Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi (38 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunijalia tena kwa mara nyingine kuwepo katika Bunge hili. Pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Musoma kwa kuweza kunipa ridhaa hii kwa mara nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2016/2017. Kazi yetu ni kuishauri Serikali. Wakati najaribu kupitia Mpango huu kwenye ule ukurasa wa 24, umesema wazi kwamba malengo mahususi ni kuimarisha kasi ya ukuaji na kuongeza uchumi. Hii ni pamoja na uchumi huo uweze kuwanufaisha wananchi waliyo wengi, pamoja na kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango. Kusema kweli amepanga mipango yake vizuri. Ukisoma kwenye huu ukurasa wa 24 mpaka 26 na kuendelea mbele, mipango iliyopangwa ni mizuri sana. Wenzetu wamekuwa wakitubeza kwamba sisi ni wazuri kwa kupanga mipango, lakini tuna tatizo la utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia Mpango na kusoma ukurasa wa 37, kwamba mojawapo ya mikakati ya kutekeleza mipango hii ni pamoja na kuwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa maana ya Public, Private Partnership. Mashaka yangu yawezekana pamoja na mipango yetu mizuri, lakini bado tukakwama kwa sababu ya ukwasi wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka tu kushauri au kuchangia katika maeneo manne, nilitaka kuchangia katika eneo la viwanda, kilimo, uvuvi pamoja na mifugo kama muda utaniruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuendeleza viwanda, maana Mpango huu mlisema umebainisha namna ambavyo hivi viwanda vinavyotakiwa kwa maana ya vile viwanda vitakavyosaidia kuajiri watu wengi zaidi. Kwa upande wa viwanda, kama tunahitaji kuona Matokeo Makubwa ya Sasa, nashauri tujielekeze kwenye vitu vitatu; kwanza, tuendelee kupanua hivi Vyuo vyetu vya VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Musoma kipo Chuo cha VETA kimoja ambacho kinachukua wanafunzi kila mwaka wasiozidi 200, sasa ukiangalia wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba pamoja na Kidato cha Nne wale ambao hawapati nafasi ya kuendelea Kidato cha Tano, maana yake tuna wanafunzi wasiopungua 6,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Chuo cha VETA kinachukua wanafunzi wasiozidi 200 tafsiri yake ni kwamba watoto zaidi ya 5,000 wanakaa Mtaani na hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo, nadhani tukiongeze wigo wa Vyuo vya VETA pamoja na Vyuo vya Ufundi kuchukua wanafunzi wengi, matokeo yake tutapata wanafunzi wengi wenye elimu ya kawaida ya ujasiliamali, elimu ya kawaida ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka hapo kama tumepanga kujikita kwenye viwanda, ningeshauri tufufue lile shirika letu la viwanda vidogo (SIDO)..
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba leo tukipata Mkurugenzi Mtendaji mzuri wa SIDO, mfano kama alivyo yule Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba, akaangalia namna gani mafunzo mengi yanaweza kutolewa kwa vijana wengi zaidi; yale mafunzo yatawasaidia kuwajenga vijana wetu, wapate elimu ya ujasiriamali, tena kwa gharama nafuu. Maana kama wote mmetembea; Waheshimiwa Wabunge nadhani ninyi ni mashahidi, mafunzo mengi ya watu wanayojifunza Kule SIDO, kitu kikubwa kwanza wanajifunza usindikaji. Kama ni usindikaji wa alizeti, watajifunza; kama ni wa unga watajifunza, lakini ni pamoja na ufundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani watakapoenda pale watajifunza usindikaji pamoja na mambo ya packaging. Kwa kufanya hivyo sasa itawapa nafasi ya kuwa na bidhaa ambazo sisi wenyewe tutazitumia na hata nchi zote zinazotuzunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda nchi kama Kenya kuna hawa wanaoitwa Juakali. Juakali Kenya ina nafasi kubwa sana na inawasaidia watu wengi sana. Kwa hiyo, ukiangalia hili Shirika letu la SIDO kama tukilifufua na likapata mwendeshaji mzuri, ni dhahiri kwamba tutakuwa na vijana wengi ambao watakuwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri. Kwa utaratibu huo sasa, hata hizi taasisi zetu za fedha ni rahisi kuwapa fedha kwa kuwakopesha kwa sababu tayari wanao ujuzi utakaowasaidia katika kusukuma maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine basi, hebu tuendelee kuimarisha hizo Ofisi zetu za Ubalozi. Maana Ofisi zetu za Ubalozi ni kwamba tukiwa na wale ma-business attache wataweza kujua kwamba bidhaa gani zinazotakiwa huko ili waweze kutusaidia watu wetu hawa waweze kuuza huko.
Eneo lingine ni eneo la kilimo, mfano pale Mara, tunalo eneo kama lile shamba la Bugwema ambalo ni heka 20,000, mashamba kama haya yako mengi katika nchi hii. Leo ukitangaza tenda ya nani yuko tayari kufanya irrigation katika eneo hilo, labda katika kipindi cha miaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali inawalipa fedha za kufanya irrigation, matokeo yake ni kwamba lile bonde lenyewe linaweza kuzalisha mazao mengi kama mpunga, alizeti ambayo itasaidia sana watu wetu, siyo wa Musoma peke yake wala si wa Mara, lakini maeneo kama haya yako mengi ambapo Serikali nadhani kwamba ikijikita katika utaratibu huo itaweze kusaidia watu wetu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapozungumza kwenye suala la mifugo, nini kifanyike? Tunahitaji tutenge maeneo madogo, maana Mpango huu umesema tunahitaji tufungue Vituo vya Uhamilishaji.
Ni kweli kwamba tatizo kubwa tulilonalo, ng‟ombe wetu; sisi ni wa tatu katika Afrika, lakini ng‟ombe wetu thamani yao ni ndogo. Tunachohitaji, ni lazima tufanye crossbreed ili tuzalishe mifugo ambayo itakuwa na tija.
Kama hivyo ndiyo basi, sasa ni lazima tuwe na vituo kama vile ambavyo vitazalisha ng‟ombe wanaokuwa haraka ndani ya kipindi cha miaka miwili unaweza kuuza ng‟ombe kwa Shilingi milioni moja, mpaka Shilingi milioni mbili kuliko hawa wetu unawachunga miaka mitano mpaka minane lakini unauza kwa Sh. 500,000/= ambazo hazina tija. Kwa hiyo, tunadhani hilo nalo katika mipango yetu linaweza likatusaidia katika kuhakikisha kwamba tunaendelea. nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuweza kunipa nafasi na mimi niweze kuwa mchangiaji siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia kuwepo katika hii siku njema ya leo, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi yake nzuri anayoifanya. Ni ukweli usiopingika, wote tunayafahamu na hata yale ambayo yalikuwa ni mambo magumu ambayo tulikuwa tunadhani kwamba hayawezekani ameweza kuyatekeleza katika kipindi kifupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mfano suala la kuhamia Dodoma ilikuwa ni hadithi ya toka miaka ya 70 lakini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na huu wa pili tayari wote tumekubali na Serikali nzima imehamia Dodoma.

Vilevile kuna suala la nidhamu ya uwajibikaji, nadhani hilo ni suala ambalo halipingiki kila mmoja anakubali kwamba sasa ile nidhamu imekuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni sisi hawa hawa tulikuwa tunapenda kusema kwamba katika nchi hii wapo wale vigogo hawashughulikiwi wanapokosa lakini leo imedhihirika kwamba nchi hii ni ya kila Mtanzania, uwe mkubwa ama mdogo ukikosea sheria inafuata mkondo wake. Kwa hiyo, hiyo yote ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na jukumu letu sisi ni kuendelea kumwombea uzima katika hii kazi nzuri anayoendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa maana ya uwasilishaji wake wa Mpango huu ambao ni wa 2018/2019. Nadhani ukiangalia katika ukurasa wa tano ameweza kusema vizuri kwamba yeye kama Waziri ameweza kutuletea sisi kama Wabunge tuweze kushauri lakini vilevile tuweze kutoa maoni kwa namna bora zaidi ya utekelezaji wa Mpango huu. Kwa hiyo, kumbe sasa ameanza na yale aliyoyaona kwamba yanastahili halafu ametupatia na sisi tuweze kuchangia kwa maana ya kujaziliza. Nikiangalia kuna ile Kamati ya Bajeti imeweza kusema mambo mazuri sana na katika hayo basi kazi yetu ni kuendelea kujaziliza pale penye ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza, pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya lakini tuna tatizo moja kubwa kwamba Watanzania hali ya uchumi wetu imeendelea kudorora. Huo ni ukweli usiopingika karibu kila mmoja wetu ukimgusa iwe mkulima wa kawaida hali ya uchumi imekuwa mbaya, lakini hata wafanyabishara, biashara nyingi zimesimama na zimefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nini kinachangia haya yote, pamoja na vile viashiria vizuri vinavyoonesha kwamba uchumi wa nchi unakua lakini unapokuja kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja bado hali inaelekea kuwa mbaya. Hii moja, leo Serikali imezuia uuzaji wa mazao ya
chakula hasa mahindi na mchele. Kwa wale wenzetu ambao bahati nzuri wamebahatika kulima na wakavuna, Serikali imeweka mpango mzuri wa kuzuia kile chakula kisiende nje ili kije kitusaidie Watanzania, kumbe Serikali ilikuwa na kila aina ya sababu ya kununua kile chakula iweke kwenye maghala ya Taifa halafu iendelee kusambaza katika yale maeneo ambayo yana upungufu wa chakula.

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika tumemzuia asiuze lakini vilevile hatuko tayari kununua, kwa kweli hali hii tafsiri yake ni kwamba imeendelea kumpa yule mwananchi wa kawaida hali ngumu ya maisha. Kwa hiyo, hilo ni kati ya suala ambalo Serikali inahitaji iliangalie na ione ni kwa kiasi gani inaweza ikawasaidia hawa wananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeambiwa na wote tumeendelea kufahamu kwamba mazao kama mbaazi hayana soko, lakini wale wakulima walishalima na wanayo kwenye maghala. Zao kama tumbaku halina soko, wakulima walishalima na tayari yapo kwenye maghala. Tafsiri yake ni kwamba lazima hali ya uchumi, ya kipato iendelee kuwa duni na maisha yao yaendelee kuwa magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika huu Mpango wa leo ambao umeletwa mbele yetu nami nina ushauri ufuatao. Ukiangalia katika nchi yetu zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima lakini pamoja na hayo huu Mpango haujasema unafanya nini katika kipindi kifupi na kirefu kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushauri wangu leo wa nini kifanyike ni lazima tuwe na mpango na muda mfupi, wa kati na muda mrefu. Katika mpango wa muda mfupi leo ungeniuliza na kama Dkt. Mpango atakubaliana na ushauri huu ili ikiwezekana ndani ya mwaka kesho na mwaka keshokutwa tuanze kuona matokeo tena matokeo makubwa, hebu tutambue mabonde mazuri yanayostahili kilimo katika kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika, mfano sisi pale Mara tunalo shamba lisilopungua ekari 20,000 linaitwa shamba la Bugwemu. Maeneo kama hayo yote tukiyatambua, kazi ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kwenye hayo maeneo yote inapeleka maji, bahati nzuri tunayo REA. Kwa hiyo, tukiweka mkakati wa muda mfupi kwamba yale mabonde yote yatambulike na maji yaweze kwenda pale itasaidia sana na hiyo ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, ukiangalia vijana wengi leo wanaomba kwenda kujiunga kwenda JKT wakitegemea wakitoka hapo kwanza watapata mafunzo lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuja kupata kazi. Sasa hebu tusiwafundishe zaidi kushika bunduki kule JKT, tuwafundishe zaidi kulima na kazi za mikono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokijua ndani ya kipindi kifupi, wale JKT tukiwawezesha vijana wengi wakaweza kwenda kule wakajifunza kilimo na kile kitakachopatikana na hicho kilimo kikaja kuwa mtaji wao kwa maisha ya baadaye watakapotoka pale waende kuanza maisha. Mimi naamini tatizo kubwa la chakula litakuwa limekwisha lakini hata hili ambalo linatuzuia kupeleka chakula katika nchi jirani kumbe tutakuwa tumezalisha chakula sasa ambacho kina soko kila mahali.

Mheshimiwa Spika, leo ukizungumza suala la mchele, katika nchi zote zinazotuzunguka mchele wa Tanzania una soko kubwa sana, lakini mchele wenyewe ndiyo huo wakitaka kupeleka hawaruhusiwi kwa sababu hautoshelezi. Kwa hiyo, tunadhani kwamba katika mpango wa muda mfupi, hiyo ni namna pekee inayoweza kutuwezesha au kuwawezesha watu wetu wakaweza kupata kipato ambacho kinaweza kikawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu tuone namna ya kuendelea kuisaidia SIDO, kuendelea kuiongezea uwezo ili itoe mafunzo kwa watu wengi zaidi. Mnajua kwa bahati mbaya sana yawezekana hili wengi hatulifahamu, bidhaa nyingi kinachotakiwa ni ile packaging. Labda nitoe mfano
mdogo, ukienda pale sokoni utakuta kuna ile asali ya Pinda, kwa jinsi ilivyokuwa packed ile robo kilo bei yake ni zaidi ya kilo nzima ya asali inayotoka Tabora. Kumbe kilichofanyika pale ni packaging na utaalam huo SIDO wanao, kwa hiyo wanaweza kuwafundisha watu wengi zaidi na wakawafanya watu wengi zaidi wakapata ujuzi na wakawa wanafanya packaging ya bidhaa mbalimbali tulizonazo na wakawa wanajipatia kipato kizuri na hata katika masoko ya export. Kwa hiyo, tunadhani kwamba SIDO yetu tukiendelea kuisaidia basi nayo itatusaidia zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda wa kati, kati ya eneo ambalo nadhani tunahitaji kulifanyia kazi ni pamoja na elimu yetu. Leo tumesikia hapa juhudi kubwa tuliyonayo ni kuhakikisha kwamba mikopo inapatikana, vijana wetu wanamaliza vyuo vikuu lakini tumesahau kwamba tuna tatizo kubwa leo la kuwapatia hao vijana ajira. Maana masomo mengi wanayoyasoma baada ya pale uwezo wa kuwaajiri hatuna. Kwa bahati mbaya vijana wengi wa Kitanzania huko nje wanashindwa kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda duniani kote, kila ukikutana na watu weusi watatu wanafanya kazi mahali popote pale duniani, wawili lazima utamkuta ni Mkenya, sanasana utamkuta ni Mganda lakini kwa Watanzania ni wachache sana. Hiyo tafsiri yake ni nini? Ni kwamba inaonekana kumbe ile elimu tunayoitoa haiwapi nafasi kubwa ya ushindani wa ajira katika masoko ya nje. Kwa hiyo, leo watoto tunawasomesha, wanamaliza chuo halafu wanarudi hapa sasa hakuna ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike? Hebu tuangalie namna ya kuboresha vyuo hivi vya kati. Wale wanaomaliza kidato cha nne, wanaomaliza kidato cha sita, tuongeze hivi vyuo vya VETA na vyuo vya ufundi ili wanafunzi wengi zaidi wapate ujuzi. Tunadhani kwa kufanya hivyo itawafanya sasa hao vijana wajiajiri wao wenyewe. Kwa utaratibu tulionao wanafunzi wengi wanasoma sociology na political science, maana yake ni kwamba wakimaliza tunaendelea kukaa nao mitaani. Kwa bahati mbaya sana unakuta kuna baadhi ya wanafunzi wamemaliza chuo kikuu lakini anazidiwa na aliyemaliza kidato cha nne akaenda VETA kwa sababu yeye tayari anao ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunang’ang’ana na tunajitahidi kusomesha lakini naamini kwamba baada ya muda tutafika mahali tunatengeneza bomu kubwa na tunayo mifano ya nchi. Ukienda kwenye nchi kama Nigeria, ni kati ya nchi ambazo zina wasomi wengi lakini walioajiriwa huko duniani ni wachache. Sasa inaonekana huo ndiyo mfumo wa elimu tulionao. Kwa hiyo, nina imani kwamba kama hatukuuangalia vizuri basi itatusumbua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo tunahitaji kulifanya, ukiangalia kwetu sisi Tanzania ni kati ya nchi ambayo ina madini kushinda nchi nyingi, inashinda Kenya, Uganda, Rwanda, karibu nchi zote zinazotuzunguka. Cha ajabu unakuta katika nchi kama Kenya wana-export zaidi madini kutushinda sisi na hizo nchi nyingine zote hizo za Rwanda, lakini haya tunaendelea kuyasema mwisho wa yote yanabaki kama yalivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hatuna udhibiti kamili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono Mpango.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Kwa sababu ya muda, naomba tu niende moja kwa moja kwa kusema kwamba kwa upande wa mifugo kusema kweli Wizara wala Serikali haijafanya chochote kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia katika kitabu chetu kwamba fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji, yaani ni kituko kabisa. Kwa hiyo, tunadhani Serikali ina changamoto kubwa, ione ni kwa kiasi gani, inahitaji ijipange kuhakikisha kwamba inawasaidia wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la mbegu bora. Mifugo mingi ya Tanzania pamoja na kwamba Tanzania ni nchi ya tatu, tuna ile mifugo ambayo ni aina ya zebu. Kwa hiyo, tunaifuga kwa muda mrefu lakini tija yake ni ndogo. Kwa hiyo, ushauri wangu, hebu Serikali iangalie kupitia hizi ranch zake iweze kuzalisha ng’ombe bora wa mbegu na iweze kusambaza kwa gharama nafuu. Tunadhani kwa namna hiyo, itaweza kuwasaidia Watanzania wengi waweze kufuga kwa tija kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu ushauri, kwa sababu sisi mojawapo ya kazi yetu ni kushauri, ukiangalia hata ranch zetu za Serikali zote tulizonazo, nenda Kongwa na hizo za NARCO, zote zimekufa. Yaani ni kwamba zile ranch hazina tija. Ni vizuri wale Mameneja wa Ranchi zile badala ya kuteua tu kwamba tunadhani fulani ni mwaminifu tumkabidhi ranch, Mheshimiwa Waziri atangaze nani anaweza kusimamia? Naamini atapata watalaam wazuri wanaoweza kusimamia na wakaziendesha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani ranch inaweza kubeba ng’ombe 16,000, unaipatia ng’ombe 4,000. Tafsiri yake ni kwamba tunawasaidia tu wale Mameneja pamoja na wale wahusika walioko kule, lakini hazina manufaa yoyote na hata sisi hatuwezi kujifunza kupitia zile ranchi. Kwa hiyo, huo ndio ushauri wangu kwa upande wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uvuvi, yawezekana nikatofautiana kidogo na wenzangu. Binafsi napongeza suala la ukomeshaji wa uvuvi haramu, kwa sababu gani? Maana wanasema penye ukweli lazima tuseme ukweli kwa sababu tunahitaji kuisaidia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu Musoma Mjini, baada ya zoezi la kukomesha uvuvi haramu kuendelea kwa muda, leo ukienda pale ukimwuliza kila mmoja anakubali kwamba sasa samaki wameongezeka. Kwa hiyo, hilo ni jukumu ambalo tuna kila sababu ya kupongeza kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, kuna yule ambaye ni DC wangu wa pale mjini, anasaidia sana suala la uvuvi haramu. Nimefanya mikutano mingi, wale wale waliokuwa wanachukia wakati ule wakisema wanakandamizwa, leo kila mmoja anakubali kwamba kweli samaki wanapatikana. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na haya mafanikio, yako matatizo na changamoto ambazo lazima tujipange tuone namna ya kuzimaliza. Ile timu ya Mheshimiwa Waziri inayofanya kazi ile, wako wengine wanafanya kazi kwa uaminifu, lakini wengine wanatumia nafasi zile kuwaumiza wale wavuvi pamoja na wale raia wa kule. Shida iliyoko pale, wakati mwingine naweza kuita ile timu, kama ilivyokuwa Operesheni Tokomeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe mfano, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na mimi tumewasiliana mara nyingi. Moja, unakuta labda wale watu wanapofanya operesheni zao, wakikuta tu kwenye ile gari labda hawana ile koleo ya plastic, anaambiwa faini shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tatu, wakati vile vitu ni vya kuelimishana tu. Mtu yule hana gumboot anapigwa faini ya shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tatu. Kwa yule mvuvi wa kawaida anayefanya biashara hiyo, maana yake ni kwamba tunamfilisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nimekwenda kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na wafanyabiashara wa Musoma wanaosafirisha samaki. Wote tunafahamu, samaki wote tunaokula huku hatuna magari yenye refrigerated system yanayoweza kusafirisha samaki. Wanaweka kwenye Fusso, wanafunga kwenye maboksi wanasafirisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale samaki wakiwa kule Musoma, kabla ya hawajaondoka, wanaenda pale kwenye Kituo cha Uvuvi, ndipo wanapakilia, wanakaguliwa. Wanapofika Singida, hatuna storage system. Ile Fusso inafunguliwa, wanacheki box moja moja, zinakutwa kilogram tatu kwenye tani 14. Wakikuta kilogram tatu wanapiga faini shilingi milioni sita. Hivi hiyo ni tokomeza au ni kuendeleza uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi, bahati nzuri mimi na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiwasiliana na kusema kweli mambo mengine amekuwa akiyamaliza. Nitoe mifano kwa machache ambayo tumewasiliana na tuone namna ya kuyarekebisha ili mambo yaende. Hili gari moja walipofungua pale Singida wakakuta hakuna kilogram tatu, ni under size walipigwa faini ya shilingi milioni sita. Waliponiambia, nikazungumza na Mheshimiwa Waziri. Akaniambia hiyo gari kama ina kilogram tatu peke yake hebu iachieni.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale watu walionesha kiburi wakasema wanarudi ku-check upya. Badala ya ile sampling waka-check upya. Kwenye kilogram 14, maana yake ile kazi waliifanya kwa siku mbili. Tafsiri yake ni kwamba hilo gari siyo refrigerated. Kwa hiyo, matokeo yake wale samaki wote walifika Dar es Salaam sokoni wakiwa wameharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi walipo-check tena kila box, wakapata kama kilogram 30 zikiwa ni under size. Ile faini ikarushwa kutoka shilingi milioni sita mpaka shilingi milioni 20. Hivi tunategemea hiyo ni Operesheni Tokemeza au hiyo ni kusaidia kumaliza tatizo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana nasema kwamba pamoja na nia nzuri ya Serikali, ihakikishe kwamba samaki wanapatikana, lakini lazima tuangalie namna ya utendaji wa kazi unavyofanyika. Kibaya zaidi, wale watu wakisikia tu kwamba Mheshimiwa Waziri kaambiwa jambo, kalalamikiwa hapo ndipo wanakuja zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili, maana ni vizuri tukaenda kwa mifano. Ilitokea kwa mtu mmoja, kwa kawaida wale wanaofanya biashara ya kununua samaki, akinunua samaki anapaswa awe na watu wengine nadhani kama wanne hivi. Kwa bahati mbaya wakati anakata leseni akalipia wale watu wote lakini jina likaandikwa la kampuni yake peke yake. Walipomshika mtu wake wakati yeye hayupo, matokeo yake akapigwa faini. Kwa bahati nzuri nilimweleza Mheshimiwa Waziri na akafuatilia. Hapo sasa ndiyo wakasema wanamtafuta na mwenye mzigo naye wanataka wampige faini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana tunasema kwamba ukiangalia zoezi lenyewe ni nzuri, lakini kwa maana ya kwamba tunategemea kama sisi watu wa Musoma pale tuna viwanda visivyopungua vinne vya samaki ambavyo vyote vimekufa. Hata hivyo, leo furaha yangu ni kuona kwamba viwanda sasa vinachipuka kwa maana vinafunguliwa na samaki wanapatikana. Sasa kupatikana kwa samaki huku lazima kuendane na kuwapa watu wetu elimu kuliko hiki kinachofanyika sasa, badala ya kuwaendeleza badala yake tunawamaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine hata zile nyavu tunapozishika, Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua; tunashika nyavu haramu, zile nyavu tuna haki ya kuziteketeza. Sasa hebu tuelezwe, ile boti, zile engine, tuna haja gani ya kuziharibu? Maana yake ni kwamba unachoma ile boti, tafsiri yake ni kwamba unataka yule mtu afilisike. Kwa hiyo, huyo mtu unapotaka afilisike, sasa kesho ataendeshaje maisha yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kazi nzuri ambayo ndugu zetu wanaifanya, lakini hebu waone namna gani wanaweza wakaifanya kwa uzuri zaidi. Ushauri wangu, ni vizuri kwenye ile timu watu wengi wakahusika mle; watu wa usalama, Polisi na wenyewe wakawemo mle. Ule mchanganyiko tunadhani utasaidia kuwafanya watu wawe na mbinu nzuri za kufanya ile Operasheni ambayo kazi…

TAARIFA . . .

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo taarifa naipokea kwa maana kwamba, Mheshimiwa Waziri ajue sasa kwamba hizo ni changamoto ambazo anahitaji kuzirekebisha kwa haraka, otherwise badala ya huu uvuvi kutusaidia, basi utaendelea kuwa kero.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami naunga mkono hoja, lakini hayo yote yarekebishwe ili mambo mazuri yaendelee kufanyika. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika haya maandalizi ya mpango wa bajeti 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nianze kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja Naibu wake kwa maandalizi ya mpango mzuri na niseme tu kwamba katika mpango huu yapo yale mambo ambayo yamepewa kipaumbele kama kuendelea kufanya kazi ya ununuzi wa ndege, lakini vilevile mradi wa Stiegler’s Gorge pamoja na wa reli ya kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo katika nchi yetu Tanzania ni nchi ambayo tuna vivutio vingi vya watalii, lakini ni kwamba wenzetu Wakenya wanatushinda watalii kwa wingi na mapato ya utalii ni kwa sababu hatuna direct flight za kuja Tanzania. Kwa hiyo, leo nilipoona humu tunataraji kwa na direct flight za kutoka China kuja Tanzania, kutoka India kuja Tanzania huo ni mwanzo mkubwa na mwanzo mzuri unaonyesha tunatarji na sisi kupata mapato ya fedha za kigeni kutokana na watalii kwa hiyo nasema big up katika hilo. Lakini ukiangalia mradi wa Stiegler’s Gorge ambao baadhi yetu tunaubeza tunatambua kwamba ili nchi yetu iweze kuendelea inahitaji muwekezaji na mwekezaji yoyote akitaka kuwekeza moja wapo ya factor kubwa anayoingalia ni gharama ya uendeshai ambayo anakwenda kwenye umeme.

Kwa hiyo, wote tunafahamu gharama za umeme wa maji kwa namna zilivyo chini, kwa hiyo, matokeo yake ni kwamba tuna nafasi kumbe ya kuvutia watu wengi wawekezaji wengi kuleta viwanda vyao nchini. Kwa sababu ya gharama za umeme tunatarja kuwa chini, kwa hiyo, tunaendelea kuishukuru Serikali kwa mpango huo. Lakini Mheshimwa Dkt. Mpango nikuombe tu ufanye jambo ambalo ni la haraka na litaonesha matokeo ya haraka. Kwenye huu mpango wa reli ya kisasa leo Watanzania wengi tukiwemo Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera pamoja na wote ambao usafiri wa Dar es Salaam kuja kwenye mikoa yetu tunatumia zaidi ya siku moja maana yake abiria lazima walale njiani.

