Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Agnes Mathew Marwa (27 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama katika Bunge hili Tukufu siku ya leo. Kwa umuhimu zaidi nawashukuru sana wapiga kura wangu, wanawake wa Mkoa wa Mara, walionipigia kura nyingi sana za kishindo hadi leo hii kuwepo hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru kwa upekee mama yangu mzazi na baba yangu, pamoja na Mashirika ya Kikristo yaliyonifanyia maombi, pamoja na Mashekhe na wanamaombi wote na watu wote wa Mkoa wa Mara waliokuwa wanafurahia leo hii niwe Mbunge. Nawashukuru sana, nawaahidi sitawaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kunukuu kidogo Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sababu sikupata nafasi ya kuongea siku ile. Kwa ruhusa yako naomba ninukuu. Hotuba ya Mheshimiwa Rais iliwakumbusha watumishi wengi wa umma ambao wengi walijisahau wajibu wao, hivyo aliwakumbusha watumishi wengi kuwajibika kwa umma kwa taaluma na weledi kwa kuzingatia usawa bila upendeleo kwa watu wote, bila kujali itikadi ya vyama na dini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, nampongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa hotuba yake ambayo imehimiza kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma (integrity). Hivyo basi, kwa hotuba hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais tunatarajia kwamba kila mtumishi mahali pake pa kazi atimize wajibu wake ipasavyo na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania walio wengi hasa wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kwa kuongelea au kuchangia kwa suala la ujasiriamali. Wajasiriamali au ujasiriamali ni suala ambalo linatakiwa liangaliwe kwa macho ya ziada, kwa maana katika Mpango wa Taifa au Mpango wa Maendeleo, wajasiriamali ndio wanatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa hili; na haswa naanzia na akina mama wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wa Mkoa wa Mara ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, ikiwemo wafanyabishara wa dagaa, ikiwemo wale wanaouza mboga mboga na wengine wa masokoni wananyanyasika sana kutokana na kutozwa ushuru usiokuwa na sababu. Kwa hiyo, naomba tuangalie sana hawa wajasiriamali kwa macho ya huruma, kwa maana na wao wanatoa mchango mkubwa sana katika Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niende kwenye suala la maji. Suala la maji limekuwa ni ni kilio cha kudumu katika Taifa hili la Tanzania. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangazie sana macho yake na itoe kipaumbele katika suala la maji, kwa maana suala la maji limesababisha matatizo na majanga makubwa hasa kwa wanawake wetu wa Mkoa wa Mara, kwa kuvuruga au kuachanishwa kwa ndoa zao kutokana na umbali mrefu wanakwenda kutafuta maji. Vilevile limekuwa likiwasababishia ulemavu wa migongo, limekuwa pia likiwaletea shida sana katika uzazi. Kwa hiyo, kwa namna ya kipekee sana liangaliwe suala la maji na hasa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia naungana na Waheshimiwa walioongea jana, Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Mheshimiwa Lugola, kuhusiana na suala la reli. Ni kweli katika mazingira ya kawaida, utaratibu ambao unatakiwa katika kuunganishwa kwa reli ili nchi ya jirani au ndugu zetu wa jirani wapate unafuu, ni kitu ambacho siyo kizuri sana, kwa sababu kwanza itatupotezea sisi Pato la Taifa na wao kwa ujanja wao, wanachotaka kukifanya ni kwamba wataunganisha kule juu kwa juu nchi nyingine ili malipo haya yasije Tanzania. Kwa hiyo, hilo suala liangaliwe au lipewe kipaumbele, liwe kama lilivyoongelewa na Mheshimiwa Zitto au Mheshimiwa Lugola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie sana suala la polisi kuhusiana na makazi au vituo vya kazi. Vituo vya kazi na masuala ya makazi ya polisi wetu imekuwa ni shida sana. Hivyo, Serikali ingechukua taratibu za ziada ili iingie mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa ili kuwajengea nyumba za kudumu hata baadaye watakapomaliza kuzilipa ziwe za kwao hata pale wanapokuwa hawapo kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba ndugu zangu wa upinzani, tumtie moyo Rais wetu Mheshimiwa Magufuli. Ameanza vizuri. Siyo kila kitu tunaongea maneno machafu, maneno ya kashfa, maneno ya dharau, kiasi kwamba hata wewe ukiombwa kitu huwezi ukakubali kama mtu ameongea maneno ya dharau. Hata Mwenyezi Mungu anatoa pale unapomsifia; ndiyo maana unasema; “Baba yetu uliye Mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimie, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni,” ukimaliza unampiga kibao Mungu, halafu ndiyo unamwomba, “utupe riziki yetu ya kila siku.” Siyo ninyi kila siku mnatoa matusi tu. Kesho msipofanyiwa maendeleo mnalalamika.
Ndugu zangu Wapinzani nawaomba sana; mmefanyiwa mambo mengi sana kwenye Majimbo yenu kuliko hata sisi wa CCM. Mfano ni Arusha au Mkoa wa Kilimanjaro, uko wazi kabisa, mmefanyiwa mambo mengi mazuri, hata barabara mlizonazo ni kama barabara za Kimataifa, mikoani kwetu, hatuna. Mnatakiwa muwe na Shukurani, lakini pia mnatakiwa mkubali kwamba aliyeshinda, kashinda, ninyi mmeshindwa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi hii. Kwa kweli utendaji wake umetukuka, kuna haja ya kumsifia na kumfagilia sana sana. Pia nampongeza sana Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu. Mheshimiwa Rais tunamwita Bulldozer, sijui yeye tutamwitaje? Maana ni baba zaidi ya Baba. Anapiga kazi kuliko chochote. Yeye tumwongezee tumwite Tingatinga. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu, anastahili pongezi za hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia katika Wizara ya Uvuvi. Hili suala la uvuvi kwa kweli linawaumiza wananchi wengi sana na limewakosesha wananchi wengi sana ajira kwa uonevu ambao uko wazi kabisa na Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi anapaswa akae na Watendaji wake au wale wadau wa uvuvi ili wamweleweshe kwa undani zaidi, inawezekana kuna mambo mengine hayajui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nilikuwa ni mvuvi. Kwa uvuvi wa dagaa ukisema ile milimita nane, ni milimita nane ile inavua wale furu wadogo wadogo, siyo dagaa. Labda kama sasa tunaambiwa tusile dagaa, dagaa wawe chakula cha samaki. Kwa hiyo, hili suala kwa kweli halikubaliki kabisa kwa kuwaonea hawa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai kwamba uvuvi haramu ni kweli kabisa haukubaliki, nasi tunahitaji tule samaki wakubwa. Sasa imefikia hatua uonevu umepitiliza, umekithiri, umevuka mipaka. Hawa watendaji wanatakiwa waangaliwe kwa undani zaidi. Naweza kusema nao pia ni Wapinzani kwa sababu siyo kweli kwamba yaani wao wanawaonea tu wananchi wakati wao wanafanya utekelezaji wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye suala la afya. Kwenye suala la afya, nazidi kusisitiza katika bajeti ya Serikali muiangalie sana Hospitali yetu ya Rufaa, Hospitali yetu ya Mkoa wa Mara ili izidi kuboreshwa na iishe kwa haraka zaidi ili kusudi wananchi wa Mkoa wa Mara na majirani zetu wapate huduma nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Hospitali ya Wilaya ya Bunda, Hospitali ya DDH. Kulikuwa kuna malipo ya wafanyakazi ambao baada ya kwenda kuwasikiliza, nilikuta wana madai. Yale madai yalikuwa ni kipindi kile cha uhakiki wa vyeti, bahati nzuri naishukuru sana Serikali yangu sikivu ilisikiliza na wakaanza kulipwa mishahara. Ila walipoanza kulipwa mishahara kulikuwa kuna malimbikizo yao ya miezi kama mitano, minne hivi ambayo hawajalipwa na mpaka leo hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimsikia juzi juzi tu Mheshimiwa Rais akisema ametoa pesa ambazo zinatakiwa zilipe madeni au mabaki ya watu au wafanyakazi wanaodai madeni yao. Hao wafanyakazi wa DDH ni kati ya wale wanaodai hayo madeni. Basi naiomba Serikali iliangalie sana hili, wakalipwe hayo madeni yao wafanyakazi wa DDH hospitalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye suala la madini. Bado nampongeza tena na tena Mheshimiwa wetu Waziri Mkuu maana tulizunguka naye kwa kweli kwa vijiji vya Mkoa wa Mara sana, mpaka alikula ugali wa mtama kwenye nyumba ya bibi mmoja hivi wa Mkoa wa Mara, ule ugali wetu mkubwa pamoja na furu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya. Nilifika naye mpaka kule kwenyeJimbo langu la Nyamongo. Nasema Jimbo la Nyamongo kwa sababu mimi ndio Rais wa Wabunge wa Mkoa wa Mara. Kwa hiyo, Majimbo yote yangu. Tulifika naye kule, akaenda kuangalia matatizo ya wale wananchi. Baada ya kuangalia matatizo ya wale wananchi kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukua hatua za haraka kuongea na wale wawekezaji na kufanya mambo mengine ambayo yanatakiwa wale wananchi walipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, hili suala limetumia muda mrefu sana na ndiyo maana leo nalisisitiza hapa, naamini Serikali yangu ni sikivu, basi wale wawekezaji ambao tunawapenda sana Tanzania kwa sababu wanaongeza kipato cha nchi, lakini sasa wasipitilize wakawa wao wameota mapembe. Kule kwetu tunaita kuota mbhekela yaani kuota mapembe. Kwa hiyo, tunaomba wasiote mapembe kwa maana ya kwamba wasifanye uonevu sana kwa wananchi, basi wawalipe fidia yao wale wananchi wa Nyamongo kule mgodini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye suala la maji. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iangalie sana Mkoa wetu wa Mara na hasa katika Wilaya yangu ya Serengeti, Bunda, Tarime, Musoma Vijijini, Rorya na kwingineko kwa maana ya kwamba suala la maji limekuwa ni muhtasari ambao unaandikwa na mtoto wa darasa la kwanza. Kwa maana ya kwamba sisi tuna Ziwa la Victoria ambalo linatuzunguka lakini maji yanatoka pale kwetu Musoma, yanatoka pale kwetu Ziwa Victoria yanapelekwa wilaya nyingine au mkoa mwingine, wakati sisi pale pale ndiyo wenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, wewe ndio mke wa kwanza, lakini mke wa pili anapewa nyumba ya urithi wakati wewe mke wa kwanza ndio unapaswa kupata urithi wote. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ingalie sana hili suala la maji kwa kweli kwani Mkoa wa Mara tuna haki kabisa kwanza ya kuenziwa kutokana na kwamba sisi ndio tulikuwa na Mwasisi wa Taifa hili au Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo, tunapaswa kuenziwa kwa kutokosa umeme wa REA, ukipita tunatakiwa tupate, maji tunatakiwa tupate, basi hata ikiwezekana Mkoa wetu wa Mara uwe Mkoa wa maonyesho kwamba huu ndiyo Mkoa aliotoka Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni kuhusu Serikali kuangalia Watendaji wa Vijiji na Kata wa darasa la saba waliotolewa kazini. Naomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi; Mheshimiwa Waziri Mkuu amfikishie Mheshimiwa Rais haya maombi yetu kwamba hawa Watendaji wa darasa la saba ni tumetoka nao mbali sana. Wengi wao wanakaribia kumaliza muda wao na wengine wanakaribia kustaafu. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, warudishwe kazini hao Watendaji wa Darasa la VII kwa sababu sasa watakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametutoa mbali, kwa sababu hawa Watendaji ndio waliotusababisha kujenga Shule za Kata, kujenga hospitali zetu na vituo vyetu vya afya. Kwa hiyo, tunapowaacha njiani namna hii, ni kama vile tumewatia jiti wakati wamesimama, tena jiti lenyewe la machoni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu hili suala tunapaswa kuliangalia kwa undani zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuangalia sana kwa undani hili suala la watu wanaoishi na VVU. Kwa kweli mmetoa msaada mkubwa sana, Wizara ya Afya imewapa kipaumbele hawa wagonjwa wa VVU, lakini kipekee kama inawezekana kwa sababu sasa hivi ni watu ambao wanajitambua sasa; katika mikoa yote na wilaya zote ukiwemo Mkoa wangu wa Mara wana vikundi vyao vya ujasiriamali mdogo mdogo. Basi zile asilimia kumi ambazo zinakwenda kwenye Halmashauri, waangaliwe angalau nao wawe wanakopeshwa. Wanafanya biashara zao au shughuli zao ndogo ndogo ili kusudi waweze kujiwezesha kwa vitu vya dharura ambavyo vinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, nawashukuru sana ndugu zangu wa Upinzani kwa sababu kwa kweli wameongea kitu kizuri sana hata mimi kimenigusa. Sasa kutokana na kwamba na wao ni kati ya watu wanaohamasisha, tusitumie vibaya pesa za Serikali, kuliko kusema tena tuanze huu mchakato wa Katiba kwa sababu ni mchakato ambao sisi Wabunge tutakaa chini na watu wengine kuongelea habari za Katiba, tutakuwa tunalipwa hapa chini. Nafikiri wazo aliloongea pale Mheshimiwa Cecilia Paresso, kwa kweli ni zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nawashauri na kuwaomba kwamba sasa wao wahame tu kwenye hicho Chama chao, wahamie CCM haya mambo yaishe, ionekane moja kwamba CCM ni chama kimoja, kwa sababu inaonekana hata wao wameshakubali kwamba CCM ndiyo chama kimoja, kuliko tukaanza malumbano huku ndani, mara tuandike sijui barua, mara vitu gani, au mmoja kati yao ajitolee basi aandike pale barua aitume kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akishaituma pale kwa Msajili wa Vyama vya siasa, basi itakuwa ime…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii ili nichangie Wizara hii kwa sababu na mimi pia ni mvuvi. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwatetea Watanzania na kuwajali Watanzania na hasa Watanzania masikini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuchaguliwa katika Wizara hii. Kipekee zaidi nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii na Wataalam wake kwa kuwasababishia Watanzania umaskini uliokithiri na hasa Watanzania wafugaji, narudia. Nimpongeze sana Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na wataalam wake kwa kuwasababishia wavuvi wa Tanzania umaskini uliokithiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea na mengine nianze kwa kuishauri Serikali. Kutokana na mapato waliyofanya na hasa yale waliyofanya baadhi yao ya unyang’anyi kwa wavuvi hawa niiombe Serikali sasa imuagize CAG aende akakague hizo pesa walizowanyang’anya hawa wavuvi ili iweze kufanya maendeleo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili niishauri pia Serikali kwamba kutokana na kwamba, tuna matatizo mengi sana ya maji, elimu na mambo mengine Wizara hii safari hii kwa bajeti hii isipewe pesa, hiyo pesa iende kwenye elimu na mambo mengine, kwa sababu pesa waliyokusanya, ukisema uwaongezee pesa nyingine ni kwa ajili ya kusafiri na kwenda kuwapiga mabomu ndani ya bahari na ndani ya ziwa wavuvi na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Mpina ananisikia na narudia tena kumwambia Mheshimiwa Mpina ameingizwa chaka na Waziri Mkuu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameingizwa chaka na Katibu Mkuu wake pamoja na hawa wasaidizi wake, kwa nini, Katibu Mkuu, yeye ni Mtaalam wa mambo haya na ndiyo maana amechaguliwa kuwa Katibu kwa sababu yeye kasomea. Hata kama Waziri hajasomea mambo haya ya uvuvi basi Katibu Mkuu na wataalam wake wanaelewa; lakini kwa nini wanafanya vitu bila kuangalia shida au matatizo yanayowapata wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ndio wapiga kura wetu, hawa ndio wapiga kura wa Mheshimiwa Magufuli. Naamini kabisa hata Mheshimiwa Dkt. Magufuli jinsi alivyo active Mheshimiwa Rais wetu akinisikia leo atatuma tume haraka sana iende kuangalia haya mambo, kwa sababu hiki tunachokilalamikia hata Mheshimiwa Rais wakati mwingine haelewi ni nini kinachoendelea huko ziwani. Ni kama wakati ule wa operation ya bomoa bomoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa operation ya bomoa bomoa kuna watu walivyosikia tu bomoa bomoa wakaingia na wengine ambao hata hawakuwa wanafanya au wanabomoa kihalali wakaanza kubomoa hovyo hovyo. Hata hivyo Mheshimiwa Rais kwa sababu ya kuwajali Watanzania, aliposikia vizuri na aliposikiliza kwamba watu hawa wanaonewa alienda kuangalia na kweli sasa watu hawaonewi tena. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Rais hili suala alichukulie kwa umakini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe Bunge lako Tukufu liunde kamati kwa ajili ya uchunguzi wa haya masuala ya uvuvi ili kusudi tuwasaidie wavuvi hawa. Wanaumia, wanaumizwa sana, kwa sababu kuna baadhi yao wanachomewa nyumba, wanachomewa nyavu, lakini bila sababu za msingi. Tunakubali kwamba sheria zipo na sheria zenyewe tulizitunga sisi wenyewe, lakini wanapitiliza sasa wanavuka wanaenda nje ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe sana Serikali iliangalie hili suala kwa umuhimu zaidi; kwa sababu kuna mambo mengine yanatokea kwa mfano Mheshimiwa Waziri leo amesema kwamba milipuko imepungua kwa wavuvi haramu. Ni kweli kabisa Mheshimiwa Waziri milipuko imepungua kwa wavuvi haramu, lakini milipuko imeongezeka kwa wale wataalam wake wale wanaokwenda kule kwenye operation.

