Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zaynab Matitu Vulu (8 total)

MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-
Zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wa mijini hupata chakula chao cha asubuhi, mchana na jioni kwa mama lishe, lakini mama lishe hao wananyanyaswa sana na askari wa mgambo wa majiji na miji kote nchini.
Je, kwa nini Serikali isiandae mazingira mazuri na masafi ya kufanyia kazi zao na wao wakatozwa ushuru mdogo kuliko hali ya kuendelea kuwanyanyasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, mama yangu huyu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabisahara wadogo walioko katika sekta isiyo rasmi katika kukuza kipato na ajira. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo mama lishe karibu na maeneo walipo wateja wao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu askari mgambo wanaonyanyasa mama lishe, jambo hili halikubaliki pia ni kinyume cha Sheria ya Polisi Wasaidizi ya mwaka 1969 inayowazuia kuwapiga, kuchukua au kuharibu bidhaa au mali za wananchi. Askari mgambo kama ilivyo kwa watumishi wengine wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na bila manyanyaso wala dhuluma wakati wa kuwaondoa wafanyabisahara katika maeneo yasiyoruhusiwa. Mheshimiwa Spika, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa askari mgambo yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa mama lishe na wafanyabisahara wengine wadogo, kwa sababu vitendo hivyo ni kinyume cha sheria. Aidha, napenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wote kufanya biashara zao katika maeneo yaliyotengwa rasmi na Halmashauri na kuacha kufanya bisahara hizo katika maeneo yasiyoruhusiwa.
MHE. ZAYNAB M. VULLU aliuliza:-
Serikali imeona umuhimu wa kuchukua hatua kali zaidi kwa mwanaume anayempa mimba mwanafunzi wa shule kwamba apatiwe kifungo cha miaka 30:-
Je, Serikali itamhakikishiaje mwanafunzi aliyepewa mimba kuwa ataweza kuendelea na masomo baada ya kujifungua?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vullu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na mambo mengine, imeweka mkazo juu ya kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wote. Aidha, sera inatamka wazi kuwa Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na hivyo kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika na kwamba itahakikisha kuwa usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo, Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo utakaofuatwa na wadau mbalimbali ili kuwawezesha wasichana waliopata ujauzito kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua. Mwongozo huu pia, baadhi ya mambo yaliyowekwa ni utaratibu utakaofuatwa kwa wasichana waliojifungua kuendelea na masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia ya Serikali kuondoa vikwazo kwa mtoto wa kike ili kuendelea na masomo, wito unatolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walimu, viongozi wa elimu pamoja na dini na jamii kwa ujumla kwa pamoja kuchukua hatua za makusudi za kuzuia na kudhibiti tatizo la mimba shuleni na katika umri mdogo kwani kwa kiwango kikubwa inamvunjia heshima mwanafunzi mwenyewe na kuwa chanzo cha upotevu wa maadili na pengine kupoteza dira yake ya mafanikio katika maisha.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-
Kwa sasa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo Jijini Dar es Salaam kimezidiwa uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo vingine kikanda ili kuboresha huduma za usafiri wa mabasi yanayoingia na kutoka mikoani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ipo katika mipango ya kuanzisha vituo vingine mbadala vya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani baada ya kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi kama ifuatavyo:-
(a) Kituo cha mabasi Mbezi Luis, chenye eneo la mita za mraba 68,000 kitahudumia mabasi yatokayo katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Rukwa, Iringa, Ruvuma na Njombe); Kanda ya Ziwa (Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Geita na Simiyu); Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Manyara); Kanda ya Magharibi (Tabora, Kigoma na Katavi) na nchi za jirani za Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, Zimbabwe na Zambia.
(b) Kituo cha mabasi cha Boko Dawasa chenye eneo la mita za mraba 63,121 kitahudumia mabasi yatokayo mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Mashariki (Arusha, Kilimanjaro na Tanga) na nchi za jirani za Kenya na Uganda.
(c) Kituo cha mabasi cha Kanda ya Kusini, kitatafutiwa eneo sehemu ya Kongowe kwa ajili ya kuhudumia mabasi yatokayo Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
MHE. ZAYNAB M. VULU aliuliza:-
Kilimo cha mwani kinalimwa baharini na asilimia kubwa ya wakulima wa zao hilo ni wanawake:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha zao hilo?
(b) Je, Serikali inamsaidiaje mkulima wa mwani kupata soko la uhakika hususani nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kilimo cha zao la mwani kinachofanyika katika mwambao wa Bahari ya Hindi ni miongoni mwa shughuli za sekta ndogo ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji ambapo jumla ya tani 1,197 zenye thamani ya shilingi milioni 412 zilivunwa na kusafirishwa nje ya nchi mwaka 2016/2017. Aidha, tani 1,329 zenye thamani ya shilingi milioni 469 zilivunwa mwaka 2017/2018. Mwani hulimwa zaidi na wanawake wanaokadiriwa kuwa asilimia 90 ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 Serikali iliandaa Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kilimo cha mwani zikiwemo kiasi kidogo cha mwani kinachozwalishwa na wakulima pamoja na mapato duni. Malengo mahsusi ya Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani ni pamoja na kujenga uwezo wa wakulima kujitegemea; kuongeza mwamko juu ya kilimo cha mwani kama shughuli inayozalisha mapato mazuri; na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanachochea uwekezaji wa kisasa na kudumisha matumaini ya wadau wote wa tasnia ya mwani.
(b) Mheshimiwa Spika, mwani unaozalishwa nchini unauzwa katika masoko ya nchi za Ufilipino, Uchina, Ufaransa na Denmark. Pia kiasi kidogo cha mwani husindikwa hapa nchini na wadau kwa kutengeneza sabuni za mche, sabuni za maji na shampoo. Pia, mwani husindikwa ajili ya chakula na dawa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango Madhubuti wa Maendeleo ya Mwani ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji; kusaidia wananchi kuingia mikataba yenye tija na makampuni ya mwani; pamoja na kutafuta masoko mapya ya nje ili kusaidia wakulima kupata bei bora zaidi.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-

