Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zaynab Matitu Vulu (36 total)

MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nami naomba niulize maswali mawili ambayo yanafanana na barabara ya Arusha - Simanjiro. Kwa kuwa barabara ya kutoka Mkuranga hadi Kisiju ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na Awamu ya Tano, kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na kwa kuwa hadi leo hii wananchi wa Wilaya ya Mkuranga na Wilaya ya Mafia wanaitegemea sana barabara hiyo: Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa katika Kisiwa cha Mafia wananchi wake wanapata shida sana ya usafiri wa kutoka Mafia hadi kwenda nchi kavu ambayo ama ni Bandari ya Kisiju ama Bandari ya Nyamisati, lakini pia bado wana matatizo ya barabara za lami katika kisiwa hicho. Je, Serikali haioni sasa ni vyena ikatimiza ahadi yake ambayo ilitolewa na Rais ya kujenga barabara kuanzia Kilindoni hadi Rasinkumbi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ya Mkuranga hadi Kisiju ilitolewa ahadi na Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa kuanzia Rais wa Awamu ya Nne na sasa Rais wa Awamu ya Tano. Naomba nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Vulu, kama ambavyo tumekuwa tukiongelea hili suala mbele ya Waziri wangu, nami nampongeza sana kwa juhudi hizo za kufuatilia hizi barabara pamoja na mwenzake kwamba barabara hii kama ambavyo tumemwahidi tutaijenga kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa na Viongozi wetu Wakuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la lini tutaanza, naomba Mheshimiwa Zaynab Vulu utupe muda, maana yake tuna miaka mitano, ndiyo tumeanza tu, nikuhakikishie katika kipindi hicho ambacho kazi yetu kubwa itakuwa ni kuwajengea miundombinu Watanzania, tutahakikisha tunakupa jibu kamili la lini tutaanza kwa vitendo kwa maana ya kupitia bajeti zinazokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili la kuhusiana na barabara inayoanzia Kilindoni ambayo ni sehemu muhimu sana ya kuunganisha mawasiliano kati ya wenzetu wa Mafia pamoja na Kisiju, naomba nayo nikuhakikishie kwamba tutaijenga kwa kiwango cha lami kama ambavyo imeahidiwa na unafahamu kwamba barabara hii kwa pale Mafia tumeashaanza sehemu kuijenga, tutahakikisha tunaikamilisha kujenga na hatimaye wananchi waweze kunufaika na matunda mazuri ya Serikali ya Awamu ya Tano aliyoiweka madarakani ikiongozwa na Jemedari, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye nia ya dhati ya kuwasaidia watu wenye kipato cha chini ili waweze kuinuka na kupata maisha mazuri.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ni kutaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia akina mama walioanzisha VICOBA kwa kuongezewa mtaji wao? Pia Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha taasisi binafsi zinazotoa mikopo kuacha kunyanyasa akina mama wanapochelewa kulipa mikopo yao kwa kuwanyang‟anya vifaa vyao vya matumizi na vinavyowaendeshea maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itashawishi mabenki kutupelekea benki kwenye Wilaya ya Mafia na Jimbo la Utete? Kwa sababu Makao Makuu ya Wilaya ya Rufiji ni Utete lakini mpaka leo hapo Utete hakuna huduma inabidi waende Kibiti kufuata huduma. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili japo yameonekana kama manne ya Mheshimiwa Zaynabu Vulu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni akina mama kuongezwa mtaji kwa kuwa wameanzisha VICOBA. Kwanza kabisa naomba niwapongeze akina mama wote nchini kwa kuonesha ujasiri wao katika kuungana katika vikundi na kuanzisha VICOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba Serikali imeweka mazingira mazuri na tayari taasisi za kifedha au benki za jamii zinaanzishwa hivyo nawashauri akina mama hawa na mimi nitashirikiana nao kama mama kuhakikisha kwamba tunaanzisha taasisi au benki yetu ya kijamii ya wanawake sehemu yoyote ile. Naomba nitoe nafasi hiyo, tushirikiane kwa pamoja Wabunge wanawake ili tuweze kuungana na akina mama hawa kuanzisha benki ya wanawake ya kijamii sehemu yoyote ile ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ya swali hili la kwanza ilikuwa ni taasisi za kifedha zinazokopesha ziache kuwanyanyasa akina mama. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba kama nilivyojibu wiki moja iliyopita Serikali inaanzisha rasimu ya sera kwa ajili ya taasisi hizi ndogo za fedha ili sasa kuweza kuzikagua na kuziwekea sheria na taratibu ya kuweza kufanya kazi na kuacha kuwanyanyasa akina mama. Sera hii itakapokuwa tayari, nina uhakika kabisa taasisi hizi zitaacha kuwanyanyasa akina mama. Pia naomba niwashajihishe taasisi zote hizi zinazotoa mikopo kwa akina mama ziache utaratibu huu wa kuwanyanyasa akina mama. Tufuate taratibu zote za utoaji wa mikopo kama vile kuangalia uwezo wa mlipaji anayekopa kabla hujamkopesha kuliko kumkopesha tu kwa kuonekana wako kwenye kikundi halafu baadaye unakuja kuwanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nilisema ameuliza maswali mawili lakini yanaonekana kama manne, kwa hiyo, kulikuwa na sub-questions. Napenda kulijibu swali hili, kwamba ni lini Serikali itaweza kuzishawishi benki kupeleka matawi yao Mafia na Rufiji?
Namuomba Mheshimiwa Zaynabu Vulu tushirikiane tuone ni jinsi gani ya kuongea na benki zetu na hasa benki yetu ya NMB na CRDB, nina uhakika wakienda ku-access mazingira ya Mafia wataenda kufungua tawi lao sehemu hii. Naomba tukae na Mheshimiwa Zaynabu Vulu tuone ni jinsi gani ya kushughulikia suala hili.
MHE. ZAINAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza:-
La kwanza, kufuatana na maelezo ya Wizara husika kwamba mashamba yasipimwe viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Je, hawaoni kwamba wananchi watanyimwa haki zao kwa sababu mtu anapokuwa na mashamba yake ana ndugu zake, ana watoto wake, ana wake zake atataka awagawie maeneo ya kuweza kujiendeleza na kukwepa ujengaji holela katika miji yetu, Serikali haioni kwamba itamnyima haki huyo mhusika wa hilo shamba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na tatizo la mgogoro wa mipaka kati ya Ikwiriri na Nyamwage kwa maana ya Kata ya Mbwara na ni wa muda mrefu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuutatua mgogoro huo na kuwawezesha wananchi wa Wilaya ya Rufiji kuweza kuwa na mji mdogo katika Jimbo la Rufiji? Naomba majibu na tuambiwe lini wananchi hao watatatuliwa mgogoro huo na kupewa majibu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge kulingana na swali alilouliza kwamba mashamba yasipimwe, kutopimwa mashamba hayo kufanywa viwanja kutanyima haki ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuelewe kwamba tamko la Wizara lililotolewa ni kwa ajili ya faida na manufaa ya halmashauri zetu wenyewe kwa sababu watu wamekuwa wakitumia njia hiyo kujinufaisha katika kupima, kununua mashamba baadaye wanapima viwanja na wanaviuza katika bei kubwa sana, square meter moja inauzwa 20,000 na kuendelea na ni baadhi ya Wabunge pia wamelalamika katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa na wakati mwingine pia unaporuhusu hiyo, watu wanaanza kuanzisha miji ambayo haiko katika utaratibu wa mipango miji kulingana na mipango kabambe ambayo imewekwa katika maeneo hayo. Kwa hiyo, hatuwezi kuruhusu hilo liendelee, kama kazi hiyo itakuwa iko ndani ya mpango wa Halmashauri inaweza ikafanyika hivyo ,lakini suala kubwa hapa ni kwamba, halmashauri zetu zinaibiwa au Serikali inaibiwa na haipati pesa. Hakuna tatizo lolote la yeye kupeleka mpango wake halmashauri na halmashauri ikafanya kazi hiyo ya ugawaji viwanja na mapato ya Serikali yakaingia kuliko yeye kudanganya kwamba anataka shamba baadaye anapima na kupunja wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu mgogoro wa Kijiji cha Ikwiriri na Nyamwage, samahani Mheshimiwa kama nitakuwa nimetaja vibaya. Nyamage?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Nyamwage! Naomba niseme migogoro hii iko mingi kama ambavyo tumeelekeza sasa inakuwa ngumu sana kwenda leo, kwenda Ikwiriri, kesho unarudi unaitwa tena kulekule katika eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunafanya uratibishi kama Wizara kuweza kujua migogoro yote hii ili timu inapokwenda kufanya utatuzi wa mgogoro huu wa Ikwiriri ikatatue na migogoro mingine katika maeneo hayo badala ya kwenda mgogoro mmoja baada ya mwingine ambayo inagharimu Serikali pesa nyingi ya mtu kwenda na kurudi kwa hiyo tutafanya utatuzi huu katika migogoro yote kama jinsi ambavyo tutakuwa tumeikusanya ambavyo tumeleta kitabu na bado mnaendelea ku-update taarifa zilizoko humu.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kauli yake ya kuruhusu wafanyabiashara ndogo ndogo wafanye biashara bila kubughudhiwa. Sasa naomba nijikite katika maswali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kutokana na majibu ya swali la msingi; naomba Serikali iniambie mama lishe na wafanyabiashara ndogo ndogo wangapi ambao walikamatwa na bidhaa zao zikaharibiwa au kuchukuliwa ambao tayari wamepewa fidia?
