Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anna Joram Gidarya (13 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia lakini pia ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jengo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, ndugu zangu naomba nitangulize neno la utangulizi. Naomba tujifahamu kwamba sisi ni Wabunge lakini utumishi wetu unalenga nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo machache na kwanza naomba nianze na afya. Katika hili kabrasha nimesoma pesa zilizowekwa kwa ajili ya on call hasa kwa Mkoa wangu wa Manyara, Babati TC hazitoshi kabisa. Pesa hizi ni kidogo sana ukizingatia idadi ya madaktari waliopo. Babati TC ina daktari mmoja wa anesthesia, sidhani kama huyu daktari mmoja anajitosheleza na hii on call.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la elimu. Babati TC ina takribani shule za sekondari zisizopungua 36 lakini tuna walimu wa masomo ya sayansi wachache mno. Shule moja ina mwalimu mmoja wa masomo ya sanyansi, kwa wiki ana vipindi 49, sijui mwalimu huyu anajigawaje katika maandalio ya somo na mpaka hatua ya kukamilisha hii kazi ya kuwafundisha wanafunzi. Tuna upungufu mkubwa sana wa walimu, kuna shule zilizopo maeneo ya mijini walimu wamerundikana humo kwa kigezo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya walimu hao wapimwe. Walimu wengine wa vijijini wanapiga mizigo, siku nzima mwalimu halali mpaka saa kumi na mbili lakini muda wa kazi uliopangwa unajulikana. Kwa nini wengine wawe wana kula bata mjini na wengine wapo vijijini wanakula mzigo, haiwezekani! Namshauri Waziri mwenye dhamana hii walimu hao wapimwe. Mfano mzuri ni shule ya Babati Day, kuna walimu zaidi ya 22 wamerundikana pale lakini shule za pembezoni hazina walimu na tunasema elimu bora, tutaipataje?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye utawala bora. Mkoa wa Manyara kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambayo chanzo chake ni watawala wakuu wa maeneo hayo husika. Kwa nini nasema hivyo? Eneo lenye migogoro mikubwa ya ardhi ni maeneo yenye hifadhi mfano Galapo. Eneo hili watawala wana maeneo, imagine Mkuu wa Mkoa ana hekari 400 halafu Mkuu huyo huyo wa Mkoa ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, anasuluhisha nini? Anaendaje kwanza ku-face wale wananchi wenye matatizo? Mkuu wa TANROAD ana heka 500, RPC ana heka 300, leo hii mnawahamisha wale watu mnawapeleka wapi, inawezekanaje? Tumejibeba mno kuliko wale wadhaifu ambao wametuweka sisi tuwatawale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Waziri wa Ardhi aende Galapo, akinihitaji mimi anitafute nitampeleka na nitamuonyesha hayo mashamba. Mwezi wa pili tulienda na Naibu Waziri wa Maliasili kuangalia mipaka ya watu wa Ayamango, wanampeleka sehemu ile ambayo haitakiwi, kisa wanajificha. Waziri wa TAMISEMI, nakuomba baba yangu kawamulike Wakuu wa Mikoa. Iweje mimi niteuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa halafu miezi mitatu, minne tayari nina heka 200, nimepewa kwa sababu nimefanya kazi gani, lazima tujiulize. Mnasema migogoro haiishi, migogoro ya Manyara ni ya muda mrefu ni kwa sababu watawala wakija wametanguliza mikono. Unachukua hapa, unapeleka pale halafu wewe ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Waziri akija anapapaswa huko anaambiwa maneno mengi, ndiyo imeshatoka hivyo. Tunaomba twende kwa wale wadau wa ngazi ya chini tujue matatizo yao yako vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende eneo lingine la kilimo. Kumekuwa na Maafisa Kilimo na Maafisa Mifugo kazi yao wanayojua ni pembe za ng‟ombe zikiota akakate, hakuna kutoa elimu, hakuna kuhangaika watu wake wafuge vipi. Hapa mmeandika mafunzo, haya mafunzo kwa nini msiyafute kama wao hawataki kujituma? Tumekuwa wavivu wa kufikiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huu mradi wa ng‟ombe wa TASAF hawaelekezwi hata nini wafanye. Kazi yao ni kuwaambia jenga banda, lakini kuna mifumo mingi ya ufugaji, sisi wengine ni wajasiriamali tumetoka huko. Kuna mfumo wa kufuga kisasa huhangaiki na malisho ya ng‟ombe wala huhangaiki kumtafuta kijana wa ngo‟mbe. Unafunga vyombo vya kisasa ng‟ombe wako anakula, anakunywa maji na kwa kiwango. Watu hawa wamekaa kazi yao ni kuomba vibustani huko kwenye mashamba ya watu. Wako watu kule Magugu wamekaa ni Maafisa Kilimo na wao wana mashamba kawamulike Afisa Ardhi nakuomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la mwisho ni barabara. Miundombinu yetu ni michafu. Tuna kilio cha muda mrefu, tuna barabara inayotoka Mbuyuni – Magara, tuna eneo linalohitaji daraja. Rais wa Awamu ya Nne, huyu aliyemaliza muda wake alituahidi mwaka 2010, sasa sielewi daraja lile linafanyiwa uchunguzi wa aina gani miaka kumi iliyopita? Mpaka sasa daraja hilo limekuwa kikwazo kwa watu wanaotoka Mbulu kuja Arusha, kuja Babati na maeneo yale ya Magara. Mheshimiwa Waziri, tunakuomba utusaidie lile daraja ni muhimu kwa watu wa Mbulu Mjini na Babati Vijijini. Tunaomba miundombinu hii ya daraja ikamalike kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema, ndugu zangu utawala siyo kutawala kwa mabavu, tunatakiwa tutawale kwa hekima. Tujiulize kwa nini watu kwenye Majimbo yao wakulete wewe hapa uwe Mbunge, uwawakilishe, una nini hasa wewe, una nini ulichowazidi, una elimu au, hapana, ni Mungu amekupanga uwe mtawala wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusitumie utawala wetu vibaya. Wako waliotumia utawala vibaya na wameanguka. Hatuhitaji tuanguke kwa sababu utawala unatoka kwa Mwenyezi Mungu, tutawale kwa hekima. Tumegeuza huu ukumbi kama chumba cha ku-debate, kila siku ni debate hapa, ni taarabu hapa sasa haieleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu yangu Mheshimiwa Nape mimi nakujua wewe ni kaka yangu, tumefanya kazi sana nikiwa CCM, kwa hiyo, nakuomba wakati mwingine kuna uhuru, huu uhuru uuachie, hautakukwaza wewe, cha msingi ni kutengeneza sheria ya huu uhuru unatumikaje lakini tuki-debate humu ndani hatutasogea. Huu siyo utawala, kwanza turudi tujiridhishe katika maandiko, maandiko yanasema aliyeteuliwa kuwa mtawala ni Mwenyezi Mungu mwenye ametaka awe mtawala, sasa tusitumie hivi vipaji vibaya. Hakuna aliye zaidi ya mwenzake hapa, wote tumetokana na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Nape suala la vyombo vya habari uliachie. Siyo kwa maslahi ya hawa Wabunge wa Upinzani ni kwa maslahi ya Watanzania na kwake pia ili tuwe na mbio ambazo zinaelezeka. Tusikimbie mbio ambazo sio zetu, ukichagua mbio ukimbie mbio zako mwenyewe, hizo mbio kaka yangu siyo za kwako zitakudondosha njiani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza kabisa naomba nipongeze hotuba ya Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na naomba nichangie maeneo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Wizara yenyewe ya Katiba na Sheria. Wizara hii sasa imekuwa kubwa ina taasisi kama tano ndani yake ambazo zina uwezo wa kufanya kazi zake kwa kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Tume ya Kurekebisha Sheria. Tume hii inafanya kazi nyingi, inaleta marekebisho mengi ya Katiba na Sheria, lakini Tume hii inaonekana kazi zake hazifanyiwi kazi kwa wakati.
