Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anastazia James Wambura (12 total)

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza:-

Je, ni kwa kiasi gani eneo la EPZ lililotengwa na Mamlaka ya Bandari Mkoani Mtwara kwa ajili ya uwekezaji limetumika kwa shughuli iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ujenzi wa Bandari Huru ya Mtwara (Mtwara Free Port Zone) unahusu ujenzi wa sehemu maalum ya Bandari yenye gati na sehemu ya ugavi kwa ajili ya kuhudumia Sekta za Mafuta na Gesi. Madhumuni ya kuanzishwa kwa Eneo la Uwekezaji katika eneo la Bandari Huru ya Mtwara ilitokana na hitaji la makampuni yanayotoa huduma kwa Makampuni yanayofanya shughuli za utafutaji wa Gesi na Mafuta katika mwambao mwa Pwani ya Nchi za Tanzania, Kenya na Msumbiji ambayo yalikuwa yanahitaji kuwa na kituo cha ugavi (supply base) karibu na Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, Eneo la Mradi wa Uwekezaji lenye ukubwa wa jumla ya hekta 110 katika Bandari Huru ya Mtwara (Mtwara Free Port Zone) linaendelezwa kwa awamu. Katika awamu ya kwanza, eneo la ukubwa wa hekta 10 limeendelezwa kwa asilimia mia moja kama ilivyopangwa. Shughuli za utekelezaji wa mradi huo zimehusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ndani na nje (offsite and onsite infrastructure) ikiwemo barabara kwa kiwango cha lami, umeme na mfumo wa usambazaji wa majisafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uendelezaji wa miundombinu katika eneo hilo kukamilika kwa asilimia mia moja (100%), kwa sasa shughuli za uwekezaji katika eneo hilo zinaendelea vema na makampuni matatu (3) yanafanya shughuli hizo za uwekezaji.
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza:-

(a) Je, nini sababu ya barabara ya Kibiti – Lindi kuharibika mara kwa mara licha ya kufanyiwa ukarabati?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatiza hilo ili kuzuia ajali za mara kwa mara katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibiti – Lindi kwa sasa inabeba magari mengi na yenye uzito mkubwa zaidi ya ilivyokusudiwa wakati wa usanifu uliotumika kujenga barabara hiyo. Hali hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa wa viwanda na migodi katika Mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini uliojitokeza miaka ya hivi karibuni baada ya ujenzi wa barabara hii kukamilika. Aidha, ujenzi wa viwanda vikubwa kama cha Dangote, Mkoani Mtwara na uwepo wa migodi mikubwa ya Makaa ya Mawe, Mkoani Ruvuma kumechangia ongezeko la magari yanayobeba uzito mkubwa kuliko ilivyotarajiwa wakati barabara hii inafanyiwa usanifu.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo kwa sasa, Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati mkubwa utakaowezesha barabara hiyo kustahimili wingi na uzito wa magari kwenye barabara hii. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 7,500 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Aidha, pamoja na juhudi za Serikali zinazoendelea, ninaomba nitoe wito kwa wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara ambayo upanuzi wake umekamilika na hivyo kuwa na uwezo wa kupokea meli nyingi na kubwa kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, kutumia bandari hii ya Mtwara itasaidia sana kupunguza usafirishaji wa mizigo mikubwa kwa njia ya barabara na hivyo kunusuru barabara hiyo kuharibika mara kwa mara.
MHE. ESTHER N. MATIKO K.n.y. MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza:-

(a) Je, nini sababu ya barabara ya Kibiti – Lindi kuharibika mara kwa mara licha ya kufanyiwa ukarabati?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatiza hilo ili kuzuia ajali za mara kwa mara katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na
(b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibiti – Lindi kwa sasa inabeba magari mengi na yenye uzito mkubwa zaidi ya ilivyokusudiwa wakati wa usanifu uliotumika kujenga barabara hiyo. Hali hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa wa viwanda na migodi katika Mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini uliojitokeza miaka ya hivi karibuni baada ya ujenzi wa barabara hii kukamilika.