Mheshimiwa Naibu Spika, wao sasa ndio kabla hawajaenda kuwakamata wavuvi wanaanza kulipua mabomu. Hivi lengo lao ni kwenda kuwakamata au lengo lao ni kuwauwa wananchi? Hali ngumu Mheshimiwa Waziri, wananchi wana maisha magumu, kwa hiyo wananchi wengi sasa hivi wana ugonjwa wa pressure, sukari; hivi wanaposikia yale mabomu wanajisikiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya masuala yananiuma sana kwa sababu na mimi nimetokea kwa wavuvi, hawa wavuvi wanapata shida. Wavuvi wa nchi hii, fikiria ukianzia Zanzibar, Dar-es-Salaam, Mara na sehemu nyingine, huu ni uonevu unaopitiliza. Hebu Serikali ichukue hatua za lazima waende wakasaidiwe, waende wakaangaliwe, kwa sababu haya mambo yanayofanywa ni mambo ambayo ni ya uonevu tena uonevu uliokithiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri Mpina, anaona hii Wizara hawezi kuitendea haki Mheshimiwa Mpina amwambie tu Mheshimiwa Rais atoke ili kusudi amchague mvuvi kabisa aende akaangalie haya mambo anaelewa uvuvi. Wakinichagua hata mimi ambaye sijasomea hayo mambo kwa sababu, nilikuwa mvuvi naweza, kuliko hawa wataalam wanadanganya, wanakudanganya.

mimi najua wanamwingiza chaka, Mheshimiwa Mpina ni mtendaji mzuri, lakini wanamwingiza chaka kuna mambo mengine alitakiwa, kwa mfano… (Makofi)

TAARIFA . . .

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa mfano bei za nyavu zile nyavu zinazohitajika kuvuliwa dagaa au samaki zilikuwa kati ya Sh.16,000/= lakini sasa hivi zimefika Sh.45,000/=. Pia kuna maboya ambayo kwa bundle ilikuwa ni Sh.30,000/= lakini sasa ni Sh.130,000/=. Kwa hiyo inaonesha ni jinsi gani haya mambo sasa yanavyokuwa ni magumu kwa hawa wavuvi. Wanachomewa vitu vyao, lakini pia bado wanapewa, wanawekewa tozo nyingi zisizokuwa na sababu au na maana. Pia kuna gharama nyingine ambazo kwa kweli zinakuwa ngumu sana kwa wavuvi na hasa wale wa hali ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kama hii leseni kweli aliitoa yeye kwa huyu mfanyabiashara ambaye ni mmoja tu anayetoa na kuuza nyavu hizi; yule Mhindi ambaye yuko Arusha, Mheshimiwa Waziri akaongee naye sasa arekebishe hizi bei kwa sababu hizi bei zinawaumiza hawa wananchi. Kwa hiyo itabidi waendelee angalau kutumia zile, watatumia hata vile vyandarua ambavyo wanapewa wajawazito na watoto wadogo kwa sababu inakuwa ni ngumu sasa kuzinunua ni bei ghali. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hili suala aliangalie ili kusudi hawa wananchi waweze ku-afford kununua hizi nyavu kwa ajili ya shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni mtoto wa mkulima na ni mchapakazi. Mheshimiwa Waziri hili suala la uvuvi na hasa hawa wanaotoza ushuru kwenye magari au wanaotoza ushuru hawa samaki hata yeye mwenyewe anaweza tu akaliangalia hili suala, kwa sababu kwa mfano kuna vibambala. Mheshimiwa Waziri vibambala wale huwa ni samaki wakubwa ambao ni wale Sangara wakubwa kidogo huwa wanataka kuwa kama reject, samaki ambao si fresh sana lakini ni samaki ambao hawaingii kiwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wale wananchi wanatengeneza vibambala, si samaki wadogo. Sasa Mheshimiwa Waziri kama hata hawa samaki vibambala wanakamatwa na wanatozwa ushuru anategemea nini , kwamba sasa tutakula nini. Au wananchi hawa wafanyabiashara, maana hivyo vibambala wanaouza wengi wao ni wale wamama wajasiriamali wadogo wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afuatilie haya masuala kwa ukaribu kama nilivyoshauri, kwamba iundwe kamati maalum toka Bungeni ili iende ikasimamie na kushughulikia haya mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi juzi kuna gari ilikamatwa la kuku. Kuku wana ushuru, hapo Singida. Kuku wamekatiwa ushuru, kutoka tu kituo kimoja kwenda kituo kingine wanataka ushuru mwingine, kutoka kituo kimoja tena kwenda kingine wanataka ushuru mwingine. Mheshimiwa Waziri hivi kweli hata kama ndiyo operation hii ni operation chukua pesa au operation tokomeza? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri hili suala aliangalie sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lile la hawa hawa wafanyabiashara wenye mitumbwi. Kwenye mtumbwi anakuwepo boss na wafanyakazi wake. Kwa mfano anakuwepo boss mwenye mitumbwi na wafanyakazi wanaopanda mle kwenye boti wanaokwenda kuvua wanakuwa watano hadi kumi. Sasa kila mmoja anatakiwa awe na leseni, boss awe na leseni, wale 10 ambao pia ni wavuvi wake wanatakiwa kila mmoja awe na leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mheshimiwa Waziri katika mazingira haya inakuwaje? Ni kwamba sasa hata kama, mimi siamini kama Mheshimiwa Rais kweli atakubaliana na hili suala kwamba kila mwananchi, hata yule ambaye anaajiriwa aende akakatiwe leseni. Hiyo leseni yeye anaifanyia kazi gani wakati boss wake ana leseni? Au siku hizi labda kuna leseni za vibarua ili uajiriwe lazima uwe na leseni ndipo uajiriwe. Hata kazi za kuvua samaki, hata kazi za kuuza dagaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ndivyo basi tunatakiwa hata sisi tuwe na leseni. Mheshimiwa Spika anatakiwa awe na leseni, wewe Naibu unatakiwa uwe na leseni, sisi Wabunge tunatakiwa tuwe tuna leseni ili kusudi ndipo tuingie bungeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunijalia kuchangia siku ya leo katika Wizara ya Afya. Namshukuru kwa nafasi ya kipekee Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya yeye na Serikali nzima, kwa kuonesha kwamba anaweza na kwa kuonesha kwamba sasa Tanzania mpya yenye matumaini inawezekana.
Meshimiwa Mwenyekiti, Mkoani kwangu Mara kuna matatizo makubwa sana ya vituo vya afya, ukizingatia kwamba Mkoa wa Mara umepakana na mipaka mingi ambayo wenzetu wa nchi za jirani pia wanategemea huduma za afya kutokana na Mkoa wetu wa Mara. Kwa mfano, Wilaya ya Tarime kwa sasa imegawanyika katika sehemu mbili; tuna Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya. Hospitali tuliyonayo ni moja tu, ambayo haikidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu waliopo Wilayani hapo Tarime. Kutokana na hali halisi ya matatizo hayo ya hospitali, Mgodi wa Acacia uliopo Wilayani Tarime, ambao uko chini ya North Mara wameamua kutujengea Kituo cha Afya katika Kijiji cha Nyamwaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kaka yangu Mheshimiwa Luoga, alikaa nao chini wakafanya maongezi, pamoja na Halmashauri ya Tarime. Wakaongea wakakubaliana kwamba badala ya kutengeneza au kujenga Kituo cha Afya, wakakubaliana kwa majengo yale yale na kwa gharama zile zile, tuiombe Serikali ikubali majengo yale baadaye yawe Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa dada yangu Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla bahati nzuri mpo hapa, nawaomba watukubalie Wilaya ya Tarime, yale majengo yatakayojengwa na Kampuni ya Acacia yawe ni Hospitali ya Wilaya kwa sababu wamejitolea wao wenyewe. Kwa hiyo, pia yanakuwa yametusaidia sisi kupunguza gharama ambazo tungezipata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya kipekee zaidi, kama mnakumbuka, naamini hata Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliopita wameiongelea sana Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kwangwa. Hospitali ya Kwangwa ilikuwepo hata kabla hatujazaliwa, tunasikia historia yake. Kama mnavyojua, Mkoa wa Mara kuna matatizo mengi sana, ukizingatia kule kwetu kulikuwa na mfumo dume ambao hadi sasa haujakwisha, kwa hiyo, kuna matukio mengi sana ambayo yanategemeana na Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma Hospitali ya Kwangwa, wanawake, watoto na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kwa ujumla wanapata shida sana. Tangu mwaka 2012, mkoa ulikuwa unaomba shilingi bilioni mbili na point, lakini hizo fedha zilikuwa hazifiki kama zilivyokuwa zinaombwa. Toka kipindi cha mwaka 2012, mwisho imekuwa 2013; na mwaka 2014, Serikali imejitahidi kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mara, wamejenga hospitali, imefikia ilipofikia, lakini mpaka sasa imekuwa kitendawili; na fedha ambayo imeshatoka ilikuwa ni sh. 3,334,967,000/= na fedha nyingine za kipindi hicho bado hazijatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu zaidi, wananchi wa Mkoa wa Mara, kwa kuiona Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina umuhimu, pamoja na kuwa baadhi ya Majimbo wamewachagua Wabunge wa Upinzani, lakini Rais wetu aliongoza kwa kura za kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Rais aiangalie sasa hospitali ya Mkoa wa Mara ili sasa ifikie mwisho kwa sababu ni hospitali ambayo inaweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini pia ikapunguza matatizo ya wananchi wa Mkoa wa Mara kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mkoa wa Mwanza, wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza pia inazidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, wananchi wa Mkoa wa Mara wengi wao akinamama ndiyo wanaotunza familia zao na akinamama hao hawana vipato vya kutosha; wanakosa hata nauli ya kuwatoa kutoka Mkoa wa Mara kwenda Mwanza. Kwa nini hili suala Serikali isiliangalie kwa nafasi ya kipekee zaidi ili hospitali hiyo itengewe sasa kiwango cha kutosha ili kuisaidia japo ianze kufanya kazi, hata kama majengo mengine yatakuwa bado, basi yatamaliziwa baadaye, lakini ianze kazi, iitwe Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, baada ya Bunge, kama inawezekana twende wote Wilayani Tarime, aende akaangalie yale majengo ambayo Acacia imeshakubali kujenga ili muipe hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kwa nafasi ya kipekee sana, kuna wanawake wenzetu ambao ni ma-nurse mishahara yao ni midogo sana, haitoshi. Mwaangalie na mwaongezee mishahara. Pia Wizara ya Afya kwa ujumla muiangalie bajeti yake iongezwe kwani bajeti iliyopo ni ndogo sana, haitoshi kukidhi mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi nyingine tena ya ziada, nasema MSD ni jipu kwa sababu, ni kweli kuna baadhi ya maeneo wanakosa pesa ya kuwalipa, lakini kwa mfano Wilayani Serengeti wametenga bajeti ya kuwalipa lakini wao madawa ndiyo hawana. Kwa hiyo, naomba kama inawezekana, urudishwe utaratibu wa zamani, twende tukanunue madawa au hospitali ziruhusiwe kununua madawa kwenye maduka makubwa ya wengine, ambapo madawa yanapatikana, kuliko wananchi wetu wanakufa wakati madawa hakuna MSD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusiana na Bima ya Afya, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida sana na wamekuwa mstari wa mbele kujiunga na Bima ya Afya. Katika mazingira ya kawaida, unapojiandikisha, kwa mfano umejiandikishia hapa hapa Bungeni, ukienda kituo kingine huwezi kutibiwa. Kwa hiyo, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara wanapata shida. Mwanamke akijiandikishia Nyamongo mgodini au akijiandikishia Mtaa wa Mkendo, hawezi kwenda kutibiwa Mtaa wa Ilingo, kwa sababu Bima yake inaishia kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Nape Nnauye kwa jinsi alivyoanza vizuri katika Wizara yake, anaonesha ni jinsi gani anavyopenda michezo na jinsi gani anavyoiweza Wizara hii kwa sababu anaonekana kabisa kwamba anaitendea haki, Mheshimiwa kaka Nape tunakutia moyo, watu wasikuvunje moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee sana naomba niongelee kuhusu suala la Miss Tanzania. Miss Tanzania ni kati ya sanaa inayoitangaza nchi yetu, ni kweli kwamba kulikuwa kuna madoa ambayo wanapaswa kurekebisha, wanatakiwa wayarekebishe, lakini Mheshimiwa Waziri unatakiwa ukae nao, wewe na Wizara yako kuweka sawa ili sanaa hii isipotee, waendelee kuonesha mashindano ya Miss Tanzania kwa sababu ni kati ya mashindano yanayoitangaza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za wasanii ni kazi ambazo zinapaswa kutetewa sana na Waheshimiwa Wabunge na nchi kwa ujumla. Nchi za wenzetu sanaa ndiyo inayoleta uchumi wa nchi, kwa mfano Nigeria na nchi nyingine, sanaa ni kitu cha muhimu sana.
Kwa hiyo, tunatakiwa tuangalie wasanii kwa macho mawili au kwa macho ya mbele zaidi ili tuwape moyo wasanii wetu. Tuangalie kazi zao, tuangalie jinsi ya kutengeneza utaratibu ili jasho lao na kazi zao zionekane, wasiwe wanafanya kazi halafu watu wanatoka tu huko pembeni, wanapata pesa kutokana na jasho la wasanii. Namuomba sana Mheshimiwa Rais awaangalie wasanii hawa kwa macho ya huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wasanii wa Tanzania wako chini sana, wanadharaulika sana ni kwa sababu hawana mtetezi. Mheshimiwa Waziri uliangalie sana hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee zaidi narudi kwenye suala la kuonesha matangazo ya Bunge live. Kuhusiana na suala la kuonesha matangazo ya Bunge live hii ilipelekea Wabunge tukawa (Wabunge waliopita) maana nisiseme tukawa sikuwepo kipindi hicho, mimi pia nilikuwa naagalia televisheni. Wabunge walikuwa wanakaa tu hapa kwenye tv wakiuza sura hapo! Hawaendi kufanya kazi majimboni mwao! Kwa hiyo, ni suala ambalo wananchi wanatakiwa waelewe, utaratibu huu umefanyika ili kuwarudisha Wabunge waende kufanya kazi majimboni mwao! Siyo wanang‟ang‟ania kuonekana kwenye tv! Wanataka waonekane ili iweje? Mkitaka muonekane nendeni mfanye kazi majimboni kwenu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu mbaya sana, Wabunge tunawadanganya wananchi kwa sababu wananchi hawajui. Sasa hivi mnaonekana majimboni kwani uwongo? Mnakwenda majimboni sasa hivi na mnatakiwa muende mkafanyekazi majimboni! Siyo mnadanganya wananchi waungane na ninyi wawa-support eti ooh, Serikali ya CCM, Serikali ya CCM haitaki muone maovu! Maovu mbona ninyi ni waovu kuliko mtu yeyote!
Mheshimiwa Naibu Spika, natamani hata kulia! Mnatutia aibu! Najisikia uchungu sana! Mnadanganya wananchi….
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana ndugu zangu wananchi waliotuchagua waelewe kwamba huu utaratibu katika mazingira ya kawaida ni kweli, wanaweza wasielewe lakini waelewe kwamba sasa hivi Wabunge tunatakiwa turudi kwao kufanya kazi na tukae karibu nao wananchi, ndiyo maana na wananchi wanatakiwa na wao wafanye kazi zao watakuwa wanatuangalia kwenye tv baadaye. Utaratibu huu ni mzuri sana na utawafaidisha wananchi na kuwanufaisha, tutakwenda kila siku majimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina la zaidi ahsante sana na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kipekee zaidi naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Muhongo kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli Mheshimiwa Muhongo unastahili sifa na nafasi hiyo ulistahili hasa ndiyo maana umerudishwa tena pamoja na majungu yote yaliyotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuishukuru au kupongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa wanayomsaidia Waziri Muhongo pamoja na Naibu wake kwa sababu kumekuwa kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya wananchi wa Tarime kule mgodini na wawekezaji wa Mgodi wa Acacia. Lakini Mheshimiwa Waziri amekuwa ni chachu kubwa ya kuonyesha yeye anasababisha ule mgogoro unafikia mahali anaumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo basi Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake nilizoziona au wananchi walizoziona Mheshimiwa Waziri alituma watu waende wakaangalie matatizo ya wananchi, Mheshimiwa Waziri alimteua akiwemo Mbunge wa kule kule mgodini kaka yangu Heche na yeye pia alikuwa kati ya watu walioenda kule kuangalia matatizo ya wananchi, kwa hiyo nafikiri mambo yatakuwa mazuri tu nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri endelea hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hapa kwenye mkataba wa Mgodi wa Acacia. Mgodi wa Acacia ulikuwa na leseni ya utafutaji wa madini ndani ya Halmashauri ya Tarime katika Kata ya Turwa na Kinyamanyori. Kwakuwa leseni hiyo muda wake ulishakwisha naiomba Serikali ikabidhi maeneo yale kwa wananchi ili waendelee na uchimbaji mdogo mdogo. Na Serikali kwa mpango wake endelevu iliyonao mzuri wa kuwasaidia hao wachimbaji wadogo wadogo, wachimbaji hao watakaporudishiwa eneo hilo iwasaidie mashine za kisasa kama ilivyo kwa maeneo mengine ili uchimbaji wao uwe na tija na uwanufaishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi zake kubwa sana za kuanzisha mradi wa REA ambao umewasaidia ndugu zetu wengi sana Vijijini ikiwemo Mkoa wa Mara; Mheshimiwa Waziri nikuombe kuna baadhi ya vijiji mkoani Mara ambavyo vimebaki; kwa mfano Wilayani Rorya kuna vijiji vya Kemwame, Kibui, Mkengwa na Baraki Tarafa ya Suba vimekwama baada ya kuwa vimewekewa nguzo toka mwaka 2015 na kinachoendelea wananchi wale hawakijui mpaka sasa hivi wamebaki kwenye sintofahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakapofunga hoja yake anipe majibu juu ya suala hili la umeme, ni lini wananchi wa Wilaya ya Rorya wataupata umeme? Lakini pia anipe majibu ya kuwarudishia wachimbaji wadogo wadogo wa Tarime eneo lao ili nao waifadike nalo? Kwa sababu kuna wachimbaji wengi wadogo wadogo kule ambao wanaitwa tu wachimbaji wadogo wadogo lakini hawana maeneo ya kuchimba kwa sababu yale maeneo ni ya watu, watu ndio wameyamiliki. Kwa hiyo, nikuombe kipekee zaidi unishughulikie sana suala, hili usiliache.
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu zangu wapendwa, Wabunge wenzangu; mwisho naomba kumalizia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao wameniwekea wimbo kwenye simu yangu unasema CHADEMA, CHADEMA peoples power nina imani kabisa ni wale majirani zangu. Lakini watani wangu naomba niwaambie mimi ni nyara ya CCM, kwa hiyo huo wimbo hautafanya chochote. Tunapoingia humu ndani Bungeni bangi tuweke pembeni na kazi tuweke pembeni.
Kwa hiyo, ndugu zangu niwaambie hamtanikatisha tamaa, CCM ina vijana, ina wazee ina watoto ina kila mtu na CCM ni ile ile mwaka 2020 mtaisoma namba. Ahsante mimi ndiye Agness kutoka Mkoa wa Mara, nyara ya CCM ahsanteni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi. Imefikia hatua sasa vijijini watoto wengi wanakwenda shuleni, hakuna watoto wanaokaa majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kipekee nimpongeze Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako. Kwa kweli mama anafanya kazi nzuri sana, tuko nyuma yake na Mungu amsimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Magufuli ampe Mheshimiwa Profesa Ndalichako pesa ya kutosha ili arekebishe mambo mengi ndani ya elimu ili mambo mengine ambayo yanaleta shida ndogo ndogo yakae sawa. Kwa mfano, elimu ya shule za Serikali, shida siyo kwamba eti wanafunzi hawaelewi au Walimu hawafundishi. Hata kama wewe nyumbani kwako ukiwa una njaa huwezi kufundisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iwaangalie hawa Walimu kwa macho mawili kwa sababu Walimu ndiyo wamemfundisha Rais, wamemtoa Mbunge lakini Walimu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niongelee suala la kupandishwa madaraja kwa Walimu. Ni muda mrefu sasa Walimu wanalalamikia suala la kupandishwa madaraja na hasa vijijini. Mkoani kwangu Mara Walimu wengi wanalalamika hawajapandishwa madaraja. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie sana hili kwa macho mengine kwani hawa Walimu wanapopata motisha wanaweza kufundisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine Mkoani kwangu Mara, Wilaya ya Rorya, Kijiji cha Kinesi, Tarafa ya Suba, kuna shule moja ya Isango. Hiyo shule ameuziwa sijui ni mtu gani, tangu mwaka 2014. Shule hiyo ilikuwa inasaidia watoto wengi sana na Mkoa wa Mara tuna uhaba wa shule.

