Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia (27 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na wote walioshiriki katika kusababisha nikawa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutumia fursa hii adhimu kabisa kuchangia katika mjadala huu na napenda nianze na wenzangu wa TAMISEMI. Nimepitia vitabu vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati lakini kwa masikitiko makubwa ukiangalia vitabu hivi, nyuma kabisa huku vinasomeka Kamati ya Bunge ya Utawala na Sheria za Serikali za Mitaa Aprili, 2015. Kile kingine cha Utawala Bora nacho hivyo hivyo kinasomeka Aprili, 2015. Tunaweza tukasema labda ni makosa ya uandishi lakini kwa mujibu wa taarifa ambazo ninazo bahati mbaya sana hata Kamati yenyewe haikupitia taarifa hii. Kwa hiyo, yawezekana makosa haya yapo wazi ni kwa sababu Kamati nayo kwa bahati mbaya sana haikushirikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msingi uleule wa Bunge kuishauri na kuisimamia Serikali itategemea zaidi kama Kamati zako zitatimiza wajibu wake na zitafanya kazi kwa mujibu wa Kanuni. Tukiwa na utaratibu huu kwamba zinaletwa taarifa zinasomwa hapa halafu wanakamati hawashirikishwi sidhani kama ni utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye mapendekezo ya Kamati, pendekezo namba 13, linasema kwa kuwa ukusanyaji wa ushuru na majengo katika Halmashauri za Manispaaa utatekelezwa na TRA, ni vyema Serikali ikawa makini na uamuzi huo hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka hiyo haikupata mafanikio huko nyuma ikilinganishwa na mafanikio yaliyoonyeshwa na Serikali za Mitaa. Naamini kabisa kama Kamati ingekuwa imeipitia taarifa hii naamini wasingekubali kuunga mkono kwa sababu taarifa inaonyesha ufanisi umepatikana kwenye Manispaa lakini vilevile wanakubaliana kupeleka TRA, mantiki haikubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika ukusanyaji wa mapato takwimu zinaonyesha Manispaa wamekusanya vizuri sana na mimi nikiangalia takwimu za Manispaa yangu ya Kinondoni miaka mitatu imekusanya vizuri sana, asilimia 75, asilimia 80, asilimia 116. Sasa leo kuamua kodi hii kurudishwa tena TRA watu ambao watategemea watendaji wale wale wa Manispaa kwa kweli hili ni jambo ambalo linanifanya kwa namna moja ama nyingine nisiunge mkono hoja hii. Nashauri Serikali wafanye marekebisho kodi hii ikusanywe na Manispaa kwa sababu imeonekana bado wanaendelea kukusanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la milioni 50 au tunaweza tukaziita mamilioni ya Mheshimiwa Rais kwa kila kijiji na kwa sisi watu wa mjini kila Manispaa na kila mtaa. Katika Jimbo langu nina mitaa 52, tafsiri yake mapesa haya tunatarajiwa kupewa bilioni 2.6 wakati Mfuko wa Jimbo wa Mheshimiwa Mbunge wengine milioni 70, wengine milioni 50. Mbaya zaidi pesa hizo wakati tunazipeleka tuna historia ya mapesa ya mabilioni ya Kikwete ambapo hakukuwa na utaratibu mzuri wa pesa zile kuwafikia walengwa. Wasiwasi wangu ni kwamba hizi pesa tunazipeleka kisiasa na bahati nzuri nashukuru hatujaona kwenye maandishi hizi pesa zimetengwa wapi. Ni bora sasa kabla pesa hizi hazijapelekwa huko tukaonyeshwa kama Bunge utaratibu gani utatumika kuhakikisha walengwa wanazipata pesa hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu, nimepata tabu sana wakati mwingine tunatamani kupongeza Serikali lakini kwa hali ilivyo tunashindwa. Mfano uhaba wa matundu ya vyoo kwamba mpaka hapa tulipo Serikali yetu haijaweza kumudu kuchimba vyoo kwenye shule zetu. Serikali inatupa taarifa kwamba mwaka 2010 mpaka mwaka 2016 tofauti ya vyoo tulivyochimba ni 57,092 wakati mahitaji ya vyoo ni 464,676. Tunapokuwa na Serikali ambayo ina upungufu wa mashimo ya vyoo katika shule zetu 464,000 unakosa cha kupongeza. Kama tunashindwa kuchimba walau matundu ya choo maana yake tusistaajabu tunapopata kipindupindu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nitamuomba Waziri ajitahidi tuondokane na aibu hii. Haiwezekani tukaja bajeti ya mwaka ujao tukaendelea kusema tuna matatizo au tuna upungufu wa matundu ya vyoo. Serikali iliyopata uhuru miaka 50 hili ni jambo haliwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi katika elimu, tuna programu ya elimu bure, tunasema alhamdullilah lakini kama mwenzangu alivyosema siyo elimu bure ni elimu kwa kodi. Hata hivyo, tujue kwamba ruzuku ya elimu tunayotoa mashuleni ya mtoto mmoja Sh. 500/=, shule yenye watoto 1,000 mwalimu anapewa Sh. 500,000/= kwa mwezi. Shilingi 500,000 kwa mwezi hata matumizi ya Mbunge ndani ya nyumba yake hayapatikani. Wizara lazima ije na suluhisho na katika nafasi yangu ya kushauri angalau basi tuweke sh. 2,000/=, hii sh. 500/= ni pesa ndogo sana. Leo imefika mtu anaogopa kuwa Mwalimu Mkuu kwa sababu ni mateso, ni presha, turekebishe hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya, akina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee hawahudumiwi bure kama tulivyoahidi. Nina ushahidi, mimi katika Jimbo langu tuna Hospitali yetu ya Mwananyamala, kama hiyo haitoshi hospitali zetu tumeweka viingilio kama kwa waganga wa kienyeji kwamba ukitaka kwenda hospitali lazima uwe na sh. 6,000/=. Kwa hiyo, Serikali iondoe hili tozo la kiingilio na kama kuna ulazima wa kuweka basi isizidi sh. 1,000/= ili mwananchi aweze kwenda hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Tunaposema utawala bora kwa kweli inatupa tabu sana hasa tukiangalia uchaguzi wa Zanzibar, tunakuwaje na utawala bora katika uchaguzi ule tulioufanya? Uchaguzi ule umetutia aibu, nafikiri Serikali imefika mahali sasa warudi, siyo vibaya mtu kulamba matapishi yako. Uchaguzi ule ulivyofanywa watu wanajua, bahati nzuri niliongea na kaka yangu Mheshimiwa Keissy, msema kweli sana kaka Keissy yeye anajua kabisa kwamba uchaguzi ule wamepiga kura watu 48, hatuwezi kuwa na uchaguzi kama huu, ni aibu. Lazima tujitahidi turudi nyuma tutazame tulipokosea ili tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utumbuaji wa majipu. Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu Rais ndiyo akawa anatumbua majipu. Rais ana kazi nyingi, vyombo vyake vinafanya kazi gani? Tume ya Maadili inafanya kazi gani? Imetengewa pesa hapa shilingi bilioni 6 sijui bilioni ngapi ya kazi gani, wanashughulikia Maadili gani, kwa nini wasitumbuliwe wao? TAKUKURU hawapewi uwezo na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi gani mpaka Rais leo ndiyo anatumbua majipu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuruka live, kama kuonekana usiku ndiyo watu wanapatikana na siye tubadilishe muda.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Tubadili Kanuni tufanye kikao usiku.
MWENYEKITI: Muda wako umemalizika.
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Ili tuonekane. Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pili, nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba siku ya Alhamisi sawa na tarehe 19 kaka yangu Iddi Mohamed Azzan kwa hiari yake aliamua kufuta kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kinondoni. Namshukuru sana Mungu, namshukuru naye kaka yangu kwa ukomavu, maana sisi watu wa Pwani tunasema “mtu mzima akivuliwa nguo, basi huchutama.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wametoa sifa nyingi sana kwa Mzee wangu, Mzee Lukuvi. Imenipa tabu hata mimi mchangiaji nisije nikaharibu shughuli hii nikaonekana kituko. Kabla sijafika huko, nianze na maswali mawili ambayo naomba Mheshimiwa Lukuvi wakati akifanya majumuisho ayagusie. La kwanza, ujenzi wa mji wetu mpya wa Kinondoni status yake ikoje? Wananchi wa Kigamboni wana mashaka, hawajui. Nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri atuondoe shaka hii katika majumuisho atakayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, anaonaje; mimi nina mashaka kidogo na hasa ukizingatia sasa tunatarajia au tumeshapitisha kuwa na Manispaa au Wilaya ya Kigamboni. Sasa tutakuwa na Kigamboni Municipal Council, lakini vile vile kuna kitu kinaitwa Kigamboni Development Agency: Je, hatutakuwa na vyombo viwili vyenye mvutano ili kuhakikisha Kigamboni yetu inakuwa nzuri? Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kinondoni, nimekumbwa na suala la bomoa bomoa. Bomoa bomoa ile imenikuta kwenye Kata yangu ya Magomeni, Mtaa wa Kwasuna, Kata yangu ya Hananasif Mtaa wa Kawawa; tena Mtaa umepewa jina la Mzee wetu, namheshimu sana; amepewa Mtaa wa Mabondeni ambapo Serikali wameona pale hawastahili kukaa watu, wakaenda kuvunja bila kujali jina lake walilompa yule mzee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, siku mbili, tatu nimemsikia kaka yangu Mheshimiwa Waziri January Makamba alikuwa na mkutano wa hadhara kule Segerea, amesema Serikali haina mpango tena wa kuendelea na bomoa bomoa. Vile vile ikasemwa kwamba Serikali ina mpango wa kufanya mabadiliko ya sheria ya mazingira ya kupunguza mita 60 baada ya kuona kwamba utekelezaji wake umekuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo hoja yangu. Hoja yangu ya msingi; hawa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kinondoni nyumba zao zimevunjwa na mbaya zaidi kuna wengine mpaka leo wanaishi pale kwenye vile vibanda. Mheshimiwa Waziri, kibinadamu Serikali lazima ije na suluhisho. Kwa sababu ninavyojua, jukumu la Serikali pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha watu wake wanapata mahali pazuri pa kuishi. Sasa wale watu wanaishi kwenye vijumba vibovu pale. Tumevunja nyumba zao nzuri, tumewabakishia vijumba vya mabati. Lazima Serikali itumie au itekeleze wajibu wake kuhakikisha wale watu wanapata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wale watu waliovunjiwa nyumba zao, lazima Serikali ije na mpango, tunawapeleka wapi? Hatuwezi kuwa na Serikali ambayo inapomkuta mtu ana nyumba ya vyumba vitatu na sitting room, inamvunjia halafu anabaki kwenye kibanda cha bati. Tulisema tunawavunjia nyumba zao kwa ajili ya usalama, lakini leo wanaishi katika mazingira magumu zaidi kuliko zile tulizovunja. Mheshimiwa Waziri kama atapenda, nina takwimu za watu waliopata maradhi ya shinikizo la damu kutokana tu na nyumba zao kuwekewa X na waliopoteza maisha. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inatakiwa ihakikishe wananchi hao wanapata mahali pazuri pa kuishi. Nami napenda kushirikiana na Mheshimiwa Waziri katika maeneo yafuatayo:-
Moja, tuna maeneo ya squatters kwenye Kata ya Hananasif na Kata ya Tandale. Tukiamua kufanya maendeleo tukabadilisha kutoka squatters tukafanya mji wa kisasa tukajenga majumba marefu, maana yake hawa watu wote waliokaa mabondeni wanaweza kupata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafikiri Serikali ifike mahali hasa sisi Wabunge wa Mjini ambao hatuna mashamba ya kupewa na Serikali wala sitakuja hapa nikaomba shamba Mheshimiwa Waziri, najua hana shamba la kunipa. Ninachokitaka, ni lazima Serikali tuje na mpango wa namna gani ya kubadilisha makazi yetu haya ya squatter tuwe na majumba yaliyokuwa kwenye mpango na majumba ya kwenda juu. Aliweza Mheshimiwa Mzee Karume! Mzee Karume kafanya Zanzibar, sisi tunashindwa kwa sababu gani? Kama tutashindwa kufanya Kinondoni, tunataka tukafanye wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana Shirika lake la Nyumba. Hili Shirika limebadilishwa kabisa kutoka kutengeneza nyumba kwa ajili ya wananchi wanyonge, mpaka sasa wanatengeneza nyumba za kibiashara. Unaambiwa nyumba ya bei nafuu ni sh. 40,000,000 ya bei nafuu ni sh. 60,000,000. Kwa wananchi wetu wenyewe wana uwezo wa kujenga nyumba kwa sh. 30,000,000 ikawa bora kuliko hiyo ya sh. 40,000,000 inayojengwa na Shirika. Sasa kama Shirika hili nalo limekuwa kama la kibepari ambalo lengo lake ni kupata faida, imetokana na lengo la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, tena wananchi wanyonge. Kwa kweli Shirika limetoka kwenye mwelekeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliwahi kusema Shirika lisijenge tena nyumba za kibiashara, lakini lazima Shirika lirudi lijenge nyumba za bei nafuu kweli ambazo wananchi wa hali ya chini wanaweza kukaa. Siyo nyumba za bei nafuu za kiini macho za sh. 30,000,000 au sh. 40,000,000 ambazo wananchi hawawezi kukaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikiamua kutekeleza haya naogopa kusema, Mheshimiwa Lukuvi namheshimu sana mzee wangu, lakini namwomba sana, wale watu wanaoishi pale Kinondoni Mkwajuni wanaiaibisha Serikali yetu. Siyo wa kwenda kuwafukuza! Lazima sasa Serikali ionane na mwakilishi wa wananchi; tuje na mpango wa namna gani tutawaondoa pale ili nao wapate mahali pa kuishi, wasikie. Wakisikia Mheshimiwa Lukuvi ana roho nzuri, anapendwa, anapigiwa makofi na Waheshimiwa Wabunge, nao waone sababu ya Mheshimiwa Lukuvi kupigiwa makofi na Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni niko tayari kushirikiana na Serikali, niko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Waziri kuhakikisha tunalitatua tatizo hili ambalo naamini linanitia aibu kama Mbunge, linamtia aibu yeye kama Waziri na linaitia aibu Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Serikali ya wananchi, madaraka yake imepata kutoka kwa wananchi na lazima itumike kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana na naunga mkono hoja ya Upinzani.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa na kuchangia jambo hili. Pili, nikushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwanza, nianze kusema naunga mkono taarifa zetu hizi nzuri kabisa zilizoandaliwa na Kamati zetu hizi kubwa mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuweka rekodi sawa lakini kubwa kuliko yote kuonesha kwamba sisi watu wa Kinondoni tuliwahi kuonja matunda ya UKAWA. Matunda yale tuliyaonja katika gogoro kubwa linaloonekana kwamba Manispaa na Halmashauri hazichangii 10% za vijana na wanawake. Chini ya aliyekuwa Meya wetu wa UKAWA, Ndugu Boniface Jacob, Manispaa yetu ya Kinondoni ambayo imeitwa manispaa sugu imefanikiwa kutoa pesa shilingi bilioni 2.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie wenzangu kama sisi Wabunge tukishirikiana na Madiwani wetu na Wenyeviti wetu wa Halmashauri au Mameya tukawa na nia ya dhati, hizi pesa zinatoka na sisi kwetu Kinondoni zimetoka. Niwaahidi wananchi wa Kinondoni vyovyote itakavyokuwa bila kujali mabadiliko yoyote yaliyotokea tutahakikisha mwaka huu wa fedha 2016/2017 tutatoa pesa shilingi bilioni 6.4 kwa sababu makusanyo yetu ya ndani ni takribani shilingi bilioni 64. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masikitiko hapa, tulikuwa tumekadiria kukusanya property tax shilingi bilioni 10 kwa Manispaa yetu ya Kinondoni. Leo Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi hii kutoka manispaa ameipeleka TRA na mpaka sasa ndiyo kwanza wamepeleka vibarua vya kuwataarifu watu kwamba wanadaiwa, tuna masikitiko makubwa sana. Kwa kuondoa hii shilingi bilioni 10 maana yake wananchi wa Kinondoni, vijana na wanawake mmewakosesha shilingi bilioni moja ambayo kama wangegaiwa shilingi milioni hamsini, hamsini, ni wananchi 20,000 mmewakosesha pesa hizi. Ni hasara kubwa sana kwetu sisi watu wa Kinondoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri kama atashindwa kurejesha hii property tax kukusanywa katika Halmashauri basi walau arejeshe katika Manispaa. Kwa sababu kwenye Manispaa pesa nyingi zitapotea, kwa sababu Majiji yana majengo makubwa yenye thamani kubwa tofauti wakati mwingine na Halmashauri yenye majengo madogo. Kwa hiyo, tusije tukaipoteza hii fursa kwa kupoteza mapato mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda niishauri Serikali kama wajibu wetu wa msingi, imeelezwa hapa katika ripoti ya PAC tuna Shirika letu la NSSF. Katika mashirika yetu ya hifadhi hili ni shirika kubwa sana. Hili shirika lina utajiri wa shilingi trilioni 3.8. Shirika hili lina miradi 40 ambayo tayari iko kwenye utekelezaji. Shirika hili limepata mabadiliko, limepata Mkurugenzi mpya na ni mtu mwenye uwezo, Profesa, lakini kwa masikitiko makubwa Wakurugenzi nane ambao walikuwa wanafanya kazi na Mkurugenzi huyu wamesimamishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, yawezekana kuna mambo yamesemwa na nashukuru ripoti imeeleza vizuri, lakini imekuja kueleza vizuri suala la Dege Eco Village na imeeleza kwamba si kweli ardhi imenunuliwa kwa milioni 800 kama inavyoandikwa kwenye magazeti wakati mwingine, kilichotokea pale ni kwamba ardhi ile heka 300 imeingizwa kama capital na yule mwekezaji Azimio amepata 20% ya mradi kwa kutoa viwanja 300; siyo kapewa pesa milioni 800 kwa heka, siyo kweli. Kwa thamani ya mradi share atakayopata 20% wameigawanya kwa viwanja ikaonekana milioni 800 wakati siyo utaratibu. Utaratibu na huu sio mgeni, hata National Housing wamewahi kuingia mkataba na TPDC na wamepata 25% katika jengo lile kubwa pale la Mkapa Tower na kiwanja cha heka moja ni sawasawa na bilioni 4.5. Sasa huu ni utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masikitiko yangu au ushauri wangu naotaka kumpa dada yangu pale Mheshimiwa Waziri mhusika ni kwamba shirika kubwa kama hili akapewa Director mgeni, Wakurugenzi wake nane ambao walikuwa wanasaidiana na Mkurugenzi aliyeondoka, wanaojua uendeshaji wa shirika hili wakakaa pembeni akawa Mkurugenzi mpya anachukua na Wakurugenzi wake wengine wapya, tunapoteza pesa zetu, yaani shilingi trilioni 3.8 tunaziweka rehani. Hawa watu wanatakiwa wawepo wamsaidie, kuna kaka yangu Magoli, kaka yangu Kidula, Wakurugenzi wapo pale waende wakamsaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunapata hasara kwenye mashirika yetu ni kwa sababu hatujali thamani ya kile kitu tulichonacho. Hii inatuletea matatizo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afanye kila hali Wakurugenzi hawa wamsaidie Mkurugenzi wetu Mkuu ili uchumi wetu usiyumbe.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza shukrani kwa Allah (S.W.) kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii ya mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018. Nikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri katika maeneo yafuatayo:-
(a) Kupambana na wafanyakazi hewa, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na Idara zake zote;
(b) Kuendelea na mapambano dhidi ya ufisadi uliokuwa ukifanyika katika nchi yetu; na
(c) Kupambana na kuzuia mfumuko wa bei katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango kuandaliwa vizuri na kitaalam, bado kuna upungufu ufuatao:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza msingi wenyewe wa viwanda ni jambo linalohitaji maandalizi makubwa na mapema. Kwa kweli, dhana ya viwanda inataka fedha za kutosha kama mtaji, rasilimali watu wenye ujuzi na miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mawazo yangu, Serikali bado haijawa kwenye wakati mzuri kutoa fedha kwenye viwanda. Badala yake fedha zipelekwe kwenye miundombinu ya kuwezesha viwanda, badala ya kuanzisha viwanda na hasa ukizingatia Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kwenye sekta hii ya viwanda.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuwa na mahusiano mabaya na wafanyabiashara wakubwa na wadogo, hatuwezi kujenga nchi bila kushirikiana kati ya Serikali na wafanyabiashara.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wafanyakazi wa Serikali ni watu muhimu sana kwa ujenzi wa Taifa letu. Naomba Serikali yetu iwaangalie kwa jicho la huruma.
(d) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na mkakati wa kubadilisha watendaji wake. Jambo hilo ni zuri, lakini linahitaji umakini na hasa watendaji wawe na weledi wa kutosha na hasa wasiwe wakereketwa wa Chama, bali wawe watu wanaoweza kufanya kazi bila ya kuathiriwa na siasa na upendeleo wa kivyama.
(e) Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu amejikita katika usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali za kila siku. Kwa mawazo yangu, kazi hii inaweza pia ikafanywa na Waziri Mkuu na hasa baada ya Rais kuonesha nini anataka katika utendaji wa Serikali na Waziri Mkuu ameona nini Rais anataka ili naye aige.
(f) Mheshimiwa Naibu Spika, demokrasia ni dhana kubwa katika maendeleo ya nchi. Mfano Uchaguzi wa Meya, Tanga, Kinondoni na uchaguzi wa Zanzibar. Kama demokrasia ikiheshimiwa itaongeza mahusiano ya ndani, pia itatoa fursa ya kupata fedha za MCC za Marekani, mfano Dola milioni 698.1 kwa mwaka.
(g) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi ya majengo kukusanywa na TRA. Jambo hili lilikuwa linafanywa na Manispaa vizuri sana, hivyo tunaiomba Serikali jambo hili la Kodi ya Majengo lirejeshwe kwa Manispaa na Halmashauri, kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kwa Serikali yetu:-
(a) Kujenga miundombinu ya viwanda na siyo kujenga viwanda na kuendesha mashirika ya ndege;
(b) Pesa ya Sekta ya Kilimo kufikia 10% ya bajeti ya nchi;
(c) Serikali ihakikihe mchango wa madini kwa pato la Taifa mpaka kufikia 10% ya pato la Taifa;
(d) Kuleta utengamano wa kisiasa kwa Zanzibar, Tanga na Kinondoni;
(e) Ajira kwa vijana, hasa tuongeze fedha kwenye mabenki, kilimo, uvuvi na ufugaji; na
(f) Kuondoa VAT katika mizigo ya nje na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kunijalia uzima. Lakini pili nikushukuru sana Mwenyekiti kwa kuamua kuwa mimi niwe mchangiaji wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Kamati hasa hii Kamati ya Serikali za Mitaa kwa kueleza na kwa kutimiza wajibu wao wa kuishauri Serikali; kueleza mambo kwa kina sana, nawashukuru sana muwasilishaji na wanakamati kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kamati ya Katiba na Sheria. Katika Wizara yetu ya dada yangu pale anayeshughulikia ajira na walemavu; dada Jenista. Ukiangalia Kamati imejikita sana kwenye mambo ya kisheria, lakini mahali pengine kwenye taarifa hawajagusa chochote kwenye suala la vijana na walemavu. Ukiambatanisha vijana, walemavu na ajira maana yake hili ni kundi muhimu sana; vijana ni kundi muhimu ambalo linahitaji ajira na walemavu ni kundi muhimu ambalo linahitaji uwezeshaji. Lakini sijui kutokana na Kamati kuwa na mambo mengi bahati mbaya sana sikuona kwamba suala la ajira limepewa uzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, tuna tatizo kubwa sana la ajira na hasa kwa vijana. Mimi kama mwakilishi wa Jimbo la Mjini, Jimbo la Kinondoni linapambana sana na tatizo la vijana na hasa vijana kukosa ajira. Nilitegemea ama wakati mwingine Kamati itueleze Wizara yetu imefanya jambo gani katika ajira; katika kupitia utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji ndani ya mwaka mzima wa Kamati, ningefurahi sana kama Kamati ingetuonesha. Tuna tatizo kubwa sana la ajira, vijana wetu hawana ajira, Serikali lazima ijitahidi ihakikishe inatoa ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiliunganisha hilo la ajira na mikopo ya vijana, kwamba watendaji wetu wa Halmashauri na Serikali za Mitaa hawatoi umuhimu unaostahiki katika ile asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo inatakiwa iende kwa wanawake na vijana. Wakati mwingine wawakilishi tunagombana na watendaji kuonesha kwamba lazima tutenge hizi pesa, lakini wakati mwingine watendaji wanaona kwamba pesa ikibaki ndipo ipelekwe kwenye kundi lile la asilimia 10 ya wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe na niishauri Serikali na nikubaliane na Kamati utengenezwe utaratibu au waraka maalum wa kuwasisitiza watendaji wote wa Halmashauri kwamba suala la asilimia kumi si hisani ni suala la sheria; kwamba Halmashauri zote zitenge asilimia kumi; kiwe ni kipaumbele na isiwe mpaka matatizo au bajeti inapoonekana inaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TAMISEMI napenda kutoa ushauri kwa Serikali. Suala la TAMISEMI kuwa chini ya Ofisi ya Rais sisi wananchi bado halijatunufaisha na nadhani ni busara sasa kama Mheshimiwa Rais ataiona ni vizuri hii TAMISEMI ikarudishwa tena kwa Waziri Mkuu, ili Waziri Mkuu aweze kulisimamia. Kwa sababu kwa mtazamo wangu naamini Mheshimiwa Rais ana majukumu mengi sana na hili jambo linahusu Halmashauri na Manispaa zetu, hivyo Mheshimiwa Rais abaki katika kujikita kwenye kusimamia Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zisimamiwe na Waziri Mkuu. Huu ni ushauri ambao naamini mtani wangu ataupokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, leo Makao Makuu yamehamia Dodoma, Dar es Salaam tunabaki kama jiji. Serikali ifike mahali sasa itambue kwamba ina wajibu wa kuyajenga majiji. Tuna Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, na Mbeya. Haya ni majiji, ukiachilia mbali Tanga na mengineyo, ni majiji ambayo Serikali lazima ije na mpango wa kuhakikisha majiji haya yanakuwa ni majiji kweli yanafanana na majiji mengine na hasa ukizingatia kwa sisi watu wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuhama yote tutabaki sisi kama sisi watu wa Jiji la Dar es Salaam na tunatakiwa tujengewe uwezo wa kutosha ili kuhakikisha Jiji letu la Dar es Salaam ambalo ndilo jiji kubwa kuliko majiji yote liwe ni jiji la mfano katika East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utawala bora. Tuna tatizo la utawala bora. Kamati imesema vizuri sana na mimi naipongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukianza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, Mheshimiwa Rais alisema magari yote ambayo sio ya mwendo kasi yanayopita katika njia ya mwendokasi yakikamatwa yang‟olewe matairi. Mheshimiwa Rais mtani wangu, mimi najua Kiswahili yeye hajui na mara nyingi anapenda kutumia Kiswahili kwa lugha ya picha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba kwa kusema magari yang‟olewe matairi nilivyomfahamu mimi, kwa kuwa hajui Kiswahili, nilitegemea kwamba anaonesha ni tatizo gari zisipite na gari itakayopita ikamatwe ipelekwe kwenye vyombo vya sheria, ipewe hukumu kali kwa mujibu wa sheria. Si kwamba wang‟oe matairi kama walivyong‟oa. Kwa sababu hata akisema mtu anatumbua naamini huwa anatumia lugha ya picha, hatumbui kwa maana ya kutumbua, anamwajibisha mtu aliyefanya makosa kwa kutokufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuaje leo vyombo vya dola, polisi wanashindwa kumfahamu Mheshimiwa Rais kwamba ana matatizo ya kutofahamu vizuri Kiswahili badala yake wanawakamata mapikipiki wanayang‟oa matairi kisha wanawapeleka mahakamani, sasa huyu mtu umeshang‟oa matairi umemuadhibu, unampeleka mahakamani kwenda kufanya nini? Jeshi la Polisi lazima lielewe lugha ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alipoambiwa kule njaa, aliwaambia mimi niwapikie, alikuwa na maana kwamba hii njaa ya Tanzania kila mtu atimize wajibu wake kuhakikisha anaepukana na njaa. Niwaombe watu wa Jeshi la Polisi wamwelewe sana mtani wangu huyu kwamba hakukusudia wang‟oe matairi ya watu na wale vijana waliong‟olewa matairi yao warudishiwe. Mahakama ndiyo yenye uwezo wa kumtia mtu hatiani, si Jeshi la Polisi wala si tamko la Mheshimiwa Rais ambalo watu hawakulielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Kinondoni tuna tatizo na wakati mwingine ndiyo maana hatupendi sana Mheshimiwa Rais kuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka kwa kukubali kunipa nafasi hii badala yake. Pili, nakushukuru wewe Mheshimiwa Mtemi Chenge, kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na namna bora unavyotuendesha katika mjadala wetu huu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza, napenda nianze na kuelezea hali halisi ya uchumi na hasa nikichukua Jimbo langu la Kinondoni kama case study. Mimi kama mwakilishi nilijitahidi kupita kwa watu wangu; hali ni mbaya sana kwa wananchi wetu. Imefika mahali katika Manispaa yetu ya Kinondoni, mahoteli yanafungwa, nyumba za wageni zinafungwa, saluni watu hawaendi; hata sasa hivi tumerudi mtu ananunua nyembe anamtafuta mwenzie anampa kitana, anamnyoa nywele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale waliokwenda saluni sasa hivi hawafanyi tena scrub. Akiambiwa afanyiwe scrub, anasema hana muda, ana jambo anawahi. Hali imekuwa mbaya zaidi mpaka kwa akinamama lishe. Dar es Salaam imefikia sasa vijana hawali mchana. Mimi mwenyewe nimeshawahi kukaa na vijana nikawakuta wamechanga, wamesonga ugali wenyewe na samaki wa kukaanga wanakula. Wanakwepa mpaka kwenda kula kwa mama lishe. Hawa akinamama lishe wamekopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza hapa, mzunguko wetu wa pesa kwa wananchi ni mdogo sana. Nimesikitika umetolewa mchango hapa na Mbunge mwenzangu kijana, nimekatishwa tamaa sana. Kwa sababu sisi vijana tunategemewa kuja kuwa viongozi wa baadaye na inapofikia kijana haamini, analeta porojo kwenye suala la kiuchumi, mimi imenikatisha tamaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme suala la bajeti ya nchi yetu siyo suala la vyama, ni suala la Kitaifa. Tunapolichukua suala hili tukalifanya ni la vyama matokeo yake inakuwa mchezo wenu ni mauti yetu. Napenda tuangalie kwanza msingi wa bajeti yetu, kwa sababu inaonekana tulipotoka na tulipo ni tofauti. Hivi msingi wa bajeti yetu ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeambiwa msingi wa bajeti yetu ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi; wakati mwingine ni hotuba ya Mheshimiwa Rais; Mpango wa Miaka 25 wa Maendeleo na mengine mengi yanaingizwa hapa. Turudi tuangalie misingi yetu tunayoitumia katika kutengeneza bajeti zetu. Kama utaratibu ndiyo huu, hatuwezi kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bajeti ya nchi tukaikabidhi kuwa eti kigezo kikubwa ni ilani ya chama wakati hili jambo linahusu nchi nzima; nafikiri hapa ni mahali pa kuanza kubadilika. Lazima suala la uchumi wa nchi yetu liwe ni suala la kitaifa, tukubaliane tunataka kwenda wapi na kwa namna gani. Vyama vya siasa vipimwe kwa kutekeleza mpango kwa ufanisi, visiwe vyama vya siasa vinatuletea mipango hapa ya kila siku ya kuibuka. Leo ikipangwa ilani hii, nasi tunaitikia ilani hii, kesho akija Mheshimiwa Rais akatoa hotuba hii, nasi tunafuata hotuba hii. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mpango wa uchumi wa nchi yetu usiwe wa kikundi cha watu wachache, tukubaliane; halafu vyama vya siasa vipimwe utekelezaji wa mpango wetu wa uchumi tuliokubaliana. Wananchi watamchagua mtu kwa kutekeleza mpango wetu tuliokubaliana. Isiwe mtu akipata nafasi ya kuongoza nchi hii, basi yeye ndio awapangie watu waende wapi. Hili nafikiri kuna mjadala hapa inabidi tufanye ili tupate muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna tatizo kubwa la nidhamu ya bajeti yetu. Ukiangalia bajeti yetu tulichokubaliana na watekelezaji wetu, watu wetu wa Serikali wanavyotekeleza, ni tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye bajeti, tulikubaliana hapa tutanunua ndege nne; lakini leo unaweza ukasikia mtu anajigamba eti tumeshalipa hela ya ndege sita. Msingi wa bajeti uko wapi? Kwa nini bajeti inapitishwa kama sheria? Leo nchi ya Tanzania imekuwa kama genge; mtu anaamua kufanya matumizi kwenye genge lake na siyo suala la Tanzania kuendeshwa kwa msingi wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweza ukamsikia kiongozi wetu anakwenda mahali anasema nyie nitawapeni shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie Magereza nawapa shilingi bilioni moja hapa mjenge; nyie Magomeni, nawapa shilingi bilioni 10 hapa mjenge; nyie sijui Katavi au wapi, nitawapeni hapa mjenge TRA ya shilingi bilioni ngapi! Hatuwezi kwenda kwa mtindo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nidhamu yetu ya matumizi ni muhimu sana na lazima Bunge liheshimiwe kwa kuwa linapitisha bajeti na inakuwa sheria na ihakikishe inafanya kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti. Hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli wa mipango yetu; hivi tumeongeza mipango yetu ya maendeleo ya bajeti kutoka 26% au 27% tukaweka asilimia 40; ni kweli tulikuwa tunakusudia kutekeleza? Hivi kweli tunachokipanga tunakusudia kukitekeleza? Kwa nini hatuwi wakweli? Imefika mahali na sisi Wabunge tunapenda kuongopewa. Inafika mahali sisi Wabunge wenyewe tunataka Serikali ije kutuletea muujiza hapa. Nitafanya hivi asilimia 200, nitafanya hivi asilimia 300 mpaka mtu mmoja siku moja akasema kwanza asilimia mwisho 100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatuwi wakweli katika mipango yetu? Hivi wachumi wetu hawa hawajui projection ya mapato yetu? Leo inafika bajeti yetu, tumepeleka mipango yetu, fungu la maendeleo asilimia 20, tena inapelekwa kwenye quarter ya tatu mwezi wa 12. Hivi kweli watendaji wetu, wapangaji wetu wa mipango hawajui uhalisia wa hali yetu? Kama tunataka tubadilike tutoke hapa tulipo, tuwe wakweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono sana Kamati ya Bajeti, imeeleza mambo mengi mazuri sana na kwa kweli kama Serikali itayafanyia kazi tutatoka. Nawaomba Wabunge wenzangu, bajeti ijayo na mipango ijayo; mpango ambao siyo realistic tuukatae. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mapato tuliyotegemea kutoka kwa wafadhili imekuja asilimia 16 tu na mapato tuliyokuwa tunayategemea kutoka kwa wafadhili ni zaidi ya shilingi trilioni 10.08. Asilimia sita ni sawasawa na shilingi trilioni moja. Kamati inatuambia kwamba hawajui kwa nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali na kuliomba Bunge lako Tukufu; tuna tatizo sisi na tatizo letu hatutaki kuambizana ukweli. Kuna jambo linasemwa kwamba sisi Zanzibar hatuko vizuri. Sisi ni Watanzania, ni wenyewe kwa wenyewe; hivi Wazanzibari wale wakikaa pamoja kuna tatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Rais aliyepita Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alitumia nguvu kubwa sana na muda wake mwingi kuwaunganisha Wazanzibari, Wazanzibari wakafika wakawa na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa. Hivi jamani sisi kama Taifa tunakwenda mbele au tunarudi nyuma? Baada ya kufika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, leo tunakwenda tunarudi nyuma? Naomba hili jambo lizungumzwe wale wenzetu wakae pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naamini kabisa, hizi pesa za nje zinakawia; miongoni mwa sababu ni pamoja na huu utengamano wa Zanzibar, inaweza ikawa ni sababu. Hili jambo tusilichukulie kishabiki; ni jambo la Kitaifa, ni letu; sisi ni wenyewe kwa wenyewe, kwa nini tusikae kama Taifa tukatatua tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wote wapo na wote walikuwa ma-senior katika uongozi wa nchi hii. Nani asiyemjua Mheshimiwa Maalim Seif, nani asiyemjua Mheshimiwa Mzee Shein? Wote hawa wanajua na wote wana malengo ya kuhakikisha Wazanzibari wanafika mahali pazuri. Tukizungumza kama Taifa, naamini tutatoka na pesa hizo tutazipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kwamba mipango yetu haizingatii hali yetu ya kimazingira. Hivi sisi tangu nchi hii imeumbwa, kuna samaki kule baharini wanapita, wanavuliwa huku juu Somalia, South Africa, wanapita wale samaki kila siku. Nimeongea na wataalam wa samaki wanasema, wale wanakua na wakishakua wanakufa. Sisi tangu tumepata uhuru nchi hii hatujawahi kutumia resource ile ya samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kuna kipindi aliikamata ile meli, wakapatikana samaki wengi, yule mtaalam anawaambia Watanzania hawajui hata resources zilizopo kwenye bahari yao, wananchi waliambiwa waende wakachukue samaki watu wamekwenda na mabeseni, kumbe samaki mmoja beseni halitoshi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, kwa nini hatuangalii mazingira yetu, Tanzania kwa jiografia yetu tunapokuwa maskini wenzetu hawatuamini, hawatuelewi, hawaelewi kwa nini tumekuwa maskini sisi, lakini sisi tukipanga mipango hatuangalii jiografia yetu, hatuangalii vitu gani sisi tunavyo wengine hawana, tunataka kufanya vitu wanavyofanya watu wasiokuwa na vitu kama vya kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaimba tu hapa viwanda, hivi sisi kweli tunaweza kwenda kwenye viwanda, kwa nini tusiende kwa yale tunayoyaweza. Sisi tunaweza kulima na watu wetu wanakuwa kwenye kilimo na tuliambizana hapa kilimo ndiyo uti wa mgongo, hayo ni majina – Kilimo Kwanza, kilimo cha kusonga mbele, majina yalikuwa mengi, lakini kimsingi kilimo ni uti wa mgongo. Kwa nini hatu-invest kwenye kilimo? Leo tunategemea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MAULID S. ABDALLAH MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Allah (S.W.) kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya nchi yetu ni kitu muhimu sana na yasipolindwa bila shaka madhara yake yanaweza kutuathiri sote kama Taifa bila ya kubagua nani amesababisha au nani hakusababisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira ni sisi wenyewe tunaoishi na kuyatumia mazingira haya mfano, kilimo kisichozingatia uharibifu wa mazingira; kama vile kulima kwenye misitu yetu ya hifadhi, kilimo kwenye vyanzo vya maji, kulima kwenye maporomoko bila ya kufuata kanuni ya kilimo hasa kwenye maeneo ya maporomoko. Aidha, mifugo isiyozingati mbinu za kisasa, mfano, kufuga na kulisha kwenye hifadhi za misitu na mbuga za wanyama, kufuga wanyama wengi kuliko uwezo wa ardhi iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bahari, Mito, Maziwa na Mabwawa kutumia uvuvi haramu wa mabomu au nyavu ndogo maarufu kama jalife. Katika yote haya tusisahau ukataji wa mkaa na kuni kama nishati hasa kwa ajili ya Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hayo, bado tuna tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira katika majiji na njia kuu kwa uzalishaji wa taka ngumu na majitaka kutoka majumbani na viwandani. Aidha, vifungashio vya bidhaa za viwandani na vibebeo mfano, mifuko ya plastiki, maboksi na plastiki ngumu na sehemu kubwa yanayochafua na kuharibu mazingira yetu. Mfumo mbovu wa utiririshaji wa maji taka kutoka viwandani na majumbani kwenda maeneo maalum kwa ajili ya kuhifadhi, kuyatupa au kuchakata ili uweze kutumika tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni au ushauri;
(i) Mifugo yetu iwe kwa kiwango kisichoharibu mazingira hivyo basi, wafugaji wetu waelimishwe ufugaji wa kisasa wenye tija yaani mifugo kidogo tija kubwa.
(ii) Wafugaji wasihamehame kiasi ambacho wanaweza kuharibu mazingira kwa sehemu kubwa badala ya eneo dogo kama hawatahama. Pia wafundishwe kupanda nyasi kwa ajili ya malisho ya wanyama wao.
(iii) Wavuvi wadogowadogo na wale wanaotumia zana haramu, wafundishwe uvuvi bora na Serikali iwapatie vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki ili waweze kupata mavuno mengi ya samaki jambo ambalo ndicho kivutio kikubwa cha kutumia uvuvi haramu.
(iv) Wakata mkaa; katika hili Serikali naishauri yafuatayo:-
• Mosi, Serikali iwafundishe wakulima njia mbadala ya kujipatia kipato kinyume na kuuza mkaa. Wanakijiji wengi hawana njia mbadala ya kupata fedha zaidi ya mkaa.
• Pili, kusambaza gesi majumbani katika Majiji ya Dar es Salaam na mengine. Aidha, tuna kila sababu ya kupunguza bei ya umeme ili watu wapike kwa jiko la umeme.
(v) Serikali iwe na takwimu zote za wazalishaji taka wa viwanda au majumbani na kila mtu achangie gharama za usafi na utunzaji wa mazingira kulingana na kiwango chake cha uchafuzi wa mazingira.
(vi) Serikali iwe mfano bora wa kutunza mazingira na kusimamia mazingira kwa kutumia vyombo vyake mfano mzuri, utunzaji wa mikoko Jangwani na daraja la Salenda. Serikali isiache mikoko na uoto wa asili ukifa maeneo ambayo Serikali au Ofisi ya Makamu wa Rais ni karibu yake.
(vii) Serikali isiweke ubaguzi wa utekelezaji wa Sheria. Mfano, Sheria ya mita sitini ya Mito. Kwangu Dar es Salaam Ofisi ya DART Jangwani na Jengo la MOI Muhimbili ni majengo yaliyo karibu na mito ndani ya mita sitini, lakini hayaguswi badala yake Serikali imeenda kubomoa nyumba za wananchi ambao Sheria imewakuta, jambo hili si utaratibu wa Serikali.
(viii) Serikali ishirikiane na Manispaa za Mijini zenye kuzalisha taka nyingi ili ziweze kujenga mitambo ya kuchakata taka na kuwa mbolea na manispaa zitalipa kidogo kidogo kwa Serikali; jambo hili lina faida ya mazingira, ajira, mbolea na kadhalika.
(ix) Sheria itungwe ya kudhibiti uzalishaji wa plastiki ngumu na laini ili kupunguza au kuondoa taka ambazo si rahisi kuzidhibiti.
(x) Wakulima wetu waelimishwe kilimo bora cha kisasa chenye tija. Bila shaka wananchi wakielimishwa vizuri hawana haja kwenda kwenye vyanzo vya maji, maeneo ya hifadhi na maeneo ya maporomoko.
(xi) Kuanzisha operation ya kupanda miti mingi kuliko kasi ya wakata miti na wavuna misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyenzi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kunijalia uzima.

