Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile (96 total)

MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Katika miaka ya 70 kulikuwa na Community Centres ambapo wananchi wa rika tofauti walikuwa wakikutana na kubadilishana mawazo na maeneo hayo yalikuwa ya muhimu kupata huduma za jamii kama afya ya akili, wananchi wenye msongo wa mawazo, ugonjwa wa kisukari, kifafa, pumu na shinikizo la damu:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha Community Centres?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa siku hii ya leo, lakini namshukuru vilevile Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu. Niwashukuru pia wananchi wa Kigamboni kwa kuendelea kuwa na imani nami kama mtumishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali Namba 72 la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na pia namuunga mkono Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri kuhusiana na suala zima la kurejesha majumba ya maendeleo na umuhimu wake ulionekana hapo awali katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa dhumuni la kuwapatia wananchi taarifa mbalimbali, maarifa, burudani, lakini pia stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mapendekezo yaliyotolewa na Wizara yangu ya kuimarisha sekta ya maendeleo ya jamii ya mwaka 2007, pamoja na mambo mengine yaliyopendekezwa suala la kuyafufua majengo ya maendeleo na kuyarejesha katika matumizi yake ya awali lilitiliwa mkazo. Hata hivyo, Halmashauri 135 ndizo zilizokuwa na majumba ya maendeleo yaliyojengwa mwaka 1961 na mwaka 1962. Zipo Halmashauri zimerejesha matumizi ya awali ya majumba hayo, ikiwa ni pamoja na Iringa Manispaa, Dodoma Manispaa na Mpwapwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Halmashauri ambazo zimebadilisha matumizi ya majengo haya na hayawezi yakarudishwa katika matumizi ya awali. Kwa mfano, Manispaa ya Temeke imekuwa Hospitali ya Rufaa, Manispaa ya Mtwara imeendelezwa na kuwa Ofisi ya Ardhi na Maendeleo ya Jamii na Manispaa ya Ilala imeendelezwa na kuwa Ofisi za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara yangu imekuwa ikifanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI mara kwa mara, juu ya kukumbusha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kurejesha matumizi ya majengo ya maendeleo kwa lengo la kutumika kama sehemu ya kujadili masuala ya maendeleo, kupata taarifa mbalimbali, burudani na stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa, hili ni jukumu la kila Halmashauri, hivyo niwaombe tunapokutana katika vikao vyetu kujadili mipango mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zetu, basi tulisisitize suala hili muhimu na lipewe uzito unaostahili ili kulitekeleza kwa vitendo.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanasababisha vifo vingi, hasa kwa Watanzania wanaoishi vijijini ambako madaktari bingwa na huduma za vipimo vya maabara havipatikani:-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha programu maalum ya kupeleka Madaktari Bingwa na maabara zinazotembea vijijini?
• Je, Serikali ina mpango wa kutoa ruzuku ya tiba kwa Watanzania wasio na uwezo wanaougua magonjwa yasiyoambukizwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, iliunda kikosikazi ambacho kina wataalam na vifaa tiba vya kutosha ambacho hushirikiana na timu za mikoa kupima na kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Kwa kuzingatia kuwa wataalam ni wachache hapa nchini na huduma lazima ziwafikiwe wananchi, Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza kimetengeneza mpangokazi na ratiba ya kuzunguka mikoa yote ili kuelimisha na kutoa huduma hizo bila malipo.
Mheshimiwa Spika, kampeni ya kwanza ilizinduliwa tarehe 17 Desemba, 2016 na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwenye Viwanja vya Leaders Club, Mkoani Dar es Salaam. Kampeni kama hizi zimefanyika katika Mikoa ya Dodoma, Katavi, Kilimanjaro na Ruvuma. Hadi hivi sasa utaratibu huu umeweza kuwafikia wananchi takribani 14,896.
Mheshimiwa Spika, aidha, upimaji huambatana na wagonjwa kuchukuliwa vipimo vinavyotoa majibu kwa haraka (rapid test), teknolojia ambayo inaruhusu vipimo kufanyika na majibu kupatikana katika mazingira husika. Hivyo, Serikali haina mpango wa kuweka maabara zinazohamishika (mobile clinics) kwa sasa.
(b) Mheshimiwa Spika, Sera ya Serikali kwa magonjwa sugu, yakiwemo yasiyo ya kuambukiza, ni kwamba matibabu yanatolewa bila malipo kwa wagonjwa kama vile wa kisukari, kansa na shinikizo la damu. Hivyo, Serikali haitoi ruzuku kwa wagonjwa wasio na uwezo, bali inagharamia matibabu kwa wagonjwa wanaogundulika kuwa na magonjwa yasio ya kuambukiza bila malipo. Nashauri wananchi kufika katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili kupima afya zao na kupata ushauri wa matibabu mapema.
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:-
Wananchi wengi hapa nchini hasa wanawake hutumia vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu. Pamoja na jitihada za Serikali kuzuia bidhaa hizo lakini bado vinaingizwa nchini na kutumika.
(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuzuia uingizwaji na utumiaji wa vipodozi hivi?
(b) Je, Serikali inaweza kutumia fedha kiasi gani kuzuia bidhaa hiyo kuingia nchini?
(c) Je, adhabu gani inatolewa kwa yeyote atakayekamatwa akiingiza nchini vipodozi visivyofaa kwa matumizi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye sehemu (a) (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, TFDA imekuwa ikichukua hatua zifuatazo kudhibiti uingizwaji na utumiaji wa vipodozi. Vipodozi vyote hutakiwa kusajiliwa kabla ya kibali cha kuingiza nchi kutolewa. Mpaka sasa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3,179 ambavyo ndivyo vinavyorushusiwa kuingizwa na kutumika nchini. TFDA imefungua Ofisi saba za Kanda katika Mikoa ya Arusha kwa maana ya Kanda ya Kaskazini, Dar es Salaam - Kanda ya Mashariki, Dodoma - Kanda ya Kati, Mbeya - Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mtwara - Kanda ya Kusini, Mwanza - Kanda ya Ziwa na Tabora - Kanda ya Magharibi kwa lengo la kuimarisha ukaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 maeneo 3,648 yalikaguliwa ambapo kati ya hayo maeneo 120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi kwa binadamu na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Vilevile jumla ya tani
407.82 za vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania bilioni 1.36 ziliteketezwa na TFDA na kesi 52 zilifunguliwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo, wakaguzi wa TFDA wamewekwa katika vituo vya forodha kwenye mipaka ya Namanga, Holili, Horohoro, Tunduma, Sirari, Kasumulu, Mutukula, Rusumo, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere na vituo vingine vya forodha vilivyoko katika Mkoa wa Da es Salaam kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi vinavyoingizwa nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 TFDA ilitenga na kutumia jumla ya shilingi milioni 154.8 kwa ajili ya operation maalum ya ukaguzi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na vipodozi. Aidha, katika mwaka 2017/2018, mamlaka imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 132.16 ambazo zimekuwa zikitumika katika operation za kubaini na kukamata vipodozi haramu.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 91(b) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura ya 129 kinatoa adhabu isiyopungua miezi mitatu au kulipa faini isiyopungua shilingi 500,000 au adhabu zote mbili kwa pamoja kwa yeyote atakayekamatwa akiingiza vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya binadamu. Sambamba na adhabu hii, vilevile mtuhumiwa anapaswa kugharamia uteketezaji wa vipodozi vyote vilivyokamatwa na wakaguzi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko la watoto wa mtaani katika miji na majiji mengi hapa nchini.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na sheria zitakazoibana jamii kuwa na wajibu wa kulea watoto hawa badala ya kuwaachia majukumu Mashirika yasiyo ya Kiserikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna ongezeko la watoto wa mitaani katika miji na majiji mengi hapa nchini. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatekeleza Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inabainisha majukumu ya familia, jamii pamoja na Halmashauri za Miji na Majiji hapa nchini katika kutekeleza wajibu wa matunzo na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 95(1) cha Sheria ya Mtoto kinaelekeza na naomba kunukuu; “Ni jukumu la kila mwanajamii ambaye atakuwa na ushahidi au taarifa ya kuwa haki za mtoto zinavunjwa na wazazi, walezi au ndugu ambao wana jukumu la kumlea mtoto lakini wameshindwa kufanya hivyo au wameacha kwa makusudi kutoa huduma za chakula, malazi, haki ya kucheza au kupumzika, mavazi, haki ya matibabu na elimu atatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri husika.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 95(2), kinamuelekeza Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri husika kupokea taarifa ya malalamiko na kumwita mlalamikiwa ili kujadili tatizo hilo. Maamuzi yatatolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kwa kuzingatia maslahi mazima ya mtoto husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mlalamikiwa atapuuza maamuzi yalyotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii, shauri hilo litafikishwa Mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 95(5) ambacho kinaelekeza na naomba kunukuu; “Mtu yeyote atakayekiuka kifungu cha 95(1) atakuwa ametenda kosa, na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa faini isiyopungua shilingi elfu hamsini za Kitanzania au kifungo cha miezi mitatu jela au vyote viwili”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini kutunga Sheria Ndogo zitakazodhibiti watu wanaosababisha watoto kuishi na kufanya kazi mitaani. Aidha, Waheshimiwa Wabunge na sisi tutoe elimu ya uwepo wa sheria hii kwa wapiga kura wetu.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ilimaanisha nini kusema kuwa matibabu ni bure kwa kinamama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mama wajawazito ni moja ya makundi maalum wanaostahili kupata huduma za matibabu bure kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Uchangiaji wa Huduma za Afya wa mwaka 1997. Aidha, mwongozo umeweka bayana kuwa akina mama wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila malipo na sio zile tu zinazohusu huduma za ujauzito.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwongozo uliopitiwa mwaka 2009/2010, imetamkwa bayana kuwa huduma ya afya kwa mama wajawazito ni bure ikiwa na maana kwamba mara tu mwanamke anapokuwa na ujauzito, huduma zote kuanzia kliniki ya ujauzito, pale atakapougua maradhi yoyote pamoja na huduma ya kujifungua, sanjrari na kumuona daktari, kupatiwa vipimo, kupewa dawa na kufanyiwa upasuaji pale utakapohitajika kufanyiwa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuondoa adha kwa wananchi, Wizara imeanzisha utaratibu wa kutenga bajeti itakayotumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vinavyohitajika wakati wa kujifungua (delivery parks), delivery parks hizo watapewa akina mama wajawazito wanapokaribia kujifungua ili wawe wanatembea na vifaa hivyo. Hii itapunguza kero kwa akina mama kujinunulia vifaa vyao wao wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inazikumbusha halmshauri kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hii ili akina mama wajawazito wapate huduma za matibabu bure kama Mwongozo wa Uchangiaji wa Mwaka 1997 na Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inavyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wananchi wanaombwa kutoa taarifa kuhusu hospitali zinazotoza fedha kwa ajili ya matibabu kwa akina mama wajawazito ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Sasa hivi baadhi ya watumishi wa Halmashauri kama vile Wakurugenzi na wengine wanapostaafu hupatiwa kadi ya bima ya afya pamoja na familia zao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia kadi kama hizo watumishi na viongozi wa Serikali waliostaafu kabla ya utaratibu huo kuanzishwa ikizingatiwa kuwa wengi wao walilitumikia Taifa hili kwa uadilifu na uaminifu mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango wa wastaafu waliowahi kuwa watumishi na viongozi wa Umma katika maendeleo ya Taifa hili. Kwa sababu utaratibu wa kuwapatia bima ya afya wastaafu waliowahi kuwa viongozi na watumishi wa Umma ni kupitia Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura Namba 395, Toleo la Mwaka 2015 kwa kuzingatia vigezo na masharti yafuatayo:-
(i) Mstaafu husika lazima awe alikuwa mwanachama mchangiaji wa mfuko kabla ya kustaafu.
(ii) Mstaafu awe amefikisha umri wa kustaafu kwa hiari miaka 55 au kwa lazima au miaka 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia utaratibu huu, wanachama wastaafu wanaokidhi masharti na vigezo vilivyoainishwa, hupatiwa bima ya afya inayomuwezesha kupata huduma za matibabu yeye mwenyewe pamoja na mwenza wake hadi mwisho wa maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia uhitaji wa huduma za afya na changamoto za upatikanaji wa huduma hizi kwa wastaafu na wananchi wengine walio nje ya utaratibu huu, mfuko umeweka utaratibu wa kujiunga kwa hiari kupitia utaratibu wa mwanachama binafsi.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Liko tatizo la uhaba wa dawa na madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa dawa na Madaktari wa kutosha wanakuwepo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kanyasu Constantine John, Mbunge wa Geita Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu zilizopo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto zinaonyesha kuwa Hospitali ya Mkoa wa Geita ilipandishwa hadhi kutoka iliyokuwa Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018. Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya walengwa wa huduma kwenye hospitali hiyo, hospitali ya Wilaya ya Geita imekuwa ikipata mgao mkubwa wa fedha za kununulia dawa, vifaa tiba na vitendanishi kuliko hospitali za Mkoa isipokuwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga na ile ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hali hiyo, Hospitali ya Geita katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitengewa fedha za Kitanzania shilingi 141,939,184 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilipokea kiasi cha shilingi 278,666,525 kiasi ambacho ni takribani mara mbili ya mgao wa mwaka wa fedha 2015/ 2016. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Hospitali hii baada ya kupandshwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, mgao wake umeongezeka na kufikia fedha za Kitanzania shilingi 368,287,841; hadi kufikia mwezi Desemba 2017, Hospitali hii ilikuwa imepokea kiasi cha milioni 168,609,586.94 kwa ajili ya kununua dawa kupitia bohari ya dawa. Hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ni asilimia 90 kwa zile dawa muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kuna jumla ya Madaktari Bingwa 451 nchi nzima. Wizara imeweka utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo ya Uzamili kwa Madaktari Bingwa kila mwaka wa fedha kwa uwiano wa wanafunzi 100 ndani ya nchi na 10 nje ya nchi. Jumla ya madaktari 236 wanaendelea na masomo na tunataraji ndani ya miaka mitatu watakuwa wamehitimu na kurudi vituoni. Wizara imeanzisha utaratibu wa kuwatawanya Madaktali Bingwa ili kuweka uwiano katika Mikoa yote nchini na sasa jumla ya Madaktari Bingwa 74 ambao walikuwa wakifadhiliwa na Wizara walihitimu masomo ya udaktali bingwa kwenye fani mbalimbali, taratibu za kuwapandisha vyeo na kuwatawanya kulingana na uhitaji katika Mikoa zinaendelea. (Makofi)
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
(a) Je, kwa nini Serikali haina utaratibu wa kuwachukua wagonjwa wa akili wanaoranda randa barabarani na mitaani na kuwapeleka kwenye hospitali za wagonjwa wa akili kupatiwa matibabu?
(b) Je, Serikali inafahamu idadi ya wagonjwa wa akili waliopo barabarani na mitaani kwenye wilaya za nchi yetu ambao wanahitaji huduma ya matibabu na inatoa maelekezo gani kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kuhusu kuwahudumia wagonjwa hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la kwanza la kulinda afya ya jamii kuanzia katika ngazi ya familia. Aidha, jamii zetu zimekuwa zikiwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatenga wagonjwa wa akili kunakopelekea wagonjwa hawa kurandaranda mtaani. Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 inawataka na ndugu na jamii wawaibue wagonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ili wapatiwe matibabu na wakishapata nafuu, huruhusiwa kwenda kukaa na familia zao na kwenye jamii wanazotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Sehemu ya Tatu, kifungu cha sheria Namba 9 (1-3) kimeeleza wazi kuwa, Afisa Polisi, Afisa Usalama, Afisa Ustawi wa Jamii ngazi ya Wilaya pamoja na Viongozi wa Dini, Afisa Mtendaji wa Kata na Afisa Mtendaji wa Kijiji, wana jukumu la kubainisha mtu yeyote anayerandaranda na kutishia amani na usalama au vinginevyo kumkamata na kumfikisha katika sehemu ya magonjwa ya akili na ikithibitika taratibu za kumpatia matibabu huanza kama ilivyoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Kifungu cha 11(7) na kifungu Namba 12 cha sheria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa idadi kamili ya wagonjwa wa akili haifahamiki nchini, inakadiriwa kwamba wagonjwa wa akili ni asilimia moja tu ya Watanzania wote. Kwa idadi ya Watanzania milioni 50 inafanya wastani wa wagonjwa laki tano. Kati ya hao asilimia 48 ndiyo wanafika katika vituo vya kutolea huduma za afya, asilimia 24 wanakwenda kwa waganga wa kienyeji na asilimia iliyobaki, wanapelekwa kwenye tiba za kiroho kwa maana Makanisani na Misikitini na wachache ndiyo wanarandaranda mitaani bila msaada wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahamasisha Jamii, Watendaji Kata na Serikali za Mitaa, wawaibue watu wanaoonekana kuwa na dalili za ungonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya afya ili wapatiwe matibabu, kwani huduma hii bila gharama yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitoe rai kwa jamii waache kuwanyanyapaa wagonjwa wa akili na badala yake wawafikishe kwenye vituo vya tiba mara wanapoona kuwa wana dalili za ugonjwa huo ili wapatiwe matibabu stahiki na waache kuhusisha na imani za kishirikina. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Je, ni lini Benki ya Wanawake Tanzania itaanzisha tawi lake Zanzibar kwa madhumuni ya kuwapatia huduma za kibenki na mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuwainua kiuchumi wajasiriamali wanawake wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009 kwa lengo la kuwawezesha wanawake kupata huduma za kibenki, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu ili kujikwamua kiuchumi. Mpaka sasa, Benki imefungua matawi mawili yaliyopo jiji Da es Salaam na vituo vya kutolea mikopo na mafunzo 305 katika Mikoa Saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Mwanza, Ruvuma na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa benki ni kuhakikisha kwamba huduma zake zinawafikia wanawake waliopo katika mikoa yote ya Tanzania ikiwemo Zanzibar. Hata hivyo, utekelezaji wa mpango huo unakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa mtaji wa benki hivyo, benki imekuwa ikipanua huduma zake katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa awamu kwa kufungua vituo vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali. Aidha, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha benki zinajiendesha kwa ufanisi na kukuza mtaji ikiwemo kufanya mabadiliko katika Benki kwa kuweka uongozi na watumishi waadilifu wenye uwezo pamoja kutafuta fedha kwa ajili ya mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Benki ya Wanawake Tanzania itaendelea kufungua vituo vya kutolea mikopo na mafunzo katika Mikoa yote ya Tanzania, ikiwemo Zanzibar kulingana na upatikanaji wa mitaji.
MHE. SUZAN A. LYIMO aliuliza:-
Makazi ya Wazee yapo katika hali mbaya sana pamoja na kuhojiwa Bungeni muda mrefu sana:-
(a) Je, Serikali inawaeleza nini wazee hao walioshiriki katika ukombozi wa nchi hii?
(b) Je, ni lini makazi haya pamoja na miundombinu itaboreshwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa waliotoa Wazee katika ukombozi wa nchi hii. Aidha, Wazee ni rasilimali muhimu katika ustawi na maendeleo ya nchi. Serikali inawahakikishia wazee wote nchini wakiwemo wale walioko kwenye makazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo huu wa Serikali umejidhihirisha kwa kuweka sehemu kwa maana ya subsection ya wazee katika Idara Kuu ya Ustawi wa Jamii na katika jina la Wizara, ambalo linasomeka, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Wazee na Watoto. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka mkakati kuboresha maisha ya wazee.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha hali ya miundombinu ya Makazi ya Wazee kwa kufanya ukarabati kwa awamu. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa mabweni ya Wazee katika makazi ya Kolandoto – Shinyanga, imekarabati Makazi ya Wazee ya Kilima- Kagera na kujenga uzio katika makazi ya Njoro- Kilimanjaro kwa jumla ya Sh.285,120,383.25. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha jumla ya Sh.568,000,000 ili kukarabati Makazi ya Wazee Ipuli – Tabora, Nunge – Dar es Salaam na Kibirizi – Kigoma.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Kwa takwimu zilizopo inakisiwa kuwa watu wote wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania ni zaidi ya milioni moja na laki tano na inaaminika kuwa na wanawake ndio waathirika wakubwa zaidi ikilinganishwa na wanaume.
Je, ni sababu gani za kataalam ambazo zimesababisha W anawake kuwa ni waathirika zaidi kuliko Wanaume?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa Mbunge wa Mtambwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za kitaam zinazosababisha wanawake kuathirika zaidi na maambuzi ya VVU na UKIMWI zipo kama nne na naomba nizitoe kama yafuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ni ya kimaumbile na kibaiolojia. Mwanamke yuko katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU ukilinganishwa na wananume kwa kuwa maumbile ya mwanamke ni rahisi kupata michubuko wakati wa tendo la ndoa na hivyo kurahisisha virusi vya UKIMWI kupenya. Aidha, maumbile ya mwanamke hupokea mbegu za kiume kutoka kwa wanaume wakati wa tendo la ndoa. Iwapo mwanamke atafanya mapenzi na mwanaume mwenye VVU, mwanamke huyo anaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili kwamba kuna tabia na mazingira hatarishi ambayo husababisha hatari zaidi kwa wanawake kuambukiwa VVU, ikiwa ni pamoja na kufanya biashara ya ngono na kuanza mapenzi katika umri mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya tatu ni mfumo dume uliokuwepo katika jamii yetu unaowapa fursa wanaume ya kuamua kufanya ngono na wanawake wengi, kutotumia kondomu, kuoa wasichana wenye umri mdogo na na hata kufanya ukatili wa kijinsia. Mfumo huu unasababisha baadhi ya wanawake kuambukizwa VVU na hata kushindwa kueleza hali zao za maambukizi kwa wenza wao kwa kuhofia kuachika, kutengwa au kufukuzwa kutoka kwenye familia. Kwa kawaida mfumo dume huambatana na wanyanyapaa na ubaguzi ambao pia ni kikwazo kikubwa kwa wanawake kuwa wazi kuhusu hali zao za maambukizi ya VVU na hasa na hasa kutengwa na familia yao au jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu ya mwisho ni kwamba wanawake wengi hujitokeza kupima kuliko wananume. Nitoe rai kwa wanaume kujitokeza kupima, tusitumie wenza wetu kama kipimo cha maambukizi yetu sisi.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Vifo vya mama katika Mkoa wa Mwanza pamoja na mambo mengine huchangiwa na kukosa huduma za upasuaji, damu salama na upungufu wa watumishi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza vifo vya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vifo vinavyotokana na uzazi bado ni changamoto nchini. Tafiti zilizofanyika mwaka 2015/ 2016 zinaonesha kwamba kuna idadi ya vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Mwanza ulikuwa na vifo 305 kwa kila vizazi hai 100,000. Katika kukabiliana na tatizo hili Wizara yangu imeandaa mpango mkakati wa kuboresha huduma ya afya kwa wanawake wajawazito wa mwaka 2016 mpaka 2020 na mpango maalum wa kutekeleza afua muhimu zenye matokeo makubwa ambao umezinduliwa mwezi Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo muhimu yaliyomo katika mpango mkakati huu ni pamoja na kuimarisha huduma kwa wanawake wajawazito ikiwemo huduma ya dharura wakati wa ujauzito wakati wa kujifungua hadi wiki sita baada ya kujifungua. Sanjari na hiyo tumeimarisha mifumo ya afya ikiwemo kuwa ajili watumishi wenye ujuzi vifaa tiba pamoja na dawa ili kuhakikisha kwamba huduma inayotolewa ina ubora unaokidhi viwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepata ufadhili wa World Bank na Canada kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu katika vituo vya afya ili kuwezesha kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwemo upasuaji wa kumtoa mama mtoto tumboni. Katika Mkoa wa Mwanza vituo vya Kome (Buchosa), Karume (Ilemela), Kahangara (Magu), Malya (Kwimba), Kagunga (Sengerema) na Bwisya (Ukerewe) vimepata jumla ya bilioni 2.6 kwa ajili ya ukarabati wa au kujenga vyumba vya upasuaji, wodi ya wazazi, chumba cha kijifungulia, maabara ya damu na nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kibali cha ajira cha watumishi wa afya takribani 3152 kilichotolewa mwezi Disemba, 2017 Mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya watumishi 78. Aidha Wizara imeupatia Mkoa wa Mwanza magari ya wagojwa manane kwa ajili ya huduma za rufaa za wajawazito kwenye vituo vya afya, vilevile tunaendelea kuhamasisha akina mama wajawazito kujifunguliwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na changamoto zinazoikabili za kuwa na wagonjwa wengi, kukosekana kwa Hospitali za Wilaya, kupokea majeruhi wa ajali mbalimbali lakini hadi sasa hospitali hiyo inatumia X-ray za zamani ambazo ni chakavu hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray ya kisasa (Digital X- ray) ili kuondokana na adha kubwa wanayopata wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali namba 13 lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua umuhimu wa huduma ya uchunguzi kwa kutumia mionzi ya rediolojia. Aidha, Wizara inatambua changamoto ya uchakavu wa mitambo ya radiolojia na gharama kubwa za matengenezo inayoathiri upatikanaji wa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kuleta mashine mpya 34 za kisasa za digital ambazo zinatengenezwa na Kampuni ya Philips, na hii inatokana na mkataba wa matengenezo wa mwaka 2012 na 2016 ambao mbali ya matengenezo waliyotakiwa kufanya walitakiwa vilevile kubadilisha mashine chakavu na kuweka mashine mpya. Mashine hizi zitafungwa katika hospitali za rufaa zote za mikoa Tanzania Bara ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Awamu ya kwanza ya kuletwa mashine hizi inatarajiwa kuwa ni Juni, 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na gharama kubwa ya kununua na kufanya matengenezo ya vifaa vya uchunguzi Wizara imeanza kufanya uchambuzi ikiwa ni pamoja na kuangalia uzoefu wa nchi nyingine ambazo zilishaanza kuweka utaratibu wa kukodisha vifaa na kulipia huduma. Wizara inatarajia kutumia uzoefu huo kuandaa miongozo itakayowezesha kutekelezwa kwa utaratibu huo kwa ufanisi.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo la udhalilishaji kwa watoto katika jamii na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana nalo ikiwemo kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za matukio ya aina yoyote ya udhalilishaji kwa watoto wakiwemo watoto wa kike. Kupitia Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009, Serikali imekuwa ikielimisha jamii wakiwemo wazazi na walezi kuelewa wajibu wao wa kuripoti matukio ya udhalilishaji punde yanapotokea. Sheria hii imeelekeza kutolewa kwa adhabu kali kwa watuhumiwa wote wanaopatikana na hatia ya udhalilishaji wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha mwaka 2021/2022 umeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa. Kamati hizi wajumbe wake wamehusisha Idara za Mahakama, Jeshi la Polisi, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii pamoja na Idara ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti matukio ya udhalilishaji katika maeneo husika na kuyashughulikia kisheria. Aidha, Wizara imekwishatoa mafunzo ikiwamo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wapatao 50 kutoka katika mikoa yote 26. Ili kuratibu uanzishwaji wa Kamati hizo, tayari mikoa tano wameshaanzisha Kamati hizo. Vilevile, Serikali imekwishaanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika vituo 417 katika Jeshi la Polisi ili kuwezesha kushughulikia pamoja na masuala mengine vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vya udhalilishaji watoto vinaweza kudhibitiwa pia kwa kupitia mtandao maalum wa mawasiliano kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za udhalilishaji. Namba hiyo naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge inapatikana kupitia namba 116 na Waheshimiwa Wabunge wanaweza kupiga namba hiyo na kuwajulisha wapiga kura wao kuhusiana na namba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ya kutumia namba hii na mtandao huu ni kwa mtoto mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba ya mtoto kuweza kuripoti tukio lolote la udhalilishaji wa mtoto. Mtandao huu huwasilisha taarifa la tukio hilo kwenye vyombo husika ambapo mwathirika hupata huduma stahiki za kiafya na unasihi na mtuhumiwa kufikishwa katika mamlaka husika za kisheria. Katika kipindi cha Januari mpaka Disemba 2017, matukio 1,072 yaliripotiwa katika mtandao huu na kushughulikiwa.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ambao ni mkoa mpya hauna Hospitali ya Rufaa, hivyo wagonjwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 140 kufuata huduma hiyo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Shinyanga na Mwanza; mwaka 2015/2016 Mkoa wa Simiyu ulipokea fedha kidogo ya kuanzisha jengo la OPD.
