Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Marwa Ryoba Chacha (34 total)

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naitwa Mwalimu Marwa Ryoba Chacha ni Mbunge wa Jimbo la Serengeti.
Kwa kuwa tatizo ambalo liko Temeke ni sawasawa na tatizo ambalo liko ndani ya Jimbo la Serengeti. Katika barabara ambayo ni lami ya kutoka Makutano – Butiama - Nata - Tabora B - Loliondo na kadhalika, ilishafanyika upembuzi yakinifu na evaluation kwa wananchi ambao barabara hiyo inapita ambapo hiyo barabara haikuwepo. Tangu mwaka 2005 mpaka leo wananchi hao hawajalipwa.
Je, Serikali inasema nini kuhusu fidia ya wananchi ambao wako kando kando mwa hiyo barabara ambao walishafanyiwa evaluation lakini hawajalipwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba awe na subira kwa sababu kuna swali hilo hilo limeletwa na litajibiwa katika Mkutano huu kabla haujaisha. Kwa hiyo, nitaomba muda ukifika wa kulijibu hilo swali tuyajibu hayo yote kwa pamoja.
MHE. MARWA R. CHACHA: Nina maswali mawili. Kwanza, naomba niwaambie tu kwamba Serengeti wanaishi binadamu, siyo wanyama peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija Serengeti ni aibu sana, yaani utafikiri haipo Tanzania. Hatuna maji, hatuna lami, hatuna chochote, yaani faida tunayoipata sisi kuishi Serengeti National Park ni tembo kula mazao ya wananchi na kuua watu. Hiyo ndiyo faida tunayoipata.
Sasa mimi nimeuliza kwamba kwanini Wizara tusipate sehemu ya gate fee au bed fee? Hivyo vilikuwa ni vyanzo vya mapato vya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti haina chanzo chochote. Ukija kwenye kwenye service levy, wamechukua vyote, hakuna kitu. Sasa sisi own source tunatoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye maelezo ya Naibu Waziri, amesema kwamba wamewahi kuisaidia Wilaya, mimi nimekuwa Diwani tangu mwaka 2010 sijaona mradi wowote wa TANAPA.
MHE. MARWA R. CHACHA: Swali la kwanza, kwa kuwa ni majirani zetu, ninyi watu wa TANAPA naomba mtujengee game post kila kata katika kata kumi, ili kuzuia tembo, sisi tulime tu, hamna shida. Tunahitaji game post. Hata gari la kufukuzia tembo hatuna.
Swali la pili.

MHE. MARWA R. CHACHA: Swali la pili, kwa kuwa sasa makampuni haya yameenda Mahakamani kuishitaki Serikali, Mwanasheria wetu unasemaje kuhusu hili? Maana sasa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti hatuna own source? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuacha siku nyingine, jana nilikaa na wananchi wa Serengeti katika ofisi yangu wakiandamana na Mheshimiwa Mbunge kuelezea tatizo la single entry katika Pori la Serengeti ili ifanyiwe marekebisho, wananchi wa Serengeti ambao wana WMA waweze kufaidika zaidi na pori la Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikiliza na tatizo lao tuko kwenye hatua ya kulitatua. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba wananchi wa Serengeti hawafaidiki na kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyo na hizi WMA ambavyo vinapakana na Serengeti vinapata shilingi milioni 300 kila mwezi kutokana na biashara ya WMA hizi. Kwa hiyo, siyo kweli kabisa kwamba hawafaidiki na kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tuko tayari kuongeza ulinzi katika maeneo ya mipaka na katika mwaka huu unaokuja wa fedha tumepanga tujenge vibanda vitatu kwa ajili ya askari ili kuhakikisha kwamba tunasaidiana na Wilaya katika kuwalinda wananchi na hivi sasa tayari tuna magari ambayo yanazunguka kule kuhakikisha kwamba tunasaidia kupunguza hasara ambazo wananchi wanaweza kupata kutokana na wanyama waharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na Wilaya ili kuhakikisha kwamba tunapunguza madhara haya.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Makutano – Mugumu – Mto wa Mbu imetengewa fedha kuanzia mwaka 2012 - 2013 ili kujenga kilometa 50 kuanzia Makutano mpaka Sanzate.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoongea, tangu mwaka 2013, hii ni 2016, hata kilometa moja ya lami haijawahi kukamilika. Sasa kama kuanzia mwaka 2013 mpaka sasa ni miaka mitano...
Miaka mitano kilometa 50 haijakamilika. Uki-cross multiplication it will take 45 years kukamilisha kilometa 452.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali, nataka Mheshimiwa Waziri awaambie wananchi wa Serengeti, ni lini watakamilisha ujenzi wa lami kuanzia Makutano mpaka Mto wa Mbu?
Swali la pili, ninavyoongea, sasa hivi hakuna mawasiliano kwenye hii barabara, imekatika! Daraja la Mto Robana limekatika. Serikali iko tayari kuji-commit sasa hivi kupeleka hela zikajenge yale madaraja ambayo yamebomoka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha kwa kusimamia kwa ukamilifu Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imekusudia na imeweka barabara hii katika Ilani yake na tunaanza kuitekeleza kwa mwaka ujao wa fedha ukiacha kile ambacho kimeshafanyika katika kipindi kilichopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka ujao wa fedha, bajeti yetu itakapofika, Waheshimiwa Wabunge naomba muikubali ili tuweze kutekeleza Ilani hii ya Chama cha Mapinduzi. Katika barabara hii shilingi bilioni 12 tumezitenga kwa ajili ya kujenga kipande hiki anachokiongea na shilingi bilioni nane tumeitenga kwa ajili ya kujenga upande wa pili wa Arusha ambayo nimeiongelea.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kutokana na uhifadhi unaofanywa na wananchi wa Serengeti umesababisha tembo kuongezeka kwa wingi sana.

Mheshimiwa Spika, kwa sensa ambayo imefanyika 2006, kulikua na tembo 3000 na kwa sensa ambayo imefanyika mwaka 2014 tembo wako 7000 na wengi wamehamia maeneo ya West – Serengeti sasa kwa kuwa tembo wameongezeka imekua sasa ni laana kwa wananchi wa Serengeti.

Mheshimiwa Spika, swali, kwa vyote hivi ambavyo Waziri amesema ni ukweli hakuna hata kimoja ambacho kimetekelezwa. Sasa swali kwa Waziri, la kwanza; tungetamani Wanaserengeti kila Kata iwe na game post ambayo game post itakua na gari, itakua na Maaskari na silaha. Je, Wizara iko tayari kujenga game post kwa kila Kata, ziko Kata 10 zinazozunguka hifadhi, mko tayari kutujengea game post na kila game post na askari wake wanalinda mipaka ya Kata husika dhidi ya tembo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nimepitia Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sheria Na. 5 ya Mwaka 2009, kuna kifuta machozi hakuna fidia. Na kifuta machozi kama tembo ameua mtu ni shilingi 1,000,000/= na kama wewe umeua tembo ni 25,000,000/=. Swali, kati ya tembo na mtu nani wa thamani?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Serikali katika hatua ya kwanza kabisa inampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jitihada za Serikali katika uhifadhi. Takwimu za ongezeko la tembo ni faraja kwa Taifa hili kwa sababu kila mmoja wetu anafahamu faida za uwepo wa wanyamapori na faida za uhifadhi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la hatua zilizochukuliwa napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ni wiki mbili tu zilizopita nilikuwa Serengeti na haya niliyoyasema hapa sikuyaandika tu kutoka kwenye karatasi isipokuwa nimeshuhudia yakiwa yametekelezwa katika hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake la uanzishwaji wa game posts katika kila Kata hili ni wazo jema, unapotaka kuanzisha jambo ambalo ni jipya ni lazima kujipa fursa kwanza ya kufanya utafiti uliokamilika uweze kujiridhisha juu ya umuhimu na uwezekano na ukaangalia kila aina ya jambo ambalo ni la umuhimu kabla ya kutekeleza mpango wowote unaoufikiria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunalipokea, tutalifanyia kazi na itakapoonekana kwamba ni jambo ambalo ni vema tukalitekeleza basi Serikali italitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kifuta machozi kuwa kidogo, katika jibu langu la msingi nimeeleza pale mwishoni kwamba Serikali inatambua juu ya changamoto ya kwamba kifuta jasho au kifuta machozi vyote kwa pamoja hivi kila kila kimoja havitoshi, yeye ameangalia tu upande wa maisha lakini pia hata kwenye mali, mali zinazoharibiwa wakati mwingine ukiweka ulinganifu wa kiasi cha mali kilichopotea na kiwango kile kinacholipwa mara nyingi kinakuwa ni kidogo.