Naomba niende kwenye Sheria ya Vijiji kuhusu ardhi sheria ya mwaka 1999 Na. 5. Sheria hii ya Ardhi ilipitisha Hati za Kimila lakini kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika maeneo yetu, tunaomba sheria hii irekebishwe hata ikiwezekana Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wapewe nakala halisi kwa kufanya mikutano ya hadhara kuwaelimisha wananchi ili kuondoa mgongano kati ya Wenyeviti wa Vijiji na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi imetumika vibaya. Tangu Vijiji kugawiwa kwa wananchi, Operesheni Vijiji wananchi walipewa maeneo, lakini inavyoonekana hao wawekezaji, wahifadhi walikuja baada ya vijiji kugawiwa, leo hii inaonekana wananchi katika maeneo yale hawatakiwi kukaa pale wanaoneka wamevamia maeneo. tunajiuliza, nani alikuwa mkaaji wa kwanza katika hii ardhi kati ya mwekezaji na mwananchi. Tunaomba sheria hii irekebishwe ili kuondoa mgongano, wananchi wetu waishi kwa amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika eneo la tozo za kodi ya ardhi na nyumba. Kumekuwa na tabia mwananchi wa kawaida amejenga nyumba yake ya kawaida ya nyasi yuko kwenye Halmashauri ya Mji, hana elimu yoyote kuhusu kukuza Mji wala plan ya Mji, lakini mwananchi huyu pamoja na kuishi kwenye nyumba ya nyasi analipishwa shilingi 2,000 na kiwanja chake kama cha ardhi anakilipia, tunaomba hizi sheria zirekebishwe, zinatuletea matatizo, kumekuwa na manung‘uniko makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo la Mahakama. Mahakama nyingi za Mwanzo hazifanani na mahakama na hata wanaoingia humo hawafanani na majengo halisi. Miundombinu ya mahakama ni michafu, mahakama imekuwa ni mbovu, majengo yanataka kuanguka. Pia hata miundombinu ya vyoo, hakuna vyoo kabisa, maeneo mengi wanahifadhi mahabusu zaidi ya 60 wanatumia choo kimoja, jinsia ya kiume na ya kike, hapa tunahifadhi maradhi na sisi tunasema adui mkubwa ni maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende eneo la utawala. Kumekuwa na mgongano mkubwa sana hususani kwa Babati TC, mgongano huu unatokana na DC anaingilia mamlaka ya Kibunge, DC huyo amekuwa kero kwa Mbunge wa Babati Mjini. Tunaomba DC aelekezwe mipaka yake ya ki-DC.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Sheria ya Ndoa aliyozungumzia dada yangu Kiteto, lakini naomba niende kwenye magereza. Hali ya magereza yetu ni mbovu na ni mbaya. Kwanza kuna mrundikano wa mahabusu, pili hawapati lishe nzuri, hasa kwenye mahakama zenye vitengo vya watoto. Kumekuwa na vitendo vya kikatili wanafanyiwa wale watoto, tunaomba mahakama za watoto zitengewe eneo lake peke yake, sheria hii iwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la ajira; Kumekuwa na matatizo mengi katika eneo la ajira, vijana wengi hawaajiriwi, wanamaliza vyuo lakini kumekuwa na dana dana nyingi. Tunaomba hizi sheria zote zirekebishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende katika eneo la Sheria ya Walaji na Watumiaji. Kumekuwa na matatizo ya hapa na pale katika matumizi ya vyakula tunavyokula hasa vinavyotoka nje ya nchi. Hata hivyo kumekuwa na tabia ya TFDA kwenda kwenye maduka ya wale wanaouza bidhaa za vyakula. Unakuta bidhaa ina- expire mwaka 2016 mwezi wa sita, lakini hilo kontena limepita wapi? Utashangaa TFDA wanakuja kuvamia maduka ya watu wanatoa vyombo, wanachoma na wanatoza faini. Lakini tunajiuliza hili kontena limepita wapi? Sheria hii haiko sawa tunaomba hawa wa TFDA watueleze na Waziri mwenye dhamana ashughulike na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la uvunjaji wa sheria na haki za binadamu. Mwaka jana tumetoka kwenye uchaguzi, tumefanya uchaguzi vizuri lakini tarehe 26 kulitokea na tukio kwa upande wa Upinzani. Vijana wetu walikamatwa, kompyuta zao zilichukuliwa kisa tu wanakusanya matokeo. Huu ni uvunjaji wa haki za binadamu, halafu bado tunasema hii haki tunaitumia. Haki hapa haijatumika! Vijana hawa wamebambikiwa kesi, bado tunalia tunasema haki imetendeka!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa kumalizia. Ni hatari sana kuanzisha familia ambayo uwezi kuitunza. Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, tumeona Bajeti ya Tume ya Haki za Binadamu, bajeti hii hairidhishi hata kwa mtu wa kawaida unaona ni jinsi gani hii Tume haihitajiki katika Serikali hii.
Mheshimiwa Waziri, Fungu namba 55 tunahaja ya kulishikilia, huwezi kubeba mzigo mzito ambao huwezi kuutekeleza! Tume hii inafanya kazi nyingi, Kazi nyingi zinaletwa kwenye Wizara husika lakini kazi hizi zinazimwa kwa sababu maalum. Sasa kwa nini hii Tume mmeiweka? Tume hii kwenye bajeti yake haina maeneo mengine zaidi ya OC, sasa kama ina OC na hawana jengo wanapangisha wana kazi gani ya kulipwa mishahara? Kwa kazi ipi wanayofanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema posho ya Wazee wa Mahakama. Wazee wa Mahakama wanalipwa shilingi 5,000; wanahudhuria mahakamani mwezi mzima halafu bado Serikali inawakopa! Tunaomba muwalipe hawa wazee na ikiwezekana wazee hawa wapandishiwe posho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia eneo linguine ni eneo la haki za wazee. Ahsante, siungi hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu inakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwepo ya kuandaa miundombinu ya elimu yenyewe. Changamoto nyingine ni:-
(i) Ubora wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu;
(ii) Uhaba wa madarasa na Walimu kwa shule nyingi hasa Walimu wa masomo ya sayansi;
(iii) Upandishaji wa madaraja mserereko kwa Walimu;
(iv) Uhamisho wa Walimu holela pasipo kulipwa haki zao stahiki na hata posho za uhamisho; na
(v) Uhaba wa nyumba za Walimu/mazingira magumu wanayoishi Walimu;
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu yetu Tanzania haina ubora kuanzia ngazi ya msingi kwa kuwa tunabadilisha mitaala ya elimu kila mara jambo ambalo ni kinyume na taaluma halisi ya Walimu waliyosomea. Hii ni changamoto kubwa kwa Walimu hata katika maandalio ya somo. Haya ni mazingira magumu sana kwa Walimu hata katika maandalio ya somo. Haya ni mazingira magumu sana kwa Walimu na wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara ni mmojawapo ya Mikoa inayokabaliwa na changamoto ya uhaba wa Walimu na majengo ya nyumba za Walimu na madarasa ya kufundishia watoto. Walimu wengi wanaishi katika mazingira ambayo ni hatarishi na si rafiki kabisa kwa Walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia Wizara kuwapandisha Walimu madaraja kwa mkupuo (madaraja mserereko) bila kupandishiwa mishahara. Kwa muda mrefu na hadi sasa bado kero hizo zinaendelea na bado Wizara imekaa kimya bila kutoa tamko kama Walimu hawa watalipwa madai yao ya kupandishwa madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya Wizara kuhamisha Walimu pasipo kuwa na sababu za msingi lakini pia Walimu hawa hawapewi posho za uhamisho wala disturbance allowance. Mpaka sasa katika Mkoa mzima wa Manyara zaidi ya Walimu 160 wanadai hayo madeni ya msingi kwa Serikali hii takribani miaka zaidi ya kumi na mbili (12) bila kufikiriwa na hata kupatiwa majibu yanayoleta matumaini kwa Walimu hawa, wamebaki na maumivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa nyumba za Walimu ni kero kubwa kwa Mkoa mzima wa Manyara. Katika shule moja ya msingi Haraa iliyoko katika Mji wa Babati, Walimu wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Nyumba yenye vyumba viwili wanakaa Walimu nane (8) wa kiume, nyumba yenyewe haina madirisha wala haijasakafiwa ni nyumba ya udongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo yafuatayo:-
(i) Serikali itoe rai kwa Wizara ya Elimu kuhusu mambo yote ambayo ni kikwazo kwa sekta nzima ya elimu kushughulikiwa haraka ili kuokoa muda na kuokoa jahazi la elimu;
(ii) Posho za Walimu zilipwe kwa wakati baada ya madai hayo kufanyiwa uhakiki na malipo yafanyike kwa kila Mwalimu anayedai madai yake;
(iii) Nyumba za Walimu zijengwe za kutosha ili kuondoa kero na adha wanayopata Walimu wetu na kuwaondoa Walimu wetu katika mazingira hatari ya ufundishaji; na
(iv) Serikali irudishe utaratibu ule wa mwanzo wa wanafunzi kufundishwa masomo ya elimu ya kujitegemea ili wapate elimu bora ya kukabiliana na mazingira pindi tu wanapomaliza elimu ya msingi na hata elimu ya sekondari na kupunguza mzigo wa kutegemea ajira ya Serikali tu. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugafji na hifadhi ya Tarangire, kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi na hifadhi ya Tarangire, Mkoani Manyara jambo ambalo limewagharimu wananchi na hata kukosa makazi ya kuishi baada ya kutolewa katika maeneo yao kwa madai kuwa wamevamia Hifadhi ya Tarangire.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2007 wananchi wa vijiji vya Ayamango, Gedamara na Gijedabung‟ hawana makazi maalum wala maeneo ya kulima kujipatia kipato na hata chakula kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na kuwa Serikali inasema kuwa wamepata eneo mbadala ya kuwahamishia wananchi hao ambao ni shamba la mmiliki Ufyomi Gallapo Estate. Shamba hilo ni dogo sana, halitoshi kukidhi mahitaji ya wananchi hao kulima na maeneo ya kujenga nyumba bora.