• Je, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
• Je, ni lini Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukukaribisha tena katika Bunge letu tukufu. Tumefurahi sana kukuona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, Wizara inapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kutambua jitihada ambazo Serikali imefanya katika kuendeleza mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ukiwa ni mmoja wa mikoa mipya ulioanzishwa mwaka 2012. Kutokana na uhitaji wa huduma za afya ngazi ya rufaa katika ngazi ya mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu iliandaa na kupeleka andiko Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuzingatia mahitaji ya kitabibu kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, niongeze hapa tu kwamba, pamoja na andiko hili hospitali hii sasa kwa agizo la Mheshimiwa Rais, zimeletwa tena katika Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha na hadi sasa jumla ya shilingi 2,087,268,672 zimeshatolewa. Kati ya fedha hizo, shilingi 299,896,185 zilitumika kununua ardhi yenye ukubwa wa ekari
(a) Shilingi milioni 595,650,815 zilitumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na utawala katika awamu ya kwanza na shilingi 1,191,721,672 zilitumika kuendeleza ujenzi wa jengo la OPD katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika Hospitali za Rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Simiyu. Hii inaenda sambamba vilevile na kupatiwa ahadi ya fedha ya shilingi bilioni 10 ambayo zilitolewa na Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu tarehe 11 Januari, 2017.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Serikali iliipandisha hadhi Hospitali ya Temeke kuwa Hospitali ya Mkoa ambayo sasa inastahili kuhudumiwa na Wizara badala ya Halmashauri ili huduma inayotolewa hapo ifanane na hadhi ya Hospitali ya Mkoa.
Je, ni lini Serikali itaanza kuihudumia hospitali hiyo kwa kiwango kinachostahili ili kuipunguzia mzigo Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Serikali iliipandisha hadhi Serikali ya Temeke kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hiyo ni moja ya hospitali tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam zilizopandishwa hadhi kuwa Hospitali za Rufaa za Mkoa ikiwa ni pamoja na Hospitali za Mwananyamala na Ilala. Lengo ni kuhakikisha kuwa huduma za afya za kibingwa zinawafikia wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mheshimiwa Spika, katika mwendelezo wa kuboresha huduma za kibingwa kwa wananchi, tarehe 25 Novemba, 2017 Hospitali ya Temeke ni miongoni mwa hospitali 23 za Rufaa za Mikoa ambazo zilikabidhiwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka TAMISEMI wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua Hospitali ya Mafunzo ya Mloganzila. Wizara yangu imekabidhiwa hospitali hizi kutoka TAMISEMI tarehe 15 Machi, 2018.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha hospitali hii inatoa huduma kulingana na hadhi iliyopewa, Serikali imeweka vipaumbele vya kuboresha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na:-
• Vipaumbele vya kuongeza madaktari bingwa wanane katika fani za magonjwa ya akinamama, upasuaji, mifupa, mama na watoto na magonjwa ya ndani. Hospitali ya Temeke kwa sasa ina wataalam hao.
• Kuhakikisha upatokanaji wa dawa na vifaatiba.
• Kuhakikisha mipango ya hospitali inawekwa wakiasaidiana na Wizara katika kukarabati vyumba vya upasuaji, maabara na vyumba vya wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha hospitali hii ili kukidhi mahitaji ya wananchi kulingana na uwezo uliopo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2015/2016 wanawake 85 Mkoani Singida walipoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi. Aidha, inaelezwa kitaalam asilimia 35 ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa na kuimarishwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi wa mpango kwani utumiaji wa huduma hizo kwa sasa unatekelezwa kwa asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 27?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu rasmi za sensa mwaka 2012 zinaonesha vifo vitokanavyo na uzazi katika Mkoa wa Singida ni 468 kwa kila wanawake 100,000. Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya afya na Malaria Tanzania za mwaka 2015/2016 (Tanzania Demographic Health Surveys 2015/2016) matumizi ya uzazi wa mpango katika Mkoa wa Singida yalikuwa asilimia 38.4 wakati wastani wa Kitaifa ni asilimia 32.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya afya katika Mkoa wa Singida wameweza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma 77 katika kipindi cha mwaka 2015 na idadi watoa huduma ilikuwa 121 kwa mwaka 2016 ili waweze kutoa huduma sahihi za uzazi wa mpango kwa kuzingatia miongozo ya utoaji huduma za uzazi wa mpango zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango kwa kutumia simu za viganjani, huduma hiyo hujulikana kama m4RH na ili kupata elimu hiyo, mhusika anatakiwa kutuma ujumbe wa m4RH kwenye namba 15014 na hapo mtu yeyote ambaye ana umri wa miaka 15 hadi 49 wanaweza kupata ujumbe wenye elimu ya uzazi wa mpango. Katika Mkoa wa Singida wateja waliopatiwa huduma ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2015 walikuwa 198,822, mwaka 2016 walikuwa wateja 209,511 na
mwaka 2017 walikuwa wateja 173,587.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuboresha huduma za dharura za uzazi ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni katika Mkoa wa Singida ambapo vituo vya afya vinne vya Ndago katika Halmashauri ya Iramba, Ihanja katika Halmashauri ya Ikungi, Itigi katika Halmashauri ya Itigi na Kinyambuli katika Halmashauri ya Mkalama vimeweza kupata kila kimoja kimepata fedha zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari ambapo matibabu yake ni ya muda mrefu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa dawa za ugonjwa wa kisukari bure kama ilivyofanya kwa ugonjwa wa kifua kikuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inatambua uwepo wa wagonjwa wasio na uwezo wa kuchangia gharama za huduma za afya ikiwa ni pamoja na wale waliokuwepo katika makundi maalum ya kijamii, wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 60 ambao hawana uwezo wa kipato, watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, watoto walio katika mazingira hatarishi, wanawake wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kundi hili pia wapo wagonjwa wenye magonjwa sugu kama saratani, wanaoishi na virusi vya UKIMWI, kisukari, magonjwa ya moyo, pumu, selimundu, kifua kikuu, ukoma na magonjwa ya akili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Ugonjwa wa Kisukari Nchini, inaendesha Programu ya Kitaifa ya Kisukari ambayo inajulikana kama National Diabetic Program, ambapo imeanzisha vituo vya matibabu ya kisukari vipatavyo 169 katika Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha, jumla ya madaktari na wauguzi 1,925 wamepatiwa mafunzo maalum ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa kisukari. Lengo ni kuwapatia wagonjwa wote wa kisukari huduma bora na za bure za matibabu kama ilivyoainishwa katika Sera ya Taifa ya Afya. Hadi hivi sasa Serikali imetoa matibabu na dawa ya bure kwa wananchi wapatao 5,386.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko katika mchakato wa kuainisha idadi na mahitaji ya wagonjwa wa kisukari nchini. Pindi kazi hii itakapokamilika Serikali itatoa mwongozo utakaosimamia vizuri zaidi matibabu ya wagonjwa wa kisukari nchini.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Mpaka sasa inadaiwa kuwa hakuna dawa sahihi za kutibu ugonjwa wa kisukari.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti kuhusu dawa za kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa kisukari ni moja kati ya magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza. Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa kichochezi kiitwacho insulin. Aidha, kwa kushindwa kutengenezwa kabisa na kongosho au kwa jina kitaalam unaitwa pancreas au kwa kufanya kazi chini ya kiwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna aina tatu za kisukari. Kisukari ambacho kinategemea insulin ambayo tunaita type one ambacho huanza utotoni; kisukari kinachotegemea insulin ama type two ambacho huwapata watu kuanzia miaka 35 na kuendelea ingawa watoto na vijana wameanza kupata aina hii kutokana na kutaozingatia misingi ya lishe; na kisukari cha mimba hii ni aina ya tatu ambayo inatokea wakati wa ujauzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ambayo yanachangia mtu kuugua kisukari ni pamoja na kuwepo historia ya kisukari ndani ya familia, magonjwa ya kongosho kama saratani na maambukizi, uzito unaozidi na unene uliokithiri, shinikizo la damu, mtindo wa maisha usiofaa hususani kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa , uvutaji wa bidhaa za tumbaku na masuala mengine kulingana na aina ya kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mpaka sasa duniani kote haijagundulika dawa ya kutibu ugonjwa wa kisukari na kupona kabisa. Matibabu yote yanayotolewa mpaka sasa ni yale yanayompatia mgonjwa kiwango bora cha kuishi ikiwemo kuhakikisha kwamba kiwango chake cha sukari mwilini kinakuwa ndani ya kiwango cha kawaida kila siku ili kuvilinda viungo vingine vya mwili visidhurike na hivyo kumpunguzia mgonjwa magonjwa ya mara kwa mara, kulazwa wodini mara kwa mara na kupunguza uwezekano wa kifo. Dawa hizi ni pamoja na sindano ya aina ya insulin ambazo mgonjwa hulazimika kuchoma kila siku kwa maisha yake yote na vidonge ambavyo kila mgonjwa humeza kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tafiti nyingi ambazo zinaendelea duniani kote kutafuta dawa itakayoweza kutibu kabisa ugonjwa huu, lakini tafiti hizi bado hazijazaa matunda. Tafiti hizi ni pamoja na zile za kujaribu kutengeneza cell za kongosho na kuzipandikiza kwa maana ya Pancreas Stem Cell Transplantation ili kuweza kuweka cell mpya za kongosho na kuipa kongosho uwezo wa kutengeneza insulin kwa wingi zaidi. Njia hii pekee ndiyo itakuwa ufunguzi wa kudumu wa tiba dhidi ya ugonjwa huu. Mara tu tafiti hizi zitakapokamilika na kuonesha mafanikio, Serikali ya Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma hii inapatikana hapa nchini.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Imebainika kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) umeendelea kuathiri jamii ya Watanzania.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa TB?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, TB au Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukizwa na huambukizwa kwa njia ya hewa. Ugonjwa wa TB hushambulia mapafu na viungo vingine ikiwa ni pamoja na mifupa, uti wa mgongo, ubongo, moyo, ngozi na sehemu nyingine za mwili. Kwa ujumla TB inaweza kushambulia kila kiungo katika mwili. Ugonjwa huu husababishwa na vimelea aina ya bacteria na mgonjwa akitibiwa kwa dawa tulizonazo anaweza kupona kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote anaweza kuambukizwa au kuugua TB lakini makundi yafuatayo yako katika hatari kubwa zaidi kuugua ugonjwa huu ni pamoja na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, watoto wadogo chini ya miaka mitano, wazee, watu wanaougua magonjwa ya muda mrefu ikiwemo saratani, kisukari, wenye utapiamlo, wafungwa, wachimbaji wadogo wadogo migodini na wale wanaotumia madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumweka katika matibabu ndiyo njia kuu ya kupambana na kushinda tatizo la kifua kikuu. Hivyo basi, mikakati ya Serikali imejikita katika afua za kuongeza uwezo wetu wa kuwafikia watu wote wanaohitaji huduma za TB ili kuwagundua wagonjwa hawa mapema na kuwatibu kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati na hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kama ifuatavyo:-
(a) Kufanya upimaji wa TB kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI;
(b) Kuingiza teknolojia mpya nchini ya upimaji na ugunduzi wa uhakika na uharaka wa vimelea vya TB kwa kutumia Gene Xpert. Hadi hivi sasa mashine 97 zimeshafungwa katika Hospitali za Mikoa na baadhi za Halmashauri na mashine nyingine 90 zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kufungwa kwenye Hospitali za Wilaya zilizobakia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia hii inawezesha sasa hivi badala ya siku za nyuma ambapo mgonjwa alihitaji kupima makohozi mara tatu kwa siku tatu, sasa hivi ugunduzi unaweza ukanyika ndani ya masaa mawili badala ya siku tatu kama ilivyokuwa awali.
(c) Tumewezesha maduka muhimu na Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kufanya utambuzi wa dalili za TB na kutoa rufaa kwa wahisiwa wote kwenda katika mfumo wa tiba.
(d) Kufanya uchunguzi kwa wafanyakazi wote migodini na kwenye mahabusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena, Wizara yangu inatoa wito na kuwahimiza Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kutokomeza TB na kuhakikisha kwamba TB inakuwa ni ajenda yao ya kudumu katika vikao vyote vinavyoendelea na wanavyovihutubia.
MHE. JAMES F. MBATIA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa huduma ya afya nchini kwa ubia na Mashirika ya Dini na/au Taasisi Zisizo za Kiserikali:-
(a) Je, ni kwa asilimia ngapi ya ubia huo kwa kila upande kati ya Serikali na Mashirika ya Dini au Serikali na Taasisi nyingine Zisizo na Kiserikali?
(b) Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita ubia huu umepata mafanikio kiasi gani na kwa kutumia vigezo gani kwa Hospitali ya Kilema?
(c) Kwa kipindi hicho tajwa hapo juu, je, ubia huo umepatwa na changamoto kiasi gani kwa kutumia vigezo gani kwa Hospitali ya Kilema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania inatambua mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini. Aidha, Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi ilitunga Sera ya Ubia kati za Sekta ya Umma na Binafsi, (Public Private Partnership, 2009) pamoja na Sheria Na.103 ya mwaka 2010 iliyorejewa mwaka 2014 na kanuni zake za mwaka 2011 ambazo zimerejewa mwaka 2015.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Machi 2018, jumla ya vituo vya kutolea huduma vilivyopo ni 7,215 (vya umma vikiwa ni 5,361 sawa na asilimia 74 na sekta binafsi ni 1,854 sawa na asilimia 26). Aidha, kati ya vituo binafsi 1,854, vituo 900 sawa na asilimia 13 vinamilikiwa na Mashirika ya Dini. Kati ya vituo hivyo vinavyomilikiwa na Mashirika ya Dini ambavyo vimesaini makubaliano ya kutoa huduma za afya baina ya Serikali na Mashirika ya Dini ni 130 sawa na asilimia 1.8 ambapo hospitali ni 85, vituo vya afya na zahanati ni 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inadhihirisha kwamba sekta binafsi ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini. Aidha, takribani asilimia 40 mpaka 70 ya gharama za uendeshaji wa Hospitali za Mashirika ya Dini zinatoka Serikalini kwa ajili ya mishahara ya watumishi, dawa, vifaatiba pamoja na gharama nyingine za uendeshaji wa hospitali hizi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Kilema ilianza kutumika kama Hospitali Teule ya Halmashauri ya Moshi Vijijini mwaka 1984. Katika kipindi hiki kuna mafanikio mengi yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi;
(ii) Kuongeza idadi ya vifaatiba ambavyo vimeboresha utoaji wa huduma;
(iii) Hospitali hii ina jumla ya watumishi 156 walioajiriwa na Serikali ambao wanafanya kazi katika hospitali hii;
(iv) Watoa huduma hususani Madaktari wameongezeka hadi kufikia watumishi tisa; na
(v) Wanapata mgao wa madawa kutoka MSD.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki chote ambapo Hospitali ya Kilema imekuwa ikitumika kama Hospitali Teule imekuwa ikipata changamoto ambazo zimekuwa zikitatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na mmiliki ambaye ni Jimbo la Moshi la Kanisa Katoliki. Baadhi ya changamoto hizo pamoja na kufanyiwa kazi kwa kushirikiana ni ufinyu wa bajeti; upungufu wa watalaam pamoja na uwekezaji katika hospitali hiyo.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:-
Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kigoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma inahitaji Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili iweze kutoa huduma za kibingwa. Aidha, Wizara inatambua kuwa, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kwa sasa ina Daktari Bingwa mmoja tu katika fani ya watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuzihamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya Madaktari Bingwa na fani zao katika hospitali zote za mikoa, kanda, hospitali maalum na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha tathmini hii, Wizara itawapanga upya Madaktari Bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya hospitali za mikoa, kanda maalum pamoja na Taifa. Lengo ni kuwa hospitali ya mkoa iwe na Madaktari Bingwa ikiwemo pamoja na Hospitali za Rufaa ya Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali imegharamia mafunzo ya Madaktari Bingwa 125 ambao wameingia mkataba wa kutumikia katika maeneo watakayopangiwa baada ya kuhitimu masomo kwa lugha ya kitaalam bonding. Mkoa wa Kigoma utakuwa ni moja ya mikoa itakayonufaika.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:-
Serikali inatekeleza sera inayohusisha huduma bora za afya ya mama na mtoto.
Je, utekelezaji huo umenufaishaje Jimbo la Tunduru Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ramo Matala Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya mama na mtoto ni moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika Sera ya Afya mwaka 2007. Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2016 hadi 2020, ambao unajulikana kama National Road Map Strategic Plan to Improve Reproductive Maternal, New Born, Child and Adolescent Health in Tanzania, unaolenga kuboresha afya ya uzazi ya mama mtoto na vijana. Katika kutekeleza mkakati huu, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa uzazi na huduma wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, Serikali imehakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za uzazi na mtoto ikiwemo dawa ya uzazi wa mpango kwa maana ya (sindano ya depoprovera, vipandikizi na vitanzi) dawa za watoto (ORS zinc) kwa ajili ya kutibu kuharisha na dawa za antibiotics za watoto ya amoxyllin kwa ajili ya kutibu nimonia) dawa za uzazi salama ikiwepo dawa ya kuongeza uwingi wa damu kwa maana ya Fefol, dawa ya kuzuia mama mjamzito kupoteza damu baada ya kujifungua kwa maana ya oxytocin na dawa ya kuzuia kifafa cha mimba kwa maana ya magnesium sulfate.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mpango wa kukarabati na kupanua vituo vya afya 208 nchini ili viweze kutoa huduma za uzazi wa dharura, ambapo Kituo cha Afya cha Mkasale kilichopo katika Wilaya ya Tunduru kimepewa fedha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ikiwemo chumba cha upasuaji, jengo la huduma za mama na mtoto, maabara na nyumba ya mtumishi. Kituo cha Afya cha Matemanga kimetengewa fedha katika awamu inayofuata.
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini bado ni tatizo kubwa:-
Je, Serikali inasema nini katika kupambana na wanaume wanaodhalilisha wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kuipongeza sana Timu ya Simba. Wahenga wanasema; mla mla leo, mla jana kala nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa lipo ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa mujibu wa matukio yaliyoripotiwa katika vyombo vya dola na vyombo vingine vya umma. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau inachukua hatua zifuatazo:-
Moja, Serikali imezindua Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Vitenda vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/2018
– 2021/2022. Kupitia mpango huu, Serikali imedhamiria kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ukeketaji wa watoto wa kike kutoka asilimia 15 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia saba mwaka 2022. Utekelezaji wa mpango huu umeanza kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote na baadhi ya Asasi Zisizo za Kiserikali yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza mpango huu.
Pili, tumeanzisha madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi ambavyo kwa sasa tuna jumla ya madawati 417 ambayo yamewezesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kujiamini na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti kwa watoto na udhalilishaji wa wanawake katika maeneo yao.
Tatu, tumeanzisha vituo vya one stop center na vituo hivi vimekuwa na madawati ya polisi, ushauri nasaha na huduma za afya katika eneo moja, tofauti na sasa ambapo wahanga inabidi waende kwanza polisi wachukue fomu waende hospitali wapate ushauri nasaha, jambo ambalo linapoteza muda. Vituo hivi tumevianzisha katika Hospitali ya Amana kule Mbeya; Hai, Mkoa wa Kilimanjaro; na Kahama katika Mkoa wa Shinyanga.
Nne, Serikali inaendelea kuhamasisha utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Adhabu, Sura Na. 16 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 na kuhimiza wazazi, walezi, jamii na wahanga wa vitendo vya ukatili kutokaa kimya pindi wanapoona watoto au mwanamke anafanyiwa vitendo vya ukatili ili kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaowatendea watoto na wanawake vitendo hivyo vya kinyama vinavyopelekea madhara ya kimwili, kiafya, kisaikolojia, hata kifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2017, Jeshi la Polisi limeripoti jumla ya matukio 41,416 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake. Kati ya matukio hayo, matukio 13,457 ni ya ukatili wa kijinsia kwa watoto. Serikali inakemea udhalilishaji na ubakaji wa aina yoyote kwa wanawake na watoto. Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawashawishi na kuwashauri wananchi kutomaliza mashauri yaliyopo katika vyombo vya dola katika ngazi ya familia.
MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:-
Hepatitis ni ugonjwa hatari usiofahamika vizuri kwa wananchi walio wengi:-
(a) Je, dalili za ugonjwa huo ni nini;
(b) Je, ugonjwa huo una chanjo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Aloyce Bura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maambukizi ya Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu hushambulia ini pekee na hivyo kulifanya kushindwa kufanya kazi vizuri. Katika hatua za mwisho mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata saratani ya ini. Virusi vya homa ya ini vipo katika makundi matano, yaani (A), (B), (C), (D) na (E).
Mheshimiwa Naibu Spika, dalili za homa ya ini ni pamoja na ngozi na macho kuwa na rangi ya njano, kukojoa mkojo wenye rangi nyeusi, joto la mwili kupanda, kuwa na mafua, kichwa kuuma, kukosa nguvu, kupata kichefuchefu, kutapika, tumbo kuuma upande wa juu kulia na kupungua uzito.
Mheshimiwa Spika, maambukizi ya homa ya ini yanategemeana na kundi la Virusi. Kundi la B, C na D huambukizwa kwa niia ya kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na vitu vingine vyenye ncha kali, utumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano yenye virusi vya ugonjwa huo, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine ambaye ana kidonda, pia mama anaweza kumwambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aina ya homa ya aina ya ini inayosababishwa na virusi vya kundi (B) Hepatitis B (HBV) ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini. Aina ya Kirusi cha A na E huambukizwa kwa njia ya kinyesi na kutokuwa na majisafi na salama (faecal oral) ambazo hufanana kwa kiasi kikubwa na uambukizwaji wa magonjwa ya kuhara.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa Hepatitis B unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo na chanjo hii hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake. Hapa nchini chanjo hii inapatikana kwa watu wazima na watoto wachanga. Kwa watoto wachanga, chanjo hii ipo katika mchanganyiko wa chanjo ya pentavalent ambayo watoto wachanga hupatiwa, katika mwaka 2017, asilimia 98 ya watoto walipata chanjo hii. Kwa wenye maambukizi ya virusi aina (C), kwa sasa hakuna chanjo. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KITETO Z. KOSHUMA) aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Bugando inatoa huduma kwa Mkoa wa Mwanza na Mikoa jirani ikiwemo Simiyu na Mara lakini Hospitali hiyo haina CT Scan:-
Je, ni lini Serikali itapeleka CT Scan katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua umuhimu wa kuimarisha huduma za uchunguzi katika hospitali za Kibingwa ngazi ya Kanda na Taifa ikiwemo hospitali ya Bugando. Hii ni pamoja na kuhakikisha hospitali hizi zinakuwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi vikiwemo kuwa na CT Scan na MRI. Wizara ipo katika hatua za utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa vifaa vya uchunguzi kupitia mradi wa ORIO ambapo Hospitali ya Bugando ilipangiwa kupata MRI na CT Scan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakati Wizara ikiendelea ukamilishaji wa mradi huu, Hospitali ya Bugando nayo ilinunua CT Scan kupitia mipango yake ya hospitali na tayari ilishasimikwa, kuzinduliwa na kuanza kazi tangu tarehe 26 Januari, 2018. Wizara inaipongeza Hospitali ya Bugando kwa juhudi hiyo. Serikali kwa sasa itaendelea na mpango wa kuitafutia Hospitali ya Bugando mashine ya MRI.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:-
Je, nini chanzo cha ugonjwa wa Lupa na ni watu wangapi wameugua na wangapi wamefariki kutokana na ugonjwa huo hapa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa Lupa au kwa jina la kigeni unajulikana kama Systematic Lupus Erythematosisni ugonjwa wa kinga za mwili ambao hushambulia viungo vya mwili vikidhania kwamba ni vitu vigeni (foreign bodies). Viongo ambavyo hudhurika zaidi ni ngozi, figo, ubongo, chembechembe za damu, moyo, mapafu na viungo vingine vya mwili kama joints. Watafiti hadi sasa hawajaweza kubaini chanzo cha ugonjwa huu. Inasadikiwa kwamba mgonjwa mwenye vinasaba vya Lupa hupata ugonjwa huu pale anapokutana na visababishi kwenye mazingira vinavyochochea kuanza kwa ugonjwa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vinavyoweza kuchangia kuanza kwa ugonjwa huu ni miale ya jua, maambukizi ya bakteria, matumizi ya baadhi ya dawa za shinikizo la damu, dawa za kifafa na antibiotic. Wagonjwa wenye ugonjwa wa Lupa unaotokana na dawa hupona haraka mara wanapoacha kutumia dawa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, visababishi vingine vinavyoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu wa Lupa ni pamoja na jinsia. Ugonjwa huu huwapata zaidi wanawake kuliko wanaume. Katika masuala ya umri, Lupa huwapata zaidi watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45. Asili, Lupa huwapata zaidi Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, Wahispania na Waasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili za ugonjwa huu siyo rahisi kubainika kirahisi. Baadhi ya dalili kuu ni maumivu ya viungo, uchovu wa mara kwa mara, homa, vidonda vya mdomoni na vipele vinavyofanana na mabawa ya kipepeo kwenye mashavu. Ugonjwa huu hauna tiba, dawa zinazotolewa hulenga kupunguza athari za ugonjwa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili takribani wagonjwa wawili hugundulika na ugonjwa wa Lupa kwa mwaka na hufuatiliwa katika Kliniki ya Ngozi. Mpaka hivi sasa kuna wagonjwa takribani 10 wanaofuatiliwa katika hospital hii. Katika mwaka 2017/2018 kumeripotiwa kifo kimoja kutokana na ugonjwa huu. Kuna uwezekano wa vifo vingi zaidi kutokana na ugonjwa huu, lakini havijaripotiwa kutokana na dalili za ugonjwa huu kutobainika kirahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nimalizie kwa kusema kuwa ugunduzi wa ugonjwa wa Lupa ni mgumu sana na wakati mwingine mtu hutibiwa kama mgonjwa wa ngozi tu. Ni kutokana na ugumu uliopo wa kugundua na hata mtu kujua kama na ugonjwa wa Lupa, wagonjwa wengi hufika katika Hospitali wakiwa na matatizo mengine kama ya ngozi, viungo na hutibiwa matatizo waliokuja nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua kitu chochote kisichokuwa cha kawaida katika miili ili waweze kupata tiba mapema kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA (K.n.y. MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI) aliuliza:-
