Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza (18 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CHONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia machache juu ya Mpango huu wa Serikali ambao umeletwa mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Mheshimiwa Silinde kusema kwamba tunayo maneno mengi na mipango mingi lakini utekelezaji ndio umekuwa tatizo kubwa sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye gharama za uendeshaji wa miradi katika nchi yetu. Kwa muda karibu wa miaka miwili ndani ya Bunge hili tumekuwa tukiishauri Serikali kufanya marekebisho katika Sheria ya Manunuzi. Ukitazama tangu Naibu Waziri wa Fedha alipotusomea hapa mwelekeo lakini katika vitabu vyote hivi ambavyo vimeletwa na Waziri malalamiko yao na maoni yao yamegusa namna ya kudhibiti manunuzi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya tatizo kubwa ni Serikali kushindwa kuleta sheria hii ili tuirekebishe. Tumelalamika sana, Wabunge wamepiga kelele kuhusu namna sheria inavyosababisha ukiritimba na kuifanya Serikali miradi yake kuwa ya bei kubwa, miradi mingi inashindwa kukamilika na inayokamilika inakuwa na gharama ambazo zimeifanya Serikali iwe na madeni makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize ni lini sasa Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Manunuzi? Wakati mwingine nakuwa na wasiwasi kwamba mnashindwa kuleta sheria hii kwa sababu wako watu ndani ya Serikali ambao wananufaika na matumizi ya sheria hiyo. Mmeongelea suala la kudhibiti mtadhibitije kama sheria bado ni ileile. Kwa sababu sasa imekuwa ni kawaida ya Serikali manunuzi yake hayaendani na soko. Kalamu ambayo inauzwa kwa shilingi 200/= wao watainunua kwa shilingi 1000/=. Mradi wa Serikali ambao ungeweza kutekelezwa kwa shilingi 50,000,000/= unatekelezwa kwa shilingi 100,000,000/=. Naiomba Serikali ibadili sheria hii na iilete haraka sana ili tuweze kuifanyia marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu elimu. Yako mambo mengi na Waziri wa Elimu ametuambia kwamba atakuja na mipango hasa ya upande wa ukaguzi, lakini mimi naomba niongelee kuhusu mgawanyo sawia wa walimu katika nchi yetu. Unaweza kukuta kuna shule ambazo zina walimu 30 na shule nyingine zina walimu wawili.
Naomba nitolee mfano katika Jimbo la Bukoba Vijijini katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba. Halmashauri hii katika Mkoa wetu imekuwa ya mwisho kielimu, lakini hata shule ambayo imekuwa ya mwisho kiwilaya na kielimu inatoka katika Halmashauri hii inaitwa Kamkole ipo katika Kata ya Rukoma, ina wanafunzi 215 ina walimu wawili tu. Mwaka jana Halmashauri ya Wilaya iliomba walimu 280, haikupata mwalimu hata mmoja. Mwaka huu tunakwenda kuomba walimu 300, tunaomba Wizara ifikirie namna ya kupeleka walimu katika Halmashauri hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakumbuka siku za nyuma yuko Mkuu wa Wilaya ambaye amewahi kupiga baadhi ya walimu viboko 20 lakini tatizo hakuna walimu katika Halmashauri hii, wanapoomba walimu hamuwapi, shule ina walimu wawili au watatu. Kama Waziri wa Afya alivyotuambia kwamba anakwenda kufanya sensa ya kuona kwamba madaktari wanakwenda sawia hata katika mikoa ya pembezoni, tunaomba walimu nao wagawiwe kwa usawa siyo shule moja inakuwa na walimu 300 na hasa shule za mijini. Pamoja na kwamba tunatetea wanawake lakini na wanaume nao wawe wanaomba uhamisho kufuata wake zao ili waende katika shule hizo isiwe kila siku sisi wanawake ndiyo tunawafuata wanaume ifike mahali na ninyi mtufuate huko tuliko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maoni yangu kuhusu hii retention. Kamati ya Bajeti imekubaliana na mapendekezo ya Serikali. Inawezekana Serikali ina jambo ililoliona labda kuna matumizi mabaya ya fedha hizo lakini naomba niwakumbushe. Mwaka 1972 wakati Serikali imefuta Local Government ikaleta utaratibu wa madaraka mikoani, baada ya miaka kumi Serikali ilishtuka kwamba imeondoa huduma kwa wananchi na ikarudisha Local Government. Hata hivyo, baada ya kurudisha Local Government, Serikali imekwenda kufuta vyanzo vya mapato ambavyo vilikuwa vinasaidia halmashauri hizi kuweza kujiendesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita mimi nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI, katika kupitisha bajeti, Wakuu wa Mikoa wote wamelia jinsi Serikali inavyoshindwa kurudisha ruzuku ya vyanzo hivi. Ukipitia bajeti ya mwaka jana, karibu mikoa yote Serikali ilishindwa kupeleka fedha mpaka wengine walipata asilimia 28 – 30, hii imesababishwa na Serikali Kuu kubeba pesa zote. Mimi nina wasiwasi na naungana na wale wanaosema Serikali inakwenda kuuwa mashirika haya. Serikali kwanza ituambie imeona mpaka ikaondoa retention? Hata ndani ya Halmashauri, kwa mfano, Idara ya Ardhi, vyanzo vyote vya mapato vinakwenda Wizarani lakini Wizara ya Ardhi imeshindwa kurudisha pesa hizo na unakuta halmashauri zinashindwa kupima viwanja kwa sababu hawana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii retention ina maana gani? Ina maana kwamba pesa yote itakusanywa Hazina na tujue hii Serikali ina wakora, kuna watu wengine ni wakora huko, wanaweza kutumia mwanya huu kuhakikisha kwamba hizi fedha hazirudishwi inavyotakiwa. Serikali itueleze, ina mpango upi sasa ambao utawezesha fedha hizi kutoka Makao Makuu Hazina kuzirudisha katika wilaya ikiwa ni pamoja na Halmashauri. Halmashauri zinalia na mmekwenda kuziua na zinakwenda kufa. Serikali ifikirie namna ya kurudisha baadhi ya vyanzo. Kama inashindwa kupeleka fedha za bajeti irudishe vyanzo vile ambavyo vilikuwa vinawezesha Halmashauri kuweza kupata mapato yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya chama chetu cha CHADEMA ya 2010 tulikuwa tumepanga kurudisha Serikali za Majimbo, CCM ikapiga kelele na kusema ni ukabila siyo ukabila, hii nchi ni kubwa. Ndiyo maana watu wanaiba mpaka CAG atambue wizi umetokea mahali fulani inakuwa imepita miaka mitano. Nchi hii ni kubwa, inahitaji chombo kingine hapa katikati ambacho kitahakikisha wananchi wanapata huduma zao na kudhibiti mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele ya kwanza imeshalia, naomba niongelee juu ya utawala bora. Nitaongelea Wilaya ya Kyerwa, mimi ni Mbunge wa Viti Maalum naruhusiwa kuongelea mkoa mzima. Utawala bora ni pamoja na mambo ambayo mmeona yanafanyika katika uchaguzi. Mtu anashinda kiti chake lakini anatangazwa ambaye hakushinda. Wasimamizi wa Uchaguzi ni Wakurugenzi, Mkurugenzi anatangaza matokeo halafu anapitia dirishani. Tume na ninyi mnafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachotaka kuwaambia haya mambo yanaweza kuwa ni kung‟ang‟ania kupata madaraka sawa lakini mnalea kizazi ambacho hakiwezi kuvumilia mambo haya. Kizazi cha sasa hivi hakina siasa za mwaka 1947, tunao watoto na vijana wapya. (Makofi)
MHE. CHONCHESTA L. RWAMLAZA: Msifikirie kung‟ang‟ania madaraka ni jambo jema. Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa CHADEMA ilipata Madiwani 13 wakati CCM ilipata…
MWENYEKITI: Ahsante, kwaheri.
MHE. CONCHESTA L. LWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. CONCESTTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuongea machache kutoa maoni yangu juu ya taarifa za Kamati ambazo zimetolewa leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC kwa hiyo nianze kwa kuunga mkono maamuzi na mapendekezo ambayo yametolewa na Kamati yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maneno mengi yameshasemwa lakini ni muhimu na sisi tuendelee kuyasema, tuyawekee uzito wake lakini na kuwekea msisitizo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako nilirudishe nyuma wakati Serikali imefuta Serikali za Mitaa mwaka 1972 na kuweka mfumo wa madaraka Mikoani. Serikali ilifanya hii decentralization lakini baadae Serikali iligundua kwamba ilishindwa kutoa huduma kwa wananchi. Kwasababu Serikali za Mitaa ni vyombo ambavyo viko pale kutoa huduma kwa watu wa ngazi ya chini, lakini pia vinatekeleza Sera ambazo zinaelekezwa na Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama wenzangu walivyosema, kama Halmashauri zitakwenda katika mwenendo huu tunakwenda kuziua na kuzifuta kama ilivyokuwa mwaka 1972. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mfumo wa ukaguzi katika Halmashauri. Wakaguzi wa Ndani hawana kasma, Wakaguzi wa Ndani wako chini ya Mkurugenzi. Katika ukaguzi wetu tumegundua Mkaguzi wa Ndani mmoja ambaye alijitokeza kujibu hoja za uhasibu wa Halmashauri. Sasa tukajiuliza, huyu ni auditor wa ndani lakini yeye amejitokeza kujibu hoja za mhasibu ambazo tumemuuliza, je, huyu anaweza kusimamia kweli ukaguzi katika Halmashauri yake?
Kwa hiyo tunachoishauri Serikali, ihakikishe inaimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili Halmashauri hizi na Wakurugenzi waweze kukaguliwa na hata wenyewe hawa ma-auditors wa ndani waweze kushauri Halmashauri zao katika mambo ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee Mfuko wa Wanawake na Vijana wa asilimia 10. Mfuko huu uko very sensitive, kila Mbunge anauhitaji, anahitaji kuona Halmashauri inatoa mchango wa asilimia tano kwa vijana na aslimia tano kwa wanawake ili waweze kuwa na shughuli za kufanya. Tuwaweke vijana wawe busy, wasiingie kwenye panya road, tuwaweke akina mama waweze kupata kazi za kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu katika ukaguzi wetu na kuhoji Halmashauri, kila Halmashauri ina deni kubwa la mifuko hii, lakini madeni hayo yamesababishwa na maagizo yanayotoka juu ambayo yanawapa deadline yaani yanawapa ultimatums ku-raise tengeneza madawati Halmashauri, katika miezi miwili tunaomba madawati yako tayari. Wananchi? Hawana pesa za kuchangia. Halmashauri ifanye nini? Kwa hiyo, wanachukua mafungu kutoka own sources, wanachukua mafungu kutoka katika development wanatengeneza madawati na kwa kweli kama walivyosema wenzangu imekuwa ni mwanya wa kuiba hela za Serikali. Ukiwauliza wote wanakuambia kwamba sisi tumechukua hizi pesa kwa sababu tuliambiwa tutengeneze madawati katika miezi miwili, tumetengeneza maabara katika miezi miwili, kwa hiyo, matokeo yake pesa zinapotea bure.