Barabara ya Vikindu – Vianzi hadi Sangatini ni muhimu kwa wakazi wa Jimbo la Mkuranga na Kigamboni:-

Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Vikindu - Vianzi hadi Sangatini yenye urefu wa kilomita 18.65, inaanzia Kijiji cha Vikindu -Vianzi na Kitongoji cha Sangatini (Mkuranga) Mkoa wa Pwani na kuungana na barabara ya Kibada, Mwasonga hadi Tundisongani iliyopo Wilaya ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga inahudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini (TARURA) na kwa upande wa Wilaya ya Kigamboni inahudumiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, TARURA Wilaya ya Mkuranga wameiomba Serikali shilingi milioni 270 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 za kuifanyia matengenezo maeneo korofi kwa urefu wa kilometa 18 na kujenga boksi kalvati moja lenye midomo miwili. Aidha, TARURA watafanya tathmini ya ujenzi kwa kiwango cha lami kipande wanachokisimamia na itakapokamilika, Serikali itazingatia matengenezo hayo kwa kutegemea na upatikanaji wa rasilimali fedha. Ahsante.
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-

Kazi zote za Utawala na fedha katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya zinasimamiwa na Mganga Mfawidhi wa Wilaya wa eneo husika:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa elimu ya Utawala na Usimamizi wa Fedha Madaktari hao ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri Wahasibu Wasaidizi 335 na kuwapanga kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha usimamizi wa fedha kwenye Vituo vya Afya kupitia mfumo wa kielektroniki wa Facility Financing, Accounting and Reporting System (FARS). Aidha, ili kukabiliana na upungufu uliopo wa wataalam hao wa utawala na usimamizi wa fedha, Waganga Wafawidhi katika Hospitali za Halmashauri, Vituo vya
Afya na Zahanati wamepatiwa mafunzo ya utawala na usimamizi wa fedha yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 Desemba, 2018 hadi tarehe 22 Januari, 2019 katika kila Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo wataalam hao kwenye masuala ya fedha na utawala katika vituo wanavyovisimamia. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imewasilisha maombi ya kibali cha kuajiri zaidi watumishi wa kada za Wahasibu Wasaidizi kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa fedha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
MHE. ZAYNABU M. VULLU aliuliza:-

