Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ester Amos Bulaya (20 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuwashukuru baba zangu, mama zangu wa Jimbo la Bunda Mjini kwa unyenyekevu mkubwa, bila kujali umri wangu, bila kujali jinsia yangu, mkasema ng‟wana Bulaya ndiye chaguo sahihi la Jimbo la Bunda Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushindi wangu umetoa fundisho kwa wale wote wenye kiburi cha kukaa madarakani muda mrefu. Pia ushindi wangu umetoa fundisho, wananchi wataangalia product bora inayopelekwa na chama husika na si ukubwa wa chama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitoe pongezi kwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Wale ma-senior kama mimi asilimia 30 tuliorudi, mnajua kwamba isssue si Mipango, issue ni utekelezaji wa Mipango. Issue si Serikali ya awamu hii, ni utekelezaji wa Serikali husika. Issue si Ilani ya 2015, ni utekelezaji wa Ilani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia tena mapinduzi ya viwanda. This time don’t talk too much, fanyeni kazi. Rais wa Awamu ya Nne alipokuwa akizindua Bunge, alisema mapinduzi ya viwanda, kwenye Ilani ya mwaka 2010 ukurasa 171, imezungumzia mapinduzi ya viwanda. Hatuhitaji tena mzungumzie, tunahitaji mtende. Tunataka mtende! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kwetu sisi tu, Taifa hili linatuangalia, tutembee kwenye maneno yetu. Wenzetu wanachukua Mipango yetu wanaenda ku-implement kwenye nchi zao. Please, wapeni Watanzania wanachokitarajia. Tuache kusema, tutende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wote waliozungumzia reli ya kati na naungana na hoja ya kuhakikisha tuna viwanda, tuvifufue vya zamani, tuwe navyo. Ni jambo la msingi sana, lakini leo hii tunazungumzia mapinduzi ya viwanda. Tumemaliza ujenzi wa VETA kila Wilaya? Mambo haya yanakwenda sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ma-graduate wenye masters, wenye degree wale ni ma-superviser. Tunahitaji kuandaa product nyingine ya certificate, ya diploma tuipeleke kwenye viwanda. Tunatakiwa tuwe na VETA, VETA na mapinduzi ya viwanda yanaenda sambamba. China ilifanikiwa kwa mtindo huo. Please tuwe na VETA, tuwe na viwanda, tunatoa watu huku kwenye VETA tunaingiza viwandani tunatatua tatizo la ajira kwa vijana. Tupange kwa makini, tutekeleze kwa makini kwa maslahi ya vijana wa sasa na wajao, please mkaangalie tena. Tusiseme tu VETA kwenye kila Wilaya ziko wapi tumezungumza miaka mitano iliyopita, this time mara ya mwisho tuongelee mapinduzi ya viwanda Watanzania waone viwanda si maneno, do not talk too much, tendeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakapoamua kwenda kuwekeza kwenye viwanda, kuna mmoja alisema angalieni na jiografia, sisi kwetu kule Kanda ya Ziwa hatuhitaji katani kule ni pamba, ng‟ombe na uvuvi. Hiyo niliyosema ya VETA mwenye degree ataenda kusimamia samaki wanasindikwa vizuri yeye hataenda kusindika. Mwenye degree, mwenye masters hataenda kutengeneza viatu atasimamia viatu vimetengenezwa vizuri, ni ushauri chukueni ufanyieni kazi. Hamtaimba tena 2020 hapa, fanyeni kazi siyo maneno, it is not about slogan ni utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlikuja hapa na Maisha bora kwa Kila Mtanzania yako wapi? Leo hapa kazi iko wapi? Siyo maneno ni vitendo. Siyo tu wingi kwa kuandika kwenye Ilani mmeziandika sana tendeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumezungumzia kuhusiana na Shirika letu la Ndege jamani kuwa na Shirika la Ndege ni ufahari tukiwa kwenye nchi za wenzetu. Tunapishana tu na ndege za Kenya, Rwanda, sisi tunasema tu tutafufua, tutafufua lini? Nchi ndogo kama Malawi wana ndege. Baba wa Taifa aliacha ndege tunahitaji ndege. Mnaenda Dubai mnapishana na ndege za Kenya, Rwanda na kadhalika tunahitaji ndege. Kuwa na ndege jamani unachangia pia kwenye sekta ya utalii, watu mnaosafiri mnajua. Ukishuka pale Kenya wazungu wote wanaishia Kenya halafu wanakuja Kilimanjaro, tungekuwa na ndege wangeshukia Dar es Salaam fedha zile wanazoziacha Kenya wangekuja kuacha kwenye nchi yetu lakini ndege moja, sijui mtumba kila siku tunazungumzia ndege, ndege ziko wapi? Kwa nia njema tutende ili tulitendee haki Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapozungumzia sekta ya utalii watu wanajua utalii ni tembo tu, siyo tembo, wenzetu kule wametengeneza visiwa, sisi mashallah Mungu ametupa hatuhitaji kuvitengeneza, tunavitumia kwa aina gani vile visiwa? Tunaboresha maeneo yetu mengine ya utalii, tuna Mbuga pale ya Saa Nane, ukienda kule unaona Mwanza nzima jinsi ilivyo nzuri lakini cha kushangaa hata hoteli kule hatuna. Tungetengeneza huu Ukanda wa Kaskazini na Kanda ya Ziwa ungekuwa sekta ya utalii. Mtu anatoka Ngorongoro, anaenda Serengeti, anaenda Saa Nane anaenda kwenye visiwa vyetu ambavyo Mungu ametujalia. Wenzetu nchi nyingine wanatengeneza visiwa na maeneo ya utalii lakini sisi tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ashakum si matusi wengine wanasema visiwa vyetu wanaenda kujificha wake za watu na wanaume za watu. Visiwa vyetu tunatakiwa tuvitumie kwenye utalii ndugu zangu. Tunayaongea haya kwa uchungu mkubwa, Mungu ametupa mali hatuzitumii. Haya ni mambo ya msingi tumeyasema na Mwenyekiti wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Utalii. Watu wanakuja wanayalalamikia haya, mambo kama hayo lazima tuyaweke katika mipango yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie deni la Taifa, nakubaliana kabisa hakuna nchi isiyokopa. Kukopa ni jambo lingine, kwenda kuwekeza katika kile ambacho wamekikopea pia ni jambo lingine. Leo hii tunadaiwa US Dollar milioni 19. Nimesema kukopa siyo shida, je, tunazitumiaje hizo fedha tunazokopa? Tunakopa tunaenda kuwekeza kwenye eneo gani? Fedha zetu za ndani tunaweza kuwekeza katika maeneo ya huduma za kijamii hizi fedha tunazokopa twende ku-invest katika maeneo ambayo yatazalisha na tutaweza kulipa deni kwa mujibu wa mikataba tuliyoingia na kuondokana na mlundikano wa riba kama ambavyo upo humu kwenye ripoti. Hilo ni jambo la msingi sana. Tatizo hata katika hii Mifuko yetu ya Hifadhi ya humu ndani ambayo tunaikopa na hatuilipi, tunaenda kuwekeza sehemu ambazo hatuzalishi. Hilo ni jambo la msingi ukikopa nenda kawekeze eneo ambalo litakuwezesha kulipa deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtende, msiendelee kuongea, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kupongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, wajibu wetu ni kuwashauri kama tunavyowashauri kwenye mambo mengine; mkitaka yachukueni, lakini mnapoyaacha na madhara yake yanatokea kama yaliyotokea kwenye kikokotoo na kwenye mambo mengine. Kwa hiyo, Waziri na Naibu Waziri Mheshimiwa Jesca Kishoa ambaye leo ni birthday yake wamefanya kazi yao, wamelitendea haki Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa term ya pili, na tangu nimeingia kwenye Bunge hili Serikali ya Chama cha Mapinduzi haijawahi kutoa pesa za REA zote, mbali ya kwamba pesa zipo kwenye uzio na tunajua pesa zikiwekwa kwenye uzio zinatakiwa ziende zote kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa taratibu zetu tulizojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naanza na awamu ya nne; mwaka 2010/2011 tulitenga bilioni 56.883, zilizotolewa ni bilioni 114; mwaka 2013/2014 zilitengwa bilioni 53.158, zilizotolewa ni bilioni 6.757; 2015/2016 zilitengwa bilioni 420, zilizotolewa ni bilioni 141, sawa na asilimia 34; 2017/2018, awamu ya tano sasa ya majigambo mengi… (Makofi)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: …zilitengwa bilioni 499, zimetolewa bilioni…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, subiri. Taarifa Mheshimiwa Dkt. Mollel.

MHE. JOHN W. HECHE: Wanataka kuharibu Bunge hawa...

T A A R I F A

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa dada yangu mpendwa taarifa kwamba ameanza…

(Hapa Mheshimiwa John W. Heche alizungumza bila kufuata utaratibu na bila kutumia kipaza sauti)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, siyo vizuri unavyofanya.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Charles Wegesa, tulia.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, naomba utulie jamani na wenzio. Mheshimiwa Dkt. Mollel, naomba umalizie taarifa yako.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumpa taarifa dada yangu kwamba ameanza vizuri na ameonesha jinsi ambavyo kwa awamu ya nne kumekuwa na kwamba inatengwa hela lakini tunahitaji kufikia lengo hatufikii, ndiyo maana tunaweka miradi ya kimkakati, kama ya Stiegler’s na mingine ambayo itahakikisha tuna-boost viwanda na chanzo mapato ya ndani yaweze kuongezeka ili tuweze kubadilisha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha wanaongea kizalendo wakidai kwamba ni makosa kufanyika hayo ambayo yangetusaidia tuweze kufikia lengo yeye analolitaka. Kwa hiyo, wakati tuna-address issues hizo anazolalamikia anapinga kwa hiyo tunafikiri dada yangu ungetusaidia sasa kuunga mkono Stiegler’s na nyingine ili mwisho wa siku tuweze kufikia lengo ambalo unataka tufikie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, taarifa hiyo.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uchanga wa kuingia Bungeni unamsumbua, ni njuka siyo size yangu, siwezi kumjibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo trend ya Serikali…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Nitaanza vibaya mama.

MHE. ESTER A. BULAYA …ya Chama cha Mapinduzi kushindwa…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Halima Mdee yuko wapi kwanza nikushtaki kwake?

MWENYEKITI: Waheshimiwa naomba tutulizane, tusikilizane Waheshimiwa, Mheshimiwa Ester naomba uendelee tafadhali.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema, kwamba pesa zikiwekwa kwenye uzio ni tofauti na pesa zingine anazozisema yeye, hizi zinaenda kwenye matumizi maalum, lazima ziende zote, ndiyo hoja iliyopo hapa. Ziko kwenye ring-fenced, ndicho ninachokisema, na hiyo trend ilianza tangu Bunge lililopita mpaka hili la Serikali ya Awamu ya Tano bado hamjafanikiwa kutoa pesa zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu hii imejipambanua inashughulika na ufisadi, imeanza na mishahara hewa…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(f) na (g). Kuwa Mheshimiwa Mbunge ametumia lugha ya kuudhi na inayodhalilisha wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa anayechangia amemwambia Mheshimiwa Dkt. Mollel kuwa ni ushamba wa kuingia Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, umezungumza maneno ya ushamba? Haya, endelea.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge mnaosema ushamba nitawatoa nje, Mheshimiwa Ester endelea.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Amenivurugia ndoa yangu huyu unajua, Halima Mdee mke wangu halafu ukaolewa…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati pesa za REA…

MWENYEKITI: Waheshimiwa tuwe na nidhamu jamani, hebu Mheshimiwa Ester naomba umalizie.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati pesa za REA Serikali hii inachelewa kupeleka, lakini bado…

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa Chief Whip amesimama bado mnapiga kelele ya nini?

Mheshimiwa Chief Whip endelea.

