Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aida Joseph Khenani (65 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kushiriki Bunge hili kwa mara ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki sana, dakika kumi naziona chache, napenda kuanza kuzungumzia suala la utawala bora. Tunapozungumzia utawala bora tunamaanisha, usiwe utawala bora wa maandishi uwe wa vitendo. Tunapozungumzia vitendo, amezungumza mzungumzaji aliyepita sasa hivi, kazi yetu sisi siyo kupongeza Serikali, kazi yetu ni kuikosoa na kuisimamia Serikali. Hatuwezi kuogopa polisi pale ambapo tunaona kuzungumza ni haki yetu, hatuwezi kuogopa kupigwa pale tunapoona Serikali imekosea, tutaisimamia na tutaikosoa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utawala bora, nianze na suala la maslahi ya walimu. Walimu wa nchi hii ni watumishi kama watumishi wengine. Kama kweli utawala ni bora, kwa nini madai yao imekuwa ni wimbo wa nchi hii? Kila Mbunge anayesimama hapa akizungumzia Jimbo lake anazungumzia masuala ya walimu. Leo ukitazama hata kwenye vyuo, kwa sasa wanachuo wakikosa haki zao muhimu, wanaposimama kudai haki yao wengi wanafukuzwa vyuoni, je, huo ni utawala bora? Tukisimama hapa tukidai haki zetu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa tuisaidie Serikali na nchi yetu kuboresha mapendekezo ya Mpango. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniongoza kwa sababu najua ni kazi yako. Ninapozungumzia suala la utawala bora hatuzungumzi kwa sababu ya uoga na nidhamu ya uoga sisi wengine hatuna. Mnapozunguka mnatazama nchi zinazounda Umoja wa Afrika utawala bora wanafanyaje, lakini utawala bora wa Tanzania tunauzungumzia kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele mlivyoleta kwenye Mpango, Serikali makini haiwezi kuwa na vipaumbele vingi visivyokuwa na idadi. Inaonyesha ni jinsi gani mmeandika tu lakini utekelezaji ni sifuri. Nikianza na suala la kilimo. Natokea Mkoa wa Rukwa, tunalima sana mahindi na maharage. Leo hii wakulima wa Mkoa wa Rukwa wanajiona kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Pembejeo ni tatizo kwao lakini hata vile vichache wanavyopata kwa nguvu zao ili angalau kuzisaidia familia zao kuna ushuru usiokuwa na tija. Tunapozungumzia ushuru, huyo Mtanzania wa Rukwa ambaye ni mkulima, amekosa pembejeo, amejikongoja akalima kilimo chake tena kwa mkono lakini na kilekile kidogo Serikali inatoza ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini watakapoanza kuwathamini wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa? Wamelima mahindi na mnajua walikosa soko, mmezungumzia hapa, lakini huyu mkulima wa Tanzania ili ajue kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamthamini, inamthamini kwa lipi, kwenye pembejeo ni shida, kwenye masoko ni shida.
Naishauri Serikali, kama kweli tunaamini asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima, tutengeneze mazingira rafiki ya wakulima hawa. Isibaki stori za kwenye madaftari na vitabu yanabaki kwenye makabrasha, tunataka vitendo vifanyike. Kama kweli ni kazi tu mmemaanisha mfanye kazi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la maji, nikiwa natazama Bunge kwa njia ya TV, Mheshimiwa Keissy imekuwa ni wimbo wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, iko Mkoa wa Rukwa. Watu wa Nkasi Kaskazini na wenyewe ni Watanzania kama Watanzania wengine, kwa nini kila siku iwe ni wimbo tu wa maji? Kwenye Mpango mnaoleta mtuambie ni mikakati gani mipya mliyokuja nayo ukiachana na nyimbo mnazoimba kila siku. Mikakati mipya iko wapi ambayo itatufanya sisi tuwaamini kama kweli mnakwenda kutenda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wananchi, imefikia mahali wamechoka na nyimbo hizi sasa wanataka utendaji. Ukitazama Bunge hili Wabunge wengi wanasimama wanazungumzia suala la maji, sawa, yawezekana tunazungumza na tunaleta kwa maandishi kama hivi, ni kitu gani kinawazuia sasa mnapoandika mnashindwa kutenda? Kama kweli ni Serikali sikivu na siyo kinyume, tendeni sasa, muache kupiga story.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu. Mkoa wa Rukwa umesahaulika kwa kila kitu. Watu wa Rukwa siyo Watanzania? Ukizungumzia Nkasi Kaskazini na Kusini barabara ni hadithi. Amezungumza hapa Mheshimiwa Mipata na anazungumza kila siku lakini sisi tunapozungumza hatuombi, tunaitaka Serikali ifanye kwa sababu ni wajibu wenu kufanya na msipofanya tunajua hamsikii na hamuelewi. Msifikiri Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza ni kwamba mnapendwa sana, no, lazima mjitafakari. Pale mliposhinda kwa haki mjitafakari lakini mapito mliyoyapata katika kipindi hiki mnajua kwamba ni jinsi gani mmekosea step, lazima mjipange. Sasa kwenye Mpango mnaokuja nao tunahitaji mikakati madhubuti ambayo kweli inamaanisha kwenda kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu. Suala la elimu haliwezi kufanikiwa kama mnakurupuka lazima mtafakari kabla ya kusema. Mnasema elimu bure, elimu bure itakujaje wakati walimu wenyewe madai yao yako palepale? Sawa wanafunzi wamefika shuleni lakini sasa hivi wanafunzi idadi yao ni kubwa kuliko walimu. Hii elimu bure inakwenda sambamba na yale mnayoyasema au mnasema tu ili kutimiza wajibu? Mimi naamini hata hili mmeibuka tu kulisema, hamjajipanga. Ni mipango gani madhubuti ambayo mmetuonyesha hapa kama kweli mmekusudia kutoa elimu bure? Mimi nawashauri msiwe mnakurupuka, mjipange kwanza. Mkiona UKAWA wamekuja nayo wanazungumza msifikiri na nyie mnaweza mkafanya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi yangu kuiambia Serikali pale walipokosea lazima wajirekebishe na wasikurupuke lazima wajipange. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa na maneno mengi kuliko kutenda na Watanzania wanaona. Haya wanayoyazungumza inaonyesha ni jinsi gani kweli wamekurupuka, hawajajipanga. Vipaumbele ambavyo wanashindwa kuvitekeleza, vipaumbele vingi, hakuna Serikali inayoendeshwa kwa staili hii. Lazima uwe na vipaumbele unavyojua utatekeleza. Ni kipi ambacho mlikileta kwenye Mpango uliopita na mmetekeleza kama mlivyokuwa mmepanga, hakuna! Imekuwa ni maneno ya kila siku ya kuandikwa yanashindwa kutekelezeka. Tunaitaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi iachane na porojo, ifanye kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Napenda kushauri mambo machache katika Wizara hii ya Ardhi. Mheshimiwa Waziri imeonekana kama ana mikakati kabambe kwenye maandishi yake, lakini sijajua alivyojipanga kwa sababu suala la migogoro ya ardhi lipo kila sehemu nchini na halijaanza leo na sitapenda sana kama Waziri anasubiri na Mkoa wa Rukwa yatokee kama yanayotokea Morogoro ndiyo achukue hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wamekuwa na utaratibu mmoja wa kusubiri matukio ndiyo wamnakuja na matamko na mikakati. Nafikiri ni vema kwenye maeneo ambayo haijatokea migogoro, wakaweka mikakati thabiti kuonyesha kwamba wako serious na suala hili. Tatizo wanasubiri matukio ndiyo wanakuja na kauli ambazo hazisaidii chochote, watu wanakuwa tayari wameangamia, wamepoteza maisha, hawana tena cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mgogoro wa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na mwekezaji EFATHA, limekuwa ni kero sana kwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Rukwa, tumezungumza mara nyingi sana. Mheshimiwa Waziri amezungukia maeneo mengi lakini Mkoa wa Rukwa bado hatujamwona. Hili suala limeleta shida sana kwani kuna watu wameumia sana pale, kuna watu wamefungwa, sijajua shida ni nini? Hili suala sijui halijafika mezani kwa Mheshimiwa Waziri au kama limefika ni kitu gani kinazuia asije Mkoa wa Rukwa kuangalia nini kifanyike? Nimeona jitihada za Waziri, lakini napenda kuziona pale atakapofika kuzungumza na wananchi wenyewe. Napenda kumshauri ili afanikishe masuala haya, asifanye kazi kama Wizara nyingine wanaopewa maandishi wanaridhika kwa maandishi yale bila kwenda sehemu husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ambayo inaendelea mpaka sasa, Jimbo la Kalambo kuna mauaji yametokea hivi karibuni. Migogoro hii iliyopo kwa Wafipa ilikuwa haipo sana kwa sasa ipo kati ya Wafipa na Wasukuma lakini shida siyo makabila, elimu mnaitoa kiasi gani? Mmegundua shida ya migogoro hii ni nini? Yawezekana mmekosa suluhisho kwa sababu hamjaja na njia ya kusuluhisha migogoro hii ila mnakuja na matamko ambayo hayana tija. Ni vema mkajua tatizo la migogoro ni nini na mkaja na suluhisho la kudumu siyo la muda mfupi kwa ajili ya kampeni, mkaja na suluhisho ambalo litaondoa migogoro kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la kuwapa ramani viongozi wa Serikali alilozungumzia hapa Mheshimiwa Waziri. Mkoa wa Rukwa nimeangalia hapa pesa zilizorudishwa kwao, kwenye kitabu cha hotuba, ukurasa wa 83 anasema marejesho, ile asilimia 30, Manispaa nzima ya Sumbawanga kiasi ambacho kimerejeshwa pale sijajua kama kinaendana na Manispaa, kuna shida kubwa sana hapa. Yawezekana ni mawasiliano mabovu kati ya Wizara yenyewe ya Ardhi na Manispaa husika. Kama siyo rushwa basi kuna shida kubwa sana kwenye Wizara au kwenye Manispaa pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanaowaweka kwenye Manispaa na Halmashauri zetu wamekuwa wakijitukuza kama Miungu watu ambapo wananchi wanapokuwa na shida wanashindwa kuwahudumia kwa uharaka, wanaangalia ni nani anasema, anasema nini, ana kiasi gani. Sasa nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama eneo ninalotoka mimi Kata ya Chanji, ni ya muda mrefu sana kwenye Manispaa ya Sumbawanga, iko katikati ya mji lakini Mheshimiwa Waziri akitazama maeneo yaliyopimwa atashangaa lakini property tax inakusanywa! Halafu baadaye ndiyo watakuja na hili la bomoabomoa, Sumbawanga haijafika lakini wananchi wako kwenye tension kubwa sana kwamba sijui mimi nitaondoka au nitabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ni vizuri elimu ikatolewa kwanza kwa watu hawa na elimu tunayoizungumzia ni bora wakapewa Wenyeviti wa Serikali au Vitongoji na Vijiji, wale ndiyo wako karibu na wananchi kuliko hawa mnaowapeleka. Hawa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji au Vijiji wataweza kueleweka vizuri na wananchi wao kwa sababu wanajua maeneo na wanajua ramani vizuri za maeneo hayo. Kama tutachukulia mambo haya juu juu hatutaweza kukomesha tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana Waziri ana nia njema lakini watendaji wake wa chini ndiyo wanaomwangusha lakini yawezekana na wao ni kwa sababu elimu hawana au yawezekana hawa watu ambao wanaweza wakafikisha ujumbe ni wachache kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, kuna haya mambo yanawezekana yanakurudisha nyuma kwa sababu aidha, watu kwenye Halmashauri ni wachache au hata waliopo hawatimizi wajibu wao. Kwa hiyo, ni vizuri katika haya anayotaka kuyafanya akagundua kitu gani kinakwamisha pengine ni bajeti anayopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia mahali nchi hii haitambui kwamba migogoro hii inapelekea kukosa amani katika nchi yetu, kwa sababu unapotokea mgogoro kati ya shule na wananchi unategemea ni nini kinaendelea? Siyo kwamba wale Walimu wanatambua maeneo yale wao wamekwenda pale kufundisha, lakini nani anayatambua yale maeneo? Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa haelewi ramani halisi ya pale ikoje. Sasa inapotokea migogoro kama hii nani alaumiwe Serikali, Halmashauri ya Mji au Manispaa ambayo inahusika na lile eneo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kabla hatujachukua hatua na migogoro mingine haijajitokeza, elimu itolewe kwa watu wetu na elimu hiyo tusi-base tu kwa watu ambao wako Wizarani, tu-base kwa watu ambao wako na wananchi wetu ambao ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la asilimia 20 kwa Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa, yawezekana maeneo mengine wanapewa, Manispaa ya Sumbawanga kuna shida katika suala hili. Inafikia mahali Watendaji wa Kata wanasema wanaopaswa kukusanya ni mgambo, sheria inasema nini juu ya suala hili, ni akina nani wanaokusanya hii property tax? Sheria inasema nini, inawezekana ni mkanganyiko. Sasa Wenyeviti wanapata shida, wanakusanya pesa hizi kwa amani kabisa, wanapokwenda kule hawapewi, sasa shida nini Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naona kwamba Waziri ana nia njema katika maelezo yake, lakini yawezekana watendaji wake ndiyo wanaokwamisha mambo anayotaka kufanya. Pia hata bajeti anayopewa haifanani na migogoro ambayo ipo kwenye nchi yetu, haifanani kabisa. Ndiyo maana muda mwingine tunaona kama kiini macho au kama story za miaka yote. Yawezekana ana kusudio jema, tunataka tuone haya mambo kwa vitendo na pale Waziri anapoona amezidiwa asisite kusema. Kazi yetu hapa siyo kumshangilia, tutamshangilia pale atakapofanya vizuri, lakini kama atakuja na haya mabegi aliyotupatia leo na documents nyingi halafu akashindwa kutimiza kile alichopanga, haitatusaidia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kusema ni kwamba, suala la rushwa kwenye Wizara hii ni kubwa sana. Yawezekana hata Waziri katika maeneo aliyokwenda ameliona lakini maeneo mengine akashindwa kuona kwa sababu sijajua kama anapewa ushirikiano wa kutosha. Huu ushirikiano ni lazima kuwepo na semina elekezi ili Mwenyekiti wa Serikali ajue wajibu wake, ajue anapata nini na anapaswa kufanya nini kwenye suala la ardhi, lakini ajue wananchi wake wanapaswa kutimiza wajibu gani kwenye kumiliki majengo yao au wanapokuwa wanataka umiliki wa ardhi. Mheshimiwa Waziri wananchi kwa sasa wanatamani maeneo yao yapimwe lakini anapokwenda pale mpaka aje apate hiyo hati ya kumiliki ardhi ni shida, tatizo ni nini, kuna shida gani hapa na bado inakuwa ghali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri hata hizi nyumba tunazosema za National Housing bei wanazotoa hazifanani na mazingira halisi ya maeneo husika. Huwezi ukauza nyumba kwa shilingi milioni 30, kwa Manispaa ya Sumbawanga, unategemea Mfipa anayepata gunia tatu kwa mwaka ataweza kununua hiyo nyumba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hizo nyumba zijengwe kulingana na mazingira halisi ya eneo husika. Kama ni Manispaa ya Sumbawanga waaangalie watu wa Manispaa ya Sumbawanga uwezo wao wa kipato ni kiasi gani. Wasichukue mazingira ya Dar es Salaam wakayapeleka Manispaa ya Sumbawanga haitawezekana. La sivyo hizo nyumba watakwenda kujenga kwa ajili ya wafanyabiashara lakini kusudio la zile nyumba ilikuwa ni watu wa hali ya chini waweze kupata nyumba za kuishi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri katika hilo, awatazame watu wa Sumbawanga kwa jicho lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumaliza hii migogoro, Mheshimiwa Waziri ana nia njema na ameonesha njia, napenda kushauri tena kuwe na ushirikishwaji. Manispaa ya Sumbawanga siyo lazima twendaemahakamani, sisi tunaheshimu sana mila na desturi, anaweza akaa na watu wa pande zote mbili wakamweleza shida ni nini badala ya kusubiri migogoro mpaka ifike mahakamani na watu kuuawa. Kwa hiyo, ushirikishwaji ni suala jema sana na litasaidia kumaliza migogoro hii. Yawezekana sheria zipo, lakini zimepwaya au usimamizi ni mbovu. Kwa hiyo, hata kama zitakuja hapa zikawekwa kwa staili nyingine, inawezekana ikawa ngumu kwenye utekelezaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijaalia uzima, kuweza kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu. Pia napenda kupongeza na kushukuru kwa dhati Ofisi yako kwa kuweza kuokoa maisha yangu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru pia Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano waliouonyesha na nitakuwa sio mtu mwema sana nisipowashukuru Wabunge wa Mkoa wa Rukwa na Katavi kwa upendo waliouonyesha bila kujali itikadi za vyama vyao.

Mheshimiwa Spika, pia naungana na wazazi, Walimu, ndugu na jamaa katika kuomboleza msiba uliotukuta juu ya wanafunzi ambao walituacha. Tunasema kazi ya Mungu hatuwezi kuhoji, lakini tumepokea, ingawa mambo haya hayazoeleki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda kuchangia mambo machache nikianza na upande wa habari. TBC ni Television ya Taifa wote tunajua, lakini inachangiwa na walipa kodi wa nchi hii wakiwepo wa Mkoa wangu wa Rukwa, leo tunapokuwa tunajadili bajeti, wanashindwa kujua wawakilishi wao wamezungumza nini? Je, wamezungumza yale waliyowaambia? Kwa sababu hawawezi kuona tena Bunge live.

Mheshimiwa Spika, yawezekana hata nia njema ya Serikali hasa anapokuwa anazungumza Mheshimiwa Rais kwamba watu wafanye kazi, lakini tunafahamu fika kwamba Rais anapokuwa anafanya jambo lolote anaonekana live. Rais huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alichaguliwa kwa kura za Watanzania, Wabunge wamechaguliwa kwa kura za Watanzania. Sijajua utofauti mkubwa uliojitokeza hapo katikati.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri pamoja na sisi Wabunge, mimi bado linanichanganya kwenye kichwa changu. Tofauti ni nini? Ni nafasi au ni kazi kama alivyozungumza? Kwa sababu ule muda anapoonekana yeye, wananchi wanaacha kazi wanamsikiliza, basi angalau hata kipindi hiki cha bajeti sasa ili wananchi waweze kuwaona Wawakilishi wao wanafanya nini? Je, wanazungumza yale waliyowaambia wazungumze au inakuwaje? Sidhani kama itakuwa busara au uzalendo anaousema yeye aonekane, Waheshimiwa Wabunge wasionekane, wakati wote walikwenda kuomba kura na wananchi ni wale wale ambao wanatakiwa waone nini kinazungumzwa na nini kinatendeka. Sidhani kama uzalendo uko mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri labda aje atuambie kwamba pesa zinakuwa nyingi sana kuonyesha Bunge, lakini upande wa Rais na vitu vingine pesa zinakuwa siyo nyingi. Wakati huo huo TBC inaweza kuonyesha mambo mengine. Napenda tupate taarifa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up kwamba kwa mara ya mwisho ni lini taarifa za Upinzani zilionyeshwa TBC? Nimekuwa mfuatiliaji sana wa TBC. Sasa kama TBC imekuwa na ubaguzi, ni vyema Mheshimiwa Waziri aje kutuambia tujue. Ni lini kwa mara ya mwisho TBC ilionyesha habari za Upinzani, wakati wote ni Wabunge na wote ni Wawakilishi wa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili kwa upande wa habari, ni juu ya Waandishi wa habari. Pamoja na Bunge kutoonyeshwa live, Watanzania hawa wanategemea kupata habari kwenye vyombo mbalimbali. Leo waandishi wa habari wanakuwa na hofu ya kutoa habari. Hatujasikia tamko kutoka kwa Mheshimiwa Waziri linaloonesha moja kwa moja uzito juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari. Tumeangalia matukio kadhaa, achana na hayo ya huko nyuma ya akina Mwangosi na watu gani, lakini bado hatujaona jitihada za Serikali juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie mikakati yake aliyoipanga juu ya Waandishi wa Habari. Wananchi hawawezi kujua chochote bila kuwaona au kuwasikiliza Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wangu wa Rukwa kuna maeneo hakuna TV, wanategemea kusikiliza redio. Hizo redio zenyewe sasa hivi habari haziendi kama zilivyo; sijui mpaka zichujwe wapi, zifanywejwe! Sasa haya mambo inafikia mahali yanakuwa na ukakasi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ni mikakati gani ameiweka juu ya ulinzi wa Waandishi wa Habari pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari? Sambamba na hilo, ile ripoti ya Mheshimiwa Nape tunataka tuisikie, kwa sababu hapa ndiyo mahali pake, aje atuambie nini kinaendelea juu ya kile kitu? Kama kuna kiini macho tujue kwamba imeshindikana, lakini imeshindikana kwa nini?

Mheshimiwa Spika, upande wa michezo, hatuwezi kuboresha michezo tukiwa hatujaboresha viwanja vya michezo. Hapa tutapiga story siku zote na kutafuta mchawi. Kwa sababu huwezi kusema watu waje wacheze, unategemea kwamba waje wacheze Dodoma tu; kwa sababu hawa watu wanatoka kwenye Wilaya na Mikoa. Huko kwenye Wilaya na Mikoa hali za viwanja ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, katika viwanja hivyo kuna viwanja vinamilikiwa na Chama Tawala; siyo dhambi, basi viendelezeni. Viko kwenye hali mbaya! Shida ni nini? Yawezekana bado hakujawa na mikakati thabiti kwa sababu hatutegemei kuangalia Serengeti boys wale wale wakae miaka 20, tunataka mikakati ya wale ambao wanaandaliwa sasa kuja kuwa Serengeti Boys wa mwaka 2020. Hawa watu wanapatikana wapi? Wanapatikana kwenye Wilaya na Mikoa. Ni utaratibu gani umewekwa ambao utakuwa rafiki kwa hawa vijana wanaotoka kwenye mikoa na wilaya?

Mheshimiwa Spika, siamini kwamba Mkoa wangu hakuna wachezaji wazuri. Mkoa wa Rukwa wanakula samaki, kuna watu wanacheza vizuri sana. Ni lini utawajua? Utawajua kwa kufuata ule utaratibu uliokuwepo zamani. Kulikuwa na michujo inafanyika shule za msingi na sekondari. Nakumbuka kwa mara mwisho UMITASHUMTA pamoja na UMISETA wakiwa wanakwenda Geita nafikiri, ilitokea tamko hawarudi wale watoto. Tunaomba mtuambie sasa, hiki kitu ndiyo kimefutwa moja kwa moja au kuna mikakati gani inaandaliwa juu ya suala hili? Maana imeshakuwa sasa hatuelewi, tupo tu.

Mheshimiwa Spika, siamini kama wachezaji wengi wanatoka Dar es Salaam na Mwanza tu; na Mikoa mingine wachezaji wapo. Wekeni mikakati, wekeni mazingira rafiki ya kuwapata wachezaji wazuri na wapo, wanapatikana maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, vile vile tusiwekeze kwenye mpira peke yake. Kama tumeshindwa kwenye mpira, lazima tuwe na plan B. Tutafute mchezo mwingine ambao hatutaitwa shamba la bibi Tanzania, haiwezekani! Naamini vipaji vipo vingi tu, lakini ni namna ya kupata hivyo vipaji na kuvifuata kule viliko. Kwa hiyo, kumekuwa na shida kidogo.

Mheshimiwa Spika, vazi la Taifa limekuwa likizungumzwa sana. Siamini kwamba mpaka leo tumeshindwa kupata vazi la Taifa. Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kufanya majumuisho atuambie, maana nimeona huku pembeni nyuma ya hiki kitabu, lakini haijaonesha kwamba ndiyo hili, sijui! Nafikiri ndiyo utaratibu unaandaliwa. Muda umekuwa mrefu, mpaka lini kwa mwendo huu unaokwenda? Kama ndiyo hili limepitishwa, basi mtuambie lilivyopitishwa.

Mheshimiwa Spika, hiki kitu inatokea, hata ukiangalia kwenye muziki, watu wengi hasa wanawake unakuta mavazi wanayovaa pale ni tofauti na wanaume, wao watavaa suti nzuri na tai safi kabisa, lakini wanawake wanavaa vibaya! Leo mtawaambia nini wakati hakuna vazi lililoteuliwa? Tunaomba mtakapokuja, tena Mheshimiwa Naibu Waziri,yeye ni mwanamke, kwa sababu inapotokea kudhalilishwa, hawadhalilishwi wale walioko pale na wanawake wengine wote wanaozunguka kwenye jamii hizi tunapata aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, lilizungumzwa sana siku ya Ijumaa suala la Mwenge. Naomba Mheshimiwa Waziri aje anipe ufafanuzi kidogo. Kwenye Mkoa wangu wa Rukwa Wenyeviti wamekamatwa kwa kutochangisha pesa za Mwenge. Naomba kujua, ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa kwa kutochangisha pesa za Mwenge? Kwa sababu kitu kinachoitwa mchango kwa mimi ninavyoelewa, ni hiari siyo lazima. Sasa ni sheria ipi ilitumika kuwakamata Wenyeviti hao wa Serikali ambao hata mshahara hawalipwi; na kila siku tunajadili hapa, hakuna siku imepitishwa Wenyeviti wataanza kulipwa mshahara au posho. Sasa ni sheria gani ilitumika kuwakamata Wenyeviti hawa? Naomba kauli ya Serikali Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kichwa changu bado hakijakaa vizuri. Ahsante kwa nafasi uliyonipa kutoa mchango huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini napenda pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunifikisha siku ya leo salama na kuchangia Wizara muhimu sana kwa wananchi wangu wa Mkoa wa Rukwa. Tunapozungumzia kilimo, tunazungumzia kitu muhimu sana ndani ya Taifa letu, tunazungumzia kitu muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa, lakini pia tunatazama hali ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika haya mazingira tunapozungumza kilimo kunajambo la msingi ambalo ni bajeti. Bajeti ni tatizo; na hata tutakapochangia mambo mengi hapa tunarudi pale pale kwenye bajeti, tutatoa maelezo mengi ushari mwingi suala linarudi pale pale kuhusu bajeti.

Naomba utakapokuja Mheshimiwa Waziri wa Kilimo utuambie mikakati uliyonayo tofauti na miaka iliyopita. Hali ya chakula umeiona, hali ilivyo mbaya unajua ingawa imefikia mahali sasa mnatoa kauli za kufurahishana tu unamfurahisha aliyekutua wakati wananchi wanaumia, tukizungumza hapa zinakuwa story tu kama story zingine za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kilimo; sasa hivi ukiwatazama watumishi wa Serikali hawategemei tu mshahara, wamejiingiza kwenye kilimo kwa sababu wanajua kilimo kinalipa; kilimo ndiyo kila kitu. Sasa kama tutashindwa kuwekeza kwenye kilimo tutaondokaje kwenye hii hali tuliyonayo? Pembejeo ni shida, kuna suala tunazungumzia kila kipindi cha bajeti; Benki ya kilimo. Kama maeneo ambayo yanazalisha hiyo Benki haipo, hata wakulima hawaijui tunamalizaje tatizo hili? Hawajui waanzie wapi wala waende wapi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kila tunapozungumza majibu yanakuwa ni yale yale. Mimi naomba utakapokuja utuambie angalau mikakati mipya ambayo unayo ili kukitoa kilimo hapa kilipo na hatimaye tuinue uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuzungumzia kilimo kwamba wananchi wa Rukwa wananufaika wakati hujawaambia kwamba kwa kipindi hiki ambacho wanategemea kuvuna watauza wapi. Suala la masoko ni muhimu kuliko suala lingine. Sasa hivi tunaendeshwa kwa matamko tu, akipita Mheshimiwa Rais anasema hivi, halafu wewe Waziri wa Kilimo unakuja na matamko mengine, sasa hawa wakulima wamebaki dilemma, yaani hawajui wamsikilize nani? Wamsikilize Mheshimiwa Rais wakusikilize wewe Mheshimiwa Waziri wa Kilimo?

Mheshimiwa Naibu Spika, na haya mambo lazima yawekewe utaratibu. Tunajua itifaki zilivyo, lakini tunapozungumzia uchumi kuna watu ambao ni wataalamu panapokuwa na siasa pia tuwasikilize wataalamu hawa, wakulima tunawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo tumekuwa tunalizungumza kila siku na hakuna majibu ambayo yanaonesha mwelekeo moja kwa moja wa kuondokana na haya matatizo ambayo wanayapata wakulima juu ya pembejeo. Tunaomba Serikali ipeleke pesa kwa wale wanaonunua pembejeo kwa wakati ili muda ukifika yale maduka yauze kwa bei ya ruzuku na wasaidie wale wakulima. Nilizungumza hapa, ukitazama Mkoa wa Rukwa mkiwapa pesa wale wakulima wanaopata shida, hawana hata pesa za pembejeo, mkiwapa kipindi cha mwenge hamjawatimizia malengo yao; wapeni kipindi cha kilimo ziwasaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, zitawasaidia wanawake zitawasaidia vijana pia. Kuhusiana na suala hilo utakaa tu wewe na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, mkatoa tu mwongozo ukafika kule. Sijajua Kiswahili ambacho kinaweza kikawasaidia ni kipi kwa sababu kama maneno tunasema mambo mengi tunazungumza lakini bado utekelezaji unakuwa mgumu. Kipindi nasema nakuja kuchangia Mbunge mmoja akaniambia unaenda kuchangia nini? Nikajiuliza maswali kwa nini ananiambia naenda kuchangia nini, nikamwambia naenda kuchangia kilimo; nini kwenye kilimo, bajeti yenyewe ndio hii! Nimetafakari sana, lakini tutasema tu kwa sababu ndiyo kazi yetu kusema, kama mtasikia sawa msipo sikia sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira Tanzania ni shida kwa vijana, vijana hawa wanategemea kilimo, kilimo chenyewe kina matatizo, tuambieni hawa vijana mnawapeleka wapi? Yaani kilimo hamjawasaidia, ajira hakuna mnataka waende wapi?

Mheshimiwa Waziri tunaomba mikakati ya kutosha, yaani hali ya kilimo haifurahishi ingawa unakuja hapa unatuambia hali ya chakula iko vizuri, siju iko vizuri wapi? Kwa sababu ukiangalia bei ya mahindi ya mwaka wa jana, bei ya mahindi kwa kipindi hiki sasa msimu huu wa kilimo bei yake unaiona halafu unasema hali ya chakula, Mheshimiwa Waziri unamfurahisha nani yaani?

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani haya mambo unakuwa unamfurahisha nani kwa sababu hali halisi inaonekana. Ni bora ukasema ukweli tukusaidie kama suala ni bajeti hupewi pesa sema tukusaidie ndiyo kazi yetu. Lakini ukija hapa ukafanya mambo ya kufurahishana hatimaye tutaanza kuonana wabaya hapa, tunaweza tukakutuhumu kumbe kosa si wewe kosa ni bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya wakulima na wafugaji yaani umekuwa waimbo, hivi mnataka mtuambie kwamba mmeshindwa kabisa kuwa na mikakati ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji? Wataalamu wanafanya kazi gani? Yawezekana ninyi ni wanasiasa, wataalam wenu wameshindwa kuwasaidia jinsi ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji au mpaka leo hamjajua tatizo lililopo kati ya wakulima na wafugaji ni nini? na kuna migogoro mingine inachangiwa na ninyi wenyewe Serikali kwa kutokufanya maamuzi haraka ya kumaliza midogo kabla haijawa mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali tena leo yawezekana ikawa mara ya mwisho. Suala la ardhi, ardhi tunajua ni ndogo na watu wanazidi kuongezeka tupeni sasa mikakati ya kumaliza migogoro hii yawezekana ndugu zenu hawajaumizwa, lakini kuna watu wamekufa .
Roho inakuwa inauma tunapokuja kuwaambia nyinyi hamsikii mnataka tuseme nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningefurahi kama Mheshimiwa Waziri wangu vile ambavyo huwa anaonyesha anasikia tukizungumza leo tunapokuja kipindi kingine tunakuja na kauli nyingine lakini kauli ni hizi hizi na mambo haya haya hivi usikivu unafanyika wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishauri tu, yale maamuzi ya kwenda kununua ndege yawezekana yalikuwa sahihi, lakini kama kilimo ni kipaumbele maamuzi yale yalikuwa batili. Huwezi kupanda ndege una njaa, huwezi kupanda ndege una utapiamlo, kama kilimo kilikuwa cha kwanza ni bora basi mngechukua nusu kwanza muingize kwenye kilimo na nyingine iende huko kununua hiyo ndege. Kwa sababu tunasema kilimo ndiyo kipaumbele. Sasa maji ni shida, kilimo cha umwagiliaji kinapatikanaje?

Pembejeo ni shida, bajeti yenyewe uliyopewa shida, haya kwenye masoko yenyewe mpaka leo hamjasema lakini toka acha wakulima wauze bei wanayotaka, sawa watauza halafu wakiuza hiyo bei kwa sababu shida sio bei shida ni pesa hakuna hata hiyo bei atakayopanga nani ataenda kununua hela hamna. Kwa hiyo, kunamazingira mengine matamko haya hayasaidii na yenyewe yanatengeneza migogoro tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya hali ya hewa imekuwa ndiyo kisingizio, hawa watabiri wa hali ya hewa nao wanaweza wakatusaidia au wakatuathiri, kwa sababu wakulima wanapokuwa wanakwenda kulima wanataka kujua mwaka huu mvua ni nyingi au chache, wanatakiwa kuambiwa walime nini kulingana na hiyo hali ya hewa ya kipindi hicho. Sasa hayo mazingira yanapokuwa yanajitokeza na wakulima nao wanaanza kulima kwa mazoea. Ukitazama hii bajeti ina maana kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017 wakulima walikuwa wanafanya kazi wao binafsi, ni kama Wizara haipo, kwa utekelezaji huu, Wizara haijawasaidia chochote.

