Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amina Saleh Athuman Mollel (46 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tena katika Bunge hili la bajeti.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako wewe kwa kuondokewa na mwenzetu Mheshimiwa Dkt. Elly Macha lakini vile vile nitoe pole kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Wabunge wote.
Mheshimiwa Spika, kwetu sisi kama Wawakilishi wa Watu Wenye Ulemavu ni pigo kubwa kwa sababu ni miongoni mwa mwenzetu ambaye tulikuwa tukitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba yale masuala ya watu wenye ulemavu basi yanazungumzwa hapa Bungeni. Nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge pamoja na viongozi na Mawaziri kuhakikisha kwamba tunamuenzi Dkt. Elly Macha kwa kuyatimiza yale aliyokuwa akiyapigania humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nichukue nafasi hii kwa kuipongeza Serikali pamoja na Mawaziri wote.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tena katika Bunge hili la bajeti.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako wewe kwa kuondokewa na mwenzetu Mheshimiwa Dkt. Elly Macha lakini vile vile nitoe pole kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Wabunge wote.
Mheshimiwa Spika, kwetu sisi kama Wawakilishi wa Watu Wenye Ulemavu ni pigo kubwa kwa sababu ni miongoni mwa mwenzetu ambaye tulikuwa tukitoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba yale masuala ya watu wenye ulemavu basi yanazungumzwa hapa Bungeni. Nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge pamoja na viongozi na Mawaziri kuhakikisha kwamba tunamuenzi Dkt. Elly Macha kwa kuyatimiza yale aliyokuwa akiyapigania humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nichukue nafasi hii kwa kuipongeza Serikali pamoja na Mawaziri wote. kwa kazi kubwa wanayofanya kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano. Pia natoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa kutambua na kuthamini mchango wa Watu Wenye Ulemavu na kuchukua uamuzi wa kuwapa nafasi katika nyanja mbalimbali na hii inaonesha kwamba kuwa na
ulemavu siyo kulemaa. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nijikite tu kwa kutoa ushauri kwa Serikali na hasa nianze kwa suala zima la elimu. Napenda kuishauri Serikali kwamba kwa sababu Serikali imetoa elimu bure kwa elimu ya msingi mpaka sekondari; na hii imekuwa ni faraja kwa sababu miongoni mwa watu ambao
walinyimwa elimu kutokana na mila na tamaduni za jamii za kiafrika na hasa sisi wenyewe. Mfano mzuri tu, hata katika jamii ninayotoka. Kwa
maana hiyo basi, mpango huu wa elimu bure, umesaidia sana kuhakikisha kwamba jamii inawapeleka watoto wenye ulemavu kupata elimu. Katika shule mbalimbali hivi sasa watoto wenye ulemavu wengi wanatambua na wanapata elimu. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hilo.
Mheshimiwa Spika, naishauri pia Serikali kuhakikisha kwamba inatimiza wajibu wake kwa kupeleka fedha kwa wakati unaotakiwa ili kuepusha usumbufu na kuhakikisha kwamba hata ile mianya yote ambayo wamekuwa wakitumia baadhi ya watu wasio waadilifu wanaosababisha
fedha hizi kupotea katika njia zisizoeleweka, basi Serikali iwabane na kuweza kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Spika, naungana na Serikali na naipongeza pia kwa kutambua haki ya msingi ya kikatiba kwa Watu Wenye Ulemavu kupata haki ya msingi ya kupata taarifa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza dhahiri kwamba Serikali imevitaka vyombo vya habari vihakikishe kwamba vinaajiri Wakalimani ili wenzetu nao waweze kupata taarifa.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali na naviomba tu vyombo vya habari kuhakikisha kwamba vinatimiza agizo hili la Serikali kuhakikisha kwamba linaajiri. Namwomba Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa George Mwakyembe, ahakikishe kwamba vyombo vya habari vinatimiza wajibu kuajiri wakalimani ili basi viziwi nao waweze kupata taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuishauri Serikali katika Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu; katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mfuko wa watu wenye ulemavu haukutengewa fedha.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, hii ni haki ambayo nchi imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu na nchi yetu imeridhia mkataba huo ambao baada ya kuridhia ni kuhakikisha zile haki za watu wenye ulemavu zinatimizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mfuko huu katika bajeti iliyopita inayoishia katika Bunge hili haukuweza kutengewa fedha, kwa hiyo, naishauri tu Serikali kuhakikisha kwamba mwaka huu fedha hizo zinafanya kazi, kwa sababu mfuko huu utakapotengewa fedha ni kwamba Baraza la Watu
wenye Ulemavu litaweza kufanya kazi na litakuwa ni msaada mkubwa katika kuishauri Serikali katika nyanja mbalimbali na hasa masuala mbalimbali yanayowahusu Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano ina nia ya dhati kabisa katika kuhakikisha kwamba inashughulika na masuala ya watu wenye ulemavu, kwa hiyo, nisisitize tu kwa kusema kwamba, hili ni jambo jema, lakini tuhakikishe kwamba linaendana na fedha ili basi Baraza hili liweze kufanya kazi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeelezea ni jinsi gani basi ambavyo inatambua na itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu. Pamoja na kauli hii, kumekuwa na
changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali imekuwa na utaratibu mzuri tu kwa watoto wasioona, zipo shule maalum ambazo zimetengwa na shule hizo wamekuwa wakienda hawa watoto kupata elimu na wamekuwa wakilipiwa gharama mbalimbali na hasa nauli kwa sababu jamii
haitambui mchango wa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwapa nauli na kuwapeleka katika shule zilizotengwa. Mfano Shule ya Uhuru Mchanganyiko, lakini kuna shule nyingine ipo Iringa.
Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo hivi sasa wale watoto wanapokwenda na inapofika wakati wa likizo hawawezi kwenda nyumbani na matokeo yake wanabaki mwaka mzima huko huko. Kwa sababu wazazi wengi hawatambui hilo na tayari walikuwa wamezoeshwa hivyo, kwa hiyo, wale
watoto wanakuwa hawana tena nafasi ya kurudi majumbani.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ije na majibu kwamba je, ni kweli wao ndio wametoa agizo hilo kwamba hakuna fedha kwa ajili ya watoto hawa au ni baadhi ya Walimu wa hizi shule ambao wamekuwa wakijichukulia madaraka wao wenyewe na kuamua maamuzi kwamba watoto hawa wasirudi nyumbani?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitamwomba sana Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha bajeti hii basi aweze kutoa hizo taarifa ili tuweze kujua ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia watoto hawa ili na wao pia waweze kupata elimu; na kama mnavyofahamu elimu ndio ufunguo wa
maisha.
Mheshimiwa Spika, unapomsaidia mtoto mwenye ulemavu akapata elimu, umemwokoa na mambo mengi. Mara nyingi nimekuwa nikitoa mfano kwamba sisi tusingesoma hizi nafasi hapa tusingeweza kupata. Kwa hiyo, ili tuweze kujikomboa sisi wenyewe elimu ndiyo msingi na
elimu ndiyo silaha yetu ili tuweze kujisaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, nisemee suala la Mahakama. Katika suala la Mahakama tuhakikishe tu kwamba zile kesi ambazo walikuwa wamehukumiwa wale watu au kesi ambazo zinaendelea katika Mahakama mbalimbali nipate tu takwimu ni wangapi wamehukumiwa? Wangapi ambao bado kesi zao zinaendelea? Vile vile tujue kama kumekuwa na taarifa nyingine za mauaji ya watu
wenye ulemavu wa ngozi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia mawili matatu katika hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunijalia afya njema lakini pia familia yangu, pamoja na wote wa UWT walioniwezesha kufika hapa.
Baada ya kusema hayo naomba nianze kwa kuchangia kwanza kabisa kwa kumpongeza Rais, kwa kuteuliwa kwake, lakini nimpongeze sana kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa sababu katika kipindi cha miezi mitatu siku 100 ndizo hizo ambazo hivi sasa zinaelekea kutimia, tumeona mengi ambayo ameweza kuyafanya kwa kipindi kufupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa kabisa kwa niaba ya watu wenye ulemavu kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada za kutambua kundi hili kuliwezesha katika sekta mbalimbali. Tumeshuhudia kwa mara ya kwanza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaye mwakilishi na vilevile masuala ya watu wenye ulemavu kuyahamishia katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Hiki kilikuwa ni kilio cha watu wenye ulemavu kwa kweli tunamshukuru sana kwa hili. Vilevile tunamshukuru sana kwa kutupa Mawaziri hawa na nina imani kabisa kama waswahili asemavyo uchungu wa mwana aujuae mzazi, ninaamini kabisa Mheshimiwa Jenista Mhagama atakuwa msaada mkubwa kwa kweli, kwetu sisi katika kundi hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja nianze kuchangia baada ya shukrani hizi kwa sababu ningekuwa mchoyo wa fadhila. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake aligusia masuala ya watu wenye ulemavu na kama nilivyosema awali ameanza kuonyesha kwa vitendo. Tunafahamu tunapozungumzia umasikini katika nchi hii watu wenye ulemavu ndilo kundi linaloongoza kwa umaskini, na hata unapokutana na watoto wenye ulemavu wengi wao pia wametoka katika familia maskini. Kwa hiyo, suala la elimu ni muhimu sana, kwa kundi hili, ukimuwezesha kupata elimu kwanza mtu huyu anaweza kujitegemea yeye mwenyewe, lakini pia hata unapomwezesha katika nyenzo mbalimbali inakuwa ni msaada mkubwa kwake yeye ili kuweza kujitafutia riziki kwake yeye, lakini pia katika familia yake kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa nchini Tanzania ni 4% tu ya watoto wenye ulemavu ndiyo wanaopata elimu, na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwamba amefanya elimu kuwa bure, tunaamini kabisa mojawapo ya vikwazo ambavyo wazazi wengi walikuwa wanaona taabu kuwapeleka watoto wao shule, kama ana watoto wawili mwenye ulemavu na asiye na ulemavu anaona ni afadhali ampeleke asiye na ulemavu na huyo mwenye ulemavu abaki nyumbani. Kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba hivi sasa wazazi wengi watawapeleka watoto wao shule ili waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali ichukue hatua kali, sheria ifuate mkondo kwa wale wazazi ambao mpaka hivi sasa bado wanawaficha watoto wenye ulemavu nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mzazi wangu angenificha mimi tusingekuwa na Amina hapa Bungeni, tusingekuwa na akina Mheshimiwa Ikupa, tusingekuwa na Waheshimiwa wengine wote kama wazazi wetu wangetuficha. Lakini walitambua thamani ya sisi ndiyo maana leo hii tuko hapa. Kwa hivyo, ninaamini kabisa kukiwepo na sheria ambayo itawabana wazazi wote wanaowaficha watoto wao majumbani na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupata elimu ninaamini kabisa watoto hawa wataweza kufika mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la elimu, hivi sasa elimu katika shule za msingi na sekondari ni bure, lakini tunafahamu kwamba wanafunzi wanaokwenda Vyuo Vikuu kuna mikopo. Hivi kuna utaratibu gani mzuri ambao unaandaliwa kwa wanafunzi hao wenye ulemavu ili waweze kupata elimu? Kwa sababu wengine hawapati hizo asilimia za mikopo. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu na ninaamini kabisa mwanzo mzuri tumekwisha uona, ianze kutoa ruzuku kwa wanafunzi wenye ulemavu, wanaokwenda Vyuo Vikuu, sekondari na hata form five na six, ili basi waweze kujikimu, lakini pia ule mzingo ambao wengine ni walemavu na familia zao ni masikini zaidi wataweza kwenda shule. Ombi langu ni hilo kwa Serikali.
Mheshimwia Naibu Spika, lakini pia mimi ni mwanataaluma, nimetoka katika taaluma ya habari. Hawa waandishi huko wanakotoka wengi wao mishahara yao ni midogo na mimi nimuombe sana kaka yangu Mheshimiwa Nape, nakuomba sana kuhakikisha kwamba waajiri wengi kunakuwepo na utaratibu mzuri ambao utawawezesha Waandishi wa Habari waweze kuifurahia kazi yao. Wananchi wanafaidika kwa sababu ya hawa Waandishi wa Habari. Tukiwa katika misafara, wakiwa katika shughuli zozote za kitaifa muda wote wako busy kufanya kazi zao, lakini waajiri wengi hawatambui thamani ya Waandishi wa Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ombi kwa Serikali, tuwaangalie sasa ili waandishi hawa waweze kufurahia taaluma yao, waweze kuifanya kazi yao ipasavyo kwa kuboresha maslahi yao, lakini vilevile kwa sababu wanakumbana na changamoto nyingi wanapofanya kazi, tuangalie utaratibu pia wa kuwaandalia bima, kwa sababu waandishi wengi na hata katika matukio mengi wao ndiyo wanaokuwa waathirika wa kwanza. Kukiwa na matukio ya milipuko mabomu, tukio lolote lile wao ndiyo wa kwanza kwa sababu mwajiri ili aweze kupata taarifa lazima huyu mwandishi awepo pale.
Kwa hiyo, kaka yangu Mheshimiwa Nape, ninakuomba sana uangalie ni kwa jinsi gani tutaweza kuboresha maisha mazuri kwa hawa Waandishi wa Habari.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Molel muda umekwisha.
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu mapitio na mwelekeo wa Serikali na Makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Ofisi yako wewe mwenyewe, kwa maana ya Ofisi ya Spika, kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanafanyiwa kazi. Pia pongezi za kipekee kabisa zimwendee Mheshimiwa Waziri Mkuu ambapo amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba haki za watu wenye ulemavu zinatimizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais amefungua milango na kuthamini haki za watu wenye ulemavu kwa kuona kwamba kuwa na ulemavu siyo kulemaa na ndiyo maana leo hii katika Idara mbalimbali watu wenye ulemavu wamepewa nafasi kuonesha uwezo wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpe pongezi za dhati kabisa kwa kuhakikisha kwamba Wizara yetu inahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Hiki kilikuwa ni kilio cha watu wenye ulemavu kwa muda mrefu. Kana kwamba hiyo haitoshi ni furaha iliyoje kuwa na Naibu Waziri katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri Mkuu imejitosheleza. Ni hotuba ambayo imegusa maeneo yote. Sisi watu wenye ulemavu tunaona ni fahari kubwa kwa sababu masuala yetu mengi yamezungumzwa na yameguswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba tu nishauri mambo machache ambayo naamini kabisa kwa jitihada zilizoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano mambo haya yatafanyiwa kazi hasa katika suala la elimu. Naomba nitoe mapendekezo yangu kwa Serikali hasa kipindi hiki ambapo Mheshimiwa Rais ametoa kipaumbele cha elimu na kuhakikisha kwamba watoto wa Kitanzania wanasoma bure, ni jambo muhimu sana kuhakikisha kwamba sasa ni wakati wa kuboresha miundombinu ili watoto wenye ulemavu waweze kupata elimu pasipo vikwazo vyovyote. Pia ni wakati muafaka sasa kuboresha vyuo vyetu ili kuhakikisha kwamba navyo mazingira yanakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mambo mengi yameorodheshwa humu na kwa kuwa matarajio yetu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pande zote mbili kugusia mambo haya ya watu wenye ulemavu ambayo siku zilizopita yalikuwa nyuma sana, lakini sasa tumeona yanapewa kipaumbele. Tulitarajia Kambi ya Upinzani pamoja na vyama vingine vyote ambavyo vinawakilishwa hapa Bungeni vingekuwa mstari wa mbele kuunga mkono hotuba hii kwa kushauri ili kuboresha kwa namna moja au nyingine na kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanasonga mbele na kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya hapa kazi tu. Ni jambo la kuhuzunisha hasa tukizingatia kwamba tunapokuja hapa Bungeni tunategemea kupata mambo yenye msingi, matokeo yake upande wa pili unatoa vitu ambavyo haviendani na wakati uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vyombo vya habari kurusha moja kwa moja matangazo ya Bunge ndiyo hoja yao hivi sasa. Tunapozungumzia suala zima la habari, habari zinapatikana wakati wowote na katika matukio yoyote muhimu. Hatujaona vyombo vya habari kama vimekatazwa kurusha habari na matangazo yanaendelea kutolewa Mheshimiwa Mwenyekiti, kinacholiliwa hapa ni kule kurushwa habari moja kwa moja. Hata ukiangalia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna sehemu ambayo imezuia kurusha matangazo ya Bunge na matangazo haya yanaendelea kurushwa. Hata kama hayajarushwa moja kwa moja lakini si yanaendelea kurushwa kwa wakati mwingine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri ni wakati muafaka wa kujiuliza ni kwa nini wenzetu wanalilia matangazo haya kurushwa moja kwa moja. Pengine ni kutokana na ajenda zao kwa hivi sasa zimeweza kufanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Awamu ya Tano na kujikuta hivi sasa hawana la kusema. Ndiyo maana hata wakati mwinginge wanaona kwamba ni bora wafanye yale ambayo yamefanyika na tumeshuhudia leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale masuala ya ufisadi waliyokuwa wakiyapigia kelele hivi sasa mafisadi wanashughulikiwa. Wamekuja hapa na kuzungumzia kuhusiana na matumizi ya fedha ambazo hizi fedha Waziri mwenye mamlaka husika sheria inamruhusu. Ni kwa vipi sheria inamruhusu, hivi hata nyumbani baba anapotoa fedha na zikabaki zikatumika kwenye matumizi mengine kuna ubaya? Katika sheria hii ambayo tumewasikia leo wakizungumzia ya Appropriation Act ya mwaka 2016 iko wazi kuhusiana na Waziri kutoa Fedha na kwenda kutumika sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeona Sherehe za Uhuru fedha zile zimetumika kutengeneza barabara ya Mwenge, kuna ubaya gani? Vile vile tumeona fedha za Muungano zitatumika kufanyia ukarabati barabara ya kwenda uwanja wa ndege kule Mwanza. Katika hili Serikali inapoamua kutekeleza mambo muhimu ambayo yataleta unafuu kwa wananchi hivi tatizo liko wapi? Ajenda yao hapa ni nini? Tumeona jitihada za Rais katika kutumbua majipu. Nafikiri kwa upande mwingine hata hawa pia ni majipu ambayo yanapaswa kutumbuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine wanapozungumzia utawala bora hapa Tanzania ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikilivalia njuga suala hili na utawala bora upo, upo kwa maana gani? Hebu tuangalie hata katika vyama vyetu. Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeshuhudia kabisa kwamba kila kipindi cha miaka mitano uchaguzi upo, miaka kumi uchaguzi upo na hata Rais anayekuwa Mwenyekiti katika chama husika anapomaliza muda wake unafanyika uchaguzi. Hata hivyo, tangu upinzani umeanza hapa nchini hebu tuangalie hawa Wenyeviti kwa muda wote wamekuwa Wenyeviti wa vyama hivyo na wao ndiyo wa kwanza kuzungumzia demokrasia, lakini ndiyo wavunjaji wa demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumzia Upinzani kwa chama cha CUF, tangu kimeanza Maalim Seif ndiye Mwenyekiti, hivi hakuna wengine ambao wana sifa za kuwa Wenyeviti?
MHE. AMINA S. MOLEL: Kuwa Katibu Mkuu, amekuwa Katibu Mkuu kwa muda wote kwani hakuna wengine wenye sifa?
Sasa mnazungumzia demokrasia ipi? Ni demokrasia ipi mnayoizungumzia wakati ninyi ndiyo wa kwanza kuivunja hiyo demokrasia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, linapokuja suala la uongozi wakati mwingine Mwenyezi Mungu ndiye anayeteua viongozi…
MHE. AMINA S. MOLEL: Siyo kila mtu tu atakuwa kiongozi, siyo kila mtu tu atakuwa Rais, miaka yote hujawa Rais basi achia ngazi wapishe wengine. Mnafurahisha sana, mlisusa uchaguzi, uchaguzi umefanyika wa haki, halali kabisa mmewaumiza wengine ambao hivi sasa wanalia ambao kwa namna moja au nyingine wangeweza kuendeleza Taifa hili, lakini leo hii mmewazuia. Kwa maana hiyo ninyi ndiyo wa kwanza kuvunja demokrasia kwa sababu hamuitimizi hiyo demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe tu Rais wetu na tuzidi kumpa moyo, aendelee kufanya kazi, aendelee kuyatumbua majipu, Watanzania wanayaona. Wanaona jitihada za Rais, wanaona jitihada za Mawaziri wetu, kazi kubwa wanayoifanya na hicho ndicho tunachokihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine wanasema kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji. Naomba kuwatia moyo muendelee kufanya kazi, kazi inaonekana na wananchi wanaifurahia, kila siku umaarufu wao unazidi kushuka. Tunapoelekea sasa mwaka 2020 ni dhahiri kabisa hizi row ambazo hivi sasa mmeongezeka zitapungua kwa sababu matarajio makubwa ya wananchi ni kufanyia kazi matatizo yao, lakini hivi sasa mmekwenda kinyume kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, naomba kuwapa moyo Mawaziri wetu, naomba kumpa moyo Waziri Mkuu, naomba kumpa moyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunamwomba aendelee kufanya kazi kwa mwendo huo huo. Kauli mbiu ya hapa kazi tu iendelee isirudi nyuma, tunachotaka sisi ni maendeleo. Wananchi kwa muda mrefu walikuwa na kero nyingi hivi sasa basi hizo kero ziweze kufanyiwa kazi, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwepo hapa, niishukuru pia familia yangu walitambua umuhimu wa mimi kupata elimu ndiyo maana nikawepo hapa, lakini vile vile naomba nimpongeze Waziri mwenye Wizara husika Mheshimiwa Waziri Ndalichako kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nianze kwa kunukuu. Kama tunavyofahamu elimu ni maarifa na maarifa ni maisha. Maana yake jamii ikipata elimu, watoto wakipata elimu ,basi watakuwa na maisha bora. Natambua jitihada za Serikali katika kuboresha elimu tangu uhuru. Kwa mfano, mwaka 1961-1984 kwa falsafa ya Elimu ya Kujitegemea; lakini vile vile Sera ya Elimu mwaka 1995 ambapo Serikali ilikuja na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; mwaka 2002-2006 ikaja na MMEM na MMES na mwaka 2014 Sera ya Elimu imeasisiwa, lakini pamoja na jitihada hizo za Serikali bado elimu bora kwa Watanzania na nalenga hasa kundi la watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimnukuu mtu ambaye ni miongoni wa watu wenye ulemavu ambao wamefanikiwa sana, Bwana Nicolaus James maarufu kwa jina la Nick Vujicic ambaye yeye ni mlemavu kutoka nchini Australia, hana miguu, hana mikono, lakini pamoja na yote hayo mafanikio yake ni makubwa na ni mfano wa kuigwa na walemavu wote duniani kutokana na jitihada zake. Hata hivyo, Bwana Nicolaus James au Nick Vujicic yeye amefanikiwa kutokana na Serikali yake kutambua kwamba kuwa na ulemavu siyo kulemaa, kwa maana hiyo iliboresha miundombinu na kuhakikisha kwamba Bwaba Nicolaus Vujicic anapata elimu, ili elimu ndiyo iwe mtaji katika maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie changamoto za watu wenye ulemavu na hasa watoto wenye ulemavu kwa hapa nchini Tanzania. Hii sio kwamba kwa nchi hii ya Tanzania tu, ni Afrika yote, lakini kwa sababu mimi ni Mtanzania naomba nizungumzie nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kwa kusema kwamba; kama familia yangu isingetambua umuhimu wa mimi kupata elimu, leo hii nisingekuwa hapa, lakini walitambua umuhimu wa elimu ndiyo maana leo niko hapa na pengine isingekuwa hivyo, ningekuwa ombaomba mitaani. Kwa maana hiyo, siyo walemavu wote wanaoomba wanapenda, yote hiyo ni kutokana na maisha, ni kutokana na wao kutokupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi najiuliza swali; ni kwa nini watoto wengi wenye ulemavu wanatoka katika familia maskini? Hili ndilo ambalo linatukosesha sisi elimu kwa sababu katika familia kama kuna watoto watatu na yupo mtoto mwenye ulemavu, familia itaona ni afadhali iwapeleke watoto wasio na ulemavu ili wakapate elimu na kwa maana hiyo yule mwenye ulemavu anabaki nyumbani. Kwa maana hiyo, huyu ambaye ana ulemavu, asipopata elimu ndiyo tunamuandaa na kumpeleka katika kundi la kuwa ombaomba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina furaha kwa sababu mama Ndalichako ni mwananmke na wanasema “uchungu wa mwana, aujuaye mzazi” na hasa mama! Wewe ni mama! Nakuomba kwa moyo wangu wote, angalia watoto wenye ulemavu. Waandalie mazingira mazuri ili waweze kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa naibu Spika, changamoto ni nyingi. Miundombinu sio rafiki kwa maana hiyo hata anapokwenda shule bado ni shida huyu mtoto! Ukienda vijijini watoto wanatembea kilometa saba, kama ni mtoto mwenye ulemavu atawezaje kutembea kilometa saba kwenda kupata elimu? Kwa hiyo hii inakuwa ni changamoto, hawezi kwenda kupata elimu!
Mheshimiwa Naibu Spika, yuko mtoto mmoja aliamua yeye kila siku awe anambeba mdogo wake, kumpeleka shule kwa sababu alijua hii ndiyo njia ya kumsaidia mdogo wake! Lakini alifika mahali kwa sababu yule binti anakua na uzito, alishindwa. Kwa hiyo, yule kijana alishindwa kumsaidia mdogo wake na mdogo wake akaishia hapo hakupata tena elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda katika shule zetu, mfano watoto wenye ulemavu wasioona, hawa wanahitaji vifaa ambavyo vinawawezesha mfano mashine za braille, katika shule nyingi hakuna hizo mashine. Huyu mtoto ili aweze kupata elimu inakuwa ni vigumu kwake. Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba hivi vifaa vinapatikana na kwa sababu Waziri wa Fedha yuko hapa viko vifaa ambavyo ni muhimu vya kupunguziwa kodi au vikaondolewa kodi kabisa ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vyuo vyetu na vyuo vya ualimu, kwa nini Serikali isione umuhimu wa lugha za alama zikafundishwa ili Walimu wote wanapotoka shule wawe na ufahamu wa lugha hizi za alama, kwa sababu wakijua hivyo, mwanafunzi mwenye uziwi kule kijijini hatakuwa na haja ya kutafuta shule nyingine. Ndiyo maana ukienda hata katika vyuo vikuu ni nadra sana kuwakuta wanafunzi viziwi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu hakuna Walimu wenye utaalam huo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kuhakikisha kwamba mitaala ya lugha za alama inafundishwa Walimu wote waweze kufahamu, lakini pia kuna ubaya gani kuingiza katika syllabus ili hata hawa wanafunzi wengine waweze kuwasiliana kwa sababu watajua kwa kujifunza hizi lugha za alama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko shule za binafsi na hapa Serikali tungeweza pia kuzitumia hizi shule za binafsi kwa kupunguza baadhi ya kodi ili watoto wenye ulemavu na wao wakapata nafasi. Ukimpunguzia kodi, atawachukua watoto, watano, wane; tayari hawa watoto wamepata elimu! Katika vyuo vyetu sio rafiki na hasa vyuo binafsi na hata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chenyewe ukinipeleka hata mimi pale mazingira sio rafiki ili niweze kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuhakikishe kwamba vyuo vyetu vyote na hii sheria ipo na nakumbuka mwaka 2013/2014, Waziri Lukuvi wakati huo tukiadhimisha siku ya watu wenye ulemavu duniani pale Iringa, alilizungumzia hili kuhakikisha kwamba majengo yote yanakuwa rafiki. Nashangaa ni kwa nini mpaka leo hii baadhi ya majengo hayaangalii hilo, lakini pia katika Vyuo Vikuu, tunawaandaa vipi hawa wanafunzi katika suala la mikopo? Wengine hawawezi hata kufuatilia. Tuwe na tangazo maalum, tuwaelekeze wanafunzi wanaomaliza elimu ya form six kuhakikisha kwamba wanapotaka kwenda kujiunga utaratibu mzuri umeandaliwa kwa ajili yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ni mengi, changamoto ni nyingi, lakini nimalizie kwa kusema kwamba; elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Ukimwezesha mtoto mweye ulemavu, umemkomboa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana katika Wizara hii kwa hotuba yake. Nampongeza sana kama mwanamke kwa kazi nzuri anayoifanya na nazidi kumtia moyo kwamba wanawake wote wa Tanzania wanamtegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la afya, tunafahamu kwamba afya ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Tunapozungumzia afya, tunafahamu kwamba bila ya kuwa na afya huwezi kufanya jambo lolote la kuleta maendeleo. Tunakumbuka kabisa kwamba mojawapo ya mambo yaliyokuwa yakipigiwa kelele ni suala la maradhi na maradhi haya ndiyo maana tunasisitiza sana suala la afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Afya na hasa Serikali kwa kuleta Mfuko wa Bima ya Afya. Pamoja na hayo, naomba nizungumzie machache hasa changamoto zilizopo katika Mfuko wa Bima ya Afya ambayo kwa namna moja au nyingine, umekuwa ni kikwazo kwa baadhi ya wanachama wanaokwenda kupata huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na vizingiti kwa maana kwamba katika baadhi ya card hizi za Bima wanapokwenda kupata huduma ya afya na hasa kama tunavyosisitiza siku zote, ni vyema kwa mwananchi kujua afya yake. Atakapojua afya yake, anajua kabisa kwamba yeye ana matatizo gani ili aweze kukabiliana nayo mapema ili aweze kupata matibabu mapema. Wanachama wengi wa Mfuko wa Bima ya Afya wanalalamika kwa sababu wanapokwenda kwa ajili ya kufanya check-up ya miili yao, wanakataliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakataliwa pamoja na kwamba wao ni wanachama wazuri na wamekuwa wakichangia. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa, atuambie ni kwa nini Mfuko wa Bima ya Afya umekuwa ukiwakatalia wanachama kuangalia afya zao ili waweze kujua na pengine kuchukua hatua mapema kutokana na matatizo wanayoyapata? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dawa pia; kama Mfuko wa Bima ya Afya wamekubali kubeba dhamana ya Watanzania, kwa nini wazuie baadhi ya dawa wasizitoe wakati wanachama wote wanaotibiwa wanachangia Mfuko huo? Namwomba Mheshimiwa Waziri na naishauri Serikali na Waziri, atakapokuja kuhitimisha, atueleze ni kwa nini Mfuko huu wa Bima ya Afya umekuwa na hivyo vikwazo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwa Madaktari. Madaktari pesa waliyopangiwa na huo mfuko wa afya kama consultant fees wanalipwa sh. 2,000/=. Hivi kwa wakati huu tuliopo na Madaktari hawa ambao ni wataalam wetu, tunawategemea, mabingwa, hivi kweli unakwenda kumlipa sh. 2,000/=! Ni aibu kwa Mfuko wa Bima ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia Mfuko wa Bima ya Afya, naomba moja kwa moja niende katika masuala ya watu wenye ulemavu. Nawapongeza Wabunge wote ambao wamezungumzia suala la watu wenye ulemavu na hasa katika Mfuko wa Bima ya Afya na kuona umuhimu wa wao Serikali kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kupata card za Bima ya afya ili waweze kutibiwa. Nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nawaomba pia Wabunge wengine katika Majimbo yao waone umuhimu wa kuwachangia hawa watu wenye ulemavu ili basi wanapokwenda hospitali wasipate tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la vifaa saidizi. Tunafahamu kabisa ulemavu siyo kulemaa; na katika ulemavu unapomsaidia mtu mwenye ulemavu vifaa saidizi kwa wale wanaovitumia, tayari umepunguza vikwazo. Isipokuwa katika Bima ya Afya wanapokwenda, bado halipo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri alione hili kwamba ni muhimu na aone ni kwa jinsi gani atawasaidia watu wenye ulemavu ili waweze kupata vifaa saidizi na kuweza kutimiza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba nizungumzie katika hospitali zetu na hasa wanawake wenye ulemavu wanapokwenda kujifungua. Vitanda siyo rafiki; na wakati mwingine hata Madaktari wenyewe au Manesi kwa namna moja au nyingine kauli zao siyo nzuri. Wanapowaona watu wenye ulemavu na hasa mwanamke amekwenda ni mjamzito, maneno ya dhihaka yanakuwepo mengi. Hivi katika suala la mama kumleta mtoto, hata kama mtu ni mlemavu hana ule uhitaji? Kwani wana kasoro gani? Si wanayo maumbile kama wengine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba, nasimama mbele yao kama mwanamke mwenye ulemavu na naomba kuwatetea hawa, kuwasilisha kilio chao kwa sababu sio wote ambao wanaweza kufika huku na kuwasilisha kilio chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia masuala ya watu wenye ulemavu, wana changamoto nyingi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hili pia, aangalie ni kwa namna gani basi tutafanya, kama ni kutoa elimu ili kwa namna moja au nyingine lugha hizi waziangalie, wasiwadhihaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuone umuhimu na hasa nimwombe Mheshimiwa Waziri kuona umuhimu wa kuweka Wakalimani katika hospitali zetu. Wanapokwenda watu wenye ulemavu hasa viziwi, inakuwa ni vigumu kwa wao kuweza kuwasiliana. Lugha inakuwa ni gongana! Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Waziri, wakati mwingine tunapoajiri basi tuone umuhimu wa kuajiri hawa watu ambao ni wakalimani wa lugha za alama ili waweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Zahanati ya Nduruma. Zahanati hii ya Nduruma tayari imepandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya. Zahanati hii inahudumia Vijiji vya Marurani, Manyire, Mlangarini na maeneo mengi katika Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Arumeru; lakini mpaka hivi sasa hakuna wataalam na hakuna gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inakuwa ni tatizo kwa hata akinamama wanapokuwa wajawazito kwenda hospitali ya Mount Meru inakuwa ni shida, wanajifungulia njiani. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu na hasa Waziri mwenye dhamana kutuletea gari la wagonjwa katika Zahanati ya Nduruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la watoto wa kike kwa sababu mimi ni mdau na vile vile niungane na ndugu yangu Mollel aliyesema kwamba shujaa ni yule anayejali mtoto wa kike. Katika shule zetu nyingi, watoto wa kike kwa mwezi hawaendi shule kati ya siku nne mpaka siku kumi. Naomba tu Mheshimiwa Waziri na nimwombe pia kwa sababu Waziri wa Fedha yuko hapa, aone basi umuhimu wa kupunguza…
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga hoja mkono.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kwanza kabisa naomba niseme kwamba mimi nimekulia katika taaluma ya habari, na naomba kwa heshima na taadhima niitendee haki taaluma ya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika, kwa kazi nzuri naamini kwamba atafanya mambo mazuri kadri muda unavyokwenda. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ndugu Reginald Mengi, kwani yeye ndiye ambaye kwa kiasi kikubwa amechangia mimi kufika hapa, nilianzia ITV na Radio One wakati huo bado binti mdogo na baadae nikaenda Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Nichukue nafasi hii pia kumshukuru, Mkurugenzi wakati huo Ndugu Tido Dunstan Muhando, ambaye ninaamini kabisa naye amechangia mafanikio yangu hapa.
Niwashukuru pia na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Shirika la Utangazaji Tanzania kwa kazi nzuri na ninaomba niwatie moyo, na niwaambie kwamba mwenzao nipo humu na nipo kutetea maslahi ya waandishi wote kwa ujumla na mwisho ni kwa wanahabari wote popote pale walipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo katika utangulizi wangu, basi siku zote wanasema mcheza kwao hutunzwa na mimi naomba nitunzwe kwa kuanza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa kuwa ndipo ambapo nimetokea huko. Shirika hili la Utangazaji Tanzania (TBC) ni shirika ambalo kusema ukweli ni kama limesahauliwa na hata ukiangalia katika bajeti ambayo imepangiwa kwa hivi sasa ni bajeti ambayo haitoshi kitu chochote; kwa mwezi mmoja tu Shirika la Utangazaji Tanzania gharama ya kulipia umeme inakwenda karibia shilingi milioni 70. Sasa kama mwezi mmoja tu na bajeti hii ambayo Shirika hili la Utangazaji (TBC) limepangiwa, utaona ni dhahiri kabisa kwamba fedha hizo hazitoshi kuweza kuikwamua (TBC) kutoka hapa ilipo ili Watanzania waweze kujivunia shirika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote haya na watu wamekuwa wakilalamikia ni kwa sababu Shirika hili tumelisahau, ndiyo maana kila siku linazidi kuwepo hapa lilipo. Mimi nimpongeze tu Mheshimiwa Rais kwa kutupa Mkurugenzi sasa hivi Dkt. Ayoub Rioba ambaye ninaamini kabisa ni mbobezi katika fani hii ya taaluma ya habari, ni msomi, kwa hiyo ninaamini ili aweze kufanya kazi vizuri, ni lazima haya mambo yaendane na fedha, ikiwa ni pamoja na kuboresha mitambo, kuboresha hata hayo majengo tu miundombinu katika Shirika hili imechoka tangu miaka hiyo atujazaliwa mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Redio Tanzania pale mitambo ni hiyo, ofisi ni zile zile tangu miaka hiyo, sasa hata kama ni kijana ari ya kufanya kazi, atawezaje kufanya kazi wakati vifaa vilivyopo ni duni. Ukienda hata katika mitambo iliyopo ya Kisarawe, bado hali ni mbaya. Nashukuru kwamba kwa miaka ya hivi karibuni wameweza kuboresha angalau Redio Tanzania ambayo sasa hivi ni TBC Taifa, kidogo imeboreshwa mitambo yake, lakini hili ndilo kimbilio la Watanzania walio wengi na hasa unapozungumzia taaluma hii, hawa wa huko vijijini walitarajia mambo mengi kutoka katika Shirika hili la TBC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali yenyewe imeisahau TBC utawezaje kuboresha? TBC ina wafanyakazi wazuri, wana taaluma lakini vifaa vimechoka. Wengine hata ofisi hawana, ukienda Shirika la Utangazaji TBC hivi sasa majengo yako pale lakini majengo hayo miunombinu hakuna chochote. Kwa hiyo, naiomba Serikali, na ninaishauri Serikali iliangalie Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa jicho la pekee, hebu tujifunze kutoka kwa wenzetu, mashirika kama CNN, BBC ambao wanajivunia hilo mashirika yao na ndiyo maana hata ukiangalia katika vita, vinapotokea vita wanachokimbilia cha kwanza ni chombo cha Taifa, kwa nini na sisi tusijivunie Shirika hili!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya Shirika hili la TBC vilevile wafanyakazi wa Shirika hili la TBC wamekuwa wakidai marupurupu na mishahara yao kwa muda mrefu. Kumekuwepo na scheme mpya ya mishahara ambayo tangu mwaka 2012 mpaka leo madai ya wafanyakazi wa TBC hayajatimizwa. Mheshimiwa Waziri Nape ninaamini kabisa haya umeshayapata na kwa sababu wewe ni kijana nakuomba uangalie kwa jicho la pekee, wasaidie hawa wafanyakazi wa TBC ili waweze kutimiza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni Startimes, hili ni jipu! nasikitika kwa kweli. Hawa Startimes, kupitia kampuni ya Star Media ambao waliingia mkataba wa miaka mitano. Mkataba ule hivi sasa tayari muda wake umekwisha, hawa Star Media ambao ndiyo wanaimiliki kampuni hii ya Startimes, hakuna malipo yoyote yanayolipa kwa Shirika hili la TBC. Kama huu uwekezaji ulikuja na ulikuwa na nia njema, ungeweza kwa kiasi kikubwa kulisaidia shirika hili kupunguza makali, kujenga mitambo iliyopo hapo. Kwa hiyo ninamuomba Waziri atakapokuja atuambie kuhusiana na mkataba huu wa TBC, vilevile aje atueleze, kwa sababu ndani ya Star Media hawa Startimes hivi sasa wanasema kwamba wamepata hasara. Hebu tujiulize wakati tunatoka kwenye analogia kuingia kwenye digital ni nani walioongoza kwa kuuza ving‟amuzi? Nitamuomba Waziri atakapokuja atusaidie katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie waandishi wa habari. kila mmoja wetu hapa, hata mmoja wetu hapa asiyetegemea waandishi wa habari. Tunapokwenda popote pale msafara wa waandishi wa habari upo nyuma yetu, tukitarajia kwamba hawa ndiyo ambao waweze kufikisha taarifa kwa wananchi. Kwa nini hatuwathamini wanahabari? Kwa nini tumewasahau wanahabari? Ukiangalia hata hawa wanaofanya kazi hapa muda wote wamesimama wanafanya kazi, lakini mishahara yao ni midogo, hakuna anayewatetea.(Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze ni lini Muswada wa Habari utakuja hapa ili tuweze kutetea maslahi ya waandishi wa habari, tuangalie pia kuhusiana na suala la bima kwa ujumla kwa hawa waandishi wa habari ili basi waweze kufanya kazi zao vizuri na ukiangalia baadhi ya wanahabari, kwa jinsi ambavyo wanatembea hata viatu vyao soli zimeisha. Kwa hiyo, mimi nina imani sana na Mheshimiwa Waziri, nina imani sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nina imani kwamba atawatendea haki waandishi wa habari ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie suala la michezo, tunaposema michezo, michezo hii siyo tu kwa timu hizi kubwa, lakini pia hata watu wenye ulemavu wanahitaji michezo. Watu wenye ulemavu wamesahauliwa hakuna anayezungumza kwa niaba yao, kwa heshima na taadhima naomba nizungumze kwa niaba yao ili basi kilio chao kiweze kufika na Serikali iwaangalie hata kwa kuandaa viwanja ambavyo michezo hii wataweza na wao pia kushiriki na kulitangaza Taifa hili. Mwanariadha Oscar Pistorius wa Afrika Kusini, ameweza kuitangaza nchi yake ni kutokana na kuwezeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara ya Ardhi, kwa sababu mimi pia ni miongoni mwa wananchi ambao wanaguswa na migogoro ya ardhi nikitokea katika jamii yangu ya Wamasai. Kwa hiyo, moja kwa moja naomba nigusie baadhi ya maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine yamechangiwa na migogoro hii, hasa kutokana na kwamba Serikali ama viongozi husika kutokuvalia njuga migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya mambo ambayo kwa namna moja au nyingine yamechangia sana migogoro baina ya wafugaji na wakulima ni Sheria ya Utambuzi wa Mifugo ya mwaka 2010 ambayo inashindwa kutambua wafugaji wa asili na hasa katika maeneo yao husika. Pia Sera ya Wanyamapori ya mwaka 1998 na yenyewe pia imekuwa ikizuia mifugo katika maeneo ya wanyamapori ilhali maeneo hayo siku za nyuma yalikuwa ni wazi kabisa kwa ajili ya wafugaji na wafugaji hawa walikuwa hawabugudhiwi na kitu chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine pia ni hizi sheria ambazo ni nyingi, mfano Sheria ya Mazingira ya mwaka 2007 na yenyewe pia kwa sababu inaainisha kuwa ufugaji wa asili ni moja ya vyanzo vya uharibifu wa mazingira, hii pia imechangia kuwepo kwa migogoro baina ya wafugaji na wakulima. Maeneo mengi yaliyokuwa yakitumika na kutambuliwa na wafugaji, nakumbuka tangu nikiwa mdogo maeneo hayo wafugaji walikuwa wakiyatumia na wafugaji hawa wamekuwa wakilisha mifugo yao na kumekuwepo na amani baina ya wafugaji na wakulima, hakukuwepo na migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu sheria hii sasa haiwatambui wafugaji na haithamini ile mifugo yao na kuona kwamba mifugo hii ya asili ni chanzo cha uharibifu wa mazingira, sheria hizi zimekuwa zikichangia migogoro hiyo na kwa sababu haitambui imekuwa ni chanzo cha uharibifu huu au migogoro hii baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba yapo maeneo mengi ambayo yametengwa, migogoro hii pia inachangiwa na baadhi ya viongozi, viongozi wa Kiserikali, viongozi wa kisiasa, viongozo wa kimila, viongozi wa kidini, wote hawa wamekuwa wakichangia migogoro hii. Kwa mfano, katika Ranchi ya Manyara ambayo hata wakati huo akiwa Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa, eneo hili la Ranchi ya Manyara lilitamkwa wazi kwamba litumike kwa ajili ya mifugo, lakini mpaka leo hii baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakilitumia hili eneo na kuwanyima hata wafugaji ambao na wenyewe wanatoka katika jamii hiyo, kuwazuia kulisha mifugo yao na hata wakati mwingine maeneo haya ambayo mifugo inatakiwa ipite na kwenda kunywa maji imekuwa ni shida pia. Hili ni eneo la Ranchi ya Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine wanasema kwamba kabla ya kutoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako, ni vema basi ukatoa boriti kwenye jicho lako. Ijumaa, miongoni mwa walichangia hapa na hasa nizungumzie eneo la Monduli ambako mwaka jana nilipata bahati ya kuzunguka katika Kata zote katika Uchaguzi Mkuu, yapo baadhi ya maeneo ambayo baadhi ya viongozi wenyewe kama nilivyosema wamechangia, lakini pia hata viongozi wengine hao ambao tunaowatarajia na …
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunapokuja huku tukitarajia kwamba wao ndio faraja kuweza kuishauri Serikali ndiyo wamekuwa hao wanaochangia migogoro. Mfano katika Milima ya Nanja, mmoja wa viongozi ambao wakati huo alikuwa ni Diwani wa CCM na kwa hivi sasa yuko upande wa pili, ameuza eneo hili la Mlima Nanja na hivi sasa eneo hilo linatumika kwa uchimbaji wa kokoto na eneo hili limeuzwa pasipo ridhaa ya wananchi wenyewe. Kwa hiyo, wakati mwingine tunapozungumzia kuhusiana na hii migogoro, ni vema na pia tukajiangalia, je, tumechangia kwa kiasi gani, tumetatua migogoro kwa kiasi gani ili basi tuweze kuwanyooshea vidole wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi katika Wilaya ya Monduli na hasa nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye mamlaka husika kwa jitihada zake, ambapo Februari na Machi mwaka huu, aliweza kufika Wilayani Monduli katika ziara yake na kufuta baadhi ya vibali 13 vya mashamba ambayo yalikuwa yametelekezwa na mashamba hayo kugawiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kwamba pamoja na kwamba jitihada hizi zipo, lakini bado tuiombe Serikali yenyewe ili iweze kushughulikia migogoro hii ambayo imekuwa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi hao kama nilivyosema, baadhi yao viongozi wa Kiserikali, vile vile viongozi wa kisiasa ambao wamehodhi maeneo makubwa na matokeo yake wananchi wanapata shida ya kuweza kumiliki ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya ya Arumeru ambako hasa ndiko huko ninakotoka, yapo mashamba makubwa na hayo mashamba, mfano shamba la Gomba Estate na kwa bahati nzuri katika moja ya nakala tulizopewa na Mheshimiwa Waziri yameorodheshwa. Mashamba haya tangu tunakua yamehodhiwa na ukienda hata kwa hivi sasa mashamba haya hayatumiki, wananchi wa kule hawana maeneo wakati mwingine ya kulima na hata juzi tu wananchi moja ya mashamba ambayo yapo katika maeneo hayo ya Malalua, maeneo ya Gomba walijikatia baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vema kama hawa wafanyabiashara au hawa ambao wamehodhi maeneo haya hawawezi kuyamiliki, nafikiri ni vema kabisa huu utaratibu ukaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wanapewa mashamba haya ili waweze kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mashamba haya na hasa ukizingatia mfano kwa Mji wa Arusha ambao kila siku umekuwa ukipanuka. Mji huu na maeneo mengi sasa yamekuwa ni maeneo ambayo wananchi wengi nao wanazidi kuvamia na bado yamehodhiwa na hawa watu ambao hawaitendei haki Serikali. Mheshimiwa Waziri kwa dhamana aliyonayo kama alivyofanya katika Wilaya ya Monduli namwomba pia afike katika maeneo ya Vijiji vya Mlangarini afike katika maeneo ya vijiji, Kata ya Manyire ili aweze kufuta baadhi ya vibali hivi ambavyo vinawakosesha wananchi wetu haki ya kumiliki ardhi, vilevile inawakosesha wananchi wetu kupata maeneo kwa ajili ya kulisha mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda katika Jiji la Dar es Salaam, katika Jiji hili la Dar es Salaam na hasa tukikumbuka mvua za mwaka 2011/2012 ambazo zilileta maafa kwa kiasi kikubwa, Serikali kwa wakati ule iliwatafutia eneo la Mabwepande na wananchi wakaweza kupewa viwanja ingawa bado wako wengine ambao wamerudi tena katika bonde la Msimbazi, wamerudi katika mabonde ya Mkwajuni, tuangalie kwamba sheria hizi wapo kweli ambao wameshalipwa, lakini wapo kweli ambao miaka nenda miaka rudi wapo maeneo hayo. Tuangalie ni kwa jinsi gani Serikali inaweza kuwasaidia ili kuepusha migogoro hii ambayo kwa namna nyingine imekuwa ikikosesha amani wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema kwamba tunafahamu umuhimu wa ardhi, kila mmoja wetu anatambua thamani ya ardhi na ardhi imekuwa ikipanda thamani kila leo. Ili kuepusha migogoro hii ya ardhi, tusiwasubiri wananchi mpaka wanajenga, wanamaliza kujenga halafu bado wanapelekewa huduma zote muhimu, utakuta umeme wamepelekewa ,matokeo yake baadaye wanakuja kubomolewa. Hii inakuwa ni kero kwa wananchi na wananchi wanakosa imani na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba tu Mheshimiwa Waziri na kwa sababu ameingia katika Wizara hii na ameanza vizuri, hebu naomba arekebishe pia hata hao watendaji ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakisababisha migogoro hii ya ardhi kwa kutoa vibali maeneo ambayo siyo halali kujenga, matokeo yake pia wananchi wamekuwa wakijenga na baadaye wanakuja kuwabomolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nimwombe tu Mheshimiwa Waziri kwamba, kwanza nimtie moyo kwa kazi nzuri anayoifanya na aendelee kufuta mashamba haya ambayo yamekuwa ni kero na hasa ukizingatia kule Bwawani pia kule Lucy mashamba haya yapo namwomba afike pia katika Kata ya Nduruma ufike pia huko Lucy ufute hivi vibali ili wananchi waweze kumiliki ardhi hii. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nimpongeze Waziri kwa kazi nzuri na hasa kwa hatua yake ya kuwatimua baadhi ya watumishi wasio waaminifu katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Nampongeza sana Waziri kwa hili na namwomba aendelee kwa sababu bado wezi wapo wengi na ndiyo maana kwa kiasi kikubwa fedha nyingi zinazopatikana za utalii zinaishia mikononi mwao. Nampongeza sana kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Niwapongeze baadhi ya Wabunge na hasa wale ambao kwa namna moja au nyingine wametambua jitihada, uhifadhi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya makabila ambayo yanaishi katika hifadhi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu turudi nyuma kidogo. Nimefurahishwa na baadhi ya michango na baadhi ya michango mingine kwa kweli inaniweka katika wakati mgumu. Ni kweli, wanasema kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake; najua kunguni wake, kwa sababu hata mimi pia nimesomeshwa na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo kati ya wafugaji na wakulima linahitaji busara, kwa sababu kila mmoja anavutia upande wake. Wengine wanasema kwamba wafugaji ni waharibifu na ndiyo chanzo cha uharibifu wa mazingira. Katika kumbukumbu zangu, Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa inatiririsha maji kwa kipindi chote cha mwaka mzima, lakini leo hii hata mkoa huu kwa kiasi kikubwa hayo maji ambayo siku za nyuma Mwanamuziki Salum ambaye alikuwa ni mzaliwa wa Morogoro aliimba kwamba Mji wa Morogoro unatiririsha maji safi, lakini leo si kama ilivyokuwa zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni kutokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa na wakulima katika vyanzo vya milima; je, hapa wafugaji wanaingia vipi? Kwa sababu wafugaji ndiyo wanaohesabika kwamba ni waharibifu wakubwa wa mazingira; ndiyo maana nikasema hili jambo linahitaji busara. Humu ndani kila mmoja atavutia upande wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wetu wasipokaa, wakaandaa mipango ambayo itawawezesha wafugaji waweze kufuga kwa amani na utulivu, wakulima waweze kulima pasipo usumbufu wowote ili pasiwepo na malalamiko ya watu mifugo yao kuuawa, kusiwepo na malalamiko ya wananchi nyumba zao kuchomwa moto, tutapata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tu tulishuhudia ukatili uliofanywa kwa baadhi ya mifugo kule Morogoro. Kwa maana hiyo, kama busara isipotumika, narudia tena kama busara isipotumika, wataalam wetu wakakaa, mipango hii ikapangwa kuhakikisha kwamba kila mmoja anafuga katika eneo ambalo Serikali imeweka mipaka, inatambua lile eneo na linatambuliwa eneo hili ni kwa ajili ya wakulima, hii migogoro itaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanasema ng‟ombe ni wadudu, lakini utashangaa ndiyo hao hao wanakula nyama. Ikifika Jumamosi Waheshimiwa wengi tunakimbilia mnadani, tunakwenda kula nyama hivi kama wafugaji wasingefuga tungekula wapi hizo nyama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vyema tukatambua kwamba kila mmoja ana nafasi yake katika nchi hii na hata hao wanaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine hakuna anayependa; hebu fikiria kutoka Mwanza mtu mpaka anakwenda Lindi mwendo huo ni wa siku ngapi? ni kutokana na kutokuwepo na mipango ambayo inawafanya hawa watoke sehemu moja kwenda eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo narudia tena busara itumike ili tuweke mipango ya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania ana haki ya kuishi katika nchi yake, popote pale anapoweza, ili mradi tu kwamba sheria hazivunjwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, zipo sheria za tangu mwaka 1959; pamoja na kwamba ipo Sheria ya 2009 au 2010 lakini je, hii sheria ya tangu enzi za ukoloni ni lini sheria hii italetwa ili ifanyiwe marekebisho? Kwa kufanya hivyo tutapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro, tutawaacha watu wanaoishi katika jamii ile, hasa ya wafugaji ambao ni Wamasai, wataishi lakini pia wakitunza mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri pia Serikali, kuhakikisha kwamba katika haya mapori tengefu, yapo maeneo mengine ambayo tuwaachie wafugaji, kwa maana kwamba, kama kweli yakitengwa na kuhakikisha kwamba wafugaji na wao wanafuga; kwa sababu tangu tunazaliwa wananchi, babu zetu, mama zetu, baba zetu, walikuwa wakiishi huko. Kwa hiyo, tuangalie ni maeneo gani ambayo ni mapori tengefu, tutawatengea wananchi wetu ili waweze kuishi na mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nije katika suala la utalii. Katika suala la utalii nimwombe Mheshimiwa Waziri, hebu aiangalie Bodi ya Utalii, sioni kama kuna kazi wanafanya, kwa sababu tuliwatarajia hawa waweze kutangaza kwa kiasi kikubwa utalii wetu, lakini mpaka leo kitu gani kinachofanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende katika Jiji la Dar es Salaam, hivi mtalii anaposhuka katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kuna kituo gani pale anakwenda kupata maelezo kuona kwamba Tanzania kuna utalii huu? Hakuna! Akitoka katika uwanja wa ndege anapoingia barabarani anakaribishwa na mabango ya simu yanatusaidia nini sisi Watanzania? Kwa nini tusitumie haya mabango kuhakikisha kwamba ni njia mojawapo ya kutangaza utalii wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jiji la Dar es Salaam, wengi na ndiyo maana kila siku wanazidi katika hili jiji la Dar es Salaam. Hivi katika sheria za mipango miji na hasa kwa sababu utalii si lazima twende mbugani tu, hata baadhi ya majengo yakihifadhiwa vyema ni utalii. Leo hii katika majengo ya Posta ambayo yalijengwa kabla hata hatujazaliwa, yanabomolewa yanajengwa mengine, kwa nini tusitenge eneo ambalo haya majengo yakahifadhiwa ili kiwe ni kituo cha utalii tuje tuone haya majengo ya miaka nenda miaka rudi yasaidie hata vizazi vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi suala la utalii lina mapana sana na naumia sana ninapoona nchi ya Kenya inatumia advantage ya sisi kulegalega, vivutio vilivyoko Tanzania wanavitangaza wao. Ndiyo maana siku za karibuni, tulimwona Mkenya amesimama kabisa anasema bonde la Olduvai Gorge lipo nchini Kenya, Serikali imejibu nini? Itumie nafasi hiyo wakati mwingine kuhakikisha kwamba wanaeleza, huo utalii upo Tanzania; lakini Serikali imekaa kimya. Huu ni utalii wa kwetu; ni vitu vya kwetu ambavyo tunajivunia. Mlima Kilimanjaro, mara ngapi wameutangaza, kwa kujivunia kwamba njoo Kenya uone Mlima Kilimanjaro, lakini ukweli ni kwamba Mlima huu upo Tanzania tunajipanga vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, mtalii anapotoka katika hifadhi tumejipanga vipi kuhakikisha kwamba anapata maeneo mengine ya kwenda kutembelea? Kwa mfano, Mbuga ya Kruger nchini Afrika ya Kusini, Mtalii akitoka pale atakwenda katika Mji wa Soweto. Kule ataweza kushuhudia, wakati mwingine hata mauaji ya watoto yaliyofanyika mwaka 1976; ni vivutio pia wanakwenda kule kuangalia na kujifunza historia. Historia ya Nelson Mandela, katika vitu vingine tofauti tofauti, pesa zinaendelea kubaki, je, sisi tumejipanga vipi? Mtalii anapotoka Ngorongoro, anapotoka kupanda Mlima wa Kilimanjaro anapotoka huku Gombe, anakwenda wapi? Utamaduni wetu ni upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu ili nami niweze kuchangia mawili matatu katika kuishauri Serikali yangu. Vilevile nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza zaidi katika kutoa ushauri na ushauri wangu utakwenda hasa kwa kuzingatia Wizara mbili ili kuweza kuishauri Serikali yangu katika mpango huu kwamba tunapoandaa mpango huu wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 ni mambo gani ya msingi ambayo yanahitaji kuzingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 45 naomba kunukuu kwamba, hapa Waziri anasisitiza Maafisa Masuuli wanapaswa kujumuisha masuala mtambuka katika mipango na bajeti ya mwaka 2017/2018 na kwamba, ili kufanikisha lengo hili kila Wizara, Idara Zinazojitegemea na Wakala, Sekretariati za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma zinasisitizwa kutenga fedha za kutekeleza vipaumbele kwenye masuala mtambuka. Vipaumbele hivyo ni pamoja na masuala ya kijinsia, vilevile masuala ya watu wenye ulemavu katika kuangalia hasa suala zima la ajira, afya, elimu na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Naomba nijikite katika haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu au mwongozo huu wa bajeti umeeleza tu in general kwa sababu haujaweza kufafanua na kusisitiza masuala hayo kwamba yatatekelezwa vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, tunapozungumzia huduma muhimu za kijamii na hivi sasa katika Serikali yetu tunatoa elimu bure, lakini suala la kijinsia hasa kwa watoto wa kike na katika bajeti iliyopita, halikupewa kipaumbele kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba mahitaji muhimu kwa watoto wa shule hasa wasichana yamezingatiwa kwa kiasi gani. Mfano, tunafahamu kabisa watoto wa kike na hasa watoto wa kike wa vijijini na hata wale wa mijini tunafahamu kwamba, kwa mwezi wanakosa kuhudhuria masomo kwa siku nne, tano mpaka saba na hii ni kutokana na siku zao zile ambazo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali na najua Mheshimiwa Waziri ni baba na baba ana watoto na watoto hao wapo watoto wa kike wa kwake, lakini pia jamii yote kwa ujumla hao watoto wa kike tunawaangalia vipi! Mfano, katika vyoo, vyoo hivi vya shule na hasa maeneo mengi unakuta kwamba shule nyingi zina matundu matano mpaka saba na katika Sera ya Elimu inasema kwamba, matundu ya vyoo vya shule kila choo idadi ni 20 kwa 25, ishirini kwa watoto wa kike na ishirini kwa wavulana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watoto wa kike wana mahitaji muhimu mfano, tunazungumzia huduma za maji, mtoto huyu wa kike akiwa katika siku zake anahitaji pia maji, je, tumejipanga vipi katika bajeti zetu kuhakikisha kwamba maji yanakuwepo ili watoto hawa wa kike waweze kujisitiri vizuri!
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, katika bajeti yetu pia tumejipanga vipi na je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kupunguza kodi au kuondoa kodi kabisa katika suala zima la pedi ili hawa watoto wa kike waweze kupata pedi na hata ikibidi Serikali ilibebe hili kuhakikisha kwamba, wanagawa pedi kwa watoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huduma za afya tunajua kabisa na tumesikia mengi tu na tumeona maeneo mengi hata ya Vijijini vituo vingine vya afya akinamama wanajifungulia kwenye nyumba za nyasi (full suit). Je, bajeti hii imeangalia vipi mchanganuo wake kuweka vipaumbele katika kujenga vituo vya afya na zahanati ambazo wanawake wamaeneo yote ya vijijini watajifungua salama na kuondoa tatizo la vifo kwa mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii tunasema kwamba, kama wanawake haya ndiyo masuala muhimu ya kuzingatiwa na tunafahamu kabisa katika Wizara hii tunaye mwanamke na huyu mwanamke tunatarajia kabisa kwamba yeye ndiye atakuwa jicho la wanawake wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabila la Warangi wana msemo unasema kwamba, mwana wa mukiva amanyire michungiro, kwa maana kwamba mtoto wa maskini hata awe na shida vipi anajua jinsi gani ya kuhimili ile shida. Kwa maana kwamba kama ni khanga imechanika huku nyuma ataishona mbele ataiunga atajifunga na maisha yatakwenda mbele. Kwa maana hiyo, natumia msemo huu kwa kusema kwamba, Naibu Waziri katika Wizara hii yeye ndiyo jicho la kuangalia Wanawake wa Tanzania kwa sababu amebeba dhamana yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekitiki, katika suala la watu wenye ulemavu. Tumetaja tu ujumla ajira, elimu, afya lakini, je, tumejiandaa vipi kuhakikisha kwamba bajeti kadhaa itakwenda katika kununua vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu? Bajeti kadhaa itakwenda katika kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa rafiki ili watoto wote waweze kupata elimu na hasa watoto wa vijijini ambao miundombinu siyo rafiki. Je, Bajeti hii tumejipanga vipi kuhakikisha kwamba tunaorodhesha idadi kamili ambayo itatimiza mahitaji ya watoto wenye ulemavu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la ajira. Sheria na Wizara pia na yenyewe kama Wizara ya Fedha bado ina jukumu hilo. Je, tunawekaje mipango yetu katika kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu na wenye sifa wanapata ajira, vilevile mitaji kwa ajili ya kuwawezesha ili waweze kujiajiri. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kama baba, lakini kama Waziri mwenye dhamana katika Wizara hii kuhakikisha kwamba haya mambo katika hii bajeti ijayo ili kusiwepo na maswali haya tuone kwamba tumejipanga vipi ili katika kila kipengele kimoja kijitosheleze katika kusaidia mahitaji hayo ya makundi haya niliyoyataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema; siku zote katika maisha unapokuwa mwongo basi ni vema pia ukawa na kumbukumbu. Tumesikia michango mingi sana ya Waheshimiwa Wabunge, lakini naomba nikumbushe tu mambo yaliyojiri kwa kasi sana mwaka jana, tuliambiwa kwamba: “Nawashangaa sana wanaochoma moto vibaka kwa kumuacha Lowassa akitanua mitaani.”
Mwingine akasema kwamba; “CCM wamempatia Fisadi fomu ya kugombea Urais ni hatari sana.” Swali langu, je, kati ya CCM na wao ni nani hatari katika hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanasema kwamba “nina ushahidi wa kutosha kuhusiana na wizi na ufisadi wa Lowassa na Rostam Aziz.” Leo hii ni nani ambao walimbeba na kumtangaza nchi nzima kumsafisha na wakati huo huko nyuma walisema kwamba ni fisadi? Ndiyo maana nikasema kwamba ukiwa mwongo uwe pia na kumbukumbu ya yale maneno unayosema. Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwa hizi dakika tano zilizosalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wale wote walio katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na michango iliyotolewa Bungeni nawashukuru sana, niendelee katika vipengele vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu ni tatizo na wengi wamezungumzia katika vyuo vikuu ambako pia kuna changamoto kubwa lakini pia tukiangalia katika shule za msingi na sekondari changamoto bado ni kubwa sana, mfano mabinti wengi hasa vijijini kutokana na uhaba wa mabweni hawafiki mbali zaidi. Pia kama tunavyofahamu mabinti wanakabiliwa na changamoto mbalimbali mfano tu binti anapokuwa katika siku zake za hedhi nayo ni changamoto kubwa hata Kamati imeeleza basi Wizara iangalie ni jinsi gani inaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa wototo wenye ulemavu ambao ni changamoto kubwa sana. Naishukuru Serikali kwa suala zima la elimu bure kwa wote ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwaandikisha watoto hawa shule. Siku za nyuma mzazi kama ana watoto wawili, watatu lakini ana mtoto mwenye ulemavu ni afadhali awapeleke hawa wengine, mwenye ulemavu anabaki nyuma. Kwa utafiti mdogo ambao binafsi nimeufanya watoto wenye ulemavu wengi hivi sasa wameandikishwa shule lakini changamoto ni nyingi katika shule zetu mbalimbali. Kwa hiyo, niiombe tu Wizara ihakikishe kwamba watoto wanaweza na wao kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza hata juzi katika vyuo vyetu vikuu changamoto bado ni kubwa kwa wale wanafunzi wenye ulemavu wanaopata bahati ya kwenda vyuo vikuu. Niiombe tu Serikali kupitia Wizara husika hasa katika vyuo vikuu na mfano mojawapo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho miuondombinu ni tatizo. Kwa wanafunzi wanaopata bahati kwenda katika vyuo vikuu na hasa chuo hiki cha Mlimani ni tatizo kubwa kutoka darasa moja kwenda darasa lingine. Ukiangalia mazingira yenyewe katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hawawezi kupata elimu ipasavyo na wanafunzi hawa wengi wao hata matokeo yanapokuja siyo mazuri sana. Wanaopata matokeo mazuri ni bahati.
Kwa hiyo, kutokana na changamoto hii, naiomba Serikali kuangalia ni jinsi gani itaboresha miundombinu ili wanafunzi wenye ulemavu waweze kusoma pasipo changamoto yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie pia katika Shirika la Utangazaji Tanzania na ni-declare tu interest kwamba mimi mwenyewe nimetoka huko. Nasikitika sana kwa Serikali kwa jinsi ambavyo kwa muda mrefu imekuwa ikisuasua kupeleka fedha na hata katika ripoti hii ukiangalia ni kwamba kila mwaka bajeti hiyo inapungua. Mimi nina imani sana na viongozi wetu walioko katika Wizara hii lakini watawezaje kutekeleza majukumu yao endapo bajeti hizi haziwezi kufika? Mheshimiwa Rais amemteua Ayub Rioba kuwa Mkurugenzi nina imani naye, lakini kama hakuna bajeti miundombinu ni chakavu, mitambo imechoka na iliyopo imezeeka ya tangu mwaka 1999...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba tu Serikali kuhakiksha kwamba bajeti hii inaifikisha katika Wizara hii ili waweze kutoa kwa TBC.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu dakika ni chache kwanza kabisa mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, hongera sana Dada yangu Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri Kigwangalla kwa kazi nzuri mnayoifanya, nina uhakika kabisa tunapoelekea vifo vya wanawake na watoto, lakini pia matatizo pamoja na ukatili wa kijinsia utapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa dakika ni tano, naomba nijikite katika suala moja ambalo limezungumzwa hapo jana kwa kirefu na aliweza kulizungumza Mheshimiwa Faida, na mimi pia naomba nijikite katika suala hilo. Suala la ukatili kwa watoto ni kubwa, kwa kiasi kikubwa sana na ukatili huu dhidi ya watoto katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri pia imeelezwa katika ukurasa wa 55.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite na kwa kutoa mifano katika suala hili. Utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Maimamu kule Zanzibar unaonyesha kwa kiasi kikubwa ukatili dhidi ya watoto, watoto wamekuwa wakilawitiwa, watoto wamekuwa wakinajisiwa kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanywa mwaka 2014/2015 umebainisha kuwa suala hili ni janga. Watoto wameharibiwa kwa kiasi kikubwa, watoto wa miaka kuanzia minne na kuendelea. Kwa mujibu wa utafiti huu uliofanywa, unaonesha kwamba nchi za Magharibi kwa kiasi kikubwa zimetumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kwamba nchi za Afrika zinaidhinisha mapenzi ya jinsia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mila, tamaduni na desturi zetu imekuwa ni vigumu. Kwa maana hiyo, ipo nguvu kutoka nje ambayo kwa mujibu wa utafiti huu inawatumia baadhi ya walimu wa madrasa kule Zanzibar, lakini pia walimu wa shule za msingi inawatumia. Walimu hawa wanapewa pesa na kuhakikisha kwamba wanawalawiti watoto ili kuandaa kizazi ambacho itakuwa ni rahisi baadaye kuwa na kizazi cha watoto ambao wanashiriki mapenzi ya jinsia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huu nipo tayari kuuthibitishia Bunge hili na kukutanisha na wale ambao tayari wamekwisha fanya utafiti huu na kubaini ni kwa jinsi gani watoto wetu wameharibiwa na watoto wengine wameshakuwa wazoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utafiti huu Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alishakabidhiwa ripoti, pia katika Siku ya Wanawake Duniani pia walizungumzia hawa maimamu kuonesha ni kwa jinsi gani wazazi, walezi, lakini pia walimu wa madrasa ambao ndio tunawategemea kuwalea na kuwakuza watoto wetu katika maadili ndio wanaoshiriki, lakini pia walimu wa shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu angalizo kwamba sisi kama wazazi, hata wageni wanaokuja nyumbani kwetu tusijenge tamaduni za kuhakikisha kwamba wanalala na watoto wetu kwa sababu ndiyo hao wanaowaharibu watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia kwa undani zaidi ukazungumza na watu ambao wanashiriki mapenzi ya jinsia moja, atakuambia mjomba ndiye aliyeanzisha tatizo hilo, mwingine atakuambia ni ndugu wa baba ndiye aliyeanzisha tatizo hilo. Kwa hiyo, tujenge tamaduni watoto wetu tusiwaweke karibu na ndugu wanaofika katika familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo ni kubwa na ni janga, ni janga la kitaifa. Tunaandaa kizazi ambacho baadaye kitakuwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya malengo ya milenia ilikuwa ni kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, watoto wachanga pamoja na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Pamoja na kuwepo lengo hili, Tanzania bado tuna changamoto kubwa ya vifo vya wanawake na wajawazito pamoja na watoto wachanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 16 ameeleza na kuthibitisha kuwa vifo hivi bado ni changamoto kubwa, ambapo kwa mwaka 2015 idadi ya vifo ilikuwa 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Hili ni tatizo kubwa ambalo linahitaji nguvu ya pamoja kati ya wanawake na wanaume. Wanaume wakielimishwa na wakawa karibu na wake zao kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza vifo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mila potofu katika jamii zetu ni tatizo. Kwa mfano katika baadhi ya makabila mwanamke mjamzito hawezi kwenda kujifungulia hospitali mpaka apate ruhusa ya mama mkwe au wifi ndipo aende hospitali au kwa waganga wa kienyeji. Hili ni tatizo na elimu ni muhimu kutolewa kwa jamii hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Arusha takwimu zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito vimeongezeka kwa asilimia 31 kutoka vifo 49 kwa mwaka 2015 na kufikia vifo 72 kwa mwaka 2016. Kwa upande wa vifo vya watoto kwa mwaka wa jana kulikuwa na vifo 978 waliopoteza maisha sawa na kifo kimoja kwa kila vizazi hai 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya vifo hivi ni kutokana na upungufu wa vituo vya afya katika Halmashauri za Mkoa wa Arusha ambapo kwa jamii za wafugaji kama inavyoeleweka wanaishi mbali na miji, hivyo naomba Wizara isaidie kwa kutimiza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa WHO duniani kote hasa nchi zinazoendelea wanawake 300,000 hufa wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua, na zaidi ya watoto milioni mbili hufa katika siku 28 za mwanzo na wengine zaidi ya milioni mbili wakiwa si riziki. Kwa upande wa watoto takwimu za WHO zinasema kuwa watoto wachanga na wale wanaozaliwa wanakufa. Vifo hivi vinaweza kuzuilika kwa kuwa na huduma bora za afya wakati wa ujauzito na kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana vifo vinavyorekodiwa ni kwa wale tu wanaofika hospitali na wengi hujifungua majumbani kutokana na umbali pamoja na mila na desturi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na naomba tu kwanza kabisa ni-declare interest kabisa kwamba na mimi ni mwanahabari, kwa hiyo, Wizara hii ni ya kwangu na inanihusu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kutupa afya na kuweza kujumuika hapa. Kwanza kabisa nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya. Pili, nampongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, dada yangu pamoja na Mheshimiwa Mwakyembe kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia masuala mawili. Kwanza nianze na TBC kwa sababu ndiyo ambayo imenifanya mimi nikawa Amina hapa nilipo. Nimefanya kazi TBC kwa miaka nane. Shirika la Utangazaji TBC lina hali mbaya kiasi ambacho jitihada zinahitajika kwa kweli ili kuona ni kwa jinsi gani tunawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC ni chombo cha umma, ni shirika pekee la habari la umma katika nchi hii na ndiyo chombo cha Serikali na siku zote wanasema kwamba ni vyema ukaanza na nyumbani kwako. Huwezi kwenda kwingine pasipo kuanza na nyumbani kwako. Inatia uchungu unapoangalia vyombo vingine vya habari vina hali nzuri wakati sisi chombo chetu kina hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali halisi naijua sana TBC, mitambo yake imechoka mno, inahitaji siyo kufanyiwa marekebisho, bali inahitajika mitambo mingine mipya ili kuweza kwenda na wakati huu uliopo. Hata kama hao wafanyakazi, kwa kweli wakati mwingine ile morally ya kazi inashuka. Siku moja mjitolee tu mwangalie hata wanapokuwa katika matukio mbalimbali ambayo wao wanahusika muone ni kwa jinsi gani wanavyojitoa katika kuhakikisha kwamba jahazi linakwenda, lakini ndani yake maumivu na mateso wanayopata kwa mitambo ilivyo chakavu, inatia uchungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba na nina imani sana na Serikali na nina imani sana na Mheshimwa Dkt. Mwakyembe. Kwanza yeye ana taaluma hiyo ya habari lakini vilevile ni mwanasheria. Kwa maana hiyo, ni matarajio yangu makubwa sana kwa Serikali na wewe pamoja na dada yangu mpendwa Mheshimiwa Anastazia kwamba mtaliangalia kwa jicho la huruma na kwa jicho la pekee Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba maslahi ya wafanyakazi wa TBC yaangaliwe. Wana miezi saba hawana posho na kama mnavyojua, watu wanategemea kwa kiasi kikubwa sana hizo posho. Mishahara mara nyingi tunakopa; na kama umekopa mshahara, unategemea ile posho ndiyo iweze kukusaidia. Sasa kama hata hiyo posho hupati miezi saba! Juzi juzi wamelipwa posho ya miezi minne na bado wanadai posho ya miezi saba. Jamani hebu tuwe na huruma tuwafikirie wafanyakazi hawa wa TBC ambao wanajitoa. Kwanza hawa ni wazalendo wa hali ya juu ambao wanahakikisha kwamba TBC inasimama na kwenda, pamoja na changamoto zote zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atuambie hivi tangu StarTimes wameingia ubia na TBC mpaka leo ni miaka mitano tayari imepita na nilijua ule mkataba ni wa miaka mitano, lakini kumbe unakwenda mpaka miaka kumi. Naomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie kwamba TBC tangu imeingia ubia na StarTimes imefaidika nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wako pale, wanatumia eneo lile la TBC pamoja na kwamba tunawahitaji sana wawekezaji, lakini hatuhitaji wawekezaji ambao wanakuja kutunyonya. Tunataka wawekezaji ambao na sisi tutafaidika. StarTimes kama kweli katika yale makubaliano ya Mkataba wao wangetimiza vyema, leo hii Shirika hili la Utangazaji la TBC lisingekuwa na shida iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi sana kwamba Mkurugenzi wa TBC ataweza ku-perform vizuri endapo mtamwezesha. Tido alipoingia alikuta TBC ina shilingi bilioni sita ndiyo maana TBC ikapanda juu kwa haraka sana, lakini ameingia Mkurugenzi wa sasa, hakuna fedha, madeni chungu mzima, atawezaje ku-perform? Mimi nawaomba sana mhakikishe kwamba mnaisaidia TBC ili iweze ku-perform vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba kaka yangu Rioba, kwa upande mwingine ni shemeji yangu, dada yangu ameolewa huko Ukuryani huko Musoma, Mara. Namuamini sana na nina matarajio makubwa sana naye, lakini pia kaka yangu Rioba punguza ukali. Umekuwa mkali mno kiasi kwamba hata wafanyakazi wakikuona wanakukimbia kama panya. Punguza ukali tushirikiane. (Makofi)

