Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (28 total)

MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y. MHE. ALI HAFIDH TAHIR) aliuliza:-
Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa hususan Mawaziri Wakuu Wastaafu ambao wameaminiwa na kuchaguliwa na wanachama wa chama fulani lakini baada ya kupata madaraka wakahama vyama hivyo na kwenda kunufaisha vyama vingine:-
Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati sasa wa kuifanyia marekebisho sheria husika ili kufuta stahiki za Mawaziri Wakuu Wastaafu wanaohama vyama vyao kwa kuwa stahiki hizo zilitokana na nguvu za chama alichohama, na kwamba kuendelea kumpa stahiki hizo ni sawa na kuwakejeli na kuwadharau wananchi waliomchagua?
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali. Tahir, Mbuge wa Dimani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mawaziri Wakuu Wastaafu wanahudumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafao kwa hitimisho la kazi kwa viongozi, Sheria Na. 3 ya mwaka 1999. Sheria haielezi hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu atakayeamua kuhamia chama kingine cha Siasa tofauti na chama kilichomweka madarakani na kumwezesha kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.
Mheshimwa Spika, mbali na sheria hiyo kutoweka zuio lolote kwa Viongozi wa Kifaifa Wastaafu kujiunga na chama kingine cha siasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inalinda haki za msingi za binadamu ikiwemo haki ya uhuru wa mtu kujihusisha na masuala ya Siasa. (Makofi)
Kwa mujibu wa Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatamka kwamba mtu yeyote anayo haki ya kujihusisha na mambo ya kisiasa na kuweza kujiunga na chama chochote. Mawaziri Wakuu Wastaafu kama walivyo watu wengine, wanao uhuru wa kujiunga na chama chochote cha kisiasa wanachopenda ili mradi hawavunji sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haki ya kujiunga na chama chochote au kujihusisha na masuala ya kisiasa ni haki ya Kikatiba, na kwa kuwa haki hizi haziwezi kuzuiwa au kuingiliwa, ni wazi kwamba suala la kufanyia marekebisho Sheria ya Mafao kwa Viongozi wa Kitaifa Wastaafu, Sheria Na. 3 ya mwaka 1999 kwa lengo la kuwazuia Mawaziri Wakuu Wastaafu au Viongozi wengine wa Kitaifa Wastaafu kujiunga na chama chochote cha kisiasa itakuwa ni kwenda kinyume na Katiba ya nchi. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi ya walimu kulipwa mishahara midogo ambayo hailingani na gharama halisi za maisha:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha maslahi ya walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mshahara wa Watumishi wa Umma wakiwemo walimu hailingani na gharama halisi za maisha. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa nyongeza ya mishahara kila mwaka kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu. Aidha, wakati wa kutoa nyongeza hiyo ya mishahara walimu hupewa nyongeza kubwa kuliko watumishi wengine wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2015/2016, mshahara wa walimu wenye cheti au astashahada uliongezeka kutoka shilingi 163,490/= hadi kufikia shilingi 419,000/= kwa mwezi ambayo ni sawa na asilimia 156.28.
Kwa upande wa mwalimu mwenye stashahada, mshahara uliongezeka kutoka shilingi 203,690/= hadi shilingi 530,000/= ambayo ni sawa na asilimia 160.20.
Kwa upande wa mwalimu mwenye shahada mshahara uliongezeka kutoka shilingi 323,900/= hadi kufikia shilingi 716,000/= sawa na asilimia 121.05.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inafanya tathmini ya kazi au job evaluation katika utumishi wa umma ili kubaini uzito wa kazi kwa watumishi wa umma wakiwemo walimu ili kupanga upya mishahara kwa kulingana na uzito wa kazi. Kazi hii imeanza mwezi Oktoba, 2015 na inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 15 ijayo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Mwaka 2002 Serikali ilipitisha Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na Marekebisho yake ya mwaka 2008 yaliweka Mfumo wa Wazi wa Upimaji na Ujazaji wa Mkataba wa Utendaji Kazi (OPRAS):-
(a) Je, ni kwa kiasi gani mfumo huu umetekelezwa nchini?
(b) Ni lini mfumo wa kupima taasisi (institutional performance) utaanzishwa na kuanza kutangazwa hadharani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kupima utendaji kazi kwa uwazi ulianzishwa mwezi Julai, 2004 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kutekeleza Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 kama ilivyohuishwa mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma ilifanya Tathmini ya Uzingatiaji na Utekelezaji wa Mfumo wa OPRAS katika taasisi za umma. Tathmini hiyo ilihusisha taasisi za umma 110 katika kipindi cha awamu tatu. Katika tathmini hiyo, lengo lilikuwa ni kufuatilia taasisi zilizokuwa na utekelezaji wa kiwango cha juu. Napenda tu kuliarifu Bunge lako kwamba matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kwamba utekelezaji uko katika asilimia 51.
Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha kwamba mfumo huu unatekelezwa na watumishi wote, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora iliagiza waajiri kuhakikisha kwamba mtumishi atapandishwa cheo tu kwa kuzingatia matokeo ya OPRAS. Hatua hii imesaidia sana kuongeza kiwango cha utekelezaji kwani sasa kila mtumishi anatekeleza mfumo huu kama sharti la kupandishwa cheo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu lini Serikali itaanzisha na kutangaza mfumo wa kupima taasisi (institutional performance) hadharani, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa Mikataba ya Utendaji kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017. Mikataba hii itatekelezwa na taasisi zote za umma ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za umma. Mfumo huu utaiwezesha Serikali kupima utendaji kazi kwa kila taasisi ya umma kwa kila mwaka.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Ingawa kuna tatizo la ajira Serikalini, lakini inasemekana kuwa ziko nafasi nyingi zilizo wazi katika ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya hata Vijiji:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali inalificha jambo hili na ni lini sasa itajaza nafasi za ajira zilizo wazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika sekta za Utawala kama vile VEO, WEO ambapo wananchi huwalipa watumishi wa kukaimu kwa fedha zao wenyewe kinyume na taratibu?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isipandishe mishahara ya kima cha chini kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya nafasi za ajira mpya Serikalini hufanyika kwa uwazi kupitia bajeti ya Serikali ambayo huidhinishwa na Bunge hili. Ajira hizi hufanyika baada ya waajiri kuwasilisha maombi yao Serikalini na kuidhinishwa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilitengewa nafasi za kuajiri Watendaji wa Vijiji (VEO) kumi na Watendaji wa Kata (WEO) Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nafasi hizo Serikali itaendelea kujaza nafasi wazi kila mwaka kulingana na uwezo wa kibajeti na vipaumbele vilivyowekwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipandisha kima cha chini cha mshahara kulingana na uwezo wa bajeti au mapato ya ndani na kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za maisha. Kutokana na hatua hii, Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo kwa sasa hulipa kima cha chini cha mshahara sawa na asilimia 80 ya kiwango cha gharama za chini za maisha (minimum living wage).