Mheshimiwa Waziri hii kesi iko Mahakamani muda mrefu sana, nimwomba sana alisimamie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Magufuli huko aliko namwomba, yeye ni mtu wa vitendo aangalie suala hili la Shule ya Isango ili irudi mikononi mwa Serikali na wananchi. Wananchi wa Rorya wanaweza wakaiendesha shule ile na wako wadau ambao wako tayari kwa ajili ya kuiendeleza. Sasa hivi imekaa kama gofu wakati Mkoa wa Mara tuna upungufu wa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la ongezeko la tozo chefuchefu kwa hizi shule za watu binafsi. Nasema tozo chefuchefu kwa shule za watu binafsi kwa sababu, hizi shule zimeongeza na kupandisha kiwango cha elimu, kwa hiyo, tunapowawekea kodi nyingi ina maana kwamba tunataka kuwakwamisha wasiendelee au tunawakomesha wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tunawakomesha wananchi kwa sababu hizi tozo zinapokwenda kwa hawa wakuu wa shule au wamiliki wa shule anayezilipa ni mwananchi. Yule Mkuu wa Shule unapomwongezea na yeye zile asilimia anaongeza ada kwa mwananchi. Katika mazingira ya kawaida tunawaonea wananchi, hatuwaonei hawa wenye shule. Kwa hiyo, hili suala tuliangalie mara mbili kwa ajili ya kupandisha kiwango cha elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Waziri wangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, kipekee na-declare interest kwa sababu mimi pia ni mwanafunzi ambaye nimesoma hayo masomo ya QT. Wameongea humu Wabunge wengi lakini hawajaongelea suala hili. Kipekee nimwombe Waziri aangalie vile viwango vya ufaulu vishuke kidogo kwa hawa wanafunzi wanaosoma masomo ya jioni kwa sababu wanapokuwa wanawekewa marks za juu sana na wengi wao ni watu wazima, wanatoka maofisini, wanakuwa wamechoka wanawaza mambo mengine inakuwa ni vigumu kufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri washushe kidogo viwango hivi ili watu wengi wapate moyo wa kusoma. Mheshimiwa Waziri naamini hili atalichukua kwa mikono miwili ili hata wale ambao ni vilaza wenzangu na wao wakasome hii elimu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mara tuna upungufu mkubwa sana wa walimu wa shule za msingi na sekondari na hasa vijijini. Wilaya ya Rorya, Tarime, Serengeti, Bunda, Butiama na Musoma Vijijini, nimwombe sana kiongozi wangu atuongezee Walimu ili wale wanafunzi na wao waweze kufundishwa vizuri. Kwa sababu wanakuwa wanafunzi wengi sana lakini unamkuta mwalimu labda mmoja au wawili. Kwa hiyo, kipekee nimuombe Waziri atusaidie kutupatia Walimu Mkoani Mara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kunipa nafasi hii ya kipekee ili nichangie Wizara hii. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Tizeba kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Wizara yake nzima kwa sababu kwa kuanzia nimeona kwa kweli mnafanya kazi. Kuna mambo ambayo tumewaomba siku si nyingi sana lakini mmeshayarekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama mvuvi; mimi nimetokea kwenye dagaa dagaa kwa hiyo mimi pia ni mvuvi; nimeona hapa kuna baadhi ya tozo tulizokuwa tunazilalamikia. Kwa mfano kuna hii tozo ya movement permit, kuna hizi ada za ukaguzi wa kina wa viwanda na maghala zimepunguzwa, vilevile kuna tozo za vyeti vya afya ambayo ilikuwa inawasambua sana wavuvi hawa. Pamoja na hayo vile vile pia kuna ada za usajili wa vyombo vya uvuvi ambayo ni kati ya vitu ambavyo Mheshimiwa Tizeba na Wizara yake wamevishughulikia, kwa kweli pongezi sana nakupa na Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee bado niendelee kuomba baadhi ya vitu ili waviangalie, pia vipate punguzo kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi hawa au hawa wafanyabiashara wa samaki. Kwa mfano sasa hivi ushuru umeongezwa ambapo gunia moja kutoka shilingi 1000 kwenda shilingi 2000, kitendo kinachowapelekea wale wafanyabiashara kukosa faida ambayo wangeitegemea na faida yao ni kidogo sana. Kwa hiyo, wanapotozwa tozo kubwa inasababisha faida zao kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kipekee nimuombe sana Mheshimiwa Tizeba, Mkoa wetu wa Mara ni Mkoa uliozungukwa na Ziwa Victoria, lakini ni kati ya mikoa ambayo mara kwa mara huwa tunakuwa na upungufu wa chakula. Nimuombe Mheshimiwa Tizeba ashughulikie suala hili kwa kushughulikia kilimo cha irrigation, kwa maana ya kwamba tuwe na kilimo cha kudumu mkoani kwetu ili sasa tuepukane na hili suala la shida ya chakula cha mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala ambalo limezungumziwa jana na Mbunge mwenzangu wa Jimbo la Serengeti, Mheshimiwa Ryoba, kwa kweli Mkoa wa Mara kumekuwa na upungufu wa chakula na ni hali ambayo ipo nchi nzima na dunia nzima ya mabadiliko ya hali ya hali ya hewa. Lakini Mbunge mwenzangu aliongela kwamba chakula sasa hivi hakuna kabisa kwa sababu ya tembo. Mimi nimwambie Mheshimiwa Ryoba, Serikali sikivu, Serikali ya Mheshimiwa Magufuli imeshapeleka chakula mpaka sasa tani 500 na mimi nilimuomba Mheshimiwa Tizeba ambaye aliomba chakula Ofisi ya Waziri Mkuu na wamela na wataleta katika Mikoa mingine yote walioomba. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Ryoba kwa kuwa yeye ni Mbunge wa Serengeti, mimi ni Mbunge wa Mkoa kwa hiyo kuna taarifa nyingine anapaswa kuniambia mimi ili niwe nampa kwa sababu ameshindwa kusimamia wananchi wake na mimi ndiye nasimamia mambo hayo na nimeomba na wameshaleta chakula. (Makofi)

Lakini kutokana na hili suala la tembo, ni kweli linasumbua lakini wanakuja kwa msimu, sio wanakuja siku zote, tembo huwa wanakuja wakati mvua hazinyeshi, yaani wakati wa kiangazi.

T A A R I F A . . .

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei hiyo taarifa kwa sababu Mheshimiwa anaongopa mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, chakula kimeletwa tangu juzi na ripoti ipo, lakini yeye ameomba Mwongozo siku ya jana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ryoba nikuombe unishukuru kwa kazi ninayokufanyia jimboni kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hili suala la tembo. Ni kweli suala sumbufu kwa Wilaya ya Serengeti na Wialaya zingine. Hawa tembo huwa wanakuja wakati wa kiangazi, wakati mvua zikinyesha hakuna tembo anayekuja kutafuta maji kwa sababu huwa wanakuwa wana maji. Hata hivyo Serikali yetu sikivu imelishughulikia pia suala hili na inaendelea kulishughulikia, na mimi niliongozana na Mheshimiwa Ramo Makani, Naibu Waziri kwa ajili ya kufanya mipango jinsi ya kuziba au kuzuia yale maeneo ili hawa tembo wasiwasumbue wananchi. Nafikiri Mheshimiwa siku hiyo sijui alikuwa na mawazo mengi, lakini tulikuwa naye, sijui kama alisahau. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo mimi nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kwamba tukae na tuongee na wananchi wetu, tuwaombe lakini pia tuwaeleweshe kwa sababu ukweli ni kwamba sisi tunapokaa yale maeneo ni maeneo ambayo yamepakana na hifadhi, ambako zile ndizo njia za tembo, kwa mfano, kuna Robanda, Manchila, Kisangula, Sedeko, Mbalibai, Mashoswe, Nata, Mosongo, Nyamatale, Uwanja wa Ndege (maeneo ya Ngalawani), haya yote ni maeneo ya ukanda wa hifadhi. Ki ukweli ni kwamba yale maeneo tunayokaa sisi ni kweli tunaathirika lakini ni maeneo ambayo sisi ndo tumewafuata wale tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niwaombe ndugu zangu Wana-Serengeti, kwa hali hii tuvumilie katika kipindi hiki ambacho Serikali yetu inalishughulikia suala hili, na nina imani kabisa ni suala ambalo litaisha na haya matatizo yote yataisha. Hata hivyo tusiwape imani wananchi wote kwamba eti njaa inaletwa na tembo, kuna maeneo mengine ambayo tembo hawafiki, je, huyu Mheshimiwa ambako tembo hawafiki anawapeleka yeye?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mambo ambayo tunapaswa sisi kuyaongelea kama Wabunge, lakini kuna mambo ambayo hatupaswi kuyalalamikia na kulia kwa muda wote. Tukiwa tunalia sisi wananchi wetu watafanya nini? Tunapaswa sisi tuongee na Serikali yetu kwa lugha ya kuwaonesha au kuwaelekeza kwamba kuna matatizo kwa sababu sisi ndio tunaishi kule, isiwe tu tunakuja tunasema kwamba ooh kuna hiki kuna hiki, kibaya zaidi tunaenda kufanya kule siasa. Wananchi sasa hivi hawataki siasa wanataka vitendo.

Mheshimiwa Mbunge mwenzangu, basi mimi na wewe tujipange, kile chakula kimeshaletwa, twende tukawagawie wananchi wetu kusudi waepukane na hili tatizo lililokuwepo kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongea mabaya na mema pia tuongee. Kuhusu hili hili suala la tembo, kuna fidia ambazo zimeshalipwa na Serikali, sijamsikia Mheshimiwa Mbunge mwenzangu hapa anaisifia Serikali, na bado kuna pesa nyingine ambazo Mheshimiwa Rais ameandaa zitakazokuja kwa awamu nyingine ya pili. Kwa hiyo, wanasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Serikali yetu ni sikivu, Serikali yetu ina nia njema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa bajeti hii iliyosheheni weledi na kuonesha kuwajali wananchi na hasa wananchi wa hali ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali katika bajeti hii iangalie jinsi ya kupata fedha mahali, shilingi hamsini au arobaini ili kumtua mwanamke ndoo kichwani na hasa mwanamke wa kijijini. Kule kwetu Mkoani Mara inafikia hatua wanawake wa kijijini inapofika jioni wanakosa hata hamu ya kuwapa mapenzi waume zao, kwa hiyo, niiombe sana Serikali ijitahidi kwa hili na iliangalie sana suala la maji na ikiwezekana hii pesa ya makinikia basi itakapokuja suala la kwanza liwe ni maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushie suala la ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli lile la shilingi milioni 50 kwa wajasiriamali. Kwa kweli wananchi wetu wanaiulizia sana hiyo pesa na ninaamini Mheshimiwa Magufuli hadi sasa kafikisha asilimia kama 98 hivi ya utekelezaji wake imebakia hiyo asilimia mbili ambayo ni hiyo shilingi milioni hamsini hamsini, Mheshimiwa Magufuli tunaiomba ili kusudi hawa ndugu zetu walale kabisa vitandani wajue hawana chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee zaidi naiomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kushughulikia hili suala la kilimo, basi benki ya kilimo ipewe pesa na Serikali ili wapeleke mitaji vijijini, wananchi wangu wa Mkoa wa Mara mara kwa mara wanalalamika vyakula ni kutokana na hali halisi ya uchumi. Lakini pia ni kutokana hali halisi ya kwamba wanakuwa hawana mtaji na hawana vifaa, kwa mfano, wanatakiwa wakopeshwe na Benki ya Kilimo ili wafanye kilimo cha irrigation, kinaweza kusababisha kupunguza shida na matatizo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia kaka yangu Mheshimiwa Heche akiongea kuhusu suala la kuwaandamanisha wananchi kule mgodini, ni kweli hakuna asiyejua kwamba wananchi wa Tarime kule mgodini wameumia, wamepata makovu, lakini hili suala Serikali imeshalishughulikia kwa kiasi kikubwa sana, lakini pia Mheshimwia Heche anapaswa kujua yale malipo au zile fidia za wale wananchi Mheshimwa Rais muda si mrefu sana wananchi wote watalipwa na Mheshimiwa Magufuli hakubali wananchi wa hali ya chini wanyanyasike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya labda hana ripoti hiyo na mimi ntakapoenda kule kuwakabidhi wale wananchi malipo yao nitamwita Mheshimwa, kwa sababu Jimbo lake sasa hivi amemwachia Mheshimwa DC wa Tarime ndio mwenye Jimbo anaitwa Mheshimiwa Luoga, ikiwezekana Mheshimiwa Rais muangalie sana huyu umpe hata Ukuu wa Mkoa maana kwa kweli ana kazi kubwa sana ya kufanya kule Ubunge badala ya u-DC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Hawa wanaombeza Mheshimiwa Rais kwamba ooh! Sijui ananunua ndege! Mlitaka awanunulie magari ma- vogue ili kusudi muendee Majimboni kwenu. Wananchi wa hali ya chini wanapanda hizi ndege na bei au gharama za ndege zimeshuka na sisi Wabunge tuna uwezo wa kwenda Dar es Salaam kufanya shughuli zetu na asubuhi tukarudi Bungeni. Isitoshe hizo ndege ninyi wenyewe mnazipanda, kila siku tunakutana ndani ya hizo ndege, kwa nini msiache kupanda? (Makofi)

