Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Agnes Mathew Marwa (20 total)

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hospitali ya Kwangwa ya Mkoa wa Mara iliyopo Musoma Mjini imekuwa ni ya historia kila siku tunaisikia ipo tokea hatujazaliwa hadi leo; na kwa kuwa wanawake na watoto wanapata shida sana na vifo vingi vinasababishwa na umbali wa kutoka Hospitali ya Musoma hadi Mwanza, je, Serikali inaonaje sasa kwa sababu imeshaitengea bajeti Hospitali ya Kwangwa kumalizia suala hilo au kuipa kipaumbele Hospitali ya Kwangwa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imepokea suala zima la Hospitali ya Kwangwa. Maelekezo yetu ni kuhakikisha Hospitali za Wilaya na Mikoa zinafanya vizuri na zile ambazo zina changamoto kama vile miundombinu haijakamilika, changamoto za kibajeti zilizojitokeza katika kipindi cha nyuma kwamba bajeti zimetengwa lakini hazikufika, tunaenda kusisitiza suala zima la ukusanyaji wa mapato, huduma ya afya tumesema ni jambo la msingi ili kila mwananchi apate huduma bora ya afya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Marwa, Serikali imejipanga na katika kipindi hiki tutaangalia bajeti inasemaje katika hospitali hii. Lengo letu ni kuipa nguvu wananchi wa eneo hilo wapate huduma kwa manufaa ya Serikali yao.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Swali langu la nyongeza lilikuwa ni hilo aliloliongelea Mheshimiwa Ryoba, labda swali (b), kutokana na hizo posho kusuasua na wananchi wanakuwa hawazipati kwa muda, ni lini sasa Serikali itakaa na wale wananchi ili kuongea nao au kuwapa uhakika wa kuwapa hizo fidia kwa muda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa mdogo wangu Agnes Marwa na wifi yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sisi Wizara ya Kilimo kama nilivyosema kwenye jibu langu lile la nyongeza, ni kwamba hatuwezi tukafanya Wizara ya Kilimo peke yetu sisi kama Wizara ya Kilimo kwa sababu inawahusu wakulima kwa sababu hii inahusisha Wizara tatu; Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ningependa kuwaasa Maafisa Kilimo wetu, Maafisa Ugani wetu kule kwenye halmashauri wajaribu ku-review zile posho na viwango vya posho ambavyo huwa wanavifanyia tathmini kwa wakulima wetu kabla hawajapeleka Wizara ya Maliasili na Utalii ili wakulima hawa waweze kupata haki zao stahiki. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea majibu kwa yale Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ameyajibu vizuri sana. Basi katika hili suala ambalo nimelisema Wizara ya Maliasili na Utalii sasa hivi inafanya mapitio ya zile kanuni zetu za kifuta jasho za mwaka 2011 ambazo ndizo zinaongoza namna ya kutoa kifuta jasho, si fidia kama inavyosomeka, ni kifuta jasho kwa wale wananchi ambao wameathirika. Kwa hiyo, baada ya hizi taratibu kukamilika basi mambo yatakuwa yamekwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu hili suala lake kwamba ni lini watalipwa, kama nilivyosema katika jibu langu la kwanza kwamba tarehe 29 na tarehe 30 mwezi uliopita maafisa wetu wameshakwenda kufanya tathmini. Baada ya tathmini hiyo kukamilika basi taratibu za kuwalipa hao wote walioathirika zitafanyika mara moja.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Bado sijaridhishwa na majibu hayo ya Mheshimiwa Waziri. Kutokana na sintofahamu ya wananchi hao wa Bunda, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri, nina evidence hapa nisome. Kutokana na kituo hicho cha afya kwa mwaka 2006, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Rais Mstaafu aliweka jiwe la msingi. Aliweka jiwe la msingi ili kusudi huo upembuzi yakinifu na hivyo vitu vingine vikikamilika ipewe hati ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufanya huo upembuzi yakinifu anaousema hapa Mheshimiwa Waziri, mochwari imeshatengenezwa tayari na ipo, chumba cha dharura Mheshimiwa Waziri kipo, X-Ray tayari ipo, Ultra Sound tayari ipo na barua hii nitamkabidhi nikitoka hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, ya Wilaya ile lakini pia chumba cha