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wake wa umma kulingana na uwezo wake wa kiuchumi.
MHE. DOTO M. BITEKO aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali inachukua muda mrefu sana kurekebisha mishahara ya Walimu baada ya kupandishwa vyeo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko, Mbunge wa Bukombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba miaka ya nyuma kulikuwepo na ucheleweshaji wa kurekebisha mishahara kwa kuwa mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara wa wakati huo ulimtaka kila Mwajiri kuwasilisha marekebisho ya Watumishi wake Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2012 Mfumo huu wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara uliimarishwa kutoka Toleo la 7 kwenda Toleo la 9 la Lawson ambapo mwajiri alisogezewa huduma ya kufanya marekebisho mbalimbali ya kiutumishi yanayotokea katika ofisi yake bila ya kulazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam. Utaratibu huu umekuwa na manufaa ambapo kwa sasa mabadiliko mbalimbali ya kiutumishi yanafanywa na mwajiri kwa kuzingatia mzunguko wa malipo ya mishahara kwa kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utaratibu huu mzuri, mazingira machache yanayoweza kuchelewesha marekebisho ya mishahara kufanyika kwa wakati, kutokana na kuingizwa kwa taarifa za watumishi kwenye mfumo baada ya orodha ya malipo ya mishahara katika mwezi husika kufungwa, au waajiri kufanya mabadiliko bila ya kuweka taarifa muhimu hususan viambatisho kama vile barua za kupandishwa cheo na taarifa kutumwa, zikiwa na makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupitia Bunge lako Tukufu, kuwataka waajiri wote kufanya marekebisho ya mishahara kwa watumishi wote kwa wakati kama ambavyo imekuwa ikielekezwa na Serikali ili kuepusha ucheleweshaji wa haki za watumishi.
MHE. PAULINE P. GEKUL (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Kuwepo na matukio ya vifo visivyokuwa vya lazima kunatokana na kutokuwepo kwa motisha kwa madaktari na wauguzi kwa kulipwa viwango duni vya mishahara na kutolipwa posho zao kwa wakati.
Je, Serikali inakabiliana vipi na changamoto ya maslahi kwa watumishi wa sekta hii muhimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na madaktari, matabibu pamoja na wauguzi nchini ambapo Serikali imeendelea na jitihada zake za kuboresha mishahara ya watumishi wake mwaka hadi mwaka ikiwemo ya wataalam wa sekta ya afya kwa kuzingatia uwezo wa Serikali wa kulipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi na punde tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi wote wa umma wakiwemo wa sekta ya afya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni shilingi 390,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kutokana na ukweli huu kati ya mwaka 2010/2011 hadi mwaka 2016/2017 vianzia mishahara kwa kada za wauguzi vimeongezwa kutoka shilingi 614,000 hadi kufikia shilingi 980,000 kwa mwezi kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada. Aidha, shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 zimekuwa zikilipwa kama kianzio cha mshahara kwa wahitimu wa astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vianzia mishahara kwa kada za madaktari na maafisa tabibu katika kipindi hicho vimeongezwa kutoka shilingi 886,800 hadi shilingi 1,480,000 kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na mwisho shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2016/2017, vianzia mshahara hivi ni vikubwa zaidi ikilinganishwa na vile vya watumishi wa Serikali Kuu na walimu kwa kuzingatia ngazi ya elimu zao kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali Kuu kwa watumishi wenye astashahada wameanzia na shilingi 309,000; kwa walimu wameanzia na shilingi 419,000, kwa wauguzi wameanzia na shilingi 432,000; na kwa matabibu na madaktari wameanzia na shilingi 432,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa stashahada, Serikali Kuu kianzia mshahara kimeanza na shilingi 525,000, kwa upande wa walimu wenye stashahada ni shilingi 530,000, wauguzi shilingi 680,000/= na tabibu na madaktari shilingi 680,000. Kwa upande wa shahada, Serikali Kuu wameanzia na shilingi 710,000, walimu shilingi 716,000, wauguzi shilingi 980,000 na kwa upande wa matabibu na madaktari wenye shahada shilingi 1,480,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wataalam wa afya na watumishi wote kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia viapo na maadili ya kazi zao. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kadri uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Kumekuwa na mlundikano wa madeni ya watumishi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyalipa madeni hayo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa hakuna madeni tena?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mishahara na kuyalipa kwa kadri ya uwezo wake wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya mshahara ya shilingi 56,293,372,627.37 ambayo yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yaliyotokana na kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma ambapo hadi kufikia mwezi Juni, 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi 28,929,095,373.89.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya shilingi 13,754,462,429.29 tayari yamehakikiwa na yameshaingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara na yanasubiri kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya watumishi 8,776 yenye jumla ya shilingi 15,590,586,474.69 yanaendelea kuhakikiwa ili yaweze kuingizwa kwenye mfumo tayari kwa kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa, lakini ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba madeni haya yanalipwa mara yanapojitokeza.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais amepunguza idadi ya Wizara kutoka 23 hadi 18 ili kupunguza gharama za uendeshaji:-
Je, ni kiasi gani cha fedha za walipa kodi zilizookolewa kwa kuwa na idadi ndogo ya Wizara.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya Mheshimiwa Rais ya kupunguza Wizara kutoka Wizara 28 hadi 18 ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake, ya kupunguza gharama za uendeshaji na ukubwa wa Serikali aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na katika Hotuba yake wakati akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lengo likiwa ni kuboresha huduma kwa wananchi wetu kwa kuelekeza matumizi makubwa ya Serikali katika huduma za kijamii, kama vile afya, elimu, maji, miundombinu na mawasiliano pamoja na miradi ya maendeleo.
