Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Atupele Fredy Mwakibete (121 total)

MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naridhika sana na majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa ununuzi au uwekezaji wa hizi ndege 11 lazima uendane sambamba na mafunzo kwa wafanyakazi wake. Sasa Je, kuna juhudi gani za makusudi za kuhakikisha kwamba Serikali inasomesha wafanyakazi hao na hasa marubani, wahandisi na ma-cabin crew ili kuhakikisha kwamba hizo ndege 11 zinakuwa na wataalam wa kutosha wa kuziendesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna wafanyakazi wastaafu wengi wa ATCL wanadai stahiki zao ambazo kwa muda mrefu sana hawajalipwa. Pamoja na ukweli ya kwamba Serikali mwaka 2016 waliliridhia kuchukua deni hilo, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo hii mwaka 2022 madeni hayo hayajalipwa. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na kadhia hii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abbas Ali Mwinyi, kama ifuatavyo : -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue namna ambavyo Mheshimiwa Abbas Mwinyi kwamba yeye ni bingwa hasa kwa maana ya masuala haya ya U-pilot na ana licence aina ya ATPL. Ni kweli kwamba Serikali imewekeza sana kama ambavyo nimejibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba imewekeza zaidi ya trilioni 1.44 na kwa msingi huo Serikali imejipanga ipasavyo kusomesha wale wote ambao kwanza marubani, na hivi sasa kupitia chuo chetu cha NIT, Chuo cha Usafirishaji Serikali imetenga zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya ununuzi wa ndege ambazo zitatumika kwa ajili ya mafunzo kwa ajili ya marubani kwa kuzingatia kwamba kozi hizo zilikuwa zinatolewa nje ya nchi na kwa bei kubwa zaidi. Tunategemea kwamba ifikapo mwezi Agosti na Septemba, kozi hii itaanza kutolewa na tayari Serikali imeshatoa hizi fedha zote bilioni nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali la pili ambalo amezugumzia suala la maslahi hususan kwa wastaafu, ambao walikuwa watumishi wa kampuni hii ATCL na sasa wanadai maslahi yao. Ni kweli mwaka 2016 Serikali ilitoa commitment ya kulipa madeni hayo na mwaka 2017 kupitia CAG alihakiki hayo madeni.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2021, Wizara ya Fedha kwa mujibu wa sheria pia imehakiki hayo madeni na wanadai zaidi ya bilioni nne na sasa hatua za mwisho kwa ajili ya kuwalipa wastaafu na watumishi ambao walikuwa ATCL ipo kwenye hatua za mwisho ili waweze kulipwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimpongeze sana Naibu Waziri kwa namna anavyojibu maswali kwa umakini na umahiri mkubwa. Ingawaje leo ni siku yake ya kwanza, Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Serikali imejipangaje kuongeza ndege nyingine ili kuweza kukidhi ushindani wa soko la ndani ya nchi na nje ya nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye majibu ya awali kwamba Serikali imenunua ndege 11 na sasa imejipanga kununua ndege zingine tano, ambazo zitagharimu trilioni 1.7. Nimpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa hizi fedha na hizi ndege zitaingia ndani ya nchi mwaka 2022. Kwa hiyo tutaendelea kuboresha shirika letu la ndege nchini na ndege hizo ni ndege zile kubwa kwa maana ya moja aina ya boeing Dreamliner aina ya 787-8 ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 262. Pia ndege zingine mbili aina ya Airbus A220-300 zenye uwezo wa kubeba abiria 181 na ndege ya mizigo yenye kuweza kubeba tani 51 pamoja na ndege aina ya Dash 8400 aina ya Bombadier ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 76. Kwa hiyo, kutoka zile 11 za awali jumlisha tano ambazo tutanunua na Serikali tayari imesha-approve bajeti zitakuwa ndege 16 jumlisha na ndege moja iliyokuwepo awali kabda ya hizi ndege 11 zitakuwa ndege jumla 17. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri kwenye Serikali yetu. Je, ni lini bandari hii itaanza kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameanza kufuatilia tangu nilipoteuliwa tu, alikuja ofisini kwangu kufuatilia suala la Bandari hii ya Isaka iliyopo Mkoani Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza ni lini itaanza hasa. Changamoto kubwa ilikuwa ni kwamba bandari hii ilikuwa haina vitendea kazi. Ilikuwa haina mabehewa, hatuna injini na sasa tumekwishanunua. Nimefanya mkutano jana na Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Bandari pamoja na TRC na nimewaagiza ya kwamba ndani ya wiki hii wanipe ripoti, wafanyabiashara wote ambao wanatumia Bandari ya Dar es Salaam na wanatoka Nchi za Congo, Rwanda na Burundi wakae nao ili waone umuhimu sasa wa kutumia Bandari hii ya Isaka badala ya kuchukulia mizigo yao Dar es Salaam kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kumekuwa na mashindano makubwa sana katika bandari za majirani zetu hasa Mombasa, Kenya na Beira, Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha bandari yetu ya Dar es Salaam ili iweze kuweza kushindana na Bandari hizo za nchi za jirani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimpongeze pia Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni lango la uchumi wa nchi yetu. Sasa anataka kujua je, tuna mikakati gani ya ushindani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika sekta hii ya usafirishaji hususan bandari tuna washindani ambao ni Beira, tuna Durban pamoja na Mombasa. Hivi ninavyosema, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais awali alitoa shilingi bilioni 210 kwa ajili ya kununua vitendea kazi katika ile Bandari ya Dar es Salaam, lakini vifaa vile vilikuwa bado havitoshi na ameongeza shilingi bilioni 290 na kufanya bilioni 500 kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika Bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo vifaa hivyo kwa kuwa tayari tumeshaagiza na nina hakika kuingia Dar es Salaam tayari, pia tunatengeneza njia za reli kwa ajili ya kwenda kuchukua mzigo na kupeleka katika Bandari hizo ambazo nimezitamka hapo kama Isaka pamoja na nchi jirani za kwenda Zambia. Kwa hiyo tunagemea kwamba ushindani utaimarika zaidi mara tu baada vifaa hivi kuja ili tuwe bora katika nchi zetu za Afrika Mashariki. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona. Swali langu litahusu TEMESA na nimeshawasilisha changamoto zake kwa Kamati husika, lakini kwa fursa hii uliyonipa naomba nimuulize Waziri swali moja dogo. Je, kutokana na ucheleweshwaji na gharama kubwa zinazotumiwa na halmashauri zetu wanapopeleka magari na mitambo mingine TEMESA.

Je, Waziri yupo tayari kuiagiza TEMESA kuruhusu halmashauri zenye karakana zake kutengeneza magari yake yenyewe, hasa inapokuwa ni matengenezo madogo madogo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hili swali la TEMESA ni kwa mujibu wa sheria kwamba magari yote ya Serikali yatengenezwe chini ya TEMESA kwa hiyo, nachukua concern yako kama ambavyo umesema ili nasi tuweze kujadili upande wa Serikali. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri au majibu ya Serikali.

Kimsingi majibu ni mazuri sana, ila uhalisia ulivyo ni kwamba, abiria anaweza kuwa na mzigo akatakiwa kulipa, lakini akiuliza alipie ofisi gani, akakosa hiyo ofisi na akatakiwa kumpa fedha mkononi mchukuzi ambaye ndiye atamlipia itakapofika saa 1.30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya nyongeza; kwanza, naomba kujua ni mzigo wenye uzito kiasi gani ambao mtu akipita nao hapo bandarini atatakiwa kulipa? (Makofi)

Pili, je, Serikali haioni umuhimu wa kupunguza au kuondoa kabisa ushuru wa wafanyabiashara wadogo wadogo wanaotoka Zanzibar kuja kuchukua biashara zao hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukurani za Mbunge kwa niaba ya Serikali. Pili, naomba kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza amezungumzia suala la uzito; anataka kufahamu ni uzito kiasi gani ambao anastahili ama anapaswa kulipa anapopita pale bandarini? Ieleweke kwamba Mamlaka yetu ya Bandari nchini inaongozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2004 na miongozo mbalimbali ikiwepo Mwongozo wa Mwaka, 2003 na Aya ya 12(1) na aya ya 71(1). Miongozo hii inatuelekeza kwamba mzigo wa abiria yeyote anayetoka Bara ama kwenda Visiwani au Visiwani kuja Bara inatakiwa atozwe ukiwa hauzidi kilogram 21. Hilo la kwanza kupitia Mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, inaelekeza kwamba inatakiwa ujazo wa huo mzigo kwa maana ya cubic measurements usizidi moja, kwa maana ya ujazo wake ama nafasi inayochukua huo mzigo wako ni kiasi gani? Kuhusu wafanyabiashara wadogo kupunguziwa gharama pale bandarini; nataka nimhakikishie Mbunge ya kwamba kama wewe una bidhaa, kwa mfano, una baiskeli au TV ya matumizi yako binafsi, haitakiwi utozwe ushuru pale bandarini. Ila kama una zaidi ya hivyo, hii sheria itatuhusu sote. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, tunajua bandari yetu ni miongoni mwa chanzo cha mapato, na kumeibuka kuwepo kwa bandari bubu zaidi ya 58 katika Mikoa mbalimbali ambapo Serikali yetu inakosa mapato. Naibu Waziri ulikuwa Mwenyekiti wa Kamati na huu ni mfupa mzito ambapo mapato ya Serikali yanapotea.

Je, ni lini sasa mchakato wa kuangalia hizi bandari zote kama walivyokuwa wameahidi walipokuja kwenye kamati. Ni lini sasa mtazirasimisha rasmi ikiwemo na badari ya Mbweni ili Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha na kupeleka maendeleo kwa Watanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue Mheshimiwa Ester Bulaya kama ulivyosema nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma changamoto hizi tuliziona na hivi sasa kati ya bandari zote nchini tuna bandari 693 nchi nzima ya Tanzania ambazo ni bandari bubu. Na tunazo bandari 66 tu ambazo ni rasmi. Bandari ya Mbweni ambayo ni miongoni mwa bandari 24 ambazo tutakwenda kuzirasimisha hivi sasa ninavyosema.

Mheshimiwa Spika, badari hizi zinaingiza fedha kwa mwaka shilingi milioni 200 kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana wa kurasimisha bandari bubu ambazo zinaingiza fedha Serikalini. Nitoe wito pia kwa kuwa siyo kila sehemu tutaajiri kama TPA kwa maana tutashirikiana na halmashauri husika katika maeneo hayo ili hizo bandari ziewe kurasimishwa. Ahsante.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaleta matumaini kwa wananchi wa Singida kwa kufufua reli hii ya Singida – Manyoni. Pamoja na majibu hayo, ninayo maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kupata commitment ya Serikali, nataka kujua ni fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa lengo la reli hii lilikuwa ni kukuza uchumi, kubeba mizigo ambayo ipo katika ukanda huu na hasa ililenga sana wakati huo Mwalimu Nyerere akianzisha reli hii ni kubeba ngano ambayo iko kule Basutu katika Mkoa wa Manyara. Sasa kwa sababu tunakuza eneo la kilimo na tuna madini yako pale kwenye Mkoa wa Singida, ni mpango gani wa Serikali sasa kuujenga kwa kiwango cha SGR ili iwe na uwezo mkubwa wa kubeba mizigo katika eneo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2022/2023, tumetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.45 kwa ajili ya ukarabati wa tuta pamoja na makalavati na uwekaji wa tabaka la kokoto na tutajenga kama ambavyo tuliboresha reli ya kutoka Tanga kwenda Arusha kupitia Moshi kwa maana ya kutumia force account.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anapenda kujua ni lini sasa hii reli itakuwa katika kiwango cha standard gauge? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa jitihada zake pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine wa Mkoa wa Singida, Serikali mara baada ya kufanya ukarabati huu wa awali, tukifungua malango/tukifungua njia, ndipo tutakapoanza sasa kufanya tathmini, feasibility study kwa ajili ya SGR. Ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, ni lini treni ya mwendokasi itaanza kufanya kazi kati ya Dar es Salaam na Morogoro? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, matarajio yetu yalikuwa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro yenye urefu wa kilometa 300 tulitegemea ingeanza mwezi huu wa Septemba kama ambavyo tulijibu hapo awali wakati wa Bunge la Bajeti. Lakini kutokana na changamoto mbalimbali hususan katika kusafirisha vipuri na mabehewa ambayo kulikuwa kuna changamoto ya kupata meli ya usafirishaji kutoka nchini Ujerumani kuja Tanzania, lakini habari njema kwa Watanzania wote watambue ya kwamba tayari vichwa vya treni, mabehewa ya abiria na mizigo, hivi ninavyosema vimekwishapakiwa kwenye meli kuja nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunataraji kwamba ifikapo mwezi Novemba, mwaka huu vitakuwa vimeshaingia na tutafanya majaribio mpaka mwezi Januari. Kwa hiyo, mwezi Februari mwakani standard gauge kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro itaanza rasmi, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami niulize maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Serikali kwa hatua ya awali ya kutenga fedha, lakini sote tunajua; kutenga ni jambo moja na kutekeleza mpaka ujenzi ukamilike na meli ianze kutumika ni jambo lingine: Nataka kujua ni lini ujenzi wa meli hizo utakamilika na kuanza kutumika kwenye Ziwa Tanganyika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imewekeza fedha kujenga Bandari ya Kasanga, Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kipili, Bandari ya Kigoma pamoja na Karema, lakini hatuna usafiri wa uhakika wa Ziwa Tanganyika wa kubeba mizigo pamoja na mazao ambayo yanazalishwa kwenye hii mikoa mitatu. Nataka kujua kwa sababu huu muda ni mrefu wa kutengeneza hizo meli: Mna mpango wowote wa dharura wa kutuletea usafiri ili kuepusha tatizo la kila siku kupoteza maisha ya Watanzania kwa sababu ya kutumia maboti?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala usafiri ndani ya Ziwa Tanganyika. Nami nimeshuhudia nilikwenda kule, kuna changamoto kubwa hiyo. Nataka nimhakikishie Mbunge na Wabunge wote wa mikoa yote mitatu; Mkoa wa Rukwa, Katavi pamoja na Kigoma, suala la kukamilika, kwanza kama ambavyo nimesema kwenye jibu langu la msingi, tumeshatangaza tenda tarehe 19 ya mwezi huu wa Tisa, tunategemea zitafunguliwa tarehe 2 Novemba na tayari Mheshimiwa Waziri wangu, Profesa Mbarawa alishakwenda kule kuonesha hata sehemu ya kujenga chelezo kwa kampuni ambazo zimeonesha kwamba zina nia ya kwenda kutengeneza ama kujenga hizi meli mpya mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, kwamba ni namna gani tunaweza kama Serikali tukafanya jambo la dharura kwa ajili ya wananchi wa mikoa hii yote mitatu; kwanza, tumejipanga katika kukarabati meli zote mbili. Kuna meli ya Liemba pamoja na Mv Mwongozo. Tenda ya Mv Liemba, inatangazwa tarehe 26 ya mwezi huu na tunategemea kwamba itachukua muda wa mwaka mmoja. Kwa Mv Mwongozo ambayo inabeba abiria 500 na tani 150 yenyewe itachukua muda wa miezi sita. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu kwamba ifikapo mwakani mwezi wa Kumi mwaka 2023 meli hizi za dharura zitakuwa zimeanza kufanya kazi ndani ya Ziwa Tanganyika. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nilitaka kujua, ni lini meli ya MV. Kaliasi itaanza tena safari zake kutoka Bandari ya Mwanza, Kwenda Bandari ya Nansio Visiwani Ukerewe? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna meli katika Ziwa Victoria ambayo ilipata shida katika mifumo yake ya kuongozea meli, na tulishaagiza kifaa hicho nje ya nchi; na ndani ya mwezi wa Kumi mwanzoni tunategemea kitakuja, kinaitwa mouse controller. Kwa hiyo, mwishoni mwa mwezi wa Kumi meli hii itaanza kufanya kazi zake ndani ya Ziwa Victoria. Ahsante sana.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza sana Serikali kwa kupokea ushauri na kuanza kuufanyia kazi, lakini naipongeza kwa kununua ndege za mizigo. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali imekubali kupokea ushauri, je, Serikali iko tayari kutangaza Uwanja wa Kimataifa wa KIA kuwa uwanja wa kimkakati wa kusafirisha mazao ya kilimo na mifugo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari Serikali imeshatenga fedha na utaratibu wa kuanza kujenga common use facility ndani ya Jimbo la Hai. Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kujenga kiwanda cha kutengeneza maboksi kwa ajili ya kusafirishia bidhaa zinazotokana na mifugo na kilimo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Saasisha Elinikiyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la ndege za mizigo. Katika maswali yake mawili ya kwanza anasema je, Serikali tuko tayari kutangaza uwanja huu kuwa ni wa kimkakati. Sisi Serikali kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri tunatangaza rasmi uwanja wa KIA kuwa ni uwanja wa kimkakati kwa mazao, hususan maua, matunda, mboga mboga pamoja na nyama pamoja na viwanja vingine kama cha Songwe International Airport kilichopo Mkoani Mbeya pamoja na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anataka kufahamu ni kwa namna gani tunaweza tukashirikiana pia na wenzetu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika kukuza eneo hili na kujenga viwanda vidogo.

