Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Flatei Gregory Massay (42 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na afya tele. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kwa kunileta humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze kabisa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa, nami nimeisoma mwanzo mwisho. Nasema mimi nitakuwa wa kwanza na naendelea kuwa wa kwanza kumuombea aishi maisha marefu, awe na afya njema lakini pili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri na mimi nitamsaidia kwa asilimia mia moja kwenye eneo ninalohusika kule Jimboni kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana na yeye mwenyewe kumtegemea Mungu kwenye kazi zake ambazo wananchi wa Jimbo langu wanaziona na watu wa Mungu wengi tunamuombea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie maeneo machache hasa kwenye ukusanyaji wa kodi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha makucha yake kwenye eneo ambalo linaonekana kuna tatizo la ukusanyaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo ambalo kimsingi naomba niliseme hapa leo kuhusu barabara au miundombinu. Kule kwetu Mbulu ni Wilaya iliyoanza tangu mwaka 1905 lakini hatujawahi kabisa kuiona barabara ya lami. Ukitaka kumfundisha mtoto leo kuhusu barabara walimu wanapata shida, ni lazima amtoe mtoto nje ya Wilaya ampeleke Babati au Karatu ili kuweza kuona mfano wa barabara ya lami. Namshukuru Mungu barabara hii ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu. Kwa kuwa Rais ameiahidi barabara hii, niombe sana Wizara hii ya Miundombinu iiangalie maana barabara hii ni muhimu sana kwetu ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na mkoa wetu, kutoka Karatu – Mbulu, Mbulu- Hydom, Hydom –Singida, kilomita 180 zimeandikwa pale. Namuona Mama Nagu akiniambia eleza na ile ya kwangu, mama nitafika huko. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni inayotoka Babati - Dongobesh pale kuna kilomita 63. Bila kuisahau barabara ya Mbuyu wa Mjerumani, Magara kufika Mbulu Mjini na hii ya Hanang kuja Hydom. Tukipata barabara hizi zitatusaidia sisi ambao ni wakulima wa vitunguu pale Mbulu Bashay. Vitunguu hakika vina soko maeneo mengi na eneo maarufu ni pale kwetu Bashay ambapo vitunguu vile zinauzwa maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Zanzibar na Uarabuni. Barabara hii itasaidia sana kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo yale na kupunguza pia umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, pamoja na ahadi kubwa ambayo tumepewa mara nyingi na Mheshimiwa Rais wetu wa awamu uliyopita lakini naamini kabisa Mheshimiwa Rais huyu wa Awamu ya Tano ambaye leo nampongeza hapa kutokana na hotuba yake, yako mabwawa makubwa ambayo yamejengwa pale Dongobesh. Naamini ahadi aliyotoa siku ya kampeni pale Dongobesh ataitekeleza. Kwa nini nasema hivyo? Kilimo chetu sasa kimeingiwa na ukakasi wa ukame lakini tukipata namna ya kutengeneza mabwawa na kuyakinga maji yanayopotea hasa kipindi hiki cha mvua nyingi, mabwawa haya yakiwa tayari yanaweza kusaidia sana kilimo cha umwagiliaji na tukavuna mara mbili kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwaa Mwenyeki, najua eneo langu la Mbulu Vijijini, hakika lina changamoto nyingi. Changamoto ya maji ni kubwa mno. Nashukuru Mheshimiwa Rais ameahidi kupatikana kwa maji katika Mji Mdogo wa Hydom, Dongobesh, Bashay na maeneo mengi ya Laabay. Nina hakika nchi nzima tuna tatizo la maji lakini nafikiri Waziri amekwishakuniahidi miradi iliyotengenezwa au iliyofadhiliwa na World Bank ambayo imesimama katika maeneo hayo itafanyiwa kazi. Mbulu tunahitaji shilingi bilioni tatu tu ili kuweza kumaliza miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna tatizo moja kubwa mno nalo ni umeme vijijini. Mimi nasimama hapa naweza kuwa ni Mbunge wa sita Wilayani Mbulu Vijijini lakini tangu zamani mpaka leo tuna kata tatu tu ambazo zimeweza kupata umeme. Tumeleta maombi na Mheshimiwa Waziri Muhongo ni jembe na nimeongea naye na napenda kumhakikishia atakapofika kule nitamtembeza maeneo mengi sana. Kwa kuwa najua wewe ni jembe utafika maeneo hayo na nakukaribisha sana maeneo ya Maretadu, Tumat, Bashay, Maseli na naeneo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wangu umekuwa mdogo, naomba sasa nishukuru hasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, dada yangu Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama. Juzi wananchi wangu walipata njaa hasa Wahadzabe wa Eda Chini, umewasaidia tani 400, zimekwenda kule, zimesaidia Wilaya nzima, nakushukuru sana, hili lazima niliseme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sitendi haki kama sijasema jambo linaloniuma moyoni. Mwenge wa Uhuru ni jambo imara sana. Mwenge huu aliuanzisha Baba wa Taifa, ni ishara kubwa sana na una maudhui ya kutosha. Mimi kama nisingekimbiza mwenge nisingewajua watu kutoka Zanzibar, tusingekuwa na umoja, nimefahamu nchi hii kwa vile nilitembea sana na mwenge. Nasikitika sana kusikia watu wanasema tuufute mwenge. Kama tatizo ni gharama tutafute namna nzuri ya kuupeleka mwenge bila gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana mwenge umewekwa katika maeneo mengi ya nchi hii na kuna siri kubwa. Viongozi wa majeshi yote nchini wale wenye wenye vyeo vikubwa, vyeo vyao vina alama ya mwenge. Hata motto wa Mheshimiwa Rais wetu wa Hapa Kazi Tu kuna alama ya mwenge. Leo unafutaje kiholela namna hii jambo ambalo Baba wa Taifa amelianzisha?
Mimi nisingewafahamu akina Mwashibanda, Vuai wa kule Zanzibar ni kutokana na kutembea na mwenge. Mwenge unaleta umoja, amani na unamulika mafisadi. (Makofi)
Namuomba Mheshimiwa Rais auongezee nguvu Mwenge wa Uhuru ili uweze kufanya yale ambayo yametokea wakati sijazaliwa, ing‟oe mafisadi, ilete amani na imulike hata nje ya mipaka yetu kama inavyofanywa na ilete tumaini mahali ambako tumaini halimo. Najua wengi watapiga vita sana jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala moja tu, ninaomba niishauri Serikali hii inayoingia sasa tunayo manpower Tanzania yaani idadi kubwa ya watu, China wanatumia idadi yao kubwa kuzalisha. Sisi inabidi kwa kweli Serikali ilete sheria hapa Bungeni, zamani kulikuwa na kitu, watu wanakamatwa wanapelekwa sehemu ambayo nilikuwa siijui, nimepata kwenye historia ya Gezaulole sijui ni wapi huko! Vijana wanaokutwa wanahangaika wanapelekwa Gezaulole, leo vijana wengi tunacheza pool kuanzia asubuhi, bao na karata. Ni lazima kutumia nguvu yetu kuzalisha uchumi kama wa China ili uweze kuendelea na uchumi huu uweze kutusaidia sisi vijana tunaokua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kabisa hotuba hii na kumpongeza na Mheshimiwa Rais, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii lakini pia namshukuru Mungu sana kwa kupata afya nzuri ya kusema hapa sasa. Kwanza nianze kushukuru sana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwa nini nasema haya? Kimsingi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu wake kwa kufanya kazi hii ambayo imekuwa kero sana kwa wananchi wetu hasa kwenye migogoro ya ardhi. Mheshimiwa Lukuvi amejitahidi sana kwa kweli kama wachangiaji waliotangulia walivyosema, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake binafsi zinazoonekana na Wizara yake kwa ujumla kuonesha moyo dhahiri kabisa wa kutatua matatizo ya ardhi; hasa amefika kule kwetu Mbulu, alisaidia Halmashauri ya Mji kwa kweli kurudishiwa ardhi yake na amesaidia kwenye Bonde la Yaeda Chini kutatua mgogoro ulioko pale ambao nimeuona pia ameuandika katika kitabu chake hiki cha migogoro kwenye ukurasa wa 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kwamba kwa kuwa sasa Sheria ya Ardhi inataka watu wengi au majority kupiga kura ili kutoa adhi, lakini kuna maeneo mengine wapo watu ambao ni minority, naomba wale pia wazingatiwe. Kwa mfano, kwenye eneo letu kule kuna watu wanaoitwa Wahadzabe; wale mara nyingi wanakula kwa kufanya kitu kinachoitwa uwindaji. Kwa hiyo, wana tabia ya kuhama na kurudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba waangaliwe, kwani ardhi yao katika lile bonde ni ndogo sana. Nashukuru kwanza kwa kufanya hatua ile, lakini angalau wale watu wawe considered katika ardhi ambayo kimsingi iko kule ambayo ni eneo pekee katika maeneo ambayo wanayo katika Mbuga ile ya Yaeda Chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, amezungumza Mbunge mwenzangu wa Mjini, kama kuna maeneo yenye migogoro Tanzania hasa ya ardhi, nafikiri ni kule kwetu Mbulu. Namshukuru Waziri kwa kweli kwa kutusaidia na kutuambia kwamba yuko tayari sasa kuja kuanzisha Baraza la Ardhi ambalo litafanyika kule kwetu Mbulu. Nami nimwambie kabisa, jana Jumapili nilikuwa nyumbani, wamekubali, wameshapanga majengo ya kumpa kuanzisha Baraza la Ardhi na Halmashauri imeshamwandikia barua, nafikiri ataipata na nafikiri mwenzangu amezungumza, sina sababu ya kuendelea na hilo, lakini nakushukuru sana, Mungu ambariki kwa sababu kwa kweli akileta maendeleo yale ya kusikiliza kero za wananchi kwa haraka, migogoro yote itakuwa rahisi kutatulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kuishauri Wizara hasa katika upimaji wa ardhi. Ili kuondoa migogoro, ni vyema basi Wizara ikajielekeza kuipima ardhi hasa ardhi yote ya Tanzania, pawe na Land Bank ambayo itaondoa kitu kinachoitwa migogoro mingi. Ardhi ya Tanzania ikipimwa ni rahisi kuondoa migogoro; tutaelewa kabisa huu ni mwisho na mpaka wa mji na hapa panaelekea kuwa kwa wafugaji na hapa ni wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi yetu ikipimwa, kwa sababu sasa hivi kuna GPS, kwa hiyo, ni rahisi sasa kutumia GPS, kwa mfano ile ya Tume ya Uchaguzi, hivyo, ni rahisi sana kupima ardhi yote ya Tanzania. Ardhi ile ikipimwa ni rahisi pia kujua nani anaishia wapi, migogoro mingi itapungua kwa ajili hii. Kwa hiyo, naishauri Wizara yetu hii ya ardhi, pamoja na kazi nzuri inayofanya, ipime ardhi hizi na ardhi ikishapimwa basi, inaweza kutatua migogoro kwa wingi sana kila mtu akijua mipaka yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie jambo la utaratibu wa kupata hatimiliki. Naiomba Wizara ifupishe kidogo utaratibu au iende kasi ya upatikanaji wa hatimiliki kwa wananchi wetu. Maana sasa hivi ukitaka kupata hatimiliki, kwa kweli unatumia utaratibu mrefu sana mpaka kuipata hati hii. Kupata wapimaji kwenye maeneo yetu ni kazi. Kwa mfano, katika Mkoa wa Manyara hasa Wilaya ya Mbulu, hatuna wapima ardhi, kwa hiyo, inachukua muda mwingi sana mpaka mtu apate hatimiliki ya kiwanja chake ili aweze kukiendeleza au kuombea mkopo au kufanyia maendeleo fulani. Nashauri haya, basi Wizara ijitahidi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna jambo lingine ambalo napenda kulieleza. Kuna upimaji wa miji na upimaji wa miji midogo. Niombe sasa Wizara ijikite na ielekeze namna nzuri ya upimaji wa miji. Miji ikipimwa; kwa mfano, miji midogo ikipimwa na miji ikapimwa itakuwa rahisi sasa matumizi bora ya ardhi kufanyika. Sasa hivi maeneo mengi yanavunjwa kwa sababu hatuna plan management ya ardhi katika miji yetu midogo na mikubwa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ijikite katika hali hii ya kupima miji yetu ili pawe na plan ya mji wowote unaoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwetu kuna Miji ya Haidom ambao sasa tumeuombea kuwa mji na Mji wa Dongobesh ambao unazidi kuwa mji na Mji wa Mbulu ambao kimsingi ni wa siku nyingi, lakini una ramani nyingi ambazo nashukuru Mheshimiwa Waziri alipokuja alisema kabisa kwamba atatusaidia kutupatia mpima atakayesaidia kupima ule Mji wa Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa miji hii midogo ambayo sasa inakua, ufanyike upimaji mahususi wa mwanzo na miji mingine Tanzania ili migogoro isiwepo kwa sababu Maafisa wengi wa ardhi wanapata shida. Maeneo mengi hasa ya makorongo, maeneo ya kutoa maji yanaleta shida sana katika maeneo haya, kama ardhi isipopimwa hasa kwenye miji hii ambayo tunategemea kuwa miji mikubwa baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hela ambazo zinaitwa retention ambazo kimsingi Halmashauri zinakusanya kama maduhuli na zinakuja Wizarani, basi Wizara ihakikishe zile hela zinarudishwa kule ili Halmashauri zetu ziweze kujiendesha kwa kutumia hela za retention ambazo Serikali kuu inakusanya kupitia Hamashauri zetu. Maana Halmashauri zetu pia hicho ni chanzo cha pato na ni pato mojawapo ambalo likirudishwa kule kwa haraka basi, Halmashauri zinaweza kujiendeleza, zikaendelea kufanya mpango wa upimaji katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kujielekeza kwenye habari hii ya nyumba zenye bei nafuu. Tumeona mpango mzuri wa Mheshimiwa Waziri; kwanza nampongeza sana. Nina Bag hapa, yuko mchangiaji alisema hapa, sitaki kumtaja jina, anasema Wizara haikujipanga. Wizara imejipanga. Nimelisoma hili Bag! Yaliyomo humu ukiyasoma kama Mbunge ukayaona yalivyokuwa yanaelekeza, ni rahisi kuona kuwa Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wamejipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko Sheria za Ardhi huku, tukasome tuelewe tuwasaidie wananchi wetu ili waelewe. Sisi kama Wabunge tunaweza kuwa rahisi kuwaelekeza wananchi, kuwafundisha katika maeneo ili angalau waweze kuondoa migogoro. Hiyo itakuwa ni rahisi kuliko kulaumu kwamba Serikali haijajipanga. Serikali imejipanga, wametuletea mambo yako humu, migogoro imepangwa, Mheshimiwa Waziri ameandika nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Serikali tusaidie sasa kueleza wananchi wetu ile namna bora, maana hakuna Serikali mahali popote duniani inayoweza kufanya kazi kwa upande mmoja tu. Ni lazima upande mwingine wa sisi Wawakilishi tufanye kazi ya kuelimisha watu wetu ili migogoro hii nayo ipungue tufikie katika hali ambayo itasaidia Wizara na Serikali kwa ujumla, maana Serikali tu haiwezi kutatua migogoro kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro pia inatatuliwa na Wanasiasa ambao ni sisi wenyewe. Nasi Wanasiasa yaani Wabunge na wengine wanaotusikia wanaochaguliwa, tusaidie kuelekeza watu ili wasiwe wa kwanza kuvunja sheria. Maana tukianza kuvunja sheria, tutakuwa wa kwanza kuilaumu Serikali, kwa sababu mpaka Serikali ije inatumia muda mwingi na gharama nyingi, watu wengi wamefariki, wamepoteza maisha kwa migogoro hii ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia, Serikali kwa upande mwingine ijitahidi. Wakuu wa Wilaya; namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, anatatua migogoro kwa kuiona mwenyewe physically. Natoa rai yangu kwa Wakuu wa Wilaya wa maeneo mengine, Wenyeviti wa Vijiji, ni tatizo. Inafika mahali wako Matajiri wanaotaka ardhi kwa muda mwingi, lakini inafika mahali wakipewa kitu kidogo, yaani rushwa wanachanganyikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufika mwenyewe na hadanganywi. Hadanganywi kwa sababu anaiona ile migogoro inavyokwenda, anaona jinsi ya uhaulishaji wa ardhi na wakati huo basi anafika mahali anaweza kustopisha zile ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, lakini naomba pia, amalizie ile migogoro ambayo kimsingi iko Manyara na Mbulu. Naamini Mungu atamsaidia, atakuja tena. Najua Tanzania ni kubwa na lazima tuongee worldwide.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naipongeza Wizara, pia naunga mkono hoja hii. Nakuachia pia muda uendelee na Mungu akubariki sana. ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia Mpango huu au Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya mwakani yaani 2017/2018 ni vema sasa tukafika mahali tukaongea uhalisia ambao utatupeleka katika maendeleo ya kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri sana Mpango huu, unaonekana kwa kweli ni mzuri, lakini mimi nina walakini kwa kuangalia mipango ambayo ipo na imeandikwa hapa hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda vidogo vidogo. Pia kuna mipango mikakati ambayo imeelezwa hapa katika mpango huu ambayo kimsingi nimekuwa nikisikia mimi kabla sijawa Mbunge na sasa nimeingia humu bado naendelea kuisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna mpango huu kwa miradi hii ya Kinyerezi, mipango hii ya Special Economic Zone, ni kweli Tanzania tunahitaji umeme na tunaona maeneo mengi yana ukosefu wa umeme. Lakini tunaona kabisa hapa mpango huu unaonesha kwamba utakuwa na faida ya kuongeza megawati 600, lakini tumekuwa na mipango mingi hatuoni utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia miradi hii ambayo imeoneshwa kwenye mpango wa Serikali hapa, vituo vya biashara vya Kurasini imekuwa ikisemwa muda mwingi, lakini sasa ukiangalia fidia imeshatolewa na mamilioni yako hapa yanaoneka sitaki kuingia in detail, lakini hoja yangu ni hii tu Serikali imeshaweka fedha nyingi hapa sasa na muda unaanza kwenda, ituambie basi ni lini inaanzisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina wasiwasi unaweza ukabeba mpango huu ukaelekea tena mwakani kwa sababu naamini kwenye mpango uliopita ulikuwepo, Kurasini, Kinyerezi, viwanda vidogo vidogo ambavyo vimekuwa vikielezwa hapa na hii SEZ, tunapiga maswali kwa wale wengine ambao tunakaa mbali na maeneo haya. Umeme tunahitaji kweli, viwanda tunahitaji kweli lakini ni lini sasa unaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila tunapoona mipango tunategemea kwamba Serikali itakwenda kuifanya, tunaposoma vitabu hivi tunaamini kabisa mipango hii ya Serikali inakwenda kutekelezwa, lakini kinachotutia kichefuchefu ni kwamba tuna tatizo moja hapa kwetu la kutenda, tunatenda lini? Maamuzi tunayafanya lakini wakati wa kwenda kutenda hapo ndio tunaanza kuona danadana, leo, kesho, kesho kutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vizuri upande wa kilimo unaona kabisa mipango mizuri, ipo katika vitabu vyetu hivi na unaisoma vizuri sana, kwa mfano ukiangalia mpango wa kilimo umeiandika vizuri sana Mheshimiwa Mpango, je, wakati wa kwenda kutekeleza tunatekeleza kama tulivyoandika? Hilo ndilo tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia kwa uhalisia wa mwaka huu, tunaposema tunakwenda kusaidia sekta ya kilimo wananchi wetu wanajua tunakwenda kweli kusaidia tukiwa tumeamua kwa sababu mpango huu umeelezwa humo, na Wabunge kazi yetu kubwa ni kuishauri Serikali, hapa tunaposhauri naomba ushauri huu uchukuliwe, na ukafanyiwe kazi wakati tumeamua kushauri, kwa sababu sisi ni Bunge na wao ni Serikali tunaamini ya kwamba tunafanya kazi katika three pillars of the one government (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tufanye kazi moja rahisi tu, tunapoingia huku tunaingia kama tuna vyama, lakini tunapokuja huku tunawakilisha wale wasiokuwa na vyama, na wale wenye vyama. Mimi naomba lingine niwashauri ndugu zetu wa upinzani mara chache tunapoingia humu, tunaanza kukashifiana kwa lugha ambazo sio nzuri, hizi lugha zinatuondoa kwenye mood wa kuangalia fact issues ambazo zinafanya sisi Watanzania kule waone kwamba tumekuja huku kuwatetea. Tunapojadili habari hii kwa mfano kilimo sasa, hali halisi mpaka sasa hivi kwa sisi Wabunge tunaotoka maeneo ya kilimo hakuna pembejeo, hakuna ruzuku sijui ni lini tutapata. Sasa tukianza kuongea hatuna maana ya kusema jambo lolote mbadala na hili, ni hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo kwa mfano, mimi kule nategemea kilimo, tunategemea mifugo, pembejeo za kilimo hazipo, Serikali imekwisha kuahidi, Mheshimiwa Rais alikwisha kusema je, hebu tuambiane mpango huu unaeleza pia, kuna fedha imetengwa, je tunapatiwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi mvua zimeaza kunyesha je, hizi pembejeo tutakapopeleka baada ya mvua kunyesha; kwa mfano ukipeleka mahindi au ruzuku yeyote na pembejeo hizo, mbolea wakati msimu umeshapita unampelekea nani? Je, tukipata mwezi wa pili inafaa kupikiwa kande? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba tu tufike mahali tuende kwenye uhalisia wenyewe, lakini hata mkulima huyu, ukiangalia takwimu zinaonesha asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, angalia leo kilimo hiki hakimsaidii na leo kuna maswali mengi yameulizwa asubuhi kuhusu kilimo na hali inaonekana kabisa kilimo ndiyo tegemeo. Lakini ukiangalia miradi yote ya umwagiliaji imesimama tatizo ni hela hakuna, hapa imeandikwa vizuri sana, sasa nina-declare tunafanyaje ili kuisaidia nchi yetu kama tunashauri halafu yale ambayo tunashauri hayatekelezwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali yetu tunaipenda sana ninaona kabisa jitihada za Waziri, naona jitihada za Rais, naziona kabisa jitihada zinazofanyika, tukafanye kazi ya kufanya kazi ambayo tumeamua kuifanya kweli. Angalia wakulima sasa hivi wamechoka, sisi vijana ambao tumekuja kuwatetea vijana tumeanzisha SACCOS zetu kule lakini utaangalia nimshauri sana ndugu yangu Waziri Mpango, kuna kodi ambayo imeanza kuua katika maeneo yetu kule. Kodi hii inaenda kuwalenga wakulima wadogo wadogo wanaochajiwa VAT, tumeanzisha SACCOS, AMCOS katika maeneo yetu kule, lakini kodi hii ukiangalia ndiyo kodi ambayo Mheshimiwa Rais amesema kodi kero tuondoe. Hivi leo mkulima mmoja mmoja anadaiwa zuio la kodi hii haistahili na hii siyo sahihi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iangalie maeneo ya kuweka kodi na maeneo ambayo hayapaswi kuwekwa kodi. Tuliingia huku tukisema habari ya kodi kwa watalii kwenye maeneo yetu ya kule, lakini tazama leo tunaona athari zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu wakati mwingine tunaposhauri kama Wabunge Serikali ichukue ule ushauri ikaufanyie kazi, bahati nzuri Tanzania tuna wasomi leo, tufanye research tuone kabisa je haya tunayoshauriwa na Waheshimiwa Wabunge ndiyo hasa yale ambayo wanaona kwa ushauri wao na kama wanakataa wakatae kwa hoja na sisi tunapoeleza tunaeleza kwa hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye suala la miundombinu imeelezwa hapa, uboreshaji wa miundombinu, imeelezwa habari ya ATCL, imeelezwa habari ya TAZARA, imeelezwa habari ya ndege na yameelezwa mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine naangalia ninapoingia huku kule maeneo ya kwetu hatuwezi kukutana na hiyo ATCL, hatuwezi kukutana na hiyo TAZARA, hatuwezi kukutana na meli kwa sababu hatuna maziwa, hatuwezi kukutana na chochote ambacho mnasema, standard gauge ndio kabisa huku kwetu haipiti, sina maana ya kujitenga katika Tanzania, lakini nina maana ya kuuliza swali moja tu kama hamtatusaidia sisi barabara zetu zikaonekana kwenye huu mpango tutakuwa tumeingia kufanya nini huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa maeneo ya pembezoni tuangaliwe kama tunagawa rasilimali ya nchi hii tuigawe kwa usawa, haiwezekani maeneo fulani yanaonekana miradi mikubwa imeenda huko na maeneo fulani yamenyimwa kabisa. Ninajua wazi kwamba tutafaidi wote lakini tufaidi basi hata barabara. Sisi kwa Mikoa yetu ya Kaskazini ukiacha barabara hatuna kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine napenda kuishauri Serikali, hasa hili la mabenki ambayo kwa kweli sasa hivi tunaona crisis imetokea mimi sio mtaalamu wa uchumi lakini katika study yangu nime-study kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia tumekuwa tukishauri hapa habari ya vyanzo vya mapato, tunapenda sana kukusanya mapato, lakini naomba nishauri Serikali iangalie hii habari ya kukopa ndani ya nchi Serikali iangalie kwa sababu kuna fursa ya kukopa nje, kwa nini Serikali isitumie nafasi hii ambayo inayo ya kukopa nje ya nchi kuliko ndani kwenye mashirika ya kwake yenyewe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie basi kwa sababu ninaamini kwamba Serikali ina nafasi ya kukopa nje, Serikali inaweza kufanya jambo lingine ione kama kukopa ndani na kukopa nje ipi nafuu. Lakini kwa sababu nimesikia kengele ya mwisho niseme kidogo katika suala la fluctuation hili suala la kufanya fixing rating. Tufanye utafiti wa kweli, tunaweza kuangalia tukaishauri Serikali ikaamua kubadilisha mtindo wa sasa wa kuangalia soko la dunia katika upandaji wa dola na kushuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali moja tukiamua kubadilisha mfumo huo, je, Benki Kuu ya Tanzania inaweza kweli kuhimili mapigo ya kushuka kwa uchumi hasa inaposhuka itapata wapi fedha ya kufidia ile sehemu na ile gape? Kwa hiyo, naomba Wizara ijipange, Serikali iangalie kama imekuwa tayari kweli kuingia katika mtindo huu, ikiingia hapa lazima nayo Benki Kuu imejiandaa katika kuziba gape la kiuchumi, vinginevyo uchumi wa dunia ukishuka, Tanzania hatupo nje ya dunia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba kuchangia hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa afya ya kusimama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, naomba kwanza niipongeze Wizara hii hasa Mawaziri hawa Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kufanya kazi hii kubwa na pia nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Labda niseme pia kwa nini natoa pongezi hizi, Makatibu hawa kweli wapo wawili lakini naamini wanafanya kazi kwa umoja wao. Wizara hii imefika kule kwetu ambako kimsingi ni Mbulu Vijijini, wamefika kwenye hospitali ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukiiomba ipandishwe hadhi kuwa hospitali ya Kanda, Hospitali ya Rufaa ya Lutheran ya Haydom. Kwa sababu hii basi kwa kweli napenda kuwashukuru na wananchi wangu waliniambia nikifika hapa cha kwanza niishukuru Wizara hii kwa kufika pale na kuangalia changamoto za Hospitali ya Haydom. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Nasema haya pia kwa sababu nataka kuleta ombi kwenye Wizara hii tena kwa ajili ya wananchi hawa wa Wilaya ya Mbulu ambao pia Hospitali ya Haydom inazungukwa na inatoa huduma kwa maeneo mengi na mikoa mingi ambayo kimsingi inategemea hospitali hiyo. Kwa hiyo, kwa kuwa hospitali hii inategemewa na mikoa mingi hasa Mkoa wa Singida wanaitegemea Hospitali ya Haydom, Mkoa wa Arusha, Mkoa huu wa Dodoma, Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mara, niiombe Wizara iendelee kufanya process ya kutosha ili kwa haraka na wakati ufaao tuweze kuipandisha hadhi Hospitali ya Haydom iwe Hospitali ya Kikanda ili iweze kupata msaada kutoka Serikalini wa kuweza kuhudumia maeneo haya yote niliyoyataja. Wako Wabunge hapa wanasikia ninayoyasema, naamini wanakubaliana nami hospitali hii inatibu wananchi wetu wa maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hotuba ya Waziri ameitaja Hospitali ya Haydom katika ukurasa ule wa 19 kwamba iko kwenye ngazi ya Mkoa, ni kweli. Kwa nini nazungumzia sana hospitali hii? Tatizo lililopo pale katika mkoa wetu, tunayo pia Hospitali ya Mkoa wa Manyara ambayo kimsingi RAS anapoomba maduhuli kwa sababu ya kuisaidia hospitali hii, hawezi kuomba bajeti mbili na kuiombea Hospitali ya Haydom ambayo kimsingi ipo kwenye level moja na hospitali hiyo ya mkoa na hii ya Haydom bado ipo kwenye level ya mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tunasubiri ujio wake Haydom na watu wanakusikia na ameniahidi atafika Haydom. Namkaribisha sana ili aone juhudi za wale watu wa Haydom tunavyofanya kazi ya kuisaidia hospitali hiyo, karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, lipo tatizo ambalo naamini wengi wetu tumesema, tatizo la watumishi. Hili nafikiri ni tatizo la kimfumo hasa kwenye suala la ajira na nani wa kuwasimamia. Wako watumishi wengine wanasimamiwa na halmashauri, wako wengine wanaajiriwa na RAS na wako wengine wanaajiriwa na Wizara. Sasa tuombe itafutwe namna rahisi na nzuri ya kuweza kufanya watumishi hawa wawe na mtu mmoja anayeweza kuwasimamia kwa sababu umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikufichi, ukitaka kumtuma mbwa muache aende na awe na mtu mmoja wa kumpigia miruzi. Ukimtuma mbwa akatafute mawindo huo ni mfano tu, ukishampigia miruzi na miruzi mingi humpoteza mbwa. Sifananishi hawa wataalam wetu kama mbwa hapana, nina maana kwamba anayepokea order apokee kwa mtu mmoja na hali hii itakuwa nzuri na Wizara yetu ya Afya itaweza kuwa na miguu na watakuwa na ari ya kufanya kazi na kazi hiyo wataifanya kwa uaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo lingine la kusema kuhusu call allowance za hawa watumishi wa Wizara ya Afya. Ukiangalia sasa hivi inavyosadikika na inavyosemekana watumishi hawa wanakatwa kodi kwenye call allowance hasa hawa wa private sectors. Kwa hiyo, niombe kama kuna namna yoyote iangaliwe vizuri na kwa sababu sasa hivi Mheshimiwa Rais ameshaamua kuteremsha kiwango kile cha kodi katika mshahara basi tuangalie kwa kina namna gani ya kupunguza basi tozo linalokatwa katika call allowance hasa kwa hizi sekta binafsi. Naomba sana Wizara iangalie sehemu hizi, hizi allowance wanazopewa kwanza ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye bajeti mwaka huu inaonekana hapatakuwa na hizi call allowance za kutosha. Kwa hiyo, niombe basi kwa hizi sekta binafsi ambazo zinawapa wale watumishi wao zile call allowance tuangalie vizuri namna ya kuzikatia kodi. Kwa sasa hivi takwimu zinaonesha wanakatiwa kodi kwa asilimia 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuone namna ya kupunguza zile asilimia ili ile call allowance yule mtu anapomuacha mke wake, kwa mfano Nesi au Daktari anapoitwa usiku, anaacha familia yake, anakwenda kumtibu mgonjwa. Sasa anapopewa zile fedha hizo allowance halafu baadaye inakatwa kodi kubwa kwa asilimia 30, nafikiri siyo sahihi. Tuone ni namna gani ya kuwa-encourage hawa watu hasa wanaohusika na kuzihudumia roho zetu. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie pia sehemu hii kwa umakini na kwa jicho kali kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu bima ya afya. Mimi ni mdau mzuri na napenda sana bima ya afya kwa sababu inasaidia wale wanyonge kupata matibabu kwa urahisi. Hata hivyo, bima ya afya iendane pia na upatikanaji wa dawa. Yupo mzungumzaji mmoja amesema kwamba bajeti ya dawa ni ndogo, nimetazama Fungu 52 na nakiri kwa kweli ni ndogo. Nawashawishi Wabunge wenzangu na nawahamasisha tufanye namna yoyote ile, piga ua galagaza, tuisaidie Wizara hii ipate fungu lingine au sijui tufanyaje, tu re-budget ili tuone kwamba tunalipangia hili eneo la dawa pesa zaidi maana uhai ndiyo unaotakiwa katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda wangu haujakwisha, nimeona pia Wizara hii inakwenda na Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Maendeleo ya Jamii ni Wizara pekee, sisi tumesomea huko, tumechukua digrii zetu huko na wengine tunaendelea kusoma huko. Tukiangalia miundombinu ya hivi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ni mibaya, haifai na ukiangalia kwenye bajeti yetu hapa hasa bajeti ya maendeleo ina zero. Hakika kama tumeshindwa kuvifanya vyuo hivi vikawa ndani ya Wizara hii ya Afya basi tuitengee Wizara! Maana maendeleo ya jamii ndiyo community base ya kuwasaidia watu wetu, wanapomaliza hivi vyuo wanakwenda kuwasaidia wananchi wetu kuwajengea uwezo, kubuni miradi, kuendeleza miradi iwe sustainable.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Chuo cha TICD - Tengeru kimekuwa pale tangu mwaka 1963 kabla ya Muungano, leo hii kuna lami tangu mkoloni pale haijawahi kufanyiwa rebuilding yoyote, hakina maabara, maabara imeanza kujengwa pale miaka tisa haijawahi kumalizika. Mheshimiwa Waziri wa Afya alishakuwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Kwa hiyo, niwaombe kabisa mtembelee chuo kile, mkisaidie na muone namna gani special ya kusaidia vyuo hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye vyuo hivi vya FDC wako walimu wanafundisha lakini mishahara yao ni midogo wakati wana elimu sawasawa na walimu wa vyuo vikuu. Kwa hiyo, naomba muangalie walipwe kutokana na elimu zao maana sasa hivi wanalipwa sawasawa na walimu wa sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wangu umekwisha, basi niombe kabisa kabisa, Mheshimiwa Waziri FDC ndiyo ngome, hawa ndiyo CDO wa kutosha katika nchi hii, ni viraka maana yake anaweza kufanya kazi yoyote, uwasaidie kwa namna yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini kwa consideration ya haya niliyoyasema. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijasahau na muda haujakwisha nipongeze hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kweli imelenga kila mahali na kwa mimi mwenyewe nimekosheka kwa maana ya kwamba imegusa maeneo mengi sana. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwanza kwa kasi aliyoanza nayo na pia kwa kazi anayofanya, kwa kweli maarufu sana kwa kutumbua majipu. Sisi wanyonge na maeneo ambayo kimsingi tulikuwa tumesahaulika sasa tunaanza kupata ahueni ya kupata maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Mawaziri ambao wamekuja kwenye Jimbo letu la Mbulu ambalo lilisahaulika kwa muda mrefu sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi, Waziri wa Ardhi kwa kusaidia kutatua matatizo au mgogoro wa ardhi ulioko katika Bonde la Yaeda Chini kule eneo la Wahadzabe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kuja kuisaidia Hospitali ya Haydom ili iweze kupandishwa kuwa Hospitali ya Kanda ambapo inaweza kuhudumia Mikoa yetu ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu na Meatu. Pamoja na pongezi hizi kwa kweli niwapongeze Mawaziri wote wanaofanya kazi na kwenye kasi hii ya hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa kweli naomba nizungumzie kwenye sekta ya miundombinu. Tunayo barabara moja kubwa sana kule Nyumbani ya Mbulu - Karatu- Haydom – Singida - Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu - Dareda-Dongobesh. Barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya mawasiliano ya Wilaya ya Mbulu Vijijini ili kukutana na Hanang na Katesh. Barabara hii inahitajika sana kwa wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Mbulu Mjini, Katesh, Babati, Mkalama na kwenye Majimbo ya Singida ili kupata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Haydom kwa sasa ni ya rufaa na ina wataalam wa kutosha barabara hii inahitajika sana ili iweze kufikiwa na watu wetu wa maeneo haya niliyoyazungumzia wapate tiba. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alinijibu kwenye swali langu nililouliza Bungeni Na.76, kwenye Bunge la Februari kwamba, ataweka kwenye Mpango ili barabara ile itengenezwe kwa kiwango cha lami, naomba kwa kweli azingatie hili ili wananchi wa Mbulu Vijijini na maeneo niliyoyataja waweze kupata mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo moja la kushauri Serikali. Kuna taasisi mbili za RITA na NIDA. Ili kubana matumizi, nadhani taasisi hizi mbili zinafanya kazi moja, kwa sababu RITA inasajili vizazi na vifo na NIDA hali kadhalika inafanya kazi hiyohiyo. Ni vyema basi ili kupunguza matumizi ikafanywa kuwa taasisi moja katika hali ya kubana matumizi ili Serikali ipeleke pesa kwenye maeneo mengine kwa ajili ya maendeleo. Huu ni ushauri wangu kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la umeme. Suala la umeme ni jambo ambalo limezungumziwa sana na Wabunge wengi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, Mbulu tangu kumekucha yaani imezaliwa 1905 sawa na Nairobi lakini kwa masikitiko yetu Mbulu umeme umepatikana mwanzoni mwa miaka ya 90 kwenye Kata moja ya Haydom lakini mpaka leo haujasogea kijiji hata kimoja. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwenye REA III tafadhali angalia sana Mbulu ili mtusaidie Mbulu tuondokane na tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata leo hii ukiwaambia wananchi wa Mbulu waangalie TV wataionea wapi, umeme katika kata 18, kata tatu tu ndiyo zina umeme. Kama Mheshimiwa Joseph Musukuma alivyosema, leo hii hata nikiongea hapa hawawezi kuniona labda wawashe jenereta. Naamini katika mpango wa Serikali na kasi hii, umeme utafika kwenye Vijiji vyetu vya Endadubu, Masieda, Endanyawish, Endanaichan na maeneo mengi ambayo kwa kweli hata nikiyasema leo naona kabisa napoteza wakati lakini nina hakika Mheshimiwa Waziri ananisikia na nimeshampelekea orodha ya Vijiji vya Mbulu ambavyo havijapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la mawasiliano. Kama unavyojua mawasiliano yanahitajika sana kwa ajili ya kuwasiliana na wananchi wetu. Sisi kule ni wakulima wa vitunguu swaumu ambavyo vinakwenda hata nje ya nchi kama vile Uarabuni na maeneo mengine mengi. Kule kwetu wamekuja watu kutoka Zanzibar kwa sababu biashara hii inauzika lakini tuna shida ya mitandao ya simu maeneo ya Tumati, Dongobesh, Maretadu na maeneo mengi hasa ya Masieda basi tungeomba Mheshimiwa Waziri aone maeneo haya hasa Kata ya Tumati kutupatia minara michache ili walau tuweze kuwasiliana na watu wetu. Mimi kama Mbunge wa Mbulu Vijijini nikitaka kuwasiliana na wananchi wangu kutoka hapa siwezi mpaka nifike manually niweze kuzungumza na watu wangu kule. Kwa hiyo, naomba sana Waziri wetu wa Ujenzi na Mawasiliano alione hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo la kushauri kuhusiana na suala la michezo. Mimi ni mwanamichezo, napenda ku-declare interest. Mbulu ni Wilaya ambayo ilikuwa inatoa wanamichezo wengi sana hasa maarufu ambao wamevunja historia na kuweka rekodi katika Olympic hasa kwa michezo ya riadha. Ndugu Filbert Bayi anatoka Mbulu, Gidamis Shahanga anatoka Mbulu, John Bura anatoka Mbulu, hawa wote wameweka rekodi ya dunia. Kwa hiyo, nishauri hivi vyama vya michezo viangalie wapi hasa historia ilipo ili viisaidie Tanzania iweze kujulikana Kimataifa kama ulivyokuwa miaka ya 70. Hii inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape ni rafiki yangu sana najua ananisikiliza katika hili. Kambi nyingi zimewekwa mijini, nature ya Mbulu inafanya vijana wengi waweze kujiingiza katika michezo na waweze hakika kuzinyemelea hizo medali, sasa hivi Tanzania ni vigumu sana kushinda katika jumuiya yoyote hata Olympic kwa sababu tu michezo mingi imewekwa mijini, mtukumbuke na kule. Wananchi na vijana wa Mbulu wamenituma niwaeleze hili ili muweke kambi kule, historia ya akina Filbert Bayi haijavunjwa mpaka leo, rekodi yake ya dunia iko pale. Ni vema tutafute na kuinua vipaji vya kina Filbert Bayi na wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hotuba nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimpongeze rafiki yangu msanii mwenzangu Profesa Jay na wenzake ambao wamebaki humu. Kwa kweli huu unaonekana ni uzalendo wa kutosha. Nawapongeza na Wapinzani wengine ambao wamebaki hapa. Sina sababu ya kusema sana kuhusu upinzani lakini najua dozi wamepata na wanaelewa nini maana ya kubaki na kuendelea kuzungumza, kusikiliza na kuchangia hoja hii.
Naomba tuwe na kitu kimoja tu kinachoitwa uzalendo. Uzalendo hauwezi kuonekana katika vyama vyetu, unaonekana katika mtu kufanya jambo. Ndiyo maana nimekupongeza Profesa Jay kwa sababu najua tulipotoka, tulikuwa tunaimba mimi na wewe unakumbuka (huku akiimba madawa bangi ni saa utajiri kuuchuma mashangingi) mambo kama haya, leo tupo Bungeni. Kaka usitoke hapa, ukitoka mwanangu kule watakuchimbia mbali na mimi Flatei si unajua mwana sarakasi sitoki hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumkumbusha tu kwamba na yeye aangalie, kwa nini nasema haya? Leo hii tunatakiwa kufanya kitu kinachoitwa maendeleo katika Majimbo yetu, leo hii TV kule haionekani ni vizuri tukashauriana humu ndani, tukitoka hapa nenda Jimboni watakuangalia. Muombe Waziri hapa akifika kule atakusaidia umeme utakwenda na maji yatakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye maji. Jimbo langu la Mbulu Vijijini tuna miradi mitatu ya maji ambayo imefadhiliwa na Benki ya Dunia. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Maji nadhani ananisikia, miradi ile ya World Bank imesimama, naomba basi tusaidie iongezee pesa ili miradi ile iweze kutekelezeka wananchi wa Haydom, Bashay na maeneo ya Masieda na Dongobesh waweze kupata maji ili yale maji tuyatumie katika kilimo na kilimo kiweze kuwapatia wananchi wetu faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda wangu nao umeanza kusogea sana. Mwisho, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa, ni Waziri wa kwanza kwa miaka 10 iliyopita amefika Jimboni kwangu akiwa Naibu Waziri, hakuwahi kutokea Waziri mwingine mpaka awamu hii imekwisha. Nakushukuru sana umefika kule na sasa basi nawashukuru Mawaziri ambao wanategemea kufika na wengine wameniahidi kufika katika Jimbo la Mbulu. Ni kweli barabara yetu haipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mimi na Mheshimiwa Jitu tulisukumwa na wananchi baada ya mvua kunyesha. Walipojua tunakuja Bungeni wakasema basi tuwatoe hawa kwenye matope ili wafike Bungeni, tulitumia saa tano kutoka kule kuwahi hapa Bungeni kutokana na jinsi miundombinu ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuendelea sana lakini kubwa zaidi nataka kuonesha tu umuhimu wa kuiona na kurudi Mbulu na Wilaya ile ni kongwe. Haya maeneo matatu niliyoyasema naomba mtusaidie sana Serikali. Kwa nini nasema haya ni kwa sababu naona uchungu. Mimi ni mjukuu nimekuja huku, alikuja Sarwatt, Marmo na Akunaay sasa kumbuka mimi ni mjukuu nimekuja kuwaambieni Mbulu muiangalie kwa jicho la pekee sana. Mbulu ni Wilaya mama imezaa Hanang kwa Mama Nagu, imezaa Babati kwa mtu anayeitwa Jitu, imezaa Babati Mjini kwa mtu anayeitwa Pauline Gekul na imezaa Karatu kwa mtu anayeitwa Willy. Jamani, sasa leo wote hao wana lami wana kila kitu, wana umeme, Mbulu kata tatu, mtuonee huruma jamani, hatuna hata kipande cha kilometa moja cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kabisa kwa asilimia mia moja, naunga mkono hoja hii ili Serikali ifike Mbulu ikanifanyie haya. Ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu kwa waandishi wa habari kwamba wamekuwa na mazingira magumu ya kufanyia kazi na Serikali haijaweka mazingira mazuri ya kiajira na kimaslahi kwani hali hii inadidimiza tasnia hii ya habari, kuna wakati waandishi hulazimika kufanya kazi na kutoa habari ile ambayo haina maslahi kwake na kwa umma, ila ni kwa kuwa tu hana ajira inayoeleweka na mkataba wa kudumu. Hivyo ni kuidhalilisha tasnia hii, kwani mara nyingi wamekutana na risk mbalimbali za kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali isaidie kuwapa mwelekeo mzuri waandishi hawa ambao pia wanasaidia Taifa katika kuelimisha jamii.
Pili, TBC ingeangalia pia kuweza kuongeza channel na pia kutokana na hayo, ni vyema ikaongezewa fedha ili ifike katika Wilaya 82 kama ilivyo katika bajeti yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Taasisi ya Sanaa ya Bagamoyo inatoa stashahada, lakini Serikali haijaweka mitaala katika shule za chini ili somo la sanaa liweze kupanda kielimu. Masikitiko yangu ni kuwa Serikali imeanzisha taasisi hii bila kuwa na base au msingi toka chini. Kwa hiyo, naitaka Serikali ije na majibu ya kina kuhusu suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nianze kwa kupongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya kwa kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana kwa kufika na kutatua changamoto sugu jimboni na Mkoani Manyara. Pamoja na pongezi hizi tunazo changamoto na ahadi tulizopewa na Serikali kupita viongozi wetu wa Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Miundombinu; tunaomba kujengewa barabara ya kutoka Karatu –Mbulu, Haydom Singida/Sibiti maana inasaidia ikiwa itajengwa kwa lami. Barabara hii inapita katika majimbo matano na hata itasaidia sana wananchi kufika katika Hospitali ya Kilutheri
ya Haydom ili kupata matibabu na pili itasaidia wananchi kiuchumi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekjiti, kupandishwa hadhi hospitali ya Kilutheri ya Haydom iwe ya Kanda kama ulivyoahidi. Jambo hili la kupandishwa hadhi itasaidia sana kuhudumia jamii inayozunguka. Mikoa ya Simiyu, Manyara, Arusha, Singida, Tabora na sehemu ya Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la miradi ya maji ambayo imekwama kutokana na kutopata fedha kwa wakandarasi. Hoja, mradi wa maji Hydom- Tumati, tunaomba Serikali ifanye mkakati wa kuwasaidia wakandarasi. Mifugo/Kilimo katika jimbo langu kuna wizi wa mifugo ambao umepelekea kufariki kwa kuuawa zaidi ya wananchi wanne na zaidi ya mifugo 500 kuibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iimarishe usalama katika Bonde la Yaeda Chini/Eskesh Kilimo. Tunaomba sasa mbegu na mbolea zinazotolewa kwa wakulima zije kwa muda muafaka yaani kabla kunyesha mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya ipo katika ilani ya CCM kujenga zahanati kila kijiji. Naomba nitoe ushauri ni bora Serikali kutoa maelekezo mahususi kujikita katika kujenga kituo kimoja cha afya kila Halmashauri kwa mwaka wa fedha ili baada ya miaka mitatu tutakuwa tuna vituo ziadi ya 500 hapo ndipo tutaona matokeo ya haraka katika Sekta ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawapongeza sana, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono Hoja ya Serikali au Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo malalamiko katika eneo hili la Mahakama. Hatuna Mahakama katika eneo la Haydom ambapo pana watu zaidi ya hamsini elfu na wapo pembezoni na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ni kilomita 86 toka Makao Makuu ya Wilaya ambapo ipo Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho Kituo cha Polisi Haydom ambapo tunaomba tujengewe Mahakama hata ya Mwanzo. Tumekwisha tenga kiwanja cha kujenga Mahakama. Kituo cha Polisi kinafanya kazi ya kukamata wabadhirifu na kuwasafirisha Mbulu zaidi ya kilomita 86 hivyo kuipa Serikali gharama kubwa sana ya kupeleka mahabusu/ watuhumiwa zaidi ya kilometa nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tujengewe Mahakama Haydom maana wakati mwingine Polisi hutumia mabasi kusafirisha watuhumiwa na wakati mwingine kutoroka na kupotea. Hivyo naomba sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami niungane na wenzangu wote ambao wametoa pole kwa wafiwa wote na kweli Mungu azilaze roho za Marehemu watoto wetu mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitoe pongezi zangu kubwa sana kwa Mheshimiwa George Huruma Mkuchika ambaye alikuwa DC katika Wilaya yangu ambayo mimi nilikuwa mdogo sana kwa kujenga uwanja wa michezo, ambao umefanya mimi kama Flatei Massay kuwa mwanamichezo kutokana na viwanja ambavyo huyu mzee wetu ambaye ni Mbunge humu ndani ameifanya kazi hiyo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini naamua kusema haya? Nasema haya kwa sababu kuna watu wanatakiwa kuenziwa katika Taifa letu. Kwanza, wamefanya kazi nzuri, uwanja wa Julius Nyerere ulioko Mbulu umejengwa kwa nguvu kazi ya kwake mwenyewe. Namkumbuka alikuja mimi nikiwa mtoto sana, nina miaka kama sikosei mitano. Nilikuwa naona jinsi akivaa magwanda yake ya kijeshi akiwa Captain na kuhamasisha wananchi wa Mbulu kujenga ule uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa uwanja umekuwa mzuri na naamini wachezaji wengi wametokea pale na wana riadha wengi wametoka pale. Sasa niiombe Wizara iangalie namna gani ya kuweza kusaidia viwanja hivi vya michezo? Kwa sababu wanariadha wengi ambao kimsingi wameonekana katika Taifa letu kuleta zawadi ya ushindi katika medali za Kimataifa wametokea pale, mfano, Filbert Bayi, John Stephen
Akhwari, John Bayo, hawa watu wote wamefanya kazi na kulitangaza Taifa hili katika ulimwengu huu wa Michezo na wameweka rekodi ambayo mpaka sasa naamini haijavunjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara iangalie sana uwanja ule, hata ikiwezekana basi waangalie namna ya kusaidia hata kwa kutumia maeneo ya ushauri tu nini kifanyike ili angalau michezo iweze kuendelea katika maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, pia nataka kusemea hawa wazee wetu waliotusaidia sana kuitangaza Tanzania. John Stephen Akhwari, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, alifika akamtembelea mzee yule. Ana vikombe kama 15, Mheshimiwa Naibu Waziri aliona mwenyewe. Kwa sababu alifika, yule babu sasa anazeeka na hawezi kuishi miaka mingi kutokana na umri wake sasa. Naamini historia yake inaonekana na Mheshimiwa Waziri anayo. Hebu angalieni basi namna ya kuangalia malalamiko yake ambayo alimpa Mheshimiwa Waziri. Mimi ni Mbunge wake lazima nimwambie leo. Asingeweza kupata nafasi yoyote, nafasi ya kumsaidia ni wakati huu akiwa hai.