Sasa kwa sababu tumeona kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro ni kilometa 300 na mpaka sasa umeshatengeneza 24% ni mategemeo yangu by mwaka kesho au mwaka kesho kutwa mwanzoni kile kipande kitakuwa kimekamilika. Sasa nini kifanyike wakati huu ujenzi unaendelea hebu tuanze kabisa kununua vichwa vya tayari tayari kwa ajili ya treni, kwa ajili ya kuleta abiria hapo, pamoja na mabehewa lakini pamoja na stand kwa ajili ya mabasi, matokeo yake yatakuaje kutoka Dar es Salaam treni iwe inaondoka saa 11 naamini saa 12 itakuwa Morogoro, abiria wote wa mikoani wakipanda pale saa 12 tafsiri yake kwamba hakuna abiria hata mmoja atakayelala njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini huo mpango peke yake utaanza kuonesha matokeo ya haraka wakati huo ujenzi wa reli kadri unapofika kwenye kituo kimoja mfano ukifika Dodoma utaratibu mwingine unaendelea yaani huduma zote zinaendelea kupatikana kuliko tutakaposema tusubiri tujenge kwa muda mrefu au kipande kirefu halafu ndipo hizo huduma zianze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kuwa nimesema hayo sasa katika mpango huu wa 2019/2020 wote tunafahamu kwamba kilimo ndio uti wa mgongo, kilimo kinachukua 70% ya Watanzania, nini kifanyike kwenye upande huo hebu kama tunahitaji kuajiri watu wengi na maisha yetu yawe mazuri lazima tujikite kwenye kilimo cha umwagiliaji na tutakapojikita kwenye kilimo cha umwagiliaji na tutakapojikita kwenye kilimo cha umwagiliaji tutambue mabonde yaliyopo katika nchi hii na mabonde hayo leo tunaweza kuamua mfano tusema tunalima mpunga, katika mabonde yote tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kuwa nimesema hayo sasa katika mpango huu wa 2019/2020 wote tunafahamu kwamba kilimo ndio uti wa mgongo, kilimo kinachukua 70% ya Watanzania, nini kifanyike kwenye upande huo hebu kama tunahitaji kuajiri watu wengi na maisha yetu yawe mazuri lazima tujikite kwenye kilimo cha umwagiliaji na tutakapojikita kwenye kilimo cha umwagiliaji na tutakapojikita kwenye kilimo cha umwagiliaji tutambue mabonde yaliyopo katika nchi hii na mabonde hayo leo tunaweza kuamua mfano tusema tunalima mpunga, katika mabonde yote tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuzungumza zao la mpunga kwanza ni zao la biashara, lakini vilevile ni zao la chakula, lakini vilevile nchi zote zinazotuzunguka ni nchi ambazo zinahitaji mchele wa Tanzania. Ukienda Kenya, Uganda, Rwanda, Kongo na Zambia, mchele wa Tanzania ukiruhusiwa tu kuuzwa unao kila nchi unaupenda. Sasa nini kifanyike tukishaanisha hayo mabonde wakati mwingine tunaweza kutangaza wakandarasi kama tunavyotangaza kazi za bararaba. Tukasema tunahitaji mkandarasi hekta 2000 hizi zipo hapa, basi tunachohitaji wewe mkandarasi weka miundombinu ya irrigation watu watalima mfano zao moja kama niilivyosema la mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia zao la mpunga, mpunga ni zao hakuna kinachotupwa yale mabaki yake kwa maana ya majani mifugo inakula, zile pumba hata wale wachoma matofali sasa hawataharibu mazingira kwa kukata mita watatumia kuchomea matofali. Lakini sisi wote ni mashaidi zile wanaita rice polish kwa maana zile chenga zake ndio tunakula vitumbua, lakini na mchele wake tunauza.

Kwa hiyo, kumbe ni imani yangu kwamba kwa kulima mpunga ni zao ambalo linaweza likamsaidia Mtanzania yeyote yule na likapandisha kipato chetu na hela yenyewe haina kwamba soko limeanguka kwa sababu mahitaji ya soko yapo ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo ni imani yangu tukikipa kilimo kipaumbele cha kwanza hasa kilimo cha umwagiliaji itatusaidia sana katika kuukomboa na kunyanyua kipato cha Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipaumbele cha pili tufanye nini1 Kwangu mimi kipaumbele cha pili tukipeleke kwenye suala la uvuvi. Kwa bahati mbaya watanzania wengi kila fursa tunayoipata inabadilika tena inakuwa hatari kwa watu wetu. Leo wale watu waliopo baharini, waliopo Ziwa Tanganyika, waliopo Ziwa Victoria ni kilio kitupu. Ni kilio kitupu kwa sababu badala ya yetu sisi tuone namna kuwasaidia, kazi yetu ni kwamba mtu amekosea anapigwa faini ambayo haiwezi. Kwa hiyo, wale watu wetu wengine wanafungwa, kwa hiyo hali ya maisha inakuwa ngumu, lakini nini kifanyike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ili watu wetu tuweze kuendeleza uvuvi, ili wale watu wetu waweze kuthamini maana ya uvuvi, kinachopaswa kufanyika hebu Serikali itenge fedha, tuwe na uvuvi ule ufugaji wa kufugia ziwani, ufugaji wa kufugia baharini kwa maana ya kutengeneza zile cage, ukishalianzia lile kwa vyovyote vile uvuvi haramu hautakuwepo kwa sababu wale wananchi wenyewe ambao ni wafugaji wa samaki wao wenyewe ndio watakaokuwa walinzi wa ziwa letu na walinzi wa bahari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwa kufanya hivyo kwanza watakuwa wanapata kipato lakini vilevile watakuwa walinzi wazuri katika maziwa yetu na bahari zetu kwa kuhakikisha kwamba uvuvi haramu haufanyiki. Lakini hata zile fedha ambazo watu wa patrol huwa wanawatoza wakienda kuwakamata wakati mwingine huwa wanawatoza shilingi milioni mbili mpaka shilingi milioni tano zile fedha zinapaswa ziwarudie, zirudi kwa kutengeneza miundombinu kama hiyo ili watu wetu waendelee kuona umuhimu wa uvuvi na imani yangu kwamba mambo yatakuwa mazuri na wale watu wetu watafanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo katika ushauri wangu tunapaswa tujikite, katika kuwasaidia wananchi wetu na Watanzania wetu, ni ukweli usiopingika kwamba leo yupo mtoto anasoma mpaka chuo kikuu, anatoka na bachelor yake ya sociology, lakini huyo mtoto ukimchukua na yule mtoto ambaye amesoma VETA akamaliza, huyu wa VETA bado yupo better of kuliko yule ambaye ana degree yake ya sociology.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kwamba mpaka leo kipaumbele kikubwa tunakitoa zaidi kuhakisha kijana asome mpaka degree yake, kumbe kati ya eneo ambalo tunahitaji kuliendeleza tunapaswa kuendeleza maeneo ya vyuo kwa maana hivi vyuo vya certificate na diploma ambavyo watu wetu wataendelea kupata ujuzi na itawasaidi zaidi katika kujiajiri kuliko huu utaratibu ambao tunathamini zaidi wale watu ambao wana bachelor kumbe wakati mwingine bachelor yake anazidiwa na mtu mwenye certificate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja na kupongeza sana, ahsanteni sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuweza kuwa mchangiaji wa mwisho katika hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango. Napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli naipongeza sana Awamu ya Tano kwa maana ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mipango pamoja na Mawaziri wenzake kwa kazi nzuri ambayo wanaitendea haki Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tulipoenda kwenye uchaguzi mwaka 2015 tulikuwa tunawaahidi wananchi maendeleo. Kusema kweli, mimi binafsi Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, nikizungumzia katika Jimbo langu la Musoma, ingekuwa leo ndiyo tunaenda kwenye uchaguzi hasa tukiwa tunazingatia yale tuliyoyaahidi, basi naweza nikasema utekelezaji umefanyika kwa zaidi ya asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni ukweli usiopingika, hata unaposafiri barabarani utakutana na magari mengi ya nguzo kwa maana ya nguzo ya umeme, mabomba ya maji, lakini hayo yote ni mambo ambayo yanafanyika katika lengo zima la kuhudumia wananchi. Ndiyo maana hata ndugu yetu Mheshimiwa Bwege pale, yeye mwenyewe ameshukuru na ameweza kusema wazi kwamba mambo ambayo yamefanyika katika awamu hii ni mambo ambayo ni ya wazi wazi kwa maana ya mambo ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wasiwasi wangu ni mmoja tu ambapo katika Mpango huu wa leo sijaona kama tumeuzungumza sana. Pamoja na juhudi hizi kubwa za maendeleo tunazofanya, lakini bado mahitaji hata tungepeleka maji, hata tungetengeneza barabara pamoja na elimu, lakini mahitaji mwaka baada ya mwaka yapo pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mifano michache. Pale kwenye Jimbo langu la Musoma, ile mwaka 2005 tulijitahidi sana kujenga sekondari karibu kila Kata, lakini ndani ya muda mfupi tu, leo kuna Kata ambazo zina sekondari zaidi ya tatu. Hapo ni kwamba mahitaji ya sekondari bado yako pale pale. Ukienda kwenye Shule za Msingi, leo unakuta kwa sababu ya ufinyu wa maeneo ya kujenga, pale pale tumezibananisha, ilikuwa ni shule moja, sasa ziko shule mpaka nne. Kwa hiyo mahitaji haya, mashaka yangu ni kwamba inaonekana hayatakaa yapungue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, sijui labda hili watu wengi tunaogopa kulisema, maana nimejaribu kuangalia hata katika nchi za wenzetu zinazoendelea, suala la uzazi wa mpango; ni kwamba kwa namna ambavyo Watanzania tunaongezeka siku kwa siku, katika mtazamo wangu ni kwamba pamoja na juhudi zote ambazo tutazifanya, lakini bado mahitaji yataendelea kubaki pale pale. Kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba, hata kama tunadhani kama hatulioni; nitoe mfano kwetu sisi watu wa Mara ambao tunaruhusiwa kuoa wanawake mpaka watano, maana yake ni kwamba familia zetu zinaendelea kupanuka siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ninyi Wasukuma, upanuzi wa familia unaendelea siku hadi siku. Sasa hayo yote ukiyaangalia, kama hatuwezi ku- address suala la uzazi wa mpango ni tatizo ambalo ninaamini kwamba pamoja na juhudi za awamu hii, lakini mahitaji bado yataendelea kubaki kama yalivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia wale wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba, maana kwa namna ninavyoliona ni tatizo la ajira. Wanafunzi wanamaliza Darasa la Saba, zaidi ya asilimia 50 wanaingia mtaani. Wanafunzi wanamaliza Kidato cha Nne, zaidi ya asilimia 70 wanaingia mtaani; wanafunzi wanamaliza mpaka Vyuo Vikuu, zaidi ya asilimia 80 hakuna kazi. Hii yote, katika mtazamo wangu ni kwamba wanafunzi wote hawa wanakosa ajira kwa sababu hawana skills. Yaani asilimia kubwa ya wanafunzi hawana mafunzo yoyote yanayoweza kuwawezesha hata kujiajiri. Hali hii ni hali ambayo inaendelea. Sasa nini kifanyike katika huu Mpango wa muda mfupi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali awamu hii, ilianzisha mpango wa kuchukua wanafunzi wengi au vijana wengi kwenda JKT. Kusema kweli wale vijana wamekaa kule miaka mitatu na wamejifunza mafunzo mbalimbali; mafunzo ya ukakamavu na badhi ya mafunzo mengine labda ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika mtazamo wangu, Serikali inapaswa iongeze nguvu zaidi. Nini kifanyike? Moja, wale vijana wanaoenda JKT, kwanza waendelee kuchukuliwa wengi zaidi, nami nakubali kwamba wakae miaka mitatu. Pia katika kipindi cha miaka mitatu hiyo wajifunze mafunzo mbalimbali; ujasiriamali, mifugo na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kila mwezi tuwe na utaratibu kama tunawalipa mshahara, lakini fedha hizo tunaziweka kule. Hata kama tungekuwa tunawawekea shilingi 200,000/=, baada ya miaka mitatu, yule kijana atakuwa na pesa zisizopungua shilingi milioni saba. Sasa ile siku tunapomwambia sasa kijana umemaliza miaka mitatu JKT, hebu nenda kaendelee na maisha, tafsiri yake ni kwamba akiondoka pale na shilingi milioni saba na huku ameshajifunza mafunzo mbalimbali, lazima atapata mahali pa kuanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, baada ya miaka mitatu tunawaambia, tunawachukua wachache Jeshini, wachache Polisi, halafu wengine tunawaambia wakaanze maisha. Kwa kweli tunawapa ugumu wa maisha. Hii sioni kama inawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akaliangalia na hilo aliweke katika Mpango tuone namna ya kuchukua vijana wengi zaidi kwenda JKT wakajifunze, lakini mwisho wa siku waondoke na chochote, waondoke na ujuzi ili wakaanze maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naona na lenyewe tunahitaji kuliweka katika Mpango, tunajitahidi sana kuwasomesha vijana mpaka kwenye elimu ya juu. Tunapowapeleka mpaka kwenye elimu ya juu, kuna baadhi ya degree ambazo vijana wakitoka nazo kule ukimleta kwenye maisha ya kawaida anazidiwa na kijana ambaye ametoza VETA au mwenye Diploma ya Mifugo. Hii yote ni kwa sababu kuna baadhi ya degree ambazo kama hakupata ajira ya Serikali, hawezi kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kama ambavyo tumejitahidi sana kujenga shule za sekondari, kama ambavyo tumejitahidi sana kujenga Vyuo Vikuu, hebu tuwe na mikakati mahsusi ya kujenga hivi vyuo katika maeneo yetu. Mfano Vyuo vya Mifugo, Vyuo vya Kilimo, Vyuo vya VETA na Vyuo vya Ufundi Uchundo. Tunadhani kwamba hawa vijana wanaomaliza Darasa la Saba, wanaomaliza Kidato cha Nne, wakiondoka na huo ujuzi, basi unaweza ukawasaida zaidi kwenda kuanzisha maisha kuliko katika hali ya sasa ambayo wanaendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ndiyo maana vijana wetu wengi leo wakishamaliza hizi elimu mbalimbali, unawakuta tu wako Mitaani wala hawajui wafanye nini. Ndiyo maana sasa kila ukiwauliza kila kijana anazungumza hali ya maisha ni ngumu kwa sababu anashindwa namna gani anavyoweza kuendesha maisha yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu mwingine ambao Mheshimiwa Dkt. Mipango aendelee kuuweka katika mipango ni huu utaratibu wa uendelezaji wa bandari. Bahati nzuri tumeendeleza Bandari kama ya Dar es Salaam, ya Mtwara na Tanga. Ziko bandari ambazo leo zimesinzia. Ukienda kama kule Kanda ya Ziwa, pale Musoma bandari imelala; ukienda Mwanza bandari zimelala na ukienda Bukoba bandari zimelala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa najaribu kuangalia Serikali ilipoanzisha utaratibu wa bulk procurement, huu wa ununuzi wa mafuta kwa pamoja. Katika utaratibu wake wa kudhibiti nadhani kama magendo na vitu kama hivyo na kuwa na mafuta bora; ilichokifanya, ilianzisha kwenye eneo moja tu la Dar es Salaam. Ikafika mahali ikafanya vizuri, Serikali eneo la Tanga ikafika mahali wakafanya vizuri na Serikali imepeleka Mtwara, imefika mahali wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia kule Kanda ya Ziwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Ulikuwa na hoja nzuri sana, muda ndio huo.

