Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe (39 total)

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Asilimia 90% ya wakazi wa Mkoa wa Singida wanategemea maji ya visima ambapo vingi vya pump za mkono na wengine wanachota maji kwenye malambo na mabwawa na hasa maeneo ya vijijini, lakini maji hayo hayakidhi viwango na pia hayatoshelezi mahitaji. Je, Serikali haioni imefika wakati wa kutafuta wawekezaji wakubwa ili kupunguza adha hii ya maji katika Wilaya zote za Mkoa wa Singida na hasa ikizingatiwa Wilaya ya Singida ni wilaya ambayo ina hali ya ukame kijiografia? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sitaki nibishane naye kuhusu takwimu anazosema kwamba asilimia 90% ya wananchi wa Singida wanatumia pump za mkono. Hili ni jambo ambalo kitakwimu itabidi tulizungumze na nitalileta wakati nawasilisha bajeti yangu, atajua ni wangapi wanatumia pump za mkono na wangapi wanatumia taratibu zingine ili kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la msingi ni kwamba katika Programu ya Maji, wa kuamua chanzo cha maji cha kutumia tuliwaachia wao wenyewe wananchi hasa halmashauri kulingana na teknolojia na gharama za mradi, kwa hiyo, maeneo mengi walichagua visima lakini katika programu hii tulikuwa hatutumii pump za mkono. Pump za mkono ni katika miradi ile ambayo inafadhiliwa na wafadhili kama Water Aid na mashirika madogo madogo kama yale au NGO’s, ndiyo wamekuwa wanatoa pump za mikono. Kama Tigo nimekwenda juzi Singida nimefungua mradi wa vijiji 12 kwa pump za mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Programu ya Maji tunatumia aidha ni pump za umeme wa generator au kama kuna grid karibu ndiyo wanaunga, kitu cha namna hiyo. Kwa hiyo, tutajaribu kuangalia, kuna baadhi ya maeneo ambayo wako karibu na mito, tunaweka mradi mkubwa ambao unaweza kwenda kusambaza maji katika vijiji vingi. Sasa ili kusudi Mheshimiwa Mbunge upate jibu zuri, naomba unisubiri nitakapowasilisha bajeti yangu, nitaonesha ni miradi ya namna gani inakuja kwa Mkoa wa Singida kuangalia vyanzo na nini tutatumia.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Njombe - Makete haina tofauti na barabara ya Manyoni - Itigi.
Swali, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara kilometa mbili zilizobaki kutoka njia panda inayokwenda Tabora na ile inayokwenda katikati ya Halmashauri ya Mji Mpya wa Itigi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anakumbuka katika Bunge hili hili tumejibu maswali mbalimbali na maswali ya nyongeza kuhusiana na kile kipande kidogo cha kilomita 8.3 cha kutoka Njia Panda hadi Itigi, Makao Makuu ya Halmashauri mpya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kile ambacho tulieleza wakati tunajibu swali hili hapa Bungeni; kwamba tutakapojenga ile barabara inayokwenda mpaka Rungwa, mpka Makongorosi kipande hiki kitajengwa, na unafahamu kwamba tumeshatenga fedha katika kutekeleza suala hili.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya nina maswali mengine kwake.
Kwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ndiyo tegemeo kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Singida hususan wanawake katika kupata huduma za afya, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Hospitali hii ya Rufaa inapata wataalam na madawa ya kutosha pamoja na vifaa tiba kama MRI, ultra sound na x-ray pamoja na gari la kubebea wagonjwa. (Makofi)
Kwa kuwa tayari kuna jengo ambalo limeainishwa kwa ajili ya kuanzishwa duka la madawa karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kinachokosekana ni fedha za ukarabati wa jengo hilo?
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo ili lianze kufanya kazi mara moja?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
(a) Jibu letu la kwanza ni kwamba Serikali ina mikakati mingi kama ambavyo tulieleza wakati wa kipindi cha bajeti hapa Bungeni, miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza bajeti yetu ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye bajeti hii ya mwaka 2016/2017 kutoka takribani bilioni 26 zilizokuwepo kwenye bajeti ya mwaka uliopita mpaka bilioni takribani 252 kwenye bajeti hii mpya. Kwa hiyo, tukishakuwa na fedha za kutosha tutaweza kukidhi mahitaji ya hospitali zote nchini.
Mheshimiwa Spika, pili tunaendelea kuzishauri Halmashauri na Mikoa yote nchini watumie vizuri pesa wanazopata kutokana na user fees wanazo-charge kwa wagonjwa wakati wanaenda kupata huduma kwenye hospitali, pia pesa wanazopata kutoka kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili waweze kuzitumia vizuri kwa ajili ya manunuzi ya vifaa tiba, kwa sababu tunalenga katika muda mrefu kuhakikisha hospitali zetu za Wilaya na hospitali za Mikoa zinajitegemea zenyewe na ndiyo malengo ya Decentralisation by Devoluton.
(b) Kuhusiana na ukarabati, hili nimuachie Mheshimiwa Mbunge akashauriane na Katibu Tawala wa Mkoa wake, waone ni namna gani wanaweza wakafanya ukarabati wa hospitali hii wa jengo hili la theater na maabara na vitu vingine.
Mwisho nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wote kwamba katika mwaka huu unaoendelea tuna mradi mkubwa wa vifaa tiba unaoitwa ORIO ambapo tutaweza kupata vifaa kama MRI, CT Scan, ultra sound na x-ray machines ambavyo amevitaja Mheshimiwa Mbunge na tutavigawa kwenye hospitali mbalimbali nchini.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu. Nataka tu kuongeza sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe kwamba ni lini tutapeleka wataalam.
Mheshimiwa Spika, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi karibuni tutaanza kutangaza nafasi kwa hiyo tutapeleka wataalam katika hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili tumekubaliana kwamba tunataka kuzifanya kweli hospitali za Rufaa za Mikoa ziwe Hospitali za Rufaa kwa hiyo tumetangaza nafasi tutafundisha wataalam watano katika kila Mkoa kwenye masuala ya usingizi, magonjwa ya akina mama, magonjwa ya watoto, upasuaji na mifupa.