Pili, nikushukuru nawe kwa kunipa fursa hii adhimu nami kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu sana. Nimpongeze kidogo Mheshimiwa dada yangu Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayofanya, hasa kwa uwasilishaji mzuri aliyoufanya jana. Kwa kweli wakati anawasilisha Dada Ummy niliamini kabisa kwamba matatizo yetu yamekwisha. Vilevile nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati kwa kutuonyesha wazi kwamba pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Dada Ummy lakini Wizara hii bado ina matatizo lukuki, hata bajeti waliyopewa haikufika zaidi ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kabisa hotuba ya Kambi ya Upinzani. Nimpongeze Dada yangu Mheshimiwa Ester kwa uwasilishaji mzuri na kuonesha matatizo yaliyopo kwenye Wizara yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina Sera ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo imetolewa mwaka 2007. Katika sera yetu hii ukienda ukurasa 10 ambao unaeleza afya ya msingi ukienda kwenye ukurasa wa 11 nitayasoma madhumuni ya sera yetu hii. Madhumini ya sera yetu hii ni kupanua dhana ya afya ya msingi na kuwa na huduma bora za afya zinazoendana na wakati, endelevu na zinazowafikia wanachi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye tamko la sera namba moja na namba mbili, tunaambiwa Serikali itahakikisha wananchi na sekta mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya katika ngazi zote ili kuboresha afya.
Pili, Serikali itaimarisha uendeshaji na usimamizi wa huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera hii imeingizwa kwenye utendaji kwa kutumia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tumeambiwa mara nyingi hapa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itajenga zahanati kila kijiji. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema itajenga kituo cha afya kila kata. Tumeambiwa mara nyingi hapa kwamba hii Ilani ndiyo imefanya wananchi kukiamini Chama cha Mapainduzi. Na mimi kwa kweli nitakuwa Wakili wa wananchi kuhakikisha Chama cha Mapinduzi wanatekeleza Ilani yao hii, Ilani ambayo ilikuwa ndiyo sababu wananchi kuwaamini. Wasipotekeleza tafsiri yake wamewarubuni wananchi, wamewalaghai wananchi, hawatekelezi yale ambayo ilikuwa ndiyo sababu ya kupewa madaraka ya kuongoza nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makubaliano ya Abuja ya mwaka 1989 Serikali zetu za Afrika walikubaliana Wizara ya Afya itengewe walau basi asilimia 15 ya bajeti, bajeti yetu hapa ni shilingi trilioni 31, asilimia 15 ni shilingi trilioni
4.5. Sisi tumetenga shilingi trilioni 1.1. Kwa utaratibu huu hivi kweli tuna malengo ya dhati ya kuhakikisha tunapunguza vifo vya akina mama? Hivi kweli tuna malengo ya dhati ya kuhakikisha tunapeleka afya ya msingi kwa wananchi wote kama sera yetu ilivyosema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe wakweli, tuhakikishe basi walau niungane na senior kaka yangu Mheshimiwa Mbatia pale, bajeti hii basi walau tufanye asilimia tano ambayo itakuwa ni shilingi trilioni 1.5, na hii asilimia tano tukiiweka tuongeze madaktari, tuna madaktari wanazungukazunguka tumewasomesha kwa gharama kubwa, kwa nini tusiwaajiri madaktari na wahudumu wa afya, wafanyakazi wote wa idara za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tushirikiane na Halmashauri kuhakikisha tunajenga hizo zahanati kila kijiji, tuhakikishe tunajenga vituo cha afya kila kata. Kama tuna nia ya dhati ya kumsaidia mama na mtoto, kuwasaidia watu wetu hawa, tuwe na zahanati kila kijiji kwa sababu kule ndiyo huduma itamfikia mwananchi. Vifo vya akina mama vinasababishwa na kutokwenda kliniki, hawapati huduma za kliniki, huduma ya kliniki zahanati isipokuwepo kijijini ataipatia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hospitali yetu ya Mwananyamala, mimi ni Mbunge wa Jimbo Kinondoni, hospitali ya Mwananyamala imepandishwa hadhi, imekuwa ya rufaa, jambo la kusikitisha Serikali hawatoi fungu lolote la uendeshaji wa hospitali ile, badala yake imekuwa gharama kwa Halmashauri na Manispaa ya Kinondoni. Uendeshaji wa hospitali ya Mwananyamala inatugharimu karibu shilingi bilioni 6.9 kila wiki. Mbaya zaidi tumepewa tena jukumu, kwa kuwa hospitali yetu imekuwa ya rufaa tunatakiwa tujenge hospitali ya Wilaya. Serikali ipo kimya haitusaidii chochote kwenye ujenzi ya Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali yetu ya Kinondoni kwa maana ya Mwananyamala katika Jimbo letu na Wilaya yetu ina zaidi ya watu milioni moja. Msongamano umekuwa mkubwa na msongamano ukubwa wake unatokana na kwa sababu hatuna Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, naomba Wizara ije kutuambia ama wapeleke fedha za ruzuku kwenye Hospitali ya Mwananyamala au watusaidie kujenga hospitali ya Wilaya ambayo ipo Mabwepande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hali ngumu sana katika Hospitali yetu Mwananyamala. Dawa tunapata MSD, wakati mwingine dawa tunazozitaka wakati mwingine MSD hawana, Wanapokuwa hawana MSD hamna njia mbadala. Hakuna chombo kingine kinafanya ushindani na MSD. Ukitaka kununua dawa nje ya mfumo wa MSD unatakiwa ufuate mfumo wa manunuzi. Hivi leo dawa tunatumia kama tunataka kununua kipuli cha gari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Wizara ituletee njia mbadala ama MSD ipate mtu wa kufanya naye kazi mbadala wake au itupe kibali tunapokuwa tunahitaji dawa tusifuate utaratibu huu wa manunuzi ambao unatupa taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hatuna vifaa na gharama za hivi vifaa vya upimaji ni gharama kubwa, Serikali ituambie ina mpango gani wa kutumia utaratibu wa PPP (Public Private Partnership) kwamba watu binafsi hasa hospitali zetu za Mjini, watu wana fedha wanataka kutibiwa matibabu mazuri, wako tayari kuchangia gharama na watu binafsi wanaweza wakatoa kununua mitambo kwa gharama zao, tukafanya partnership. Serikali inasemaje, imeshindwa hilo basi Serikali kutudhamini kwenye mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ukitaka kununua kitu kwa mkopo, ukitaka kukopa banki lazima upate dhamana kutoka Serikali, Serikali inasemaje katika hili, lazima Serikali itudhamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni afya ya msingi. Elimu ya msingi Mheshimiwa Magufuli amesema bure namshukuru sana na nampongeza. Je, afya ya msingi kwa nini isiwe bure? Hivi wananchi hawa wanaoenda kutibiwa kwenye zahanati kuna shida gani hawa wakitibiwa bure? Ukiangalia kundi kubwa ambalo linakwenda hospitali mara kwa mara tayari linatibiwa bure, wanawake, watoto chini ya miaka mitano, wazee wanatibiwa bure, wagonjwa wa kifua kikuu, wagonjwa wa HIV, kisukari, wanatibiwa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu tunachangia huduma katika Mifuko ya Kijamii ya Afya. Sasa ukiangalia ukiondoa makundi hayo ambayo ndiyo yako mengi hospitali huyo anayelipia ni nani? Kwa nini Serikali sasa isikubali kwa afya ya msingi watu wetu wakapata huduma ya bure? Na kwa sababu tayari tunatoa bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Hospitali yetu Mwananyamala tunataka tuongezewe wafanyakazi. Sisi kwa kutwa tunahudumia watu 2,500 ukiondoa watu 1,500 wa methadone jumla tunahudumia watu 4,000.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi kwa kunijaalia uzima hatimaye nami nimepata fursa ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu katika Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, napenda nianze kuchangia kwenye Wizara hii kwa kuzungumzia Hospitali ya Mwananyamala. Hospitali yetu ya Mwananyamala imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa, lakini kwa masikitiko makubwa bado Serikali haitoi ruzuku ya kuiendesha hospitali hii, badala yake, mzigo wote wa uendeshaji umeachiwa Manispaa ya Kinondoni peke yake. Kwa ukubwa wa hospitali, Manispaa inatumia kiasi cha Shilingi milioni 69 kwa wiki jambo ambalo ni mzigo mzito kwa Manispaa ya Kinondoni yenye changamoto lukuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini basi Serikali itaanza kutoa ruzuku ya uendeshaji wa Hospitali ya Mwananyamala kwa sababu sasa siyo Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni tena? Aidha, kwa kuwa Hospitali ya Mwananyamala imepandishwa hadhi: Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Mabwepande hasa ukizingatia kuwa Hospitali ya Mwananyamala imezidiwa na mlundikano na wagonjwa, bila kusahau wakazi wa maeneo ya pembezoni, itakuwa ni mkombozi wao hasa kutokana na umbali na msongamano wa foleni za magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali yetu ya Mwananyamala ina changamoto na matatizo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida Hospitali ya Mwananyamala inahudumia wagonjwa 2,500 kwa siku, wagonjwa wa kawaida na wagonjwa 1,500 vijana walioathirika na madawa ya kulevya. Hivyo kufikisha jumla ya wagonjwa 4,000 kwa siku, jambo ambalo limepelekea upungufu wa Madaktari na Wauguzi, vifaa tiba na hata uhaba wa vitanda. Hivyo tunaiomba Serikali ituongezee Madaktari Bingwa 10 ili tuwe na 26; Madaktari wa kawaida (General Medical Officer) 20 ili tufikie 100 na Wauguzi 100 ili tuwe na Wauguzi 350.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba haya kwa kuwa hospitali hii inatuhudumia watu wote wa kutoka mikoa yote kwa sababu Kinondoni ndiyo Dar es Salaam na Dar es Salaam ndiyo Tanzania. Hivyo basi, Kinondoni ndiyo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa zinazotumika kwenye hospitali zetu, zinatoka katika maghala ya MSD. Wakati mwingine MSD inakuwa haina dawa inayotakiwa kwa wakati muafaka, hata kupelekea maduka yetu na hospitali (za Serikali) kukosa dawa. Kwa bahati mbaya, hakuna ushindani katika jambo hili kwa maana ukikosa dawa MSD, basi unaweza kuzinunua kwa wengine kama Wakala wa Serikali, badala yake unatakiwa ufuate utaratibu wa kawaida wa Manunuzi ya Umma, jambo ambalo lina mlolongo mrefu wa kuchukua muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwamba, kwa nini isiweke ushindani katika biashara hii ya dawa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wakati? Mfano MSD iwepo na Wakala mwingine kama MSD. Aidha, kwa nini Serikali isiweke masharti nafuu ya kununua dawa bila ya kufuata mfumo wa manunuzi wa kawaida endapo MSD haina dawa inayotakiwa kwenye hospitali zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mwananyamala haina mashine ya CT-Scan na nyingine kwa ajili ya kupima baadhi ya wagonjwa. Wote tunajua hali za hospitali zetu na Serikali kwa ujumla. Aidha, hospitali ya Mwananyamala wanataka kumaliza jengo la Bima ya Afya na kununua mashine ya CT-Scan kwa mkopo kutoka Shirika la Afya kwa makubaliano ya kulipa kidogo kidogo kutokana na kukusanya malipo ya kuchangia gharama za matibabu hospitalini hapo: Je, Serikali iko tayari kuidhamini Hospitali ya Mwananyamala ili iweze kukopesheka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vifaa vya vipimo ni ghali sana; na vinahitajika sana hasa katika Hospitali yetu ya Kinondoni: Je, Serikali iko tayari sasa kutumia mfumo wa PPP (Public Private Partisanship) ili wafanyabiashara na wanaotaka kushirikiana na Taasisi zetu za Umma waruhusiwe kwa makubaliano ya kugawana faida inayopatikana kutokana na uchangiaji wa gharama za vipimo?

