Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anna Joram Gidarya (15 total)

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi wa Tanzanite uliopo Mkoa wa Manyara ni mgodi ambao unachukua idadi kubwa
ya vijana, lakini kumekuwa na vifo mfululizo miaka tisa sasa ambavyo havijawahi kufanyiwa utafiti wa kina ni kwa nini vifo hivi vinatokea.
Je, ni lini sasa Serikali itakaa na hawa wawekezaji wa vitalu husika ili kuanzisha utaratibu wa kifuta jasho kwa
familia zile ambazo zinapata maafa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa yapo madhara yanayotokana na uchimbaji, siyo katika mgodi wa Tanzanite One peke yake, hata katika migodi mingine. Sheria zinataka kama kuna mtu ameathirika na uchimbaji au na dhuluma yoyote, taratibu za kisheria lazima zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tumelichukua kwa muda mrefu, tunashirikiana na Wizara ya Kazi pamoja na
Kitengo cha Maafa ili kutathmini ukubwa wa tatizo la namna hiyo ili hatua zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, tumeunda timu inayojumuisha Wizara yetu, Wizara ya Kazi pamoja na
Halmashauri husika ili mwezi wa tano tuanze kuyatathmini madhara hayo. Baada ya tathmini itakapofanyika
Mheshimiwa Mbunge, tutakujulisha hatua kamili zitakazochukuliwa.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ugonjwa wa fistula ni ugonjwa ambao umeenea karibu Tanzania nzima. Ugonjwa huu unawadhalilisha akinamama, hususan mikoa yetu ambayo ina jamii ya wafugaji, watu ambao hawahudhurii mara nyingi kliniki. Je, Wizara ina mpango mkakati gani wa kutoa elimu hii kwa kila Wilaya, hasa kwa jamii hii ya wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Gidarya kwamba ugonjwa wa fistula unawadhalilisha sana mama zetu, shangazi zetu, dada zetu katika jamii. Ni jambo ambalo mwanaume yeyote ambaye anawapenda mama zetu na dada zetu hawezi kukubaliana nalo. Nami kama Balozi wa Wanawake nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuboresha huduma za uzazi kwa sababu ndiyo kisababishi kikubwa cha ugonjwa wa fistula ili kupunguza cases za fistula ambazo zimekuwa zikijitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango tulionao kwa sasa ni kutumia kliniki zetu za uzazi ambazo zipo kwenye kila kituo cha kutolea huduma za afya, kuanzia ngazi ya zahanati kwenda ngazi ya kituo cha afya, ngazi ya hospitali ya wilaya mpaka ngazi ya hospitali za rufaa, kutoa elimu kwa akinamama wote na akinababa wote ambao wanafika kuhudhuria kliniki za uzazi salama katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto zinazojitokeza za tiba zimekuwepo na tunaendelea kuzipunguza kwa kuendelea kutoa ujuzi, lakini pia elimu kwa umma juu ya kuwahi kupata huduma za uzazi ili wasipate madhara yanayotokana na mchakato wa uzazi.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Matatizo yaliyoko Katavi yanafanana sana na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Babati Vijijini kata ya Duru vijiji vya Endagwe, Hoshan, Ameyu, Eroton na Wikanzi maeneo haya hayana mawasiliano ya simu. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri ni lini maeneo haya yatapewa vipaumbele ukizingatia uwanja wa ndege wa Manyara unapelekwa Mwikanzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara tutakapopata fedha tutahakikisha tunapeleka mawasiliano katika maeneo haya ya Mkoa wa Manyara na hasa maeneo hayo ambayo tuna kusudia kujenga uwanja wa ndege kama ambavyo Mheshimiwa Anna umeyaeleza.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ya Waziri na swali la msingi kumekuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya wanawake, pia inaonekana kuna matatizo makubwa sana ya kisaikolojia kwa wale watoto wanaokulia pale gerezani kwa sababu mazingira siyo rafiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga kituo maalum kwa ajili ya wale wanawake wanaofungwa wakiwa na mimba na wakiwa na watoto wachanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mazingira ya magereza ya wanawake, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya magereza yetu kila mwaka kadri hali ya uwezo wa bajeti inavyoruhusu ikiwemo maeneo ambayo magereza ya wanawake yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza, tumekuwa tuna utaratibu wa kufanya ziara kwenye magereza haya. Naomba nikiri hapa kama kuna maeneo ambayo yana mazingira mazuri ni magereza ya wanawake kuliko wanaume.
Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwapongeza sana akina mama inaonekana siyo tu katika hali ya maisha ya kawaida lakini hata hali ya gerezani maeneo yao yanakuwa ni maeneo ambayo yanakuwa safi na mazuri zaidi kimazingira pia Serikali inafanya jitihada kwa kutoa kipaumbele maalum katika maeneo ambayo magereza ya akina mama wenye watoto yapo.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na kuwa lugha yetu ya Taifa ni kiswahili lakini kumekuwa na mkanganyiko katika mfumo wetu wa ufundishaji wanafunzi. Shule nyingi za Serikali kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba wanafundisha kwa kiswahili lakini wakifika sekondari wanaambiwa wazungumze lugha ya kiingereza. Sambamba na hilo, tatizo hili liko kwenye vyuo vyetu vya Serikali ya Mitaa hususan Hombolo. Masomo yote yanafundishwa kwa kiingereza ilhali watu hawa wanaenda kusimamia watu ambao hawajasoma.
Je, Serikali haioni ni muhimu kubadilisha mitaala hii kuondoa mkanganyiko huu katika sera ya ufundishaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunamshukuru kwa kuwa ni mdau wa kiswahili na kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kuwa Balozi wa Kiswahili Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya msingi kiswahili imekuwa ndiyo lugha ya kufundishia na kiingereza inakuwa kama somo. Tunafanya hivyo kwa sababu tunaamini Watanzania wengi lugha ya kiswahili japokuwa ni lugha ya pili, lakini wana uelewa zaidi na hivyo kuwawezesha kuelewa vizuri elimu yao ya msingi katika lugha ambayo wamekuwa nayo. Hali kadhalika tunapokwenda kwenye sekondari ndipo sasa wanapotumia lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia na kiswahili kama somo na hiyo sasa inaenda vilevile kwa upande wa zile shule zinazotumia lugha za kiingereza toka awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu hakatazwi kuweka msisitizo katika lugha ile ambayo anafahamu inaeleweka na wanafunzi kwa uzuri zaidi ili kumfanya yule mwanafunzi kile kilichofundishwa aweze kukitafsiri katika lugha yake iliyo rahisi na kukielewa vizuri zaidi. Ieleweke kwamba lugha pekee siyo maarifa. Lugha pamoja na yale maarifa unayofundishwa ndiyo yanayomfanya mwanafunzi kuwa imara na kuweza kutumika katika nyanja mbalimbali zinazohitajika. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo. Kwanza, Mheshimiwa Waziri kwenye majibu yake amesema wameunda madawati 516, pamoja na madawati haya ni idadi ya watoto wangapi waliokufa kwa kukeketwa?
Pili; Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na takwimu zinazoonesha 2016/2017, ni hatua zipi na ni watuhumiwa wangapi ambao wamechukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza, kuhusu takwimu za watoto waliokeketwa, mpaka sasa hatuna takwimu halisi za watoto ambao wamekeketwa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa vitendo hivi vinafanyika katika zama hizi katika mazingira ya usiri mkubwa kwa sababu Serikali imetoa jicho lake kila kona kwamba vitendo hivi toka tumevi-criminalize kwenye Sheria ya Mtoto mwaka 2006. Mpaka sasa tumekuwa wakali, tumeanzisha hayo madawati, tumetoa mafunzo kwa Polisi na kwa kiasi kikubwa kila mtu sasa amekuwa aware kwamba hili ni tatizo na sio mila tu ambayo tunairuhusu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, vitendo hivi sasa vimehamishwa kutoka utaratibu wa kizamani wa kimila ambapo vilikuwa vinafanyika wazi na kwa sherehe na sasa vinafanyika katika taratibu za usiri. Kwa hivyo imekuwa ngumu kwa kweli kuweza kutengeneza takwimu halisi za namba ya watoto ambao wamekeketwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni watu wangapi ambao wamewahi kukamatwa kwa vitendo vya ukeketaji. Mpaka sasa pia sina takwimu halisi mahsusi hasa za kuhusu wakeketaji, kwamba wangapi wamewahi kushtakiwa na wangapi wamewahi