Mheshimiwa Spika, pia niambiwe askari mgambo wangapi, kutokana na sheria ambayo ametueleza Mheshimiwa Naibu Waziri, wameshakamatwa, wamehukumiwa au bado wako wanaendelea na kifungo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwanza Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo ambayo haya ni lazima yazingatiwe na kila mmoja wetu katika maeneo yetu. Lakini pia kwa mujibu wa sheria hii ni kweli wafanyabisahara ambao wengine kwa kweli ni jambo baya, utakuta mtu amechukua mkopo, ameenda kufanya biashara yake, lakini kwa makusudi mtu mwingine, hata hawa mgambo wanalichukua hizi bidhaa nyingine, waliamua kuchukua na wakazitumia kwa maslahi yao binafsi hata bila kuzi-report katika Halmashauri zetu, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi siwezi kutoa takwimu ni wangapi waliokamatwa, lakini katika maeneo hayo na maeneo mbalimbali, maana yake nchi nzima hii, tukizungumzia Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, hili limejitokeza katika maeneo mbalimbali na hata hivyo maeneo mengine hatua zimeshachuliwa. Kwa mfano ukienda katika Jiji la Arusha kwa rafiki yangu Mheshimiwa Lema, kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao bidhaa zao zilichukuliwa na baadhi ya mgambo waliohusika kwenye hilo wameshapelekwa kwenye vyombo vya sheria. Mheshimiwa Spika, na juzi juzi kule Mwanza ambako tukio kama hilo limetokea, na ninashukuru sana dada yangu Angelina Mabula naye alikuwepo kule site, kuna kazi kubwa ambayo imefanyika. Wale wote ambao wameonekana kwamba wamedhulumu mali za watu, kukatakata mapanga mapapai pamoja na matikiti hivi sasa wanachukuliwa hatua zile za kisheria.
Mheshimiwa Spika, na ni kwamba katika eneo la pili ni askari mgambo wangapi ambao hivi sasa wamefikishwa; niseme hili ni suala la kitakwimu. Jukumu letu kubwa ni kusimamia sheria. Wale ambao watakiuka sheria ambazo zimewekwa ni lazima tuwachukulie hatua za kisheria. Lengo kubwa ni kwamba mwananchi wetu aweze kushiriki katika yale mazingira halali yaliyotengwa na Serikali. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipati nafasi hii. Nami naomba niulize swali linalofanana na swali na msingi. Kwa jina naitwa Zaynabu Matitu Vulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi niulize swali linalofanana na swali la msingi. Kwa kuwa Mafia ina uwanja wa ndege; na kwa kuwa Mafia ni eneo ambalo linapokea watalii wengi sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka taa ili wasafiri hao waweze kutumia ndege wakati wowote na kuweza kuunganisha na ndege zao kwa ajili ya safari zao za Kimataifa?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, uwekaji wa taa katika kiwanja cha ndege cha Mafia utafanyika pale mahitaji yatakapojitokeza. Kwa sasa hatuna ndege zinazotua usiku. Needs hiyo itakapojitokeza, wataalam watafanya mpango huo na taa hizo zitawekwa.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa REA inapeleka umeme vijijini na wakandarasi ndiyo wanaosimamia uwekaji wa vifaa vya umeme kwenye vijiji, je, Serikali inaweza ikatuambia kuna tatizo gani katika Kijiji cha Zegero, Kata ya Kurui?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna transformer imekaa pale zaidi ya miezi sita na wakati napita kwenye ziara nimeikuta pale toka 7 Aprili, je, Serikali inasema nini? Wananchi wanaiona ile transformer pale wana mategemeo ya kupata umeme lakini mpaka leo hii hawajapata umeme. Mbali ya hayo, transformer ile inaharibika kwa kunyeshewa na mvua bila kupata usimamizi na watoto kuichezea. Naomba majibu
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa sipendi kukataa, kama kuna transformer imeharibika na iko pale muda mrefu, Mheshimiwa Vulu naomba sana tukitoka hapa mimi na wewe tuongozane tukaone hiyo transformer na ikiwezekana ifanyiwe ukarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue fursa hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia sasa Serikali imekusudia ma-transformer yote yanayotengenezwa hapa nchini ndiyo yatakayokuwa yanatumika kwa ajili ya kuunganishia umeme wetu. TANESCO sasa haitaagiza transformer kutoka nje, itakuwa inanunua ma-transformer kutoka hapa nchini. Kampuni ya TANELEC sasa hivi ina uwezo wa kuzalisha transformer 883 kwa mwezi ambapo mahitaji ya TANESCO ni ma-transformer 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Vulu nikuombe sana, kama transformer bado ipo mimi na wewe tukitoka hapa tuongozane sambamba, tukae tujadiliane tufanye marekebisho ya transformer hiyo ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, kwa kuwa usalama barabara ni sio tu kuangalia magari bali pia na kuhakikisha wale wanaoangalia usalama wa barabarani wanakuwa katika mazingira mazuri.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea askari hawa wa barabarani vibanda ili wajihifadhi wakati wa mvua badala ya kuwa wanakaa chini ya miti na sio hivyo tu na watawasaidiaje hasa kina mama wale askari wanapohitaji kujisitiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake aliyokuwa nayo kwa askari wetu hawa wa usalama barabarani ambao wanafanya kazi zao katika mazingira magumu ambayo ameelezea. Lakini Jeshi la Polisi lina changamoto nyingi na changamoto za vituo vya kudumu na changamoto ya vituo vya dharura.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba kadri ya hali ya uwezo wa fedha ya Jeshi la Polisi utakavyokuwa unaruhusu tutaendelea kutafuta changamoto hizi moja baada ya moja kulingana na kipaumbale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo kuna hatua ambazo za dharura kwa mfano tuna utaratibu wa mobile police post ambazo tumekuwa tukizitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kupitia mradi wa BRN ambao tumechukua case study ya Mkoa wa Kinondoni mtaona kwamba tumeyazingatia hayo mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema uwezo utakaporuhusu ile case study ya kinondoni tutaitawanya au kuisambaza maeneo mengine ya nchi.
MHE. ZAINAB M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Pwani hususani Wilaya ya Rufiji naomba nirudi kwenye swali la msingi.
Sote tunafahamu Rufiji ina mto na ina bonde zuri sana la kilimo; tuna Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Rufiji kwa maana ya RUBADA. Je, Serikali itaweza kutuambia nini kazi za hiyo mamlaka? Kwa sababu bonde liko pale, maji yapo pale hakuna kinachoendelea katika uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali.
Je, kuna sababu ya hii mamlaka kuendelea kuwepo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba ipo haja ya mamlaka hiyo kuwepo. Kilimo cha umwagiliaji katika nchi hii kimeanza mwaka 1940 na kilianzia Rufiji, wakati huo ilikuwa hekta 160 ndio zilianza kutumika kule Rufiji. Baada ya hapo muda uliofuata tuliahamia Mbarali, hiyo ilikuwa ni mwaka 1960. Kutokana na mamlaka hiyo kuwepo uboreshaji kuhusu kilimo cha umwagiliaji umeendelea kutokana na hiyo mamlaka, hatimaye mpaka tumekuja kuwa na Tume ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeipitisha mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na data ambazo zilikuwa zinaandaliwa na hiyo mamlaka ndiyo imetufikisha hapa tulipo sasa hivi. Tayari Serikali imeshaainisha maeneo mengi kama nilivyojibu katika swali la msingi kuhakikisha kwamba sasa bonde hili la Mto Rufiji ambalo linatokana na Mto Ruaha na mito mingine ya Kilombero na kutokana na mamlaka hii imeainisha hayo maeneo na sasa hivi maeneo mengi yamesanifiwa sasa hivi tunachosubiri ni fedha kuanza utekelezaji. Kwa hiyo, mamlaka hii uwepo wake ni wa muhimu, data zote kuhusu kilimo cha umwagiliaji zina hii mamlaka.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza niseme nilitarajia angeniambia Mwongozo huo utaanza lini ukizingatia Wizara inaongozwa na Waziri mwanamke, Naibu Waziri mwanamke na Katibu Mkuu mwanamke. Je, Sheria ile ya SOSPA haoni kwamba inakinzana na sera ambayo wanaleta na vipi mtawasaidia hao watoto waweze kuendelea na utaratibu ambao mmeuweka? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mtoto wa kike na wanawake wote kibaiolojia kuna siku ambazo lazima tuzitumikie. Watoto wa shule wengi wanaacha kwenda shule kati ya siku sita mpaka saba, ukipiga kwa mwaka mmoja mtoto wa kike anapoteza zaidi ya siku 60 au 70. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuweza kupeleka mataulo ya kuweza kuwasaidia na kutenga chumba maalum kwa ajili ya wao kuweza kujihifadhi wakati wanapohitaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikiri kwamba ni heshima kubwa sana Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupewa sisi wanawake kuiongoza ambao tuko jirani sana na mahitaji au matatizo ya wanawake na ndiyo maana tunasema kwamba mwongozo tayari umeshaandaliwa. Kama mazungumzo yote tunayoendelea kuyafuatilia yatakuwa yamekamilika, tunatarajia tarehe Mosi, Machi, 2017 mwongozo huo uwe umekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanawake ni mtambuka. Tunapozungumzia kuwawezesha vijana katika demokrasia na katika kushiriki shughuli mbalimbali za kiuongozi, tunachozungumzia ni kwamba lazima watoto wa kike wasiachwe nyuma. Kutokuwa na sehemu za kujihifadhia wanapokuwa shuleni ni tatizo. Mwongozo ulishatolewa kwamba kila shule lazima itenge chumba maalum kwa ajili ya wanafunzi hao kujihifadhia wakati maalum lakini hali kadhalika tunasema kwamba hata hizi fedha za elimu bure zinazotolewa ni vema ikatengwa sehemu ndogo kwa ajili ya kuwasaidia hawa watoto wa kike pale inapotokea mambo yametokea kwa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema bila kuficha wapate pedi zao kwa sababu tumekuwa tukificha mambo haya ya wanawake, matokeo yake hata kwenye bajeti hayawekwi. Tuseme wazi kwamba mahitaji ya mwanamke ikiwemo pedi ziwekwe kwenye bajeti ili hawa watoto wa kike waweze kusaidiwa.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee jibu zuri la Naibu Waziri. Napenda nitoe taarifa kwa Bunge lako Tukufu kwamba imekuja teknolojia ambapo taulo nzuri za bei nafuu zitatengenezwa. Zaidi nitoe taarifa kwamba kuna Wabunge wawili wamejasiria, tunawaongoza kusudi watengeneze viwanda hivyo.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; sambamba na wenzangu ni lini Serikali itakwenda vijijini kukutana na akina mama ambao wanahodhi maeneo mengi na maeneo hayo wanaweza wakaanzisha viwanda vidogo vidogo lakini unakuta wanakwama kwa kuwa hawana hati za kimila au zile za kiserikali ambazo zinaweza zikawasaidia kuwapa mikopo na wao kuingia katika uchumi wa viwanda? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumalizia kazi la Mheshimiwa Mdee, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri kwamba ni kweli sheria hazibagui, lakini pia hata kama akipata mwanaume hati ya kimila au hati ya muda mrefu, wakati wowote ule mwanamke ajue ile hati ni salama. Hii ni kwa sababu kwa utaratibu wa sasa mwanaume akitaka kuuza au kubadilisha ile hati hatumkubalii mpaka tumuulize mkewe na vilevile mwanamke akitaka kuuza lazima tumuulize mumewe ili kuonyesha kwamba mali haipotei whether imeandikwa mwanaume au mwanamke wakati wa kupoteza lazima yoyote aulizwe. Kwa hiyo, mwanamke amelindwa sana katika sheria za sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Vulu nataka kukushauri tu kwamba hayo mashamba na maeneo ambayo wanawake wanamiliki au yapo kwenye mtaa au vijiji, washauri hao wanawake wajihusishe na mamlaka zinazohusika ndani ya Halmashauri ili wawapimie waweze kupata. Kama wapo mijini hawapati hati za kimila wanapata Title Deed za muda mrefu, lakini kama wapo vijijini wapete hati za kimila. Ardhi inapimwa na inamilikishwa na Halmashauri za Wilaya. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Swali langu ni kwamba, kwa kuwa Mkoa wa Pwani wanalima sana matunda ya aina mbalimbali na kwa kuwa kiwanda kipo eneo moja tu Mkuranga ambacho sasa hivi kinazalishana kiwanda kingine kinajengwa Chalinze. Je, ni lini Serikali itawashawishi wenye Kiwanda hicho kuhakikisha wanakuwa na maeneo maalum ya kuwasaidia wakulima kwenda kupeleka mazao yao na kuuza badala ya kutafuta magari na kupeleka mpaka kwenye kiwanda? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kiwanda cha Evelyne kinachokausha matunda asilia na Kiwanda cha Sayona kitakachochakata matunda ya aina zote, mara wanapoanza uzalishaji wataweka collection point. Evelyne wakati wowote atazinduliwa na kuanza kazi, mboga tunategemea aanze mwezi wa Tisa. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri inaelekea Serikali haijajipanga kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo. Kwa kuwa suala la ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mbezi Luis ni la miaka mingi na kwa kuwa msongamano uliokuwepo pale Ubungo umekithiri na haileti sura nzuri kwa sababu sasa hivi nchi yetu inatakiwa iwe na kituo chenye hadhi ya Kimataifa. Swali la kwanza, je, ni lini Serikali iko tayari kuanza kujenga kituo cha mabasi katika maeneo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyataja kwa maana ya mabasi ya Kusini, Kaskazini na yanayotoka Kanda ya Kati na nchi jirani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kituo cha mabasi ya Kusini kinatarajiwa kujengwa Kongowe na ukiangalia eneo la Kongowe halina nafasi ambayo watajenga kituo bila kutumia pesa nyingi za Serikali.
Je, atakubaliana na mimi kwamba majibu haya hayako sahihi kwa sababu vikao vimeshaanza kufanywa kati ya Wizara ya Maliasili na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga? Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuanza kufanya upembuzi yakinifu katika hilo eneo la Vikindu au Mwanambaya huko Mkuranga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imejipanga sana na ndiyo maana nilisema pale awali mipango yoyote lazima ipangwe katika utaratibu sahihi. Wiki iliyopita nilijibu swali la Mheshimiwa Mnyika linalofanana na swali hili. Kinachotokea ni nini? Serikali kupitia Jiji la Dar es Salaam imeweza kupata eneo la Mbezi Luis. Bahati nzuri Kamati yenye kuhusika ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iliamua kwenda kujihakikishia na imejiridhisha kuwa ni eneo muafaka. Bahati nzuri sasa LAPF wameshakubali uwekezaji wa kituo hicho cha kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo kuna mambo ya msingi lazima yafanyike. Wiki iliyopita Jiji pamoja na LAPF na wadau wengine walikaa kikao kujadili ujenzi wa kituo hicho ambao utagharimu takribani shilingi bilioni 28. Walikuwa wanajadili katika hicho kituo cha Mbezi Luis daraja litapita juu au chini kwenda katika kile kituo cha mabasi cha kawaida cha daladala. Hiyo haitoshi, tarehe 19 Mei, Kamati hii itakutana tena kufanya mjadala mpana kuona ni jinsi gani kituo hiki kinaenda kujengwa. Kwa hiyo, ndiyo maana nimesema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imejipanga sana na tutahakikisha tunajenga vituo katika Jiji la Dar es Salaam ili kusaidia wananchi waweze kupata usafiri mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kituo cha watu kutoka Kusini ni kweli, Jiji la Dar es Salaam sasa hivi linafanya tafakari kwa sababu yeye anaangalia mipaka yake. Walivyoangalia eneo lililokuwepo la Kongowe waliona kwamba ni lazima kulipa fidia. Kwa hiyo, kwa mkakati unavyokwenda, kwa mfano Kongowe mbele pale Vikindu kuna eneo kubwa, Serikali itaangalia jinsi gani stand ile itaweza kujengwa pale kwa watu wa Kanda ya Kusini na itahakikisha mipango hii yote inafanyika vizuri. Hata hivyo, agenda hii itaenda awamu kwa awamu lakini lazima tumalize kujenga vituo vyote.
Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaweza kujenga vituo imara kabisa kama tulivyojenga pale Msamvu, Mpanda na maeneo mengine. Lengo kubwa ni wananchi waweze kusafiri vizuri katika nchi yao.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Makambako - Songea halina tofauti na tatizo la barabara ya Kimanzichana – Mkamba, Mkamba – Mkuruwili, Mkuruwili – Msanga hiyo ni kwa Wilaya ya Mkuranga na tatizo la Mpuyani - Mwanarumango, Mwanarumango – Msanga -Vikumbulu na hiyo inatokana na tatizo kubwa la mvua iliyonyesha na kupelekea barabara kukatika hadi kufanya wafanyabiashara ya kusafirisha abiria na magari ya mizigo yanayobeba malighafi kupeleka viwandani kushindwa kufanya safari zake.
Je, Serikali kwa kuwa haina pesa na lengo lake ni kuweka lami kwa barabara hizo, ni lini Serikali itakuwa tayari kuweka changarawe na kukarabati yale maeneo korofi ili kuweza kusaidia jamii ya maeneo hayo waweze kupita kwa usalama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli lazima nitambue juhudi za Mheshimiwa Zaynabu Vulu katika kufuatilia barabara hizi na hasa hiyo barabara aliyoitaja ambayo inaharibiwa na magari makubwa yanayobeba malighafi zinazokwenda viwandani. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Vulu, kama ambavyo tumekuwa tukimhakikishia mimi na Waziri wangu wakati anafuatilia masuala hayo Ofisini kwetu mbele ya wataalam vilevile, aendelee kufanya kwa namna anavyofanya ili hatimaye yeye na sisi tufike hapo tunapotaka kufika. Tunajua katika barabara hii moja aliyoitaja ni ile barabara niliyosema ni kipaumbele namba mbili cha kuhamasisha viwanda au cha kuwezesha viwanda. Nikumhakikishie tuna nia thabiti na wakati wowote tutakapopata fedha tutahakikisha barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyosema kwa sasa tumeshatoa maelekezo kwa Mameneja wote wa Mikoa wa TANROADS, barabara zote zilizokatika zirudishiwe kwa kutumia fedha za emergence. Washirikiane TANROADS pamoja na Mfuko wa Barabara kuhakikisha wanarudisha mawasiliono katika maeneo yote ambayo mawasiliano yamekatika. Maelezo hayo tumeyatoa na nina hakika Meneja wetu wa Mkoa wa Pwani atahakikisha maeneo hayo anayoyataja Mheshimiwa Mbunge ambayo barabara zimekatika mawasiliano yanarudi. (Makofi)
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, bado inaonekana kuna tatizo la uhaba wa Walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inatoa Walimu wa kutosha ili waweze kufika kwenye Halmashauri zetu. Pia kuwa uwezo wa kupata Walimu wengi kwa sasa hivi haupo, je, hakuna haja ya kwamba wachukue Maafisa Afya kwenye Kata zetu waweze kusaidia watu ambao wana watoto wenye matatizo ya akili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, tatizo la ugonjwa wa akili au usonji linaongezeka nchini. Je, chanzo cha tatizo hilo ni nini, ni lishe duni, uhaba wa madini wakati mama anapokuwa mjamzito au ni nini kinachopelekea mpaka kuwa na idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa wa akili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba kwa kiasi fulani kuna changamoto ya kuwa na Walimu wa kutosha kwa ajili ya kuwafundisha watoto wenye matatizo ya akili na usonji. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto hiyo Wizara imejipanga kuhakikisha kwamba katika siku za huko mbele tatizo hilo linaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo imeanza kwa kujenga chuo cha kisasa cha kufundishia Walimu cha Patandi. Tunajenga The State of Art College kwa ajili ya kufundisha Walimu watakaotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba siyo kwamba Serikali haijajipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wazo lake alilopendekeza kwamba tuwatumie Maafisa Maendeleo ya Jamii tutalifikiria kuangalia namna tutakavyoweza kufanya kazi pamoja na kwamba tunafahamu kwamba unahitaji watu maalum ambao wanajua saikolojia na namna nzuri ya kuwafundisha watoto hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na chanzo, kuna vyanzo mbalimbali vinavyosababisha watoto wazaliwe wakiwa na hayo matatizo. Mojawapo ni suala la alcoholic disorders hasa kwa akinamama wajawazito. Ni muhimu sana kujua kwamba tayari kuna tafiti zinaonesha kwamba kama mzazi akiwa mjamzito atakuwa mlevi sana inasababisha mara nyingi mtoto kuzaliwa akiwa na haya matatizo. Sababu ya pili ni kwamba magonjwa mengine ni ya kurithi, kwamba watoto wanazaliwa kwa sababu wamerithi kutoka kwa wazazi na kuna sababu nyingine, kwa vyovyote vile nina uhakika wenzetu wa afya wanaweza wakawa na taarifa sahihi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kama wameongezeka au hawajaongezeka, kama Wizara ya Elimu tunachofahamu na tunachofanya ni kwamba, tunajua tumeendelea kuongeza uwezo wetu wa kuwapokea wengi zaidi. Ndiyo maana kama ninavyosema, tumeendelea kutenga fedha kila mwaka; mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 3.5 kuhakikisha kwamba wanafunzi wale katika shule za msingi na sekondari wanapata vifaa vya kuwafundishia. Vilevile hata katika ujenzi wa majengo wa sasa ukienda kwenye shule za msingi yanajengwa ili yaweze kukidhi mazingira maalum ya wanafunzi wa aina hii. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, nataka kuongeza maelezo mafupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa hivi ina mkakati, imeonekana kwamba siku 1,000 za mwanzo za mtoto baada ya kuzaliwa iwapo atapata tatizo la utapiamlo zinamuathiri sana katika kukua vilevile kiakili. Kwa hiyo, sasa hivi Serikali kupitia Taasisi yake ya Lishe, imeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba siku 1,000 za mwanzo mtoto anapata lishe nzuri ili kuhakikisha kuwa anakua vizuri na anapata uwezo mzuri wa kuweza kuwa na akili sawasawa.