Mfano, hata sisi huku tunafanya kazi vizuri sana na Spika. Ukiweka ukaribu vizuri na wafanyakazi, pamoja na kwamba ndiyo huo ukaribu uwe na mipaka ili muweze kushirikiana na kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kujibu baadhi ya hoja kuhusu uhuru wa habari; na mimi hapa nitanukuu tu mambo machache. Kwa mfano, tofauti na mawazo ya wenzetu ambao wanasema kwamba nchi hii haina uhuru wa vyombo vya habari, naomba ninukuu kwa kusema kwamba nchi hii ina idadi ya vyombo vya habari na njia nyinginezo za mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Tanzania ina magazeti na majarida 428, redio 148, televisheni 32 na watumiaji wa internet wapatao milioni 20, yaani nusu ya nchi; na kuna lines za simu zilizosajiliwa na zinazotumika zipatazo milioni 41; robo tatu ya idadi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ripoti mbalimbali duniani, Tanzania iko juu duniani na Afrika. Ukiacha jinsi ambavyo wanazungumza hapa, Tanzania kwa mfano, taarifa ya mwaka huu ya Chama cha Wanahabari Wasio na Mipaka (Reporters Without Borders) ambayo inasema kwamba, kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 bora katika uhuru wa habari Afrika. Ya kwanza katika Afrika Mashariki ikiwa ni ya 83 duniani ambapo Kenya ni ya 95, Uganda ni 112, Sudan Kusini 145, Congo-DRC ni ya 154, Rwanda ya 159 na Burundi iko katika nafasi ya 160. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti hii, Tanzania Kimataifa pia imezizidi baadhi ya nchi kubwa ya huko Ulaya. Katika nchi hizo mfano, Marekani na Asia katika uhuru wa kujieleza na habari; Tanzania imezidi nchi za Ugiriki, Israel, Brazil, Paraguay, Uganda, Falme za Kiarabu, Cameroon, Tunisia na Guinea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ambayo ilitungwa mwaka 2016 hapa ya Huduma ya Habari namba 12 ya 2016 ni sheria ambayo imeleta mageuzi makubwa sana katika kutetea uhuru wa habari kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, imebainika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kama wasemavyo wahenga kwamba kila kiongozi basi anakuwa na baraka za Mwenyezi Mungu. Kwa kusema hivyo, naomba nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mimi nasema wazi kwamba ni chaguo la Mwenyezi Mungu na ni chaguo la Mwenyezi Mungu kutokana na uthubutu wake hasa kwa tukio kubwa leo hii ambalo amelithibitishia Taifa la Watanzania ni kwa jinsi gani kwa muda mrefu tumekuwa tukiibiwa madini yetu na sisi Watanzania tukiendelea kuwepo katika limbwi kubwa la umaskini. Kweli huyu ni chaguo la Mwenyezi Mungu, nampongeza sana kwa uthubutu wake, kwa kile ambacho amedhihirisha leo hii, basi yale aliyokuwa akiyafikiria, kwamba ni kweli, kwa hili tuzidi kumuombea Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu ili aweze kuyabaini mengi na hatimaye Watanzania wafurahie rasilimali zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nichukue pia nafasi hii kuipongeza Wizara, nampongeza Waziri, nampongeza pia na Naibu Waziri, niwapongeze pia na Wakurugenzi wa TANAPA, lakini pia Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, pamoja na changamoto zote hizo na lawama nyingi lakini kazi wanayofanya ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwa nini naipongeza Serikali na naipongeza pia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwanza kwa hatua yake ya mfumo mpya wa kielektroniki wa kukusanya maduhuli, ambao unaitwa NCAA Safari Porto ambao umeonyesha ni kwa jinsi gani wameweza kukusanya shilingi bilioni 81 hii ni faraja kwetu, kwa maana kwamba endapo katika maeneo mengi kuhakikisha kwamba mfumo huu unafanya kazi pesa zitakazo ingia katika sekta ya utalii zitakuwa ni nyingi na zitaweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishauri Serikali na niseme tu kwamba uzuri wa Bonde la Ngorongoro na sababu ya Ngorongoro kuingia katika maajabu saba ya dunia ni kutokana na upekee kwamba wanyama pamoja na binadamu wanaishi pamoja na kwa maana hiyo basi pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo mimi naishauri tu kwamba Wizara itekeleze maagizo ya Waziri Mkuu ya kuhakikisha kwamba katika Bonde la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wanatenga maeneo ili mifugo isiingie katika bonde lile na badala yake waende kunywesha maji katika maeneo hayo ambayo yatakuwa yametengwa tofauti na hivi sasa kwamba ndio tunataka kuwaondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwaondoa pasipokuwa na mbadala, je, tumewasaidia kweli hawa wananchi? Kwa hiyo tutimize tu hili agizo la Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba tunatenga maeneo na hayo maeneo basi hao wafugaji watakwenda kunywesha mifugo yao na badala yake hakutakuwa na mifugo itakayoingia katika Bonde la Hifadhi ya Ngorongoro kwa sababu uzuri wa Ngorongoro ni ile Crater yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia ambalo napenda niishauri Wizara, kwa mfano siku ya Jumapili hapa kulikuwa na semina na tulielezwa ni kwa jinsi gani ambavyo baadhi ya wanyama wapo hatarini kupotea, na hii ni kutokana na muingiliano kati ya binadamu na hao wanyama. Ni kweli nakumbuka siku za nyuma ukiingia tu eneo la Monduli ulikuwa unakutana na wanyama wengi katika maeneo hayo, lakini hivi sasa hakuna na hii inaonyesha kwamba ni kweli ni kutokana na muingiliano baina ya binadamu na wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa pamoja na yote hayo kama kweli katika hifadhi zetu, kama kweli katika mfano Bonde la Ngorongoro tunataka kweli wale wanyama waendelee kuwepo kule tuhakikishe kwamba hata haya magari yenyewe mfano, msimu wa utalii kwa siku zinaingia mpaka gari 200. Sasa Serikali iangalie jinsi gani itaweza kupunguza hayo magari na hata ikiwezekana pamoja na kwamba tozo la kodi lipo basi tuone uwezekano wa kuweka tozo kubwa ili magari yasiingie kwa wingi kule na badala yake tuendelee kuhifadhi mazingira tofauti na hivi sasa ambapo magari ni mengi sana katika Crater ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine pia tunafahamu kwamba Serengeti, hifadhi zilizopo Kaskazini ndizo ambazo hasa kwa kiasi kikubwa zinasaidia hata kuendesha hizi hifadhi nyingine, lakini ni pengine ni kutokana na miundombinu ambayo ipo katika maeneo hayo. Katika hizi hifadhi nyingine ambazo zipo naishauri Serikali kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ili basi hifadhi hizi ziweze kufikika kwa urahisi na watalii waweze kwenda kule, lakini pia kuhakikisha kwamba inatangaza vivutio vingi ili watalii waweze kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukienda Kigoma kuna hifadhi ya Gombe na Mahale na kwa bahati nzuri hifadhi hii ina chimpanzee ambao katika hifadhi nyingine ni vigumu sana kuwapata. Sasa watalii wengi wanashindwa kufika kule kutokana na miundombinu ambayo sio rafiki. Kwa maana hiyo endapo tutaboresha miundombinu na kuhakikisha kwamba wanafika kule kwa urahisi na kwa bahati nzuri hivi sasa tunayo bombardier ambayo inakwenda kule, lakini je, katika kwenda huko Gombe na Mahale miundombinu ikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawahamasishaje watalii ili waweze kufika huko hii ikiwa ni pamoja na kutangaza zaidi na hata kwa kutumia vyombo vyetu vya humu ndani lakini pia vyombo vya nje kama ambavyo kwenye ripoti yenu mmeonyesha. Kwa kufanya hivyo tutaweza katika hifadhi zetu kupata watalii wengi zaidi na kuingiza pato kubwa kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia utalii sio kwamba ni hifadhi tu, utalii hata majengo ndio maana Zanzibar wanakwenda kule kwa sababu ya Mji Mkongwe wa Zanzibar. Ukienda katika Jiji la Dar es Salaam mfano Posta ni eneo ambalo lingefaa sana ule mji badala ya kuubomoa yale majengo ya zamani, majengo yale tungeyaacha ili uwe ni mji ambao utakuwa ni kumbukumbu. Tofauti na hivi sasa tunabomoa majengo yale ya zamani na kujenga majengo mapya, tupanue kwa kwenda katika maeneo mengine ambayo yatatengwa ili basi tuweze kujenga zaidi na hata kuwekeza vivutio zaidi ambavyo vitawavutia wawekezaji na sio kubomoa tu yale majengo ambayo ni majengo yamekuwepo kwa muda mrefu na majengo hayo tunayapoteza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wangeweza kufanya hivyo leo hii kusingekuwa na watalii wengi ambao wanakwenda, umebaki kuwa ni mji wa kihistoria, Mji Mkongwe wa Zanzibar. Kwa hiyo, mimi naishauri sana Serikali kuhakikisha kwamba inazingatia haya lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba miundombinu inawezesha watalii wengi kuweza kufika kule. Lakini pia katika huu mfumo unaotumika na Ngorongoro tuhakikishe kwamba tunaongeza mashine katika lile eneo la geti pale ili kuepuka ule mrundikano wa watalii wanapofika pale kwa wingi, kwa sababu wakati mwingine mtalii anapokuja yeyeanataka afike pale amalize zile taratibu mara moja aweze kuingia, lakini matokeo yake anafika pale anapanga foleni kwa kweli inakuwa ni usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuangalie ni jinsi gani mzee wetu Maghembe pale kwamba tunaboresha vipi kwa kuweka kama ni hiyo mifumo ya kielektroniki inakuwepo ya kutosha ili wanapofika pale kusiwepo na huu usumbufu, lakini kwa wale ambao wanasema kwamba tozo hizi za kodi kwamba zimesababisha watalii...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na hatimaye kuweza kusimama leo hii katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwape pole wazazi wote waliopoteza watoto wao katika ajali mbaya ya gari la shule iliyohusu shule ya Lucky Vincent, Mkoani Arusha. Niwape pole sana na Mwenyezi Mungu awajalie ili waweze kuendelea na mambo mengine na wale watoto pia waliokwenda jana kupata matibabu nje, Mwenyezi Mungu awajalie wapone na warudi kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nitoe pongezi za dhati kwa sababu amechangia kwa kiasi kikubwa watoto wenye ulemavu na hasa wazazi lakini walezi kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shule ili waweze kwenda kupata elimu. Miongoni mwa watu ambao walikuwa ni waathirika wakubwa katika suala zima la elimu ni watoto wenye ulemavu ambao kutokana na mila, desturi na tamaduni zetu wazazi kwa mitazamo tu hasi waliwaacha na kuwafungia nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa ujio wa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kuleta elimu bure hata wazazi wenyewe wameona kwamba ni wakati muafaka wa kuwapeleka watoto wao shule. Kwa hiyo, nampongeza sana na niseme tu kwamba kwetu sisi tunaona Mheshimiwa Rais Magufuli ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Waziri pamoja na Naibu wake na hawa ni akinamama. Wanasema siku zote uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Niwapongeze sana lakini pamoja na pongezi hizo na pongezi za ujumla kwa Serikali vilevile basi nizungumzie changamoto zilizopo katika suala zima la elimu na hasa kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu pamoja na kwamba hivi sasa shule nyingi watoto wamejitokeza na kwenda kupata elimu lakini nikianza na suala zima la miundombinu pamoja na kwamba Serikali imetoa vifaa, pongezi sana kwa hilo Mama Mheshimiwa Profesa Ndalichako lakini bado miundombinu ni tatizo na ni kikwazo kwa watoto wenye ulemavu kuweza kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia miundombinu ni kwa ujumla kuanzia madarasa lakini pia umbali na tatizo lingine kubwa zaidi ni vyoo. Pamoja na jitihada ambazo mmezionesha mnakwenda kujenga vyoo katika shule za msingi na shule za sekondari watoto wenye ulemavu wanapata shida sana wanapokuwa shuleni kwa sababu miundombinu ya vyoo inawafanya wasiweze kufika katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika vyoo vingi ambavyo vinatumiwa na wanafunzi wote kwa ujumla na hasa ukiangalia tundu moja wakati mwingine linatumika mpaka na watoto 25-30 kwa huyu mtoto mwenye ulemavu, mfano tu mtoto mwenye ulemavu anayetambaa, niambie mazingira yale anafikaje chooni? Inakuwa ni vigumu sana. Kwa hili, niwaombe tulete sheria kwamba kila shule ni lazima kuwepo na vyoo ambavyo vitawawezesha watoto wenye ulemavu kupata huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, nalishukuru sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nimshukuru Katibu pamoja na Spika kwa sababu wanaelewa kwamba Bunge hili limetujumlisha wote lakini pia miundombinu ni rafiki inayotuwezesha kwenda katika maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na kwa sababu watu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania na wao wanakarabati hizi shule muwape mwongozo kuhakikisha kwamba katika kila shule wanayokwenda kukarabati wahakikishe vyoo viwili vinakuwepo kwa ajili ya watoto wenye ulemavu na Walimu Wakuu waweke utaratibu maalum ambao utawezesha hawa watoto peke yao wenye ulemavu kwenda katika vile vyoo na wasiweze kuingia hao wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ni kweli kwamba Serikali imetoa vifaa kwa ajili ya watoto wenye ulemavu lakini kwa walimu bado ni tatizo. Ni tatizo kwa sababu gani? Kwa mujibu wa mwongozo wa huduma kwa watumishi wa umma wenye ulemavu ambao unasema nyenzo na vifaa vya kuongezea uwezo wenye ulemavu Wizara, Idara, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe kwamba watumishi wenye ulemavu wanapata huduma zitakazowasaidia kutekeleza majukumu yao kikamilifu kama vile nyenzo na vifaa ili kuwasaidia kuongeza kiwango chao cha kujitegemea katika maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwongozo huu unawataka waajiri na siyo kwa Wizara ya Elimu peke yake ni waajiri wote kwa ujumla na bahati nzuri yupo hapa Mwenyekiti wa Waajiri hili pia alibebe na kusisitiza waajiri wote wanaowaajiri watu wenye ulemavu wanahakikisha ni kwa namna gani watu wenye ulemavu wanaweza kufika katika sehemu zao za kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu nachangia Wizara ya Elimu, hawa Walimu wana changamoto nyingi, hawana nyenzo muhimu ambazo zinawawezesha wao kuweza kufanya kazi zao kwa ukamilifu. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuoimba na kuishauri pia Serikali kuhakikisha kwamba inawawezesha Walimu hawa.

