Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Devotha Methew Minja (41 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Awali ya yote niwashukuru akinamama wa Mkoa wangu wa Morogoro kwa kunipa fursa ya kuwa mwakilishi wao. Hali kadhalika nikishukuru Chama changu kwa kuniona kwamba nafaa kuwakilisha katika Bunge hili, bila kuwasahau wapambanaji wenzangu wa ITV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vizuri sana Mpango ulioletwa mbele yetu. Yako mambo mengi sana, lakini hakika mambo haya nilikuwa nikijiuliza tu, mikakati na mipango mingi kiasi hiki tunaifanya kwa ajili ya watu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikapata jibu ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa lao, lakini hivi tunavyojadili mambo haya muhimu ambayo yanakwenda kulenga kuleta maendeleo ya wananchi, tukiwa tumejifungia, lakini wananchi hawajui ni kitu gani kinachoendelea, kwa kuzuwia chombo cha umma kutangaza matangazo haya moja kwa moja, naona kama hatuwatendei haki wananchi. Hali kadhalika naona kama tutakwama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mataifa mbalimbali yaliyoendelea ni yale ambayo yametumia vizuri vyombo vya Habari. Mfano Malaysia, ukienda ukimuuliza hata dereva tax, National Goal ni ipi na ni njia gani ya ku-achive National Goal? Watakueleza kwa sababu wako informed na wanatumia vyema vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakuja na Mpango hapa tunasema ni kwa ajili ya wananchi na maendeleo ya Taifa, lakini wananchi hawa hawana fursa ya kupata na kuelewa tunajadili nini! Tumezungumza mambo mbalimbali ambayo ni ya vyanzo vipya vya mapato, tumezungumza habari ya mambo ya retention, lakini mambo hayo hamuoni kama wananchi wangepata fursa ya kufuatilia moja kwa moja kujua na sisi tunafanya nini, ingeweza kutusaidia pengine mipango hii ikaweza kutekelezeka kwa uzuri na kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata taarifa hapa kwamba, TBC Chombo cha Umma ambacho kilianzishwa kwa lengo la kutoa huduma kwa umma; TBC inasema ni gharama kuendesha matangazo haya ya moja kwa moja! Hata hivyo, tumekwenda mbali zaidi kuangalia mchakato, ukiaangalia Air Time kwa TBC kwa kipindi cha saa moja gharama yao ni 7,080,000/=, lakini tukiangalia saa ambazo tumekuwa tukizitumia hapa kuanzia masaa sita mpaka saba kuendesha Bunge live. Pia tumejaribu ku-calculate kwa vipindi vinne vya Bunge kwa maana ya vipindi vitatu vifupi na kipindi kimoja cha Bunge la Bajeti ambacho ni kirefu, tukapata ni sawa na saa 290 za kurusha Air Time na ukizidisha unapata 2.2 billion na siyo 4.2 kama tulivyoelezwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika tunakumbuka Serikali, kamera tunazoziona huku zilifungwa na Star TV enzi hizo, lakini hivi sasa ikatokea mambo mengine mengine hapo wakasema siyo vema ni lazima taarifa hizi zirushwe na vyombo vya umma. TBC ikajengewa uwezo kwa kupewa bilioni 4.6 inunue vyombo vya kisasa na kutumia kamera hizi ambazo zimefungwa na Star TV, lakini matokeo yake hiyo 4.6 haijafanya chochote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii TBC wanakuja na crew ya watu 20 kurusha live hapa, kitu ambacho kinaongeza gharama. Hamuoni sasa ni wakati wa kuruhusu hivi vyombo binafsi vifanye kazi vizuri, kuhakikisha vinasaidia kusukuma mipango hii kama TBC imeshindwa? Hamuoni kama sasa ni wakati wa Serikali kupunguza hivi vikwazo kwa vyombo hivi binafsi na kupewa hizi ruzuku ambazo TBC inashindwa kufanya kazi? Ruzuku zielekezwe kwa vyombo binafsi vifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niende kwenye mipango mbalimbali niliyoiona kwenye kitabu hiki; nimeona habari ya reli, miundombinu, barabara, lakini sijaona mahali popote ambapo tumezungumza jinsi ya kusaidia wananchi ambao wameathirika kutokana na miundombinu hii. Nikizungumzia Kilosa hivi sasa kuna wananchi wanaishi kwenye mahema kwa zaidi ya miaka mitano, wameathirika kwa sababu reli ya kati ilikatika katika eneo la Godegode, tuta la Kidete lilivunjika ambalo nimeona mpango mnalitengeneza, lakini kuvunjika kwa tuta lile ambalo lilisababisha mafuriko kwa wananchi hamjaweka mpango wa kuwapa hata viwanja wananchi leo hii, tangu 2010 wanaishi kwenye mahema, wakiwemo wananchi wa Kidete, wananchi wa Mateteni na wananchi wa Magole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati umefika wakati tunaandaa mipango hii tuwafikirie na wananchi hawa ambao waliathirika kutokana na kuharibika kwa miundombinu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mna mpango wa kufanya Tanzania kuwa ni Tanzania ya Viwanda. Tunavyozungumza hivi Morogoro viwanda vilikuwa vingi, leo hii viwanda mbalimbali vimekufa, lakini hamjatueleza kwamba, viwanda hivi vitafufuliwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Canvas, kiwanda cha UNAT cha matunda ambacho akina mama walikuwa wanatumia kwa ajili ya matunda yao! Leo hii akinamama ndiyo wanaotembea na mabeseni kichwani, haikuwa kazi yao! Kiwanda cha Asante Moproko, Kiwanda cha Ceramic, Kiwanda cha Tanarries, ambavyo vyote hivi vilikuwa vinatoa ajira kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye suala la maji; limezungumzwa kila mahali, lakini Mkoa wa Morogoro ni Mkoa ambao una mito mingi sana, lakini Mkoa wa Morogoro ndiyo unaoongoza kwa kukosa maji. Nikianza katika Manispaa ya Morogoro pekee, ambayo kwa sasa inategemea Bwawa la Mindu ambalo limejengwa mwaka 1984 wakati huo idadi ikiwa ndogo sana; leo hii Serikali imekuja na mkakati mpya wa kujenga Bwawa la Kidete, hatukatai! Imekuja na mpango mpya wa kujenga mabwawa mengine ya Vidunda, hatukatai! Lakini kweli mipango hii ni kwa manufaa ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii inatumia mito ya Morogoro ambayo maji yatakwenda sehemu nyingine, sisi wana-Morogoro wenye mito yetu tunabaki bila maji! Nenda katika Manispaa nimesikia majibu ya Naibu Waziri leo asubuhi, Kihonda, Area Five, Kilakala, kote huko hakuna maji japo anasema kwamba, mpango wa MCC ulisaidia, lakini tunavyozungumza hivi sasa huo mpango wa MCC wananchi hivi sasa ni kuandamana kila wakati wakienda MORUWASA kudai maji! Kwa nini sasa kwa mito hii mingi wasifikirie kujenga bwawa jipya kwa kutumia hii mito yetu iliyopo, ili kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili la maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji, nazungumza hili kwa masikitiko makubwa. Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari tumesikia jinsi mauaji ya mifugo na wananchi yakiendelea katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero.
Hivi karibuni nimetembelea vijiji vya Kunke kule Mvomero, wananchi wa vijiji sita wamechangishwa shilingi mia tano kila mmoja eti kwa ajili ya kufanya operation ya kuwaondoa wafugaji. Kazi ya kufanya operation ya kuwalipa Polisi ni kazi ya wananchi? Wananchi kila mmoja alitozwa shilingi mia tano ili wawaondoe wafugaji, zoezi ambalo linapaswa kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara husika, lakini leo hii wananchi wanaambiwa kama ninyi hamtaki migogoro hii basi wachangie ili wafugaji waondolewe. Hii ni kuendelea kuongeza uhasama katika makundi haya mawili kwa kuwa yote yanafanya shughuli halalli ambazo zinachangia pato kwa Serikali.
Tukirudi kwenye suala la Mpango wa NFRA wa kuuza mazao, hivi sasa Serikali imeanzisha soko la Kibaigwa ambalo linatoa huduma kuwezesha wakulima wa Morogoro, Dodoma na Manyara kufanya biashara ya mazao, lakini hivi sasa wakulima wa Morogoro hawapeleki mazao yao pale kwa sababu ushuru...
MWENYEKITI: Nakushukuru sana.
MHE. DEVOTHA MATHEW: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja zangu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa Walimu hauwiani katika ya shule za mijini na vijijini ambapo katika Wilaya ya Kilosa Shule ya Msingi Mabwegere kwa zaidi ya miaka 10 ilikuwa na Mwalimu mmoja hali iliyosababisha baadhi ya wazazi wasio na taaluma ya elimu kujitolea kwenda kufundisha watoto wao, hali hii ilisababisha shule hiyo kushindwa kufanya vizuri. Ipo haja ya kuangalia upya mgawanyo huu wa Walimu badala ya kurundikana katika Manispaa ya Morogoro wakati Wilayani hakuna Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la X-ray mashine katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro unategemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili kutoa huduma za matibabu zilizoshindikana katika Wilaya saba za Mkoa lakini X-ray mashine iliyopo imenunuliwa zaidi ya miaka 14 iliyopita na haina ufanisi hali inayolazimu wagonjwa kwenda nje ya hospitali (private) kufanya kipimo hiki. Aidha, kutokana na matukio mengi ya ajali wajeruhi pia wanategemea hospitali hiyo. Naomba Serikali ione umuhimu wa kununua X-ray machine mpya kwa ajili ya hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya zahanati zimefunguliwa na Mwenge miaka mitano iliyopita na baada ya Mwenge zimefungwa badala ya kutoa huduma kwa wananchi licha ya kuwa zimejengwa kwa nguvu za wananchi. Mfano wa zahanati hizi ni Bigwa iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la mafuriko ya mara kwa mara katika Mto Mkondoa, Wilayani Kilosa. Serikali iliahidi tangu mwaka 2010 kuwa wangejenga tuta ili kuzuia mafuriko lakini mkandarasi alipewa fedha kazi haijaisha na wananchi wanaendelea kupata madhara makubwa ya nyumba kujaa maji kila msimu wa masika pamoja na kusomba reli ya kati maeneo ya Godegode.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa TASAF katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero, baadhi ya kaya zisizo maskini zimepewa fedha bila utaratibu na wenye shida na maskini wanakosa nafasi hizo. Ipo haja kwa watathmini wa TASAF kufanya upya uhakiki wa kaya maskini zinazostahili kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wa Viti Maalum kukosa ofisi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kama Waziri wa TAMISEMI alivyoeleza Bungeni. Ipo haja ya Waziri wa TAMISEMI kuwaandikia Wakuu wa Mikoa kutoa ofisi hizo ili kuwezesha Wabunge wa Viti Maalum kufanya kazi zao za kisiasa kwa wananchi badala ya kutumia ofisi za chama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji wa watumishi wa umma bila kutumia haki za msingi za binadamu. Tumeshuhudia Serikali ikiwafukuza watumishi kwa madai ya kutumbua majipu, hatupingani na utumbuaji huu, lakini haki za msingi za binadamu zizingatiwe. Mfano, Mkurugenzi Kabwe wa Dar es Salaam kutumbuliwa mbele ya mkutano wa hadhara bila kujali staha yake, familia, mke, watoto na marafiki, hali hii ni ya kukemewa. Utaratibu mwingine ungeweza kufuatwa kwa Waziri mwenye mamlaka kumshughulikia badala ya kumuaibisha hadharani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufukuzaji huu wa watumishi umewakumba pia Mabalozi ambao walipewa saa 24 wawe wamerudi nchini. Lazima haki za mtumishi zizingatiwe mfano kuangalia utu na familia. Mfano, kuna watoto ambao wapo shuleni nje ya nchi na wazazi wao bila kumpa muda wa kujiandaa kuhamisha familia inakuwa sio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuiaji wa vyombo vya habari kufanya kazi zake mfano waandishi wa TV hawaruhusiwi kuingia Bungeni na kamera badala yake wanapewa taarifa ambazo ni edited. Huu ni ukiukwaji wa Katiba na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi juu ya Bunge lao linaloendeshwa kwa kodi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama kubwa za Mwenge. Mwaka huu uzinduzi wa Mwenge umefanyika Mkoani Morogoro ambapo tumeshuhudia kila halmashauri zimeelekezwa kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi hayo na halmashauri zote zimetoa fedha za wananchi na kuzipeleka katika shughuli za Mwenge. Kama hiyo haitoshi Walimu wa shule za msingi na sekondari wamelazimishwa kutoa mchango wa Sh.10,000 ili kuchangia maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge. Hii si sahihi, si haki fedha za wananchi walipa kodi kutumika kukimbiza Mwenge ambao bado hauna tija kwa wananchi huku wanafunzi wakikosa masomo ili kuhudhuria shughuli za Mwenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hewa kudumu katika Wizara mbalimbali kwa miaka mingi ni udhaifu kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana na Serikali. Badala ya kuwakamata watuhumiwa pekee ni muda muafaka kuwatia hatiani wasimamizi na maafisa wa idara tofauti walioshindwa kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo la Rais kuhusu watumishi kulipwa mshahara usiozidi milioni kumi na tano ni lini utekelezaji huu utaanza?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Naomba na mimi nichangie mawili, matatu kwa dakika hizi tano ambazo umenipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa uzito wa bajeti hii ya kilimo ambayo tunafahamu pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 70 inategemea kilimo. Ninachokiona katika kujadili bajeti hii, wakulima na wafugaji hawajui ni nini tunachojadili, ikizingatiwa kwamba changamoto ni nyingi katika sekta hii. Nafikiri, hatuzungumzii habari ya televisheni tu, tunazungumzia pia habari ya redio. Mkulima anapaswa akiwa shamba leo hii ajue mpango wa Serikali wa kununua maelfu ya tani za mahindi; mkulima ajue kwamba ni kiasi gani cha fedha kimetengwa kwa ajili ya kusaidia pembejeo, lakini leo hii tunawanyima fursa wakulima hawa kujua wakati tunakabiliwa na matatizo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo suala tu la kusikiliza redio mkulima akiwa analima, watu wako kwenye bodaboda wanasikiliza redio, wako kwenye daladala wanasikiliza redio, wanajua ni nini hatma ya sekta hii muhimu ambayo inachangia pato zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro. Hivi karibuni Waziri wa Kilimo alifika Mkoani Morogoro; mauaji makubwa yametokea, wananchi wameuawa, mifugo imeuawa, lakini hatma ya kutatua migogoro hii kule Mvomero wameamua kujenga korongo la kilometa 13 linalogharimu shilingi milioni 147, lenye urefu wa futi zaidi ya sita kwenda chini, upana zaidi ya ekari moja kutenganisha wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi shilingi milioni 147 zingejenga Zahanati mbili, zingejenga malambo matatu ambayo yangesaidia wananchi hawa ambao migogoro yao mikubwa ni kutokana na kukosa vitu muhimu ikiwemo haya malambo. Leo tumeamua kuanza kuwagawa Watanzania hawa badala ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, enzi za Mwalimu Nyerere migogoro hii haikuwepo, lakini hivi sasa watu wamehodhi maeneo makubwa, wakulima hawana sehemu ya kulima, ranchi zilizokuwa za Serikali zimehodhiwa, Serikali ilitoa maamuzi kwamba zaidi ya ekari 5,000 zigawiwe wananchi hawa lakini hakuna kitu, wamegawana vigogo, sasa hivi wanakuja kuamua kuwatenga wakulima na wafugaji. Sijui tunakwenda wapi katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Berlin wameamua kuvunja ukuta ili kuwaunganisha watu, leo sisi tunasema tunajenga korongo kumtenganisha mkulima na mfugaji! Watu hawaombani chumvi, hawaombani kibiriti! Shule wanafunzi wanashindwa kuvuka upande wa pili! Naongea kwa masikitiko makubwa; wananchi hawa wangejengewa mikakati ya kutatua migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu alifika pale, wananchi wanamnyooshea vidole Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, RPC, DC, migogoro inatokea hawana habari kinachoendelea, matokeo yake Mahakama ilitoa rulling kutengeneza buffer zone Halmashauri/Serikali iliamua kujenga korongo kwamba sasa korongo litengenezewe. Hata mipaka ya nchi zetu, hakuna makorongo. Inasikitisha sana! Fedha hizo ambazo ni mapato ya wananchi ambayo yangesaidia lakini sasa hivi yanakwenda kutengeneza makorongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, korongo hili halikuzingatia hata ushauri wa Madiwani wala NEMC zaidi ya kuharibu mazingira. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie upya jinsi ya kusaidia jamii hizi kurudisha utamaduni.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kwa maandishi tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro katika Kijiji cha Kambala. Serikali imeshindwa kutatua mgogoro huu. Serikali imejenga korongo la kuwagawa wakulima na wafugaji kufuatia migogoro ya mara kwa mara. Korongo hili limetumia zaidi ya shilingi milioni 147, fedha za mapato ya halmashauri ilizokuwa inadai Kiwanda cha Mtibwa Sugar.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zingeweza kusaidia kujenga zahanati na majosho ya mifugo badala ya kujenga korongo la kuwatenganisha wakulima na wafugaji, tunatengeneza Taifa la namna gani? Tunahubiri amani na ushirikiano lakini tunakuja na maamuzi ya kuwagawa Watanzania kwa kutenganisha jamii hizi. Nashauri Serikali itumie busara kupitia maamuzi haya ili kurudisha mahusiano kwa jamii hizi. Tatizo la wakulima na wafugaji lingeweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano badala ya kutumia nguvu. Serikali iangalie mashamba yaliyohodhiwa bila kuendelezwa kwa muda mrefu pamoja na ranchi zikiwemo za Wami Dakawa zitumiwe na wananchi baada ya Serikali kufanya utaifishaji na kugawa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliyopita iliagiza zaidi hekari 5,000 zigawanywe kwa wananchi ili kuondoa kero ya upungufu wa maeneo ya kilimo na ufugaji. Eneo hilo limechukuliwa na vigogo wamegawana badala ya kutolewa kwa wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ichukue hatua kama ilivyoagizwa wananchi wapate ardhi hii badala ya vigogo kujinufaisha na maamuzi ambayo yameshatolewa na Serikali. Ni wakati wa Serikali kusimamia maamuzi yake yaliyokwishatolewa na si kuyabatilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA - stakabadhi ghalani. Ukopaji wa mazao kwa wakulima mwaka jana umesababisha usumbufu mkubwa na wakulima walikopwa mazao kwa muda mrefu lakini walicheleweshewa malipo yao. Wengine wamelazimika kutumia nguvu kudai jasho lao. Tumeshuhudia wakulima wa maeneo ya Kibaigwa, Mbeya, Morogoro waliandamana kudai malipo yao. Zoezi la kuwalipa wakulima hao limechukua muda mrefu huku wakulima wengi wakipata hasara katika taasisi za fedha walizokopa kwa ajili ya kilimo na walitegemea kurejesha baada ya msimu wa kilimo badala yake iliwachukua miezi na miaka kudai malipo pasipo kupata jibu.
Nashauri Serikali iwalipe fidia wakulima kwa kuwa mazao waliuza kwa shilingi 500 na kuuza kwa 800, Serikali ilitengeneza faida kwa nini Serikali isingetoa fidia/kifuta jasho kwa wakulima hao? Mfumo huu wa NFRA unapaswa kuangaliwa upya na kwa mwaka huu Serikali ije na mpango/mfumo mpya wa kuwalipa wakulima mara baada ya kuuza mazao yao. Pia ikiwezekana NFRA iwe na mfumo wa kuwakopesha pembejeo na mbegu wakulima ili walipie baada ya kuvuna mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mazao, hii imekuwa kero ya muda mrefu kwa wakulima na ni ukandamizaji wa wakulima ambapo kuna milolongo ya ushuru wa mazao kutoka shambani kwenda sokoni, sokoni kwenda stoo za soko na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri huu unaendelea kuwakandamizi, wakulima wanakata tamaa badala ya kuuza mazao yao sokoni mfano soko la mazao Kibaigwa sasa wanakwepa ushuru na wanauza mazao mashambani kama lumbesa na kuendelea kupata hasara. Imefikia wakati sasa Serikali kuangalia upya viwango vya ushuru wa mazao, kuondoa mageti ya ushuru kwenye vijiji ili kuwezesha wakulima kuwa na ushuru mmoja tu usiowaumiza na pengine ushuru mwingine wapewe wafanyabiashara wanaonunua mazao toka kwa wakulima au kwenye masoko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa njia ya maandishi juu ya hoja ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufa kwa viwanda Morogoro; Mwalimu Nyerere alipendekeza Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa viwanda tangu miaka mingi iliyopita kwa lengo la kusaidia Jiji la Dar es Salaam kutokana na miundombinu iliyopo ikiwemo umeme, barabara, reli, maji na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vilitegemewa na wananchi wa Morogoro, vilisaidia kupunguza tatizo la ajira, ambapo hata wananchi wale waliweza kuendesha maisha na kupeleka watoto shule, hali hii ilisababisha population na kupelekea kuwepo kwa vyuo vingi vikuu ambavyo vilitengeneza wanafunzi waliofanya kazi katika viwanda, lakini viwanda hivi leo hii vimekufa baada ya Serikali kuvibinafsisha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kubinafsisha lilikuwa ni kuongeza uzalishaji na kupanua viwanda, lakini hivi sasa viwanda vimebaki kuwa magodauni, vingine vinafuga mbuzi na vingine vimebaki tupu baada ya wawekezaji wasio na nia njema kuuza vyuma vilivyopo ndani ikiwemo kiwanda cha Kanivas cha maturubai na kiwanda cha Asante Moproko kilichokuwa kinatengeneza mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijitapa kuwa inataka kuingia katika uchumi wa viwanda, lakini tutafikaje bila ku-review upya matatizo yaliyosababisha kufa kwa viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Serikali, ipitie upya mikataba ya ubinafsishaji, ambapo baadhi ya wawekezaji wasio na nia njema walichukua viwanda kwa lengo la kujinufaisha ambapo wengine walichukua viwanda kwa lengo la kupata mikopo katika mabenki, ambapo wengine walichukuwa mikopo na kufungua biashara zingine zikiwemo biashara za mabasi na malori badala ya kuwekeza kwenye viwanda na matokeo yake viwanda vimekufa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi zaidi ya 4000; mpaka sasa wengine wameshakufa, walikuwa wanadai fidia baada ya ubinafisishaji kwa lengo la kuwaendesha na kulipa vinua mgongo, lakini wafanya biashara hawa hawakuwalipa Wananchi hao hadi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ama kupitia upya mikataba, ukaguzi wa viwanda vya Komoa, Kanvas, Asante Moproco, Ceramic Unats, Tanaries, Tanzania Shoe, ambavyo vyote vimekufa na vimegeuzwa kuwa mazalia ya popo na kufugia mbuzi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kufungia viwanda vya Plastics nchini; hivi sasa kuna zaidi ya viwanda 20 vya kutengeneza plastics vinavyotengeneza mifuko, ambavyo vingi vimefungiwa kwa sababu vinasababisha uchafuzi wa mazingira, kiwanda kimoja cha mfuko wa plastic kinaajiri watu 200 kwa viwanda, hivi 20 tunawanyima ajira watu 4000! Kwa nini Serikali isije na plan B ya kuwataka wawekezaji hawa wa viwanda vya biashara kama vya mifuko kuagiza material ya kuozesha mifuko badala ya kuja na hoja ya kuongeza micro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imevifungia viwanda hivi kwa kuvitaka vitengeneze mifuko minene yenye unene wa macro 50 kutoka kwenye micro 30 ya hivi sasa. Wawekezaji hao wana mikopo na walifuata utaratibu wote wa kupata vibali na kuwekeza, lakini badala ya kuja na mkakati rahisi kusaidia nchi iendelee kuwa na viwanda sasa inaua viwanda!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Uingereza, Kenya, Ethiopia, viwanda vya Plastics ndiyo vinasaidia kuongeza ajira na kuinua uchumi. Katika hili wamefanikiwa kutokana na ubunifu ambapo ungesaidia kuwezesha mifuko hii badala ya hapa nchini kuja na mkakati wa kufungia viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ije na plan B ya kusaidia viwanda hivi kwa kuruhusu ku-import material kuwezesha mifuko na hii itasaidia hata bidhaa zingine zinazotumia mifuko kama chumvi, viroba, sanzu na kadhalika. Lakini tukija na mpango wa kuwa na mifuko macro 50 mifuko hii itakuwa ghali na watu wa kawaida hawataweza ku-afford.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote niipongeze kwa namna ya pekee hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo imefafanua mambo muhimu na imeitendea haki sekta hii ya habari. Nianze kwa kupongeza kazi nzuri ambazo zinafanywa na waandishi wa habari hapa nchini, kazi zinazofanywa na wasanii, kazi zinazofanywa na wanamichezo mbalimbali hasa wale wanaojitolea kwa nguvu zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Mheshimiwa Zitto kwamba hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kuisahau timu ya Taifa Stars hata Twiga Stars wamefanya kazi nzuri sana na walifuzu South Africa baada ya kuichapa Eritrea kwa bao nne kwa mbili, tulipaswa tuwaenzi kinadada hawa ambao wanafanya vizuri na wapo katika list ya timu nane bora za Afrika zinazofanya vizuri.
Baada ya kusema hayo vilevile Mheshimiwa Waziri ameshindwa hata kutueleza ni jinsi gani hii Wizara inaendelea kuwaenzi wanamichezo ambao wametumia nguvu na jasho lao kwa mfano Ndugu Francis Cheka, ambaye baada ya kumchapa Mserbia, hivi sasa Ndugu Francis Cheka, anaokota chupa, ndiyo ajira yake aliyonayo hivi sasa mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka Morogoro ninamfahamu, nimekuwa mwandishi na nimekuwa nikiandika habari zake, kungekuwa na mpango wa kuendelea kuwaenzi watu hawa siyo tu pale baada ya kumaliza pambano, angalau awe role model aendelee kufanya kazi zake vizuri na vijana wengine wavutiwe na kazi nzuri ambayo anaifanya kwa maana tuone ni yapi manufaa ya yeye kupigana na kupata ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende kwenye suala ambalo mwaka huu Aprili 15, Idara ya Habari, Mawasiliano ya Bunge ilitoa taarifa zake kwa vyombo mbalimbali vya habari, kwamba inaanza mpango wa kuwa na feed maalum ambayo tv itakuwa inarushwa na Bunge. Hali kadhalika Waziri naye alifika Bungeni na akatudhihirishia hilo, kwamba hivi sasa taarifa za Bunge zitakuwa zinawafikia wananchi kwa uhalisia, kwa high quality na tukawa tunaamini hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu ambao wanasema wameutoa katika Mabunge ya Jumuiya za Madola, utaratibu huu hapa kwetu kidogo ni tofauti, feed maalum zinatumika kwa nchi ambazo hasa waliangalia wingi wa vyombo vya habari, kuondoa congestion ya waandishi wa habari wote kuingia kwenye Bunge kupiga picha, ikizingatiwa kwamba waandishi wa television lazima awe mwandishi na mpiga picha, achana na redio achana na magezeti, sasa wakawa na mpango maalum ambao utasaidia Bunge liwe na television yake isaidie vyombo binafsi kila mmoja kwa wakati wake aweze ku-rely hizo information na kuzisambaza katika vyombo vyake. Wakati huo huo wananchi wawe na uwezo wa ku-access hiyo television na kuangalia ni kitu gani kinachojiri Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu ni tofauti na kinachofuata hivi sasa, tangu kuanza kwa mpango huu tumefanya monitoring ya day to day, kuna vitu ambavyo tumevibaini, mojawapo ni kufanya editing ya kupitiliza, taarifa tunazozizungumza, taarifa ambazo zinakosoa Serikali hazipewi nafasi, uchujaji huu wa namna hii ambao mwishoni mnatoa vitu vile ambavyo tu vinapendeza Serikali hatuwatendei haki wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeangalia hata uwiano wachangiaji wa upande wa Serikali na kambi pinzani, hakuna uwiano sahihi, tuna ushahidi, tunarekodi, na tumefanya monitoring za kutosha. Waziri Kivuli wa Ulinzi Mheshimiwa Juma Hamad Omar akiwasilisha taarifa yake hapa, amepewa dakika tatu tu, tena za mwishoni za kushukuru, waandishi wa habari wameshindwa kuiandika ile habari, na kama mli-monitor saa mbili habari hiyo haikuweza kutokea, sasa uchujaji wa namna hii tunakwenda wapi, kama tuna mambo ya feed maalum? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sasa waandishi wapiga picha wasiruhusiwe wakaingia wakachukua kile ambacho wanafikiri kitafaa, kuendelea kuwaruhusu waandishi wa magazeti na wapiga picha kuingia, huku waandishi wa television wakisubiri nje na baada ya kurekodi wanapelekewa clip kwenye external ambazo tayari zimeshachujwa, waandishi hawa wataandika nini, ushahidi upo na tunafuatilia na tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hilo mpango huu wa feed maalum bado quality yake ya picha siyo nzuri, mfumo unaotumika waandishi wa habari wakichukua ni lazima waende waka-condense lazima waende waka-convert kwenye adobe kwa maana hiyo wakatanue picha quality inapungua, hiyo ndiyo hali halisi. Kwa maana hiyo, kuna haja sasa ya kufikiria ili kuondoa utata kwa waandishi hawa wa television pamoja na kuwepo huu mfumo wa Bunge lakini wawe na uwezo wa kupiga picha kwa quality ambazo wanafikiri zinakidhi vigezo kwenye vyombo vyao vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isiruhusu mpango huu pamoja na hoja za awali kwamba ni gharama, Mheshimiwa Nape alituambia ni shilingi bilioni nne tulifanya assessment za kutosha, tukagundua wala haifiki bilioni Nne ilikuwa ni shilingi bilioni 2.1, wadau wamejitokeza wako tayari kusaidia wamezuiwa, mpango huu bado unaendelea kuwakwamisha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru, hili ni jambo ambalo Serikali inapaswa kuliangalia upya. Televisheni ya Taifa (TBC) inafanya nini kama inaendeshwa kwa kodi za Watanzania, kwa nini haipewi jukumu hili la kupeleka hizi taarifa kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi, katika taarifa ya Waziri amezungumza mambo mbalimbali, lakini sijaona mahali ambapo amekuja na mpango wa kuwasaidia waandishi wa habari ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu. Waandishi wa habari wanafanya kazi kutwa nzima, hawana mikataba, hawana maslahi mapana, lakini amekuja na mkakati kwamba lazima walipie Press Card kwa shilingi 30,000 ili kuingiza mapato katika Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema siyo hilo tu, Wizara kama inataka kumsaidia mwandishi wa habari ingekuja na mpango ambao ungewabana wamiliki wa vyombo vya habari walau kutenga asilimia fulani ya kuwasaidia waandishi hawa wawe na bima za afya, wawe na security za kazi, waweze kufanya kazi yao kama kweli tunatambua mchango wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnatambua mchango wake wewe mwenyewe binafsi Waziri kila unapopita, kila unachofanya, hufanyi bila waandishi wa habari, lakini inapokuja kuhusu masuala yao hapa hatujaona sehemu ambayo umejikita kupambania maslahi ya watu hawa! Zaidi ya hayo umenukuliwa ukisema sasa unataka kuja na mkakati wa waandishi wa habari kuwa na degree, ni jambo la ajabu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea nyingi watu wenye taaluma ya diploma ndiyo wazalishaji wakubwa na hata hapa nchini tunatambua mchango wa walimu wenye diploma, wauguzi, madaktari wenye level ya Assistant Medical Officer (AMO) wanafanya kazi nzuri sana, lakini ni kwa nini inapokuja kwa waandishi wa habari kije kigezo cha degree? Tulitegemea kuona mikakati kwamba nini kifanyike walau wapate muda wa kujiendeleza…
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Siungi mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nichangie katika Mpango wa Serikali wa Maendeleo 2017/2018 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, lakini ni lazima tuseme ukweli, hali ya maisha ya wananchi vijijini ni ngumu zaidi na wanaishi kwa kula mlo mmoja na wengine wanashindwa hata kupata mlo kutokana na mazingira magumu. Zipo taarifa kutoka vyombo mbalimbali yakiwemo magazeti, mitandao kwamba Septemba, 2015 mabenki yalikuwa na faida ya shilingi trilioni 64, lakini Septemba, 2016 faida za mabenki ni shilingi trilioni nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Waziri anasema uchumi umekua! Hivi kweli uchumi umekua, difference ya shilingi trilioni 60 ni gap kubwa. Serikali lazima ijitathmini, imekosea wapi? Hivi sasa mabenki yanajiendesha kwa hasara, hayatengenezi faida. Kama hayatengenezi faida, Serikali inakosa kodi na pia, hata wananchi nao wanakosa mikopo katika benki. Benki za Serikali ndiyo zipo hoi zaidi, TWB, Twiga Bancorp, TIB, ndiyo zimesinzia kabisa kwa kuwa na mtaji wa negative. Tumeshuhudia Serikali kuichukua Twiga na kuipa jukumu BOT kusimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi ya kujiuliza katika Serikali hii wakati kuna hali ngumu za maisha kwa wananchi, lakini Serikali imeshindwa kuzuia matumizi ya hovyo hovyo yanayogharimu fedha na kusababisha hasara kwa Taifa. Mfano halisi ni Benki ya TIB ambayo malengo yake ilikuwa ni kuendeleza kilimo, kutoa mikopo, kusaidia katika miradi ya umwagiliaji, kujenga na kuwekeza katika miradi ya kilimo, lakini zilizokuwa idara zake sasa hivi nazo zimekuwa ni benki kamili; TIB Cooperate, TIB Commercial, TABB Bank ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki zote hizi ma-CEO wao wote wanalipwa zaidi ya shilingi milioni 20 na kama imeshuka ni baada ya Mheshimiwa Rais kutoa tamko la kupunguza mishahara. Pia, katika hili, benki zote hizi zina Wakurugenzi wanaolipwa zaidi ya shilingi milioni 10, lakini hakuna wanachofanya; kuanzia asubuhi hadi jioni wanahudumia watu wawili au watatu tu kwa siku kwa sababu, benki hizi Makao Makuu yake yapo Dar es Salaam badala ya benki hizi kuwa vijijini kuwasaidia wakulima ambao kwa zaidi ya 80% kilimo hicho kinatengeneza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ugumu wa maisha unaonekana waziwazi katika uwekezaji wa viwanda; Bakhresa ameripotiwa na vyombo vya habari kuwa, zaidi ya 70% ya biashara zake zime-freeze na anatarajia kuhamishia hub zake katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha TTPL hivi sasa kilikuwa kinasindika zaidi ya tani 46,000, sasa hivi kiwanda hiki kinasindika tani 16,000 lakini cha kushangaza Serikali haitazami viwanda vya ndani vilivyo ndani, lakini inaangalia kujenga viwanda vipya badala ya kuangalia kwa jicho lingine viwanda hivi. Badala ya Serikali kutegemea kuanzisha viwanda vipya visivyo na tija na kuacha vya zamani vikiendelea kuteketea, lazima Serikali ikubali kuelezwa ukweli, ikae chini na kujipanga na kuweka vipaumbele vya kuendelea kutafuta mbinu za kufufua uchumi na kuwaondolea wananchi mateso ya ugumu wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, priorities za Serikali kwa wananchi wake hazieleweki. Tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu; kama uchumi umekua, kwa nini wasikopeshwe kama tunakusanya shilingi trilioni saba? Kwa nini Mfalme wa Comoro asingesaidia kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Vyuo Vikuu? Priority ni uwanja wa mpira wa kisasa Dodoma au kujengewa Msikiti na siyo kusaidia wahanga wa Kagera ambao hawajui hatima ya maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama takriban zaidi ya mwaka watumishi hawajui hatma ya maisha yao. Hawajui lini zoezi hili litamalizika; hawakopesheki na mabenki, kisa uhakiki. Hii siyo sawa. Serikali ina watumishi wa umma siyo zaidi ya 5,000, uhakiki gani usioisha? Uhakiki gani unazuia watumishi kupanda madaraja na kushindwa kupata haki yao ya msingi ya kupata mikopo?
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nikiri kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii lakini katika taarifa ya Mwenyekiti aliyowasilisha utashangaa kwamba hakuna suala lolote linalozungumzia juu ya Faru John, hakuna suala lolote linalozungumzia juu ya Loliondo, ni burning issues kwa sasa hivi, Watanzania walitaka wapate majibu, lakini Kamati haikuweza kwenda ili kuweza kupata kielelezo ili kuleta Bungeni, ni jambo la kushangaza. Sijui ni Kamati ipi ambayo inaweza ikalifanyia kazi zaidi ya Kamati ambayo ilikuwa maalum kwa ajili ya kuleta masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa haraka, niongelee suala la kulinda corridors wanakopita wanyama, kama tulivyosikia kwenye taarifa ya Kamati ya Maliasili na Utalii, Wizara iliamua kuzuia maeneo ambayo ni mapito ya wanyama. Nazungumza hili kwa sababu wanyama ambao wanatoka Saadani kwenda Wamimbiki, Mvomero, Mikumi kuelekea mpaka Ruaha wananchi wamevunjiwa nyumba zao katika Wilaya ya Mvomero wakijumuisha pia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kutokana na kupisha hizi corridor za wanyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kushangaza Serikali imewavunjia wananchi nyumba hizi, haikuwalipa fidia lakini Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imejengwa kwenye mapito hayo ya wanyama. Kama ni sheria ni lazima ikate pande zote mbili. Kuendelea kuwavunjia wananchi nyumba zao bila kuwalipa fidia huku Serikali ikiendelea kuweka majengo ya Halmashauri na kujenga nyumba za wafanyakazi si kuwatendea haki wananchi. Naomba Wizara iangalie upya suala hili na kama kuna uwezekano walipe fidia kwa wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mambo mengine ya migogoro ya wakulima na wafugaji Mkoani Morogoro. Ziko Kamati mbalimbali ambazo zimeundwa na Bunge hili lakini mpaka sasa hivi hakuna taarifa zozote ambazo zimefanyiwa kazi kusaidia kupunguza migogoro hii. Tunashuhudia watu wanapigwa mikuki ya midomoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Rais akifuta hati mbalimbali za mashamba. Tatizo ni ardhi, kwa nini mashamba hayo yasirudi yakawasaidia wananchi wa Wilaya za Mvomero na Kilosa ambako ndiko kwenye matatizo na migogoro ya kila siku? Hati hizi ambazo zimefutwa kwa nini ardhi hizi zisigawanywe kwa wananchi? Mpaka sasa ardhi zile zimeendelea kuwa mashamba pori pamoja na kufutwa huku wananchi wanaendelea kuwa na migogoro kutokana na uhaba wa ardhi. (Makofi)
Suala lingine ni kuhusu korongo lililojengwa la kuwatenga wakulima na wafugaji Wilayani Mvomero. Suluhu ya migogoro hii si kuendelea kuwatenga wakulima na wafugaji. Jamii hizi zinategemeana, hawa ni Watanzania, wanashirikiana lakini Serikali imeendelea na msimamo wake wa kuendelea kujenga korongo lile mbali na kwamba tulisema lisitishwe ili kutafuta suluhu kati ya makundi haya mawili ambayo yameendelea kuwa na migogoro ya siku hadi siku. Serikali imeendelea kutumia fedha zaidi ya shilingi milioni 17 kuendelea kuchimba korongo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo ambayo tunahitaji Wizara husika iyafanyie kazi ione. Kuna Kamati Maalum ya kutataua migogoro ya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia sana hotuba zote tatu ikiwemo ya Waziri, hotuba ya Kamati na hotuba ya Kambi ya Upinzani. Katika hotuba zote hizi, kila hotuba iligusa kuwapongeza madaktari kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa Watanzania. Tunafahamu kazi yao ni ngumu kazi ya kutetea uhai wa wanadamu siyo kazi rahisi. Kazi ya kuahirisha kifo siyo kazi rahisi ni kazi ambayo kwa kweli inatoka moyoni katika kuhudumia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia madaktari wakifanyakazi katika mazingira magumu, tumeshuhudia wengine hata waki- risk kwenye kazi zao magonjwa, kupata maambukizi, lakini madaktari hawa hawakati tamaa wanaendelea kuwahudumia Watanzania. Kwa kweli, niwapongeze sana madaktari kwa kazi ngumu wanayoifanya. (Makofi)