Uundwaji wa Serikali ya Awamu ya Tano bado unaendelea, kwa sasa Serikali inafanya uchambuzi wa kina wa majukumu ya kila Wizara, na taasisi zake ili kuainisha majukumu ambayo ni muhimu kuendelea kutekelezwa na Serikali na taasisi zake au la na kuchukua hatua stahiki. Uchambuzi huu utaiwezesha Serikali kubaini majukumu yanayofanana ndani ya taasisi, lakini yanatekelezwa na kitengo au Idara zaidi ya moja, au majukumu yanayofanana, lakini yanatekelezwa na taasisi zaidi ya moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili pia litawezesha kubaini, kama idara au vitengo ndani ya Wizara na taasisi zake, vina majukumu ya kutosha ya kuhalalisha uwepo wake. Kukamilika kwa uchambuzi huu, ndio itakuwa msingi kwa Serikali kuuhisha miundo ya mgawanyo wa majukumu wa Wizara na taasisi zake na hivyo kujua gharama halisi, zitakazotokana na kupunguzwa kwa Wizara kutoka 28 hadi kufikia 18.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMMED) aliuliza:-
Serikali imejipanga kupiga vita suala la ajira kwa watoto na imekuwa ikiunga mkono matamko ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na ajira za watoto.
Je, kupitia Mradi wa TASAF III Serikali ina mikakati gani ya makusudi kuwasaidia watoto na tatizo la ajira za utotoni kwa upande wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini au TASAF III ulianza utekelezaji wake mwezi Agosti mwaka 2012. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016, mpango umeandikisha jumla ya kaya milioni 1.1 Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya hizo, kaya 33,532 zimeandikishwa na zinapata ruzuku ya malipo kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji, mpango unatilia mkazo uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini zilizoandikishwa. Uhawilishaji wa fedha umeziwezesha kaya hizi maskini kuwa na uhakika wa chakula, kupata huduma za afya na kuwawezesha watoto walio na umri wa kwenda shule kuanza shule na kwa walio katika shule za msingi na sekondari kupata mahitaji muhimu ya shule. Aidha, kaya hizi zinapata kipato cha ziada kupitia ajira za muda kwa wanakaya wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kufanya kazi kwenye miradi midogo-midogo inayotekelezwa na TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini umewezesha watoto waliokuwa katika ajira za utotoni katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kipato cha kaya kutoka katika ajira hizo na kuweza kuhudhuria shule kwa kiwango cha 80% au zaidi. Kwa wale ambao hawajafikia umri wa kwenda shule waliweza kupata huduma za afya kwa kufuata taratibu za sekta husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliowekwa unashirikisha viongozi wa maeneo ya utekelezaji katika ngazi zote kufuatilia mahudhurio ya watoto shuleni ili waweze kufikia viwango vilivyowekwa. Kwa kaya ambazo watoto wao hawafikishi idadi ya siku zilizopangwa za kwenda shule hupunguziwa ruzuku kama njia ya kuwahimiza kutimiza masharti ya kuhakikisha kwamba watoto wao wanahudhuria shuleni ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mategemeo ya Serikali kwamba Waheshimiwa Wabunge watashirikiana na viongozi wa Serikali katika ngazi zote ili kufanikisha mpango huu kwa kuhakikisha kwamba watoto walio na umri wa kwenda shule wanaotoka katika kaya maskini wanaandikishwa na kutimiza masharti ya Mpango kwa kuhudhuria shule kama inavyotakiwa.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu suala la watumishi hewa limekuwa likiathiri sana uchumi wa Taifa na kwa kuwa waliohusika wengi wao ni maafisa na watumishi wa Serikali.
Je, Serikali inasema nini juu ya wale waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 25/10/2016 Serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wa umma 1,663 kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao walibainika kusababisha uwepo kwa watumishi hewa kwa mchanganuo ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara ni watumishi wa umma 16, kwa upande wa Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali ni watumishi wa umma tisa, kwa Sekretarieti za Mikoa ni watumishi wa umma wa sita, Mamlaka za Serikali za Mitaa watumishi wa umma 1,632 inayofanya jumla ya watumishi 1,663.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii inajumuisha kuwasilishwa kwa masuala yanayohusu baadhi ya watumishi hawa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo kufikia tarehe 25/10/2016 jumla ya watumishi wa umma 638 wamefunguliwa mashitaka polisi, watumishi 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na watumishi wa umma 975 mashtaka yao yamefikishwa kwenye mamlaka zao za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hatua hizi Serikali inaendesha ukaguzi wa mara kwa mara kwa mfumo wa taarifa za kiutumishi au Human Capital Management Information System na maafisa wanaobainika kuhusika au kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika taasisi au mamlaka zao wanachukuliwa hatua za kinidhamu kama vile kuwafungia dhamana na uwezo wa kuingia na kufanya kazi katika mfumo huo na hatua nyingine za kinidhamu. Nakushukuru.
MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:-
Kumekuwepo uhaba wa watumishi katika Halmashauri nyingi nchini ambao unaleta athari katika utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kutotoa huduma katika kiwango kinachohitajika.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hasa vijana waliomaliza vyuo ambao wanazurura mitaani kwa ukosefu wa ajira?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndilla Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi wa umma Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya ikama na mishahara na kutoa vibali vya ajira mpya kwa taasisi zote za umma ikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, kama ilivyo kwa sekta zote za ajira katika utumishi wa umma kwa kutegemea kiwango cha kukua kwa uchumi. Kwa kuzingatia sera za kibajeti, Serikali imetenga pia nafasi za ajira mpya katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo zitajazwa kwa awamu, ambapo watumshi wa umma wapatao 5,074 hadi sasa wameshaajiriwa, ikiwemo watumishi wa hopsitali mpya ya Mloganzira. Aidha, tayari Serikali imetoa kibali cha kuajiri walimu wa masomo ya hisabati, sayansi, mafundi sanifu wa maabara za shule za Serikali wapatao 4,348.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kutoa rai kwa mamlaka za ajira kutumia vizuri rasilimali watu walizonazo kwa kuwapanga watumishi wa umma kwa kuzingatia uwiano sahihi ili kuweza kukabiliana na changamoto za upungufu wa watumishi wa umma.
MHE. JAPHET N HASUNGA aliuliza:-
Kwa kuwa watumishi na viongozi wengi wamekuwa wanaingia kwenye madaraka mbalimbali ya nchi bila kupewa mafunzo ya kuwaandaa kama ilivyo katika nchi nyingi duniani na kama ilivyo kwenye vyombo vya majeshi yetu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa viongozi wote wanapewa mafunzo ya awali kabla ya uteuzi wa madaraka yoyote katika utumishi wa umma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwapatia mafunzo ya awali watumishi na viongozi wa umma kabla ya uteuzi wa madaraka yoyote katika utumishi wa umma ili waweze kuuelewa utumishi wa umma na kufahamu misingi yake, sheria, kanuni na taratibu za utendaji kazi na kuwapatia stadi za uongozi zinazowezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Katika kutekeleza azma hii Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
(a) Imeandaa na kuendesha mafunzo elekezi kwa watumishi wanaoteuliwa kushika nafasi za uongozi ili waweze kumudu madaraka mapya.
