Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Nicholus Matiko (55 total)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwenye swali langu la msingi nimeelezea dhahiri kwamba hospitali ya Mji wa Tarime inatoa huduma kwa Wilaya nzima ya Tarime na baadhi ya wananchi wa Serengeti na Wilaya ya Rorya. Serikali imekuwa ikileta fedha za OC na bajeti ya dawa, kwa kufuata population ya Mji wa Tarime ambayo ni watu 78,000. Ppia imekuwa ikileta, fedha la kapu la pamoja kwa maana ya basket fund, milioni 106 tu ambayo haikidhi haja na zamani tulikuwa tukipokea zaidi ya milioni 500 bado huduma za afya zilikuwa siyo dhahiri.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwa nini Serikali sasa, isiweze kuleta fedha za OC na za basket fund kwa kufuata population walau ya Tarime Rorya na siyo ya Mji wa Tarime, ukizingatia kwamba tunatoa huduma kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaopata huduma ya afya kwenye hospitali ya Mji wa Tarime, wamekuwa wakitozwa sh. 6,000 lakini wakifika ndani hawapati madawa, hawapati huduma zinazostahili, ni kwa nini sasa Serikali kwa maana katika Hospitali ya Mji wa Tarime tayari tuna jengo ambalo liko tayari, kuweza kufungua duka la dawa kwa maana ya MSD ni kwa nini sasa Serikali isiweze kuja na kufungua hilo duka pale kwenye hospitali ya Mji wa Tarime ili wananchi waweze kupata huduma ya madawa wanavyoenda kutibiwa pale kuliko kuhangaika tena wanatoa sh. 6,000 halafu akitoka nje anaambiwa hamna dawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, swali la kwanza ni kwa nini Serikali, isichukulie takwimu kwamba Hospitali hii ya Mji wa Tarime inatibu pia wateja kutoka Rorya na maeneo mengine ya jirani. Jibu ni kwamba Serikali siku zote inapopanga Mpango wake wa Bajeti kwa ajili ya kuzihudumia hospitali zote nchini ina formula maalum ambayo inazingatia kigezo anachokisema cha idadi ya watu wanaohudumiwa katika hospitali. Pia, pesa zote zinazotoka kwa wafadhili zinapangwa kwenye bajeti kutokana na burden of desease, mzigo wa magonjwa ambao unahudumiwa katika eneo la kijiographia ambapo hospitali hiyo inatoa huduma.
Kwa hivyo, watu wote wanaofanya planning kwenye sekta ya afya, wanazingatia kigezo cha idadi ya watu, lakini pia mzigo ambao hospitali husika inaubeba kwa maana ya kutoa huduma zake. Kwa maana hiyo, niseme tu maelezo ya ziada hapa kwa Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, kwamba changamoto ya kuwahudumia Watanzania kwenye eneo hili la dawa, vifaa na vifaa tiba ni kubwa sana, kwa maana ya mzigo wa kibajeti ambapo Sekta ya Afya inabeba. Changamoto hiyo itaweza kutatuliwa kwa jitihada ambazo tunazifanya sasa hivi za kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na bima ya afya, hili ni jambo ambalo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi pesa tulizonazo sasa ni ndogo haziwezi kubeba mzigo wa kutibu Watanzania wote kama ambavyo tunatamani iwe, sasa tunakuja na jitihada mpya ya kuhakikisha Watanzania wote wanaingia kwenye Mfuko wa Bima ya Afya ili hospitali zenyewe ziweze kukidhi mahitaji ya madawa, vifaa tiba na vitendanishi kama ambavyo zinajipangia.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu duka la dawa la MSD. Nimpongeze Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko na wataalam wetu wa sekta ya afya kwenye hospitali ya Mji wa Tarime, kwa kuandaa eneo kwa ajili ya kuanzisha duka la MSD. Kwanza nitumie nafasi hii kwa namna ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kuanzisha mkakati, wa kufungua maduka ya MSD yaani MSD Community outlets.
Maduka haya kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanatoa huduma kwenye hospitali ya Taifa na hospitali za Kanda kwa maelekezo yake, lakini kwa kuzingatia mahitaji ya Mikoa na Wilaya zote nchini kwamba wangependa kuwa na maduka ya MSD, ili waweze kuhakikisha wananchi wanapata dawa kwa ukaribu na kwa gharama nafuu zaidi, ndani ya hospitali kuliko kuzifuata nje ya hospitali. Wizara yetu imewaelekeza MSD waandae Mpango Mkakati wa kutoa utaalam wa kiufundi wa namna ya kuanzisha maduka ya dawa, katika mfumo huu wa MSD community outlets. Taasisi yetu ya MSD, imejipanga kuwasaidia Milkoa.
Pia Taasisi yetu ya NHIF imejipanga kuingia kwenye mkakati wa kuwakopesha hospitali yoyote ile iwe ya Mkoa ama ya Wilaya, fedha kwa ajili ya kuanzisha maduka haya na MSD itatoa technical support, ikiwepo mifumo ya kuendeshea maduka haya kama mifumo ya computer ili kuweza kuyaendesha kisasa zaidi na katika mtindo ule ule ambapo maduka yetu ya MSD community outlets yanaendeshwa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa masikitiko makubwa sana nimefedheheshwa na majibu ya Wizara kwa sababu amenijibu kuhusiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mimi nimeuliza kuhusiana na Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo Mnada wa Magena upo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu, kwa kuwa katika majibu yao ambayo hayajakidhi wametamka dhahiri kwamba walifunga mnada huu kwa sababu za wizi wa ng’ombe na usalama. Kwa kuwa Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi imeanzisha Kanda Maalum ya Tarime - Rorya ambapo hivi sasa usalama umeimarika ingawa bado wanaongelea suala la wizi. Vilevile wameainisha kwenye majibu yao kwamba 1996 tu waliweza kupata Sh.260,000,000 na sasa hivi 2015 wanapata Sh.212,000,000, hawaoni kuwa Serikali inapoteza mapato mengi sana kwa kutokuanzisha ule mnada ambao ulikuwa umeshajengwa ambapo kwa sasa hivi unaweza kupata zaidi ya Sh.1,000,000,000? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni dhahiri kabisa na hata kwenye majibu yao wamesema Mnada wa Mtana, Kewenja, Nyamwaga na Chemakolele ipo katika Halmashauri ya Wilaya na ni dhahiri kabisa pia kwamba huu mnada ulihamishwa kwa sababu za kisiasa kwa sababu huwezi ukasema Kirumi ipo mpakani na Kenya. Napenda kujua sasa ni lini Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itaacha siasa iweze kufanya mambo ya kimaendeleo na Mnada wa Magena ufunguliwe ili wananchi wa Tarime wafaidike? ((Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupoteza mapato, ni kweli kabisa kuna changomoto kwamba Serikali ingeweza kupata mapato mengi zaidi kwa kuendelea na mnada ule. Hata hivyo, katika hali iliyopelekea mpaka mnada husika ukafungwa, ukweli wa mambo ni kwamba hata kukusanya mapato ilikuwa haiwezekani. Kwa sababu Serikali ina jukumu la msingi la kulinda amani na usalama, kwa kweli ilikuwa haiwezi kuendelea kuruhusu mnada ule utumike wa sababu watu mali zao zilikuwa zinapotea na walikuwa wanatishiwa maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, hakuna shughuli za kiuchumi ambazo zilikuwa zinaenda kama ilivyotarajiwa. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ingeweza kupata mapato lakini haikuwezekana kuendelea kuwa na shughuli yoyote katika hali ambayo si salama. Hata yeye mwenyewe amekiri kwamba kulikuwa na hali ya kutishia amani na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mnada husika kufungwa na mwingine kuanzishwa kisiasa, nimhakikishie tu Mheshimiwa Matiko kwamba kilichopelekea mnada huu kufungwa na mwingine kuanzishwa siyo sababu za kisiasa ni kwa sababu ulinzi na usalama wa wananchi wa Tarime ulikuwa ni wa muhimu zaidi. Vilevile nimhakikishie tu kwamba kwa hali ya sasa mnada ule mpya unafanya kazi kama ile iliyokuwa inafanywa na mnada wa awali. Cha maana ni wananchi kupata fursa ya kuuza mifugo yao kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna mnada ambao unafanya kazi ileile vizuri zaidi na hauhatarishi usalama, kwa vyovyote vile Serikali itachukua uamuzi wa kuhakikisha kwamba mnada huo unaendelea badala ya kufikiri kwamba ni lazima kurudi kwenye mnada ambao kwa kweli uendeshaji wake ulikuwa unatishia ulinzi na usalama.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kweli majibu yaliyopatikana leo, ni dhahiri kabisa hata Serikali haijui mipaka ya Kata. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwa kinywa kwamba wanatwaa ardhi kwa kufuata Sheria ya mwaka 1999 na kwa kuwa JWTZ hawakufuata sheria, mwanzoni waliomba hifadhi ya miezi mitatu katika Kata ya Nkende, walivyopewa wakaamua kuhodhi na Kata ya Nyamisangura na Nkende na Nyamisangura, siyo eneo la Nyandoto. Kikosi cha Jeshi kinatakiwa kukaa Kata ya Nyandoto na siyo Nyamisangura na Nkende.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu hawakufuata Sheria ya mwaka 1999, kama alivyotamka mwenyewe, haoni sasa kwamba ni dhahiri wananchi hawa wanatakiwa kuhodhi maeneo yao kama mlivyoyateka mwaka 2008 mpaka sasa hivi, mwaache waendeleze shughuli zao za kiuchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Waziri anasema kwamba wanaenda kukamilisha utathmini, ifahamike kwamba waliwazuia wananchi hawa kufanya shughuli za maendeleo kuanzia mwaka 2008, hawafanyi shughuli zozote za maendeleo. Sasa hiyo tathmini ambayo Waziri anakiri kwamba anaenda kuikamilisha mwaka huu, napenda kujua na wananchi wa Tarime wajue kwamba mtazingatia hali halisi ya mwaka 2007, ambapo Wanajeshi hao waliwakataza wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo; nyumba zimebomoka, vyoo vimebomoka, mashamba yameshakuwa chakavu sasa hivi ni ardhi tu; huo utathmini ambao mnaenda kuufanya sasa hivi, unazingatia vigezo vipi? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba wananchi walizuiliwa kuendelea na shughuli za uchumi kwa sababu ya kuweka Kiteule cha Jeshi.
Napenda Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba amani na usalama katika eneo nalo ni muhimu kwa ajili ya shughuli za uchumi. Kwa hiyo, maelewano yalifanyika kwamba wananchi wapishe Jeshi hapo kwa ajili ya shughuli za usalama ili na wao waweze kupata fidia.
Kwa hiyo, hatua tuliyofikia ni nzuri naweza nikasema, kwa sababu sasa tunasema kwamba fedha za uthamini zimeshapatikana na zimeshatumwa kwenye Halmashauri. Ni jukumu la Halmashauri kukamilisha uthamini ili wananchi hao waweze kulipwa fidia inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu tathmini kuchukua viwango vya mwaka 2007 au sasa, kwa mtazamo ni kwamba viwango vya sasa vitakuwa vikubwa zaidi kuliko mwaka 2007.
Kwa hiyo, tunachosema tu ni kwamba, kwasababu uthamini huu unafanywa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, ni vyema Mheshimiwa Mbunge ukashirikiana na Halmashuri yako pamoja na watendaji wa Wizara yangu ili kuweza kupata tathmini stahiki bila ya mtu yeyote kuonewa. Kama kweli kuna nyumba ambazo zilikuwepo ambazo zimebomoka, tutalizingatia hilo ili kila mtu aweze kupata fidia yake anayostahili.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba, posho za Madiwani kwa maana ya vikao na posho za Wenyeviti wa Mitaa, Vitongoji na Vijiji zinalipwa na Halmashauri na kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwamba wanatambua kuna Halmashauri zingine hazina uwezo, makusanyo ya ndani ni madogo kama ilivyo Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini sasa Serikali isione ni vema mathalani kwenye vikao vya Madiwani ambavyo tumeona vinatofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine, wengine wanalipwa 60,000, wengine 80,000 wengine 250,000 wengine 300,000, kwa nini wasi-standardize iwe kama tunavyolipwa posho Wabunge kwa Tanzania nzima na iweze kutenga fedha, isitegemee mapato ya Halmashauri ili Madiwani wanavyokaa vikao vyao waweze kulipwa fedha ambazo ni uniform kwa Tanzania nzima, vilevile kwa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kuhusuiana na suala la Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji na Vijiji. Tumeshuhudia wananchi wakienda kupata huduma majumbani kwao. Serikali inajibu kwamba, inategemea mapato ya Halmashauri. Narudi pale pale tuna Halmashauri zingine mapato ni madogo sana na haiwezi kujenga Ofisi za Wenyeviti. Kwa mfano, kwangu Halmashauri ya Mji tuna Mitaa 81 Halmashauri ya Mji wa Tarime haiwezi ikajenga hizo ofisi. Kwa nini sasa Serikali isione umuhimu kuwapatia hawa Viongozi ofisi zao iwajengee, itenge fungu kutoka Serikalini ishuke chini kwenye Halmashauri zote nchini iweze kujengewa ofisi ili kuepuka adha ambayo inaweza kupelekea hata wengine kushawishika na kutoa na vitu vingine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vitongoji lakini pia Wenyeviti wa Vijiji wanafanya kazi nzuri sana na kila mmoja anajua. Lakini pia ndiyo ambao wanazisaidia sana hizi Halmashauri katika kutekeleza shughuli zake ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa hayo mapato yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni jambo la kusikitisha na linashangaza na tutachukua hatua kali sana kusema ukweli kwa Halmashauri zote ambazo hazitaheshimu formular ile ya asilimia 20 ya mapato ya ndani kuzipeleka kwa hawa watu muhimu sana wanaowasaidia katika kutekeleza miradi lakini pia kukusanya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itahakikisha inalisimamia jambo hili, lakini tusaidiane Waheshimiwa Wabunge ninyi ndiyo Wajumbe wa Halmashauri zenu huko. Haya yanafanywa na watu ambao wako chini yenu kabisa kinidhamu, kwahiyo ni vizuri tukasikia huko mnachukuliana hatua kwa sababu mna hiyo mamlaka na sisi tukaja kusaidia pale tu ambapo huyu mtu amekuwa ni tatizo sugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vigumu pia kuweka standard formula na standard formula tulioiweka kama Serikali tumesema ni asilimia 20 ya mapato ya ndani, kwa sababu kwanza kabisa ili uweze ku-establish Halmashauri lazima vigezo kadhaa uweze kuvifikia ikiwa ni pamoja na hali ya uchumi wa eneo husika. Sasa tulipokuwa tunaomba Halmashauri, tunaomba tu ili tuweze kuzipata, lakini tunakuja kupata shida pale inapokuwa vigezo vile tulivyovisema siyo halisi kwa sababu huko kiwango cha uwezo wa ndani ndiyo unao-determine uanzishwaji wa Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naamini kwa Halmashauri zilizoanzishwa na kama kweli zilikidhi vigezo vilivyopo kwa mujibu wa sharia, basi haziwezi zikashindwa kabisa kuweza kuwalipa posho hawa watu muhimu sana katika ngazi ya Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Kwa sababu hawa watu kama nilivyosema ndiyo wanaosaidia kukusanya mapato hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili juu ya ofisi za Viongozi hawa muhimu ni kweli tungeweza kusema ni jambo zuri kwamba nchi nzima tukawa na utaratibu wa kujenga ofisi hizi zote, lakini kama mnavyofahamu bajeti yetu ni hiyo moja na kupanga ni kuchagua, ndiyo maana tumeziachia Halmashauri kwa dhana ya kupanga vipaumbele vyao, basi kama kipaumbele cha Halmashauri fulani ni ofisi hizi tunaweza tukaanza na hizo na sisi Serikali Kuu tutatenga kwenye bajeti yetu kwa kadiri ya sealing ilivyopangwa kuhakikisha kwamba, tuna-facilitate au tuna-fund miradi ambayo imeibuliwa kutoka huko chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Halmashauri kuhakikisha kwamba kutokana na makusanyo yao ya ndani ambayo hayana masharti kutoka Serikali Kuu, basi wanapanga kupunguza upungufu huo wa ofisi kila mara wanapopanga katika bajeti zao.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo yaliyopo kwenye Kituo cha Afya cha Chamwino ni sawa sawa na matatizo yaliyopo kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo inahudumia takribani wananchi zaidi ya 500,000, hawana kifaa cha ultra sound. Ningependa kujua sasa ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa dhati kabisa wa kuleta huduma hii ya kifaa cha ultra sound kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ili kuondoa hizi adha kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimemsikia Mheshimiwa Esther, lakini katika jibu langu la msingi alishasikia pale awali. Mimi naamini kwamba ni kweli changamoto hii ni kubwa na ndiyo maana katika mwaka huu ukiangalia katika bajeti yetu ya TAMISEMI, development budget karibuni ni shilingi bilioni 182.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hiyo kuna sehemu zingine watu wameweka vipaumbele vya vifaa tiba, wengine wameweka magari ya wagonjwa, wengine wameweka miundombinu kujenga wodi za wazazi. Kwahiyo, japokuwa hii ni changamoto iliyopo pale Tarime naomba vilevile Waheshimiwa Wabunge tutumie fursa zinazowezekana katika mchakato wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ni kwamba mchakato wa bajeti wa mwaka huu ulivyokuja Wabunge wengi sana tulikuwa katika vikao vingine vya Kamati, inawezekana hiyo ndio ndo ikawa miongoni mwa changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huko mbeleni tunapokwenda tuangalie jinsi gani tufanye ili michakato ya bajeti itakavyoendelea sisi Wabunge tuwe mbele kuwa main stakeholders katika ile budget process. Hii itasaidia vile vipaumbele ambavyo sisi kama Wabunge wa majimbo tunaona kwamba ni jambo la msingi kuwa katika bajeti yetu viweze kufanyiwa kazi.
Hata hivyo Mheshimiwa Esther Matiko nimelisikia jambo hili, tutawaambia wadau mbalimbali kuona ni jinsi gani wanaweza wakatusaidia. Lengo letu kubwa ni kwamba mwananchi katika kila angle katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aweze kupata huduma bora na mama aweze kunusurika katika suala zima la uzazi.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa magereza mengi nchini ni kweli miundombinu ni michakavu sana; na kwa kuwa asilimia zaidi ya 75 mahabusu waliopo magereza ni wale ambao wana kesi za kudhaminika lakini wananyimwa dhamana. Swali langu linakuja kwamba Gereza la Tarime linachukua mahabusu na wafungwa kutoka Wilaya ya Rorya na unakuta ina msongamano mkubwa kutoka 209 mpaka 560 mpaka 600.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa Serikali ni lini itajenga gereza Rorya, kwa sababu ile ni Wilaya inajitegemea, ili kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa Tarime ambayo inaweza ikapelekea magonjwa mbalimbali na ukizingatia miundombinu ni mibovu sana? Lakini pia kwa haki za kibinadamu wanatoka kule Rorya kufuatilia kesi Tarime, kuja kuona mahabusu Tarime, kuja kuona wafungwa Tarime. Ni lini sasa mtajenga Gereza la Rorya kupunguza msongamano katika Gereza la Tarime? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba kuna msongamano wa wafungwa katika Gereza la Rorya na kuna umuhimu mkubwa wa kujenga Gereza pale. Lakini changamoto ya upungufu wa magereza katika Wilaya zetu mbalimbali nchini halipo Rorya tu; kwenye maeneo mengi ya Wilaya nchini bado magereza yamekuwa ni upungufu.
