Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Angelina Adam Malembeka (16 total)

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, adhabu mojawapo aliyoitaja ni kifungo cha maisha kwa wale ambao watapatikana hatia na huko gerezani tayari wameshakuwa na tabia kama hiyo, haoni kwamba kwa kuwaweka gerezani maisha wataendelea kufanya shughuli hiyo, kwa nini adhabu isiongezwe na waweze kuhasiwa ili wasirudie tena kitendo hicho?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba vitendo vya ubakaji vinajirudia mara kwa mara; Je, anaweza kunipa taarifa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ni kesi ngapi zimepelekwa Mahakamani na ngapi zimetolewa hukumu. Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge yeye anaona adhabu ya gereza haitoshi, hata kwenda jela maisha haitoshi ila anataka vile vile wahasiwe. Siwezi kuwa na jibu hapa kwa sababu hili ndilo Bunge linalotunga sheria za nchi, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge aje na hilo wazo liletwe mbele ya Bunge hapa, ni ninyi mtakaopitisha kwamba wanaume wahasiwe wanaokutwa na hilo tatizo au la, lakini siyo Serikali kuja na shauri hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anataka kujua statistics, kujua ukubwa wa tatizo hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo la kubaka na kulawiti nchi hii sasa hivi limefikia mahali pabaya kwa sababu, ukichukua takwimu za miaka mitatu au miaka minne iliyopita, tuna matukio kumi na tisa kila siku ya Mungu ya kubaka na kulawiti. Hayo matukio 19 ya kila siku ya Mungu ni yale ambayo yanaripotiwa, sasa siyo ajabu yakawa mara tatu ya hapo yale ambayo yanapita bila kuripotiwa na kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili ni tatizo kubwa, Waheshimiwa Wabunge lazima tushirikiane. Kati ya mwezi Januari mpaka mwezi Machi mwaka huu tu nimepata taarifa hapa kwamba tuna mashauri 2,031, miezi mitatu tu! Mpaka sasa naipongeza Mahakama kwamba pamoja na uchache wao wameweza kuzikamilisha kesi 111, watuhumiwa 96 wamefungwa. watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi, lakini bado kesi 1,920 kwa miezi mitatu bado hazijakamilika. Hiyo ndiyo changamoto tuliyonayo ambayo naona Waheshimiwa Wabunge wote ni kazi yetu kuweza kuitatua.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Jeshi la Polisi pamoja na kazi nyingine kazi yake kubwa ni kulinda mali na raia, nilitaka kufahamu kuna ukweli gani kuhusiana na raia kupigwa na polisi huko Pemba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Niabu Spika, sio kweli kwamba polisi wamekuwa wakipiga raia huko Pemba na ninaomba nichukue fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mfano halisi ambao ulijitokeza siku za hivi karibuni kule Pemba kwa kitendo cha maigizo na usaniii kilichofanywa na watu kutoka chama cha upinzani cha kisiasa kwa makusudi kabisa ili kupotosha jamii na dunia kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati polisi imefanya kazi yake ya kuwakamata wahalifu ambao wanafanya vitendo vya uhalifu Pemba kuna mhalifu mmoja alijifanya kwamba amekufa na amepigwa na baada ya kuhojiwa na polisi alikimbia na kukamatwa, mtu ambaye amekufa anawezaje kukimbia.
Kwa hiyo, huo ni ushahidi wa usanii ambao unafanywa kwa kulipaka matope jeshi la polisi. Naomba dunia na Watanzania watambue kwamba polisi hata siku moja hawezi kufanya kazi kinyume na sheria, maadili yake na weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kauli hiyo sio kweli kinachofanyika ni kwamba kuna raia ambao wamefanya vurugu za makusudi na polisi inachukua jitihada za kuwakamata na kupeleleza na baadae kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimalizie tukwa kuendelea kutoa wito kwamba tuendelee kuhakikisha kwamba tunalinda amani ya nchi yetu lakini vilevile tusitumie kauli ama vitendo vilivyokuwa sio vya kweli kulipaka matope Jeshi la Polisi na kuipaka matope nchi yetu mbele ya Watanzania na mbele ya Jumuiya za Kimataifa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza nilitaka kufahamu ni mikakati gani iliyowekwa na Serikali katika kuongeza vifaa tiba na wataalam katika Hospitali zote za Jeshi zikiwepo za Zanzibar?