Aidha, ujenzi wa viwanda vikubwa kama cha Dangote, Mkoani Mtwara na uwepo wa migodi mikubwa ya Makaa ya Mawe, Mkoani Ruvuma kumechangia ongezeko la magari yanayobeba uzito mkubwa kuliko ilivyotarajiwa wakati barabara hii inafanyiwa usanifu.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo kwa sasa, Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati mkubwa utakaowezesha barabara hiyo kustahimili wingi na uzito wa magari kwenye barabara hii. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 7,500 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Aidha, pamoja na juhudi za Serikali zinazoendelea, ninaomba nitoe wito kwa wasafirishaji kutumia Bandari ya Mtwara ambayo upanuzi wake umekamilika na hivyo kuwa na uwezo wa kupokea meli nyingi na kubwa kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, kutumia bandari hii ya Mtwara itasaidia sana kupunguza usafirishaji wa mizigo mikubwa kwa njia ya barabara na hivyo kunusuru barabara hiyo kuharibika mara kwa mara.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa shule za sekondari utaanza katika kata zisizo na shule za sekondari nchini ili kuendana na mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari itajenga shule mpya 1,000 za sekondari za kutwa nchini kwa kuanza na ujenzi wa shule za sekondari kwenye Kata zote ambazo hazina shule za sekondari. Mradi huo unatakelezwa kwa awamu, na katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 220 kujenga shule 310 mpya za sekondari za kutwa nchini.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani suala la kuwapatia wazee wasiojiweza vitambulisho kwa ajili ya kupata matibabu bure limetekelezwa kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge, kwa swali lake zuri na kwa mapenzi yake kwa wazee wetu ambapo nasi ni wazee watarajiwa; kwamba wanaendeleaje hawa wazee wasiojiweza kupata vitambulisho vya kupata matibabu bure, limetekelezwaje.

Mheshimiwa Spika, naomba kulijibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, zoezi la kuwatambua wazee na kuwapatia vitambulisho linaendeshwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zote hapa nchini. Hadi kufikia Desemba, 2020 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asilimia 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake ni 1,252,437. Aidha, wazee wasio na uwezo 1,087,008 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu za Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF).

Mheshimiwa Spika, vilevile, katika kuhakikisha kuwa makundi yote ikiwemo wazee wanapata huduma bila kuwa na kikwazo cha ugharamiaji, Serikali ipo kwenye hatua ya kuandaa Muswada wa Bima kwa wote utakaowasilishwa kwenye Bunge lako Tukufu ili kuundiwa sheria. Tunatarajia kwa hapa tulipofikia ni Novemba. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itajenga air traffic control tower yenye urefu wa kutosha kumuwezesha muongoza ndege kuona miundombinu yote ya runway, taxiways na maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara?

(b) Je ni lini Serikali itajenga jengo la muda la abiria lenye ukubwa wa kutosha wingi wa abiria wanaoingia na kutoka katika uwanja huo?

(c) Je, ni lini parking shade ya mitambo ya zimamoto na uokoaji itajengwa katika eneo lililopangwa kwenye master plan?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mhe. Anastazia James Wambura wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kilijengwa na kuanza kutoa huduma katika mwaka 1952/1953. Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya kiwanja hiki yanayotokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Mikoa ya Kusini, Kiwanja hiki kilihitaji kufanyiwa maboresho makubwa. Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), iliandaa Mpango Kabambe (Master Plan) uliopendekeza kupanua kiwanja hiki kutoka daraja Code 3C kwenda Code 4E (kwa mujibu wa ICAO). Kiwanja kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za ndani na nje ya nchi zenye ukubwa wa Boeing 787-8 (Dreamliner).

Mheshimiwa Spika, Uboreshaji wa Kiwanja hiki umegawanywa katika awamu mbili, ambapo kwa sasa ujenzi unaoendelea ni wa awamu ya kwanza unaohusisha baadhi ya kazi zikiwemo urefushaji wa njia ya kuruka na kutua ndege (runway), ujenzi wa maegesho mapya ya ndege (Apron) na barabara zake za maingilio (taxiway).

Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege (Air Traffic Control Tower), Jengo la abiria (Airport Terminal Building) na kivuli kwa ajili ya maegesho ya mitambo ya zimamoto (Fire Fighting Equipment Shade) vitajengwa katika awamu ya pili mara baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini wastaafu ambao waajiri wao walikuwa hawatoi michango katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii watalipwa haki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mafao ya pensheni hulipwa kwa mstaafu kwa kuzingatia kipindi kilicholipiwa michango yake. Kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya watumishi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati. Kutokana na changamoto hiyo, mifuko imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapeleka Mahakamani waajiri ambao hawawasilishi michango kwa wakati ili kuwezesha wastaafu hao kupata haki yao.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa na mifuko kukabiliana na changamoto hii ni pamoja na kutoa elimu kwa waajiri, kutengeneza namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) kupitia Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG) na kupunguza tozo zinazotokana na ucheleweshwaji wa michango hiyo. Aidha, mifuko imeingia makubaliano maalum na waajiri 63 ya namna ya kulipa madeni yao.

Mheshimiwa Spika, waajiri ambao wameendelea kukaidi kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati, Mfuko kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General) imechukua hatua ya kuwapeleka Mahakamani kwa mujibu wa sheria. Aidha, waajiri 123 tayari wamefikishwa Mahakamani, ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru wananchi wa Manispaa ya Mtwara dhidi ya vumbi la makaa ya mawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshachukua jitihada za kuweka miundombinu ya kupunguza vumbi la makaa ya mawe ili kuwanusuru wananchi. Tayari Mamlaka ya Bandari Tanzania imefunga mfumo maalum wa dust suppression system unaotumia maji kupunguza vumbi. Pia, limetengwa eneo maalum kwa ajili ya kujenga conveyor belt itakayotumika kupakia makaa ya mawe katika meli. Aidha limetengwa eneo maalum nje ya mji takribani kilometa 34 katika Kijiji cha Kisiwa Mgwao kutoka Mtwara Mjini kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya namna hiyo. Hatua hii itasaidia kupunguza, kusambaa kwa vumbi katika mazingira.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NEMC, kwa kushirikiana na Manispaa ya Mtwara na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwa pamoja tunaendelea kufuatilia na kusimamia usafirishaji wa uhifadhi wa mazingira katika maeneo hayo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Mangopacha Nne ili kuwanusuru Akina Mama na tatizo la ukosefu wa huduma wakati wa kujifungua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha Shilingi bilioni 86 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 234 kwenye kata za kimkakati kote nchini. Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara imepokea Shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Mkunwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya kutolea huduma za afya kwenye kata za kimkakati zenye uhitaji mkubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kata ya Mango Pacha Nne.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni shule ngapi za sekondari zimejengwa katika Mkoa wa Mtwara ambao una zaidi ya kata 50 ambazo hazina shule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari imejenga shule 231 za kata na shule 10 za wasichana za kitaifa katika mikoa 10. Hii ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari.

Mheshimiwa Spika, katika awamu hii ya kwanza Mkoa wa Mtwara umeshajengewa shule 10 za kata katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi na kata ambazo zilikuwa hazina shule.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini Shule ya Sekondari Mkalapa itatambuliwa kuwa shule ya vipaji vya michezo ya mpira wa wavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea ombi la Mheshimiwa Mbunge la kutambua shule ya Sekondari Mkalapa kuwa shule ya vipaji vya mchezo wa wavu.

Nielekeze wataalam wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kutembelea shule hiyo ili kuona miundombinu iliyopo na namna shughuli za michezo zinazofanyika shuleni hapo ili kuona kama inakidhi vigezo vinavyotakiwa.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni kiasi gani Halmashauri zinahakikisha 30% ya fedha za manunuzi zinakwenda kwenye kampuni za wanawake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 inaekeleza taasisi nunuzi zote kutenga asilimia 30 ya bajeti inayotengwa katika manunuzi kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni makundi ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia Mei, 2022 jumla ya Halmashauri 24 kati ya 184 zimekwishavitambua na kuwezesha usajili wa vikundi 88 katika Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA) ikiwa ni kigezo cha lazima cha kisheria cha kuwezesha kundi hilo maalum kupata zabuni za ununuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzielekeza Halmashauri zote nchini kuhamasisha vikundi kujisajili na kutenga kiwango cha asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa vikundi hivyo vikiwemo vikundi vya wanawake. (Makofi)