Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile (37 total)

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Moja ya chanzo cha migogoro ya ardhi hapa nchini unatokana na kwamba katika nchi yetu sasa hivi kuna umiliki wa asili ambao unatambulika kwa mujibu wa sheria kama customary right of occupancy na umiliki kwa kupitia hati ambao unajulikana kama granted right of occupancy. Changamoto imekuwa ni kwamba katika umiliki wa asili umekuwa haupewi uzito ule ambao unastahili je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba umiliki wa asili unatambuliwa, unalindwa na kuhakikisha kwamba wamiliki wa asili wanaweza kutumia hati zao zile kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Swali la pili, ujenzi holela kwenye maeneo mengi hususani katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa ni kero kubwa sana. Sasa na moja ya changamoto ni kwamba kumekuwa na hali ambayo watumishi wapimaji pamoja na watumishi Maafisa Ardhi kushiriki katika mikakati hiyo.

Je, Serikali ina mkakati gani na nakumbuka kwamba Mheshimiwa Waziri alishawahi kutoa kauli ya kuwawezesha baadhi ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na Waheshimiwa Madiwani kusimamia shughuli ya Mipango Miji na kuwapa ramani ili waweze kusimamia maeneo ya umma na kuzuia uvamizi, je, utekelezaji wa jambo hili umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, sehemu ya kwanza Mheshimiwa ameulizia swali la miliki za asili ili kuwawezesha wananchi wetu, Wizara yangu iko katika mpango kabambe ambao unaendelea katika Halmashauri zote za kuwezesha upimaji katika maeneo ambayo yapo watu waweze kupimiwa na kumilikishwa kulingana na hali halisi katika maeneo wanayoishi. Aidha katika vipao mbele vya upangaji wa miji pia, mpaka sasa Wizara yangu imeshapima Majiji matano, Manispaa 15, Miji 15 na Miji midogo 79, yote hii ni katika kuhakikisha kwamba kunakua na mipango mizuri ambayo itaepusha ujenzi holela na ukuaji holela wa Miji yetu katika maeneo ya nchi hii.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, niliuliza kuhusiana na umiliki wa asili na mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba umiliki wa asili unalindwa, kuenziwa na kutumika kwa wananchi kwa ajili za maendeleo. Lakini la pili, ni kuwawezesha wananchi, Serikali ilitoa tamko kupitia Waziri kwamba Wenyeviti wa Serikali za Mitaa watawezeshwa na kupewa ramani ili waweze kusimamia maeneo yao na kuzuia uvamizi wa maeneo, hilo swali halikuweza kujibiwa.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nadhani katika kujibu nimeeleza pengine labda hakusikia vizuri, naomba niseme kwamba, suala la maeneo kulindwa kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alielekeza tayari katika Jiji la Dar es salaam kwa kuanzia Wenyeviti wote wale wa Mitaa watawezeshwa kupewa ramani za maeneo yao, ili waweze kila mmoja kulinda eneo lake, aweze kutambua wapi ni eneo la makazi, wapi ni eneo la wazi, wapi ambapo pamepangwa kwa ajili ya kujenga ili watu waepukane na kuvamia viwanja na kufanya ujenzi usio na utaratibu.

Mheshimiwa Spika, swali lake lingine aliongelea suala la umilikishaji wa asili kwa maana ya kupata zile hati za kimila, nadhani nimeliongelea kwamba Halmshauri zinaendelea katika utaratibu huo na ndiyo maana kumekuwa na msisitizo wa kuwa na zile masjala katika maeneo yao ili pale ambapo mwananchi anakuwa amepimiwa eneo lake na tayari Kijiji kinakuwa au Mtaa unakuwa na hati yake, basi waweke pia na eneo la kuhifadhi. Maana yake huwezi kuwa na Mmliki wa Asili na kutoa hati ambazo huna namna ya kuweza kuzihifadhi, maeneo yote wameelekezwa kuwa na masjala ambazo zitatunza na tunaimani kwamba hati hizi zinawapa uwezo wananchi kiuchumi kwa hiyo suala hilo Wizara inaitilia kipaumbele ni wajibu wa Halmashauri zote kuzingatia na kufuata utaratibu huo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ndugulile na wa mwisho jirani yako Mheshimiwa Keissy.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kigamboni lina jamii kubwa sana ya wavuvi lakini sekta hii ina changomoto kubwa sana. Wavuvi wana leseni za chombo, wana leseni za baharia, wana leseni ya aina ya samaki wanayovua lakini wavuvi hawa hawa wakitoka Dar es Salaam wakiingia Mafia kuna leseni nyingine ambayo wanatakiwa kukata. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya mzigo wa leseni ili kuondoa hizi kero kwa ajili ya wavuvi hawa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Faustine Mbunge wa Kigamboni kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana suala la wavuvi, nakumbuka alishakuja ofisini mara kadhaa. Niseme tu kwamba Wizara na Serikali kwa ujumla inayaangalia maeneo yanayolalamikiwa katika kazi zinazowapatia Watanzania kipato hasahasa yanayohusu makato mengi yanayokwenda kwa mtu anapofanya shughuli yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amelisemea hili la leseni nyingi na nilipokutana na Wabunge wanaotokea maeneo ya uvuvi upande wa Kanda ya Ziwa walisema hata mtu akitoka Nyamagana akiingia Ilemela anatakiwa atoe leseni nyingine. Lingine wavuvi ni Watanzania na maji ni ya Tanzania lakini leseni inatolewa kwa dola na lenyewe tumepokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge kwamba vikao hivi tunavyofanya vya kukutana nao ni kwa ajili ya kuandaa mpango maalum ambao utatoa majawabu ya kudumu ya malalamiko hayo ambayo Wabunge wameyaleta kwa niaba ya wananchi wao. Kwa hiyo, tutalifanyia kazi na tutatoa tamko ambalo litakomesha yale ambayo yanawakwaza wavuvi, wafugaji pamoja na wakulima.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wastaafu ambao wanapitia Mfuko PSPF hivi karibuni Serikali iliongeza kiwango, lakini wastaafu hawa wanakuwa hawalipwi kwa wakati na kwa kiwango ambacho Serikali ilitangaza.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuwalipa wastaafu hawa kwa kiwango sahihi na kwa wakati muafaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tatizo hili lilkuwepo PSPF, lakini kuanzia Disemba 2015 mpaka leo wastaafu hao wamekuwa wakilipwa pesa zao inavyostahili. Kuanzia Disemba hiyo tumeanza kulipa hao wastaafu shilingi 100,000/= kama ambavyo Serikali iliongeza kiwango hiki kupitia Mfuko wa PSPF na arrears zao mpaka kufikia mwisho wa mwezi huu wa nne wote watakuwa wamelipwa zile arrears za kutoka Julai hadi Disemba.