Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Atupele Fredy Mwakibete (21 total)

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-
Kwa muda mrefu wananchi wa Busokelo wamekuwa wakikumbana na adha kubwa ya ubovu wa barabara ya Katumba - Mbando - Tukuyu yenye urefu wa kilometa 82 inayoanzia Katumba (RDC) kupitia Mpombo, Kandete, Isange, Lwangwa, Mbwambo (BDC) hadi Tukuyu (RDC) na barabara hii imekuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa muda mrefu na Mkandarasi yuko eneo la ujenzi wa kipande cha kilometa kumi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha barabara hiyo kwa kujenga sehemu iliyobaki yenye kilomita 72?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Katumba - Mbwambo - Tukuyu yenye urefu wa kilometa 82 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya. Barabara hii ni ya changarawe na ipo kwenye hali nzuri kwani inapitika vizuri isipokuwa maeneo machache yenye miteremko mikali inayoteleza wakati wa mvua. Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya aina mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika wakati wote bila matatizo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika mwaka wa fedha 2009/2010, Serikali kupitia Wakala wa Barabara ilianza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulikamilika mwezi Februari, 2012.
Baada ya usanifu wa kina kukamilika katika mwaka 2013/2014 kiasi cha shilingi milioni 1,270 kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilomita 2.5 kwa kiwango cha lami. Aidha, baadaye Serikali iliamua kujenga kilimeta 10 ambapo mwezi Aprili, 2014 Wakala wa Barabara uliingia mkataba na kampuni ya CICO kujenga kilometa 10 kuanzia Lupaso hadi Bujesi kipande kilichopo
Wilayani Busokelo kwa gharama ya shilingi milioni 8,929.724. Ujenzi wa Kipande hicho unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa kilometa 72 zilizobaki kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-
Wananchi wa Bonde la Mwakaleli, Kata za Kandete, Isange na Luteba wanaoishi kando ya Hifadhi ya TANAPA wamekuwa wakinyanyaswa sana na watumishi wa TANAPA kwa kisingizio kwamba wamevamia Hifadhi wakati TANAPA ndio waliovamia makazi ya wananchi kwa kuweka mipaka mipya tofauti na ile ya zamani hali inayofanya baadhi ya shule na taasisi zingine kuonekana kuwa ndani ya Hifadhi ya TANAPA kwa sasa:-
Je, ni lini Serikali itarudisha mipaka ya zamani ili wananchi wasiendelee kuishi kwa wasiwasi, lakini pia waendelee na shughuli za kilimo kama ilivyokuwa zamani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa Livingstone ulikuwa Msitu wa Hifadhi yaani Forest Reserve ulioanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 1940, kwa lengo la kutunza vyanzo vya maji vya Ziwa Nyasa na baianuwai nyingine muhimu. Wananchi wa Kata za Kandete, Isange na Luteba katika Jimbo la Rungwe Mashariki mnamo mwaka 1945 walianza taratibu kuingia katika msitu huo na kufanya shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na makazi, kilimo na ufugaji, kinyume na Tangazo la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kunusuru vyanzo muhimu vya maji vya Ziwa Nyasa na baianuwai muhimu ndani ya msitu, Serikali iliamua kubadilisha hadhi ya Msitu wa Livingstone kutoka Forest Reserve kuwa Hifadhi ya Taifa Kitulo, iliyotangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Na. 279 la mwaka 2005, baada ya hatua zote muhimu za Kiserikali kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Tangazo hilo la Serikali la mwaka 2005, mnamo mwaka 2007 lilifanyika zoezi la uhakiki na uwekaji wa mawe ya mipaka ya hifadhi zoezi ambalo lilishirikisha wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau wengine muhimu ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Kitulo na viongozi wa vijiji husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la uhakiki na uwekaji mipaka kwa eneo lote la hifadhi lilikamilika mwaka 2010. Aidha, katika zoezi hilo ilibainika kuwa baadhi ya mashamba, makazi na miundombinu ya taasisi kama vile shule na kanisa, vimo ndani ya mipaka ya hifadhi na hivyo kusababisha migogoro kati ya hifadhi na wananchi, mgogoro ambao unahitaji kupatiwa ufumbuzi wa pamoja baina ya Serikali na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wa kudumu wa suala hili unafanyiwa kazi na Shirika la Hifadhi za Taifa, kwa niaba ya Wizara yangu kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na uongozi wa Mkoa wa Mbeya na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja. Wakati suala hili likisubiri kupatiwa ufumbuzi, wananchi wawe wavumilivu kwa kutofanya shughuli za uharibifu wa mazingira katika maeneo husika.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Busokelo hasa katika Kata za Kandete, Isange, Lutebe Lwangwa, Mpata, Kabula, Mpombo, Lufilyo Kambasegela, Ntaba, Lupata, Itete, na Kisegese wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji safi na salama; na kuna maeneo mengi ambayo mabomba uyamepita lakini maji hayatoki kutokana na kukosekana kwa matenki ya maj:-
(a) Je, ni lini Serikali itatatua kero hiyo ya maji kwa kujenga matenki ya maji kwenye Kata hizo?