MHE. ZAINAB M. VULLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya wavuvi wa Uvinza haina tofauti sana na hali ya wavuvi wa Ukanda wa Pwani ya Mkoa wa Pwani. Naomba nizungumzie hasa Kisiwa cha Mafia ambapo wanawake wengi wanajitahidi kulima kilimo cha mwani si kwa wao tu kwa mtazamo wa nje kwamba kinawapatia mapato lakini pia kilimo cha mwani kinasaidia kukuza samaki kuzaliana, kutunza mayai na hata kuhifadhi mazingira bora ya bahari. Kilimo hicho kinalimwa kwa shida sana,
Je, ni lini Serikali itahakikisha inawapatia nyenzo kama viatu, kamba na vifaa vingine vya kulimia mwani ili wananchi hao waweze kulima vizuri? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vizuri sana Zanzibar katika kilimo cha mwani hasa kwa kuwatumia wataalam wetu hawa wa COSTECH pamoja na IMS. Tutapeleka wataalam wetu hawa katika eneo hili analolizungumza Mheshimiwa Mbunge ili waweze kwenda kuwafundisha wakulima wetu wanaolima zao la mwani ambalo tunalipendekeza sana sasa hivi kwa wakulima na kulipigania lifanyike kwa ajili ya kuongeza thamani za zao hilo na kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo eneo hilo ambalo wakulima wanalima kwa shida tunatahakikisha kwamba tunaelekeza nguvu huko kuhakikisha wafugaji wale tunawapa mafunzo, tunawaonesha soko na vilevile tunawaunganisha kimtaji ili kuhakikisha kwamba zao hilo wanalilima vizuri zaidi kwa sababu lina soko la uhakika duniani. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa swali la msingi limetaja Mto Rufiji ambao upo kwenye Mkoa wa Pwani ninaotoka, na kwa kuwa watu wa Mkoa wa Pwani wamezungukwa na mito mingi, na kaulimbiu ya Serikali ni kumtua ndoo mwanamke. Je, Serikali ina mpango gani kwa kuanzia na Mto Rufiji kuweza kusambaza mabomba ya maji kwa wananchi na kuwaondoa na adha ya kuliwa na mamba mara kwa mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kwamba tayari tunatenga fedha kila Halmashauri na zimeshaanza kutekeleza miradi ya maji, upo ushahidi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wengi wanaliwa na mamba kwa Mto Rufiji, wale wanaokaa pembezoni na Mto Rufiji, lakini kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba tunatafuta fedha ili tuweze kufanya utafiti tutengeneze mradi mkubwa wa maji tuyatoe maji kutoka Mto Rufiji tuwapelekee wananchi pembezoni mwa huo Mto Rufiji ili wasiwe na haja tena ya kushuka kwenda kule mtoni kuchukua maji.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi zake za kuhakikisha viwanda vinakuwa vingi nchini.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yake ya swali la msingi amegusia upatikanaji wa faida kwa kuhusisha kwa kuwa na miundombinu rahisi kwa kufikisha malighafi kwenye viwanda.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba hadi sasa baadhi ya maeneo miundombinu ya barabara si rafiki kwa magari yanayobeba bidhaa, hali kadhalika miundombinu hiyo haileti tija kwa wafanyabiashara wa viwanda na wanaokwenda viwandani kununua na kupelekea walaji kwa maana ya wananchi kuwauzia?
Je nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha miundombinu hiyo itaboreshwa na kuimarishwa ili kuwapa nafuu wale wanaozalisha na wanunuzi wa hizo bidhaa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua, viwanda vinapoanza kunakuwa na utaratibu wa kuangalia hali ya mazingira rafiki kwa wananchi. Viwanda vile vinapoongezwa kwa maana ya wanavyopanua au kuongeza idadi ya miundombinu ya uzalishaji mali.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuangalia usalama wa raia wanaozunguka kiwanda, hali kadhalika na wale wanaofanya kazi katika viwanda vile? Tumeshuhudia wengi wakiathirika, naomba majibu ya maswali hayo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba Mheshimiwa Mbunge yupo Tanzania. Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika suala la miundombinu yeye mwenyewe ni shahidi, kila kona zinajengwa barabara za lami ili kuunganisha Mikoa na Wilaya kwa barabara imara zinazopitika mwaka mzima.
Mheshimiwa Spika, kuhusu upande wa umeme, maana mali ikishazalishwa inahitaji kusafirishwa kwenda kwa wananchi inatumia barabara, lakini pia kuna miundombinu imara na Wizara ya Nishati na Madini inaendelea kuweka umeme wa msongo mkubwa ili viwanda visipate shida kwa ajili ya kupata power, pia pamoja na matumizi ya gesi. Kwa hiyo, suala la miundombinu, Mheshimiwa Mbunge linakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ni mwaka huu tu kupitia TAMISEMI tayari na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, tumeunda Rural Road Agency ili kuhakikisha sasa utekelezaji wa barabara zile ndogo (feeder roads) zinafika kila kona ili mali zinazozalishwa viwandani ziweze kwenda kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la usalama viwandani; kuna usalama kupitia kwenye mazingira, lakini kuna usalama wa watumishi wanaofanya kazi ndani ya viwanda. Suala hili linashughulikiwa vizuri sana na idara husika ya mazingira kuhakikisha kwamba matatizo yanayojitokeza ndani ya viwanda hayaathiri wananchi wanaoishi katika mazingira ya pembezoni mwa kiwanda kama tulivyojibu katika swali la msingi, lakini pia yapo masuala ya usalama yanayokuwa-addressed ndani ya watumishi kwenye viwanda.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na Mheshimiwa Vulu kwa maswali yake mazuri sana ya mazingira hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, ameuliza swali linalohusu miundombinu. Actually, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyoeleza, kwamba tunafanya tathmini ya mazingira kabla kiwanda hakijaanza ili kuona kwamba kiwanda hicho mahali kinapowekwa kama hakitakuwa na madhara yoyote katika mazingira au kwa wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, sasa pale inapojitokeza kiwanda kinataka kupanua miundombinu yake katika eneo husika, tunafanya tena tathmini ya athari kwa mazingira ili kujiridhisha, je, upanuzi na miundombinu inayoongezwa haitakuwa na athari yoyote ile kwa mazingira? Kwa hiyo, Mheshimiwa Vulu wala asiwe na wasiwasi, kila kiwanda kinapopanua miundombinu huwa tunashiriki na kujiridhisha kwamba hakuna athari yoyote ile kwa mazingira.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na napongeza majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilitaka kujua, je, ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kuhakikisha inatoa pilipili nyingi ili kuweza kuchoma na kukimbiza tembo hao kwenye maeneo wanayoishi watu hasa ukizingatia kwamba kwanza kuchoma moto misitu ni kuharibu mazingira?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichosema ni kwamba katika maeneo yale yanayozunguka hifadhi zetu au yale ambayo yapo jirani na hifadhi zetu tunajaribu kuwahamasisha wananchi kwamba wapande pilipili na pia pale ambapo pana kinyesi cha tembo tunakichukua kile tunachoma. Nataka niseme kwamba tutaangalia namna na tutazungumza mikakati ambayo tumeiweka katika kuhakikisha kwamba pilipili zinatosha katika maeneo hayo hasa pale tutakapowasilisha bajeti yetu hapo tarehe 21 na 22 Mei.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kilimo cha mwani kimekuwa hatarishi kutokana na mazingira kinapolimwa na kinalimwa na wanawake wanaoishi katika visiwa na ukanda wa bahari. Kutokana na mazingira hayo hatarishi, je, Serikali ina mpango gani kupitia benki, mashirika au taasisi zinazoendesha masuala ya bima ili kuweza kwenda kuwafikia wanawake hao na kuwapa elimu ya kuweza kuwapatia fedha za kutosha ili waweze kujikwamua katika vifaa na halikadhalika kuweza kujikinga na athari zozote zinazotokana na kilimo hicho kwa kuwa kinakuwa baharini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kilimo cha mwani mavuno yake ni mengi sana kutokana na zao lenyewe linavyofyonza maji mengi, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili zao hilo liweze kuchakatwa na kuweza kusafirisha kwa wingi na kupata bei inayoweza kumkomboa mkulima wa mwani? Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya mama yangu, Mheshimiwa Zaynab Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoani kwetu Pwani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni uhatarishi wa kilimo chenyewe cha mwani ambacho kinalimwa kama ulivyosema Msheshimiwa Spika ni pamoja na Jimboni kwangu Mkuranga katika Kata ya Kisiju kwenye Kisiwa cha Koma.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati njema sana Shirika letu la Bima la Taifa (NIC) limekuja na mpango la kuhakikisha kwamba linaanzisha Bima ya Kilimo. Kwa hivyo, kwa kutumia dirisha hili la Bima ya Kilimo kutoka NIC na kwa kutumia mpango wetu wa ushirika kwa vikundi vya wakulima, naomba mimi na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum mama yangu Mheshimiwa Zaynab Matitu Vulu na Wabunge wengine wakulima wa mwani tuwahamasishe wakulima wetu wa mwani kule vijijini wajiunge katika ushirika na hatimaye tuwaunganishe na Shirika letu la Bima ili kuweza kupata nafuu hii endapo litatokea lolote la kutokea.