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba Serikali ya Awamu ya Tano ifanye ujasiri kama ilivyofanya kwa uchangiaji wa gharama za elimu, yaani kufuta uchangiaji wa gharama ya matibabu ya msingi iwe bure. Naomba hayo kwa sababu zifuatazo:-

(1) Idadi kubwa ya wagonjwa wetu katika afya ya msingi ni kutoka katika makundi maalum, yaani watoto wa chini ya miaka mitano, wazee wa zaidi ya miaka 60 na akinamama wajawazito. Hawa wote wametibiwa bure.

(2) Wagonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Kisukari wote wanatibiwa bure. Hili nalo lina idadi kubwa.

(3) Vijana walioathirika na madawa ya kulevya, nao wanatibiwa bure.

(4) Maskini wanapaswa kutibiwa bure kwani asilimia 70 ya Watanzania ni maskini, wanaishi chini ya dola moja na hasa Watanzania wa Vijijini, wanastahili kupata huduma ya afya bila malipo.

(5) Serikali inatoa dawa (fedha za dawa) kwa Vituo vya Afya nchi nzima, dawa ambazo zinaweza kuwatibia wagonjwa bure.

(6) Utaratibu wa Bima, wananchi wengi wakijiunga na Bima inatosha kugharamia wachache waliobaki kuweza kupata huduma bure.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pili, nakushukuru nawe Spika wangu kwa kunipa fursa ya kuzungumza katika Wizara yetu hii muhimu sana kwangu nikiwa kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni mwanachama wa Simba Sport Club na kadi yangu ni hai. Kuna maneno yamesemwa hapa lazima yawekwe sawa. Nashukuru uligundua kwamba yanayosemwa hayako sawasawa, ukaamua kusimamisha sasa mimi kwa sababu nakuja kusema sawa sasa, record tuna-balance story. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza timu ya Simba ndiyo timu bora kabisa Tanzania. Vile vile ndiyo timu ambayo imecheza vizuri na imeshinda mechi zake na hasa mechi zote ngumu. Wanaodai kwamba tunapendelewa, record zinaonesha tumewafunga Zanzibar, tumewafunga juzi pale na wanamkumbuka sana Kichuya na kona zake. Kwa hiyo, suala la upendeleo kwa Simba halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hiyo mbao iliyowatoa machozi, ikawafanya wasicheze fainali, sisi tuliwafunga Mwanza na wao wakafungwa Mwanza. Kwa hiyo, ukitafuta timu ambayo ina kiwango kidogo na ambayo siku ukienda kwenye mechi za Kimataifa wanatutia aibu sana hawa wanaobebwa halafu… (Makofi)

TAARIFA...

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, taarifa hii siipokei, kwa sababu record zinaeleweka kwamba Simba siyo muda mrefu tu ilikuwa inashiriki na imeshiriki kwa ufanisi na ukizungumza timu ambayo inatambulika nchi hii, hakuna kama Simba. Tunawashinda kwa kuanza hata kuvaa viatu, sikwambii kuvaa jezi. Kwa hiyo, Simba ni timu ambayo haiwezi kusahaulika na timu ambayo watu hawawezi kuisahau. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha msingi hapa ambacho nataka tukieleze ni kwamba mpira wa miguu una sheria na taratibu. Bahati nzuri msemaji kasema kabisa anataka Wizara iachane na soka, ifuate michezo mingine. Bila shaka yeye ana mchezo mwingine zaidi ya soka, japokuwa hajausema, naamini utakuwa labda kuogolea au kuvuta kamba. Kwa hiyo, hafahamu vizuri Sheria za Soka.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Soka imewekwa kabisa kwamba mchezaji akipata kadi tatu, haikupaswa hata Simba kukata rufaa, ni automatic kwamba mtu amevunja sheria, wasimamizi wa sheria wanatakiwa Simba wawape points zao. Kama hili halitoshi, sisi leo tunakwenda Gabon kule, kwa sababu wale ambao walipata ushindi kinyume na utaratibu walinyang’anywa zile points. Sasa nashangaa leo hao hao wanashangilia Gabon lakini utaratibu huo huo ukiwa kwa Simba inakuwa nongwa.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niweke hayo mambo sawa, Simba ni timu makini, itachukua ubingwa, makombe yote mawili, bila kubebwa na huyo Yanga tunamsubiri tutaonana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hili, naiomba Wizara isaidie sana timu zetu hizi kubwa Simba na Yanga. Nikiri kwamba Wizara hasa Mheshimiwa Waziri, tumekubaliana tupate muda tukae tujadiliane kuhusu michezo na mambo ya sanaa katika Jimbo langu la Kinondoni, lakini timu zetu hizi za Simba na Yanga ni timu ambazo zinaunganisha umoja wetu. Leo mimi na ndugu yangu Mheshimiwa Mtolea nahitilafiana naye, lakini naungana na Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa wengine wa CCM. Leo usishangae Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akakaa pamoja na kiongozi wangu Mheshimiwa Mbowe katika soka. Sasa hizi timu zina umuhimu mkubwa sana, kwa sasa hizi timu zinalinda mpaka utaifa wetu, tunaweza tukahitilafiana kwenye vyama, lakini tukakutana kwenye mpira.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa yako hatuhami timu hizi. Unaweza kuhama vitu vingine vyote, lakini ni ngumu sana kuhama timu. Sasa kama timu hizi zimefika mahali zinalinda utaifa wetu, Wizara sasa izisaidie hizi timu. Msaada ambao nautaka kwa Wizara; hizi timu zimeanza miaka ya 1930, 1936 ni timu ambazo zimeanza siku nyingi, lakini inaonekana huko nyuma viongozi walifanya kazi kubwa. Wamejenga majengo. Clubs zote zina majengo makubwa. Wamejenga imani ya watu, Clubs zote zina wapenzi wengi, lakini inaonekana sasa hivi viongozi wetu wameshindwa kututoa pale walipotufikisha wazee kutupeleka kule tunakotamani. Nahisi kuna tatizo la menejimenti, kuna tatizo la ufahamu wa uendeshaji hizi clubs zetu kama wanavyoendesha wengine.

Mheshimiwa Spika, timu ambazo zina wapenzi wa kutosha, lakini ndiyo timu ambazo zinaongoza kwa kuombaomba, ni timu ambazo zinaishi kwa kutegemea wafadhili. Wakati mwingine inashindwa hata kututumia sisi wanachama wake na wapenzi wake. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kukaa nao na atumie wataalam wake wa Wizara kuzisaidia hizi timu ili ziweze kutumia rasilimali zake ilizokuwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye muziki. Mimi natoka Jimbo la Kinondoni, Jimbo la Ma-star, nina Wasanii wa kutosha kabisa. Kama nilivyosema, Mheshimiwa Waziri ameniambia tutafanya vikao vyetu na vijana hawa. Naomba jambo la kwanza ni-declare interest kwamba mimi ni mpenzi mkubwa wa wanamuziki wangu wa Kinondoni, nikianza na mtu mzima Diamond; na kwa sababu Diamond na Ali Kiba wanakuza muziki huu wa kizazi kipya, naye namtambua na nampenda sana.

Mheshimiwa Spika, pia mimi ni mpenzi wa muziki mpya unaitwa singeli. Huu huwezi kumsahau Msaga Sumu, kijana Manifongo, hata Profesa J, ametoa muziki wake mmoja anasema Kazi, Kazi. Anasema watu wafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, hawa vijana wakati wanafanya hizi kazi zao, Wizara yetu inatakiwa iwalinde. Niliwahi kuzungumza na Diamond, yeye kama yeye muziki wake unatumika kwenye Makampuni ya Simu kama milio ya simu, lakini malipo anayoyapata hayaendani kabisa na thamani ya muziki wake. Wizara sasa iingilie, iwahoji, wanatumia vigezo gani kuwalipa hawa vijana wetu?

Mheshimiwa Spika, la pili amelisema Profesa J, nimeongea na Diamond TRA wanampelekea anadaiwa milioni 400, hivi ukidaiwa milioni 400 maana yake yeye mwenyewe mapato yake basi ni karibu shilingi bilioni 1.2. Sasa haya mapato kama ndio hivyo TRA wanasema yeye alipe kodi shilingi milioni 400, mapato yake ni mabilioni hayo, yamekwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, vile vile vijana hawa wanahitaji kusaidiwa kwenye menejimenti. Leo Diamond katoka alikotoka, kafika pale. Hivi tunamwacha pale pale adumae au tunamwendelezaje? Yeye ameshakua sasa hivi ni kama model kwa wasanii wa Tanzania, East Africa na hata Afrika kwa ujumla. Wizara lazima iangalie namna gani inaweza kumtoa pale; na wakati mwingine siyo kwa kutoa pesa, ni kukaa nao hawa vijana na kuwasaidia katika mambo ya utawala. Kwa sababu tuna viongozi wetu wa mambo haya ya sanaa, washiriki katika kuwasaidia wasanii wetu kwa mambo ya utawala.

Mheshimiwa Spika, pia niseme, pamoja na mapenzi yangu makubwa kabisa na wanamuziki hawa na wasanii wa maigizo, bado nahimiza wasanii wetu lazima wajikite kwenye nidhamu. Nidhamu ndiyo mafanikio ya kila jambo. Haina maana ukiwa msanii ukose nidhamu. Leo wasanii wamekuwa ndio katika watu wanaoandikwa andikwa kwenye magazeti na wengine wanaamini wakifanya utovu wa nidhamu ndio majina yao yatatajwa. Mimi Mbunge wao siamini katika hilo. Naamini kwamba wafanye kazi kwa juhudi, walinde vipaji vyao, wafanye kazi kwa umakini.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kwamba malipo wanayoyapata hayaendani na kazi wanayoifanya. Leo wasanii wa maigizo, wanatengeneza filamu wakati mwingine kwa shilingi milioni 15, shilingi milioni 12; anakwenda kuingia mkataba shilingi milioni 20, kazi ndio imeuzwa kabisa! Maana yake hawezi hata ku-print tena ile kazi. Kazi ndiyo imeuzwa, imeenda kwa Step Entertainment au nani au nani na huyo mtu anayenunua kazi ni kikampuni kimoja tu. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, iangalie hawa watu wanaonunua kazi za wasanii na kupora kabisa kazi na kuchukua hati miliki ya kazi, lazima waangaliwe.