dhararu kipo. Je, ni nini sasa kinachosababisha hii Wilaya ya Bunda na hicho Kituo cha Manyamanyama kisipewe hadhi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa usimamizi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Bibi Janet Mayanja akiwa na Madiwani wake chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri kutokana na mapato na makusanyo ya Halmashauri wameweza kuweka vitu hivyo na vinginevyo. Ni kwa nini sasa hospitali hiyo isipewe hati? Kama mnatuelezea kwamba vituo vya afya vinatakiwa vibaki palepale ziwepo Hospitali za Wilaya, Mheshimiwa Waziri naomba majibu leo kwamba kama fedha ipo… (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali bado halijakwisha, naomba Mheshimiwa Waziri niambiwe kwamba ni lini sasa na sisi mtatuletea hiyo pesa ya kujenga Hospitali ya Wilaya ili tujue kile ni kituo cha afya? Mheshimiwa Naibu Waziri, tafadhali naomba majibu ya kutosha. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli idadi ya wagonjwa wanaokwenda kupata huduma katika Kituo cha Afya cha Manyamanyama ni wengi sana na ndiyo maana kumekuwa na concern ya kwamba ni vizuri kituo cha afya kile kikapandishwa hadhi ya kutoka kituo cha afya kikawa hospitali ya wilaya. Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba uhitaji wa vituo vya afya bado uko pale pale na ujenzi wa hospitali za wilaya bado uko pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na kazi nzuri ambayo anaifanya ya kuhakikisha afya za watu wake zinaimarika, ni vizuri tukahakikisha tunaheshimu ramani inayohusu hospitali ya wilaya ambayo ni tofauti na ramani inayohusu kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hospitali za wilaya ambazo tunakwenda kuzijenga kwa mwaka wa 2018/2019, Bunda DC ni miongoni mwa Wilaya ambazo zinakwenda kupata hospitali za wilaya. Kwa taarifa nilizonazo Bunda DC na Bunda Mji, Bunda DC mpaka sasa hivi bado hawajajua wapi Halmashauri yao itakuwa. Kwa hiyo, pesa hiyo ambayo itakuwa ipo tayari kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya busara itumike ili pale ambapo papo tayari tuanze kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata fursa ya kuongea na Mkurugenzi jana, pamoja na Kituo cha Afya cha Manyamanyama tayari Halmashauri imeanza kutafuta eneo lingine la ukubwa wa hekari 40. Kwa hiyo, thinking yao ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na eneo mbadala kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa kwa Mheshimiwa Getere. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hata wapiga kura wa Mheshimiwa Getere wako hapa ndani leo wamesikia na wanausubiri huo umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali hilihilo niulize kwa Mkoa mzima wa Mara, kuna Wilaya ya Rorya ambako mimi nimezaliwa, Wilaya ya Msoma Vijijini pia nilikozaliwa lakini pia kuna shangazi zangu wa Wilaya ya Serengeti na Tarime. Swali langu sasa, ni lini Serikali itapeleka huduma za umeme wa REA katika huduma za shule, zahanati, vituo vya afya kwa maeneo mengine yote yaliyobaki ya Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Agness, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Mbunge Agness anavyofuatilia masuala haya ya umeme katika taasisi za umma. Napenda kusema tu kwamba mkandarasi katika Mkoa wa Mara atapeleka umeme kwenye vijiji vyote 172 vya Mkoa wa Mara pamoja na vitongoji 318 na yuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha msingi kabisa, katika Wilaya ya Rorya ameshapeleka umeme kwenye vijiji 17 na shule za sekondari 18. Katika Wilaya ya Msoma Vijijini, mkandarasi anaendelea na kazi. Niseme kwamba vijiji vyote vitapelekewa umeme kuanzia sasa na kuendelea na mwezi Juni, 2020 miradi yote itakamilika.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza lenye vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, kutokana na shilingi na vifaa vya ujenzi kupanda thamani kila mwaka, deni la wananchi wa Nyamongo wanaodai fidia ni miaka sasa. Je, watakapolipa hizo fedha watawalipa pamoja na riba kwa sababu sasa vifaa vya ujenzi vimepanda?

