Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Flatei Gregory Massay (33 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Kutokana na wizi wa mifugo uliokithiri katika Bonde la Yayeda Chini, Serikali ilianzisha kituo cha polisi na sasa kimeondolewa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirudisha kituo hicho ili wananchi wapate huduma za ulinzi wa mifugo na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kituo cha polisi cha Bonde la Mto Yayeda Chini kilianzishwa kutokana na matukio ya kukithiri kwa matukio ya wizi wa mifugo. Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi lilipeleka gari PT Na. 1008, Landrover kituo cha polisi cha Hydom kinachotoa huduma ya ulinzi wa eneo hilo na kuanzisha doria za mara kwa mara ili kupambana na wimbi la wizi wa mifugo. Kwa hivi sasa, hali ya wizi wa mifugo na uhalifu mwingine katika eneo hilo umepungua.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kituo hicho hakijaondolewa bali taratibu za kutoa huduma za ulinzi zimebadilika; ambapo askari hupangwa kwa kazi za ulinzi wa doria eneo hilo kwa kipindi maalum na kwa awamu. Jeshi la Polisi litaendelea kutathmini na kuzingatia hali ya uhalifu wa eneo hilo katika kutoa huduma stahiki za ulinzi na usalama.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Barabara ya Mbulu – Hydom – Babati – Dongobeshi, imekuwa na miundombinu mibovu na haipitiki muda wote wa mwaka na kumekuwepo ahadi ya kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Je, Serikali itatekeleza lini ahadi hiyo ambayo pia imetolewa na Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbulu – Hydom ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Kilimapunda – Mbulu – Hydom – Kidarafa yenye urefu wa kilometa 114. Aidha, barabara ya Dareda – Dongobesh yenye urefu wa kilometa 60, ni barabara ya Mkoa na inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) na barabara zote hizi mbili ni muhimu sana kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara, na hasa wa Jimbo la Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Mbulu – Hydom – Kidarafa imejumuishwa kwenye mradi wa upembuzi yakinifu wa barabara inayopita kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Seringeti (Southern Bypass) ya Mbulu Route unaojumuisha barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Kidarafa hadi Sibiti. Mradi huu upo kwenye hatua ya ununuzi ili kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu na usanifu chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) ambapo kazi ya kuchambua Zabuni inaendelea.
Aidha kuhusu barabara ya Dareda kwa maana ya Babati hadi Dongobeshi yenye urefu wa Kilomita 60, imejumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 katika Mradi wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na itaweka katika mpango wa utekelezaji kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa miaka minne mfululizo kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika kwa muda wote wa mwaka wakati maandalizi ya kuzijengwa kwa kiwango cha lami yanaendelea. Mathalani, fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 zilikuwa ni shilingi milioni 1,254.163; mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi milioni 1,425.163; mwaka 2014/2015 zilitengwa shilingi 1,258.876 na mwaka huu wa 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 1,655.504.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali kupitia Benki ya Dunia ilianzisha mradi wa maji katika Miji ya Haydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika baada ya fedha kusitishwa:-
Je, Serikali imejipangaje kumaliza miradi hii ili wananchi wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ya Hydom, Masieda, Tumati Arri na Bwawa la Dongobesh ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ifuatavyo:-
(i) Mradi wa maji wa Hydom umefikia asilimia arobaini na tano. Mradi huu utapokamilika utahudumia wakazi wapatao 16,737.
(ii) Mradi wa Maji wa Masieda umefikia asilimia tisini na tisa na wananchi wapatao 3,137 wanapata huduma ya maji.
(iii) Mradi wa maji wa Mongahay - Tumati umefikia asilimia kumi na sita. Hata hivyo, mkataba umevunjwa kutokana na mkandarasi kushindwa kutekeleza mkataba. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu inaendelea na taratibu za kupata mkandarasi mwingine. Mradi huu utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 8,679.
(iv) Mradi wa Arri utahudumia wananchi wapatao 17,580. Ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia arobaini na tano.