Pamoja na juhudi za Serikali kuwahaminisha wananchi hao hakuna makubaliano kati ya Serikali na mmiliki huyo na wala hakuna mkutano wa hadhara uliokaa kwa vijiji vyote hivyo kuwaeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kumfutia mmiliki wa Ufyumi Gallapo Estate. Ni lini Serikali itamaliza mgogoro huu kwa kuwakabidhi wananchi hao eneo mbadala ili waendelee na maisha ya kila siku ya kujitafutia riziki zao za kila siku katika shughuli za kilimo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya wanyama Burunge, mgogoro wa vijiji vya Maweni Magara, Manyara Kisangaji na Kazaroho ni wa muda mrefu sana kati ya Juhibu na wafugaji pamoja na wakulima. Jumuiya ya Juhibu inaundwa na vijiji kumi ambayo ni Minjingu, Mdori, Kisangaji, Kazaroho, Maweni, Magara, Manyara, Ngoley, Mwanda na Nkaiti. Huo ndiyo muunganiko wa vijiji kumi vilivyounda Jumuiya ya Hifadhi ya wanyama Burunge kwa makubaliano ya kutenga matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya wakulima, wafugaji na uhifadhi ambayo ndiyo Juhibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yatokanayo na Juhibu hugawanywa kwa vijiji wanachama kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya vijiji husika. Lakini cha kushangaza leo hii wakulima na wafugaji wanaondolewa katika maeneo yale kwa nguvu ya dola jambo ambalo ni la kikatili na unyanyasaji hata kufikia wananchi kuchomewa nyumba na mifugo na askari wa Juhibu na kuwataka wananchi hao kuhama ifikapo tarehe 1/6/2016 kwenda kwenye eneo mbadala la Mfula Ng‟ombe ambao ni eneo la madimbwi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kuhusu wananchi wa vijiji vya Ayamango, Gidamara na Gijedabung‟ Serikali ifanye jitihada za haraka sana kuwapatia wananchi wale eneo mbadala lililotengwa hata kama ni vipande ili waendelee kuiamini Serikali yao na kuipa matumaini mapya ya kujikwamua kiuchumi na kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vijiji vinavyounga Juhibu naishauri Serikali eneo lililotengwa kwa ajili ya wananchi wale kuhamia halifai kwani eneo lile la Mfula Ng‟ombe lina historia ya kuwa na kichocho kutokana na madimbwi ya maji yaliyozunguka eneo lile. Hivyo halifai kwa makazi ya binadamu kuishi eneo lile.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu wa maandishi katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na migogoro ya mipaka kati ya wafugaji na wakulima (vijiji). Kumekuwa na migogoro ya mipaka ya muda mrefu kati ya hifadhi zetu na wafugaji na wakulima ambao wako jirani na hifadhi. Migogoro hii imekuwa kero kubwa sana hata kusababisha madhara makubwa sana kwa wananchi, kupigwa risasi na askari wa hifadhi na kusababisha vifo vingi vya wananchi, wanawake wengi kubakwa na askari wa hifadhi. Katika kata za Aya Mango, Gedamara na Gijedabung’ walibakwa hadi kufa na mpaka sasa Wizara haikushughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ifanye mpango wa haraka wa kumaliza migogoro hii katika vijiji vya Gijedabung’, Aya Mango, Gedamara, Maweni, Mdori, Nkaiti, Mwada - Kisangaji na Sangaiwe ambao umedumu kwa takribani miaka kumi sasa. Kwa sasa hali ya mahusiano ya wananchi na wafanyakazi wa hifadhi ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sheria ya kulipa fidia na kifuta jasho, ni jambo la kawaida sana na la hatari sana kwa Wizara hii kwani mpaka sasa pesa inayotolewa kama kifuta jasho ni ndogo kwa waathirika walioathiriwa na wanyama. Kwa mfano, tembo kuharibu mazao, kuua watu, simba kuua watu na kukamata wanyama wafugwao. Naomba Wizara iangalie namna ya kuongeza kifuta jasho hicho kwani madhara ni makubwa sana ambayo haiendani na hiyo shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Utunzaji wa Mazingira (EMA) na Sheria ya Ardhi kuhusu mita 60 kutoka katika kingo za mito na bahari.