Mheshimiwa Spika, uwanja wa KIA tayari tumeshatenga hekari ama hekta 711 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogovidogo, lakini pia kwa kushirikiana na wawekezaji na tayari tumeshaanza kufanya hiyo hatua. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imejipanga kupanua bandari za Mwanza na Bandari zile za Nansio; je, Serikali imechukua hatua gani za haraka kuhakikisha wanakamilisha hizo bandari ili ziweze kuwasaidia wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema na tayari ilishaanza kufanya kazi; je, ni lini Serikali itaanza kuleta meli kwenye eneo la Bandari ya Karema, meli za kimataifa na meli za ndani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikipanga fedha katika bajeti mbalimbali hususan kupitia TPA kwa bandari hizi za Mwanza, Nansio, Mwanza Kusini na Mwanza Kaskazini. Na hivi navyosema Bandari ya Nansio tayari tumeshafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja a Bandari za Bukoba pamoja na Kemondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusiana na meli za Kwenda kwenye bandari yetu ambayo imezinduliwa hivi karibuni na hususan katika Ziwa Tanganyika, tunataraji hivi karibuni tutafanya mkutano na washirika ambao ni wadau muhimu katika usafirishaji wa bandari za Ziwa Tanganyika kutoka Congo, Zambia, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo hivi karibuni utaanza kuona meli zikienda katika bandari hiyo mpya ya Kalema. Ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bandari ya Nansio ina hali mbaya na inaweza kuleta matatizo muda wowote, Mheshimiwa Waziri uko tayari baada ya Bunge hili utembelee Jimbo la Ukerewe ili uone umuhimu wa kuharakisha matengenezo ya bandari ile ya Nansio? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari mara baada ya Bunge wiki ijayo tutembelee bandari hii ya Nansio na kujionea; na nitaambatana na wataalam ili washauri vizuri zaidi. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ningependa kufahamu, ni lini Serikali inatarajia kujenga vituo vya kupumzikia abiria na mageti ya kushushia abiria kwenye vituo vya Kilondo, Lupingu na Manda?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ziwa Nyasa tumeshafanya upembuzi yakinifu katika Bandari za Nyasa pamoja na Mbamba Bay. Kwa hiyo katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga katika maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwanza kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Katosho wamepisha eneo la ujenzi wa bandari ya nchi kavu kwa zaidi ya miaka sita sasa na majibu haya ya usanifu yamekuwa yakitolewa kwa zaidi ya miaka sita na kuwaumiza sana wananchi: Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuharakisha huu upembuzi yakinifu ili eneo hilo lifanyiwe kazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili bandari ya nchi kavu iweze kuwa na tija kwa Taifa lazima kuwe kuna miundombinu wezeshi ikiwemo uwepo wa reli, uwepo wa meli, uwepo wa mabehewa ya kutosha na barabara za uhakika. Ukizingatia Mkoa wa Kigoma bado tuko nyuma sana kimiundombinu: -

Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kuhakikisha miundombinu wezeshi inatekelezeka ili bandari hii iwe na tija?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba bandari hii imechukua muda mrefu, lakini tangu mwaka 2019 tulijenga uzio ama ukuta wa eneo hili. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Kigoma kwamba ifikapo Aprili mwakani 2023 upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unakwenda kukamilika na tayari tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bandari hii.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili angependa kufahamu miundombinu wezeshi katika kufanikisha bandari yetu kavu na miundombinu hiyo wezeshi ni pamoja na reli, barabara na kupata mzigo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, bandari hii kavu tayari ipo karibu kabisa na bandari nyingine ya Kigoma, pia ipo karibu kabisa na barabara kuu inayokwenda Kigoma Mjini. Pia tumewaelekeza mamlaka ya bandari nchini pamoja na TRC, wapo kwenye majadiliano kwa ajili ya kupeleka reli ili iwe rahisi kupeleka mzigo utakaokuwa unahudumiwa na nchi rafiki na nchi jirani kati ya Congo, Rwanda, Burundi pamoja na Zambia. Ahsante.
MHE. HASSAN HAJI KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Hata hivyo, kwa kuwa utaratibu uliokuwepo sasa hivi, wa abiria ambao wanasafiri wanasubiria sana nje kabla ya kuingia ndani. Je, ni lini Serikali hii itatoa maelekezo ya wale abiria ambao tayari wana tiketi, wasisimame pale nje, waingie ndani moja kwa moja na kusubiria usafiri ndani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo ama jengo lilipo la kusubiria abiria pale Dar es Salaam Kwenda Zanzibar lina uwezo wa kubeba abiria 150 na jengo ambalo tutajenga litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 400.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hatua ambayo Serikali inachukua tunaweza ratiba maalum, mahususi kwa boti zote mbili ambapo boti ya kwanza kama ambavyo iko inaondoka saa moja asubuhi, boti ya pili itaondoka saa tatu na nusu, boti ya tatu itaondoka saa sita, nyingine saa nane mpaka saa kumi na mbili. Kwa abiria wote ambao wanakuwa nje na wana tiketi, hawa ndio wanatakiwa waingie kwenye jengo hili ili kuruhusu wasafiri kuliko mwingine yeyote kwa sababu eneo lile bado ni dogo. Kwa hiyo, ni maelekezo kwa Serikali kwa abiria wote, lakini pia wale wote wanaosimamia eneo hili.
MHE. ASIA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Changamoto hii ambayo inaonekana kwa abiria wetu kwa upande wa Dar es Salaam hali kadhalika changamoto hii imejitokeza sana kwa upande wa Zanzibar. Je, Serikali ina mpango gani wa upanuzi wa Bandari ya Zanzibar ama kuijenga bandari mpya ili kupunguza changamoto hii kwa abira wetu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa suala la Bandari ya Zanzibar ni suala ambalo lipo kwenye Wizara ya Wenzetu kule, tutawasiliana nao ili tuone namna gani ya kupanua ujenzi wa Bandari hii ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na bora kabisa ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sisi tayari tunalo eneo letu la kibiashara: Je, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha juu ya uwezo wa ufanisi na uwezo wa mtaji wa Kampuni ya DP World ili kuja kuongeza soko katika bandari zetu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha uwezo wa kuweza kuongeza ushindani kwa kuwa tayari tunazo Bandari za Beira (Msumbiji), Mombasa (Kenya), na Durban (South Africa) ambazo tunashindana nazo? Mmepima uwezo wa DP World kuja kuongeza ushindani katika eneo hili la ukanda wa SADC na ukanda wa Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali pasi na shaka imejiridhisha kwamba DP World Port ina uwezo wa kuendesha bandari zetu nchini hususan Bandari yetu ya Dar es Salaam. Tumejiridhisha kwa maana ya kwamba, kwanza, inafanya kazi katika mataifa yasiyopungua 69 duniani, na pia wataalamu wetu wametembelea mataifa hayo ikiwemo Uingereza, Canada, India, Dubai kwenyewe na mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, vile vile Bandari hii ya Dar es Salaam hivi sasa inapata wateja wake kwa njia ya mfanyabiashara kuleta meli yake, lakini kupitia DP World, wao wana connection, au mtandao mpana wa kibiashara huko duniani, kwa hiyo, watatutafutia masoko. Zaidi ya yote, wamejenga bandari kavu katika nchi ambazo tunahudumia kama Taifa hususan kule Congo pamoja na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujiridhisha kuhusu ushindani na uwekezaji ambao atafanya DP World. Ni kweli kwamba ushindani katika bandari zetu ni mkubwa hususan katika ukanda wetu wa Bahari ya Hindi. Tuna Mombasa, ni washindani wetu; tuna Beira (Msumbiji), pamoja na Durban (Afrika Kusini). Kupitia DP World, Bandari ya Dar es Salaam, itaongeza ufanisi kwa ushindani kwa sababu kwanza ataleta vifaa na vyombo vya kisasa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mifumo ambayo tumekuwa tukizungumza miaka mingi katika Bandari yetu ya Dar es Salaam ili taasisi zionane kupitia mifumo ya electronic single window system, pia itawekezwa na itakuwa automated ili kuongeza ufanisi. Sasa hivi ukienda bandarini utakuta meli ni nyingi lakini muda wa kupakua na kushusha mizigo ni mrefu. Hili ndilo tunataka sasa tuongeze ufanisi kwa kupunguza huo muda ili Bandari yetu ya Dar es Salaam iendane na ushindani wa bandari hizi nyingine ambazo nimezitamka.

Mheshimiwa Spika, tunakushukuru. (Makofi)
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Usalama wa vyombo vya majini ni lazima kwa maisha ya watu na mali zao. Je, Serikali inafanyaje kila baada ya muda kuvifanyia ukarabati kisheria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba usalama ni jambo la msingi na ni lazima lifanyike. Kwa sheria yetu tunafanya ukaguzi kila mwaka kwa vyombo vyote vya majini na kwenye maziwa makuu, na huwa tunatoa cheti kinachoitwa seaworthiness certificate. Hata hivyo, hatulazimiki tu kwa mwaka, tunaweza tukafanya pia kwa wakati wowote inapobidi shirika lijiridhishe na vyombo hivyo. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Je Serikali haioni umuhimu wa kuwaelimisha watumiaji wa bandari ikiwemo ya Kemondo na Mwanza juu ya Sheria za Tozo zinazo zinazotungwa kuliko kukutana nazo barabani? (Makofi)

Swali langu la pili je, ni aina gani za tozo? Napenda kujua hilo, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutoza tozo ama kutunga Sheria za Tozo kwanza unaanzishwa na Mamlaka ya Bandari yenyewe TPA na hatimaye unapelekwa kwa mdhibiti ambaye ndiye TASAC na TASAC ana wajibu wa kuitisha wadau wote wa sekta hiyo ama maeneo ambako hiyo tozo itakuwa inagusa katika tozo.

Sasa ninamuelekeza ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini pamoja na TASAC watoe elimu, waende katika hizi bandari za Kemondo pamoja na bandari zingine nchini kwenda kutoa elimu kwa jamii ili waeleze ni aina gani ya tozo wakienda bandarini watakutana nazo na kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili anataka Mheshimiwa Mbunge afahamu aina ya tozo ambazo bandari inatoza; tuna tozo ya aina nyingi, lakini zimegawanyika katika makundi mbalimbali; kuna tozo za lazima ambazo tunaita ni ports statutory charges, lakini kuna tozo tunazoziita wharfage, wharfage ni aina ya tozo ambayo ukitumia miundombinu ya bandari unatozwa, lakini kuna tozo za show handling hizi ni tozo ambazo meli inapokuja mpaka kwenye gati la bandari inapokuwa inashusha mzigo ama kupakia mzigo pia unatoza na kuna tozo za ziada, ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; ni lini Serikali itaweza kupitia upya tozo hizi ambazo zimekuwa nyingi bandarini na kuleta uwekezaji kutochochewa kuhusiana na hizi tozo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bahati Ndingo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunauchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kimsingi tumeshaanza kukaa na wadau na mamlaka ambazo zinahusika kwa maana ya Tanzania ni TASAC, lakini kwa wenzetu Zanzibar ni ZMA ambako zina mahusiano ya moja kwa moja na vikao hivyo vinaendelea, na wewe Mheshimiwa Mbunge ukipata nafasi tutakukaribisha kama mdau ili utoe maoni ya Waheshimiwa wengine, ahsante.
MHE.KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa hatua ambayo inachukua, hata hivyo ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, uzoefu unaonyesha kwamba wanaponunua mabehewa mapya wanayapeleka katika route nyingine na route hizo mabehewa yaliyochakaa huko ndiyo wanayaunga kwenye route ya Kigoma. Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba mabehewa haya 22 mapya yatakayokuja yatawekwa kwenye route hii?

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa sababu mabehewa yanayokarabatiwa ni 39 na mapya ni 22 jumla ni mabehewa 59 na bado ni machache na ukizingatia kwamba Serikali ina mkakati wa kuhama kutoka kwenye narrow gauge kwenda standard gauge; je, Wizara ina mpango wa kukarabati mabehewa zaidi ili yaweze kutumika badala ya kununua mapya ambayo tukianza standard gauge tutayaacha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shaban Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka kujua commitment ya Serikali kwamba mabehewa hayo 22 mapya je, yatakwenda Kigoma. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mabehewa haya 22 yenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 14.9 yatakwenda Kigoma na namwalika siku yatakapofika nchini Septemba mwaka huu awe sehemu ya kuyapokea haya mabehewa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema reli inayotengenezwa ni ya standard gauge na tuliyonayo ni ya meter gauge tunaonaje kwamba hizi reli ziweze kufanya kazi kwa pamoja, lakini pili ziendane na uhitaji wa mabehewa tuliyonayo. Turn worksheet ya Mheshimiwa Mbunge kwamba reli ya sasa ya meter gauge ina meter moja na standard gauge ina meter 1.475 kwa namna yoyote ile reli tuliyonayo tutaendelea kuitumia hadi hapo itakapokuja kukamilika ya standard gauge. Hata ikikamilika, lakini bado hii pia tutaendelea kuitumia. Kwa maana hiyo bado tutaendelea kukarabati mabehewa tuliyonayo kwa sababu tender ya kutangaza kutoka Tabora kwenda Kigoma ili ijengwe standard gauge bado itachukua muda. Kwa hiyo bado tutaendelea kutumia ya meter gauge. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Reli ya Kaliua – Mpanda ni mbovu na ndiyo maana inasababisha mabehewa nayo kuwa mabovu Serikali inasema nini katika hili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli reli ya kutoka Kaliua – Mpanda ina changamoto, lakini kama Serikali kupitia shirika letu la reli nchini kila mwaka tumekuwa tukitenga fedha kwa ajili ya kukarabati reli hii. Pia habari njema ni kwamba Mheshimiwa Rais ameridhia kwamba kitangazwe kipande hiki cha Kaliua - Mpanda mpaka Karemi ili kiwe standard gauge. (Makofi)
MHE. DEOGRATIUS P. MWANYIKA : Mheshimiwa Naibu spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na uwekezaji anaouongelea wa bilioni 13 changamoto kubwa ya reli ya TAZARA ni kwamba hata ukiwekeza hizo fedha, uendeshaji kibiashara ni tatizo. Sasa Serikali ina mpango gani wa muda mfupi ili reli hii iendeshwe kibiashara iondoe maroli mengi ambayo yako barabarani badala ya kutumia mzigo uende kwa treni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tuliambiwa hapa na kulikuwa na ushauri wa Kamati ya Bajeti, kwamba mkataba wa uwekezaji wa Reli ya TAZARA ndilo moja ya tatizo kubwa sana linalotufanya tusiweze kuitengeneza reli hii vizuri. Sasa swali, Serikali ina mpango gani na imechukua hatua gani mpaka muda huu kurekebisha mkataba huo au kuu-terminate kabisa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa ujenzi na uchukuzi napenda kujibu Maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanyika kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la Reli ya TAZARA, pamoja na Wabunge wote wa Nyanda za Juu Kusini wamekuwa kila mara wakifuatilia jambo hili. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini, mpango wa muda mfupi ndio huo ambao tumetenga fedha kiasi cha Shilingi bilioni 13.1 na tutafanya manunuzi ambayo nimejibu kwenye jibu langu la Msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mkataba, mkataba ama Sheria Namba 4 ya mwaka 1995 ya TAZARA ndiyo ambayo inakwamisha tusiendelee hasa katika uwekekezaji kama nchi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zambia walipokutana walielekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tukutane na wenzetu wa Zambia. Mikutano hii imefanyika mwezi uliopita tarehe 14/10/2022 mpaka tarehe 15/11/2022 na mimi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri nilimwakilisha Lusaka Zambia kwa ajili ya kujadili Sheria hii. Mwishoni mwa Desemba tutakutana tena ili tuihuishe halafu baadae tutaileta kwenye Mabunge yote mawili ya nchi ya zambia pamoja na nchi ya Tanzania ili sasa kila nchi ipate fursa ya kuwekeza upande wake.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nilikuwa naulizia iwapo Serikali inaweza kuthibitisha au inaweza kutuhakikishia kwamba huyu mbwa kwa namna walivyom-train hataweza kupata hicho kichaa cha mbwa, ahsante. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo hili ambapo kuna meli kubwa za mzigo zinazotoka huku Bara kwenda Zanzibar na kwenda Comoro hususan eneo la Azam Sealink na Lighter Key linahitaji kufungwa mzani mkubwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayokwenda na inayoingia pia Dar es Salaam. Serikali ilikwisha tangaza tenda tangu mwaka jana mwezi wa kumi na bahati mbaya hakuna aliyeweza kukidhi vigezo vya tenda hiyo kwa maana ya scanner ama mdaki ambao tunahitaji kama Serikali. Maana tunahitaji scanner iwe kubwa na kwa maana hiyo sasa, tutatangaza tenda upya tarehe 3 ya mwezi wa pili tuweze kufunga midaki miwili katika eneo hili la Azam Sealink na Lighter Key kwa ajili ya meli kubwa za mizigo zinazokwenda Zanzibar pamoja na Visiwa vya Comoro, ahsante.. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nampongeza kwa jibu lake zuri ambalo linaridhisha. Swali langu la kwanza; kwa kuwa deni hilo la wastaafu lilirithiwa kabla ya mpango maalum wa kufufua ATCL, nilitaka kujua sasa hivi Serikali ina mpango gani wa kuzuia kuzalisha madeni mengine mapya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imejikita zaidi katika kutoa mafunzo mbalimbali katika vyuo vyake ikiwepo Chuo cha Usafirishaji, nilitaka kujua hadi sasa tuna marubani wangapi wazalendo ambao wako katika ndege zetu za ATCL? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami niweze kujibu maswali mawili ya nyongeza, ya Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala haya ya ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua mpango wa kuzuia madeni mapya baada ya kuanza mpango ule wa ufufuaji wa kampuni hii yetu ya ndege nchini. Serikali imejipanga kuzuia ama kutozalisha madeni mengine. Hadi sasa tangu mwaka 2016 tumekuwa tukilipa wafanyakazi wote na hakuna deni jipya; lakini kwenye mwaka wa fedha huu 2022/2023 ambao tunaendelea nao tumetenga takribani kiasi cha shilingi bilioni 10 ili kulipa wafanyakazi wote waliokuwa wa ATCL kama deni la nyuma.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua idadi ya marubani tulio nao hapa nchini hususan wanawake na wanaume. Tuna takribani ya marubani 106. Kati ya hao marubani 11 ni wanawake na marubani 95 ni wanaume; kwa maana ya kwamba hawa wanawake wanarusha ndege zote kwa sababu hapa nchini tuna ndege aina tatu ambapo tuna Dash 8Q400, Bombardier al maarufu Bombadier ama sasa hivi inaitwa DeHaveland lakini pia tuna Airbus 220-300 ambapo pia wanawake wanarusha na tuna Boeing 787-8 ambayo pia wanawake wanarusha hizi ndege. Na kati ya hao 106. 105 wote ni watanzania, ni mmoja tu ambaye sio Mtanzania.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru sana majibu ya Serikali, lakini sisi humu sote ndani wote ni watu wenye ulemavu watarajiwa na lazima tukiri kwamba mtu mwenye ulemavu hawezi kutoka point A kwenda point B kwa kutumia vyombo vya usafiri kwa sababu miundombinu haikidhi haja kabisa na katika jibu la Waziri amesema kwamba kuna TBS kuna LATRA ambao wanatakiwa kuangalia hivyo viwango;

Je, ni ipi sasa kauli ya Serikali kutoka na hili jambo ili watu wenye ulemavu na wenyewe wapatiwe haki ya msingi ya kupanda haya mabasi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, watu wenye ulemavu wamekuwa wakinyanyapaliwa sana katika vituo vya mabasi na madaladala wakati wa kuingia katika hivi vyombo, kwa sababu kuna watu wasioona kuna watu ambao hawawezi kutembea unaona kwamba wanapata manyanyaso makubwa sana.

