Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asha Mshimba Jecha (6 total)

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu yenye kutia moyo ya Mheshimiwa Waziri, hivi anafahamu kituo hiki sasa hivi kimefunga huduma zake na wanatoa huduma kwenye jengo la kuazima? Je, ni lini tathmini hii itafanyika ili gharama ijulikane na umuhimu wa kukijenga pia uonekane? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia anawahakikishia vipi wananchi wanaotumia kituo hiki umuhimu wa kujengwa na kuweza kukitumia kama walivyozoea? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Asha, kwa kweli kwa kufuatilia sana suala la kituo hiki. Mbali na swali la hapa amekuwa pia akiulizia mara zote anapopata fursa ya kutembelea ofisini ama kwenye shughuli za Kamati.
Mheshimiwa Spika, niseme tu, kwa umuhimu huo na kwa ufuatiliaji wake, jambo hili tumesema lifanyiwe tathmini kwa upekee kwa maana ya Kituo cha Dunga kama kituo peke yake mbali ya vituo vingine kwenye maeneo mengine ambavyo vinafanana kama kituo hicho.
Mheshimiwa Spika, mara tathmini hiyo itakapokuwa imekamilika ambapo tunaamini ni katika kipindi hikihiki, basi utaratibu wa upatikanaji wa fedha utaanza na hapo ndipo tunaposema tunatoa rai hata kwa wadau mbalimbali ili tuweze kufanya kama ni jambo mahsusi kufuatana na mazingira ya pale.
Mheshimiwa Spika, mara ukarabati wake utakapokamilika basi niwahakikishie wananchi kwamba matumizi yake yatarejea katika hali ya kawaida na wataendelea kumpongeza na kumpigia kura Mheshimiwa Mbunge ambaye amelitetea sana jambo hili. (Makofi)
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza niipongeze kupitia mradi huu, kwa kweli imejitahidi sana kwa haya waliyoyasema na wanachi tayari wameonesha matunda na uzalishaji umekuwa. Mheshimiwa Jenista ni shahidi alikuja kutembelea maeneo ya Kongoroni na akajionea jinsi gani wananchi walivyoimarika katika uzalishaji wa kilimo cha ndimu. Kwa taarifa niliyonayo sasa hivi kwamba mitambo ya kiwanda cha ndimu tayari imefika na tayari imejaribiwa bado ufungaji tu naamini kazi hiyo itafanyika. Kwa kuwa mradi huu umeonesha maendeleo makubwa na bado kuna maeneo mengine yanahitaji mradi kama huu.
Je, Serikali kupitia mradi iko tayari kuendelea kwa yale maeneo mengine ambayo hayajafikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swala langu la pili elimu haina mwisho; kwa kuwa vikundi hivi vineonesha mwelekeo mzuri na bado vingali na changamoto ya kuyafikia masoko lakini hata kuongeza ujuzi wao.
Je, mradi huu uko tayari kuendelea na vikundi hivi ili kufikia lile lengo la kuondokana na uchumi mdogo na kuingia uchumi wa kati katika ulimwengu huu wa sasa hivi wa viwnda? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kama Serikali kupitia mradi huu utaendelea kuyafikia maeneo ambayo hayafikiwa. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba mradi huu ambao una lengo la kwenda kurekebisha miundombinu ya barabara na masoko maeneo ya vijijini na kuongea tija katika mazao unaendelea kuwanufaisha Watanzania, na kadri ambavyo miradi inazidi kuibuliwa basi tutayafikia pia na yale maeneo ambayo bado hayaguswa kutokana na maelekezo na mwongozo wa mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusu suala la mafunzo na kuviendeleza vikundi ambavyo vimeshapatiwa fedha kupitia mradi huu. Kwa mujibu wa utaratibu wa mradi huu wa MIVARF miradi hii ikisha ibuliwa katika halmashauri kazi sisi tunayoyanya ni kuwezesha na baadaye kazi ya kuendelea kuvilea vikundi hivi inabaki katika halmashauri husika. Kwa hiyo niendelee tu kumuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa sababu tayari mradi huu umeshafanya kazi yake eneo la uendelezaji wa vikundi hivyo pia na wenyewe kwa nafasi yao waweze kushiriki kuhakikisha kwamba vikundi hivi vinakuwa endelevu na viweze kuleta tija kwa Mtanzania. (Makofi)
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Kama alivyoeleza kwamba ugonjwa huu hapa kwetu upo, pamoja na kwamba anasema wanaoathirika zaidi ni Marekani, lakini hapa kwetu tayari umeingia na mazingira yake tumeona kwamba wanawake waathirika zaidi lakini na umri ni miaka 15 mpaka 45.