Mheshimwa Naibu Spika, sasa wasiwasi wangu, hii mifuko, Halmashauri zote zinadaiwa mamilioni ya pesa, je, wana uwezo wa kulipa madeni haya? Kwa sababu kama walivyochangia wenzangu Halmashauri hizi zimekatwa mikono, haziwezi kuwa na pesa, Serikali Kuu imechukua vyanzo vyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Katika bajeti ya mwaka jana kama mnakumbuka katika kitabu cha Waziri wa Ardhi, alionesha kwamba walikusanya shilingi bilioni 54 lakini walipeleka bilioni nne tu katika Halmashauri karibu 138. Mkoa wangu wa Kagera tulipewa shilingi milioni 138, Halmashauri ya Ngara ilipewa milioni nne kitu kama hicho. Sasa unaweza kuona kama wameweza kukusanya pesa zikaenda kule juu hazirudi, hizi kwa mfano za kodi ya majengo zitarudi? Nina wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana katika kitabu chetu tumependekeza kwamba iundwe sheria ya mfuko huu. Hakuna sheria ni agizo sawa, lakini hata sheria yenyewe itazame ni jinsi gani mfumo huu unaweza kuwekwa na unaweeza kutumika. Kwa mfano, tumegundua kwamba hata makundi mengine yanayopewa mikopo ni hewa na yanayopewa hayarejeshi, kwa hiyo hiyo, mifuko haiwezi kurotate, hairudishi pesa tena. Kwa hiyo, mimi nashauri kwamba Serikali iziangalie hizi Halmashauri upya ziweze kupata makusanyo na ziweze kukata 5% kwa ajili ya vijana na 5% kwa ajili ya wanawake vinginevyo, itabaki katika hoja za ukaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Na namwomba Waziri mwende nalo hili kwamba, tuangalie upya namna ya kuweka mfuko huu, ili tuweze ku-materialize yaani uweze kuona kama unaweza kuleta impact kwa wanawake vinginevyo Halmashauri zitashindwa, mtazituhumu hapa na zitashindwa kabisa kukusanya hizi fedha na hawatakuwa na uwezo wa kuwasaidia wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye hoja ya Serikali kutokupeleka fedha. Serikali haipeleki fedha, lakini ziko Halmashauri nyingine zinapelekewa fedha nyingi nje ya bajeti. Kwa mfano katika kukagua tuligundua katika Halmashauri ya Mpanda katika mwaka wa fedha 2014/2015 walikuwa wametenga bajeti ya shilingi milioni 432 lakini wakapewa fedha shilingi milioni 303.8 ya ziada. Kwa hiyo, wakawa na fedha karibu milioni mia saba na kitu. Ukiuliza Hazina kwa nini mmewapa fedha ya ziada ambayo haipo kwenye bajeti? Hawana majibu, ukiuliza Mkurugenzi, hana majibu, tuonyeshe mmetumiaje hawana majibu. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba, inawezekana kuna chain ya wizi kuanzia Hazina, TAMISEMI mpaka kwa Mkurugenzi. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ilijue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kama fedha zinaweza kutolewa za ziada basi CAG apewe maelezo na hata Kamati ipewe maelezo. Kwa hiyo, kuna mambo kama hayo ambayo yanafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uteuzi wa wakurugenzi, watu wamesema sana. Si wote ni baadhi, lakini naomba niseme hapa kuna Chuo cha Hombolo. Serikali za Mitaa zina chuo cha kuweza kufundisha watu wake, sasa imekuwaje chuo hiki hakiwezi kutumika kufundisha watu? Kiko pale purposely kwa ajili ya kufundisha namna ya kuendesha Serikali za Mitaa, ni kwa nini watu hawapewi mafunzo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mafunzo pia yatolewe kwa Madiwani. Madiwani wetu wanakuja hata sisi hapa Wabunge, kuna wapya, kuna wa zamani, mnatuweka kwenye semina tunajifunza. Hata Madiwani wafundishwe ili waweze kukabiliana na executive. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakukaribisha siku moja uje kwenye kamati yetu huko ya LAAC, yako ma-book pale, yanakuja wale wataalamu wanakuandikia, book linalingana hivi, yaani unalinganisha biblia tatu, nne, tano unalitazama mpaka unaanza kujiuliza nianzie wapi? Na watu hawa wanafanya purposely ili ukienda pale utazametazame macho tu uwe kama buibui usielewe hata cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtindo huo ndio ulio ndani ya Halmashauri mimi nimekuwa diwani tangu mwaka 2000, najua, wanaleta ma-book yaani madiwani wanaanza kuyatazama up side-down, na wale wanakuwa ile executive ina hawasomi. Unakuta Mkurugenzi ana degree, Bwana Mipango ana ma-degree, wengine wana CPA, wengine wana nini; halafu Madiwani wanaweka pale wanachanganya changanya. Madiwani wapewe mafunzo. Halafu wanakuta wameandika kwa kimombo bwana. Sasa wewe unaleta taarifa hii kwa madiwani unaandika kimombo wakati hata sheria ya uchaguzi inasema mtu ujue kusoma na kuandika. How? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachoshauri Serikali isitazame haya mambo ya kubana matumizi haya, mnabanabana kitu gani? Na mnabana nini, hamjapata chochote, kwa sababu sisi LAAC tunafanya paper work. Huwezi kufanya paper work kwa hizi Kamati, wakati una watu huku wanajua kuchodoa, yaani ninyi hamuwajui watu wa Halmashauri. Huwezi kufanya paper work, wanakuja wameandika vitabu vizuri kabisa, wanapewa hata zile ripoti za CAG zile za ukaguzi, hati safi. Hati safi unakuta mtu amelamba shilingi milioni 300, shilingi milioni 500, utawauliza hata CAG, mnawapaje hati safi hawa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kuona kinachotokea. Kwa hiyo, tunaomba na wale madiwani wapewe mafunzo. Serikali isiseme kubana matumizi. Watanzania wana tabia moja, wana tabia ya kufanya mambo kimya kimya. Wanaweza kukubali kutii, bila kuwa na utii. Kwa hiyo Serikali hii itaendelea kuibiwa, haki ya Mungu mpaka mtakoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu gani? Kwa sababu huku chini sisi tunafaya pepar work. Tunashinda mle ndani ya kamati, kuanzia saa moja mpaka saa tatu usiku hatuna hata chakula, Naibu Spika, tupe na chai basi, maji moja, tunakagua vitabu vile mpaka tunachanganyikiwa lakini uko wizi mkubwa, na sisi tunawaambia haya kwa heri mwende, hatuendi kukagua, what do you expect? Mnachotegemea ni nini? Mtaibiwa yaani hata huku kutumbuana hakutakuwa na faida yoyote. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Halmashauri naomba msiziue. Kama mkiendelea na mtindo huu wa kuwanyima fedha, mtindo huu wa kuhakikisha kwamba makusanyo yote mmewanyanganya, halafu ninyi mnawaambia kwamba jamani hamkusanyi mapato, wanakusanya wapi? Hakuna mapato ndani ya Halmashauri. Hakuna 5% za wananwake, hakuna 5% za vijana. Sana sana mtakuwa mnafukuza wakurugenzi mnatumbua na anayekuja mnatumbua wote mtawatumbua kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kuchangia hii 5%.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze na Mfuko wa Barabara. Halmashauri zetu zinapokea fedha kidogo kwa ajili ya matengenezo ya barabara, kwa sababu fedha hizo ni kidogo, hawawezi kutengeneza barabara ambazo zina viwango kama zile zinazotengenezwa na TANROAD. Uwiano wa utoaji wa pesa za Mfuko wa Barabara kwa kila shilingi laki moja inayotoka kwa ajili ya Mfuko wa Barabara, Halmashauri inapewa sh. 30,000 which is 30 percent, kwa hiyo unaweza kuona Halmashauri wakipewa fedha, ni zile fedha ambazo zinaweza kufanya grading peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawawezi kutengeneza mitaro, hawawezi kuweka karavati, kwa hiyo mwaka hadi mwaka tutabaki kulaumu hizo Halmashauri. Serikali imekuwa ngumu kubadili sheria hii ili kusudi Halmashauri ziweze kupata fedha angalau hata asilimia 40 waweze kutengeneza barabara ambazo zinawiana, kwa kuangalia jinsi walivyotueleza ukisoma katika hotuba ya Waziri, anasema kuna zaidi ya barabara mtandao wa kilomita laki moja na kitu na nafikiri inawezekana ni zaidi ya hizo, maana yake sina uhakika wamefanya lini research.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya kuongeza maeneo mapya ya utawala, hizi barabara za Halmashauri zina mitandao mikubwa ambayo kwa kweli Serikali inapaswa ifikirie namna ya kuwapa Halmashauri fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia hili jedwali ambalo tumepewa na Waziri, nitoe mfano tu wa Mkoa wa Kagera peke yake. Mwaka 2014/2015, Mkoa wa Kagera ulikuwa umetengewa bilioni 9.1, lakini ulipewa bilioni 3.9, mwaka 2015/2016, Mkoa wetu tulitengewa bilioni 6.9 lakini tulipewa milioni 366, kwa hiyo ukichukua pesa zote hizo tulizopewa katika miaka hii miwili, tumepewa 4.2 bilioni. Unaweza ukaona ni jinsi gani, pesa zinavyokwenda katika Halmashauri na katika Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ifikirie namna ya kupeleka pesa ili tuweze kusaidia hizi Halmashauri, ziweze kutengeneza barabara kwa kuzingatia kwamba watu wote wako kule katika Halmashauri na huduma zinahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili naomba niongelee, ni kuhusu elimu. Ukurasa wa 24 wa kitabu cha Waziri, ameongelea kuhusu mambo ya elimu, mipango ni mizuri, lakini naomba nijielekeze katika hizi shule maalum ambazo zinafundisha watoto wenye matatizo, walemavu wa ngozi, walemavu wa viungo, pamoja na wale wasioona. Naomba nitoe mfano wa shule ambayo iko katika Mkoa wa Kagera inaitwa Ngeza Mseto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 8 Machi ilikuwa ni Siku ya Wanawake Duniani, Chama chetu cha CHADEMA kilisherehekea sherehe hiyo kwa kwenda kutoa huduma katika sehemu mbalimbali ikiwemo shule hiyo. Tulichokikuta pale kuna watoto walemavu wa ngozi, kuna wale walemavu wa viungo, lakini pia kuna watoto wasioona. Tulichokikuta pale, wale wamama walioenda pale, walikuta vitanda vimejaa vinyesi, watoto hawaoni wale, wanalalia vinyesi, yaani mizinga ya vinyesi imejaa kwenye vitanda vyao, Walimu wapo, Matroni yupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, worse still, nakumbuka mwaka 2000 nilikuwa Diwani, wakati ule Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuwa Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI, alifika kwenye shule hii na kwa kweli aliomba Hazina, Hazina wakawa wanatoa fedha extra money milioni 60 kila mwaka, yaani milioni 15 kila baada ya kota moja. Je, naomba niulize TAMISEMI na nimuulize Waziri wa Elimu, pesa hizo bado zinakwenda na kama zinakwenda zinafanya nini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchungu mkubwa kabisa wale watoto wanavaa mpaka lisani zinatazama huko hawana mtu wa kuwaambia au kuwavisha, mabweni yao yote yamezungukwa na vinyesi, uchafu, wale watoto wanaishi kama wanyama. Ninyi mmetamka katika kitabu hiki kwamba mtahakikisha kwamba watoto wenye mahitaji maalum watapewa elimu na wataangaliwa afya zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli shule ya Ngeza Mseto iko Manispaa ya Bukoba, tunaomba Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri nendeni mkaiangalie hiyo shule, mhakikishe kwamba inapewa pesa. Siyo hiyo tu, hata vile vituo vingine ambavyo vina watoto ambao wana matatizo ya namna hiyo Serikali iweke mkono wake. Halmashauri peke yake ya Manispaa ya Bukoba haiwezi kabisa ku-manage shule hii, kwa sababu shule inabeba watoto wa Mkoa mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu taarifa ya Mdhibiti, mimi niko kwenye Kamati ya LAAC na hapa wameongelea kuhusu asilimia 20 ya fedha za Serikali ambazo zinazotoka kama ruzuku ambazo zinapaswa kwenda katika Vijiji, zingeweza kulipa mishahara ya Wenyeviti wa Vijiji au posho zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tulichogundua Kamati yetu imepitia Halmashauri 30, Halmashauri zote 30 zimeshindwa kupeleka hiyo asilimia 10, hizo Halmashauri zina jeuri! Zile pesa siyo mapato ya ndani ya Halmashauri, zile fedha zinatokana na ruzuku ya Serikali ambayo ni fidia ya vile vyanzo vya mapato, lakini Halmashauri hazipeleki hizo fedha na zikipeleka zinapeleka kwa asilimia kidogo. Mheshimiwa Simbachawene anajua na nafikiri Mheshimiwa Jafo anaelewa, waliona maoni yetu ni kwamba hizi fedha haziendi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ihakikishe na kusimamia pesa hizi ziwe zinakwenda na ninachotaka kuwaambia hata Vijiji vyenyewe havijui, havina taarifa kuhusu fedha hizo, inawezekana hata zikipelekwa zinaweza kulambwa na Wenyeviti wa Vijiji pale au na Watendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema juu ya utawala bora. Nisimalize bila kuongelea kuhusu haya mambo mnayosema hapa kuhusu TBC na nashangaa sana, wenzangu CCM msije mkafikiri kurudi ndani ya Bunge hili, mjitazame ninyi huko nyote kuna watu hawakurudi almost 60 percent kwani matangazo hayakuwepo? Kurudi au kutorudi haina maana kwamba wasiangalie matangazo yao (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii inaendeshwa kwa demokrasia ya uwakilishi, ndiyo maana kuna vyombo kama Bunge, Bunge siyo mali ya Serikali, Bunge ni mali ya watu, ni chombo cha watu na ukitazama dunia nzima huwa kunakuwa na mvutano mkubwa kati ya Serikali na Bunge. Serikali hailipendi Bunge, kwa sababu Wabunge mnaisema Serikali, mnaisahihisha, mnafichua, kwa hiyo itafanya kila mbinu kuhakikisha kwamba hili Bunge linadhoofika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii, viongozi wote nawaambia, Naibu Spika upo hapo na Spika, hebu igeni hayo Mabunge ya nyuma yalikuwa yanafanya kazi gani, igeni hata nyuma, mnakumbuka Wabunge mliokuwepo, ilikuwa ni kazi kubwa sana kuanzisha Kamati ya Bajeti ndani ya Bunge hili, tunamshukuru Madam Spika pamoja na kwamba tulikuwa tunamkoa makwenzi humu, lakini yule Mama alisimama imara kuhakikisha Kamati ya Bajeti inaanzishwa. Serikali ilikuwa haitaki Kamati ya Bajeti lakini Bunge lilisimama imara,na Spika alisimama imara na Naibu wake. Kwa hiyo na ninyi msikubali Serikali kutuyumbisha, tutashindwa kusimamia watu.