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mwongozo wako, kwanza kuhusu aina ya taarifa zinazotolewa hapa Bungeni, lakini pamoja na hayo, Mbunge anachangia lakini Mbunge mwenzake anawasha microphone na kutukana. Na bahati mbaya sana inawezekana Kiti chako hakisikii, lakini maneno ambayo yamesemwa ni maneno makubwa sana na yameingia kwenye microphone. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba mwongozo wako; hivi hii miongozo inayotolewa kwa ajili ya dhihaka tu pamoja na matusi na nini, unairuhusu iendelee kwenye Kiti chako ili vilevile iamshe hasira za watu? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini, nimekuelewa. Waheshimiwa tutulizane. Waheshimiwa tulizaneni, wote Wabunge hapa mnaelewa vizuri Kanuni na mnajua nini mnafanya, kwa hiyo mnafanya makusudi, mnaposema wawili, watatu, wanne mimi huku sisikii kinachozungumzwa na mtu mmoja, siyo ninawaachia, ukiongea wewe na mwingine na mwingine hakuna kinachosikilizika, kwa hiyo, mimi nashindwa kutoa maamuzi. Ila ninyi Wabunge mnaelewa Kanuni na mnafanya makusudi, yeyote ambaye atakwenda sasa hivi kinyume atatoka nje hana ruhusa ya kuchangia, naomba umalizie muda wako.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mbali ya kwamba fedha za REA haziendi zote, lakini kumekuwa na ufisadi, kuna malipo hewa. REA imeipa Kampuni ya HIFAB fedha za ziada, zilizozidi, Dola za Kimarekani 81,000 na ushee wakati ilipaswa kulipa dola 9,000; na hili jambo halijafanyika mwaka 2010, 2011, limefanyika mwaka 2017 kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wizi kama wizi mwingine, wahusika wanatakiwa washughulikiwe na mpaka sasa hivi na kwenye hotuba yetu tumesema bado Dola za Kimarekani 44,000 hazijarudishwa ambapo huko Serikali hii inasema ya wanyonge ndiko pesa za wanyonge zinapigwa. Huko ndiko ambako tunahitaji umeme vijijini, huko ndiko ambako Serikali hii imewapa Wakuu wa Mikoa waanzishe viwanda; wakati kuna uchafu huu hivyo viwanda vitakamilikaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna ukaguzi ulifanywa kwa mikataba mitatu iliyogharimu shilingi bilioni 984 ambapo imegundulika vijiji 55 kwenye Mikoa ya Tanga, Mwanza, Arusha na Manyara tayari vina umeme lakini wakandarasi wamelipwa tena waende wakaweke umeme. Huu ni wizi, na tunaposema wizi hatuwezi kunyamaza eti tukachagua awamu, huu ni wizi kama wizi uliofanyika awamu zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji ukaguzi maalum ufanywe ili hiyo dhamira sasa ya kuzima vibatari mikoani huko na vijijini itekelezwe. Kwa hiyo tutahitaji majibu sahihi. Sasa kama vijiji 55 hivi, je, kwa nchi nzima tunaingizwa mkenge kiasi gani, huo wizi upo kiasi gani? Kwa hiyo haya lazima yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa pia na malalamiko kwenye suala zima la kuunganishiwa umeme vijijini. Wanasema wenye pesa ndio wamekuwa wakipewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme. Wananchi wa kawaida huko majimboni kwetu wanalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni kuhusiana na suala la TANESCO. Mpaka sasa hivi Shirikia TANESCO linajiendesha kwa hasara kwa bilioni mia tatu na. Kipindi cha awamu ya nne wakati inaondoka madarakani hasara ilikuwa bilioni 124, yaani kuna ongezeko la bilioni 122. Sasa tulitegemea Serikali hii inayokusanya kodi ingeenda kuondoa zile hasara na kuleta faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado madeni; madeni kutoka bilioni 700 mpaka bilioni 958 na TPDC peke yake inaidai TANESCO bilioni 340. Ndiyo maana Kambi Rasmi ya Upinzani tulisema shirika hili litakufa, sisi siyo wa kwanza, tumeshauri ligawanyeni, kuwe kuna mashirika mawili, limezidiwa uwezo na athari ya madeni, athari ya kujiendesha kwa hasara inakwenda kuathiri kwenye mtaji. Haya ndiyo ambayo tunayasema… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tunapoamua kupanga katika mipango mbalimbali ya kitaifa, dhamira ni kuhakikisha mipango inatekelezeka kwa lengo la kukuza uchumi wetu, kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza pato la Mtanzania mmoja mmoja na kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza ajira kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua, katika mipango yote suala la Mpango wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma ni takribani zaidi ya miaka 20 linaongelewa katika Bunge hili. Liganga na Mchuchuma ilikuwepo katika mipango yote. Lazima tujiulize Serikali ya Chama cha Mapinduzi mna dhamira, mikakati na malengo ya kuhakikisha mnamuondoa Mtanzania kwenye umasikini na mna lengo la kuinua pato la Mtanzania mmoja mmoja au tunafanya kazi kwa mazoea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaliwa kuwa na madini ya chuma takribani tani milioni 126. Tumejaliwa kuwa na madini ya makaa ya mawe takribani tani milioni 428. Leo tunajenga reli ili ule mradi ukamilike unatarajiwa kutumia shilingi trilioni 17 na katika hizo ziko pesa za mikopo lakini tunaagiza chuma kutoka nje wakati Mwenyezi Mungu ametupa chuma chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza kupitia Shirika letu la NDC ambalo lina hisa asilimia 20 na kampuni ya Kichina tumeingia mkataba zaidi ya miaka saba lakini hakuna kinachoendelea katika Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Sheria ya Madini, kifungu cha 47(2) kimeweka wazi ukipewa mkataba na leseni unatakiwa utekeleze ndani ya miezi 18. Tuna hisa asilimia 20 kupitia NDC, kuna Mchina ana asilimia 80 amevunja sheria, anafichwa. Kuna interest gani, kuna nini kinajificha huku pesa tunakwenda kukopa nje, tunaagiza chuma kwa kukopa nje halafu kuna mtu tunambeba, tuna madini tumepewa na Mwenyezi Mungu, tuko serious? Halafu tukihoji mnatupa tu maneno, timizeni wajibu wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kule wa Njombe na Ludewa hawaendelezi maeneo yao. Wamesema wapishe eneo la mradi…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, upewe taarifa; Mheshimiwa Waziri nimekuona.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuwa Mradi wa Liganga na Mchuchuma una vipengele sita. Vipengele vitano vimeshafanyika, kimebaki kipengele kimoja ambacho kinahusu mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii mikubwa ina maslahi makubwa kwa nchi. Unapoingia mikataba na mashirika ya kimataifa lazima uwe makini. Kwa hiyo, majadiliano yanaendelea na yapo katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba mkataba huu unakuwa na maslahi mapana. Kwa hiyo, anavyosema hakuna kinachoendelea siyo sahihi kwa sababu ina mambo sita, matano yameshafanyika, limebaki jambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apokee taarifa hiyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, pokea hiyo taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa, najua ni Waziri mgeni. Hili jambo tangu enzi za mama Mary Nagu, vipengele vitano miaka 20 brother? Hii ni taarifa ya sasa hivi ya Waziri na inasema hiyo kampuni haina uwezo wa kuwekeza dola za Kimarekani bilioni 2.9. Shame! Okoeni pesa za Watanzania, tunaagiza chuma kutoka nje, Mwenyezi Mungu ametupa chuma chetu; tunahitaji nini? Halafu unajibu majibu kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ludewa, Njombe, maeneo haya takribani zaidi ya miaka saba wameshindwa kuyaendeleza. Mnasema Serikali ya wanyonge wakati kuna watu kule mnawasimamisha zaidi ya miaka saba hawaendelezi maeneo yao, hawajalipwa fidia, mnamlindwa mwekezaji mnasema maslahi ya nchi; yako wapi wakati huyu amevunja Sheria ya Madini, kifungu cha 47(2) miezi 18 imeisha, like seriously? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtimize wajibu wenu. Haya madeni wanakuja kuyalipa Watanzania. Kuna mtu alisema dunia ni chuma, chuma tunacho tunaagiza nje kwa hela za mikopo; kweli? Halafu tunakuja tunafanya mzaha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Najua Serikali imekwenda kuchukua pesa tena kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenda kuwekeza kwenye viwanda. Hatukatai kuchukua fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye viwanda kama kuna dhamira njema na Serikali mnalipa hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Ripoti ya CAG, inaonesha hali ya Mifuko ni dhoofulihali, mifuko iko taabani. Ripoti ya mwanzo…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, upokee taafifa kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka leo napoongea hapa kama Waziri wa sekta, thamani ya Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii imeshapanda mpaka shilingi trilioni 11.510. Sasa kama thamani ya Mifuko hii imeshafika shilingi trilioni 11.510 mpaka sasa, hicho ni kiashiria kwamba sekta inakua na siyo inakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nani mwenye majukumu ya kusema kwamba sekta inakufa? Ukitaka kuwa na mamlaka ya kusema mifuko inakufa ni lazima ufanye actuarial. Sasa hivi ndiyo tupo kwenye huo utaratibu wa actuarial. Mtathmini ameshaanza kufanya utathmini wa Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, manunuzi ya Mtathmini kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa sekta binafsi yameshakamilika. Kwa hiyo, taarifa ya Mthamini ndiyo itakayokuja kutupa uelekeo mzima wa sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka haya Mheshimiwa Ester ya kusema kwamba mifuko imekufa kabla Mtathmini hajatoa ripoti anayatoa wapi? CAG anafanya ukaguzi wa mwenendo wa fedha, Mtathmini kwa vigezo vya Umoja wa Mataifa na Shirika la Kazi la ILO ndiye atakayetupa mwelekeo wa Mifuko na sekta. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester asubiri, asianze kuwahisha shughuli mapema. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Ester Bulaya, unaipokea?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amejichanganya mwenyewe, naye amejuaje hiyo thamani kama bado tathmini haijafanywa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya kwanza kabla Mifuko haijaunganishwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali wa kwenu amesema mifuko haina uwezo wa kulipa madeni yake pamoja na madeni ya wastaafu. Amefanya tena ukaguzi na wewe unajua tarehe moja hapa tulipitisha Sheria ya Kikokotoo ukaliahidi Bunge na wewe ukaponea chupuchupu akaondolewa yule Mkurugenzi mwingine, ukaahidi hapa Bungeni mnakwenda kufanya tathmini ya madeni, huu mwaka wa nne sister, hukufanya. (Makofi)