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hii hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyoonyesha na kwa muonekano wake, anaonekana amejiandaa na yuko tayari kulitumikia Taifa hili katika kuhakikisha kwamba katika kipindi chake cha miaka mitano basi suala la viwanda linakuwepo katika nchi yetu, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya. Mahali popote unapopita, kwa kweli kila mmoja anaona kwamba sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeanza kwenda mchakamchaka. Sisi kazi yetu ni kuendelea tu kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kuwa na maisha marefu, lakini na kazi yake iweze kuendelea vizuri kwa kadri inavyoonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, pale kwangu kwa maana ya Jimbo la Musoma Mjini, kwa bahati mbaya sana tuko pembezoni. Huwezi kupita Musoma kwenda mji wowote ule, ili uje Musoma lazima ufunge safari ya kuja Musoma na hatuna economic activity yoyote zaidi ya biashara ndogondogo na viwanda. Ombi langu la kwanza, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri hebu apange, tukae siku kama tatu hivi pale Musoma maana tulikuwa tunasaidiwa na Kiwanda cha Mutex, Kiwanda cha Nguo, nacho hivi leo ninavyozungumza kinaenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, viko viwanda kama vinne vya samaki, kwa bahati mbaya sana sasa hivi tunacho kiwanda kimoja tu nacho kinasuasua. Kwa hiyo, kwa maneno mengine, watu wa Musoma Mjini leo hawana ajira, vijana hawana kazi za kufanya, matokeo yake sasa ni kuongeza vibaka lakini na uchumi wa mji unaendelea kudorora. Kwa hiyo, hilo ni ombi langu la kwanza ambalo naomba kwamba hebu tufike kule ili tuweze kusaidiana tuone tutafanyaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Mutex kilipobinafsishwa, kuna mafao ya watumishi ambayo nimeyapigia kelele katika Bunge hili toka mwaka 2005 hadi leo, wale waliokuwa wanadai wengi wao wamepoteza maisha, lakini hata watoto wao wanaendelea kudai. Kwa hiyo, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri tutakapofika pale, tupate nafasi ya kuzungumza nao na Serikali sasa itoe majibu yao ya mwisho ili wajue kama hayo mafao yao wanayapata au la kama hawayapati basi waweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili zoezi la kuendeleza viwanda, tunavyo viwanda vya ngozi hapa nchini. Hivi viwanda vinaonekana vimekufa kwa sababu mpaka leo ukiangalia kwa wafanyabiashara au wachinjaji ngozi zao wanatupa bure. Kwa sababu leo anauza kilo ya ngozi kwa bei isiyozidi sh. 200, tafsiri yake ni kwamba, hakuna wanachokipata. Kwa hiyo, tunadhani na hili nalo Mheshimiwa Waziri ajaribu kutuambia, hivi viwanda vilivyopo mkakati wake ni nini katika kuwasaidia wananchi wetu wa Tanzania maana vinginevyo tutajikuta wale Watanzania tulionao ambao wanafanya biashara hizo basi wanaendelea kufilisika siku baada ya siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo na kwa ufupi hili suala ambalo Serikali imezungumza kwamba tunahitaji kukuza viwanda. Mchango wangu ni kwamba, kama leo tunakubaliana kwamba Tanzania tunahitaji iwe ya viwanda, lazima tukubaliane hivi viwanda tunavyovihitaji ni viwanda vya aina gani. Leo ungeniuliza mimi vile viwanda vikubwa vyote vinavyokuja, kwanza vingi ni automation, utakuta kiwanda ni kikubwa lakini watu kinaowaajiri ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu la kwanza pamoja na kuanzisha viwanda na kwa kuwa lengo letu ni ajira tungeiangalia vizuri sana SIDO, tuangalie namna ya kuiwezesha kwani kule vijana na akinamama wanapata mafunzo mbalimbali. Ni imani yangu kwamba yale mafunzo wanayoyapata, ukiangalia wanaweza kuzalisha bidhaa nzuri sana, zile bidhaa zinaweza zika-compete katika masoko mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuendelea sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri akawa na mkakati maalum, kwanza kuhakikisha kwamba wataalam wanaendelea kuwepo SIDO na mafunzo yanaendelea kutolewa. Bahati nzuri SIDO ipo karibu katika kila mkoa, kama ni vijana pamoja na akinamama tayari wameshajifunza, wamepata mafunzo sasa tuna nafasi ya kuwapa mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ni kwamba hata vile viwanda ambavyo tunaona vinaleta bidhaa nyingi, maana Mheshimiwa Waziri leo amejibu hapa kuhusiana na suala la toothpick, amesema kwamba kile kiwanda kinagharimu siyo zaidi ya dola 28,000, wako Watanzania wengi tena wenye uwezo wa kawaida wanazo hizi fedha, lakini tatizo letu sasa ni kwamba hawa Watanzania wengi hawana exposure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe kinachotakiwa sasa, tukishatoa haya mafunzo, wakati mwingine Mheshimiwa Waziri hawa Watanzania hebu waulizwe, naamini watakuwa tayari kupata exposure kwa fedha zao, waende kwenye nchi za wenzetu kama India, China na hizi nchi Asia, viko viwanda vidogo vidogo huko ambapo wakirudi watavianzisha hapa kwa fedha zao na kwa kusaidiwa na benki na vingi viwe vile ambavyo vinaweza kuzalisha bidhaa zinazoweza kutumika humu nchini. Kwa hiyo, tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo tunaweza kusaidia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo mimi binafsi nalifahamu na hizo ni hisia zangu, ni kwamba, Serikali yetu haijawa tayari kuhakikisha kwamba inawasaidia hawa Watanzania ambao wanaibukia kwa kuwajengea uwezo ili na wao waweze kufanya biashara. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tukienda kwa utaratibu huo hii SIDO itafanya kazi nzuri. Hebu tuzalishe zile bidhaa ambazo tunaweza kuziuza humu humu nchini na kwenye hizi nchi za jirani kuliko kuanza kupambana na yale masoko ya wenzetu, masoko ya Ulaya ambayo ushindani ni mkubwa kwa hali yetu kusema ukweli siyo rahisi sana tukaweza kuingia huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye nchi za wenzetu mfano kama Syria, kila mwaka kuna bidhaa ambazo wanaleta hapa nchini. Zile bidhaa zote zinatengenezwa na viwanda vidogo vidogo kama SIDO. Ukienda kwenye nchi jirani ya Kenya, kuna hivi viwanda wao wanaita Juakali, Juakali ina mchango mkubwa sana Kenya na inatengeneza bidhaa nyingi, nzuri na ambazo zinaweza zikashindanishwa katika masoko mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu ni hilo kwamba hebu tuangalie namna ya kuweza kuisaidia SIDO, watu wakapata mafunzo na baada ya kupata mafunzo tuone namna ya kuwasaidia, lakini namna wanavyoweza kupata exposure na wakaja kufanya biashara zao mbalimbali na tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia sana Watanzania wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango wangu kwa leo, lakini niendelee tu kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, kusema ukweli wale watu wetu wa Musoma kule wanahitaji msaada mkubwa wa Serikali ili waweze kuendelea. Nina uhakika vijana na akinamama wakisaidiwa wanaweza kujikwamua. Maana hayo mengine nazungumza kutokana na uzoefu wangu kwamba pale tulipojaribu kuwasaidia vijana, pale tulipojaribu kuwasaidia akinamama wanaweza kwenda, lakini tatizo kubwa ni kwamba vijana hawana ramani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa TAMISEMI pamoja na Waziri wa Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijalia kuwepo katika siku hii njema ya leo. Pia naungana na wasemaji wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Unajua wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Sisi wanadamu wengi tuna ile hali ya kutoridhika na kwa bahati mbaya sana wenzetu tukishukuru huwa wanakereka hivi lakini huo ndiyo ukweli wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme machache ambayo yananifanya niendelee kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Mimi nakumbuka wakati amekuja Musoma wakati ule anatafuta ridhaa, alipofika nilimuomba mambo matatu ya muhimu kwa niaba ya wananchi wa Musoma. Nilimwambia kati ya kero kubwa ya watu wa Musoma tuliyonayo ni kwamba maji ya Ziwa Victoria yako hapa na kuna huu mradi ambao niliuanzisha kabla sijaondoka, lakini mradi huu umeendelea kusuasua kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, alichosema akishakuwa Rais, Waziri atakayemteua asipoleta hayo maji, huyo Waziri atageuka kuwa maji. Leo nashukuru kuliambia Bunge hili kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli alipokuwa Rais mwaka jana, moja kwa moja zoezi lile la uwekaji wa maji lilienda kwa speed. Hivi leo ninavyozungumza mwezi huu wa sita karibu Musoma nzima itapata maji safi na salama. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema nina kila aina ya sababu kushukuru katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, sababu nyingine au jambo lingine nililomuomba, nilimwambia tuna Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali ile inahitaji zaidi ya shilingi bilioni 50 lakini kila mwaka inatengewa shilingi bilioni moja. Nikamwambia Mheshimiwa hii hospitali itatengamaa lini? Kwa mwaka huu peke yake nimeangalia kwenye bajeti tumetengewa toka shilingi bilioni 1 mpaka shilingi bilioni 5.5. Ndiyo maana tunasema wakati mwingine lazima tuwe na ule moyo wa kusema ahsante na ndiyo maana naposimama nasema naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendelea kuangalia hata kwenye sekta zingine, maana wakati ule Rais anasema elimu sasa ni bure kuna baadhi ya watu walibeza lakini nitoe tu mfano halisi ulioonyesha umuhimu wa ile bure aliyoisema Mheshimiwa Rais. Kwenye ile kata yangu ninayoishi peke yake, ambayo ni Kata ya Nyakato, darasa la kwanza walioandikishwa ni watoto wasiopungua 800, tafsiri yake ni baada ya kuona kwamba ile elimu sasa inatolewa bure. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya lakini tunaendelea kusema na hii ni kawaida yetu sisi wanadamu kwamba lazima ushukuru lakini haikumaanishi kwamba uache kuomba maana yeyote aliyeko hapa hata kama angekuwa na fedha kiasi gani bado kesho anahitaji na mahitaji yake hayaishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu kuna vitu ambavyo Mheshimiwa Waziri lazima tuviangalie sana. Moja, ni vyumba vya madarasa lakini pili ni madawati. Pamoja na kwamba yapo madawati ambayo Wabunge tutapewa kwa ajili ya kupeleka majimboni lakini bado tuna upungufu mkubwa. Kwa hiyo, naiomba kabisa Wizara na Serikali kwa ujumla iendelee kuangalia na kutathmini itafanyaje ipunguze tatizo la madawati pamoja na vyumba vya madarasa. Maana kama leo kweli shule moja ina wanafunzi wasiopungua 800, hilo ni darasa la kwanza, tafsiri yake ni kwamba darasa hilo tu ni shule. Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo na kwa sababu kwenye bajeti hapa hatujaona kama kuna fedha za kutosha kwa ajili ya vyumba vya madarasa pamoja na madawati tujue kwamba hiyo ni changamoto ambayo tunahitaji kuifanyia kazi na tuone ni kwa kiasi gani Serikali itajipanga kulitatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo bado tuna tatizo la upungufu wa dawa katika zahanati na vituo vyetu vya afya. Wakati mwingine inatia aibu, watu wetu ambao wana uwezo wa chini anapokwenda hospitalini anakuta hakuna dawa za kutosha. Nadhani Serikali yetu ina kila sababu kuendelea kuhakikisha kwamba tunakuwa na hizi zahanati katika maeneo yetu yote sambamba na vituo vya afya kwa ajili ya kuboresha huduma za wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuendelea kuiomba Serikali, pamoja na kwamba jana nililiuliza katika swali la nyongeza, kusema kweli naomba Mheshimiwa Waziri alitilie maanani maana nayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba zile shule zetu zote za sekondari tumeziweka pembezoni mwa kata zetu, upande mmoja. Mfano kutoka pale kwenye Kata ya Bweli mpaka Kata ya Makoko zipo sekondari zisizopungua 14, zile sekondari zote barabara hazipitiki. Kwa hiyo, tukaomba barabara moja ya lami ikaziunganisha hizo shule zote ili turahisishe hata usafiri wa wanafunzi kwenda shuleni kwa maana kwamba tutaruhusu daladala kupita huko. Kwa hiyo, tunadhani kwamba barabara hiyo ikipewa kipaumbele basi itaweza kutusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naiomba Serikali ni kutokana na zile fedha ambazo tunataraji kuzipata, shilingi milioni 50 kwa kila kijiji lakini kwetu sisi mjini tunahesabu ni shilingi milioni 50 kwa kila mtaa. Kama kuna kazi kubwa tuliyonayo ambayo tunahitaji kuifanya sasa ni kujenga uchumi wa vijana, ni kujenga uchumi wa akina mama kwa maana kwamba akina mama ndiyo wenye jukumu kubwa la kulea familia zetu. Kama hivyo ndivyo hebu tuhakikishe kwamba wale watu wetu wamepata elimu nzuri, wamepata mafunzo mazuri maana tulijifunza kidogo kwenye yale mabilioni ya JK na sasa tunadhani kwamba kwa yale tuliyojifunza kule tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika hizi milioni 50 zinazokuja kwa ajili ya kila kijiji na kila mtaa. Nadhani fedha hizi zikisimamiwa vizuri kwa ajili ya vijana na akina mama, zitaleta impact kubwa na zitajenga uchumi wa watu wetu kwa maana ya mtu mmoja mmoja na maisha yao yatakuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kutokana na uzoefu wangu baada ya kuwa nimelijaribu maana nilichukua kama pilot study, nikajaribu kwa vijana tukawaanzishia mradi wa kujitegemea. Naomba kulihakikishia Bunge hili kwamba zoezi lile linakwenda vizuri na wale vijana ambao hawapungui 200 wanafanya kazi zao za kulima vizuri na tunataraji kwamba baada ya mwaka mmoja watakuwa model wa vijana wengine kujifunza. Nadhani kwa utaratibu huo sasa wale vijana watakuwa wamepata ajira na maisha yao yatakua yamekwenda vizuri. Nazungumzia uzoefu nilionao ikiwa ni pamoja na kwasaidia akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi hoja zote mbili za Kamati. Nijikite zaidi katika taarifa hii ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Na mimi nakubaliana kabisa na Kamati ya LAAC kwa changamoto ilizoziona mojawapo ikiwa ni pamoja na baadhi ya Halmashauri kutochangia kabisa ule mfuko wa vijana na akina mama. Pia Halmashauri kutopeleka fedha kwenye kata na vijiji na uzembe wa ukusanyaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tutambue tu jambo moja kwamba mwaka jana ndiyo tulikuwa na uchaguzi na zaidi ya asilimia 70 ya Madiwani ni wapya lakini na hawa Wakurugenzi ni kweli kwamba zaidi ya asilimia 50 ni wapya, kwa hiyo, hata ile namna ya usimamizi wa fedha ni tatizo.
Kwa hiyo, nadhani cha kwanza kinachopaswa kufanyika hawa Madiwani pamoja na Wakurugenzi wanahitaji kupata mafunzo ambayo yatawasaidia au litawawezesha kuwa na udhibiti na usimamizi mzuri wa hizi fedha zao. Pia hii itasaidia kuondoa ile migongano iliyopo kati ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa sababu hawa Madiwani wanajua majukumu yao lakini na Mkurugenzi naye atakuwa anajua majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hata sisi Wabunge tulipokuja humu Bungeni bado tulipata orientation. Sasa leo inakuwaje hawa Wakurugenzi wapya wanachaguliwa wengine kutoka maeneo ambayo hawajawahi kuhusika kabisa na masuala ya uongozi halafu wanafika wanapewa majukumu na tunategemea kwamba wanaweza ku-perform. Kwa hiyo, nadhani hiyo ni dosari ya kwanza pamoja na kwamba Serikali inabana matumizi lakini ione uwezekano wa kuendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya Madiwani na hawa Wakurugenzi ambao ni wapya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makusanyo kuchukuliwa na Serikali, ukiangalia kwenye ile Sheria Na. 7 na Na. 8 zilizounda Halmashauri za Miji pamoja na Halmashauri za Wilaya ilikuwa inasema wazi kwamba lengo la Serikali ni kuzijengea Halmashauri uwezo ili ziweze kujiendesha.
Sasa mimi najiuliza kama tunafika mahali tunachukua vyanzo vya Halmashauri tunavirudisha Serikali Kuu huko ndiko kuijengea ile Halmashauri uwezo? Kwa hiyo, tunadhani kwamba huu utaratibu wa Serikali Kuu kuona kwamba kuna chanzo hapa ambacho inaweza ikakusanya zaidi ikachukua halafu tukaiacha Halmashauri, halafu tunarudi kuilaumu kwamba haikusanyi wakati huo hata zile fedha ambazo tumeahidi tunapeleka hatuwapelekei mimi sidhani kama tunatenda haki hata kidogo. Kwa hiyo, nadhani tuna kila aina ya sababu ya kuendelea kuzijengea uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mapato yote au kodi zote ambazo zinadaiwa na Serikali Kuu ni za lazima yaani ukiletewa barua na Serikali Kuu kwamba kodi hii unapaswa ulipe, unapewa siku tofauti na hapo ni kwamba hatua kali zitachukuliwa. Ndiyo maana ukiangalia TRA wanapoenda kukusanya mapato yao wanaandamana na polisi, lakini ukiangalia hawa Halmashauri ambao tunategemea wakusanye siku zote mapato yao ni ya ku-negotiate yaani ni majadiliano na sana akiwa na askari atumie askari mgambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba haya mapato tunayotegemea kutoka kwenye Halmashauri haziwezi ku-perform kwa asilimia tunayotegemea kwa sababu mapato ya Halmashauri inaonekana ni hiari lakini mapato ya Serikali Kuu hayo ni lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo nalo lazima tuliangalie na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuzijengea uwezo hizi Halmashauri au Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha zenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni maslahi ya Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani. Nadhani hilo tunatakiwa kuliangalia zaidi ili nao waweze kujisikia kama viongozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakupongeza kwa hotuba yako nzuri, nami naunga mkono hoja. Pamoja na pongezi hizo napenda kupata ufafanuzi mdogo, mwaka jana Jaji Mkuu alipokwenda Musoma pamoja na shida mbalimbali na hoja zilizotolewa mbele ya Jaji, moja ilikuwa posho za Wazee wa Baraza kulipwa 5,000/= kwa kesi, vilevile kucheleweshwa malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jaji Mkuu aliwaahidi wale Wazee wa Baraza kulipwa 10,000/= badala ya 5,000/=. Mpaka sasa wale Wazee wa Baraza wanalipwa 5,000/= na cha ajabu toka mwaka jana mwezi Septemba hawajalipwa hadi leo. Mheshimiwa Waziri, ikumbukwe kwamba, wazee hawa wanakwenda Mahakamani tangu asubuhi hadi mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi na majibu ya maslahi ya wazee hawa. Ahsante na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi yake nzuri. Mheshimiwa Waziri, kama atakumbuka miezi miwili iliyopita alipata nafasi ya kutembelea Uwanja wa Musoma ambapo aliahidi kuujenga kwa kiwango cha lami. Nashukuru kwamba ametenga fedha kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja inawasumbua watu wa Musoma kwa sababu wataalam walikuja kuangalia maeneo ya kupanua uwanja huo, wakavuka barabara upande wa pili wakasema hapo patafanyiwa tathmini. Napenda kufahamu ni kweli uwanja huo utavuka barabara kuelekea upande wa magharibi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuna kitega uchumi chetu cha mwalo wa kupokelea samaki Mwigobero. Mwalo huu ulichukuliwa na bandari na tuliomba turudishiwe; tulimweleza Mheshimiwa Waziri na akatukubalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa tunasubiri bado hatujapata jibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Nategemea majibu mazuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo katika hii hotuba ya bajeti ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba wote tunajua kazi kubwa ya ulinzi inayofanywa na Jeshi letu, ni kazi nzuri na niseme tu kwamba hasa kwetu sisi ambao wakati mwingine tumekuwa watembezi tembezi kidogo katika nchi za wenzetu, ukija Tanzania ndiyo unaweza kujua kwamba kweli Jeshi letu linafanya kazi nzuri kwasababu ukilala una uhakika wa kuamka kesho yake. Kwa hiyo baada ya kuwapongeza kwa hiyo kazi nzuri lakini kuna baadhi ya mambo ambayo tunapaswa tuendelee kuwasaidia na ambayo yatahakikisha kwamba kazi zao zinakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; Jeshi letu bado lina matatizo makubwa ambayo ni pamoja na madeni. Tunaamini kwamba wanashindwa kufanya mipango yao mizuri kutokana na madeni na kwa maana ya ukwasi wa fedha. Kwa mfano kati ya miradi mizuri waliyonayo ni pamoja na kile kiwanda cha kutengeenza magari kile cha Nyumbu, ni kiwanda ambacho tulitakiwa tuone matokeo yake ya haraka, lakini naamini kwamba kinasua sua hii yote si kwa sababu nyingine lakini ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia ili waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba Jeshi wanayo madeni, kwa maana ya wale wazabuni. Kwa hiyo, napo kuna tatizo kubwa kwa sababu fedha wanazopata hazikidhi mahitaji yao, kwa hiyo, Serikali inahitaji kuangalia namna ya kuendelea kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu niseme kwamba katika miradi waliyonayo, kwa mfano hawa wenzetu wa JKT; JKT kwangu mimi ninavyofahamu leo tukiamua kuitumia vizuri inaweza ikaleta impact kubwa hasa kwa vijana wetu. Nadhani Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi kwamba kila linapotoka tangazo kwamba sasa kuna nafasi za kwenda JKT katika kila Wilaya unakuta wapo vijana zaidi ya 1,000 wanajipanga pale msululu kwa ajili ya kuomba waende JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wote tunakubaliana kwamba katika nchi hii kama kuna tatizo kubwa tulilonalo ni tatizo la ajira kwa vijana. Sasa basi JKT kwanza wanafundisha maadili, lakini wanaendelea kufundisha vijana kuipenda nchi yao. Kwa hiyo, katika yale mafunzo wanayofundisha ambayo ni pamoja na mafunzo ya kufanya kazi ambayo ni ya ujuzi ni imani yangu kwamba kama Serikali itaweka nguvu kubwa kwa JKT basi kwa kiasi kikubwa itapunguza tatizo la ajira kwa hawa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba kwa yale mafunzo ambayo vijana wangekuwa wanayapata pale mfano unazungumzia mafunzo ya kilimo. Ingekuwa ni rahisi zaidi vijana wakafika pale wakapata mafunzo ya uvuvi na mafunzo mbalimbali, sasa wakitoka hapo ni rahisi zaidi wakasaidiwa kidogo na wakaenda kuanza maisha yao kuliko hivi ambavyo tunavyowaacha vijana wanahangaika mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaamini kwamba JKT ni mahali pekee ambapo panaweza pakaleta impact kubwa. Unaona tunafikia mahali tunakuwa na upungufu wa chakula, lakini tunayo mabonde mazuri, na mengine; labda niseme tu moja, kwa mfano ukiangalia pale kwenye Wilaya ya Musoma walipewa eneo kubwa lakini hawakupewa uwezo; kwa hiyo, mwisho wa yote wameendelea tu kuliangalia lile eneo mpaka mwisho. Kwa hiyo, tunadhani kwamba hayo ni baadhi ya mambo ambayo Serikali ikiwasaidia basi wataweza kufanya mambo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja karibu na mwisho; kwa bahati nzuri hili tulishalizungumza na Mheshimiwa Waziri; ni suala la fidia kwa ajili ya wale wananchi walioombwa waondoke kwenye eneo ambalo Jeshi imelichukua, eneo la Makoko. Hili ni suala ambalo tumehangaika nalo sasa zaidi ya miaka 15. Tangu mwaka 2005 tumekuwa tukilizungumzia lakini hadi leo. Jeshi walishakubali kwamba wanalipa fidia, kwa maana ya Serikali, lakini hadi leo kila leo wale wananchi wameshindwa kuyaendeleza maeneo yale, lakini vile vile wameshindwa kuhamia mahali pengine kwa sababu bado hawajalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho, nadhani ni wiki tatu zilizopita wale wananchi walituma wawakilishi wao, bahati nzuri baada ya kuona nimezidiwa niliwapeleka moja kwa moja tukakaa na Mheshimiwa Waziri na akahaidi kwamba kwenye bajeti hii tutawalipa fidia. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba commitment yako utakaposimama kuzungumza uwahakikishie hawa wananchi ili wakae wakijua, kama ulivyoniambia siku ile, wawe na uhakika kwamba kama kweli watapata hizi fedha zao. Maana sasa ukiangalia ni muda mrefu na hata kati ya hao wenye hizo familia wengine walishafariki, sasa familia zao nazo zipo pale zile nyumba zinaelekea kuanguka lakini wameshindwa waende wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba baada ya kupata hayo majibu mazuri kwa mwaka huu tunaweza kumaliza hilo tatizo la wananchi ambalo limewasumbua kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na mimi naungana na wenzangu kusema naipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri ambayo inaifanya, na ninaendelea kusema tupo pamoja na ni jukumu letu sisi kuendelea kuisaidia ili waendelee kutekeleza majukumu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE.VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia machache kwenye hii Wizara yetu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya. Natambua wako baadhi ya watu wanabeza yale mafanikio yanayopatikana, lakini hii ni kwa sababu tu kwamba kila mmoja ana uhuru wa kutoa mawazo yake, ndiyo maana anaweza kuzungumza hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais, kwanza ya kukusanya mapato, lakini na kusimamia mapato hayo, hiyo tu inaonesha kwamba Rais wetu amedhamiria kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Hata nilikuwa napitia hiki kitabu chake, Mheshimiwa Waziri, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu; moja, nataka tu kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kuhusiana na Kiwanda cha MUTEX cha Musoma. Kama unakumbuka, kiwanda hiki tumekizungumza kwa muda mrefu, toka mwaka 2005 nazungumzia hatima ya wafanyakazi waliokuwa wa Kiwanda cha MUTEX. Wale wafanyakazi baada ya kile kiwanda kubinafsishwa, hadi leo hawajalipwa haki zao. Kwa hiyo, wengine wako pale, hawana namna ya kuishi. Sasa Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hili tumeshalizungumza wote, kesho namsubiri tu kwenye shilingi, kama hajatoa majibu sahihi, basi sina namna ya kuweza kuiachia shilingi yake. Hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni hii Idara au Shirika letu la Viwango (TBS). Sasa hivi huko mjini kuna msako mkubwa unaoendelea na wanafanya kazi ya kuharibu zile bidhaa zote ambazo hazikukidhi viwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja; zile bidhaa zote ni bidhaa ambazo zinapita katika njia halali, lakini hawa watu wetu wa TBS wanao wawakilishi kule kutoka kwenye nchi husika ambao wana-certify kwamba zile bidhaa zina haki ya kuingia nchini. Sasa zikishafika humu, mtu kalipa na ushuru lakini kinachofuatia, tunasema hizo bidhaa zote zinateketezwa, yakiwemo mfano, mabati na bidhaa nyingine kama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati mwingine unajiuliza, hivi kweli hilo bati hata kama basi makosa yameshafanyika, hilo bati ni gauge labda tuseme 34 badala ya 32, hivi ukililinganisha na nyasi, ni lipi bora? Kwa hiyo, nilidhani unahitaji utueleze una mikakati gani kuhakikisha kwamba zile bidhaa tunazizuia kule kule, kuliko vile ambavyo Watanzania tunaziingiza ndani, halafu zinakuja kutupatia hasara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, naomba nizungumzie suala la viwanda. Ni kweli kwamba hii nchi uchumi wake unaweza ukajengwa na viwanda. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri mwenyewe amesema tunavyo viwanda vya aina tatu; viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa.

Waheshimiwa Wabunge wenzangu, mimi binafsi, nisingependa sana tuka-support hivi viwanda vikubwa na ninazo sababu za kimsingi ambazo nasema ni vizuri nguvu zetu tukazielekeza kwenye viwanda vidogo. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri kwenye page ya tisa, yeye mwenyewe ametoa ushahidi hapa akasema, katika Tanzania asilimia 99.5 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeangalia hata katika nchi nyingine, mfano Kenya ni asilimia 98, Malaysia asilimia 97, Ujerumani asilimia 99 pamoja na nchi nyinginezo. Kwa hiyo, huo tu ni ushahidi tosha ambao unadhihirisha kwamba kumbe tunahitaji nguvu kubwa zaidi tuelekeze katika vile viwanda vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuzungumzia viwanda vidogo bila kuzungumza habari ya SIDO. Kwenye page ya 68 Mheshimiwa Waziri amesema hivi; “Shirika la SIDO ndiyo Taasisi ya Serikali yenye thamani ya kuendeleza viwanda vidogo nchini.” Sasa kama hivyo ndivyo, Mheshimiwa Waziri ameizungumzia SIDO nusu page, lakini tunakubaliana kwamba asilimia 99 ya viwanda vya hapa nchini vinapaswa kujengwa au kusaidiwa na SIDO. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba hebu tuisaidie SIDO, tuipe uwezo ili iweze kusaidia hivi viwanda vidogo vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie tu jambo moja, kwamba asilimia kubwa ya kazi inayopaswa kufanyika katika viwanda, ni suala la packaging. Labda nitoe mfano mdogo; ukienda hapo sokoni, kuna ile asali imeandikwa “Asali ya Pinda,” tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mstaafu kwa kazi nzuri aliyofanya. Robo ya bei ya ile asali ni sawasawa na lita moja ya asali inayotoka Tabora. Hiyo yote ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu ya packaging. Kwa hiyo, kumbe tukiendelea kuwasaidia hawa SIDO, maana yake ni kwamba watasaidia watu wetu wengi; kwanza, katika kupata mafunzo ya packaging na zile bidhaa karibu nusu tutaendelea kuzitumia hapa kwetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naendelea kushauri zaidi kwamba Mheshimiwa Waziri tuangalie uwezekano wa kuendelea kuisaidia SIDO na kuijengena uwezo. Tena kwa yale mafunzo ambayo wanayapata, yataleta tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, juzi tuliona Rais wa Afrika Kusini alipokuja hapa, alikuja na wafanyabiashara wasiopungua 80, lakini kwetu sisi jambo hilo hatulifanyi. Ni ukweli usiopingika kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wafanyabiashara ambao tunawafahamu elimu yao kama wameenda sana, ni elimu ya sekondari. Kwa hiyo, ni kwamba viko baadhi ya viwanda vingi wangeweza kuvileta, lakini kwa sababu ya ile exposure ambayo wangesaidiwa, wangeweza kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kubwa, leo Tanzania hakuna incentives kwa ajili ya viwanda vidogo, isipokuwa ipo kwa ajili ya viwanda vikubwa. Kwa hiyo, nadhani hilo nalo Serikali ilipaswa iliangalie, ione namna ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hii Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba aliyetangulia amesema hatupaswi kupongeza, lakini wanasema usiposhukuru kwa kidogo, hata kwa kikubwa hutashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo imefanywa na Wizara hasa ya kuondoa hizo tozo ambazo ndizo kero kubwa kwa wananchi wetu, ni kazi nzuri ambayo inahitaji kupongezwa. Vilevile naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa nzuri. Taarifa nzuri kwa maana gani? Wizara imeendelea kuzungumza aidha madhaifu au mafanikio, yote wameendelea kuyaweka bayana. Hii siyo kwa sababu nyingine; wamefanya hivyo ili waweze kupata ushauri. Mheshimiwa Waziri, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, ninachohitaji tu kusema, mfano ukisoma kwenye ukurasa wetu wa nne unasema, kilimo kinachangia asilimia 65 ya ajira; lakini ameendelea kusema, kwenye upande wa chakula kilimo kinachangia asilimia 100 na kwenye pato la Taifa kinachangia asilimia 29. Hii ameisema kwa sababu ya kuonesha hali halisi na umuhimu wa kilimo. Tunapokuja kwenye ukweli ni kwamba kwa kweli Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Wizara ambayo haikupewa fedha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kupitia kwenye hiki kitabu, ukiangalia pale page number 27 na 28, kwenye miradi ya maendeleo ya mwaka 2016/2017, zile fedha za maendeleo zilizokuwa zimetengwa, shilingi bilioni 800, zilizotolewa ni 4% peke yake, kwa maana ya shilingi milioni
280. Fedha za wafadhili ndiyo zimetoka kidogo kama shilingi milioni 900 ambayo ni asilimia 12. Kwa hiyo, hii tu inaonesha kwamba ni kweli tuna changamoto kubwa kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia, leo sisi hasa watu wa Kanda ya Ziwa tunalia sana tatizo la kilimo kwa maana hatuna chakula. Siyo kwamba ni wavivu lakini ni kwamba tunalima, tukishalima kwa sababu ya kukosa maji, kile chakula kinakufa. Bahati nzuri ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, ukipita tu pale Magu utawaona wako pale vijana wa Kisukuma wanahangaika na vi-pump vya maji, tena vile vya petrol, vi-pump vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe kinachopaswa kufanyika pale ni kwamba, ukiangalia kwenye mabonde kama haya tuliyonayo mengi, ni kwa nini basi tusianzishe zile irrigation scheme tena kwa utaratibu rahisi tu, tunatangaza tender kama tunavyotangaza tender za barabara? Nani anataka hizi hapa ekari 3,000 aje afanye irrigation! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ya kuwalipa, ule mpunga wenyewe kama ni mpunga ambao ukiangalia mchele una soko kubwa Kenya, Uganda, Rwanda na tuna soko kubwa la ndani. Kwa hiyo, ni kwamba wale wakulima wenyewe wataweza kulipa zile gharama za kuendesha shamba lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya maeneo tuliyonayo yako mengi. Nilidhani tu kwamba kupitia ile Benki ya Kilimo ni vizuri basi tukaweka mkakati mahsusi kwa ajili ya kilimo cha irrigation na hii itatupunguzia adha ya chakula; hii ambayo kila leo tunaipigia Serikali kelele kusema Serikali ilete chakula. Tunaamini kwamba Serikali kwa majukumu iliyonayo na kwa shughuli ilizonazo, fedha za kuweza kutuletea chakula hazipo. Kwa hiyo, nilidhani kama Mheshimiwa Waziri atauchukua huo ushauri, atakuwa ametusaidia katika upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumze kidogo kuhusu uvuvi. Sisi pale kwetu Musoma Mjini tunavyo viwanda visivyopungua vitano vya samaki. Kwa taarifa yako na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri anafahamu, vile viwanda vyote vimekufa. Vile viwanda vimekufa siyo kwa sababu nyingine, ni kwa sababu ya uvuvi haramu, wale samaki wameisha, vile viwanda kwa Musoma Mjini vilikuwa vinachangia uchumi kwa kiasi kikubwa sana, lakini siyo Musoma tu, hata Mwanza vile viwanda vya samaki vimekufa, hata kule Bukoba vile viwanda vya samaki vimekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi nini kifanyike? Njia pekee ni kwamba lazima uvuvi haramu uendelee kupigwa vita. Mheshimiwa Waziri yeye anao ushahidi, pale kwetu Musoma Mjini bahati nzuri tunaye DC mmoja anaitwa Anney Vincent. Ni DC ambaye hata Mheshimiwa Waziri anajua amefanya kazi nzuri sana. Kwa Musoma Mjini, uvuvi haramu haupo; lakini sasa cha ajabu ni kwamba ukiondoka tu pale Mjini, ukianzia Bunda na kuelekea kwenye maeneo mengine, ule uvuvi haramu unaendelea kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ndio hivyo, maana yake ni kwamba hata ile juhudi anayoifanya ya kuhakikisha kwamba huu uvuvi haramu unaisha, maadamu anafanya katika eneo moja, tafsiri yake ni kwamba hao samaki watakuwa wanaenda maeneo mengine na wataendelea kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa kazi ile iliyofanyika, mpaka hivi sasa, angalau kwa pale mjini samaki tunaokula ni wale wazuri. Sasa kinachotakiwa kufanyika ni kumwangalia mtu kama huyu tukampa overall ya Ziwa Victoria akahakikisha kwamba anapata resources. Naamini wale wenye viwanda watachangia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanazuia uvuvi haramu. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, tunadhani kwamba itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine dogo, hebu tuanzishe vile vikundi vinavyofuga samaki kwa njia ya caging ambapo wakifuga vile wale wenyewe watakuwa walinzi wakubwa wa wale wanaovua uvuvi haramu. Kwa kufanya hivyo, itatusaidia sana kuhakikisha kwamba hilo tatizo la uvuvi haramu linaisha, viwanda vyetu vinafufuka na uchumi wetu unakua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niguse kwenye upande wa ufugaji. Kwa kweli kwenye ufugaji bado hatujafanya kitu. Hatujafanya kitu kwa sababu gani? Tunazo ranch nyingi, nimeangalia hapa kwa haraka haraka, tuna Sao Hill, Mabuki, Kitulo mpaka ranch yetu ya NARCO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisoma kwenye ukurasa wa 110 pale, Mheshimiwa Waziri mwenyewe anasema kwamba kwa mwaka 2016 tumeweza kuzalisha mitamba 634. Sasa hizi ranch zote zina uwezo wa kuzalisha mitamba 634 peke yake? Tafsiri yake ni kwamba zile ranch tumewapa watu wachache wafaidike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenyewe bahati nzuri ni mfugaji, unapozungumza mitamba 634 hiyo, ukienda kwenye zizi langu pale kwenye wale ng’ombe nilionao, unawapata hao mitamba 634, tena mitamba wazuri na wa kisasa. Hata siku moja niliweza kuleta ng’ombe wangu hapa Dodoma machinjioni, bahati nzuri nikamwalika Mheshimiwa Naibu Waziri, alifika akawaona. Ng’ombe mmoja nilikuwa nauza siyo chini ya shilingi 1,200,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumbe tunachohitaji kufanya katika kusaidia mifugo, ushauri wangu ni kwamba hizi ranch nyingi tulizonazo, hebu tuwachukue wale wafugaji wanaofanya kazi ya kunenepesha. Hata ukipita pale Mwanza baada ya Coca Cola hapo njiani utakuta Wasukuma wapo pale wanahangaika, wanalisha mashudu, hakuna eneo la malisho. Ukiangalia hizi ranch nyingi tulizonazo hizi, zimekaa tu. Hivi kwa nini tusiwapangishe waka-lease, halafu wakaweza kufuga mifugo ya kutosha, mingi tukaweza kuendelea?