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, nataka kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali haijawekeza kikamilifu katika sekta ya uvuvi na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kodi zinazotozwa wavuvi ni nyingi sana na zisizokuwa na mpangilio. Nataka nitolee mfano wa Mafia ambapo Wilaya hiyo imesema kwamba kila boti itakayokuwa inaingia pale inatozwa shilingi milioni tano; whether wamevua au hawajavua. Je, Serikali itakuwa tayari katika bajeti ijayo kutuletea majibu ya kina katika Finance Act kuhakikisha kwamba kodi hizi zote zimehuishwa na zile kodi ambazo ni kero kufutwa? Swali la kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika ardhi ya Kigamboni tulikuwa na taasisi inaitwa TAFICO (Tanzania Fishing Company) ina majengo na ilikuwa inafanya kazi ya uvuvi pale Kigamboni. Majengo yale yapo pale mpaka sasa hivi hayafanyi kazi yoyote. Je, Serikali itakuwa tayari kubadilisha majengo ya taasisi ile kuwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuongeza ajira na kuongeza thamani ya mazao ya bahari?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kodi kama nilivyosema kwenye maswali yaliyotangulia na katika swali hili, zipo nyingi na kwa kweli Mheshimiwa Rais alikwishatoa maelekezo kwamba ni lazima zipitiwe upya na hizo ambazo zinastahili kuondolewa kwa sababu zina kero mbalimbali ziondolewe siyo kwenye mazao ya uvuvi peke yake, lakini kama nilivyosema awali hata kwenye mazao ya kilimo pia. Kwa hivyo, kodi zile ambazo zitaondolewa na zisiwe na madhara yoyote ya kibajeti baada ya ile Kamati kukamilisha kazi yake zitaondolewa na zile ambazo zitakuwa na madhara ya kibajeti hizo zitasubiri sasa utaratibu wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni wazo na mimi nalichukua, nitakwenda kuzungumza na wenzangu katika Wizara na Serikali kuona pendekezo hili la Mheshimiwa Dkt. Ndugulile linaweza kutekelezwa namna gani.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto ya ajira imekuwa kubwa sana nchini hususan kwa upande wa vijana na kwa kuwa Halmashauri zimekuwa zinatenga asilimia 10 kwa ajili ya kukopesha akina mama na vijana lakini katika baadhi ya Halmashauri kumekuwa na changamoto kubwa. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kutenga kati ya asilimia 10 - 30 ya tenda zote za Serikali ili kuweza kuwapatia fursa za kujiajiri vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli imekuwepo asilimia 5 ya mikopo katika kila Halmashauri kwa ajili ya vikundi vya akina mama na vijana na ambapo kwa kiasi kikubwa vijana na akina mama wengi wamekuwa wakinufaika kupitia mfuko huu. Pia kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeelezwa wazi kabisa kwamba moja kati ya mipango ambayo tunatazamia kutekeleza mwaka huu ni kuhakikisha tunatengeneza utaratibu ambapo kila Halmashauri itatenga asilimia 30 ya manunuzi yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya akina mama na vijana.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji imekuwa ikiongezeka, wakulima, wafugaji dhidi ya hifadhi na ukuaji wa miji kama swali la msingi lilivyokuwa limeulizwa. Nakumbuka kwamba katika Bunge hili swali hili limeshawahi kuulizwa na ikatakiwa kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Ardhi; Wizara ya Maliasili; wakae pamoja kuangalia utaratibu wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi. Je, Wizara hizi zimeshakaa na hatua waliyoifikia ni ipi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba migogoro ya aina hii imekuwa mingi sana katika nchi yetu, lakini vile vile ni kweli kwamba tayari tulishaahidi na tulielekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wizara zile zinazohusika na suala hili zikutane ili kujaribu kutafuta suluhu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huo bado upo, lakini tulisema ni baada ya Bunge la Bajeti. Kama anavyofahamu bado hatujarudi hasa maofisini kukaa kwa pamoja, lakini nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo bado tunalipa kipaumbele kikubwa sana, ni tayari ni maagizo kutoka kwa viongozi wetu. Kwa hiyo, tukitoka kwenye Bunge hili nimwahidi tu kwamba hilo ni moja kati ya masuala ya kwanza ya kwenda kutekeleza kama Wizara mbalimbali na kama Serikali. Nashukuru sana.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na suala la elimu bure na changamoto ambazo zinakabiliana na suala hili, katika Wilaya ya Kigamboni, Wilaya ya Temeke na naamini katika Wilaya nyingi Tanzania, kuna changamoto kubwa sana ya Walimu hususani upande wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu hawa walikuwa wanagharamiwa kwa michango ambayo ilikuwa inakusanywa pale shuleni ambayo ilikuwa inalipia hawa Walimu wa part time. Serikali imesema imetoa mwongozo wa jinsi ya kusimamia suala hili, je, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa maelezo ya mwongozo huo kwa Waheshimiwa Wabunge ili na sisi twende kuwasimamia zoezi hili kwa ukamilifu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba, dhana ya elimu bure imekumbana na changamoto nyingi, lakini changamoto hizi ni changamoto za mafanikio. Kwa sababu kama mwanzo kulikuwa na suala la ulipiaji wa Walimu, vijana waliokwenda sekondari wanashindwa kwenda kusoma kwa sababu ya ada au michango mbalimbali. Nimeshuhudia sehemu mbalimbali zilizopita miongoni mwa vijana hao wengine walikuwa madereva wa bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii na Wabunge ni mashahidi; naamini Wabunge wengi walishakopwa na kuombwa sana na wananchi wao kuwalipia watoto ambao matokeo yao hawakuweza kuyapata kwa sababu ya ada ya mitihani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baada ya kuyachukua madeni na katika mpango wake mkakati, hasa kama ulivyojielekeza kwa Walimu wa sayansi, ni kwamba mwaka huu katika suala zima la ajira; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora siku ile ilivyozungumza, kwamba katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2015/2016 kulikuwa na tengeo kwa ajili