Ukiangalia katika Wizara ya Elimu hawa Walimu wenye mahitaji maalum wengi ndiyo wanaopata ajira kwa wingi huku, kwa hiyo, tuhakikishe tunawawekea miundombinu pamoja na kuwapa nyenzo ili waweze kufanya kazi zao pasipo usumbufu. Vilevile kuhakikisha wanawekwa maeneo ya karibu ili basi wasipate shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kwamba kumekuwepo na utaratibu ambapo Serikali inaratibu wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika shule tofauti, tofauti, mfano, shule ya Buigiri na Furaha kule Tabora na nyinginezo. Wanafunzi wenye ulemavu ambao wanakwenda kusoma kwenye shule hizo kwa sababu ya mila, tamaduni, desturi na mitazamo, wazazi wengi wanaona kwa nini ampeleke mtoto lakini sasa hivi wanakwenda na Serikali ikaweka utaratibu kwamba hawa wanafunzi wakati wa likizo inawasafirisha kuwarudisha nyumbani lakini mwaka jana mmefuta huu utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mama yangu anapofuta huu utaratibu hawa watoto wanabaki kule shuleni mwaka mzima. Kwa mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu mfano shule iliyopo Shinyanga ambayo sasa hivi imekuwa kama ni kituo wengi wamekwenda kuwatupa pale watoto hawarudi hata nyumbani. Sasa ule utaratibu wakiondoa kwamba hawawachukui tena kuwarudisha nyumbani yaani pale ndiyo inakuwa nyumbani kwao na kama mnavyojua tukasome lakini pia turudi nyumbani ili kujumuika na wazazi wetu. Wakituacha maeneo ya shule wasipoturudisha nyumbani ni sawa na wametutupa kwa maana kwamba sisi tunakuwa sasa ni watoto wa pale pale mpaka tumalize shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, yeye ni mama na siku zote mama ndiyo mwenye uchungu, apigane hawa watoto warudi nyumbani kwao, kuwepo na usafiri utakaowapeleka na kuwarudisha nyumbani. Ndiyo wamewaandalia mazingira lakini pia wakiwaacha kule miaka yote inakuwa ni kama vile adhabu au ukizaliwa mtu mwenye ulemavu basi inakuwa ni kama vile ndio mkosi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunasimama hapa na kutoa michango ni kwa sababu jamii ilituwekea mazingira mazuri, wazazi wetu walikuwa wanajua umuhimu huo na ndiyo maana wakatusomesha na leo hii tuko hapa. Sasa tusipowaandalia mazingira mazuri tutawapata wapi akina Amina na Ikupa wengine.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema, lakini kipekee kabisa niwapongeze wenzetu waliopata nafasi za uteuzi. Kipekee kabisa nimpongeze pacha wangu Mheshimiwa Ikupa Stella Alex kwa nafasi uliyoipata, nina imani na wewe na nina amini kabisa utasaidia kuishauri Serikali hasa katika masuala ya watu wenye ulemavu. Waswahili wanasema; kitanda unachokilalia ndio hapo utakapojua kunguni wake. Kwa hiyo wewe unajua, unajua adha na shida mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa sababu hata wale wanaochangia ni wanachangia kwa nia njema kuona kwamba ni kwa namna gani mpango huu utakwenda kunufaisha Taifa la Tanzania na kufanya uchumi wetu uendelee kukua. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ni kweli kwamba katika Bara la Afrika uchumi wa nchi ya Ethiopia unakua kwa kasi sana lakini pia Tanzania tunakua kwa uchumi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Tanzania kuwepo katika ukuaji wa uchumi, bado pato la wananchi wa kawaida ni dogo sana kwa maana kwamba maisha ya wananchi wa kipato cha chini hali zao bado ni duni sana. Kwa hiyo, katika mpango huu tulitarajia kuona kwamba mikakati madhubuti ambayo itakwenda kusaidia mbali ya kukua kwa Pato la Taifa, lakini tuone ni kwa kiasi gani kwamba mpango huu unasaidia kukuza pato la mwananchi wa kipato cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia imezungumzia mfumuko wa bei, lakini katika mfumuko wa bei huu pamoja na kwamba wanasema umeshuka, lakini je, kwa kipato cha mwananchi wa kawaida pato hili limeshuka kwa kiasi gani. Tunaona kwamba bado hali iko pale pale. Kwa hiyo tuone kwamba ni kwa jinsi gani tunaboresha maisha ya wananchi wetu, kwa mfano kwa kuangalia ni vitu gani ambavyo ni muhimu kwa mwananchi wa kawaida. Bei ya mafuta inapokuwa juu ni dhahiri kabisa kwamba inaumiza watu wengi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona kwamba katika muda wa mwaka mmoja, bei ya sukari imekuwa ni tatizo kubwa sana ambapo bei yake pia imekwenda mpaka wakati mwingine imefika shilingi 3,500 mpaka shilingi 4,000. Sukari inategemewa na kila mwananchi wa kawaida, kwa hiyo tunapozungumzia kwamba mfumuko wa bei umeshuka, tuangalie kwa huyu mwananchi wa kawaida umeshuka kwa kiasi gani, tunawasaidiaje wananchi wa kawaida ili uchumi wao na wao pia uweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika suala zima la watu wenye ulemavu. Hapa katika ukurasa wa 53 ambapo wameweka vijana, ajira na wenye ulemavu nilitarajia kuona mambo mengi ambayo yangekuwa na manufaa, mpango huu ungeeleza ni kwa jinsi gani unakwenda kujikita kusaidia kundi zima la watu wenye ulemavu. Kwa mfano, hatuna idadi kamili ya watu wenye ulemavu na ili upange mpango wako uweze kukamilika kwamba utafanya nini kwa kundi fulani au kwa vijana ni vema basi tujue kwamba je, tuna watu wangapi mfano walemavu wasioona, kwa mfano tuna walemavu wa viungo, viziwi na wengine wengi. Kwa kujua idadi yake tunapanga mipango kulingana na idadi ya watu ambao tunakwenda kuwasaidia kukwamua kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu tunapozungumzia pato la chini na hasa kwa kundi la watu wenye ulemavu ni watu ambao maisha yao ni ya duni sana. Hasa unapokwenda vijijini, hali zao bado ni duni. Katika mpango huu nilitarajia tuone kwamba kulingana na idadi hii ni mikakati gani Serikali mpango huu unakwenda kuwasaidia vipi watu wenye ulemavu.

Kwa hiyo, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuona kwamba ni kwa jinsi gani mnapokwenda kuongezea zile nyama ambazo zimechangiwa na Wabunge tuone kwamba basi mpango huu unakwenda kuwasaidiaje watu wenye ulemavu badala ya jinsi mlivyoweka hapa kwamba vijana, ajira na wenye ulemavu. Wenye ulemavu wana mahitaji yao muhimu tofauti ni vijana, lakini wana mahitaji yao muhimu tofauti na wengine. Huwezi kulinganisha na kijana wa kawaida. Tunawawekea mipango gani, mikakati gani ya kuwasaidia watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwa sababu suala la chakula limezungumziwa sana, naomba nizungumzie kwangu mimi hasa katika suala la kuboresha kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo. Wengi wetu hapa tumesomeshwa na kilimo, pia na mifugo tumetoka huko. Sasa tunapoelezea katika mpango huu tungeona kwamba katika kilimo tunaboresha vipi kilimo chetu. Ni kweli wananchi wanalima, lakini kilimo chenyewe bado ni kilimo duni. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi hali ya hewa hivi sasa baadhi ya maeneo mvua zimekuwa shida. Je, tunawashauri vipi wananchi wetu ili walime kulingana na hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaangalia suala la pembejeo ambalo kwa wakati mwingine limekuwa likifika kwa muda ambao sio sahihi, je tunajipangaje? Miundombinu ni suala muhimu sana kwa sababu hata wanapozalisha kama miundombinu sio rafiki, sio mizuri mfano barabara. Kule kwetu ukienda kuna baadhi ya maeneo vijana wanalima nyanya sana, lakini kwa sababu barabara ni mbaya na wachuuzi wanaokwenda kuchukua katika maeneo yale wananunua kwa bei wanayotaka, kwa hiyo, bado hatujawasaidia vijana wetu kuwakomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika mpango huu, tuone kwamba kutakuwa na mikakati ya elimu kwamba katika eneo fulani kwa mfano yanajulikana maeneo ambayo ukienda Mkoa wa Rukwa, Katavi, ukienda Ruvuma ni baadhi ya maeneo ambayo wanapata mvua nyingi. Je, maeneo yale ambayo hawapati mvua tunawaandaaje wananchi wetu ambao tunajua kabisa kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo, tunawaandaaje ili wao waweze kulima mazao kulingana na mvua. Waweze kulima mazao ambayo yataendana na eneo husika, katika mpango huu sijaona kwamba ni kwa namna gani tunaweka hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mitaji ni muhimu, siku hizi kila kitu kinahitaji mitaji, je, tunaandaaje kuhakikisha kwamba tunawawezesha. Mfano, kama ni vijana ambao ndiyo nguvu kazi tunawaandaaje kwa mitaji ili vijana hawa tunataka kwamba wajiajiri wao wenyewe na kwa sababu tunakwenda katika sera ya viwanda, tunawaandaaje kwamba ili hizo malighafi hao vijana wanaokwenda kujiajiri wenyewe, je, mitaji wanapata wapi. Katika mpango, mpango haujaeleza wazi kwamba vijana hawa tunawaandaaje katika suala la kilimo na kwa sababu kilimo ndiyo ajira pekee ambayo inaweza kuwaajiri vijana wengi wakajiajiri wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji pia kwa sababu hata hawa wakulima wadogo wadogo bado wanahitaji wawekezaji wakubwa ili kwa namna moja kila mmoja anamuhitaji mwenzake. Mipango gani inawekwa ili kuvutia hawa wawekezaji ambao na wao pia waweze kuwasaidia hawa wakulima wadogo wadogo. Vyote hivyo ni vitu ambavyo Mpango ungeweza kueleza kwa uwazi ili basi yeyote yule anayekamata Mpango huu na yeye anasoma anajua kabisa kwamba nchi imeandaa kitu fulani, kwa hiyo vijana au wananchi tujiandae kwa jambo hili kutokana na Mpango jinsi ulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuboresha ufugaji na kwa mfano, tuliona hivi karibuni bilionea mmoja Bill Gates ambaye anaamini kabisa kukuza uchumi wa wananchi ukiwawezesha katika suala zima la ufugaji kwa mfano kuku. Kuku hivi sasa ni mali, kuku ni pesa. Tunawaandaaje wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba na wao wanajiingiza huko kwa kuamini kabisa kwamba ukiwa na kuku hata watatu, nakumbuka siku moja Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofika kijijini kwetu alisema kwamba wananchi ili kulipia umeme wa REA ukifuga kuku watatu tu tayari umeshalipia gharama ya kupata umeme wa REA. Je, sasa katika mpango ambao ndiyo tunategemea huku tunawaandaaje wananchi ili hawa wananchi waweze kujikita zaidi katika suala zima la ufugaji kwa sababu ufugaji kama nilivyosema kuku ni pesa. (Makofi)

Vilevile katika suala zima la uvuvi kuna ufugaji wa samaki hivi sasa. Ufugaji wa kisasa ambao ili kukuza mitaji yao na kipato cha wananchi pia nilitarajia kwamba Serikali yenyewe imejiandaa vipi. Kwa hiyo, katika Mpango huu tungeweza kuona kwamba wananchi watasaidiwaje katika ufugaji wa samaki ili kuhakikisha kwamba tunapunguza makali ya maisha jinsi yalivyo kwa hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona kuna uvuvi katika Bahari Kuu. Mfano, zipo meli nyingi zinakuja hapa nchini na zinakwenda katika bahari kuu kuvua. Je, zile leseni ambazo wanapewa je leseni hizo zinatolewa kulingana na ukubwa wa meli jinsi ulivyo au watu wanapewa tu wanakwenda kuvua kadri yeye anavyoweza na ukubwa wa meli yenyewe. Kwa hiyo, kama tunataka kukuza uchumi wetu katika suala la uvuvi, kwenye Bahari Kuu basi tuone kwamba hizo leseni ziendane kulingana na ukubwa wa meli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa sababu Serikali yetu hivi sasa imeweza kununua ndege, basi tuone ni wakati sasa wa kufikiria mbali zaidi kuwa na meli ya kwetu wenyewe ya uvuvi ili tuweze kuvua wenyewe kwa sababu mahitaji ya samaki hivi sasa watu wengi wanaondoka katika ulaji wa nyama za ng’ombe na ulaji wa nyama nyingine, kwa hiyo wanakimbilia zaidi kwenye samaki na kuku. Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Waziri wa fedha jambo ambalo ningetarajia kuliona katika Mpango pia kwamba Serikali katika miaka miwili/mitatu ijayo pengine tumejikita katika kununua meli yetu wenyewe ili basi nasi katika uvuvi wa Bahari Kuu tuweze kwenda kuvua wenyewe na sio kila siku wavue tu wageni wanaokuja hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ile Sera ya Huduma za Fedha kwa ajili ya wananchi. Tuone kwamba hivi sasa inafanyiwa kazi ili basi wananchi waweze kufaidika na hilo. Kwa mfano hili tuangalie kwenye Halmashauri zetu kwa sababu tayari tunawaandaa wananchi ili wananchi waweze kuzalisha kwa wingi. Mfano, katika viwanda, tunapokwenda kwenye viwanda, je, tumewaandaaje katika suala zima mfano kwenye jamii tumeandaaje katika wataalam wa afya maji vijijini ili wananchi basi wawe na afya njema. Vyote hivi ni vitu ambavyo vinahitaji kuzingatiwa kwa umakini kwa sababu wakati mwingine watu wetu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Kwa hiyo, kukiwepo na mipango thabiti na katika Halmashauri zetu, kwa mfano Maafisa Biashara hawa wakawezesha kuandaa vikundi kwa ajili ya watu wenye ulemavu na kwa sababu sasa hivi kuna ile asilima nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.

Kwa hiyo, Maafisa Maendeleo Jamii na wao wahakikishe kwamba wanaandaa na kutoa mafunzo kwa makundi yote hayo ili kuhakikisha kwamba kila mmoja anajitegema na kuongeza pato yeye mwenyewe lakini pia katika kukuza uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la mikopo kwenye mabenki ni kweli kwamba tumeona Benki Kuu kwa mfano imepunguza riba kuanzia asilimia 16 lakini vilevile ikashuka mpaka asilimia 12 na sasa asilimia tisa, lakini bado mabenki yanatoza riba kubwa mfano, mpaka asilimia 20, 22. Sasa tunawaandaaje hawa wananchi kama kweli Benki Kuu imepunguza kutoka asilimia 16 imekwenda asilimia 12, imekwenda asilimia 9 kwanini mabenki yaendelee kutoza riba ya asilimia 20 mpaka 22 huku sio kumsaidia mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naishauri sana Serikali yangu kwa upendo kabisa kuhakikisha kwamba kama kweli na hili pia ndiyo maana tumeona kwamba kutokana na jinsi uhaba hivi sasa biashara nyingi ambazo hazijaenda vizuri lakini pia wananchi wengi hawana fedha. Tumeona jinsi ambavyo watu wanauziwa nyumba. Kwa hiyo, kama Serikali katika Mpango tuweke kwamba ndiyo muda umefika muda fulani mtu aongezewe kulipa ili basi kuepusha watu kuwatia katika umaskini. Tukifanya hivi tutawasaidia sana wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ufugaji, ninaiomba Serikali na hasa katika mpango huu kwa sababu wakati mwingine tunawatia wananchi umaskini.