Mheshimiwa Spika, pili, kutokana na uthamini kila siku kufanyika kwa haohao wakazi wa Nyamongo lakini hawalipwi ukizingatia hali halisi kwamba na wao wana familia zao, wana watoto wanawasomesha na biashara zao na mahitaji yao ambayo yamesimama kusubiria kuondolewa katika maeneo yale. Je, Serikali ina mpango gani wa kulimaliza hili suala sasa ili wale waliobaki walipwe fedha zao?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agness Marwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nieleze kwamba tumekuwa karibu sana Mheshimiwa Agness Marwa kushughulikia masuala ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo. Kwa kweli, amekuwa mstari wa mbele kuwapigania kila wakati na kutualika mara kwa mara kwenda Nyamongo kwa ajili ya kukutana na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ziko fidia ambazo fedha zilishatolewa muda mrefu lakini bahati mbaya hazijalipwa kwa wananchi. Hii ni kwa sababu tu wako wananchi ambao walikataa zile fedha, kwa hiyo, zikawekwa Halmashauri. Kwa hiyo, nadhani si sahihi sana kuupa tena mzigo mgodi kwamba wao walipe na fidia ya interest kwa sababu fedha hazijachukuliwa. Wale wananchi waliokataa mwanzo walikuwa 138, wale wananchi wengine 70 wakachukua cheque zao wakabaki 64, niwaombe wakachukue cheque zao kwa sababu tayari uthamini ule ulikwishafanyika muda mrefu na fedha zao shilingi 1,900,000,000 ziko pale kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili ambalo ameuliza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba jambo hili la fidia sasa lifike mwisho. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Mgodi wa Barrick kuingia pamoja na Serikali kama mbia, tunachukua kila hatua kufuta yale makosa ambayo yalikuwa yanafanyika ACACIA. ACACIA walikuwa na utaratibu, mnaweza mkafanya uthamini leo kesho wakakataa kulipa tu kwa vigezo vingine. Nataka nimhakikishie kwamba tumeshazungumza na mbia mwenzetu Barrick anayekuja, jambo hili sasa litafika mwisho na Mthamini Mkuu ameshawasilisha vitabu vya uthamini ambavyo nimetaja wananchi zaidi ya 1,838 wamekwisha kufanyiwa uthamini. Kwa hiyo, tutalipa kwa wakati baada ya taratibu hizo kukamilika. Ahsante.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Naibu Waziri huyu mkandarasi kama ameomba muda wa nyongeza na atapewa na Serikali, je, ikifikia muda huo ikiwa barabara hiyo haijamalizika nini kitafanyika? Je, atapewa muda tena aendelee au atapewa muda mkandarasi mwingine ili aimalizie hii barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Agness amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo ya Mkoa wa Mara juu ya barabara nyingi ambazo kimsingi Serikali imepeleka miradi mingi sana katika Mkoa huu na hivi karibuni Mheshimiwa Marwa unakumbuka Mheshimiwa Rais ameongeza miradi kadhaa ya ujenzi wa barabara ya lami katika Mkoa wa Mara, kwa hiyo nakupongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake anasema kwamba endapo tutamuongezea mkandarasi huyu kwamba muda na asipokamilisha itakuwaje; kimsingi niseme kwamba zoezi la kumuongezea muda linazingatiwa kitaalam ili kuona nini kazi iliyo mbele ya safari ili kukamilisha mradi huu. Kwa hiyo, ninaamini muda ambao utaongezwa utakuwa ni muda ambao utawezesha kutekeleza mradi huu kwa wakati kulingana na utaalam kulingana na taratibu. Kwa vile suala hili ni la kimkataba nikuhakikishie Mheshimiwa Marwa kwamba sisi tunatasimamia vizuri mkataba huu ili kazi ikamilike na zipo hatua za kuchukua kulingana na utaratibu wa kimkataba kama wakandarasi hawa watakiuka mkataba basi sheria itachukua nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba mradi huu unajengwa kwa kutumia joint venture na nia ya Serikali kuwasadia wakandarasi wazawa ili waweze kujenga uwezo, ili waweze kujenga mitaji, lakini ili waweze kusababisha ajira nyingi kwa vijana wetu lakini hili pia ile faida inayopatikana iweze kubaki hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni nia ya Serikali kuwawezesha hapa, sasa watumie fursa hiyo ambayo Serikali niwaombe sana wakandarasi hawa wakiingia kwenye joint venture watumiea fursa hii nzuri ili kuhakikisha kwamba tunawasidia kama Serikali na kama watashindwa basi Serikali itaendelea na taratibu ambazo zipo. Kwa maana hiyo kwamba kulikuwa kuna changamoto za kiuendeshaji na za kiutawala katika JV hizi ambapo tumeelekeza wenzetu au pande wa CRB na wenzetu wa ERB kwamba ndio walezi wa hizi taasisi wawasimamie vizuri na wahakikishe ubora, wahakikishe nidhamu ili tuwajenge vizuri waweze kusaidia nchi yetu, ahsante sana.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, sambamba na hilo swali la Mheshimiwa Robert Maboto nauliza je, ni lini Serikali itakamilisha lami kutoka Kinesi yaani Wilaya ya Rorya inayounganisha kutoka Rorya mpaka Tarime ambayo pia ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa wetu Hayati Magufuli? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi za viongozi wetu wakuu tutaendelea kuzitekeleza kulingana na fedha itakavyopatikana ikiwa ni pamoja na hiyo barabara ya kutoka Rorya hadi Kinesi, ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali kuhusu kuongeza vifaa tiba kwenye Kituo cha Afya Nyamwaga, Wilaya ya Tarime ili kipandishwe hadhi kiwe Hospitali ya Wilaya, ikizingatiwa Wilaya ya Tarime ina uhitaji mkubwa kutokana na jiografia ilivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ambacho Mheshimiwa Mbunge ameomba tu hapa ni kwamba, lini Serikali tutaongeza fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Nyamwaga ili kiweze kuendelea kuhudumia watu? Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imesikia ombi lake na tutafanya tathmini tuone ni vitu vingapi ambavyo vinahitajika kwa wakati huu ili viweze kutoa ile huduma stahiki. Ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika Wizara hii. Niombe na kuishauri Serikali ifanye hivyo kwa Mikoa yote ya Tanzania nzima ukizingatia wanawake wenzetu na wao wanatakiwa wazae katika uzazi salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza liko hivi, Mkoa wa Mara, ni kati ya Mikoa yenye changamoto yenye uhitaji huu wa vyumba vya kujifungulia wanawake wenzetu wenye uhitaji maalum.

