Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. James Kinyasi Millya (17 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya watu wa Simanjiro, kwanza kwa sababu nasimama mara ya kwanza niwashukuru sana kwa kunichagua na kunipa heshima ya kuwa Mbunge wao na kusaidia kuwaondolea kelele hapa Bungeni. Mimi namshukuru Mungu sana kwa hilo na nawashukuru kwa ajili ya heshima waliyonipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Frantz Fanon wakati fulani alinukuliwa akisema haya, nanukuu kwa kiingereza; “every generation out of relative obscurity must find it’s own mission and either fulfill it or betray it.” Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi sana kwamba kila jamii kwa wakati fulani lazima ikubali kutafuta njozi yake na labda waamue kuikamilisha au kuikataa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la nchi yetu ni kubwa na tatizo hili kwasababu limetokea CCM wakati fulani si lingine bali ni unafiki na uongo. Unakuta viongozi wanaotegemewa na Taifa hili wanaongea uongo kwa sababu ya kujipendekeza, nilishindwaga mimi, nilishindwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasemahaya? Ugonjwa huu ni mkubwa kwa sababu unakuta makada ninaowafahamu kwa majina wanajaribu kujivua u-Membe, wanajaribu kujivua u-Lowassa kwa kujipendekeza na Serikali iliyoko madarakani wanawaacha wananchi wanateseka hawasemi ukweli. Huu ugonjwa ni mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mifano michache wengine wanasema nisitaje lakini kwasababu sitaki kuwa mnafiki, alikuja Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba, ugonjwa huu ni mkubwa. Katoka kwa wananchi akatetea Katiba nzuri, iliyotoka kwa wananchi kwa mapendekezwa ya wananchi baadaye alipoguswa mahali na CCM akakana matokeo ya wananchi, ni unafiki mkubwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa na kama viongozi hatutapona katika hili nchi hii itaenda pabaya. Ninamkosa Baba wa Taifa kama Nyerere, kama Sokoine ambao wakisimama kwa ukweli, watasimamia hiyo kweli na hiyo kweli itawaweka huru milele. Nimewakosa watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye hoja za madini. Sisi watu wa Simanjiro tuna madini ya Tanzanite, kwa miaka mingi sana ukienda Naisinyai, kuienda Mererani – Simanjiro watu ni maskini kweli kweli. Eneo lenye watu karibu 50,000 Mererani na Naisinyai hawana maji, Tanzanite ipo pale, wanachukua wazungu, wanachukua wazawa, watu wetu wanaachwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Profesa Muhongo ninakuheshimu sana na unajua, nikuombe hata kutokana na yale ambayo yanasemekana si hasara, corporate social responsibility, tusimamie, watu wetu wanaumia sana, wanaonewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa leo hii niongee kwa masikitiko makubwa. Tulikuwa na mgodi mkubwa unaoitwa Tanzanite One, hata Kamati imegusia na kwenye taarifa mbalimbali ipo. Mgodi ambao Serikali ni mbia, STAMICO na mwekezaji uliuzwa kiholela na mimi najiuliza kama Mbunge na ningeomba nipate majibu wakati unakuja kuhitisha hotuba na hoja yako; hivi mgodi ule na ubia ule ulipatikanaje kwa Kampuni ya Sky Associates ambayo nimeaminishwa na najua kwenye maandiko si Kampuni ya Tanzania, wametokea wapi watu hawa? Je, tender hii ilitangazwa lini ili watu wote wa-compete fairly halafu wapewe. Sky Associates kama alivyokuwa anasema Dkt. Mwakyembe kuwa wakati fulani aki-present hoja yake ya DOWANS hii ni kampuni ya mfukoni, ni ya watu wachache waliotengenezewa ulaji na baadhi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa, sintachelea kusema Simbachawene anahusika kwenye hili. Kampuni hii leo hii inanyanyasa wananchi wote, wachimbaji wadogo naomba niwataje kwa majina, Simbachawene amesainije mkataba kampuni iingie kwenye ubia na Serikali lakini hakuna mtu alieshindana naye? Eti walitangaza kule London Stock Exchange, Watanzana wangapi wangeweza kuona London Stock Exchange? Leo wachimbaji wadogo wanaonyanyaswa kwenye mkataba huo, Mathias Mnama, Sunda, One, Olomi, Mwarabu na mwingine kapoteza maisha kwa sababu ya mitobozano. (Makofi)
Mheshimiwa Profesa, wewe uliunda Tume wakati fulani, Tume mbalimbali zimeundwa kwa ajili ya mitobozano huko ardhini lakini bahati mbaya kuna Tume yako wewe, kuna Tume ya Dkt. Kipokola, kuna Tume ya Jenerali Mboma, wachimbaji wadogo wanaonewa na mgodi huu kwa muda mrefu.
Ninaomba kwa mara ya kwanza unisaidie kama Mbunge na unisaidie kama mwananchi mwakilishi wa wananchi wengi wanaotaka kunufaika na mgodi wao. Hawa Sky Associate waundiwe tume, ni wezi, hawanufaishi Simanjiro. Ninakuomba, wanaiba madini, wananunua mpaka Maafisa wetu wa Serikali, wengi! Naomba Mheshimiwa Profesa utusaidie kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine; Mheshimiwa Profesa madini yanaibiwa kila siku na kampuni hii. Na bahati mbaya, mimi nimeahidi mara nyingi nitakuwa mkweli mpaka nitakapokufa. Wanapata wapi kiburi cha kufukuza wafanyakazi 201 halafu wamewafukuza, baada ya kuwafukuza wanawapeleka mahakamani hawajawalipa mafao na sheria za kazi zinajulikana, bahati mbaya mama yetu Mhagama naye anatajwa humu ndani kwamba ni shemeji wa mmoja wa mbia wa hapo. Dada anaitwa Asia Gonga ameolewa na Martin Mhagama au Yusuph Mhagama, sasa sijui….
TAARIFA...
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba ukoo wake ni mkubwa na mimi ni kwamba nimepata taarifa. Nimetaja taarifa tu kwamba anatajwa. Angesema tu mimi huyo sihusiki naye, simple. Lakini watu hawa wanapatiwa kiburi na nani? Wanafukuza Watanzania halafu sekta yako inayosimamia wafanyakazi haiwasaidii, kwa nini nisihusishe jina hilo na jina lako? (Makofi)
Baada ya kusema haya mgodi huu tunataka tunufaike nao. Madini haya yamechukuliwa kwa muda mrefu lakini kampuni hii ya kitapeli iondolewe mara moja, Wanasimanjiro na Mheshimiwa Waziri nikuombe ukutane na wananchi hawa ukutane na wachimbaji wadogo usikie kilio chao. Tanzanite kwa mara ya kwanza na EPZA, kwa nini msijenge EPZA, madini yetu yanatoroshwa kila siku. Tumeto aeneo kama Simanjiro, liko eneo la EPZA, mnachelewa kulijenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi naomba nichangie haya yafuatayo:-
(a) Mashamba pori na kutapeli ardhi ya watu ambao hawakuridhia; na
(b) Makazi, ujenzi wa NHC na tatizo la mishahara midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba pori na ulaghai kupitia Wenyeviti. Kuna mashamba pori Simanjiro naomba utusaidie kwani wananchi wanateseka na mifugo yao na hivyo kusababisha migogoro kati ya wananchi na mbuga za wanyamapori (National Park). Shamba Namba 24 linasumbua wananchi wa kijiji cha Lobosoit „A‟. Mheshimiwa Waziri anafahamu tatizo hili na tayari maelekezo yale tumeshaanza kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa zaidi ya miaka mingi shamba hili halitumiki na halilimwi na juzi kwenye Kikao Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Bwana Brown Ole Suya alileta barua ya kubatilisha matumizi ya ardhi kutoka kwenye kilimo na mifugo kwenda mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba siyo suala la mazingira na wananchi wa kijiji cha Lobosoit “A”, siyo tu hawakumpa mtu huyu hiyo ardhi ya kilimo na mifugo lakini hawapo tayari ardhi yao ihalalishwe ili mtu huyu aiuze ardhi hii kwa wageni (wazungu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Vijiji Simanjiro ambao sio waaninifu wameuza ardhi ya wanakijiji bila ridhaa yao na hili limepelekea mpaka wao kupata hati miliki. Waliomilikishwa kimakosa wamepewa mpaka hati miliki na Wizara ya Ardhi. Tutasaidikaje ili wale Wenyeviti wa Vijiji ambao sio waaminifu wachukuliwe hatua na wananchi warudishiwe ardhi yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Laangai, mbali na tamko la mahakama la kuzuia ardhi ya wafugaji isiibiwe na isigeuzwe kuwa eneo la mapambano kama ilivyotokea Kiteto, naomba Wenyeviti na Serikali za Vijiji vya kitapeli zichukuliwe hatua. Iandaliwe orodha ya Wenyeviti wezi wa ardhi ili wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya ardhi inapandisha bei za nyumba; riba za kibenki ni tatizo kubwa la bei ghali za nyumba hizi. La pili, mwanafunzi aliyepata kazi/ajira mwaka huu atapataje nyumba iwapo mshahara wake ni mdogo sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya Angola wana mpango mzuri wa kuiwezesha jamii yake kupata makazi bora. Naomba mkajifunze hayo ili wananchi wasaidiwe kupata nyumba bora na nzuri kwa mishahara yao midogo. Hawawezi kukodi nyumba za NHC kwa bei za sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze masikitiko yangu makubwa kwamba wafugaji wanapambana na nini? Wanapambana na dola nyingi dhidi ya uhai wa watu. Wizara hii ni Wizara pekee yenye dola nyingi kweli ambazo interesting group, zingine ambazo ziko nje ya nchi zina-interest, na mimi hapa imebidi nitoe kidogo leo elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumeanza utalii nchini mwetu? Mwaka 1892 alikuja Muaustralia mmoja anaitwa Oscar Bowman, mwaka 1913 akaja mwingine anaitwa Stewart Edward White mzungu wa Kiingereza, akaja mwingine anaitwa Bernard Dimezec pamoja na mtoto wake anaitwa Michael wakaandika kitabu kimoja kinachoitwa Serengeti shall never die. Baada ya wazungu hawa kuandika vizuri kitabu hicho, Waingereza, mwaka 1959 wakaamua kuwaondoa wafugaji wa Kimasai Serengeti, wakasema wala hawafai. Tumewatunzia mazingira hayo kwa damu na jasho letu tukiwapa na ng‟ombe wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe takwimu nyingine, kwa nini kuna migogoro ya wafugaji na wakulima nchi hii! Serengeti zimeondoka square kilometers 14,750 kutoka kwa wafugaji, Mkomazi - square kilometers 3,500 za wafugaji, Ngorongoro zimeondoka square kilometers 8,300 za wafugaji, Tarangire National Park zimeondoka square kilometers 2,850 za wafugaji, watu hawa mnawapeleka wapi! It’s