(i) Sheria ya Ardhi (Land Act 4/5 1999) inaeleza juu ya mita 60,
(ii) Land Survey (Act Cap 324 RE. 2002); na
(iii) Planning Act (No. 8 2007).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2000 kifungu namba 57 imeelezea mambo haya ya utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo pamoja na sheria hizi ni nyingi sana, kumekuwa na uharibifu unaotokana na mmomonyoko wa ardhi katika maeneo mengi, hasa katika maeneo ya ukanda wa Bonde la Ufa. Kunapotokea hali hiyo ya tendo la asili la ardhi kumomonyoka, kingo zinasogea na zile mita 60 zinapungua, wakazi wa maeneo husika kusumbuliwa kuondolewa katika maeneo hayo, Wizara inajipangaje kuelimisha wananchi kuhusu madhara yatokanayo na mmomonyoko wa ardhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na ushauri; Wizara iandae utaratibu wa kujenga mahusiano mazuri katika kutangaza utalii na hifadhi zetu kwa kushiriki shughuli za kijamii katika maeneo yote yenye hifadhi. Kwa mfano, kujenga vyumba vya madarasa (shule), kujenga zahanati, huduma za maji, kuanzisha timu za mpira, michezo ya riadha na mashindano ya mavazi ya asili ili jambo hili liwe chanzo na mwanzo mzuri kwa Wizara hii kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka. Hili ni jambo muhimu ambalo litajenga mahusiano makubwa mazuri na kuwajengea uwezo mpana na uelewa juu ya hifadhi zetu, faida za hifadhi zetu kupitia huduma wanayopata kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nitoe pole zangu za dhati kwa wananchi wote wa Tanzania na wana wa Arusha kwa msiba mkubwa uliowapata kwa watoto wetu. Pia naomba nipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitangulize maneno haya, kwa macho ya kawaida tunawaona walimu wanayo furaha, lakini katika mioyo yao walimu hawa wanaandamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa elimu ni mfumo ambao hauna tija kwa maslahi ya Taifa hili. Kumekuwa na mitaala mbadala kila Waziri anapokuwa kwenye sekta hiyo. Kila Waziri anayepewa Wizara anakuja na mitaala yake. Sasa sijui Bodi hiyo ya Elimu ina kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatuwezi kupata elimu bora bila kuwa na afya, maji na lishe bora lakini pia na miundombinu bora ya elimu. Ni ukweli usiopingika kwamba tuna uhaba wa walimu, nyumba za walimu, matundu ya vyoo lakini pia shule nyingi za sekondari za kata hazina maabara na mabweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kutaratibu kwa wanafunzi wa shule za kata kwenda kupanga kwenye nyumba za watu binafsi hususan vyumba vinavyoitwa geto. Unawezaje kupata elimu bora kwa kumweka mtoto ambaye ana umri wa miaka chini ya 13 au 18 amepanga, anaishi mwenyewe, anaishi group na vijana wa kiume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe ni mashahidi watoto hawa ukweli ni kwamba wako kwenye foolish age, unatarajia nini? Unatarajia “A” na zero ngapi? Mazingira haya yaboreshwe, kama Serikali ilivyoamua kujenga shule za kata wahakikishe mabweni yanakamilishwa ili wanafunzi wetu wapate elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la uhaba wa nyumba za walimu. Kwa macho yangu nilishawahi kushuhudia walimu wanakaa kwenye nyumba za udongo. Nyumba yenye room tatu wanakaa walimu sita mpaka tisa, wakike watatu na wanaume sita. Hebu niambieni walimu hawa wakiingia darasani wanafundisha nini kama siyo wanawaza mazingira yale mabovu ya makazi yao na mishahara midogo na kutokulipwa pesa zao za sitahiki zao halali lakini Waziri akija hapa akiulizwa swali anasema wamelipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache kudanganyana, hawa ni Watanzania, tumewapa kazi hii. Sisi zote humu ndani ni kazi ya walimu, lakini leo hii wenzetu wa upande wa pili mnafanya siasa juu ya afya na akili za Watanzania. Kumekuwa na Taifa la vuguvugu si Taifa la watu wasomi kwa sababu kila mtu ana yake kichwani akija ni kubadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye viwango vya ufaulu. Hebu tuelezane ukweli wa mambo, mwanafunzi kutoka darasa la kwanza mpaka la saba ameshindwa kupata marks 100, unampeleka form one kufanya nini? Ana tofauti gani na baba yake anayefuga ng’ombe na yeye jioni akirudi anakunya maziwa, maana hata kusoma hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuanze na form one mpaka form four mmepandisha daraja la ufaulu mnasema division four mpaka point 35, mmelenga kufanya nini? Mmeipeleka huko ya nini? Tunafuga watu ambao watatulemea katika Taifa hili. Tunalia na ajira za vijana, mnasema East African Community haiajiri vijana wa Tanzania, unaajirije Mtanzania mwenye vyeti kama hivi? Tumebaki kuwa walalamikaji, tumebaki kufanya siasa kwenye maisha ya Watanzania, kila kitu ndiyoooo, mpaka lini, hata kwenye elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa ambalo watu wake hawajali elimu hakuna uchumi, maendeleo na hakuna afya. Madaktari hawa hawa leo mnakuja na uhakiki wa vyeti fake nani kawatengeneza kama sio ninyi? Alikuja Mungai nikiwa darasa la pili alifuta michezo, leo mnalia na michezo? Kwa nini mnakuwa mnakana vivuli vyenu, mnakimbia vivuli, Serikali inakimbia kivuli chake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni niende kwenye elimu ya mtoto wa kike. Tunaomba tuelimishe watoto wa kike, mtoto wa kike ni hazina. Angalieni akina mama ambao hawajasoma, kila mwanaume aliyesimama hapa mbele yake kuna maendeleo ni mwanamke amemshauri vizuri. Je, hawa wanawake wakisoma, natumai asilimia ya maendeleo itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iache utaratibu wa kutuletea elimu ya vuguvugu. Kulikuwa na mpango wa vodafaster, mmetuzalishia watoto wengi kupitia hao walimu wa vodafaster leo hii mnasema watoto hawa ni mbulula na ni vilaza, ukilaza huu mmetengeneza ninyi Serikali. Nani kautengeneza kama sio ninyi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyeti fake, wadau wakubwa wa kuzalisha hivi vyeti feki ni Baraza la Mitihani, hizi namba fake ni Baraza linagawa. Anzeni kule msianze na wale ambao siyo wahusika, alipataje namba ya mtihani, nani aliyemuandikia zile marks na nani aliyempa kile cheti bandia ambacho hakina alama ya twiga, ni watu wa Baraza. Mheshimiwa Waziri usimung’unye maneno ulikuwa mama mzuri sana lakini wamekuweka kwenye mtego na wamekuweka mtu kati kwenye siasa, acha siasa kwenye elimu ya Watanzania. Tunahitaji Watanzania wenye elimu na afya ya kutosha kwa sababu madaktari wanatokana na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema hata wale walimu wa UPE waliofukuzwa Serikali imewatendea dhambi. Serikali wenyewe ndiyo iliwaajiri wale walimu, leo unasema sio walimu, wameishia ngazi ya diploma, wametumikia Taifa hili na walifundisha vizuri, kuna watu waliotokana na walimu hawa wa UPE, leo unasema hawa walimu sio? Muogopeni Mungu mkawalipe wale watu na wengine wameshastaafu wapate stahiki zao. Msitujengee Taifa linalobeba laana kwa sababu utakapokuwa umejiwekeza kwenye laana na uhakikishe kwamba laana hiyo itakuwa inakutafuna wewe. Hatuhitaji laana ya walimu hao, walipwe pesa zao. Ahsante.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, hizo dakika zangu mbili zilizoliwa ulinde. Kwanza kabisa naomba niunge mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hata hivyo kwa kuwa muda ni mchache naomba nijielekeze kwenye hoja mahsusi katika Wizara hii. Kwanza kabisa naomba niende kwenye mgogoro wa ardhi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Tarangire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii imezungumzwa muda mrefu lakini inavyoonekana hakuna mafanikio. Nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba leo hii nimekuja na document ambayo inaonesha Sheria iliyounda vijiji hivyo na GN ya Serikali. Naomba nimkabidhi kitabu hiki ili aende akatatue mgogoro wa Gijedabou, Gedamara na Ayamango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye shamba la mwekezaji Hamir Estate iliyofutwa umiliki wake na Mheshimiwa Rais mwaka 2015, Novemba. Shamba hili lilifutwa na Mheshimiwa Rais tarehe 4 Novemba, 2015, lakini cha kushangaza mwekezaji huyu pamoja na kusitishwa umiliki wa shamba hili bado anaendelea kulitumia shamba hili, jambo ambalo linaibua mgogoro mpya kwa wanakijiji na wananchi wa Bonde wa Kiru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili wakati Mheshimiwa Rais analifuta, hakukuwa condition yoyote iliyowekwa, hakuna maelekezo yaliyoelekezwa kwamba lipelekwe kwa wananchi au liende wapi. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri hili jambo alifanyie kazi, shamba limefutwa, tujue linakwenda kwa wananchi au linakwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye Wizara husika sasa atuletee sheria mpya ya kubadilisha matumizi ya ardhi. Kwa mfano, sasa hivi kumekuwa na sheria inabadilishwa matumizi ya ardhi ya kilimo inakuwa ardhi ya makazi, hii imeleta mgogoro. Kwa mfano Babati Bonga ilikuwa ni matumizi ya kilimo, Arusha Usa River kulikuwa ni matumizi ya kilimo, leo ukikuta ni majumba matupu. Vile vile mfano mzuri, unaweza ukahamisha watu wakakaa jangwani ukawapelekea maji na wanaweza kuishi, lakini huwezi ukapelekwa jangwani ukalima ukaivisha mazao. Sheria hii iletwe hapa iingizwe katika moja ya sheria ya matumizi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nyaraka hizi Mheshimiwa Waziri naomba nimkabidhi barua ya ubatilisho wa umiliki juu ya shamba la huyu mwekezaji Hamir Estate kitalu namba 1396 eneo la Bonde la Kiru, Wilayani Babati.