Pamoja na kazi hii sasa wanayoifanya lakini kuna mambo ambayo tukiyaangalia yanakatisha tamaa. Daktari anafanya afanyavyo kuhudumia wagonjwa walio wengi, lakini inatokea viongozi kama DC, RC anamtumbua hadharani Daktari - DMO akishasikiliza malalamiko ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara, anasema kuwanzia leo hana kazi. Nafikiri ifike mahali tuwape moyo watu hawa ambao wanajitoa kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wana madai yao ya msingi, kwa zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa Daktari Bigwa kwenye zile call allowance kwa maana mgonjwa kazidiwa saa nane saa tisa ya usiku analipwa shilingi 25,000 na dakitari wa kawaida analipwa shilingi 15,000. Madaktari hawa kwa zaidi ya mwaka hospitali nyingi hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwa Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa wa Morogoro inahudumia wagonjwa 500 kwa siku na hii ni baada ya hospitali ile kuwa ya rufaa kwa maana inahudumia wagonjwa wanaoshindikana katika Wilaya zake zote. Hospitali hii pamoja na ukubwa kuhudumia wagonjwa 500 ni sawa na wagonjwa 15,000 kwa mwezi, lakini hospitali hii haina x-ray machine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, x-ray machine iliyopo ni ambayo imenunuliwa tangu vita ya pili ya dunia, kwa sababu hospitali ile ilikuwa ya Jeshi. X-ray inagharimu siyo zaidi ya shilingi milioni 100, hospitali hii haina. Wagonjwa wanatoka na drip wanakwenda Mazimbu, wanakwenda hospitali ya Jeshi kwenda kufanya x-ray. Hilo nimelishuhudia mwenyewe na tumefuatilia na tumewahi hata kusema hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mortuary, hivi leo ndugu yako akipoteza maisha katika Mkoa wa Morogoro utalazimika kumsitiri pasipo hata kusubiri ndugu, kwa sababu mortuary hazifanyi kazi. Kweli kwa hospitali hii ambayo ina hadhi ya kuwa ya rufaa inashindwa kutengeneza tu mortuary kwa ajili ya kuwaifadhi wapendwa wetu ili basi walau waweze kuagwa kwa heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala lingine la Madaktari Bingwa. Tumekuwa na ajali nyingi sana Mkoa wa Morogoro, Daktari Bingwa wa mifupa hakuna, theatre kwa ajili mifupa hakuna, theatre iliyopo ni moja na inategemewa kwa maana ya magonjwa yote, akina mama wanaojifungua ndiyo hiyo hiyo. Watu wenye vidonda ndiyo hiyo watu wa ajali ndiyo hiyo. Nafiki Waziri alitizame kwa namna nyingine suala hili ili kuipa hadhi hospitali ya Mkoa wa Morogoro iweze kuwa na theatre room.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la sakata la madaktari. Serikali ya Awamu ya Nne, kipindi cha nyuma ilikuwa ikihamasisha kwa maana ya ule mpango wa brain bridge kutoka nje, madaktari wetu ambao wamesomeshwa na kwa fedha za Tanzania watoke nje, waje nchini, tena nakumbuka Rais wa Awamu ya Nne, ndiyo ulikuwa mkakati wake wa kuwaomba Watanzania walioko nje warudi hapa nchini watoe huduma kwa Watanzania wenzao. Nakumbuka walikwenda Cuba, Botswana Uingereza na kwingineko na baadhi ya madaktari nafikiri waliitika wito wa Rais wa Awamu ya Nne wakarudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii cha kushangaza Tanzania ambayo ina upungufu wa madaktari, inawachukua madaktari kwenda kutoa huduma kwa Wakenya. Tumeushangaza ulimwengu kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia daktari mmoja kwa takwimu nimepitia hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa vijijini daktari mmoja anahudumia watu zaidi ya 78,000 na nane, kwa mjini anahudumia watu 25,000. Wenzetu Kenya daktari mmoja anahudumia watu 15,000. Leo hii sisi ndiyo wa kupeleka Madaktari Bingwa, madaktari wetu, watoto wetu, waende wakahudumie kuwaponyesha Wakenya wakati wamesomeshwa na kodi za Watanzania! Kuna mahali ambapo tunabidi kukubali kwamba tumefanya makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, najaribu kuwatizama wale ambao hawakujitokeza kwa maana walikuwa na nia pengine ya kutoa matibatu kwa Watanzania, kuwaajiri madaktari 258 kati ya wale ambao walitahiniwa na kuwaacha wale wazalendo ambao walikuwa na nia ya uzalendo siyo sawa. Nafikiri priority ingekuwa kwa wale ambao walisema wana nia ya kuwatumikia Watanzania zaidi, kubaki nchini na kusaidia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali inasema ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya, hivi sasa tuna kata zaidi ya 3,900, hospitali ambazo zinamejengwa katika kata hizi ni hospitali 448 ambayo ni sawa na asilimia 11 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu unatekelezeka kwa namna hii? Yako mengi ambayo tunataka kuyajua, flyover ndiyo ni maendeleo, flyover moja ambayo ni shilingi bilioni 100 ni sawa na kujenga hosptali ngapi za Kata? Ni zaidi ya hospitali 250. Priority kwa Watanzania walio wengi ni flyover au ni kupata hospitali ili wapate huduma za afya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la upungufu wa vifaa. Ukienda kwenye hospitali kifaa cha kupima wingi wa damu baadhi ya hospitali za private unapata, siyo hospitali za government. Ukienda kupima hospitali za government itakuchukua siku tatu kufahamu wingi wa damu, private ndani ya saa kadhaa unapata jibu, kwa sababu hospitali za government zinazidiwa na wagonjwa, ni kwa nini vifaa hivi muhimu visiwepo kwenye hospitali za government zikaweza kuwasaidia wagonjwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa naliangalia sana suala...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niwapongeze waandishi wa habari ambao wanafanya kazi yao vizuri sana. Tuna kila sababu ya kuwapongeza waandishi kwa sababu tujiulize tu kama Taifa hili lingekuwa halina waandishi hakuna vyombo vya habari sijui tungekuwa kwenye giza la namna gani. Tunapenda tuwapongeze kwa kazi ambayo wanaifanya, japo tunajua wanafanya kazi katika mazingira magumu kuliko ilivyo kawaida. Tunaendelea kuwapa moyo waendelee kupambana kuendelea kutoa elimu na kuelimisha taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani (Waziri Kivuli) alikuwa ametoa pongezi nyingi kwa harakati mbalimbali ambazo Waandishi wa Habari wanaendelea kufanya katika kujaribu kujitetea na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuifanya kazi yao. Pamoja na kwamba hotuba ile imechinjiwa baharini lakini mimi nawapa comfort kwamba tutaendelea kuwasemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri wakati wa hotuba yake, amewasifu wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari, wanamichezo lakini sijasikia mahali akizungumza kuhusu habari ya mateso ya waandishi wa habari. Waandishi wa habari ambao walivamiwa na kuumizwa wakiwa katika press conference ya Chama cha Wananchi (CUF) ambao nao ni wadau muhimu nilitarajia angewapa pole. Hali kadhalika kwa wasanii, Ney wa Mitego na Roma Mkatoliki nao waliteswa ambao nao pia ni wadau wake, alipaswa nao awape pole kwa kazi kubwa ambayo wanafanya pamoja kupitia madhila mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri amenukuliwa akisema kwamba yeye ni msikivu na yupo tayari kuhakikisha kwamba anaendelea kusaidia tasnia hii ya habari iendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni zaidi ya waandishi 30 wamepitia manyanyaso makubwa, wengine wakiwekwa ndani na Wakuu wa Wilaya, vyombo vya habari vikivamiwa ikiwemo redio ya Clouds, tunamuomba Mheshimiwa Waziri wakati ana windup hapa atueleze ni nini hatma ya ripoti iliyoandaliwa na Mheshimiwa Nape Nnauye wakati akiwa Waziri kuhusu sakata la kuvamiwa Clouds. Si hiyo tu pia atuambie ni sheria ipi ambayo inamruhusu DC kumzuia mwandishi wa habari asiingie katika Wilaya eti apate kibali cha kuandika habari.

Tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwa hii sheria ambayo RC, DC ana uwezo wa kumuweka mtu rumande kwa saa 48 iletwe Bungeni irekebishwe kwa sababu imekuwa ikitumika kama kigezo cha kuwaumiza waandishi wa habari. Tumeona Ndugu Mnyeti ambaye ni DC wa Arumeru amewaweka Waandishi wa Habari ndani kisa wameingia katika eneo lake la kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo waandishi wa habari walitambuliwa rasmi kwa maana ya kuhakikisha professional hii ya waandishi wa habari inafanya vizuri. Tunashukuru hivi sasa Serikali inatambua kwamba tasnia ya habari ni muhimu na inafanya kazi. Hata hivyo, yapo mambo mengine ya msingi ambayo tunajiuliza, kama uandishi wa habari ni tasnia muhimu kama ilivyo professional zingine mfano za udaktari, wanasheria kuna mambo ya msingi sana ambapo yanatufanya tunashindwa kuielewa sheria hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea mwandishi wa habari amefanya makosa ya kitaaluma sheria hii inasema akamatwe na polisi afikishwe mahakamani, lakini taaluma kama ya udaktari, endapo daktari atafanya makosa ya kitaaluma kuna sheria kwamba bodi inapitia, inamuajibisha lakini hakuna harakati za haraka haraka za kumpeleka polisi na kumfikisha mahakamani. Imewahi kutokea daktari ambaye alikuwa afanye operesheni ya kichwa akafanya ya mguu, lakini alifikishwa mahakamani? Kwa nini tunapokuja kwenye suala la uandishi wa habari wakamatwe na polisi wafikishwe mahakamani, tunaona hapa kuna double standard. Tunaomba kama kweli hii ni sheria na tumeamua kuitambua tasnia ya waandishi wa habari basi kama mtu atakuwa amefanya kosa la kitaaluma bodi zihakikishe zinamwadhibu kwa kuangalia taaluma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu ukata wa hivi sasa kwa vyombo vya habari, hii haijawahi kutokea. Hivi sasa waandishi wa habari hawana kazi za kufanya, kuna poromoko kubwa la waandishi kuachishwa kazi. Kampuni za The Guardian, Free Media, Azam na New Habari Cooperation zimepunguza waandishi. Ni kwa nini waandishi hawa wanapunguzwa? Ni kwa sababu hali imekuwa ngumu, wanafanya kazi katika mazingira magumu. Gazeti ambalo lilikuwa linatengeneza nakala 26,000 sasa hivi linatengeneza nakala 5,000. Hali hii inakuwa ngumu zaidi kwa sababu Serikali haipeleki matangazo kwenye hivi vyombo vya habari hususani vya private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Rais akihitaji kufanya press conference anaita vyombo vyote, Mkuu wa Wilaya au RC wakitaka kufanya press conference anaita vyombo vyote lakini ikija kwenye suala la matangazo vyombo vya binafsi vinabaguliwa. Kwa nini tusitende haki tuwezeshe hizi private sector zifanye kazi zipate matangazo ziweze kuhudumia Taifa hili? Kama kuna mkakati wa kuhakikisha kwamba tunadumaza vyombo hivi tuelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali iangalie imetoa mamlaka hivi hivi sasa kwa Idara ya Habari - Maelezo yenyewe ichuke jukumu la kuratibu matangazo yote. Katika matangazo ambayo yanakwenda kwenye vyombo vya habari, Idara ya Habari - Maelezo ambayo imepewa jukumu ya kuratibu matangazo inapata commission ya asilimia 10, kwa hiyo imeacha kazi yake ya msingi sasa hivi inahakikisha inatafuta matangazo. Hii ni kama ilivyo sasa hivi traffic ambapo wameacha kazi zao za msingi za kuhangaika na ajali inahangaika na tochi za kukusanya. Tunaomba tusaidiwe tujue kama kweli suala hili la kuratibu matangazo ambalo linakwenda kwa njia ambayo ni ya kibaguzi kupitia Idara ya Habari - Maelezo, ni kwa nini utaratibu wa zamani usitumike na vyombo vyote vipate haki katika kupata matangazo ili viweze ku–retain waandishi ambao wameajiriwa katika vyombo hivi vya habari. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, tukitoka hapo tuzungumze kuhusu hofu iliyopo hivi sasa kwa vyombo vya habari. Hakuna uhuru kabisa wa vyombo vya habari hapa nchini. Tumemsikia Mheshimiwa Rais katika ziara zake Mkoani Shinyanga alisema yapo magazeti matatu ambayo yupo karibuni kuyafungia, japo hakuyataja lakini hii moja kwa moja kama mkuu wa nchi inaleta hofu kwa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kuona kwamba pengine ni mimi au yule. Kwa hiyo, waandike habari ya kuipendeza Serikali na kuacha kuandika habari za kukosoa Serikali pale ambapo inakwenda kinyume na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sakata la Bashite kuvamia Clouds, Rais alinukuliwa kwamba vyombo vya habari haviko huru kwa kiasi hicho na kutoa karipio kali. Tulitegemea kwamba Rais angesaidia kwa mtu kama huyu ambaye amekiuka maadili ya utumishi wa umma kwa sheria ya mwaka 1995 mpaka sasa hivi asingekuwa kazini. Kwenda kuivamia studio na waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao kihalali na kuhakikisha waandishi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, sekta hii muhimu kwa uchumi wa Taifa. Kiwango cha kutangaza utalii kipo chini hali ya kuwa na tozo nyingi zinazotozwa zikidaiwa matumizi yake ni promotion kupitia Bodi ya Utalii mfano watalii wanalipa dola moja per head wanapolala kwenye hoteli per night na zinapelekwa Bodi ya Utalii. Matozo mengi yanafanya watalii wengi kukimbilia Kenya na mpaka Kenya wana-captalize Mlima Kilimanjaro ni wao na watalii wanafikia kwao due to number of charges zisizo na sababu. Katika eneo la matangazo mfano ndege za Kenya zimeandikwa Kilimanjaro na zinakwenda nchi nyingi duniani, kwa hiyo, ni rahisi kuwaaminisha wageni kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na strategies nzuri za ku-promote utalii na kuondoa siasa kama za kusema tunanunua ndege kubwa ya Dreamliner itakayoruka Ulaya mpaka Kilimanjaro ikiwa na watalii is this a strategy? Hapo hapo mkoa wenye utalii umejaa siasa za chuki mpaka kukera wageni, kwa mfano RC kaweka mtu ndani muda mrefu kwa zaidi ya miezi minne bila dhamana kwa kesi ambayo ina dhamana, yote haya wageni wanayaona na wanatushushia value.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA wafanye kazi na kupunguza matumizi yasiyo na lazima. Kwa mfano kuna Mawaziri walikuwa wanatumia mali za TANAPA kama magari, ndege kama mali zao binafsi na zikatumika mpaka kwenye kampeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Faru John na Faru Fausta ambapo Faru Fausta gharama za matunzo yake ni kubwa wakati matukio ya ujangili ni makubwa na yanaendelea. Hata taarifa ya Faru John namna alivyopotea inajulikana ila imefunikwa funikwa na imepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli nyingi za kigeni zina- charge gharama kubwa na masharti yake ni magumu. Hoteli hizi zinawalenga hata wazawa ambapo huendi bila appointment na ndiyo hao faru wanapotelea kwenye hizo hizo hoteli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maliasili na nishati, matumizi ya mkaa yanaendelea kuongezeka nchini na hii inatokana na kupanda kwa gharama za gesi. Serikali huwezi kuhimiza matumizi ya nishati mbadala wakati gesi na umeme gharama yake ipo juu. Makaa ya mawe,
wawekezaji kama Dangote amepewa achimbe kwa nini yasitumike pia kwa wazawa kama nishati ili waache kuchoma mkaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro maeneo ya hifadhi namna ambayo wawekezaji wanapewa vipaumbele kuliko wazawa na mwisho huwa ni migogoro isiyoisha. Wawekezaji wana viwanja vidogo vya ndege ndani ya hifadhi mfano Serengeti wanavifanyia nini kama siyo vinatumika kuhujumu uchumi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi ambayo ipo Mtwara tulihakikishiwa kuwa itakuwa muarobaini wa mambo mengi ikiwemo matumizi ya nyumbani ili kunusuru ukataji misitu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya gesi ya majumbani na bei itakuwa chini. Kuna sehemu kama Dar es Salaam yalitandazwa mabomba ya gesi mitaani lakini hakuna lolote, mkaa tani na maelfu ya tani kila siku yanapelekwa Dar es Salaam.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu kwa maisha na maendeleo ya Watanzania. Vision ya viwanda, Mwalimu Nyerere aliwahi kuiona na ilikuwa implemented kuanzia miaka 1967, ambapo mikoa mbalimbali ilionesha kwa vitendo kwa kuwa na viwanda na vilikuwa vikifanya kazi. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa ambayo ilinufaika na vision hiyo kwa kuwa na viwanda zaidi ya 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunavyozungumza viwanda vilivyokuwa vimewekeza katika Mkoa wa Morogoro kwa miaka hiyo ya 1960 viliwezesha wananchi wa Mkoa wa Morogoro kupata fursa za kupata ajira. Ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupata house girl; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta watu wanacheza bao; ilikuwa siyo rahisi kwa Mkoa wa Morogoro kupita kukuta Wamachinga; ilikuwa siyo rahisi kupita Mkoa wa Morogoro ukakuta watu wamekaa vijiweni, kwa sababu kulikuwa na viwanda na viwanda vile vilikuwa vikitoa ajira kwa wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo sasa, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimejaribu kupitia sana katika taarifa yake hii, iko wapi mikakati ya kufufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro vilivyokufa? Ubinafsishaji wa viwanda badala ya kuongeza efficiency, ubinafsishaji wa viwanda umekuwa ni wa kunufaisha watu wachache ambao wamechukua viwanda kama collateral kwenda kukopa katika mabenki, kunufaika wenyewe na wananchi kukosa ajira. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha, atuambie uko wapi mkakati halisi wa kuvirudisha viwanda vya Mkoa wa Morogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Morogoro hivi sasa kuna viwanda, kwa mfano, Kiwanda cha Canvas ambacho kilikuwa kikinua hata pamba kutoka kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa, lakini hivi sasa wameacha kulima pamba kwa sababu kiwanda kimekufa. Kipo kiwanda cha Asante Moproco cha Mafuta; kiwanda hiki wananchi walikuwa wanalima alizeti kwa sababu walikuwa na uhakika wa sehemu ya kuuza. Hivi sasa wananchi hawalimi alizeti kwa kuwa hakuna kiwanda. Kipo kiwanda cha Komoa, kipo kiwanda cha CERAMIC, Morogoro Leather Shoe, UNNAT cha Matunda ambacho kilikuwa kikinunua matunda ya wananchi wa Mkoa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atupe mkakati wa kufufua viwanda hivi. Siyo hivyo tu, atuambie Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua wawekezaji hawa ambao kwa makusudi waliviua viwanda hivi? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha watu hawa ambao wengine kwenye viwanda vile wameuza vipuri, hivi sasa yamebaki kuwa magodauni na wengine wanachunga mbuzi. Je, ni sahihi kwa watu hawa kutumia collateral kupata faida lakini wanaviua viwanda badala ya kunufaisha? Atuambie, Mheshimiwa Rais alipita Morogoro akasema atalishughulikia, tunataka kuona kwa vitendo kwamba hawa wamiliki wa viwanda ambao wameziweka ajira za wananchi wa Mkoa wa Morogoro mfukoni, wanachukuliwa hatua gani kama kweli mna nia ya kuleta viwanda kwa nchi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la nyumba. Wakati wa ubinafsishaji zipo nyumba ambazo zilikuwa zinamilikiwa na viwanda vile na zilikuwa ni nyumba za Serikali. Zile nyumba hivi sasa zinamilikiwa na watu ambao ndio waliobinafsishiwa viwanda, lakini hivi sasa wafanyakazi wa Serikali hawana nyumba, hawana pa kuishi. Wale watu wamepeana nyumba zile kinyemela, hawalipi pango na hawalipi kodi. Maofisa wanakosa mahali pa kuishi lakini watu waliobinafsishiwa wanang’anga’nia kuishi kwenye nyumba hizi. Hii siyo sahihi kabisa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri amulike, aangalie ili hatua mahususi ziweze kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia biashara ya mwendokasi; mabasi ya Dar es Salaam, tuna mengi ya kujiuliza. Biashara hii imekuwa kama ni ya watu wachache. Serikali imeamua kuleta mabasi ya mwendokasi kwa lengo la kusaidia kupunguza msongamano, lakini kuna wazawa, kuna Watanzania ambao walikuwa wakifanya biashara za daladala ambao nao walikuwa na uwezo wa kupata fursa ya kuwekeza katika mwendokasi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichukue dakika tano kuchangia bajeti. Nilimsikiliza sana Waziri wakati akiwasilisha bajeti ile, suala la kufuta motor vehicle na kurudisha shilingi 40 kwenye mafuta ni kama umeiba kutoka mkono huu na kupeleka mkono wa kushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani asiyefahamu kwamba ukigusa mafuta umegusa kila mahali. Ni nani asiyefahamu umuhimu wa mafuta kwa nchi hii mnatuambia tunakwenda kwenye nchi ya viwanda. Hiyo motor vehicle ambayo imefutwa sijui Waziri alifanya research kiasi gani nakuona kwamba labda iwe compansated na shilingi 40 na ni kwa nini 40 tunataka kufahamu, kwa nini isiwe shilingi 10 au tano?.

Mheshimiwa Mwenyekiti kuna mambo ya msingi ambayo lazima niyaangalie. Ukizungumza habari ya mafuta unazungumza maisha ya watu. Hatuwezi kwenda kwenye viwanda kama mafuta bado yako juu. Huwezi kugusa uzalisaji wa namna yoyote kama mafuta bado yako juu. Kwa hiyo, ni lazima Waziri aangalie upya suala hili la kuongeza shilingi 40 kwenye mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia pia katika kitabu cha bajeti ya Waziri. Anazungumzia kwamba kufutwa kwa hizi road licence pengine zitasaidia na hakutakuwa na shida na itawezesha watu wengi wenye magari waweze kuendelea kufanya kazi zao vizuri. Lakini ninachotaka kukuambia analysis ambazo tumezifanya shilingi 40 kwa mtu mwenye scania au basi anatoka Dar es Salaam anakwenda Mbeya anatumia may be lita 600, go and return lita 600 ukizidisha mara arobani tunazungumzia shilingi 24,000 kwa siku. Kwa mwezi tunazungumzia shilingi 720,000, kwa mwaka nzima tunazungumzia shilingi 8,640,000 wakati hiyo motor vehicle ilikuwa haizidi shilingi 500,000. Kwa hiyo, tunachoona ni kwamba watakaokwenda kuumia ni Watanzania, kwa sababu kila mtu lazima atumie usafiri kwa vyovyote vile iwe kusafirisha mazao, kwenda kokote anakoweza lakini tutakwenda kuwaumiza Watanzania, kwa hivyo naona hii shilingi 40 haina tija. Otherwise angetuambia ni kwa nini shilingi 40 na isiwe shilingi tano au isiwe shilingi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye bajeti ya Waziri kila mwaka sigara, pombe zinapanda. Siku Watanzania watalala waamke, wamwelewe vizuri Naibu Waziri Kigwangalla na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kuhusu suala la no smoking hatutakuwa na bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema sigara hizi ndiyo zinaleta madhara, ndiyo zinazotuletea kansa, kifua kikuu, tunakiwa na maadhimisho ya siku kifua kikuu. Fedha hizi hizi zinazosema tunazosema tuna-save huku tunakwenda kutibia watu wetu ambao wanaugua magonjwa yanayotokana na sigara na pombe. Kwa hiyo, ifike mahali tutatafute sources nyingine ambazo zinaweza zikasaidia Watanzania na siyo kucheza na afya za Watanzania, kuendelea kupandisha kila wakati haizuii mtu kutumia sigara. Lakini tungetafuta vyanzo mbadala ambavyo ni reliable vitakavyosaidia Taifa hili kupata mapato halali bila kuwa na athari kwa wananchi wanaotumia vitu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine la bandari, ni aibu. Hotuba ya Kambi ya Upinzani imesema kwamba lazima kuwe na vyanzo vingine ambavyo vitalisaidia Taifa hili. Tukiangalia nchi zingine zinafanya vizuri, angalieni Bandari ya Beira, angalieni Mombasa wanavyofanya vizuri na World Bank wamewahi kusema endapo tutatumia vizuri bandari, zaidi ya asilimia 30 tunaweza tuka-save kwenye bajeti yetu. Sasa hivi bandari imegeuka siasa. Viongozi wa Serikali wanaamka asubuhi na vyombo vya habari wanakwenda bandarini kutumbua watu.

Mheshimiwa Waziri kwa nini tusikubali kwamba tunahitaji watu professional watusaidie tufanye nini ili bandari zifanye kazi vizuri. Tuna Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara yenye kina kirefu lakini bado hazisaidii mchango kwenye hii bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuangalie haya mambo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru lakini siungi mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia sana kitabu cha Waziri Mpango, nisikitike tu kusema mambo mengi tunayoyaona ni yale yale, hakuna mambo mapya. Mheshimiwa Mpango nilitegemea ungekuja na mikakati mipya kuhusu suala la bandari. Tukizungumzia bandari, tumeambiwa bandari ikisimamiwa vizuri inaweza ikasaidia kuongeza Pato la Taifa hili tukaachana na kukimbizana na watu wanyonge, wafanyabiashara wadogo ambao hawana nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ilivyo hivi sasa ukiwauliza wafanyakazi wa bandari wanakwambia hawaijui siku yao wala saa. Bandari imegeuka kuwa siasa, viongozi mbalimbali wanakwenda na camera kwenda kutumbua viongozi wa bandari, wakurugenzi wa bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango atuambie asione aibu, kama unahitaji kusaidiwa kwenye bandari usione aibu sema. Nchi zingine zenye bandari zinafanya nini zinafanikiwa, kwa nini Tanzania hatufanikiwi? Tafuta experts wa kusaidie tufanyaje bandari yetu iweze kusonga mbele ichangie Pato la Taifa. Kila siku Mheshimiwa Mpango wewe unazungumzia, ooh, kodi zitaongezwa kwenye sigara na kadhalika, kumbe tuna bandari ambayo ingeweza kusaidia hata hizi sigara ambazo tunasema zina madhara tukaachana nazo kwa sababu kuna siku Watanzania wataamka watalielewa neno “no smoking” na sijui mapato tutapata wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Bandari ya Mtwara, yenye kina kirefu, lakini tumeifanyia kazi kwa kiasi gani? Leo tulikuwa tukisikia TRA wanatangaza mapato yao wamepata kiasi gani, lakini ukienda bandarini hakuna meli, meli utakayoikuta imebeba kokoto inapeleka Qatar kwenye kuandaa Kombe la Dunia. Kwa nini meli zisiwepo pale ambazo tunajua zime-import tunahakikisha tunapata mapato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango usione aibu, tafuta namna ambayo utashauriwa na wataalam waweze kusaidia tufanyaje bandari ya Tanzania iweze kusaidia kuongeza pato na kuwapunguzia mzigo Watanzania ambao wanakimbizana huko, mtu unamkuta ana kamtaji kake ka laki mbili anaambiwa anunue EFD machine ya shilingi laki nane, hii ni ajabu sana. Kamtaji ka laki mbili, laki tano unaambiwa nunua EFD machine ya laki nane, are we serious? Bandari isimamiwe na ifanye kazi yake vizuri iokoe jasho na vilio vya Watanzania. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa siipokei, nilifikiri ananiambia kwamba bandari inafanya kazi kwa zaidi ya asilimia 100, ananiambia 40? Bandari tunayo miaka mingapi toka uhuru mpaka sasa hivi tunazungumzia bandari hiyo hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu fine za barabarani. Traffic wametoka kwenye lengo la kusaidia kupunguza ajali za barabarani, sasa hivi wamegeuka kama maofisa wa makusanyo wa TRA. Nikizungumza hayo wanaotoka Dar es Salaam wanaelewa, shida wanazokutana nazo watu wenye magari, traffic hivi sasa wanafungua mpaka bonnet kuhakikisha wanakusanya mapato na kila mwisho wa mwezi wanatoa tathmini, tumekusanya milioni kadhaa kwa sababu ya matatizo na makosa mbalimbali ya barabarani, hivi hii ni faida ni hasara? Hivi hili ni tatizo au? Kwa sababu huwezi ukasema umekusanya mapato kwa fine za barabarani maana yake hujafanya kazi yako ipasavyo. Tulitegemea wangekuja na taarifa kwamba ni namna gani wamepunguza ajali kutoka asilimia fulani kwenda asilimia fulani na siyo kutuletea mapato, hii sio kazi yao, ni kazi ya TRA hii. Kama tuna nia ya kukuza uchumi ni lazima tuangalie vitu hivi na sijui kama Mheshimiwa Mpango kwenye hili amewawekea traffic wapi maana wanaonekana nao wanafanya kazi ya kukusanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu habari ya viwanda. Nimesikia kwamba hivi sasa mikoa inatakiwa kuwa na viwanda 100. Hivi ni viwanda vipi? Tunasema mtu akiwa na cherehani tano tayari ni kiwanda, are we serious? Tuna viwanda vingapi ambavyo vimekufa hivi sasa havieleweki? Mkoa wa Morogoro wenyewe una viwanda zaidi ya 20 vime-collapse, hakuna ajira, wengi wanafugia mbuzi hivi sasa. Viwanda vya Morogoro watu walichukua wakafanya kama collateral kwenda kuchukulia mikopo kufanya shughuli zao zingine lakini viwanda vimekufa. Kwa nini tusivitazame viwanda hivi ambavyo tayari vipo ambavyo vilianzishwa kwa nguvu ya Mwalimu Nyerere? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa siikubali. Mimi nilifikiri angenieleza kwamba tayari viwanda vimeanza kufanya kazi. Hizi hadithi anazosema tumeanza kuzisikia siku nyingi tu. Kusema leo tutafufua, kesho tutafufua, watu wa Morogoro tulishazoea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie kwenye sekta ya utalii. World Bank wanatuambia sekta ya utalii ikisimamiwa ipasavyo ina uwezo kabisa wa ku-cover budget yetu kwa mwaka. Hivi sasa tunajiuliza pamoja na vivutio tulivyonavyo, hifadhi tulizonazo lakini bado hakuna kitu ambacho tunaona kama vile tunafanya kwa malengo ya kuhakikisha sekta hii inanyanyuka na inachukua nafasi kusaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hoja zinazoendelea hivi sasa tunataka kuona Waziri anasimamia pale kwenye sekta ya utalii kutoa ushauri na kuangalia tufanyaje tuende mbele badala yake sasa Waziri anayepata nafasi yeye ana kazi ya kuangalia aliyetoka alifanya nini na vijembe. Aje na mkakati kwamba yeye atafanya nini kutupeleka wapi ili sekta hii itusaidie, si kufufua makaburi Mawaziri wengine wamefanya kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kuna mahali ambapo tumekosea, ni lazima tuwe na mipango mikakati ambayo itatusaidia ili sekta hii ya maliasili na utalii iende kuwasaidia Watanzania kama vile…