Mheshimia Naibu Spika, suala hili sasa hivi mawakala kule Mkoa wa Rukwa hawajalipwa mpaka leo, kuna watu wameuziwa nyumba zao, kuna watu wamefilisiwa. Lakini kosa sio la kwao ni kosa la Serikali kwa nini inashindwa kuwalipa. Mheshimiwa Waziri ni vyema ukawa mkweli na muwazi tukusaidie. Tukiwa tunazungumza hapa masuala ya kilimo uti wa mgongo sijui kilimo kwanza yaani kauli nyingi ambazo haziendani kabisa na mazingira ya kilimo chenyewe kinavyokwenda. Ni vyema mkawa mnatoa matamko yanayoendana na mazingira mliyonayo. Lakini ukisema hamna pesa wala si dhambi kwa sababu utakuwa umesema ukweli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, lakini na mimi napenda kupongeza mzungumzaji aliyetoka kuzungumza sasa kwa kutimiza wajibu wetu kama Wabunge kwa kuwa ni muhimili unaojitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia hotuba ya Waziri Mkuu cha kwanza tunaangalia uhalisia wa Watanzania. Tukitazama uhalisia wa Watanzania tumeangalia jambo la msingi ambalo ni maisha ya kawaida wanayoyaishi kila siku. Maisha waliyonayo Watanzania hayaendani na hiki kilichosomwa au kilichoandikwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, hali ya maisha ni ngumu sana. Tunapozungumza kwamba hali ya uchumi ni nzuri wakati Watanzania hali yao ni mbaya, tunaomba hayo maandishi yaende kwenye uhalisia kwa Watanzania, hali ya maisha haifanani na kile kilichoandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia ajira mpya tunatazama vijana wengi ambao wamemaliza vyuo wapo mtaani. Leo vijana wetu wanajiingiza kwenye vitendo mbalimbali ambavyo si makusudi yao, ni maisha. Leo tumetazama taarifa mbalimbali hasa kwa jana, yaani imefikia mahali mpaka makanisani sadaka zimeanza kuibiwa. Hatutasema ni vijana peke yao ndio wanaoiba, lakini ni vyema Serikali ikajielekeza kwa kuangalia kundi kubwa la Watanzania ambalo ni vijana linawapeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi viongozi wetu wapo Segerea, tumeenda kutazama kule robo tatu ya wafungwa waliopo kule ni vijana, na hapo inajidhihirisha kabisa kwamba Tanzania suala la ajira imekuwa ni kidonda ndugu sasa. Ni vyema kama tunategemea kuleta amani tunayoizungumza kwenye Taifa letu tukatazama kundi kubwa la Watanzania na tukatafuta suluhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka kwenye Mkoa wa Rukwa ambao tunategemea kilimo, kilimo hicho ninachokizungumza ndicho ambacho Watanzania wengi tunategemea kuendesha Taifa. Leo wamesimama Wabunge wengi wakazungumzia kuhusu ununuzi wa ndege, si jambo baya, lakini ni wakati gani umenunua na je ndio uhitaji mkubwa wa Watanzania? Watanzania wangapi ambao watafaidika na hiyo ndege? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anaulizwa Mkurugenzi wa ATCL leo amesema nje ya kupanda ndege Watanzania watanufaika kuuza vipuli; mambo haya ni fedheha kwa Watanzania. Ni kweli ndege ingenunuliwa lakini kwa kuangalia kipaumbele cha Taifa letu ni ndege? Ni kweli taifa letu kipaumbele cha kwanza ni ndege?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapouzungumzia Mkoa wetu wa Rukwa ukiacha suala la usafiri wa anga kuna usafirishaji wa majini. Amezungumza Keissy pale kuhusu meli, hiyo meli imekuwa ni wimbo. Meli ile ingewasaidia Watanzania wa kawaida hata kufanya biashara, kutoa mazao yao Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine kupeleka hata nchi ya Congo; lakini leo ni Mtanzania gani wa Rukwa atakuja kupanda ndege hiyo iliyoletwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mkumbuke unapozungumzia ndege huzungumzii wananchi wa Dar es Salaam, unazungumzia wananchi wa Taifa la Tanzania na hizo ni kodi za Watanzania wote. Tungeomba mambo ambayo tunakuwa tunazungumza kama Wabunge yachukuliwe kama vile tunavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafikia mahali tunapata shida sana, kwamba hivi tunazungumza kwa kutimiza wajibu au tunazungumza kama mhimili ambao tunatakiwa tuisimamie Serikali? Kwa sababu yale tunayozungumzia hayawezi kwenda kama vile tunavyozungumza na mnakuja hapa matokeo yake sasa watu wamejaa hofu. Niwaombe Mawaziri, hata Mungu ni mkubwa lakini ana washauri wake ambao wako chini sana, Malaika; kaeni na Mheshimiwa Rais mumshauri uhalisia wa Taifa letu na Watanzania wanakabiliana na nini. Mkiwa waoga tukija hapa tutazungumza kumbe mkifika kule mnakuwa na hofu mnashindwa kutimiza wajibu wenu wa kumshauri Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza hivi, kabla hatujapitisha bajeti tayari bei ya petrol imepanda, bei ya mafuta ya taa imepanda, bei ya dizeli imepanda. Sasa unaanza kujiuliza huu uchumi uliokuwa ina maana shilingi ya Tanzania imeshuka thamani. Sasa hii tunayozungumza hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu, najua hata mama yangu ameondoka lakini yupo Naibu Waziri pale; tunapozungumza kama Wabunge angalau basi muwe mnafungua masikio mnatusikiliza tunachokizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hapa, tulizungumzia mambo ya petroli hapa, tulizungumza mambo ya mafuta ya taa; hivi leo ukipandisha bei kwenye petroli unategemea Watanzania wangapi wanaoathirika? Hiyo inakwenda kuwaathiri moja kwa moja Watanzania wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha Watanzania wanaishi vizuri kwa kupewa mambo yao ya msingi. Mlipo kuja hapa mkazungumza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama kama Waziri, kama Kiongozi wa Serikali akazuia wakulima wasipeleke mazao yao nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni haki yenu na ni wajibu wenu kama Serikali kuhakikisha taifa lisipate njaa, lakini kama unaweza kupata nguvu ya kuzungumza kuzuia kwa nini usipate hiyo nguvu ya kuhakikisha Watanzania wanapata soko la uhakika la kuuza mazao yao? Kama hatujui pembejeo zao, yaani mpaka Mheshimiwa Rais anaweza kuzungumza kwamba sasa mnataka mbolea ziende wakati Waziri wa Kilimo yupo, tafsiri yake ni nini? Waheshimiwa Mawaziri wote mmeshindwa mpaka yeye aseme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa tumeenda kuwahamasisha, Mheshimiwa Rais amezungumza watu wafanye kazi, tumeenda kuwahamasisha wafanye kazi, wamekwenda kuchukua mikopo benki, wamezalisha kilimo cha kisasa, wakazalisha kwa wingi. Matokeo yake hivi ninavyozungumza kuna wakulima wameuziwa nyumba zao, kuna wakulima wanadaiwa na benki kwa sababu ya uzembe wa Serikali. Kwa sababu ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wakulima wake wanapata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mtanzania wa kawaida amekwenda kuathirika kwa uzembe ambao umetokana na Serikali yenyewe. Kwa nini msiwasimamie wale mnaowalipa mishahara, mnawasimamia hawa ambao hatujui wamepataje pembejeo, hatujui wamefanyaje kuweza kupata hicho chakula? Hata viwanda tunavyoviimba ni viwanda ambavyo vitabaki kwenye historia tu kwenye maandishi, huwezi kuzungumzia viwanda wakati umeshindwa kuimarisha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda ni lazima leo kama Serikali mjiwekeze, mhakikishe kabisa kwamba kipaumbele cha sasa ni kilimo, hivyo tutabadilisha wakulima wetu kwenda kuweka kilimo cha umwagiliaji, waachane na kilimo cha mazoea. Leo unasema asilimia kumi ndiyo mliyopeleka, huu ni utani, utani sana tu. Na tunapozungumza tukizungumzia Serikali tunazungumzia Chama cha Mapinduzi, ndicho chenye Serikali na Wabunge wanaposimama kuzungumza lazima wajue chama chao ambacho kinaongoza Serikali kimesababisha maumivu makali kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uvuvi, yaani leo ikitokea kipindupindu kimetokea kwenye Mkoa wangu wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, wakulima pamoja na wavuvi wameenda kuchomewa nyavu zao pamoja na makazi, yaani leo hakuna njia ya kudhibiti kipindupindu mnawachomea watu makazi yao. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imewafikisha Watanzania mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani alikwambia kudhibiti kipindupindu ni kuchoma makazi? Yaani leo mmekosa kabisa njia mbadala ya kuzuia kipindupindu mnawaondoa watu wakawe maskini? Haya mambo ikifikia mahali kuna watu hawawezi kusema, sisi tuliotumwa leo kama wawakilishi wao kusema tukisema msiposikia kuna wakati mwingine watasema kwa milango ambayo hamtajua wanasemea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye utawala bora na unapozungumzia utawala bora lazima uzungumzie utawala wa sheria. Leo unapozungumzia Mbunge wa chama cha upinzani ni kama unazungumza mtu ambaye ni adaui wa Taifa. Msajili wa Vyama vya Siasa kazi yake ni kulea vyama vya siasa, leo amekuwa muuaji wa vyama vya siasa. Katiba mpya imeelekeza maandamano ni haki ya Kikatiba, yeye anapaswa kuwaambia kwamba mnataka kuandamana kwa sababu gani, ameona kuna mvurugano wa vyama asimame katikati kuhakikisha vyama vinakwenda salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo CHADEMA wanaandamana, anasema ni kwa nini nisiwafutie usajili, na anajua Katiba inaelekeza kwamba maandamano ni haki ya msingi. Mbona wale wanaoandamana kumsifia Rais hawaambiwi waondoke nchini? Ila wewe ukiandamana kwa kutaka kumkosoa Mheshimiwa Rais wewe ni adui wa Taifa hili. Utawala bora bado kwa Tanzania ni jambo ambalo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naunga mkono taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo na taarifa zote zilizowasilishwa. Siko mbali sana na wajumbe waliotangulia, kwanza nampongeza Mheshimiwa Goodluck kwa mara ya kwanza ameonesha ukomavu wa kisiasa kwamba msimamo wake unabaki pale pale. Kila mhimili unapaswa kuheshimiwa na lazima tulisimamie hilo, hatuwezi kukubali. Kuna kitu kimenishangaza sana, Maazimio ya juzi tu hapa lakini naona kuna watu wameanza kugeuka, Bunge hili hili, juzi tu hapa, kuna nini kimetokea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tutaendelea kusema ukimtuhumu mtu ambaye ana watu wengine nyuma hujamtuhumu yeye, tunachokizungumzia sisi ni kwamba sheria zifuatwe. Kuna watu wanaohusika na hayo mambo wafuate utaratibu, sheria ziko wazi. Makonda hawezi kumwita mtu yeyote angeagiza Jeshi la Polisi lifuate utaratibu kuwaita hao watu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika mazingira ya kawaida kama kuna Mbunge ametuhumiwa, sisi tulivyoambiwa tunalala msifikiri ni mtu mmoja alisikia, ni wananchi ambao wako nyuma yetu wamejua kwamba sisi tunalala usingizi. Sasa kama tunakubaliana na Makonda kwamba kweli tunalala usingizi, kiukweli mimi binafsi kama Aida, sisi Wafipa tuna misimamo yetu, mimi siwezi kukubaliana hata siku moja. Kama kuna mtu anajua amefanya vizuri kwa kusubiri uteuzi, sisi wengine hatusubiri uwaziri hata siku moja hatusubiri, tutasimamia ukweli. Kama kuna watu wanafanya hayo mambo hakuna mtu anafurahishwa ila afuate utaratibu mambo mengine yaendelee. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye taarifa ya Kamati, niongelee kuhusu Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Ndugu zangu Wabunge pale ndipo sheria zinachapwa, mtu yeyote ambaye unahusika na mambo haya ukienda kuona pale na ukaacha unafiki, ukatimiza wajibu wako kama Mbunge utaelewa hiki ninachokizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Jenista Mhagama kama kweli kuna utumbuaji kitu gani kinazuia kumtumbua yule mtu pale kwa sababu mambo yako wazi kabisa inakuwaje siri za Serikali zinakwenda kutolewa nje, kuna kitu gani kinaendelea? Tunaishauri Serikali ifanye utaratibu unaowezekana, kama mmefanya haraka kuhamia Dodoma mpaka kwenda kwenye Chuo cha UDOM, fanyeni haraka kutafuta utaratibu wa kudhibiti mazingira ya pale, kwa sababu tu moja, kwa maslahi ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la wanasheria wetu, yawezekana shida ni taaluma waliyo nayo au hakuna utaratibu wa kuwaangalia hawa wanasheria wa Halmashauri jinsi wanavyowajibika. Kuna watu wamehukumiwa kwa sheria hizi za Halmashauri ambazo ziko kinyume kabisa na sheria mama. Tunaishauri Serikali kuna kila sababu ya kufanya semina kwa hawa wanasheria wa Halmashauri kama kweli tuna nia njema. Kwa sababu yawezekana wanafanya kwa kutojua au kwa makusudi kwa sababu wanajua mmewatelekeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia hata kesi nyingi za Halmashauri, nimewahi kukaa siku moja nikajiuliza kwa nini kesi nyingi za Halmashauri tukienda mahakamani tunashindwa? Kuna mambo mawili hapa, yawezekana wanasheria wenyewe wanapiga deal na hawa watu waliopeleka kesi mahakamani au Wakurugenzi wanapokuwa wanafanya shughuli zingine wanashindwa kuwashirikisha wanasheria. Haya mambo lazima tuyatazame kwa maslahi ya Taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawasiliano ya Simu. Kulingana na umuhimu wa mawasiliano kwa binadamu ili kuweza kutimiza malengo yao kwa wakati ni vema Serikali ikamaliza tatizo kwa kupeleka minara ya simu kwenye maeneo ambayo bado hayajapata mawasiliano. Kwa mfano Jimbo la Nkasi Kusini, Wilaya ya Nkasi iliyopo Mkoa wa Rukwa, Kata ya Kala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Meli ya MV Liemba. Meli hii imekuwa ya muda mrefu na imechoka, Serikali kwa nini isituletee meli mpya ili kuokoa maisha ya wananchi wa Ziwa Tanganyika? Suala la barabara inayotoka Sumbawanga – Kanazi limechukua muda mrefu na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotoka Namanyere, Kilando, Kabwe na maeneo mengine ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Kiwanja cha Ndege cha Manispaa ya Sumbawanga. Mpaka sasa wananchi wa Sumbawanga wanashindwa kuendelea na shughuli zao wakisubiri kulipwa baada ya tathmini. Nashauri Serikali baada ya tathmini, iwalipe wananchi hawa na kama kuna matatizo ya kifedha basi waruhusiwe kuendelea na shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Usalama katika Bandari; kuna kila sababu ya Serikali kufanya tathmini ya kutosha katika maeneo ya bandari, kwa sababu kumekuwa na changamoto na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wafanyakazi wa bandari. Suala la fedha kutofika kwa wakati, nalo linakera, ni tatizo kwenye maeneo mengi nchini na kupelekea usumbufu mkubwa kwa kutomaliza miradi mbalimbali ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Barabara Kujengwa Chini ya Kiwango; suala hili limekuwa endelevu katika mikoa yetu. Nashauri Serikali iwachukulie hatua wakandarasi wote wanaofanya kazi chini ya kiwango na kutoa taarifa kwenye maeneo mengine ili wawafahamu wakandarasi wazuri na wabaya ili wasirudie kuwapa kazi wakandarasi wasio na sifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia hotuba ya Waziri Mkuu kwenye mambo makuu matatu. Sehemu ya kwanza ni ajira kwa vijana, jambo ambalo imekuwa ni kilio kwa vijana wa Kitanzania. Kwa sasa kumaliza elimu ya chuo kikuu imekuwa ni kama laana kwenye nchi yetu. Mpaka nasimama kuchangia hapa message za vijana waliotuma kwamba hebu waambie watuambie hatma ya sisi tuliomaliza vyuo vikuu toka mwaka 2015 ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la ajira ukiangalia ajira inayotokea kwa mwaka hailingani na idadi ya wahitimu kwa mwaka kwenye nchi yetu. Nataka Serikali ije ituambie nini hatma ya vijana hawa wa toka mwaka 2015 mpaka leo? Kwa sababu kitu kingine ambacho kingewasaidia kujiajiri ni upande wa kilimo, suala la kilimo liko hoi bin taabani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la ajira kwa vijana sasa kumekuwa na suala la ubaguzi. Kwa sasa watu wanapotafuta ajira kuna maeneo imefikia wanaambiwa waoneshe Kadi yao ya Chama cha Mapinduzi. Naomba suala hili Serikali iliangalie kwa sababu ubaguzi huu hautaishia kwenye chama peke yake, athari za ubaguzi ni kubwa sana, zikianzia kwenye vyama zitakwenda kwenye makabila, zikitoka kwenye ukabila zitakwenda kwenye udini, ni vizuri Serikali ifuatilie jambo hili. Si kwamba limejificha kiasi kwamba hamuoni, kama mlikuwa hamjui mimi nawaambia kwamba kuna hili jambo kwenye suala la ajira sasa watu wanaambiwa wapeleke Kadi za Chama cha Mapinduzi jambo ambalo kwenye Katiba yetu ya nchi halipo. Sasa kama ni utekelezaji wa Ilani ya Chama ya Mapinduzi pia tujue kwamba ajira kwa sasa lazima uwe na kadi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nitaenda kulizungumzia ni suala la kilimo. Tunapozungumzia kilimo, ni lazima tuzungumzie masoko na pembejeo.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani ukae. Mheshimiwa Antony Mavunde, kanuni iliyovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 64(1)(a) ambayo inazuia Mbunge kutotoa taarifa ambazo hazina ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge anayezungumza, anatoa taarifa kwamba kuna ubaguzi mkubwa kwenye eneo la ajira na kwamba ni lazima mtu aoneshe kadi ya CCM ndiyo aweze kupata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili siyo kweli. Matangazo yote ya ajira, huwa yanatoa vinavyohitajika kwa maana mwombaji awasilishe nini. Kwa hiyo, kwa sababu taratibu zimewekwa vizuri kabisa katika kila ajira ambazo zinatangazwa na mwombaji anatakiwa awasilishe nyaraka ambazo zimesemwa; na katika nyaraka hizo haijawahi kuwemo kadi ya Chama cha Mapinduzi kama kigezo cha mtu kupata ajira; hivyo kwa mujibu wa kanuni; na kwa sababu mimi nimethibisha kwamba siyo kweli, tunamtaka mtoa taarifa aondoe maneno yake au lah, athibitishe mbele ya Bunge lako tukufu na kanuni za Bunge hili ziweze kuchukua hatua. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira na Vijana, akitumia kanuni ya 64(1)(a) inayozungumzia mambo yasiyoruhusiwa Bungeni, lakini amesoma kifungu kidogo cha
(1) kinachosema Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Sasa ukishazungumza kuhusu taarifa ambazo hazina ukweli zinakupeleka kwenye kanuni ya 63 inayohusu kutokusema uongo Bungeni.

Sasa ukiisoma kanuni ya 63, huwa inamtaka anayemwambia Mbunge mwingine kwa maana ya mchangiaji kwamba amesema uongo, yeye anatakiwa kusema maelezo yake yanayoonesha kwamba yule Mbunge aliyetangulia kusema kabla yeye hajasimama na kusema kuhusu utaratibu, alikuwa akisema uongo.

Kwa maelezo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri na amesema kuhusu matangazo yanayotolewa na vigezo vinavyowekwa na kwamba kigezo ambacho alikuwa anakitaja Mheshimiwa Mbunge aliyekuwa akichangia hakipo kwenye ajira kama ambavyo yeye amekisema. Sasa kwa masharti ya kanuni inayokataza kusema uongo Bungeni, Mheshimiwa Mbunge anapewa fursa ya kufuta usemi wake ama kuthibitisha.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa Kanuni zetu tulizojiwekea nitampa fursa Mheshimiwa Aida Khenani kufuta kauli inayosema ajira Serikalini inataka mtu awe na kadi ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni vizuri tukaacha hofu. Nimesema wakafuatilie, ndiyo jambo nililozungumza, Hansard ziko wazi. Kwa kuwa umeniongoza, nayafuta, ila mimi nimesema na ni wajibu wa Serikali kwenda kufuatilia jambo hilo. Mitandao iko wazi, mambo hayo yako wazi kabisa yanaonekana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khenani, ili Taarifa zetu Rasmi za Bunge zikae vizuri, kama unasema unafuta kama ulivyozungumza, huwezi tena kuendelea kutoa maelezo juu ya jambo hilo hilo ambalo unalifuta. Kwa hiyo, lifute ili taarifa zikae rasmi, halafu uendelee na mchango wako.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuta maelezo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazidi kusema, kama kuna nchi wanalia njaa kwenye Taifa lao, vijana wa Tanzania wanalia na ajira kwenye Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kwenye suala la kilimo ambalo tunaamini vijana wengi walikimbilia huko kujikita, lakini nako hali ni mbaya kupita kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la kilimo nitazungumzia masoko. Suala la masoko ya mazao mchanganyiko na mazao yote nchini, imekuwa ni shida kubwa sana kwa wakulima na sasa wanajiona ni kama hawana uhalali wa kuendelea na kilimo, hasa wakulima wa zao la mahindi wa Mkoa wangu wa Rukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumza mwaka 2018 kwamba kabla ya tamko la Mheshimiwa Waziri Mkuu ndani ya Bunge kukataza wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi hali ya mazao yao na bei halisi ilikuwa ni shilingi 75,00/=. Baada ya tamko lile, baadaye akaja kuruhusu wakati huo tayari nchi ambazo zilikuwa zina uhitaji, hazihitaji tena, inakuwa ni hasara kwa mkulima. Ni vyema Serikali kabla ya matamko yake ikafanya kwanza tafiti kuliko kuwapa adhabu wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo bado ni shida kwa wakulima wetu. Serikali ya Awamu ya Tano, slogan yake ni Serikali ya viwanda. Kwa nini sasa wasiweke kipaumbele cha kujenga viwanda zizalishwe pembejeo hapa ili kupunguza hali ngumu ya bei kwa wakulima wanaopata shida? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu watakapokuja watuambie, wana mkakati gani wa kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza pembejeo nchini ili kupunguza bei kubwa ya pembejeo ambayo inaenda kuwaumiza wakulima wetu? Bei kubwa ya pembejeo haiendani na hali ya bei ya mazao ambayo wanazalisha. Kwa hiyo, ni vyema, wakipunguza bei ya pembejeo itawasaidia hata uzalishaji wa kulima ambapo kilimo chetu sasa kitakuwa ni chenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahindi kwetu ni siasa, mahindi ni maisha na mahindi ni biashara. Hapa nataka kuzungumzia jambo moja, kwenye korosho fedha zimetoka kwenye Benki ya Kilimo. Sasa mimi sijui kama ile benki imebadilika imekuwa ni Benki ya Korosho. Kama ni mazao mchanganyiko, haya mazao mengine utaratibu ukoje? Ningependa kujua, Serikali ina mkakati gani na mazao mengine? Je, huu utaratibu utakuwa ni wa kila mwaka wa kuchukua pesa kwenye Benki ya Kilimo kwenda kununua mazao ambayo yatakosa soko?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiambie Serikali tu kwamba baba akinunua chakula nyumbani hapongezwi kwa sababu ni wajibu wake. Kwa hiyo, tunategemea Serikali ni wajibu wenu kuhakikisha mnawatengenezea soko wakulima wanchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuzungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mpaka leo mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa. Jana limejibiwa hapa kwamba Wenyeviti wa Serikali wanalipwa shilingi 20,000 kama posho. Kabla sijamaliza muda wangu wa miaka mitano, nimezungumza hili jambo mara tatu ndani ya Bunge. Hili jambo inategemeana na makusanyo ya Halmashauri, kwa nini Serikali isilete heria hapa ambayo itakuwa uniform kwamba hawa Wenyeviti watalipwa posho kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri sasa hali ni mbaya na huwezi kufananisha Mwenyekiti wa Sumbawanga Mjini ukamfananisha na Mwenyekiti wa Kinondoni kwa sababu zile Halmashauri za Mjini zitakusanya tofauti na Halmashauri za Vijijini. Sasa kama Serikali ina uwezo wa kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi, kwa nini wasitenge fedha kwa ajili ya kuwalipa posho Wenyeviti wa Serikali? Kama jambo hili halijaandaliwa, ni vizuri kwa ushauri tu, kabla hawajajipanga na uchaguzi, wajipange kwanza ni namna gani wataanza kuwalipa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa? Hili jambo…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla uchaguzi wa Serikali za Mitaa haujafanyika, wananchi wenye sifa wanajipanga kwa nafasi ambazo wanahitaji; ama kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au wa Kijiji, au wa Kitongoji au Mjumbe wa Serikali ya Kijiji au Serikali ya Mtaa. Utaratibu ni kwamba kazi za Uenyeviti wa Mitaa ni kazi za kujitolea na ni lazima awe na kipato ambacho kinamwingizia maisha yake halali ili aweze kufanya kazi bila kumdhulumu mwananchi na bila kuiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mazingira hayo, hata kabla posho haijapangwa, anakuwa anapanga na anakwambia kwa sababu zipi na ataishije?

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya pili ni kwamba…

NAIBU SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa. Mheshimiwa Aida Khenani, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza najua wana muda wa kujibu, sijui ana pressure ya nini; lakini pia alikuwa Mwenyekiti mwenzangu, anajua kwa nini hiyo nafasi ameikosa kwa wakati huu. Kwa hiyo, aniache Mwenyekiti nizungumze kwa sababu nawajua Wenyeviti wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la ukusanyaji wa mapato linategemea na uwezo wa Watendaji kwa maana ya Wakurugenzi, anaweza kubuni vipi vyanzo vya mapato? Kwa hiyo, hii hali itaweka utofauti mkubwa sana wa Wenyeviti juu ya posho zao. Kama Serikali inaweza kumwamini Mwenyekiti akaandika barua ya kumdhamini mtu, inakuwaje ashindwe kutambua kwamba ana mchango gani ndani ya nchi hii? Ni kiongozi pekee wa Serikali wa Mtaa ambaye hana usiku, hana mchana, hana jua, hana mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaambia tu Serikali, kama bado hawajatambua mchango wa Wenyeviti, ni bora wafute suala hili la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wabaki wabaki Madiwani tu ambao wanapata posho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima kuweza kupata tena nafasi hii kuzungumza ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote waliosema kuna umuhimu wa kuwa na agenda za kitaifa. Kuna maana kubwa ya kuwa na agenda za kitaifa. Tunatambua kuanzia Awamu ya Kwanza mpaka sasa tuko Awamu ya Sita, kuna mambo ambayo yaliibuliwa na awamu zote, lakini unaona umaliziaji unakuwaje. Tunapokuwa na agenda za kitaifa kila anayekuja, hatujui kesho atakuja Rais wa namna gani, atatokea chama gani, kukiwa na agenda za kitaifa zinam-guide kwamba Taifa tunakwenda hivi. Kwa hiyo, ni vizuri jambo hilo likaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taifa letu limebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, ukiangalia ndani ya Bunge, tika nimeingia Bunge lililopita, tukianza kuzungumza suala la maji kila Mbunge anasimama anazungumza uchungu ulivyo.

Mheshimiwa Spika, nchi hii tuna mito ya kutosha, tuna maziwa ya kutosha, tuna bahari za kutosha, nini kimekosekana kwenye nchi yetu? Je, wataalam wetu hawatushauri vyema? Au tumetanguliza siasa zaidi hata mambo ambayo yanahitaji utaalam? Ni vizuri tukajipima tuangalie shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisimama wiki iliyopita kuuliza Habari ya maji; Ziwa Tanganyika na kina chake, lakini kutoka Kilando kuja Namanyere ni kilometa 64 tunazungumza habari ya maji miaka nenda rudi, shida ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tumeanza kufikiria maji kutoa Ziwa Viktoria tumefikisha Tabora tufikiri mikoa hii mitatu, tufikir Katavi, tufikiri Rukwa, tufikirie Songwe hawa wote wanaweza kufaidika na maji kutoka Ziwa Tanganyika badala ya kutimia fedha kidogokidogo kwenda kuanzisha miradi ambayo haiwezi kutatua changamoto ya maji. Ni bora tukafikiria kitu ambacho tunaamini tunakwenda kumaliza changamoto ya maji na suluhisho ni kutumia maji kutoka Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Ziwa hilo Tanganyika ukiachana na kufaidika na maji tuna uvuvi pale. Slogan ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa ni Serikali ya Viwanda, tujiulize tuna viwanda vingapi leo kwa ajili ya uvuvi kutoka kwenye maziwa yetu kama kweli tunachokisema ndio tunachokimaanisha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba, Serikali imekuwa inakuja na slogans mbalimbali, lakini siamini kama slogans hizo zinakuwa zimeshirikisha kikamilifu wataalamu wetu na kama zinaweza kutekelezeka. Leo kama tunaweza kusimamia kwenye kilimo lazima tujue kabla hatujafikiri viwanda tunazungumzia raw material. Mashamba yapo, maeneo yapo, shida ni nini kwenye Serikali yetu ya Tanzani? Ni vizuri kuwashirikisha kikamilifu wataalamu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kumekuwa na ilani mbalimbali, kuandaa ilani ni jambo moja na kutekelea ilani ni jambo jingine. Tukianza kuzungumzia utekelezaji tunakuja kwenye mpango huu ambao tunausema. Na mpango lazima uendane sambamba na hiyo ilani ambayo mnakuwa mmeipanga ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ziwa Tanganyika pamoja na kwamba, hatujalitumia vizuri hilo eneo la Ziwa Tanganyika, tuna-share zaidi ya nchi moja; tuna nchi ya Tanzania ambayo sisi tunamiliki kwa ukubwa zaidi, lakini kuna Kongo, kuna Zambia. Leo unapokuja na utaratibu wa kanuni juu ya wavuvi kutumia nyavu gani ni vizuri kabla ya kuja na hayo maamuzi mjiulize hizo nchi nyingine wanatumia nyavu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Samaki hawajui kwamba, mpaka huu leo tuko Tanzania, kesho tuko Kongo. Inawezekana tunakuwa na sheria na kanuni ambazo zuinatuadhibu sisi wenyewe tunashindwa kutumia rasilimali tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo leo wakati tunafikiria viwanda tumewawezeshaje wavuvi wetu ambao wanaweza kutumia hizo teknolojia na kuwawezesha, sio kuwapa tu hizo kanuni na sheria kwasababu, lazima Serikali tujue tuna wajibu kwa wananchi wetu. Pamoja na kwamba, tunawaambia waende kutumia nyavu za milimita nane na hatujui zile nchi nyingine ambazo tuna-share kwenye ziwa moja hilohilo Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tujiulize ni kwa nini wakati tunafikiri viwanda na kipaumbele chetu ni kuwaambia wananchi au wavuvi wetu watumie milimita nane tumejiwekeza kiasi gani sisi wenyewe kutengeneza hizo nyavu ambazo tunafikiri ni halali, ili tuweze kuwawezesha wavuvi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inafikia mahali sio kila mvuvi ni mtaalamu, akienda dukani akauliza kwamba, hii ndio milimita nane, anapewa kwamba ndio yenyewe. Akifika kule, kwa bahati mbaya zaidi, Serikali badala ya kukamata kiwanda ambacho kinazalisha wanakwenda kwa mlaji wa chini kabisa ambaye hajui, yeye ameambiwa ni milimita nane anakwenda kutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na miongoni mwa kanuni ambazo ni vizuri tukaziangalia kama lengo ni kuwasaidia wavuvi wetu na Watanzania, sisi hapa tunazungumzia milimita nane kwamba, ndio wakatumie kuvua Samaki, wavuvi hawa wanatumia hizo milimita nane. Wakifika kule wakiwa wanavua samaki, wametega wale samaki, ile nyavu haizuii chini ya ile sentimita ambayo wanaitaka wao Serikali, unakuta Samaki wale wengine wamefuata. Kwa bahati mbaya zaidi watendaji walipo huko chini anapofika kwa mvuvi huyu badala ya kuangalia kwamba, ile nyavu ndio iliyosababisha sio mvuvi. Kwamba, ni kweli ni milimita nane, lakini Samaki waliongia pale labda wawili au watano, mvuvi anapigwa fine milioni mbili, milioni tano, milioni kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yawezekana lengo la Serikali ni kweli ni kukomesha uvuvi haramu, lakini ni vizuri tukajua chanzo, ili tuje na suluhisho kama Taifa badala ya kuja na hizi operations ambazo hazieleweki, matokeo yake watendaji wamekuwa wamekuwa mahakama, wamekuwa ndio askari. Sasa kama tunataka hapa tunafikiri kwamba, namna gani sekta ya uvuvi imesaidia Taifa kwa pato, lakini tufikiri pia tunapotaka kupata pato kubwa tumeandaaje juu ya kesho? Hawa wavuvi tumewajengeaje mazingira rafiki, ili kesho tuendelee tena kupata fedha zaidi kwa ajili ya kukuza uchumi wa Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitarudi kwenye jambo ambalo ni la muhimu zaidi. Kwenye ileile ya kwanza kwamba, agenda za kitaifa. Kumekuwa na wimbo usioisha Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, ni jambo jema Liganga na mchuhcuma, lakini limekuwa linazungumzwa halina majibu. Ni vizuri leo Mheshimiwa Waziri uje utuambie nini kimejificha kwenye hili jambo ili tuweze kujua tunachokizungumza. Kwasababu, kama jambo ni jema nini kinazuwia hili jambo lisitekelezeke? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika tuliambiwa tunaenda kwenye uchumi wa gesi. Gesi ya Mtwara imeishia wapi? Mje mtupatie majibu hapa nini kinaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunaangalia zawadi nyingine ambayo Mungu ametupa Mkoa wa Rukwa, helium gas, tunajua kwamba Serikali imefanya hatua mbalimbali, lakini tunataka kujua ukitazama kiuhalisia bado hatuko serious na uchimbaji wa gesi hii kuanzia miundombinu, kuanzia elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo lile, tunataka tena mambo ya Mtwara yaje yajitokeze na Mkoa wa Rukwa. Ni vizuri tujipange vizuri na lengo ni jema, lile suala sio la Mkoa wa Rukwa ni suala la kitaifa. Makosa yaliyojitokeza iwe ni fundisho tunapoandaa jambo jingine kutokea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia, tumekuwa na utaratibu ambao tunatamani kumuokoa mtoto wa kike. Kumekuwa na mkanganyiko kidogo wa sheria zetu, sheria ya ndoa na sheria ya mtoto. Kwenye Mpango wa Miaka Mitano tunatamani akina Mheshimiwa mama Samia wengine, wajengewe mazingira rafiki ili tupate Marais wazuri wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kila sababu leo, natambua kwamba, sheria zipo, lakini kuna mianya ambayo bado watu hawa wanatumia kuwaumiza watoto wa kike. Ni vizuri tukalinda ndoto za watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeangalia kuna namna ambavyo Mkoa wa Shinyanga wameanza, pamoja na kwamba ndio walikuwa wanaongoza wakiwa na asilimia 59 kwa takwimu ambazo zimetokea 2006 nafikiri.

Mheshimiwa Spika, wale watu wamekuja na mikakati mbalimbali ambayo ni mizuri kuiga kama Taifa. Cha kwanza wamekuja na utaratibu wa kujenga shule ya girls, kwa maana ya kwamba wameamini mazingira pia yalichangia watoto wa kike kupata mimba za utotoni na ndoa za utotoni. Jambo hilo si baya kama likawa ni mpango wa kitaifa, kwamba kila Halmashauri angalau ikawa na shule moja ya girls ili tuone namna gani tunaweza tukalinda vipaji vya watoto wetu wa kike.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la kubadilisha vipengele hivyo ambavyo vimekuwa ndio uchochoro, yaani mtu amebaka, anafika pale mtoto wa kike anaulizwa anasema ni kweli, wazazi walikubaliana lakini mimi nilikuwa nataka kusoma. Akija kwenye sheria hiyo ya ndoa wanamuuliza mlalamikaji kwamba wewe kuna taasisi ambazo zimejitolea kwa ajili ya kutetea haki za watoto wa kike, anapofika pale anaambiwa ulipoenda huko mpaka unataka kufunga ndoa ulikuta kwamba wameandaa sherehe kwa maana ya vyakula na nini anakubali kwamba ni kweli. Wanamwambia soma sheria ya ndoa ina maana kulikuwa makubaliano ya wazazi na ndiyo maana hatua hiyo ikafikia hapo.

Mheshimiwa Spika, bado bado narudi, pamoja na kwamba sheria tulitunga ndani ya Bunge kama lengo ni kumlinda mtoto wa kike, tufanye marekebisho ya sheria hizo ambazo bado zina mwanya ambao watoto wetu wa kike wanaendelea kuangamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazingira hayo hayo, namalizia kusema; kama kilimo tuna uwezo wa kulima Tanzania, kama uvuvi tuna uwezo wa kuvua zaidi kuliko maeneo mengine, tayari Serikali imewekeza kwenye Bandari mbalimbali ikiwemo Bandari ya Kagwe, tutumie Ziwa Tanganyika, kwasababu Mpango wa Serikali Awamu ya Tano ilikuwa ni kufua Meli ya MV Liemba; ile itasaidia kusafirisha minofu, kusafirisha mazao mbalimbali badala ya kupiga kelele habari ya soko. Leo Zambia wameanza kuchukua eneo la Kongo na sisi tupo jirani tunashindwa kutumia hiyo nafasi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima kuweza kusimama tena ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, nitachangia mambo machache kulingana na umuhimu wenyewe wa Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini mambo mengine ninaweza kushauri kwenye Wizara nyingine za kisekta..

Mheshimiwa Spika, nitaanza na suala la ajira, sote tunajua kwamba, suala la ajira bado ni changamoto kubwa sana kwenye Taifa letu. Tukitazama wahitimu wa kada mbalimbali kwa mwaka na idadi ya ajira zinazotolewa ni vitu viwili tofauti, lakini pamoja na kwamba, Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali namna ya kuwasaidia vijana, imekuja na Habari ya Mfuko wa Vijana bado haijaweza kumaliza changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na mfuko uliopo ambao uko chini ya TAMISEMI ambao unazungumzia asilimia 4 kwa vijana, asilimia 4 kwa wanawake na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu ni vizuri suala hilo likaangaliwa upya. Najua kuanza hatua moja inatufanya turudi na turekebishe makosa yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza changamoto inaanzia kwenye asilimia mbili ya watu wenye ulemavu. Watu wenye ulemavu wako wa aina tofauti na hapa kumekuwa na shida sana kwenye hili jambo. Kwa kuwa, Wizara hii pamoja na kwamba, tulipitisha hiyo asilimia 2 ni vizuri tukaangalia sera yetu kwasababu, lengo ni kuwasaidia watu wenye ulemavu na lengo ni kuwasaidia vijana pamoja na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na ushauri kidogo, leo tuna VETA na tuna vyuo vya ufundi, wale watu wakishamaliza pale wamepewa knowledge shida yao inakuwa ni suala la capital. Na kwasababu, kumekuwa na changamoto kwa vijana wengi ambao wanamaliza vyuo hawana uwezo wowote wa kwenda kufanya biashara wa kwenda kufanya jambo lolote kwa hiyo, inakuwa ni changamoto kurudisha ile fedha ambayo wamekopa. Ni kweli wanajikusanya huko wanaona namna gani ambayo wanaweza wakajisaidia ili wakakope, wanakopeshwa. Kurudisha fedha ile inakuwa ni ngumu, lakini hali tukiangalia halmashauri zetu ni mbaya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni nini kwenye jambo hili; wale watu wanaokuwa wamemaliza vyuo vya ufundi au waliotoka VETA tayari wamepewa ujuzi na ninazungumza leo ni kwa mara ya tatu ndani ya Bunge. Wale watu wakipewa mkopo na tutoke kwenye asilimia 4 tufikiri zaidi ikiwezekana vijana peke yake wapewe asilimia 10. Lengo ni kwamba, kwasababu, wameshapewa ujuzi wakienda kule kwasababu wana uwezo wa kujiajiri wao wenyewe wanaajiri vijana wengine kupitia kazi ambazo wamezifanya. Kutakuwa na tija na lengo ambalo tulikuwa tunafikiri kuwa-empower vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hata wanawake. Wanawake sasa wamejitoa wameamua kuingia kwenye ujasiriamali na shughuli mbalimbali, tukizungumzia asilimia 4 ni wanawake wangapi ambao wanapewa huo mkopo?

