Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Agnes Mathew Marwa (7 total)

MHE. AGNESS M. MARWA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la dawa katika Hospitali ya Manyamanyama iliyoko Wilayani Bunda na hii ni kutokana na hospitali hiyo kutokuwa na hati rasmi ya kuwa Hospitali ya Wilaya:-
(a) Je, ni lini Serikali itaipa Hospitali ya Manyamanyama Hati rasmi ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili kuongeza mgao wa dawa na kupunguza shida kubwa wanayoipata wananchi?
(b) Je, ni lini Serikali itaongeza Waganga na Wauguzi katika hospitali hiyo ili kuongeza ufanisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Manyamanyama hakijakidhi vigezo vya kupewa hati ya kuwa Hospitali ya Wilaya kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na timu ya ukaguzi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto uliofanyika mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu uliobainika ni pamoja na ukosefu wa jengo la utawala; jengo la huduma za mionzi; jengo la kliniki ya macho; jengo la huduma za dharura; jengo la kufulia; ujenzi wa wodi ya upasuaji ya wanaume na wanawake; jengo la ufundi wa vifaa vya hospitali kwa maana (karakana); jengo la kuhifadhia maiti na nyumba za watumishi. Hivyo, kituo hicho kitapata hadhi ya kuwa hospitali endapo miundombinu yote inayohitajika itakamilika ili huduma za msingi zenye hadhi ya hospitali ziweze kutolewa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya watumishi wa afya katika Kituo cha Afya Manyamanyama ni 165, watumishi waliopo ni 78 na upungufu ni watumishi 87. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kituo kimepokea watumishi watano (5) akiwemo Daktari mmoja. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi wa afya 48 ili kupunguza pengo hilo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. AGNESS M. MARWA) aliuliza:-

Wananchi wengi walibomolewa nyumba zao na Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo, Mkoani Tarime na wengine hawajalipwa fidia ya maeneo yao mpaka sasa. Aidha, Mgodi huo pia umeanza kuchimba chini ya ardhi ya maeneo ya watu (underground mining):-

Je, ni lini Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa ambalo limeulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kusimamia sekta ya madini kwa kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miradi na uendelezaji wa migodi inatake kufanyika na kulazimika kupisha maeneo yao wanalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na wanapewa makazi mbadala ambayo yana hali bora kuliko makazi waliyokuwa nayo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uthaminishaji katika maeneo yanayozunguka Mgodi wa North Mara na ulipaji wa fidia umegawanyika katika awamu nyingi kwa kuzingatia vijiji husika kuridhia. Kijiji cha Nyabirama wakazi wake waliothaminiwa wote walilipwa fedha zao isipokuwa wakazi 138 ambao fidia yao iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 3 waliikataa na hundi zao zilitolewa na mgodi na ziko kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Tarime. Eneo la Kijiji cha Nyabichune lilithaminiwa katika awamu ya 47 lakini wananchi walikataa fidia husika iliyoidhinishwa. Aidha, eneo la Mrwambe lilithaminiwa katika awamu ya 30, 32, 32A na 32B na taarifa yake bado haijaridhiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Taarifa hiyo ikisharidhiwa itawasilishwa kwa mwekezaji ili aweze kufidia wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Nyamichele ambacho nacho kina waathirika ambao wanatakiwa kufidiwa kuna changamoto ya uwepo wa taarifa mbili tofauti za uthaminishaji. Katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mara tumekubaliana ifanyike tathmini mpya katika eneo hilo. Pia uthaminishaji utafanyika katika eneo tengefu la mita 200 (buffer zone 200 meters) lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa maji ya kemikali na mabaki yanayotokana na shughuli ya uchenjuaji wa madini unaofanyika mgodini hapo. Kazi hii ikikamilika wahusika watalipwa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji kutoka uchimbaji wa wazi (open pit) kwenda kwenye uchimbaji wa chini (underground mining), uamuzi huo ulifanyika baada ya mgodi kufanya utafiti ulioonesha kuwa ilikuwa ni rahisi kutumia njia hiyo badala ya kuendelea na mgodi wa wazi. Niwatoe shaka wananchi wa Tarime kuwa Wizara yangu inafuatilia kwa karibu uchimbaji wa underground unaofanyika hivi leo. Uchimbaji huo unafanyika katika eneo la Gokona kuelekea Nyabigena ndani ya maeneo yao ya zamani ambayo walikuwa wameshachimba toka awali. Hivyo, hakuna eneo ambalo mgodi wa underground unachimba kwenye makazi ya wananchi.
MHE. MARWA R. CHACHA (K.n.y. MHE. AGNESS M. MARWA) aliuliza:-