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu inayohusiana na bomba la mafuta kutoka Uganda mpaka Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kila jambo huwa linakuwa na mapingamizi, lakini tuseme tu kweli kwamba kwa kazi hii aliyoifanya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba bomba hili tunaweza kupewa huu mradi ni kazi ambayo anastahili kupongezwa sana, kwasababu kwanza ni mradi ambao umechukua muda mfupi sana, lakini wote tunafahamu ni kwa kiasi gani wenzetu wa Kenya walivyokuwa wanautaka mradi huu kwa udi na uvumba, lakini imekuwa bahati nzuri tuimeweza kuupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako manufaa ya wazi wazi ambayo yatatokana na mradi huu maana hili bomba litakapojengwa maana yake ni kwamba hata barabara katika maeneo hayo yote zitapita na watu wetu ambao wako katika maeneo hayo watafaidika zaidi katika biashara zao mbalimbali, watafaidika na ajira ambazo zitatokana na mradi huu. Hii ikiwa ni pamoja na Serikali itaendelea kupata kodi katika mradi huu, lakini na ile tozo ya upitishaji wa mafuta kwa sababu lile bomba linalopita katika nchi yetu, kwamba tuta-charge kile kitu kinaitwa throughput ambayo kwetu sisi vilevile tutafadika nayo mbali na kodi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba katika hili bomba linaliopita kama ingewezekana, maana nimeambiwa kwamba bomba hili tunalijenga sisi, Serikali ya Uganda pamoja na Kampuni za mafuta ikiwemo Total. Basi kama tungeweza ni vizuri na sisi nasi kama Serikali tungeongeza nguvu zaidi au mtaji mkubwa ilio kwenye lile gawiwo tutakalokuwa tunapata basi tuweze kupata kiasi kikubwa zaidi kuliko ambacho tunachoweza kupata kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, jambo lingine ambalo limenifurahisha ni pale ambapo Serikai iliamua kuweka nafasi kubwa ambayo itapitisha bomba la gesi, ikiwezekana na miundombinu mingine labda bomba la mafuta ghafi lakini ikiwezekana na bomba la gesi

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme, kama inawezekana hebu Serikali ione uwezekano wa kupitisha bomba la mafuta kutoka Tanga litakalokwenda sambamba mpaka kule Uganda. Hilo bomba kama endepo litakuwepo vilevile litakuwa na manufaa makubwa. Kwanza, kama ni gharama za fidia tutakuwa tumeshalipa kwa hiyo tayari eneo tutakuwa nalo. Hata hivyo leo itoshe tu kusema kwamba wenzetu majirani mafuta yanafika Mombasa lakini wanaweza kuuza Uganda, Rwanda, Burundi na hata DRC kushinda sisi siyo kwa sababu nyingine, ni kwa sababu wana bomba la mafuta linalotoka Mombasa mpaka Kisumu; Mombasa mpaka Eldoret.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu na sisi nafasi hii tumeipata, ukweli wa ni kwamba ukiweka bomba kutoka Tanga la mafuta likaenda mpaka Uganda maana yake sisi tutakuwa tumeshaminya zaidi ya kilometa 400, tutakuwa tuna kilometa 400 chini ya wao. Kwa hiyo tafsiri yake ni kwamba gaharama za mafuta kufika kwenye hizo nchi zitakuwa ni ndogo kwahiyo vilevile tutaendelea kufaidika zaidi kuliko wao kwa hiyo, hiyo kwetu itakuwa competitive advantage kama nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitahadharishe tu juu faida ambayo tunayo lakini hatuiangalii sana, kwamba sambamba na hili bomba la mafuta gahfi tulilonalo tunayo miradi kama hii. Kwa mfano liko bomba hili la TAZAMA ambalo linatoka Dar es salaam mpaka kwa wenzetu kule Zambia pale Kapirimposhi na Ndola.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili bomba hatulitumii sana, ni bomba la mafuta ghafi pamoja na mafuta masafi, lakini cha ajabu ni kwamba tunaacha kutumia lile bomba lakini malori mengi yanapitisha mafuta kupeleka huko na mtokeo yake ni kwamba kwanza yanaendelea kuharibu barabara lakini na gharama za uendeshaji nazo zinakuwa kubwa. Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia namna tunavyoweza kutumia hii miundombinu ambayo kwangu mimi ninaamini kabisa kwamba tukiitumia vizuri inaweza ikatuletea faida zaidi; ukilinganisha kwamba kwa Tanzania kijiografia tumekaa vizuri, kwamba inatupa nafasi nzuri zaidi ya kufanya biashara na wenzetu wanaotuzunguka kuliko wenztu ambao wako pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bada ya kusema hayo, na mimi naunagana na wenzangu kwa kuipongeza Serikali kwa kazi hii ambayo wameifanya kwa haraka, lakini niseme tu kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hili suala linalohusiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi lakini vilevile na watu wengi tumekuwa haturidhiki sana na maendeleo ya nchi hii kwa maana ya mafanikio yanayopatikana. Na mimi hili limekuwa likinisumbua sana kujua hivi shida ni nini, hasa ukiangalia kwenye hii Awamu ya Tano, ni awamu ambayo kila mmoja anakubali kwamba ukusanyaji wa mapato umeongezeka, lakini vilevile kumekuwa na nidhamu ya matumizi. Hata hivyo, bado kila ukiangalia kila upande, upungufu upo, kwenye upande wa elimu, upungufu upo; afya, upungufu upo; maji, upungufu upo; na kwenye huduma zote za jamii. Ukija kuangalia upande mwingine wa bajeti, ukiangalia awamu iliyopita na awamu hii, fedha zimeongezwa maeneo mengine zaidi ya asilimia 300, mfano kwenye afya, tulikuwa tunazungumzia chini ya shilingi bilioni 50 kwa mwaka lakini leo tunazungumzia zaidi ya shilingi bilioni 200. Hizo ni fedha ambazo zimeenda kwenye afya, lakini bado kwenye elimu na kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti wangu kuna jambo ambalo nimeona kama hatujalitambua wala hatuli- address ambalo nadhani kama tusipolizungumza basi tutaendelea kuathirika. Hayo maendeleo tutayategemea na bado hatutayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu ninaona kama tunahitaji ku-address suala la uzazi wa mpango. Tunahitaji ku-address suala la uzazi wa mpango kwa nini? Nitoe tu mifano michache; nakumbuka mfano mwaka 2016 pale kwenye Jimbo langu kulikuwa na uhaba wa madawati, tukatengeneza madawati yasiyopungua dawati 3,000, lakini mwaka 2017 tu mwishoni tunaambiwa kulingana na wanafunzi ambao wameendelea kujiunga, bado hizo dawati tunaambiwa tena zinatakiwa karibu dawati 3,000 nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwenye shule yangu moja tu nakumbuka kule nakotoka, shule ya Nyakato, lile darasa la kwanza peke yake wamejiunga wanafunzi 800 kwenye darasa la kwanza. Kwa hiyo, ukiangalia kutokana na ongezeko la watu kila mwaka, kwa hiyo, ni kwamba chochote kile tunachokifanya lazima upungufu uendelee kuwepo. Kutokana na hali hiyo, ndio maana najiuliza, labda Mheshimiwa Waziri atatusaidia kwamba hivi ni kwa nini hili suala la uzazi wa mpango hatutaki kuli-address?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukijaribu kuangalia katika nchi za wenzetu, ukitafuta nchi yoyote ile ambayo inaonekana imepiga hatua au inaendelea, unakuta watoto wadogo wanaozaliwa ni wachache kuliko watu wazima. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema kwamba nadhani tukiendelea na hali hii na kwa kutambua kwamba nchi ni ile ile, maeneo ni yale yale, kwa hiyo, kila siku itakuwa tuna upungufu mkubwa, pamoja na juhudi za Serikali ambazo itakuwa inafanya, lakini bado shida yetu itakuwa iko pale pale na bado changamoto zitaonekana kuwa bado ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilidhani Serikali inahitaji ilifanye ni suala la bima ya afya. Ukiangalia hasa katika nchi nyingine za kiafrika, mfano ukienda hata Rwanda hapo, suala la bima ya afya ni compulsory.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inajitahidi kupeleka vituo vya afya na zahanati, lakini kulingana na idadi kubwa ya watu tulionayo, kila leo zile huduma za afya unakuta ni mbovu, na kwa sababu ni mbovu ndiyo maana sisi kama Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa kawaida tunaendelea kuona tu kwamba hakuna ambacho hii Serikali ya Awamu ya Tano inafanya, kwa sababu bado upungufu ni mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nadhani watu wengi zaidi sasa tumejitahidi kuongeza kuzaa, kwa sababu leo una uhakika kwamba mama akipata ujauzito hata chandarua atapata bure kule kwenye zahanati. Akishajifungua mpaka miaka mitano mtoto atatibiwa bure. Akitoka hapo, kule shule ataenda atasoma bure. Kwa hiyo, mzazi kama mzazi wala haoni shida yaani anaona jukumu lake yeye ni kuzaa tu, akishazaa, Serikali itaendelea.

Kwa hiyo, ndiyo maana nasema lazima tufike mahala tuamue na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuendelea. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri sana ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kubwa Musoma Mjini kwani wananchi waliombwa kupisha eneo la Jeshi katika eneo la Makoko na wameendelea kupata ahadi ya kulipwa fidia. Sasa ni zaidi ya miaka kumi hadi leo bado hawajapata chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakumbuka wale wananchi walituma mwakilishi wao. Na mimi nilimleta kwake na tukakaa pamoja akaahidi kwamba katika bajeti hii hao wananchi wa Musoma watalipwa fidia. Naomba kauli yake hapa Bungeni, kwani wamehangaika kwa muda mrefu sana ili suala hilo tulimalize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Waziri wa Ujenzi. Awali ya yote, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini na kwa namna ambavyo ameweza kujipambanua katika kitabu hiki maana miradi yote inaonekana na iko wazi, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nitaenda kwa haraka sana. Namba moja, nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri alikuja Musoma na kama alivyokuwa ametuahidi Mheshimiwa Rais kujengewa uwanja wa ndege zoezi hilo limeanza na nimeona kwenye kitabu chetu hiki ziko kama shilingi bilioni 11, hongera kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu moja tu kwamba, kama Mheshimiwa Waziri alivyokuja tukazunguka katika maeneo yale kuna nyumba kama 106 ambazo zinahitaji fidia. Naomba atuambie lini tutawalipa hawa watu fidia ili waweze kuanzisha maisha yao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla ya hizi nyumba 106 tulikuwa na mpango wa kuchukua eneo kubwa zaidi ambalo lilichukua zaidi ya nyumba 300. Zile nyumba zote ziliwekewa X na kwa sababu sasa tulipunguza tukarudi nyumba 106, naomba Mheshimiwa Waziri awaambie watendaji wake waende kufuta zile X kwa sababu nyumba zile watu wamehama na hawawezi kupanga tena wakiamini kwamba wakati wowote zitabomolewa. Mbaya zaidi hata benki sasa, wale wenye zile nyumba zingine hawakopi kwa sababu mabenki yanaamini kwamba nyumba zile nazo ziko katika mpango wa kuondolewa. Kwa hiyo, hilo nadhani ni vizuri likafanyika kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni barabara ya Nata – Mugumu – Klein’s Gate - Mto wa Mbu. Barabara hii tumekuwa tukiizungumza kwa kipindi kirefu lakini safari hii hata kuonyeshwa kwenye kitabu hiki Mheshimiwa Waziri hajaonyesha. Kwa hiyo, naomba tufahamu kama barabara hii imeondolewa maana ilikuwa inajengwa katika kiwango cha lami, kama imeondolewa basi ni vizuri tukajua kuliko kukaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la muhimu kwetu ni ile barabara inayotoka Musoma Mjini – Makojo. Barabara hii tunashukuru kwamba angalau safari hii imepata kama shilingi bilioni tatu lakini ina zaidi ya miaka 10 kila leo ni upembuzi yakinifu sijui fedha hizi ndiyo zitaanza lami au bado tuko kwenye upembuzi yakinifu. Kwa hiyo, hilo nalo ningependa kupata maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la reli ya kutoka Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Mimi ile naingia hapa Bungeni mwaka 2005 kulikuwa na mpango huu wa hii reli ya kuja Musoma, lakini mpaka leo hivi tunavyozungumza kila siku inapewa tu fedha ndogo mfano kama safari hii nimeona kuna shilingi bilioni mbili. Sasa ni zaidi ya miaka 15 suala la upembuzi yakinifu bado linaendelea. Napenda Mheshimiwa Waziri atoe maelezo ya kina kuhusiana na hiyo reli ya Tanga – Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho linahusiana na hawa wakandarasi wetu wa ndani. Kwa kweli wazo na mipango ya Serikali ni mizuri kuwawezesha wakandarasi wa ndani, lakini hawa wakandarasi wa ndani kwa utaratibu tunaoenda ni kweli kwamba hawawezi kukomaa. Mfano, ukiangalia barabara ya Makutano - Nata ni zaidi ya miaka mitano inajengwa katika kiwango cha lami lakini haisogei. Kwa hiyo, wakati mwingine tunakuwa na mashaka kwamba wale wakandarasi ndiyo hawana uwezo kwa maana kwamba ndiyo hawajengi lakini ukiangalia kwa kiasi kikubwa inachangiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachangia kwa sababu gani? Kama kweli tumedhamiria kwamba tunahitaji kuwa-empower ni lazima hata pale wanapoomba zile advance payment tuwe tunawapa kwa wakati. Kwa hiyo, anapojikuta kwamba akiomba advance payment hatuwezi kuwapa na inachukua muda mrefu na tunatambua kwamba hawana uwezo hayo ndiyo matokeo kwamba mradi mmoja unachukua muda mrefu na matokeo yake badala ya kumsaidia mkandarasi yule tunaendelea kumdhoofisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie sana suala la namna ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hii hotuba ya Waziri wa Mipango na Fedha. Kwanza, nashukuru kwa hotuba nzuri ambayo hasa ukiangalia imelenga kuwasaidia sana watu wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mambo mawili ya muhimu ambayo ndiyo kama maneno yangu ya utangulizi. Moja, natambua kwamba Serikali hii ni Serikali ya wanyonge, ni Serikali ambayo ingependa kuendelea kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, wala hilo halina ubishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuulize tu Mheshimiwa Waziri wa Mipango; swali la kwanza ni suala la watumishi waliokuwa wa kiwanda cha MUTEX. Hao watumishi toka waachishwe kazi ni zaidi ya miaka 20. Toka walipoachishwa kazi wamekuwa na madai yao ya kimsingi. Vile vile hawa watumishi wametoka katika mikoa mbalimbali. Wote mnafahamu kwamba fedha hizo zilitengwa, lakini hawajalipwa hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikilisema hili hata nakumbuka mwaka huu mwanzoni Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Musoma. Alipokuja, wananchi wa Musoma walimpokea kwa mabango, akaahidi kwamba atahakikisha wamepata mafao yao. Mheshimiwa Waziri anafahamu, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekwenda kwake mara nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii Serikali ya wanyonge inashindwa nini kumaliza tatizo dogo hili la watumishi ambao waliitumikia Serikali hii kwa uwezo wao wote katika kipindi chao kikubwa, lakini mpaka leo wanataabika wanatolewa kwenye nyumba hata walizokuwa wanaishi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati wa uhitimishaji kusema kweli, hili lazima Mheshimiwa Waziri alitolee maelezo ya kina ambayo wale wananchi labda yanaweza yakawatia moyo, ambayo yataonesha hizo fedha zao kama safari hii wanaweza kuzipata ili waendelee na maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine ni suala la kuwaondoa kazini watumishi hewa. Hakuna mwenye tatizo na hilo, lakini namna ya watumishi wengine jinsi walivyoondolewa. Ukiangalia katika Majimbo yetu mbalimbali, wako baadhi ya watumishi ambao waliondolewa tu kwa sababu ya upotoshwaji. Mfano, kuna mtu ambaye alisoma darasa la saba, baada ya hapo akaajiriwa, akaendelea kujiendeleza, akapata Certificate, akapata Diploma, mwingine mpaka akapata Degree. Wakati ule wanajaza zile taarifa zao binafsi, alipofika kwa Afisa Utumishi pale akaambiwa wewe sasa elimu yako siyo ya darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu, elimu yako siyo ya darasa la saba andika kwamba una elimu ya kidato cha nne. Leo huyo tumemwondoa kazini, tumeacha mtu wa darasa la saba. Hivi kweli ukiangalia tu katika ule utendaji wa kawaida, umemwacha wa darasa la saba halafu umetoa mtu ambaye ni graduate. Hao leo wanahangaika mtaani, hawana pa kwenda, wala hawajui wafanye nini, wala hawajui hatima ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani hii Serikali yetu ambayo ni Serikali sikivu, hebu itoe majibu sahihi na ione namna gani ya kuwasaidia hawa watu ambao wengi wao walipotoshwa. Badala ya kusema kwamba amemaliza darasa la saba akaambiwa kwamba kwa sababu amejiendeleza, basi elimu yake ni zaidi ya darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda na watu wengi kusema kweli tunalizungumzia ni kwamba nchi yetu kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri, uchumi wetu umekua. Tukija kwenye hali halisi katika kuangalia wananchi wa chini, wale wananchi wa kawaida katika maisha yetu ya kawaida, huo uchumi hatuuoni. Hiyo nami nakubaliana kwamba inawezekana uchumi wetu umekua katika zile sekta ambazo haziajiri watu wengi. Sasa kwa sababu hiyo, ndiyo maana kila mara tukiangalia hali ni ngumu. Sasa kwa sababu, sisi Wabunge jukumu letu ni ushauri, nami napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri Mpango, kama ataona ushauri unafaa, basi waweze kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, sifahamu ni kwa nini Watanzania wengi hatupendi kulizungumza hili. Kusema kweli suala la uzazi wa mpango ni suala ambalo halikwepeki kama tunahitaji kukuza uchumi wetu. Kwa sababu, ukiangalia fedha nyingi sasa pamoja na kuzipeleka kwenye huduma za jamii, lakini inaonekana kule nako hatujafanya kitu. Mfano, ukiangalia kwenye afya peke yake zimetoka shilingi bilioni thelathini na kitu, leo tunazungumzia shilingi bilioni mia mbili na kitu, lakini ukienda kule hospitali, bado dawa hazitoshi, bado huduma za afya hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule, mfano kwenye shule moja, katika Kata yangu moja, darasa la kwanza peke yake wanaandikishwa watoto wasiopungua 800. Kwa hiyo, ni kwamba hata kama tutaongeza bajeti, bado maisha yataendelea kuwa magumu kwa sababu fedha nyingi tunaendelea kuzimalizia kwenye huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba hebu tuone namna ya kuli-address. Maana katika nchi nyingine, asilimia kubwa ya watu ni wale wenye manpower ya kufanya kazi, lakini katika Tanzania asilimia 60 wote ni watu ambao ni tegemezi. Kwa hiyo, tunadhani
kwamba bila kuli-address hili litaendelea kutupa tabu na kila siku fedha zitaonekana hazitoshi na uchumi wa nchi bado utaendelea kuwa ambao siyo mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni ushauri, wote tunakubaliana kwamba siyo chini ya 60% ya Watanzania ni wakulima. Kama hivyo ndivyo, nini kifanyike?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie yale mazao ambayo kwanza masoko yake yanapatikana. Nami nije na mfano wa zao moja tu la mpunga. Zao hili ukiangalia katika nchi zote zinazotuzunguka, ukienda Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo na Zambia ni watu ambao wanahitaji mchele. Kwenye suala la kilimo cha mpunga kinahitaji maji, mbolea na hakina majira. Sasa kumbe kitu ambacho tungeweza kufanya, tungeweza ku-identify katika mabonde tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewapeleka huko JKT wakawapeleka vijana huko, wale vijana wakafanya kazi, watavuna ule mpunga. Kwa hiyo, tungekuwa na masoko ya uhakika ambayo tunadhani kwamba wale vijana watakuwa wamejipatia ajira na ni kwamba maisha yao yataboreka kuliko hivi ambavyo tunaendelea kuhangaika na bado maisha yetu au maisha ya watu wetu yanaendelea kuwa magumu. Kwa hiyo, kama tutaona ni jambo jema, basi na lenyewe tukilichukua ni imani yangu kwamba litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naona kama bado hatujajipanga vizuri sana ni elimu. Leo ukiangalia kwenye upande wa elimu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, nimalizie tu kwa kusema kwamba, naomba mwisho Serikali ione uwezekano wa kulipa wale Wazabuni wote ambao wamei-supply Serikali, wametusaidia, lakini mpaka leo wale watu wanadai na hawajawahi kulipwa. Kwa hiyo, Serikali iweze kuwalipa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hii hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya yeye na wasaidizi wake kwa maana ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na viongozi wote wa Serikali. Mambo haya kusema kweli yako wazi kwa maana ya maendeleo ambayo yameendelea kufanyika hasa katika kuboresha huduma za jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nizungumzie kwanza ushahidi huo katika Jimbo langu la Musoma, kwamba ni kwa kiasi gani katika kipindi hiki kifupi huduma za jamii zimeendelea kuboreshwa sana. Leo unapozungumza upande wa elimu, nakumbuka Mheshimiwa Rais aliposema kwamba sasa elimu itatolewa bure, kiwango cha uandikishwaji wa watoto kimekuwa kikubwa sana na mpaka kimepelekea darasa la kwanza kwenye shule mbalimbali wanaenda mpaka watoto 800 kwa darasa moja badala ya yale madarasa matatu. Hiyo yote inaonesha ni kwa kiasi gani wanafunzi wengi zaidi wamejiunga katika elimu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata unapozungumza habari ya afya, mfano mwaka jana tu achana na miaka mingine tumepata shilingi milioni 400 kwa ajili ya huduma ya afya lakini tumepata zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya Hospitali yetu ya Rufaa. Kwa hiyo, hayo yote ni matokeo ya uongozi mzuri na kuwajali wananchi ndiyo maana yameendelea kujitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, hata upande wa habari ya maji, kwa Musoma Mjini tulikuwa na tatizo kubwa la maji lakini leo shida kubwa tuliyonayo ni tatizo la mabomba kupasuka shauri ya pressure ya maji. Kwa hiyo, hii yote inaonesha ni kwa kiasi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeendelea kushughulikia matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi nakumbuka katika hiki cha miaka miwili pale kwangu nimepata shilingi bilioni 12 kwa ajili ya barabara, lakini hata kwa mwaka huu tu nimepata shilingi bilioni 4. Hata ile Kamati ya Bunge iliyokuja Mjini Musoma nadhani iliweza kuona maana ilizitembelea zile barabara iliona ni kwa kiasi gani ule Mji wetu wa Musoma umekuwa mzuri kwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami. Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema tuna kila aina ya sababu ya kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mbunge wa Jimbo la Musoma nimeona nizungumzie tu yale ya pale mjini zaidi ya yale makubwa ambayo yanaonekana katika nchi nzima. Mfano leo ukipita wakati wa usiku kwenye maeneo mengi utadhani kama ni mjini kwa sababu karibu kata na miji inazo taa kwa maana kwamba umeme umesambaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwetu sisi kama nchi matumizi yetu ya umeme ni wastani wa MW 1,100 lakini umeme ambao unazalishwa sio chini ya MW 1,600. Kwa hiyo, hii tu inaonyesha ni kwa kiasi gani tumejitahidi lakini Serikali ina jukumu la kuhakikisha ule umeme unasambaa katika maeneo mengine ambayo bado hayajapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilisafiri nilipofika pale Airport saa 12.00 wakati na-board, ukiangalia ule uwanja wa ndege umepambwa kwa ndege za Air Tanzania. Katika siku za nyuma ulikuwa unakuta hata kile kibao kile kimoja tu cha Air Tanzania kilikuwa hakiwezi kuonekana. Haya yote ni mambo makubwa tuna kila aina ya sababu ya kuyasemea wala hatuhitaji kumung’unya maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wajitahidi sana kama ambavyo speed kubwa imeelekea kwenye hii reli ya mwendo kasi, mwaka jana nilisema na mwaka huu nasema, pale reli itakapofika Morogoro tu basi na vichwa pamoja na mabehewa vianze kutembea ambayo yatakuwa yanaleta abiria pale na abiria kuanzia saa 1.00 wanachukuliwa kutokea pale. Matokeo yake kila Mtanzania atakuwa siku hiyo ametoka Dar es Salaam na atalala nyumbani kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sana leo watu wa Kanda ya Ziwa wakiondoka Dar es Salaam lazima walale njiani kwa sababu ya urefu wa barabara. Kwa hiyo, tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo, ndivyo Serikali inavyoendelea kushughulikia matatizo ya wananchi wake ili waendelee kuishi kwa amani na raha mustarehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo mafanikio mengi maana nilidhani nizungumzie machache lakini niendelee kuzungumzia changamoto ambazo bado zinawasumbua Watanzania lakini na watu wa Jimboni kwangu, wa Jimbo la Musoma. Kwangu mimi pale Musoma Mjini sasa yamebaki matatizo mawili makubwa. Tatizo la kwanza Mheshimiwa Waziri Mkuu analifahamu vizuri, niendele tu kumkumbusha na hili sasa badala ya kumkumbusha wale wananchi nitawaleta katika Bunge kwake waje wamuone yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako wafanyakazi waliokuwa wa Kiwanda cha Mutex ambao malipo yao nimekuwa nikiyasemea kila leo lakini hayo malipo yamekuja kufanyika ambapo kile kiwango walichokitaa ambacho hawakupewa miaka ishirini iliyopita leo wamekuja kupewa tena nusu ya hicho. Kwa hiyo, hilo kwa kweli kwa wale wananchi ni kero kubwa, ni kero ambayo inawasumbua na kwa sababu Serikali imeahidi kulishughulikia kwa muda mrefu na mpaka leo haijalishughulikia nitawaleta wenyewe waje kuzungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni suala la kiwanja cha ndege. Tuliomba kiwanja cha ndege na Mheshimiwa Rais aliridhia na tathmini ya fidia ilishafanyika lakini mpaka leo wananchi hawajalipwa na kuna sintofahamu kama kiwanja kitajengwa au hakitajengwa. Naiomba Serikali iseme kama hakijengwi tufute zile alama za ‘X’ ili wananchi waendelee na maisha yao kama kinajengwa basi fidia ilipwe ili ule uwanja uweze kujengwa. Kwa hiyo, hilo nalo nategemea katika kikao hiki au Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itakapokuwa inajibu italijibu suala hilo ili wananchi waweze kupata taarifa za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni tatizo la ajira. Pamoja na juhudi zote ambazo tumeendelea kuzifanya za kuongeza viwanda lakini tunatambua kwamba ajira pekee au sehemu pekee itakayopunguza tatizo la ajira ni Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, mimi bado sijaona kama Serikali imeweka vipi nguvu kwenye Wizara ya Kilimo katika kupunguza tatizo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, njia pekee ni kuhakikisha kwamba tunaweka nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji. Leo ukienda katika Kanda ya Ziwa na hata katika hizi Kanda zingine, Manyara au Arusha maeneo mengi sasa leo ni kiangazi na vyakula vimekufa. Hiyo inaonesha kabisa kwamba kama tungekuwa na kilimo cha umwagiliaji nguvu zile walizozitumia wananchi leo lisingekuwa tatizo. Wananchi wamelima, mvua hazikupatikana matokeo yake yale mazao yao yanakufa. Hii inaonesha moja kwa moja kwamba yawezekana mwaka huu kutakuwa na njaa kubwa, si kwamba wananchi hawakulima ni kwa sababu mazao yao yamekufa kwa sababu ya kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza nikupongeze kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani. Nampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Lugola, pamoja na Naibu Waziri Masauni pamoja na uongozi wote wa Jeshi la Polisi na Majeshi yote kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuwatumika watanzania hongereni sana. Yako mambo ambayo ya waziwazi katika hiki kifupi tumeweza kuyaona ambayo watanzania wote naamini watakubaliana na mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja suala la ajali kusema kweli Jeshi la Polisi limezisimamia na zimepungua kwa kiasi kikubwa. Lakini kama hiyo haitoshi leo inaweza kufika saa hizi saa mbili nikaondoka hapa kwenda zangu Musoma saa mbili za usiku nikafika Musoma salama pasipokuwa na matatizo yoyote kwa sababu Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri sana. Naendelea kazi yangu ni kuendelea tu kuwaombea kwamba hebu endeleeni kufanya kazi hiyo nzuri watanzania waendelee kuishi kwa amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe mambo machache ambayo yamezungumziwa katika hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Kati ya matatizo ambayo Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani inapaswa kuyafanyia kazi imesema hapa vizuri kwenye ukurasa wa 11 kwamba Mheshimiwa Rais bilioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 400 za maaskari wetu na ni ukweli usiopingika kwamba maaskari wetu ni kati ya watu ambao maeneo yao ya kuishi si mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano pale Musoma kwamba ziko nyumba bahati nzuri baada ya kuwa nimepiga kelele toka mwaka 2005 kweli Serikali ikawa sikivu ikaanza kujenga maghorofa mawili pale ambayo yangebeba maaskari wa kutosha. Lakini nakuambia hadi leo tunavyozungumza yale maghorofa yamekamilika kwa asilimia zaidi ya 85 lakini yameshindwa kumaliziwa mara wanaiba milango, mara wanaiba mabomba ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini hizi nyumba zitakamilika ili walau wale maaskari wachache waweze kujistili kuliko wanavyoishi sasa wanaishi kwanza wengine uraiani, lakini wengine wanaishi kwenye zile nyumba za full suit ambapo wanaishi kwa tabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine Mheshimiwa Waziri wewe unafahamu kwamba pale Mjini Musoma pale ndipo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara. Kuna jengo ambalo lilijengwa toka mwaka 2013 jengo la RPC lile jengo limeishiwa kwenye basement hadi leo jengo hilo liko hapo hapo. Sasa nataka nifahamu mpango wa kulijenga jengo hili ili Jeshi la Polisi waweze kufanya kazi zao vizuri. Lakini halikadhalika askari Magereza wote bado hawana nyumba na hata maeneo yao ya kuishi si mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni mategemeo yangu kwamba Mheshimiwa Waziri haya majibu utaweza kutufafanulia ili watu wa Musoma waweze kujua namna tunavyoweza kuwasaidia katika haya majengo yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo moja kubwa ambalo Mheshimiwa Waziri binafsi nilishalileta kwako, na nilishakuja na Mkurugenzi wa maji, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara pamoja na Magereza Polisi wenyewe wanadaiwa zaidi milioni 850 za maji na Magereza wanadaiwa zaidi milioni 360.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matokeo yake katika baadhi ya maeneo mengi ya Musoma Mjini kwenye zile Kata za pembezoni kama Rwamlimi, kama Bweli kule Kwanga mpaka kule Makoko tunakosa maji kwa sababu ziko fedha ambazo Jeshi la Magereza pamoja na Polisi walipata huduma lakini ni kwamba wameshindwa kulipa n hizo fedha kama zingepatikana zingetusaidia katika kuboresha maji katika Mji wetu wa Musoma. Sasa ningependa kufahamu mpango wa kulipa haya madeni katika bajeti hii utaweza kutulipa ili walau haya matatizo yaweze kupungua. Pamoja na hayo madeni baada ya kuwa yamelipwa ni imani yangu kwamba yatatusaidia sana katika kuboresha Mji wetu wa Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nichangie vilevile kidogo kwenye upande wa Jeshi la Magereza. Nashukuru na tumeangalia pale katika page 28 Mheshimiwa Rais alifanya kazi kubwa ya kuweza kusema kwamba sasa Jeshi la Magereza lazima wajitosheleze kwa chakula na akaonesha kwamba sasa hivi wanalima mnalima kama eka 4,000 na kitu sasa zitalimwa mpaka eka 12,000 na kusema kweli hii ni kazi nzuri ni kazi ya kupongezwa na niseme tu kwamba Jeshi la Magereza wakijipanga vizuri tatizo la chakula hata kwenye Taasisi zetu za Serikali kama shule hilo tatizo litaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kusema kweli mtu anapofungwa anafungwa mwaka mmoja anafungwa miaka mitatu kulingana na speed ya maendeleo, akitoka kule ndani tunategemea kwamba akienda kule ndani apate nafasi ya kujifunza mambo mengi ambayo ni pamoja na kilimo ni pamoja na ufundi. Sasa tunapowafunga tu na kuwaweka kule ndani akitoka huku nje baadhi ya wafungwa wengi wakiachiwa huru wanatamani warudi ndani ya gereza kwa sababu sasa wanakuta huku nje huku maisha yameenda speed mambo mengi hawayafahamu sasa wanaona kwamba ni afadhali tena arudi magereza kwa sababu kule magereza anapata chakula cha bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kushauri kwamba mbali na suala la kuwafunza kilimo, vilevile Magereza wanayo nafasi kubwa ya kujifunza mafunzo mbalimbali yanayoweza kuboresha maisha yao. Lakini watakapotoka kule sasa watakuja kwanza wamejirudi lakini watapata mahala pa kuanzia kuliko vile wanavyofungwa, wanakaa mle ndani akitolewa hapo anaenda kusafisha mtalo matokeo yake anatoka kule pasipokuwa na ujuzi. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tunapokuwa tunawapeleka mtu anapofanya makosa na akapelekwa Magereza tafsiri yake ni kwamba tunataka ajirudi vilevile ajifunze na baada ya hapo aje kuwa raia mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba tukiendelea kuwasaidia hawa Jeshi la Magereza wanaweza wakafanya kazi nzuri zaidi ya kuzalisha na kukuza uchumi wa nchi hii. Baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nitumie nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Kamati ya Miundombinu pamoja na Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nawapongeza sana watu wa miundombinu na naipongeza sana Serikali kwa namna ilivyoweza kutoa fedha za kutosha kuhakikisha kwamba barabara na bandari zetu nyingi zinaweza kufanya kazi. Ndiyo maana kwa ushahidi ukiangalia katika bajeti iliyopita ilikuwa shilingi trilioni 4.2 lakini kwa mwaka huu tumeenda almost 4.9. Hongereni sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mafanikio makubwa ya Serikali lakini bado yapo mambo ya kimsingi ambayo yanahitaji kuangaliwa na hasa katika kipindi hiki. Wote tunatambua hiki ni kipindi ambacho katika nchi nzima mvua nyingi zimenyesha na kutokana na hali hiyo, barabara nyingi sasa zimeharibika kwa maana ya miundombinu. Kutokana na hali hiyo, hata zile barabara ambazo zilikuwa zimejengwa ambazo zilikuwa na hali nzuri zimeendelea kuharibika.Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupata ufafanuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu kwamba hivi wamejipangaje? Maana leo ukienda kwa mfano kule Musoma Jimboni kwangu nadhani mafuriko yameongoza kuliko mahali pengine popote pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye zile Kata kama za Nyakato, Bweri, Kitaji mpaka kwa bahati mbaya sana kumetokea maafa katika Jimbo langu kutokana na haya mafuriko, sasa ile miundombinu yote imeharibika. Napenda kufahamu Kamati ilijipangaje katika kusimamia Serikali kuhakikisha kwamba katika hiki kipindi kifupi tunarudisha ile miundombinu iliyokuwepo katika hali yake maana vinginevyo hali itakuwa mbaya zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kulielewa sambamba na hilo ni kwamba Serikali imekuwa na utaratibu mzuri wa kutenga fedha ambazo zinatengeneza hasa barabara katika kiwango cha lami. Fedha hizi zimekuwa zikipatikana aidha kutoka Serikalini na nyingine kupitia misaada kutoka maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake kwenye zile barabara za Manispaa pamoja na Halmashauri zinazojengwa kwa kiwango cha lami, wote tunatambua kwamba Halmashauri zetu hazina uwezo wa kuendelea kuziimarisha. Sasa kutokana na hali hiyo, zile barabara za lami zinapokuwa zimeanza kuharibika maana yake zinaachiwa hata yale mashimo tunashindwa kuyaziba. Kwa hiyo, badala ya kutumia fedha kidogo kwenye kutengeneza zile barabara, matokeo yake zile barabara zinaendelea kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano hai, siku moja kamati yako ikipata nafasi ikaja pale Musoma Mjini, kuna barabara kama ya Shabani, kama yale mashimo yangeweza kuzibwa ile barabara ingeendelea kupitika, lakini leo hii ukienda pale tunatamani tu bora ile lami yote iondolewe ibaki kuwa barabara ya vumbi kuliko ilivyokuwa barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kwenye ile barabara yetu ya Mkenda ambayo ndiyo kioo cha mjini, nayo imeanza kutoboka, Halmashauri haina uwezo wa kuziba yale mashimo. Matokeo yake baada ya miezi sita ile barabara yote itakuwa haipo na nguvu kubwa iliyotumika itakuwa imepotea bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo, binafsi naishukuru Serikali kwa maana ya toka mwaka juzi 2018 tumeweza kupata fedha za kutosha. Maeneo mengi sasa pale Musoma Mjini tumejenga kwa kiwango cha lami. Ila kwa bahati mbaya sana, yale maeneo ambayo yapo usoni mwa Mji wa Musoma ndio yameendelea kuharibika. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba atakaposimama atapata nafasi ya kutuambia wamejipangaje kwenye fedha za kuboresha barabara zinazoharibika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, napenda kuchangia kuhusu uwanja wa ndege. Tunatambua Serikali imefanya juhudi kubwa na nzuri za kuendelea kuboresha viwanja vya ndege. Nimesikitika wakati nasoma hapa kwenye taarifa yake kwenye viwanja vya ndege ambavyo vinajengwa, Kiwanja cha Musoma hakimo, lakini kimekuwa kikisemwa na tuliona hata katika bajeti kwamba kitajengwa, lakini nimeanza kupata mashaka makubwa kwanza baada ya kuona hapa kwenye hii hotuba hakimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nakumbuka toka mwaka jana mwanzoni uthamini ulifanyika. Kwa kawaida sisi wote tunatambua kwamba uthamini unachukua miezi sita baada ya hapo una-expire. Sasa madhara ambayo wale watu wa Musoma wameyapata toka uthamini ufanyike, zile nyumba zao sasa ziliwekwa X, hakuna watu, wapangaji wamekosekana wala hakuna shughuli zinazoendelea na wale watu bado hawajalipwa fidia. Halafu tunapokuja kwenye vitabu, hapaoneshi juhudi zozote za Serikali kwa ajili ya kujenga ule uwanja wa ndege wa Musoma. Sasa hata tunapata tabu kubwa katika kusafiri, lazima tuje Mwanza ili tuweze kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu atakaposiamama atuambie, ule uwanja wa Musoma unajenga ama haujengwi? Kama haujengwi ni vizuri wakaenda wakafuta zile X na wakawaelimisha watu ili waweze kuendelea na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kidogo kwenye suala la bandari. Katika hili, mimi binafsi naiomba Kamati yako ipate nafasi wakati wa ziara za Kamati itembelee pale Mjini Musoma. Pale tunayo bandari ambayo nayo ilishakufa kwa sababu hakuna meli inakuja wala hakuna activity yoyote inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tulikua pale na mwalo wetu wa Mwigobero. Ule mwalo ndio watu wetu walikuwa wanafanya biashara ndogo ndogo, mitumbwi yote na samaki walikuwa wanagoa pale na biashara mbalimbali zilikuwa zinafanyika pale. Kilichotokea, watu wa bandari walikuja pale na wakatuambia wakati huo kwamba wanategemea watusaidie kuboresha ile bandari na wakasema wataiboresha bandari ifanane na ile Bandari ya Kirumba. Nasi tukafurahi tukaona kama ingeweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ile bandari wameichukua na hakuna kinachoendelea na wale watu wote waliokuwa wanafanya biashara pale wamefukuzwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia.