(b) Mji wa Lwangwa ni Makao Makuu ya Halmashauri mpya ya Busokelo na kuna ongezeko kubwa la watu ukilinganisha na miundombinu ya maji iliyopo; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu mipya ya uzalilshaji wa maji kwenye eneo hilo jipya la mipango miji?
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilipokea shilingi milioni 907 ambazo zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Mpanda katika Kata ya Lupata na miradi wa maji Kasyabone na Kisegese katika Kata ya Kisegese. Miradi hii inahusisha ujenzi wa matanki yenye ujazo wa mita za ukubwa 90 kwa Kata ya Lupata na matanki wawili ya mita za ukubwa 45 kila moja katika Kata ya Kisegese. Katika bajeti ya mwaka 1015/2016 Serikali imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 171.94 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Kanyelele Kata ya Kabula, Ilamba katika Kata ya Kambasegela na kijiji cha Mpata katika Kata ya Mpata.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Lwangwa tayari Halmashauri imekamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha maji Mano Sekondari. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 Serikali imetenga shilingi milioni 280 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiahidi kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na Zahanati kwa kila Kijiji na Kituo cha Afya kila Kata na Hospitali kwa kila Wilaya ili kuwaondolea kero wananchi wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na wengine kupoteza maisha wakiwa njiani:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza mpango huo wa kuwa na Zahanati kwa kila Kijiji, Kituo cha Afya kwa kila Kata na Hospitali kwa kila Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Zahanati kwa kila kijiji, Vituo vya Afya kila Kata na Hospitali kila Wilaya, unafanyika kwa ushirikiano kati ya wananchi na Halmashauri kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD).
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu kubwa ya miradi hii huibuliwa na kutekelezwa na wananchi wenyewe na Halmashauri huchangia nguvu kidogo ili kukamilisha miradi hiyo. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi, inaendelea na ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali kila Wilaya. Ujenzi huo unafanyika chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi yaani MMAM, ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kwa mwaka 2016 hadi 6,935 katika mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 31.9. Aidha, utekelezaji wa program hii unaendelea, ambapo katika mwaka 2016/2017 Halmashauri zimetengewa shilingi bilioni 182.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele kimetolewa katika kukamilisha miradi viporo, badala ya kuanzisha miradi mipya. Ofisi ya Rais TAMISEMI, inafanya tathmini ya utekelezaji wa MMAM ili kujua idadi ya vijiji ambavyo havina Zahanati. Kata ambazo hazina Vituo vya Afya na Wilaya ambazo hazina Hospitali. Lengo la tathmini hiyo ni kuhakikisha maeneo haya yanapewa kipaumbele na kutengewa bajeti ili kuongeza huduma za afya karibu na wananchi.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
(a) Je, Serikali itakubali kujenga Hospitali ya Wilaya ya Busokelo hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wametoa eneo tayari na wako tayari kushirikiana na Serikali?
(b) Je, kama Serikali inakubali, ni lini kazi hiyo itaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni sera ya Serikali kuhakikisha tunajenga hospitali kila Wilaya, ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Utekelezaji umefanyika kupitia mpango wa Halmashauri kwa kushirikisha nguvu za wananchi, hivyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Hospitali ya Wilaya inajengwa katika Halmashauri mpya ya Busokelo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali hiyo umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo zimetengwa shilingi bilioni 2.0 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Halmashauri ya Busokelo ina changamoto za miundombinu ya barabara ambayo hairidhishi, na ukizingatia kuwa wananchi wake wanategemea zaidi shughuli za kilimo na usafirishaji wa gesi asilia ya carbondioxide.