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, mtashindwa kuwa na legacy kwa sababu mkimaliza miaka yenu mitano au kumi watu watawakumbuka kwa sababu ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana haya mambo ya watu kusikia taarifa ni namna ya kuwaelimisha Watanzania. Katika kitabu hiki, wametuambia kwamba kuna watoto zaidi ya laki mbili na sitini na kitu, hawakuweza kufanya mtihani wa darasa la saba, tunawa-damp huko ndani na inawezekana hawawezi kujiendeleza tena. Watu wanapaswa kupata elimu kupitia majarida, ndivyo wanavyoweza kujua namna Serikali yao inavyoendeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawaambia watoe kodi, watajuaje maana ya kodi, watajuaje zinasimamiwaje hizo kodi, mnawarudisha Watanzania katika ujima. Hatuwezi nchi hii kwenda hivyo, mngefanya miaka ya 60, sasa hivi Watanzania ni waelewa, wanataka kusikiliza Bunge lao, wanataka kujifunza na tuwasaidie kujifunza, tusiwadumaze Watanzania kwa kuwarudisha katika kuvaa ngozi, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, lakini nakuomba tena ninyi ni wasomi…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CONCHESTA L. LWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache kuhusu hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongea kuhusu halmashauri kuweza kupima viwanja na kupanga miji. Ni kweli halmashauri zimepewa jukumu la kupanga miji, kupima mashamba, kupima viwanja, kuweka makazi kwa ustawi wa watu wao, lakini kwa muda mrefu halmashauri hizi nchini zimeshindwa kufanya kazi hii kwa sababu ya ukosefu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nyuma halmashauri zilikuwa zina retain pesa yake ile asilimia 30 inayotokana na kodi za ardhi na hivyo wanapata uwezo wa kufanya kazi ya kupima viwanja. Baada ya kuwaondolea mapato hayo kwenda katika Wizara ya Ardhi, fedha hizi hazirudi na kama zinarudi zimechelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nafuatilia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa tisa umeweza kutuonyesha mapato ambayo yametokana na kodi za ardhi. Ametuambia kwamba wameweza kukusanya bilioni 54.35, lakini tukienda ukurasa wa 83 unaotuonyesha mgao uliorudi katika halmashauri wa asilimia 30 yaani utaona maajabu, asilimia 54 bilioni zimekusanywa, lakini halmashauri 138 zimepata bilioni nne nukta nne. Kwa hiyo, naweza kuangalia uwiano na nimekwenda mbali nikaangalia Mkoa wa Kagera ambao ni mkoa wangu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mgao wa mwaka huo tumeweza kupata milioni 113 na point, lakini unaweza kuona katika trend hii ni namna gani halmashauri zinaweza kupata fedha ya kuweza kupima viwanja. Siyo hivyo, nashauri Serikali itazame upya hata hii asilimia 30 ni sawa hata kwenye barabara halmashauri zinapewa hela ndogo, lakini kama ni sheria ibadilishwe ili hawa watu waweze kupata angalau hata asilimia 40 hata kama ni nusu kwa nusu kwa sababu kazi nyingi ziko ndani ya Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupima viwanja ndani ya halmashauri kuendana na ubia hata kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Wizara inafikiria au tayari imeanza kufanya ubia. Halmashauri nyingi zinakopa pesa kwa ubia tuseme na UTT, lakini fedha hizo ambazo mara nyingi halmashauri wanakopa nani anazisimia. Kumekuwa na malalamiko katika hali hii ya Wizara ya Ardhi, haieleweki maana yake inasimamiwa na TAMISEMI, Wizara ya Ardhi inasimamia vyake, kwa hiyo, matokeo tunakuwa na mkanganyika mkubwa. Halmashauri ziko TAMISEMI zinakwenda kukopa pesa, pesa hiyo inatumika vibaya, nani anasimamia mikopo hiyo? Wizara ya Ardhi inawekaje mikono yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, naweza kukupa mfano katika halmashauri yetu ya Manispaa ya Bukoba, kulizuka mgogoro mkubwa nafikiri mlihusika wanakopa pesa za kulipa fidia, lakini fidia zinazolipwa wanalipwa wale watu ambao wana ardhi na hata CAG alienda kukagua akaona kitu kama hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI tulienda kuona hivyo hata Lindi imefanyika hivyo, kwa hiyo fedha zinakopwa. Je, nani kati ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ambao wanaweza kusimamia mikopo hii ili fedha zitumike kadri inavyotakiwa. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie hili maana yake TAMISEMI wanasema wao mikopo ipitie kwao, Wizara ya Ardhi ni vipi, kwa hiyo, naona kuna mkanganyiko hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwenye kodi ya majengo. Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani upande wa ardhi amejaribu kusema, yeye anafikiria na sisi kambi kwamba inawezekana mnapenda kutuchonganisha na hizi halmashauri zetu ambazo tunasimamia kama upinzani lakini siyo hivyo. Kwa mfano, tuchukue Dodoma hapa hii halmashauri ni ya Chama cha Mapinduzi, mnafikiri mnaondoa majengo hii manispaa itajiendesha namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri msipeleke ushuru au kodi ya majengo kwa Serikali Kuu. Miaka miwili ya mwisho kwenye Bunge nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI tumekwenda pale Dar es Salaam tuliona jinsi TRA walivyoshindwa kukusanya kodi ya majengo walikuwa wanafanya uthamini wa upendeleo yaani yule mwenye kajumba kadogo ndiyo anawekewa fedha nyingi nani atafanya uthamini ili kwa kweli kupata hali halisi ya mapato ya majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA walishindwa na kama walishindwa kipindi hiki mimi sioni sababu, mnakwenda kuua halmashauri hizi hata za kwenu ambazo sio za upinzani peke yake zote mtakwenda kuziua. Kwa hiyo, mwangalie kwa makini kwamba kodi za majengo zirudishwe, halmashauri ziweze kujiendesha kama kweli mnakwenda kufanya D by D na kwamba kweli hapa Halmashauri zifanye nini ziweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye wawekezaji, Wabunge wengi sana wamelalamika kuhusu wawekezaji lakini wawekezaji hawa wako hata wanasiasa ambao nao wanakwenda kwa ulaghai wao, wanakwenda kuhodhi ardhi kubwa katika maeneo ya halmashauri zao. Mfano katika Mkoa wa Kagera tuna mgogoro mkubwa katika Wilaya ya Muleba, mgogoro huo nina uhakika uko mezani kwa Mheshimiwa Waziri, kama haupo nina documents hapa akihijtaji kama hana nitampa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Kitene, Kata ya Kasharunga uko mgogoro kati ya kijiji na aliyekuwa Waziri wa zamani marehemu Edward Barongo. Mwaka 1990 aliomba kijiji kimpe ardhi eka 2000 sasa hivi ana eka zaidi ya 11,000. Tuje kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi sijui nimtaje jina, aliyemfuata huko nyuma, Mheshimiwa Waziri anamjua. Yeye kwenye kata hiyo hiyo katika Kijiji cha Kamyora aliomba ardhi eka 1098 sasa hivi anahodhi ardhi zaidi ya eka 4000, kwa hiyo, uko mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namtaja si Profesa Tibaijuka ni dada yangu si kwamba namsema ndani ya Bunge, lakini nakataa hii tabia ya kila kitu changu, kila kitu changu, hapana. Ukiwa kiongozi wakati mwingine na wewe uwaachie wengine. Kama ni kiongozi huwezi kuhodhi ardhi, watu wanakuja kukodi kwako au watu hawawezi kufanya nini, ni tabia mbaya ambayo lazima tuikemee. Hatujasema kwamba kiongozi wa siasa hawezi kumiliki lakini, naomba tumiliki kwa ustaarabu, tumiliki ili tuwaachie na wenzetu wale ambao tunawaongoza, ndiyo hoja yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachomwomba Mheshimiwa Waziri, mgogoro huu tunaomba waende wapime upya hiyo ardhi ili kusudi kama mtu aliomba eka 1098 abaki na hizo, ili zile zinazobaki wananchi wapate maeneo ya kutumia. Hivyo hivyo katika kile Kijiji cha Kitene, japokuwa marehemu Edward Barongo, alishafariki, Mungu amweke mahali pema, lakini ana watoto wake. Kwa hiyo, kama aliweza kuomba eka 2000, kwa nini ahodhi eka 11,000? Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri aende kwa kutumia vyombo vyake wakapime upya hiyo ardhi ili haki iweze kutendeka na migogoro hii iweze kwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nimalizie kuhusu wataalam wa ardhi ni kweli mna vyuo lakini vyuo hivi wataalam hawatoshi. Nimegundua kwamba inawezekana watu hawaoni maana ya kwenda shule kujifunza haya mambo ya ardhi. Mwendeshe kampeni maalum, vijana wetu waweze kuona kwamba wanastahili kwenda kusoma mafunzo haya na muwahakikishie ajira ili kusudi vijana wetu wa Kitanzania waende kwenye vyuo hivi, wasome wapate utaalam ili muweze kuajiri wataalam wengi katika halmashauri zetu. Kusema ukweli halmashauri hazina wapimana hazina wachora ramani. Kwa hiyo, tunaomba kwa hayo machache muweze kutangaza watu waende wasome na waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache juu ya hoja hizi za taarifa za Kamati, Kamati ya Katiba pamoja na TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na taarifa ya Kamati ya Katiba. Napenda tu kuongelea kuhusu utawala bora na nitajielekeza katika chaguzi zinazoendelea katika nchi yetu. Kuchagua viongozi na uchaguzi ukiwa huru na haki ni sehemu mojawapo ya kupanga viongozi na njia mojawapo ya kulea demokrasia katika nchi yoyote iliyopo duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, magomvi mengi ambayo yanatokea katika nchi tunazozisikia duniani zilizo nyingi inatokana na uchaguzi usio huru na haki na dhuluma zinazotokea katika uchaguzi, manyanyaso yanayotokana na uchaguzi, wakati mwingine kulazimika kutangaza matokeo ambayo siyo halali na hufanya wananchi wachukie na baadaye wanaamua kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu nimeshiriki chaguzi hizi za juzi ambazo zimemalizika za Madiwani. Tulikuwa na Kata moja tu katika mkoa wetu, Kata ya Kimwani na nilishiriki kikamilifu mpaka mwisho. Mambo niliyoyaona napenda niyaseme hapa, kwamba sasa hivi uchaguzi katika nchi yetu umegeuka, Jeshi la Polisi limekuwa Chama cha Siasa na wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matendo niliyoyaona, bunduki, mabomu na vitisho ni dhahiri kwamba Watanzania hawawezi kuingia katika uchaguzi wakijiamini na matokeo ninayoyaona watu watakuja kuchoka na haya mambo ambayo yanafanywa na Jeshi la Polisi. Ukiisoma vizuri, mimi hakuna mahali ambapo nimeona katika Sheria ya Uchaguzi ambapo Askari wanahusika kwenda na mabomu, ninachojua wanakwenda kulinda vituo, wako Mgambo, wako Polisi, wanakwenda kulinda vituo. Kipindi hiki nimeshuhudia Polisi wanakuja na mabomu wanazuia wananchi kutoka vijijini kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako hapa vijana wa bodaboda ambao unakuta wakati mwingine wale wapigakura wanatoka mbali mno na vituo, kutokana na jiografia mbalimbali jinsi nchi yetu ilivyo. Mtu analipa bodaboda kwenda kupiga kura Polisi wanamzuia njiani yule bodaboda kumpeleka huyo mtu kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo machafu ambayo nimeyaona na kwa kweli sisi Waheshimiwa Wabunge tunapaswa kukemea mambo haya. Uchaguzi ni jambo huru, uchaguzi ni watu wanakwenda kuchagua viongozi wao, tunajua katika nchi yetu kwamba tunakwenda kwa mfumo wa Vyama Vingi, ni lazima vyama vifanye ushindani na hata kiongozi atakayepatikana ajue kwamba hicho cheo amekifanyia kazi. Hakuna sababu ya kufikishana tunakofikishana, nina wasiwasi kwamba sasa kadri tunavyokwenda tunalea vijana wetu katika kuleta chuki na baadaye huko mbele yanaweza kutokea mambo ambayo tunayaona katika nchi hizi za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshuhudia Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, ma-OCD, yaani kwenye Kata moja tu yenye wapigakura 8,000, lakini Serikali nzima ipo pale na watu wakishasikia kwamba Mkuu wa Mkoa yuko pale, Mkuu wa Wilaya yuko pale, kuna watu wengine hawakuzoea hayo na Watanzania walio wengi wako tofauti huwezi ukalinganisha na Wakenya, hawapendi mambo ya ugomvi. Kwa hiyo, unapokwenda kuwanyanyasa watu mwishowe wanaona hawana haja ya kwenda kupiga kura, matokeo yake watu wanashindwa kupata haki yao. Naomba Serikali iyatazame na hata Tume ya Uchaguzi iyatazame ili tuweze kupata viongozi wetu wazuri na tuendelee kulea demokrasia katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kauli ambazo zinatolewa na viongozi wa juu ambazo mimi naziita kama kauli za mzaha, zinaweza kutolewa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya, lakini zinapotolewa na viongozi wetu wa juu kwa kweli zinashangaza, siwezi kusema zinatisha au zinashangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Mkuu wa Nchi alipotembelea Mkoa wa Kagera na mnajua Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tetemeko, katika mkutano huo alikuwepo Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Wilfred Lwakatare ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini, alipewa nafasi ya kuongea na nafasi hiyo aliitumia kutoa mawazo kwa niaba ya wananchi, mawazo aliyoyatoa ndiyo mawazo tunayopaswa kutoa sisi Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotoa mawazo lazima Serikali ione kwamba huyu mtu ni mwakilishi wa wananchi, aliiomba Serikali na alishasema hata ndani ya Bunge hili kwamba tungependa katika Mkoa wa Kagera, tunajua hamuwezi kujengea watu wote, lakini Serikali inaweza ikatoa ruzuku katika viwanda vya mabati, viwanda vya nondo na viwanda vya saruji ili wananchi wa kule waweze kupata vifaa kwa bei ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo siyo la ajabu, wakati Mamlaka ya Kuuendeleza Mji wa Dodoma (CDA) enzi zile za Awamu ya Kwanza, jambo hili limewahi kutokea, vifaa vilijengwa na ikapigwa chata kuonesha kwamba ni ofa ya kuja kutengeneza Mji wa hapa Dodoma. Kitu hicho kinaweza kufanyika hata Mkoa wa Kagera na hata mahali pengine ambapo watu wanaathirika namna hiyo. Majibu yaliyotolewa na viongozi wa juu – maana yake hatuwezi kutamka majina, ukitamka hapa utakutwa hapo mlangoni, niseme Serikali, nikitamka hapa Askari wanaweza kunisubiria hapo maana yake na wenyewe mmeshawafanya wamekuwa wanasiasa, alisema anamwambia Mheshimiwa Lwakatare akajenge kiwanda!