Mheshimiwa Spika, wakati ule walikuwa wanawasikiliza Taifa, ilikuwa ni ngumu sana kupata zile hela ambazo wanatunzwa wanaposhinda katika zile medali ambazo zimeisaidia nchi hii kusifika wakati huo. Kwa kweli walikuwa wanasaidia Tanzania na kuipatia heshima kama nchi. Hawakuwa wanapata jambo lolote.

Mheshimiwa Spika, sasa basi waje wasaidie kwa sababu wamekuja wale watu wa olympic kutoka nchi ya Australia ikitaka kumjengea huyu baba au babu uwanja wa michezo, lakini kwa sharti moja tu, ni kwa jina lake. Kwa bahati mbaya sana Serikali wakati uliopita haikukubali kabisa jina la uwanja huo kuitwa kwa jina lake. Wale wafadhili wamekuwa kila siku wakijaribu kutafuta namna rahisi ya kufanya muunganiko kati ya Serikali yao na sisi ili kumsaidia kumjengea mzee huyu ambaye ametangaza Tanzania katika ulimwengu huu wa michezo.

Mheshimiwa Spika, basi naomba Serikali ione namna gani ya kusaidia. Nafiri Mheshimiwa Naibu Waziri siku ile mzee yule alimwambia masikitiko yake makubwa. Sasa kabla hajafika mahali Mungu akamchukua kwa sababu ni mzee, waje basi wamsaidie haraka ili angalau jina lile lisifutike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka niliseme, Mbulu tumetoa wanamichezo wengi wa Kimataifa, siyo kwa sababu tu ni maarufu sana, hapana! Ni kwa sababu ya nature ya eneo lenyewe. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, sasa hivi wanamichezo wengi hasa wanariadha kutoka Mbulu wanachukuliwa maeneo mengi mengi na watu hufadhili mmoja mmoja. Sasa naomba Wizara ijaribu kufanya jambo moja tu, isiondoe sasa eneo la michezo ya mazoezi kutoka Mbulu kuipeleka Dar es Salaam. Kwa sababu sasa mnavyofanya namna hiyo saa hizi, historia inaweza kufutika kwa sababu moja tu.

Mheshimiwa Spika, ukimtoa mtu Mbulu kwenye kitu kinachoitwa uwanda wa juu, sisi kule bahati nzuri hali ya hewa inatu-favour na milima inawasaidia wachezaji. Sasa ukimtoa mchezaji toka Mbulu ukamfanyia kambi Dar es Salaam ili aende kushinda, anashindwa kushinda kwa sababu ya mvuto anaotumia, upepo ule au hewa ya Dar es Salaam iko zero degree wakati huku Mbulu kuna 1,500. Sasa ukimtoa pale akafanye mazoezi Dar es Salaam akienda Ulaya, hawezi kushinda.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sababu hizo nafikiri ni za kitaalam sana; mimi sio Daktari lakini naziona na ninazijua. Kwa hiyo, wasaidie basi kuliko Chama kile cha riadha kiamue moja kwa moja kwa sababu wao ndio viongozi waamue kambi kufanyika Dar es Salaam, wanaweza kufanya hivyo kwa sababu wao ni viogozi, lakini waone, Filbert Bayi wakati huo walikuwa wanafanya mazoezi na kufanyia pale Mbulu na wakashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii basi, walishinda kutoka na hali ya hewa iliyoko pale na nature ya mazingira ya kule ni milima na miinuko, ili akifika kule aweze kumaliza zile mbio akiwa na nguvu na kuisaidia nchi yetu tupate medali. Nimeona niseme hii moja kwa moja hapa kama mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nielezee sasa eneo la michezo. Michezo ni lazima uanzie ukiwa mdogo. Wenzetu ukiangalia historia ya michezo kwa sisi wanamichezo utaona watoto wetu wanafundishwa wakiwa watoto. Nami niungane na wenzangu kwa msingi huo ni vizuri kumfundisha mtoto akiwa mdogo akafahamu na kumjengea ile behavior akaweza akafanya michezo akiwa utotoni. Leo hii ukimfundisha punda mzee kulima, hawezi. Ni lazima basi hii michezo irudishwe shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, linguine, liko jambo ambalo nataka niseme kwenye sanaa na hasa Bodi ya Filamu. Bodi ya Filamu ina harufu ya rushwa. Naomba nirudie, ina harufu ya rushwa kwa sababu kwa sisi wasanii, nami nataka nikwambie, mimi ni msanii, lakini ukitaka kuomba chochote kwenye Bodi ya Filamu, wanaweka hali ambayo haimruhusu msanii kupata anachotaka. Kwa mfano, mpaka Bodi ikae unahitaji miezi mitatu.

Mheshimiwa Spika, ukitaka kufanya inter-connection wewe msanii wa Tanzania na Msanii aliyeko Ulaya, akija Tanzania inabidi aache kabisa kila kitu, anatakiwa asije na camera. Nashangaa sana, unamruhusu asije na camera wakati huo unamkubalia aingie na simu, sasa kama ni usalama wa nchi, sijui inawezekana. Simu nyingine zina capacity kubwa. Kama ukitaka asichukue hiyo picha, ataweza hata kutumia simu, si atachukua tu!

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimepeleka malalamiko katika Ofisi yake na nimeandika mwenyewe. Walikuja Wabunge kutoka nchini Norway, ni wafadhili wa miradi mingi nchini, lakini Bodi ya Filamu ikawazuia wale Wabunge wasiingie na camera jambo ambalo nililishangaa sana, likanifanya nipate mshtuko kwa sababu wale Wabunge walipoingia, walikuja wakiwa watupu wakisema, kwa nini hatukupewa?

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri walifuata sheria za Tanzania, wamefuata sheria za mambo ya nchi za nje, wamefika Wizarani, wameandika, wametumia Ubalozi wa Norway, wametumia Ubalozi wetu ulioko Sweden, wameruhusiwa; wamekuja kwenye Wizara yako, wameomba kibali. Kilichowafanya wakatazwe wasipate kibali hicho ni Bodi ya Filamu. Wameomba, muda unatosha na bahati mbaya hawakupata majibu. Kwa nini hawakupata kibali cha kuingia na camera? Hiyo tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye Bodi ya Filamu kuna shida pale; nami na-declare ninao ushahidi na nimempa kwa maandishi na nimesema kwa maandishi na Balozi pia amenipa barua yake kwa maandishi na nimempa copy yake. Naomba akachunguze Bodi ya Filamu, kuna shida pale. Bahati nzuri nimekwenda mwenyewe pale, ni mara tatu nimeshindwa kupata ninayotaka kuyafanya. Mara moja tu Mheshimiwa Nape alipokuwa Waziri alipiga simu ndiyo nikasaidiwa kwa sababu tu mimi ni Mbunge. Je, wasanii wangapi wana shida pale? Aangalie Bodi hii, kwa nini inatoa masharti magumu? Kama ni shida, tujue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona nilisemee vizuri hili na nilisemee kwa uchungu mkubwa kwa sababu tunapoteza heshima. Anapokuja mtu anayefadhili nchi hii, lakini inafika mahali anakwamishwa kwa jambo dogo tu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naunga mkono hoja, lakini naomba kama hataleta majibu haya, nitashika shilingi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali na Mawaziri wote. Tuna tatizo la barabara ya lami ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya kutojengwa kwa kiwango cha lami kabla ya mwaka 2020 kama tulivyoahidi. Tunaomba kujengewa barabara hii Karatu
– Mbulu – Haydom – Lalagu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano naomba minara ya simu katika Kata ya Endahagichan, Endomilay, Nqorati, Geterer, Endamasak, Eshkesh, Arri Tumat. Pia naomba mnara wa Maghang ufunguliwe na wa Yaeda - Ampa maana muda umepita sana. Naomba sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipongeze Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2020/2025 ambao umeletwa hapa. Mpango huu nimeusoma vizuri sana, ni mpango mzuri sana, lakini ninayo machache ambayo napenda kuyaelezea katika mpango huo. Ukiangalia mpango uliopita wa pili utaona jinsi ambavyo uchumi ulikuwa unasogea kidogo kidogo, lakini pia uwekezaji katika mpango huu katika eneo letu la kilimo haujawa vizuri sana. Sasa naomba na kushauri kwamba; Dkt. Mwigulu Nchemba umesoma vizuri sana. Ukiangalia sasa wakulima wetu ndio walio wengi, na zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Sasa ni vyema tukaangalia namna gani mpango utawa-favor watu wengi hawa ambao kimsingi uchumi wao unategemea kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia saa hizi kilimo kimekuwa kwa asilimia tatu peke yake. Kwa nini iko hivyo? Ni wazi kwamba mpango uliopita haukwenda vizuri sana katika eneo hili ili ku-favor Watanzania katika suala la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini? Wizara zote hizi ambazo zipo katika Serikali zinatakiwa ziende zikipangilia kuendana na mpango unaowekwa kwa kila mwaka.

Mheshimwia Naibu Spika, na sasa ukienda kuangalia Tanzania kama nchi hatuko pembeni ya dunia. Ukiangalia sisi bahati nzuri tunapata mvua za misimu na hatuwezi kabisa kulima kupitia mvua hizi kwa sababu kuna wakati unafika mvua zinaisha.

Kwa hiyo nishauri, kwenye Wizara ya Kilimo mkija na bajeti muweke bajeti ambayo itasaidia kujenga mabwawa katika maeneo yote ya nchi hii ambako utaweza kuzuia maji kwa wingi ili basi tukawa na kilimo cha uhakika, na kilimo hiki kikishakuwa cha uhakika maana yake uvunaji wa uhakika unaonekana; pale ambapo mwananchi anaweza kunyeshea mazao yake na akavuna kwa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia leo tuna mikopo ya wakulima, unamkopesha mkulima huyu kutoka benki aende akalime, lakini anakwenda kulima kwa kutegemea mvua za masika, mvua zikiisha au zisipofika wakati wake mvua ikawa kidogo maana yake ni kwamba yule mkulima sasa anakutana na kitu kinachoitwa deni, na hilo deni lazima alipe. Lakini kumbe Serikali ikijiandaa vizuri ikaenda kuweka mabwawa katika maeneo yetu kule vijijini wakulima wale wakaweza kunyeshea yale mazao kwa hiyo utakuwa umemsaidia yule mkulima kwanza, atakuwa na uwezo yeye mwenye wa kulima na ataweza kuvuna na kulipa Serikali. Kwa hiyo utakuwa umemuinua mwananchi moja kwa moja kutoka chini katika mazingira ya kujenga mabwawa ya kunyeshea.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi yana maeneo hayo ya kunyeshea lakini si kila mahali. Ukiangalia nchi nyingi za nje zimekopa mambo mengi toka Tanzania. Ukiangalia kilimo cha korosho ukienda Cuba utakuta walichukua mbegu kwetu. Pia ukienda katika suala la mbegu na pembejeo hizi za kilimo imekuwa tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kununua mbegu ni ghali; na mbegu zote zinatoka nje ya nchi, mbegu zinazotoka nje ya nchi zinakuwa ghali zikifika kwa wakulima wetu; kwa mfano sasa hivi mbegu zinatoka Kenya. Lakini ebu tujiangalie sisi kama Watanzania, tumeshindwa kweli kuzalisha mbegu nchini? Na kwa nini tusizalishe mbegu nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna Watanzania wengi vijana wameenda shule hawana kazi, tunalia namna ya kuwatafutia ajira, lakini kumbe tunayo ajira. Ajira tuliyonayo ni ipi, ukienda ukawapatia eneo kubwa tu vijana hawa ukawawezesha wakalima mbegu, mbegu hiyo itashuka thamani, na ikishuka thamani ni wazi kwamba wakulima wetu watanunua mbegu katika hali ambayo iko chini. Leo hii mbegu ni ghali, inapotokea mbegu zinakuwa ghali vijana wetu hawawezi kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya China imeendelea kwa sababu ya wingi wa watu wake, imewapa kazi ya kufanya na kazi hiyo wanayofanya inawaletea kipato katika nchi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe kabisa, Mheshimiwa Mwigulu nakumbuka maneno yako ulipokuja kusoma kwa mara fulani bajeti hii hapa ya kwako ulisema hivi; ‘ukitaka mali utaipata shambani’, mwisho wa kunukuu hotuba yako, wakati huo ukiwa Waziri wa Kilimo na Mifugo enzi hizo. Sasa ndugu yangu leo umepewa Wizara hiyo angalia namna gani ya kusaidia kilimo moja kwa moja. Ukifanya hili utakuwa umeisaidia sana Serikali kunyanyua watu wote na kuwa katika kipimo kile cha uchumi wa kati ambao sasa tunakwenda kuinua watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wowote ukitaka upande, eneo lolote, katika nchi zozote; na katika nchi zilizoendelea waliangalia swala la miundo mbinu. Miundo mbinu ikishakuwa salama na mizuri maeneo yoyote yale inasaidia uchumi wetu kupanda. Kwa mfano ukienda moja kwa moja katika maeneo ambako uchumi umekwenda juu ni kwa sababu ya miundo mbinu. Tunapogawa rasilimali kupitia mpango huu, tuna hakika tunatakiwa kuangalia. Nimshukuru sana Hayati John Pombe Joseph Magufuli, ameangalia sana miundo mbinu na katika maeneo haya ameunganisha mikoa mingi sana kwa barabara za lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maeneo yale mambo yameenda vizuri sana. Sasa na kwasababu unajua Mheshimiwa Mwigulu kuna barabara yetu ambayo ingesaidia kuinua uchumi wa Tanzania. Barabara ya Karatu, Mbulu, Hydom, Singida, Sibiti kule mpaka Simiyu na Meatu wamekaa huko. Barabara hiyo ni barabara ya kimaendeleo. Najua resources au rasilimali zetu si kubwa sana, lakini barabara hii ikifunguliwa na mpango huu ukajielekeza hapo, ni wazi kwamba utakuwa umeinua sehemu hii ya uchumi wa nchi yetu kama Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana mpango huu unaonekana namna hii, na jimboni kwako kumbuka ni kule. Kuna mtu mmoja alisema hapa hutarudi, mimi nikuombee 2025 urudi, lakini kwa masharti haya. Mpango huu uelekeze moja kwa moja kwenye barabara hii ninayoisema ambayo inapita jimboni mwako. Na bahati nzuri Mungu alivyokubariki…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatey Masey, kwani anakuja kugombea…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina…

NAIBU SPIKA:… Maana umesema barabara hii ikitengenezwa ndio atarudi atakuja kugombea kwako kwa hiyo wewe hutarudi?

MHE. FLATE G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara hii inapita jimboni kwangu, halafu inakwenda jimboni kwake. Kwa maana hiyo basi barabara hii asipoiangalia isipopita wananchi watajua Flatey Massey Mbunge wa Mbulu Mjini kaisema barabara hii na Mwigulu Lameck Nchemba yeye ni Waziri katika Wizara hii na katika mpango uliopita barabara ilikuwepo haijatengewa fedha, sasa hivi amekuwa Waziri wa Fedha ataiwekea fedha; na kwa bahati nzuri wamewekwa pamoja. Waziri naibu wake anaitwa Masauni hawa wote ni vijana mwingine yuko yanga mwingine yuko simba unaona hiyo! Mwingine yuko bara mwingine yuko visiwani unaona hiyo! Hawa wote ni vijana. Sasa itakuwa hatari kama mpango huu hautakuja kwenye bajeti ikiwa na fedha katika barabara hii ambayo nimetaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo inapita kwenye majimbo tisa. Jimbo la Karatu, Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini, Iramba kwake mwenyewe, inaenda Meatu, inakuja Sibiti inakutana mpaka Lalago kule, mpaka Maswa, Bariadi wananisikia kwa hapa. Kwa hiyo nimesema hii tu ili tukitoka hapa tuwe na knowledge; baadaye pasije pakawa na kwamba aah! Unajua katika mipango hii inayopangwa hapa, resources nyingine imeenda upande fulani na upande mwingine umesahaulika. Sina maana ya kujitenga katika nchi hii, napanga tu na kusema ili ninapokuja katika bajeti aje na hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na akishakuja na hiyo ni wazi kabisa mipango hii itakuwa inakwenda vizuri, kwasababu hamna uchumi wowote mahali popote unaweza kuendelea kama huna miundombinu. Mazao kutoka shambani kwenda viwandani unapelekaje? Ni lazima tuwe na miundombinu ya kutosha. Na kwasababu hiyo ukiangalia maeneo yote yale hakuna barabara ya kutosha. Hakuna barabara ambayo unaweza kusema utapeleka mazao kwenye viwanda, na ukiangalia viwanda vyetu viko mijini na kwa maana hiyo basi niombe sana sana sana sana Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba na ndugu yangu Masauni, sisi wote ni vijana na vijana wengi tumeingia humu; tuwasaidie vijana wetu kwa kupeleka mazao yao kwenye viwanda kwa kuwawekea barabara hizi ambazo nimezisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naona kabisa muda umeondoka lakini niombe kama nchi ni vizuri kujiwekea sheria ili sheria hizi zitusaidie. Nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusema kabisa tunakwenda kupigilia maendeleo katika miradi mikakati iliyowekwa. Mungu ambariki sana na ninaendelea kumuombea ili tuendelee vizuri katika mipango ambayo imewekwa wote wawili wakiomba kura katika ilani ya CCM kwasababu barabara iko kwenye ilani ya CCM…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. FLATEI G. MASSAY: …na nafikiri itakwenda vizuri Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii Mungu akubariki sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia nafasi hii pia kwa kuzisemea barabara ambazo kimsingi zimeshakuwa kwenye ahadi za ilani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu ilani ni mkataba wetu sisi na wananchi na hasa kwa Chama Cha Mapinduzi ambapo 2015 kuja mwaka 2020 tuna barabara ambayo imewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi, barabara ya Karatu – Haydom – Dongobesh kuja Singida kwenda Sibiti, Lalago.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeiona katika kitabu chetu hapa, na barabara hii imeahidiwa na Rais wetu mpendwa, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kutoka 2015 kuja 2020. Lakini pia juzi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Sita amekuja Dongobesh ameahidi barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara moja tu iliyobaki ambayo inaunganisha mikoa minne ambayo haikujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii inatoka Jimbo la Karatu kuja Jimbo la Mbulu Mji, maana yake inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inatoka Mbulu Mjini kuja Haydom kwenda Singida, maana yake inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. Na kutoka pale inaelekea Maswa, maana yake unakutana na Mkoa tena ule wa Simiyu, na kwenda pia Shinyanga kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nieleze kwamba barabara hii ndiyo barabara iliyosahaulika moja kwa moja. Ni barabara chache mno ambazo hazikuunganishwa kwa lami kwa mikoa hii. Kwa hiyo, masikitiko yangu nataka nioneshe Mheshimiwa Waziri aelewe.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Yahaya Massare.

T A A R I F A

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumpa taarifa mchangiaji anayechangia sasa hivi, Mheshimiwa Flatei, si barabara hiyo tu iliyosahaulika, ni pamoja na barabara ya Mkiwa – Itigi – Rungwa – Makongorosi kutokea upande wa Mkoa wa Singida, imesahaulika toka Uhuru. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Naona taarifa za nyongeza za barabara. Sasa sijajua na mimi nikupe taarifa nyongeza ya barabara nyingine; Mheshimiwa Flatei Massay, unapokea taarifa hiyo?

