Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anna Joram Gidarya (6 total)

MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mkoa wa Manyara ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa ukeketaji wa watoto wa kike; takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza Kitaifa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kukomesha ukatili huo wa kijinsia pamoja na kutoa semina elekezi kuhusu madhara yatokanayo na ukeketaji wa mtoto wa kike hususan Wilaya ya Hanang, Simanjiro, Kiteto na Mbulu?
(b) Kwa kuwa, Ngariba sasa wanatumia mbinu mbadala za kuwakeketa watoto wa kike wa kuanzia miezi sita (6) hadi mwaka mmoja na miezi sita. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakamata Ngariba wote wanaofanya ukatili huo na kuwachukulia hatua za kinidhamu, hatua za kibinadamu ili wawe sehemu na fundisho la kukomesha ukatili huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango madhubuti wa miaka mitano wa kutokomeza vitendo vya ukatili ujulikanao kama Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/2018 – 2021/2022) ulioandaliwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na asasi mbalimbali za kiraia. Kupitia mpango kazi huu, Serikali imedhamiria kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji wa watoto wa kike kutoka asilimia 32 ya mwaka 2016 mpaka kufikia asilimia 11 ifikapo 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango kazi huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, iliwapatia mafunzo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote 26 na baadhi ya asasi za kiraia yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza mpango kazi huu. Aidha, kuanzishwa kwa madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi ambapo hadi sasa kuna jumla ya madawati 516 kumeongeza mwamko wa wananchi kujiamini na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji wa watoto wa kike katika maeneo yao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na watoa huduma wa afya ya mama na mtoto, Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa iliyoshamiri vitendo vya ukeketaji ikiwemo Mikoa ya Manyara na Dodoma imeweza kusambaza dodoso ili kuwatambua wale watoto waliofanyiwa kitendo cha ukeketaji pale wanapopelekwa kliniki. Katika zoezi zima la upimwaji wa maendeleo ya mtoto watoa huduma hao huwachunguza watoto kama wamekeketwa. Aidha, zoezi hili pia hufanyika kipindi mtoto anapoenda kuanzishwa darasa la kwanza, ikitokea mtoto amekeketwa wazazi/walezi huchukuliwa hatua kali za kisheria.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mgodi a Tanzanite ulioko Mererani, Wilaya ya Semanjiro ni mgodi wenye idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi katika mgodi huo na kumekuwa na historia ya matukio ya maafa kila mwaka ya vifo vya watu wengi.
(a) Je, Serikali imefanya utafiti gani ili kubaini chanzo cha maafa hayo yanayolikumba Taifa kila mwaka na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa letu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha utaratibu maalum kwa wamiliki wa vitalu vya Tanzanite kuwalipa kifuta jasho wahanga wote wanaopatwa na maafa wanapokuwa kazini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya taarifa za ajali yanaonesha kuwa ajali nyingi husababishwa na wachimbaji wadogo kutokuzingatia tahadhari ya usalama wanapotekeleza majukumu yao ya uchimbaji madini. Hivyo, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji na kuwaelimisha wachimbaji kuchukua tahadhari za usalama wakati wa kufanya kazi pamoja na kuwahamasisha kuunda timu za wakaguzi katika maeneo yao kutoka miongoni mwa wachimbaji ambao hupewa elimu ya ukaguzi na wataalam wetu wa Wizara ya Madini. Hivyo, nawasihi wachimbaji wa madini kutambua umuhimu wa kuzingatia taratibu na usalama wa kazi kwa uchimbaji ili kulinda afya na uhai wao.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kupitia Sheria Namba 20 ya mwaka 2008 ya Fidia ya Wafanyakazi. Wizara itahamasisha wamiliki wa leseni na wachimbaji kujiunga na mfuko huu ili kupata kifuta jasho wanapopatwa na maafa wanapokuwa kazini.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Kituo cha Wazee Sarame kilichopo Magugu, Wilaya ya Babati Vijijini ni kituo cha muda mrefu ambacho kinahudumiwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya. Kituo hiki kina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi, usafiri wa dharura, huduma ya kwanza, vifaatiba na miundombinu ya barabara:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma zote za msingi katika kituo hicho ikizingatiwa kuwa wazee wengi ni walemavu wa viungo, vipofu, waliopooza na viziwi pia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa huduma za msingi katika makazi ya wazee na watu wenye ulemavu, wasiojiweza ikiwa ni pamoja na wanaotunzwa katika makazi ya Magugu yaliyopo katika Halmashauri ya Babati Vijijini. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 Serikali imepeleka fedha kiasi cha Sh.14,631,935.47 kwa ajili ya chakula na Sh.900,000 kwa ajili ya dharura zinazojitokeza, bajaji moja katika makazi hayo kwa ajili ya kurahisisha usafiri.
Mheshimiwa Spika, aidha, makazi ya Magugu yamepata huduma ya upulizaji wa dawa za kuuwa wadudu kwa maana ya fumigation mwezi Mei, mwaka huu 2018. Wizara imeendelea kupeleka vifaa vya usafi na huduma ya kwanza kwenye makazi yote ya wazee ikiwa ni pamoja na makazi ya Magugu. Aidha, uboreshaji wa huduma na miundombinu katika makazi utaendelea kufanyika kadri ya fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, sambamba na haya, Serikali bado inatambua kuwa zipo changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za msingi kwenye makazi ya wazee na ili kukabiliana nazo Serikali katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, imetenga jumla ya fedha Sh.27,032,000 kwa ajili ya chakula na Sh.3,600,000 kwa ajili ya dharura. Aidha, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilitenga bajeti ya Watumishi wa Ustawi wa Jamii wapatao 24 na katika bajeti ya Mwaka 2018/2019, Wizara imetenga bajeti ya watumishi 60. Wizara inaahidi kuwapeleka baadhi ya Watumishi hawa kwenye makazi ya wazee Magugu yaliyopo Sarame-Babati Vijijini pale tu tutakapopata kibali cha ajira zao.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mkoa wa Manyara ni moja kati ya maeneo yanayokubaliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi katika wananchi wa Babati Vijijini hasa katika Vijiji vya Amayango, Gedamara na Hifadhi ya Tarangire kwa takribani miaka 11 sasa bila ufumbuzi wowote, migogoro hiyo imesababisha wananchi kukosa elimu, afya na uchumi kushuka ambapo majengo ya jamii yaliyopo ni madarasa manne, bweni moja, matundu 13 ya vyoo vya shule na jengo la zahanati na majengo haya yote yamejengwa kwa nguvu za wananchi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro hiyo iliyodumu kwa muda mrefu na kurudisha maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na hifadhi?
• Endapo itabainika mipaka kati ya vijiji na hifadhi iliyooneshwa kwenye ramani ni batili. Je, Serikali husika iko tayari kuwalipa fidia wananchi wote walioathirika na migogoro hiyo kwa muda wa miaka 11?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uhakiki wa mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire na Vijiji vya Gedamar na Ayamango ulifanywa na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 2004 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 160 la mwaka 1970 lililoanzisha Hifadhi ya Taifa Tarangire. Baada ya uhakiki huo eneo hilo lilisimikwa vigingi (beacons) vya kuainisha mpaka wa hifadhi na vijiji husika ambao unafahamika kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika uhakiki huo ilibainika kuwa kaya 245 za vijiji vilivyotajwa hapo juu zilikuwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa Tarangire kimakosa. Ili kuwaondoa wananchi wa vijiji hivyo kutoka kwenye eneo la hifadhi, Serikali iliamua kuwalipa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la hifadhi kifuta jasho kilichohusisha fidia ya mali, posho ya usumbufu, posho ya makazi na gharama za usafiri.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Vijiji vya Gedamar na Ayamango walilipwa jumla ya shilingi 137,845,592 tarehe 2 Februari, 2011 kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati. Baada ya malipo ya kifuta jasho wananchi wengi waliondoka isipokuwa kaya 42 ambazo ziliomba kupewa eneo mbadala la kuhamia. Halmashauri ya Wilaya ya Babati ilikubali kuwapatia wananchi hao eneo maeneo ya kuhamia kwenye shamba la Ufyomi lililopo Gallapo ambapo wananchi hao wameshapatiwa maeneo katika shamba hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Vijiji vya Gedamar na Ayamango na Hifadhi ya Tarangire na mpaka uliopo kati ya hifadhi na vijiji hivyo ni sahihi.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-