Kwa hiyo, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na kwa taarifa yenu kinakuja kitu kipya tena mwezi ujao. Hiyo ni kuonyesha jinsi gani Mheshimiwa Rais anavyotekeleza utekelezaji wake au kutekeleza Ilani aliyoiahidi. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuhusiana na masuala ya miundombinu hasa barabara. Hivi ni kweli kwamba hamuoni wakati tunawaona huwa mnaondoka hapa siku ya Jumamosi na Jumapili mnarudi hapa na Jumatatu mnakuwa Bungeni tena kwa magari. Zamani mlikuwa mnaenda hivyo kukiwa kuna mabonde?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kutoka hapa Dodoma mpaka Musoma kupitia Singida ilikuwa inatumika siku tatu lakini leo unaondoa asubuhi, jioni unafika na kesho yake unarudi unafika Bungeni na kipindi hicho Mheshimiwa Magufuli alikuwa ni Waziri wa Barabara. Kwa hiyo, mnapaswa kujua kwamba ametekeleza kwa kiasi gani au ametekeleza amefikia hatua gani. Hata wewe ukiamka nyumbani kwako sio kila kitu unachokitekeleza kwa siku moja! Mambo yanaenda taratibu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango. Kwanza kabisa, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wangu kwa kutuhudumia Watanzania kwa upendo, kwa kweli ni chaguo la Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nirudi sasa kwenye Mpango nimeona wameongelea suala la afya. Kwenye suala la afya niishauri Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi iangalie sana hospitali nyingi na hasa hospitali za rufaa ambazo hazijakwisha huko vijijini kwetu, wilayani na kwenye mikoa mingine kwa ujumla ili kuboresha huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa ya Mkoa wa Mara imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu sana. Hospitali ya Kwangwa imekuwa ikijengwa tangu sijazaliwa mpaka leo inaendelea kujengwa, pesa yake inakuja kwa matone matone kama ya mvua. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu iangalie sana suala la afya na kuangalia pia jinsi ya kuboresha zile hospitali zetu ndogondogo za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Mpango nimeona wameongelea kuhusiana na suala la maji, niiombe sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi iangalie sana hili suala la maji. Kama tulivyoomba Wabunge wengi na hasa Wabunge wanawake suala la kumtua mwanamke ndoo kichwani basi Serikali yetu katika Mpango huu ujao iangalie sana suala la maji kwa upana wake ili kusudi kumtua ndoo mwanamke kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Mpango wameongelea mambo ya Serikali kwa ujumla kwa mfano kuna Mahakama, magereza na vitu vingine. Sijui kwa mikoa mingine kwa Mkoa wangu wa Mara kuhusiana na suala la Mahakama kwa kweli kumekuwa kuna shida sana na hasa vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Wilaya ya Rorya kuna pesa ilishatolewa kwa ajili ya Mahakama lakini hadi sasa Mahakama haijajengwa hivyo kumekuwa na msongamano mkubwa katika Mahakama iliyopo Wilaya ya Tarime na kusababisha usumbufu na pia kuwasababisha wananchi wengi kushindwa kuhudhuria kutokana na umbali na kipato cha kwenda kule au nauli inakuwa ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala pia la magereza, magereza zimejengwa muda mrefu sana toka kipindi cha Mwalimu Nyerere. Hivyo tuangalie suala la magereza katika Mpango huu kwa nchi nzima kutokana na ongezeko la watu. Kwa mfano, Wilaya ya Tarime watu kipindi hicho walikuwa wachache sana lakini siku hizi kwa kweli watu ni wengi sana na tunazaliana kwa speed ya hatari, kwa hiyo magereza ya Wilaya ya Tarime kwa kweli hayatoshi kabisa watu wanabanana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niongelee suala la madini. Humu kwenye Mpango wameongelea suala la madini na sheria zake na mambo mengine. Katika madini tunaiomba Serikali au mimi Mbunge wa Mkoa wa Mara naishauri Serikali iangalie sana suala la kulipa fidia kwa wananchi ambao wanakuwa wamechukuliwa maeneo yao na wawekezaji waliowekeza katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika,Kwa mfano, Mgodi wetu wa North Mara umechukua maeneo ya wananchi kwa muda mrefu sana kwa kweli, watu walikufa, wengine hawana pa kuishi mpaka sasa, wengine ni wazazi wetu, wengine ndugu zetu lakini hawana pa kuishi. Hivyo, niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ifuatilie suala hili ili kuweka kwenye Mpango kuwalipa wananchi hao wa mgodini malipo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya kwa sababu nimemuona Mbunge wangu wa Tarime ambako ndiyo huko Nyamongo, Mheshimiwa Heche, yeye anawashwawashwa na uwanja wa ndege ulioko kwa Mheshimiwa Rais, anashindwa kuwaombea wananchi wetu walipwe fidia zao. Sasa yeye anatakiwa ajue kwamba wale wananchi wanahitaji yeye awatetee siyo awashwewashwe na mikoa mingine kitendo ambacho kwa kweli siyo kizuri sana na ni kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo kwa sababu yeye alitaka uwanja wa ndege uende nyumbani kwake? Au ni kosa Mheshimiwa wetu Rais kuzaliwa eneo ambalo uwanja wa ndege umepelekwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwanza kutokana na Mpango hili suala nina imani kabisa limeangaliwa kwa undani zaidi, kwanza kurekebisha au kubana matumizi. Kubana vipi matumizi basi na wanananchi wetu wanapaswa walisike hili. Ule uwanja ungepelekwa Shinyanga inamaanisha kwamba wananchi wangebomolewa nyumba, kwa hiyo ili kubana bajeti kule kulikuwa na maeneo ya wazi ni kwa nini uwanja usijengwe?

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mambo mengine tunapaswa na sisi kupeleka siasa mitaani siyo tulete siasa Bungeni. Kwa hiyo, niwaombe sana Wabunge wenzangu mambo mengine yanapokuwa ya heri tufurahie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nishukuru sana, sina zaidi ila nasema Mbunge wangu Heche asiwashwewashwe, awatetee wananchi wa Nyamongo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Afya. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kwa kweli suala la afya sasa Tanzania tumefika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Ummy, wewe ni Jembe. Kwa kweli unatosha. Hukuchaguliwa kimakosa katika nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa kuipongeza na kuishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikiliza maoni ya Wabunge wao na hasa kwa kunisikiliza mimi Mbunge wa Wanawake wa Mkoa wa Mara na Mbunge ambaye ni Rais wa Wabunge wote wa Mkoa wa Mara. Kwa kuwa niliongelea suala la Hospitali ya Rufaa ambayo ni Hospitali ya Kwangwa, kwa kweli nilipoingia tu Bungeni niliongelea na baada ya kuongelea sasa tupo kwenye bajeti. Kwa kweli nami katika Mkoa wa Mara nitaandikwa kwenye wino wa dhahabu. Nashukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini, ananiona ni Mbunge ninayefaa na kutosha ndiyo maana nakuwa mwakilishi mzuri Mkoa wa Mara, amekuwa akinipa vifaa ambavyo nimekwishapeleka katika Wilaya za Bunda, Tarime, Serengeti, Rorya na Wilaya nyingine. Kwa kuwa wale wananchi wanaponituma mimi nafanya kweli, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ananiona kupitia kwa Mheshimiwa Ummy. Kwa kweli ninajisifia kwamba ninatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba suala lingine, namwomba Mheshimiwa Waziri Ummy aangalie sana sasa suala la zahanati zilizopo kwa Mheshimiwa Getere ambaye sasa naye anatakiwa apate huduma hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali yangu kwa sababu inawahudumia sana Wapinzani. Majimbo yote iliyopeleka vifaa ni ya Wapinzani. Sasa na hili Jimbo la Mheshimiwa Getere jamani ambalo halina kitu chochote ambalo ndiyo la CCM, chama kilichopo madarakani sasa na lenyewe lipelekewe vifaa kwa sababu halina vifaa katika zahanati zake zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna zahanati ya Hunyali ambayo aliifungua Waziri Mkuu, haina vitanda, mashuka na kadhalika, ambapo vyote hivyo Mheshimiwa Rais alinipa kupitia Mheshimiwa Waziri Ummy na nikavipeleka kwenye Majimbo ya Wapinzani ambayo ni Bunda, Tarime na Serengeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye hiyo zahanati ya kwa Mheshimiwa Getere katika Kata ya Kihumbu kuna hospitali ambayo inatakiwa finishing ambayo ni madirisha na milango. Mheshimiwa Ummy nakuomba uandike tafadhali, nina imani unanisikiliza. Pia kuna dispensary ya Hunyali, kipekee naomba Mheshimiwa Waziri aichukulie kwa umuhimu zaidi kwa sababu jiwe la msingi aliweka Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ambaye ametoka kule siku siyo nyingi sana. Sasa Mheshimiwa Ummy akimaliza tu kwenye hii Wizara yake, nina imani kabisa nitapeleka hayo mashuka na vitanda kwa maana sasa hivi bajeti imekaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali yangu kwa kweli iko vizuri inafanya kazi nzuri. Kwa kweli tumetoka kwenye asilimia 50 mpaka sasa hivi tuko kwenye asilimia 98, anayebisha simuoni wala. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanazozifanya na hasa Mheshimiwa wetu Dkt. John Pombe Magufuli kupitia jembe lake la ukweli Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchagia siku ya leo ukizingatia na mimi ni mjumbe wa Kamati wa Miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa moyo wake wa dhati wa kujali Watanzania lakini pia wanyonge kwa kukubali kwa kutoa shilingi trilioni 15 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Kipekee niishukuru sana Kamati yangu ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Kakoso na Naibu wake ambaye sasa hivi ni Meneja, kwa kufanya kazi nzuri sana ya kutuongoza na kutupitisha katika mambo mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli narudia tena kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Magufuli na kumpongeza sana sana. Kwa mtu kama mimi ambaye nimekuwa Mbunge kipindi cha kwanza kwa kutokea moja kwa moja kule Nyachalakenye tena nilikuwa muuza dagaa lakini sasa na mimi naweza kutunga sheria, kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mungu na kumpongeza Rais wetu anaonyesha ni jinsi gani anavyofanya kazi na kuwakwamua Watanzania. Nami sasa ni msomi kati ya wasomi na nipo vizuri kwa sababu tulipoanza tu Kamati alitutumia wanasheria wakatufundisha, wakatupika tukaiva tukawa vizuri na sasa tunaweza kutunga sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa mafaniko makubwa, tukianza na mafanikio upande wa barabara na madaraja. Kwa upande wa barabara sasa Tanzania nzima barabara zinatengenezwa tena kwa kiwango cha lami; ni barabara ambazo zinapitika vizuri na zinasaidia kuunganisha sehemu moja na nyingine hata kufikia vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma kwetu kule Mara ilikuwa ukitoka Musoma kufika Dodoma ni lazima utumie zaidi ya siku tatu lakini ukifika pale Singida kulikuwa kuna watu wanawaimbisha watu mtaji wa maskini sasa hivi naamini kuna barabara ya lami na hawawezi tena kufanya matukio hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madaraja kwa kweli Serikali imefanya kazi nzuri sana hata kama wale jirani zetu hawaoni wanasema mwenye macho haambiwi tazama basi Watanzania wapiga kura wanaona kwamba ni kazi kubwa sana imefanyika. Mfano ni kule kwetu Mkoa wa Mara kuna lile daraja na Mto Mara ambalo linaunganisha Tarime na Serengeti. Kwa kweli ilikuwa siyo sehemu nzuri na imeua sana watu lakini pia ilikuwa ni sehemu ambayo ulikuwa huwezi kupita mpaka uzunguke, hata uchumi ulikuwa huwezi kukua kutokana na kutumia muda mrefu barabarani kwa ajili ya kuzunguka kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Sasa hivi barabara ile imeunganishwa kutokana na lile daraja na limetengenezwa na wazawa tena wazawa wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba sana ndugu zangu Watanzania na haswa wale mnaofanya shughuli kama hizo muwe wazalendo kama wale waliotengeneza Daraja na Mto Mara tutafika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niishukuru sana na kuipongeza tena Kamati yangu ya Miundombinu kwa kazi nzuri tuliyoifanya. Tumeweza kuzunguka karibu mikoa yote ya Tanzania, tulizunguka mwezi mzima tukiwa tunafanya kazi za kuangalia minara simu, madaraja, barabara na ubora wake na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiwa tunazunguka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?

MWENYEKITI: Ndiyo maana yake, unga mkono hoja.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC. Hii ni heshima kubwa kwetu kama Wabunge, lakini ni heshima kubwa kwa Watanzania na nchi kwa ujumla. Mimi niseme hii nafasi sasa imempata mkunaji maana sasa imefika mahali pake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ameanza vizuri. Ukweli ni kwamba Watanzania bado lugha ya kigeni Kiingereza na lugha nyingine, zilikuwa ni lugha ambazo zilikuwa zinaleta shida sana kwenye mikutano na sehemu mbalimbali kutokana na kwamba ni lugha ambazo tulikuwa hatuzijui vizuri, tulikuwa hatufundishwi tangu utotoni. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, niungane na Mbunge mwenzangu kusema kwamba ni kweli atakuwa ameacha legacy katika Jumuiya hii ya SADC.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwa Tanzania tumekuwa mstari wa mbele chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kutafuta uhuru wa baadhi ya nchi za SADC. Kwa kweli tumewasaidia nchi nyingi sana kiasi kwamba Uenyekiti ulipofikia umefikia mahali pake, kwamba nasi sasa tuonekane kwa yale tuliyoyafanya, kwamba sasa hivi tunaweza kufanya kitu gani.

Mheshimiwa Spika, sina shaka sana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi alioupata wa SADC, kwa sababu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli naamini kabisa ataondoa ukiritimba katika masoko ya biashara. Kwa mfano, kule kwangu Mkoani Mara unaweza ukafanya biashara ama za nafaka au biashara ya dagaa niliyokuwa naifanya mimi kutoka nchini kwetu kuvuka mpakani kunakuwa na ukiritimba lakini kunakuwa pia na masuala ya rushwa. Sasa naamini kabisa chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli rushwa itakoma na hizo nchi washirika naamini kabisa watamtambua kwamba huyu ndiyo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais wetu ni kati ya vivutio na hasa katika nyanja ya uongozi, kwa sababu ni kiongozi bora, ana uongozi uliotukuka, Wabunge pia tumeiga kutoka kwake, mfano; Kama unakumbuka safari hii likizo ya Bunge lililopita kila Mbunge amekuwa akifanya kazi na hii yote ni kutokana na uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwamba asiyefanya kazi na asile na ambaye hajafanya kazi kwa kweli kuliona hili Bunge mwaka 2020 asahau. Kwa hiyo, huu uongozi safari hii umempata mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hili suala la viwanda maana yeye alipochaguliwa tu alisema kaulimbiu yake ni Tanzania ya Viwanda, lakini kumbe ni Rais ambaye ana maono makubwa na ndiyo maana tunasema tumepewa Rais ambaye ametoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu hapohapo ukiangalia imeunganishwa kwamba sasa SADC pia wameongelea suala la viwanda na kukubaliana. Hivyo, naamini kabisa viwanda sasa vitakuwa vingi sana, mfano wake nimwambie hata Mheshimiwa Neema Mgaya kile kiwanda chake cha vyerehani Kumi sasa akianzishe kwa sababu haya mambo yote yanafanyika kutokana na makubaliano ya SADC.

(Maneno hayo yalifanyiwa marekebisho na Mheshimiwa Neema W. Mgaya na kusomeka Vyerehani 370 na siyo Vyerehani Kumi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wabunge wenzangu au wapiga kura wangu wa NEC ambao ndiyo Wabunge, pamoja na wananchi wangu wa Mkoa wa Mara, na hasa Wabunge wa CCM, napongeza sana kwa kweli uongozi huu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imani yangu ni kwamba sasa atafanya mabadiliko makubwa na watauona uongozi wake uliotukuka ambao Tanzania tunajivunia.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa wangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunda Tume ya Mawaziri nane; Waziri wa TAMISEMI, Ardhi, Maji, Ulinzi, Kilimo, Maliasili, Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni Mazingira; kwa lengo tu la kuhakikisha kwamba matatizo ya ardhi yanashughulikiwa ipasavyo. Kwa kweli Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri sana na ndiyo maana imefikia hatua wananchi wamekaa kimya. Wale wanaosema wao wanataka Katiba mpya mambo yote yametendwa, mambo yote Mheshimiwa Rais anayafanya sasa yale waliyokuwa wanahitaji wao yafanywe katika Katiba mpya.

Mheshimiwa Spika, lakini haitoshi hiyo, mimi niwe kidogpo tofauti na wenzangu badala ya bomoabomoa namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jenga jenga. Kakijenga Chama chetu Chama cha Mapinduzi, kaijenga Tanzania kwa ujumla na ndiyo maana bomoabomoa imebadilika imebomoa vyama vya upinzani.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa wetu Waziri Lukuvi, Mheshimiwa Waziri wetu hongera sana kwa kweli kwa kazi nzuri unayoifanya ya kutembelea wanachi na kushughulikia migogoro yao wewe pamoja na Dada yangu Mheshimiwa Angelina Mabula; na ndiyo maana badala ya kuzeeka sasa mnakuwa vijana kwa ajili ya kutembea sana na kushughulikia kero za wananchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni nyeti sana katika hali halisi ya uchumi wa Watanzania. Kwetu Serengeti Mkoa wa Mara kumekuwa na shida na migogoro mingi sana; katika Wilaya ya Tarime na Wilaya ya Bunda lakini yote haya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wameyashughulikia kwa undani zaidi na kwa uzuri; kwa kweli Mheshimiwa Waziri hongera sana. Tunawashukuru sana kwa kusababisha ile ardhi iliyokuwa inatuletea shida, sasa mmeiweka katika mipango mizuri, kwamba sasa iwe katika matumizi bora ya ardhi. Mimi niwaombe tu mfanye haraka ili wale wananchi waliokuwa wanapata shida kutokana na ugomvi au migogoro ya ardhi sasa waweze kuitumia ardhi yao. Migogoro yote iliyokuwepo sasa imekwisha hivyo tunaomba wagawiwe ili waweze kuitumia vizuri.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu Tarime wanawake tulikuwa haturuhusiwi kumiliki ardhi; kumiliki ardhi ilikuwa ni kama kosa la jinai, lakini kutokana na utendaji mzuri na upendo wa Mheshimiwa Rais na Mawaziri wake kwa wananchi wake wa hali ya chini sasa tunaweza kumiliki ardhi ambazo wanawake pia tunakwenda kuchukua hati, tena tunachukua hati kwa muda. Kwahiyo ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba hata sisi watu wa hali ya chini na haswa wanawake wa Mkoa wa Mara sasa wanaweza kuimiliki hii ardhi.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara hii; pamoja na mambo yote kuna changamoto ambazo bado wanatakiwa wazishughulikie. Kuna baadhi ya wafanyakazi au watendaji wa Wizara hii ambao hawaoni kwamba wao wanapaswa kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais; bado wamekuwa ni wasumbufu sana katika Wizara hii. Wamekuwa bado wakiowaomba rushwa wananchi bila kujali kwamba wananchi wana hali mbaya au hali ngumu, lakini pia wamekuwa hawafanyi kazi ipasavyo na kwa muda; na ni wachache tu wanaosababisha hii Wizara ionekane kama vile bado ina matatizo matatizo. Mheshimiwa Waziri Lukuvi Mungu akikubariki hebu ingia sasa na kwa hao wafanyakazi warudishe tu angalau na wao vijijini wakalime ili kusudi wale wanaoweza kufanyakazi; kuna wananchi wengi sana ambao hawana kazi; nao wapate kazi za kufanya.