Kwa hiyo tutajaribu kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano huo kwa kujenga magereza katika Wilaya ambazo zina upungufu katika nchi nzima, na utekelezaji wa mpango huo utategemea upatikanaji wa rasilimali fedha, kwani mpaka sasa hivi kati ya Wilaya 92 ni Wilaya 43 nchini ndio ambazo zina magereza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi tunalifahamu hili tatizo, niombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira pale ambapo hali itakapo ruhusu tutashughulikia pamoja na hizo Wilaya nyingine 43 ambazo nimezizungumza zenye mapungufu hayo. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Askari Magereza wapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa kuwa Askari Magereza na wenyewe wanajiendeleza, wanapata shahada, wanapata elimu ya juu zaidi, lakini mishahara yao imekuwa ikibaki kuwa ile ile ambayo haitofautiani na askari wa kawaida aliye na cheti cha form four. Ukiangalia Jeshi la Polisi mtu mwenye shahada anapata sh. 860,000 lakini pia anapata posho ya ujuzi asilimia 15, kwa Askari Magereza wanalipwa sh. 400,000 wakikatwa inabaki 335,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao maana imekuwa ikiwaahidi kwamba itawaongezea mshahara kulingana na ujuzi wao, lakini mpaka leo bado. Ni lini sasa itakwenda kuwalipa Askari Magereza kulingana na ujuzi wao ili kuwapa motisha kama askari wengine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko hususan katika masuala mazima ya kupanga mishahara ya Askari Magereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua katika kada mbalimbali si wote ambao wanapata mishahara ambayo inaendana na kazi zao. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Esther Matiko, tayari tumeshaanza zoezi la tathmini ya kazi na hata ninavyoongea hapa watu wangu wa Bodi ya Mishahara wako hapa Bunge, wameshaongea na Tume ya Huduma za Bunge, lakini vilevile wameshazunguka nchi nzima kuongea na kada mbalimbali. Ifikapo mwezi wa Pili zoezi hili litakuwa limekamilika na baada ya hapo tukae sasa kupanga uwiano wa kazi pamoja na uzito wa majukumu kwa kada moja baada ya nyingine tukitambua ugumu wao wa kazi pamoja na majukumu yao. Vile vile tutaweza kupanga pia miundo yao pamoja na madaraja yao katika ngazi za mshahara. Kwa hiyo, nimhakikishie zoezi hili litaweza kufanyika kwa Askari Magereza, lakini vilevile kwa watumishi wote wa umma kwa ujumla wake.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa tatizo la maji lililopo Jimbo la Mpwapwa linaonesha uhalisia wa ukosefu wa maji Tanzania nzima likiwepo Jimbo la Tarime Mjini, na kwa kuwa maji safi na salama ni muhimu kwa afya za binadamu; ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaona kuna umuhimu wa kuwapatia maji wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini maji safi na salama kwa kutekeleza bajeti ambayo tuliipitisha hapa, ambayo bado hamjaanza kuitekeleza mpaka sasa hivi, ili wananchi wa Tarime Mjini na Tanzania kwa ujumla waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokisema ni kweli, tatizo la maji sio Tarime tu, ni nchi nzima, na ndiyo maana katika mipango ya Serikali tumejielekeza jinsi gani tutafanya kuhakikisha tatizo la maji tuweze kulipunguza. Hata sasa hivi katika halmashauri zetu ukiangalia, takribani shilingi bilioni 25 zimepelekwa ili miradi ya maji iweze kufanyika katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba sisi dhamira yetu ya dhati ni kuhakikisha katika bajeti ta mwaka huu ambayo Serikali inafanya mpango, utaratibu mzuri wa kupeleka hizi fedha, utafikia mahali pazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Matiko asiwe na hofu katika hili, tutasimamia bajeti za Halmashauri, lengo letu ni kwamba ile bajeti ya karibu halmashauri zote na TAMISEMI, zaidi ya shilingi trilioni 6.4 ziweze kutekelezeka katika mwaka huu wa fedha. Na hili ni wazi kwa sababu mchakato wa ukusanyaji wa mapato unavyoendelea Serikali tuta-pump hizo pesa lakini sisi tuliopewa dhamana ya kusimamia tutahakikisha tunasimamia wananchi waweze kupata huduma ya maji.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kiukweli majibu ya Mheshimiwa Waziri yapo kiujumla zaidi na inasikitisha kwa sababu tunapokuwa tunatoa maswali yetu tunatarajia mwende sehemu husika kujua uhalisia wa sehemu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mahabusu waliopo Gereza la Tarime, zaidi ya asilimia 65 ni kesi au makosa ambayo yanatakiwa yapewe dhamana; na kwa kuwa kesi nyingi ni kesi za kisiasa za kubambikwa na nyingine ni kesi za watoto chini ya miaka 15; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alikuja Tarime na hakupata muda wa kuingia Gerezani, ningependa sasa leo mtuambie ni lini Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkurugenzi wa Mashtaka watakuja Tarime kuangalia hali halisi ya mahabusu walioko Gereza la Tarime ili waweze kuondoa zile kesi ambazo jana Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba nyingine ni za juice, ili Watanzania warudi uraiani na wafanye kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna msongamano mkubwa sana kwenye Gereza la Tarime, capacity yake ilikuwa ni watu 260 wakiwa wamezidi sana. Sasa hivi ni zaidi ya watu 600; na kwa kuwa ukitokea mlipuko wa magonjwa tutapoteza Watanzania wengi waliopo kwenye lile Gereza; na kwa kuwa gereza lile linahudumia Wilaya ya Rorya na Tarime: ni lini sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi mtajenga gereza katika Wilaya ya Rorya, mtajenga Mahakama ya Wilaya kule Rorya ili wale Watanzania wa Rorya waweze kushtakiwa kule na kuhudhuria kesi zao kule ili kuondoa msongamano ambao upo katika Gereza la Tarime?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwape pole timu yangu ya Magereza (Tanzania Prisons) kwa kushindwa jana kwa figisu za Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda zilipocheza na Ndanda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Katiba na Sheria tutalifanyia kazi jambo hilo; huo ni wajibu wetu na tumekuwa tukifanya hivyo. Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria ameshafika Mkoa wa Geita, ameshafika Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Kagera na anakuwa na Ofisi ya DPP na anakuwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani. Nikubaliane nalo, hilo tutafanya, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba wale ambao kwa kweli wanaweza wakapata namna ya kwenda nje waende nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitofautiane na Mheshimiwa Mbunge kwenye takwimu, anasema asilimia 75 ya kesi ni za Wanasiasa. Natofautiana naye kwa sababu amesema asilimia 75 ni za wanasiasa na wakati ule ule ni za watoto. Huwezi ukawa na asilimia 75 ya wanasiasa na watoto. Kwa hiyo, kwenye hilo siyo kweli na kama kuna issue specific ya kesi ya mtu mmoja mmoja, Waheshimiwa Wabunge ninyi ni Viongozi, tusaidiane kupeana taarifa ili tuweze kufanya intervention inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga gereza Rorya hata Mheshimiwa Mbunge wa Rorya amelisema mara nyingi na ameongelea matatizo wanayopata wananchi wake. Ni kweli wanapata shida kwa sababu mashahidi wanatakiwa kutoka Rorya na ni gharama hata kwa Serikali kuwatoa watu Wilaya nyingine kwenda kutoa ushahidi katika Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo tumelipokea na kama Serikali tunachukua hatua kwa Wilaya zote mpya ambazo zimeanzishwa, ambazo bado hazina huduma hizo za Mahakama pamoja na Magereza, kuhakikisha kwamba tunawapunguzia usumbufu wananchi na sheria iweze kuchukua mkondo wake kwa wakati.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kiukweli nasikitika kwa majibu ya Waziri wa Katiba na Sheria kuhusiana na umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Rorya. Tangu Bunge la Kumi nakumbuka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nimekuwa nikiongelea suala zima la kupatikana kwa Mahakama ya Wilaya ya Rorya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kukiwa hakuna Mahakama Wilaya ya Rorya, Mahakama ya Wilaya ya Tarime inakuwa na kesi nyingi na ndiyo maana mwisho wa siku tunakuwa na mrundikano wa kesi ambazo hazifanyiwi uamuzi kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Rorya tayari wana ardhi na kwa sababu tumekuwa tukiongea umuhimu kuwa na Mahakama ya Wilaya ya Rorya tangu Bunge la Kumi, ni vegezo vipi ambavyo vilitumika kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 wasipeleke Mahakama ya Wilaya Rorya wakaamua kupeleka sehemu nyingine Tanzania ikizingatiwa jiografia ya Wilaya Rorya ni kubwa, watu wanatoka mbali sana kuja Wilaya ya Tarime. Naomba kujua ni vigezo vipi vimetumika kwa Serikali isiweze kujenga Mahakama ya Wilaya ya Rorya mwaka huu wa fedha hadi waseme ni mwaka ujao wa fedha?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nimetamka mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tuna tatizo kubwa la miundombinu ya mahakama, kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu katika nchi yetu. Nimelieleza wazi hili na tatizo hili haliko Rorya tu!
Mheshimiwa Spika, nilimeshaeleza wakati ninajibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge watatu katika Mikutano iliyopita kwamba ninalishukuru Bunge lako Tukufu limetupitishia shilingi bilioni 46.76 kwenye Mfuko wa Mahakama na hizo shilingi bilioni 46.76, tutatumia shilingi bilioni 36 kujengea mahakama hii haijapata kutokea. Vilevile, tuna fedha ambayo mapema mwaka huu, mnakumbuka Mheshimiwa Rais aliagiza wapewe zote mahakama shilingi bilioni 12.3 jumla ni bilioni 48.3.
Mheshimiwa Spika, tumesema tunaanza kwa ujenzi wa mahakama 40 katika mwaka huu wa fedha, ninaomba utuamini kwa sababu mahakama sasa hivi imeshaanza ujenzi wa kisasa wa mahakama tena nafuu, lakini ujenzi uliyo bora kwa miezi mitatu anapata mahakama ya kisasa kama tulivyofanya mahakama ya Wilaya ya Kibaha.
Namuomba Mheshimiwa Mbunge avumilie tu, tumeipanga Rorya katika mwaka wa fedha 2017/2018, wavumilie kama Wilaya zingine zinavyovumilia kwa sasa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naitwa Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kabisa kwamba ukosefu wa nyumba za walimu na kukaa mbali na shule unasababisha kutokuwa na kiwango kizuri cha ufundishaji kwenye shule zetu. Hivi karibuni tulisikia kauli ya Waziri Mkuu akitoa msisitizo kwamba walimu waishi kwenye shule ambazo wanafundisha. Kwa majibu ya Naibu Waziri ni dhahiri bado Serikali haijawa na mpango madhubuti wa kuhakikisha walimu wanakaa kwenye maeneo ambayo wanafundisha.
Ni nini mpango mkakati wa Serikali hasa kwa pale ambapo wananchi wamejenga maboma wanashindwa kuyamalizia ili watoto wetu waweze kupata elimu mbadala kwa Walimu kukaa maeneo ya shule. Napenda kupata mkakati ambao unatekelezeka siyo wa kuandikwa tu kwenye makaratasi, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza na kuongezea kwenye swali la msingi pia ambalo limejibiwa na Naibu Waziri vizuri kabisa, Mheshimiwa Jafo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna mahitaji makubwa ya madarasa, tuna mahitaji makubwa ya nyumba za walimu. Kwa mfano, tuna upungufu wa madarasa katika shule ya msingi kwa sasa 127,745. Tuna upungufu wa madarasa kwa shule za sekondari 10,204. Hali kadhalika tuna upungufu wa nyumba za walimu. Mipango yote, mpango uwe mpango mkakati, uwe mpango wa haraka, uwe mpango wa dharura, inafanyika kwenye Halmashauri zetu. Tusitegemee kwamba tutakuja na mpango fulani nje ya mipango ile ya Halmashauri, kwa sababu Serikali kwa mujibu wa Katiba, kwa mujibu wa sheria, tunatekeleza dhana ya ugatuaji wa madaraka.
Mheshimiwa Spika, kugatua madaraka maana yake ni kwamba tupange vipaumbele sisi tulioko huko kwa wananchi. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kwanza kuwapongeza sana wananchi wote wa Tanzania wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, kwa namna tulivyoshirikiana vizuri sana katika suala la kupunguza upungufu wa madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo sasa, tuangalie namna ya kwenda kwenye mchakato wa kupunguza tatizo la nyumba za walimu na madarasa. Tukifikiri kuna njia nyingine nadhani tutakuwa tunajidanganya, ukweli ni kwamba lazima tujipange wenyewe kwa kutumia rasilimali zilizopo na ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu tunayoiandaa, msisitizo mkubwa ambao tumeelekeza Halmashauri sisi TAMISEMI ni kwamba wajipange sana kuweka fedha nyingi na mipango mikubwa kwenye madarasa na nyumba za walimu. Hii itatusaidia ili hata Serikali kama ikitoa fedha yoyote ile, itakwenda kwa njia hiyo ili kutekeleza upungufu uliopo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Tarime Mjini lina kata nane na kati ya kata nane, kata nne ziko pembezoni na hazina umeme kabisa na kata mbili zina umeme kwa asilimia chache. Ningependa kujua commitment ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini wanapata umeme kwa asilimia zaidi ya 90.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Esther, tumeshirikiana naye sana kwenye mradi wa REA Awamu ya Pili na ni kweli kuna kata nne na kata nyingine mbili ambazo hazijaguswa kabisa. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Esther kwamba Jimbo lako pamoja na Mkoa wa Mara tumeshaanza kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu wa desification. Hapa ninapozungumza wiki ijayo mkandarasi ata-report kwake ili amwelekeze maeneo mahususi. Kwa hiyo, kata zake nne na zile tatu ambazo anazungumza Mheshimiwa Mbunge zitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza mwezi wa Tatu na kuendelea.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru. Kwa kweli niendelee kusikitika kwamba Serikali inashindwa kuona barabara ambazo zinaweza zikaongeza chachu ya ukuaji wa uchumi kwenye nchi yetu kupitia utalii.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua ni lini Barabara ya Tarime – Nata kwa maana ya kwenda Mugumu itakamilika kwa kiwango cha lami? Mheshimiwa Naibu Waziri anatueleza
kwamba upembuzi yakinifu unakamilika 2018, watalii wengi wanaotoka Kenya wanapita Tarime wanaenda Serengeti, tukiboresha ile barabara kwa kiwango cha lami tutakwenda kukuza uchumi wetu kwa sababu watalii wengi watapita
kwa sababu barabara inapitika. Ni lini sasa Serikali itajicommit, isiseme leo itamaliza upembuzi yakinifu 2018, ione kuna uhitaji wa haraka sana wa kujenga barabara ya Tarime – Mugumu na iweze kumalizika ndani ya mwaka mmoja kama ikiwezekana tuweze kukuza uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa barabara tuna hatua tatu muhimu na hatua hizi ni lazima zikamilike. Hatua ya kwanza ni upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Baada ya Serikali kuiona barabara hii kwamba ina umuhimu na inaongeza mapato yetu katika utalii imeamua kuianza hiyo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hiyo itakamilika mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, baada ya kazi hiyo kukamilika,
hatua ya pili itakayofuata ni kutafuta fedha za ujenzi wa barabara hiyo. Huwezi ukajenga barabara bila fedha. Kwa hiyo, Serikali itatafuta fedha ili tuanze kujenga barabara hiyo.
Tukishapata fedha tutatangaza tumpate mkandarasi wa kuanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nasikitika kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani leo hii inaita kwamba ni Wilaya ya Tarime/Rorya haijui kwamba ni Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masikitiko yangu, nipende kumwambia Naibu Waziri kwamba tayari tuna miuondombinu kwa maana ya mtandao wa TRA pale, tayari wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamejenga hilo jengo na tuna rasilimali watu. Sasa nataka kujua ni lini sasa baada ya kutambua kwamba Tarime/Rorya ni Mkoa wa Kipolisi na hivyo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Kipolisi, ni lini mtakuja kufunga huo mtambo ili kupunguza adha ya wananchi kwenda kwenye Mkoa wa Polisi wa Mara kutafuta huduma? (Makofi)
Swali la pili ni kuhusiana na kujenga ofisi ya Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ambao Mheshimiwa Waziri amesema ni mkoa mpya. Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ni wa siku nyingi ukilinganisha na Katavi, Simiyu na Geita. Kwa mikakati yenu ya ndani ningependa kujua ni lini mtakuja kujenga jengo zuri lenye hadhi ya Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya ili kuondokana na kukaa kwenye magodauni ambayo wanakaa sasa hivi na kushusha hadhi ya Kipolisi Mkoa wa Tarime/Rorya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nirudie majibu yangu ya msingi ambayo nimejibu kwamba, changamoto kubwa ambayo inakabili kutokukamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi na miundombinu mingine ikiwemo hii miundombinu ya utoaji wa leseni ni ufinyu wa kibajeti. Azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba mikoa na wilaya zote nchini zinapata huduma hizo muhimu. Changamoto nyingine kubwa ambayo nimeizungumza ni katika mikoa ile mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue fursa hii kumhamasisha Mheshimiwa Mbunge, nimefanya ziara katika maeneo mbalimbali ikiwemo hii mikoa mipya na nimeona jitihada mbalimbali ambazo viongozi wa maeneo hayo wamekuwa wakifanya ili kuhamasisha wananchi, pamoja na sisi tupo tayari kuweza kuwasaidia nguvu kazi kupitia Jeshi la Magereza kuanza mchakato wa ujenzi wa vituo vya kisasa kwa mikoa mipya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati hayo yakiendelea tutaendelea kuhakikisha kwamba tunajitahidi itakavyowezekana kadri ya bajeti itakavyoruhusu kwa upande wetu kujenga vituo hivyo vya Polisi, wakati huo huo kuzungumza na mamlaka ya TRA kuhakikisha kwamba huduma za utoaji leseni zinapatikana katika mikoa na wilaya zote nchini Tanzania, ikiwemo sehemu ambayo Mheshimiwa Mbunge anatoka.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Tarime miundombinu yake ni mibovu sana na haina hadhi ya kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Kwa bajeti ya mwaka jana 2016/2017, Serikali iliahidi hapa kwamba Vyuo vyote vya Wananchi vitapandishwa hadhi na kuwa VETA. Napenda kujua sasa ni lini Serikali itaenda kutimiza azma yake ya kupandisha Vyuo hivi vya Wananchi kuwa VETA kwa kuanzia na Chuo cha Wananchi cha Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kuna dhana ya kufikiria kwamba labda mafunzo yanayotolewa na VETA ni bora zaidi kuliko yale yanayotolewa na Chuo cha Wananchi. Nitake tu kusema kwamba Vyuo vya Wananchi vina uwezo mzuri na mkubwa sana katika kutoa mafunzo isipokuwa kwa muda mrefu vilikuwa havijapewa haki yake ya kuendelezwa na kufanyiwa ukarabati unaostahili pamoja na kuwekewa miundombinu na vitendea kazi vya kufundishia kama inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kufuatilia vyuo hivyo na kuvirekebisha. Kwa hali hiyo, tutafuatilia pia Chuo cha Tarime kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge ili kiweze kusaidiwa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina Hospitali ambayo ni Hospitali ya Mji, lakini inahudumia Wilaya nzima, ningetaka kujua ni lini Serikali itajenga Hospitali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati inasubiria kujenga, iipe ile hadhi kama Hospitali ya Wilaya na kuweza kuleta mahitaji kama inavyotakiwa kwa idadi wa watu wa Tarime nzima na siyo Halmashauri ya Mji tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kesi anayoizungumzia Mheshimiwa Esther hapa inafanana na ya ndugu yangu Mheshimiwa Chumi, tuna Halmashauri zile za Mji na Halmashauri za Wilaya, kwa bahati mbaya ukiangalia Tarime Halmashauri ya Mji ndiyo ina hospitali, Halmashauri ya Wilaya haina hospitali na bajeti mnayopata ni ndogo, hali kadhalika ukiangalia Mufindi na Mafinga, Mafinga kuna Hospitali ya Wilaya bajeti ikienda inakuwa ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita maeneo mbalimbali niliwapa maelekezo watu, kwa nini maeneo ambayo hakuna Hospitali ya Wilaya kama kuna hospitali zingine zile za mission tunaweka DDH na tunapeleka funds pale kwa nini kunapokuwa kwa mfano katika Halmashauri ya Tarime kuna Hospitali ya Wilaya, kwa nini watu wa Halmashauri ya Wilaya pale, fedha tunazozipeleka ambao wana bajeti kubwa sana wasielekeze fedha zingine kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba katika Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo nadhani hasa Wakurugenzi wetu katika maeneo husika na viongozi mliopo huko tuangalie haja ya wananchi wetu kuweza kuwahudumia, hili ni jambo kubwa na shirikishi. Kwa hiyo, naomba niagize, katika maeneo ambayo yana scenario kama hii, lazima viongozi mkae muangalie ni jinsi gani tutafanya tuweze kuhudumia eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nakuunga mkono Mheshimiwa Esther Matiko ni jambo lenye mantiki na lina busara zaidi, naomba maagizo haya yachukuliwe sehemu zote kama ni jambo la kujifunza, nini tufanye tuwasaidie wananchi wetu katika suala la afya. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, wakati Naibu Waziri anajibu alielezea ni jinsi gani moshi wa bangi unamuathiri si tu mtumiaji bali hata watu wa pembeni.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiona wakati Serikali inafanya operation ya kukata au kuzuia bangi, inavuna yale mabangi yaliyokwisha komaa, na wanaenda wanachoma zile bangi, sasa Naibu Waziri atueleze ni kwa kiasi gani Jeshi la Polisi wameweza kuathirika na ile bangi na je, hawaoni kwamba zile bangi zinawaathiri ndio maana wanatenda kinyume na wajibu wao wanavyowatakiwa kufanya?(Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwamba kwanza sio jambo la mzaha kuzungumzia masuala yanayohusu dawa za kulevya, kwa sababu zinaathiri vijana wetu, zinaharibu umakini na utimamu wa nguvu kazi ya Taifa letu.