(a) Je, Mfuko wa Bima ya Afya una wanachama wangapi na ni asilimia ngapi ya Watanzania wamejiunga na bima hiyo?
(b) Je, kwa nini baadhi ya hospitali, hasa za binafsi, hazikubali malipo kwa kutumia kadi hizo za Bima ya Afya?
(c) Je, Mfuko wa Bima ya Afya umefikia malengo ya kuanzishwa kwake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kepteni Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulianzishwa mwaka 2001 kwa Sheria Sura ya 395. Hadi kufikia Juni, 2018 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa una wanachama wachangiaji 858,137 ambao wanaufanya mfuko kuhudumia jumla ya wanufaika 3,918,999 sawa na 7% ya Watanzania wote. Katika kipindi hicho hicho Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na jumla ya wanufaika 13,398,936 sawa na 25% ya Watanzania wote hivyo, kufanya wananchi wanaonufaika na Mpango wa Bima ya Afya nchini chini ya NHIF na CHF kufikia 17,317,935 sawa na 32% ya Watanzania wote, lengo la mfuko ni kufikia 50% ya Watanzania wote ifikapo mwaka 2020.
(b( Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hospitali zinakataa kadi za NHIF kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo hospitali kutosajiliwa na mfuko, kufutiwa usajili na kufanya vitendo vya udanganyifu na kukataa bei za huduma za NHIF.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unahudumia watumishi wote wa umma, kama ilivyokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwakwe pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa rasilimali fedha katika sekta ya afya, mfano, zaidi ya 80% mpaka 90% ya mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya zinategemea fedha za NHIF.
Hata hivyo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea kutekeleza mkakati wake wa kuongeza wigo wa wanachama kwa kuandikisha makundi mbalimbali katika sekta rasmi na isiyo rasmi, ikiwemo wajasiriamali wadogo wadogo na watoto chini ya miaka 18 chini ya Mpango wa Toto Afya Card na makundi ya wakulima kupitia Mpango wa Ushirika Afya ambao mpango huu ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Shinyanga, hivi karibuni.
MHE. HAWA M. CHAKOMA (K.n.y. MHE. AMINA S. MOLLEL) aliuliza:-
Baadhi ya mila na tamaduni katika jamii za wafugaji hapa nchini haziwapeleki watoto wa kike shule, badala yake wanawaozesha katika umri mdogo kinyume na ridhaa yao, hivyo kukiuka sheria za nchi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa mila na tamaduni hizo haziwanyimi watoto wa kike haki yao ya kupata elimu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua haki za msingi za mtoto ikiwemo ya kupata elimu na kuendelezwa ili kupata nguvu kazi yenye tija itakayochangia kujenga uchumi unaotarajiwa katika nchi yetu. Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa mila na tamaduni zenye madhara zinazosababisha watoto kushindwa kwenda shule zinashughulikiwa ipasavyo. Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inayoelekeza kutoa haki kwa mtoto bila kubaguliwa ikiwemo kuendelezwa kielimu na kutokomeza mila zinazoruhusu ndoa katika umri mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekezaji wa Sheria Namba 21 ya mwaka 2009 inayoelekeza utoaji wa haki na huduma ya msingi kwa mtoto ikiwemo elimu, malazi na huduma ya afya na utekelezaji wa Mpango wa Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha mwaka 2021/2022 ambao umelenga kushirikisha jamii kutokomeza mila na tamaduni zenye madhara kwa watoto na hasa watoto wa kike ili kumuwezesha kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2017/2018 Wizara imetoa elimu kuhusu mila na desturi zenye madhara, ikiwemo ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kwa jumla ya wananchi 13,020 yakiwemo makundi mbalimbali ya mangariba, viongozi wa jadi na jamii ya wafugaji katika Mikoa ya Dodoma, Arusha, Mara, Shinyanga, Tabora, Lindi, Tanga, Dar es Salaam na Katavi. Aidha, Wizara imeandaa mdahalo mkubwa wa Kitaifa mwezi Oktoba mwaka huu utakaojumuisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na viongozi wa kimila ili kujadili na kupata muafaka wa Kitaifa wa namna ya kutokomeza matatizo ya ukatili kwa watoto yakiwemo ukeketaji, ndoa na mimba za uototoni, ambayo yamekuwa yakiongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia, imeanzisha klabu za watoto na mabaraza ya watoto na kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi mbalimbali za utendaji kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa masuala ya ukatili wa wanawake na watoto, yakiwemo masuala ya mila na tamaduni zenye madhara kwa watoto.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka sheria kali zitakazowabana wazazi ambao wamekuwa wakitelekeza watoto na familia zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto ni haki ya mtoto kwa mujibu wa Sheria Na. 21 ya mwaka 2009. Aidha, kifungu cha 7 mpaka cha 9 kinatoa majukumu kwa mzazi/mlezi na mtu yeyote mwenye jukumu la kumlea mtoto kuhakikisha kwamba anawatunza na kuwalea watoto ikiwemo kuwapatia huduma zote muhimu kama chakula, malazi, mavazi, elimu na kuwalinda na vitendo vya nyanyasaji, ukatili, unyonyaji na utelekezaji. Kifungu cha 14 cha Sheria ya Mtoto kinatoa adhabu kwa mzazi/mlezi yeyote atakayekiuka kifungu hiki atatozwa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya mashauri 6,557 yanayohusu matunzo na malezi ya watoto na wanawake yalishughulikiwa katika ngazi mbalimbali za Halmashauri na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wazazi/ walezi na wote wenye jukumu la kutoa malezi na matunzo kwa watoto wahakikishe wanatimiza wajibu wao kikamilifu. Vilevile familia zote ambazo zimetelekezwa zitoe taarifa katika Ofisi za Ustawi wa Jamii zilizoko katika Halmashauri wanapoishi ili mashauri yao yaweze kusikilizwa na watoto kupata huduma stahiki kwa ajili ya makuzi yao.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote za Serikali kuhakikisha kuwa wanashughulikia kwa haraka mashauri yanayowasilishwa kwenye ofisi zao kwa kutumia sheria na taratibu zilizopo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu linaendelea kuwa kubwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hii kubwa hasa katika Jiji la Mwanza?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukijengea uwezo Kitengo cha Ustawi wa Jamii kukabiliana na changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali hili la msingi kwanza nikushukuru sana na kukupongeza na wewe kwa kushirikiana pamoja na Serikali katika kuhakikisha kwamba tunarudisha ule uzuri wa asili, nakushukuru na kukupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, kifungu cha 16, msamiati unaotumika katika kubainisha watoto hao ni watoto walio katika mazingira hatarishi na si watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali inatekeleza Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2021/2022, ambapo umebainisha majukumu mbalimbali ya wadau katika kuondoa changamoto hiyo. Moja ya shabaha ya mpango huo ni kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021/2022 ikiwemo katika Jiji la Mwanza.
Mheshimiwa Spika, katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Jiji la Mwanza limeunda kamati 11 za ulinzi na usalama kwa wanawake na watoto katika mitaa 11; makao ya watoto manne yamesajiliwa; jumla ya watoto walio katika mazingira magumu (hatarishi) 5,843 walibainishwa, wakike wakiwa 3,337 na wanaume, 2,506. Kati ya watoto hao, jumla ya watoto 2,381 walitengenezewa kadi za bima ya TIKA, watoto 27 walipelekwa katika Vyuo vya VETA na watoto 741 wanasomeshwa katika shule za sekondari. Aidha, zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika kata zote 18 umefanyika mwaka 2018. Jumla ya watoto 426 wanawake wakiwa ni 21 na wanaume 405 walitambuliwa. Kati yao watoto 135 walipelekwa kwenye makao ya watoto ya muda, watoto 120 waliunganishwa na familia zao, watoto 165 walirejeshwa kuendelea na masomo na watoto 323 walipata huduma za matibabu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuona umuhimu wa huduma za ustawi wa jamii, imeanzisha Kitengo cha Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lengo likiwa ni kuboresha huduma hizi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto, haki za mtoto na uendeshaji wa mashauri ya watoto. Serikali pia imeimarisha mipango ya bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuanzisha kifungu cha malipo (cost center) na kuingiza huduma za ustawi wa jamii katika mfumo ulioboreshwa wa mipango na bajeti katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Improved Plan Rep.). (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Baadhi ya wanawake wameathirika na vipodozi vikiwemo kucha na kope kubandika.
Je, ni wanawake wangapi wameathirika macho kutokana na matumizi ya kope bandia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa kucha za kubandika na kope za kubadnika siyo vipodozi. Kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura ya 219 inayosimamiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kipodozo ni kitu chochote kinachotumika kwenye mwili au sehemu ya mwili kwa njia ya kupaka, kumimina, kufukiza, kunyunyiza au kupuliza kwa ajili ya kusafisha, kuremba, kupamba, kuongeza uzuri, mvuto au kubadili muonekano. Takribani wagonjwa 700 kwa mwaka hupokelewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili…
Mheshimiwa Spika, takribani wagonjwa 700 kwa mwaka hupokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na matatizo ya ngozi yanayotokana na kumeza vidonge vinavyobadili rangi ya mwili mzima pamoja na vipodozi vyenye kemikali. Imeelezwa kuwa watu hao wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani na magonjwa ya ngozi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara kupitia TFDA haina utaratibu wa kudhibiti kope wala kucha za kubandika kwa sababu hakuna sheria inayoipa mamlaka ya kudhibiti bidhaa hizo. Hivyo basi, kutokana na hilo, Wizara kwa kupitia TFDA haina takwimu za kuonesha madhara yanayotokana na matumizi ya bidhaa hizo kwa kuwa hakuna mfumo wa kupokea taarifa za matumizi ya bidhaa husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa maana ya miezi tisa ya ujauzito au wenye uzito pungufu chini ya kilogramu 2.5 huwa katika hatari zaidi ya kupoteza maisha kuliko wengine kutokana na kushindwa kupumua, kupoteza joto, kupata uambukizo wa bakteria kwa haraka, kushuka kwa sukari mwilini (hypoglycemia) kutokana na kushindwa kunyonya, ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga na kadhalika. Tatizo la uzito pungufu unachangia asilimia 25 ya vifo vya watoto wachanga hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizo za kiafya zinazotokana na kuzaliwa kabla ya wakati, Wizara imeendelea kuboresha huduma za watoto hao kwa kutekeleza afua mbalimbali kama vile moja, kuwapatia wajawazito dawa ya sindano ya dexamethasone injection kusaidia mapafu ya watoto kukomaa kwa haraka iwapo dalili za mama zinaonesha anaweza kujifungua kabla ya wakati ili kumsaidia mtoto anapozaliwa kuweza kupumua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili; huduma ya kumsaidia mtoto kupumua (helping baby to breath) kwa wale wenye shida ya kupumua mara tu baada ya kuzaliwa. Huduma hii imefundishwa kwa wafanyakazi wa vituo vyote vya kutolea huduma hapa nchini na kila kituo ambacho kuna huduma za kujifungua kuna vifaa vya kumsaidia mtoto kupumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; kuanzishwa kwa huduma ya mama kangaroo (kangaroo mother care) ambayo humsaidia mtoto kutunza joto na ya nne; kununua vifaa vya kuhudumia watoto njiti ambayo wana matatizo ya kiafya kama vile oxygen concentrator, mashine ya kutibu manjano, mashine za kufuatilia hali ya mgonjwa kwa maana ya pulse oximeter na mashine za kuongeza joto.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Wastani wa juu wa kuzaa kwa mwanamke wa Kigoma ni mara saba juu ya wastani wa kitaifa, lakini wanawake hawa wana hatari ya kupoteza maisha wakiwa wanajifungua kutokana na miundombinu mibovu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha uzazi salama na kutokomeza kabisa vifo vya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO atajibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kigoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wastani wa wanawake kuzaa katika Mkoa wa Kigoma ni 6.7 wakati wastani wa kitaifa ni watoto 5.2 kwa kila mwanamke. Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa kuanzia mwaka 2016 – 2020 kwa jina la kitaalam linajulikana kama (National Road Map Strategic Plan…
Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2016 – 2020 (National Road Map Strategic Plan to Improve Reproductive Maternal, New Born, Child and Adolescent Health in Tanzania) unaolenga kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana.
Katika kutekeleza mkakati huu, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu…
:…Wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua. Wizara katika kuhakikisha inatokomeza vifo vya mama na watoto katika Mkoa wa Kigoma imeweza kutekeleza afua mbalimbali kama vile:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mpango wa kukarabati na kupanua vituo vya afya 208 nchini ili viweze kutoa huduma za uzazi wa dharura, ambapo katika Mkoa wa Kigoma vituo vitatu vilipata fedha za ukarabati wa shilingi milioni 400, ambavyo ni Uvinza, Mwamgongo na Janda…
… na vituo vya afya sita vilipata kila kimoja shilingi milioni 500 ambavyo ni Mabamba, Nyakitonto, Kiganamo, Nyamidaho, Lusesa na Gwanumpu.
Aidha, Kituo cha afya cha Kagezi na Kimwanya vinajengewa vyumba vya upasuaji na jengo la kuhudumia mama na mtoto kupitia wadau wa Global Affairs Canada chini ya Shirika la World Vision.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuimarisha huduma ya uzazi wa mpango kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya afya, na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango. Kwa Mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka miwili watumishi 150 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma za dharura kwa mama mjamzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kupandisha hadhi vituo vya afya ili viweze kutoa huduma ya upasuaji na damu salama, ambapo kati ya vituo 16 vilivyopo 11 vimepandishwa hadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, kuboresha huduma ya rufaa kwa kununua magari na boti za kubebea wagonjwa katika vituo vilivyopo katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Kituo cha Wazee Sarame kilichopo Magugu, Wilaya ya Babati Vijijini ni kituo cha muda mrefu ambacho kinahudumiwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya. Kituo hiki kina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi, usafiri wa dharura, huduma ya kwanza, vifaatiba na miundombinu ya barabara:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma zote za msingi katika kituo hicho ikizingatiwa kuwa wazee wengi ni walemavu wa viungo, vipofu, waliopooza na viziwi pia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa huduma za msingi katika makazi ya wazee na watu wenye ulemavu, wasiojiweza ikiwa ni pamoja na wanaotunzwa katika makazi ya Magugu yaliyopo katika Halmashauri ya Babati Vijijini. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 Serikali imepeleka fedha kiasi cha Sh.14,631,935.47 kwa ajili ya chakula na Sh.900,000 kwa ajili ya dharura zinazojitokeza, bajaji moja katika makazi hayo kwa ajili ya kurahisisha usafiri.
Mheshimiwa Spika, aidha, makazi ya Magugu yamepata huduma ya upulizaji wa dawa za kuuwa wadudu kwa maana ya fumigation mwezi Mei, mwaka huu 2018. Wizara imeendelea kupeleka vifaa vya usafi na huduma ya kwanza kwenye makazi yote ya wazee ikiwa ni pamoja na makazi ya Magugu. Aidha, uboreshaji wa huduma na miundombinu katika makazi utaendelea kufanyika kadri ya fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, sambamba na haya, Serikali bado inatambua kuwa zipo changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za msingi kwenye makazi ya wazee na ili kukabiliana nazo Serikali katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, imetenga jumla ya fedha Sh.27,032,000 kwa ajili ya chakula na Sh.3,600,000 kwa ajili ya dharura. Aidha, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilitenga bajeti ya Watumishi wa Ustawi wa Jamii wapatao 24 na katika bajeti ya Mwaka 2018/2019, Wizara imetenga bajeti ya watumishi 60. Wizara inaahidi kuwapeleka baadhi ya Watumishi hawa kwenye makazi ya wazee Magugu yaliyopo Sarame-Babati Vijijini pale tu tutakapopata kibali cha ajira zao.
MHE. CECILIA D. PARESO aliuliza:-
Serikali ilihusika kikamilifu katika uanzishwaji wa kituo kijulikanacho kama International Graet Lakes Woman Research Centre ambapo kwa Tanzania kituo hicho kuliazimiwa kiwe Tengeru Arusha:-
i. Je, mpaka sasa utekelezaji wake umefikia wapi?
ii. Je, ni mafanikio gani yamepatikana tangu kituo hicho kianzishwe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Pareso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Great Lake Woman Recherch and Documentation Centre kilianzishwa mwaka 2009 ikiwa ni utekelezaji wa maazimio kikao cha Mawaziri, wanaosimamia masuala ya wanawake kutoka nchi za Maziwa Makuu kilichofanyika mwezi Julai, 2008 Kinshasa, Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nchini kituo hicho kilianzishwa chini ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii, Tengeru kwa malengo ya kufanya utafiti kuhusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake hapa nchini, kuhifadhi matokeo ya tafiti hizo ili kuwasaidia watunga sera na wafanya maamuzi kukusanya taarifa na takwimu mbalimbali zinazohusiana na jinsia na wanawake pamoja na kusambaza taarifa hizo kwa njia mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zilizofikiwa katika kuanzisha Kituo hicho, ni pamoja na kutenga eneo maalum ndani ya taasisi linalotumika kwa ajili ya kituo; kukipatia Kituo hicho rasilimali watu ikiwemo Mratibu wa Kituo pamoja na Mkutubi kwa ajili ya kuendesha na kusimamia shughuli za kituo; Kukipatia kituo vifaa ikiwemo computer ishirini na nne, mashine ya fax na simu; kuanzisha tovuti ya kituo inayopatikana kwa anuani ya www.wrdc. or.tz kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuanzishwa kwa kituo hicho baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kwa wanawake na wanaume ili kuwajengea uwezo wa kuendesha shughuli zao na kujiongezea kipato kwa ufanisi na hivyo kupunguza umasikini kwenye jamii. Aidha, chuo kimetoa mafunzo kwa wanafunzi mia mbili wa shule za sekondari ili kuwajengea uelewa wa masuala ya ukatili wa jinsia na madhara yake katika kujenga uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kituo kimewahudumia zaidi ya watu mia tatu ishirini kati ya hao wanawake mia mbili thelathini na moja na wanaume sabini na tisa; na kuwawezesha kupata taarifa walizozihitaji zenye kuelimisha kuhusiana na masuala ya haki za umiliki wa ardhi kwa wanawake, ukatili wa kijinsia na elimu ya ujasiriamali kupitia tovuti na machapisho mbalimbali yaliyopo kwenye Kituo.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Moja kati ya matatizo makubwa yanayoikabili nchi yetu ni maradhi ya figo na idadi ya wagonjwa wa figo inazidi kuongezeka siku hadi siku:-
(a) Je, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hupokea wagonjwa wangapi kwa siku?
(b) Je, Serikali ipo tayari kutoa elimu kwa umma juu ya chanzo cha ugonjwa huo na namna ya kujikinga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 wakati wa huduma za utakasaji wa damu kwa wagonjwa wa figo zilipoanzishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kulikuwa na wagonjwa wa figo chini ya 10 waliokuwa wakihitaji huduma hii, lakini kwa sasa tuna wagonjwa 240 waliopo kwenye huduma hii. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili inatoa huduma ya utakasaji damu kila siku isipokuwa siku ya Jumapili na kuna jumla ya vitanda 42 vya kutolea huduma ambapo kwa siku wanahudumiwa wastani wa wagonjwa 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kiliniki ya wagonjwa wa figo ambayo inafanyika kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imekuwa ikiona wastani wa wagonjwa wapatao 60 kwa siku. Sanjari na hilo, Serikali kupitia hospitali zake za kibingwa imefanikiwa kuanzisha huduma za kupandikiza figo ambapo jumla ya wagonjwa 10 wameshapata huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mgonjwa mmoja katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na upandikizaji huu utaendelea kwa wagonjwa watano kila mwezi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wakati huohuo Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiendelea kujengewa uwezo.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Magonjwa ya Figo Tanzania tunaendelea na jitihada za kutoa elimu za kujikinga na madhara ya magonjwa ya figo kwa kuzingatia kanuni za afya na kupima mapema ili kutambua na kupata matibabu kwa wakati. Elimu juu ya uelewa wa madhara yatokanayo na matumizi ya vileo, lishe isiyozingatia misingi ya afya bora na kutofanya mazoezi vinaweza kusaidia sana kuzuia magonjwa ya figo. Elimu hii imekuwa ikitolewa kupitia vyombo vya habari, ikiwemo makala kwenye magazeti, vipindi vya runinga na redio, vipeperushi, utoaji wa elimu za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na pia kwenye kampeni mbalimbali za magonjwa yasiyoambukiza.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imekuwa na mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Mafunzo yanayohusiana na tafiti hizo maeneo ya Amani Muheza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza azma hiyo?
(b) Kama Serikali haipo tayari, je, itakuwa tayari kukabidhi majengo yaliyopo Amani - NIMR kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
i. Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inayosimamia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (National Institute of Medical Research kwa maana ya NIMR Act 2002, Cap 59, haiipi mamlaka ya kuanzisha au kutoa shahada lakini inaruhusu utoaji wa mafunzo mafupi na elimu kwenye maeneo yanayohusiana na tafiti za kiafya. Wizara kupitia NIMR inalenga kusimamia utekelezaji wa jukumu hili la msingi kwa taasisi kwa kuanzisha mafunzo mafupi yatakayoendana na mamlaka na majukumu ya taasisi.
ii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa taasisi haipo tayari kukabidhi majengo yaliyomo NIMR Amani kwa Halmashauri ya Wilaya na Muheza, kwa kuwa Wizara kwa kupitia NIMR ina mpango wa kuyatumia majengo hayo ikiwemo majengo ya ofisi, karakana, maabara, hosteli na watumishi waliobobea katika nyanja mbalimbali kutoa mafunzo ya muda mfupi kwenye eneo la tafiti za afya ili kuwajengea uwezo wataalamu katika sekta ya afya nchini.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Katika Hospitali ya Rufaa ya Rukwa kumekuwepo na tatizo la wanawake wajawazito na waliojifungua kulazwa katika kitanda kimoja.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto, naomba kujibuswali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge, Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto ya akina mama wajawazito na waliojifungua kulala katika kitanda kimoja inayochangiwa na ufinyu wa nafasi katika jengo la wazazi lililopo kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma hizi hasa kwa kuwa hospitali hii ilianza kama kituo cha afya mwaka 1974. Vilevile tatizo hili linachangiwa na ukosefu wa Hospitali za Wilaya katika Halmashauri za Kalambo na Sumbawanga hali inayosababisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuhudumia wateja wote wanaotoka kwenye halmashauri zote mbili.
Mheshimiwa, Mwenyekiti, Wizara imeweka mikakati ya ufumbuzi wa changamoto hii kama ifuatavyo:-
a) Kupitia Mpango Kabambe wa Hospitali wa mwaka 2017/2018 yaani Comprehensive Hospital Operation Plan, Wizara imekamilisha ukarabati wa wodi mbili na hivyo kuongeza nafasi ya vitanda kwa ziada 20 ambavyo tayari vinatumika na hivyo, kupunguza msongamano uliokuwepo.
b) Serikali inafanya ujenzi na upanuzi wa miundombinu katika vituo vya afya sita ambavyo ni Mazwi, Nkomolo, Kirando, Mwimbi, Legezamwendo na Milepa ndani ya Mikoa hii. Kupanua wigo wa kujifungua kwa njia ya upasuaji. Hatua hii itapunguza tatizo la akina mama wajawazito wengi kupewa rufaa kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
c) Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imetenga jumla ya shilingi bilioni 100.5 katika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya upanuzi wa Hospitali za Halmashauri 67 ambapo kila moja imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.5. Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zinatarajiwa kunufaika na fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu kwamba Serikali kupitia mikakati hii itatoa tatizo la msongamano wa akina mama wajawazito waliojifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inakabiliwa na upungufu wa Madaktari Bingwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Shinyanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Azza Hillal Hamad kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kuwatetea wananchi wa Shinyanga hususani katika sekta ya afya nataka kumpongeza sana kwa jitihada zake hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwezesha kutoa huduma za kibingwa Hospitali za Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inahitaji kuwa na Madaktari Bingwa wa fani sita muhimu ambazo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama na Wajawazito, Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Daktari Bingwa wa Mionzi, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto. Aidha, Serikali inatambua kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina Madaktari Bingwa watatu tu ambao ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama na Wajawazito, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuzihamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya mahitaji ya Madaktari Bingwa na fani zao katika Hospitali zote za Mikoa, Kanda Maalum na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Baada ya kukamilisha tathmini hii Wizara itawapanga upya madaktari bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kila hospitali ya mkoa, kanda, hospitali maalum na zile za Taifa, lengo ni kuwa kila Hospitali ya Mkoa iwe na Madaktari Bingwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Hospitali ya Kibena ni kongwe sana na imechakaa sana:-
Je, ni lini Serikali itaifanyia ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuifanyia maboresho Hospitali ya Kibena katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2018/2019. Kwa sasa Serikali inafanya upanuzi wa jengo la radiolojia ili kusimika mashine mpya ya X-Ray. Ujenzi huu utagharimu jumla ya Sh.39,750,000. Vile vile upanuzi wa jengo la upasuaji unaendelea chini ya ufadhili wa Shirika la UNICEF.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe katika eneo la Wikichi ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali ilipeleka kiasi cha Sh.3,234,787,370 ambazo zimeweza kutumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambao umekamilika kwa asilimia 95.
Mheshimiwa Spika, vile vile, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo kwa kujenga majengo ya X-Ray, upasuaji, uchunguzi wa maabara na kichomea taka hatarishi. Sanjari na hilo, kupitia fedha za Global Fund, hospitali itajengewa jengo la huduma ya mama na mtoto na hivyo kuifanya hospitali hii kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu za afya katika Mkoa wa Njombe.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambalo hata akinamama wajawazito wawili hawawezi kupishana kwenye corridor?