kuhukumiwa. Kwa sababu pia toka tumetunga hiyo sheria kama nilivyosema awali hata wale Mangariba ambao walikuwa ni mashuhuri kwa kukeketa nao pia hawakeketi waziwazi na hawakubali pia kukeketa kwa sababu wanajua ni kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumeona kwa sababu bado vitendo vinaendelea kwa njia za kichini chini ni vema tukatumia njia mbadala za kufanya kazi na Mangariba kwa kuwaelimisha, kuwajengea uwezo lakini pia kuwapa tahadhari kwamba kitendo hiki ni kosa la jinai na kwamba akikutwa anafanya kitendo hicho, yeye, wazazi wa mtoto, ndugu wa mtoto na watu wote ambao wamesherehekea kitendo hiki kifanyike, wanachukuliwa hatua kali za kisheria. Kwa hivyo, hata Mangariba nao wamekuwa wanasita kushiriki kufanya vitendo vya ukeketaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tumeanza mradi wa kufanya njia mbadala ya kufanya graduation ya watoto kwenda kwenye ujana ambayo inajulikana kama Alternative Rights of Passage (ARP) ambapo tunatumia sasa Viongozi wa Kimila zaidi, hao Mangariba pamoja na Viongozi wa Kimila kama Malaigwanan, Machifu na Watemi kwenye maeneo mbalimbali ili kuwaelimisha kuhusu jambo hili na kuwaambia kwamba mtoto anaweza akahitimu kutoka kwenye utoto kwenda kwenye utu uzima bila kukatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo, anapata mafunzo yote ambayo yanahusu mambo ya kiutu uzima kwa sababu sasa anakua bila kukatwa na tunapata mafanikio makubwa na ndio maana vitendo hivi vimepungua kwa kiasi kikubwa.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Waziri kumekuwa na tatizo la viwanja katika maeneo mengi, kwa mfano Mkoa wetu wa Manyara ni Mkoa unaoongoza Tanzania nzima kwa kuiletea nchi hii medali hasa kwenye michezo ya riadha. Lakini kumekuwa na tatizo la viwanja vya muda mrefu, wachezaji hawa wanaenda kufanya mafunzo Arusha.
Ni lini sasa Serikali itatujengea kituo cha mafunzo kwa ajili ya kuendeleza vipaji hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema katika majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tumezitaka Halmashauri zote nchini kutenga viwanja vya michezo ya aina mbalimbali hiyo ni hatua ya kwanza. Lakini hatua ya pili, Serikali tumeanzia na kujenga complex ya michezo kwa ajili ya michezo yote hapa Dodoma na nadhani tukiwa tunapita kuelekea Dar es Salaam tunaiona.
Mheshimiwa Spika, kimsingi niseme tu kwamba hata Sera yetu ya Michezo inaelekeza kwamba masuala ya viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali yanatakiwa ushiriki wa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni na taasisi mbalimbali, hivyo niombe Halmashauri ishirikiane na wadau mbalimbali ili kuweza kuanzisha kituo cha michezo. Ahsante.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa pia na kero katika sekta ya uwindaji katika utoaji leseni hasa kwa wazawa. Soko hili limemilikiwa zaidi kwa wageni kuliko wazawa. Kwa mfano, leseni ya uwindaji kwa mwaka unalipa dola 600 na tena unalipa dola 200.
Je, Wizara haioni umuhimu wa kuwapa wazawa zaidi ili pia waweze kulinda hifadhi zetu? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka uliopita wa uwindaji unaoishia mwezi Juni, 2017 vitalu vilivyokuwa vimetolewa asilimia 85 walipewa wazawa na ni vitalu asilimia 15 tu ambavyo walipewa wageni. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba utoaji wa vitalu unawapendelea wageni.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na utaratibu wa Serikali pindi tu mawe yanapotoka kulazimisha wamiliki kupitisha mawe hayo kwenye chumba maalum (strong room) kabla ya kuuzwa mnadani, jambo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa wamiliki wa vitalu kutokuwalipa wafanyakazi hao kwa wakati.
Je, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuondoa usumbufu huu kwa wamiliki wa mgodi huu wa Tanzanite?