Mimi ni mtoto ambae nimekulia kwenye familia ya ufugaji. Tumeona juzi huko Rukwa wakati mwingine wafanyakazi au hawa Watumishi wa Serikali wawe na moyo wa huruma. Tumeona wanawafungia ng’ombe kwenye mazizi kweli? Wanawafungia ng’ombe miezi sita, mwaka ng’ombe wanakufa na wengine bado wanaendelea kuwepo pale wazima jamani! Hivi ni kwa sheria zipi? Je, hawa watu tunawafikiria vipi? Kuna mambo mengine ambayo kwa kweli tunaomba wakati mwingine tutanguliwe na huruma zaidi katika kuwasaidia wananchi wetu. Hali ni ngumu, unaenda tena kummaliza huyu mtu. Tuwe na huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia na nakupongeza sana Mheshimiwa Kigwangalla, Waziri wa Maliasili, wananchi wa Arusha tumechoka na mgogoro wa Loliondo. Kwa hiyo, miongoni mwa mambo ambayo tunakuomba yaishe sasa ni mgogoro wa Loliondo tumechoka nao. (Makofi)

Mhshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nakushukuru sana. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na moja kwa moja kwa sababu dakika ni chache niende kwenye kile nilichoandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba watu wote wana haki sawa mbele ya sheria na Mtanzania yeyote hapaswi kuchukuliwa kama mhalifu mbele ya sheria mpaka atakapotiwa hatiani na mamlaka husika ambayo ni mahakama. Vilevile Ibara ya 107 inasema kwamba inatambua mamlaka pekee yenye haki na wajibu wa utoaji haki ni mahakama ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenukuu vipengele hivi na hasa nikienda katika Wizara ya Katiba na Sheria ambayo ndio inayohusika na marekebisho ya sheria mbalimbali na mimi nitazungumzia Sheria ya Usalama barabarani (Road Traffic Act) ambayo ni ya zamani sana ya mwaka 1968 na moja kwa moja naomba nizungumzie kero iliyopo ambayo imekuwa sasa hivi ni kero kubwa sana inayosababishwa na askari wa usalama barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema Ibara hiyo ya 13 na 107 lakini niulize tu na wakati Mwenyekiti wa Kamati husika atakapokuja hapa pengine atusaidie sisi ambao kwa namna moja au nyingine mambo ya sheria siyo sana. Ni mamlaka gani hasa ambayo inamruhusu askari wa usalama barabarani pamoja na kwamba taratibu hizo zipo lakini nataka kufahamu ni sheria gani ambayo inamruhusu anaposimamisha tu gari moja kwa moja kudai leseni? Vilevile hapo hapo kuanza kuandika notification kutokana na vitu mbalimbali ambavyo ameviona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hivi sasa na hata ukiangalia katika Jiji la Dodoma hebu watusaidie ni sheria gani ambayo inamtaka dereva asimame wakati wowote anapofika kwenye zebra crossing. Kwa sababu ni busara tu kwamba anapofika kwenye zebra crossing kama kweli kuna watu ambao wanavuka pale barabara sawa lakini wakati mwingine hakuna hata mtu anayevuka barabara na anapopita katika eneo hilo moja kwa moja tayari askari anamsimamisha na kumwandikia faini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu askari anapofika kitu cha kwanza anaomba leseni. Sasa mtusaidie sisi ambao hatujui sheria na Watanzania wengine wote kwamba ni sheria gani ambazo zinamfanya askari wa usalama barabarani kujichukulia sheria yeye na kuandika faini na wakati mwingine mtu anaandikiwa makosa mpaka manne, matano na hasa anapokuona kwamba kwa namna moja au nyingine wewe kidogo unauelewa wa sheria anachukulia kama ni kisasi na ndipo hapo anapoandika makosa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mtu anakwambia washa taa kwa mchana hivi jamani tuna haja kweli ya kuwalazimisha watu kuwasha taa na kama hiyo taa labda ina matatizo tayari moja kwa moja hapo hapo anakwandikia notification. Tumeona hapa kama nilivyosema hizo Ibara ya 13 na 107 vyote hivyo angalau basi mamlaka zinazohusika ndizo ambazo zinapaswa kuhakikisha kwamba makosa hayo yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu sheria hizi ni za muda mrefu sana tunaomba mabadiliko ya sheria yaletwe na kama Serikali bado inaona kwamba kuna wakati mgumu au kuna kigugumizi tuombe basi mwenyekiti wa Kamati husika, kwa sababu na wao pia kwa mujibu wa sheria zinamruhusu kufanya hivyo waahirishe na kuleta kwamba vile ambavyo vinahitaji kufanyiwa marekebisho ili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kuhusiana na taarifa iliyowasilishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Mendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumze mambo machache tu. Moja ni kuhusiana na ule Mfuko wa Maendeleo hasa kwa Wanawake ile asilimia kumi.

Nakumbuka mwaka jana katika bajeti tulipendekeza kwamba katika ile asilimia tano kwa wanawake na vijana pamoja na watu wenye ulemavu wakasema kwamba iende mbili. Naiomba Serikali iweze kuleta sheria kwa sababu wengine wanafanya kwa mapenzi tu, naomba kwamba iwe sheria. Vile vile lakini vilevile Watu wa Maendeleo ya Jamii wasaidie kutoa elimu ili hata wanapopewa hiyo mikopo waweze kuitumia katika malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie katika ukurasa wa hamsini ambao wamelizungumzia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na nakubaliana kabisa na maoni ya Kamati kwamba TBC ni shirika pekee la Serikali ambalo linategemewa kwa kazi nyingi na hata katika habari na matukio mbalimbali ya Serikali, TBC wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba jamii inapata taarifa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani na maoni yao kwamba TBC ikajifunze kwa Azam TV na kwa nini sikubaliani nao. Miongoni mwa mshirika ambayo yana waandishi na wataalam wenye weledi ni TBC. Changamoto kubwa ya TBC wanayokutana nayo ni kwamba tangu mitambo imefungwa mwaka 1999 hatimaye TBC mwaka 2000 mpaka leo mitambo bado ni hiyo hiyo. TBC inakabiliwa na changamoto kubwa ya mitambo iliyochakaa na imechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo Serikali itaamua kweli kuwekeza kwa shirika hili la TBC kufunga mitambo ya kisasa na vilevile hasa kwa kuzingatia wakati tulionao hivi sasa, naamini kabisa TBC itafanya kazi vizuri na ipasavyo. Naomba niseme tu nimekuwepo kwa miaka nane katika shirika hili na nimeshuhudia, inasikitisha baadhi ya mitambo ukienda TBC wafanyakazi wa TBC wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2008 ndipo ambapo mbali na ile studio ya awali kabisa ya mwaka 1999, baadaye wakaja wakafunga studio nyingine ndogo ambayo ndio wanayotumia kusomea habari na vipindi vya asubuhi vya jambo. Hakuna studio na mfano mzuri tu, kwa bahati nzuri tunaona wakienda kuhojiwa na hasa kipindi cha tunatekeleza, wenyewe wanashuhudia ubovu na uchakavu wa mitambo iliyopo ya TBC. Hiyo studio iliyopo ni ya tangu mwaka 1999. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba inazingatia umuhimu wa kuwekeza mitambo ya kisasa ili TBC iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kabisa vituo vingine kwa mfano hata Azam ilivyokuwa inaanzishwa ni wataalam hao hao wa TBC ambao waliweza kwenda kusaidia katika uwekezaji wa mitambo ya kisasa. Hatuwezi kulinganisha na TBC kwa sasa kwa sababu wao wana mitambo iliyo bora zaidi na vilevile TBC mitambo yao imechoka sana. Kwa hiyo, Serikali izingatie hili, tusipende tu kumkamua ng’ombe maziwa pasipo kumlisha ipasavyo. Ikiamua kuwekeza TBC ina wafanyakazi na watumishi wenye weledi na uzoefu mkubwa na itaweza kufanya kazi zake kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na Wizara ya Habari, mchangiaji mmoja alisema kwamba Wizara ya Habari hivi sasa na hasa Idara ya Habari (Maelezo) wamekuwa wakitumika sana kuhariri au kufungia vyombo vya habari. Utaratibu uliopo na kama inavyofahamika, endapo wanataaluma wakizingatia weledi na umakini zaidi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa mzungumzaji)

Hayatoweza kutokea hayo.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwepo hapa tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuwapongeza Mawaziri na hasa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake. Nimpongeze sana pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa mshauri mzuri kwa Waziri na hatimaye kutuletea bajeti yenye tija na inayojali maslahi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kondoa wana msemo usemao kwamba mwana wa mukiva amanyire michungiro. Usemi huu una maana kubwa sana na ndiyo maana nikampongeza Naibu Waziri kwa sababu ya ushauri wake mzuri na kuweza kumsaidia majukumu Mheshimiwa Waziri na hatimaye tumeletewa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze sana Serikali kwa hatua zake katika kujali maslahi ya kundi la watu wenye ulemavu. Kubwa zaidi niipongeze Serikali, kuondoa kodi katika vifaa vya watu wenye ulemavu, ukurasa wa 71. Vifaa hivi ni muhimu sana. Vifaa hivi ndivyo vinavyowasaidia watu wenye ulemavu kuweza kutekeleza majukumu yao lakini pia ni sawa na miguu au mikono ya watu wengine ambayo wamepewa na Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, kwa kitendo hiki cha kuondoa kodi katika vifaa vya watu wenye ulemavu ni faraja kubwa sana kwa sababu hivi sasa vifaa hivi vitakuwa na bei angalau afadhali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, calipers ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu wenye ulemavu zinafika kwenye Sh.400,000/= mpaka Sh.500,000/= lakini nina matarajio makubwa sana kwamba baada ya kuondolewa ushuru wa kodi kwa vifaa hivi, basi vitapungua na walemavu wengi wataweza ku-afford vifaa hivi. (Makofi)

TAARIFA . . .

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na kwa sababu mwenzangu amekuwa akitumia sana vifaa hivi, kwa hiyo, anachokizungumza anakifahamu kwa undani zaidi. Kwa hiyo, niungane naye tu katika kuipongeza Serikali kwa maana kwamba sasa hiyo gharama ambayo imekuwa ikitozwa itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika Hospitali ya CCBRT, Hospitali ya KCMC lakini pia Hospitali ya Seliani ambazo zimekuwa zikihudumia sana watu wenye ulemavu, naamini kabisa kwamba msamaha huu wa kodi uwatawasaidia. Kwa maana hiyo pia tutaweza kuboresha hospitali yetu ya Muhimbili ili basi na wenyewe waweze kuboresha zaidi kitengo hiki cha huduma ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza kwa moyo wa dhati kabisa Serikali na niendelee tu kuipongeza Wizara, Mama yangu Ndalichako, Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye pia hivi karibuni alipokea vifaa vya watu wenye ulemavu ambavyo vimesambazwa katika shule na vyuo mbalimbali. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba Serikali hii imekuwa ikijali maslahi na kuangalia kundi hili la watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi na kuishukuru Serikali, nitoe tu pia ushauri kwa Serikali kwa sababu kuhusu Kitabu hiki cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016. Pamoja na kwamba tumepunguza kodi lakini bado kuna mahitaji mengi ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, ni vyema katika bajeti ijayo tuone ni kwa jinsi gani tutasaidia zaidi kundi hili. Kwa mfano, maisha ya watu wenye ulemavu ni ya chini sana na hasa maeneo mengi ya vijijini hali zao za kiuchumi ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokuja na bajeti tuone kundi hili tunaliangalia vipi? Kwa mfano, kwa hivi sasa tulipo katika Sera ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inajikita zaidi katika viwanda, pia tuangalie hivyo viwanda ni kwa jinsi gani vitaweza kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu, kuwasaidia na hali ngumu au maisha magumu waliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambapo nilizungumza kwa undani zaidi na nimekuwa nikilipigia sana kelele suala la TBC kutokana na uchakavu wa mitambo. Kwa sababu ni Serikali sikivu Mheshimiwa Rais alifanya ziara katika shirika hili na kujionea hali jinsi ilivyo lakini pia akaweza kutatua baadhi ya changamoto zilizopo katika shirika hili, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote haya, sasa ni wakati muafaka kabisa kwa wafanyakazi na watumishi wote wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutoa ushirikiano, kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha kwamba shirika hili linarudi katika hali yake iliyokuwepo hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri aliyoifanya ambayo hivi sasa Afrika inafahamu kwamba Tanzania inaye Rais anayeitwa Dokta John Pombe Magufuli. Kitendo alichokifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kitendo cha kuungwa mkono na Watanzania wote, ni kitendo cha kuungwa mkono na wale wote wapenda maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu mimi katika kundi ninaloliwakilisha na naomba nijikite kulizungumzia hili, ni watu wenye maisha duni sana. Rasilimali hizi zikitumika ipasavyo ni dhahiri kabisa kwamba tutatatua changamoto nyingi za watu wenye ulemavu na kupunguza ukali wa maisha waliyonayo. Kwa maana hiyo, naomba sana nimpongeze Rais. Pia naamini kwanza ni fundisho ambalo tumejifunza lakini pia tutakuwa makini katika kupitisha mikataba ili mikataba hiyo isije ikatufunga sisi na ikatuumiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya hivyo pia, ni wakati muafaka sasa na ningemwomba Mheshimiwa Rais aangalie mkataba na mwekezaji wa Pori la Loliondo ambao kwa muda mrefu umekuwa ni mgogoro unaoumiza ndugu zangu wa jamii ya Kimasai. Kwa hiyo, namwomba pia kuangalia ni kwa jinsi gani watapitia mkataba huu ili kama kuna vipengele ambavyo vinawabana au vinawaumiza wananchi vifanyiwe marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia ambalo napenda kuishauri Serikali, kwanza nampongeza Mheshimiwa Spika kwa kuunda Kamati kupitia Mkataba wa Sky Associate pamoja na State Mining Companies Limited (STAMICO) ili kuweza kurekebisha upungufu uliopo. Kabla Mkoa wa Manyara haujagawanywa madini haya yalikuwa ndani ya Mkoa wa Arusha na nafahamu kabisa ni kwa jinsi gani yamekuwa yakisaidia wakazi wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ukienda hali ni ngumu sana kwa vijana wengi ambao walizoea kuchimba madini haya na kujipatia kipato, hali imekuwa tofauti. Kwa hiyo, kwa kitendo hiki cha Mheshimiwa Spika kuunda hii Kamati kupitia mkataba huu, ni faraja kubwa na naamini kabisa sasa mikataba hii itaangalia ni kwa jinsi gani itakwenda kuwanufaisha wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishauri Serikali katika Halmashauri na Mikoa yetu kuangalia kwa mfano, ndiyo, tumepunguza kodi katika vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu lakini tunawaandalia mazingira gani mazuri ya kuwawezesha watu hawa kufanya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Seriakli yetu kwa kazi nzuri inayofanya, na hapa nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa jitihada anazofanya katika kuwatetea wanyonge wa taifa hili; Waswahili wanasema kwamba mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe na hili tunalishuhudia. Nimpongeze pia Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, nimpongeze sana Dada yangu Jenista Mhagama kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na wasaidizi wake Mheshimiwa Ikupa pamoja na Mheshimiwa Mavunde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia hotuba hasa katika ukurasa wa 24 ambako kumezungumziwa huduma kwa watu wenye ulemavu. Tumeona jitihada za Seriakli katika kusaidia kundi hili la watu wenye ulemavu, na nitoe pongezi za dhati kwa jitihada zinazofanywa. Kwa mfano, tumeshuhudia kuanzia mwaka jana vifaa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum vimepelekwa katika shule mbalimbali ingawa bado uhitaji ni mkubwa, kwa hiyo, niisisitize tu kwamba Wizara kuendela kuangalia na hasa maeneo mengi ya vijijini kwa kweli bado uhitaji ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia kwa kuona umuhimu wa kuboresha vyuo vya watu weye ulemavu, kwa mfano Chuo cha Yombo ambacho kilikuwa ni msaada mkubwa sana katika kuwajengea uwezo, kuwapa ujuzi watu wenye ulemavu ambao walikuwa wakitoka hapo wanakwenda kujiajiri wao wenyewe na si kutegemea tena ajira.

Kwa hiyo, hiki chuo ni muhimu sana na niisisitize Wizara katika kuhakikisha kwamba kweli wanaboresha na kukirudisha katika ule ubora uliokuwepo pale awali na kuongezea pia na wakati huu tulionao hivi sasa wa karne ya sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize tu pia kwamba katika vyuo hivi mbali ya chuo hiki cha VETA, lakini tuone pia katika Vyuo vya VETA ambavyo tunaona kabisa kwamba vinazalisha vijana na vinawajengea uwezo. Katika vyuo hivi nitoe mfano tu ambapo katika kipindi kilichopita nilikuwa Mjumbe katika Kamati ya PIC ambako tuliweza pia kukutana na VETA. Mimi masikitiko yangu ni kwamba VETA kwa kweli hawana kipaumbele kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, hapa nisisitize Serikali kuhakikisha kwamba vyuo vyote hivi vinajali kundi hili ili kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo kuwapa ujuzi wakitioka pale waweze kwenda kujiajiri wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu asilimia mbili; tangu jana pia tumeona hata katika maswali ya Waheshimiwa Wabunge tumeona uhitaji wa kundi hili. ni kweli kabisa kwamba katika bajeti ya mwaka jana, Waziri alitoa ahadi na alitoa tamko kwamba sasa ile asilimia 10; asilimia nne iende kwa wanawake na asilimia mbili iende kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu. Sasa hili lilikuwa ni tamko, ninasisitiza na kuona uhitaji kwamba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa tunahitaji sheria, kwa sababu kukiwepo na sheria, sheria hii itatoa muongozo, itawaelekeza wakurugenzi na hakuna Mkurugenzi ambae sasa ambaye atafanya kwa utashi wake bali atafanya kwa kzuingatia kanuni, sheria na taratibu zilizopo kwa ajili ya watu hawa wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye ulemavu kwenye mabenki hawakopesheki na hawakopesheki kwa sababu dhana iliyopo miongoni mwetu bado watu wengi wana ile dhana potofu ya kuona kwamba huyu mwenye ulemavu hawezi kurudisha huo mkopo, kwa hiyo, hii asilimia mbili mimi nasisitiza tuone umuhimu kwamba hili ndilo kimbilio lao, ndilo tegemeo lao kwa kuwapa asilimia hii mbili waweze kujiajiri kwa kufanya biashara mbalimbali.

Tumeshuhudia; hizi zitawawezesha wao kuondokana na hali ngumu ya maisha na wakati wenyewe uliopo hivi sasa. Kwa hiyo nasisitiza umuhimu na ninaomba sana dada yangu mpendwa, dada mkubwa Jenista Mhagama utakapokuja hapa basi uje kutupa majibu na nitafurahi nikisikia ni tamko na utueleze kama ni sheria au kanuni na taratibu zitaandaliwa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Wizara hasa Ofisi yangu hii ya Dada yangu Jenista Mhagama kwa jitihada wanazofanya kwa kuhakikisha kwamba kundi la vijana linawezeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo, kilimo hiki tunaangalia ni kwa namna gani tunawawezesha vijana, vijana ndiyo nguvukazi ya Taifa. Vijana hawa mikopo ambayo ipo na tumeona kwamba mikopo hiyo baadhi wamekuwa wamefaidika na vijana wengi hivi sasa wanahamasika tuone sasa ni kwa jinsi gani tutawajengea hawa vijana na kuwapa hii mikopo wajiingize kwenye kilimo. Kilimo chenyewe ambacho tunakihitaji hivi sasa ni kilimo cha kisasa, kilimo biashara. Kilimo hiki biashara kitawawezesha vijana waweze kujiajiri wao wenyewe na kupunguza basi lile tatizo la ajira. Kwa mfano, hizi green house ni muhimu sana, vijana wengi tumeshuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakiwezeshwa kwa kupitia hii mikopo na vijana hawa wakaandaliwa mafunzo kupitia ujasiriamali mbalimbali wataweza wao wenyewe, kwa sababu kikubwa kinachohitajika pia ni elimu. Katika kilimo wakiwezeshwa; tunaona kwamba kuna ufugaji wa kuku, kuna ufugaji wa samaki vyote vinaingia katika kilimo biashara. Kwa hiyo naisisitiza sana na naiomba sana Serikali tuone umuhimu wa kuwawezesha vijana hawakwa kuwapatia hiyo mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia kwamba program ya kuwawzesha vijana katika Vyuo vya VETA, tuangalie sasa, tunapokwenda katika sekta ya utalii kwa wenzetu utaratibu mzuri wanaoweka ni haa kuhakikisha kwamba vijana hawa kwa mfano, wanaofanyakazi katika sekta hii ya utalii wanapata elimu ambayo customer care ni muhimu sana. Ukienda nchi za Kenya jinsi ambavyo wenzetu wanavyoweza kuhudumia ile customer care ni muhimu sana; kwa hiyo na sisi huku kwetu kama tumedhamiria kuona kwamba tunawawezesha vijana wetu kwenda katika mafunzo hayo kwa mfano kupitia programu ya Chuo cha Utalii, vijana wetu watumike kupata ujuzi lakini pia wafundishwe jinsi ya ule ukarimu wa kuwapokea wageni wanaofika hapa. Tunafahamu sekta ya utalii ni pana na inaongeza pato katika nchi hii, kwa hiyo, tuwawezeshe katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu, kuwepo na programu, kwa mfano; Wizara hii husika kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu hata madereva taxi wapatiwe mafunzo, kwa mfano wanapokwenda kumpokea mteja ajue ile namna gani ya kuweza kumpokea mteja kwa ukarimu ili kwamba anapoondoka ibaki ile sifa yetu kuwa Watanzania kama ilivyo kwamba sisi ni wakarimu. Kwa hiyo, kwa kupewa mafunzo hayo hata hawa madereva taxi watajua, hata mgeni kama anasahau kitu kwenye gari ni rahisi sana kuangalia ni kwa namna gani ya kuweza kumsaidia huyo mgeni anayefika hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie katika ukurasa wa 18, suala la ajira. Ninasisitiza ni kazi nzuri, mpango mzuri ambao umeandaliwa wa kukusanya kanzidata kwa wahitimu wenye mahitaji maalum. Nasisitiza tena kwamba wapo vijanaa wengi wamemaliza vyuo vikuu wenye ulemavu, wasioona, viziwi na wengine wengi tuone kwamba ile asilimia tatu inazingatiwa siyo kwa Taasisi za Serikali tu hata katika private sector. Sasa hivi tupo katika suala zima la viwanda, katika viwanda hivi je, tunawaandaaje watu wenye ulemavu ili na wao basi waweze kuingia huko, wapate ajira na kuweza kufanyakazi huko kuhakikisha kwamba tunawaondoa katika dimbwi kubwa la umaskini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu itusaidie katika Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Arumeru katika kijiji, Kata ya Oldonyowasi maji yenye fluoride yanatuumiza watu wa kule. Ukienda kule utakuta watoto wanapinda miguu na wazazi/wamama na vikongwe wanapinda migongo. Naomba sana watalaam mbalimbali wameshafanya utafiti tatizo ni kubwa naomba sana. Na Mheshimiwa Dada yangu Jenista utakapokuja naomba pia utueleze kwa sababu mwaka jana tumeona Waziri Mkuu kweli ametupatia mradi na kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 50 tumepata maji. Kwa hiyo, naomba sasa katika Kata hii ya Oldonyowasi tuone ni kwa jinsi gani tunaweza kupunguza tatizo la madini ya fluoride. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii. Naomba niende moja kwa moja katika mazingira, niwapongeze pia Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo katika msimu wa mvua na katika msimu huu wa mvua tumeshuhudia ni kwa jinsi gani baadhi ya wenzetu walivyoathirika, tunawapa pole. Hata hivyo, haya yote ni kutokana na baadhi ya wenzetu ambao utendaji wao wa kazi uliwezesha kutoa vibali ambavyo havikustahili kutolewa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukienda katika Bonde la Msimbazi kuna baadhi ya wananchi ambao leo hii ukienda wana vibali vinavyowaruhusu kuwepo maeneo hayo. Kama hawa watu wasingetoa vibali hivyo ni dhahiri kabisa mafuriko haya yasingewakumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mazingira yetu tunaharibu sisi wananchi wenyewe. Twende katika mito yetu ambayo kwa namna moja au nyingine tumekuwa tukimwaga taka ngumu lakini sio hiyo tu hata katika mitaro tumeona kuziba kwake ni kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi wenzetu wenyewe. Kwa hapa niwaombe wenzangu wananchi wa kawaida tujue umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaona mafuriko na kama tunavyofahamu katika mafuriko maji mengine yanatoka katika vyoo na takataka mbalimbali zimechanganyika. Baada ya mafuriko kunakuwepo na tahadhari ya ugonjwa wa kipindupindu. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa jukumu hili sio la Serikali peke yake, hata sisi wananchi tunapaswa kuhakikisha kwamba tunashuhudia na kuyalinda mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania sera iliyopo sasa ni kuhakikisha kwamba ujengaji wa viwanda, nakubaliana kabisa na naunga mkono, lakini katika viwanda hivyo tuangalie kwamba ni kwa jinsi gani tunahitaji viwanda lakini viwanda ambavyo vitalinda mazingira yetu. Tunafahamu Mataifa makubwa kama Marekani na China ambayo yalikataa kusaini Mkataba wa Kyoto kutokana na uhitaji wa viwanda vikubwa vilivyopo kwao, lakini pia ndio chanzo cha uharibifu wa mazingira. Kwa hiyo na sisi wakati huu tunapoanzisha ujenzi wa viwanda, tuhakikishe kwamba viwanda sio chanzo cha uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa air pollution ni tatizo kubwa na sio Tanzania tu, maeneo mengi. Kwa hiyo, katika viwanda naiomba Wizara inayohusika kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinakuwa sio chanzo cha uharibifu wa mazingira bali vinakuwa ni chanzo cha utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tatizo kubwa la ukataji wa miti ni kutokana na uhitaji mkubwa wa mkaa. Hivi sasa Tanzania Mwenyezi Mungu ametujalia tuna gesi, basi tuone ule uharaka wa kuhakikisha kwamba hii gesi inakuwa ni chanzo cha utunzaji wa miti yetu, miti yetu isikatwe na kusiwepo na uharibifu wa mazingira kwa sababu wananchi wengi watakwenda katika utumiaji wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili waende katika utumiaji wa gesi tunahitaji gesi kwa gharama nafuu, kwa maana hiyo tutaweza kulinda mazingira yetu, watu na hasa kwa sababu mkaa usipohitajika kwa kiasi kikubwa mjini, ni dhahiri kabisa wale waliopo kule Vijijini hawatoharibu miti yetu, hawatokata miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa. Kwa hiyo, ni uharaka unahitajika kwa hivi sasa kuhakikisha kwamba mazingira, gesi inakuwa ni chanzo cha kuhifadhi misitu, ni chanzo cha utunzaji wa misitu ili wananchi wasiweze kuharibu kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi pia ya maeneo yamekuwa na uharibifu mkubwa na hasa tunavyofahamu wananchi wenyewe ndio chanzo kikubwa. Itumike elimu na kuhakikisha kwamba kwa mfano wanaochimba mchanga maeneo mengi wanakuwa ni chanzo cha uharibifu. Yale maeneo kama tulivyoona Makamu wa Rais alichokianzisha hapa Dodoma, basi elimu hiyo ya upandaji wa miti iendelee katika maeneo mengi kwenye mikoa mingine ili kulinda mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Waziri. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa hapa, pili naomba nifafanue na kuweka taarifa sahihi kwenye Hansard. Nilimaanisha saa tatu asubuhi mpaka saa nne na nusu kipindi cha maswali na majibu ndiyo lilikuwa lengo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kama sijaenda mbali zaidi naomba nizungumzie kidogo alichozungumzia mwenzangu aliyemaliza kuongea. Katika habari lengo kuu la tasnia ya habari ni kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha. Kwa hiyo katika TV kuna vipindi vya kuelimisha, kuna vipindi vya kuburudisha na kuna vipindi ambavyo vinajumuisha kwenye michezo, burudani lakini vya kuhabarisha ni kama habari. Kwa hiyo, allipozungumzia kuhusu taarifa ya habari dakika tatu, taarifa ya habari unakuta ni nusu saa na inajumlisha matukio yote hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya habari, habari nyingine kwa mfano habari kubwa kama ya Rais itakwenda dakika tatu mpaka dakika tano, lakini habari nyingine zitakwenda dadika moja moja au dakika mbili na kama kuna tukio maalum la Rais wanachofanya ni kusema kwamba kutakuwa na kipindi maalum na katika kipindi hicho maalum wanarudia hiyo taarifa katika kuelezea. Kwa hiyo, nataka tu kuweka ufafanuzi huo kwa sababu TBC hawana nafasi ya kuja kujadili hapa na kwa sababu na mimi pia ni mwanataaluma na nimetoka huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo napenda pia nimshukuru Mwenyekiti wa Bunge wa Michezo, Mheshimiwa Ngeleja na Kamati yake kwa ujumla kwa kuniteua kuwa Msemaji wa Timu ya Bunge, kwa hili nashukuru sana na mimi nasema kwamba kipele kimepata mkunaji na mimi nitakikuna sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nianze na maswali kwa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku- windup aje kutufahamisha. Mheshimiwa Waziri timu yetu imekwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola kule Australia. Taarifa nilizonazo mpaka hivi sasa ni kwamba miongoni mwa wachezaji waliokwenda huko mmoja ametoroka kambini na amezamia huko nchini Australia. Jina lake nimelipata anaitwa Fathiya kutoka Ukonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup atufahamishe kwamba hizi taarifa je, zina ukweli wowote kwamba huyu mchezaji ametoroka kambini na kuzamia huko nchini Australia? Pia nataka kujua kwamba kama ni kweli ametoroka ni vipi mahusiano yetu kati ya Tanzania na Australia, hili haliwezi kututia doa kwa sababu sisi tunafahamu Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikipokea sana wakimbizi, lakini siyo Watanzania kutorokea kama huyu mwenzetu alivyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo kwa sababu dakika ni chache, moja kwa moja niende kwa maslahi ya Waandishi wa Habari. Tunafahamu kwamba tuna mhimili mitatu, Mihimili wa Bunge, Mahakama na Serikali lakini tasnia ya Habari pia ni mhimili ambao tunauhesabu kama mhimili wa nne, lakini waandishi wa habari wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu sana. Wengi wao hawalipwi ipasavyo na hata katika ile mikataba yao, ukienda kwa mfano anapofanya miaka miwili hakuna chochote kinachoingizwa katika mifuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mifuko kabla haijavunjwa sasa hivi na kuwa mifuko miwili; tunafahamu kulikuwa kuna PPF na mifuko mingineyo, ilikuwa haipelekwi huko. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba atakapokuja atufahamishe hapa ni vyombo gani ambavyo vimekuwa haviwalipi Waandishi wa Habari ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waandishi wa Habari wanafanya kazi kubwa sana. Popote pale ulipo Waandishi wapo na ndiyo wanaowahabarisha wananchi, matokeo yake hawapati hiyo mishahara kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atufahamishe amechukua hatua gani.

