Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (2 total)

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa umeme wa REA utaanza kutekelezwa katika Jimbo la Busanda?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Jeremia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu umeanza rasmi nchi nzima tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu unajumuisha vipengele-mradi vya densification, grid extension na off-grid renewable. Mradi huu unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima, vitongoji vyote, taasisi zote za umma na sehemu za pembezoni ikiwa ni pamoja na maeneo vya visiwa. Usambazaji wa umeme katika Jimbo la Busanda utafanyika kupitia vipengele-mradi vya densification na grid extension utakaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Busanda pamoja na Wilaya yote ya Geita itajumisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 184.7; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 582 na ufungaji wa transfoma 109. Mradi huu utaunganisha wateja wa awali 8,834. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 25.6. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:-
Maeneo mengi ya Wilaya ya Kakonko yanaonyesha kuwepo kwa madini yenye thamani kama dhahabu na almasi.
(a) Je, kuna tafiti zozote zilizofanyika kuhusu upatikanaji wa madini Wilaya ya Kakonko?
(b) Kama zipo, je, ni madini gani yanapatikana na ni katika maeneo yapi?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia miaka ya 1970 Serikali kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za kubaini uwepo na upatikanaji wa madini katika Wilaya ya Kakonko. Baadhi ya tafiti zilizofanyika ni pamoja na upimaji na uchoraji wa ramani za kijiolojia katika eneo la Kakonko. Maeneo mengine yaliyofanyiwa kazi hiyo ni Kalenge na sehemu ya Kibondo. Aidha, kati ya mwaka 1980 na 1985, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la UNDP walifanya utafiti mwingine wa madini ya chokaa katika eneo la Bumuli Wilayani Kakonko.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti hizo zilibaini uwepo wa madini ya dhahabu katika maeneo ya Mwironge, Mwiruzi na Nyakayenze; chokaa katika eneo la Bumuli na katika eneo ya Keza, Kibingo, Nkuba pamoja na maeneo ya Kasanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti za kina zinahitajika ili kujua kina cha madini yaliyogunduliwa. Serikali inaendelea kuhamasisha makampuni mbalimbali binafsi ili kufanya utafiti wa kina na kuendeleza uchimbaji katika Jimbo la Kakonko.