Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Devotha Methew Minja (36 total)

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa Naibu Waziri kuhusu kushughulikia tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali imekuja na mpango wa kuanzisha Bwawa jipya la Kidunda ambalo litakuwa likitoa huduma ya maji katika mikoa mingine lakini siyo kwa Mkoa wa Morogoro. Serikali haioni kama si vyema kuanzisha bwawa hilo pasipo kwanza kushughulikia kero ya maji ya wananchi hasa wa Manispaa ya Morogoro kuliko kuitumia mito yao kuendelea kutoa huduma katika mabwawa ambayo yatahudumia mikoa mingine nje ya Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema si vyema kuanzisha Bwawa la Kidunda, Serikali iliona ni muhimu sana tuwe na Bwawala Kidunda kwa ajili ya kuhakikisha kwanza wananchi wa Dar es Salaam watapata maji ili muda wote Mto Ruvu uwe unakuwa na maji ya kutosha. Bwawa lile pia tumeshalifanya usanifu siyo kwa ajili ya maji tu lakini pia pamoja na kuzalisha umeme. Kwa hiyo, lina manufaa mengi na hivi sasa tupo mbioni kupata wawekezaji tunaoweza kushirikiana nao tuweze kujenga bwawa lile. Maeneo yale mengine ambayo hayana maji, Naibu Waziri ameshasema vizuri kwamba kwenye programu yetu awamu ya pili tunakwenda kushughulikia tatizo la maji katika maeneo hayo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Kwa kuwa matatizo ya ukosefu wa huduma katika Hospitali za Mkoa wa Morogoro hayana tofauti na matatizo ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Morogoro una Hospitali ya Rufaa ambayo inatoa huduma katika wilaya zake zote lakini cha kusikitisha hospitali hiyo haina huduma ya X-ray. Huduma ya X-ray iliyopo ni ya zaidi ya miaka 20 iliyopita hali ambayo inawalazimu wagonjwa waliolazwa hata wodini kwenda kupata huduma za X-ray nje ya hospitali hiyo katika Hospitali za Mzinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapeleka huduma hizo za X-ray katika Hospitali hii muhimu ya Rufaa ambayo inategemewa na wananchi wa Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, hiki kilio tumekisikia na tunajua Morogoro ni center. Ukisema huduma ya X-ray pale Morogoro hakuna wakati tukijua Morogoro ni muungano wa barabara mbili, inayotokea Dodoma na ile inayotokea Iringa, na katika njia moja au nyingine kama kesi za ajali za magari lazima mgonjwa moja kwa moja atapelekwa katika Hospitali ya Mkoa. Sasa kama changamoto hii ni kubwa kiasi hiki, naomba niseme katika zoezi letu la kupeleka vifaa vya upimaji tutahakikisha Morogoro inapewa kipaumbele. Naomba aiamini Serikali yake itaenda kufanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri kwa majibu yake, amesema mwaka 2018 ndio mradi huo utakamilika, ni nini commitment ya Serikali kwa kuwa hadi kufikia mwaka 2018 na wananchi wanaihitaji nishati hii muhimu kwa ajili ya maendeleo. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia njia mbadala kuweza kusaidia wananchi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tatizo la nishati ya umeme katika Mkoa wa Katavi linafanana kabisa na matatizo ya umeme katika Mkoa wa Morogoro hasa katika Manispaa ya Morogoro katika Kata za Mindu, Kihonda na Mkundi ambapo wananchi hawa kwa muda mrefu hawana nishati ya umeme ingawa wanapitiwa na Gridi ya Taifa. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kuhakikisha wananchi hawa wanapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment ya Serikali kwa Mkoa wa Katavi pamoja na Sumbawanga kwa kweli ni kubwa sana. Hadi sasa mbali na mradi huu wa kupeleka umeme wa kilovolti 400 hivi sasa Serikali imeanza kukarabati majenereta mawili yaliyokuwa na matatizo pale Mpanda. Yale majenereta yalikuwa na uwezo wa megawati 2.6 lakini yalikuwa yanatoa umeme wa megawati 2.3, ukarabati wa majenereta hayo umekamilika tarehe 5 mwezi huu kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mpanda pamoja na maeneo ya jirani umeme utapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatua ya pili sasa hivi ujenzi umeanza kufunga jenereta mbili mpya ambazo pia zinatengenezwa, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, kupitia mradi wa ORIO. Jenereta hizi zina uwezo wa kufua megawati 2.5 kwa ujumla wake kwa hiyo, Mji wa Mpanda pamoja na Sumbawanga sasa watakuwa na jumla ya megawati 5.1 ambapo matumizi yao kwa sasa hivi ni megawati 2.6. Kwa hiyo, vijiji vyote sasa vya Mchangani, Dilifu, Longililo, Mpakani, Gereza la Kakalankurukuru, pamoja na Kalamsenga vyote vitapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji vya Morogoro vikiwemo Mindu pamoja na Kihonda, vijiji hivi vinapelekewa umeme kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu unaoanza tarehe 15 Disemba, 2016. Na vijiji vyote vya Kihonda na maeneo ya jirani ikiwemo pamoja na Mindu vitapelekewa umeme wa uhakika mwaka huu.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikiliza majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambapo amesema hivi sasa Serikali ime-stick kupima kwenye Sh. 300,000/= kwa hekta moja lakini pia amesema Serikali inashirikiana na wapima binafsi. Je, Serikali imeweka mikakati gani ya kuzuia hao wapima binafsi wasiendelee kuongeza bei kwa maana ya kuwaumiza wananchi ambao wanahitaji huduma hii ya kupimiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali inasema nini juu ya wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi katika Manispaa ya Morogoro ambao walifuata taratibu zote za kupata hati, lakini hivi sasa wamevunjiwa nyumba zao na wengine wanalala nje huku wakiwa na hati zao mikononi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kulipa fidia kwa wananchi hao ambao wana hati?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza habari ya Serikali imeweka mikakati gani kuweza kudhibiti hawa wapima binafsi ili wasiwe na bei ambazo zinaumiza wananchi. Serikali inaweka viwango kutegemeana na hali halisi ya bei inayotakiwa kutozwa mwananchi wakati wa upimaji. Sekta binafsi nayo ipo na inafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali na ndiyo maana juzi tu walikuwa na mkutano wao ambao uliwakutanisha wapima wote ambapo hili pia lilijitokeza kama kero kwa wananchi wengi ambao wanalalamika kwamba gharama zao ziko juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachofanyika ndani ya Serikali, kwanza ni kuzungumza nao na pengine kuweza kuelekeza bei ambazo zitaweza kutumika ili kutompunja au kumuumiza zaidi mwananchi. Kwa sababu ukishaachia soko huria wale wanakwambia wana gharama nyingi na kubwa kama ambavyo tumesema vifaa vyao jinsi vilivyo, lakini kama Serikali hatuwezi kuwaachia waendelee kulitawala soko na wakati huohuo tunahitaji ardhi iwe imepimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara tunajadiliana nao na nadhani Waziri aliongea nao na akaelekeza vizuri nini cha kufanya ili waweze kuja na taratibu ambazo hazitamuumiza mwananchi wa kawaida. Kwa sababu gharama za upimaji zinafahamika na wao wasiwe na visingizio vya kutaka kutoza fedha nyingi bila sababu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tulivyokuja kwenye bei ya viwanja, vivyohivyo na gharama za upimaji lazima nazo zitakuwa na bei elekezi pamoja na kwamba ni soko huria, lakini ni bei ambazo zinalinda mlaji ili kuondokana na tatizo hili. Lengo letu ni kuhakikisha ardhi yote imepimwa. Gharama ni kubwa lakini na Wizara haiwezi kupima ardhi yote peke yake bila kushirikiana na taasisi binafsi, inaweza ikawa ngumu zaidi. Kwa hiyo, naomba mtupe muda, tunazungumza nao tuweze kufikia muafaka namna gani ya kuweza kutoza gharama za upimaji kwa maeneo yote hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea habari ya wale ambao wamevunjiwa na walifuata taratibu. Serikali ilishaelekeza, kama kuna watu walikuwa na hati na walizipata kihalali, watu wale walitakiwa kutambuliwa. Kwa sababu zoezi hili ni kama lile lililofanyika Dar es Salaam ambapo Wizara ilielekeza wale waliokuwa na hati za halali za umiliki walitakiwa kuleta hati zao Wizarani wakatambuliwa. Kwa hiyo, hili linaweza likafanyika hivyohivyo na Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Morogoro tuna ofisi yetu, wapeleke hati zao tuweze kuzipitia, kama zilikuwa ni halali basi tutaona nini cha kufanya, kama ni viwanja vingine au kufuata utaratibu mwingine. Kwa sababu wakati mwingine kuna watumishi ambao hawakuwa waaminifu, anaweza akawa anasema ana hati kumbe hati yenyewe siyo halali. Kwa hiyo, tutazipitia zile hati zote, aliyekuwa na hati halali amevunjiwa kimakosa, basi taratibu za kisheria zitazingatiwa na atapata haki yake.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la maji Ngara linafanana kabisa na tatizo la maji katika Mkoa wa Morogoro, licha ya Mkoa Morogoro kuwa na mito mingi, lakini wananchi wa Morogoro hawapati maji safi na salama. Je, Serikali haioni kama kuna haja sasa ya kujenga bwawa lingine liweze kusaidiana na Bwawa la Mindu ili kutosheleza maji kwa wakazi wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la Mheshimiwa Devotha Minja kuhusiana na kuongeza kiwango cha maji katika Bwawa la Mindu; kwa bahati nzuri pia nimeuzunguka Mkoa wote wa Morogoro, nimeenda Bwawa la Mindu.
Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Minja kwamba tayari Benki ya Ufaransa imetupa Euro milioni 70 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kuongeza kiwango cha Bwawa la Mindu ili Bwawa la Mindu liweze kuwa na maji mengi. Wakati nafanya ziara kule, nilikuta uzalishaji wa maji ni lita milioni 25 badala ya lita milioni 45 zinazohitajika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi makabrasha ya zabuni yamekamilika, tumeshasaini mkataba wa mhandisi mshauri ambaye atapitia nyaraka zilizopo kwa muda wa miezi sita na baada ya hapo tunatangaza tenda ya kuanza ujenzi ili tuweze kuongeza kiwango cha maji katika Mji wa Morogoro. Kwa hiyo, suala hilo la Mheshimiwa Minja tunalifanyia kazi, lakini naomba Mheshimiwa Mbunge anisaidie. Wakati nafanya ziara pale tumekuta lile bwawa linachafuliwa sana.
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tunaimba kila siku kuhusu uchafuzi wa mazingira, naomba tusaidiane. Watu tayari wanafanya kilimo cha umwagiliaji juu ya mito ambayo inaingiza maji katika Bwawa la Mindu. Tusaidiane, tuwatengenezee utaratibu mwingine ili tuwe na uhakika wa maji katika Bwawa la Mindu.
MHE DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kukuniona. Licha ya Mkoa wa Morogoro kuwa na mito mingi na hatimaye kuweza kulisha Mikoa mingine kama Pwani, Dar es Salaam na Mkoa wa Tanga lakini Mkoa wa Morogoro hauna maji safi na salama. Sasa ni lini Serikali itahakikisha Manispaa ya Morogoro hususan katika Kata za Bingwa, Kiegea A na B, Mkundi, Kingolwira na Kihonda zinapata maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza swali lake linazungumza kiujumla kwamba Mkoa mzima hauna maji salama hili si kweli, si kweli kabisa. Ni kweli kuna upngufu wa maji lakini huwezi kusema Mkoa mzima hauna maji salama, watu wangekuwa wameshakufa. Kwa hiyo, kazi ziko na kuna miradi inayoendelea na eneo analolizungumza pale Manispaa ya Morogoro tunao mradi mkubwa wa kupanua mradi ule ambao upo. Tutaongeza ukubwa wa lile bwawa la Mindu tutaongeza mtandao; hivi sasa kazi imeshaanza kwa awamu ya kwanza ya kupeleka hayo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata fedha kutoka Benki ya Ufaransa ya kuweza kuweka miundombinu ya kutosha kabisa kuongeza upatikanaji wa maji, huu wa sasa mara mbili zaidi. Kwa hiyo, Serikali inatambua tatizo hilo na inalifanyia kazi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya kazi.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa na viwanda vingi sana. Baada ya ubinafsishaji, viwanda vingi vimekufa na vingine vimegeuka kuwa ma-godown. Je, Serikali ina mpango gani wa uhakikisha inafufua viwanda hivi viweze kutoa ajira kwa wakati wa Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Devotha nawe umewahisha shughuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isionekane mimi ni bingwa wa kukwepa maswali, Mheshimiwa Devotha hakuna kiwanda kitabaki godown Morogoro. Tajiri namba moja alisimama Morogoro na microphone, akasema kama ningekuwa na Waziri wa Viwanda, Viwanda vya Morogoro vingefanya kazi, alikuwa ananisema mimi. Viwanda vyote unavyovisema, vinafanya kazi sasa. Kiwanda cha Canvas kitaanza ku-role Kiwanda cha MOPROCO kitaanza kutengeneza mafuta nami mambo yataendelea kuninyookea. (Kicheko/Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Magereza mengi nchini yanaendeshwa kinyume kabisa na Kanuni Namba 10 ya Umoja wa Mataifa ambayo inazungumzia namna ya kuwahifadhi wafungwa kwamba ni lazima wakidhi vigezo ikiwemo afya, hali ya hewa, joto na nafasi ya kutosha. Magereza mengi nchini likiwemo Gereza la Songea ni mojawapo ya magereza kongwe nchini ambalo lilijengwa tangu mwaka 1948. Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba gereza hili nalo linakidhi vigezo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tangu Rais aseme maneno ka-ta yameleta athari kwa magereza mengi nchini ikiwemo magereza 14 ya Mkoa wa Morogoro ambayo hivi sasa yako kwenye giza tororo. Serikali haioni kama magereza haya kuendelea kuwa na giza ni kinyume kabisa na haki za Umoja wa Kimataifa na pia inasababisha Askari Magereza kushindwa kufanya kazi zao vizuri? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, nimpongeze kwa kuonyesha concern ya msongamano wa wafungwa kwenye magereza na ameuliza Serikali tuna mkakati gani. Moja ya mkakati wa muda mrefu tunaofanya ni wa kuhahakisha kwamba tunajenga magereza hasa kwenye maeneo ambayo ni ya kilimo yawe na ukubwa wa kutosha na magereza ya mijini yawe kwa ajili ya mahabusu ambao wanahitajika kuwa karibu na mahakama kwa ajili ya usikilizaji wa kesi zao. Kwa hawa ambao walishahukumiwa wawe katika magereza ambako kazi ya kuwarekebisha inaweza ikafanyika huku kukiwa na kazi ya uzalishaji inayoendelea katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la umeme kukatwa, jambo hilo lilishashughulikiwa kwa sababu tayari Hazina ilishatoa fedha kwa ajili ya mafungu yetu ya Polisi, Magereza pamoja na maeneo mengine. Mimi niwasisitizie Waheshimiwa Wabunge, nia na maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Rais yanarekebisha kwa kiwango kikubwa Maafisa Masuuli wanapopewa fedha zilizokuwa zimeelekezwa kwa ajili ya utilities waweze kutumia katika maeneo yale ambayo yalikusudiwa fedha hizo ziweze kutumika. Kwa maana hiyo, badiliko hili linaweza likaathiri katika kipindi ambacho tu madeni yalikuwa yamelimbikizwa lakini itajenga nidhamu ya kudumu ya Maafisa Masuuli kuweza kuelekeza fedha zilipokuwa zimeelekezwa ili kupata jawabu la kudumu la matumizi bora ya fedha zinazotolewa na Serikali. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inaitaja kazi ya uandishi wa habari kuwa ni jukumu la kisheria. Serikali inawachukulia hatua gani watu wanaowazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi zao kama vile RC kuvamia kituo cha Clouds, baadhi ya waandishi kuvamiwa wakiwa kwenye mkutano wa CUF, baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuwakamata waandishi wa habari na kuwaweka ndani na hata jana kule Arusha katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent waandishi wa habari kumi walikamatwa wakiwa wanatimiza majukumu yao. Ni lini Serikali itaacha tabia hii mbaya ya kuwakamata kamata waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana kwa maswali yake na kwa kutambua kwamba Sheria ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 inahimiza kwamba kazi ya waandishi wa habari ni jukumu la kisheria, nadhani sote tunakubaliana na hilo. Hata hivyo, anaposema kwamba kuna watu wanaozuiwa kufanya kazi zao, mimi naamini kwamba kama kweli waandishi wa habari wanafuata maadili na wanatafuta habari kwa ajili ya kujenga na siyo kuvuruga nchi, siamini kabisa kwamba kuna watu wanaoweza kuwazuia.
Sera yetu ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 inahimiza kwamba taasisi zote za Serikali na wadau wote wa habari kutoa taarifa kwa wanahabari na inahimiza kabisa kwamba wale Maafisa Habari katika Mikoa na Halmashauri wawe tayari kutoa ushirikiano kwa wanahabari ili kusudi wanahabari waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kuna hili la watu wanaozuia, mimi naomba baadaye tuonane na Mheshimiwa Devotha Minja aweze kuniambia ni wapi kwa sababu ndiyo kwanza nasikia hilo. Sera yetu inahimiza kwamba ni wajibu kwa Maafisa wa Habari kuwapa ushirikiano wanahabari kwa sababu jukumu lao linatambulika kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili Mheshimiwa Waziri alilitolea ufafanuzi vizuri sana wakati anahitimisha hotuba yake hapa Bungeni. Kwa hiyo, naomba nisirudie tena maneno ambayo aliyasema Mheshimiwa Waziri hapa Bungeni.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara ya Kichangani - Tubuyu katika Manispaa ya Morogoro ambayo ina urefu wa kilometa nne imejengwa kwa kilometa moja kwa shilingi bilioni tatu yaani kilometa nne imejengwa kwa shilingi bilioni 12. Je, Serikali iko tayari kupeleka wataalam kwenda kubaini ubadhirifu wa ujenzi wa barabara hii ambayo imejengwa kwa Mfuko wa Benki ya Dunia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata concern hii kutoka kwa Wabunge hasa wa Mkoa wa Morogoro na hasa barabara hizi zinazojengwa under Strategic Cities Project pamoja na barabara zingine ambazo zinajengwa katika Manispaa. Bahati nzuri kwa taarifa za Morogoro tunazifanyia kazi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kufanya verification kuangalia value for money katika eneo lile lakini zoezi hilo tutalifanya maeneo mbalimbali ikiwemo katika Mji wa Hai, Mkoa wa Kilimanjaro. Lengo letu ni kwamba thamani ya fedha ipatikane ili wananchi waweze kupata huduma inayolingana na thamani ya fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kilio chake kimesikika tutaenda kulifanyia kazi eneo hili.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Waziri amesema Serikali haitarajii kuwepo kwa ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita mamia ya wanafunzi wenye vigezo walikuwa wakishinda katika Bodi ya Mikopo wakifuatilia upatikanaji wa mikopo. Wengi wa wanafunzi hao wanatoka katika familia maskini, na Bodi ya Mikopo vigezo wanavyoviangalia ni ufaulu. Wanafunzi wengi ambao wanasoma katika shule binafsi zikiwemo Feza na nyinginezo wana ufaulu wahali ya juu ukilinganiswa na shule za Serikali. Hata hivyo hivi sasa wanafunzi hao wanaotoka kwenye shule za private ambao wana ufaulu mkubwa wanapata fursa hii ya mikopo ikilinganishwa na wanafunzi maskini wanaotoka katika shule za Serikali. Je, ni lini Serikali sasa itaangalia vigezo stahiki vya wanafunzi ambao wana uhitaji wa kuingia vyuo vikuu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ilikuwa ni kwa wenye uhitaji, lakini sasa lengo lile limebadilika na sasa hivi mikopo inatolewa kwa kozi, kwa mfano wanaosoma udaktari, engineering wanapata mikopo kwa asilimia 100. Ni nani amesema kwamba nchi hii haihitaji accountants? Nani amesema nchi haihitaji waandishi wa habari? Nani amesema haihitaji lawyers? Naomba majibu ni kwa nini sasa Serikali isiangalie namna ya kutoa mikopo kwa kuangaliwa mahitaji ya wanafunzi wa hali ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba leo hii Wizara yetu itatoa Kauli ya Serikali kuhusiana na masuala ya udahili na mikopo, kwa hiyo tutaelezea kwa kirefu kidogo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo itoshe tu kwa ajili ya maswali ya nyongeza niseme yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu wanafunzi kuandamana kwa sababu ya kucheleweshewa mikopo, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Bunge hili lilipitisha shilingi bilioni 427 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea.