Naomba nimkabidhi nyaraka hizi kwa sababu muda wangu hautoshi ili aone ni jinsi gani yeye anadanganywa. Mgogoro wa Bonde la Kiru umekuwa ni VICOBA vya baadhi ya viongozi. Mgogoro huu ni wa tangu mwaka 1998, mwaka 2009 mfanyakazi wa mashamba ya Kiru mchana kweupe saa kumi alikatwa shingo akaletwa Mrara; leo hii tunasema tunashughulikia mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namjua Mheshimiwa Waziri anafanya kazi, hata haya matokeo ya hili shamba kufutwa ni pamoja na juhudi zake. Kwa sababu ameanza, aende akamalizie hii ngoma. Amepongezwa sana lakini haimaanishi kwamba mimi simpongezi lakini kuna mambo mengine yanatuumiza. Hiki kitabu ukiangalia kuna magofu ya nyumba za watu, watu wanaishi kwenye nyumba za nyasi hawaruhusiwi kuendeleza makazi yao, hawaruhusiwi kulima miaka 11. Hebu ajichukulie sasa, ni miaka 11, wewe ni baba na una watoto sita, chakula chako ni cha kuombaomba, inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Waziri atakuwa amenisikia kwa haya machache, naomba Mheshimiwa Waziri nimkabidhi hizi nyaraka. Naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi naomba nijikite kwenye hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyoko mezani inaonesha kwamba Watanzania ni jinsi gani akili zetu zinachezewa. Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018 inaonesha ni trilioni 1.7 lakini ya mwaka huu ni shilingi 886,236,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, unawezaje kuhudumia Watanzania kwa bajeti hii, nchi ambayo watu wake hawana afya nzuri, hawana lishe bora, ni nchi ambayo watu wake kiuchumi na kiafya hakutakuwa na nguvu kazi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajinasibu kwamba wanafanya mambo mazuri, ni kweli upande mwingine kuna mambo yanaenda sawa. Kuna mambo hayaendi sawa, kwenye Idara ya Afya kuna mambo ambayo tunaona ni kama mchezo wa kuigiza kila mwaka. Issue ya watumishi kwenye hii idara ni issue ambayo imezoeleka, Wabunge wanaleta maswali ya msingi, majibu ya Mawaziri inaonyesha ni kutuchezea akili za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kitabu cha Kamati, TWAWEZA wameleta takwimu inaonesha kwamba kila baada ya dakika 12 mtoto mmoja wa Kitanzania anapoteza maisha kwa sababu ya kukosa lishe. Ukienda tena zaidi wanasema mpaka masaa ya jioni ni watoto 35 wanakufa kutokana na lishe duni, sasa tunajiuliza hii bajeti mmepunguza kwa nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni idara nyeti, hakuna msomi anayesoma kama hana lishe bora. Hakuna mtu yeyote anayeweza kwenda kwenye Serikali ya viwanda kama hana lishe bora. Tusileteane maigizo ambayo yanaweza yakaleta hasira kwa Watanzania, tunahitaji Watanzania wenye afya njema, tunahitaji Watanzania wenye akili ambazo zina afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna habari ya matibabu bure kwa wazee. Nakubaliana ni kweli kuwe na matibabu bure kwa wazee lakini Serikali haikuangalia ni wapi mtu anapokuwa na magonjwa ya kudumu. Unapokuwa kijana kuna magonjwa si nyemelezi, lakini umri unavyozidi kukua na unapozidi kuzeeka mwili unapoteza nguvu. Kuna watu wanaumwa magonjwa ya figo, kuna watu wanaumwa magonjwa ya tezidume, haya mambo yote yana-compare kwenye uzee, kwenye umri mkubwa, lakini suala la matibabu bure kwa wazee ni paracetamol kwenye vituo vya afya. Kwa namna moja au nyingine tunawapoteza wazee wengi kwa sababu ya huu mwamvuli wa matibabu bure.

Tunaomba sasa mje na mkakati mwingine namna ya kuokoa maisha ya wazee wa Kitanzania ambao wamefikia umri mkubwa na wana mashambulizi ya magonjwa ya kudumu ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zahanati zetu kuanzia ngazi ya vituo, zahanati zimejengwa kwa mahitaji ya mtu kama mimi ambaye sina mahitaji maalum. Hawa watu wenye mahitaji maalum hawajawekewa kipaumbele kwenye zahanati zetu, ninategemea Waziri atakapokuja hapa atuambie ana mkakati gani wa kujenga maeneo katika zahanati yetu kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine ambalo ni eneo nyeti, matumizi ya madawa ya kupunguza makali ya VVU, matumizi haya mna…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika bajeti hii kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kunukuu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 8(1), inasema:-

“(a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.

(b) Lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; na

(c) Serikali itawajibika kwa wananchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imeletwa na tunaisifia ni bajeti nzuri. Maandishi ni mazuri, matendo ni mabaya kuliko tunavyofikiria. Hata Biblia inasema, heri yule aliyejenga juu ya mwamba kuliko yule aliyejenga juu ya mchanga. Ndugu zangu Taifa linaenda kuangamia. Uchumi wa Taifa unaenda kuangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, simulizi hizi za kusema uchumi umepanda amepata wapi? Wizara ya Kilimo mwaka 2016/2017 mpaka Machi fedha zilizopelekwa ni shilingi bilioni 2,252 sawa na asilimia 2.22, asilimia 98 ya bajeti haikutekelezwa. Katika Wizara ya Mifugo, makadirio yalikuwa ni shilingi bilioni 4 lakini pesa iliyotolewa ni shilingi milioni 130 sawa na asilimia 3.25, asilimia 97, haikutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye maji, pesa zilizotengwa ni shilingi bilioni 913, iliyotolewa ni shilingi bilioni 230,997 sawa na asilimia 25, asilimia 75 haikutekelezwa. Hizi ni simulizi alizoandika Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye kitabu hiki. Kama hizi za huku nyuma zimeshindikana kutekelezwa lakini amekuja tena na 2017/2018 Mifugo na Uvuvi wametenga fedha ileile ya mwaka 2017 lakini pesa iliyotolewa mpaka sasa ni sifuri. Hizi ni simulizi, Watanzania wana hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Mheshimiwa Waziri hamshauri Rais wakasimamia hata kwenye zile ahadi 10 za Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi alitoa ahadi 10. Kwanza, alisema ataboresha mfumo wa kiutendaji Serikalini. Pili, ataboresha Huduma za Afya. Tatu, ataboresha maslahi ya wafanyakazi lakini wafanyakazi wameishia kutumbuliwa, wala hawajaongezewa hata senti tano kwenye mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya nne alisema, anaboresha elimu na elimu bure. Elimu bure imekuwa ni majanga katika Taifa letu. Ahadi ya tano alisema ataboresha maji, maji yako wapi? Namuuliza Mheshimiwa Dkt. Mpango, bajeti ya maji iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya sita akasema ataboresha kilimo, uvuvi, mifugo na viwanda. Kilimo na Mifugo ndiyo hiyo ya sifuri sifuri. Mheshimiwa Dkt. Mpango ameleta simulizi isiyosahaulika ndani ya Bunge. Saba, Mheshimiwa Rais alisema kuwe na kipato kizuri cha kuongeza uchumi, uchumi uko wapi? Nane, akasema kuongeza fursa za ajira, ajira ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya tisa akasema, kupunguza tozo na kodi zisizo za lazima hasa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Sasa tozo imekuwa ni mwiba, mshike mshike mtaani. Watu wanaingia wanakagua mpaka draw za watu. Umetusakizia mbwa mkali wa mapato, TRA. Leo hii mpaka mabeseni ya vitunguu yanakamatwa, ukiwa na nyanya tano, ushuru, ukiwa na nyanya 10 ushuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango, asifikiri tunamchukia, tunamwambia kwa sababu Bunge ndilo lenye dhamana ya wananchi. Vichwa vyote hivi unavyoviona, watu hawa wanajibika kwa Watanzania. Kwa nini Waziri mmoja tu aliangamize hili Taifa? Baba yangu yangu Mheshimiwa Waziri tulia, kaa, mshauri Mheshimiwa Rais, timizeni hizi ahadi. Hizi bajeti za kisekta zinaendana na ahadi za Mheshimiwa Rais, kwa nini hamtaki kumshauri? Mnasema viwanda, viwanda mtavipata wapi wakati kwenye kilimo kuna sifuri, elimu ndiyo hakuna, kila siku tunalalamika.