(b) Je, Serikali haioni kuwa kupanua eneo la jengo hilo kutaenda sambamba na kuhamasisha wanaume kwenda kliniki na wenza wao na kupata ushauri pamoja?

(c) Katika eneo la kujifungulia la akinamama ni rahisi kuona kitanda cha jirani yako; je, Serikali haioni hali hii ni udhalilishaji pamoja na kuingilia uhuru wa mwingine kujihifadhi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuboresha huduma za akinamama wajawazito, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, mnamo mwaka 2016 alielekeza kuwa Ofisi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto zilizokuwa eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhama na jengo hilo kutolewa kwa Hospitali ya Taifa ili kupunguza msongamano wa akinamama wajawazito katika jengo la Maternity I. Hivyo basi, ikumbukwe kuwa jengo hili lilikuwa ni Ofisi na lilibadilishwa matumizi kuwa jengo la mama na mtoto, hivyo, miundombinu ya jengo hili hairuhusu kufanyiwa upanuzi.

Mheshimiwa Spika, jengo hili limewekwa viti vya kutosha katika corridor ambayo vinatosheleza kukaa akinamama pamoja na wenza wao. Natoa rai kwa wanaume kuambatana na wenza wao kliniki ili kupata elimu ya kutunza ujauzito; maandalizi ya kujifungua na matunzo ya mtoto ajaye, mwitikio kwa sasa kwa wanaume sio wa kuridhisha.

Mheshimiwa, Spika huduma za akinamama hasa za kujifungua zinahitaji usiri mkubwa. Hiki ni kipaumbele cha Serikali na kwa Watumishi wa Afya katika vituo mbalimbali nchini. Hivyo, katika jengo hili eneo la kujifungulia lina vitanda 20 ambavyo vimetenganishwa na mapazia imara (screen folds) ambapo akinamama hawaonani wakati wa kujifungua na hivyo kutunza faragha zao.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI aliuliza:-

Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Wizara ya Afya iliomba na kutengewa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la maabara na ununuzi wa vipimo vya kisasa kama CT Scan na MRI Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kimeshatolewa mpaka sasa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo?

(b) Kwa kuwa bajeti inayohitajika imeshatengwa; je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilipeleka shilingi bilioni moja, na baadaye katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliomba na kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa jengo la huduma za radiolojia na ujenzi wa Jengo la Wazazi Meta katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya. Hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni tatu zimeshapokelewa kwa ajili ya kazi hizo ambapo shilingi bilioni mbili ni kwa ajili ya kumalizia mradi wa ujenzi wa jengo la radiolojia na ununuzi wa baadhi ya vifaa vya radiolojia na bilioni moja kwa ajli ya kugharamia ujenzi wa jengo la wazazi katika Hospitali ya Rufaa Meta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi umeshakamilika kwa asilimia 90 na kwa sasa mafundi wanakamilisha kuingiza umeme katika jengo baadhi ya ununuzi wa transofoma. Hivyo, hadi kufikia mwezi Machi 2019 jengo litakuwa limekamilika rasmi. Aidha, Serikali tayari imeshanunua CT- Scan kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo inasubiria kukamilika kwa jengo maalum ili iweze kusimikwa rasmi. Vilevile hospitali hii inategemea kupatiwa mashine ya MRI kupitia Mradi wa ORIO wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Taratibu za manunuzi wa vifaa hivi unaendelea.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi linazidi kuwa janga la Kitaifa nchini huku jitihada za kulikabili zikionekana kutopewa kipaumbele; hali ni mbaya katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambapo idadi kubwa ya watoto hao hujihusisha na kuomba pamoja na matukio ya uhalifu ikiwemo wizi wa vifaa vya magari kwenye maegesho.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ya kukabiliana na tatizo hili kwa nchi nzima ikiwemo kuwaweka kwenye vituo maalum na kuwapatia huduma za msingi?