ya Walimu ambao tulikuwa tunatakiwa tuwaajiri na kipaumbele kikiwa ni kuwaajiri Walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukaenda mbali zaidi, kwa upande wa Walimu wa sayansi kuna wengine ambao wako nje ya system, lakini wana uwezo Serikali itaangalia kwa ukaribu zaidi namna ya kufanya ili Walimu wale waweze kutumika pamoja na wale ambao wamestaafu lakini wana uwezo wa kufundisha masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunaweza kuangalia vilevile vijana wetu waliosoma Bachelor of Science in Chemistry, Bachelor of Science in Physics, Statistics, au Bachelor of Science in Mathematics. Watu hawa hawaitwi walimu, ni watu waliosomea fani nyingine lakini akienda shuleni anaweza kufundisha. Ndiyo maana tumesema kwamba watu hawa tutawabainisha vilevile. Vijana hawa wengine wametembea mpaka soli za viatu zote zimekatika, hawaitwi Walimu lakini ni wataalam wazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda katika mpango wetu mpana kabisa wa kuhakikisha jinsi tutakavyowaingiza vijana hawa katika utaratibu mzuri angalau wapewe hata short course ya teaching skills ili tuongeze idadi ya Walimu wa Sayansi na kuondoa tatizo hilo, kwa sababu tumejenga maabara nyingi hivyo lazima tupate Wataalam ambao watafundisha maeneo hayo. Nadhani hayo ndiyo maeneo ya kuweka msisitizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeipeleka katika Halmashauri zote miongozo yote ya Sera ya Elimu, kwamba kila eneo ada kiasi gani, gharama za ukarabati kiasi gani. Miongozo hii tumepeleka katika Halmashauri zote ili watu wapate ufahamu ile pesa inayopelekwa inaenda katika kipengele gani kwa sababu kila kipengele kimewekwa asilimia yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Kigamboni au Wilaya mpya ya Kigamboni inakua kwa kasi sana. Umeme kwa wakazi wa Kigamboni unatoka katika Wilaya ya Ilala na ku-supply baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ilala, Temeke, Mbagala yote, Mkuranga yote na Kigamboni yote. Je ni lini sasa Serikali itajenga kituo cha umeme katika Wilaya mpya ya Kigamboni ili kuendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kigamboni ni mpya na kwa sasa unatumia umeme kutoka Ilala na umbali uliopo ni zaidi ya kilometa 50. Kwa nguvu iliyopo kwa sasa hivi, uwezo wa kupeleka umeme kwa Kigamboni hautoshi. Mpango wa Serikali utakapokuwa unasambaza umeme kwenye REA awamu ya tatu, utajenga pia kituo cha kupozea umeme kwenye Wilaya ya Kigamboni ili kuhakikishia upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa Kigamboni.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Wilaya ya Kigamboni ina askari takribani 100, magari yanayofanya kazi matatu na nyumba chache sana za askari. Je, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ina mkakati gani wa kuongeza askari katika Wilaya mpya ya Kigamboni ili kukidhi mahitaji, hususan tukizingatia kwamba, Wilaya mpya ya Kigamboni ina changamoto kubwa sana ya uvuvi haramu, uhamiaji haramu pamoja na ongezeko la uhalifu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilitaka kujua; katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba ujenzi wa kituo kipya cha Wilaya utajengwa katika Kata ya Kibada mara fedha zitakapopatikana. Je, Wizara inaweza ika-make commitment kwamba itaingiza ujenzi wa kituo kipya cha Polisi cha Wilaya katika bajeti hii inayokuja ya mwaka wa fedha 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na pendekezo la Mheshimiwa Mbunge kuhusu haja ya kuongeza idadi ya Askari Kigamboni, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeliona hilo na tunategemea pengine katika askari ambao wanaweza wakaajiriwa katika mwaka ujao wa fedha tuweze kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya askari katika maeneo yote ambayo kuna upungufu wa askari ikiwemo Kigamboni.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ametaka kujua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwamba fedha hizo za ujenzi wa Kituo cha Kigamboni zitaingizwa. Naomba kwanza nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi hatua ambazo zimefikiwa ni hatua za kuridhisha kwani mbali na kupatikana eneo la ujenzi wa kituo, lakini tayari hatua za awali ikiwemo utayarishaji wa ramani kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho umeshafanyika.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake tutazingatia ingawa inawezekana ikawa kwa bajeti ya mwaka huu ikawa tumechelewa, lakini tutaangalia utaratibu mwingine wa kuweza kuangalia jinsi gani ya kupiga hatua zaidi na pale ambapo tutaweza kuingiza katika bajeti ya mwaka mwingine wa fedha, tutaziingiza kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru
sana. Kwa kuwa, ulevi wa pombe hizi za kienyeji sasa hivi kumekuwa na
ongezeko la matumizi makubwa sana ya pombe aina ya viroba ambavyo
vifungashio vyake na bei yake imekuwa ni nafuu sana ambapo imepelekea hata
watoto wa shule wanaweza kumudu kati ya shilingi 300 mpaka 500 kuzinunua.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kupiga marufuku pombe za viroba ili
kunusuru Taifa hili?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kinachofanyika sasa ni utaratibu, lakini ukweli ulio wazi ni kwamba viroba
vitapigwa marufuku na tutaanzisha packaging ya pombe kali kwenye ujazo
ambao itakuwa ni vigumu kwa mtu kuficha. Watoto wa shule kwa sababu ni
rahisi wanaweza kuficha. Tutaweka kwenye chupa ya glass, ujazo utakuwa
mkubwa kiasi kwamba mtoto ashindwe kununua lakini hata dereva wa daladala
ashindwe kuficha. Ni suala la muda na Waziri wa Mambo ya Mazingira
alizungumzia jana.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa mtazamo huo mpya na ninaamini sasa huo ndiyo mtazamko chanya ambao tunapaswa kwenda nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa hivi katika ununuzi wa vifaa tiba tumekuwa tukivinunua bila kuwa na mpango wa matengenezo kwa maana ya Plan Preventive Maintenance, kuwekwa katika mpango wa
manunuzi.
Je, sasa Serikali mtakuwa tayari kuhakikisha wakati mna-negotiate kununua zile mashine mnaweka mpango wa Preventive Maintenance kwa sababu sasa hivi gharama zinazotumika kutengeneza vifaa tiba ni za juu sana?