Pili, ni lini Waziri atafanya ziara katika vituo hivyo ili kuona hali halisi ya utendaji kazi katika vituo hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali katika kuongeza vifaa tiba, dawa na watumishi kwenye Vituo vya Afya vya Kijeshi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali kwenye bajeti zake kila mwaka imekuwa ikiongeza bajeti ya huduma za afya kwa ajili ya makamanda na wapiganaji wetu kwa sababu wanapewa umuhimu wa kipekee katika nchi yetu, lakini sambamba na kuongeza bajeti Serikali pia imeongeza mikakati ya kufundisha wataalam mahsusi kwa ajili ya majeshi na hivi karibuni tumepata wafadhili kutoka Ujerumani kupitia Serikali ya nchi hiyo ambao ni marafiki zetu ambapo wametujengea chuo kikubwa na cha kisasa cha kijeshi kwa ajili ya kutoa wataalam kwenye sekta za tiba na chuo hiki nikupe taarifa Kamati yako ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Adadi mwezi Aprili, 2016 ilitembelea kwenye chuo hiki ambacho kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Ujerumani na wakajionea namna kilivyo kizuri na cha kisasa.
Mheshimiwa Spika, pia Kamati ilitupa ushauri kwamba kituo kile badala ya kuishia kutoa stashahada kiende mpaka ngazi ya degree na Jeshi likachukua ushauri ule na limekubali kukipandisha hadhi chuo hicho na mkakati wa kukiweka sawa inaendelea.
Sambamba na mkakati huo ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi kwenye jeshi kwa sababu ya umuhimu wao tayari mikakati ya kuajiri wataalam wapya wakimemo madaktari bingwa na madaktari wa kawaida pamoja na wataalam wengine imeendelea kutekelezwa. Mpaka kufikia mwezi Machi madaktari takribani 143 waliajiriwa mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma majeshini.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kupitia chuo hiki ambacho kimeaznishwa tunaamini katika miaka ya karibuni kutakuwa hakuna changamoto ya watumishi lakini pia kupitia kwenye kuongeza bajeti yetu tunaamini changamoto ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi nayo itakuwa imepatiwa ufumbuzi. Lakini suluhisho la kudumu ambalo Serikali inalifanya kwa sasa ni kutengeneza Bima ya Afya mahsusi kwa ajili ya makamanda na wapiganaji wetu na bima hii tayari imeshapata baraka za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na sasa hivi ndani ya Serikali mchakato wa kuirasimisha unaendelea ili ufike katika ngazi ya Baraza la Mawaziri na utekelezaji ufanyike.
Swali lake la pili, kwamba je Waziri itakuwa tayari kwenda kufanya ziara ninaomba nilichukue na nilifikishe kwa Waziri mwenye dhamana ili aweze kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge na pengine kumpa majibu mahsusi kwamba ni lini ataenda kuvitembelea vituo hivi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza, nilitaka nifahamu kwa wale waandishi na wachapishaji ambao wamechapisha vitabu vyenye maadili mabovu au wametoa taarifa za uongo kupitia vitabu hivyo wamepewa adhabu gani?