Mheshimiwa Spika, katika utendaji wa Mheshimiwa Lukuvi kuna maeneo ambayo yamepakana na hifadhi ambapo ni Wilaya ya Bunda, maeneo ya Nyatwali. Ni muda mrefu sasa hilo eneo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Agness.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa hii nafasi adhibu uliyonipa ya kuchangia hotuba wa Mheshimiwa Rais. Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunisababisha kurudi tena Bungeni kwa kipindi cha pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru mume wangu mpenzi Anold Wanyambelwa kwa kunisaidia kukaa vizuri na kuishi vizuri na Wajumbe mpaka Wajumbe wakanielewa. Nashukuru sana na Mungu akubariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu kipenzi kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Mheshimiwa Rais Mungu ambariki sana kwa sababu kwanza amefanya kazi ya kujenga nchi na uchumi wa Watanzania na sasa tumetoka kwenye uchumi wa chini, tuko kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kafanya kazi ya pili ya kukijenga Chama cha Mapinduzi kikaimarika kupitia kazi nyingi na nzuri alizozifanya zilizopelekea tukapata kura za kishindo. Mungu akubariki sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Rais wetu kipenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania hatuhitaji Katiba Mpya bila maendeleo. Watanzania tulikuwa tunahitaji barabara tumeletewa barabara na Mheshimiwa Rais. Tena bahati mbaya jamani, pamoja na Ubunge wangu, yawezekana kidogo nimesababishwa kuwa mshamba na Mheshimiwa Rais nilipofika Dar es Salaam juzi nimepotea. Nimekutana na barabara nzuri sana ambazo zimetengenezwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliona ni vyema akafanya maendeleo kwa Watanzania; kajenga Vituo vya Afya. Badala ya kuchukua shilingi bilioni 400 na kuzipeleka kwa Wabunge wakae kwa ajili ya kujadili Katiba mpya, akaona ni vyema apeleke kwenye maendeleo ya wananchi. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunataka uzazi salama na siyo Katiba na sasa wanawake tunazaa salama. Ndiyo maana katika Bunge moja tu mimi nimezaa watoto wawili kwa kipindi cha miaka mitano na sasa niko salama. Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Mungu akubariki sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli ameona zile shilingi bilioni 400 badala ya kutuletea sisi kujilipa wakati wa kujadili Katiba mpya, amesababisha tumepata maji vijijini. Mheshimiwa Dkt. Magufuli sasa wanawake umewatua ndoo kichwani. Mungu akubariki sana kwa kuimarisha ndoa za wanawake, kwa sababu ndoa nyingi zilikuwa zinavunjika kwa kufuata maji mbali, kusubiri maji na kukaa muda mrefu kwenye vituo vya kutafuta maji. Mungu akubariki sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli, tunakuombea uendelee na mwendo huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kipekee nimshukuru sana Rais wangu kwa kuwajali wajasiriamali wadogo wadogo, wakiwemo mama ntilie, bodaboda, baba lishe, mama lishe kwa kuboresha vitambulisho vyao hadi kupanda hadhi kuonekana kama vitambulisho vya Taifa ili na wao waweze kukopesheka katika mabenki pamoja na kampuni na mashirika mengine ya kifedha. Niseme Mwenyezi Mungu ambariki sanaMheshimiwa Magufuli adumu miaka 200. Ingekuwa siku zinarudishwa nyuma tungemrudisha nyuma sasa ndiyo akawa unaanza mwaka wa kwanza ili mbele bado miaka kumi inayofuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana ndugu zangu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Magufuli kafanya kazi nyingi na kubwa sana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Alifanya kazi kama Mbunge, kama Waziri, alifanya kazi kama Diwani na kiongozi wa chini kabisa na ndiyo maana tumesimama imara na ndiyo maana Chama Cha Mapinduzi leo tunajivuna kwa kazi nzuri Mheshimiwa Magufuli alizozifanya ambazo zimetusababishia kutembea kifua mbele na kupata ushindi wa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi kama alivyowaambia Mheshimiwa Rais sasa hivi wanatakiwa mfanye kazi. Hizo nafasi alizowapa ni deni sio kwamba eti amewachagua kwa sababu humu watu wengine hawatoshi, kuna wengine hapa tunawasubiria ili kusudi tu ushindwe kufanya kazi ili na sisi tupate nafasi hizo. Niwaombe sana, wamsaidieni Mheshimiwa Rais kufanya kazi kwa nguvu zote kwa juhudi, sasa hivi sio muda wa kukaa ofisini. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwajali akinamama. Mheshimiwa Rais kwa kweli Mungu ambariki sana, sana na ndiyo maana sasa hivi wanawake wengi tuko Bungeni, tumekuwa asilimia kubwa sana lakini kwa wale waliokwenda majimboni wameshinda, ushindi wa kishindo. Kwa hiyo, tunasema wanawake tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana ndugu zangu, tunapokuwa tuna mihemko ya kisiasa tuiache pembeni sasa tufanye kazi kwa manufaa ya Watanzania wote. Fimbo aliyowachapa mwanzoni ndugu zetu wale rafiki zetu majirani msije mkaitamani tena maana kipindi kijacho wakiendelea kutoka nje maana yake hata wao wawili waliopo humu basi wataondoka jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia rasimu ya Mpango. Wizara hii imeweka mambo mengi sana ambayo ni mazuri na naamini kabisa ni mwendelezo wa mafanikio ya miaka mitano iliyopita ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye rasimu hii nimeona wakizungumzia viwanja vya ndege, kikiwemo kiwanja cha Mkoa wa Mara. Kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Mara ningeishauri Serikali katika Mpango wake kipewe kipaumbele na ikiwezekana wakiangalie kwa macho ya ziada kwa sababu, kule kwetu Mkoa wa Mara ndipo alipotoka muasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo, ni sehemu nzuri ambayo ingelikuwa ni ya mfano na hasa ukizingatia Mkoa wa Mara tunachangia Taifa hili pato kubwa sana kutokana na madini, lakini pia utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara tuna kiwanda ambacho kiko Musoma Mjini, Kiwanda cha MUTEX. Kiwanda cha MUTEX kimekufa muda mrefu sana. Kiwanda hiki kilikuwa kinatengeneza kanga nzuri sana na kubwa ambazo ukiangalia watu wa kule Mkoa wa Mara tumejaliwa zile kanga zilikuwa zinatutosha vizuri tu. Kwa hiyo, niseme na sasa hivi pia ni vizuri zaidi kile kiwanda kikiangaliwa kwa jicho la ziada ili kifunguliwe kwa manufaa ya kuongeza ajira kwa vijana na watu mbalimbali ambao wanaweza kupata ajira na kupunguza upungufu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wazee wetu wa muda mrefu sana ambao wanaitwa wastaafu walifanya kazi kipindi hicho kiwanda kile kikiwa Serikalini. Wana madai yao ya muda mrefu sana ni miaka sasa, kila wanapoenda mahakamani wanakata rufaa, wanashinda, wanakata rufaa wanashinda, nimwombe sana baba yangu, Mheshimiwa mpendwa wetu sana Rais, naamini kabisa ataiangalia siku ya leo; akawaangalie wale wazee wetu wa Kiwanda cha MUTEX kwa jicho la huruma, walipwe mafao yao ya muda mrefu kwa sababu, kuna wengine wao wameshafariki, kuna wengine wamepata ulemavu, lakini hata wale waliopo hali zao sio nzuri sana. Naamini anajali wanyonge na wale ni kati ya wanyonge ambao naamini kabisa daddy atanisikiliza leo na ataenda kuwaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la maji; Mkoa wa Mara wilaya zetu zote zimezungukwa na Ziwa Victoria, lakini baadhi ya wananchi wetu wanalia sana shida ya maji kutokana na miradi mikubwa ambayo Serikali imeshaiandaa kwa ajili ya Mkoa wa Mara. Pia, kwenye rasimu nimesikia wakiitaja, kwa kweli nawapongeza sana wako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Mkoa wa Mara ni mkoa aliotoka muasisi ulitakiwa uwe mkoa wa mfano, asiwepo mwananchi hata mmoja analalamika shida ya maji. Hivyo basi, ningeomba miradi hiyo mikubwa inapopita; upite Bunda, upite Serengeti, upite Tarime, upite Rorya, upite Musoma Vijijini, upite Musoma Mjini, lakini upite maeneo yote lengo ni kwamba, kutoa haki sawa na hasa kwa wale ambao wamekaa karibu na uaridi. Wanasema unapokuwa karibu na uaridi unanukia. Sisi wenyewe Mkoa wa Mara ndio wenye uaridi ambalo ndio maji ya ziwa, pamoja na kuwa Taifa zima ni haki yetu na ni haki yao, lakini sisi hasa Mkoa wa Mara tuwe wa mfano tusikose maji nyumba hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la miradi mikubwa ya umeme. Huu mradi wa umeme umekuwa kwa wananchi na hasa wananchi wa vijijini umekuwa changamoto sana huu mradi wa umeme wa shilingi elfu 27. Wananchi kila wanapoenda kwenye ofisi zao, wanaambiwa kwamba, bajeti bado haijaandaliwa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana, pamoja na kazi nzuri anazozifanya, nimwombe aangalie hili suala kama ni bajeti sisi Wabunge tutampitishia harakaharaka ili hili suala liende kwa wananchi wakapate huu umeme wa shilingi elfu 27 kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja tu.

MWENYEKITI: Muda wetu umeisha.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii. Kwanza nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy kwa kuteuliwa. Naamini kabisa wewe ni jembe, unaweza na yale mazuri yote yaliyoanzishwa naamini kabisa utayaboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa hapo ulipo presha inakupanda, unasema, huyu ndio Agnes wangu za zamani! Hivi kweli nini kinaendelea? Ila mimi ni Agnes mpya, nimefundwa na wewe, sasa hivi niko vizuri, usiwe na wasiwasi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, dada yangu Mheshimiwa Waziri Ummy, , kama vile ulivyokuwa unafanya ziara kipindi kilichopita, nakuomba sana, ukipata nafasi dada yangu njoo Mkoa wa Mara, ikiwezekana niite nami nikuoneshe baadhi ya vichochoro kule kwetu vijijini; Wilaya za Serengeti, Rorya, Tarime, Bunda, Musoma Vijijini, Mwibara na kwingine uone jinsi barabara zetu zilivyokuwa mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi ili unielewe kwamba TARURA wana mzigo mzito sana. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, bajeti ya TARURA ikiletwa ndogo kwa kweli inabidi tumrudishe kidogo Mheshimiwa Waziri aende akachakate ili airekebishe iongezwe. Kwa sababu TARURA wamepata mzigo mkubwa sana, lakini kutokana na kazi zao wanazozifanya, kwa kweli huwezi ukawalaumu kwa bajeti wanayopewa. Bajeti yao ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kubeba jukumu la kujenga kwenye mitaa na bajeti waliyopewa iwe ndiyo hii ambayo tumeiona, halafu tuseme kwamba TARURA watafanya vizuri, siyo kweli. Tutabaki kuwalaumu kila siku TARURA bila kujua tatizo liko wapi? Tunapaswa kwanza kutatua tatizo halafu baadaye tuone utendaji kazi wao ukoje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakuomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, jipinde sana uangalie kuhusiana na hili suala la TARURA. Siku ukirudi hapo mezani, basi utuelezee vizuri hili suala limekaaje na bajeti yao umeirekebisha vipi?

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu. Kwa kweli hotuba yake ya jana ilikuwa nzuri sana. Binafsi nilifurahi kusikia akisema kwamba ataboresha mishahara ya wafanyakazi. Kwa kweli wafanyakazi hawa mama yetu wana imani sana na wewe. Siyo tu kwamba wana imani sana na wewe kwa sababu eti utawaongezea mishahara au kuboresha mishahara yao. Wana imani kubwa kwa sababu utendaji kazi wa mama wanaujua toka kipindi kilichopita akiwa na baba yetu Hayati JPM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kabisa wafanyakazi wana imani na wewe mama, kaa vizuri mama, angalia vizuri, chakata chakata na Wizara yako, hawa wafanyakazi kama ulivyosema nao wafurahi, kwa sababu kila kukicha bajeti zinazidi kubadilika na hasa bajeti za kifamilia zinakuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa upande huo wa wafanyakazi, nakwenda kwa Madiwani. Ndugu zangu, Wabunge wezangu, Madiwani wetu ndio wanaotulindia magoli. Wana kazi kubwa sana. Bila Diwani wewe ukitoka hapa Bungeni ukienda, unamwuliza Diwani, sehemu fulani kuna nini?

Mheshimiwa Spika, sehemu fulani kuna tatizo gani? Huyo ni Diwani, naye ndio yuko kule muda wote. Mtu akiugua anaenda kumdai yeye Diwani; akitokea Mjumbe amekuja; wale ambao si mnajua tena, Wajumbe noma, lakini Diwani anamtuliza yule Mjumbe wako. Pia hawa Madiwani ndio wametuweka sisi madarakani na ndio wameiweka Serikali hii madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa maana ya kwamba wao ndio wanaishi moja kwa moja kwa siku zote kule Majimboni kwetu au kwenye Kata zao na wananchi wetu. Kwa hiyo, ukweli ni kwamba Madiwani wanapaswa kuongezewa posho zao, kwani hazitoshi, hazikidhi mahitaji yao, kwa kweli wanapata kiasi kidogo sana ukilinganisha na majukumu waliyonayo.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Waziri Ummy, hili suala sasa aliangalie zaidi. Ikiwezakana jamani, kwenye Wizara basi mwangalieangalie, kwa sababu mmeshaona kule kwa Wakurugenzi kuna shida, basi mlipe moja kwa moja kutoka Wizarani wale Madiwani angalau wajue kwamba tuna mshahara wetu unatokea huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hata kwangu, Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa ambayo ni wahanga wa Madiwani kukopwa. Jamani, kweli tunawakopa Madiwani ambao ndio wanaofanya kazi kubwa sana. Hata huyo Mheshimiwa Mkurugenzi mwenyewe anamtegemea Diwani kule chini na Mheshimiwa DC anamtegemea Diwani kule chini, lakini bado. Siyo tu kwamba wanawakopa, hawajatuambia hizo fedha wanazowakopa ziko wapi? Wamepeleka wapi?

Mheshimiwa Spika, nakuomba dada yangu, Mheshimiwa Ummy, ukienda kawaangalie hawa Wakurugenzi, ukawafanyie ukaguzi. Utakuta uharibifu mwingi sana na upotevu mwingi sana wa fedha ambao wanaufanya na hasa pale wanapowafanyia uonevu Madiwani. Kwa kweli haikubaliki, Wabunge wenzangu, haikubaliki, tukatae kabisa wasiwaonee hawa Madiwani.