Kwa hiyo, kujibu swali lake sasa ni kwamba wanapoenda kuchoma huwa wanakuwa wamejifunika vifaa maalum na hata kama hawajajifunika vifaa maalum, wakati wanateketeza bangi wakawa passive smoker wa cannabis bado ile bangi ikiingia kwenye mwili wao itakuwa catabolized na kupotea ndani ya miili yao ndani ya siku 30 kwa sababu metabolism ya bangi inadumu ndani ya mwili ndani ya siku 30 baada ya hapo inaisha kabisa inakuwa imekuwa katika form nyingine ya salt inatoka pamoja na mkojo.(Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo hata kama wataathirika lakini madhara yake hayatakuwa ni ya kudumu unless huyo mtu atumie bangi leo, iingie kwenye damu atumie na kesho na kesho kutwa na mwezi ujao awe chronic smoker wa cannabis hapo anaweza akapata madhara. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini Waheshimiwa Wabunge ambao wanashughulikia tatizo hili la kupambana na dawa za kulevya wanakumbuka, Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Dawa za Kulevya, mara kadhaa imeenda kwenye kamati hiyo kuelezea matumizi ya sheria na kanuni zilizotungwa chini Ofisi ya Waziri Mkuu, ambazo pia zinaongoza utaratibu mzima wa kuteketeza dawa hizi za kulevya katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, unapoona vikosi vile vinafanya
kazi ya uteketezaji wa bangi ziko technics ambazo wanazitumia katika kufanya kazi ya uteketezaji ikiwemo wakati wa uteketezaji pia, wanazingatia uelekeo wa upepo na uelekeo wa hewa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Wajumbe wa Kamati wanaelewa jambo hilo wanazingatia kwa mfano uelekeo wa upepo na maandalizi mengine ya aina ya matumizi ya vyombo vya uteketezaji ikiwepo aina ya moto utakaotumika katika uteketezaji na aina ya mafuta yatayotumika katika uteketezaji.
Kwa hiyo, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge si kweli kabisa na naomba Bunge lako liondoke hapa likijua kwamba si kweli eti kukitokea tatizo ndani ya Jeshi la Polisi ni kwa sababu wameshiriki katika kuteketeza bangi, na hivyo wameathirika na matumizi ya bangi, ninaomba hilo tuliweke wazi, kikosi kazi kimefundishwa vizuri, polisi wetu ni waadilifu na wanapofanya kazi ile wanafanya kitaalam na kwa kutumia uadilifu mkubwa na kwa kufuata utaratibu.(Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ametueleza kwamba waliondoa watumishi hewa 19,708. Ni dhahiri kwamba kuondolewa kwa wafanyakazi wenye vyeti fake kumeathiri zaidi maeneo ya elimu na afya. Napenda kujua statistically ni vipi Serikali, maana yake ametuambia wataajiri; mpaka sasa hivi Serikali imeajiri walimu wangapi na wafanyakazi wa sekta ya afya? Maana yake kuna zahanati nyingine hazina kabisa watumishi.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine unakuta shule zina walimu watatu tu, tunaweza kuona ni madhara gani watoto wetu watapata. Sasa kama walikuwa na hili zoezi la vyeti fake, walijiandaa vipi ku-replace hawa wafanyakazi kwenye sekta ya elimu na afya? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa kama nilivyoeleza, tumeshatoa vibali hivyo 10,184 na sasa hivi kwa upande wa elimu, tayari Wizara ya Elimu imeanza zoezi la kuchambua, wanatuma vyeti wale ambao walikuwa ni wahitimu na wanaostahiki kuingia, baada ya hapo watahakikiwa na kuweza kuingia katika ajira.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika walimu kwa ujumla wake, katika ku-replace watumishi ambao wameondoka kwa walimu, ni zaidi ya walimu 3,012 wataweza kuajiriwa katika zoezi hili. Pia katika suala zima la sekta ya afya, tutaajiri zaidi ya watumishi 3,152. Hili ni katika kuziba pengo la walioghushi vyeti feki. Baada ya hapo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 ajira bado ziko pale pale 52,436 na ni kutokana na hali ya uwezo wa kibajeti.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni kweli kabisa kwamba wastaafu wanateseka sana na wengi wao wanapoteza maisha. Ni katika Bunge hili hili, Mheshimiwa Naibu Waziri aliliahidi Bunge kwamba wastaafu wote wanaodai malimbikizo baada ya marekebisho ya kima cha chini kutoka shilingi 50,000 kwenda shilingi 100,000 watalipwa fedha zao kwa maana arrears zote lakini ni takribani miaka miwili sasa wastaafu hawa hawajalipwa fedha zao sana sana ni wale ambao walikuwa kwenye PSPF na PPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningetaka kujua ni kwa nini Serikali haijaweza kuwalipa hawa wastaafu haya malimbikizo kama ambavyo Naibu Waziri uliahidi Bunge hili na je mnavyoenda kuwalipa…
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukanusha kwamba ni miaka miwili wastaafu hawa hawajalipwa ile nyongeza, siyo sahihi hata kidogo. Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii wameanza kulipa kima cha chini kilichoongezwa na Serikali kuanzia mwezi Januari, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili aliloli-quote yeye kwamba niliahidi hapa, nakumbuka wakati najibu swali hili nililieleza Bunge lako Tukufu kwamba kulingana na Sheria ya SSRA, regulator anaye-regulate Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii, ni Bodi za Wadhamini za mifuko husika baada ya actuarial valuation ndizo zinazoamua sasa kulipa kiwango hiki na ndipo baada ya kufanya actuarial valuation Bodi zote zimeidhinisha na tumeanza kulipa kwa kipindi chote kuanzia Januari mpaka leo tunapoongea wote wanalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua yapo malalamiko wanasema kwamba wengine hawaoni hizo transaction lakini naomba niwaambie kwamba hasa kwa wastaafu wetu wanaolipwa na PSPF siku za nyuma pensheni zao za kila mwezi zilikuwa zikianza kulipwa kabla ya hii addition kwa hiyo kulikuwa kunaonekana kuna two transaction ndani ya mwezi mmoja kwa utofauti wa wiki moja au wiki mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali yetu inalipa nyongeza hii kwa sababu nyongeza hii hasa kwa PSPF hulipwa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina, tunalipa kwa wakati na wanalipwa siku moja pensheni yao pamoja na ile nyongeza yao. Kwa hiyo, hakuna sehemu yoyote ambapo hawalipwi.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kufuatia majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni dhahiri kabisa imeonyesha ni jinsi gani miundombinu ya kujifunzia na kujifunza katika Halmashauri ya Mji wa Tarime hairidhishi na inapelekea matokeo mabaya kwa ufaulu wa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Tarime wameitikia sana wakishirikiana na wadau mbalimbali ikiwepo mimi mwenyewe Mbunge. Tumejenga madarasa mengi lakini mengi yamekaa bila kuezekwa na kwa kuwa kuna Shule ya Msingi Mtulu ambayo imejengwa na wananchi kwa kujitolea madarasa sita pamoja na ofisi lakini Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji amezuia ile shule wananchi wasiendelee kujenga kwa kile anachokiita kwamba ni mgogoro wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sasa kupitia Wizara hii ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais na Rais ana mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi, wawatie moyo wananchi wale waliojenga yale madarasa ili sasa waweze kuamuru ile shule iendelezwe ili kupunguza adha ya upungufu wa madarasa katika Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Halmashauri ya Mji kuna shule moja ambayo inatumiwa na shule tatu, Shule za Msingi Azimio, Mapinduzi na Sabasaba. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kipindi hicho akiwa Naibu Waziri alitembelea sisi kama Halmashauri ya Mji tunataka ile shule ijengwe ghorofa ili sasa walimu wasikae kwenye mti kama Ofisi, wanafunzi wasifundishiwe nje chini ya mti, wanafunzi wasirundikane 120 kwenye darasa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini sasa Serikali isiweze kutumia ile asilimia tano ambayo walisema Waziri anaweza akapeleka kwenye matumizi mbalimbali kama tulivyoona ilivyoenda Chato kwenye uwanja wa ndege. Kwa nini msijenge ghorofa katika shule ile kwenye zile asilimia tano ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.7 ili sasa kupunguza adha ya ukosefu wa madarasa katika Mji wa Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema ukisikia upande mmoja, hakika upande ambao haujasikilizwa utakuwa lazima umekosa. Itakuwa ni vizuri tukajiridhisha sababu ambazo zimesababisha Mkurugenzi azuie uendelezaji wa hiyo shule ili tunapokuja kutoa taarifa iwe ni taarifa ambayo iko balanced. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie mbunge, miongoni mwa maeneo ambayo nitatembelea ni pamoja na kwenda kutazama uhalisia wa hiki ambacho nakisema kwa sababu lengo ni kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano wa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaase Waheshimiwa Wabunge na viongozi kwa ujumla, kwamba katika Wilaya ya Tarime, vijana ambao wanamaliza kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba wapo 25,000 lakini vijana ambao wanajiandaa kuingia darasa la kwanza wapo 13,000; kwa hiyo, unaweza ukaona sisi kama taifa kuna mambo ambayo lazima tu-address namna ya population growth inavyokwenda, tukiacha tukatizama hivi tukidhani kwamba Serikali peke yake inaweza hakika haiwezekani. Ni vizuri tukashirikishana pande zote ili kutatua matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali lake la pili juu ya ujenzi wa ghorofa, ghorofa jambo zuri na ningependa na mimi nijiridhishe halafu tuone na uwezo wetu maana unapotengeneza chakula lazima ujue na unga upo kiasi gani kwa sisi tunaokula ugali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na juu ya asilimia tano nitaomba niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge tuone hiyo asilimia tano na tutayamaliza ili tatizo hili liweze kutatuliwa lakini siamini kwamba asilimia tano inajenga ghorofa. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mkoa wa Mara una shughuli nyingi sana ambazo zingeweza kuliongezea Taifa letu uchumi kwa maana ya utalii, tuna Ziwa Victoria lakini pia makumbusho ya Baba wa Taifa. Katika majibu yake Naibu Waziri ametueleza kwamba wamefanya usanifu pia kwenye uwanja wa ndege wa Musoma, ningependa kujua uwanja wa ndege wa Musoma na wenyewe upo kati ya viwanja vilivyopewa priority maana yake umetaja Tanga tu kama ndiyo umepewa kipaumbele na unaanza kukarabatiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Kwenye jibu langu la msingi wakati najibu kuhusu uwanja wa ndege wa Tanga nilieleza viwanja 11 ambavyo vimeshafanyiwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na uwanja wa Musoma ukiwemo. Ni kweli kwamba viwanja vyote vimepewa kipaumbele kinacholingana na pesa itakapopatikana kama nilivyoeleza tutafuta mkopo kutoka Benki ya Dunia, pesa itakapopatikana basi viwanja vyote vitapewa kipaumbele kujengwa kwa sababu tunahitaji viwanka vyote vya Mikao viwe na kiwango kizuri ambacho ndege yoyote inaweza ikashuka, ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ingawa kwa kweli majibu ya Waziri, Naibu Waziri yanakatisha tamaa maana tumekuwa tukisikia siku zote kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa raia na mali zao ni muhimu sana katika nchi yetu. Kwenye Jimbo la Tarime Mjini katika Kata zote nane tuna kituo cha poilisi kwenye Kata ya Bomani tu, na Kata zingine ambazo za pembezoni wananchi wamejitolea kujenga vituo vya polisi. Tunataka kujua mkakati thabiti wa Serikali katika ku-support zile juhudi za wananchi hasa Kata ya Nyandoto, Kenyamanyoli, Nkende na Kitale ambazo ni mbali na mji, na kuna gari moja tu ambayo inafanya patrol.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati wa Serikali maanake mnakusanya mapato mengi, muweze kuelekeza kwenye kumalizia vituo vya poilisi ili tuweze kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nieleze tu kwa ufupi, ni kwamba changamoto ya vituo vya polisi haipo tu katika vituo vya polisi vya ngazi ya kata na tarafa, tuna Mikoa ya kipolisi takribani 34 nchi nzima. Kati ya hiyo majengo ambayo ya makamanda wa mikoa yaliyopo nchini ni 19. Kwa hiyo takribani mikoa 15 haina Ofisi ya Makamanda wa Mikoa. Mikoa miwili Manyara na Mara ndiyo ambapo ujenzi wa Ofisi mpya za makanda unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtaona changamoto hii ni pana sana, na ndiyo maana wakati wote tumeendelea kuwashawishi wadau werevu ikiwemo ninyi Waheshimiwa Wabunge ambao wengi wenu mmekuwa mkijitolewa na sisi tumekuwa tukichukua jitihada mbalimbali kuhamasisha wananchi kujitolea kuchangia ujenzi wa vituo hivyo vya polisi ili kabiliana na changamoto hii; wakati ambapo Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya ujenzi pamoja na ukarabati wa vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii haiwezi kumalizika kwa wakati mmoja. Naamini wewe Mheshimiwa Mbunge ni Mbunge wa Jimbo na una fedha za Mfuko wa Jimbo. Unaweza ukatumia hizo vilevile kusaidia jitihada hizi za Serikali katika kuhakikisha kwamba ina punguza changamoto ya upungufu wa vituo vya polisi nchi nzima kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata na Tarafa. Serikali kama ambavyo tunasema pale fedha zitakapopatikana tutapunguza tatizo hili hatua kwa hatua, hatuwezi tukamaliza kwa wakati mmoja.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru kwamba, Wizara inatambua kwamba Mji wa Tarime unatakiwa kupimwa, lakini pia inatambua kwamba una upungufu wa watumishi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maeneo mengi ya Mji wa Tarime yalikwishaandaliwa ramani ya Mipango Miji, lakini mpaka sasa hivi hayajapimwa, na kwa kuwa wananchi wanaendelea kujenga kiholela na kuharibu ramani ambayo tulikwishaandaa hapo awali, ni kwa nini sasa Serikali msiweze kuunda kikosi kazi kwa ajili tu ya kuja kupima maeneo yote ambayo yameshaandaliwa ramani ya mipango miji ili sasa tusiharibu hii ramani ambayo imeshaandaliwa?
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Tarime haina vifaa vya kuweza kupima ardhi na tumekuwa tukikodi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, na kwa kuwa, Halmashauri ya Mji wa Tarime hatuna fedha za kuweza kununua vifaa hivi ambavyo vinauzwa bei ghali sana, ni kwa nini sasa Serikali isiweze kufadhili ununuzi wa vifaa hivi ili kuweza kupima maeneo mengi zaidi na kuweza kuharakisha umilikishaji wa ardhi kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema maeneo mengi ya Tarime yalikuwa yamepimwa, yana michoro tayari, lakini upimaji wake pengine haujakamilika na yameanza kuvamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali hilo naomba nijibu kwamba kwanza niwaombe Halmashauri yenyewe husika kwa sababu ndio kwanza inazidi kukua sasa hivi, kama maeneo yale hayajakamilika katika upimaji niombe Halmashauri iwe makini katika kulinda yale maeneo yasivamiwe, kwa sababu katika maeneo yote yenye michoro wananchi wanapovamia, hapatakuwa na upimaji mpya. Maana yake wakikutwa wamevamia kiwanja kimoja watu wawili/watatu, maana yake pale lazima mmoja itabidi apishe apewe kile kiwanja na mwingine atafutiwe eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanya lile eneo lisiingiliwe na watu wengi zaidi niwaombe sana Halmashauri kwanza wakamilishe ile taratibu kwa sababu ni jukumu pia la Halmashauri, lakini watasaidiwa pia na Ofisi yetu ya Kanda ambayo sasa hivi wamesogezewa, itakuwa iko Simiyu. Kwa hiyo, tukishafanya hivyo tutakuwa tumelinda yale maeneo. Urasimishaji unaofanyika hauwezi kufanyika katika yale maeneo ambayo tayari yalikuwa yamepimwa, unafanyika katika maeneo ambayo yapo katika ule utaratibu upo.
Kwa hiyo, suala la kuwa na vikosi kazi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kazi hii inafanyika haraka ni jukumu pia la Kanda husika kwa sababu, tunaweza tukatumia Wataalam walioko katika Halmashauri jirani wakiratibiwa na Ofisi ya Kanda, suala hilo linaweza likafanyika na inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la vifaa; suala hili nilishalijibu pia katika majibu ya nyuma katika Bunge hili. Niombe sana Wizara haiwezi kununua vifaa vya upimaji katika Halmashauri zote, ni jukumu la kila Halmashauri kuweka bajeti zake, Wizara imejipanga katika Kanda zake na vifaa vile katika Kanda vinaweza kutumika katika Halmashauri yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi vifaa vile vina bei kubwa sana, lakini ninaomba na nimekuwa nikielekeza wale wenzetu walioko kwenye Kanda, kila mmoja ana Halmashauri zake ni kiasi cha kupanga utaratibu mzuri, mkiwa na vikosi kazi ambavyo vinaweza vikasaidia katika kwenda Halmashauri moja baada ya nyingine itaturahisishia katika kupunguza kero ya upimaji.
Kwa hiyo, naomba pamoja na private sector ambao wanatumika, bado Ofisi zetu za Kanda kwa kutumia watumishi katika Halmashauri kwenye Mkoa husika tunaweza tukapunguza tatizo hilo. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ningependa Serikali ituambie kwa muktadha wake kabisa kwa sababu haya ambayo wameelezea kuyafanya it is a peanut! Ni madogo sana. Kujenga kituo cha Makumbusho, kuwafadhili watu kupata fani ya malikale ni hela ndogo sana! Mjusi huyu tangu apelekwe kule ni kiasi gani, kwa maana ya faida kutokana na utalii, umeiingizia Serikali ya Ujerumani? Kwa nini Serikali ya Tanzania tusiingie angalau mkataba tuwaambie angalau asilimia tano au 10 ya mapato watuletee kutokana na mjusi ambaye anaingiza fedha za utalii kule Ujerumani kuliko hizi peanut package ambazo wanatupa ambazo hazisaidii nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshauri tu Dada yangu kwamba, masuala yanayohitaji utafiti na takwimu ni vizuri kusubiri utafiti na takwimu utoe matokeo badala ya kutoa kauli za jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda niseme tu kwa kifupi kwamba, mjusi huyu au mijusi hawa waliotoka Tanzania kule Ujerumani na bahati nzuri wako baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa wamefika pale mahali na mmojawapo ni Mheshimiwa Dkt. Kafumu ni kwamba, mijusi hawa wawili ni sehemu tu moja ya vivutio vingine vya malikale vilivyoko katika jumba la makumbusho kule Ujerumani ambalo ni kubwa na lina vitu vingi na kiasi ambacho hata kukokotoa kwamba, mijusi wawili wa Tanzania wanazalisha nini ndani ya jumba ambalo watu wanakuja kuangalia vitu vingi ambavyo Wajerumani hawa walivitoa katika nchi za Afrika walizotawala wakati huo katika maeneo mengi na wako wengi kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo matatu ambayo yanafahamika tayari ni kwamba, viingilio katika makumbusho ya Elimu Viumbe huko Berlin ni Euro 3.5 hadi Euro nane, kwa jumba zima ambalo lina vivutio vingi ambapo wanafunzi, watafiti na wazee wanaingia bure, hilo la kwanza.
Pili, asilimia 95 ya Bajeti ya Makumbusho ya Elimu Viumbe Berlin kule, inatoka katika Serikali Kuu na Serikali ya Mji wa Berlin, maana yake ni kwamba, hiyo makumbusho haina hata uwezo wa kuweza kujiendesha yenyewe.
Tatu, Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin ina kumbi nyingi za maonesho, Ukumbi wa Dinosauria ukiwa ni mmoja tu, kwa hiyo, ni vigumu kujua kiasi halisi cha fedha kinachopatikana kutokana na kuingia na kuona masalia ya mijusi wa Tanzania. Vilevile kwenye makumbusho hii kuna nakala ya masalia ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapozungumzia suala la kuboresha eneo hili ambako mijusi wametoka, ili liweze kuwa eneo la utalii si sahihi kusema kwamba, kipato kitakachotoka pale kitakuwa peanut. Pia, pili, ukifundisha watu kwenye taaluma hiyo ya malikale ambayo itaendelea kufanya tafiti katika nchi nzima hii, athari yake ni kubwa. Kwa hiyo, kiufupi unaweza kusema tu kwamba, watu hawa sasa badala ya kutupa samaki wanataka kutupa boti, wanataka kutufundisha kuvua, ili tuweze kuvua wenyewe samaki tupate faida zaidi kuliko kupewa samaki wa siku moja tu. (Makofi
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu alitueleza kwamba kuna Madawati ya Jinsia 117. Hii inaonesha dhahiri kwamba kuna Wilaya nyingine hazina haya Madawati ya Jinsia. Ni ukweli kabisa kwamba kiwango cha ubakaji kwa maana ya watoto wa kike lakini na ulawiti wa watoto wa kiume kimekuwa kikiongezeka sana na tunajua sheria zipo. Ni kwa nini hawa watu wanaendelea kufanya hivi labda ni kutokana na mianya ambayo ipo kuanzia kwenye Jeshi la Polisi na kwingineko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua kwa sababu sheria zipo lakini bado vitendo hivi vinaendelea, ni kwa nini sasa Serikali isije na njia mbadala kama tiba kabla ya hili tukio kutokea, kuwafanyia kama counseling hao wanaotenda kwa maana kwenye maeneo husika wazazi au jamii husika ili tuwe na tiba mbadala kabla ya tukio kutokea kwa sababu tunaona haya mambo yanatokea na sheria zipo ni kwa nini msibuni …
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inafanya njia mbadala nyingi tu na niweke tu kumbukumbu sawa kwamba Madawati ni zaidi ya 417 na kwenye Vituo vya Polisi vyote tumeweka Madawati ya aina hiyo ili kuongeza idadi iwe kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu njia mbadala, kama Serikali tumeendelea kuongeza jitihada za kutoa elimu licha ya hatua kali tunazozichukua. Ndiyo maana tunaendelea kuwasihi hata viongozi wa kiroho kwenye nyumba za ibada kuendelea kutoa elimu hiyo kwa sababu matukio haya maeneo mengi yanaambatana na imani za kishirikina. Wengine wanaamini wakifanya hivi watapata utajiri, wengine wanakuwa na kesi wanaamini wakifanya hivyo watakuwa wamesafishika kwenye kesi hizo na wengine wanaamini watapona magonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, jamii kwa ujumla wake katika maeneo tofauti tofauti tumeona tupanue elimu hasa hasa zikiwepo nyumba hizo za ibada kwa sababu maeneo ambapo nyumba za ibada watu wameshika sana mienendo ya Kimungu matukio haya ya kikatili yamekuwa pungufu zaidi. Kule ambapo kuna imani nyingi za kishirikina ndiko ambapo matukio haya ya ajabu ajabu yamekuwa yakiendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kazi hiyo kuwapa viongozi wa kiimani tunaendelea kutoa rai kwa wananchi kutoa taarifa ili sisi kwa upande wa Serikali tuweze kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika wamefanya hivyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kabisa kwamba msongamano kwenye Magereza yetu Tanzania, Tarime na hata Segerea nilipoenda ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ambalo nauliza hapa, Mheshimiwa Waziri wakati anatoa takwimu za gharama kwa wafungwa, amesema ni shilingi 1,200 kwa chakula. Nilipokuwa Segerea kwenye swali langu ninaloenda kuuliza, kule kuna wamama wamefungwa wanadaiwa shilingi 150,000 mathalani, lakini amefungwa miezi sita. Kwa gharama ambazo amezitoa Mheshimiwa Naibu Waziri unakuta zinavuka pale tena mpaka shilingi 270,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mama ambaye amefungwa miezi sita, anaumwa ugonjwa wa fibroid ana-over breed, kila siku jioni ambulance inampeleka Amana.
Je, ni kwa nini Serikali isitumie busara ya zaidi kwa hawa akina mama ambao wengine wana watoto wachanga ambao unakuta wanafungwa kwa kesi za shilingi 100,000 au 200,000 wasiweze kuzi-waive uki-compare na gharama ambazo wanaenda kuhudumia kwenye ile jamii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, suala la kwamba fedha ambayo wanadaiwa ni kidogo, ni suala la kisheria. Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge anafikiri sheria ile imepitwa na wakati na haitendi haki, ni rahisi yeye kuleta hoja Bunge hili libadilishe sheria kwa sababu sheria ndiyo zinasema hivyo. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nipongeze kwa majibu mazuri yaliyotolewa. Nataka tu kumuomba Mheshimiwa Mwalongo kwa ile hoja ya jambo mahususi alilolileta kwamba baada ya Bunge, basi tuonane ili nilipate vizuri kwa sababu jambo lake alilolileta lile ni mahususi ili tuweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambazo tumezipata, niweke tu kumbukumbu sawa, siyo kila Magereza yana msongamano. Tuna baadhi ya Magereza ambako katika mikoa ile kiwango cha uhalifu ni kidogo, hata msongamano Magerezani ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilienda Mkoa wa Lindi, Gereza lilikuwa na uwezo mkubwa kuliko kiwango cha wahalifu. Hivyo hivyo, nilienda kwa Mheshimiwa Shangazi kule, kiwango cha Gereza la kule ni kikubwa kuliko wahalifu walioko mle.
Kwa hiyo, nitoe rai kwa Watanzania na jamii nzima ya Watanzania kuepuka kufanya uhalifu kwa kweli, kwa sababu sisi kama Serikali hatupendi watu kuwa magerezani, lakini tunawapeleka kwa sababu ya uhalifu wanaoufanya.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi tukaacha wahalifu wakawa nje na kama watu watafanya uhalifu, ni kwamba wataenda magerezani. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nioneshe masikitiko yangu na kwa namna gani Serikali haiwezi kuweka kumbukumbu. Mwaka 2016 niliuliza swali hili na majibu walinipa haya haya licha ya kwamba aliyekuwa Waziri alikuja Tarime na akajionea hali halisi na akatoa agizo kwamba ule mnada ufunguliwe, lakini leo mnaleta majibu ya kumbukumbu za mwaka 1997. Maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wafanyabiashara wa ng’ombe wanapeleka ng’ombe nchini Kenya kwa mnada ambao upo mpakani wa Mabera kupelekea upotevu mkubwa wa mapato ambayo yangekuja Tanzania kupitia multiplier effect, Wakenya wangekuja kununua zile ng’ombe Tanzania kwa sababu wanategemea ng’ombe za kutoka Tanzania kuliko ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini Serikali hamkutaka kutumia rejea ya muhtasari ya kikao cha mwaka 2016 ambapo tulikaa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Tarime, Waziri na watendaji wa Wizara husika pamoja na mimi Mbunge na baadaye tukaongea na wananchi? Kwa nini hamkutumia ule muhtasari ili mweze kufuata maamuzi yaliyofikiwa kuweza kufungua Mnada wa Magena?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wafanyabiashara wa ng’ombe ambao wanapeleka Kenya wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa sana kwenye kuvusha ng’ombe hizi. Kwa kuwa mnada ambao wameuweka rejea wa check point ya Kirumi hautoi suluhishi, kwa sababu wakinunua ule mnada siyo wa mpakani wanapokuja kuvusha ng’ombe kwenda Kenya wanasumbuliwa sana.
Ni kwa nini sasa Waziri (maana yake inaonekana hamtunzi kumbukumbu) husika usije tena kwenye Mnada wa Magena uweze kujionea uhalisia na maamuzi yale ili sasa uweze kuruhusu mnada huu kufunguliwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Matiko na kwa hakika Mheshimiwa Esther Matiko anashiriki kikamilifu katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais juu ya ulinzi wa rasilimali za nchi yetu na ndiyo maana anasisitiza sana kuhakikisha rasilimali za mifugo zinaweza kudhibitiwa pale ili ziweze kuinufaisha nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anatusisitiza kwa nini tusitumie Mnada wa Magena sawa na muhtasari wa mwaka 2016 ilipokaa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya kule
Mara na Wizara yetu; na swali la pili, kwa nini Mheshimiwa Waziri asiende Magena?
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie kwamba hivi sasa Wizara yetu imeunda tume maalum ambayo inapitia maeneo yote katika nchi yetu kufanya tathmini ya minada tuliyonayo ya awali zaidi ya 480 na minada ya upili na mipakani ili kuweza kujiridhisha na maombi yaliyoletwa. Nataka nimwambie kwamba moja ya eneo ambalo tutalifanyia kazi baada ya tathmini hii inayokwenda kukamilishwa na Wizara na wataalam wetu, ni hili alilolileta hapa Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Spika, kwa kumhakikishia ni kwamba tutafika Magena pia. Mimi kama Naibu Waziri na Waziri wangu tutakubaliana, tutakwenda Magena kujiridhisha na hiki anachokisema. Kwa faida ya nchi yetu, tukiona kwamba jambo hili lina faida nasi, tutalitekeleza sawa na ushauri wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Tarime Mjini, Kata za Nkende, Kenyemanyori, Kitare, Nyamisangura na Turwa pamoja na Nyandoto hazina umeme kabisa, Bunge lililopita niliuliza swali kama hili na Naibu Waziri akaahidi atatembelea Tarime ili kuweza kuona wakandarasi wa REA ambao tangu mwaka 2016 walitakiwa watekeleze huu mradi, lakini mpaka leo ni Kata ya Nyandoto ndiyo tumeona sasa wameanza kufanyakazi.
Je, ni kwa nini Naibu Waziri hukuweza kutekeleza ile ahadi ambayo uliahidi kwa wana Tarime ili waweze kupata huu umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru kwa kutambua kwamba kazi imeanza ka Kata ya Nyandoto kama alivyoitaja, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi yangu ya kutembelea Jimbo la Tarime Mjini na Mkoa wa Mara iko pale pale ila kutokana tu muingiliano wa ratiba, lakini kwa kuwa kazi zetu ziko site naomba nimthibitishie baada ya Bunge hili nitatembelea Wilaya hiyo ya Tarime na Wilaya zingine za Mkoa wa Mara kuhamasisha na kukagua miradi hii na kuwapa shime wakandarasi wafanyekazi kwa haraka na kama inavyokusudiwa. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hili swali la kuuliza kuhusu uwanja wa ndege na kuiomba Serikali ione umuhimu wa kuupandisha hadhi huu uwanja utoke kwenye Halmashauri na uende kwenye Tanzania Aviation Authority; kwa sababu kwa sasa hivi ilivyo kumkodisha Coastal Aviation kwa milioni 20 kwa mwaka anakuwa ana-monopolize na kodi ambazo anawataja aviation zingine wanavokuja kutoa pale ni nyingi sana; kwa hiyo Serikali tunapoteza mapato mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni kwa nini sasa Serikali haioni umuhimu wa kupandisha hadhi huu uwanja na kuukarabati kwa sababu tunapata watalii kutoka maeneo mbalimbali, lakini pia unaweza kutumika kwa ndege kutoka pale kwenda hata nchi jirani ya Kenya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwa nini sasa wameeleza hapa kwamba wamekarabati barabara ya kilometa 1.2, lakini kuna barabara ya kutoka Tarime kupita Magena unaenda mpaka Kata ya Mwema kule ambapo kuna daraja la Mto Moli ni bovu sana hata Clouds Tv walionesha…..
…linahatarisha maisha watu wanaotumia ile barabara. Ni lini sasa Serikali itaweza kujenga daraja lile la Mtomoli sambamba na ile barabara ambayo inaenda Magena kwenye huu uwanja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya kuomba kupandishwa uwanja huu kuchukuliwa na iwe miongoni mwa viwanja ambavyo vinamilikiwa kitaifa haina ubaya. Hata hivyo ni vizuri tukajua chimbuko la uwanja huu. Uwanja huu mwanzo ulikuwa unatumiwa na kampuni hii ambayo inajiita COGFA ambao wanajenga barabara ya kutoka Sirari kwenda Makutano. Na wao baada ya kumaliza matumizi yake walimkabidhi Mkuu wa Wilaya, lakini baadae bali katika kugawanyika Halmashauri ya Mji na halmashauri ya Tarime Town Council na DC ikaonekana kwamba uwanja ule ambao uko kilometa tisa ubaki chini ya umiliki. Ukitazama katika mkataba wao ambao ni suala la wao ndani ya Halmashauri, kwa sababu mkataba umeingiwa kati ya Coastal Aviation na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo linaongeleka, kwa kadri watakavyopisha kwenye vikao vyao na wakaridhia kwamba sasa ownership ihame sisi kama Serikali hatuna ubishi na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la pili la kujenga daraja, kama ambavo tumekuwa tukitengeneza miundombinu kwa kadri bajeti inavyoruhusu, naomba nimehakikishie Mbunge bajeti ikiruhusu tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba mazingira rafiki kwa ajili ya watalii kwenda mbuga yanajenga, ni pamoja na kujenga kwa daraja.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Soko la Kimataifa la Lemagwi ambalo lilikuwa limejengwa na baadaye kutelekezwa, liko Wilayani Tarime, ambalo lingeweza kusaidia kuuza mazao mbalimbali. Tungependa kujua, ni lini Serikali itamaliza kujenga hilo soko ambalo limetumia zaidi ya billions za Watanzania na baadae limetelekezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali wka kuzitaka halmashauri zote ambazo zina miradi ya kimkakati ambazo wana uhakika katika uwekezaji pesa inakwenda kupatikana ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya kwao, ni vizuri wakahakikisha kwamba andiko linakamilika ili kama kuna sehemu ambayo Serikali inahitaji kuwekeza nguvu yake tujue exactly nini ambacho tunakwenda kukipata kama halmashauri kabla ya nguvu kubwa haijawekezwa huko.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba ikigundulika askari wanaowaweka kituoni wananchi kwa muda watachukuliwa hatua. Wakati nachangia bajeti iliyopita ya Wizara ya Mambo ya Ndani nilieleza bayana kabisa kwamba kuna baadhi ya mahabusu kituo cha Kawe waliwekwa ndani kwa zaidi ya miezi mitatu na nikasema kabisa na nikamtaja na askari aliyehusika mpaka leo hajachukuliwa hatua.
Je, ni kwa nini Mawaziri wanatumika kwenye Bunge Tukufu kuwadanganya watanzania bila kuchukua hatua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hii hoja ya mahabusu Kituo cha Kawe, tulishawahi kutoa maelekezo, uchunguzi ufanyike ili hatua ziweze kuchukuliwa, lakini kama Mheshimiwa Mbunge atataka kulithibitishia Bunge hili tukufu mpaka kama hatua hazijachukuliwa, basi nimuahidi kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia nijue ni kwa nini hatua kama hazijachukuliwa ama pengine wanastahili kuendelea kukaa ndani kwa mujibu wa sheria.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Mwaka 2016 mwezi wa kumi, Mkoa wa Mara ndiyo walizindua REA Awamu ya Tatu na densification. Mpaka naongea sasa hivi, Jimbo la Tarime Mjini maeneo mengi, maeneo ya Kanyamanyori, Kata ya Nyandoto, Kitale na Nkende mradi huu haujaanza na ni kwa asilimia 90 hawa watu hawana umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa ni lini Serikali itaenda kuelekeza maana imepita takribani miaka miwili ili miradi iweze kufanyika kwa ufanisi na wananchi waweze kupata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko kuhusu masuala ya umeme katika Mkoa wa Mara hususan katika Jimbo lake, kwanza, kwa kuwa nimeona ndani ya Bunge bado changamoto za wakandarasi kuanza kuendelea na kazi, inaonekana Wabunge wengi hawaridhiki kwamba speed inaonekana ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kutupitishia bajeti yetu, sisi tunaendelea na ziara. Ndiyo maana leo Mheshimiwa Waziri hayupo, ameshafanya ziara pia katika Mkoa wa Mara. Kutokana na tatizo hili, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara Mkoa wa Mara tena ili kuona kwa nini wakandarasi mpaka sasa hivi wanasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba wakandarasi hili ni onyo la mwisho kwa kweli kama speed itaendelea Serikali ya Awamu ya Tano itasita kuvunja mikataba nao kKwa sababu miezi iliyobaki ni michache na tumeshawapa hela kwa nini inashindikana. Nashukuru ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na wananchi, kama alivyosema ipo nchi nzima, lakini nimekuwa nikizungumzia utatuzi wa mgogoro kati ya Jeshi la Wananchi na Mtaa wa Bugosi na Kenyambi kule Tarime ambao umedumu kwa muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri anaelewa; ni lini sasa Serikali itaona kwamba imeshindwa kupata fedha za fidia kuwalipa hawa wananchi, ukizingatia Jeshi la Wananchi limetoka kwenye Kambi yao, limekuja kwenye makazi ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, kama hakuna fedha, tunaomba warudishe hii ardhi kwa wananchi ili waendelee na shughuli zao za maendeleo. Ni lini Serikali itawarudishia ardhi wananchi hawa wa Tarime?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna tatizo la mgogoro wa ardhi katika eneo hili la Tarime la muda mrefu, ninayo taarifa hii, tumeshazungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Mbunge. Wataalam wameshauri na tathmini ya fidia imefanyika, kinachosubiriwa ni fedha ili ziweze kulipwa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, katika mwaka huu wa fedha, bajeti yetu ilikuwa ni shilingi bilioni 20 katika kulipa fidia na upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali. Bahati mbaya sana tumepokea kama shilingi bilioni tatu ambazo tumeshazilipa kule Kilwa, lakini mwaka wa fedha haujaisha, tuna matumaini kwamba fedha zitapatikana na zikipatikana tutaendelea kulipa katika maeneo haya ambayo uhakiki umeshafanyika.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Esther avute subira, ajue kwamba Jeshi nalo lina umuhimu wa kuwepo maeneo haya. Katika ulinzi wa nchi lazima tuone umuhimu wa taasisi hii ya Jeshi kuwepo. Siyo vizuri au siyo rahisi tu kusema kwamba kila ambapo tunashindwa kulipa fidia kwa wakati, basi Jeshi liondoke wananchi warudishiwe ardhi; ulinzi utafanywa na nani? Kwa hiyo, naomba subira iendelee na bila shaka tutalimaliza tatizo hili kwa haraka iwezekanavyo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa majibu yanayotia matumaini kama yatatekelezeka, kwa sababu mradi wa Ziwa Victoria kuanzia wakati wa Mheshimiwa Eng. Kamwelwe alisema mnafanya upembuzi yakinifu na mradi ungeenda kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mji wa Tarime ndiyo Makao Makuu ya Wilaya Tarime na umekuwa na matatizo ya maji kwa muda mrefu na kusababisha wananchi wasifanye shughuli zao za maendeleo; na kwa kuwa vyanzo vikuu katika Mji wa Tarime ni Bwawa la Nyanduruma na lile la Tagota ambalo halitoi majisafi na salama na Wizara tuliowaomba hata angalau wajenge treatment plant wakasema wanategema mradi mkubwa wa Ziwa Victoria:

Ni lini sasa mtahakikisha kwamba ule mradi ambao tumeuanzisha Gamasara ambao tumesha-rise certificate, Mkandarasi amesimama kuanzia Novemba tumeleta Wizarani mpaka leo hajalipwa, ni lini yule Mkandarasi atalipwa ili angalau ajenge lile tenki la lita 100,000 kuweza kusaidia wananchi wa Gamasara na Kata ya Nyandoto na Kata za pembezoni kwa kipindi hiki tukisubiria huu mradi wa Ziwa Victoria ambao mmesema unakwenda kuanza mwaka 2019/2020?

La pili, hawa DDCA wameshakamilisha na walileta certificate na hata Mheshimiwa Eng. Kamwelwe mimi mwenyewe nilimpa document, lakini mpaka leo inavyosemekana, hawajalipwa fedha na ndiyo maana hata hawajaanza kufanya huo utafiti wa maji ya chini ya ardhi kama mlivyo-report hapa. Napenda sasa nihakikishiwe leo kwamba hawa DDCA watalipwa fedha ili wananchi wa Tarime hasa zile Kata za pembezoni waweze kuchimba visima na wapate majisafi na salama. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimtoe hofu dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko, Serikali ya Awamu ya Tano ikiahidi inatekeleza na ikichelewa kutekeleza, basi kunakuwa na sababu maalum ya kueleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ninalotaka kusema, pamoja na mradi mkubwa huo wa Ziwa Victoria katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji Tarime, lakini tuna mradi pale Gamasara wa asilimia 25, lakini tunatambua kabisa utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri, tulikuwa na madeni ya Wakandarasi zaidi ya shilingi bilioni 88, lakini tunamshukuru Mheshimiwa Rais amewaagiza watu Wizara ya Fedha kutupa zaidi ya shilingi bilioni 44 kwa ajili ya kuwalipa Wakandarasi na tumeshazipata na tumeshazigawa. Tuna shilingi bilioni 44 nyingine tutakazopewa mwezi huu wa Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, katika maeneo yote ambayo Wakandarasi wanadai, tutawalipa ili miradi iendelee kutekelezeka na ahadi ya kumtua mwana mama ndoo kichwani iweze kitimilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la DDCA, sisi pale tumeona haja ya uchimbaji wa visima. Sasa katika mgao huo wa shilingi bilioni 44, watu ambao wamelipwa ni watu wa DDCA. Tunawaagiza waende Tarime haraka katika kuhakikisha hii kazi inafanyika ili ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwana mama ndoo kichwani inatimilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba endeleeni kutuunga mkono bajeti yetu katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo ahadi kwa Jimbo la Bukene, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni zake na hata Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya Tarime Mugumu ambayo ni kilometa 89 kwa kiwango cha lami; na kwa kuwa hii barabara ikijengwa itakuza uchumi siyo tu wa Tarime au Mara, bali wa Taifa, maana yake watalii watakao toka Kenya wataweza kupita kwenye njia ile:-