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Kwa hiyo, naomba Kamati yako nayo ikiweza kupata nafasi ya kuja pale, itatusaidia kutatua hilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsanteni sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuchukua nafasi hii kwanza kukushukuru kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi hoja zetu mbili za Kamati ya Afya pamoja na Huduma za Jamii. Mimi binafsi naendelea kuipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo wameendelea kuboresha katika haya maeneo mawili. Nilishazungumzia maeneo mengine lakini leo kwa sababu tuko kwenye elimu pamoja na afya naomba nijikite upande huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninakumbuka katika mafanikio mengi tuliyoyapata, na naomba nijielekeze zaidi katika Jimbo langu la Musoma. Hata kwenye upande wa elimu peke yake nakumbuka hata kwa mwaka jana tu tumepata shilingi milioni 700 kwa ajili ya Shule ya Msingi Mwisenge, shule aliyosoma Hayati Baba wa Taifa. Shule hii haikuwa kwenye bajeti lakini kwa sababu Mheshimiwa Rais alikuja kule basi akaitembelea na akaweza kutupatia fedha hizo, kwa hiyo pongezi hizo ziweze kumfikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile hata kwenye zile shule zetu kongwe tulipata 1.2 bilioni kwenye shule yetu ya Musoma Teki. Tumeendelea kupata mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali kwenye upande wa elimu. Walimu wameongezeka pamoja na kwamba bado kuna upungufu mkubwa wa walimu kutokana na wingi wa wanafunzi; maana ukiangalia kwenye taarifa ya Kamati wamesema wanafunzi tu wameongezeka kwa asilimia 27.7, kwa hiyo inaonesha dhahiri kwamba baada ya kuwa tumepata mfumo wa elimu bure au elimu bila malipo sasa haya haya ndiyo matokeo yake, kwamba wanafunzi wengi zaidi wameendelea kujiunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ungeangalia kwenye elimu ya juu bado kwa mwaka huu peke yake imetolewa mikopo ya thamani zaidi ya bilioni 49. Hii ni kwa sababu ya wale watoto, wale watoto wasiokuwa na uwezo waweze kuwa na uhakika wa kusoma. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa kazi hiyo nzuri

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi hata ukizungumzia kwenye idara ya afya yako mambo mengi ambayo yemefanyika. Uilinganisha sasa na kipindi cha nyuma utakubaliana na mimi kwamba hata upungufu wa dawa katika vituo vyetu vya afya pamoja na kwenye zahanati umepungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Kwa pale Musoma Mjini kwa mwaka jana peke yake tuliweza kupata fedha isiyopungua milioni 400 kwa ajili ya kituo chetu cha afya cha Makoko naipongeza sana SerikaliPamoja na fedha za bajeti jambo ambalo limetufurahisha sana wananchi wa Musoma na wananchi wa Mkoa wa Mara tumekuwa na hospitali ya Rufaa ambayo tumehangaika nayo kwa zaidi ya miaka 20. Kwa mwaka huu peke yake tumepata bilioni 15 kwa ajili ya ile hospitali na tunategemea wakati wowote ule ile hospitali itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya si maendeleo ya kubeza, ni maendeleo ambayo ni maendeleo makubwa ambayo tunadhani kwamba kwa kadri tunavyoenda hivi basi kusema kweli tunaenda vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe tu kusema kwamba pamoja na hayo maendeleo ambayo yameendelea kupatikana; lakini liko suala moja ambalo bado ninategemea Kamati iweze kuli-address, kwamba kutokana na ongezeko kubwa la watu mimi nilitegemea Kamati ya Huduma za Afya iweze kulizungumzia hili suala la uzazi wa mpango. Maana kama hatuwezi kulizungumza kila leo huduma zitakuwa zinaongezeka lakini baada ya miaka miwili, mitatu zile huduma zinaonekana tena hazitoshi kwa sababu ongezeko letu la watu bado ni kubwa sana. Sasa hilo nalitegemea, kama hatuwezi kulizungumza na tunaendelea kulikalia kimya kwa hiyo tuendelee kutambua kwamba kazi kubwa ambayo itakuwa inafanyika bado tutakuwa tunaonekana tu bado tuko nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo ningependa kufahamu Kamati ilivyojipanga hasa kwenye mapungufu ya kuondoa tatizo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, tuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi katika shule zetu. Hii hata kwenye vile vyuo vyetu vya ufundi, VETA; kati ya matatizo mengine tuliyonayo, mfano tuna Chuo cha VETA pale kinachukua wanafunzi 280. Ukiangalia kile ni chuo ambacho mwanafunzi wa Darasa la Saba anaweza kwenda, wa Kidato cha Nne anaweza kwenda, wa Kidato cha Sita anaenda. Sasa kwa sababu wanachukuliwa wachache, matokeo yake ni kwamba tunapeleka wanafunzi wengi mpaka Vyuo Vikuu, lakini wakifika kule matokeo yake ni kwamba wanakosa ajira. Kumbe tungeweza kuboresha na kuongeza zaidi kwenye hivi vyuo vya ufundi kama VETA vingeweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Serikali ilianza na utaratibu wa kupeleka wanafunzi JKT na wengine wamekaa huko miaka mpaka mitatu. Nadhani ilikuwa ni nafasi nzuri ya kutumia mafunzo ya JKT katika kuwafundisha vijana wetu stadi mbalimbali. Mambo ya kilimo wangeweza kujifunza kule, mambo ya ufundi wangeweza kujifunza kule. Kwa sababu JKT ni mahali pekee ambapo mwanafunzi anaweza kuishi kwa gharama nafuu, lakini akajifunza mambo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba baada ya kuwa wamejifunza kule, badala ya kuwaacha tu kwamba sasa hebu rudini majumbani, nilitegemea kabisa kwamba ni mahali ambapo wangeweza kujifunza stadi mbalimbali, mafunzo mbalimbali na baada ya hapo, wale vijana wakapewa mitaji wakaingia wakaja huku kwenye ujasiriamali wakaweza kujiajiri katika ajira mbalimbali. Kile kitendo cha kuwaweka pale halafu baada ya muda tukawaondoa, kusema kweli sioni kama inawasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; nikushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hii hotuba ya bajeti ya Waziri Mpango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake kwa ujumla; kusema kweli wanafanyakazi nzuri na ni kazi yenye kutukuka. Mimi nikuombe tu Waziri Mpango kwamba mnapoona kule upande wa pili wanajaribu kubeza haya mafanikio wanabeza tu kwa sababu ni utaratibu kwamba lazima wazungumze. Kusema kweli kazi ambayo mnaifanya ni kazi nzuri ni kazi ambayo inawapa matumaini makubwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mimi ninachoweza kusema katika mchango wangu; ni kweli kwamba pamoja na maendeleo yote ambayo yanafanyika lakini Watanzania wangependa kuona huko kukua kwa uchumi kukiwa kunaonekana katika maisha ya kawaida ya watu. Kama hivyo ndivyo labda mimi nichangie tu katika maeneo machache ambayo tunaweza kuyafanya katika mpango wa muda mfupi, mengine tukaweka kwenye mpango wa muda wa kati, na mengine tukayaweka kwenye mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na mpango wa elimu, nakumbuka mwezi uliopita Mheshimiwa Rais alienda Malawi, akaenda Afrika Kusini, akaenda pamoja na Namibia. Pamoja na mambo mengine aliyokuwa anayazungumzia lakini alikuwa anasisitiza zaidi kuona namna ya kuboresha au Kiswahili kuwa lugha ya Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Waziri unaweza ukatenga kiasi kidogo cha fedha na kiasi hicho ukakipeleka kwenye ofisi zetu za Ubalozi zile ofisi za Ubalozi zile tukatengeneza tu crash program kwa ajili ya walimu wanaofundisha Kiswahili wakawa na vyumba pale kwenye Ubalozi wetu. Kiswahili ambacho nchi zetu za Afrika wanahitaji kufundishwa ni kile cha kujua kusoma na kuandika. Sasa hii crash program inaweza ikawa inaanza asubuhi mpaka jioni. Kwa hiyo utajikuta kwamba yale mataifa mengine wanaotaka kujifunza Kiswahili wanajiandikisha pale ubalozini, na walimu wetu wako pale na wanawafundisha. Kwa hiyo tutajikuta kwamba mambo mawili tutayafanikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tutakuwa tumepata ajira kwa ajili ya walimu wetu kwa ajili ya mpango wa muda mfupi, lakini la pili tutakuwa tumepata mapato. Hilo nalisema; leo ukienda pale British Council pale Posta pale, unakuta unakuta pale Serikali ya Uingereza imeanzisha mfumo huo na kila siku zaidi ya wanafunzi 200 wanapata pale elimu na kwamba wale wanaotaka kujifunza Kiingereza wanajifunza, lakini vile vile Serikali yao inapata kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunadhani kwamba pamoja na mpango wa muda mrefu, lakini naamini kwamba huo ni mpango wa muda mfupi ambao Mheshimiwa Mpango ukiuamua leo tayari ndani ya miezi miwili ni zoezi linaloweza kufanyika na tayari watu wetu wakapata maisha, na mambo yakaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilipenda nichangie, katika kukuza ajira; maana mojawapo ya kazi yoyote ile ya Serikali, pamoja na mambo mengine lakini ni pamoja na ku-create ajira kwa wananchi wake. Leo ukiangalia tunao vijana wengi wa Kitanzania hawana ajira. Sasa kwenye upande wa kilimo kinaweza kikachukua watu wengi zaidi katika kuwasaidia wakajipatia ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo mojawapo Serikali imeanzisha mpango mzuri wa kuchukua vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi cha miaka miwili. Hivi sasa kuna in-take ambayo sasa nadhani kama sikosei huu inaelekea mwaka wa tatu. Mimi ushauri wangu ni kwamba, wale vijana pamoja na kazi zingine wajikite zaidi kwenye uzalishaji wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hili suala la JKT kwanza ni vizuri likawepo katika kila mkoa, na kulekule wakachagua mazao. Pia tusikalie tu yale mazao ambayo tunasubiri soko la dunia liseme, yako mazao ambayo tunaweza kuyauzia katika nchi zetu hizi za Afrika. Kwa mfano leo tukilima zao kama la mpunga tunaweza kuuza Kenya, Uganda Rwanda na Zambia. Kwa hiyo basi kama hivyo ndivyo hawa vijana hawa, badala ya kuwaingiza JKT miaka miwili halafu tukawaondoa ni vizuri wakatumia muda mwingi wakazalisha na wakapata mtaji na kwa hiyo tunapowaondoa wawe wamejifunza maisha ya kijeshi lakini vile vile sasa tuwape mitaji ili wakaendelee na maisha yao. Kwa hiyo nadhani hii ni nafasi nzuri ya kuwatumia wale vijana ili waweze kujipatia ajira lakini vile vile waweze kujipatia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi hata leo ukija kwenye mifugo; katika nchi hii tunayo mapori mengi tena ni ranch za Serikali. Kwenye zile ranch leo ukienda ni miti tu inakua kiasi kwamba hata mifugo haiwezi kuchungwa. Kwa hiyo zile ranch zile tukizitumia vizuri; na tunaweza kuzitumia vizuri kwa maana ya kuzikodisha; na katika kuzikodisha leo Watanzania wengi wanayo mifugo, wengi wanafuga lakini hawana mahala pa kufugia. Kwa hiyo zile ranch zile tukizikatakata vipande na Serikali ikawakodishia wananchi, watanenepesha mifugo yao humo na baada ya kunenepesha ile mifugo, tunayo masoko makubwa; kule Comoro kuna soko kubwa sana la mifugo, kule Uarabuni nako soko ni kubwa. Shida moja tu ni kwamba Watanzania wengi hawana mahala pa kufugia mifugo yao, kwa maana ya kunenepesha ili waweze kuuza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo maana wakati mwingine tunalalamika au watu wetu wanalalamika wanasema uchumi mgumu kwa sababu tu kwamba kuna maeneo ambayo yangeweza kuwachukua ku- accommodate watu wengi lakini hizo fursa wanashindwa kuzipata. Kwa hiyo,naamini kwamba tukitumia na hiyo nayo itawasaidia sana Watanzania wengi kuweza kujipatia uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la uvuvi, ambalo nalo; leo ukiangalia samaki kama sato wanatakiwa kila mahali lakini uwezo wetu wa ku-supply ni mdogo. Kwa hiyo nadhani kwamba haya ni baadhi ya maeneo ambayo leo tukiyasimamia vizuri, yataleta matokeo ya haraka. Baada ya kusema hayo, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa sababu ya muda nitakwenda moja kwa moja kwenye hotuba ambayo tunaijadili hapa.

Mheshimiwa Spika, nimesoma vizuri hotuba zote mbili; ya Bunge la Kumi na Moja na Bunge la Kumi na Mbili. Kusema kweli kama ukizipitia vizuri unaona dhahiri kwamba yale mambo aliyoyasema Mheshimiwa Rais katika Bunge la Kumi na Moja na utekelezaji wake katika Bunge la Kumi na Mbili unathibitisha kwamba Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kutembea katika maneno yake. Kwa hiyo, tunampongeza sana kwa kazi hiyo nzuri na kwa namna ambayo sasa nchi inakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja; Watanzania wengi tunafika mahali tunasahau, zamani hata katika nchi zingine walikuwa wanasema Tanzania ni nzuri kwa kuweka mipango mizuri, ikishaweka ile mipango inatekelezwa katika nchi za wenzetu, majirani zetu. Lakini leo hao waliokuwa wanasema hivyo hiyo nafasi hawana maana wanashangaa jinsi ambavyo tunapanga mambo na jinsi ambavyo utekelezaji wake unavyokwenda. Kwa hiyo ukiangalia nchi zote, ziwe na Afrika mpaka kwa wale wenzetu wa Ulaya, wanatutamani, wanatamani Tanzania jinsi inavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hivyo ndivyo sasa ni vizuri tukaendelea tu kufanya tafakari kwamba hata huko tuendako hivi baadae mambo haya tutaendelea ku- maintain hii pace tuliyonayo au baadae mambo yatakuja yatushinde. Nadhani hilo ni jambo ambalo huko mbeleni tunahitaji kuendelea kulitafakari katika mustakabali wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo sasa mimi nitoe tu mchango katika maeneo mawili kwa sababu ya muda. Eneo la kwanza ambalo tunahitaji sasa tuliangalie katika hiki kipindi tunachoenda nacho kwa kweli tatizo la ajira kwa vijana wetu bado ni tatizo kubwa kwa sababu vijana wengi wanamaliza chuo, lakini mwisho wa yote ajira imekuwa ni tatizo.

Kwa hiyo, ninadhani ni vizuri sasa Serikali ingejiangaliza huko, itengeneze programu maalum kwa ajili ya vijana hawa wanaotoka sekondari, wanaoshindwa kuendelea, lakini na wale vijana wanaomaliza vyuo vikuu, kwamba namna gani sasa tunaweza kuwa-accommodate katika kupunguza hili tatizo la ajira. Kwa hiyo, hilo ni moja ya eneo ambalo tunahitaji kuliangalia.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, viko vitu vingine ambavyo vilevile hata sasa hivi yawezekana hatuoni impact yake lakini bado impact yake ni kubwa. Leo ukipita katika vituo vyote vya polisi, maana yake vilevile tumezungumza kwamba kati ya watu tunaohitaji kuwasaidia ni hawa waendesha bodaboda. Kuna bodaboda zaidi ya 1,000 katika kila kituo cha polisi. Sasa ukija kuzijumlisha katika nchi nzima ziko nyingi sana na ziko pale zinaoza. Na unakuta wakati mwingine bodaboda mwingine alishikwa na ile bodaboda alikuwa hana leseni akakimbia na ameshindwa kwenda kuitoa ile pikipiki.