Je, Serikali ina mpango gani wa kwenda kujenga vyumba hivyo katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara ukizingatia ni Mkoa special alikotoka muasisi wa Taifa hili Baba yetu Mwalimu Julius Nyerere?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maelekezo ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan hasa alipokuwa anatusisitiza kuhusu eneo la kupunguza vifo vya akina Mama na Watoto mojawapo ni eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala siyo kujenga maeneo maalum kwa ajili ya wao kujifungulia, lakini ni suala la ndani ya ramani yenyewe na huduma yenyewe ambayo akina mama wengine wote wanapata huduma ndani humo kuhakikisha kwamba kuna usaidizi mazingira infrastructure inawasaidia wao kuweza kupata huduma hiyo. Lakini kunakuwepo na vifaa ambavyo vinaweza vikawasaidia wenzetu wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Afya kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kwamba sasa Waganga Wakuu wa Mikoa yote wanapokwenda kufanya usimamizi shirikishi eneo hilo liwe sehemu yao ya hadidu rejea ya kufuatilia kuhakikisha kila Wilaya, kuhakikisha kila Kituo cha Afya kila Zahanati wamezingatia hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itashughulikia migogoro ya wafugaji na wakulima inayoendelea katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Serengeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa katika Hifadhi ya Serengeti na wananchi ama vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo na changamoto hizi zimesababisha kuwepo na vurugu nyingi ikiwemo wananchi kuuawa lakini pia na askari wameendelea kuuawa.