Mhshimiwa Mwenyekiti, pia, nivipongeze vyombo ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuwalipa na hasa mimi nitolee mfano Azam, nawapongeza sana TBC, lakini pia, hata ITV.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje atueleze, mwaka jana nakumbuka mwenzangu ambaye sasa hivi ni Naibu Waziri alishika shilingi kwa ajili ya kutaka wakalimani katika taarifa za habari. Naomba kufahamu mchakato huo umefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanamuziki wetu tunafahamu kwamba, muziki wa dansi tulikotoka mpaka hivi sasa, lakini kwa mfano kwa hivi sasa kumbi nyingi za burudani zinatakiwa zifungwe saa sita kamili usiku, kama unavyofahamu saa sita kwetu watu wazima ndiyo kumenoga kwelikweli, lakini hawa pia ndiyo ajira yao wanaambiwa kwamba muda huo wafunge. Mpaka wamefikia kuwaweka wasanii ndani kwa mfano mwanamuziki mkongwe King Kikii aliwekwa ndani. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aje kutufahamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu lingine ni kwamba, Maafisa Utamaduni, tunafahamu wapo chini ya TAMISEMI. Nataka kujua hivi sasa je, ule ufanyaji kazi wao ukoje na Wizara husika kwa sababu, mambo ya sanaa, utamaduni na michezo yako katika Wizara yake, aje kutuambia kwamba, wamefikia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maadili, naomba Waziri aje kutufahamisha, Mheshimiwa Waziri nimemwonesha katika Night Clubs zetu kumekuwa na mchezo ambao wanahamasishwa labda kama ni mwanamke au mwanaume kucheza na wakati mwingine mpaka kufikia kuvua nguo na kufanya tendo la ndoa na Mheshimiwa Waziri nimemwonesha kilichotokea hivi karibuni. Nataka atakapokuja hapa aje atueleze wamechukuliwa hatua gani na ni mikakati gani ipo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, utamaduni wetu na maadili yetu tunayalinda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TBC, naweza kusema ni miongoni mwa mashirika ambayo yana wataalam waliobobea, wakongwe tangu miaka hiyo. TBC tunafahamu popote pale katika shughuli zote za Kitaifa, TBC ndiyo ambao wamekuwa wakitegemewa sana, lakini wakati mwingine tunawalaumu TBC wakati makosa siyo ya kwao. Makosa siyo ya kwao kwa sababu hatujaliangalia ni kwa jinsi gani tunawekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni shirika la umma, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze ni kwa jinsi gani analiwezesha Shirika la Utangazaji (TBC) ili basi liwe kweli ni Shirika la Umma, liwe kweli shirika ambalo linaweza kufanya majukumu yake na hizi lawama zinazotokea zote ni kwa sababu, tumelisahau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika taarifa kwamba, wamesema wanakuja kujenga studio ya kisasa hapa Mjini Dodoma, lakini je, kwa wakati huu ambapo bado wapo Dar es Salaam tunawawezesha vipi? Naomba kwa sababu ndiyo shirika tunalolitegemea sana katika utendaji wa kazi wamebobea. TBC ndiyo ambao wamefunga mitambo ya vyombo vingine vyote, kwa maana kwamba, wamewatoa wataalam TBC na wamekwenda kufunga huko. Kama wanaweza kufunga huko kote kwa nini washindwe wao kufanya vizuri? Ni kwamba, hatujaamua kuwekeza ipasavyo katika Shirika la Utangazaji (TBC). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, leo hii mimi najivunia uwepo wangu hapa ni kwa sababu nimelelewa katika taaluma, nimetoka huko ndiyo maana najivunia uwepo wangu hapa bila kusahau nilipotoka, siku zote tulipotoka ndipo ambapo pameweza kutufikisha hapa. Naipongeza sana TBC na naomba tuwawezeshe ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Online TV. Nafurahi kwa sababu, vijana wengi wamepata ajira hivi sasa, lakini katika kila kitu kisipowekewa msingi mzuri ni dhahiri kabisa kwamba hata maadili wakati mwingine yanaweza kukiukwa, ndiyo maana hata ukiangalia nyingine zinafanya vizuri sana, lakini sasa utaratibu ambao amekuja nao Mheshimiwa Waziri, nafurahi kwamba, tutaweka sasa zile guidelines na kuwafahamisha vizuri ili wasiweze kwenda kinyume na maadili ya Mtanzania, kwa sababu ile ni njia mojawapo pia ya habari, tuone kwamba ni kwa jinsi gani wanafuata misingi, sheria na taratibu zilizopo katika kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuuhabarisha umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu sanaa na utamaduni. Sipingani na maamuzi ya Serikali katika kuwafungia Wasanii. Hapa kuna sehemu tulikosea kwa sababu haiwezekani mwanamuziki anatoa single yake, ametoa wimbo wake unapigwa halafu wanakuja kumfungia! Hili haliwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujikumbushe siku za nyuma wanamuziki wengi, wakati huo Redio Tanzania Dar-es- Salaam, walikuwa wakitoa nyimbo zinakuwa edited, baada ya hapo ndiyo zinapigwa. Je, hawa wataalam sasa hivi wako wapi? Tuweke misingi mizuri tuwasaidie wasanii wetu ili wakikiuka baada ya kupewa hiyo misingi mizuri na kulelewa vizuri, hapo ndipo tunaweza tukawahukumu. Kwa hiyo, nawapongeza akina Diamond, nampongeza Monalisa na wengine wote ambao wameweza kupeperusha vizuri bendera ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa pia ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu Mkataba wa Star Media pamoja na TBC. Nafurahi kwamba, mkataba ule umekuwa renewed hivi sasa na kwamba matakwa yamezingatiwa, lakini sikubaliani na walichosema kwamba kwa miaka yote saba Star Media wamepata hasara! Hii naona kwangu ni aibu kwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka mwaka 2013, TBC na Star Media ndiyo walikuwa wa kwanza kuanza kuuza ving’amuzi, wote ni mashahidi na tunajua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa na kipekee kabisa niipongeze Serikali, nimpongeze Waziri wa Maji kwa jitihada kubwa anazofanya na tumeshuhudia ni kwa jinsi gani ambavyo amekuwa mstari wa mbele kutembelea maeneo mbalimbali kushughulikia tatizo la maji. Pamoja na yote haya maji ni shida sana na tunafahamu kwamba maji ni uhai na maji ni kwa wote, uwe mwenye ulemavu, usiye na ulemavu kila mmoja anahitaji maji.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana alikuja kuzindua mradi wa maji katika Kata ya Nduruma, Vijiji vya Maroroi, Mlangarini pamoja na vijiji vingine vya jirani, tunashukuru sana kwa hili kwa sababu ndani ya miaka 50 hatukuwa na maji ya bomba zaidi ya maji ya mito ambayo tulikuwa tumeyazoea, kwa hili naishukuru sana Serikali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote tunafahamu Mkoa wa Arusha tumejaaliwa Mlima Meru na katika huu Mlima Meru baadhi ya maeneo wanapata maji lakini maeneo mengine tunafahamu kama katika Jimbo la Longido, Jimbo la Ngorongoro kote huko maji ni shida na wanaopata shida kubwa ya maji ni akina mama kwa sababu wao ndiyo wachotaji wakubwa wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti, ninaomba nizungumzie shida kubwa iliyopo katika Hamashauri ya Arusha DC ambapo tuna tatizo kubwa la madini ya fluoride yanayowaathiri wananchi kwa kiasi kikubwa. Inasikitisha sana kwa sababu watoto wanapinda miguu, akina mama wanapinda migongo na hata hao watoto ukiangalia mahudhurio yao shuleni siyo mazuri kwa sababu maji yenye madini ya fluoride yamewaathiri kwa kiasi kukubwa sana. Eneo kubwa ambalo limeathirika na maji ni katika Kata ya Oldonyosambu pamoja na Oldonyowasi ambako huku kuna athari kubwa sana ya madini haya ya fluoride, maji yanapatikana kwa kiwango kidogo lakini hata hayo yanayopatikana kwa kiwango kidogo bado ni shida sana.

Mheshimiwa mwenyekiti, ulemavu unaepukika na ulemavu huu tunafahamu upo ulemavu wa kuzaliwa, upo ulemavu wa ajali na changamoto nyingine lakini ulemavu huu unaosababishwa na maji yenye madini ya fluoride haukubaliki kwa sababu tuna uwezo wa kupeleka maji na kuwaondolea shida akina mama na watoto ambao wanapata athari kubwa, wanapinda miguu na wanapata athari pia hata kwenye kusoma inakuwa ni shida. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri nilikuonesha video ambayo inaonesha ni kwa jinsi gani watoto wameathirika na maji haya yenye madini yenye fluoride na kwako wewe pia ilikuwa ni jambo la kushangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwamba umeahidi lakini kwa kweli tunahitaji jitihada za haraka katika kuhakikisha kwamba tunawasaidia wakazi hawa katika hizi Kata za Oldonyosambu pamoja na Kata ya Oldonyowasi ili basi tuondoe tatizo hili la ulemavu unaotokana na maji yenye madini ya fluoride.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo hili ni kubwa na kwa kuwa sasa katika Wilaya ya Longido chanzo kingine cha maji cha Mto Simba kutoka Wilaya ya Siha, basi tunaomba hivi sasa kwamba chanzo cha maji ambacho ni cha Engutoto na tunafahamu kabisa kwamba kulikuwa kuna mradi unaofadhiliwa na DFID kwa kushirikiana na Water Aid Tanzania, tunaomba katika Halmashauri hii ya Arusha kile chanzo cha maji ambacho awali kilikuwa kipeleke maji katika Jimbo la Longido na hatimaye chanzo hiki tumekiacha, tunaomba sasa chanzo hiki kiweze kupeleka maji katika Kata hii ya Oldonyosambu pamoja na Kata ya Oldonyowasi ili tuondoe tatizo hili la madini ya fluoride. Tukipeleka chanzo hiki cha maji tutasaidia vijiji vya Losinoni ambavyo hali yake ni mbaya sana, tutasaidia vijiji vingine ambavyo ni vya Lengijave lakini siyo hiki tu kuna kijiji cha Lemanda ambacho kimeathirika kwa kiasi kikubwa sana.

Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana ili basi uweze kuhakikisha kwamba tunapeleka fedha, tunakishughulikia chanzo hiki cha maji ili tuweze kutatua madini haya ya fluoride. Kuna baadhi ya wenzetu wakati mwingine hata kucheka inakuwa ni shida kwasababu ya meno yameathirika na maji. Mheshimiwa Waziri, hatupendi kwahiyo tunaomba sana mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunafahamu katika Mkoa wa Arusha, tumesomeshwa wengine na bustani kwa sababu tulikuwa na kilimo cha umwagiliaji kwa miaka yote kutokana na maji yanayotoka katika Mlima Meru. Hivi sasa hatuwezi tena kulima kwa sababu wamiliki wa mashamba makubwa ya maua sasa hivi wanayahodhi yale maji yote, matokeo yake wananchi ambao walitegemea kilimo kutokana na kilimo hiki cha umwagiliaji sasa hivi hawawezi tena kulima. Tunawapenda wawekezaji, tunawahitaji wawekezaji, lakini wawekezaji hawa wasitufikishe hapo wananchi wetu wanapata shida. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri ili uweze kushughulikia na kupitia basi kwa sababu wengine wamehodhi maji na wanasema kwamba wana hati miliki ya kuhodhi maji hayo kwa miaka 100 yaani kwa maana 99.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wetu wanaangamia, ndugu zangu nimesoma mimi kwa kulima bustani, hivi sasa imekuwa ni shida kwa hiyo tunaomba sana mashamba ya maua yaliyopo katika eneo la vijiji vya Chekereni, lakini pia njiapanda ukienda Mlangarini, mashamba ya maua yale wamiliki wote wamehodhi maji, tunaomba tunayahitaji haya maji ili wananchi wetu waweze kurudi na kulima kilimo cha umwagiliaji tofauti na sasa ambako tunasubiri mvua mpaka mvua na siku hizi kumekuwa na mabadiliko ya tabianchi maji haya yanakuwa ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, hiki ni kilio cha wananchi cha muda mrefu, tunawahitaji wawekezaji kama nilivyosema, lakini wawekezaji hawa wasihodhi maji yote, kwa hiyo ninaomba sana Serikali ipitie haya... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie. Sekta ya utalii ni muhimu sana katika nchi yetu na sekta hii ni miongoni mwa sekta mojawapo ambayo inachangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa. Mwenyezi Mungu ametujalia nchi yetu ya Tanzania kuwa na hifadhi pamoja na vivutio vingi ambavyo endapo vivutio hivyo vitatatuliwa changamoto ndogo ndogo zilizopo, Tanzania tutafika mbali katika sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuipongeza Serikali, natambua jitihada wanazofanya na ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri tangu umeingia katika Wizara hii na tunamatarajio makubwa kwamba kutakuwa na mabadiliko katika sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Spika, mimi natoka Mkoa wa Arusha na kwa bahati nzuri katika Mkoa wetu wa Arusha ni Mkoa namba moja ambao tunapozungumzia hifadhi, Kanda ya Kaskazini ndio inayoongoza.Tunafahamu kwamba Tanzania tuna hifadhi 16. Katika hifadhi hizi hifadhi namba moja inayoongoza kwa mapato makubwa ni KINAPA ambayo ipo chini ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi nyingine zote za Kanda ya Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hifadhi hizi kufanya vizuri bado hizo hifadhi nyingine 11 hazifanyi vizuri kiasi kwamba haziweze kuongeza Pato la Taifa. Hifadhi hizi hazifanyi vizuri kwa sababu ya miundombinu. Kwa mfano Ruaha National Park. Ruaha National Park mbali ya ukubwa wa eneo hili la Ruaha ambalo tukingalia kwa Afrika, Kruger National Park ya Afrika ya kusini inaoongoza kwa ukubwa na Ruaha inafutia kwa sababu ya eneo kubwa. Hata hivyo hii Ruaha bado haijafikia hifadhi zilizopo kaskazini ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia pato la Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, katika ziara yake Mheshimiwa Rais hivi karibuni akiwa Mkoani Iringa amesisitiza umuhimu wa kuboresha uwanja wa ndege wa Nduli ili kuhakikisha kwamba watalii wanafika katika mkoa huu wa Iringa ili waweze kufika Ruaha. Pia si tu kwamba uwanja huu wa ndege wa Nduli, tuone pia ujenzi wa barabara ya kwenda Ruaha National Park, barabara hii pia ijengwe ili watalii waweze kufika kwa wingi katika Hifadhi hii ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo ambazo, Wizara inapaswa kuhakikisha kwamba haya yanafanyiwa kazi, lakini bado hatujatangaza ipasavyo hifadhi zetu, vivutio vyetu, utalii wetu na kwa mfano ukienda Kigoma kuna Gombe na Mahale ambapo hapa Tanzania wanapatikana sokwe (chimpanzee), lakini miundombinu bado inakuwa ni tatizo. Kwa hiyo, Wizara tuone ni kwa kiasi gani tunaharakisha uboreshaji ili watalii wengi waweze kufika mpaka huko.

Mheshimiwa Spika, ukienda Katavi ambako nako pia kuna hifadhi na bahati nzuri sasa hivi asilimia kubwa barabara imefika, lakini je, huku Gombe na Mahale ambako hawa chimpanzee walioko kule ni kivutio tosha kabisa cha kuweza kutangaza utalii na watalii wengi wakafika huko.

Mheshimiwa Spika, si hilo tu, pia kuhakikisha kwamba Wizara inatenga fedha na kuhakikisha kwamba Bodi ya Utalii Tanzania ambayo ndiyo yenye jukumu la kutangaza utalii wetu, fedha wanazopewa ni kidogo, tunawawezeshaje kwa sababu unapotaka kitu kizuri lazima wewe mwenyewe ufanye jitihada, toa pesa upate pesa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukiwawezesha Bodi ya Utalii kwa kuwapa fedha wakaweza kutumia nafasi ya kutangaza, ku-brand utalii wetu nina imani kabisa kwamba, Tanzania tutapanda juu na hifadhi hizi zitaweza kuingizia pato kubwa la Taifa.

Mheshimiwa Spika, ukienda katika uwanja wetu wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hebu nenda pale, kwa mfano unapoingia katika barabara hii kubwa ya Mwalimu Nyerere, barabara hii mgeni anapoingia ni vivutio gani, matangazo yamewekwa ili kumuwezesha, mbali ya kile ambacho yeye ametoka huko anataka kwenda kukitembelea, lakini je, kuna kitu gani kingine cha ziada ambacho kitamfanya yeye aweze kutoka na kwenda kutembelea? Tuone umuhimu wa ku-brand hifadhi zetu, tuone umuhimu wa ku-brand utalii wetu pamoja na vivutio mbalimbali.

Mheshimiwa Spuka, tunazo mali kale nyingi, kwa mfano tu hapa katika Mkoa huu wa Dodoma ukienda hapo Kondoa kuna utalii upo, lakini haujatangazwa ipasavyo kuhakikisha kwamba watalii wanafika. Hivi sasa Dodoma ni Jiji, sasa kama Dodoma ni Jiji tunai-brand vipi Dodoma ili kuhakikisha kwamba vivutio vingi vinakuwepo?

Mheshimiwa Spika, katika matukio mengi nimeshuhudia, kwa mfano tu shughuli mbalimbali, ngoma zinazochezwa na wagogo, hizi ngoma zikitumika ipasavyo ni utalii tosha ambao utawawezesha watalii mbali ya kuona vivutio vingine hata hizi ngoma tu na kwa sasa kwa sababu Dodoma ni Jiji, tuone umuhimu wa kuwekeza katika mila, desturi na tamaduni zetu ili watalii wanapokuja wawe na vitu vingine vya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hoteli zetu, kwa bahati nzuri sijatembea sana lakini nimefika nchi ya Nepal. Katika nchi ya Nepal unapokwenda katika sehemu yoyote ile na hasa wakati wa jioni katika hoteli zote wa kitalii kuna utaratibu wa ngoma, mila na tamaduni zao, ambapo wanashuhudia pale, na ni kivutio. Kwanza inawawezesha wale wananchi wanapata kipato, lakini pia Serikali inapata kipato. Kwa hiyo wakazi wanaoishi maeneo ya karibu na pale wanafaidika kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu kwa mfano jamii ya Wamasai, Mmasai tu yeye mwenyewe ni kivutio, lakini je, tunawatumiaje hawa ndugu zetu Wamasai kuhakikisha kwamba ule utamaduni, mila na desturi zao zinawafaidisha hawa Wamasai lakini pia inakuwa ni njia mojawapo ya kuiongezea Serikali pato la Taifa?

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia katika mapori tengefu. Tunayo mapori mengi ninaiomba sasa Serikali kwa kupitia Sheria ya mwaka 2009/2010 ambayo inampa dhamana Waziri mwenye dhamana kuhakikisha kwamba anatenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima ili kuepusha hii migogoro ambayo imekuwa ni shida. Ukisikia hawa wote wanaolalamika juu ya mifugo, mimi wakati na kwenda form one mama yangu aliuza ng’ombe Kwa hiyo ninajua thamani ya ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, leo hii mnavyowafilisi hawa na hasa kwa watendaji ambao si waaminifu inakuwa ni pigo na tunawaingiza kwenye umaskini hawa wafugaji. Tunahitaji wafugaji, tunahitaji hifadhi zetu kwa sababu tunaelewa umuhimu wa hifadhi zetu, tunaelewa umuhimu wa mifugo, lakini pia hata wakulima.

Mheshimiwa Spika, mimi nina imani kubwa na Waziri, tuone ni kwa jinsi gani hawa wafugaji hawaumii, wanakuwa ni sababu ya wao kuweza kulinda hizo hifadhi na wanyama lakini pia wakulima nao wanafaidika na haya maeneo yaliyopo. Tuone kwamba haya ni maeneo gani ambayo tutayatenga kwa ajili ya wafugaji na kwa ajili ya wakulima. Vile vile tuangalie jinsi ya kuisuluhisha migogoro hii yote kwa amani na utulivu ili kuepuka haya malalamiko ambayo yanawaumiza wananchi, na hasa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, niipongeze pia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hasa kwa ujenzi wa maktaba mpya ya kisasa kabisa ambayo itasaidia na inasaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mali kale.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni…

SPIKA: Makumbusho, sio maktaba.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Makumbusho ambayo inasaidia kuhifadhi hizi mali kale. Kwa mfano hivi sasa tayari imegundulika kwamba mtu wa kwanza duniani aliishi Afrika; na kwa bahati nzuri huyo mtu wa kwanza imegundulika aliishi Tanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru, naunga mkono hoja ahsante
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi nichangie bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya na nampongeza Mheshimiwa Rais na Waziri mwenye dhamana. Vilevile nampongeza sana Spika wa Bunge pamoja na Katibu wa Bunge Bwana Kagaigai, kwa sababu wamekuwa ni mfano wa kuigwa kwa kuzingatia haki za msingi na kufuata Sheria za Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mwaka 2006 juu ya haki za watu wenye ulemavu. Nampongeza sana Mheshimiwa Spika na Katibu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, katika suala zima la elimu bure kwa watu wenye ulemavu limekuwa na faida kubwa sana. Nasema hivyo kwa sababu siku za nyuma katika suala zima la elimu katika jamii zetu, hasa wazazi walikuwa wanaangalia kwamba kipaumbele apewe nani. Kipaumbele hiki apewe mtu mwenye ulemavu. Kwa hiyo, kama kuna watoto wawili katika familia, mzazi yuko tayari kumpeleka mtoto asiye na ulemavu na mtoto mwenye ulemavu anaachwa nyumbani na wengi wao walikuwa wanafichwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba haki ya kupata elimu ni ya msingi na ni haki pia kwa watu wenye ulemavu. Katika Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Waziri sijaona, bado sijaridhika hasa katika kundi hili la watu wenye ulemavu kuzungumzia ni kwa jinsi gani. Kwa maana hiyo naiomba tu Serikali na Mheshimiwa Rais, kwa sababu pamoja na kwamba jitihada nzuri na kazi nzuri imefanyika katika kuhakikisha kwamba elimu ni bure mpaka kidato cha nne, lakini bado naomba elimu kwa watu wenye ulemavu iwe ni bure kuanzia elimu ya msingi mpaka elimu ya chuo cha Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivyo? Kama nilivyosema hapo awali, mtu mwenye ulemavu tegemeo lake kubwa liko katika elimu, hana namna nyingine yoyote ambayo inaweza kumwezesha huyu mtu akaweza kujitegemea mbali ya elimu. Kwa sababu ukimpa elimu umemkomboa na elimu hii ndiyo itakayomsaidia aweze kupata ajira. Vile vile bila ajira kwa mtu mwenye ulemavu na hasa hata wale ambao wamesoma, asipopata ajira bado inakuwa ni shida. Kwa hiyo, ile elimu aliyopata itamsaidia aweze kuona ni kwa jinsi gani anaweza akajiajiri kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba inatoa elimu bure kwa watu wenye ulemavu kuanzia elimu ya msingi, sekondari na vilevile elimu ya chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mzuri tu, nawaombea mapumziko mema mapacha wawili ambao walifariki hivi karibuni, Maria na Consolata. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika suala zima la mkopo, aliwapa watoto hawa ruzuku ambayo siyo mkopo, kwa sababu aliona umuhimu wa watoto hawa kwa jitihada zao mpaka wakafika elimu ya chuo cha kikuu. Kwa hiyo, akaona ni namna bora kabisa kuhakikisha kwamba anawapa ruzuku ili waweze kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtu mwenye ulemavu mpaka anapofika chuo kikuu au anapobahatika kumaliza elimu ya sekondari akaenda kidato cha nne, cha tano na cha sita na baadaye kwenda chuo kikuu ni sawa na usemi wa Kiswahili unaosema: “Ukimwona nyani mzee, ujue amekwepa mishale mingi.” Kwa hiyo, changamoto wanayopata watoto wenye ulemavu na watu wenye ulemavu ni kubwa na ni mara mbili ya wenzetu wasio na ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kuona umuhimu wa kuwapa elimu bure watu wenye ulemavu kuanzia elimu ya awali mpaka chuo kikuu. Siyo hayo tu, tuone ni kwa jinsi gani tunawawezesha kwa kupata vifaa. Nafurahi sana Waziri mwenye dhamana ni mama, wanasema: “Uchungu wa mwana aujuae mzazi.” Tuone sasa ni kwa jinsi gani tunawezesha vifaa vipatikane katika shule zote. Pia hawa Walimu ambao wanasoma katika Vyuo, tuone ni kwa jinsi gani tutawawezesha wapate vifaa vya kuwasaidia pia katika kufundishia ili basi tutatue zile changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana na namwomba sana Mheshimiwa Rais aone ni kwa jinsi gani atalikomboa hili kundi la watu wenye ulemavu. Natambua jitihada zake, tumeona ni kwa jinsi gani katika Wizara mbalimbali wapo watu wenye ulemavu na hawajamwangusha. Hata katika Bunge lako, katika Baraza tumeona Mheshimiwa Ikupa anavyofanya kazi vizuri na hii imetuonesha kwamba watu wenye ulemavu ukiwapa nafasi wanaweza. Sasa usipowapa elimu itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Naomba sana katika hilo ili basi tuweze kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ukurasa wa 15 wa Bajeti ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza kuwa asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira na vijana 800,000 wanaohitimu Elimu ya Chuo Kikuu ni vijana 40,000 tu wanaopata ajira. Kwa miaka mitatu ina maana kwamba tutazalisha watu 2,280 wasio na ajira. Kwa sababu kati ya hao 40,000 ukiondoa katika hiyo 800,000 wanabaki watu 760,000. Kwa hiyo, utaona ni kwa jinsi gani tatizo la ajira lilivyo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri aliendelea kwa kusema kwamba Sekta ya Kilimo ambayo ni tegemeo, inaajiri asilimia 66 ya Watanzania. Pamoja na kwamba kuajiri asilimia hiyo bado inachangia pato lake kwa wastani wa asilimia 30, lakini pato hili linakua kwa kasi ndogo sana ya 3% mpaka 7%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hivi karibuni tumeona jitihada zake, ambapo amezindua mpango mkakati wa kilimo. Katika suala hili sasa tuone ni kwa jinsi gani kilimo chetu tunakifanya kuwa cha kisasa. Nchi ya Misri ambayo inategemea maji kutoka Mto Nile, wameweza kwa kiasi kikubwa sana kufanikiwa katika suala zima la kilimo. Siyo hao tu, ukienda nchi ya Israel mapinduzi ya kilimo ni makubwa sana na hata Mheshimiwa Mama Mbene siku akichangia bajeti hii alielezea pia nchi ya Vietnam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa nchini Tanzania mvua ni shida na hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, je, tunajipangaje kuhakikisha kwamba kilimo chetu, mbali ya kuajiri asilimia hiyo 66, lakini vijana hawa 800,000 ambao wanahitimu vyuo vikuu, tuone kwamba wale wanaobaki ni kwa jinsi gani wanaweza kujiajiri katika suala zima la kilimo. Vile vile katika kilimo tuone kuna mpango mkakati gani wa kuwawezesha vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tumeona kwamba vijana wengi wameingia katika kilimo cha kisasa ambacho ni kilimo cha kibiashara kwa kulima hasa kwa kutumia hizi green house. Je, Serikali sasa inawawezesha vipi hawa vijana na hasa ukizingatia kwamba nchi ya Tanzania tuna maeneo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya maeneo makubwa tunawawezesha vipi vijana ili waweze kujiajiri wao kwa kulima kilimo chenye tija ambacho kitaweza kuwasaidia wao na familia zao? Hili ni jukumu ambalo Serikali inapaswa kuhakikisha kwamba inajipanga na itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira. Kwa sababu vijana tukianza kuwawezesha na kuwafundisha tangu chuo kikuu; na tumeshaona kwamba sasa hivi Mheshimiwa Rais ana dhamira ya dhati kabisa kuwakomboa vijana na hasa katika mapinduzi haya ya kilimo, sasa basi twende kuwawezesha vijana waingie katika hicho kilimo cha biashara ambacho kitawasaidia kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona baadhi ya vijana ambao wamefanya vizuri na wanasafirisha bidhaa za shambani ambazo wanalima mpaka nje ya nchi. Mmoja wa vijana hao ni Khadija Jabir ambaye amekuwa ni mfano wa kuigwa. Sasa tunawaandaaje vijana wengine, tuwapate kama akina Khadija Jabir ili nao waweze kujiingiza katika mapinduzi haya ya kilimo? Kwa sababu pia tunakwenda katika viwanda rasilimali nyingine hasa malighafi nyingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimalizie kwa kusema kwamba napongeza pia kwa kuona umuhimu wa kufuta kodi katika baadhi ya vifaa ambavyo vinachanganywa katika vyakula vya kuku. Kuku hivi sasa ni tegemeo kubwa sana la wajasiriamali. Kwa hiyo, kwa kuondoa kodi hizi zitawasaidia sana wanawake ambao ndiyo wajasiriamali wakubwa na jamii yote kwa ujumla ili waweze kuwekeza katika ujasiriamali wa kufuga kuku. Siyo hilo tu, hili pia litawasaidia waweze kuendeleza na kuwasomesha watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushuru sana na naunga hoja mkono.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza mawazo mazuri yaliyotanguliwa na Wabunge wenzangu hasa wa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa wamedhamiria kuweza kuunga mkono na kumtia moyo Rais na jemedari wetu mzalendo namba moja Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote na vilevile pongezi za pekee ziende kwako wewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuwa wewe umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba Mheshimiwa Rais anakwenda kufanya na kutimiza yale aliyoahidi, aliwaambia Watanzania alipokuwa akiomba kura mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika mpango Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. Nina furaha kuona kwamba katika bajeti ya elimu ni kwa jinsi gani ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano na hasa ilivyojidhatiti katika kuhakikisha kwamba elimu ni bure, tumeona kwa jinsi ambavyo hivi sasa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi na sekondari imeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia imewawezesha hata wale wanafunzi ambao kwa namna moja au nyingine hawakuweza kupata elimu wazazi wao hivi sasa wamepata ahueni ya kuwaandikisha watoto wao na ndiyo maana leo hii tunajivunia kwa kuona kwamba idadi kubwa imeongezeka, pongezi za dhati kabisa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na mpaka kufikia hivi sasa kwa mujibu wa taarifa ya jana inaonesha kwamba ni bilioni 20.9 ambazo zinatolewa kwa kila mwezi. Utaona kwamba hizi kwa mwaka mzima zinakwenda bilioni 250.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya mpango tumeona kwamba kuhusiana na suala zima la umeme wa REA ni kwa jinsi gani ambavyo Serikali imeweka nguvu kuhakikisha kwamba wananchi na hasa wa maeneo ya vijijini kuelekea uchumi wa kati wanapata umeme. Tunafahamu umeme na hivi sasa katika suala zima la viwanda umeme unahitajika sana. Jumla ya vijiji 557 tumeona kwamba hivi sasa tayari vimekwishapata umeme huu wa REA na hii itawawezesha wananchi waweze kujikita katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais wetu ambaye anawapenda na anawapigania wananchi wake kuhakikisha kwamba anatutoa hapa tulipo na kufika katika uchumi wa kati mwaka 2025. Hili ni jambo la kujivunia na nawapongeza tu Mawaziri na Waziri mwenye dhamana ya umeme basi endeleza jitihada hizo na sisi tunakuunga mkono tupo nyuma yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mabadiliko ya Sheria za Madini tumeona ni kwa jinsi gani zimeongeza pato na hasa katika ujenzi wa ukuta kule Mererani. Kwa mujibu wa taarifa tumeona kwamba hapa ukuta huu ambao una kilometa 24.5 mapato yameongezeka toka bilioni 194.4 kwa mwaka 2015 na kuendelea lakini hadi mwaka 2018 sasa hivi ni bilioni 301.2. hizi ni jitihada njema kabisa za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kwamba madini yanawafaidisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema tu kwamba nimpongeze pia hata katika Bunge la Afrika nilimuona mmoja wa Wabunge kwa kweli Mheshimiwa Silinde nikupongeze umeona jitihada hizi na ukapongeza kwamba kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa mabadiliko ya sheria zilizoletwa hapa Bungeni zimewezesha na ukawataka pia Wabunge kutoka Mabunge mengine ya Afrika nao waige mfano kwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Hii ilikuwa ni jitihada na credit nzuri kwa nchi yetu na hongera sana kwa huo uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ni kwa jinsi gani katika vituo vya afya vimeboreshwa, wananchi wengi maeneo mengi walikuwa hawapati huduma ya afya. Mimi naamini kabisa kwamba jitihada hizi zitakwenda kupunguza vifo vya wanawake na watoto, lakini vilevile wananchi wengi watapata huduma hii kutokana na vituo hivi vinavyojengwa maeneo mengi hakukuwa na hivyo vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa Rais kuhakikisha kwamba tunatumia nguvukazi ya wananchi, vituo hivi vimejengwa katika ubora na vilevile gharama zake zimewezesha kupatikana yale majengo yote yaliyotakiwa. Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa jitihada hizi kuhakikisha kwamba wananchi wake kwa sababu ili tuwe na uchumi ulio imara tuweze kuzalisha mali tunahitaji afya na kwa wananchi wakipata afya basi uzalishaji mali utaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali kwamba kutokana na jitihada hizi na vilevile kwamba wenzetu wanasema Serikali imewekeza sana katika vitu, ni kweli tunawekeza katika vitu kwa mfano barabara ili tuwawezeshe wananchi waweze kufika kutoka eneo moja na lingine. Vilevile wananchi hawa wataweza kusafirisha biashara zao na kusafiri wao wenyewe tofauti na hapo awali ilivyokuwa na ndiyo maana leo hii ukitoka Arusha mpaka Tunduma kwenda mpakani mwa Zambia na Tanzania ni barabara ya lami kutokana na jitihada nzuri za Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunaona kwamba katika suala zima la kilimo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu jitihada zinavyofanyika hivi sasa ambapo amekuja na mipango/mikakati ya kuhakikisha kwamba wanawawezesha vijana katika kilimo. Wao wamedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunaingia katika kilimo cha vitalu (green house). Huu ni mpango mzuri na jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ili vijana waweze kujiingiza kwenye kilimo na siyo kwa kufanya hivyo tu. Serikali yenyewe inawawezesha vijana hawa kwa kupitia mikopo mbalimbali ili waweze kujipanua zaidi katika suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema ni kwamba na masoko pia tayari kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wamekwishaanza kuwatafutia vijana hawa. Kwa hiyo, napongeza sana jitihada hizi kupitia kwa Waziri Mkuu, kupitia kwa dada yetu Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wako kutokana na kazi nzuri mnayofanya. Nina imani kubwa kabisa na Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile vikundi vya ujasiriamali vimewezeshwa na siyo hao tu, nina furahi sana kupitia sheria ya 442 ambayo itawawezesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo na tayari baadhi ya Halmashauri zimekwishaanza kutekeleza hili, hii itatusaidia pia kupunguza umaskini. Pia itatusaidia kupunguza ile hali ya kuwa tegemezi na yote haya ni kutokana na mipango mikakati mizuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema hakuna usalama, nchi hii ni miongoni mwa nchi ambazo zinaongoza kwa amani. Wenzetu waliopo nchi jirani wanajivunia Tanzania na kuitolea mifano, ndugu zangu tuendeleze amani tuliyonayo na amani hii ndiyo itakayotuwezesha kufika katika uchumi wa kati mwaka 2025. Kwa maana hiyo kwamba kukiwa na amani watanzania wataweza kwenda kufanya shughuli zao mbalimbali za ujasiriamali lakini vilevile kwenye kilimo na shughuli zingine ambazo zitawawezesha wao kuongeza kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais wetu mzalendo namba moja, Rais ambaye katika dunia hii wanamtolea mfano na waswahili wanasema kwamba kwenye miti, hapana wajenzi. Mimi nasema kwamba wajenzi ni sisi wenyewe na ni kutokana na Rais huyo basi atatufikisha katika uchumi tunaoutarajia kufikia uchumi wa kati mwaka 2025. Tumuombee Rais wetu na tumuunge mkono ambaye ameruhusu wajasiriamali waweze kuingia maeneo mbalimbali kujipatia kipato. Hivi sasa hata wizi umepungua kutokana na vijana wengi wanajishughulisha katika shughuli za kujiletea vipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge wenzangu tuendelee kuungana na Mawaziri na kumuunga mkono Rais wetu kuhakikisha kwamba yale aliyoyaahidi mwaka 2015 anayafanyia kazi na kuyatimiza. Jambo la muhimu ni kuona kwamba ni kwa jinsi gani amedhamiria miradi mikubwa ya umeme kwa mfano Stiegler’s Gorge na mradi wa reli ambao tayari umekwishaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ssa katika Jiji la Dar es Salaam hata foleni zimepungua kutokana na miundombinu inayojengwa na kwa mfano daraja la TAZARA. Hizi ni jitihada zinazoonyeshwa na Rais wetu kwa kipindi kifupi, tunatarajia kwamba kwa miaka mitano itakayokuja kutakuwa na mafanikio makubwa zaidi na endapo tutaendelea kumuunga mkono. Mungu akupe maisha marefu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, tunakupenda, tunakuhitaji sana na tunaona kwamba wewe umedhamiria kuwakwamua wananchi wako na una dhamira ya dhati kabisa katika kuhakikisha kwamba unatutoa hapa tulipo kufika katika uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Niende moja kwa moja katika kuchangia kwenye Kamati ya Miundombinu, nianze nayo kwanza. Naipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa ambazo imefanya na hasa Mheshimiwa Rais katika kulifufua na kuiendeleza TTCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa TTCL ilikwishakufa lakini kwa jitihada na weledi mkubwa wa Rais wetu tumeona sasa shirika hili tayari limekwishafufuka. Ni matarajio yangu kwamba sasa litakwenda kujiendesha kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili shirika hili liweze kujiendesha kwa faida naishauri Serikali kuona ni namna gani Wizara na Taasisi zinaweza kulipa yale madeni ili pia liweze kuendelea kutoa gawio kama walivyoweza kufanya kwa mwaka jana. Pasipo kulipa haya madeni bado itakuwa ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika viwanja vya ndege. Naipongeza pia Serikali na Kamati kwa jinsi ambavyo wametuletea ripoti inayoonyesha jitihada za Serikali katika ujenzi huu wa uwanja wa ndege na hasa Terminal III. Uwanja huu utakapokamilika utapokea kwa siku watu zaidi ya 2,000, hili pia litasaidia kuleta watalii na wageni wengi kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nina ushauri kwa Serikali kwa sababu pamoja na jitihada hizi nzuri lakini suala la miundombinu hasa kwa watu wenye ulemavu bado ni tatizo. Katika viwanja vyetu vya ndege hakuna lift ambazo zinaweza kuwasaidia watu wenye ulemavu. Mara nyingi ukienda katika uwanja wa ndege hata ile lift iliyopo wakati mwingine unakuta haifanyi kazi. Kwa hiyo, watu wenye ulemavu, wagonjwa inakuwa shida kufika katika viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, wakati mwingine tumeona kwamba wengine wanalazimika kuwabeba, siyo kila mtu atapenda kushikwashikwa kubebwa kupandishwa kwenye ndege kutokana na ule umbali. Kwa hiyo, niwaombe sana Serikali na hasa Wizara husika kuona ni jinsi gani tunaweka hii miundombinu ili angalau basi na watu wenye ulemavu waweze kufurahia mazingira hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi sana ukifika maeneo mengine kama Dubai unapotua tu kwenye uwanja tayari unakuta kwa mtu mwenye ulemavu miundombinu imeandaliwa na mtu huyu inakuwa ni rahisi kufika eneo ambalo anataka. Kwa hiyo, naishauri Serikali kuona ni kwa jinsi gani wataboresha miundombinu na kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu. Naipongeza sana Serikali kwa ujenzi wa miundombinu ambayo tumeona sasa Tanzania yetu ni kwa jinsi gani tunaunganishwa na barabara ambazo zimejengwa. Barabara hizi zitaweza kukuza uchumi, kipato kwa mtu mmoja mmoja lakini kwa maeneo mengi wananchi wataweza kusafirisha bidhaa zao kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itawasaidia wao badala ya kuuza bidhaa zao katika maeneo yale ambayo kwa namna moja au nyingine hawezi kupata fedha ambazo wanatarajia wao lakini wakitoka pale na kwa sababu kwa hivi sasa miundombinu tayari ipo itasaidia sasa kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja lakini pia kuongeza pato kwa kwa Serikali yetu kwa sababu itapata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye barabara, naomba tu Serikali kwa sababu nimechunguza na kuona wamejitahidi kuweka alama za barabarani na alama hizi zipo kuhakikisha kwamba hapa kuna watu wenye mahitaji maalum wanataka kuvuka, tumeona sasa hivi zebra zinaheshimika sana. Hata hivyo, maeneo mengi ambapo kuna alama zinazowawezesha watu wenye ulemavu waweze kuvuka bado ni tatizo Watanzania hawaheshimu alama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote, naipongeza Serikali kwa umamuzi wake wa busara kwa kuleta Azimio hili katika kuyabadilisha Mapori haya ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika pamoja na Orugundu kuwa sasa Hifadhi za Taifa. Kwa maana hiyo basi Hifadhi za Taifa zitaongezeka kutokana na upandishwaji wa mapori haya.