Mheshimiwa Spika, kubwa nawaunga mkono vijana wangu, nawaandaa, tutafanya kikao na Wizara, lakini kubwa waangalie nidhamu na maadili ya Kitanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MAULID S. MTULIA: Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami nipate fursa ya kuchangia katika Wizara hii nyeti sana ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wenzangu walivyolalamika na kuonesha kwamba bado tuna tatizo kubwa la maji, nami Dar es Salaam tatizo lipo; na ukingalia takwimu za Mheshimiwa Waziri, zinaonesha kwamba katika maji tumetoka asilimia 72 tumekwenda asilimia 75, lakini kwa masikitiko makubwa, sisi watu wa Dar es Salaam hatuna mbadala wa maji. Unapotupa maji asilimia 75 maana yake hii asilimia 25 nyingine tunaitoa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna mito kusema kwamba tutakwenda kuteka maji kwenye mito, hatuna maziwa, hatuna visima. Kwa hiyo, maana yake kutoa maji asilimia 75 Dar es Salaam ni kuwaambia wananchi wa Dar es Salaam asilimia 25 watumie maji machafu; na hata hivyo visima ukichimba havichimbiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Dar es Salaam kuna maeneo mengi hakuna maji. Mengi sana, Majimbo yote, Dar es Salaam yote; ukienda kwa kaka yangu Mheshimiwa Mnyika utakuta kuna maeneo mengi hakuna maji, ukienda kule Kigamboni hakuna maji, ukienda huku Kawe hakuna maji. Sasa sisi tuna tatizo hilo kubwa sana la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo lingine ambalo hatuwezi kulalamika sana ambalo ni tatizo la fedha na Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa wamechangia kwamba tuongeze tozo ya sh.50/=. Mimi bahati nzuri nipo kwenye Kamati ya Nishati na Madini na kama kuna jambo ambalo lina tozo kubwa, basi mafuta yana tozo kubwa sana. Sipingi kuongezwa sh.50/= lakini nataka nitoe njia mbadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hii Mamlaka yetu ya EWURA ambayo inasimamia tozo hizi za kwenye mafuta; na kuna vinasaba ambavyo tunavigharamia, lakini katika tozo la vinasaba kwa Tanzania tunafika mpaka shilingi sita na senti kidogo, lakini ukienda wenzetu wa Kenya na Uganda wana shilingi moja na shilingi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua teknolojia yawezekana ni ya juu sana kwa sababu sisi tunatumia chemicals, wenzetu wanatumia marking kwa maana wakati mwingine ni kubadilisha tu rangi ya mafuta, inajulikana kwamba haya yamechakachuliwa, haya hayajachakachuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali sasa wanapokwenda kukaa, watazame; wakati umefika sasa, ni bora kutumia teknolojia ambayo tunadhani itakuwa na gharama nafuu hata kama ubora wake utakuwa siyo sawa na ubora wa sasa ili isiwe tu kila tunapopata tatizo tunaongeza tozo la mafuta ambayo athari yake kimsingi ni lazima itarudi kwa mwananchi. Huyo mwananchi tunataka kumkomboa ili apate maji, lakini huyo huyo tunamwongezea mzigo. Kwa sababu huduma zote mwananchi anazopata kijijini lazima atatumia mafuta. Hakiendi chochote lazima mafuta itatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, badala ya kutumia shilingi sita, tutumie zile shilingi mbili au shilingi moja ili sasa upungufu iwe ndiyo pesa ambayo tunaweza tukaitumia tukaingiza kwenye maji ili mwananchi asipate mzigo wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tuna tatizo la ukosefu wa maji na takwimu hapa ninazo. Ukiangalia vitabu vya Mheshimiwa Waziri, ameeleza hapa. Mwaka 2016 maji ilikuwa kila mwananchi anaweza kupata mita ya ujazo 1,952, lakini katika kitabu chake cha 2017 ameonesha kwamba inapungua mpaka 1,800. Ukiangalia 2025 inakadiriwa maji yatapungua mpaka millimeter 1,500.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi kuchangia. Nashukuru kwa michango mizuri iliyotolewa na wenzangu, lakini na wawakilishi wetu wa Kambi Rasmi ya Upinzani na hasa kuonesha tofauti kwa sababu mara nyingi watu wengi wanafikiri upinzani ni kupinga tu, lakini leo upinzani umeonesha kabisa siyo lengo letu kupinga tu, mambo mazuri tunayaunga mkono. Kwa hiyo, hili nashukuru sana. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, na mimi naunga mkono hizi itifaki, lakini nina maeneo ambayo nayaona lazima tuyaangalie na tuyarekebishe.

Mheshikiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, Wajumbe wa Kamati na hata watu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wamelalamikia suala la muda, kwamba wakati mwingine Serikali inaingia itifaki muda mrefu takribani miaka sita, bado hawajaleta Bungeni kwa ajili ya kuridhia hilo Azimio. Hili siyo jambo zuri. Naiomba Serikali itambue kwamba, Wabunge kwa ujumla wao wapo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Tutajitajhidi kufanya lolote lile kwa maslahi ya nchi yetu, kwa hiyo, hata jambo lolote wakiliona zuri wasihofie wala tusiviziane, walete Bungeni na Wabunge huku kama kawaida yetu tutalichangia vizuri.

Kwa hiyo, hili jambo liangaliwe isiwe kawaida ya Serikali kuwa na wasiwasi wa kuleta jambo, jambo lolote lenye maslahi mapana ya nchi yetu wasiwe na kigugumizi, walilete tutalichangia, penye kasoro tutawaeleza, penye kuunga mkono tutaunga mkono, tuwe na utamaduni huo. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, wewe unajua sisi tuko Dar es Salaam pale, tunapozungumzia itifaki ya mambo haya ya bahari mimi nakubaliana na itifaki, lakini nina mashaka na utekelezaji wetu wa kazi zetu wenyewe.

Mheshimiwa Mwneyekiti, wewe Jimbo lako la Ilala pamoja na Jimbo langu mimi la Kinondoni tunaungana pale Salender Bridge, tuna mikoko na Serikali tunayo pale Dar es Salaam. Wizara ya Mazingira iko pale Dar es Salaam, lakini mikoko yetu inakufa pale Jangwani na maeneo mengine yote! Sasa haya yataondoshwa kwa itifaki haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kwamba, tuna mto wetu pale Msimbazi, tuna Mto Ng’ombe na mito mingine, inaleta uharibifu mkubwa wa mafuriko ni kwa sababu tu ile mito hatuiangalii. Kwa taarifa tu mwaka huu Jangwani pale tumepita salama sana, nilitumia pesa zangu za Mfuko wa Jimbo kusafisha Mto na hatimaye mafuriko mwaka huu Jangwani pale hayakutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuna utaratibu wa kulinda mito yetu hii, hizi itifaki sidhani kama zitatusaidia sana. Ni vizuri sasa kama Serikali yetu, kama Viongozi, tujikite katika kutatua matatizo yetu wenyewe, hizi itifaki ni jumla tu, itifaki haiwezi kuja kutuondolea matatizo yetu ya ndani ambayo sisi wenyewe hatufanyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka sheria ya mita 60, hivi hii sheria ya mita 60 kuiacha bahari, hii bahari anaisafisha nani? Tunapokaa umbali wa mita 60 anayetegemewa sasa Serikali ndio ikafanye kazi za kusafisha mito. Je, inafanya? Tunapokaa umbali wa mita 60 inategemewa sasa bahari yetu Serikali ndio ikasafishe, matokeo yake bahari yetu inanuka. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, lakini ukienda nchi zilizoendelea, Paris hata ukienda Dubai, watu sasa hivi wanajenga mpaka kwenye bahari. Hizi sheria sisi tunaangalia kulingana na hali ya sasa au sheria tunaleta tu ili mradi? Lazima tutoe sheria ambazo zitaendana na wakati. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, watu wetu waruhusiwe kujenga kwenye bahari kwa lengo la kutunza hiyo bahari yenyewe. Watu wetu waruhusiwe kukaa karibu na mito kwa lengo la kutunza hiyo mito yenyewe, kwa sababu hiyo Serikali inayotaka watu wakae mbali, wao hawawezi kwenda huko wala hawawezi kwenda kutunza, badala yake tunakuwa na fukwe chafu, tunakuwa na mito michafu ni kwa sababu ya kutengeneza sheria ambazo wakati mwingine hatuna uwezo wa kwenda kuzisimamia. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, mfano watu wangu wa mabondeni pale wanatakiwa wahame, hivi pale Jangwani mtu anahama vipi wakati watu Dubai wanakaa baharini? Wewe unamhamishaje mtu Jangwani! Una mhamisha mtu Jangwani akakae Mabwepande wakati Jangwani anaenda Posta hata Kariakoo kwa mguu, Mabwepande anatumia nauli shilingi 2,000 na anatumia saa matatu! Mimi nafikiri hii siyo sawa, tutoke huko tuende katika ulimwengu wa kisasa. (Makofi)

Mheshikiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam, Jangwani, watu wako wana uwezo wa kuendelea kukaa pale hakuna madhara yoyote. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kupata fursa hii adhimu kabisa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge wa Jimbo, vilevile Kiongozi wa Kitaifa nitagawa mchango wangu katika maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza nitazungumzia kama mwakilishi wa Jimbo langu, lakini naamini nikipata fursa nitazungumza mambo yote haya nitachangia kitaifa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiniuliza kuhusu bajeti naionaje? Nitakubaliana kabisa na wenzangu wengi kwamba bajeti ina sehemu imefanya vizuri na ina sehemu kwangu mimi imenikwaza. Sasa kwa sababu sehemu iliyofanya vizuri watu wameshazungumza na kuisifia, nitajikita zaidi katika sehemu ambazo zimenikwaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kifupi katika ile kuondoa kodi ya leseni ya barabara nimezungumza na wapiga kura wangu, watu wa bodaboda, taxi drivers kimsingi wanashukuru sana. Wanasema hii kodi imewasaidia sana na niliwahi kuwauliza mnasemaje kama Serikali ikiamua kuirudisha tena kule mnasemaje? Wengi hasa wa pikipiki wamesema bora hivi ilivyo sasa hivi, huu mtazamo wanauunga mkono sana. Kwa hiyo, hili nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mimi kwa jimbo langu la mjini nina tatizo sana la umaskini na umaskini kwangu mimi ninaupima katika mzunguko wa pesa. Mheshimiwa Waziri mzunguko wa pesa katika Mji wa Dar es Salaam umeshuka sana. Nashukuru kwamba umefanya juhudi za kufuta kodi mbalimbali pale bandarini, ambayo naamini kwa namna moja ama nyingine itaweza kuchochea uchumi, lakini naomba uyaangalie haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watu wa Dar es Salaam utatusaidia sana kama utaleta ajira mpya. Ninapozungumzia ajira mpya nakusudia kuna walimu wengi wamesoma, wamemaliza course zao mbalimbali wanasubiri ajira. Kuna eneo la afya wanasubiri ajira, kuna wataalam wa kilimo, bila kusahau majeshi yetu yote vijana wanasubiri ajira na bahati mbaya sana hawa watu wanaotarajia kuajiriwa hawataki kukaa vijijini, wanakuja kukaa mjini. Kwa hiyo tuna kundi kubwa la watu liko pale Dar es Salaam linatumia lakini halizalishi.

Mheshimiwa Waziri utanisaidia sana kama ukioanisha na hili la kupandisha madaraja watumishi wetu, kutoa increment kwa watumishi wetu, bajeti haisemi. Nimewahi kuzungumza na walimu, wafanyakazi wa afya wanalalamika kwamba sasa hivi increment hakuna, sasa hivi watu hawapandishwi madaraja, kwa hiyo Mheshimiwa waziri hili utakuwa umenisaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri utanisaidia sana kama benki zetu zikiwa na fedha. Mikopo kwenye benki zetu za baishara, watu wa Dar es Salaam wengi wao wanaishi kwa kufanya biashara na wanakopa katika benki hizi za kibiashara, benki hizi ndogondogo mitaji yao ni midogo. Natambua kwamba Serikali imekopesha mpaka bilioni 500 lakini tunapenda ingekuwa ni vizuri tukafika angalau trilioni moja.

Natambua Serikali tumeshusha riba kutoka asilimia 16 mpaka asilimia 10, lakini mimi natamani kwa nini tusishushe mpaka asilimia tano kwa sababu hii mikopo inayokopwa na mabenki, ni mikopo ambayo risk yake ni ndogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kama atayafanya haya atakuwa amenisaidia kwa kiwango fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atanisaidia sana mimi mtu wa Dar es Salaam kama atalipa madeni au madai. Bajeti inaonyesha mwaka jana baada ya kufanya uhakiki tulikuwa na madai yanayofika trilioni 1.9 na tukalipa bilioni 700 maana yake kuna pesa zimebaki kama trilioni 1.2. Mheshimiwa Waziri ukilipa hizi tena tumelipa deni la nje, takribani trilioni saba, sasa kama tunalipa deni la nje trilioni saba ni vizuri tukamaliza haya madai ya ndani kwa sababu haya madai ya Wakandarasi, madai ya Wazabuni, madai ya Bohari Kuu ya Madawa, madai ya watumishi, madai ya huduma mbalimbali haya yataleta mzunguko pale Dar es Saalam na wananchi wetu wataanza kuona nafuu ile unayoikusudia kuipeleka. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ninasikitika sana, Dar es Salaam pale ninakabiliwa na hali ngumu, chakula kikipanda. Mwaka huu ndani ya kipindi kuanzia mwezi wa tatu mpaka tunakuja hapa mwezi wa sita iliwahi kufika kilo ya unga shilingi 2,400, na unga ndio chakula nafuu kwa watu wa Dar es Salaam, kwa sababu ugali hauchagui mboga. Sasa unapopanda unga maana yake mwananchi wa kawaida atapata hali ngumu, wamejitahidi kupunguza matumizi wameacha mambo yote yasiyokuwa ya lazima, lakini mtu hawezi kuacha kula. (Makofi)

Sasa Mheshimiwa Waziri utatusaidia sana ukiongeza hifadhi ya chakula na hasa mahindi ili inapofika kipindi kama hiki cha ukame hifadhi yetu ya chakula iwe inauzwa kwa bei nafuu kwa wafanyabiashara wetu ili bei ya vyakula isipande. Kwa sababu bei ya vyakula ikipanda kunasababisha hali ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wanapokuwa na njaa, wakati mwingine hawaoni umuhimu wa standard gauge. Mheshimiwa Rais anaweza akafanya mambo makubwa ya kujenga reli hayo, makubwa ya umeme na kuleta ndege lakini hivi mwananchi mwenye njaa atathamini vipi haya? Na kwa kweli kama tunataka kuleta mtengamano, kama tunataka wananchi wa kawaida waone Rais anachapa kazi lazima tutatue suala la njaa na kutatua suala la njaa ni kushusha bei ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ni kwa maana hiyo bei ya chakula lazima ishuke, lazima hifadhi yetu ya chakula itumike kama kiwango ambacho kitaenda ku-regulate pale ambapo mazao yanapokuwa hayapatikani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya Halmashauri, kwenye mapato ya Halmashauri mimi nasikitika sana, kwa kweli wachangiaji wengine wanachangia lakini wengine sio wahusika wa moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua sisi watu wa Dar es Salaam ni wahusika wa moja kwa moja. Katika property tax, Kinondoni mwaka uliopita tulikusanya shilingi bilioni 7.8, baada ya Serikali kutukusanyia mwaka huu wametupa shilingi bilioni moja. Kuna hela zinapotea hapa jamani, wengine tunaposema kwamba tunataka kusaidia nchi yetu, inakuwaje tunapoteza mapato kama haya kwa sababu tu ya kugombania nani akusanye? Kwa nini basi Waziri kama anaona inafaa lazima hizi peza wakusanye wao, kwa nini katika haya Majiji hasa Jiji la Dar es Salaam kwa nini Halmashauri zisiwe kama agent, kwamba wao ndio wakusanye halafu wakukabidhi wewe ufanye unavyotaka? Si lazima zile pesa zote shilingi bilioni 7.8 tutumie sisi Kinondoni lakini roho inauma kwamba mnatoka kwenye mapato ya kukusanya shilingi bilioni 7.8 mnarudi mnapewa bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongeza kodi ya mabango ambayo nimemuuliza Mhasibu wangu ambaye nimempigia simu leo hii akaniambia ni shilingi bilioni tatu tumelenga. Sasa kwa kulenga shilingi bilioni tatu ninyi wenzetu mtaichukua mnaenda kuifanyia majaribio wakati hii kodi ya majengo hatujafika mbali, tunaongeza na kodi ya mabango tunaenda kupoteza shilingi bilioni tatu?

Mheshimiwa Waziri, fikiria kama vipi, Manispaa za Kinondoni kwa sababu nayo ni Serikali zikusaidie ili tusipoteze hizi fedha, kwa sababu tunaweza kupoteza fedha zaidi shilingi bilioni 30 kwa Dar es Salaam tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabadiliko ya sheria, nimesoma hapa katika kitabu cha Financial Bill hapa kuna mabadiliko ya sheria yanakuja, Sheria Na. 290…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia kuwa na afya njema na kupata fursa hii ya kuchangia katika mjadala huu muhimu sana. Pili, nitoe mkono wa Baraka na kuwatakia Ramadhan Mubarak Waislam wote na hasa wa Jimbo la Kinondoni na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili la Ramadhan vile vile niseme kwamba katika kupeana mkono wa baraka, ndugu zetu, kwa taarifa nilizonazo Zanzibar na hasa Pemba kuna uhaba mkubwa wa nafaka, kwa maana ya viazi mbatata pamoja na mihogo. Mheshimiwa Mwijage kwa sababu ni Waziri wa Biashara anasikia hili achukue fursa kuwahakikishia wafanyabiashara wetu wa bara wanajitahidi kupeleka vyakula haraka iwezekanavyo ili kupunguza ugumu huu na Ramadhan iwe nyepesi kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mwijage kwa usomaji mzuri wa taarifa ya bajeti na niombe mzee wa uchumi wa diplomasia kama wakati mwingine akiwa anamu-opt anaweza akafanya mambo yakawa mepesi sana, ameisoma vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati yangu, Mheshimiwa Dotto Biteko, kiongozi kijana, kamati yake iko makini na amesoma ripoti nzuri sana ambayo hata wachangiaji imewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nizungumze, mimi mbunge wa Mjini na sina tatizo sana na REA I, II na III lakini mimi nina tatizo kubwa sana la bei ya umeme, tuna tatizo umeme ni bei juu sana. Bei juu ya umeme inatokana na gharama ya uzalishaji ambayo TANESCO wanaipata bila kusahau gharama za usambazaji. Hata hivyo, tuna umeme wa maji ambao gharama yake ni shilingi 36 tofauti na umeme wa gesi ambao ni shilingi 147na umeme wa mafuta tunaambiwa shilingi 368.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha, Waziri Kivuli alisema kwamba umeme unanunuliwa kwa shilingi 500 na TANESCO wanauuza kwa shilingi 280.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia gharama hizi za uzalishaji kama tungetumia umeme wa maji na umeme wa gesi, gharama zetu za umeme zingeshuka kwa chini ya asilimia 50 ya sasa. Umeme wetu unakwenda juu sana, ni kwa sababu ya haya makampuni yanayozalisha umeme kwa njia ya dharura tuliyoingia mikataba, umeme wa mafuta, ni makampuni ambayo yananyonya sana nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna makampuni haya yanajulikana Songas, Dowans, Pan African; ni makampuni ambayo yanazalisha umeme kwa gharama kubwa na leo nimepata nafasi ya kuwauliza watendaji wetu, je, tukiacha kutumia umeme wa mafuta tukitumia umeme wa maji na gesi na njia nyingine hatuwezi ku-survive? Wanasema tunaweza, lakini tuna kikwazo kikubwa cha mikataba, mikataba tuliyoingia na makampuni ya uzalishaji umeme ni ya ajabu sana, ni mikataba ambayo mimi nashindwa, mikataba gani tunaingia, wataalam wetu wanaingiaje kwenye mikataba ambayo haina room ya kutoka? Hii ni ndoa ya aina gani? Au ndiyo ile ndoa wanayosema ya Kikatoliki?