(v) Ujenzi wa tuta la bwawa la umwagiliaji la Dongobesh umekamilika kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii imechelewa kukamilika kutokana na kukosekana kwa fedha za kuwalipa wakandarasi. Serikali itaendelea kutoa fedha kila zinapopatikana ili kukamilisha miradi hiyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika maeneo ya Tarafa za Jimbo la Mbulu za Manetadu, Tumatu Arri, Masieda na Yayeda chini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inagharamia utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini (REA), kupitia mpango huu wa REA Vijijini (REF). Mradi huu unatekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Manyara. Mkandarasi, CC International Nigeria Limited, hivi sasa anaendelea na utekelezaji wa mradi huo katika Wilaya za Mkoa wa Manyara ikiwemo Wilaya ya Mbulu Vijijini. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 84, ambapo tayari transformer zimeshafungwa na pia wateja 354 wameunganishiwa umeme katika Mkoa mzima wa Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unategemea pia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu 2016. Lengo kubwa la mradi huu ni kupeleka huduma za umeme kwa wananchi na hivyo kurahisisha shughuli za kiuchumi pamoja na kijamii. Tarafa za Manetatu, Masieda, Tumatiadi na Yaeda Chini zimejumuishwa katika Mpango wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, utakaoanza mara baada ya bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Haydom kwa sasa inatumika kama Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kupitia Tangazo la Serikali namba 828 la tarehe 12 Novemba, 2010. Serikali imeweka utaratibu wa kuipatia hospitali hii ruzuku ya Serikali kwa ajili ya dawa na vifaa tiba kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya, pamoja na kulipa mishahara ya baadhi ya watumishi wanaotoa huduma katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 134.04 kwa ajili ya dawa na uendeshaji wa shughuli za hospitali, kati ya fedha hizo, zilizopokelewa ni shilingi milioni 111.5. Vilevile hospitali hii imetengewa shilingi milioni 570.6 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa watumishi wa Serikali wanaofanya kazi katika hospitali hiyo. Kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba wa utoaji huduma ya afya, lengo likiwa ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ambayo inahudumia Mkoa wa Manyara pamoja na Mikoa jirani.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Hospitali ya KKKT Hydom ilipanda hadhi kuwa Hospitali ya Mkoa muda mrefu, sasa inahudumia Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Singida, Arusha na Simiyu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipandisha hadhi ili iwe Hospitali ya Kanda kuiwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Hospitali ya KKKT Haydom ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa mwaka 2010. Aidha, hospitali hii haikupandishwa hadhi ili iwe Hospitali ya Mkoa. Mkoa wa Manyara una Hospitali yake ya Rufaa ya Mkoa. Madhumuni ya kuipandisha hadhi Hospitali hiyo yalikuwa ni kuifanya itoe huduma za ngazi ya rufaa ya Mkoa ikisaidiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. Ili hospitali iwe ya rufaa ngazi ya Kanda, ni lazima iwe na miundombinu bora tofauti na iliyopo sasa, pamoja na watumishi waliopata mafunzo yanayohitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Kaskazini tayari kuna hospitali zinazotoa huduma za kibingwa kama KCMC ila kwa vigezo vingine Hospitali hii imeshakaguliwa na imeonekana ina upungufu kadhaa, pale utakapokamilika itatoa huduma hizo. Aidha, hosptiali ya KKKT Hyadom toka awali ilikuwa inahudumia wananchi wa mikoa iliyotajwa. Hali hii inachangiwa na sehemu ya kijiografia iliyopo hospitali hiyo kwani inafikika kirahisi na wananchi wa mikoa hiyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo.
Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom yamejadiliwa katika vikao vya awali vya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira tarehe 25/09/2012, Baraza la Madiwani katika kikao cha tarehe 19/10/2012 na Kamati ya Huduma za Uchumi katika kikao cha tarehe 13/06/2014. Kimsingi, vikao vyote hivyo vimekubaliana na wazo la kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Haydom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri mapendekezo hayo sasa yawasilishwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili hatimaye yawasilishwe kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kupata kibali. Hivyo, taratibu hizo zikikamilika na kuonekana mamlaka hiyo imekidhi vigezo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haitasita kuanzisha mamlaka hiyo kisheria.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Wananchi wa Mbulu Vijijini hawana mawasiliano ya simu wala minara katika Kata za Tumati, Yaeda, Ampa, Gidhim na Gorati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka minara katika Kata hizo ili kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, iliainisha maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Mbulu likiwemo Jimbo la Mbulu Vijijini na kuyaingiza maeneo hayo katika miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa. Kijiji cha Yaeda Ampa kutoka Kata ya Yaeda Ampa kimeingizwa katika zabuni ya mradi wa kufikisha huduma ya mawasiliano kwa maeneo ya mipakani na kanda maalum. Zabuni hii ilifunguliwa tarehe 27, Aprili, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yetu kuwa Kijiji cha Yaeda Ampa kitapata kampuni ya kufikisha huduma ya mawasiliano na kuondoa kabisa tatizo la mawasiliano katika kata hiyo. Aidha, Kata za Tumati, Gidhim na Gorati zimeingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali kupitia Mradi wa Vijijini kumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia iliahidi kupeleka maji Maretadu, Labay, Gidmadoy, Qamtananat, Garbabi, Magana Juu na Qatabela:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri zote nchini. Utekelezaji wa programu hii unafanyika kwa awamu. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji kwa Halmashauri ya Mbulu Vijiji vya Singu, Masieda, Arri-Harsha, Dongobesh, Mongahay, Tumati, Haydom na Moringa vilihusika. Hadi sasa miradi ya maji katika Vijiji vya Singu na Masieda imekamilika na ujenzi unaendelea katika vijiji vilivyobaki. Serikali katika kuhakikisha inakamilisha miradi ya maji na kuanzisha mingine mipya kiasi cha shilingi bilioni 2.09 zimetengwa kwa Wilaya hiyo katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu ya pili ya utekelezaji wa WSDP iliyoanza Julai, 2016, Halmashauri zote nchini ikiwemo ya Mbulu zimewasilisha mipango ya utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa maana 2016/2017 - 2020/2021 ambapo miradi mingi ya maji itatekelezwa kulingana na mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu vilivyopo katika mpango huo ni Maretadi, Labay, Didmadoy, Quantananat, Garbabi, Magana Juu na Qutabela. Kwa kuanzia Vijiji vya Meretadu, Labay na Garbabi vimepewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2017/2018 ikiwa ni pamoja na Vijiji vya Genda, Ng’orat na Endahagichan. Vijiji vingine katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu vitaendelea kutekelezwa kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Hydom umechukua muda mrefu kumalizika na wananchi wanasubiri maji huku muda wa mkataba na mkandarasi ukiwa umeisha.