Pili, ninataka kujua kwa kuwa wananfunzi wanaotoka Visiwa vya Unguja huwa wanafanya mitihani ya Kitaifa sambamba na wenzao wa Tanzania Bara; je, Wizara inafanya utaratibu gani kuhakikisha kwanza mihtasari na vitabu kwa maana ya mitaala na vitabu inawafikia wanafunzi wa Zanzibar mapema ili na wao waweze kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi vitabu vyote kabla ya kupitishwa vinatathminiwa na baada ya kutathminiwa, vinaangaliwa katika suala la maadili inayoendana katika misingi ya kwamba huyu mwanafunzi atafundishwa vipi. Lakini vilevile siyo maadili tu hata uchapishaji wake kitabu kilivyochapishwa kinaleta uhalisia wa yale yanayokusudiwa kufundishwa au laa! Kwa mfano, kama tuna lengo la kumfundisha mtoto kwamba haya ni mayai, basi tunategemea kwamba na kitabu hicho hata picha itaonyesha mayai ambayo ni meupe na itaonyesha kweli yale ni mayai, hayataonyeshwa mayai wakati hapo imechorwa embe. Kwa wanaokuwa hawajatekelza wajibu wao ipasavyo vitabu hivyo vinakuwa haviruhusiwi kupelekwa au kusambazwa au kuchapishwa kwa maana hiyo wanatakiwa kurekebisha hayo makosa. Hayo yalishafanyika hata katika vitabu ambavyo sisi wenyewe tulikuwa tukivishughulikia na tulivizuia visiweze kuendelea.
Pili; kwa upande wa Zanzibar kimsingi Zanzibar wao wanayo mamlaka yao ya elimu ambayo inashugulikia masuala yote hayo ya mitaala pamoja na vitabu. Lakini kwa kuwa sisi wote ni ndugu na tuna masuala ya ushirikiano wa kielimu huwa pia tunaweza kusaidiana katika masuala ya kitaalam lakini pia hata kuchukua best practice katika kutoka upande wowote wa nchi kwa faida ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ningependa kuongezea kidogo majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri wa Elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nitoe tu ufafanuzi kuhusiana na mitaala ya elimu ya sekondari kwa upande wa Zanzibar. Kama alivyoelezea Mheshimiwa Naibu Waziri kwa upande wa elimu ya msingi mitaala inatengenezwa na upande wa Zanzibar, lakini kwenye upande wa sekondari mitaala inatengenezwa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo utaratibu ni shirikishi wakati wa mitaala inapotengenezwa tunawashirikisha upande wa Zanzibar na vilevile hata katika Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania kunakuwa na uwakilishi wa Wajumbe wa kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu wa usambazaji wa vitabu ili vifike Zanzibar kwa wakati, utaratibu ni kama unavyotumika Bara kwamba kwanza zoezi ni shirikishi la vinapokuwa tayari Wizarra ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar huwa inafanya hilo jukumu.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri niliyopewa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya kutoa elimu ili fedha zitakazotolewa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa taasisi nyingi za fedha zimeonekana zinatoa mikopo kwa wanawake na vijana, Serikali imejipanga vipi katika kuinua uchumi au kuwawezesha kiuchumi wazee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa wajasiriamali wote hasa ukizingatia kwamba moja ya changamoto zilizopo kwa Mifuko ya mwanzo ilikuwa ni elimu ya ujasiriamali. Kwa hiyo, hilo tayari limeangaliwa na Serikali imejipanga vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wazee, bado Serikali inaangalia changamoto mbalimbali na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia kwa mfano namna ya kurasimisha pensheni ya wazee, lakini suala hili linafanyiwa kazi na pale litakapokamilika basi taarifa rasmi itatolewa na ikibidi sheria rasmi itatungwa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
La kwanza, kumekuwa na utaratibu wa Watanzania wanaofariki nje ya nchi, ndugu zao wanaokuwepo hapa nchini hupata taabu, adha na kucheleweshwa kuletewa maiti. Inafikia familia za kimaskini zinauza hata vitu vyake ili kuweza kuleta ile maiti nchini. Je, ofisi za Ubalozi zimejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wenye hali duni maiti zao zinapopatikana kule ziletwe nchini haraka? (Makofi)
Swali la pili, kuna baadhi ya Balozi zina utaratibu wa kupanga siku maalum za kuwahudumia Watanzania, hususan tabia hiyo ilikuwepo katika Ubalozi wetu wa Afrika Kusini. Tabia ile ilileta matatizo na usumbufu kwa Watanzania ambao wanataka huduma katika ofisi za Ubalozi.