Mheshimiwa Spika, naomba nitaje faida zitakazopatikana kutokana na hifadhi hizi zilizoanzishwa. Kwanza kabisa, pato litakalopatikana litaongezeka katika pato la Taifa na vilevile ajira zitapatikana na hivyo vijana wanaoishi katika maeneo yale kwa namna moja au nyingine itawasaidia sana hasa katika zile kazi kwa mfano za kuongoza watalii na shughuli nyingine mahoteli yatakapojengwa wataweza kupata hizo ajira.

Mheshimiwa Spika, miradi ya ujirani mwema inayotekelezwa na TANAPA na nichukue fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wa TANAPA kwa jinsi ambavyo wanatekeleza sera ya ujirani mwema. TANAPA wamekuwa wakisaidia wananchi wanaoishi maeneo majirani na hifadhi zetu kwa kujenga hospitali na kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo haya. Kwa hiyo, niwapongeze sana TANAPA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwepo wa Uwanja huu wa Ndege ambao kwa kweli kwa muda mrefu umekuwa ukizungumzwa sasa tunaona busara za Mheshimiwa Rais wetu kwa kuona mbali kwamba sasa watalii wataweza kufika kwa haraka zaidi pale na kuweza kutembelea hizi hifadhi zetu. Tunafahamu Geita imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na madini, kwa hiyo, wawekezaji wataweza kufika kwa urahisi zaidi. Madini haya pia yataweza sasa kutangazwa kwa undani zaidi kutokana na hifadhi hizi kwa hiyo wawekezaji wengi watapenda kwenda kule kuwekeza mahoteli na miradi mbalimbali. Kwa hiyo, kwa kweli tunaona kabisa kwamba Geita itakwenda kubadilika lakini na maeneo mengine jirani na uwanja huu sasa ndiyo utakaokuwa chachu kubwa ya maendeleo. Vilevile uanzishwaji wa hifadhi hizi kutachangia utunzaji wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende tu haraka katika kuishauri Serikali kwa sababu tunafahamu kwamba faida ni nyingi. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua channel ya kutangaza utalii Channel ya Safari pale TBC na Waheshimiwa Mawaziri walikuwepo. Kwa hiyo, sasa ni wakati muafaka kabisa wa kuitumia hii Safari Channel kuweza kutangaza utalii wetu na hasa hifadhi hizi mpya ili wananchi waweze kutambua na kupata ule muamko wa kwenda kutembelea hifadhi zetu. Kwa maana kwamba wananchi watakapokwenda kutembelea hifadhi hizi, kwanza ni njia mojawapo ya kupunguza msongo wa mawazo unapokwenda kule unasahau mengine na kuona utalii uliopo kule. Kwa hiyo, nashauri sana kuitumia hii channel ili iweze kutagaza huo utalii wetu.

Mheshimiwa Spika, wito wangu vilevile wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi hizi kuona kwamba wao ndiyo wanakuwa chachu ya kutunza mazingira na kuhifadhi hifadhi hizi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Amina.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii, Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu, bariki Baraza la Mawaziri, wewe mwenyewe Spika na Watanzania wote kwa ujumla. A Luta continua, mapambano bado yanaendelea. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Kamati zote hizi mbili. Awali ya yote, naunga mkono Kamati zote mbili. Vile vile namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia na hatimaye kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kabisa, naishukuru Serikali hasa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kweli niwapongeze sana kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuhakikisha makundi maalum na hasa kundi la watu wenye ulemavu ambalo leo hii nitapenda zaidi nilizungumzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nisiisahau pia Wizara ya Katiba na Sheria, nawapongeza sana kwa jinsi ambavyo wamekuwa nao katika suala la Sseria kuzingatia masuala ya watu wenye ulemavu. Vilevile kwa kuwa katika ukurasa wa 25 wamezungumzia makundi maalum, wakiwemo pia watoto, nichukue nafasi hii pia kukemea mauaji yanayoendelea huko Mkoani Njombe hasa ya watoto na Mwenyezi Mungu pia awajalie familia ambazo zimepoteza watoto. Pia wale watoto waliotangulia mbele ya haki, basi Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema Peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa kuzungumzia suala zima la michezo kwa ajili ya watu wenye ulemavu; na nitapenda pia kunukuu Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Ibara ya 30 unaelekeza nchi wanachama kushirikisha watu wenye ulemavu kwenye michezo. Vilevile Sheria yetu ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 Sheria Na. 9 inatoa haki ya watu wenye ulemavu kushiriki kwenye michezo kupitia Kifungu cha 52.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Kimataifa inazungumzia inclusive policy ambayo Tanzania pia imekubali na imeridhia. Ni kweli nchini kwetu tumekuwa tukizungumzia masuala mbalimbali, hasa katika michezo, tunazungumzia kwa ujumla na hasa mpira na michezo mingine ambayo inawahusisha wenzetu ambao kwa namna moja au nyingine wako kamili kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa watu wenye ulemavu, kwa kweli Serikali bado imekuwa nyuma pamoja na kwamba tumeridhia hii sheria, bado michezo kwa watu wenye ulemevu haijapewa kipaumbele na wala haijatiliwa mkazo. Nasema hivyo, kwa sababu hakuna fungu lolote, hakuna mahali ambapo Serikali imejitoa katika kusaidia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; walikuja wenzetu ambao ni kutoka katika Chama cha Watu Wenye Ulemavu ambao wanahusika na michezo. Kwa bahati nzuri sana mwaka huu kuna mashindano yatafanyika hapa nchini kwetu mwezi wa Sita yatahusisha watu wenye ulemevu kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati. Jumla ya nchi 12 zitashiriki, lakini mpaka sasa bado wanahangaika hawajui wapi ambako kwa kweli wanaweza wakasaidiwa. Ni heshima kubwa kwa michezo hii kufanyika hapa nchini mwetu, lakini ningeiomba Serikali katika majibu yao watakapokuja kutueleza, watueleze kwamba katika hili wamejiandaje basi ili kufanikisha michezo hii, lakini kama tunavyofahamu michezo ni ajira, michezo ni afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia michezo hii inatukutanisha kwa pamoja walemavu kutoka sehemu mbalimbali. Kwa hiyo katika ile michezo inakuwa ni faraja kwetu pia, kwa hiyo niombe tu kwamba Serikali ione kwamba inatekeleza sera hizi katika kusaidia hawa watu wenye ulemavu kwenye michezo kwa sababu pia itawasaidia kuongeza kipato cha kwao wao binafsi pia na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili naomba sana Serikali waweze kuliona kwa sababu katika Kamati yetu ni kweli tunasimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na kipekee mimi nawapongeza kwa sababu kuna jitihada kubwa sana ambazo zimefanyika na niseme tu kwa kweli kwa Mheshimiwa Rais wetu nampongeza sana kwa moyo wangu wa dhati kabisa, kwa jinsi ambavyo ameyapa kipaumbele masuala watu wenye ulemavu. Hilo kwa kweli tunajivunia na hata kwa Afrika Mashariki kitendo cha kuwa na Naibu Waziri katika Baraza la Mawaziri, hii ni faraja kubwa sana na ni mfano ambao hata wengine wenye ulemavu wakiona kwamba kwenye Baraza kuna mtu ambaye amefikia hatua hiyo, wanapata ile ari ya kusoma na kuweza kuwa na ndoto kwamba na wao siku moja watakuja kufika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Rais wangu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, nampongeza sana kwa hili kwa kutambua na kuwapa umuhimu na niseme tu kwamba sasa hivi watu wenye ulemavu tumekuwa na heshima kubwa hata wazazi wale ambao walikuwa wanaona kwamba kuwa na mtoto mwenye ulemavu ni tatizo, sasa hivi wanaona kwamba kumbe akipata elimu na kwa kuzingatia kwamba sasa hivi elimu ni bure, kwa kweli hizi pongezi namwombea sana Mheshimiwa Rais wetu, Mwenyezi Mungu aweze kumpa maisha marefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kuzungumzia mwishoni mwa mwaka jana nilipata bahati ya kuhudhuria kama mdau katika Ofisi ya Waziri Mkuu, walikuwa wanaandaa mwongozo ambao utawezesha kuwa na Mfuko Maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu na hili nimelizungumzia sana katika Bunge hili, ni matarajio yangu kwamba Mheshimiwa dada yangu mpendwa Jenista kwamba kwa mwaka huu ni matarajio yangu kwamba kwa sababu katika Bunge na hasa Ofisi ya Waziri Mkuu tuna fungu kwa ajili ya Bunge, tuna fungu kwa ajili ya vijana, tuna fungu kwa ajili ya masuala mengine, lakini hakuna fungu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu kwa kweli nitakuwa mpinzani wa Mheshimiwa Waziri endapo hatokuja na fungu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Matokeo yake kwamba sasa tumekuwa tukidandia tu katika haya mafungu mengine, vijana wanalo fungu lao na katika fungu hili mpaka katika mikoa yote wana ofisi zao. Sasa kama masuala haya tumeshayachukua na tumeshayapa kipaumbele ni muhimu sasa na hili pia wakati mwingine hata Naibu Waziri aweze kufanya kazi zake vizuri inakuwa ni busara zaidi akiwa na fungu lake, anajua kabisa kwamba hapa Mheshimiwa Waziri nitamshauri tufanye hivi, nitamshauri tuendeleze hivi, lakini pasipokuwa na fungu wakati mwingine unaweza ukaambiwa kwamba hakuna fedha kwa ajili ya masuala hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo dada yangu mpendwa namjua uwezo alionao, Mheshimiwa Jenista Mhagama namfahamu yeye ni mwanamke shupavu, ni mwanamke hodari amekuwa mfano bora na isitoshe kama mama basi hili atalibeba kwa hekima kubwa na ataliangalia pia kwa jicho la ziada kuhakikisha kwamba katika bajeti ya mwaka huu tunakuwa na fungu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu na sio kudandia katika mafungu mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia kuhusiana na watu wenye ulemavu, naendelea kupongeza kwa sababu naona mabadiliko makubwa na ndio maana naendelea kujivunia, mwaka jana tulipitisha sharia…

MWENYEKITI: Ahsante kengele ya pili.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na kuwepo hapa, bila yeye tusingekuwepo hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa naomba na naonesha kutokana na jinsi ambavyo Ofisi hii ya Waziri Mkuu na pia Rais kupitia Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya kazi na hasa katika masuala ya watu wenye ulemavu yalivyopewa kipaumbele. Hii inaonesha kwamba Serikali yetu ni sikivu, inasikiliza wanyonge na inasikiliza hoja mbalimbali ambazo zinatolewa na kwenda kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwa kuanza kuzungumzia Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu; tarehe 2 Februari, 2017 niliuliza swali kuhusiana na Mfuko huu na nilisema kwamba kwa sababu Mfuko huu na masuala yote ya watu wenye ulemavu yapo pia katika mkataba wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2006, lakini pia Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 inazungumzia pia haki za watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia na kuishauri Serikali kuona ni kwa jinsi gani wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu na tulidai Mfuko kuhusiana na watu wenye ulemavu lakini pia tukadai bajeti kuhusiana na Wizara hii kwamba tayari tunaye Naibu Waziri na kama tunaye Naibu Waziri tulihitaji kwamba kuwepo na bajeti maalum. Kwa mfano mfuko huu kwa mwaka 2017 haukutengewa fedha, lakini mabadiliko makubwa tumeyaona katika bajeti hii ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nampongeza mwenzangu Mheshimiwa Naibu Waziri, Ikupa Alex, kwa ushauri mzuri ambao ameweza kuutoa kwa kushirikiana kwa pamoja hatimaye sasa kwa kweli tunajivunia kuona kwamba kitengo cha watu wenye ulemavu kimetengewa fedha. Kwa kuanza kwa mwaka huu ambayo ni subvote 2034 na imetengewa zaidi ya bilioni moja na naamini kabisa huu ni mwanzo, tunapokwenda ni pazuri na tutaweza kuongezewa pia hiyo bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili kwa kweli nampongeza sana Waziri mwenye dhamana, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama yeye ni jembe lakini pia niwapongeze Manaibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa. Jembe lingine ambalo limeongezeka katika Ofisi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Angella Kairuki, lakini pia naamini kabisa ni kutokana pia na Makatibu Wakuu waliopo ambao na wao kwa kweli kipekee nawapongeza sana kwa mchango wao katika kuwasimamia na kuwashauri vizuri Mawaziri hatimaye tunakwenda pamoja sasa. Nawapongeza sana na nimpongeze sana Katibu Mkuu baba yangu Massawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo na kazi nzuri ambazo kwa kweli zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, napenda kushauri mambo mawili, matatu ili basi kuona kwamba ni kwa jinsi gani na kama ilivyo sisi ni kiunganishi katika ya Serikali na wanachi na wajibu wetu ni kuisimamia Serikali na kuishauri. Napenda kuishauri Serikali katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwamba tumeona tunacho kitengo na tayari tumekwishatengewa fedha. Naishauri Serikali kuona umuhimu sasa kutoka kwenye kitengo na kwenda kwenye idara kamili ambayo idara hii ndiyo itakuwa Idara ya Watu Wenye Ulemavu na siyo kitengo. Huu ni ushauri wangu naomba sana watakapoendelea basi waone kwamba ni kwa jinsi gani tunakwenda kufikia huko na kuwa Idara ya Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu bado siyo rafiki katika majengo mengi na hata ya Serikali pia kwa watu wenye ulemavu. Bado miundombinu siyo rafiki na hata baadhi ya majengo mengine watu hawazingatii. Nawaomba waliopewa dhamana ya kulisimamia hili kuona kwamba tunaweza kuondoa changamoto zote hizi ambazo zinawakwamisha watu wenye ulemavu kuweza kushindwa kutimiza majukumu yao au kwenda maeneo ambayo wanapaswa kwenda kufuatilia haki zao au kushughulikia yale mambo ambayo ni muhimu kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimpongeze Naibu Waziri wa Kazi, Ajira pamoja na Mkurugenzi wa Ajira, Bwana Msaki kwa kazi nzuri wanayofanya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na tunaisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu. Tumeshuhudia ni kwa jinsi gani ambavyo Waziri mwenye dhamana, kwa ujumla Ofisi hii kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi na tumesikia kwamba watu wakilalamika kuhusu suala la ajira na tunapoelekea hata Marekani bado tatizo la ajira lipo na ni nchi zilizoendelea. Kwa kuona kwamba Serikali haiwezi pia kuwatimizia wananchi wake wote kuwapa ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira wao wameandaa utaratibu mzuri ambao wanakusanya maoni na hasa vijana mbalimbali ambao wamemaliza Chuo Kikuu, wanatuma maoni na maombi hatimaye Ofisi hii kwa utaratibu mzuri ulioandaliwa wanapelekwa katika Taasisi mbalimbali ikiwemo mabenki. Kule wanakwenda wanapata ujuzi na wengi tayari hivi sasa kule walikopelekwa wamekwishapata ajira na kuchukuliwa na mabenki na maeneo mengine tofauti tofauti. Hii ni kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile bado utaratibu mzuri ambao umeandaliwa katika suala zima la kilimo na tumekuwa tukizungumza hapa kilimo cha kutegemea msimu wa mvua siyo kilimo ambacho kitaweza kutukomboa. Serikali yetu imekuja na utaratibu mzuri wa kuona ni kwa jinsi gani tunalima katika kilimo biashara, kilimo chenye tija kwa kuona ni kwa jinsi gani tunalima kwenye kilimo cha kutumia maji hasa kilimo cha umwagiliaji. Ofisi hii utaratibu mzuri iliyoandaa katika Halmashauri zetu hivi sasa katika kila Halmashauri vijana wanatakiwa zaidi ya 100, Halmashauri zetu zimeandaa baadhi ya maeneo na vijana hawa wanapewa ujuzi, wanajengewa nyumba-vitalu yaani green house ambazo wanapewa ujuzi kuweza kujua ni kwa jinsi gani wataweza kulima mazao ya kule ndani kwenye bustani hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mazao hayo yatakuwa ni mazao ambayo kwanza ni yenye ubora, ni mazao ambayo yataweza kuuzwa katika maeneo tofauti tofauti na yataweza kuwakwamua vijana wale na vijana hao watakaokuwa wamepata huo ujuzi watatoka sasa pale. Tunayo mabenki yetu, naamini kabisa Serikali itawawezesha vijana hawa ili basi waweze kujitegemea badala ya kutegemea hasa ajira kutoka Serikalini. Huu ni utaratibu mzuri unaoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na tayari vijana wapo site wanafanya kazi hiyo. Halmashauri zetu tunaziomba sana zihakikishe kwamba zinasimamia zoezi hili na kutoa ushirikiano kwa walengwa ili waweze kufanyia kazi hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama kweli sitawazungumzia OSHA pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Tulikuwa na malalamiko mengi kwa OSHA, lakini hivi sasa OSHA wameondoa vipengele vingi ambavyo vilikuwa ni kero kwa wawekezaji na vipengele hivyo vimeondolewa hivi sasa na tumeona kwamba, pamoja na kuondoa vipengele hivyo, wawekezaji sasa wengi wamekwenda, vibali vinatolewa kwa muda muafaka, lakini pia wanapata fedha kutokana na vibali hivyo. Kwa hiyo, napongeza sana huu utaratibu unaofanywa na nimpongeze sana Mkurugenzi wa OSHA, Bi.Khadija kwa kazi nzuri sana anayofanya.

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naishukuru sana Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na hatimaye kusimama mbele yako kuweza kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya. Vilevile nawashukuru sana Makamu wa Rais, Waziri wetu Mkuu ambaye amekuwa ni kiongozi wetu na mshauri wetu kwa kazi kubwa anayofanya na katika kumshauri pia Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Mawaziri, nampongeza sana Mheshimiwa Mkuchika na siku zote wanasema penye wazee hapaharibiki neno; amedhihirisha yeye ni baba, amedhihirisha pamoja na yote hayo na kama wanavyosema Waswahili kwamba, mkubwa akivuliwa nguo basi anachutama. Yeye ni jalala, lakini tunaona, tunamkubali na tunaona yale yote anayoyafanya. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri kwa ushauri mzuri na kazi nzuri anayomsaidia Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Jafo. Ameonesha umahiri mkubwa sana hasa katika kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wanawake. Ameweza kumsaidia na kumshauri Rais na hatimaye sasa tunaona matunda mazuri yanayofanyika, nampongeza sana na namwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumtia nguvu, kumpa ujasiri na afya aendelee kuwatumikia Watanzania. Waheshimiwa Manaibu Waziri pia na wao tuwapongeze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kuchangia kuhusiana na asilimia mbili ambayo katika Bunge la Bajeti mwaka jana tuliipitisha. Asilimia hii mbili tumeona ni kwa jinsi gani ambavyo imekuwa na mafanikio katika kusaidia makundi maalum na hasa kundi la watu wenye ulemavu. Niombe tu kwamba, kuna baadhi ya Halmashauri ambazo bado hazijatimiza matakwa ya Sheria hii ya Fedha (Finance Act); naomba sana azisimamie ili basi ziweze kutoa hiyo asilimia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nishauri kwamba, kumekuwepo na changamoto baadhi ya watu wenye ulemavu ambao wako maeneo tofautitofauti, naomba kwamba, busara itumike tuangalie ni kwa jinsi gani ikibidi basi kama ni mmoja mmoja basi tuwakopeshe kwa sababu, wapo ambao tumeona wamefanya vizuri sana. Kwa hiyo, kusiwe na kigezo kwamba, lazima wajiunge kwenye vikundi naomba sana ofisi iweze kuangalia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya hasa katika kutoa elimu bure. Nami nimekuwa siku zote nikithibitisha kwamba, elimu hii bure imesaidia baadhi ya watoto wenye ulemavu kupelekwa shule ambao walifichwa majumbani, lakini kwa sababu elimu ni bure wametolewa na sasa hivi wako kule. Changamoto iliyopo ni miundombinu, bado ni tatizo. Naiomba sana Serikali kuona ni kwa jinsi gani watasaidia katika kutatua changamoto hii ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika shule zote za sekondari tumeona na nashukuru sana wananchi kwa ujumla wamejitoa sana, Wabunge wamejitoa sana katika kuiunga mkono Serikali. Naomba kuona kwamba, ni kwa jinsi gani sasa katika shule hizi za sekondari, zile shule ambazo zina mabweni basi watoto wenye ulemavu waweze kupelekwa kule ili wasipate shida wakasome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo pia watoto wenye ulemavu ambao wanakwenda katika shule ambazo ni maalum na Serikali ilikuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba, inatoa fedha wakati shule zinapofungwa, lakini hivi sasa watoto wale imekuwa ni shida kwa sababu wengine wanalazimika kukaa muda wote shule mpaka inapofika Disemba. Namshauri Mheshimiwa Jafo, ameonesha umahiri mkubwa, naomba awaangalie watoto hawa kwa jicho la pekee, wapewe nauli ili unapofika wakati wa kurudi nyumbani basi waweze kurudi nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hostel zitasaidia sana kwa sababu, kwa mfano kule kwetu jamii ya Wamasai, kama mnavyofahamu, mtoto wa kike akiwepo nyumbani ni rahisi sana kuolewa. Naomba sana hostel kwa ajili ya shule ambazo zipo kwa mfano Shule ya Sekondari ya Oldonyowasi ambayo ni mpya imejengwa hivi karibuni na ndio wameanza kidato cha kwanza. Naomba ujenzi wa hostel katika Shule hii ya Oldonyowasi, ili basi waweze wanafunzi wale ambao wengi wao ni kutoka katika jamii yetu hii ya wafugaji waweze basi kukaa hostel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naenda haraka haraka, vilevile naomba nizungumzie suala la Walimu; Walimu kwa kweli, kukopa kunasaidia na asiyekopa hafahamu nini maana ya kukopa, lakini baadhi ya taasisi za kifedha zinawaumiza Walimu na baadhi ya Walimu wamekwishaacha shule. Naomba niitaje Baypot imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa Walimu ambao kwa kweli, wengine wamelazimika kuacha shule na kukimbia ili kukwepa hiyo mikopo ambayo imekuwa ni kero kubwa kwao. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha uko hapa, alitazame hili ili kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana TARURA na kipekee kabisa kwa sababu, natoka Mkoa wa Arusha, nampongeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha, nampongeza Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Arusha DC. Niombe tu sasa kwamba, kweli wanahitaji kuangaliwa ni kwa jinsi gani tunawaongezea bajeti ili waweze kutimiza yale malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo kwa kweli ni la kutolewa mfano. Ni jambo ambalo kwa kweli, la kushukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kujenga vituo vya afya na vituo hivi vya afya vinakwenda kutatua changamoto ya vifo vya wanawake na watoto. Haijawahi kutokea, tuna kila sababu ya kujivunia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye, tumeona fedha zinazopatikana zinatumika katika kuhakikisha kwamba, zinafanya yale ambayo yamekusudiwa. Vituo hivi pamoja na hospitali za wilaya zinazokwenda kujengwa haya ni mapinduzi makubwa ya maendeleo, naipongeza sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu pia tumeona ni kwa jinsi gani Rais wetu kutokana na utawala bora amedhihirisha miradi hii mikubwa kama kusingekuwa na utawala bora, basi isingewezekana; leo hii kuna Stieglers Gorge, tunaona kwamba, nikwa jinsi gani tatizo changamoto ya umeme itakwenda kutatuliwa. Tumeona Mradi wa REA, lakini sio hilo tu, ujenzi wa reli ya kisasa, vyote hivi ni maendeleo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuangalie pia katika Jiji la Dar es Salaam, tuangalie Ji la Dodoma jinsi ambavyo unapendeza na majengo yale ya Serikali. Hii yote ni kutokana na utawala bora na matumizi sahihi kabisa ya fedha katika kuhakikisha kwamba tunasimamia na kuleta maendeleo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, mimi naipongeza sana Serikali na Mawaziri kwa vifua walivyonavyo vya kuweza kuhimili yote hayo na msivunjike moyo. Kama ndani ya miaka mitatu ambapo sasa hivi tupo mwaka wa nne, Rais Magufuli ameweza kufanya yote hayo, wapo wengine ambao ndani ya miongo zaidi ya miwili mpaka leo hii hawana hata ofisi ya chama, kwa nini tusimpongeze Rais wetu Magufuli kwa kazi kubwa aliyofanya. Nampongeza sana, tunamtia moyo Rais wetu ili kuhakikisha kwamba anazidi kuwaletea Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Watanzania wanaona na 2020 siyo mbali mwakani tutaona Watanzania watakachoenda kufanya na nina uhakika kwamba CCM itaendelea kutawala. Upinzani bado upo nyuma sana kwa hiyo sisi tutaendelea kutawala kwa sababu ya sera nzuri na utawala bora tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Waheshimiwa Mawaziri hongereni sana, msivunjike moyo tuendelee kufanya kazi na sisi Wabunge kumbukeni ni askari miamvuli wenu humu ndani kwa hiyo kabla hamjafikiwa nyie sisi tutakuwa wa kwanza. Alluta continua, mapambano yanaendelea CCM iendelee kutawala. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie bajeti ya Wizara ya Habari. Kama alivyosema mwenzangu Mheshimiwa Juma Nkamia na kwa sababu sisi wote ni wanataaluma, tumekuwa katika taaluma ya habari, naomba niseme kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, Tanzania ni nchi ya pili kwa Afrika Mashariki kwa uhuru wa habari, pamoja na kwamba imeshuka nafasi 10. Kwa mujibu wa report ya Without Borders na The Press Freedom Index ya 2018 Tanzania kwa Afrika na kwa dunia pia ni ya 93. Kenya yenyewe ni ya 96, Uganda ni 117, Rwanda ya 156 na Burundi ni ya 159. Kwa hiyo, utaona kwamba, Tanzania bado sisi ni kinara, tuko vizuri katika uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, Tanzania pia imeshika nafasi ya pili kwa kuenzi uhuru wa habari na wa kisiasa. Imetanguliwa na Kenya kwa Afrika Mashariki na hii ni kwa mujibu wa report ya Freedom House ambayo ni ya mwaka huu wa 2019.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa sababu hiyo, tunakumbuka kwamba mwaka 2018 Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alichaguliwa pia kama kiongozi bora. Ni maoni na kura kutoka kwa wananchi katika Bara hili la Afrika ambao wametambua utendaji wa Rais wetu mpendwa kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niendelee kwa kuchangia. Ninaomba niende moja kwa moja kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). TBC ni Shirika la Umma na mashirika yote duniani hata ukienda CNN, BBC, yote hayo yamefikia pale kutokana na jitihada nzuri za Serikali. Na mimi nina imani kubwa sana na Serikali na jitihada kubwa anazofanya Rais wetu katika kuhakikisha kwamba TBC inasimama.

Mheshimiwa Spika, zile fedha tulizopitisha mwaka 2018, hata kwa bajeti ya mwaka huu utaona ni kwa jinsi gani tunaliboresha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili liweze kuwa kama zamani lilivyokuwa pamoja na maslahi ya wafanyakazi wa TBC.

Mheshimiwa Spika, naomba pia, nizungumzie Waandishi wa Habari wa Tanzania. Hali ilivyo sasa ni mbaya. Waandishi wengi bado hawalipwi maslahi yanayostahili na wanafanya kazi katika mazingira magumu. Namwomba Waziri tuone ni kwa jinsi gani tunavyowasaidia Waandishi wa Habari ili basi na wao waweze kufurahia kazi yao.

Mheshimiwa Spika, sisi hapa bila Waandishi wa Habari, wananchi hawawezi kupata habari zinazoendelea.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba…

SPIKA: Mheshimiwa Amina, Kuhusu Utaratibu.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kanuni ya 64(1)(a) inasema, “Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge:-

(a) Hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.”

Mheshimiwa Spika, mchangiaji anayeendelea kuchangia saa hizi amelieleza Bunge hili kwamba, Rais alichaguliwa kuwa Rais bora. Sasa naomba atusaidie tu kwa uelewa mpana kwamba hizi taarifa naona kama haziko sahihi, hizi kura zilipigwa wapi? Atusaidie tu kwa sababu, naona kama taarifa kidogo hazina…

SPIKA: Kanuni zetu zinasema wewe kwa kuwa umesema hajasema ukweli, wewe unausema ukweli sasa. Yaani wewe ndio uliambie Bunge ukweli ni upi? (Makofi)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu, hili jambo sijawahi kulisikia, nataka tu kusema kwamba kwa nini Mbunge anayecha…

SPIKA: Sasa mbona umesimama kumbe hata hulijui! Basi huna hoja kaa. Endelea Mheshimiwa Amina, endelea na mchango wako. Endelea na mambo mengine tu. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa kumsaidia tu aende katika Jarida la African Leadership Magazine ambalo lina Makao yake Makuu London, Uingereza, atapata taarifa hizi, lakini pia taarifa ziliwekwa wazi kwa vyombo vya habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kuchangia. Niliishia pale kwa kuzungumzia Waandishi wa Habari. Naiomba Serikali na ninajua Serikali ni makini kuangalia kwamba hata baadhi ya wamiliki ambao hawawalipi Waandishi wa Habari ambao ni waajiriwa wao maslahi wanayostahili. Wapo ambao bado wanadai mishahara yao. Waandishi wa Habari kwa kweli wana hali ngumu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kulisimamia hili kuhakikisha kwamba hawa waandishi wa habari wanaweza kulipwa maslahi yao.

Mheshimiwa Spika, tuzungumzie pia suala zima la wasanii. Wasanii wa kizazi kipya wamekuwa na mchango mkubwa sana katika nchi hii. Nakumbuka wakati nafanya kazi ya Uandishi wa Habari miaka ya 1990 nyimbo zilizokuwa zimetawala ni kutoka Congo, kutoka Mataifa ya nje, lakini muziki wa kizazi kipya umebadilisha hiyo mentality na hivi sasa katika vyombo vyetu vya habari, redio, TV na hata maeneo mbalimbali ni muziki wa kizazi kipya.

Mheshimiwa Spika, ukienda Kenya, utaona jinsi ndani ya Afrika Mashariki, Tanzania tunavyoongoza kwa muziki huu wa kizazi kipya. Tuone sasa ni kwa jinsi gani tunawapatia haki zao, ambapo nakumbuka tulipitisha sheria kuona ile percentage wawe wanalipwa. Je, napenda kufahamu kwamba ile sheria tuliyopitisha, tayari imeshaanza kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, je, tunajiandaa vipi katika kujenga kumbi za kisasa kama walivyo wenzetu, nchi zilizoendelea? Ukienda India kuna Bolywood, ukienda Marekani pia hivyo hivyo. Sasa je, tunafanyaje kwa nchi yetu hapa Tanzania? Tunaona sasa hivi filamu zimeporomoka hapa nchini kwa kweli, siyo kama ilivyokuwa. Naomba Waziri atuambie kwamba ni kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, niende pia kwa Msemaji Mkuu wa Serikali. Mimi binafsi nampongeza kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuhakikisha kwamba yale yanayofanywa na Serikali yetu jamii na Watanzania wanatambua; lakini tuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba Ofisi hii ya Msemaji Mkuu wa Serikali inakuwa siyo idara, iwe ni ofisi maalum ambayo itakuwa na uhuru mpana zaidi.