Mheshimiwa Spika, na kwa bahati mbaya hata hiyo asilimia 4 kuna halmashauri zinashindwa kuwapa wanawake kwa sababu ya hali iliyopo kwenye halmashauri zetu. Kwa hiyo, ni vizuri ikiwezekana itoke TAMISEMI tukaona namna bora ambavyo tunaweza ku-control jambo hili, ili tuweze kuwasaidia wanawake ambao tuliwalenga pamoja na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuja kidogo kwenye kilimo kwasababu, nitakuja kluchangia kwenye Wizara ya Kilimo. Tunapozungumzia uwekezaji, tunapozungumzia viwanda, tunapozungumzia uchumi wa kati huwezi kuacha sekta ya kilimo Tanzania kuizungumzia ili kufikia uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia palepale ambapo nazungumza kila siku, ili kuboresha kilimo chetu na kiwe kilimo chenye tija lazima tuwekeze kwenye utafiti. Nategemea leo tunapozungumzia kilimo cha Tanzania cha kwanza tuangalie vyuo vyetu vya utafiti viko vingapi, lakini tunapeleka fedha kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hata tukija na njia mbadala kwamba, tunahitaji mazao ambayo yatakuwa labda mbadala wa mahindi, kwa mfano Nyanda za Juu Kusini. Kabla ya kufanya hivyo mmefanya utafiti kiasi gani wa udongo? Mmefanya utafiti kiasi gani juu ya mbegu ambazo zinapelekwa kwa ajili ya kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mbadala wa mahindi kwa mfano nyanda za Juu Kusini kabla ya kufanya hivyo mmefanya utafiti kiasi gani wa udogo, mmefanya utafiti kiasi gani juu ya mbegu ambazo zinapelekwa kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba mwaka uliopita ni asilimia 20 tu ya mbegu bora ambazo zilipelekwa kwa wakulima wetu. Ukipeleka mbegu ambazo si bora kwa hali ya kawaida unategemea mazao yake yatakuwaje? Kama tutawekeza kwenye utafiti lazima pia tutatafiti ni zao gani ambazo linaweza likasaidia Taifa, ni zao gani ambalo linaweza kupandwa kulingana na aina ya udongo ambayo tumepata majibu kutoka kwa watafiti.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaendelea cha mazoea sana, ukiangalia kwenye shina moja labda nitolee mfano zao la mahindi, wanachukua kile kifuniko cha maji au kisoda wanapimia mbolea wanaweka pale, nani alifanya utafiti kwamba lile tundu linafaa kwa kile kizibo kimoja kuweka mbole? Lakini wananchi wengi wanatumia ni kwasababu ukiangalia hata Maafisa wa ugani wetu ni wangapi wanafika kule kwa wakulima wetu kuwapa elimu na kwamba wamefanya utafiti ni kiasi gani kinafaa kutumika kwenye shina moja la mahindi.

Mheshimiwa Spika, bado ninarudi Ofisi ya Waziri Mkuu. Pamoja na kwamba Wizara zote zinaweza kuzungumzia kulingana na sekta zao ni vizuri kuangalia uchumi wa kati wa Taifa hili tunaenda kuangalia kwenye vitu gani? Leo tunazungumzia uchumi wa kati ukienda kwa Mtanzania mmoja mmoja wa chini kabisa kwa mfano kule Nkasi ukimwambia tupo kwenye uchumi wa kati atakushangaa uchumi wa kati upo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunataka hii hali Mheshimiwa Waziri Mkuu hizi takwimu ambazo tunasoma kwenye vitabu zikaonekane kwa wananchi moja kwa moja kwenye uhalisia wa maisha yao ya kila siku na hapa tutakuwa tunazungumzia lugha moja. Ni kweli kwamba yawezekana wataalam wetu wanatuambia hivyo, lakini nataka uhalisia.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida hata mimi Aida ukiniambia kwamba uchumi wa kati, bado najiuliza uchumi wa kati ninaangalia nini? Vigezo gani ambavyo naviona kwangu kwamba kweli tumefikia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nataka kwenda kuzungumzia habari ya Tume Huru nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na kwamba nimezungumza mara kadhaa…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Getere

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Ahsante naomba nimpe taarifa Mbunge ya Nkasi, anasema uchumi wa kati umekujaje aende akaangalie vigezo vya IMF na World Bank, kwamba uchumi wa kati unapatikana kwa capital income per capital income na GDP; kwa hiyo angalia tu hivyo vigezo mama utajua kwamba vinaendaje Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Aida.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. Sisi hatujazoea kukaririshwa tumezoea kuona na kuyaishi maisha yenyewe ya uchumi wa kati; kwa hiyo hatuwezi kuelewana lugha zipo tofauti kidogo.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kumkumbusha Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba tumekuwa na ahadi ya muda mrefu kuhusu suala la MV Liemba kwenye ziwa Tanganyika. Ni vizuri wakati unahitimisha; kumekuwa na kelele nyingi kwamba yawezekana wale watu wamejitoa, sijui mkataba umefanya nini, ni vizuri mkaja hapa mkatueleza hatua ya MV Liemba imefikia wapi na nini kinaendelea ili na sisi tupate kujua watu tunaotokea kwenye Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, kwasababu ya muda naomba nizungumzie Tume Huru ya Uchaguzi, Fungu la 61. Miongoni mwa Wabunge wa CHADEMA waliotangazwa ni mimi hapa kupitia Tume hii iliyopo sasa hivi, natambua hilo. Lakini pamoja na kutambua kwamba nilitangazwa si kwamba nilikuwa Mgombea bora kuliko wagombea wengine wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lakini ni miongoni mwa wale wachache, au mimi niliyepenya kwenye tundu la sindano. Naomba nizungumze mambo machache kwa ajili ya Taifa letu, kwa nia njema kabisa,. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia Tume Huru ya Uchaguzi tulianza na mchakato wa kutaka Katiba mpya ambayo ilikuwa ni maoni yetu. Natambua kwamba yalitokea yaliyotokea, lakini pamoja na hayo mlifikia hatua kubwa sana ya Katiba mpya. Ndiyo maana leo tunasema kwakuwa kelele ni nyingi na tunahitaji umoja wa Taifa letu tuangalie vipengele ambavyo bado vinashida, hasa kwenye eneo la Tume Huru ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Tume Huru ya Uchaguzi tukisema tuongeze idadi ya watu kuna gharama ya fedha, lakini kama lengo ni kuponya taifa ni vizuri tukazungumza.

Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya Wakurugenzi ambao sheria imekataza kabisa kwamba Msimamizi wa Uchaguzi hatakiwi kuwa kiongozi wa Chama cha Siasa, lakini sote tunajua wapo Wakurugenzi ambao walikuwa viongozi wa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Spika, lakini hata ningekuwa mimi leo nimepewa ukurugenzi kila mtu alikuwa anajua Aida ni kada wa CHADEMA katika wagombea wa Chama cha Mapinduzi lazima nitalinda maslahi ya chama changu, na lengo ni jema tu. Naomba nitolee mfano mdogo tu wa kama yangu alikuwa Mkurugenzi hapa Dodoma, alikuwa mkurugenzi Dodoma amekwenda Jimbo la Mlimba Mheshimiwa Kunambi…

SPIKA: Unamchokoza. (Makofi)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, aaah! nimesema ni mfano, na nia ni njema tu alikuwa Makao Makuu pale kila mtu anajua.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa hali ya kawaida yaani ukiangalia suala hili ambalo nataka kuzungumza Mheshimiwa Waziri Mkuu kuanzia mchakato wa awali habari ya watu kunyang’anywa fomu, habari ya watu fomu zao zina matatizo. Msimamizi wa Uchaguzi hakai pale kwa ajili ya kuvizia nani amekosea kwenye fomu yake anatakiwa awepo pale kumwelekeza mgombea kwamba hapa unatakiwa kufanya hivi, ufanye hivi Uchaguzi wa mwaka 2020…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa, iko wapi taarifa, Nimekuona Mheshimiwa Kunambi.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, Hakuna mashaka na Tume yetu ya Uchaguzi. Na labda nimueleze tu kama Tume yetu ya Uchaguzi isingekuwa Tume ya kutenda haki yeye asingekuwepo hapa. Nimpe tu taarifa kwamba Tume yetu ya Uchaguzi inazingatia misingi ya demokrasia. Naomba kuwasilisha. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana, Aida muda wako umekwisha, dakika moja tu ili uweze kupokea taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Kunambi anatakiwa kujua kwamba mimi sikupita bila kupingwa hilo la kwanza ajue…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. AIDA J, KHENANI: ….lakini la pili…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: … nataka nitoe ushauri kwenye jambo hili…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa nipo huku…

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma taarifa.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi nazidi kumweleza mchangiaji kwamba, ni kweli hatuna mashaka na Tume ya Uchaguzi na imetenda haki na mfano mzuri huko Kilimanjaro Mheshimiwa Anna Mghwira ni ACT, lakini tumewapiga, kwa hiyo naomba waondoe mashaka na Tume yetu. (Makofi)

SPIKA: Pokea taarifa.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Hajajibu hamuwezi kumpa taarifa juu ya taarifa

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Ayayayaaa!

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimwambie kaka yangu Musukuma kwamba Mheshimiwa Anna Mghwira sio ACT ni CCM lakini, tafakari ninayoiacha ninapohitimisha kila Mbunge aliyekuwa humu ndani anajua alishinda, kama alishinda alishinda kwa namna gani, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Tatizo lenu, nikusaidieni, mimi huwa ninakaa nawasikiliza habari ya tume huru lakini hata siku moja hajawahi kusimama mtu akasema hiyo tume huru mnayosema nyinyi inafananaje? Mnasema neno Tume huru tume huru kwani iliyoko hapa sio huru…

MHE. AIDA J. KHENANI: (Alizungumza bila kutumia kipaza sauti)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimepata hii nafasi kuweza kuchangia wizara hii muhimu na ninaomba niendelee alipoishia mchangiaji kwamba, pamoja na kwamba tunatambua kwamba wafugaji nao wanahaki na tunatambua kwa kwenda kuchukua ushuru kutoka kwao, lakini bado wafugaji hawajatendewa haki kama inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi zote zipo kwenye Serikali, leo ukiangalia namna wanavyotendewa wafugaji wa nchi hii, wakati tayari wizara inawajibu hamuwezi kuwa na haki ya kuchukua ushuru halafu mnashindwa kutimiza wajibu wenu kwa wafugaji, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo jambo kwamba, pamoja na hizo wizara mbili ambazo nimezungumza, lakini bado kuna wafugaji ambao ng’ombe zao zilikamatwa bila utaratibu wakaenda mahakamani na mahakama ikaamua kwamba hao wafugaji warudishiwe ng’ombe zao, mpaka leo hawajapewa ng’ombe zao. Ni wajibu wenu wizara kwa sababu mnachukua ushuru na tozo mbalimbali kuhakikisha wafugaji wa nchi hii ambao mahakama imeshaamua wanapewa haki zao za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba wanatakiwa kurudishiwa mifugo bado mnawajibu kama wizara kuhakikisha kwamba hawa watu, minada pale panapostahili, nitazungumzia eneo moja tu, wafugaji wangu ambao wapo ziwani, Ziwa Tanganyika ili wafikishe mifugo yao mnadani lazima wapite kwenye hifadhi na wakipita kwenye msitu ule wanakamatwa sasa ni wajibu wa nani, lazima muwapelekee huduma jirani na kule waliko kwa sababu ni haki yao na ni wajibu wenu Wizara kufanya hivyo. Kwa hiyo tunaomba minada kwenye maeneo ambayo yana wafugaji kwa sababu ni haki yao kupata huduma za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuzungumzia uchache tu kwa hao wafugaji, naomba niende kwa wavuvi, miongoni mwa changamoto ambao zinawakumba wavuvi wetu ni pamoja na kanuni zilitungwa 2019/2020, kuna changamoto kubwa kwenye eneo hilo, Mheshimiwa Ulega ulikuwepo kwenye utungaji wa hizo kanuni na wakati Mheshimiwa Rais anasema anakurudisha hapo alitamka maneno fulani. Hata hivyo, wakati naangalia CV zako nikagundua kwamba eneo hilo linakuhusu sana la uvuvi na akasema amekuleta urekebishe na sisi tunaimani kwamba Mama hakuja tu kwamba kukurudisha alikuwa amepitia na akagundua kwamba kuna shida. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hicho alichokifanya tuna mategemeo makubwa kwa kuwa waziri ndio ameingia wewe ulikuwepo utamsaidia zaidi kuweza kuboresha yale makosa ambayo yalifanyika kipindi kilichopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuzungumzia habari ya uvuvi haramu. Mimi Aida siyo muumini wa kuwasaidia wanaofanya uvuvi haramu, lakini kumekuwa na makatazo kadhaa kutoka kwa wizara na Serikalini, lakini makatazo hayo hayaendani na njia mbadala namna ya kuwasaidia wavuvi wetu kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la nyavu, wakati waziri anawasilisha hapa amesema uvuvi haramu umepungua kwa asilimia 80 tunashukuru kwa sababu umepungua, lakini umepungua umewaacha wavuvi wetu kwenye hali gani kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ilikuja na utaratibu wa kwamba wanahitaji kutumia nyavu ya milimita nane na kumekuwa na mkanganyiko kwenye hiyo taarifa, wengine milimita kumi, wengine milimita nane. Pamoja na milimita nane hiyo nyavu wanapokwenda kutumia hao wavuvi kuna maeneo ambayo haizuii hiyo nyavu Samaki ambao wizara haitaki waingie kwenye ile nyavu, kinachotokea ni nini? Huyu mvuvi ambaye ni mtu wa mwisho kabisa ikitokea wale Samaki ambao inaonekana ni halali wapo robo tatu labda pale wamepenyeza Samaki kumi au watano hawa watendaji wanapofika kule wanawatoza faini, faini ambazo hazina uwiano, milioni mbili, milioni tano, milioni kumi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wavuvi pamoja na kuchangia pato la Taifa hizi nyavu zinapoingia nchini Serikali mpo, nyinyi ni wajibu wenu kuhakikisha mnafuatilia nyavu hizo zinazalishwa wapi. Kinachofanyika sasa hivi kwenye nchi yetu ni sawa na msafara wa ng’ombe, ng’ombe wa mbele akisimama anayepigwa ni ng’ombe wa nyuma ndiye anaye adhibiwa. Hawa wanao adhibiwa leo wavuvi wetu ni watu wa chini kabisa hizi nyavu zimepita sehemu ngapi mpaka kumfikia mvuvi wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri nikuombe sana, niwaombe sana na Mheshimiwa Waziri kuna haja ya kufanya utafiti wa kutosha juu ya jambo hili na kwa sababu tumekuwa na utaratibu tukiamini ndiyo njia halali, au ndiyo suluhisho la kuchoma nyavu ni vizuri tukajifunza. Nitatolea mfano wa Ziwa Tanganyika, Ziwa Tanganyika tuna-share zaidi ya nchi tatu, hivi mmejiuliza nchi nyingine ikiwemo Kongo, Burundi na Zambia wamefanya nini na wanatumia nyavu gani badala ya kuja kuwaadhibu hawa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza kwenye Bunge lililopita na leo narudia kusema hawa Samaki wanavyokuwa mle ndani kwenye ziwa hawajui kwamba wapo Tanzania, wapo Kongo au wapo Burundi kwa hiyo kuna wakati mwingine tunatunga kanuni ambazo zinakwenda kuwanyonga wavuvi wetu bila kuangalia kwamba wenzetu wanafaidikaje na hilo jambo.(Makofi)

T A A R I F A

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Spika, taarifa nakuruhusu.

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza kuhusu nyavu hizi ambazo zinatakazwa na wizara ni nyavu aina ya Makira, hizi nyavu aina ya Makira neno lenyewe limetoka Kongo ni neno la kifaransa kwa hiyo linakatazwa huku kwetu Ziwa Tanganyika, lakini kule Kongo wanavua kwa kupitia nyavu hiyo, kwa hiyo, tunahifadhi samaki huku kwetu kule tunawaachia waweze kuwavua hao Samaki. Ahsante sana.

SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Aida?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya wavuvi wetu ninapokea kabisa, kabisa hiyo taarifa na kuna haja ya wizara kujitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye jambo hili twendeni tukafanye utafiti wa kutosha kwenye nchi ambazo tuna-share kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, kuangalia wenzetu wanafanya nini kabla ya kuja na kanuni ambazo hazitusaidii. Lakini tuboreshe pia sera zetu na sheria ambazo tunaamini zitaleta manufaa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uvuvi ring net, kulingana na umaskini wa wavuvi wetu wanatumia ring net utakuta mle ndani kwenye hicho kifaa kuna wavuvi kumi, kumi na moja mpaka kumi na tano. Sheria zetu zinataka kila mvuvi aliyopo kwenye kile chombo awe na leseni, hili jambo Mheshimiwa Waziri nataka tu kwamba, kama tuliweza kuangalia zile sheria au kanuni za wafanyabiashara wadogo ambazo zilikuwa ni kero twendeni tukaangalie na kwa wavuvi wetu jambo hili ni kero bado kwa wavuvi wetu, naamini inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye jambo lingine kuhusu mikopo, mikopo kwa wavuvi. Pamoja na kuwachomea nyavu hawa watu wamekuwa maskini ni wajibu wa Serikali sasa tuende tukawapatie mikopo ambayo itawasaidia kuwa na nyavu halali ambazo zimeidhinishwa na wizara ziweze kuwasaidia watokane na uvuvi walionao leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba hili jambo ipo kwenye sera, nashukuru nimeona wizara mmeanza juzi Mwanza nilikuwa na Naibu Waziri yupo kule, tunataka kuwaona na wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanapewa mikopo, mikopo ambayo itawawezesha waondokane na umaskini ambao mwingine ulitokana na maamizio na mambo yenu ambayo mlikwenda kuyafanya ambayo hayatatusaidia kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niende kwenye suala la mipaka ndani ya ziwa. Kama kuna sehemu kinatumika kama kichaka leo hii cha kukusanya kodi kwa wavuvi ni hicho kitu kinaitwa mipaka, hifadhi ndani ya ziwa. Hawa wavuvi wetu wanapoingia ziwani kuvua hakuna alama yoyote inayoonyesha kwamba hapa niihifadhi, matokeo yake wale watendaji badala ya kutoa elimu wamekaa pale kama mtego wanasubiri mvuvi aingie kisha wampe adhabu kwamba hapa umeingia kwenye hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili halikubaliki, ni vizuri tukajikita kutoa elimu na kutimiza wajibu wetu wa kuweka mipaka, alama zinazoonyesha hii ndiyo mipaka hapa ni hifadhi, badala ya kwenda kuwapa nanii adhabu wavuvi wetu. Na hili jambo wapo watendaji wenu ambao siyo waaminifu, inawezekana zile fedha hazifiki kwa sababu hata wanapotoza hawatoi risiti, naamini Serikali hainufaiki na chochote kwenye jambo hili. Kuna kila sababu pamoja na sheria zenu ziwe wazi na mjikite zaidi kutoa elimu kwa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi ni suala ambalo watu wanataka kujikimu kimaisha yale maji yalivyo yasigeuke leo kuwa laana kwa wananchi wetu lazima maji yale kuwa karibu leo na Ziwa Tanganyika wananchi wanataka kunufaika iwe baraka, siyo leo inavyoonekana kuwa laana kuwa karibu na Ziwa Tanganyika, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, kuna wamama ambao wamejikita kuuza Samaki hawa Samaki ambao leo inaonekana ni haramu wanapita na mabeseni na sinia wanauza zile Samaki. Jambo ambalo linatokea leo Maafisa Uvuvi akikuta yule mama anauza Samaki, yule mama hajui kwamba huyu Samaki anaruhusiwa au haruhusiwi anakamatwa na sinia lake, anatozwa faini milioni moja, laki tano, laki nane, niwaombe wizara kuna kila sababu ya kuwaangalia...(Makofi)

SPIKA: Ahsante sana

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia uzima na mimi kuweza kuchangia mpango siku ya leo. Niwapongeze Kamati kwa kazi kubwa ambayo wameifanya Kamati ya Bajeti, wamefanya kazi kubwa sana kwa uzalendo kwa ajili ya Taifa letu, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na matumizi bora ya rasilimali za nchi tulizonazo, nitaanza na Ziwa Viktoria na Ziwa Tanganyika. Maziwa yote mawili tuna-share zaidi ya nchi moja. Pamoja na kwamba ndani ya ziwa kuna vitu vingi ikiwemo maji, ikiwemo samaki, dagaa na vitu vingine vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na mfano wa Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika pamoja na kwamba leo kwenye mpango tunazungumzia upatikanaji wa maji mjini malengo ambayo hayajafikiwa toka tulipoanza kutengeneza mipango yetu, lakini kwenye mpango nilitegemea kuona ni namna gani Serikali imejipanga kutumia maji hayo tuliyonayo kwenda kutatua changamoto za maji kwenye Taifa letu, sijaona kwenye mpango, mmezungumza kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo fedha inatumika vibaya ni maeneo ambayo watu wanakwenda kwa ajili ya kufanya survey ya kutafuta maji. Zinatumika fedha nyingi wanaacha mashimo tu kule, lakini kuna vyanzo vya uhakika ambavyo ni Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria. Hatujaona mpango ukionesha hasa kwamba wamewekeza fedha kule ili kufikia malengo ya kupunguza changamoto ya maji Vijijini na Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha suala la maji tu kuna suala la uvuvi, kama wanaweza wakatumia Congo, Zambia, Burundi, tunapozungumza namna ya kuongeza Pato la Taifa ni lazima tuwawezeshe wavuvi wetu waweze kuvua kisasa, pamoja na kuwawezesha, lakini bado lazima tuondoe sheria kandamizi zinazowakandamiza wavuvi wetu

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea tunapozungumza kuongezeka kwa pato tutengeneze mazingira rafiki ya watu ambao wanatakiwa kuongeza Pato la Taifa. Leo pamoja na kwamba nia njema ya Serikali ya kuondoa uvuvi unaoitwa uvuvi haramu, tukachoma vile vifaa lakini lengo ni kuongeza pato, tukawachomea vile vifaa walivyokuwa navyo ambavyo walikuwa wanaongeza pato kupitia hivyo vifaa vinavyoitwa haramu lakini tukawaacha bila hivyo vifaa, mkumbuke wale samaki na dagaa hawajui kwamba hapa ni Tanzania au hapa ni Congo. Kwa hiyo, badala ya kuwasaidia wavuvi tumewatia umaskini. Nilitegemea kwenye mpango tuseme tumejipanga namna gani kwenda kuwaondoa wale wavuvi ambao waliondolewa vile vifaa ambavyo vilikuwa vinaitwa haramu, kuwapa vifaa halali ambavyo ni vya kisasa ili tukaingie kwenye competition na nchi hizo nyingine ambazo tuna-share Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwenye mpango huu kwa kuwa tunajua kuna fedha zinapatikana kwenye uvuvi, tutafute namna bora, kwanza zikiwemo meli za kisasa kwa kuwa tunashindana, tuko kwenye ushindani. Lazima tutengeneze mazingira rafiki tukiamini kwamba kweli malengo ambayo tunatarajia tumeonesha kwa mifano kuwasaidia wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya ziwa ukiangalia Ziwa Tanganyika ukiacha maji na uvuvi kuna suala la mafuta. Kwenye Mpango hapa nilitegemea nione mmejipanga namna gani kuvuna yale mafuta ya Ziwa Tanganyika ambayo yangesaidia kuongeza Pato la Taifa letu. Tumezungumza kidogo tu na kuna mambo ambayo hatuwezi kuwa na vyanzo vilevile. Kuna rasilimali ambazo tunazo lakini hatujazitumia kama inavyotakiwa. Mungu ametujaalia maziwa kama hayo yapo, lakini hakuna mipango ambayo inaonesha kweli namna gani tumejipanga kutumia rasilimali hizo kuweza kusaidia Taifa letu ikiwemo suala la Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria. Nimezungumza mara nyingi na leo nitaendelea kusema bado hatujatumia inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndani ya hayo maziwa mawili bado kuna suala la mipaka. Wavuvi wanapoingia ili wakachukue mazao yao yaliyopo mle ndani kwa maana ya samaki, wanaambiwa kuna sehemu ambazo ni za hifadhi. Ukiangalia kwenye mpango hakuna sehemu wamesema wanaweka kiasi gani kwenda kuweka mipaka kwa kuwa hakuna alama yoyote inayoonesha kwamba hapa ni mpaka. Lakini, toka wameanza kusema hayo maeneo ni hifadhi, hatujawahi kuambiwa kwenye hifadhi hiyo, hao samaki wamefika wangapi zaidi ya wananchi kukamatwa na kupewa adhabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye jambo jingine kwa sababu ya muda kuhusu matumizi bora ya ardhi, kabla sijafika huko, tunatambua nia njema ya wale Mawaziri, Tume iliyoundwa kwenda huko kupitia mipaka. Kuna maeneo ambayo leo kwa sababu kwenye mpango hapa Mheshimiwa Waziri ametuambia idadi ya watu inavyoongezeka na kwa neema ya pekee wanawake wanaongezeka kwa asilimia 51 alivyotusomea hapa, lakini ukiangalia kama idadi inaongezeka tulitegemea kwenye mpango watuambie kwa sababu ardhi iko pale pale na idadi ya watu inaongezeka kuwe na Mpango maalum kwa ajili ya kuongeza maeneo ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yamewekwa hayana faida yoyote, hakuna hata mdudu unaweza ukatembea mchana, asubuhi ukakutana nae lakini wananchi wangeozewa hayo maeneo wangeongeza uzalishaji. Kwa hiyo, kuna haja ya Serikali kuwa na mpango maalum wa kupitia angalau kila mwaka kuangalia maeneo ambayo hayana sababu ya kuwa pori tengefu warudishiwe wananchi ili waendelee kuzalisha na waongeze Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza kuna maeneo ambayo yamekuwa na migogoro mara nyingi, hifadhi na wananchi. Pamoja na kuwa hifadhi, lazima tujue hivi wanyama wale wako wangapi, wanaingiza kiasi gani na kama tungeweza kuwapa wananchi wangeingiza kiasi gani kwenye Pato la Taifa. Leo hatuwezi tukawa tunazungumzia mipango ambayo tunathamini pekee wanyama halafu tukaacha wananchi na tunajua kweli idadi inaongezeka na aridhi iko pale pale. Kama kweli tunategemea matokeo chanya ni lazima tuwe na utaratibu maalum wa kuongeza maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye matumizi bora ya ardhi, hapo lazima tuzungumze tumepima eneo kiasi gani kwa ajili ya kilimo. Tumezungumza kwamba hapa inasaidia Pato la Taifa asilimia 26 lakini tulitegemea kwenye mpango hapa mtuambie mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kwenda kuongeza kwenye Vyuo vya Utafiti, hatujaona hapa! Kwa hiyo, hakuna suala lolote ambalo linaonesha kilimo ni kipaumbele. Ni lazima tuone kwenye mpango hapa kwa sababu huwezi kuboresha kilimo wakati hujaweka fedha kwenye utafiti. Lazima tutafiti tujue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimaliza kwenye utafiti ni lazima fedha itengwe kwa ajili ya kupima udongo. Leo mnatuambia kuna mazao ambayo soko lake ni gumu lakini mnapokuja na mazao mbadala lazima ardhi iwe imepimwa kwamba udongo huu unafaa kwa ajili ya zao hili. Kama hatujapeleka fedha kwa ajili ya kupima udongo hakuna kilimo hapo na lazima mjue kwamba hivi tunaposema kilimo tunazungumza kitu gani. Kuna suala la kupima udongo, kuna suala la pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru tu kwamba kuna fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kujenga madarasa, ni jambo jema sana, miongoni mwa maeneo ambayo watu wake wameathirika ni pamoja na wakulima wa nchi hii kwa sababu nchi ambazo zilikuwa zinazalisha mbolea na wao walikumbwa na janga hili kwa hiyo, bei imekuwa kubwa ya mbolea. Tulitegemea kipaumbele cha kwanza mngepeleka kuweka ruzuku kwenye pembejeo ili Watanzania na wao waone! Mheshimiwa Waziri huwezi kumpeleka mtoto darasani wakati hajala, lazima ale chakula ashibe ndiyo aende huko darasani. Kwa hiyo, tunategemea kwenye mpango hapa mtuambia mpango wa Serikali pamoja na slogan ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Viwanda, lakini viwanda vingekuwepo hapa vingezalisha mbolea. Mbolea ingezalishwa Tanzania bei ingekuwa nafuu na ingeweza kumsaidia mkulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira yote haya tunaomba busara ile iliyotumika kwenda kwenye madarasa ni jambo jema na mimi nakubali lakini turudi kwa hawa wakulima ambao hiyo asilimia 26 nikueleze tu ni wakulima wa mkono na kama nia ni njema ya kwenda kumsaidia mtu huyu ni lazima tuoneshe hiyo nia njema ya kumsaidia mkulima wa kawaida kabisa. Ruzuku ni lazima na mimi niseme tu, Serikali iliyopewa dhamana ni lazima muangalie namna ya kuwasaidia hawa wakulima. Hii siyo favor, lazima tujue kwamba tuna dhamana ya kuwasaidia wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujue athari ya hili jambo, huu ni mwezi Novemba na kama ni Novemba, wakulima wa Nyanda za Juu Kusini zaidi ya Mikoa Saba huu ndiyo mwezi wa kupanda, mbolea haipo! Tutakuja kuingia gharama mara mbili ya kuagiza mazao nje ya nchi badala ya leo kuweka ruzuku kwenye mbolea iweze kuwasaidia Watanzania. Lazima tuchukulie jambo hili kwamba ni jambo muhimu sana na lazima tuone kwamba Watanzania hawa ambao leo tunaamini zaidi ya asilimia 60 tunawapeleka wapi. Wakati nazungumzia hiyo mbolea lazima mjue pia kuna competition ya masoko hao wenzetu na wao hawajalala. Hawa majirani zetu Zambia mfuko wa mbolea ni 65,000 wao wanatoa wapi? Tanzania tunasubiri nini? Lazima tuone yale mambo mazuri ambayo wenzetu wanafanya siyo vibaya kuiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia. Kabla ya yote nipongeze taarifa zote za Kamati Tatu na niwapongeze Wajumbe kwa namna ambavyo walijitoa kuchakaka na kujadili kwa kina taarifa hizi.

Mheshimiwa Spika, kulingana na umuhimu wetu kama Muhimili wa Bunge, kuna sehemu pekee ambayo sisi tumepewa hiyo neema ya kuisimamia Serikali. Kama kuna eneo Taifa letu linapata hasara na kupoteza fedha ni eneo la mikataba, nami nitajikita eneo hilo la mikataba.

Mheshimiwa Spika, wakati tunajadili hapa taarifa iliyopita ya Kamati yetu ya PAC, ilijadili kuhusu mkataba ambao ulikuwa unahusiana na NFRA wa ujenzi wa vihenge, mpaka leo nazungumza hakuna kitu kimefanyika, kwa namna nyingine alizungumza Mheshimiwa Getere hapa kwamba tunamwambia nani? Unaweza usimuelewe, lakini kama tunazungumza tunaleta taarifa kama Kamati ya Bunge ili Bunge lipitishe na Bunge likapitisha tunakuja kutoa taarifa kwa mara nyingine jambo lile halijatekelezwa, inatia uchungu wakati mwingine.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, yule Mkandarasi hatujui anafikiri nini mpaka leo, lakini wakati Wabunge wanajadili yale matrekta mabovu, ndiyo huyo huyo msumbufu Mkandarasi ambae hakuna maamuzi yoyote yamefanyika mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nazungumzia suala la mikataba nilikuwa najiuliza machache sana, kwa nini tunaingia mikataba mibovu? Je, nchi yetu inashida ya Wanasheria? Je, ni kweli nchi yetu imeshindwa kuwashirikisha kikamilifu wanasheria wetu washauri vizuri tunapoingia mikataba? Ni kweli Wanasheria wanapitia hiyo mikataba kabla hatujaingia kwenye hiyo mikataba? Na ni kweli wanatoa usahuri wa kina? Je, huo ushauri ni kweli Wizara inazingatia?

Mheshimiwa Spika, ukianza kutazama hasara hizo ambazo tunazipata kama Taifa kupita mikataba, utapata maswali mengi ambayo hayana majibu. Aidha, Wanasheria wetu wanatumika kuhujumu nchi yetu, kwamba wanajua kwamba mkataba huu tumwambia yule mtu apite uchochoro ambao anaweza kutokea. Ninatoa mfano tu wa vitu vichache kwa sababu ni vitu vingi ambavyo tunapata hasara kama Taifa. Ukitazama Shirika letu la Umeme TANESCO, Symbion namna walivyoingia huo mkataba na hasara ambayo tumeipata kama Taifa ya malipo ya Dola za Kimarekani Milioni 153.43.

Mheshimiwa Spika, ni huzuni na inaumiza sana, yaani wameshaingia mkataba, umeanza kutekelezeka, wanafika katikati wanagundua kuna makosa, wanaamua sasa ngoja tujiondoe kwenye huo mkataba. Hawajui madhara yanayoweza kutokea baada ya wao kujiondoa, ndiyo hapo ninaposema, Je, ni kweli Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inashirikishwa kwenye mikataba hii? Hasara hii ya Dola za Kimarekani, Milioni 153 ingesaidia Watanzania wangapi huku kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri watu wawe wanaangalia ikitokea mkataba kama huu umeingiza hasara kwenye Serikali yetu, ni watu gani wameshiriki, wakiwa wanachukuliwa maamuzi mapema inawezekana tukaokoa fedha zingine kwenye mikataba mingine inayokuja na wengine wakajifunza, kwamba kwa kupelekea hasara kwenye Taifa, yeye mwenyewe anaweza akatolewa pale kama mfano, lakini unaona mambo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya tumewahi kushauri Bunge lililopita, kwamba ni vizuri Bunge lishirikishwe kwenye mikataba hii, kwa sababu hasara inayotokea kwenye Taifa ni wananchi wetu wanaoenda kuumia. Ni vizuri kama Bunge litashiriki yawezekana tukashauri mambo kadhaa kabla ya kupata hasara kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano wa pili ambazo zinaingiza hasara pia kupitia mikataba ni TANROADS. Kwa hali ya kawaida, siamini kwamba TANROADS wanaweza kukosa Wanasheria makini wa kushauri kuingia kwenye mikataba. Mara nyingi tunapata hasara kwenye TANROADS sehemu gani? Ni pale ambapo, TANROADS inashindwa kuwalipa Wakandarasi kwa wakati. Wanasheria kama wameshirikishwa ni lazima washauri. Ukitazama kila Bunge hili jambo litazungumzwa. Sasa kama linazungumzwa kila Bunge halafu tunakuja tena tunazungumza, ndiyo maana tunarudi kulekule kwa Mheshimiwa Getere, tunasema nini na tunamshauri nani? Lakini kwa sababu ni wajibu wetu tutaendelea kushauri.

Mheshimiwa Spika, TANROADS pekee yake, wameingiza hasara ya Bilioni 68.73 kwa kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. Hizi fedha ambazo Mheshimiwa Rais anazunguka kutafuta, kwamba watoto wasihangaike kwa ajili ya madarasa, lakini kuna nyingine hasara za ajabu na za kizembe tu zinafanyika kwenye Taifa letu. Kuna haja ya kuangalia vizuri mikataba yote kuna shida gani, nani anakubaliana na hili jambo, nani yuko nyuma ya haya mambo yanayofanyika. Mimi siamini kama Wanasheria wanashirikishwa kikamilimu na kama wanashirikishwa wao wenyewe wanahusika kutuhujumu kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la vihenge nimkwishalizungumzia. Yule mkanadarasi hatujui mpaka leo anawaza nini na fedha alishalipwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 33, yuko huko na hatujui nini kitaendelea mpaka leo; kwa sababu yeye alikuwa ametishia kupeleka mahakamani lakini sisi kama taifa tupo tu na kuna vihenge havijamalizika mpaka leo. Kwa hiyo kuna haja sasa ya kufanya maamuzi kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nataka nishauri kwenye jambo hili. Ninashauri Serikali ichukue hatua za makusudi kwa watendaji wote waliosababisha hasara hizo kwa makosa ya uzembe au kwa makosa ya kuruhusu kuingia mikataba kama hiyo ambayo inaleta hasara kwa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanapokuwa wanasikia kuna mkataba umesainiwa, wanaambiwa tu hivyo; lakini baadaye ukija kukuta mambo yaliyopo; lile kundi ambalo linakuwepo pale wakati mkataba unasainiwa; sisi tunaamini kabla ya kusaini kuna watu wameshakaa, jopo la wataalamu mbalimbali likapitia ule mkataba, unamaslahi kwa taifa? Je, ni hasara gani ambayo tunaenda kuipata kama taifa? Je, hakuna eneo lingine ambalo tunaweza tukapata fedha mpaka kuingia kwenye mkataba mbovu?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba hatua zichukuliwe, pia zichukuliwe kwa wakandarasi wote ambao wanafanya makusudi na uzembe wakiamini kuna uchochoro wa kutokea; kwamba kuna sehemu watatokea tu. Ndiyo maana nasema na wanasheria wanakuwa wanahusika kwa wakati mwingine. Kwa sababu kama mkataba wameupitia na wanajua lazima washauri vizuri, wakiwashauri vizuri tutajua kwamba shida ipo kwa wataalamu wetu na hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimezungumzia kwenye suala la mikataba, narudia tena kusema. Kuna haja ya uchunguzi wa kina tunapokuwa tunaingia kwenye hii mikataba kama wanasheria wetu au Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashirikishwa kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, naomba nihame hapo kidogo, niende kwenye kamati ya LAAC. Katika miradi ambayo inaendelea hivi sasa kwenye halmashauri zetu, ikiwemo ujenzi wa madarasa; ni jambo jema sana ambalo analifanya Mheshimiwa Rais. Ukitazama jambo hilo jema, tuna ma-engineer wachache sana; wamezungumzia changamoto ya watumishi.