(b) Je, Serikali inatambua idadi kamili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2021/2022 ambapo miongoni mwa shabaha zake ni kuhakiksha watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanapata huduma stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kuwaunganisha watoto hawa na familia zao na pale itakapobainika kuwa wazazi hawapatikani, watoto hawa wataunganishwa na familia za kuaminika wakati taratibu nyingine za kudumu zikiendelea kufanyiwa kazi na mamlaka husika ikiwemo utaratibu wa malezo ya kambo, kuasili au kuwapeleka katika makao ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya utafiti ili kubaini idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika mikoa sita nchini, kwa maana ya Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa ambapo jumla ya watoto 6,393; wanaume wakiwa 4,865 na wanawake 1,528, wametambuliwa. Watoto waliotambuliwa walipewa huduma za chakula, malazi, mavazi na matibabu na kati ya hao ambao walitambuliwa, watoto 930 waliunganishwa na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa mwongozo wa utambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwaunganisha na huduma. Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Juni, 2018, jumla ya waoto 864,496 walitambuliwa kuwa wanaishi katika mazingira hatarishi katika mikoa yote nchini kasoro Mikoa ya Lindi na Ruvuma.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-

Tatizo la kukosekana kwa mafuta yanayosaidia kukinga ngozi dhidi ya mionzi kwa watu wenye Ulemavu wa ngozi hapa nchini limekuwa kubwa na hivyo kuwa chanzo cha magonjwa ya saratani kwa watu hao na kusababisha vifo. Inakadiriwa kuwa asilimia 70 hadi 75 ya vifo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinatokana na saratani.

Je, ni lini Serikali itatoa huduma hiyo bure kwa watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo yote nchini kama inavyotoa dawa za kufubaza virusi kwa watu wenye maambukizi ya UKIMWI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua uwepo wa watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa maana albinos (albinism) nchini na umuhimu wa wao kupata mafuta hayo ili kuwasaidia kukinga ngozi yao dhidi ya mionzi. Kwa kutambua umuhimu wa mafuta hayo, kwa jina la kitaalam tunaita Sun Protection Factor 30, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kuanzia mwaka 2013 iliingiza mafuta hayo kwenye orodha ya Taifa ya dawa muhimu ili ziweze kununuliwa kutunzwa na kusambazwa na Bohari ya Dawa nchini kote.

Aidha, Bohari ya dawa tangu mwaka 2015 imekuwa ikinunua mafuta hayo kadri ya maombi yalivyowasilishwa na vituo vya kutolea huduma ya afya. Baadhi ya taasisi kama vile Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Mirembe
- Dodoma, Hospitali ya Kisarawe na Ilemela zilipata mafuta haya kutoka MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hali ya ualbino ni hali ya kudumu na hivyo kuangukia katika kundi la magonjwa sugu, ambapo Sera ya Afya mwaka ya 2007 inatamka wazi kuwa kundi hili litapata huduma bure, hivyo basi, nitoe rai kwa hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mikoa ya Halmashauri kuingiza bajeti ya mafuta hayo katika mipango yao ili iweze kuagiza mafuta hayo kutoka bohari ya dawa.
Aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha wazalishaji wa ndani ya nchi wa mafuta hayo katika kiwanda kilichopo katika Hospitali ya KCMC.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-

Tanzania haina wauguzi walisomea kuhudumia watoto njiti.

(a) Je, ni lini sasa Serikali itasomesha wauguzi kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti?

(b) Je, kuna hospitali ngapi na vituo vya afya vingapi nchini vyenye chumba atamizi (incubator)?

(c) Gharama za kuwatunza watoto njiti ni kubwa na wanakaa hospitali muda mrefu kwa miezi mitatu hadi minne, je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya kuwahudumia watoto njiti yapo katika Mtaala wa Mafunzo ya Wauguzi na Madaktari na wanafundishwa wakiwa vyuoni. Ili kuboresha ufanisi katika kuwahudumia watoto njiti na upatikanaji wa elimu hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, imetengeneza mtaala wa mafunzo haya utakaotumika kuwafundishia wauguzi waliopo makazini kuanzia mwezi Februari, 2019 nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia Mafunzo ya Huduma Muhimu kwa Watoto Wachanga (Essential Newborn Care), watoa huduma kwa maana ya Madaktari na Wauguzi 1,453 kutoka vituo vya kutolea huduma 653 katika Mikoa ya Tabora, Simiyu, Shinyanga na Kigoma walio makazini wameshapata mafunzo. Lengo ni kutoa mafunzo haya katika mikoa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma atamizi kwa maana incubators hutolewa kwa watoto wote njiti pamoja na walio na uzito pungufu ili kuzuia kupoteza joto ambapo kwa sasa huduma hii inapatikana katika baadhi ya hospitali za Mikoa na Halmashauri tu. Mpaka sasa ni hospitali za mikoa 20 pamoja na Hospitali 24 za Halmashauri ambazo zina vyumba vyenye huduma atamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha huduma za kumhudumia mtoto njiti zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma. Serikali inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na mtoto njiti. Aidha, elimu kuhusu maandalizi kwa ajili ya kujifungua hutolewa kwa wazazi, mama na mwenza wake, wakati wa kliniki za ujauzito ikiwa ni pamoja na matunzo ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua.

Hivyo, Serikali haina kusudio la kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaojifungua watoto njiti. Wizara itaendelea kuboresha miundombinu ya kuwatunza watoto njiti katika vituo vya kutolea huduma za afya na kutoa elimu ya kulea watoto njiti kwa jamii.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-

Kumekuwepo na kero kubwa ya wananchi wanaotumia Bima ya Afya kunyimwa dawa katika zahanati na maduka ya dawa nchini kwa kisingizio cha malipo kutoka NHIF kuchelewa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kimkakati wa kuhakikisha malipo yanafanyika kwa ufanisi ili kuboresha mfumo mzuri wa matumizi ya kadi za Bima hususani kwa wazee nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele leo ni Siku ya Saratani Duniani na naomba kuwakumbusha Watanzania kwamba saratani ni tatizo kubwa ndani ya nchi yetu takribani watu 55,000 kwa mwaka wanapata ugonjwa huo wa saratani na ni 13,000 tu ambao wanafika katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ikiwa ni takribani ni asilimia 25 na asilimia 70 wanafika wakiwa na hatua ya mwisho kabisa ya ugonjwa. Kwa hiyo, nilikuwa nataka kutumia fursa hii kuwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata huduma na upimaji na matibabu ya saratani ni bure.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya huingia mkataba na vituo vya kutolea huduma , mkataba ambao huanisha makubaliano juu ya utaratibu wa kutoa huduma bora kwa wanufaika wake na uwasilishaji wa madai ya gharama ya huduma za afya zinazotolewa kwa wanachama wake. Utaratibu huo huwataka watoa huduma kuwasilisha madai yao kwa wakati ndani ya siku 30 baada ya mwezi husika wa madai ili kuwezesha kuanza kwa mchakato wa madai hayo kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, sheria inautaka mfuko kukamilisha malipo ya madai ya watoa huduma ndani ya siku 60 toka siku ambayo madai husika yamewasilishwa katika Ofisi za Mfuko zilizopo katika mikoa yote nchini. Kwa sasa mfuko unalipa madai kwa wastani wa siku 45. Hata hivyo baadhi ya madai yamekuwa yakichelewa kulipwa kutokana na ucheleweshaji wa kuwasilisha madai kwa baadhi ya watoa huduma. Watoa huduma kutozingatia miongozi ya tiba kama ilivyoainishwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa maana ya Standard Treatment Guidelines. Vitendo vya udanganyifu na baadhi ya watoa huduma kutozingatia makubaliano yaliyoainishwa katika mkataba wa huduma baina yao na mfuko.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mfuko kwa sasa unaendelea kufanya maboresho ya huduma zake ikiwa ni pamoja na kufanya mambo yafuatayo:-

(i) Kutumia zaidi TEHAMA katika utayarishaji wa madai na kuwezesha watoa huduma kutayarisha madai kwa wakati;

(ii) Kuimarisha ofisi za mikoa na kugatua zaidi shughuli za mifuko hasa malipo kwa watoa huduma, viwango vya malipo mikoani vimeongezwa ili kuzipa ofisi za mikoa uwezo wa kulipa madai makubwa;

(iii) Kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma wote waliosajiliwa na mfuko ili kuwasilisha madai kwa wakati na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu;

(iv) Mfuko unaendelea kuwakumbusha watoa huduma kuzingatia miongozo ya tiba na maelekezo mengine yanayotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa lengo kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta sheria ya kuwataka wananchi wote kujiunga Mifuko ya Taifa ya Bima ya Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na maandalizi ya utaratibu wa kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa katika mfumo wa bima na hivyo kuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wote wanapohitaji bila ya kuwa na kikwazo cha kifedha. Katika kulitekeleza jambo hili Wizara imeandaa mapendekezo ya kuanzisha bima ya afya moja, kwa maana ya Single National Health Insurance na kuwasilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi Serikalini. Pindi Serikali itakaporidhia mapendekezo haya suala hili litawasilishwa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, endapo Bunge lako litaridhia muswada huo kutakuwa na ulazima wananchi wote kujiunga na bima ya afya. Matarajio ni kuanza kutekeleza mwaka huu 2019. Kwa sasa Wizara inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya na CHF iliyoboreshwa. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya na CHF zilizoboreshwa wakati tunasubiri muswada huo kupitishwa.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Sera ya Afya imebainisha makundi yenye msamaha wa matibabu ambayo ni wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea, watoto chini ya miaka 5, watoto wanaoishi na TB na UKIMWI:-

Je, ni lini Serikali itaweka Watu wenye Ulemavu kuwa miongoni mwa watu wanaohitaji msamaha wa gharama za matibabu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mhesimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 na kuandaa mapendekezo ya Sera mpya ya Afya. Katika mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 changamoto mbalimbali za matibabu kwa makundi ya msamaha ziliibuliwa na watoa huduma pamoja na watumiaji huduma hizo. Moja ya changamoto iliyojitokeza ni hospitali zetu kuwa na wagonjwa wengi wa msamaha na hivyo kushindwa kuboresha huduma za afya. Kutokana na changamoto hiyo ya kuwa na makundi mengi ya msamaha, Wizara iliona ni vyema ikaboresha utaratibu wa msamaha kwa kuhakikisha kuwa watu wasio na uwezo tu ndiyo wanaopatiwa msamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mapendekezo ya Sera mpya na Afya kila mwananchi mwenye uwezo atapaswa kugharamia huduma za afya. Sera pendekezwa inaainisha njia mahsusi zitakazowezesha Serikali kubaini wananchi wote wenye uwezo ili waweze kuchangia gharama kabla ya kupokea huduma, kwani ni wazi kuwa si kila mlemavu ana kipato duni. Hivyo, wananchi watakaothibitika katika maeneo yao kuwa hawana uwezo wa kuchangia wakiwemo walemavu wataendelea kupatiwa matibabu bila kuchangia gharama za matibabu. Aidha, Serikali inatambua changamoto ya uchangiaji wa huduma za afya na inaandaa utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kundi la walemavu.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

MSD kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa za kuongeza damu kwa mama mjamzito na dawa za usingizi:-

Je, ni lini changamoto hiyo itatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeboresha upatikanaji wa dawa muhimu hadi kufikia wastani wa asilimia 90 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Upatikanaji wa dawa hizi kwa kiasi kikubwa umetokana na ongezeko la bajeti ya dawa hadi kufikia bilioni 269 katika mwaka wa fedha 2018/2019 toka bilioni 31 kwa mwaka wa fedha 2015/2016, pia kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa dawa hizo katika mnyoroo wa ugavi.

Mheshimiwa Spika, dawa za kuongeza uwingi wa damu (Ferous sulphate/fumerate + Folic acid) na dawa za usingizi (Anaesthesia drugs) ni kati ya dawa zilizo katika orodha ya dawa muhimu zaidi ambazo upatikanaji wake umeimarika hadi kufikia asilimia 90. Kwa sasa dawa hizi zote mbili zinapatikana kwa kiasi kikubwa katika Bohari ya Dawa. Kutokana na umuhimu wa dawa hizi kwa mama wajawazito na katika kuhakikisha tunapambana na vifo vya mama wajawazito, Wizara inawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha dawa hizi zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-

Moja ya Dira ya Taifa kupitia Wizara ya Afya ni huduma bora ya afya ya wazazi na kupunguza vifo vya watoto na wazazi:-

Je, ni kwa kiasi gani Dira hii imetekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huandaa Sera na miongozo mbalimbali yakiwemo masuala ya afya ya uzazi na mtoto. Kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga ni suala linalopewa kipaumbele cha kwanza katika Wizara. Dhamira hii inaonekana na kuthibitishwa katika miongozo mbalimbli ya Serikali kama vile Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007; Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025; Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); Mpango Mkakati wa Nne wa Afya; Mkakati wa Kupunguza na Kuimarisha Afya ya Uzazi, Watoto na Vijana; na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Wizara ni kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 292 kwa kila vizazi hai 100,000 na kupunguza vifo vya watoto kutoka 21 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi 16 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanikiwa kuongeza kiwango cha akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 51 mwaka 2012 hadi asilimia 73 mwaka 2018. Aidha, wanawake wajawazito wanaohudumiwa na watoa huduma wenye ujuzi wameongezeka kutoka asilimia 40 mwaka 2012 hadi asilimia 72 mwaka 2018. Idadi ya wanawake wajawazito wanaohudhuria kliniki, mahudhurio manne na zaidi wameongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 57 mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanyika mwaka 2015/2016 unaonesha kwamba vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, vimepungua kutoka 90 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010 na kufikia 67 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016. Vilevile, vifo vya kina mama vimepungua kutoka 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010 na kufikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016. Ni matarajio yetu kuwa utafiti unaofuata wa mwaka 2019/ 2020 utatupa matokeo chanya zaidi katika kupunguza vifo vya akinamama na wajawazito Tanzania.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la matumizi ya dawa za kupunguza maumivu zenye Codeine, Valium, Morphine, Amphetamine, Phenorbabitone ambazo zinauzwa bila cheti cha daktari na zinatumiwa kama mbadala wa dawa za kulevya:-

(a) Je, Sheria zinasemaje kuhusu hilo linalosababisha vijana kuwa mateja wa dawa za kawaida?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hakuna prescription drugs inauzwa bila cheti cha daktari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Sheria ya Chakula na Dawa, Sura Na. 219 katika kifungu chake 77(2) inatambua makundi matatu ya dawa ambayo ni:

(i) Dawa zinazodhibitiwa ama kwa jina la kigeni inaitwa controlled drugs kama Morphine, Pethidine na Diazepines kama vile valium:-

(ii) Dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari, prescription only medicines mfano dawa za antibiotic, shinikizo la damu, kisukari, za saratani na dawa zenye viambata vya Codeine; na

(iii) Dawa za kawaida ambazo kwa lugha ya kigeni tunaita Over the counter/general medicine dawa hizi hazihitaji cheti cha daktari. Mfano kama dawa za kikozi, mafua na maumivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria hiyo ya Mamlaka ya Chakula na Dawa, Sura 219 kifungu cha 77(4) kinatoa adhabu ya faini au kifungo kwa mtu yeyote atakayekutwa akitoa dawa za zinazodhibitiwa na zinahitaji cheti cha Daktari.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa pamoja na uwepo wa sheria na adhabu hizo bado kumekuwa na changamoto za uuzwaji wa dawa zinazohitaji cheti cha daktari pasipokuwa na chetu hicho. Wizara imeandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na suala hili kwa kufanya yafuatayo:-

(i) Kuandaa kanuni za usimamizi na udhibiti wa dawa za cheti ambapo pamoja na mambo mengine zitaainisha namna dawa zinazodhibitiwa (Tramadol, Diazepam, Pethidine na Morphine) ambapo kwa sasa rasimu ya awali imeshakamilika. Aidha, adhabu kali zimebainishwa kwa watakaokiuka taratibu hizo;

(ii) Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa mifumo ya udhibiti ukaguzi katika meneo yanayotoa huduma za dawa nchini; na

(iii) Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara yanayoweza kupatikana kutokana na matumizi holela ya dawa.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-

Masuala ya kunajisi na ubakaji kwa watoto pamoja na mapenzi ya jinsia moja yamekithiri nchini na kuongezeka siku hadi siku:-

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti wa kina na kuona athari zinazoendelea kuikumba jamii katika suala zima la usagaji (lesbianism)?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza kuandaa sheria ya kuwaadhibu wanawake wanaoharibu vijana wa kiume chini ya umri wa miaka 18 na wale wenye kuwafunza na kuwaharibu watoto wetu wa kike katika masuala ya usagaji (lesbianism)?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 inakataza vitendo vilivyo kinyume na maadili ikiwemo mapenzi ya jinsia moja. Hadi sasa Serikali haina takwimu za hali ya usagaji na ushoga nchini. Hivyo, Serikali inaona umuhimu wa kufanya utafiti wa kina kuhusu masuala ya mapenzi ya jinsia moja ikiwepo usagaji ili kubaini ukubwa na athari za suala hilo.

(b) Mheshimiwa Spika, pindi utafiti utakapofanyika, Serikali itaangalia uwezekano wa kuzifanyia marekebisho na kuboresha sheria zilizopo ili kubaini na suala hilo?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali inatambua kuwa sheria pekee haitoshi kutatua tatizo hili, hivyo inaendelea kutoa elimu kuhusu malezi chanya yanayozingatia maadali ya Kitanzania?
MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR aliuliza:-

Vitendo vya ukatili kwa watoto vimezidi kuendelea kwa kasi siku hadi siku kama vile ubakaji, kunajisiwa kwa watoto wa kiume na kuingiliwa kinyume na maumbile watoto wa kike:-

Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria Bungeni ili kurekebisha sheria hiyo iwe kali zaidi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mussa Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla sheria zilizopo zinajitosheleza kabisa kuwashughulikia wale wote wanaokutwa na hatia katika makosa ya ubakaji, kunajisi watoto wa kiume na wa kike. Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 1985, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, imeelekeza adhabu kali kwa yeyote atakayebainika kutenda kosa la kumdhalilisha mtoto au kumbaka mtoto ikiwemo kifungo cha miaka 30.

Hata hivyo, imekuwa vigumu kuwatia hatiani wakosaji hawa kwa sababu wengi wanatoka ndani ya familia na kwa kukosekana ushahidi ikizingatiwa matukio mengi hufanywa na watu walio karibu na familia. Wengi wao wanaogopa kutoa ushahidi kutokana na hofu ya kupoteza mmoja wa wanafamilia kutokana na adhabu za vifungo vya maisha. Aidha, kutokana na mtazamo hasi wa jamii, familia nyingi huhofia kudhalilika na kunyanyapaliwa baada ya kubainika mkosaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kuweka mikakati ya kusaidia kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hili, lakini bila ushirikiano katika ngazi zote kuanzia familia haitakuwa rahisi. Serikali inatoa rai kwa jamii kutomaliza masuala ya ukatili wa kijinsia ndani ya familia na badala yake ishirikiane na Serikali ili sheria ichukue mkondo wake.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari wa kutibu magonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeajiri Madaktari 11 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara katika ajira mpya za mwezi Julai, 2018. Kwa sasa hospitali imeshapokea Madaktari nane na kufanya jumla ya Madaktari wa kada kuwa 17. Sanjari na hilo, katika kupunguza tatizo la uhaba wa Madaktari Bingwa, Hospitali ya Ligula kwa kupitia utaratibu wa kuendeleza watumishi wake inatarajia kumpokea Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Koo, Pua na Maskio (ENT Surgeon) ambaye anatarajiwa kumaliza mwezi Oktoba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2017/2018, Wizara iliwapeleka Madaktari Bingwa wa fani ya Upasuaji wa Kawaida na Mifupa (General Surgeon na Orthopaedic Surgeon) katika Chuo cha Muhimbili ambapo wanatarajia kumaliza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021. Aidha, Wizara itaendelea kutenga bajeti ya kuwasomesha Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili kufikia azma ya Serikali na kuhakikisha kwamba hospitali zote za rufaa za mikoa zinakuwa na Madaktari Bingwa wa kutosha.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. GODFREY W. MGIMWA) aliuliza:-

Taarifa mbalimbali za kitafiti zinaonesha kwamba Mkoa wa Iringa unaongoza kwa tatizo la utapiamlo:-

(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kufikia kwenye takwimu hizo?