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ni lazima tutoe taarifa kwa sababu watu wasipotoshe mambo humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya Mtathmini wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ilifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2016/2017. Tathmini ile tuliifanya baada ya kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali na walitushauri namna ya kwenda kwenye merging. Tulipitisha sheria hapa ndani kwamba mwaka mmoja, miwili baada ya merging ndiyo sasa tutafanya tathmini yenye uhaliasia wa kujua baada ya merging mifuko yote na sekta inakwendaje. Sasa asichanganye tathmini ya merging na tathmini hii baada ya merging tunakwendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo masuala mengine ya kupona au kutokupona siyo kazi yake, iko mamlaka ya kutathmini haya yote. Mimi nasimama kama Waziri wa sekta namwambia Mheshimiwa Ester, tathmini ni mbili; ya merging ilishakwisha, tunasubiri ya mwenendo tunaokwenda sasa hivi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, taarifa hiyo, ipokee.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu atulie tu, hayo mambo mimi hayanihusu ila ninachomwambia, mlipe madeni. Mnakopa hamfanyi tathmini, wastaafu hawalipwi humu ndani kila Mbunge anapiga kelele. Haya, kwa tathmini tu aliyoifanya CAG Serikali mnadaiwa shilingi trilioni mbili na bilioni mia nne kumi na saba, fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo sijazungumzia deni la PSPF, takribani shilingi trilioni 11, mliwaamrisha wawalipe watu ambao hawachangii. Leo kwenye viwanda 12 mmekwenda kuchota tena fedha shilingi bilioni 339 kuendelea kuwekeza huku mnadaiwa shilingi trilioni mbili.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MBUNGE FULANI: Eeeh.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, tafadhali.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, utanisamehe sana. Unajua ni lazima Bunge hili lielewe mwelekeo wetu ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria, kazi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya kwanza ni kuandikisha wanachama, ya pili ni kukusanya michango. Huwezi ukakusanya michango ukaitunza benki eti isubiri tu watu watakapostaafu uwape. Kazi ya tatu ni kuwekeza na unapowekeza michango unaongeza thamani ya ile michango muda utakapofika uweze kuwalipa wastaafu kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazowekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali inajichoteachotea tu, hapana. Serikali inawekeza kwenye uwekezaji wenye tija ili muda unapofika mafao yaweze kupatikana.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Sasa kama
anataka hiyo michango iwekwe tu benki bila kuongeza thamani utapata wapi fedha? Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester aelewe hesabu hizi za hifadhi ya jamii, azielewe vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Halima, haiwezekani taarifa juu ya taarifa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Ester Bulaya, unapokea taarifa?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei. Halafu anajua mimi nilikuwa Waziri Kivuli wa Sera na Uratibu wa Bunge, anajua nilivyomkimbiza humu ndani kupitia Sheria ya Kikokotoo na Mheshimiwa anazungumzia michango, anataka nije huko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta zenu za Kiserikali, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi mliacha kupeleka michango shilingi bilioni 85; Mfuko wa Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni 61; Mfuko wa Bima ya Afya bilioni 24 michango mlichelewa ninyi ndani ya siku 30, unazungumzia michango? Nazungumzia mlipe madeni, muwekeze kwenye maeneo ya mikakati. Hizi pesa siyo zenu, ninyi ni wasimamizi, pesa hizi za wastaafu wa taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hatuoni dhambi kila Mbunge akisimama humu kuna wastaafu wana miaka miwili, wengine miezi sita hawajalipwa halafu hela zao mlizokopa hamlipi, mnachukua zingine mnakwenda kuwekeza, kwanza mmefanya tathmini hivyo viwanda vinalipa; mmefanya? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipeni pesa za wastaafu wa nchi hii, wamelitumikia taifa hili kwa jasho la damu. Mnataka morali iongezeke kwa hawa waliopo kazini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, muda hauko upande wako, muda umekwisha. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni lini Serikali kwanza, itamteua Kamishna wa Dawa za Kulevya ili kuleta ufanisi wa kazi katika Tume, maana ni muda mrefu tangu aliyekuwa Kamishna muda wake kwisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa nini Serikali mmeamua kupeleka fedha za methadon (MDH), badala ya kupitia kwenye Tume ya Dawa za Kulevya kama ilivyokuwa zamani? Serikali haioni kuwa fedha hizo zitakuwa hazifiki kwa wakati kwenye vituo husika vinavyotoa huduma hiyo ya methadon kwa vijana walioathirika na dawa za kulevya?
Tatu, kumekuwa na mkakati wa kuvuruga utaratibu mzima wa kuwarudisha vijana walioathirika na dawa za kulevya kurudi kwenye hali yao ya kawaida, ambapo wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya huenda kwenye vituo vinavyotoa huduma ya methadon kwa kuwashawishi vijana kuanza kutumia tena dawa za kulevya. Kitendo hicho kinarudisha nyuma jitihada za kupambana na dawa za kulevya. Je, Serikali mna mkakati gani wa kuhakikisha mkakati huo unakwama?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza kabisa Waziri akija kutujibu hapa jioni, ningependa atufafanulie katika hizi fedha za maendeleo ni kiasi gani kinakwenda kulipia madeni ya Wakandarasi ambayo natambua yameanza kulipwa, ni kiasi gani kinakwenda kumalizia miradi tuliyopitisha bajeti ya mwaka jana na kiasi gani kinakwenda kwenye miradi mipya, isiwe kiujumla hivi. Tunaomba, mmesema hapo kazi na sisi tunataka tuwasimamie muifanye kazi kiufasaha, siyo jumla jumla hivi, aje atuambie, kwenye randama sijaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningetaka kulizungumzia na hili pia nitasema kama Waziri kivuli wa Sera, Uratibu, Bunge na mazagazaga mengine. Mwaka uliopita kwenye Mfuko Mkuu, Wizara hii ilipitishiwa bilioni 199, leo kwenye kitabu chake Mheshimiwa Waziri amekiri mpaka Aprili amepokea bilioni 600. Kwa utaratibu wa kuheshimu mihimili amepata zote na ziada, alimpitishia nani? Huku ni kuvunja Katiba na kudharau Bunge, alipata zote, kuna Wizara zingine hazijapata, kaka yangu Mheshimiwa Nape wamempa bilioni mbili, mwaka jana tulimpitishia bilioni tatu hizi bilioni 500 nani alimpitishia?
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Bunge liheshimiwe, lazima tufuate Kanuni, lazima tufuate Katiba, kuna Wizara nyingine hazipata hata asilimia 50, yeye amepata 200 tofauti na tuliyompitishia humu, hatusemi asipewe pesa, tunataka utaratibu ufuatwe ili kujenga nidhamu ya matumizi. Leo kuna akinamama kule wanaomba gloves tumepitisha bilioni mia na, amepata 600 nani kampitishia? Tunapoyasema haya tunataka tutengeneze nidhamu, hatuna hila, mimi mwenyewe nataka apate fedha, angekuja kuomba sasa hivi tupitishe leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea, Mheshimiwa Rais wetu mtukufu, mpenzi sana amesema tunataka tujifunge mkanda tubane matumizi fedha nyingi ziende kwa wanyonge. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri naona kuna residential house, Ikulu, JK ametoka miezi sita iliyopita imeharibika lini? Kila mwaka hapa tunapitisha fedha za ukarabati, je, amemtuma?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwambalaswa amesema ukimtazama moyoni dhamira yake ni kwa wanyonge, hizi fedha mngepelekea TEA aende akatengeneze miundombinu ya elimu. Sasa hivi Wahisani wamegoma kuleta pesa, kipaumbele siyo kujenga residential house Ikulu, tupeleke kwenye miradi ya maendeleo wangempa Mheshimiwa Nape, wangepeleka TBC, wangepeleka na maeneo mengine. Kipaumbele residential house Ikulu, Dar es Salaam? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, jambo lingine nimesoma ripoti ya CAG, kuna halmashauri tano zimetoa mikataba ya utengenezaji wa barabara zaidi ya bilioni moja na milioni mia saba bila kujua dhamana ya hawa Wakandarasi, kweli! Ndiyo maana kule kwenye Halmashauri zetu mtu anaomba tenda hana hata greda, kwa nini wasilime barabara kama mashamba? Huu ni wizi, lazima usimamiwe, tukisema wizi usimamiwe tunataka biashara hii ikome ili Jimboni kwangu kule wananchi wangu watengenezewe barabara, mambo yaende hatuwezi tukasema funika kombe mwanaharamu apite, halafu hapiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakuja Jimboni. Mwaka jana walitupa bilioni moja utengenezaji wa barabara ya kuanzia kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Kangi, Kisolya – Bulamba – Bunda – Nyamswa, na hili nilimwambia Mheshimiwa Waziri, mwaka jana ilipitishwa kwa kiwango cha lami leo naona imewekwa kwenye changarawe, tuchukue lipi? Wananchi wa Bunda kuanzia Mwibara kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Boniphace Mwita, tueleweje, ni kiwango cha lami au cha changarawe? Hata hivyo, Mkoa wa Mara umekuwa ukipewa fedha ndogo kila mwaka, Mheshimiwa Rais alivyoomba kura alisema hizi ni kiwango cha lami hapa mmetuwekea changarawe, lipi ni lipi? Maneno yanakwenda huku, vitendo kule, tuamini kipi hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa kuna ukarabati, upanuzi wa barabara kubwa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Musoma, Mheshimiwa Waziri wananchi wangu waliridhia kupisha upanuzi wa barabara wameshafanyiwa tathmini huu mwaka wa nne pamoja na baba yangu Mzee Wassira nyumba yake iko Manyamanyama, mnawalipa lini? Sasa mtuambie hapa lini mnawalipa hawa? Yuko na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Gimano anadai humu, lini mnawalipa? Kuna wazee maskini mmoja babu yangu, mpaka amekufa jana hajalipwa, kwa nini mliwafanyia tathmini mpaka leo hamjawalipa, naomba majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri Halmashauri yangu mimi ni mpya barabara nyingi haziko sawa, kupitia TANROADS Mkoa wa Mara mmejipanga vipi kuhakikisha hizi Halmashauri changa mnazisaidia. Kwanza kama mnavyojua Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa Wilaya maskini, Wizara kupitia TANROADS Mkoa wa Mara mnajipanga vipi kuhakikisha hizi Halmashauri mnazipa support kuhakikisha barabara zinapitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuna nyingine zimeshaanza kufanyiwa kazi kama Balili – Mgeta, namshukuru Mkurugenzi wa TANROADS Mkoa wa Mara na maeneo mengine ya Kangetutya, Manyamanyama, sasa hizi nyingine hizi mna mkakati gani wa kuhakikisha mnazisaidia ?Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia sekta hii muhimu sana. Kwanza kabisa kwa moyo wa dhati nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, dada yangu Ummy Mwalimu kwa uteuzi wako. Tunaamini mwanamke akipewa nafasi hasa katika sekta ya afya ambayo ina changamoto kubwa sana zinazowagusa wanawake, sisi tunakuombea ili uingie katika historia ya kuondoa matatizo ya wanawake. Pia nichukue fursa hiyo kumpongeza kijana mwenzangu kwa uteuzi Dkt. Kigwangalla, naamini usipofuata siasa, ukifanya kazi kwa profession yako ya Udaktari utasaidia sana kuboresha sekta ya afya katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, niwapongeze Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushiriki zoezi la kutoa damu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuwasaidia watoto waliokuwa wamekosa damu wakati wa kufanyiwa upasuaji wa moyo ili waweze kufanya hivyo. Tunaamini bila kujali itikadi zetu, tukifanya hivyo tutasaidia sana kuchangia kwenye benki ya damu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ningependa unipe ufafanuzi kwa nini fedha za methadone zinapitia MDH (Management and Development for Health)? Nauliza hivyo kwa sababu mwanzo zilikuwa zikienda Tume na ilikuwa rahisi sana kufika katika hivi vitengo ambavyo wanatoa hizi dawa kwa ajili ya kuwasaidia wale walioathirika na dawa za kulevya. Sasa hivi imeenda MDH na nafikiri ni mlolongo mkubwa sana kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Mheshimiwa Spika, pia hivi sasa hawa watu wa drugs wana mkakati maalum ambao nchini Italia watu wanaouza dawa za kulevya waliutumia. Baada ya kuona kwenye mianya mbalimbali wameanza kuziba na nichukue fursa hii kuwapongeza Kitengo cha Usalama wa Taifa wanaoshughulikia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuziba hiyo mianya, sasa hivi wana mkakati wa kwenda kuuza dawa za kulevya katika hivi vitengo vya kutoa dawa za kuwarudisha wale vijana. Sasa tunataka kujua kama mnajua mna mkakati gani wa kudhibiti ili hii methadone iwasaidie vijana siyo wanatoka kunywa dawa wanarudi katika chemba za kuwarudisha tena katika kutumia dawa za kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kitengo cha magonjwa ya watu wenye matatizo ya akili pale Muhimbili, hakuna wodi ya watoto wa matatizo ya akili, wanakwenda kuchanganywa kwa wagonjwa wengine, moja wanaweza wakaumiza wenzao au wao wakaumizwa, kwa hiyo, ni changamoto kubwa sana hakuna wodi ya watoto.
Mheshimiwa Spika, kingine hata katika hiyo wodi ya watu wazima tunajua watu wenye matatizo ya akili, ambao wanakwenda hawajawahi kutumia dawa, wako active zaidi kuliko wale ambao wameshaanza kutumia dawa.
Serikali ina mkakati gani wa kuongeza wodi na kuwagawa, wale walioanza kutumia dawa, wanaoanza kupona wanakuwa kwenye wodi zingine na hawa ambao bado hawajaanza kutumia dawa wawe kwenye wodi zao ili tuepushe madhara ya kuumizana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ukipitia taarifa ya CAG, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), mwaka jana kuna mzigo wa shilingi bilioni 4.6 umeingia bila kukaguliwa, hapo ndiyo zinaingia cerelac fake, zinaingia S26 fake, maziwa ya kopo, zinaingia sorry pads fake, zinaingia pampers fake, zinaingia juisi fake na kadhalika. Mwisho wa siku tunawaona kwenye TV wanakwenda kusema tumekagua vitu fake vilivyoingia, je, ni jitihada gani ambazo zimefanywa kudhibiti kwanza visiingie kabla ya kusubiri vinafika dukani na kuleta madhara kwa watoto na kuleta madhara kwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka kulizungumzia hapa kuhusiana na hospitali yetu ya Ocean Road, nakumbuka mwaka jana nilileta hoja binafsi na Mheshimiwa Waziri aliyekuwa Naibu Waziri Dkt. Kebwe alijibu yafuatayo; “tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua mashine.”
Mheshimiwa Spika, leo napongeza taarifa ya Kamati imeeleza ni uzembe umefanywa na Serikali, ile mashine haijaja, mbali na kutambua jitihada ya kujenga maeneo ambayo zitakaa zile mashine. Mheshimiwa Waziri mashine zilizokuwepo, zile mbili ni mbovu, zinafanya kazi kupita uwezo wake. Kwa siku zinahudumia wagonjwa zaidi ya 300 na tunajua ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi unavyomsumbua mwanamke na tunajua matibabu ya kansa yalivyo ya gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Ocean Road waliomba Bohari ya Dawa, dawa tofauti tofauti 53 wamepata 17 tu, sawa na asilimia 35. Tunaomba kuwe na mkakati maalum wa kuhakikisha fedha zinazokwenda Ocean Road ziwe ring fenced ziende zote, pamoja na dawa zinapotengewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tuwe na mkakati sasa wa kutanua wigo wa matibabu katika kanda zetu ili ile Ocean Road isielemewe. Hata katika takwimu ukiangalia wengi wanaopata hayo magonjwa ni watu maskini wanaotoka kwetu kule Manyamanyama na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia, nimelizungumzia sana nikiwa Mbunge wa Viti Maalum kuhusiana na kupandishwa hadhi Kituo cha Afya cha Manyamanyama kuwa Hospitali ya Wilaya. Hili ni jambo la muda mrefu, tunajua kuna changamoto ya kukosa chumba cha kuhifadhi maiti, lakini kama unavyojua Halmashauri yetu bado changa, tunaomba Wizara mtusaidie na uingie katika kumbukumbu. Hili ombi tangu enzi za Mama Anna Abdallah na wengine, naamini kwako wewe ni jambo dogo halitakushinda. Tunaomba utusaidie wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini, akinamama wasihangaike sana iwe Hospitali ya Wilaya kwa sababu inahudumia hata Wilaya ya jirani pamoja na mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine natambua umuhimu wa Mfuko wa Afya, ni kuboresha sekta ya afya na kuboresha vituo vya afya na natambua kuna ufadhili wa DANIDA pamoja na fedha za Serikali, kuna Halmashauri 23 hazifanyi vizuri, natambua zingine zilizokaguliwa kati ya 160, 138 zinafanya vizuri. Hizi 23 kutofanya vizuri na kufuata masharti zimesababisha hasara ya bilioni moja na milioni mia moja tisini na tisa.
Mheshimiwa Spika, hizi fedha zingeweza kujenga vituo vya afya vingine, hizi fedha zingeboresha katika sekta ya afya hasa kule vijijini ambako tunatoka sisi. Mfano Halmashauri moja tu, kwenye taarifa yake imesema imetumia milioni 55 kwenda kununua dawa na vifaa tiba, lakini katika ripoti ya CAG alivyofanya ukaguzi, wametumia milioni 31, milioni 20 ni wizi mtupu. Sasa tunaomba kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara na uangalizi kuhakikisha hizi fedha zinatumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunajua kuna upungufu katika Mfuko wa Afya wa wafanyakazi 32,000 katika Halmashauri zetu na hawa wafanyakazi ni pamoja na wataalam, kule Mheshimiwa Kigwangalla ambako hakuna hata mlango wa kwenda kumfungia mfanyakazi wala mfanyakazi wa kumfungia, kule ndiko tunatakiwa tupeleke wataalam, tuepushe vifo vya akinamama wajawazito, tuepushe matatizo ambayo yanawakumba wananchi wetu wa vijijini. Huu Mfuko ni mzuri, nia njema lakini lazima tufuatilie mara kwa mara, fedha zinazotengwa zitumike kwa malengo husika, ili tuweze kutatua changamoto za afya katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani na pia nikupongeze kwa kusoma vizuri hotuba yako, lakini changamoto kubwa dada yangu uliyonayo, hicho ulichokisoma upate fedha na ziende katika utekelezaji. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii nami kwa dakika chache niweze kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza kabisa, ningependa Mheshimiwa Waziri atupe status ya umeme nchini ikoje? Kumekuwa na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara. Tuliambiwa hakuna mgao, je, mgao umerudi kinyemela? Hapa Dodoma peke yake umeme ulikuwa unakatika kila Jumapili kuanzia asubuhi unarudi saa 12.00. Siku hizi unarudi saa 9.00 kwa sababu Wabunge tupo Dodoma. Tunaomba hilo utuambie. Pia atujibu, kwenye fedha hizi za umeme, kiasi gani kinaenda katika kumalizia viporo? Kiasi gani kinaenda kwenye miradi mipya? Hilo pia tunaomba atufafanulie, siyo hivi tu kama ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wale asilimia 30 tuliorudi humu ndani, mwaka 2015 nilipokuwa nikichangia Wizara ya Fedha, nilisema fedha zilizopaswa kwenda REA zimeenda kutumika kwenye matumizi mengine. Nilisema, Waziri kama huyo anaweza aka-survive kwenye nchi yetu. Kavunja Katiba, kavunja Sheria ya Bajeti, kavunja kanuni za nchi! Leo athari tunaiona hapa, miradi ya REA Awamu ya Pili haijatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti anasema, shilingi bilioni 70 ilikopwa, Serikali yetu sijui nini! Imevunja taratibu, hapa hakuna kutafuna maneno, wamekwenda kutumia fedha zilizokuwa kwenye ring fence. Maana ya kuwa kwenye ring fence, hazipaswi kutumika kwenye matumizi mengine. Leo tutamnyooshea kidole Mheshimiwa Muhongo wakati hatukumpa hela, watu wamekwenda kunywea chai na maandazi huko ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliyasema haya mwaka 2015 nikiwa Chama cha Mapinduzi. Leo Makamu Mwenyekiti wa Bajeti ameyasema. Tunapozungumzia haya jamani, kwenye mambo ya muhimu ya kuondoa Taifa letu kwenye giza, kweli tumeshindwa kuchukua maeneo mengine, tunaenda kuchukua fedha zilizowekewa uzio? Leo hapa kila mtu akisimama, vijiji vyangu vya Awamu ya Pili havijakamilika. Hakupewa hela. Pesa zimekwenda kutumika kwenye matumizi mengine. (Makofi)
Nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge ambao mmeingia sasa hivi, kama tusipoibana Serikali, huu utaratibu ukiendelea, Bunge lako Tukufu linapitisha fedha, Serikali inaenda kutumia kwenye matumizi mengine, hatuwatendei haki wananchi. Tukatae Bunge hili kuwa rubber stamp, tuseme mwisho, tuazimie pesa za REA, ile trilioni moja tunayoipitisha hapa iende, mwakani tuzungumzie mambo mengine tena, siyo umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya hayana Chama! Wabunge wengi nyie tunatoka vijijini huko, tunajua hali halisi ikoje. Mimi Jimbo langu la Bunda Mjini, baba yangu alikata Kata saba vijijini alijua zitamsaidia na ndiyo nimemchapa. Kata saba ziko vijijini kule, nataka umeme uwake. Kaleta Kata saba Jimbo la mjini, nimemkunguta huko ndiyo nimemshinda vibaya hajaambulia hata Kata moja! Ndiyo nasema hizo zote ziwake umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Babu yangu, hapa hakuna cha viwanda kama hakuna umeme. Halafu tunazungumza mambo kama haya, Waziri wa Fedha hayupo! Hayupo! Lazima awepo! Mambo ya msingi kama haya, mwenzake alikula, hakupeleka fedha. Tunahitaji fedha hizi tunazotenga kwa mambo yanayogusa maisha ya Watanzania. Leo Vijiji vyangu kule vya Kangetutya, Kamkenga, Guta, Nyamatoke, Miale kote huko kuwe na umeme. Sasa leo shilingi bilioni 70 zile hazikwenda, halafu tunaongea lugha nyepesi eti Serikali umekopa hela iliyokuwa kwenye ring fence! This is the shame. Mpeni pesa Mheshimiwa Muhongo tumalize biashara ya kusambaza umeme vijijini. Sasa tunakula bila kunawa halafu tunakuja kufanya kazi tena ya kupitisha kumalizia viporo hapa! Bunge letu lazima liwe kali kwa maslahi ya Taifa. Hii tabia iwe mwisho! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri kingine, Jimboni kwangu Kata ya Kabasa Kung‟ombe kuna mgodi pale. Naomba tutembelee ule mgodi, wanafanya kazi katika mazingira hatarishi. Kwanza hauwanufaishi wananchi wa Kata ya Kung‟ombe lakini mazingira yale siyo mazuri, hawafuati taratibu, kemikali zinawaumiza wananchi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine pale kwenye Kata ya Mjini, umeme kwa wananchi ni shida, gharama kubwa, wananchi wa Bunda masikini…
NAIBU SPIKA: Tunaendelea.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi nijikite katika masuala ya Jimboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake najua wananisikiliza. Moja, kama ambavyo nilimsaidia Waziri wa Viwanda na Biashara babu yangu kwa wezi wale wa EPZ nawaambieni mkashughulike na wezi wa miradi ya maji, mmoja ni mtoto wa aliyekuwa kada wenu na Waziri mwenzenu wa zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo kama wale wanaotajataja wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa zaidi ya shilingi milioni 800 Kata ya Kabasa, shilingi milioni 800 pesa za walipakodi, huyu mtoto, maji hakuna, kashughulikieni hilo tatizo. Nyamswa kwa Boni niliwaambia, ameharibu Mtwara ameharibu na maeneo mengine, huu mradi mkubwa ndiyo usiseme kabisa ilikuwa kila Serikali ikiweka hela wanakata benki moja kwa moja kwa huu utapeli. Rorya kule walimfukuza, wananchi wangu wa Bunda wanataka maji, nimeshasafisha Baba yao nasafisha na uchafu wote, sitaki nataka wananchi wa Bunda wapate maendeleo, hilo limeshaisha, nadhani mmeshanielewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunda kuna njaa, Baba wa Taifa alisema anayeficha maradhi kilio humuumbua, tuna njaa. Narudia, Bunda tuna njaa au niseme tu lugha laini, tuna upungufu wa chakula kwa kata zaidi ya sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, njaa hii siyo ya kujitakia, tatizo la tembo kuharibu mazao ya wananchi, dada yangu Mheshimiwa Jenista alishakuja kutembelea tukampeleka katika mashamba na moja ya shamba aliloenda kwenye Jimbo langu na akaahidi ataitisha kikao pamoja na Waziri wa Maliasili mpaka leo hicho kikao hatujafanya, dada yangu sijui kikao tutafanya lini, utanijibu uniambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Bunda wamesema hawataki kuomba chakula, wana uwezo wa kulima msiwatengenezee njaa wasiyoihitaji. Tembo wenu wanatoka wanakula mazao kule sijui ndovu, sijui tembo, sijui mazagazaga gani mtajijua wenyewe, halafu tena tukiwaambia tuna njaa hamtaki tuseme tuna njaa. Naomba wananchi wangu biashara ya kuombaomba hawataki na ninyi mmesema Serikali yenu hamtaki kuombwa sisi hatutaki kuomba, mnatuchokoza wenyewe, tembo wenu wanakuja kula mazao yetu, marufuku. Nimeshasema hivyo na mtuelewe, tunaomba mlete chakula kwa sababu tembo wenu ndiyo wamesababisha matatizo yote haya. Hayo ndiyo yaliyonifanya nisimame nizungumze. Wananchi wangu wanataka chakula, kwa sababu kuna njaa iliyosababishwa na Serikali kwa tembo wao kuja kula katika mazao ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko kwa hotuba yake nzuri ambayo inaonesha wanawake tunaweza, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Maghembe kwamba tutakayoyachangia hapa ndiyo atatudhihirishia ule msemo wa Kinana kumwita ni mzigo au lumbesa ni kweli au atudhihirishie hapa yeye ni mwepesi kama tissue.