Je, sasa hivi wamejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wanaotaka huduma kwenye Balozi zao nje ya nchi yetu wanapata huduma haraka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa nyakati tofauti kumeripotiwa baadhi ya Watanzania ambao wamefiwa na ndugu zao kupata taabu katika kusafirisha miili, lakini katika hali ya jumla Balozi zimekuwa zikisaidia sana pale wanapopata taarifa sahihi kwa wakati. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwamba mara nyingine ucheleweshaji unatokea kutokana na Balozi zetu kuweza kupata taarifa kwa wakati, lakini katika hali ya jumla, kati ya masuala ambayo Balozi wetu zinatakiwa zishughulikie ni kuhusu maslahi ya Watanzania wanaoishi huko ikiwa ni pamoja na pale wanapopata taabu, wanapopatwa na matatizo ikiwa ni pamoja na kifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna changamoto ambazo zimetokea, kila wakati Wizara imekuwa ikichukua changamoto hizo na kuzifanyia. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakoelekea, changomoto hizi zitaendelea kupungua na hasa sasa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejikita katika kuleta ufanisi na nidhamu katika utumishi wa umma. Kwa hiyo, tunaamini upungufu na changamoto ambazo zimekuwa zikitokea nyuma, zitapungua kama siyo kuondoka moja kwa moja.
Ni rai ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu Balozi zetu kupanga siku maalum kwa ajili ya kuwatumikia na kutoa huduma kwa Watanzania, pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri, Wizara italiangalia, lakini ifahamike kwamba hakujaripotiwa kwa kiwango kikubwa kuhusu Watanzania kushindwa kupata huduma za kibalozi, lakini kama nilivyosema tutalipeleka na kuliangalia na iwe ni moja kati ya njia za kususluhisha changamoto ambazo zinatokea.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa utaratibu aliousema ulishawahi kufanyika katika wilaya mbalimbali hapa nchini na baadaye tukaambiwa utaratibu huo umesitishwa, je, ni lini zoezi hilo litaanza tena ili vijana waweze kujiunga na Jeshi?
Mheshimiwa Spika, pili, ni nini kauli ya Serikali juu ya ajira ya Jeshi kwa vijana wenye maadili mema na uwezo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Tanzania kwa ujumla?Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, utaratibu niliousema haujasitishwa, bado utaratibu huu unatumika, kila mwaka tunachukua vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia katika wilaya na mikoa yao. Kwa hiyo, utaratibu huo bado unatumika. Mwaka huu tumefanya zoezi hilo mwezi Desemba na tunategemea tutakapopata fedha baada ya bajeti basi awamu inayofuata utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana anaowazungumzia Mheshimiwa Malembeka, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, ni kwamba tutakapotangaza tena kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, nitawaomba vijana hao waombe kupata nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa na ajira kwenda Jeshi la Wananchi zinapitia katika Jeshi la Kujenga Taifa. Si Jeshi la Wananchi peke yake, kwa sasa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeamua kwa makusudi kwamba ajira zao zipitie JKT. Kwa hiyo Polisi, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Jeshi lenyewe la Wananchi wa Tanzania wote wanachukua vijana waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hiyo nitawaomba wajiunge huko ili hatimaye waweze kupata ajira hizo.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Angelina mwenzangu, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa naibu Waziri amekiri kuwa wananchi wanavamia na kuyamega maeneo ya Serikali kinyume na utaratibu; na kwa kuwa ametoa rai wananchi waondoke maeneo hayo kabla sheria haijachukua mkondo wake, sasa isije ikawa kwa wananchi kilio, kwa watendaji vigelegele.
Je, Serikali ina kauli gani juu ya watendaji ambao wanalipwa mshahara kwa kazi ya upimaji na katika maeneo yao hawajafanya lolote hadi sasa?
Swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya msingi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema gharama elekezi za huduma ya upimaji siyo kubwa kama inavyoonekana au inavyodhaniwa.