TAARIFA . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu naye ni Mjumbe mwenzangu kwenye Kamati mimi ninashangaa sana kwenye Kamati anasema vile huku leo anasema hivi. Yeye juzi hapa amesema Mheshimiwa Kigawangalla akae vizuri vinginevyo atatumbuliwa kama Mheshimiwa Maghembe au siyo, sasa sasa hivi anatupa taarifa ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuzungumza kukuza uchumi bila kuangalia jinsi ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja. Ukiangalia hali ilivyo hivi sasa huwezi kuwatoa watu ambao ni matajiri wanaoishi kama malaika useme waishi kama mashetani, haiwezekani, hivi vitu vyote vinategemeana. Sasa ifike mahali watu waangalie sekta binafsi zinafanya nini na Serikali ione ni jinsi gani ya kusaidia sekta hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunaona hasara ambazo zinapatikana kwa hivi sasa kwenye sekta nyingi. Kwa mfano, Club Bilicanas iliyokuwa inamilikiwa na Mheshimiwa Mwenyekiti Mbowe ilivunjwa kwa jazba na kadhalika lakini hivi sasa club ile magari yana-park; kulikuwa kuna migahawa, kuna Gazeti la Tanzania Daima, watu wangapi wamepoteza ajira? Wafanyakazi wangapi walikuwa wanategemea pale kuishi maisha yao? Leo hii kweli, taxi ndiyo zina-park pale? Hatuwezi kujenga uchumi kwa kuumiza watu.

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi niulize kilimo cha green house kina conserve mazingira lakini watu wa Kagera wanaolima kwa jembe wameambiwa walime mpaka mtoni hawaharibu mazingira. (Makofi)

Kilimo cha green house ambacho kinatumia water drip, ni maji kidogo sana, lakini matokeo yake ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi. Kutokana na muda mfupi, naomba nianze kwa kupongeza taarifa za Kamati zote mbili, tumefatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze waandishi wa habari kwa kazi ambazo wanaendelea kuzifanya. Waandishi wa habari kwa sasa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, hilo lazima tuseme. Wanafanya kazi katika mazingira ya kutishwa, vitisho vikali, lakini sisi tunaendelea kuwaeleza waendelee kupambana kwa ajili ya Taifa hili. Zipo nchi nyingi zimepata uhuru kutokana na waandishi wa habari kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawapa moyo na tunawaambia, ukweli utaendelea kuliweka huru Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia sana taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii. Waandishi wakiwa katika kundi hili, kuna mambo ambayo nimeona hata Kamati haikuwatendea haki. Katika taarifa nilitegemea kuona taarifa ya hali halisi za waandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza leo Mwandishi Azory Gwanda wa Mwananchi, ana siku ya 79 hajaonekana, hajulikani alipo. Gazeti la Mwananchi limekuwa likiandika kila siku mtu huyu yuko wapi na hatuoni juhudi zozote. Tulitegemea Kamati ingeelezea kuhusu wadau hawa muhimu kwenye tasnia hii, waandishi hawa ambao wamepotea, ambao wametekwa, taarifa zao ikiwemo ile ya kina Roma Mkatoliki ambapo Mheshimiwa Waziri alituahidi hapa kwamba ataleta taarifa kamili kwamba tukio lile lilitokeaje? Tulitegemea kuyaona hayo ndani ya Kamati hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba nizungumzie suala la press card. Nimesoma taarifa hii inaeleza kwamba waandishi 54 ndio wamepata press card na kati ya hao 14 ni waandishi wa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini waandishi? Sheria inawatambua waandishi, inatambua taaluma ya uandishi wa habari, wanashindwa kupata press card. Press card ni shilingi 50,000. Mwandishi wa habari shilingi 50,000 kwa mwaka; driving licence ni shilingi 40,000 kwa miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuhakikisha waandishi wa habari wanapata press cardkwa bei nafuu? Passport hizi ambazo tunatumia, ambazo zinakwenda kwisha muda wake, ni shilingi 50,000 ndani ya miaka 10, lakini mwandishi wa habari anakuwa na press card ambayo atalipa 50,000 ndani ya mwaka mmoja. Huu ni uonevu na tunasema, labda watuambie kama TRA imeahinisha press card ni moja ya vyanzo vya mapato, ndiyo tunaweza tukawaelewa. Vinginevyo kwa kuwa taaluma hii imeshafahamika, wapewe nafuu ili waweze kutambulika na wawe na vitambulisho vya kueleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu Habari Maelezo. Habari Maelezo imegeuka kuwa wahariri, wametoka kwenye majukumu yao ambayo yameelekezwa na sheria tuliyoipitisha, hivi sasa ndio wanaofanya editing kwenye vyombo vya habari. Hivi karibuni Habari Maelezo imeiandikia Gazeti la Tanzania Daima barua lijieleze ni kwa nini lina-cover story za Kinondoni za upande wa upinzani peke yake? Hiyo siyo kazi ya msingi ya Habari Maelezo. Kwa nini Habari Maelezo isiiandikie Gazeti la Uhuru kwa nini linaandika habari za CCM? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti binafsi yanaangalia story zinazouza, yanaangalia yaandike nini ambacho kitauzwa ili wafanye biashara. Kuwalazimisha kwamba waweke front page habari za CCM na wasipouza, mbona gazeti la Uhuru haliuzi? Lina nakala ngapi hivi sasa na linatembea wapi? Kwa hiyo, watu wanaangalia, watu wanataka nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Habari Maelezo kwenda kusimamia kuhakikisha Tanzania Daima inaandika habari za uchaguzi siyo; kwa sababu kwa mujibu sheria, wakati wa uchaguzi vyombo vya habari vinakua chini ya Tume. Ilikuwa ni jukumu la Tume kusema kwa nini chama hiki kinakosa fursa kwenye gazeti? Siyo kazi ya Habari Maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Habari Maelezo wafanye kazi zao na siyo kuhakikisha wanafuatilia magazeti mengine kwa maana kwamba inatupelekea kuona kama kuna maelekezo fulani ambayo hatuyaelewi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuyafungia magazeti. Magazeti yameendelea kufungiwa kila kukicha. Naomba kufahamu na Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha atueleze; anatoa wapi mamlaka hii ya kufungia magazeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Vyombo vya Habari tuliyoipitisha hivi karibuni, haijampa mamlaka Waziri kufuta magazeti. Haijampa mamlaka hayo na atueleze ni kwa kutumia Kanuni zipi na Kipengele kipi? Kwa sababu tulisema mwamuzi wa mwisho atakuwa ni mahakama. Mahakama itakuwa na room ya kusikiliza upande huu na upande huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo sheria baada ya kusainiwa, kanuni zipo tayari, walitakiwa kuandaa yale mabaraza matatu ambayo kazi yake ilikuwa ni kushughulika endapo kuna mwandishi amepotosha, kuna mtu ambaye amekwenda kinyume na maadili. Kwa nini Serikali inaona kigugumizi kuunda mabaraza haya ikiwemo Baraza la Ithibati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema unaadhibu gazeti kwa kulifungia, ni sawa na kusema kwamba eti unaifungia hospitali kutokana na daktari mmoja kuua mgonjwa. Huwezi kuifungia hospitali kwa sababu ya daktari mmoja; badala yake uta-deal na yule daktari. Ndivyo ilivyo kwa waandishi wa habari. Kama utalifungia gazeti, wapo wafagizi, wapo maafisa masoko, wapo watu ambao wao ni makarani na wahasibu; chain zaidi ya watu 300. Mtu mmoja kweli akoseshe watu 300 ajira? Haiingii akilini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja.

Mheshimiwa Spika, nimepitia vizuri kitabu cha hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nilitegemea ningeona mambo mengi humu; nilitegemea Waziri Mkuu angetueleza hali halisi ya siasa ya nchi hii kwa wakati huu.

Mheshimiwa Spika, kwa yale ambayo yanaendelea katika nchi hii, ukandamizaji wa demokrasia unaoendelea katika Taifa hili, kuendelea kunyimwa kwa vyama vya siasa kufanya haki yake ya msingi ya kufanya mikutano; tunaelewa, kazi ya chama chochote cha siasa katika Taifa hili ni kuendelea kutafuta wanachama wapya na kupima afya yake, lakini hivi sasa hali ya siasa iliyoko Tanzania haifananishwi na nchi yoyote ambayo iko katika nchi za Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, kwa nini nasema hali ya siasa si nzuri? Ni kwa sababu ya uonezi wa waziwazi na ukandamizaji wa waziwazi. Mfano mzuri tunaouzungumzia hapa ni baadhi ya viongozi wetu wa chama ambao waliwekwa mahabusu wakala Pasaka mahabusu, akiwemo Mwenyekiti wetu wa Kambi ya Upinzani ilhali Mahakama ya Kisutu ilishatoa dhamana, kwa kisingizio kwamba gari ya kupeleka mahabusu ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nje ya Mahakama ya Kisutu ukiangalia wakati tunapewa taarifa hizo zilikuwepo defender zaidi ya 30, magari ya washawasha yalikuwemo katika eneo la Kisutu. Unajiuliza, ni magari hayo hayo ya Polisi yameharibika, yameshindwa kuwaleta watuhumiwa Mahakamani, lakini magari hayo hayo yanazunguka Kisutu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike mahali tuseme ukweli kwamba Taifa hili tunataka kulipeleka wapi. Mwanzoni niliposikia kwamba upo mkakati kwamba tukiingia madarakani tutahakikisha tumeumaliza upinzani. Nilijua kuumaliza upinzani maana yake ni kufanyia kazi hoja za msingi za upinzani, ni kuhakikisha malalamiko ya upinzani wanayoyatoa dhidi ya wananchi kwa Serikali yanafanyiwa kazi, ndiyo namna ya kuiua upinzani, lakini namna ya kuua upinzani sio hivyo, ndiyo hivi tunavyoviona sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna matamko yanayoendelea. Mimi juzi nimemsikiliza Rais akiwa Arusha. Anawaambia Askari wa Jeshi la Polisi fanyeni mtakavyo, nipo nyuma yenu, nawa- support. Tunajua kazi ya Jeshi la Polisi na amewapongeza kwa jinsi walivyoshughulikia watu kwenye maandamano. Ukiangalia maadamano yale, watu walivyoumizwa wakiwa kama majambazi, watu wameishia kupigwa risasi, wengine wamekufa; sasa kauli za namna hii zinaipeleka wapi Taifa hili? Kwa maneno mepesi ni kwamba ukiwaambia unawa- support kwa maana hiyo waendelee na kazi hiyo ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza wachangiaji wa wiki iliyopita. Kuna mchangiaji mmoja alisema wapinzani wanalalamika, bilioni sita za uchaguzi it’s peanuts! Bilioni sita kwa nchi maskini kama hii ambayo inaishi chini ya dola moja; bilioni sita tunaona ni sawa kwenye uchaguzi?

Mheshimiwa Spika, nilishangaa kwa sababu unaposema hizi bilioni sita za uchaguzi unazungumzia zile za Tume. Hivi umehesabu gharama nyingine ambazo zinaendana na uchaguzi? Umehesabu nauli za wananchi ambao wanatoka maeneo hayo kwa siku 30 wanapanda daladala wanaenda kwenye uchaguzi? Umehesabu Wabunge ambao wanatoka maeneo yao wanaweka mafuta wanakwenda kwenye uchaguzi? Umehesabu gharama…

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, hivi bilioni sita, Mwananyama watu wanalala chini, bilioni sita ingefanya kazi yake, hiyo bilioni sita anayoiona ni ndogo. Bilioni sita hiyo anayoiona ni ndogo ingefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kule kwa Manjunju ambako maji yanafurika kila wakati zingesaidia kuleta plan watu wakae vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziko gharama nyingine zinazotokana na chaguzi hizi. Unapozungumzia hiyo bilioni sita peke yake hujaweka gharama nyingine, misafara mikubwa kuliko hata ya Waziri Mkuu ya Mkuu wa Mkoa, hujaweka misafara ya magari ya washawasha, hujaweka misafara yanayobeba mbwa kwa ajili ya chaguzi. Vile vile hujaweka gharama za watu waliokufa/waliopoteza maisha ambao wamezikwa kwa gharama za Serikali akiwemo yule binti Akwilina.

Mheshimiwa Spika, hujaweka gharama za Katibu wetu wa CHADEMA Hananasif ambaye naye alifariki, zile zote ni gharama. Kwa hiyo, tusiione bilioni sita tu tukaiona, tukifanya tathmini tunaweza tukaona in reality unaweza ukaogopa kuingia kwenye uchaguzi. Nafikiri kungekuwa kuna namna tu mtu akatoka huko, akaingia huku, tukaendelea! (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, naomba kwa ajili ya muda niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona Waheshimiwa Wabunge wamechangia sana kuhusu ununuzi wa ndege. Hakuna mtu ambaye anasema ununuzi wa ndege ni mbaya, lakini tunachokilalamikia na kukisema siku zote ni gharama za ununuzi wa ndege. Taifa kama hili kununua ndege tatu cash kwa hali ambayo tunayo.

Mheshimiwa Spika, mataifa yaliyoendelea yote hivi sasa yanaanza ku-withdraw kuingia kwenye biashara za ndege kwa sababu biashara ya ndege returns zake si za karibu hivyo. Ni hasara ku-run ndege. Sasa sisi kwa Taifa maskini kama hili tunaenda kununua kwa cash, tungejifunza hata kwa wenzetu Precision na Fastjet ndege zao wamenunuaje. Ukiangalia zote hizo watu wamenunua kwa mikopo, watu wananunua hisa.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ukiangalia hata huo unafuu wa ndege tunaoambiwa kwamba zimenunuliwa kwa kodi zetu, ukiangalia leo ATCL kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma unazungumzia karibu, lakini saba lakini ukipanda Fastjet kwenda Dar es Salaam – Mbeya na kurudi ni 230,000. Sasa unafuu uko wapi? Tunaweza tukasema kweli tunaunga mkono ununuzi wa ndege?

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, hivi ndege tulizonazo hizi zinatoka nje ya nchi? Hata hivyo, ningeweza nikaelewa kama tumenunua ndege ambayo inatoka hapa inakwenda Marekani, inaleta watalii, wanakuja moja kwa moja hapa. Hivi niulize hata hiyo ndege kutoka Canada mpaka kufika Tanzania ilichukua siku ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kuhusu suala la Serikali kujinasibu kwamba inakwenda kupambana na ufisadi.

Mheshimiwa Spika, pale Manispaa ya Morogoro iko barabara ambayo imejengwa kutoka Kichangani kwenda Tubuyu ina kilometa nne. Kilometa moja tu imejengwa kwa shilingi bilioni 3.4. Barabara hiyo haina mito, haina kona, haina makorongo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia dakika tano hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia watu wanasifu Wizara inafanya vizuri, lakini kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro hawawezi kuwasifia hata mara moja. Ni kwa nini nasema haya? Kuna barabara ya Tubuyu – Kichangani katika Manispaa ya Morogoro. Barabara ile ina kilometa nne tu imejengwa, kilometa moja imejengwa kwa shilingi bilioni 3.4; kilometa nne zimejengwa kwa shilingi bilioni 13.6. Barabara imenyooka kama chuma cha pua; barabara unaweka rula unanyoosha, haina milima, mabonde wala mito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao waliungana nami pamoja na baadhi ya Madiwani wa CCM. Mwaka 2017 nilisema na kwa bahati nzuri baada ya kuona kwamba hela hizi zimepigwa; tuliamua kwenda kwa wataalam wa TANROAD tukawaambia hebu tuambieni, sisi sio wataalam, tunataka kujua barabara hii kwa nini imejengwa kwa gharama hizi nyingi kiasi hiki? Nao wakawa wanashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatuambia kilometa moja standard yaani barabara concrete inajengwa kwa shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja tena kwenye maeneo ambayo ni korofi. Tukawaambia hapa zimetumika shilingi bilioni 13.6. Wakatuambia hatujawahi kuona, pengine ni kwenye barabara za ahera ndiyo zinaweza kuwa na gharama kubwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaanza kupambana ndani ya Halmashauri yetu, tukajaribu kuuliza matumizi ya fedha hizi. Ikumbukwe fedha hizi ni mkopo wa World Bank ambao uliletwa kwenye nadhani Halmashauri kadhaa kama saba hivi na Halmashauri ya Morogoro ikiwemo, ambazo tunategemea kwamba Watanzania watakuja kuzilipa kwa jasho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuja na hoja hiyo Halmashauri, viongozi wa Halmashauri wakaanza kutembeza rushwa kwa Madiwani na Madiwani wakasema hawakubaliani na hali hii, wakaandika barua kwa Mkuu wa Mkoa kuthibitisha wamepewa rushwa ili wanyamaze kwenye jambo hili. Nakala wakapeleka kwa DSO na RCO wakasema sisi hatupo tayari, tupo tayari kuhakikisha kwamba tunataka kujua hatma ya fedha hizi. Ukimya mpaka leo, hakuna kilichoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, tukaja Bungeni, nikazungumza, nikamwomba Mheshimiwa Jafo wakati huo akiwa Naibu Waziri. Akaenda Morogoro akaiona barabara ile, akaunda Tume. Hata Tume aliyoiunda mwaka 2017 mpaka sasa hivi hakuna kitu ambacho kimefanyika mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Jafo alikuja ameunda Tume akashangaa barabara kutumia fedha nyingi kiasi hiki, lakini mpaka sasa amekuwa Waziri ni kimya.

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema baadhi ya Madiwani na ambao walikwenda TAKUKURU kutoa ushahidi kabisa kwamba wamepewa ili wanyamaze.

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa. Watu wamefanya Mkoa wa Morogoro ni shamba la bibi, ni lazima tuseme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukawa tunavizia tukutane kwenye Kikao cha RCC tuweze ku-raise hoja zetu kuhusu barabara hizi, lakini tumepigwa ile inaitwa nini?