Je, ni utaratibu gani mzuri sasa ambao umewekwa kuhakikisha kwamba hawanyanyaswi na wanawekewa mpango mzuri wa kupanda katika hivi vyombo vya usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa balozi mwema wa watu wenye ulemavu. Kwa swali la kwanza anataka asikie kauli ya Serikali, kauli ya Serikali ni hii; kwanza natoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya usafiri, daladala pamoja na mabasi na kwa kushirikiana na LATRA pamoja na TBS wahakikishe ya kwamba wanaweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu hususan katika maeneo ya stendi ama mabasi, hili tunatoa onyo kali sana kwa sababu watu wenye ulemavu ni binadamu kama binadamu mwingine yeyote na ahaki zote za msingi. Kwa maana hiyo, kupitia vyombo vyetu vya sheria na kupitia Jeshi la Polisi pamoja na TARURA pamoja na TANROADS kuhakikisha kwamba miundombinu yote wezeshi hususan barabara pamoja na mabasi kwa maana ya vyombo vya usafiri kwa wale wamiliki tunaweza kuhakikisha hivyo vinawekwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nisisitize hapa suala la kisheria kwa mtu yeyote atakayeonewa, tutahakikisha tunachukua sheria kali sana na itakuwa fundisho kwa watu wengine wote wanaonyanyapaa na kuwanyasa watu wenye ulemavu.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, inaonesha kwamba Serikali huenda haifahamu vizuri barabara hii.

Mheshimiwa Spika, barabara hii inahudumia kata 18 za Bukoba, inahudumia wilaya mbili; Wilaya ya Bukoba na Wilaya ya Misenyi, inahudumia nchi mbili; inaziunganisha Tanzania na Uganda na vita ya mwaka 1978 ya Iddi Amini ilipiganwa kwa kutumia barabara hii.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kwenda Bukoba kuangalia barabara hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara hiyo kuna Daraja la Kalebe, daraja kubwa ambalo ni la zamani sana, ni bovu, linaruhusiwa uzito wa tani saba, lakini kwa vile hakuna ulinzi wala kizuizi wanapita magari ya tani 15 mpaka 20.

Je, tunasubiri watu wafe pale ndio mtengeneze daraja hilo na barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rwekiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri Mheshimiwa Mbunge amekuja mara kadhaa Wizarani akifatilia ujenzi wa barabara hii pamoja na daraja lake. Kwa niaba ya Serikali napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ya kwamba nipo tayari kuongozana naye kwenda jimboni Bukoba Vijijini ili nikashuhudie na kuona barabara hii pamoja na daraja hili mara baada ya vikao hivi vya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili suala la Daraja la Kalebe ni sehemu ya barabara hii ya kutoka Kyatema- Kanazi, Bwela, Katoro – Kyaka; na kwa maana hiyo kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekwishakamilika na mwaka ujao wa fedha tumeweka mapendekezo kwamba barabara hii na daraja hili vijengwe.

Kwa hiyo, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikifika aipitishe ili pia daraja tuweze kulijenga, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuiuliza Wizara, wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanataka kujua ni lini barabara ya njia nne itaanza kujengwa ambayo ilisaidiwa kwamba kuanzia Uyole mpaka Mbalizi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua umuhimu wa barabara hii ya Mbeya mpaka Tunduma na tayari Serikali ilikwishaitangaza na mkandarasi amepatikana na tunachosubiri na hata kwa maelekezo yako ni kwamba hivi karibuni hususan ndani ya mwezi huu wa pili tutasaini mkataba ili barabara hii ianze kujengwa kwa njia nne kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoahidi alivyotembelea Mkoa wa Mbeya, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali ambayo pamoja na kwamba hayatoi matumaini ya karibuni, lakini napenda nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali kwamba barabara hii iko chini ya TANROADS kwa matengenezo ambayo yanaendelea inawezesha walau kupitika na barabara hii ni shortcut kwa ajili ya kutoka Magila – Turiani – Mziha - Handeni - Mziha, Kibindu -Mbwewe kwenda Mikoa ya Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali yangu kama yafuatavyo; je, Serikali ipo tayari kuielekeza TANROADS katika matengenezo yanayoendelea kutenga pesa kwa ajili ya matengenezo ya mifereji, kwa sababu eneo hili lina mvua nyingi ili barabara hii iendelee kupitika na kwa kuwa kuna vyakula vingi katika eneo hilo ili uweze kufika sokoni?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Serikali imepanga mpango mzuri wa kuendelea na upanuzi wa ujenzi wa njia sita kutoka Kibaha mpaka Chalinze na ilishafanya tathmini; je, Serikali inasemaje ina mpango gani juu ya fidia kwa maeneo ambayo barabara hiyo itapita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii kwanza ina umuhimu mkubwa sana kwa mikoa hii yote miwili ya Morogoro pamoja na Pwani, na katika mwaka huu wa fedha ili iweze kupitika tumetenga fedha takribani kiasi cha shilingi milioni 346.981 na wakandarasi wawili wapo site.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba suala la ujenzi wa mifereji pia tutajenga kwa kuwa tayari wakandarasi wako site ni sehemu ya scope ya kazi tuliyompatia mkandarasi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa ajili ya barabara kutoka Kibaha – Chalinze kuja Morogoro kwa ajili ya fidia, tayari barabara hii wizara imekusudia tutafanya kwa mfumo wa EPC+Finance, lakini sasa tumebadilisha kwa tutafanya kwa njia ya Public Private Partnership (PPP). Tayari mtaalam mwelekezi Kampuni kutoka Korea ya Kusini yupo site na tunategemea tutakabidhi kazi hii kati ya mwezi wa tatu ama wa nne na kupitia ripoti atakayoleta kwa ajili ya fidia na gharama zote, Serikali itatumia hiyo ripoti kwa ajili ya kulipa wale wote watakaokuwa wameathirika na barabara hii, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Zanzibar inatembelewa na watalii wengi sana kwa kipindi cha mwaka mzima na wengi wanatamani kuja Bagamoyo kuja kuangalia vivutio vilivyopo pamoja na kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Saadan, lakini kikwazo kikubwa wanachokipata ni sehemu ya kupaki boti kwa ajili ya kushuka ili waweze kufanya utalii. Je, Serikali ina mpango gani kuliingiza suala hili katika bajeti ya mwaka ujao ili kuunga mkono juhudi za Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan katika suala zima la Royal Tour?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa shughuli nyingi sana za usafiri kati ya Bagamoyo na Zanzibar za mizigo pamoja na abiria zinafanyika kwa boti za kawaida na majahazi ya kawaida. Je Waziri yuko tayari kutembelea Bagamoyo ili aone shughuli zinazoendelea pale ili alitilie umuhimu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo.

Sasa napenda kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka kujua nini committent ya Serikali katika bajeti ijayo kwa ajili ya ujenzi wa haya magati. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa na mpango kabambe wa kuainisha bandari zote nchini ikiwemo na Bandari ya Bagamoyo katika ujenzi wa hizi gati na nimhakikishie kwamba tayari kwenye mwaka wa fedha ujao, ambako tutasoma bajeti yetu, tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga gati katika Bandari hii ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, kwa mwaka huu wa fedha ambao unaendelea, tayari tumetenga kiasi cha Shilingi milioni 68 kwa kushirikiana na wenzetu wa Maliasili na Utalii ambapo tumeweka front dock yard kwa ajili ya kupokea majahazi, lakini pamoja na boti kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua ama anaomba nitembelee Bandari ya Bagamoyo na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na yeye mara baada ya Bunge la Bajeti, nitafika Bandari ya Bagamoyo kujiridhisha. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kumekuwa na mrundikano sana wa abiria katika stesheni ya Tabora Mjini na Stesheni zinazofuata za Goweko, Tula na Malongwe wakienda pale wanakosa tiketi au tatizo la mfumo. Je, Serikali haioni haja ya kuongeza mabehewa ili wananchi wanapokwenda kupata huduma hiyo waweze kupata huduma na seat ili waweze kusafiri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na changamoto ya mfumo wakienda pale mfumo ukiwa chini hawawezi kupata tiketi na wakipanda kwenye treni wanapigwa faini asilimia 100. Je, Serikali haioni haja ya kuboresha hii mifumo ili abiria akienda pale asipate usumbufu wa kupata tiketi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igagula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala haya ya mifumo pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Tabora. Hata hivyo ameomba suala zima la kuongezewa mabehewa ili kuweza kuwa na route nyingi katika kusafirisha wananchi ama abiria kutoka Tabora mpaka Dar es Salaam, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari alishatoa idhini na tulishasaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa mengine mapya 22 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 14, lakini pamoja na hilo tutakarabati behewa 37 ili kuongeza safari za kutoka Tabora kuja Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema changamoto za mfumo; ni kweli wakati mwingine kunakuwa kuna changamoto za mfumo kwa sababu ya internet. Nilishatoa maelekezo kwa uongozi wa TRC kwamba sasa wafikiri nje ya mfumo huu ili watumie mfumo unaoitwa USSD kwa maana ni Unstructured Supplementary Service Data ili kuweza kupatikana mfumo wakati wote, lakini hata hivyo mfumo tulionao unaruhusu kufanyakazi kwa njia ya offline mode.

Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo na maagizo kwa Ma- TT pamoja na wote wanaohusika na masuala ya booking clerk kwamba wahakikishe tiketi zinapatikana hata kama mfumo haupatikani kwa sababu unaruhusu mfumo wa offline mode.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa mradi huu upo katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Je, Serikali inaweza kuona kuwa kuna haja sasa ya kuharakisha upatikanaji wa huyo Mwekezaji. Pia kufanya mazungumzo makini ili mradi huo uweze kuanza kwa haraka kwa muda uliokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuharakisha mazungumzo ambayo yanaendelea kwa ajili ya mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Ni kweli majadiliano yameendelea na bahati nzuri sana nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba majadiliano yako katika hatua za mwisho kabisa ili mradi huu uanze utekelezaji wake. Na kwa maana hiyo mara tu mazungumzo yatakapokamilika na sisi upande wa TRC kwa kuwa tayari fedha kutoka Umoja wa SADC wametuahidi kutoa hizo Dola 6,000,000 na sisi tutaanza utekelezaji wa mradi huu kwa ujenzi wa standard gauge.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kufahamu kwamba ni lini sasa mradi huu utaanza. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara tu mazungumzo yatakapokamilika mradi huu tutaanza utekelezaji wake. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza hivi sasa shirika letu la Ndege Tanzania limeanza safari zake za kubeba mizigo kwa ajili ya safari Guangzhou China, inaondoka China na kupitia Zanzibar na baadaye inarudi Zanzibar. Shirika hivi sasa wanatumia ndege yake ya Boeing 787 kwa ajili ya kubeba mizigo hiyo. Ndege hii imeundwa kwa ajili ya kubeba abiria na mizigo lakini eneo kubwa ya ndege hii ni kwa ajili ya kubeba abiria. Shirika letu sasa linabeba mizigo bila ya abiria kwa kwenda huko China.

Je, Shirika halioni hivi sasa kuendelea kufanya hivyo ni kuendelea kulitia hasara?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria kati ya Zanzibar, Pemba na Dar es Salaam. Je, ni lini Shirika la Ndege la Air Tanzania litaanza safari zake katika Kisiwa cha Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Juma Mohamed Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna Ndege aina ya Dreamliner 787-8 ambayo inafanya biashara kati ya Tanzania na China na Ndege hii imekuwa ikibeba abiria lakini kipindi cha Covid 19 China kama tunavyofahamu kuingia abiria yeyote ndani ya nchi ya China. Kwa hiyo tukaona ni heri na bora Ndege hii aina ya 787-8 Dreamliner ambayo ina uwezo wa kubeba tani 40 ifanye biashara ya kubeba mizigo kuliko tungeiacha kuwa grounded na ingekuwa gharama zaidi kuliko hivi sasa ambavyo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anatamani ama anapenda kwamba tuanzishe safari za kwenda Pemba. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wa Zanzibar kwamba Shirika letu la ATCL litaanza safari zake za Pemba mwaka wa fedha 2023/2024 kwa maana ya kwamba mwaka ujao, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imetambua uwepo na umuhimu wa Bandari Kavu ndani ya Mji wa Tunduma na tayari Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetenga zaidi ya ekari 2,000 kwa ajili ya uwekezaji wa bandari kavu. Sasa nataka kujua je, ni sekta ngapi binafsi ambazo zimefikiwa mpaka sasa ili kuja kuwekeza bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Taifa sasa lipo katika ushindani wa kibiashara; je hatuoni kuchelewachelewa tunaweza tukaleta matokeo hasi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Halmashauri ya Tunduma ina eneo la kuweza kujenga bandari hii kavu na sekta ambazo ziko tayari kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hili la bandari kavu, kuna Sekta ya Kilimo, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, suala la kuchelewachelewa. Kimsingi Serikali imechukua hatua za kuongea na watu binafsi na ndio maana hadi sasa tupo kwenye majadiliano ya mwisho ili eneo la Mpemba ambalo litakuwa linaunganisha upande wa Malawi pamoja na Zambia na DRC liweze kujengwa Bandari hii kavu, ahsante.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Spika, Morogoro ina barabara mbili kuu zinazounganisha nchi za SADC na Afrika Mashariki. Morogoro ilitenga hekari 500 kwa ajili ya bandari kavu, je Serikali ina mpango gani wa kujenga Bandari Kavu katika Mji wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Abdul-Aziz, Mbunge wa Morogoro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Morogoro pia tuna eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu na kwa kuwa reli yetu SGR itaanza kazi hivi karibuni na katika mwaka wa fedha ujao nimwombe Mheshimiwa Mbunge apitishe bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi kwa kuwa ni miongoni mwa Bandari Kavu zitakazojengwa katika mwaka wa 2023/2024. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pamoja na hayo majibu ambayo hayaridhishi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege, awali upanuzi ulikuwa ni mita 300 na upanuzi huo umeanza mwaka 2016. Mpaka tunavyozungumza sasa, ni miaka saba, wamepanua mita 150. Mita nyingine 150 waliwazuia wananchi wa Kata ya Makole kutokuendeleza maeneo yao, na mpaka sasa tunavyoongea nyumba zile zimekuwa ni magofu, watu walihama mle: Je, Serikali haioni wana sababu ya kuwalipa wananchi wa Kata ya Makole, kaya 50 zilizobaki kifuta jasho, ili waweze kufanya ukarabati wa nyumba zao na warudi kwenye makazi yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni sera ya Serikali kwamba, inapotwaa maeneo ya wananchi, inatakiwa ilipe fidia kwanza ndipo iendelee na utekelezaji wa miradi. Imekuwa ni kawaida ama ni tabia ya Serikali kuendelea kutwaa maeneo ya wananchi bila kuwalipa fidia na kuendeleza utekelezaji wa miradi, na matokeo yake wananchi wengi wamekuwa wakidhulumiwa. Hivi tunavyoongea…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa Kunti?