Je, kwa nini gharama hizo zisiwekwe wazi ili wananchi na taasisi nyingine wafahamu na kuzitambua na waweze kujipanga kwa ajili ya kulipia? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza ameulizia habari ya adhabu kwa watendaji ambao wanafanya makosa na tunaadhibu pengine wananchi. Kama nilivyomjibu muulizaji wa swali namba 44 majukumu na uwajibishaji yako chini ya mamlaka husika hasa katika maeneo yetu kwenye Halmashauri za Wilaya. Kwa hiyo, haya yanapobainika basi tuyachukulie hatua papo hapo ili tusiweze kuwafanya wananchi waumie zaidi kwa makosa ya watendaji wetu.
Swali la pili, ametaka kuewekewa gharama za upimaji wazi. Naomba niseme tu tutazitoa na tutawagawia Waheshimiwa Wabunge wote, lakini kwa kifupi tu nikianza kuzungumzia habari ya miji kwenye Mamlaka za Miji na Manispaa katika gharama za upimaji kuanzia square meter moja mpaka square meter 400 gharama yake kwa maeneo ya residential ni shilingi 65 lakini maeneo ya commercial ni shilingi 350 kwa square meter, kwenye industrial ni shilingi 450 na kwenye maeneo ya social services ni shilingi 150. Kwa miji yetu ya kwaida kwenye township ni shilingi 200 kwa makazi, maeneo ya biashara ni shilingi 300, maeneo ya viwanda 350 na maeneo ya services ni shilingi 100. Vivyo hivyo kwenye trading center ni shilingi 100 kwa makazi, shilingi 200 kwa commercial, shilingi 200 tena kwa industrial na shilingi 100 kwa services. Kwa sababu mlolongo pia unategemeana na ukubwa wa kiwanja vina-range kuanzia shilingi 300,000 mpaka milioni 14 kutegemeana na ukubwa kuanzia hekari moja mpaka 10 ni shilingi milioni tatu, zinakwenda zinaongezeka kadri ya ukubwa, tutaziandaa na tutawasambazia Waheshimiwa Wabunge wote.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la kutelekezwa kwa watoto ni jambo ambalo wanawake/ Wabunge hatuwezi kulifumbia macho; ili kupata uhakika na ukweli kuhusu watoto wanaotelekezwa na Waheshimiwa Wabunge wanaume, kwa nini tusifungue Kituo cha Ustawi wa Jamii hapa ili kuweka mambo sawa? Ahsante. (Kicheko/ Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana suala la utelekezaji wa watoto hapa Bungeni ni changamoto kubwa sana. Naomba nirudie majibu yangu ya msingi kwamba sheria ya mtoto imeweka utaratibu mzuri tu wa kushughulikia mashauri ambayo yanahusu utelekezwaji ama watoto kutopata matunzo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza kwamba madawati yetu ya Halmashauri katika ngazi ya Halmashauri yatumike katika masuala haya.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, yenye data na yamenifurahisha. Pamoja na majibu hayo mazuri nina swali moja la nyongeza na ombi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais juu ya kujenga viwanda ili kutoa ajira, kujenga uchumi na kutumia malighafi za eneo husika lilizungumzwa bila ubaguzi wowote na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amesema jukumu la Serikali ni kuhamasisha na kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji na ujenzi ni jukumu la sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimekuwa nikisikia Wizara hiyo ikisema hapa na kupiga debe kuhusu ngozi, pamba, matunda, sukari, ndizi, mihogo hadi pilipili sijasikia hata siku moja Wizara hiyo ikizungumza kuhusu mchakato wa karafuu. Ni lini sasa Mheshimiwa Waziri ataanza kuweka hamasa ya kasi ili Zanzibar tupate kiwanda cha kuchakata karafuu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu sasa, kwa kuwa suala la viwanda ni la nchi nzima bila kujali suala la Muungano na kuna vitu ambavyo vimefanyika Zanzibar bila kujali suala la Muungano nikitolea mfano wa barabara iliyojengwa round about ya Amani hadi Mtoni ambayo ilijengwa kwa fedha ya Muungano na kupewa jina la Mkapa Road, kwa nafasi hii kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja naomba tujengewe kiwanda cha karafuu Zanzibar ili vijana wetu wapate ajira. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge lile la kwanza ambalo litajibu na namba mbili, kuhamasisha uchumi wa viwanda nchi nzima ni jukumu la Wizara yangu na nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge twende Zanzibar niweze kuhamasisha kwa nguvu ileile ambapo nimeanzia sehemu nyingine. Katika utaratibu huo nitawahasisha wawekezaji ambao najua wapo kusudi tu- take advantage ya karafuu, mwani na michaichai kusudi tu- take advantage ya viungo hivi na manukato. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na pia namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amekiri kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na msingi vinavyotumika upande wa Zanzibar ni tofauti na vya Bara.