Mheshimiwa Spika, kipekee niende moja kwa moja kwenye suala la shule. Shule zetu na hasa za vijana wetu wa kike zimekuwa ni nzuri sana ambapo kwa sasa vijana wa kike wamejitahidi, kiasi fulani kwa kweli wamepanda katika ufaulu, wameanza kuwa na ufaulu mzuri, lakini changamoto inayokuja ni pale ambapo vijana wetu wa kike wengine ambao hawawezi ku-afford kupata taulo za kike, inawapa shida, wanapata shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu, moja kwa moja kama vile tunavyoweka bajeti nyingine za shule kwa watoto wa shule kama watoto wa kiume wanavyowekewa zile packages zao, basi tuangalie na kwa watoto wa kike wawekewe moja kwa moja. Kama vile ambavyo Serikali inakuwa imewalipia ada, basi waangalie pia na kwa hawa watoto wa kike wawekewe ili wale watoto ambao hawajiwezi, umri ambao wanakuwa wameanza kupata hedhi, basi waweze na wao kujiangalia kwamba wanaweza kusoma na hawawezi kupata matatizo madogo madogo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia wizara hii kwanza niwapongeze sana waziri na watendaji wote katika wizara hii, lakini pia nimpongeze kipekee dada yangu kwa awamu iliyopita daktari wa covid Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi kubwa aliyoifanya kipindi kilichopita pamoja na Serikali nzima akiwemo Mheshimiwa wetu Hayati John Pombe Magufuli pamoja na mama yetu Samia kwa kazi nzuri waliyoifanya kipindi kilichopita ambayo sasa mama anaiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa kweli hotuba ya juzi ya mama alipokuwa na wazee nampongeza sana Mheshimiwa wetu Rais kwa moyo huohuo Mwenyezi Mungu amwongezee sana na azidi kumpa hekima na sisi tunamuombea sana aliposema kwamba huduma ya afya kwa wazee iboreshwa. Naamini kabisa mama yetu wewe ni mama na bahati nzuri ulianza na baba, baba katuacha na wewe, kwa hiyo, tunaamini kabisa wazee hawa wanategemea faraja kutoka kwako kama ulivyosema Mheshimiwa Rais wetu kwamba huduma hii itaboreshwa tunaamini kabisa suala hilo litasimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe waziri na watendaji wako, Mheshimiwa Rais ametoa maagizo huduma kwa wazee iboreshwa sio sasa mpaka aje kuanza kutumbuatumbua ndio muanze kufanya vizuri. Niwaombe sana hili suala mliangalie kwasababu hawa wazee pia watoto wao ni wapiga kura wenu na wao wenyewe ni wapiga kura wenu lakini pia kwa kura za kishindo walizozitoa sasa hivi watanzania wanasubiri na kutegemea matokeo chanya kwa wabunge wao na kwa serikali yao. Kwa hiyo, niseme tu naamini kabisa Mheshimiwa Waziri uliyechaguliwa ni jembe na ninaamini kabisa wewe ni mtendaji mzuri, hawa wazee watapata faraja kutoka kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuombe sana, Mheshimiwa Waziri sasa aangalie hili suala la watoto wa chini ya miaka mitano. Kule kwetu Mkoa wa Mara na hasa katika hospitali nilizokwenda kukutana na malalamiko haya kwamba watoto wa chini ya miaka mitano wanalipishwa wakati watoto wale wanatakiwa wapate huduma bure. Nafikiri sio jambo zuri Mheshimiwa Waziri lifatilie na ikikupendeza naomba tuongozane nikakupeleke maana ushahidi ninao na baadhi ya stakabadhi walizolipia nilichukuwa kabis ushahidi ninao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ila tu ukifika usiwatumbue urekebishe tu mambo ili yakae sawa kwa hiyo niseme tu kwa kweli wananchi wetu wanaumia, tusimamie vitu tunavyokuwa tunaviahidi lakini pia tufanya kwa kadri ya mapenzi ya Mungu tukiwa tunajua kwamba kesho ahera tutajibu nini, sio tu watupigie kura wakimaliza kutupigia kura watanzania hawa vitu vingine tunakuwa kama vile hatuwaatendei haki wakati sisi wenyewe ndio tumeahidi kutoka midomoni kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niishukuru sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi kilichopita na sasa hivi kwa kutejengea hospitali nzuri sana ya rufaa hospitali ile kwa kweli ilikuwa na muda mrefu sana na sasa imejengwa iko vizuri, na imeanza kutoa huduma lakini tu kama alivyosema Mbunge mwezangu Mheshimiwa wetu waziri tungeomba sana kwasababu Mkoa wa Mara kiukweli ni kwamba ni mkoa ambao mnatakiwa muuweke ukae kimkakati kwasababu ndio mkoa uliomtoa Mhasisi wa Taifa hili Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi ile hospitali ya rufaa irekebishwa vitu vilivyobaki ili kusudi sasa na mkoa wa mara wale wanaojua wale watu wanaojua maana kule sisi kuna bibi zetu ambao mpaka leo wanajua Mwl Nyerere yupo Butiama hawajui kama ameshakufa mpaka leo ukienda kule vijijini saa nyingine wanakuambia ah sisi tunaenda kuchagua chama cha Mwl Julius Kambarage Nyerere. Sasa kwasababu hiyo basi mazingira yaboreshwa hata sisi tuonekane kwamba akina Agnes tunatoka Mkoa wa Muhasisi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa wangu waziri ufanye kweli nakuamini sana waziri najua utafanya kweli. Lakini kipekee zaidi niseme tu hivi sasa, hivi tumejenga hospitali nyingi sana na nzuri sana tena za kimkakati zinazoweza kuwasaidia wananchi wengi sana, katika sehemu zote mikoa yote vijiji vyote hospitali zetu jamani ni nzuri sana. Lakini Vituo vya Afya vimejengwa vingi sana. Mheshimiwa Waziri kama vilevile ardhi walivyokaa kamati nane, basi Mheshimiwa Waziri na wewe pia ukakae chini na waziri au Wizara ya Ujenzi ili muangalie hizi hospitali ziweze kufikika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama anataka kwenda hospitalini lakini sasa unakuta sehemu zenyewe hazipitiki ni mabonde kuinama sasa kama ni mabonde kuinama inakuwaje yani mabonde kuinama namaanisha kwamba hapa kuna shimo mara hapa kuna mtaro umekaa vibaya mara hapajarekebishwa. Kwa hiyo, niombe sana hii Serikali yetu naamini ni Serikali Sikivu, na haya mambo ambayo tunayashauri naamini kabisa yatatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana mama yetu Mheshimiwa Rais mama yetu kipenzi Raisi wa kwanza mwanamke Tanzania kwa mambo haya yote tunayoyasema hapa mawaziri wake kama watayafuata na kuyashikiria naamini kabisa wakiyatekeleza, na hizi pesa zitoke kwa wakati sio tu tuwe tunaongea hapa maneno tunasema weeee! Pesa mara zimetoka kidogo.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. AGNES M. MARWA: …mara mkandarasi, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii adhimu. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa wetu Rais kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya. Nasema anazoendelea kuzifanya maana ni kazi ambazo alikaa kama vile Mungu alivyokaa na utatu wake mtakatifu wakaumba wanadamu na mambo yote duniani na yeye alikaa na utatu wake na Mheshimiwa wetu Hayati wakapanga mipango yote hii iliyokuwepo na miradi yote hii inayoendelea, kwa hiyo ni vitu ambavyo anaendelea navyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao wanadhani na wanauliza ngoja tusubiri Mama atafanya nini? Wanapaswa kujua kwamba, hata haya yanayoendelea yeye ndiye aliyekaa pia na kuyapanga na Hayati na anaendelea kuyatekeleza. Sasa tunapaswa kum-support na kumpa nguvu ili kusudi aendelee kufanya mengi mazuri baada ya kuyamaliza haya waliyoanza nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa wetu Waziri mtani wangu Mwigulu Nchemba kwa kukalia kiti hiki cha fedha. Kwa kweli, naamini kabisa fedha yetu iko mikono salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la umeme. Kipindi kilichopita tulikuwa tuna vijiji 12,312 ambavyo vilikuwa havina umeme, lakini Mama kwa mapenzi mazuri na Tanzania yetu ameona kwa mwaka huu vijiji 10,317 vyote vipate umeme. Basi kwa maana hiyo ninaamini kabisa kwa kasi hiyo, kipindi kijacho, bajeti ijayo basi hata hivi vijiji vilivyobaki 2,005 naamini kabisa vyote vitapatiwa umeme kiasi kwamba, hata Mkoa wangu wa Mara utapata umeme Mkoa mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa wasambaza umeme. Umeme upo, umeme umetolewa, lakini sasa kasi ya usambazaji ni ndogo. Ukiingia ndani kule vijijini unawakuta watu hawajasambaziwa umeme, kwa hiyo umeme unabaki tu kuwa jina kwamba tuna umeme. Kwa hiyo, mimi niwaombe sana Ndugu zangu wasambazaji wa umeme wafuatilie sana susla la kusambaza ili kusudi wasaidie vijiji vyote na maeneo yote yapate umeme ili kuleta pato zuri kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la miradi ya maji. Ninamshukuru sana Mheshimiwa wangu Rais kwa kuweka miradi na kuendelea kujenga au kutekeleza miradi mizuri ya maji ya kimkakati. Kwa kweli, Mungu ambariki sana kwa sababu miradi ya maji yote ikitekelezeka, akimtua ndoo mama kichwani atakuwa ameponya ndoa za wanawake asilimia 98 ambazo zilikuwa zinavunjika kwa ajili ya kufuata maji mbali au umbali mrefu. Wanawake wengine walikuwa wanachoka sana wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya ndoa, lakini pia wanawake wengine walikuwa wanaenda kwenye maji mbali sana, wanapokuwa wameenda mbali wanachelewa kurudi nyumbani kwa hiyo, inawaletea conflict ndani ya familia zao, suala ambalo Mama yetu naamini kabisa yeye kama Mama sasa ameona kwamba, alimalize kabisa ili kusudi liende vizuri kwa hiyo, mimi niseme Mungu ambariki sana.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Watanzania, niwaombe Watanzania wenzagu tumuunge Mama mkono, tum-support Mama, tuwe na umoja na ushirikiano, asitokee mtu mwingine wa nchi nyingine akaibeza Tanzania na wewe ukakubali. Mtu yeyote anayembeza Mama amelibeza Taifa la Tanzania. Mtu anayebeza Taifa la Tanzania amekubeza wewe Mtanzania.

Kwa hiyo, mimi niseme umoja wetu ndio ushindi wetu ili malengo yetu yatimie tufikie malengo yetu, tufikie uchumi wa kati na ikiwezekana tufikie uchumi wa juu zaidi, kama tunavyoona kasi ya Mama ni kubwa sana sio kama watu wengine wa huko nje walivyokuwa wanategemea na wachache waliokuwa wana nia mbaya na Tanzania walivyokuwa wanategemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama anaenda kwa kasi ya ajabu, Mama anapiga kazi, Mama yuko vizuri kwa sababu, wao wenyewe ni mashahidi na mashuhuda. Walidhani kwamba, miradi iliyokuwa imeanzishwa kipindi cha Hayati, kipindi kilichopita kwamba, italala, mama amesema miradi yote itatekelezwa. Na ikishatekelezwa atafanya mengine makubwa zaidi ambayo tumeshaona sasa hivi mama anaendelea kufanya mambo makubwa zaidi hata yale ambayo watu hawakutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Watanzania tuwe wamoja, tulilinde Taifa letu kwa nguvu zote. Niwaombe sana watu wetu wa dini zote bila kujali ni dini ya aina gani, watu wa imani zote, kila siku kukicha, asubuhi, mchana na jioni tuliombee Taifa letu la Tanzania ili tufikie malengo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeongelea vizuri sana kwenye suala la wachimbaji wa madini lakini la wawekezaji kwa ujumla wa Tanzania. Ombi langu, niombe sana kuna watu ambao waliathirika katika mgodi wa North Mara kule kwetu Tarime kipindi kilichopita, kwanza kabisa maeneo yao walipoyatoa walitarajia at least watabadilisha kidogo maisha, lakini waliheshimu sana Serikali yao kwamba wanapotoa yale maeneo na wao watahifadhiwa vizuri, naishukuru sana Serikali yetu kwamba walisikiliza vizuri na baadhi yao walipewa fidia lakini hawajapewa fidia wote, mpaka leo kuna wengine wameingia umaskini kwa kile kinachoitwa uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeongelea vizuri sana kwenye suala la wachimbaji wa madini, na wawekezaji kwa ujumla Watanzania. Ombi langu niombe sana, kuna watu ambao waliathirika katika mgodi wa North Mara kule kwetu Tarime kipindi kilichopita kwanza kabisa; maeneo yao walipoyatoa walitarajia at least watabadilisha kidogo Maisha. Lakini waliheshimu sana Serikali yao kwamba wanapotoa yale maeneo na wao watahifadhiwa vizuri. Naishukuru sana Serikali yetu kwamba walisikiliza vizuri na baadhi yao walipewa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hawajapewa fidia wote mpaka leo kuna wengine wameingia umaskini kwa kile kinachoitwa uwekezaji, unapokuwa uwekezaji Tanzania basi mawaziri wetu, waangalie hili suala la wawekezaji, waangalie watanzania wanashida gani, na uhitaji gani ili hawa Watanzania walipwe fidia zao kutokana na mali zao walizozitoa. Siyo watoe wao eneo halafu wabaki kuwa maskini kila siku wanalia siyo jambo zuri hata kwa Mwenyezi Mungu Tanzania tunahitaji baraka. Kwa hiyo, niombe sana kwa wale waliobaki watu wa Tarime Mheshimiwa Waziri ufuatilie hili suala ili wakalipwe maeneo yao na wao waifaidi mali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikuombe sana Mheshimiwa Waziri au Waheshimiwa Mawaziri katika wawekezaji wanaokuja Tanzania ninaimani kabisa mnajitahidi sana. Kuna jambo moja naona kama tunafeli hivi inapokuwa kuna uwekezaji mkubwa mahali basi maeneo hayo yang’ae yatakate kutokana na uwekezaji ule siyo tu watu wanawekeza kuna madini sisi tunaonekana kwenye madini. Lakini Mheshimiwa Agnes nikitoka kule Tarime vumbi limeshanipiga mpaka basi. Eti! Mpaka tusubirie bajeti ya Serikali! Kwani wale wawekezaji jamani! Si wangetutengenezea hata lami kidogo hata kuonyesha wamechukua fedha kutoka kwetu, kuchukua pesa kwetu maana yake ni kwamba wanapopata mali kutoka kwetu wanakwenda kuuza wanapata fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi wanapopata pesa nyingi na sisi wanaotuacha pale angalau basi tunukie nukie na sisi ile dhahabu siyo tu tuna barabara mbaya maji, hatuna sisi tunaitwa tu tuna wawekezaji jamani hili suala niombe sana mawaziri wetu mkae karibu na hawa wawekezaji muwaambie ukweli kwamba faida wanazofaidika nazo kutokana na nchi yetu ya Tanzania na wao pia watufaidishe.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuongea siku ya leo. Kwanza nikupongeze wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Zungu kwa kuchaguliwa na Chama chetu; Chama cha Mapinduzi, kuwa mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi kwa nafasi ya Unaibu Spika. Naamini kabisa, kama kawaida, hiyo imekwisha hiyo, yeye ndiye Mungu amemeoneshea njia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja na kuchangia katika Wizara yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Mimi niseme tu namshukuru sana Mheshimiwa wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutukubalia sisi wanakamati kwa kurasimisha ardhi kwa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa wale wanaouliza Mheshimiwa Rais, Mama Samia kafanya nini; wanapaswa kujua kwamba kati ya shughuli au kazi nzuri au upendo mkubwa aliotuonesha Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ni huu wa kumtaka kila Mtanzania amiliki ardhi yake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampongeza sana mama, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki, unaupiga mwingi. Wale waliokuwa wanafikiri huwezi, unaweza, unatosha na chenji inabaki. Naamini 2025 kwa mapenzi ya Mungu mama tutakupa kura nyingi sana. Sisi kama Wana- Mara, nami kama mwakilishi wa wanawake kutoka Mara tutampa Mheshimiwa Rais kura za kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niongelee suala la ardhi. Kwa kweli Mabaraza ya Ardhi yamekuwa yakileta kero nyingi sana tena kero zenyewe ni chefuchefu na hasa pale Mabaraza yanapoendesha kesi kwa muda mrefu sana. Mabaraza haya yamekuwa yanaendesha kesi kwa muda wa miaka 10, 20 mpaka 30. Hii wakati mwingine hupelekea mtu mwenye kesi hiyo anafikwa na umauti hajafaidi ardhi yake; mtu mwingine anakuwa ameshazeeka na mtu mwingine anakuwa ameshazaa watoto na watoto wameshakuwa na wajukuu. Ni suala ambalo siyo zuri sana na ambalo linaleta shida kila siku kwenye ardhi na migogoro isiyokwisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wao kama viongozi, kama waosimamia wasimamizi wa kesi za ardhi, tunawaomba wabadilishe taratibu zao. Hii yote ni kwa ajili ya kutengeneza rushwa ambazo hazijaisha katika ardhi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Waziri wetu, Mheshimiwa Mabula, lakini naomba afanye kazi kubwa sana katika mabaraza haya. Ikiwezekana awabadilishe badilishe, wasikae muda mrefu na ikiwezekana pia afuatilie kujua kwamba ni nani anayesababisha shida hizi zinaendelea? Kwa sababu shida hizi zinazoendelea ni baina ya masikini na matajiri. Ikionekana katika ardhi hiyo masikini au mtu wa hali chini alikuwa anaimiliki ardhi hiyo kama mmiliki namba moja, halafu akatokea tajiri, naye anakuwa na Hati, tena unaiona hati yenyewe inafanana kama ya wiki mbili, lakini inakuwa eti ni Hati ya miaka 20. Ni kitendo ambacho siyo kizuri sana, ni uonevu kwa Watanzania. Tum-support mama yetu Mheshimiwa Samia kwa upande wa umilikishaji kwa ili kila Mtanzania aweze kumiliki ardhi na hasa Watanzania wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; naiomba Serikali ifanye auditing ya mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia kesi hizi: Je, zimetumia muda gani? Zinaendaje? Kusudi kesi hizo ziwe zinatumia muda mfupi kwisha, siyo kesi zinakaa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, suala la ardhi limekuwa ni tatizo kubwa sana na hasa hapa Dodoma. Nasema Dodoma kwa sababu naamini kabisa hata sisi wenyewe Wabunge huku ndani, wengi sana tuna matatizo hayo. Sisi tunataka kulipia malipo ya Serikali ili tupate Hati, tulipie kodi za Serikali lakini wao wanakaa nazo maofisini muda mrefu bila ya kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili sulla linatakiwa liondolewe kwenye maofisi, wamekuwa wanakula rushwa kupitiliza. Kama wamepewa kazi mtoto wa baba, mtoto wa shangazi kwamba wote ni wakazi wa hapa hapa ambao hawatoki ndani ya ofisi hizo, basi wapishe, kuna watu wengi sana wanatembea na vyeti wamesoma Vyuo Vikuu, wengine ni Maprofesa wanatembea na vyeti vyao mkononi, wapewe kazi hizo wafanye kama wao kazi za ardhi zimewashinda.

Mheshimiwa Spika, pia mimi niseme tu kuhusu viongozi wangu wa Dodoma. Imefikia hatua viongozi kutoka ardhi muone aibu na haya. Kuna vitu mnavifanya vinapitiliza. Mimi kama Mbunge nina mfano hai. Nilinunua kiwanja miaka 10 iliyopita, lakini hawakuwa wanajua kama ni kiwanja cha Mbunge, bahati mbaya kipindi hicho mimi sikuwa Mbunge. Nikiwa Mbunge sasa nimekuja kufuatilia, eti kiwanja changu kimechukuliwa, kimepelekwa Polisi, kwamba Polisi wanafanya uchunguzi. Hivi sasa uchunguzi unachukua miaka, badala ya waniambie kwamba hiki kiwanja kama ni cha mtu, basi mimi kama Mbunge nitakubali mtu masikini akapewe kile kiwanja. Hata hivyo, ninavyo vielelezo vyote na document zangu ambazo ni original, ni kwa sababu tu kuna mtu alikuwa anataka kumilikishwa ambaye ameshawapa rushwa, sasa yamewakwama wameshindwa la kufanya.

Mheshimiwa Spika, kama natendewa mimi Mbunge, hivi raia wa kawaida wanatendewa nini? Wanafanyiwa vitu vingapi? Sisi kama Wanakamati kutoka Kamati ya Ardhi tumeshauri mara nyingi, basi wale Maafisa au viongozi walioko hapa maofisini, tunaamini kabisa wala rushwa wanawajua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala linatokea kote ikiwepo hata kwangu Mkoa wa Mara. Kuna wamama masikini wanalia sana, wanaonewa. Kama yeye ni mmiliki namba moja, huyu mmiliki namba mbili anayekuja na Hati ambayo inaonekana ni kama Hati ya jana, lakini huyu mama ana Hati yake ya miaka mitano hadi sita ambayo yeye ndiye mmiliki namba moja. Basi yeye awe na haki kwenye haya Mabaraza ya Ardhi ili kusudi yeye apewe haki yake na huyu namba mbili wakamtafutie hivyo viwanja vya matajiri amilikishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ardhi imenuka rushwa, imejaa rushwa. Naomba Mheshimiwa Waziri iwe ni sehemu yake ya kwanza sasa kuchanganua au kuwatoatoa wale watu ambao ni wala rushwa na wanafahamika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii.