(b) Je, jitihada gani zinachukuliwa na Serikali kunusuru tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa ni kweli kabisa Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa tatizo la udumavu kwa asilimia 42. Wastani wa Kitaifa ni asilimia 34, kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa demografia na afya wa mwaka 2015/2016 uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Wadau wa Maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vilivyotumika kufikia takwimu hizo ni pamoja na kuchukua sampuli za kaya zilizochaguliwa kushiriki kupitia utaratibu maalum wa kitaalaam ili kuziwakilisha kaya nyingine katika Wilaya. Kwa kaya zilizochaguliwa watoto chini ya miaka mitano walipimwa urefu au kimo, uzito, kupimwa wekundu wa damu pamoja na kuhoji maswali kwa Mkuu wa Kaya au mlezi kwa kutumia dodoso maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kunusuru tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Afua za Lishe (National Multisectoral Nutrition Action Plan) wa mwaka 2016/2017 ambayo itaisha mwaka 2021/2022 ambao una vipaumbele vinavyolenga kupunguza utapiamlo ifikapo mwaka 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa lishe inaendelea kutekeleza afua za lishe zenye matokeo makubwa ambayo ni pamoja na:-

(i) Utoaji wa vidonge vya madini chuma na asidi ya foliki kwa wajawazito;

(ii) Utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo;

(iii) Uongezaji wa virutubishi vya madini na vitamin kwenye vyakula hususani unga wa ngano, mahindi, mafuta ya Kula pamoja na urutubishaji wa kibiolojia wa mazao katika viazi vitamu, mahindi, maharage na mihogo;

(iv) Kutoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto chini ya miaka mitano;

(v) Utoaji wa elimu na huduma ya lishe kwa wanawake, wasichana na watoto wachanga na wadogo, elimu ya ulaji wa vyakula mchanganyiko na mtindo bora wa maisha; na

(vi) Utoaji wa Ajira Maafisa Lishe katika ngazi za mikoa na halmashauri.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi, uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji safi na maji taka ikiwemo na ukosefu wa gari la wagonjwa:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia hospitali hiyo watumishi wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ni tegemeo la watu wengi hasa akinamama wajawazito?

(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na vitendea kazi vingine ikiwemo CT Scan na MRI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2018/2019, imeajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya 52, katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi na kufikia asilimia 45. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara inategemea kuomba kibali cha kuajiri watumishi 197 wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiendelea kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Mpaka sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imeshapelekewa mashine mpya ya kisasa ya X-ray (digital x-ray) na imeanza kufanya kazi. Sanjari na hilo, hospitali mpya, itakapokamilika itasimikwa vifaa vya kisasa ikiwemo CT Scan ili kuiwezesha kufanya kazi kwa hadhi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa magodoro, vitanda na vifaa tiba Wizara itaendelea kuhakikisha Hospitali inatenga bajeti kupitia mpango kabambe wa Hospitali Comprehensive Hospital Operational Plan (CHOP) kwa ajili ya ununuzi wa vitanda, magodoro na vifaa tiba ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, tayari imetumia kiasi cha Sh.673,575,168.58/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na vitendea kazi kama magodoro, mashuka, vitanda, mashine ya kufulia, ultra sound pamoja na vifaa kwa ajili ya chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwahudumia wagonjwa wa akili wanaozurura mitaani katika masuala ya matibabu, mavazi na makazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuimarisha huduma za afya nchini ikiwemo huduma ya afya ya akili. Uimarishaji wa huduma ya afya ya akili umekwenda mpaka katika ngazi ya afya ya msingi ambapo ndipo jamii ilipo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuongezeka kwa wagonjwa wa akili wanaorandaranda barabarani, Sheria Afya ya Akili ya mwaka 2008 inawataka ndugu na jamii kuibua wagonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ili wapate matibabu. Wagonjwa wakishapata nafuu huruhusiwa kwenda kukaa na familia zao kwenye jamii wanazotoka. Jukumu la kwanza la kulinda afya ya jamii huanzia ngazi ya familia lakini jamii zetu zimekuwa zikiwanyanyapaa, kuwabagua na kuwatenga wagonjwa wa akili na kupelekea wagonjwa wa akili kurandaranda mtaani.

Mheshimiwa Soika, kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, Sehemu ya Tatu, kifungu cha sheria namba 9(1)(3) imeeleza wazi kuwa Afisa Polisi, Afisa Usalama, Afisa Ustawi wa Jamii ngazi ya Wilaya pamoja na viongozi wa dini, Afisa Mtendaji wa Kata, Afisa wa Kijiji wana jukumu la kubainisha mtu yeyote anayerandaranda kwa kutishia amani au vinginevyo na kumfikisha kwenye sehemu ya uchunguzi wa magonjwa ya akili na ikithibitika taratibu za kumpatia matibabu huanza kama ilivyoainishwa kwenye Sehemu ya Tatu ya Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008, kifungu namba 11(7)(12) cha sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa rai kwa jamii kuibua watu wanaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa wa akili na kuwapeleka kwenye vituo cha afya ili waweze kupata matibabu kwani huduma hii ipo na inatolewa bila gharama yoyote. Magonjwa ya akili yanatibika, hivyo, nitoe rai kwa jamii waache kuwanyanyapaa wagonjwa wa akili na badala yake wawafikishe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuwa ugonjwa wa akili hauna uhusiano na imani za ushirikina.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo watoto wengi njiti huzaliwa na akinamama wanaojifungua watoto hao njiti wengi wao ni waajiriwa ambao hupata changamoto ya likizo ya uzazi inayotosha kwa malezi ya awali ya watoto hao njiti:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha akinamama hao wanaongezewa likizo ya uzazi?

(b) Akinamama hao wanapojifungua pia, hupata changamoto ya vifaa kama vile vifaa vya kukamulia maziwa, dawa na gharama za matibabu; Je, Serikali imejipangaje kuwasaidia gharama za vifaa hivyo?

(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kudumu wa kutokomeza suala la akinamama kuzaa watoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kazi ya Mwaka 2004, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 inaelekeza kuwa mama aliyejifungua mtoto mmoja apewe likizo ya malipo ya siku 84 na siku 100 kwa mama aliyejifungua watoo pacha, sheria hiyo pia imeweka wazi kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kupewa saa mbili kwa siku, ili apate muda wa kunyonyesha. Serikali haina muda wa kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa sasa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza sera ya Afya ya Mwaka 2007 ya Kutoa Huduma Bila Maipo kwa Makundi Maalum wakiwepo akinama wajawazito na mwongozo wa uchangiaji unaeleza wazi kuwa, kundi hili halipaswi kugharamia huduma za afya pale wanapohitaji. Hivyo, basi, Wizara inafanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma kwa akinamama wajawazito, hususan, wanapojifungua kwa kutumia njia mbalimbali. Kwa sasa Wizara inatekeleza Mpango wa Pili wa kuboresha afya ya uzazi na mtoto, yaani One Plan II ya mwaka 2016 mpaka 2020 ambapo imeweka vipaumbele mahususi vya kuboresha afya ya watoto wachanga ikiwemo watoto njiti nchini. Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 Wizara imetenga fedha bilioni 22.5 kwa ajili ya huduma ya mama wajawazito na katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 inatarajia kuomba idhini ya Bunge kutumia fedha kiasi cha bilioni 29.5 kwa ajili ya kundi hili na hivyo hakuna akinamama wanaojifungua wanaoripotiwa kukosa huduma za dawa na vifaa tiba kabla na baada ya kujifungua katika vituo vya Serikali.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kujikita katoka afua mbalimbali kwa lengo la kudhibiti visababishi vya kuzaliwa watoto njiti, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha akinamama wajawazito wanaanza kliniki mapema mara tu wanapohizi kuwa na ujauzito, kuhudhuria kliniki ipasavyo, ili kuchunguza na kutibiwa magonjwa mbalimbali, ikiwa yatabainika kwa kuzingatia vilevile ushauri wa lishe n.k. Afua nyingingine zinazolenga kuokoa maisha ya watoto wachanga kama vile uanzishwaji wa vyumba maalum vya matunzo na matibabu ya watoto wachanga, kwa maana ya neonatal care units, sambamba na upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, kwa ajili ya watoto wachanga ikiwemo watoto njiti.
MHE. AMINA N. MAKILAGI Aliuliza:-

Baadhi ya watu katika jamii bado wanaendeleza vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwadhulumu wanawake:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza kabisa vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua ukatili wa kijinsia ni pamoja na vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwadhulumu wanawake na watoto. Aidha ukatili wa kingono na kisaikolojia ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali za kuzuia na kutokomeza ukatili huo. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kuandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha mwaka 2021/2022. Mpango huo unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000; Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia wa mwaka 2005; na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008. Kutokana na utekelezaji wa mpango huu, hadi kufikia 2018, jumla za Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto 10,988 zimeanzishwa katika ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata, Vijiji na Mitaa. Kamati hizi zina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa mpango kazi katika ngazi husika.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Jeshi la Polisi 420 kwa kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia. Aidha, Serikali imeanzisha huduma za One Stop Center kwenye Mikoa saba ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Shinyanga, Pwani, Iringa Mbeya na Mwanza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imewezesha kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Namba 1 ya mwaka 2017. Sheria hii inatoa fursa kwa wanawake waliofanyiwa unyanyasaji au kudhulumiwa kupata haki zao kupitia vyombo vya usimamizi wa sheria pasipo kujali uwezo wao wa kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa elimu kwa jamii. Mfano katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara imetoa elimu ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kwa Wahariri na Waandishi wa Habari ili waweze kuelimisha jamii kuhusu suala hili pamoja na kufichua matukio ya ukatili wa kijinsia. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali imeratibu midahalo kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na kuwasilisha wasanii katika kampeni za kutokomeza ukatili huo.
MHE. ESTHER N. MATIKO (K.n.y. MHE. HAWA S. MWAIFUNGA) aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na changamoto kubwa za majengo, Wauguzi, Madaktari na Wahudumu wengine wa Hospitali, pia kuna uhaba mkubwa wa vitanda hali inayosababisha wajawazito kuzalia chini:-

(a) Je, katika mwaka huu wa fedha Serikali imejipanga vipi kuwasaidia Wananchi wa Tabora kupata ahueni kwa kutatua kwa kero za Hospitali hiyo inayotegemewa na zaidi ya robo tatu ya wakazi wa mji wa Tabora?

(b) Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kuwa Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui nazo zinapata hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora katika ajira mpya za mwezi Julai, 2018 imeajiri watumishi wapya wapatao 49 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kati ya hao wakiwemo wauguzi, wateknolojia, wafamasia na madaktari na kufanya hospitali kuwa na jumla ya watumishi 357 kwa kada zote kati ya watumishi 468 wanaohitajika kulingana na ikama ya hospitali ambayo ni sawa na asilimia 76.3 ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hospitali haina tatizo la vitanda na magodoro lakini kuna ufinyu wa majengo unaopelekea kuwa na vitanda vichache. Hivyo basi kwa kuwa hospitali za rufaa za mikoa zimekabidhiwa rasmi chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 wizara imetenge bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ambapo itaweza kupunguza uhaba wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka fedha 2018/ 2019 Serikali imepanga kujenga hospitali za wilaya 67 nchi nzima katika jitihada za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa upande wa Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui nazo zimepatiwa fedha kiasi cha bilioni 1.5 kwa kila moja kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imeboresha vituo vya afya 13 katika Wilaya ya Uyui DC, Tabora MC, Nzega TC, Kaliua DC, Igunga DC, Skonge DC, Urambo DC na Nzega DC. Kukamilika na kuanza kutumika kwa hospitali na vituo vya afya hivi vitapunguza sana msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI aliuliza:-

Udumavu na Utapiamlo mkali ni tatizo kwa watoto wengi nchini:-

Je, Serikali ina mpango gani unaotekelezeka wa kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuzijengea uwezo Kamati za lishe za kata?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuhu Mwamwindi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeazimia kutekeleza malengo la Baraza la Afya Duniani (World Health Assembly) la kutokomeza utapiamlo ifikapo mnwak 2025, pamoja na kutekeleza maazimio mbalimbali ya kupunguza utapiamlo ya kitaifa kikanda na Afrika Mashariki. Kitaifa, Serikali kupitia sera ya Taifa ya afya mwaka 2007 ambayo kwa sasa inapitiwa imeeleza wazi kuwa itaboresha huduma za lishe kwa wananchi wake. Kwa miaka ya karibuni Serikali imeongeza juhudu katika kupambana na tatizo la utapiamlo nchini kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi mbalimbali zilizofanyika ni pamoja kuandaa na kutekeleza mpango mkakati jumuishi wa kitaifa wa Utekelezaji wa Afya za Lishe (National Multi-sectoral Nutrition Action Plan ya mwaka 2016/ 2017 ambayo itaisha mwaka 2021/2022 ambayo una vipaumbele vinavyolenga kupunguza utapiamlo kufikiapo mwaka 2021 ambavyo ni pamoja na:-

(i) Kupunguza viwango vya hudumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kutoka asilimia 34 mawaka 2015 hadi 28.

(ii) Kudhibiti viwango vya ukondefu kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na kufanya viendelee kubakia chini ya asilimia 5 iliyopo sasa.

(iii) Kupunguza viwango vya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.

(iv) Kupunguza idadi ya wanawake walio katika umri wa uzazi miaka 15 - 49 wenye upungufu wa damu kutoka asilimia 44.7 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 33.

(v) Kupunguza tatizo la upungufu wa vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 59 kutoka aslimia 33 hadi kufikia asilimia 26.

(vi) Kudhibiti tatizo la uzito uliozidi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kubakia chini ya asilimia 5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianzisha muundo wa kada ya Maafisa Lishe chini ya Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2012 ambapo jumla ya Maafisa Lishe 114 wameajiriwa katika mikoa na halmashauri za Serikali. Sanjari na hilo, Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais - TAMISEMI ipo katika mchakato wa kuangalia utaratibu wa kuajiri wahudumu wa afya, ngazi za jamii angalau wawili wawili kila kijiji ambapo pamoja na shughuli nyingine watatoa huduma za lishe katika ngazi ya kaya.
MHE. MARIAM NASORO KISANGI aliuliza:-

Wapo watoto wanaoishi Gerezani na huenda shule na kurudi Gerezani kulala na mama zao. Hali hiyo siyo nzuri kwa malezi ya mtoto hasa mambo wanayoyaona na kusikia wakiwa Gerezani:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia watoto hao waondokane na hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto kuwepo magerezani inatokana na mama zao kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo wakiwa katika hali ya ujauzito au kuwa na mtoto aliye chini ya umri wa miaka miwili ambaye anapaswa kupata haki ya kunyonya maziwa ya mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutoa maelezo ya ufafanuzi kama ifuatavyo: hakuna watoto wanaokwenda shule wakiwa magerezani isipokuwa kuna watoto walio chini ya miaka miwili wanaolazimika kubaki gerezani na mama zao ili kupata haki yao ya kunyonya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yapo mazingira yakiwemo kukosekana kwa malezi mbadala kwa watoto zaidi ya miaka miwili na wasiozidi miaka mitano kubaki na mama zao gerezani, hivyo kulazimika kuhudhuria katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Day Care Centres) kwa madhumuni ya kupata huduma ya malezi changamshi ya awali ili kuchochea ukuaji na maendeleo ya kiakili, kimwili, kihisia, kijamii na kimaadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2015 kulikuwa na watoto 150, mwaka 2016 tulikuwa na watoto 85 na mwaka 2017 kulikuwa na watoto 108. Watoto hawa ni kwa mgawanyiko wa akina mama walioko mahabusu na wafungwa katika magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 Kifungu cha 114, Kanuni za Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mwaka 2015 na Sera na Uratibu wa Ulinzi na Mtoto katika Magereza ya Mwaka 2018, imeweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa mtoto anapata malezi yanayohitajika ikiwemo mlo kamili, virutubisho, huduma za afya pamoja na chanjo kwa watoto wa chini ya miaka miwili. Utaratibu wa watoto chini ya miaka mitano kuhudhuria kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, unalenga kupunguza muda watoto kukaa gerezani na kutumia muda wa zaidi ya masaa sita katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009, Serikali imeanzisha program ya malezi mbadala kama vile walezi wa kuaminika, malezi ya kambo na kuasili. Lengo ni kuhakikisha watoto wote wanaolelewa katika taasisi wanapata malezi ya kifamilia. Pia watoto walio na mama zao gerezani ambao wamekosa malezi mbadala, wanapata fursa ya kupokelewa katika makao ya watoto kwa muda wakati jitihada nyingine zikiendea. Program hizo zinahakikisha watoto wa zaidi miaka mitano wanaondolewa gerezani na kuunganishwa na watoa huduma wa malezi.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-

Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kwenye suala la ubakaji (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho yaliyofanywa mwaka 2017 yote yana lengo la kukomesha vitendo vya ubakaji wa watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi (kifungo miaka 30) na watoto chini ya miaka 10 (kifungo cha maisha):-

(a) Je, tokea kupitishwa kwa sheria hii (SOSPA) na marekebisho yake, ubakaji umepungua au kukoma hapa nchini?

(b) Je, kama bado changamoto ipo Serikali ina mpango mkakati gani mpya katika kupambana kutokomeza ubakaji Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Giga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Makosa ya Kujamiana (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho yaliyofanyika 2002 imeingiza vifungu vya makosa ya kujamiana kwenye Kanuni za Adhabu ili kukomesha vitendo vya ubakaji kwa watoto ambapo yeyote akipatikana na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela au kifngo cha maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na adhabu hii ambayo ni kubwa ambayo ingeweza kufanya watu waogope kujihusisha na vitendo vya ubakaji lakini vitendo vya ubakaji kwa watoto nchini vimeendelea kuongezeka. Kwa mujibu wa Takwimu ya Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani, matukio ya ubakaji yameongeza kutoka matukio 394 Desemba 2015 hadi kufikia matukio 2,984 Desemba 2017. Hii ni kutokana na jitihada kubwa ambayo Serikali imefanya na wadau ambalimbali ya kuhamasisha jamii kutoa taarifa ya masuala ya ubakaji pindi yanapotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza afua mbalimbali katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 10, 988 katika ngazi za Halmashauri, Kata na Vijiji; kuanzisha vikundi vya malezi 1,184 na kuwezesha huduma ya simu kwa watoto ambapo wanaweza kupiga simu namba 116 ili watoto na jamii waweze kutoa taarifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017/ 2018 - 2021/2022 ambapo kupitia mpango huu Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kutoa elimu bure, kuandaa na kutoa elimu juu ya malezi chanya kupitia vitini vya malezi na makuzi na kuandaa mkakati wa mawasiliano wa kuelimisha wananchi kuachana na mila potofu.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa ukamilifu Sera ya Afya ya kutoa huduma za afya bure kwa wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano pamoja na wazee wenye umri zaidi ya miaka 60?

(b) Mwaka 2014 Serikali ilianza utaratibu wa kuwapatia wazee vitambulisho kwa ajili ya matibabu bure kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali. Je, ni Wilaya ngapi zimekamilisha zoezi hilo muhimu ili kuokoa maisha ya wazee yanayopotea kwa kukosa huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada katika kutoa huduma bora za afya na zenye kufikiwa na watu kwa kuandaa sera na miongozo na kusimamia utekelezaji wake. Katika kutoa huduma hizi, Serikali imekuwa ikiyapa kipaumbele makundi maalum kama vile wajawaziti, watoto chini ya miaka mitano, wazee wasio na uwezo na wenye ulemavu ambao kwa namna moja au nyingine hawawezi kujishughulisha na shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato kwa kuanzisha sera za matibabu bila malipo kwa makundi hayo. Tangu kuanzishwa kwa sera hii Serikali imekuwa ikisimamia kwa ukaribu kuhakikisha inatekeleza ipasavyo na watoa huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya katika kuwapatia makundi haya matibabu bure, bado kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa sera hii kutokana na kuongezeka kwa magonjwa na idadi ya watu walio katika makundi maalum. Hali hii inasababisha watoa huduma kuwa na idadi kubwa ya watu walio katika makundi maalum wakati rasilimali kwa ajili ya kuwahudumia ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali iko katika hatua ya maandalizi ya mkakati wa ugharamiaji wa huduma za afya ambao lengo lake ni kuibua vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kugharamia huduma za afya kwa maana ya health care sector financing. Moja ya vyanzo vilivyopendekezwa katika mkakati huo ni uanzishwaji wa Bima ya Afya moja (Single National Health Insurance) ambayo uchangiajikatika bima hiyo itakuwani ya lazima kwa wote walio na uwezo wa kuchangia. Kulingana na taifiti zilizofanywa, njia hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza rasilimali fedha katika sekta ya afya na kuweza kugharamia makundi maalum yatakayohitaji msaaha wa kulipia huduma za afya. Mkakati huu unatarajia kukamilika na kuanza kutekelezwa mapema mara baada ya taratibu za Serikali za kufanya maamuzi zitakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa maagizo kwa watoa huduma watenge madirisha maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee na Halmashauri ziwatambue na kuwapa kadi za wazee kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo utekelezaji wa utaratibu huu umekuwa na changamoto ambapo takribani asilimia 40 tu za Halmashauri zote zimeweza kutekeleza agizo hilo. Natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la Serikali la kutoa vitambulisho kwa Wazee.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Kuna wagonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Damu na Kansa wanapata shida kubwa ya kiafya:-

Je, Serikali ina mpango gani katika kuwapatia huduma ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisukari, Shinikizo la Damu na Saratani ni kati ya magonjwa yajulikanayo kama magonjwa sugu au magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka sana duniani kote ikiwa ni pamoja na Nchi Zinazoendelea, Tanzania ikiwepo. Ongezeko hili lilianza kuonekana tangu miaka ya tisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007, ilitoa tamko la kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, mnamo mwaka 2009, Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilianzisha kitengo cha kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kutengeneza mpango mkakati wa mwaka 2009 – 2015 na hivi sasa tunatekeleza mpango mkakati wa mwaka 2016 – 2020. Mwongozo huu unatekelezwa kuanzia ngazi ya hospitali ya kanda hadi zahanati. Huduma za Magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la Damu pamoja na Saratani ni huduma ambazo katika hatua za awali zinapatikana katika ngazi ya kituo cha afya. Mgonjwa anapokuwa na magonjwa haya ambayo yapo katika hatua ya juu, hulazimika kupatiwa huduma za matibabu ambazo zinapatikana Hospitali za Kanda, Taifa, Rufaa za Mikoa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeboresha huduma ya magonjwa ya moyo ikiwemo Shinikizo la Damu kwa kufungua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali za Ocean Road, Bugando, KCMC, Benjamin Mkapa na ipo mbioni kufungua huduma za saratani katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya ili kupunguza mzigo kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambayo kwa miaka mingi ni yenyewe pekee imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa hao. Aidha, Serikali iko mbioni kuanzisha programu ya magonjwa yasiyoambukiza kama ilivyo kwa Programu za UKIMWI, TB na Malaria ili kufikisha huduma hizi katika ngazi ya zahanati na kuzipa mwonekano wa kipekee huduma za magonjwa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, natoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanajikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kula mlo unaofaa, kutotumia tumbaku na bidhaa zake na kupunguza matumizi ya pombe.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Sera ya Wazee imeelekeza kuwapatia wazee matibabu bure lakini utekelezaji wake haueleweki na pia una urasimu mkubwa.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa uhakika wa kuwaondolea kero na shida hizo wanazozipata wazee katika suala zima la matibabu yao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007 iliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba wazee wanapata huduma bora za afya. Katika kutekeleza uamuzi huo Serikali ilitoa tamko la makundi maalum wakiwemo wazee wasio na uwezo kupatiwa huduma za afya bila malipo. Hata hivyo, changamoto iliyopo katia utekelezaji wa Sera hii ni ufinyu wa bajeti ikilinganishwa na mahitaji ya kuwapatia huduma za afya makundi hayo bila wao kuchangia gharama za huduma hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya Mkakati wa Ugharamiaji wa Huduma za Afya ambao lengo lake ni kuibua vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya kugharamia huduma za afya (Health Care Financing).