Swali la pili, kwa kuwa, gharama za utengenezaji wa vifaa hivi ni kubwa sana, kwa maana ya
Preventive Maintenance na pale vinapokuwa vinaharibika kwa hali ya kawaida:-
Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuingiza gharama za PPM ama Plan Preventive Maintenance katika gharama za vitendanishi, badala ya kutenga peke yake ambazo ni mabilioni ya hela ambapo mara nyingi Serikali inaishia kutozilipa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakubaliana na wazo lake kwamba gharama za Planned Preventive Maintenance ni vema zikawa sehemu ya mkataba mkuu wa ununuzi wa vifaa tiba. Hivyo, ndiyo maana mikataba yote mipya ambayo itafungwa na Serikali na Private Contractors kwa sasa itahuisha uwepo wa section maalum ambayo ina Planned Preventive Maintenance katika costs zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili pia tunakubaliana naye kwamba ni lazima tuziingize gharama za PPM kwenye manunuzi ya vitendanishi. Pia tunakubaliana naye kwamba ni wazo zuri, naomba nilichukue na nitalifanyia
kazi ndani ya Serikali.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bima kwa Wote ni utaratibu ambao ungeweza kusaidia sana wananchi wanyonge kuweza kupata huduma nzuri za afya kwa gharama nafuu, lakini vilevile ingesaidia serikali kupata mapato ya kuendesha huduma za afya, sasa nataka kuuliza ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria wa Bima ya Wote (Universal Coverage) kwa ajili ya kujadiliwa hapa Bungeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lipo katika negotiation ambapo wadau mbalimbali wameenda kushiriki na Wizara ya Afya na Wizara yetu inaangalia utaratibu mzuri, naomba niseme kwamba Serikali imejipanga katika hili na si muda mrefu baada ya wataalam kupita katika ngazi mbalimbali basi Serikali itakavyoona kwamba huu muswada sasa umeiva, basi utakuja hapa Bungeni kwa ajili ya kufanya maamuzi hayo.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nimesikiliza kwa makini sana majibu ya Mheshimiwa Naibu Wazir; swali langu la kwanza: Je, ni lini sasa Serikali italeta azimio hilo Bungeni kuweza kupitishwa? Maana amesema kwamba ni nchi mbili tu ambazo zimepitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sisi Tanzania tuna Sheria ya Kazi nadhani ya mwaka 2004. Je, ni lini sasa kulingana na mazingira ya sasa mtaileta tena ili iweze kufanyiwa mapitio?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza ameuliza, ni lini? Katika majibu yangu ya msingi, nimesema Serikali bado tunaendelea kupitia maudhui ya mkataba huu ili baadaye baada ya kujiridhisha tuweze kuuleta kwa ajili ya kuwa ratified.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Convention hii namba 189; katika utaratibu wa hizi Conventions huwa pia wanatoa vitu vinaitwa recommendation. Katika Convention hii kuna recommendation namba 201 ambayo inatoa mazingira ya nchi zile wanachama kuona namna bora ya kuweza kuandaa baadhi ya mechanism ili mikataba hii iweze kuridhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mambo mengi ambayo yapo katika mkataba huu tayari yapo ndani ya sheria zetu. Ukiangalia katika article ya kuanzia 13 mpaka 18 imezungumza kuhusu masuala ya Freedom of Association, masuala ya mikataba ambayo kwa mujibu wa sheria zetu, tayari yako covered.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika nchi kama Kenya, ziko baadhi ya Conventions ambazo hawajazi-ratify kwa sababu wanaona sheria yao ni nzuri zaidi kuliko ile mikataba. Kwa hiyo, nasi bado tunaona kabisa kwamba yako maeneo mengi sana ambayo sheria yetu ime-cover.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni mapitio ya sheria.
Kwa mujibu wa utaratibu wa masuala ya kazi, sisi tunafanya kazi katika mfumo ambao tunaita ni tripartism kwamba ni Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Inapotokea kwamba kuna jambo lolote ambalo linahitaji marekebisho au mapitio ya sheria, wadau huwa wanafanya taratibu hizo. Nasi kama Serikali mara zote tumekuwa flexible kuhakikisha kwamba sheria zetu za Kazi zinakuwa intact ili ziwe msimamizi mzuri katika masuala ya kazi katika nchi yetu.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatupa matumaini wananchi wa Kigamboni hususani kwa changamoto ambayo inatukabili. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika mwaka
wa fedha 2017/2018 Wilaya ya Kigamboni haikupata miradi mipya na hii inatokana na kwamba miradi ya mwaka jana (2016/2017) haikutekelezwa kikamilifu. Changamoto moja ilikuwa ni hali ya upatikanaji wa vifaa kwa maana ya transfoma, nguzo ndogo pamoja nyaya. Je, Naibu Waziri anaweza akatuhakikishia kwamba katika mwaka huu wa fedha transfoma zaidi ya 30, nyaya kilometa zaidi ya 30 na nguzo takribani 1,000 ambazo tunazihitaji tunaweza tukazipata ili kutekeleza miradi hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kigamboni iliingizwa katika REA Awamu ya Pili na kuna vijiji ambavyo vilirukwa. Je, utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu kwa maeneo ambayo yalibaki unaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni jinsi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wa Kigamboni.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la vifaa, kwanza kabisa tukiri kwamba kulikuwa na shida ya upatikanaji wa nguzo, transfoma pamoja miundombinu ya TANESCO, lakini kuanzia mwezi Juni kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni na Watanzania wengine wote, sasa nguzo zinapatikana hapa nchini na zinatosha kupeleka miundombinu katika maeneo yote. Nitoe tu tamko kwamba katika nchi nzima tulikuwa na wateja 29,000 ambao hawajaunganishiwa umeme wakati wameshalipia kuunganishiwa umeme, lakini wananchi hao wamepelekewa umeme bado wananchi 32 tu. Kigamboni eneo ambalo ni muhimu sana hadi sasa tumepeleka nguzo 2,100 na wateja waliobaki ni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wananchi wako wa Kigamboni Mheshimiwa Ndugulile kule Mwanzo Mgumu tumeshawapelekea nguzo, Msongozi kwa Mpika Chai na Cheka tumeshapeleka nguzo. Kwa hiyo, wananchi wataendelea kuunganishiwa umeme kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na miradi mingine ya Jimbo la Kigamboni, ni kweli kabisa tulipeleka miradi ya REA katika vijiji viwili Kigamboni kwa sababu Kigamboni kimsingi ni mitaa kwa sababu ipo Jijini Dar es Salaam, lakini tulipeleka mradi wa REA Kisarawe II kwenye eneo la Cheka pamoja na Kimbiji. Tuna mradi mwingine ambao upo chini ya TANESCO na umeshaanza ambao utapeleka umeme kwenye vijiji vya Mheshimiwa Ndugulile. Vijiji ambavyo vitapelekewa umeme ni pamoja ni Changanyikeni, Gezaulole pamoja na maeneo yote ya Dege.