Je, kwa nini Serikali isimfukuze mkandarasi huyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Mji wa Haydom ulianza kutekelezwa mwaka 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha utekelezaji ulisimama mwaka 2015/2016. Hata hivyo, pamoja na mkataba wa mkandarasi kuisha muda wake, napenda nimsifu na kumshukuru Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Chelestino Mofuga na Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Hudson Kamoga kwa kufanya kikao kati yao na mkandarasi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Wizara ya maji Profesa Kitila Mkumbo tarehe 2/11/2017, ambapo muafaka wa mkandarasi kuendelea kutekeleza mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2018 ulipatikana. Kwa maana hiyo, wakazi wa vijiji vya Haydom na Ng’wandakw vinavyounda Mji wa Haydom wenye wakazi 17,406 wataanza kupata maji baada ya mradi huo kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza yangu kuhusu taarifa tulizozipata usiku wa leo zinazohusu changamoto za Mkandarasi zinazohitaji utatuzi wa haraka namwomba Mheshimiwa Flatei Massay na mwenzangu Naibu Waziri wa Maji tukutane hapa Bungeni baada ya kipindi cha asubuhi ili tupate utatuzi wa haraka wa mradi huo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho au mishahara Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kurahisisha ufanisi wa shughuli zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa katika maendeleo ya Taifa. Serikali imezingatia na kuweka utaratibu wa kushirikisha viongozi hawa wanaolipwa posho maalum kwa motisha kupitia asilimia 20 ya mapato yanayorejeshwa na Halmashauri kwenye vijiji. Asilimia 17 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika kwa shughuli za utawala, ikiwemo kulipa posho ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa na asilimia tatu kwa shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kuboresha utaratibu huu kwa kuingiza katika mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ili kuweka utaratibu mzuri wa urejeshaji wa asilimia 20 kwenye vijiji na kuwanufaisha walengwa. Aidha, tumeimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zote ili kujenga uwezo wa kutenga asilimia 20 kwenda kila kijiji.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya Simu katika Kata za Yayeda, Ampa Arr, Tumati, Gidilim Gorati, Endaagichan na Haydere katika Jimbo la Mbulu Vijijini ili wananchi waweze kuwasiliana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliyaainisha maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mbulu vijijini yakiwemo maeneo ya Yaeda, Tumati, Gidilim Gorati, Masieda, Endaagichan, na Hyadere na kuyaingiza katika zabuni ya awamu ya tatu iliyotangazwa tarehe 5 Juni, 2018. Zabuni hii inategemewa kufunguliwa tarehe 23 Julai, 2018. Endapo mzabuni atapatikana, mkataba kwa ajili ya kazi husika unatarajiwa kusainiwa tarehe 29 Agosti, 2018 na ujenzi wa minara unatarajiwa kuchukua miezi tisa tangu kusainiwa kwa mkataba.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Kutokana na sera ya Serikali kujenga vituo vya afya kila kata.
Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo katika Kata za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer, Masieda na kupandisha hadhi Zahanati ya Hayderer kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imejenga vituo vya afya 210 nchi nzima kwa gharama ya shilingi bilioni 93.5 vikiwemo vituo vya afya saba vilivyoko Mkoa wa Manyara kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipewa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Dongobeshi na Halmashauri ya Miji Mbulu ilipewa shilingi bilioni moja kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Tlawi na Daudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutimiza azma ya kuwa na kituo cha afya kila kata hapa nchini Serikali imeweka vigezo maalum juu ya ujenzi wa vituo vya afya, lengo mahsusi ni kusogeza huduma za afya ili zipatikane ndani ya umbali wa kilometa tano kama ilivyoelekeza kwenye Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandishwa hadhi kwa Zahanati ya Hayderer kuwa kituo cha afya miundombinu iliyopo katika zahanati hiyo haikidhi vigezo vya kuhuishwa kutoa huduma kama kituo cha afya. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imeendelea kufanya uhamasishaji kwa wananchi kujitolea kujenga vituo vya afya katika kata zilizotajwa za Maretadu, Maghangw, Endamilay, Dinamu, Geterer na Masieda. Hadi sasa wananchi wa Maretadu wametenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi kulingana na upatikanaji wa fedha na rasilimali nyingine kama watumishi na vifaa tiba.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Serikali iliahidi vijiji vingi vya Jimbo la Mbulu Vijijini umeme wa REA III.
Je, ni lini sasa umeme utafika katika vijiji vya Endahargadat, Endahagichani, Qamtananat, Mewadan, Endalat, Gidbiyo na Manghay?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote Tanzania Bara visivyokuwa na miundombinu ya umeme ifikapo mwezi Juni, 2021. Jimbo la Mbulu vijijini lina vijiji vipatavyo 76, kati ya vijiji hivyo 12 vimepatiwa umeme. Vijiji 13 vya Qaloda, Getesh, Endesh, Labay, Maretadu, Hayderer, Endanachan (Haydom), Muslur, Dirim, Simha, Yaeda Ampa, Endoji na Gidhim vimejumuishwa katika mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Mkandarasi Kampuni ya Angelique International Limited kutoka India ameshaanza utekelezaji wa mradi na anatarajia kukamilisha kazi hiyo mwezi Juni, 2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilometa 45.87 za njia ya umeme wa msongo wa Kilovolt 33 na kilometa 35 za nja ya umeme wa msongo wa 0.4 kilovolt, ufungaji wa transfoma 16 na uunganishwaji wa wateja wa awali 347. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 2.6. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili utakaoanza kutekelezwa Julai, 2019 hadi mwezi Juni, 2021. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Serikali iliahidi kuanzisha Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu. Aidha, wataalam wa Serikali walifika Mbulu na kukabidhiwa majengo kwa ajili ya Baraza hilo katika Mji wa Dongobesh na Mheshimiwa Mbunge akachangia shilingi milioni tatu za kuongeza miundombinu.

Je, ni lini Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu litaanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi sasa tuna jumla ya Mabaraza 97 ambayo yameundwa, ambapo kati ya hayo Mabaraza 53 yanatoa huduma na Mabaraza 44 likiwemo Baraza la Mbulu hayajaanza kutoa huduma kutokana na changamoto za uhaba wa rasilimali watu. Ili Baraza liweze kuanza kufanya kazi linahitaji kuwa na angalao Mwenyekiti mmoja, Katibu Muhtasi, Msaidizi wa Kumbukumbu, Msaidizi wa Ofisi, Dereva na Mlinzi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imeipatia Wizara Wenyeviti 20 ambao ni wajiriwa wapya. Wenyeviti tisa kati ya hao ni kwa ajili ya kuongeza nguvu katika maeneo hayo yaliyoelemewa kwa wingi wa mashauri katika Wilaya za Mbulu, Sumbawanga, Kibondo, Kigoma, Temeke, Bukoba, Mwanza, Musoma na Ulanga. Wenyeviti 11 kwa ajili ya mabaraza 11 ambayo hayana Wenyeviti katika wilaya za Ukerewe, Maswa, Kilosa, Same, Kyela, Shinyanga, Lindi, Iramba, Nzega, Lushoto na Tunduru. Taratibu za mafunzo ya awali zinafanywa ili Wenyeviti hawa waweze kupangiwa vituo na kuanza kazi katika Mabaraza hayo ambayo yana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba Baraza la Mbulu linaanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo, Wizara imeshatuma barua kwenda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupata mapendekezo ya wananchi wenye sifa, ili Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aweze kufanya uteuzi wa Wazee wa Baraza la Ardhi na Nyumba kwa Wilaya ya Mbulu.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zitakazopata Wenyeviti wapya wa Mabaraza kutuma mapendekezo ya Wajumbe wa Mabaraza kwa wakati, kila wanapotakiwa kufanya hivyo, ili wananchi wasikose huduma kwa kukosekana Wajumbe wa Baraza. Aidha, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanashauriwa kuangalia uwezekano wa kutoa maeneo ya ofisi kwenye majengo yaliyo katika hali nzuri ili kurahisisha uanzishwaji wa Mabaraza katika Wilaya ambazo Mabaraza hayajaanza kazi.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Madiwani nchini wanafanya kazi kubwa sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea posho na mishahara au maslahi yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa wanayofanya Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao. Kwa kuzingatia ukweli huo, Serikali imekuwa ikipandisha posho na maslahi ya Madiwani kwa kadri mapato ya Halmashauri yanavyoongezeka. Kuanzia mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali ilipandisha posho ya Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2012 kutoka shilingi 120,000/= hadi 250,000/= kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 108.3. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali ilipandisha tena posho za Madiwani kupitia Waraka wa mwaka 2014 kutoka 250,000 hadi 350,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 40.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inalipa pia posho ya madaraka kwa Wenyeviti wa Kamati kiasi cha shilingi 80,000/= kwa mwezi na posho ya kikao kiasi cha shilingi 40,000/= kwa mujibu wa Waraka wa Mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kikubwa kinachotumika kupandisha posho za Madiwani ni uwezo wa Halmashauri kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri husika. Serikali itaendelea kuthamini na kutambua kazi kubwa na nzuri inayotekelezwa na Waheshimiwa Madiwani na kuongeza posho hizo kadri makusanyo ya mapato yanavyoongezeka.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Wakulima wa vitunguu saumu wanayo changamoto ya soko la kuuzia zao hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la vitunguu saumu nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitunguu saumu vinavyozalishwa nchini hutumika ndani ya nchi na vilevile huuzwa nje ya nchi vikiwa ghafi. Aidha, baadhi ya mataifa ambayo hununua vitunguu saumu vinavyozalishwa nchini ni Shelisheli, Visiwa vya Comoro, Msumbiji, Zambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Falme za Kiarabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo ikiwemo vitunguu swaumu, Serikali inakamilisha upatikanaji wa simbomilia (barcode) na kiwango cha ubora wa bidhaa zinazotokana na vitunguu saumu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, Wizara imeanzisha Kitengo cha Masoko chenye jukumu la kutafuata mahitaji ya masoko ya wakulima ndani na nje ya nchi ikiwemo vitunguu swaumu kwa kufahamu kiwango kinachohitajika, ubora, bei na muda wa unaohitajika sokoni wa mazao na bidhaa hizo sokoni ili kutoa taarifa kwa wakulima na hivyo kuzalisha mazao yanayokidhi mahitaji ya soko.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ilivijengea uwezo vikundi vya wakulima katika Bonde la Bashay na kuwawezesha kusindika vitunguu saumu na kuwa katika bidhaa mbalimbali zikiwemo mafuta na unga wa vitunguu saumu. Jitihada hizo zimesaidia kuongeza thamani ya zao la vitunguu saumu muda wa kuhifadhi bila kuharibika ubora wake na kuimarisha soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima na wasindikaji wa vitunguu saumu wa Mbulu huwezeshwa kushirki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kila mwaka ili kutangaza na kutafuta masoko ya viunguu saumu na bidhaa zake ndani na nje ya nchi. Serikali kwa kushirikiana na Asasi Isiyo ya Kiserikali ya Global Communities iliandaa Kongamano la Vitunguu Saumu lililofanyika katika Bonde la Bashay tarehe 16 Aprili, 2019 katika AMCOS ya DIDIHAMA ambapo wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali za nchi walialikwa lengo likiwa ni kutafuta soko la vitunguu saumu.

Aidha, Serikali inaendelea kudhibiti uuzaji holela wa vitunguu saumu kwa kutumia magunia ya lumbesa, mabeseni na ndoo ili mizani itumike katika minada ambayo hufanyika katika ghala la vitunguu saumu Bashay Wilayani Mbulu na hivyo kuratibu soko na bei ili kumnufaisha mkulima. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Serikali aliahidi kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Jimbo la Mbulu Vijijini kupitia REA III kwa sababu REA II haikufanya vizuri katika jimbo hilo:-

Je, vijiji vingapi vitafikiwa na umeme wa REA Awamu ya III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kufikisha umeme katika vijiji vyote visivyo umeme nchini ifikapo Juni 2021. Jimbo la Mbulu Vijijini lina vijiji vipatavyo 76 na kati ya vijiji hivyo 12 vimepatiwa umeme. Vijiji 13 vya Qaloda, Getesh, Endesh, Labay, Maretadu, Hayderer, Endanachan(Haydom), Muslur, Dirim, Simha, Yaeda Ampa, Endoji na Gidhim vimejumuishwa katika mradi wa REA III mzunguko wa kwanza. Mkandarasi Kampuni ya Angelique International Limited kutoka India anaendelea na kazi za kusambaza umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vilivyopelekewa umeme zitakamilika mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na kusimika nguzo, kuvuta nyaya na kufunga transfoma katika Vijiji vya Qaloda, Getesh, Endoji, Endesh, Labay, Maghang Juu, Getagujo na Simahha. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 6 vya Getesh, Endoji, Qaloda, Labay, Getagujo na Maghang Juu vitawasha umeme mwisho wa mwezi Mei, 2019. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilometa 45.87 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 na kilometa 35 za njia ya umeme wa msongo kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 16 na uunganishaji wa wateja wa awali 347 na gharama za mradi ni shilingi bilioni 2.6.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyobaki katika Jimbo la Mbulu vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa pili utakaoanzwa kutekelezwa mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Wananchi wa Hydom wameandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama kwa sababu Polisi wakikamata watuhumiwa huwapeleka Mbulu Mjini kilomita 86 ilipo Mahakama ya Wilaya:-

(a) Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Hydom?

(b) Je, Serikali haioni kuwa inapata hasara sana kupeleka Mahabusu Mbulu Mjini umbali wa kilomita 86 kutoka Hydom?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uhaba wa majengo ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili Mahakama ya Tanzania, mahitaji ya majengo ya kuendeshea shughuli za mahakama hapa nchini ni makubwa, kwa msingi huo, Mahakama imejiwekea utaratibu wa kujenga majengo haya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Manyara, Wilaya za Mbulu, Hanang, Kiteto na Simanjiro hazina majengo ya Mahakama za Wilaya. Aidha, Wilaya ya Mbulu ina Mahakama za Mwanzo tatu tu zinazofanya kazi, ambazo ni Daudi, Endagkot na Dongobesh, licha ya ukubwa wa Wilaya yenye Tarafa tano. Hivyo, Tarafa mbili za Hydom na Nambisi hazina Mahakama za Mwanzo changamoto inayowafanya wananchi wa Hydom kutembea umbali mrefu kufuata huduma za mahakama katika Mahakama ya Mwanzo Endgkot ama Dongobesh.

Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kuainisha maeneo ya kipaumbele ni pamoja na umbali, idadi ya watu, wingi wa mashauri na shughuli za kiuchumi ambazo mara nyingi ni kiashiria cha kuongezeka kwa idadi ya mashauri. Kwa kuzingatia vigezo hivyo na mpango wetu wa ujenzi, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama ya Mwanzo Hydom imepangwa kujengwa mwaka 2020/2021.
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Karatu – Dongobesh – Hydom hadi Singida iliyotengewa fedha katika bajeti iliyopita utaanza?
NAIBU WAZIRI WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala kama hili lilijitokeza, swali namba 7 ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Mbulu Mjini, kwa hiyo, inaonyesha ni kwa kiasi gani barabara hii ni muhimu na majibu yangu ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mbulu – Haydom yenye urefu wa kilometa 70.5, ni sehemu ya barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Lalago – Maswa (km 398) inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali (Preliminary Design) wa barabara hii (kupitia mradi wa Serengeti Southern Bypass) ili kuijenga kwa kiwango cha lami, umekamilika. Kazi hii ilifanywa na kampuni iitwayo H.P. Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG mwaka 2016 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).

Mheshimiwa Naubu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii ambayo itawezesha wananchi wa Mbulu kupata huduma katika Hospitali ya Haydom, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya Mbulu – Haydom (km 50) kwa kiwango cha lami; ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021, shilingi bilioni tano zilitengwa. Utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua za manunuzi na ujenzi wake utafanywa kwa njia ya Kusanifu na Kujenga (Design and Build). Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga fedha shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay, swali la nyongeza.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba barabara hii ina umuhimu na sasa kwa miaka miwili imekuwa ikiwekwa kwenye bajeti na haikujengwa na amesema imetegwa shilingi bilioni 5, je, atuambie ni lini atatangaza tenda ili barabara hii ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa anajua wazi kwamba bilioni 5 haiwezi kujenga barabara na barabara hii iko kwenye Ilani ya uchaguzi mwaka 2015-2020 na 2020-2025 na Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni juzi hapa, je, yupo tayari kuweka fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ili kumaliza kilomita zingine 20 kufika 70 kufikia eneo la Haydom?
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza:-

Je, ni lini minara ya simu itajengwa katika Kata za Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni siku yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa katika Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini ili nikatetee na kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo la Bariadi. Pia naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Bariadi kwa kunichagua kwa kishindo na hakika hawajapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuniamini na kuniteua kuwa msaidizi wake katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa jumla ya kata 633 zimekwishapata huduma za mawasiliano nchi nzima ambapo ujenzi unaendelea katika kata zingine 361 kupitia ruzuku ya Serikali. Watoa huduma kwa uwekezaji wao wamefikisha huduma za mawasiliano katika kata 1,692.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tarehe 25 Januari, 2021 tuliwekeana sahihi ya mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 59 zenye vijiji 166 katika zabuni ya awamu ya tano. Vilevile mwezi huu tunatarajia kutangaza zabuni nyingine ya awamu ya sita ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 74 zenye vijiji 206.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) una miradi 15 katika Jimbo la Mbulu Vijijini katika kata 13. Kata zenye miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ni pamoja na Yaeda Ampa, Yaeda Chini, Maghang, Masieda, Bashay, Eshkesh, Geterer, Gidihim, Hayderer, Maretadu, Masqaroda, Endamilay, na Tumati. Jumla ya minara 14 imekamilika kujengwa katika kata 12 kati ya minara 15 inayopaswa kujengwa, hii ni sawa na asilimia 87.5 (87.5%) ya utekelezaji wa miradi hiyo. Bado mnara mmoja ambao unatarajiwa kujengwa na Shirika letu la Mawasiliano Tamnzania (TTCL) ambao utakamilika kabla ya mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado kuna takribani kata 1,365 kati ya Kata 3,956 zilizopo Tanzania Bara zikiwemo kata za Jimbo la Mbulu Vijijini na wadi 16 kati ya wadi 111 zilizopo Zanzibar ambazo bado zina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inavifanyia tathmini vijiji vingine vyote Tanzania Bara na Visiwani vikiwemo Vijiji ambavyo viko katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambavyo ni Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat, na hatimaye vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji ambavyo vitajumuishwa katika kutangaza zabuni katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Mbulu Vijijini ili vijana wapate ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitenga jumla ya shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kujenga vyuo 29 vya VETA katika ngazi ya Wilaya ambavyo kwa sasa vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbulu kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango ambacho pia hutoa mafunzo ya ufundi stadi. Chuo hiki kinaendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu utakaogharimu jumla ya shilingi milioni 605.2 ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani humo, nashauri wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kuendelea kutumia vyuo vilivyopo maeneo yote nchini, ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - Tango na Chuo cha VETA Manyara. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Mahakama Hydom katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mahakama ya Hydom ni moja ya miradi ambayo Mahakama imesaini mkataba Machi, 2021 na tayari Mkandarasi ameanza kazi. Mradi huu utakamilika ifikapo mwezi Agosti, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitano 2016/2017 – 2020/2021, Mahakama inafanya maboresho makubwa ili kukabiliana na changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo. Maboresho hayo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo katika maeneo mbalimbali kwa ngazi zote za Mahakama. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mbulu – Haydom – Singida kwa lami, ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mbulu - Hydom hadi Singida yenye urefu wa kilometa 160.5 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Barabara hii imegawanyika katika sehemu kuu mbili za Mbulu – Haydom urefu wa kilometa 70.5 na Haydom – Singida urefu wa kilometa 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sehemu ya pili ya Mbulu –Haydom imetangazwa kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kwa kuanza na kilometa 25 na sehemu zingine zilizobaki zitaendelea kuongezwa wakati sehemu ya kwanza ya kilometa 25 ikiendelea. Sehemu iliyobaki ya Haydom – Singida ipo katika hatua ya manunuzi ili kumpata mhandisi mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kabla ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Mradi wa Ujazilizi katika Mkoa wa Manyara na Jimbo la Mbulu Vijijini ili kuwafikia wananchi wengi ambao hawakupitiwa na Mradi wa REA I, II na III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ujazilizi kupitia mpango wa kupeleka umeme vijijini, ili kufikisha umeme katika vitongoji vya Tanzania Bara vikiwemo vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini. Miradi hii inatekelezwa awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Mwaka 2021/2022, jumla ya vitongoji 246 katika Mkoa wa Manyara vikiwemo vitongoji vyote visivyo na umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini vinatarajiwa kufikishiwa umeme. Gharama ya Mradi ni shilingi bilioni 45. Zoezi la kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu linalotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TANESCO.