Waheshimiwa Wabunge ninyi mtajenga viwanda? Mimi nimekua, sasa hivi nina umri mkubwa wa kutosha tumejifunza kuhusu madini ya tin yaliyopo Kyerwa Karagwe tangu nikiwa mtoto wa miaka nane tu niko darasa la tatu, sijawahi kuona Mbunge ambaye anajenga kiwanda pale na wamekuwepo Wabunge mbalimbali pale. Kwa hiyo, kiongozi wa nchi anapotamka maneno ya namna hii, mimi nayaita ni maneno ya mzaha lakini pia inatonesha vidonda vya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema Mheshimiwa Mbunge akileta mawazo, hata kama anatoka opposition alichaguliwa! huwezi kumwambia basi nenda kajenge kiwanda hata mimi nitakusaidia, Mheshimiwa Lwakatare hela ya kujenga kiwanda ataitoa wapi, wengine wananiambaia eti yeye alijenga wapi, Chato hakuna kiwanda cha mabati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya, hatuwezi kuacha kusema tutakuwa waoga mpaka lini? Maana yake Rais wa Nchi au Kiongozi Mkuu wa Nchi au hata kama ni Waziri ni dhamana anawakilisha watu wake na Mkoa wa Kagera hatupendi sana kuomba omba na mara nyingi hamleti msaada kule, miaka nenda rudi hamjatuletea misaada. Tuna uwezo wa kujitegemea, lakini hii imetokea na tetemeko tunajua siyo la Chama, ni maafa ya nchi lakini wananchi hawakupewa kauli za kuwastahi waweze kukaa vizuri, wakitulizwa wanajua kwamba Rais wao amewaambia maneno mazuri. Kwa hiyo, ningependa Viongozi kauli hizi sizifurahii na watu wengine katika Mkoa wa Kagera kusema ukweli hawakufurahishwa na kauli hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kuongelea kuhusu suala la TAMISEMI kidogo, labda niongelee kuhusu elimu tu. Kwamba elimu ni bure sawa, inatolewa au labda ni ya malipo lakini niongelee Bukoba Vijijini tu ambako nafanyia kazi na Mheshimiwa Rweikiza nafikiri na yeye ataniunga mkono pale. Mnakumbuka huku nyuma kuna Mkuu wa Wilaya moja anaitwa Mnari, amewahi kuwapiga Walimu wa Bukoba Vijijini viboko. Pamoja na kuwapiga au asiwapige, mazingira ya kule siyo mazuri na pia hakuna Walimu. Katika kipindi cha bajeti hapa niliomba kwamba mtusaidie Walimu Bukoba Vijijini. Mwaka huu tumepewa zawadi ya Kinyago. Pale Mkoani wanatoa vikaragosi vile, tumepewa hicho, tunaomba Mheshimiwa Simbachawene atusaidie, atupe Walimu Bukoba Vijijini. Hilo ndilo ombi langu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo katika hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nagawana muda Mheshimiwa Heche basi nitachangia point moja tu kuhusu Mfuko wa Wanawake na Vijana wa asilimia 10 ambayo inapaswa kukatwa katika mapato ya own source ya Halamashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya LAAC tumeona kwamba huu Mfuko una umuhimu wake na kwa ujumla wake unaweza ukachochea maendeleo ya vijana na wanawake pale ambapo ukitumika kwa hali inayostahili ili hawa vijana na wanawake waweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotoka own sources ya Halmashauri ni kodi za wananchi. Utaratibu wa kuzitoa kama mikopo kwa vijana na wanawake haueleweki, walengwa ambao wanastahili kupata mikopo hii wengine hawapati kwa sababu gani. Hii ni kwa sababu tumegundua kwamba hata vikundi vingine ambavyo vinapewa hiyo pesa vinakuwa ni vikundi hewa, lakini katika Halmashauri nyingi hakuna hata zile Kamati ambazo zinapaswa kukaa na kutoa pesa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kushangaza kuna baadhi ya Halmashauri hata Wakurugenzi wengine hawajui component ni watu gani ambao wanapaswa kuwa kwenye Kamati hiyo. Kuna Mkugenzi mmoja alisema kwamba Mbunge ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ilhali Wakurugenzi ndio Wajumbe, kwa hiyo mnaweza kuona ni namna gani mifuko hii inavyotekelezwa bila hata Wakurugenzi kujali kinachoendelea katika Halmashauri zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utaratibu wa kusimamia urejeshwaji wa pesa hiyo, hizi pesa tumekuwa tukisimamia kwa karibu Kamati zote, Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya LAAC tunasimamia kuhakikisha Halmashauri wanapeleka pesa ya asilimia tano kwa wanawake na asilimia tano kwa vijana katika akaunti zao ili waweze kukopeshwa. Ninachotaka kusema ni kwamba pesa hizi hazirejeshwi, huu mfuko unakwenda kisiasa kabisa, ni kama upo upo tu basi, watu wanapata pesa wanajiondokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea maoni na ushauri au alichokiona CAG katika hesabu zake za mwaka wa fedha 2015/2016 kuna pesa zaidi ya bilioni nne zinadaiwa zipo nje, zipo katika vikundi na hizi pesa ni nyingi. Hata hivyo, ni kwamba hizi pesa ambazo zipo zinatolewa na Halmashauri hazina ukomo. Tunaona kwamba hizi pesa zitolewe halafu hii mifuko iwe na kiwango fulani na pia iwe na ukomo, iwe ni rotation fund yaani tukisema Halmashauri moja inajiwekea malengo kwamba sasa tunakusanya ama tunakopesha mpaka tunafikisha bilioni mbili au tatu basi tunaweka ukomo na pesa zingine zinaendelea kufanya maendeleo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu nasema kwamba mfuko huu wa kisiasa tu, pamoja na kwamba ni mzuri lakini malengo yake hayatekelezwi. Sioni sababu mfuko huu kuendelea lakini pesa za wananchi zikapotea ina maana Serikali inataka kutuambia nini. Katika ripoti ya mwaka jana, Kamati ya LAAC tulitoa ushauri kwamba itengenezwe sheria maalum ambayo itaweza kuonesha mfumo thabiti wa kuweza kukusanya hizo pesa, kukopesha na baadaye kuzirejesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haikutoa majibu na wala haikutengeneza sheria hii. Hata mwaka huu tumerudia tena maoni hayo kwamba itengenezwe sheria ili kuwezesha mfuko huu kuwa endelevu na kuweza kusaidia wanawake na vijana kwa malengo ambayo yanastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mapendekezo aliyoleta Mheshimiwa Zitto hapa hata kama ni mapema kwa sababu ilikuwa kwenye mchango wangu, kwamba ingekuwa vema basi kama Serikali ikiona haitaweza kuweka utaratibu mzuri basi ianzishe Benki ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa ili kuwezesha Halmashauri kuchangia ndani ya benki hiyo na benki ikakopesha vijana na wanawake ili hizi pesa zionekane zina manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoona kule tunapokwenda kukagua ni kwamba vijana wanachukua pesa, wanawake wanachukua pesa basi imeishia hapo, huu mfuko umekuwa shamba la bibi. Kuna baadhi ya Halmashauri wameamua kuziweka kwenye SACCOS lakini ukifuatilia kuona hata wale walioweka kwenye SACCOS hizi pesa wanaopewa siyo walengwa wenyewe. Ukipeleka kwenye SACCOS wanakopa wale wenye uwezo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tumekwenda kwenye Jiji la Dar es Salaam wamepeleka zaidi ya bilioni moja kwenye SACCOS yao, sijui kwenye Benki huko ya Dar es Salaam, lakini hizo pesa hazijarejeshwa mpaka leo, kwa hiyo unaweza kuona kwamba hata Halmashauri zenyewe hazina usimamizi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuweza kunipatia nafasi kidogo nami niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa mawazo yangu napenda nichukue nafasi hii kwanza kuunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani, pia napenda tu kuwashukuru Viongozi wetu wa kambi, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Riziki S. Mngwali pamoja na James Francis Mbatia kwa kazi nzuri wanayoifanya na niwaambie kwamba kufanya kazi ya upinzani katika nchi zetu za Kiafrika inataka moyo. Kwa hiyo, tuendelee tu kupambana na matokeo ya kazi yetu yanaendelea kuonekana na kuleta mabadiliko katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maji katika bajeti hii, nikiamini kabisa kwamba tumekaa hapa takribani miezi miwili, tukifanya mipango na kutafsiri mipango hii katika pesa ndiyo maana ya bajeti, tunapanga halafu tuna tafsiri mipango katika pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunahitaji kuona mafungu tunayoyagawa yanaleta matokeo mazuri, kwa vikundi vya wananchi na mwananchi mmoja mmoja na tunapima matokeo haya tunaona bajeti yetu tuliyoipanga imeleta matokeo yapi, imeweza kuleta maendeleo ya nchi na watu wake imeweza kupeleka mbele maendeleo ya mtu mmoja mmoja katika makundi yao na baadaye tunarudi mwaka kesho tunakuja kushangilia na kupiga makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiria kwamba hii bajeti inapaswa kujibu matatizo ya maji, kwa sababu tulikaa hapa na hasa wanawake, tulipanga mkakati mzuri na tukafanya lobbying, Wanaume wakatusaidia tukasema Serikali iongeze tozo ya Sh.50/= kwenye mafuta iende kwenye maji ili tuweze kuwatua wanawake ndoo, lakini cha kushangaza Serikali imekataa maombi yetu. Kwa lugha nyingine Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi isitudanganye haipo tayari kuwatua wanawake ndoo, badala yake mmetuletea sasa hoja nyingine ya Sh.40/= ambazo wanasema zitaongezwa kwenye mafuta baada ya kufuta road license. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiuliza Mheshimiwa katika kitabu cha bajeti cha Waziri mbona hajatuonesha hii Sh.40/= kama inakwenda kwenye maji? Hii Serikali inaelewa vizuri mafuta yanayoingia nchini kwa sababu wanaagiza mafuta kwa bulk procurement, kama wanafanya hivyo wanajua ni lita ngapi, kwa hiyo mngeweza kukokotoa kutueleza ni fedha kiasi gani zitapatikana, hakuna jambo kama hilo katika vitabu vyao. Sasa tunakaa hapa tunaanza kupigwa wananchi kiini macho kwamba unajua hiyo Sh.40/= itakwenda kwenye maji, wapi na wapi watuoneshe mahali ambapo mmeandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atuonyeshe ni shilingi ngapi ambazo zitatokana na mafuta hayo. Wanajua kwa nini wameshindwa kufanya calculation ni kwa sababu walikuwa hawakuipanga kwenye bajeti hata kidogo ni wazo limeletwaletwa tu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani kwamba hii Sh.40/= haziwezi kupandisha maisha ya watu. Nilikuwa nafanya simple calculation, kwa basi ambalo linatoka Dodoma kwenda Mwanza, mtu tu ambaye anaweza kutumia lita 200 analipa road license zaidi milioni mbili, kwa hiyo na wao watufanyie mahesabu tuone haya mafuta ambayo wanaagiza kwa bulk procurement yanaleta pesa kiasi gani ambazo wanasema zitakwenda kwenye mafuta, otherwise wanachofanya wanajaribu kutetea hii hoja, wakijua wanafanya siasa, sawa tunafanya siasa hapa, lakini wasifanye siasa za kwenda kudanganya au kuwaweka sawa au kuwaweka vibaya wananchi wa chini na hasa akinamama wanaotumia vibatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye Halmashauri, siwezi kuchangia bila kugusa Halmashauri. Bajeti ijibu matatizo ya wananchi, tukienda kwenye Halmashauri tunatazama pesa za barabara ambazo zinatolewa na Serikali Kuu katika Mfuko wa Barabara, ukienda kwenye kitabu cha ujenzi ukurasa wa 172 kinaonesha kwamba wao mwaka huu watakusanya bilioni 832.4. TAMISEMI wanapewa pesa bilioni 249.7, pesa hizo siyo kwamba zinakwenda zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona bajeti ya mwaka huu Serikali imeweza kutoa fedha za maendeleo asilimia 38, kwa hiyo tunaona ni namna gani Serikali ilivyoshindwa kabisa hata kufika asilimia 50. Kama pesa hizi zinakuwa ndogo na mara nyingi tumekuwa tukiwaambia kwamba waongeze pesa katika Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutengeneza barabara na barabara hizi zikipitika ni njia ya kusaidia wananchi kuweza kusafirisha mazao yao lakini pia kusaidia wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemwona Mheshimiwa Waziri Ummy hapa anahangaika kutafuta ambulance, hizo ambulance zinakwenda kupita barabara gani, kama Halmashauri barabara zake hazitengenezwi? Kuna mtu ameuliza hapa kwamba inawezekana Serikali Kuu wana mpango wa kutoa huduma wenyewe badala ya Halmashauri ndiyo maana wanachukua vyanzo vyote. Wanachukua vyanzo vyote vya Halmashauri Je, ninyi wana mpango ngani mbadala wa kutoa huduma kwa Halmashauri hizi. Nina wasiwasi mkubwa haya mambo yote tunayoyapanga yatakwenda kushindwa kutoa majibu sahihi na kusaidia wananchi ili waweze kuinua maisha yao kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama barabara hazitengenezwi za Halmashauri, Serikali Kuu watakwenda kuona mashimo yaliyomo kwenye mitaa? Wanaweza wao wenyewe kukaa Dar es Salaam pale au kukaa Dodoma hapa wakajua mimi kwetu kule Kamachumu Makongola Kijijini kwangu nilikozaliwa kwamba kuna barabara mbaya, hamna barabara ni mbaya za Halmashauri hazitengenezeki, hakuna mahali pa kupitisha mazao, wananchi wanahangaika lakini bado Serikali inatoa pesa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kutamka kuhusu percentage ya pesa ambazo zinakwenda Halmashauri kwenye Mfuko wa Barabara, Serikali inakaa kimya Mawaziri wanakaa kimya, ni kwa nini hawaleti sheria, wasilete Sheria za Madini tu na hizi wazilete tuzibadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo niongelee kuhusu madini na mikataba, watu wengi wanasema mchawi mpe sifa yake, mimi namshukuru sana Mheshimiwa Bashe amesema mtu akifanya kitu kizuri asifiwe wakati mwingine kwa kitu kizuri, kama wanavyosema tumuunge mkono Rais wetu, mimi nafikiri wazo siyo baya, pia hata Mheshimiwa Lissu amefanya kazi kubwa sana kuhusu mambo haya ya mikataba, amesimamia kesi mbalimbali. Kwa hiyo siamini kama kuna mtu ambaye anaweza kushindwa kutambua kazi ya Mheshimiwa Lissu ambayo ameifanya tangu mwaka 2004 mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema walete sheria na wakubali tumewaambia kwamba hakuna sababu ya kupigiana makofi, kufanya kosa kitu kibaya ni kulirudia, kama CCM walitufikisha hapa kwa miaka 50, basi wawaombe radhi Watanzania na wakubali tusahihishane humu ndani. Waende walete sheria maana yake hata Ndugu Ludovick Uttoh, aliyekuwa CAG amewaambia kwamba nchi iliingia kwenye mikataba ya kipumbavu, siyo maneno yangu yako kwenye magazeti, alisema tulipitisha sheria ambazo zinaruhusu madini na kila kitu kiende. Kwa hiyo, waende walete sheria, hata tukiongea maneno ya namna gani hapa, kama hakuna sheria wale jamaa wataendelea kubeba mabonge ya dhahabu kwa asilimia 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani Waziri ambaye anaweza kwenda kwenye uwanja wa ndege hapa? Nenda kwenye machimbo, kwenye uwanja wa ndege hakuna anayekanyaga pale hata Waziri wa Fedha hakanyagi, hata wewe Mwenyekiti wa Bunge leo hukanyagi mle, ni sheria tulizoziunda zinatupeleka. Walete sheria hapa tubadili ili tuweze kwenda na jambo hili vizuri kwa sababu ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba ni kwamba tuhakikishe bajeti hii inajibu matatizo ya Watanzania, inaangalia kilimo kwa mfano, hebu tuangalie kilimo kwa undani, wameanzisha mashamba darasa hayafanyi kazi, mimi ninapoishi nyumbani kwangu kijijini natazamana hivi na shamba darasa hamna kitu, kwa sababu hakuna Extention Officers hawatuoneshi katika bajeti kwamba wanaenda kuajiri Extention Officers hawatuambii wanakwenda kufanya mikakati ipi kwa ajili ya kilimo ili wananchi waweze kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wangekubali issue yetu ile ya Sh.50/= wangeweza kutuambia tutapata pesa kiasi gani, tutajenga malambo, tutajenga mabwawa, tutafanya umwagiliaji and then wananchi watalima, tutapata chakula lakini hata lishe, hatuwezi kuongea ya lishe wakati watu hawashibi, watu hawana chakula na utegemee watu wafanye kazi wakati watu wana njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu, bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na meli au usafiri katika Ziwa Viktoria. Waziri Mkuu ametueleza namna walivyoweka mkataba ili kuweza kujenga meli katika Ziwa Viktoria. Tangu meli ya Viktoria iharibike ni karibu miaka saba. Wananchi wa Mkoa wa Kagera wameteseka sana na hasa wanawake ambao walikuwa wanatumia meli ile ili kuweza kusafirisha bidhaa na hasa za kilimo na kufanya biashara kati ya Mkoa wa Kagera au Bukoba na Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli hii sasa imekuwa ni hadithi. Tunaomba Waziri Mkuu atueleze pamoja na kusema kwamba wameweka meli kubwa ambayo itaweza kusafirisha abiria zaidi ya 1,000 na mizigo, je, hii meli itakamilika lini? Wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa kweli tumeteseka kiasi cha kutosha kwa sababu bidhaa zote zinazokwenda Mkoa wa Kagera zinasafiri kwa njia ya barabara. Kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Kagera wanateseka sana na kwa kweli tusingependa kulalamika kwamba labda mkoa wetu haupendwi, mnatutupa sana kutokana na matukio mbalimbali hata yale ya tetemeko majibu tuliyoyapewa, tunaonekana kwamba sisi ni watu ambao hatustahili sana kupata huduma kutoka katika Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara vijijini. TARURA ni wakala ulioanzishwa ili kuona barabara za vijijini zinaweza kutengenezwa. Barabara hizi zilikuwa zinatengenezwa na Halmashauri za Wilaya, ikaonekana kwamba huu Wakala ungeweza kusaidia barabara hizi zikatengenezwa na zikaweza kupitika mwaka mzima. Mimi niseme, TARURA wanafanya kazi nzuri tatizo walilonalo ni ukosefu wa fedha. Serikali haitoi fedha za kutosha kwa TARURA ili waweze kutengeneza barabara vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano mdogo tu. Mimi ninafanya kazi katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini, wana mtandao wa barabara kilomita 593 na wanapewa bajeti ambayo ni shilingi milioni 800.09 tu kwa bajeti ya mwaka mzima. Ukigawa hizo hela kwa kilomita 593 kila kilomita inapewa karibu shilingi milioni 1.4. Unaweza kuona, je, hiyo pesa inatosha TARURA kuweza kutengeneza barabara nzuri? TARURA wanaweza kutengeneza barabara kama zile zilizokuwa zinatengenezwa na Halmashauri, wanapitisha magreda na mvua ikinyesha zinarudi kule kule zinakuwa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiambie Serikali kwamba pamoja na kutengeneza huu Wakala wa TARURA, basi wapewe pesa za kutosha. Mjue kwamba kule vijijini ndiyo kuna mtandano mkubwa sana wa barabara na wananchi wanataka huduma hiyo ili waweze kusafirisha mazao yao na kuweza kuinua kipato na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee kuhusu Tume ya Uchaguzi. Waziri Mkuu ametuonesha jinsi vituo vilivyoongezeka Tanzania Bara, Tanzania Visiwani kule lakini Tume hii ya Uchaguzi naiona kama ndiyo Taasisi pekee ambayo inaweza kudumisha amani katika nchi yetu; ni Taasisi ambayo kazi yake ni kupanga safu ya uongozi katika nchi hii; ni Taasisi ambayo inasimamia moja ya kigezo cha demokrasia katika nchi, kwa sababu uchaguzi ndiyo mwisho wake unaleta matatizo katika nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume hii kwa kuangalia uchaguzi mdogo uliofanyika, wote uliofanyika baada ya uchaguzi wa 2015, wamefanya mambo ya ajabu na ya kushangaza sana. Mimi nina jina langu ambalo ningeweza kuita Tume, lakini naogopa msije mkaniambia futa maneno, kwa sababu hii Tume nimeipima nikasema ni kitu gani hiki? Tumekuwa na Tume miaka nenda rudi lakini siyo Tume hii tuliyonayo sasa hivi. Hawa watu nao wamejitoa ufahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia chaguzi Wilaya ya Muleba katika Kata ya Buhangaza. Nilimwona Mkurugenzi anakuja na Polisi nikiwepo kwa macho yangu. Polisi sita, bunduki sita, anakuja kubeba boksi kama mwizi. Huyo ni Mkurugenzi ambaye anasimamia uchaguzi, yuko chini ya Tume. Wakurugenzi walio wengi ni makada wa Chama cha Mapinduzi, inawezekana wamepewa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa tahadhari kwamba Tume inawaona Watanzania kama watu legevu, Watanzania ambao wamelelewa katika misingi ya kutopenda kufanya vurugu, Ninachotaka kuwaambia, Tume isitupeleke Watanzania kwenda kufanya mambo yasiyostahili katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Monduli, nimeshuhudia kwa macho yangu, nilikuwa Mto wa Mbu, nimeona ni jinsi gani Polisi wameweka magari zaidi ya 15, niliyahesabu, magari ya washawasha, wanatisha wananchi. Hatuwezi kufanya uchaguzi wa vitisho. Unatisha wananchi wanashindwa kutoka nje kwenda kupiga kura halafu unasema umeshinda, umeshinda kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Tume sasa iwe huru na pale ambapo uchaguzi utafanikiwa kwa uhuru na haki, mtu atakubali kwa sababu kwa miaka yote ya nyuma mbona tulikuwa tunakubali mtu akishinda anamshika mwenzake mkono! Kinachotokea sasa, nami nashangaa Serikali iliyoko madarakani, tazama mlivyo wengi ndani ya Bunge, mnahofia nini? Kama mnajigamba kwamba mnafanya kazi nzuri, mnasema maneno yenu, mmefanya kazi, sasa mna wasiwasi gani? Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama wewe unajiamini, unaendaje kwenda kufanya madhara ambayo yanafanywa na Tume? Sasa hivi katika siasa za Tanzania sisi upande wa Upinzani tunashindana na dola, hatushindani na Chama cha Mapinduzi. Nami nimeona kwa style hii kumbe ninyi ni wepesi kama hamna Polisi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Tume, Waziri Mkuu atueleze: Je, BVR zimenunuliwa katika nchi yetu? Ziko ngapi? Zinatosheleza? Tunaomba kujua wananchi wanajiandikisha lini? Tunaomba kujua ni lini Watanzania wataweza kukagua majina yao katika daftari la wapiga kura? Kwa sababu tangu mwaka 2015 hili daftari la wapiga kura halijawahi kuboreshwa. Sasa kama linaboreshwa, je ni lini?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rwamlaza, kuna taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tu kupunguza pressure kidogo ya suala la daftari kwa Mheshimiwa Mbunge, naomba tu nimpe Taarifa kwamba Serikali hii sikivu ambayo inafanya kazi kwa umakini sana, suala la uboreshaji Daftari la Wapiga Kura kwa mujibu wa sheria na Katiba, kazi hiyo imeshaanza. Sasa hivi Tume iko kwenye hatua ya awali ya kufanya majaribio ya vifaa vyake na mfumo mzima na kanuni zilizopitishwa na Vyama vya Siasa. Wameshaanza hiyo kazi Wilaya ya Kisarawe na hapo Morogoro. Kwa hiyo, Kata mbili sasa hivi ziko kwenye majaribio na mwezi wa Tano tunaanza uboreshaji wa Daftari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge pressure itulie, BVR ziko za kumwaga, kila kitu kiko tayari kabisa. Tuko tayari kabisa kwa kuanza kuboresha Daftari. (Makofi)

MWENYEKITI: Mhesimwa Rwamlaza, taarifa hiyo.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jenista Taarifa hiyo Mheshimiwa Jenista wasifanye siri, uchaguzi siyo siri, uchaguzi siyo msiba bwana kwamba hautakuwa na maandalizi. Semeni basi Watanzania wajue mnachokifanya, mpaka uulizwe hapa? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wakijua, watajua kwamba sasa uchaguzi wetu utafanyika kwa uhuru na haki. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Si umeshasikia lakini sasa!

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kwa mzungumzaji.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba ni kweli daftari la mfano limeshaanza na ukiwemo Mkoa wangu wa Morogoro, mimi kama Mwenyekiti wa Chama, CHADEMA Mkoa wa Morogoro na Mjumbe wa Kamati Kuu, tumeingia kwenye hilo zoezi kwenye Kata moja ya Kihonda. Sisi kama wadau wakubwa wa Daftari hili tumezuia kabisa na Tume kuhamasisha wananchi waende wakajiandikishe isipokuwa Tume wametangaza siku moja tu na hawakufika kwenye maeneo ya mbali ambayo wananchi walipo. Kwa hiyo, Daftari limeenda kwa kusuasua sana, mpaka limemalizika juzi ni wananchi 6,000 tu ndio waliojiandikisha. Kwa hiyo, ni CCM tupu ndiyo wanaofanya hiyo kampeni. (Makofi)

Hiyo nakupa… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rwamlaza.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo, kwa sababu najua lazima mizengwe ifanyike katika uchaguzi huu. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, hakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri. Wewe ni mwanamama kwa sababu nchi hii ikiingia kwenye matatizo kuna matatizo kuna siku utakuja kusimama na kuomba samahani kwa wananchi kama Rais wa Algeria alivyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mnapofanya matendo haya msijue kwamba baadaye huko Mungu akikujalia ukafika miaka 90 kwamba hutaweza kulaumiwa na baadaye ukasimama mbele ya watu kuomba msamaha kwa matendo machafu yaliyofanyika. Kama watu wataingizwa katika hali mbaya au katika mapigano au katika malalamiko na mambo mengine ambayo hayastahili kutokea kutokana na uchaguzi mbaya unaotokea katika nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ngoja nibadili uelekeo kidogo basi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti ya TAMISEMI na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia na mimi nakuombea angalau hukuwa na hasira leo, mambo yameenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, nina machache sana kuhusu bajeti ya Wizara hii. Kwanza nianze na fedha za Mfuko za Wanawake na Mfuko wa Vijana zile asilimia kumi ambazo zinapaswa kukatwa katika mapato ya Halmashauri (own source) ili ziweze kusaidia wanawake na vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu katika Kamati zetu ambapo TAMISEMI tumekuwa tukisisitiza sana kwamba Halmashauri hizi ziweze kutenga fedha hizi ili 5% na 10% iweze kuwasaidia wanawake na vijana katika kuboresha maisha yao, kufanya biashara na hivyo kujiajiri na kuwaondoa mitaani ili waweze kuwa na shughuli za kufanya.
Mheshimiwa Spika, baada kuweka msisitizo huo, Halmashauri nyingi sasa zinaanza kutenga fedha hizo. Binafsi nimekuja na mawazo yangu haya nikiitaka TAMISEMI na kuuliza swali. Fedha hizi ambazo zinatolewa kwa makundi mbalimbali ya wanawake na vijana huwa zinarudishwa au tunatoa zaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ziko fedha nyingi ambazo zinatolewa kwa vikundi katika nchi hii, lakini mifuko hii iko wapi? Zinarejeshwa wapi? Katika akaunti ipi? Je, kama hatutoi sadaka au kama hatuzitoi kama ruzuku, kama TASAF ni kwa nini hazina return yake?
Mheshimiwa Spika, ukienda katika Halmashauri utawaambia toa fedha na hata CAG hata siku moja hajawahi kuonyeshwa namna fedha hizi zinavyorejeshwa.
Fedha zinapelekwa kwa makundi, basi zinaishia pale. Kila mwaka Halmashauri itasisitiza, tunaziweke msimamo kwamba mchange fedha hizo mpeleke kwa makundi, lakini hatuangalii hizi fedha zinarejeshwa vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, binafsi nilikuwa nawaza kwamba kama mabenki yanaweza kukopesha fedha kwa watu na baadaye mwisho wa mwaka wanatuonyesha kwamba sasa benki hii tulikopesha shilingi bilioni tano, lakini tumezalisha hivi, tumekuwa na mfuko endelevu. Ni kwa nini ndani ya Halmashauri yetu hakuna kitu kama hicho?
Mheshimiwa Spika, nimegundua kwamba fedha hizi zinapotea kiholela, hakuna anayeziona na hata kwenye Halmashauri hatukuambiwa kwamba ziko kwenye akaunti ya deposit, wapi? Kwa hiyo, naomba Wizara itazame ni jinsi gani huu mfuko unaweza ukasimamiwa ukawa endelevu.