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. ESTER A. BULAYA: Nasema hivi, kama „tissue’ linakwaza namaanisha „wepesi‟ basi „tissue’ litoke „wepesi‟ libaki pale pale. Atuambie kama yeye ni mzigo au mwepesi. (Makofi)
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kujua, nilipomaliza uchaguzi nilienda Ngorongoro, sikwenda South Africa kama wanavyoenda wengine, kuna mbuyu pale una eneo kama sebule, majangili walitengeneza ndani ya hifadhi ya Tarangire. Nataka kujua, tangu Wizara yake imegundua nchi yetu imepoteza tembo wangapi? Yaani majangili wanaenda kwenye mbuga, wanatengeneza mbuyu unakuwa kama sebule na askari wapo halafu tunaambiwa baadaye ndiyo waligundua. Tunataka kujua waliohusika na eneo hilo walichukuliwa hatua gani? Hilo ni jambo la msingi. Akitujibu hayo, nitajua yeye mwepesi au mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limeongelewa kwenye Kambi ya Upinzani kuhusiana na kampuni iliyopewa kuwinda, Waziri ametoa barua tena wakati Waziri aliyehusika aliinyima. Miongoni mwa waliokuwa Wajumbe kwenye Tume ya Uwindaji jana alipokuwa akichangia Mheshimiwa Nsanzugwanko alisema watu wale walikuwa hawafuati taratibu na inasemekana walishaua mpaka na simba. Sasa ni sababu zipi ambazo Wizara hiyohiyo moja ina maamuzi mawili tofauti kwenye hiyo kampuni inayolalamikiwa haifuati taratibu, huyu ananyima kibali, huyu anakuja kurudisha, kuna kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kimezunguka hapo? Yaani huyo mtu anachezea tu sharubu za Wizara anavyotaka. Tunaposema haya, tunayaongea kwa sababu hatuhitaji Serikali ichezewe na hao mapapa. Haiwezekani Wizara hiyohiyo moja mnakuwa na maamuzi mawili kwenye kampuni moja yaani mnapingana na Tume yenu ya Wanyamapori? Kweli, atujibu mzigo au mwepesi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukichangia humu ndani kuhusiana na mambo ya wakulima na wafugaji. Jimboni kwangu nina hifadhi, wakulima na wafugaji, yote nayahitaji. Kama kiongozi, siwezi nikaja hapa nikasema nahitaji uhifadhi halafu eti najitoa wazimu nasema nawachukia wafugaji, sitakuwa natenda haki. Wala sisemi kwamba napenda wafugaji halafu niseme sihitaji uhifadhi, sitakuwa nalitendea haki Taifa langu. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili hili hawezi akalimaliza kwa kauli, hawezi kulimaliza peke yako, lazima Wizara zote tatu zikae na tukubali kwamba tulikosea, hatukuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alisema kukiri kukosea siyo shida, ni mwanzo wa kujipanga upya. Taifa letu lilikuwa halijajipanga kwa future kwenye matumizi bora ya ardhi. Leo hii ukiwa unatoka Hong Kong ukapanda treni unaenda Guangzhou utaona upande huu ni mashamba ya kilimo na upande huu kuna mashamba ya mifugo, hakuna mwingiliano pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua hatujapanga matumizi bora ya ardhi na hawa wafugaji bado hatujawafatutia soko la kutosha. Tujiulize leo tuna viwanda vingapi? Tunalalamika wengi, tuna mkakati gani wa kuhakikisha wanafuga mifugo ya kisasa na wanapata soko ndani ya nchi yao kuliko kuja hapa kama viongozi tunapasuka humu ndani, hivi tukitoka nje tunaweza kulisaidia Taifa letu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi lazima Mheshimiwa Waziri wa Maliasili akae na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Waziri wa Ardhi ili kuona ni namna gani tunaweza tukalitatua tatizo hili lakini kwa Wabunge kutupiana mpira humu ndani hatuwezi kufika na tusicheze na vita ya ardhi, ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri, hili ni jambo nyeti, jambo linalohusu Taifa letu, kama tumeshindwa kugombana katika uchaguzi, hatuhitaji ardhi yetu ije itugombanishe. Lazima tutengeneze mazingira mazuri ya vizazi vyetu siyo kuja kugombana humu ndani ya Bunge. Sisi ni viongozi, lazima busara itutawale katika kutatua migogoro hii, siyo kwa kauli tu ondokeni, mnakowapeleka kuna malambo au mazingira yakoje? Hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la tozo kwenye hoteli, nilikuwa Mjumbe wa Kamati, naomba jambo hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa muktadha wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther amezungumzia hapa kwamba kuna shilingi bilioni tatu zinapotea lakini tangu kesi ilipokuwa mahakamani Serikali imepoteza zaidi ya shilingi bilioni nane. Leo Wizara hii inashindwa kukazia hukumu wakati Jaji amekuwa mzalendo kwa Taifa lake, kuna nini hapa au hawa watu wenye hoteli bado na wenyewe wanaichezea Serikali wanavyotaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kusisitiza, duniani kote hakuna utaratibu wa double entry, utaratibu ni single entry. Mheshimiwa Waziri, mtalii anaingia akitoka lazima alipe tena, tunaona katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nije Jimboni. Nilizungumzia suala la wananchi wangu kuhusu tatizo la mamba, Naibu Waziri akajibu amekwenda kupeleka swali langu katika Halmashauri ya Wilaya, mimi niko ya Mji ndiyo maana alipewa yale majibu. Mimi mwenyewe ofisi yangu ya Mbunge nimehudumia zaidi ya wananchi wanne Mheshimiwa Maghembe, kuna tatizo hili na nashukuru Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba ataenda kulifuatilia. Peleka tu watu wa kuvua hatujaomba pesa ili wananchi waondokane na tatizo hili la mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wananchi wangu hawataki kuomba chakula. Wanalima lakini tembo wanakuja kuharibu mazao ya wananchi. Hawa nao wameingia kwenye hifadhi? Mheshimiwa Maghembe, please wananchi wa Mara wanaona haya kuomba, tunalima! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa Nyatwali, Tamahu, Serengeti, Kunzugu, Mihale, Bukole, Mihale nilienda na Mheshimiwa Jenista ameona mwenyewe shamba lilivyoharibiwa. Mkasema mtapeleka magari kule hawafanyi patrol, juzi tembo wamekula heka 20, please, tafuteni ufumbuzi wa kudumu. Watu hawafanyi patrol tuone ni namna gani hawa wananchi wataondokana na tatizo la kuliwa mazao yao. Namwomba sana Mheshimiwa Maghembe ashughulikie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wananchi wangu wa Kijiji cha Serengeti, Tamahu, Nyatwari wanataka kujua hatma yao maana wanatishiwatishiwa kuhama. Hawajapewa fidia, hawajashirikishwa na kuna maendeleo kule kuna shule, zahanati na kuna kila kitu. Haiwezekani mtu akaamka tu akawambia leo mnahama bila kuwashirikisha wananchi. Kuna wazee pale wa miaka mingi lazima haya mambo yawe wazi. Wanahama mnawapeleka wapi, kwa fidia ipi, mbona hamjawashirikisha? Hayo ni mambo ambayo nataka anipatie majibu ili nimpime yeye ni mzito au mwepesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Mpango huu muhimu wa leo. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kuwashukuru Wabunge wenzangu wa CHADEMA kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisaidiana hapa Bungeni na nimepata taarifa kuna karatasi zinatembea hapa upande mwingine wa kumchangia mpiga kura wangu Mzee Wassira na mimi Mbunge wake naombeni pia nishiriki kumchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba niende kuzungumzia Mpango…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tunapopanga mipango kama Taifa lazima tupange maeneo yanayogusa watu wengi na katika Taifa letu maeneo yanayogusa watu wengi ni sekta ya kilimo, takribani asilimia 80 ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa miaka mitatu mfululizo tumekuwa tukipanga trilioni 2.7 kwenda katika sekta ya kilimo, lakini zikatengwa bilioni 371, zilizotoka milioni 250 sawa na asilimia tisa, sasa kama tunapanga kutoka trilioni 2.7 kwenye sekta inayoajiri watu wengi tunatoa asilimia tisa tuna dhamira ya dhati ya kumkomboa Mtanzania! Haya ndiyo mambo ya msingi Wabunge wenzangu tujiulize na hasa sisi tunaotoka Majimbo ya Vijijini ambayo yanaitwa Mjini leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipanga hapa huko kwenye sekta ya kilimo tufikie asilimia 10 hatukufika, tukapunguza asilimia sita hatukufika, ikawa asilimia 3.2, leo kwenye sekta ya kilimo iko asilimia 2.3, tunaenda mbele tunarudi nyuma. Tuna mpango kweli wa kuhakikisha hii sekta inaondoa umaskini katika Taifa letu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitatu mfululizo asilimia tisa kwenye sekta inayowaajiri watu wengi, halafu tukija kuongea hapa watu tunapiga bla bla! Please Mheshimiwa Mpango naomba apange na atekeleze kama kazi yake ni kupanga ajifunze na kutekeleza ili haya mambo yaende katika hii sekta nyeti, Watanzania wanufaike nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeangalia katika mipango mbalimbali, Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hapa naongea kama Waziri Kivuli, inadaiwa trilioni saba, kwenye hii mipango sijaona mkilipa. Trilioni sita ziko PSPF, Mfuko ambao hali ni hohehahe, tukisema Serikali mtachangia kwenda kufilisi Mfuko huu, mtajibu nini? Miongoni mwa fedha hizo ni fedha za mikopo takribani miaka 10 hamjalipa, lakini hamna mpango wa kulipa. Serikali inadaiwa mbele, inadaiwa nyuma, inadaiwa kushoto, inadaiwa kulia, lini sasa haya mambo yatakwisha? Hakuna humu katika mpango, jamani hii Mifuko tunatambua kuna mambo ya msingi ambayo inachangia, lakini tunahitaji hii Mifuko isaidie wanachama wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inadaiwa trilioni sita katika Mfuko mmoja ambao tumeambiwa unakaribia kufilisika, huna mpango wa kuonesha unaanza kulipa lini na ni deni la muda mrefu, tunajua deni lingine mlilirithi kwa watu ambao walikuwa hawajaanza kuchangia. Sasa haya mambo lazima tuoneshe kuna mikakati dhahiri ya kulipa, ndiyo kwanza mnapanga kukopa tena, tena ndani trilioni 6.8 wakati tunajua mkiendelea kukopa ndani mzunguko wa fedha unakuwa finyu. Hali ya umaskini ni kubwa wananchi ni hohehahe, uchumi umeshuka, huko kitaa hali ngumu, Wabunge hali ngumu, kila mtu kapauka tu, pesa hakuna. Haya lazima tuyaseme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili naomba nimwambie ukweli, duniani kote kama Waziri wa Fedha hakuwa stable nchi inayumba, hatuhitaji Taifa letu liyumbe. Tunaomba mipango inayopangwa itekelezwe kwa maslahi ya Taifa letu, ni jambo la msingi sana. Leo hii tunazungumzia masuala ya viwanda lakini ukiangalia huku hakuna connection yoyote kati ya sekta ya kilimo, sekta ya viwanda pamoja na Wizara ya Elimu na Wizara ya Mafunzo na Ufundi, hivi vitu vinakwenda sambamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaambia kwenye bajeti tulijua basi leo mngeleta katika Mpango, hakuna. Tukitoka mnasema, tukibaki tukiwashauri mnasema, mnataka nini sasa? Chukueni basi hata haya mazuri maana unajiuliza haya hatukuwepo uchumi umekua! Mikutano ya hadhara mmezuia uchumi umekua! Mmetufukuza Bungeni uchumi umekua! Kwenye mipango mmeshindwa kupanga sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bunge, kama Taifa tunaomba tuweke maslahi ya Taifa mbele tusijiwekee sisi kulinda nafsi zetu wenyewe, tumshauri Mheshimiwa Rais vizuri. Hali ya uchumi haiko vizuri, bandarini kumekauka kila sehemu kumekauka. Tuliongea katika briefing hapa, leo hii Bunge ni aibu ukiangalia kule majani ile green yote imekauka sasa hivi shida kila kona, wananchi wana njaa, Wabunge wana njaa, kila sehemu kuna njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwambia Mheshimiwa Mpango apange na kutekeleza, huko kwenye Halmashauri ndiyo kabisa, yeye asipopanga vizuri, asipotekeleza Wizara zingine na zenyewe hali yake ni ngumu. Kwenye Halmashauri zetu mpaka leo fedha hazijafika, kwangu pale Bunda Mjini kwa sababu nimeamua kuongoza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunda Mjini hata photocopy tu wanakuja kutoa kwenye ofisi ya Mbunge kwa sababu nimeamua kuongoza. Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi; wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kwa moyo wa dhati kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama, mimi mwenyewe, Dkt. Ndugulile ndio tulioanza kushughulikia dawa za kulevya humu ndani kwa kutunga sheria ya kupambana nao, sio kutafuta sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nizungumze yafuatayo, sipingani na watu wanaopingana na suala la kupambana na dawa za kulevya, wale wote wanaotaka kupambana na dawa za kulevya wasimuongopee Rais, tumshauri Rais amteue Kamishna wa chombo cha Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ambacho tulipitisha sheria yake humu ndani na nilisema kabisa nimempongeza dada yangu Jenista Mhagama na Dkt. Ndugulile sisi ndio tulianza huu mchezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tutakapohakikisha hiki chombo kinapata Kamishna kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya, wale mapapa, hao wanaokamatwa sasa hivi waathirika wanatakiwa wapeleke Muhimbili na Mwananyamala wakapate tiba, wale ni waathirika sio kwenda sero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndio nililotaka niliseme na mdogo wangu Makonda akitaka kupambana na dawa za kulevya aende magerezani akakutane na akinamama Leyla atamwambia mapapa ili tuungane wote kwa pamoja na tunamkaribisha katika hili lindi kuhakikisha nchi yetu inapambana vikali dhidi ya dawa za kulevya kwa sababu mimi mwenyewe mdogo wangu anayenifuata yupo Mwananyamala anakunywa dawa methadone. Kwa hiyo, ninachokisema nina uchungu nacho na nimekifanyia utafiti wa kina na nilileta maelezo binafsi katika Bunge hili Tukufu na ninashukuru Mheshimiwa Jenista akalisikiliza alipoingia tu katika hiyo wizara tukaleta muswada na tukatunga sheria nzuri sana ambayo leo hii katika watu watakaokutwa nyumbani kwao wanafunga zile dawa za kulevya kuna fine lakini wanaenda jela zaidi ya miaka 20. Kwa hiyo, tulianza hiyo vita kwa vitendo kwa kutunga sheria kali sio kwa kukamata waathirika ambao wanatakiwa waende wakanywe dawa kama ambavyo inafanyika hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tangu mwaka jana mwezi wa kumi na moja hivi vituo vinavyorudisha watu katika hali yao ya kawaida, hawa waathirika ambao wapo sero sasa hivi, hivyo vituo tangu mwaka jana havijapokea watu wapya. Ningependa kujua kwa sababu gani hawajapokea watu wapya na inasemekana dawa ya methadone haiendi kwa wakati. Lakini pia mkifuata ile hoja yangu binafsi niliiambia Serikali ihakikishe hivi vituo viende nchi nzima, tusiishie Dar es Salaam peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunajua tatizo la dawa la kulevya yanachangia sana katika maambukizi mengine ya magonjwa ya HIV. Kwa mfano, watu tu wa kawaida maambukizi ya ugonjwa wa HIV ni asilimia 5.1; kwa watu ambao wanatumia dawa za kulevya ni asilimia 25 mpaka 50. Kwa hiyo, sio issue ya kuwapeleka waathirika sero, hili janga ni zito. Kwa hiyo, mtu anaetaka kupambana tupambane na mapapa na sio waathirika ambao wanawekwa sero badala ya kuwapeleka katika vituo vya kurudisha katika hali yao ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na haya ni maazimio ya UN ya mwaka 2006 ukitaka kupambana na dawa za kulevya pambana na watu wale mapapa wanaoleta nchini, hilo ndio jambo la msingi. Kwa hiyo, nilitaka niliweke hili sawa; tusifanye siasa katika vita ya dawa za kulevya. Tusimwongopee Rais kwa kutaka kuhakikisha vyeo vyetu, tumwambie ukweli na ili tumsaidie Rais amteue Kamishana wa hii Tume maana tangu tulipoipitisha hii sheria hiki chombo hakina Kamishna. Hilo ndio jambo la msingi ili tuungane kwa pamoja tuhakikishe tunatokomeza vita ya dawa za kulevya hapa katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imesema Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya haina fedha, ni aibu kwa nini hawa watu wengine wasiojua haya mambo wasifanye vitu kienyeji kama hatuwapi pesa za kutosha, tuipe hii Tume pesa ipambane na huu muziki kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Mahakama ya Mafisadi, niliiomba Serikali hizi kesi zinachukua muda mrefu, kuwe na Mahakama Maalum ambayo itashughulika na hii mipapa ambayo wako ndani na haipelekwi mahakamani. Kuwe na Mahakama Maalum inayoshughulika na hizi kesi za dawa za kulevya, hilo ni jambo la msingi sana katika Taifa letu, lakini sio kutafuta sifa na sio kutaka kuhalalisha vyeo vyetu pasipo sababu katika janga ambalo linaharibu kizazi cha watu cha vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie kabisa Waziri anayehusika, hivi sasa hivi wale mapapa wanaoingiza wanataka kuanza kuangalia soko kwenye hizi centre zinazotoa huduma yaani dawa za methadone, wale ambao Serikali imeamua kuwarudisha katika hali ya kawaida wao sasa hivi wanataka kwenda kuwauzia dawa katika vile vituo. Serikali ina mkakati gani ya kuhakikisha hawa watu hawafanyi hivyo? Ni mbaya sana lakini sasa hivi baada ya kuona hii sheria kali na tumeweza kuhakikisha kwenye ile sheria zile kemikali na zenyewe tumeziingiza katika sheria kuwa ni moja ya makosa, sasa hivi zile kemikali hawa vijana wanatengeneza hapa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mdogo wangu Makonda watafute wale vijana wanaotengeneza hizi kemikali tuanze ku-deal nao, wanatengeneza viwanda vidogo vidogo halafu wale waathirika sasa tuwapeleke kwenye vituo tusiwaweke sero. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami kwa moyo mkunjufu, napongeza kwanza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa yale mambo mazuri ambayo yameandikwa na tumeendelea kuyasisitiza, Serikali myachukue myafanyie kazi maana kazi yetu ni kuwashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza Majiji yote na Halmashauri zote zinazoongozwa na Upinzani. Mbali ya ufinyu wa fedha lakini wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana na hiyo inaonesha ni namna gani Watanzania hawakukosea kutupa kura na tunawahakikishia wakiendelea kutupa kura, haya mambo ya kuwaza mawasiliano ya simu, hakuna. Sisi tutawaza flyovers zenye nafasi na underground. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, sasa naomba niende katika Jimbo langu la Bunda. Kwanza, natambua kazi nzuri ambayo inafanywa na TANROADs Mkoa wa Mara, lakini pia nashukuru kwa baadhi ya barabara kwenye Jimbo langu ambalo tayari zimeshapandishwa hadhi, ila tu Mheshimiwa Waziri najua yeye ni mchapakazi na alikuja Bunda. Kuna barabara ambazo hazijapandishwa hadhi katika mwaka huu wa fedha, please, naomba mwakani ziangaliwe ziweze kupandishwa hadhi. Naomba sana, kwa sababu bado Halmashauri yetu ni changa, inahitaji kulelewa na inahitaji support yenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo ni Sazira – Misisi – Kitaramanka, barabara ya Bitaraguru – Kiwasi na barabara nyingine zote hizo tunahitaji zipandishwe hadhi ili ziweze kupitika ili akinamama wanapokwenda kujifungua waweze kupita katika miundombinu iliyo salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie Mfuko wa Barabara. Katika Mamlaka ya Mji wa Bunda, mwaka 2016 tulitengewa shilingi milioni 710 mpaka sasa hivi zilizofika ni shilingi milioni 73 tu. Shilingi milioni 700 ndizo zilizokuwa zimetengwa, zilizofika ni shilingi milioni 73, tutazifanyia nini jamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni asilimia ngapi hiyo? Kumi kati ya 100! Please! Halmashauri yetu ya Bunda ni changa; na ukizingatia kwenye hizi Halmashauri, vyanzo vya mapato Serikali Kuu mmevichukua ambavyo vingesaidia hizi Halmashauri changa kujitahidi angalau basi kukarabati hizi barabara. Hamkuleta pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADs Mkoa wa Mara na wenyewe ni kilio. Mkoa wa Mara barabara zinazokarabatiwa sasa hivi ni vyanzo vya ndani. Kwenye RCC iliyopita, mpaka tuliunda Kamati ndogo kuja Wizarani kudai pesa. Miaka mitatu mfululizo mnachelewa kutupa pesa, Mkoa wa Mara tumewakosea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nazungumzia Majimbo yote; na huu mkoa una historia katika kutafuta uhuru wa nchi yetu. Mara unazungumzia Baba wa Taifa, lakini leo hii Mkoa wa Mara, Makao Makuu ya Mkoa tukizungumza Uwanja wa Ndege, mara mnauweka katika ujenzi wa kiwango cha lami, mara mnautoa. Tatizo liko wapi? Please, tunaomba Uwanja wa Ndege wa Musoma ujengwe kwa kiwango cha lami, biashara ya kuuweka na kuutoa na kuanza kuukarabati kwa kiwango cha changarawe tumechoka. Mara ndege zinakuja, mara zinasimamishwa kwa sababu ya uwanja mbovu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa alianza kuusema Veda one, Veda two karudi. Sasa akaja tena Nyerere One; sasa sijui akirudi tena Nyerere two, ataendelea kuongelea huu uwanja!
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunazungumzia barabara ya Kisolya – Bunda – Nyamswa; barabara ya Nata ambayo inatokea Musoma Vijijini kwenda Serengeti, barabara ya Tarime – Mtomara mpaka Ngorongoro; lakini pia tunataka hizi barabara ambazo zinaenda katika mbuga zetu, kama kweli utalii ndiyo unaongoza katika pato la Taifa, kwa nini sasa tusitengeneza barabara ambazo zinaenda katika hizi mbuga zetu ili watalii waongezeke, Serikali iendelee kupata mapato tuweze kufanya mambo mengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa pia nimeona kwenye kitabu chako, nakupa hongera, barabara ya Tanga – Saadani – Bagamoyo, isiishie kutengewa fedha, zijengwe kwa kiwango cha lami. Barabara ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, kutoka pale Tarangire, zote hizo ziwekwe lami ili utalii wetu ukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nizungumzie tu barabara ya Iringa kwenda Ruaha, zaidi ya kilometa 120, leo hii watu wanashindwa kwenda kule. Mvua ikinyesha wanatumia zaidi ya saa manne na hii Mbuga ya Ruaha ndiyo mbuga ya kwanza Afrika Mashariki kwa ukubwa na ina wanyama wengi. Kwa Afrika ni mbuga ya pili kwa ukubwa, lakini ni miongoni mwa mbuga tano zinazochangia mapato ya Serikali. Sasa kwa nini tunashindwa kuweka lami kwenye hizi barabara ambazo zinaenda katika mbuga zetu ili kukuza utalii wetu? Hilo pia ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie fidia ya barabara ya kutoka Mwanza kwenda Musoma. Katika kipande cha Jimbo langu wananchi wamedai fidia kwa muda mrefu katika kupisha ule ujenzi na tena barabara ndiyo ilifuata nyumba za wananchi, siyo wananchi walifuata barabara, watalipwa lini? Hapa pia nimetumwa na mpiga kura senior, baba yangu Mzee Wasira, ana nyumba yake pale Manyamanyama, mlipeni. Lini sasa mtawalipa hawa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ukarabati wa hii barabara unaendelea, imekwisha, haijakamilika, tayari barabara zimeanza kuharibika. Hivi hawa Wakandarasi mnaowapa tender mnatumia vigezo gani? Kabla tu barabara haijakabidhiwa, tayari kuna mashimo kama mahandaki. Juzi niliuliza swali, hii barabara ya Dodoma, hapa Dodoma Waheshimiwa Wabunge wenyewe mnajua katika maeneo yetu, kila siku zinakarabatiwa. Kule Ununio, barabara ile ya Mbagala kule Dar es Salaam na yenyewe hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuone ni namna gani hawa Wakandarasi wetu wanajenga barabara zenye viwango! Hilo ni jambo la msingi sana Mheshimiwa Waziri. Kama wanashindwa kazi, washughulikieni. Siyo kwamba Wakandarasi wanachezea tu Serikali; mmewapa tender, hawafanyi kazi kama vile ambavyo inatakiwa na fedha za Serikali zinaenda bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni madeni ya Wakandarasi. Barabara nyingi zimesimama kwa sababu Serikali hamjalipa Wakandarasi fedha. Naomba sana… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri achukue, alikuja Bunda, tunahitaji Mkoa wa Mara tupate fedha za kutosha… barabara zetu. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa nishukuru katika Jimbo langu la Bunda kituo cha afya cha Manyamanyama tumepata gari la kubebea wagonjwa, ahsante sana; lakini katika yote usisahau kinahitaji kupandishwa hadhi. Imemshinda mama Anna Abdalah, Mwakyusa na ni sasa ndugu yangu Kigwangalla na Mheshimiwa Ummy dada angu mbali na kazi zote anazozifanya Manyamanyama tunahitaji iwe hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tukizungumza humu ndani tutamsulubu Ummy, tutamsulubu Kigwangalla, lakini wote tunatakiwa tuibane Serikali itimize, Azimio la Abuja la kutenga asilimia 15 ya bajeti ya Serikali Kuu iende kwenye Sekta ya Afya. Hawa hata kama wawe na misuli ya kufanya kazi kiasi gani wasipopewa fedha, hawawezi kutimiza majukumu yao.