Mheshimiwa Spika, pia, kama ilivyokuwa Dar es Salaam tunaona Serikali imehamia hapa, lakini je, hapa Dodoma Hakuna Idara ya Habari Maelezo? Wakitaka kuzungumza, wengi tutawasikia wamekwenda Dodoma Hotel na maeneo mengine. Tunahitaji kuwa na ukumbi wa kisasa ambapo watu mbalimbali watakwenda hapo kwa ajili ya kwenda kuzungumza na Waandishi wa Habari na sivyo kama ilivyo sasa hivi ambapo hatujui na hatujaona Ofisi Maalum ambayo ni ya Mtendaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Msemaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up atueleze ni kwa namna gani basi Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba tunapata Ofisi Maalum ya Msemaji wa Serikali ambaye anafanya kazi nzuri sana katika kuweka mambo mazuri yanayofanywa na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kutokana na utendaji huo ndiyo maana waafrika wengi wanatambua jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais wetu. Nasi pia tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya na tunazidi kumtia moyo kuona kwamba tunakwenda katika nchi ya viwanda ambayo uchumi wake unakua. Pamoja na changamoto hizo tulizonazo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Tanzania Rais Magufuli na Serikali yake nawaombea Mungu na iendelee kusonga mbele. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, kila tunaposimama hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, natangua tu kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kifo cha mpendwa wetu Dkt. Reginald Mengi. Natambua mchango wake hasa kwa sisi watu wenye ulemavu, alitupenda, alituthamini na alitusaidia. Kwa kweli tutamkumbuka kwa mengi. Kipekee kabisa Dkt. Reginald Mengi ataendelea kuishi ndani ya mioyo yetu. Ninamfananisha Dkt. Reginald Mengi na Mama Theresa wa Calcutta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, inshallah Mwenyezi Mungu hapo kesho tutakwenda nasi kujumuika nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema kwamba kwa wanafunzi wenzetu wanaosoma Vyuo Vikuu, niombe kwa Wizara kwa sababu kuna utaratibu wa Bima ya Afya ambayo wanakatiwa au wanakata wanafunzi wale na huu ni utaratibu mzuri ambao umeandaliwa na Serikali. Kipekee kabisa nampongeza mwanamke jasiri, shupavu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pamoja na Naibu wako, Katibu Mkuu, pamoja na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hakika matunda tunayaona na Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa Afya ili mwendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri kufuatilia Bima za Afya kwa sababu vyuo vingi hapa nchini, pamoja na kwamba wanafunzi wanatoa pesa, lakini hawapati hizo Bima za Afya kwa wakati. Pia wengine wanatoa zaidi ya kile kiwango kinachohitajika, wanatoa shilingi 100,000/=. Hawa wanafunzi wakati mwingine wasipotoa hawaruhusiwi hata kufanya mitihani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba sana dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu alifuatilie hili na hata ikibidi, basi uwe utaratibu wanafunzi wanapoanza mwaka wa kwanza kuwepo na watu wa Bima ya Afya ili waweze kuwakatia vitambulisho kutokana na mikopo wanayopata ili kuondoa usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili lipo kwa shule za sekondari na hata hizi English Medium, tuwasaidie wazazi. Kama kweli zinatolewa hizo pesa, basi ziweze kukatiwa bima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia nizungumzie kuhusiana na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, vingi vimechoka, vimechakaa na vinahitaji ukarabati. Namuomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuhakikisha kwamba Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii vinafanyiwa ukarabati. Pia ikiwa ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweza kuwasaidia vitendea kazi ili waweze kufanya kazi ambayo wamepatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakemea pia baadhi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu na hili hata Mheshimiwa Rais pia amelizungumza, baadhi ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu wanaowanyanyasa watoto wa kike kingono na wamediriki wakati mwingine hata kuwafelisha kwa sababu tu wamekataliwa kingono, tumefika mahali pabaya sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri yeye ni Waziri pamoja na afya lakini jinsia, alisimamie hili kuwanusuru watoto wetu wanaokwenda shule ili waweze kusoma kwa amani na utulivu kama nchi yetu ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitalizungumzia kwa mapana zaidi suala la mapambano dhidi ya UKIMWI. Hali ya mapambano dhidi ya UKIMWI ni mbaya. Takwimu zinazoooneshwa na zimesomwa hapa, hivi sasa kila mwaka watu 72,000 wanaambukizwa virusi vya UKIMWI na ni kati ya miaka 15 mpaka 64. Miaka kuanzia 15 mpaka 24 hao ni vijana ambao maambukizi yako kwa asilimia 49 na kati ya hao ni watoto wa kike ndio wameathirika, tunalipeleka wapi Taifa letu? Nchi yetu tunasema nchi ya viwanda na viwanda tunategemea pia hata hawa ambao wako vyuoni waje kwenda kule, je, vijana hawa ambao hivi sasa wapo katika janga la maambukizi ya virusi vya UKIMWI tunawasaidiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie ni mkakati upi unaandaliwa ili kuona kwamba tunanusuru maisha ya watoto wetu na hasa watoto wa kike, ndio ambao wanaangamia kwa kiasi kikubwa. Naomba sana tuone ni kwa jinsi gani tunawasaidia, leo hii tunasema kwamba mpaka tunapomaliza siku watu 197 wanaambukizwa virusi vya UKIMWI. Hili sio jambo la mzaha ni jambo kwa kweli pamoja na jitihada nzuri za Serikali na hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Dawa za Kulevya na bahati nzuri na Kifua Kikuu hali ni mbaya huko tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu ambao tunafanya kampeni kwenye shule zetu, lakini maeneo mengi wale wahusika wamejisahau, tunaomba wawakumbushe ili tuone ni kwa jinsi gani basi kama ni kampeni au ni jinsi gani ya kuweza kukinusuru kizazi hiki ili kiepukane na hili janga la UKIMWI. Mimi naumia sana kama mwanamke, watoto ambao tunawategemea kwamba ndio viongozi tukiondoka hapa, wanakwenda chuo wanakwenda shule, wakirudi badala yak u-graduate na A wanarudi na virusi vya UKIMWI. Hili linaumiza sana, namwomba Mheshimiwa Waziri pia na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na hizo jitihada na nipongeze sana pia Serikali yetu kwa jinsi ambavyo inalichukilia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kondomu hazipatikani, Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba atuambie ni kwa nini kumekuwa na uhaba mkubwa wa kondomu na pengine hili ndilo linalosaidia au linalochangia kuendelea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, tujue ni idadi ngapi pia wanapokea kwa mwaka hizo kondomu, kwa sababu najua siku za nyuma walikuwa wanapokea zaidi 18,000, lakini ni taarifa zilizopo ambazo Mheshimiwa Waziri atakuja kutuambia walipata kondomu 9000. Je, tatizo liko wapi, atueleze Mheshimiwa Waziri ili tuweze kunusu kizazi hiki ambacho kinaangamia na ugonjwa huu wa UKIMWI?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia malengo haya ya 90, 90 kwa kweli Serikali inafanya kazi kubwa, lakini watendaji kule chini bado ni tatizo. Tulipokwenda kwenye kampeni baadhi hawajui unapomwambia 90, 90 anakwambia ni kitu gani na wakati mwingine ni mtu mwenye dhamana ya kuweza kusaidia katika hili. Kwa hiyo, naomba sana kwa kweli, mimi nalia sana na UKIMWI na hasa watoto wa kike tuone ni kwa jinsi gani tutawasaidia watoto wetu ili kuwaepusha na huu ugonjwa wa UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nimalizie tu kwa kusema kwamba, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake bado pia hili ni tatizo katika maeneo mengi. Mwisho kabisa niseme kwamba, kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii tunaiona na Mheshimiwa Ummy anaacha alama katika Wizara hii pamoja na Naibu wake. Kikubwa tunachokifurahia na tunaona kabisa kwamba kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais kwamba yupo hapo lakini Dkt. Ndugulile, ni Daktari, kwa hiyo hakuna mtu atakayeweza kuwadanganya katika Wizara. Tunawaomba sana waendelee kusaidia na kuhakikisha kwamba vituo vya afya ambavyo Serikali hii ya Awamu ya Tano imeviboresha, basi tuone vifaa vinapelekwa ili tuweze kupunguza tatizo la vifo vya wanawake na watoto kwa sababu hawa wanawake ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwa mara nyingine tena, tuendelee kumwombea Dkt. Reginald Mengi. Pia tujiulize kwa sababu tunao matajiri wengi, sisi wenyewe binafsi je, tunasaidiaje watu wenye uhitaji? Katika maeneo mengi tunao tunawaona na wana shida ambayo kweli wanahitaji kusaidiwa na hata matajiri waliojaliwa tunawasaidiaje, tunaacha alama gani, Dkt. Reginald Mengi, kilio cha Watanzania na huko anakokwenda basi Mungu anaona. Kwa hiyo na sisi iwe ni somo kwetu ni jinsi gani tunakwenda kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, nampongeza sana Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote Wizarani, waendelee kuchapa kazi, tuko pamoja na wao, a luta continua, mapambano bado yanaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia mpango wa mwaka 2020/2021. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa Miaka Mitano, nianze tu kwa kupongeza katika suala zima la elimu kwa sababu tangu Rais wetu alipoingia madarakani alifanya elimu bure na wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne mwaka huu ndiyo wanafunzi ambao kwa kweli katika hiyo miaka minne wamenufaika na elimu bure. Kwa hiyo, napongeza sana jitihada hizi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ni mzuri na tunaona ndani ya miaka minne pia iliyopita utekelezaji umekuwa ni mzuri kwa sababu ipo miradi ambayo kwa kweli wanasema mwenye macho haambiwi tazama. Tunapongeza kwa jitihada hizi ambazo ni Mapinduzi makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano iliyofanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Imani yangu kubwa ni kwamba miradi hiyo itakapokamilika Tanzania tutaelekea kabisa katika ule uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kupitia viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa 2020/2021 ningependa nizungumzie katika suala zima la Uwekezaji, tunafahamu Uwekezaji ni jambo zuri sana na kwa kweli nipongeze Wizara husika Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Ofisi ya Waziri ya Mkuu nawapongeza sana kwa sababu tunaona kwa kweli baadhi ya vikwazo ambavyo tayari kwa sasa vimeondolewa na tumerahisha huduma ambazo sasa zinapatikana katika eneo moja badala ya ule usumbufu uliokuwepo hapo awali. Tunapoelekea kwenye uchumi wa kati ni dhahiri kabisa vikwazo hivyo vingeweza kupunguza kasi ya Wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia wawekezaji katika upande wa Maliasili, tunawahitaji sana, lakini ningependa kuishauri Serikali kwamba katika Mpango huu na hata tunaelewa kabisa kwamba tangu tumeweka concession fees kwa kweli pato limeongezeka kwa kiasi kikubwa sana makusanyo yamekuwa ni makubwa, kwa mfano tu TANAPA kwa Hifadhi ya Serengeti kwa kipindi cha tangu Julai mosi mpaka mwezi wa 10 walikusanya zaidi ya bilioni 49 na yote hii imewezekana kutokana na concession fees ambayo tuliipitisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana na niwapongeze sana Wizara ya Maliasili na Utaliii kwa kazi hiyo nzuri, lakini ningependa kushauri kwamba katika uwekezaji huu sasa tuangalie ni kwa jinsi gani tunapunguza hoteli nyingi ambazo zipo ndani ya Hifadhi zetu. Kwa sababu tunaelewa kabisa utajiri huu tulionao hata wenzetu wa jirani wanatamani wangekuwa nao na tunapoweka hoteli nyingi katika maeneo hayo wanyama nao pia wanakimbia kwa sababu ya kuona mazingira ambayo ni tofauti na yale waliyoyazoea. Kwa hiyo ningeishauri Wizara ya Maliasili na Utalii, tunapokwenda huko labda sasa, tuone kwamba ndiyo tunahitaji, lakini waweke mazingira mazuri kwamba kupunguza hoteli ndani ya Hifadhi angalau zikajengwa pembezoni mwa Hifadhi ili basi wanyama wale waendelee kuwepo na hatimaye waendelee kuongeza pato la Serikali kama ilivyo pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia sana Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa sababu katika suala zima la mikopo tumeona kwamba mikopo ya elimu kwa vyuo vikuu imeongezwa na ukiniuliza kipaumbele changu ni kipi hasa katika Bunge hili, basi sifichi nitasema kwamba ni watu wenye ulemavu, watu wenye ulemavu. Kwa sababu gani nasema hivyo? Watu wenye ulemavu kwa kweli katika Awamu hii ya Tano Serikali imekuwa na jicho la ziada katika kuhakikisha kwamba wanatimiziwa mahitaji yao. Pia katika suala zima la Uongozi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kweli ni Rais wa mfano na tunampongeza sana kwa hilo na nawapongeza pia hata Mawaziri ambao kwa kweli wamekuwa na ushirikiano mkubwa sana katika suala zima la watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sasa basi tuweze kupata viongozi wengi ambao wanatokana na kundi hili la watu wenye ulemavu, napendekeza katika Mpango huu kuona ni kwa jinsi gani kwamba tunaongeza bajeti hii ya mikopo ili wanafunzi wenye ulemavu waweze kupata ruzuku badala ya mikopo, kwa sababu Waswahili wanasema ukimwona nyani mzee, ujue amekwepa mishale mingi. Mtu mwenye ulemavu mpaka anafika Chuo Kikuu kuna changamoto nyingi sana amezipitia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu katika nchi zilizoendelea wanatoa ruzuku badala ya mikopo kwa sababu hata anapomaliza Chuo Kikuu kupata ajira inakuwa ni ngumu sana, kwa hiyo kurudisha ile mikopo bado inakuwa ni ngumu na ni mzigo mkubwa kwake.

Kwa hiyo ningeomba kwamba hawa watu wenye ulemavu tuangalie Serikali ni kwa jinsi gani tunawapa ruzuku badala ya kutoa mikopo kwa kweli ambayo hapo baadaye kwao inakuwa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiamini Serikali yangu kwa umakini ilionao na ombi langu hili basi katika Mpango huu tunapoelekea tuone kwamba bajeti hiyo inazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu na hata wale watoto ambao wamezaliwa na familia za watu wenye ulemavu kipato chao kinakuwa ni duni. Naiomba Serikali tuone kwamba ni kwa jinsi gani tunawa-accommodate hawa watu wenye ulemavu na familia zao ili basi angalau ruzuku hiyo itasaidia, lakini kuona ni kwa jinsi gani sasa tunaboresha shule, naipongeza kwa kweli Serikali kwa sababu tayari imekwishaanza na matunda tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado mimi kama Mwakilishi wao ninawasilisha ombi la kuona kwamba ni kwa jinsi gani tunaboresha shule zetu ambazo zita wa- accommodate na watoto wenye ulemavu. Kwanza kwa kuangalia katika ajira ambazo tayari wamekwishaanza kufanya, lakini tuongeze pia Walimu ambao wana ujuzi na utaalam wa kufundisha watu wenye mahitaji maalum ambao ni wanafunzi wenye ulemavu. Shule nyingi za vijijini bado miundombinu yake siyo rafiki kabisa, kabisa, kwa hiyo naiomba Wizara iangalie ni kwa jinsi gani miundombinu hii inawawezesha watoto wenye ulemavu hasa vyoo, imekuwa ni shida, wakati mwingine unakwenda vijijini ukienda kwenye hizo shule kwa kweli inahitaji moyo ambao kwa kweli ni mgumu kwa sababu watoto wale wanalazimika kwenda kwenye vyoo ambavyo wanatambaa, wakati mwingine akitoka kwa kweli anatia huruma na ni rahisi sana kupata magonjwa, kwa hiyo tuone ni kwa jinsi gani tutaboresha hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ajira kwenye Ofisi ya Waziri ya Mkuu, nimeona kwa kweli jitihada kubwa na natambua na nampongeza sana Mheshimiwa Jenista yeye ni mwanamke shujaa, jasiri kwa jicho lake la ziada ambalo amekuwa karibu sana na watu wenye ulemavu. Sasa naomba basi katika Mpango huu tuone ni kwa jinsi gani zile Taasisi au Wizara ambazo bado hazijatimiza asilimia tatu, asilimia tatu kwa ajili ya watu wenye ulemavu tuzingatie.

Ningeomba hata Bunge letu pia kwa kweli limekuwa la mfano na Mheshimiwa Spika popote alipo nampongeza sana kwa kazi kubwa kwa sababu miundombinu amekuwa ni mfano na wengi waje kuiga hapa, lakini sasa naomba pia katika suala la asilimia tatu, matarajio yangu ni kuona napishana na watu wenye ulemavu katika Taasisi yake ambayo kwa kweli watakuwa ni mfano bora na watatoa elimu ambayo itasaidia wengine pia ambao bado kwa namna moja au nyingine wako nyuma sana katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la uwekezaji, wawekezaji wanaokuja tumeona kwamba wanaajiri watu wengi na ajira zipo nyingi, lakini na wao pia asilimia tatu nayo izingatiwe pia ili watu wenye ulemavu wale ambao wamepata elimu, wamesoma waweze hizo ajira na hatimaye kuweza kujikomboa wao wenyewe na kusaidia familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza kwa sababu mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na nimeshuhudia mengi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi wanayofanya hasa kwa kuzingatia kwamba kitalu nyumba kinawasaidia sana, vijana wengi wamewezeshwa. Nawaomba sasa katika Mpango huu tuone ni kwa jinsi gani tunafika maeneo mengi zaidi katika nchi hii ili vijana tuweze kuwawezesha katika kilimo hasa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Vijana, vijana wengi waweze kupata mikopo ambayo itawawezesha kujiajiri badala ya kutegemea ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayaona mengi kupitia Kamati hii, vijana ambao wamewezeshwa na sasa hivi wengine mitaji yao imefika zaidi ya bilioni. Kwa hiyo kwa kweli tukiwawezesha vijana wengi na maeneo mengi tukawafikia na pia tukawatumia hata baadhi ya Wabunge huku katika Majimbo yao, naamini kabisa vijana wengi sasa hawatokuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mollel kwa mchango wako na ushauri wako.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nilishawahi kusema hapa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sisi wote Watanzania na hili kweli tumelishuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu tumepata uhuru hatujawahi kuwa na Naibu Waziri katika Baraza la Mawaziri mwenye ulemavu, lakini ndani ya Serikali hii ya Awamu ya Tano tunaye Mheshimiwa Ikupa ambaye anatuwakilisha vyema. Na hili ni jicho pevu la Rais wetu, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, lakini sio hilo tu; tunao makatibu wakuu, sio hayo tu, tunaye mpaka Balozi ambaye ni mtu mwenye ulemavu. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, ameandika historia katika nchi hii na tuna kila sababu ya kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunachangia kuhusiana na ndege, wakati ndege zinanunuliwa wapo waliopinga, lakini leo hii tunapambana nao kule tukiweka mizigo yetu ambao walikuwa wanapinga. Kwa hiyo, haya yote ni ya kujivunia kutokana na jemedari huyu tuliyenaye, Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, 2020 kura yangu chukua, sasa nifiche ya nini Magu uongozi anaujua. Mungu ambariki sana Rais wetu!

WABUNGE FULANI: Asaweeee!

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninamshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kusimama hapa mwaka huu wa 2020. Ninapongeza na kuunga mkono kamati zote tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Jambo kubwa ambalo nawapongeza sana kwa jinsi ambavyo wameweza kuizungumzia asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ambayo ni kazi kubwa pia inafanywa na Serikali yetu. Kipekee kabisa kwa kweli nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Serikali yake kwa jinsi ambavyo leo hii miaka minne tunasimama tukizungumza huku tukijidai kwa yale mambo mazuri aliyofanya katika nchi hii kwa kipindi kifupi, haijawahi kutokea na hii ni historia imeandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona matunda mazuri, tumeona ni kwa jinsi gani ambavyo Rais huyu amejitoa kwa Watanzania. Pamoja na lawama zote lakini hata siku moja hajawahi kurudi nyuma amesimama katika kile anachokiamini. Kutokana na mazuri anayoyafanya Mheshimiwa Rais ndio maana hata kelele zinakuwepo nyingi na ukiona kwamba unaporusha jiwe ukasikia kuna kelele ujue kwamba, tayari kuna mtu limempata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Rais wetu tunaona kwamba ni kwa jinsi gani hata hiyo demokrasia ambayo wenzetu wamekuwa wakiizungumzia, na kwa miaka zaidi ya miango sasa miwili sijawahi kuona hiyo demkorasia ambayo wao wanaizungumzia kwa upande wa pili, lakini kwao wenyewe utekelezaji umekuwa ni ngumu. Unapozungumzia jambo wanasema kwanza kabla hujanyoosha kidole kwa mwenzako angalia hivyo vidole vingine inarudi wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunasimama hapa tangu miaka hiyo na leo hii tuko katika Bunge, tangu tumeanza kumsikia Mheshimiwa Mbowe ni Mwenyekiti na mpaka sasahivi ni Mwenyekiti. Je, hii ni demokrasia gani? Kama si kwamba, ni kuisema upande wa pili wa Chama Cha Mapinduzi ambao ndio wana Serikali? Serikali ambayo inafanya mambo makubwa katika kuwatetea wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakipinga ndege, lakini leo hii wao ndio wa kwanza kupanda hizo ndege, pamoja na kwamba, wanazipinga hizo ndege na wamekuwa wakizikimbia kamera zisiwarekodi kwa ajili ya hizo ndege. Sisi kama Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi tuna kila sababu ya kujivunia kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati ninaomba nimpongeze Waziri wa Mambo ya Nje kwa kazi nzuri aliyoifanya, pamoja na lawama nyingi, lakini umeonesha kwamba, wewe ni mwamba usiotetereka. Sisi kama Wabunge tuna kila sababu ya kumpongeza na leo hii tunajivunia yale ambayo yalikuwa yanapingwa, leo hii tunayo Twiga ambapo Barrick wamebwaga manyanga na hatimaye kuona ni kwa namna gani washirikiane na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ili Watanzania waweze kufaidika na asilimia 16. Yote hii ni kwa sababu ya Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye hababaishwi na hajawahi kuyumba hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tuna kila sababu ya kujivunia. Walisema kwamba, hapa sisi tungeweza kuwekewa vikwazo kwa kuvunja mikataba, hakuna mikataba iliyovunjwa, sheria zimeletwa hapa na tumezipitia. Mwaka wa nne leo tuna kila sababu huu mwaka wa tano kujivunia yote yaliyofanywa na Serikali ambayo inaongozwa na Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapiga kelele sana, lakini ukweli ni kwamba baadhi yao wamekimbia hata majimbo yao. Sasa unategema nini? Siku zote utavuna ulichopanda, mwaka 2020 tunakwenda kuonesha kwamba Watanzania wanaelewa sasa pumba ni zipi na mchele ni upi. Kwaajili ya kazi nzuri iliyofanywa na Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Wabunge wa CCM wana asilimia kubwa ya kurudi katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unajiuliza hivi mtu mzima inakuwaje leo anazungumza anasema tutashiriki kikamilifu kwenye huu uchaguzi, lakini dakika za misho maji ya shingo anasema hatushiriki kwenye uchaguzi? Hebu tunaomba safari hii kama kweli ninyi ni wanasiasa mahiri msuse uchaguzi wa 2020.

Mheshimiwa MwenyekitiKazi kubwa itafanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na wengi wanakwenda kufa kifo cha taratibu. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana. Ninawapongeza sana Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya na wao ndio wanaotufanya tutembee vifua mbele. Vituo vingi vimejengwa, barabara tunaona zimetengenezwa; waulize upande wa pili, hawajui hata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwa kusema kwamba, Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa wanayoifanya, iwe wa Viti Maalum, wa Majimbo, tumeshuhudia ni kwa jinsi gani wanajituma. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuniwezesha kusimama hapa. Awali ya yote ninaunga mkono Kamati zote mbili Kamati ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu nitaanza moja kwa moja na Kamati Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kuzungumzia kutoa ushauri kwa Shirika la Utangazaji Tanzania TBC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni-decrare interest kwamba mimi ni Mwanahabari na kabla ya hapo pia nilikuwa TBC. Kwa hiyo ninapozungumzia TBC naizungumzia TBC kwa upendo kwa kutambua changamoto zilizopo katika Shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitakuwa mchoyo wa fadhili endapo sitaipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa wanayoifanya; Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza lote la Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mwakyembe ninakupongeza sana hasa baada ya kuona jitihada kubwa unazozifanya katika kukagua mitambo ya TBC na kuweza kuiboresha pale ambapo ina changamoto. Kwa kiasi kikubwa sana Mheshimiwa Waziri hii itasaidia katika kutatua changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yoyote ile inajivunia Chombo chake cha Habari na TBC ndilo Shirika la Umma. Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia uhuru wa kupata habari, lakini vilevile inaendelea mpaka kuzungumzia katika uhuru wa kutoa mawazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo hakuna uhuru usiokuwa na mipaka; hivyo nipongeze sana Serikali pale ambapo inasimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba Vyombo vya habari vinafuata maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC ni Shirika kongwe, na tunafahamu Shirika hili la Utangazaji Tanzania (TBC) liliendelea kutumia majengo ambayo yalikuwa ni majengo ya filamu kwa miaka hiyo; na kwa muda mrefu kwa kweli limekuwa likihitaji marekebisho na mabadiliko makubwa hasa katika mitambo pamoja na mazingira yenyewe kwa ujumla, lakini hasa mitambo. TBC bado inahitaji uboreshwaji mkubwa wa mitambo ili basi kiweze kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi pasipo kuwa na hizo changamoto, na hata kama zitakuwepo basi changamoto ziwe ni chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi najivunia Shirika hili la Utangazaji Tanzania na pamoja Mkurugenzi wa TBC, Bwana Ayoub Ryoba kwa jitihada kubwa wanazozifanya. Wafanyakazi hawa wa TBC ni Wafanyakazi ambao kwa kweli wanahitaji pongezi hasa kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli ulio wazi maeneo yote katika ziara zote za Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Jemedari Dkt. John Joseph Pombe Magufuli TBC tumekuwa tukiwaona wakituhabarisha kile kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kweli nimpongeze aliyekuwa Msemaji wa Serikali Dkt. Hassan Abass kwa kazi kubwa aliyokuwa anaifanya katika kuwahabarisha wananchi nini ambacho Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali, inayoongozwa na Dkt. John Joseph Pombe Magufuli inachokifanya na tumeshuhudia kwa kweli hata wananchi sasa hivi wanamwelewa vizuri sana Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kutokana na kazi kubwa ya Dkt. Abass.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii basi wanasema pengine ndiyo ambayo imempendezesha Rais na kumpa nafasi hiyo. Mimi ninampongeza akaendeleze jitihada hizo hizo katika kuhakikisha kwamba anasimamia misingi ya taaluma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali, na nimpongeze Spika wetu kwa sababu hivi sasa katika Bunge letu kipindi cha maswali na majibu watu wanafatilia, hata wenzangu viziwi wanafatilia kwa sababu wapo Wakalimali wanaotafsiri lugha ya alama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hao tu, tumeanza vizuri katika taarifa zetu za habari televisheni mbalimbali nazo pia wanafanya kazi hiyo kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma. Mheshimiwa Waziri na Naibu wako nakupongeza sana kwa hili jambo unalolifanya katika kuhakikisha kwamba tunazingatia na mikataba yote ambayo nchi yetu imeiridhia.