Chenga ya mwili. Mkoa wa Morogoro haukufanya kikao cha TANROAD wala hatukufanya kikao cha RCC. Tumekuja Bungeni tunakutana na vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa anakwepa kujibu hoja hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipeleka wapi Taifa hili?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Kivuli, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miezi mitano jela, tunampa pole kwa anayopitia. Kambi ya Upinzani ikiungana na Watanzania ambao wanalitakia mema Taifa hili, wanaungana naye na wanasema kwamba yampasa apitie hayo anayopitia ili aweze kupata ukombozi kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza sana maoni ya Kamati ya Wizara hii ambayo inasema kwamba inashangazwa, tangu kuundwa kwa Sheria hii ya Huduma za Vyombo vya Habari, ni kwa nini mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri anaona kigugumizi kutunga kanuni? Ili sheria iweze kufanya kazi yake vizuri ni lazima iwe na kanuni ambazo zitaongoza sheria ile iweze kufanya kazi. Matokeo yake hivi sasa kinachoendelea, Mheshimiwa Waziri anachokifanya sasa hivi ni kufungia magazeti kazi ambayo siyo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anafungia magazeti kwa kusema ni kosa la uchochezi. Tunaelewa kosa la uchochezi ni kosa la jinai na Mahakama pekee ndiyo ya kutoa hukumu hiyo. Tuliomba kanuni hizi ziundwe ili kuwe na yale mabaraza likiwemo la ithibati ambalo ndilo litakuwa na room ya kuzungumza na Mwandishi na kutoa adhabu inayostahili kulingana na alichokifanya. Siyo kama hivi sasa Mheshimiwa Waziri akilala, anaamka asubuhi ni kufungia gazeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha na wakati mwingine kunakuwa na double standard. Yale magazeti ambayo yanaandika habari mbaya za kupiga Upinzani, za kutukana viongozi wa Upinzani likiwemo Gazeti la Tanzanite, Mheshimiwa Waziri sijui halioni? Ikifika kwenye magazeti kama hayo, anavaa miwani ya mbao, lakini ikifika Tanzania Daima anavaa miwani yake ya kawaida na anayafungia magazeti. Tunasikitika sana kama kunakuwa na double standard katika matukio haya na tunataka atupe majibu ni kwa nini kanuni hazitengenezwi mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakumbukwa tuliambiwa hapa Bunge Live halitakiwi kwa sababu kutakuwa na msongamano wa waandishi na nini, hawataweza kufanya kazi yao vizuri, tukaambiwa mwarobaini itakuja Bunge TV na itakuwa na uwezo wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata habari, tukakubaliana na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, toka hiyo Bunge TV ianze mpaka sasa outreach yake ni wapi? Kwa sababu hata pale barabarani haifiki. Yaani hii Bunge TV inakuwa kama kioo cha ndani, tunakaa hapa ndani tunajitazama tukitoka nje hatuwezi kujiona. Hivi kwa nini hii Bunge TV isiunganishwe ikaingia mpaka kwenye ving’amuzi Watanzania wakaona kinachoendelea ndani ya Bunge lako? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni issue ya bajeti, tulitegemea hata Mheshimiwa Waziri angeizungumzia sasa hii Bunge TV iweze kupewa, ifanye kazi yake vizuri, iweze kufikisha habari kwa Watanzania. Kwa sababu walitupa mifano, wakatuambia angalia hata South Africa kuna channel ya Bunge. Ni sawa hatujakataa, lakini tunataka tuione kwenye frequency, watu wenye ving’amuzi waione. Hata ikiwezekana wale wenye TV za local wawe na uwezo wa ku-access, wakati mwingine wa-relay kwenye Bunge TV wawaoneshe Watanzania kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu waandishi kukosa access, pamoja na hii Bunge TV kuwepo. Tunaelewa kwamba lipo Kikanuni, Mbunge anapozungumza hapa yapaswa kila kitu kiingie kwenye Hansard, lakini Mbunge akiongea jambo ambalo lina ukakasi kwa Serikali linakuwa- edited.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri, ni vigezo vipi vinavyotumika? Kwa sababu ukienda kwenye written Hansard utakuta kila kitu kinaandikwa vizuri kabisa, lakini kile ambacho kinachukuliwa hapa kinarekodiwa, wanapewa waandishi huko, hawana access na baadhi ya information zinakatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi upo Mheshimiwa Waziri akitaka nitamwonesha.

TAARIFA . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mwandishi professional, siwezi kumjibu, naendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kuhusu suala la usajili wa magazeti. Wote tunaelewa usajili ni kitu ambacho ni permanent. Usajili wa magazeti hivi sasa kuna sheria eti kila mwaka magazeti lazima yasajiliwe, tumewahi kuona wapi? Katiba yetu Ibara ya 18 inasema, ni haki na ni uhuru kwamba kila mwananchi ana uwezo wa ku-access information. Sasa wanapokuja na vigezo kwamba kila gazeti, kila mwaka lisajiliwe upya tunaomba watuambie, hivi Serikali wakati inapitisha bajeti zake, TRA ilionesha kwamba moja ya vyanzo vyake ni usajili wa magazeti? Ina maana hapa kuna ukiukwaji wa Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua usajili ni permanent na hii tunajua ni makusudi tu. Yale magazeti ambayo hayataandika mapambio ya kuitukuza na kuisifu Serikali hii ya CCM baada ya mwaka yatafungiwa, hayatapewa usajili. Hali hii inasababisha wamiliki wa vyombo vya habari kuwa na uwoga. Watu ambao wanataka hata kuingia kwenye biashara hii ya vyombo vya habari, wanashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuhoji, hii wamei- copy wapi? Nimejaribu kufuatilia nchi za Afrika Mashariki, nimeona ni Rwanda pekee yenye element ya namna hiyo, kwamba kila mwaka wanasajili magazeti. Ni kwa nini tunachukua utaratibu ambao siyo utamaduni wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata blogs nazo eti zinaambiwa zinatakiwa zisajiliwe na zilipe, tena kwa hela nyingi; kati ya laki moja mpaka laki mbili. Mtu kafungua blog yake ambayo anategemea Watanzania watapata taarifa, lakini shilingi 200,000/= anaipata wapi? Haya ni masharti ambayo wanawawekea watu, wananchi watakwenda kuumia kwa sababu hawatakuwa na access ya kupata information.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA tulitegemea wangesaidia kusimamia sheria iliyopo ya kuhakikisha habari zinawafikia Watanzania, lakini TCRA imekuwa kama ni barrier sasa. Yaani kitu kidogo TCRA tayari ni kupiga faini magazeti, ni kupiga faini TV, ni kupiga faini redio, hali ambayo wakiangalia, na wao wana takwimu, waangalie tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano, ni watu wangapi wameingia kwenye ku-invest kwenye media?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna kasi kubwa sana ya watu ku-invest kwenye media katika kipindi cha Awamu ya Nne, lakini siyo sasa hivi. Ni kwa nini? Masharti magumu, lakini tunajua behind ni kuangalia vile vyombo ambavyo haviimbi mapambio, ndiyo vipewe fursa ya kuhakikisha kwamba vinaendelea kufanya kazi, vile vinavyokosoa Serikali kuhakikisha kwamba havipati fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo tunajiuliza, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake. Katika hotuba yake tulitegemea angetuambia ni nini kinachoendelea katika matukio haya ya Waandishi wa Habari kupotea, kutekwa, kunyanyaswa na waandishi wa habari wamekuwa kama vifaranga vya kuku ambavyo havina mchungaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, hata mwezi haujapita, Mwandishi wa Gazeti la The Guardian alitekwa, alipigwa, alinyanyaswa, lakini hata Mheshimiwa Waziri hana habari. Hawa ndiyo watu wake ambao anafanya nao kazi. Kwa nini hawasemei Waandishi? Serikali kwa nini haitoi matamko kuhusu matukio ambayo Waandishi wa Habari wanafanyiwa, ikiwemo Azory ambaye sasa hivi amepotea ni miezi mingi mpaka sasa hatujasikia hata tamko la Serikali. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri akizungumza habari za sanaa, za nini, lakini kuzungumza habari za Azory ambaye amepotea sijawahi kumsikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahoji haya matukio ambayo Waandishi wa Habari wamekuwa wakiyaripoti, Serikali inaendelea kukaa kimya. Tunashuhudia watu wanapigwa risasi mchana kweupe, media zinaripoti, lakini hakuna kinachoendelea. Tunashuhudia watu wanatolewa bastola, Waandishi wa Habari wamepiga picha zinaonekana kabisa, mpaka sasa hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maiti zinaokotwa tunaoneshwa kwenye media, kwenye kila namna ya magazeti, lakini hakuna chochote kinachoendelea. Sasa ifike mahali Mheshimiwa Waziri, Wizara yake itambue mchango mkubwa wa kazi ya Wanahabari ambao wana kazi ya kulielimisha Taifa hili, kazi ya kutoa taarifa za Taifa hili ili Serikali iweze kufanyia kazi na kutoa matamko ya mambo yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuhusu suala…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niungane na Watanzania wapenda mema, watakia mema Taifa hili, kumpongeza Waziri wangu kivuli Mheshimiwa Joseph Mbilinyi kwa kumaliza kifungo chake, lakini tunamwambia kwamba alipaswa kupitia hayo ili kuleta ukombozi katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu Mwalimu Nyerere aliamua kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ni wa viwanda. Tukiacha Mkoa wa Dar es Salaam mkoa wa pili kuwa na viwanda vingi ilikuwa ni Mkoa wa Morogoro. Na kuanzia miaka ya 1960, 1970 kuendelea mpaka ya 1980 kwa Mkoa wa Morogoro huwezi kumkuta house girl kutoka Morogoro anaenda kufanya kazi, huwezi kuwakuta vijana wamekaa vijiweni, huwezi kuwakuta hata wazee wanakunywa kahawa vijiweni kwa kuwa watu wote walikuwa na fursa ya kuingia kwenye viwanda, kufanya kazi kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali lengo la kubinafsisha viwanda ni kuongeza efficiency, lakini cha kushangaza, kwa makusudi mazima watu wale waliihakikisha Serikali kwamba watavichukua viwanda, wataviendeleza na kuhakikisha ajira inaendelea kuongezeka na kuongeza. Sasa badala ya ku-expand viwanda, kuongeza ajira watu wamevitumia viwanda kama collateral kwenye kukopa na kufanya biashara zao zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo viwanda vya Morogoro vimekufa kwenye mikono ya watu, watu wamekosa ajira na tunategemea na Waziri wakati anahitimisha atuambie, Serikali imechukua hatua gani kwa watu hao ambao wameua viwanda kwa makusudi kabisa. Serikali imechukua hatua gani kwa watu hao ambao wamewanyima Watanzania ajira? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na ninaamini Waziri amemsikia vizuri Mheshimiwa Kuchauka alichokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tegemea Waziri na hitimisha atuambia hivi Morogoro tunahitaji viwanda vingine vipya, kama anavyosema ama tunahitaji kwanza tufufue vilivyoko? Kwa sababu rasilimali ya viwanda tayari tunavyo. Lakini sasa hivi vimekaa tu kwa hiyo tunataka kuona mpango wa Serikali katika kuhakikisha wanafufua viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumza kuhusu viwanda ambavyo vilikuwa vikitengeneza malighafi, nimemsikia Waziri pale wakati anawasilisha, katuonesha na viatu ambavyo vimetengenezwa, hivi Mheshimiwa Waziri nikuulize, ngozi zinaharibikia Morogoro hatuwezi kuzitumia unatuonesha viatu, tunashindwa ku-export ngozi pale Morogoro, nilikuwa nauliza lengo lilikuwa ni nini kama kweli tuna ngozi ambazo tunashindwa kuzitumia, unatuonesha sample ya viatu vichache. Ungetupa mikakati ni nini Serikali imejipanga kufanya kuhakikisha hata Viwanda vya Ngozi vilivyopo Morogoro ambavyo vimesheheni ngozi ambazo wanashindwa kuziuza mpango wako ni nini vitengenezwe viatu kama ulivyotuonesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda cha Mbigiri, tumesikia Serikali inataka kuanzisha Kiwanda cha Sukari. Lakini fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo hilo ni kilio mpaka sasa hivi. Kwa kweli watu ambao waliendeleza maeneo haya ambayo yaliachwa na Serikali miaka mingi wanakuja kuambulia patupu, halafu mnawaambia eti mtawafundisha kuwa ni out growers ambao hawana maeneo, hii si sahihi kabisa. Na nishukuru nilimuona Mheshimiwa Waziri anajaribu hata kulima kule anawaonesha jinsi ya kulima, lakini watalima wapi Mheshimiwa Jenista? Maeneo mengi yamechukuliwa, hawana pa kulima mnategemea out growers watatoka wapi Mbigiri? Kwa hiyo, Serikali inapojipanga ione namna gani yakuwasaidia na wananchi ambao wanazunguka maeneo ya viwanda ambavyo mnataka kufanya kazi ili wale watu waweze ku-support viwanda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia Serikali ikisema ina mpango wa kuweka viwanda 100 kwa kila Mkoa. Hivi najiuliza, hivi viwanda tunavyovizungumzia ni vipi? Ni viwanda plant, tunazungumzia viwanda vidogo au tunazungumzia viwanda vya aina gani? Kwa sababu hivi sasa kuna viwanda vikubwa Dar es Saalam ili kifanye production ni lazima umeme ukatike Dar es Salaam nzima. Sasa tunataka kupeleka viwanda vya namna gani kama hatua umeme wa uhakika, hatua barabara zinazoeleweka, hatuna maji ya kutosha, hivi ni viwanda gani mia tunapeleka katika Mikoa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anaelewa kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo wawekezaji wanaombwa leo mzalishe usiku ili Watanzania wengine wapate umeme. Kwa sababu wakizalisha umeme wote unaotumika mkubwa unalazimika kuingia kwenye kiwanda. Kwa hiyo, mimi nafikiria kabla ya kuja na idea ya viwanda hakikisheni tuna umeme wa kutosheleza, hakikisheni zipo barabara za kutosheleza zitakazokwenda vijijini kuchukua mazao. Lakini zaidi barabara pamoja na kuhakisha maji yanatosha katika hivi viwanda. Tunaelewa hivi viwanda vinahitaji maji ya kutosha. Kwa hiyo, idea ya kusema tu viwanda, viwanda tunaona hii ni kama tu kuwadanganya Watanzania Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huwezi kwenda kwenye viwanda huna mipango sahihi ambayo tukitizama tunaona kweli tunaelekea kwenye viwanda. Unless utuambie twende kwenye viwanda vya vyerehani, vyerehani havihitaji maji, vingine hata havihitaji umeme tutakuelewa. Lakini plant tunazozitaka sisi ziende sambamba na miundombinu ya kuwezesha viwanda hivi viendelee kutoa ajira kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kupata fursa hii niweze kuchangia bajeti kuu. Wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti hii, nilikuwa najaribu kumwangalia sana hata usoni kwamba anachozungumza na kilichomo ndani ya moyo wake kinaonekana ni tofauti kabisa. Nina wasiwasi sana kama Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha haya hivi anakwenda field au anatuletea tu taarifa hapa ambazo hajui hali halisi ya uchumi wa nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri anatuletea taarifa ambayo Deni la Taifa ni shilingi trilioni 46, sisi tunakusanya shilingi trilioni 32, hawa watu wanaotudai wakicharuka, kitakachofanyika ni kwamba nchi itauzwa na sisi tutauzwa. Kwa maana hiyo, sioni realistic ya bajeti yake hapa. Tulitegemea kwamba angekuja na mipango ambayo inatuonesha ni jinsi gani tunakwenda kupunguza hilo deni na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati bajeti inawasilishwa tulikuwa tuki-observe pia nchi nyingine zinavyowasilisha bajeti zake. Ukiangalia Kenya, Uganda, Mawaziri wako serious wanaonesha ni jinsi gani wamejipanga kuhakikisha bajeti wanayokwenda kuiwasilisha inakuwa na impact kwa wananchi wao. Ukija ukiangalia kwetu huku, bajeti siasa, Waziri ashukuru na wananchi wake na majirani zake wa Zuzu na kadhalika. Hakuna mwaka ambao bajeti imekosa mvuto kama huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata waliokuwa wanafuatilia kwenye televisheni, wananchi unawauliza hivi kwa nini hamfuatilii bajeti? Wananchi wanasema aah, ni business as usual, hakuna jipya, maisha ni magumu. Hawana hata muda watu wa kutoka maofisini wakakae waangalie bajeti ya Serikali inasemaje, kwa sababu hawategemei kuongezewa hata senti tano ya mshahara. Kwa hiyo, lazima tujiulize ni kwa nini wananchi hawako na sisi wakati tunawasilisha vitu muhimu vya Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba pato la Taifa limepanda. Hivi, kweli limepanda kwa watu gani? Mheshimiwa Waziri aende field aone kwa macho yake mawili, pato la Taifa limepanda unapita kila nyumba unakuta imeandikwa inauzwa kwa mnada wa benki fulani? Pato gani hili ambalo limepanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapita huko mtaani, maduka yamefungwa, pato la Taifa limepanda! Mheshimiwa Waziri atuambie, pato la Taifa limepanda, benki zinashusha riba! Namwambia hata zikifikisha asilimia mbili, Watanzania hawana nguvu ya kukopa. Kwa nini? Biashara hazifanyiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata mabenki yakazane kushusha riba, kama huu uchumi haujarekebishwa, bado namna ya wananchi kurudisha fedha hizo hawana, wataendelea ku-default na ndiyo maana wanaogopa. Ndicho kilichobaki kwa mabenki sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pato la Taifa limepanda, sasa hivi mpaka Benki za Serikali zenyewe zinashindwa kufanya kazi. Twiga Bankcorp juzi wame-merge na Postal Bank, haina mtaji, imefilisika. Benki ya Wanawake hivi sasa inachechemea, hata kulipa mishahara haiwezi. Pato la Taifa limepanda! (Makofi)

Mheshimimiwa Mwenyekiti, tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie, hivi hili pato la Taifa kupanda, kuna impact gani kwa mwananchi wa kawaida? Tuwe na huruma na hawa wananchi ambao wanakamuliwa, sisi tunapata kulipwa mishahara, kama kweli hatuwezi kuwasemea na kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia wananchi hawa wakanyanyuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri anasema, katika mipango yake, kwenye bajeti hii TRA wakakusanye shilingi trilioni 20. Hivi, shilingi trilioni 20 zinakwenda kupatikana kwa namna gani? Nimeangalia kama kuna vyanzo vipya ambavyo wame-identify, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo ni vile vile, watu ni wale wale; hii tunakwenda kuwakamua wananchi mpaka jasho la damu. Kwa sababu ukiangalia TRA sasa hivi; namwona Kamishna wa TRA anazunguka kama pia; yuko Dodoma, wapi na wapi, eti anaenda kuvizia na yeye watu gani wamenunua bidhaa bila risiti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Kuna shida somewhere. Hakuna hela! Kwa hiyo, anatoka ofisini hakukaliki, anakwenda mikoani naye anakaa vichochoroni kama hawa junior officers wanavizia wananchi ambao ni wateja wametoka kununua bidhaa. Haiwezekani! Lazima wafike mahali waone hili kwamba hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika watu wanao-frustrate wafanyabiashara ni pamoja na TRA.Hivi siku wafanyabiashara wakiamua sasa hawafanyi tena biashara, wanauza kunde kwa sababu hazina kodi; hivi watapata wapi mapato? Ndipo wanakoelekea hivi sasa, kwa sababu TRA sasa hivi wanazunguka na mifuko ya sulphate imejaa makufuli kwamba wakikukuta na kikosa kidogo wanafunga kwa sababu wamepewa majukumu kuhakikisha wanakusanya. Kwa hiyo, wafanyeje? Wanatumia nguvu! Kwa hiyo, wanakomoa ili kuhakikisha kwamba makusanyo yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna tena kuelimisha wafanyabiashara kuhusu TRA. Mfano mzuri, wengine nasi ni wafanyabiashara, tunajua. Maofisa wa TRA wanakuja kwenye biashara yako, asubuhi wanakwambia print Z Report na Waziri anaelewa, Z Report inatolewa baada ya mtu kuwa amemaliza mauzo yake, anafunga siku. Sasa wewe saa mbili unataka Z Report. Kwa maana hiyo unaua system nzima ya makusanyo. Halafu wanafungua draw wanaangalia una shilingi ngapi? Wana compare na Z Report. Hivi tunapeleka wapi wafanyabiashara hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaelewa mfumo wetu wa kutoa risiti za EFD machine uko slow. Imefika mahali TRA mpaka wanapandikiza watu. Wanawaleta purposively ili kuhakikisha kwamba akishanunua bidhaa, kwa sababu mfumo wetu siyo kama petrol station kwamba ukijaziwa mafuta inatoka, hapana, lazima utumie mikono, dakika tano wakati mwingine system iko down, uweze kupata risiti. Wanachokifanya, anachukua bidhaa anaondoka, wanakuja Maofisa wanakwambia hujatoa risiti. Kwa hiyo, huu ni uonezi wa hali ya juu. Kama kweli Serikali imeamua kukusanya mapato siyo kwa kuwaonea wafanyabiashara kwa kiwango hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la importation na exportation, nimesikia eti wanataka ku-discourage importation ili kulinda viwanda. Viwanda vipi? Leo tunasema kwamba mafuta, mtu anakaa kwenye gari hawazi, anasema, kuanzia leo hakuna kuingiza mafuta nchini. Uzalishaji wetu wa mafuta ya kula ni asilimia 30. Asilimia 70 tunaipata wapi? Tunategemea watoe kauli hizo wakati wameshapandisha uzalishaji kwa asilimia 100, ndiyo watuwekee hizo restrictions kwamba mafuta yasiingie nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la importation na exportation ni la kimahusiano zaidi kwa Mataifa na Taifa. Hivi leo tunaweka restriction, bidhaa zetu huko nje zinakoenda, zisipopokelewa inakuwaje? Kwa maana hiyo kama mtu anaamua kwamba sasa hakuna kuingiza mafuta kutoka asilimia 25 wamepandisha mpaka 35 mafuta hakuna, nchi ina uwezo asilimia 30, hivi wanataka kuwarudisha wananchi kula chakula bila mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza, hivi traffic kwenye makusanyo, wako upande upi? Kwa sababu traffic speed waliyonayo wanawazidi hata TRA. Hizi tochi zilikuja kwa lengo la kupunguza ajali au kuongeza mapato, watuambie! Kwa sababu tangu tochi zimekuja, nashangaa unawasikia ma-RTO wanaeleza tumekusanya kiasi hiki, si kutuambia ajali zimepungua kwa kiasi hiki, wanatuambia tumekusanya kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi lengo la tochi watuambie kumbe siyo kupunguza ajali ni kukusanya! Labda ni indirect way ya kukusanya, atueleze Mheshimiwa Waziri. Maana inafika mahali sasa Traffic wanapanda juu ya miti, wanatokea porini, ni fine. Imefika mahali madereva wanasema; ah, mimi sasa nalazimika ninunue tochi. Maana ya kununua tochi ni nini? Unaweka pesa mfukoni, kila unapokutana nao Sh.30,000/= unatoa unaendelea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika,nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nimepitia vizuri kitabu hiki cha Waziri Mkuu hasa katika ukurasa wa tisa ambapo amezungumzia mafanikio ya miradi ambayo imefnywa na Serikali hii ya Awamu ya Tano. Moja ya mafanikio aliyoyazungumza ni kuhusu ujenzi wa Standard Gaugeunaoendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatupingani kabisa na mradi huu, tunachokizungumza ni kuhusuproper planning za mradi huu. Ili nchi yoyote iendelee lazima iwe na mikakati endelevu, nchi za uarabuni ambazo zina mafuta, ukiwauliza hata kesho yao baada ya mafuta kwisha, wanafahamu. Kwa sababu wanaingia gharama ku-implement teknolojia ambazo zinabaki kwa wazawa.