Swali la pili pamoja na wamiliki wa migodi wa Tanzanite kuwa na vibali halali kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuuza mawe hayo kwenye mnada kwa bei ya kutupa; je, Serikali haioni kama wamiliki hawa wa migodi wanapata hasara kubwa pamoja na kuwa wanalipa kodi ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka nieleze tu kwamba tunawalazimisha watu kupitisha mawe kwenye strong room kabla ya kuuzwa, lengo letu ni moja tu kutaka kujua uhakika wa kiasi gani cha mawe yamezalishwa ili Serikali iweze kupata kodi zake na tozo zake mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili hatuwezi kurudi nyuma madini haya ya Tanzanite yamekuwa yametoroshwa na nchi hii imepata aibu kubwa. Asilimia 20 tu ya madini yote ya Tanzanite yanayochimbwa ndiyo tunaweza kuyaona yameingia kwenye mfumo wa Serikali. Kwa hiyo, tumeweka nguvu kubwa ya udhibiti na usimamizi na hili Mheshimiwa Anna ninamwomba aunge mkono juhudi za Serikali kwenye jambo hili tusirudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili utaratibu wa kuuza mawe haya kwenye mnada ni utaratibu ule ule na umekuwepo kwa muda mrefu, bei iliyopo pale sio bei ya kutupwa ni bei ya ushindani wale wanaotaka kununua wote wanakwenda kwenye eneo la mnada wanatoa bei zao yule anayeshinda anapewa kwa bei nzuri. Hili tunataka kulifanya kwa uzuri zaidi na litakuwa katika Mkoa wa Manyara ili lisimamiwe vizuri zaidi Serikali iweze kupata kodi zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ya Waziri na swali la msingi kumekuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya wanawake, pia inaonekana kuna matatizo makubwa sana ya kisaikolojia kwa wale watoto wanaokulia pale gerezani kwa sababu mazingira siyo rafiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga kituo maalum kwa ajili ya wale wanawake wanaofungwa wakiwa na mimba na wakiwa na watoto wachanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mazingira ya magereza ya wanawake, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya magereza yetu kila mwaka kadri hali ya uwezo wa bajeti inavyoruhusu ikiwemo maeneo ambayo magereza ya wanawake yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza, tumekuwa tuna utaratibu wa kufanya ziara kwenye magereza haya. Naomba nikiri hapa kama kuna maeneo ambayo yana mazingira mazuri ni magereza ya wanawake kuliko wanaume.
Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwapongeza sana akina mama inaonekana siyo tu katika hali ya maisha ya kawaida lakini hata hali ya gerezani maeneo yao yanakuwa ni maeneo ambayo yanakuwa safi na mazuri zaidi kimazingira pia Serikali inafanya jitihada kwa kutoa kipaumbele maalum katika maeneo ambayo magereza ya akina mama wenye watoto yapo.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mazingira yaliyopo Kondoa yanafanana na mazingira yaliyopo Babati Vijijni. Zahanati ya Galapo ni Zahanati ya muda mrefu, imepandishwa kuwa Kituo cha Afya, lakini mpaka sasa hatuna jengo la upasuaji. Kwa nguvu za wananchi tumejitahidi mpaka tumepaua hilo jengo. Mpaka sasa tuna vifaa vya hicho chumba cha upasuaji lakini tuna changamoto ya kumalizia hilo jengo ili litumike. Ni lini sasa Serikali itapeleka pesa za kumalizia hilo jengo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeze dada yangu Mheshimiwa Anna kwa swali zuri, lakini nawapongeza Wabunge wa Babati na kaka yao Mheshimiwa Jitu Soni kwa pamoja. Nafahamu Babati Vijijini ina changamoto kubwa ya afya na ndiyo maana kwa Zahanati ya Galapo ambayo imepandishwa lakini kwa sasa kipaumbele chetu kwamba tumeanza na vituo viwili vya afya, kile ni cha kwanza na sasa hivi tunaenda katika Kituo cha Magugu, kwa sababu tunajua pale Magugu ni center kubwa sana gari nyingi zinapita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo tumeweka kipaumbele na hata hivyo ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Kituo cha Afya cha Galapo tutafanya kila liwezekanalo kwa mipango ya Serikali tuweze kukiimarisha kwa ajili ya wananchi wa Babati Vijijini waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, natambua kazi kubwa wanayofanya Waziri wa Afya na Naibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri waliyompelekea haya majibu wamemdanganya, kwa sababu mimi ni tomaso, naomba niambatane naye, nikapapase mwenyewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyoko kwenye hiki kituo ni matatizo makubwa sana. Kama kuna kitu ambacho Wizara haifahamu katika kile kituo kuna wazee 52 na katika hao 52 kuna wazee wanne ni kati ya wazee waliyopigania Vita vya Pili vya Dunia.