Kwa hiyo, nadhani Serikali inahitaji izianglie kwamba badala ya zile rasilimali kuendelea kupotelea pale, basi ni vizuri ikaangalia utaratibu mzuri wa kuunda tume au kamati fulani hivi ambayo inapita katika kila Wilaya iziangalie zile bodaboda zote zilizoko pale pamoja na makosa waliyofanya halafu waamue kwamba badala ya kufia pale ama Serikali izitaifishe au basi wale wa kurudishiwa waweze kurudishiwa kuliko ambavyo tunaendelea kutumia fedha za kigeni kuagiza bodaboda zingine, lakini tuna bodaboda nyingi zimejaa kule kituoni. Kwa hiyo, nadhani upande huo napo Serikali inahitaji kuliangalia namna ya kulisaidia zaidi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ukienda kwa hawa vijana wetu wa JKT, kusema kweli mimi ule mpango niliupenda na ni mpango ambao niliufurahia kwamba wale vijana wanakaa pale JKT ile miaka mitatu baadae kati ya hao vijana wanapata ajira. Lakini wale vijana wakitumiwa vizuri, wakifundishwa vizuri elimu ya ujasiriamali, wao wenyewe wana uwezo wa kuzalisha na kile watakachokizalisha na kwa kuwa watakuwa wamepata mafunzo, basi hicho hicho bado wanaweza kupewa tena baada ya ile miaka mitatu na wakaenda kuanza maisha na tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo itawasaidia sana kuliko ile ambayo wakishatoka pale chuoni, wakishatoka JKT baada ya ile miaka mitatu halafu wengine tunawarudisha nyumbani.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kwanza kwa kunipa nafasi. Vile vile nimepitia hotuba ya Mpango, umekaa vizuri pamoja na kwamba yapo marekebisho na ndiyo maana tuko hapa kwa ajili ya kuweka sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunapanga mipango hii, lazima ianzie kule kwetu kwa maana ya Halmashauri zetu. Wakati mwingine yako mambo ambayo yako kwenye uwezo wa Serikali, lakini kunakuwa na ukiritimba ambao unakwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikianzia na Jimbo langu la Musoma Mjini, huwezi kuamini lile jimbo ambalo lina wakazi wasiopungua laki mbili lakini lina ukubwa wa square kilometer zisizopungua 63. Kwa maana kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine haizidi kilometa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya shida kubwa ambayo tumeendelea kuipata toka miaka na miaka, maana pale mimi nimekuwa Mstahiki Meya toka 2000 mpaka 2005, lakini vile vile nikawa Mbunge toka wakati huo 2005. Tumekuwa tukipambana au tukijitahidi sana kuongeza maeneo, kwa sababu kusema kweli square kilometer 63 kwenye wakazi 200,000, maana yake ni kwamba leo ukija pale Musoma unataka tu uwanja; kuna mwekezaji amekuja anataka uwanja ajenge tu hata shule. Hiyo nafasi haipo. Hakuna chochote utakachotaka kufanya kwa sababu ya eneo kuwa dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaratibu unasema tuzungumze na halmashauri husika. Tumezungumza lakini mwisho wa yote hawako tayari kutoa yale maeneo. Sasa athari kubwa tunazozipata ndizo hizo kwamba leo hii hatuwezi kujipanua, hatuwezi kufanya uwekezaji, kwa hiyo, hata namna ya kuongeza mapato katika Mji wetu wa Musoma imekuwa ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inalifahamu hili. Tumejaribu kupitia katika vikao vyote mpaka RCC lakini suala hili hadi leo tunazungumza limeshindikana. Ukiangalia, hata wale wenyewe wanaokatalia hayo maeneo, unamkuta mtu, pale tulipo kwa sababu ni kata za jirani, kuja mjini kwa maana ya Makao Makuu, anatembea, ni kama kilometa tano. Kwenda kwenye Makao Makuu ya Jimbo lake, anaenda kilometa 80. Kwa hiyo, ukiangalia kwa namna moja au nyingine, yule mwenyewe kwa maana ya mwananchi, anapata adha kubwa kwa kwenda kuhudumiwa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuja kwenye hizi huduma za jamii, mfano leo ukizungumza hospitali, hawa wote wanakuja wanakuja pale mjini. Anapotaka kwenda shule, anaacha shule mita 200, lakini anaenda shuleni kilometa tano mpaka saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizo juhudi ambazo tumezifanya, tunajikuta kwamba wale wananchi hata tulipowazungukia katika kuzungumza nao, wote wanataka kuja mjini. Pamoja na kwamba wanataka kuja mjini, ukifika tu kwenye Baraza la Halmashauri, basi mnakaa vikao lakini wanasema watawajibu, wakijibu wanasema hatukukubaliana na hilo ombi lenu. Ndiyo maana wakati mwingine tunasema, Serikali kwa sababu inayo nafasi ya ku- intervene katika kuhakikisha kwamba vile vile inatusaidia ili tupate maeneo makubwa, wawekezaji wakija wapate. Watu wakitaka viwanja wapewe. Basi hiyo itatusaidia sana katika kukuza Mji wetu wa Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia Musoma, naamini umefika pale umeona, Musoma lazima ufunge safari kwamba unaenda Musoma. Yaani huwezi tu kupitia kwamba unaenda Mwanza, unaenda Sirari, lazima ufunge safari kwamba unaenda Musoma. Pale uchumi pekee tulionao, kidogo ni ziwa ambapo lile ziwa nalo liko vijijini. Kwa hiyo, hakuna uchumi ambao tunaupata kutokana na lile ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji tufanye biashara, yaani watu wetu wawe na zile biashara ndogo ndogo zinazowapa uchumi. Sasa unapotaja biashara, watu 200,000 halafu wameji-confine katika square kilometer 63, kwa hiyo, unakuta tatizo la ajira Mjini Musoma ni kubwa sana. Ndiyo maana tunasema kwamba Serikali inahitajika ku- intervene ili tuweze kupata maeneo na kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia watu wetu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza sana kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mchemba pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Masauni kwa namna walivyoweza kuwasilisha Mpango huu. Karibu yote nakubaliana nayo, lakini yako mambo ambayo nadhani nimeona kama hayajakaa vizuri sana na tunahitaji tuone namna bora zaidi ya kuyaweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, nchi yoyote ile mojawapo ya jukumu lake kubwa kushinda yote ni kuhakikisha kwamba watu wake wanapata ajira. Kwenye suala la ajira ninyi wote ni mashahidi, vijana wengi wanamaliza darasa la saba, kidato cha nne, vyuo vikuu na vyuo mbalimbali vya kati lakini ukija kwenye ajira ni tatizo. Kwa hiyo, lazima Mpango huu tunapoupanga ujielekeze namna gani utaendelea ku-solve tatizo la ajira katika nchi yetu ambalo kwa kusema kweli sasa hivi hilo ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia suala la ajira lazima tuangalie kilimo, viwanda, uvuvi na ufugaji. Labda leo mimi nichukulie mfano kwa pale Musoma; pale Musoma ni kwamba vijana wetu wengi hawana ajira kabisa kwa sababu viwanda vimekufa na vingine kwa bahati mbaya sana ninyi wenyewe Serikali ndiyo mnaviuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na kiwanda pale cha MUTEX na kilikuwa kinafanya kazi na bahati nzuri mwekezaji wake ni mkubwa ni huyu Mohamed Enterprise, lakini tulimnyang’anya kwamba ameshindwa kukiendesha vilivyo, tukasema tunampa mwekezaji mwingine. Mpaka leo hivi tunavyozungumza huu ni mwaka wa pili kile kiwanda kina makufuli, watu wetu hawana ajira na wako mtaani. Mimi niseme tu kwamba itakapofika wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Mheshimiwa Mwigulu, niseme ni mjukuu wangu, lakini nitalia na shilingi yake kama hatakuja na majibu kamili ni kwa kiasi gani atatusaidia ku-solve tatizo la ajira kwa watu wetu wa Musoma, hasa kuhakikisha kwamba kile kiwanda cha MUTEX kinafunguliwa lakini sambamba na viwanda vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza kati ya mambo tunayohitaji kuyaangalia sana katika kuwasaidia watu wetu, nimezungumzia suala la mifugo, kilimo pamoja na uvuvi. Shida yetu kubwa ni kwamba kila leo hizi fedha zinazotengwa na Wizara badala ya kwenda kwenye ukulima zinaenda kwenye kilimo. Fedha zinapoenda kwenye kilimo hizo ndizo zinaishia kwenye zile mnaita facilitation; kununua magari, computer na kwenye mambo kama hayo. Tunategemea kwenye bajeti ya sasa fedha zielekee kule kwenye ukulima, kwa maana kwamba watu waweze kupata mabwawa ya kutosha kwa ajili ya irrigation, lakini waweze kupata pembejeo nzuri na zilizo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaingia kwenye duka la pembejeo za kilimo ziko bidhaa fake zinauzwa mle, matokeo yake ni kwamba mtu anakuja kunyunyizia vile viuatilifu vyote ni fake. Kwa hiyo, yeye mwenyewe amehangaika halafu anarudi kupata hasara ya pili. Tunapozungumza suala la uvuvi ni kwamba fedha ziende kwa wale wavuvi wenyewe kwa kuhakikisha kwamba walau tunaweka mikakati ya kuona watu wanakuwa na uvuvi endelevu, unaoweza kusaidia watu. Mfano, vijana wetu wa pale Musoma wamesaidiwa vizimba vingapi ili waweze kupata ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unakuta vyakula vya samaki lakini yule mfugaji anaambiwa kwamba labda baada ya miezi sita yule samaki atakuwa amefikisha nusu kilo, matokeo yake anafuga mwaka mzima kutokana na chakula anachowalisha, lakini gramu 500 au nusu kilo wale samaki hawajafikisha. Shida kama hizo ni kwa sababu fedha haziendi kwenye uvuvi badala yake zinaenda tu katika usimamizi ambao hausaidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata unapozungumza suala la ufugaji, unakuta badala ya fedha kwenda kwa wafugaji ili wapate majosho, dawa bora, waweze kuwa na unenepeshaji mzuri matokeo yake ni kwamba hata dawa za mifugo nyingi ni fake. Haya yote ni baadhi ya mambo ambayo tunahitaji tuyaangalie na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunavyoweza kuwasaidia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo tunapozungumzia viwanda, yawezekana tukawa tunaangalia tu vile viwanda vikubwa kama MUTEX, MWATEX na vinginevyo, lakini naamini kabisa kwamba tukilisaidia Shirika letu la SIDO ambalo ndilo linaloshughulika na viwanda vidogovidogo na bahati nzuri Baba wa Taifa aliliweka karibu katika kila mkoa, lingesaidia sana suala hili la viwanda. Kazi kubwa ya SIDO inafundisha habari ya usindikaji na packaging. Bidhaa nyingi hata tungeenda kwa wenzetu walioendelea kama China viwanda vyao ni vile vidogovidogo ambavyo kazi kubwa ni kusindika na packaging, wanaweka ile bidhaa yao katika hali nzuri ya kuvutia. Kwa kufanya hivyo basi ni rahisi watu wetu wakaweza kufanya biashara zao ndogondogo pasipokuwa na shida. Tatizo SIDO zetu zote zimekufa. Kumbe SIDO ingeweza kutoa mafunzo mbalimbali ambayo yangewasaidia sana watu wetu wa Musoma, lakini na watu wetu wa Tanzania kwa ujumla katika kuendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nadhani hili kwangu ni suala la ushauri, ni hili suala la TRA. Kama tunavyofahamu suala la TRA ni kweli wakati mwingine wanachukua fedha kwa nguvu na wananyanyasa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Hayati John Pombe Magufuli amelikemea sana suala hili lakini na juzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu naye amekuja amepigilia msumari wa mwisho kwamba kuwe na utaratibu mzuri wa ukusanyaji. Hata hivyo, kumbuka kuna bajeti ambayo tunategemea Waziri atatukusanyia, lengo ni shilingi trilioni mbili. Lengo la shilingi trilioni mbili si fedha ndogo, yaani unahitaji kwenda extra mile kuona namna ya kuweza kuzikusanya.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ushauri wangu, ili uweze kuweka check and balance, kwa maana ya kwamba wale TRA wafanye kazi yao, ushauri wangu ebu imarisha ile Board of Appeal iwe active, ifanya kazi ipasavyo. Ili TRA wanapombana yule mlipa kodi kama anaona ameonewa basi aweze kupata mahala pa kwenda, na majibu ya pale yakitoka haraka maana yake kama anadaiwa basi, maana siamini kama TRA anaweza kumuonea mtu halafu ukaenda na kule kwenye Board of Appeal na penyewe napo ukaonewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale huwa kuna kakipengele, kwamba kama unataka kwenda huko kwenye Board of Appeal nadhani unapaswa kulipa one third ya kile ulichokadiriwa. Sasa, nimekadiriwa bilioni tatu, one third maana yake nilipe one billion sina.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunadhani kwamba hicho kipengele mkikiondoa hicho ili hata yule ambaye anadhani kwamba ameonewa aweze kusikilizwa katika ile Board of Appeal, na itakapokuwa active sasa itamsaidia sana katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka, unapata kodi yako lakini na huko kwa mlipa kodi anapata haki yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii bajeti ya Wizara ya Miundombinu. Kusema ukweli bajeti tumeiona, kwangu mimi leo ninachoweza kusema ni masikitiko yangu. Ni masikitiko yangu kwa maana kwamba, yako mambo ambayo yanazungumzwa ambayo tunataraji kwamba ndani ya muda mfupi yanapaswa yapate utekelezaji. Kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya mambo ambayo naamini kwamba watendaji wetu aidha wanayapuuza au basi tu wanayawekwa kwa muda ambao hata haukustahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Musoma Mjini tuna tatizo la uwanja wa ndege na tatizo hili ni la muda mrefu kwa sababu ule uwanja wetu ni wa vumbi na sasa hivi hakuna ndege ya abiria ambayo inatua pale. Sasa kinachonisikisha ni kwamba katika awamu iliyopita kwa maana ya marehemu John Pombe Magufuli aliahidi kwamba tutajenga uwanja wa ndege. Kwa hiyo nikashukuru kwamba ndani ya muda mfupi, mpaka fedha za fidia zikaja shilingi bilioni 4.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha ni kwamba, fedha hizo zimekuja toka mwaka jana, lakini mpaka leo yaani zililipwa tu fedha kidogo kama bilioni mbili hivi na kitu, watu wengine walitathminiwa gharama za fidia, lakini mpaka leo ni zaidi ya mwaka hawajapata fidia, fedha zile 4.2 bilioni ziko kwenye akaunti pale Musoma. Sasa unajiuliza kwanza Sheria yenyewe ya Fidia inasema baada ya miezi sita inatakiwa ifanyike evaluation mpya. Sasa wale watu wameendelea kukaa pale hawajalipwa, wamelipwa watu kiasi na fedha zipo, sasa tafsiri yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonipa mashaka kabisa ni kwamba, leo Waziri huyu ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo. Kwa maneno mengine nasema yeye ndiye ametoa zile fedha, leo tena amekuja, bahati nzuri amekuwa Waziri, kwa nini hawa watu wasilipwe ili wakaendelee na maisha yao kuliko kuwaacha wakaendelea kupata adha ambayo watu hawa wanaendelea kuipata hadi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake ni kwamba, siku watakuwa tayari kulipa fidia, maana yake kwamba miezi sita imeisha na kwa kuwa miezi sita imeisha evaluation mpya inapaswa ikafanyike na zile nyumba kwa sababu watu walishahama wanasubiri walipwe fidia zitakuwa zimeanguka, kwa hiyo labda huyo mtu badala ya kulipwa milioni 100 au milioni 200, sasa atalazimika kulipa milioni 50 au chini ya hapo. Kwa hiyo na hilo ningependa Mheshimiwa Waziri aweze kulitolea ufafanuzi, ni lini hao watu watalipwa fedha yao mara moja ili maisha yao yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo vilevile linanifanya nishindwe kufahamu, kama tulisikia ripoti ya CAG japokuwa labda muda wake bado wa kuizungumza, kati ya jambo alilolisema ni kwamba Shirika la Ndege ni shirika ambalo limefanya vibaya katika kipindi sasa cha miaka mitano. Sasa nimejiuliza, nimejaribu kusikiliza katika hotuba ya Waziri yote na kuipitia, hakuna mahali ambapo pameonesha kwamba ni hatua gani ambazo Wizara imechukua kwa ajili ya kulinusuru shirika lile la ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa haraka haraka nilichokifahamu ni kwamba, aidha basi yawezekana habari hiyo labda haikuwa sahihi na kama ilikuwa sahihi, mbona basi suala hilo Wizara haijazungumza chochote katika kulinusuru hilo Shirika la Ndege. Naenda mbali zaidi naanza kujenga mashaka yawezekana kuna habari zingine za upotoshwaji ambazo labda wakitueleza vizuri tunaweza kuelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naunga mkono hoja lakini nasubiri majibu sahihi kuhusu fidia ya watu wa Musoma. (Makofi)


Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Waziri wa Nishati. Kusema kweli na mimi niungane na wenzangu waliotangulia kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika toka aliposhika Wizara hii. Hii inonesha kabisa kwamba katika kipindi kifupi kwa maana baada ya mwaka mmoja nchi nzima ya Tanzania itakuwa imepata umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nijielekeze tu kwenye Jimbo langu la Musoma. Mheshimiwa Waziri anafahamu, bahati nzuri nilimwalika na alikuja Musoma na tukawasha umeme kwenye Mtaa wa Bukoba. Baada ya kuwa tumewasha umeme Mtaa wa Bukoba pale pale akatoa agizo kwamba kuanzia sasa kwenye maeneo yote ya pembezoni yatapata umeme. Naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri toka alivyotoka, lile eneo la pale Bukoba hawajapata umeme zaidi ya ule aliowasha. Mitaa ya Nyabisale, Songambele, Kwangwa A, Kwangwa B, Mugalanjabo, Zanzibar, Bukanga hivi ninavyozungumza hawajapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Waziri amechukua hatua za kuzungumza na Meneja wa TANESCO na akamuagiza, bahati mbaya tu sasa hivi hayupo Mwenyezi Mungu amrehemu lakini hilo tatizo kwangu ni kubwa. Nadhani mwezi uliopita Naibu Waziri Mheshimiwa Byabato alikuja Musoma aliweza kushuhudia alikaa mpaka na Wenyeviti wa Mitaa wanamweleza hali ya umeme ulivyo wa shida pale Musoma Mjini.

Mheshimiwa Spika, TANESCO tunapowauliza wao wanasema hivi, ni mita 30 toka pale nguzo ilipo kulia na kushoto zaidi ya hapo hawatoi umeme. Kikubwa zaidi TANESCO kila tunapowauliza wanasema hawana bajeti sasa Mheshimiwa Waziri leo ataniambia nini kwa sababu kwenye vitabu hata kwenye ile miradi ya Peri-Urban sisi Musoma hatumo, sasa endapo Musoma hatumo na TANESCO wanasema hawana bajeti yetu tunafanyaje? Waziri ametangaza hapa kwamba hakuna mwananchi kulipia nguzo sijui wale watu wa Musoma watafanyaje. Naomba baada ya Bunge hili tukubaliane kwamba tukishaahirisha twende wote akawaambie kwamba ndugu zangu ile ahadi aliyotoa kwamba watu wa Musoma watapata umeme wa Sh.27,000 haipo badala yake walipie tu zile gharama za kawaida za shilingi laki tatu na kitu tofauti na hapo tutaendelea kuonekana sisi wengine ni waongo.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri labda atoe maelekezo ili fedha ziweze kupatikana kwenye maeneo kama haya ya Peri-Urban kama ambavyo imetokea kwenye mikoa mingine na ameweza kuonesha ili na sisi watu wa Musoma tuweze kupata umeme. Faida za umeme kila mmoja anazifahamu na kwa sababu watu wetu sasa walishajua kwamba umeme wa Sh.27,000 unakuja kila siku inaonekana mimi Mbunge ndiye ninayewakwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri aangalie fedha zile zinazokwenda kwenye mfuko wa REA ziweze kwenda kwa Mameneja wa TANESCO wa Mikoa ili zile ahadi ambazo Serikali inazitoa basi iweze kuzitekeleza. Kusema kweli pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo imeendelea kuonekana lakini kwetu sisi wengine hali si shwari kabisa. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba atakapokuwa anajibu basi suala la Musoma asiweze kulisahau.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa sababu ya muda naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika mpango ulioko mbele yetu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha na Mipango kwa namna ambavyo amejitahidi sana kuwasilisha mpango wake kama maandalizi ya bajeti ya mwaka kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia hali halisi katika mazingira ya kawaida ya wananchi. Maana mimi nafika mahali najiuliza, yawezekana ni mimi tu kule Musoma au ni nchi nzima ndivyo ilivyo? Hali halisi ya maisha sasa hivi ni ngumu, kwa sababu vitu vimepanda sana bei. Nimeona hapa katika mpango Mheshimiwa Waziri anasema mfumuko wa bei siyo mkubwa, nikashindwa kuelewa kwamba yawezekana vigezo tunavyoviangalia siyo vigezo vinavyogusa hali halisi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano hai; leo ukiangalia bei ya chakula, nakumbuka mwaka 2021 mwezi Julai, mchele kwa pale Musoma ulikuwa unauzwa shilingi 1,100; lakini leo hivi tunavyozungumza, bei ya mchele ni shilingi 2,500. Hali hii ikiendelea kuja kufika mwezi Desemba, ni ukweli usiopingika kwamba utakuwa unauzwa siyo chini ya shilingi 3,000. Sasa kama bei ya chakula kama mchele ambao ni wa lazima, unaweza ukapanda mara tatu, halafu unawezaje kusema kwamba mfumuko wa bei siyo mkubwa! Unapozungumza habari ya mahindi Musoma mwaka 2021, tulikuwa tunanunua shilingi 50,000, leo hivi tunavyozungumza gunia moja la mahindi ni shilingi 120,000. Bei imepanda zaidi ya mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa namna yoyote ile, ni vizuri tuangalie kwamba hali halisi ya uchumi wa watu wetu wanapolia, wana haki ya kulia, kwa sababu kwanza fedha zenyewe hazipatikani, lakini bei yake ndiyo hiyo tu kwamba maisha yameendelea kuwa magumu kulingana na mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kwanza naishukuru Serikali kwa maana ya Waziri wa Kilimo, wiki hii nimwomba chakula na ametupatia kiasi cha kutosha ambacho kiko njiani kinaenda Musoma kwa ajili ya kwenda kupunguza yale makali ya bei ya vyakula. Ombi langu ni kwamba basi wajitahidi hicho chakula kiendelee kwenda mara kwa mara, kwa sababu tofauti na hapo, naamini yawezekana chakula kitauzwa mpaka shilingi 150,000 kwa gunia na ukilinganisha na kipato cha watu wetu, hali ya maisha itaendelea kuwa ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sasa hivi tunachangia mpango kwamba nini kifanyike katika kuhakikisha kwamba angalau kwenye bajeti ya mwaka kesho tunaendelea kuboresha; kati ya maeneo ambayo tunadhani tunahitaji kuwekeza fedha sana, moja ni eneo la kilimo. Tunashukuru kwamba Serikali imeongeza kwenye bajeti iliyopita, lakini iendelee kuongeza zaidi. Kwa sababu tukiongeza fedha kwenye kilimo, kwanza tafasiri yake ni kwamba itawafanya wale watu wetu kule kwa maana ya Serikali iendelee kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji. Maana hata kama tungeweka fedha kwenye kilimo halafu tukajikuta kwamba hatutengenezi miundombinu ya umwagiliaji na hali ya ukame ambayo inalisumbua Taifa letu, wakati mwingine tutajikuta kwamba fedha zimeongezeka, watu wamelima na matokeo yake bado shida inabaki pale pale kwa sababu ya ukosefu wa mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema, katika nchi yetu kwa namna ilivyokaa, imezungukwa na nchi nyingi ambazo vile vile zinaitegemea Tanzania ili iweze kuilisha. Sasa tunadhani nini kifanyike katika mpango ujao? Hebu tujaribu kuwa na aina mbili za mazao; mazao ya chakula na mazao ya biashara. Kwa sababu leo ninavyojua, kama sisi watu wa Mara kwa mfano, mchele wetu mwingi unaliwa na watu wa Kenya na Uganda ambapo kwa kusema kweli wanatusaidia katika kutupatia fedha, lakini sasa, hata kama tunauza kule chakula, lazima tuwe na akiba yetu ya kutufanya tuendelee ku-survive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ungeniuliza ushauri wangu ningesema, kila mkoa uandae mazao yao ya chakula na mazao ya biashara. Kwenye yale mazao ya chakula hebu tujaribu kuwa strict tusiyauze nje. Mfano, kwa pale Mara, leo tukianzisha mfano, kilimo cha mihogo ambacho mpaka leo tunalima mihogo na tukawa strict kwamba mihogo tusii-export nje na Serikali ikaweka nguvu pale katika kusaidia wale wakulima wa mihogo kama ambavyo inasaidia kwenye maeneo mengine…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Fedha, umesikia mihogo! (Kicheko/Makofi)

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafasiri yake ni kwamba sisi Mara tutajua kabisa kwamba zao letu la chakula, tunalima mihogo na mtama; ambapo ukichanganya mhogo na mtama ni chakula safi kabisa kuliko hata mahindi. Kwa hiyo, kwa sababu wenzetu wa Kenya wanahitaji mahindi, sisi Mara tutalima mahindi, tutawasafirishia, tutalima mpunga kwa maana ya mchele tutawasafirishia. Kwa hiyo, tutamaliza sasa katika kuondoa tatizo. Kumbe sasa tukishakuwa na huo utaratibu wa zao la chakula na zao la biashara, basi itatusaidia sana kuhakikisha kwamba tunaendelea ku- survive na mfumuko wa bei unaendelea kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine lililopo ambalo ni kubwa sana ni tatizo la ajira. Yaani ukiangalia kadri vijana wanaozalishwa kuingia kwenye soko la ajira, lakini wakati huo hakuna ajira, siyo mjini, wala vijijini. Hata zile ajira za mjini kwa sisi watu wa mjini ni zile biashara ndogo ndogo. Ukizungumza biashara ndogo ndogo tunafika mahali tunasema Wamachinga watengewe maeneo. Kumbuka kwamba wale ni watu wenye mitaji midogo, lakini tunawatenga mbali na soko, mbali na watu. Matokeo yake ni kwamba tunapofanya hivyo, ndiyo maana kila leo wanalazimisha kurudi mjini. Kwa hiyo, wanakukwa ni kama wakimbizi katika nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani katika mpango huu ni vizuri vile vile tukaangalia katika yale maeneo ambayo yana mikusanyiko ya watu, hata kama kuna taasisi ya Kiserikali pale tuone namna ya wao kupata eneo ili waweze kufanya biashara. Tofauti na hapo, maana yake ni kwamba maisha yanaendelea kuwa magumu na Wamachinga hawawezi kufanya biashara, lakini hata kule kijijini ambako wangeweza kwenda, bado nako hawataweza kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo naishukuru kwamba Serikali imeanza kuliona, lakini hebu iongeze bidii ni kwenye eneo la uvuvi. Tunakubali kwamba angalau kwa sasa hivi, Serikali imeweka mpango wa kukopesha wale wavuvi wadogo wadogo. Tunadhani watu wengi suala la elimu bado linawasumbua sana na vile vile namna ya kuweza kuipata mikopo. Kwa hiyo, ombi langu, tuweke katika mpango namna ya kuendelea kuelimisha wananchi wetu ili waone namna bora zaidi ya kuweza kupata mikopo. Pia baadhi ya maeneo Serikali inapaswa iwekeze. Mfano, leo unapozungumza pale kwangu mjini, eneo kama la Makoko, ni eneo ambalo ni zuri sana kwa biashara ya dagaa, utawakuta akina mama wamebeba mabeseni wanaenda kuanika halafu wanauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe Serikali ikiwekeza pale, wale akina mama wakaweza kuwa wanakaushiwa dagaa zao vizuri, tafsiri yake ni kwamba wale wavuvi watawekeza kwenye vifaa vizuri vya kuvulia. Hata akina mama ambao wanahangaika na mabeseni kichwani, wataweza kukausha dagaa zao pale pale na hatimaye watauza katika maeneo yote ambayo tunadhani yanahitaji hao dagaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakushukuru sana kwa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hii hotuba ya Waziri wa TAMISEMI. Nakushuru sana Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Naibu Mawaziri mnafanya kazi nzuri ni imani yangu kwamba tukiendelea hivi basi tutaweza walau kutatua changamoto nyingi zinazowahusu wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naendelea kuishukuru sana Serikali kwa maana ya Mheshimiwa Rais Samia tumeweza kupata fedha za kutosha kujenga vyumba vya madarasa, kujenga zahanati, vituo vya afya pamoja na barabara. Kwa hiyo, nawapongezeni sana, lakini bahati nzuri ni kwamba fedha zimekuja na tumezisimamia vizuri, lakini huu usimamizi mzuri huu kwa namna yoyote ile tusingeweza kusimamia pasipokuwa na madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, hiyo kazi nzuri ambayo inafanyika na hata kwa sasa safari hii inaonekana tena fedha nyingi zaidi zitakuja, sasa mimi ombi langu ni vizuri na wale Waheshimiwa Madiwani tukaendelea kuwajali, lakini hali kadhalika na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa sababu hao ndiyo wanaofanya kazi kubwa huko hasa tunapokuwa hatupo majimboni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo katika kuteleleza hayo, maana mimi bahati nzuri nimekuwa Diwani mwaka 2000 kabla sijawa Mbunge mwaka 2005 mojawapo ya mambo yaliyokuwa yanafanyika ilikuwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya Madiwani lakini na kuwajengea uwezo ili waweze kuzisimamia. Sasa umezungumza vizuri katika hotuba yako, lakini bado hujazungumza namna ya kuendelea kuwajengea uwezo pamoja na maslahi yao kwa sababu wale watu wanasimamia fedha nyingi sasa, lakini ni kwamba uwezo wao kiuchumi ni mdogo sana. Kwa hiyo, nadhani hilo utakapokuwa unajibu ni imani yangu kwamba utalijibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine pamoja na miradi mingi na fedha nyingi tulizozipata kwangu pale Mheshimiwa Waziri, aidha, mambo yalifanyika kimakosa, aidha, kwa makusudi mfano, kwenye zile fedha zilizokuja fedha za tozo na fedha za UVIKO kwenye barabara mimi nipata shilingi milioni 500 peke yake nilipokuja kuuliza kulikoni nikaambiwa kuna fedha za TACTICS pamoja na miradi ya kimkakati. Sasa at least katika majimbo mengine zilipatika shilingi bilioni 1.5 mimi nimeambulia shilingi milioni 500 lakini mpaka leo hivi ninavyozungumza hakuna dalili ya fedha za kimkakati wala za TACTIC. Kwa hiyo, nitaomba wakati unasimama unieleze hilo, vinginevyo mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kuanza na shilingi yako Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ipo ile miradi mfano; fedha zimekuja, lakini vile vituo vya afya vya zamani vilivyochoka, ninacho Kituo cha Afya cha Bwiru pale, leo ukikiona ni afadhali hata zahanati, lakini zipo shule za msingi kama Mtakuja yaani imechoka yaani ile inahitaji tui-condemn. Kwa hiyo, pamoja na mengine yote ningekuomba utakapopata nafasi baada ya Bunge hili twende Musoma nikutembeze na hivi wewe ni mjukuu wangu nitakutembeza mradi kwa mradi uweze kuiona ili uweze kuona kwamba ni kwa kiasi mtaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilidhani kwamba kwenye upande huo Mheshimiwa Waziri hebu basi angalia namna ambavyo tutakavyopata fedha kwa ajili ya kufidia yale mapengo ya barabara ambazo hazikujengwa. Lakini cha ajabu zaidi sasa kwa miaka mitano mfululizo Musoma hatujawahi kupata fedha za maendeleo kwa ajili ya barabara hatujawahi yaani tofauti na fedha tulizo bahatisha za World Bank ambazo tumezipigania kwa muda mrefu hakuna fedha yoyote ambayo imeshakuja na ukiangalia kwa muda wa miaka mitano kwa namna ambavyo Madiwani wangu wanafanyakazi nzuri hatujawahi kupata hata hati chafu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ni imani yangu kwamba katika yale yote ambayo ni ya kimsingi katika kutusaidia mji wetu wa Musoma ili nao uweze kuendelea basi katika bajeti hii utaweza kusema namna ya kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme jambo moja ambalo ninadhani aidha tunaliona, lakini tunajifanya kama hatulioni. Mheshimiwa Waziri umetoa takwimu nzuri kwamba darasa la saba wanamaliza wanafunzi zaidi ya 1,130,000; kidato cha nne wanamaliza wanafunzi zaidi ya 880,000; kidato cha sita wanamaliza wanafunzi 80,000; tafsiri yake ni nini? Kwamba kumbe basi kila mwaka wanafunzi au vijana zaidi ya milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira, yaani wanapaswa waanze maisha lakini ukiangalia sasa kama wanapaswa waanze maisha na jukumu mojawapo kubwa la Serikali ni pamoja na kuwapatia wananchi wake ajira, sasa leo ni tatizo ambalo linatutesa, kwangu mimi pale Musoma vijana wangu wengi hawana ajira, lakini hawana ajira sijasikia kwenye bajeti yako ni namna gani mmewatengenezea mazingira kwamba sasa kila wanapomaliza hawa zaidi ya milioni moja wakimaliza shule mmewaandalia mazingira gani ya ujasiriamali aidha, mazingira gani ya kuweza kupata ajira.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilipomuuliza Mheshimiwa Bashe hapa swali la nyongeza alisema kwenye bajeti hii ameandaa fedha kwa ajili ya miradi ya kilimo kwa ajili ya vijana ili waweze kujiajiri, lakini wanatatizo moja kubwa la maeneo sasa nilitegemea kabisa kwamba na wewe hapo ungeweza ku-chip in kwa maana ya kutenga fedha kwenye kila halmashauri ili tuweze kuandaa maeneo ili atakapokuwa na fedha kwa ajili ya vijana basi tayari tuna maeneo ya kuweza kuwa-accomodate.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine sambamba na hilo wapo vijana wetu wa kimachinga, wapo vijana wetu wa bodaboda, nashukuru kwamba hilo nililipigia kelele mwisho tukawa- official rise wanaendelea na shughuli zao pamoja na kwamba bado yapo mambo ya kurekebisha, lakini wale wamachinga wale ni watu ambao wao ili waweze kufanyabiashara wanatafuta watu walipo, sasa cha ajabu kila mnaposema mnawapanga tunawapanga kwenye maeneo ambayo hakuna watu na wao kwa sababu biashara yao ni ndogo ndogo maana yake ni kwamba lazima tuwaandalie maeneo ambayo tayari wapo watu. (Makofi)