Mheshimiwa Spika, lakini nimesema kwenye jibu la msingi kwamba Serikali inachukua hatua ya kupitia viwango hivyo na upitiaji wa Kanuni utakapoonekana kwamba, iko haja ya kuweza kufanya mabadiliko basi tunaweza kufanya mabidiliko hayo kwa mujibu wa sheria.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa majibu ya nyongeza baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ningependa sana niwapongeze wananchi wa Serengeti kwa moyo wao na juhudi zao katika kuhifadhi wanyamapori, ninaamini kabisa kama wananchi wa Serengeti wangekuwa hawahifadhi wanyama wale walioko pale ingekuwa vigumu sana kwa pori lile kuwa zuri na pori ambalo lina kiwango cha pili kwa ubora dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu ambao wanaua tembo ni majangili siyo wananchi wa Serengeti na ndiyo maana watu ambao wanawaua wale tembo kama wanaua kwa makusudi kama ambavyo inatokea mara kwa mara ndiyo maana wanachajiwa fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, lakini malipo haya hayalinganishi binadamu na wanyama. Lengo ni kuhakikisha kwamba watu wenye nia mbaya hawauwi wanyama bila sababu, lakini pia ni kuhakikisha kwamba Serikali inashirikiana na wananchi katika kuomboleza matukio ambayo yanaweza kutokea kwa wanyama kuwaua wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Wilaya ya Serengeti ni Wilaya ambayo kimsingi tunazungukwa na wanayama kila kona na zao pekee ambalo kimsingi Tembo hali ni tumbaku, Mheshimiwa Spika, unakumbuka nimekuandikia barua kuhusu issue ya Tembo wamehamia Serengeti wamekula mazao yote; wananchi kwa sasa hawana chakula, zao ambalo kimsingi lilikuwa likiwanufaisha na kuwaokoa wananchi wa Serengeti ni tumbaku, kwa sasa tumbaku haina soko hata kampuni ya Alliance One iliyopo nasikia mwakani inaondoka.
Sasa swali Mheshimiwa Waziri Serikali hii ya Awamu ya Tano kipaumbele chake ni viwanda ni lini mtajenga kiwanda cha ku-process tumbaku Tanzania?
La pili, uko tayari wewe Waziri na mimi Mbunge wa Jimbo la Serengeti kuambatana na wewe kwenda kuwasikiliza wakulima wa tumbaku wa Serengeti na kuwatafutia hayo makampuni uliyosema?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakiri kabisa kufahamu changamoto inayoletwa na wanyama waharibifu kwa wakulima wa Serengeti kama ilivyo katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Mimi nafahamu maeneo ya Serengeti kwa sababu ni jirani zangu, sisi Ngorongoro tulichokifanya ni kwamba wanyama tumewatumia kama fursa ili hata pale wakituletea taabu tuone kwamba tunaweza vilevile tukanufaika na hao wanyama.
Hata hivyo changamoto ya tumbaku kama zao la biashara wote tunafahamu, tumbaku ndio zao la pekee duniani ambalo hata wale wanaotaka wanufaike nalo hawakubali kulipigia debe linunuliwe. Leo hii nina hakika Mheshimiwa Mbunge na hata wale wanaotoka maeneo mengine wanaolima tumbaku nikiwaambia twendeni nje tukapige debe ili watu wanunue sigara nina hakika hawataungana na mimi, ndio changamoto ya tumbaku, ni zao ambalo limeshetanishwa duniani yaani limekuwa demonized.
Mheshimiwa Spika, ni zao ambalo pamoja na kwamba tuko tayari kunufaika nalo lakini dunia nzima inapiga vita tumbaku na hii imesababisha bei ya tumbaku iendelee kudorora na wanunuzi wa tumbaku wameendelea kuwa wachache siku baada ya siku. Leo hii nchini tuna wanunuzi wanne tu kampuni hiyo anayosema ya Alliance One, tunao Premium, TLTC na GTI na duniani kote makampuni makubwa hayazidi manne yanayonunua tumbaku. Kwa hiyo, ni shida ambayo ni ya dunia nzima lakini pamoja na changamoto hiyo Serikali inaendelea kutafuta fursa katika masoko ambayo yanaelekea kuanza kujitokeza hasa soko la China. Wizara inaendelea na majadiliano na Ubalozi wa China tuone ni namna gani tunaweza tukapata fursa katika soko la China.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunaangalia uwezekano wa kupata fursa katika soko linaloibukia la shisha katika maeneo ya Uarabuni, nchi kama Misri lakini kwa sasa wananchi wetu tunaendelea kuwaeleza umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kulima mazao mengine kwa sababu inavyoelekea soko la tumbaku duniani litaendelea kushuka kwa sababu ya aina ya zao lenyewe, ni zao ambalo linapigwa vita, zao ambalo lina madhara kiafya, kwa hiyo, tunaendelea kuwashauri kwamba tutafute mazao muafaka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa kiwanda cha kuchakata tumbaku nchini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inaweka mazingira wezeshi pamoja na kushawishi sekta binafsi kujenga viwanda vya tumbaku.
Mheshimiwa Spika, tuna baadhi ya viwanda vya tumbaku, kuna kiwanda kikubwa kipo Morogoro lakini tunaendelea kuwahamasisha sekta binafsi kama wanaweza wakaanzisha kiwanda cha kuchakata tumbaku sina hakika kama hata nikiandamana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Serengeti kwamba mimi ninaweza nikapeleka kiwanda kule lakini tutaendelea kuwahamasisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Serikali inafanya nini kuhusiana na uharibifu ambao unaendelea, nilishaongea na Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi niko tayari kuongea na Wizara ya Maliasili ili kuangalia ni namna gani Serikali inaweza ikawafidia wananchi ambao mazao yao yanaharibiwa na Tembo.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Serengeti kwa kujitahidi kukamilisha vyumba vya maabara kwa asilimia 81.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wamekamilisha kwa asilimia 81, Mheshimiwa Naibu Waziri uko hapa na umekuja pale Jimbo la Serengeti na umeona hali ilivyo; kwa kuwa wananchi hawa wamejitahidi kwa hali hii. Je, Serikali kupitia hizi fedha za P4R mko tayari kukamilisha hivi vyumba 12 ambayo ni sawa na asilimia 19? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ujenzi wa maabara ulipaswa pia kuendana na upungufu wa vyumba vya madarasa: Je, kupitia hizi pesa za P4R, mko tayari kupeleka sehemu ya fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwapongeze kwa kazi kubwa waliyoifanya; na kama kuna deficit ya vyumba 12, niseme kwamba Serikali tutashirikiana, siyo na watu wa Serengeti peke yake, isipokuwa jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunapata maabara katika kila sekondari zetu zilizokamilika. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge nilikwambia hiyo juhudi iendelee, lakini Serikali na sisi tutatia nguvu yetu kuhakikisha maeneo yote yale ya Serengeti yanapata maabara kama tulivyokusudia.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimezungumza hapa kwamba tumetenga karibu shilingi bilioni 16. Lengo ni kwamba zile maabara ambazo wananchi wamejitolea kwa nguvu kubwa kuzijenga, lazima ziwe na hivyo vifaa. Kuanzia mwezi Machi mpaka mwisho wa mwaka hapa tutajikuta tumekamilisha suala zima la maabara siyo Serengeti, lakini katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, suala zima la ujenzi wa vyumba vya madarasa, ni kweli. Tuna changamoto ya vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali ikiwepo kwako Serengeti, nami nakupongeza sana, nilikuwa nawe siku ile. Tutajitahidi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu ukiangalia katika michakato mbalimbali, tulikuwa na madarasa ambayo yapo katika program ya P4R ambayo tumejenga kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu, lakini tulikuwa na madarasa ambayo tulikuwa tunayajenga kwa mpango wa MES II lakini kuna mipango mingine mbalimbali ambayo takriban shilingi bilioni 29 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vingi vya madarasa, zaidi ya vyumba 3,000.
Mheshimiwa Spika, katika harakati hizi, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo maeneo ya Serengeti, lakini nchi nzima kwa ujumla kwa hii mipango mipana ya Serikali ili tuondoe changamoto ya madarasa. Lengo kubwa ni wanafunzi wetu wapate maeneo mazuri ya kusomea.


WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Jafo kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imeshanunua vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kwa ajili ya maabara zote nchini zilizokamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaanza zoezi la usambazaji wa vifaa hivyo. Kwa hiyo, natoa tu wito kwa Waheshimiwa Wabunge ambao katika maeneo yao maabara hazijakamilika, waendelee kuzikamilisha kwa sababu utaratibu wa Serikali ni kwamba tutakuwa tunapeleka vifaa pale ambapo maabara zimekamilika.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, pengine Waziri wa Maliasili na Utalii au Waziri; katika Wilaya ya Serengeti ndani ya mbuga yetu ya wanyama ya Serengeti kuna mahoteli mengi na makampuni mengi ambayo kisheria wanatakiwa kulipa service levy, lakini kwa muda mrefu walikuwa mahakamani wakikataa na kupinga kulipa ushuru wa service levy. Sasa Serikali imewashinda, tumewashinda yale makampuni lakini mpaka sasa yale makampuni yanagoma kulipa ushuru wa service levy. Je, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Maliasili na Utalii inaweza kutusaidiaje sisi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ili waweze kulipa arrears?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hapo siku za nyuma tumekuwa na hiyo changamoto ya hotels kutofuata utaratibu ambao tulikuwa tumeshauweka na kwa kweli ni kwa mujibu wa sheria kwamba, walipaswa kulipa zile kodi mbalimbali kwa utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge anauzungumzia lakini ni kweli suala hili lilifika mahakamani na hukumu ilitolewa na mahakama sasa kwa bahati mbaya utekelezaji wa hukumu haukuweza kuendelea kwa sababu tulikuwa na changamoto ya kutokuwa na bodi ambayo kwa mujibu wa sheria ndiyo inayopaswa kufanya maamuzi na kuchukua hatua. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa kwa ujumla kwamba tayari bodi imekwishaundwa, Mheshimiwa Rais alishateua Mwenyekiti wa Bodi na bodi imekamilika iko tayari na kwamba hivi karibuni suala hilo litapatiwa ufumbuzi na majibu yatapatikana na bila shaka hakuna mashaka tutakwenda kutekeleza ile hukumu kama ilivyotolewa na mahakama.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza swali langu limejibiwa nusu, mimi nimeuliza ni lini ujenzi wa chujio na usambazaji wa maji utakamilika? Kwa hiyo, yeye amejibu upande mmoja wa ujenzi wa chujio, hajajibu upande wa usambazaji wa maji. Na ujenzi wa chujio hili unasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Maji pengine ndiyo maana Mheshimiwa Naibu Waziri hana picha halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza; la kwanza ni kuhusu usambazaji wa maji katika Mji wa Mugumu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa chujio hili. Nataka kumuuliza Naibu Waziri, bahati nzuri ulikuja mwaka jana pale Jimbo la Serengeti pale Mugumu na uliyaona yale maji, ninataka kujua kama kata zote za Mamlaka ya Mji mdogo wa Mugumu, kata saba Kata ya Morotonga, Kata
ya Mugumu, Kata ya Stendi Kuu, Kata ya Getaisamo, Kata ya Kisangura kama zote zitapata maji, pamoja na vijiji vinavyozunguka lile bwawa, Kijiji cha Miseke, Kijiji cha Rwamchanga na Kijiji cha Bwitengi. Hilo ni swali la kwanza, ningependa kujua kwamba wakati wa usambazaji wa maji
haya maeneo yote yatapata?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; huyu mkandarasi ambaye anajenga chujio hili (PET) anadai sasa hivi ana certificate ambayo iko Wizarani ya zaidi ya milioni 200 na kimsingi mradi ule unasuasua pengine kwa sababu hana fedha. Je, Wizara iko tayari kumlipa certificate anayodai ili aendelee na hii kazi mradi ukamilike haraka huo mwezi wa sita?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa hii awamu tulianza kujenga chujio ili kuongeza uzalishaji wa maji ifikie lita milioni tano kwa siku, ambazo zinatosha kwa wakazi kwa sasa kwa wale wa mjini, lakini Serikali kwa kutumia mkopo wa dola milioni 500 tumetenga milioni nane US dollars ambazo ni sawasawa na shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kuboresha usambazaji katika maeneo ya vitongoji vya Mji wa Mugumu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na shaka, tatizo la kupata maji ya uhakika kwa Mji wa Mugumu na vitongoji vyake linashughulikiwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili kuhusu madai ya mkandarasi; madai hayo tutamlipa mara tu baada ya kupata hizo certificates, hakuna shaka ya fedha, fedha tunazo.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Vilevile katika Wilaya ya Serengeti ni moja ya Wilaya kongwe ambayo kimsingi ni Wilaya ambayo iliizaa Bunda; na ni Wilaya ambayo ina changamoto kubwa sana kijiografia, ni Wilaya ambayo ni kubwa kwa eneo, pia, ni Wilaya ambayo ina kata nyingi kweli.
Je, ni lini Wilaya hii itagawanywa kuwa Wilaya mbili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba tuweke kumbukumbu sawa, hapa ukiwa unajibu maswali haya lazima kidogo akili yako ikae vizuri. Kwa sababu Wabunge wengine wanasema maeneo yasigawanywe, wengine
wanasema maeneo yagawanywe.
Mheshimiwa Mbunge, nadhani unakumbuka siku ile tulienda wote mpaka usiku tumetoka kule tukiwa Serengeti kwako. Ni kweli Kata zako zimekuwa scattered sana, ndiyo maana nalifananisha Jimbo lako na lile Jimbo la Ngorongoro, ukiingalia jiografia yake ni jiografia yenye changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa sababu Serikali hii hatuwezi kugawanya kila maeneo tu, ni lazima kuangalia jinsi gani kuweza kuyahudumia yale maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale kwenye haja na michakato halali na vikao vyetu huko ambako mamlaka tulizopita mamlaka za Wilaya na mamlaka za Mikoa, zikifanya maamuzi hayo basi jambo hilo litakuja katika Ofisi ya Rais TAMISEMI na Waziri wangu ataliangalia, atalipima, pale atakapoona linakidhi basi atafanya maamuzi sahihi, kutokana na uhalisia wa eneo hilo.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye Jimbo langu la Serengeti katika process za kuongeza vijiji, vitongoji na kata, kuna baadhi ya maeneo ambayo utaratibu haukufuatwa, baada uchaguzi kuna Serikali za Vijiji walijiuzuru. Kwa hiyo, kimsingi kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji na mpaka ninavyoongea hakuna uongozi kwenye vijiji hivyo. Nini tamko la Wizara kuhusu maeneo ambayo yana migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba iko migogoro mbalimbali lakini migogoro inatofautiana, iko mipaka ya kijiji kwa kijiji, kata kwa kata, iko ya aina nyingi na kwenye orodha tumeorodhesha zaidi ya 250 kwa nchi nzima.
Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mazingira ya migogoro hii inatofautiana kutoka mgogoro mmoja hadi mwingine hatuwezi kuwa na tamko la pamoja kwa hiyo atuletee ili tuweze kuona hiyo scenario ikoje ili tuweze kutatua mgogoro husika ikiwa ni pamoja na mamlaka za uongozi wa maeneo husika.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, kwa tatizo lililoko Nzega huko ni sawasawa na tatizo lililoko Serengeti. Sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba Wilaya ya Serengeti kwa ukubwa wake; je, ina-qualify kuigawa kuwa Wilaya mbili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, qualification ya Wilaya inategemea vigezo kadhaa ikiwepo population ya watu, ikiwepo area size na mambo mengine. Kwa hiyo, kwa sababu ombi hilo hatuna rasmi katika ofisi yetu, maana ingekuwepo limefika, tungeenda kufanya uhakiki kuangalia, je, vile vigezo vyote vya kuanzisha Wilaya mpya vinakidhi au vipi? Ndiyo tungeweza kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hili naomba niliache kwa wananchi wa Serengeti wenyewe watafanya maamuzi kwa kadri watakavyoona inafaa na sisi kwa mujibu wa ofisi yetu, itakwenda kufanya tathmini kama hilo litkuja kuangalia kama nini kinafanyika. Ila tufahamu wazi kwamba Serengeti japokuwa eneo ni kubwa lakini idadi ya watu ni wachache, kwa sababu eneo kubwa sana liko katika sehemu ya hifadhi. Kwa hiyo, mambo hayo yote tutayazingatia. Lengo kubwa ni mustakabali wa nchi yetu iwe vizuri.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kuna huu utaratibu wa MSD kwenda kwenda vituo vya Afya wamebeba, wanapeleka kondomu na mseto pakiti nane unaenda kwenye zahanati unakuta wamepeleka kondomu na mseto nane, huu utaratibu unasafirisha hivi vitu kutoka Mwanza mpaka kule Serengeti haukubaliki. Je, ninyi kama Wizara mnaona huu utaratibu uendelee?
Swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri umekuja pale Serengeti na Serengeti sasa ni Wilaya ya kitalii, tunapata watalii wengi lakini tulikupeleka kwenye ile Hospitali ya Wilaya ukaona umaliziaji wa ile OPD. Wizara mpo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia ile OPD? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la upelekaji wa dawa MSD naomba nitoe ufafanuzi ifuatavyo:-
Ni kwamba dawa zinapofika kule kwanza kuna request ya kawaida inayopelekwa, lakini dawa zinapofika lazima Kamati ya Afya ya kituo husika lazima ihisike katika upokeaji wa dawa, lakini nitoe wito kwa Halmashauri ya Serengeti kwa sababu japo kuwa tumepeleka fedha nyingi pale kuna baadhi ya fedha zingine bado hazijatumika katika ununuzi wa dawa, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Mbunge najua kwamba kwa sababu pale eneo lako lina changamoto kubwa tushirikiane vema kwamba kuhakikisha tunasukuma MSD dawa ambazo zimebakia karibuni za shilingi milioni 180 zifike pale site, lakini hali kadhalika mnao pesa nyingi zaidi za basket fund bado hazijanunua dawa, nitoe maelekezo hayo kwa Serengeti haraka iwezekanavyo dawa zipatikane kwa sababu tayari Serikali tumepeleka fedha.
Lakini katika suala la pili ni suala zima la hospitali tuliofika, ni kweli na mimi nimefika pale na tulivyoenda kuangalia tukasema ajenda ya Mheshimiwa Rais alipofika pale ni kuahidi kwamba atawahudumia wananchi na ndio maana katika kipindi cha sasa tumefanya commitment zile wodi mbili tutazifanya two wards in one, tutafanya zoezi kubwa pale la kupeleka takribani tutaweka nguvu karibu shilingi milioni 700 lengo kubwa ni kufanya ahadi ya Mheshimiwa Rais katika maeneo mbalimbali iweze kutekelezeka. Kwa hiyo hili ni jukumu la Serikali tunaenda kulitekeleza. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza tarehe 24 Mei, 2017 wakati Naibu Waziri akijibu swali langu lililokuwa linahusu kupeleka dawa kwenye vituo vya afya niliuliza swali la nyongeza lililokuwa linahusu hospitali hii ya Wilaya. Bahati nzuri Naibu Waziri amefika kwenye hospitali ile akaona, alisema kwamba wametenga shilingi milioni 700 kwenda kumalizia OPD ambayo hiyo ingekuja kabla ya mwaka wa fedha 2016/2017 haujaisha. Mwaka wa fedha 2016/2017 umeisha. Alitamka kwenye Bunge hili, wananchi wa Serengeti walisikia zinaenda shilingi milioni 700 kumalizia OPD. Je, alilidanganya Bunge na wananchi wangu wa Serengeti? Kama siyo kwamba alidanganya, nini kilitokea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, mantiki ya kupeleka fedha Serengeti ilikuwa siyo kulidanganya Bunge na zoezi hili tutalifanya maeneo mbalimbali. Kama Serikali, tuna mpango na tumezungumza kwamba katika programu ya Serikali kwamba tutafanya katika sekta ya afya hasa vituo vya afya vile ambavyo vimeonekana ni changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha sasa, takribani vituo 142 tutavifanyia ujenzi huo ambayo ni equivalent pesa yake karibuni shilingi milioni 700 katika kila center kwa ajili ya kutengeneza miundombinu na kupeleka vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kudanganya Bunge, jambo hilo halipo isipokuwa ni commitment ya Serikali. Kwa hiyo, jambo la msingi ni kwamba watu wa Serengeti wavute subira kwa sababu Serikali ina mipango yake na inatekeleza.
Katika ujenzi huu sehemu nyingine tunafanya bulk procurement kuufanya ujenzi huu tupate mkandarasi wa pamoja kuhakikisha ujenzi huu unaenda sambamba katika maeneo yote na lengo letu kwamba tupate value for money na ubora wa majengo ule unaokusudiwa tuweze kuupata vizuri. Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba inapeleka huduma za afya kwa wananchi wake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, barabara hii ambayo inaunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha imetengewa fedha mwaka 2016/2017, shilingi bilioni 12. Tender ikatangazwa kuanzia mwezi wa Disemba, 2016, hivi ninavyoongea ni mwaka mwingine wa fedha bado mkandarasi hajapatikana. Wananchi wa Jimbo la Serengeti, wananchi wa Mkoa wa Mara na Arusha wanataka kusikia, ni lini compensation na ujenzi wa barabara hii utaanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa sasa kipande cha Barabara Nata – Mugumu hakipitiki, kimesababisha mfuko wa cement sasa hivi ni shilingi 22,000. Mna mpango gani wa kutengeneza kipande hiki kwa kiwango cha changarawe kwa wakati huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kuwa Serikali inafanya juhudi ya kufanya barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ambayo inatoka maunganiko ya barabara kwenda Sanzate - Mugumu - Nata mpaka Arusha kama alivyotaja ina urefu wa kilometa 472.
Kwa hiyo, kwenye Awamu ya Kwanza barabara hiyo ya maunganisho imeshakamilika lakini sasa kwa eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge anataja ni kweli kuna fedha zilitengwa katika mwaka 2016/2017, shilingi bilioni 20, hii ilikuwa ni sehemu ya barabara nzima, lakini kwa mwaka huu wa fedha pia kuna shilingi bilioni 17.397 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Spika, hatua za ujenzi ni process, ni hatua ya tathmini na kulipa fidia ni hatua ya ujenzi wa barabara hii. Kwahiyo, baada ya tathmini ambayo imeshapelekwa, kiasi cha kama shilingi bilioni 4.1 ambazo zinahakikiwa kwa sababu zoezi la kuhakiki ni kujihakikishia kwamba malipo yanafanyika kwa uhalali, kumekuwa na matatizo kwenye utathmini, saa nyingine kumekuwa na rekodi ambazo sio sahihi, kwahiyo baada ya kukamilisha zoezi hili, process ya manunuzi itakuwa inakamilishwa na ujenzi utakuwa unaendelea kwenye awamu hii ya pili.
Mheshimiwa Spika, nitoe tu agizo kwa upande wa TANROADS, kama eneo hili halipitiki basi TANROADS Mkoa wa Mara waende waliangalie eno hili ili warekebishe maeneo wananchi waendelee kupita wakati hatua za ujenzi zinaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri anasema ujenzi unaweza kuanza mwaka 2018/2019, unaweza kuanza. Sasa wananchi wa Mji wa Ujiji na Kasulu kwa ujumla wanataka kupata uhakika, yaani ile commitment ya uhakika kwamba utaanza 2018 au unaweza maana ukisema unaweza, unaweza usianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Mji wa Mugumu tulipewa kilomita mbili mwaka wa fedha uliopita lakini kilomita mbili hizi tumetangaza mara tatu hazijapata mkandarasi kwa sababu ya kilometa chache. Je, Wizara iko tayari kwa mwaka ujao wa fedha kutuongezea kilomita iwe rahisi kwa ajili ya wakandarasi kufanya mobilization?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumesema kwamba ujenzi unaweza ukaanza kwa sababu bajeti haijapitishwa na Bunge. Naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane naye kupitisha kwanza bajeti ndiyo ujenzi uweze kufanyika vinginevyo kama Bunge halitapitisha bajeti hiyo, ujenzi hauwezi kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba wamepata ugumu kupata mkandarasi kwa sababu ya ufupi wa barabara ya kilomita. Ningemwomba Mheshimiwa Mbunge amshauri Mkurugenzi wake wa Halmashauri aweze kutembelea Halmashauri za jirani ambazo zimeweza kujenga hizo hizo kilomita mbili na zimepata wakandarasi. Ahsante sana.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ndani ya Wilaya ya Serengeti hatujawahi kushuhudia mvua kubwa kama hizi zinazoendelea kunyesha. Barabara za halmashauri hususan madaraja yamesombwa na maji na ruzuku tunayopata kutoka Road Fund, haitoshi. Je, Wizara iko tayari kutusaidia kujenga madaraja yale ya halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ombi lake na kwa kweli kabla hatujaiandaa bajeti itakayokuja kusomwa na Waziri wangu hapa, bajeti hiyo imezingatia matatizo makubwa ya uharibifu wa madaraja na barabara sehemu mbalimbali nchini na hasa kwa kuzingatia viwango tulivyojiwekea vya mgawanyo wa fedha za Road Fund za 30% kwa 70%, siyo rahisi sana kwa upande wa Serikali za Vijiji kuhakikisha kwamba madaraja yote yaliyobomoka pamoja na barabara zote zilizokatika znarudishwa katika hali yake ya kawaida. Tusubiri majibu atakayoleta Mheshimiwa Waziri wakati bajeti itakaposomwa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa NJaibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, mradi huu umechukua muda mrefu sana. Ukiangalia kwenye swali la msingi ni tangu 2008, lakini ukija kwenye majibu anasema usanifu umekamilika tangu 2013. Pamoja na kwamba Serikali inasema wako kwenye evaluation wananchi wa Wilaya ya Moshi na hususan wa Kata ya Tela wanataka kujua, huu mradi umetengewa shilingi ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Wilaya ya Serengeti kuna miradi ya maji kwenye Vijiji vya Nyagasense, Rung’abure na Kibanchebanche. Mradi wa Nyagasense hautoi maji na walishalipa retention yote. Pia Mradi wa Rung’abure hautoi maji. Mradi wa Kibanchebanche mkandarasi ametokomea na nimemwambia Mheshimiwa Waziri twende Serengeti, hatukwenda mpaka leo, wameshalipa mpaka retention lakini miradi haitoi maji. Ni nini tamko la Wizara dhidi ya matatizo haya ambayo yametokea, wamelipwa fedha zote miradi haitoi maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimjibu swali kaka yangu Mheshimiwa Marwa Chacha, moja alitaka kujua gharama ya mradi; gharama ya mradi itagharimu kiasi cha milioni mia nane ishirini na mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; kuna baadhi ya miradi ambayo imeshalipwa fedha za Serikali lakini haitoi maji. Nataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji na kama viongozi; maana unapokuwa Naibu Waziri, ni jukumu lako kuhakikisha wananchi wanapata maji. Sisi hatutamwonea haya yeyote ambaye amefanya ubadhirifu wa fedha za Serikali. Kama kweli kuna fedha ambazo kuna mtu amezila, basi ajiandae kuzitapika ili wananchi waweze kupata maji. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, baada ya kupata janga la tembo kuharibu mazao ya wananchi wa Serengeti na Bunda nilimwomba chakula, kwa kweli tulipata mahindi nimshukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza lakini kimsingi swali hili lilikuwa lijibiwe na Wizara ya Maliasili na Utalii. Sasa kwa kuwa Serikali ni moja naomba niulize maswali yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016, baada ya tembo kuharibu mazao sana na kupiga kelele hapa Bungeni ikaonekana hatua haichukuliwi nilimwandikia Spika wa Bunge barua dhidi ya madhara na hatua ambayo wananchi walikuwa wameamua kuichukua. Mheshimiwa Spika akamwandikia Waziri wa Maliasili na Utalii aliyekuwepo, Mheshimiwa Maghembe ambaye tuliondoka naye kwenda naye Serengeti akaona madhara makubwa na akakabidhiwa tathmini ya uharibifu wa mazao na mauaji ambayo yameyosababishwa na tembo.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazao na mauaji hauwezi ukaisha mwezi mtu hajauawa na tembo. Mashamba yanaharibiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ilishaahidi kuweka uzio au fence kuzunguka makazi ya wananchi, sasa miaka mitano inaelekea kwisha hakuna hatua yoyote, hakuna chochote kilichofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaweka mpaka fedha kwenye bajeti yake kuweka game posts kwenye maeneo ya makazi ya wananchi ili kuzuia tembo, lakini mpaka leo hakuna chochote kilichofanyika. Nini tamko la Serikali dhidi ya uharibifu unaosababishwa na tembo kwenye mazao ya chakula na mauaji ya wananchi wa Serengeti, Bunda na Tarime na maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo ameliuliza. Ni kweli kabisa kumekuwa na matatizo katika maeneo mengi na hilo eneo alilolisema ni mojawapo ya maeneo ambayo kumekuwa na tatizo sana la tembo kuvamia katika mashamba ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita tarehe 29 na tarehe 30 tulipeleka Maafisa wetu kwenda kufanya tathmini katika yale maeneo ili kuangalia uharibifu mkubwa ambao umefanyika na ili tuone ni hatua gani ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala ambalo amesema kwamba tuna mpango wa kuweka uzio, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali bado inafanya jitihada kuhakikisha kwamba tunachukua hatua za tahadhari na kuona ni nini kifanyike katika kuweza kuhakikisha kwamba tunawalinda wananchi wale ambao wanazunguka hifadhi zetu. Kwa hiyo, tutaendelea kulifanyia kazi. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake dogo la nyongeza, lakini kwa niaba pia ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa pongezi alizozitoa naomba nizipokee. Vile vile naomba pia niongezee katika majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili amejibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza kwa sababu linahusu wakulima, mazao na chakula naomba niseme kabisa kwamba sisi kama Wizara ya Kilimo kwa vile inahusu wakulima na mazao, basi tutashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, vile vile na Ofisi ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba tunahakikisha wakulima wetu wanapewa stahiki zao zinazostahili ili tatizo hili lisiweze kujitokeza tena. Nashukuru.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo la Serengeti, Vituo vya Afya vya Iramba na Nata vimetengewa fedha kwenye mwaka huu wa bajeti pamoja na Hospitali ya Wilaya ambayo imetengewa shilingi milioni 700. Leo ni tarehe 21, tarehe 30 mwaka wa fedha huu tulionao unaisha; na Mheshimiwa Waziri alipokuja pale Jimbo la Serengeti, alituhakikishia kwamba fedha zitakuja. Nini tamko lake kuhusu fedha hizi kutokufika mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilikuwa na Mheshimiwa Ryoba Jimboni kwake na tulitembelea ile Hospitali ya Wilaya, nami nilikuwa najua kwamba jana ndiyo angeunga mkono Bajeti ya Serikali kwa sababu ndiyo fedha zenyewe hizi zinazopelekwa kwa wananchi. Sasa tunapokuja site pale tunakubaliana fedha ziweze kwenda, tunapokuja huku katika kupitisha mafungu wenzetu mnasusa hamtaki kupitisha, sio jambo zuri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ryoba, tumekwenda pale tumeona matatizo ya wananchi. Sawa! Suala la fedha tutakwenda kulitekeleza na kama tulivyoongea kwa kirefu zaidi, pale ukiangalia kupitia Ofisi yetu na Wizara ya Afya katika lile jengo la pale Mugumu tunafanya ile two in one sword, tutafanya lile na wananchi watapata huduma. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Bunda la Mheshimiwa Getere, halina tofauti sana katika Jimbo langu la Serengeti katika Vijiji vya Rwamchanga, Masinki, Ring One na maeneo mengine, ambapo kuna jamii ya Wakisii, Wanandi, ambao wamekuwepo kabla ya uhuru. Je, ni lini Serikali itawafanya kuwa raia wa Tanzania? Maana tumeona maeneo mengine wakimbizi…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimjibu babu yangu Mbunge wa Serengeti kwamba, kwa wale wote ambao wameshakaa tangu enzi ya uhuru na wako Tanzania na wangependa kuwa raia wa Tanzania, pana taratibu. Wafike kwenye Ofisi za Uhamiaji watapewa taratibu za kuhalalisha uraia wao kwa sababu, uraia hatuwapi tu kwa kutamka, lazima wapite kwenye taratibu zile ili kuweza kuweka kumbukumbu sawa kwamba, wameshakuwa raia.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba yetu ya nchi hii ya 1977, Afisa wa Tume ya Uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. Wakurugenzi na Watendaji wanaosimamia chaguzi ni wanachama wa CCM kwa ushahidi. Wengi waligombea Ubunge, walioshindwa wameteuliwa kuwa Wakurugenzi na hakuna sehemu yoyote ambapo wamejiuzulu uanachama wao na ndiyo wanaosimamia chaguzi hizi na imepelekea wagombea wa vyama vya upinzani wanaongombea Ubunge na Udiwani wananyimwa ama fomu ama wakirudisha fomu Wakurugenzi wanajificha. Je, hii ndiyo Tume Huru ya Uchaguzi? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mimi mwenyewe nimeshiriki kwenye hizi chaguzi. Nimeenda sehemu moja inaitwa Nyabubinza kule Maswa Magaharibi. Mimi Mbunge, Mkuu wa Wilaya, Ma-green guard na Polisi wanadiriki kututeka tunaofanya kampeni kutoka upinzani. Hivi hii ndiyo Tume huru ya Uchaguzi? Huko mnakotaka twende ni wapi? Mnataka mpaka damu imwagike? Mnataka mpaka damu imwagike? Swali la pili… Sawa, naenda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Marwa Chacha Ryoba, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua kama kweli hii ni Tume Huru ya Uchaguzi kwa mifano aliyotoa. Nikirejea katika majibu yangu ya msingi unaipimaje Tume ya uchaguzi ni huru. Uhuru wa Tume ya Uchaguzi unapimwa kutokana na majukumu ya Kikatiba yaliyopo ambapo utekelezaji wake ndiyo unaashiria kwamba Tume hii ni huru au siyo huru.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Ibara ya 74(6) imeainisha majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo kimsingi hasa majukumu hayo yakiingiliwa ndiyo unasema Tume hii imekosa uhuru. Jukumu mojawapo ni kubwa ni la kuratibu na kuendesha uchaguzi ambao ndiyo umefanya hata Marwa Ryoba Chacha leo yuko Bungeni. Kwa hiyo, sitaki kuamini kwamba majukumu haya ya Tume yanaingiliwa kwa mujibu wa swali ambalo amelileta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema kwamba alikwenda kwenye kampeni Maswa wakatekwa na je hii ndio Tume Huru ya Uchaguzi? Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa tuelewane kimsingi kabisa, tukizungumza Tume ya Uchaguzi maana yake ni Tume ambayo inayotokana na Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Unazungumza kuhusu kutekwa jambo ambalo la kijinai na ulipaswa kuliripoti Polisi lichukuliwe hatua na siyo jukumu la msingi la Tume la kushughulika na kutekwa kwa watu. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali kuhusu ununuzi wa pamba, Mkoa mzima wa Mara, Wilaya za Serengeti, Bunda, Musoma Vijijini na maeneo mengine mpaka sasa hawajaanza kununua pamba. Tuliomba hapa kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwamba mtindo uliokuwa unatumika zamani wa kununua pamba uendelee kuliko huu wa kulazimisha mwananchi atembee kutoka Kilometa ngapi akafungue akaunti benki jambo hili limekuwa gumu kwa wananchi.