Mheshimiwa Spika, leo walimu wameingizwa kusimamia ujenzi wa hiyo miradi kwenye halmashauri zetu. Mwalimu anajua taaluma yake ni kufundisha, unampeleka akasimamie jengo ambalo, tena ni la pressure. Ukitazama zile fefdha za COVID, wote mnajua presha iliyiokuwepo kwenye ujenzi wa yale madarasa. Umemuweka mwalimu, tena kwa bahati mbaya zile kamati zote nne walimu wapo. Kwa hiyo walimu zile siku 90 zote badala ya kufikiri kuwafundisha wanafunzi wetu wanafikiri kuhusu miradi ya ujenzi. Kwa bahati mbaya zaidi, yeye kwa sababu si taaluma yake, ukitazama yale madarasa ya COVID, nafikiri Waheshimiwa Wabunge wote wameshapita kwenye maeneo yao wameona. Mimi sijajua kama ni lile jina, au ni nini.

Mheshimiwa Spika, kabla hayajakamilika, yana ufa. Unaanza kuwaza ni jina hili lenyewe COVID ndilo limeendana na hii kasi inayokwenda ya madarasa kuharibika au kuna nini?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kunakuwa na masharti mengi, ni vizuri tujue, tuko hapa leo kuna madarasa ambayo yalijengwa na wazazi wetu yapo imara; lakini madarasa ya sasahivi yanajengwa, yaani ni kama watu hawawi na mtazamo kwamba hivi tunajenga hili darasa tukitazamia miaka mingapi mbele? Wanatazama kumaliza, ukifika pale utaona rangi inapendeza, ndani ya miezi mitatu ufa umetokea pale, yaani mambo hayaeleweki.

Mheshimiwa Spika, na kama ni wajibu wetu sisi kama Bunge, kuisimamia Serikali, kuna haja ya kuona kwamba mikopo tunayokopa, tunalenga nini? Tunataka kua-achieve nini? Tunataka ku-achieve kwa muda gani ambao tunafikiri kwamba angalau lile lengo ambalo tumelenga litaonekana kwa muda fulani.

Mheshimiwa Spika, leo tunamaliza ndani ya mwaka mmoja hali ni mbaya; kuanzia kwenye sakafu, ukuta na unaanza kujiuliza ni kwanini? Ni kwa sababu ya pressure tuliyokuwa nayo ya kujenga madarasa au shida ni kwa sababu wataalamu wetu hawakutosha. Tulitumia walimu wenye taaluma nyingine kuwapeleka kwenye taaluma ambayo si ya kwao labda ndiyo maana hayo mambo yametokea.

Mheshimiwa Spika, hapo nataka nizungumze kidogo kwenye suala la hawa watu ambao wanaitwa maafisa manunuzi kwenye halmashauri zetu. Yaani kama unavyoona changamoto hizi zingine, ukienda kwenye halmashauri, yaani kila mradi ukienda lazima utakuta kuna madudu tu kwa hawa watu wanaitwa maafisa manunuzi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, kuna haja ya kufuatilia kwa kina, je, wale maafisa manunuzi waliopo kule ni kweli wana taaluma hiyo? Kwa sababu fedha hizi zote ambazo tunapeleka, mabilioni na mabilioni, wasimamizi ndio hawa wanaoenda kuhusika na manunuzi. Ni kweli wanayo elimu ya kuweza kusimamia hizo fedha? Kama sivyo kuna haja sasa ya kuendelea kupitia upya, kwenda kuwatazama, halmashauri kwa halmashauri ili kama shida ni maafisa manunuzi kwamba hawapo wenye sifa, Serikali ifanye kazi ya ziada ya kuwaajiri hao kwanza kwa kuwa wao ndiyo wanaokwenda kuhusika na manunuzi ya kila kitu.

Mheshimiwa Spika, kuna wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema hapa, kwamba ni vizuri yale mabaraza na kamati za fedha wanapokutana na Wabunge wahusike. Muda mwingi tupo hapa Bungeni. Ulipokuwa unazungumza asubuhi, kwamba na ninyi Wabunge muone huko mnakotokea, kiukweli hali ni mbaya, na ukifika huwezi kuwaambia mlikopita hapa hamkufanya vizuri watakushangaa. Kwa hiyo kwa sababu wewe unaingia automatically kwenye kamati hiyo inabidi uliache tu lipite, liende, eeh!

Mheshimiwa Spika, na kwa mazingira ya kawaida huwezi kusimama mle ukaanza kukosoa, wanasema wewe ni mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango, lakini hukuwepo wakati hilo jambo linafanyika.

Mheshimiwa Spika, naomba na hilo jambo mliangalie tena, kwa sababu tukipunguza hayo mambo wenyewe kule hapa tuatapunguza mambo mengine ambayo hayana sababu. Wabunge tutakwenda huko sisi wenyewe kwenda kusaidia haya badala ya kuja kuleta hoja nyingine ambazo hazina sababu ya kuwepo hapa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kusimama wakati huu nikiwa na afya njema. Napenda kumshukuru aliyewasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani na Waziri kwa kutambua umuhimu wa kilimo nchini Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napenda kusema miongoni mwa wakulima tunaowazungumzia leo ni pamoja na wakulima wa Mkoa wa Rukwa. Kuna shamba ambalo Wabunge wangu wa Mkoa wa Rukwa wamelizungumza kwa miaka kadhaa humu ndani, tena ni wa Chama cha Mapinduzi, yawezekana hamkuwasikiliza kwa sababu ni Chama cha Mapinduzi leo nasimama kupitia CHADEMA kuzungumzia shamba hilo hilo ili mtambue kwamba ni suala ambalo linawagusa wananchi moja kwa moja, shamba la EFATHA, Manispaa ya Sumbawanga, Kijiji cha Isesa imekuwa ni sehemu ya watu kwenda kufanya kampeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili limetamkwa hapa ndani akiwa Waziri Mkuu Pinda kwamba anakwenda kulishughulia, lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika. Sijajua speed mlionayo Chama cha Mapinduzi na kama mna nia njema na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Wananchi wale kwa sababu ni miongoni mwa watu waliowapa kura na sasa mnajiita ni kazi tu mmeacha porojo nendeni mkashughulikie suala lile, muache story mfanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitazungumzia suala moja ambalo ni kero kubwa kwa Watanzania hasa wakulima. Mimi ni miongoni mwa watoto waliotoka kwa wakulima tena wanaolima kilimo cha mkono. Nasikitika Waziri hayupo hapa alisema anataka jembe likae kwenye jengo la kumbukumbu, lakini angejua kwamba Manispaa ya Sumbawanga asilimia kubwa ya wakulima wanalima kwa mkono wanapata gunia mbili au tatu kwa mwaka lakini wanalipa kodi kwenye nchi hii wakati huo huo ni miongoni mwa wakulima ambao wanapata mateso mpaka wanajiona ni kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Analima kwa mkono, kutoa mazao yake shambani kuyapeleka sokoni anakamatwa njiani alipie kodi. Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Rais alipokuja hapa alipokuwa anazindua Bunge alizungumzia habari ya tozo zisizokuwa na tija, lakini mpaka leo kama mlikuwa serious mngekuwa mmeonyesha hatua. Hakuna kitu, zimekuwa ni story za miaka yote.
Mimi nawashauri, siku hizi Watanzania wanaelewa mnapotamka kitu mwende kwa vitendo, msitamke tu halafu mkanyamaza, mnapotamka tayari Watanzania wamesikia wanabaki kusubiri utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao haya tunayozungumzia ndugu zangu Wabunge tukiwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo kuna mkulima analipia mpaka mwenge, huu mwenge unakwenda kumsaidia nini mkulima, unammulikia nini shambani? Imefikia mahali hizi tozo hata wanaosimamia inaonekana kama kuna hali fulani ya upofu wa kutokutazama mbele. Wakulima hawa ni miongoni mwa watu ambao wanachangia pato kubwa la Taifa katika nchi hii, mmekuja na kauli mbiu nyingi sana lakini kauli mbiu hazijasaidia chochote imebaki story tu na mnaongoza kwa kupanga vitu kwenye karatasi, lakini utekelezaji mna zero positive. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la masoko, unapozungumzia viwanda, Waziri wangu naona ametoka, alisema Sumbawanga atajenga kiwanda, mimi nataka nimwambie Mkoa wa Rukwa tunalima mahindi, maharage, ngano na ulezi na pia kuna wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapozungumzia Serikali ya viwanda mpaka leo mmetoa elimu kiasi gani kuonesha kwamba mko serious na viwanda mnavyovizungumza? Kwa sababu hata wakulima wataona mnachokizungumza ni sawa na story za siku zote walizowahi kusikia. Kama elimu hamjatoa, halafu mnawaambia kwamba wao wanatakiwa kujenga viwanda wakati hawajaona utofauti wa wao walivyokuwa wanalima na leo unavyowaambia kwamba wapeleke kwenye viwanda, viwanda vinawasaidia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikaji wa pembejeo, sidhani kama huwa hamsikii siku zote tunavyokuwa tunawashauri. Kabla sijaingia kwenye hili Bunge mmeshauriwa mara nyingi sana. Kuna sehemu mpaka mnawaambia Wenyeviti wa Serikali washiriki kuandaa zile Kamati. Ukitazama Mkoa wa Rukwa hasa Manispaa ya Sumbawanga, huyo Mwenyekiti anayeshughulikia pembejeo, halafu mnapokuja mnakuwa mmeweka watu wenu mnaowajua, analipwa shilingi 5,000 baada ya miezi mitatu. Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa leo inamkopa hiyo shilingi 5,000 kwa miaka mitano..
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niwaambie Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama mko serious na mnatambua umuhimu wa kilimo katika nchi hii nendeni mkafanye utafiti kwanza. Unapozungumzia viwanda lazima ujue kabla ya viwanda wananchi walikuwa na changamoto zipi. Kama soko mlishindwa kutafuta mlipokujana na kauli mbiu ya kilimo kwanza ikawa kilimo mwisho, viwanda leo vitakwenda kumkomboa Mtanzania kwa style ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la hawa Maafisa Kilimo kuna wengine wako mjini na Mkoa wa Rukwa utakuta wale wakulima hawamfahamu. Yeye faida yake kuwepo kule ni nini, hakuna faida ambayo mkulima anaiona. Inabidi tusiwalaumu wataalam hawa, yawezekana hamjawawezesha wanawafikiaje wakulima hawa. Kwa hiyo, nawashauri Chama cha Mapinduzi kama mna nia njema na wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa wawezesheni hawa Maafisa Kilimo wakatimize wajibu wao wa kutoa elimu kwa wakulima hawa ili kilimo hiki kilete tija ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la utabiri wa hali ya hewa, yawezekana ni Nyanda za Juu Kusini peke yake, Mkoa wa Rukwa kipindi cha nyuma walikuwa wanalima kutumia utabiri wao wa kawaida, wa Kifipa ule, wakitazama ndege wanajua kwamba safari hii kuna mvua nyingi au chache lakini walikuwa wanapata vizuri kuliko leo wakiambiwa kuna mvua nyingi wanapolima mvua haiji. Naomba hawa watabiri wa hali ya hewa utabiri wao uwe ni wenye tija, usiwe na hasara kwa Watanzania na wanapofanya utabiri wasifanye utabiri wa Dar es Salaam kwani huko hakuna wakulima, wafanye utabiri kwa kuangalia wakulima wa vijijini hasa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la uvuvi kwa sababu wavuvi pia wako Mkoa wa Rukwa. Wavuvi katika Taifa hili hususani Mkoa wa Rukwa imekuwa ni Mkoa ambao wamenyang‟anywa sana vifaa vyao kwamba ni haramu, hivi viwanda vinavyozalisha hivi vitu hamjui viko wapi? Yawezekana hata kodi mnachukua lakini mkifika mnawaambia vifaa vyao ni haramu, kwa nini msiende kwenye viwanda vinavyozalisha?
Mimi naomba kuwaambia hawa Watanzania wapo kama ninyi ambao leo ni Mawaziri lakini mlikuwa kama wao na mlitazame hili kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia kwamba na wao wanastahili kuishi kwa amani katika nchi yao wasijione kama wakimbizi ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Ziwa Rukwa amelizungumza jana Mama Maufi, yule ni Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, hili suala limesemwa sana humu ndani na Mbunge wa Kwela, sasa tunaomba tunapowaambia mchukue hatua. Inafikia mahali mnapokuwa mnajiita ninyi ni Serikali sikivu hata mtu ambaye alikuwa haelewi anajitokeza kuja kusikiliza kwamba huyu anayesema anasema kitu gani kwa sababu kama mmeambiwa mara moja, mmeambiwa mara ya pili kitu gani kinazuia msiende kutekeleza, shida ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti ya kilimo mnayokuwa mnatenga kama mna nia ya kuboresha kilimo, hizi fedha ni za wapi, mkitegemea fedha za nje mnakwenda kufanya nini au mnakuja kucheza comedy hapa ndani ya Bunge na kutudanganya? Huwezi kupanga kwenda kufanya kitu unategemea mhisani akupe fedha wakati wewe hujajipanga una kiasi gani? Kama mko serious kweli basi Taifa litazame kwamba kilimo ni uti wa mgongo kama mlivyokuwa mmesema mara ya kwanza. Mambo mnayofanya hayafanani na hiki mnachokizungumza. Niombe kauli mbiu zenu ziendane na kile mnachokifanya. Hatutachoka kuwashauri lakini msiposikia tutatumia kauli nyingine ya kuwaambia maana kauli ya kawaida naona ni ngumu sana kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, hivi mnaweza mkaboresha kilimo bila kuwa na miundombinu ya uhakika? Kwa mfano, Wilaya yangu ya Nkasi pale Namanyere toka Mheshimiwa Rais wa leo akiwa Waziri alitamka hapa akasema Wafipa hawajawahi kuona hata lami, nilijua anatania maana alisema watani wangu mpaka leo hakuna lami, kwa hiyo, alikuwa serious kwamba kweli Wafipa watabaki kuwa hivyo. Kwa hiyo, nawashauri hawawezi kulima halafu hawana barabara ambayo itawafanya wafike sokoni kupeleka mazao yao. Muwe serious kutazama kwamba kilimo kinakwenda sambamba na miundombinu na mfanye hayo mkiwa mnamaanisha kwamba kweli mpo serious kuboresha kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri mambo kadhaa katika Wizara hii muhimu katika maendeleo ya nchi yetu ili kuleta tija kwa kizazi hiki na kizazi kijacho, kuboresha maslahi ya Walimu kulingana na umuhimu Mwalimu katika kuboresha elimu nchini ni lazima Mwalimu aweze kulipwa stahiki zinazostahili kulingana na hali halisi ya maisha kwa sasa. Kulipa madai ya Walimu kwa wakati kulingana na Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapocheleweshwa kulipwa madai yao kwa wakati inapelekea Walimu wetu wengi kukosa utayari wa kufundisha kama ilivyokuwa mwanzo, wanakata tamaa. Mfano, Manispaa ya Sumbawanga iliyoko Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya kutowalipa Walimu pesa ya likizo na kupelekea kuona kama wanatengwa. Suala la Afisa Elimu kumwadhibu Mwalimu, hali hii imeendelea kuonyesha manyanyaso makubwa kwa Walimu wetu kwa mfano dalili iliyojitokeza hivi karibuni katika Wilaya ya Sumbawaga Mkoa wa Rukwa. Serikali inachukua hatua gani kwa Afisa Elimu huyu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuleta ufanisi katika Wizara ya Elimu katika Taifa letu, suala hili la kodi kwenye Wizara hii imepelekea ada kuwa kubwa zaidi na hivyo Watanzania wa hali ya chini kushindwa kumudu katika ada husika. Mwingiliano wa Wizara kuwa na chanzo cha tatizo kutokana na changamoto nyingi zinazowapata Walimu wanafuzi pamoja na miundombinu kutokana na mambo hayo kutoshughulikiwa na Wizara moja, imekuwa changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Kitengo cha Ukaguzi kutokuwa na vifaa vya kuweza kuwafikia Walimu na kutimiza majukumu yake na kupelekea kuleta matokeo chanya katika Wizara moja ambayo itashughulikia haya yote, suala la mikopo katika Elimu ya Chuo Kikuu kuna vigezo gani vinavyotumika kutoa mikopo hii ambayo imekuwa na malalamiko makubwa hasa kwa watoto wanaotoka familia za kimasikini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI, upandishwaji wa madaraja katika Sekta hii ni lazima Wizara ifanye marekebisho. Suala hili linaleta mkanganyiko mkubwa hasa katika Manispaa ya sumbawanga. Hii ilitokana tu na uzembe wa vyombo husika. Hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Waraka Na. 5, elimu bure, liende sambamba na miundombinu, ada elekezi kulipa madai yote ya Walimu, mikopo hata kwa Walimu walioamua kujiendeleza ili kuondokana na ujinga na kukomboa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha elimu tujiulize mambo yafuatayo katika Wizara hii ya Elimu. Nini chanzo cha elimu yetu kushuka? Nini kinazuia kulipa madai ya Walimu? Kwa nini Walimu hawawezeshwi katika matibabu? Kwa nini mitaala yetu ni tatizo? Kwa nini ada elekezi leo? Lini Wizara itatoa Motisha kwa Walimu wa vijijini? Ni lini Serikali italeta mashine ya kuchakata vyeti nchini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na umuhimu wa Wizara ya Ardhi napenda kushauri mambo yafuatayo ili kuepukana na migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika Mkoa wa Rukwa na nchi nzima kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi yaboreshwe kulingana na utendaji wanapokuwa katika Mabaraza ya Ardhi. Kutokuwa na elimu ya kutosha kumepelekea kupata migogoro mingi katika Halmashauri zetu. Hati za kimila, mara nyingi zimekuwa hazitambuliki kwa baadhi ya watendaji katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Manispaa ya Sumbawanga iliyopo katika Mkoa wa Rukwa na Wilaya zake, kata na vijiji pamoja na mitaa na vitongoji vyake. Serikali ina mkakati gani wa kuwapa semina watu hawa ili kuondoa migogoro, kuwawezesha Maafisa Ardhi, kwa kuwapa vitendea kazi. Maafisa Ardhi hawa wamepelekea migogoro mikubwa sana katika Halmashauri zetu kwa kutomaliza mogogoro kwa wakati na mahali pengine kutokea migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya wawekezaji na wananchi, kulingana na migogoro hii kutokea kila eneo katika nchi yetu, nashauri Serikali kutafuta njia sahihi ya kumaliza migogoro hii ya wawekezaji na wananchi kwa kuweka njia shirikishi kuanzia ngazi ya chini ili kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro kwa wananchi wa Isesa na mwekezaji, huu ni mgogoro wa muda mrefu uliopo katika Manisapaa ya Sumbawanga Mjini na Vijijini, suala hili limechukua muda mrefu hata kwenye kitabu cha Waziri mgogoro huu haupo, naomba Wizara ichukue hatua haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia kutokuwa wazi, kutokuwalipa wananchi fidia kwa muda muafaka inapelekea migogoro mingi katika Halmashauri zetu kutokana na taarifa tufauti na kupelekea migogoro isiyo ya lazima, nashauri Serikali kutoa fidia kwa wananchi na kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kutoa hati kuchukua muda mrefu, kutokana na hali hii kushamiri hasa katika Mkoa wa Rukwa, Manispaa ya Sumbawanga na ili kuondoa tatizo hili Serikali imegundua tatizo hili, imegundua ni nini linalochelewesha? Pia migogoro kati ya wakulima na wafugaji nashauri Serikali kupima maeneo nchi nzima ili kuepukana na tatizo la migogoro inayoendelea na kupelekea vifo mbalimbali vinavyotokana na migogoro hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ya ardhi katika Manispaa ya Sumbawanga kulingana na suala hili kuwa na hali ya kutokuwa na usimamizi mzuri wenye uwazi ili kuondoa migogoro isiyokuwa na tija. Suala la ushirikishwaji ngazi za mitaa, hali hii ya kutokushirikishwa hasa kupewa ramani na kuyajua maeneo ya wazi ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza bila sababu.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa watumishi katika hospitali zetu nchini suala hili limekuwa ni tatizo kubwa sana katika Wilaya zetu. Kwa mfano, Wilaya ya Kalambo, Nkasi, Sumbawanga Mjini na Sumbawanga Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, suala hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wanawake wa Kitanzania na kasi yake ni kubwa sana, lakini bado hatujaona Serikali ikiipa kipaumbele kulingana na tunavyopoteza wanawake wengi hasa walioko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukosefu wa dawa kwenye hospitali zetu, hili limekuwa ni tatizo kubwa, Serikali ifanye utaratibu wa kufuatalia kama dawa zipo katika hospitali za vijijini. Wizara ipeleke dawa ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sheria ya Ndoa, kuna sababu ya kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ili kuokoa maisha ya watoto wetu wa kike kwa kukosa mambo ya msingi ikiwemo elimu, kwani wakiingia kwenye ndoa wakiwa na miaka 18 itapelekea kukosa elimu.

Kuhusu ukatili kwa wanawake, kwa kuwa ukatili huu umekuwa ukiendelea kwa kasi hasa kwa watoto wa kike wakiwa shuleni, mitaani na nyumbani, je, Serikali inaleta mkakati gani wa kumaliza tatizo hili la ukatili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifo vya wanawake wajawazito hakuna mkakati wa dhati wa kumaliza tatizo hili na kuona wanawake hasa waliopo pembezoni na wanawake wa vijijini, Serikali iweke kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi wa mpango, kuna kila sababu ya Serikali kutoa semina elekezi hasa kwa maeneo ambayo bado elimu hii haijawakomboa kwani kumekuwa na upotoshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa kupitia Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Afya ili kuboresha na kujenga vituo vya afya kwa kila kata na hospitali za Wilaya hasa katika Mkoa wa Rukwa hakuna Hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kuzingatia, kukosekana kwa hospitali hata moja ya Wilaya katika Mkoa wa Rukwa kunapelekea mlundikano wa wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Rufaa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naungana na wachangiaji wote waliopita kwa suala la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Tusipoanzisha Wakala wa Maji Vijijini, tutaimba nyimbo za siku zote ambazo hazitapatiwa majibu. Tukianzisha wakala tutaepusha malalamiko mengi ambayo yanajitokeza kwenye vijiji.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo ni vigumu sana kuweza kuyakamilisha kwa sababu suala la maji linahitajika maeneo yote. Wanafunzi hawawezi kukaa darasani kwa muda wote kama maji hayapo. Pia, kilimo tunachokisema kila siku kama uti wa mgongo na majina mengi ambayo tumejipa, hatuwezi kukidhi malengo kama suala la maji halitapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali, unajua tumekuwa na vipaumbele vingi, hebu tukae tuangalie kipaumbele ambacho Watanzania wanakizungumza. Leo kama maji ni kipaumbele cha nchi hii, hatuwezi kupunguza bajeti, tungeongeza bajeti. Inaonesha ni jinsi gani mambo tunayoyazungumza hapa ni kama kuna watu wengine washauri tena tofauti na Bunge. Suala la maji tulizungumza, tunazungumza tena, lakini kuna mambo ambayo yanapewa vipaumbele nje na yale ambayo Wabunge wanazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Serikali, ni vyema wakazingatia basi yale ambayo tunayazungumza. Ukitazama hili suala la maji haliko upinzani, haliko chama tawala, wote tunazungumza maji, maji, maji. Tunaomba basi tupate mikakati ya Serikali, angalau basi wawe wanatusikia na kutusikia ni pale wanapojibu yale tunayoyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia vyeti fake, kuna bili fake, sijui kama Waziri anajua. Kama maji hayapo lakini bili zinasoma, zinasomaje? Kwa hiyo, kipindi wenziwe wanazungumzia vyeti fake, yeye ajue kuna bili fake! Naomba aje hapa atuambie kama maji hayapo bili zinakujaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Mkoa wa Rukwa lazima wakae pamoja Wizara tatu, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Mazingira. Mkoa wa Rukwa hatujawahi kulia njaa hata mwaka mmoja lakini kinachotokea saa hizi kwa ajili ya kufurahishana, yaani anakuja mtu wa mazingira, wananchi wamelima mahindi, anawaambia wakate wamelima kwenye vyanzo vya maji. Ni kweli hatukubali kulima kwenye vyanzo vya maji lakini watuambieni Serikali wametenga eneo gani mbadala wananchi wakalime? Hatulimi bangi bali mazao ya chakula. Tunahitaji wakae pamoja waje na majibu ya kueleweka ya kuwasaidia Watanzania. Ni kweli wanaepusha vyanzo vya maji visiharibiwe lakini wanataka watu wafe na njaa? Waje watupe majibu ya uhakika Watanzania wa Rukwa wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimwambie kwa taarifa tu Mheshimiwa Waziri, mwaka jana tu wanawake 12 wamepoteza maisha kwa kufuata maji umbali mrefu. Leo tunazungumzia maji hayohayo tena tayari bajeti imepungua wakati maji bado hawajapata. Leo mimi nakujaje


namshangilia hapa Mheshimiwa Waziri wakati wanawake walionipigia kura wanapoteza maisha na bado hana mikakati yoyote ya kuonesha mazingira rafiki ya kuwasaidia maji. Tunaomba majibu ya kuridhisha ambayo yatawasaidia Watanzania.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huu tunazungumza kuna wanawake ambao wamefariki, kuna wanawake ambao wamebakwa, kuna wanawake ambao wameathirika kuhusiana na ndoa zao, kuna wanawake ambao wamepoteza mapato, huu muda wanaofuata maji wanashindwa kufanya biashara wanaanza kuhangaikia maji. Mheshimiwa Waziri tunaomba na Waziri anayehusika na upande wa watoto, Wizara ya Afya, hakuna kitu kitawezekana bila maji. Kwa hiyo, wanapokaa pamoja waangalie basi, maji ni kipaumbele hakuna mambo mengine. Nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa aliyemaliza amesema anaunga mkono hoja lakini amezungumzia suala la mahindi, mimi nasema mapema kwamba siwezi kuunga mkono hoja wakati wananchi wangu mahindi yanaoza yako nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbolea, tumezungumza suala la Mfumo wa Pamoja wa Kununua Mbolea, nataka nimwaambie Waziri na Wizara kwa ujumla kwamba, mfumo huu ume-fail, haujafanikiwa hata kidogo. Mkafanye tathmini upya juu ya ugawaji wa mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa Mkoa wangu wa Rukwa, juzi tulikuwa kwenye semina mkazungumzia Minjingu, yaani kwetu Minjingu tunaichukia kama ugonjwa wa UKIMWI. Imeleta umaskini kwa wakulima na imeleta shida kwa wakulima wetu. Kwa hiyo, kama lengo la Serikali ni kujenga viwanda, waiteni wawekezaji waje kuzalisha urea, waiteni wawekezaji ambao watakuja kuangalia hitaji la wakulima wanataka nini, Minjingu Mkoa wa Rukwa hatuihitaji, labda kama mtarudi kufanya maboresho ya mbolea hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la bei elekezi. Bei elekezi ni kizungumkuti tu. Mkoa wetu wa Rukwa mbolea imekuja kwa bei tofauti na ile ambayo ilikuwa imepangwa. Kwa hiyo, niseme tu kabla hamjatoa tamko lolote au kuzungumzia bei elekezi kama hamna uhakika muache kwanza mkafanye tafiti badala ya kuwaletea ugomvi wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi tamko la Serikali linatoka hapa la kuzuia kuuza mazao nje ya nchi, Sumbawanga Mjini bei ya gunia ilikuwa Sh.70,000, hivi ninavyozungumza leo gunia la mahindi Mkoa wa Rukwa ni Sh.18,000 mpaka Sh.24,000. Naomba niwaambie tu Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama mmeamua kwamba zao la mahindi halifai njooni na zao mbadala badala ya kuwafanya wakulima wawe maskini. Kama hamna zao mbadala muwaambie kwamba wao ni Watanzania au wanatoka nchi gani? Mbolea mnaleta kwa kuchelewa, yaani wakati tunahitaji mbolea za kupandia hamleti, wakati tunahitaji mazao yakue ndiyo mnaleta mbolea ya kupandia kwa hiyo mnakwenda vice versa tena kwa bei tofauti na ile ambayo mlikuwa mmepanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiambie Serikali, kama nia yetu ni kujenga viwanda, kama mnavyosema kauli mbiu ni kujenga viwanda, mambo yanayotendeka na Wizara ya Kilimo ni tofauti na kauli mbiu. Huwezi kujenga viwanda umeshindwa kutengeneza mazao ambayo unajua ndiyo ambayo yanakwenda kuzalisha hivyo viwanda vyenu mnavyovizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yanasikitisha sana. Leo unapozungumzia kilimo ambacho kinaajiri watu wengi kwenye Taifa hili ndiyo mmepeleka asilimia 18. Tunaomba Waziri utakapokuja hapa utuambie nini kilitokea mpaka mkapewa asilimia 18. Mkumbuke kwa kuwa, ninyi ndio mlizuia wananchi wasiuze mazao yao nje ya nchi yale mazao yao ya mwaka jana kwa sababu tunaenda kwenye msimu mwingine wa mavuno, ambayo ninyi ndio mlisababisha wao wakashindwa kuuza, mnayafanyaje? Mnayanunua au mnawaruhusu wapeleke sehemu nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kizungumkuti kidogo kwenye suala la mawakala. Bajeti ya 2015/2016 ilikuwa ni shilingi bilioni 35, kwenye chombo chao cha mawakala wanazungumza kwamba hilo ndiyo deni, lakini watu wenu kwenye Wizara wanasema ni shilingi bilioni 67 na ndiyo maana mpaka sasa hivi hamjawalipa mnaendelea kuhakiki. Sasa tunata Waziri atakapokuja atuambie ipi ni sahihi? Kwa sababu, kama bajeti ilikuwa shilingi bilioni 35 hiyo shilingi bilioni 67 imetoka wapi na hizo vocha zilitengenezwa kwa pesa gani? Zile vocha zilizorudi zimerudi kwa nani na kwa utaratibu gani? Waziri atakapokuja hapa atuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kutengeneza vocha zaidi ya bajeti ilivyotengwa, lazima uendane na bajeti. Kwa hiyo, kama kweli mna hakika mnashughulikia mafisadi tunataka uwazi wa jambo hili, ni kipi kati ya shilingi bilioni 35 na shilingi bilioni 67?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na umuhimu wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambayo inachangia pato kubwa kwa Taifa letu, kuna kila sababu ya kubadilisha utaratibu wa kuendesha Wizara hii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadilisha aina ya matangazo kutokana na hali ya ushindani ni mkubwa sana, ni vyema Serikali ikabadilisha utaratibu wa matangazo kwa vivutio vilivyopo nchini kwa kutumia njia kama shuleni, ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vikuu na vyuo vya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu ili kupata watalii wengi nchini kwa kutengeneza miundombinu ambayo itakuwa rafiki kwa watalii wanaokuja nchini ili kuongeza idadi ya watalii na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wananchi kulingana na migogoro ambayo inaendelea nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo Simanjiro ambao umechukua muda mrefu sana kupeleka mifugo na wananchi kuuawa, ni vyema migogoro hii ikamalizwa kwa wakati na bila kuathiri haki ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya hifadhi ichunguzwe upya kwani idadi ya watu imeongezeka lakini maeneo ya hifadhi pamoja na mapori tengefu wakati ardhi ni ile ile. Hivyo, nashauri Serikali kupitia upya mipaka hiyo ya maeneo ya hifadhi ili kuwatendea haki wananchi wanaoishi karibu na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na uzoefu na matatizo mengi yanayotokea katika maeneo ya hifadhaji ili utekelezaji wa yale waliyokubaliana yafikie malengo, suala la bajeti kufika kwa wakati kulingana na umuhimu wa Wizara hii ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi katika nchi yetu, ni vyema bajeti ikatolewa kama ilivyotengwa na kupitishwa na Bunge na iende kwa wakati.