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa vyanzo vilivyopendekezwa katika Mkakati huo ni uanzishwaji wa Bima ya Afya Moja (Single National Health Insurance) ambapo uchangiaji katika bima hiyo utakuwa ni wa lazima kwa wote walio na uwezo wa kuchangia.

Kulingana na tatifi zilizofanywa, njia hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza rasilimali fedha katika sekta ya afya na kuweza kugharamia makundi maalum yanayohitaji msamaha wa kulipia huduma za afya. Serikali inatarajia kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wote mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwataka watoa huduma kutenga madirisha maalum kwa ajili ya kwuahudumia wazee na halmashauri ziwatambue na kuwapa kadi za wazee kwa ajili ya matibabu.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y JOSEPHINE T. CHAGULA) aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Geita haina jenereta la dharura pindi umeme unapokatika na hivyo kusababisha vifo vingi kutokea:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka jenereta la dharura katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jenereta lililokuwa linatumika katika hospitali ya Mkoa wa Geita lilipata hitilafu na hivyo kufanya hospitali ya Mkoa wa Geita kutokuwa na jenereta la dharura.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hospitali ya Mkoa wa Geita imepata jenereta mbadala lenye ukubwa wa KVA 400 ambalo linakidhi mahitaji yote ya hospitali. Jenereta hili lilipatikana kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita kupitia Mgodi wa GGM.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza Madaktari Bingwa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jin sia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za huduma nchini ikiwa ni pamoja na hospitali yetu ya Taifa Muhimbili. Katika Mwaka 2017/2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilitenga kiasi cha shilingi bilioni Mbili zilizotumika kwa ajili ya kusomesha Madaktari Bingwa 125 wa fani za kipaumbele katika Chuo cha Muhimbili (MUHAS) ambao wanatarajia kukamilisha masomo yao mwaka 2020/ 2021. Aidha, katika mwaka 2018/2019, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ili kuendelea kugharamia mafunzo ya ngazi ya kibingwa katika kada mbalimbali za afya 127 katika Chuo cha MUHAS. Aidha katika mwaka 2018/2019 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ili kuendelea kugharamia mafunzo ya ngazi za bingwa kwa kada mbalimbali za afya 127 katika Chuo cha MUHAS.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni, 2019 jumla ya watumishi wa sekta ya afya 458 walikuwa wanaendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za taaluma kwa idadi hiyo, 435 wanaendelea na masomo yao ndani ya nchi na 23 nje ya nchi kwa ufadhili wa Serikali; katika idadi hiyo, jumla ya madaktari bingwa 365 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo kuanzia mwaka 2019/2020, 2020/2021, 2021/2122. Wataalam wote hawa watasambazwa katika hospitali mbalimbali nchini kulingana na uwiano wa wataalam waliopo na kwa kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya watalaam bingwa katika fani za kipaumbele. Kutokana na uhaba uliopo katika hospitali za rufaa za mkoa Wizara itahakikisha fedha hizi zinatumika vyema katika kusomesha wataalam wanaotoka katika maeneo yenye uhaba mkubwa. Aidha Wizara kupitia hospitali za rufaa za Taifa na taasisi za nje inaendelea kuendesha kambi za udaktari bingwa hapa nchini kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa na kuwajengea uwezo wataalam wetu.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD aliuliza:-

Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) inafanya kazi zake kwa weledi na uadilifu mkubwa lakini haina mamlaka ya kujitegemea kama zilivyo BRELA na RITA.

Je, ni lini Serikali itaipa Mamlaka Idara hiyo kuwa Taasisi inayojitegemea?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Ofisi ya Waziri Mkuu iliandaa kikosi cha kupitia, kuchambua na kushauri juu ya namna bora ya uratibu wa mashirika yasiyo ya Serikali. Moja ya mapendekezo yaliyotolewa ni kuifanya Idara ya Mashirika Yasiyo ya Serikali kuwa Taasisi inayojitegemea. Hata hivyo, suala hilo ni la kimuundo na linahitaji maandalizi ya kutosha. Serikali inatoa rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha pamoja na vitendea kazi muhimu ili kumwezesha Msajili kufanya kazi yake na umadhubuti chini ya usimamizi wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Serikali. Serikali inayafanyia kazi pasipo kuingiliwa na pia ina wawakilishi wa Serikali na NGO’s.

Mheshimiwa Spika, katika hatua za kuboresha uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Serikali. Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Serikali, Sheria Na. 3 ya mwaka 2019 na kuweka masharti yote ya kusajili chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Serikali na hivyo kumpa mamlaka mbalimbali Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Serikali ikiwemo kusimamia Shirika husika, kufanya kazi pale linapopatikana na makosa wakati ikisubiri uamuzi wa Bodi. Aidha, mashirika yametakiwa kuwasilisha kwa Msajili taarifa ya utekelezaji ya robo mwaka, taarifa za ukaguzi wa fedha za mwaka na mikataba ya fedha ambayo mashirika yanaingia na wafadhili na kuweka bayana kwa umma taarifa za mapato na matumizi ili kongeza uwazi na uwajibikaji.

Mheshimiwa Spika, nyenzo hizo ni muhimu katika kumfanya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Serikali kufuatilia utendaji wa mashirika hayo na hivyo kuchukua hatua stahiki. Hivyo kwa sasa Serikali haina mpango wa kuifanya Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Serikali kuwa Taasisi inayojitegemea.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa mtaani ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani ambao wanaishi katika mazingira magumu. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2019 jumla ya watoto 36,548 wakiwemo watoto wa kiume 17,894 na wa kike 18,654 walitambuliwa. Kati ya hao jumla ya watoto 1,178 walipatiwa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na jamii, msaada wa kisheria, kuunganishwa na familia zao na kuwapatia elimu ya ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa kuwaunganisha watoto na familia na kuwatafutia malezi mbadala wale wasio na familia katika Mkoa wa Mwanza. Programu hii imeanza kutekelezwa mwezi Novemba, 2019 na inatarajiwa kufika mikoa yote ambayo ina wimbi kubwa la watoto wanaoishi mitaani.

Mheshimiwa Spika, mwisho nichukue nafasi hii kuikumbusha jamii kuwa jukumu la matunzo, malezi, ulinzi na usalama wa mtoto ni la familia na jamii kwa ujumla. Vilevile Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinapaswa kusimamia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ili kuwawajibisha wazazi wanaotelekeza majukumu yao na badala yake wanawaacha watoto kuzurura mitaani.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka x-ray machine mpya katika Hospitali ya Rufaa ya Mtwara – Ligula?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Hospitali ya Ligula inakabiliwa na uchakavu wa mashine ya x- ray ambayo uharibika mara kwa mara. Katika ziara yangu ambayo niliifanya katika hospitali hii mnamo tarehe 4 Disemba, 2018 nilijionea uchakavu wa mashine na hivyo tulitoa ahadi ya Serikali ya kuipatia hospitali hii mashine mpya ya digital x-ray.

Mheshimiwa Spika, mashine tano mpya za x-ray za kidijitali (digital x-ray) zimeshaingia nchini kupitia utaratibu wa managing equipment services tarehe 14 Januari, 2020. Taratibu za ugomboaji zikikamilika zitapelekwa na kusimikwa katika Hospitali za Rufaa za Njombe, Iringa, Tabora, Temeke pamoja na Mkoa huu wa Mtwara katika Hospitali ya Ligula.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-

Huduma za matibabu ya madaktari bingwa zipo katika kanda zote isipokuwa kanda za Magharibi na Kusini:-

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hizo Mkoani Katavi ili kusaidia wananchi wa Kanda ya Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Katavi kuna uhitaji wa Madaktari bingwa 24 kulingana na ikama na kwa sasa kuna Madaktari Bingwa wawili. Madaktari hao ni Madaktari bingwa wa Watoto na Wanawake. Ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali imepanua wigo wa mafunzo kwa ajili ya Madaktari bingwa. Lengo la Serikali ni kuwa na Madaktari bingwa angalau wawili wawili katika fani za magonjwa ya kina mama, watoto, magonjwa ya dharura, mifupa, usingizi na upasuaji. Wataalamu hawa watakapomaliza mafunzo watapangiwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwa ni pamoja na Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ina kusudio la kujenga Hospitali ya Kanda ya Magharibi Mkoani Tabora ambayo inategemewa kuhudumia wakazi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora pamoja na Kigoma.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga bado ni tatizo nchini:-

Je, Serikali inafanya jitihada gani kupunguza na ikiwezekana kuondosha kabisa vifo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeboresha Vituo vya Afya zaidi ya 352 na vingine kujengwa upya ili vitoe huduma zote za afya ya uzazi kabla na wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua ikiwemo kumtoa mtoto tumboni kwa njia ya operesheni na kuzijengea uwezo wa kutoa huduma ya damu salama kwa watakaohitaji. Aidha, Hospitali 67 za Halmashauri zinajengwa ili huduma ziwafikie wananchi wote wa vijijini na mjini kwa usawa na urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vinakuwepo muda wote, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 270 mwaka 2018/2019. Juhudi hizi zimewezesha wajawazito kuendelea kupata huduma za afya ya uzazi na mtoto ikiwemo kinga tiba dhidi ya Malaria (SP), Fefol ambayo ni madini ya chuma na folic acid ambayo ni kinga tiba dhidi ya upungufu wa damu, vipimo vya shinikizo la damu, kaswende, wingi wa damu, sukari na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, aidha, mwezi Agosti 2019, Wizara ilizindua na kusambaza nchi nzima mwongozo wa kitaifa wa matibabu ya watoto wachanga na uanzishwaji wa vyumba maalum vya matibabu ya watoto wachanga “National Guideline for Neonatal Care and Establishment of Neonatal Care Units” mwongozo huu unalenga kuwajengea uwezo watoa hudumu juu ya huduma muhimu kwa watoto wachanga. Vilevile Wizara kwa kushirikiana na wadau wa UNICEF wameanza kusambaza vifaa mbalimbali kwa ajili ya vyumba hivyo maalum vya watoto wachanga kwa baadhi za hospitali za mikoa na Halmashauri.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-

Ugonjwa wa Mguu Kifundo unatibika katika Hospitali ya Rufaa Kitete – Mkoani Tabora ambapo hupokea zaidi ya Watoto 40 wenye tatizo hilo kila mwezi:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa vya kutosha kama vile POP, bandeji, pamba, kiatu na gongo-pinde ili kusaidia watoto hao?

(b) Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo kwa watoto Mkoani Tabora na familia nyingi hazina uwezo wa kufika Hospitali kupata huduma; je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ili watoto wengi zaidi waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma hizi, vifaa tiba vya huduma za utengemao vimeingizwa katika mfumo wa ununuzi wa Bohari ya Dawa (MSD) kuanzia mwaka 2018/2019 na hivyo kufanya upatikanaji wa POP bandeji, pamba na viatu na gongo- pinde kupatikana kwa uhakika. Aidha, Wizara imeagiza waganga Wafawidhi na Wafamasia katika vituo vya kutolea huduma za afya kupeleka mahitaji yao mapema Bohari ya Dawa ili pasiwepo na upungufu wa aina yoyote wa vifaa tiba ikiwa ni pamoja na vifaa hivyo vinavyotumika katika kutoa huduma za utengamao.

(b) Mheshimiwa Spika, kutokana na ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini, Wizara yangu imeandaa Mpango Mkakati wa muda wa Kati (Medium Term Strategy: 2017-2021) unaolenga kufikisha huduma za utengemao hadi ngazi ya Wilaya ifikapo Juni 2021, ambapo kwa sasa huduma hii hupatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Ujenzi wa Jengo la Utawala na vyumba vya madarasa katika Chuo cha Uuguzi Korogwe bado haujakamilika:-

Je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Jengo la Utawala na vyumba vya madarasa katika Chuo cha Uuguzi - Korogwe bado haujakamilika kutokana na changamoto za fedha za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vya afya hapa nchini. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali haikutenga fedha kwa ajili ya ujenzi katika vyuo vya afya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuona changamoto hii, Serikali inaandaa zoezi la uhakiki wa miradi yote ya maendeleo iliyokuwa inatekelezwa katika vyuo mbalimbali vya hapa nchini ili kupata taarifa za hali ya sasa ya miradi hiyo. Lengo ni kupata taarifa zitakazosaidia katika kuandaa maandiko na mipango itakayotumika kutafuta fedha pamoja na mgawanyo wa fedha kulingana na vipaumbele na mahitaji ya kila chuo. Hivyo basi, mara pesa zitakapopatikana chuo hiki pamoja na vile ambavyo ujenzi umesimama vitapewa kipaumbele cha ukamilishaji.
Kumekuwa na tatizo kubwa katika jamii yetu la ubakaji wa watoto wadogo chini ya miaka mitano na vikongwe:-

Je, Serikali imeshawahi kufanya utafiti ili kujua chanzo cha tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili hasa ubakaji kwa watoto na vikongwe. Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi za mwaka 2018 za makosa ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, hali ya vitendo vya ukatili kwa watoto nchini imeongezeka kutoka matukio 13,457 mwaka 2017 hadi matukio 14,419 mwaka 2018 ambalo ni ongezeko la makosa 1,034 sawa na asilimia 7.7. Mikoa inayoongoza kwa matukio haya ni pamoja na Tanga ikiwa na matukio 1,039, Mbeya 1,001, Mwanza 809, Arusha 792 na Tabora 618. Makosa yanayoongoza ni ubakaji (5,557), mimba za utotoni (2,692), ulawiti (1,159), shambulio (965) na kujeruhi (705).

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2009 Serikali kwa kushirikiana na UNICEF ilifanya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto. Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 60 ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hufanyika majumbani ambapo vitendo hivi hufanywa na watu wa karibu na watoto wakiwemo baadhi ya wazazi, walezi, watoa huduma wa vyombo vya usafiri, majirani na wanafamilia na asilimia 40 ya vitendo hivyo vya ukatili hufanyika shuleni. Aidha, sababu kubwa ya vyanzo vikubwa vya ukatili ni pamoja na imani potofu, elimu au hali duni ya umasikini, kutetereka kwa misingi ya malezi ndani ya familia, mila na desturi potofu na utandawazi. Aidha, hakuna utafiti uliofanyika kuhusu ubakaji wa vikongwe ingawaje vyanzo vya ukatili vinashabihiana na ule wa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua jukumu lao la malezi na matunzo kwa watoto na wazee ambao ni hazina na tunu muhimu katika Taifa letu. Mwisho, napenda kutoa rai kwa jamii kutoa taarifa na ushirikiano kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wahusika hao.
MHE. SUSAN A. LYIMO aliuliza:-

Serikali ina utaratibu wa kutoza gharama miili ya marehemu iliyohifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti (Mochwari) Hospitalini na hivyo kusababisha vikwazo na simanzi kwa wanafamilia wasiokuwa na uwezo wa kulipa gharama hizo:-

Je, ni lini Serikali itaacha kutoza gharama miili ya marehemu wanaofia hospitali na kuhifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhiwa maiti (Mochwari) ili kupunguza simanzi kwa wafiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili miili ya marehemu wanaofia hospitali au nje ya hospitali iweze kuhifadhiwa na kustiriwa kwa heshima inahitaji kutunzwa kwenya majokofu yenye ubaridi mkali na wakati mwingine kuwekewa dawa za kusaidia isiharibike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2017, wananchi wanapaswa kuchangia gharama za afya ikiwa ni pamoja na matibabu na hata huduma za uhifadhi wa maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, panapotokea changamoto ya mwananchi kushindwa gharama za uhifadhi wa maiti mwananchi huyo anapaswa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali husika ili kupata maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hiyo. Ili kuondokana na changamoto kama hizi wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima ya Afya kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu toka mfukoni.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-

Wananchi wengi wamekuwa wakiathirika kisaikolojia:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya ushauri nasaha.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bubu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiathirika kisaikolojia kutokana na matukio na changamoto mbalimbali za maisha ikiwemo magonjwa, umaskini wa kipato, kufiwa, ukosefu wa ajira, kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, ukatili na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia huduma watu walioathirika kisaikolojia imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha uwepo wa wataalam wa kutosha wa kutoa huduma ya ushauri wa Kisaikolojia. Kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Serikali imeajiri Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zote 185, kwa baadhi ya Halmashauri nyingine Maafisa hao wako hadi katika ngazi ya Kata. Lengo la Serikali ni kuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii hadi ngazi ya Kata katika Halmashauri zote ili wananchi waweze kufikiwa na kupata huduma kwa urahisi na kwa haraka ili kuwaondolea athari zitokanazo na matatizo ya kisaikolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wenye matatizo ya kisaikolojia wanaata huduma zenye kiwango cha ubora, Serikali imeandaa mwongozo wa utoaji msaada wa kisaikolojia wa kijamii kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana wa mwaka 2014 (The National Guideline for Psychosocial Care and Support Services for MVC and Youth 2014), na mwongozo wa Utoaji wa Msaada wa Kisaikolojia na Jamii (The National Guideline for Provision of Psychosocial Care and support Services of 2019) pamoja na taratibu za uendeshaji (Standard Operating Procedure (SOP). Pia Maafisa Ustawi wa Jamii na Wataalam wengine wameendelea kujengewa uwezo katika eneo hili la utoaji wa Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii ili waweze kutoa huduma bora na kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kusisitiza wananchi watumie wataalam wetu wa Ustawi wa Jamii waliopo katika Ofisi ya Halmashauri ili waweze kupata huduma za ushauri wa kisaikolojia. Aidha, Serikali itaendelea kuajiri wataalam kadri inavyowezekana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii muhimu.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Eneo la Chamazi Mbagala katika Kitengo cha Afya ya Akili limetelekezwa na hakuna ukarabati wa majengo yaliyopo wala uendelezwaji wa eneo hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo na Chamazi lina ukubwa wa ekari 165 na linaendelea kutumika kwa shughuli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ngo‟mbe, kuku wa mayai na nyama. Shamba hili pia linatumika kwa kilimo ambapo zaidi ni mazao ya mboga za majani, mahindi na nazi yanazalishwa. Pia kazi mbalimbali za mikono zinafanywa katika eneo hili zikiwemo kazi za ususi wa vikapu, mifuko, mikufu, bangili na mapambo mbalimbali kwa kutumia malighafi za asili. Kazi nyingine ni pamoja na ufumaji wa vitambaa, kofia na utengenezaji wa nguo za batiki.

Mheshimiwa Spika, shughuli hizi ni sehemu ya tiba kwa wagonjwa wa akili waliopata nafuu ili waweze kurudi katika hali ya kawaida na kushiriki katika shughuli za kiuchumi wanaporudi katika jamii. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeajiri Watalaamu wa Mifugo na Kilimo ili kuweza kusimimia shughuli za ufugaji na kilimo. Aidha Hospitali imekuwa ikisafisha shamba hilo kila mwaka kwa kuondoa vichaka na kukata majani.