Zao la nazi ni zao ambalo pia lina faida nyingi sana kuanzia mti, matawi, na nazi yenyewe:-

(a) Je, ni lini Serikali itatafuta soko la kudumu la zao hilo?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo kama ilivyokuwa zamani?
NAIBU WAZIRI WAKILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, soko la kudumu la zao la nazi lipo nchini kwa sababu kiasi cha nazi kinachozalishwa bado hakikidhi mahitaji ya soko la ndani la nchi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya zao hilo ikiwemo ulaji wa madafu na watumiaji wa nazi. Aidha, mafuta mwali yanayotokana na nazi yanaendelea kupata umaarufu kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa ndani na nje ya nchi ambayo lita moja inafikia hadi shilingi 40,000. Bidhaa kama fagio, mbao, ka mbao na samani zinazotokana na mti wa mnazi na uwezo wa zao hilo kutunza mazingira huongeza thamani ya zao la minazi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha soko la zao la nazi nchini msimu wa mwaka 2018/2019 wakulima wapatao 74 katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wamefundishwa namna ya kukamua mafuta mwali. Vilevile, kikundi cha wanachama 50 katika Wilaya ya Bagamoyo kimepewa mashine yenye uwezo wa kukamua lita 500 za mafuta ya mwali kwa mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha masoko ya mazao yote ya kilimo likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi kupitia vyama vyao ushirika, masoko ya moja kwa moja na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya zao la nazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa zao la nazi kuendelea kupanda mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na zenye tija kubwa. Tanzania ni nchi ya 10 Duniani kwa uzalishji wa nazi ikiongozwa na nchi ya Indonesia na kwa Afrika ni nchi ya kwanza ambapo huzalisha wastani wa tani 530,000 za nazi kwa mwaka, ikifuatiwa na Ghana ambayo huzalisha wastani wa tani 366,183.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha minazi nchini ambapo imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo kidogo cha utafiti cha Mbezi Wilaya ya Bagamoyo ili kuzalisha miche bora ya minazi yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa kunyong’onyea kwa minazi (Coconut Lethal Disease) na kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahamasisha kilimo cha minazi katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini ambapo msimu wa 2018/2019 ilizalisha na kusambaza jumla ya mbegu ya miche 11,000 kwa wakulima katika Mikoa ya Rukwa na Mwanza. Aidha, Serikali inafanya mazungumzo ya Jumuiya ya Asia – Pacific Coconut Community) ambayo hutunza ‘‘germplasm” ya minazi kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za minazi zenye kuongeza tija na uzalishaji mkubwa kwa wakulima. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU aliuliza:-

Serikali inajenga reli ya standard gauge na itapitia baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani?

Je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuboresha vituo vya zamani na hasa vituo vidogo vidogo ili kuimarisha njia ya usafiri na vituo hivyo vidogo ni vipi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Matitu Vulu, Mbunge wa Viti Maalum - Pwani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa reli iliyopo meter gauge inaendelea kukarabatiwa ili kuhakikisha inatoa huduma za uchukuzi hasa kwa mizigo ya ndani ya nchi, hivi sasa Serikali inaendelea na ukarabati wa reli hii kutoka Dar es Salaam hadi Isaka kupitia mkopo wa Benki ya Dunia wa dola za Kimarekani milioni 300.

Mheshimiwa Spika, kwa ukarabati huo, wakati ukarabati huo unaendelea katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetenga fedha kupitia kifungu namba 4216 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati ikiwemo stesheni ya Soga, Ruvu na Kwala zilizopo katika Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ukarabati huu, mpango wa Serikali ni kuunganisha stesheni za zamani na mpya zinazoendelea kujengwa kupitia mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa yaani SGR. Yapo maeneo yatakayounganishwa kwa barabara na pia kwa madaraja ya juu kwa baadhi ya maeneo yanayokaribiana na vituo hivyo, kwa mfano, Stesheni ya Soga ya zamani ya Mkoa wa Pwani itaunganishwa na daraja la juu la Stesheni mpya ya SGR.