Mheshimiwa Naibu Spika,leotunafanya Standard Gauge, asilimia 20 ya labour skills ni Watanzania, asilimia 80 ni Waturuki. Tunasema kwamba mradi huu unatoa ajira kwa Watanzania kwa kiwango kikubwa, labda watuambie Watanzania wataishia kufanya zile kazi ndogondogo za mamantilie na zinginezo, asilimia 80 ya teknolojia kubwa zinafanywa na Waturuki. Kwa hiyo, tunachosema sisi, tuwe na miradi ambayo ina proper planning, tuandae watu wetu kwanza kuingia katika hiyo teknolojia, tupate watu professionals ambao sasa kwa asilimia 90 watakuwa…

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA):Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Devotha Minja kuna taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifadada yangu Mheshimiwa Devotha Minja kwamba, akizungumzia mambo ya ajira wakati wa ujenzi wa SGR, ni very short term yaani kama kuzungumza leo na wakati ule mradi ni wa miaka nenda rudi. Kwa hiyo, azungumzie labda impact ambayo nchi itapata kupitia mradi huu, badala ya kuzungumzia vitu vya leo wakati ule ni mradi wa muda mrefu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Devotha Minja unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ana muda baadaye anaweza akajibu kama Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokisema, tulitegemea, neema ambayo aliisema Rais, kwamba ajira zitabaki kwaWatanzania, asilimia zaidi ya 90 kazi hizi zifanywe na Watanzania, lakini sasa zinafanywa asilimia 20 ambao ni Watanzania. Hoja yangu ni kwamba, tulitakiwa tujiandae kabla ya kuingia kwenye mradi huu, kwa maana kuwaandaa watu ambao wana uwezo wa kufanya hizi kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la mataruma, mataruma hivi sasa ya reli yanatoka China. Hivi tulikuwa na sababu gani ya kukimbiliakuanza mradi huu, badala ya kufufua miradi ya Mchuchuma na Liganga, tukapata mataruma, yakatusaidia, tukaweza kupunguza gharama ya fedha nyingi ambayo sasa hivi inakwenda China badala ya kubaki hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza miradi hii, inaleta maswali kwa wananchi. SGR, unazungumzia bilioni 16, kwa wananchi wa kawaida tu, ukiwauliza kipaumbele ni nini sasa hivi watakwambia tunataka huduma za afya, ni suala la kisera kwamba, kila kata iwe na kituo cha afya. Katika vituo vya afyakata 4,420, kuna vituo vya afya 513 na katika hivyo 513, vituo 115 ni vya private.

Kwa hiyo, kwa mwananchi wa kawaida ukimwambia unapeleka bilioni 16 kwenye SGR, ambapo hana huduma yoyote ya afya, wananchi wa kawaida hawatuelewi.

Mheshimiwa Naibu Spika,tunasema yote ni mipango, lakini lazima tuangalie basic needs kwa wananchi. Kuna maeneo hivi sasa yanapata maji kwa asilimia tatu, lakini ukimwambia mtu habari za SGR hakuelewi, anataka maji, anataka huduma zaafya. Kwa hiyo, tunasema niproper planning Tanzania kuangalia priorities za nchi na kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika,Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuhusu mradi wa kufua umeme wa Stiegler’sambao utagharimu takriban trioni 6.5. Tulikuwa na mradi wa Kidunda, ambao ulikuwa una uwezo wa kuzalishamegawatts 20 za umeme, ulikuwa na uwezo wa kuzalisha maji yatakayotumika kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa ajili ya viwanda, kwa ajili ya mashamba ya umwagiliaji, lakini hivi sasa tumeacha huku, tunakimbilia kwenye Stiegler’s. Kwa hiyo, ni wakati ambao tunataka kusema ni kwanini Serikali inakuwa na miradi mingi halafu implementation yake, mingine inaachwa, mingine inapewa kipaumbele!

Mheshimiwa Naibu Spika,kama suala ni umeme, tungeanza na Kidunda, watu walishalipwa fidia, ndipo twende kwenye Stiegler’s, tuangalie kwamba tuna upungufu wa umeme kiasi gani, ndipo tungeanza mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo tukijiuliza, umeme wa maji siyo reliable siku hizi, kwa nchi nyingi sasa hivi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Tungeweza tukafikiria zaidi hata kuwa na umeme, sisi tuko chini ya equator, kuwa na umeme wa jua, umeme wa upepo na kadhalika, badala ya hivi sasa nguvu zote, Kidunda wananchi wamelipwa, wameachwa kama walivyo, sasa hivi nguvu za Serikali zinaenda kwenye Stiegler’s.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Waziri Mkuu pia amesema suala la ununuzi wa ndege. Ndege nneBombardierzimegharimu zaidi ya bilioni 280, lakini hivi karibuni tumeambiwa, maintenance ya ndege hizi zimetumika zaidi ya bilioni 14, hivi tunatengeneza faida? Hivi ni biashara kwenye ndege! Airbus moja ambayo ni takribani bilioni 200 iliyokuja juzi, tunajiuliza iko wapi! Tuliambiwa italeta watalii kutoka Marekani, kutoka Uingereza kutoka wapi, hivikwa nini hatuioni ikifanya shughuli hizo, kwa nini hatuioni sasa hivi ikifanya shughuli hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri atakapokuja kujibu atueleze iko wapi hiyo ndege. Kwa sababu ukisoma kwenye mitandao unaambiwa mara imeuzwa Kenya, mara iko kwenye matengenezo, mara iko garage, mara inapakwa rangi. Ndege iliyokuja juzi, shughuli zote za nchi zikasimama kwa sababu ya ndege moja, ambayo imekuja nchini. Leo hatuelewi kwamba huo uzalishaji wa ndege hii mpaka sasa umeingiza faida kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo taarifakwenye mitandao, mara inaonekana inabeba nyama kutoka Mwanza, tunataka tuambiwe, kwa sababu zimenunuliwa na kodi za Watanzania, ziko wapi ndege hizi za kuleta watalii ziinue utalii wa nchi hii, inafanyakazi gani hivi sasa?Ndiyo ugomvi wetu, tunahitaji fedha za Serikali zitumike vizuri, badala ya kuleta ndege miezi mitatu toka Januari, ime- ground, badala ya kwenda huko nje, ikafanya yale ambayo Serikali imesema, matokeo yake tunayasikia tu ya mitandao yanayoendelea. Kwa hiyo, watu wanataka kufahamu specificni kitu gani kinaendelea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Devotha Minja, unapokea taarifa hiyo.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ana muda wa kutosha kuja kujibu. Nilitegemea angeniambia airbus iko wapi sasa hivi ambayo Watanzania wanataka kujua. Sheria za kimataifa zinasema ili uende nchi kama Amsterdam na kwingineko kwenye mataifa yaliyoendelea lazima uwe na ndege tatu, kwa maana ya mbili ziwe angani na moja iwe reserved. Sasa ya kwetu tutaiweka reserved tukisubiri zingine zije ndipo zianze kuruka, tunasema ni kuilaza pesa chini. Nafikiri atakuwa na muda mzuri wa kunieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye hali ya kisiasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, kengele ya pili imeshagonga nilikuwa nampa dakika yake moja ili aweze kumalizia sentensi. Kwa hiyo, naomba tumruhusu amalizie sentensi yake, Mheshimiwa Devotha Minja dakika moja.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Watanzania wanataka kujua kuhusu ndege yao kubwa iliyokuja ambayo ilifanya shughuli zote nchi nzima zikasimama, watu wakaenda kuipokea mpaka kwenye runway wamekaa wanashangilia, iko wapi ndege hiyo, inafanya nini, imeingiza nini toka imeingia hapa nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilimsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake, alisema kwamba kwa sasa tuna magazeti 216 na redio 163. Hoja si wingi wa kuwa na media nyingi. Hoja, media hizi zinafanya kazi kwa uhuru au ndiyo zile ambazo Waziri akiamuka asubuhi anafungia kwa sababu tu hazijaandika habari nzuri za kumpendeza mwenye nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Habari Maelezo hivi sasa imegeuka kama ni kitanzi kwa Waandishi wa Habari. Kazi kubwa ya habari maelezo sasa hivi, ukienda katika News Media zote, utakuta kuna mafaili ya maonyo ya kuwaambia kwa nini wasifutiwe, ya kujieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, habari maelezo badala ya kuwaelekeza vyombo vya habari vifanye nini, Wahariri wafanye nini, sasa hivi imegeuka kama kitanzi kwa ajili ya kuhakikisha inafungia magazeti yoyoteyale ambayo hayaandiki habari nzuri ambazo zinaipendeza Serikali, badala yake yanahangaika na magazeti ambayo yanaandika habari za kuikosoa Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, CAG alizungumza na Media, kama haitoshi, Mwenyekiti ACT naye akaitisha media kwa lengo la kuchambua taarifa ya CAG, Dkt. Abasi, anawaandikia wahariri ambao waliandika habari ambazo ni za uchambuzi zilizofanywa na chama cha ACT. Haki iko wapi, CAG ambaye ndiye aliyekuwa chanzo cha taarifa hizo, asichukuliwe hatua, lakini kwa sababu Zitto ametoa ufafanunzi na waandishi wameandika, basi vyombo hivyo havina mamlaka, vinataka kufungiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuendesha nchi kwa nama hii. Maana yake ni nini, kwamba sasa hata vyama vya upinzani, visifanye press, maana yake ni hiyo kwa sababu kama umepewa onyo usifanye press za upinzani, maana yake ni kwamba tunataka kuvinyima uhuru vyombo vya habari vifanye kazi za kuchagua, zifanye kazi za Serikali tu peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kulikuwa kuna defamation yoyote, ilipaswa, kabisa, angewajibika Zitto na si vyombo vya habari! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya muda, suala la Bunge Live, tuliambiwa Bunge Live hatuonyeshi kwa sababu wananchi wako busy kufanya kazi. Sasa hivi Rais anafanya ziara, ziko live, je, hao wananchi sasa hivi hawafanyi kazi! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoyazungumza haya, tunataka kuangalia upande mwingine wa shilingi, lakini kama haitoshi, hata hapa Bungeni tulipo, tukichangia chochote hapa, kinakatwa! Wakati mwingine clips za Wabunge hazitolewi kwa wandishi, kwa nini? Tunaogopa nini! Hili Bunge ni huru tumekuja kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi, taarifa zinazoandikwa kwa maandishi hazikatwi, lakini ikifika kwenye jambo ambalo tunaikosoa Serikali, clip haitaonekana! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna haja gani ya kuendelea kuwa na Bunge ambalo, tuna haja gani ya kuendelea kuwa na waandishi ambao wanafanya kazi ya Bunge hapa ambao mwishoni clips zote zinafutwa, hakuna kazi iliyofanyika. Hili halikubaliki na tunasema kwa masikitiko makubwa, tuna haki ya kupewa kile tulichochangia hapa. Kama ilivyo upande wa CCM wanapewa na sisi Upinzani tuna haki ya kupewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumza kuhusu kufungiwa kwa magazeti, sijui Waziri anatoa wapi mamlaka ya kufungua magazeti. Kwa mujibu wa Sheria ya Habari tuliyoipitisha 2016, hakuna sehemu ambayo inamtaka waziri kufunga magazeti. Anapofanya kosa Mwandishi kama Mwandishi, anawajibika yeye, unapokifungia chombo, kuna wafanyakazi wengine, kuna madereva, kuna wahudumu, kuna watu wengine Waandishi, wanawajibika kwa kosa la moja mmoja, si sawa! Haya ndiyo mambo ambayo tunasema Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mimba kwa watoto wa kike walio chini ya miaka 18 waliopo shuleni, lazima Serikali ikubali kwa kuweka mkakati maalum wa kuwaendeleza watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni. Kupata mimba hatukubaliani nako, si kitu kizuri, lakini sasa tuwalaani watoto wa kike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pamoja na kuja na sheria ya kifungo cha miaka 30, lakini bado watoto wanaendelea kupata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu kwa shule za msingi zinaonesha wanafunzi 251 wamepata mimba, takwimu hizo bado kwa wanafunzi wa shule za sekondari. Kuwaondoa shule watoto kwa kupata mimba bila kuwa na mpango wa kuwaendeleza ni sawa na kuendelea kutengeneza Taifa la mbumbumbu. Tujue watoto wanaopata mimba ni dhahiri hawajapata uelewa wa masuala ya afya ya uzazi kwa maana ya kujua uzazi wa mpango, afya ya mama na mtoto, elimu ya kulea mtoto, umuhimu wa chanjo na kadhalika. Ni wakati wa Serikali kuweka mkakati wa mpango wa kuwarudisha shule watoto wa kike wanaopata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwiano wa walimu katika shule zilizopo mjini na vijijini haupo sawa. Ipo haja Serikali kuona jinsi ya kugawa walimu kwa uwiano ili kukidhi mahitaji ya walimu kwani shule nyingi vijijini zina upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la mkanganyiko wa vitabu, kutokana na makosa makubwa yaliyopo kwenye vitabu na bado vinaendelea kutumika kuharibu watoto wetu, ni vizuri Serikali ikachukua hatua kuvikusanya vitabu vyote na kuviondoa kwenye shule na kuja na utaratibu wa haraka wa kutengeneza vitabu vingine visivyokuwa na makosa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii muhimu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Nimefuatilia sana taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji lakini katika hotuba yake hakuzungumza mkakati wa kufufua viwanda vilivyokufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Tanzania ya Viwanda lilikuwepo na Mwalimu Nyerere miaka 1967 alikuwa na vision hiyo na ali-implement wakati ule kwa kuhakikisha viwanda vingi vinaanzishwa katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro pekee ulikuwa na viwanda zaidi ya 40, lakini hivi sasa viwanda vingi vimekufa vikiwemo viwanda vya Canvas, Komoa, Asante Moprocco, Ceramic Tanzania, Leather Shoe, Unnats na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aje na majibu, upi mkakati wa Serikali wa kufufua viwanda vya Mkoa wa Morogoro ambavyo vilikuwa vikitoa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro?

Mheshimiwa Naibu Spika, ubinafsishaji wa viwanda ulikuwa na lengo la kuongeza ufanisi wa uzalishaji na si kuua viwanda. Sasa kwa nini uwekezaji umetumika kuongeza tija kwa mwekezaji na kuua ajira? Wawekezaji kwa masikitiko makubwa wametumia viwanda hivi kama Collateral kuchukua mikopo mikubwa katika mabenki badala ya kuendeleza kwenye biashara za malori, mabasi na kuua viwanda hii sio sawa. Tunataka kuona Serikali inachukua hatua mahsusi kwa wawekezaji hao kwa makusudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba za Serikali zilizonunuliwa na wawekezaji hata baada ya kuua viwanda kwa nini wawekezaji hawa wasirudishe nyumba hizo zikatumika kwa wafanyakazi wa Serikali? Hawalipi kodi hawalipi pango, huku wameua viwanda; ni kwa nini Serikali isichukue nyumba hizi zikatumika kwa maofisa wa Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya Mwendo Kasi Jiji la Dar es Salaam, ni kama imekuwa monopolized na watu wachache. Kabla ya mwendo kasi wapo wamiliki wa mabasi ya daladala ambao walikuwa wakifanya biashara tena kwa mkopo na wengine wakijifunga mkanda kuuza nyumba, mali na kuingia kwenye biashara ya daladala. Serikali imekuja na mpango wa mabasi yaendayo kasi; kwa nini wasiwape fursa wafanyabiashara wa daladala nao kama wana uwezo wawekeze katika mabasi hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa mabasi ya mwendo kasi ambayo yalikuwa yanatoa huduma kwenye njia pekee sasa hivi yanafanya biashara kwenye njia ambazo si maalum; wa mfano Mbezi Louis, Muhimbili; hali hii inawaweka pembezoni wafanyabiashara wanyonge wa daladala ambao nao wangeweza kupata fursa hizo kama wazawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya viwanda sasa itekelezwe kwa vitendo ambapo tunatarajia kuona Serikali inafanya kazi kwa pamoja na Wizara nyingine mtambuka kama vile Wizara ya Kilimo na Mifugo, Nishati na Madini pamoja naWizara ya Maji na Umwagiliaji. Hakuna viwanda bila uhakika wa umeme na malighafi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa maandishi Wizara hii muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu importation ya mbegu za kilimo, kwa nini tunaendelea kuruhusu makampuni makubwa kama Panner SIDCO ambayo hurb zao zipo nje ziendelee kushika kasi katika soko la mbegu? Serikali lazima ifikirie kuwezesha makampuni ya ndani na wakulima wetu kupitia Vyuo vya Utafiti kama Ilonga, ASA, kuwasadia wakulima kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhakika wa chakula unaenda sambamba na uhakika wa mbegu. Lazima Taifa lijitafakari na kutenga bajeti ya kudumu kuwezesha makampuni ya ndani kuyajengea uwezo wa kutengeneza mbegu hasa zinazoendana na hali ya hewa ya mazingira tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko ya wananchi juu ya mfumo wa NFRA na hii inatokana na urasimu wa Viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao wanatumia mfumo huu kuwapa fursa wafanyabiashara wa mazao kuuza mazao badala ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Maafisa Kilimo katika ngazi za Kata watumike kusaidia kuwatambua wakulima na kuwawezesha kupata fursa badala ya sasa hivi ilivyo kwa mfumo huu kwa nje unaonekana kuwasaidia wakulima, lakini wengine wanaumizwa na urasimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu feki masokoni; mamlaka zinazohusika kwa nini zinashindwa kufanya kazi? Wakulima wananunua mbegu madukani hawana utalaam wa mbegu, lakini hakuna hatua za dhati za kuwakamata, kukagua maduka ya pembejeo za kilimo
na mifugo ili kubaini mbegu feki na mbegu zilizoisha muda wake wa matumizi. Mfano, viuatilifu holela vinavyoingia madukani kwa njia ya panya, mfano Mkoani Mbeya na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Morogoro katika Wilaya ya Kilosa, Mvomero, Kilombero na Wilaya ya Morogoro Vijijini. Serikali, Wizara ya Ardhi isaidie kufuta mashamba pori yasiyoendelezwa kwa miaka mingi. Mfano, Mvomero na Kilosa, Serikali ichukue hatua kubadilisha matumizi ya mashamba hayo. Mfano, NAFCO Kilosa yagawiwe kwa wakulima na wafugaji ambao migogoro yao inatokana na uhaba wa maeneo ya kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa kodi au ushuru wa mazao kwa wakulima mfano, soko la mazao Kibaigwa. Ni kilio cha wakulima wengi wa Mikoa ya jirani na Morogoro; Kiteto na Dodoma ambao wanashindwa kupeleka mazao yao kutokana na ushuru wa mazao wa kila kituo cha kizuizi cha ushuru wa mazao. Ushuru huu ukiondolewa, utawasaidia wakulima kuacha kuuza mazao yakiwa mashambani na badala yake ushuru huu watozwe wafanyabiashara. Vinginevyo, wakulima wataendelea kuuza mazao yakiwa shambani na kwa lumbesa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie kwa maandishi hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Baada ya kumsikiliza sana kwenye uhamasishaji wa Wabunge kuunga mkono hoja ya Wizara hii ni lazima tushauri ili kusaidia maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara kama wadau muhimu wanaotegemewa na Taifa kuongeza mapato, wako katika wakati mgumu sana na wengi wamefunga biashara zao hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kuelemewa na kodi nyingi zisizo na tija. Kwa nini wafanyabiashara wasipewe fursa wezeshi za kuwezesha wafanye biashara hizi wapate faida na waweze kulipa kodi bila kukimbizana? Serikali lazima ifungue milango ya biashara na kuwaona wafanyabiashara ni marafiki na wadau muhimu wanaotakiwa kusaidiwa ili biashara zao kuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Waziri, kwa nini hajaleta taarifa za hali za biashara, kwa nini hajasema wafanyabiashara wangapi wamefunga biashara, wawekezaji wangapi wamehamisha uwekezaji au wamesitisha uwekezaji wao? Waziri angeleta status ya hali ya biashara nchini na challenges zilizopo ili tuone mikakati ya Serikali ya kufufua biashara hizi au kuhamasisha wafanyabiashara kurudi kwenye biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za Afrika Mashariki mfano Rwanda mifumo yao ya kukusanya mapato ni rafiki na kila mfanyabiashara anajikuta anaona umuhimu wa kulipa kodi/mapato kwa faida ya Taifa lake. Kwa nini tusiige mfumo huo ambapo hata ukitokea biashara imekufa wanapeleka wataalam wa biashara, wanazungumza nao na kuwapa indoor training jinsi ya kufufua biashara badala ya hivi sasa biashara ikifa hamna anayejali hata Serikali haioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake (TWB), tumesikia hadithi za kuwa benki hii itapeleka matawi mikoani. Je, kwa nini Benki hii ya Serikali iliyoanzishwa kwa ajili ya kutoa ahueni kwa wanawake imebaki kuwa ya watu wachache kwa maana ya mikoa michache? Benki zingine zimeanzishwa nyuma baada ya TWB sasa hivi zina matawi karibu kila mkoa, kuna shida gani kwa nini benki hii ya Serikali isifungue matawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, interest ya Benki hii ya Wanawake ni kubwa hata kuzidi Benki ya Posta, kwa nini? Lengo la benki hii ni kusaidia wanawake wapate fursa za kukopa na kuendeleza ujasiriamali lakini cha kushangaza inaonekana kuwa na interest za juu hali inayopelekea wanawake wengi kushindwa kumudu gharama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe na mipango mipya ya kupata vyanzo vya mapato, wataalam wabuni vyanzo vipya vya mapato kupitia miradi mipya ya kilimo, uvuvi na mifugo ambapo zipo nchi zimeendelea kwa kutegemea blue economy yaani uvuvi tu. Kwa nini Serikali isifikirie uwekezaji kwa maana ya kuwa na wataalam ambao watalipatia Taifa mapato badala ya hivi sasa inakimbizana na wavuvi haramu na kuingia gharama nyingi za kuharibu nyavu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wawekezaji wameanza kufunga viwanda. Kwa nini Serikali haifanyi utafiti na kuja na mawazo/mbinu za ku-retain wawekezaji badala ya kukaa kimya na kusubiri wawekezaji wapya?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Waziri kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wa Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha ardhi inawanufaisha Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo baadhi ya mambo ambayo lazima tuseme ili kusaidia kusukuma Wizara hii muhimu kwa Watanzania. Ofisi za Ardhi za Kanda, mpango huu ulipoanzishwa ulikuwa na nia ya kusogeza huduma karibu na wananchi. Kanda ya Kati, Mkoa wa Morogoro ndipo yalipokuwa Makao Makuu na Wizara/Serikali ilijenga Ofisi za Ardhi za Kanda kwa gharama kubwa. Ofisi hii zimesaidia sana chini ya Kamishna imepunguza kwa kiasi fulani migogoro na malalamiko ya ardhi hususan Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri amesema katika hotuba yake, Serikali imebadilisha/kuhamisha Ofisi ya Kanda Morogoro na kuhamishia Dodoma, hii si sawa. Kwa kipekee Mkoa wa Morogoro utazamwe kwa namna nyingine kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi ya mara kwa mara ambayo imegharimu maisha ya watu kwa kusababisha vifo na majeruhi hasa katika Wilaya za Kilosa, Kilombero, Mvomero na Morogoro Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa vifaa vya kupimia ardhi; Maafisa Ardhi wanafanya kazi katika mazingira magumu ambapo unakuta mfano, Mvomero ina kifaa kimoja tu cha kupima, hali inayosababisha ucheleweshaji wa upimaji wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kero ya bomoa bomoa; katika vitu vinavyolalamikiwa na wananchi ni uvunjaji wa nyumba za wananchi wanaojenga kwa jasho kwa vibali vyote kwa kuzingatia masharti mbalimbali hasa waliopo kando ya barabara ambapo hivi sasa Serikali kupitia TANROAD wanakusudia kuvunja nyumba za wananchi na barabara ya Dar es Salaam, Morogoro kwa zaidi ya mita 20 kila upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hizi zinafanyaje kazi Ardhi na Miundombinu? Kwa nini kusiwe na mpango wa kuzuia wananchi kujenga badala ya kusubiri wananchi wajenge kisha waje kubomoa. Yapo maeneo ambayo wananchi nao wamepelekewa huduma muhimu kama maji, umeme na kadhalika
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa maandishi hoja hii muhimu ya elimu. Kwanza nianze na motivation kwa walimu. Serikali imeshindwa kutoa motisha kwa walimu wa shule za sekondari na msingi ndiyo maana ufaulu umeshuka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu madai ya msingi ya walimu kupandishwa madaraja, kulipwa arreas (malimbikizo), likizo, uhamisho na kadhalika. Madai hayo yote yasiposhughulikiwa kwa wakati hali ya ufaulu katika shule za Serikali itaendelea kuwa mbaya na kamwe hazitaweza kushindana na shule binafsi ambazo kwa sasa zimechukuliwa role ya Serikali badala ya shule za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uhamisho walimu wa arts kwenda shule za msingi. Tumeshuhudia walimu wengi wakiripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba wamejinyonga na wengine kufa kwa msongo wa mawazo. Kuendelea kuwashusha walimu kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi pasipokuwaandaa kisaikolojia (counseling) bado wanajiona kama ni demotion kwao na inawavuruga moyo. Inahitajika motivation ya aina yake kwa walimu hao ili waweze ku-cope na mazingira mapya wanayoenda kukutana nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifikirie namna ya ku-motivate shule binafsi ambazo zinatoa aibu Taifa hili. Shule binafsi zimesaidia kupandisha kiwango cha ufaulu kwa kiasi kikubwa kwenye Taifa hili na hii imefanya wazazi wengi sasa wanasomesha watoto kwenye shule za private badala ya kupeleka Kenya, Uganda na Malawi kama ilivyokuwa zamani, hivyo pesa zilizokwenda nje ya nchi sasa zinabaki hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isipunguze masharti katika shule hizi hasa kuwapunguzia gharama zilizokuwa muhimu ili kuziwezesha shule hizi kuendelea kufanya vizuri? Badala ya Serikali kupambana na shule za private kuweka masharti magumu, sasa wazipe fursa na kuwajengea uwezo na mazingira rafiki ili waendelee kuwekeza kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure bado haijaisaidia nchi hii. Sasa hivi imekuwa ni malalamiko kila kona, bado Serikali imeshindwa kupeleka huduma muhimu kwa wanafunzi katika shule za msingi; chakula mashuleni hamna. Moja ya sababu zilizotolewa na Taarifa ya Kamati ya Wizara ya Elimu ni kukosekana kwa chakula mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure wanafunzi wana njaa; elimu bure wanafunzi hawana madawati shuleni, wazazi bado wanachangishwa, elimu bure bado wazazi wanalipia gharama za ulinzi, maji, umeme na kununua vitabu. Hiyo siyo elimu bure, ni lazima Seriklai ingefuta ghrama zifuatazo; chakula, ulinzi, vitabu mashuleni na kadhalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa taarifa za uchangiaji wa bajeti ya Maji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Mindu nimeona katika kitabu cha Waziri anasema yupo kwenye majadiliano na Wafaransa ili kufanya ukarabati wa bwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa population ya Morogoro sasa Bwawa la Mindu haliwezi kuwa ni suluhisho sahihi, lazima Serikali ifikirie kuwa na bwawa lingine ambalo litasaidiana na Bwawa la Mindu ili kutosheleza wananchi wa Manispaa ya Morogoro pamoja na viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bwawa la Kidunda, fidia zilizotolewa na Serikali kwa wananchi ni ndogo, hazikidhi na bado yapo malalamiko ya wananchi wa ndani kupunjwa. Ni vyema Wizara ikajiridhisha na fidia hizo hata kama zimefanywa na evaluator wa Serikali lakini bado mradi huu ili ufanikiwa lazima Wizara ijenge mahusiano na wananchi ambao watakuwa ndio wanufaika na walinzi wa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gharama za ku-drill visima, suala la kupeleka maji kwa wananchi ni jukumu la Serikali, lakini cha kushangaza sana, mtu anakosa huduma ya maji anaamua kukusanya pesa ili kuchimba kisima; gharama za kufanya survey na kupata kibali cha kuchimba maji ni shilingi 250,000. Pia kila mwaka wananchi waliochimba kisima wanalazimika kulipa shilingi 250,000 kila mwaka, hiyo siyo sawa. Kama mwananchi amechimba kisima, analipia umeme kusukuma maji, automatically kwenye umeme analipa kodi, kwenye jenereta na analipa kodi ya dizeli kusukuma maji. Hivi kwa nini Serikali inalipisha kodi nyingine tena shilingi 250,000? Hii haikubaliki. Watu wa bonde wanapaswa kuangalia upya malalamiko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuendelea ku-harass vijana na akinamama ambao wanaweka pump za maji ili kumwagilia mboga mboga katika mashamba ambapo Morogoro akina mama na vijana walinyanganywa pump zao za umwagiliaji tu wanatakiwa kulipa kodi maji ambayo ni ya mto yanayoenda kupotea baharini.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanaamua kuya- utilize maji hayo ambayo yangeweza kupotea badala yake wananyang’anywa pump za umwagiliaji, tena vikundi vya akina mama wenye mkopo benki. Hii siyo sawa. Pengine Serikali ingeweza kusubiri wavune mboga mboga na walipe ushuru sokoni badala ya kuvi-harass vikundi vya wanawake na vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipaumbele cha Serikali bado siyo maji na ndiyo maana fedha zinazotengwa haziendi kwenye Wizara na hii imezua mashaka baada ya kubaini baadhi ya maeneo. Mfano, Mkoa wa Katavi umepelekewa miradi mingi kuliko mikoa mingine, hii haikubaliki. Lazima miradi hii ya visima igawanywe kwa usawa kwa kuwa tatizo la maji ni la nchi nzima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwa maandishi, kwanza ni kuhusu pembejeo za kilimo. Wizara imeshindwa kusimamia utaratibu wa ugawaji pembejeo za wakulima kwa wakati badala yake imekuwa kilio na kupata pembejeo za kilimo kwa kuchelewa ikizingatiwa kuwa wakulima wengi hawana uwezo wa kumudu gharama kubwa za mbolea na wanategemea mbolea ya ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikiri wazi kuwa mfumo wake wa kupatia wananchi mboleo ume-fail na watafute mbinu nyingine ya kufikisha mbolea hizo kwa wakulima kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya uhakika wa mazao bado. Bado kuna changamoto, Serikali imekazana kudhibiti uuzwaji wa mahindi nje ya nchi huku Serikali ikishindwa kuwa na mfumo mbadala wa kusaidia wananchi wake kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya mahindi yameharibika, wananchi wamepata hasara ikiwemo Mkoa wa Morogoro. Serikali imewaweka wananchi katika mazingira magumu sana wengine kupata hasara. Cha kushangaza, mahindi kutoka Zambia yanapita Tanzania na yanaenda Kenya kuuzwa, hiyo siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya mawakala wa pembejeo za kilimo ambao wamefanya kazi ya kupeleka huduma kwa wakulima mpaka sasa hayajalipwa. Hii ni aibu na uonevu kwa wakulima. Serikali iliahidi kupitia madai yote na kubaini madai hewa na halali, mpaka sasa hamna majibu. Tatizo hili kama Serikali haitatenda haki kwa mawakala halali, hii itaendelea kujenga chuki kati ya Mawakala na Serikali yao. Ni vyema Serikali ikapitia upya madai hayo na kutoa haki kwa mawakala.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kwa maandishi kama ifuatavyo:-