(a) Je, ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Njombe kupitia Mwakaleli, kata za Kandete na Luteba?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga barabara inayounganisha Jimbo la Busekelo (kijiji cha Kilimansanga) na Jimbo la Rungwe (kijiji cha Suma)?
(c) Vyanzo vya Halmashauri haviwezi kujenga barabara zote na hivyo kulazimika kuomba msaada TANROADS; je, ni lini maombi ya Halmashauri ya Busekelo, kuhusu kupandishwa hadhi ya barabara zaidi ya tano tulizoomba ili ziwe chini ya TANROADS yatajibiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Jimbo la Busokelo lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Njombe kupitia Mwakaleli, kata ya Kandete na Luteba inapitia Katumba – Lusanje – Kandete – Ikubo hadi Luteba. Sehemu ya barabara ya Katumba - Lusanje – Kandete – Ikuba ambayo ni kilometa 34 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na TANROADS, na sehemu ya Ikuba hadi Luteba inahudumiwa na Halmashauri ya Busokelo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS inaendelea kufanyia matengenezo kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 271.805 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Katumba - Lwangwa hadi Mbambo na shilingi milioni 38.086 zimetengewa kwa ajili ya barabara ya Lusanje - Kandete hadi Ikubo. Mpango wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuzifanyia mategenezo barabara hizi ili zipitike wakati wote wa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na milima yenye miinuko mikali kwa sasa hakuna barabara inayounganisha Jimbo la Busokelo na Jimbo la Rungwe kupitia vijiji vya Kilimansanga na Suma. Serikali haifikirii kufungua barabara ya kuunganisha maeneo hayo kutokana na milima hiyo mikali, hivyo barabara zilizopo tunaomba ziendelee kutumika kuhudumia maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, maombi ya Halmashauri ya Busokelo kuhusu kupandishwa hadhi barabara zaidi ya tano zilizoombwa ili ziwe chini ya TANROADS yanafanyiwa uchambuzi pamoja na maombi mengine yaliyopokelewa kutoka nchi nzima kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwenye Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009. Mara taratibu za uchambuzi zikikamilika barabara ambazo zina kipaumbele kiuchumi na kijamii zitapandishwa madaraja kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itayakubali maombi ya wananchi wa Halmashauri ya Busokelo ya kuifanya Halmashauri hiyo iwe Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali GN Namba 286 ya tarehe 9 Septemba, 2011 ikiwa ni sehemu ya Wilaya ya Rungwe kwa lengo la kusogeza karibu huduma zilizokuwa zikitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo ya kuifanya Halmashauri ya Busokelo kuwa Wilaya yaliwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) iliyokutana tarehe 4 Julai, 2013. Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Mkoa kupitia maombi hayo ili kujiridhisha kama Halmashauri hiyo inakidhi vigezo kuwa Wilaya kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekretarieti ya Mkoa ilifanya tathmini ya maombi ya wananchi wa Busokelo ya kuwa Wilaya kamili kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua nia njema na juhudi kubwa ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa kuzingatia taarifa ya tathmini iliyofanywa na Sekretarieti ya Mkoa, hususan katika idadi ya watu, ukubwa wa eneo pamoja na kuwepo kwa tarafa moja pekee, imesababisha kutokidhi vigezo vya uanzishwaji wa Wilaya ya kiutawala ya Busokelo.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Ajira kwa sasa ni tatizo hapa nchini hasa kwa walimu wa sanaa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri katika sekta mbalimbali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanywa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) mwaka 2015/2016 umebaini kuwepo na ziada ya walimu wa masomo ya sanaa wapatao 7,463 katika shule za sekondari. Kutokana na hali hii Serikali inaendelea na zoezi la kuwagawanya walimu hao (redeployment) kwa kuzingatia uwiano na mahitaji halisi ya walimu wa sanaa kwa kila mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kila shule iweze kupata Walimu wa masomo ya sanaa badala ya kuajiri walimu wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 watumishi wa umma 9,721 wameshaajiriwa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya kila mwajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali inatarajia kuajiri Watumishi 52,436 wa sekta mbalimbali kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa pamoja na kuimarisha sekta na maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Tunatambua juhudi za Serikali za kujenga Chuo cha Kilimo na Mifugo katika Kata ya Lufyilo.
Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa bwalo la nyumba za walimu ili chuo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa majengo ya madarasa yalishakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busokelo kama ifuatavyo:-
Wizara ya Kilimo ina jukumu la kusimamia na kuviendeleza vyuo vya kilimo hapa nchini. Hiki ni kituo kidogo cha kutoa mafunzo ya kilimo kwenye scheme za umwagiliaji kwa maana ya World AgricultureResource Center. Kituo hiki kilijengwa kwa jitihada kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki Profesa Mark Mwandosya ambapo mwisho alikabidhi kituo hicho kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili wakamilishe sehemu iliyobaki.
Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua uwepo wa kituo hicho na inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ili kupata fedha za kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa ajili ya kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, vyuo vya kilimo vinavyosimamiwa na Wizara ya kilimo vipo 14. Vyote hivi vimejengwa muda mrefu na hivi sasa vinakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ikiwemo ofisi za walimu, madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu, maktaba pamoja na karakana. Changamoto nyingine ni uhaba wa wakufunzi na watumishi wa kada nyingine pamoja na vifa vya kufundishia.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo Wizara imeweka kipaumbele cha kuboresha vyuo vilivyopo badala ya kufikiria kuongeza vyuo vingine. Vyuo hivyo vikikarabatiwa vitaweza kuchukua wanafunzi wengi hivyo kuwezesha Serikali kufikia lengo la kuwa na mtaalam mmoja wa kilimo katika kila kijiji na pia kuzalisha maafisa ugani wenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa wakulima. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali imeshatenga shilingi 773,208,000 kwa kuanzia kwa ajili ya kufanya ukarabati katika Vyuo vya MATI.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Hapa nchini kumekuwepo na ukuaji na utumiaji wa mifumo mingi mipya ya teknolojia kwa ukusanyaji wa kodi na malipo mengine kwa njia ya mtandao (electronic):-
(a) Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na wizi wa kimtandao kwa wananchi?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuundwa kwa Bodi ya wana TEHAMA nchini ili kuwa na udhibiti na ufanisi wa watumiaji wa mitandao nchini wanataaluma wa TEHAMA waweze kuwa na Bodi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, lenye sehemu
(a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususani kwenye mitandao kama ifuatavyo:-
(i) Mwaka 2015 ilitungwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Miamala ya kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao pia kutambua makosa yanayofanyika kwenye mtandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo.
(ii) Kimeanzishwa kitengo cha uhalifu wa mitandao chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao ikiwemo wizi kwenye mitandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Kurugenzi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali.
(iii) Kupitia Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kimeanzishwa kitengo cha uratibu, ufuatiliaji na usimamizi wa matukio yanayotokea kwenye anga ya mtandao TzCERT. Kitengo cha TzCERT kinashirikiana kwa ukaribu na taasisi mbalimbali kama vile sekta ya fedha, mawasiliano, nishati , uchukuzi na jamii. Pia kinashirikiana na taasisi za kiintelijensia na kuhakikisha anga ya mtandao inakuwa salama.
(iv) Imeandaliwa mikakati ya Taifa ya usalama wa mitandao ambao unaweka bayana muundo wa Serikali kukabiliana na uhalifu wa mitandao.
(v) Mwisho elimu kwa umma imeendelea kutolewa.
(b) Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa matumizi ya TEHAMA nchini yemeongezeka ikiwa ni sambasamba na ukuaji wa sekta ya TEHAMA kama mojawapo ya sekta zinazokuwa kwa kasi. Kwa kutambua changamoto ya kutotambuliwa kwa wataalam wa TEHAMA nchini Serikali imefanya yafuatayo:-
(i) Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambayo inaatamka kuwepo kwa mfumo wa kuwatambua na kuwaendeleza wataalam wa TEHAMA ili kuwa na rasilimali watu ya kutosha nchini ambayo inazingatia maadili na yenye uwezo wa kufanikisha jitihada za TEHAMA katika kujenga jamii maarifa na;
(ii) Kwa tamko la Rais la mwezi Novemba 2015 imeanzishwa Taasisi ya Tume ya TEHAMA (ICT Commission) ikiwa na lengo kuu la kukuza TEHAMA ambapo moja ya majukumu yake ni kusajili, kusimamia na kuendeleza utaalam wa wataalam wa TEHAMA nchini.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y MHE. FREDY A. MWAKIBETE) aliuliza:-
Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali na Jimbo la Busokelo pia limebarikiwa kuwa na madini hayo.