Sambamba na hilo, tumepeleka mradi mwingine, kule Kigamboni kulikuwa na transfoma moja yenye uwezo wa MW 5 tu, sasa tumeing’oa tumeweka yenye MW 100 ambayo itapeleka umeme kwenye vijiji vyote vya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpe tu faraja mhesimiwa Mbunge wa Kigamboni kwamba matatizo ya umeme Kigamboni sasa yanaelekea kuisha. Utekelezaji wa REA umeshaanza tangu Juni, 2017 na utakamilika Machi, 2019.(Makofi)
kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeanzisha utaratibu mzuri wa kuwashirikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kuwapatia ramani za maeneo husika, je, Serikali itaweza kwenda mbali zaidi na kuwajengea uwezo pamoja na kuwapatia elimu Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Madiwani ili waweze kusimamia maeneo yale ya wazi na ujenzi holela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hivi karibuni Serikali imeweka zuio katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa watu ambao wamejihamasisha kubadilisha mashamba yao na kupima viwanja ili waweze kujenga na kuuza. Kwa sababu Serikali yenyewe imeshindwa ama kwa kiasi kikubwa haina uwezo wa kukidhi mahitaji ya ujenzi wa viwanja kwa ajili ya wananchi, haioni sasa ni muda muafaka kuweka utaratibu wa jinsi ya kupata kodi badala ya kuweka zuio?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile katika swali lake la kwanza ameishukuru Serikali kwa kutoa ramani kwa Wenyeviti wa Mitaa ili kuweza kulinda na kuhifadhi maeneo yao lakini akataka kujua kama Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuwajengea uwezo. Naomba niseme tu kwamba swali lake ni la msingi sana na kama nilivyokuwa naeleza muda mfupi uliopita, watu hawa wanahitaji pia kupewa elimu ya kutosha kuweza kutambua ramani zile na namna ya kuzisimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Wizara imeonyesha dhamira ya dhati kutaka kulinda maeneo ili yasivamiwe kwa kushirikisha elekezi kwa sababau tumeona maeneo kama Kigamboni kuna makampuni zaidi ya matano yamepima maeneo yale lakini kila kampuni ina bei yake ya kiwanja. Kuna wanaouza square meter moja shilingi 25,000/=, kuna wanaouza shilingi 20,000/= na kuna wanaouza kwa shilingi 10,000/=. Ni nani Mtanzania wa kawaida ataweza kununua? Serikali pia huwa inapima lakini gharama zake hazijafikia hata shilingi 10,000/= kwa square meter moja, iweje wao wapime na kuuza katika bei kubwa za namna hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imeamua kwa maana ya Wizara kusitisha kwanza zoezi hili na wiki hii bei elekezi itakuwa imeshakamilika na itatoka ili viwanja hivi hata kama wanapima, tunashukuru kwa sababu wanasaidia katika kupanga miji yetu, lakini wapange miji na kuweza kuuza viwanja katika bei ambayo mlaji wa kawaida ataweza kumudu, isiwe ni bei ambazo zinakwenda kubeba wale watu wenye pesa na wasio na pesa watajikuta hawana viwanja. Kwa hiyo, dhamira ya Serikali ni njema na naomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono na wiki hii bei elekezi itatoka na viwanja vitaendelea kupimwa kama kawaida lakini kwa maelekezo mazuri ya Wizara. wahusika wenyewe, niwaombe Halmashauri husika kwa sababu Wenyeviti hawa sio wengi sana kwa kushirikiana na Wizara yangu waweze kuweka utaratibu mzuri ili watu hawa waweze kupewa angalau ABCs za kuweza kusoma na kutambua ramani zile ili waweze kufanya kazi yao kwa ufasaha zaidi. Maana tukishawawezesha hawa, kwa sababu pia siyo wote wanaofurahia namna ambavyo miji yao inaharibika, wengi wanachukia, watakuwa katika position nzuri ya kuweza kusimamia jukumu ambalo wamepewa sasa ambalo linastahili kusimamiwa katika maeneo yao. Kwa hiyo, niseme tu Wizara yangu itashirikiana na Halmashauri kuandaa mipango mizuri ili watu hawa waweze kupewa elimu ili waweze kusimamia vizuri maeneo yao kama ambavyo wameelekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili amezungumzia habari ya zuio la Wizara kwa upimaji unaoendelea katika maeneo mbalimbali. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge watambue kwamba hatua iliyochukuliwa na Wizara ina lengo zuri na hasa la kutaka kuwalinda walaji wa kawaida kwa maana watu wa kawaida ambao wanatafuta viwanja kwa ajili ya kuweza kupata maeneo yao. Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya mwaka 2007 inaruhusu watu binafsi kupima maeneo hayo lakini kwa kuzingatia taratibu za maeneo hayo.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NGUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dhana ya kupunguza matumizi ya fedha na kubana matumizi katika Serikali, Serikali imekuwa inanunua magari kutoka kwa ma-dealers, magari haya huwa yanakuja na warrants ya kilometa laki moja au miaka mitatu matengenezo yanakuwa bure, lakini warrant hii Serikali imekuwa haitumii na badala yake imepeleka magari kwenye garage za watu binafsi na kutumia gharama kubwa sana.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwanza inasimamia hizi warrant, ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa kununua magari kutoka kwa manufactures?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri wake tutaenda kuufanyia kazi na baadae tutamletea majibu stahiki.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nimesikiliza kwa makini sana majibu ya Mheshimiwa Naibu Wazir; swali langu la kwanza: Je, ni lini sasa Serikali italeta azimio hilo Bungeni kuweza kupitishwa? Maana amesema kwamba ni nchi mbili tu ambazo zimepitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sisi Tanzania tuna Sheria ya Kazi nadhani ya mwaka 2004. Je, ni lini sasa kulingana na mazingira ya sasa mtaileta tena ili iweze kufanyiwa mapitio?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza ameuliza, ni lini? Katika majibu yangu ya msingi, nimesema Serikali bado tunaendelea kupitia maudhui ya mkataba huu ili baadaye baada ya kujiridhisha tuweze kuuleta kwa ajili ya kuwa ratified.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Convention hii namba 189; katika utaratibu wa hizi Conventions huwa pia wanatoa vitu vinaitwa recommendation. Katika Convention hii kuna recommendation namba 201 ambayo inatoa mazingira ya nchi zile wanachama kuona namna bora ya kuweza kuandaa baadhi ya mechanism ili mikataba hii iweze kuridhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mambo mengi ambayo yapo katika mkataba huu tayari yapo ndani ya sheria zetu. Ukiangalia katika article ya kuanzia 13 mpaka 18 imezungumza kuhusu masuala ya Freedom of Association, masuala ya mikataba ambayo kwa mujibu wa sheria zetu, tayari yako covered.