Mimi siupingi, naupenda sana, lakini fedha za walipa kodi ndani ya Halmashauri zinapotea bila ninyi kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu jaribu kufanya research kidogo muone kama hizi fedha huwa zinarejeshwa au zinapotea jinsi zinavyopelekwa? Maana yake Halmashauri zina-respond sasa hizi, zinapeleka shilingi milioni 200, shilingi milioni 300, shilingi milioni 400, that is the end of the story, zinaenda wapi? Hakuna mahali ambapo zinarejeshwa, hakuna return yoyote, hakuna Bunge hata kuelezwa kwamba Halmashauri ya mahali fulani ilikopesha shilingi milioni 500, mwisho wa mwaka tumekuwa na shilingi milioni tano na tumeweza kuendeleza mfuko huu na kama tungefanya hivi, tumekuwa tumeacha hii biashara. Hii biashara ya kuwaambia Halmashauri itenge kila mwaka, kuwasisitiza, kungekuwa na mfuko wao ambao umekuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nimegundua, hii mifuko haina sheria. Hii mifuko inaendeshwa kiholela ndani ya Halmashauri. Kwa vile hakuna sheria, hakuna kanuni na hakuna kamati. Hizo kamati zinaundwa hata Madiwani wa Viti Maalum hawapo. Kwa hiyo, unaweza
kuona ni kwamba pamoja na kusisitiza kwamba fedha hizi zipelekwe, lakini hazina uangalizi hata kidogo. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali na TAMISEMI kwamba sasa twende mbali, tutunge sheria, tuwe na kanuni, lakini mifuko hiyo iwe endelevu, ionyeshe faida, izae tupate mfuko maalum ndani ya Halmashauri ambapo fedha zake zinakwenda zina-rotate zinakopeshwa kwa wadau.
Mheshimiwa Spika, kama Serikali hii inaamua tuzitoe kama zaka, tuwatangazie watu wote ziwe sadaka tujue kwamba Halmashauri inatoa sadaka kwa watu na hazirudishwi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwenye kodi ya majengo. Amesema vizuri Msemaji wa Kambi ya Upinzani, amejaribu kutoa ushauri. Ninachotaka kukwambia ni kwamba kweli Kamati ya Bajeti imetuambia kwamba hizi fedha zitakuwa zinarejeshwa kwenye Halmashauri kutokana na jinsi
walivyoweka makadirio. Binafsi nikajiuliza, je, kuna sheria inayo-guide kwamba Halmashauri inaweza kupata kiwango fulani? Maana yake mimi nilikuwa kwenye RCC tarehe 2 Machi katika Mkoa wangu wa Kagera, wakatupa taarifa kwamba fedha za kodi ya ardhi hazijarejeshwa mpaka Disemba mwaka 2016, mkoa ulikuwa haujapata hata senti tano.
Mheshimiwa Spika, pale kuna sheria ambayo inasema kwamba asilimia 30 itarudi katika Halmashauri na hata Mfuko wa Barabara una sheria yake; ni kwa nini kwa upande wa majengo hakuna sheria ambayo ina-guide kiasi ambacho kitarudishwa ndani ya Halmashauri? Tunaacha tu holela. Ni kwamba Serikali inaweza ikaamua. Nilikuwa naongea na Mbunge wa Tunduma hapa, ameniambia karibu shilingi milioni 78 za ardhi hazijarudishwa katika Halmashauri yake. Kwa mtindo huo na kwa style hiyo ni kwamba hata hizi fedha za majengo hazitarudishwa, kwa sababu hakuna sheria, hakuna kitu chochote kinacho-guide Halmashauri ikajua kwamba itapata kiwango hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali ifikirie namna ya kuweka sheria ambazo zitawezesha Halmashauri wajue angalau katika kodi itakayokusanywa ndani ya Halmashauri yetu tunastahili kupata asilimia au asilimia 50. Kutoka hapo hata Wabunge wanaweza kuwa mandate ya kusaidia kudai ili Halmashauri zao ziweze kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ngoja niendelee.
Mheshimiwa Spika, leo limetoka swali hapa linalohusu miradi ya maji la Mheshimiwa Kaboyoka, tukapewa majibu; majibu haya wakati mwingine ya kimzaha mzaha hii Serikali ya CCM inatoa.
Mheshimiwa Spika, nilianzia katika Kamati ya TAMISEMI, leo niko kwenye Kamati ya LAAC kwa hiyo, napata chance ya kukagua miradi. Tena nashukuru wewe huendi huko, kwa sababu ungekuwa unaenda, ungekuja huo upara umeota nywele. Hakuna miradi ya maji.
Mheshimiwa Spika, tena nakusihi usijaribu kwenda kule. Nakwambia karibu asilimia 43 ya miradi ya maji haifanyi kazi katika nchi hii.
Ukienda kule utakuta mambo ya ajabu. Hakuna umwagiliaji, hakuna mabwawa, mabilioni ya pesa yamelipwa yaani unabaki kushangaa. Mimi nataka Serikali iwe inatujibu swali kwa nini? Msituambie michakato. Ni kwa nini Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilishindwa kusimamia miradi hiyo?
Mheshimiwa Spika, kuna mkanganyiko kati ya Wizara ya Maji, kuna mkanganyiko katika Halmashauri; ukienda wale wanakwambia aah, sisi wapembuzi yakinifu walitoka kwenye Wizara ya Ardhi. Wamekuja pale wamefanya Wizara ya Maji, wamekuja wamefanya upembuzi yakinifu wanaondoka, wameacha Wakurugenzi hawajui cha kufanya hata fedha wakati mwingine... Halafu na ninyi mna tabia ya kuingilia ingilia mambo ya watu, msini-distract mimi.
Taarifa...
Mheshimiwa Spika, halafu hii tabia ya Mawaziri kujibu kabla ya majumuisho kwa kweli inatupa shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilichosema, nilikuwa kwenye RCC yangu Mkoa wa Kagera tarehe 2 Machi taarifa ile ninayo. Mimi naenda kwenye vikao mwenzako, nilikuta wanadai tangu Disemba Mkoa wangu wa Kagera hakuna chapa; sasa kama umepeleka jana, hewala. Kwa hiyo, ninachojua ni kwamba hizo fedha haziendi na siyo kwangu tu. Sehemu zote mkifuatilia mtakuta hizi fedha haziendi; na siyo ajabu hata
kwako. Kama umepeleka, basi ni ubinafsi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, nilikuwa naongelea kuhusu mambo ya miradi ya maji, akanipeleka huko, mnani-distract memory kitu ambacho sipendi kwa kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama miradi ya maji haitekelezeki, Waziri atuambie ni kwa nini Serikali inashindwa kusimamia? Wasituletee mambo ya michakato hapa. Watuambie ni kwa nini, miradi hiyo imekwama?
Mheshimiwa Spika, maji ni kero katika nchi hii. Ninyi hamjaona, nendeni katika majimbo yenu labda mahali pengine hamuendi. Kuna mahali nimewahi kwenda kusimamia kampeni sitawasema, watu hawaoshi vyungu, yaani kile chungu kinapika maharage, kinapika na kahawa
ya kunywa. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni namna gani nchi hii ilivyo katika matatizo makubwa ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachowaomba hakikisheni nchi hii iweke priority katika kazi hii na msimamie mabilioni ya pesa, mabilioni; na mabilioni hayo ni pesa za watu, ni mikopo, watakwenda kulipa Watanzania. Kwa hiyo, kama mnaona kuna miradi hewa, unakwenda Mkurugenzi anakutembeza hata mradi haujulikani mahali ulipo.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo mambo ambayo nilisema nichangie machache…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ya pili eeh, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia japo muda kwa mfupi, lakini nitoe machache kuhusu hoja yetu iliyo mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii kuungana na Wabunge wote na waliochangia kwamba Wizara hii ipewe fedha za nyongeza katika bajeti yake. Hatuwezi kuongea mengi. Waheshimiwa Wabunge wameongea mengi kuhusu matatizo ya maji katika nchi yetu. Maji yamekuwa ni janga katika nchi na nitashangaa Wabunge ambao wanasema bajeti inatosha. Bajeti haitoshi, iliyotolewa haikutosha, basi tuombe Serikali iweze kukubaliana na maoni ya Wabunge kwamba tozo ya sh.50 iongezwe ili tupate sh.100/= kutokana na lita za petrol na diesel. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo ambalo naona linatukabili sisi ni namna ya kusimamia fedha ambazo zitatolewa katika bajeti. Tunapoongelea miradi ya maji, siyo kwamba miradi ya maji haijawahi kuwepo. Inawezekana katika nchi yetu, tusingekuwa na kilio kikubwa cha matatizo ya maji kama fedha ambazo zilitolewa huko nyuma kutengeneza miradi ya maji katika kupitia mradi wa World Bank pamoja na ile miradi ya vijiji kumi, zingesimamiwa inavyotakiwa. Zingesimamiwa, ina maana tungekuwa tumepunguza kwa kiwango kikubwa matatizo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, pamoja na kwamba tunatoa kilio fedha ziongezwe, fedha hizi Waheshimiwa Mawaziri zisimamiwe ili tusije tukarudi kule nyuma kama ilivyokuwa katika miradi ya awali. Nashangaa pale watu wanapokuja hapa na kuimba nyimbo za kujisifu, lakini walioharibu na kushindwa kusimamia miradi hii ni Serikali iliyoko madarakani. Tunasifu Awamu ya Tano, lakini kulikuwa na ya Pili, ya Tatu na ya Nne. Ina maana wao walikuwa hawafanyi kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka ni kwamba miradi isimamiwe. Fedha tunazoomba kama Bunge tunawapa Serikali mafungu, basi mafungu hayo yasimamiwe kikamilifu ili miradi iweze kuleta matokeo mazuri na iweze kuonekana. Kwa mfano, kama sisi ambao Kamati zetu zinazunguka kutazama miradi hii, iwe ya umwagiliaji, iwe ya mabwawa ya matumizi, haifanyi kazi vizuri. Fedha zinatumika vibaya!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, aende pale Tabora, kuna ule mradi wa Nala, ni mabilioni ya pesa. Kuna miradi mingine ambayo Halmashauri inashindwa kulipa Wakandarasi na inapaswa ilipe fidia au ile hasara ya kuchelewesha kulipa. Kwa hiyo, unakuta Halmashauri hizi nazo zinajikuta zimeingia katika malipo makubwa kwa sababu ile miradi ya awali haikulipwa inavyotakiwa. Kwa hiyo, mambo yanakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachoomba tulie kuongeza pesa, Serikali itusikie iongeze pesa hiyo, lakini isimamiwe inavyotakiwa ili miradi hii iweze kuleta matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka kusema ni kwamba katika mikoa mingine kwa mfano Mikoa ya Kagera, Mungu alikuwa ametujalia vijito vidogo vidogo ambavyo wanawake walikuwa wanavitumia kuchota maji, lakini vijito vyote hivyo vimekauka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu katika hivyo vyanzo vidogo vidogo. Hii hali inapotokea, wanasiasa wananyamaza hasa katika ngazi ya Halmashauri. Hata ile Wizara inayohusika na Mazingira haichukui hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake, ile mito midogo midogo iliyokuwa inatiririsha maji mazuri ambayo watu walikuwa wanatumia kabla ya kupewa haya maji ya bomba, kulikuwa na hiyo mito, lakini sasa hivi yote imekauka. Imekauka kwa sasabu hakuna juhudi maalum za kuelimisha Watanzania, watu wamejisahau na mara nyingi wanasiasa wanaogopa kuchukua hatua kwa sababu ya kufikiria kwamba labda hawatachaguliwa tena.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwa dakika tano. Naomba nianze na kitu kilichotokea hapa wakati Waziri anatoa kauli. Mimi naona mnatu-confuse kwa sababu gani? Tulitegemea kwamba majibu aliyoyatoa Waziri angeyapeleka kwa CAG afute hoja. Mnachotaka kutuaminisha hapa, mimi naaminai kwamba CAG anafanya kazi kwa kupewa vielelezo, kama hakupewa vielelezo Naibu Spika ataandika kitu alichokiona.

Naomba nijadili sasa mambo machache kwa sababu ni dakika tano kwanza nianze na utoaji dawa katika hospitali. Dawa zipo, ninachotaka kuongelea ni namna wale Wafamasia wanavyotoa dawa kwa wagonjwa. Wafamasia wanatoa dawa kwa wagonjwa bila kutoa maelekezo ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko dawa ambazo ukisoma leaflet yake ukishapewa dawa wanakwambia kwamba labda hii dawa unapaswa uiyeyushe kwenye maji kabla ya kumeza au utumie hiyo dawa kabla ya kula au masaa fulani kabla ya kula au hizi dawa zinaendana na chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea Wafamasia wetu wamekuwa wakitoa dawa hizo kwa kuonesha kwamba unatumia moja mara moja, mbili mara tatu na kadhalika bila kutoa maelekezo ya kutosha kwa wagonjwa. Kwa hiyo, unakuta wakati mwingine mtu anakwenda kumeza dawa ambavyo haitakiwi na kwa kweli haileti tija katika matibabu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu uzazi wa mpango, Mheshimiwa Waziri nimepitia kitabu chake hicho ameandika maneno mazuri na anafanya kazi sio mbaya, lakini hakuna mahali alipogusa kuhusu uzazi wa mpango. Huku nyuma kulikuwa na kitengo wakati wa Awamu ya Kwanza kulikuwa na kitengo kinaitwa UMAT (Uzazi na Malezi Bora Tanzania).