Jimbo la Babati Vijijini linakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya mawasiliano ya simu hasa katika Vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso ambako hakuna kabisa mnara wa mawasiliano ya simu:-

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo katika maeneo ya vijiji husika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuratibu utekelezaji wa jitihada muhimu za kuwezesha maeneo yote nchini kufikiwa na huduma za mawasiliano sawasawa na maelekezo ya Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016. Kupitia Mfuko wa Mawasiano kwa Wote Serikali itaviainisha Vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso kwa kuangalia ukubwa wa eneo, idadi ya wakazi wake pamoja na kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya ruzuku kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini kukamilika, vijiji hivyo vitajumuishwa katika orodha ya miradi itakayoingia katika zabuni zinazotarajiwa kuingizwa katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. ANNA J. GIDARYA) aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa Serikali imekaa kimya kuhusu ajira kwa vijana, kumekuwa na wimbi kubwa la vijana mitaani wasio na ajira waliomaliza vyuo mbalimbali takriban miaka mitatu iliyopita.

(a) Je, ni lini Serikali itafungua milango ya ajira kwa vijana wa Kitanzania walioteseka kwa muda mrefu?

(b) Je, Serikali imefanya tathmini ya kiwango cha madhara yaliyotokana na vijana kukosa ajira?

(c) Je, ni vijana wangapi wameathirika na kujiingiza katika makundi mabaya kwa kukata tamaa ya kupata ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya Mbunge wa (Viti Maalum) lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008, Miongozo ya ILO na Kikanda, Ajira inajumuisha shughuli zinazokubalika kisheria ambazo ni za uzalishaji mali, zenye kufanikisha malengo ya kazi zenye staha na zinazozalisha kipato. Hivyo, ajira ni hali ya mtu kuajiriwa au kujiajiri kwa ajili ya kujiingizia kipato halali.

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kama mmoja wa waajiri wakuu imeendelea kuajiri kupitia Taasisi zake mbalimbali kila mwaka kwa kuzingatia mahitaji na bajeti. Hata hivyo, kupitia Sera na Mipango mbalimbali ya Serikali katika kuchochea Uwekezaji na Viwanda, shughuli nyingi za kiuchumi zimeongezeka hali ambayo pia imesaidia katika upatikanaji wa nafasi za ajira hasa katika kundi hili kubwa la vijana. Utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati imekuwa ni chachu kubwa katika kuongeza wigo mpana wa upatikanaji ajira. Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 jumla ya ajira Serikalini ikijumuisha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma zilikuwa 184,141. Aidha, katika ajira za miradi ya maendeleo ya Serikali zilikuwa 787,405, na ajira zilizozalishwa na Sekta Binafsi zilikuwa ni 646,466.

(b) Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba ukosefu wa ajira kwa vijana una madhara kiuchumi na kijamii. Ukosefu wa ajira unapunguza mchango wa nguvukazi isiyo na ajira katika Pato la Taifa pamoja na jitihada za Serikali kupunguza umasikini. Aidha, kunapunguza uwezo wa nguvukazi hiyo kuweza kujitegemea na kuendelea kuwa tegemezi kwa jamii. Ili kupunguza tatizo hilo Serikali imeandaa mikakati mbalimbali za kuwawezesha vijana kuajiriwa au kujiajiri. Mikakati hiyo ni pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo katika kipindi cha Mwaka 2017-2019 jumla ya vijana 47,585 wamewezeshwa kiujuzi na kujiajiri katika sekta mbalimbali.

(c) Mheshimiwa Spika, suala la vijana kujiingiza katika makundi mabaya ni suala la maadili na makuzi. Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana imekuwa ikiandaa miongozo ya maadili na makuzi kwa vijana na imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kwa vijana nchini.