Je, haoni kuwa kitendo hicho kinafifisha na kudhoofisha uwezo wa wanafunzi ambao wanaanza mitaala mipya badala ya kuendeleza ile waliyokuwa nayo na kusababisha wanafunzi kutoka Zanzibar kutofaulu vizuri mitihani yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar huendesha mitihani ya elimu ya awali na msingi Zanzibar, na kwa kuwa Baraza la Mitihani Zanzibar lipo, Serikali haioni kuwa ni wakati muhimu sasa iruhusu mitihani ya kidato cha nne na cha sita ikatungwa na kusahihishwa na Baraza la Mitihani la Zanzibar na kupewa hadhi sawa ya Kitaifa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, kwa kuwa vitabu katika eneo hili la mafunzo katika elimu ya awali na msingi vimekuwa vikitungwa upande wa Zanzibar, basi kwa kushirikiana imeonekana kwamba ni vyema wao wenyewe kuendelea kutunga hiyo mitihani. Hata hivyo tuelewe kwamba suala la Baraza la Mitihani ni suala ambalo lipo katika mambo ya Muungano katika jedwali la kwanza namba 16.
Kwa hiyo, kwa misingi hiyo pale inapotokea kwamba kuna haja ya kufanya marekebisho ina maana ni suala la Kikatiba ambalo inabidi kufuata taratibu za Kikatiba katika kupata marekebisho kama hayo. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ninampongeza na ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake zuri ambalo limeleta uelewa na kuonesha nia ya kukufua ranchi zetu. Nilikuwa na maswali mawili ya ziada kama ifuatavyo:-

(i) Kwa kuwa katika maelezo yake amesema lengo kubwa ilikuwa ni kutoa mifugo bora kwa ajili ya nyama ndani ya nchi na kuuza nje ya nchi, na kwa kuwa Zanzibar inategemea kitoweo cha nyama kutoka Tanzania Bara, je,
Serikali ina mpango gani kupeleka nyama Zanzibar kwa utaratibu maalum?