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ameniuliza juu ya viwanda vidogovidogo. Ni kweli kwamba tunahitaji kutengeneza viwanda vidogovidogo. Changamoto kubwa inayoonekana hivi sasa pamoja naye kusema kwamba uzalishaji ni mkubwa lakini kwa soko la kimataifa bado tunayo changamoto kubwa ya uzalishaji mdogo lakini na ubora wenyewe wa lile zao letu. Ndiyo maana tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunazalisha zaidi na pili tunazalisha kilicho bora.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa viwanda vidogovidogo tumekuwa tukivisaidia sana pale Bagamoyo maeneo ya Mlingotini ni eneo mojawapo ambalo Wizara yangu inasaidia vidogovidogo. Kipo kiwanda kidogo ambacho kinafanya uchakataji na ku-pack mazao yanayotokana na zao hili la mwani. Sisi Serikalini tupo tayari kuhakikisha kwamba tunaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vidogovidogo na kuwapa support wakulima wetu.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara ya Nzasa – Kilungule – Kwa Mwanagati na Buza ni muhimu sana kwa wakazi wa Mbagala, kwa maana ya Jimbo la Temeke na vile vile kwa wakazi wa Jimbo la Ukonga. Je Serikali, ina mpango gani wa muda mfupi wa kuweza kuboresha barabara hiyo ili wakazi hao waweze kupita kwa ufasaha na wepesi kusafirisha mazao na huduma za kijamii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wilaya Kisarawe, imepakana na Mkoa wa Dar es Salam na Jimbo la Ukonga; na kwa kuwa barabara inayopita Msimbu inaanzia Chanika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha au kujenga lami ya muda mrefu barabara inayoanzia Chanika – Msimbu hadi Masaki ambapo itaungana na barabara ya Mwanaromango ili kusaidia ujenzi wa taifa na kuendana na speed ya Mheshimiwa Rais kwa sababu tuko kwenye awamu ya viwanda na biashara? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi utaona jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali kwa kupitia mradi wa DMDP kuhakikisha kwamba Dar es Salam inajengeka, kwa maana ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge kuna jumla ya shilingi bilioni 260 kati ya shilingi bilioni 660 imetengwa kwa ajili ya mradi huu. Naomba nimwondoe hofu, katika mipango ambayo inafanywa na taratibu karibu zote zimekamilika; tukishakamilisha ujenzi wa barabara hiyo ambayo na mimi nimeenda kuitembelea tutaenda mpaka Kisarawe.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Kwa kuwa, biashara mara nyingi ni muuzaji na mnunuaji; na kwa kuwa, biashara ya ukahaba mara nyingi inaita machangudoa; na kwa kuwa, katika bahari kuna changudoa, kuna changuchole, kuna changufatundu. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya hawa machangu wengine wakakamatwa na wakapewa elimu ya kutosha, waachane na vitendo vya ukahaba kwa sababu, wao kama hawakwenda sokoni, hii biashara haitakuwepo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha wasichana wote wanawawezesha kwa mikopo na elimu ya ujasiriamali, pamoja na juhudi alizozisema Mheshimiwa Naibu Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na juhudi za Serikali, Taasisi Zisizo za Kiserikali, na baadhi ya raia kumekuwa na mkusanyiko mkubwa wa biashara hii maeneo mbalimbali, ikiwemo eneo maarufu kwa Uwanja wa Fisi, Mburahati, Dar-es-Salaam na biashara hii inafanyika katikati ya maeneo wanayoishi wananchi. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kwenda katika maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuvunja hayo maeneo, kujenga miundombinu ambayo itawawezesha wasichana waliojiingiza katika biashara hizo kwa kutokutarajia kutokana na hali ngumu ya maisha na pia wataepukana na maradhi ya UKIMWI; Serikali ikiweza kujenga hiyo miundombinu na kuwapa mikopo hawa wasichana haioni kwamba, tutakuwa tumekwamua Taifa ambalo tunalitegemea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza swali lake na concern yake Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na janga hili. Naungana mkono na yeye kabisa kuhusiana na umuhimu wa kushughulika sio tu na wauzaji, lakini wanunuzi, lakini si tu na wanunuzi, mpaka na mazingira ambayo wale wanayaweka. Maana kuna wengine sio wanaouza, kwa mfano wenye madanguro, ni watu ambao sio wauzaji na sio wanunuzi, lakini wanahamasisha hivi vitendo. Kwa hiyo, yote hayo na wote ambao wanashiriki kwa namna moja ama nyingine katika hii biashara kuna haja ya kuhakikisha kwamba, tunachukua hatua na ndivyo ambavyo Serikali inafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo nadhani Bunge hili ni wakati muafaka wa kuzitafakari. Moja ni changamoto ya sheria; labda nitoe mfano wa sheria ambazo pengine zinakwaza mapambano dhidi ya vita ya makahaba. Ukiangalia kwenye Kanuni ya Adhabu Namba 176(a), Sura ya 16, adhabu ambayo inatakiwa itolewe kwa watu ambao wanafanya biashara ya madanguro wanasema ni fine isiyozidi 500/= ama iwapo ni kosa la mara ya pili na kuendelea atatozwa fine isiyozidi 1,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtaona kwamba, adhabu kama hii inaweza kuwa inahamasisha utendaji wa huu uhalifu. Kwa hiyo, kuna haja ya Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuangalia na kutafakari juu ya sheria hizi ambazo zimepitwa na wakati ili hatimaye kazi kubwa ambayo inafanywa ya kuwakamata hawa makahaba kila siku, pamoja na wahamasishi wanaoshiriki na wanunuzi iweze kuwa na tija kwani mara nyingi wanapokamatwa wanarudia tena makosa kwa sababu, ya wepesi wa sheria zilizopo. Kwa hiyo, kimsingi hilo ni jibu la swali lake la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na elimu; nimhakikishie kwamba, tunaendelea kutoa elimu, lakini vilevile na mamlaka nyingine kama ambavyo nimezungumza katika swali la msingi kwamba, kwa sababu, suala hili ni mtambuka tumekuwa tunashirikiana kama Serikali na mamlaka nyingine na taasisi mbalimbali, ili kuweza kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara haya, ikiwemo kuwashirikisha vilevile viongozi wa dini ambapo nilizungumza kwamba, viongozi wa dini ni sehemu muhimu sana katika kutoa elimu ya maadili juu ya wananchi.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa swali la msingi linafanana na hoja nitakayoitoa na kwa kuwa ujenzi wa barabara ni kiungo muhimu kwa ajili ya maendeleo na pia kuboresha hali halisi ya mwananchi; na kwa kuwa Serikali iliahidi kutoka kwenye Ilani yake ya 2005, 2010 na 2015 ujenzi wa barabara kutoka Makofia kwenda Mlandizi, kutoka Mlandizi kwenda Mzenga, kutoka Mzenga kwenda Vikumburu na Manerumango; na kwa kuwa hadi leo barabara hiyo haijajengwa kwa kiwango cha lami. Je, Serikali itaanza lini ujenzi angalau, narudia tena angalau kwa kiwango cha changarawe ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kupata usafiri mzuri na hali kadhalika ukizingatia Mkoa wa Pwani tunaongoza kwa viwanda vya uchumi? Naomba kauli ya Serikali tumesubiri mpaka leo haijajengwa, ni lini Serikali italisimamia jambo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba Mheshimiwa Zaynab Vullu ni Mbunge ambaye amekuwa akifuatilia sana barabara nyingi sana za Mkoa wa Pwani ambazo ziko kwenye ahadi ya Serikali ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Nampongeza sana kwa jitihada zake hizo, naamini kwamba Serikali tumeshasikia na nimhakikishie Mheshimiwa Vullu kwamba mpaka sasa hivi kuna pesa imekwishapitishwa kwenye bajeti hii ya Wizara yetu kutengeneza barabara husika kwa kiwango cha changarawe. Taratibu zinaendelea kufanyika ili pesa itakapopatikana wakati mwingine ujao tujenge kwa kiwango cha lami.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa zao la mchikichi linafanana na zao la nazi; na kwa kuwa watu wa Pwani wanategemea sana zao la nazi; kwa kipindi kirefu zao hilo limekumbwa na ugonjwa ambapo minazi inanyauka na Serikali iliahidi kufanya utafiti. Je, utafiti huo umefikia wapi na kuna mkakati gani wa kuhakikisha zao hilo litafufuliwa upya? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Naomba nimjibu Mheshimiwa Zaynab Vulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyauko ni ugonjwa ambao unakumba mazao mengi na mbinu iliyopo mpaka sasa ya kukabiliana na mnyauko ambayo inaeleweka ni kwa kufanya usafi (sterilization). Mbinu hii imekuwa ikiandamana na hasara na vimelea hawa kuendelea kubaki kwenye maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasayansi sasa hivi duniani wanaelekea kwenye mbinu nyingine bio-control ambapo enzymes zinazalishwa kwa ajili ya kimelea mahsusi kilichosababisha mnyauko kwenye zao au mmea fulani. Utafiti huu umeendelea kufanyika katika vituo vyetu vya utafiti na sasa hivi tuko katika hatua ya kujenga kiwanda cha kuzalisha hivi vimelea (enzymes) zitakazokabiliana na aina mbalimbali ya minyauko katika mimea yetu.
MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, bandari ya Nyamisati na bandari ya Kilindoni zimekidhi kigezo cha Serikali; na kwa kuwa wananchi wa kutoka Nyamisati kwenda Mafia au kutoka Mafia kwenye Nyamisati wanapata shida ya usafiri, uwezo wa majahazi yao hauzidi abiria 50 pamoja na mizigo yao. Je, ni lini Serikali itaondoa kadhia hiyo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo kwa kuwapelekea boti ambayo itakuwa salama na uhakika wa kusafirisha, ukizingatia kunakuwa na wazee, akinamama wajawazito, watoto, wanaokaa sana bandarini na kukosa usafiri wa uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi anavyofuatilia hasa Bandari ya Nyamisati mpaka nimeshaizowea kuisikia kutoka kwake na Mheshimiwa Dau na wadau wote ambao wako Mkoa wa Pwani bila kumsahau Makamu Mwenyekiti wa Kamati yangu Mheshimiwa Hawa Mchafu.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna vyombo vinafanya kazi maeneo yale, lakini niwapongeze sana Wabunge wa eneo lile kwa sababu vyombo karibu vyote vinavyofanya safari kati ya Mafia na Nyamisati vimesajiliwa na ndiyo maana hata ikitokea ajali, huwa kuna utaratibu maalum ambao tunaweza kupata taarifa rasmi za ajali hiyo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ina mpango wa kupeleka boti muda huu wakati tunaendelea na utengenezaji wa land craft kubwa tumewapatia TEMESA Sh.3,800,000,000 kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Spika, hivyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Pwani wasiwe na wasiwasi Serikali ina utaratibu wa kutengeneza kivuko kile pamoja na boat la kuwasafirisha abiria. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu umeme kupelekwa Mafia, naomba kujua nini harakati na mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme katika Visiwa vya Jibondo, Chole na Jiwani huko huko Mafia? Kwa sababu Jibondo, Chole na Jiwani vyote hivyo ni visiwa ndani ya Kisiwa kikuu cha Mafia. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa, kwa kuwa REA kupitia miradi ya kupeleka umeme vijijini upo mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya off-grid ikiwemo visiwa; visiwa alivyovitaja Jibondo, Jiwani na Chole vipo katika mkakati huo na kama miezi minne iliyopita REA ilifanya tathmini katika maeneo mbalimbali ya visiwa vikiwemo Visiwa vya Kibiti, Mkiongoroni, Mbuchi, Salale, Saninga, Koma na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimthibitishie mradi huo upo na bahati nzuri wafadhili ambao ni Serikali ya Norway pamoja na Sweden wapo ku-support maeneo yote ya visiwa ikiwemo hata Visiwa vya Ukerewe na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba mradi huo upo. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali sasa hivi ina ndege zaidi ya sita; na kwa kuwa ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria wengi; na kwa kuwa Mafia ni kisiwa ambacho kiko katika ramani ya Tanzania kutokana na shughuli zake za utalii, utalii wa samaki aina ya potwe ambapo kila mwaka watalii wengi wanakwenda, je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kuongeza ukubwa wa kiwanja na kuhakikisha Shirika la Ndege la Tanzania linapeleka ndege zake kwa ajili ya abiria wanaosafiri na wanaokwenda kuangalia utalii huko wanakokwenda?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa bado hakuna utaratibu wa Serikali kupeleka ndege kubwa; na kwa kuwa wananchi wa Mafia wana adha kubwa ya usafiri wa baharini na ndege. Je, huoni sasa kuna haja ya kuongeza speed ya kupata meli au boti ambayo itasaidia na kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mafia?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mafia ni eneo muhimu na kuna vivutio vingi sana vya utalii katika eneo hili, lakini nimuhakikishie tu Mheshimiwa Vulu, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba hatua madhubuti Serikali inazichukua ili kuhakikisha kwamba tunaboresha usafiri wa Mafia ikiwemo usafiri huu wa ndege na usafiri wa vyombo vya majini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Vullu usiwe na wasiwasi kwa sababu kama nilivyosema tunakwenda kuufanya uwanja huu uwe katika kiwango cha daraja C. Lakini kikubwa ambacho kama Serikali tutafanya kwa sababu tumeendelea kuongeza kununua ndege pia tutaongeza idadi ya miruko katika kisiwa hiki. Tukiongeza idadi ya miruko katika kisiwa hiki tutaweza sasa kuweka uwiano wa abiria na huduma ambayo inahitajika Mafia kwa hiyo sisi kama Serikali tuko makini kuhakikisha kwamba tutakwenda kuhuduamia kisiwa cha Mafia kulingana na mahitaji ya wakati ili tuweze kusaidia pia kuchangia uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuwa na usafiri wa majini kama Mheshimiwa Vullu alivyosema Serikali inayo Mpango wa kutengeneza boti maalum ambayo itakuwa inatoka Nyamisati kwenda Kilindoni Mafia. Kwa hiyo, utaratibu wa manunuzi Mheshimiwa Vulu zinaendelea , kwa hiyo baada ya muda ambao siyo mrefu wananchi wa Mafia wataweza kuunganika vizuri na upande huu wa bara. Kwa maana hiyo kwamba Mheshimiwa Vulu na wananchi wa Mafia wasiwe na wasiwasi tunatambua umuhimu wa kuhudumia kisiwa cha Mafia kwa umaridadi wa hali ya juu.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mheshimiwa Ally Seif Ungando na wananchi wa Kibiti, napenda kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa juhudi ilizofanya, lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili. Kwa kuwa umeme umeshafikia hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameielezea, ningependa kujua ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye maeneo ya Nyatanga, Kingwira, Zimbwini, Runyozi na Makaoni?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali iliahidi kaya 90 katika eneo la Kitembo na katika kaya hizo 90, kaya 40 bado hazijapata umeme, ningependa kujua Serikali imejipangaje katika hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Zainab Vullu, Mbunge mwenzangu wa Viti Maalum wa Mkoa wa Pwani.

Katika maswali yake mawili ya nyongeza, amepongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge Ally Seif Ungando na mimi nimepokea kwa niaba ya Wizara, kwa kazi ambayo inaendelea katika maeneo ya Wilaya ya Kibiti na katika maeneo mbalimbali, lakini ameulizia maeneo ya Nyatanga, Zimbwini, yatapata lini umeme. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge mama Vullu kwamba katika REA III mzunguko wa pili unaoendelea, maeneo haya yameingizwa katika orodha na kazi inatarajiwa kuanza 2019 mwezi wa Saba. Nalitarajia Bunge hili wakati wa kuwasilisha Bajeti yetu ituunge mkono ili kazi ya kumaliza vijiji ambavyo vimesalia katika mradi wa REA III mzunguko wa kwanza viweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameelezea eneo la Kitembo nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na kumshukuru kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo tunayatembelea kwenye ziara mimi pamoja na yeye Kitembo tumewasha umeme kama anavyosema, tumeshawaunganishia kaya 50, hizi kaya 40 kwa sababu mradi unakuwa na wigo wa wateja wa awali. Mradi unakuwa na kazi za awali, kaya zinazobaki TANESCO inaendelea na kazi yake ya kusambaza umeme. Kwa hiyo, naomba nielekeze TANESCO kuzingatia kwamba mradi unapokamilika na kukabidhiwa waendelee kuwasambazia umeme wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inaongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uamuzi wa kisera, kwamba kwa sasa umeme utakaosambazwa na TANESCO, REA na wadau wowote, bei ya kuunganisha ni shilingi 27,000/=. Kwa hiyo hakuna kikwazo kingine kwamba kutakuwa na bei nyingine pengine shilingi 177,000/=, bei ni moja shilingi 27,000/=; kwa hiyo TANESCO waendelee na kazi ya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ambao mradi wa REA umekamilika. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mkuranga na wanaotumia barabara hiyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi wanozunguka eneo hilo; na kwa kuwa kuna haja ya kuiboresha; na kwa kuwa Serikali imesema wanasubiri TARURA wafanye tathmini ndiyo barabara hiyo ijengwe, je, hawaoni kwamba wakati wakifanya tathmini barabara hiyo iweze kutengenezwa angalau kwa kiwango cha kokoto?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii inaungana na barabara ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam ambayo iko TANROADS. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya barabara hii kuipandisha hadhi na kuiweka TANROADS ili iweze kupata huduma ambazo zinalingana na kule inapoishia ambapo inahudumiwa na TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, jirani yangu Mheshimiwa Zaynabu Vulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kwamba barabara hii inaweza ikapata matengenezo wakati tunasubiri mpango wa fedha ujao. Naomba niwaelekeze TARURA wa Wilaya hii ya Mkuranga wafanye utaratibu wa kukarabati maeneo korofi. Bahati nzuri katika mwaka huu wa fedha wametenga fedha shilingi milioni 270 ili zipelekwe katika eneo hili lakini tunaomba wafanye kazi hiyo mapema ili iendelee kupitika wakati wote na wananchi wasiendelee kupata shida katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kupandishwa hadhi kwa barabara hii. Suala la kupandishwa hadhi lina taratibu zake na mwongozo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Halmashauri yake wawasiliane na TANROADS, watafanya tathmini kama ikikidhi vigezo basi itakuwa ni vizuri ikapandishwa hadhi ili kupata huduma kubwa kidogo kulingana na mgao wa fedha ambao unatolewa. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na ukizingatia leo ni siku ya kwanza kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nawatakia kheri wale wote ambao wamejaaliwa kufunga na wasiojaaliwa Mungu awape tahfifu waweze kufunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua, Serikali ina mpango gani au ina mkakati gani kwa wale watoto ambao wamehukumiwa na kupelekwa magerezani ikiwa ni gereza la pale Upanga au kwa jina lingine Kisutu? Nini wanapewa katika masuala ya kujiendeleza kielimu ya kawaida au elimu ya ufundi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipate majibu katika maswali haya.