Kwa hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha Madaktari walio katika mikoa yao walete maombi, hatutampeleka mtu ambaye hatoki katika hospitali hizi za Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.(Makofi)
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo la Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ni sawasawa na matatizo yanayoikabili Hospitali ya Rufaa ya Singida. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiboresha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ikiwa ni pamoja na kuipatia watumishi wa kutosha, vifaa tiba kama X-Ray na kufanya ukarabati mkubwa wa majengo ya hospitali hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ili pia kutowasimamisha Waheshimiwa Wabunge wengine, kupitia Mradi wa Orion kama nilivyosema tumetenga shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kununua vifaa tiba, hasa vifaa vya uchunguzi katika Hospitali za Rufaa ikiwemo Sekou Toure na Singida Regional Referal Hospital, Iringa Regional Referal Hospital na Musoma Regional Referal Hospital. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa hawa wanaotoka katika mikoa hii wasisimame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kwamba ni lini sasa tutaweza kupeleka watumishi wa kutosha, kama nilivyosema tumeomba kibali cha kuajiri watumishi 30,000 katika sekta ya afya na tumeruhusiwa kuajiri watumishi 10,000. Kwa hiyo, mara taratibu zitakapokamilika, basi tutaweza pia kupeleka Madaktari Bingwa na watumishi wengine wa sekta ya afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Miradi ya maji iliyopangwa kutelekezwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini ya ukarabati wa miundombinu ya visima ya Sagara, Mdilu, Ihanuda na Mwasawiya pamoja na ile inayotumia pampu za mkono ya Vijiji vya Muhamo, Mkimbii, Mwanyonye, Mitula, Mwakiti, Ndugwire, Gauri na Kinyeto haijatekelezwa mpaka sasa na hii ni kutokana na ukosefu wa fedha:-
Swali; ni lini na wakati gani fedha zitaletwa kukamilisha miradi hii? Je, ni lini Serikali itawatua ndoo wanawake wa Mkoa wa Singida?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aysharose swali la nyongeza, unauliza moja tu. Kwa hiyo, chagua kati ya hayo maswali, unalotaka ujibiwe.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Je, ni lini na wakati gani fedha zitaletwa kukamilisha miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya visima Singida, nimeeleza katika Bunge hili kwamba kuanzia sasa hivi Serikali haitapeleka fedha kwenye miradi ya maji kabla miradi haijatekelezwa. Kinachotakiwa ni kwamba lazima kwanza ulete certificate ili tuwasilishe Hazina kuomba fedha tuweze kuzileta.
Swali lake, ni lini fedha zitaletwa? Fedha tutapeleka kulingana na upatikanaji wa fedha katika Serikali na nina hakika kwamba mwaka wa fedha unaokuja, akituletea certificate kuhusu hivi visima, kwa vyovyote vile fedha tutapeleka.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililopo katika Mkoa wa Rukwa halina tofauti na tatizo lililopo katika Mkoa wa Singida.
Swali; je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Hospitali za Wilaya za Mkoa wa Singida na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inapata vifaa tiba vya kutosha kama vitanda vya kujifungulia ili kuwasaidia wanawake wajawazito ambao hutumia muda mrefu wa kutembea kufuata huduma hizo za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Mheshimiwa Aysharose atambue kwamba, mimi kama daktari na kama baba wa wanawake na kama mume wa mwanamke, nina passion ya kipekee na mambo yote yanahusu wanawake na ndiyo maana nikapewa jina la Balozi wa Wanawake. Kwa msingi huo, toka nimeteuliwa kwenye nafasi hii, nimezunguka kwenye zaidi ya vituo 120 vinavyotoa huduma za afya nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara zangu nimekuwa nikihamasisha ujenzi wa theatre na maabara ambazo zitakwenda kuboresha huduma ya mama na mototo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini. Hivyo, namhakikishia kwamba vifaa tiba ni sehemu muhimu ya mpango huu ambao tumeuanzisha wa kuboresha huduma za upasuaji na huduma za akinamama wajawazito kwa ujumla wake. Kwa hiyo, Mkoa wa Singida nimeshafika mara mbili toka nimeteuliwa na katika ziara zangu nimekuwa nikihamasisha mambo haya yatekelezwe na Halmashauri zenyewe, maana mpango huu siyo wa kwetu.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi wa Wilaya ya Singida Vijijini wanataabika sana kutokana na shida kubwa ya maji na matumaini yao waliweka katika ukarabati wa miundombinu ya maji ya visima inayogharamiwa na chanzo cha fedha cha LCDG ambapo fedha hizo hazijaletwa hata senti moja kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa, miradi hiyo inahusisha Vijiji vya Mughamo, Sagara, Kinyeto, Mkimbii, Kihunadi, Mwanyonye…

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Kijota na Semfunga: Swali; je, Serikali itapeleka lini fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 300 ili kuvikarabati visima hivyo na kuondolea kero wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mji wa Itigi ni miongoni mwa miji midogo inayokua kwa kasi sana na ni Makao Makuu ya Jimbo la Manyoni Magharibi, lakini mji huu hauna kabisa mtandao wa maji: Je, sasa Serikali ipo tayari kutenga fedha za kutosha kwa mwaka ujao wa fedha, 2017/2018 ili kuwawezesha wananchi wengi kupata maji safi na salama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto kubwa ya maji katika Wilaya ya Manyoni, ni ombi…

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Matembe, hoja yake anayoizungumza katika Bunge siyo hapa tu; ananifuata ofisini, tukikutana huko mtaani, anazungumzia kuhusu maji Singida. Tumeshaongea kuhusu mikakati yote itakayohakikisha kwamba Mkoa wa Singida sasa matatizo ya maji tunayakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza awali, ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji tuliamua kuhakikisha kila Wilaya tunaipatia fedha ili pamoja na miradi mikubwa ambayo inatekelezwa moja kwa moja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Halmashauri pia ziweze kutekeleza miradi kwa kujipangia wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Itigi; napo tumefanya utaratibu huo huo, lakini pamoja na hilo, Itigi tumekamilisha ujenzi wa Bwawa la Itagata ambalo litahudumia kilimo, lakini pia Halmashauri inaweza ikaona uwezekano kama maji yanatosha, basi yaweze kusambazwa kupelekwa na kwa matumizi ya majumbani.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika uanzishwaji wa viwanda ili kuzalisha ajira za kutosha kwa vijana, je, Serikali ipo tayari sasa kuupa Mkoa wa Singida kipaumbele cha kwanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili. kwa kuwa Tanzania tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda: Je, ni lini sasa
Mfuko huu wa SME Credit Guarantee Scheme utaletwa Singida ili vikundi vya wanawake na vijana viweze kunufaika na mfuko huo? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Aisharose maswali yake mawili ya nyongeza na nianze na hili la pili ambalo ni rahisi. Mfuko wa SME Guarantee Scheme umeshafika Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema kwa sababu yeye anashughulika na akina mama na vijana,
namuagiza Meneja wa Singida awasiliane na Mheshimiwa Mbunge, halafu namuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO wawasiliane, zile mashine zinazotengenezwa na TEMDO huyu mama ndiye awe mhamasishaji wa kuwaonesha watu namna gani wakope. Tumeshusha riba mpaka 17%. Mashine ya kwanza Singida uanze nayo wewe, utembee kijiji kwa kijiji ukiwalenga vijana na akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi ni kwamba Singida tayari wako kwenye
uchumi wa viwanda. Tumeshatenga maeneo ya kujenga viwanda na Mbunge wa Singida, Mheshimiwa Kingu,
anajasiria kupitia e-scheme, mradi wa kiwanda cha maziwa.