Kwa hiyo, naomba kuuliza ni lini pamba itaanza kununuliwa Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu wa pamba ulifunguliwa tarehe 1 Mei na ununuzi unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kutegemeana na upatikanaji wa pamba ulivyo. Pamba haikomai kwa mara moja nchi nzima, inakomaa tofauti kulingana na ukanda wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi ununuzi katika Mkoa wa Mara umeshaanza, nimezungumza leo asubuhi na Mkuu wa Mkoa. Tatizo lililoko Mara ni wale wanaohusika kununua wanawatapeli wananchi kwamba akilipa taslimu anapewa Sh.800 badala ya Sh.1,100 bei iliyotangazwa ya kununua pamba msimu huu. Sasa hivi maelekezo yapo, watafutwe wanaofanya huo udanganyifu ili wananchi wapate haki yao kwa mauzo halali wanayoyafanya.
MHE MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Serengeti, Kata za Ikoma hususani ndani ya hifadhi maeneo ya Robo, Kata za Sedeko, Nyansurura na Nyambureti, hakuna mawaliano ya simu. Mheshimiwa Naibu Waziri anasema nini kuhusu kupeleka minara katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe maelezo kwa ujumla tu kwamba tunayo changamoto kwenye maeneo ambayo yanapakana na Hifadhi ya Taifa na tuko kwenye mawasiliano mazuri sana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yako kwenye hifadhi tunaweka minara kwa mapatano maalum. Tunapata changamoto kwa sababu wanaohudumia ile minara hatuwezi kuwa na control nao ya moja kwa moja. Tunajipanga kuhakikisha kwamba tunakuwa na control nao ya moja kwa moja ili hata mnara unapowekwa kwenye hifadhi, basi usalama wa hifadhi zetu unaendelea kuzingatiwa lakini wakati huo huo wananchi wanapata huduma ya mawasiliano bila kukwamishwa. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Waziri, wananchi wa vijiji vya Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikili, Bonchugu, Miseke na Pakinyigoti wamenituma nimwombe Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli aende akawasikilize matatizo yao, lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni Mheshimiwa Waziri.
Je, uko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi kwenda kusikiliza matatizo yao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wananchi wa vijiji vilivyopo kando kando ya Hifadhi ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikorongo na Gurumeti pamoja na Ikoo na WMA kazi yao kubwa ilikuwa ni uwindaji, ufugaji na kilimo. Uwindaji sasa hivi hawawindi, maana wakienda kuwinda hawarudi; mifugo yao imetaifishwa; mazao yao ya kilimo tembo wanakula; ninyi kama Wizara, nini mbadala mnaowasaidia wananchi wa maeneo haya ili waweze kujikimu kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwanza naomba nimhakikishie tu kwamba niko tayari wakati wowote pale ambapo muda utaruhusu tutapanga, lazima twende tukatembelee katika yale maeneo. Hiyo inatokana na kwamba sasa hivi tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba maeneo yote yanayopakana na Hifadhi za Taifa, lazima vijiji vyote vile vipimwe vizuri, tuweke mipaka vizuri lakini pia tuimarishe ule ulinzi katika yale maeneo hasa kule ambako kumekuwa na changamoto nyingi ambapo wanyamapori wamekuwa wakiharibu mazao na shughuli za wananchi wanazofanya katika yale maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia tutaweka minara, pamoja na kutumia ndege zisizokuwa na Rubani. Kwa hiyo, mambo mengi tutayafanya kuhakikisha kwamba haya yanafanyika. Ili kufanya hayo, lazima tufike na tuone kwamba wananchi wanaondokana na hizi changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hatua mbadala; sasa hivi tunatoa elimu ni nini kinaweza kufanyika katika yale maeneo yaliyo jirani na hifadhi? Kwa sababu ukipanda yale mazao ambayo wanyamapori wanayapenda, ni wazi kabisa kwamba yataliwa na wanyamapori. Ukipanda yale mazao ambayo wanyamapori hawayapendi, wanayaogopa, basi kidogo hii itasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakwenda kukaa pamoja na Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwa pamoja, tutashauriana kuona ni aina gani ya mazao ambayo wananchi wa maeneo yale watashauriwa kwamba wayapande ili kuondokana na hii migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza katika hayo maeneo. (Makofi)
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Katika hifadhi Serengeti National Park pamoja na Ngorongoro, hali ya barabara siyo mzuri na hususan kwenye kipande cha barabara kuanzia Ngorongoro getini mpaka lango la Serengeti National Park kuna udongo wa Volcano ambao hata watengeneze vipi, kwa muda mfupi unakuta ule udongo unaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haina mpango wowote wa kutengeneza ile barabara hata kwa kiwango cha zege ili kuondoa shida kubwa ambayo tunaipata watu tunaopita kwenye hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampa hongera sana, amekuwa ni mdau mkubwa sana kwa sababu maeneo mengi, maliasili na hifadhi nyingi ziko katika eneo lake. Nafikiri nitakapokwenda kule, nitajua maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi Serikali inapitia maombi mbalimbali, inapitia utaratibu wa kuweka barabara ya kudumu ambayo inaanzia Karatu kupitia Ngorongoro mpaka Serengeti. Mara baada ya taratibu hizo kukamilika na clearance zote kufanyika, kwa sababu ni maeneo ya hifadhi, kumekuwa na mabishano makubwa juu ya aina ya barabara ambayo inatakiwa ijengwe.