Je, Serikali haioni haja ya kuelimisha juu ya ugonjwa huu kwa sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kama ilivyo katika magonjwa mengine, wajibu wetu Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa mbalimbali, vyanzo vyake, dalili zake na matibabu yaliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuhamasisha jamii kupata uelewa wa kina katika jambo hili, Serikali kupitia Kitengo chake cha Elimu ya Afya kwa Umma, tutaweka utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii ili wananchi nao waweze kupata uelewa vizuri wa ugonjwa huu.
Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, siyo ugonjwa ambao unabainika kirahisi, wala chanzo chake kinajulikana kirahisi na wala matitabu yake siyo rahisi kama nilivyogusia katika jibu langu la msingi. Kwa hiyo, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutazingatia katika mpango wetu wa elimu ya afya kwa umma.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina suala moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango mizuri ya Serikali lakini bado wavuvi wana hali ngumu, uduni wa vifaa, utaalam na kadhalika. Je, ni lini Serikali itaanzisha vyuo vya uvuvi vingine kwa sababu navyofahamu chuo kilichopo ni kimoja tu lakini hata wahitimu wake hawapati nafasi ya kuajiriwa pamoja na kwamba tumezungukwa na ukanda mkubwa wa bahari na maziwa. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwatumia wataalam wanaomaliza katika chuo hicho lakini pia kuanzisha vyuo vingine kwa lengo la kuwanyanyua wavuvi ili waweze kuwa na tija na bahari na maziwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili mazuri sana ya nyongeza ya Mama yangu Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali tunao mpango wa kuhakikisha tunafungua vyuo vingine. Hapa karibuni tumefungua chuo cha uvuvi katika Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara Mikindani, Chuo cha FETA ambacho kinafanya kazi ya kutoa elimu. Mipango mingine ya Serikali ni pamoja na kuboresha chuo chetu kilichopo pale Pangani maarufu kama KIM kwa kushirikiana na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Halmashauri ya Pangani kwa lengo la kuhakikisha wananchi hasa vijana walio wengi wa maeneo haya ya ukanda wa bahari wanapata elimu. Kwa upande wa Ziwa Victoria chuo chetu kilichopo katika Wilaya ya Rorya pale Gabimori na chenyewe tunakwenda kukiongezea nguvu ili kusudi kitoa elimu zaidi kwa wananchi wengi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza mipango yetu tuliyonayo ya kuhakikisha wale wataalam wanaotoka katika vyuo hivi wanakwenda kupata kazi na kuisaidia jamii yetu. Katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kuwa Serikali inao mpango wa kufufua Shirika letu la Uvuvi la TAFICO na tayari tumeshalifufua, hivi sasa tunakwenda katika hatua ya kununua meli. Tayari tumepata msaada kwa maana ya grants kutoka Serikali ya Japan wa takribani bilioni nne ambazo tunakwenda kununua meli na kutengeneza miundombinu ya kuhifadhia samaki katika eneo la ukanda wa pwani. Hii ni chachu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wale wengi wenye utaalam wataajiriwa na mashirika haya.

Vilevile tunao mpango wa kuhakikisha wanajiajiri wao wenyewe kwa kufanya kazi za uvuvi endelevu wa kisasa na vilevile ufugaji wa samaki.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa tatizo hili sio mara ya kwanza kutokea hapa nchini, je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuzuia jambo hili lisitokee tena kupunguza usumbufu kwa wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Serikali mikakati iliyonayo ni kusimamia sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 kama inavyoelekeza kuhusu unazishwa na usimamiaji wa uanziswaji wa taasisi za kifedha ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, na Serikali mmeona kwa sasa imekuwa, imeweka udhibiti wa hali ya juu kuhakikisha taasisi zote za kifedha zinafanya kazi kulingana na sheria ili kuzuia changamoto hizi wanazozipata wateja wetu.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilielekeza TANESCO kwamba vijiji vyote ambavyo umeme umepita juu vipatiwe umeme. Miongoni mwa vijiji 74 ambapo kuna Vijiji vya Buyungi, Imenya, Itwangi na Nyambui, je, Serikali itavipatia umeme lini katika huu msimu wa 2019/ 2020? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Naibu Waziri aliahidi wananchi wa Nyambui atawapatia umeme. Je, ahadi hiyo itatekelezwa lini? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi lakini nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali kwa wananchi wa Shinyanga kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe taarifa Kijiji cha Itwangi kimewashwa umeme tangu juzi ingawaje swali wakati linajibiwa kilikuwa hakijawashwa umeme, kwa hiyo, kimeshawashwa umeme. Kwa hiyo, wananchi wa Itwangi sasa wanapata umeme kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Buyubi pamoja na Minyami kitawashwa tarehe 17 mwezi huu wa Septemba. Kwa hiyo, wananchi wa maeneo hayo wategemee kuunganishiwa umeme katika maeneo hayo kwa wiki inayokuja. Ahsante.