Kwa hiyo, Singida viwanda siyo jambo geni, tunahangaika Singida kwenye viwanda kuona ile malighafi ya saruji kama tunaweza kutengeneza kiwanda angalau cha ku-blend saruji kutafuta crinker na kuchanganya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuwe wote, Singida wako kwenye viwanda.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa miundombinu na hasa barabara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo; je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hii kutoka Ilongero Mudida, Kungi Kidarafa hadi Haydom kutoka kilomita 1.6 ambazo zinajengwa kwa sasa kwa mwaka hadi kufikia kilomita tano ili kuharakisha ujenzi huo na kufungua fursa za kiuchumi kwa mikoa ya Manyara, Arusha na Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ni viongozi wa chama changu ndiyo walitoa ahadi hii nina imani kubwa na Serikali ya chama changu chini ya Jemedari Dkt.John Pombe Magufuli. Je, Waziri yuko tayari sasa kufanya ziara ili kujionea hali halisi ya barabara hii na kuona sehemu iliyofikia ili kuwajengea upya imani wananchi wa Wilaya ya Singida Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ni muhimu sana na kama tulivyoeleza inaunganisha mikoa miwili ya Singida na Manyara; na pale Haydom pana mambo mazito sana ukitoka Haydom unaenda kwenye ile hospitali kubwa ambayo tunategemea sana watu wa maeneo yale kuanzia Singida mpaka Manyara yote. Kwa hiyo, umuhimu wake tunaufahamu na kwa sababu hiyo tutaangalia kuongeza kasi ya kujenga barabara hii kadri tutakavyokuwa tunawezeshwa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge mimi barabara ile nilipita lakini bahati mbaya katika ziara zangu huwa naangalia kazi tu; lakini kwa sababu ni vizuri vile vile kwenda kufanya ziara pamoja na Wabunge, nitaangalia muda mwingine nitakapokwenda katika barabara hiyo nimhusishe na Mbunge ili na yeye ajue kwamba huwa napita katika barabara hiyo. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa wanannchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki wanategemea maji ya mabwawa na visima na kwa muda murefu sana wamekuwa wakitaabika na kero kubwa ya ukosefu ya maji safi na salama. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Jimbo la Manyoni Mashariki linapata maji safi na salama kwa uhakika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa program ya maji hapa nchini na tumeanza awamu ya pili Julai mwaka huu 2017. Tumeweka utaratibu wa kutenga fedha kwa kila Halmashauri ili zenyewe zihakikishe kwamba zinabuni na kutekeleza miradi ya maji. Zaidi ya hapo, kuna bwawa kubwa tumejenga katika Halmashauri ya Manyoni Mashariki ambalo lile litafanya kazi mbili, moja ni umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga, lakini pili litasaidia katika maji ya matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wala asiwe na wasiwasi, tunaendelea na utelekezaji kuhakikisha kwamba wananchi wa Manyoni Mashariki wanapata maji. Nimshukuru kwa sababu yeye ni mama wananchi wake wa Singida anawapenda ndiyo maana anawatetea. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa malengo makuu ya kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake ni kumkomboa mwanamke wakiwemo wanawake wa Mkoa wa Singida. Swali la kwanza, je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha dirisha maalum la wanawake kwenye benki ambazo inamiliki hisa kama NMB ili kuwawezesha wanawake wa Mkoa wa Singida kupata mikopo nafuu wakati Serikali ikiendelea kujipanga?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wanawake wengi wamejikita katika shughuli za ujasiriamali lakini hawana dhamana za kukopa; Je, Serikali inatoa maelekezo gani kwa SACCOS na benki binafsi ili kuwawezesha wanawake wengi kupata mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mwaka huu akinamama wa Singida wana bahati kwa sababu tunaanza hatua ya awali ya kufungua kituo cha kutolea huduma za Benki ya Wanawake. Singida ni katika mikoa mitatu ambayo tumeamua kuwekeza mwaka huu. Sambamba na mkakati huo tulionao, wazo lake tunalichukua, kwamba Benki yetu ya Wanawake Tanzania iangalie uwezekano wa kufungua madirisha maalum kwenye benki mbalimbali ambazo zipo katika maeneo mengi zaidi nchini. Ni wazo zuri, tunalichukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie, teknolojia ambayo imeingia sasa hivi kwenye huduma za kibenki hapa nchini ya kutumia mitandao lakini pia ya kutumia simu za mkononi, nayo itatusaidia kuwafikia Watanzania wengi zaidi na huduma za kibenki na hata huduma za kimikopo huko tunakoelekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tuna management mpya ya Tanzania Women’s Bank ambayo imeanzisha mazungumzo na wenzetu wa TTCL pamoja na wa Halotel kwa ajili ya kutengeneza mifumo ya kibenki ambayo inatumia simu za kiganjani ili kuwafikia wananchi walio wengi zaidi na mikopo pamoja na huduma mbalimbali za kibenki katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu SACCOS na benki binafsi; tunazishauri ziendelee kufanya kazi kwa ukaribu na wataalam wetu wa Benki ya Wanawake Tanzania ili waone ni namna gani wanaweza wakashirikiana kwa pamoja kuwahudumia wanawake ambao ni wajasiriamali.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana ndiyo kundi muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa letu, je, Serikali ina mpango ganiwa kuwapatia vijana nchini wakiwemo wa Mkoa wa Singida vitendea kazi na mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha kujikita katika shughuli za ujasiriamali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina Maafisa Maendeleo vijana kote nchini lakini maafisa hawa hawana vitendea kazi kuweza kuwafikia vijana wengi walioko vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Maafisa vijana hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aysharose kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutetea maendeleo ya vijana katika Mkoa wa Singida na mimi binafsi nimeshuhudia kwa sababu alishanialika kuwa mgeni rasmi kwenye mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana wa Mkoa wa Singida. Naomba aendelee hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi hatuna shida ya kuwasaidia vijana wetu vitendea kazi na mikopo na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu ni ofisi ambayo inasimamia suala zima la uwezeshaji wananchi kiuchumi, kama nilivyosema tunayo mifuko 16 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na mimi, tutaendelea kumuelekeza jinsi ya kufanya pamoja na kutumia mfuko wa maendeleo ya vijana kutoka katika Halmashauri zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ni kwa kiasi gani tutawasaidia Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweza kusimamia shughuli za maendeleo ya vijana. Ni hivi juzi tu Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alinialika na tulianza kikao cha kwanza cha kuwapa nguvu na kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii nchi nzima. Tutaendelea kufanya hivyo kwa Maafisa Vijana pia katika nchi nzima ya Tanzania. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo Mtwara halina tofauti na tatizo lililopo katika Jimbo la Singida Kaskazini. Vijiji vingi vya Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo vilikuwa katika Mpango wa REA II mpaka sasa havijapatiwa umeme. Vijiji hivyo ni Mrama, Madasenga, Mipilo, Meria, Mitula na Msange. Kwa kuwa sasa tunaelekea kwenye Tanzania ya Viwanda; je, ni lini sasa Serikali itavipatia vijiji hivyo umeme ukizugatia kwamba tupo katika Mpango wa REA III? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida mkandarasi ambaye alipewa kazi alikuwa na jukumu la kukamilisha masuala ya mikataba. Taratibu za mikataba amekamilisha juzi, siku ya Ijumaa, na hivyo ataanza kuingia site kuanzia Ijumaa wiki hii, kwa hiyo wananchi wa Singida na maeneo mengine watapata mkandarasi huyo.