(ii) Kwa kuwa Ranchi ya Ruvu likuwa inajengwa machinjio kubwa ya kisasa lakini mpaka sasa hvi imesimama na haijulikani itakamalika lini. Serikali ina kauli gani juu ya Ranchi hiyo ya Ruvu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya upelekaji wa kitoweo cha nyama ya ng’ombe Zanzibar hivi sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya biashara ya kuchukua nyama ya ng’ombe na kupeleka Zanzibar na ziko kweli changamoto kadha wa kadha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mara changamoto tulizonazo huwa tunazifanyia kazi ya kuhakikisha tunazitatua na hatimaye kuweza kuwasaidia wenzetu kuweza kupata kitoweo cha nyama ng’ombe, mbuzi kwa uhakika na hilo tutaendelea kulifanya kadri litakavyokuwa likiibuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, juu ya machinjio ya Ruvu. Tupo kwenye mkakati mzuri wa kuhakikisha machinjio ya Ruvu inajengwa. Hivi sasa tumeshafanikisha kuona juu ya athari ya mazingira na hatua zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati tulionao ni kutafuta pesa ya kuhakikisha kuwa mradi ule unakamilika na kuwaweza kuwasidia Watanzania kupata nyama ya uhakika, lakini vilevile kuweza ku-export nje ya nchi na hata kutengeneza vitu vingine kama vile mazao yanayotokana na ngozi za ng’ombe wetu.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri na kumpa pongezi kwa majibu yake ambayo yanaonyesha nia ya dhati ya Serikali kuwasaidia wafungwa wanawake. Maswali yangu mawili yanyongeza ni kama ifuatavyo:-

(a) Je, Serikali inawasaidiaje watoto ambao wapo gerezani na mama zao kielimu na kisaikolojia kwa kuzingatia haki za watoto husasan wanapotumikia kifungo hicho ambacho watoto wao hawahusiki nacho?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa wanawake wafungwa ambao ni wajawazito wakatumikie kifungo hicho nje ili waweze kuwalea watoto wao katika familia huru badala ya kuwa gerezani?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kwa jina maarufu Nyoka wa Kijani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo akina mama wafungwa ambao wanajifungua watoto wakiwa magerezani. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Nyoka wa Kijani, Nyara ya CCM kwamba utaratibu wa Jeshi la Magereza kupitia kanuni za Jeshi la Magereza watoto ambao wamekwishazaliwa magerezani wanpofikia umri wa kuanza awali wamekuwa wakisoma kwenye shule za awali zilizopo kwenye magereza zetu. Pia kwa kupitia watumishi wa magereza ambao wana utaalamu wa masuala ustawi wa jamii wamekuwa wakiwapa elimu pamoja na kuwafariji watoto hawa ili wajione wao siyo wafungwa ndani ya magereza isipokuwa wamezaliwa katika wakati ambao mama zao wapo magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba kwa nini wafungwa ambao wanajifungua magerezani wasipate adhabu nyingine badala ya kuwafunga magerezani. Tunao utaratibu kupitia sheria yetu ambayo inaitwa Probation for Offenders pamoja na Community Services, wale ambao wana vifungo chini ya miaka mitatu tumekuwa tukiandaa utaratibu wa kuwaondoa magerezani ili wawe na vifungo mbadala. Hata hivyo, kuna utaratibu watoto wanaokuwa magerezani wanapofikia umri ambao wanaweza wakaishi uraiani bila kuwa na mama zao ndugu zao wamekuwa wakishirikishwa ili waweze kutoa malezi kwa watoto ambao mama zao wapo magerezani. Ahsante sana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonesha kabisa Serikali ina nia nzuri ya kusaidia wananchi wake. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja nilikuwa nina maswali mawili ya kuongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilitaka kujua: Je, huduma ya uokoaji na kuzima moto kuna gharama zozote ambazo mhudumiwa anatakiwa alipe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili: Je, kama gharama hizo zipo, ni utaratibu gani unatakiwa ufanywe ili aliyepatiwa huduma aweze kulipa bila kuwa na taharuki? Maana kipindi kile anakuwa amechanganyikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Malembeka kwa kazi nzuri ambayo anayoifanya katika Mkoa wake wa Kaskazini. Kwa kweli anawatendea haki wapiga kura wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nikijibu maswali yake pamoja, kwanza huduma za kuzima moto ni za bure, hakuna gharama. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Uokoaji na Zimamoto ya mwaka 2007 Sura ya 427, inaeleza kwamba Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lina Mamlaka ya kuweza kutoa leseni kwa makampuni binafsi kutoa huduma hizo ikiwemo huduma ya kuzima moto pamoja na vifaa.