Je, ni lini Serikali itapeleka wawekezaji wa kiwanda cha marumaru katika Kata ya Lufilyo kwenye Mto Makalya?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete Mbunge wa Busokelo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Atupele kwa jinsi ambavyo amekuwa akishirikiana na Serikali kufuatilia ili kuona madini ya eneo tajwa yanapata mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano ambao moja ya sekta ya kipaumbele ni sekta zinazotumia malighafi zinazopatikana nchini ikiwa ni pamoja uonezaji wa thamani madini ikiwemo madini aina ya granite. Katika Jimbo la Busokelo Kata ya Lufilyo, Kijiji cha Kikuba eneo la Mto Makalya kuna mashapo ya madini aina ya granite ambayo ni malighafi ya kutengeneza marumaru zenye ubora wa kimataifa. Kampuni ya Marmo Granite Ltd. ya Jijini Mbeya ilikuwa ikichimba mawe ya granite kutoka eneo hilo na kutengeneza marumaru na baadae ilisitisha shughuli hizo kwa madai kubwa barabara ya kwenda kwenye machimbo ni mbovu hivyo kutowawezesha kupata faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuhamasisha upatikanaji wa mwekezaji mwingine katika mradi huo. Nimuombe pia Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete aendelee kutupa ushirikiano mpaka hapo mwekezaji mwingine atakapopatikana. Vilevile Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI itawasiliana na TARURA ili barabara hiyo iweze kurekebishwa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Busokelo ni miongoni mwa Halmashauri zinazozalisha maziwa ya ng’ombe kwa wingi ambapo kwa mwaka inazalisha zaidi ya lita milioni 50:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kumalizia Kiwanda cha Maziwa kinachojengwa Kata ya Isange ili kunusuru maziwa mengi yanayoharibika kwa kukosa soko?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Maziwa cha Isange kilianza kujengwa na Serikali mnamo mwaka 2012 chini ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Kwanza (Agricultural Sector Development Programme – ASDP – Phase I). Kupitia programu hiyo shilingi milioni 140 zilitolewa na kutumika kujenga jengo la kiwanda, kuingiza umeme, maji na ununuzi wa tenki la kupoza maziwa (chilling tank) lenye uwezo wa lita 2,030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uibuaji wa ujenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Isange ulitokana na ukosefu wa soko la maziwa na hivyo kufanya maziwa mengi kuharibika. Hata hivyo, ujenzi wa kiwanda ulikwama baada ya kumalizika kwa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Kwanza (ASDP I) ambayo ilikuwa ikifadhili mradi wa kiwanda hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ilitangaza fursa ya uwepo wa jengo la Kiwanda cha Maziwa kwa ajili ya wawekezaji ambapo mwekezaji ASAS DAIRIES LTD alijitokeza na kuomba kuwekeza katika jengo la Kiwanda cha Maziwa. Mwekezaji baada ya kuingia mkataba na halmashauri ameanza kutumia jengo hilo kama Kituo kikubwa cha kukusanyia maziwa yanayonunuliwa kutoka kwa wafugaji kupitia Ushirika wa Wafugaji wa Maziwa wa UTAMBUZI. Kwa sasa mwekezaji anakusanya jumla ya lita 3,600 za maziwa kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji ameahidi kufunga mitambo ya kuchakata maziwa kama kiasi cha maziwa kitaendelea kuongezeka. Hivyo, naomba kutoa wito kwa wafugaji wa huko Busekelo kutumia fursa hii kuongeza uzalishaji wa maziwa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa wa madini na gesi asilia aina ya carbon dioxide:-
Je, ni lini Serikali itaenda kufanya utafiti wa kutosha kwenye Kata ya Lufilyo ambapo kuna madini aina ya marble (marumaru)?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa madini ya marble katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo ambapo Kampuni ya Marmo Granito inamiliki leseni moja ya uchimbaji wa kati yenye Namba ML 250 ya mwaka 2006 na leseni 10 za uchimbaji mdogo wa madini hayo zenye namba PML 0007657 – 0007666 za mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utambuzi huo ni kutokana na utafiti wa awali uliofanywa kati ya mwaka 2005 hadi 2007 na Kampuni ya BGR ya Ujerumani kwa ushirikiano wa taasisi za Serikali (STAMICO na GST). Utafiti huo ulipelekea kugunduliwa kwa madini hayo yenye rangi ya kijani na nyeupe katika Kijiji cha Kipangamansi kilichopo katika Kata ya Lufilyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itaendelea kufanya utafiti wa awali wa kijiolojia ili kubaini maeneo mengine yenye madini hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Vilevile utafiti wa kina utafanyika ili kubaini ubora na wingi wa upatikanaji wa madini hayo na kuishauri Serikali. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-