Lakini cha pili Singida tunawapatia mkandarasi aliyeshindwa kukamilisha kazi katika REA II, Kampuni ya SPENCON iliondolewa kwa hiyo, tunawapa mkandarasi mwingine. Kwa hiyo, Mkoa wa Singida utapata wakandarasi wawili pamoja na mkandarasi wa REA III.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililoko Iramba Mashariki halina tofauti na tatizo lililoko Singida Kaskazini, Manyoni Magharibi, pamoja na Jimbo la Ikungi. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwa vijiji vilivyobaki ambavyo vilikuwa katika mpango wa REA II, ukizingatia sasa tuko mpango wa REA III, ili wananchi wa maeneo hayo waweze kunufaika na Sera ya Viwanda? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza sana Mheshimiwa Aisharose kwa swali lake zuri. Naomba nimtaarifu tu katika maeneo ambayo ameyataja, Singida Kaskazini, Manyoni Magharibi, Ikungi, Mkandarasi ambaye anaenda kufanya kazi hizi zilizoachwa na Mkandarasi Spencon ameshateuliwa ambaye ni Emek Engineering and Dynamic na System Company Limited. Kwa hiyo, wako katika mchakato wa kumalizia tu masuala ya manunuzi ya kutoa Performance Bond, lakini kazi itaanza muda siyo mrefu na kwamba vijiji vyote ambavyo viliachwa awamu ya pili vitapatiwa umeme. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuniona. Tatizo lililopo Ruangwa halina tofauti na tatizo lililopo Manyoni Magharibi, kwa kuwa sasa kuna Sera ya Madini inayotaka kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo wa madini ruzuku.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa ruzuku kwa wajasiriamali wachimbaji wa gypsum wa Wilaya ya Itigi ili kuongeza uzalishaji na hata kuanzisha viwanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa Matembe, Mkoa wa Singida na hasa katika maeneo ya Itigi kuna maeneo mengi sana ambayo kuna madini ya dhahabu na katika maeneo hao kwa mwaka jana tumepatia ruzuku wachimbaji wadogo 32, lakini tunaendelea pia kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mbunge kushirikishe tu, tutakapofikia hatua sasa ya kugawa ruzuku nyingine awamu ya tatu ambayo ipo kwenye maandalizi tutakushirikisha na tunatarajia kuanzia mwakani taratibu zikikamilika tutaanza kukamilisha utaratibu mwingine wa kuwapatia ruzuku pamoja na mikopo. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Singida wametaabika sana na kero kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu sasa. Je, Serikali haioni imefika wakati muafaka wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Igunga hadi Mkoa wa Singida ili kuwaondolea wananchi wa Mkoa wa Singida kero hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe ni mama na unawapenda akina mama na unajua jinsi wanavyopata shida ya maji. Mkoa wa Singida ni miongoni mwa Mikoa ambayo haina vyanzo vya uhakika vya maji na mabwawa yaliyopo kama Kindai, Lake Singidani yote yana maji ya chumvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa mawazo mazuri na sisi tunawaza hilo. Kupitia mradi wa maji wa Ziwa Victoria sasa tunafikisha maji Igunga tunafikiria kwamba tufanyeje kuyatoa pale Igunga tupandishe Mlima Sekenke ili yaje mpaka Singida. Hayo ni mawazo namba moja ambayo na sisi tunayapokea, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba tutayafanyia kazi. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa takwimu zinaonesha Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni na moja ya sababu ni kutokuimarishwa kwa elimu ya uzazi wa mpango.
Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuanzisha kampeni ya kitaifa ili kuwawezesha wanafunzi na hasa wa kike kuanzia shule za msingi hadi sekondari kuweza kujitambua na kuepukana na mimba za utotoni? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa hospitali za Mkoa wa Singida pamoja na vituo vya afya vina uhaba mkubwa wa wataalam na vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hospitali na vituo vya afya vya Mkoa wa Singida vinapatiwa wataalam na vifaatiba vya kutosha ili kuziwezesha hospitali hizo kufanya kazi kwa ufanisi na kuokoa vifo vya akinamama wajawazito na watoto? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Matembe kwa kuwa mpiganaji mkubwa sana wa masuala ya afya ya akina mama na watoto katika Mkoa wa Singida na kwa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba tuna changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni na takwimu ambazo tunazo zinaonyesha kwamba wastani wa asilimia 27 ya vijana ambao wapo kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha, wameshapata watoto au ni wajawazito, hii idadi ni kubwa sana na baadhi ya Mikoa inakaribia asilimia 50. Kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mkakati na Wizara tumeanzisha kampeni inayoitwa “Mimi ni Msichana, Najitambua, Elimu Ndio Mpango Mzima.” Hii kampeni tayari tumeshaizindua na inaendelea kusambaa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ndani ya Wizara sasa hivi tunakamilisha kuandaa mkakati wa afya ya uzazi kwa vijana, ambao itatoa dira na mwelekeo wa nini tunahitaji kufanya hususan katika yale maeneo ambayo mimba za utotoni zimeshamiri. Sambamba na hilo, tumeanzisha club katika maeneo mbalimbali hususan katika shule za sekondari kuwajengea uwezo vijana wetu hususan mabinti wa kike kujitambua na kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya kutosha kuhusiana na elimu ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, tafiti zimethibitisha kwamba tunapomnyanyua mwanamke kiuchumi vilevile tunazuia uwezekano wa wale mabinti kupata mimba za utotoni, sambamba na hili kuna miradi ambayo tunaifanyia upembuzi yakinifu sasa hivi ambayo itatoa fedha kidogo kuwajengea uwezo wale mabinti especially wale ambao wapo nje ya mfumo wa shule kuweza kujikimu kimapato na hii ni moja ya mkakati ambao tumeuona umekuwa na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha tumeweza kuongeza bajeti ya mpango wa afya ya uzazi kutoka shilingi bilioni tano mpaka shilingi bilioni 18. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza nini mkakati wa Serikali kuongeza wataalam na vifaatiba. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaatiba ni bilioni 269 na nimeongelea hapa bajeti ambayo tumeiweka katika family planning kutoka bilioni tano mpaka bilioni 18. Tatizo siyo fedha, tatizo niwaombe Waheshimiwa Wabunge watusaidie ni kuwahimiza waganga wetu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba wanaagiza vifaa na dawa ambazo zinahusiana na masuala ya uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni tabia ya baadhi ya watoa kutoagiza vifaa hivi kwa sababu wanaona kwamba havina tija au havitoki haraka katika hospitali zao, lakini ni sehemu ya tiba muhimu na dawa muhimu sana hususan katika upande wa uzazi wa mpango, lakini Serikali itaendelea kutoa elimu hiyo na kuhamasisha watoa huduma kuhakikisha kwamba wanaagiza dawa hizo na sisi kama bohari ya dawa tunazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kweli tumekuwa na changamoto ya uhaba wa watumishi na tunaamini kwamba kadri vibali vinapopatikana tutakuwa tunaongeza wigo wa watoa huduma katika hospitali hizi. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Morogoro Mjini halina tofauti na tatizo lililopo Manyoni Magharibi. Wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika na kero kubwa ya ukosaji wa maji safi na salama na maeneo yaliyoathirika ni Itigi Mjini, Songareli, Mlowa, Tambukareli, Majengo na Zignal.