Suala la kushirikiana na Wizara nyingine ambayo ni Wizara ya Ardhi, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ili kuweza kuwa na mkakati wa kudumu wa kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi na watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, manyanyaso kwa wananchi wanaopita katika hifadhi kulingana na hali iliyopo katika maeneo mbalimbali wanatakiwa kupewa elimu na siyo maamuzi na hatua kali zinazochukuliwa kwa mifugo na wananchi wetu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini pia ninampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo kwa kuendelea kulisaidia Taifa hili kwa kupitia taaluma yake na uzoefu wake ndani ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba hata kuna baadhi ya Wabunge hawajui majukumu ya Kamati ya Sheria Ndogo na hata kutamka hili neno unakuta mtu anasema sheria ndogo ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge linatunga sheria, lakini sheria inapotungwa na Bunge haiwezi kwenda kutumika bila kutungwa kanuni. Kanuni hizo zimekasimishwa kwenye taasisi kuanzia kwenye Halmashauri hasa kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tunapotunga sheria, sheria nyingine zinakuja zinapitishwa kwa haraka sana lakini kanuni zinachelewa zaidi na pamoja na kuchelewa zinakuja na makosa mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kanuni zikitungwa zikawa kinyume na sheria mama na tunaamini sheria mama ndiyo dira yetu ndiyo katiba tunayoitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilichangia hapa kuhusu suala la sheria ndogo kwenda kinyume na sheria mama na nikaomba Wizara ya TAMISEMI ambayo iko chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiyo inayoongoza kwa makosa na madudu mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa sehemu wamefanyia kazi lakini ningependa wajue kwamba tunapozungumza haya mambo tumefanya utafiti. Yawezekana suala la kubana matumizi limepelekea hasara kubwa sana. Hawa watu hawapewi semina elekezi na inapotokea sheria hizi zikawa zimeshaanza kutumika ndiyo tunakuja kugundua Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo sisi sio watunzi wa sheria, lakini makosa yanayokuja yanaanzia kwenye utunzi wa kanuni yenyewe na inakuwa tayari imeshaanza kutumika. Makosa haya mengine yanafanyika kwa makusudi na hili jambo limeongezeka zaidi kwenye awamu ya tano kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, ile tamaa ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanatunga kanuni mpaka wanakwenda kinyume na sheria mama. Sasa ningependa kuishauri Serikali, ni vyema, hasa Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Fedha waende kufanya utafiti upya. Aidha, wanasheria wetu uwezo wao ni mdogo au kuna watu wanawaendesha ina maana wanaacha taaluma zao wanafuata maagizo ya kutunga hizi kanuni ambazo zinakwenda kuwaathiri Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo kuwa na makosa ya kiundishi hii Sheria Ndogo mpaka ije ipite inakuwa imepitia kwenye hatua mbalimbali, hatuamini kwamba mpaka inaanza kutumika hawa watu wote hawajaona. Tungeomba Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali ifuatilie kwa kina, aidha, kuna kuna upungufu mkubwa wa waandishi wa sheria au hatuna kabisa au hakuna vigezo sahihi mnavyovitumia kuwapata hao waandishi wa sheria. Kama na huko mtaingiza siasa ndiyo hali inakuwa ngumu zaidi kwa sababu hizi sheria zinakwenda kuwaathiri Watanzania wa chini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo kutorejea kanuni sahihi; bado wanarudia makosa yale yale, kwa sababu mpaka ianze kutumika imepita hatua kadhaa; hawa watu wako wapi? Mbona hatujaona hatua kadhaa zikichukuliwa kama watu wengine wanavyochukuliwa makosa ambayo yanakuwa yanafanyika ni ya kawaida kabisa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutorejea jedwali sahihi, yaani hawa watu, inapita kwa mtu wa kwanza, mtu wa pili mpaka inaanza kutumika jedwali tu kwamba anarejea jedwali ambalo si sahihi na kile kitu anachokizungumzia. Hivi ni suala la kuja kujadili ndani ya Bunge, hayo ni mambo ambayo tunayafanya Sheria Ndogo sisi tunajeuka kuwa waandishi wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijasoma law nimesoma Community Development inabidi utumie akili nyingi kufikiri. Sasa Mwanasheria Mkuu utuambie, aidha na wewe umeshindwa kutimiza wajibu wako au ofisi yako inapwaya. Kwa sababu hizi sheria tunaposema hatuzungumzii kwa sababu Waziri kama sheria imepita hapa ndani ya Bunge yeye ana mamlaka ya kutunga kanuni; unatunga kanuni ambayo inakupa mamlaka zaidi na mpaka inaanza kutumika ina makosa mpaka tunarudi ndani ya Bunge tunazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri ni vema sasa kwa kuwa Bunge limekasimu mamlaka yake kwenye Kamati, kabla sheria hizi hazijaanza kutumika, hazijawa gazetted, sheria ikishatungwa kanuni ziletwe hapa mara moja baada ya kwamba sheria zimepita ili tuweze kupitia kanuni hizo kama zina usahihi na baadae ndiyo ziwe gazetted zianze kutumika kwa Watanzania kwa sababu zimewathiri Watanzania wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama kuna uharaka kiasi hicho, yaani manaleta tayari zimeshaathiri watu, kwa hiyo tunataka ziletwe kabla hazijaanza kutumika tuziangalie kama zimekwenda sawa sawa na sheria mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kanuni la Baraza la Sanaa la Taifa. Mheshimiwa Mwakyembe nafikiri hili jambo uliangalie vizuri. Hawa wasanii mnakuja kuwaangalia wakiwa wameshatumia nyingi ndiyo mnatunga kanuni ambazo wala hazieleweki. Wakati mwingine hili jambo linakuwa gumu kwa sababu ushirikishwaji wa wadau unakuwa mdogo na mkiwashirikisha mnawatafuta wale makada makada wale ambao wakija wanapitisha tu halafu baadae zikianza kuwaathiri ndiyo wanaanza kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu msanii ili afahamike kwamba ni msanii anatumia nguvu zake za ziada sana na hakuna mkakati wowote ambao wizara mmeuweka wasanii wale wa chini, ila ninyi kazi yenu ni kuandaa kanuni ambazo zinawafanya ninyi mkusanye pesa. Ni jinsi gani mnawasaidia hamna utaratibu wala mkakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara ya Habari kama nia yao ni kuinua vipaji na michezo vya watanzania, wasijikite kwenye kukusanya pesa na kuweka adhabu ambazo zitawazuia wao kukuza na kuondoa vipaji vyao kwa sababu kuna wakati mwingine tumeshuhudia huyu Diamond ni msanii mkubwa, kuna kanuni nyingine mnatunga kwamba anavyoenda kwenye tangazo alipie milioni tano. Kuna msanii wa hali ya chini kabisa, hiyo milioni tano anaitoa wapi ina maana mnamzuia yeye mnakwenda kumtafuta mtu ambaye tayari ameshafahamika na hao ndiyo watakuwa wanaendelea kukua kila siku, wale wa chini kabisa ni vigumu sana kuweza kuonesha vipaji vyao kwamba wao wanafahamika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tena Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumieni ofisi yenu vizuri. Kama shida ni fedha za kuwapa semina elekezi watendaji wenu huko chini, hali ilivyo kwenye Halmashauri ni mbaya sana. Kama Rais alikuja kuzungumza ndani ya Bunge kuhusu tozo, zile tozo kama hamjui tunawaambia tena kanuni zilizotungwa huko chini zinakwenda kinyume kabisa na yale aliyozungumza hapa ndani na wanaoathirika ni watanzania wa hali ya chini kabisa. Kwa hiyo, ni vyema mkafuatilia yale mnayoyazungumza na siyo kuzungumza kwa ajili ya kujiridhisha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa dakika tano ni chache sana kuna mambo nategemea Waziri atakuja kutoa ufafanuzi ili tuweze kuelewa. Unapozungumzia kukua kwa uchumi leo katika kilimo wakulima wa mahindi ambao mwaka jana waliweza kuuza mahindi yao gunia Sh.60,000 leo ni Sh.24,000. Kwa hiyo, unapozungumzia kukua kwa uchumi mtuambie umekua sehemu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika Taifa hili nimekaa nimefanya tafakari kubwa ni nani ana amani, mfanyakazi hana utulivu kwa sababu alitegemea sheria itamlinda kuongezeka kwa mshahara wake leo mshahara hauongezwi, mkulima hana amani kwenye Taifa hili, hali ya kilimo ni mbaya, njoo kwa wavuvi, njoo kwa wafanyabiashara, nani ana utulivu kwenye Taifa hili. Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ndiyo unaweza kumshauri Rais vizuri kama unaweza kusikiliza mawazo ya Wabunge tunayozungumza humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mfanyabiashara anajiona ni kama mkimbizi ndani ya Taifa lake. Ni kwa nini mmeshindwa kutengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ni kutoza kodi zisizokuwa na sababu. Leo TRA wanajua hali ya uchumi ni mbaya lakini wakiamua kufunga wanafunga, huwezi kukamua maziwa ng’ombe usiyemlisha, unategemea wao wanapata wapi pesa. Taifa hili tunategemea wakulima, wavuvi, wafanyakazi, leo watu hawa wote wako kwenye wakati mgumu Taifa tunaliendeshaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera ya kulinda uchumi wa Taifa. Tuliopo humu ndani siyo kwamba wote tumesoma uchumi tuko kwenye facult tofauti tofauti lakini ni pale ambapo unaweza kuchukua mawazo yetu ukaoanisha na taaluma yako kuweza kulipeleka Taifa mbele. Kama utachukua mawazo yako binafsi ndiyo haya tunarudi tena kuzungumza ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana kama mimi wana wakati mgumu kwenye Taifa hili, ajira ni shida, wamejiingiza kwenye kilimo, kilimo hicho ndiyo imekuwa taabani hili Taifa tunalipeleka wapi? Waziri wa Fedha ukisema uchumi unakua wewe ndiyo unayempotosha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hali ni mbaya kuliko hiki unachokiandika, hii hali ni nzuri kwa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ni lazima tuangalie hawa wafanyabiashara wanapolipa kodi wanategemea wayaone matokeo ya kodi wanayoilipa. Leo hakuna matokeo yoyote ambayo yanaweza yakawaletea tija na wao kujisukuma kuweza kulipa kodi. Leo wanaona ukiwa mfanyabiashara ni bora ukae nyumbani. Hili suala ambalo tunazungumza kwamba mfanyabiashara ukimuelimisha akajua umuhimu wa kodi na akayaona matokeo hakuna ugomvi utakaotokea kwa sababu faida ya kulipa kodi anaiona. Leo mnatumia nguvu kuliko kutumia busara na maarifa inatuweka kwenye wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili Taifa sio la Waziri wa Fedha ni Taifa la Watanzania, hiki unachokiandika unategemea kodi za Watanzania wakiwemo wakulima, wafanyakazi pamoja na wafanyabiashara. Ukijifungia mwenyewe ukaja na hizi takwimu unazozileta hapa zitaisha kwenye kitabu na haitakusaidia. Kwa sababu ulipoteuliwa na Rais aliamini ukija humu ndani utasikiliza mawazo ya Wabunge na sio mawazo yako. Haya mawazo tunayokwambia sisi kwamba unapozungumza hali ya uchumi umepima kwenye kipimo gani, ni kipimo gani ambacho umekitumia, wafanyakazi wanalia, wakulima wanalia, wafanyabiashara wanalia, wewe hizi takwimu unazipata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Bunge pia tuna wakati mgumu na ndiyo maana tunasema Mheshimiwa Waziri wa Fedha zungumza ukweli. Ni lazima mbadilishe approach na Taifa lolote makini linakuwa na vipaumbele na kipaumbele sio cha kwako ni kipaumbele ambacho kinawagusa Watanzania na maisha halisi ya watanzania. Leo ukienda kwenye uhalisia hiki ulichokiandika haujaonesha mkakati wowote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na elimu. Kulingana na umuhimu wa kuwa na viwanda nchini kwetu, ni lazima kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuanzisha viwanda na faida zitakazopatikana baada ya kuwa na viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuboresha kilimo. Kulingana na utaratibu wa viwanda ni vyema wananchi wakabadili utaratibu wa kilimo cha mazao na badala yake walime au kuanzisha kilimo chenye tija kwa ajili ya kuhudumia viwanda vitakavyokuwa vinazunguka maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na ajira kwa vijana. Ili suala la viwanda lifanikiwe ni vyema elimu ikatolewa zaidi kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa ambao watanufaika na viwanda badala ya kuchukuwa vijana wa nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha elimu ya viwanda mashuleni. Kulingana na umuhimu wa suala la kuanzisha viwanda ni vyema kama wanafunzi katika masomo wakawa na elimu au mada juu ya kuanzisha na kuendeleza viwanda nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwawezesha wakulima. Kwa kuwa viwanda vingi na kwa asilimia kubwa vinategemea kilimo na ili suala hili la viwanda lifanikiwe ni vema wanawake wakulima wawezeshwe kuanzisha viwanda hata kama ni vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda na mazao ya biashara. Ni vema Wizara ya Viwanda na Biashara kuwa na mkakati wa kudumu na endelevu kwa kuwa na viwanda bora vya kuandaa mazao ya biashara ili kilimo kiweze kuwakomboa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha vyuo vya VETA Mkoa wa Rukwa. Vyuo hivi vitasaidia vijana kupata ujuzi utakaosaidia kuendesha viwanda vitakavyoanzishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ni tatizo kubwa kwa wakulima hasa wa Mkoa wa Rukwa mpaka wanaelekea kukata tamaa kutokana na changamoto hii. Naomba Serikali ishughulikie suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ifufue viwanda vilivyokufa vya nguo, nyama, maji na kilimo (pembejeo).

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, bili ya maji. Kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba bili za maji ni tofauti na ilivyokuwa awali, pia hata kusoma wanakuwa wanakadiria tu na kupelekea kuleta hali ya sintofahamu kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mita za maji kuchezewa. Suala hili limekuwa ni tatizo na mambo haya yanafanywa na watumishi wenyewe wa Idara ya Maji au watu wanaokuwa wafanyakazi wa Ofisi za Idara ya Maji kwenye Halmashauri zetu na mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uharibifu wa vyanzo vya maji. Elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi wetu ili wajue athari za kuharibu vyanzo vya maji kwani hatuwezi kukomesha tatizo hilo bila kutoa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya maji ni mibaya. Suala hili linahitaji Wizara tatu kukaa kwa pamoja ili kuimarisha tatizo la maji katika Halmashauri zetu. Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya uvunaji maji ya mvua. Kumekuwa na matatizo sugu ya ukosefu wa maji katika Mkoa wa Rukwa wakati mvua zimenyesha na kusababisha mafuriko na kuua watu na maafa. Kwa nini Serikali isiwe na utaratibu wa kuhifadhi maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo, Mifugo na uvuvi na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kukaa pamoja na kupanga utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka vyanzo vya maji kulima mazao ambayo hayataathiri vyanzi vya maji na pia kutowaathiri wananchi kupata njaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa Idara ya Maji wasio waaminifu wamepelekea malalamiko makubwa kwa wananchi kwa kuwapa vifaa vibovu au kuchezea mita na kusababisha bili zisizo na uwiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji itengeneze mita kama ilivyo LUKU za umeme ili kuondoa malalamiko kwani kila mtu au mteja anajua amelipa kiasi gani na ametumia kiasi gani kumaliza kabisa malalamiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu. Ili kulinda vyanzo vya maji, wananchi wakielimishwa vizuri juu ya kulinda vyanzo vya maji matatizo mengi yataisha au kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa iliyotengwa ni ndogo iongezwe kulingana na umuhimu wa maji katika maeneo mengi nchini. Pesa iliyotengwa haiwezi kumaliza tatizo la maji nchini. Nashauri Serikali iongeze pesa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na nchi yetu kuwa na mahusianao na nchi mbalimbali duniani kuna kila sababu ya kuboresha maeneo muhimu ili kudumisha mahusiano makubwa na yenye manufaa kwa nchi yetu ikiwemo yafuatayo:-

Kwanza, kuunganisha soko la ndani ya nchi yetu na masoko ya nje kwa kufanya uboreshaji wa mazao yanayozalishwa nchini, kuyapandisha thamani ili yaweze kutumika nchi nyingine ambazo tuna uhusiano mzuri na nchi yetu, kupata manufaa kwa kupitia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kupeleka wanadiplomasia wenye uwezo. Kutokana na mazingira halisi ya nchi yetu ni vema wanadiplomasia nafasi zao zikawa na faida kwa nchi yetu, kwa kutumia uwezo wao kuchukua mambo ya nchi nyingine na kuyaleta nchini kwetu yalete manufaa. Kuwa na utaratibu wa kuunganisha Watanzania wanaoishi nchi za nje kulingana na kauli mbiu ya Awamu ya Tano, kauli mbiu ni viwanda ni vema Wizara hii ya mambo ya nje kuangalia ni jinsi gani watasaidia Taifa kuendana na kauli mbiu ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni namna gani Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kubeba ajenda ya utalii ili Taifa letu liweze kunufaika na watalii, endapo kama Wizara itaweza kutangaza na kubeba ajenda ya utalii ili kupata fedha za kigeni pamoja na kujenga uhusiano mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Watanzania wanaoajiriwa nje ya nchi hususan kazi za ndani, wamekuwa wakiuawa na kuteswa na kunyanyaswa ni vema Wizara ikawa na mipango endelevu ya kumaliza na kufuatilia kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi ni mdogo sana, Wizara ni vema pamoja na Mabalozi waweze kuangalia kwa ukaribu wanafunzi wote na kuwapa misaada ambayo inaweza kuwa ndani ya uwezo wao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ni kitu muhimu sana katika nchi yetu na dunia nzima kwani kila kiumbe kinachoishi duniani kiko chini ya ardhi ambapo kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zinaikabili Wizara hii ambayo ni lazima kuwepo na mikakati ya makusudi kumaliza changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji; suala hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi yetu ambayo imesababisha madhara makubwa sana ikiwemo vifo kwa wakulima na wafugaji na pia kwa wawekezaji hasa kama hakukuwa na ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mipaka, ni vyema Wizara ikawa na utaratibu madhubuti wa kupitia upya mipaka ya maeneo mbalimbali ikiwemo vijiji na vitongoji lakini maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji pamoja na maliasili zote ili kuondoa migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza katika maeneo yetu. Upatikanaji wa hati miliki, suala hili limekuwa na changamoto kubwa hasa kwa wananchi wa vijiji ambao makazi yao hayajapimwa, na kumekuwa na urasimu mkubwa kwa maafisa wa ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Mkuu wa Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Maafisa Ardhi kwenye Halmashauri ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga; nashauri Serikali kuongeza Maafisa Ardhi kwenye Halmashauri mbalimbali nchini ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima. Kutolewa mafunzo kwa Maafisa Ardhi na Maafisa Mipango Miji ili kuweka ufanisi katika maeneo na kazi zao ambao hazitaleta usumbufu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upimaji wa ardhi, suala hili limekuwa na changamoto kubwa, lakini linatokana pia na maafisa ambao sio waaminifu kwa kujipatia viwanja ambavyo Halmashauri na Serikali kwa ujumla hazinufaiki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati kuchukua muda mrefu na kupelekea mianya ya rushwa suala hili limekuwa likiwakatisha tamaa wananchi ambao hawana hati miliki. Nashauri Serikali kufuatilia suala hili kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba; kuna changamoto kubwa hasa kwa suala la gharama kwani gharama za nyumba zinazojengwa ni kubwa ambazo wananchi wakiwemo wa Mkoa wa Rukwa hawawezi kumudu kabisa nyumba zijengwe kulingana na jiografia husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wapewe ramani ili wayajue maeneo yao. Hii kwa kiasi kikubwa itachangia kuondoa migogoro isiyo na sababu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na kauli mbiu ya Serikali ya viwanda ni vyema tukaboresha Benki ya Kilimo na kuifikisha mikoani ili wakulima waweze kukopesheka ili waweze kujikomboa kimaisha na kufikia malengo ya viwanda katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu soko la uhakika la mazao, kutokana na nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wananchi ambao ni wakulima wamejikita kwenye kilimo cha mazao ya chakula na mazao ya biashara ambayo yamekosa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta binafsi, Serikali inapaswa kushirikisha sekta hii katika taratibu za kukuza uchumi katika nchi yetu ili waweze kuwa mfano na wengine waweze kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya maliasili na utalii, kulingana na umuhimu wa sekta hii ya utalii ni muhimu ikatazamwa kwa umakini mkubwa kwani tukiwekeza kwa kufanya tafiti za kutosha tutaweza kupata fedha nyingi za kigeni kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo ipewe kipaumbele katika shughuli zote za maendeleo kwa kuwawezesha wakulima kwa kuwapa pembejeo, mtaji na elimu ya kuachana na kilimo cha mazoea badala yake kiwe cha kisasa. Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Serikali ijielekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuelekea kwenye nchi ya viwanda kuepuka kilimo cha msimu ambacho hakitabiriki na kinaweza kisifikie malengo ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya madini, kulingana na umuhimu wa viwanda ni vyema Serikali ikawekeza kwenye utafiti ili wanavyuo wanapomaliza masomo yao waweze kusaidia Taifa la Tanzania kwa upande wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Deni la Taifa, ni vyema kama Taifa tukawa na utaratibu wa kukopa mikopo ambayo haiwezi kuwatesa Watanzania wote. Tutaweza kuepuka kero hiyo kwa kukopa kwa wazabuni wa ndani ambayo haitakuwa na kero kubwa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo kulingana na changamoto hii, imekuwa ikiwaathiri wakulima wengi kulingana na changamoto ya bei ya pembejeo yenyewe, upatikanaji wake, kwani suala hili linawaathiri sana wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha umwagiliaji; pesa nyingi zimepotea katika mabwawa. Suala hili haliwezi kufanikiwa, kwa sababu bado ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti ni muhimu sana ili tuweze kuinua kilimo chetu kuwa chenye tija kwa kuwa utakuwa umefanyika utafiti kuwa wapi panafaa na panafaa kwa kilimo gani katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la soko limekuwa changamoto kubwa kwa wakulima wengi nchini ikiwemo watu wa Mkoa wa Rukwa ambao wanalima mazao ya chakula, lakini Serikali ilitoa tamko au katazo juu ya wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi wakati huo Serikali imeshindwa kuwatafutia soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa bei elekezi kwa mbolea zinazopelekwa mikoani ikiwemo Mkoa wa Rukwa. Suala hili limeshindwa kutekelezeka kwani suala la barabara limekuwa linachangia bei elekezi, haitawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na uzoefu ambao tumekuwa nao, suala la wakulima wetu kusubiri msimu wa kilimo, ni vyema Serikali ikajenga mazingira rafiki kwa wakulima kuwa na kilimo cha umwagiliaji.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu; kwa sasa elimu yetu nchini imekuwa ni bure kuanzia ngazi ya msingi na sekondari. Suala hili limekuwa na mkanganyiko mkubwa kwani mapokeo ya wananchi wanajua kwa sasa hakuna mchango wowote ambao wanatakiwa kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Walimu kupandishwa, ni utaratibu tuliozoea katika nchi yetu Mwalimu anapojiendeleza anategemea kupandishwa daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vyuo, kuna baadhi ya mikoa haina chuo hata kimoja katika kozi mbalimbali kitu ambacho kinakuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wanaohitimu katika maeneo mbalimbali. Ushauri wangu kwa Serikali kuhakikisha vyuo vinajengwa kwenye mikoa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Walimu, jambo hili limekuwa changamoto sana kwa Walimu wetu. Jambo hili ni hatari kwani sote tunatambua ualimu ni karama hivyo kutapelekea matokeo mabaya katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukariri madarasa, jambo hili ni vizuri Serikali ikafanya tafiti za kutosha kabla haijazuia kwani suala hili lina athari kubwa sana kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Wauguzi; baada ya Serikali kuja na suala la vyeti feki kumebaki na upungufu mkubwa wa nafasi mbalimbali katika hospitali nyingi nchini kwani jambo hili ni hatari sana kwa kitengo hiki muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi wa mpango; suala hili limekuwa na changamoto kwani elimu kwa watu wa vijijini bado haijatolewa kikamilifu, lakini pia Serikali ifanye tafiti juu ya baadhi ya njia za uzazi kwani zinalalamikiwa sana kuwa zinaleta madhara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti inayopitishwa na Bunge ipelekwe kwenye maeneo husika na muda muafaka ili kuondoa changamoto wanazokutana nazo wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hasa maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na ongezeko kubwa la watoto wa mtaani Serikali iongeze maeneo ambayo watu watapewa msaada pale inapobidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapungufu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zetu ni jambo ambalo limekuwa changamoto katika huduma mbalimbali za kijamii kulingana na uchache wa watumishi katika maeneo mbalimbali nchini. Pia upungufu wa Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa katika Mkoa wa Rukwa na hospitali hii inazidiwa na wagonjwa kwa kuwa hatuna Hospitali ya Wilaya hata moja katika Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu dirisha maalum kwa ajili ya wazee; hospitali nyingi hazina dirisha maalum kwa ajili ya wazee na maeneo ambayo wamejitahidi kuweka dirisha kwa ajili ya wazee hakuna huduma. Nashauri Serikali kufatilia suala hili kwani wazee wetu wanapata taabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu afya ya akili; Serikali iwekeze kwenye utafiti kujua nini kinasababisha suala hili kuendelea kwani idadi ya waathirika wa akili inazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Serikali ikawekeza kwenye lishe kwani tusipowekeza kwenye lishe tunakwenda kuzalisha watoto wenye udumavu wa akili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Rukwa tunategemea Uwanja wa Sumbawanga Mjini kwa ajili ya usafiri wa anga ambao umefanyiwa uthamini lakini mpaka sasa hatujui kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Nkasi, Makao Makuu ya Wilaya ambayo yako Namanyere, tunaomba maboresho makubwa ili wananchi wake wanufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara ya Ntendo – Muze ni barabara muhimu sana kwani ikiboreshwa itawasaidia wananchi wa maeneo hayo wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo na kuwainua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bomoa bomoa inawaacha wananchi wengi wanaathirika na sheria iliyopo ambayo inazungumzia mita 15 kwa mjini na mita 30 kwa vijijini. Tunaomba sheria hii iletwe ndani ya Bunge ifanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kala haina mawasiliano kabisa pamoja na Kata ya Ninde bado mawasiliano yake siyo ya uhakika. Naomba Serikali ipeleke mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TARURA wapewe fedha za kutosha ili waweze kufanya kazi zao kwa haraka na uhakika. Pesa zikipelekwa kwa muda muafaka itaepusha madhara ambayo yanajitokeza kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zinazounganisha mikoa zipewe kipaumbele ili kuleta baraka kwa wananchi kwa kuwainua kiuchumi, lakini kuepusha vifo vya wanawake na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya Ziwa Tanganyika (MV Liemba) imekuwa ya muda mrefu ambayo hata ikifanyiwa matengenezo bado imechakaa. Naishauri Serikali kutafuta meli nyingine mpya ambayo itawasaidia Watanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanja vya michezo. Viwanja vya michezo vingi katika halmashauri mbalimbali hali yake ni mbaya sana, ili kuboresha michezo ni lazima tuboreshe viwanja vyetu katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukuza vipaji kuanzia shuleni ili tuwe na matokeo chanya ni lazima tuwekeze kwa watoto wadogo hasa kuandaliwe syllabus maalum zitakazowajenga wanafunzi wakiwa mashuleni ili kuwakuza kulingana na vipaji walivyonavyo ili kulisaidia Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vazi la Taifa. Kulingana na umuhimu wa jambo hili ni vyema suala la Vazi la Taifa lipewe kipaumbele kwani kutokuwa na Vazi la Taifa ni vigumu kumhukumu kwa kosa la mavazi, sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suala la Kufungia Magazeti; jambo hili liangaliwe upya kwani magazeti yanasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii. Naiomba Serikali ibadilishe utaratibu, badala ya kufungia gazeti apewe adhabu Mhariri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasanii kufungiwa wakati nyimbo tayari zimepigwa kwenye redio na TV, jambo hili si sawa kwani huwezi kufuta wakati wimbo huo unakuwa umesambaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo irejeshwe mashuleni, UMISETA na UMITASHUMTA miaka iliyopita vyombo hivi vilichangia sana kukuza michezo na kuibua vipaji vingi kwa wanafunzi wetu shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya michezo ifanyiwe marekebisho ili kuleta ufanisi katika michezo nchini kwani tumekuwa tukifanya vibaya mara kwa mara katika Taifa letu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kuongelea kuhusu upungufu wa walimu wa sayansi. Suala hili limekuwa ni changamoto katika maeneo mengi nchini kwani mpaka sasa idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ni tofauti na wanafunzi wanaosoma masomo ya sanaa. Hivyo, Wizara ichukue jambo hili na kulifanyia kazi ili tuweze kumaliza tatizo hilo la walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni nizungumzie shule binafsi. Kulingana na mchango wa shule binafsi katika Serikali suala hili liangaliwe kwa kupunguza kero zile zinazowafanya watu wa shule binafsi wavunjike moyo ili kuboresha elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni suala la elimu bure. Naomba suala hili liangaliwe upya kwani kuna changamoto ambazo zinaikabili sekta ya elimu ikiwemo kutopeleka pesa shuleni jambo ambalo linawakwamisha kufanya mambo ya msingi ambayo wamejipangia kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu madai ya walimu. Ili tuwe na matokeo chanya ni lazima kuwe na mazingira rafiki kwa walimu pamoja na wanafunzi. Madai ya walimu yamekuwa ya muda mrefu ambayo kwa sasa yanawaathiri wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, walimu wa sekondari kupelekwa kufundisha shule za msingi. Suala hili halijawahi kutokea katika nchi yetu na linaweza kuathiri wanafunzi kwani wanafunzi wa shule ya msingi wanahitaji kujengewa msingi na walimu wenye level hiyo.

Suala la sita ni upungufu wa vitabu. Kulingana na umuhimu wa vitabu katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi, Wizara iweke kipaumbele kununua vitabu na vitabu viandaliwe kwa ubora ili wanafunzi wapewe elimu sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, kiandaliwe chombo maalum kwa ajili ya kusimamia elimu ili kuleta tija. Jambo

hili likisimamiwa vyema litaleta matokeo chanya kwa Wizara ya Elimu na itakuwa rahisi kumaliza matatizo yanayoikabili Wizara kwani watakuwa wanatembelea na kujua matatizo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na uchakavu miundombinu. Kulingana na miradi mingi ya umwagiliaji kutekelezwa ikiwa chini ya kiwango na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na kuwa chanzo cha upotevu wa pesa za wananchi wanaolipa kodi halafu zinaliwa na watu wachache ambao Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu wale wote waliochukua na kutumia pesa za walipa kodi wa nchi hii.

Miundombinu ya maji imekuwa changamoto kubwa na kusababisha upotevu mkubwa wa maji pale ambapo inatokea mabomba kupasuka na kusababisha upotevu mkubwa wa maji katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali inapaswa kulitafutia ufumbuzi ili kumaliza suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi nyingi kuendelea kudaiwa na kusababisha maumivu makali kwa Watanzania ambapo wanaotakiwa kulipa ni Serikali. Inapochelewa kulipa madeni hayo kwani kunakuwa na ubaguzi kwani wananchi wa kawaida wasipolipa bili japo ya mwezi mmoja wanakatiwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutumia Ziwa Tanganyika hususan kusambaza maji katika mikoa inayozunguka Ziwa Tanganyika, suala hili likikamilika litasaidia kumaliza changamoto zinazokabili mikoa ya Rukwa, Kigoma, Katavi kwani wananchi wakitumia ziwa hilo ambalo litakuwa la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bili hewa, kumekuwa na utaratibu mbovu sana wa bili za maji kuja wakati maji hayatoki. Hizi mita zinakuwa na shida au watu wote walipe madeni ambayo ni halali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tafsiri na upotoshaji wa maana halisi ya viwanda vidogo. Tunaomba kupata tafsiri sahihi, maana ya viwanda na aina ya viwanda vinavyozungumziwa na Wizara husika ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yana viwanda vingi na kuna maeneo ambayo hayana viwanda kabisa. Napenda kujua kigezo kinachotumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wawekezaji kukata tamaa ni vyema likaangaliwa upya kuhusiana na mazingira ya wawekezaji ili kukuza uchumi wetu. Aidha, ni vyema kama Taifa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wetu wanaotaka kuwekeza nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema umeme uwe na uhakika ili kuendesha viwanda na kuwapa wawekezaji nchini kuwa na uhakika na uwekezaji wao kwa kuwa kila mtu anawekeza ili apate faida, inapotokea changamoto ya umeme na maji wawekezaji wanaweza kukata tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa kiwanda cha dawa ni muhimu sana kwani kukiwa na viwanda vingi vinavyozalisha dawa za binadamu kutasaidia Taifa na wananchi wa kawaida kwani bei itakuwa nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kuanzisha Kiwanda cha Mbolea. Mbolea inahitajika sana nchini lakini kumekuwa na changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kutolewa semina elekezi kwa wafanyabiashara na TRA juu ya kulipa kodi badala ya hii hali ambayo inajitokeza sasa kwa kuonekana uadui mkubwa kati ya wafanyabiashara na TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya sasa kiuchumi katika nchi yetu ni tete mno hasa kwa wananchi wa chini kabisa. Ni vyema kukawa na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wafanyabiashara kuhama kutokana na changamoto wanazokutana nazo Serikali iweke utaratibu mpya utakaosaidia wafanyabiashara wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi haramu, jambo hili ni vyema likatolewa tafsiri sahihi vifaa ndio haramu au watu ambao ndio wavuvi ndio haramu kulingana na mkanganyiko uliopo katika maeneo mengi nchini na suala la kukomesha lifuate taratibu, sheria na haki za binadamu.

Mheshimiwa Spika, suala la kuchomea wavuvi nyavu; utaratibu wa kutokomeza uvuvi haramu muafaka wake sio kuchoma nyavu kwani kwa kuchoma nyavu ni kusababisha wavuvi kupata umaskini pia jambo hili linatakiwa kudhibitiwa viwandani na sio ziwani au bandarini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tozo za kero kwa wavuvi, ni vyema Serikali ikapitia tozo zote ambazo ni kero kwa wavuvi wetu kwani suala la uvuvi nalo linachangia pato la Taifa letu na pia kupata kitoweo kwa wananchi wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, suala la utaratibu mbovu wa kusafirisha mifugo, kulingana na changamoto wanazokutana nazo wafugaji, mfugaji anapokuwa anatoa na kupeleka mifugo yake mnadani hata kama ni wachache wanamtaka kusafirishwa kwa gari (lori sio sawa).

Mheshimiwa Spika, leseni ya wavuvi itolewe moja kwa moja kwa kila ziwa au bahari. Jambo hili limekuwa na changamoto kwa wavuvi kwani kwa sasa leseni zinatolewa kwa kila Halmashauri jambo ambalo ni gumu kwani samaki wanahama kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine.

Mheshimiwa Spika, suala la operation zinazoendelea zinaleta madhara makubwa sana kwani haifuati haki za binadamu, haki za wanyama pamoja na kupeleka migogoro.

Mheshimiwa Spika, mifugo mingi inayokamatwa haipewi matunzo mazuri kama vile chakula na maeneo ya kutunzia inakuwa sio rafiki na kusababisha mifugo hiyo kufa na kusababisha maumivu kwa mfugaji.

Mheshimiwa Spika, kutopelekwa kwa pesa ya maendeleo, hakuna shughuli yoyote inaweza kufanyika bila kupeleka fedha iliyotengwa kwenye eneo husika ili kazi ilivyokuwa imetengwa ikienda kwa wakati ni rahisi kumaliza changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, nashauri kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ili kuondokana na migogoro iliyopo katika nchi yetu.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, mipaka inayozunguka hifadhi ipitiwe upya. Kulingana na idadi ya watu kuongezeka nchini kumekuwa na muingiliano mkubwa sana kati ya wananchi na wanyama na kupelekea mahusiano mabaya kati ya wananchi wanaozunguka hifadhi na watumishi wanaohusika na kuhifadhi wanyamapori. Nashauri Serikali kupitia upya mipaka yake ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Spika, sheria ya fidia ibadilishwe, suala hili limekuwa na malalamiko makubwa kwa wananchi pale inapotokea mtu au watu kuuawa, kujeruhiwa au mazao, makazi ya wananchi kuharibiwa, fidia au kifuta jasho haviendani na adhabu inayotolewa kwa mtu au watu wanapokamatwa wakiwa wameua mnyama au wanyama.

Mheshimiwa Spika, kuwekwe mazingira rafiki kwa wawekezaji, kumekuwa na changamoto za wawekezaji waliopo na wanaotaka kuja kuwekeza nchini kwetu. Kwa kuwa Taifa letu tunategemea utalii kukusanya na kupata pesa za kigeni ni vema kama Wizara kukawekwa mkakati wa makusudi utakaokuwa rafiki kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kuja.

Mheshimiwa Spika, tozo na malipo kwa watalii ziangaliwe upya ili kuleta tija kwa Taifa letu kwa kuangalia tozo zote zenye kero ambazo zinaweza kufanya watalii wetu wakaweza kushindwa kuja kutalii na kusababisha Taifa letu kukosa mapato na kupeleka nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, suala la ugawaji vitalu, kumekuwa na malalamiko mengi kwa wananchi wanapokuwa wanataka kumiliki vitalu kwa kufuata taratibu na sheria tulizojiwekea, kumekuwa na ukiritimba mkubwa na kupelekea mianya ya rushwa na kufanya waone kuwa wageni wanapewa nafasi kubwa kuliko wageni wenyeji.

Mheshimiwa Spika, huduma za kijamii ziboreshwe kwa vijiji vinavyozunguka au karibu na hifadhi. Kumekuwa na changamoto kwa wananchi wanazunguka hifadhi ili kulinda wanyama hasa pale ambapo wananchi wanafuata huduma za maji na vitoweo mbali. Nashauri Wizara kuweka utaratibu mbadala wanapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara itoe elimu kwa maeneo yanayokuwa karibu na hifadhi ili kujua umuhimu wa uhifadhi na wao wananchi wajue kuwa wao ni walinzi wa kwanza kuliko ilivyo sasa wanavyojiona kama wanyonge.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mazingira na Wizara ya Maliasili na Utalii kuna umuhimu wa kukaa pamoja ili kupitia suala la mipaka na shughuli za binadamu, kwa kuwa Serikali ni moja endapo kama mtakaa pamoja mtamaliza tatizo hilo kwa umakini.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kubadilisha kutangaza vivutio vyetu ubadilishwe kwani utaratibu unaotumika kwa sasa haujaleta matokeo makubwa na ya haraka kwa Taifa letu kulingana na faida wanazozipata nchi nyingine zinazotuzunguka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, usalama wa Watanzania wanaoishi nchi za nje, suala hili limekuwa na changamoto kubwa sana kwa Watanzania wenzetu wanaojishughulisha na mambo mbalimbali ikiwemo kutafuta kazi za ndani na masuala mbalimbali yanayohusiana na biashara. Wanapopata matatizo wanaobeba jukumu ni ndugu zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutumia diplomasia kwa wafungwa kwenye magereza zilizopo nje ya nchi kuwaomba waje watumikie kifungo kwenye nchi yao kwa maana ya Tanzania ili kuendelea kujenga ushirikiano mzuri. Kutumia balozi zetu kunufaisha Taifa letu. Serikali ifuatilie kwa karibu utendaji wa Mabalozi na kuwapa semina elekezi kwa kutazama uhitaji wa Taifa letu kwa wakati huo na kuwakumbusha wajibu wao ili Taifa letu liweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la diplomasia ya uchumi; jambo hili ni vyema likapewa kipaumbele kwa kuwa Taifa letu bado linakua na kujenga ukaribu kwa mataifa ambayo ni marafiki zetu ili kukuza uchumi wa Taifa letu. Kutumia diplomasia Serikali itumie fursa hiyo kutafuta masoko ya mazao ya biashara. Suala hili halijatunufaisha kama Taifa kuwa na manufaa ni pale ambapo tutatumia nafasi hiyo inapotokea na ziada ya kutosha na tukawa na ziada.