Halmashauri ya Busokelo ina maporomoko ya maji (waterfalls) maeneo mbalimbali na jotoardhi (geothermal):-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia maporomoko hayo ya maji (waterfalls) na jotoardhi (geothermal) kuweza kuzalisha umeme ili kupunguza changamoto ya umeme nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika Halmashauri ya Busokelo kuna maeneo yenye maporomoko ya maji yanayoungana na maporomoko yaliyoko Wilaya ya Makete katika Mto Rumakali. Upembuzi yakinifu katika maeneo hayo ulifanywa na Serikali mwaka 1998 kwa ushirikiano na Serikali za Norway na Sweden.

Mheshimiwa Spika, kulingana na upembuzi yakinifu huo maporomoko ya Mto Rumakali yanaweza kuzalisha umeme wa MW 222. Kwa sasa TANESCO inaendelea na kazi ya kuhuisha upembuzi yakinifu kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kabla ya kuanza hatua za utekelezaji. Utekelezaji wa mradi utaanza Aprili, 2020 na kukamilika Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya jotoardhi ya Ngozi, Kiejo-Mbaka Mkoani Mbeya na Songwe Mkoani Songwe. Miradi hii yote imefikia hatua ya uchorongaji visima vya majaribio ili kuhakiki kiasi na ubora wa rasilimali ya jotoardhi katika maeneo hayo. Aidha, TANESCO kupitia Kampuni Tanzu ya Jotoardhi inaendelea na utafiti wa vyanzo vya umeme wa jotoardhi katika eneo la Mbaka katika Halmashauri ya Busokelo.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti huo yataonyesha hali halisi ya uwezo wa kuzalisha umeme kwa nguvu za jotoardhi itakayopatikana katika eneo husika. Kazi ya utafiti na uchorongaji huo inatarajiwa kukamilika mwaka 2022.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-

Wananchi wa Busokelo katika Kata ya Luteba walianza kutengeneza barabara inayounganisha Mikoa ya Mbeya na Njombe kupitia Mlima ya safu za Livingstone:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kuunga mkono juhudi za wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua Barabara ya Njombe-Makete-Isyonje Mbeya (kilometa 203.6) kama barabara rasmi inayounganisha Mikoa ya Njombe na Mbeya. Barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge inayounganisha Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe na Rungwe, Mkoa wa Mbeya ambayo ni barabara ya Mkoa. Aidha, kutoka Luteba hadi Ipelele katika Wilaya ya Makete kilometa 7.5, hakuna barabara inayoonekana wazi ni eneo la Milima mikali ya Livingstone.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Njombe-Makate kilometa 107.4 ambayo ni sehemu ya barabara ya Njombe-Makate- Isyonje-Mbeya inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya. Sehemu hii ya barabara hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, barabara inayopita katika safu ya Milima ya Livingstone inahitaji upembuzi yakinifu ambao ndiyo itakuwa msingi wa kufanya maamuzi. Kuhusu sehemu inayotengenezwa na wananchi katika safu ya Mlima Livingstone, Serikali itaangalia namna ya kusaidiana na wananchi waliojitolea kutengeneza sehemu hiyo ya barabara pamoja na upatikanaji wa fedha.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-

Wananchi wa Kata za Mpombo, Kandete, Isange na Luteba pamoja na Kata za Kabula, Lwanga na Lupata wanalima zao la chai kwa wingi lakini bei ya zao hilo ipo chini:-

Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la Chai ambalo litasababisha kupanda kwa bei kuliko bei ya sasa ya Shilingi 315 kwa kilo?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Chai Tanzania iliitisha kikao cha wadau wa chai kilichofanyika Aprili, 2019 kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za wakulima ikiwa ni pamoja na kupanga bei elekezi ya chai kwa mwaka 2019 kwa kuwashirikisha wadau wote. Mkutano huo wa Wadau wa zao la chai ulifanyika tarehe 3 Aprili, mwaka 2019 Mufindi Mkoani Iringa na Wajumbe walipitisha bei elekezi ya majani mabichi ya chai kwa mwaka 2019 kuwa ni shilingi 315 kwa kilo.

Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali kutafuta masoko ya mazao ya kilimo nchini ni jukumu endelevu. Kwa upande wa zao la chai, jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kuwa chai inayozalishwa inauzwa hapa nchini bila kuwalazimu Wakulima kusafirisha chai yao kwenda kwenye mnada wa Mombasa. Katika kutekeleza hilo, Serikali inakamilisha mkakati wa kuanzisha soko la chai Tanzania kwa kuanzisha mnada wa Kimataifa wa Chai Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza uanzishwaji wa mnada wa chai nchini Tanzania kikosi kazi kiliundwa ambacho kinajumuisha Bodi ya Chai (TBT), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi wa Ghala, Chama cha Wakulima wa Chai Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) pamoja na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai Tanzania yaani (TSHTDA). Maandalizi ya mnada huo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 ili tuwe na mnada wetu utakaosaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa chai nje ya nchi na faida inayopatikana iongeze bei ya mkulima.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-

Katika eneo linalopatikana gesi aina ya carbondioxide (CO2) kwenye Jimbo la Busekelo, Kijiji cha Mpata kuna visima ambavyo ni hatari kwa binadamu na viumbe hai wengine kwani huwa wanakufa wakivuta hewa ya sehemu hiyo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha ya binadamu na viumbe katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busekelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa katika Jimbo la Busekelo, katika Kijiji cha Mpata kuna visima vya gesi ya ukaa (Carbondioxide) vinavyomilikiwa na Kampuni ya Tanzania Oxygen Limited. Kampuni hiyo inamiliki leseni mbili za uchimbaji wa gesi ya ukaa ambazo ni ML 139/2002 iliyotolewa tarehe 17/11/2002 na ML 379/2009 iliyotolewa tarehe 21/08/2009. Kisima cha Mpata Kipo katika leseni Na. ML 139/2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Mpata kuna visima viwili. Kisima kimoja kilichimbwa na kimefunikwa madhubuti na Kampuni ya Tanzania Oxygen Limited ambayo inavuna gesi ya ukaa. Kisima cha pili kimetokana na nguvu za asili zilizosababishwa na mlipuko wa volkano na hivyo kupelekea uwepo wa kisima cha asili. Kutokana na uwepo wa kisima hicho kilichotokana na njia ya asili, tafiti za awali zinatoa tahadhari ya kisima hicho kikifunikwa kinaweza kutoa gesi hiyo kupitia njia nyingine na hivyo kuleta madhara yasiyotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo hayo ili kudhibiti athari inayoweza kutokea. Hatua za udhibiti zilizochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na TOL ni pamoja na kuweka vizuizi madhubuti, uzio na ulinzi wakati wote kwa watu na wanyama ili wasiweze kufika katika eneo la kisima sambamba na kuweka mabango ya tahadhari katika eneo hilo. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na TOL inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari za gesi ya ukaa katika maeneo yanayozalishwa gesi hiyo. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa Daraja la Mto Mbaka linalounganisha Jimbo la Busokelo na Rungwe litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Mbaka ambalo lipo katika barabara ya Katumba - Lwangwa - Tukuyu yenye jumla ya kilometa 81, linaunganisha Halmashauri ya Busokelo na Mji wa Tukuyu. Barabara hiyo ni ya mkoa na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, hapo awali daraja hili lilikuwa la chuma (Bailey) lakini kwa kuzingatia umuhimu wa daraja hilo lililopo kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mazao ya misitu, Serikali iliamua kulijenga kwa kiwango cha zege kuanzia mwaka 2018. Hata hivyo, wakati ujenzi ukiendelea kulijitokeza changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na usanifu ambao ilibidi urudiwe kuendana na hali halisi ya eneo husika. Usanifu huo ulikamilika mwezi Oktoba, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mkandarasi anaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo ambapo kazi za ujenzi zimefikia asilimia 68 na kazi zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busekelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajiridhisha kuwa inatoa mikopo kwa wanafunzi walengwa, kupitia vigezo vilivyowekwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura178) ambayo inawalenga wanafunzi wa Kitanzania wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu, lakini kutokana na hali ya kiuchumi hawana uwezo wa kumudu gharama. Vigezo hivyo ni mwombaji anatakiwa awe Mtanzania mhitaji; awe amepata udahili katika taasisi inayotambulika; asiwe na ufadhili wa masomo yake ya elimu ya juu kutoka taasisi nyingine; na awe ameomba mkopo kwa usahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ili kuwafikia wahitaji wengi zaidi Sheria ya Bodi ya Mikopo imetoa mamlaka kwa Bodi kuweka vigezo vya ziada ambapo katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ilitangaza Mwongozo wa Utoaji wa Mikopo uliotaja sifa na vigezo vya ziada kama ifuatavyo: Yatima; mwombaji au mzazi mwenye ulemavu; mwombaji aliyefadhiliwa katika masomo yake ya sekondari au stashahada; na mwombaji aliyetoka katika familia ya kipato cha chini au kaya maskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia sifa na vigezo hivi, katika mwaka wa masomo 2020/2021, jumla ya waombaji wapya 66,374 wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu waliomba mkopo na kati ya hao waombaji 55,318 sawa na 83% walipangiwa mkopo kwa mchanganuo ufuatao: Yatima walikuwa 1,137 sawa na 2.06%; waliofiwa na mzazi mmoja walikuwa 8,683 sawa na 15.7%; waombaji wasiofahamu wazazi au waliolelewa katika Vituo vya Ustawi wa Jamii walikuwa ni 71 sawa na 0.17%; waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu walikuwa ni 92 sawa na 0.13%; waombaji waliofadhiliwa na taasisi zinazotambulika walikuwa 1,992 sawa na 3.6%); na waombaji kutoka kaya maskini walikuwa 43,343 sawa na 78.35%. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Maji kutoka Mto Rumakali katika Kata ya Lufilyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) inatekeleza Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rumakali, Mkoani Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha megawati 222 na njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilomita 150 kutoka Rumakali hadi Kituo cha Kupoza Umeme cha Iganjo, Mkoani Mbeya. Gharama za mradi ni takriban shilingi bilioni 913.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikiwa sasa ni kukamilisha taratibu za manunuzi ya Mkandarasi wa ujenzi wa mradi. Kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2021 na kukamilika mwezi Juni, 2024.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa wananchi maeneo ya Hifadhi ya Kitulo ambayo hayatumiki ili wayatumie kulisha mifugo yao hususani eneo la Kwipanya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo ilianzishwa kwa GN. Na.279 ya mwaka 2005. Maeneo yote yaliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Kitulo likiwemo eneo la Kwipanya yamehifadhiwa kisheria kulingana na umuhimu wake kiikolojia, kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Miongoni mwa sababu zilizopelekea Serikali kuanzisha Hifadhi hii ni pamoja na:-

(i) Kuhifadhi vyanzo vya maji ambavyo vinatoa maji yanayoenda kwenye Bonde la Ziwa Nyasa na Bonde la Mto Rufiji ambapo kwa sasa maji hayo yanachangia kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Maji uliopo katika Bwawa la Julius Nyerere pamoja na Bwawa la kufua umeme wa maji la Mtera;

(ii) Eneo hili linahifadhi uoto adimu wa asili wa misitu na maua uliopo katika eneo husika;

(iii) Kutunza makazi ya wanyama adimu duniani kama vile Kipunji na Minde; na

(iv) Pamoja na kuhifadhi mandhari ya asili ya milima kwa ajili ya shughuli za utalii.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhifadhi eneo hili la Taifa la Kitulo kutokana na umuhimu wake. Ahsante.