Mheshimiwa Spika, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaotegemea kupata mikopo ni 30,000. Tayari Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 29,578. Tofauti na huko nyuma wakati huu fedha ilitangulia kwenye bodi, wanafunzi ndio wanaenda kuomba, wakati huko nyuma fedha zilikuwa zinachelewa. Tayari Serikali imeshatoa shilingi i bilioni 147 kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka. Kilichotokea ni kwamba taratibu za udahili ambazo wakati huu wanafunzi wenyewe ndio walikuwa wanachagua vyuo ndizo zimechelewesha utolewaji wa mikopo na ndiyo maana kuna hawa wanafunzi wachache ambao bado hawajapata mikopo. Lakini kama ninavyokwambia tayari wanafunzi 29,578 wameshapata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili linalohusu vigezo vinavyotumika. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna vigezo vikuu vinne vinavyotumika kwaajili ya kutoa mikopo.
Mheshimiwa Spika, kigezo cha kwanza ni uyatima, kigezo cha pili ni ulemavu, kigezo cha tatu ni uduni halafu kingine ni ile kuangalia masomo ya kipaumbele kulingana na mipango ya maendeleo ya taifa. Sasa wanapochanganya vigezo hivi vyote ndipo tunapata idadi ya wale wanafunzi ambao watapata mikopo. Kwa hiyo baadaye Mheshimwa Waziri atakapotoa taarifa atatoa takwimu kuonesha kwamba vigezo hivi vimezingatiwa na wanafunzi wale ambao tunasema wanastahili zaidi ndio hasa wamekuwa walengwa na ndio wamepata mikopo. Nashukuru sana.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la Ranchi ya Mbarali linafanana kabisa na tatizo la Ranchi ya Mkata iliyoko Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambapo Ranchi ile hivi sasa imegeuka kuwa pori na Serikali imeshindwa kuiendeleza. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kubinafsisha Ranchi ile, mashamba yatolewe kwa wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro ya muda mrefu?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi na naomba nijibu swali la nyongeza ambalo ameuliza Mheshimiwa Devota Minja na kama ambavyo Naibu wangu amejibu vizuri sana maswali hapa Bungeni, tunataka Wabunge watuelewe. Kwanza Serikali haijashindwa kusimamia ranchi hizi, tunachokifanya kama Naibu Waziri alivyozungumza tunafanya tathmini sasa tupitie ranchi zetu zote tujue shughuli zinazofanyika.
Mheshimiwa Spika, tunajua upungufu uliopita kwamba zipo ekari sasa hivi, unakuta ekari moja imekodiwa mtu analipa Sh.500/= kwa mwaka. Kuna ekari zimekodiwa mtu analipa Sh.1,000/= kwa mwaka; kuna mahala ambapo uwekezaji hauendani na eneo lilivyo. Kwa hiyo tunafanya tathimini ili tuje na mpango mkubwa kwa sababu gani ranchi hizi shabaha ya kuanzishwa kwake haijaondoka toka tulivyoanzisha na ndio maana tunataka kupitia ranchi hizi tufanye mageuzi makubwa ya kuwa na viwanda vikubwa nchini kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wenye viwanda nchini wanapata mahali pa kutunzia mifugo yao kabla hawajachinja.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunataka tuwa- transform wafugaji wetu, hatuwezi kuruhusu huu ufugaji wa mtu anafuga mifugo leo, anamchunga ng’ombe mpaka anakufa mwenyewe. Lazima tuwabadilishe wafugaji wetu tuwe na maeneo ambayo tutazalisha mitamba ya kutosha, tutazalisha ndama wa kutosha, tutazalisha mifugo ambayo inaweza ikagawiwa kwa wafugaji ili wafugaji wetu waweze kupata neema ya ufugaji huu.
Mheshimiwa Spika, kupitia ranchi hizi tunategemea kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika Taifa hili na kwa wafugaji Tanzania. Kwa hiyo, tuungeni mkono tutakapoleta mabadiliko yetu na Wabunge muache hili la kila mmoja kuhitaji ligawiwe kwa wananchi; tunataka ranchi hizi zitumike kwa faida ya Taifa na kwa mapana zaidi (Makofi).
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa ni Sera ya Serikali kwa Wazee kupata matibabu bure, Kambi ya Funga Funga ya Mjini Morogoro, ambayo inahudumia wazee wengi hivi sasa wanakosa huduma ya matibabu kutokana na hospitali ya Mkoa wa Morogoro kukosa madawa ya kutosha, hivi sasa wazee wale wakifika hospitali wanapewa panado na madawa mengine wanaambiwa wakanunue kwenye pharmacy za nje ya hospitali. Nataka kujua, je, Sera hii ya matibabu bure kwa Wazee inatekelezeka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 imetamka wazi kwamba matibabu kwa Wazee wasiojiweza itakuwa bure na hili tunalitekeleza kwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hatuna uhaba wa dawa sasa hivi, bajeti ya dawa imeongezeka sana kutoka bilioni 30 kufikia takribani bilioni 270, dawa zote za muhimu zinapatikana. Kama kuna suala mahsusi kuhusiana na Kambi hii Mheshimiwa Devotha Minja ningependa kupata maelezo ya ziada ili tuweze kuchukua hatua stahiki. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kukosekana kwa mipaka limeendelea kuleta migogoro na kuwaumiza wananchi wengi hapa nchini. Tatizo hilo limeendelea kuwaumiza wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi pale Manispaa ya Morogoro ambao wamevunjiwa nyumba zao, takribani miaka miwili imepita baada ya kuambiwa kwamba wamejenga kwenye Hifadhi ya Msitu wa Kundi. Hata hivyo wananchi wale walikuwa na vibali halali na walipewa ramani zote na mji kujenga nyumba zao. Je, Serikali ipo tayari kuwalipa fidia wananchi hawa wa Mtaa wa CCT Mkundi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na matatizo katika msitu wetu ule wa Mkundi ambapo wananchi wengi walikuwa wameondolewa kwa sababu walikuwa wamevamia katika maeneo haya. Kama nilivyokuwa nimesema, hata jana ambapo tumekuwa tukitoa maelezo kwa muda mrefu, kwamba yapo maeneo ambayo yalikuwa yamepimwa katika hifadhi za Taifa, maeneo ni mengi, na jana nilisema kwamba vijiji takribani 366 vimepimwa kwenye hifadhi za misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili eneo pia wananchi hawa kweli walikuwa wamepewa katika hayo maeneo lakini tulipogundua kwamba wamepewa kimakosa ndiyo maana jitihada zikafanyika katika kuwaondoa.
Kuhusu fidia, kwa sababu taratibu zilikuwa zimekiukwa, kwa kweli Wizara tutaangalia kama kweli wanaweza waka-qualify kupata fidia, lakini tunaamini kabisa kwamba kama walivamia na kama Serikali hawakupewa kihalali kwa kupitia, kwa sababu ule ni msitu, basi fidia inaweza isitolewe, lakini kama tutakuta kwamba waliondolewa kimakosa basi tutalitafakari na kuona namna bora ambavyo tunaweza tukalitatua hilo tatizo la wananchi wake.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoeleza Naibu Waziri, kazi za wasanii ni kuburudisha, kuelimisha, kuonya na kukosoa, wasanii wamekuwa wakifanya kazi hizi hata wakati wa kampeni tulishuhudia wasanii walivyofanya kazi yao vizuri na wakati mwingine waliimba nyimbo za kuponda upinzani na mlikuwa mkishangilia. Jambo la kushangaza hivi sasa wasanii wakiimba nyimbo za kukosoa Serikali wanashughulikiwa na mfano mzuri ni Ney wa Mitego pamoja na Roma Mkatoliki.
• Swali la kwanza, je, ni wakati gani sasa kazi hizi za wasanii zinathaminika?
• Swali la pili, kwa bahati mbaya sana Rais ametoa maagizo ya wale ambao wamehujumu kazi za wasanii na kuacha kabisa kuwawajibisha Serikali yake ambayo imeshindwa kabisa kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na Marehemu Mzee Francis Ngosha ambaye amekufa akiwa maskini wa kutupwa.
Je, Serikali inataka kukamata kazi za wasanii wakati ninyi wenyewe mmemuhujumu Mzee Francis Ngosha ambaye mpaka sasa hivi hana lolote, amekufa na hakuacha alama yoyote katika familia yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maswali yake yako nje kidogo na swali la msingi, lakini kwa sababu tu ya kumbukumbu tulizonazo, swali lake la kwanza linalouliza kwamba ni wakati gani kazi za wasanii zinathaminiwa? Kama alivyosema mwenyewe, kwamba kazi ya sanaa ni kuburudisha, kuelimisha, kuonya, kukosoa na kadhalika, niseme tu kwamba kazi za wasanii tunazithamini wakati wote hasa wakati zinapoelimisha, zinapoburudisha na kufanya kazi zile ambazo zinalijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kusema kwamba wasanii huwa wanashughulikiwa wakiikosoa Serikali, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hizi za sanaa zinasimamiwa na sheria. Tunayo Sheria ya BASATA Namba 23 ya mwaka 1984, tuna Sheria nyingine Namba 4 ya Bodi ya Filamu ya mwaka 1976 na tuna Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Namba 7 ya mwaka 1999. Kwa hiyo, tunachohitaji ili tuweze kuzithamini kazi hizi ni kwamba wasanii wazingatie sheria, wafuate sheria na taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa wasanii ambao tunaona kwamba wameenda kinyume, hatua huwa zinachukuliwa na hatua zenyewe, kwa mfano kuna msanii mmoja anaitwa Nikki Mbishi ambaye alipewa tu onyo kutokana na kuweka picha ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne katika wimbo wake I am sorry JK. Hizo ni hatua tu ambazo huwa tunazichukua ili wasanii hawa wafuate sheria. Sheria ya BASATA inahitaji wasanii hawa wapitishe nyimbo zao BASATA ili ziweze kukaguliwa kabla hazijatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakiwa wamepitia kule ina maana kwamba watatoa kitu ambacho kinazingatia sheria na kinafuata maadili, sasa huu ni ukiukwaji wa maadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwingine ambaye ameshawahi kupewa onyo ni Diamond kupitia kwa Meneja wake, ambaye alitumia majina ya viongozi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Ney wa Mitego, huyu aliimba wimbo wake wa Wapo ambapo ulifungiwa na BASATA kwa muda, lakini baadaye ulifunguliwa baada ya kuwa na makubaliano ya jinsi ya kuuboresha huo wimbo. Huyo mwingine Roma, hakuna hatua ambayo imechukuliwa na Serikali kwa mwaka huu kuhusu msanii huyo na ninadhani ninyi ni mashahidi kwamba alijieleza yeye mwenyewe kwa vyombo vya habari na Mheshimiwa Waziri pia alikuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ambalo linamhusu Marehemu Francis Ngosha na Mheshimiwa Devotha anadai kwamba Serikali imemhujumu, hii siyo kweli, hakuna hujuma. Kimsingi yapo majina mezani mpaka sasa kama matatu hivi yanayohusiana na ubunifu wa nembo tunayoitumia, ambayo ni nembo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpaka sasa bado haijajulikana ni nani hasa ambaye ni mbunifu wa nembo hii. Kwa sababu kwa mfano, yupo Marehemu ambaye alishatangulia mbele za haki muda mrefu anayeitwa Abdallah Farhan wa Zanzibar, yeye vielelezo tayari vimeshakutwa katika kumbukumbu zake jinsi alivyokuwa akibuni nembo yetu ya Taifa, nembo ya Kenya pamoja na nembo ya OAU kipindi hicho alipokuwa akisoma Makerere University. Kwa hiyo, yapo majina ambayo yanadaiwa kwamba yalishiriki katika kutengeneza nembo hii. Ninaomba sana… (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wataalam wafanye kazi ya kutambua ni nani hasa ambaye alishiriki kubuni. Kwa sababu Marehemu Francis yeye anajulikana kama ni mchoraji, lakini siyo mbunifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme tu kwamba labda swali la Mheshimiwa Devotha Minja ni ishara ya wazi kwamba kuna uhitaji mkubwa sana wa kuwa na orodha ya wasanii na kazi ambazo wamezifanya na ni kitu ambacho sasa hivi Wizara tumeanza kukifanya ili kusudi tuwe na orodha ya wasanii wote katika nchi yetu na kazi ambazo wanazifanya ili mwisho wa siku utata kama huu usiweze kutokea tena. (Makofi)
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Matatizo ya afya katika Mkoa wa Songea yanafanana kabisa na matatizo ya afya katika Hospitali ya Mkoa Morogoro ambapo licha ya kazi nzuri inayofanywa na Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro lakini hospitali ile inaelemewa na wagonjwa wengi. Kwa mwezi mmoja Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro inatibu zaidi ya wagonjwa 15,000. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kupeleka vifaa muhimu kama MRI, CT- Scan na X-ray machines za kisasa ili kuwapunguzia mzigo wagonjwa ambao wanalazimika hivi sasa kwenda Muhimbili kwa matibabu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Mheshimiwa Mohamed Abood kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye hospitali ile lakini pia kwa kutumia pesa zake za mfukoni kuweza kununua baadhi ya vifaa tiba ambavyo vinatumika katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumwaga sifa hizo kwa Mheshimiwa Abood, naomba nijibu sasa swali la Mheshimiwa Devota Minja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkubwa kupitia mradi wake wa ORIO wa kupeleka vifaa tiba kwenye Hospitali za Mikoa nchini, Hospitali za Wilaya na baadhi ya vituo vingine maalum vya kutolea huduma za afya nchini. Mradi huo ulisuasua mwaka jana kwa sababu tulikuwa hatujalipa counterpart funds kwa Serikali ya Netherlands ambao ndiyo wafadhili wa mradi ule. Sasa tumeshaanza kukamilisha sehemu yetu ya fedha ambazo tunapaswa kulipa ili mradi uanze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika baada ya miezi mitatu mradi huu utaanza kutekelezwa. Mradi huu ukitekelezwa, tutaweza kupata CT-Scan, MRI, Ultra-sound, digital X-rays na vifaa vingine vingi vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa kwa ajili ya hospitali zetu hapa nchini. Sina hakika mgao umekaaje mahsusi na Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, lakini naamini kwa vile ni kati ya hospitali kubwa hapa nchini inawezekana ikapata badhi ya vifaa hivi vikubwa ambavyo vinatarajiwa kuja lakini nitaangalia na akipenda nimpe taarifa nitampa baadaye.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijinasibu kuwa ina mpango wa kujenga viwanda 100 kwa kila mkoa...
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikieleza kuwa ina mpango wa kujenga viwanda 100 kila mkoa na mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa na viwanda vingi tangu enzi za Mwalimu. Lakini hivi sana viwanda vingi vimekufa na vimegeuka kuwa ma-godown, mfano wa viwanda hivyo ni Kiwanda cha Komoa, Kiwanda cha Tanzania Leather Shoes, Kiwanda cha CERAMIC, Kiwanda cha U-nuts, sasa Serikali haioni kama kuna umuhimu wa kufufua viwanda vilivyokuwa ndipo ije na wazo la kujenga viwanda vipya. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza tunamshukuru kwa ufuatiliaji. Ni kweli Serikali iko serious kuona kwamba viwanda vingi vinajengwa Tanzania hasa katika kuongeza thamani mazao ya wananchi tulio nao jirani na viwanda hivyo kama ambavyo nimekuwa nikisistiza kila wakati viko katika ngazi za aina mbalimbali. Kuna viwanda vidogo sana, viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa. Kwa hiyo, wananchi wenye mitaji midogo wanao uwezo pia wa kuanzisha viwanda kulingana na hali inayowezekana.
Sasa suala la viwanda vya zamani ambavyo havifanyi kazi, kwanza tufahamu kwamba kiwanda kina tabia sawa sawa na binadamu. Kiwanda kinapokosa mazingira mazuri na wezeshi kinaweza kufa sawa na binadamu anavyokufa. Kwa hiyo, ni wajibu wetu sasa hivi kuhakikisha kuwa tunajenga mazingira wezeshi ikiwemo kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya viwanda na hiyo ndiyo kauli mbiu na hiyo ndiyo jitihada inayofanyika ndiyo maana unakuta jitihada mbalimbali zinaendelea.
Kwa hiyo, Morogoro ni sehemu mojawapo ambayo tayari tumeshaitembelea na hivyo viwanda ambavyo unasema vimekuwa havifanyi kazi vizuri kama Leather Industries tayari tuko katika mchakato wa kuhakikisha kwamba makongano mbalimbali ya leather yanafanyika ili kuhakikisha viwanda hivyo vinakuwa vizuri na kuleta tija kwa Taifa. Na nizidi kuwaomba watanzania wengi msitishike, nimetembelea viwanda. Zaidi ya viwanda nilivyotembelea asilimia 90 vingi vinaendeshwa na sisi Watanzania wenyewe. Kwa hiyo, tujitoe hata sisi Wabunge tuanzishe viwanda kadiri inavyowezekana kulingana na mahitaji ya maeneo yetu.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Imekuwa ni kawaida kwa Seriikali kutoa matamko ambayo hayatekelezeki. Hivi tunavyozungumza, matumizi ya dola yako pale pale. Bado zipo Taasisi za Serikali ambazo zinapata huduma au kutoa huduma kwa dola.
Je, ni lini Serikali itapitia upya sheria zake na kuona uwezekano wa kulinda shilingi kama ilivyo nchi ya Kenya au nchi ya Afrika Kusini ambapo huwezi kupata huduma bila kutumia rand? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, utitiri Bureau De Change hapa nchini umeongeza mdororo wa shilingi na imekuwa kama ni vichaka vya kutakatisha fedha.
Je, Serikali haoni kama kuna haja ya kuwa na sheria mahususi za kubana Bureau De Change?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa lazima tufahamu ni Bunge hili ndilo linalopitisha sheria na hivyo kama upungufu wowote, Bunge hili litaleta mapendekezo na Bunge liweze kupitisha sheria au kufanya mabadiliko kwenye sheria zinazotumika hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tufahamu kwamba katika misingi ya kiuchumi, matumizi ya fedha za kigeni hayasababishi kushuka au kudorora kwa thamani ya fedha yoyote ile duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tufahamu, Mheshimiwa Mbunge ametaja nchi ya Afrika ya Kusini; napenda kuliambia Bunge lako Tukufu katika fedha ambayo imepita katika misukosuko mikubwa ni fedha ya nchi ya Afrika ya Kusini pamoja na kwamba wana sheria ya kutotumia fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba wananchi na Watanzania waelewe kwamba yapo mambo muhimu ambayo yanasababisha misukosuko ya thamani ya fedha ya Taifa lolote, nayo ni haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni nakisi ya urari wa biashara; pili, mfumuko wa bei na tatu, ni tofauti ya misimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu limefanya vizuri sana katika hatua hizi ambazo nimezitaja; nakisi ya urari wa biashara; na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza kwenye kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili tuweze kusafirisha bidhaa zile ambazo zina thamani kubwa na kuhakikisha kuwa nakisi ya urari wa biashara ndani ya Taifa letu unakuwa ni mdogo na tumefika hatua nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naliomba Bunge lako tukufu waendelee kuipa support Serikali yetu, Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Serikali ya viwanda inayosisitiza kuongeza thamani ili tuweze kuhakikisha kwamba thamani ya shilingi yetu inakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, amesema utitiri wa Bureau De Change. Kama Mheshimiwa Mbunge amekuwa ni mfuatiliaji mzuri, Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza usimamizi katika Bureau De Change. Tumefunga zaidi ya maduka 92 ya kubadilishia fedha hapa nchini ikiwa ni katika jitihada za kuhakikisha kwamba maduka haya hayawi ni vichaka vya kusafirisha fedha zetu na hayawi ni vichaka vya kutakatisha fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kusimamia, tumepewa dhamana ya kusimamia sheria mimi na Mheshimiwa Waziri wangu, sheria zote za kifedha, sheria za Taasisi za kifedha, tutaendelea kusimamia na kuhakikisha thamani ya shilingi yetu inaendelea kuimarika. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali imekuwa ikipanga miradi mingi ya umwagiliaji katika mkoa wa Morogoro ambayo haitekelezeki, je, Serikali sasa haioni kuna haja ya kwuaatumia wataalam ambao wanatoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) waweze kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuendeleza kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizarani pamoja na changamoto ambazo tumeziona tukaona haja sasa ya kupitia ule mpango kabambe, na tumejipanga katika kuhakikisha tunakuwa na miradi michache lakini yenye tija ya uzalishaji katika nchi yetu. Kwa hiyo, wazo lako na ushauri wako tumeupokea katika kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya umwagiliaji ili iweze kuwa na tija katika nchi yetu.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya tatizo la maji safi na salama kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro bado ni kizungumkuti. Bwawa la Mindu ambalo limekuwa likitegemewa na wananchi wa Manispaa kwa sasa halitoshelezi. Kwa kuwa Mkoa wa Morogoro una mito mingi, je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga bwawa lingine ili iwe mwarobaini kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro ambao wanakosa maji kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge dada yangu Devotha, ni kweli Morogoro kumekuwa na changamoto kubwa sana ya maji na tunajua kabisa tunaelekea Tanzania ya Viwanda, lazima tuwe na mahitaji ya maji kwa maana ya maji yenye utoshelevu. Sisi kama Wizara ya Maji tumeliona hilo, tupo kwenye majadiliano ya dola milioni 70 katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji safi na salama katika Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumezuka tabia mbaya ya Jeshi la Polisi, wanapokwenda kumkamata mtuhumiwa wakimkosa wanakamata mtu mbadala akiwa mke au watoto.
Naomba kufahamu Jeshi la Polisi linatoa wapi mamlaka haya ambapo wanashindwa kutumia mbinu zao za kiintelijensia kukamata mtuhumiwa badala yake wanarahisisha na kukamata mke au watoto na kuwatesa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Devotha Minja, shemeji yangu na niseme tu kwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria na niseme hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya adhabu kwa mbadala. Kosa linabaki kuwa la mkosaji. Kwa hiyo, nielekeze tu popote pale ambapo pana mtu amefanya kosa atafutwe yule yule aliyekosa na kama wengine wanaweza wakasaidia basi wasaidie katika namna ya kuelezea jinsi wanavyoweza kufahamu, lakini siyo kuchukua adhabu ya mtu mwingine aliyekosa.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilitegemea Waziri angeniambia kwa sababu kutaifisha ni suala lingine na kuendeleza ni suala jingine, kwamba hizi ekari zaidi ya elfu 67 ambazo zimetaifishwa Serikali hii imeziendeleza vipi? Sasa maswali yangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kumekuwa na matumizi mabaya ya hii sheria ya kutaifisha mashamba. Wapo watu ambao walikuwa wakimiliki mashamba kihalali na wana hati, lakini wamenyang’anywa mashamba hayo. Wapo watu ambao walishinda hata kesi Mahakamani, lakini mashamba yao wamenyang’anywa. Ni lini Serikali hii itaacha uonevu kwa wananchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Kata ya Tungi, eneo la Kiyegeya katika Manispaa ya Morogoro tangu mwaka 1984 walikuwa wakimiliki mashamba ya Tungi Estate, lakini mwaka 2014 wananchi wamenyang’anywa mashamba yale kwa maana ya kuachia ujenzi wa Star City.
Kwa kuwa, Serikali mpaka sasa haina lengo la kuanzisha mji ule wa Star City, lakini vilevile mpaka sasa Serikali haijalipa fidia. Naomba kufahamu ni kwa nini Serikali isiwaache wananchi hawa wakaendelea na shughuli zao za kilimo?

Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko na tumekuwa tukifuatilia hata kwenye vyombo vya habari. Baadhi ya mashamba ambayo yanafutwa na wamiliki ambao wamekuwa wakilalamikia kwamba, walikuwa na mashamba hayo kwa muda mrefu, lakini wamenyang’anywa. Kwa hivyo, naomba Waziri anayafahamu vizuri, yakiwemo ya Mvomero, yakiwemo ya Hananasifu…
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali hatujataifisha mashamba. Nilimsahihisha kidogo kwenye swali lake nikasema, yaani kwa Kingereza ni revocation, revocation siyo kutaifisha. Rais anaweza akayachukua mashamba kwa manufaa ya umma, lakini hajafanya hivyo. Haya mashamba yote tuliyochukua niliyoyataja ni yale mashamba ambayo waendelezaji wamekiuka sheria.
Mheshimiwa Spika, kila mwananchi anapopewa shamba au kiwanja lazima azingatie sheria na masharti aliyopewa kwenye hati yake yameandikwa. Kama amepewa shamba kwa ajili ya mifugo, lazima alitumie kwa mifugo na alipe kodi stahili na aliendeleze. Kamishna ana uwezo wa kulipima uendelezaji wake kila mwaka ameendeleza kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, nataka kukuhakikishia mashamba haya niliyoyataja hayakutaifishwa kama anavyosema Mheshimiwa Devotha, isipokuwa wenye mashamba haya na wana hati. Ukisikia Mheshimiwa Devotha shamba limefutwa maana yake lina hati, kumbe afutiwe nani?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hawa watu wenye hati wamefutiwa kwa sababu, wamekiuka masharti ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 99, Sura 113, wakiwemo hao unaowasema, mimi siwajui, lakini hao ambao anafikiri tumewaonea, hakuna hata mwananchi mmoja ameonewa katika utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Spika, nataka kuwahimiza wamiliki wote wa mashamba nchini, mtu yeyote ambaye ana shamba amepewa, lazima afuate masharti. Kama haliendelezi, kama halipi kodi stahili, shambapori, sheria itafuata mkondo wake. Sheria inaanzia kwenye Halmashauri husika, Afisa Ardhi husika anatoa notice kwa mhusika ya siku 90 ajieleze kwa nini hatua zisichukuliwe. Wengine hawa wote hawajibu hata notice, baada ya hapo Halmashauri inapandisha zoezi hilo mpaka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na mimi nampelekea Mheshimiwa Rais anatimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Devotha Minja jambo hili wakikusikia wenye Halmashauri zao watakushangaa kweli kwa sababu wao ndiyo wamefanya, Halmashauri hizi ndiyo zimeleta maombi ya kufuta mashambapori. Nasi tutaendelea kutekeleza hili jambo na ninawahimiza Waheshimiwa Wabunge mahali popote mtakapokuta mashamba yasiyoendelezwa, bila kujali ya nani, bila kujali siasa, bila kujali mashamba haya alikuwa anamiliki mkubwa gani au mtu gani, yaleteni kwa mujibu wa sheria na sisi tutachukua hatua.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Shamba la Tungi. Shamba hili la Tungi ni la watu, linamilikiwa kwa mujibu wa sheria, lina mmiliki halali. Nataka nimwombe tu kwa sababu, maelezo haya ni mengi, nimwombe Mheshimiwa Devotha Minja aende pale kwa Mkuu wa Mkoa atampa maelezo mengi kwa sababu, mimi mwenyewe nimeshakaa na timu ya Mkoa, hawa wananchi walipelekwa tu pale kulima wakati wa siasa ya Kilimo cha Kufa na Kupona, lakini walikuwa wanalima kwenye shamba lisilo lao.
Mheshimiwa Spika, pale pana hati ya mtu na Mkuu wa Mkoa amefanya jitihada sana, Mheshimiwa Dkt. Kebwe ya kuwatetea wale wananchi na wenye shamba wamewapa ardhi wale wananchi wa pale ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa hiyo, jambo hili Serikali imeshalishughulikia.