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria, watoto chini ya miaka 18 hawapaswi kufungwa magereza ya watu wazima. Kwa hiyo, kuna utaratibu wa Serikali kuwa na mahabusu za watoto, lakini vilevile kuna maeneo ambayo tunaita Gereza la Watoto, ambapo wale watoto wanatuhumiwa kwa mujibu wa sheria wamehukumiwa kifungo gerezani, basi wanapelekwa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuwarekebisha kitabia, siyo kuwaadhibu wale watoto, la hasha, Serikali ina lengo la kuhakikisha kwamba tunawarekebisha kitabia. Kwa hiyo, kule wanapata huduma zote za matunzo, lakini wanapata huduma za elimu na huduma za kuweza kuwasaidia kuwarekebisha kitabia ili hata baadaye wakitoka basi wawe ni sehemu ya raia wema katika jamii hii.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kwa kuwa swali la msingi linahusu muunganiko wa daraja na barabara; na kwa kuwa sote tumeshuhudia kwa macho au kupitia vyombo vya habari jinsi Mji wa Dar es Salaam ulivyoharibika kwa mafuriko; na kwa kuwa ujenzi wa madaraja na barabara umechangia kuhakikisha kwamba usafiri umekuwa siyo mzuri kwa watoto wetu, kwa watu wazima na kwa wagonjwa kutokana na mafuriko yaliyokuwepo: Je, Serikali itachukua hatua gani za dharura kuhakikisha mafuriko hayo hayataendelea tena na hayatatokea; na kuhakikisha Mji wa Dar es Salaam unarudi kama ulivyokuwa hapo awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi sote ni mashuhuda kwamba mvua ambazo zinanyesha Dar es Salaam sasa hivi ni nyingi sana ambazo hatukuzitarajia. Kwa hiyo, kwanza ni sisi wote kushiriki kuhakikisha kwamba tunapambana na tabianchi ambayo inaleta mwongezeko wa mvua ambazo hatuwezi kuzitarajia. Sasa tunafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kipekee nichukue fursa hii kupongeza UDART jinsi ambavyo wamekuwa wakipambana na hali hii pale ambapo maji yanakuwa yamezidi, tunalazimika kusimamisha usafiri ili kusije kukawa na madhara makubwa, lakini immediately zinafanyika juhudi za kuhakikisha maji yale yanaondolewa na usafiri unarejea kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, ni ukweli usiopongika, kwa mvua ambazo zinanyesha sasa hivi; na bahati nzuri watabiri wa hali ya hewa walitufahamisha kwamba mvua zinatarajiwa kunyesha nyingi sana, kwa hiyo, hakuna namna ambavyo tunaweza tukasema tutafanya kuzuia mvua kwa sababu ni calamity ambayo inaweza ikatokea muda wowote. Kwa hiyo, tuwe na subira, hali ya Dar es Salaam itarudia katika hali yake baada ya mvua hizi kukoma kama ambavyo wametuambia.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa ruhusa yako naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Jemedari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa juhudi zake na msimamo wake wa kuhakikisha Watanzania tunapata huduma za afya. Ukiangalia kwenye Mkoa wetu wa Pwani, Vituo vingi vya Afya, Zahanati na Hospitali za Mkoa zimepata vifaa tiba na wataalam mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza: Kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonyesha njia ya kutaka Watanzania wapate huduma bora na sahihi kwa wananchi wake: Je, hawaoni kwamba kwa kuwafanya Waganga Wafawidhi na wa Vituo vya Afya au Zahanati kusimamia masuala ya Uhasibu ni kuipelekea kada hiyo kuacha kazi zake za kutibu na kuhangaika maeneo mbalimbali kwenda kununua dawa, kwenda kufuata vifaa tiba na kuacha kutibu wagonjwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa Serikali imeonyesha nia ya kuomba kibali kwa ajili ya Wahasibu na mpaka leo hii hicho kibali hakijapatikana; kwa nini msichukue wataalam wa uhasibu ambao wamemaliza masomo yao, wako maeneo mbalimbali Tanzania na wakafanya kazi hizo kwa kujitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge ametoa. Naye amekuwa ni miongoni mwa champions ambao wamekuwa wakipigiania suala zima la afya, naye anastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika swali lake anaongelea suala zima la kwamba Waganga wanaacha kazi zao za kitaaluma na wanaanza kufanya kazi ya fedha; katika majibu yangu ya msingi nimemwambia kwamba tumeajiri watumishi wa Kada ya Uhasibu 335.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kwa muda mfupi ambao tumewapa hiyo taaluma ni ili wawe na uelewa wa jumla, lakini Uhasibu ni professional ambayo haiwezi ikasomewa ndani ya muda mfupi huo. Kwa hiyo, hawaachi kazi yao ambayo wameajiriwa nayo kuanza kufanya kazi ya usimamizi wa fedha, lakini ni vizuri at least wakajua nini ambacho kinaendelea kulikoni kutojua kabisa. Huo ndiyo msingi wa elimu ambayo imetolewa kwa hao Waganga.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anasema kwamba ni vizuri, pamoja na kwamba tumeomba kibali cha kuajiri, sasa kuna wengine ambao wamemaliza taaluma ya Uhasibu wako Mtaani tuwaajiri wajitolee. Sina uhakika sana na kwa sera yetu haijatokea mahali hata pamoja ambapo tunataka mtu afanye kazi asilipwe.

Mheshimiwa Spika, tuendelee kuwa na subira, Serikali ni sikivu na jana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya utawala alisema tunaenda kuajiri watumishi mbalimbali 45,000. Ni imani yangu kubwa katika hao watakaoajiriwa ni pamoja na Wahasibu wakaokwenda kufanya kazi hizo.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imebaini kwamba kuna tatizo la soko; na kwa kuwa Serikali imebaini kuna uhaba wa zao lenyewe na watumiaji. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuweka mkakati madhubuti wa kuwatafutia wakulima hawa soko la nje waweze kusafirisha nazi zao kwenda nje ya nchi kwani hapa Tanzania kwa mujibu wa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri inaonekana kwamba soko limepungua? Pia wangeweza kutoa elimu ya kutosha watu wakajua matumizi na thamani ya zao la nazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; bila shaka Naibu Waziri anajua thamani ya zao la nazi, zao la nazi lina thamani kubwa sana. Kwanza mti wenyewe unatumika kama mbao, unatumika kwa kutengenezea furniture, mti wenyewe unatoa nazi, nazi inatoa tui ambalo linapikiwa, nazi ina maji ambayo yanatumika kwa afya zetu; nazi machicha yake yanatumika kwa ajili ya kutengenezea kashata na vitu vingine, lakini pia mnazi huohuo unatoa makuti ambayo yana thamani katika utalii wetu wa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo mnazi huo huo unatoa kitu kinaitwa kitale, kitale kina thamani kubwa sana watu wa afya wanaweza wakajua na watu wa Pwani wanaweza wakaelewa thamani ya kitu kinachoitwa kitale. Sasa ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha zao hili la nazi halipotei nchini kwetu kwa kurudisha vituo vya utafiti vilivyokuwa Dar es Salaam, Mafia, Bagamoyo na Lindi ili wakulima wale wasiweze kupoteza thamani ya zao la nazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kutafuta soko la nazi nje ya nchi; ni kweli kwamba kama Serikali tuna mikakati mbalimbali lakini tufahamu kwamba matatizo makubwa ya soko la nazi sio bei, tatizo kubwa ni kipato kidogo wanachopata wakulima wa nazi na kipato hicho kinaweza kuongezeka kutokana na bei kubwa au tija kuongezeka au kuongeza uzalishaji, lakini pia kupunguza gharama za uzalishaji wakulima hao wa nazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali moja ambalo ndiyo tumeanzisha vituo vya utafiti hivi 16, kimojawapo ni Kituo chetu Cha Utafiti cha pale Mikocheni ambacho kimepewa mahususi kwa ajili ya utafiti wa zao la nazi. Lengo ni kuja kupunguza gharama za uzalishaji, lakini kupata mbegu bora zinazoweza kuhimili ukame na magonjwa kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua ni lini Serikali tutaanza kurudisha vile vituo vyetu vya utafiti kama zamani. Kama nilivyosema katika majibu yetu ya msingi, kwanza zamani hatukuwa na vituo vile vya utafiti zaidi ya hiki cha Mikocheni, tulikuwa na vituo vya kuzalisha miche ya minazi na baadaye kuisambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo utaratibu mpaka sasa hivi tunao, tunacho kule Zambezi Bagamoyo, tunacho pale Mkuranga na tutaendelea kufungua vituo hivyo Mafia na sehemu zingine kwa wakulima wakubwa wa nazi, lakini hasa baada ya kupata taarifa za utafiti kutoka kwenye kituo chetu hiki cha TARI pale Mikocheni ambacho tumewapa mahususi kwa ajili ya kufanya utafiti wa zao la nazi ili kuja sasa na mbegu ambayo inahimili ukame na magonjwa tuachane na mbegu yetu ile fupi tuliyoletewa kutoka nje ambapo kule ni nchi ambazo ni za baridi, haiwezi kuhimili kutokana na hali ya joto na hali ya mazingira ya nchini kwetu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wakulima wote; sasa hivi tunasisitiza tutumie mbegu yetu ile ya asili ya East African Tall ambayo inahimili ukame, joto na mazingira yetu.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na nazi kuwa na mandhari nzuri inayovutia inapopandwa, lakini zao lake limekuwa likiporomoka bei mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka jana bei ya jumla ya nazi ilikuwa inauzwa shilingi 400 au zaidi lakini nazi hiyo hiyo mwaka huu inauzwa kwa shilingi 50. Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kumsaidia mkulima kwa kuweza kudhibiti bei na kuweza kupata faida ukizingatia zao la nazi linavunwa mara nne kwa mwaka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa nazi ina faida nyingi ikiwemo mafuta na nyingine Mheshimiwa Naibu Waziri amezielezea. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuwasaidia wakulima wa zao la nazi kuweza kuanzishiwa viwanda vidogovidogo ikiwemo ya mafuta, tui la nazi au vifuu kutengeneza mkaa mdogo mdogo ili kudhibiti mazingira ya nchi ili na wao wakulima wa zao hilo waweze kupata faida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza Serikali kwa ajili ya kuongeza bei pamoja na kutafuta soko kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. Soko bado lipo kubwa ndani ya nchi na ndio maana tunalazimika wakati mwingine kuagiza tui la nazi kutoka nje ya nchi kuonyesha kwamba bado kuna mahitaji makubwa ya nazi. Lakini tatizo kubwa linalokuja si bei, tatizo kubwa ni tija ndogo wanaipata wakulima kutokana na kipato kidogo wanachokipata kwenye kuchukua nazi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mzee Bakhresa yuko tayari kuwekeza na mashine zimeshaingia zina miaka minane lakini anashindwa kupata mali ghafi ya kutosha kuweza kuzalisha tui la nazi hapa nchini kwa muda wote wa mwaka. Kwa sababu kama ulivyosema ni kiasi kidogo kutokana na matatizo unayokumbuka.