Mheshimiwa Spika, mipango inaendelea katika mwaka wa Fedha 2019/2020. Hospitali ya Taifa Muhimbili imepanga kuanza ujenzi wa uzio kwa kuanzia eneo linapaka na maeneo yanamilikiwa na wananchi wanaoishi karibu na shamba hili. Sanjari na hilo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Kituo cha Afya cha Uwekezaji inaendelea kufanya mazungumzo na wabia kwa ajili ya kutumia sehemu ya shamba hili kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa tiba na dawa. Hospitali imeshafanya mazungumzo na wadau kutoka China, Hong kong, Uturuki, Tunisia na Jamhuri ya Czech.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-

Ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado unaendelea kwa kiwango kikubwa hapa nchini:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahudumia kwa unasihi na unasaha wahanga wa ukatili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq (Viti Maalum) kutoka Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini. Kwa kuliona hilo, Serikali iliandaa mpango kazi wa kitaifa wa miaka mitano wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao unatekelezwa kwa kipindi cha 2017/2018 na utaisha mwaka 2021/2022. Mpango mkakati huu unaainisha mikakati mbali mbali ya kupambana na kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha vituo 11 vya mkono kwa mkono (One Stop Centres) ambapo huduma za ushauri nasaha, huduma za kipolisi na huduma za matibabu zinapatikana katika eneo moja kwenye mikoa ya Dare es Salaam, Pwani, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Arusha, na Simiyu kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Katika vituo hivi huduma za kipolisi, ushauri nasaha na huduma za afya zinatolewa kwenye kituo kimoja. Lengo la Serikali ni kuwa na kituo angalau kimoja kwa kila Mkoa na hii inaenda pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu katika eneo la utoaji huduma husika.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko kubwa la Watoto wa Mitaani Jijini Dar es Salaam hali ambayo inakosesha Watoto hao haki zao za msingi kama elimu na malezi bora?

Je, Serikali imechukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kufiwa na wazazi, migogoro ya familia, kutengana kwa wazazi, vitendo vya unyanyasaji na ukatili na umasikini katika ngazi ya kaya, vimesababisha ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya utafiti ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani iliyofanywa mwezi Mei mwaka 2018, inayohusisha mikoa sita nchini ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha na Iringa, jumla ya watoto wapatao 6,393 wakiwemo wa kiume 4,865 na wa kike 1,528 wanaoishi na kufanya kazi mitaani, walitambuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2018 hadi mwezi Machi, 2019 jumla ya watoto 2,702 walipatiwa huduma mbalimbali katika mikoa ifuatayo: Arusha, watoto 330; Dar es Salaam 475, Dodoma 337, Iringa 313, Mwanza 770 na Mbeya 447. Huduma zilizotolewa ni pamoja na huduma za, chakula, afya, malazi, kurudishwa shuleni, stadi za ufundi, stadi za maisha, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto wakiwemo walio katika mazingira hatarishi. Pia itaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kwenye eneo la stadi za malezi na ulinzi wa watoto. Aidha, Serikali itaendelea kufanya tafiti ili kubaini kiini cha tatizo na kupanga mipango mahsusi ya kupambana na kutokomeza tatizo la watoto wa mitaani nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba jukumu la matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto linatekelezwa ipasavyo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI) aliuliza:-

Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi ni muhimu kwa mustakabali wa afya ya wananchi.

Je, Serikali ina mpango gani wa ugawaji wa fedha za mkupuo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa kipaumbele katika ujenzi wa Hospitali za Rufaa za mikoa mipya mitano ya Njombe, Katavi, Songwe, Simiyu na Geita ambayo haina Hospitali za Rufaa za Mikoa. Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi umeanza katika eneo jipya lenye ukubwa wa ekari 243.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi. Serikali itaendelea na ujenzi wa hospitali hii kwa awamu kwa kutegemea na hali ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-

Baadhi ya watoto wakubwa wenye uwezo wameamua kuwatelekeza wazazi wao pasipo kuwapa matunzo wanayostahili:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawajibisha watoto waliotelekeza wazazi wao na kuhakikisha wanatoa matunzo stahili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ipasavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wazee katika ustawi wa Taifa letu. Sote tunatambua kuwa wazazi walitumia rasilimali walizokuwanazo kuhakikisha watoto wanapata huduma za matunzo na malezi ili kuwawezesha kukua na kufikia ndoto zao.

Mheshimiwa Spika, kufuatia mifumo ya hifadhi ya jamii ya asili, jukumu la kuwatunza na kuwalea wazazi au wazee ni la wanafamilia, hususan watoto. Kutokana kudhoofika kwa mifumo hiyo ya asili, mmomonyoko wa maadili na utandawazi, jukumu hilo limekuwa na changamoto nyingi na kusababisha wazazi kutelekezwa.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuhakikisha maslahi ya wazee yanalindwa na wanapata haki zao ikiwemo matunzo, Serikali iliandaa Sera ya Wazee ya mwaka 2003 ambayo inaelekeza jamii kuwajibika kutoa matunzo kwa wazee.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna sheria ya kuwawajibisha watoto wanaotelekeza wazazi wao. Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua jukumu lao la malezi na matunzo kwa wazazi ambao ni hazina na tunu muhimu ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kutoa rai kwa watoto na jamii kwa ujumla kuhakikisha wazazi na wazee wanapatiwa malezi na matunzo yanayostahili.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Wakunga wa Jadi ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto hasa maeneo ya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania iliridhia Mkataba wa Uzazi Salama mwaka 1994 katika mkutano uliofanyika nchini Misri. Mkataba huo unaelekeza kwamba kila mama anayejifungua atahudumiwa na mtaalamu mwenye ujuzi kwa kutilia maanani kwamba matatizo yatokanayo na uzazi hayatabiriki na yakitokea uhitaji kutatuliwa na wataalamu wenye ujuzi katika kuokoa maisha ya mama na mtoto mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inawatambua wakunga wa jadi kama watu muhimu katika jamii. Hivyo, Wizara kwa kutambua umaarufu wao katika jamii, inawatumia kufanya uhamasishaji wa wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya na ikibidi kuwasindikiza.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-

Sheria ya NHIF inamtambua Mtumishi wa Umma ambaye amechangia kwa miaka 10 pale anapostaafu kuwa atahudumiwa na Mfuko yeye na mwenza wake hadi mwisho wa maisha yao:-

Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu kama huo kwa Viongozi wa Umma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu ni moja ya makundi ya wanachama ambayo yametajwa katika Sheria ya Mfuko. Kundi hili linapata huduma bila ya kuendelea kuchangia hadi mwisho wa maisha kwa sababu fedha za kugharamia kundi hili zinatokana na mapato yatokanayo na uwekezaji wa michango ya wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa utaratibu wa fao la wastaafu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unalenga mwanachama ambaye ni Mtumishi wa Umma, amechangia katika Mfuko huu kwa kipindi kisichopungua miaka kumi katika utumishi wake. Hata hivyo, idadi ya wastaafu imeendelea kuongezeka na gharama za madai kuzidi kuwa kubwa kwa kuwa magonjwa ya kundi hili ni yale yenye gharama kubwa. Mfuko umefanya tathmini ya kugharamia kundi hili na kupendekeza kubadili kigezo cha muda wa kuchangia kabla ya kustaafu kutoka miaka 10 hadi miaka 15 ambapo mabadiliko yameanza kutumika kuanzia tarehe 1 Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa matibabu kwa Viongozi wa Umma waliostaafu unatekelezwa kwa kufuata miongozo ya utumishi wa umma iliyopo. Kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge huduma za matibabu kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji Bunge (The National Assembly (Administration) Act) ya mwaka 2008 ambapo kupitia Kanuni zake, Mheshimiwa Mbunge hupata huduma za matibabu kwa kipindi chake cha Ubunge. Aidha, Mfuko umekamilisha utaratibu unaowapa fursa wananchi mbalimbali kujiunga na Bima ya Afya kupitia mpango wa Vifurushi unaomwezesha mwananchi kujiunga kulingana na aina ya huduma na uwezo wa kuchangia.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana imeshatenga eneo kwa ajili ya kujenga chumba cha utakasaji. Hospitali ipo kwenye mchakato wa ununuzi wa mashine kubwa ya kufulia kupitia mkopo kutoka NHIF wenye thamani ya shilingi 80,000,000. Kwa sasa hospitali imenunua mashine ndogo mbili kwa ajili ya kufulia nguo zinazotumika katika chumba cha upasuaji zenye thamani ya shilingi 300,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke imeagiza mashine ya kufulia automatic washing machine yenye uwezo wa kufua kilo 70 kwa awamu moja na pasi yake kwa jumla ya shilingi milioni 83,348,950. Na Hospitali ya Mwananyamala imeagiza mashine mbili za kufua kupitia MSD zenye thamani ya shilingi 71,000,000 na tayari mashine moja imewasilishwa katika Hospitali ya Mwananyamala na ipo katika utaratibu wa usimikwaji. Aidha, kwa sasa huduma za ufuaji katika Hospitali ya Temeke na Mwananyamala zinafanywa kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mkataba wa ufuaji mpaka pale watakapokamilisha taratibu zote.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mtoto mwenye ugonjwa wa sickle cell hutakiwa kupata matibabu mfululizo ambapo kwa familia zisizo na uwezo hushindwa kulipia gharama za matibabu na hivyo kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wagonjwa wa sickle cell kupata matibabu bure?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa watoto wenye ugonjwa seli mundu au kwa jina la kitaalam sickle cell, wanahitaji matibabu mfululizo kwani huwa wanapata upungufu wa damu na maumivu ya mara kwa mara. Familia, jamii na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitahidi sana kuwahudumia watoto hao kwa kuwapatia mahitaji maalum. Hata hivyo, misaada hiyo haikidhi mahitaji ya wagonjwa wote na kuna baadhi ya familia hazina uwezo wa kuwahudumia watoto wenye seli mundu.

Mheshimiwa Spika, kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeandaa mwongozo wa kutoa msamaha kwa makundi tofauti yasiyo na uwezo likiwepo kundi la watu wenye magonjwa sugu kama sickle cell. Kwa kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, familia zisizo na uwezo huhakikiwa na kupatiwa kibali cha huduma bila malipo. Aidha, Serikali inaanzisha Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza (National Non-Communicable Diseases Control Programme) ambayo ugonjwa wa sickle cell utakuwa ni moja ya magonjwa yatakayokuwa yakiratibiwa kitaifa.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kipimo cha MRI katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwongozo uliokuwepo huduma za CT-Scan na MRI hazikuwepo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya kiuchumi na uhitaji wa huduma hizi kwa wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilifanya mabadiliko ya mwongozo kwa kutengeneza mwongozo mpya wa vifaa vya Radiolojia nchini wa mwaka 2018 (Standard Medical Radiology and Imaging Equipment Guidelines) ambapo pamoja na mambo mengineyo huduma za CT-Scan na MRI zitapatikana katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na huduma za MRI zitapatikana katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko hayo Serikali inakusudia kufunga CT-Scans katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwa ni Mwananyamala, Temeke na Amana.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Ligula inakabiliwa na upungufu wa Madaktari Bingwa:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Ligula inapata Madaktari Bingwa wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Hawa Abdulrahamani Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula) inahitaji kuwa na Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili kuwezesha kutoa huduma za kibingwa. Aidha, Wizara inatambua kuwa, Hospitali hii kwa sasa ina Madaktari Bingwa mmoja tu wa fani ya Udaktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wakawake (OBGY).

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uamuzi wa Serikali kuzihamishia Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara imefanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya mahitaji ya Madaktari Bingwa na fani zao katika Hospitali zote za Mikoa, Kanda, Maalum na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tathmini hii, itawezesha utekelezaji wa uamuzi wa kuwapanga upya Madaktari Bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kila Hospitali ya Mkoa, kanda maalum na Taifa. Lengo ni kuwa, kila Hospitali ya Mkowa iwe na Madaktari Bingwa wa fani nane za kipaumbele ambazo ni Daktari Bingwa wa Uzazi na Wanawake, Daktari Bingwa wa Watoto, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa, Daktari Bingwa wa Huduma za Dharura na Magonjwa ya Ajali, Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi na Daktari Bingwa wa Huduma za Radiolojia katika Hospitali za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Ligula.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara imewapeleka Madaktari Bingwa wa fani za Upasuaji wa kawaida na Upasuaji wa Mifupa 125 katika Chuo cha MUHAS ambao wanatarajia kumaliza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021. Madaktari hawa watapangwa katika Hospitali ya Rufaa za Mikoa ikiwemo Ligula. Wizara itaendelea kutenga bajeti ya kuwasomesha Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha Hospitali zote za Rufaa zinakuwa na Madaktari Bingwa wa kutosha. Kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019 Serikali inagharimia masomo ya madaktari bingwa 127 katika Chuo cha MUHAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kipindi hiki cha mpito, Serikali imekuwa ikiendesha kambi za udaktari bingwa ikiwa ni pamoja na upasuaji kwa lengo la kufikisha huduma za madaktari bingwa kwenye mikoa isiyokuwa na huduma hizo.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mkoa wa Katavi hauna kifaa cha kumsaidia kupumua mtoto aliye dhaifu (ambubag):-

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi kifaa hicho?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ambu bag na maski ni vifaa vinavyompatia hewa mtoto mchanga aliyezaliwa na tatizo la kushindwa kupumua na ni moja ya afua inayolenga kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini. Serikali imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha siyo tu kuna watoa huduma wenye ujuzi, lakini pia dawa na vifaa tiba muhimu vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya hapa nchini. Kwa kipindi cha mwaka 2018, Serikali ilipokea na kusambaza vifaa mbalimbali vya kumsaidia mtoto mchanga mwenye matatizo ya kupumua ikiwemo ambu bag na maski 3,735. Vifaa hivyo vilipekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya 3,500 katika Halmashauri 109 za mikoa 16 ya Tanzania Bara. Usambazaji huo ulienda sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma namna ya kutumia vifaa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inategemea kupokea ambu bag na maski nyingine 2,500 ambazo zitasambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwenye mikoa ambayo haikupata mgao hapo awali. Utaratibu wa ugawaji wa vifaa hivyo umeandaliwa kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ambapo Katavi imeorodheshwa katika mgao huo. Nizitake mamlaka husika kuagiza vifaa hivyo kutoka Bohari ya Dawa. Aidha, Bohari ya Dawa itaendelea kuvinunua vifaa hivyo ili vipatikane sambamba na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ikiwemo afya ya watoto wachanga.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-

Wazee ni hazina ya Taifa lakini wapo wazee wasiojiweza ambao Serikali imewapa hifadhi katika kambi mbalimbali ikiwemo Kambi ya Fungafunga ya Mjini Morogoro. Hata hivyo, kambi hiyo ni chakavu kwa muda mrefu hali inayosababisha wazee kuendelea kuishi katika mazingira magumu:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati kambi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa waliotoa wazee katika ujenzi wa Taifa hili. Aidha, wazee ni rasilimali muhimu katika ustawi na maendeleo ya nchi. Kwa kutambua hili, Serikali inatoa matunzo kwa wazee wasiojiweza katika kambi 17 nchini ikiwemo makazi ya Fungafunga Mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma katika makazi haya, Serikali imefanya tathmini ya hali ya utoaji wa huduma na miundombinu. Taarifa ya tathmini imebainishwa na kuainisha hali ya majengo na miundombinu katika makazi haya ikiwemo makazi ya Fungafunga na imeweka mkakati wa kuboresha hali ya majengo na miundombinu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inajali haki na ustawi wa wazee kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 na itafanya ukarabati wa kambi hizi kwa awamu kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-

Kuna kundi kubwa la watoto wenye mazingira magumu ambao wanazurura tu na hivyo kukosa haki zao za msingi ikiwemo elimu na malezi bora:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuokoa kizazi hicho ambacho kinapotea?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufiwa na wazazi, migogoro ya familia na kutengana kwa wazazi, vitendo vya unyanyasaji na ukatili na umaskini katika ngazi ya kaya vimesababisha ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Utafiti wa Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mitaani uliyofanywa na Wizara mwezi Mei, 2018 uliohusisha Mikoa sita nchini ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa, jumla ya watoto wapatao 6,393 wakiwemo wa kiume 4,865 na wa kike 1,528 wanaoishi na kufanya kazi mitaani walitambuliwa.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2018 hadi mwezi Machi, 2019, jumla ya watoto 2,702 walipatiwa huduma mbalimbali katika Mikoa ya Arusha (330), Dar es Salaam (475), Dodoma (337), Iringa (313), Mwanza (770) na Mbeya (447). Huduma zilizotolewa ni pamoja na huduma za afya, chakula, malazi, kurudishwa shuleni, stadi za ufundi, stadi za maisha, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na jamii.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto wakiwemo walio katika mazingira hatarishi, pia itaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kwenye eneo la stadi za malezi na ulinzi wa mtoto. Aidha, Serikali itaendelea kufanya tafiti ili kubaini kiini cha tatizo na kupanga mipango mahsusi ya kupambana na kutokomeza tatizo la watoto wa mitaani nchini.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha jukumu la matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto linatekelezwa ipasavyo. Vilevile nizitake Mamlaka za Serikali za Mitaa ziandae mipango na mikakati madhubuti ikiwemo kutenga rasilimali za kutosha katika kukabiliana na tatizo hili la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-

Watu wenye ulemavu wamekuwa wakipata adha kubwa katika kupata matibabu ikiwemo kukosa fedha kwa ajili ya matibabu:-

Je, ni lini Serikali itahakikisha inawapatia bima ya afya watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imefanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 na kuandaa mapendekezo ya Sera mpya ya Afya. Katika mapitio ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007, changamoto mbalimbali za matibabu kwa makundi ya msamaha ziliibuliwa na watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma hizo. Moja ya changamoto iliyojitokeza ni hospitali zetu kuwa na wagonjwa wengi wa misamaha na hivyo kushindwa kuboresha huduma za afya. Kutokana na changamoto hiyo ya kuwa na makundi mengi ya msamaha, Wizara iliona ni vyema ikaboresha utaratibu wa misamaha kwa kuhakikisha kuwa wananchi wasio na uwezo tu ndio wanaopatiwa msamaha.

Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo ya Sera mpya ya Afya kila mwananchi mwenye uwezo atapaswa kugharamia huduma za afya. Sera pendekezwa inaainisha njia mahsusi zitakazowezesha Serikali kubaini wananchi wote wenye uwezo ili waweze kuchangia gharama kabla ya kupokea huduma, kwani ni wazi kuwa si kila mlemavu ana kipato duni. Hivyo, wananchi watakaothibitika katika maeneo yao kuwa hawana uwezo wa kuchangia ikiwemo walemavu, wataendelea kupatiwa matibabu bila kuchangia gharama za matibabu.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inatambua changamoto za uchangiaji wa huduma za afya na inaandaa utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kundi la walemavu.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Iringa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya madaktari bingwa na hivyo kusababisha madaktari hao kuishi mbali na hospitali:-

Je, ni nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ina madaktari 26 kati ya hao, madaktari wanne ni madaktari bingwa. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, hospitali ilitenga kiasi cha Sh.40,000,000 kwa ajili ya kuwapa motisha madaktari wa kulipia gharama za nyumba kila mwezi kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani na fedha kutoka Serikali Kuu kwa maana ya OC. Hadi kufikia mwezi Mei, 2019 kiasi cha Sh.25,500,000 kimelipwa kwa ajili ya malipo ya kodi ya nyumba zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya motisha ya watumishi.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-

Ndoa za utotoni ni tatizo kubwa katika jamii zetu hususan katika jamii zenye umaskini:-

Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa umma hasa katika maeneo ya vijijini ili wananchi wafahamu athari za kuozesha watoto katika umri mdogo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa umma katika kupambana na ndoa za utotoni ambazo zina madhara makubwa kwa watoto wa kike ambapo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo TV, redio, magazeti na jarida imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kuandaa ujumbe kuhusu madhara ya mimba za utotoni sambamba na kusisitiza wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kutoozesha watoto mapema. Aidha, mwaka 2017, Tarime Mkoani Mara, Serikali ilizindua kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ijulikanayo kama “Mimi Msichana Najitambua: Elimu Ndiyo Mpango Mzima”.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hiyo ililenga kutoa elimu kwa watoto kuhusiana na mimba za utotoni na umuhimu wa kuelekeza muda wao mwingi katika elimu, kujitambua na kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki zao. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2018, jumla ya wananchi 13,234 walifikiwa na kampeni. Kati ya hao, wanafunzi 8,546, walimu 476, viongozi wa dini 110, wazee wa mila na wazee mashuhuri 90, ngariba 38, waendesha bodaboda 261, wazazi/walezi 3,600 na watendaji wa kijiji 113. Kampeni hii imefanyika katika Mikoa ya Shinyanga, Mara, Tabora, Lindi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam na Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto. Sambamba na mpango huo, mwaka 2018, uliandaliwa Mdahalo wa Kitaifa ambao ulikuwa na lengo la kujadili vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo ndoa za utotoni. Mikoa yenye kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto ilijumuishwa katika utaratibu wa kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa kampeni ambayo umeainisha jumbe za kipaumbele zitakazotumika na mikoa katika kuelimisha jamii katika mikoa husika kwa kuzingatia mazingira yao. Mikoa sita ilijumuishwa ikiwa ni pamoja na Shinyanga, Dodoma, Tabora, Mara, Katavi na Singida.