MHE. KUNTI Y. MAJALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, watu 46 walioko Mkonze hawajafanyiwa uthamini na Waziri hapa anasema waendelee kuvuta subira. Ni lini wananchi 46 waliobaki Mkonze watalipwa fidia yao kwa sababu tayari maeneo yao yameshachukuliwa na mradi umeshatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Yusuph Majalla, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mwaka 2016 Serikali ilikuwa na nia kwa ajili ya ujenzi ama upanuzi wa uwanja wetu wa ndege wa hapa Dodoma, lakini Serikali ilipoanza ujenzi mwingine mpya, hususan katika kiwanja cha Msalato, ikaona haina sababu ya kuendelea kupanua uwanja mkubwa zaidi wakati uwanja mkubwa wa Kiwanja cha Msalato unaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ilipofika mwaka 2018 na kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo pamoja na timu yake na wataalamu wetu kutoka TAA walipewa taarifa wananchi hawa kwamba eneo hilo, na kusudio la Serikali kuendelea kuupanua uwanja huu halitakuwepo tena, bali tutalipa zile fidia za mita 150 ambazo tayari tumeshalipa kwa kiasi cha Shilingi 1,900,000,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, kuhusu Mkonze, ni kweli kwamba, katika ujenzi wa TRC, kawaida unapojenga SGR, tunasema ni Design and Build, maana yake huwezi kufanya tathmini yote na ukalipa wananchi wote. Maana yake, inafanyika tathmini na wakati huo huo ulipaji unaendelea. Kwa maana hiyo basi, ifikapo tarehe 17 ya mwezi huu wa Aprili, wananchi wote wa eneo la Mkonze ambao hawajalipwa fidia zao tukutane eneo la SGR Station hapa Mkonze na waje na nyaraka zao, ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Tabora Mjini ni moja kati ya majimbo ambayo reli ya SGR imepita kwenye maeneo ya Ndevelwa. Wananchi wamefanyiwa tathmini ndogo, lakini pamoja na udogo wa tathmini hiyo, bado hizo fedha mpaka sasa tunavyozungumza wananchi hao hawajalipwa fedha zao: Ni lini Serikali itawalipa wananchi hawa fedha zao ili watafute maeneo mengine ya kuweza kujihifadhi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa suala la fidia katika eneo hili la SGR mara baada ya maswali na majibu tuonane ili tuweze kuwasiliana na wale wote ambao wanafanya zoezi hili la ulipaji kwa sababu, tunaendelea kulipa katika eneo hili, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwanza sikubaliani na majibu ya Serikali kwenye swali langu la msingi kwa sababu ukizingatia kwamba sheria ni mwaka 2007, leo ni mwaka 2023 miaka 16 sasa bado Serikali inasema inatafuta fedha na huku wameweka vigingi kwenye maeneo ya wananchi lakini ingekuwa ni mwananchi ndiyo ameingilia kwenye hilo eneo Serikali ingeenda kumwondoa kwa nguvu. Baada ya maelezo hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, ni lini sasa Serikali itawalipa fidia wananchi hawa? Swali la pili, kama Serikali haina uwezo wa kulipa fidia, kwa nini isiwaruhusu wananchi hawa wakaendeleza maendeleo hayo mpaka watakapokuwa tayari kuwalipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa wale wote ambao waliathirika na ujenzi huu wa Arusha Bypass kwa maana hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Arusha waendelee kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi waruhusiwe kujenga maeneo haya. Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na sheria ya kuhifadhi barabara ambayo ilianza tangu mwaka 1932 enzi za ukoloni na ikarudiwa mwaka 1967 na tukatunga sheria mpya mwaka 2007 ambayo inataka hifadhi ya barabara kutoka kati kati ya barabara mpaka upande wa pili iwe mita 30 na kutoka kati kati tena upande mwingine iwe mita 30 kwa maana ya kwamba jumla ni mita 60.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwamba sheria hii lazima tuilinde na ikizingatiwa kwamba Arusha ni mjini tunahitaji pia kuendeleza miundombinu mizuri pale Arusha ili jiji hili la kitalii na kwa maana hiyo tuna hakika tukifanya vizuri katika suala la miundombinu hata watalii pia wataongezeka zaidi.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE : Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, gati la kuegesha meli katika Kisiwa cha Godzba baada ya maji kushuka ya Ziwa Victoria, kuegesha meli za Songoro Marine na hiyo Clarias imekuwa ni shida. Serikali mnaonaje haraka mtujengee gati lile liweze kuhimili kupokea meli zetu maji yanapopanda na kupwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza; visiwa vya Ikuza bandari ya Magarini, Mazinga, Bumbile Kerebe havijahusishwa kwenye mpango wa Serikali ulioutaja. Je, ni lini Serikali itaangalia gati za visiwa hivyo na kuweza kuzitekeleza kusudi Muleba nzima iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika gati hili la Godzba kuna changamoto ya maji kushuka na hivyo kusababisha gati hilo kutotumika ipasavyo na meli hizi. Kwa maana hiyo, Serikali inatoa maelekezo kwanza kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini kutuma timu ya wataalam ili kulirekebisha gati hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa hatua za awali kwa kuwa wenzetu wa MSCL wana-floating dock tatu (tishari), nataka moja ije eneo hili la Godzba ili lianze kufanyakazi wakati meli hii inafanya kazi eneo hili na tishari nyingine itaenda katika kisiwa cha Gana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anataka kujua ni lini tutapeleka huduma katika visiwa vya Kerebe Bumbile, Kyamkwikwi, Godzba na maeneo mengine. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa meli hii ya MV Clarias tayari tumeshakamilisha matengenezo yake jana na tunategemea ndani ya wiki hii, namuelekeza mkurugenzi wa TASAC atume timu yake ya wataalamu ili wakajiridhishe na hatimaye meli hii ianze kufanya kazi. Kwa maeneo ya visiwa ambavyo umevitamka Mheshimiwa Mbunge nako tutaanza kupeleka huduma kama ambayo inafanya sasa maeneo mengine. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Tanganyika ukianzia Kigoma mpaka Kalambo tulikuwa tukitegemea meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo, ni muda mrefu sana hatuna usafiri wa meli.

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuhakikisha kwamba inapatikana meli kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Ziwa Tanganyika tuna changamoto za meli, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuelekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya Uchukuzi kwamba mwaka huu wa fedha tunakwenda kusaini mikataba minne ya ujenzi wa meli tatu pamoja na chelezo kubwa katika Ziwa hili la Tanganyika kwa maana ya meli tatu, meli mbili zitakuwa Ziwa Tanganyika na chelezo na meli moja itakuwa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa ukanda wa Kigoma kwamba kwa meli hii ya MV Liemba ambayo tayari tupo hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi pia itakarabatiwa.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo (a) na (b): -

(a) Ningependa kujua kwa kupata commitment ya Serikali, ni lini sasa vituo hivi vitarejeshwa?

(b) Wananchi wa maeneo haya Njage na Itongowa wamekuwa wakipata adha kubwa sana ya usafiri hasa ukizingatia wakati huu wa masika sisi Wananchi wa Mlimba usafiri wetu mkubwa ni treni ya TAZARA. Sasa namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri lini atakuwa tayari kuambatana nami tupande treni hiyo ya TAZARA anaposema hapo Ifakara mpaka Mbingu tushuke kwenda Njabi umbali wa kilometa tisa halafu apate hiyo adha na yeye ataona najua atachukua hatua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wanaotumia vituo hivi vya Stesheni ya Reli ya TAZARA kwamba tarehe 28 Ijumaa ya wiki hii tunatuma timu ya wataalam kwenda kufanya tathmini ya kina. Itafanya kazi hii kwa wiki moja, mpaka tarehe 06 ya mwezi wa tano, na watatoa taarifa ama ripoti ambayo hiyo itakuwa msingi wake katika kufanya maamuzi. Hata hivyo swali lake la pili ni lini kwenda huko, Mheshimiwa Mbunge mimi na wewe nitakwenda pamoja na wewe siku ya weekend wakati vikao vya Bunge vinaendelea, tutaomba ruhusa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Spika ili twende kuona adha hii kwa wananchi na hatimaye kufanya maamuzi sahihi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, swali langu ni dogo; kwa kuwa huduma ya treni ya mwendokasi nchini inasubiriwa kwa hamu kubwa sana.

Je, ni lini shirika hili litaanza kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Reli yetu ya TRC hususan katika mradi wetu wa SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma awamu ya kwanza tutaanza kutoa huduma kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro. Hivi ninavyosema tumeshafanya testing katika vituo vyote signal na treni la Mkandarasi na kwa maana hiyo tunachosubiria sasa ni kuja vichwa na hivi vichwa tunategemea vitakuja ndani ya mwezi ujao ili ianze kufanya hii station ya SGR, ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naomba nitoe pole nyingi kwa wananchi wa Jimbo la Hai kutokana na mafuriko yanayoendelea sasa hivi kwenye maeneo mbalimbali. Swali langu, ni lini Serikali itajenga kituo kidogo cha treni eneo la Rundugai sokoni?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambau kwamba kituo hiki cha reli, treni ya abiria inayotoka Dar es Salaam kwenda Arusha ni miongoni mwa maeneo ambayo pia tunashusha. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaweka fedha kwenye bajeti ijayo, nitaomba wakati wa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tuunge mkono ili tujenge kituo hiki kiweze kutumika, ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante. Viwanja hivi vilitumika kwa kupigania uhuru Kusini mwa Bara la Afrika. Je, ni nini tamko la Serikali hasa kwamba viwanja hivi lini vitawekwa lami vyote viwili?

Swali pili, Je, ni lini wananchi waliotwaliwa maeneo yao kwa ajili ya kuongeza eneo kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea watalipwa fidia zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni lini vitajengwa viwanja hivi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo hayo kwamba katika bajeti ya mwaka huu Kiwanja cha Lindi kimetengewa ama tumetenga takribani bilioni 2.5 na fedha hizi zitatumika kwa ajili ya Mkandarasi Mshauri ambae ataandaa document kwa Ajili ya kutangaza viwanja hivi ili viweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, suala la pili anataka kuja ni lini wananchi watalipwa fidia. Ni kweli tathmini imekwishafanyika na mwezi Machi daftari ambalo limeshaandaliwa kwa ajili ya malipo liliwasilishwa kwa Mthamini Mkuu na Mthamini Mkuu ataleta Wizarani na Wizara tutapeleka Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hawa katika kiwanja hiki cha Nachingwea. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na umuhimu wa Serikali kukuza utalii hususani katika mbuga yetu ya Burigi – Biharamulo, naomba kujua ni lini sasa uwanja wa ndege wa Biharamulo sasa utakarabatiwa ili uweze kuwa kiungo muhimu cha kuleta watalii katika eneo letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiwelesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Kiwanja cha Ndege cha Biharamulo ni miongoni mwa viwanja 11 ambavyo tumevitengea fedha na kwa kiwanja cha Biharamulo pekee tumetenga takribani Milioni 400 kwa jili ya ukarabati kiwanja hiki cha Biharamulo. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Je, ni lini uwanja wa ndege wa Bukoba Mjini utawekewa taa na mnara wa kuongoza ndege ili kuongeza usalama wa watumiaji wa uwanja huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kiwanja cha ndege cha Bukoba kwenye mwaka wa fedha ujao na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais tumetenga takribani bilioni 2.9 kwa ajili ya ujenzi wa control tower pamoja na taa za kuongozea ndege katika kiwanja hiki, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mbogwe ni kubwa iliyo na vyanzo vingi vya mapato, tumeshatenga eneo la kujengewa uwanja wa ndege tayari. Lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Mbogwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge naomba mara baada ya kipindi cha maswali na majibu nionane naye ili niweze kuangalia bajeti kiasi gani tumetenga kwa bajeti ijayo katika eneo lake. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Lake Manyara Airport utajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, uwanja alioutamka Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa viwanja ambavyo vipo chini ya Benki ya Dunia na tayari tupo katika mchakato wa kutangaza tenda ili viwanja hivi viweze kujengwa kikiwemo na Kiwanja cha Tanga, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo tunavyoongea mpaka ule unatumika lakini kwa kiasi kidogo sana na hili tatizo limetokana na upande wa pili wa Zambia ambapo wafanyakazi kama walivyo TRA Tanzania, ZRA wamekuwa hawaishi pale. Je, Serikali kwa kutumia ushirikiano uliopo na Zambia haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuongea na upande wa pili ili watumishi wa ZRA wawepo muda wote ili kusiwe na shida kwa wasafirishaji wa mizigo.

Swali la pili; ukitaka kwenda Congo ya Lubumbashi njia iliyokuwa rahisi kabisa ni kwa kupita Kasanga Port ambayo naomba niipongeze Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana. Kazi ndogo ambayo imebaki ni upande wa pili kwa maana kupitia Mlilo kule na kwa wakati huu ambao ni rahisi kabisa kutumia PPP.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kutangaza mradi huu ambao economically unaonekana kwamba viable? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mpaka wetu wa Kasesya ambao una taasisi mbalimbali, kuna taasisi za Uhamiaji, Polisi, watu wa kilimo, TRA, kwa hiyo tunafanya kazi masaa 24, lakini upande wa wenzetu Zambia haufanyi kazi masaa 24, Serikali imechukua juhudi za kuwasiliana kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na hata mwaka jana tulifanya mikutano Tarehe 14 na 15 mwezi wa Kumi, kuhakikisha mpaka huu tunauhuisha na unafanya vizuri, waliahidi Serikali ya Zambia kwamba watafanya kama ambavyo tunafanya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekti, swali la pili kuhusu PPP hususan katika Bandari yetu ya Kasanga ambayo ni kweli imegharimu zaidi ya Bilioni 4.7 na Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumekuwa tukifanya mikutano mbalimbali kuishirikisha sekta binafsi ili upande wa pili wa Congo waweze kutengeneza barabara ili bandari yetu ya Kasanga Port iwe na tija. Kwa hiyo, haya tunaendelea kuyafanya, tunataendelea pia kuwasiliana na wenzetu wa Serikali ya Congo ili kuhakikisha miundombinu upande wa kwao inafanya vizuri, ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mpaka wa Namanga ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu lakini kuna msongamano mkubwa wa malori. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha huduma katika mpaka huu wa Namanga ili basi kuleta tija? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na suala la mpaka wa Namanga kuwa na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mipaka kama Tunduma pamoja na Namanga ni mipaka ambayo ina msongamano mkubwa na ni kwa sababu ya bidhaa zinazoingia na kutoka kwenda nchi jirani. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba kwanza maeneo haya tumepanga utaratibu na scanner ambazo ziko katika maeneo hayo, kabla zilikuwa zinafanya masaa 12 na sasa tumeweka mpango wa zifanye kazi masaa 24 maana yake usiku na mchana ili magari ya kwenda Kenya na magari ya kuingia Tanzania kusiwe na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tumeweka eneo maalum kwa ajili ya kuegesha magari hususan ya mizigo ili yasisongamane sana eneo lile la mpakani, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikumi idadi ya malori ni kubwa msongamano ule unasababisha hatari na usalama wa maisha ya raia na mali zao. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetoa Milioni Mia Moja kwa ajili ya kutatua tatizo hilo la malori kwa kutenga eneo na kusaidia ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini commitment ya Serikali kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika kutatua tatizo la malori ambalo linasababishwa na mizani pale Mikumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F.
MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo la Mikumi kuna msongamano wa malori mengi na Mheshimiwa Mbunge ninakupongeza kwa kufatilia jambo hili, alipolileta Serikalini tukawapa eneo ambalo ni la TRC kwamba waendelee kulitumia na tayari tulishatoa kibali hicho kama Serikali, kinachosubiriwa sasa ni wao kama Halmashauri kulifanyia hilo eneo ukarabati ili malori yaliyoko pale barabarani yahamie eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninakupongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zako hizo. Ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ukweli uliokuwepo, Shirika la Nyumba la Bara halitumi fedha kupitia Shirika la Nyumba la Zanzibar hadi muda huu.

a) Je, kuna ushirikiano gani sasa ya kuliwezesha shirika la Nyumba la Zanzibar kwa kulipatia fedha kwa ajili ya kuwajengea watumishi wa bara?

b) Je, kuna mkakati gani wa ushirikiano kati ya ZBA pamoja na TBA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyo kwisha kusema, ni kwamba nyumba za Zanzibar kwa watumishi wa umma zinajengwa chini ya Wakala wa Majengo wa Zanzibar lakini wana ushirikiano wa karibu sana kati ya ZBA pmoja na wakala wa majengo Tanzania Bara. Ushirikiano huo ni pamoja na kwamba Wakala wa Majengo Zanzibar wamekuja mara kadhaa huku Bara kujifunza namna ambavyo TBA wameweza kuendesha miradi mbalimbali happa nchini ikwemo miradi ya Dar es Salaam Magomeni quarter hapa Dodoma pamoja na mji wa kiserikali.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa swali lake la pili ni kwa kiwango gani TBA iipatie fedha ZBA. ZBA fedha zake zinatengwa kwenye Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi kule Zanzaibar. Na kwa mwaka wa fedha ujao, kwa maelezo ya ZBA ni kwamba wametenga takribani kiasi cha shilingi bilioni 56 ili kujenga nyumba takriban 400 zitakazo jengwa kwa Zanzibar nzima kwa maana ya Unguja na Pemba, na walau kila Wilaya watagusa kupitia mradi huu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa nyumba kadhaa zilizo chini ya mamlaka ya TBA hasa hapa Dodoma ni chakavu, miundombinu ya maji taka imechoka, maji ya karo na vyoo yanafurika hovyo na hivyo kuwa tishio kwa afya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuisimamia mamlaka hii ya TBA ili kuhakikisha nyumba hizi ziko katika hali ya usalama na si tishio kwa wakazi, na hasa kwa vile wanalipwa kodi na hawakai bure?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Asha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli badhi ya nyumba za TBA hapa Dodoma ni chakavu, na nikushukuru Mheshimiwa Spika, kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali wanadaiwa. Na kwa kuwa wanadaiwa wanakila sababu ya kulipa ili tukarabati nyumba hizi ambazo ni chakavu, ukizingatia kwamba TBA fedha zake zinakata kutoka ruzuku za Serikali lakini pia na kodi za mpangaji, inapokusanywa ndipo inapokarabati nyumba hizi za TBA, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Uko ujenzi unaoendelea na TBA kule Temeke, tunaita Temeke quarter.