Mheshimiwa Menyekiti, hilo ndilo jambo la ukweli lazima tuseme, asilimia 15 na hapa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha upo na wewe na mama unalisikia hilo, lazima uhakikishe Azimio la Abuja na Tanzania tumesaini linatekelezwa, kwa sababu zikitengwa asilimia 15 angalau changamoto ya Sekta ya Afya nchini itapungua na imekuwa ni kubwa; kuna tatizo la madawa, kuna kansa ya uzazi, kuna matatizo ya ugonjwa wa akili ambayo yamesahaulika kabisa. Yote hayo hayawezi yakafanikiwa kama tusipotimiza lile Azimio la Abuja la kutenga asilimia 15 kwenye bajeti kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nchi za wenzetu South Africa, Zambia, kuna mambo ambayo wameyafanya, fedha za dawa na vifaa tiba zinatokana na matumizi ya kawaida, ambazo ni fedha ndani, ni Bunge hili sisi kuamua, taratibu siyo misaafu, tukihakikisha pesa za dawa tunaziweka katika fungu la matumizi ya kawaida, uhakika wa fedha zetu za ndani kwenda katika madawa na vifaa tiba utakuwa mkubwa. Hapa nimpongeze mdogo wangu Upendo Peneza, aliomba kuleta hoja binafsi katika Bunge hili Tukufu lakini hakupata nafasi. Kwa hiyo lazima tubadilishe utaratibu na sisi si wa kwanza, tukifanya hivyo, si tu tutakuwa tumetatua changamoto katika sekta ya afya, tutakuwa tumeokoa vifo vya akinamama na watoto na tutakuwa tumetatua matatizo mengi ambayo yapo katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri Vyuo vya Maendeleo ya Jamii. Kabla Wizara hii haijaunganishwa unakijua Chuo cha Kisangwa Bunda kina matatizo lukuki. Naomba chuo hicho mhakikishe kinapewa fedha za kutosha ili kutatua matatizo yaliyopo. Kingine gari ambalo limechukuliwa kinyume na taratibu, Wizara ilishaagiza gari lile lirudishwe, aliyekuwa Mkuu wa Chuo alijiuzia kinyume na utaratibu na barua ziko Wizarani, hakuna shangingi linalouzwa kwa shilingi laki tano, niliwaambia, naomba wizi huo mimi Jimboni marufuku sitaki nimeshaanza kusafisha. Kama ulikuwa kipindi hicho cha nyuma nimeshaingia mimi, sitaki biashara ya wizi Jimbo la Bunda, ni maendeleo tu. Naomba mambo hayo yote yazingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na ndugu yangu Dkt. Kingwangalla, yeye ni Daktari na tulikuwa wote, back benchers huko. Suala la tatizo la afya ya akili pale Muhimbili, kila siku kati ya wagonjwa 150 mpaka 200 wanaenda pale, zile dawa ni ghali, sasa hivi wanachangia. Ukiangalia moja ya matatizo hayo yapo kwenye kurithi na yanachangia umaskini mkubwa, lakini kitengo hiki kimesahaulika kabisa. Mimi si daktari lakini wanasema matatizo yale kuna stage, lakini sometimes mgonjwa anaruhusiwa kwenda kwa sababu tu hakuna vitanda, hakuna maeneo ya kutosha ya kuwahifadhi wale. Kwa hiyo naomba mlifanyie kazi sana, tuwape…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina jambo dogo tu la kumkumbusha Mheshimiwa Maghembe, kwanza kabla ya yote najua moja ya mambo ambayo yanachangia kutoendelea kwenye sekta ya utalii ni pamoja na miundombinu. Mimi naomba nikuambie ni mtalii mzuri tu hata Easter yangu nilienda kula pale Ruaha National Park.

Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Miundombinu hakikisheni hizi mbuga zetu zinapitika vizuri, barabara mpaka katika maeneo ya mbuga yapitike vizuri ili sasa tuweze kuvutia watalii wengi zaidi. Hilo ni jambo la msingi sana kama tunataka kupunguza kwanza gharama na kuhakikisha kunakuwa na watalii wa ndani zaidi; na wa nje kufika kirahisi katika mbuga zetu za wanyama, hilo ni jambo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende jimboni; Mheshimiwa Waziri nilichangia mwaka jana na mwaka huu narudia, mimi napenda sana uhifadhi, lakini haya mambo yanategemeana na nilisema hatuwezi tukalinda mbuga zetu kwa mtutu. Watu ambao wanaweza wakawa walinzi wazuri ni wananchi wanaozunguka hizi hifadhi. Kule kwetu Mara, jimboni kwangu tuna Mbuga ya Serengeti lakini kila siku tembo wamekuwa wakitoka wakila mazao ya wananchi, wakiharibu nyumba za wananchi na kuua wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hili nimekuwa nikilizungumzia sana. ukienda Kunzugu, Miale, Nyamatoke na maeneo mengine, ukija kule kwa kaka yangu Boni pia jimboni kwake na kwenyewe kuna matatizo hayo hayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niwapongeze Wabunge wa Afrika Mashariki wanawake waliochaguliwa jana, na bila kujali itikadi zetu tukiungana katika mambo ya msingi, tutakuwa tunaitendea haki nchi yetu. Pili, nipongeze kabisa jitihada zinazofanywa na Jiji la Dar es Salaam kwa kudhibiti huo wizi ambao umesemwa na aliyenitangulia chini ya UKAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama ambavyo tumeungana jana na kuweka historia ya kuwapeleka Wabunge wanawake wengi kwenye Bunge la Afrika Mashariki, ninaamini tutaungana tena kuibana Serikali kuhakikisha tunaitendea haki bajeti hii ya maji ambayo ukizungumzia watu ambao wanaumia katika suala zima la kutafuta maji ni mwanamke. Ninaamini tutaacha itikadi zetu pembeni ili tulitendee haki Taifa letu na tuwatendee haki wanawake wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina sababu kubwa za kusema hivi. Waheshimiwa Wabunge mwaka jana zilitengwa shilingi bilioni 937 fedha za maendeleo ni shilingi bilioni 915, zilizotoka ni asilimia 19 tu ya zaidi ya shilingi bilioni 900. Sasa tujiulize tupo kwenye kipindi hiki ambacho leo hii Waziri na Naibu wake shemeji yangu wanaomba tupitishie hapa bajeti. Hiyo asilimia 81 mtaileta lini kuwatendea haki watanzania na wanawake wa Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaposema tunaikataa bajeti naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani si kwamba tunawachukia, si kwamba hatutaki maji, no, tunaitaka Serikali na tunamtaka Waziri wa Fedha aende afanye anavyofanya mkae mjipange upya mjue sasa mtakapopata fedha mtuletee ili sasa sisi wanawake na wanaume wote na Waheshimiwa Wabunge wote ndio tuungane kuipitisha bajeti yenu. Haiwezekani tunasema tuna mkakati wa kuhakikisha tunamtua mwanamke ndoo ya maji kichwani mijini na vijijini, halafu mpaka leo zaidi ya asilimia 81 haijaenda kwenye Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilishasema nitasema ukweli, fitina kwangu mwiko. Nakupenda shemeji yangu na nakupenda mzee wa site, katika hili kwa sababu ninawapenda ninahitaji asilimia 81 mpate Serikali iende ikakae, ikatafute pesa iwape. Kuunga mkono hapa siwezi nikawapaka mafuta kwa mgongo wa chupa, hiyo si desturi yangu mimi. Si desturi yangu na kama mama, kama mwanamke na kama Mbunge wa Jimbo ambaye Jimboni kwangu..., nimesoma kitabu chako umeweka, umetenga hela. Mwaka jana ulitenga na miaka kumi iliyopita huo mradi ulikuwepo yaani leo wana Bunda kama ni birthday ni birthday ya kuanzishwa mradi wa maji kwa miaka kumi bila kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa biashara ya kutenga pesa ambazo hazifiki na kila siku nimekuwa nikisema mkandarasi huyo ni mwizi, amekataliwa Kigoma na Rorya. Mimi nilisema simtaki alienitangulia akawa ananibishia, wananchi wa Bunda wakasema mwana Bulaya jaga, nimekuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi sitaki jimboni kwangu; wizi jimboni kwangu sitaki, silindi wezi, ninachotaka mimi ni maslahi ya wananchi wangu kwanza.