(i) Uchomaji nyavu haramu; hatupingi operation za kuchoma nyavu lakini hoja ni kwa nini wavuvi ndiyo watu wa mwisho kuadhibiwa, nyavu hizi haramu zinaingiaje nchini? Nyavu zinapitaje na kuingia nchini? Endapo Serikali imeweza kudhibiti mahindi kuuzwa nje ya nchi inashindwa nini kudhibiti uingizwaji wa nyavu haramu nchini?

(ii) Kiwanda cha nyavu haramu Arusha, tuliona Waziri alifika katika kiwanda na kubaini utengenezaji wa nyavu hizi haramu. Je, ni hatua zipi Serikali imechukua dhidi ya kiwanda hicho? Kama wavuvi wakikamatwa na nyavu zinachomwa, je, kiwanda kilichozitengeneza kinachukuliwa hatua gani?

(iii) Migogoro ya wakulima na wafugaji Mkoa wa Morogoro bado ipo. Kwa nini Serikali isitafute suluhisho la kudumu? Kwa nini Ranchi ya Mkata, Kilosa ambayo imegeuka kuwa pori lisigawiwe kwa wakulima na wafugaji ili kukidhi upungufu wa ardhi na malisho kwa wakulima na wafugaji Wilayani Kilosa?

(iv) Usafirishaji wa ng’ombe toka Shinyanga hadi Dar es Salaam wanyama wanakufa njiani. Kwa nini Serikali isijenge kiwanda cha kisasa au machinjio ya kisasa wanapotokea ng’ombe na nyama ikasafirishwa magari yenye air conditioner na ikapelekwa Dar es Salaam badala ya ilivyo sasa? Kuendelea kusafirisha mifugo siku nyingi njiani ni kuwatesa mifugo na ni kinyume na haki za wanyama. Kama Dodoma kupitia machinjio yake wamesafirisha mbuzi toka Dodoma hadi Dar es Salaam na wamesafirishwa kwa ndege kwenda Uarabuni ndani ya saa 24, kwa nini Shinyanga, Kanda ya Ziwa washindwe kusafirisha nyama badala ya mifugo?
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia hoja kwa njia ya maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tatizo la GN kutokutambulika katika hifadhi nyingi nchini inaongeza migogoro isiyo ya lazima kati ya wananchi na hifadhi, utatuzi wa haraka unahitajika. Wahifadhi/askari wanyamapori wanatumia GN kama fursa ya kuwaumiza wananchi kwa kigezo kwamba wameingia kwenye hifadhi na kuwalipisha faini zilizo onevu.

Mheshimiwa Spika, bado Wizara haijaweka dhamira ya dhati kwa kuimarisha utalii wa fukwe hapa nchini kama ilivyo nchi za Mauritania/Morocco na nchi nyingine. Hapa nchini fukwe zetu kama Coco Beach ambazo zinatumika kuuza mihogo kwa nini Wizara isiziboreshe kwa kujenga hoteli za kitalii, beach za kisasa, hasa watalii wanapotua Dar es Salaam wakati wakisubiri kwenda kwenye hifadhi wakapumzika beach, wakaongeza mapato badala ya ilivyo sasa kwamba wanabaki hotelini wakisoma vitabu huku wakisubiri kwenda kwenye hifadhi?

Mheshimiwa Spika, malipo kwa wananchi wanaouawa na tembo au wanyama wengine ni kidogo, ipo haja Sheria ya Fidia kuletwa Bungeni ibadilishwe. Kwa sasa kifuta jasho ni kati ya shilingi 100,000 ni kidogo ikilinganishwa na thamani ya utu/mwanadamu. Tembo akigongwa na gari faini ya USD 1500 zaidi ya shilingi milioni 30 kwa tembo mmoja, lakini ukilinganisha mtu akiuawa na tembo eti kifuta jasho shilingi 100,000 sio sawa kabisa.

Mheshimiwa Spika, Wami Mbiki ni potential kwa hifadhi, wanyama wapo wa kutosha, Sweden imewahi kusaidia hifadhi ile na Mwenyekiti wake ni Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Kwa nini Wizara isiendeleze hifadhi hii ambayo ina rasimali za wanyama za kutosheleza? Sasa hivi wananchi wameingia kwenye hifadhi wanalima, wanawinda wanyama na wanakata miti, sasa badala ya hifadhi imegeuka mashamba. Wanyama wanavamia makazi ya wananchi kula mazao kwa sababu hifadhi inakosa sifa. Tunaitaka Serikali kurudisha hifadhi hii kwenye hadhi yake ili kuongeza kipato kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika Hifadhi ya Mikumi wanyama wanaendelea kuuawa kwa kugongwa na magari. Ulikuwepo mpango wa barabara ya Morogoro – Mikumi ku-divert Kilosa mpaka Mji wa Mikumi. Kwa nini mpango huu hautekelezeki?

Mheshimiwa Spika, kuzibwa kwa shoroba; Hifadhi ya Saadani kupitia Wami Mbiki kwenda Mikumi hadi Selous kuna wanyama wanatembea kwa mfano tembo wanatoka Saadani hadi Selous, lakini shoroba zimezibwa. Mbaya zaidi Serikali imejenga majengo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, wameziba shoroba. Vilevile Serikali hiyo imevunja nyumba za wananchi Mtaa wa CCT Mkundi kwa madai kuziba shoroba wakati majengo ya Serikali Wilaya ya Mvomero yapo, hayajavunjwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja zifuatazo kwa Wizara mbili zilizowasilishwa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijinasibu kuwa inashughulikia rushwa. Manispaa ya Morogoro ujenzi wa barabara ya kilometa nne kutoka Kichangani – Tubuyu. Barabara hii imejengwa kwa fedha za mkopo wa World Bank ambayo tunatarajia fedha hizo zitalipwa na kodi za jasho la Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza barabara hiyo kilometa moja imejengwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 3.4 kwa kilomita nne, hivyo imegharimu 13.8 bilioni, wakati haina mto, korongo wala milima imenyooka kama rula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Madiwani walihoji matumizi mabaya ya barabara hiyo kwa fedha, matokeo yake rushwa za wazi zilianza kutolewa kwa Madiwani wa CHADEMA na CCM. Kuna kigugumizi gani katika kufuatilia ubadhirifu wa fedha waziwazi zilizotafunwa na wakandarasi wakishirikiana na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii niliileta Bungeni nikamuuliza swali Waziri wa TAMISEMI ambaye wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Jafo mwaka jana alienda kuitembelea barabara hiyo na akaunda Kamati ya kufuatilia baada ya kutoridhika na pesa zilizotumika ikilinganishwa na thamani ya barabara yenyewe lakini cha kushangaza hadi sasa hakuna kitu kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufisadi huu wa wazi wazi Serikali imeuona lakini hakuna hatua zozote zimechukuliwa. TAKUKURU wamehoji Madiwani wa Manispaa wamekiri kupokea rushwa kwa nini Serikali haichukui hatua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wamevunja nyumba za wananchi Mtaa wa CCT Mkundi kwa madai ya kujenga kwenye hifadhi ya lami lakini wananchi hawa wana hati halali za viwanja pamoja na vibali vya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika Serikali ilipeleka huduma za maji, umeme, ujenzi wa shule, Ofisi ya Mtendaji wa Kata na wana vitambulisho vya makazi na walipiga kura. Sasa hivi Serikali inawahamishia wananchi wa Mtaa wa CCT katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Haki haikutendeka kwa wananchi na imesababisha usumbufu na taharuki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, usahili wa vyuo; Serikali tumeona imefungia baadhi ya vyuo visivyo na sifa hali iliyosababisha usumbufu kwa watoto, wazazi wamepoteza fedha na wanafunzi wamepoteza muda, pia Serikali imechukua hatua gani kulipa fidia kwa usumbufu huo kwa maana hiyo hadi chuo kianze kudahili wanafunzi kuna uzembe pia kwenye mamlaka zilizotoa kibali, je, hatua zipi zimechukuliwa kwa watendaji walioruhusu vyuo hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa wahitimu mtaani ambao hawana ajira, je, Serikali haioni sasa kuna haja kuweka somo la kujitengemea katika vyuo vikuu ili kuwajengea wanafunzi wanaomaliza vyuo kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira toka Serikalini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya Walimu kutopandishwa mishahara na kupanda madaraja bila kupewa haki za kuongeza mishahara yamekuwa ya muda mrefu. Mazingira magumu ya Walimu kuanzia shule za msingi vijijini yanakatisha tama; Serikali kwa nini isije na mpango wa kujenga nyumba za Walimu kama ilivyowahi kuja na mpango kujenga vyumba vya maabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, motivation kwa Walimu wanaojitolea tumeona katika vyombo vya habari, shule za kata zimetoa watoto bora, pia shule za kata Walimu ni wachache wanaofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamisho wa Walimu pasipo kulipwa haki na stahili zao; Serikali iliangalie hili, Rais amewahi waambia Walimu wasikubali kuhama kama TAMISEMI haina fedha ya uhamisho. Yapo malalamiko bado ya uhamisho wa Walimu especially Walimu wa sekondari waliopewa shule za msingi kufundisha, Serikalini iangalie upya malalamko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wengi wapo mijini zaidi kuliko vijijini Serikali iangalie uwezekano wa kuwa na uwiano sawa wa Walimu; inashangaza unakuta shule za msingi vijijini walimu ni wachache, wanalazimika kufanya kazi ngumu kugawana masomo na wengine kulazimika kufundisha masomo wasio na uwezo nayo, hawajasomea mfano sayansi kwa walimu wa Arts. Masomo ya sayansi ndio wanapewa kipaumbele kulinganisha na wanafunzi wanaosoma michepuo mingine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, uendeshaji wa ndege nchini. Serikali iliagiza ndege kubwa (Dreamliner) iko wapi? Mbona hatuoni ikifanya kazi? Inanunuliwa ndege ya maonyesho kwa cash money, kodi za wananchi halafu hatuoni ikifanya kazi kwa kuinua uchumi wa nchi kama ilivyoelezwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, zipo taarifa kuwa ndege hiyo imekodishwa Kenya. Kama ndivyo, hayo ndiyo tunayolalamikia kuwa Serikali ina tatizo katika kusimamia na kupanga priorities. Hivi kulikuwa na sababu gani kukimbilia Dreamliner, ku-invest kwenye ndege ambayo return zake haziwezi kuonekana kwa haraka? Ni bora Serikali ingewekeza kwenye project kama za afya, maji na kadhalika, ndege bora ingetumia PPP.

Mheshimiwa Spika, matengenezo ya ndege ndogo tatu (Bombardier) zaidi ya shilingi bilioni 14, hivi kweli ndege zinajiendesha kwa faida? Kwa nini Serikali isingeachia private sector au nchi zenye uzoefu wa biashara za ndege mfano Ethiopia na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, SGR, kwa sasa ajira kwa Watanzania ni asilimia 20 na asilimia 80 ni Waturuki. Hiyo siyo sawa, Serikali ilipaswa kuandaa watu wetu kuingia kwenye ajira kabla ya kuanzisha mradi wa SGR. Kazi ambazo ni professional/technical skills zingefanywa na Watanzania kuliko hivi sasa Watanzania wanaishia kwenye kazi ndogo ndogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ubinafsishaji viwanda vya Serikali ambavyo havifanyi kazi hususani viwanda vya Mkoa wa Morogoro mfano Asante Moproco, Canvace, Morogoro Shoes Tanaries na kadhalika, iko haja Serikali kuangalia upya uwekezaji huo kwani kwa sasa kuna malalamiko kuwa wawekezaji wameuza vipuri mfano, Morogoro Canvas vipuri havipo Serikali ifuatilie. Hivi ilikuwa ni uwekezaji, ubinafsishaji au ufilishaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tumbaku Morogoro kilichokuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji na kutoa ajira, sasa hivi kimepunguza uzalishaji na ajira na kinadai Serikali tax returns za zaidi ya bilioni 25. Serikali irudishe fedha hizo viwanda viweze kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, importation ya bidhaa zinazozalishwa nchini kwa wingi mfano maziwa hatuna sababu ya kuendelea kuruhusu uingizaji wa maziwa ya nje na yanauzwa bei ndogo ikilinganishwa na maziwa yanayozalishwa nchini. Hatuwezi kukuza uchumi kama Serikali haiweki mazingira rafiki kwa viwanda vyetu vya ndani kwa kuvilinda ili viweze kukabiliana na ushindani. Vilevile, returns za tax kwa viwanda vingi hapa nchini hazirudi hii inaweza kushusha fursa za uwekezaji kwa viwanda vingi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara nyingi zinafungwa kutokana na mazingira magumu ya biashara Kariakoo na katika mikoa mingi. Juzi Mtwara tumeona kwenye TV wafanyabiashara wamerudisha leseni za biashara, hii siyo sawa. Kuna mzigo mkubwa wa kodi mfano OSHA, leseni, tax leavy, Manispaa na kadhalika. Mzigo huu mkubwa wa kodi siyo afya na biashara nyingi zinakufa. Serikali iangalie jinsi ya ku-harmonize hali hii kwani uchumi wa nchi yoyote unategemea mapato yanayotokana na wafanyabiashara wadogo ambao wapo wengi nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jeshi kutumika kisiasa, wakati wa uzinduzi wa Makao/ Ofisi za Serikali Dodoma Mkuu wa Majeshi alinukuliwa akisema kuwa Jeshi linafuatilia kauli tata zinazoashirika uvunjifu wa amani. Sio kazi ya Jeshi la Polisi kushughulikia au kupeleleza kauli tata za kuashiria uvunjifu wa amani, ni vyema Jeshi likafanya kazi yake ya kulinda mipaka ya nchi na sio kuingilia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uimarishaji mipaka ya nchi, Jeshi la Ulinzi lipo lakini idadi ya wahamiaji haramu kupitia njia ya panya katika mipaka ya nchi jirani yanaogezeka siku hadi siku, kwa nini hatua zaidi zisichukuliwe na hii imebainika hasa kwenye mapango ya Tanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya mipaka kati ya wananchi na Jeshi la Ulinzi, ipo migogoro mingi kama Pangawe, Kizuka, Mzinga na Kilombero ambayo imesababisha hata mauaji kwa askari na wananchi, iko haja mipaka ya Jeshi ikahakikiwa upya kwa kuwashirikisha wananchi waliopo kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia kwa askari wanaopoteza maisha wakiwa kwenye vita nchi za nje ikilinganishwa na nchi zingine za Afrika Mashariki ni ndogo na zinalalamikiwa na ndugu, pia ipo shida ya urasimu katika kulipa fidia za wajane waliopoteza waume zao wakati wa vita.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, Utafiti wa mbegu mpya na TARI–GMO ya Malindi katika Kituo cha Makutupora Dodoma. Napongeza hatua hiyo lakini kumekuwa na kauli kinzana Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo alinukuliwa akisema Serikali imepiga marufuku majaribio ya GMO, huku hotuba ya Waziri ikionesha kuwapongeza Wizara imegundua mbegu mpya za mahindi inayostahimili magonjwa.

Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Wizara ya maendeleo inayoombwa na Wizara ya kiasi inayopelekwa ni asilimia 48.74. Hata nusu ya asilimia hamsini haifiki kama nchi, kilimo sio kipaumbele na hii inajidhihirisha kutokana na bajeti ndogo iliyopelekwa na hata hii inakiuka makubaliano ya Malabo kuna bajeti ya kilimo lazima itengwe na kufikiwa kwa asilimia 10 ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, ASA; Serikali iongeze nguvu kusaidia utafiti wa mbegu katika vituo vya utafiti. Sasa hivi mbegu nyingi zilizopo nchini hazitoshelezi badala yake makampuni binafsi kama SEDICO, Panner na kadhalika ndio makampuni yanayosambaza mbegu nchini. Ikumbukwe kuwa Harb za makampuni haya ya nje zipo nje ya nchi hivyo ikitokea siku wakagoma ku-supply mbegu nchini hatutakuwa na sustainable agriculture, lazima Serikali ifikirie.