Sasa hivi tumefikia hatua nzuri, makubaliano yanakuja na ninaamini kabisa kwamba baada ya muda mfupi tutaanza kuweka barabara ya kudumu ambayo ndiyo suluhu ya hilo tatizo ambao Mheshimiwa Mbunge amelisema.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Vijiji vyenye mgogoro wa mipaka na Hifadhi ya Serengeti ni vijiji vinane, Kijiji cha Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisalala na Bonchugu. Ukiona wananchi wa vijijini wameungana, wameenda mahakamani, wameishinda Serikali, halafu Serikali imekata rufaa ni kama kuwaonea na wananchi hawana shida na mambo ya rufaa.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Serengeti imeanzishwa kwa GN namba 235 ya mwaka 1968 na ikatengenezewa ramani iliyosajiliwa kwa registration namba 14154. Ramani hii imefichwa, imeanza kutengenezwa ramani nyingine na ndio kisa cha wananchi kushinda mahakamani. Sasa tunataka kujua kwa nini Serikali haitaki kwenda kukaa na wananchi wa vijiji hivi ili kukubaliana mpaka, sio kupoteza muda kukaa huko mahakamani na wananchi wanaumia. Kwa hiyo ni lini Wizara na Wizara ya Ardhi wataenda kukaa na wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ni kweli imekiri kwenye barua kwamba ilifanya makosa kwenye kutekeleza mipaka kwenye GN iliyoanzisha Pori la Ikorongo, wamekiri na wanahitaji utaratibu tu wa kwenda kurekebisha ile mipaka. Kwa nini Wizara pamoja na Wizara ya Ardhi wasiende kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya kurekebisha ile mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haiwezi kuwa na lengo la kuonea wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema, lakini taasisi hizi zilipokuwa zinapitia mipaka na baada ya migogoro hii kuwepo na baada ya wananchi kushinda kwenye kesi yao ambayo walikuwa wamefungua, Taasisi kwa sababu ilikuwa inafahamu mipaka yake ya awali iliamini kwamba ikikata rufaa inaweza ikabadilisha matokeo. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi sisi Serikali baada ya kesi hii kwenye Mahakama ya Rufaa kuamuliwa tutatumia hukumu hiyo kuweka mipaka ambayo itamaliza mgogoro huu na kama mipaka hiyo itakuwa ni hii ya sasa ambayo vijiji vinatambua, hatuna pingamizi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi tutakwenda kupitia upya hii mipaka ya Ikorongo na kuweka alama kwa kutumia Wizara ya Ardhi pamoja na ushirikiano na Wizara yetu ili kumaliza mgogoro huu kwenye suala lake la pili.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kampuni ya Alliance One iliyokuwa inanunua tumbaku Serengeti iliondoka wakati ambapo wakulima wako kwenye peak ya kilimo cha tumbaku. Baada ya kuondoka wakulima wakashindwa wapi wauzie tumbaku yao. Kwa kuwa Serikali ina jitihada ya kuwatafutia wananchi wa Serengeti kampuni nyingine ya kununua tumbaku, kwa nini wakulima wanaolima sasa hivi tumbaku wasiruhusiwe kuuza kokote watakako tumbaku yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ryoba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumtoa wasiwasi Mheshimiwa Ryoba pamoja na wakulima wa pamba, Serikali inayo mikakati mizuri ya kuhakikisha tunawasaidia katika kupata masoko ya uhakika na nitumie nafasi hiui kumpongeza Balozi wetu Mheshimiwa Mbelwa Kairuki, Balozi wa China tunawasiliana nae na kuna ujumbe unaondoka mwezi huu mwishoni kwenda China kwa ajili ya kutafuta masoko ya tumbaku. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Ryoba awe na subira, karibuni tutaweza kuwapa uhakika wakulima hawa wa pamba katika Jimbo lake.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka tu kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwenye Jimbo langu la Serengeti Kata ya Busawe, Kijiji cha Busawe, wananchi wamejenga kituo cha afya wameweka mpaka na vifaa vinavyostahili kwa ajili ya kituo cha afya, lakini ni muda mrefu sasa tangu waombe usajili wa kituo chao cha afya. Maombi yamekaa Wizarani muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inawaambia nini wananchi wa Kata ya Busawe na Kijiji cha Busawe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza sana Mheshimiwa Ryoba, Mbunge wa Serengeti na wananchi kwa kujenga kituo chao cha afya. Sisi kama Serikali tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunaungana na nguvu za wananchi pale ambapo wao wenyewe wametoa nguvu zao na wamejenga kituo chao cha afya. Ni wajibu wetu kama wataalam kwenda kukagua na kuhakikisha kwamba kinakidhi vile vigezo na kuweza kutoa huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu suala hili ndiyo nalisikia hapa kwa mara ya kwanza; na Mheshimiwa Ryoba ni rafiki yangu, siku zote tunakaa tunaongea, namwomba baada ya kipindi cha maswali na majibu awasiliane nami tujue tatizo ni nini na nimhakikishie ndani ya muda mfupi kituo chake kitapata usajili.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kwanza nichukue nafasi, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, na Naibu wake Waziri wanafanya kazi nzuri sana, na ni kazi ambayo itaisaidia sana CCM 2020 tunakoenda kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza Mheshimiwa Waziri wa Nishati alipokuja Serengeti mwaka huu mwanzoni alihaidi maeneo ya yafuatayo yatapa umeme; shule ya Sekondari Inagusi ilipo Kata ya Isenye, Kijiji cha Nyamatoke na Mosongo vilivyopo Kata ya Mosongo pamoja na Kiyakabari Kata ya Stendi Kuu.

Ni lini maeneo haya yatapata umeme ambao ulihaidiwa na Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini TANESCO au REA watapeleka umeme Kata ya Morotonga katika Vitongoji vya Mutukura na Romakendo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza tupokee pongezi zake, lakini naamini pongezi ni kuhitaji zaidi huduma. Kwa hiyo, tumepokea kwa ahadi kwamba tutaendelea kufuatilia hiyo miradi. La pili pia nimpongeze yeye Mheshimiwa kwa namna ambavyo anavyofuatilia masuala ya nishati katika Jimbo lake na sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini masuala yake mawili yamejielekeza kwanza kwenye ziara ambayo imefanywa na Mheshimwia Waziri wa Nishati katika Jimbo la Serengeti na ahadi aliyoitoa katika shule ya Sekondari Nagusi na maeneo ya Kiyabakari. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nishati alipotoa ahadi hii alikuwa na uhakika wa utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya III mzunguko wa kwanza unaoendelea na kwamba mkandarasi Derm wa Mkoa wa Mara ni miongoni mwa wakandarasi wanaofanya vizuri tulivyo wa-rank na kwamba inatarajiwa itakamilisha kazi kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maeneo aliyoyataja mara tu Julai 2019 mradi wa REA Awamu ya III unaanza na kazi ndiyo itafanyika. Kwa hiyo nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwa kipindi hiki cha kuendelea 2019 maeneo haya yote ataiona kazi inaanza na nguzo zitapelekwa na ninaomba nimuelekeze mkandarasi Derm azingatie maelekezo ya Mheshimiwa Waziri pamoja na Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Mara na msimamizi wa mradi wa REA katika Mkoa wa huo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge ameulizia masuala la kwa mfano Marotonga na eneo ambalo umelitaja Mgumu Mjini, yanaonyesha haya maeneo ni ya ujazilizi. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Agnes Serikali baada ya kuona pana changamoto baada ya miradi ya REA kukamilika na kwa kuwa lengo lake Serikali ni kusambaza umeme palikuwa na changamoto ya gap ya usambazaji wa umeme. Na ndiyo maana ikabuni mradi wa ujazilizi na bahati nzuri Mkoa wa Mara ulikuwemo katika ujazilizi Awamu ya kwanza ambao ulikuwa kama mradi wa majaribio.

Mheshimiwa Spika, na Serikali imekuja na mradi wa ujazilizi Awamu ya pili, Awamu ya II(a) ambayo itakuwa na Mikoa tisa na Awamu ya II(b) itakuwa na Mikoa 16, ikiwemo Mkoa wa Mara na kwa kweli tunauhakika Awamu ya II(a) utafadhiliwa na Serikali za Norway, Sweden na Umoja wa Ulaya na hela zake tunazo bilioni 197 na Awamu ya II ya ujazilizi two (b) itafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa mpaka sasa tunauhakika wa kiasi cha bilioni 270 kati ya bilioni 400 ambazo zitaanzia kazi na mchakato tupo hatua ya manunuzi na mradi huu utaanza 2019/20 kwa ajili ya kufikisha umeme katika maeneo ya Vitongoji ili kuweza kusambaza umeme, nikushukuru sana.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa niaba ya Wananchi wa Serengeti naomba kuuliza ni lini barabara ya Makutano Sanzate, Mugumu, Tabora B, Kilensi, Loliondo Mto wa Mbu itakamilika na nilini watapata fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tu Mbunge kwa sababu anafuatilia hii barabara na anafahamu hatua nzuri ambayo barabara hii muhimu imefikiwa kwa sababu tunao mradi wa kutoka makutano sanzate ambapo tupo karibu asilimia 85 ya Ujenzi wa barabara hiyo na muda mrefu tunaendelea kuijenga lakini tunatoka Sanzate tunakwenda Nata tunafahamu kwamba tupo kwenye hatua ya kumpata mkandarasi ili ujenzi uendelee lakini kutoka Sanzate kwenda Mugumu na sehemu ya barabara pia upande ule wa kutoka Loliondo kwenda Salensi Junction kuna mradi unaendelea. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu harakati za kuijenga barabara hii kutoka makutano kwenda hadi Mto wa Mbu ahsante.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi, nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri, mwaka jana tulikwenda Jimboni Serengeti na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Kamati ya Miundombinu, moja eneo tulilowapeleka sisi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ni kutembelea uwanja wa Mugumu ambao ilikuwa ujengwe na mwekezaji mmoja anaitwa Grumet, lakini Grumet akawa ameacha; sisi kama halmashauri tunakibari cha NEMC, tunakibari cha Mamlaka ya Viwanja vya ndege tuna Hati Miliki ya kiwanja, TANAPA kwa kushirikiana na halmashauri wameamua kujenga uwanja ule.