Mheshimiwa Spiaka, swali lake la pili kuhusu mkakati wa kuweza kuongeza thamani ni kweli tuna mkakati wa kwanza kama nilivyosema kwenye kuongeza tija na uzalishaji ili kuweza kuwavutia wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani wan je kuja kuweka viwanda vidogo, vya kati na vikubwa baada ya uhakaika wa upatikanaji wa malighafi.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa kwanza ni kuendelea kuongeza shughuli za utafiti ili kuja na mbegu ya minazi ambayo itaweza kukinzana na mabadiliko ya tabia nchi na huu ugonjwa uliokuwepo ili wananchi hawa wakazalishe nazi nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa pili ni kutoa elimu kwa wakulima kwa ajili ya kuchanganya mazao mbalimbali kwenye mashamba ya minazi kama miembe, michungwa na mazao mengine ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato kwa wakulima hao.

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea kuwaelimisha wananchi waache kutegemea ile minazi ambayo iliyokuwa walirithi kutoka kwa mababu zao sasa hivi tunawahimiza kupanda mbegu mpya ili wawe na minazi mipya ambayo italeta tija na uzalishaji mkubwa itaenda kuongeza kipato chao.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri na juhudi za Serikali kuhakikisha kunakuwa na kituo maalum cha kuzalisha mitamba, nina maswali yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hilo ni kubwa, na kwa kuwa eneo hilo tayari limeshakuwa na wakazi zaidi ya 300 kwenye sehemu inayoitwa Vingunguti na wakazi hao wako kwa muda mrefu sana, na wanajiendeleza na wamejiendeleza kwa muda mrefu. Je, haioni sasa ni wakati wa Serikali kulitoa eneo hilo na kuwapa wananchi hao ili waweze kuishi kwa usalama na amani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa suala hili linahusu mambo ya mifugo na ardhi, hii Tanzania ni nchi ya amani, upendo na ushikamano, na Tanzania yetu ina wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na wafanyakazi sehemu mbalimbali. Kumekuwa na tatizo la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Je, Serikali haioni sasa ikatafuta mbinu mbalimbali mbadala za kuepukana na migogoro hiyo kwa kuwapatia maeneo wafugaji wakakaa wakaweka mifugo yao na wakulima na wananchi wengine wakaishi kwa amani na utulivu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo hili lilikuwa na hekta zaidi ya 1,000 na baada ya Serikali kugundua kwamba wananchi wameshaingia eneo hili, wamejenga, wamejiendeleza, tumefanya tathmini, tumewaachia wananchi zaidi ya hecta 2,900 ili waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo.

Sasa naomba tupokee pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge ya kwenda kufanya tathmini tuangalie kazi ya kuzalisha mitambo ambayo inafanyika eneo hili, faida yake, lakini pia na huduma za jamii za wananchi halafu tutaona busara tunafanye ili tuweze kuamua, ama tuwaachie au tuendelee kuweka mifugo pale ya kuzalisha mitambo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili anazungumzia migogoro ya ardhi; muda mfupi uliopita Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoka kuzungumza hapa namna ambavyo Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla wamepokea jambo hili la migogoro na kwamba haipaswi kuendelea. Mheshimiwa Waziri umefanya kazi hiyo, lakini pia wakuu wa mikoa na wilaya wamepewa maelekezo, lakini Wizara ya Ardhi inafanya pia mpango mahususi wa matumizi bora ya ardhi, sasa hili nalo kama kuna mgogoro pale unaendelea naomba tulipokee tuwasiliane na wenzetu mamlaka katika eneo lile tulifanyie kazi. Nia ya Serikali ni kwamba migogoro isiwepo, tunahitaji wakulima, tunahitaji wafugaji na wananchi na shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo biashara ili waendelee kufanya kwa amani na waweze kuchangia pato ikiwa ni pamoja na kulipa kodi. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu yaliyokuwa na uhakika kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hapo zamani stesheni ndogo ndogo za reli zilikuwa zina stawi sana miji yake kutokana na kwamba reli zilikuwa zinasimama kwa mfano Stesheni ya Mpiji na Stesheni ya Kikongo na nyinginezo hadi Mwanza, Kigoma na Tabora na kwa kuwa ujenzi huu wa reli sasa hivi hakuonyeshi dalili ya kwamba kutakuwa na treni itasimama.

Je, kuna mpango gani na mkakati gani angalau kwa Stesheni ya Kikongo ambayo stesheni hiyo inaunganisha barabara inayotoka Makofia hadi Mlandizi, Mlandizi hadi Mzenga, Mzenga hadi Mwanarumango, Serikali haioni kwamba barabara hii na stesheni hii ikiboreshwa na treni zikasimama itasaidia kusafirisha abiria na mizigo ambayo wananchi wanataka kuipeleka kokote kule? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali na ninaishukuru na kuipongeza, imepanga Stesheni ya Soga na Kwala kuwa stesheni kubwa; je, Serikali haioni sasa kuna haja na umuhimu wa Halmashauri hizo kupewa ardhi, ardhi hiyo ikapimwa, ikagaiwa kwa wananchi, wananchi hao wakajenga na wakawa na miradi ambayo itaendeleza ule mji na wao kuwapatia kipato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ametaka kujua status ya vituo vya zamani kupitia meter gauge. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro ambako tunapitia Mkoa wa Pwani kuna vituo vya zamani 14. Nimhakikishie tu kwamba vile vituo vitaendelea kuboreshwa kupitia mradi wa TIRP ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa dola milioni 300 na mpaka sasa hivi vimekwishaanza kurekebishwa na kuwekwa katika hali nzuri. Reli itakapokuwa inapita ile meter gauge itahudumia vituo vyote vile 14 kati ya Dar es Salaam mpaka Morogoro.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa SGR kuna vituo sita, Dar es Salaam mpaka Morogoro kuna vituo sita, vinne viko katikati na kimoja ni cha Dar es Salaam na kingine ni cha Morogoro. Vinne kuna Kwala, Soga, Kingolwira na Ngerengere. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kuunganisha vituo hivyo na vile vituo vya zamani unaendelea vizuri na reli ya kisasa inayojengwa kwa asilimia 70 itakwenda na ile reli ya zamani ya meter gauge.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, Mheshimiwa alitaka kujua suala la upimaji wa ardhi kwa ajili ya maeneo yale. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mamlaka ya Mji wa Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi wamekwishaendelea kupanga mji ule wa maeneo ya Kwala, Soga na Kingolwira kwa ajili ya kuwa-accommodate watu watakapata viwanja pale. Kwa sababu vituo vile vitakuwa ni vya kisasa ambavyo vitakuwa na huduma zote za kijamii na tunategemea hata wananchi nao waende wakae pale maeneo yao kwa ajili ya kufanya shughuli za kijamii.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa swali la msingi linazungumzia suala la kufundisha Kiswahili na kwa kuwa Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli anakitangaza Kiswahili dunia nzima na kwa kuwa Serikali inajua umuhimu wa kukitangaza Kiswahili.

Je, kuna mkakati gani wa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kukitangaza Kiswahili, kwani nchi jirani wanachukua nafasi ya kuonekana wao ndio wamejipanga katika kuuza soko la lugha ya Kiswahili? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli hakika amekuwa ni Balozi mzuri sana katika kuhakikisha kwamba Kiswahili kinatumika na amekuwa akikitumia katika mikutano hata nje ya nchi na ameongeza chachu ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata katika Mikutano ya Umoja wa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeendelea kukitangaza Kiswahili kwa kuhakikisha kwanza kinatumika katika shughuli mbalimbali za kiserikali, lakini vilevile hili suala la kwenda kufundisha katika nchi za nje ni mojawapo ya hatua muhimu ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili na hata katika mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tumeona kimekuwa kinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba fursa yoyote inayopatikana ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili tunaendelea kuitumia, lakini vilevile Wizara yangu itaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha ufundishaji wa somo hili la Kiswahili kwa sababu kadri ambavyo tutakuwa na watalaam wengi wa Kiswahili hiyo pia ni sehemu moja wapo ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili.