Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Esther Nicholus Matiko (3 total)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa na mimi nimwulize Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni dhahiri kwamba wanafunzi hawatakiwi kufanya siasa Vyuoni, lakini kumekuwepo na ama mkakati au maelekezo ambapo Menejimenti ya Vyuo inawanyanyasa wanafunzi wanaokuwa hawapendezwi na siasa ya Chama cha Mapinduzi. Je, ni kweli kwamba kuna hayo maelekezo? Kama hakuna maelekezo, Serikali inazieleza nini sasa Menejimenti za Vyuo kuhusu hii tabia ambayo imejengeka ya kuwanyanyasa vijana na hata kuthubutu kuingilia Uongozi wa Serikali za Wanafunzi? Mojawapo ya Chuo ambacho kimekithiri ni Chuo Kikuu cha Dodoma.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo:-
Kwanza nataka nikanushe kwamba siyo kweli kwamba kuna maelekezo kwenye Vyuo vyote vya Elimu ya Juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, hakuna unyanyasaji wowote unaofanywa kwenye Vyuo kwa wanafunzi ambao... (Makofi/Kelele)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanao uhuru wa kujiunga na vyama vyovyote wanavyovitaka, lakini kila eneo limeweka utaratibu wake. Hakuna zuio la wafanyakazi kujiunga na vyama vyovyote lakini liko zuio la mtumishi anapokuwa kazini kuendesha siasa. Hakuna zuio la mwanafunzi yeyote kama Mtanzania kujiunga na Chama anachokitaka yeye, lakini zuio ni kwamba hutakiwi kufanya siasa wakati wa masomo ili u-concentrate na masomo yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inaweza kutokea labda vijana wawili wenye itikadi tofauti huko wakafanya mambo yao, wakatofautiana huko, huo siyo utaratibu wa Serikali, ni utaratibu wao wao wenyewe. Kwa hiyo, nawaomba sana niwasihi Viongozi wa Vyama vya Siasa, tusilione hili kama ni msimamo wa Serikali, badala yake tulione hili kama ni mapenzi ya watu wengine, kama ambavyo vijana wafanyabiashara huko wanavyoweza kukorofishana mahali pao, lakini haina maana kwamba yule wa Chama Tawala anapokorofishana na mtu mwingine wa Chama cha Upinzani huko kwenye biashara zao tukasema labda soko lile, Chama Tawala kimepeleka watu wake kuzuia watu wa Vyama vingine wafanye vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, niwasihi Watanzania wote; Tanzania hii ni yetu sote na tunahitaji maendeleo ya Watanzania wote. Kila mmoja anao uhuru wa kupenda Chama anachokitaka. Kama kuna maeneo yanabana kisheria na kwa utaratibu wa matumizi au matakwa hayo kuyapeleka maeneo hayo, lazima yazingatiwe. Serikali hii itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali Vyama vyao; tutaendelea kuwahudumia Watanzania wote bila kujali Vyama vyao; pia tutatoa elimu kutoka ngazi ya awali mpaka elimu ya juu bila kujali mapenzi ya Chama chako. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikusihi tu uamini bado kwamba Serikali hii haina jambo hilo wala haina maagizo hayo mahali pa kazi na uwe na amani. Nami nasema Watanzania hawa ni ndugu, wanaishi pamoja na bado tunapenda washiriki kikamilifu katika masomo yao. Ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nakushukuru Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni ukweli kabisa kwamba, hawa askari hawapewi hizi sare na hata wakifanya parade utaona uniform zao ziko tofauti-tofauti kwa texture, lakini hata kwa rangi.

Mheshimiwa Spika, nilitaka pia kujua, maana hujajibu swali langu lile jingine, fidia ambazo watarudishiwa gharama ambazo wakati mnaendelea kujiratibu kuhakikisha wanapewa hizi uniform. Je, wataweza kuridishiwa gharama ambazo wamekuwa wakizitumia kujinunulia uniform zao wenyewe?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu umelieleza hilo na unaonesha unazungumza kama una uhakika wa kwamba, askari wetu wananunua. Na ungependa kujua je, kama askari hao wanaweza kurudishiwa fedha zao kama sera ya kuwapa vifaa bure ipo?

Mheshimiwa Spika, basi naomba nilichukue hilo niwasiliane na Wizara husika, ili tuone msingi wa ununuzi wa vifaa hivyo, halafu tutaweza kuzungumza vizuri na Wizara ya Mambo ya Ndani na tutakupa taarifa Mheshimiwa Mbunge, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.

Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.