a calculated genocide, mnataka maisha yetu yasiwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hii, Edward Moringe Sokoine, kati ya mwaka 1948 na 1958 ndipo wakati alikuwa anamaliza shule ya msingi na sekondari. Mikataba hii inaingiwa, mnaondoa maeneo haya makubwa kutoka kwa watu wetu. Where were there any informed consent? Naongea hivi, kuna wafugaji wako Zambia wanasuka watu nywele, kuna wafugaji wako Dar es Salaam wamekuwa walinzi, Serikali mnawaonaje, tunaanza kuwa watu wabaya kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnatupiga, tumewahifadhia mazingira haya yote tukiamini kwamba tunatunza maisha yetu. I declare interest, siamini kwamba utalii ni mbaya, lakini utalii mbaya unaoumiza maisha yetu ni utalii usiokubalika na nitakuwa wa mwisho kukubali utalii wa namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanauliza maswali mengi, wanasema mifugo inaharibu mazingira, mmoja amezungumza hapa, hivi ni ng‟ombe gani anayeua tembo, ni ng‟ombe gani anayeua simba. Lakini geuzeni swali upande wa pili, watu wanaotegemea mifugo, karibu watu milioni mbili nchi hii, geuzeni usemi kwamba hawa mifugo wamekufa, its their livelihood, leo Serikali ianze kuwalisha hawa, mnaongelea 17 percent ya GDP ya nchi. Je, mkianza kuwalisha watu hawa kwa sababu hawana mifugo, hawana maisha, itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitika kwenye kauli ya Mheshimiwa Waziri juzi na bahati mbaya wafugaji wa Kimasai wamekupigia kura kwa takribani miaka15 kule Same. Unasema mifugo haifai, mifugo inaumwa, wanyama wasisafirishwe. Sasa nina maswali mawili; maana yake ni kwamba hawafai kuliwa na kwamba maisha ya watu ni ya bei rahisi kuliko pesa? Swali la pili, je, tuambiwe kwamba ni kauli ya Serikali kwamba wale wote wanaotegemea nyama nchi hii na wale wanaosafirisha kwenda Mataifa mengine wasisafirishe nyama kwa sababu wanaumwa, itoke kauli ya Serikali? Mheshimiwa Waziri amenisikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kuna WMAs, tunachoomba wafugaji wa Kilindi, Mheshimiwa Msigwa ameongea hapa milioni 25, ndugu yangu naomba upate hili, tuna ng‟ombe milioni 25, hatutaki kuongezewa eneo, mipaka ambayo iliwekwa kabla sisi hatujawa na akili ya kisheria na ndiyo maana unaona Wamasai wengi, Mheshimiwa Ole-Nasha, wengine wote wanasoma sheria kwa sababu ya uonevu mkubwa. Sisi hatuli wanyamapori hao, hatuli simba, hatuli swala, tunawatunzia, lakini basi let it be fair, na ninyi msituumize. Kimotorok mnatufukuza, Emoret mnatufukua, Same mnatufukuza, Kilosa mnatufukuza, Bukombe mnatuumiza, Hanang‟ nina picha hapa, maskini wa Mungu mfugaji anatoka Katavi ameumizwa, kuna PF3 hapa. Mnatuumiza, mmetufanya watumwa kwenye nchi yetu. Naomba Serikali mkae chini mtufikirie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba utalii ni kitu kizuri, lakini Waheshimiwa Wabunge iwe fair. Naomba Sheria za WMA zilianzishwa na jamii, Kifungu kile cha 12 kilichoanzisha sheria hiyo badilisheni. Tunapata hela zetu, Simanjiro tumekataa WMA, lakini Kiteto na Longido wanafanya WMA. Mheshimiwa Waziri, hela zinachelewa sana, tunaomba mtume hizi hela mapema. Lakini kile Kifungu cha 51 cha sheria hiyo, ongezeni percentage, imekuwa ni kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeumia sana, Wamasai hawajasoma nchi hii, sheria za nchi hii hazijaangalia bado watu hawa. Kule Afrika Kusini wakati wa ukombozi, mwaka 1994 wakasema tuleteni an affirmative action. Tunacholilia hapa, wengine tumesoma siyo kwa sababu ya sera za CCM, ni bahati za makanisa na bahati za wengine wazungu tu. Mmetusahau muda mrefu, mnatuumiza muda mrefu, naombeni mfikirie kwamba Bunge hili lianze kutenda haki kwa ajili ya watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, fikirieni mifugo, its not about business, it is a livelihood. Mimi nisipokuwa na ng‟ombe siangalii kuhusu hela. Lakini lingine ni lile linahusiana na Mheshimiwa Lowassa na Mheshimiwa Sumaye, Wakili mwenzangu ameongea, ninasikitika sana, watu hawa wanasahau records. Mwaka 2006 Lowassa akiwa Waziri Mkuu wa CCM alifukuza mifugo Ihefu, hapakuwa hata siku moja na tamko la Kiserikali kutoka kwa Lowassa na Sumaye kutapanya mifugo yote nchi hii, msipotoshe umma. Nimuombe Wakili mwenzangu anapoanza kusimama aongee na authority, tunatetea utu, hatutetei biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, Mungu awabariki sana. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina nafasi gani katika ushirikiano wa kibiashara kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wa kifugaji wanaokwenda Zambia na Afrika ya Kusini, wamekwenda kwa ajili ya kusuka nywele za akinamama kwa “style ya kimasai.” Ni sisi pekee nchi hii na Afrika ambao tunaweza kusuka nywele hizi na hazisukwi na mtu mwingine yeyote. Matatizo na adha wanayokumbana nayo wenzetu wa Kimasai katika nchi hizi mbili ni haya yafuatayo:-
(1) Wanakatwa, wanapigwa na kuhukumiwa bila kupewa usaidizi wa kisheria;
(2) Zambia kama nchi, imekuwa ikiwahukumu “Wamasai” bila kuwapa msaada wowote wa kisheria “fair hearing” trial hazifanyiki.
(3) Tunaiomba nchi ya Zambia ituambie wafugaji hawa wafanye nini ili wakidhi vigezo vya kufanya kazi nchini huko?
(4) Balozi wa Tanzania (Lusaka) amekuwa “reluctant” katika kuwasaidia vijana wetu wanaopata matatizo nchini Zambia. Naomba Balozi wa SADC atazame hili ili watusaidie kuwaondolea vijana wetu shida wanayokumbana nayo.
(5) Tunaomba vijana wetu waliofungwa kwenye Magereza ya Zambia wasaidiwe. Wapo wengi Magerezani na sijui kama Wizara ina takwimu zozote. Please hili lifuatiliwe pia.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niweke msimamo kwamba na mimi pamoja na Kambi yetu Rasmi tunakubaliana kimsingi kwamba mkataba huu kwa muda huu usisainiwe na Serikali.
Mheshimiwa Spika, lakini hilo lisitunyime nafasi ya kuweza ku-criticize mkataba mzima objectively. Maprofesa watatu walikuja Jumamosi, ninawaheshimu sana. Mheshimiwa Profesa Kabudi, ni mwanasheria nguli, ni mwalimu wetu kwa namna yoyote, lakini walipowasilisha upande mmoja wa shilingi, kisomi haikubaliki.
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye article 101 pale inaposomeka; “resources mobilization.” Nataka tu niwaoneshe faida ya mkataba huu pamoja na madhaifu yake mengi, lakini kuna faida fulani.
Mheshimwa Spika, nenda kifungu cha pili; “The objective of joint resource mobilisation is to complement, support and promote in the spirit of interdependence, the efforts of the East African Community Partner States in pursuing alternative sources of funding to support regional integration and the development strategies, in particular the EPA Development Matrix.” Hiyo matrix hatujaletewa.
Mheshimiwa Spika, Maprofesa wangetuonyesha Waheshimiwa Wabunge hiyo development matrix ni kitu gani? Tunapoungana na EU tunakuwa na nafasi kubwa ya ku-negotiate for funding kwa ajili ya miradi ya maendeleo; mkataba huu unasema hivyo. Mkataba huu kwa kiwango chochote una madhaifu makubwa lakini sisi kama nchi tusifikie mahali tukawa ni watu wa kukataa siku zote.
Mheshimiwa Spika, alipoanza Profesa siku ile, alisema kitu kimoja kwamba nchi ya Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla, itapoteza revenue.
Waheshimiwa Wabunge, naomba niwakumbushe kitu kimoja, mwaka 2004 tuliingia mkataba wetu na Kenya na Uganda; East African Customs Union Protocol. Tuliwaachia nchi ya Kenya kwa miaka mitano walipe kodi.
Mheshimiwa Spika, mkataba huo uliisha mwaka 2009. Mwaka 2009 Kenya ikaanza kuingiza bidhaa zake bila kulipa kodi Tanzania, baada ya Tanzania na Uganda kuruhusiwa kuingiza Kenya bidhaa zao wanazotengeneza kwa miaka mitano bila kodi yoyote.
Mheshimiwa Spika, tujiulize kama nchi, hivi baada ya ule mkataba mwaka 2009, viwanda vingapi Mheshimiwa Mwijage tumeanzisha kuanzia siku hiyo? Tumepeleka nini Kenya? Leo hii mnatutuhumu wengine, tumepeleka kabichi, nyanya na vitunguu lakini hatujaanzisha viwanda vya aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, wengine mnasema tunautetea mkataba huu kwa sababu tuna maslahi binafsi na nchi za Ulaya, wala siamini hata kidogo. Mimi ni mzalendo na ninaamini ni mzalendo, lakini hivi mfano Tanzania, Waziri wa Fedha anajua, kati ya mataifa matano makubwa yanayochangia Tanzania bajeti yake, ni nchi zipi? Kama kati ya tano hizo, Ulaya zipo nchi tatu.
Mheshimiwa Spika, nafikiri wakati tunakataa mkataba huu, tujiulize maswali ya msingi, moja, hivi ni viwanda gani hivyo ambavyo tunavitetea kwamba tukiingia kwenye mkataba huu tunapoteza bidhaa?
Pili, kwa muda gani nchi yetu ya Tanzania itaweza kujenga viwanda vyake peke yake na kuweza kushindana na masoko haya mengine ya East Africa na Ulaya pia, itatuchukuwa muda gani kujenga viwanda kwa sababu viwanda vingi vipo mfukoni.
Tatu, kama hatutaanzisha viwanda kama nchi, hivi hamuoni kwamba Ulaya wakiingiza bidhaa zao kwenye uchumi kuna kitu kinachoitwa basket of goods, kwa sababu vitaingia kwa bei rahisi mwananchi wa kawaida atakuwa na uwezo wa kuvinunua kwa wingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunapata kutoka China tunavitoza kodi ambavyo ni vya hali ya chini kweli, lakini wote tunafahamu, leo ukiletewa bidhaa kutoka Ulaya na China, wote ambao mmesafiri humu duniani, mtakubaliana na mimi kwamba bidhaa ya China na Ulaya vinatofauti kubwa, quality wise, I will go for European goods for sure!
Mheshimiwa Spika, nne, naomba pia nishauri badala ya kukutaa mkataba huu, Bunge tumshauri Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais kwenye kikao cha mwisho cha Marais wa Nchi za Afrika Mashariki -Summit ya juzi Arusha au Kenya kikao kimoja cha mwisho, ndiye aliyewaomba wenzake kwamba jamani mkataba huu sisi hatujapitia, ninaomba niunde Technical Committee ambayo itapitia mkataba huu itushauri kama nchi.