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatamani na tunafikiria wataalam wetu wanapoingia kwenye mikataba waweke na mlango wa dharura wa kutoka, lakini leo mikataba yetu hii ukiingia, ukitoka, unapelekwa mahakamani. Nina habari kwamba Dowans wamesimamishiwa mkataba na wako mbio wanakwenda mahakamani na kuna hatari tukalipishwa pesa nyingi. Sasa kwa utaratibu huu nafikiri tatizo liko kwa watendaji na wataalam wetu. Inakuwaje mikataba tukiingia hatuwezi kutoka? Nafikiri hili jambo si sawa na kwa kweli umeme umekuwa ghali lakini sababu kubwa ni huu umeme wa mafuta ambao hatuwezi kujitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Songas tungeweza kuachana nao, hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Leo Dowans mnataka tuachane nao, hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Leo Pan African tunataka kuachana nao hatuwezi kwa sababu ya mikataba. Hivi hii ni mikataba gani ambayo hawa wataalam wanaingiaje mikataba ambayo hatuna room ya kutoka? Napata taabu sana mimi hapa na kwa kweli kwa utaratibu huu nchi hii tutakuwa tunasokota kamba nyuma inaungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO ina deni kubwa linalofikia kiasi cha bilioni 800, inadaiwa. Kama TANESCO inadaiwa zaidi ya bilioni mia nane, lazima umeme upande na ili ushuke lazima tutoke kwenye mikataba hii. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aje kutueleza ni namna gani tutatoka kwenye hii mikataba ya kinyonyaji, mikataba ambayo inapandisha bei ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nimuunge mkono dada yangu, Mheshimiwa Najma leo amezungumza jambo zuri sana kuhusu Zanzibar. TANESCO inawa-treat ile Kampuni ya Umeme Zanzibar kana kwamba ni mtumiaji wa kawaida, wanamuuzia umeme kana kwamba wanamuuza Mr. Juma, Mr. Ali, hawazingatii kwamba yule naye anakwenda kufanya biashara. Wanamtozea mpaka Kodi ya VAT wakati na yeye alipaswa atengeneze aweze kuuza aweke na kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono, ni vizuri wakapewa huo u-agency, au kama itashindikana wao wana uwezo wa kununua umeme wenyewe, wanunue kutoka katika makampuni yanayozalisha umeme wafanye transfer kwenda kwao Zanzibar ili na wao liwe ni shirika ambalo linaweza kujinunulia umeme kwa watengenezaji umeme na badala yake lisiwe shirika ambalo linapitisha umeme halafu linatozwa bei ya mtumiaji wa kawaida, hii siyo fair. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nilizungumze, tulikuwa katika bajeti ya maji, wachangiaji wengi hapa walivyochangia walionesha kwamba ili bajeti yetu ya maji ipate pesa nyingi tuongeze tozo kwenye mafuta, shilingi hamsini na mimi nilisema kuongeza tozo ya shilingi hamsini kwenye mafuta tafsiri yake hatumsaidii mwananchi wa kawaida, kwa sababu yeye atakwenda kuilipia hii kwenye upatikanaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikapendekeza kwamba, tuna hawa jamaa zetu wa EWURA, wao wanasimamia vinasaba na juzi tu hapa kulikuwa na mchakato wa kumpata mzabuni wa vinasaba. Tenda imefanywa, makampuni yamejitokeza, makampuni matatu yaka-qualify kwa kutumia vigezo walivyoviweka EWURA na Makampuni yaliyo-qualify ilikuwa ni SICPA, SGS na kampuni nyingine ambayo jina lake sikulipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya makampuni ukiangalia tenda waliyoweka hii kampuni ambayo inaonekana imeshinda tenda bei yake ni kubwa. Nilipendekeza hapa, ni vizuri sasa watu wa EWURA wakaisaidia nchi kutafuta mkandarasi ambaye ame-tender kwa gharama ya chini ili… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia mimi pamoja na Wabunge wenzangu kuonana mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kutoa mawazo yangu kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19. Tumeletewa mapendekezo nakumbuka Waziri Mpango ametusisitiza sanasana tumpe maoni yetu na mimi kama Mbunge tena Mbunge wa Dar es Salaama tena Kinondoni kwa wajanja, nimefurahi sana kupata nafasi hii na nitayazungumza na nayaangalia kwa kina sana mambo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napenda tuliangalie kwa kina ni umaskini ambao naamini mapendekezo yetu au mapendekezo yangu nitakayoyatoa yanalenga namna gani tutapunguza umaskini kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi kama Mbunge wa mjini napata nalo tabu sana ni ukosefu wa ajira, kwa hiyo nitaeleza namna gani Serikali ikifanya tunaweza tukapunguza au kuondoa tatizo la ajira. Jambo la tatu ambalo ni lengo kuu la msingi ni kuinua au kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kitabu hiki cha Mheshimiwa Mpango, nampongeza ni mtaalam mzuri, lakini baada ya kukisoma sana tumeona mpango wetu maendeleo wa mwaka 2017/2018, tumetekeleza kwa asilimia 50 katika bajeti yetu ya maendeleo. Kwangu mimi naliona hili kama ni dosari kubwa, hivi ikiwa tunatengeneza mpango halafu tunakwenda kwenye utekelezaji, tunatekeleza kwa asilimia 50 tafsiri yake ni nini? Je, ingekuwa wataalam wengine mfano wataalam wa ujenzi Mainjinia nao wakatengeneza mpango wao halafu wakatekelezeka kwa asilimia 50 jengo litakuwepo, barabara itakuwepo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namweleza Mheshimiwa Mpango kama kuna mahali tunatakiwa tujirekebishe katika mapendekezo yangu mapendekezo haya tunayotoa mpango atakaotuletea 2018/2019 ahakikishe hatuwezi kutekeleza chini ya asilimia 80. Kupanga mpango ambao akautekeleza kwa asilimia 50 maana yake ametekeleza chini ya kiwango na kama mpango ni lengo kuleta maendeleo tusitegemee maendeleo kama yatakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukuaji wetu wa uchumi ukiangalia hapa kuna chati ukurasa wa saba wa mapendekezo ya mpango inaonesha tulivyokuwa tuna grow chati inaonekana kuna kipindi tulifika mpaka 9.1; tukashuka, tukapanda mpaka 8.8 mwaka 2014; 2016 tulienda mpaka
7.7, 2017, tumeshuka; 2018 tumekwenda mpaka 7.0; mwaka 2017/2018 sasa hivi tunapanga kwenda 7.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa tunakuwa au tunaongeza ukuaji wa uchumi kwa 7.1 kutoka 7.0 maana yake Mheshimiwa Mpango anatukatisha tamaa kwamba hatuendi. Sasa mapendekezo yangu ni kwamba, lazima tujitahidi tuonekane curve inapanda twende angalau basi turudi pale tulipotoka 2016 tuje angalau 7.7 ili ionekane uchumi wetu unakua, kinyume chake atakuwa amekubaliana na matokeo kwamba sasa tunaanza kwenda chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia umaskini kwetu sisi Dar es Salaam, tunazungumza ukosefu wa ajira kwa vijana, vijana wengi hawana ajira. Serikali ukizungumza mpango hapa wanakwambia kuna vijana 1,000 wako VETA; kuna vijana 2,000 wako wapi; kuna vijana 3,000 wako wapi! Hivi kwa idadi ya vijana tuliyokuwa nayo Tanzania na kwa takwimu tunazopewa za vijana 2,000, 3,000 au 4,000 tutaondoa ukosefu wa ajira kwa vijana wetu lini? Hivi kama tunashindwa Dar es Salaam kwenye idadi ya watu milioni sita tunakuwa na Chuo cha VETA kimoja, idadi ya watu milioni sita, Dar es Salaam una chuo cha VETA kimoja, huu ukosefu wa ajira tunauondoaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natamani sana Mheshimiwa Waziri akija, atuoneshe namna gani tatizo la ajira tutalipunguza kwa vijana wetu wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu taarifa, ukitembelea Manispaa za mjini leo, Ilala, Kinondoni, Temeke, watendaji wetu (wataalam wetu wa biashara) wamefungua file la kufunga biashara…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana mtoa taarifa, dada yangu lakini taarifa yake inanipa tabu kwamba tuna programu nyingi za mafunzo ambazo hazitegemei VETA, tunategemea hawa vijana wanapelekwa kwa Profesa Maji Marefu? Si lazima hawa vijana wapate stadi? Namwambia Dar es Salaam tuna VETA moja, labda ningepewa taarifa kwamba ziko nane. Sasa hivi tuna Manispaa tano, VETA ziko tano, ningeichukua taarifa hiyo, lakini ananipa taarifa kwamba sehemu nyingine tusitegemee ufundi stadi peke yake, sasa tutegemee uganga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mategemeo yangu ni kwamba ajira za vijana wetu zitatokana na weledi na ufundi watakaopewa na Serikali yetu sio kwa ujanja ujanja. Nakushukuru sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la umaskini, katika jimbo langu pamoja na kwamba tuko mjini lakini wananchi wetu ni maskini sana. Umaskini huu unasababishwa wakati mwingine, Serikali haituangalii vizuri. Tuna pesa zimetengenezwa kwa ajili ya kuboresha Mji wa Dar es Salaam, tumeweka mabasi yaendayo kasi lakini tunashindwa kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia mifereji midogo midogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mto Msimbazi na wewe unaguswa moja kwa moja, juzi imenyesha mvua ndogo tu watu wana hali mbaya, maji yanaingia majumbani, wananchi wanapata hasara, vifaa vyao vinaharibika. Tuna Mto Kibangu na Dar es Salaam imeshakwisha labda mngetuambia mnataka kutupa viwanja Dar es Salaam mtatupa Dar es Salaam gani viwanja? Dar es Salaam viwanja vimekwisha! Hivi Serikali katika kutupunguzia umaskini inashindwaje kututengenezea angalau mifereji midogo midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Benki ya Dunia DNDP wametuletea mradi wa kutengeneza Mto Ng’ombe au Mto Sinza…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Leo wote wanaonipa taarifa ni katika watu ninaowaheshimu sana, lakini kati yangu mimi na yeye sijui nani na data. Mimi wikiendi hii nilikwenda Dar es Salaam, kamvua ka juzi tu kale tumeenda kuokoa vyombo. Hivi ninavyozungumza kijiko kinasafisha mto tena kwa hela ya Mfuko wa Jimbo – Mto Kibangu, nazungumza Mto Msimbazi! Sasa nani hana taarifa, ni mimi niliyetoa hela ya Mfuko wa Jimbo na kukodi kijiko kwa hela ya Mfuko wa Jimbo na kukodi kijiko kwa pesa ya Mfuko wa Jimbo? Au Mheshimiwa Waziri anazungumzia Wailes wakati mimi nazungumzia Mto Msimbazi? Nani ana taarifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema nawaheshimu sana viongozi wangu hawa lakini ninachokisema, nasema kitu ambacho nimepata kwenye field. Nakushukuru sana na nategemea kwa sababu na wewe unahusika kwenye matatizo haya utakuwa makini sana kulinda muda wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Serikali inaondoa vipi Watanzania kwenye umaskini kwa kudharau kilimo? Hivi tunawaondoa vipi Watanzania kwenye umaskini kwa kuweka masharti yaliyopitwa na wakati kwenye kilimo? Enzi zile za zamani, enzi ambazo Tanzania hatujitoshelezi kwa chakula, enzi zile za wakulima wadogo wadogo wanaolima kupata gunia sita, Serikali ilikuwa inahakikisha wananchi wakilima wasiuze mazao yao kwa sababu wakiuza hizo gunia sita ndani ya miezi miwili wanahemea njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo Serikali inatoa amri ya kutokuuza mahindi kwa mfanyabiashara kama Sumry aliyeacha biashara ya mabasi akaenda kuwekeza kwenye kilimo, akalima heka 1,000 akalima heka 1,500 amepata mahindi unamwambia asiuze kwa ajili ya njaa? Huyu hakulima kwa sababu ya kutaka kula, alilima kwa sababu akauze! Sasa imefika wakati Serikali tusi-generalize, tusitoe order ambazo zimepitwa na wakati. Hizi order zilikuwa enzi zile za watu kuhemea njaa. Leo watu wanakwenda kulima kama biashara unamzuiaje asiuze? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kaka yangu Harun pale kalima mchele wake unamwambia asiuze atakufa njaa, Harun amelima kwa sababu ya kula? Sasa lazima Serikali iwe wazi, matamko ambayo tuna generalize kipindi hiki wananchi wanakwenda kulima kwa ajili ya kufanya biashara, tusiwakatishe tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hivi utaondoaje umaskini bila ku-invest kwenye kilimo? Kilimo ndicho ambacho kina uwezo wa kuajiri watu wetu kwa asilimia zaidi ya 70. Kilimo ndicho ambacho kinaweza kikachukua kwa sababu sisi tuna eneo kubwa, sasa leo Serikali kama tulivyojikita kwenye Shirika letu la Ndege, kama tulivyojikita kwenye miundombinu, kama tulivyojikita kwenye umeme, vile vile Serikali ioneshe nia yake ya dhati kujikita kwenye kilimo kwa sababu huko ndiko vijana wetu watakwenda kupata ajira ya kutosha. Sio kwamba watu wanakwenda kulima halafu unaleta Sheria ambazo sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye kilimo hivi Serikali mpaka sasa hivi inashindwa kutuambia Watanzania tulime nini? Leo Watanzania tumewaambia wakalime mbaazi, mbaazi hazina soko. Leo Watanzania wanabuni, kuna watu nimesikia wanatoka mikoa ya mbali wanakwenda Mtwara kununua maeneo kwa ajili nao walime korosho kwa sababu baadhi ya mazao imeonekana bei haidumu, bei inayumba, sasa kwa nini Serikali isifanye utafiti, ikatuambia Watanzania limeni kitu fulani. Tusishangae baada ya Watanzania wengi kwenda kuamua kulima korosho tutaambiwa nayo korosho imeshuka bei, hili si jambo ambalo tunalitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango yeye ndiye kazi yake, ndiyo kazi yake kutuelekeza Watanzania tulime nini kitu ambacho tutapata maslahi. Leo tunaambizana tulime mbaazi kumbe hata mkataba na Wahindi hamjaingia. Leo kuna watu wanaleta habari hapa kwamba Wachina wanataka mhogo, hivi ninyi Serikali mmeshazungumza na Wachina? Mmefanya nao mikataba? Tumekubaliana? Hivi leo kwenye kilimo hatuwekezi, leo kwenye uvuvi tumeshindwa kuweka mpango wa kununua meli, tulikubaliana hapa uvuvi wa bahari kuu, hamsemi chochote kwenye bahari kuu hapa zaidi ya kutoa elimu ndogo ndogo, hatuna meli hatuna viwanda vya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo wafugaji, wafugaji hawa tunawaambia wapunguze ng’ombe wao, wanapunguzaje? Hilo soko la nyama liko wapi? Hivyo viwanda vya nyama viko wapi? Leo nyama yetu ya Tanzania inafika mahali hata kwenye migodi haikubaliki. Nyama ya Tanzania mpaka sasa hivi inakwatwa kwa shoka, hivi kweli Serikali mnafikiri umaskini huu tutauondoa kimuujiza? Umaskini huu utaondoka kwa Serikali kuhakikisha tunaangalia maeneo ambayo Watanzania wengi wapo tena wanafanya kwa gharama zao na Serikali kwenda kuwasaidia. Kama tutakuwa hatufanyi hivi, tutakuwa tunapotea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo suala la elimu tumelifanya kama biashara. Zamani enzi za mwalimu vijana wote walikuwa wanasomeshwa na Serikali, imefika mahali Serikali ikasema vijana wanasoma wengi hela hatuna tunawakopesha, unamkopesha mtu ili alipe, si lazima achague cha kusoma? Tunawasomesha chochote, hela amechukua ya mkopo, ikishakuwa hela ya mkopo maana yake ni business, hivi sasa wewe umemsomesha mtu kwa hela ya mkopo halafu unamsomesha kutunga mashairi. Haya wamesoma watu 2,000 kutunga mashairi utawaajiri wapi? Unayo industry ya watunga mashairi wewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini sasa Serikali hatuji na sera, hatuji na maelekezo, Watanzania wanasoma kwa gharama ya kukopa ili alipe lazima aajiriwe, unamsomesha chochote, lazima tuwaelekeze Watanzania, wasome kitu gani ili wapate kuajiriwa, waweze kulipa zile pesa, lakini tunawaacha tu mtu anakuja anachagua chochote cha kusoma, akienda kwenye soko la ajira, anaambiwa hakuna ajira, halafu huyu mtu anatakiwa alipe mkopo na ndiyo maana haya mapesa…

T A A R I F A . . .

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimepata bahati, wote wanaonipa taarifa watu wangu ninaowaheshimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilichokisema; hivi wewe unasema mashairi ni fani nzuri inaheshimika, mimi siidharau lakini je wewe unaheshimu kama unavyoniambia mie? Unawaajiri wangapi? Kwa sababu ninachosema, huyu mtu umemkopesha na ukishakopa dawa ya deni kulipa! Je, unahakikisha anachokisoma kitamwezesha kulipa? Hawa watu mtawaajri nyie Serikali hawa watunga mashairi? Kwa nini tusisomeshe madaktari ambao tunaweza kuwapeleka Zimbabwe, tunaweza tukawapeleka Malawi, kwa nini tusisomeshe Ma-engineer wa gesi ambao wana soko kubwa ulimwenguni, kwa nini tusisomeshe fani za kilimo ambazo zinaenda kutumika. Tunasomesha chochote! Halafu then akija kijana anatafuta ajira unamwambia Aah! Unajua hii fani yako hii kwenye ajira kweli haitakiwi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na mimi kuwa sehemu ya wazungumzaji siku ya leo. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima wa afya njema na kuwepo kwenye Bunge hili Tukufu nikapata fursa ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge nimeapishwa juzi tu hapa, nimeingia kupitia dirisha dogo na mara nyingi wachezaji wanaosajiliwa katika dirisha dogo ni wachezaji wazuri sana. Nikishukuru Chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa hatimaye kuwagaragaza jamaa zetu kule na kupata ushindi wa kishindo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano Dokta John Pombe Magufuli, mimi namuita field marshal. Niliwaambia kuwa nampenda balaa na nampenda kweli kweli kwa namna anavyochapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijafanya sawa nisipomshukuru mama yetu, Mheshimiwa Samia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyomsaidia Rais wetu kutekeleza majukumu yake. Pia sasa nikushukuru wewe Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri sana ambayo imetoa mwelekeo wa namna gani Serikali yetu katika mwaka wetu huu mambo yatakavyokuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana Kinondoni wana matumaini makubwa sana na bajeti hii ya mwaka huu. Wana Kinondoni tuliwaeleza kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli ni Serikali ambayo imedhamiria kuleta maendeleo kwa Watanzania wote na wao ikiwa ni sehemu ya Watanzania. Niwaahidi wana Kinondoni kwamba uchaguzi umeshakwisha, tumepata ushindi unatosha na wote wawe kitu kimoja kushirikiana na Mbunge wao kuhakikisha wanaleta maendeleo katika Jimbo lao la Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze tu ndugu zangu wa kipande cha kule kwamba uamuzi nilioufanya Katiba ya Chama nilichokuwa nipo kule unaruhusu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu. Kwa sababu na wao siku hizi wamekuwa waumini wakubwa wa kutaka Katiba basi jambo hili wasilionee, usichokila usikitie hila, kwa maana kwamba, tumefanya kwa mujibu wa Katiba na siye ni waumini wa Katiba tusiwe na maneno maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine watazungumzia gharama hapa, uchaguzi umegharimu bilioni sita lakini siye au nyie siyo ndiyo mnataka twende kwenye Katiba Mpya, hivi Katiba Mpya tukiiingia kwenye hiyo kura ya maoni hatutotumia gharama? Hivi gharama yake itakuwa ndogo kuliko hiyo bilioni sita? Kama tunataka kweli kuwa waumini wa Katiba tuanze kuishi kwa mujibu wa Katiba tusianze kusemana kwa mtu ambaye amefanya maamuzi ambayo yanatekelezwa kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri tu, ushauri wa kwanza kwa chama changu kile kilichonilea kwamba kibaya chako chema kina wenyewe. Ushauri wa pili kwa Chama Kikuu cha Upinzani, CHADEMA waache kulialia wagangamale, kulonda kazi ya Jeshi kugangamala. Kama umeingia kwenye uchaguzi umepigwa unafanya tathmini unajipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao. Mwisho wa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwingine, tuonane 2020 na Inshallah Maulid Mtulia mtamkuta pale pale Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu chapa kazi. Chama cha Mapinduzi ndiyo chama chenye Serikali na ndiyo chenye jukumu la kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa Tanzania na wengine jukumu lao ni kukosoa, kushauri, lakini bahati mbaya sana hili la kukosoa ndiyo wanalipenda, kwa hiyo usishangae wakija na maneno ya aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jamaa yangu mmoja mtani wangu anatoka hapa Ifakara, anakebehi kununuliwa ndege, basi okay wewe watu wako hutarajii kupanda ndege basi hata Daraja la Kilombelo hujaliona? Hata ile barabara inayojengwa kutoka Ifakara - Kidatu nayo hujaiona? Kwa hiyo, watu kama hawa wasimtoe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kinondoni katika kuhakikisha tunatunza mazingira, tunainua uchumi wa wana Kinondoni na kuhakikisha tunashirikiana na Serikali kuleta ustawi tumekuja na mradi mkakati wa kuhakikisha Coco Beach tunaiendeleza. Tunahitaji Serikali itupatie pesa shilingi bilioni 7.2 ambayo tuna uwezo wa kuirejesha ndani ya mwaka mmoja. Tafsiri yake nini? Tafsiri yake ni kwamba kila baada ya mwaka mmoja tuna uwezo wa kutumia hicho kama chanzo cha ndani cha kuingiza shilingi bilioni 7.2. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliahidi kwamba tunataka kujenga barabara na sisi Dar es Salaam na hasa Kinondoni tunatarajia sana kwamba barabara zetu zitajengwa. Tuna magari mengi na tunapojenga barabara na kuondoa foleni kiuchumi magari haya yanaweka mafuta na tozo ya mafuta sasa hivi ndiyo inaingia moja kwa moja kama kodi, maana yake magari yatakapotembea sana mafuta yatatumika sana na tutapata kodi sana. Kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tunaondoa foleni katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna suala la masoko. Niishukuru Serikali imetutengea shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya soko letu la kisasa la Magomeni, lakini vilevile itenge pesa kwa ajili ya soko la Tandale ambalo ndiyo soko kubwa la chakula Dar es Salaam, pia na soko la Makumbusho na Mapinduzi ambayo ni masoko makubwa Dar es Salaam. Tukiyafanya haya yote, tutaongeza ajira kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Rais amehimiza kwamba wawekezaji wetu wa ndani na hasa katika masuala ya dawa na vifaa tiba wapewe kipaumbele. Mimi nina mwekezaji pale Jimboni kwangu, mpiga kura wangu ana kiwanda cha vifaa tiba pale Mwananyamala kinatengeneza gozi, hakijapata kupewa kipaumbele na badala yake MSD bado wanaendelea kununua kutoka nje. Sasa hii ndoto ya Mheshimiwa Rais tutaifika lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu kabisa na mimi kupata kuchangia kwenye hoja iliyopo Mezani. Nitakuwa sijafanya sawa kama nisipomshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima. Lakini si mimi peke yangu na Wabunge wenzangu tukakaa hapa tukajadili haya mambo ambayo ni mazuri kabisa kwa mustakabali wa maendeleo yetu na Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake, Manaibu wake, kwa kazi kubwa, nzuri wanayofanya. Niwashukuru kwamba na sisi Dar es Salaam maeneo mengi tunaona kuna fedha zimetengwa, tunaamini zitaenda kuleta maendeleo kwa watu wetu wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mchache na kama unavyojua watu wa Jimbo la Kinondoni wana mategemeo makubwa sana na bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na kuwaletea ili Kinondoni mpya tuliyokuwa tukiinadi kwenye kampeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na ujenzi wa nyumba kongwe za Magomeni. Nyumba hizi Mheshimiwa Rais alifanya uzinduzi pale akawaaminisha wananchi wangu wa Jimbo la Kinondoni, hasa wale waliokuwa wanakaa Magomeni, lakini vilevile na mimi nilitumia fursa ile kumuomba Mheshimiwa Rais nyumba hizi zikiisha watu wetu waliovunjiwa nyumba zao na wao wapate nafasi za kusihi, lakini nimeangalia kwenye kitabu cha bajeti hapa ukurasa wa 160 imeoneshwa kwamba kuna ujenzi unaendelea lakini nimeenda kutafuta pesa kule nimeona kuna shilingi milioni 200 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba Wizara walitazame hili kwa jicho la rehema kwa sababu watu hawa wana matumaini makubwa sana na ujenzi wa hizi nyumba na kwa sababu Mheshimiwa Rais alishatoa offer kwamba watu watakaa miaka mitano bila kulipa kodi, sasa tusipojenga kwa haraka inaweza ikafika hiyo miaka mitano hata Rais mwenyewe asiwawahi watu wake wakati wanakaa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ituongezee fedha pale na ujenzi uishe kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Dar es Salaam na hasa Kinondoni ambako mji ulikuwepo zamani tulikuwa na barabara nyingi nzuri za lami, hivi sana tuna barabara zetu zimechafuka sana, zina mashimo mengi. Lakini unaona kwamba tunatengewa mpaka barabara za changarawe na vumbi, pale Kinondoni utaweka wapi barabara ya vumbi? Ni barabara ambazo nyumba zimesongamana, unapoweka vumbi maana yake vumbi unawapelekea wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sasa Waziri aangalie namna gani atazipandisha daraja barabara zetu za Manispaa ya Kinondoni. Mfano, tuna barabara muhimu sana, hii hapa ya Ndugumbi inakwenda pale Mwananyamala ya zamani sasa hivi inaitwa Makumbusho, Daraja la Harubu limevunjika, ile barabara tukiijenga tutasaidia watu kutoka katika njia kuu. Michepuko kwenye barabara inakubalika, labda kwenye mambo mengine huko ndiyo sina uhakika, lakini michepuko kwenye barabara ni jambo ambalo linasaidia sana kuondoa foleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa najikita, tuna barabara zetu za Tandale, kwa Bi. Mtumwa pale, tunahitaji ile barabara ipandishwe daraja ili ijengwe kwa kiwango kizuri. Tuna barabara zetu pale kwa Dunga, hii barabara ya Biafra ni barabara inatoka Biafra inakwenda kule Mwananyamala, ni barabara inayotumika sana. Lakini tuna barabara yetu nyingine inaitwa ya Biafra inayotoka pale kwenye mataa inakwenda mpaka Best Bite. Tuna barabara zetu za Kijitonyama - Akachube ni barabara ambayo Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka bahati nzuri ni kwamba katika Jimbo langu la Kinondoni Wabunge wengi ni wakazi lakini vilevile hata wanaokaa nje wanapita pale. Kwa hiyo, barabara ile ya Akachube, barabara ya Mabatini ni barabara muhimu sana. Lakini Magomeni kuna matoleo, watu wa mwendo kasi pale Morocco pale karibu na Kanisa Katoliki ukitaka kuzunguka uje Manispaa au uende Chalinze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakaa chini, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata fursa hii adhimu na mimi kuchangia. Pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyofanya na tunakubali kibinadamu kwamba kuna yaliyopungua na ndiyo maana na sisi tumepata fursa hii ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika Jiji la Dar es Salaam na bahati njema nawe ni wa Dar es Salaam. Dar es Salaam ni kitovu au chemchem ya mabadiliko kwa Tanzania. Dar es Salaam ilitoa ushiriki mkubwa kabisa katika kuleta mageuzi na uhuru wa nchi. Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alianza Dar es Salaam na wazee wake wa Pwani pale kupigania uhuru. Kwa hiyo, Dar es Salaam tuna kila sababu ya kuhakikisha unakuwa mji wa kisasa na chemchem ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Takwimu zinaonesha makusanyo ya kodi ya nchi yetu nusu yanatoka Dar es Salaam. Kama tutapanga mipango yetu mizuri zaidi, kuna uwezekano mkubwa kabisa Dar es Salaam ikaongeza mapato. Kama tunavyofahamu Dar es Salaam ina zaidi ya ya watu milioni sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka nini sisi watu wa Dar es Salaam? Dar es Salaam tunataka Serikali ituwekee miundombinu ya kisasa ambayo itaweza kupunguza foleni. Uchumi wa Dar es Salaam unaweza ukaenda mara mbili zaidi endapo watu wa Tegeta, Mbondole na Pembamnazi wanaweza kufika Kariakoo kwa wakati na mtu wa Kongowe anaweza kufika Tegeta kwa wakati. Ili hili lifanyike, lazima Mheshimiwa Waziri aitazame Dar es Salaam kama Special Zone, kama sehemu ambayo uchumi wa nchi unaweza ukaimarika kupitia Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza hivi kama Mbunge wa Kinondoni, niko katikati pale, lakini watu wanaokwenda Tegeta wanategemea barabara za kwangu pale Magomeni, Ndugumbi, Makumbusho, Kijitonyama, Kinondoni yenyewe, Hananasifu, Kigogo lazima wapite. Tunapokuwa na miundombinu mibovu katika maeneo hayo ya kati, wewe shahidi, tunapokuwa na miundombinu mibovu Ilala mtu hawezi kufika pembezoni. Kama tunataka maendeleo ya kweli, basi lazima tujikite kuhakikisha tunaleta mabadiliko Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wangu wa Dar es Salaam siwezi kuwaombea pembejeo hapa kwa sababu kazi yao kubwa wamejikita katika sehemu ya kujiajiri wenyewe. Tunapozungumzia uchumi wa Dar es Salaam, tunazungumzia biashara. Lazima Mheshimiwa Waziri ahakikishe anatuwekea mazingira bora ya biashara. Zamani Jiji la Dar es Salaam tulikuwa tunapokea wageni kutoka Burundi, Rwanda, Congo wanakuja kununua bidhaa zao pale sasa hivi wale watu hawapatikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napozungumza hivi naamini Mheshimiwa Waziri hili analitambua. Sasa tusiweke mazingira magumu mpaka ikapelekea wageni hawa wakaona ni bora kulichukua kontena kulipeleka kwao kuliko kuja pale Dar es Salaam. Kwa sababu wakija Dar es Salaam watu wa Ilala, Kinondoni na Temeke guest zao zitapata watu, uchumi unazunguka. Kwa hiyo, hili ni muhimu ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine watu wetu wa Dar es Salaam wamejiingiza katika sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo. Tunapozungumzia Wizara ya Michezo kwetu sisi inafanana na Wizara ya Kilimo kwa sababu asilimia 60 ya watu wa Dar es Salaam shughuli zao ni za kujiajiri wenyewe, sanaa, habari na michezo. Vijana wamefungua ma-blog mengi, wako kwenye social media, wanaigiza, wanaimba na wanacheza. Ukienda katika Wizara ya Michezo katika fungu la maendeleo, utakuta kuna shilingi bilioni 8, shilingi bilioni 3 kwa ajili ya TBC, shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya viwanja, sasa unakuta hawa vijana hatujawatengea kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati wenzetu wengine wanadai pembejeo kwa watu wao, sisi watu wa Dar es Salaam tunataka vijana wetu watengenezewe studio waingie watoe muziki safi. Tunataka vijana wetu watengenezewe jumba kwa ajili ya kwenda ku-act na wapate hatimiliki ya kazi zao. Hizi ndiyo kazi ambazo nadhani watu wa Dar es Salaam tukifanyiwa uchumi wetu utakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu mafanikio ya bajeti yetu. Kuna watu wanazungumza hii ni bajeti hewa, bajeti ya kufikirika na kadhalika, lakini jamani tuwe wa kweli, bajeti hii ni nzuri na lazima tujue tulikotoka. Sisi wengine tunakumbuka tuliingia kwenye siasa kwa matatizo gani? Tuliingia kwenye siasa wakati huo barabara ya Kibiti – Lindi haipitiki, hakuna Daraja la Mkapa. Tuliingia kwenye siasa mtu akitaka kutoka Dodoma kwenda Arusha lazima afike Chalinze. Mtu akitaka kutoka Dodoma kwenda Mbeya lazima afike Morogoro. Kulikuwa hakuna Daraja la Kikwete wala Daraja la Ifakara. Tumetoka mbali sana jamani, lazima tuone tulikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeondoa riba kwa vijana. Mimi nikienda Misikitini kuwahamasisha watu wangu namna gani wataitumia Serikali, nikiwaambia mikopo, walikuwa wananiuliza sasa hii riba itakuwaje na sisi hatutaki kutumia riba? Leo Serikali imesikia imeondoa riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye miradi mikubwa, sisi watu wa Dar es Salaam ndiyo watumiaji wakubwa wa umeme. Hizi propaganda ya kuacha huu mradi wa Stiegler’s Gorge zinatoka wapi? Watu wa Dar es Salaam tunatumia umeme zaidi ya nusu ya umeme wote unaozalishwa. Tunajua kuzalisha megawatt moja ya umeme wa gesi ni ghali kuliko umeme wa maji, dola milioni 1.2 na hii nyingine ni dola milioni 1. Hata uzalishaji wake, megawatt moja inauzwa kwa Sh.136 wakati ya maji ni Sh.36. TANESCO leo wananunua umeme kwa unit moja Sh.148 wanauza kwa Sh.200, tukitengeneza umeme wa maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei itashuka na watu wa Dar es Salaam watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, lakini nianze kabisa kwa kuwashukuru Watendaji Wakuu wa Wizara hii, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na kaka yangu Yussuf Masauni kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha nchi yetu bado ipo na ulinzi na usalama na amani ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Kamanda Sirro, Kamanda wangu wa Mkoa wa Kanda ya Dar es Salaam, Mambo Sasa na Kamanda wangu wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamanda Jumanne. Kwa sisi ambao tumetoka kwenye hekaheka za chaguzi muda siyo mrefu tunajua umuhimu na thamani ya kazi za Watendaji wetu wa Ulinzi na Usalama. Kwa kweli nawapeni pongezi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwa mkweli. Nimefurahishwa sana na nimejifunza kitu kikubwa sana kutoka kwa kiongozi wangu, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa alipokuwa anaongea mbele ya Mheshimiwa Rais. Kwa kweli nimejifunza kwamba sisi kama Wabunge, kama Wanasiasa pamoja na hitilafu zetu za Vyama, pamoja na tofauti zetu bado tunahitaji kuheshimiana. Nam-promise kwamba kwa kuwa amemheshimu kiongozi wetu wa nchi, amemheshimu ni kiongozi wangu wa Chama nami nam-promise nitamheshimu kiongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mchango wangu katika Jeshi la Polisi. Pamoja na kazi nzuri wanayotufanyia Polisi wetu, bado wana changamoto nyingi. Kwetu pale Dar es Salaam bado tuna changamoto ya vituo chakavu vya ofisi za vituo vidogo vya Polisi, tuna changamoto ya samani za Watendaji wetu wa Polisi na changamoto ya usafiri. Polisi pamoja na Magereza wote wana changamoto ya usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wenzangu, bajeti hii sitegemei upande ule kule kwamba wataikataa kwa sababu itaenda kutatua matatizo ya kuongeza magari. Tuliona lilitokea tatizo hapa, kiongozi wetu na wale baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wenzetu watuhumiwa walicheleweshwa kwenda Mahakamani wakakosa dhamana ikabidi walale ndani kwa sababu ya kukosa magari na mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna nzuri ya kuondoa tatizo lile ni kupitisha hii bajeti ikawa ni bajeti ambayo inaenda kufanya kazi badala ya kwenda kwenye Balozi za watu wengine na kuomba labda watusaidie, kwa sababu hapa ndiyo mahali pake. Nategemea kwamba bajeti yetu itapita bila shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wetu walikuwa wanapata ration na wanaendelea kupata lakini wanapata mwisho mwezi na majeshi yetu mengine haya. Ni vizuri kwa sisi ambao tunafanya nao kazi, tunazungumza nao, wanaomba sana hii ration itolewe kati ya mwezi na isiwe mwisho wa mwezi, kwa sababu ikitolewa katikati ya mwezi ina manufaa makubwa sana kwao. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu alichukue hili kwamba ni hitaji la vijana wetu wa ulinzi na usalama, wanaomba ration zao zipatikane katikati ya mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge, vijana wangu wa Dar es Salaam pale wengi wanaendesha bodaboda. Hivi sasa imekuwa bodaboda na Jeshi letu la Polisi wanawindana kama chui na paka. Namwomba kiongozi wetu wa Jeshi la Polisi badala ya kuwatazama vijana wale kama maadui na badala ya kuwawinda kama chui anavyowinda mnyama, wawafundishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua vijana damu inachemka kuna makosa mengi wanakosea, wakati mwingine wanashindwa kufuata sheria, kuvaa kofia ngumu, kuendesha wakiwa na ndala, natambua na hata mimi mwenyewe najitahidi sana kuwaelimisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Jeshi la Polisi lichukue hili kama ni task maalum, kwa sababu wale vijana ni wetu, wamejiajiri, wanatoa service na wanahudumia watu wetu. Huu upungufu wao basi, Jeshi la Polisi kama walivyoanza kufanya kuandaa baadhi ya semina mbalimbali, kuanza kuwaelimisha kuhusu Sheria ya Usalama Barabarani; pili, kuwafundisha maadili ya usafirishaji; na tatu, kuwaeleza kwamba watakapofanya kinyume na utaratibu, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili vijana wale wapate kujifunza. Naamini wakijifunza wanaweza kukafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami natambua kwamba Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa sana katika operation mbalimbali. Nakumbuka kuna kipindi Panya Road walisumbua pale siku moja tu mji mzima uliharibikiwa. Hata wale ambao wanatazama hii dhana ya ulinzi na usalama na kutazama Polisi kama ni watu ambao hawana faida sana, nawashangaa kwa kweli. Nawashangaa kwa sababu naamini Polisi kama wangepata kupumzika siku moja tu na wahalifu wangeijua siku hiyo moja wanayopumzika Polisi, nafikiri tungeijua thamani ya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulipokuwa kwenye kampeni, wakati tunamaliza pale Polisi walitusaidia sana. Wakati mwingine wakijua kwamba chama fulani wanapita njia fulani wanakuja kutuzuia sisi wengine tusiingie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana siku lilipotokea tukio lililotokea laiti sisi vyama tungekutana pale, kwa kweli lingetokea jambo moja kubwa sana. Nafikiri tusingesema tunayosema sasa. Kwa juhudi zao Jeshi letu la Polisi wamefanya kazi kubwa, nami nasema waendelee kufanya kazi kubwa. Huu upungufu unaotokea, siupuuzi na wao wasiupuuze, wautazame kwa jicho kubwa, waondoe upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wajumbe wenzangu wengine wamesema kwamba watu waliokufa wakaokotwa beach wamefika 1,000 na wengine wanaamini wale walikufa Tanzania, wengine tunaamini sio Watanzania kwa sababu mahali wanapokufa watu 1,000 Tanzania hii wenye ndugu zao wangeonekana. Haiwezekani leo tunazungumzia mfano suala la Benny Saanane, tunazungumzia mfano suala yule mwandishi aliyepotea, halafu tukaacha kuzungumzia watu 1,000 waliopotea, kwa kweli haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoonekana, tukubaliane na kama tulivyopewa taarifa, hawa ni watu wahamiaji haramu wanaotupana, watu wanasafirishwa kwenye malori, wakishakufa wanatafuta mahali pa kuwa- dump. Haiwezekani kwamba wale wawe Watanzania halafu ndugu na jamaa wasionekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo kwa kweli siyo sahihi. Tusije tukalipaka tope Jeshi letu kwa ajili tu ya kutaka kutia uzito wa jambo. Kimsingi tuzungumzie hoja iliyopo, kuna watu wamepotea na watu wakipotea Polisi wanashirikiana nasi kutafuta, haina maana kila aliyepotea kafichwa na Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa limesemwa, jambo kubwa sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia mimi pamoja na Wabunge wenzangu kukutana mahali hapa leo na kupata fursa ya kuchangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Sambamba na hilo nitumie fursa hii kuwatakia watu wa Jimbo langu la Kinondoni, Ramadhan Mubarak na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, niseme wazi naipongeza sana Wizara hii ya Ardhi kwa kazi kubwa wanayofanya. Nimtaje kwa jina mzee wangu Mheshimiwa Lukuvi na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa. Kwetu sisi Kinondoni hakuna asiyefahamu kwamba tulikuwa na migogoro mingi sana ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri alikuja pale tukaenda mpaka katika maktaba yetu ile ya ardhi tukaangalia pamoja, tukaona namna gani baadhi ya watendaji wetu wanavyokiuka utaratibu katika kutafuta namna ya kuwadhulumu wanyonge wenye ardhi yao na badala yake kuwapa umiliki huo matajiri. Kwa kweli, wamefanya kazi kubwa sana, tunawashukuru sana mwendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo najikita kwenye jambo moja tu. Jambo langu, kama mnavyojua, Jimbo langu la Kinondoni ni Jimbo ambalo lina kata 10 na kati ya kata hizo 10, kata tisa zote zimepitiwa na mabonde na wananchi wangu katika hizo kata tisa wote wanaishi katika maeneo yasiyokuwa rasmi. Kwa hiyo, unapozungumzia suala la urasimishaji, suala la uendelezaji wa miji, suala la upangaji miji na wakati mwingine hata suala la kuleta bomoabomoa kwa ajili ya kutengeneza mji mimi ni mhanga na wananchi wangu ni wahanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitajikita sana hapa na kuiomba Serikali iangalie namna gani inaweza ikatusaidia sisi watu wa Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla ambao mji wetu maeneo mengi watu walienda kama ni mashamba, lakini leo ni mji na yamepangwa katika mpango usiokuwa bora, tunafanyaje kuboresha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri na nimevutiwa na maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ukurasa wa 38 Mheshimiwa Waziri anazungumzia Mpango Kabambe wa Utekelezaji wa Miji na katika mpango huo kabambe amelitaja Jiji letu la Dar-es-Salaam. Kwa hiyo, tuna mategemeo makubwa sana watu wa Dar-es-Salaam tutanufaika katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika ukurasa wa 41 ameanzia ukurasa wa 40 ameendeleza urasimishaji wa makazi holela Jijini Dar-es-Salaam. Kama mnavyoelewa, kama nilivyotangulia kusema katika Jimbo langu la Kinondoni hayo makazi holela yapo. Kwa hiyo, kwa kweli, nina mategemeo makubwa sana kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda tena ukurasa wa 47, Mheshimiwa Waziri ameelezea maendeleo ya sekta ya nyumba na hapa napenda kunukuu; Mheshimiwa Waziri anasema:-

“Wizara yangu ina jukumu la kuratibu uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini, sekta hii huchangia kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia hayo Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi, ili kuvutia uwekezaji katika sekta hii na kuwezesha wananchi kumudu gharama za nyumba zilizo bora.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimevutiwa hapa katika Serikali kuwezesha wawekezaji kuja nchini. Sisi watu wa Dar es Salaam, tena hili niseme kwamba naungana na Mheshimiwa Waziri kabisa, tunashirikiana katika Mto wetu Msimbazi. Tunaathirika vile vile katika Mto Msimbazi, lakini vile vile tumeathirika katika Mto Ng’ombe, Mto Kibangu, mito mingi. Jambo hili limesababisha wananchi wangu kuishi katika maeneo ya mito na hata kuvunjiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kwenye kampeni tulizungumzia Dar es Salaam mpya. Namwomba Mheshimiwa Waziri aje na mkakati sasa kwa sababu, tukisema kila anayekaa bondeni tumvunjie, katika jimbo langu tutavunja asilimia 60 ya nyumba zote zilizokuwa katika Jimbo la Kinondoni. Kama nilivyotangulia kueleza kata tisa zote zina mabonde, tukiamua kwenda kuvunja nyumba maana yake zaidi ya asilimia 60 ya nyumba zote tutakuwa tunavunja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Waziri anazungumzia kutengeneza mazingira mazuri ya wawekezaji kuingia; Mheshimiwa Waziri ana mpango gani wa kuhakikisha tunarasimisha makazi haya ya Jimbo la Kinondoni, ili Kinondoni ile ya kisasa tuliyokuwa tumeihubiri katika kampeni ipatikane?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi nimezungumza nao, wako tayari kutoa maeneo yao kama atapatikana mwekezaji kwa ajili ya kushirikiana. Wao wanatoa maeneo mwekezaji anajenga nyumba za kisasa, ili tuondoe kabisa squatter katika Jimbo langu la Kinondoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vile vile tumeambiwa katika Mto Msimbazi kama kuna mtu, kuna mtu kajitokeza anataka kuwalipa fidia wale watu wanaokaa mabondeni, ili yeye alitumie jengo lile kwa ajili ya maendeleo. Sasa Waziri anatuambia nini kuhusu kuwapa fursa hawa wawekezaji? Kwa sababu, sisi kama Serikali tukiamua tufanye sisi, maana yake itabidi tukakope hela benki, lakini mwekezaji ameamua aje kuwekeza kwa gharama zake mwenyewe; Serikali ina mpango gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itambue kwamba, Jiji la Dar-es-Salaam lina zaidi ya watu milioni sita, lakini watu hawa wanataabika kwa mifereji ya Mto Msimbazi ambayo Serikali inapaswa kujenga miundombinu wezeshi, miundombinu ambayo itafanya Dar-es-Salaam iwe ya kisasa. Angalia juzi pale imenyesha mvua Jangwani, jiji lote limesimama; hivi kweli, tunasimamisha jiji kwa mradi ule Mto Msimbazi? Hivi kweli Mto Msimbazi hautibiki? Inafika mahali Dar-es-Salaam inasimama kwa Mto Msimbazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na maelezo ya kutosha namna gani Dar-es-Salaam yetu mpya tunaijenga na hasa wananchi wako tayari kutoa maeneo yao kushiriki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mto Msimbazi kama kuna watu wanajitokeza kuwekeza na Serikali ikajiweka mbali wakalipwa fidia wananchi wetu hili jambo litakuwa lina manufaa kwa wananchi na lina manufaa Serikali.

Nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kusimama kwenye Bunge lako Tukufu. Pili, nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyoliendesha Taifa letu kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri Mkuu nimeisikiliza na kwa kweli ilikuwa hotuba nzuri yenye mwelekeo na yenye matumaini. Nianze na ukurasa wa 66 hasa kwa kaka yangu pale Mheshimiwa Mavunde kwa maana nazungumzia vijana na ajira. Sisi watu wa Kinondoni tunakupongeza sana, lakini katika kipengele ambacho amenivutia sana ni kile cha kuhakikisha anatoa ajira kwa vijana; vijana wanapata ajira na mafunzo na hasa mafunzo ya kilimo cha kitalu nyumba. Nasi Kinondoni kwa maana ya Manispaa tumejenga kituo Mabwepande, vijana wanakwenda kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna jambo moja tu naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie pale, atuletee angalau madarasa mawili kwa ajili ya vijana wanaotoka mbali waje kukaa pale na inaweza ikasaidia kwa watu wa Temeke, Ubungo, Ilala na Kigamboni. Vijana wote wa Dar es Salaam watakuja kujifunza pale kwa sababu kutakuwa na mabweni kwa ajili ya wasichana na wavulana. Akitufanyia hilo, kaka yangu Mheshimiwa Mavunde atakuwa ametusaidia sisi pamoja na Jiji la Dar es Salaam na kwa ujumla wake atakuwa ameisaidia sana nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna walemavu. Kwa kweli natamani sana kama Serikali ikija na ruzuku kwa ajili ya walemavu kwa sababu maisha ni mapambano. Kama sisi wengine tunapambana tukiwa tupo timilifu, wenzetu wanaopambana na viungo pungufu maana yake uwanja siyo fair. Kama tumetoa mkopo kwa ajili ya wanawake na vijana ambao ni wazima, haiwezekani na walemavu tukatoa mkopo kwa condition hiyo hiyo, kwa sababu hawa ni watu wenye upungufu. Kwa upungufu huu lazima tutafute namna ya ku-subsidize.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natamani sana Serikali ije na ruzuku kwa ajili ya walemavu, ije na vifaa kwa ajili ya walemavu wa kutembea kama vile baiskeli, magongo, vifaa vya kuongeza usikivu na kila namna. Lazima walemavu hao tuonyeshe kama jamii tunawajali na tunajua kwamba wenzetu wapo kwenye mapambano haya wakiwa na upungufu. Uwanja uko fair.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye uwekezaji. Kuna uwekezaji wa watu, kuna uwekezaji kwa maana ya ndani na uwekezaji wa nje. Nina hamu kubwa sana tuzungumzie uwekezaji wetu wa ndani. Kwanza naipongeza Serikali yangu kwa kuhakikisha imekuja na miradi mkakati mikubwa, tukianza na mradi wa standard gauge. Huu mradi ni mradi mkubwa na mtu yeyote anayeubeza mradi huu kwa kweli tutakosa kumwelewa. Hata leo mradi unakwenda una miaka; wewe mpaka leo unakuja kuubeza mradi huu maana yake utakuwa unajipotezea muda. Huu mradi ni mzuri. Vile vile tuna mradi wetu wa umeme, ACT na tuna miradi mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi hii, tuje na mkakati wa kuona ni namna gani miradi hii inaweza kuwajenga Watanzania? Mfano, tunajenga reli kutoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma – Rwanda na Burundi wameomba wanataka nao tufike. Haiwezekani tukajenga kwa kutumia Kampuni ya Kituruki tu, lazima tuwe na ajenda. Baada ya Waturuki kuondoka, transformation of knowledge inapatikana? Haiwezekani tena wakiwa Congo wanataka kujenga reli kama ile, wakamtafute tena Mturuki, wanatakiwa waje Tanzania wawakute Watanzania wapo tayari kwa ajili ya kujenga reli.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kama huu uende kwenye viwanja vya ndege. Tuna mpango wa kujenga viwanja vya ndege vya kanda vingi kweli. Viwanda vya Songwe, Dodoma, Iringa, Mtwara na Lindi. Tuna viwanja vingi tunajenga. Hivi viwanja tunavyovijenga tutakwenda na viwanja vya mikoa, haiwezekani mpaka leo hatuna kampuni hata moja ambayo tunailea kwamba wakati viwanja hivi tunajenga kwa kutumia Wakandarasi wa nje, tukimaliza tukianza viwanja vyetu vya mikoa Watanzania wawe wana uwezo wa kujenga hivi viwanja wao wenyewe na hiyo ndiyo transformation of knowledge. Hili hatuwezi tukafanyiwa na mtu, lazima tuwe na mkakati nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapeleka umeme vijijini, makampuni tunayotumia mengi katika vijiji vingi; hivi kweli tukimaliza mradi wa umeme vijijini Watanzania washindwe kwenda kufanya oparesheni za miradi ya umeme kwa ajili ya nchi ya Burundi, Congo na nchi nyingine? Tuendelee tu kuwa sisi kazi yetu ni kutumika!

Mheshimiwa Naibu Spika, mtazamo wangu kwa miradi yote mikubwa tunayoweka fedha nyingi, lazima tuje na mpango wa kuhakikisha elimu inabaki ili Watanzania waende mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sisi tunajenga reli, lakini tuna mradi wetu wa kimkakati wa Mchuchuma na Liganga. Ni mradi wa muda mrefu. Mchuchuma na Liganga umesimama. Ukiangalia, kuna changamoto. Changamoto ya kwanza, mbia aliyekuja kampuni ile ya Kichina ambayo yuko na NDC hakuja na capital ya kutosha. Mradi unataka capital ya shilingi bilioni tatu yeye amesema anaweza akaja na capital ya dola milioni 600. Kwa maana hiyo, anataka atumie mradi wetu kama collateral kwa kukopa hela benki. Huo ukawa mgogoro wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa pili, umeme utakaozalishwa kutoka pale Mchuchuma, Megawatt 600, 250 itumike kwenye kiwanda, 300 iingie kwenye grid ya Taifa; na ile inayoingia kwenye grid ya Taifa, anataka Megawatt moja atuuzie kwa senti 12 mpaka senti 15 ambayo ni ghali. Umeme wa gesi tunanunua kwa senti 6 na TANESCO wanauza kwa senti 11. Ukiangalia hapo unaona mgogoro mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa migogoro hii yote, ndiyo tusitoke? Kwa sababu tukiweza kutengeneza kiwanda cha Liganga, tukatoa chuma cha pua tungeweza kutumia kujenga kama mataruma. Vilevile tunapokwenda kwenye ulimwengu wa Tanzania ya Viwanda, visiwe viwanda vya juice tu, viwe viwanda vya chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mawazo yangu ni kwamba lazima Serikali ikae na hawa wabia wetu na NDC tutatue huu mgogoro, kwa sababu hiki kiwanda kwetu kina umuhimu mkubwa sana. Chini ya kile chuma kumechanganyika na madini muhimu sana. Kuna madini yanaitwa vanadium na titanium; ni madini muhimu na ghali kuliko hicho chuma, lakini inapatikana tu baada ya kuchimba chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ile reli ya kusini ambayo tunataka kuijenga Mtwara mpaka kwenda Songwe ni reli ambayo inategemea mzigo huu mkubwa utakaotoka Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo, tusipopatana na tukaja na suluhisho, maana yake ile reli ya kusini itabaki kuwa ni ndoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, imefika mahali Serikali sasa, nimeona kwenye mpango tumetenga fedha kwa ajili ya fidia, lakini kulipa fidia peke yake haitoshi. Namwombe dada yangu Mheshimiwa Angellah, namuamini sana, alichukue hili kama ni jambo la msingi ambalo anaweza akalisaidia Taifa, akatusaidia na sisi pia. Kwa maana mradi huu ukifanikiwa utakuwa ni mradi mkakati wa kuhakikisha kweli tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda na siyo viwanda vya juice na maji tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima na mimi kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Pili, nikushukuru wewe Mwenyekiti wetu. Tatu, niwashukuru Watendaji wote Wizara ya Maji nikianza na Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Maji ni nyeti sana kama Wabunge wengi walivyosema lakini vilevile tujikumbushe Wizara hii katika Awamu hii ya Tano tu wamepita Mawaziri wengi na wamefanya kazi kubwa. Ameanza Mzee wetu Mheshimiwa Maghembe, Mheshimiwa Eng. Lwenge, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe na sasa tunaye Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Kwa kweli wote wamefanya kazi nzuri lakini sasa hapa kwa Profesa kwa kweli mambo yanakwenda kweli kweli. Wakati mwingine Profesa unamkuta ananing’inia kwenye ngazi unapata raha kabisa, mzigo unapigwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine matatizo yetu yanaonekana kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe na umuhimu katika jamii yetu. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuwaunge mkono wenzetu hawa kuhakikisha kwamba tunawapa nguvu, tunawatia moyo hili jambo liende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu Kinondoni maji tunapata, yako mengi na ukichukua Mradi wa Ruvu Chini na Ruvu Juu hatuna shida sana ya maji, shida yetu ni mtandao wa maji tena kwa baadhi ya kata. Niiombe Wizara ishirikiane na watu wetu wa Dar es Salaam kwa ajili ya Kata zetu za Tandale, Mwananyamala, Makumbusho, Kigogo, Hananasifu na Mzimuni. Hizi ndiyo kata ambazo tunaamini mtandao wa maji ukiwekwa itakuwa ni vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru tu kwamba bajeti ya mwaka huu inakwenda nzuri na itatekelezeka. Kama nilivyosema pesa zimesainiwa lakini zile shilingi trilioni 1.2 ambazo hata kaka yangu Mheshimiwa Mnyika amezisema asiwe na wasiwasi mwaka huu ndiyo mwaka wa mavuno, mihela itakuwa inashuka kwenye Wizara ya Maji kwa maana shilingi bilioni 330 ipo, shilingi trilioni 1.2 zipo, wasimamizi wapo, RUWASA inakwenda kuanzishwa mwezi Julai, tuhakikishe mapanya wote wanaokula pesa za maji wanakwenda kudhibitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati wetu sasa, hakuna wakati mzuri ambao tunatakiwa tuungane, tushikamane kuwasaidia wenzetu hawa kwa sababu wameonyesha dhamira ya kweli.Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi kila Mbunge ametembelewa na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri au na Katibu Mkuu au na kiongozi yoyote. Hili jambo kwa kweli siyo dogo, ni jambo ambalo sisi kama viongozi na wawakilishi wa wananchi lazima tuwape moyo; mnyonge, mnyongeni, haki yake mpeni.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, unga mkono hoja.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu nami kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na salama. Pia nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wka kazi kubwa na juhudi yake na hasa kutuelekeza katika Tanzania ya viwanda. Hakika Tanzania ya viwanda inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili tuna msemo wetu “mzigo mzito mpe Mnyamwezi” na sina shaka Waziri wa Wizara hii ni Mnyamwezi. Namwombea kila la heri afanye kazi hii tukimtegemea kwamba atatuoa hapa tulipo. Ushauri tu; Mheshimiwa Waziri Wabunge wenzangu wengi wamesema akae na wadau, lakini naanza kusema Mzee wangu akae na wafanyakazi wake, Wakuu wake wa Idara. Kuna tatizo limetokea wakati mwingine mabwana wakubwa hawatoi nafasi za kutosha kwa wataalam wetu kutoa ushauri. Sasa haya yote yaliyosemwa na Wabunge ni vizuri wakaenda wakakaa na wataalam, naamini wataalam wana njia ya kututoa hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja hapa na kilio chetu cha watu wa Dar es Salaam. Dar es Salaam kilikuwa ni kitovu chetu cha biashara, lakini leo iko wapi Dar es Salaam yetu ya biashara? Iko wapi Kariakoo yetu? Namtaka Mheshimiwa Waziri aturejeshee Kariakoo yetu ya Wanyarwanda, ya Warundi, ya Waganda na Wakongo. Kariakoo ambayo tulikuwa tunafanya biashara na mimi kama Mbunhge wa Kinondoni nanufaika sana na biashara inapochangamka katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwaje na biashara katika Jiji la Dar es Salaam kama hatuna miundombinu inayoweza kutuwezesha kufanya biashara? Nichukue fursa hii kuwapa pole Wanadar es Salaam wote kwa mafuriko yaliyotokea kutokana na mvua kubwa iliyonyesha. Dar es Salaam barabara zetu zinapitika kiangazi tu. Juzi tu hapo barabara ya Jangwani imefungwa kwa sababu ya mafuriko, barabara ya Mkwajuni imefungwa kwa sababu ya mafuriko na niseme kwamba tunawaomba sana wenzetu wa Wizara ya Fedha, ule mpango wa DMDP waliokubali kutuongezea Dola milioni 100 kwa ajili ya kufanya mabadiliko, kujenga daraja vizuri pale, kufanya Dar es Salaam ipitike mpango ule ufanyike, kwa sababu haya ndiyo yanayoiua Dar es Salaam yetu na haya ndiyo yanayoiua Kariakoo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kariakoo ilikuwa ni kitovu cha uchumi, ilikuwa ndiyo Dubai yetu, lakini leo wapi haipo tena. Kwa hiyo namtaka Mheshimiwa Waziri asiulize tufanyeje kwa sababu ni jambo lililokuwa wazi kwamba Kariakoo imedorora, milango iko wazi, frame hazina wapangaji, biashara haifanyiki, Watanzania wanakwenda kuchukua mzigo kutoka Uganda, it is shamefull. Unatoka hapa unakwenda kufuata mzigo Uganda watu ambao hawana bahari, kwa nini? Kwa sababu bandari yetu inasemekana kodi kubwa, watu wanapita Mombasa, wanapeleka mzigo Uganda. Sasa mambo haya mengine maana yake ni lazima tuyafanyie kazi. Haiwezekani Kariakoo inakufa ndani ya mikono yetu, haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka nizungumzie watu wangu wa sanaa (COSOTA); COSOTA wanasimamia hati miliki na hati shiriki, leo vijana wangu wacheza filamu, vijana wangu waimba muziki, vijana wangu wafanya sanaa kazi zao zinafilisiwa, kazi zao zinaporwa, zinadhulumiwa, wameingizwa mikataba ya Chief Mangungu. Msanii anakwenda kwa mtu ambaye anamtazama kama sponsor, anamwambia kazi hii bwana kwa vile umeileta kwangu unataka nikudhamini, sasa hii kazi itakuwa ya kwangu na wewe utakuwa msimamizi, hiyo ndiyo mikataba walioingia vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kazi zao zote zinasomeka ni kazi za mtu mmoja haiwezekani na Sheria ilikuwepo ya mwaka 1999. Ifike mahali Serikali iwatetee hawa watoto wa kimaskini, kazi zao zirejeshwe kwao wenyewe. Haiwezekani kama mtu ameingizwa mkataba wa kitapeli unasema aliuza mwenyewe, aliuza akiwa na uelewa? Aliuza kwa usahihi? Kama ameuza, ana mkataba wa kuuza? Hakuna. Mkataba uliokuwepo ni kwamba yeye, msimamizi na mjanja mmoja anajiita yeye ndiyo mmiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ifike mahali Serikali yetu iwe na uwezo wa kutoa maamuzi na hasa tunapowatetea vijana wetu wanyonge. Haiwezekani vijana wanyonge wanafanya kazi zao kwa jasho lao, halafu hawapati matunda ya kazi zao, haiwezekani. Lazima ifike mahali vijana wetu wapate matunda kutokana na jasho lao, siyo kurubuniwa rubuniwa. Hili jambo mimi kwa kweli nina-appeal kwa Mheshimiwa Waziri na COSOTA lazima ifanye jambo ambalo vijana watahisi kwamba Serikali ipo pamoja nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema biashara; biashara lazima iwe na miundombinu. Hivi sisi leo tuna biashara za viwanda, viwanda lazima uuze. Leo nimeona kwenye kitabu saruji zinakwenda nje, lakini sijaona nondo. Hivi kweli Congo, Nchi za nje zinachukua saruji zinashindwa kuchukua nondo, lakini tunawezaje kupeleka nondo Congo kama hatujatengeneza miundombinu ya kutoka hapa Tanzania kwenda Congo? Tunawezaje kulitumia soko la Congo? Tunapokuwa sisi hatutengenezi miundombinu kwenda kulifuata soko, nilitegemea viwanda vyetu vinavyozalisha cement ile cement ipite iende mahali ikafanye biashara. Mimi nategemea Wachina wanaingiza nondo Tanzania siyo kwa ajili ya soko la Tanzania, iwe ni transit, ipite kwa ajili ya kwenda kwenye masoko mengine na haiwezi kwenda kwenye masoko haya mengine lazima sisi tutengeneze miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo miundombinu ya kwenda Congo ni muhimu sana kwa sababu kuna soko kubwa, soko ambalo linaweza likawa ni suluhisho la biadhaa zetu za nondo, biadhaa zetu za cement, mahindi yetu, mchele wetu na bidhaa zote zinazozalishwa. Sasa tunapokosa kutengeneza hii miundombinu na kutengeneza kwamba vitu vinavyoingia viwe vinapita vitajaa hapa na vikijaa hapa badala yake vinaleta mzigo mkubwa kwa viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimengalia kwenye kitabu hapa kuna watu tunafanya biashara India, sijaona biashara Uturuki kitabu hiki hakijasema na Watanzania wengi sasa hivi wanachukua biashara Uturuki, lakini kitabu hiki hakijaeleza kwamba biashara ya Tanzania na Uturuki ikoje...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtulia kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuchangia Mpango huu. Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya. Nitakuwa sijafanya sawa kama sitampongeza sana Jemedari wetu, Mheshimiwa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ufanisi mkubwa katika kipindi kifupi cha miaka minne ya utendaji kama Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tuliona mbali na tuliona ile kasi kwa mbali kabisa tukajua kwa mwendo huu wa Mheshimiwa Rais haya yanayotokea sasa tuliyajua kwamba yatakuja kutokea. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyofanya na kwa kututengenezea njia ya kupita katika kujadili Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie maendeleo ya watu, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu na nataka nijikite wenye eneo la mazingira. Katika mazingira hapa sisi maeneo ya mijini kule tunasumbuliwa sana na mafuriko, mito inakuja kuharibu miundombinu na wakati mwingine Dar es Salaam kuifanya inasimama kabisa. Kwa hiyo, katika hili napenda nijikite mfano mzuri katika Mto Msimbazi na mito mingine mingi ya Dar es Salaam. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri tunapokwenda kutengeneza Mpango huu tutolee macho katika ile mito inayotusumbua na hasa Mto Msimbazi. Najua kuna mipango inaendelea na najua kuna bajeti kubwa ambayo haiendani na uhalisia wa jambo lenyewe, lakini naamini Mheshimiwa Waziri atatupitisha vizuri hapa ili tukija kwenye bajeti tutokee vizuri tusikae hivi hivi, lazima tuje na suluhisho na hasa ninachozingatia ni kwa ajili ya kutengeneza mto na kulipa fidia kwa wananchi waondoke lile eneo tulitumie kisasa na kisayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mazingira wezeshi, sisi watu wa Dar es Salaam pale tuna mpango wa kutengeneza barabara za kuondoa msongamano na kupunguza foleni. Mpango mzuri sana na kwa kweli tunaipongeza sana Serikali yetu na kwa kweli katika hili tumenufaika nalo sana kwa maana ya barabara, fly over Mfugale pale, hapa Ubungo, nyingine itakuja Magomeni, nyingine itakwenda Mwenge, nyingine zitasambaa. Kwa kweli tunapokwenda tunategemea sasa kwenye bajeti hii itakayokuja jambo hili lipewe uzito mkubwa kabisa ili tutakapoondoa msongamano na foleni Dar es Salaam tunakuza uchumi. Watu wakiweza kupita kutembea kurudi kufanya mambo yao kwa wakati uchumi wetu utaongezeka bila wasiwasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nisisitize katika ile mipango yetu ya kipaumbele mitatu, lazima tuweke fedha tuhakikishe tunamaliza kwa wakati. Kujenga Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere tukisuasua faida haitapatikana, itachelewa kwahiyo tuhakikishe tutakwenda kwa speed. Kujenga standard gauge tukisuasua reli inachelewa kufika Dodoma hatutapata matunda. Tukiwahi kufanya hivyo maana yake na uchumi wetu utachemka na hata mapato yetu yataongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechungulia ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi katika kifungu cha 160(A), Serikali ilielezea ujenzi wa viwanja vya michezo cha Mwanza na cha Mbeya kwa hiyo, tusiondoke hapa lazima tufanye jambo. Mheshimiwa Rais anawapenda sana wasanii, anawapenda wana michezo. Lakini vilevile ukienda kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, Fungu 162 tunazungumia ujenzi wa Arena wa jengo la changamano la michezo na ambalo hili nitafurahi sana tukilijenga Dar es salaam kwa ajili wasanii wako wengi, iddai ya watu wako wengi na jengo kama hili limejengwa Rwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jengo ambalo unaweza ukafanya ukumbi, ukafanya boxing, ni jengo ambalo ukaondoa ukaja uwanja wa mpira mkacheza, ni jengo ambalo ukaondoa ukafanya stage watu wakafanya burudani zao, miziki, vijana wakafanya Tamasha na hivi, ni jengo ambalo la kisasa. Na Mheshimiwa Rais aninavyomjua mie, vijana wake hawa anawapenda kweli kweli na sisi tumsaidie hili jambo lifanikiwe kwasababu ni jambo ambalo linagusa watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Utawala Bora; nimemsikiliza sana Mwenyekiti hapa, Mzee wangu Mzee Mheshimiwa Mbatia amezungumza mambo mazuri sana lakini mimi ninachosema tu, watuonyeshe mifano hawa wazee, waonyeshe mifano. Chama cha Mapinduzi
ndiyo chama pekee kimeonyesha demokrasia pana tunapofika mambo ya uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vingine hawana hiyo demokrasia. Wakati mwingine mambo haya yanawaharibikia kwasababu viongozi ni wale wale wa tangu tumeanza vyama vingi ni wale wale hawawapishi wengine sasa jamani kama utaratibu ndiyo utakuwa huu basi hata nyie wenyewe tu kujifanyia mabadiliko kwamba toke fulani, aje fulani, atoke fulani, hawa vijana mnawandaaje? Sasa viongozi wa vyama vya upinzani wanazeeka na wengine watakufa na vyama vyao kwasababu hakuna succession plan sasa anakuja kwenye Serikali ya Mtaa sehemu ambayo sisi tumeweka utaratibu, tumeweka Sheria, tumeweka miongozo wanafikiri Serikali ya Mtaa itakwenda kama wanavyofanya wao kule, haiwezekani. Huku kwenye Serikali za Mitaa kuna taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, watu wakijitoa mimi naona wameogopa aibu tu kwasababu pale kwangu tulikuwa na mitaa 52 na hawa waliojitoa wana mitaa miwili nilikuwa na hamu nao sana. Nilikuwa na hamu nao tuje kuwanyoosha. Wewe mitaa imepunguzwa, kwa mfano, kwangu kuna mitaa 20 tunakwenda kupiga kura sasa si ndiyo vizuri hiyo mitaa 20 ushinde yote ili uonekane mmenifanyia figisu. Mngeniachia mitaa mingi ningeshinda yote, mmeniachia 20 nimeshinda yote 20 hamna, wana mitaa miwili na kuna maeneo mengine mfano kwa Ndugu yangu pale Mheshimiwa Deo Ngalawa kule hawakuchukua hata form wanalalamika nini hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti ukienda kwa Kalanga kule wamekimbia, hapa kwa ndugu yangu hapa James Millya hapa wamekimbia sasa wakati mwingine lazima haya mambo tuyaangalie halafu mtu anakuja anasema kujenga amani, amani yetu, amani vipi? Sisi tunaolinda amani ndiyo unatusukumia tunafanya fujo na nyie mnaokata mahindi ya watu mnaonekana nyie ndiyo mnapenda amani, hili haliwezekani kwasababu kama nyie ndiyo mnakata mahindi ya watu, nyie ndiyo mnaokwenda kuvunja nyumba za watu, nyie ndiyo mnawafukuza watu kwenye upangaji halafu mkigeuka mkija hapa mnajisema nyie ndiyo mnalinda amani na siye tunafanyakazi ya kulinda amani usiku na mchana tunaonekana ndiyo tunaokuja kuleta vurugu hili jambo siyo fair. Nilikuwa nataka Mwenyekiti lazima awe fair asiwe anakionea tu Chama cha Mapinduzi, lazima tuwe fair.(Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo sijalielewa, tuna shida gani pale Liganga na Mchuchuma? Liganga na Mchuchuma tuna shida gani pale? Pale tunakwenda kutengeneza umeme wa Makaa ya Mawe, pale tunakwenda kutengeneza chuma, hivi ulimwengu wa sasa bila chuma viwanda hivi si vitakuwa viwanda vya juice tu?

Mhesheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nadhani sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango aje ahakikishe tunakwenda kukwamuka pale Liganga na Mchuchuma kwasababu kwanza ule umeme unaotumika kwa ajili ya kutengeneza viwanda vya chuma tutaungeteneza pale kwenye Makaa ya Mawe. Kwa hiyo, ni jambo ambalo lina faida kubwa sana. Na tukianza kutengeneza chuma hata viwanda vikubwa vikubwa vitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imeelezea kufufua Shirika la uvuvi TAFICO. Mheshimiwa Dkt. Mpango nilikuwa naomba sasa tuje kwasababu tukifufua Shirika letu hili la uvuvi by automatic hata ile dhana ya kununua meli za uvuvi itapatikana. Tukishanunua meli za uvuvi viwanda vya samaki vitapatikana, tunakwama wapi? Kama tumeona kwenye Ndege, cha kwanza tulifufua Shirika la Ndege, tukishafufua Shirika la ndege tumeleta ndege na huku kwenye uvuvi tufufue lile Shirika letu la uvuvi tukishafufua Shirika letu la uvuvi tunakuja sasa na kununua meli za uvuvi hapo mimi nafikiri tutakuwa tumekwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuja jambo lingine, tumeendelea sana kwenye mambo ya afya sasa hivi lakini lazima sasa tuje na uta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia mimi pamoja na Wabunge wenzangu leo kupata fursa ya kujadili hoja zote mbili zilizotolewa na Wenyeviti wetu wa Kamati; pili nikushukuru na wewe kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wangu mimi naunga mkono hoja zote mbili na Maoni ya Kamati. Hata hivyo nilikuwa nataka niseme hapa, kama kuna Kamati amabzo zinaonyesha namna gani Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ilivyotekeleza Ilani na inavyojali maendeleo ya watu, basi hoja za leo zinathibitisha kwa wazi kabisa kwamba Serikali si tu inajali maendeleo ya vitu bali pia imezingatia sana maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii adhimu kabisa kumpongeza Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kusimamia kwa dhati, kwa umahiri mkubwa kabisa, kujenga na kuleta maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema hayo ukizingatia kwamba hivi sasa pesa za elimu bure kila mwezi Serikali inatoa bilioni 23. Ukipiga hesabu kwa Mwaka unapata biloni 276, na ukizidisha miaka mitano ya Awamu hii unapata trilioni 1.38

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo; ukienda kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, tumetoka katika bilioni 337 mpaka bilioni 450; na kama nayo utaizidisha mara miaka mitano unapata trilioni 1.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya, haya matrilioni nayataja kwasababu ukienda kwa lile jambo ambalo linasemwa sana la ndege si zaidi ya trilioni 1.2. Kwahiyo utaona kwa haya mambo mawili niliyoyataja ya Wizara hii ya Elimu imezidi gharama tulizoziweka kwenye ndege kwa sababu tu Serikali inajali maendeleo ya watu na inahakikisha watu wentu wanapata maendeleo sambamba na maendeleo ya vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kwenye afya huko ndiko hatari kabisa. Utakumbuka huko nyuma iliwahi kutokea Mtu alifanyiwa operation ya kichwa badala ya operation ya goti; lakini leo Serikali yetu imenunua vifaa vikubwa kabisa. Kuna angle-suit inanunuliwa pale MOI kwa ajili ya kufanya operation ya Ubongo kwa kutumia mshipa wa paja. Kwahiyo leo Mtu unaweza kumkuta anafanyiwa operation kwa kutumia mshipa wa paja lakini operation ya kichwa, mambo ya kwenda kufumua ubongo sasa hayapo tena. Haya yanapatikana Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia gharama za vifaatiba na dawa za Wizara ya Afya inafika trilioni 1.35. Sasa wakati mwingine wenzetu wengine wanaweza wakasema hatufanyi hiki, hatufanyi kile, hatufanyi vile lakini lazima tuwaoneshe Serikali inafanya vitu gnai ambavyo vinaleta maendeleo kwa Wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye michezo; leo tu umemtambulisha yule kijana bondia amekuja na mkanda wake hapa; lakini najua kuna Bondoa Mwakinyo amekuja na mkanda hapa. Mwaka jana tumekwenda kule Misri kwenda kuipeleka timu yetu; ambapo tangu miaka ya 1980 hatujawahi kwenda katika Mashindano ya Afrika, lakini tumeenda katika Utawala huu. Mimi nasema kwamba Utawala huu umekuja na mavumba, umekuja na kismati unafanyakazi kweli kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Simba mambo waliyoyafanya ni makubwa. Wewe unajua kwamba tumefika robo fainali kwenye robo fainali kwenye Mashindano ya Afrika. Hivi tunavyozungumza, Bwana Ally Samatta yuko Uingereza; kwa mara ya kwanza tumepeleka mchezaji kule anapiga soccer katika Premier League ya Uingereza. Mtu mwingine anaweza akayaona haya yanatokea kama uyoga. Wakati wenzetu wengine wanasema hatuhajafanya huki, hatujafanya hiki sisi tunaenleza tumefanya hili, tumefanya hili, kazi inapigwa kweli kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda wkenye Maoni ya Kamati; Kamati inaitaka serikali sasa kwenye michezo waje na uboreshaji wa viwanja vyetu vya michezo; lakini si uboreshaji peke yake na kuongeza idadi ya viwanja vya michezo pale Dar es salaam na Mafia, lazima Mafia tupeleke viwanja vya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili, tunataka sasa tuje na Kampuni, viwanda ambavyo vitaleta nafuu katika gharama za vifaa vya michezo (Sports industry). Tukifanya hivi kwenye michezo tutafika mbali sana. Nchi nyingine zote, katika idara ya michezo, idara ya sanaa, idara ya mambo ya music ni miongoni mwa idara tajiri sana, lakini kwetu bado inaonekana kuna umasikini. Serikali ikiongeza nguvu kwenye michezo hapa tunaweza kupoata ajira nyingi sana kwa vijana wetu na vijana wetu wakapata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imesisitiza umuhimu wa Baraza letu la Kiswahili kushirikiana na Wizara ya Elimu kutengeneza vyuo vingi vya kufundisha walimu wa Kiswahili kwenda kuwafundisha Kiswahili wasiokuwa Waswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama utakumbuka Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amejaribu kukimiliki Kiswahili na kuuonesha ulimwengu kwamba Kiswahili wenyewe ni Watanzania, na amefanya juhudi kubwa sana. Vilevile kuna soko kubwa sana East Africa, kuna soko kubwa sana SADC, kuna soko kubwa sana Afrika nzima na ulimwenguni. Tunapokuwa hatuna vyuo vingivya kutoa walimu wengi wa kufundisha Kiswahili kwa wasio waswahili, soko hili litachukuliwa na watu wengine na sisi tutakosa fursa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumefika mahali, tunakwenda kwenye uchumi wa kati, lakini uchumi wa kati una utamaduni wake. Ifike mahali Wizara yetu ya Elimu na Serikali kwa ujumla itengeneze chombo kitakachopitia mitaala yetu yote ili tuje na kitu ambacho kitatupeleka latika uchumi wa kati. Uchumi wa kati hauwezi kwenda kwamba wanaume wako wanawakata masikio wake zao, uchumi wa kati hauwezi kwenda wanaume wako wanawabaka watoto wadogo, wanawalawiti, uchumi wa kati una ustaarabu wake. Ili tuingie kwenye ustaarabu wa uchumi wa kati lazima na mitaala yetu iwa-shape watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya zamani tulikuwa tunafundisha sayansi kimu watu wapige mswaki, watu wafanye hivi lakini leo lazima tuwafundishe watu utamaduni huu wa kiulimwengu wa watu kuwa wastaarabu, kwasababu uchumi wa kati unataka watu
wafanyakazi, wawe wastaarabu, wawe wavumilivu, wawe hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunazungumza hapa kwamba kuna watu wanazidai hospitali maiti, hospitali watu wapate matibabu, wazee na vijana; suluhisho ni kuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote; isiwe leo Watanzania mtu akijijua ana tatizo la figo ndipo anakwenda kukata bima. Tunapokuwa na watu wa bima ambao tayari wameshajijua wagonjwa, na ni wengi ndipo wanakwenda kukata bima, hapana. Tuje na nima ya watu wote kwasababu watu wengi watachangia na wachache wenye matatizo ndio tutakaowatatulia matatizo yao. Leo unamkuta mtu anasema hapa tupeleke watu nje, Serikali haijakosa kupeleka watu nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa tunapeleka watu zaiid ya 600 kwenda kutibiwa nje, leo tunapeleka watu 65 sasa ukipiga mahesabu ya kipesa hapa, pesa tunazookoa ni zaidi ya trilioni 1.835. Haya ni mambo ya fedha. Uthibitisho kwamba watu wanapelekwa nje Mheshimiwa Lwakatare yule pale amepelekwa nje, na uthibitisho wa kwamba watu wanafanyiwa opetation za figo, siku hizi operation za figo ziko hapa Dodoma. Mtu akipata tatizo la figo, wala Wanyamwezi hawaji tena Dar es salaam, wanaishia Dodoma hapa hapa, wanafanyiwa operation ya figo, hayo Mabusha ndiyo usiseme wanamaliza kabisa, kule kwetu hakuna fujo siku hizi mambo yanakwenda vizuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaj)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa muda wako umeksiaha, ahsante sana.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja zote mbili za Kamati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijaalia uzima na kuweza kuchangia kwa maandishi. Nawapongeza watendaji wote kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wote ambao sikuwataja kwa ajili ya kulinda muda.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla. Wizara hii ikiunganishwa na Wizara ya Kilimo zina uwezo wa kuongeza ajira na kuondoa umaskini. Zaidi ya hapo Wizara hii inaweza kuondoa umaskini na utapiamlo kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha hayo inabidi tufanye yafuatayo:-

i. Kutenga maeneo ya wafugaji bila kuingiliana na wakulima.

ii. Kutoa elimu ya kutosha kwa wafugaji wetu namna bora na ya kisasa itakayowezesha kuvuna na kupata mapato ya wanyama.

iii. Wavuvi wetu waelimishwe namna bora ya kisasa zaidi ya kuvua samaki wengi.

iv. Kuanzisha viwanda vya kusindika samaki na nyama.

v. Kujenga machinjio ya nyama kwa kiwango cha kisasa ili nyama zetu ziuzwe mahotelini, migodini na hata kwenye super market za ndani
na nje.

vi. Kupunguza mifugo yetu ili tuweze kuitumia na kuwa bora.
vii. Kufuga kisasa ili kupata mifugo mingi na yenye ubora kuliko ilivyo sasa.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa salama kuonana na wenzangu hapa lakini pili nishukuru kwa kupata fursa hii adhimu kabisa ya kuchangia katika sheria hii muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli sheria hii ni miongoni mwa sheria zilizokuwa zinahitajika sana katika ustawi wa Taifa letu. Hata ukisikiliza michango ya wenzangu waliotangulia wote wanaonesha umuhimu wa sheria hii. Kubwa kuliko yote wanajaribu kuonesha sehemu ambapo kuna upungufu ili yafanyiwe marekebisho hatimaye tupate sheria ambayo italeta ustawi kwa jamii yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakwenda mbali, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa hili lakini nataka nirudi nyuma zaidi. Jumatatu tulikuwa Dar-es-Salaam pale na Mheshimiwa Waziri, tulikuwa na shughuli moja kubwa sana ambayo ilimjumuisha na Mheshimiwa Rais, ilikuwa ni kuja kuzindua mpango wa kuhakikisha zilizokuwa nyumba kongwe za Magomeni zinajengwa na wananchi wale ambao walikuwa hawana mahali pa kukaa, wanakaa kwa shida, wanarudishwa katika nyumba zao zile kongwe. Kwa hili nasema nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu wanufaika ni watu wa Jimbo langu moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka niongeze hapa kwamba wale wananchi wa Magomeni wa zilizokuwa nyumba kongwe, nyumba zao zilivunjwa kwa lengo la kuboresha zile nyumba, wajengewe nyumba nzuri na ikiwezekana Manispaa waweke miradi pale kwa ajili ya mapato. Kilichofanya nyumba zile zisijengwe hakisemwi ni kwamba baada ya kupatikana yule mwekezaji TAMISEMI hawakutoa ridhaa ya ule mradi kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa namna moja ama nyingine isije ikaonekana ni Manispaa ya Kinondoni ilikuwa haitaki wale watu wajengewe nyumba kumbe ilikuwa ni mipango kutoka TAMISEMI haijakamilika. Sasa mambo kama haya ya watu wa TAMISEMI kuzuia jambo halafu burden yake au hasara yake kwa Manispaa ya Kinondoni na juzi Meya wangu amesulubiwa sana kwamba alishindwa kuwatetea wananchi wale, napenda record ziwekwe wazi kwamba TAMISEMI ndiyo ilikuwa haijatoa idhini au ridhaa ya kuendelea kwa ule mradi, ndiyo maana wananchi wale wameshindwa kupatiwa zile nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine niseme kwamba, wakati tunawarudisha wale waliokuwa wapangaji wa nyumba kongwe walikuwa wanaishi kwa kulipa kodi tukumbuke tuna wananchi tumewavunjia nyumba zao mabondeni. Kwangu mimi hawa kama ni wapiga kura wangu vilevile naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri amshauri Rais kwamba nyumba zile zinazojengwa Magomeni kipaumbele cha pili baada ya wale waliokuwa wamevunjiwa nyumba zao hawajarudi kiende kwa wale wakazi wa mabondeni waliovunjiwa nyumba zao. Ikiwa tunaona huruma kwa wapangaji wetu kurudi kwenye nyumba zetu, basi kwa hisia hiyo hiyo tuwaonee huruma na wale tuliowavunjia nyumba za kwao wenyewe ili nao warudi pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shughuli ile kwa masikitiko makubwa na Mzee wangu Lukuvi, nampenda sana baba yangu anatuelekeza, sisi vijana tunajifunza kazi kutoka kwa wakubwa, lakini kuna tukio limetokea pale sikulipenda kwa kweli. Sisi tumekwenda pale wawakilishi wa wananchi na mimi ni mwakilishi wa Kinondoni na tukio linafanyika Kinondoni, lakini Wizara ya Mzee wangu Lukuvi na uongozi uliokuwepo pale umeshindwa kutambua uwepo wa mwakilishi wa Jimbo husika, hii inatukatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisafiri umbali mrefu kwenda kushiriki shughuli ile nikifahamu kiongozi wetu wa nchi atakuwepo pale na viongozi wetu watakuwepo pale. Kwa sababu mimi ni mwakilishi wa wananchi na nilivyolelewa kwenye chama changu kwamba natakiwa niheshimu uongozi, sasa inapofika wenzetu wakubwa hawa ambao tunategemea tujifunze kutoka kwao anafika Mbunge wa Jimbo husika, Mheshimiwa Lukuvi yeye ni mgeni pale, anashindwa ku-recognise kuwepo kwa Mbunge, imenisikitisha sana. Nafikiri sio namna nzuri, itatukatisha tamaa sisi kama vijana, itatukatisha tamaa sisi kama wapinzani kushirikiana na Serikali katika matukio ya Kitaifa. Kwa kweli, sikuipenda nimeona niieleze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukirudi sasa kwenye jambo letu hili, sheria hii pamoja na uzuri wake lakini kuna mambo yanayotakiwa yafanyiwe marekebisho. Siku za nyuma kulikuwa na kawaida, mfano, hawa wathamini wanaweza wakathamini jengo au mali inayotaka kuuzwa na baada ya kuthamini TRA wanapokuwa wanataka kwenda kuchukua kodi yao nao huwa wanapeleka watu wengine kwenda kufanya tathmini. Hii ni repetition isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sasa itambulike kwamba huu uthamini utakaokuwa unafanywa na hawa Wathamini wetu, ile document itakayotokea iwe ni document ya kisheria asitokee mtu mwingine tena akamtafuta mthamini wake, tafsiri yake itakuwa wale waliofanya kazi ile hawaaminiki na tutakuwa tunapoteza nguvu bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, katika huu Muswada kuna suala la Wajumbe wa Bodi, tumeambiwa kutakuwa na Wajumbe wa Bodi tisa na Kamati nne. Muswada haujaeleza moja kwa moja wajumbe wa Kamati hizi nne wote watakuwa wanatoka kwenye ile Bodi ya watu tisa? Kama itakuwa ndivyo, idadi yao itakuwaje? Kila Kamati itakuwa na Wajumbe wa Bodi wawili au vipi? Kwa hiyo, naomba ufafanuzi ili tujue hawa wajumbe wa hizi Kamati nne ni walewale wa Bodi tu peke yao au wengine wanatoka wapi kwa sababu sheria haijaeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna hii stop order. Mara nyingi wananchi wetu wanapowekewa stop order wanatakiwa wasifanye maendelezo yoyote. Hii stop order ni kwa muda gani kwa maana ni muda gani mwananchi anatakiwa asiendeleze? Tukisema hiyo miaka mitatu maana yake mwananchi huyu atapata athari kubwa. Kwa hiyo, mawazo yangu mimi ni bora basi ile stop order isizidi miaka mitatu kwa sababu mwananchi akishapewa ile haruhusiwi kufanya maendeleo yoyote. Kwa hiyo, tuipunguze irudi angalau iwe mwaka mmoja badala ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napata tabu sana, ardhi Tanzania imekuwa mali ya Serikali au mali ya Rais. Sisi Kinondoni pale tuna eneo letu kubwa sana, Mheshimiwa Waziri amemshauri Rais walichukue, nilitegemea TAMISEMI kuwa chini ya Rais hata ile ardhi angeweza kuisimamia akiwa kulekule TAMISEMI, sasa hivi imeporwa imepelekwa Serikali Kuu, sasa hii ardhi maana yake inakuwa haina mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar-es-Salaam unapowapora ardhi Manispaa, leo Manispaa ya Kinondoni ikiamua kufanya maendeleo, ikiamua hata kubadilisha ofisi yake inabidi ikamwombe Mheshimiwa Lukuvi kuchukua ile ardhi, nafikiri hili si sawa. Ifike mahali hizi Manispaa ziachiwe ziwe na ardhi na ifike mahali hata wananchi ardhi za kwao ziwe ni za kwao. Isiwe leo mwekezaji anaenda Wizarani anachagua eneo halafu mwananchi hapewi taarifa analazimishwa tu kufanyiwa tathmini.