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tozo za TRA ambazo zinatuletea shida, TRA wamekuwa kama wezi. Umetoka na TV yako nyumbani unapeleka kwa fundi, anakwambia nipe risiti. Mimi nimenunua TV tangu mwaka 2008, risiti najua iko wapi? Msituchonganishe, mnavunja mahusiano baina ya TRA na watu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za sikukuu, wanusanusa kwenye maduka ya watu wanataka nini? Saa 4.00 asubuhi anakwambia naomba ripoti, ripoti inatolewa pale mtu anapofunga mahesabu ya siku, hiyo ya saa 4.00 yeye anatoa wapi ripoti? Kwa hiyo, saa 4.00 anatoa ripoti, saa 7.00 akifunga duka akienda kula akirudi anatoa ripoti. Kwa nini hamjatengeneza utaratibu wa kuelimisha wafanyabiashara? Hii ni dhambi kubwa sana, itamtafuna Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii issue ya Polisi, tunataka watuambie Polisi wamegeuka kuwa wakusanya ushuru wa nchi hii? Polisi wamejazana barabarani, kila mtu ana mashine, wameongeza idadi ya magari, kila siku magari matano, utakamata magari ya nani? Wanasababisha nchi hii kuangamia kwa sababu ya maarifa. Serikali haijakokotoa vyanzo vya mapato ambayo tunafikiri kwamba tutapata mapato wamekuja tu wana-hang halafu sasa wameelekeza kwa wale wanaofikiri wataleta hela, Polisi hawataweza kuinua uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna issue ya standard gauge. Mradi huu hauwezi kutekelezeka. Kama tunataka kuingia kwenye ushindani wa soko, Kenya wanatengeneza standard gauge inayotumia mafuta sisi tunatengeneza inayotumia umeme kwa kutegemea umeme wa Stiegler’s Gorge. Tutatoka humu Bungeni mpaka huo mradi utimie, wote tumekufa. Tukifika kule, tutakuta na Kenya nao wameshatuwahi hakuna tena habari ya standard gauge. Nani anayekuja kwenye gharama kubwa wakati kuna standard gauge inayotumia mafuta yenye gharama nafuu? Hakuna standard gauge inayoweza kujengwa kwa ajili ya kubeba tu abiria. Kama huo ndiyo mpango wenu, tutakuwa tumefeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengine siyo lazima tuyaseme kwa sababu macho yanaona lakini inabidi tuyaseme. Kwa nini Serikali isije na vipaumbele vinne tu ambavyo vinaweza kutekelezeka kuliko kuja na mlolongo wa vipaumbele ambavyo havitekelezeki? Leo nchi hii inahema kwa ajili ya sigara na pombe. Kila mwaka kodi ya pombe na sigara inapandishwa, japo wameandika ni hatari kwa afya zetu. Hakuna vyanzo vingine vya mapato? Wameacha kuweka wasimamizi katika zile sekta tunazofikiri zinatuletea pesa, wamekuja na hizi hela ndogo ndogo za kuokoteza, hizi ni pesa za kuokoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri akajipange, tunataka bajeti inayotekelezeka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi naomba nichangie katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji katika maeneo mawili.

Mheshimiwa Spika, maji ni uhai wa kila kiumbe chenye uhai katika uso wa dunia, lakini nchi yetu imekuwa ni kinyume na matarajio, maji yamegeuka kuwa mtego wa umaskini kwa uchumi wa Mtanzania wa kawaida. Maskini analipia maji bill kubwa kuliko mtu mwenye uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja kutokana na muda naomba niende kwenye mpango wa maji vijijini. Tuna vijiji vingi katika nchi hii ambavyo havina maji tofauti na sisi tunaokaa katika maeneo ya mjini. Naomba nitolee mifano miwili tu katika Mkoa wangu wa Manyara.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia pato la kawaida la Mtanzania kwa mwaka ni shilingi 2,131,299; hii ni kutokana na takwimu ya Juni, 2017 ili uone ni jinsi gani tuna hali mbaya katika sekta hii ya maji, tuna vijiji katika Wilaya ya Hanang, tuna vijiji vinaitwa Gehandu na Laganga, vijiji hivi umbali wa kupata maji ni kuanzia kilometa mbili mpaka kilometa nne watu wanatafuta maji. Hata hivyo pale unapopata hayo maji pipa la lita 200 ni shilingi 7,000. Sasa ndio ujiulize ukiwa na familia ya watu sita utakuwa unagharimia katika uchumi wako shilingi ngapi? Halikadhalika vijiji vya Endakiso na Nkaiti maji yanauzwa kwa gharama hizo hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pato la huyu mkulima na mwananchi wa kawaida badala ya kufanya masuala ya kiuchumi pato lake linaishia katika manunuzi ya maji. Hapa tunasifiana, lakini hata Biblia inasema kusifu kunawapasa wanyoofu wa moyo, hivi mnasifu nini katika hili? Wanaokufa ni akina nani? Tuna watoto tuna ndugu zetu, hata kama sisi tunaishi mjini, tumewaacha babu zetu na mama zetu huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, familia moja inahitaji angalao pipa moja kwa kubana matumizi, lakini mwananchi huyu anahitaji takribani shilingi milioni 2.5 kwa mwaka ili watoto wake wale, waoge, wapige mswaki na matumizi mengine, lakini pia familia ya watu sita wastani wa hicho kipato ni asilimia 16 ya kipato cha kila mwanafamilia. Kwa muktadha huu hata mtoto aliyezaliwa leo wa siku moja anahusika katika manunuzi ya maji. Hebu tujiulize kwa Tanzania nzima na vijiji vyote hali hii ya adha ya maji uchumi wa Watanzania tumeukaba kiasi gani na tumewarudisha kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba Waziri utakapokuja utuambie umeongea vipi na watu hao wa Wizara ya Fedha? Tunajua tatizo haliko kwenu, tatizo liko Hazina. Kwenye Kamati za kisekta watu wa Hazina wanakuwepo, mara waje kwanza na ukomo wa bajeti, mmeweka ukomo wa bajeti kile kidogo mlichokiweka hamkitoi. Kwa nini mnatuchosha kukaa kwenye Kamati tunachambua nini? Unawezaje kuwa na akili nzuri hujaoga, hujala, wewe utapata wapi hiyo afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hii Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kwa kuwapa pole viongozi wangu, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe na dada yangu Mheshimiwa Ester Matiko, kwa muda mrefu kuwepo mahabusu kwa ajili ya dhuluma ama kutokufuata utaratibu na miongozo ya utawala bora kwa watu wanaoshikilia hayo madaraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitangulize kwa kusema utawala bora ni matokeo ya msingi bora wa maadili mema. Misingi hii inakubalika na inatokana na mtawaliwa na yule anayemtawala mtu mwingine. Kumekuwa na vurugu nyingi kwa baadhi ya watendaji wa Serikali hususan Wakuu wa Mikoa na ma-DC. Kumekuwa na mkanganyiko kati ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi katika halmashauri nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, tumekutana na kesi nyingi, mwaka jana tumeshauri, lakini bado mwaka huu hizo vurugu zinaendelea, natumai Waziri akija atatuambia hizi kero za kila siku zitakwisha lini? Utawala bora ni pamoja na kulinda wale watu unaowaongoza, lakini katika nchi yetu imekuwa ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanayoudhi, kuna mambo mengi ambayo yanaleta hitilafu tunasema rais anafanya kazi nzuri nami nakubali ni kweli anafanya kazi, lakini wao wenyewe humu ndani ndiyo wanaomwangusha rais. Tusifurahishane hapa hata Rais mwenyewe anajua kwamba wao ndiyo wanaomwangusha, wanamwangusha vipi? Amepewa dhamana kubwa yeye kwenda kutawala kwa ile ngazi ambayo inampasa yeye lakini hawampelekei ripoti nzuri. Huku chini wanakuja kwa ajili ya kukamiana, kila mtu kwa nafasi yake akatekeleza wajibu wake, wanatuletea Wakurugenzi ambao hawajui hata mipaka ya kazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa vile vile, kila mtu kwenye hizo nafasi zao amejifanya Miungu watu, tena wengine wamewaleta wanathubutu kabisa wanakwenda kwenye shughuli za ufunguzi wa miradi, ni DED amevaa shati ya CCM. Tukisema haya mnatuombea miongozo, kuhusu utaratibu kwamba siyo kweli, kwamba ma- DED na ma-DAs ni makada wa CCM, hata hilo mnakataa? Ushahidi tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shida kubwa, kuna issue ya TAKUKURU, nchi hii watu wanaogopa hata kufanya biashara. TAKUKURU wakikuweka ndani leo hii utakaa miezi miwili wanasema uchunguzi bado, lakini kesi wamezibadilisha. Hivi mtu ambaye hana hata shilingi milioni 10 benki unambadilishiaje kesi kwamba ni uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, anatakatisha makaratasi? Wasaidieni watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala ni kitu cha msimu tu, tutapita, tutarudi mitaani, tutakoseana heshima, lakini at least ungali wewe kama unajua unaishi je, watoto wako unawabakizaje huku nyuma? Tumejenga athari, mioyo ya watu inalia, wamekuwa waonevu, uchumi kama unashuka wasiende kuumiza watu kwa ajili ya kuwakamata wanatafuta pesa. Tufungiane humu ndani tutafute namna bora ya kuuinua uchumi wa nchi hii. Hivi wanavyowakamata hawa wafanyabiashara, wanafikiri kwamba hawa wafanyabiashara ndiyo wachangiaji wakuu wa mishahara. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna subiri taarifa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Wenyekiti, nataka kumpa taarifa dada yangu anayezungumza kwamba, waliokuwa makada wa CCM kuwa ma-DC na Wakuu wa Mikoa wala siyo shida, kwa sababu hata yeye alikuwa kada wa CCM lakini leo hii ni Mbunge wa CHADEMA, anaamini katika kazi yake mpya.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona alikuwa anataka nimwone tu, kwa sababu mdogo wangu nataka tu nimwambie katika hizo ngazi, mimi nilikuwa CCM na najua utaratibu unaoendelea ndani ya CCM. Kwa hiyo ninachokizungumza siyo kwamba nabuni, nina jua.(Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye tume ya haki za binadamu, kumekuwa na mazuio ya mikutano ya hadhara. Hivi leo hii kama Mbunge wa Upinzani wa Jimbo ananyimwa asifanye mikutano kigezo kikuu nchi nzima kumekuwa na sababu wanasema, intelejensia, hivi intelejensia iko kwa Wabunge wa CHADEMA tu, halafu mnawatuma polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe. Naomba niendelee asinipotezee muda.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J.NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, subiri taarifa hiyo.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hakuna Mbunge wa Jimbo anayezuiwa kufanya mikutano kwenye maeneo yake. (Makofi)

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna umeisikia hiyo taarifa? Hakuna Mbunge anayekatazwa kufanya mkutano kwenye Jimbo lake.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa.

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA: Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Haya Kuhusu Utaratibu.

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a) Mbunge hapaswi kutoa taarifa za uongo.

Mheshimiwa mwenyekiti, Mbunge aliyesimama sasa hivi hapa anasema Wabunge hawazuiwi kufanya mikutano kwenye maeneo yao. Mimi nimekuwa mhanga na nimelalamika mara nyingi nakataliwa, Wabunge wengi tunakataliwa kufanya mikutano kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anasimama hapa anasema uongo, kwa nini Mbunge unasema uongo na Wabunge wenzako tupo? Tunaomba afute uongo huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Peter Msigwa hata na mimi naelewa kwamba Mbunge hakatazwi kufanya mkutano kwenye eneo lake.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Tuendelee Mheshimiwa Anna.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu ulindwe. Mimi sijazoea kujibizana na watu wenye umri wa baba zangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu, twendeni tukajenge nchi kwa maslahi mapana ya vizazi vyetu vya baadaye, tutasifiana humu lakini ukweli wanaujua mioyoni mwao na Biblia inasema, ole wako mnafiki. Sasa tusinafikiane humu ndani, mikutano ni kweli wanazuia lakini kwa nini wanakimbia vivuli? Hilo wanalijua kwa nini wasituruhusu tukafanya mikutano, tukutane jukwaani kwa hoja, wasitufungie kwenye chupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie mambo machache tu kwa ajili ya Taifa hili. Huku ndani watu tunaenda na interest za vyama lakini hao hao wanaopiga kelele humu ndani kwenye maeneo yao hakuna kitu. Kuna halmashauri nyingi hazifanyi vizuri katika mapato ya ndani, tuache vyama twendeni kwenye halmashauri zetu, wananchi wanataka nini. Maendeleo yanaletwa sisi tumetumwa huku kwa ajili ya kutetea wananchi, tumekuja hapa tunapongezana, ni interest tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni halmashauri kama sita hazikufanya vizuri na wamo humu wanaotetea. Mfano mzuri ni Mkoa wa Mtwara, Halmashauri ya Masasi imefanya kwa asilimia 10.95, Nanyumbu asilimia 10.44, Tandahimba asilimia 13.22, wastani ule wa mkusanyo ni 11.53. Leo tunasifiana huku wanasema wamefanya kazi nzuri, kwa nini hawakushauri huko kwenye halmashauri zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nsimbo ni halmashauri mojawapo imetuangusha 23.5, Mlele 26.3, Tunduru 27, sasa leo hii hapa tukisema tuambizane kwa nini tunahangaika humu kupeana taarifa kusifiana tu, haiwezekani, tusemane humu ili tukajenge kule kwa wananchi. Tumekosa umoja humu kwa ajili ya hili Taifa kwa sababu kuna watu wanajipendekeza huko. Halafu wanaojipendekeza huko kwa taarifa yao jamaa mwenyewe anapiga mzigo, sasa wafanye kazi na wao wasimfurahishe furahishe humu. Bahati nzuri yeye huwa haendi na upepo anafanya kazi, haya twendeni. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya malizia dakika moja.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ni halmashauri mojawapo pia yenye madeni makubwa. Halmashauri inadaiwa milioni 112 na CRDB benki, asilimia 20 ile ya vijiji haipelekwi, leo hii hapa tunasema kila kitu kimefanyika, kimefanyikaje? Halmashauri inadaiwa, makusanyo ya ndani yanaenda kulipa madeni ya mikopo ya Madiwani, mtapata wapi maendeleo. Halafu huku mnaogopana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie issue moja ya mwisho tu dakika zangu hizo zilizobaki. Kuna issue ya Mfuko wa Jimbo, Wakurugenzi wamekuwa wamiliki wa Mifuko ya Jimbo, Mkurugenzi ana uwezo wa ku-host pesa za Mfuko wa Jimbo na kule kuna akinamama wanakufa kwa ajili ya kukosa dawa. Hawataki hizi pesa zifanye maendeleo na kazi ya Mfuko wa Jimbo siyo kwenda kumaliza miradi ni kwenda kuchochea maendeleo. Sasa kwanini Wakurugenzi hawa wasichukuliwe hatua? Au basi kama hawajui waambiwe utaratibu na mipaka yao ya kazi, Wakurugenzi wanasigana mno na ma-DC na Wabunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anna, ahsante sana.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kwanza kabisa niungane na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo machache katika Wizara hii ya Afya, nianze na eneo la maboma wazi katika maeneo yetu ya vituo vya afya. Tuna maboma wazi katika maeneo mengi nchini na maboma wazi haya yamejengwa na wananchi, lakini Serikali haipeleki hela kwa kile kiwango ambacho kimeridhiwa kwamba, wananchi wanajenga maboma na Serikali inamalizia. Mpaka sasa kuna maboma zaidi ya 3000 nchi nzima ambayo hayajaezekwa na ni nguvu za wananchi zinapotea bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na miradi isiyokidhi hadhi. Miradi hii ipo mingi, lakini unaenda kwenye zahanati unaenda kukagua zahanati unakuta kuna mapungufu mengi na zahanati nyingi zimejengwa chini ya viwango, huu ni ubadhirifu wa pesa za umma. Tunaomba Wizara iangalie ni jinsi gani wanaweza kwenda mbele zaidi kwa kutafuta wakandarasi wenye elimu na wenye utaalam mzuri katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la ukusanyaji wa damu salama. Katika maeneo mengi ya mikoa kulianzishwa vituo vya ukusanyaji damu salama, lakini tangu mwaka 2015 mfadhili aliyekuwa wa mradi huu alikabidhi magari ya Red Cross Serikalini, lakini magari hayo mpaka sasa hayajawahi kufanya kazi, jambo ambalo linasababisha vifo vingi kwa sababu vituo hivi vimeshindwa kukusanya damu salama katika maeneo mengi. Mfano mzuri ni Mkoa wa Kagera na Mkoa wangu wa Manyara damu salama haiko kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la ustawi wa jamii. Kumekuwa na tabia ya ukatili wa watoto katika maeneo mengi, lakini tuna mabaraza yanayohusika katika maeneo mengi, kwenye kata kwenye mikoa kwa ajili ya kusikiliza hizi kesi za watoto, lakini mabaraza hayo hayafanyi kazi vizuri. Tuna kesi nyingi ambazo hazitatuliwi kwa wakati, lakini nyingi zinazimwa na watoto tayari wameshapata madhara makubwa. Sasa Wizara ituambie wana mpango gani wa kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii katika maeneo mengi nchini, ili waende sasa wakafanye hii kazi kwa weledi?