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua na kama siku tatu zilizopita Serikali ya Mkoa ilienda kuzungumza na wananchi ili kutatua mgogoro huu. Kimsingi hakuna mgogoro wowote isipokuwa wananchi hawataki kukubaliana na mipaka iliyopo na kibaya zaidi tunapoweka vigingi wananchi wanaenda wanang’oa vile vigingi na kuendelea kufanya vurugu ikiwemo kuingiza mifugo hifadhini.

Kwa hiyo, niendelee kuwaomba wananchi wafuate sheria na taratibu zilizopo nchini, kwenda kinyume na sheria ni kujitakia sababu nyingine ambazo Serikali itachukua hatua.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri namshukuru sana, lakini naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba eneo la Serengeti ni miongoni mwa maeneo ya vivutio vyetu ambavyo vinajulikana kimataifa. Hili ni eneo ambalo tunapaswa kulilinda na kuliendeleza, lakini hili ni eneo pia ambao kumekuwa na changamoto kama alivyosema Naibu Waziri, askari wetu mara kwa mara wamekuwa wakipigwa mishale na wananchi wanaozunguka.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Askari Deus mwenye umri wa miaka 42 amepigwa mshale wa sumu eneo lile na tumekuwa tukiendelea wananchi na kutoa matamko na kulaani hali hii.

Mheshimiwa Spika, hivyo nitumie nafasi hii kusema kwamba kimsingi Serengeti haina mgogoro wowote wa mpaka, wananchi wanapaswa kufahamu na niishukuru sana Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara wamepita juzi na wataalam wetu, kuwaonesha wananchi eneo la mpaka ili wasipate kuingia katika hifadhi.

Hivyo ni muhimu kuheshimu maeneo haya ya hifadhi ili hifadhi zetu ziwe salama, wafugaji wawe salama na wakulima wawe salama. Nimeona niongeze msisitizo huo, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

Je, Serikali itakuja lini na mpango wa kusambaza maji katika vijiji vya Wilaya za Mkoa wa Mara zinazozunguka Ziwa Victoria ukizingatia tayari vyanzo vya maji viko wazi kutokana na Ziwa Victoria na vijiji vingi havina maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Dada yangu Agnes Marwa na atakubaliana na mimi Wizara ya Maji tumewekeza miradi mikubwa sana katika Mkoa wa Mara. Tuna mradi wa Mugangu, Kyabakari Butiama, zaidi ya Bilioni 70. Pia tuna mradi pale Bunda ambao umekwishakamilika kwa ajili ya chanzo.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie kila ambapo bomba kuu litakapokuwa linapita vijiji jirani tutahakikisha vinapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya ya Rorya ni kati ya wilaya ambazo ziko nyuma sana kimaendeleo kutokana na changamoto ya miundombinu. Sasa;