Sasa kila mara hilo nalo hatujalitekeleza vizuri sana na hata katika bajeti yako sijasikia namna gani umeweza kuwagusa. Kwa hiyo, mimi niombe hapa sasa kwamba pamoja na Wizara yako na wizara zingine ni vizuri kipaumbele chetu kuliko yote ni pamoja na ajira kwa watu wetu ni imani yangu kwamba kila Wizara, juzi nilisikia hapa mfano; TRA wametangaza ajira 1000 napo wanajigamba kwamba ajira nyingi zimetoka ajira 1,000 hivi ninyi ajira 1,000 katika watoto zaidi milioni moja ambao kila mwaka wanakuwa tayari kwa ajili ya kuanza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba kila Wizara iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba inatoa ajira kwa kila mwaka na kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia vijana wetu.

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nawashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Musoma Mjini, Jimbo langu lilibahatika kupata na lenyewe ule mpango wa umeme wa REA hasa katika yale maeneo au mitaa ya pembezoni pamoja na kwamba liko mjini. Baadhi ya mitaa iliyofaidika na mpango huo iliyoanza kufaidika ni pamoja na ule Mtaa wa Bwiribukoba, Nyabisare, Songambele, Kwangwa, Zanzibar, Bukanga ni mitaa ambayo ilibahatika na ilianza kubahatika na huo mpango. Baada ya 2015 - 2020, tulipoanza 2021 mpaka leo ule mpango kwa pale Musoma Mjini ukaondoka na baada ya kuondoka tunaishukuru kwamba TANESCO imeendelea kusambaza hata zile transformer katika hiyo mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu yale maeneo mitaa ya pembezoni ni maeneo ambayo yanafanana na maeneo ya vijijini. Kwa hiyo unakuta transformer imepelekwa lakini watu walioweza ku-tap pale umeme hawavuki watu watatu, wanne na sababu ni rahisi tu kwamba sasa kwa sababu ile miji inakaa mbali mbali lazima mwananchi aweke nguzo zaidi ya mbili. Sasa nguzo mbili unazungumzia zaidi ya shilingi 500,000. Sasa hebu tuliangalie hili kwamba yule aliyebahatisha 2015 - 2020 aliweka umeme kwa shilingi 27,000. Leo huyu mwingine jirani yake ambaye wakati ule aliomba lakini hakupta nafasi anaambiwa aweke umeme kwa zaidi ya shilingi 500,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutokana na hali hiyo, kwa hiyo watu wangu wengi wote walioko maeneo ya pembezoni wameshindwa kuweka umeme na kama tunavyofahamu mahitaji ya umeme ni makubwa na hasa katika mazingira ya sasa, wananchi wangependa wapate huo umeme. Sasa leo cha ajabu sasa ukija pale Musoma Mjini na nimwombe Mheshimiwa Waziri Makamba aje pale Musoma mwenyewe ashuhudie kwamba leo jirani yangu ni Butiama, pale kuna Kijiji cha Nyabange, pale wanapata umeme wa shilingi 27,000, hapa kwangu Bwiribukoba wanapata umeme wa shilingi 500,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo matokeo yake leo watu badala ya kukimbilia mjini watu wengi wanahamia pale jirani kwa sababu pale ndipo sasa gharama za kuishi zimekuwa nafuu. Sasa kutokana na hali hiyo, watu wangu wameshindwa kufahamu kwamba hivi wao kumbe kuingia mjini tena imekuwa adhabu kwao? Sasa natambua kabisa na wote tunatambua kwamba bado ile miradi ya peri urban bado ipo na kama ipo, sasa sisi ambao tayari tulibahatika kuingia kwenye huo mpango wa REA, leo tuna dhambi gani, badala ya kuendelea kulipa kwa shilingi 27,000 ili watu wote waweze kupata hiyo huduma sasa matokeo yake wao wanalipa umeme kuanzia shilingi 300,000 mpaka zaidi ya shilingi 500,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningependa wakati Mheshimiwa Waziri anajibu, ni vyema awaambie kabisa watu wa Musoma watambue kwamba sasa ule mpango utarudi au ndiyo wameendelea kuusahau. Kama wameendelea kuusahau hata umuhimu wa zile transformer haupo kwa sababu Serikali inapoteza resource pale inapopeleka transformer halafu wanaweza ku-tap watu wanne au watu watatu peke yake. Kwa hiyo nadhani kuna haja ya kuliangalia hilo ili tuone namna ya kuwasaidia watu wetu wa Musoma kwa sababu nao wangependa kupata hiyo huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, liko jambo ambalo vile vile huwa linanichanganya kidogo. Leo unakuta kwamba kuna mtu anahitaji umeme na kwa sababu anahitaji umeme akienda TANESCO, wanamwambia hawajawa tayari au hawana bajeti kwa mwaka huu kwa ajili ya kumsogezea umeme. Yule mwananchi anasema sawa, mimi nina hiari sasa kulipia in advance. Sasa akikubali kulipia in advance, TANESCO wanasema ukishalipia kwa hiyo gharama labda ya kupeleka pale umeme kununua transformer pamoja na zile nguzo labda unakuta ni Sh.20,000,000. Sasa najiuliza kama yule mwananchi amekubali kulipia huo umeme in advance, ni kwa nini TANESCO wasiendelee kumrudishia aidha kwa kumkata pole pole mpaka zile fedha zake zitakapoisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tofauti na hapo anaambiwa wewe kaa subiri siku tukiwa tayari na bajeti tutakuwekea umeme. Kwa hiyo nadhani kuna kila aina ya sababu kwa yule ambaye ameshajitolea amelipa in advance walau TANESCO wakubali kuja kumrudishia hizo gharama kuliko kusema kwamba hawako tayari tena kuja kumlipa hizo gharama wakati bado wanaendelea kumchaji ile bili yake ya kila mwezi. Kwa hiyo nadhani hapo napo kuna haja kidogo ya Serikali kuendelea kuliangalia hilo tatizo la kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye upande wa madini. Tunatambua kwamba STAMICO ni caretaker kwa ajili ya wale wachimbaji wadogo na kama kweli tunapenda kuwasaidia wale wachimbaji wadogo, hivi STAMICO Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inawasaidia STAMICO uwezo kwa kuwapa fedha za kutosha ili waweze kuwakopesha wale wachimbaji wadogo wadogo waweze kujenga uwezo? Kwa sababu leo hii ukiangalia hata katika takwimu wale wachimbaji wadogo ni kati ya watu ambao wanachangia sana pato la nchi hii, lakini wapo tu wala hakuna namna wanayosaidiwa ili waendelee kukua, waendelee kukuza mitaji na kutokana na hali hiyo wachimbaji wadogo uzuri wao ni kwamba leo ukimsaidia akijenga uwezo anarudi ku-re invest humu humu nchini tofauti na wale wachimbaji wakubwa ambapo unaambulia tu kile kifaida, fedha nyingine yote inayobaki anaipeleka kwao. Kwa hiyo kuna kila aina ya sababu ya kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo kwa sababu akishapata fedha hapo ataendelea kujenga hoteli, ataendelea kufanya miradi mikubwa ambayo itaendelea kuisaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani kuna kila aina ya sabau ya kuona namna ya kuwasaidia. Kwanza kuisaidia STAMICO, lakini vile vile aweze kuwasaidia wale wachimbaji wadogo na kwa kufanya hivyo watasaidia sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuwa mchangiaji wa mwanzo katika Wizara hii ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa maana ya bajeti yao nzuri, kwa namna walivyoweza kuwasilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuchangia katika maeneo mawili ambayo kwangu nadhani wanapaswa kuya-consider. Ukiangalia hii Wizara ya Elimu, maana yake ni kwamba hao ndio wanaoanza kuwandaa vijana wafike mahali waanze maisha. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile katika haya maandalizi yao lazima wawe wameangalia zaidi kwamba mwisho wale vijana wakimaliza shule wanahitaji wapate ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli katika nchi yetu hapo ni kati ya mahali ambapo tuna tatizo kubwa, kwamba vijana wengi wanamaliza shule na wanahitaji waajiriwe ili waendeleze maisha yao. Kwa bahati mbaya sana na hata ukiangalia katika nafasi ambazo zinatokea, wanaopata nafasi ni wachache lakini wanaomaliza shule ni wengi zaidi. Kwa hiyo, nilidhani kwamba ninyi kwa sababu ndio waandaaji wa sera na miongozo, ni vizuri mngejikita sana kuangalia namna gani wale vijana wanaomaliza shule wataweza kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo ukiniuliza kwenye elimu hasa ya Chuo Kikuu ambapo sasa hivi ndipo mmeangalia sana, pamoja na ile elimu ya vyuo vya kati, hebu tujitahidi kuweka nguvu kubwa katika vyuo vya kati. Ni ukweli usiopingika kwamba leo ukimchukua kijana, mfano aliyemaliza Chuo cha VETA, halafu ukamchukua mwingine ambaye amemaliza Political Science Chuo Kikuu, ukiwapeleka duniani, yule mwenye elimu ya certificate anaweza kuendesha maisha yake kushinda yule wa Chuo Kikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kwa sababu ukienda kwenye hivi vyuo vya kati, wanafunzi wengi wanajifunza moja kwa moja yale maisha ya kawaida. Mfano, ufundi makenika, ufundi wa magari, useremala pamoja na fani mbalimbali. Kwa hiyo, nilidhani kwamba pamoja na hizo juhudi za Serikali kuviangalia hivi vyuo vya kati, ingeweka hapo nguvu zaidi kuliko inavyoangalia sasa vile vyuo vikuu. Nitoe mfano hai kwamba pale kwangu Musoma Mjini tunacho Chuo cha VETA, kimejengwa vizuri, lakini ukiangalia idadi ya namba za watoto ambayo wanachukuliwa pale ni wachache sana ukilinganisha na mahitaji, lakini wale watoto ambao wanasoma vyuo vikuu wapo wengi sana, lakini mwisho wa siku wanarudi mtaani hawana ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ingejitahidi kuongeza vile vyuo kwa maana ya kuviongezea fani mbalimbali na wale watoto waweze kujifunza kwa njia ya vitendo. Leo ukienda pale mfano Musoma unakuta kuna gari moja, yaani wapo wanafunzi wanachukua kozi ya Umakenika, lakini gari lililopo pale ni moja tena bovu. Sasa wanafunzi karibu 200 waliopo pale, maana yake ni kwamba kuja kujifunza namna ya kufunga injini tafsiri yake ni kwamba vijana wengi wanatoka pale hawana ujuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana tunasema hebu mjitahidi kuangalia namna bora zaidi ya kwanza kuvipanua hivyo vyuo na ikiwezekana viende kila Jimbo na vile vile mwendelee kuviongezea fani na facilities za kuwafanya waendelee kujifunza kwa njia ya vitendo. Kwangu mimi nadhani hilo linaweza likasaidia zaidi kwenye upande huo ili vijana wengi waendelee kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, lipo suala ambalo tunahitaji tuendelee kuwasaidia wale vijana wetu wanaomaliza vyuo vikuu pamoja na vyuo vya kati hasa kwenye kada hii ya Ualimu. Leo Mheshimiwa Waziri akiamua hilo, nadhani linaweza likaleta impact ya haraka. Tanzania tuna bahati moja kwamba unapozungumza lugha ya Kiswahili, hii lugha ya Kiswahili sisi ndio waasisi wa hiyo lugha, lakini ukienda duniani katika nchi nyingine wako majirani zetu hapa wa Kenya wanatoa walimu wa kwenda kufundisha katika nchi nyingine lugha ya Kiswahili, lakini kumbe hiyo ni opportunity ambayo kwetu sisi kama Tanzania tungeweza kuitumia. Mfano watu wengi katika Mataifa mbalimbali wanachohitaji kujifunza ni kusoma, kuandika na kuongea lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo sisi hatulazimiki kutafuta wale Walimu ambao wamesomea Kiswahili peke yake, hao ndiyo wakafundishe lugha ya Kiswahili katika Mataifa mengine; kumbe watu tunaowahitaji ilimradi awe anajua Kiingereza, halafu anajua Kiswahili, maana yake ni kwamba anaweza akaenda na akafundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ungeniuliza tufanyeje? Tunaweza kufanya kitu kimoja kwamba katika zile ofisi zetu za mabalozi zote zilizopo katika nchi mbalimbali, tukaweka pale kitengo ambacho kinafundisha Kiswahili kwa muda mfupi. Kwa kufanya hivyo kumbe tunaweza tukawapeleka kule walimu wetu wengi na wakafanya kazi hiyo ya kuweza kuwafundisha Mataifa mengine. Kwa hali hiyo wakapata ajira na maisha yakaendelea kuliko hivi sasa ambavyo tunakaa nao humu pasipokuwa na ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku za nyuma wakati nakua, ilikuwa ukitembea huko duniani, ukikutana na asilimia kubwa ya watu ambao ni Watanzania walikuwa wa Taifa moja la Nigeria. Nigeria ilikuwa inasifika kwa kuwa na vyuo vingi karibu kushinda nchi nyingine yoyote ile, na hiyo ni kwa sababu wao walikuwa wanaonekana walikuwa na mfumo kama wa hapa kwetu na madhara yake makubwa ambayo walikuwa wanayapata walikuwa wanaonekana sio miongoni mwa nchi Taifa ambalo watu wake sio waaminifu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo inatokana na nini? Ni kwa sababu walikuwa wamesoma, lakini elimu waliyosoma ni elimu ya kusoma ambayo haiwasaidii katika ku-create ajira. Sasa mimi nina mashaka sana kwamba leo Watanzania wengi na kwa elimu tunayoipata ndiyo hiyo tu kwamba kila mmoja unakuta amemaliza Chuo Kikuu lakini haajiriki. Shida kubwa ambayo wanaipata hawa wasomi, hawezi kufanya hizi kazi za kawaida, lakini anafika mahali ajira zinazopatikana huwezi kuamini leo analipwa mpaka shilingi 300,000 mtu mwenye degree ya Chuo Kikuu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara yetu ya TAMISEMI. Sina shaka kabisa na utendaji wa Waziri pamoja na wasaidizi wake. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyoweza kutupa fedha za kutosha katika Manispaa yangu au Jimbo langu la Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa leo ninayo maombi matatu machache. Ombi la kwanza, kama nilivyosema namshukuru Mheshimiwa Rais ameweza kutupatia fedha Shlingi milioni 500 kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Sambamba na hilo, ameweza kutupatia Hospitali iliyokuwa ya Mkoa baada ya kuwa tumejenga Hospitali ya Rufaa. Sasa tumekabidhiwa rasmi kuwa Hospitali ya Manispaa ya Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu sasa, kwa sababu tayari tunazo Shilingi milioni 500 kwenye akaunti; na wakati huo huo tayari tunayo hospitali ambayo sasa tumekabidhiwa, lakini hospitali ile ina upungufu mwingi, haina fensi, mawodi yamechoka pamoja na miundombinu mbalimbali; ombi langu dogo kwa Mheshiiwa Waziri, hapa nilipo ninayo barua ya kuomba kubadili matumizi ya zile fedha zikatusaidie kuboresha ile hospitali iweze kuwa hospitali ya kisasa kwa ajili ya Manispaa ya Musoma. Naomba watumishi wetu waje wachukue wakupatie ili hilo tuwe tumelimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la pili, pamoja na hiyo hospitali yetu ambayo sasa ni Hospitali ya Manispaa, kulingana na ikama yake, inahitaji iwe na watumishi 200, lakini mpaka hivi tunavyoongea ina watumishi 45 peke yake. Kwa hiyo, ninayo barua ya pili hapa ya kukuomba tuweze kupata watumishi, kwa sababu mpaka hivi sasa tuna zahanati nzuri, na tumepata fedha za kutosha. Tuna vituo vya afya vizuri, tumepata fedha za kutosha, hebu sasa tuboreshe hiyo hospitali yetu ya Manispaa ili watu wetu wa Musoma waweze kupata huduma nzuri ili waweze kuendelea na maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la tatu, mwaka jana 2022 nilisema hapa Bungeni kwamba pale kwetu Musoma kwenye ile Shule ya Mtakuja, ni shule ya siku nyingi, shule kongwe. Sasa shule ile imechoka na kusema kweli kwa mwaka huu bahati nzuri tumepata fedha Shilingi milioni 90 kwenye shule ile, lakini hizi fedha ambazo tumepata ni kwa ajili ya ukarabati. Ombi lingine ninaloomba Mheshimiwa Waziri ukipata nafasi njoo ujionee mwenyewe ile shule. Kama ingekuwa ni shule ya private tungekuwa tumei-condemn haina sifa za kuwa shule, kwa sababu mabati yametoboka, makenchi yamechoka, yameliwa na mchwa, lakini baadhi ya vyumba vya madarasa havina hata lenta kwa sababu ni madarasa ya zamani. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba zile fedha badala ya kukarabati, kitu ambacho hakikarabatiki tunaomba zile fedha zitumike kujenga vyumba vipya vya madarasa, lakini tuongeze fedha nyingine ili ile shule yote iweze kujengwa vizuri na watoto wetu waweze kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni madawati. Leo kama kuna tatizo tunalo katika nchi hii hasa kwa shule za msingi, ni madawati. Watoto wetu kama pale kwangu, nusu ya watoto wa shule za msingi wanakaa chini. Sasa Serikali imesema hivi, wazazi wasichangishwe, lakini wakati huo huo Serikali haitoi madawati. Hata ukiangalia katika hii bajeti tuliyonayo mpaka leo haioneshi kama kuna madawati tutayapata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wakati anasimama, azungumze kinagaubaga ni namna gani tunamaliza tatizo la madawati? Tofauti na hapo, Mheshimiwa Waziri, wewe jua Shilingi yako lazima niing’ang’anie. Haiwezekani tumepata fedha za kutosha, madarasa mapya yamejengwa, lakini ukiona mle watoto wanakaa chini. Hii ni aibu na ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najaribu kuzungumza kwa haraka haraka ili niweze kumaliza ya kwangu. Lingine ni suala la hizi ajira kwa walimu. Tunaipongeza sana hii Serikali ya Mama Samia kwa ajira nyingi ilizozitoa. Sasa leo ukiangalia wakati mwingine ni vitu vya ajabu sana. Tunao walimu wengi ambao Serikali imewasomesha, halafu wamekaa tu pale, hakuna ajira. Upande huu wa pili wanafunzi wetu wako madarasani lakini hakuna walimu. Upande huu walimu wapo, Serikali imewasomesha, hakuna ajira. Upande huu wanafunzi wapo, na miaka inaenda lakini hakuna walimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi la kwanza, ajira kama hizi zinazopatikana, wewe angalia tu; gawa ratio, angalia Musoma ni ajira ngapi? Tuambiwe Musoma tunawapa ajira 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kwamba wale walimu wanaojitolea, tuwe tunawapa kipaumbele. Advantage yake ni moja. Leo inatokea kwamba yuko mwalimu ambaye alipomaliza miaka minne iliyopita, alienda kulima au alienda kufanya shughuli nyingine, lakini yuko mwalimu ambaye amejitolea toka alivyomaliza shule. Leo nafasi inapatikana unakwenda kumchukua yule ambaye alikaa miaka minne bila kutusaidia, wakati yuko mwalimu aliyejitolea.

Mheshimiwa Spika, kwanza hata huyu aliyejitolea tu yeye mwenyewe kwanza imemfanya aendelee kuwa current, kwa sababu ameendelea ku- practice. Kwa hiyo, tunadhani hilo bahati nzuri kwa sababu liko kwenye uwezo wako, hebu tusaidie kuhakikisha kwamba linakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niweze kuchangia katika hii Wizara ya Madini. Nitaungana na wenzangu tu kumshukuru Ndugu yetu Waziri Biteko pamoja na Naibu Waziri. Kusema kweli kazi yao inaonekana na hasa pale ambapo wameweza kujitahidi kuhakikisha kwamba ndani ya muda mfupi wachimbaji wadogo wanaweza kuchangia kwa 40%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli katika nani yangu nitajikita tu kwa hawa wachimbaji wadogo maana ninawaona wako majirani zangu pale wa Buhemba naona ni namna gani wanahangaika. Wako majirani zangu wa Sirorisimba lakini hata kule kwa Kinyigoti. Tunaona kwamba ni kwa kiasi gani ambavyo wanapambana sana wanajitahidi lakini wanakumbana na vikwazo vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Wizara imejitahidi sana kuwasaidia lakini tunadhani inahitaji ifanye zaidi ya hapo. Uzuri wa wachimbaji wadogo kwanza uzuri wao ni kwamba wana multiplier effects. Yaani mchimbaji mdogo akipata, yaani utaona amejenga nyumba, akipata ameendelea kufanya biashara nyingine yaani ile fedha anayoipta anarudi ku- reinvest. Kwa hiyo, hii inasaidia sana katika kwanza mzunguko wa fedha lakini na kukuza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na wale wawekezaji ambao wanatoka nje wakubwa tunawahitaji lakini wao ni kwamba zaidi ya ile kodi ambayo tunabahatisha tunapata, hata CSR yenyewe wanatoa kwa mbinde sana. Kwa hiyo, tuna kila aina ya sababu na nikuombe Mheshimiwa Doto, umefanya kazi nzuri na kazi kubwa, nawewe kama kiongozi wa Wizara hii mojawapo ya kazi kubwa ya kiongozi ni kufanya mambo yafanyike. Sasa kati ya jambo moja ambalo unahitaji ulifanye hebu jipe malengo ndani ya miaka miwili, mitatu hawa wachimbaji wadogo sasa watoke 40% waende 60%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo ni jambo ambalo najua leo ukiamua Mheshimiwa Waziri Doto ni jambo linalowezekana sana. Wachimbaji wadogo hawa yako baadhi ya changamoto ambazo wanapambana nazo. Moja yaani yeye kwanza wao ndiyo wavumbuzi wa madini hasa ya dhahabu. Anachokifanya huwezi kuamini, mchimbaji mdogo anahangaika huko porini anakuja anakutana na mwamba, wa pili anakuja, mwingine anakuja mwisho wanakuwa wengi pale. Anatokea tu mtu wa kawaida anaenda pale na GPS anachukua coordinates akitoka pale anaenda kwenye portal tayari analipa shilingi 50,000 lile eneo linakuwa ni la kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake wale wachimbaji wadogo waliokuwa wanachimba pale wote wanaondolewa, lile eneo unapewa wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli yaani tunawapa adha kubwa. Kwa hiyo, ombi langu Mheshimiwa Waziri ambalo linawezekana, hebu yeyote yule wachimbaji wadogo wakishaanza pale, kwanza wanatambulika mpaka kwenye vijji vile wanavyofanya kazi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inapotokea tukitaka kuwasaidia inapotokea kwamba kuna mtu ameenda pale ameingiza kwenye GPS amepata coordinates na amechukua lile eneo, kabla hamjampa, hebu tuangalie nani alianza, ni wale wachimbaji wadogo au ni yeye. Kama ni wachimbaji wadogo ndiyo walianza, hebu tuwasaidie wale wachimbaji wadogo ndiyo waendelee kuchimba pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo tutawasaidia sana maana shida kubwa ambayo wanaipata ni kwamba wao yaani wakishatafuta, wakipata wanaondolewa hapo. Wakienda mahali pengine wakitafuta wakipata, wanaondolewa hapo. Sasa kusema kweli hii haiwasaidii sana katika kuwa kuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizao lao la pili ambalo wanakumbana nalo ni namna ya kupata ile miamba. Yaani wao wanakuwa tu ni kama waganga wa kienyeji. Anaenda anahangaika hapa miezi sita hajapata kitu anahama. Anaenda mahali pengine anahangaika hajapata kitu anahama. Mwisho anakuja kubahatisha kamchirizi kamwamba kidogo basi ndipo anapata hapo fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nini kifanyike katika kuwasaidia? Natambua kwamba ndugu zetu wa STAMICO ndiyo caretaker wa hawa wachimbaji wadogo. Lakini ukiangalia leo majukumu waliyonayo STAMICO wanamajukumu mengi. Wana majukumu makubwa na kusema kweli wanafanya kazi nzuri sasa tukisema tena wao waendelee kuwa ma-caretaker wa hawa wachimbaji wadogo hiyo nafasi hawana kwa sababu wakifanya huku ni bure lakini sasa unaachaje uzalishaji wako halafu utumie muda mwingi kwa ajili ya kuwasaidia hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaweza kufanya vitu viwili; moja, aidha tukatafuta chombo kingine kama labda GST wakawa wanafanya hiyo kazi ya kuwatafutia miamba. Maana unakuta yeye mchimbaji mdogo yule leo anachimba hapa, akikosa anaenda mahali pengine. Lakini kumbe ingekuwa mfano leo ukija kama pale Buhemba watafiti wakaja pale kama ni GST au chombo, taasisi yoyote ile ikawaonyesha kwamba mwamba ni huu maana yake ni kwamba wangeweza kufanya kazi kubwa sana kuliko ambavyo wanahangaika hivi sasa. Kwa hiyo, kama ombi langu tuone namna ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo katika kutambua ile miamba halafu wao waendelee kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza yaani mchimbaji mdogo hata akipata mwamba tu wa sentimita 50 yaani huo tu umetosha kumtajirisha. Kwa sababu wanatumia muda mwingi kufanya kazi ya kubahatisha na ndiyo maana wanaendelea kupoteza na unakuta siku hizi wanakuja watu sijui tuwaite matapeli au ndiyo hivyo tena, wanakuja kwamba na vimashine vya kudanganya na anapitapita hivi nadhani ni metal detector, kakishasema hapa anaambiwa chimba hapa. Anaenda mita 30 hamna kitu, anaenda pengine hamna kitu, kwa hiyo hali hii nadhani haiwasaidii sana wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri kama utauchukua huo ushauri wa kuhakikisha kwamba tuna chombo ambacho kazi yake ni kuwatafuta yaani leo nikisema pale Sirorisimba uchimbaji wa pale unakuja unawatafutia.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mathayo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji kwamba ili waweze kufanikiwa hawa wachimbaji wetu wadogo, GST pamoja na STAMICO wapunguze gharama za utafiti. Mfano, mita moja sasa hivi wana-charge shilingi 432,000. Kwa kufanya utafiti wa mita 60 ni sawa na shilingi 29,000,000. Mchimbaji mdogo atazipata wapi? Kwa hiyo wapunguze hizo gharama ili wananchi wetu waweze kufanikiwa.