Ni lini sasa hii ahadi ya Mheshimiwa Rais itatimilika kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Tarime Mugumu almaarufu kama Nyabwaga Road?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali iliahidi kujenga kipande cha kilometa 44 kutoka Tarime mpaka Mugumu kwa kiwango cha lami. Naamini hata Mheshimiwa Mbunge anajua kwamba upembuzi yakinifu ulishafanyika, usanifu wa awali ulishafanyika na usanifu wa kina ulishafanyika. Sasa hivi tunatafuta pesa kwa ajili ya kumpa Mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekitik, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo, tutajenda hiyo barabara kwa sababu ya umuhimu wa utalii wa nchi yetu kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Halmashauri ya Mji wa Tarime, kata zote zilikuwa haina kituo cha afya bali walikuwa wanategemea Hospitali ya Mji. Tunashukuru tumepata Kituo cha Nkende ambacho kinaendelea kujengwa; lakini kuna kata nne za pembezoni ambazo zina zahanati tu, kwa maana ya Kata ya Kitale, Kata ya Kanyamanyori na Nanyandoto. Wananchi wa katia ya Kanyamanyori wameamua kuchangishana ili kuendeleza kile kituo cha afya kwa maana kujenga maternity ward na maabara:-

Ni lini sasa Serikali itawatia moyo wananchi wale kwa kutoa fedha kuweza kujenga kituo afya cha ili kupunguza vifo vya mama na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na nikatembelea Hospitali ya Wilaya ambayo mwanzo ilikuwa inahudumia maeneo mengi sana kiasi kwamba kukawa kuna congestion kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge mwenyewe anakiri na anashukuru kwamba kimeanza kujengwa kituo cha afya na imebaki hizo kata ambazo yeye amezitaja. Naomba aendelee kuiamini Serikali kwamba kama ambavyo tumeanza kujenga katika hiyo kata kwa kadri bajeti itakavyoruhusu, tumeahidi tutatekeza na katika kata nyingine kwa jinsi bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hospitali ya Wilaya ya Mji wa Tarime ambayo kiukweli inatoa huduma kama Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa naweza nikasema na Kanda Maalum Tarime Rorya, Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea na akaona ni jinsi gani inaelemewa kwa utoaji wa huduma. Hivi ninavyoongea chumba cha kuhifadhia maiti kwa maana ya mortuary kwanza ni kifinyu lakini pia mashine yake kwa maana ya compressor haifanyi kazi na wale ndugu zetu ambao tunawahifadhi pale wakikaa muda mdogo wanaharibika. Nataka kujua commitment ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inasaidia ukarabati au upanuzi wa mortuary ikiwemo kusaidia hiyo mashine ya compressor kwa sababu Halmashauri ya Mji wa Tarime haina kipato cha kutosha. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge nilipata fursa ya kutembelea hospitali ile ambayo ina congestion kubwa na bahati nzuri nilipata fursa nikiambata na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Maelekezo ambayo yalikuwa yametolewa, kwanza ni kuhakikisha kwamba dawa za kutosha zinatolewa ili kukidhi haja kwa sababu wananchi ni wengi wanaopata huduma pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili ambalo amelisema kuhusiana na chumba hicho cha kuhifadhia maiti ambacho mashine imeharibika kiasi kwamba sasa mwili unaharibika ndani ya muda mfupi, naomba seriously tukitoka hapa tuwasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili tuone hatua za haraka za kuchukua kuhakikisha kwamba mochwari ile inafanya kazi.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa Serikali imekiri kwamba imetenga bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa na nafikiri na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwangu itakuwepo. Na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna ufinyu wa majengo katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora kupelekea hata vitanda kukosa sehemu ya kuweka na hivyo kupelekea msongamano wa wagonjwa na kudumaza utoaji wa huduma ya afya kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua sasa kati ya hizi bilioni 12 ni kiasi gani cha fedha kimetengwa specifically kwa ajili ya Hospitali hii ya Mkoa wa Tabora ili sasa kuondoa ufinyu wa majengo na kuweza kuondoa msongamano na vitanda viweze kupata mahala pa kuweka na wananchi wa Tabora waweze kupata huduma stahiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni dhahiri kabisa inatambulika kwamba tuna uhaba wa wauguzi kwa maana ya madaktari, manesi na madawa katika hospitali zetu nyingi nchini. Na tunatambua kwamba uhaba huu umepelekewa na sababu mbalimbali ikiwepo zoezi la vyeti feki ambalo Serikali ya Awamu ya Tano iliendesha, vifo na kustaafu. Hospitali yangu ya Mji wa Tarime ina ukosefu wa daktari ni wengi lakini specifically daktari wa meno ambaye amefariki kuanzia mwaka jana na nimekuwa nikiongea hapa. Ningetaka kujua sasa ni lini Serikali itaweza kutuletea daktari wa meno ili wananchi wa Tarime waendelee kupata huduma hii ya meno?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza specifically kiasi gani ambacho tumekitenga katika Hospitali ya Rufaa ya Mko wa Tabora hususan katika kuboresha miundombinu ile. Hiyo data sinazo hapa kwa hiyo nitamwomba tu Mheshimiwa Mbunge tukishamaliza kikao hichi tuongee na watendaji wetu ili waweze kutupatia hizo taarifa na niweze kumpatia taarifa ambayo kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili ameulizia kuhusiana na daktari wa meno ni kweli Serikali imekuwa inaendelea na jitihada za kuziba mapengo wa vyeti feki na zile ajira nyingine. Na katika awamu ya kwanza tuliajiri takribani watumishi 3152 kuziba pengo la watumishi feki na Serikali baadaye ikaongeza watumishi takribani 8000 na sasa hivi tuko katika hatua za mwisho kuangalia hawa ambao walistaafu, wamefariki ili nao nafasi zao ziweze kuzibwa na tuko katika hatua za mwisho kabisa kuweza kuziba haya mapengo ya wale ambao wamefariki na wamestaafu ili sasa nafasi zao ziweze kujazwa. Na nikuhakikishie kwamba Tarime huyo daktari ambaye wamemwitaji wa meno naye atapatikana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa sasa tunajua kwamba tuna mradi wa REA ambao ndiyo umejielekeza kupeleka umeme vijijini. Katika Kijiji cha Sazira katika Jimbo la Bunda Mjini ambalo lina Vitongoji vitatu cha Nyamungu, Wisegere na Kinamo havijawahi kupitiwa na mradi huu wa REA phase I, phase II na hata phase III. Sasa ningependa kujua hawa wananchi wa Kijiji cha Sazira ni lini watapatiwa umeme ili na wenyewe waweze kupata umeme katika shughuli zao za kimaendeleo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Mji wa Tarime pia tumepitiwa na umeme wa REA ambao unapita kwenye aidha Kijiji sehemu ndogo tu au kata. Ningependa kujua maeneo ambayo yana Taasisi kama sekondari, zahanati au vituo vya afya na shule ya msingi kama vile Kitale tuna Kijiji cha Nkongole ambacho kina hizo Taasisi zote, Kenyamanyori Senta tuna Kibaga ambayo ina mgodi pale haijapitiwa na umeme wa REA. Ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba inapeleka huu umeme wa REA kwenye yale maeneo ambayo hayajaguswa kabisa na Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kwamba ungeweza kwenda Tarime kujihakikishia hayo maeneo ambayo kila siku nayauliza hapa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameulizia Kijiji cha Sazira ambacho kipo Bunda Mjini ambacho kina vitongoji vitatu na hakina umeme. Kama ambavyo tumepata kujibu maswali hapa ya msingi kwamba mpango wa Serikali ni kupeleka umeme vijiji vyote. Kwa sasa tuna mradi huu unaoendelea wa REA awamu ya tatu ambao unahusisha vijiji 3,559 lakini ukichanganya na miradi mingine yote ya Ujazilizi, BTIP tunatarajia kufikisha umeme ifikapo Julai, 2020 kwa vijiji 9,299.