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC hivi sasa wana channel ambayo inatangaza utalii ninaiomba Serikali kuhakikisha kwamba inawawezesha TBC kwa kiasi kikubwa na hata ikibidi kuongeza bajeti ili basi wao ndio wawe wa kwanza katika kutangaza utalii wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia ni mjumbe wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI, TB bado ni tatizo kubwa hapa nchini; kwa mwaka watu zaidi ya 75,000 wanakufa kutokana na ugonjwa huu wa kifuu kikuu. Niiombe Serikali kuhakikisha kwamba jitihada zinaongezwa ili kuweza kunusuru wananchi wa Tanzania wengi wasiangamie na ugonjwa huu wa TB.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia elimu iendelee kutolewa na tulishirikishe Shirika letu la Utangazaji Tanzania (TBC) kutoa elimu juu ya madhara gani au nini basi hasa chanzo cha ugonjwa huu ili wananchi waweze kufahamu na vilevile kuchukua tahadhari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulipitisha sheria kuhusiana na upimaji kwa watoto chini ya miaka kumi na nane mpaka kumi tano; ninaiomba Wizara iharakishe kanuni na pia kutoa elimu ili wazazi watambue umuhimu wa kuwapima watoto wao hasa chini ya miaka kumi na nane mpaka kumi na tano ili basi malengo ya 90 90 90 yaweze kukamilika na kufanyiwa kazi kwa jitihada kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekuwa tukitegemea sana vyanzo au wafadhili kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI; sasa ni wakati wa Serikali; naishauri Serikali kuhakikisha kwamba tunapata vyanzo vya uhakika vya kuweza kutunisha mfuko wa UKIMWI ili basi tuweze kujitegemea angalau kupunguza misaada mikubwa ambayo kwa wakati mwingine kwa kweli tunapata misaada hiyo kutokana na masharti magumu. Kwa hali ilivyo kwa sasa hivi kwa kweli tuharakishe mfuko huu na kwa kupata vyanzo katika bajeti ya mwaka huu ili basi tuweze kupunguza misaada kutoka kwa wafadhili wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda umekwisha ninakushukuru sana kwa kweli, naipongeza Serikali tena Mheshimiwa Harisson Mwakyembe na Naibu wako hongereni sana. Vilevile Mheshimiwa Ummy Mwalimu Mungu akubariki sana, A luta continua mapambano yanaendelea, ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kuhusiana na Azimio hili la Mkataba wa Marrakesh.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 14 Novemba, 2017, niliuliza swali ambalo lilihusu Mkataba huu wa Marrakesh. Katika majibu yao, Serikali waliahidi kulifanyia kazi na kulileta hapa ili mkataba huu uweze kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kutoona. Kipekee kabisa naishukuru Serikali imeonesha wa vitendo kwamba kile walichokiahidi wamekifanyia kazi. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jitihada hizi ambazo kwa kweli zinaleta faraja kubwa sana kwa watu wenye ulemavu pamoja na Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Marrakesh? Marrakesh ni kwa sababu mkutano huu ulifanyika nchini Morocco katika Mji wa Marrakesh na nchi 20 zikaridhia Azimio hili ambapo katika mkataba huo waliridhia kuhusiana na kuweza kuruhusu vitabu mbalimbali viweze kutafsiriwa kwa kuchapishwa katika maandishi ambayo yatawasaidia wenzetu wenye uono hafifu na wale wasioona. Kwa kweli kama ambavyo wengine wamesema, Serikali imefanyia kazi jambo hili haraka sana na tunawashukuru kwa hilo kwa sababu wanafunzi wengi waliokuwa wakisoma katika vyuo vikuu walikuwa wakilazimika kutafsiriwa na wakati mwingine kutafsiriwa huwezi jua nini ambacho wakati mwingine kimekosekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mkataba huu watu wasioona utaweza kuwasaidia kwa mapana zaidi ili basi maandishi mbalimbali iwe kwenye michoro, vitabu au kwa lugha nyingine zozote zile uweze kutafsiriwa na kuwasaidia kupata elimu. Elimu ndiyo kila kitu na hasa kwa watu wenye ulemavu elimu ndiyo mtaji wake. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kuleta Mkataba huu wa Marrakesh ili basi watu hawa waweze kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu tunafahamu kabisa kwamba hapa nchini kwetu haki ya kupata taarifa hasa kwa watu wenye ulemavu wa kutoona ilikuwa ni shida hapo awali. Kwa hivi sasa, kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano tunaona kabisa Mheshimiwa Rais amekuwa na jitihada kubwa. Kwa hiyo, Baraza la Mawaziri pia na kwa kuwa tayari katika Baraza hilo la Mawaziri tunaye pia mtu ambaye anatuwakilisha, tunaona sasa haya yote yakifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli Awamu hii ya Tano imekuwa na jicho la ziada katika kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma wakiwemo watu wenye ulamavu. Ni pongezi za pekee kwa kweli nazitoa kwa Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza la Mawaziri na Serikali yote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kutafsiri huku wakati mwingine wako wengine ambao watataka kujinufaisha. Naomba Serikali iwe makini kuhakikisha kwamba kile ambacho kimekubaliwa basi watu wenye ulemavu wa kutoona waweze kusaidiwa kwa haki na vile vingine ambavyo havitokuwa na manufaa basi sheria iweze kufuata mkondo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sheria ya Hakimiliki ambayo iko chini ya COSOTA tuone sasa kwamba sasa ni kwa jinsi gani iendane na mkataba huu wa Marrakesh; na yenyewe pia tuna haja na kila sababu ya kuweza kubadilisha vile ambavyo vinahitaji viingie huko na kusiwepo na kipingamizi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwakweli kutokana na hili lililofanyika, langu kubwa ni pongezi lakini pia kuona kwamba sasa wakati huu tunapokwenda tuone na mikataba mingine ambayo kwa namna moja au nyingine bado imeachwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Bajeti hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia vitu vitatu, lakini awali ya yote niipongeze Wizara, nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kanyasu, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nimpongeze pia Katibu Mkuu wa Wizara hii pia kwa kazi nzuri na ushauri mzuri, pamoja na watendaji wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa niwapongeze Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Ndugu Manongi pamoja na wa TANAPA Ndugu Allan Kijazi, kwa kweli wamekuwa na mchango mkubwa sana kwa Tanzania na hasa kwa mimi ninayetoka Mkoa wa Arusha nawapongeza sana kulingana na kazi nzuri wanazofanya za kijamii, na hasa katika kuwasaidia wanawake. Hongera sana Ndugu Manongi pamoja na Ndugu Allan Kijazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia katika upande wa promotion na advertisements na hapo ndipo tunapojiuliza nini maana ya utalii. Maana ya utalii pasipokuwa na promotion pamoja na advertisements ni sawa na kazi bure. Tunafahamu umuhimu wa haya mambo mawili katika kuhakikisha kwamba tunautangaza utalii wetu, tunaitangaza Tanzania kimataifa na hapo basi ndipo ambapo tunapoweza kupata watalii wengi kuja nchini Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri, Nchi ya Tanzania Mwenyezi Mungu ametujalia na tuna kila sababu ya kujivunia kutokana na maliasili zilizopo pamoja na vivutio vingi vilivyopo katika nchi hii. Wakati mwingine ndipo tunapojiuliza kwamba tunasemwa ni nchi maskini, au sisi maskini; umaskini wetu unatoka wapi wakati tuna utalii, tuna maliasili na tuna mambo mengi ambayo yanaweza kutuletea fedha za kigeni na hatimaye kumkomboa Mtanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, jana tuliona wageni waliofika hapa ambao kwa namna moja wamechangiwa na Wizara hii kuweza basi kuja hapa na kwa namna moja au nyingine, hasa yule Miss Ukraine. Hata hivyo, nitakwenda kwa upande wa hapa nyumbani kwetu kuona ni kwa jinsi gani tunawatumia Watanzania ambao wameonesha mafanikio makubwa katika kuwa-brand na wao sasa wakatumika kama mabalozi wetu kuweza kuutangaza utalii wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilisimama kwa Mbwana Samatta na nitaendelea kumzungumzia Mbwana Samatta kutokana na kazi nzuri aliyoifanya ya kuitangaza ramani ya Tanzania kupitia soka la kulipwa kule Nchini Ubelgiji. Wizara inapaswa sasa basi kumtangaza kama huyu ni balozi ili aweze kuendelea kuutangaza utalii wetu kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbwana Samatta kwa bahati nzuri sana amefanya mazungumzo na daktari wa hiyo timu na amehamasika kuja kutembelea Tanzania. Kama ameweza kufanya hivyo, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, kaka yangu, Mheshimiwa Kanyasu, kwa nini tusimtangaze huyu na kumtumia kuwa kama ni brand Balozi, kuweza kuitangaza nchi yetu na kuutangaza utalii wetu kwa kupitia soka analocheza? Kwa kufanya hivi, Mbwana Samatta ataweza kwa kiasi kikubwa pia kuweza kuwaleta watalii wengi kuja kutembelea nchi yetu na hatimaye kupata pesa kutokana na wale watakaokuja hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzijuzi tumemuona mwanadada Azara Charles ambaye tumekuwa tukimuona ni mtu wa kawaida akikaa chini na kupiga zile danadana. Lakini Azara ameweza kumhamasisha kiasi kwamba mpaka Rais wa Taifa kubwa la Marekani, Donald Trump, kuweza kumzungumzia mwanadada huyu ambaye sisi Watanzania tumemwona kwa muda mrefu tukimchangia vipesa vidogovidogo na tayari sasa Azara ameingia mkataba na Kampuni ya Nike.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa je, sisi kama Watanzania tunamtumiaje Azara ili kuweza kuutangaza utalii wetu huko atakakokwenda? Hii itasaidia kwa Watanzania. Lakini pia wasanii wetu na wanamuziki mbalimbali na wao pia mbali ya kufaidika, lakini Taifa tutaweza kufaidika mara mbili zaidi kutokana na kazi zao au vipaji vyao wanavyovifanya. Na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Amina.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mawili matatu katika Sheria hii ya Manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuleta Muswada huu. Nampongeza pia Waziri mwenye dhamana, Waziri Mpango kwa mipango mizuri ambayo ninaamini kabisa inatupeleka kwenye uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja lakini vilevile niipongeze tena Serikali kwa sababu imeona umuhimu wa kuleta sheria hii na hasa kwangu mimi nafurahia sana kwa kuona ni kwa jinsi gani makundi maalum yameainishwa katika sheria hii. Vilevile niombe tuangalie, je, katika makundi haya maalum ni utaratibu upi mzuri utakaoandaliwa ili kuhakikisha kwamba makundi haya na yenyewe yanapata nafasi hii na kuweza kushiriki katika mchakato huu mzima pasipo kuachwa nyuma na tunapoelekea katika uchumi wa kati tuhakikishe kwamba hakuna anayeachwa nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende sasa katika ukurasa wa 13 katika kipengele cha 27 ambapo kinasema kwamba marekebisho haya yana lengo la kuifanya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya kufungia. Naomba tu nishauri hapo kwa sababu kama ni kampuni, kwa mfano kampuni „A‟ ikifungiwa inaweza kuanzisha kampuni nyingine na wakaendeleza kufanya mchakato huu au kuendelea na kazi. Vilevile kama ni Wakurugenzi hawa wakifungiwa wanaweza pia kutumia wenza wao au ndugu zao kuhakikisha kwamba wanaendeleza suala hili. Hapa niiulize Serikali itadhibiti vipi jambo hili lisiweze kujitokeza. Naomba sana Serikali izingatie suala hili ili kuhakikisha kwamba kama kweli kampuni imefungiwa au kama kweli Wakurugenzi fulani wamefungiwa basi wasipate nafasi tena ya kutumia mlango wa nyuma kushiriki katika kuweza kupata hiyo tenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile sheria hii itapunguza zile 10% zilizokuwa zikitumiwa na ofisi za Serikali na mfano mzuri tu ni katika matangazo. Matangazo mengi ambayo yanatoka Serikalini au katika Wizara mbalimbali unakuta yamechajiwa gharama kubwa na hii ni kwa sababu ya wale watu ambao wanaweka zile 10% au kwa wale wafanyakazi/watumishi wa umma ambao siyo waaminifu wanatumia hii 10% kuhakikisha kwamba wanavyopeleka matangazo na cha kwao kinarudi ili waweze kujipatia. Kwa hiyo, mimi naona hii ni faraja kubwa sana na niiombe tu Serikali kuhakikisha kwamba sheria hii kweli inakuwa ni msumeno ambao unakula pande zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile sheria hii itasaidia pia kuhakikisha kwamba vitu vingi vinakuwa vya viwango. Wakati mwingine wakandarasi hawa wamekuwa wakikubali kuingia makubaliano lakini katika makubaliano hayo kunakuwa na zile 10% ambazo zinasababisha washindwe kutimiza wajibu wao mfano ni katika ujenzi wa barabara mbalimbali. Barabara mojawapo katika Jiji la Dar es Salaam ni ya Baracuda ambayo imetengenezwa hivi karibuni tu lakini tayari hivi sasa imekwishakuwa na mashimo mengi tu. Siyo hiyo tu lakini barabara ya Tabata ambayo inapita katika Shule ya St. Marys ilitengenezwa kwa muda mfupi na ikaharibika na hii ni kutokana na hizo hizo 10% ambazo zinaiingizia gharama kubwa Serikali. Pamoja na mabadiliko haya ya sheria niiombe Serikali iweke adhabu kali kwa wale wakandarasi ambao kwa namna moja au nyingine watapewa tenda hizo na matokeo yake wakafanya kile kitu katika kiwango ambacho hakikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niungane na maoni ya Kamati ya Bajeti na nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, tuzungumzie hili ambapo katika ofisi nyingi za Serikali ambapo unakuta kuna idara takriban nne/tano na idara hizo zote zina Wakurugenzi Wasaidizi na hawa wasaidizi wamekuwa wakitumia magari ya Serikali na mafuta ya Serikali lakini cha kusikitisha mwisho wa mwezi pia utakuta wana posho kwa ajili ya mafuta. Sasa hapa niulize tu kama mtu kapewa gari, dereva yupo bado mwisho wa mwezi ana posho ya mafuta, haya mafuta ni ya nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile baadhi ya watumishi ambao siyo waaminifu wamekuwa wakiyatumia vibaya na pengine hili pia litawapunguzia adha baadhi ya madereva mfano wale wa Jiji la Dar es Salaam. Dereva huyo analazimika kuamka saa kumi alfajiri kwa ajili ya kumfuata bosi na wakati mwingine bosi huyu inawezekana anakaa mbali Bunju, amfikishe ofisini. Gari hilo ni la Serikali, mafuta ya Serikali, mwisho wa mwezi kuna posho ya mafuta. Kwa hiyo, naipongeza kwa kweli Serikali yangu na nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mpango kwa mipango mizuri ambayo naamini kabisa ina lengo la kututoa hapa tulipo kutupeleka katika uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana naunga mkono hoja 100%.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na kutukutanisha tena hapa na vilevile ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Muswada huu wa Haki ya Kupata Taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kumueleza tu kwanza Mbunge wa Tandahimba kwamba wakati wa kuchangia alisema nchi ya Tanganyika, hakuna nchi ya Tanganyika, naomba kwenye Hansard hili waweze kulibadilisha hakuna nchi ya Tanganyika, pia nimfahamishe kwamba kama jinsi ambayo imeelezwa Muswada huu unahusu Tanzania Bara, hili siyo suala la Muungano, kwa maana hiyo Zanzibar inayo Wizara ya Habari inayojitegemea kule na masuala yao yatabaki kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nijikite kwa kuanza kueleza nikianzia na harakati za kupata Muswada huu. Itakumbukwa kwamba Muswada huu ulianza miaka kumi iliyopita (mwaka 2006) wakati huo lilipoanza vuguvugu la haki ya kupata taarifa. Kwa wakati huo ulipotolewa kwa mara ya kwanza katika tovuti ya Wizara ya Habari mwaka 2006, Muswada huu ulipingwa na wadau mbalimbali, hata wadau walipokutana na Wizara walizungumza na kutoa mapendekezo yao na wakakubaliana kwamba Muswada ule kwa wakati ule urudishwe ili uweze kufanyiwa maboresho. Serikali ilisikiliza baadhi ya maboresho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena Muswada huu uliletwa mwaka 2015 kwa hati ya dharura na ulikuwa pia na baadhi ya mapungufu, ulirudishwa Muswada huo na wadau walipewa nafasi ya kuweza kuupitia ili kuuboresha kwa kutoa mapendekezo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mapendekezo ambayo tayari yapo katika Muswada huu mojawapo ilikuwa ni kuweka utaratibu wa kumwezesha mtu kuomba na kupata taarifa, jambo ambalo Serikali kwa hivi sasa imelizingatia. Vilevile kulikuwepo na sharti kwa taasisi za umma na watu binafsi, kuwa na Maafisa Habari ambao watakuwa na wajibu wa kuwapa watu taarifa wanazozihitaji, jambo ambalo katika Muswada huu imezingatiwa.
TAARIFA....
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa yake, naomba ulinde muda wangu na ninaendelea.
Katika maeneo ya baadhi ya vifungu mbalimbali vya Muswada ambao uliwasilishwa mwaka jana, Muswada huu kwa mara ya kwanza baadhi ya maoni ya wadau wa habari yamezingatiwa na maoni yao ninayo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya maoni hayo, kwa mfano, Muswada uliopita mwaka jana kulikuwa kuna kipengele ambacho kiliupa upendeleo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambao ulivitaka vyombo vya habari vyote viweze kupewa taarifa katika chombo kile. Jambo hili lilipingwa na kwa hivi sasa limeondolewa na hii ni kwa mujibu wa maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18 ambacho kilielekeza kuwa taarifa iliyotolewa kwa mtu aliyeomba kutoka kwa mwenye taarifa haitatolewa kwa umma kimeondolewa vilevile, na kifungu hicho kilikuwa kimeua kabisa nia na madhumuni ya sheria lakini katika Muswada huu wa mwaka 2016 kifungu hiki kinaruhusu matumizi ya taarifa kutumika vilevile kutaka habari hizi zisipotoshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kingine ambacho kimeboreshwa na kipo katika Muswada huu wa Haki ya Kupata Taarifa ni kifungu ambacho umefanya mabadiliko mawili makubwa katika rufaa. Mfano, awali rufaa ya mwanzo kutokana na kunyimwa kupewa taarifa ilikuwa imepelekwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwa sasa rufaa ya kwanza ya kunyimwa taarifa itaenda kwa Mkuu wa taasisi husika ambapo taarifa iliombwa na ngazi ya pili ya rufaa vilevile itakwenda kwa Waziri, hata hivyo bado kuna maboresho ambayo kwa namna moja au nyingine yanahitaji kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 10 kinaelekeza jinsi gani waombaji taarifa wanaweza kufanya hivyo kwa kutumia maandishi au kupitia njia za kielektroniki za mawasiliano kama barua pepe, vilevile kina maelekezo ya kusaidia waombaji taarifa ambao hawajui kusoma au kuandika na wenye ulemavu kuomba taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele hiki kimeboreshwa kwa maana kwamba na ninaiomba pia hapa Wizara husika kuangalia ni kwa jinsi gani makundi maalum yataweza kupewa taarifa. Mfano, kama watu wenye ulemavu wa kutosikia (viziwi) wahakikishe kwamba watu hawa wanapewa vipi taarifa na zinawafikia kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende katika kipengele cha sita ambacho kinapigiwa sana kelele. Ni kweli, na ni ukweli ulio dhahiri kwamba kuna baadhi ya vipengele ambavyo vinahitaji kufanyiwa marekebisho, lakini Muswada kwa kiasi kikubwa umezingatia maoni na ushauri wa wadau wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kipengele cha sita na hapa nijikite zaidi katika kipengele ambacho kinazungumzia taarifa, mfano katika majeshi, taarifa za kiusalama, ni ukweli ulio wazi kwamba kwa mfano, ukiangalia kwamba katika mambo ya usalama, baadhi ya taarifa ambazo zimeshawahi kutolewa, mfano unapotoa taarifa kwamba kifaru cha Jeshi kimeibiwa, hizi taarifa, kwa sababu hata katika taaluma tunaambiwa kwamba kuna taarifa ambazo lazima uangalie national interest, kwa maana kwamba unapotoa taarifa hizi unawaambia nini maadui wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipengele hiki kiendelee kubaki kwa ajili ya maslahi ya Taifa, kipengele ambacho kinazungumzia majeshi, kipengele ambacho kwa mfano ilizungumziwa kwamba rada ni mbovu, hivi, je, hauoni kwamba taarifa zako unazitoa kwa maadui ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kuvamia na kuweza kutumia nafasi hiyo! Kwa hiyo, kipengele hiki kinastahili kubaki hivyo kwa sababu ya interest ya Taifa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni kweli kama ambavyo na wengine pia wamesema, kwamba kuna baadhi ya vipengele ambavyo vinahitaji kurekebishwa kwa mfano, haki hii ya kupata taarifa unaposema kwamba kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi sasa tunaelekea katika nchi ya viwanda, kwa maana hiyo wapo wengine ambao ni wawekezaji na wanapokuja hapa kuna taarifa nyingine ambazo ni muhimu wanahitaji kuzipata, unapoweka muda mrefu wa siku 30 kwa maana hiyo kama ni taarifa ambazo ni muhimu utakuwa umembana huyo mtu asiweze kupata hizo taarifa. Kwa hiyo, siku 30 ni nyingi sana na ziangaliwe ni kwa namna gani basi wanaweza kupunguza hizo siku ili taarifa zipatikane kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kipengele kingine ambacho kinahitaji maboresho ni kipengele kwa mfano, kipengele kinachozungumzia upendeleo ambacho nilikizungumzia kuangalia kwamba ni namna gani mfano mtu anapokwenda kutafuta taarifa na zile taarifa akazikosa na vilevile anapotaka kukata rufaa kwamba Waziri ndiyo mwenye dhamana ya mwisho, napendekeza kwamba kiweze kuboreshwa kuangalia kwamba ni kwa namna gani kuwe na tume au mamlaka nyingine ambayo inaweza zikapelekwa zile taarifa na mtu ambaye anatafuta taarifa aweze kupata hizo taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kusema kweli kwa mara ya kwanza kabisa Muswada huu umezingatia maoni mengi ambayo yana manufaa kwa Taifa hili na hata maoni ya wadau wa habari wameyatoa humu na wameelezea na kuridhishwa kwao ni kwa jinsi gani kwa mara ya kwanza Serikali imeweza kuzingatia hayo maoni yao. Kwa maana hiyo, ninaamini kabisa Muswada huu utakapopitishwa utaweza kwenda kufanya kazi lakini pia katika nchi yoyote ina utaratibu wake na katika hizi nchi mfano duniani kote mataifa makubwa na madogo yanaweka zuio kwenye taarifa zake ili kulinda maslahi yake. Kwa maana hiyo wale watu ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakipata taarifa na kuzitumia hizo taarifa pasipo kuzingatia; mfano hata katika taarifa wanaposema kwamba habari ni nini, lazima uzingatie vitu vitano, kwamba hiyo habari ni nani, imetoka wapi, ni nani ametoa hiyo habari tofauti na wengine ndiyo utatumia kwamba ni habari za uchunguzi lakini hizo habari za uchunguzi wakati mwingine ukiangalia ni nani katoa bado jibu inakuwa huwezi kupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile itawazuia hata wale watendaji wa Serikali ambao kwa namna moja au nyingine wanaiba taarifa za siri na kuzitoa kwa nia isiyo njema. Muswada huu utakwenda kuwabana kwa maana kwamba itawataka pia hata hawa wanahabari kuhakikisha kwamba wanapata habari katika vyombo vinavyohusika kuwatoa habari ambayo ni mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunapozungumzia hapa ni vyema basi wakati mwingine watu tukajikita katika kuangalia kweli, wanasema kwamba mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, yapo mambo ambayo Serikali ina nia njema kabisa na wadau wa habari pia wametoa maoni na yameweza kuzingatiwa, afadhali wakati mwingine, ndiyo, mnapozungumza tuangalie kwamba kweli tuishauri Serikali ni vipi ambapo hapa wamekosea tuboreshe hivi badala ya kuwa ndiyo namba moja katika kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Muswada huu wa Huduma kwa Vyombo vya Habari. Kwanza kabisa naomba ni-declare interest kwamba na mimi ni mwanahabari na ni mwanahabari ambaye nina sifa kwa sababu nina degree ya uandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kuleta Muswada huu wenye heshima kwa taaluma hii ya habari. Kwa muda mrefu waandishi wa habari wameitwa majina mengi, wamedharauliwa na wapo wengine ambao walikuwa wakijiita critical thinker lakini waandishi wa habari na nakumbuka hata nikiwa chuo tulikuwa tunaambiwa sisi siyo ma-critical thinkers kwa maana hiyo Muswada huu utaleta heshima kwa wanahabari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi lakini nianze tu kwa kusema kwamba siku zote ukiona jambo zuri, ukiona jambo linapigiwa kelele ujue basi hilo jambo ni zuri na limewakamata pabaya wale wasiopenda. Sisi ni wanasiasa basi tuwe wavumilivu tunapozungumza. Kelele za chura huwa hazimzuii ng’ombe kunywa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia baadhi ya vipengele la kwanza niipongeze kwa mara nyingine Serikali kwa kuondoa vile vipengele ambavyo vilikuwa na utata na kwa maana hiyo inadhihirisha kabisa kwamba ni Serikali sikivu na kwa maana hiyo imeondoa vile vipengele ambavyo kwa namna moja au nyingine vimezua mjadala mkali na hasa kwa wanahabari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taaluma ya habari inakwenda kuwa na heshima kwa maana kwamba wengi ambao walikuwa wakifanya kazi hii kwa namna moja au nyingine wamepitia changamoto mbalimbali. Lingine kubwa zaidi ni kutokana na malipo madogo au malipo kiduchu waliyokuwa wakilipwa na hasa kutokana na kutokuwa na sifa. Kwa maana hiyo Muswada huu utawabana wamiliki wa vyombo vya habari, utavibana vyombo vya habari kuhakikisha kwamba Mwandishi wa habari ambaye ameajiriwa katika chombo husika basi atalipwa kulingana na taaluma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la waandishi wa habari kuwa na bima ni jambo muhimu sana na hivi karibuni, nitumie mfano tu wa Mwandishi wa habari mmoja ambaye kwa muda takriban wa miaka miwili alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya saratani. Waandishi wa habari walimuunga mkono sana mwenzao katika kumchangia ili kuhakikisha kwamba mwenzao anapata matibabu, lakini kwa sababu Mungu alimpenda zaidi hatimaye hatunaye hivi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama naye huyu angekuwepo katika mfumo huu wa malipo au wa bima hizi kwa waandshi wa habari, kwa namna moja au nyingine ingemsaidia sana pale tu alipogundua matatizo kuweza kuyashughulikia na bima hiyo ingeweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la uchochezi kwa urefu kidogo na nitakwenda kwa kutoa mifano ambayo leo hii tunapozungumza tunayo, mifano halisi ya wale ambao kwa namna moja au nyingine wametumia kalamu yao vibaya. Tunajua kwamba media is powerful na kalamu hii inapotumika vizuri inaleta maendeleo na kwa maana hiyo Muswada huu utakwenda kusaidia pia waandishi wa habari kuhakikisha kwamba habari zipi ambazo tunamsaidia Rais wetu zenye kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994, nchi ya Rwanda iliingia katika mauaji ya Kimbari na mojawapo ya mambo ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa ni mwandishi ambaye pia alikuwa ni Mhariri wa Gazeti la Kangura na huyu siyo mwingine ni Hassan Ngeze. Wengi tunamfahamu Hassan Ngeze ambaye kwa wale wanahabari ambao wanafuatilia habari wanajua leo hii yupo katika mahakama ya The Hague nchini Uholanzi amefungwa maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hassan aliandika habari katika gazeti la Kangura kuhusiana na amri 10 za Hutu. Katika hizo amri ni kwa jinsi gani zikiwahamasisha hawa Wahutu kuua Watutsi na kwa hiyo habari ambayo iliandikwa katika gazeti hilo ndiyo ambayo iliyomsababisha Hassan Ngeze akafungwa maisha leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi karibuni tu nchini Ufaransa gazeti la Charlie Hebdo ambalo lilichapisha vikatuni vya Mtume Muhammad (S.A.W) na kwa maana hiyo vile vikatuni vilisababisha mauaji makubwa kwa waandishi wa habari. Hii inaonesha kwamba waandishi wa habari tusipotumia kalamu zetu vizuri zinaweza kutuingiza katika matatizo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu suala la Richmond na katika suala hilo la Richmond mengi yaliandikwa na tuliaminishwa mengi sana. Naomba tu ninukuu baadhi ya mifano michache ambayo ilitumiwa katika vichwa vya habari katika magazeti. Mfano, katika gazeti la Mwanahalisi, gazeti hili la terehe 18 Januari, 2012 liliandika “Lowasa anajua uzalendo au ni machozi ya mamba?” Huu ni mfano mmojawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gazeti la Mwanahalisi la terehe 6 Aprili, 2011 liliandika “Lowasa hasafishiki”, huu ni mfano mwingine. Lakini hapo hapo gazeti la Mwanahalisi likaja pia kuandika kwamba; “Lowasa karibu CHADEMA”. Tuna haja gani ya kuwa na waandishi kama hawa ambao leo hii wanaamka, wanaandika habari kwamba huyu mtu ni mbaya, lakini kesho hiyo hiyo uwongo huo huo unabadilika na kuwa ukweli? Tunahitaji kuwa na Miswada na sheria kama hizi ambazo zitaweza kulinda taaluma ya habari. Taaluma ya habari, tunapokwenda kuupitisha Muswada huu ni kwa manufaa ya Wanahabari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2017
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia muswada huu wa Sheria mbalimbali ambao kwangu binafsi naona kwamba ni muswada wenye manufaa na utakwenda kutatua masuala mengi hasa kwenye suala zima la migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Hata inapokuja miswada hii ni katika kuhakikisha kwamba yale anayoyapigania basi kusiwepo na vipingamizi, kwa hili namshukuru sana na nazidi kumtia moyo Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu ili aweze kuwatumikia Watanzania na hasa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sehemu ya pili ambayo inahusu migogoro ya ardhi na mabadiliko na kama nilivyosema katika mabadiliko haya ya sheria yatakwenda kusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na hasa kwa kuzingatia kwamba baadhi ya watu wametokea kwamba kudhulumiwa haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa mabaraza haya ni chachu, pamoja na kwamba yalikuwepo lakini hivi sasa kwa mujibu wa sheria hii, mabaraza haya yameboreshwa zaidi. Kwa hiyo, ni faraja kubwa sana kwa Watanzania hasa wanyonge wa maendeo mengi ya vijijini ambao watakwenda sasa kunufaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo kubwa ambalo limenifurahisha ni kwamba tofauti na ilivyokuwa hapo awali, file lilikuwa likienda kwa Msajili linaweza likakaa muda mrefu sana wakati mwingine hata mwaka au miaka miwili bado halijarudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria hii mabadiliko tumeona kwamba watapewa siku 14 kwa maana hiyo katika siku hizi 14 zitasaidia sana kupunguza mlolongo wa kusubiri muda mrefu kwa wale watu ambao wamekuwa katika matatizo haya ya migogoro ya ardhi. Na tunaona kwamba katika siku hizi 14 pia itakuwa imesaidia kwamba kama ni file hili kama kwa upande mwingine ataona kwamba linahitaji kwenda mbele zaidi litakwenda huko. Kwa hiyo, ule mlolongo ambao ulikuwa ni mrefu utapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kipengele kingine ambacho ni sehemu ya tatu kwamba cha upimaji wa ardhi maeneo mengi. Tumeshuhudia kwamba baadhi ya maeneo yamekuwa na vibali viwili viwili na hii ni kutokana na kwamba wakati mwingine kutokuwepo na mtu maalum ambaye anahusika ni nani hasa anayepaswa kuhakikisha kwamba anatoa vibali ili eneo hilo liweze kupimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika sheria hii mpya tumeona kwamba kutakuwa na Mpima Ardhi wa Kanda. Kwa maana hiyo kama usipokuwa na kibali maalum ambacho kitaonyesha kwamba wewe lazima upate kibali ili kuweza kupima ardhi, hutoweza kufanya hivyo tofauti na siku za nyuma na hili ndilo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa sana, kwa mfano watu wa mabondeni ambao wamekuwa wakibomolewa na watu hao kwa upande mwingine utakuta kwamba wanazo hati kabisa ambazo wamepewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na kwamba kwa namna moja au nyingine, watu ambao walikuwa wakipima kwa upande mwingine hawakuwa na vibali maalum ambavyo walikuwa wakivipata kutoka kwa wahusika. Kwa hiyo, sheria hii naona kwamba itakwenda kutatua migogoro ambayo sio ya lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa hasa kwangu mimi ambacho kimekuwa ni faraja kubwa na kwa moyo wangu wa dhati kabisa naipongeza Serikali, nakupongeza sana Mwanasheria Mkuu, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ndio wanasimamia mifuko hii ya fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili mimi ndilo ambalo ndilo limenifanya hasa nikanyanyuka kuipongeza Serikali kwa moyo
wa dhati kwa sababu sasa tunaona kabisa mbali na Rais ambaye amekuwa mfano katika awamu hii ya tano kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mpaka Mawaziri hivi sasa tunao ambao wana ulemavu na sisi tunaamini kwamba na siku zote nimependa kutumia mfano huu,kitanda usichokilalia huwezi kujua kunguni wake. Uwepo wa Waziri katika Baraza la Mawaziri ni chachu kwa sababu ataweza kushauri. Kwa hiyo, hapa sasa katika mfuko huu wa fidia ambako Sura 263 inayojumuisha kifungu cha 34 hadi 36 cha muswada.

Mimi nimefarijika sana kuona kwamba watu wenye ulemavu pia watashiriki katika hiyo bodi. Na hapa kwa mujibu wa maoni jinsi inavyozungumza, kwamba wawakilishi kutoka Chama cha Watu Wenye Ulemavu ingawa nakubaliana na maoni ya Kamati kwamba wanasema kusiwepo na masharti. Kama umeshasema mtu mwenye ulemavu, huyu anajua ni jinsi gani ya kuweza kuwasaidia wenzake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na itasaidia sana kwa sababu katika Vyama hivi vya Watu Wenye Ulemavu sio wote tuseme kwamba wana ujuzi huo wa masuala haya ya mifuko. Kwa hiyo kwa kuweka hapa kwamba lazima awe na ujuzi, mimi naiomba Serikali iondoe kwa sababu tayari umekwishasema ni Chama cha Watu Wenye Ulemavu, tayari hawa watu wana ujuzi mpana zaidi, wana uelewa mpana zaidi wa masuala ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, wataweza kuishauri vyema Serikali kuhakikisha kwamba inatenda haki na kuwasaidia wale watu ambao wamepata ulemavu katika sehemu za kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba sisi wote ni walemavu watarajiwa. Na kama unavyofahamu, siku hizi ajali zimekuwa nyingi lakini hasa kwa wafanyakazi, hasa kwenye viwanda, wengi wamekuwa wakipata matatizo na wengi wametelekezwa ambapo hakuna kile ambacho kweli wanastahili kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtumie aliyekuwa mwandishi wa habari waGazeti la Habari Leo, Athumani Hamisi, kama mfano, ambaye alipata ajali wakati akienda kufanya kazi Kibiti na gari ikapinduka. Mpaka leo hii, pamoja na kwamba inawezekana Kampuni ya Serikali ndiyo inamlipa mshahara kidogo sana, lakini ni mtu ambaye amesahaulika, ana maisha magumu sana katika nchi hii. Ni mtu ambaye aliitumia taaluma yake vizuri kuhabarisha na kukosoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile leo hii kwa hali aliyoipata ambayo amekuwa ni mlemavu wa kudumu, kama hii sheria ingekuwepo ninaamini kabisa angepata fidia ambayo leo hii ingemwezesha kuishi maisha ambayo angeweza kuishi maisha tofauti kama awali alivyokuwa akifanya kazi. Lakini leo hii amesahaulika huyu mwandishi na maisha yake ni magumu sana. Ninaiomba pia Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imwangalie kwa jicho la pekee kwa sababu ni mtu ambaye ameitumikia kwa muda mrefu. Imuangalie kwa jicho la pekee na hata ikibidi kwa kweli kuweza kumjenga nyumba, kwa sababu anaishi maisha magumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mfuko huu mimi naona kwamba sheria hii itakwenda kuboresha na wale ambao watapata ajali katika maeneo ya kazi watafidiwa. Kwa hiyo mwakilishi kutoka katika Vyama vya Watu Wenye Ulemavu atatoa ushauri ambao utakuwa ni mwafaka, utaweza kuisadia Serikali. Ninachoomba tu ni kwamba hapa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hebu ondoa hiki kipengele kinachosema mwenye ujuzi na uzoefu katika mambo ya kazi ya hifadhi za jamii. Ninakuomba uliondoe hili ili basi hawa watu waweze kuingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili limekuwa ni faraja kubwa sana na ndilo ambalo limenifanya mimi nisimame kuweza kuchangia. Na kwa moyo wangu wa dhati naipongeza Serikali katika hili kuhakikisha kwamba sasa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma na hii ni kutokana na kuridhia hii mikataba, Sheria Na. 9 ambayo inaitaka Serikal
kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeona sasa sio tena kwa maneno ni kwa vitendo. Kwa hiyo hili mimi nasema Serikali hongera sana na msiishie hapo, na Rais wetu nampongeza sana, imekuwa ni faraja, na ninaamini kabisa kwamba watashirikishwa katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo katika nchi yetu. Sisi tunasema katika maendeleo tuhakikishe kwamba hakuna anayeachwa nyuma, na mimi nafurahi kuona kwamba watu wenye ulemavu hakuna anayeachwa nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naipongeza sana Serikali, nawatakia kila la heri katika sheria hii, lakini Mwanasheria Mkuu naomba sana uzingatie hiki kipengele cha ujuzi, hebu kiondoe. Tayari huyu mtu, kwanza kuwa tu na ulemavu tayari huo ni ujuzi, ana uzoefu katika masuala ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, ushauri wake utakuwa ni wa busara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsante
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa hizo dakika tano, ninaomba nichangie mambo makuu matatu, moja katika usajili wa line za simu, kwanza nakubaliana na mapendekezo yaliyoletwa na Serikali kwa sababu ninaamini kabisa yatakwenda sasa kusaidia kupunguza tatizo kubwa la wizi ambao umekuwa ukifanyika kwenye mitandao, na kwa upande mwingine, wizi huu umechangiwa pia na Makampuni ya simu, simu wao wenyewe, ambao wafanyakazi kwa namna moja au nyingine wanaofukuzwa au wafanyakazi ambao siyo waaminifu ndiyo ambao wamekuwa wakifanya zoezi hili la kuwaibia wananchi wasiyo na hatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Sheria hii sasa Serikali katika mabadiliko haya yatakwenda kudhibiti wizi huo. Nina swali tu kwa Serikali kwamba katika usajili huu wa, unaoendelea na hasa kwa kutumia alama za vidole kuna mambo ya msingi ambayo hayajazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wapo watu ambao wamepata ajali na kwa bahati mbaya wamekatika mikono, lakini viungo vingine wanavyo na wanasikia vizuri wanahitaji kutumia simu. Mtu huyu amewekewa utaratibu gani wa kwenda kusajili kwa kutumia alama za vidole, hapo naona kwamba hawakuangalia kwa jicho hilo kuona kwamba tunawaandalia utaratibu gani watu wenye ulemavu, watu waliopata malazi ya ukoma wakakatika vidole, lakini pia hata wale ambao siku hizi ajali ni nyingi wamepata madhara hayo madole gumba wanayapata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika Sheria hii ya Baraza la Sanaa. Naipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya lakini siku za mbele naomba waangalie kwa sababu sheria hii ni ya muda mrefu kuona kwamba wanaileta ili iweze kufanyiwa marekebisho tukaweka huko huko COSOTA, BASATA na haya marekebisho ambayo yanafanyika mara kwa mara basi tutakuwa tumesaidia sana. Kwa ujumla wake, sheria hii inakwenda kusaidia kwa kiasi kikubwa sana; wezi mbalimbali, maharamia wa kazi za wasanii, tunalalamika wasanii wetu kwamba hawafaidiki na kazi hizo lakini wizi ndiyo ambao kwa kiasi kikubwa umesababisha wasanii wetu wawepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize wasanii kama msanii mkongwe kwa mfano, Nguza Viking au King Kikii, King Kikii kwa nchi za wenzetu sasa hivi angekuwa ni billionaire kwa kazi nzuri ambayo ameifanya, tangu ameanza kuimba miaka hiyo nyimbo za mtindo wa Masantula na nyimbo nyingine nyingi lakini mpaka leo bado ni maskini. Kwa hiyo, sheria hizi zote zimeangalia hilo, kwa hiyo, BASATA watazuia sasa wizi, wataweza ku-destroy hizo kazi za maharamia ambao wamekuwa wakifanya kazi hiyo na kujinufaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu pia kupata majibu, tumeona kwamba mwanamziki maarufu Beyonce ametoa wimbo na filamu ambayo ina baadhi ya mandhari ya Mlima Kilimanjaro lakini pia hata Serengeti, the Lion King. Napenda kupata majibu kama Serikali inalifahamu suala hilo na imefaidika na nini? Hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya sheria na hasa Sheria hii ya Filamu tuliyofanya hivi karibuni, kwanza Serikali inalijua hilo lakini imefaidika vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba niishie hapo. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naanza kwa kuipongeza Serikali kwa mabadiliko haya ya sheria ya mara kwa mara ambayo yamekuwa na tija kubwa. Kabla ya Sheria ya Madini kufanyiwa marekebisho, tulikuwa tunakusanya kati ya bilioni 130 –150, baada ya marekebisho mwaka 2018/2019 tulikusanya zaidi ya bilioni 328. Mwaka huu lengo kwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ni kukusanya bilioni 470 na tayari mafanikio yanaonekana kwamba tutafika huko. Hii inaonesha kwamba, mabadiliko haya ya sheria yamekuwa na tija kubwa sana na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu yale yaliyosemwa kwa mfano ACCACIA kwamba tungeshtakiwa, lakini sasa hivi tunaona matokeo mazuri ambapo sasa ubia tayari unakwenda kuingiwa na kwa kuanzishwa kampuni nyingine ambayo itakuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapongeza sana mabadiliko haya ya sheria na sisi kama Wabunge, Bunge kazi yake ni kutunga sheria. Wakati wowote sheria zitakapoletwa sisi kama Wabunge tutawajibika. Kwa hili nimpongeze Mheshimiwa Spika na Kamati yetu ya Katiba na Sheria ambayo imekuwa ikifanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba, katika maambukizi ya Virus vya UKIMWI asilimia kubwa ni vijana na ni kuanzia miaka 15 – 24, na Serikali imeleta mabadiliko kushusha mpaka miaka 15. Naipongeza kwa mabadiliko haya. Mabadiliko haya yatakuwa na tija kwa sababu vijana wengi kwangu naona kwamba hasa wale wa sekondari tayari wana ufahamu mkubwa na utawasaidia wao wenyewe kwenda kufanya mabadiliko haya kupima ili tuweze kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambazo zinatolewa mfano ikiwemo nchi ya Afrika Kusini ambayo wao wameshusha mpaka miaka 12, matarajio ilikuwa ni kuona ni kwa jinsi gani wanapunguza lakini matokeo yake maambukizi yapo juu zaidi. Kwa hiyo, miaka hii 15 kwa Serikali kuleta mabadiliko haya ni mwanzo mzuri, na endapo kutakuwa na changamoto kazi ya Bunge ni kutunga sheria na niwajibu wetu basi sheria hizo zitakapokuja, tutaweza kufanyia marekebisho ili kunusuru kizazi hiki ambacho hivi sasa kimekuwa na maambukizi makubwa ya Virus vya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali katika ule mpango wa 90, 90, 90, ni kuhakikisha kwamba watanzania wengi wanapima. Wakishapima 90 ya pili, ni wanapata dawa kwa ajili ya kunusuru/kupunguza makali ya Virus vya UKIMWI. 90 ya tatu wale wanaotumia dawa maambukizi yanakuwa ni madogo kwa sababu tayari dawa zile zinafanya kazi. Hatuwezi kufanikiwa hii 90 ya tatu pasipo 90 ya kwanza kuweza kukamilisha na ndiyo maana katika sheria hii, Serikali imeleta sheria hii ili basi vijana ambao ni kuanzia miaka 15 – 24 ambao 80% wameathirika kwa kiasi kikubwa tutaweza kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wakishajua vijana miaka hiyo 15 chini ya wazazi wataweza kuanza kutumia dawa ambayo tunakwenda katika 90 ya kwanza, wakitumia dawa 90 ya pili kwa sababu bado vijana wana matamanio mengi 90 ya pili, kama anatumia dawa ipasavyo 90 ya pili itamsaidia kuweza kutumia dawa. 90 ya tatu dawa hizi zitasaidia asiweze tena kuambukiza Virus vya UKIMWI au hata yeye mwenyewe kwa sababu tayari atakuwa amepitia zile stage za ushauri na chini ya uangalizi utamsaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo marekebisho haya ya sheria, ninaipongeza sana Serikali kwa kutuletea mabadiliko haya na kazi yetu sisi Wabunge ni kutunga sheria. Tuko hapa tutaendelea kutunga sheria, Mheshimiwa Rais wetu aendelee kufanya kazi sisi kama Wabunge atuletee sheria tutabadilisha hizo sheria ili ziweze kumsaidia. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaelekea katika uchumi wa kati, uchumi wa viwanda mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nasema kwamba, Serikali pamoja na sisi Wabunge tuko pamoja, tutaendelea kuisimamia Serikali, kuishauri pale tunapohitaji kuishauri lakini vilevile kuhakikisha kwamba mabadiliko yote ya sheria tunayafanyia kazi, 90, 90, 90, ili iweze kufanikiwa ni pamoja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.