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wengi wameathirika na wamefanyiwa vitendo vya kikatili. Mfano mzuri ni Hanang ambapo ni Basutu, Balangalalu na Babati pia wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la utatuzi wa migororo ya ndoa na matunzo ya watoto. Kila siku hapa Bungeni tunalia na hali ya kusema watoto wa mitaani. Watoto wa mitaani tunawatengeneza sisi wenyewe, kwa nini tunawatengeneza sisi wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inayotakiwa isimamie unakuta kesi nyingi zinaendeshwa, lakini kwa sababu unakuta mama au mzazi mmojawapo hana uwezo mzuri kesi tayari imepelekwa Mahakamani, kesi inaamuliwa mtoto aende kwa upande mmoja wa mzazi mmoja. Matokeo yake ule mgogoro kama haukutatuliwa vizuri ndio maana unaona unasikia kesho mkoa fulani watoto wamechinjwa, mkoa fulani baba ameuwa mtoto, haya ni mambo yanayoumiza Taifa, lazima yaangaliwe kwa wakati na lazima yasimamiwe na wizara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumechoka kusikia vifo vya watoto kila siku watoto wanachinjwa, Tanzania nzima hakuna siku mtoto hachinjwi ni kwa sababu ya ubadhirifu wa kutokutumia sheria. Hongo zinatembea huko, mzazi anasema ana uwezo wa kumchukua mtoto wake, anamchukua anampeleka kwa mama wa kambo, yule mtoto anaendelea kunyanyasika, mwisho wa siku kisaikolojia anaathirika halafu tunasema tuna watoto wa mtaani, hiyo haiwezekani. Nendeni mkakae mliangalie hili namna ya ku-solve watoto wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la vyumba vya wagonjwa mahututi. Hospitali nyingi za wilaya hazina vyumba ambavyo vinakidhi mahitaji ya mgonjwa mahututi; mfano mzuri ni Hospitali ya Mrara chumba cha wagonjwa mahututi ni sawa na gereji ya magari. Nendeni mkaangalie pale Babati, mkashuhudie hili ninalozungumza, boresheni hizi huduma mtusaidie, tuwasaidie Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie eneo moja ambalo nafikiri litakuwa ni la mwisho. Maeneo mengi ukienda kwenye hospitali za wilaya, kila unapomfikisha mgonjwa, hasa wale wagonjwa wanaopata ajali wanasema damu haipo. Sasa kwenye hotuba ya Waziri ameandika amesema damu sijui lita elfu ngapi hizi, hizi damu kwa nchi nzima hazitoshi na tunasema tunachangia damu salama kwa hiyari, ile kampeni endelezeni, ili tusaidie Watanzania walio wengi. Hii idadi ya damu uliyoandika hapa Mheshimiwa Waziri haitoshi kwa nchi nzima Tanzania kila siku watu wanahitaji damu salama na wanahitaji kuongezewa damu kupitia magonjwa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru wewe kwa haya machache niliyochangia. Kuna eneo hili la maendeleo na uwezeshaji wa wanawake. Eneo hili sidhani kama Wizara inafuatilia vizuri katika maeneo yake. Hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye maeneo yao wamekuwa miungu watu. Hii mikopo mnayosema namna ya kuwezesha wanawake VICOBA, hawa watu hawafanyi hii kazi kwa weledi. Afisa Maendeleo anataka rushwa ili mradi tu wanawake wapate mkopo. Hii siyo sahihi! Hii ni haki yao ya msingi akina mama kupata huu mkopo na upo kwenye sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, angalieni hivi vitu ambavyo vinagusa jamii. Kila siku tunaimba hapa issue ya dawa lakini kuna mambo ambayo tukiyasimamia mambo mengine yanaweza yakaenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu uhaba wa walimu. Walimu ni nyenzo muhimu katika nchi yetu lakini kwa muda mrefu kumekuwa na uhaba wa walimu. Pamoja na kuwa vyuo vingi vimetoa idadi kubwa ya walimu waliokidhi vigezo vya kuajiriwa, lakini Serikali imeshindwa kuwaajiri walimu hawa. Katika shule za sekondari zote nchini kuna uhaba mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi. Nashauri Serikali ifanye mkakati wa haraka na wa makusudi kuondoa tatizo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni walimu wa sekondari kupelekwa kufundisha shule za msingi. Tunatambua kuwa tuna uhaba wa walimu katika shule zetu. Kitendo cha Serikali kuwachukua walimu hawa wa sekondari kwenda kufundisha katika shule za msingi si sawa kabisa kwa kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo ya namna ya ufundishaji kwa masomo husika na madarasa yanayofundishwa na walimu wenyewe. Ni vema sasa Serikali ianze upya utaratibu wa kuajiri walimu kulingana na madaraja yanayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa watoto wenye ulemavu. Katika maeneo mengi nchini miundombinu ya madarasa haikuzingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu, jambo ambalo linawafanya watoto hawa kusoma katika mazingira magumu mfano miundombinu ya madarasa, vyoo na hata njia za kupita siyo rafiki kabisa. Nashauri Serikali ihakikishe kuanzia sasa shule zote zinazotarajiwa kujengwa ziwe na mfumo maalum kwa watoto wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu Vyuo vya Ufundi (VETA); kwa kuwa kwa sasa kwa kipindi kirefu Serikali haina mpango wa kuajiri pamoja na changamoto nyingi za watoto wengi kutofaulu wanapomaliza elimu ya msingi na hata kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo jambo ambalo limesababisha wimbi kubwa la vijana mtaani na kuzurura hovyo. Serikali imepoteza nguvu kazi ya Taifa kwa kushindwa kujenga vyuo vingi vya ufundi. Nashauri Serikali ijenge vyuo vingi vya mafunzo ya ufundi kwa kila mkoa kadri iwezekanavyo ili kunusuru kundi hili la vijana wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.