Mheshimiwa Spika, Technical Committee ndiyo ile nafikiri ambao wamewasilisha upande mmoja wa shilingi nafikiri siyo vema sana tukawa ni nchi ya kususa na kukataa wakati hatuchukuii hatua madhubuti ya kuweza kubadilisha nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nishauri kitu kimoja…
TAARIFA...
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, naomba nipokee taarifa hiyo kwa nia njema kwamba anajaribu kuniambia kwamba ni kweli Mheshimiwa Rais alivyoomba kwamba iiundwe Technical Committee ya kuishauri Serikali imeundwa, lakini bado haijawasilisha mapendekezo yake.
Mheshimiwa Spika, hilo halitunyimi fursa kama Bunge kuiomba Serikali, mkataba huu kwa sasa usitishwe lakini tusikatae moja kwa moja. Uende ukapitiwe tena tuangalie kama negotiating team ya Tanzania inaweza ikabadilisha baadhi ya mambo ambayo tunayataka na bidhaa ambazo tunataka kuzitetea kwa muda na baadaye urudishwe Bungeni.
Mheshimiwa Spika, pili, ninaomba Serikali yetu badala ya kupiga kelele ya kusema tunaandaa viwanda, sasa ifikirie ni muda sahihi wa kuwekeza kwenye viwanda. Hili jambo la kukimbia na kuwa na protection policy kila saa hautatufikisha mahali. Waingereza wanasema, you better run the hard way kwa sababu the easy way you do not go it, kwa sabubu ninyi hamuwezi hata kidogo. Tukiwaachia hata miaka 100 humuwezi kuanzisha viwanda vya kushindana na Ulaya. Ni changamoto kama nchi kwamba, ni lazima kwa muda huu tuamue wote kama jamii tuungane tuwaambie Mawaziri hawa wenye viwanda mifukoni, walete viwanda ili tusiwe wapiga kelele kwenye soko la Afrika Mashariki.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo Arusha ukienda kwenye maduka yote vifaa vya Kenya vimejaa, ukiuliza tunapeleka nini Kenya? Utaambiwa maembe na machungwa ya Tanga na unga wa Azam.
Mheshimwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba mkataba huu usisainiwe, lakini kama nchi tuangalie faida ambazo tunaweza tukazipata kutokana na mkataba huu, badala ya kuanza kulialia na kupiga kelele kwamba sisi hatuwezi, hatuwezi siku zote! Muda unatosha ni muda sasa wa kushindana na Mataifa mengine kama nchi.
Mheshimiwa Spika, tumeingia kwenye AGOA, mmesikia jana Mheshimiwa Mwakyembe amesema tumeuza asilimia nne soko la Marekani, wakati Kenya wameuza 98% they are taking advantage of their industrial power na Tanzania tunabaki kulalamika ni nchi ya kulalamika tu Kiongozi analalamika, wananchi wanalalamika, kama alivyosema Mheshimiwa Lowassa wakati fulani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nimshukuru saana Mungu kwa kunipa nafasi hii leo lakini niendelee kuwashukuru watu wa Simanjiro kwa kuniamini kuwa Mbunge wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye Wizara hii na kuanza na maneno haya tu, kwamba ni lazima Wizara hii itambue pamoja na maslahi mapana ya nchi ni muhimu kutambua pia kwamba wale waliosaidia sekta hii ya kiuchumi ya maliasili kutunzwa mazingira yake na wenyewe waheshimiwe; maana imekuwa na fikra kubwa sana kwamba wale ambao wanaishi pale, maslahi yao sio mapana sana na sio makubwa kwa Taifa ukilinganisha na Taifa kubwa. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie sana kwasababu mimi ni mfugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niungane na Wabunge wenzangu, mipaka hii kuanzia mwaka 1954 mpaka leo haijaangaliwa tena, jamii imeongezeka na mimi niko kwenye msimamo mmoja kwamba haiwezekani tufike mahali kwamba kesho tukiwa bilioni moja kama Wachina tuseme na mbuga zetu ziliwe, haiwezekani! Ni lazima tukubaliane.Lakini wakati mipaka hii ikiandaliwa watu wetu walikuwa hawajui kinachotokea, hawajui thamani ya ardhi, hawajui nini maana ya mipaka hii na wanyama hawa. Ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri na zile Wizara ambazo zimeungana Wizara tano, mifugo, kilimo tuje na wawakilishi (wote sisi wawakilishi) tukae pamoja tuweke mipaka ya kudumu na tuwafundishe wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Simanjiro vijiji vya Kimotoro, kijiji cha Lobosiret, Emboret na baadhi ya maeneo ambayo mbuga hizi zimezunguka nipo tayari kuwaongoza wananchi wangu tutakapokubaliana na Serikali kwamba mipaka hii sasa huu ndiyo uwe mwisho, kwa maisha ya sasa na maisha ya baadae ya watoto wetu. Ni muhimu sana tukae wadau wote tukubaliane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nitambue kimsingi kazi kubwa iliyofanyika Ngorongoro, Loliondo. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini bahati mbaya nimeona pia kwenye Kambi yetu Rasmi ya Upinzani. Wananchi wamekaa na watumishi wa Serikali, wamekubaliana njia ya kwenda mbele ili kumaliza migogoro. Mheshimiwa Waziri ninaona hutaki kutambua nguvu hii. Mimi nafikiri ni vyema sana wanyamapori na Wizara yako ikae na wananchi tukubaliane wote kwamba kuanzia sasa na maisha ya baadae tunakaaje ili kuhifadhi wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mtalii, nikuambie tu ukweli, mimi nazunguka sana lakini namshukuru Mheshimiwa Nape na yeye siku moja nimeenda mbuga moja nikasikia na yeye yupo kwenye hoteli mojawapo. Ni lazima sisi kama Bunge, hii Wizara tuibebe, kazi kubwa tuifanye. Viongozi hamtalii, hamuendi mahali, lakini ni vyema sana Wizara hii iwepo Ngorongoro Conservation Area Authority, iwepo TANAPA kwa ujumla wake, kina KINAPA wote, mfanye juhudi za kipekee za kusaidia Watanzania watalii na viongozi wa nchi hii muanze kutalii kwenye mbuga zetu ili tupate mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nitambue leo Simanjiro, kijiji cha Kimotoro pamoja na kupoteza maisha ya mfugaji mmoja, kuuawa na wanyama, anafidiwa kijana wetu mmoja leo kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe. Mimi naendelea kusema fidia hii haitoshi, lakini leo anafidiwa mmoja. Naomba Wizara muangalie uhalali wa binadamu, heshima ya binadamu vis a vis mnyamapori. Haiwezekani anapouawa, shilingi milioni moja tu! Badilisheni sheria hizi, tubadilishe ili tuheshimu ubinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa kwenye Wizara hii, leo mimi sitaongea sana against you,kubwa na imeandikwa kwenye Biblia na Qurani amri kubwa kushinda yote ni upendo. Ninyi wahifadhi kaeni na sisi, nami nitambue kazi kubwa ya Tarangire iliyofanya pale Kimotoro wakati mnapitapita pale Kimotoro tumeweka mahusiano mazuri, Mhifadhi na Afisa Uhusiano wa Tarangire ninaomba nitambue kwamba tumeanza kukubaliana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niongelee Makumbusho ya Taifa. Bahati nzuri nimesoma mwaka 2006/ 2007 Misri, nimetembelea makumbusho yao. Watu hawa wanaingiza watalii wengi sana kwa Makumbusho ile ya Cairo. Lakini Ujerumani wanaongoza pia kwa ajili ya makumbusho.

Ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuanzia ukurasa wa 12 mpaka 51 inaongelea wanyamapori, ukiangalia ukurasa wa 53 mpaka 89 kurasa 36 na 39 inaongelea nyuki. Lakini Makumbusho yetu ya Taifa mnaongelea kwa kurasa saba tu, hamuipi uzito utamaduni wetu wa nchi yetu. Makumbusho ya Dar es Salaam hayana maana kubwa ukilinganisha na makumbusho mengine yanayotuzunguka kwenye nchi yetu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, weka nguvu kubwa kwenye makumbusho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Misri pale bajeti ya 2017/2018 wanapitisha almost one billion USD wamepata msaada kutoka JINCA wanaboresha makumbusho yao. Mwalimu Nyerere na ninyi bahati nzuri wazee kama ninyi mmeishi na Mwalimu Nyerere sisi wengine tunamuona kwenye makumbusho tu. Kwa nini hampendi kuutunza utamaduni wetu, alianzisha Makumbusho ya Taifa letu. Ninaomba kwa nguvu zote, bajeti ya Makumbusho iongezwe. Ninaombeni tuwape Watanzania heshima hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili kuna suala la utozaji, lakini Mabalozi wetu nimeshuhudia nchini Canada, Balozi wa Kenya anaenda kwenye shule za sekondari na vyuo vikuu vya nchini Canada anawaita watalii wakati wa low season wanafunzi anatangaza utalii, imefika wakati sasa nchi yetu tunapomteua Balozi wetu pamoja na hadidu za rejea za kumpa moja ni kutangaza nchi na kutangaza nchi yetu kwenye mataifa ambayo wanaenda. Haiwezekani Mabalozi wakakaa kule maofisini na ofisi kubwa na wanapewa kila kitu, lakini hawatangazi nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu hatupati watalii wa kutosha Zanzibar is just amazing, ukiangalia Ngorongoro ni nzuri, ukiangalia Mlima Kilimanjaro, hamna mlima kama huo duniani. Lakini hatutangazi vizuri, mabalozi wetu ni vizuri Serikali iweke hadidu za rejea za kusaidia utangazaji wa utalii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu mbili naomba nimpe Mheshimiwa Ester.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nianze kuwapongeza rika langu, ndugu zangu wote, ma-korianga popote walipo nchini kwa kufikia hatua ya muhimu ya maisha yao, tunakwenda kukabidhi madaraka. Hata hivyo, niwatakie heri wenzetu wale wa Kimnyak, Irkimayana kwa namna ambavyo wanapokea madaraka kutoka kwetu kwa mila za kimasaii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimshukuru kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kufika jimboni kwangu na kuniahidi jambo moja, kwamba VAT ya asilimia 18 inayotozwa kwa mnunuzi wa tanzanite kwenye soko huria itaondolewa. Nina imani kwamba Waziri anapokuja kuhitimisha hii VAT ataiongelea. Ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike pia kuhusu ruzuku, hamjatoa kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Mererani hususani akinamama ambao na wenyewe wana wawakilishi wao kila mahali wanajaribu kujipambanua katika suala la kiuchumi lakini wamefanya application na Wizara yenu haijatoa hata ruzuku moja kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niingie kwenye suala la tanzanite. Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo na wewe unaifahamu imeweka bayana kwamba madini ya vito yatachimbwa na wazawa lakini leseni yoyote itakayotoka haitazidi square kilometa moja. Kwenye application iliyofanyika 2013 application ya leseni HQP26116 ya Tanzanite One iliiomba Wizara kutoa leseni ya madini, wao wenyewe wamempa square kilometa 7.6 kinyume na sheria. Kuna majadiliano makubwa ya kisheria kati ya Wizara yako na watumishi, wengine wakikataa lakini kulikuwepo na shinikizo mwaka 2013 na ushahidi huo upo naomba niulete acheni kufisidi nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu mmemwelewa Mheshimiwa Tundu Lissu vibaya. Ninyi mnafahamu kesi ya Dowans tumepoteza kama nchi na kesi ya Richmond tumepoteza kama nchi. Mheshimiwa Rais, Wabunge wa Upinzani hawakatai kwamba kuna madudu nchi hii kuhusu mikataba lakini nendeni kwa style ambayo nchi haitapata hasara kwa baadaye. Eleweni hivyo Wabunge wenzangu wa CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Tanzanite One ilipewa leseni kinyume na masharti ya sheria na aliyehusika katika hilo, aliyesaini leseni hiyo ni ndugu Engineer Ally Samaje na anajulikana yupo, naomba Serikali ifuatilie. Walichokifanya ndugu zangu, kwa sababu sheria ya 2010 inaruhusu yeyote anayechimba mable na graphite aruhusiwe kupewa takribani square kilometa 10; wakasema kwenye leseni yao hiyo wana–apply mable na graphite na si tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ukienda kwenye documentation zote Kampuni ya Tanzanite One haijawahi hata siku moja kusafirisha nje mable na graphite. Ujanja huu ulitumika na ninyi mnatakiwa mwelewe nchi yetu inavyoibiwa. Mtu anaomba leseni ya kitu kingine lakini anachimba kitu kingine, ipo kwenye documentation. Anaomba leseni ya mable na graphite lakini anakwenda kuchimba tanzanite. Niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nchi yetu inamalizwa; tusiposimama kama wananchi wanaoipenda nchi hii, tutaimaliza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kampuni iliyoingia mkataba na Serikali 2013/2014 inaitwa Sky Associate, sasa huyo Sky Associate ni nani? Ni kampuni iliyosajiliwa mahali panaitwa Virgin Island ambayo inafanya kazi zake Hong Kong. Kampuni hii haipo Tanzania na haijasajiliwa Tanzania. Mheshimiwa Ngonyani anafahamu kwa sababu taarifa aliyotoa kwa umma wakati yupo Wizarani pale; Mheshimiwa Ngonyani aliwaambia watu kwamba ndugu Faisal Juma Shabash ambaye ni Mtanzania anamiliki asilimia 25, alisema Hussein Gonga anamiliki asilimia 35, Ridhiwan Urah, si huyu Ridhiwan anamiliki asilimia 40. Hakuna popote, si TIC, sio kwenye usajili wetu wa makampuni Tanzania, watu hawa wanaonekana. Hii kampuni ni ya kitapeli na Serikali inawalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu lingine, hawa jamaa wanafanya minada. Kampuni hii ya Tanzanite One imeuzwa kwenda Sky Associate kwa dola milioni tano ya kulipana kwa mafungu. Minada miwili waliyofanya Agosti na Februari wameuza takribani dola milioni saba…

T A A R I F A . . . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili, nimwombe Mheshimiwa Rais atumie mamlaka yake leo asimamishe uzalishaji wa kampuni hiyo, lakini na Mheshimiwa Ngonyani pia ashughulikiwe. Pia niombe STAMICO inayohusika kufisadi nchi yetu, wewe tulia…

T A A R I F A. . . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niombe tu kwa heshima kwamba sipokei taarifa hiyo, lakini kwa sababu nimeomba Tume ya Rais iundwe na haya yote anayoyasema yataonekana kwa sababu kwa kawaida na yeye atahojiwa; haya yote atakuja kuyaeleza kwamba, je, kampuni hii ni ya Kitanzania au sio ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea kitu kimoja, akanushe mtu yeyote hisa hizo zimeuzwa kwa dola milioni tano tu, lakini kwa masoko ya Agosti 2016 na Februari watu hawa wameuza madini kwa milioni saba, tayari almost bilioni 16 na capital gain hawalipi, ndugu zangu nchi yetu inaibiwa sana. Hata hivyo, Kampuni ya Tanzanite One Limited imekuwa ikitoa taarifa za uongo kwa mbia mwenza, yaani STAMICO tangu alivyoanza uzalishaji wa tanzanite hapa nchini. Kwa mfano, kuanzia Julai 13 hadi Julai 16, STAMICO ameripoti mauzo ya jumla ya dola za kimarekani milioni 16 wakati kiukweli ni milioni 17, tayari kuna dola almost kati ya milioni moja mpaka laki kadhaa zinaibiwa, ndiyo maana tunasema watu hawa wanaiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hilo halitoshi, minada inayoandaliwa yote, nilimwandikia barua Kamishna Msaidizi wa Madini pale Arusha, ndugu Ali Adam, tarehe 20 mwezi wa pili 2017, kwamba ninaomba uniambie tenda ya kwanza na tenda ya pili waliyouziwa madini yetu kwenye tenda ni akina nani? Alichonijibu officially, tarehe 24 Februari, ipo kwenye documentation na barua imegongwa; wameuziwa Gemoro Company Limited, kampuni ya India, Viber Global Limited Kampuni ya India, Kala Jewels Kampuni ya India, Shree Narayan Gems ya India, hiyo ni tenda ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tenda ya pili ameuziwa Arwi International ya India, Shree Narayan ya India na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge watu hawa wote wana mahusiano ya karibu na kampuni ambayo imesajiliwa Virgin Island inayofanya kazi zake Hong Kong. Waheshimiwa Wabunge nchi yetu inaibiwa, ni muda muafaka madini haya ya tanzanite wengi wenu hamyafahamu, ni madini ambayo yangeweza kubadilisha maisha ya watu wa Simanjiro lakini yangeweza kubadilisha maisha ya watanzania wengi. Ninaomba kwa ukubwa wetu tuingilie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyeiti, muda wa dakika tano ni mdogo sana nifanye mambo mawili, moja nimkaribishe sana Mheshimiwa Lukuvi Simanjiro, matatizo ya Simanjiro Wizara ina takwimu inaongoza Tanzania kwa kuporwa kwa ardhi yake, lakini la pili kwa sababu Wizara yako imesogezwa tarehe, wananchi walikuwa wapo tayari kuja kukuletea matatizo yao, ninaomba hata baada ya kupitisha bajeti yako wananchi wachache waje kukusalimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mwaka 2005 nilikuwa kijana peke yake wa Wilaya nzima aliye graduate degree ya kwanza, baada ya miaka mitatu baadae ndio mwingine mmoja anapatikana. Kwa nini ninasema hivyo, Wilaya ya Simanjiro imejaa watu wengi ambao hawajasoma, wale wachache wanaojua kuandika na kusoma waliopewa Tarafa; waliopewa kuwa Wenyeviti vya Vijiji wame-take advantage ya hali ile na kuwaumiza wananchi na kuwachukulia ardhi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri fika Simanjiro hali ni mbaya kweli kweli, lakini niseme tu kitu kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mashamba makubwa, shamba namba 24 Lorbosoit ya aliyekuwa Katibu Tarafa ya Emboreet Mzee Brown ambaye bahati mbaya au nzuri ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, amechukua heka 8,000 lakini kama haitoshi, baada ya kushindwa kulima na kufugia amebadilisha shamba lile anataka kufanya ni la wanyamapori na kuwauzia Wazungu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri umetoa directives nakumbuka kama Waziri ulisema hakuna kubadilisha ardhi yoyote, kubadili matumizi yake bila idhini yako, huyo Mzee anafanya ujanja kutumia nafasi yake ya CCM kubadilisha mazingira hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Muhindi mwingine Kata ya Loiborsiret, Kijiji cha Loiborsiret eneo la Motio, ameamua kuchukua ardhi kubwa ya wananchi kununua moja, moja heka mia, mia mbili lakini sheria zipo wazi, haiwezekani kijiji kikawa na uwezo wa kugawa zaidi ya heka 50 haiwezekani, Mheshimiwa Waziri nakuomba usaidie hilo. Kuna kijiji kingine cha Narakauwo mtu anaitwa Jerry Hoops amekuja ameingia kama mbia mwenzake na Mtanzania mmoja, alichukua heka 2,000, shamba lile lipimwe lina zaidi ya hekta 10,000 mpaka sasa hivi naomba uliingilie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Kilombero kuna zaidi ya mashamba 50,000, maelfu na maelfu ya hekari ambayo yamechukuliwa. Mheshimiwa Waziri tatizo hili hatuwezi kukusaidia kwa dakika hizi tano ninakuomba Mheshimiwa Waziri ninakukaribisha uje Simanjiro, umeenda Arumeru, umeenda Monduli, umeenda Babati naomba uje Simanjiro wanakusubiri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Naberera kuna Mwenyekiti wa Kijiji amekuwa ni mtu wa ajabu naomba uangalie, kwa kweli mimi kwa ufupi niongee kwenye hilo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo pale Wizarani kwako una watu mahiri kweli, kuna mtu anaitwa Ndugu Lwena ninamfamu ni mwanasheria mahiri kweli hali rushwa ni mtu ambaye sijawahi kuona, nimeishi naye nimefanya naye kazi mwaka 2009, anaweza kukusaidia. Kuna kesi ya Lekengere, Faru Kamunyu and others versus Minister of Natural Resources and Tourism ya mwaka 2002, Mahakama ya Rufani ilisema huwezi ukachukua ardhi inayomilikiwa kimila bila kupata idhini ya Rais. Rais peke yake ndiye mwenye uwezo wa kufanya hivyo. Ukisoma pamoja na Sheria ya Land Acquisition Act ya mwaka 1967, pamoja na kuwapa wananchi fidia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri naomba utusaidie Simanjiro imeoza, waliotutangulie wengine kwenye madaraka hayo hawajatumia vizuri, ninaomba tusahihishe historia, watu wangu wanaumia, ardhi inaumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudie kwenye suala la ardhi Mkoa wa Arusha kwa ujumla. Kuna watu walioletwa na Mwalimu Nyerere kwa nia njema ya kuwekeza, baada ya kumaliza uwekezaji na kuchukua ardhi yao, sasa wanayageuza mashamba yale kama mtaji. Inawezekanaje Mtanzania akanunua ardhi yake peke yake, sana Serikali muingile, kuna watu wakubwa wana mashamba makubwa pale Arusha, Arumeru na unafahamu. Mzungu anataka kwenda ulaya kwenda ku-retire kukaa kwenye nyumba ya wazee, anabadilisha ardhi yetu kama sehemu ya kiinua mgongo chake, badala ya ninyi kusimamia arudishiwe machinery na gharama ambazo ametumia kwenye shamba lile, anatuuzia mashamba yetu, NHC walinunua kule Kisongo, ninampongeza Ndugu Msechu ni kijana mzuri mwenzetu anafanya kazi kubwa ninaomba tembelea Angola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamchanganya kama Serikali, hamjui kama mpo kwenye ubepari, hamjui mpo kwenye ujamaa you just confuse, philosophy mnaichanganya mpeni afanye biashara ili atakapopata faida aendelee kusaidia watu maskini wengine, lakini mnamchanganya ni mtu mzuri mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mungu awabariki sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu pale ambapo rafiki yangu na ndugu yangu Mheshimiwa Nape alipoishia. Alipoanza kutoa takwimu nyingi za kuhusu wafugaji kunyanyaswa nchi hii, labda kukumbusha tu wiki mbili zilizopita Kamati hii ya Ardhi Maliasili na Utalii ilizuia Muswada ambao ulikuwa unakuja kwa ajili ya kuwaadhibu wafugaji tena ya kum-charge kila mfugaji, kwa mfugo mmoja kama ni ng’ombe au mbuzi shilingi 100,000 wanapoingia kwenye hifadhi ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi naipongeza sana Kamati hii kwa kufanya juhudi kubwa na kuzuia jaribio hilo baya kwa ajili ya wafugaji tena wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu nyingine, jana Mahakama ya Wilaya ya Same imetaifisha ng’ombe 36 wa wafugaji. Ni ongezeko la takwimu ambazo ametoa kaka yangu Mheshimiwa Nape na mimi naomba Bunge hili liangalie sasa kwa historia ya nchi hii wafugaji kunyanyaswa kwa muda mrefu. Hii imekuwa sasa ni too much! Naomba mtusaidie ili haya mambo yaishe, maana wakati Mheshimiwa Jaji Nyalali akihukumu ile kesi ya Mkomazi miaka fulani na hukumu yake naijua vizuri sana, mfugaji aliyehamishwa kwenye mbuga ile alilipwa shilingi 250,000; yaani haya ni manyanyaso ya miaka ya 1990 mpaka sasa hivi, wafugaji wanaendelea kutaabika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tu suala la Kamati, kwenye ukurasa wa 14 Kamati imeongelea suala la Ngorongoro na wanasema hivi: “Kuna uharibifu wa vyanzo vya maji, uoto wa asili unaosababishwa na ongezeko la binadamu Ngorongoro tangu mbuga ile iamuliwe kuwa mbuga mwaka 1956, maana wakati ule wakazi walikuwa 8,000 na sasa wako 93,000, kwa hiyo, kuna upungufu wa watalii kwenye Mbuga ya Ngorongoro.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni uongo mkubwa na mwendelezo wa Serikali hii kuwaumiza wafugaji. Kwa nini nasema hivyo? Mwaka 2014 takwimu sahihi zilizopo Ngorongoro ongezeko la mapato ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, imeongezeka shilingi bilioni 63 na mwaka 2017 ni shilingi bilioni 102. Hili hata Mheshimiwa Waziri Maghembe alikiri, Kamati inajua, imepewa mpaka taarifa na Chama cha Wafugaji wa Ngorongoro, lakini Kamati hii haijataka kunukuu kwa makusudi ya kutaka kupotosha kwa sababu hawataki kuwasaidia wafugaji wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu barua waliyopewa ya tarehe 8 Machi, 2017. Serikali hii inaingia kwenye record tangu Uhuru wa nchi hii kuwanyanyasa wafugaji na wakulima kwa vitendo. Naomba data hizi ambazo zipo na Kamati imekabidhiwa, wafugaji wa Ngorongoro wameonewa vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mwaka 2013 Hifadhi hii ya Ngorongoro, Mamlaka ya Ngorongoro iliibuka mshindi wa Umoja wa Mataifa baada ya maajabu ya saba ya asili inaitwa One of the Natural Wonders of Africa, kwa sababu wafugaji na wanyamapori wanaishi sehemu moja, lakini najua target ya Serikali ni kutaka kuwaondoa wafugaji wale. Tunaomba kwenye Bunge hili muwasikilize wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Nape kwamba kwa mara ya kwanza tuunde tume itakayoshughulikia masuala ya wafugaji na uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la mipaka. Kama hoja ya Kamati inavyosema, kuna maeneo mengi ambayo yalitolewa kwa wanyang’anyi wa nchi hii, kuna ranchi nyingi nchi hii zilitolewa kwa wafanyabiashara. Kwa nini msiwarudishie wafugaji ili tuendelee na sisi kupata maeneo ya wafugaji? Kwa mfano, kama mmechukua Tarangire sehemu fulani, mtupe mbuga yoyote au eneo lolote, kama ni Kongwa au Kilimanjaro na sisi wafugaji tupewe na maeneo ya kufugia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la maji. Inasikitisha sana, mamlaka inayodaiwa kuliko yote ni mamlaka za Serikali na ninyi mmeshindwa kuzilipisha. Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 34 wa kitabu hiki utaona kuna barabara ya Arusha – Orkesumet - Kibaya mpaka Kongwa. Wakati upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unafanyika kwenye barabara ile, inapita Wilaya ya Simanjiro, lakini walipofika kwenye Kijiji cha Nadonjukin wataalam wanatoa sababu ya kupindisha barabara ile isipite Terrat kuelekea Orkesmet wakidai kwamba kuna wanyamapori wanaopita kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia kwenye nchi yetu barabara ya Morogoro –Mikumi – Ilula – Iringa, pale katikati panapita wanyamapori. Pia barabara ya kutoka Minjingu kwenda Babati, kuna Mbuga ya Tarangire na Manyara katikati. Kimataifa, kuna barabara ya Kruger Park inayopita katikati ya National Park ya Afrika Kusini ya Kruger National Park. Barabara hizi zote zinapita katikati ya Mbuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa TANROAD wanapitisha barabara ile wakiiacha Simanjiro yenye vijiji vya Terrat, Sukro, Narkawo, Loiborsiret. Huu ni uonevu na ubaguzi wa hali ya juu. Naiomba Wizara, Mheshimiwa Waziri kwa kitabu chake hiki, ajaribu kuangalia upya kwamba lazima barabara ile ipitike. Tunavyosema nyumbu anapita kwa miezi mingapi; wanakuja mwezi wa Tatu tu kuzaliana pale. Kwa hiyo, naomba ubaguzi huu usifanyike hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara tangu barabara zake zipandishwe hadhi, mara ya mwisho ni mwaka 2009. Kuna barabara ya kutoka Msitu wa Tembo kwenda Korongo kuelekea mpaka Vijiji vya Nyumba ya Mungu mpaka Ngage. Barabara hizi kwa fedha za ndani za Halmashauri na TARURA haiwezi kuhudumia barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wajaribu kuangalia namna gani Mheshimiwa Waziri apandishe hadhi barabara zetu ili TANROADS waangalie barabara hiyo yote inaenda mpaka Ruvu-Remit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye ATCL. Kwenye ripoti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ukurasa wa nne, Afisa huyu anasema ATCL hesabu zake hazijawahi kukaguliwa kwa muda mrefu sana, lakini sababu hiyo hiyo ndiyo inatupelekea sisi tuseme kwamba inawezekana one point five trillion ambayo haionekani kwenye Hazina ya Serikali, inawezekana imetumika kwa sababu ya kutokagua mahesabu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka, wale wanaomshauri Mheshimiwa Rais, washauri vizuri. Mheshimiwa Magufuli hatadumu milele, ataondoka kwenye madaraka. Ninyi ambao hamumwelekezi kwamba anakosea saa nyingine, kama yeye ndio kachukua hizo fedha, ni muhimu ndugu zangu mumshauri vizuri. Fedha za umma ni za umma na mtu huwezi kuzichukua kama unavyotaka fedha zako za mfukoni. Kuna taratibu za kuchukua fedha hizi. Ni vizuri mshauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanafanya hivyo Waheshimiwa Mawaziri, wakumbuke kwamba akina Yona walikuwa Mawaziri, wakumbuke kwamba akina Mramba walikuwa Mawaziri iko siku Watanzania watakuja kuwaulizeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nafanya Mahakama ya Kimataifa, Rwanda, watu waliokuwa wakimzunguka Rais Habyarimana mwaka 1994, walimshauri vibaya na ndiyo maana mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 yakatokea. Nawaomba Waheshimiwa Mawaziri, watu wa karibu walioko karibu na Mheshimiwa Rais, washauri Mheshimiwa Rais kwamba nchi hii ni nchi yenye sheria, haiwezekani ukaweza kuchukua fedha zote kutoka kwenye Hazina ya Taifa ukapeleka mahali ambapo hazionekani. Ni muhimu ufuate sheria ili nchi hii iweze kuwaheshimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi…

KUHUSU UTARATIBU . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabila la Kimasai kati ya vitu ambavyo hatuwezi ni unafiki. Najaribu kushawishi kwa nia njema kwamba inawezekana hawa ambao wako madarakani sasa, kama hawamshauri vizuri Rais, nitoe mfano mmoja; Police Ordinance, Political Parties Act, The Constitution haimpi mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukataza mikutano ya hadhara na hawa ambao wako karibu naye wanamnyima fursa ya kumshauri vizuri. Hivyo, ni vyema waliomzunguka Mheshimiwa Rais wakamshauri vizuri. (Makofi)

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu waliokaa upande wa pili ambao kwa muda mrefu nimekaa na ninyi CCM, saa nyingine muwe mnakumbuka Kanuni ya 64 hiyo hiyo, mnapojaribu kushawishi Bunge kwa kumsifia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa moyo wa dhati na ninyi ndio mtakaokaa upande wa pili kumpiga mawe baadaye Watanzania wakianza kuuliza maswali. Sisi wengine tuko upande huu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, hili la Stieglers’ Gorge halihitaji wala akili nyingi, ukifananisha eneo la UDOM na Dar es Salaam kwamba kulikuwa na wanyama pori na kwenyewe na hili eneo la Stieglers’ Gorge ambalo ni Selous, haihitaji kusoma hata kidogo kujua kwamba kule hakuna wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wafugaji wa nchi hii kwa muda mrefu wameonewa sana. Mwaka 1968 Mwalimu Nyerere alipokuwa Rais wa nchi yetu, alipotembelea eneo la Indumiet kule Longido, ambayo kwa sasa ni Siha aliwaambia Serikali kwamba wafugaji watengewe ekari 5,500 kwa ajili ya kufuga, mwaka 1968. Mwaka 1973 Bunge hili likatunga sheria na kuiagiza Serikali mwezi wa tatu, mwaka 1973 kwamba wafugaji wapewe eneo hilo. Serikali kupitia GN Na. 59 mwaka huohuo wakatenga ekari 5,500 kwa ajili ya wafugaji, lakini TANAPA kwa kukaidi maagizo ya Mheshimiwa Rais Nyerere, Marehemu, Baba wa Taifa, waliwanyang’anya wananchi wale ile ardhi wakairudisha Kilimanjaro National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 1998 Mahakama ya Rufani chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Nyalali iliiagiza Serikali ya Tanzania kuwapatia wafugaji wa Mkomazi eneo lingine mbadala la kufugia. Mpaka leo miaka 20 tayari kamili wafugaji wale wanahangaika wako pale juu, wanahangaika hawana eneo la kufugia.

Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi, juzi mwezi Februari, 2018 Mheshimiwa Kigwangalla alienda Wilayani Simanjiro, Kijiji cha Kimotorop, najua unafahamu kwa sababu, ulitembelea muda mrefu sana, Kijiji cha Kimotorop. Amekuta vigingi wanyama pori wamepiga kuanzia pale zahanati, shule ya msingi na kuchukua kaya 3,000 akatoa tamko kama Waziri kwamba wafugaji wale wote wafukuzwe na waondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike mahali sasa mnajiuliza kwa nini Tanzania tunashika nafasi ya 110 duniani kati ya nchi 133 kiutalii, mnajiuliza ni kwa nini pamoja na vivutio vikubwa ambavyo tunavyo. Jibu ni dogo, laana na vilio vya wafugaji nchi hii na wananchi wanaolia kwa sababu ya kuonewa kwa muda mrefu sasa. Ifike mahali wananchi hawa wasikilizwe, watu wanaumia kwelikweli, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi saidiana na Wizara hii maana mliambiwa, Bunge lilitoa tamko la Wizara tano mkae kwa ajili ya kusaidia wananchi, mpaka leo hamjakaa, mmeweka vigingi wenyewe, wananchi waaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, kuna dada yangu kutoka Arusha aliongelea kuhusu Loliondo, mgogoro wa Loliondo miaka 26 leo halina majibu Bunge, Serikali haina majibu, Loliondo wananchi wanaumia sana. Ifike mahali niungane na Mheshimiwa Mbunge aliyesema unda kamati malum kama ambavyo umeunda ia Tanzanite, ya madini mengine, ili tusaidie nchi hii kuwanusuru wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale juu kuna mfugaji mmoja anaitwa Julius Tisho amepoteza ng’ombe 240 ambao wameswagwa na wahifadhi kwenye Mbuga ya Selous, wakalipia risiti, hizi hapa kwa ajili ya faini, lakini mwisho wa siku pamoja na kulipa risiti hizo ng’ombe wale walipigwa risasi na wahifadhi, CD ninayo hapa nitakukabidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua Wasukuma wameonewa, najua Wagogo wameonewa ambao ni wafugaji, Wamasai wameonewa ambao ni wafugaji, Wabarbaig, lakini wengine na Wakurya, itafika mahali tutaweka tamko na ninyi Chama cha Wafugaji mko hapa ndani, tufike mahali tuseme kwa sababu utalii unaathiri maisha yetu tufike huko Ulaya na Marekani, twendeni China na mahali popote duniani tuwambie kwamba tunawaombeni msije Tanzania kwa sababu mnapokuja Tanzania maisha yetu yanaathirika, tutaweza. Tukaeni pamoja, tuunganishe pamoja na sisi Wabunge tuko tayari kuitangaza Tanzania kwamba utalii huu unaathiri maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado hatujafikia hapo, lakini tutafikia mahali fulani tunaumia sana, inauma sana. Naombeni Serikali hii isikie kwa mara ya kwanza. Bahati mbaya kule Loliondo ambako 2015 ndilo Jimbo pekee Arusha ambalo mmechagua CCM watu wanaumia sana. Wafugaji nchi hii naomba sasa ifike mahali wasikilizwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru.
Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kunukuu kitabu ambacho asubuhi tumeambiwa kinauzwa pale nje na Mheshimiwa Spika kwa sababu wengine wanapenda sana kunukuu vitabu vya nje, lakini hapa ndani wanaviacha wakijidai kama hawaoni, naomba nianze kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu chenyewe kinaitwa Corruption in Agony, Contemporary Nyerere of our time, by Jacob Roman Lubuva. Kinaanza hivi naomba niendelee; “many people in Africa in beyond consider the President’s personal character, attitude and leadership style peculiar to his predecessors. Some equate his leadership qualities to leadership ethos of the founding father of Tanzanian Nation, his excellent, the late Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Some commentators have yet compared President Magufuli to some known architects of African Nations like Kwame Nkurumah and Nelson Mandela with reference to his hate of corruption, a sense of self-reliance and pro-poor attitude.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini anaendelea, “The President remarkable achievement immediate and radical pro-citizen’s socio-economic transformations and unprecedented fast truck of political campaigns. Consequently, the President has been and presence of pre- electric and social media global being committed.”Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Zitto…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zitto…

MHE. JAMES K. MILLYA: …mimi najua Kimasai vizuri na unajua hilo, lakini Mheshimiwa Zitto wakati fulani nilipokuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Tumaini ulikuwa mtu wa kawaida/ Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa hiyo, unajua kwamba najua kiingereza vizuri, najua kimasai na kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa kuanza hili, Mheshimiwa Rais amefanya mikutano miwili; mmoja, Ikulu kuhusu wafanyabiashara Tanzania nzima, lakini bado Mheshimiwa Rais juzi alifanya mkutano na wachimbaji wa nchi nzima wadogo wadogo kuhusu biashara ya madini. Lakini wenzetu hawa kwa sababu hawaoni na hawataki kutambua, bado wanaponda nguvu za Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimetaja rushwa? Kampeni za wenzetu mwaka 2002, 2005, 2010 walisimamia ajenda ya rushwa, rushwa, rushwa! Ametokea mtu ambaye anapigana dhahiri kwa ajili ya rushwa kwa sababu hawa wafanyabiashara siyo wengi wazuri. Ukiona mtu anatoa mapovu kuwatetea ujue inawezekana amerambishwa kidogo, lakini ukweli ni kwamba wengine na naomba nieleweke vizuri, siyo wafanyabiashara wote wabaya, lakini kuna wafanyabiashara kweli imedhihirika pale mfano, madini pale airport, Tanzanite wameshakamata zaidi ya watu wengi wanaiba madini, na hao unawatetea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, naomba nitoe takwimu za Tanzanite tangu ukuta huu uwekwe mambo ambayo yalikubalika kuhusu Marekani miaka hata kabla ya mimi kuanza shule ya msingi. Ukuta huu Mheshimiwa Dkt. Magufuli baada ya kuona kwamba madini yetu yanaibiwa sana akaamua kuweka ukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye Kamati Teule ya Bunge leo hii watu wa Mererani na hii kauli ichukueni, watu wa Mererani wanapendelea ukuta, wanafurahia ukuta, madini yameongezeka bei. Mimi ni Mbunge, kauli hii inaweza ikanihukumu mwaka 2020 lakini uhakika watu wangu wanafurahia ukuta. Ukuta hauna shida na ukuta nauunga mkono sana, kwa hiyo, watu wengine wanaokuja kuongea kuhusu ukuta hiyo waache kabisa kwa sababu ukuta uko sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitengo kinaitwa TANTRADE kwenye Wizara ya Biashara. Mheshimiwa Rais juzi juzi hapo aliwaambia watu hawa hawasaidii Serikali yetu vizuri kabisa. TANTRADE inaongozwa na mtu anaitwa Edwin, naomba nitoe ushuhuda, kuna EXCO itafanyika China mwaka huu. Kuna vijana wa Arusha wameomba kuhudhuria na wanasema Serikali hatutaki hata shilingi moja kwenu. Wameomba tangu mwezi wa Oktoba, 2018 mpaka leo isingekuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje juzi Arusha, isingekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara huyu kijana asingesaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, watu wetu hawa ambao wamepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania kukuza biashara zao wawasaidie kweli kweli. Niombe kitengo hiki cha TANTRADE kiangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani vita ambayo saa nyingine Mheshimiwa Dkt. Magufuli anapigwa ni ya nini? Ni kwa sababau kama Mheshimiwa Dkt. Magufuli anaingilai interest ya Wamarekani, interest ya Wabelgiji, interest ya Wajerumani kwa sababu wafanyabiashara wao wamesimamishwa na Canada na wengine ndiyo maana wanasukuma. Ninaomba Serikali yangu tuwaangalie wafanyabiashara tuwasaidie haswa, tuwasaidie, tuweke mifumo rafiki ya kusaidia wafanyabiashara kwa sababu nchi hii kiuchumi tutafahamika tu kama ni wazuri kama tuki- compete mfano na Kenya na nchi nyingine kiuchumi. Ninaomba nia njema ya Mheshimiwa Rais kwa kuita ile mikutano miwili ipo, ninaomba watu ambao wanasaidia kwenye kitengo cha biashara wasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitika asubuhi sana, kama mtu anataka maamuzi ambayo yanafanywa kwenye nchi na yanufaishe na watu wa Msumbiji nilisikitika kidogo. Mheshimiwa Zitto nikikosea ni faida yako wewe mpinzani kwa hiyo wewe ninaomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ni moja, kama Serikali imepitisha bei elekezi kwa ajili ya korosho kuwaokoa watu wetu wa kawaida, kwa nini mtu mmoja ambaye anajua…

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa kangomba utawafahamu tu. Na ni kweli wangependa korosho ya Mozambique inunuliwe ili ya watu wetu isinunuliwe waanze kupiga kelele ndiyo nia yao. Lakini hujuma hiyo imeshafahamika na hakika hamtaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara husika, biashara ni muhimu sana na Mheshimiwa Rais ana nia njema sana. Niombe kama ikiwezekana Bunge hili liweze kuunda Kamati Maalum ya Wafanyabiashara ambayo inaweza ikasaidia kumuongoza Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri kutanzua matatizo ya kwenye sekta hii ya biashara, ningeomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona, naomba niwasilishe, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, nami nimshukuru Mungu kwa nfasi hii, lakini kipekee kwa sababu ndiyo nasimama kwa mara ya kwanza tangu tumpoteze Mheshimiwa Mzee Mengi, marehemu, niendelee kumuombea Mungu ailaze roho yake pema peponi. Alikuwa kiongozi mzuri sana.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze watumishi wa Wizara wamefanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Mpina alipita juzi Simanjiro na akongea na wafugaji halafu akakagua baadhi ya mabwawa yetu na Mheshimiwa Waziri ukasema utasaidia fedha kwa ajili ya kuboresha yale mabwawa. Mimi kama Mbunge wa eneo hilo nikushukuru, lakini niishukuru Serikali yangu sana kwa kuwajali wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa Ole-Gabriel. Siku fulani mifugo ya Simanjiro ilikamatwa kwenye Pori Tengefu la Mkungunero, yeye na Naibu Waziri, Mheshimiwa Ulega, walikuwakilisha vizuri, walitusaidia ng’ombe 540 na punda 10 wakaondoka mikononi mwa hifadhi, kwa negotiation za Wizara, na mimi kama Mbunge ambaye napenda kushukuru kwa yale ambayo yamefanywa na Serikali ninawashukuru sana yeye pamoja na viongozi wa TAMWA kwa ujumla na viongozi wa Wizara ya Maliasili, wametusaidia na mifugo ile iko huru. Ninawashukuru na wafugaji wa Simanjiro wanawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais, tuendelee kumpa moyo sana kwa kazi kubwa anayowasaidia wafugaji. Wafugaji wengi wako hapa, kwenye hizi gallery zote wafugaji wapo. Mheshimiwa Rais ametamka kwamba wakati tunapata uhuru wa nchi yetu taifa lilikuwa na wakazi na Watanzania milioni tisa tu na mifugo ni michache, tumeongezeka kwa takribani milioni 55. Baada ya kuona haja hiyo, ameona yale maeneo ambayo wahifadhi hawayatumii kwa ajili ya mbuga za wanyama amesema kwa upendo mkubwa wa wafugaji yagawiwe, ifanyike timu maalum ya Mawaziri imepita ili wafugaji wapate maeneo hayo. Huu ni upendo gani kwa mkuu wetu wa nchi, anatupenda sana. Mimi kama mfugaji na Mbunge anayetokana na CCM nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, wafugaji wamelipokea hili kwa mikono miwili. Anapenda na wafugaji wako na yeye siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine; kuna ugonjwa unaitwa ugonjwa wa ndigana. African Union miaka fulani pale Adis Ababa waliamua kujenga kiwanda cha kuzalisha dawa ya ndigana pale Malawi; lakini hapa nchini mtu aliyepewa tenda hiyo ni mtu anaitwa Dokta Mbwile. Ninapoongea leo mifugo katika Ukanda wote wa Simanjiro, Arusha, Manyara wanakufa kwa sababu dawa hii haipo sokoni. Wizara sijui mmetumia hekima gani, mnatoa tenda hii kwa mtu mmoja tu nchi nzima. Niiombe Wizara kama ushauri hii tenda igawiwe kwa watu wengine kwa sababu, ule ugonjwa ukimshika ndama au ng’ombe haiwezekani kumtibu tena. Ninawaomba mfikirie namna ya kuongeza wadau wa kuchukua dawa hii kutoka Malawi wailete Tanzania.