Je, Serikali mna mkakati gani wa kuwapatia nyumba wale ambao walikuwa wakiishi pale kabla ya ujenzi huu unao endelea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Temeke Mwisho na Temeke quarter kuna mradi unaendelea na mradi huu tutajenga majengo takribani saba ya ghorofa yatakayo kuwa na uwezo wa kubeba familia 1,008 na kwa maana hiyo sasa wale wote ambao watakuwa ni waathirika wa maeneo

hayo pia TBA tutaona ni namna gani ya kuwafanya hawa waishi katika maeneo hayo.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, suala la upembuzi yakinifu limechukua muda mrefu sana, ndiyo kwanza saa hizi Serikali imejipanga kuanza kutenga fedha.

Je, Serikali haioni kwamba ujenzi wa bandari katika mwambao wa Bahari ya Hindi ungerahisisha sana na kupunguza suala la ukosefu wa ajira kwa wananchi wa Tanzania, hususan wa Mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mkoa wa Mtwara unalima mazao ya mihogo, njugu, mbaazi, nazi, mazao ambayo yanahitajika sana kule Comoro. Je, Serikali haioni kwamba kama kungekuwa na meli hii uwepo wake ungechechemua sana uchumi wa watu wa Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imechukua muda mrefu kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na ulianza tangu mwaka 2019 na 2021. Hii ilikuwa ni kwanza lazima ilitakiwa tujiridhishe – na huu ulikuwa upembuzi yakinifu wa awali – tujiridhishe kiasi cha mzigo utakaotoka Mtwara kwenda Comoro ili tujue ni aina gani ya mali na ukubwa wake, ambaye Serikali kwayo itakwenda kujenga ama kutengeneza.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo, kwa kuwa katika Mwaka wa Fedha ujao tumetenga fedha sasa kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa kina wa mwisho ili tupate uhalisia wa aina gani ya meli hii.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili; Serikali inatambua juhudi za wakulima wa Mtwara, hususan wale wote ambao wanalima mazao mbalimbali. Na kuna kila sababu ya kwamba wawe na meli inayosafirisha mazao yao kutoka Mtwara kwenda Visiwa vya Comoro.

Mheshimiwa Spika, na kwa jitihada hizo, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ziara aliyoifanya Ufaransa, ndiyo maana meli hizi sasa zimeshaanza kuja nchini, hususan katika Kampuni ya CMA, CGM pamoja na UFL Express, maana kwamba Mtwara itakuwa hub, na Nchi jirani kama Comoro, Mozambique pamoja na Malawi watakuwa wanachukua mizigo pale kwenda maeneo yao, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja, kwa nini Wizara na TRC waliacha bei ya ushindani ya shilingi bilioni 9.1 kwa kilometa moja ya standard gauge na kuamua kumpa kampuni ya CCECC kwa shilingi bilioni 12.5 kwa kilomita moja ya standard gauge na kuisababishia hasara Serikali ya shilingi trilioni mbili ambayo ni kinyume na matakwa ya single source kama alivyoeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni kwa nini Serikali isivunje huo mkataba baina ya TRC na CCECC wa ujenzi wa kipande cha Tabora - Kigoma kwa sababu hata hiyo Lot III, Lot IV anayoi-refer CAG ameshatuambia kwamba tayari walikiuka utaratibu wa sheria. Kwa nini Serikali isifute huu mkataba wa kinyonyaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei ya ushindani, bei zilizopo ni tofauti sana na zilizotumika miaka ya 2017 wakati nchi inaanza ujenzi wa standard gauge. Kila kitu kimebadilika, hususan katika suala la asilimia zaidi ya 65 ya SGR, inatumia chuma. Bei ya Soko la Dunia ya chuma, imeongezeka kwa robo tatu ya gharama yake. Pia mwaka 2017 bei ya mafuta ilikuwa takribani shilingi 1,900, sasa hivi imekwenda mpaka shilingi 3,000 na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo gharama anazolinganisha Mheshimiwa Mpina, ziko tofauti sana na gharama za leo. Hata hivyo, hapa tumesema katika jibu letu la msingi kwamba tumeokoa takribani shilingi bilioni 632.74. Katika nchi za Afrika Mashariki, sisi Tanzania peke yake, kwa gharama ya ushindani, ndiyo tumeweza kuwa na kiwango kidogo zaidi cha kutengeza kilomita moja kwa dola za Kimarekani milioni nne, wakati nchi jirani na hata ukisoma ripoti ya Benki ya Dunia, ni zaidi ya dola za Kimarekani kwa kilomita moja milioni 7.69. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nihakikishie Watanzania na Bunge lako tukufu kwamba hakuna hasara yoyote, zaidi tumeokoa fedha hizi ambazo nimezitamka hapa. Engineering estimate zilikuwa dola za Kimarekani bilioni 3.006 sawa na shilingi trilioni 7.2, nasi tumesaini mkataba wa shilingi trilioni 5.2. Maana yake tumeokoa tena shilingi trilioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwa nini mkataba usivujwe? Huu makataba hatuwezi kuuvunja kwa sababu kwanza ni wa gharama nafuu; na pili, ni mkataba na CCECC. Ukiangalia rank za Makampuni yote duniani, perfomance ya kampuni hii, inaonesha kufanya vizuri, ni ya 10 kwa mwaka 2021, na ni ya 11 kwa mwaka 2022. Kwa hiyo, hata kipande kile cha kutoka Isaka - Mwanza ambacho ni kilomeeta 341, wana asilimia zaidi ya 30. Kwa hiyo, wanafanya vizuri na ndiyo maana tuliwapa mkataba huu wa kutoka Tabora kwenda Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika kutokana na ahadi mbalimbali za viongozi wa Serikali, tangu Serikali ya Awamu ya Tatu, yaani mika 23 mpaka sasa uthamini wa maeneo hayo tayari umeshafanyika zaidi ya mara tatu. Sasa naombe nijue;

Je, ni lini wananchi wa maeneo haya watalipwa fidia ili waweze kupisha ujenzi wa barabara hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali jingine, kulingana na uwingi wa malori kulazimika kupita katikati ya mji wa songea hivyo kulazimisha msongamano ajari na uchafuzi wa mazingira.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara ile ili kuweza kupunguza adha inayowakuta wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hususani wakazi wa Songea Mjini, kuzingatia kwamba bajeti ya Serikali ya Wizara hii bado haijapitishwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tathmini tumekwisha kufanya mara tatu, na hii ni kutokana na sheria ya tathmini; kwamba inapofika baada ya miezi sita na kama hakuna malipo yamefanyika inatakiwa tathmini ile iweze kufanyika tena, vinginevyo ilipwe kwa fidia.

Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi ambao wataathirika katika ujenzi huu ni kwamba tayari sasa tathmini imekamilika, hii ya mwisho, na daftari lipo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali ili aweze kusaini na hatimaye Serikali itafute fedha kwa ajili ya kulipa fidia hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana kwa kushirikiana na Benki ya Dunia Serikali imepata mkopo kwa ajili ya ujenzi katika kipande hiki cha Songea - Lutukila na tupo katika hatua za manunuzi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, mara baada ya manunuzi kukamilika tunaanza kujenga, na iko ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake japokuwa hali ni mbaya sana wakati wa mvua katika lile eneo naomba wajitahidi kufanya haraka sana.

Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza; kwa kuwa barabara ya Kinyanambo C - Mapanda mpaka Ukami na Kinyanambwa A Saadani – Igoma katika Jimbo la Mufindi Kaskazini ni ya kiuchumi na pia ni ya ahadi ya Mheshimiwa Rais; je, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?

Swali la pili, barabara ya Iringa – Kilolo - Idete ni ya mkoa na Serikali iliahidi muda mrefu sana kuiunganisha na mkoa wa Morogoro kupitia kata ya Idete, Itonya, Muhanga mpaka Mungeta; je, ni lini ahadi hiyo itatimia kwa sababu uchumi wa mkoa wa Morogoro na Iringa uweze kukua kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la barabara ya Kinyanambo C-Mapanda mpaka Ukome. Ni ahadi ya viongozi wetu wa kitaifa na ahadi zote za viongozi wa kitaifa sisi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tutahakikisha tunazitekeleza na tunaziweka katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2023/2024, hususani kwenye barabara hii ya Kinyanambo C -Mapanda-Ukoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, barabara hii ya Iringa – Kilolo – Idete kipande cha Ipogolo – Kilolo chenye kilomita 33 ni barabara ambayo inafadhiriwa na Benki ya Dunia na mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao, wapo katika hatua za manunuzi na kilometa 67 zilizobaki nazo zimekwishafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa maeneo haya kwa sababu unaunganisha kati ya Mkoa wa Iringa pamoja na Morogoro kwamba inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulipitisha bajeti hapa ya kujengwa kipande cha Haydom mpaka Labay kwa kiwango cha lami na bajeti ya Waziri bado hatujapitisha.

Je, ni lini atasaini mkataba ule ili barabara ile ijengwe kipande hiki nilichosema kwa kiwango cha lami au tuje na sarakasi kwa namna nyingine tena kwenye bajeti hii ya Jumatatu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye mwaka huu wa fedha tunatakiwa tujenge barabara hii aliyoitamka Mheshimiwa Mbunge na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha kwa sababu mwaka wa fedha wa Serikali ni mpaka tarehe 30 Juni, nina hakika tutakuwa tumesaini barabara hii ili mkandarasi aanze kufanya kazi pale. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, wananchi wa Mkoa wa Katavi hususan wa eneo hili wamekuwa wakizunguka umbali mrefu kupitia Eneo la Mpanda mpaka Inyonga kutokana na kwamba barabara hii kipindi cha masika imekuwa haipitiki kabisa.

Swali la kwanza; je, Serikali haioni sasa umuhimu wa haraka wa kufanya ujenzi wa barabara hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali inafanya ujenzi wa Barabara ya kutoka Mpanda – Uvinza mpaka eneo la Lulafe. Je, ni lini Serikali itakamilisha kilometa zilizobaki mpaka Uvinza ili tuweze kuunganishwa na wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa ujenzi wa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii aliyoitamka ni kilometa hizo 60 ambazo zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini Serikali iliona umuhimu kwanza kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Kavuu ambalo lilikuwa la chuma sasa tunakwenda kuweka zege na kazi hii inaendelea. Katika mwaka wa fedha sasa tutakamilisha hizo kilometa zilizobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwa Barabara hii ya Mpanda – Uvinza; barabara hii ipo na mkandarasi anaitwa CHICO na tayari tumeanza ujenzi wa kiwango cha lami kilometa 25 na tunategema kwamba mkataba huu utaisha baada ya mwaka mmoja na miezi sita. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo hayo yote, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekeleza mradi huu na utakamilika kwa wakati, ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, barabara ya Kwa Sadala – Isuke kilometa 15 imekuwa ni ahadi ya muda mrefu kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais; je, ni lini sasa barabara hii ya Kwa Sadala – Isuke kilometa 15 itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara hii ya Kwa Sadala – Isuke na kwa kuwa ni ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa kama nilivyokwishajibu swali la Mheshimiwa Martha kwamba, ahadi zote za viongozi wa Kitaifa, sisi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumeziweka katika mpango wa bajeti ijayo. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge apitishe bajeti itakayosomwa hapa tarehe 22 na 23 ili barabara hiyo iwe sehemu ya utekelezaji huo, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Chombe – Igonda – Kaoze mpaka Ilemba? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii aliyoitamka kadri Serikali itakavyopata fedha, tutakwenda kuitekeleza barabara hii.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wananchi wa Mkoa wa Songwe wana changamoto wanapokwenda kuhitaji huduma kutoka mkoani imewalazimu kwenda kupitia Mkoa wa Mbeya na kuanza usafiri kuelekea Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Barabara kutoka Mloo – Isasa – Magamba mpaka Mkwajuni ili kurahisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyotamka Mheshimiwa Mbunge iko katika mpango wa Serikali wa kujenga na sasa tunatafuta fedha ili tuanze ujenzi wa barabara hii, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya vivuko ambavyo vinasababisha mkwamo wa kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine. Kuna changamoto kubwa sana kutoka Kijiji cha Itogwamolo kwenda Kijiji cha Bandari, lakini hivyo hivyo kutoka kitongoji cha Shilabela kwenda Isaka Stesheni na hivyo hivyo kutoka kwenye Kata ya Isaka kwenda ya Jana. Sasa swali langu la kwanza; ni lini Serikali itaweza kutenga fedha ili iweze kujenga vivuko vitakavyowawezesha wananchi kufika kwenye maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa katika eneo la Isaka hasa kwenye suala la bandari.

Je, ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja kwenye Kata ya Isaka ili aweze kufanya mkutano wa hadhara awasikilize wananchi wa Isaka kero kubwa ambayo inayozuka katika maeneo haya ya bandari, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu sana masuala ya kivuko katika eneo hili. Serikali itaanza ujenzi katika vijiji hivyo alivyovitamka vyote, hususan katika Kijiji cha Isaka na Isakajana, Isaka Stesheni na Kitongoji cha Shilabela na Kijiji cha Itogwa hadi Kijiji cha Bandari. Tutaanza ujenzi wa kuunganisha vijiji hivi tarehe 27 ya mwezi huu wa tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwenda kukagua, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na yeye, mara baada ya kuanza ujenzi tutaenda kukagua eneo hili pamoja na eneo la Stesheni ya Kisaka, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa kipande hiki kilichobaki ndio kinaunganisha mkoa wa simiyu na Mkoa wa Arusha na ni muhimu sana katika kufungua uchumi wa wananchi wa Karatu lakini wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla wake.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kuanza ujenzi wa kipande hiki cha Karatu-Orudeani Matara hadi Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ya Karatu-Odoyani hadi Mataralalago kujengwa kwa kiwango cha lami. Serikali imekwisha fanya tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, na sasa kazi iliyobaki ni kutafuta fedha ili barabara hii ijengwe.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika nakushukuru. Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii ya uchumi, ni nini hasa mkakati wa Serikali kuhakikisha inajenga barabara hii kwa haraka?

Swali langu la pili, Jimbo la Mtwara Mjini lina changamoto kubwa sana ya barabara; je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuliangalia jimbo hili kwa jicho la tatu ili iweze kulijengea barabara nyingi za lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua umuhimu wa barabara hii kama Serikali na ndiyo maana tumeshafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na tunahakikisha ya kwamba barabara hii inapitika kila mwaka. Katika mwaka wa fedha ujao imetengewa takribani shilingi milioni 188.435 na katika mwaka ujao pia tutafanya usanifu wa kina ili iwe maandalizi katika kujenga katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, barabara katika Mkoa wa Mtwara hususan Mtwara Vijijini na Mjini, Serikali inatambua umuhimu wa barabara kuboreshwa katika Mkoa huo. Ndiyo maana hivi sasa kuna miradi ile ya EPC + Financing, kuna barabara ambazo pia ziko katika Mkoa wa Mtwara na ambazo hivi karibuni tutaenda kusaini mkataba kabla ya mwezi wa sita mwaka huu, 2023, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Barabara ya Mbulu – Karatu – Haydom – Sibiti mliahidi kujenga kwa kiwango cha lami na kipande hiki cha Mbulu – Haydom, Mheshimiwa Waziri uliahidi utasaini mkataba kabla ya bajeti yako Jumatatu. Hebu tuambie leo na uwambie wananchi wa Mbulu, mkataba huo utasaini lini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia sana suala la barabara hii na wewe ni shahidi kwamba Mheshimiwa Mbunge, katika Bunge lililopita alipiga sarakasi kuhusiana na suala hili la barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Sikivu. Sasa, tunakwenda kusaini mkataba kesho na tutasaini pale Haydom. Kwa hiyo, niwatangazie wananchi wa jimbo hili kwamba kesho ni siku muhimu kwao katika kushuhudia kusainiwa mkataba wa ujenzi wa barabara hii. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kufuatilia barua hii.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya Singida – Ilongero hadi Haydom upembuzi yakinifu umekwishafanyika; je, Serikali itakamlisha lini barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekwisha kamilika na sasa Serikali inatafiuta fedha ili tujenge kwa kiwango cha lami barabara hii, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kufuatia ujenzi wa bandari ya uvuvi unaoendelea pale Kilwa Masoko. Nini mpango wa Serikali kupanua barabara ya kutoka Kilwa Masoko mpaka Nangurukuru ili iweze kukidhi haja ya wakati wa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli pale Kilwa Masoko tunajenga bandari ya kisasa ya uvuvi na katika mipango yetu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TANROADS, tutaboresha pia barabara hii kutoka eneo la bandari ri kwenda katika eneo la pale mjini na kwa maana hiyo Mheshimiwa Mbunge katika mwaka wa fedha ujao barabara hii tumeitengea fedha kwa ajili ya kuboresha katika ujenzi wa kiwango cha lami. Ni sehemu ya mradi huu wa uijenzi wa hii Bandari ya Kilwa Masoko, ahsante.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya kutoka Igawa kuelekea Mbeya inapita Jimbo la Makete. Ni barabara yenye volume kubwa ya magari na inachangia uchumi wa Tanzania kwa kiwango kikubwa sana. Je, ni ipi commitment ya Serikali ili iweze kujenga barabara hii ambayo pia anaitumia Mheshimiwa Spika na imekuwa ni nyembamba kwa kiwango ambacho inahatarisha sana usalama wa wapitaji wa barabara ile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii aliyoitamka ya Igawa kwenda Makete inapita milimani na ni barabara muhimu sana katika uchumi wa wananchi wa maeneo hayo. Pia amesema kwamba ni barabara ambayo Mheshimiwa Spika anapita. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo hayo kwamba, hii barabara ni miongoni mwa barabara ambazo ziko kati ya huu Mradi wa EPC + Financing kuanzia Igawa – Mbeya mpaka Tunduma.

Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ambazo zinakwenda kusainiwa, kwa ridhaa yako naomba nizitaje hapa ili Waheshimiwa Wabunge wasipate nafasi ya kuwa na mashaka.

(i) Ifakara – Malinyi – Lumecha hadi Songea;

(ii) Igawa - Mbeya – Tunduma;

(iii) Karatu – Haydom – Mbulu – Sibiti hadi Maswa;

(iv) Mafinga – Mgororo;

(v) Masasi – Nachingwea – Liwale;

(vi) Kongwa – Kibaya – Arusha; na

(vii) Handeni – Kiberashi – Chemba - Kwa Mtoro hadi Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi zitasainiwa mwezi wa sita, na tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, katika historia ya nchi hii tunakwenda kusaini kilometa zaidi ya 2000 na Mheshimiwa Waziri alikwisha tamka akiwa pale Singida.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nilitaka nimuulize tu Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa mtakuja Kiteto kusaini mkataba wa hii barabara ya Kongwa – Kiteto mpaka Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hii ni miongoni mwa barabra ambazo nimezitamka hapa kwamba zitasainiwa kabla ya mwezi wa sita. Barabara ambazo ziko katika EPC+ Financing, ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na umuhimu mkubwa wa kiuchumi na shughuli za kijamii kwa wananchi wa Ngoreme hasa upande ule wa Majimoto, Busawe na Iramba. Ni lini sasa barabara ya Musoma kutoka pale makutano ya Nyakanga mpaka Sirori Simba kupitia Iramba - Majimoto mpaka Nyasirori itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitamka Mheshimiwa Mbunge, ni barabara ambayo katika mwaka huu wa fedha tulikuwa tumeifanyia upembuzi yakinifu wa awali na katika mwaka wa fedha ujao tutaifanyia upembuzi yakinifu wa kina kama maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza niseme sijaridhishwa na majibu ya Serikali kwa namna ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema. Kwa sababu tarehe 17 mwezi huu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi akiwa Singida akisaini mikataba aliitaja barabara yetu ya Makongolosi kuelekea Mkiwa kuwa na yenyewe itajengwa kwenye mradi huu wa barabara ambazo amezitaja hapa lakini majibu ya Serikali yanaonekana kugongana.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo niweze kuuliza sasa. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri, alikwishasema fedha zipo za kuweza kujenga zaidi ya kilometa 2300. Je, ni lini sasa Serikali itatoa pesa hizi ili barabara yetu ya Makongolosi kwenda kuunganishwa mpaka Mkiwa iweze kujengwa kwa kuwa barabara hii ni muhimu sana kiuchumi kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Singida?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kuanzia Makongolosi kupita mpaka Mkwajuni mpaka Mbalizi ni barabara ya vumbi na imeahidiwa muda mrefu kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na tayari Serikali imeshatenga kilometa 50 kuweza kujengwa. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kuanzia Makongolosi hadi Mkwajuni ili iweze kuunganishwa mpaka Mji mdogo wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Njelu Kasasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Lupa, kwa kufuatilia barabara hii ambayo ni shortcut ya kwenda katika Mkoa wa Mbeya kutokea Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii kama nilivyokwisha jibu kwenye majibu yangu ya awali yenye kilometa 503, tumekuwa tukijenga awamu kwa awamu. Pia hadi sasa tumesaini mkataba wa kipande hiki cha Noranga - Doroto kilometa sita na Itigi – Mkiwa kilometa 25.6. Maana yake nini? Maana yake tunaendelea na ujenzi mpaka Makongolosi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nikuhakikishie ya kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaendelea kujenga barabara hii na katika mwaka wa fedha ujao pia tumetenga fedha kwa ajili ya kutoka Makongolosi kwenda Singida.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, barabara ya Makongolosi – Mbalizi. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kila mwaka na mwaka huu imetengewa kilometa 50 na mwaka ujao pia tumewekea fedha za kuanza ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba barabara hii katika mwaka ujao wa fedha itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Majita – Musoma – Busekela yenye urefu wa kilometa 92 imechukua muda mrefu sana kukamilika. Hadi sasa imekwishajengwa kwa kilometa tano tu.

Je, Serikali ni lini ina mpango wa kupeleka fedha za kumalizia barabra hiyo ukizingatia itaongeza au kukuza uchumi kwa wana Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara kwa Ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, Agnes Marwa, kuhusiana na suala la barabara hii ya Majita – Musoma. Ni kweli tumekwishajenga kilometa tano na suala la kupeleka fedha tutaendelea kupeleka fedha katika barabara hii ili ikamilike kwa ukamilifu wake, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na foleni inayotokana kati ya Mkoa wa Morogoro na Pwani. Ni lini ujenzi wa barabara nne kuanzia Chalinze mpaka Morogoro Mjini utajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ya Chalinze kwenda Morogoro ni barabara ambayo tumeifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kupitia makampuni ya Korea Kusini na mwezi wa nne walileta ripoti maalum inayoonesha ni kwa kiwango gani tujenge. Je, iwe ni kwa mfumo wa PPP ama iwe ktika mfumo wa EPC + Financing? Sasa Serikali imeona umuhimu wa barabara hii iwe katika mfumo wa PPP. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge niwahakikishie na wananchi wote wa eneo hilo kwa sababu ni barabara kuu, kwamba barabara hii itajengwa kwa mfumo wa PPP na tayari tumeshaanza ku– engage na wakandarasi, ahsante.
MHE. ALILY A. MLAGHILA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Barabara ya Uyole – Kasumulu ina zaidi ya miaka 35 sasa, muda ambao imekwishapita design age yake. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuanza kuiwekea hata layer ya juu badala ya kusubiri ibomoke yote?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa kufuatilia barabara hii na nimhakikishie tu kwamba kwa kuwa hapa Kasumulu ni lango muhimu la kwenda katika Nchi Jirani ya Malawi. Katika bajeti zetu za TANROADS kupitia Mkoa wa Mbeya tumetenga fedha kwa ajili ya kuboresha barabara hii iweze kupitia wakati wote, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. nilitaka kuuliza swali la nyongeza kwamba barabara itokayo Malagarasi kwenda Uvinza, kipande cha kilometa 51 kimekuwa na muda mrefu sana na sasa kimeanza kutengenezwa lakini kinasuasua sana.

Nini mpango wa Serikali kuhakikisha wanamaliza maana barabara hiyo ni kipande hicho ndicho kilichobaki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kati ya maeneo ambayo barabara imechukua muda mrefu ni pamoja na kipande hiki
cha Malagarasi – Uvinza ili Mkoa wa Kigoma uweze kuunganishwa na mikoa jirani ikiwemo Tabora.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa Kigoma. Mtakumbuka ziara aliyoifanya Mheshimiwa Rais, alipokuwa Kigoma ni miongoni mwa barabara hizi ambazo alizotoa maelekezo kwamba ni lazima ikamilike. Sisi Wizara ya Ujenzi katika bajeti hii inayoendelea na inayokuja tumetenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru Serikali kwa barabara yetu ya Kiberashi – Handeni – Chemba hadi Singida lakini ili barabara hiyo iweze kutumika vizuri kuna interchange mbili. Kwanza ni kutoka Zamahelo mpaka Donsee nyingine ni kutoka Goima hadi Bicha. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha interchange hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Monni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pongezi za Serikali nazipokea kwa niaba lakini pongezi hizi ziende kwa Mheshimiwa Rais, maana yeye ndiye anayetoa hizi fedha na hususani katika ujenzi wa barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge umeizungumzia. Kwa kuanzia kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii nafikiri itakuwa vema zaidi tukianza kama ambavyo Serikali imepanga ndipo tuanze na hizo zingine kwa kuwa hii ndio itakuwa lango muhimu

la kuunganisha kati ya Mkoa wa Dodoma na Mkoa jirani, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Mpanda – Kaliua – Ulyankulu mpaka Kahama yenye urefu wa kilometa 472 iko kwenye Ilani ya Uchaguzi 2015/2020 lakini iko kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025. Je, barabara hii sasa ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya kilometa 472 ni kweli iko kwenye Ilani ya 2025 na Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza ilani hii ya 2025. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba kwa kuwa bado tunaendelea na utekelezaji wa ilani hii, uwe na uhakika kwamba pia barabara yako itajengwa.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Ipo barabara ya kutoka Mbezi kwenda Mpiji Magohe au barabara ya Victoria Road. Ni barabara ambayo iko ndani ya mpango kwa miaka mingi na bajeti lakini iko chini ya ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini ndani ya ilani kwa miaka 10. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii iko kwenye Ilani lakini pia tumekwisha ifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na katika bajeti ijayo nikuombe Mheshimiwa Mbunge tutakayoisoma jumatatu na jumanne, tuipitishe bajeti hiyo ili barabara hii iweze kujengwa kwa kuwa ni miongoni mwa barabara hizo pia, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nilitaka ifahamike kwamba meli ya MT Sangara ambayo imefikia asilimia 90.7 ni meli ya mafuta siyo ya abiria wala mizigo, inabeba mafuta tu na kwa maana hiyo haina msaada mkubwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa imekuwa kawaida kwa Serikali kila mwaka kutenga bajeti na kuleta hapa kwenye Bunge lakini hakuna utekelezaji, na kwa kuwa, katika Ziwa Tanganyika kwa sasa hakuna meli hata moja ya Serikali inayofanya kazi. Nataka commitment ya Serikali kwamba bajeti itapungua kwenye eneo lingine lolote la Wizara na siyo kwenye meli hii, kwamba lazima meli hizi zitatengenezwa na kurudi majini, nataka commitment ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri wetu wa Ujenzi na Uchukuzi amesoma bajeti ya Wizara yetu na ameonesha commitment ya kiwango cha juu kabisa kuhusiana na namna ambavyo Ziwa Tanganyika tunakwenda kujenga meli mbili mpya pamoja na chelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi, commitment nyingine ya Serikali ni hizi meli ambazo hazifanyi kazi kwa sasa na tayari kwa mfano, hii MV Mwongozo ambayo tayari Mkandarasi ameshapatikana, ni Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) pamoja na hii meli ya MT Sangara ambayo amesema kweli ni ya mafuta lakini inafanya kazi katika Ziwa Tanganyika na iko asilimia 90. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa fedha ujao inakwenda kufanya haya ambayo imeahidi hapa. Ahsante. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Reli ya Kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay ni miongoni mwa miradi midogo iliyopo katika Mradi huu mkubwa wa Mtwara Corridor. Serikali imesema itatekeleza mradi huu kwa ubia. Mimi nataka kujua kwa nini Serikali isitekeleze mradi huu yenyewe ikizingatia umuhimu wake kuliko kusubiria ubia ambao hauna uhakika utapatikana lini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, mwaka 2004 Lilongwe – Malawi kulisainiwa mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu wa Mtwara Corridor na Tanzania inatakiwa iitishe Mkutano ili kutathmini utekelezaji wa mradi huu umefikia hatua gani? Mpaka leo Tanzania haijaitisha: Nataka kujua, ni lini Serikali ya Tanzania itaitisha mkutano huo wa nchi nne; Msumbiji, Malawi, Zambia na Tanzania yenyewe ili kutathmini mradi huu umefikia hatua gani kwa sababu ni mradi muhimu sana katika mikoa ya kusini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uamuzi wa kuzishirikisha sekta binafsi ili kuongeza tija. Pia, kwa sababu Serikali ina commitment nyingi, inaweza ikachelewa kupata fedha kwa ajili ya huu mradi. Hata hivyo, kuna makampuni zaidi ya manne kutoka China, South Africa, Australia pamoja na Marekani, ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika mradi huu wa ubia, ukizingatia kwamba eneo hili tayari ni potential kubwa. Uwepo wa makaa ya mawe pamoja na chuma unasababisha wawekezaji hawa waje. kwa sababu tayari mzigo upo metric ton zaidi ya milioni 428 ambapo tunaweza tukachimba zaidi ya miaka 100. Kwa hiyo, sekta binafsi tayari imeonesha utayari huo. Kwa hiyo, tutaendelea kuwa-engage ili mradi huu uweze kuanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua ni lini sasa Mkutano wa Wakuu wa Nchi utaitishwa. Tarehe 15 ya Mwezi wa Sita kutakuwa na mkutano wa wadau wote wa sekta na Wizara ya Madini, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Uchukuzi, wadau kutoka sekta binafsi pamoja na taasisi zote za Serikali hususani TRA, MSCL, TPA, RAS Mtwara, RAS Lindi na Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara na Lindi mnakaribishwa kwa ajili ya kujadili jambo hili kama maandalizi ya kuzi–engage nchi zingine za Msumbiji pamoja na Malawi, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunujibu swali langu kwa ufupi na kwa malengo ambayo niliyakusudia. Ninapenda nishauri barabara hii ianze kujengwa toka Nangurukuru kuelekea Liwale kwa sababu itatengeneza muunganiko wa lami inayotoka Dar es Salaam – Kilwa Masoko pamoja na Mkoani Lindi kuelekea Liwale na kugusa majimbo yote yalipo katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kupata kujua;

Je, katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii, itajengwa kilometa ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna barabara ya kutoka Njianne kwenda Kipatimu yenye urefu wa kilometa 50, imekuwa ikijengwa kwa urefu wa mita 700 mwaka 2021, mita 700 2022 na mita 600 2023;

Je, ni lini Serikali itakuja na mradi wa kimkakati ili iweze kujenga kwa urefu mrefu katika barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa karibu katika barabara hii. Lakini pia tumeupokea ushauri wake, kwamba ianze kujengwa kutoka Nangurukuru kwenda Liwale, naamini haya tutaweza kuyazungumza. Mkandarasi huyu mmoja anaweza akaanza upande wa Nangurukuru – Liwale ama Liwale – Nangurukuru, yote yanawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake mawili ya nyongeza, la kwanza anataka kujua ni kilometa ngapi katika ujenzi huu utakaoanza Mwaka wa Fedha 2023/2024; ni kilometa 72 kati ya kilometa 230.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anataka kujua barabara hii ya Tinga – Kipatimu, ni kweli kwamba barabara hii tumekuwa tukiijenga sisi kama TANROADS kidogokidogo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuijenga barabara hii hadi ukamilifu wake, na sasa tumetenga jumla ya takribani milioni 281.81 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii katika Mwaka wa Fedha ujao, 2023/2024, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bandari iweze kufanya kazi vizuri, inahitaji kuwa na barabara ya lami kutoka bandarini, lakini pia inahitaji kuwa na reli kwa ajili ya kubeba mizigo. Kwa kuwa barabara ya lami kutoka Karema kwenda Mpanda bado haijakamilika, na kwa kuwa Serikali bado haijajenga reli kutoka Karema kwenda Mpanda;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kujenga reli pamoja na barabara ya lami ili kuwezesha kubeba mizigo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuwa na bandari ambayo haifanyi kazi, ambayo haina meli, ni sawa na kuwa na nyumba ambayo haikaliwi na mtu. Ziwa Tanganyika halina meli inayofanya kazi sasa hivi, MV. Liemba haifanyi kazi na MV. Mwongozo haifanyi kazi;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inajenga meli ili ziweze kubeba mizigo kutoka Kongo na nchi za jirani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Bandari yetu ya Karema inatakiwa ifungamanishwe na barabara kwa kiwango cha lami pamoja na reli. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka wa fedha ambao tunauanza wa 2023/2024, kati ya kilometa 112 zote zimekwisha tangazwa na itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuifungua bandari hii ya Karema – Ikola mpaka Kagwira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anataka kujua meli katika Ziwa Tanganyika. Kama ambavyo tuliweza kuwasilisha bajeti yetu siku ya Jumatatu na Jumanne, tuliweza kutoa commitment kwamba kati ya Ziwa Tanganyika, meli tatu tunaendelea kuzikarabati, hususan Meli ya MT. Sangara inayobeba mafuta ambayo iko asilimi 90, pia kuna Meli ya MV. Liemba ambayo tayari mkataba wake tutasaini mwezi Juni, na MV. Mwongozo tumepata mkandarasi mshauri atakayeweza kuishauri Serikali namna gani ya kuifanya hii meli i-balance maana ilikuwa na shida ya stability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo pia tumetenga fedha kwa kutengeneza meli kubwa mbili, moja ya mizigo itakayobeba tani 3,500 na nyingine ni ya kubeba abiria 600 pamoja na tani 400 ambayo kwa ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma, mlisema ikiwezekana ziwe mbili, na sisi Serikali tukasema tunakwenda kulifanyia kazi hili. Kwa hiyo hii ni mipango na tunakwenda kufanya katika mwaka wa fedha ujao, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ambayo ameegemea zaidi kwenye mtazamo wa Sheria badala ya hali halisi ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Je, ni lini mmechukua hatua kwa meli zilizozidisha abiria na kusababisha vifo vingi zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inavyombo vingapi? Vinavyotoa huduma za abiria na mizigo baharini na maziwa makuu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, Mwantumu Dau Haji, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya vyombo huwa vinakiuka sheria kwa kuzidisha uzito wa abiria na mizigo. Kupitia TASAC tunatoa elimu kwa wamiliki wa vyombo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spaka, pili; sheria inatutaka kwa yeyote atakayezidisha uzito kulipa faini na kabla meli haijaondoka kuna Maafisa ambao wanahakikisha mstari wa ujazo haujazidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, faini hizo zinatofautiana kulingana na urefu wa chombo na chombo. Chombo chenye urefu wa mita zaidi ya 24 wanalipa faini ya shilingi laki nne na chombo chenye urefu chini ya mita 24 wanalipa faini ya shilingi laki mbili lakini ikithibitika pia huyo mmiliki ameshindwa kulipa faini hiyo anapelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza idadi ya vyombo tulivyonavyo hapa nchini. Kwa Sensa ambayo ilifanywa na TASAC mwaka 2021 kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu wa Taifa (NBS) inaonesha vyombo vyote tulivyonavyo hapa nchini kwa ukanda wa bahari, maziwa makuu yote, mito na maziwa madogo ni 52,189; hii ndiyo takwimu iliyofanyika mwaka 2021. Na kati ya vyombo hivyo asilimia 53.6 vipo Ziwa Victoria, asilimia 13.4 vipo Bahari ya Hindi, asilimia 10.2 vipo Ziwa Tanganyika, asilimia 7.6 vipo Ziwa Nyasa na asilimia 15.2 vipo maeneo ya Maziwa Madogo pamoja na Mito. Ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa maamuzi hayo mazuri na jibu zuri ambalo wameweza kutujibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati barabara hii inapanuliwa kuna wananchi ambao walikuwa wamejenga pale na walibomoa nyumba zile ili kupisha ujenzi wa barabara ile; je, ni lini watapata fidia yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naishukuru Serikali kwa sababu imeleta taa za barabarani katika barabara hii ya Kenya Road. Lakini taa hizi zimewekwa kwa mbali sana kiasi kwamba hazimuliki vizuri.

Ni lini sasa zile sehemu ambazo hazina taa za barabani zikiwemo za Masara, barabara ya Musoma pamoja na Magena watawekewa taa za barabarani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia kwa wale waliobomolewa kupisha ujenzi wa barabara hii ni kweli kwamba wale wote waliobomolewa ni kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 2007 Na. 13, kwamba waliokuwa ndani ya hifadhi ya barabara kwa maana ya mita 22.5, hawa ndio walioguswa, lakini waliokuwa nje ya hifadhi ya barabara, mpaka mita 30 hawakuguswa. Kwa hiyo hapa hakutakuwa na fidia kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la taa za barabarani; tumewaelekeza managers wote wa TANROADS nchi nzima kwamba lazima watenge fedha kwa ajili ya kuweka bajeti za taa barabarani na kwa maana hiyo kwenye mwaka wa fedha ujao katika eneo hili la Tarime Mjini, tumetenga shilingi milioni 270 kwa ajili ya kusimika taa za barabani na mitaa yake yote. Na hata hivyo, kuna taa nyingine ambazo zimeshasimikwa lakini tutaongeza zaidi ili huu mji uweze kupendeza zaidi, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwa nini ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Magole – Turiani – Mziha – Handeni umeanzia Magole na kuishia Turiani na kuacha kipande cha Handeni – Mziha – Turiani?

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kwagilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii aliyoitamka kwamba imeanzia sehemu hiyo kipande na kingine kimeachwa, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali ni kujenga yote. Kwa hiyo tumeanza hicho kipande, lakini hata kipande kingine pia tutakimalizia, ahsante.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka taa za barabani katika Mji wa Nyamilangano ambao tayari umewekewa kilometa tatu za lami?

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, taa za barabarani katika maeneo ambayo ameyasema tumetenga kwenye bajeti ambayo imepitishwa na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo tutamuwekea katika eneo lake Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni za Rais wa Awamu ya Tano, aliahidi katika Mkoa wa Shinyanga atatujengea barabara kilometa 10, na juzi, mapema mwaka huu, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, aliahidi wakati akizindua Hospitali ya Rufaa ya Mwawanza pale Shinyanga, kwamba atatujegea kilometa 10.

Nini mpango wa Serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi hizo za viongozi wa Kitaifa, hasa katika mwaka huu wa fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zote za viongozi wa Kitaifa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika bajeti ya mwaka huu tumezizingatia kwa kiwango kikubwa. Na kwa maana hiyo, hata barabara aliyoisema Mheshimiwa Salome Makamba ni miongoni mwa barabara ambazo tunakwenda kuzijenga, ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kuanzia Kalela – Munzeze mpaka Buhingwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitamka kuanza Kalela na kuendelea ni barabara ambayo katika bajeti ya mwaka ujao tumeitengea fedha kwa ajili ya kufanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ahsante.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, barabara ya kutoka Kibena – Lupembe – Madeke hadi Taveta, Mheshimiwa Swalle, Mbunge huyu, amekuwa akiizungumza sana barabara hii. Ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa kwa lami ili wananchi wa Lupembe wapate imani na Serikali yao?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii inaunganisha Mikoa ya Njombe, Iringa na inakwenda mpaka Morogoro, na katika mwaka wa fedha huu ambao tutaanza, ni miongoni mwa barabara ambazo tumezitengea fedha, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kuwahakikishia Wana-Singida Magharibi kwamba kabla ya mwezi ujao tutakuwa tumesainiwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya lami, kilometa 76; tunaipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; je, Serikali sasa iko tayari kuifanyia upembuzi yakinifu barabara ambayo inatoka Singida – Mtunduru – Ighombwe – Iyumbu mpaka Tabora ambayo itaunganisha na barabara inayokwenda Kwamtoro – Kiteto mpaka Tanga ili kuwarahisishia wananchi wa Singida mawasiliano ya Tanga, Singida na Tabora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali iko tayari kuipandisha hadhi barabara ya Puma – Ihanja – Iseke – Mwintiri – Igelansoni mpaka Itigi ili kuwapunguzia adha wananchi kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara hii unaotokana na hali za mvua zinapokuwa zikinyesha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu katika barabara hizi zote na hatimaye tunakwenda kusaini mkataba mwezi ujao (Juni).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza kuhusu upembuzi yakinifu katika hii barabara ya Singida – Mtunduru – Ighombwe – Ngungira mpaka Iyumbu yenye kilometa 113, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida Magharibi kwamba katika bajeti ya mwaka tutakaoanza 2023/2024 ambao mlipitisha bajeti siku ya Jumanne, tumetenga fedha takribani shilingi 165,041,665 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, na kwa maana hiyo barabara hii ipo katika mpango kama maandalizi ya kuja kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kupandisha hadhi barabara ya Puma – Ihanja – Mwintiri – Iyumbu; barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) na sisi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tuko tayari kama itapandishwa hadhi kwa kufwata utaratibu ule ambao umewekwa, kwa maana ya kupitia kwenye vikao maalum, kupitia DCC, inakwenda kwenye Road Board ya Mkoa, na hatimaye Mwenyekiti wa Bodi anaandika barua kwa Mheshimiwa Waziri ili Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi atume timu kwenda kuikagua hii barabara na hatimaye tutoe hiyo ridhaa ya kupandishwa hadhi barabara hii, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na ya kuleta tumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza;

a) Je, ni lini sasa mtaanza mchakato wa kuwashirikisha wadau kuhusu ujenzi huo?

b) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari sasa kuambatana na Mheshimiwa Manyanya na Mheshimiwa Agnes Hokororo, ili kwenda kufanya mikutano kwenye maeneo haya mawili ili wananchi waelewe kabisa kwamba, huo mradi sasa ni kweli utaenda kuanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa kwanza katika ujenzi huu wa standard gauge kupitia mfumo huu wa Public Private Partnership kwa njia ya ubia, tayari tumeitisha kikao tarehe 15 ya mwezi wa sita, mwezi huu, ambapo kitashirikisha Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi, pamoja na Wizara ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara na Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake zote pamoja na wadau wote ambao wanashiriki katika uchimbaji wa makaa ya mawe. Na kwa hivyo basi, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa hii ya Ruvuma pamoja na Mtwara kushiriki katika mkutano huu pamoja na Lindi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu kuambatana kwenda site; niko tayari kuambatana na Waheshimiwa aliowatamka, Mheshimiwa Angelina Manyanya pamoja na Agnes Hokororo na yeye mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Ntara, ili tukapate kutoa elimu na kuwaelimisha wananchi katika maeneo hayo kuhusu uwepo na ujio wa mradi huu muhimu katika Mtwara Corridor.
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. M. A. KABUDI: Mheshimiwa Spika, nashukiuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kujua ni lini Serikali itakarabati reli kutoka Kilosa – Mikumi hadi Kidatu, ili ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Palamagamba Kabudi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amefuatilia jambo hili kwa ukaribu. Tumetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa reli hii ya Kilosa – Mikumi, na tutaanza rasmi mwezi wa saba mwaka huu kwa ajili ya kuihuisha tena reli hii ianze kufanya kazi kama ilivyokuwa inafanya kazi miaka ya zamani. Ahsante.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Watanzania tuna shauku kubwa;

Je, ni lini reli yetu ya kisasa ya mwendokasi itaanza kutoa huduma kwa wananchi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Reli hii ya mwendokasi (SGR) kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro, kilometa 300 itaanza kutoa huduma mwezi wa saba. Hivi sasa mwezi huu wa sita tunategemea kupokea mabehewa yenye ghorofa na hatimaye mwezi wa saba tutapokea kichwa. Na kwa kuwa tayari miundombinu yote testing na kila kitu kimeshafanyika katika njia hii ipo tayari kwa ajili ya kuanza mara baada ya mabehewa haya yatakayoingia mwezi huu wa sita na vichwa vitakavyoingia mwezi wa saba.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mpango wake wa kujenga reli kutoka Tunduma mpaka Bandari ya Kasanga na Kabwe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, reli hii ya kutoka Tunduma mpaka Rukwa, katika mwaka wa fedha ujao tutaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa awali, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninataka kujua, je, ni lini mabehewa 37 yaliyokuwa kwenye karakana ya reli yakikarabatiwa kwa ajili ya safari za Kigoma – Dar es Salaam yataingia kwenye reli na kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mabehewa aliyoulizia Mheshimiwa Mbunge ni kweli tunakarabati mabehewa 37, na kila mwezi tunakarabati mabehewa 22, 20 za mizigo na mbili za abiria. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wasafiri wote kutoka Kigoma kwamba mwezi ujao mabehewa haya yataanza kufanya kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma umejaliwa kuwa na makaa mengi sana na inasemekana kwamba makaa yaliyopo yanaweza kuchimbwa kwa miaka isiyopungua 80; na sasa Liganga Mchuchuma imefunguka: Je, kwa nini Serikali isitafute mwekezaji kwa mfumo wa BOT (Jenga, Endesha na Kabidhi) kwa base ya makaa ya mawe yaliyopo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa kwa sasa kumekuwa na usafirishaji wa makaa ya mawe kwa malori mengi sana, malori 250 kwa siku na tani 360,000 kwa mwezi na kumekuwa na malalamiko ya wananchi kwamba Mkoa wa Ruvuma na Mtwara tunafaidikaje: Je, Serikali inaweza kuja na taarifa rasmi, yaani tani ngapi mpaka sasa hivi zimeshasafirishwa na Mkoa wa Ruvuma umepata nini; na Taifa linapata nini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la ujenzi wa reli katika ushoroba huu wa Mtwara. Ni kweli kwamba tayari Serikali tumeshaanza ku-engage ubia kwa maana ya PPP na kuna nchi zaidi ya tano ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza, kwa maana ya kuna nchi ya Marekani, Afrika Kusini makampuni kutoka katika hizo nchi, Morocco, Italy, Croatia pamoja na Canada, kwa maana ya kwamba makampuni haya yapo tayari kushirikiana na Serikali katika kujenga reli hii kwa mfumo wa ubia.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu manufaa na kuja na taarifa rasmi hapa Bungeni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Njombe kwamba Serikali ipo tayari kuja na taarifa ya manufaa ya uwepo wa makaa ya mawe katika maeneo hayo tangu tulipoanza kuchimba mpaka sasa. Kwa kupitia pia wenzetu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Fedha tutashirikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha, Shilingi bilioni 15 kwa kuanza malipo na fidia kwa maeneo haya la Liganga na Mchuchuma na tayari wameanza kutoa elimu katika maeneo haya. Ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Anachokieleza Naibu Waziri uhalisia kule si kweli kwa sababu mabasi yanayotoka masafa marefu unakuta yana abiria lakini yanasingizia hayana abiria matokeo yake yanawaacha wananchi juu kwa juu. Kwa mfano, pale Igunga maeneo ya mnadani wananchi wanafika wanashushwa tu wanaachwa wanaanza kuhangaika kutafuta bajaji na bodaboda kurudi Mjini.

Je, ipi ni kauli ya Serikali katika hili ili kuepusha adha kwa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, moja ya mwongozo wa Serikali ni kuhakikisha Halmashauri zetu zinakusanya mapato na Halmashauri nyingi vyanzo vyetu vya mapato ni pamoja na hizi stendi za mabasi lakini mabasi yanatumia kigezo cha kusema hawana abiria lengo wasiingie Halmashauri ili tusipate mapato. Pia naomba kauli ya Serikali katika hili, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nicholaus Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha kujibu kwenye jibu langu la msingi kwamba Sheria ya Usalama Barabarani, lakini pamoja na wadau, tulikaa na wadau mwaka jana tarehe 24, Mwezi wa Nne 2022, wadau wote wa usafirishaji, tulikubaliana kwamba ili kupunguza gharama kwa abiria ni pamoja na mabasi haya ambayo hayana abiria wa kushusha ndani wala hakuna anayepakia yasiingie ili kupunguza muda wa mabasi hayo kwenda kwa sababu wanasafiri umbali mrefu.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kama kuna basi lolote ambalo limeshusha abiria njiani na wakati eneo hilo kuna kituo cha mabasi kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu cha 50 (1) na Sura ya 168 kimeelekeza wazi kwamba dereva huo lazima achukuliwe hatua za kisheria. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na jeshi la polisi tutaendelea kusimamia jambo hili ili mabasi haya yafuate utaratibu huu kama ambavyo tulikubaliana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu suala la mapato katika Halmashauri zetu hususan katika vituo hivyi vya mabasi, ni kwamba siyo kila basi kama nilivyokwisha kusema litaingia kwenye kituo, lakini kwa mabasi yale ambayo yataingia kwa masafa mafupi yana wajibu wa kulipa ushuru katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ninataka kufahamu Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi mpya ya mabasi Bukoba Mjini? Ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa stendi katika Mkoa wa Kagera, Bukoba tutawasilina na wenzetu TAMISEMI ambao wanasimamia jambo hili na naamini katika bajeti yao mwaka huu huenda wamepanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi hii. Ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu ni sehemu ya mpango ambao upo kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya nchi yetu Awamu ya Tatu ambao mwezi Julai unafikia hatua ya miaka mitatu ya utekelezaji. Ni maandalizi gani ya awali ambayo Serikali imeyafanya kuonesha kwamba ina dhamira ya dhati kujenga mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu ni sehemu ya mradi funganishi wa Mtwara Development Corridor ambayo makubaliano ya mradi huo ulifanyika Lilongwe - Malawi Novemba, 2004 na marais wanne wa hizi nchi nne.

Je, ni lini Serikali sasa kama mnufaika mkuu utarudisha utaraibu wa marais hao wanne kukutana na kuweza kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huu wa reli pamoja na miradi mingine ndani ya Mtwara Development Corridor? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Masasi Mjini, Mheshimiwa Idelphonce Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa mradi huu na Wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara na kwa swali la kwanza anapenda kujua maandalizi ya awali ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali tumeanza maandilizi ya awali, kwanza tumeanza vikao ndani ya Serikali pamoja na kufanya vikao na wadau mbalimbali na hivi ninavyosema tutakuwa na kikao kingine ambacho kimeitishwa na Mamlaka ya Bandari nchini kitakachofanyika tarehe 22 hadi 23 pale Mtwara na Waheshimiwa Wabunge mnakaribishwa katika mkutano huu kwa sababu ndio unaenda kuifungua Mtwara Corridor yote na wadau wengine ni pamoja na RAS kwa maana ya Mamlaka ya Mkoa wa Lindi, Mtwara yenyewe pamoja na Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi, ni kwamba mradi huu kwa kuwa kwanza kuna makampuni zaidi ya matano kutoka nchi mbalimbali kutoka nchi ya Uingereza, Canada, Marekani, Afrika Kusini, Croatia, Morocco wameonesha nia katika uwekezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na kwa maana hiyo, changamoto kubwa ilikuwa katika kikwazo ambacho kilichokuwepo kupitia Sheria ya PPP ambayo Bunge lako tukufu wiki iliyopita imepitisha na kufanya mabadiliko madogo kwenye sheria hiyo.

Kwa hiyo, tunaamnini mapatano na mikutano itakayofuata sasa katika makampuni kutoka nchi hizi watakuja moja kwa moja kuwekeza kwa kuwa tayari tulishaanza kufanya nao mikutano hiyo, ahsante.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwamba hivi karibuni Bunge lako tukufu limefanya marekebisho ya Sheria ya PPP ili kuwezesha miradi kama hii kutekelezwa kwa urahisi.

Je, Serikali inatoa kauli gani sasa katika kuharakisha utekelezaji wa mradi huu ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wananchi wa maeneo hayo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikota kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina hamu kubwa sana katika kutekeleza mradi huu na ndio maana Serikali imeanza pia kulipa fidia. Nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya takribani shilingi bilioni 15 katika kulipa huu mradi wa Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, Serikali inaona umuhimu mkubwa wa mradi huu na ndio maana pia tumeitisha vikao hivi mara moja mara baada ya kubadilisha sheria yetu ya Public Private Partnership kwa maana ya ubia, ahsante. (Makofi)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwamba kazi ya mshauri ilifanyika toka mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na uthamini kwenye eneo ambalo reli hii itakwenda kupita.

Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa fidia kwa wananchi waliopo kwenye eneo ambalo reli hii ambapo mradi unaenda kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekwisha kusema kwamba upembuzi yakinifu ulikwishafanyika tangu miaka hiyo ya 2016 na Serikali hatua iliyofikia sasa ni kumuajiri Transaction Advisor kwa maana ya Mshauri wa Kifedha ambaye ndiye atakayetupa miongozo yote hadi kulipa fidia, lakini pia kupitia mthamini mkuu kwa sababu hili jambo lilishafanyika miaka mingi kwa vyovyote vile kutakuwa na haja ya kurudia kupitia daftari ambalo lilikuwa limeandaliwa kipindi hicho, nashukuru.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, miaka mitatu iliyopita Serikali katika mpango wake wa maendeleo ilijielekeza kwamba itajenga SGR kwa reli hii ya kuanzia Tanga – Moshi - Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo bado upo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali itajenga reli hiyo ya Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha, lakini kwa sasa tuna awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza na awamu ya pili kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma. Mara tutakapokamilisha hizi ndipo tutakapokuja katika hii reli ya kutoka Dar es Salaam – Tanga - Moshi mpaka Arusha na mpango huo uko vilevile.

Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo kwamba Serikali ina nia hiyo, lakini kwa sasa tunakamilisha hizi ambazo tumekwishaanza, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa ajali ni jambo ambalo sometimes haliepukiki, linaweza likatokea wakati wowote. Swali la kwanza; ili kuhakikisha usalama na kuepuka ajali za majini, je, TASAC inachukua hatua gani za kila siku za kuimarisha uokozi kwa ajili ya ajali za majini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani katika kuwekeza kwenye dhana kama vile boti za mwendokasi, vifaa na kuwawezesha kwa kuwapa utaalam wa uokozi wakati wa ajali za majini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdallah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Shirika letu la TASAC Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali hususani katika uokozi maeneo ya majini, ziwani pamoja na baharini kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza, huwa tunatoa elimu kwa wadau wote wanajishughulisha na masuala ya uvuvi baharini ama baharia. Hatua ya pili, kupitia TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini) ambako tunatoa taarifa ya hali ya hewa kila siku kwa Maziwa yote Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa pamoja na Baharini ili kujua mwenendo wa upepo pamoja na hali ya Maziwa hayo na Bahari kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine, tunafanya uchunguzi wa ajali ili kubaini vyanzo vya ajali hizo na itatusaidia katika ajali nyinginezo zitakazojitokeza na kuzuia zisitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumefanya mafunzo kwa Mabaharia kupitia International Maritime Organization na kupewa vyeti (Ithibati) kwa Mabaharia wote ambao wako katika maeneo hayo ya maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu vifaa, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali katika mwaka wa fedha ujao imetenga takribani bilioni 1.74 kwa ajili ya ununuzi wa boti mbili kwa ajili ya uokozi ambapo boti moja itakuwa kama ambulance katika kutatua changamoto zote ndani ya maziwa na baharini, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa vifo vingi vinavyotokea Ziwa Tanganyika vinatokana na wananchi kutumia usafiri ambao sio salama, kwa sababu hatuna usafiri wa uhakika kwa maana ya meli. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka usafiri wa kisasa Ziwa Tanganyika ili kuokoa vifo vya watu vinavyotokea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khenani, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliyosomwa tarehe 22 na 23, tulifanya Commitment kwamba mwaka wa fedha ujao 2023/2024 tunakwenda kujenga na kununua meli mbili za kisasa. Vilevile, hivi karibuni tulikuwa na vikao na Waheshimiwa Wabunge wote wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi kuhakikisha kwamba haya ambayo Serikali imefanya commitment katika bajeti, tunakwenda kuyafanya na naamini tutayatekeleza, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa mustakabali huo huo kwa jinsi zinavyotokea ajali nyingi si baharini tu hata pale panapotokea barabara inapokutana na reli kuna ajali nyingi sana zinatokea na kusababisha madereva wa treni sasa hivi wanapiga horn usiku kucha na kusababisha watu kutokulala hususani pale treni inapopita ili kuepusha ajali za barabarani zinazotokea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka automatic gates katika kila barabara na reli inapokatiza ili kuondoa ajali na kutokupiga horn usiku zinazowafanya watu kukosa usingizi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa sana kati ya maeneo ambapo barabara inapita na reli inapita. Kwa kutambua hilo, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika letu la Reli Nchini, tumetangaza tenda kwa ajili nya kuweka mifumo mipya automatic systems ambayo itakuwa ni gate way inajifunga na kufunguka automatic. Vile vile, tenda hii mwisho wa ku–submit ni kesho.

Kwa hiyo, wale wote ambao wako interested na ni international tender, wanakaribishwa kuomba ili tuweze kutengeneza mifumo yote na maeneo yote ya mapitio kati ya barabara na reli, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza na nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa hatua hiyo, lakini niombe mchakato wa malipo sasa uharakishwe kwa sababu uthamini huu umefanyika kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kumekuwa na changamoto katika umakini wa uhakiki hususani uliofanyika katika kipindi hiki cha pili ambapo wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wanapunjwa, kucheleweshwa kwa malipo haya na malalamiko mengine mengi. Je, Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili atakuwa tayari kuambatana nami kwenda Kilwa Masoko kukaa na wananchi hawa kuwasikiliza kero zao na hatimaye kuwapatia majawabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mradi na Mpango huu ni wa muda mrefu, je, ni lini sasa upanuzi na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa jambo hili la fidia kwa wananchi wake na Serikali imeendelea kulifanyia kazi. suala la kuambatana naye nimhakikishie nitaambatana naye mara baada ya vikao vya Bunge. Vile vile, nitakuwa na ziara katika Mkoa wa Lindi (Kilwa) Morogoro, Ruvuma pamoja na Iringa. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge hata huko Kilwa nitafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini hasa upanuzi wa kiwanja utaanza. Ni kwamba tayari tumekuwa na awamu mbili za upanuzi wa kiwanja hiki ambapo awamu ya kwanza ilikuwa kwa ajili ya kutanua ile run way kuweka moramu na sasa hivi tumejenga jengo la abiria lililogharimu takribani milioni 137. Awamu ya pili itafadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo iko katika mpango wa Serikali wa mwaka wa fedha ujao. Kwa hiyo, baada ya hapo kiwanja hiki kitakuwa kimekamilika, ahsante sana.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wananchi wanaozunguka Uwanja wa Ndege wa KIA wamekwishafanyiwa tathmini ya baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kupisha Uwanja wa Ndege wa KIA. Swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanza kulipa wananchi hawa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Saashisha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo alilolisema katika uwanja huu Serikali imefanya tathmini na uthamini na kinachoendelea sasa tumeshapeleka lile daftari kwa Mthamini Mkuu wa Serikali, tayari kwa ajili ya malipo na kwenda kupeleka Hazina. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wawe wavumilivu wakati wanasubiri malipo yao, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja, kwa kuwa Bunge lilishazimia Kampuni ya KADCO kurejeshwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, sasa ni lini Serikali itafanya hivyo kutii Azimio la Bunge? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sawali la pili, ni lini sasa Serikali itakamilisha mchakato wa sheria kuipa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kusimamia kuendeleza viwanja vya ndege nchini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) : Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli mwezi Novemba, 2022 Bunge lako tukufu liliazimia KADCO kuwepo chini ya viwanja vya ndege nchini. Swali la pili, uanzishwaji wa Sheria ya Viwanja vya Ndege nchini. Ninaomba nijibu yote kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya Bunge lako tukufu kuazimia kwamba lazima KADCO iwe chini ya TAA, hatua ambayo Serikali tumefanya mpaka sasa, kwanza tuliielekeza TAA kuandaa draft kwa maana ya mapendekezo ya sheria, na tayari draft hiyo imeshakuja Wizarani na tuliyapitia, kuyaboresha na kuyapeleka kwa Mwanasheria Mkuu ili kupata idhini au kibali. Tayari Mwanasheria Mkuu alishatoa kibali na sasa ipo ngazi ya wataalamu kwa maana ya Makatibu Wakuu.

Mheshimiwa Spika, tunategemea tutaomba kibali kwenye Baraza la Mawaziri ambalo litafanyika mwezi wa saba na hatimaye matarajio ya Wizara mwezi wa tisa sheria hiyo iweze kuwasilishwa hapa Bungeni. Sheria hii itaweka msingi wa viwanja vyote vya ndege nchini kuwa chini ya TAA.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna viwanja vya ndege vilivyo chini ya TANAPA, kuna viwanja vingine viko chini ya mamlaka nyingine za Serikali. Sasa sheria hii itaweka msingi kwamba viwanja vyote vya Serikali hapa nchini viwe chini ya TAA, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, andiko la TMA kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni latokea mwaka jana mwaka wa 2021; na sasa tunakwenda kukaribia mwaka wa 2022. Nilitaka commitment ya Serikali kujua kwamba hatua hii inaweza ikakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, jambo hili litasaidia katika kuleta maendeleo ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mmejipangaje kuendelea na maboresho wakati mkisubiri maamuzi yale ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shabani Ng’enda, Mbunge Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee kufuatilia Chuo hiki cha Hali ya Hewa pale Kigoma jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema maandiko yalianza tangu mwaka 2021; kimsingi maandiko tumeandika mwaka huu na tumepeleka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe 14 Aprili, 2022 lakini mwaka jana tulianza mazungumzo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hivi sasa tunavyosema tulitegemea Seneti itakapokaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndipo tupate mrejesho pengine ndani ya miezi miwili ijayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka afahamu tumejipangaje namna ya kuboresha chuo hiki. Ni kweli kwamba chuo hiki ni mkombozi mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa na chuo ni kimoja na Serikali kupitia bajeti zake mwaka wa fedha 2021/2022 tulitenga kiasi shilingi milioni 450 na tumejenga majengo pale kwa maana ya madarasa, maabara pamoja na computer room ama computer lab. Lakini hata hivyo, mwaka wa fedha na Waheshimiwa Wabunge mlitupitishia hapa tumetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga jengo la utawala, na tunahakika mwakani chuo hiki kitaboresha zaidi.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua ni mpango upi wa Serikali kuweka miundombinu shindani kwenye Chuo hiki cha Hali ya Hewa Kigoma; hasa ukizingatia kwamba chuo hiki kwa nchi za Afrika ni nchi chache sana ambazo zinatoa taaluma hii na sisi kuweza kulitumia hilo soko la kuweza kupokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali Afrika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bakar Hamad kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali tumejipanga vyema kukiboresha chuo hiki ili kiwe shindani katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na ukizingatia kwamba hiki ni chuo pekee kinachotoa elimu hii ya hali ya hewa; na kwa msingi huo tumeingia makubaliano na Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT) ili kianze kutoa elimu ya TEHAMA lakini zaidi ya yote kwa sababu pia Chuo chetu cha NIT kitaanza kutoa mafunzo ya urubani na mafunzo ya urubani yanaendana na hali ya hewa. Kwa hiyo, hata hiki pia kitakuwa sehemu ya hayo mafunzo; na zaidi ya yote pia chuo chetu tunakitangaza hata nchi jirani kwa maana ya Rwanda pamoja na Burundi, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, andiko la TMA kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni latokea mwaka jana mwaka wa 2021; na sasa tunakwenda kukaribia mwaka wa 2022. Nilitaka commitment ya Serikali kujua kwamba hatua hii inaweza ikakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, jambo hili litasaidia katika kuleta maendeleo ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mmejipangaje kuendelea na maboresho wakati mkisubiri maamuzi yale ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shabani Ng’enda, Mbunge Kigoma Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee kufuatilia Chuo hiki cha Hali ya Hewa pale Kigoma jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema maandiko yalianza tangu mwaka 2021; kimsingi maandiko tumeandika mwaka huu na tumepeleka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe 14 Aprili, 2022 lakini mwaka jana tulianza mazungumzo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hivi sasa tunavyosema tulitegemea Seneti itakapokaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndipo tupate mrejesho pengine ndani ya miezi miwili ijayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka afahamu tumejipangaje namna ya kuboresha chuo hiki. Ni kweli kwamba chuo hiki ni mkombozi mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa na chuo ni kimoja na Serikali kupitia bajeti zake mwaka wa fedha 2021/2022 tulitenga kiasi shilingi milioni 450 na tumejenga majengo pale kwa maana ya madarasa, maabara pamoja na computer room ama computer lab. Lakini hata hivyo, mwaka wa fedha na Waheshimiwa Wabunge mlitupitishia hapa tumetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga jengo la utawala, na tunahakika mwakani chuo hiki kitaboresha zaidi.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua ni mpango upi wa Serikali kuweka miundombinu shindani kwenye Chuo hiki cha Hali ya Hewa Kigoma; hasa ukizingatia kwamba chuo hiki kwa nchi za Afrika ni nchi chache sana ambazo zinatoa taaluma hii na sisi kuweza kulitumia hilo soko la kuweza kupokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali Afrika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bakar Hamad kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tumejipanga vyema kukiboresha chuo hiki ili kiwe shindani katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na ukizingatia kwamba hiki ni chuo pekee kinachotoa elimu hii ya hali ya hewa; na kwa msingi huo tumeingia makubaliano na Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT) ili kianze kutoa elimu ya TEHAMA lakini zaidi ya yote kwa sababu pia Chuo chetu cha NIT kitaanza kutoa mafunzo ya urubani na mafunzo ya urubani yanaendana na hali ya hewa. Kwa hiyo, hata hiki pia kitakuwa sehemu ya hayo mafunzo; na zaidi ya yote pia chuo chetu tunakitangaza hata nchi jirani kwa maana ya Rwanda pamoja na Burundi, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; naomba commitment ya Serikali, ni lini ujenzi huo wa daraja utaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Mheshimiwa Waziri tutaongozana nami ili twende kwenye eneo husika ambalo tunalizungumzia la kujenga daraja apate ufumbuzi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza anataka commitment ya Serikali kwamba, lini ujenzi huu hasa utaanza katika daraja hili la Mto Ruvuma, eneo la Kilambo. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia suala zima la daraja hili katika Mto huu Ruvuma, sababu tunatambua kwamba, daraja hili ni kiungo muhimu kati ya Nchi yetu ya Tanzania na Nchi ya Msumbiji. Kwa maana hiyo, mazungumzo ambayo tutayaanza hivi karibuni pamoja na Nchi ya Msumbiji kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nje, tutafanya commitment kupitia pia Wakala wetu wa Barabara Nchini (TANROADS) ili tuanze sasa mchakato mzima wa kuanza kujenga daraja hili, maana daraja hili lazima lijengwe na nchi mbili kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kwenda naye kuona hili eneo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya Bunge hili la Bajeti, mwezi Julai nitakuwa na ziara, hivyo nitakwenda kwa Mheshimiwa Mbunge kutembelea eneo hili. (Makofi)
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante nilikuwa naomba pamoja na majibu mazuri na mambo yanayoendelea katika hii Wizara kwa hawa wananchi, nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri; ni lini hawa wananchi watapata barua ya kuwaambia kwamba sasa wanakwenda kufanyiwa tathmini upya, ni lini maana yake mlikuwa mkiongea kila siku?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilikuwa nataka nijue ni lini hiyo tathmini itaanza kufanyika, wapate barua rasmi lakini pia wapate tarehe na mwezi ambao wataanza kufanyiwa tathmini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Kamoli, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini barua tutapeleka kwa wananchi ili wajue, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshakwisha andika barua kwenda Jiji na Jiji wao watachukua wajibu wa kwenda kuwajulisha na kuwahabarisha wananchi kwamba zoezi hili la tathmini linaanza rasmi, na ninaamini na kwa kuwa Jiji tumeshawaandikia tangu mwezi Aprili naamini watakuwa wamelifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, zoezi lenyewe swali lako la pili linaanza lini? Linaanza mwezi Julai na litakamilika mwezi Septemba, 2022. (Makofi)
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba je, fedha zilizotengwa za ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege Pemba zimejumuisha pia malipo ya fidia kwa wananchi ambao wameingia kwenye eneo hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bakar Hamad kuhusu uwanja wa Pemba; katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha utakaoanza mwezi wa Julai na tunashukuru Bunge lilipitisha tumetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa uwanja kwa Pemba lakini pamoja na fidia eneo lile ambalo tutatwaa kwa ajili ya ujenzi huo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, ni kwa muda mrefu sana wananchi wa Mkoa wa Singida wameelekezwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mkoa wa Singida. Nataka kujua ni lini Serikali itaanza uboreshaji na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Kishoa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nimemsikia mara kadhaa Mheshimiwa Mbunge akizungumzia suala la Uwanja wa Ndege wa Singida na sisi kama Serikali kupitia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi tunasema tuainishe eneo la ujenzi wa Uwanja wa Ndege na kufanya tathmini kwa maana ya kujua gharama halisi. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 tumetenga bajeti kwa ajili ya kufanya hizo tathmini kwa ajili ya eneo la ujenzi wa uwanja wa ndege hapa Singida.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru ninalo swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu spika, naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba vijana hawa wamekuwa wakifanya kazi nzuri nafahamu wapo ambao walifanya toka enzi za TRL. Je, Serikali inasema nini katika kuzingatia mafao yao wakati wa kuajiri?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali nipokee hizo pongezi za Mheshimiwa Mbunge na nipende kujibu swali lake la nyogeza kuhusu namna ambavyo Serikali inazingatia hawa vibarua kwa ajili ya maslahi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kusema kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali kupitia Waraka Namba Moja wa mwaka 2004 wa Utumishi wa Umma kwamba anayestahiki ama anastahili kuajiriwa katika ajira za kudumu inatakiwa awe amemaliza kidato cha nne, na hawa kwa kuwa wako darasa la saba na wengine hawajamaliza tunaendelea kuwashawishi na kuwashauri na kupitia Shirika letu la Reli nchini tutaendelea pia kuwaendeleza ili wafikie hicho kiwango na hatimaye kuajiri.