Kwa hiyo kijiji ambacho amekitaja kwenye Wilaya ya Bunda Mjini hapo vipo katika mpango wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili ambao utaanza Julai, 2019 na kukamilika 2021. Kwa hiyo niwatoe hofu tu wananchi wote nchi nzima, mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kupeleka umeme katika vijiji vyote nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameulizia suala la Jimbo lake la Tarime; ni kweli niliahidi kutembelea Jimbo hilo kama utaratibu wetu ndani ya Wizara, lakini nitazingatia angalizo lako kwamba kwa ruhusa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini nimtoe hofu tu Mheshimiwa Esther kwamba katika maeneo ambayo ameyataja na hasa Taasisi za Umma, Wizara imetoa maelekezo mahususi na naendelea kurejea hayo maelekezo kwamba Taasisi za umma ni moja ya kipaumbele katika kuzipelekea umeme iwe shule ya msingi, sekondari, kituo cha afya au miradi ya maji.

Kwa hiyo naomba niwaelekeze Wakandarasi kuzingatia maelekezo hayo na Mameneja wote wa TANESCO na wasimamizi wa miradi hii ya REA kwamba umeme ufikishwe kwenye Taasisi za Umma ili kuboresha utoaji wa huduma ambazo zinatokana na hizo Taasisi za umma.

Mheshimiwa Spika, katika haya maeneo aliyoyasema Mheshimiwa kwanza mojawapo lipo katika REA awamu ya tatu, mradi unaoendelea na Mkandrasi Derm yupo, anaendelea vizuri na ni moja wa Wakandarasi ambao kwa kweli wanafanya kazi vizuri na nimhakikishie tu mpaka Juni, 2019 hii miradi itakuwa imekamilika. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni dhahiri kwamba Serikali imekuwa haitoi kipaumbele kwenye huduma muhimu za binadamu badala yake wamekuwa wakiwekeza zaidi kwenye vitu.

Mheshimiwa Spika, magereza ni moja ya sehemu ambazo inatakiwa wapewe vipaumbele na wapewe huduma stahiki kama inavyoelekeza. Wazabuni wengi wanadai na wameacha kutoa huduma za vyakula na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha zaidi nilitaka nijue, Serikali ni lini itatoa nguo kwa wafungwa ambao mnasema kabisa wakishafungwa wavae yale mavazi. Niliona hiyo nikiwa Segerea, lakini juzi nilivyotembelea Gereza la Tarime pamoja na matatizo mengi ambayo yametokana na kutokulipa madeni ya wazabuni na kuweza kutoa vifaa hivi unakuta mpaka Askari Magereza anachukua nguo zake anavisha mfungwa kama anavyotoka nje.

Ni lini sasa Serikali itaondoa hii fedheha ihakikishe kwamba wafungwa ambao wanastahili kuvaa nguo waweze kupewa zile nguo ambazo wataweza kujihifadhi? Na wajue kabisa kwamba waliopo Serikalini leo magereza ni yao kesho. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimsahihishe siyo sahihi kwamba Serikali haitoi kipaumbele kwenye huduma mbalimbali ikiwemo za wafungwa. Nimhakikishie kwamba wafungwa hawa tumekuwa tukiwapatia uniform na siyo wote kama ambavyo umetaka ieleweke kwamba hawana uniform, lakini changamoto hii itaendelea kupungua hatua kwa hatua. Hata hivyo, sehemu kubwa ya wafungwa tayari wameshaanza kupatiwa nguo kwenye magereza.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mji wa Tarime wameendelea kupata adha kubwa ya maji safi na salama na hasa upatikanaji wake. Kupitia Bunge hili nimeshauliza maswali mengi sana na kuchangia na Serikali ikaahidi kwamba, itatoa suluhisho la muda mfupi la kuchimba visima 23 kandokando ya Mji wa Tarime kuweza kuboresha Mradi wa Gamasara na Bwawa la Nyanduruma, lakini zaidi kwenye bajeti iliyopita waliahidi Mradi wa Ziwa Victoria ambao unatokana na mkopo kutoka India kwamba, unaenda kuanza ambao ni suluhisho la muda mrefu.

Sasa napenda kupata majibu kutoka kwa Naibu Waziri, ni lini sasa hii miradi yote inaenda kutengemaa ili wananchi wa Mji wa Tarime waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, dada yangu Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tuna Mradi pale wa Gamasara ulikuwa ukifanya kazi kwa kusuasua, nilifika na tumechukua hatua kubwa ya kushughulikiana na yule mkandarasi. Wiki hii tunafunga pampu ili kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma hii ya maji, lakini tunatambua kabisa Mkoa wa Mara ni maeneo yenye changamoto.

Mheshimiwa Spika, tumepata fedha takribani kwa mikoa 17 mmojawapo ukiwa Mkoa wa Mara na tumekwishatuma fedha zaidi ya Sh.8,345,000,000. Katika jimbo lake mpaka sasa tumekwishatuma pesa zaidi ya Sh.1,345,000,000, hizo fedha ni kwa ajili ya utekelezaji. Kwa hiyo, hizo fedha ziende zikatumike katika kuhakikisha zinachimba visima katika maeneo yenye changamoto ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, pia katika kuhakikisha tunatatua kabisa tatizo la maji Rorya pamoja na Tarime ni moja ya maeneo ambayo tumeyaweka katika miji 28 kupitia fedha za India. Tunasubiri kibali kutoka Exim Bank ili tuweze kutangaza tenda kwa ajili ya kuwapata wakandarasi na Mradi ule mkubwa wa kuyatoa maji Ziwa Victoria ili wananchi wa Tarime waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza napenda kumshukuru Naibu Waziri maana tarehe 07 Agosti, alikuja Wilaya ya Tarime na kuna maagizo aliyatoa kwenye Mradi wa Gamasara na wa Nyanduluma, lakini nataka kujua ni lini sasa vile visima 23 ambavyo Bunge lililopita niliuliza hapa na ukaelekeza kwamba, ni DCA wanaenda kuanza kuvichimba mara moja, lakini mpaka sasa hivi hamna chochote ambacho kinaendelea kwenye Jimbo la Tarime Mjini, ili kuweza kutoa suluhisho la la muda mfupi wakati tukisubiri ule mradi wa Ziwa Viktoria? Ahsante?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, nikiri nimefika Tarime na moja ya changamoto kubwa kiukweli changamoto kubwa ipo pale Tarime. Na moja ya changamoto ambayo tumeona jambo la kulifanya haraka kwanza tume-terminate mkataba wa yule mkandarasi wa Mradi wa Gamasara, mradi ule tutaufanya kwa sisi wenyewe kuwapatia fedha wataalam wetu waweze kuutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna suala la uchimbaji wa visima. Tumekwishawaagiza watu wa DDCA na sisi tumejipanga kuwapatia fedha ili uchimbaji wa visima 23 uweze kuchimbwa pale wakati tunasubiri mradi mkubwa wa fedha zile za India. Sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wa Tarime kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Adha iliyopo Urambo ya Hospitali ya Wilaya kuhudumia population nje ya eneo linalohitajika ni sawa na ile ya Hospitali ya Mji wa Tarime ambayo kwa kweli na nimeshaongea mara nyingi sana hapa Bungeni, inahudumia watu nje ya population ya Mji wa Tarime, wanatoka Shirati, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Kinyemanyoli waliamua kujenga kituo cha afya ili kupunguza ile population ambayo inaenda kupata huduma ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na nilishauliza hapa akaahidi kwamba angeweza kupeleka fedha. Nataka kujua sasa ni lini Serikali itapeleka fedha ku-support nguvu za wananchi ili tuweze kuwa na kituo cha afya Kinyemanyoli kupunguza adha wanayopata wajawazito na watoto?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa maswali yaliyoulizwa hapo awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Mkoa wa Mara umekuwa na changamoto mbalimbali za sekta ya afya lakini tumefanya investment kubwa katika mkoa huo na tukifahamu kwamba eneo la Tarime Mji napo kuna changamoto hizo. Ni jukumu la Serikali kuangalia nini kifanyike katika maeneo hayo kama tulivyofanya kazi katika Mkoa mzima wa Mara. Kwa mfano, kwa sasa hivi tunajenga Hospitali za Wilaya takriban tatu na kuimarisha vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Esther Matiko kwamba tunaifahamu changamoto zilizopo kule na tunazishughulikia. Kikubwa zaidi naomba nimuagize Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kwenda kufanya tathmini na kutuletea taarifa ili katika mchakato wetu wa bajeti unaokuja mwezi wa tano tuangalie jinsi gani tutaweza ku-address matatizo ya maeneo hayo kwa sababu lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Tarime Mji wanapata huduma vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwamba wanadhurika vijana mahabusu kwa kuona tabia za wale wafungwa wabakaji, wezi na madawa ya kulevya lakini tumeshuhudia akina mama wanakuja wajawazito wanajifungulia gerezani, kuna akina mama wanakamatwa wakiwa na watoto wanakuwa nao gerezani wanachangamana na hao watu ambao wanatabia za tofauti tofauti na tunajua kabisa kwamba mtoto mchanga kuanzia zero age mpaka five years anakuwa ndiyo muda ambao anajifunza na kuweza kuweka vitu akilini, mtoto yule anakua kwenye makuzi ya gerezani anafuata zile tabia ambazo hazina maadili kabisa.

Je, Serikali ni kwa nini sasa isitafuta mbadala kama inashindwa kuwapa dhamana hawa mahabusu wenye watoto ni kwanini isitenge sehemu kabisa ya wamama wajawazito na wamama wanaonyonyesha waweze kukaa na wale watoto mpaka watakapofikia umri wa kuweza kuwatoa gerezani, kuliko kuchangamana wanaona wale akina mama saa nyingine wako uchi, wako hivi ni tabia mbaya na haiwatendei haki hawa watoto. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wanaruhusiwa kuchukuliwa na familia zao, kwa hiyo, watu wengi ambao wanafungwa, wakinamama ambao wana watoto wanapofikia umri baada ya kuacha kunyonyesha, mara nyingi huchukuliwa na jamaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa wale ambao watakuwa wanaendelea kubakia magerezani aidha kwa sababu ya kukosa jamaa wa kuwaangalia nje, kuna utaratibu mzuri ambao unaandaliwa na mimi binafsi nimetembelea magereza mengi sana na ninapotembelea kwenye magereza hayo hutembelea katika maeneo ya wanawake na katika mambo ambayo tunaangalia moja ni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahakikisha kwamba watoto wale wanapata elimu, wanaandaliwa mazingira mazuri na wanasoma katika shule za nje ya gereza. Kwa hiyo, kimsingi jambo hili tunaliangalia kwa uzito wa aina yake ili kuhakikisha kwamba watoto wale hawapati madhara ya kisaikolojia wakati wanapokuwa gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niendelee kutoa wito kwa wakinamama kujiepusha na kufanya vitendo vya kiharifu ili kuepusha kuwaingiza katika matatizo watoto hawa hasa wanapokuwa katika umri mdogo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Mji wa Tarime tuna Migodi midogo ya Buguti na Kibaga, tumekuwa tukishuhudia migogoro kwa wachimbaji wadogo kwenye mgodi wa Kibaga na Mgodi ule wa Kibaga leseni yake iko na Barrick kwa muda mrefu na nimeshawahi kuuliza hapa, Serikali ikasema kwamba ina- revoke leseni ya Barrick. Na kwa sababu leo Naibu Waziri imekiri kwamba zile leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi mtaenda kuzifuta na kuwapa wachimbaji wadogo. Ningetaka kujua specifically, kwa wachimbaji wadogowadogo wale wa Kibaga, ni lini sasa ile leseni itaondolewa kwa Barrick ili waweze kupewa wachimbaji wadogowadogo wa Kibaga waweze kufanya kazi zao kwa ufasaha zaidi na bila kubughudhiwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumekwishakutoa tamko, kwa leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi, na hasa ambazo ziko kwenye utafiti na hazifanyiwi kazi, zirejeshwe, zirudishwe na sisi tuweze kutafuta namna ya kuwagawia wachimbaji wadogo na tunawagawia katika vikundi. Mheshimiwa Mbunge ameniuliza swali hilo lakini hakunipa specific namba ipi, naomba tu nilichukue suala hili, tuone ni leseni ipi, aidha ni ya uchimbaji, au ni leseni ya utafiti. Kama leseni ni ya utafiti na haifanyiwi kazi, sisi tutazirudisha, lakini nimhakikishie tu kwamba kuna leseni nne ambazo zilisharudishwa na watu wa Barrick maeneo hayo na wameshaturudishia sisi na walishaandika barua, tutaangalia namna ya kuangalia kuwagawia wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu, ameonesha m ikakati iliyopo kwa Butiama, Kiabakari, Mugango na Vijiji 13 vya Musoma Vijijini lakini katika swali la msingi la Mheshimiwa Sokombi aliweza kuonesha adha ya maji Mkoa wa Mara na akataja na Serengeti. Ningependa kujua mkakati uliopo kwa Wilaya ya Serengeti hasa maeneo ya vijijini ambayo kwakweli wananchi wa pale hawana maji kabisa. Ni mkakati gani Serikali mko nao ikiwemo wa kupeleka visima maeneo ya Serengeti Vijijini, sio pale Serengeti Mji. Mkakati gani upo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mwezi wa tatu wakati Mheshimiwa Naibu Waziri ukijibu swali langu kuhusiana na adha ya maji Tarime kwa muda mfupi wakati tukisubiria mradi unaotoka ziwa Victoria, niliweza kuulizia vile visima 23 ambavyo Serikali ilisema itakuja kuchimba na DDCA alikuwa ameshafanya usanifu wa awali. Ulinihakikishia kwamba sasa tatizo lilikuwa ni hela na ukaagiza DDCA waende. Lakini ninavyoongea sasahivi ni takriban mwezi mmoja na nusu unaenda bado DDCA hawajafika katika Tarime Mji kuhakikisha kwamba wanatuchimbia vile visima 23 wananchi wa maeneo ya pembezoni waweze kupata maji tukisubiria Mradi wa Ziwa Victoria.