Mheshimiwa Waziri huyo mkandarasi ana madeni mengi, mkiweka hela kidogo badala ya kwenda kufanya shughuli za kukamilisha ule mradi wa maji ambao sasa hivi una miaka kumi haukamiliki, halafu mimi leo nije hapa hata kama nakupenda kiasi gani siwezi kukubali kuja kuunga
mkono wakati wananchi wangu wanaona tu mwaka wa kumi sasa hivi mradi wa maji haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ni changa lakini Mamlaka ya Maji Bunda ni class c, inapaswa kupata ruzuku Serikalini na ndiyo maana wanashindwa kulipa bili ya maji kwa sababu hampeleki fedha kwa mujibu wa taratibu anahitaji kupata ruzuku. Kwa sababu kuna neno kata, wanakata! Nilimuomba kaka yangu nashukuru umenisaidia na baba yangu Muhongo. Neno kata linatumiwa vibaya. Mnashindwa kupeleka fedha wakisikia kata wanakata bila kujua wanaathiri mamia ya wanawake na maelfu ya watanzania kwa kukosa huduma ya maji hicho kidogo ambacho kinapatikana, please! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nadhani kwenye Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani mmeambiwa kuna miradi hewa, nendeni mkaishughulikie kule, mkichelewa mimi nitawaumbua. Nilishasema kule kwa kaka yangu Mheshimiwa Bonny, mradi ule wa Mgeta – Nyangalanga amepewa mtoto wa mpigakura wangu senior, kala milioni 800 haujakamilika wakawa wanalazimisha apokelewe kinguvu, Makalla alikataa wakataka kumtumia DC nikamwambia wewe utaondoka wewe mradi hautapokelewa, haukupokelewa. Shughulikieni hawa wezi, msipowashughulikia nitawaumbua hapa, sicheki na mtu mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wizi Jimboni kwangu sitaki. Mradi wa Mgeta, shughulikieni. Wizi, conflict of interest, unatoa tender kwa mtoto wako, hana vigezo, kakataliwa maeneo kibao mpaka Mtwara kule, ondoeni wizi, nimesafisha mtu sitaki na mtoto wake, nataka mambo yangu yaende vizuri ili wananchi wangu wapate maendeleo kupitia binti yao, Ester ngw’ana Bulaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba sana Mheshimiwa Waziri, mzee wa site na shemeji yangu wa Kantalamba, sana, mbali ya kwamba kuna hii miradi mingine imeanzishwa kama kule Rwabu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Ester Bulaya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kwa moyo wa dhati kabisa kutokana na changamoto za maji nchini, Taarifa ya Kamati imeelezea changamoto kwa kina na Waheshimiwa Wabunge humu ndani wote tunajua umuhimu wa maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 174. Kwanza tu naomba nimwambie ukweli kwa sababu Mradi wa Bunda maji ni kama mtoto wangu niliyemlea tangu nikiwa Mbunge wa Viti Maalum, naujua vizuri sana na kwa sababu nataka kulisaidia Taifa hili, nitasema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, hivyo vituo ambavyo vinasemwa hapa vilivyojengwa ni Nyasura, Balili Msikitini, Balili Stoo na Kunzugu. Makubaliano katika ujenzi wa mradi huu wa maji, vituo vilikuwa vianzie kwenye chanzo cha maji Nyabehu. Hilo halijafanyika na kilichotokea Mamlaka yetu ya Maji Bunda ikaamua kujenga kituo kimoja Nyabehu. Vituo vingine vilivyokuwepo kama Tairo ni kituo ambacho chanzo chake ni ile miundombinu ya zamani, siyo mradi huu mpya, hilo Mheshimiwa Waziri naomba ulizingatie kweli kweli. Mradi huu wa maji Bunda kilikuwa kichaka cha watu kula fedha za Serikali ambazo ni kodi za wananchi kushirikiana na watoto wa vigogo na wewe unajua. Lazima tuseme haya, tunahitaji hii miradi ya maji ikamilike mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani miaka nane tunazungumzia chujio. Kuna habari nimezipata huko Wizarani kwako, aidha mmepigwa au mlikuwa mnataka kupigwa. Chujio la shilingi bilioni tatu mlikuwa mnaambiwa lijengwe kwa shilingi bilioni 12. Tunaipeleka wapi nchi hii? Kweli dhamira ya kumtua ndoo mwanamke kichwani itakamilika kwa ufisadi wa namna hii wakishirikiana na baadhi ya watendaji, ambao wengine mnawatoa Mtwara mnawaleta Bunda, mnawatoa Bunda mnawaleta Wizarani. Wizarani ambapo ndiyo kunasimamia miradi lukuki ya maji, hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mradi wa Maji tu Bunda unachukua miaka kumi na bado haujakamilika ina maana mnahitaji miaka 100 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji katika majimbo kumi, hilo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, huu mradi wa Bunda ni wa muda mrefu sana. Akisimama Mheshimiwa Boniphace atakwambia hivyo hivyo, akisimama Mheshimiwa Kangi atakwambia hivyo hivyo. Hatuhitaji Bunda Mkoa wa Mara kuwa kichaka cha wezi, tumechoka na hili tutaendelea kusema na tunaomba wachukuliwe hatua. Kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi walisema na Ofisi yangu ilitoa ushirikiano na bado baadhi ya wakandarasi na watumishi wengine wanapeta. Wanakula na nani? Please, huu wizi sisi hatuhitaji, tunahitaji miradi ikamilike wananchi wapate huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwako kunahitaji maji, Waheshimiwa Wabunge wote wanahitaji maji katika maeneo yao na hili nasema kwa dhamira ya dhati. Itokee sisi Wabunge na Mawaziri tukatiwe maji miezi mitatu, tu-feel pinch ambayo wananchi wetu wanaipata ya kukosa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kumsaidia mwanamke kutua ndoo ya maji kichwani. Waheshimiwa Wabunge kwa miaka mitatu mfululizo mwaka 2015/2016 fedha zilizotengwa zikapitishwa na Bunge hili ni zaidi ya shilingi bilioni 485, zilizotoka ni shilingi bilioni 136 sawa na asilimia 28. Mwaka 2016/2017 fedha zilizotengwa shilingi bilioni 913, zilizotoka shilingi bilioni 250 sawa na asilimia 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Aprili mwaka huu fedha zilizotengwa za maendeleo ni shilingi bilioni 673, zilizotolewa ni shilingi bilioni 135. Tunaenda mbele, tunarudi nyuma. Ile dhamira ya kuhakikisha mwanamke hatembei umbali mrefu kutafuta maji iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitatu mfululizo! Yaani badala ya kupanda, tunashuka. Asilimia 28, 25, 22, why? Halafu tunakuja hapa tunasema kweli tuna dhamira ya dhati ya kuhakikisha tunamaliza tatizo la maji katika Taifa hili. Kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwenye Majimbo ya Vijijini kwenye mahospitali yetu kuna operesheni hazifanyiki kwa sababu maji hakuna hospitali. Naomba hili jambo mliangalie kwa umuhimu wake. Wanawake wanateseka.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani sasa hivi bora umpelekee mgonjwa ndoo ya maji hospitalini kuliko chakula. Kama wawakilishi wa wananchi hali hii hatutaikubali. Hii figure nimetoa za miaka mitatu mfululizo, nikiwatajia hiyo ya miaka nane ni aibu tupu! Halafu bado tunakuja tunasema tuna dhamira ya dhati, kweli! Hata asilimia 40 tu tumeshindwa kufikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza sekta ya umwagiliaji; tunawahamasisha vijana graduate kwenda kulima kilimo cha umwagiliaji. Mwaka 2015/2016 mahitaji ni shilingi bilioni 400. Bunge hili tulipitisha shilingi bilioni 53 kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Fedha zilizotoka ni shilingi bilioni tano; asilimia 10, shame! Shilingi bilioni tano! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wangu wa Nyatwali wana project kubwa sana ya kilimo cha umwagiliaji; kwa pesa hii inawezekanaje? Wale wa kwa Karukekere kwa Mheshimiwa Kangi, Mgeta kwa Mheshimiwa Boniphace na maeneo mengine! Lazima tuseme haya mambo, hatuwezi kuyafumbia macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zimekosekana, vijana wamehamasika kwenda kuwekeza kwenye kilimo. Kwa pesa hizi! Haya mwaka huu Bunge tulipitisha shilingi bilioni 24, zimetoka shilingi bilioni nne tu kwenye kilimo cha umwagiliaji. Four billion, halafu tunakuja hapa kwa mbwembwe nyingi kwamba tunataka kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Kweli tuko serious? Tunaguswa na maisha ya Watanzania? Tunaguswa na tatizo la ajira la vijana wa nchi hii ambao wameona Serikali haiwezi kuajiri, wameenda kujiajiri kwenye kilimo cha umwagiliaji, kwa pesa hizi tutazigawaje? Hata kama sungura mdogo kiasi hiki, hata mkia hauwezi ukatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine miaka yangu yote nane ya Ubunge nimesikia upotevu wa maji DAWASCO ni ule ule asilimia 47. Ukienda kwenye ripoti ya CAG wamesema walishauriwa kununua chombo ambacho kitasaidia kudhibiti tatizo la upotevu wa maji. Mpaka leo kimya. Wizara yako inasemaje? Au kuna mradi wa watu hapa? Tunataka tujue.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti. Naomba nianze na TANESCO na muda ukiniruhusu nitaenda maeneo mengine. Wabunge tuliokuwa katika Bunge hili kipindi kilichopita na ripoti mbalimbali za Kamati ikiwepo kamati ya Mashirika ya Umma ambayo mimi nilikuwa mjumbe, Mwenyekiti wangu alikuwa Mheshimiwa Zitto Kabwe, tulizungumzia namna gani TANESCO inajiendesha kwa hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani, TANESCO ilikuwa ikipata hasara shilingi bilioni124. Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, TANESCO inapata hasara shilingi bilioni 346. Hasara hizi zinatokana na upungufu wa maji ya uzalishaji umeme pamoja na gharama za uendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hapo tu, Mwenyekiti wa Kamati ametoka kuelezea madeni ya TANESCO ambayo yamepanda kwa asilimia 23 kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani kutoka shilingi bilioni 738 mpaka shilingi bilioni 958. Haya si maneno ya Ester Bulaya, ukisoma ripoti ya CAG na imesema kabisa madeni haya hayana uwiano kati ya mali za Shirika la TANESCO pamoja na madeni. Kwa namna nyingine TANESCO imefilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati haya yanatokea kulikuwa na ushauri wa Kamati yetu chini ya Mheshimiwa Zitto Kabwe ya Mashirika ya Umma na taarifa mbalimbali ya Serikali kulikuwa na mikakati mbalimbali na ambapo nchi mbalimbali pia zinafanya, kwamba, hili Shirika ni wakati muafaka sasa likagawanywa yakawa mashirika mawili. Likawepo Shirika linalo-deal na masuala ya uendeshaji na lingine masuala ya uzalishaji, dunia nzima inafanya. Leo hii tusingekuwa tunaendelea kuzungumzia umeme wa kwenye vibaba wakati tuna-plan kuwa na nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Hong Kong hawasheherekei miaka 50 ya Uhuru wanasheherekea miaka 50 umeme hata siku moja haujakatika kwenye nchi yao. Ni kwa sababu wana mipango mizuri katika uzalishaji na usambazaji. Sisi hatutakuwa wageni, South Africa wanafanya, jirani zetu Kenya wanafanya na hii mikakati ipo kwa nini, Serikali ya Awamu ya Tano hamtaki kufanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mambo haya yanafanyika, hapo sijaenda deni la Standard chartered la Euro zaidi ya milioni 10 na gharama za kesi takribani bilioni 7.5, hilo naliacha wataongea wengine. Wakati haya yanafanyika na hali ya TANESCO ilivyo dhoofu, TANESCO pia inashindwa kukusanya madeni makubwa. TANESCO inaidai hospitali ya Tumaini dola za kimarekani milioni 9.4 sawa na bilioni 18 za Kitanzania na ni kodi ya pango. Tangu mwaka 1998 hawajawahi kulipa. Kulikuwa na kesi Mahakamani TANESCO imeshinda tangu mwaka 2016 na maamuzi ya Mahakama yanasema hivi, waondoke na kisha walipe TANESCO hizi Fedha. Mpaka hivi tunavyozungumza pamoja na maamuzi ya Mahakama TANESCO hawajachukua hatua yoyote pamoja na kuwa mfilisi wanahitaji fedha. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, lakini kingine TANESCO kwa masikitiko makubwa imetoa zabuni kwa mzabuni asiye na vigezo kinyume na mkataba. Masharti ya mkataba yanasema hivi, mzabuni awe na uzoefu wa miaka mitano, lakini sasa huyo mzabuni mwenyewe ana leseni ya kusambaza pembejeo yaani majembe, mbolea, kazi aliyopewa ni ya kusambaza nguzo ya umeme na keshakula dola milioni moja zaidi ya bilioni 2. Mkataba unasema awe na uzoefu wa miaka mitano na hii ni kinyume cha Sheria Na. 3 ya Mwaka 1972 ya Leseni na Biashara. Serikali ya Awamu ya Tano aibu, shame, shame, sasa haya tunayasema kwa sababu tunapenda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati haya yanatokea mikakati ya kushindwa kugawanya TANESCO, mmeshindwa kulisimamia shirika vizuri, mmeshindwa kufuata ushauri uliotolewa na mikakati ya Serikali inashindwa kutekelezwa mnaenda kwenye mambo mengine ya Stiegler’s Gorge ambayo mmeitengea bilioni 700, hizo ni fedha zetu za ndani wakati hizo fedha mngepeleka kuboresha Shirika la TANESCO, mngeligawa mara mbili na pesa nyingine zingeenda kwenye REA. Hapa Mwenyekiti wa Kamati ameeleza wazi, mbali ya kwamba TANESCO inadaiwa, bilioni 700 zimetengwa kwenye Stiegler’s Gorge ambayo hatima yake hatuijui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye REA kwa mwaka huu wa fedha, kwenye fedha zote za maendeleo hiyo Stiegler’s Gorge imetengewa karibia asilimia 40 ya fedha za maendeleo. REA ambayo at least mbali na changamoto zake imefanya vizuri asilimia 20 na bajeti iliyopita REA wamepata asilimia 49. Waheshimiwa Wabunge wote tunajua sheria, fedha zilizowekewa uzio hazipaswi kutumika kwa matumizi mengine. Fedha zinatakiwa zitolewe zote, kufanya hivyo ni kuvunja sheria na ni mfululizo wa Serikali ya Awamu ya Tano kutokutii sheria, amesema pale Mheshimiwa Nape, mnaendelea tena kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitakiwa hizi pesa zitolewe zote, sisi Wabunge tunaotoka mikoani tunajua umuhimu wa umeme wa REA kukamilika. Timizeni wajibu wenu, tuache hizi mbwembwe ndogo ndogo halafu hapa mnasema mnataka kuwa na Serikali ya Viwanda, kwa mtindo huu, kweli? Haiwezekani! Mimi niwaambie baada ya kufikiria miradi mipya una uwezo wa kuacha legacy kwa kukamilisha miradi uliyoikuta ya umeme wa upepo, makaa ya mawe, tukamilishe haya kwanza halafu twende huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo wakati pori la Selou linatangazwa kuwa urithi wa Dunia nchini Qatar na dunia ikakubali kutusaidia kutupa fedha nyingi. Leo tunaenda kukata miti milioni mbili huko kwenye huo mradi halafu nasikia mkiulizwa mnasema ooh, tumechukua eneo dogo, jamani ni kama mwili moyo ni mdogo lakini mwili mkubwa, toa moyo kama binadamu utaishi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu sisi Wabunge ni kushauri na kusimamia Serikali ifanye kazi yake ipasavyo kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo. Tunalipenda Taifa hili, hatuhitaji deni la Taifa liongezeke kwa sababu hakuna mipango thabiti ya kuivusha nchi yetu. Ukiona mpaka wengine tunasema hivi yametuchosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, timizeni wajibu wenu, acheni mbwembwe ndogo ndogo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza kabla sijaanza kuchangia, lazima nisisitize mambo ya msingi na kama Bunge lazima tuvae viatu vyetu katika kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na tabia ya kutofanyia kazi Maazimio ya Bunge na Kamati yetu tumesema, na changamoto inayotokana na kutofanyia kazi maazimio ya Bunge lako tukufu ni kusuasua kwa uwekezaji na utendaji wa mashirika yetu, hilo ni jambo baya sana na inaonesha Serikali hii inalidharau Bunge na tumesema kwenye Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Wabunge wenzangu, kuna suala la Kikanuni hapa kama ambavyo Kamati ya PAC na Kamati ya LAAC inavyofanyia kazi taarifa ya CAG sisi tunafanya kazi na Msajili wa Hazina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea hatujawahi kupewa ripoti na Msajili wa Hazina, hili ni jambo la kikanuni na tulipohoji tukaambiwa taarifa inakwama Wizara ya Fedha, aibu, mnatufanya sisi tushindwe kufanya kazi yetu vizuri kwa niaba ya Bunge kwa kusimamia mashirika na kuja kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na shirika letu pendwa la ndege, ni jambo jema kufufua Shirika la Ndege na hakuna mtu anayepinga. Lakini tujiulize tunafufua wakati gani, tuna mipango gani, kwa malengo gani ya ushindani wa kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika letu la Ndege kwa miaka mitatu mfufulizo wametengeneza hasara ya bilioni 316, mnajua ni kwa sababu gani! Shirika halina mpango wa kibiashara. Kwa nini tusibebe kitimoto, tusibebe mbuzi, tusibebe samaki kwenye ndege ya abiria? Haya mambo hayatutendei haki kama Taifa, kwa mfano, tumewekeza. Kwa mfano trilioni moja kununua ndege, lakini hivi karibuni tumeambiwa shirika letu limeingiza bilioni nne halafu limeenda kufanyia ukarabati ndege mbili kwa bilioni 13. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi tuna upungufu wa marubani, Mwenyekiti wa Bodi alikuja kutuambia kwenye Kamati na ma-engineer yaani hivi ninavyowaambia marubani wa bombadier ndio wanaorusha dreamliner. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani ni kama dereva wa Noah mkabidhi basi la Shabiby abebe abiria, ndio mambo hayo! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Shirika letu la Ndege lakini lazima mambo kama haya yafanyiwe kazi ili Shirika letu liwe na ufanisi, lijiendeshe kibiashara, lakini tuwe na usalama wa abiria wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imewekeza takribani shilingi trilioni 54 kwenye Mashirika ambayo yana hisa kuanzia asilimia 50 mpaka 100, lakini imepata faida asilimia moja tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewekeza trilioni 54 faida kwa mwaka 2017 ilipata bilioni 800 sasa hivi, kwa hesabu za Juni, 2018 faida iliyopatikana bilioni 600 pungufu ya bilioni zaidi ya 200. Hizo bilioni 200 mngenipa bilioni tano ningemaliza mradi wangu wa maji Bunda. Hizo bilioni 200 hapa kila Mbunge ana matatizo lukuki au basi at least mngeenda kupunguza ahadi yenu ya shilingi milioni 50 kila kijiji ambayo hamjaitekeza, tangu muingie madarakani. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Bashungwa, Mheshimiwa Esther taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niu-junior unamsumbua sio type yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililotaka kulisema hapa, tumesema Serikali haitoa mitaji kwenye mashirika mbalimbali. Nitoe mfano, tumeanzisha Benki ya Kilimo, Benki yetu ya Kilimo, lengo kubwa la kuanzisha ni kusaidia wakulima wetu, Benki yetu ili isimame ilikuwa inahitaji Mtaji wa bilioni 800, lakini sasa hivi ina bilioni 60 tu. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge mnakumbuka Kilimo ndio kinaajiri asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania na kuna habari chini ya carpet kwamba benki hii, ambayo ina mtaji, wa bilioni 60 ndio alikuwa amepewa kazi ya kwenda kununua korosho za bilioni 900 wapi na wapi? Aibu haiwezekani na ni kwa sababu Serikali haifatilii mashirika yake haifuatilii vyombo vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na hili pia sijui mnabisha?