Mheshimiwa Naibu Spika, lugha ya Kiswahili, suala hili tumelizungumza sana, nashauri Serikali kupitia diplomasia kushawishi nchi marafiki kutumia lugha ya Kiswahili ambayo itasaidia kwa Taifa letu kwa wakufunzi ambao watakuwa Watanzania na kama Taifa tutanufaika kwa kupata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutumia Ziwa Tanganyika, Victoria na Ziwa Nyasa kwa kuwa mazingira haya kushirikiana katika uvuvi ni vyema kama Taifa tukawa na uvuvi wa kisasa utakaoleta tija kwa Taifa letu badala ya kuchoma nyavu zetu za wavuvi. Kutumia Watanzania wanaoishi nje ya nchi kunufaisha Taifa letu. Tukiwatumia vizuri Watanzania hawa katika biashara na katika elimu tutapata manufaa makubwa hasa pale ambapo na wao watatambua kuwa Taifa linatambua uwepo wao kule waliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, waliopelekwa kusoma nje ya nchi, Serikali kupitia ubalozi watumie nafasi zao kushawishi na kuomba wanafunzi hawa kupunguziwa ada au kufutiwa kabisa ili kuwatia moyo wazazi na walezi ambao wamejitolea kuwapeleka watoto au ndugu kusoma nje ya nchi kwani ni kwa manufaa ya nchi nzima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali ya usalama nchini; kwa sasa hali ya usalama wa nchi yetu siyo salama sana, kumekuwa na matukio ambayo hatukuyazoea nchini kwetu, ambayo ni watu kupotea, watu kutekwa na kuuawa. Wananchi wameingia taharuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuhoji uraia wa watu wanapoipinga Serikali, jambo hili linaleta sintofahamu kabisa haijawahi kutokea toka tawala mbalimbali zilizopita, jambo hili halikubaliki kwani linajenga hofu miongoni mwa Watanzania ambao wanatumia haki yao ya Kikatiba kutoa maoni yao kulingana na mwenendo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasiojulikana jambo hili limekuwa kama kichaka cha wahalifu kujificha kwani kuna matukio yamejitokeza hivi karibuni ambayo wahusika hawajatambulika na ndiyo wanapewa majina hayo ya watu wasiojulikana, ni vema Wizara ya Mambo ya Ndani wakatueleza hawa ni watu gani, wako wapi na wanafadhiliwa na nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya Polisi katika Mkoa wa Rukwa; kuna ujenzi wa vituo vya Polisi katika Jimbo la Kwela, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini. Kama Mbunge nimetembelea vituo hivyo, Serikali nayo itimize wajibu wake kwani wananchi wamechanga mpaka lenta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Polisi kubambikizia watu kesi ni jambo ambalo linaondoa weledi kwa Jeshi la Polisi na mambo hayo yanafanywa na baadhi ya askari wasio waaminifu; ni wajibu wa Wizara kulitazama jambo hili kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuondolewa kwa kanuni ambazo ni kandamizi kwa Polisi hasa wadogo wasiokuwa na nafasi zozote katika Jeshi kwani wanafukuzwa hovyo jambo ambalo linaweza kuongeza wahalifu mitaani, kwani watu hawa wanakuwa hawana kazi mtaani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu watu kuteswa wanapokamatwa na na Polisi kabla Mahakama haijasema kama mtu huyo ana kesi ya kujibu au la. Je, nikifungu gani cha sheria kinachompa Askari Polisi haki ya kumpiga mtuhumiwa na kumtesa kabla ya Mahakama kuamua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kubambikiziwa kesi. Hivi sasa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wanabambikiziwa kesi na hawapelekwi Mahakamani kwa wakati. Je, kwa kufanya hivi siyo kuvunja sheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto kubwa katika ujenzi waMahakama katika Wilaya mbalimbali nchini. Jambo hili linapelekea wananchi wengi kuanza kutumikia kifungo kabla ya kufikishwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki ya kupata taarifa. Sheria iliyotungwa imepelekea maumivu makali kwaWatanzania. Kupata habari/taarifa ni haki yao ya msingi wakati wote watakaohitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndoa za utotoni. Sheria inayoruhusu ndoa za utotoni imekuwa kandamizi kwa wananchi wa Tanzania kwani kwa kiasi kikubwa kwa sasa inatumika vibaya kukandamiza watoto wa kike na kuzima ndoto zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya mikataba mibovu tunayoingia. Suala hili la kuingia mikataba mibovu inapelekea Taifa kuingia kwenye hasara kubwa na kupelekea umaskini kwa uzembe kwa kutopitia mikataba hii vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa Mahakimu kuanzia Mahakama ya Mwanzo. Kulingana na kazi wanazofanya za kuhukumu watu ni vyema jambo hili likaangaliwa upya kwani watu hawa wanahitaji ulinzi wakiwa kazini na nje ya kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nianze na hoja ya uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea naomba niweke record sawa kwamba Tanzania Daima imefungiwa mara kadhaa na kupewa onyo mara kadhaa. Tunachotaka, Serikali isikae upande mmoja. Tunapokuwa tunalalamika ndani ya Bunge, tunategemea Serikali itachukua maoni yetu na kuyafanyia kazi. Watu wanapoitwa ni hatari; na vyombo vya habari vinasomwa na watu wengi. Tunategemea Serikali aidha ichukue hatua inayowezekana kama ilivyochukua hatua kwenye vyombo vingine vya habari ikiwepo Gazeti la Tanzania Daima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la uhuru wa vyombo vya habari tunategemea Serikali ije na mkakati wa kuweza kuwalinda hawa wenye vyombo vya habari pamoja na Waandishi wa Habari. Mpaka nasimama hapa kuzungumza, kuna Mwandishi wa Habari ambaye mpaka leo yamekuwa malalamiko ya Waandishi wa Habari wenyewe pamoja na sisi Wabunge na wananchi wengine. Azori mpaka leo hatujasikia Serikali inasema nini juu ya huyu Mwandishi wa Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania wana haki ya kupata habari kwa mujibu wa Katiba yetu, lakini Waandishi wa Habari wana haki ya kutoa habari. Ni lazima tujue hapa ni kweli kwamba uhuru wa habari una mipaka yake, lakini hiyo mipaka isiwe pale ambapo Serikali inatakiwa kukosolewa. Serikali lazima ikosolewe. Ni kweli lazima kuwe na mipaka kwa sababu kila kitu kikipita kiasi ni sumu. Waandishi wa Habari wanahitaji ulinzi. Sasa hivi wanatishwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, anaweza akaja Mwandishi wa Habari kwamba tunaomba azungumzie utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano. Anapoanza kuzungumza, anakwambia aah, hayo siwezi kutoa kabisa. Sasa umeniruhusu nitoe mawazo yangu; hili suala litaleta shida sana kwa sababu, Waandishi wa Habari wanaweza kutoa habari kwenye chanzo chochote. Sasa kama watawekewa mipaka na vitisho, sidhani kama tutalisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tumetoka kwenye hali ambayo sasa tunaamini kwamba ni Taifa huru na uhuru wenyewe ni pamoja na Waandishi wa Habari kuwa huru kutoa kile ambacho wanaona kinastahili kutolewa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni BASATA. BASATA majukumu yao ni pamoja na kukuza wasanii wetu, lakini tunaona sasa majukumu ya BASATA yamebadilika. Wasanii hawa wanapokuwa wanaanza kule chini, jukumu la BASATA ni kuhakikisha wanakuza vipaji vyao, lakini leo tunaona wanaanza kuwafungia wasanii. Huyu msanii mpaka anaanza kutambulika na Taifa huko chini ana mikakati aliyojiwekea.

Mheshimiwa Spika, napenda nijue Serikali ina mkakati gani wa kuweza kukuza vipaji vya vijana wetu? Siyo wanakuja kuwatambua pale ambapo sasa ana uwezo wa kulisaidia Taifa kwa pesa zake kwenda nje. Kwa sababu sasa hivi kama msaanii anataka kwenda nje ya nchi lazima atoe taarifa kwa BASATA, lakini BASATA mbona hawajaja na mkakati wa kuwasaidia kuwatafutia huko nje; aidha kuwaunganisha na network ya wasaanii wengine ambao wako nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunategemea chombo hiki kiwasaidie na siyo kuwakandamiza. Jambo lingine ni viwanja vya michezo. Tunatambua kuna viwanja vingi ambavyo vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi, sitataka kuhoji sana kwa nini wanamiliki viwanja hivi, lakini nilizungumza Bunge lililopita kama wameamua kuvimiliki waviboreshe. Kuvimiliki tu halafu mkashindwa kuviboresha sidhani kama mnawasaidia Watanzania, kwa sababu viwanja hivi vingine kabla, tulipokuwa kwenye mfumo wa chama kimoja vilikuwa vinaendeshwa na Watanzania wote siyo Chama cha Mapinduzi peke yake. Sawa, mmevichukua, tunaomba basi mviboreshe ili viweze kuwasaidia vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kujua, tunapokuwa tunazungumzia mara nyingi hapa, Wizara imekuwa inaleta watu tunawapongeza waliofanya vizuri, ikiwemo Taifa Stars. Taifa Stars ilifanya vizuri na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akatoa promotion ya pombe ambayo iliuzwa nusu bei.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri, labda inawezekana tunatafuta njia nyingine ya kuweza kuwasaidia vijana wetu, lakini sidhani kama ile njia ilikuwa sahihi sana. Kwa nini Wizara isije na mkakati; na hamuwezi kuja na mkakati kama hamjajua kwa nini tunashindwa. Kama wameshinda, Serikali ije sasa na mkakati, siyo wa nusu bei ya pombe kwa sababu watu walilewa na sidhani kama ilisaidia mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, sasa sidhani kama huo ni mkakati wa Wizara au ni yeye tu alikuja na ile style na hamjasema chochote mpaka leo. Kama itakuwa hivyo, basi tujue kama ni style ya Awamu ya Tano kwamba watakuwa wanawapa nusu bei ili vijana wetu waweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena kusisitiza, Serikali makini haiogopi kukosolewa. Naamini kuna mambo mazuri yanafanyika, sasa ili yaonekane ni mazuri lazima waruhusu mawazo ya watu wengine waseme. Hamwezi kufanya wenyewe, mnataka kujipongeza wenyewe, lakini anayetaka kukosoa haruhusiwi. Inajenga tafsiri ambayo siyo nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie amejipangaje kuweza kuwalinda wamiliki wa vyombo vya habari, pamoja na waandishi wa habari. Ni namna gani hawa watu wanalindwa? Kwa sababu, hivi vitisho vimekuwa vingi sana.

Mheshimiwa Spika, mwandishi mwenzao wa habari, Serikali inasema nini? Imefikia wapi mpaka leo? Huyu mtu yuko wapi? Lazima Serikali iseme, kunyamaza kimya mnawafanya watu wanakuwa na sintofahamu. Wao hawawezi kusema, sisi ambao tupo kwa niaba yao lazima tuseme.

Mheshimiwa Spika, umezungumza vizuri kipindi anazungumza Mheshimiwa Mwakajoka. Narudia kusema ni vizuri kama sheria inafuatwa kwenye vyombo vya habari, wasiangalie baadhi ya vyombo vya habari. Hili jambo la kutaja watu hadharani kwamba hawa watu ni hatari, kuna mambo mpaka ya ushoga yameandikwa kwenye magazeti.

Mheshimiwa Spika, kuna viongozi ambao wameaminiwa na watu, ni vizuri Serikali ije iweke sawa jambo hili. Kama kweli kuna watu wanafanya mambo hayo, sheria iko wazi, kwa nini wasipelekwe huko kwenye vyombo vya sheria ili sheria ikatafsiri kwamba huyu mtu anafanya kosa la ushoga? Sheria iko wazi, kwa nini chombo hiki kinaandika na Serikali inakaa kimya. Je, tuamini kwamba ni kweli Serikali imepeleka hayo mawazo ili gazeti liandike? Kama sivyo, Serikali isimame hapa itoe maamuzi juu ya chombo hiki. Ukisema hawa watu ni hatari, uhatari wake uko wapi? Umewataja majina na picha zao ziko pale.

Mheshimiwa Spika, wengine ni viongozi ambao tunawaamini, wanaongoza watu wengi ambao wako huko nje. Vinapotokea vitu kama hivi, hatari siyo mpaka mwone watu wanaandamana. Ukiona watu wanasema wengine wanaandamana mioyoni.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri huo mwongozo uliotoa ukautoa na kwenye Wizara. Haya malalamiko ya kila siku, hili gazeti ni la nani? Linasukumwa na nani? Nani yuko nyuma ya chombo hiki cha habari? Kama kuna ukweli, hatua zichukuliwe siyo kunyamaza kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru japo kwa dakika chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo tunazungumzia kiungo kikubwa sana ndani ya taifa. Nitapenda kuchangia vyuo vya utafiti. Hakuna maendeleo ya kilimo kama hatujapeleka fedha na vyuo vya utafiti kuwekwa kipaumbele. Naomba nishauri tu Wizara ya Kilimo, kwamba, kama hamna kipaumbele kipaumbele cha kwanza kwenye Wizara yenu iwe ni vyuo vya utafiti. Huwezi kufanya chochote kwenye kilimo bila kuweka kipaumbele kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyuo vichache vya utafiti, lakini hata vilivyopo havipelekewi fedha, na hata fedha zikitengwa hazipelekwi kwa wakati. Kilimo kinachoendelea Tanzania ni kilimo cha mazoea, ukiangalia mbolea inayotumika kwenye mazao mengi wanatumia vile vidude vya visoda au vikopo vya maji. ni lini walifanya utafiti kwenye udongo kwamba kile ndicho kipimo sahihi? Ni kwa sababu ya mazoea. Hivyo, hatuwezi kuendelea bila kufanya utafiti, ni bora leo tukatenga fedha nyingi kwenye utafiti ili tuweze kuinua kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la vituo vya rasilimali za kilimo. Lengo la kuweka vituo hivi lilikuwa ni kupeleka huduma kwa wakulima; na hivi vituo vilipaswa viwekwe kama vituo vya afya vya kila kata; lakini leo nitolee mfano mdogo tu, Mkoa wa Rukwa una kata 97 hivi vituo vipo 9, kuna kilimo hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la masoko; suala la masoko tumezungumza sana. Wajibu wa mkulima ni kuhakikisha analima au anzalisha kwa tija. Wakulima wetu wamejitoa lakini Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake kuwatafutia masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, uamuzi mlioufanya kwenye korosho ni uamuzi wa dharura sana lakini kama ni uamuzi endelevu wa kutumia Benki ya Maendeleo ya Kilimo mtuambie kwamba itakuja kutumika na kwenye zao la mahindi, kwa sababu ilianza kwenye korosho na ile siyo benki ya korosho peke yake. Kwa hiyo, nashauri Serikali busara iliyotumika itumike tena, kama ilikuwa ni dharura tafuteni soko kabla ya msimu wa mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la miradi ya umwagiliaji; hatuwezi kuwa na kilimo ambacho kinategemea mvua peke yake, lazima wajielekeze kwenye mabwawa ya umwagiliaji. Mengi yaliyopo mengine yamekufa, mengine yamesimama, kosa ni la nani? Serikali wana wajibu wa kupeleka fedha na mambo haya yanafanyika hivi ni kwa sababu Serikali inakosa kipaumbele; inashika pale, inashika hapa, matokeo yake kilimo chetu sijui wanakwenda kukipeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Maafisa Ugani; nimefuatilia kidogo – akija Waziri atanisahisha, yaani mpaka sasa tuna upungufu wa Maafisa Ugani 20,100, hali ya kilimo itakuwaje kama Maafisa Ugani kuna upungufu huo. Nawaomba Wizara ya Kilimo kipindi wanapeleka mapendekezo yao kwa Serikali cha kwanza waombe idadi halisi ya Maafisa Ugani ambao watakwenda kutoa ushauri kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kumekuwa na shida sana kwenye Wizara ya Kilimo; bei ya pembejeo haiendani na hali halisi ya bei ya mazao. Naomba nishauri kwa kuwa slogan ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda, viwanda wajenge hapa ili bei ya pembejeo ipungue, sasa hivyo viwanda watajenga viwanda gani, hivyo viwanda vitahifadhi nini kama upande wa materials wenyewe tumefeli, upande wa umwagiliaji tumeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara ya Kilimo iwe na vipaumbele, kipaumbele cha kwanza kabisa kiwe kuimarisha miradi ya umwagiliaji na hii itasaidia wakulima wetu. Suala pia la danadana la kutokuwalipa mawakala kwa suala la kwamba eti wanafanya utafiti; wanafanya utafiti kwa miaka mingapi? Wale wenye makosa basi wasipewe, wale ambao wanabainika hawana makosa walipwe fedha zao. Uhakiki huu pia ni kama njia mojawapo ya kutegeategea hivi, Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake, kama fedha hakuna waseme kwamba fedha hakuna. Kuna watu wameuziwa nyumba zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la bima za wakulima lifanyike haraka ili Serikali wajue maumivu ambayo wanayapata wakulima ili makosa wanayofanya Serikali wawe wanawajibika kwa wakulima hawa. Hili jambo liende sambamba na matamko ambayo yanatolewa. Nazungumza hivi kwa sababu, narudia tena leo kwamba tamko la Serikali lililotoka… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kuongelea kuhusu viwanja vya michezo. Kulingana na changamoto za viwanja vingi nchini kuwa chakavu, jambo hili linatakiwa kupewa kipaumbele na Wizara ili kuweza kukuza michezo katika ngazi mbalimbali nchini na pia italeta chachu kwa vijana wenye vipaji mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kuhusu kuboresha usikivu. Kwa sasa kuna shida kubwa ya usikivu wa chaneli zetu, hasa kwenye maeneo ya mipakani. Naomba maboresho yafanyike ili kuwasaidia wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kupata habari za taifa lao badala ya kupata habari za nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, tatu ni usalama wa waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari. Kwa sasa kumekuwa na vitisho na watu kupotea, je, Wizara ina mkakati gani wa kuwalinda kwani kuwepo kwa waandishi wa habari ni muhimu sana katika taifa lolote lile.

Mheshimiwa Spika, nne, vazi la taifa. Mpaka sasa vazi la taifa halijajulikana na imekuwa ni malalamiko ya muda mrefu kwa wananchi katika ngazi mbalimbali nchini kuhusu vazi hili. Je, Wizara mpaka sasa imefikia hatua gani kuhusu vazi la taifa?

Mheshimiwa Spika, tano, chuo kikuu kwa ajili ya walimu wa michezo. Nashauri kijengwe chuo kikuu cha walimu wa michezo ili kuweza kukuza michezo nchini kwani kwa sasa kuna uhaba wa walimu bora wa michezo. Hii pia itasaidia kuinua michezo nchini.

Mheshimiwa Spika, sita, wanamichezo wanaofanya vizuri ndani na nje ya nchi. Kumekuwa na malalamiko kwa kiasi wanachopewa baada ya ushindi kwamba wanapewa kiasi kidogo sana ambacho hakiendani na kiasi walichopata, jambo ambalo linapunguza morali kwa wanamichezo wetu.

Mheshimiwa Spika, saba, nashauri Wizara iweke utaratibu mzuri wa kuibua vipaji mbalimbali kuanzia huko wilayani na mikoani ndani ya nchi yetu. Ni imani yangu kuwa wilayani na mikoani kuna vipaji vingi.

Mheshimiwa Spika, nane, kufungia magazeti. Suala hili limekuwa likileta sura mbaya kwa mataifa mengine yanayotuzunguka. Suala la kufungia magazeti linaathiri wamiliki, waajiriwa pamoja na wananchi wanaopata habari ambayo ni haki yao.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Ninamshukuru Mungu nami kupata nafasi kuchangia bajeti muhimu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yoyote makini ina kipaumbele, Serikali yoyote makini kipaumbele chake ni kipaumbele cha wananchi wake. Tunapozungumza hapa bajeti iliyopita na bajeti hii tunawatazama Watanzania ambao wametupa dhamana leo tunazungumzia hali ya uchumi kwenye vitabu kila siku inaonekana uchumi unakua lakini ukienda kwenye uhalisia hali ya Watanzania inazidi kuwa mbaya hasa katika hii Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni vizuri takwimu hizi zinazoongezeka kwenye vitabu zipelekwe kwenye uhalisia wa maisha ya Watanzania na baada ya kupeleka huko na haya mambo yote itaonekana kama yana ufanisi endapo utawala bora utazingatia Sheria ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo watakaosema kwamba Serikali imefanya nini Watanzania kupitia Wawakilishi. Kwa mujibu wa Katiba tuna haki ya kufanya mikutano kuwaeleza Watanzania nini kinaendelea kwenye nchi hii. Mikutano imezuiliwa, kwa hiyo ninyi mtatengeneza wenyewe na mtakuja kujisifia wenyewe, lengo letu ni moja kuijenga nchi yetu, pelekeni takwimu hizi ziende kwenye uhalisia kwa Watanzania, maisha ya Watanzania bado ni magumu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosababisha uchumi wa nchi hii uonekane bado ni butu, ni kero zinazoendelea kuhusu tozo na ushuru ambao unakuwepo kuanzia kwenye bandari na maeneo mbalimbali. Nitolee mfano mmoja tu, leo ukiagiza gari kwa milioni kumi na moja, mpaka ukaichukue pale bandarini bei yake inafanana na ile uliyoagizia.

MBUNGE FULANI: Kweli. (Makofi)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nini tunafanya? Ukiangalia kero ambazo wafanyabiashara walienda kuzungumza Ikulu kwa Mheshimiwa Rais inaonesha ni jinsi gani Wabunge tumeshindwa kutimiza wajibu wetu. Zile ni kero ambazo wanazipata Wafanyabiashara na kama unataka kukuza uchumi wa nchi yetu lazima tuangalie watu ambao wanaweza kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza wanazungumzia kilimo ambacho ndiyo kinaajiri vijana wengi na watu wengi kwenye Taifa letu, tumejipangaje kwenye kilimo chetu. Serikali ya Awamu ya Tano ilikuja na slogan ya Serikali ya Viwanda, tumejipangaje kwenda kwenye viwanda, ni lazima tuboreshe kilimo nchini. Leo tunapozungumzia kilimo hali ni ngumu sana kulingana na pembejeo ambazo wakulima hawawezi gharama bado ni kubwa sana, kama slogan ni Serikali ya Viwanda lazima tuwekeze kwenye viwanda, viwanda hivyo vikijengwa nchini vitapunguza gharama za pembejeo ambazo zitawaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama pembejeo bado ni ghali kwa wakulima hawa lakini rudi kwenye hali halisi ya soko ambayo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inatafuta masoko kwa hawa wakulima, bado Serikali haijajikita kutafuta masoko. Ushauri wangu, tunatumiaje Muungano wetu wana Umoja wa Afrika Mashariki kuweza kuuza mazao yetu ambayo wanaweza kuyalima Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niliona kwenye hotuba kuna tozo zimeondolewa lakini ukitazama sekta ya uvuvi haijaguswa kabisa. Hawa wavuvi wanapata leseni kutoka Serikalini na wanalipa kodi inakuwaje wao wasiguswe na wana kero nyingi sana kwenye nchi hii? Tusijivunie kukusanya kodi bali tujivunie kutengeneza mazingira rafiki kwa wavuvi na wakulima wetu, hapo ndiyo tutazungumzia ukuaji wa uchumi ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa napozungumza leo ziwa tunalotumia sisi la Ziwa Tanganyika suala la usafirishaji ni mgumu. Nategemea Serikali itakuja ituambie hapa suala la MV Liemba mmefikia wapi mpaka sasa ambapo ni usafiri ambao utatusaidia kwenda kuuza mazao yetu Burundi, Congo na maeneo mengine, hiyo mtakuwa mmetusaidia kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini tumejipanga sisi kukusanya kodi kwa hawa wavuvi badala ya kujipanga kuwatafutia masoko kwanza. Hawa Watanzania leo kama mkulima na mvuvi analia, huo uchumi unakua kutoka wapi? Ni vizuri Serikali ikaangalia Watanzania hawa, kama tunataka kukusanya kodi na wao waone faida ya kodi wanazozitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, katazo la mikutano ya Vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa inasajiliwa kwa kuangalia vigezo toka mwaka 1992 tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini tumeshuhudia kwenye Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na zuio kwa vyama vya siasa kutimiza majukumu yao. Tunaomba Serikali itujibu inatumia sheria gani kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Spika, Askari kuwaadhibu wahalifu; Je, ni sheria gani inampa mamlaka Askari anapokuwa na mhalifu ambaye hajahukumiwa kuadhibiwa? Kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi juu ya polisi pale wanapowakamata wahalifu jambo ambalo linaondoa upendo kati ya Jeshi la Polisi na raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti; Askari wa Usalama Barabarani kugeuka kuwa wakusanya mapato; hivi sasa kumekuwa na utaratibu kwa Askari wa Usalama Barabarani wakiwa na EFD machine na risiti muda wote, je, huo ndio mpango wa Wizara ili kuweza kumaliza ajali barabarani au ndiyo chanzo cha rushwa na kupelekea ajali zaidi?

Mheshimiwa Spika, Vituo vya Polisi vinavyojengwa na nguvu ya wananchi; wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini jitihada hizi za wananchi haziungwi mkono na Serikali na kupelekea kuwavunja moyo wananchi hawa wanaojitolea.

Mheshimiwa Spika, vitambulisho vya Taifa; sio Watanzania wote ambao wamepata vitambulisho hivi, kwa hiyo jambo lolote litakalofanyika kwa sasa kwa kigezo cha kuwa na utambulisho litakuwa la ubaguzi, nashauri Serikali kwa kuwa bado kuna changamoto kwenye uzalishaji wa vitambulisho, Wizara iweke mkakati mahususi wa kuweza kumaliza changamoto hizo kwanza ili kuwapa haki wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, suala la askari wenye sifa na waliotimiza vigezo kupandishwa vyeo; kumekuwa na malalamiko kutoka kwa askari wanaojiendeleza kielimu kushindwa kupandishwa vyeo pale ambapo ameshajiendeleza, suala hili linashusha morali kwa askari wetu kwani nao wana stahiki kupewa haki kama watumishi wengine nchini.

Mheshimiwa Spika, pesa za likizo; pamoja na uhamisho kwa askari wetu kumekuwa na malalamiko makubwa kwa askari kuhusu pesa za likizo na pesa za uhamisho, Wizara iangalie upya utaratibu wa kuwasaidia askari kuwapatia pesa hizo kwa kuwa ipo kisheria na ni haki zao.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijaalia uzima kufikia siku ya leo, lakini niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Nkasi Kaskazini kwa kuniamini na leo niko ndani ya Bunge kuwasilisha mawazo waliyonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulingana na dakika tano nitazungumza kwa uchache sana. Siku alipokuja Mheshimiwa Rais ndani ya Bunge nilikuwepo hapa na leo tunazungumzia hotuba yake ambayo ni mwelekeo kwa Taifa letu. Ukitazama nchi yetu ya Tanzania kila kanda ina vitu ambavyo vipo vinaweza vikasaidia Taifa. Kanda yetu ya Nyanda za Juu Kusini na kwenye hotuba Mheshimiwa Rais amezungumzia zaidi kujikita kwenye kilimo. Nyanda za Juu Kusini tunajishughulisha na kilimo. Lakini pamoja na kilimo hicho ni namna gani kinanufaisha Taifa kwa ujumla. Ukizungumzia Nyanda za juu Kusini unazungumzia mikoa mitano ambayo inazalisha chakula na mazao ya biashara lakini sisi tumebahatika pia kupya bandari ya Kabwe, bandari ile ingetumika vizuri kulingana na mazao yanayozalishwa kwenye Nyanda za Juu Kusini sio tu kusaidia Nyanda za Juu Kusini, ingesaidia pia Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kupitia bandari ile ambayo tayari Taifa limewekeza fedha nyingi tunategemea kupata matokeo ambayo yatakuwa ni matokeo chanya yatawasaidia wananchi wanaozunguka eneo lile la bandari lakini pia yatasaidia Taifa. Ili tuweze kusafirisha mazao ambayo tunaamini tunaweza tukapeleka nchi za jirani ambao wanaweza kutumia bandari yetu ya Kabwe ni lazima kiwe ni kilimo chenye tija. Wakati nazungumzia kilimo kwenye Nyanda za Juu Kusini tayari Serikali imeweka fedha nyingi kwenye miradi ya umwagiliaji, lakini ni miradi mingapi inafanya kazi mpaka leo? Unaitazama dhana ya Serikali kuwekeza fedha lakini namna gani tunakwenda kumalizia hizo fedha au viporo ambavyo tayari tumekwisha vianzisha?

Mheshimiwa Spika, wakati nazungumzia kilimo si kuwasaidia tu wakulima, lakini ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais naye amekiri kwamba ajira zinazopatikana kwa mwaka haziendani na uhitimu wa wanafunzi kulingana na level mbalimbali. Tunaamini kilimo ndiyo ingekuwa muarobaini wa kuweza kumaliza jambo hilo. Kilimo tunachozungumzia hatuzungumzii kilimo cha mazoea. Kama tumeanzisha miradi ya umwagiliaji wanakwenda kuazalisha nini? Je, wanachozalisha watauza wapi? Mheshimiwa Rais baada ya kuzungumza ndani ya Bunge ni kazi ya Mawaziri sasa. Kwa mfano, natambua kwamba janga la Corona limepita dunia nzima hatufurahishwi nalo, lakini sisi tumebahatika wananchi wetu wameendelea kulima wamezalisha kwa wingi. Mpaka sasa tunatumiaje fursa hiyo kuweza kuwasaidia wananchi wetu ambao ni wakulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, wakati tunazungumza hapa pia tayari Serikali imewekeza fedha kwenye vyuo mbalimbali na hapa mimi nategemea TAMISEMI na Wizara ya Elimu hii asilimia nne ya kwenda kuwasaidia vijana hawa ambao wamemaliza level mbalimbali hawana ajira haisaidii sana, haileti yale matokeo ambayo tulikusudia. Leo hivi vyuo vya VETA wanakuwa wameshapata ujuzi. Kwa nini pale wanapokaribia kuhitimu wasipewe fedha kwa ajili ya mikopo na fedha hiyo ni rahisi kurudisha tofauti na sasa ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo wanamaliza wanakwenda kukaa tu mtaani. Kwa hiyo inakuwa haina utofauti na wale ambao wametoka shuleni hawajafundishwa namna ya kujiajiri. Lakini hawa tayari wameshapewa ni namna gani wanaweza kujiajiri. Kwa hiyo tunaweza tukatumia ile fedha badala ya kuwapa kiasi kidogo tukaangalia wahitimu ni kiasi gani watapewa fedha hizo waweze kusaidia na wale mataajiri watu wengine kupitia mafunzo ambayo wameyapata na itakuwa na maana Zaidi juu ya kwenda kuwa empower vijana pamoja na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tukirudi kwenye kilimo hapo hapo hivi Vyuo vya Utafiti vikiwezeshwa kikamilifu watu watakuwa na uhakika wa kulimo wanachokilima. Watakuwa na uhakika wa mbegu zinazotoka kwa sababu tayari zimefanyiwa utafiti. Lakini leo hata ukiangalia maeneo ambayo watu wanalima, mtu anaamua kwamba yule alipata gunia 10 na mimi leo nitalima gunia 10. Hapana, tuambieni aina ya udongo huu mnaweza kulima zao fulani. Mkituambia pia tutajua soko la zao hilo liko wapi. Kwa hiyo, hata mtu anapoingia kwenye kilimo hawezi tena kufikiri ajira. Leo tutakwenda kuwafundisha vijana namna bora ni namna gani wanaweza kujiajiri. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu kuboresha maslahi ya walimu. Suala hili la kuboresha maslahi ya walimu wetu ni muhimu ili kuleta morali kwa walimu na matokeo chanya kwa watoto na hasa kizazi hiki ambacho kinakabiliwa na kuzungukwa na utandawazi ambao unawaathiri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri mitaala yetu iendane na teknolojia yetu. Kutokana na suala la teknolojia kubadilika kila wakati hivyo mitaala yetu ni vyema kuzingatia mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha za alama kwa wanafunzi wenye ulemavu. Wanafunzi hawa wanahitaji kupata elimu kama wanafunzi wengine ili kuleta usawa na kuondoa malalamiko miongoni mwa wanafunzi ambao wako kwenye jamii zetu zinazotuzunguka. Kwa hiyo, ni muhimu lugha hizi ziwepo katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna upungufu wa walimu wa lugha za alama. Nashauri ili kumaliza tatizo hili Serikali iongeze vyuo maalum kwa ajili ya walimu wa lugha za alama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji wa wadau wa elimu wanapotaka kufanya mabadiliko katika masuala ya elimu. Kumekuwa na matokeo hasi kwenye maamuzi mbalimbali yaliyotokea katika masuala ya elimu sababu kubwa ni kutowashirikisha kikamilifu wadau wa elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo maalum kwa walimu. Kulingana na mabadiliko yanayojitokeza kwenye elimu ni vyema walimu wetu wakawa wanapewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vya ufundi. Bado kuna upungufu mkubwa wa vyuo vya ufundi nchini kulingana na wahitimu wa ngazi mbalimbali kuwepo mitaani lakini hata vile vichache vilivyopo vina changamoto za walimu kuwa wachache pia hawapelekwi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza pesa kwenye suala la ukaguzi kwa kuwa matokeo chanya ya elimu yatatokana na ukaguzi. Nashauri Serikali ili kuboresha elimu yetu ni vyema kuboresha Kitengo cha Ukaguzi pia Wizara ishughulikie kero zinazotokana na ukaguzi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu ina mkanganyiko sana. Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza sera hizi ambazo zimekuwa na mkanganyiko mkubwa?
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia afya niweze kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya dakika tano, nitazungumza kwa uchache. Tunapozungumzia Mpango wa Miaka Mitano tunazungumzia Dira ya Taifa. Napozungumzia Dira ya Taifa lazima nitazame wimbi kubwa la vijana ambao wamekosa ajira. Tunapozungumzia wimbi kubwa la vijana lazima tutafute suluhisho kupitia Dira ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ajira ambazo zinatolewa Serikalini lakini bado tunarudi kwenye kilimo kwamba inawezakana ikawa mwarobaini au ikasaidia angalau kwa hili tatizo la ajira. Ukizungumzia kilimo cha Tanzania, nitatoa takwimu ya 2019 – 2020, wakulima ambao walilima 2019/2020 waliotumia mbegu bora ni asilimia 20 tu; waliotumia mbolea za viwandani asilimia 20, hapo ndiyo tunarudi kwenye lengo kweli kilimo ni uti wa mgongo, kitakwenda kutatua tatizo hili la ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumza hivyo siyo kwamba tuna shida ya ardhi kwenye nchi yetu, ardhi ipo na wataalam wapo wanalipwa fedha, shida nini kwenye Serikali yetu ya Tanzania kwenye suala la kilimo? Kama bajeti tunapitisha na mipango inaletwa hapa na inapoletwa naamini kabisa wanakuwa wamewashirikisha wataalam wetu huko chini, shida inakuwa ni nini Zaidi? Kupanga mpango ni jambo moja na kupeleka fedha ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia 2015-2020, hekta zilizoongezeka kwenye umwangiliaji ni 233,339. Leo kwenye Mpango huu tunazungumzia kwenda kufikia hekta milioni moja na laki mbili. Nilitamani kujua tu kuna miujiza gani utakaotumika hapo wa kufikia hekta milioni moja na laki mbili wakati kwa miaka mitano tunazungumzia laki mbili na thelathini na tatu mia tatu thelathini na tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ya kushauri, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais nilijikita hapo na leo narudia. Kama tunataka kuboresha kilimo chetu ni lazima kwenye Mpango fedha zitengwe kwa ajili ya kupelekwa kwenye vyuo vya utafiti. Kama kweli tuna nia njema ya kuokoa Taifa letu lazima tutenge fedha za kutosha tupeleke kwenye vyuo vya utafiti. Tukipata fedha za kutosha mbegu zenyewe zitakuwa bora, tukipata mbegu bora lazima tutatenga fedha kwa ajili ya kupima udongo kujua udongo huu unafaa kwa zao lipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia ngano, ukitazama Mkoa wa Rukwa tunalima ngano sana lakini kama tunasema hitaji la Taifa letu ni ngano Serikali imejipangaje kwenye Mpango huu kwenda kupima maeneo ambayo yanaweza kufaa kwa kilimo cha ngano ili iendelee kuzalishwa kwa wingi Tanzania? Utakuta ni wimbo ambao tunauimba tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, kuna mikoa ambayo inazalisha sana mpunga, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwao lakini ukiangalia kwenye Mpango hapa hakuna kitu ambacho kimetengwa kwa ajili ya kwenda kuongeza uzalishaji wa mpunga na ili twende kwenye viwanda ni lazima tuboreshe raw material. Kwenye raw material mbolea leo Mkoa wa Rukwa mfuko mmoja Sh.65,000 wakati gunia la mahindi Sh.30,000, unaweza ukafikiri hapo huyu mkulima auze gunia ngapi ndiyo anunue mfuko mmoja wa mbolea? Je, kilimo kitakua au kitarudi nyuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunazungumzia viwanda nashauri tujue Tanzania tunahitaji viwanda vya aina gani. Viwanda vya kwanza vinavyohitajika ili tupunguze gharama za mbolea lazima tuwe na kiwanda kinachozalisha mbolea Tanzania ili wakulima wapate mbolea kwa bei rahisi. Tukiwa tumepeleka na mbegu bora tunazungumzia sasa kilimo cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili lazima tupeleke Maafisa Ugani wa kutosha kwenye kata ambazo zinazoongoza kwa kilimo. Leo kuna Maafisa Kilimo wapo mjini, hatukatai haa na mjini wanalima lakini kwa sababu ni wachache basi hao wachache wapelekeni maeneo ambayo wanazalisha, maeneo ambayo wanaendesha kilimo tujue kwamba tuko serious na kilimo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miradi ya umwagiliaji tunatambua kwamba Serikali imepeleka fedha nyingi ikiwemo Mkoa wa Rukwa lakini miradi hiyo haifanyi kazi. Lengo la Serikali ni nini? Kabla leo hatujabuni miradi mipya tupeleke fedha tukamalizie miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambayo ni Wizara muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu kwenye maeneo tofauti ili kuinua uchumi kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, TARURA waongezewe fedha. Suala hili limekuwa na changamoto kubwa sana, kwani TARURA wana barabara nyingi za mitaa na vijiji lakini wanashindwa kumaliza kazi hizi kwa muda muafaka kwa sababu ya fedha kidogo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni usafiri wa meli kwa Ziwa Tanganyika. Kumekuwa na changamoto kubwa ya usafiri wa majini kwa wananchi wanaotumia Ziwa Tanganyika kwa usafiri na biashara. Naomba kujua Serikali imefikia wapi katika suala la Meli ya MV Liemba?

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko ya Wakandarasi wengi kutokulipwa fedha zao kwa wakati. Kwa nini Serikali isiwalipe Wakandarasi ili kuleta ufanisi kwa kazi na miradi wanayopewa ili kuinua uchumi wa nchi?