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika nchi kama Kenya, ziko baadhi ya Conventions ambazo hawajazi-ratify kwa sababu wanaona sheria yao ni nzuri zaidi kuliko ile mikataba. Kwa hiyo, nasi bado tunaona kabisa kwamba yako maeneo mengi sana ambayo sheria yetu ime-cover.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni mapitio ya sheria. Kwa mujibu wa utaratibu wa masuala ya kazi, sisi tunafanya kazi katika mfumo ambao tunaita ni tripartism kwamba ni Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Inapotokea kwamba kuna jambo lolote ambalo linahitaji marekebisho au mapitio ya sheria, wadau huwa wanafanya taratibu hizo. Nasi kama Serikali mara zote tumekuwa flexible kuhakikisha kwamba sheria zetu za Kazi zinakuwa intact ili ziwe msimamizi mzuri katika masuala ya kazi katika nchi yetu.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya TFDA ikiwa ni pamoja na Baraza la Wafamasia ni udhibiti wa dawa. Sasa hivi kumekuwa na tatizo kubwa sana la uuzaji wa dawa holela ikiwa ni pamoja na hizi dawa zinaitwa P2. Nini mkakati wa Serikali wa kudhibiti uuzaji holela wa dawa katika maduka bila kuzingatia misingi na matumizi ya dawa hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza kwamba kuna uuzaji wa dawa kwa namna holela. Kikubwa wala hilo halihitaji kusema tunajipangaje. Hilo liko wazi, zipo hizo taasisi, yupo Mfamasia wa Serikali, ipo Pharmacy Council, wapo TMDA ambao ndiyo wanahusika kufanya hiyo kazi. Straight forward ni kwamba hatutaki kuliona hilo. Waanze kusimamia miongozo na sheria na taratibu za kusimamia masuala mazima ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kimsingi ni agizo tu linatoka hapa kwamba inatakiwa hili analolisema Mbunge lisiweze kuonekana tena likitokea kama lipo. Tutakwenda kulifuatilia kama lipo, wanaofanya hivyo watawajibika na vile vile tutaenda kusimamia sheria kama ambavyo ilishapitishwa na Bunge. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia stahiki wananchi wa mitaa ya Mwasonga, Madege na Sharifu wanaoguswa na mradi wa uchimbaji wa madini ya mchanga kupitia Kampuni ya Nyati katika Wilaya ya Kigamboni.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna kampuni ya uchimbaji wa madini ya mchanga mzito unaitwa heavy sands katika Jimbo lake, na kampuni husika inaitwa Nyati na hivi sasa ninavyojibu swali lake majedwali yote ya malipo ya fidia yameshakamilishwa, wapo watakofidiwa wapatao 1,198 na Mdhamini Mkuu wa Serikali ameshamaliza kazi yake na hivyo mpango wa malipo yao unaweza ukafanyika ndani ya miezi miwili ijayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika,
nianze kwa ushauri mdogo kwamba Serikali iende ikaziangalie hizi gharama, bado ni kubwa sana na zinadumaza ubunifu. Maswali mawili yangu ya nyongeza; vijana wengi wamejiajiri kupitia ubunifu na wengi wanafanyakazi na taasisi za nje, changamoto imekuwa ni malipo.

Je, ni lini sasa Serikali itaruhusu mfumo wa pay poll ili vijana hawa ambao wamejiajiri na kufanya kazi za consultancy huko nje ya nchi waweze kupata malipo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; tuna vijana wengi wabunifu ambao wanaandaa mifumo ya software. Software ambazo tunazinunua online hazitozwi VAT, lakini zile ambazo zinatengenezwa nchini, zinatozwa VAT. Ni lini sasa Serikali itafanya mapitio ili kuhakikisha kwamba wabunifu wa ndani ya nchi wanapata nafuu katika mifumo ambayo wanaitengeneza hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndugulile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Ndugulile kwa kiasi ambacho anapigania wananchi wa Jimbo la Kigamboni na Watanzania kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Paypal bado haujazuiliwa na unaendelea kutumika nchini. Mwaka 2016 wawakilishi wa Paypal walifika Benki Kuu ya Tanzania ili kupata taratibu zinazotakiwa katika kutekeleza huduma hiyo. Hata hivyo, Serikali ipo tayari kupokea maombi ya leseni kwa sababu hawawezi kuendesha huduma hiyo bila kuwa na leseni. Serikali iko tayari kupokea leseni hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli kabisa. Naomba nikiri kwamba ni kweli huduma hii ya software au huduma za mtandao hulipiwa VAT ni suala la kweli kabisa kwamba lazima ilipiwe VAT na ni tofauti, yaani VAT ambayo inalipiwa kwa software ambazo zinatengenezwa nchini, zinakuwa na ongezeko hilo la thamani tofauti na ambazo wananunua ndani ya mtandao online.

Mheshimiwa Spika, suala hili tayari utafiti umeshafanyika kwa kina na mapendekezo yake tayari. Nalihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba mapendekezo hayo yatawasilishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/ 2023 mwaka huu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Ujenzi wa barabara ya mwendokasi kwenda Mbagala pamoja na magari yanayotoka bandarini na kuingia bandarini na uwepo wa mizani katika eneo la bandari linaleta usumbufu mkubwa sana kwa wakazi wa Kigamboni ambao wanatumia Daraja la Nyerere. Je ni nini mkakati wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha kwamba adha wanazozipata wananchi zinaondokana na changamoto hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara zote na hasa za mjini zinajengwa na kupanuliwa kwa maana ya magari yaweze kupita ama mawili ama matatu ama manne. Hata hivyo, kama kuna suala ambalo liko very specific kwa barabara ambayo ameainisha Mheshimiwa Mbunge, nitamwomba tuweze kuonana naye kama Wizara ili tuone kama kuna changamoto yoyote ambayo iko tofauti sana tuweze kuwa na mpango wa haraka kuweza kuondoa changamoto hiyo kwa hiyo barabara ambayo ameainisha Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Wizara ya Ujenzi na majibu yenye faraja kwa wakazi wa Kigamboni hususan maeneo ya Mwasonga, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ilifanya ujenzi wa kipande kidogo cha kilometa moja kutoka Kibada junction kwenda Mwasonga. Sasa hivi ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu, kipande kile cha kilometa moja hakijakamilika.

Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa kile kipande cha kilometa moja ambao ujenzi wake umeanza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; barabara nyingi pale Kigamboni zimemeguka kutokana na kukosa kingo kutokana na magari mazito kuchepuka nje ya barabara na kwingine barabara zimekatwa kashata kutokana na ubovu lakini hazijakarabatiwa. Sasa ni lini barabara zile zitakarabatiwa lakini vile vile kuwekwa kingo ili barabara zile zisiendelee kumomonyoka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mkandarasi ambaye alipewa kazi ya kukamilisha kipande cha kilometa moja amechelewa na tayari ameshaandikiwa barua na anatumikia adhabu ya liquidated damage na kama atakuwa hajakamilisha ndani ya siku 100, tunafunga mkataba kumtafuta mkandarasi mwingine. Hivi tunavyoongea yupo anakamilisha hiyo kazi na yuko kwenye 75%-80%.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mashimo na kingo za barabara, tayari tumesham-engage mkandarasi, Mark Construction na ameshaanza kazi na kuharibika kwa barabara hii ni kweli ni barabara ya zamani, traffic imeongezeka sana na magari mengi makubwa yanapita. Kwa hiyo tayari mkandarasi yupo kwa ajili ya kukarabati barabara hizo za lami. Pia hata hizo za changarawe tumeshamweka mkandarasi kuhakikisha kwamba anakarabati hizo barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na Wilaya 63 ambazo mnatarajia kujenga VETA katika mwaka huu wa fedha.

Je, Wilaya ya Kigamboni ni moja ya Wilaya hizo unaweza ukalithibitisha hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni, kaka yangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwamba katika orodha na mimi nimeipitia vizuri na Wilaya ya Kigamboni ni miongoni mwa Wilaya ambazo ziko kwenye mpango wa kujengewa vyuo hivi na bahati nzuri maeneo yameshatengwa kwa ajili ya ujenzi na mimi Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili kwa vile niko karibu pale tutakwenda kulitembelea na kuona namna hani tunaweza tukafanya. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mgogoro kama huo huko vilevile katika Jimbo la Kigamboni katika Kata ya Kimbiji eneo la Kijaka.

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ndugulile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kulifuatilia suala hili kwa karibu, kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni na ninapenda kumfahamisha kwamba mgogoro huu tayari na wenyewe unashughulikiwa na upimaji ulishafanyika, kwa hiyo tunasubiri tupate hati na baada ya hapo hatua zinazofuata zitaendelea. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kigamboni katika Hotuba ya Bajeti ya Mwaka jana ilitajwa kwamba ni moja ya wilaya ambayo mtakwenda kujenga chuo cha VETA na imebakia miwezi miwili. Ni lini sasa ujenzi ule utaanza ili wananchi wa kigamboni waweze kunufaika na chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kigamboni ni miongoni mwa wilaya 64 zilizobaki katika ujenzi wa vyuo 64 zilizobaki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba geotechnical survey, topographical survey, environmental impact assessment tayari tumeshafanya. Tunasubiri majibu kwa maana ya results ya tafiti hizo na baada tu ya majibu hayo, tunaenda kuanza ujenzi katika mwaka huu wa fedha, nimuondoe wasiwasi kazi hiyo inakwenda kufanyika.
MHE. DKT. FAUSTINE NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba kuna nguvu kubwa sana imepelekwa katika ukanda wa Maziwa katika suala zima la ufugaji wa samaki kwa vizimba. Je, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba na Ukanda wa Pwani ikiwa ni pamoja na Kigamboni zinanufaika na uvuvi wa samaki kwa njia ya vizimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa 2022/2023 upande wa Mikoa ya Pwani kwenye programu hii ya ufugaji wa samaki tulipeleka pesa zaidi upande wa ukulima wa mwani Takribani Bilioni 2.1zimenufaisha wakulima wa mwani kutoka Tanga kule Moha mpaka Mtwara kule Msimbati, sasa katika mwaka wa 2023/2024 kupitia programu maalum ya blue economy tunatarajia kupeleka tena nguvu kwa maana ya uwezeshaji, kwa lengo la mwani vilevile unenepeshaji wa Kaa na ufugaji wa Majongoo Bahari. Kwa hivyo, wakulima na wavuvi wa ukanda wa Pwani wakiwemo wa Kigamboni na wenyewe makundi ya vijana na akina mama yatapata kunufaika na programu hii. Ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, naomba nimuulize Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mwaka wa fedha 2023/2024 umebaki miezi miwili.

Je, ni lini wananchi wa Kigamboni watarajie vivuko hivyo viwili vidogo kama Mheshimiwa Naibu Waziri anavyoongea?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa TEMESA ni Taasisi ya Umma inayotoa huduma za ufundi na umeme pamoja na huduma za vivuko.

Je, Serikali haioni sasa umefika muda muafaka wa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma ya vivuko ili kuongeza ufanisi na kuongeza wigo wa huduma hususani kwa wananchi wa Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, mwaka huu tulitegemea tuanze manunuzi ama utengenezaji wa kivuko na kazi hiyo tumeshaanza, kwa sababu tulitangaza tenda kununua hivi vivuko viwili lakini ilionekana watu hawa walikuwa wame-bid, wote walikuwa wame-tender bei za juu wakati wa kufanya evaluation, hivyo tunatangaza upya tena tenda, kwa hivyo tupo kwenye utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kigamboni na Magogoni kwamba hizo taratibu zinaendelea tutakapopata Mkandarasi sahihi shughuli hizo zitaanza mwaka huu wa fedha na tayari tumeshaanza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, tayari yalikuwa pia ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba taasisi zote ambazo zinafanya biashara kama kuna uwezekano wa watu binafsi kufanya biashara basi waruhusiwe, hivi ninavyoongea tayari Azam ameshaonesha nia ya kutaka kufanya shughuli katika kivuko hiki cha Kigamboni na sasa itakuwa ni kwa vivuko vyote tunategemea Serikali ikishakamilisha taratibu basi wale wafanyabiashara ambao wanataka kufanya biashara sambamba na TEMESA taratibu zikishakamilika wataruhusiwa kufanya hivyo. Ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kigamboni ina mtandao wa barabara za TARURA takribani kilometa 1,000, lakini ni kilometa tano tu ambayo ni asilimia 0.5 percent ambazo zina kiwango cha lami. Bajeti ya TARURA pale ni shilingi bilioni 3.5.

Je, nini mkakati wa TARURA kuongeza bajeti ili barabara za Wilaya ya Kigamboni zifanane na barabara nyingine za Jiji la Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA itaendelea kuongeza fedha katika Wilaya ya Kigamboni na Jimbo la Kigamboni kwa Mheshimiwa Ndugulile kadri ya upatikanaji wa fedha. Ni lengo la Serikali hii ya Awamu ya Sita kuhakikisha TARURA inakuwa na nguvu ya kutosha kutengeneza barabara nyingi zaidi za lami katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo kule Kigamboni.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu haya ya Serikali. Katika dhana hiyo ya utayari katika masuala ya uokozi, Wilaya ya Kigamboni ina matanki makubwa ya mafuta na hatuna gari ya zimamoto wala Kituo cha Zimamoto.

Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na Kituo cha Zimamoto na gari la Zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina mpango wa kuendelea kuimarisha Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vifaa na utaalam ili kutekeleza majukumu hayo. Kama mazungumzo yetu na wakopeshaji yataenda vizuri, tunaweza kupata magari zaidi ya 150 kwa ajili ya shughuli za Zimamoto na Uokozi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya Kigamboni ambayo Mheshimiwa amefanya marejeo yake na umuhimu wa uwekezaji uliopo pale hasa matenki ya mafuta, kipaumbele kitawekwa kuhakikisha kwamba kunapatikana magari ya kuzima moto na kuimarisha Ofisi ya Zimamoto upande wa Kigamboni ili kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi, nashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itaanza mpango wa kujenga soko jipya la kisasa la samaki katika Wilaya ya Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la nyongeza Mheshimiwa Ndugulile, anataka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko jipya Kigamboni. Ujenzi wa soko jipya Kigamboni utategemea uwezekano wa kibajeti. Kama Serikali itapata bajeti, basi iko tayati kuanza ujenzi wa soko hilo jipya pale Kigamboni, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Kigamboni ina ukanda wa bahari takribani kilomita 70, nataka kujua nini mkakati wa Serikali wa kukuza kilimo cha mwani na jongoo bahari katika Wilaya ya Kigamboni kama mkakati wa kuchochea uchumi wa bluu na kuongeza ajira nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mkakati wetu mkubwa ni kuhakikisha tunafikia maeneo yote ya ukanda wa pwani na ndio maana hivi karibuni tumepata fedha kutoka maeneo mbalimbali. Juzi tumesaini mkataba wa fedha karibu dola milioni 13 na watu wa USAID na sehemu ya hizo fedha ni pamoja na kuhamasisha kilimo cha mwani na majongoo bahari katika Ukanda wa Pwani ikiwemo Kigamboni. tumefanya hivyo Ifani, Tanga, kwa hiyo ni jambo ambalo lipo katika mchakato. Ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Mkoa mkubwa na ni Jiji la kibiashara, kwa kuzingatia vigezo vyote, kwa maana ya idadi ya watu, kiuchumi na idadi ya magari ni kubwa sana. Je, nini mtazamo wa Serikali wa kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya Dar es Salaam Metropolitan Authority?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ndugulile la kwa nini Serikali isianzishe Mamlaka ya Usimamizi wa Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tunalipokea kama ushauri na tayari Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa maelekezo yake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angellah Kairuki, kuna timu ambayo inaliangalia hili na kuona ni namna gani linaweza kufanya kazi, pale timu hii itakapowasilisha ripoti hii kwa Mheshimiwa Waziri, basi tutaona hatua zinazifuata za kuchukuliwa.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ya Ujenzi ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vivuko vipya: Ni lini ujenzi huo wa vivuko vipya utaanza pale Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mwaka huu unaoendelea, Serikali ilitenga fedha za kujenga vivuko vingi, vikiwemo vya maziwa na vya pale Kigamboni alivyovisema Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunategemea kujenga kivuko kimoja kikubwa, lakini pia kumetokea maombi kadhaa na Serikali inafanya tathmini kuona baada ya kupata uzoefu wa vivuko hivi vidogo vya Bakhresa, namna ambavyo tunaweza kufanya ni kujenga kivuko kibwa na pia kuwa na vivuko vidogo. Kwa hiyo, kinachoendelea sasa hivi, tuko kwenye taratibu za manunuzi kuhakikisha kwamba kile tulichokipanga tunakifanya pia katika mwaka huu, pamoja na kuongeza vivuko vidogo ambavyo tumeona vinakwenda kwa haraka sana kati ya Kigamboni na Kivukoni, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi katika swali hili ambalo limetoka kwa Mheshimiwa Mariam Kisangi, umesema kwamba barabara ile inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami, tunashukuru kwa hilo, lakini barabara hii kwa sasa hivi imeharibika sana kutokana na uzito wa magari yanayopita pale pamoja na mvua ambazo zimenyesha: Ni lini ukarabati wa barabara hii utafanyika wakati tunasubiri barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara nyingi za Dar es Salaam, hasa ambazo ni kwa kiwango cha changarawe, zimepata changamoto kutokana na mvua ambazo zimekuwa zinaendelea kunyesha katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika barabara zake hizo alizozitaja, tayari tumesham-engage Mkandarasi, Ibra Construction Company ambaye amepewa barabara ya kutoka Mji Mwema kwenda Kimbiji na pia huyu huyo atafanya kazi kutoka Kibada – Mwasonga – Kimbiji na kuendelea mbele ili kurejesha mawasiliano na kuondoa changamoto ambazo zinaendelea kwa sasa. Kwa hiyo, mkandarasi tayari ameshakuwa site, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wastaafu wengi wamekuwa wanapata adha ya kufanya uhakiki wa mara kwa mara kuthibitisha kwamba bado wako hai, proof of life na wanahitajika kwenda makao makuu ya Wilaya au ama katika taasisi ambazo walistaafu kwa ajili ya kwenda kufanya hiyo proof of life?

Je, ni mkakati gani ambao Serikali mtachukua kuhakikisha kwamba kunakuwa na mfumo wa kisasa wa kuweza kufanya hiyo proof of life badala ya usumbufu ambao unaendelea kwa hivi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndugulile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwa na changamoto sana ya wastaafu wetu kwenda kuambiwa kwamba anaenda kuhakikiwa taarifa na kadhalika, lakini tuliliona hilo na tukaanzisha mfumo maalum wa kuwahitaji wao kuwa na namba zao za mawasiliano za kiganjani, lakini pia kuanzisha portal maalum ya kutoa taarifa za wanachama na hatua ya pili tuliyoichukua ni kwamba kuhakikisha sasa taarifa hizi zinaenda on monthly basis kuhakikisha kwamba taarifa zake kwa wakati wote zinapatikana kwa Mfumo wa TEHAMA. Kwa hiyo, tumejihimarisha kwenye TEHAMA na tunafanya vizuri na sasa tumekwishakuanza kuwahudumia vizuri, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ilitenga Shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Sangatini eneo la Tundwi Songani kule Pemba Mnazi katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa ujenzi ule haujaanza: Ni lini ujenzi wa daraja Sangatini utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Sangatini lilishatengewa fedha na fedha ipo. Tender ilitangazwa lakini ali-tender mtu mmoja na akawa ame-tender bei ya juu na tumeshalitangaza tena. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tender zitafunguliwa wiki hii na baada ya hapo daraja hili litaanza kujengwa kwa bajeti ya mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.