Ni lini sasa wataenda? Maana mpaka sasa hivi DDCA hawajaenda. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, dada yangu lakini kikubwa ninachotaka kukisema sisi kama Wizara ya Maji tunatambua changamoto, si Serengeti tu kwa maana ya Mkoa wa Mara na ndiyo maana katika Miji 28 ambayo tumeiorodhesha kwa ajili ya kutatua tatizo la maji tumeipa kipaumbele zaidi ya miji mitatu kwa maana ya Tarime, Mugumu ambayo ipo Serengeti lakini pia Rorya katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nataka nikuhakikishie tumekwishasaini mkataba katika kuhakikisha utekelezaji huu unakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia yale maeneo ambayo yapo kandokando na Ziwa Victoria hususan Vijijini tunafanyia usanifu ili kuhakikisha vijiji vile ambavyo vipo pembezoni na Ziwa Victoria ili viweze kupata huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la uchimbaji visima katika Jimbo lako la Tarime tulikwishaagiza na tumepewa agizo hilo kuhakikisha kwamba linatekelezeka lakini kuna mabadiliko tu ya kiutendaji katika Wakala wetu wa Maji na wa Uchimbaji Visima DDCA lakini sasa hivi ameshapatikana Mkurugenzi, tunamuagiza kwa mara nyingine aende kuchimba visima vile ili wananchi wale waeze kupata maji. Kuhusu mradi wako wa Salasala pia tumekwishawalipa. Tunamtaka mkandarasi atekeleze m radi ule na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Mji wa Tarime kwa hadhi ya kuwa mji ulitakiwa kuwa na umeme kwa zaidi ya asilimia 90, lakini maeneo yenye umeme ni chini ya asilimia 40. Na kwa sababu, Waziri wakati anajibu baadhi ya maswali hapa amehakikisha kwamba, na akatoa instructions kwamba, vituo vya afya, zahanati, shule kama sekondari vihakikishwe vinapewa umeme.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu Kata ya Nkende kuna kituo cha afya, kuna sekondari na kuna shule za msingi, lakini hazina umeme. Kata ya Kenyamanyori ina shule ya sejkondari, ina shule za msingi, ina kituo cha afya hakina umeme na Kata ya Kitale kuna Sekondari ya nkongole na Mogabili na vituo vya afya pale, zahanati hazina umeme, vilevile na Kata ya Nyandoto.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa ni lini, na nimekuwa nikiuliza haya maswali, ni lini huu umeme wa REA utaweza kufika kwenye hayo maeneo ambayo hayana umeme kabisa, ili sasa hizo zahanati, vituo vya afya, sekondari na shule za msingi ziweze kupata umeme, pamoja na Wananchi? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza pamoja na kuwapongeza Wananchi wa Tarime kwa kupelekewa umeme katika vijiji vyote iko changamoto katika kata ambazo amezitaja, hasa Kata ya Nkende pamoja na Kenyamanyori na Kitale. Nimeshazungumza mpaka na Mkurugenzi alipie zahanati na shule zipelekewe umeme kwa sababu, vijiji na vitongoji vya maeneo hayo vina umeme. Kwa hiyo, nikupongeze Mheshimiwa kwa kufuatilia, lakini nikuombe uwasiliane na Mheshimiwa Mkurugenzi na Halmashauri ya Kijiji cha Nkende pamoja na Kijiji cha Kitale na Kenyamanyori waweze kulipia ili shule na zahanati zipelekewe umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, nyongeza ya hilo, nitapenda nitembelee mimi mwenyewe ili nikatoe maelekezo kwa wakurugenzi waweze kulipia. Mheshimiwa Esther hata akibaki nitakwenda mwenyewe ili kusudi maeneo hayo na zahanati ziweze kupatiwa umeme, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nisikitike kwa majibu ya Serikali ambayo yametolewa na Naibu na Waziri sasa hivi Serikali ya Awamu ya Tano tunasema tunaelekea kwenye Tanzania ya Viwanda na kwa kasi kubwa sana ununuzi wa ndege ambao tuahitaji pilot na Ma-engeneer, mnajenga SGR, stiegler’s gorge zote zitahitaji wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya majibu hayatoi uhalisia ni mwezi Mei mwaka huu tumepewa mwalimu mmoja wa sayansi sasa kama Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia walimu toka Tanzania tupate uhuru kweli tunao walimu 59, na upungufu ni mkubwa. Maswali yangu sasa.

Ningependa kujua katika sekondari tisa ambazo zipo ndani mji wa Tarime ni sekondari mbili ambayo ni High School ya Tarime na sekondari ya Mogabili ndio maabara zimekamilika sekondari saba zote maabara hazikamilia majengo ni yale ambao wananchi wamejenga na kwa kufanya hivi inazorotesha ufaulu wa wanafunzi. Ningependa kujua Serikali ni lini mtaleta fedha ili tuweze kukamilisha maabara ya hizi sekondari saba ambazo hazijakamilika zikisubiri Serikali ikamilishe pamoja na vifaa?

Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime tuna sekondari moja tu A-Level na kama unavyojua kwamba tuna sekondari tisa. Wanapomaliza form four wanafunzi wetu wengi na hasa wasichana wanashindwa kupata nafasi kuendelea na high school. Ni lini sasa Serikali itapandisha hadhi walau Mogabili Sekondari au Nyandoto kuwa A-level nayo ili kuchukua wanafunzi mchanganyiko kwa maana wavulana na wasichana ili watoto wetu wa kike waweze kwenda High School?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upole kabisa haya ndio majibu ya Serikali, yeye Mheshimiwa Esther kama ana majibu yake nadhani abaki nayo. Majibu ya Serikali majibu haya yanaandaliwa kutoka Halmashauri ya Tarime. Hakuna taarifa za uwongo ambazo zinatolewa hapa mbele ya Bunge letu Tukufu na ndio taarifa ya hali halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili suala la kupeleka walimu na kupeleka vifaa vya maabara haliwezi kabisa kulinganishwa na miradi mingine ya maendeleo kwa sababu kila kitu kinajitegemea na vyote ni muhimu sana na vinafanyika sambamba. Tumeajiri walimu awamu hii ya juzi 4500 ndio imepata walimu wachache, awamu iliyopita walimu walipelekwa Tarime lakini bahati nzuri na mimi nimefika wanazungumza ukifika Tarime pale tunazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala shule kupandishwa hadhi Waheshimiwa Wabunge mnafahamu ni suala la mchakato ni lazima ninyi wenyewe kama Mbunge wa eneo husika kupitia halmashauri yako kupitia vikao vya halmashauri kamati ya fedha, bajeti ya ndani na wadau mbalimbali ikiwepo na mfuko wako wa jimbo mleta maoni TAMISEMI Wabunge walioleta maoni yakupandishwa shule zao kuwa high school yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaomba nitoe taarifa kuanzia mwezi mwaka huu tuna shule nyingi zinaanzishwa ambao tumepata maoni kutoka kwa Wabunge wenyewe kwa vyanzo vya ndani tumpelekee Serikali na walimu tunawapeleka katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.

Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.

Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali imekiri kabisa kwamba wananchi wa Tarime asilimia 20 ndiyo wanaopata maji. Tatizo la maji ni Tanzania nzima. Sasa napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa miradi ya muda mfupi; visima virefu, Mradi wa Bwawa la Nyanduma ambalo tumekuwa tukilitengea fedha lakini haziendi na miradi mingine kama ya Gamasala na kwingineko kwa Tarime Mji, napenda kujua, ni lini Serikali itaenda kuchimba vile visima 23 ambavyo wameahidi kuanzia mwaka 2016 viweze kuwa suluhisho la muda mfupi kwenye Kata ya Kitale, Nyandoto, Kenyamanyoli na Mkende wakati tunasubiria Mradi wa Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, jana wakati wameweka Mpango hapa, Serikali imekiri kabisa kwamba imepeleka maji vijijini kwa asilimia 70.1, wamechimba visima miradi 1,423 ambapo kuna vituo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther, naomba uulize swali tafadhali.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Miradi hiyo ina vituo 131,000. Kwa Rorya tuna mradi mkubwa kule Kirogo ambao umetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.3, ulitakiwa kuwa na vituo 23…

NAIBU SPIKA: Swali Mheshimiwa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: … lakini kuna vituo vitatu tu ambavyo vinatoa maji. Ni lini sasa Serikali itahakikisha maji yanatoka kule Kirogo kwa vituo vyote 23 na siyo vituo vitatu tu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi, salama na ya kutosheleza kwa maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alikuwa ziarani hapo Tarime na aliweza kuwasiliana na kuambatana na Mbunge wa Tarime Mjini ambaye ni Mheshimiwa Kembaki na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mheshimiwa Naibu Waziri Waitara na Mheshimiwa Waziri ametoa ahadi hivyo visima vyote vitachimbwa ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa kuanza, katika mwaka wa fedha ujao, visima vitachimbwa na maji safi na salama yatapatikana bombani kwa wananchi wote wa Tarime. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la awali ambalo ni jibu langu la msingi. Eneo la Rorya visima hivi vitatu kwa sasa hivi vinapata maji kati ya 27. Vijiji hivi vinakwenda kupatiwa huduma kupitia Mwaka wa Fedha 2021/2022 lakini vile vile tayari Wahandisi wetu wa eneo lile wanaendelea na hii kazi na visima vile ambavyo vilisalia vinakwenda kuchimbwa na kuhakikisha kuona kwamba vinakwenda kutoa maji ya kutosheleza kwa wananchi wote wa Rorya.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mtaa wa Kenyambi na Bugosi katika Mji wa Tarime wana mgogoro wa muda mrefu na Jeshi la Wananchi na Serikali imeshafikia hatua nzuri tu ya kufanya tathmini na ikarudia tena kufanya tathmini bado imebakiza malipo. Napenda kujua ni lini wananchi wale wataenda kulipwa fidia yao ili waweze kuondoka maeneo yale na kuwaachia Jeshi la Wananchi wa Tanzania? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua kwamba tunaendelea kuwajali wananchi wetu wa Tanzania na niseme tu kwamba migogoro hii ilikuwepo kadhaa lakini niseme kwamba kati ya migogoro hiyo, zaidi ya asilimia 50 ya migogoro tumeshaitatua. Yako maeneo ambayo tumeyatambua kwa ajili ya fidia na wananchi wameshalipwa, yapo maeneo mengi ambayo tayari tumeshalipa. Hii inaonesha tunao mwendelezo mzuri wa kuendelea kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi hawa wa Tarime wavute subira kwa sababu tunatafuta fedha. Tukipata fedha kwa maeneo yote ambayo tumeyatambua yanahitaji fidia kwa wananchi wetu tutakwenda kuwafanyia malipo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge kuvuta Subira na wakati mwingine tunaweza tukaonana ili nimueleze kwa kinagaubaga namna tunavyokwenda kutatua matatizo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Kicheko)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara yanaonyesha uhalisia wa Wilaya zote ndani ya Mkoa wa Mara kwenye kadhia ya umeme na kwa sababu umeme unaweza kuimarisha usalama na kuweza kukuza uchumi kwa maana kupitia uanzishwaji wa viwanda na vitu vingine. Ningependa kujua ni lini sasa Serikali itahakikisha umeme unapatikana katika wilaya zote ndani ya Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wilaya zote Tanzania Bara zina umeme, maeneo machache katika wilaya hizo ndiyo hayajafikiwa na umeme, kwa hiyo nimhakikishie kwamba maeneo hayo machache ambayo bado hayajafikiwa na umeme kwa maana ya vijiji yatakuwa yamepatiwa umeme katika miezi 18 ijayo. Kama ni umeme wa uhakika kama nilivyotangulia kujibu maswali yaliyotangulia ya msingi, Serikali inaendelea kuwa na jitihada za kuhakikisha inatenga bajeti kuhakikisha inawawezesha TANESCO kuendelea kurekebisha miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, pia Serikali inatekeleza miradi mikubwa sana ya ufuaji wa umeme Tanzania bara ikiwemo ya Mwalimu Nyerere itakayozalisha megawatt 2,115, Rusumo megawatt 80, Kagati megawatt 14, Ruhudji megawatt 358 na Rumakali megawatt 222. Miradi yote hiyo ikikamilika tutaweka umeme mwingi sana kwenye grid yetu ya Taifa na kuweza kumpatia kila mmoja umeme wa kutosha. Kwa hiyo tunawahakikishieni Wabunge wote kwamba umeme upo na utaendelea kuongezwa, tutarekebisha miundombinu yetu ili kila moja aweze kufikiwa na umeme ili Tanzania ya viwanda iweze kuwa ya kweli.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali imeweza kutoa fedha nyingi sana za walipa kodi masikini kwenda kwenye miradi ya maji, lakini uhalisia ni kwamba miradi mingi sana haitoi maji kwa ukamilifu au mingine haitoi maji kabisa. Ningependa kujua, ni lini Serikali itafanya ukaguzi kwenye miradi yote nchi nzima ambayo haitoi maji ili sasa iweze kutubainishia bayana ni miradi ipi kwa fedha kiasi gani zimewekezwa na haitoi maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli fedha nyingi zimeelekezwa katika miradi ya maji na ndiyo maana tatizo la maji linaendelea kupungua. Namna ambavyo tatizo lilikuwa huko awali ni tofauti na sasa hivi, na tayari sisi Wizara tunafanya kazi kwa makusudi kabisa usiku na mchana ili kuhakikisha kuona kwamba miradi yote ambayo haitoi maji itatoa maji. Tayari miradi ambayo ilikuwa ya muda mrefu haikuweza kutoa maji. Baadhi tayari inatoa maji na tayari watendaji wetu wanaendelea kufanya kazi. Tutahakikisha miradi yote ambayo maji hayatoki maji yatatoka bombani.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kufuatana na majibu ya Naibu Waziri anasema kwamba mahabusu wana hiari ya kufanya shughuli mbalimbali; kwa sababu mahabusu wengi wanakaa muda mrefu Gerezani; miaka mitatu, nane, wengine mpaka tisa, wengine mpaka 12: Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupeleka vifaa mbalimbali ambavyo watakuwa wanajiendeleza mle ndani kama ni kushona cherehani; yaani ujuzi mbalimbali wakiwa mle mle ndani, siyo kwenda kufanya kazi nje, kwa kipindi ambacho wanasubiria kesi zao kama zimemalizika wameachiwa huru au kama wamefungwa. Kwa kipindi hiki, kwa nini msipeleke waendeleze ujuzi wao wakiwa mle gerezani? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamza Chilo, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mahabusu hawapaswi kufanya kazi kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa na pia sheria za nchi yetu. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kwamba katika maeneo ambayo tumepita na kuangalia, wengine wanapenda kufanya zile shughuli za hiari yao kabisa na wanapenda kufanya kazi. Nakubaliana na Mheshimiwa Matiko kwamba katika maeneo ambako tumekuwa na shughuli ambazo haziwaruhusu kutoka nje, kwa sababu mahabusu wanategemeana na aina ya kosa alilolikosa.

Mheshimwia Spika, kwa makosa ya kawaida unaweza kumruhusu hata kutoka kidogo, lakini kwa makosa yale magumu, makubwa, siyo rahisi kumruhusu. Sasa katika maeneo ambayo tumefungua bakeries kwenye maeneo ya Magereza na Shule za Kushona ambazo ziko ndani ya Magereza, kwa kweli wanazifurahia na wanafanya.

Mheshimiwa Spika, tunachukua maoni yake hapa kwamba hicho anachokisema ndicho kinachofanyika hata kwa sasa. Tutajitahidi tu kuongeza uwekezaji kuhakikisha kwamba tunapeleka mashine hizo za kushona au zinazofanana na shughuli za kawaida zinazoweza kufanyika ndani ya Magereza ili waweze kujishughulisha kwa sababu kusema ukweli mtu kukaa bila kufanya shughuli yoyote kwa muda mrefu inakuwa siyo jambo ambalo kibinadamu linakubalika. Hata wao unaona kabisa nimesema nao, wanasema tuleteeni shughuli za kawaida tufanye. Kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge. Ahsante. (Makofi)