Mheshimiwa Spika, la pili; maeneo ya wafugaji ni maeneo makame sana, yanapokea mvua kidogo kila mwaka. Namna pekee ya kuwasaidia wachungaji na wafugaji kwa ujumla nchi hii ni kuanzisha mabwawa makubwa.

Mheshimiwa Spika, wakati wa uhuru kulikuwa na mabwawa, natoa mifano miwili, Kata ya Narkawo na Kata ya Komolo pale Skuro; mabwawa ambayo Mheshimiwa Waziri wa Mifugo ulitembelea; ni mabwawa makubwa ambayo Mheshimiwa Nyerere, Baba yetu wa Taifa aliyaanzisha kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji. Kwenye maeneo mengi ya wafugaji ardhini hakuna maji, mtusaidie tupate mabwawa makubwa kila eneo ili wafugaji wapate nafuu ya adha ya ufugaji wao.

Mheshimiwa Spika, lingine ni migogoro ya wafugaji. Migogoro hii imekuwa kero. Nimesoma jitihada za Wizara, wamefanya vizuri, maana wametembelea Wilaya za Uvinza, Kasulu, Kibondo, Katavi, Kalambo, Nkasi na Sumbawanga. Niombe, nchi hii migogoro ya wafugaji na wakulima mingi imekithiri eneo la Morogoro; mtusaidie sana Morogoro, muipe kipaumbele Morogoro. Na kwa sababu nimeona mmewashirikisha akina nani, niombe Kanisa la Kilutheri la Kiinjili la Tanzania pale Morogoro mlihusishe. Kuna Askofu mmoja pale anaitwa Askofu Mameo; ni mtu mwema anaweza kuisaidia Serikali kwa ajili ya kutatua tatizo hili la wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Spika, jana nimefarijika sana nimeongea na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na yeye anasema yupo tayari kuingia Morogoro kwa sababu ni mkazi wa Morogoro na kusaidia migogoro hii kwisha. Kwa hiyo, shirikianeni na Naibu Waziri wa Kilimo yuko tayari kusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, lingine; Ranchi za Taifa kwa awali kabisa zimechukuliwa kutoka kwa wafugaji. Leo hii kwa takwimu Ranchi za Taifa zinamiliki hekta laki mbili kwa mifugo elfu 30 tu. Kwa sababu kuna ranchi nyingine hazitumiki na Serikali wafikirie namna gani ya kuwagawia wafugaji, lakini wangalie, waweke angalizo moja, wasiwape watu wenye nguvu tu, wachukueni wafugaji wa kawaida wagawiani ranchi hizi. Kuna Kilimanjaro kule, kuna hapa Mpwapwa, kuna nyingine Kanda ya Ziwa. Mtusaidie wafugaji ili tuondokane na hizi shida na kumsaidia Mheshimiwa Rais ili hatimaye tusipate shida ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Suala la Maziwa. Ninaipongeza sana Wizara kwa kuamua kulinda viwanda vya ndani. Leo hii pale Arusha ukijaribu kununua Brookside au maziwa ya Afrika ya Kusini ni bei ghali sana. Kwa hiyo Wizara nia yake na Serikali ni kukuza viwanda vya ndani. Nimeona maziwa yetu ya Azam, maziwa yetu ya Tanga Fresh, kama Mheshimiwa Rais alivyotembelea, yanaanza kupata soko kwenye nchi yetu. Endeleeni hivyo hivyo tuwaunge mkono wazalishaji wa maziwa, nendeni chini muwagundue wengine ambao wanataka kuanzisha biashara hii wapeni support.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niombe linguine. Juzi nimeona clip moja, na mimi nilisema mara nyingi sitaki kuongelea upinzani sana, lakini mara nyingine wanapoanza kufanya siasa za ajabu inabidi mtu uondoke kwenye mstari ambao hukutaka kuukanyaga. Nimemwona Mwenyekiti wa Taifa wa Chama kinachoitwa CHADEMA. Mheshimiwa Mzee Lowasa alipoondoka na kurudi nyumbani kwake CCM aliwashukuru CHADEMA na akanyamaza; lakini cha ajabu sana Mzee Mbowe juzi anasema Lowasa ameondoka na mke wake peke yake. Ninaomba apate ujumbe mzuri huu, kura za Serikali za Mitaa mwaka huu mtaona jibu lake, kwamba CCM imara ile ambayo tunaijua kuanzia miaka ya elfu mbili, sabini, sasa mtaiona. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ole-Millya. Nakushukuru sana asante.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuwapongeza watumishi wa Wizara wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri wetu Dkt. Kigwangala kwa kazi kubwa wanayofanya kufufua na kuendeleza sekta hii ya utalii nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia kidogo hoja za wenzetu, mtu anasema kwa kawaida miaka yote tumekuwa tukipokea watalii kutoka nchi ya Israel kila msimu, unapata shida kidogo kwa sababu mtu hataki kusifia yale mazuri yanayofanywa kwa wakati huu. Kama hivyo ndivyo, kwa nini mtu asigusie watalii takriban 340 waliofika juzi wa kutoka China? Hili ni eneo jipya ambalo hatukuwa nalo, Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wamefanya vizuri na uongozi wa nchi hii. Tungeona watu waungwana wataje na hayo. Kwamba siyo lazima utaje ya Russia au utaje mahali pengine kama Ukraine, taja na China kwamba hili ni soko kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri kwa kuboresha kidogo hilo, ningeomba ushirikishe balozi zetu nchini. Balozi zote zilizopo mataifa mengine ya nje watuandalie ili watu wetu wanaofanya utalii hapa ndani kama Arusha au maeneo mengine tuwapeleke na wafanyabiashara wakakutane na wale ambao wanauza biashara ya utalii duniani kote wakutane na watu kama ambavyo nchi ya Kenya inafanya mara nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee hoja kubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais. Vijiji vyetu vya wafugaji kwa miaka mingi sana baada ya uhuru na hata wakati wa uhuru na Mheshimiwa Waziri umegusia kwenye hotuba yako. Tumeumia muda mrefu kwa miaka mingi, Mheshimiwa Rais baada ya kusikia kilio cha vijiji takriban 350 nchi hii, akaamua kuelekeza Wizara karibu nane zikae pamoja na akawatuma Mawaziri kila mahali, walifika Kimotoro Mawaziri nane. Nia ya Mheshimiwa Rais ni kutatua hii hali iliyokuwepo ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wenzetu wakiendelea kuuliza hivi itawezekana kufanyika kweli? Nia ya Mheshimiwa Rais ni njema, niombe sasa Wizara yako Mheshimiwa Waziri msukume jambo hili ili lisijelikawa ni jambo ambalo halitatekelezeka, wananchi wanasubiri kwa hamu Kimotoro, Simanjiro na nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma vizuri hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa 18 na 19; wenzetu bado hawaweki imani kwamba Serikali hii ni Serikali ambayo haiongei tu bali inatenda na hizi zote ni sifa za Mheshimiwa Rais. Ukiona kwenye hotuba yao wanagusia suala la Stiegler’s Gorge; Serikali inataka umeme wa kutosha. Wanaongelea pia suala la hizi hifadhi, kwamba kwa nini tumege eneo fulani la hifadhi halafu tuwape wananchi; wenzetu mmeuliza tayari SGR tunafanya nini? Mnauliza bado masuala ya ndege. Mimi niseme kitu kimoja, nimepata bahati ya kupanda ndege hizi mpya za Serikali, ni ndege za kisasa zitatuongezea utalii na nimeambiwa kuanzia mwezi ujao mtaanza kwenda India na Afrika ya Kusini, huu ni mwanzo mzuri sana. Na crew yetu mimi nilivyoisikiliza kwa uzoefu wangu wa masuala ya ndege, ni crew nzuri, tutaongeza utalii kwenye nchi hii na Mungu aendelee kuwabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kitu kimoja, nchini Ghana baada ya kupata uhuru, Kwame Nkurumah alianzisha miradi mikubwa sana. Tulipata wasaliti waliompinga Kwame Nkurumah wakati ule. Lakini mnakumbuka pia katika ukombozi wa Congo, wakati Congo inakombolewa kulikuwa na mtu anaitwa Patrice Lumumba akatokea msaliti mmoja anaitwa Moise Tshombe wakati wa kugawa Jimbo la Katanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasaliti duniani hawakosekani wala Mheshimiwa Rais asiache kufanya miradi mikubwa ya kusaidia nchi kwa sababu ya kusikiliza kelele za wale ambao hawatakii mema nchi hii, aendelee kupambana na sisi wengine ambao tupo upande huu, tunajua anafanya mema kwa ajili ya nchi hii, tupo tayari kusaidia Taifa hili na tutamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, na Mheshimiwa Dkt. Kigwangala usitishwe na maneno yoyote ya watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nigusie suala la Makumbusho ya Taifa letu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, bajeti tunayotenga ni ndogo sana, Makumbusho ya Taifa yanaisaidia Serikali na sisi Watanzania kuhifadhi kumbukumbu ya leo, kesho na miaka ijayo. Inawezekana mambo mengine yanafanyika kwa sababu ya kutaka kutufurahisha tulioko duniani sasa, tuna watoto na wajukuu wanaokuja keshokutwa wanataka kujua Tanzania imetoka wapi, inaenda wapi na miaka mingine inaenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, bajeti ya makumbusho iongezwe, ni ndogo kweli. Hii ni taasisi muhimu ambayo haipigiwi kelele mara nyingi. Mimi nimepata bahati ya kuzunguka kwenye makumbusho mbalimbali, kuna makumbusho mazuri sana duniani, naomba usaidie ya kwetu, ya kwetu ipo hoi bin taaban. Ninaomba Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha hoja yako ugusie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lingine ni Kuhusu Ujangili. Nimeona umesifiwa kuhusu ujangili. Mimi Simanjiro nimepata ujumbe jana, wafugaji wanalalamika kuhusu ujangili, ujangili umeongezeka Simanjiro eneo la Terat, Sukro mpaka Kimotoro, ninaomba usaidie. Lakini nimesikia kwenye hotuba yako umeongea mambo mazuri, umesema unaanzisha hunting blocks tena na unagawa vibali vipya, hilo litasaidia kwa sababu kwa kugawa hunting blocks, wale ambao umewapa hunting block watasaidia kushirikiana na Serikali kulinda wanyamapori wasiuwawe. Wachungaji wetu wa Simanjiro wanashindwa kuchunga kwa sababu wanahisi wanaweza kupigwa risasi na majangili, ninaomba muongeze taskforce ile National Taskforce ya Anti-poaching ipelekwe Simanjiro sasa hivi wanyama wanauwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la fidia. Hatuwezi kumfidia binadamu, juzi Simanjiro kijana mmoja mtoto wa shule ya sekondari alienda machungani akauwawa na tembo. Ninaomba msaidie mfikirie kuleta sheria hapa Bungeni tubadilishe at least tupate kidogo kifuta machozi kizuri. Mngechukua mila zetu za kifugaji za Kimasai, mtu akiuwawa kwa namna yoyote bahati mbaya, sisi tulikuwa tunatoa fidia mpaka ng’ombe 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mfikirie ni namna gani basi, kwa sababu katika mila za Kiafrika, mimi ninavyofahamu kama wafugaji wa Kimasai, mtoto ni kama kiiunua mgongo cha mzazi, akishaondoka binadamu mtu unamtegemea ni mtoto wako. Ninaomba msaidie hili suala la fidia mlirekebishe kidogo, halijakaa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kuna lingine, kuna mfugaji wa Morogoro, Game Reserve ya Matambwe aliuwawa ng’ombe wake 200 kwa kupigwa risasi na watumishi wa Wizara yako mwaka 2015, ametozwa faini lakini bado maaskari wale wakapiga risasi; ninao ushahidi hapa maaskari wa wanyamapori wakipiga ng’ombe 200 risasi; mpaka leo mfugaji yule hajapewa fidia yoyote, hajaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri nitakuletea ushahidi huu wote uwasadie, nina majina ya hawa walioamuru ng’ombe hawa wapigwe risasi. Jina la huyu aliyepiga risasi na mtu aliyechukua video lakini naomba kwa muktadha wa hoja hii nisitaje majina yake lakini nitakuletea ili wewe kama kiongozi wetu wa kisiasa katika Wizara usaidie hilo lipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya ujirani mwema. Asilimia 70 ya wanyamapori wako nje ya hifadhi, tunawatunza sisi lakini hatuoni faida gani mnatupa kama kuchimba maji, hospitali, kuhudumia shule mnatoa kidogo sana. Mheshimiwa Waziri naombeni mfikirie kwenye Wizara yako ili hili tupate na lenyewe kwa sababu mkitushirikisha tukapata faida ya wanyama hawa, tutawatunza kwa sababu tunaona faida yao, ninaomba Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja, kwamba unafanya kazi nzuri kwa kweli Wizara haipo kama ilivyokuwa mara ya kwanza, hizi sifa tukupe na Serikali imejitahidi sana. Baada ya kusema hayo nawatakia heri katika utekelezaji wa majukumu yenu, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze sana Wizara kwa ujumla wake kwa kazi kubwa wanayofanya.