Mheshimiwa Spika, kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu mfano Kenya ilivyofanya kwamba Agricultural Institute zinatengewa bajeti ya kutosha na kuwekeza nguvu kwenye utafiti wa mbegu za kilimo, mbogamboga matunda.

Mheshimiwa Spika, kodi nyingi kwenye kilimo, mfano kilimo cha tumbaku zimezidi mfano (Cess/city service, skills development levy, tozo ya Bodi za Kusindika, tozo Bodi ya Kununua Zao Mbichi, export levy, radiation levy, ushuru wa ushirika, ushuru wa research, halafu mkulima alipwe malipo ya pili all on top of the price, nchi nyingine mkulima analipwa bei anahangaika na kodi kwani yeye sio mnunuzi.

Mheshimiwa Spika, Viwanda vya Tumbaku Morogoro vinapunguza ununuzi wa tumbaku kutokana na Serikali kushindwa kulipa 25 bilioni returns VAT; iko haja Wizara ya Kilimo na Viwanda na Biashara kufanya kazi kwa pamoja maana viwanda vikifa wakulima hawatakuwa na wanunuzi wa mazao yao.

Mheshimiwa Spika, upotevu wa mavuno (post harvesting) wakulima wengi wanapoteza mazao yao kutokana na ukosefu wa maghala ya kuhifadhi mazao. Hali hii ya kukosekana maghala kunasababisha wakulima kulazimika kuuza mazao yao kwa bei ya kutupwa/bei ya hasara. Ushauri, Serikali ifikirie kujenga maghala makubwa katika maeneo ambayo yana kiwango kikubwa cha mazao.

Mheshimiwa Spika, mikopo ya matrekta kwa wakulima; bila kufanya utafiti wa kutosha wakulima wengi wanashindwa kurejesha mikopo. Mfano wakulima waliopo milimani wamekopeshwa matrekta hawawezi kuyatumia hali inayosababisha wakulima kupaki matrekta juu ya mawe, mfano wakulima wa Mgeta, Mvomero Mkoani Morogoro ni vyema utafiti wa kina wa matumizi ya matrekta hayo ukafanyika kabla ya kutoa mikopo hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Umeme wa REA. Tumeshuhudia Mawaziri wakizindua umeme kwenye nyumba za tembe, nyumba za nyasi, nyumba ambazo kwa upepo kidogo tu zitaanguka. Hivi kuna haja gani kuweka umeme ambao siku nyumba zikianguka mnaweza kusababisha madhara? Tumeshuhudia mijini tu shoti ya umeme nyumba zinaungua na kuteketea. Kwanini Wizara isingeshirikiana na TASAF kwanza zikaboreshwa nyumba za Watanzania (kaya) maskini kabla ya umeme?

Mheshimiwa Spika, umeme REA Phase ll. Katika Manispaa ya Morogoro Kata ya Mindu inapitiwa na umeme wa grid ya taifa lakini wananchi wake hawana umeme katika baadhi ya maeneo. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Morogoro na wananchi walitoa malalamiko hayo; kwanini mpaka sasa wananchi hawapati umeme?

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Stieglers George Project. Watanzania wanapaswa kuona mkataba huo. Tafiti zilizofanywa na World Energy Resource zinaonesha kuwa project hiyo itatumia fedha nyingi zaidi ya kiwango kinachotarajiwa. Ni vyema Watanzania tukawekwa wazi.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kidunda Morogoro uliokuwa na mpango wa uzalisha umeme MW 20, ulikuwa na mkakati wa kuendeleza kilimo, kutoa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam, Pwani, Tanga na kadhalika. Kuna haja gani Serikali kuanzisha project hazi-take off mna-jump kwenye new project? Kidunda bado tupo Stiegler’s, gesi bado tumekimbilia Stieglers?
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Na mimi nichukue fursa hii kuchangia muswada uliopo mbele yetu. Katika Bunge lililopita Mheshimiwa Waziri alikuja na mikakati yake akisema atakuja na muswada hapa ambao utakuwa ni mwarobaini; muswada wa habari. lakini matokeo yake sasa imekuwa ni muswada wa taarifa, sijui imekuwaje ghafla ukabadilisha gia hewani. Lakini tunachosema tu ni kwamba huu ni mkakati si muswada kama vile tunavyoufikiria; huu ni mkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa muswada huu, kwa hali halisi na mambo yanavyoendelea hivi sasa ni kwamba unakwenda kupewa rungu. Tumeshuhudia mengi ikiwemo wewe mwenyewe binafsi kuvifungia vyombo vingi vya habari. Na muswada huu unakwenda kufunga midomo; muswada huu unakwenda kukupa mamlaka ya kufanya utakavyoweza kufanya kwasababu kuna baadhi ya vipengele ambavyo vinaonesha kwamba endapo mtu hataweza kupewa taarifa, Waziri ndiye msemaji mkuu na ndiye mwenye mamlaka ya mwisho. Muswada huu unakwenda kukupa wewe mamlaka hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, endapo mtu atakosa taarifa sahihi atakwenda kukumbana na Waziri ambaye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Na kwa mamlaka hayo sasa haitoi fursa kwasababu Waziri anasimami Wizara. Inawezekana kabisa taarifa zinavyotafutwa zipo chini ya Wizara, sasa itakuwaje Waziri aweze kutetea hili? Tunaomba, kwa mujibu wa sheria kwasababu mahakama ndio yenye kuingilia kati, yenye mamlaka; suala hili lingekwenda huko badala ya kumuachia Waziri kuwa ndio msemaji mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikianza kifungu kile cha 19 ambacho kinamtaka Waziri kuwa wa mwisho katika…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 107A ambayo inaitaka Mahakama kuwa ndicho chombo pekee cha kutoa haki inayogombaniwa na si Waziri sasa. Endapo Waziri atapewa mamlaka haya, endapo mtu atakuwa amenyimwa taarifa mahali fulani pa kwenda kulalamikia isiwe ni Waziri; itoe fursa kwamba mtu aweze kwenda mahakamani na mahakama itoe haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 4 kina mgongano juu ya ni nani anapaswa kupewa taarifa. Kifungu hiki kinasema kwamba mpewa taarifa awe ni raia na si mtu. Tafsiri yake ni nini hapa? Wakati Mheshimiwa Waziri anaeleza alisema kwamba mlijaribu ku-relay nchi nyingine kwa mfano South Africa, Malaysia, Uingereza na kwingineko ambapo mnasema kwamba mtu yeyote anapaswa kupewa taarifa. Kwa hizo nchi za wenzetu kwa maana ya Uingereza, Malaysia na South Africa sheria zao zinasema hivyo. Lakini hapa mmekuja na hoja kwamba mtu anayepaswa kupewa taarifa ni raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni raia sisi wenyewe tunaji-contradict kwasababu gani? Yapo matukio kadhaa, kwa mfano issue ya RADAR, wakati huo sisi Tanzania tuliomba information kutoka Uingereza, na imetusaidia kupata taarifa kwa wenzetu; zikatuwezesha kupata change ya dola milioni 12. Sasa kama sisi tutasema mtu anaetaka kupata taarifa ni lazima awe raia kwa maana hiyo tunajifunga. Kama kuna watanzania ambao ni wawekezaji wapo hapa na wakafanya madudu; wakahitaji kupata taarifa hapa hatuwezi kuwapa taarifa kwasababu sheria hii itakuwa inawabana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahivyo, tunacho sema ni kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 18(d) kwamba:-
“Kila mtu ana haki ya kupata taarifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi tunasema kila raia kwa mujibu wa muswada huu. Kwahivyo, kuweka neno raia ni kwamba ni kichaka ambacho tunakwenda kujificha. Tumeona issue mbalimbali mfano sakata la ESCROW tuliweza kupata taarifa kwa wenzetu kutoka Malaysia kwasababu gani? Wao Katiba yao inasema kupata taarifa ni mtu yeyote na si raia. Sasa tutakapokuja na kipengele kwamba tunasema kwamba ni raia sasa tutakuwa tunajifunga kwamba baadhi ya taarifa hatuwezi kuzipata lakini pia hii ni kuleta ubaguzi; hamuwezi mkaja na muswada huu mnatuambia nchi zingine zimefanikiwa kwa mfano Malaysia na South Africa ambazo sheria yao ni tofauti na hii; haizungumzii raia inasema mtu kupata taarifa ni haki ya kila mtu. Hata Katiba yetu inasema hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kifungu cha kwanza kinasema sheria ianze kutumika mara tu Waziri anapoitangaza. iko miswada mingi ambayo imepita, zipo sheria nyingi ambazo zimepitishwa na Bunge hili lakini bado hazijaanza kufanyiwa kazi. Lakini kwenye hili kwasababu ni mkakati ikishapitishwa tu tayari ianze kufanya kazi; lakini kwanini isingepewa muda kanuni zikatengenezwa? Sisi tunasema ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge lazima tuungane katika hili kwasababu muswada huu unakwenda kunyamzisha vyombo vya habari; ni lazima tufikirie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii vyombo vya habari vinafungiwa, mtu akiamka tu asubuhi anavyoamua anafungia vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tanzania kwa level tuliyofikia sasa maendeleo tuliyo nayo tunajivunia ni vyombo vya habari. Ni nani ambae sasa hivi atakubali kuwekeza kwenye vyombo vya habari kama tunakwenda kuwa na sheria ya namna hii? Radio moja ikifungiwa ina waajiriwa permanent labda 20, hujaweka wale ambao wanakwenda kujifunza, hujaweka watu wale ambao wanakuwa wanafanya mawasiliano ya moja kwa moja; kwa maana kuchangia hoja, hujaangalia familia za hao watu. Tunaathiri zaidi ya watu 100 kufungia redio moja; wafanyakazi tu peke yake achana na Watanzania. Sasa leo hii tunakuja na sheria hii ambayo mtu akifanya kosa tu dogo lazima afungiwe. Kwahiyo, tunasema, kwa wakati tulionao na hali tulizonazo tunaona huu ni mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini vilevile kifungu cha sita tunapendekeza kiondolewe kabisa, kwanini? Mnasema kwamba mtu ambaye ata-distort information yoyote anapaswa kuhukumiwa kama zilivyo Sheria za Usalama wa Taifa. Ni kwanini tujifiche nyuma ya hizi sheria za usalama wa taifa wakati tunayo sheria ambayo inazuia hali hiyo ya mtu kama akisema uongo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunasema kwamba mtu atafungwa kifungo cha miaka 15 mpaka 20. Kwanini mtu kama ametoa information tu akakutane na kifungu kikubwa namna hii? na hakuna sehemu ambayo inazungumzia kwamba endapo hakuna fine, moja kwa moja kwamba mtu ni lazima akakumbane na kifungo cha ndani kwa maana miaka 15 mpaka 20; kwanini hakuna fine katika hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine kwa mfano informers wanakupa habari nzuri ambazo zinaweza zikasaidia na zikajenga lakini kama siye msemaji atakumbana na kifungo hiki. Sisi tunasema kifungu hiki kiondolewe kwasababu kitakwenda kutunyima kupata taarifa; so long mtu ambaye ana information ambazo ni reliable zinaweza zikasaidia nchi, zikasaidia taifa; kwa mfano issues za njaa na mafuriko; tukasubiri afisa ambaye ameteuliwa na Serikali aende akatoe taarifa hizi. Hii ni kwenda kunyima vyombo vya habari kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye uchaguzi, tutakwenda kwenye uchaguzi mwaka 2020, kwa maana hiyo taarifa za awali za uchaguzi mwandishi hataruhusiwa kuzitoa ni mpaka asubiri Afisa Habari wa Wilaya? Tunachosema kwamba kuna mambo ya msingi ambayo kwa hofu tu ya kukumbana na hili ni lazima tuyaangalie, na tunapendekeza kabisa kifungu hiki cha sita kiondolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mmezungumzia kuhusu utoaji wa taarifa kwa maana ya mtu atakapoomba taarifa apewe siku 30, hivi hiyo itakuwa ni taarifa au itakuwa ni kitu gani, kwa sababu uende uombe taarifa kwenye taasisi, ukae siku 30 usubirie kupata jibu kwamba hiyo taarifa ipo au haipo, ni kwa nini msingeweka siku tatu au siku moja kama ilivyo TAMISEMI. Siku 30 halafu unajibiwa kwamba taarifa unayoihitaji haipo. Tunachotaka kumuambia Mheshimiwa Waziri, Muswada huu utakwenda kunyamazisha vyombo vya habari, utakwenda kuumiza wamiliki wa vyombo vya habari, utakwenda kuvunja morali kwa watu ambao wana interest ya kuwekeza kwenye tasnia ya habari, tunaomba kama kuna uwezekano wowote Muswada huu uondolewe tusubiri tupate maoni upya. Wadau mbalimbali wa habari walishiriki lakini maoni yao hayamo humu, hayakuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunasema, mtaupitisha kwa sababu ya wingi, lakini tunachosema kwamba tutafika kwenye hali ambayo, kama wenzetu Uganda ilivyo Rais anaamka asubuhi anafunga magazeti, anafunga redio. Sasa kwa sasa hivi graph ya vyombo vya habari ambapo kwa Afrika, Uganda ilikuwa inashika nafasi kama ya sita, sasa hivi inakaribia kuwa mwishoni kwa sababu ya vyombo vya habari kufungwa midomo na Serikali. Tunaomba ili Muswada huu uwe na maana, ni lazima Serikali ikubali kwamba kuna baadhi ya vitu ambavyo ni lazima vifanyiwe marekebisho makubwa, vinginevyo uwekwe pembeni tusubiri mpaka muda utakapofikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania ya leo hii, kwa teknolojia ilivyokua sasa hivi, mtu akipata taarifa mtu ataogopa, watu wataingiwa woga, tutakosa taarifa muhimu. Mbona tunashuhudia kwenye baadhi ya vyombo ambavyo vinakuwa biased, matukio makubwa wanaacha kwa sababu ya woga. Kwa hiyo, tunakwenda kutengeneza sheria ambayo itaendelea kudidimiza vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba ni kwamba Serikali iko haja ya kuangalia upya jambo hili. Yapo mambo mengi ambayo tungeweza tukayafanyia kazi kwanza kabla ya kuja na muswada huu, zipo haki nyingi za watu za kupata taarifa, mngeangalia badala ya kujificha…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza sana Waziri wakati anawasilisha Muswada huu. Waziri amesema anaenda kuandika historia, nikubaliane nae anaenda kuandika historia ya kutengeneza Muswada ambao wadau hawakushirikishwa. Tumewahi kuona wapi? Tumejaribu kujifunza na kuangalia katika Mataifa mengine yenye sheria kama hii; wadau wanapewa nafasi, wadau wanapewa kipaumbele kwa maana ya kutoa mawazo yao na michango yao, lakini kwa Muswada huu tunakwenda kuupeleka kwa jinsi ambavyo Serikali imeamua, watekelezaji wa sheria hii wako kando. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iingie tu kwenye rekodi na ieleweke hivyo kwamba wadau waliomba waongezewe muda, ni kwa nini wadau wanataka muda? Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza tarehe 16/9/2016 wadau wakaomba watoe mawazo yao, wakafika kwenye Kamati, wakaomba waongezewe muda. Kwa nini wanataka muda? Kwa sababu tasnia hii ya habari ina wadau wengi wakiwemo waandishi wa habari ambao ndiyo watekelezaji wa Sheria hii. Tunazungumza hivi sasa tukiwa na redio zaidi ya 200 ziko vijijini, tunahitaji kupata michango yao badala ya kupata michango ya waandishi walioko mjini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wakaomba waongezewe muda, Muswada huu uje Bungeni hapa katika Bunge lijalo lakini waliongezewa siku kumi. Hii imekuwa novel ya kusoma kwa siku kumi? Hii ni Sheria ambayo kila mmoja alipaswa aje na mawazo. Utaweza kuona katika Muswada huu Waziri anatuambia kwamba una maslahi mapana ya waandishi. Yako wapi maslahi ya waandishi hapa? Tumeshuhudia waandishi wa habari wakipigwa, wakiuawa, wakimwagiwa tindikali, sheria hii inasema wapi kuhusu kuwalinda hawa waandishi wa habari wakiwa kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo, Waziri anasema kwamba anakwenda kutengeneza historia. Historia gani ambayo hakuna michango na mawazo ya hawa waandishi? Historia gani ambayo hakuna popote palipozungumza hata kima cha chini cha mwandishi wa habari alipwe nini, iko wapi? Tuseme basi Muswada huu unatetea kwa maana ya kuwa na sehemu ambayo inaonesha mwandishi wa habari alipwe kiasi gani, awe na mazingira gani ya kutekeleza kazi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu ya wadau ni nini? Hofu ya wadau Mheshimiwa Waziri ameandika historia ya peke yake. Katika kipindi cha mwaka mmoja ya Uwaziri wake, amekwenda kufunga magazeti, amefunga redio, hana mikono misafi na ndiyo maana waandishi wana hofu, wanataka wahakikishe kwamba Muswada huu wanausoma vizuri, wanatoka na majibu ambayo watajua ni nini hatma ya vyombo ambavyo ndivyo wanavyovitumikia na ndivyo vinavyowapa kula yao asubuhi na jioni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu nyingine ya wadau katika hili, ni kwa nini Serikali haikuona kwamba kuna haja ya kuwapa nafasi. Nimeshiriki kwenye hii Kamati, baadhi ya michango ya wadau ambayo niliiona ni kutoka kwa TWAWEZA na kutoka kwa TLS, halafu tunasema hii ni michango ya wadau. TLS anafahamu, TWAWEZA wanafahamu shida, adha ya waandishi wa habari ambao wanatembea kwa miguu barabarani wakitafuta habari? TWAWEZA wanayaelewa haya? Ungeniambia UTPC wanaelewa, ungeniambia TAMWA wanaelewa, ungeniambia MCT wanaelewa, ningeelewa, lakini TWAWEZA?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TWAWEZA wanafahamu a, b, c za uandishi wa habari? TWAWEZA wanajua shida waandishi wanayoipata? Kwa hiyo, tunakuja na mawazo kwamba TWAWEZA wametoa na TLS wametoa. Hii tunaifananaisha na kama, wao ni wadau walioalikwa tu kutoa mawazo yao lakini wadau halisi ambao walipaswa kuingia hapa hawakushirikishwa. Ni kama tuseme mtu unaandaa harusi waalikwa wanashiriki lakini bwana harusi na bibi harusi hawamo halafu unaita ni harusi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu unakwenda kumpa mamlaka Waziri ya kuamua ni nini ambacho waandishi wa habari wanataka waripoti, kwa nini? Kuna vipengele ambavyo vinasema kwamba Waziri ndiyo mwenye mamlaka ya kuangalia ni kitu gani kinaripotiwa kwa muktadha, kwa maslahi ya usalama wa Taifa, usalama wa Taifa ambao una sheria zake, ambazo zinafuatwa lakini Waziri ndiyo anasema kwamba yeye ndiye atakayeenda kupewa mamlaka ya kuhakikisha kwamba kila kinachoripotiwa yeye ana mamlaka ya kujua ni kitu gani ambacho kinaenda kuandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tumeona kwenye hotuba yake Mwenyekiti wa Kamati anasema mazingira mazuri yanayoenda kutengenezwa kwa waandishi wa habari ni pamoja na kuweka dressing code. Leo hii Taifa hili ambalo tunaona umuhimu wa vyombo vya habari tunahitaji kwenda kuwa na dressing code? Waandishi wa habari wamekuwa wakifanya kazi za utafiti, wanahitaji kuvaa nguo kufahamika wanafanya nini? Tunafikiri ni vitu ambavyo Serikali imejenga mikakati kuhakikisha wanaenda kudhibiti, kuhakikisha waandishi wa habari hawafanyi kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Bima ya Afya kwa waandishi wa habari tumeliona na sisi tunasema kwamba hilo halitoshi pekee kusema kwamba ndiyo maslahi ya waandishi wa habari. Tumeweza kuweka misingi gani ambayo itawabana hawa wamiliki wa vyombo vya habari kuwasaidia hawa waandishi wa habari kwa maana ya kuwalipa mishahara ambayo inaendana na kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kuna kipengele kingine kwamba Waziri ndiyo atakwenda kutengeneza kanuni ambazo zitakwenda kusaidia baada ya Sheria hii kutungwa. Tuliomba kwamba iwekwe wazi hapa tujue ni regulation zipi ambazo zinawekwa kwa sababu ya matamko mbalimbali ya Waziri ambayo amesikika akiyazungumza kwenye vyombo vya habari kwamba anataka uandishi wa habari lazima uanze na level ya degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Taifa gani ambalo lina sheria hizi ambalo limeweka kwamba kigezo cha mwandishi wa habari lazima awe na degree. Tumeona Mataifa mengi ambayo hata uchumi wake unaimarika, kuna level mbalimbali, kuna watu wa certificate, wapo watu wa diploma, wapo watu wa degree lakini wanatambulika kutokana na michango yao wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani tukizungumzia suala la kazi za udaktari, kuna madaktari wa AMO, kuna madaktari wa MD, kuna madaktari wenye masters lakini wote wanafanya kazi, lakini council ndiyo yenye mamlaka ya kuhakikisha kwamba wanatengenezaje madaraja ya hawa waandishi wa habari, lakini kuja na vigezo vya degree kama mbinu ya kuwagawa waandishi wa habari, leo hii wazee ambao wamefanya kazi iliyotukuka hasa ya kupigania uhuru wa Taifa hili basi wasionekane kama nao ni waandishi wa habari kisa hawana degree ya uandishi wa habari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunataka Sheria iseme wazi kwamba ni kanuni zipi ambazo zinakwenda kutengenezwa kwa ajili ya kusimamia sheria hii. Kanuni ziwe wazi, zieleze kwamba mwandishi wa habari atakwenda kuwa ni mtu wa namna gani na sisi tunasema kwamba mwandishi wa habari awe ni mtu yeyote ambaye amemaliza form four, mtu yeyote ambaye amesoma certificate, advanced certificate ya uandishi wa habari, mtu ambaye hata ana diploma atambulike, hata ana degree atambulike kwa sababu vyuo hivi vilisajiliwa na NACTE, kwa maana hiyo Serikali inatambua ni vyuo ambavyo vinafanya kazi ya kuwatengeneza waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuja na mkakati wa kwamba sasa tunakwenda kukomesha kwa kuleta suala la degree katika uandishi wa habari, hii itafanya waandishi wengi wenye passion ya kufanya kazi hii kuhakikisha wanatoka kwenye hii na sijui; tunasema tuna mpango wa kuongeza ajira lakini tunaenda…
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.