Mheshimiwa Spika, lile la mwisho ulilotaka kuuliza ushahidi la Mvomero, anajua Mvomero kuna shamba limefutwa na naamini bado limefutwa na Mheshimiwa Rais ametimiza wajibu wake. Mashamba yote yaliyofutwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya tunawaomba watupe mapendekezo namna bora ya kuyatumia katika Wilaya zao.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuamrishi tunataka mashamba yaliyofutwa wayapange viongozi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ili wananchi wale ambao wameyachungulia kwa muda mrefu na hawana nyenzo za mashamba ya kulima waweze kugawiwa yale mashamba. Kwa hiyo, kama kuna shamba Mvomero limefutwa, namwomba Mheshimiwa Murad na Viongozi wote wa Mvomero wapange utaratibu wa kutumia lile Shamba la Mvomero lililofutwa.
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali iliwazuia wananchi wa Kata ya Bigwa, Kilakala na Kola wasifanye maendeleo yoyote kwenye maeneo yao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo. Nataka kujua, kwa kuwa tathmini imekwishafanyika, ni kwa nini Serikali isiwalipe fidia wananchi hawa badala ya kuwaacha kwa zaidi ya miaka 14 mpaka sasa wanashindwa kuendeleza maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mpango wa kujenga barabara hii muhimu sana kutoka Biggwa kwenda mpaka Kisaki. Barabara hii niliipita kutoka Biggwa nimeenda mpaka Dutumi kuangalia miundombinu iliyopo katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Devota kwamba pia tutaitumia hii barabara kwa ajili ya kupitisha vifaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya access ya kwenda kwenye ujenzi wa Stiegler’s Gorge kule tunapokwenda kutengeneza umeme. Kwa hiyo, tunaona umuhimu wa barabara hii pamoja na barabara inayotokea Ngerengere kuja Mvuha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi kwa kweli kwa kuacha maeneo wazi kwa sababu itatuwia urahisi wa sisi kuanza taratibu kwa sababu ujenzi wa barabara unaanza katika hatua ya usanifu, kufanya michoro na hatua ambayo ilikuwa inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Devotha avute subira na nitalifuatilia suala hili kuona wananchi wanalipwa haki zao, lakini pia ni fursa kwetu kuweza kushughulikia barabara hii kwa sababu barabara ni huduma. Tutakapowapa barabara wananchi wake pia watanufaika na barabara hii.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, licha ya Mkoa wa Morogoro kuwa na mito mingi lakini wananchi wa manispaa ya Morogoro hawana maji ya kutosha. Kwa kuwa idadi ya watu katika Manispaa ya Morogoro imeongezeka. Je, Serikali haioni kama kuna umuhimu wa kujenga bwawa lingine lisaidiane na Bwawa la Mindu ili kutosheleza maji kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nikubaliane na dada yangu na Mheshimiwa Mbunge ni ukweli sasa hivi katika mji wa Morogoro watu wameongezeka, uhitaji wa maji umekuwa mkubwa sana. Na sisi kama Wizara tumeona hilo tupo katika harakati katika kuhakikisha tunatafuta fedha ili tuweze kuongeza miundombinu ya maji na wananchi wa Morogoro waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro umetokana hasa na kutokuwepo na mipango mizuri ya matumizi ya ardhi. Maeneo yanayofaa kwa kilimo wamepewa wafugaji na maeneo yanayofaa kwa wafugaji wamepewa wakulima. Je, Serikali inampango gani kuainisha upya maeneo hayo ili kuwapa wananchi na kuondoa hii migogoro?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa migogoro hii ya wakulima na wafugaji mingi imechangiwa na Watendaji wa Ardhi katika Vijiji na Kata: Serikali haioni sasa kuna haja ya kuwalipa fidia wananchi ambao wamebaki na makovu kutokana na migogo hii?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameongelea habari ya matumizi bora ya ardhi katika maeneo na amesema kwamba maeneo ya ufugaji wamepewa wakulima na maeneo ya wakulima wamepewa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda nimdhibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba upangaji wa matumizi ya ardhi haufanywi na Wizara. Upangaji wa matumizi wa ardhi, mdau wa kwanza ni mwananchi wa eneo husika. Tunapokuja ku-facilitate lile zoezi la upangaji, wananchi wenyewe wanakuwa wameshaainisha maeneo yao kwa ajili ya ufugaji na maeneo kwa ajili kilimo. Kwa hiyo, kinachofanyika pale ni kuweka mipaka kwa maana ya kwamba maeneo ya ufugaji yafahamike na maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pale inapotokea vurugu, ni kati ya watumiaji wa ardhi wanapokiuka makubaliano ya awali, kwamba mfugaji anatoka kwenye eneo lake la ufugaji anakwenda kwenye maeneo ya kilimo; au mtu wa kilimo anakwenda kulima kwenye maeneo ya wafugaji. Kwa hiyo, mgogoro mkubwa ulioko hapa ni kwa watumiaji wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai tu katika maeneo yote yenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji na ambapo mpango wa matumizi bora ardhi umepangwa, waheshimu maamuzi ambayo wameyafikia wao wenyewe na yanakuwa yameingia katika mpango wa matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo, hili ni jambo la watumiaji ardhi ambapo tunasisitiza waheshimu pale ambapo haijafanyika. Kwa wale ambao hawajapanga matumizi bora ya ardhi, basi nitoe rai tu kwamba mpango huo ufanyike na Wizara ipo tayari kwa ajili ya kuratibisha zoezi hilo ili angalau wananchi wote waweze kuwa na maeneo yao yaliyopangiwa matumizi kuepuka hii migogoro na inapotokea wanakiuka utaratibu, basi sheria ziweze kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika, swali lingine amesema Watendaji ambao wanachangia pengine kupata migogoro na licha ya hivyo kunakuwa na fidia za watu, niseme kwamba Watendaji hao kama wapo, ndiyo maana Wizara kuna baadhi ya Watendaji imewasimamisha kazi na wengine wameondolewa kwa kukiuka maadili ya utendaji wao.

Mheshimiwa Spika, suala la kusema kwamba kunakuwa na suala la kulipa fidia, hilo ziwezi kulitolea maamuzi sasa kwa sababu hatujawa na changamoto nalo kama Wizara na kuangalia hasa changamoto hii imetokana na nini? Kwa Watendaji waliokiuka taratibu zao, hatua zinachukuliwa. Sasa hivi tunamshukuru Mungu kwamba angalau wameanza kuwa na maadili kiutendaji tofauti na siku za nyuma.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Mheshimiwa Rais alipokuja Mkoani Morogoro kwa ziara aliagiza wananchi wa Mtaa wa CCT Mkundi ndani na Manispaa ya Morogoro wasibughudhiwe, lakini hivi sasa Maafisa wa Maliasili wameendelea kuwabughudhi wananchi wale. Je, ni kwa nini maafisa hawa wanapuuza agizo la Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minja, Mbunge wa Viti Maalum Morogoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa wetu wa Maliasili, kwa maana ya TFS, wamekuwa wakisimamia sheria hasa kuangalia mipaka ya kihalali ambayo ipo katika maeneo husika, lakini kama kuna maagizo ambayo yalitolewa na Mheshimiwa Rais kwamba, wananchi wasibughudhiwe, nitakwenda kufuatilia kuona ni kwa namna gani maafisa hao wanakiuka na tutatoa maelekezo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, lengo la Serikali kubinafsisha viwanda ilikuwa ni kuongeza ufanisi. Kuendelea kuwepo na viwanda ambavyo havifanyi kazi, Serikali haioni kama imeshindwa kutimiza wajibu wake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi kulikuwa kuna uharaka gani wa Serikali kuvitwaa viwanda hivi bila kuwaandaa wawekezaji badala yake hivi sasa viwanda vya Morogoro vimegeuka kuwa ma-godown, mahali pa kuhifadhi mbuzi na kuishi popo?