Mheshimiwa Spika, tuna matatizo makubwa ya Watumishi wa Afya tuna Watumishi wawili tu, mmoja anakaa Babati Mjini na mwingine anakaa kilometa moja na nusu kutoka kwenye kituo, maana yake usiku kukitokea dharura wale wazee hawapati huduma za haraka. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea nyumba wale watumishi wapate kuishi karibu na wale wazee?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nchi nzima idadi ya wazee inajulikana na kwa kuwa umri mkubwa wa uzee ndiyo unaopatikana na magonjwa makubwa nyemelezi pamoja na kuwa Serikali imesema huduma ya wazee ni bure. Je, Serikali iko tayari kuwapatia bima wazee wote nchi nzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, labda nianze kwa kusema kwamba kuwepo na idadi kubwa ya wazee ambao sasa hivi wanafikia milioni 2.7 ni ishara kwamba kumekuwa na maboresho makubwa sana katika huduma ambazo tumekuwa tunazitoa katika ngazi ya afya, vilevile hali ya lishe na matunzo ambayo tumekuwa tunayatoa kwenye jamii yetu, kwa hiyo ni kitu ambacho najivunia. Sasa hivi umri wa kuishi wa Mtanzania umefikia miaka 65 wastani, kwa hiyo, ni jambo jema ambalo tunapaswa kujivunia.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Anna Gidarya ni kweli tunatambua kwamba Serikali tumeendelea kuwa tunaboresha makambi haya ya wazee kadri uwezo unavyoongezeka. Pia hili ombi la kuhakikisha kwamba tunakuwa na nyumba katika kituo hichi cha Magugu, tutalifanyia kazi katika bajeti kama nilivyokuwa nimesema kwamba tuna fedha ambazo tumezitenga katika bajeti hii ambayo ipo.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, sasa hivi Serikali ipo katika mapitio ya sera ya afya. Katika sera ambayo tunaenda nayo sasa hivi ya mwaka 2017/2018 ambayo tunayo sasa hivi, tumekuwa tunasema kwamba matibabu kwa wazee yatakuwa ni bure, lakini sasa hivi Serikali tunaelekea katika mfumo wa kuwa bima ya afya kwa wote na masuala ya haki ya wazee yatazingatiwa katika sera hii mpya.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba kuhusiana na ombi lake la ziara kwenda kupapasa niko tayari kufanya Jumapili. (Kicheko)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, asante, nasikitika majibu ya Serikali kwa asilimia 90 ni uongo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi hawa walikaa kwenye hilo eneo miaka 20 iliyopita, fidia wanayosema ya kifuta jasho katika yale mabanda au tuseme zile nyumba waliwathaminishia TANAPA bila kuwashirikisha, kila mmoja fidia haikuzidi shilingi 300,000.
Mheshimiwa Spika, muda wote huo bila kuangalia riba wananchi walikaa mitaani na watoto wao waliathirika walikosa na masomo kwa sababu walifukuzwa watoto wakawa wanakaa kwenye nyumba za watu baki. Leo hii Serikali inasema imelipa, siamini katika hili. Mheshimiwa Waziri upo tayari kwenda Babati kwa ajili ya kuhakikisha kama mgogoro upo au haupo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, TANAPA imelazimisha kuweka mipaka ya kudumu bila kuwashirikisha wahusika wenyewe wa mgogoro. Mkurugenzi anayezungumziwa kwamba amelipa, walienda kutoa amri yeye na Mkuu wa Wilaya mipaka ikawekwa, wananchi hawakushirikishwa, mgogoro huo haukuisha mpaka sasa. Lakini ni kwa nini sasa Serikali katika maeneo yenye migogoro ya hifadhi wamekuwa wakatili kupitiliza, wananchi hawa ni Watanzania au sio Watanzania?