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Mathayo taarifa unaipokea?

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa mimi naipokea kwa mikono miwili, kwamba inavyoonekana hawa watu wengi iwe GST iwe STAMICO na wengineo nadhani gharama wamechukua zile gharama za zamani zile ambazo wazungu walikuwa wanazileta huku kwetu hizo ndizo wamekuja wame-copy na ku-paste. Kwa hiyo, unakuta leo unapomzungumzia mchimbaji mdogo kwamba atumie utafiti hataweza ndiyo maana wanahangaika hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo leo sasa kwa kadiri tunavyoenda.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mathayo malizia muda wako umeisha.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nasema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mosi, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na staff yote kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya, kusema kweli ukiangalia mmejitahidi sana kuboresha mifugo na mmejitahidi sana kuboresha uvuvi. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwanza kwa namna ulivyoweza katika ile awamu ya kwanza ulivyotoa vizimba mimi kwenye Jimbo langu la Musoma Mjini tuliweza kupata vikundi saba, walipata vizimba kwa hiyo wanasubiri tu mimi na wewe tuende tukawakabidhi ili waanze maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema kwamba pamoja na shukrani hizo baada ya kuwa wale wamesikia kwamba wenzao wamepata, sasa vikundi vingi zaidi vimehamasika na vinategemea kwamba kwenye awamu itakayofuata basi ni imani yangu kwamba watakuwa wengi watakaoomba ili waweze kufaidika na mpango huo wa vizimba katika Manisapa yetu ya Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nisemee tu kwa ufupi kwamba liko tatizo kidogo ambalo linatusumbua kwenye ufugaji wa samaki, tatizo hilo tunahitaji tuwe serious tuone namna ya kulitatua. Unajua watu wengi na hata wale wanaouza chakula cha samaki pamoja na wale samaki wenyewe wanatupa maelekezo kwamba samaki ndani ya miezo sita ukiwalisha hivi, watakuwa wamefika wastani wa gramu 500 na utapata biashara, lakini huwezi kuamini kwa sababu tuna watu wengi ambao ni watengenezaji wa vyakula vya samaki, wanashindwa kutupa formular kamili au kututengenezea chakula kamili kitakachoweza kuwafikisha samaki ndani ya miezi sita wapate uzito ule unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo watu wengi wanaanza kukata tamaa kwa sababu wanafuga mpaka miezi nane lakini samaki wana gramu 200, wana gramu 300. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kabisa kwamba hebu hilo ulipe uzito wake kuona kwamba ni kwa namna gani tunaweza kupata watengenezaji wazuri wa chakula cha samaki. Maana leo hii ukiagiza chakula kutoka nje ndani ya miezi sita unaweza kufikisha gramu 500, kwa hiyo nadhani hilo kwetu ni tatizo kubwa kwa sababu ni watu wachache wanaoweza kuagiza chakula cha samaki kutoka nje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo sasa hilo, ombi kwamba pale Musoma Mjini bahati nzuri wewe unapajua vizuri niko kwenye mwambao wa Ziwa Victoria na katika ule mwambao wa Ziwa Victoria ukienda pale asubuhi kuanzia Saa 12 unawakuta wakina mama wamebeba mabeseni ya dagaa vichwani na hayo mabeseni ya dagaa wakiwa wanatiririkiwa na yale maji ya dagaa, kwa maana ya kwamba wale wavuvi wa dagaa, ile kuanzia alfajiri ya Saa 11 wanafika pale hasa kwenye mwalo wangu wa Makoko, halafu wanawauzia wakina mama zile dagaa, sasa wanaanza kutembea nazo wakati mwingine mpaka kilomita tano kwa mguu. Wakifika sasa ndiyo wanaanza kuanika, tena siku hizi wamekuwa wakianika kwenye zile net, hizi net kwa maana ya chandarua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri tupate hata mashine moja au mtambo mmoja wa kukausha Samaki na dagaa pale ili samaki wakishatoka kule ziwani wanapita pale kwenye mashine wanakaushwa akina mama wetu wa Musoma Mjini waweze kufanya biashara zao kwa raha zaidi, nadhani hiyo itawasaidia kuboresha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana watu tunaowahangaikia ndio hao wenyewe, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri uone namna tutakavyowasaidia. Jambo la pili Mheshimiwa Waziri hili linataka attention kubwa sana, ndugu zangu wale wote ambao tunaishi Kanda ya Ziwa kwa maana Mara, Mwanza na Bukoba nadhani mtakubaliana na mimi, samaki wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri siku zinavyoenda ni kwamba samaki wanaendelea kupungua, kwetu sisi pale watu wa ziwani kule samaki au lile Ziwa ndiyo madini yetu, kwa hiyo watu wetu wengi wamekuwa wakipata ajira karibu zaidi ya asilimia 50 kutokana na lile Ziwa Victoria. Sasa leo pale kwangu Musoma Mjini tulikuwa na viwanda vinne, tulikuwa na Musoma Fish Park, Musoma Fish Process, tulikuwa na kiwanda cha Mzee wetu Jamaliwa lakini na Prime Catch. Leo huwezi kuamini kimebaki kiwanda kimoja cha Musoma Fish Process ambao na wao kwa sababu wanapata samaki kidogo wanalazimika kusafirisha kupeleka Mwanza katika kiwanda chao kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha nini? Kwamba kadri siku zinavyoenda yale maji yatabaki tu labda kwa ajili ya kuoga na kunywa lakini hayatakuwa maji yanayoweza kuwasaidia watu wetu kiuchumi. Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba kabisa tuangalie namna tunavyoweza kulisimamia hili Ziwa hasa kuondoa uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo najiuliza hivi kama tunaweza ile Ngorongoro ndogo tukaweka Mamlaka ya Ngorongoro kwa ajili ya kuangalia Hifadhi ya Ngorongoro, tukaweka watu kama TAWA kwa ajili ya kusaidia kuangalia wanyama, hivi tunashindwa nini kuweka mamlaka ambazo zinasimsmia haya Maziwa zinasimamia mpaka na kule baharini ili suala la vile viumbe kwa maana ya samaki waweze kufugwa vizuri. Hivyo, nadhani hilo Mheshimiwa Waziri alipe uzito ili liweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja karibu na la mwisho ni suala la hereni. Miongoni mwa wafugaji hapa na mimi naweza nikajinafasi kwamba na mimi ni mfugaji na ninafuga vizuri. Binafsi nitofautiane tu na wenzangu kidogo pale walipoanza kukataa herein, mimi binafsi naliunga mkono sana suala la hereni kuwepo katika mifugo yetu. Kwanza litatuondolea kabisa kitu kinaitwa wizi, nadhani Mheshimiwa Waziri ni kwa sababu haujaeleza vizuri ule umuhimu wa herein. Binafsi mifugo yangu yote inazo hereni lakini ni zile hereni za plastiki, wakati nikiwa kwenye mchakato wa kuweka hizo hereni za elektroniki tayari Serikali mkasema mnaleta, kwa hiyo mpaka leo mimi nazisubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza tu nikatumia nafasi moja ndogo tu ambayo itawa-convince watu wote wale ambao ni wafugaji wakubali zile hereni. Leo wako Wajumbe humu wamesema kwamba wafugaji hawakopesheki. Hawakopesheki kwa sababu namna ya ku-control ile mifugo yetu inakuwa shida kidogo. Leo Mheshimiwa Waziri tunao watu wa TEHAMA humu katika Wizara yako wamo, hebu waunganishe wale watu wa TEHAMA waunganishe na benki, wafanye tu kitu kimoja, mimi nina ng’ombe wangu 500 zote zina hereni maana yake ni kwamba zile ngo’mbe ili ziuzwe lazima tuuze kwa kutumia herein, kwa hiyo benki leo ukiwaambia kwamba mimi nina ng’ombe 500 hereni zake ni hizi wanaziingiza kwenye system, siruhusiwi yaani nikiuza huyo ngo’mbe hizo fedha lazima ziende wapi? Lazima ziende benki. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo kwanza itakusaidia kuhakikisha kwamba kila mmoja sasa anaona umuhimu wa zile hereni na ni kwamba maana anajua sasa tayari thamani ya zile mifugo zetu zinakuwa tayari ni dhamana kwetu hasa kwenye eneo la benki ambako ndiko wafugaji wengi wanapata taabu. Kwa hiyo, nadhani kama hilo Mheshimiwa Waziri utalipa uzito ni imani yangu kwamba linawezekana kwa sababu mimi nilishalifanyia research ni kitu ambacho kiko wazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Afya. Nampongeza Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu kwa namna alivyoweza kutupatia fedha za kutosha. Zahanati tumeweza kupata fedha za kutosha, hatuna shida huko, vituo vya afya tumepata fedha za kutosha, lakini kubwa zaidi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna nilivyoweza kumwomba ile hospitali yetu ya mkoa ili iwe hospitali ya manispaa na hivi sasa tayari ile hospitali ni ya kwetu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Jimbo langu la Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana kwa huduma ya hospitali yetu ya rufaa sasa, ile ya Kwangwa kwa huduma inazozitoa. Kwa hiyo leo maana yake ni kwamba tunaanzia kule kwenye kata, tunaenda wilayani na hatimaye kwa yale magonjwa ambayo yanashindikana basi tunaweza kwenda kwenye hospitali yetu ya rufaa, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli leo sina mambo mengi, ya kwangu namwomba Mheshimiwa Waziri machache tu tena yote ni mepesi ambayo naamini kwamba hata utekelezaji wake wala hautamsumbua sana. Moja, tunashukuru kwamba wameweza kutuletea CT scan pale kwenye Hospitali yetu ya Kwangwa, lakini kwa bahati mbaya sana sasa yapata miezi isiyopungua mitatu haijafungwa. Kwa hiyo sasa maana yake ni kwamba watu wetu wanapata tabu, lakini tayari Serikali ilishaweka fedha mashine iko pale. Kwa hiyo, tunaomba kwa haraka kabisa hiyo huduma iweze kupatikana kama huduma zingine zinavyopatikana leo pale, watu wetu walikuwa wa kusafishwa figo walikuwa wanasafiri leo mambo yote yanaishia pale. Habari ya mifupa watu walikuwa wanasafiri leo hizo huduma zote zinapatikana pale kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ndio maana nimesema nampa Waziri yale mepesi mepesi. Baada ya kuwa vifaa vingi vimefungwa pale, ile transformer iliyoko pale ni ndogo. Sasa vifaa vingi vinashindwa kufanya kazi. Sasa tukisema vifaa vingi vinashindwa kufanya kazi, maana yake ni kwamba kuna watu wanaendelea kukosa huduma kwa sababu ya shida ya umeme na tatizo ni transformer iliyoko pale ni ndogo. Hilo nalo naamini kwa Waziri wala si suala kubwa, alishughulikiwe mara moja kwa maana ya aidha azungumze na Waziri mwenzake Mheshimiwa January atupatie transformer kubwa, basi kama vipi waweze kununua ili tuweze kupata huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo kwetu ni la muhimu sana, ambalo na lenyewe nalo liko kwenye uwezo wa Waziri. Mji wetu wa Musoma kama nilivyokwisha sema ni mji ambao uko pembezoni. Kwa hiyo lazima tuwe na mikakati ya kuufanya mji ule ukue. Sasa liko suala ambalo mimi binafsi toka ile hospitali inajengwa pale nilianza kuomba kwamba angalau iweze kuwa sehemu ya chuo kikuu kwa ajili ya kufundisha wauguzi pamoja na Madaktari. Baada ya kuwa nimeliomba hilo Serikali imeendelea kuchelewa, lakini bahati nzuri tumekuja kivingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu chetu sasa cha Mwalimu Nyerere kimeleta ombi pale kwamba lile eneo la hospitali yetu ya Kwangwa kwa sababu ni kubwa watukatie pale hekari 20 ili tuweze kujenga pale Tawi la Chuo Kikuu ambacho kitakuwa kinatutolea wataalam kwa ajili ya magonjwa mbalimbali. Kwa hiyo naamini hilo ni suala ambalo liko kwenye uwezo wa Waziri. Akishalitolea hilo uamuzi, basi mara moja kile chuo kikuu kitajengwa pale na Mji wetu wa Musoma na wenyewe nao sasa utakuwa miongoni mwa miji mizuri iliyoko hapa kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni ushauri, Mheshimiwa Waziri sisi wote hapa tumezaliwa na wazazi na kwa sababu tumezaliwa na wazazi, wale wazazi wetu sasa wameshakuwa watu wazima wanahitaji huduma zetu na hata ukiangalia katika nchi zingine zimeelekeza zaidi katika afya au kwenye kuwatunza wazazi. Sasa sisi tulikuja na sera nzuri kwamba wazazi wale ambao wana umri zaidi ya miaka 60 waweze kutibiwa bure. Mpaka sasa wazazi wetu wengi wanataabika, maana akienda mara aombwe kitambulisho hiki, akipeleka hicho kitambulisho mara anaambiwa hizi dawa hazipo. Kwa hiyo wanapata shida sana. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba, kama kuna watu tunahitaji kuwapa bima ya afya ni pamoja na wazazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe tu Waziri kwamba katika yote hilo ujitahidi ulifanyie sana kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Manyinyi.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hii Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu, ambaye ndiye kiongozi wetu Mkuu.

Mheshimiwa Spika, lakini nampongeza na Mheshimiwa Waziri, CDF wetu pamoja na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mnaifanya kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa tulivu na inaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi ninayo maombi mawili na ushauri mmoja tu kwa ufupi. Ombi la kwanza linahusiana na wananchi wangu wa Kata ya Buhare kwenye Mtaa wa Mgalanjago. Wale wananchi kwenye hili eneo vilevile kuna eneo la Jeshi; lakini mnamo mwaka 2008 Jeshi liliweza kuongeza eneo ambalo walimega kwenye maeneo ambayo wananchi wangu walikuwa wanjipatia riziki, pale walikuwa wanafanya shughuli zao, na wakawa wameahidi kwamba watalipwa fidia. Sasa mchakato huo umeendelea kusema kweli mpaka sasa hawajapata fidia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, hawa watu wako kama 26 na barua yao ninayo hapa, naomba mhudumu aje aichukue akupatie hapo ili tuweze kuhakikisha kwamba basi hawa ndugu zetu wa Buhare ambao wanahitaji wapate hiyo fidia yao waweze kupata fidia ili waweze kuendelea na maisha yao kama kawaida.

Mheshimiwa Spika, la pili vilevile ni ombi ambalo bahati nzuri nilishakufikishia Mheshimiwa Waziri. Sasa nikuombe basi, kwamba kule eneo la Bukanga mnamo mwaka 1979 tulipata bahati ya kuwa na ulinzi pale, Jeshi lilichukua maeneo pale kwa hiyo wakahamia pale. Lakini katika yale maeneo waliyokuwa wamehamia, kumbe wakati wanapewa walipewa maeneo ambayo ni makubwa na mengine hawakuyafahamu.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba wao kwa sababu hawakuyafahamu, wale wananchi waliishi katika baadhi ya maeneo. Sasa miaka imekwenda, Jeshi hawajui kama ni ya wale lakini na wale wananchi wanajua ni maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kilichokuja kutokea miaka mitatu iliyopita watu wa MUWASA wakaja kuomba eneo la kujenga tenki la maji, sasa sisi kama wahusika wa eneo hilo tukawapa ili wajenge tenki la maji. Wakati wanaendelea ku-demarcate maeneo haya ndiyo wakagundua kwamba lile ni eneo la Jeshi. Tayari kuna familia au kaya zaidi ya 60 zimeshakaa pale; nadhani hilo linahitaji sana busara ya Serikali ili iweze kwenda na kuona kwamba wale watu tunawafanyaje, kwa sababu Jeshi hawakufahamu na wale wananchi nao hawakufahamu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ombi langu, nadhani hilo nilishakufikishia, kwamba hebu twende wote pale Musoma uende ukaangalie hali halisi halafu tushauriane tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuwasaidia wale wananchi ambao wamekaa kwenye hilo eneo ambalo ni pamoja na huruma ya Serikali kuwapatia ili waendelee kuishi basi maisha yao yaweze kuendelea salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya hiyo, mengine mawili madogo, ninapenda tu kufahamu lile Shirika letu la Nyumbu ambalo ndiyo lilikuwa shirika lililoanza kuwa linatengeneza magari, siku hizi hatulisikii kabisa. Kwa hiyo ninapenda kupata tu maelezo kwamba hivi lile shirika letu limekufa au bado linaendelea.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, niseme la mwisho ambalo ni ushauri wangu, kwamba tunatambua na huwa tunaona hata kule kwetu wakitangaza tu kwamba sasa kuna nafasi za Jeshi, JKT, wako vijana zaidi ya 1,000 wanakwenda pale kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya kuanza kujiandikisha na kuhakikisha kwamba wanapambana ili wapate nafasi ile.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea ni kwamba wale vijana watakaochukuliwa hata katika nchi nzima unakuta wanakaa mwaka au miaka miwili baadaye baadhi yao ndio wanapata nafasi ya kwenda katika vyombo vingine au katika majeshi mengine. Lakini vijana wengi baada ya miaka miwili tafsiri yake ni kwamba wanarudi nyumbani.

Mheshimiwa Spika, sasa wakirudi nyumbani, wale vijana bahati nzuri walishajifunza ukakamavu, walishajifunza ulinzi na mambo mengi ya kuwafanya waendeleze maisha yao, lakini kwa bahati mbaya sana sasa wanarudi kule hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo mimi nilidhani kwamba kuna haja kubwa ya Serikali kuangalia kwamba vijana hawa ni rasilimali kubwa ambao wakitumiwa vizuri kwanza wanaweza kusaidia sana kuendelea kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nilidhani sasa hata kwenye mpango kama huu wa BBT, huu wa kilimo, ni kwa nini Serikali isitoe fedha za kutosha ikawapa JKT ili wale vijana watakapomaliza yale mafunzo badala ya kuwatupa nyumbani wapewe maeneo ya kujiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tena bahati nzuri kwa sababu wao walishafanya mazoezi, ni vijana wakakamavu, wanaweza wakapewa kama mkopo hata kama ni kilimo hicho, wakapata fedha na baadaye wakarudisha ili wale wengine wanaokuja, intake inayofuata, nao waweze kusaidika na mpango huo.

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo tunadhani kwamba kwanza itasaidia sana kupunguza tatizo la ajira, lakini vilevile itasaidia sana kujenga uchumi wa nchi kwa sababu nchi nyingi zinazotuzunguka, majirani zetu, ukienda Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, wote wana mahitaji makubwa ya chakula. Sasa kwa sababu maeneo tunayo, vijana tunao, ardhi tunayo, kumbe tunaweza kuleta ajira kwa vijana wetu lakini vilevile tukawa tumesaidia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani hili ni vizuri Wizara lakini na Serikali ingelipa kipaumbele, kwa sababu moja wapo ya majukumu makubwa ya Serikali yoyote ile ni kuhakikisha kwamba watu wake wanapata ajira. Kwa hiyo hiyo nayo ni avenue nyingine ambayo tunadhani tunaweza tukawasaidia vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Muswada huu ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli na mimi naungana na wenzangu wengi kukushukuru sana Waziri wa Fedha, ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu kwa bajeti yako nzuri hasa hasa ulipokuja kumalizia wakati una-windup, maana watu wakiona mabadiliko yoyote yale ni utaratibu wa kawaida kwamba lazima wa-complain, kama pale walipoona umeweka Sh.100/= kwenye mafuta tafsiri rahisi ikaonekana kwamba basi kila kitu kitapanda.

Sasa ulipokuja kumalizia, nadhani wewe mwenyewe uliweza kuona kwamba kila mmoja aliweza kukupongeza. Kwa utaratibu unaoenda nao ni imani yangu kwamba karibu watu wote ni rahisi sana kuwagusa. Kwa hiyo, hongera sana kwa hilo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Serikali, wakati fulani hivi Wabunge mtaona tunalalamikalalamika kwamba tunapotoa mawazo yetu Serikali wakati mwingine inayapuuza. Ni ukweli usiopingika kwamba kila Mbunge anapokuwa anatoa mawazo huwa anaamini kwamba hayo mawazo yake ni sahihi. Kwa hiyo, wakati mwingine mna kazi ngumu ya kuona namna ya kuya-accommodate yote. Mimi ninao ushahidi thabiti ambao umeendelea kuonyesha kwamba mambo mengi ambayo tunayazungumza basi huwa mnayachukua na huwa mnayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka nilipoingia katika Bunge hili mwaka 2005 kwa mara ya kwanza, kati ya hoja ambayo niliishupalia sana ilikuwa ni hoja ya hawa ndugu zetu wa bodaboda. Serikali ilinisikiliza na hatimaye ikawaweka rasmi, ikawatambua na wakaendelea kufanya kazi kama watu wengine au kama wasafirishaji wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nakumbuka tena katika mchango wangu niliweza kusema kwamba hawa bodaboda wanalipa faini ya shilingi 30,000 anapofanya kosa lakini huyo bodaboda anabeba abiria mmoja, dereva anayebeba abiria 60 au anayeendesha gari kubwa naye bado analipa faini ya shilingi 30,000. Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana na nikuambie tu kwamba bodaboda wengi wamefurahi kuona kwamba tumeweza kuwapunguzia adhabu kutoka shilingi 30,000 mpaka shilingi 10,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kila jambo lina pande mbili; lina faida na hasara. Nilisikia humu baadhi ya concern za Waheshimiwa Wabunge wakisema kwamba kile kitendo cha kuwapunguzia adhabu sasa inawezekana kikasababisha ajali zikawa nyingi, kwa hiyo, hilo nalo linawezekana likawa tatizo.

Sambamba na hilo nilikuwa na ushauri, hivi tunadhani ni kwa nini bodaboda wanasababisha ajali? Pamoja na sababu zingine lakini sababu moja kubwa ni kwamba bodaboda wengi wanapoendesha zile bodaboda hawana leseni na kwa sababu hawana leseni akiwa amepakia abiria akimuona tu traffic maana yake ni kwamba yeye sasa hachagui mahali pa kwenda, mahali popote anaruka matokeo yake abiria wanaanguka lakini vilevile ni pamoja na kusababisha hizo ajali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tujiulize kama kweli lengo letu tunahitaji kuwasaidia hawa watu wa hali ya chini ili na wao waweze kupata maisha mazuri, maana na wao nao wana mahitaji kama ya wale watu wenye kipato cha kati na cha juu, ana watoto anataka waende hospitali, anataka waende shule, ana mke anataka amuhudumie.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu inayochangia hao bodaboda kukosa leseni ni kwa sababu ya gharama kubwa ya leseni. Gharama ya yeyote yule anayetaka leseni hata wa bodaboda sio chini ya shilingi 300,000 maana lazima aende kujifunza kwanza aidha ni VETA au mahali popote ataacha fedha hapo, akitoka hapo ndio aende kwenye kulipia gharama zenyewe za leseni kule TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hali hiyo unamkuta yule bodaboda analipa sio chini ya shilingi 300,000 lakini na yule anayetaka leseni ya kuendesha gari kubwa naye gharama zake ni hizohizo shilingi 300,000, ukiangalia hapa kuna shida. Kwa hiyo, kwa sababu hawana uwezo wa kulipa marejesho na kulipa hizi shilingi 300,000 matokeo yake anaamua kuendesha bodaboda pasipokuwa na leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba ni vizuri hilo Waziri wa Mambo ya Ndani akaliangalia na mkaona namna ya kutoa maelekezo. Hawa bodaboda wawe na utaratibu maalum ikiwezekana kwanza wafundishwe kwa muda mfupi lakini yatolewe mafunzo yao kwa Pamoja. Hili mimi nalisema kwa sababu nilishalifanya, nilishakaa na watu wa VETA na watu wa Red Cross wakakubali kudhamini pamoja na Ofisi ya RTO tukatoa mafunzo maalum kwa vijana wasiopungua 60 walipata leseni siku moja kwa gharama nafuu. Sasa hili likiwa kwa nchi nzima na tukaweka utaratibu mzuri wa namna hiyo basi unaweza ukasaidia zaidi katika kupunguza ajali kuliko hali ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri kuna jambo dogo ambalo liko kwenye ofisi yako. Kwenye ofisi yako kwa maana ya TRA mmeajiri vijana wasiopungua 600 mmewapa ile ajira ya muda, ile ya kujitolea na mnawapa ujira mdogo sana kwa mwezi na wale vijana wanafanya kazi nzuri sana lakini shida inakuja wapi? Inapofika wakati mnapotaka kuajiri hamuwapi wale vijana kipaumbele. Mnapotaka kuajiri mnatoa tangazo kwa kijana yeyote yaani ambaye ameshakaa pale na ambaye hajakaa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwamba kijana amekaa pale miaka mitatu, mnamlipa ujira kidogo halafu inapofika wakati wa kuajiri wakati mwingine huyo mnamuacha na wakati tayari ameshapata uzoefu. Nadhani hili si jambo zuri sana ni vizuri mkawapa wale kipaumbele kwa sababu mmeshawa-retain pale for three years na wamepata uzoefu na wanaweza kuwasaidia vizuri zaidi kuliko kuja kuchukua vijana wengine kutoka nje na kuwaajiri halafu wale mnawaacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hili lingine ni la huko mbele tunakoenda kwamba ni vizuri tukatambua kwamba leo katika nchi hii kama kuna mahali ambapo tuna shida, tunao vijana wengi wanaomaliza vyuo, sekondari au darasa la saba wengi wao hawana ajira. Ni lazima tuangalie mkakati wa kutumia kwamba hivi hili wimbi tunaweza kulipunguza kwa namna gani. Kwa hiyo, nadhani hilo nalo ni assignment ambayo wewe kwa nafasi yako una kila aina ya sababu ya kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)