Mheshimiwa Spika, naomba kupata majibu ya maswali haya.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Serikali haijashindwa kwa sababu kubinafsishwa kwa viwanda ni process na kuvitwaa vilevile ni process na tunapovitwaa ni lazima kuzingatia sheria, taratibu na kanuni tulizojiwekea. Kwa hiyo, tunafanya hivyo kwa kufuata taratibu zote.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili la uharaka gani, huwezi ukaanza kumtangazia mtu kwamba kuna kiwanda sasa kimepatikana ukichukue kabla hujakamilisha taratibu za awali za kukirejesha Serikalini.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Si Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya tu ambao hawafanyi vizuri, wapo pia ma-RPC ambao hawafanyi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, RPC anapotangaza kwamba wananchi wakiandamana atawapiga hadi wachakazwe, hivi kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi kwa wananchi wanaolipa kodi ili walipwe mishahara, ni kuchakaza wananchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana swali la dada yangu Mheshimiwa Devotha Minja. Nadhani kitu kikubwa kama Taifa, jambo la kwanza tuweke ushirikiano katika kila eneo. Nadhani vyombo vingine vinaongozwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni hasa katika suala zima la mambo ya ndani na sitaki kuviingilia. Kwa hiyo, imani yangu ni kwamba wananchi wote tutafuata utaratibu wa utii wa sheria bila shuruti kwa ajili ya kuepuka migongano mingine ambayo inawezekana siyo ya lazima kwa afya ya Taifa letu.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimesikiliza majibu ya Naibu Waziri na kwa kuwa Serikali imepokea andiko hilo, naamini kwamba italichukulia kwa uzito ili kunusuru wananchi hususan akina mama katika Kata za Mlimba na kata za jirani na Jimbo la Mlimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mkandarasi aliyemaliza Mradi wa Maji Msolwa - Kilombero ambaye hajalipwa fedha zake na Serikali lakini amekubali kuendelea kufanya ujenzi katika Mradi wa Mbingu. Je, Serikali ipo tayari kumlipa fedha zake za awali alizozilimbikiza na anaidai Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kulikuwepo na mpango wa kuongeza kina katika bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro kutokana na maji yaliyopo kutotosheleza wananchi wa Manispaa ya Morogoro. Kwa miaka mitatu sasa Serikali imesambaza mabomba katika Kata za Kiega A na B, Kihonda, Mkundi, je, ni lini itapeleka maji kwa wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Mimi nilipata nafasi ya kufika katika jimbo lake lakini kubwa ambalo tumeona tuna changamoto kubwa pale Mlimba lakini tumefanya jitihada ya uchimbaji wa visima lakini bado kumekuwa na changamoto. Tumeona haja sasa ya kutafuta chanzo cha kutosheleza kuhakikisha wananchi wa Mlimba wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu fedha anazodai mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji, tunashukuru sana Wizara ya Fedha ilitupatia kiasi cha shilingi bilioni 44 kwa ajili ya malipo ya wakandarasi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kumlipa fedha zake kwa wakati ili aendelee kutekeleza mradi na wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la maji Manispaa ya Morogoro, kiukweli Morogoro Mjini kuna changamoto ya maji na hii yote imetokana na sababu tu ya ongezeko la watu na hata shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Sisi kama Wizara ya Maji tumefanya jitihada kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kufanya mazungumzo na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya uwekezaji wa fedha kwa maana ya utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha. Zaidi ya Euro milioni 70 zitakazopatikana zitawekezwa katika Mji ule wa Morogoro ili kuhakikisha tunaongeza kina cha Bwawa la Mindu ili wananchi wa Morogoro waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza. Sisi kama Wizara ya Maji tutafanya jitihada za haraka ili jambo hili liweze kutekelezeka na wananchi wa Morogoro waweze kunufaika na huduma hii muhimu. Ahsante sana.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambayo inahudumia wagonjwa 500 kwa siku, hospitali hii kwa miezi minne hivi sasa haina kipimo cha full blood picture, hospitali hii kwa miezi minne haina oxygen, hospitali hii kwa miezi minne haina film, wagonjwa wakienda kupima x-ray wanapewa CD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu Serikali ina mpango gani wa haraka wa kusaidia hospitali hii iweze kutoa huduma kwa wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina taarifa ya hili ambalo analolisema sasa hivi, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki tuweze kulifuatilia na kuhakikisha kwamba, hiyo huduma ambayo ni ya msingi kwa wagonjwa iweze kupatikana katika Hospitali hii ya Rufaa ya Morogoro.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana yapo mambo ya ajabu sana, barabara hii ya Meimosi ni barabara ambayo imelalamikiwa kutumia fedha nyingi sana za walipa kodi na hili limekuwa question kwa LAAC walipokwenda kuitembelea barabara hii CAG mwenyewe ali-question barabara hii, Mainjinia wa TANROADS wali-question barabara hii na cha kushangaza mpaka sasa kama kweli Waziri anasema barabara haina shida

Ni kwa nini mpaka Serikali haijazindua barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Rais alikuja Morogoro mwaka 2018, na akamuagiza Waziri wa TAMISEMI kuunda tume ya kuchunguza barabara hii baada ya kubaini kuna ubadhirifu.

Je, ni kwa nini toka miaka hiyo miwili mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali na ukweli kwamba majibu haya kule kuna Mkuu wa Mkoa tena makini ameleka juzi karibuni kazi imefanyika kwa sasas hayo ndiyo majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili anazungumza maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais alitoa, Mheshimiwa Rais akitoa maelekezo kwamba ufanyike uchunguzi sehemu fulani aliyetoa maelekezo uchunguzi ufanyike ndiyo unapewa taarifa. Kwa hiyo, sitarajii kwamba taarifa ya Mheshimiwa Rais tutaileta Bungeni hapa labda kama Bunge litaagiza vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii imejengwa kwa makubaliano na mikataba iliyokuwepo ndiyo imepitiwa. Kama kuna jambo ambalo analizungumza yeye na tofauti na maelezo yetu haya tutalifanyia kazi, lakini kimsingi kwa sasa majibu ya Serikali ni hayo tumetuma wqatu wetu wameenda site Mheshimiwa Waziri amefanya kazi yake na haya ndiyo majibu ya Serikali kwa sasa katika eneo hili, la barabara ya Meimosi Morogoro Mjini, ahsante.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Matukio ya ajali ya za moto, malori ya matenki ya mafuta yanaendelea kughalimu maisha ya Watanzania kwa kushabisha vifo na vilema vya kudumu. Tukio la Agosti 10, 2019 katika eneo la Msamvu eneo la Morogoro watu zaidi ya 100 walipoteza maisha, lakini umbali wa Ofisi za Zimamoto pale Morogoro haifiki kilometa moja kuelekea pale msamvu lilipotokea tukio.

Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuwalipa fidia wapendwa waliopoteza maisha yao pale, kwa sababu fire ilifika pale kuzima moto wakati watu wameshateketea na kuwa majivu na kuni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Waziri Mkuu wakati wa mazishi yale pale Msamvu aliagiza kuunda Tume ya Kuchunguza Ajali ya Msamvu.

Je, ni kwa nini mpaka sasa Ofisi ya Waziri Mkuu haijatoa tamko lolote juu ya tume iliyouzwa kuchunguza ajali ya tukio la Msamvu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijajibu swali lake, naomba nisisitize majibu ya msingi ambayo niliyazungumza kuhusiana na mkakati wa Serikali ya kuimalisha Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji katika kulipatia vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mbali na jitihada ambazo nimezungumza za kutenga bajeti ambapo kwa mwaka huu peke yake tumeshapokea karibu shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari ya moto na vifaa vya uokoaji, lakini pia kuna mipango mbalimbali ikiwemo mkopo ambao nimezungumza, wa takribani Euro milioni 408 ambayo tunatarajia pamoja na mambo mengine kujenga vituo katika kila wilaya, kununua vifaa mbalimbali vya uokoaji ikiwemo magari, helkopta, boti na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba tukapokuwa tumekamilisha mikakati hii na ikawa ipo vizuri, basi changamoto zote zinahusiana na majanga ya moto ikiwemo kama hili ambalo limetokea Morogoro, yatakuwa sasa tunayakabili kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake specific kuhusu ripoti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imepewa kazi. Kwa kuwa hii ilikuwa ni Kamati ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nadhani siyo mamlaka yangu kuitolea kauli.

Mheshimiwa Spika, nina hakika kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia Ofisi yake, kuna utaratibu ambao umewekwa wa kuweza kuitolea taarifa pale ambapo mwenyewe ataona inafaa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira ambapo Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hili. Ni imani yangu kwamba Kamati ile imeendelea kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Spika, lengo na dhamira ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kuhakikisha kwamba taarifa ya ripoti ile inatupatia mapendekezo ambayo yanasababisha hatua zichukuliwe, lakini pamoja na kuepukana na matatizo kama haya yasitokeze siku zijazo.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kuwa Redio Tanzania inaendeshwa na kodi za Watanzania na kwa sasa ni zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Redio Tanzania lakini maeneo ya pembezoni haisikiki na watu wanalazimika kusikiliza redio za nchi jirani. Hivi tunakwama wapi? Ni kwa nini TCRA isiondoe vikwazo kwa redio binafsi ili zipewe jukumu la kuhakikisha zinatoa huduma na kuwafikia Watanzania katika maeneo yote nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa nashukuru, hizi zote ni neema za Mwenyezi Mungu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nitumie fursa hii kumtoa hofu kwamba TCRA kwa maana ya Serikali haijaweka vikwazo kwa redio yoyote ya binafsi kuanzisha vituo vyake vya redio. Mara zote sisi kama Wizara ambao tunasimamia masuala yote ya habari lakini kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mawasiliano, tumekuwa tukisisitiza kwamba milango iko wazi kwa mtu na taasisi yoyote ambayo inataka kuanzisha redio waweze tu kufuata zile taratibu ambazo zinatakiwa katika kuanzisha redio hizo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, sisi kama Wizara ambao tunasimamia masuala ya habari nchini Tanzania tumekuwa tukihakikisha kwamba maeneo yote ya mipakani yanafikiwa na usikivu wa Redio yetu ya Tanzania. Katika kuthibitisha hilo, kwenye jibu langu la msingi nimesema wazi kwamba katika bajeti ya mwaka 2016/2017, TBC ilifanya uwekezaji mkubwa sana katika maeneo yote ya pambezoni ikiwemo katika wilaya zote ambazo zipo mipakani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tunatambua concern yake kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuboresha usikivu wa TBC pamoja na Redio Tanzania katika maeneo yote ya mpakani.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na mkanganyiko wa matamko kutoka kwa Wakala wa Misitu nchini kwamba mtu akipatikana na kilo 50 za mkaa ni lazima awe na kibali maalum; ni marufuku kwa mtu kupatikana na kilo 200 za mkaa na adhabu yake ni kifungo cha miezi kumi au kulipa faini ya shilingi 50,000 na shilingi milioni 12. Hivi ni sahihi kabisa watu kama akina mama lishe, mama ntilie, akina mama wa nyumbani, adhabu hii inawahusu?