Nyumba nyingi za Vijijini hazikuwekewa umeme wakati wa usambazaji japo baada ya kuweka umeme kumekuwa na ongezeko la ujenzi wa nyumba na uzalishaji mali kama ujasiriamali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha nyumba zote zilizobaki zinapata umeme kabla mradi wa REA haujamaliza muda wake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kupeleka umeme katika Vijiji vyote Tanzania Bara ifikapo Juni, 2021. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imeweka kipaumbele kwa kusambaza miundombinu ya umeme katika maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme na katika Taasisi zinazotoa huduma za kijamiii kama vile Shule, Zahanati, Makanisa, Misikiti, Vituo vya Afya, Nyumba za Makazi na Biashara na Miradi ya Maji. Utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya III mzunguko wa kwanza ulianza kutekelezwa mwezi Julai, 2018 na unaendelea katika maeneo yote nchini ambapo utekelezaji wake utakamilika ifikapo mwezi Juni, 2019. Maeneo yatakayobaki ikiwa ni pamoja na nyumba za makazi, Taasisi, miradi ya maji na biashara yatapelekewa umeme kupitia mradi wa REA III Mzunguko wa pili utakaoanza kutekelezwa mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mpango huo, Serikali imebuni miradi ya ujazilizi (Densification) kwa lengo la kujaziliza katika mapungufu kwa miradi iliyotangulia. Miradi hii ya ujazilizi inalenga hasa kuhakikisha nyumba zote katika kila Kijiji na Kitongoji zinaendelea kupata umeme. Shirika la Umeme nchini (TANESCO) nalo linaendelea kusambaza na kuunganisha wateja mara kwa baada ya miradi ya REA kukamilika. Ili kuhakikisha wananchi wote wa Vijijini wanaunganishiwa umeme kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000, ahsante sana.
MHE. AGNESS M. MARWA aliuliza:-

Wananchi wengi walibomolewa nyumba zao na Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo, Wilayani Tarime na wengine hawajalipwa fidia ya maeneo yao mpaka sasa. Aidha, mgodi pia umeanza kuchimba chini ya maeneo ya watu (Underground mining):-

Je, ni lini mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi hawa?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia sekta ya madini kwa kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miradi ya uendelezaji migodi inataka kufanyika na kulazimika kupisha maeneo yao wanalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na wanapewa makazi mbadala ambayo yana hali bora zaidi kuliko makazi waliyokuwa nayo awali.

Mheshimiwa Spika, uthaminishaji katika maeneo yanayozunguka mgodi wa North Mara na ulipaji wa fidia umegawanyika katika awamu nyingi kwa kuzingatia vijiji husika kuridhia. Kijiji cha Nyabirama chenye wakazi 1,974 waliothaminiwa katika awamu ya 20, 35 na 42 wote walilipwa fedha zao isipokuwa wakazi 64 ambao fedha yao iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 1.9 waliikataa hundi zao zikabaki Ofisi ya Mkurugenzi Wilaya ya Tarime. Eneo la Nyabichune lilithaminiwa katika awamu ya 47 kwa kuidhinisha shilingi milioni 224 kwa ajili ya watu 69. Wizara iliagiza uthamini wa maeneo hayo ya Kijiji hicho cha Nyabichune urudiwe kwa sababu wananchi wale walionekana wamepunjwa. Mthamini Mkuu wa Serikali ameshakamilisha uthaminishaji wa maeneo 1,838 ambayo tayari umeshawasilishwa kwenye menejimenti ya mgodi kwa hatua zake za ulipaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji toka uchimbaji wa wazi (open pit) kwenda underground mining, uamuzi huo ulifikiwa baada ya mgodi huo kufanya utafiti ulioonesha kuwa gharama ya uchimbaji wa chini zilikuwa ndogo ukilinganisha na uchimbaji wa mgodi wa wazi. Naomba niwatoe shaka wana Tarime kuwa Wizara inafuatilia kwa karibu uchimbaji unaofanyika na mpaka sasa uchimbaji wa underground unafanyika katika eneo la Gokona kuelekea Nyabigena ndani ya maeneo waliyokuwa wakichimba toka awali. Hivyo, hakuna eneo ambalo mgodi wa underground unachimba kwenye makazi ya watu.
MHE. MARY P. CHATANDA (K.n.y. MHE. AGNESS M. MARWA) aliuliza:-

Tangu ujenzi wa barabara ya Makutano, Sanzate hadi Natta uanze umepita muda mrefu bila mkandarasi huyo kukamiisha kazi.