MHE. RICHARD P. MBOGO: Taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mbogo.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya taarifa hiyo.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei angesema hiyo pesa, hiyo pesa anayoisema ni mkopo kutoka TIB yaani Benki yenye mtaji wa bilioni 60 unaenda kukopa kuipa bilioni mia mbili naa; na hapa kwenye taarifa yetu tumesema kuna hatari ya benki kufilisika kwa sababu itashindwa kulipa deni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo nataka kusema hapa ni Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kukopa bila kulipa madeni kwa taasisi zake na kusababisha utendaji mbovu wa mashirika TANESCO inadai zaidi ya bilioni mia mbili naa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ripoti yetu utaona JWTZ inadaiwa Bilioni 8…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa muda wako umemalizika Mheshimiwa Ester.

MHE. ESTER A. BULAYA: Ya kwanza eehe.

MWENYEKITI: Ya kwanza eeh, haya Taarifa Mheshimiwa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Na ulinde muda wangu.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei kwa sababu SUMA JKT, viongozi wa Chama cha Mapinduzi wamekopa matrekta na hamjalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, JWTZ inadaiwa bilioni nane, Wizara ya Maji - DAWASA inadaiwa bilioni sita, Wizara ya Afya
- Muhimbili inadaiwa bilioni 2 na maeneo mengine. Lakini tunajua mbali ya madeni, ambayo...

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA:…TANESCO inaidai Serikali, Shirika hili linashindwa kujiendesha, kwa sababu inashindwa kulipa madeni, na hela nyingi zipo kwa Serikali. Serikali inaua Mashirika yake…

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ester taarifa tafadhali, Mheshimiwa Waziri.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndio nimesema moja ya maazimio ambayo hayajafanyiwa kazi kwenye taarifa yetu ya mwaka jana ni pamoja na Serikali kutolipa madeni, hapo sijazungumza madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, takribani…

MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti.

MHE. ESTER A. BULAYA: mmefilisi nyie.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya lazima tuyaseme kwa sababu wazalendo wanasema kwa lengo la kujenga, sisi wengine tusipokufa na ajali, tuna maisha marefu sana, tunahitaji Serikali itimize wajibu wake ili wananchi wapate huduma bora na mashirika yetu yafanye kazi, kwa ufanisi, lipeni madeni, acheni blah blah!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kama Bunge, nafikiri hatuwi wakali vya kutosha. Nadhani mnakumbuka miaka mitatu mfululizo Wizara hii imekuwa ikitengewa pesa kidogo sana, asilimia 18, 19. Bajeti iliyopita tumetenga shilingi bilioni 700 wamepata shilingi bilioni 300, hivi hizi zilizobaki zinafidiwa lini? Leo anakuja tena kuomba shilingi bilioni 600. Lazima Bunge tutimize wajibu wetu wa kuibana Serikali, unless otherwise tutakuwa tunamshambulia Mheshimiwa Prof. Mbarawa wakati Serikali haitimizi wajibu wake wa kupeleka pesa za kutosha katika Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji hayana mbadala, umeme ukikatika leo, unaweza ukawasha kibatari, lakini ukikosa maji huwezi ukatumia maziwa kuoga, huo ndiyo ukweli. Huwezi ukatumia maziwa kunywa, kiu ya maji na kiu ya maziwa ni vitu viwili tofauti. Operesheni hospitalini zinakwama kwa sababu maji hakuna na ukiuliza sababu ni nini, Serikali haipeleki fedha za kutosha katika Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutakuja tutawasulubu hawa Mawaziri lakini pesa haziendi, Bunge sasa tutimize wajibu wetu, tuwe wakali, tuhakikishe pesa zinaenda na hiyo dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani iwe kweli. Sisi tunaotoka majimbo ya mikoani, tunajua akina mama wana- suffer kiasi gani kwa kukosa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninapozungumzia Jimbo la Bunda Mjini, shame. Kuna mradi wa maji pale una miaka kumi na moja haujakamilika yaani mradi wa maji na mwanangu Brighton wamepishana miaka mitatu. Mradi una miaka kumi na moja haujakamilika, Brighton yuko form one ana miaka kumi na nne, ni aibu. Kila siku unakuja kuzungumza kitu hicho hicho, ukiuliza tanki, chujio, chujio gani miaka kumi na moja inashindwa kukamilika watu wapate maji safi na salama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni aibu, tunatesa wanawake, tunatesa akina mama vijijini huko. Wanatembea umbali mrefu wanakosa maji safi na salama. Mheshimiwa Waziri umeenda, naomba sasa usifike mwaka wa kumi na mbili, wananchi wa Bunda wamechoka kupata maji machafu. Hatuna mbadala, hatuwezi kunywa maziwa wakati tuna kiu ya maji, hatuwezi kuoga maziwa wakati tunataka kuoga maji, please. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi mwingine kwenye Kijiji cha Chakung’ombe, Mamlaka ya Mji wa Bunda ni Grade C haipati ruzuku Serikalini, kuna mradi wa shilingi milioni 800 umekamilika. Hata hivyo, kwa sababu Serikali haiwapi pesa mradi umeshindwa kujiendesha, umefungwa na gharama za maji zimepanda, kila siku wananchi wanalalamika. Haya mmeshindwa kukamilisha miradi iwezesheni basi Mamlaka hii iweze kutimiza majukumu yake. Gari haina, hamuipelekei ruzuku, mnategemea nini? Tunawapa stress tu watumishi, stress ya kuongezewa mishahara wanayo sasa wana-stress ya kupelekewa vitendea kazi ili watimize majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaombeni sana Serikali hebu tutimize wajibu wetu na sisi Wabunge tutatimiza wajibu wetu kuisimamia hiyo miradi iwe na tija kwa sababu tunahitaji kumtua mwanamke ndoo kichwani. Tunamtuaje ndoo mwanamke kichwani kama hatupeleki pesa za kutosha? Nawaomba sana Halmashauri yangu ya Mji, Mamlaka ile ya Maji ipewe ruzuku iweze kutimiza majukumu yake, watu wana morali lakini Serikali haipeleki hela, please.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika taarifa za kamati ambazo ziko mbele yetu. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rarmi ya Upinzani kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Hii inaonesha ni namna gani chama chetu kinavyotoa fursa kwa wanawake kushika nyazifa mbalimbali.v
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwenye taarifa ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Mheshimiwa Spika, mosi, ningependa Mheshimiwa Waziri wa Maji akija kujibu anieleze. Mradi wa maji wa Bunda umechukuwa mda mrefu sana, na tatizo kubwa lilikuwa ni ufisadi wa
mkandarasi aliyekuwa anaendesha mradi ule ambao sasa hivi ni takribani miaka 12 na mradi bado haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara mkoa wa mara na akapata taarifa mbalimbali kuhusiana na mkandarasi huyu Nyakirang‟anyi aliyepewa kuhudumia mradi wa maji ambayo chanzo chake ni Jabeu.

Mheshimiwa Spika mkandarasi yule Waziri Mkuu aliamuru TAKUKURU imkamate kuhusiana na ufisadi unaofanyika kwenye mradi wa Bunda. Kama haitoshi Mheshimiwa Rais alifanya ziara Mkoa wa Mara na kwenye Jimbo la Bunda Mjini akaelekeza mkandarasi yule akamatwe na akafunguliwa kesi ya kuhujumu uchumi.

Cha ajabu, mkandarasi yule ameongezewa mkataba tena ili kumalizia mradi Bunda; kwa ajabu. Yaani mtu amefanya madudu yote, Waziri Mkuu amesema Rais ameenda amesema bado tu Wizara mnampa tenda mwizi ambaye tayari mlisha declare wenyewe kwamba huyu mtu ni mwizi na amechelewesha huu mradi. Ilifikia kipindi account zake zote zikafungwa, Wizara kipindi cha Maghembe kikamkopesha pesa mwizi; leo tena mnampa tenda? Kwenye moja ya mkataba wake ilikuwa pia aanze kujenga vituo, hajajenga mpaka sasa hivi; mnamuongezea tena mkataba kwa ajili ya kusambaza mtandao wa maji?

Mheshimiwa Spika, haya si maneno yangu nikiongea kitu nina uhakika nacho nakuona mdogo wangu unatikisa kichwa, nina uhakika nacho.

Mheshimiwa Spika, niliongea na kiongozi mmoja mkubwa Wizarani; akasema tumeona tumuongezee mkataba ili amalize; Mara mia kuvunja mkataba wa wizi mkampa mtu mwingine; alizoiba zinatosha ili wananchi wa Bunda wapate maji safi na salama huu mradi ni wa muda mrefu na kuchelewa kusuasua kwa mradi huu na nyie pia mnapata hasara. Ningependa nipate majibu sahihi kwanini mmerudia kumpa mkataba mwizi ambaye aliwekwa ndani na nyie mnasema ni Serikali safi mnashughulika na mafisadi, huyu fisadi mmemuongezea mkataba tena.

Mheshimiwa Spika, ningependa nizungumzie kidogo suala la pamba. Sisi wananchi wa Kanda ya Ziwa vitu tunavyovitegemea ni uvuvi ufugaji na kilimo cha pamba. Tangu nimeingia Bunge hili huu ni mwaka wa tisa kilio kikubwa cha wananchi wanaolima pamba ambacho Serikali ya Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kutatua ni mbegu, bei, dawa ya kuulia wadudu na kulipa wakulima kwa muda mwafaka; imekuwa ni tatizo kubwa. Kama pamba ingewekewa utaratibu mzuri ingeleta fedha nyingi za kigeni, ingesaidia kumaliza matatizo mengine na kukuza uchumi wa taifa letu; lakini leo zao la pamba limeshuka. Sasa tunashindwa kuweka mikakati dhabiti ya kusaidia zao la pamba alafu tunakuja na maamuzi ya zima moto.

Mheshimiwa Spika, unakumbuka ilivyoletwa mbegu ambayo haina ubora hatima yake Serikali ilikimbizana kulipa fidia ya mabilioni ya shilingi. Kama tungefanya utafiti wa kutosha tukajua mbegu sahihi wakulima wangepatiwa leo tusingekuwa tunazungumza matatizo ya pamba.

Mheshimiwa Spika, kilimo cha pamba kinaanza mwezi wa kumi na moja lakini hivi tunavyozungumza mpaka leo wakulima hawajalipwa. Huyu mkulima anasomesha watoto, huyu mkulima ana mahitaji mengine. Tukileta takwimu hapa za wakulima wanaodai pamba si sawa, hawa nao ni binadamu. Si mnasema ni Serikali ya wanyonge? Wanyonge ni akina nani kama si hawa wakulima wanaotafuta wanaokopa kuhakikisha hawaombi wanatafuta pesa zao kwa jasho na damu? Hivi leo tukizungumzia mkoa wa Simiyu peke yake wanadai takribani billion nne; hapo bado hatujazungumzia Geita hatujazungumzia Mwanza, hatujaenda Shinyanga haujagusa Mara. Lipeni, na msimu unaanza mwezi wa tano. Jamani kama lilivyo zao la zabibu tegemeo kwa Mkoa wa Dodoma, kama ilivyo korosho tegemeo kwa Mkoa wa Mtwara na sisi wananchi wa kanda ya ziwa tegemeo letu ni pamba.

Mheshimiwa Spika, akisimama Mheshimiwa Raphael Chegeni atazungumzia pamba, akisimama Mheshimiwa Richard Ndassa atazungumzia pamba na nikisimama Ester Bulaya nitazungumzia pamba, akisimama Mheshimiwa Gimbi Masaba, akisimama Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki atazungumzia pamba na Mheshimiwa Ester Matiko atazungumzia pamba. Kilio cha pamba kimekuwa kikubwa; inawezekana ninyi Mawaziri hamjui hali halisi iliyoko kule chini.

Mheshimiwa Spika, please fanyeni utafiti wa kutosha msifanye utafiti wa kukurupuka. Fanyeni utafiti wa kutosha, lipeni wakulima kwa wakati ili tuhakikishe zao letu linakua. Kila siku kumekuwa na visingizie lukuki.

Mheshimiwa Spika, hivi vyama vya msingi ni tatizo, kuna rushwa huku. Sasa hivi kumekuwa na malalamiko, na mimi nimepata malalamiko kwenye Jimbo langu Kijiji cha Chagunge. Katibu wa cha msingi amekula pesa ya mkulima takribani milioni tatu.

Mheshimiwa Spika, vilevile havifanyi kazi kwa ufanisi, kuna mazingira ya rushwa. Mtu ili alipwe naye pia lazima atowe kitu kidogo. Tusipokuwa na mifumo mizuri huku juu inaenda kuambukiza uwozo mpaka huku chini, ndiyo maana leo vyama vya msingi navyo havitimizi wajibu wake na havifanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo kwenye suala la mizani kwenye vipimo. Tunajuwa inahakikiwa, tunajua; lakini leo hii mkulima anaenda kupima pamba yake, lets say ameweka kwenye shuka, kapeleka kg 15 anaambiwa hii shuka tu peke yake ina uzito wa kg. 3; ni wizi. Fuatilieni, pamoja na kwamba mmefanya uhakiki bado kuna rushwa ndogo ndogo zinamkandamiza mkulima wa pamba.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna kitu kingine, nimepewa malalamiko kwa baadhi ya watu ambao wanalipwa. Anasema, anaambiwa ameingiziwa milioni 300…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ESTER A. BULAYA: …akienda kwenye akaunti anaziona akitoa anakuta milioni 20 wizi na utapeli ukemewe.

Mheshimiwa Spika, ahsante.