Mheshimiwa Spika, katika swali langu la pili kwa kuwa gesi siyo ajenda tena kwa Serikali hii ya wanyonge na mtungi wa gesi hivi sasa kilo 15 ni kati ya shilingi 45,000 mpaka shilingi 50,000; hivi ni kwa nini Serikali isione kuna umuhimu wa kuondoa kodi katika gesi ili kuwawezesha wananchi waweze kutumia gesi badala ya kutumia mkaa na kuni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Devotha Minja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninakiri kwamba limekuwepo tamko kutoka ofisini kwetu linalohusiana na namna tunavyojipanga kudhibiti ukataji na uchomaji hovyo wa mkaa na tumeelekeza kwamba wahusika wa biashara ya mkaa ambao wanafanya biashara, siyo watumiaji, wahusika wa biashara ya mkaa ambao wanasafirisha mkaa kwa ajili ya kuuza wanapaswa kuwa wamepitia taratibu mbalimbali kabla ya kuchoma mkaa na taratibu hizo zinaanza katika level ya vijiji, tunaowazungumzia hapa siyo watumiaji wa mwisho kwa maana ya mama lishe na watumiaji wa ndani hawa watakwenda kununua katika maeneo maalum ambayo tumeelekeza maeneo yote yanayofanya biashara ya mkaa yatasajiliwa na wale wanaofanya biashara ya mkaa pale ndiyo watakaowauzia watumiaji wa mwisho.

Kwa hiyo, ni makosa kuwakamata watumiaji wa mkaa wa ndani ambao wamenunua kwa muuzaji ambaye ametambuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kweli kwamba gharama ya gesi iko juu na hii imesababisha watu wengi ku- opt kutumia mkaa na kuni hasa maeneo ya vijijini, lakini watafiti wanaonesha kwamba bado kwa gharama ya sasa matumizi ya gesi ni gharama nafuu kuliko matumizi ya mkaa. Kwa mfano sasa hivi gunia la kilo 50 la mkaa katika Jiji la Dar es Salaam linauzwa mpaka shilingi 60,000 wakati mtungi wa gesi unauzwa shilingi 50,000 na muda wa matumizi ya gesi ni muda mrefu kuliko matumizi ya mkaa.

Mheshimiwa Spika, lakini nimechukua mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge na tutajadiliana na Wizara husika kuona kama tunaweza tukaomba kuondolewa kwa baadhi ya kodi kwenye gesi ili kuhamasisha matumizi ya gesi na kupunguza matumizi kuni. (Makofi)
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimesikiliza majibu ya Serikali kwa namna zoezi hili linavyokwenda kwa kusuasua hivi, Serikali itafanya juhudu gani za ziada ili ifikapo Juni, 2020 kama alivyosema Naibu Waziri kwamba umeme huo umefika katika Vijiji vya Ipungusa, Msolwa, Kalengakule, Miembeni, Iduindembo, Ipungusa, Matema, Lumumwe, Uchindile, Kitete, Idandu na Mgwasi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Manispaa ya Morogoro zipo kata ambazo hazina umeme licha ya kuwepo mjini, kata hizi ni Kauzeni Juu, Kiegea, maeneo ya Mkundi, Magadu Juu, katika Kata ya Tungi maeneo ya Paranganyiki, Kambi A, na B; Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwa wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Devotha Minja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Devotha Minja ameulizia ni namna gani Serikali itafanya kuhakikisha ifikapo Juni, 2020 kwamba umeme maeneo hayo yaliyotajwa katika swali la msingi yanapatiwa umeme. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kulikuwa na kusuasua kwa mkandarasi State Grid katika Mkoa wa Morogoro lakini hivi ninavyosimama ndani ya Bunge naomba nimtaarifu kwamba kwa wiki ijayo kwanza kwa sasa alishawasha vijiji 18 kati ya 150 katika Mkoa Morogoro; na kwa kuwa kulikuwa na tatizo la nguzo, alikuwa na nguzo zaidi ya 900 ambazo zilivyopimwa zilionekana kama haizifai. Ninapozungumza ndani ya Bunge zaidi ya nguzo 700 zimeonekana zinafaa sasa zinaweza zikaendelea na mradi na wiki ijayo anapokea nguzo 2,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, wiki ijayo atawasha vijiji 16 vikiwemo 6 vya Wilaya ya Kilombero vikiwemo alivyovitaja ambavyo ni Kilama, Kalengakelu, Matema, Iduendemo, Miembeni na Msolwa. Vijiji hivi vitawashwa wiki ijayo na mimi natarajia kufanya ziara katika Mkoa wa Morogoro, tutamwalika Mheshimiwa Mbunge tuambatane pamoja. Sambamba na hilo, kwa hiyo nithibitishe tu kwamba kwa kweli kama tulivyojipanga na kwa kuwa tumejitahidi kutatua changamoto zinazojitokeza na zipo bado zinaendelea lakini tunakaa vikao mara kwa mara. Tuna uhakika mpaka ifakapo Juni, 2020 tutakamilisha mzunguko wa kwanza REA Awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameulizia kwenye Manispaa ya ya Morogoro, naomba nimtaarifau Mheshimiwa Mbunge mwenyewe nimeshatembelea Manispaa ya Morogoro kama mara mbili nikiwa na Mheshimiwa Aboud. Moja wapo ya maeneo ambayo tuliwasha ni maeneo ya Tungi, ni kweli maeneo ni mengi na kwa kuwa Mkoa wa Morogoro una kua sana katika ujenzi wa makazi. Maeneo haya kwa kuwa tumelitambua hilo, kama nilivyosema hapa Bungeni tuliona kwamba licha tu ya Wakala wa Nishati Vijijini kuendelea na kazi ya kusambaza umeme vijijini lakini pia tuitake TANESCO nayo ifanya kazi hiyo hiyo na kwa kuwa tumesema bei ya kuunganisha iwe 27,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulitambua hilo katika mpango mkakati wa ndani ya TANESCO na kwa kuwa tumeona tuna umeme wa ziada unaosalia kama Megawatts 300, TANESCO kwa mwaka wa fedha 2019 itajielekeza kwanye miradi ya distribution (usambazaji wa umeme). Takribani milioni 400 zimeidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kusambaza umeme katika maeneo ambayo yanakuwa kwa kasi yakiwemo Majiji na Manispaa, ikiwemo Manispaa ya hapa Dodoma, Manispaa ya Morogoro, Jiji la Tanga, Jiji la Mwanza, Jiji la Mbeya na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge jana nilikuwa Kondoa kukagua haya maelekezo yalivyoanza. Kweli TANESCO wameanza kazi ya kupeleka vijijini umeme na kwa kuunganisha wateja 27,000. Nimehakikisha kweli jana tu wateja zaidi ya 500 wameunganishwa baada ya maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba TANESCO sasa kazi kubwa ni kutafuta wateja na ipunguze bei ya kuunganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilithibitishie Bunge lako tunatambua mahitaji, tumejipanga vizuri na tutaendelea kusimamia na kupambana ili lengo hili lifikie. Ahsante sana.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza majibu ya Serikali na nilitarajia kwa kuwa Serikali hii inakusanya kodi basi ingetilia mkazo katika ujenzi wa nyumba hizi za wazee ambazo nyingi ni chakavu na nyingi zimegeuka kuwa magofu walau wazee hawa nao wajisikie kuwa ni sehemu katika Taifa hili. Swali la kwanza, je, ni upi mkakati thabiti wa Serikali kuhakikisha kuwa nyumba hizi za wazee zinakarabatiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali imekuwa ikitoa maagizo kuwa wazee wote watapata huduma za matibabu bure lakini hali ilivyo hivi sasa wazee wengi hawapati matibabu kama inavyopaswa katika hospitali za Serikali na hata katika vituo vya afya. Je, ni lini Serikali italeta sheria hapa Bungeni ambayo itasimamia matibabu na maslahi ya wazee hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Minja kwa maswali yake mazuri na kwa kufuatilia kwa karibu masuala ya wazee hususan katika kambi hii ya Fungafunga pale Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na naomba nitoe maelezo ya awali kwamba Serikali tuna kambi 17 za kuhudumia wazee. Hata hivyo, kwa mujibu wa sera yetu Serikali inachukua wazee pale inapoonekana yule mzee hana watoto wa kumtunza, ndugu na watu katika jamii ambao wanaweza wakamtunza. Mpaka sasa hivi tuna wazee takribani 500 ambao tunawahudumia sisi kama Serikali ambapo katika vigezo hivyo vitatu ambavyo nimevisema pale awali wametimiza na ndiyo maana tunawachukua na sisi kama Serikali tunawatunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa hii miundombinu ya vituo vyetu 17 umeshaanza na vituo ambavyo tumeshavifanyia ukarabati ni pamoja na Bukumbi, Mwanzage na Magugu. Aidha, tumejenga tena nyumba mpya pale Kolandoto na tumefanya ukarabati wa bweni pale Kilima. Ndiyo maana nasema tunakwenda awamu kwa awamu kuhakikisha kwamba hizi kambi zote tunaweza kuzifikia na kuzifanyia ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na matibabu kwa wazee, Serikali ilitoa agizo kwamba wazee wote ambao wamefika umri wa zaidi ya miaka 60 wapate vitambulisho ili waweze kupata matibabu bure. Kumekuwa na changamoto kidogo ya kusuasua katika utekelezaji kwenye baadhi ya Halmashauri kutoa vitambulisho. Nitumie fursa hii kuzikumbusha Halmashauri kuzingatia agizo hili la Serikali la kutoa vitambulisho kwa wazee ambao wamefika miaka 60 na vilevile kutenga madirisha mahsusi kwa ajili ya wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhu ya kudumu ya jambo hili ni hili jambo ambalo tunataka kulifanya kama Serikali kuhakikisha kwamba kila mtu anaingia katika mfumo wa Bima ya Afya ya Wote. Mwezi Septemba tunataka tulete Muswada ambapo utaratibu wa kuwa na bima utawekwa ili kuhakikisha wanapata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunatambua kwamba kuna magonjwa mahsusi ya wazee na sisi wataalam tuna kitu kinaitwa geriatric medicine. Ndani ya Wizara, tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba haya magonjwa ambayo ni mahsusi kwa wazee nayo tunayawekea utaratibu ili wazee waweze kupata matibabu kulingana na magonjwa waliyonayo.