Mheshimiwa Spika, ni vyema kufuatilia na kujua uwezo halisi wa Wakandarasi kabla ya kupewa tenda ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza kwa Taifa, kwani kumekuwa na malalamiko mengi sana na kupelekea vitendo vya rushwa na kupelekea hasara kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa viwanja vya ndege ni vyema liangaliwe kwa umakini kwa kuangalia aina ya watu kwa maeneo ambayo wana uhitaji wa viwanja vya ndege ili kuweza kukuza uchumi kwa eneo husika na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, suala la TBA bado kuna changamoto; miradi mingi wanayopewa haikamiliki kwa wakati. Pia napenda kuishauri Serikali ipunguze miradi kwa TBA na badala yake wapewe watu wengine ambapo kukiwa na ushindani huleta ufanisi mzuri wa kazi na uharaka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la watu kuwekewa X za kijani na nyekundu: kumekuwa na mkanganyiko katika utekelezaji wa suala hili pale inapotokea nyumba moja ina alama mbili ya kulipwa na kubomolewa, wanawaambia wananchi wabomoe. Je, suala hili likoje? Tunaomba ufafanuzi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi kwasababu ya dakika chache nitakwenda moja kwa moja Jimboni na kabla sijakwenda huko kama Wabunge wengine walivyozungumzia kuhusu TARURA naomba kushauri mambo machache.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba wahandisi waliochukuliwa kutoka kwenye Halmashauri sasahivi wako kwenye vyeo vya muundo wa TARURA. Kuna wengine ambao bado hawajaanza kulipwa kulingana na mamlaka waliyonayo. Sasa tusiweke hizo habari za mamlaka kana show. Kama tumeamua kusema kwamba huyu ni Meneja wa TARURA ngazi ya Halmashauri, alipwe kulingana na nafasi aliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba kwenye ngazi ya mkoa tuna mratibu wa TARURA Mkoa. Yule mtu kuwa peke yake pale kunakuwa na changamoto kadhaa kwa sababu akiwepo pale peke yake yeye ndiyo anayehusika na manunuzi. Huyo huyo mratibu peke yake ndiyo anayehusika na kutangaza tender. Kumekuwa na changamoto kwa hawa wakandarasi na changamoto hizo zinaenda kuathiri wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri, ni vizuri tukaangalia muundo wa TARURA upya ili kuweza kutimiza malengo ambayo tulikusudia baada ya kuanzisha chombo hiki.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo machache, kuna barabara ya Kirando – Korongo na leo nimekushuhudia Mheshimiwa Naibu Waziri ukiwa unajibu hilo swali ambalo kuna daraja la Kavune. Nitambue mchango wa Serikali kwenye jambo hili kwamba wamepeleka fedha kiasi kwa ajili ya ujenzi wa hili daraja lakini uhitaji wa daraja hili na hiyo barabara kwenye lile eneo ni muhimu sana.

Niwaombe TAMISEMI kuna mambo ambayo hayahitaji kufanya siasa, kuna maeneo tunayotoka pembezoni. Tukileta siasa kwenye afya, tukaleta siasa kwenye elimu, tukaleta siasa kwenye miundombinu tutawaumiza wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasema hivyo kwasababu leo tuna Sera ya Afya ambayo inataka zahanati kwa kila Kijiji, inataka kituo cha afya kwa kila Kata. Wilaya yangu ya Nkasi ina Kata 28, kata zenye vituo vya afya ni kata tatu tu. Tukianza kuzungumzia habari ya Ilani miaka yote walikuwa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, kwanini mlishindwa kutekeleza jambo hili. Kwasabbau hiyo, nataka nishauri tu kwa nia njema, basi hizo kata tatu zenye vituo vya afya basi zitoe huduma kulingana na level ya Kata kwa maana ya kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwa wauguzi bado kuna changamoto, pamoja na kwamba hatujatimiza, hiyo sera haijatekelezeka lakini katika hizo chache tulizonazo basi angalau tupeke huduma zinazoweza kujitosheleza kuwasaidia wananchi wetu. Natambua kwamba wananchi wamehamasika kuweza kuanzisha maboma mbalimbali kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya, ni vizuri! Pamoja na kwamba uhitaji ni mkubwa, fedha mnayopata TAMISEMI ni ndogo. Lazima tuwe na kiipaumbele, na kipaumbele ni kuanza kuheshimu nguvu za wananchi ambazo wanakuwa wamezianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Kabwe, Waziri Mkuu amekwenda pale akaahidi kwamba kituo cha afya kitafunguliwa mapema kwasababu ya bandari iliyoanzishwa kule. Mpaka leo ninavyozungumza hakuna fedha yoyote tumeona baada ya tamko lile na haya matamko sio mabaya lakini yamekuwa yanaathiri mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza nikarudi tu hapo kwenye masuala ya TARURA, unakuta kuna matamko au maagizo au ahadi za viongozi wa Kitaifa. Ahadi sio mbaya lakini ahadi hizo zinavyokuja zinatekelezwa kwa kiasi gani ahadi za viongozi wa Kitaifa na wakati mwingine zinakwenda kuharibu bajeti za halmashauri, kwa hiyo inakuwa ni ugomvi kati ya wananchi pamoja na viongozi waliopo kwenye kada hizo. Kwa hiyo, ni vizuri hata hizo ahadi zikawa kwenye kumbukumbu maalum. Tunapokuwa tunaandaa bajeti tunakuwa tunajua kuna ahadi ngapi za viongozi wa Kitaifa ili utekelezaji unakuwa unaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine naomba nizungumzie kwenye elimu. Pamoja na kwamba elimu inatolewa Tanzania nzima kuna maeneo ambayo yanahitaji mkakati za ziada, hasa sisi ambao tunatoka pembezoni. Mpaka hivi ninavyozungumza kwenye Wilaya ya Nkasi kuna kata nne ambazo watoto ili wakafanye mtihani wanatakiwa wapite kwenye maji, yaani wavuke maji wakafanye mtihani sehemu nyingine. Leo unazungumziaje matokeo chanya kwa watoto hawa? Anavyopita kwenye maji akafanye mtihani kwanza tumem-disturb, arudi tena nyumbani, kesho tena aende apande boti, maboti yenyewe hayapo, Serikali hamjapeleka boti. Lakini na sisi tunataka Marais watoke kwetu yaani mnaamini kwamba Nkasi Rais hawezi kutoka? Lakini kama tunaamini hivyo, lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa watu hawa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wanapozungumzia watu wengine kwamba kuna wengine wamekufa kwa kung’atwa na fisi, Wilaya ya Nkasi watoto wanang’atwa na mamba isivyo kawaida! Leo ni kosa la nani? Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha watoto wanatengenezewa mazingira rafiki kwa ajili ya kupata elimu kwasababu elimu sio fadhila, elimu ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kutoa elimu kwa watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Mheshimiwa Aida, unga mkono hoja. (Kicheko)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante. (Kicheko/Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nfasi hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani ambayo ni muhimu sana.

SPIKA: Atafuatiwa na Mheshimiwa Condester.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nitachangia mambo machache kwa sababu ya dakika tano. Nisipotambua mchango wa Askari wetu nitakuwa naidanganya nafsi yangu. Tunatambua mchango wa Askari wetu hasa kwa kujitolea kwenye nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna changamoto kadhaa ambazo zinawakumba Askari wanaojitolea hasa wa chini kabisa. Nitatolea mfano tu kwenye uchaguzi uliopita. Mheshimiwa Naibu Waziri nimezungumza nawe sana na jambo hili liko Wizarani. Siku ya uchaguzi siyo Jimboni kwangu, labda wanaweza wakafikiri nazungumza kwa sababu ni Jimboni kwangu. Askari amevunjika mguu siku ya uchaguzi akiwa kazini, mpaka leo nazungumza hakuna mchango wa Wizara hata kidogo. Askari wenzake wale wa chini ndio wanaojichangisha na mimi Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo kwa sababu, Wizara haijachangia, isipokuwa inaleta picha mbaya kwa Askari wengine siku nyingine kujitolea. Inaleta picha mbaya sana na watarudi nyuma, kwa sababu wataamini kwamba nikiumia, itakuwa ni mzigo wangu mimi na familia yangu. Jambo hili haliko sawa, tuwatie moyo Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Vituo kwa maana ya Ma-OCD, wale ni viongozi. (Makofi)

SPIKA: Unaweza ukamtaja jina la huyo Askari ili…

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri nafikiri anajua, kwa sababu anajua jina na ameshafanya naye mawasiliano, anajua vizuri.

SPIKA: Lakini Hansard haijui.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nikikumbuka nitalitaja, lakini hapa sina kumbukumbu nzuri.

SPIKA: Haya ahsante.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante

SPIKA: Wakati mwingine ni vizuri kutaja maana tutakapofuatilia baadaye…sana.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante

SPIKA: Ahsante, haya.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Askari hao wachache ndio wanaopata mateso makubwa; lakini Ma-OCD, wale ni maaskari ambao wana vyeo hivyo. Ukiangalia ofisi zao, wale sio wafungwa, wanastahili kupewa hizo nafasi na angalau mazingira yao yafanane. Kwa hiyo, tunapozungumzia kuboresha makazi ya askari, hata ofisi zao zifanane, angalau nao wakiwa mle ndani wajue wako ofisini, angalau watimize majukumu yao. Siyo wanapita huku kuna kunguni, kuna panya na nini. Yaani ifikie mahali kwa kweli tuwatie moyo askari wetu. Pamoja na kwamba kuna shida ya maslahi na nini, basi angalau mazingira yafanane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya dakika tano, nitakwenda kuzungumzia pia habari ya vitambulisho vya Taifa. Alipokuwa anazungumza Mbunge wa Kigoma, yawezekana alisomeka kwamba ni Kigoma. Mikoa yote ya pembezoni tuna changamoto hiyo. Mimi natokea Wilaya ya Nkansi, sisi tunapanda boti tu kwenda Kongo pale. Ikifika wakati wa uchaguzi, wale wote wanaoonekana wana mtazamo tofauti na CCM, wanaambiwa wewe sio raia. Hili jambo siyo zuri, linaleta unyanyasaji. Siyo jambo jema kabisa. Pamoja na kwamba bado tuna changamoto ya utekelezaji wa vitambulisho, basi mikoa ile ya pembezoni ipewe kipaumbele ili kumaliza hizi changamoto ambazo zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu ambao walipewa namba toka mwaka 2020, sasa kama namba wameshapata, vile vitambulisho vinachukua muda gani? Hili jambo ni lazima tulitazame. Kwanza tunawakwamisha kwenye mambo mengi. Leo unapokwenda kwenye sijui usajili wa line na vitu gani, kote unahitaji kitambulisho cha Taifa. Kwa hiyo, tunawakwamisha sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuishauri Serikali yangu ya Tanzania, sisi wote ni Watanzania. Leo hawa watu ambao wanaitwa wahamiaji au wageni ambao wamekuja kufanya shughuli mbalimbali Tanzania, tunatambua kwamba ipo sheria ya wageni wanapotaka kufanya kazi. Kipindi cha nyuma ilikuwa ni shilingi milioni sita kwa miaka miwili. Leo watu wengi hawana hivyo vibali vya kufanya kazi, wakiwemo watu wachache tu ambao wanafanya kazi saluni, hizi shughuli ndogo ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kuishauri Serikali kwenye jambo hili, imekuwa ni kama upenyo wa baadhi ya watu wa uhamiaji, wanakwenda kufika kule wanawaambia nipe shilingi 500,000/= ili nikuachie, kwa sababu sasa hawana vibali. Kwa hiyo, naishauri Serikali, ni vizuri mkawatambua wale wanaofanya kazi nchini ambao ni wageni, wako wangapi? Je, wana vibali vya kufanya kazi hizo? Yawezekana hata idadi yao hatuijui. Kwa hiyo, Serikali inakosa mapato, ila watumishi wachache wanakwenda kwa kukosa uaminifu, anaomba shilingi milioni moja, wanamalizana; naomba shilingi laki mbili, wanamalizana.

Mheshimiwa Spika, sasa hawa watu, kama kweli kuna vibali, tuangalie aidha kuna shida kwenye sheria yenyewe, tuifanyie maboresho. Ila kabla ya kufanya maboresho, tuwatambue wako wangapi? Je, kweli hizo kazi wanazofanya wanafanya kwa mujibu wa sheria? Yawezekana tukiwatambua itasaidia sasa hata kile kiasi ambacho tunakitaka kama ni kikubwa kipunguzwe. Lengo ni kwamba kifike Serikalini, kisipotee huko mtaani kama kinavyopotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante. Kwa hiyo, pia kwako kuna shida ya uhamiaji?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, eeh, wapo wengi tu.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma anayenijalia uzima mpaka siku ya leo nimesimama katika Bunge lako Tukufu. Niwashukuru sana wana Nkansi Kaskazini kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano katika kipindi kigumu nachokipitia hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na suala la Mradi wa Ziwa Tanganyika. Mheshimiwa Waziri kabla sijazungumza jambo hilo na mimi nikupongeze kwa kwa uthubutu na namna ambavyo unawajibika kwenye Wizara yako, pamoja na Naibu wako, mnafanya kazi nzuri. Hata hivyo, kazi nzuri zitaonekana kwa vitendo, tunatamani kuona maji siyo maneno.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mchango wa Serikali kwenye Jimbo langu la Nkasi Kaskazini katika suala zima la kupeleka maji lakini pamoja na jitihada hizo za Serikali bado kuna changamoto kubwa. Tunapozungumzia upatikanaji wa maji vijijini, Nkasi Kaskazini ni miongoni mwa majimbo ambayo yapo pembezoni na maeneo hayo Kata zote zinatoka vijijini. Serikali imetuletea kiasi cha fedha; Kata ya Kabwe kuna mradi wa maji wa bilioni 1.4, Kata ya Kilando bilioni 1.3, Kata ya Namanyere bilioni 1.7, lakini ukiangalia miradi yote hii, haiwezi kutatua changamoto ya maji hata robo ya Jimbo la Nkasi Kaskazini. Ndiyo maana tunasema kwa kuwa Mungu ametujalia kuwa na mito, maziwa na bahari kwa nini tusitumie vyanzo hivyo ambavyo ni vyanzo vya uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo linaniumiza naamini na wewe Mheshimiwa Waziri linakuumiza, wakati huu ndani ya Bunge tunazungumzia mafuriko na shida ya maji, kuna shida gani? Mungu ametujaliwa mvua za kutosha, lakini wakati huo ambao tunazungumzia mvua za kutosha zina athari zake lakini tunatumiaje sisi hiyo neema ambayo Mungu ametupa ya mvua nyingi kuweza kuvuna maji tukaepukana na hizi athari ambazo zipo leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Kilando ambako ndiko chanzo cha Ziwa Tanganyika kwenye Wilaya yangu ya Nkasi ni kilometa 64 kufika Namanyere, leo tunazungumza habari ya maji miaka nenda rudi. Kuna vitu ambavyo hatuhitaji kutumia nguvu zaidi, nimezungumzia kata tatu tu juu ya miradi inayoendelea hivi sasa ambayo haiwezi kumaliza changamoto hata robo kwa nini tutumie hiyo miradi midogo midogo ambayo haiwezi kumaliza changamoto badala ya kuja na fedha ambazo tunaamini kwamba tukitumia chanzo cha Ziwa Tanganyika hatutazungumzia wanufaika Nkasi peke yake, tutazungumzia Sumbawanga DC, Sumbawanga Mjini, Kalambo, mkoa mzima wa Katavi lakini itaunganisha na Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, tunazungumzia mradi wa uhakika ambao Serikali mkikaa utatusaidia. Pamoja na kwamba utatumia gharama kubwa lakini ni mradi ambao utakwenda kuwanufaika wananchi wengi na habari ya maji itakuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hiyo lakini hata hivi fedha chache tunazopeleka usimamizi wake ukoje? Pamoja na kwamba kuna mambo ya ajabu yanayofanyika kwenye miradi ya maji, lakini bado kuna changamoto ya watumishi, yawezekana hata waliopo uwezo wao ni mdogo; hao waliopo ni wachache hawawezi kutatua hizo changamoto za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali, pamoja na kwamba uhaba upo wa kutosha Serikali ni moja, Wizara ya Utumishi kama kweli maji ni kipaumbele lazima itoe vibali vya kuajiri watu hawa na watu hawa wapo shida ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda kumshauri tena Mheshimiwa Waziri hata wale watumishi wachache waliopo Wizara ya Maji wanatakiwa kupewa training. Yawezekana kuna maeneo ambayo sisi labda tuna bahati mbaya, tunapotumia wale local fundi wanafanya kazi nzuri lakini wale pia wanahitaji angalau wapewe elimu ya kila wakati waweze kutusaidia. Hata hivyo, kwa nini tutumie wale kama wapo waliomaliza wapo mitaani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie miradi hiyo ya maji, pamoja na kupeleka fedha ni vizuri tukawa na utaratibu wa umaliziaji wa miradi hiyo tunayoianzisha. Tunaanzisha miradi mbalimbali tunaiacha. Tunapopeleka fedha tunataka ku-achieve nini? Tunataka kumaliza changamoto ya maji. Kama hilo ndio lengo kwa nini hatufiki mwisho kwenye hiyo miradi ambayo tunaianzisha? Tusifikirie kuanzisha miradi mipya wakati hii tuliyonayo bado hatujaweza kufikia hitimisho na kufikia lengo ambalo tulikusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia kwa mfano ule Mradi wa Namanyere, toka mwaka jana wananchi hawapati maji. Tunaambiwa habari za pump, pump ni shilingi ngapi Mheshimiwa Waziri? Mnapokuwa mnafanya upembuzi si mnajua kwamba hapa kunahitajika pump? Inakuwaje mnafika mwisho mmefanya kazi mpaka asilimia 70 watu wanakaa miezi saba, miezi nane, mwaka mzima hawajapata maji kwa sababu ya pump, nini tunafanya? Natambua namna ambavyo unawajibika, lakini kuwajibika kama watendaji wako hawawajibiki kama wewe tutabaki kupiga story tu ambapo hazitatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nkasi Kaskazini tuna kata 17; hakuna kata hata moja yenye uhakika ambayo unaweza kusema tunapata maji. Mimi leo nitakupongeza kwa sababu ya uthubutu lakini tunapata shida sana kwenye Wizara yako ya Maji na inashangaza ni kama kilometa 64 kutoa maji Ziwa Tanganyika lakini mpaka leo tunalia juu ya maji, nafikiri hili haliko sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ugawaji angalieni utaratibu ni vigezo gani mnavitumia kwenye kugawa miradi ya maji. Kuna maeneo mengine tunapata changamoto na tunaanza kujifikiria shida itakuwa ni nini. Naomba nizungumzie katika hizohizo kata ambao zina miradi; Vijiji vya Itindi, Masolo, Lyele, Kanazi, Misunkumilo, Kolongwe, Kalila, Matine, Mkombe, Mpenge hayo maeneo yote hayana maji kabisa. Nakuomba utapokuwa unahitimisha hapa natamani na wewe ukaone yale maji yenye rangi ya njano ambayo wanakunywa wananchi wangu, uone kama kweli tunawatendea haki wananchi hawa. Ni Watanzania kama wengine na wanastahili kupata haki na ni wajibu wa Serikali kuwapelekea huduma ya maji ambayo ni safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami nizungumze machache kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na usafiri wa majini wa Ziwa Tanganyika. Ni vizuri kama Wizara, pamoja na changamoto za kibajeti na vitu vingine lazima tuwe na vipaumbele. Na Serikali yoyote makini lazima iwe na vipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba kuna ilani, kuna mpango wa miaka mitano, lakini lengo la mpango, lengo la ilani na mambo mengine, pamoja na kutenga bajeti ndani ya Bunge ni kupeleka huduma kwa wananchi wetu. Sasa kama hilo ndilo lengo, kipaumbele chetu ni nini kwa Wizara?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi ambao tunategemea Ziwa Tanganyika tukianza Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Kigoma pamoja na Songwe kule tuna wakulima, wakulima hawa Serikali imewekeza fedha za kutosha kwenye bandari. Sasa hizo bandari wakifikisha bandarini wanapelekaje tukizungumzia maeneo ya nchi za Jirani kwa mfano Kongo na Burundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea Serikali ilivyowekeza kwenye Bandari ya Kabwe, kuna kitu nilikuwa nataka kukipata kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, tunategemea kama tumewekeza kiasi cha kutosha kwenye bandari tukiwekeza zaidi upande wa MV Liemba wananchi wana uhakika wa kusafirisha mazao yao kupeleka nchi za Jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia pamoja na kwamba Nyanda za Juu Kusini tunaongoza kwa kilimo, tunatumia njia gani ya uhakika kuweza kusafirisha mazao yetu? Bado kuna shida. Kwa hiyo, tunapenda katika mgao wa hii miradi kuwe na vigezo vinavyoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Nyanda za Juu Kusini tunajua kuna kilimo lazima tutengeneze mazingira rafiki ya usafirishaji wa mazao yetu. Na njia rafiki ni pamoja na kurekebisha upande wa TAZARA. Kama hatujarekebisha TAZARA bado tunataka wananchi waendelee kulima kilimo cha mazoea ambacho hakiwezi kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha TAZARA, tuzungumzie pia hiyo MV Liemba toka imeanza kuzungumzwa. Bunge lililopita tulielezwa hapa kwamba wanasubiri huyu mnanihii asaini, lakini mpaka leo hapa nimeangalia kwenye kitabu cha Waziri anazungumzia kwamba mzabuni alikosa vigezo. Yaani toka Bunge lililopita mnazungumzia vigezo kama mnazungumzia habari ya kusaini, leo mnasema vigezo. Haya mambo hayafurahishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba kuna maeneo mengine yana vivuko, wana vitu gani lakini sisi kama hatuna speed boat, hatuna meli, lakini tunapozungumzia TAZARA bado tunahitaji ukarabati wa kutosha. Kwa maana hiyo kama kwenye ziwa imeshindikana usafiri wa uhakika, bado kwenye reli tunazungumzia ni changamoto. Tunataka kuwasaidia nini wananchi wa Mkoa wa Rukwa pamoja na Nyanda za Juu Kusini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, utakapokuja tunaomba kujua hatma ya Meli ya MV Liemba imefikia wapi na hivyo vigezo vitakamilika lini, na kwa nini muda wote huu mmechukua halafu mmegundua kwamba huyu mzabuni hana vigezo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia barabara ya Namanyere – Katongolo – Kipili. Huku kote ambako wameelekeza hizi fedha kuna bandari lakini cha ajabu hii barabara ina kilometa 64.8. Wamezungumzia kwenda bandarini lakini wameacha kilometa nane ambako kunatoa mpunga kupeleka bandarini. Sasa unashangaa tunataka kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nashauri wakati mnazungumzia kilometa 64 kama ndiyo lengo la kuwasaidia wananchi wale wavuvi pamoja na wakulima, ongezeni kilometa nane ambazo mtafika Kilando ambako ndiko wanakovuna na ndiko wanakotoa mpunga ili wapeleke bandarini, tutakuwa tunajua kwamba tumemaanisha kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilometa 64 za kutoka Lyazumbi – Kabwe; hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na ni vizuri mkawa mna rekodi nzuri za ahadi za viongozi wa Kitaifa. Haiwezekani viongozi wanaahidi lakini mambo hayo hayatekelezeki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ya kawaida hizi kilometa 64 za Lyazumbi – Kabwe hauwezi kuwekeza bandari pale ukaweka fedha zako za kutosha halafu hakuna lami ya kutoka pale kwenda bandarini. Sasa huyo mtu atakayepita kwenye hiyo bandari anataka kufanya nini? Kwa hiyo, ni vizuri kama Serikali imetangulia kuweka kitu tujue kabisa tunataka wananchi wafanikiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia tena barabara ya Chala – Mpalamawe, kilometa 40, ambayo inaunganisha Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi. Kwa kuwa ilikuwa ni ahadi na mkaingiza na kwenye ilani, sina shida na maandishi, shida yetu sisi watu wa Nkasi tunataka utekelezaji wa ahadi hizo ambazo tumewaahidi wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Sumbawanga Mjini kuja Namanyere ambayo imekwenda Katavi imetengenezwa vizuri, tena ikazinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Tunashukuru kwa mambo hayo ambayo Serikali imefanya. Lakini unawezaje
kutengeneza barabara hii halafu hakuna taa? Hivi inawezekana kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na pia namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunifikisha siku ya leo niweze kuchangia WIizara muhimu si kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa peke yake bali Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, toka nimeingia kwenye Bunge hili, Wizara ya Kilimo kila ilipowasilisha bajeti yake nimechangia toka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuzungumza niwashukuru sana kwa sababu hotuba zao zote wanapowasilisha huwa zinakuwa nzuri ila shida inakuwa kwenye utekelezaji wa hizo hotuba zao ambazo wanazileta ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na Mkoa wangu wa Rukwa, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikao inayozalisha zao la mahindi kwa kiasi kikubwa sana lakini leo Mkoa wa Rukwa tunaliona zao la mahindi ni kama zao la laana kwenye Mkoa wetu wa Rukwa. Pamoja na kwamba ni Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini na mikoa mingine Tanzania inayozalisha mahindi ningependa kujua hapa kwenye hotuba yako umezungumza kidogo sana Mheshimiwa Waziri. Kama zao la mahindi ni zao ambalo kwa sasa mmekosa ufumbuzi wa soko njooni na zao mbadala wananchi waachane na mahindi; wanatumia gharama kubwa kununua pembejeo na haiendani na bei halisi ya mahindi tunayolima sisi watu wa nyanda za juu kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mwananchi anakwenda tena kuvuna mahindi ya mwaka huu wakati msimu uliopita mahindi yapo ndani. Natambua kwamba Serikali haiwezi kuwapangia bei lakini ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha wananchi wake wanapata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo ningependa Wizara mnapokuja mtuambie ile mbegu ya mahindi inayotoka Zambia kama mmeiona ndiyo mbegu bora waambieni Watanzania na wakulima wa zao la mahindi wajue kwamba mbegu ile ndiyo inayostahili kwa sababu leo kama kweli wanafanya tafiti Wizara ya Kilimo, mbegu inayotumika na inayopendwa Zaidi ya wakulima wa nyanda za juu kusini ni mbegu inayotoka Zambia. Leo wakiamua kufanya jambo lolote mkumbuke kwamba tupo kwenye ushindani wa masoko, mnategemea wakulima wa Tanzania watakuwa kwenye hali gani. Ni vizuri mkafanya tafiti na mje na mkakati wa ziada kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi mbegu hizo zinapitishwa kwenye njia za panya. Serikali pamoja na kwamba Wizara ya Kilimo mnashirikiana na Wizara mbalimbali hapa kwenye majukumu yenu ni pamoja na kulinda hali ya wakulima pamoja na mbegu.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida kuna maazimio mbalimbali ambayo kama Watanzania tumeshiriki, Azimio la Maputo ya Nchi za Afrika la mwaka 2014 pamoja na nchi yetu ilishiriki ambapo maazimio yalifanyika kwenye kwa nchi zote za Bara la Afrika. Katika maazimio hayo ilikuwa ni pamoja na kuweka mahususi Sera za Kilimo ambazo zitaenda kuondoa umaskini kwenye Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia kwenye utekelezaji wa bajeti zetu na hayo maazimio ilikuwa ni kufikia mwaka 2025, leo tupo 2021. Nitatoa mfano tu kwenye utekelezaji wa bajeti, miaka mitano mfululizo bajeti ya mwaka 2016/2017 ilitekelezwa kwa asilimia 2.22, 2017/2018 asilimia 11, 2019/2020 asilimia 15 na 2020/2021 asilimia 26.46. Kwa maana hiyo miaka mitano imetekelezwa kwa wastani wa asilimia 19.3. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana nyingine miaka mitano Wizara ya Kilimo utekelezaji wa bajeti pamoja na kwamba tunatenga lakini imeweza ina maana kwamba asilimia 80.7 bajeti hii utekelezaji wake imeshindikana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kutenga bajeti lakini ni wajibu wa Serikali kupeleka fedha kama Bunge lilivyotenga. Na hapa kumekuwa na changamoto, kutenga bajeti ni jambo moja na utekelezaji wa bajeti hiyo ni jambo linginge. Tumekuwa na kauli mbiu nyingi Kilimo ni Uti wa Mgongo, kilimo sijui ni kitu gani sisi hatuna shida na slogan, tuna shida na utekelezaji wa kilimo. Na kama kweli lengo ni kuwasaidia vijana wa nchi hii, tunawezaje kutekeleza suala hilo kwa kupeleka fedha kama hizi kwenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine, mbegu hiyo ambayo leo kaka yangu Mheshimiwa Mhagama alisema katika vipaumbele vyenu vya Wizara kwamba ni vizuri mngeanza na masoko. Narudia tena katika michango yangu yote ya miaka yote pamoja na kutafuta masoko, lazima tuwekeze kwenye utafiti kwenye suala la kilimo. Hauwezi kutafuta masoko kama mbegu zako asilimia 60 ya Taifa hili ya mbegu tunaagiza kutoka nje, haiwezekani. Tunaingiaje kwenye ushindani wa masoko kama mbegu ndo hizi asilimia 60 unategemea kutoka nje, tunaaminije wale watu wa nje watafanya sisi tuongoze kwenye biashara kwenye mazao tunayolima wakati wao ndio wanatuletea sisi mbegu kwa asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba mnajitahidi, Waziri na Naibu wako lakini mtajitahidi kama mnapewa fedha kama tunavyokuwa tumetenga ndani ya Bunge. Haitawezekana kwa maneno matupu kufikia malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kupitia Ripoti ya CAG kuna mambo kadhaa ambayo yamezungumzwa pale na katika mambo hayo ni pamoja na udhibiti mbovu wa mbegu na pembejeo kutoka kwenye Wizara yako. Sasa kama malengo ni kusaidia Taifa letu, hatuwezi kushindwa kudhibiti tukategemea malengo/matokeo chanya kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, ni vizuri kama kweli tunaamini kipaumbele kitakwenda kukomoa umaskini wa Taifa letu, tuweke kilimo kama kipaumbele kwa kuwapatia fedha, pembejeo lakini tukawekeze kwenye tafiti kwa kupima udongo kama nyanda za juu kusini imeshindikana mahindi, tujue ni zao gani ambalo tutapeleka iwe mbadala wa mahindi lengo tu ni kuondoa umaskini na kuwasaidia wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia pamoja na hayo, wakulima hawa wana hali ngumu sana. Tunapozungumzia mikopo ya kilimo, hiyo Benki ya Kilimo hebu mje siku moja mtuambie hapa mikoa hii ambayo inazalisha sana ni wakulima wangapi wamenufaika na mikopo inayotokana na Benki ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna danadana nyingi lakini ukiangalia maneno kwenye hotuba mbalimbali inaonesha kabisa fedha zinatoka, zinakwenda, zinakwenda kwa nani mbona hatuyaoni matokeo kwa wakulima wetu kama kweli wanapewa hiyo mikopo? Kuna mazingira ambayo lazima tubadilishe pamoja na kwamba vipaumbele vinakuwa vingi, tuje na kipaumbele kimoja ambacho lengo ni kumkomboa mkulima na Mtanzania, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda ulionipatia ili niweze kuzungumzia changamoto ambazo zinawakumba wananchi wa Nkasi Kaskazini. Kutokana na umuhimu wa Wizara hii nitachangia mambo machache kwa kuwa mengi yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuhusiana na namna ambavyo Waziri pamoja na Naibu wake na Cabinet yote wanavyowajibika kwenye nafasi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mazuri ambayo mnayafanya hasa kupitia miradi ya REA bado kuna changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza, kutokana na ukubwa wa hii miradi ambapo imesambaa maeneo mbalimbali TANESCO wanakabiliwa na changamoto ya usafiri. Kama tunavyoona kuna mambo mazuri mmeyafanya lakini bado kuna changamoto kwenye uzuri wake wa jambo hilo la usafiri. Kwa hiyo, kwa sababu Serikali ina nia njema kuwafikishia wananchi huduma ya umeme, basi tuone namna bora ambayo tunaweza tukaifanya ili hawa TANESCO waweza kuwajibika inapotokea changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la REA, naungana na Wabunge wote ambao tumekwenda kufanya research ya kutosha na Mheshimiwa Waziri anajua tumekwenda Manyara, Singida na maeneo mengine, wakisema wamepeleka umeme kijiji fulani utakuta watu wachache tu ndiyo wamepata lakini lengo la Serikali ilikuwa wananchi wote sio wachache. Kwa maana hiyo turudi kwenye lile lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hii ya umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini katika tafiti chache ambazo nilizifanya kwenye Kamati yetu ya PAC tulivyozunguka si kwamba wananchi hawataki kupata huduma ya umeme au hawataki umeme majumbani mwao, kuna watu ambao hata hiyo Sh.27,000 ni changamoto. Sasa kama lengo ilikuwa ni hilo na tumeingiza fedha za kutosha ili kupeleka miradi, kwa nini Serikali isibebe jukumu hilo la kuchukua hiyo Sh.27,000 wananchi wakapelekewa huduma na wakaanza kukatwa taratibu taratibu kulingana na huduma ambazo wanazipata? Naamini wananchi wengi watafurahia jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizo, katika Jimbo langu lenye vijiji 49 vijiji 9 havina huduma ya umeme kabisa. Vijiji hivyo ni Itindi, Sentamapufi, Lyele, Matine, Mienge, Mpenge, Kalila pamoja na Mkombe. Natambua kwamba kuna maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu kama Jimbo langu, kuna vijiji ambavyo unavuka ziwa ndio unakwenda pembeni unawakuta wananchi na wale wananchi wanajishughulisha na uvuvi na leo tunasema kwamba waende kwenye viwanda lakini umeme haujafika. Kwa hiyo, bado wanaendelea na uvuvi uleule kama tunavyosoma historia ya Yesu walivyokuwa wanavua ukishapita muda fulani hawajauza samaki wale wanaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali kwa kuwa lengo ni jema pia tuangalie yale maeneo ambayo yana umuhimu zaidi. Natambua kwamba wote wanafanya kazi na wanahitaji kupewa umeme, kuna wengine wanatumia kwa ajili ya mwanga peke yake lakini tunatazama miradi hii ya REA namna ambavyo itasaidia pato la Taifa kwa wananchi kuweza kuendelea na majukumu yao kupitia suala la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia kukatika kwa umeme na hili ndilo limenifanya nisimame hapa. Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla umeme unakatika isivyo kawaida. Imefikia mahali kwa sababu watu walisahau vibatari na taa lakini wanaona ni bora walikuwa wakiweka mafuta kwenye taa anajua haya mafuta niliyoweka yatanitosha mpaka kesho nitaweza kununua mafuta mengine lakini leo umeme umekuwa haueleweki yaani unaweza ukakatika zaidi ya mara saba. Mheshimiwa Waziri na sisi watu Nkasi ni Watanzania; kuna wafanyabiashara, kuna wamama kule wameamua kutengeneza juisi na vitu vingine, tungependa kujua tatizo ni nini. Pamoja na kwamba umeme unapokatika wenye wajibu wa kutoa taarifa ni TANESCO kwamba kwa nini umeme umekatika na utarudi baada ya muda gani lakini mambo haya hayafanyiki na ni mazoea tu ambayo yanaendelea. Sasa hawa wananchi kwa sababu hii ni huduma tunahitaji basi kuwajibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye jambo hili naomba pia Kitengo cha Emergency, kama neno lenyewe emergency bado kuna changamoto hakuna emergency tena sasa hivi. Ni vizuri tukaboresha kitengo hicho kiwe emergency kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa navyozungumza Kata za Kalando na Itete toka jana mchana mpaka leo wako gizani. Sisi tupo mpakani mwa Congo na Burundi amani ya nchi yetu inakuwaje kama watu wako gizani? Ni lazima tuwape kipaumbele watu wa mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijasimama hapa kuchangia nimeongea na Meneja wa TANESCO anasema ni tatizo la nguzo kuungua toka jana, ni vizuri tukaboresha kitengo hiki. Kama lengo la kupeleka REA ni kuwahudumia wananchi basi tuboreshe na hivyo vitengo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kabla ya yote naomba kutoa pole kwa Jimbo langu la Nkasi Kaskazini na kwa wazazi wa binti huyu kwa kuwa ni mpiga kura wangu, Petronela Mwanisawa aliyenyongwa na mpenzi wake. Kwa mazingira ya kawaida miongoni mwa mikoa ambayo bado tulikuwa nyuma sana kielimu ni pamoja na Mkoa wa Rukwa. Inapotokea hasa tena kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 22, kwa mazingira ya wazazi kama wale wa Mkoa wa Rukwa, inatia uchungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua umekuwa mtetezi sana wa wanawake na umetoa mwongozo wako vizuri, lakini ni vizuri Serikali ikaliangalia jambo hili. Leo tunapoona adui wa kwanza sasa wa kumaliza maisha ya wanawake ni pamoja na mahusiano ya kimapenzi, iwe kwenye ndoa au mahusiano ya kawaida. Ni vizuri jambo hili likaangaliwa vizuri. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, nami napenda kuchangia Wizara hii na kabla sijachangia niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na cabinet yake. Nawapongeza zaidi kwa sababu Waziri na Naibu wake wamekuwa wasikivu na kuchukua hatua pale ambapo matatizo yanajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yangu ya Nkasi ni miongoni mwa wilaya ambazo zina migogoro ya kutosha juu ya wananchi na Hifadhi au Mapori Tengefu. Nitaanza na suala la mipaka katika Hifadhi kwa Mapori Tengefu. Nilizungumza ndani ya Bunge na Waziri Mkuu akatoa maelekezo kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii kulingana na uzito wenyewe, lakini hapa nazungumza kulingana na mgogoro huo, imefikia mahali sasa wananchi walifikia hatua mpaka kumuua Game, jambo ambalo siyo zuri. Leo limefanyika Nkasi, litaendelea maeneo mengine. Lazima mfanye uchunguzi wa kutosha, nini kinapelekea migogoro hii kuendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya yangu ya Nkasi nitataja kata chache tu ambazo zina migogoro. Kata ya Kabwe, Kata ya Kilando, Kata ya Kipili, Kata ya Kipundu na Kata ya Nkomoro. Nilifanya utafiti wa kutosha baada ya hii migogoro kuona inaendelea sana. Ukienda Kata ya Kirando, Kata ya Kipili, Kata ya Kabwe, mpaka wa kwanza kabisa uliwekwa mwaka 1948. Ukiangalia huo mwaka, idadi ya wakazi ilikuwa ni ya watu wachache sana. Huo mpaka ukabadilishwa mwaka 1992, ukabadilishwa tena mwaka 2002. Sasa ulivyobadilishwa mwaka 2002 ukarudishwa tena, kule kwenye ule mpaka uliowekwa mara ya kwanza mwaka 1948. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona hapo idadi ya watu imeongezeka kiasi gani kutoka mwaka 1948 mpaka leo mwaka 2021. Pamoja na kwamba mawazo ya Wabunge wengi tumekuwa tunaomba tuongezewe ardhi kutoka kwenye Mapori Tengefu au kwenye Hifadhi, jambo hilo halitakuwa suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri Wizara, kwa sababu, idadi ya watu inaongezeka, kuna haja kubwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Wizara inayohusika na mazingira, TAMISEMI, Uvuvi, pamoja na hizo Wizara ambazo Mheshimiwa Rais aliona kuna umuhimu wa wao kukaa pamoja, kuna haja ya kwenda kupitia mipaka hii upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama leo maumivu waliyonayo wananchi wetu, wanaona ni kama Serikali ya Tanzania inaheshimu zaidi wanyama kuliko binadamu. Lazima tuwaondoe kwenye hiyo dhana. Tunaiondoaje? Matamko na makatazo bila mbadala, haina maana yoyote, inaleta unyanyasaji kwa wananchi wetu. Leo mkiwaambia wananchi hawa wako kwenye Hifadhi, Serikali ni moja, mnajua kwamba idadi ya watu inaongezeka. Hiyo mipaka ya mwaka 1948 kwa hali ya kawaida, kulingana na idadi ya watu inavyoongezeka, lazima migogoro itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima Serikali ije na mbadala. Ukisema hii ni Hifadhi, lazima tuungane kwa pamoja tutenge eneo lingine. Kwa sababu, wengi wanaoathirika na hii mipaka ni wakulima, ni wafugaji na wavuvi. Lazima tutafute eneo mbadala na hapo tutakuwa tumekwenda kuondoa tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo jambo ni vizuri nikaliweka sawa. Adhabu zinazotolewa na watu wa TAWA, TANAPA na wengine wote, ni adhabu ambazo ni za ajabu sana. Wananchi wananyanyaswa. Mambo yaliyokuwa yanafanyika na Wakoloni, yanafanyika kwa watu wa TAWA. Jambo hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekwenda walipokuwa wanaadhibiwa watu wa mpaka ule wa Korongwe, nilimwambia Mheshimiwa Waziri, mzee anapigwa, amekutwa nyumbani. Pia kuna mama amejifungua, ana siku mbili, nyumba yake inachomwa. Anaenda wapi na huyo mtoto? Yaani imefikia mahali haki za binadamu hazipo tena. Haya mambo hayakubaliki, hayakubaliki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo hilo, inapotokea mwananchi ameliwa na mamba, ameliwa na kiboko, mnachelewa sana ku-react ninyi Wizara ya Maliasili, lakini ikitokea mwananchi amekamatwa na aidha, nyama nyamapori kidogo, adhabu anayopewa ni wakati huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea pia mfugaji amekamatwa kwenye Hifadhi, adhabu wanazopewa zinaanzia siku hiyo hiyo. Hapa nina risiti kadhaa za wafugaji ambao wamepewa adhabu. Ukifuatilia ule mgogoro pia kuna watu wenu ambao ni watendaji ambao sio waaminifu, wanachukua ng’ombe zilizokuwa nje huko wanazipeleka ndani kwenye Hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo, unajiuliza, kama wakazi wanaweza wakajenga nyumba, wakajenga shule, wana mashine pale za kusaga, hawa watu wa hifadhi walikuwepo. Wanakwenda kuchoma watu wamekaa zaidi ya miaka 10, miaka 20 Serikali ilikuwepo. Kwa nini mnashindwa kufanya hayo mambo mapema? Inatuonyesha kwamba kuna mambo yanayofanyika juu ya hao watendaji wachache, ambao wanawaingiza wafugaji pale kwa mkataba na siku hiyo wasipowapa fedha, wanakwenda kufanya maamuzi kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna sehemu rushwa zipo, ni pamoja na eneo hili, ni lazima liangaliwe vizuri. Nakumbuka kauli ya Mheshimiwa Rais akiwa ndani ya Bunge kwenye hotuba yake ya mwisho, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, juu ya maliasili zinazopatikana ndani ya Hifadhi. Lile jambo alilolitamka ni vizuri sana, lakini kuna haja ya kufanya utafiti wa kutosha kwenye maamuzi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama hata wale wananchi ambao wanaibua labda madini, namna wanavyochukuliwa na wale watu wa TAWA, TFS, adhabu wanazopewa; kitendo cha kusema hapa nimegundua kuna madini; pamoja na kwamba ni nia njema ya Serikali leo kuruhusu madini na vitu vilivyoko kwenye Hifadhi kuvunwa, ni lazima tuwe na utaratibu mzuri utakaotumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kugundua, pia watu ambao ni wa eneo lile waweze kuwa wanufaika wa kwanza ili tuweze kuleta uthamani. Kwa sababu mimi naamini wahifadhi namba moja ni wale watu ambao wako karibu na Hifadhi. Jambo hilo likitumika kwa busara hiyo naamini kila mtu anapenda uhifadhi. Sasa tunahifadhi kwa ajili ya nani? Tunahifadhi kwa ajili ya wananchi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Mungu akubariki. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Na mimi naunga mkono hoja ya kuridhia Mkataba huu wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania siyo kisiwa na sisi tuko ndani ya Afrika, na mimi pia najivunia kuzaliwa Afrika. Pamoja na maamuzi ambayo Serikali imefanya kupitia Wizara, tunawapongeza sana kwa maamuzi haya, lakini mimi nitakuwa na mambo machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhia ni jambo moja lakini lazima tujipe muda wa kufanya tafiti za kina, faida ambazo tutakwenda kunufaika kama nchi lakini Watanzania ni namna gani tumewaandaa ambapo wanaweza kunufaika na maazimio haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kwamba kama tunatambua tunaingia kwenye ushindani lazima tujue mshindani wetu ana nini na sisi tuna nini. Lazima kuandaa bidhaa ambazo tunaamini ndiyo hitaji kwenye biashara hiyo. Kwa mazingira hayo hayo tumekuwa na kasumba fulani tukiamini kwamba watu fulani ndio wanastahili kuwa wafanyabiashara. Kupitia hii nafasi lazima tuanze kuwandaa Watanzania ambao wanaweza wakawa ma-supplier kwenda kwenye nchi nyingine za Afrika, hiyo itakuwa ni faida mojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia ushindani lazima kuna vitu vinavyoitwa vikwazo. Lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa uwekezaji pamoja na wafanyabiashara ambao tunaamini kwetu tutakuwa tumeitumia hiyo fursa kama nchi. Pamoja na kuangalia ni kipi ambacho tunaweza tukatumia kama fursa baada ya kuridhia, lazima pia tujenge uaminifu. Tusipojenga uaminifu pia ni changamoto. Uaminifu wetu utatengeneza mazingira rafiki ya watu waliopo nje kuja kwetu na sisi kujijengea mazingira ambayo hata mtu ambaye alikuwa hajawahi kufikiri kupitia tu ile sifa ya mtu mwingine ambaye aliona uaminifu wetu tunaendelea kutangaza Taifa letu na kunufaika na hayo maazimio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la teknolojia lazima tuone kama hilo jambo ni kipaumbele. Lazima tuachane na biashara za mazoea tuanze kuwandaa Watanzania kutumia teknolojia kuweza kunufaika kwa kuangalia huu mkataba ambao tunaamini utalisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri pia tuangalie sera zetu ni rafiki kiasi gani. Mara nyingi tumekuwa na mabadiliko sana ya hizi sera, lazima tuwe na sera ambazo hazitawapa shida hizo nchi wanachama ambazo tumeamua kuingia nazo kwenye Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzungumza yote ambayo Wabunge wenzangu wamezungumza hatuwezi kukwepa biashara mtandao, lazima tujijenge kwa kuanza kuwaandaa vijana wetu, kabla ya kufikia hayo malengo ambayo tumejiwekea, lazima tuanze kuwaandaa leo. Wafanyabiashara waliopo ni wajibu wa Serikali kuona namna bora ya kuwatengenezea network lakini kuna wale ambao lazima tuwaandae sisi, tutengeneze mabilionea wengine, tusifikiri walewale ambao walikuwepo kuanzia mwaka 2010, leo tuanze kutengeneza wengine ili na sisi tuweze kunufaika kwenye huu mkataba ambao tumekwenda kuridhia.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mazingira yote ni lazima tujue sisi kwa upande wa kilimo ni mazao gani ambayo yana-pick kwa Bara la Afrika kutoka Tanzania, lazima tuwe tunatumia hiyo nafasi. Tusisubiri baadaye tukiwa tumechelewa, ni nini kinahitajika tunaanza sisi kwanza kuitumia hiyo fursa. Leo tunahangaika na mahindi, kama mahindi hayalipi lazima muwe mmeshaangalia mapema, kama siyo mahindi ni kipi mbadala? Tunakiandaa mapema kwa ajili ya kutumia hiyo nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa leo ni kupongeza na kuendelea kuwasisitiza kwamba lazima tuendelee kufanya tafiti za kina, faida ni zipi, hasara ni zipi. Lakini kuna mengine yanaweza yakawa kama challenge kwetu ikawa kama fursa lazima tuitumie kwa sababu tunaamini itasaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu kwa kuzingatia mambo muhimu ili kufikia uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda cha mbolea; kulingana na umuhimu wa kilimo katika kukuza viwanda au uchumi ni vyema kutazama hitaji kubwa la bei kubwa ya mbolea; ili kumaliza tatizo hilo tujenge kiwanda cha urea.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wafanyabiashara kufunga biashara zao; kumekuwa na mabadiliko makubwa kutoka kwa wafanyabiashara badala ya kuongeza wafanyabiashara inakuwa kinyume chake. Nashauri Serikali kufuatilia suala hili ili kuendelea kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa wapewe elimu pamoja na malalamiko mengi ya wafanyabiashara wengi nchini kwenye halmashauri zetu, lakini huko kuna Maafisa Biashara inaonekana wafanyabiashara sasa hawaoni umuhimu wa Maafisa hawa kwani miongoni mwa majukumu ni pamoja na kutoa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya sukari kuendelea kupanda; Wizara ina mkakati gani wa kuweza kudhibiti bei ya sukari kwani suala hili linaathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wa hali ya chini. Pia nataka kujua kununua sukari nje ya nchi kunapunguza bei ya sukari au inaongeza bei kwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi ya huduma; suala hili limekuwa na changamoto kubwa kwa wafanyabiashara pia lina wafanya wafanyabiashara wetu kukata tamaa na wengine kuhama. Nashauri Serikali kuleta marekebisho ya sheria hiyo ndani ya Bunge letu ili ifanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya biashara yasiyotabirika; kumekuwa na shida kubwa kwa taasisi mbalimbali zinazohusiana na mambo ya biashara, matamko ya mabadiliko ya kila wakati kuhusiana na biashara nchini. Nashauri Serikali kupitia upya kauli zake ili kabla haijatoa tamko lolote izingatie mazingira halisi ya wafanyabiashara wetu nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kulingana na umuhimu wa Wizara hii na mambo ya ugaidi yanayoendelea nchini na duniani kote, nitakwenda kuchangia mambo kadhaa ili kushauri Wizara hii ambayo ni muhimu kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazoidhinishwa na Bunge zipelekwe na kutolewa kwa wakati, naishauri Serikali kuzingatia maazimio ya Bunge ili kuleta ufanisi kwa Jeshi letu pia ufanisi wa utendaji kazi wa Jeshi lenyewe na kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya wanajeshi na wananchi, kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi hususani wale wanaozunguka maeneo ya Jeshi kunyang’anywa maeneo yao kwa nguvu na kuwatesa wananchi wanaozunguka maeneo ya Jeshi, hali sio nzuri wala haileti sura nzuri kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho ya chakula kwa wanajeshi ni vyema Serikali kulipa jambo hili umuhimu mkubwa ili kuleta motisha kwa wanajeshi wetu na familia zao, kwani wanajeshi wakiwa na manung’uniko ni hatari kubwa hasa kwa kuangalia umuhimu wao katika masuala ya ulinzi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa za mafunzo kwa wanajeshi kumekuwa na utaratibu mbaya sana kwa wanajeshi wa nchi yetu wanapotaka kujiendeleza kimasomo, wengi wao wanajitegemea wenyewe. Suala hili linaweza kuondoa utendaji bora, kwani pesa ambayo alitakiwa kusaidia familia zao ndiyo analipa masomo, inawakatisha tamaa wanaotaka kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upandishwaji wa madaraja, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wanajeshi waliokidhi vigezo vya kupandishwa madaraja, nashauri Serikali kufuatilia jambo hili kwa busara kubwa na kumaliza tatizo hili ili kuleta motisha ya kazi kwa wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanajeshi waliopata mafunzo na baadaye kuachwa mitaani bila kazi kuna athari kubwa sana kwani vijana hawa wanapewa baadhi ya mafunzo ambayo ni ya kijeshi ambayo kwa kubaki kwao mitaani inaweza kuwa hatari kubwa zaidi kwa nchi yetu, ni vyema Serikali ikabadilisha utaratibu ili kulinda nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwe inawaandalia kazi za kufanya baada ya kutoka kwenye mafunzo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kuwa ni Wizara ambayo ni muhimu sana kwa kuliletea Taifa letu fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la katazo la kutumia mkaa; bado kuna changamoto kubwa katika ukamataji, naomba Wizara hii ishirikiane na Wizara ya Muungano na Mazingira kwa Maafisa Mazingira pamoja na Maafisa Misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro kati ya wananchi na maeneo ya reserve; kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwa wananchi wetu katika maeneo yao ambayo yanazunguka reserve. Ni vema Wizara hii ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi ili kupima maeneo yao na kutatua migogoro hiyo ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ya kifuta jasho imepitwa na wakati. Ni vyema Serikali ikaleta sheria hii Bungeni ili ifanyiwe marekebisho kwani imepitwa na wakati. Ni vema Wizara ikachukua hatua ya haraka kwani wananchi wana malalamiko ya muda mrefu kuhusu mazao yao yanayoliwa na wanyama, lakini kifuta jasho hakikidhi athari zinazowakabili baada ya mazao kuharibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maporomoko ya Kalambo; Wizara ichukue hatua kwa maporomoko haya kwani tunatumia nchi mbili lakini nchi ya Zambia inafaidika zaidi. Naomba kushauri Serikali kuwekeza fedha kwenye maporomoko haya ili na sisi tunufaike kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tubadilishe aina ya matangazo yetu ya utalii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia Wizara hii ya Madini kulingana na umuhimu wake kwa vizazi vilivyopo na vijavyo katika kulinda rasilimali zetu za nchi yetu kwa kuzingatia mambo muhimu katika kuhifadhi rasilimali zetu.