Mheshimiwa Naibu Spika, kitengo hiki kilikuwa kinafundisha mambo mengi kutumia dawa ya kinga ya kuzaa, kufundisha wanawake namna ya kujitunza, namna ya kulea watoto wao na namna ya ku-space ili wasizae watoto wengi na kwa wakati muafaka. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, kitengo hiki hata kama hakitarejeshwa kama kilivyokuwa, lakini wkiangalie ili kiweze kwenda kutoa elimu ya kutosha kule chini kwa wanawake wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye lishe, ukienda kwenye ukurasa wa 89 wa kitabu chake, Mheshimiwa Waziri ameongea kuhusu lishe, ameongea mambo mazuri ambayo yanahusu mashirika mbalimbali namna ya kurutubisha vyakula ambavyo tunakula, kuweka madini ya joto na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Waziri kwamba lishe ndio msingi wa maisha ya mtu katika kukua kwake kimwili na kiakili. Kwa hiyo, ni vyema hiki kitengo cha lishe na taasisi hii iwe mtambuka, washirikiane na Wizara ya Kilimo pia na Idara ya Maendeleo ya Jamii . (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako hawa Social Workers ambao kazi yao ni wataalam wazuri kabisa wa kutoa ushauri kuhusu mambo hayo lakini hawaajiriwi, wanafundisha watu kila siku lakini hawapewi ajira na hawa watu wa muhimu sana katika maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo tu katika hizi dakika tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nianze moja kwa moja na usafiri katika Ziwa Victoria. Meli yetu ya MV Victoria iliharibika miaka mitano iliyopita na Serikali imekuwa ikiahidi kutengeneza meli hiyo. Ukitazama hata katika makadirio ya mwaka jana Serikali ilisema katika makisio kwamba ingetoa bilioni hamsini ili kuweza kununua meli mpya lakini pia kufanya matengenezo kwa meli hiyo ya MV Victoria. Pia mwaka huu wametoa bilioni tisa kwenda kutengeneza meli hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize tu Mheshimiwa Waziri, hii meli ya MV Victoria ambayo inatengenezwa katika miaka mitano inatengenezwa kitu gani? Kwa sababu inashangaza kwamba meli ambayo inahitajika; kwa sababu sisi watu wa Mkoa wa Kagera ili uweze kusafiri kibiashara na hasa akinamama ambao wanasafirisha ndizi, Avocado na bidhaa nyingine za maharage, wanatumia njia ya barabara, kitu ambacho kwa kweli kinawa-cost na gharama za kuendesha biashara hiyo inakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba majibu, tunaomba Waziri atuambie, ni lini atatutengenezea hiyo meli wakati tunasubiri meli ile ambayo wamesema kwamba itajengwa? Kujenga meli mpya kunachukua muda mrefu lakini matengenezo ya MV Victoria ni kwa nini yamechukua muda mrefu na kila mwaka wamekuwa wanatenga fedha kwa ajili ya meli hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kitabu cha hotuba cha Mheshimiwa Waziri cha mwaka jana hiki, ukurasa wa 81, alichokisema na hata mwaka huu ameongea lakini hakuna kitu chochote. Hata Watanzania wa Mkoa wa Kagera hawapewi taarifa ni kitu gani kinaendelea kuhusu meli yao ambayo ilikuwa inarahisisha usafiri kutoka Bukoba kwenda Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea hiyo nije kwenye TARURA. Japokuwa hii TARURA ipo chini ya TAMISEMI, lakini fedha zake zinatolewa na Serikali Kuu kutoka kwenye Mfuko wa Barabara. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiiomba Serikali, kwamba huu mgawanyo wa asilimia 30 ni mdogo na Halmashauri walikuwa wanashindwa kutengeneza barabara nzuri na zilizo imara. Sasa pesa hiyo hiyo asilimia 30 ndiyo inapelekwa kwa TARURA na huu ni Wakala ambao umeundwa au umeanzishwa ili kuweza kusaidia barabara za vijijini zilizo chini ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara haifikirii namna ya kuongeza pesa kutoka angalau asilimia 30 kwenda asilimia 40 ili TARURA waweze kujenga na kutengeneza barabara; na tukijua kwamba wana mtandao mkubwa wa barabara zilizo halmashauri na kuna maeneo mapya ya utawala ambayo yamekuwepo; tunaomba Serikali ifikirie namna ya kuongeza pesa kwa TARURA au mtindo utakuwa ni ule ule na TARURA watashindwa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi. Wamesema katika kitabu na hata cha mwaka jana wamesema kwamba wanataka hii Bodi ya Usajili wa Wahandisi iweze kusimamia kazi zote zinazofanywa za kihandisi, wahandisi watokane na umoja huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zinazojengwa zinakuwa chini ya viwango; naomba nitoe mfano, barabara ya Biharamulo ambayo imetoka Rusaunga inakwenda mpaka Kasindaga. Ukienda kwenye barabara hiyo pale kwenye keep left ya Biharamulo barabara imebomoka kabisa. Kilomita mbili kabla hujafika Kasindaga barabara imekwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiitazama baada ya lami kubanduka pale utaona kwamba ile barabara imetengenezwa chini ya kiwango. Kwa hiyo, naomba Wahandisi ambao tunawasifu kwamba wanafanya kazi wafanye kazi kulingana na taaluma zao. Kama Wahandisi hawawezi kusimamia miradi hii, basi hii miradi itajengwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kusisitiza kuhusu usafiri wa Ziwa Victoria, watuletee meli yetu. Nisiseme, labda niseme wana ajenda gani na watu wa Kagera pale ambapo wanatunyima meli, tunakosa usafiri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea ukurasa wa 26 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ameeleza juu ya wanajeshi wa nchi yetu kupoteza maisha wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini DRC. Jambo hili la ulinzi ni jambo jema kwa nchi yetu kushirikiana na nchi nyingine. Napenda kuishauri Serikali yetu kwa kushirikiana na nchi za Afrika kushauri Umoja wa Mataifa ili kusaidia DRC kujenga jeshi liwe imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina population ya zaidi ya milioni sitini, wana rasilimali za dhahabu, shaba, misitu na kadhalika. Ni kwa nini nchi hii imeshindwa kuunda jeshi lao na nchi zinapeleka askari na wanapoteza maisha? DRC imepigana tangu 1994 hadi leo. Nchi za Rwanda na Uganda na kadhalika zimepigana vita na wameondoa majeshi yao. Umoja wa Mataifa hutumia fedha nyingi, takribani bilioni moja Dola za Kimarekani kila mwaka kwa ajili ya matumizi ya majeshi almost 29,000. Fedha zinaweza kutumika kufundisha Jeshi la Congo kwa kusaidiana na majeshi yaliyopo. Nchi yetu inaweza kusaidia kutoa ushauri ili watoto wetu wasiendelee kuuawa huko DRC.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo kuhusu hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Serikali mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, navyoelewa mimi ni kwamba hapa tunachojadili ni mipango yetu ya maendeleo tunaitafsiri kwa minajili ya pesa. Tunapanga bajeti, tunatoa pesa au sisi kama Bunge tunaidhinisha ili Serikali iweze kutekeleza ile mipango ambayo imeletwa hapa na imepitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonisikitisha ni kwamba Bunge hapa linakaa linapanga bajeti lakini Serikali hii iliyoko madarakani kusema ukweli haina nidhamu ya kusimamia matumizi jinsi bajeti ilivyopitishwa. Tunapitisha bajeti Serikali inakwenda kutumia pesa bila hata kulishirikisha Bunge. Si makosa Serikali kuomba bajeti au supplementary budget pale ambapo kumelazimika kuwa na matumizi ya lazima na hayakuwepo kwenye bajeti lakini Serikali haileti inatumia inavyoona kitu ambacho nakiona ni dharau kwa Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye uhalisia wa bajeti. Nchi yoyote inapanga bajeti kulingana na uwezo na makusanyo yake. Ukiangalia mwaka jana, tulipitisha bajeti zaidi ya shilingi trilioni 31 lakini haikutekelezeka kwa sababu makusanyo hayakuweza kutosheleza. Mwaka huu pia tunakwenda kwenye bajeti ya shilingi trilion 32, je, tuna uhakika wa kukusanya ili bajeti iweze kutekelezeka? Nachoshauri Serikali wala isione aibu, pale ambapo wanaona makusanyo hayatoshelezi na hayatapatikana leteni bajeti ambayo inalingana na uwezo wa nchi yetu ili tusifanye kwa kuonesha wananchi kwamba Serikali inaweza kukusanya mapato makubwa na hatuwezi kufanya jinsi wananchi wanavyotegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu Halmashauri. Wengi sana wamesema kuhusu D by D, lakini mara nyingi nikisimama huwa nairejesha Serikali hii katika kitu kilichotendeka mwaka 1972 – 1982, kile kilichokuwa kinaitwa madaraka mikoani, walikuwa wanasema decentralization, sijui kama ilikuwa D by D. Zoezi hili lilishindwa kwa sababu naona Serikali hii inapenda kuongoza nchi hii kwa trial and error. Tunajaribu tunashindwa halafu sijui tuna- retreat halafu tunaenda kuanza upya. Kwa hiyo, nchi inakaa katika kupanga na kupangua tu, ni kama tunafanya experiment kwamba tujaribu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa inarudi kwenye centralization kwa sababu inachukua pesa yote inaweka katika mfuko mmoja. Dhana ya kuanzisha halmashauri hizi ni ipi? Kama zilianzishwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na kwa kuzingatia kwamba nchi hii ni kubwa, huwezi kuiendesha ukisimama Dar es Salaam peke yake, haiwezekani. Kama tulijaribu tukashindwa ni kwa nini sasa Serikali inataka kuturudisha kule. Hizi halmashauri kama Serikali iliyoko madarakani haizitaki leteni sheria hapa tubadilishe, tubaki na madaraka kule makao makuu ya Serikali halafu pesa zote ziwe zinatoka huko zinakuja kule chini, kitu ambacho hakitawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vyote vya halmashauri, kama walivyosema wengine na wewe unavijua vimekwenda Serikali Kuu. Kitu ambacho kimenisikitisha ni hata ardhi, maana halmashauri nyingi zinategemea ardhi le ya wilaya lakini hata ile asilimia 30 ambayo ilikuwa inabaki au inapaswa irudishwe kule katika halmashauri kusaidia kwa sababu inatokana na ushuru au tozo mbalimbali ambazo zinatokana ardhi na yenyewe mmebeba mmepeleka Wizarani sijui Hazina na pesa hizi hazirudishwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tutazame ile Local Government Development Grant mpaka sasa hivi hakujatolewa hata senti tano. Kibaya zaidi hata kipindi hiki Serikali haijaweka bajeti ya pesa hizo kurudi katika halmashauri. Kama pesa hizo hazirudi miradi yote ambayo ilikuwa imepangwa kufanywa na halmashauri madarasa, zahanati, imekwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeshindwa kurudisha hicho kidogo tu, je, ikiwa na mfuko mkubwa maana yake ni nini? Labda Serikali inachotaka kutuonesha ni kwamba imeweza kukusanya, siyo hivyo, la hasha, haijakusanya ni kwamba wamepora vyanzo vya halmashauri na halmashauri ziko mahututi na hatutegemei kwamba kweli wananchi wa Tanzania wataweza kupata huduma wanazostahili kama barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnaona barabara wanazotengeneza TARURA hata hapa Dodoma nendeni huku tunakokaa mitaani, wanatengeneza barabara ambazo hata ma-engineer hawafiki. Mmechukua ma-engineer wote wa halmashauri wameenda TARURA, halmashauri zimebaki hivi hivi zina wayawaya, ni kwamba hata barabara zinazotengenezwa hazipo. TARURA haiwezi kutengeneza barabara nzuri kwa sababu haipati pesa, watafanya grading tu lakini hawawezi kutengeneza barabara ambazo zitaweza kupitika ili wananchi waweze kusafirisha mazao yao. Hata huduma nyingine za afya, elimu hazitaweza kutekelezeka kama halmashauri hazipati pesa na Serikali Kuu inazikalia haipeleki pesa katika halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye kilimo. Ni jambo jema kwamba Serikali imeleta bajeti ambayo kipaumbele chake ni kilimo. Ila mimi ninajiuliza kipaumbele hiki mmeweka katika makaratasi, je, utekelezaji wake ukoje?