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu vijijini lina jumla ya vijiji 76 na vitongoji 362. Ni vijiji 42 tu ambavyo havina umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini na sasa vinapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotekelezwa katika Jimbo hilo. Kazi zinazofanyika sasa ni manunuzi ya vifaa na ujenzi wa miundombinu ya umeme. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika hatua nyingine Serikali imefanya uhakiki na kuainisha uwepo wa vitongoji takriban 37,610 visivyokuwa na umeme Tanzania Bara na inakadiriwa kuwa shilingi trillion 7 zitahitajika ili kukamilisha mahitaji ya umeme katika vitongoji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishaanza utekelezaji wa miradi ya ujazilizi unaolenga kufikisha umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, lini minara ya mawasiliano itajengwa katika Kata za Endanywish, Endagulda, Gidurdagaw, Yaeda Ampa, Hayeda na Endanilay?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kKuna mnara umejengwa katika kata ya Bashay kijiji cha Bashay kwa lengo la kutoa huduma katika kijiji cha Bashay na baadhi ya maeneo ya Yaeda Ampa. Hata hivyo, baada ya ujenzi wa mnara kukamilika, bado ilionekana kuwa Vijiji vya Arri na Hayeseng kutoka Kata ya Yaeda Ampa bado havipati huduma nzuri ya mawasiliano na hivyo viliingizwa katika orodha ya miradi ya Tanzania ya Kidigitali ambapo zabuni ya mradi huu inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni mara idhini ya benki itakapotolewa.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeziingiza Kata za Endahagichan yenye Vijiji vya Endadubu, Miqaw na Endahagichan, Kata ya Eshkesh yenye Vijiji vya Domanga na Endagulda, kata ya Geterer yenye Vijiji vya Magong na Mewada, Kata ya Haydarer yenye Kijiji cha Gidbiyo, Kata ya Masqaroda yenye Kijiji cha Harbanghet, na Kata ya Yaeda Chini yenye Kijiji cha Endajachi katika mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao kama nilivyosema zabuni yake inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata za Endanywish, Endagulda, Gidurgadaw, Hayeda na Endanilay tathmini ilifanyika na maeneo hayo yalionekana yana changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano na hivyo yataingizwa katika orodha ya miradi ambayo zabuni yake itatangazwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti matukio ya ubakaji wa akina mama uliokithiri katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada zake za kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watu wote wanaojihusisha na matukio ya uvunjifu wa sheria ikiwemo ya ubakaji. Aidha, Jeshi pia hutoa elimu kwa jamii kwa kuwashirikisha viongozi wa dini, mila na watu maarufu ili jamii iache kutenda makosa hayo. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatoa wito kwa jamii yote kushirikiana kutokomeza matukio ya uhalifu hapa nchini yakiwemo ubakaji kwani yanasababisha athari kubwa kwa jamii, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga mabwawa katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maji katika Wilaya ya Mbulu Vijijini kwa lengo la kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji. Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, ujenzi wa miradi ya maji ya visima virefu kwenye vijiji vya Ng’orati, Maretadu Juu, Labay, Genda, Masqaroda, Mewadani, miradi ya maji ya Singu na ukarabati wa visima katika vijiji vya Domanga, Eshkesh unaendelea. Miradi hiyo itakamilika Septemba, 2022 na itaboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Mbulu Vijijini kutoka asilimia 61 hadi kufikia asilimia 76 ifikapo Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mabwawa hasa katika maeneo kame unalenga kukusanya maji yaweze kutumika wakati wa kiangazi ili kuhakikisha shughuli za kilimo na ufugaji zinaimarika.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaendelea kuainisha maeneo ya ujenzi wa malambo na mabwawa madogo katika Wilaya ya Mbulu Vijijini ili kukusanya maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya Haydom kwenda Mogitu - Katesh itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Wizara kupitia TANROADS tayari imeingia mkataba na mhandisi mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kufanya tathmini ya athari za kimazingira na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Haydom – Katesh yenye urefu wa kilometa 70. Kazi ya Usanifu imeanza mwezi Februari, 2023 na inategemewa kukamilika mwezi Februari, 2024. Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa Vituo vya Afya Geterer na Masieda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na umaliziaji wa maboma ya Vituo vya Afya kote nchini. Serikali itapeleka shilingi milioni 800 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Masieda na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kituo hicho. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Markad.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa Vituo vya Afya ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa Kituo cha Afya Geterer kwa kadri fedha inavyopatikana.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA K.n.y. MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupeleka mbegu za mahindi kabla ya kipindi cha masika katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa kuwafikishia wakulima pembejeo za kilimo kwa wakati ikiwemo mbegu bora za mahindi katika Jimbo la Mbulu Vijijini na maeneo mengine nchini unahusisha kukusanya takwimu za mahitaji halisi na kuratibu usambazaji wa pembejeo hizo kupitia sekta ya umma na sekta binafsi kabla ya msimu wa kilimo kuanza.

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2022/2023 na mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ambayo ni Taasisi ya Serikali imeendelea kusambaza mbegu bora za mahindi katika maeneo mbalimbali kwa bei nafuu ambayo ina ruzuku ndani yake. Ninaomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuzishauri Halmashauri za Wilaya ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kutenga fedha zitakazowezesha kuendelea kununua mbegu za mahindi pamoja na mbegu za mazao mengine kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ambao huuza mbegu kwa bei nafuu zaidi.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, ni lini minara ya simu itajengwa maeneo ya Endahagichang, Tumati Juu, Qalodaginwe, Aidurdagawa, Qamtananat na Migwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Endahagichang imeingizwa katika mpango wa kufikisha huduma ya mawasiliano kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, ambapo vijiji vitakavyonufaika ni Endadubu, Miqaw na Endahagichan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafanya tathmini katika maeneo mapya yaliyowasilishwa na Mheshimiwa Mbunge ambayo ni Tumati Juu, Qalodaginwe, Aidurdagawa, Qamtananat na Miqaw ili kubaini changamoto za huduma za mawasiliano zilizopo.