je Serikali haioni kuna ulazima wa kuanza ujenzi wa barabara inayopita Mika, Utegi, Shirati hadi Kirongo; ukizingatia ni muda mrefu sasa, tangu 2017, 2018 ikiwa inafanyiwa upembuzi yakinifu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja inayoanzia Utegi katika Jimbo la Rorya ipo kwenye mpango wa kufanyiwa usanifu ili ikishafanyiwa usanifu tujue gharama halafu Serikali kama ilivyo kwenye Ilani tuweze kupata gharama na tuanze kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, je, ipo ruzuku ama mikopo nafuu ya kuwezesha miradi hii ya vizimba ili kufanya uvuvi kuwa wa kisasa zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Wizara ina mpango gani wa kuendelea kutoa elimu kuwawezesha wavuvi au wananchi wanaozunguka Ziwa Victoria kuwa na uelewa zaidi na haswa Mkoa wa Mara ambao bado hawajapata elimu hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge ni mvuvi na ni Mchuuzi na ni mtu ambae anaipenda sana hiyo kada. Nimhakikishie tu kwamba Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunazo fedha ambazo ni za masharti nafuu kwa ajili ya wafugaji wa samaki kwa vizimba kwa vijana. Eneo la pili ni kwamba mpango wa kutoa elimu upo na sasa hivi tumeanza na programu za vijana atamizi ambao wanakuwa wakifundishwa juu ya ufugaji wa samaki na elimu ya viumbe maji katika maeneo ambayo yanazungukwa na bahari, maziwa ambapo vijana wengi wanahusika na kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, hivyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Agnes Marwa kwamba kazi hiyo itafanyika. Ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhalisia huohuo kwamba Serikali ilikwishafanya uthamini na ikaelewa kwamba ni watu wangapi wanahaki ya kulipwa maeneo yao katika maeneo yambayo wamechukua Wawekezaji.

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hili kutokana na kwamba wao Wawekezaji wameshapata faida ya kutosha na sasa mashimo ndiyo yatakayobaki na wananchi wamesubiri kwa muda mrefu na ni tatizo la muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kwamba tathmini zote zimeshafanyika na kiwango cha malipo kinachostahili kulipwa kimeshajulikana, mchakato unaoendelea kwa sasa ni huo wa kuhakikisha kwamba wanaostahili kulipwa, kiwango wananchostahili kulipwa na maelewano ya wao kukubali malipo hayo ndiyo yanayoendelea na Wizara tutaendelea kusimamia hilo liweze kutekelezwa.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa madereva wenye uzoefu na ujuzi wa udereva kwa kuwa walikosa kigezo cha kuwa na cheti cha form four. Na kwa kuwa ajali zimekuwa nyingi katika nchi hii ambazo zinaleta ulemavu au walemavu wengi nchini: -

Je, Serikali haioni sasa sababu ya kuwarudisha madereva hao kazini kwa sababu cheti cha form four hakina uhusiano na ujuzi au utaalamu wa udereva? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuwaondoa watumishi waliokuwa hawana vyeti vya form four wakiwemo madereva ilikuwa ni Sera ya Menejimenti ya Utumishi ambao tumeridhia wote kama nchi, kwamba tuna vijana waliokwisha soma mpaka kidato cha nne na kuendelea, ni vizuri utumishi wa umma uwazingatie hao na kuruhusu wale ambao walikuwa kwenye utumishi wa Umma wajiendeleze. Serikali bahati nzuri ilitoa muda maalum wa watu wale kujiendeleza, na walioshindwa kujiendeleza ndio waliondolewa.

Mheshimiwa Spika, wale wa darasa la saba waliojiendeleza wengi walibaki kwenye utumishi wa Umma. Nadhani bado hakuna hoja ya msingi ya kurejea darasa la saba wakati tunaowahitaji kwa mujibu wa sera yetu ni baada ya kidato cha nne, na vyuo vya udereva vipo ambapo hawazuii kuingia kupata mafunzo. Kwa hivyo tunalichukulia positively kwa maana kwamba wataendelea kujielimisha na wanaokiuka wanachukuliwa hatua, ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, tokea Tanzania imepata uhuru, kuna vijiji mkoani Mara hawajawahi kuyaona maji toka Setikalini: Je, Serikali ina mpango gani kupeleka maji katika Wilaya ya Serengeti na vijiji vyake na Wilaya nyingine ambazo zinazungukwa na utajiri wa Ziwa Victoria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya aliyoyataja katika eneo la Serengeti, tayari tuna miradi ambayo tunatarajia wananchi waweze kunufaika na maji safi bombani. Nasi Wizara ya Maji, toka tumeanza kuhakikisha tunaleta mageuzi ndani ya Wizara hii, maeneo ambayo hayajawahi kupata maji, yanapata maji sasa hivi. Hivyo, wananchi wa Serengeti nao wakae mkao wa kupata maji safi na salama bombani.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Majita – Musoma – Busekela yenye urefu wa kilometa 92 imechukua muda mrefu sana kukamilika. Hadi sasa imekwishajengwa kwa kilometa tano tu.