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi maji safi na salama na kuwatua ndoo wanawake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na si mara moja amenieleza kuhusu suala hili, mambo mazuri hayataki haraka. Kwa kuwa sisi Wizara ya Maji si Wizara ya ukame tarehe 7 Mei, 2018 tunawasilisha bajeti yetu ya Wizara ya Maji; kwa hiyo namuomba sana tuwe katika suala zima la subira na subira yavuta heri, heri itapatikana katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. Ahsante sana, itatekelezeka. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa hospitali hii inahudumia wagonjwa wengi kutoka Mkoa wa Mbeya, Singida na Tabora lakini ina Madaktari Bingwa wachache; Madaktari Bingwa waliopo ni wanne tu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha hospitali hii inakuwa na Madaktari Bingwa wa kutosha ili kutoa huduma bora kwa wakati wote?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa gharama za hospitali hii ya Mission pamoja na gharama nyingine za hospitali za binafsi ni kubwa sana ambapo wananchi wa kawaida hawawezi kumudu. Kwa mfano, mama anapoenda kujifungua anatakiwa kulipa Sh.150,000 kwa kawaida lakini anapojifungua kwa operesheni anatakiwa kulipa Sh.450,000. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wilaya ya Itigi inapata Hospitali ya Wilaya? Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la kuwepo Madaktari Bingwa wa kutosha, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba wanapatikana ili waweze kutoa huduma. Hivi karibuni Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeweza kutoa tangazo kwa ajili ya Madaktari. Naamini katika wale ambao watakuwa wameomba na Madaktari Bingwa watapatikana kwa ajili ya kuwapeleka maeneo kama hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na swali hili limekuwa likiulizwa mara kwa mara na Wabunge wa Mkoa wa Singida, mnamo tarehe 7 mwezi huu swali hili liliulizwa na leo linaulizwa kwa mara ya pili. Kwa hiyo, inaonyesha jinsi ambavyo wanajali wananchi wao katika suala zima la afya.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na gharama za matibabu ambazo zinatolewa na hospitali hii na hospitali zingine binafsi, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi tunatarajia mwongozo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sababu Serikali inawekeza pesa zake, kuwe na bei ambazo wananchi wanaweza kumudu.
Mheshimiwa Spika, amechomekea na swali lingine kuhusiana na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi, naomba nimhakikishie ni azma ya Serikali baada ya kuwa tumemaliza hizi hospitali 67, katika maeneo yote ambayo hakuna Hospitali za Wilaya Serikali itaenda kujenga.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Singida unakua kwa kasi na majanga ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara, yakihusisha makazi na pia vile vile kwenye barabara kuu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuupatia Mkoa wa Singida gari la kisasa la zimamoto ili kuokoa maisha na mali za wananchi wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa gari la zimamoto lililopo ni bovu na halikidhi mahitaji; na ili kutoka Singida Mjini hadi kufika Wilayani Iramba, Manyoni, Mkalama na Ikungi kuna umbali mrefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipa kipaumbele Wilaya hizi kwa kuzipatia magari ya kisasa ya zimamoto? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni mpango gani wa Serikali wa kupeleka magari Singida pamoja na wilaya nyingine ambazo inazunguka; ni kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, kwamba, kwanza tutahakikisha tunafanya ukarabati wa lile gari bovu haraka iwezekanavyo pale tu fedha itakapopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika bajeti yetu mwaka huu tumepanga kununua gari tano, kwa hiyo tutaangalia Singida kama ni mmoja wa Mkoa wa vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kama ambavyo nimesema, ule mchakato wa kurekebisha sheria utakapokuwa tayari nadhani itasaidia sasa Halmashauri za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Singida kuweza kuchangia katika kununua magari haya yaweze kusaidia katika wilaya za nchi nzima.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Singida ni wakulima wazuri wa zao la alizeti, je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kulifanya zao hili la alizeti kuwa ni zao la kimkakati ili kuongeza tija na kipato kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la alizeti ni moja ya zao la kimkakati. Kama unavyofahamu kipaumbele cha kwanza cha Serikali ni mazao ya chakula na alizeti ni moja ya mazao ya chakula. Kwa hiyo, lipo kwenye zao la kimkakati na ndiyo maana lipo chini ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Mbulu Vijijini Iinafanana kabisa na tatizo lililopo Iramba Mgharibi. Vijiji 13 vya Jimbo la Iramba Magharibi hadi sasa havijapatiwa umeme. Baadhi ya vijiji hivyo ni Kisua, Tieme B, Kisonso, Makunda, Twinke, Tulya, Meli na Kisiriri.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme katika vijiji hivyo ili kuyawezesha makundi ya wanawake na vijana kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe kuhusu masuala ya REA katika vijiji vyake 13. Kwanza naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mkoa wake wa Singida umepata vijiji 150 kwa REA hii Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vijiji hivi kama ambavyo nimekuwa nikirejea kwenye majibu ya msingi, mpango wa Serikali ni kupeleka vijiji vyote umeme. Kwa hiyo, vijiji 13 vipo katika mpango wa REA mzunguko wa kwanza na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote wafanye ufuatiliaji wa karibu na kwa kweli nafarijika kuona Wabunge wa Viti Maalum wanachangamkia miradi hii ya REA. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kero ya maji katika Mkoa wa Singida ni ya muda mrefu na hii ni kutokana na jiografia yake ya hali ya ukame. Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba mabwawa katika Mkoa wa Singida ili kupunguza makali ya kero hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa upatikanaji wa maji katika vijiji 13 vya Jimbo la Manyoni Mashariki vikiwemo Mangoli, Ikasi, Magasi, Winamila na Ipanduka imekuwa ni kero kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima katika vijiji hivyo ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Aisharose, amekuwa ni mpiganaji na amekuwa ni mfuatiliaji wa mara kwa mara katika Wizara yetu ya Maji katika kuhakikisha wananchi wake wa Mkoa wa Singida wanapata maji safi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua eneo la Singida ni kame, Wizara yetu imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuchimba visima virefu na hata mabwawa katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wanasema unapotembea na kuzuru wengine naomba usinipite, hatutampita katika kuhakikisha wananchi wa Singida wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya maji kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji lakini mpaka sasa miradi 1,469 imekamilika kati ya miradi 1,810. Mkakati wetu wa Wizara ni katika kuhakikisha tunatekeleza miradi 387. Nimhakikishie dada yangu katika miradi hiyo sisi kama Wizara ya Maji tutampa ushirikiano mkubwa sana katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika vijiji alivyoviorodhesha.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, barabara inayotokea Singida Mjini – Ilongero – Mtinko – Mudida – Kidarafa – Ikungi - Haydom yenye urefu wa kilometa 93.4 ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekuwa ukisuasua. Kukamilika kwa barabara hii kutaharakisha sana shughuli za maendeleo kwa Singida Vijijini. Barabara hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne…