Mheshimiwa Spika, tunaomba majibu ya Serikali ili tusiumane umane hapa kila siku tunarudia suala la Ayamango na Gedamar, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia kuhusu haya maeneo na mgogoro huu, amekuwepo mstari wa mbele sana, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema, mgogoro huu umekuwepo kwa muda mrefu, lakini kilichokuwepo mwanzoni, hata hifadhi yenyewe ilikuwa bado haijajua mipaka yake na ndiyo maana mwaka 2004 walipoenda kuhakiki mipaka ilibainika kwamba hata baadhi ya maeneo ya hifadhi yalikuwa yako nje kwa sababu hata hifadhi yenyewe ilikuwa haijui. Lakini waliofanya uhakiki ilikuwa ni Wizara ya Ardhi ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuhakiki mipaka, ndio waliofanya. Sisi hatuhakiki, Wizara ndiyo wanatuonesha mipaka kwa ramani hii kuwa mipaka ni hapa na hapa, kwa hiyo, naamini kabisa kwamba walifanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kuongozana naye, naomba nimhakikishie niko tayari baada ya Kikao cha Bunge tuongozane twende tukaangalie hali halisi iliyopo ili tuone kama bado mgogoro upo tuweze kuutatua kwa pamoja na wananchi waweze kushirikishwa katika utatuzi wa huu mgogoro. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Napenda tu kulihakikishia Bunge lako kwamba migogoro ya mipaka hasa katika maeneo ya hifadhi tayari Wizara kwa kushirikiana na TANAPA, tunavyo vijiji vipatavyo 427 katika hifadhi nane ambavyo hatua za uhamasishaji kwa ngazi ya mkoa na wilaya zimeanza, baadaye zitashuka kwenye ngazi ya vijiji na kote huko kutapimwa ili kuweza kupanga pia matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo na tayari pesa, shilingi bilioni nne, zimeshatolewa katika Kitengo chetu kile cha Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi, kwa hiyo, tuna imani na Tarangire ipo, itakwenda kufanyiwa kazi ili kuondoa utata wa mipaka. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Natambua juhudi kubwa anayofanya Naibu Waziri. Michezo ni sekta muhimu, lakini pamoja na hivyo, vyuo vyetu vikuu havina vipaumbele vya miundombinu ya viwanja. Mfano mzuri ni mwaka jana, tulikuwa na mashindano ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, tulikuwa na michezo...

MWENYEKITI: Uliza swali tu Mheshimiwa.

MHE. ANNA J. GIDARYA: …kulikuwa na michezo kumi na tisa, Tanzania tulishiriki michezo tisa tu jambo ambalo
limesababisha nchi yetu kukosa vikombe vingi. Je, ni lini sasa Serikali itaboresha miundombinu na kuipa michezo kipaumbele katika vyuo vyetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Anna kwa sababu kwanza ni mwanamichezo mahiri, lakini vilevile ni Kiongozi wa CHANETA Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali lake la msingi, ametaka kujua kwamba ni lini sasa Serikali itaweza kuboresha viwanja vya michezo, hususan kwenye vyuo vikuu. Nikiri kwamba ni kweli mwaka jana tulikuwa tuna mashindano na yeye mwenyewe pia alishiriki, pamoja na kwamba tuna uhaba wa viwanja vya michezo, lakini kama ambavyo tumekuwa tukisema kwamba Sera yetu ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inasisitiza kwamba suala la michezo sio suala la Serikali peke yake, ni suala la Serikali lakini vilevile tuweze kushirikiana pamoja na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuweza kuwaambia na kuwaomba Wabunge wote kuiga mfano wa Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu kwa namna ambavyo amefanya maboresho ya kiwanja kule Lindi. Kwa hiyo suala hili la michezo sio suala la kuiachia Serikali peke yake, tuendelee kushirikiana pamoja na Serikali na sisi kama Wizara tuko tayari kuendelea kutoa utaalam pamoja na mafunzo mbalimbali namna gani ya kuweza kuboresha hivyo viwanja.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo lililoko Babati Vijijini ni tatizo pia lililoko Kiteto, Vijiji vya Makame, Ishkribo, Asamatwa, Ngaboro, ni lini sasa vijiji hivi vitaunganishwa pamoja na hivi Vijiji vya Endagwe, Hoshan, kwa ajili ya kufanya tathmini ili wananchi wapate huduma ya mawasiliano?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kijiji cha Landanai kilichoko Simanjiro na Kijiji cha Ngage, ni vijiji ambavyo vina idadi kubwa ya watu lakini mpaka sasa vijiji hivi havijafanyiwa uthamini kwa ajili ya kupata mawasiliano hayo. Ni lini sasa Serikali itapeleka huduma hii Landanai?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Gidarya, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kiteto alivyovitaja, bahati nzuri vimekwishaletwa mezani kwangu na Mbunge wa Kiteto, kupitia Chama cha Mapinduzi kwamba havina mawasiliano na tumekwishaviingiza kwenye orodha ya vijiji vitakavyopelekewa huduma ya mawasiliano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namshauri tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi vijiji alivyovitaja vitapepelekewa mawasiliano na vijiji vingine hivyo vyote alivyoviulizia Mheshimiwa Mbunge, tayari ninayo orodha yake nililetewa na Mbunge wa jimbo husika. Nimhakikishie tu Mheshimiwa tukitoka hapa tunaweza kuwasiliana ukaangalia orodha ya vijiji hivyo kuona kama vimeshaingizwa au la, kwa sababu nina hakika vyote vimeshaingizwa.