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii ya Mheshimiwa Massare naipokea kwa moyo mweupe, na ile ya kwako naipokea kwa sababu najua kuna barabara imesahaulika ya kutoka pale Mbeya kwenda mpaka Tunduma kule, hali ni mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze tu Waziri aelewe kwamba wameteuliwa na Mheshimiwa Rais sasa wamekuwa Mawaziri wako watatu, yaani Waziri na Manaibu wawili. Tangu Uhuru, Mbulu imeanzishwa 1905, haina barabara. Ukiangalia Mbulu kwa maeneo yote barabara ziko nyingi; barabara ya kutoka Dongobesh kwenda Babati, kilometa 63, imeahidiwa pale iko kwenye ilani, hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tunapouliza maswali, mimi nimeleta barabara hii mara 20 ndani ya Bunge hili, nimeuliza maswali 20, nimechangia kwenye mchango wa namna hii ninavyoongea hii ni mara ya tano. Na barabara hii acha tu nikwambie, ina magari mengi. Na kwa uchumi wa watu wa Mbulu, Singida, Karatu, Simiyu, Meatu, hakuna namna yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe, mara ya kwanza nimekuja kusema barabara hii nikaambiwa iko kwenye upembuzi wa awali, nikatulia. Nimekuja 2017 wakasema iko kwenye upembuzi wa kati, nikatulia. Nimekuja tena wakasema iko kwenye upembuzi yakinifu, nikatulia. Juzi hapa wananiambia sasa iko kwenye design and building; natuliaje sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mbulu wametutuma hapa kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. Sasa nikuombe unisikie leo; nifanyeje ile nieleweke? Kwenye ilani ipo, kwenye ahadi za Rais wetu ipo, wametuambia bajeti iliyopita iliwekwa kwenye kitabu cha bajeti inaonekana kilometa 50 zitajengwa kwa kiwango cha lami. Leo naona huku wamepunguza tena imekuja kilometa 25. Sasa nawaza kwa nini tunafanyiwa hivi. Kama rasilimali tunagawana katika Tanzania nchi yetu tugawane kwa usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani, naitwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, nimekuja huku niambie tufanyeje sasa. Kama tumetumwa, tumeeleza na uwakilishi upo eneo hili halijengwi. Leo naangalia kitabu cha bajeti hapa, sitaki kusema vibaya lakini mnielewe tu ndugu zangu kwangu hakuna barabara ya lami. Lakini wengine nimeona hapa siyo sahihi, wamewekewa bajeti ya kufanya ukarabati wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukarabati wa barabara, sisi hatujawahi kuiona barabara ya lami kabisa, wengine humu wana ukarabati. Kwa nini sisi tutakutana lini na changamoto hii kuisha? Wengine wana ukarabati; nini maana ya ukarabati? Wameshakaa na barabara, muda umefika hali yao imeshakuwa nzuri, barabara inakarabatiwa. Sisi ambao barabara hakuna hata kilometa moja lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Ujenzi ijue; nikipata nafasi kwenye kushika shilingi nitaishika mpaka ya mwisho ili kuhakikisha barabara hii inafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hii password ya kwamba kila siku upembuzi yakinifu, upembuzi wa awali, upembuzi wa kati; lini unaisha ili barabara hii ikajengwe kwa kiwango cha lami? Wananchi wanataka kusikia haya, wananchi wanataka kuona greda zinaanza kazi na barabara inajengwa.


Mheshimiwa Naibu Spika, na nimeshaomba mara nyingi, kuna Hospitali kubwa ya Haydom kule, maeneo haya watu hawawezi kupita, barabara imeharibika. Ni kweli wanajenga, sikatai, wanajenga kwa maana ya rough road, lakini kila ikijengwa, kila mwaka lazima barabara ile ijengwe ya Haydom – Mbulu – Hydom – Sibiti – Lalago, kilometa 389.

Mheshimiwa Naibu Spika, nifanyeje? Ni mtaalam wa sarakasi, au niruhusu basi sasa hivi nipande hapo nipige sarakasi tatu, nne, ili Naibu Waziri na Waziri wajue kwamba huyu Mbunge amechukia. Niruhusu basi naomba. Nipige? Nipige sarakasi kadhaa hapa? Niruhusu, mimi najua Kanuni haziruhusu, basi niruhusu nipige wajue kwamba kwamba nimetumwa na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kuiomba barabara. Nipige?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nipige?

WABUNGE FULANI: Piga!

NAIBU SPIKA: Usipige. Tunafahamu unajua sana kupiga sarakasi lakini…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, najua sarakasi, sasa nafanyaje?

NAIBU SPIKA: Mimi nakulinda, usije ukaumia kwenye viti.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ilani ipo; ahadi ya Marais ipo; ahadi nyingine zipo; nipige? Mimi naomba nipige kabisa. Nipige? Maana hali ilishakuwa mbaya, wananchi wanataka barabara, Waziri haelewi; Haydom – Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti; nifanyeje? Kwenye ilani ipo, kwenye kila kitu ipo, nifanyaje? Nipige? Sasa nafanyaje? (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri aje kwende wind up yake pale asiposema barabara hii anajenga lini kwa kweli humu ndani hatutaelewana, kama ni kuvunja sheria tutazivunja zote na kama kupiga nitapiga zote humu ndani. Haiwezekani wengine wapate barabara, sisi tunaongea kila siku habari ya barabara humu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, twende moja kwa moja kwenye eneo lolote la bajeti hii. Wenzetu wana billions kadhaa, sisi tuna bilioni tano tu; itajenga barabara lini? Kilometa 389. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, wewe ni mgeni lakini wamekuja wengi; amekuja Prof. Mbarawa kaona barabara ile, amekuja Engineer Nditiye kaona barabara ile, kaja Naibu Waziri kaona barabara ile, nampongeza amekuja kuona. Sasa akija kuona wananchi wanajua naam, barabara inajengwa, mwaka unapita, miaka inapita; inakuaje sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, principles zetu ni kwamba iko kwenye ilani, principles zetu ni kwamba ahadi za wananchi, principles zetu ni kwamba Marais wameahidi, sasa mama Samia Suluhu Hassan niwaambie ni mama mzuri sana, kashaahidi. Na amesema kazi iendelee. Sasa kazi inaendelea kwingine, Mbulu Vijijini haiendelei? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwaka huu wa fedha barabara mtangaze ili ijengwe ili wananchi wale ambao miaka yote wamekuwa wakitutuma humu, ametumwa Maru amekaa miaka 25 hakupewa; katumwa Akunayi naye kaka hakupewa, tumetumwa mimi na Issaay, tusipewe tena?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mungu awabariki. Sasa sijui niunge mkono, sijui niache? Naunga mkono kwa shida sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kumshukuru Mungu kunipatia nafasi ya pumzi na kuniwezesha kuchangia mchango kwenye Wizara hii ya Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze watumishi hawa kwenye Wizara ya Ardhi, nikianza na mwenyewe Waziri Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Angelina Mabula dada yangu Mary, Stella, Nico na wengine kwa kweli kwenye Wizara hii. Napongeza kwa sababu moja kubwa sana, Wizara wamejitahidi sana katika eneo hili la ardhi wana eneo kubwa sana. Migogoro ilikuwa mingi sana na mimi nimeishuhudia katika maeneo yangu mengi na niwashukuru sana kwanza kwa kulinda, kwa sababu gani nasema hivi? Ni kwa sababu ardhi imebaki kama rasilimali pekee ya Mtanzania aliyobaki nayo na urithi mmojawapo ni ardhi katika eneo letu hasa la kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwapongeze sana watumishi hawa kwa huku juu kama Wizara yenyewe kwa sababu wamejitahidi sana. Yuko mtangulizi amezungumza habari ya haya makampuni, nimsihi Mheshimiwa Waziri, yako mengi ambayo ameyafanya na Wizara yake, lakini machache yanaleta shida. Kwanza niliweke wazi hili kabla sijamiminika vizuri, haya makampuni ambayo kwa kweli yanakwenda kurasimisha, mara nyingi hayatumii sheria kwa jinsi Wizara ilizoziweka na hayafuati taratibu na hayasubiri miongozo ambayo wameweka Wizara kama Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mifano michache, ukiangalia wanavyokwenda kwenye halmashauri zetu, wakifika kule, kwa mfano halmashauri kama ya kwangu ina watumishi wachache wa Idara ya Ardhi na pengine hakuna kabisa. Kwa hiyo, baadaye nitampa Waziri ombi lakini aangalie haya makampuni, ushauri wangu kwake na kwa Serikali waunde Kamati ya Kisekta ambayo itasaidia kusimamia hawa warasimishaji ili walau waweze kupanga maeneo yetu vizuri. Nasema hivyo kwa sababu gani? Tanzania kama nchi lazima sasa nchi ipimwe yote na ikipimwa yote migogoro hii itaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingi inasababishwa kutokana na kwamba maeneo mengi hayajapimwa, lakini siyo hiyo tu maeneo mengi yakipimwa na yakapimwa kwa uhakika, maana yake ni kwamba hata Serikali itajipatia pesa kwa kutoza kodi ya maeneo yote yaliyopimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa hivi kila kampuni ina-charge kadiri inavyoona, iko nyingine ina-charge 150,000, nyingine 200,000 nyingine 100,000, lakini sasa basi Serikali ione namna gani ya kufanya, iwawekee utaratibu haya makampuni yanayopima ili utaratibu ule uonekane na sisi wawakilishi tujue kabisa kwamba wanapima kwa kiasi hiki na iwe kama formality ili hata mwananchi anapotakiwa kupima eneo lake ajue kipande chake anapimiwa kwa namna gani na kama ni kiwanja au chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niwapongeze sasa Wizara kweli kweli, kwa sababu wametoa mikopo kwenye halmashauri kadhaa na Mheshimiwa Waziri amesema sita zimefanya vizuri na zimerejesha hela. Nimwombe Waziri waendelee kuzikopesha halmashauri ili maeneo mengi yaendelee kupimwa, wasije wakakata tamaa kwa sababu halmashauri zingine hazikulipa. Niombe Wakurugenzi wale anmbao wamekopeshwa hizi hela na maeneo yao yamepimwa na wamepata faida kutokana na kupimwa kwa ardhi hii, basi nao warudishe hizo fedha ili halmashauri zingine zipate mikopo ambayo haina riba, wakapime maeneo yao. Ikiwa hivi basi ni wazi Serikali itapata mapato, lakini siyo hiyo tu migogoro itakuwa imepungua na miji yetu mingi itakuwa imepimwa. Siyo hilo tu, unapopima miji hakuna tena sababu ya kwenda kufanya urasimishaji kwa sababu miji ile imekwishapimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba nitoe mchango wangu katika Mabaraza ya Ardhi. Niishukuru kwanza Serikali imeanzisha baraza katika jimbo langu na Wilaya ya Mbulu. Bbaraza linafanya vizuri sana na linasaidia kutatua kero hii ya ardhi, lakini wana changamoto chache; ya kwanza baraza halina namna ya kwenda kutembea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mheshimiwa Waziri ikimpendeza aone namna gani ya kuanzisha haya Mabaraza yatembee yawe mobile zile mahakama zao zitembee, zikaone, maana wakati mwingine hazina namna ya kwenda kwenye maeneo zikaona, ni kweli kwamba hii ardhi ni ya fulani, hii ardhi ikoje kabla ya kutoa hukumu? Niombe pia wasitumie technicality za kisheria kabisa kutoa haki, waangalie vizuri namna ya kuhukumu kwamba haki iko wapi zaidi kuliko kutumia technicality. Niishukuru sana Wizara imeanza kutoa hukumu Kiswahili, kesi inasikilizwa Kiswahili na hili niwapongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana leo napongeza Wizara hii kwa sababu wananchi wetu kule wanapotoa hukumu wanasikiliza na wanakuwa wanajitetea bila kuwatumia hawa Wanasheria ambao mara nyingi walikuwa wakiwadanganya. Kubwa zaidi sasa katika maeneo haya, muwasaidie hao Wazee wa Baraza wawe na posho za kutosha…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei, Mawakili wanawadanganya wale wanaowawakilisha ama? Maana umesema walikuwa wanatumia Wanasheria ambao walikuwa wanawadanganya, kwani sasa hivi wakitumia Kiswahili wanajisimamia wao wenyewe unataka kumaanisha hivyo?

MHE. FLATEI G. MASSAY: Ndiyo ukweli.

NAIBU SPIKA: Kwa hiyo Mawakili ni waongo?

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kusema Mawakili wote ni waongo hapana, kwenye mahakama hasa hizi za Baraza la Ardhi wako wengine wanajifanya ma-bush lawyer, hawana hata hizo taaluma.

NAIBU SPIKA: Sasa ngoja, tufafanue vizuri, kuna tofauti ya mtu ambaye ameamua kukupa wewe ushauri ambaye siyo Wakili, wala siyo Mwanasheria. Sasa ukisema walikuwa wanadanganywa na Wanasheria yaani hapo maana yake ni kwamba kimsingi sheria… (Kicheko)

Wanasheria humu ndani wataandamana isipokuwa mimi, sasa hiyo kauli hiyo iweke vizuri kidogo.

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, basi niifute kabisa, najua wewe ni Mwanasheria na naelewa angle unayozungumzia.

NAIBU SPIKA: Ngoja ngoja unampa taarifa Mheshimiwa Flatei Massay au mimi?

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa anayezungumza.

NAIBU SPIKA: Basi ngoja tulimalize kwanza hili halafu nitakupa nafasi. Mheshimiwa Flatei ulikuwa unataka kusema point moja hivi sijakuelewa, hii ya pili uliyokuwa unasema kwa kuwa mimi ni Mwanasheria...

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, najua nini maana ya Mwanasheria, haya nilikuwa nataka kupongeza Wizara hii ielewe kwamba kwa sababu wananchi wetu kule hata kuweka hao Wanasheria zile gharama zinakuwa kazi kubwa sana, kwa hiyo kumtafuta mwanasheria proper kama wewe ni kazi sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Nadhani hoja imeeleweka, hoja ya gharama ni tofauti na hoja ya wale watumiaji wa hizo huduma za Wanasheria kudanganywa.

Mheshimiwa Olelekaita.

T A A R I F A

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nataka tu nimpe mzungumzaji taarifa kwamba, mawakili hatuendi kwenye Mabaraza hayo anayozungumza, kwa hivyo kama wananchi wamedanganywa huko basi watakuwa ni watu wengine lakini siyo Mawakili.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipokea taarifa kwa sababu ni rafiki yangu na isitoshe ni Mbunge mwenzangu na tunatoka Manyara wote, naipokea sana taarifa hii wala asiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuipongeza Wizara hii naomba niendele na mchango wangu. Kwa hiyo, Wizara inajitahidi sana na kwa kuwa sasa nimeomba kwa Mheshimiwa Waziri, wale Wazee wa Mabaraza, Wenyeviti wa Mabaraza wawasaidie basi wawapatie ajira za kudumu, ili mtu awe na hakika na ajira yake. Mtu anapokwenda kufanya kazi ile kubwa ya kutoa haki mahali fulani pia anatakiwa awe na security ya kutosha. Wakati mwingine anajua kabisa ajira yake inakwisha baada ya muda fulani au kwa miaka mitatu, kwa hiyo haimpi ile hali ya kujiona yeye ni mfanyakazi katika eneo hili la kutoa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali iwape hawa Wenyeviti ajira ya kudumu kwa sababu sasa hivi nadhani ajira zao siyo za kudumu. Pia niombe pia hawa Wazee wa Baraza, nao pia waangaliwe kwa namna Fulani, waletewe bajeti hapa na katika hiyo bajeti wapewe fedha ambazo zitaonyesha kabisa kwamba kweli fedha hii inaweza ikawa kama posho ya kawaida kabisa kulikoni sasa hivi ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa, niwashukuru pia kwasababu wamefanya kazi nzuri, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Stella huyu ambaye kwa kweli amekuwa akisimamia Mabaraza haya ya Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kama ushauri tu niombe Mheshimiwa Waziri aangalie kanuni katika Mabaraza haya, pawepo na namna rahisi ya kusaidia, kesi zinapoanza pawe na utaratibu ikiwezekana kesi zianze kwenye Kijiji, iende kwenye kata, lakini baadaye iende kwenye Mabaraza ya Wilaya. Kwa nini ninasema hivyo? Mtu mwingine anaweza kuwa na uhuru, akaenda kufungua kesi kwenye Baraza la Wilaya ambako anajua kabisa yule Hakimu au Mwenyekiti hawezi kuja kwenye eneo ilipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utoaji wa haki ule mtiririko na kesi ilivyoendeshwa inakuwa hawezi kujua kwa sababu yule Mwenyekiti hawezi kwenda site kuona hali hii ilivyo. Kesi ikianzia kwenye kijiji ni rahisi kujua kwamba kijijini wameamuaje, Baraza la Kata limeamuaje. Kwa hiyo ni rahisi kwa Mwenyekiti kuamua namna gani ya kutatua mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, niombe Mheshimiwa Lukuvi, iko migogoro ambayo Mheshimiwa Waziri anaweza kuitatua, migogoro iko Manyara mingi hasa ya Mkoa kwa Mkoa, Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa kengele ya pili imeshangonga.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza namshukuru sana Mungu kwa kunijalia nafasi ya kuwepo hapa. Pamoja na hayo yote, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa bajeti hii ya kwanza na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na msaidizi wake Mheshimiwa Masauni kwa bajeti yenu ya kwanza hii. Nina ushauri na kwa sababu muda ni mfupi, naomba niende haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunakuja huku mara nyingi kuwawakilisha wenzetu hasa Madiwani; kwenye maeneo mengi ya mafao yao/posho zao; sasa kwa sababu Madiwani wengi mara nyingi wamekuwa waki-suffer kutokana na namna ambayo wanalipwa, kwanza nawapongeza kwa sababu Serikali imekubali zile hoja za Wabunge ambazo zilikuwa zinaletwa humu, nawe Mheshimiwa Naibu Spika alileta hoja hapa ili walau Madiwani walipwe kwenye accounts zao kama Serikali ilivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri mwingine ambao sasa kwa kuwa Madiwani hao wana wigo mkubwa na ziko kata nyingine kwa mfano kule Mbulu Vijijini ni kubwa na ni pana, hawana uwezo wa kuizunguka kwa mara moja. Sasa naomba Serikali iangalie kwenye bajeti hii waweze nao kupewa mikopo kama tunayopewa Wabunge ili mikopo hii basi ikawasaidie. Aidha, wapewe usafiri na iandikwe kabisa na ziwe katika principal ambazo wao wenyewe wanaweza kulipa kutokana na fedha ambazo watapewa na kuongezewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiinua mgongo cha Mheshimiwa Diwani ni kidogo sana, lakini posho ile ikiongezwa ni wazi kwamba unaweza kuangalia katika mafao haya anaweza kukopeshwa nini? Aidha, kama ni gari dogo au pikipiki. Kwani hawa ni wawakilishi wetu wa kutosha katika maeneo ya kata zetu, kwa hiyo, naomba hili lizingatiwe sana. Kwa sababu hii basi, wataweza kusimamia miradi, maana miradi mingi katika maeneo yetu wanapaswa kusimamia kwa ukaribu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kamati ambayo inaweza kusimamia miradi ni Kamati ya Fedha kwa mujibu wa sheria na inapata nafasi ya kuzunguka mara nyingi katika maeneo ya Halmashauri. Kwa hiyo, unapompa na kumwezesha Diwani akaweza kuzunguka maeneo haya ni wazi kabisa miradi itasimamiwa kwa karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kuwa sasa Halmashauri imeshaondolewa mzigo wa ulipaji wa hii posho na mishahara ya Madiwani, napendekeza, tuna Wenyeviti wa Vijiji ambao bado hawajakumbukwa, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie na Serikali ione, Wenyeviti wa vijiji asilimia 20 inayotajwa kwenye kanuni zetu haziwafikii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwa sababu mshahara ule wa Madiwani umeshaondolewa kwenye Halmashauri kwa kupitia mapato ya ndani, kwa nini fedha hizi zisiende basi tukawapatie Wenyeviti wa Vijiji hata allowance kidogo tu? Hata kama siyo mshahara, basi posho ya mwezi kidogo tu ili Mwenyekiti wa kijiji aone kwamba aah; awe na utaratibu, maana ukiangalia katika mtindo wa sasa hivi, Mtendaji wa Kijiji analipwa fedha. Kwa hiyo, inaonekana Mtendaji wa Kijiji ni bosi wa Mwenyekiti kumbe kwa kawaida kabisa Mwenyekiti wa Kijiji ni bosi na ana Serikali yake ya Kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Serikali zote ambazo zimeachwa kidogo, ni Serikali ya Kijiji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Serikali kwa Wizara ya Fedha ione ni namna gani, kama siyo bajeti hii, basi bajeti ijayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wenyeviti wa Vitongoji ni wa msingi sana kwa sababu wao ndio wanaotoa habari, wanaotoa taarifa na ndio wanaoandaa mikutano, ndio wanaotekeleza sera zote na ndio wakusanya michango. Kwa hiyo, hata hao wanapokusanya michango waonekane basi. Serikali ipange utaratibu wa namna fulani, hata wao fedha chache ziwe zinawafikia. Hata wao isiwe kama bakshishi, iende kwenye account. Maana siku hizi kila mtu ana account, waelekezwe hao wapate na fedha kidogo hata kama fedha zenyewe ni chache, lakini ajue kwamba anapata kiwango fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini wakishapata utaongeza morality katika Serikali kutoka kwenye ngazi ya Taifa hasa hadi kwenye vitongoji maana hao wote ni Serikali. Ukifanya hivi, Serikali hii itakuwa imejiwekea legacy; na Mheshimiwa Mwigulu utakuwa umejiwekea legacy kwamba, kwa kweli katika wakati wako umeweza kufanya hii ya kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Madiwani sasa wanaenda kufaidika. Kwa hiyo, naomba hivi vyeo viwili visisahaulike, maana ni vyeo vya msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye miundombinu na hasa ya barabara. Duniani kote, uchumi hauwezi kwenda vizuri kama miundombinu iko vibaya na hasa miundombinu ya barabara. Naomba Serikali ione, mmeelekeza fedha kwenye barabara nimeona, lakini siyo kubwa sana, ni kidogo. Kwa hiyo, naomba elekeza maeneo haya kwa sababu wakulima wanapotoa mazao, wanapopeleka viwandani na uzalishaji unakuwa mkubwa, Serikali ni rahisi na kupata kodi na kukusanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko barabara ambayo kwa kweli nisipoisema naona kama sijafikisha ujumbe, ni barabara yetu moja ya Karatu – Hydom – Sibiti. Nashukuru kwanza Waziri amejibu swali langu leo na kwa kweli amesema inatangazwa kilometa 25. Kwa ajili hiyo nilishawahi siku moja kuomba hapa nipige sarakasi, hilo na-withdraw, leo sipigi hiyo, kwa sababu nimeona kwanza Serikali imekubali na inataka kujenga barabara hiyo. Ni vizuri kushukuru hata kwa kidogo, ni 25 zimetangazwa, nimeziona na imesemwa imetangazwa na ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, mmetangaza kilometa 25. Sasa kilometa 25 ni kipande kidogo sana. Kwa bahati nzuri hiyo barabara iko kwenye bajeti inaonyesha kilometa 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe basi, kwa sababu inaonyesha kilometa 50 na hii ni ahadi ya Rais, ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano na sasa ni ahadi ya Rais wa Awamu hii ya Sita, mama Samia Suluhu Hassan, alikuja akaisema barabara hii akiwa Dongobesh akiwa pia Haydom. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa itakuwa si vyema sana na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa sababu ni Waziri wa Fedha wewe barabara hii, lazima niseme tu ukweli kwa namna fulani ni mdau. Sasa niombe najua bajeti ni kidogo yaani rasilimali ni kidogo, lakini naomba mwakani uiwekee fedha ili walau basi isiwe katika ile hali imesemwa kwamba 25 kwa sababu barabara hii inapita Majimbo tisa; Jimbo la Karatu, Mbulu Mjini, Jimbo la kwangu la Mbulu Vijijini, Jimbo la Mkalama na inakuja mpaka Iramba na inakwenda mpaka Sibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi barabara hii itakapofunguliwa itakuwa imekidhi maeneo mengi sana kwa kuwapatia watu hawa huduma. Na unajua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu barabara hii inaleta watu wa kwako wa jimboni kwako kuja katika eneo la Haydom Hospitali. Ni hospitali kubwa sana ya Kanda ambayo iko pale, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ajue, anapoanza kujenga hiyo barabara aangalie kwa sababu pale hizi kilometa 25 sijui utaanzia wapi? Na sio suala langu linakuwa la Mkandarasi, lakini angalia eneo hili la Haydom kwa sababu eneo hili ni oevu na pale kuna maeneo ambako hayafiki na hayafikiki. Basi uone ni namna gani ya kuanza kilometa 25, sikupangii uanze wapi lakini angalia eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ukiangalia, katika mpango huu wa bajeti, ninaifurahia sana. Lakini nitashukuru kuona kwamba, bajeti ya mwaka huu nimeona pia ipo kilometa zingine 25. Sasa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wewe ni mtani wangu, unajua kabisa na yupo Mheshimiwa Msaidizi wako anayeitwa Comrade Masauni na nyinyi ni vijana wenzangu. Tumekuwa wote Jumuiya ya Vijana hebu wekeni kilometa hii 25 ijayo, ili zifike 50 na hii barabara ikamilike. Weka hiyo legacy basi bwana usitake nikaanza kuruka sarakasi huku na unajua hataniruhusu. Sasa kama haniruhusu rafiki yangu si uweke tu fedha mambo yaende vizuri. Kwa nini tuanze kuvunja Kanuni za Kibunge wakati wewe ni Mbwanee na Mbwanee ni Saitaa na Saitaa mambo yote mazuri. Brother weka hii fedha ili baadaye kule mzee tuzeeke tukiwa tuna barabara. Sasa hivi ni vijana brother na barabara hii inapita jimboni kwako, inakwenda mpaka Mkalama, inakutana kule kwa nini usiweke hii fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamaa ameishia hapo kilometa 25, bajeti hii ya kwako hii. Bajeti ya Mama Samia Suluhu Hassan ya 2022 kwenda 2023 na wewe Mheshimiwa Engineer Masauni hapo wekeni barabara hii na Mheshimiwa Naibu Spika uko hapa na najua mtaweka barabara hii na Mungu atawabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapa kwa sababu kengele imelia. Lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii na Mungu akubariki sana ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niseme machache. Kwanza namshukuru Mungu kunisaidia kusimama hapa mbele na kuchangia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu JPM, maarufu sana mzee wa kutumbua majipu. Mheshimiwa Magufuli amefanya mambo mengi na lazima tumuunge mkono. Nataka niseme leo hili, mimi namuombea kwa Mungu na namuombea kwa sababu anakutana na changamoto nyingi ambazo kimsingi sisi Wabunge tunaziona. Kutumbua majipu siyo kazi rahisi, anapotumbua majipu kuna wengine wanaumia, wengine wanalia lakini wengine tunafurahi hasa sisi ambao tunatoka katika mazingira duni, sasa tunaanza kuona ukweli na uhalisia wa Serikali inavyozidi kuwajibika. Kwa nini nimeshukuru haya. Nimeshukuru haya kwa sababu tunaona sasa walau Serikali inaanza kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi na kumshukuru Rais, namwambia aendelee. Inawezekana wapo wengine wanabeza hali hii, tulitaka Rais mkali, tulisema yule mpole, sasa amekuja mkali tumuungeni mkono jamani! Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Mimi namuombea kwa Mungu na kila siku nitasali kwa ajili hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, katika Wizara hii ya Miundombinu, napenda kuchangia eneo moja kubwa na kwa kweli hili nimetumwa na wananchi wangu. Kwa kuwa tunakuja huku kwa kura, naomba niseme hili kwamba katika swali namba 76 lililoulizwa kwenye Mkutano wa Pili wa mwezi Februari, Mheshimiwa Waziri alinijibu akasema barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom - Singida itajengwa na walau itawekwa kwenye mpango wa upembuzi yakinifu kwenye bajeti hii ya 2016/2017.
Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimeiona kwenye ukurasa wa 152 na ndiyo maana naona kweli walau Serikali inafanya kazi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, huu upembuzi yakinifu basi usiendelee kwa muda mrefu sana kwamba mwaka huu mpaka mwakani upembuzi bado unaendelea. Barabara hii ni muhimu sana kwani pia imeahidiwa na Rais aliyetangulia. Juzi wakati anaomba kura Mheshimiwa Magufuli ameahidi tena barabara hii na wananchi wamempa kura na tuna imani kwamba barabara hii itaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu halafu baadaye iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu Mbulu na Mbulu Vijijini ni wilaya ya siku nyingi sana, nimeshawahi kusema hapa imezaliwa 1905. Tukifanya kitu kinachoitwa research hapa tutakuta kuna Wilaya nyingine ambazo zimezaliwa hivi karibuni, kimsingi naamini Mbulu inapaswa kupata haki hii. Mbulu imeweza kuizaa Hanang, leo Hanang kuna kaafadhali kidogo, imezaa Babati na imezaa Karatu. Kwa hiyo, naomba niseme leo wilaya hii imekuwa bibi na kwa kuwa imekuwa bibi hebu muoneni huyu bibi basi awe kama kijana aweze kupatiwa hii miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi huwezi kutoka Mbulu ukafika makao makuu ya mkoa ambayo ni Babati, uko mlima unaitwa Magara, wakati Mkapa amekuja miaka 11 iliyopita kwenye kona za Magara alishaanza kusema mke wangu mnampeleka wapi kwa sababu zile kona zinaonyesha kama zinarudi. Kuna daraja pale linaitwa daraja la Magara, ukiitwa kikao kama unatokea Mbulu, Mheshimiwa Lukuvi naona unacheka, ina shida ile barabara, nafikiri ulipata kizunguzungu ulipopita pale, kufika Babati kuna daraja kubwa pale. Kwa hiyo, naomba ndugu zangu wapendwa muone na Wizara iangalie daraja hili ili liweze kuwekwa kwenye mpango ujao, daraja litengenezwe na ule mlima urekebishwe ili tuweze kufika makao makuu ya mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutoka pale kuna barabara ya kutoka Dareda - Dongobesh, hii barabara imewekwa kwenye Ilani ya CCM na mimi naamini huu ndiyo wakati mzuri wa kusemea sasa. Barabara nyingine ni kutoka Haydom – Katesh. Barabara hizi zinasaidia sana wananchi wetu kutoka katika maeneo yao kwenda kwenye Hospitali ya Haydom. Barabara hii haishii hapa inakwenda mpaka Sibiti inapitia Mkalama na Kidarafa inafungua Mkoa wote wa Manyara kwenda Singida, itahudumia maeneo yote mpaka Simiyu kule. Kwa hiyo, ndugu zangu Wabunge wa maeneo haya niliyoyataja, nafikiri ndiyo wakati wa kuieleza Serikali sasa kuifanya barabara hii ipitike na iweze kuleta kitu kinachoitwa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri sisi tunalima vitunguu saumu kule, mpunga na mazao mengi ambayo kimsingi sisi ndiyo tunaolisha viwanda. Ukieleza habari ya uchumi wa viwanda, Arusha hawawezi kuendelea bila kuwa na barabara iweze kupeleka mazao ghafi au malighafi katika viwanda vya Arusha. Kwa hiyo, barabara hii ikitengamaa na mkaijalia kuipangia bajeti katika mwaka wa fedha ujao baada ya huo upembuzi, hakika mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Mungu kwamba Waziri kwenye majibu yake ya mwanzo amesema kwamba Benki ya KfW, Benki ya Ujerumani imekubali kufadhili barabara hii. Niombe sana, Mheshimiwa Waziri siku akiwa na kikao na hao wanaoitwa KfW tuite basi na sisi tuweze kushauriana nao tuweze kuweka hoja zetu ili barabara hii itoke Karatu – Mbulu - Sibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu najua muda ni mdogo sana, naomba nishauri mambo machache kwenye mawasiliano. Mawasiliano ni taabu katika maeneo yetu mengi sana hasa kwenye kata za Ari, Tumati, Mangisa, Yaeda Ampa, kule sisi tuna shida hiyo na ninaamini hii inasikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala kubwa sana la kitu kinachoitwa barabara za Wilaya kupandishwa hadhi kufikia kuwa barabara za TANROADS. Manyara tuna miaka minne barabara hazijapanda hadhi. Kwa hiyo, niombe Wizara iiangalie Manyara kwa jicho la pekee na kuipandisha ile barabara hadhi maana sasa hivi Mkoa wa Manyara barabara zake zimekuwa scattered, hatuwezi kutoka wilaya kwa wilaya. Ukitoka Kiteto kuja Babati ni tatizo, ukitoka Babati kwenda Hanang ni shida hasa kutoka Mbulu kwenda pia Babati, niombe haya, naamini Wizara inasikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine kubwa katika Sheria ya Manunizi, naomba Mheshimiwa Waziri anayehusika alete mabadiliko ya Sheria hii ya Manunuzi, tufanye mabadiliko ya sheria hii hapa ili walau tuweze kujenga barabara zetu sisi wenyewe.
Halmashauri ziwezeshwe kununua vitu vinavyoitwa caterpillar, grader ili tuweze kujenga barabara zetu wenyewe. Niombe Mheshimiwa Waziri anayehusika, hizi caterpillar zinapoingia hapa zisamehewe kodi hasa sisi tukileta maombi kama wa halmashauri ili tuweze kujitengenezea barabara zetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimshukuru sana Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri na kuweka barabara zetu hapa. Nachoamini ni kwamba barabara zilizoko kwenye Ilani zitakuwa za kwanza kutengewa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda kuchangia haya tu, nasema naunga mkono haja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nianze kwa pongezi. Naomba kwanza nimpongeze Rais wetu JPM maarufu sana Mzee wa hapa kazi tu, maana hili jina la J J mara nyingi linanitatiza sana lakini kwa kweli kwanini nampongeza Rais wetu? Ameonesha namna nzuri na mwelekeo wa Awamu ya Tano ya hapa kazi tu kwa kukusanya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda wangu ni mdogo, nataka niende haraka na nitaongea mambo mengi, nakwenda moja kwa moja kwenye suala la maji. Wananchi wametutuma huku kwa sababu wanahitaji kuishi, na maji ni uhai. Kwa kuwa maji ni uhai nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Wabunge wengi tunahitaji kuleta mawazo ya wananchi wapate maji, mimi nakuwa wa kwanza ku-declare kwamba, tufanye namna yoeyote watu wapate maji kule vijijini na mbinu ya kufanya hayo ni kuongeza kale katozo kadogo tu, ka sh. 50 tu kwenye tozo ya mafuta ya petrol na diesel. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa hivi petrol imeshuka thamani yaani bei imeshuka, lakini ukiangalia kwenye bidhaa zote hakuna mahali ambako inaonekana kabisa bei ya chochote imeshuka, nauli ziko pale pale, kila kitu kiko hapo hapo. Kwa hiyo, naomba niungane na Wabunge wenzangu waliojaribu kuweka mawazo yao kwamba, tuweke sh. 50 ili basi watu wetu wapate maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anakumbuka, nilitamani kutoa Shilingi siku ile ya Wizara ya Maji wakati wana-present hapa kitu kinachoitwa bajeti yao. Kwa kuwa maji kwenye Wilaya yangu ya Mbulu Vijijini wanahitaji bilioni tatu, nikiangalia kwenye bajeti humu haimo, tunaipata wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, niombe basi, nimetumwa na Wanambulu kutafuta maji humu, tumetumwa na ndoo. Slogan ya kwamba, tunamwondolea mama ndoo kichwani tutapata wapi kama tusipokuwa makini hapa kuhakikisha kwamba, tunayapata maji? Ndugu zangu Wabunge, hebu tuongelee kwa kilio chetu eti, tunahitaji kupata maji, hatuna namna nyingine zaidi jamani, zaidi ya kutafuta mwanya wa kupeleka maji vijijini. Kwenye Mji wangu wa Hydom kuna miradi 10 ile ambayo imeshafanywa, yani Serikali imepeleka pesa pale, lakini haikamiliki kutokana na nini? Hakuna pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe, kwa kweli Serikali mkikubali kuweka mpenyezo tu huu mdogo wa Sh. 50 kwenye kila lita, naamini tukahakikisha kwamba pesa hii inakwenda kule mahali ambako tumeamua hapa Bungeni na ikasimamiwa; na sasa hivi tunajua Mheshimiwa Rais ameweka mipango mizuri, Mawaziri wote mmesoma. Mama yangu! Serikali hii ya JPM iki-fail mimi sipeleki mtoto shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Watu wameenda shule, ni Madaktari, ni Maprofesa, sisi tulioingia humu tumekuja tu kuwawakilisha tu wananchi wetu kwa kuomba haya na tunaposema haya tunamaanisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kwa sababu muda ni mfupi niende kwenye suala la afya, afya tunalo tatizo kubwa mno. Leo hii ukimwambia mwananchi achague kati ya kujenga kiwanda na kujenga zahanati au kituo cha afya, atakwambia ni kituo cha afya kwa sababu anahitaji kuona afya yake inaboreka. Kwa hiyo, nina masikitiko makubwa sana. Ukiangalia kwenye Wizara ya Afya kwenye pamflet letu hapa, inaonesha kabisa Mbulu Vijijini hata kituo kimoja cha afya hakijaingia huku wala zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe, naamini inawezekana ni typing error, kwa sababu tuna hata own source ya Halmashauri yetu tumeweka na tumetuma huko, lakini kutokana na ukomo wa bajeti natambua kwamba kuna tatizo hilo, kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri aangalie sehemu hii hasa suala la afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu ya kuzianzisha hospitali au zahanati mpya. Akifanya research vijijini kuna zahanati na hospitali ambazo zimekaa muda mrefu hazijamaliziwa. Kwa mfano kule Dongobeshi Mbulu; wananchi wamechanga wamejenga hospitali yao, wamejenga theatre, wanasubiri sasa hivi kuezeka tu. Kwa hiyo, Serikali wakiweka kitu kidogo hapa kwa bajeti hii tunamalizia, tunaanza kazi, naomba niseme haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nataka nijielekeze kwenye hii milioni 50 ambayo kimsingi ni ilani ya Chama cha Mapinduzi, tumewaahidi watu kwamba, milioni 50 zitakwenda vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kitu kimoja; ukisema leo milioni 50 iende vijiji; nimeamini kwamba, bajeti inasema wataanza kutekeleza baada ya mwezi Juni, lakini naomba ni-question, ukipeleka fedha hizi kabla ya mwezi Juni hakuna financial institutions ambazo ziko kule zitakazosaidia watu hawa kupata pesa zao as equal katika vijiji vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipendekeze tu kitu kimoja; kwa sababu ukiangalia kwenye maendeleo ya jamii hapa au kwa hawa watu wanaojiita Maafisa Maendeleo, Maafisa Ushirika, nchi nzima wako 400 na hawa hawawezi kusimamia zile fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie namna ya kuunda hizi benki za vijijini ili angalau watu wetu waweze kusaidiwa namna nzuri ya kupeleka na kuweza kukopa na kukopeshwa. Ziende kwa mtiririko kulikoni kwenda moja kwa moja kwa namna ya kisiasa, vinginevyo tutapoteza kama tulivyopoteza zile fedha za Mheshimiwa JK au maarufu sana kama mabilioni ya JK.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili ambalo kidogo linakula vichwa vya wananchi, wameanza kutupigia simu huku; suala la transaction money kwenye hizi finance institution. Mimi sina tatizo sana na ukusanyaji wa kodi, lakini naomba niielekeze Serikali iangalie sana. Hizi transaction charges ambazo zimewekewa VAT kwenye Sheria ya Kodi, niombe kabisa Serikali iwe makini isije ikawa sasa wakayatoza mabenki, haya mabenki haya baadaye yakaamua kupeleka au kuweka VAT kwenye transaction za mtoaji wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sasa hivi wanafunzi wengi wana pesa ndogo wanazopewa kwenye boom. Akienda kutoa pesa zake kuweka kwenye simu kutoka benki anachajiwa, akiangalia salio anachajiwa ikiwemo VAT ndani, akituma anachajiwa, sasa mtu wa kawaida atakuwa amechajiwa mara nne kabla ya kutumia fedha hizo. Kwa hiyo, naomba Serikali iwe makini sana kuangalia hali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine niangalie eneo moja la watalii. Kuna jambo hili la watalii tuliangalie vizuri, nimesoma bajeti ya Kenya, ukiangalia wao wamekuwa wajanja wameondoa ile VAT katika kuwaingiza watalii kwenye mbuga zao. Sasa nashauri hebu angalieni namna ya kuweka kodi hii, aidha iwekwe kwenye vitanda au kwenye mahoteli, lakini ukimwekea hapa inakuwa ni tatizo. Kenya ukiangalia wameweka pesa zao nyingi katika kuwa- accommodates watalii na pia wametangaza utalii wao; angalia bajeti ya Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimsihi sana ndugu yangu Mheshimiwa Philip Mpango, najua ana mipango mingi na yeye ni rafiki yangu sana na ni baba ambaye nimeendelea kumpenda. Basi aangalie eneo hili namna ya kuweza kuwaingiza hawa watu wetu wasitutoroke. Sisi tuna utalii kule Mbulu, asituone hivi watu wanataka kwenda kuangalia Wahadzabe, wale click language ambao wamekaa interior kule, wanafikaje ukiweka kodi kwenye hili eneo? Itakuwa ngumu, watakatia Kenya wapotelee huko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, East Afrika sasa hivi kila mtu anataka kuvutia kamba kwake. Nimsihi ndugu yangu aangalie eneo hili vizuri, wataalam wa kodi walimshauri vizuri hapa ili anapo-charge kodi asimshtue mtu anayeitwa mtalii kabla hajaingia kwetu. Bahati mbaya sana ukiangalia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii hakuna fedha nyingi aliyoweka kwa ajili ya advertisement ya utalii wa Tanzania. Kwa hiyo, niombe sana hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua muda wangu umekwisha, lakini naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza nitauelekeza kwenye sehemu hii ya TASAF. Kwanza, nikubaliane na wachangiaji wenzangu kwamba TASAF inasaidia sana kwenye maeneo yetu hasa kwa kuziinua familia hizi ambazo zina hali duni. Changamoto ambayo tunapata kwenye maeneo yetu ni kwamba wanapoleta hizi fedha za TASAF mara nyingi watu hawa au familia hizi zinapata changamoto pale ambapo kunakuwa na michango ya vijiji. Fedha zinakuja kwa ajili ya kuwawezesha hawa wafaidika wa TASAF wenyewe wakati huo huo Wenyeviti na Watendaji wa Serikali wanawatoza michango kwa pesa hizi za TASAF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe kidogo Wizara itoe maelekezo kwa sababu pia hawa ndugu zetu wengine wamesamehewa michango kwa hiyo wanapopata ule mwanya wa kupata hizi pesa za TASAF wakati huo huo wanakamatwa michango na wanatakiwa kuchanga tena kwa kutumia pesa ambazo Serikali imewapatia kwa ajili ya kujisaidia kwa maisha yao. Kwa hiyo, niombe Serikali itoe elimu katika Serikali zetu za Mitaa hasa vijiji ili Watendaji waweze kuwasamehe watu hawa ambao pia Serikali imeona wana haki ya kupata hii pesa ambayo inasaidia kuwainua hasa hizi familia ambazo zina tatizo la kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena kujielekeza kwenye sehemu nyingine hasa hii ya ajira. Namshukuru kwanza Mheshimiwa Kairuki ameeleza jinsi ambavyo ajira zinategemea kuachiwa kwenye kada mbili za afya na elimu. Kwenye Halmashauri yangu ya Mbulu Vijijini tuna shida kubwa sana ya watumishi hawa hasa kwenye kada ya VEO na WEO. Sasa hivi watumishi hasa Walimu ndio wanakaimu nafasi za Maafisa Watendaji. Hebu niambie leo hii tuna tatizo la Walimu, tena Walimu wa sayansi wanakaimishwa nafasi hizi ili kusaidia mpango mzima wa governance huku chini. Pamoja na nafasi hizi ambazo Waziri amezitangaza leo wanazotegemea kutoa ajira za afya na elimu, wajitahidi kufungua ajira kwenye nafasi za Watendaji wa Vijiji na Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nitoe mchango mwingine katika suala la property tax, hii kodi ya majengo ambayo kimsingi ukiangalia sheria sasa inakwenda kukusanywa na TRA. Kwa sababu sheria hii bado haijatungwa na Bunge na tunategemea iletwe baadaye tuone jinsi tutakavyosaidia kwa sababu TAMISEMI wametoa maelekezo ambayo siyo mazuri sana kwenye Halmashauri zetu. Kwa mfano, Halmashauri yangu imepewa waraka ambapo inatakiwa ikusanye kodi ukiangalia wameweka viwango vya kukusanya kodi kwenye maeneo ambayo hayafai. Wamepanga pia kukusanya kodi kwenye nyumba za tembe na kwenye nyumba za majani. Mimi sikatai kodi inakusanywa na ni sheria na inatakiwa kukusanywa lakini siyo sahihi sana kukusanya kodi kwenye nyumba za tembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kule nina wapiga kura wangu wananchi wanaoitwa Wahadzabe wao wamezoea kukaa porini, lakini sasa tunawaomba tuwajengee nyumba ili wakae kwenye nyumba. Wakisikia sasa Halmashauri inakusanya kodi inayoitwa kodi ya majengo hasa kwa nyumba za nyasi na tembe wanapata maswali makubwa na kutaka kuendelea kukaa porini. Mheshimiwa Waziri naomba uangalie suala hili na lipo kwenye Jimbo langu la Mbulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia pia suala zime la upandishaji wa madaraja. Wako watumishi mwaka jana walipandishwa madaraja na wengine baada ya waraka kutoka wamesimamishwa kupandishwa madaraja. Niiombe TAMISEMI iangalie namna gani nzuri ya kuwapa pia motisha watumishi hawa ambao kimsingi wenzao wameshapandishwa madaraja baada ya waraka kutoka wamesimamishwa na hawezi kupandishwa madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukija kwenye Halmashauri yangu ya Mbulu Vijijini specific asilimia 90 ya Wakuu wa Idara wanakaimu. Sasa basi niombe kwa sababu Halmashauri tumeshaleta mapendekezo ya kuwapandisha hao Wakuu wa Idara, Serikali iweze kutoa mwanya wakuu hawa wapandishwe. Mtu ameshakaimu miaka mitano unategemea nini? Naomba Serikali iangalie namna gani ya kuwapandisha na kuwarasimisha hawa Wakuu wa Idara ambao wamekaimu kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la asilimia tano za wanawake na vijana kwa habari hii tunayosema mikopo ya vijana. Ni vigumu kwa Halmashauri zetu za vijijini kuweza kutoa hizi hela kwa sababu gani? Hela za OC hazikwenda na Wakurugenzi wengi wanatumia pesa hizi hizi ili kuendeshea shughuli zao. Kwa hiyo, ni vizuri basi hizi fedha za OC ambazo kimsingi ziko kwenye kila bajeti ya Halmashauri za Wilaya ni vyema zikapelekwa kwa wakati ili Watendaji au Wakurugenzi waweze kuzitumia na hatimaye basi wasiende kwenye hela za vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye utawala bora. Mimi kwanza nishukuru sana, nina Mkurugenzi mzuri naamini hakupata semina au amepata semina lakini anafanya kazi yake vizuri, nampongeza sana. Pia nimeona wenzangu wengi wamelalamika sana habari ya Watendaji yaani Ma-DC. Mimi nampongeza DC wa kwangu anafanya kazi nzuri na nashukuru Mungu kama hajapata semina mimi naona kwa kweli anafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vibaya sana kila mtu kusema hapa Ma-DC wanafanya kazi mbaya, hapana, mimi nafikiri sio wote. Wapo wa kupongezwa na mimi nampongeza wa kwangu kwa sababu naona anafanya kazi nzuri. Pia nampongeza Mkuu wa Mkoa wangu naona kabisa anafanya kazi nzuri ambayo kimsingi ana-operate ile human right ambayo naiona mwenyewe. Pia namshukuru sana Mungu labda mimi inawezekana nimepangiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niunge mkono wenzangu waliosema wanahitaji semina elekezi. Ni vizuri basi Serikali ikaona, kama wenzangu na wengine wamepata tatizo hili la utawala bora ni vizuri hizi semina elekezi zikawekwa na zikapangiliwa kuliko kuwafanya wananchi, watendaji na Wabunge wenzetu wakawa na hali ya sintofahamu katika maendeleo, haiko vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Mawaziri wanaofanya kazi na nashukuru sana wamefika kwenye eneo langu. Nawapongeza sana kwa sababu wanafanya kazi kubwa. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwateua pia hawa Wakuu wa Wilaya, ndugu zangu Wabunge kama wasingeteuliwa Wakuu wa Wilaya wapya ingekuwa biashara kama ilivyo. Sasa hivi ukiangalia Serikali imeanza kukaa katika line yake. Leo hii watumishi wamekuwa na nidhamu. Ukienda kwenye Halmashauri zetu na maeneo mengi ya kazi hakika utaona wananchi wanatekelezewa na wanasikilizwa katika maeneo mengi. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kweli kwanza kwa kuangalia na kuiweka Serikali vizuri kwani sasa hivi Serikalini kuna nidhamu na wananchi wanasikilizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie haya tu, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba hii ambayo Mwenyekiti ameitoa ya Kamati yetu hii. Nami niseme ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na kimsingi nimetaka tu kusema machache ambayo wenzangu mengi wameyasema, nataka kukazia machache ambayo kimsingi nayaona katika Kamati yetu yamekuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hasa kuzungumzia kwenye sekta ya kilimo ambayo wengi wetu wamesema habari ya uchangiaji kwenye pato la Taifa. Ukiangalia sekta ya kilimo inategemewa na wananchi wetu wengi sana kwa kipato. Ni kweli Serikali imewekeza fedha katika eneo hili lakini kwa uchache sana. Ukiangalia sasa hivi, ukuaji wa sekta ya kilimo, mwaka wa fedha wa 2014 inaonekana ulikua kwa asilimia 3.4 lakini mwaka huu kwa robo hii ya kwanza ambayo tumeiona ina ukuaji mdogo sana wa asilimia tatu. Nashauri Serikali iwekeze zaidi katika kilimo na mifugo kwa sababu wananchi wetu wengi wanaitegemea sana sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo machache ambayo Serikali imejitahidi hasa katika kupeleka pembejeo za kilimo katika maeneo yetu lakini ukiangalia pembejeo zile zina utata, zinachelewa sana kuwafikia wakulima mara nyingi zinafika wakati ambapo mvua zenyewe zimekwisha kunyesha. Nishauri kidogo Wizara hii ya Kilimo kuangalia maeneo ambayo wanapeleka pembejeo hizi kuzipeleka kabla ya mvua ili wananchi waweze kupata pembejeo hizi mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mwaka huu Serikali imepeleka asilimia kidogo sana kwa wananchi wetu hasa pembejeo hizi ambazo kimsingi kwa sasa zimekuwa zikipiganiwa sana, Mikoa mingi imepata pembejeo baada ya mvua kunyesha. Pamoja na haya yote mazao yanayopelekwa kule, kwa mfano mahindi, yanapelekwa ya muda mrefu wakati wananchi wanahitaji mahindi au mbegu za muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Wizara iangalie wakati wanapeleka pembejeo hizi wapeleke pembejeo ambazo zinafaa kwa maeneo husika. Wataalam watusaidie kufanya research ili wajue katika ukanda fulani kama ni Nyanda za Juu Kusini, Mashariki au Magharibi, ni mbegu gani hasa inapaswa kupelekwa katika kusaidia jamii yetu. Vinginevyo wakiwa wanapeleka kama sasa kwa mfano wanapeleka hybrid maeneo ambayo yanahitaji samsung, itakuwa haina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niizungumzie moja kwa moja kwa undani kwa sababu kilimo tunakifahamu. Mara nyingi pembejeo zinazopelekwa mahali pale wakulima wanakuwa hawazipendi tena kwa sababu ni za muda mrefu na hazifai katika eneo hilo zinapopelekwa. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali iangalie upya suala hili la pembejeo tunazozipeleka katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pembejeo zinapelekwa wakati ambapo wananchi hawazihitaji tena, Serikali iangalie kama inawezekana ilete Bungeni tuone namna nzuri ya kusaidia twende kwenye mfumo wa moja kwa moja ili pesa hizi zinazotumika katika kupeleka pembejeo zitumike katika kushusha mbegu za mazao haya kuliko kupeleka msaada ambao mara nyingi unakuwa hauna tija tena katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye eneo hili la mikopo. Serikali au Chama cha Mapinduzi ukiangalia Ilani yetu tumeweza kuonesha kwamba tunaweza kuwapa mikopo hii ya shilingi milioni 50 kila kijiji. Katika maeneo haya Kamati imejadili kwa kina na niipongeze sana Kamati yetu kwa sababu tumeona na niipongeze Serikali wamejiandaa kwa pilot area. Sasa niombe zile institutions ambazo zinahusika na suala la fedha ziwe aware katika kuelekeza na kutoa elimu ambayo itasaidia katika vijiji vyetu wakati pesa hizi zikifika kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri haya kwa sababu unajifunza kutokana na makosa yanayotokea mara nyingi sana katika jamii yetu. Ukiangalia miaka iliyotangulia katika Awamu ya Nne kulikuwa na mabilioni ya pesa maarufu Mabilioni ya Jakaya. Pesa hizi hazikufanya vizuri kwa sababu hazikuwa na monitoring nzuri. Sasa niombe, ili kuwa na matokeo chanya fedha hizi zikifika katika maeneo yetu ya vijijini pawe na mpangilio mzuri na elimu itolewe kabla ya kupelekwa fedha hizi katika maeneo haya ili wananchi wajue kabisa fedha hizi ni za mikopo, wasione fedha hizi ni bakshihi wakazitumia bila kujua namna ya kuzirudisha. Kwa maana najua wazi pilot area hela zitapelekwa maeneo machache ili waweze kurudisha na maeneo mengine yaweze kupatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena kuzungumzia suala la afya au Wizara yetu ya Afya. Ni wazi tumeona jinsi bajeti ya afya ilivyokuwa na changamoto hasa kwenye masuala ya dawa. Nataka niende katika maeneo mengine ambayo kimsingi wengi tumekuwa tukihitaji kujengewa zahanati na vituo vya afya. Tulikuwa na mpango wa kujengewa vituo vya afya na zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mpango uliopo ni kujengewa zahanati, lakini kwenye maeneo yetu ya Halmashauri kuna maboma mengi sana ambayo hayajafikia kumalizika. Wananchi wengi wamejenga hospitali na zahanati na vituo vya afya ambazo zingine zipo kwenye lenta, madirisha na nyingine imebakia tu finishing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Wizara ya Afya katika bajeti ijayo ione namna gani ya kuleta bajeti ili angalau tuweze kujenga au kumalizia vituo vyetu. Kwa mfano, Wizara ya Afya ikiamua ikaleta bajeti ambayo angalau kila Halmashauri ikajengewa kituo kimoja cha afya kwa mwaka wa fedha hii itasaidia sana. Hakuna Halmashauri ambayo imo haina viporo hivi. Kwa maana hii basi tukiwa na Halmashauri 183 zikajengewa kituo kimoja cha afya kwa mwaka mmoja, kwa miaka mitano ukizidisha mara nne tutakuwa na vituo zaidi ya 800 ambavyo vimejengwa kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, kwa kufanya hivi katika miaka mitano kufikia 2020 tutakuwa tumejenga vituo vingi na vilivyomalizika. Kwa hiyo, huo ulikuwa ni ushauri wangu wa jumla katika Wizara hii ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la umeme vijijini. Itakuwa ndoto sana kwa Tanzania ya viwanda kuweza kupatikana bila kuwa na umeme wa uhakika. Inaonekana kabisa kwamba fedha ambazo zimepelekwa katika umeme (REA Vijijini) ni asilimia chache na sasa hivi tunasema REA III na REA II ambayo kimsingi inategemea kumalizika, bado maeneo mengi REA II haijafikia ukamilifu wake. Niombe Wizara iweke msukumo ili ile REA III iweze kuanza mapema, najua kwamba inakwenda kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara iwaangalie wakandarasi hawa wanapopewa tenda wawe na uwezo wa kumaliza kazi mapema. Tangu Awamu ya Nne yapo maeneo ya REA II ambayo mpaka sasa hayajakamilika kabisa. Hali hii inaweza kutudumaza zaidi sisi Watanzania na kauli ya Mheshimiwa Rais ya kutegemea kupandisha Tanzania iwe katika uchumi wa kati itakuwa ndoto kama tusipoangalia maana kiwanda hakiwezi kuendelea bila umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo niipongeze Wizara ya Maji inajitahidi sana katika maeneo haya ya kumalizia viporo vya maji. Kuna mpango ambao tunaendelea nao huu wa maji vijijini, niombe kabisa Wizara ya Maji na Waziri wa Fedha aone pia ipo miradi mingi ya maji ambayo kwa sasa ni viporo. Naomba sana Wizara ya Maji iangalie maeneo yale ili iweze kutoa fedha, hasa fedha ambazo naziona zinakuwa kizungumkuti…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kupata nafasi hii. Mchango wangu unaanza na sifa. Kwa sisi tunaoabudu na tunaosali kwa Kikristo ukitaka kuomba lazima kwanza uanze na nyimbo za sifa ili Mungu au Bwana wetu Yesu Kristo afahamu kwa kweli unamsifu ili akupe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza naanza pia kwa kumpongeza Rais wetu kwa kazi anayoifanya katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. Pia nawapongeza Mawaziri wote lakini kubwa nimpongeze Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa sababu kwanza amefika kwenye Wilaya yangu na kutatua kero za wafanyakazi zilizoko ndani ya Halmashauri ya Mbulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto ambazo zipo katika maeneo mengi hasa TAMISEMI ninao mchango mdogo ambao napenda kuuzungumzia leo. Serikali za Mitaa ilipaswa kukusanya mapato takribani shilingi milioni 332 lakini kwa bahati mbaya imekusanya shilingi milioni 232, ni sawa na asilimia 70. Ushauri wangu wa kweli katika kukusanya mapato ni vema sasa Wizara ikaelekeza msukumo
kwa Maafisa Maduuli ili kutumia mashine za EFD kukusanya mapato ambayo itasaidia Halmashauri zetu kuongeza mapato yanayoonekana kabisa. Kwa sababu research inaonyesha Halmashauri chache hazitumii mashine kukusanya mapato ya ndani. Kwa hiyo, niombe Wizara hii
iweze kupeleka moja kwa moja nguvu zake na kuwashauri Maafisa Maduuli kusaidia ukusanyaji wa mapato ili
Halmashauri zetu ziweze kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tunazo ahadi ambazo zimewekwa katika maeneo yetu ya Miji Midogo. Kwa mfano Mbulu Vijijini tuna ahadi ya Mheshimiwa Rais na naamini sasa kutokana na Road Fund mnaweza kutusaidia ahadi ya kilometa tano ya lami iliyowekwa katika Mji Mdogo wa Hyadom. Nafikiri Mheshimiwa Jafo umefika na umepata maswali ya ndugu zetu wananchi wa pale ambao wametaka ile ahadi walau itekelezwe ili mji ule upate sifa hata ya kuwa na lami na kilometa mbili za Ndongobesh. Pia nafikiri umeonana na wananchi wa Dongobesh waliokulilia hasa ule mradi wa maji umaliziwe tu, imebaki hela kidogo shilingi milioni 600. Baada ya kushukuru kwa kutupa shilingi bilioni 1.8 malizieni basi ule mtaro ili maji yawezekwenda na wananchi wafaidike katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema nimesifu mapema ili ujue kwa kweli nahitaji kuomba. Kwa kweli maji ndiyo msingi hasa wa maendeleo ya wananchi wetu hasa kwenye kilimo. Katika haya basi mtusaidie kwa sababu Serikali imeshawekeza hela ya kutosha bado tu eneo dogo la kuweka mtaro wa maji kwenda kwa watumiaji ili kilimo kianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao viongozi wetu wengine wanaotusaidia kwenye kazi kwa mfano Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani. Madiwani wako wenzangu wamezungumzia sana kwamba posho yao ni ndogo na wanasimamia miradi mikubwa ambapo kimsingi
wanafanya kazi nzuri sana. Niombe leo TAMISEMI waangalie namna nzuri ya kuwasaidia Madiwani hawa kwa kuwapandishia posho yao kidogo ili angalau wafanye kazi inayotakiwa kikamilifu kwa kusimamia Serikali za Mitaa hasa kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia vijiji vyetu, Wenyeviti wa Vijiji wanafanya kazi nzuri sana lakini bahati mbaya sana hawana hata posho. Kama inashindikana kuwalipa kwa muda wote wapatieni basi bakshishi kwa muda fulani wafurahi na waone Serikali yao inawajali. Hata ndugu zetu Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji naomba muone namna ya kuwasaidia katika mapato yetu ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo hasa katika Wizara ya Utumishi. Namuomba sana dada yangu anisaidie hasa tatizo la upungufu wa watumishi. Halmashauri yangu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi lakini pia tuna Wakuu wa Idara ambao wanakaimu kwa muda mrefu sana. Zaidi ya 80% ya Wakuu wa Idara wa Mbulu Vijijini kwenye Halmshauri yangu wanakaimu. Niombe basi wapandishwe washikilie hayo madaraka nao waone kwamba Serikali yao inawajali maana wamekaa kwa muda mrefu hawajui waende mbele au warudi nyuma. Mheshimiwa Waziri naamini wewe ni makini na unasikiliza haya, angalia Mbulu Vijijini kwa namna ya pekee sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara pia iangalie, tumeshafanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi lakini kuna sintofahamu ya kutumia force account kwenye Halmashauri. Naomba basi Wizara isaidie na ije na kanuni ya kutumia ile force account ili watumishi waelewe namna ya
kuitumia na kupunguza gharama ya miradi katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru katika ajira mmetusaidia kwa kutupatia walimu wachache wa sayansi.
Sisi tuna upungufu mkubwa sana wa walimu katika maeneo yetu. Niombe basi wakati ujao ajira za walimu hasa wa sayansi ziongezeke, lakini pia tunaomba ajira ziongezeke kwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi umetoka maelekezo na waraka kuwaelekeza Wakurugenzi wawaondoe walimu katika kukaimu nafasi za kata na vijiji. Wananchi wetu sasa wameamua kuwaweka watu ambao wanawalipa wenyewe ili wasaidie kuzikaimu nafasi hizi za Watendaji wa Kata na Vijiji. Naomba Wizara iangalie namna gani ya kuajiri Watendaji hawa wa Kata na Vijiji. Wako watu wamemaliza shule na wana weledi wa kufanya kazi hizi hasa katika maendeleo ya jamii. Ni vigumu sasa kusaidia wananchi kwa sababu wale wanaoshika nafasi hizi hawana ule weledi wa kutoka. Kwa sababu Serikali za Vijiji ndiyo zinawalipa kwa hiyo wanaajiri mtu yeyote tu wanaoona anafaa na anakaa pale ofisi walau kufungua na kufunga kwa hiyo hawezi kuwasaidia wananchi katika kuibua miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Maafisa Maendeleo ya Jamii wengi sana wamemaliza vyuo wako vijijini, Wizara iangalie tu namna ya kuwaajiri. Maana Serikali huku juu mnafanya kazi nzuri hapa katikati kwa Wakuu wa Mikoa vizuri, kwa Wakuu wa Wilaya vizuri, kwa Wakurugenzi vizuri, Wakuu wa Idara vizuri, kule vijijini wanakaimu watu wa kaiwada tu, tusaidieni basi tuleteeni wataalam ambao wataweza kufanya kaz kwa kuajiriwa na kuibua miradi, maana sasa hivi miradi inatoka juu inakuja chini. Kwa mimi niliyesoma Maendeleo ya Jamii wanasema top-down inatakiwa iwe bottom-up yaani miradi itoke chini kwa wananchi ili walau wao wenyewe waweze kujipangia miradi yao na waone miradi hii ni ya kwao na waiendeleze na wananchi wanaweza kufanya kazi hii kwa uhakika zaidi. Kwa hiyo, nilitaka niyaseme haya ili walau Serikali isaidie katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba nizungumzie habari ya mikopo ya vijana na wanawake. Katika Halmashauri zetu zile asilimia tano, tano kufikia asilimia kumi ni vigumu kutekelezeka kwa sababu hii. Fedha zinazoenda kwenye Halmashauri kama OC haziendi kwa
wakati au haziendi kabisa. Kwa hiyo, Mkurugenzi anaona kuliko undeshaji wa Halmashauri ukwame anatumia zile fedha za mikopo ya vijana ambayo anatakiwa itoke kwa mujibu wa kanuni. Hawezi kutoa kwa sababu hana fedha za kutumia, kwa hiyo basi anakwenda kutumia zile fedha za mikopo ya vijana. Naomba Serikali ijitahidi kupeleka fedha walau fedha hizo ziweze kwenda...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya leo kuchangia katika bajeti hii ambayo kimsingi nadhani itakuwa ya kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kuishauri Serikali katika bajeti hii. Yako mambo ambayo kimsingi nimeyasoma katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri ambayo kwa kweli naona tu nielezee kidogo. Masuala haya ya mipango mkakati, katika miradi ya mkakati ambayo Mheshimiwa Mpango umeeleza kwenye mipango yako, nikuombe basi kwa kuwa umeeleza miradi hii ya kiuchumi ya vipaumbele
...

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Mchuchuma ambao umeonekana kipaumbele katika bajeti yako, mradi wa mitambo ya kusindika gesi, Mradi wa Biashara ya Kurasini, mradi wa uwekezaji wa Bagamoyo, mradi wa Mtwara, miradi hii ambayo inaonekana kwenye mpango wako kwa kuwa umeweka miradi hii kama eneo la mkakati wa kuinua uchumi wa Serikali na nchi yetu basi maeneo haya nishauri tu, miradi hii sasa ifike mahali kwa pesa nilizoziona zimetengwa humu. Kwa mfano Mradi wa Biashara ya Kurasini iko bilioni 109 ambayo imeshalipwa fidia pale, pesa zimekaa pale. Niombe kutokana na mkakati huu Serikali ipange namna gani nzuri ya kuendelea na mipango hii ili walau Tanzania ikaweza kuendelea kutokana na mipango hii ambayo tumejiwekea yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kushauri katika eneo hili la maeneo hasa ya maji vijijini. Maji vijijini ukiangalia kwenye bajeti iliyopita fedha za maji vijijini imeenda kwa asilimia 19. Niombe kwa kuwa umeonesha kwenye mpango wako huu kiwango hiki cha maji basi iende kadiri ilivyopangwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. Pia angalia maji vijijini tunahitaji sana kwa sababu tozo ya maji haipo sasa na Wabunge tunapendekeza tozo hii iweze kuingia humu, Serikali ikubali basi ushauri huu ili walau maji yaweze kwenda vijijini. Hakuna eneo lolote unaweza kumwambia mtu katika eneo la vijijini hatuna maji kwahiyo tuangalie katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni habari ya REA. REA imeonekana kuchukua kasi yake na wananchi wanaifurahia, lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, pamoja na Waziri wa Nishati naamini Kalemani umefika kwenye eneo langu. Mbulu Vijijini tunahitaji umeme wa REA, hakuna viwanda bila umeme. Kwa hiyo nikuombe katika bajeti hii utuone vizuri sana sisi wananchi wa Mbulu Vijijini. Pia barabara hatuna, nimeamua kusema harakahara haya ili yaeleweke. Sisi kule barabara hatuna na umepita kule. (Makofi)

Mheshimiwa Kalemani ulifika Mbulu, ukaiona barabara ile, ulisema kabisa kwa maneno yako nanukuu; “mngeniambia barabra hii iko mbaya namna hii ningetafuta barabara nyingine” haya ni maneno yako Mheshimiwa Waziri. Sasa nikuombe kitu kimoja kwa ajili hii basi miradi hii tunayoiomba pesa ziende. Mheshimiwa Mpango anafahamu nimeleta maombo yangu kwake kuhusiana na msamaha wa kodi ya VAT katika grand ambayo tumepewa.

Narudia tusaidie basi katika mabadiliko ya sheria ambayo yanatakiwa kuja Bungeni, naomba sasa sijaona vizuri humu ulete mpango huo ili walau sheria hii ibadilishwe, pawe na mwanya wa kusamehe kodi kwa fedha za wafadhili mmoja wanaotaka kufadhili kujenga madaraja ya kwetu. Nafikiri hili unalifahamu na utaamua kulifanyia kazi na sisi Wabunge tuangalie maeneo haya, kwa sababu mfadhili anatusaidia na sisi tunasaidiwa katika bajeti yetu basi tuone namna gani sheria iruhusu kusamehe kodi kwa maeneo haya ya wafadhili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri jambo moja, wenzangu wengi wameongelea sana kuhusu madini, nimeona pia katika kitabu chako cha hotuba yako Mheshimiwa Mpango ukurasa wa 49 umeandika kwamba Serikali haitaruhusu usafirishaji wa madini kwenda nje yaani kutoka kwenye mgodi kwenda nje, hili sina tatizo nalo. Nataka nishauri kitu kimoja, ukitaka kuzuia hii madini tuanzishe soko la madini, liwepo hapa nchini ili walau soko hili likitambulika Serikali ni rahisi kukusanya mapato katika soko. Tatizo letu lililoko hapa watu wakichimba madini katika maeneo yetu wanakwenda kwa njia za panya wanauza nje kwa sababu kuna soko huko nje. Kwa hiyo, ninashauri Serikali ianzishe soko la madini yetu yote yanayoonekana yanapatikana nchini ili wananchi wasitoroshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi naomba niongee leo kama ushuhuda. Sisi wote tumeingia humu kuwakilisha wananchi wetu, lakini pia Serikali imeanza kazi na nimshukuru sana na niseme kabisa namuombea Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa sababu ameonesha nia ya kuisaidia Tanzania kwa kujitoa muhanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua hakuna anayeweza kusema anamuombea kwa upande fulani ninaoufahamu, lakini nimshukuru sana leo Mheshimiwa Mbatia amesema hapa mwenyewe kwa kauli yake na nimtaja kwa jina kwa sababu Hansard zinarekodi, anamuunga mkono Rais kwa suala hili la madini na ule mchanga ambao umesemwa sana sitaku kuusemea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Biblia inasema kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe, na sisi naomba Waheshimiwa Wabunge nataka niwahamasihe jambo moja. Kubeba msalaba wake mwenyewe kwa siye tunaoabudu kwa dini ya Kikristo na Waislamu ambao wamefunga mwezi huu wa Ramadhani tumuunge mkono Rais wetu, sheria zitakapoletwa Bungeni tuanze kuweka vizuri mipango yetu ili katika haya Mheshimiwa Rais amejilipua, anahitaji kutusaidia na ameomba ridhaa wananchi tumempa. Habari ya kwamba ametoka chama gani, chama A, chama B tumeingia kwa vyama lakini ukiangali research inaonyesha tuangalie maslahi ya nchi, kwa sababu wanachama wetu wa vyama vyote hawafiki hata robo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutee Tanzania, tumeingia humu kwa vyama vyetu lakini sasa tutee mama yetu Tanzania. Kila mtu ameapa hapa na tumeapa kuitetea Tanzania, tunateteaje sasa? Nimesikia mchangiaji mmoja akisema hapa bado wakati wa kumpongeza Rais Magufuli. Unasemaje bado wakati mwenzako ameonesha nia? Mimi ninamsikitikia sana ndugu yangu Lissu, akionyesha nia mtu mmoja mshangilie kwa nia hiyo baadaye uhoji matokeo. Lakini nikuombe kaka yangu, mtani wa Singida tumtetee huyu ndugu aliyeonyesha nia kwa sababu ni Rais hakuna Rais mwingine zaidi ya huyu. Tukimtetea kwa nia aliyoonyesha atasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote wanahitaji maendeleo, na sasa tumeibiwa kwenye madini, tunaona tumeibiwa kwenye madini, na nimuombe Rais asiishie kwenye haya maeneo tu aende kwenye maeneo yote ya uchimbaji wa madini akadhibiti huko kabisa kwenye migodi ili migodi hii ionekane, iingize pesa za kigeni ili Tanzania tupate maji, barabara pia tupate vitu vingine vya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndio nilitaka niseme ili watu waelewe na Waheshimiwa Wabunge waelewe kutoka CCM na kutoka CHADEMA kwamba Mheshimiwa Rais amesema kwamba analeta sheria ya mabadiliko ya madini huku tukasaidie hali hii kwa kutumia uwingi wetu humu.
Uwingi maana yake nini? Sisi Wabunge kwa sababu ndio tunaobadilisha sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbele zaidi ninajua kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Mpango kwanza nimshukuru sana amejitahidi sana kuelezea maeneo mengi sana lakini Serikali itusaidie katika maeneo haya ambayo imeanzisha tawala mbalimbali imeelekeza maeneo haya ya vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele ni kweli lazima tuviendee lakini kuna tozo ambayo sisi tunaiomba kama Wabunge kuongeza kwenye mafuta shilingi 40 tu. Najua yataongezeka, najua kuna tatizo kupanda na kushuka bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja tu Serikali ikubali tuongeze jambo hili la ongezeko la tozo kwenye mafuta ili tupate maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina jinsi kwa sababu muda umekwisha naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu hapa. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa afya njema ya kusimama hapa na kuchangia. Pili, niishukuru sana Serikali kwa kufanya kazi kwa jinsi hii ambayo angalau sasa kuna matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nianzie hapa alipoishia mzungumzaji aliyepita. Tunayo ahadi tumeitoa kule ya hizi milioni 50 (village empowerment), Ilani maana yake ni mkataba kati ya mtawala na mtawaliwa nasi tumeshaahidi kwamba wananchi tutawapatia mikopo ya milioni 50 na tumeandika. Kwa ushahidi zaidi naomba niitetee na kuiinua Ilani yetu ambayo tumeahidi katika uchaguzi. Ukiangalia ukurasa huu wa 112 tumeandika hapa na kwenye kifungu cha 57, kwamba tutapeleka milioni 50 kila kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Serikali ina changamoto nyingi, sikatai, lakini mwaka jana tumeahidi katika mpango ule wa bajeti kwamba tutapeleka bilioni 59, hatukuweza, mwaka umekwenda. Bilioni zile 59 tumeahidi tena nimeiona kwenye mpango wa bajeti ya sasa ya Serikali. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, iko bilioni 60, ndugu yangu naamini anafanya kazi nzuri, nafurahi kwa sababu ametenga mwaka huu. Ukitenga basi peleka, nimesema kwa kifupi namna hii ili ajue kwamba wapiga kura wanatusubiri, baada ya kutoka Bungeni kwa vyovyote tunakwenda kwa wapiga kura, wanauliza swali la kwanza kwenye mkutano lini mnatuletea mkopo wa milioni 50 mlizotuahidi. Sasa Serikali naomba tufanye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri leo hii kwamba, katika kutekeleza ahadi ndiko unakomwona mwananchi wa kawaida anakubali mwelekeo mzuri wa Serikali yetu na tukitaka tuungwe mkono tutimize ahadi. Huu ni mwaka wa pili sasa tunaenda kumaliza na ni mwaka wa kazi, basi tuanze kwa kiwango fulani ili mwananchi aelewe kwamba, ni kweli Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeanza kutekeleza Ilani yake kwa kutoa milioni 50, angalau vijiji fulani vionekane, naamini wenzangu wamesema sana kuhusu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kiuchumi. Uchumi wa nchi yoyote unahitaji maendeleo na maendeleo yanahitaji ushauri na ushauri unahitajika wa kitaalam. Ukiangalia, nimesoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, ukurasa wa 40, anaeleza jinsi Tume ya Mipango, nashauri kama inawezekana basi Tume hii iwe peke yake isiwe ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango ili inapopanga mipango yake iweze kushauri namna ya utekelezaji mzuri. Kwa sababu ikiwa pamoja inakuwa sio rahisi tena kushauri, naona kuna mkanganyiko hapo. Kama inawezekana iingie kwenye Ofisi ya Rais huko ili ikasaidie katika kutekeleza mpango wenyewe, maana wakati huu Tume ya Mipango inavyopanga na inapokuwa kwenye Wizara ya Mheshimiwa Dkt. Mpango, naona kuna mkanganyiko kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, katika uchumi wa nchi yoyote, sisi tuna benki, ni lazima Serikali iangalie benki zake. Kwa mfano, Benki tuliyonayo ya TIB Serikali isipowekeza kwenye benki yake yenyewe ambayo ina asilimia kubwa inayoendesha haiwezi kuendelea. Kwa nini nasema hivi; ukiangalia mitaji yoyote duniani Serikali ikiwekeza kwenye benki hii ni rahisi kwenda kwenye benki hii pia na kuona namna gani na hata ukienda kwenye soko la kimataifa huko ukiwa na asilimia 20 angalau umewekeza kwenye benki hiyo utaona pia mataifa mengine unaweza kufanya kazi nzuri katika biashara ya masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye research na wataalam wamsaidie Mheshimiwa Dkt. Mpango, najua ni mtaalam, nchi nyingi zilizoendelea zinalinda benki zao. Kama tatizo ni mtaji katika Benki ya TIB Serikali iwekeze pale. Kwa mfano, ukiangalia nchi ya China, China wana Exim na hawakubali pale mitaji yao ipotee, ukienda South Africa wana DBSA, hawakubali, ukienda Norway wana DNB, hawakubali, wana benki wanayoitegemea. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie hali hiyo, nimeona nishauri haraka kwa sababu dakika zangu sio nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwanza nimshukuru sana amenisaidia katika mambo mengi hasa kule Jimboni, lakini sasa tunao mkanganyiko wa sheria, Sheria ya Kodi au Zuio la Kodi (withholding tax). Sheria hii naamini katika Bunge lililopita walifanya zuio na kuondoa misamaha yote, huenda walikuwa na mapenzi mema lakini sasa mapenzi mema tumekuwa kama tumejinyonga wenyewe katika kuondoa misamaha yote na kuondoa uwezo wa Waziri kusamehe. Mheshimiwa Waziri alete ile sheria ili Bunge hili tubadilishe, tuone nafasi nzuri ya kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa. Sitaki kutoa mwanya kwa mkwepa kodi yeyote lakini nimwombe alete sheria hiyo ili tuifanyie marekebisho kupitia Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mfano hai, kama Mbunge yeyote tunaomba mara nyingi misaada na kama Serikali inavyoomba misaada, nilijaribu kuandika proposal katika Wilaya yangu kujengewa daraja na daraja hilo ni muhimu sana, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwanza ameliona, nashukuru amelishughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa na Serikali ya Norway na watu tu wanaosaidia wenye mapenzi mema milioni 125 ya mwanzo ya kujenga daraja sasa kutokana na sheria yetu, panatakiwa pawepo mtu atakayelipa zuio la kodi la asilimia 18. Sasa basi ukienda kwenye Halmashauri zetu ukitaka walipe pesa hizo hawana uwezo Halmashauri yenyewe tu haina uwezo wa kulipa hiyo pesa ya zuio la kodi kwa sababu haina chanzo kikubwa cha mapato….

MWENYEKITI: Mheshimiwa siyo zuio la kodi ni VAT

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani ni VAT asilimia 18. Kwa hiyo basi sheria hii isipoletwa hapa tukafanya mabadiliko ndipo tunapojinyonga wenyewe.

Kwa mfano, mfadhili amenisaidia ametupa milioni 152 za kujenga daraja, Serikali ya Halmashauri au Serikali ya Mitaa haina uwezo unapata wapi? Ukija kwa Waziri hawezi kusamehe kwa sababu sheria haimruhusu na ukisema yule mfadhili akalipe hiyo VAT anakataa anasema mimi nakusaidia wewe kukujengea daraja halafu wewe unataka mimi nilipe kodi yako, haiji hata kwa utaalam wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone zile sheria ambazo zinaweza kuletwa hapa Bungeni, niombe kabisa Serikali ilete tufanye kazi kwa niaba ya wananchi, tuzibadilishe Sheria hizi kwa manufaa ya nchi yenyewe kwa sababu vinginevyo tutajifungia nati mpaka msumari wa mwisho. Hii maana yake ni nini basi? Tumeweka sheria hizi lakini tusijifunge moja kwa moja tukashindwa kufanya kazi kwa ajili ya sheria na kwa sababu Wabunge ndiyo tunatunga sheria, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, naomba tena sana alete ile sheria tufanye marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kwa uchungu kwa sababu Serikali kwa bahati mbaya au nzuri haina namna ya kuleta pesa ya kujenga madaraja. Kuna kitu kinachoitwa ceiling (ukomo wa bajeti), ukomo wa bajeti ukishafika madaraja yetu kule katika maeneo ya vijijini hakuna namna, tunapopata wafadhili kama hawa, basi ni vizuri akakubali ili akatoa msamaha wa kodi katika sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimesimama ili kusudi kulisemea hili. Hata hivyo, niipongeze na kuishukuru Kamati yangu kwenye ukurasa wa 23 imeandika, hili siyo la kwangu kama Flatei, Mbunge wa Mbulu Vijijini hapana! Hili ni jambo la Kamati lipo humu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwaombe sheria itakapoletwa tuisaidie Serikali pia kuweka mwanya huu ambao utasaidia Waziri, kama ikishindikana basi Waziri Mkuu apewe hiyo authority ya kusamehe kama inakuwa shida huku chini au tujue nani anatoa au Rais apewe basi, kuliko kuondoa kabisa ule wigo na kutoa mwanya huu wa sheria ambayo kimsingi ikiwekwa itatusaidia...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na nimshukuru sana Mungu kwa kunijaalia afya njema ya kuongea hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze haraka katika mchango wangu kwenye taarifa hii au na hotuba hii iliyoletwa mbele yetu ya Waziri wa Fedha na Mipango. Nijielekeze moja kwa moja kwenye ukurasa wake huu wa 29.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kukuza uchumi wa viwanda ni lazima kabisa ujielekeze katika mpango huu moja kwa moja. Kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Mpango ameandika vizuri sana hapa kwamba kuna miradi ya vielelezo na miradi ambayo itatausaidia Tanzania kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Sasa basi ninaomba kutokana na mpango huu ambao ameandika hapa kwenye suala hili la gesi na naomba nijielekeze kabisa katika suala la gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gesi; ameandika vizuri hapa kwamba Serikali inataka kujielekeza katika kujenga mtambo wa kusindika gesi ya kimiminika. Sasa basi ni kweli kwamba miradi hii iko mingi na nimetaja huu mmoja ili walau Waziri Mpango anielewe. Leo hii gesi Mnazi Bay imezalishwa vya kutosha. Lakini ukiangalia wataalam wanatuambia gesi pale inazalishwa na inaweza kutumika kwa kipindi cha miaka 70. Ukiangalia matumizi ya gesi pale hayafiki asilimia 25 mpaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji aliyewekeza gesi pale amewekeza kwa bilioni za pesa za kutosha. Sasa ukiangalia gesi inayotumika sio ya kutosha na kwa kuwa sisi tuna gesi na tunataka sasa kutengeneza na kuisadia Tanzania kwenda kwenye uchumi huu na Mwenyezi Mungu ametujaalia kupata gesi, naomba mpango huu basi kadri ulivyoandikwa hapa ujielekeze kutumia gesi ili walau gesi hii ambayo Mungu ametupatia isaidie basi kwenda kwenye viwanda hivi vilivyoanzishwa sasa katika eneo lote la viwanda na Serikali iweke basi mazingira wezeshi ya kujengwa kwa viwanda maeneo yale ambayo bomba la gesi linapita, kwa kufanya hivi tutasaidia uchumi upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi utapanda kwa sababu ukiangalia katika bajeti ya Serikali ya mwaka uliopita, Serikali inaagiza mafuta kwenye bajeti yake zaidi ya robo inatumia kwa kuagiza mafuta nje. Kwa kuwa nishati ya mafuta inaagizwa kwa kutumia fedha za walipa kodi, nimshauri Mheshimiwa Mpango na wachumi wengine waone namna gani ya kufanya kitaalam ili walau gesi hii iweze kuendesha mitambo, tukaachana au tukapunguza kiwango cha matumizi ya mafuta, tukatumia gesi kwa sababu gesi imechimbwa pale na gesi hii ni bure tunaweza kutumia tunavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ikitokea leo Serikali inaamua hata wenyewe tu kwa magari ya Serikali ikaondoa mfumo wa kutumia petroli kwenye magari tukatumia gesi ambayo imo imezalishwa pale, Tanzania tutasogea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Serikali nayo ikiamua kutumia wachumi wetu kushauri na wataalam tulionao nchini wakajenga sheli za kutumia gesi, magari yetu na magari mengine ya Serikali yakabadilisha huo mfumo ikawekwa sheli nyingine Dar es Salaam, ikawekwa sheli
nyingine Arusha, tukawekewa sheli nyingine huko Kigoma, mtandao wa gesi ukaundwa katika nchi yetu, hii nchi ya Tanzania hii itasonga mbele kwa sababu tuna gesi asilia na wataalam wametuambia gesi yetu ni pure yaani haihitaji zaidi kubadilishwa na kitu chochote. Tunapata, tunaweka kwenye matumizi na tunaweza kujengewa uwezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ukiangalia leo hii TPDC uwezo wao wa kuuza gesi ni mdogo sana, ni mdogo kwa sababu tunaona kabisa wale wawekezaji walioko kule wanaidai Serikali pesa kubwa sana na kwa sababu pesa hii ni nyingi zaidi ya dola milioni 20 na ukiangalia uwezo wao wa kutumia siyo mkubwa na TANESCO ni shirika letu la Kitanzania linalojiendesha kwa hasara. Kama Serikali itaamua kuweka mpango huu vizuri, na mimi leo nimeamua kuelekeza mchango wangu katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuisaidia sana Tanzania kwenye sekta ile ya madini, nimuombe tena kupitia Bunge hili achungulie tena hili eneo la gesi kwa sababu eneo la gesi mimi siamini kama gesi hii inashindwa kutusaidia Watanzania. Nina wasiwasi na gesi hii ambayo kimsingi haitumiki ipasavyo. Kwa nini nasema haitumiki ipasavyo? Ni kwa sababu gesi tunayo, haitumiki ipasavyo na haiuziki. Kwa bahati nzuri sisi Kamati tumepata bahati ya kutembelea kule na tunaona jinsi ambayo rasilimali hii ya gesi haitumiki vizuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kujielekeza katika eneo hili la gesi ili walau gesi basi isaidie mitambo mingi ambayo inasubiriwa saa hizi. Ukiangalia Mheshimiwa Rais siku moja nimemsikia katika vyombo vya habari ametembelea maeneo ya Lindi na Mtwara, kuna kiwanda kikubwa pale cha Dangote, hebu angalia kwa nini mpaka sasa hivi hakijapelekewa gesi ili gesi itumike basi, maana kiwanda kile kikifanya kazi ya kuzalisha saruji bei ya saruji inashuka Mikoani na uchumi wa Tanzania unapanda kwa sababu saruji kule imeshafanyika kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona mchango wangu niuelekeze hapo kwa sababu ninafahamu vizuri matumizi ya gesi ambayo kwa kweli kwa sasa hayatumiwi inavyotakiwa. Pamoja na haya nataka nielezee jambo lingine dogo tu. Katika mpango huu, umeeleza jinsi ambavyo mikopo na jinsi ambayo mikopo chechefu inavyoleta shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana, sasa hivi kuna shida katika maeneo ya mikopo yetu katika mabenki, Mheshimiwa Mpango elekeza sasa namna rahisi ya kusaidia wananchi ili wasiende kupigwa huko katika suala la mikopo, wanapata uchungu kupewa riba ya juu sana. Sasa naomba Mpango huu basi tunapoenda mwaka huu wa 2018/2019 usaidie eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliamua kuyasema haya na huu ndiyo mchango wangu kwa leo. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kweli kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kufanya kazi kwa Awamu hii ya Tano, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri wake na Wizara kwa ujumla kwa kufanya kazi nzuri ambayo kwa kweli mimi nai-admire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri amefika kwenye jimbo langu na kutembelea Hospitali ya Haydom na kwenda pia kwenye Kituo cha Afya cha Dongobesh na kutupatia fedha za kujenga kituo kile. Nakushukuru sana Mheshimiwa Ummy na kwa kweli kwa Serikali nzima pia naishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru ametuma tume ambayo imekwenda kwenye Hospitali ya Haydom na kuangalia Hospitali ya Haydom kama inakidhi kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya kanda. Sasa niombe Mheshimiwa Ummy waone basi namna gani ya kuisaidia Hospitali ya Haydom ili iweze kupanda hadhi iwe hospitali ya kanda. Kwa nini nasema namna hii, Haydom ni hospitali inayohudumia Mikoa mitano, ikiwemo Singida, Dodoma, Manyara bila kusahau Arusha na Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hospitali hii imeshakuwa katika eneo ambalo linafikika na pande zote hizi nilizozitaja ningeomba Serikali iangalie namna nzuri ya kuisaidia hospitali hii ili kupanda hadhi. Kwa mfano leo unaangalia Dar es Salaam kufikika kutokana na mafuriko imekuwa na shida; kwa hiyo angalia tungekuwa tumepandisha hospitali ya Haydom kuwa hospitali ya kanda tungekuwa tumepeleka huduma vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yetu inapenda kusaidia watu wa vijijini, basi tusaidieni kuifanya hospitali hii iwe hospitali ya kanda ili iweze kutoa huduma nzuri kuliko kwenda kwenye hospitali kubwa ya KCMC. Kutoka Haydom mpaka KCMC kuna kilometa 400, kutoka Haydom mpaka kule tunasema Jakaya Kikwete kilometa 700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, kwa sababu tumeshaleta mapendekezo na ameshaikagua na Wizara yake tunahitaji Madaktari Bingwa sasa waliobobea waende vijijini ili wakawasaidie mama na mtoto kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya niombe sasa; maana unaposhukuru maana yake unaomba mara ya pili na hata kwenye Sala ya Baba Yetu ukiangalia sana kwa sisi Wakristo, sala nzima ya Baba Yetu inasema Baba yetu uliye mbinguni jina lako litukuzwe, yote haya ni kumsifu. Unapomsifu Baba yako aliye mbinguni maana yake baadaye unaweka ombi. Kwa sababu unaposema utuongezee mkate wetu wa kila siku maana yake unahitaji kuomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huwezi kuwa na double standard, ukawa unaomba wakati huo huo unatukana. Kwa hiyo niiombe Serikali yangu ambayo inasikia, kwa kweli ahadi alizotoa Mheshimiwa Ummy ya gari ya wagonjwa pale Dongobesh mpaka leo inasubiriwa. Vile vile kubwa nishukuru pia kwa kutupatia hospitali ya wilaya ambayo itajengwa kwenye jimbo langu na nimeona kabisa kwenye bajeti hii ametutengea bilioni moja. Kwa hiyo nimshukuru sana yeye pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ni kwamba ninao ushauri kwenye Serikali. Nimepata nafasi ya kutembelea katika kiwanda kile ambacho kinatengeneza dawa ya viuadudu. Mimi niombe, kama kweli Serikali inahitaji kumaliza Malaria au kupunguza Malaria tuweze kuhakikisha ya kwamba kile kiwanda kinakwenda kufanya kazi ya ku-supply ile dawa ili kuweza kuua vimelea vya mbu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimekwenda pale na hakika Mheshimiwa Rais alishaweza kuziagiza halmashauri zote nchini kuweza kununua zile dawa waka- spray kwenye maeneo yao ili kutokomeza vimelea vya mbu. Kwa msingi huo basi, siamini kama tuna dhamira ya dhati kumaliza tatizo hili la malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kumaliza malaria, niwashauri Wizara watafute namna, washauri hata hospitali zetu, kituo cha afya. Kwa mfano wakiviagiza au kuviomba hivi vituo vya afya, kwamba kila kituo cha afya kikanunua lita tano ya ile dawa, wakaagiza pia dispensary ikanunua kama lita tatu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: …ukaagiza maduka ya dawa yote nchini yakanunua ni rahisi kabisa kutokomeza malaria; lakini vinginevyo…