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iko katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015. Je, ni lini sasa barabara hii itakamilika kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuharakisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Singida Vijijini? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii imekuwa ikitengenezwa kidogo kidogo lakini nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba matengenezo yale aliyoyaona yalitokana na usimamizi mzuri wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida. Kila alivyobakiza fedha ameendelea kutengeneza kilometa moja, kilometa mbili na takriban sasa tuna kilometa 10 zimetengenezwa kwa mtindo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu, mwaka huu wa fedha 2018/2019, tumetenga shilingi milioni 200 kuanza usanifu wa kilometa hizi 93 kwenda Haydom. Nami wiki zilizopita nimepita kwenye barabara hii kuweka msisitizo kwamba usanifu uanze mara moja mara baada ya kupata fedha ili sasa barabara hii iungane na barabara itakayokuwa inatoka Haydom kuja Sibiti, barabara kubwa hii ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Singida na maeneo mengine ya jirani waweze kwenda kirahisi kupata huduma katika Hospitali ya Haydom.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Iramba ina changamoto kubwa hususani kwa watumishi na vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka haraka watumishi na wataalam katika afya ya uzazi wa mpango? Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake Mkoa wa Singida wamekuwa wakipigania suala zima la afya na jana nimejibu swali la Mheshimiwa Mbunge huyu ambaye leo ameuliza swali la nyongeza. Naomba nimhakikishie, kama nilivyotoa majibu alivyouliza Mheshimiwa Mwambe, mchakato wa ajira uko kwenye hatua za mwisho na lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yale yote ambayo yana upungufu yanapelekewa watumishi. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, zoezi likikamilika tutapeleka watumishi wa upande wa afya ili kupunguza hizo changamoto.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa alizeti inayolimwa Mkoani Singida ni alizeti bora Afrika Mashariki na Kati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa alizeti Mkoani Singida, kulima kilimo chenye tija kwa kuwapa pembejeo, mikopo yenye gharama nafuu pamoja na elimu ili waweze kulima kilimo bora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kilimo cha alizeti kinalimwa sana katika Mkoa wa Singida na sisi kama Serikali, tunahamasisha na tunahimiza kuwa na kilimo cha kibiashara na vile vile kuwa na kilimo kinachozingatia kanuni, kwa maana ya kilimo kilicho bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamasishe halmashauri zote nchini na wale Maafisa Ugani wetu wote kuhakikisha kwamba wanatoa na wenyewe elimu kwa umma, wasikae tu ofisini, kazi yao iko mashambani, kuhakikisha wanakwenda kwa wakulima, wanatoa elimu ili wakulima waweze kuwa na kilimo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kama Serikali tumejipanga kwamba hili zao la alizeti ambalo nalo ni zao la kibiashara na linasaidia sana katika kuleta mafuta ili kupunguza tatizo la kuagiza mafuta zaidi kutoka nje, tumejipanga katika mwaka huu wa fedha kuhakikisha kwamba litazingatiwa na litakuwa ni Kilimo Bora na cha kisasa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga linafanana kabisa na tatizo lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Kwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inatakiwa kupokea wagonjwa 50 kwa siku, lakini inapokea wagonjwa zaidi ya 200; na hospitali hii ina uhaba mkubwa sana wa Madaktari Bingwa, vifaatiba kama kama CT-SCAN, MRI, pamoja na gari la kubebea wagonjwa. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha lakini na Madaktari Bingwa pamoja na gari la kubebea wagonjwa ili wananchi wake waweze kupata huduma bora za afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inakiri kwamba kuna uhaba wa Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kama nilivyowaeleza katika majibu yangu ya msingi changamoto hiyo tunaitambua, tumeweza kupeleka madaktari wachache, lakini tunatambua kwamba bado hawatoshi. Katika kibali kipya ambacho tutakachokipata mahitaji ya Mkoa wa Singida yatazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika hili ni ameulizia suala la vifaa, niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Singida kama nilivyosema sasa hivi fedha kwa ajili ya bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaatiba tunavyo vya kutosha, hospitali zinatakiwa ziainishe vifaa ambavyo wanavyovihitaji ili kuweza kuvipata. Tahadhari yangu ni kwamba teknolojia nyingine ambayo wanaiulizia ya kwamba kuwa na CT-SCAN na MRI katika ngazi hizi kwa sasa bado hatuna uwezo na wataalam wa kuweza kuzisimamia na kuvihudumu. CT-SCAN na MRI tumeanza katika miongozo yetu zinaanza kutumika katika ngazi za Hospitali za Kanda. Kadri tutakavyokuwa tunajenga uwezo basi tutazishusha chini katika ngazi ya rufaa Hospitali za Rufaa za Mikoa.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Singida unazalisha kwa wingi mazao ya biashara na chakula kama vitunguu, mahindi, alizeti na viazi vitamu. Tatizo kubwa lililopo kwa wakulima wetu ni bei kubwa ya pembejeo pamoja na zilizopo sokoni kukosa ubora. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa bei zilizokuwa nzuri lakini zina ubora wa kutosha? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pembejeo zinanunuliwa lakini sisi kama Wizara ya Kilimo tuna Mfuko wetu ule wa Pembejeo ambao tunatoa mikopo yake kwa asilimia saba au nane kwa masharti nafuu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo Kondoa Mjini halina tofauti na tatizo lililopo Jimbo la Singida Mjini. Kwa kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ndiyo kimbilio la wananchi wengi katika kupata huduma za afya, lakini hospitali hiyo haina kabisa gari la kubebea wagonjwa. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka gari la kubebea wagonjwa ili kuokoa vifo vya akinamama na watoto? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, jiografia na maeneo yanatofautiana. Kama hitaji kubwa kwa hospitali ya mkoa ni gari la wagonjwa na kwa sasa halipo, naomba nimtake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida ahakikishe miongoni mwa gari zilizopo anateua gari moja itumike kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wakati Serikali ikijipanga kuja kupeleka gari la wagonjwa. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa takwimu zinaonesha miji mikubwa nchini inaongoza kwa idadi kubwa ya kuwa na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ili kuwalinda watoto hawa na kuhakikisha wako katika mazingira salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa chanzo kikuu cha watoto wanaoishi mitaani ni njaa katika familia na kukosekana kwa maadili mazuri katika jamii: Je, Serikali ina mpango gani wa kukazia sheria zetu na kuhakikisha kwamba wazazi na walezi wanawajibika katika malezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo amekuwa anafuatilia kuhakikisha kwamba watoto wa Tanzania wanapata haki na ustawi ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, sisi kama Wizara tulianza katika hatua ya awali kwa kufanya tathmini ya ukubwa wa tatizo ndani ya nchi yetu na kwa kupitia mpango mkakati ambao nimeuelezea wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, tumeanza sasa kazi ya kwenda hatua ya pili ya kuanza kuwaunganisha wale watoto ambao tuliweza kuwabaini wanaishi mtaani na baadhi ya familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumekuwa tunaendeleza kampeni ndani ya mikoa mbalimbali ya kuweza kuwatambua watoto hawa na kuwarudisha katika maeneo yao ya makazi, lakini vilevile kuendelea kutoa elimu kwenye jamii kuhusiana na masuala ya matunzo ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kukazia sheria; tuna Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na sheria hii imeweka msisitizo wa haki za msingi za watoto ambazo ningependa Bunge lako Tukufu nalo lizifahamu. Watoto wana haki takribani tano ambazo zimeainishwa kisheria; mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kutunzwa, ana haki ya kuendelezwa, ana haki ya kushirikishwa katika maamuzi yanayomhusu na mtoto ana haki ya kutobaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria hii, haki za mtoto zimeainishwa vizuri sana. Kikubwa ambacho sisi kama Wizara tunaendelea kusisitiza ni kuweka misingi ya kuwasisitiza wazazi kuhakikisha kwamba wanazingatia misingi hii ya haki za watoto na kuimarisha misingi ya familia.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inahudumia zaidi ya wagonjwa 300 kwa siku na inatoa huduma katika maeneo mawili tofauti, ipo hospitali ya zamani, ambayo ipo katika Kata ya Ipembe na hospitali mpya ya Rufaa iliyopo katika Kata ya Mandewa. Je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha inapeleka fedha za kutosha ili kumaliza ujenzi katika hospitali mpya ya Rufaa ya Mandewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hospitali hii inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Madaktari Bingwa wakiwemo wa wanawake na watoto pia ina uhaba wa vifaa tiba kama Oxygen Concentrator, baby warmer na phototherapy machine. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mahitaji haya muhimu katika hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aisharose Ndoghoi Matembe, amekuwa ni mfuatiliaji mkubwa sana wa maendeleo ya hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na amekuwa ni mdau mkubwa sana kwetu sisi Wizara ya Afya kufuatilia masuala mbalimbali, nataka kumpa pongezi hizo. Naomba sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aisharose Matembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumezipokea hizo hospitali za Rufaa za Mikoa na kusudio letu ni kuhakikisha kwamba tunaziboresha ili ziweze kutoa huduma za kibingwa kama zilivyokusudiwa na ni kweli kwa sasa Mkoa wa Singida una hospitali ya zamani ambayo inatumika kama hospitali ya Rufaa ya Mkoa, lakini kuna ujenzi wa hospitali mpya ambao unaendelea pale Mandawe na nilishaitembelea na kusudio la Serikali ni kuhakikisha kwamba sasa tunaikamilisha ile hospitali. Baada ya hapo ile hospitali ya zamani tuirudishe katika ngazi ya halmashauri iweze kutumika kama hospitali ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, tutaendelea kuboresha na kuongeza Madaktari kadri tutakavyokuwa tunaendelea kuzalisha. Mwaka jana tumesomesha Madaktari takriban 125, mwaka huu tena tumeshasomesha Madaktari Bingwa zaidi ya 100. Kwa hiyo, kadri wanapokuwa wanamaliza na sisi tutakuwa tunawapangia katika hospitali zetu za Rufaa za Mikoa. Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba zile huduma za msingi za magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, magonjwa ya mifupa, magonjwa ya akinamama, wataalam wa radiolojia, wataalam wa magonjwa ya dharura, kila hospitali ya Rufaa za Mkoa iweze kuwa nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na masuala ya vifaa tutaendelea kuongeza vifaa hivi kadri tutakavyoweza lakini nitoe msisitizo kwa waganga Wakuu wote wa hospitali za Rufaa wote wa hospitali za mikoa, masuala mengine wala siyo kuhitaji kusubiri Serikali, fedha wanazo waweze kuagiza vile vifaa ambavyo wanaviona ni muhimu katika utoaji wa huduma zao za afya.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Ikungi Mashariki halina kabisa kituo cha afya. Je, ni lini sasa Serikali itajenga vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anaongelea Ikungi Mashariki wakati mwingine ataongelea Ikungi Magharibi, lakini niombe tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo tumekuwa tukitekeleza na tumefikisha hivyo vituo vya afya 352, safari tunayo na tutazingatia maeneo yenye uhitaji mkubwa na sasa kama na eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analitaja kwamba lipo mbali na lina population kubwa, naomba nimhakikishie kwamba katika awamu inayokuja tutazingatia maombi yake.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Singida kama ilivyo Monduli ni mabingwa wa kufuga ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuanzisha kiwanda kikubwa cha ngozi na nyama ili kuendana na falsafa ya Tanzania ya Viwanda?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Singida juu ya kuanzishwa kiwanda cha kuchakata nyama na mazao ya mifugo katika Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba Serikali imekuwa na mkakati huo na maeneo mbalimbali katika Taifa letu hivi sasa viwanda vinajengwa. Wazo hili la kujenga pale Manyoni ni jema, naomba tulichukue tulipeleke kwa wawekezaji ili tuweze kupata kiwanda pale Manyoni ambako ni center kwa mifugo inayotoka katika Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya Bara kwa maana ya Shinyanga na hata Nzega na Tabora wote wanaweza kupata huduma hii ya kuchakata mifugo kwenye eneo hili kwa kuwa eneo hili ni la kimkakati.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Tatizo la miundombinu lipo pia katika Jimbo la Ikungi Mashariki katika barabara yetu ya Makiyungu - Misughaa. Changamoto hiyo imekuwa kubwa sana wakati wa masika. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mikoa ya Singida na Dodoma na kuharakisha shughuli za maendeleo katika maeneo hayo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aisharose Matembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Aisharose Matembe amekuwa mahiri sana kufuatilia barabara mbalimbali. Barabara hii anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya kilomita 461 ya barabara inayotoka Handeni – Kibirashi – Kijungu - Chemba - Singida. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira kwani katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu. Tukipata fedha eneo hili litapitiwa na mradi wa barabara ya lami inayotoka Handeni – Singida.