Je, ni lini ujenzi huu wa barabara utakamilika ili kuwaondolea adha wananchi wanaotumia barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makutano Juu – Sanzate – Natta ni sehemu ya barabara ya Makutano Juu – Natta – Mugumu – Loliondo – Mto wa Mbu – Makuyuni yenye urefu wa kilometa 437.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya barabara hii kuanza Makutano Juu-Sanzate kilometa 50 inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na ubia wa Wakandarasi wazawa waitwao M/s Mbutu Bridge JV kwa gharama shilingi bilioni 50.4 na kusimamiwa na Kampuni ya Mshauri Elekezi M/s UWP Consulting (T) Ltd. ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Mshauri Elekezi M/s Consulting Ltd. kutoka Afrika Kusini.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hii ulianza tarehe 5 Aprili, 2013 na ilipaswa kukamilika tarehe 16 Mei, 2015 na aliongezewa muda hadi tarehe 28 Februari, 2019.

Hata hivyo kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya usanifu wa tabaka la msingi wa barabara kutoka usanifu wa awali wa G45 kwenda usanifu tabaka la saruji (CM) kucheleweshwa kwa malipo ya fidia pamoja na mvua nyingi zilizonyesha wakati wa ujenzi huo zilisababisha maradi huu kusimama kwa muda mrefu. Kutokana na changamoto zilizijitokezo wakati wa ujenzi wa barabara hiyo, mkandarasi ameomba muda wa nyongeza utakomwezesha kumaliza ujenzi wa barabara hii mwezi Januari, 2020 ambapo maombi hayo yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa ujenzi wa barabara hii unaendelea vizuri ambapo maendeleo ya kazi kwa ujumla yamefikia asilimia 70.8. Aidha, ujenzi wa daraja kubwa la Kyaramo na madaraja madogo saba katika mradi kusika yamekamilika kwa asilimia 100, hivyo endapo Serikali itaridhia maombi ya mkandarasi kuongezwa muda, inatarajiwa kwamba ujenzi wa barabara hii utakamilika mwezi Januari, 2020.
MHE. AGNES M. MARWA aliuliza: -

Je, ni vikundi vingapi vya wanawake na vijana vimewezeshwa kufanya uvuvi wa vizimba Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kabla sijajibu swali, naomba kwa kifupi sana nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Rais ameweka mtu sahihi, mahali sahihi na kazi itafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Nyegezi Mwanza ilitoa mafunzo ya ufugaji samaki kwa vizimba kwa vijana 288 (wanaume 208 na wanawake 80). Vijana hao walitoka katika Wilaya za Nyamagana – 74; Ilemela – 54; Magu – 31; Misungwi – 21; Ukewere – 51; Sengerema - 28 na Buchosa - 29.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuwawezesha wakuzaji viumbe maji nchini. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 15.1 zitatolewa kwa wafugaji samaki kwa vizimba katika Ziwa Victoria kama mikopo ya pembejeo kwa masharti nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Jumla ya wananchi 3,154 wanatarajiwa kunufaika kwa kupata mikopo ya vizimba, vifaranga na chakula cha samaki. Kati ya hao vijana ni 241, wanawake 290 na kampuni mbili za wanawake. Ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA aliuliza:-

Je, Serikali imewatafutia eneo mbadala wananchi wa Vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitia uhifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali iliamua kutwaa eneo la ghuba ya Speke lenye ukubwa wa ekari 14,250 kwa manufaa ya umma ili kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo ikolojia wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria. Fidia itakayolipwa kwa wananachi husika, itahusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika Eneo la Virian, Kata ya Stoo ambapo wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Halmashauri ya Mji wa Bunda imeandaa mpango wa kutwaa na kulipa fidia maeneo mbadala ya makazi yenye ukubwa wa ekari 1,625 katika maeneo ya Manyamanyama, Bitaraguru, Butakale na Guta. Maeneo yote hayo yatapimwa na kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaotoka Kata ya Nyantwari.