(b) Imeendelea kutoa mafunzo ya uongozi (Leadership Development Programmes), kwa watumishi waandamizi kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, lakini pia kuwaandaa kwa ajili ya kushika nafasi za uongozi pindi watakapoteuliwa kushika nafasi hizo. Mafunzo hayo yamekuwa yakiendeshwa na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Taasisi ya Uongozi, Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA), Chuo Kikuu cha Mzumbe pamoja na ESAMI. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 watumishi waandamizi 1,397 waliweza kupatiwa mafunzo ya uongozi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Serikali imeanzisha Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College of Tanzania) kinachotoa mafunzo ya uongozi kwa Maafisa Waandamizi wa Kijeshi na Kiraia (Inter Service Training) kwa kuhusisha Maafisa wa Jeshi na wa Kiraia (Defence-Civil Staff Training) ikiwa ni pamoja na kuwapatia uelewa wa masuala ya usalama na hivyo kuwajengea uwezo wa kutambua athari za kiusalama wanapotunga na kutekeleza sera, sheria na maamuzi mbalimbali ya kiutendaji.
(d) Mheshimiwa Mweenyekiti, lakini pia, Serikali kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimetoa mafunzo kwa viongozi waandamizi 86 na kiko katika maandalizi ya kuandaa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya lazima kwa Maafisa Waandamizi katika utumishi wa umma (Mandatory Course for Senior Officers in the Public Service). Mafunzo haya ya lazima yanalenga kuwawezesha Maafisa Waandamizi kujua majukumu ya msingi ya uongozi na usimamizi katika taasisi za umma, hivyo kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu hayo pindi watakapoteuliwa kushika nafasi za uongozi.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:-
Ushirika katika Wilaya ya Siha umekumbwa na matukio ya ufisadi yakiwemo upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 840 katika Ushirika wa Siha Kiyeyu, upotevu wa shilingi milioni 337 ya SACCOS ya Sanya Juu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi, licha ya uchunguzi mzuri uliofanywa na TAKUKURU Mkoa:-
Je, ni kwa nini uchunguzi huo unaingiliwa na maslahi binafsi ya watu wachache na kusababisha matukio yanayodhalilisha Serikali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007, TAKURURU imepewa mamlaka kuwa chombo huru cha kuzuia na kupambana na rushwa nchini; na inatekeleza majukumu yake muhimu kama yalivyofafanuliwa katika Kifungu cha (7) cha sheria hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa. Kutokana na mantiki hiyo ya kisheria, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa namna yoyote ile, Taasisi ya TAKUKURU haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba TAKUKURU ilipokea tuhuma za udanganyifu wa matumizi ya fedha za umma kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali zilizokihusu Chama cha Ushirika cha Siha Kiyeyu na Sanya Juu SACCOS. Kutokana na tuhuma hizo, uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulithibitisha pasipo shaka kwamba viongozi wa Chama cha Ushirika Siha Kiyeyu bila ridhaa ya wanachama wake, waligawa mashamba kwa watu wasio wanachama wapatao 13, shamba lenye ekari 16 ambazo zililimwa kati ya miaka miwili na mitano bila ya kulipiwa gharama yoyote. Kitendo hiki kiliukosesha ushirika Siha Kiyeyu mapato ya kiasi cha sh. 1,600,000/=.
Mheshimiwa Spika, uchunguzi pia ulithibitisha pasipo shaka kwamba uongozi wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Siha Kiyeyu ulitoa maelezo ya uongo kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa William Olenasha kwa kumpatia stakabadhi za uongo juu ya matumizi ya sh.500,000/= za ushirika kwa ajili ya semina. Baada ya uchunguzi kukamilika uongozi huo ulikiri kutenda kosa hilo mbele ya wachunguzi.
Mheshimiwa Spika, tuhuma kuhusu ufisadi wa sh.337,000/= unaoihusu SACCOS ya Sanya Juu ni tuhuma mpya. Tuhuma za Sanya Juu SACCOS zilihusu kiasi cha sh.160,100,406, na tuhuma hizi zilichunguzwa na Jeshi la Polisi na kesi Na. CC 15/2016 imeshafunguliwa na ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Siha.
Mheshimiwa Spika, tuhuma za upotevu wa shilingi milioni 840 unaokihusu Chama cha Ushirika cha Kiyeyu ni malalamiko ya wanachama juu ya tozo anazolipa mwekezaji katika shamba la maparachichi ambapo anadaiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni 60 kwa mwaka. Tuhuma hizi ni mpya na Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro imezipokea kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Uchunguzi utakapokamilika, taarifa itatolewa.
MHE. EDWARD F. MWALONGO Aliuliza:-
Jimbo la Njombe lina Mahakama ya Mwanzo moja tu iliyopo Njombe Mjini. Je, Serikali ipo tayari kukarabati Mahakama za Mwanzo za Mahenye na Igominyi ili wananchi waweze kupata huduma hiyo jirani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Sheria na Katiba, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mahakama ni uhaba na uchakavu wa miundombinu. Sehemu nyingi nchini hazina majengo ya Mahakama na baadhi ya majengo yaliyopo ni chakavu na ni ya muda mrefu. Aidha, ni kweli kwamba Mahakama za
Mwanzo za Igominyi na Mahenye ni chakavu sana kiasi cha kushindwa kuendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, mpango uliopo ni kujenga majengo mapya na siyo kukarabati yaliyopo, hasa ikizingatiwa kuwa majengo haya yapo kwenye hifadhi ya barabara. Ni kweli Mahakama hizi zinahitajika sana na ni moja ya miradi ya kipaumbele katika ujenzi wa Mahakama
za mwanzo katika Wilaya ya Njombe. Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 kipaumbele ni ujenzi wa Mahakama ya Mkoa na kwa mwaka 2017/2018 imepangwa kujengwa Mahakama ya Mwanzo Mahenye-Uwemba; na Mahakama ya Mwanzo Igominyi imepangwa kujengwa katika mwaka 2019/2020 kulingana na upatikanaji wa fedha.
Pamoja na hayo, Mahakama imeshapata nafasi katika Ofisi ya Kijiji cha Uwemba kwa ajili ya kuendesha shughuli za Mahakama ya Mwanzo Mahenye ili huduma iendelee kutolewa wakati mipango ya ujenzi inaendelea.
MHE. MCH.PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) Aliuliza:-
Nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni katika kuajiri na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma. Kuna baadhi ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi na Mheshimiwa Rais, RC na hata DC bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake.
Je, Serikali inasemaje kuhusu hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za nidhamu katika utumishi wa umma hutekelezwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali. Kwa mujibu wa Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kuhusu usimamizi na
uendeshaji wa utumishi wa umma, ikiwemo kuanzisha, kufuta Ofisi na kuchukua hatua za nidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara hiyo ya 36(2) imempa Rais uwezo wa kukasimu madaraka yake kwa mamlaka mbalimbali ndani ya utumishi wa umma. Hata hivyo kukasimu madaraka hakuwezi kutafsiriwa kwamba Rais hana mamlaka hayo tena kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 36(4) ya Katiba na Kifungu cha 21(4) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale maelekezo ya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wa umma yanapotolewa na Viongozi wa Serikali, Mamlaka za Nidhamu za watumishi husika ndizo zenye dhamana ya kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 Serikali ilikamata Meli ya Uvuvi MFV TAWARIQ, nahodha wake Tsu Chin Tai pamoja na watu wengine 36 walishtakiwa Mahakama Kuu kwa kesi ya Jinai Na. 38 ya mwaka 2009. Kwa amri ya Mahakama samaki tani 296.3 wenye thamani ya sh. 2,074,000,000/= waligawiwa bure. Aidha, meli hiyo ilizama ikiwa inashikiliwa kama kielelezo. Tarehe 23 Februari, 2012 watuhumiwa wawili walihukumiwa kifungo na walikata rufaa Mahakama ya Rufaa ambapo tarehe 25 Machi, 2014 waliachiwa huru na sasa ni miaka saba tangu meli hiyo ikamatwe.
Je, Serikali itarudisha lini sh. 2,07,000,000/= ambazo ni thamani ya samaki na fedha ambazo ni thamani ya meli kwa Mawakili wa Nahodha wa Meli hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 8 Machi,
2009 kikosi kazi kilichokuwa kikifanya doria katika ukanda wa kiuchumi wa Bahari Kuu ya nchi yetu (Exclusive Economic Zone) katika Bahari ya Hindi kilifanikiwa kukamata meli ya uvuvi iitwayo Na. 68 BU YOUNG ikivua katika bahari yetu bila kibali. Meli hiyo ilikuwa ikiongozwa na nahodha aitwaye TSU CHIN TAI, raia wa Jamhuri ya Watu wa China na alikuwa pamoja na wenzake 36. Pamoja na kuwa jina la meli hiyo ni No. 68 BU YOUNG, meli hiyo ilikuwa inatumia pia jina la TAWARQ 1 na TAWARIQ 2 ili kuficha jina halisi na kuendeleza kufanya uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahodha wa meli hiyo, yaani
TSU CHIN TAI na wenzake walishtakiwa Mahakama Kuu katika kesi ya jinai Na. 38/2009 ambapo nahodha Tsu Chin Tai na ZHAO HANQUING aliyekuwa wakala wa meli hiyo, walitiwa hatiani. Wawili hawa waliomba rufaa Mahakama ya Rufani ambapo mwaka 2014 Mahakama hiyo ilibatilisha na kufuta mwenendo mzima wa kesi baada ya kubaini kuwa kulikuwa na kasoro katika taratibu za kuwafungulia mashtaka. Kwa ufupi, hawakuwahi kushinda kesi na Mahakama ya Rufani haikuwahi kutamka kuwa wako huru kwa sababu hawana hatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi wa Mashtaka alifungua mashtaka upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye kuondoa mashtaka dhidi yao tarehe 22/8/2014. Baada ya miaka miwili, yaani 2016 Wakili Captain Bendera alifanya maombi namba 108/2016 katika Mahakama Kuu akimwakilisha Bwana Said Ali Mohamed Al Araimi ambaye hakuwa mmoja kati ya washtakiwa katika kesi ya msingi akiomba apewe meli au USD 2,300,000.00 kama thamani ya meli hiyo na sh. 2,074,249,000/= kama thamani ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilikubaliana na hoja za Jamhuri na kutupilia mbali maombi hayo. Katika uamuzi wake, Mahakama ilitamka yafuatayo, naomba kunukuu: “this application was uncalled for, superfluous and amounts to abuse of court process, thus devoid of any merit.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la kisheria na wahusika wanaweza kuendelea kulishughulikia kupitia Mahakamani.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Halmashauri ya Lushoto ina mzigo mkubwa wa kulipa mishahara ya watumishi ambapo inatumia zaidi ya shilingi 28,000,000 kila mwezi kulipa mishahara ya watumishi ambao kimsingi mishahara yao ilipaswa kulipwa na Hazina kupitia Utumishi.
Je, ni lini Serikali itawatua wananchi wa Lushoto mzigo huu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri za Wilaya wapo watumishi wanaolipwa kutoka Serikali Kuu na wapo watumishi wanaolipwa kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmshauri husika (own source). Utaratibu huu ulianzishwa baada ya kuonekana kuwepo kwa mahitaji maalum yanayowasilishwa na waajiri kutaka kuwaajiri watumishi wa ziada tofauti na ukomo wa bajeti ya mishahara ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuna jumla ya watumishi 116 ambao waliajiriwa katika utaratibu huo wa mapato ya Halmashauri (own source) kwa kuwa Halmashauri hiyo iliona inaweza kumudu gharama za kuwalipa mishahara kutokana na vyanzo vyake vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Halmashauri zote kuzingatia uwezo wao kabla ya kuamua kuajiri watumishi kwa kutumia vyao vyao vya mapato.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina utaratibu gani maalum wa kuwapangia na kuwahamisha sehemu za kazi watumishi wake?
(b) Je, ni vigezo gani huzingatiwa katika kuwapanga au kuwahamisha watumishi sehemu za kazi?
(c) Je, ni kwa namna gani Serikali inahakikisha watumishi wake wanafanya kazi kwa ufanisi katika maeneo waliyopangwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha watumishi wa kada ya ualimu na wale wa kada za afya ambao utaratibu wao wa kuajiriwa ni wa kupangiwa vituo vya kazi mara tu wanapohitimu mafunzo yao, utaratibu wa ajira kwa kada nyingine hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria hii, mchakato wa ajira hufanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo hutangaza kazi kulingana na mahitaji ya waajiri, kufanya usaili na kuwapeleka katika vituo vya kazi waombaji waliofaulu usaili.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhamisho ndani ya utumishi wa umma hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Toleo la mwaka 2009 ambapo Katibu Mkuu (Utumishi) amepewa mamlaka ya kufanya uhamisho wa watumishi wa umma kutoka kwa mwajiri mmoja na kwenda kwa mwingine kwa lengo la kuimarisha utendaji ndani ya Utumishi wa Umma.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika kuwapanga au kuwahamisha vituo vya kazi watumishi wa umma ni pamoja na:-
(i) Mahitaji ya kila taasisi kutokana na kuwepo ikama na bajeti ya mishahara ya watumishi kwa mwaka wa fedha husika.
(ii) Sifa za kitaaluma kama zilivyoainishwa kwenye Miundo ya Maendeleo ya Utumishi kama inavyotolewa mara kwa mara na Serikali.
(iii) Umuhimu wa kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma.
(iv) Kupangiwa kazi au uhamisho kutokana na mtumishi kupata maarifa/taaluma mpya (re-categorization).
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa ufanisi katika maeneo waliyopangwa, zipo Mamlaka za Ajira na Nidhamu ambazo zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298. Kwa mujibu wa sheria hii, mamlaka hizi zinapaswa kuhakikisha kuwa kila mtumishi anapangiwa majukumu kulingana na mpango mkakati wa kila taasisi, ambapo kila mwisho wa mwaka upimaji wa wazi wa utendaji kazi hufanyika. Pale mtumishi anapoonekana hajatimiza malengo yake kwa sababu yoyote ile, anapaswa kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza usimamizi wa utumishi wa umma.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuja na mikakati yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakiki watumishi wa umma, zoezi ambalo halikuwekewa muda wa kuanza na kumaliza (time frame) hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa na hata kuharibu mfumo wa watumishi wa umma, ikiwemo namna ya kuajiri.
(a) Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watumishi wa umma walioajiriwa na kusainishwa mikataba ya ajira ndani ya Serikali ambapo ghafla mwaka 2016 Rais alitoa kauli ya kusimamisha ajira kupisha ukaguzi wa watumishi hewa?
(b) Je, Serikali inatambua kuwa watu hao tayari walikuwa watumishi na mchakato wa kuwaingiza kwenye payroll ulishaanza, lakini ukasitishwa ghafla na sasa wako mtaani na hawajui hatma yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wote ambao walisitishwa kuingizwa katika orodha ya malipo ya mishahara (payroll) mwezi Mei, 2016 waliokuwa wakipisha zoezi la uhakiki wa watumishi wamesharudishwa katika orodha ya malipo na sasa wanaendelea na kazi na wamekuwa wakilipwa mishahara yao kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya swali la Mheshimiwa Masele, watumishi hao wanatambuliwa kama watumishi wengine wa umma.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA (K.n.y. MHE. COSATO D. CHUMI) aliuliza:-
Serikali ina utaratibu wa kuwalipa watumishi wa umma gharama za nauli ya likizo mara moja katika miaka miwili wakati wanaenda likizo.
Je, Serikali ipo tayari kuanzisha utaratibu wa kuwalipa gharama za nauli za likizo watumishi wa umma kila mwaka katika kuongeza, kupandisha morali ya kazi na pia kupunguza makali ya maisha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, likizo ya mwaka ni haki ya kila mtumishi wa umma na haki hii imebainishwa katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini Namba6 ya mwaka 2004 na Kanuni ya 97 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kulipa gharama za nauli kwa watumishi wa umma kwa ajili ya likizo umeainishwa katika Kanuni H. 5 (1) (a), (b) na (c) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009. Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mtumishi wa umma anatakiwa kulipiwa gharama ya nauli kwa ajili yake, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne kutoka kituo chake cha kazi hadi nyumbani kwake mara moja katika kipindi cha miaka miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuwapa motisha watumishi wa umma ili kuwaongezea morali ya kazi. Hata hivyo, motisha inayotolewa inapaswa kuzingatia hali ya uchumi wetu. Hali ya uchumi wetu kwa sasa inaruhusu utaratibu huu wa kulipa gharama za nauli ya likizo kwa watumishi wa umma mara moja katika kipindi cha miaka miwili. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha motisha kwa watumishi wa umma kadri uchumi unavyoimarika.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-
Ajira kwa sasa ni tatizo hapa nchini hasa kwa walimu wa sanaa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri katika sekta mbalimbali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanywa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) mwaka 2015/2016 umebaini kuwepo na ziada ya walimu wa masomo ya sanaa wapatao 7,463 katika shule za sekondari. Kutokana na hali hii Serikali inaendelea na zoezi la kuwagawanya walimu hao (redeployment) kwa kuzingatia uwiano na mahitaji halisi ya walimu wa sanaa kwa kila mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kila shule iweze kupata Walimu wa masomo ya sanaa badala ya kuajiri walimu wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 watumishi wa umma 9,721 wameshaajiriwa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya kila mwajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali inatarajia kuajiri Watumishi 52,436 wa sekta mbalimbali kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa pamoja na kuimarisha sekta na maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-
Serikali yoyote duniani inaendeshwa na rasilimali watu wenye weledi, ari na uzalendo. Ili Watumishi hawa wafanye kazi kwa moyo wanahitaji kuthaminiwa, kutambuliwa mchango wao na kupewa stahili zao bila bughudha:-
Je, Serikali imebuni mkakati gani wa kuwapa motisha na ari Watumishi wa Umma ili wafanye kazi kwa kujituma badala ya vitisho?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, napenda kutoa maelezo kwamba utekelezaji wa shughuli za Serikali huendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayosimamia Utumishi wa Umma ambapo kila mtumishi hupaswa kuzingatia wakati wa kutekeleza majukumu yake. Hivyo, Serikali haitumii vitisho wala bughudha katika kusimamia watumishi wake, bali husimamia sheria, kanuni na taratibu hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa Watumishi wa Umma ni rasilimali ya msingi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu na malengo yake kwani nguvu na mafanikio ya Taifa lolote inategemea aina ya Watumishi lililonao na ni kwa msingi huo, Watumishi hawana budi kuendelezwa na kupewa motisha ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Kwa kutambua umuhimu wa motisha kwa Watumishi wa Umma, Serikali inayo mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza ari kwa Watumishi wa Umma na hivyo kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma. Mikakati hii ni pamoja na:-
(a) Kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye mshahara au Pay As You Earn kutoka asilimia 14 mwaka 2010/2011 hadi asilimia tisa mwaka 2016/17. Hatua hii imesaidia kuongezeka kwa kiwango cha mshahara anachobakinacho mtumishi baada ya kukatwa kodi.
(b) Kuongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh.100,000/= mwaka 2010/2011 hadi Sh.300,000/= mwaka 2015/2016 sawa na ongezeko la asilimia 200.
(c) Kupitia Waraka Na. 3 wa mwaka 2011 unaohusu utaratibu wa kuwakopesha watumishi vyombo vya usafiri, Serikali imekuwa ikiwakopesha Watumishi vyombo vya usafiri ili kuwapunguzia adha ya usafiri wakati wa kwenda kazini na kurudi majumbani.
(d) Kutoa dhamana kwa watumishi wakati wanapokopa fedha katika Benki na Taasisi mbalimbali za kifedha.
(e) Kuanzisha Watumishi Housing Company Limited kwa ajili ya kujenga nyumba za gharama nafuu na kuwauzia au kuwakopesha Watumishi ili waishi kwenye makazi yenye staha.
(f) Kupitia sera ya mafunzo katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Serikali imekuwa ikitumia rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya Watumishi wa Umma ili wawe na weledi wa kutosha.
(g) Serikali imekuwa ikiratibu nafasi za mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa Watumishi wa Umma kutoka kwa nchi na wadau wa maendeleo kama vile Ubelgiji, Uholanzi, Australia, Jamhuri ya Korea, Ujerumani, China, Japan, India, Malaysia, Indonesia, Singapore, Sweden na Jumuiya ya Madola na nchi zinginezo.
(h) Pamoja na Serikali kufanya zoezi la tathmini ya kazi kwa lengo la kubaini uzito wa majukumu ya Kada mbalimbali za Watumishi na hivyo kuwa msingi wa kupanga ngazi za mishahara. Zoezi hili linatarajiwa kukamilika katika mwaka 2017/2018.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Watumishi walio maeneo ya pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, mfano walimu wa watumishi wa afya.
Je, Serkali ina mpango gani wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa maeneo ya pembezoni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba watumishi walio katika Halmashauri zilizo katika maeneo ya pembezoni ikiwemo Wilaya ya Ukerewe hufanya kazi katika mazingira magumu na upungufu mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 Serikali ilipitisha Sera ya Malipo ya Mishahara na Motisha katika utumishi wa umma ambayo miongoni mwa malengo yake mahsusi ni kuwavutia, kuwapa motisha na kuwabakiza watumishi katika utumishi wa umma. Lengo ni kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi katika Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza sera hii mwaka 2012/2013 Halmashauri 33 za Wilaya, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ziliwezeshwa kuandaa miongozo ya kutoa motisha kwa watumishi wake. Kutokana na zoezi hilo Halmashauri 29 ziliandaa na kuwasilisha katika ofisi yangu miongozo iliyoabainisha aina za motisha zinazohitajika kwa ajili ya watumishi wake. Utekelezaji wa miongozo hiyo kwa Halmashauri zote 29 ulikadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 331.087 kwa mwaka, ambapo kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 314.372 kilihitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 16.761 kilihitajitaka kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miongozo hii ulitarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2013/2014. Hata hivyo, utekelezaji wa miongozo hii haujaanza kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Nchi nyingi duniani ikiwemo Japan, Uholanzi na Marekani hutumia wataalam wastaafu kwenye sekta mbalimbali za uchumi katika shughuli mbalimbali za kutoa ushauri ndani na nje ya nchi zao. Wataalam hao (volunteers) wanatoa mchango mkubwa kwenye kushauri.
(a) Je, ni lini nchi yetu itaiga utaratibu huo mzuri wa kuwatumia wataalam wake wastaafu ipasavyo badala ya kuwaacha tu mitaani?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka kumbukumbu ya taarifa ya wataalam wastaafu wake (directory) kwa kila mmoja kwenye fani yake (profession) ili kuweza kuwatumia wataalam wastaafu hao pale ushauri wao utakapohitajika?
WAZIRI WA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu wa kuwatumia wataalam wastaafu kwa kuwapatia mikataba pale wanapohitajika. Matumizi ya wataalam hao yamefanunuliwa katika aya ya 12.2 ya Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1998, pamoja na Kanuni ya D. 28 ya Kanuni za Kudumu (Standing Orders) katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009. Miongozo hii inaelekeza kwamba endapo utaalam wa mtumishi unahitajika sana Serikali inawajibika kumuomba mtumishi kuendelea na kufanya kazi.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuanzisha kanzidata ya wataalam wastaafu ili kuweza kuwatumia pale watakapohitajika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI) aliuliza:-

Kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuongeza uwekezaji kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa vikwazo vinavyoathiri dhana hiyo vinaondolewa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Dira ya Taifa ya mwaka 2025 ni kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutimiza dhamira hiyo tunatekeleza mipango mitatu ya maendeleo ya miaka mitano mitano ambayo imeainisha vipaumbele vya Taifa kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa sasa Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa kipindi cha 2016/2017 hadi kufikia mwaka 2020/ 2021 ambao kipaumbele chake ni ujenzi wa uchumi wa viwanda. Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha vikwazo vinavyoathiri uwekezaji na biashara nchini vinaondolewa kwa kuweka miundombinu muhimu na mazingira ya kisera, kisheria, kanuni na kiutendaji ambao ni wezeshi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, umeme na maji hatua ambayo inapunguza gharama za uendeshaji wa biashara na uwekezaji na kuleta wepesi katika uwekezaji na biashara. Aidha, Serikali imeimarisha upatikanaji wa ardhi ambapo Mamlaka za Upangaji Miji zimeelekezwa kuzingatia utengaji wa asilimia 10 ya kila aneo la Mpango Kabambe wa Mji kwa ajili ya uwekezaji wa biashara na viwanda. Vilevile Serikali inaendelea kuendeleza Maeneo Maalum ya Uwekezaji au Special Economic Zones ili kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya uzalishaji yenye miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji kwa kutekeleza programu za kuboresha mazingira ya uwekezaji na hii ni pamoja na mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa mazingira ya biashara nchini au Blueprint. Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na majadiliano na Sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) pamoja na mikutano ya wadau wa Sekta mbalimbali kwa ngazi za Kitaifa, Mikoa na Wilaya ambapo changamoto zinazobainishwa zinapatiwa ufumbuzi.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-

Kata za Bendera na Makanya zina jasi nyingi na jasi inaweza kutoa malighafi kutengeneza gypsum boards, mabomba ya maji machafu, saruji, POP na mbolea:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kupatikana kwa mwekezaji ili aanzishe viwanda hivyo katika maeneo hayo ya Wilayani Same?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Aidha, viwanda vinavyotumia rasilimali zinazopatikana nchini na kuzalisha bidhaa zinazotumika kwa wingi vimepewa kipaumbele. Kutokana na utekelezaji wa azma hiyo, nchi yetu sasa imeweza kuzalisha baadhi ya bidhaa zinazotosheleza soko la ndani na ziada kuuza nje ya nchi ikiwemo bidhaa zinazotokana na malighafi ya jasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje katika maeneo yote yenye rasilimali zinazoipa Tanzania faida ya ushindani (competitive advantage), Serikali itaendelea kuvutia uwekezaji katika maeneo yote yenye rasilimali ikiwemo jasi inayopatikana katika Kata za Bendera na Makanya Wilayani Same.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kutumia fursa hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Same kwa kutenga eneo katika Kata ya Makanya kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha saruji na kuingizwa katika Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Kilimanjaro na hatua za kutafuta wawekezaji zinaendelea. Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zingine kama vile Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Mamlaka ya EPZ, Tume ya Madini na wadau wengine tutaendelea kushirikiana kuzitangaza fursa za uwekezaji za Wilaya ya Same ili kuvutia na kutekeleza uwekezaji katika jasi iliyoko wilayani Same.

Aidha, napenda kuzikumbusha Wizara, taasisi za Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kusimamia mikakati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji katika maeneo yao ikiwemo kuainisha na kuyapembua kiyakinifu maeneo yote yenye rasilimali, kuyatenga na kuyarasimisha kwa ajili ya uwekezaji ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima na wawekezaji ili kufikia dhamira ya Serikali kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza:-

Tarehe 8 Machi, 2019, Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli, alipokuwa Ikulu kwenye dhifa ya Mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali Duniani aliutamka mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa uwekezaji: -

Je, Serikali imejipangaje katika kutekeleza tamko hilo muhimu sana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha tamko la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alilolitoa katika dhifa ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, la mwaka 2019 kuwa Mwaka wa Uwekezaji Tanzania, linatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza tamko hilo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kuweka misingi imara ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yatakayoendana na hali ya sasa ya kiuchumi duniani.

Aidha, Serikali imeongeza mkazo katika kuimarisha miundombinu wezeshi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa nishati ya uhakika na ya bei nafuu, maji, mawasiliano, ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ya reli, barabara, madaraja, anga, vivuko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mifumo ya Udhibiti wa Biashara (Blueprint Action Plan) ambapo hadi sasa Serikali imeweza kufuta na kuboresha tozo na ada 54 zilizoonekana ni kero kwa wawekezaji na wafanyabiashara kupitia bajeti ya mwaka 2019/2020. Hatua nyingine ni pamoja na kuondoa migongano na muingiliano wa majukumu miongoni mwa Mamlaka za Udhibiti kama vile Shirika la Viwango Tanzania na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo mikoani vilevile Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC) imeendelea kushirikiana na Ofisi za Mikoa kuandaa makongamano ya uwekezaji yanayonadi vizuri fursa za uwekezaji mikoani. Kwa mwaka huu 2019 kwa mikoa ambayo tayari imeshafanya makongamano hayo ni takribani mikoa 9 na kwa sasa tunaendelea na maandalizi katika Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali imejidhatiti kuhakikisha changamoto zinazokabili wawekezaji nchini zinapatiwa ufumbuzi kupitia mikutano ya mashauriano kati ya Serikali na sekta binafsi katika ngazi za Mikoa na katika sekta mbalimbali. Kwa sasa tumeshafanya mikutano hiyo katika Mikoa ya Arusha, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Aidha, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji kutoka nje kwa kutekeleza ipasavyo diplomasia ya uchumi kupitia Balozi zetu za nje pamoja na kufanya mikutano ya kimkakati na wawekezaji wa nje waliowekeza nchini ili kuvutia uwekezaji zaidi na kufanya mashauriano nao.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA Aliuliza:-

Serikali ya Awamu ya Tano imekaribisha wawekezaji wa nje na ndani kuwekeza sehemu mbalimbali hapa nchini:-

Je, Serikali ipo tayari sasa kuelekeza wawekezaji hao kuwekeza katika Mkoa wa Tabora?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uwekezaji katika sekta mbalimbali na kujenga uchumi wa kati wenye kuongozwa na Sekta ya Viwanda ni suala linalotekelezwa katika mikoa yote ukiwemo Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Tabora na uongozi wake na Mikoa mingine kwa kuwa mfano mzuri katika kutekeleza mikakati ya kuvutia uwekezaji ikiwemo uandaaji wa makongamano ya uwekezaji kama lile lililofanyika mwaka 2013 Dar es Salaam na lililofanyika mwezi Novemba, 2018 katika mjini Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia makongamano hayo, tumeendelea kuhamasisha kila Halmashauri kuandaa mradi wa kimkakati ambao utakuwa dira kwa wawekezaji wengine. Aidha, katika kutekeleza agizo la Serikali la kutenga maeneo ya uwekezaji, Mkoa wa Tabora umetenga ekari 42,053.71 katika Halmashauri zake zote nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kama sehemu ya matokeo ya jitihada za Serikali, takwimu zilizopo katika Kituo chetu cha (TIC) zinaonesha kwamba tangu mwaka 1997, jumla ya miradi ya uwekezaji 55 imesajiliwa Mkoani Tabora katika Sekta za Kilimo, Viwanda, Ujenzi, Utalii Mawasiliano na Usafirishaji. Wilaya ya Tabora Mjini inaongoza kwa kusajili miradi 19, Urambo 13, Nzega miradi tisa, Igunga 11, Sikonge miradi miwili na Uyui mradi mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kati ya miradi hiyo, miradi 30 ni ya Watanzania, miradi tisa ni ya wageni na miradi 16 ni ya ubia. Hivyo, napenda kipekee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inautambua Mkoa wa Tabora kama mojawapo ya maeneo ya kimkakati yenye fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali na tutaendelea kuwaelekeza wawekezaji kuja kuwekeza Tabora na katika Mikoa mingine nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwahamasisha Waheshimiwa Wabunge wote kushirikiana kwa karibu na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya EPZA na Taasisi nyingine katika kuibua miradi inayokidhi vigezo (bankable projects) na pia kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye maeneo yao. Lengo la hili ni kufanikisha malengo ya Serikali ya kuvutia uwekezaji wenye tija nchini kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mikoa inashauriwa sasa kuanza kutenga katika bajeti zake fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya msingi kama vile maji, barabara, umeme na kadhalika. Lengo ni kuelekea kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji. Hatua hizi zitasaidia katika kuharakisha uendelezwaji wa maeneo maalum ya uwekezaji kwa kukamilisha hatua muhimu za awali na hivyo kuvutia wawekezaji na hata ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda kuzihamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa karibu na Taasisi za Serikali zinazotoa huduma za ushauri wa kuwezesha uwekezaji nchini ili kuweka mikakati ya pamoja ya kutambua vivutio na fursa za wawekezaji wa ndani na nje pamoja na kuwasilisha miradi ya kutafutiwa wawekezaji na kushirikiana na TIC katika kuandaa makongamano ya uwekezaji katika Mikoa husika.