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ambao tuna umri kidogo unawazidi walio wengi hapa, hebu turudi nyuma tuangalie ile Awamu ya Kwanza ya Hayati Mwalimu Nyerere aliwezaje kufanikiwa kutengeneza kilimo kikasaidia nchi yetu. Si vibaya na wala si dhambi kuangalia kule nyuma huyu bwana alifanyaje kwani makaratasi hayapo, mafaili hayapo, mipango haipo? Naiomba Serikali irudi nyuma ione ni kitu gani ambacho Awamu ile ilifanya (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza walikuwa na extension officers, sasa hivi kilimo kinasemwa lakini hakuna elimu inayotolewa kwa wakulima. Hata yale mashamba darasa mnayoyasema hayapo na kama yapo yametelekezwa. Sisi tunakaa vijijini huko, mimi nikienda nakaa kijiji sijawahi kumwona extension officer wa kata na hata hao waliopo hawana huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko kwenye kamati ya LAAC kuna siku moja tumemwambia CAG hebu nenda kafanye performance auditing ya hawa ma-extension officers, kwa kweli wanapata mishahara ya bure, atuoneshe wanalipwa nini na wanafanya nini. Kama hawastahili kuwepo basi waondoke wakulima wajitegemee wenyewe wanavyoona yaani bora liende kila mkulima anafanya anavyoona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nchi yetu ina vijiji zaidi ya 19,000, je, wako ma-extension officer kiasi gani ambao wanaweza kusaidia kuongoza wakulima? Mimi nakumbuka baba yangu alikuwa analima kahama na kwenye kilimo cha kahawa walikuwa wanakuja extension officers wiki mara mbili na pikipiki sasa hivi hawana hata usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye kahawa. Niongezee kwa mchango wa Benardetha Mushashu jana …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia machache kuhusu hoja iliyo mbele yetu ya bajeti ya Wizara ya Maji. Mimi ni mjumbe wa LAAC, kwa hiyo, tunapata nafasi kubwa ya kutembelea miradi mbalimbali ili tuweze kuona utekelezaji wake lakini pia na thamani ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi kuna mtu mmoja alichangia kwa jazba akasema kuna mambo ya hovyo hovyo yanatendeka katika miradi hii ya Wizara ya Maji. Mimi labda nisitumie neno hilo, niseme katika miradi ya maji kuna mambo makubwa sana ya usanii na Mawaziri ninyi hamuwezi kufika kila mahali, kwa hiyo, tunapotoa mawazo yetu, hatuna maana kwamba tunawachukia au tunafanya mambo ya kisiasa hapa, tunatembea tunaona ni namna gani miradi ya maji inavyotekelezwa ndivyo sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi labda niulize, kuna nini kati ya Wizara ya Fedha, Wizara ya Maji na Halmashauri zetu? Hii miradi ya nyuma yote ilikuwa ina-originate Wizarani. Ina maana Wizara walikuwa wanatoa Mhandisi Mshauri, Mkandarasi, kule Halmashauri wala hawakuwa answerable na miradi hii. Walichokuwa wanafanya Wizara ya Maji wanaleta Mhandisi Mshauri ambaye anakuja kufanya uoembuzi yakinifu ambavyo sivyo. Matokeo yake atasema hapa kuna maji, halafu yule anayekuja kuchimba maji anakuta hayapo, ameshakula fedha ameondoka na miradi mingi sana ya maji ina fedha nyingi, ni ya mabilioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya mwaka ya LAAC tulipendekeza kama alivyosema Mheshimiwa aliyemaliza hapa kwamba iundwe Tume iende itazame miradi hii, iangalie ni miradi gani ambayo haikufanyika kwa ufanisi lakini pia mjue gharama zilizotumika. Inawezekana hamna ukakika hata wa gharama zilizotumika katika miradi hii. Ni jambo la kusikitisha kwa sababu Watanzania wanalipa madeni ya miradi ambayo haina ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitembelea miradi, hawa watu wa Idara ya Maji, wakishapata taarifa kwa mfano Kamati ya LAAC inakuja maji yanatoka kesho yake. Tukifika, wananchi wanatuambia Waheshimiwa Wabunge mmekuja na maji na mtarudi nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi ambayo imetengenezwa haifuati hata BOQs. Kwa mfano, tumekwenda katika mradi mmoja huko Ngara, tumekuta wametengeneza tenki ambalo BOQ inasema watatumia matofari ya block, wao wametumia mawe na wamejenga tenki ambalo walipoweka maji likanza kuvuja. Halafu mtu anakwambia mradi umekamilika. Miradi ya namna hiyo ni mingi sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe mchunguze miradi hii, acha hii miradi mipya ambayo inatengenezwa sasa hivi, hii miradi ya nyuma yote imekaa hovyo hovyo. Wananchi hawapati maji ni uongo na Wahandisi wanadanganya na mahali pengine hata Wahandisi wenyewe ambao kwa kweli wana ujuzi wa kuendesha miradi hii hawapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda mahali pengine unakuta wametengeneza miradi chini ya viwango, anaweka mabomba ambayo ni tofauti. Mimi siyo mtaalamu wa mabomba ya maji lakini wataweka mabomba membamba, wakipampu maji mabomba yote yanapasuka. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali halisi iliyoko on the ground. Kwa hiyo, tunaomba mhakikishe mnachunguza miradi hii kama Kamati ya LAAC tulivyopendekeza na wengine ndani ya Bunge from there mtaweza kuona ni miradi ipi inakwenda vizuri, ipi ambayo imetengenezwa kiusanii na gharama ni ipi, muweze kutambua kwama nchi hii imeingia katika ufisadi mkubwa kwa kupitia miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana labda Serikali haina vipaumbele, nawaomba tuhakikishe maji tunayaweka katika priority. Watanzania wanateseka, inawezekana sisi tunakaa mijini, mkienda kule vijijini mtaona watu wanavyo- suffer kusema ukweli, utawahurumia watu hawaogi. Wanawake wanalalamika, maisha hayaendi vizurio ndani ya familia, kama hamuogi mnakaaje? Hili jambo ni serious, tunaomba Waziri na Serikali ihakikishe maji ambayo watu wamesema maneno mengi, ni uhai na kadhalika kwamba miradi yote inatekelezwa na wananchi wa Tanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee kuhusu vyanzo vya maji vijijini. Nina uhakika kwamba Serikali haiwezi ku-supply maji kwa kila mtu Tanzania hii lakini iko mito ambayo ni vyanzo vya maji ambapo kutokana na shughuli za binadamu imekufa. Kwa mfano, katika mkoa wetu sisi yako maeneo mengi watu wanapanda miti na wengine ni wanasiasa, wanapanda miti wanaharibu vyanzo vya maji, kwa hiyo, huwezi kupata mito ambayo inatoa maji mazuri. Kwa mfano, Mkoa wa Kagera, tunayo mito mizuri ambayo inatoa maji mazuri, lakini yote imekufa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba wanaoangalia vyanzo vya maji ni watu wa mazingira, tunaomba na Wizara ya Maji isaidiane na Wizara hiyo pamoja na TAMISEMI kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji na mito zile chemichemi zinalindwa ili kuweza kusaidia watu wa vijijini ambao inawezekana wasipate huduma ya maji ya bomba ambayo tunaiongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la kuongeza fedha katika mafuta. Ni kweli tulipitisha miaka mitatu na mimi naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Chenge, hatukatai kukata hiyo shilingi 50, je, implementation yake itakuwaje? Hata za REA haziendi zote. Kama miradi ya REA fedha mnaziweka kwenye Mfuko Mkuu mnafanya mnavyotaka, maana Serikali hii ya CCM sasa hivi hata bajeti hamuiheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitisha bajeti hapa, tunatengeneza na sheria zile zinazofuata pale za kutekeleza bajeti lakini hata wakati mwingine haifuatwi.

WABUNGE FULANI: Wakati wote.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Wanasema ni wakati wote. Kuna miradi mikubwa mingine hatusemi ni mibaya, lakini je ilikuwa katika bajeti na kama inakomba fedha zote, zile fedha ambazo zingeweza kuhudumia jamii ya Watanzania zitatoka wapi. Je, mnatuhakikishiaje kwamba zile fedha zitakuwa kwenye mfuko wake ili wananchi waweze kupata maji. Maana Watanzania wanapojitolea kukatwa shilingi 50, ujue kwamba unawaongezea na gharama nyingine. Watakatwa ya maji, wanakatwa ya umeme, wanapenda kuleta maendeleo yao lakini fedha zitapelekwa kule ili miradi iweze kutekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi sipingani na hilo lakini lazima kama Wabunge tuhakikishe kwamba hizi fedha zinakwenda kutekeleza jambo ambalo sisi tumelipanga hapa. Sasa Serikali imekuwa haiheshimu Wabunge na Bunge na sisi Bunge tumekuwa na kauli za naomba, jicho la huruma, jicho la huruma gani, we want the government to do it! Tunaitaka Serikali itekeleze miradi hiyo kwa sababu tunalipa kodi na kodi zinakusanywa, hatuwezi kukaa kubembelezabembeleza jicho la huruma, jicho gani, Serikali tunaiombaomba, tunaomba jicho la huruma, ndiyo maana wanatufanyia haya. Tuwaambie we want the government to do this, tunakutaka Waziri Prof. Mbawala utupe maji, siyo tunakuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema haya kwa sababu maji yanaumiza na mnatulipia fedha za walipa kodi tunakwenda seriously. Watu wanakwenda kule, wengine wanavaa hata kabtula kupanda milima, unakuta miradi ya maji mpembuzi yakinifu pampu anaweka kule korogoni ambako anajua Mbunge hata wewe Mheshimiwa Jenista ukipanda kule ukitoka unakufa kwa sababu kupanda ile milima watu wengine mpaka wasukumwe. Pampu iko korongoni halafu maji yanakwenda mlimani, yanatoka mlimani yanashuka, hayo ndiyo mambo mnayotufanyia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nafasi niweze kuongea kidogo kuhusu hoja ya Kamati yetu ya LAAC ambayo na mimi ni Mjumbe. Kwa sababu nina muda mfupi naomba niende moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niongelee kuhusu asilimia kumi ya wanawake na vijana pamoja na wanawake na watu wenye ulemavu ambayo inapaswa itolewe na halmashauri kutoka na own source yake. Tumegundua na kwa muda mrefu katika ukaguzi wetu tuliona kwamba kuna madeni mengi ambayo halmashauri haiwezi kulipa kutokana na uwezo mdogo wa kuweza kulipwa madeni ya asilimia kumi, tumeishauri Serikali kuhusu kufuta madeni na Serikali imekubali kwa hili imefuta madeni yete ya nyuma lakini mwaka 2018/2019 michango hii inapaswa kuendelea kulipwa. Ukitazama kwamba Serikali imekubali kufuta hayo madeni, sasa napenda kujua Waziri atueleze kama amefuta madeni ya halmashauri kuna pesa ambazo tayari zilikuwa zimekuwa kwenye vikundi, je na zenyewe zimefutwa? Ina maana halmashauri inakwenda kupata hasara kwa kwa sababu hizi ni pesa ni za own source. Kwa hiyo tunapenda kupata majibu kuhusu hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri zinapeleka pesa katika Bohari ya Dawa, lakini wakati mwingine wanachewa kuleta dawa na wakati mwingine wanaleta dawa ambazo zinakaribia kuisha muda wake. Kwa hiyo na hilo tumeliona kwamba si kitu sahihi kuhakikisha kwamba MSD inatoa dawa ikizingatia kwamba halmashauri kazi yake ni kutoa huduma kwa wananchi ni pamoja na afya, elimu na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko miradi ya kimkakati, kwa mfano iko miradi ya hapa Dodoma ya stendi kuu ya mabasi na soko, lakini kule Morogoro kuna soko kuu, masoko haya yanachukua gharama kubwa, pia tunapenda kujiuliza pamoja na gharama kubwa zilizowekwa katika miradi hii na hasa masoko, je, watu wa chini wataweza kufaidika na masoko haya? Kwa sababu kwa mfano lile soko la Morogoro tumekuta kwamba katika ziara hilo soko halina mkopo hata kidogo ni pesa zimetoka Serikali Kuu pamoja na ule mradi wa kuboresha Miji. Tunachoishauri Serikali ili miradi hii iweze kutumika vizuri, basi halmashauri hizo zisiweke gharama kubwa katika kupangisha, waweke gharama ambazo zitasaidia watu wengi kuweza kuingia ndani ya soko mle na kuweza kufanya kazi na hatimaye halmashauri kupata mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda particularly kuongelea kuhusu Dodoma; ninayo hoja ya msingi na watu wa Dodoma watanisamehe na hasa Mbunge na Madiwani. Dodoma ina mapato mengi sasa hivi, wanapata mapato zaidi ya bilioni 60, wanayo miradi mikubwa ambayo wanatekeleza ni sawa, lakini Jiji la Dodoma limeshindwa kutengeneza barabara za mitaani, huko mitaani kumeoza. Napenda kusema kwamba, je, hizi barabara ni za nani, ni za Halmashauri ya Jiji, au ni za TARURA, na kama ni TARURA ina maana hawana sensa, hawajui idadi ya barabara zao walizonazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Sheria tuliyopitisha ni kwamba halmashauri ikiwa na pesa inapaswa kuichangia TARURA ili kuhakikisha kwamba inatengeneza barabara za mitaa. Hatukatai kwamba tuna miradi ya Word Bank, inatengeneza lami katika maeneo mbalimbali katika jiji, lakini kule kwenye mitaa hakuko vizuri. Kwa wale wanaokaa mitaani nafikiri mmeshaona kinachoendelea hapa, mimi mpaka nimejiuliza maswali mengi, hivi hawa Madiwani wa hapa huwa wanasema nini ndani ya Baraza lao la Madiwani, sielewi hata wachokisema, kwa sababu kama Jiji linaweza kuwa na pesa za namna hii, inawezekanaje wasitenge pesa za kuweza kutengeneza barabara hata zile za vumbi, kurekebisha kwa sababu Dodoma ni mahali ambapo ardhi mvua inaponyesha hali inakuwa mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema neno hili kwa sababu tumekagua juzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanayo mapato makubwa na wanajivuna kwa kweli, wamekusanya, wana hela nyingi. Kwa hiyo tunaomba Waziri na yeye anaishi hapa na wengine wote mnaishi hapa. Tunaomba Dodoma watutengenezee barabara za mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu TEMESA; yapo malalamiko ya wafanyakazi kwenye kivuko kwamba hawana mikataba ya ajira na hivyo kukosa fursa za kujiendeleza na hata hawawezi kukopa katika vyombo au taasisi za fedha kama wafanyakazi wengine walioajiriwa Serikalini. Naomba Serikali ifuatilie jambo hili ili wafanyakazi hawa ambao wengine wamefanya kazi kwa muda mrefu wapate haki wanazopaswa kupata kutokana na kazi wanayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya MV Victoria ni muhimu kwa usafiri kati ya Mkoa wa Kagera hasa Wilaya za Muleba, Bukoba, Misenyi, Karagwe na Kyerwa. Wananchi wote hawa wanategemea meli hasa kibiashara. Mkoa wa Kagera umegeuka dampo ya magari ya abiria yanayosafirisha abiria kutoka Bukoba – Mwanza kwa njia ya barabara. Biashara zote kutoka Mwanza kwenda Bukoba na Bukoba – Mwanza zinapita barabarani. Wananchi wanapata hasara kubwa. Malori yanapoharibika yakiwa yamebeba ndizi, huiva na kuharibika na hivyo kuwasababishia hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo ya meli hii ya MV Victoria yatakamilika lini na kiwango gani cha matengenezo kimefikiwa? Wananchi wa Kagera ambao maisha yamekuwa duni kwa kupambana na ughali wa maisha kwa bidhaa kupanda bei kutokana na kusafirisha kwa njia ya barabara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zoezi la kuhamisha walimu kutoka sekondari kwenda kufundisha shule za msingi; zoezi hili limewakatisha tamaa walimu kwa kuwaharibia malengo yao. Wapo walimu ambao walikuwa na malengo ya kufundisha sekondari na kuendelea kusoma zaidi ili wafundishe Vyuo vya Ualimu, hata Chuo Kikuu. Unapomrudisha mtu ambae alikuwa analenga huko ukampeleka kufundisha shule ya msingi unaharibu malengo yake kitu ambacho ni kibaya na ninaamini hamuwezi kuwafanyia watoto wenu hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, maandalizi ya zoezi hili hayakuwepo ni kwa nini Serikali haikutangaza ili wale wanaopenda kurudi kufundisha primary wajitokeze kwa hiari yao (naamini wapo) na wale wasiopenda wabaki. Ni hakika wapo walimu ambao wamebaki kufundisha sekondari bila kupenda kukaa huko. Hii ingetoa nafasi mtu kwenda kwa utashi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, zoezi hili limegubikwa na fitna, ukabila, siasa na rushwa pale ambapo Afisa Elimu na Mwalimu Mkuu hawapatani na mwalimu fulani anampeleka primary kama adhabu.

Mheshimiwa Mweneykiti, napenda pia kuongelea taratibu za uteuzi wa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kwenda sekondari hasa shule za kata. Katika uteuzi huu umbali hauzingatiwi, watoto wanatolewa kwenye shule za karibu na kuwapeleka mbali na nyumbani umbali wa kilometa saba hadi 10 kwenda na kurudi. Wazazi wanashindwa kutoa nauli kwa watoto wao. Naomba umbali uzingatiwe hasa kwa watoto wa kike ambao wanapewa mimba na bodaboda wanaowasafirisha kwenda mashuleni.