Kwanza kabisa nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa kurudishwa katika Wizara hii yeye pamoja na Naibu wake, kwa kweli naamini kabisa sasa mambo yatakaa sawa. Ambaye hamjui Mheshimiwa Ummy akaiulize Covid Ummy ni nani ndiyo mtamfahamu kwamba Ummy ni nani. Hata Covid ikimsikia Ummy inakimbia.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa hiki kitendo alichokifanya cha mabadiliko MSD, kwa kweli amefanya kitendo kizuri sana na kuwafariji Watanzania ambao wengi sana walipata maumivu makali sana ya mambo mengi maovu ambayo yalikuwa yakitokea. Na bahati nzuri amemchagua Mkurugenzi ambaye ni jembe ambaye naamini kabisa, timu yao kwa kushirikiana na Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri, sasa mambo yatakaa vizuri. Kwa hiyo mimi niseme nawaombea Mwenyezi Mungu ili watufikishe salama.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba Mheshimiwa Waziri aangalie, kuna mambo ambayo ni ya muhimu sana naomba ayatupie jicho la tatu, yeye pamoja na wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, kuna hizi gharama za kufungua faili na kumuona daktari, naziona hapa; kwa kweli hizi gharama zimepanda sana kutoka shilingi 3,000 zimefika 7,000 hadi 10,000. Kwa Mtanzania wa kawaida na haswa mwanamke ni ngumu sana ku-afford gharama hizi kutokana na hali halisi ya maisha ya Kitanzania. Kama mnavyojua, kwa mfano ukiangalia kule kwetu, vijijini, kama vile Mkoani Mara, kule shughuli zetu ni ndogo ndogo ambazo zinakuwa kidogo ni ngumu sana, na haswa mama anapouguliwa na mtoto au yeye mwenyewe anapouguliwa; na ukizingatia sisi wanawake wa Mkoa wa Mara wengi ndio sisi viongozi wa familia au tunao hudumia familia kwa ujumla. Naishauri Serikali iziangalie gharama hizi kwa jicho la pili ili kuangalia namna ya kumpunguzia mwananchi gharama hizi ili aweze sasa kwenda kutibiwa kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niongelee hili suala la dawa hospitalini. Kwa kweli hali ya dawa hospitalini hairidhishi kabisa. Zile dawa muhimu sana pale wanapoenda kutibiwa wagonjwa hospitalini na hasa wale wagonjwa wanaoenda wengine wakiwa wana bima, wanapoenda kutibiwa hospitalini wanaambiwa waende wakanunue nje ya geti la Hospitali, Zahanati na kwenye vituo vya afya. Jambo hili si zuri sana kwa kweli, hili ni tatizo, na waathirika wakubwa ni akina mama na watoto.

Mheshimiwa Spika, isitoshe Mheshimiwa Rais ametoa pesa bilioni 129 kwa ajili ya kununua madawa. Sasa je, hawa ambao wanachelewesha chelewesha au kubana bana hizi fedha hawaoni kama wanamchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi?

Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe kama mtoto wa Chifu Hangaya, msimuangushe mama yetu, amefanya kazi kubwa sana. Fedha aliyowapa fanyieni kazi, otherwise kila siku mtakuwa mnatumbuliwa na mnalalamika. Naamini kabisa, kwa huu uteuzi wa sasa wa Mheshimiwa Ummy pamoja na Mkurugenzi mpya na ofisi yake, naamini kabisa sasa mambo yatakaa vizuri. Mheshimiwa Ummy usituangushe. Waheshimiwa Wabunge tunakuamini sana, tunaamini mambo yatakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hospitali za Rufaa za Mikoa kwa kweli kipekee nimpongeze sana kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa kutuendelezea hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Mara. Mama ametoa fedha ambazo zimeendeleza hospitali hiyo. Sasa, mimi niwaombe watendaji kuwa fedha hiyo itoke ili hospitali hiyo imalizike. Pia niombe, kuna suala la wauguzi, tunaomba pia tupate madaktari bingwa ili kudumisha ile huduma ya afya zaidi. Kipekee zaidi nimpongeze pia mama yetu kwa kazi nzuri sana aliyoifanya ya kuongeza ajira kwa Watanzania. Ajira Mheshimiwa Rais alizozitoa zimeleta faraja kubwa kwa baadhi ya Watanzania, kwa kweli tunamshukuru sana na kumpongeza Mungu ambariki.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali lakini pia nimuombe mama. Mama hapa ulipokaa basi tunakuomba uongeze ajira mama kwa kuwa hazitoshi, ajira bado watu wengi wana vyeti ambavyo viko kwenye mifuko yao na wengine wameviweka chini ya kitanda. Mama tunakuomba ongeza ajira kidogo, wapo watu wengi ambao hawana ajira. Kwa hiyo mimi niseme tu nashukuru sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia zaidi nampongeza sana mama kwa kitendo alichokifanya juzi cha kuwajali Watanzania wafanyakazi kwa kuwaongezea mishahara, Mungu akubariki sana mama, tunaamini mama unaupiga mwingi, haulali usingizi unatuhangaikia Watanzania, tunasema tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. Jamani Waheshimiwa Wabunge akina mama na akina baba pigeni vigelegele jamani kwa Chifu Hangaya wakeeee!

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii kwa kuchangia Wizara hii. Kwanza nianze moja kwa moja kuomba Serikali iwaangalie sana wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu hali ya ajira kwa kweli ni mbaya sana katika Taifa letu la Tanzania na kama wamejitolea kujiajiri wenyewe basi ni vizuri au ni vyema wakaangaliwa kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna maeneo ambayo wamechukua wawekezaji wakubwa ambayo yamekaa muda mrefu na hawajafanyia kazi yamekwisha rudishwa Serikalini. Sasa basi ni vyema Serikali ikaona ni jinsi gani ya kuangalia kuwagawia maeneo hayo wawekezaji wadogo wadogo ili na wao waweze kufaidi sungura katika Taifa lao la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ni vyema sasa yakaangaliwa maeneo yote ambayo wanachimba wachimbaji wadogo wadogo wakafikishiwa umeme. Hili kwa kweli limekuwa ni tatizo kubwa sana na haswa Mkoani kwangu Mara Wilayani Bunda, Wilaya ya Musoma ya Vijijini, Wilaya ya Tarime, lakini na kote kule ambako kuna wachimbaji wadogo wadogo katika Taifa hili la Tanzania. Naamini kabisa umeme umekuwa ni tatizo kubwa sana na wao pia kwa sababu wanajisimamia ili kupata kipato basi ni vyema wakaangaliwa kwa jicho la ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu Doto Biteko pale walipokuwa wasikivu walinikubalia tukaenda nao kwenye Mgodi wa North Mara Nyamongo tukaongea na wale wawekezaji na wale wawekezaji pia ni wasikivu. Kuna mara nyingine tunawapiga lakini kuna kipindi pia inabidi tuwapongeze pale wanapofanya vizuri. Kwa kweli wamejenga baadhi ya shule kwa mfano wamejenga Shule ya Julius Kambarage Nyerere wamejenga Shule ya Bulege wamejenga pia Sekondari Nyarokoba lakini pia wamejenga Ingwe Sekondari, wamejenga hosteli ambazo baadhi wamerekebisha majengo lakini pia wamejenga hosteli na baadhi ya vituo vya afya wametujengea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tuna jambo moja ambalo kidogo lina utata, kutokana na kwamba sisi Wanamara lakini pia Wanatarime kama ninavyokuwa naongea mara kwa mara lakini hata watu wote wanajua kwamba ametokea muasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Katika mazingira hayo basi mkoa wetu unatakiwa uonekane mkoa wa mfano lakini mkoa wa kipekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,wawekezaji wamekwishwa pata faida kubwa sana kutokana na Mgodi wa North Mara lakini pia kule Butiama ambako pia walimaliza na walipata faida za kutosha. Basi ni vyema wakatuwekea barabara wao kama wawekezaji sio wawe wanasubiri tu Serikali itoe pesa ya barabara. Hata wao faida walizopata pia wanaweza kutuwekea basi barabara nzuri ya lami na sisi tukaoneka tukafanana fanana na dhahabu naamini kabisa bado hatujafanana na dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwa kuishauri Serikali kwenye hili suala la malipo ya wale wanaolipwa fidia. Haya malipo yametumia muda mrefu sana ni muda mrefu sana sasa Serikali ikiwa inavutana na wale ambao wametoa ardhi yao kwa ajili ya wawekezaji. Naamini kabisa Serikali imekwisha faidika na uwekezaji ambao umewekwa katika Mgodi wa Nyamongo (North Mara) ambako mwazo ilikuwa Barrick na sasa jina limebadilika limekuwa ni North Mara ambayo ipo ndani ya Barrick.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo sasa ni muda mrefu, toka mwaka 1995 ambapo wananchi wale walitoa ardhi yao kwa ajili ya wawekezaji. Naamini kabisa wamekwisha pata faida ya kutosha na bahati nzuri Dada yangu Mheshimiwa Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi alitoa ufafanuzi hapa juzi lakini pia wanapaswa kuliangalia hili. Basi akae Waziri wa Madini, akae na Waziri wa Ardhi waliangalie hili, ili kusudi na wale wananchi pia waweze kumaliza tatizo hili, lakini Sheria ya Ardhi inasema mtu anapofanyiwa uthamini wa ardhi yake na ardhi ikarudi Serikalini baada ya miezi sita, ikivuka miezi sita alipe pia faida ya ile ardhi yake kwa sababu haitumii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tokea mwaka 1995 ni miaka 20 na zaidi. Naamini kabisa Serikali sikivu italifanya hili na kutokana na kwamba wananchi wa Tanzania sasa wana hali ngumu sana, huo ndio ukweli hali ni ngumu, vitu vimepanda bei, gharama ni kubwa wale watu wanajenga nyumba ambazo kwa kweli inakuwa thamani yake ni ndogo sana na wengine wanashindwa kumalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nimuombe Waziri atakapokuja hapa ku wind up atuelezee ni jinsi gani atafanya ili kusudi wale wananchi, kwa sababu sasa ni miaka mingi imepita wapewa riba yao. Katika ile pesa yao, katika ardhi yao ambayo waliitowa kwa ajili ya wawekezaji ambayo naamini kabisa tunapofanya tathmini au uthamini kwa ardhi inapokuja kwetu itakuwa ni fundisho pia ambalo watalipwa haraka wanaokuwa wameshafanyiwa uthamini kwa sababu sasa hili tatizo linatokea. Naamini kabisa sio tu mkoani kwangu Mara hata maeneo mengine ya Tanzania naamini hili tatizo limekuwa ni kubwa sana la kutolipwa mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwa kusema nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, unachapa kazi Mwenyezi Mungu akubariki sana kwa kweli unaweza na unaiweza Wizara Mungu akubariki sana. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chetu kikubwa kwa Wanamara na Wanatarime tunaomba…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tulipwe pesa zetu za uthamini kwa sababu hadi sasa mashimo yamekwishwa kuwa makubwa sana, wawekezaji wamekwisha pata pesa nyingi sana. Hivyo tunaomba basi na sisi tulipwe ili kusudi na sisi tufaidi ile dhahabu yetu ambayo sisi wenzenu Tarime tulikuwa hatujui biashara ya kulima..

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, … na kilimo chetu sisi ilikuwa ni dhahabu sasa kama wametutoa kwenye dhahabu na sasa wanataka tulime au tufanye shughuli nyingine basi nafikiri ni vyema tukalipwa ili kusudi na sisi tufaidi. Tufaidi angalau kasungura ka Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na Mungu akubariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea katika Wizara hii. Kwanza nimpongeze sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya. Mama alituambia hakuna kitakacholala na kweli tunaona hakuna kinacholala kila kitu kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, na Wizara nzima kwa ujumla kwa kazi nzuri wnayoifanya. Sisi wananchama au watu wako tunasema piga kazi, chapa kazi, mama amekuamini na Watanzania tunakuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niende moja kwa moja kwa kusema namshukuru Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi mizuri aliyoileta Mkoa wa Mara, lakini pesa nyingi tulizozipata Mkoa wa Mara kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wetu. Kipekee zaidi niombe kiwanja cha ndege cha Musoma kinachoendelea kujengwa.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais ametoa pesa nyingi, lakini hadi sasa kinachoendelea ni kwamba mpaka dakika hii kuna watu ambao bado wanadai fidia zao. Basi nikuombe Mheshimiwa Waziri ujitahidi watu hawa wapate fidia zao ili na wao wafanye mambo yao mengine kwa sababu mpaka sasa mambo yao mengi yamesimama. Kwa hiyo, uchumi kidogo unakuwa unasuasua.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi niombe pia kutokana na hali halisi ya Mkoa wa Mara ndio Mkoa uliomtoa Mwasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere basi ni mkoa ambao pia unapaswa kupata upendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara hii inayotoka Majita - Musoma – Busekela ambayo imekwishajengwa kilometa tano tu na bado kilometa 87. Kilometa hizi zilizobaki ni nyingi sana na ukizingatia tangu Uhuru wa Taifa hili Wilaya ya Musoma Vijijini walikuwa hawajawahi kuiona lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, mimi nikuombe sana utuangalie kipekee Mkoa wa Mara na barabara hii ya Majita. Pia ukizingatia mimi mtoto wa Chifu Hangaya naishi huko Majita, kwa hiyo, inakuwa ni ngumu kidogo kwenda mpaka kule kwa sababu inakuwa ni ngumu kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kipkee nimpongeze Meneja Waheshimiwa Wabunge, TANROADS Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa kweli ni mchapakazi, anafanya kazi vizuri na mimi mwenyewe ni shahidi. Kuna daraja ambalo lilikuwa limeharibika muda si mrefu sana ambalo linaunganisha Musoma mpaka Mwanza, Daraja la Nyamika A pale Sabasaba. Mimi nilipita pale usiku nikamshuhudia Meneja amesimama wakati kazi zikiwa zinaendelea. Basi tukiwapata viongozi wa hivi basi naamini Taifa letu litaendelea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kipekee mimi pia niongelee kuhusu uwekezaji; uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa Taifa la Tanzania, lakini pia utaongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza kipato katika Taifa hili. Ninamuamini sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anazozifanya na ndio maana anakwenda kutafuta mahusiano nchi za nje kila kukicha. Mama halali asubuhi, mchana na usiku, anafanya kazi twenty-four-seven, yeye halali wala hapumziki kwa ajili yetu, anakwenda kututafutia wawekezaji. Naamini kabisa mama hawezi kwenda kututupa shimoni, mama ni mlezi, kwa hiyo, uwekezaji huu wa bandari mimi nina amini kabisa ni uwekezaji salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niwaombe tu hata wale waliokuwa Mawaziri kipindi hicho wanapobeza inakuwa sio jambo zuri, hata wao wakati huo walipokuwa Mawaziri na wao walikuwa wanafanya kazi kwa kipindi hicho. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki wawaache Mawaziri walioko madarakani wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala linatukera sana, unamkuta mtu alikuwa Waziri kipindi chake na yeye mwenyewe wakati akiwa Waziri hakufanya vizuri, lakini sasa hivi kwa sababu sio Waziri anaona wenzake wanafanya kazi anawazongazonga. Hawa ni wateule wa Mheshimiwa Rais, wawaache wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi kama Mbunge kilichoniuma sana, kuna Mbunge mwenzetu huku ndani ambaye kipindi hicjho alikuwa Waziri, muda wote kazi kusema sema wenzake. Mara Mwigulu ajiuzulu, Mwigulu ana makosa gani amemfanyia nini; lakini Wizara hii sio ya Mwigulu. Kwa hiyo, ni kitendo ambacho kinatuudhi sana mtu kwenda kwenye mitandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi niseme tu tunamtia moyo Mheshimiwa Waziri Mbarawa, afanye kazi uwekezaji huu ni mzuri sana. Hata sisi tulikwenda kujifunza katika Bandari hii ya Jebel Ali ambayo ni katika hii Kampuni ya DP World. Hii kampuni sisi kama Wabunge tuliangalia vitu vingi, tuliona kwa kweli ufanyaji kazi wao ni mzuri, wana vifaa vya kisasa na wako vizuri kabisa, lakini kama Wabunge tumejiridhisha. Mimi nilimuuliza Mheshimiwa Waziri, inakuwaje katika uwekezaji huu mbona Watanzania wanalalamika? Mheshimiwa Waziri, akatuelewesha kwamba Watanzania wataendelea kufanya kazi kama kawaida na wawekezaji wataendelea kuwkeza, lakini wameweka mikataba mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, hawezi kututupa shimoni. Mimi niwaombe ndugu zangu tumwamini Mheshimiwa Rais, kwa manufaa ya bandari yetu imesuasua kwa muda mrefu. Tukipata wawekezaji wazuri, lakini tukaweka mikataba mizuri inayotusaidia sisi ama kutu-support sisi kama Watanzania, mimi ninaamini kabisa ndio mikataba tunayoihitaji na ndizo kazi ambazo tunazihitaji sisi zifanywe na Mawaziri za kutafuta wawekezaji wazuri. Kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania kuweni na imani na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye ni mama, yeye ni mzazi, tena mkae mkijua na mnajua mimi naamini kwamba mwanamke ni mwaminifu kuliko mtu yeyote duniani kwa sababu yeye ni mzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii adhimu. Kwanza nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu nzima, lakini nimpongeze zaidi Mheshimiwa Rais kwa kuwateua watu hawa kwa sababu naamini kabisa yeye ana maono, ameona kwamba watatuvusha katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwa kuangalia kwenye suala la mikopo zile asilimia 10. Kuna hili suala la asilimia 10 kuna suala la umri ambao umri wenyewe unaanzia miaka 18 mpaka 34. Hiki kipindi cha sasa kwa umri ule wa nyuma uliokuwa unaanzia miaka hiyo ilikuwa ni sahihi, lakini ukiangalia mbele zaidi vijana wa sasa mpaka miaka 45 bado ni vijana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia miaka 18 mpaka hii miaka 34 wengi wao wanakuwa ni wale vijana ambao bado wanatabia zile zinaitwa tabia za utoto zaidi. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Kwa hiyo, ukiangalia kuanzia hapo miaka 36 mpaka miaka 45 kundi hili ndiyo kundi ambalo lina maono kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi binafsi ningeishauri Serikali basi iongeze umri kutoka umri ule wa miaka 18 mpaka 34 sasa ifikie kwenye miaka 45 ili kusudi hata hii mikopo wanapopewa wapewe watu wanaojifahamu wanaojielewa, ili kusudi kuleta tija katika jamii yetu lakini katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hili suala la bajeti kwa kweli mimi nimuombe tu Mheshimiwa Waziri na timu yake msione aibu kwenda kuomba bajeti na kurudi mara mbilimbili kuomba bajeti na mkirudi kwetu sisi Wabunge basi tutawapitishia kwa sababu Wizara hii ni muhimu sana na nimtambuka na haswa kwa jamii yetu kutokana na mambo mbalimbali. Kwa kweli bajeti hii ni kidogo sana, haiwezi kukidhi mahitaji au uwitaji wa bajeti hii au uhitaji wa eneo hili kutokana na kwamba shughuli zake ni nyingi sana na hasa ukizingatia kama hivi unavyoona hali ya sasa hivi ni mbaya mbaya sana. Lakini bado hao hao Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana usafiri na saa nyingine pia wanaleta usumbufu sana kwetu sisi Wabunge wanatuomba wakati sisi wenyewe na sisi wenyewe ni tia maji maji, kwa hiyo wanakuja kutuomba pesa za usafiri na nini suala ambalo tunaamini kabisa Wizara ikitengewa bajeti ya kutosha basi na wo watapata usafiri na vitendea kazi vingine ili kusudi boresha mambo mbalimbali katika wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia walivyotangulia kusema Wabunge wenzangu kwenye hili suala la mikopo midogo midogo; hii mikopo nafikiri sasa imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu ukienda sehemu nyingi wengine wanashindwa kurudisha mikopo, lakini wengine wanacheleweshwa, lakini wengine pia hawaendelei, kila siku wanakuwa pale pale ni kwa nini basi? Ni kwa sababu hii mikopo wanapopewa ni midogo sana kwa mfano shilingi milioni tano unawapa watu 10 ukigawanya nafikiri ni kidogo sana. Mimi kwenye somo la hesabu nilikimbia umande nafikiri mkiangalia mkipiga hapo hesabu mtaona kwamba ni pesa kidogo sana, kwa hiyo ni pesa ambazo hazitoshelezi kwa ajili ya mtu au mjasiriamali kujiendeleza kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na ndiyo maana wengine sasa wanaishia kula nyumbani, lakini kwa wale wenzangu na mimi wanaishia kwenda kununua carolight, anaona kwamba sasa mbona hii hela ni kidogo sana mimi itabidi nikapendeze, labda nitairudisha lakini sasa inakuja kutokea anashindwa hata kuirudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niishauri Serikali hii pesa inatakiwa iongezwe, huu mkopo at least basi wawe wanapewa kwa awamu lakini wapewe fedha ya kutosha kwa mfano hao watu 10 wanaweza kupewa awamu ya kwanza hiyo milioni tano halafu tena wakaangaliwa awamu nyingine wakaongezewa tena milioni tano, tena wakaja wakaongezewa kidogo ili kusudi ile mikopo iwe na tija na hasa kwa Watanzania. Tunamshukuru sana mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake anaotuonyesha kwa Watanzania na hasa Watanzania wajasiliamali wadogo na wanawake kwa mikopo aliyoitoa ya milioni 10 kila mkoa ombi langu au ushauri wangu kwa Serikali; mikopo hii ili iwe na tija iende ikasimamiwe vizuri kwa sababu huko kwenye Wilaya zetu au mikoani kwetu huko huwa kuna ile hali ya wanasiasa kuingilia mikopo hii wanapoingilia mikopo hii wanaweza ukakuta kuna kikundi cha shangazi, mjomba, bibi, babu unakuta yuko Mheshimiwa Meya tayari kawandaa ndugu zake au kawaandaa kikundi fulani anajua hapa sasa hapa hiki kikundi huyu Agnes ani-support, huyu ndiyo mpiga debe wangu hawa wapiga debe na wengine hawapati lakini hiyo siyo nia ya Mama Samia Watanzania wote mnapaswa kujua Mheshimiwa Wetu Rais hajali itikadi ya mtu, itikadi ya chama, wala kuangalia huyu mtu katokea sehemu gani yeye ametoa pesa imsaidie kila Mtanzania. Kwa hiyo, wale watendaji wabovu mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri nenda kashughulike nao, lakini sasa ufanyike ufuatiliaji wa kina, kwa sababu pesa hizi ukizifuatilia kwa undani zaidi utakuta ziko kwa hao hao viongozi ambao ni viongozi wetu wa pale manspaa na nipesa ambazo vikundi vingi vinalalamika sasa unajiuliza kwamba kwa nini vikundi vingi vinalalamika...

MHE. LUCY T. MAYENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agness kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Lucy Mayenga.

T A A R I F A

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kumpa taarifa itakuwa ni vizuri sana Hansard iweze kukaa vizuri ni Mheshimiwa Agnes mchangiaji wetu akaweka rekodi vizuri Maafisa ya Maendeleo ya Jamii ni watu ambao tunawategemea sana kwenye halmashauri zetu, wanatufanyia kazi kubwa sana kwa hiyo ni vizuri tu labda nadhani aweke vizuri rekodi kwamba siyo kwamba wanaomba omba, labda pengine mtu akiwa na jambo anaweza akahitaji msaada wa hapa na pale; hilo moja lakini lingine Mheshimiwa Rais akutoa fedha hizo milioni 10 kwa ajili ya mikopo huko kwenye halmashauri zetu, ahsante sana ni vizuri aweke rekodi vizuri isiye ikaonekana kwamba kuna vitu ambavyo tunaviweka havijakaa sawa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo na hapo hapo nimesahisha kutokana na maneno yake. Lakini tu mimi niseme tu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, kengele ya pili imegonga.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana haya yote pia katika hii wizara maendeleo ya jamii michezo pia ni furaha kwa maana hiyo kwa furaha hii mnyama kule Mwanza tulimpiga chini na sasa tunasema furaha ipo basi katika maendeleo ya watu nashukuru sana, Yanga oye. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini niipongeze sana Wizara, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwa jinsi alivyoitengeneza hii bajeti, inaonekana hakika ni bajeti ya Watanzania. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jambo jema alilolifanya la kuongeza elimu bure mpaka kidato cha sita. Hii inaonesha ni jinsi gani Ilani ya CCM inavyotekelezwa na ziada maana huu hakika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini ni jinsi gani Mheshimiwa wetu Rais anaonesha anawajali Watanzania na hasa akinamama, maana akinamama ndio wenye mzigo mkubwa ndani ya familia. Hili jambo ni zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kutokana na suala hili zuri liongezeke pia suala la ajira kwa Walimu ili wawe wengi kwa ajili ya kuleta tija kutokana na hii elimu bure. Isije tu ikawa elimu bure lakini madarasani Walimu hawatoshi. Ni wananchi wengi sana ambao hawana ajira wako mtaani, kutokana na suala hili mimi ninaamini kabisa Serikali imelenga huko huko, japokuwa tu tunashauri na sisi kama Wabunge, lakini naamini kabisa lengo la Serikali pia hapa ni kuongeza ajira kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee pia suala kama aliloongea Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kuhusiana na hili suala la asilimia 10. Serikali iangalie sehemu ya kutoa hii fedha asilimia hii kwa ajili ya shughuli inayotakiwa kufanyika. Ni jambo zuri na ni jambo jema, lakini naamini kabisa wajasiriamali wengi mtaani ni vijana, akinamama lakini pia wamepunguza idadi ya mambo ambayo yangefanyika hasa kwa hawa vijana ambao wanajiajiri wenyewe ambao labda wangefanya uhalifu, uharibifu, lakini wamejiajiri kutokana na hii mikopo midogo midogo.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ikiwaondolea tena hii asilimia itabaki nini kwa maana moja au nyingine ile asilimia waliyokuwa wanapata vijana asilimia nne akinamama asilimia nne na walemavu asilimia mbili na hapo sasa hatuoni kitu cha kubaki. Sidhani kama mimi ni mmojawapo wa ku-support suala hili. Kwa kweli tuiombe Serikali iondokane na wazo hili la kuondoa hii fedha ibaki pale pale na ikiwezekana bajeti ijayo wawaongezee, hii fedha ni kidogo sana haitoshi, huko mtaani watu hawana ajira na wamejiajiri wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende pia kwenye suala la kumpongeza sana mama yangu Mheshimiwa Rais kwa hili suala la kuanzisha Chuo Kikuu cha TEHAMA hapa Dodoma. Ameupiga mwingi sana, kwa kweli amefanya jambo zuri sana kwa sababu pia itaongeza ajira kwa vijana. Hata hivyo, niishauri Serikali na ombi langu kwa Serikali, Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao unatakiwa uangaliwe kipekee kwa sababu ni mkoa uliomtoa muasisi wa Taifa hili Hayati Nyerere. Katika mazingira hayo kutokana na nchi za wenzetu tunavyoziona mikoa kama hii ya watu muhimu kama hawa huwa ni mikoa ya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutukubalia suala la kuweka eneo la historia au eneo la utalii pale Butiama, lakini haitoshi na sisi pia Mkoa wa Mara tunapaswa kuwa na vyuo vya ziada ambavyo vitakuwa ni mfano, lakini vitakuwa ni vyuo ambavyo vinaonesha kabisa muasisi wa Taifa hili ametokea Mkoa wa Mara; na sisi pia Mkoa wa Mara tungeomba basi baadaye tuletewe Chuo cha TEHAMA ili kusudi kuutambulisha Mkoa wa Mara kwamba ndio mkoa aliotoka muasisi wa Taifa hili na vyuo vingine pia vya mahesabu, lakini pia na vyuo vikuu mbalimbali. Kwa hili nimpongeze sana mama yangu lakini ombi hili kwa Serikali naomba sana lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hili suala la matatizo yaliyotokea kwa wenzetu. Niwaombe ndugu zetu au majirani zetu wa nchi Jirani, sisi Watanzania tuna amani yetu ya kutosha, lakini wanapaswa kujua kabisa kwamba Tanzania ni nchi huru nchi inayojitegemea. Masuala ya kuingilia uhuru wetu haiwahusu wao washughulikie matatizo yao, sisi kama ni furaha yetu tutashughulikia wenyewe, kama ni matatizo yetu tutashughulikia wenyewe kama nchi, wao hawapaswi kuingilia masuala ya Tanzania na kuleta chokochoko zao Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hiki ni kitendo ambacho tunakilaani sana na sisi Watanzania au wawakilishi wa Watanzania tunawaambia wasirudie tena na hasa wale wenzetu ambao pia wanafikia hatua hata ya kumtusi Mheshimiwa Rais wetu, wajue kwamba yule ndio kiongozi wa nchi yetu. Wanapomtusi Mheshimiwa Rais wanatutusi sisi wenyewe Watanzania. Watanzania tushikamane kwa pamoja tuiangalie nchi yetu tukijua kabisa hii ni vita ya kiuchumi, mbona haya hayajatokea kabla mama hajaanza kutangaza Royal Tour? Wameona sasa Tanzania tunakwenda juu sana katika utalii wameona sasa waanze kuleta chokochoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tuseme tuko pamoja Watanzania tuungane kwa pamoja matatizo yetu tutayamaliza wenyewe na mambo ya Tanzania tutayashughulikia wenyewe, hatumhitaji mtu yeyote wa nchi ya jirani kuja kushughulikia matatizo ya Tanzania au kuendelea kuleta matatizo ndani ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tunawaambia wakae wakijua Tanzania ina Majeshi ya kutosha, lakini Tanzania ni nchi ambayo iko imara, wakituletea chokochoko, Mheshimiwa Rais akija akisimama akisema, wajue kabisa watakiona na wasirudie tena kumtusi Mheshimiwa Rais. (Makofi) [Maneno haya siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais
na Mheshimiwa Mpango kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuondoa ushuru kwa wachimbaji wadogo wadogo. Pia naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutusikiliza Wabunge wake tunapokuwa tunashauri. Ndiyo maana huwa tunawashauri wenzetu. Unaposhauri kwa uzuri, hata unayemshauri anakusikiliza. Kwa mfano, nilishauri kuhusu suala la malipo au fidia ya watu wanaodai madai yao Tarime, waliokuwa wanaitwa Tegesha na sasa Mheshimiwa Rais amenisikiliza; alimtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wake wa Madini na sasa wanalipwa kuanzia wiki ijayo, watapewa malipo yao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kukubali kutoa mapori ya akiba kuwa hifadhi ya Taifa kwa sababu ni suala zuri kwa maana ya kwamba tutaongeza pato la Taifa baada ya kuwa tuna hifadhi nyingi za Taifa.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wenzetu humu ndani wanatakiwa watafutiwe hifadhi ya ziada ili kusudi wakaishi huko kwa sababu wana tabia za wanyama. Hawaoni mambo yanayofanyika na Mheshimiwa wetu Rais, hawakubaliani na mambo yanayofanyika na Mheshimiwa wetu Rais, utadhani wao sijui wanaishi wapi! Aliiomba dada yetu JD, naomba ninukuu kidogo, “Hawajui walipotoka, watajuaje wanakokwenda? Ya kwao yamewashinda, yetu hawatoweza.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo,…

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Agness. (Kicheko)

MHE. AGNESS M. MARWA: Ndiyo Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Nyimbo haziruhusiwi. Endelea Mheshimiwa Agness. (Kicheko)

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia, napongeza kipekee pia Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, pia kupunguza ushuru wa mchuzi …

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Mheshimiwa Agness, kuna…

MHE. AGNESS M. MARWA: Ndiyo!

SPIKA: Kuna Mheshimiwa amesimama hapa.

KUHUSU UTARATIBU

SPIKA: Mheshimiwa Agness, kama ulisema hilo, futa tu ili uendelee.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, sawa nimefuta. (Kicheko)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi na kupitia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo mazuri anayoyafanya ya kuwatetea hasa Wajasiriamali wadogo wadogo wanyonge na haswa kwa kupunguza tozo ndogo ndogo kama vile kutoa tozo kwenye huu mvinyo ambao kwa maana moja au nyingine wajasiliamali wadogo wadogo ambao wanauza huu mchuzi wa zabibu, sasa watapa soko zuri na watapandisha kipato chao juu zaidi.

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa Mheshimiwa Mpango ataangalia pia kuondoa ushuru kwenye mahindi ili kusudi sasa hata gongo baadaye itengenezwe kwa kutumia mahindi ili kusudi baadaye ibadilishiwe jina na kupandishwa hadhi ili ipewe jina la mvinyo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kweli Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi kubwa, imefanya kazi nzuri…

(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Agness kengele imeshalia. Nakushukuru sana, ahsante sana.

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Magufuli oyee! (Makofi/Kicheko)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti,nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchangia Muswada huu wa Maji. Kwanza niipongeze sana Kamati hii kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kurekebisha muswada huu japokuwa baadhi ya vifungu vinatakiwa kurekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta muswada huu Bungeni ili kusudi Wanakamati waujadili na sisi Wabunge tuujadili na baadae tuupitishe. Mimi nauunga mkono kwa asilimia 9,999 na moja ya Mungu, kwa maana ya kwamba muswada huu ni mzuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa muswada huu ni mzuri, kuna baadhi ya vitu ambavyo tunatakiwa kujua au vinatakiwa kurekebishwa. Kwa mfano, tunatakiwa kujua matumizi yaliyo sahihi na matumizi yasiyo sahihi ni yapi? Kwa sababu ukisema tu matumizi yaliyo sahihi au yasiyo sahihi, hata sisi Wabunge mtatukuta siku moja tuko Mahakamani kwa sababu ya matumizi yasiyo sahihi. Naweza kutoka hapa Bungeni nimeshika kitu kibaya, nikaenda pale nje nikanawa mikono tu. Kwa kuwa nimenawa mikono na sijaweka bakuli kwa chini, basi yatakuwa labda matumizi yasiyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Magufuli kwa kumtua mwanamke ndoo kichwani. Kule kwetu Mkoa wa Mara ukianzia na Wilaya Musoma Mjini kupitia mradi wa Bukanga, sasa hivi mabomba ya majisafi yanapasuka ovyo. Kutokana na mradi huo wa Bukanga, kwa sababu maji yamekuwa mengi sana na kupitiliza, Mheshimiwa Magufuli amewaagiza wataalam wake, wameshatawanyika katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara na wameanzia na Wilaya yangu au Jimbo langu la Tarime Mjini na Vijijini, lakini pia wameenda kwenye Jimbo langu la Bunda Mjini, wamefanya utafiti, lakini pia wameshaweka utaratibu wa kupeleka maji hayo yanayotokana na huo mradi wa Bukanga kupeleka kote huko katika hayo Majimbo lakini pia kupeleka Mkoa wa Mara mzima kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa pesa nyingi alizozitenga kwa ajili ya mwanamke. Mheshimiwa Rais anaonyesha ni jinsi gani anavyomjali mwanamke, anaonyesha ni jinsi gani anavyomjali mzazi, anaonyesha ni jinsi gani mzazi alivyomuuma. Ndiyo maana tulimwonyesha Mheshimiwa Rais kwamba tunamwomba awatue wanawake ndoo kichwani, sasa ameamua kujikita kwenye suala la kumtua ndoo mwanamke kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe ndugu zangu, hasa kaka yangu Mheshimiwa Heche. Mheshimiwa Heche
asitupotezee muda wa kutoletewa maji Tarime. Kwa sababu muswada huu umekaa vizuri sana na Mheshimiwa Rais kauleta kaweka wazi haya mambo. Yeye anawaambia kule wananchi kwamba hakuna maji, hakuna nini kitu ambacho siyo kizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Rais kwa maombi niliyomwomba mimi Mbunge wa Tarime Mjini na Vijijini afanye haraka suala hili ili kusudi wanawake wa Tarime sasa wajue kwamba kupitia yeye Mheshimiwa Rais kwa kura walizompa, ameweza kuwapelekea maji na kuwatua ndoo kichwani, na mimi Mbunge wao sasa nimeomba na watapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sina zaidi ya hayo. Nasema naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)