Mimi ni Mjumbe wa Kamati hii najua kazi mnayofanya ni kubwa na kubwa na hongereni sana. Mheshimiwa Maftaha ameongelea wizi wa Mererani hapa ni kabla ya ukuta kujengwa. Mheshimiwa Rais baada ya kuona kwamba kuna wizi mkubwa ukuta ukajengwa kazi hii inafanyika vizuri ukuta umedhibiti uimarishaji wa kodi na ndiyo maana unaona kwenye takwimu ya Wizara baada ya ku-collect milioni 700 tu tuna-collect sasa almost two point three billion. Kwa hiyo hii ni kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya CCM, hilo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile na mimi nishukuru kwa ajili ya ujenzi wa Mererani, ule ukuta umesaidia nchi sana watu wetu wamenufaika, utajili unaongezeka. Hapo awali tulikuwa tunabezwa Mheshimiwa Rais kafanya kitu gani bwana, CCM inafanya kazi gani; lakini niwaambieni kitu kimoja mimi kama Mbunge wa Jimbo linalotokana na Tanzanite utajiri wa watu wetu miongoni mwa watu wetu unaongezeka kwa kiasi kikubwa sana, Serikali imenufaika. Hata hivyo Mheshimiwa anajua changamoto mbili tatu ambazo nitazitaja, muda hautoshi.

Mheshimiwa Spika, pale kuna milolongo mikubwa sana, Mheshimiwa Waziri unakumbuka mwezi wa nne tulikuwa wote na Katibu Mkuu, naomba msaidie kuwepo na wafanyakazi wa kuongezeka pale ili ile milolongo ya watanzania waliokuwa tayari kulipa kodi basi ipungue. Ninaomba suala la maji, unakumbuka siku ile tuliongelea.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Upinzani kidogo mimi nawashangaa. Ukurasa wa 14 wa hotuba yao ukiona, hawa watu wanasema nchi hii imekuwa shamba la bibi, ukurasa wa 14 ile aya ya kwanza. Lakini baada ya kurasa 13 baadae wanajisahau wanaanza kusema, ukurasa wa 27, Kampuni ya ACACIA iliyomiliki mgodi wa North Mara kunadhibitisha malalamiko ya muda mrefu ya wananchi na kwamba wamepigwa faini kubwa sana Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Mazingira. Sasa watu hawa huku mnasema Serikali haya madini yameachwa kama shamba la bibi lakini huku mnaona Serikali inafanya kitu gani, ninyi tuwaamini kwa kitu gani? Niwaambie kwa awamu hii ya Tano, mara ya kwanza Mheshimiwa Rais; na wewe unajua mmesimamia haya madini umeunda Kamati mbili ya Tanzanite na Diamond unakumbuka umesimamia kwa hiyo awamu hii kipekee kwa kweli ni awamu ya kipekee mmeamua kulinda rasilimali za nchi yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, kuna Kamati iliyochunguza mambo ya Tanzanite, kuna madeni ya ajabu ambayo yamelimbikiziwa watu wangu ma-Broker halafu wachimbaji wakubwa na wale ambao wanafanya masuala ya Tanzanite. Kamati hii imeamua kuchukua almost miaka kumi iliyopita kuwalipisha watu wangu madeni ambayo hayapo kabisa. Watu hawa wamekuwa ni maskini wengine hawana hata chochote. Mbali na uchunguzi uliofanyika kwenye Gold, mbali na uchunguzi uliofanyika kwenye masuala ya Diamond wameshikwa watu wa Tanzanite peke yake nchi ndiyo wanaosumbuliwa na Kamati fulani ambayo naomba nisiitaje na Mheshimiwa Waziri unajua na malalamiko yangu kama Mbunge nimeshakuambia niombeni mshughulikie kwa sababu uonevu huu haukubaliki hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja, ahsante sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, vitendea kazi vya Polisi. Jimbo la Simanjiro lina ukubwa wa square kilometer 21,000 takriban gari moja kwa wilaya kubwa kama hii, ni mateso na ni ngumu sana. Naomba jimbo hili liangaliwe kwa karibu. Kwa ukubwa huo Wilaya ya Simanjiro ni vyema pia mafuta ya mwezi wakaongezewa kutokana na ukubwa wa eneo husika.

Mheshimiwa Spika, kesi zisizo na tija; Polisi Kituo cha Msitu na Tembo eneo ambalo lina rasilimali ya asili (Mto wa Nyumba ya Mungu) Mkuu wa kituo kile amekuwa na tabia ya kubambikiza wananchi kesi kwa sababu zisizo za msingi.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano mmoja wa mtu mmoja tajiri anayedhulumu wananchi wa Loliondo ardhi yao lakini Mkuu wa Kituo hiki ili kutuliza madai ya wananchi kutetea ardhi yao, ameamua kimkakati kushirikiana na tajiri huyo anayedhulumu wananchi eneo lao, kuwafungulia kesi nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kupongeza Jeshi la Polisi kwa ujumla wake kwa kazi nzuri inayofanywa na kikosi chini ya IGP Sirro. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri. Tunayo amani ya kutosha na eneo la Mererani ambalo hapo awali lilikuwa na matukio mabaya, kwa sasa lina amani ya kutosha. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, maaskari wasio waadilifu; ni vyema Wizara hii ilinde taswira ya Jeshi la Polisi kwa kuwaadhibu maaskari ambao sio waaminifu ili kulinda heshima ya Jeshi la Polisi. Polisi ni taswira ya nchi yetu. Naomba wahudumiwe kwa uhakika na mahitaji yao yaangaliwe na Wizara.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii ya muhimu. Nawatakia kheri kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, ilikuwa nisisimame kabisa, lakini kwa namna ambavyo tumetendewa wachimbaji wadogo nchi hii na Mheshimiwa Rais imebidi nisimame kushukuru. Maana ni siku 17 tu tangu kikao hicho kiishe, leo sheria inakuja Bungeni kuwasaidia wachimbaji wadogo nchi nzima. Hii ina maana gani? Kwamba Mheshimiwa Rais ni msikivu sana, anajali watu na anawapenda sana wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umewataja wageni wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Wadogo ndugu Bina na wengine wa Simanjiro waliotoka hapa kwa kweli huu ni ushuhuda wa kipekee kwamba baada ya kulia kwa muda mrefu leo hii withholding tax ile ya asilimia 5 na VAT. Tena leo tumeletewa schedule of amendment asubuhi na Serikali baada ya kusikiliza jana kutwa nzima na Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na mamlaka zinazohusika, wamekuja na schedule of amendment ya kuondoa kabisa kusema wachimbaji wadogo wapo exempted kwa VAT. Kwa hili tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina dogo tu. Wakati msomaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani anasoma ule ukurasa wa pili anasema tunaleta marekebisho haya sasa hivi wakati tayari tumeshapitisha Bajeti ya 2018/2019. Hivi kweli kama wewe ni kiongozi wa nchi unataka watu wako waendelee kuumia usifanye marekebisho ya sheria ili usubiri mpaka bajeti ifike? Siyo sahihi. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Spika, siipokei hata kidogo kwa sababu in the first premise ile ya ku-question tu kwa nini leo yaletwe haya mabadiliko kwa sababu ina implication ya bajeti maana yake nia yao si njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye marekebisho ya Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Utunzaji wa Kodi, Sura ya 289. Kwenye Schedule of Amendment ya Serikali ile clause 9(a)(ii), naomba Serikali iongeze clause (iii) ya kusema kwamba badala ya kutoza nyumba zote, hata za residential, wa-qualify pale kwamba isiwe ya biashara tu bali na residential, wafikirie hiyo ili kuweka usawa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru sana Kamati ya Madini. Kwa muda mrefu na Mheshimiwa Waziri amekataza madini ya vito yasitoke nje bila kukatwa. Hatuna wataalam wa kutosha, tunaomba mtupe muda wa kutosha kusafirisha kwanza kwa sababu madini ya ruby na tanzanite hatuna uwezo wa kukata hapa nchini, mturuhusu kwa sasa tuyasafirishe nje. Chukueni kodi yenu nyingine yoyote lakini mturuhusu tusafirishe rough kwa muda huu mpaka ambapo Serikali na nchi itakuwa tayari kwa ajili ya kukata.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alisema kwamba kwenye regulations ambazo watatunga wadau wote wa madini watawahusishwa ili aweze kuruhusu kipengele hiki. Nimpongeze sana kuanzia jana ameanza kutoa leseni za kusafirisha madini yetu nje ya nchi, hongera sana Mheshimiwa Waziri. Naomba iwe kwenye hivyo madini ya vito, tanzanite na mengine yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)