Mheshimiwa Spika, Wachimbaji Wadogo. Kumekuwa na malalamiko makubwa kwa wachimbaji wadogo nchini. Nashauri Serikali kubadilisha utaratibu wa kuwatia moyo kwa kutatua changamoto zao kwa wakati kwani nao ni muhimu.

Mheshimiwa Spika, mikataba inayolalamikiwa ifanyiwe marekebisho. Kumekuwa na malalamiko kuwa kuna baadhi ya mikataba ambayo pia inafanya baadhi ya wawekezaji kuona kwao ni kikwazo kuja kuwekeza nchini. Ninashauri Serikali mikataba hiyo ipitiwe upya.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini. Nashauri Serikali itimize wajibu wake kikamilifu kwani Tume hii ikitimiza wajibu wake kwa uhakika na kwa muda mwafaka kutaleta matokeo chanya kiutendaji na pia kulipatia taifa letu mapato kwani wataweza kutatua kero nyingi na baada ya kutatua tutaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Utafiti ya Madini. Tume hizi ni vyema zikawa zinaleta matokeo yanayotokana na tafiti wanazozifanya kwenye maeneo mbalimbali nchini ili wananchi ambao si wataalam lakini wamekuwa wakigundua madini mbalimbali nchini. Ni vyema pia kuwatia moyo wananchi hawa kwenye maeneo mbalimbali hata kwa kuwapa maeneo ili kujua na kutambua michango yao.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na vifo mbalimbali kwenye maeneo ya uchimbaji kwenye maeneo au machimbo ambayo yamekuwa yakiathiri nguvu kazi ya Taifa. Nashauri Serikali kufuatilia kwa ukaribu mambo yanayopelekea vifo vya kila wakati kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, kutoa elimu maeneo yanayopatikana na uchimbaji wa madini. Kuna maeneo mengi ambayo wananchi wanaozunguka migodi. Serikali itoe elimu kwa wananchi juu ya athari ambazo wanaweza kupata kutokana na vifaa au sumu zinazoweza kutumika katika uchimbaji wa madini kwenye maeneo ambayo yanachimbwa popote nchini.

Mheshimiwa Spika, Soko la Madini. Nashauri Serikali itumie Umoja wetu wa Afrika Mashariki kama fursa kwa kufanya tafiti la soko kulingana na aina ya madini tuliyonayo nchini kwetu ili kuwasaidia wachimbaji wetu na kulisaidia taifa kwa ujumla. Hii itawanufaisha wananchi wanaozunguka maeneo yote ya uchimbaji madini nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia Wizara hii ya Nishati ambayo ni Wizara muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kisiasa. Sasa nitashauri mambo kadhaa katika Wizara hizi.

Mheshimiwa Spika, soko huria kwenye usambazaji wa umeme; kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu usambazaji wa umeme ukiwa wa kusuasua, hivyo nashauri Serikali kukubali suala la soko huria ili kuleta ushindani na kuleta tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, umeme wa upepo; Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza nguvu ya kipesa na kutoa kipaumbele kuwasaidia watumiaji wengi ambao wana hali ya chini ili waweze kutumia umeme ambao utakuwa wa bei nafuu na utawanufaisha wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Umeme Vijijini; kumekuwa na malalamiko makubwa juu ya mgao wa umeme unavyotekelezwa kwa kuwa kuna kuruka baadhi ya vijiji aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Ni vyema suala hili likafuatiliwa kwa ukaribu na umakini mkubwa sana ili kuondoa malalamiko yanayowakabili wananchi wengi.

Mheshimiwa Spika, TANESCO wapewe ushindani; TANESCO wamekosa ufanisi kiutendaji kwa sasa wanafanya kazi kwa mazoea, ni vyema kuwe na makampuni ili kuleta matokeo chanya na kuleta ufanisi kwa utekelezaji wa ugawaji umeme na nidhamu kwa matumizi ya pesa.

Mheshimiwa Spika, suala la umeme jazilizi; kumekuwa na ubaguzi mkubwa na watu wengine kujiona wanyonge pale wanapoona wananchi wengine wanapata umeme huku wengine wakikosa wakati wako eneo moja. Pia maeneo ya taasisi yepewe kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, wakandarasi walipwe kwa wakati; kumekuwa na changamoto kubwa katika utendaji pale ambapo inatokea mkandarasi hajapewa malipo yake inapelekea kazi na miradi mbalimbali kusimama na kupelekea wananchi kuinuka kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, bei halisi ya kuunganisha umeme; kumekuwa na mkanganyiko wa bei halisi ya umeme kwa wananchi wanapokuwa wanatakiwa kuunganishiwa pale ambapo REA inaishia bei zao zimekuwa tofauti kwa wananchi. Nashauri Serikali kufuatilia jambo hili na kutoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyobakia katika Mkoa wa Rukwa; tunaomba kujua ni lini maeneo hayo yatapata umeme kwani maeneo hayo yaliyobaki yakipata umeme yatasaidia kupunguza vifo vya akinamama na mtoto pia itawasaidia watu kiuchumi katika viwanda na biashara ndogondogo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Kamati ya Sheria Ndogo kwa kazi ambayo wameifanya na kutuletea taarifa ambayo kweli inaoneka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sheria ambazo zinawakuta wananchi moja kwa moja hasa wa kule chini ni Sheria Ndogo. Kazi ya Bunge ni kutunga sheria na baada ya kutunga sheria kabla haijaanza kutumika zinatungwa kanuni na hapo ndipo kumekuwa na shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa mjumbe wa Kamati kwa Bunge lililopita Kamati ya Sheria Ndogo kulikuwa na makosa mengi sana yakiwepo ya uchapaji, kulikuwa na makosa ya uandishi wa sheria. Lakini nimpongeze kipekee Mheshimiwa Jenista alichukua hatua kubwa sana, lakini katika mambo ambayo tumekuwa tunashauri kila wakati ni pamoja na semina elekezi kwa wanasheria wetu wa halmashauri na hili jambo bado Mheshimiwa Waziri halijafanyika ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ugundue kwamba kuna shida bado kumekuwa kuna tatizo aidha la uwezo mdogo wa wanasheria wetu kwenye halmashauri inafikia mahali yaani mtu anachukua sheria ya Tabora anaipeleka Nkasi ya Nkasi anapeleka Kalambo yaani imekuwa ni ku-copy na ku-paste hawana tena muda wa kufanya research. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja sasa ya kutokuwa na haraka ya kutunga kanuni zetu tuwape muda wa kutosha wakafanye tafiti kuangalia uhalisia kabla hawajatunga kanuni zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sheria itungwe kunakuwa kuna uhitaji sasa sasa hivi kumekuwa na shida kidogo ukizungumzia ukusanyaji wa mapato kila mtu anataka aonekane amefanya vizuri na hapo ndipo shida inapoanzia. Zinatungwa sheria ambazo ni kandamizi zinaenda kuwakandamiza wananchi ili mradi tu mtu aweze kukusanya vizuri kuna haja ya kufanya utafiti wa kina kwenye hizi sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Sheria za Ushuru, miongoni mwa Sheria ambazo ni kero kwa watanzania tena wananchi wa kawaida ni Sheria za Ushuru, Tozo pamoja na Ada. Kuna haja ya kupitia eneo hili tuliangalie upya, lakini sheria nyingine ni Sheria za Wavuvi. Nilikuwa najiuliza hivi kuna wakati tunatunga hizi kanuni kumfurahisha nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza wavuvi kwa mfano haya maziwa mawili tu; Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ukitazama Ziwa Tanganyika kuna nchi zaidi ya moja wanaotumia kwa ajili ya uvuvi hilo Ziwa Tanganyika, lakini tunatunga sheria za kuwaumiza wavuvi wetu halafu wavuvi wengine ziweze kuwanufaisha kwenye nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuachane na mfumo wa kufikiri sheria za kikoloni kama tunataka kukusanya mapato, kama tunataka tuongeze pato la Taifa kwenye uvuvi lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa wavuvi ni pamoja na sheria zetu ambazo zitawasaidia wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kanuni ambazo ni za ajabu nani za hovyo za mwaka 2009 zimeletwa hapa baadhi tunashukuru Mheshimiwa Waziri amechukua hatua kwa baadhi ya kanuni kuziondoa na kutolea matamko na nini. Lakini matamko haya kama hayatawekewa msingi hayana maana yeyote. Shida ipo kule kwenye utendaji kwa mfano kama waliokuwa wanatunga kanuni walifanya research kwenye Ziwa Victoria ukapeleka hizo kanuni ziende Ziwa Tanganyika ni kwenda kuwandamiza wavuvi wa Ziwa Tanganyika ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, kuna haja kabla hatujatunga kanuni zetu wao wanapewa muda wa kwenda kuangalia mazingira halisi kabla ya kutunga kanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili suala litakwenda vizuri hasa kabla hatujatunga tukiwashirikisha wadau, wahusika wa hiyo kanuni inayokwenda kuitunga kumekuwa na shida ya ushirikishwaji. Ukimshirikisha mtu siku moja mtu anayetoka Nkasi, anayetoka Kigoma si rahisi kuja Dodoma hapa kutoa maoni yake tutoe muda wa kutosha ili tuwashirikishe na wale wakitoa maoni yao maana yake nini, utekelezaji wake wa hiyo sheria inakuwa ni rahisi kwa sababu wameshiriki kikamilifu, wameshiriki kutoa maoni yao kulingana na uhalisia wa mazingira ambayo wanatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dosari za uandishi wa sheria, kabla sheria haijafika mwisho kuna hatua kadhaa. Sasa mpaka inakuja kuonekana mwishoni kazi ya kamati hii si kwenda kuangalia makosa ya kiuandishi si kazi yake Kamati ya Sheria Ndogo. Lakini saa hizi wamekuwa wanatumia muda mwingi kuangalia makosa yaliyopo kwenye Sheria wakati wapo watu ambao hizi sheria zimepita mikononi mwao. Lazima tuangalie tatizo lipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye Sheria hizi ukiangalia tunajikita zaidi kwenye kuweka adhabu kwenye Sheria Ndogo kwa nini tunajikita kwenye adhabu? Na imekuwa shida sana ya uandaaji wa hizi kanuni tunajikita zaidi kwenye kuweka adhabu kwenye Sheria Ndogo kwanini tunajikita kwenye adhabu, na imekuwa ni shida ya uandaaji wa hizi kanuni, tunajikita zaidi kwenye kwenda kukusanya na adhabu kwa mwananchi. Lakini hakuna sehemu ya uwajibikaji wa Serikali wanapokuwa wanatunga hizo sheria lazima tubadilishe fikra zetu tunapokuwa tunatunga hizo kanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zaidi Sheria kukiuka haki za binadamu hizi kanuni. Sheria yeyote inapokiuka haki za binadamu au kukiuka Katiba kwa maana Sheria Mama inakosa sifa ya kutumika. Lakini huko vijijini wananchi wetu wanaumia sana unakuta Sheria au Kanuni bado haijawa Gazetted imeanza kutumika na imeanza kuadhibu wananchi. Nani anawajibika kwenye jambo hilo si wananchi wote wanaweza kujua kwamba hii bado haina sifa ya kutumika hii sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Jenista amejitahidi makosa yale ya mwaka 2016 mpaka sasa tayari Sheria zile ambazo zimekuwa zimefuata utaratibu zinakuwa gazetted na analeta ndani ya Bunge mambo ambayo yanakuwa yanaeleweka unapokwenda huko unakuwa unajua kwamba hiki ni sawa hiki hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kwenye suala la uwajibikaji linahitajika kwa sababu anapoumizwa mwananchi wa kawaida kwa makosa ya uandishi, kwa makosa ya sheria kutokuwa gazetted, lazima Serikali ianze kuwajibika kwenye mambo hayo. Na ili wawajibike lazima wawe wanapitia kule chini kwenye halmashauri waone mazingira yalivyo, lakini jaribuni kuangalia kweli uwezo wa wanasheria wetu kwenye halmashauri unajitosheleza? Hapo bado kuna shida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilijikita kwenye ushauri nakushukuru kwa nafasi. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uzima kuweza kufika siku hii ya leo, lakini niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote mbili wakiongozwa na wewe Mheshimiwa Spika kwa kweli, nimewaona super woman, mambo yanavyokwenda ni moto tukiongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa nchi yetu. Na Wabunge wanaume wanaona mambo yanavyokwenda, nchi iko kwenye mstari. (kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu umesema Serikali ipo nitajikita zaidi kwenye Wizara ya Kilimo. Sitazungumza kwa sababu siwaoni, lakini kwa sababu umesema Serikali ipo naendelea.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye mradi wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kuhifadhi nafaka. Kwenye mradi huu Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia kwenye mkopo na Serikali ya Jamhuri ya Poland, mkopo wa dola za kimarekani milioni 55, ni jambo jema kwa sababu, lengo lilikuwa ni kwenda kujenga hayo maghala. Tulipata wakandarasi wawili kwenye huo mkataba. Wakandarasi hao wanatoka Poland, masharti yaliyopo kwenye mkataba vifaa vyote vitoke Poland. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkopo huu ulikopwa lini; tarehe 28 Septemba, 2015, nataka Wabunge tuangalie hapo hicho kipindi ni cha uchaguzi na mara nyingi mambo yanaharibika sana hapo kuanzia kwenye halmashauri, ukifuatilia hiyo trend utaona kuna jambo fulani hapo. Mikataba hii inatufundisha nini; kabla sijaenda kwenye kushauri tunamuona Mheshimiwa Rais anazunguka huko kwa ajili ya kutumia resources tulizonazo kwenye nchi zitusaidie kama Taifa. Lakini asiposhauriwa vizuri kwenye mikataba ya hovyo lazima ataingia chaka kama hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini wajibu wetu kwenye hili jambo; mkandarasi kati ya hao wawili ambaye alikuwa anatekeleza mradi Dodoma, Shinyanga, Makambako, Songea na Mbozi, ambaye alipata dola za kimarekani milioni 33.14 amefika asilimia 73 akaja kuomba nyongeza ya dola za Kimarekani milioni 12. Hakuna nyongeza ya aina hiyo! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Waziri wetu wa Kilimo pamoja na NFRA waligoma baada ya kuona hilo jambo, lakini wao hawakuingia kwenye huo mkataba, walioshiriki ni Wizara ya fedha. Nawashukuru kwa busara yao waliyoifanya, lakini huyu bwana kwa sababu anajua kuna nini nyuma ya pazia na yeye ameweka mguu chini kwamba, hataendelea na hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nini kinatokea; amegoma akaondoka, leo mkitaka mumchukulie hatua yoyote fedha hizo ambazo tulikopa ziko Poland. Ni kitu gani hiki kwenye Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mambo ambayo hayafurahishi hata kidogo. Kuna haja sasa ya CAG kwenda kufuatilia vizuri nini kilitokea kwenye huo mkataba. Na mikataba ya aina hii lazima sasa kuna haja ya kuwa wazi tuiangalie mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri kabla ya kuingia kwenye mikopo ya aina hii kwanza waangalie sifa za hiyo nchi. Na huko nyuma iliwahi kufanya hivyo kwa nchi ngapi?

Je, imefanya vizuri au imefanya vibaya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunajua sifa za nchi ya Poland, lakini hayo mengine hatutasema, tuache hapo, lakini tunaamini huu mkataba ulipitiwa na wasomi wetu tena wanasheria. Unakubalije mkataba wa aina hii kuliingiza Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo umenikopesha fedha halafu fedha unazo wewe mwenyewe. Vihenge havijaisha mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali ifanye haraka iwezekanavyo kumaliza mgogoro huu unaoendelea kati ya huyo mkandarasi, ili kazi imalizike. Tofauti na hapo tutaiingiza nchi kwenye Mahakama za kimataifa. Hamuwezi kujua kiburi cha huyu mtu kinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya dakika tano, nitazungumzia tena deni la bilioni 166 kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu ambalo NFRA wanadai. Tuliomba fedha kile kipindi imetokea tafrani kwa ajili ya zao la mahindi. Serikali ikaja hapa kupitia Waziri Mkuu kwamba tumepewa fedha bilioni 50, tukaona ni jambo jema, lakini kumbe ule ni mkopo amekopa CRDB. Kukopa CRDB sio jambo baya, sasa kama NFRA wanadai Ofisi ya Waziri Mkuu bilioni 166 kwa nini wasingelipa sehemu ya deni badala ya kwenda kukopa benki ya CRDB? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nakushukuru. Mengine tutaendelea kushauri, ahsante. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Azimio hili muhimu, Azimio la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Kuongezewa Mamlaka Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hili ni jambo muhimu sana na sisi kama Taifa, naona kama tulichelewa lakini kwa kuwa limekuja leo, tunashukuru kwa sababu limefika na kama Bunge tutimize wajibu wetu, lakini kuna mambo kadhaa ambayo nataka niyashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kukua kwa Jumuiya hii ya Afrika Mashariki kumepelekea kuridhia Itifaki kadhaa, Itifaki ambazo zimeshazungumzwa, Itifaki wa Umoja wa Forodha, Itifaki ya Soko la Pamoja lakini Itifaki ya Umoja wa Sarafu pamoja na Itifaki nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilitazama jambo hili leo tunapozungumzia kuongeza mamlaka, lazima jambo hili liendane sambamba na kupunguza baadhi ya mamlaka zilizopo kwenye mahakama zetu, pamoja na kwamba tunasema haitaathiri, kwa sababu tunapoongeza mamlaka kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki tunaenda kuiongezea nguvu. Ili uiongezee nguvu kuna baadhi ya vitu lazima vitoke huku viende kule kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo hayo kwa sababu na sisi lazima tuone tunanufaika vipi, unapozungumzia mahakama ni chombo ambacho kinakwenda sasa ku-balance mizani kwenye hizi Nchi Wanachama. Lazima tujue tumejiandaaje kama Taifa kuandaa Wanasheria wetu lakini na ushiriki wa Majaji kwenye mahakama hiyo ili kama Taifa tuweze kunufaika kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi tumeridhia na tumeshachunguza kwa sababu inawezekana huu muda ambao tumechelewa kuleta hapa au kuridhia walikuwa wanachunguza kwamba je, kuna athari gani kwenye taifa na mambo gani, lakini lazima tujue tunapoamua kuridhia leo lazima pia tuheshimu maamuzi yanayotolewa na Mahakama hii ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo kadhaa ambayo yalishatolewa maamuzi, mfano pekee, ni ile sheria ya vyama vya siasa, lakini mpaka leo kama Taifa hatujatekeleza yale maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hii. Ni vizuri kama tumeamua kuingia na hapa kwenye ushauri wangu kwa sababu wanachama waliopo kwenye jumuiya hii, kama tumeamua kuongeza mamlaka basi sisi nchi wanachama tuheshimu mamlaka ya hiyo mahakama na maamuzi ambayo yanatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongezewa mamlaka kwa mahakama hii ya Afrika Mashariki ni lazima iendane na kuiwezesha kwenye teknolojia, iendane na hali ya sasa. Lazima kuwepo kwa nguvu kazi ya kutosha ikiwepo nguvu kazi ya kutosha hata maamuzi yatafanyika kwa haraka na haki itatolewa kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunazungumzia kuridhia kwenye Itifaki hii, tumewaandaaje wafanyabiashara wetu kwenye hizi Itifaki kadhaa ambazo tumeshapitia na pia tumejiandaaje kuondoa huu utitiri wa kodi na tozo ambazo zinaweza zikawa vikwazo kwenye hii jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado elimu inahitajika sana hata kwa wananchi wetu, kuona umuhimu wa hii mahakama, lakini ni vizuri kama tumepitisha leo tukajikita zaidi kuwapa elimu wananchi wetu wakajua faida ya mahakama hii ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana kwa sababu tunapozungumzia jumuiya hii tunazungumzia pia soko la ajira, tumewaandaaje vijana wetu waweze kunufaika na hii fursa kwenye suala la ajira kwenye umoja wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu unapokuwa unataka fursa lazima uangalie kwamba kuna ushindani. Tumejiandaaje na huo ushindani, kama hatujajiandaa watanufaika wengine tutabaki kuwa wanachama tu, kwa sababu lazima tupime ni wapi ambapo kama Taifa tumejipima, ni kweli tunaendana na huo mfumo? Mifumo yetu ni rafiki ya kwenda ku-compete kwenye huo Umoja wa Afrika Mashariki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na umakini wa kutosha tuweze kutumia kama fursa katika nafasi hiyo ambayo tutakuwa tumeipata. Pamoja na kwamba tumeingia muda mrefu lakini kuna mambo ambayo kama Taifa tuone, ni kweli sisi hapa tulipofikia haya manufaa tunayoyapata ndiyo yanatosha kwa wananchi wa Taifa hili kama wanachama wa Umoja wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo lazima tuyatazame, leo unapozungumzia biashara tuna changamoto ya wakulima wetu kwenye biashara, hata bima tu kwa mkulima kwa ajili ya biashara yake bado ni changamoto kwenye Taifa letu. Je, tunakwenda kunufaikaje sisi na hiyo Itifaki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa leo nilikuwa nataka kujikita kwenye kushauri na nasema kwa umoja wake Kamati ya Katiba imefanya kazi kubwa sana ya uchambuzi, wamechambua kwa kina, lakini ni vizuri umakini ukaongezeka, zile ambazo tunaziona ni fursa tuzitumie na kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)