Je, Serikali ni lini ina mpango wa kupeleka fedha za kumalizia barabra hiyo ukizingatia itaongeza au kukuza uchumi kwa wana Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara kwa Ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, Agnes Marwa, kuhusiana na suala la barabara hii ya Majita – Musoma. Ni kweli tumekwishajenga kilometa tano na suala la kupeleka fedha tutaendelea kupeleka fedha katika barabara hii ili ikamilike kwa ukamilifu wake, ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wavuvi wa Mkoa wa Mara na hasa wale waliounda vikundi kwa ajili ya ufugaji wa vizimba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Zoezi la kutoa elimu ni endelevu. Kwa kuwa, vikundi bado viko vingi, basi tutawatuma tena wataalamu wetu waende kuwasaidia wafugaji wa Ziwa Victoria katika Eneo la Mara ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa wananchi waliambiwa kwamba watalipwa kwa ekari moja shilingi milioni mbili, kutokana na uhalisia wa maisha, maisha yamepanda juu sana, wananchi waliomba waongezewe kutoka milioni mbili kulipwa shilingi milioni sita. Je, nini tamko la Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbili, kwa kuwa Kata ile ya Nywatwari kuna wavuvi na wafugaji, je, wafugaji wamekwisha tafutiwa maeneo kwa ajili ya mifugo yao na wavuvi wataangaliwa vipi kwa ajili ya maeneo rafiki ya kuendeleza uvuvi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Agnes na kumpongeza kwa namna ambavyo anaendelea kutetea Wananchi wa Mkoa wa Mara akiwa kama Mbunge wa Mkoa wa Mara. Hili suala la stahili ya hawa wanaopaswa kuhama linafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ambapo Wizara ya Ardhi wamekuwa wakifanya uthamini na miongozo yote wanaitumia ili kuhakikisha kwamba suala hili linaendana sambamba na sheria na taratibu na kanuni zilizopo. Endapo kutakuwa na uhitaji wa kuangalia uthamani au namna ya kuongezewa basi tutakaa na Wizara ya Ardhi ili tuweze kujadili kama kuna uwezekano huo.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili la pili la wafugaji na wavuvi, kwenye upande wa kuwahamisha tayari uthamini umefanyika ikiwemo mifugo yao, ardhi yao waliyokuwa wanaitumia. Kwa hiyo, watakapokuwa wameenda kwenye makazi mapya yatazingatiwa hayo ikiwemo kutengewa maeneo ya mifugo lakini kwenye suala hili la uvuvi sheria za uhifadhi zitaongozwa kwa sababu maeneo ambayo tunaenda kuyatwaa mengi tutakuwa tunayahifadhi. Kwa hiyo tutaangalia utaratibu unasemaje ili tuweze kukaa pamoja na wavuvi waweze kuangaliwa. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; Mkoa wa Mara ni kati ya Mikoa iliyokaa kimkakati ukizingatia ni Mkoa uliomtoa Muasisi Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.

Je, ni lini Serikali itapeleka Umeme wa REA katika vijiji vyote vya Mkoa wa Mara ukizingatia wakati wakiomba kura Mama yetu Samia Suluhu Hassan na Hayati Magufuli waliahidi kwamba vijiji vyote vilivyobaki vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza mradi kabambe wa kupeleka umeme kwenye vijiji unaoitwa REA III Round Two unaendelea katika vijiji vyote nchini, na Mkoa wa Mara ni mmojawapo kati ya maeneo hayo. Na ninakumbuka mkandarasi anayepeleka umeme katika maeneo haya anaitwa Giza Cables, anapeleka umeme katika Mikoa ya Manyara na Mara, na tunatarajia kufikia Desemba mwaka huu vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme vitakuwa vimefikiwa na umeme kwa mkataba tuliokuwa nao na tunasimamia kwa karibu kabisa kwa sababu pesa tunayo na kazi inaendelea.