Je, Wizara iko tayari kuchangia chochote kwenye mwaka ujao wa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Serengeti ambao utakuwa unapokea ndege karibia 200 kwa siku? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu ya Kiserikali tunaomba wasilisho hilo mwambie Mkurugenzi wa halmashauri aliandike na kulipeleka kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI halafu Katibu Mkuu wa TAMISEMI atawasiliana na Katibu Mkuu wa Uchukuzi huo ndiyo utaratibu wa Serikali kwa sababu hiyo ni taarifa unaisema hapa Wizara yangu haijui ukifanya namna hiyo Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ukifuatilia trend ya utoaji wa hizi fedha za vikundi asilimia 10, mara nyingi Wakurugenzi wamekuwa wakijificha kwenye revolving fund, wakitoa ile revolving fund ambayo imerudishwa na vikundi, utadhani ya kwamba imetolewa aislimia 10. Wizara mko tayari kuweka mchakato ambao utaweka wazi revolving fund na 10% ya mapato ya kila mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba nikubali kwamba kwa maelekezo yako tutafanya hivyo ulivyosema kwa maana ya kupeleka nakala kwa kila Mbunge kueleza ufafanuzi tunamaanisha nini katika hii 10% ambayo inapaswa kuwa imetengwa.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nijibu sasa swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba, ni kweli, wakati wa mjadala wa bajeti Waheshimiwa wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI waliliona hili, na kweli imeonekana kuna halmashauri zingine wakichukua fedha wamekopesha, wakizirudisha, wengine walituambia ilionekana wanatoa taarifa ya kwamba walishapata mpaka asilimia 180, 120, wakaulizwa, hii nyingine ya ziada mmeitoa wapi. Ikaonekana kwamba, kikundi kikitoa fedha, wakikirudisha wanajumuisha wanasema imekusanywa, kwa hiyo, tukaelekeza kwamba na sasa hivi tumefungua akauti, kwenye kanuni mpya iliyotengenezwa, kutakuwa na akaunti mahususi ambayo fedha hii inaingia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, umapokusanya fedha zitaonekana, zinaporejeshwa zitaonekana kwa hiyo, hakutakuwa na kuchanganya kati ya fedha ambayo imekopesha na fedha ambayo imekusanywa, lakini Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema, na hili nalo tutaona na nakala na kanuni watazipata ili kuweza kusimamia vizuri utengaji wa hizi fedha lakini usimamizi wake na utekelezaji wake.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Bwawa la Mesaga liko Kata ya Kenyamonta na ni kata ambayo inaongoza kwa kuwa na watu wengi katika Wilaya ya Serengeti. Bwawa hili lilianza kutengewa fedha ama kutolewa fedha 2014/2015. Tumeona zimeenda shilingi milioni 200 na zikaenda tena shilingi milioni 198, ni fedha nyingi. Hata hivyo, ukiangalia majibu ya Serikali wanasema sijui kuna fidia na ni kama walipeleka waka-dump zile hela wamezitelekeza mpaka leo. Mimi nilitaka kujua, Serikali mlipeleka fedha kwenye eneo lenye mgogoro ambalo halina andiko mradi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nashukuru kwamba Wizara imetenga fedha shilingi milioni 217 kwa ajili ya Bwawa la umwagiliaji la Nyamitita, niombe fedha hizi zitoke. Niseme kwamba pamoja na fedha hizi kutengwa, kumekuwa na tendency ya fedha kutokutoka. Naomba fedha hizi zitoke pamoja na za Bwawa la Mesaga, wananchi wanataka kujua ni lini fedha za Bwawa la Mesaga zitatoka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chacha Ryoba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kama eneo hilo lina mgogoro kwa nini Serikali ilipeleka fedha? Eneo lile wakati lilifanyika andiko na hitaji la kujengwa mradi ule hakukuwa na mgogoro na hii ni baada ya kupata taarifa ya kimaandishi kutoka kwa wakulima na viongozi wa Wilaya kwamba wakulima wamekubali eneo lile liendelezwe kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, shida kubwa iliyoko pale na Mheshimiwa Mbunge anajua kwa sababu nimeshafika pale ni kwamba wale wakulima ambapo lile bwawa linajengwa, wale wa sehemu ya juu baada ya hela kupelekwa wanataka wafidiwe na wakulima wenzao waliokuwa upande wa chini. Mgogoro ulioko pale ni wale wakulima wa chini hawataki kuwamegea ardhi wale wakulima wenzao waliopisha bwawa lile kujengwa. Baada ya hali hiyo kutokea na hela tulishapeleka ndiyo maana kama Serikali tumewaelekeza kwanza wakulima wenyewe wakae na uongozi wa wilaya watatue mgogoro huo. Baada ya utatuzi huo kukamilika na tukipata taarifa kwamba hakuna mgogoro basi hatua zingine za kupeleka fedha zitaweza kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua lini sasa Serikali tutapeleka fedha kwenye Bwawa hilo la Mesaga. Kama nilivyojibu kwenye maelezo yangu ya awali, kutokana na mwongozo tuliokuwa nao sasa hivi wa kuendeleza miradi yote ya umwagiliaji, lazima tupate commitment letter kutoka kwa wanufaika wenyewe kwamba eneo linalojengwa mradi halina matatizo na wamekubaliana ili tusijepeleka fedha halafu kumbe kuna mgogoro. Kama tunavyofahamu tulipitisha wenyewe sheria hapa, ardhi yoyote haiwezi kutwaliwa bila kwanza kulipwa fidia. Kwa hiyo, wale wanaopisha eneo la ujenzi ule wa bwawa lazima kwanza wafidiwe na wenzao kule eneo la chini na baada ya mgogoro huo tutapeleka fedha.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kiukweli majibu haya hayaridhishi hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulienda Serengeti na Naibu Waziri pamoja na Kamati ya Miundombinu, Naibu Waziri gari lake lilipata pancha mara nne, matairi manne. Tukampa spare zikaisha mpaka raia wananchi wakampa spare, hali ni mbaya kwa wananchi wa Serengeti. Ukiangalia barabara imeanza kujengwa tangu 2013, miaka sita (6) imepita kilomita 50 hazijakwisha; Je, itachukua miaka mingapi kumaliza kilomita 80 kutoka Sanzate mpaka Mugumu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mugumu kwenye hiyo kandokando ya barabara walishafanyiwa tathmini na kila mtu anajua analipwa shilingi ngapi, ni lini watalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba Chacha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, pamoja na masikitiko yake lakini niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Ryoba kwa namna anavyofuatilia hasa miradi hii ya barabara. Ni kweli niseme tu kwamba barabara hii kwa historia ni barabara muhimu, hizi kilomita 452 mimi nimeipita hii barabara ina changamoto zake. Kwa historia Marehemu Baba wa Taifa alikuwa akipita barabara hii akitokea Arusha miaka ile, kwa hiyo ni muhimu na sisi kama Serikali tunaiangalia kwa macho mawili. Niseme tu pamoja na kuwa ujenzi huu umekwenda kwa hatua hiyo ya kusuasua lakini kama nilivyosema na kwa kweli kwa ushirikiano wa Wabunge wa Mkoa wa Mara nimejibu wiki juzi swali la Mheshimiwa Agness Marwa na wiki iliyopita nimejibu swali la Mheshimiwa Getere kuonesha umuhimu wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Ryoba avute subira, lakini niseme tu kwamba kama commitment nilivyosema hapa na namna tunavyosimamia vizuri sasa pamoja na kuchelewa lakini barabara hii itakamilika na kama nilivyokuwa nikizungumza hapa, kwa hiyo tunaisimamia vizuri itakamilika vuta subira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kilomita 452 tuko asilimia 41 ya commitment ya barabara, kwa Mradi huo wa Makutano Juu – Sanzate kilomita 50. Kama nilivyosema kutoka Sanzate – Natta kilomita 40 tuko hatua ya manunuzi, lakini pia kwenye bajeti Natta – Mugumu kilomita 45 tumeitengea bajeti na ujenzi wa eneo la Wasso – Sale kilomita 49. Utaona asilimia 41 tunaendelea kuisogelea kuweza kuikamilisha barabara hii, kwa hiyo avute tu subira Mheshimiwa Ryoba tutaisimamia vizuri barabara hii ili iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali lake kuhusu tathmini ya wale wananchi; kama nilivyosema, kiutaratibu tunatakiwa tulipe kabla ya ujenzi kuanza. Kwa hiyo tutazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizokuwepo, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, wananchi watalipwa haki yao kulingana na sheria, kwa hiyo avute tu subira kabla ya kuanza ujenzi wananchi hao watalipwa mara moja.