Mheshimia Naibu Spika, kwa hiyo, makampuni haya ndiyo ambayo yanaingia mikataba na Taasisi binafsi na ndiyo yanakubaliana malipo, lakini kwa maana ya huduma hizi za zimamoto ni bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu ambao unatumika, unapiga namba 114 na kikosi chetu kinafika pale haraka iwezekanavyo kutoa huduma hizo bila malipo yoyote. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake japo hayajaniridhisha kwa sababu swali langu la msingi nilihitaji kujua ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wamepata ajira katika jeshi kwa miaka mitatu, lakini amenipa jibu la jumla la Zanzibar yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka kujua ni lini vijana wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watapata ajira katika jeshi ili kuondoa malalamiko yaliyopo hivi sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa manug’uniko ni mengi yanayotokana na vijana kujitolea kwa muda mrefu lakini hawapati ajira. Ni mkakati gani ambao Serikali umeupanga ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira hiyo kwa kuzingatia pia jinsia maana hapa katika orodha yake inaonyesha wanaume 720 wanawake 280?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza anasema sikumpa takwimu za ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na B waliojiunga na JKT. Katika jibu langu la msingi nilitoa takwimu za jumla za vijana wanaochukuliwa kutoka Zanzibar na nikaeleza kwamba jukumu la kupanga idadi kwa Wilaya za Zanzibar linafanywa na SMZ. Kwa hivyo takwimu sina na Mheshimiwa akizihitaji itabidi azipate kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu wao ndiyo wanapanga kwa mujibu wanavyoamua, sisi tunakabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wao wanagawa wanavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika hilo hilo la kwanza alikuwa anauliza lini vijana watapata ajira ili kuondoa malalamiko. Nataka ieleweke kwamba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa lazima vijana waelewe kwamba siyo ajira, kujiunga na JKT ni kwenda kupata mafunzo ya kijeshi pamoja na study za kazi. Wachache watapata ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, walio wengi watabidi wajiajiri wenyewe au waajiriwe na sekta binafsi. Hili ni muhimu lieleweke, wasielewe kwamba kujiunga na JKT ndiyo ajira. Tunachukua vijana wengi na nilitoa takwimu hapa wakati wa bajeti yangu kwamba tunachukua takribani vijana 20,000 kwa mwaka. Vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa ku-observe kuchukua wote hao katika ajira, watapata wachache na walio wengi watakuwa wamepata study za kazi ili waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni mkakati gani wa kupatia ajira na kwa kuzingatia jinsia, hawa tuliowataja ni vijana wanaojiunga na JKT na siyo ajira. Kwa maana hiyo kule wanapofanya usaili kuna vigezo ambavyo vinafuatwa, mara nyingi wasichana hawajitokezi kwa wingi lakini wanaojitokeza wengine wanakosa sifa zinazotakiwa na ndiyo maana unaona kuna tofauti ya idadi hapa. Kwa hiyo, mkakati uliopo ni kuwasaidia vijana hawa, wale wanaokosa ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kuwapa study za kazi ili waweze kuajiriwa na sekta nyingine pamoja na kujiajiri wao wenyewe.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa
Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ina mpango wa kununua meli nane kubwa za uvuvi, ambapo nne zitaenda Zanzibar na nne zitakuwa Tanzania Bara. Je, ni lini meli hizo zitanunuliwa ili zianze kutoa ajira na kutoa huduma kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lake la kwanza ameelezea hiyo ujenzi wa bandari ya uvuvi, ningependa kujua je, upande wa pili wa Muungano utashirikishwa vipi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, ununuzi wa meli nane ambazo zimesemwa katika ahadi yetu ya Serikali ununuzi huu utaanza hivi karibuni kwa kuwa Serikali sasa iko katika mazungumzo na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, maelezo na mazungumzo hayo yanaendelea, yakishafanyika Wizara ya Fedha sasa itaingia makubaliano na mfuko huu ili ununuzi uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge alihitaji kufahamu kazi hii ya ujenzi wa bandari ambayo inaendelea kwa upande wa Bara na upande wa Zanzibar nini kinaendelea.

Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba mazungumzo haya yanapoendelea kwa upande wa Bara pia upande wa Zanzibar wameanza mazungumzo na nchi ya Comoro na bandari ya Zanzibar pia itaanza kujengwa na ikijengwa maana yake ajira hizi sasa zitatolewa kwa pande zote.