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote zimeleta madhara makubwa Mkoani kwangu Singida na kusababisha barabara inayoanzia Mjini Singida – Ninyuhe hadi Iyumbu yenye urefu wa kilomita 115 madaraja kukatika na kusitisha shughuli zote za kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami na kurekebisha miundombinu ya barabara hii, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii ambayo inapita maeneo ya Ngungila inakwenda kule Iyumbu ni barabara ambayo imepita kwenye bonde kubwa ambalo wananchi wa maeneo haya wanategemea sana uzalishaji wa mpunga. Kwa hiyo, tunafahamu kama Serikali lakini niseme hatua kubwa ambazo tumezichukua kazi iliyokuwa inaendelea ni pamoja na kujenga madaraja na makalavati katika eneo hili la Ngungila ili wananchi waweze kupita pamoja na kujaza vifusi kufanya barabara iwe juu katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua umuhimu wa barabara hii na tumeona uharibifu uliotokea kutokana na mvua. Lakini namuomba anikubalie kwamba hatua ya kwanza ni ya kuboresha barabara hii ili wananchi waweze kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile hatua ya kujenga kwa barabara hii kwa kiwango cha lami itafanyika baadaye lakini Mheshimiwa Mbunge unafahamu barabara hii itaunganishwa na barabara ile ya kutoka Sabasaba inapita Sepuka – Ndago inaenda kutoka Kizaga. Kwa maana hiyo tutakuwa tumeipunguza sana barabara hii kwa kiu yako ya kuijenga barabara kiwango cha lami tutaizingatia baada ya barabara hii niliyoitaja kuwa imekamilishwa. (Makofi)
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mradi wa Maji Kintinku Lusisile, ulianza kutekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa mwaka 2012, lakini hadi sasa imepita miaka saba mradi huu haujakamilika. Je, Serikali inasema nini kutokukamilika kwa mradi huu kwa wakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, mojawapo ya tatizo kubwa la kutokukamilika kwa mradi huu ni ucheleweshwaji wa malipo, mpaka sasa tumepokea shilingi milioni 750 nje ya shilingi bilioni 2.2 tangu kusainiwa kwa mkataba tarehe 23 Mei, 2018. Nataka commitment ya Serikali ni lini mradi huu utakamilika? Wananchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki wameteseka kwa muda mrefu, Mheshimiwa Naibu Waziri naomba unipe majibu, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kiukweli ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa wakipigania hasa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Singida. Na ninataka nimhakikishie moja ya changamoto kubwa sana tukiri ilikuwa ucheleweshaji wa kukamilika kwa miradi ya maji. Tunashukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kutupa rungu la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini, hatuna sababu hata moja sisi kama viongozi wa Wizara ya maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Wizara tumejipanga vizuri na wakala huu wa maji umejipanga vizuri. Tutahakikisha mradi ule tunaukamilisha kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mwezi huu tunawapa fedha, si yeye tu hapo Manyoni, na hata kwa Mheshimiwa Massare katika mradi wake ule wa Itigi ambao unatekelezwa na Nangai tutatoa fedha katika kuhakikisha miradi hii ya maji inakamilika kwa wakati na Wananchi wa Manyoni waweze kupata huduma ya maji. Pia, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Lubeleje, jana alizungumza hapa eneo la Bulima na Iyoma na Mima wote nao tutaweza kuwapatia huduma ya maji, ahsante sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, changamoto ya mawasiliano iliyopo Same Magharibi inafanana kabisa na changamoto iliyopo Singida Magharibi. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika maeneo ya Iyumbu, Ingombwe, Mtunduru, Sepuka, Mwaru, Ingriasoni, na Irisia ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo hawaachwi nyuma na mawasiliano ya simu za mkononi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama nilivyozungumza kwamba maeneo nchi nzima tunafanya juhudi za kuhakikisha kwamba tunaboresha mawasiliano na iko orodha ndefu tu katika Mkoa wa Singida. Nimsihi tu Mheshimiwa Aysharose Matembe na nimpongeze sana kwa kweli hata nilivyofanya ziara Singida nilipokea orodha ndefu sana kwa ajili ya kuboresha mawasiliano katika mkoa huu. Kwa hiyo, nikuombe tuonane tu ili tuweze kupitia hii orodha ili ufanye kazi ya kuwaelimisha wananchi kwamba Serikali inajipanga mwaka huu wa fedha kuna kazi kubwa itafanyika kwa ajili ya kuendeleza kuboresha…

MWENYEKITI: Ahsante
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Changamoto ya ukosefu wa maji iliyopo Momba inafanana kabisa na changamoto ya ukosefu wa maji iliyopo Manyoni Mashariki.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mradi wa Kintinku - Lusilile utekelezaji wake umekuwa ukisuasua, je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka fedha za kutosha ili kukamilisha mradi huo hasa ikizingatiwa kwamba kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha zaidi ya wakazi wa vijiji kumi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda nijibu swali la dada yangu Mheshimiwa Aisharose, kwanza, ni miongoni mwa Wabunge akina mama wafuatiliaji suala zima la maji katika Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa nachotaka kusema utekelezaji miradi ya maji unategemea na fedha. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji tutawaangalia kwa namna ya kipekee katika kuhakikisha wakandarasi wanao-rise certificate ya utekelezaji wa mradi wa pale Manyoni Mshariki tunawalipa kwa wakati na utekelezaji wake uendelee na wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, pia nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Manyoni kuwa na changamoto ya maji lakini sisi kama serikali na tunamshukuru Mheshimiwa Rais zaidi ya dola milioni 500 tulizozipata kwa ajili ya kutatua tatizo la maji nchi zaidi ya miji 28 Tanzania Bara na mji mmoja Zanzibar, sasa hivi Mkoa wa Singida miji mitatu tunaenda kutatua tatizo la maji. Wahandisi Washauri wameshapatikana, nataka nimhakikishie itakapofika mwezi September wakandarasi watakuwa site katika kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji na sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga vizuri sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Kata ya Iyumbu ipo pembezoni na haina kituo cha afya wala zahanati katika vijiji vyake vyote, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha afya katika Kata ya Iyumbu iliyopo Jimbo la Singida Magharibi ili kuwawezesha wananchi wake kupata huduma bora za afya na kuokoa vifo vya akina mama na Watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aysharose Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunafahamu pamoja na jitihada kubwa na kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali ya kujenga vituo vya afya, ambapo katika miaka mitano iliyopita zaidi ya vituo vya afya 490 vimejengwa bado kuna uhitaji wa vituo vya afya katika kata zetu mbalimbali kote nchini. Kwa hiyo katika eneo hilo Kata hii ya Iyumbu katika Mkoa wa Singida ni miongoni mwa kata ambazo kimsingi zina uhitaji wa kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mpango wa Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Afya Msingi ni kuendelea kujenga vituo vya afya kwa awamu katika kata zetu kadri ya upatikanaji wa fedha. Mimi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Aysharose kwamba tunachukua hoja hiyo, na kadri ya upatikanaji wa fedha tutaendelea kutoa kipaumbele katika Kata hii ili tuweze kujenga kituo cha afya na kuweza kuwahudumia wananchi ipasavyo.