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji ni kubwa sana katika nchi yetu, tunapaswa kuisaidia jamii yetu kwa kupanga namna nzuri ya kutatua tatizo hili. Kuundwa kwa Wakala wa Maji Vijijini kutatuongezea sh.50/= + Sh.50/= tutapata Sh.100/= ili kuweza kutatua tatizo hili, kama REA.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi inayoendelea kutekelezwa, tuna tatizo kubwa la fedha kwa Wakandarasi ambao wanapoleta certificates zao hawalipwi kwa muda unaotakiwa. Mfano, Mradi wa maji wa Haydom umeshindwa kulipwa na vyeti vyao vipo Ofisini kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna wakati mwingine hulipwa nusu ya walichokidai, hebu Mheshimiwa Waziri atusaidie mradi huu uishe kwa kuwapatia fedha Miradi ya Haydom, Arry, Ampa, Bashau. Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea Bwawa la Dongobesh, naomba ahadi yake aliyoitoa Haydom na Dongobesh itekelezwe kwa kuleta fedha kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutembelea Wilaya ya Jimbo langu. Ombi langu ni kuwatimizia wananchi huduma hii ya maji. Maji mengi wakati huu wa mvua nyingi hupotea. Naomba tusaidiwe na wataalam ili tupange kuyazuia maji kwa kujenga mabwawa ya kumwagilia maana kilimo peke yake chenye uhakika ni kilimo cha kumwagilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapanga bajeti lakini fedha hazitoki kulingana na tulivyopanga. Hivyo, ni vema kupeleka fedha kwa wakati ili kuona matokeo ya haraka. Narudia ili ukumbuke, “fedha za miradi ya Dongobesh – Bwawa; Haydom – Mradi wa Maji; na Arry – Tumati, Mradi wa Maji.”
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kweli kwa kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kufanya kazi nzuri kwa maeneo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, naona kwa kweli anavyofanya kazi yake, yeye na timu yake, Manaibu wake wote wawili, kwa kweli niwapongeze sana, katika Awamu hii mnafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri anazofanya, nimesoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri hapa na nimeona kwa kweli barabara ambayo tumeiomba kwa muda mrefu, Barabara ya Mbulu ambayo imeelezwa hapa; Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti mpaka Lalago na huko Maswa na Bariadi. Barabara hii imeombwa kwa muda mrefu sana na ipo kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, ukurasa wa 18. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafarijika kwamba kwa kweli leo nimeiona angalau imetambulika, ila ninavyoona hapa kadri barabara hii ilivyo na usumbufu kwa sasa ningeiomba Wizara na Mheshimiwa Waziri aone, najua hajawahi kutembelea barabara hii, najua hajafika kabisa, lakini aone kwamba barabara hii sasa ni hitaji kubwa mno la wananchi wa maeneo mengi; wananchi wa Karatu, wananchi wa Mbulu Mjini, wananchi wa Mbulu Vijijini, wananchi wa Mkalama, wananchi wa Singida, maeneo yote yale yanayopita moja kwa moja mpaka ufike Lalago, Maswa, mpaka kwako kule barabara hii inafika yenye kilometa 389. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni hiki; barabara hii itakapojengwa itafungua eneo kubwa ambalo limesahaulika kwa wingi na uchumi wa watu hawa utapanda. Nimeona kwamba mmeandika hapa kwenye ukurasa huu wa 38 kwamba itafadhiliwa na KfW, hawa Benki ya Ujerumani, sina tatizo, lakini ninachohofu; mwaka jana walisema ipo kwenye upembuzi wa awali, sasa hofu yangu mwakani watasema pia ipo kwenye upembuzi wa kati lakini baadaye mtatuambia tena iko kwenye upembuzi yakinifu, miaka mitano imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ambaye yuko sasa wa Awamu ya Tano wa Hapa Kazi Tu ameahidi barabara hii na ipo kwenye Ilani na nini maana ya ilani; ni mkataba kati ya mtawala na mtawaliwa. Tumeahidi hii, ndugu yangu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, aelewe, tumeahidi kwenye mikutano yetu, wananchi wa Mbulu na maeneo haya niliyoyataja wanaitegemea barabara hii na kule hatuna kitu kinaitwa lami kabisa, hatujawahi kuona tangu Mbulu imeanzishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe, Mbulu imeanzishwa 1905, haina barabara. Uchumi wa kule kwetu zaidi ya barabara hatuna lolote. Hatuna maziwa ambayo tungesema tungeweza kufanya usafirishaji wa maboti, meli na nini, hakuna huko na viwanja vya ndege kule hakuna. Kwa hiyo, tusipopata barabara hii ambayo naisemea sasa hatuna namna yoyote ya kufanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa ndugu yangu Mheshimiwa Waziri aweke basi hela ambayo itaonesha namna nzuri ya kufanya upembuzi yakinifu mwakani. Najua ametenga milioni 50, milioni 50 sisi Wabunge saba tuliosema hapa tukichanga tunaweza kufika hizi hela, kwa nini nasema hivi? Sina nia ya kudharau alizoziweka hizi, lakini ni kidogo sana. Milioni 50 kwa barabara hii yenye kilometa 389, jamani sawasawa hakuna kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii ni muhimu sana, muhimu mno, inaunganisha Mikoa ya Arusha na Manyara, Manyara na Singida na kutoka Singida inakwenda mpaka Meatu na Mheshimiwa Waziri anajua Simiyu iko kule. Kwa hiyo, niombe basi maana barabara hii ni muhimu na ni muhimu kwa sababu kuna Hospitali kubwa ya Haydom iko katikati ya mikoa hii ambayo watu wengi wanaitegemea kwenda katika hospitali hii. Basi nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa, anajua nampenda sana, lakini mapenzi haya yaende basi na kuweka hii barabara, awekea barabara ndugu yangu, aweke barabara narudia tena. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, najua wazi kwamba Rais wetu ni msikivu, ili asionekane Rais ambaye ameahidi halafu baadaye haikufanyiwa kazi, Mheshimiwa Waziri asimuangushe, amemweka hapa ili akamsaidie kazi hii. Aweke Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Maswa – Lalago, twende mpaka kwa Mheshimiwa Chenge kule. Kwa hiyo, naomba ndugu zangu wanielewe, Mawaziri wako watatu hapa wakumbushane katika ofisi yao basi, kwa kuwa barabara hii ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda nichangie mchango wangu wa dakika tano kwa kusemea barabara hii tu kwa sababu ndiyo kufa na kupona. Leo asipoiweka barabara hii akaiwekea fedha mwakani atakuwa hajatusaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, najua atatuwekea barabara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maeneo ya mipaka lipo katika maeneo mengi hasa mipaka ya Mbulu na Iramba; Manyara na Karatu; na Mbulu na Hanang. Tunaomba wapimaji waje kutatua na kusoma (GN) ili wananchi wajue wanapotakiwa kuwajibika kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mgogoro wa ardhi Yayeda Chini na mwekezaji aliyepora eneo la wananchi bila kupewa na Serikali ekari 3903. Mara nyingi Serikali hukubali kutoa eneo kwa wingi wa wananchi kusema apewe, lakini Wahadzabe, Wabarbaig mara nyingi jamii hizi hazijapewa elimu kuhusu ardhi, hivyo panapotokea mtu mmoja kuwadanganya wanaweza kutoa eneo hilo na baadaye mgogoro hautakwisha. Sasa kwa kuwa Wahadzabe ambao mara nyingi wana hamahama kutafuta matunda na asali pia wanahitaji ardhi hiyo na kwa bahati mbaya wapo wachache katika jamii. Ushauri wangu ni kwamba, wakati mwingine haki ya wachache izingatiwe ili jamii isipate tabu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Serikali ambayo kimsingi imeonyesha njia. Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa hii Awamu ya Tano kwa kweli nitakuwa mchoyo sana kama sijaweza kumpongeza kwa kazi anazozifanya. Ukiangalia wako wanaombeza hasa katika suala la kununua ndege, ukiangalia sasa hivi kwa kweli mimi mwenyewe nafurahia sana kuona hali hii ambako leo Tanzania tunaweza kuona huko angani ndege zinapishana na sisi tunasafiri. Naamua kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ajili ya hili. Wako wanaobeza juhudi hizi kuonekana kwamba kipaumbele chetu sio ndege lakini ukweli ukiona baba amenunua kitu fulani nyumbani unaamua kumpongeza kwa sababu tu kwanza fedha zinatumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si vibaya nikampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anazozifanya. Kwa kweli ni namuona mara nyingi katika shughuli za Serikali hasa kwenye maeneo yetu anapofanya ziara za kuhimiza maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi sasa naomba niende kutoa mchango wangu katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020. Kuna mambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango anapaswa aangalie kwenye mpango huu. Nimeangalia sana na kusoma kitabu hiki cha mpango ukiangalia miradi mingi kwa kweli imetekelezwa. Ukurasa wa 31 anaonyesha miradi 1,595 ya maji imekamilika, kwa hili nimpongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado sasa tu natakiwa kuongeza kasi zaidi kwa sababu miradi hii tunayoiita miradi ya maji, kimsingi visima vingi vimechimbwa kila mahali na maeneo mengi sana kwenye maeneo yetu miradi hii haikuisha, imeishia nusu mengine 90%, mingine 40% hasa ukiangalia miradi hii mingi imeanza miaka mingi. Kwa hiyo, tusipoweka mipango ya kuimalizia miradi hii ni wazi thamani ya shilingi inashuka na miradi hii inakuwa ghali kwa maana hiyo Serikali inapata hasara hata ukipanga bajeti ya namna gani inaweza kuwa shida kumaliza miradi hii vizuri na wananchi wakapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ni vizuri tunapopanga mipango yetu hii na tunapopanga fedha ziende kwa wakati ili wakandarasi walipwe wanapomaliza ili iweze kuhudumia wananchi na wakati huo basi inakuwa na kiwango kile kile kilichokusudiwa kumalizia mradi. Hii itasaidia pia katika uchumi wa nchi yetu, tutakuwa hatutumii fedha nyingi ambazo hazikukadiriwa kwa sababu unapochelewa kumaliza mradi ni wazi kabisa ule mradi unapanda gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye eneo hili la miundombinu. Kwanza kwa kweli naipongeza Serikali kwa eneo hili la miundombinu barabara nyingi zimejengwa, maeneo mengi sasa yanapitika. Kuna eneo ambalo nalipongeza, Mheshimiwa Rais amefungua Daraja la Sibiti ambalo ukiangalia kwa kanda hii ya Simiyu, Shinyanga kuja mpaka Singida na Manyara kwenda upande wa Arusha utakuwa umetengeneza njia nyingine ya kupeleka usafiri wa hakika kwa wakulima au wafanyabiashara. Kwa hiyo, nashauri fedha zitengwe ili walau lile Daraja la Sibiti linalojengwa limalizike ili barabara hiyo inayokuja Singida inayopita Manyara inayokwenda moja kwa moja mpaka Arusha ifanye kazi kwani ni njia rahisi utakuwa umeokoa kilomita 200 kuliko kupitia Singida kwenda Babati kwenda Arusha kwa njia ile. Kwa hiyo, nilitaka nimuongezee ndugu yangu ili alielewe hili, barabara ile inapopita maeneo yale itakuwa na tija kubwa sana kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi za Serikali, naona wazi na natambua juhudi za Serikali hasa katika suala la elimu. Niipongeze pia Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 20.9 kila mwezi kwenda kwenye elimu bure, kwa kweli kwa hili mnastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi elimu ya msingi imeboreka na mambo yanaenda si vibaya na elimu ya sekondari vilevile, lakini tunapoenda kwenye vyuo na kuhitaji wataalam kwenye viwanda tunayo kasoro kidogo katika mitaala. Ni vizuri kutafuta wataalam na kubadilisha modules zetu katika ufundishaji wa vyuo vyetu hivi, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ambayo itasaidia kupatikana kwa wataalam watakaosaidia katika viwanda vyetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafundi mchundo, mafundi sanifu, hatuwezi kuwapata kama module na ile mitaala iliyopo katika vile vyuo vyetu itabaki vilevile. Ukiangalia China waliweza kufanya kazi nzuri wakati wa mapinduzi yao kwenda kwenye uchumi wa kati. Ukiangalia historia yao walitumia ujanja wa kufundisha wataalam wao ili wataalam hao wakaweze ku-cover kwenye kufanya shughuli za viwandani. Ukiangalia leo hii hata sufuria tunazopikia nchini hapa zinatengenezwa Kenya na maeneo mengine lakini tukiwa na watu wetu tukawafundisha ni rahisi basi tukawa na wataalam ambao watatengeneza vyombo hivi na viwanda vyetu vitapata wataalam na hivyo, tutakuwa tumewapatia watu wetu kazi na vijana watapata ajira na pia viwanda vyetu vitainuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote katika kilimo tunahitaji kufanya jambo moja ambalo ni rahisi kulifikiri, hatuwezi kutegemea kilimo cha mvua. Nchi nyingine ukiangalia na sisi bahati nzuri tuna mvua nyingi za kutosha, tuangalie namna ya kuzuia mvua zinazonyesha kipindi cha masika ili kuwa na mabwawa mengi tukalima kilimo ambacho kinaweza kusaidia. Kilimo cha mabwawa, tutakuwa tunazalisha kila mwaka na kwa vipindi mbalimbali bila kutegemea mvua, kwa hali hii itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nimeona kwenye mpango huu kwa kiasi kidogo sana umezungumzia kilimo lakini kilimo kinabeba kwa kweli eneo kubwa la Mtanzania.

Watanzania wengi wanatumia kilimo zaidi ya asilimia sitini na kitu mpaka sabaini. Kwa hiyo, ukielekeza nguvu nyingi kwenye kilimo Mheshimiwa Dkt. Mpango utakuwa umesaidia Watanzania wengi ambao kimsingi tunategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niipongeze pia Serikali kwa kutekeleza huu mpango wa REA Vijijini. REA tatizo lake ni moja tu, wakandarasi wanadai hawana fedha, sasa sina hakika kama Serikali haiwalipi au ni nini kilichopo. Hakuna kiwanda bila umeme, tukitaka tuweze kuzalisha vizuri ni vizuri tukapeleka umeme kwenye viwanda vyetu na hii miradi ya mkakati kwa kweli tusipoangalia itakuwa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakandarasi wengi sana saa hizi wanalia habari ya kutokuwa na fedha, sasa sina hakika kwenye mpango uliopita nini kilifanyika, lakini sasa hivi tunaona kabisa yako maeneo mengi wakandarasi wanasuasua. Sasa niombe fedha tunazozipanga mara nyingi ziende moja kwa moja kwenye mpango na tunapopanga tupange nini tunafanya na kipi ni kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hiyo, kizuri ukishaweza kuziba sehemu hii ya wakandarasi hawa hakika mambo yataenda vizuri na Tanzania ya viwanda itapatikana ikiwa Serikali itawekeza katika suala la umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo niliwahi kushauri zamani kwenye mpango uliopita suala la gesi. Nimewahi kutembelea sana na kuangalia miradi hii ya gesi, sina hakika wapi imepotelea lakini nimeiona imendikwa kidogo kwenye ukurasa huu wa 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumepata matumaini sana gesi inaweza kusaidia nchi hii, hasa kutupatia fedha za kigeni au kwa matumizi ya kawaida. Tungeweza kusaidia lakini tuone nini changamoto hasa za gesi ili tupate namna ya kusogea mbele ili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa hili, nitakuwa mchoyo sana kama sijasema suala la mifugo na wafugaji. Tuone namna ya kuisaidia mifugo na wafugaji kwani kwa kufanya hivyo mambo yataenda vizuri sana. Mifugo yenyewe, kwa mfano ng’ombe kila kitu ni thamani kuanzia ngozi, maziwa, kwato na kadhalika, tukiweza kuweka viwanda ambavyo vitachakata mazao haya ya mifugo hakika Tanzania itasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nipongeze Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maamuzi yenye busara na haki katika kazi za kuhudumia halmashauri zetu. Pamoja na hayo nilete ombi la kutekelezwa kwa ujenzi wa kilomita tano katika Mji wa Haydom ambapo Rais aliahidi kujengwa kwa kiwango cha lami na Dongobeshi kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fedha za kituo cha Afya cha Dongobeshi. Naomba kupewa tena fedha katika Kituo cha Maretadu, Endamilay, Masieda na Maghangw kwani wananchi wanapata tabu ya kutembea mbali kutafuta huduma ya hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA; Jimbo la Mbulu Vijijini lina changamoto kubwa ya barabara na madaraja ambayo hayapitiki. Naomba TARURA Wilayani ipewe kipaumbele cha kupewa bajeti zaidi ili kutatua au kupunguza changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi; tuna changamoto ya kutokuwa na Engineer wa Maji; Idara inakaimiwa na Fundi Mchundo. Walimu wa Sayansi hatuna kwa kiwango kikubwa, hivyo tunaomba tupatiwe pia Maafisa Kilimo na Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa umuhimu wa pekee, napenda sasa kuishukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mawaziri wake wamefanya ziara katika wilaya yetu. Nawashukuru sana Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Joseph Kakunda na Mheshimiwa Joseph Kandege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; wawe na mpango wa kuwaelekeza Watendaji Wakuu mfano, DC, DED, RC, wajue sheria za Serikali za Mitaa na kuziheshimu hasa PPRA, RRA na D-by D ili wafahamu utaondoa mikanganyiko iliyopo huko maana inaleta taswira mbaya na kuchafua picha nzuri ya Serikali bila sababu kwa wananchi. Tusiposhughulikia tunaweza kupoteza ari na kutoungwa mkono kwa Serikali na chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami siku ya leo nichangie hoja hii. Kwanza naomba uniruhusu niwapongeze kwa kweli Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Watendaji Wakuu kama Katibu Mkuu wanavyofanya kazi kwenye Wizara hii ya Maji, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mdogo naomba tu nijielekeze moja kwa moja kwenye maeneo ya wakandarasi. Jimboni kwangu kwa kweli kuna miradi mitano, miradi hii yote kwa kweli mpaka sasa haifanyi kazi mmoja walau una afadhali. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri amefika kwenye Jimbo langu na ametembelea miradi hii ameona mwenyewe kwa macho yake. Kwa hiyo ninapozungumza nina hakika anajua nazungumzia nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Harsha, umesanifiwa 2012, hadi leo haujakamilika, wamejenga matenki, wameweka maeneo ya kujichotea maji lakini kwa kweli wananchi sasa wameduwaa, wanazidi kusubiri, hakuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mradi wa Tumati - Mongahay uko palepale. Nimesoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri aliyoiandika humu na nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hakika nachelea kusema tuna hali mbaya kweli kweli. Nimeleta maswali si chini ya 13 humu ndani ya Bunge, nimepata majibu, lakini miradi hii bado haifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa sababu kinachoonekana hapa tunalo tatizo kubwa la fedha na ukiangalia sasa kwa muda huu ambao mkandarasi amefanya kazi na hakulipwa, tumeshavunja mkataba maana yake mkandarasi huyu amekwishaondoka site, hayuko tena site. Nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Wakuu wake wa vitengo waangalie jinsi ambavyo wakandarasi hawa wamepewa hizi tender na hawa wanaopewa tender waangalie basi, nakumbuka kwenye hotuba ya mwaka jana alituahidi hapa kwamba wataunda tume ambayo wao wenyewe kama wataalm watakwenda kuhakiki na kuangalia miradi nchi nzima na nilitegemea basi watakuwa wamefika Jimboni kwangu Mbulu Vijijini, lakini hilo sidhani kama limetokea na kama limetokea basi Waziri atakuja kuniambia wakati anahitimisha bajeti yake hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ukiangalia tatizo lilloko katika maeneo yetu pamoja na wakandarsi kuwa na matatizo lakini shida ya ulipwaji wa certificate ambazo kimsingi zinakaa sana Wizarani, kama kuna Wizara nimetembea, nimeenda ofisini, nimetembea mno, nimeonana na wataalam wote, nimejitahidi kweli kweli, mara nyingi pia nimejaribu kwenda na Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na kusumbuka kote huku miradi hiyo bado haina namna ya kumsaidia mwananchi. Kwa hali hii katika jimbo langu lazima niseme ukweli, ni ngumu kusema kwamba unaweza kumtua mama ndoo kichwani, kwa kweli hili halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba amekuja na ameona pale Haidom, ameagiza kisima kichimbwe na juzi tarehe ya 25 nimeuliza swali la nyongeza hapa na akaagiza DDCA wachimbe visima, hali ni mbaya naomba kabisa waone namna ya Wizara watakavyosaidia Jimbo la Mbulu Vijijini kutokana miradi hii ambayo imekuwa viporo, wameshaacha certificate, zimeshakaa kwenye Wizara, lakini kubwa zaidi miradi mingine miwili wakandarasi wameshatengua mikataba, kwa hiyo hawafanyi kazi tena na tumetangaza tender. Naomba basi katika bajeti ya mwaka huu apeleke fedha ili hawa wakandarasi wanaoomba tena miradi hii waweze kuendelea kwa sababu bila fedha hakuna kinachotendeka. Kubwa zaidi niombe pia hawa Wahandisi Washauri wanaokuja katika miradi hii, nishauri tu watumie tena utaalam wao ili waweze kushauri miradi hii iishe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo hali hii ya hao Wahandisi Washauri inawezekana huenda taaluma zao siyo sawa, waangalie kwa wana-design miradi ambayo haiishi na shida ni nini? Tujue, lakini kubwa zaidi nashauri kwa mfano Mradi wetu wa Haydom umekaribia kumalizika, tumepeleka maombi Wizarani tuumalizie sisi kama halmashauri kwa kutumia Force Account kwa sababu sheria inaruhusu na inasema mradi unaweza kutumia Force Account yaani bei ya soko na sisi tukajenga tukaumalizia kuliko kuweka tena mkandarasi kwa sababu tuna uwezo wa kufanya hivyo. Mabomba yako tayari, maeneo mengi yamekwishamalizika, watuache sisi tumalizie, tumepeleka Hadidu Rejea na iko Wizarani kwa Waziri aangalie namna yoyote, nafikiri wananisikiliza, ni hela kidogo tu ni milioni isiyopungua 70, tunaweza kumaliza sisi wenyewe watuachie na mimi nina Injinia ambaye kimsingi amekuja, watuachie tumalize kwa kutumia Force Account…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKIITI: Ahsante sana.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba tu niunge hoja mkono, lakini kwa masikitiko makubwa sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa kupata nafasi ya kuongea jioni hii ya leo. Kwanza naomba nianze na kumpongeza kabisa Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa jinsi ambavyo anachapa kazi na kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sijampongeza na kuwapongeza hasa Mawaziri ambao kimsingi leo tunajadili hotuba zao. Mheshimiwa Waziri Jafo nampongeza sana kwa kufanya kazi kubwa ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lakini pia nampongeza sasa baba yangu Mheshimiwa Mkuchika, ambaye alishakuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu kwa miaka kadhaa, hongera sana mzee wangu, chapa kazi, akazie uzi hapohapo; lakini nawapongeza pia, Naibu Mawaziri katika Wizara zote mbili, ili kuokoa muda, pia na Makatibu Wakuu kwenye Wizara zote hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani pia, kwa kututengea fedha za kujenga Kituo cha Afya cha Dongobesh, Mheshimiwa Waziri nampa hongera sana. Wakati naingia jimboni nilikuwa sina kituo kabisa cha afya, lakini leo tunajenga kituo cha afya ametupatia milioni 700, Mungu awabariki sana, lakini pia wametupatia bilioni moja na milioni 500 tukajenga Hospitali ya Wilaya pale Dongobesh. Mheshimiwa Waziri namshukuru sana na nashukuru sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nashukuru juzi wametupatia fedha za maboma. Tumepata milioni 230 kwa kujenga maboma kwenye shule za sekondari tisa. Biblia inasema ni bora kushukuru nami naishukuru sana Serikali yangu kwa kweli, kwa kutujalia na kutupatia fedha nyingi kiasi hiki, hizi ni pongezi kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Biblia inasema kwa Waefeso 5:4, naomba niwakumbushe wachangiaji wenzangu. Waefeso 5:4 anasema: “Wala aibu wala maneno ya upuuzi si vema na hata ubishi hayampendezi Mungu, ni afadhali kushukuru.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama bajeti hii. Nimetazama na kusoma Wizara zote mbili, kuna mahali pa kupongeza Serikali na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyofanya kazi usiku na mchana. Kwa nini? Ukiangalia leo hospitali za wilaya zimejengwa na maeneo mengi tunapata huduma. Vituo vya afya viko vingi na sasahivi naona 57 vinakwenda kujengwa. Tusiposhukuru tutakuwa na hali ya kutorudisha fadhila na shukrani. Mimi nashukuru sana Serikali na niko kifua mbele nimetumwa humu kuwashukuru kwa ajili ya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili ninao ushauri, ukiangalia TARURA bajeti yake kwa miaka miwili iliyopita imeanza kupungua. Mwaka 2017/2018 imepungua kwa asilimia nane, lakini mwaka jana kwa asilimia 16 na mwaka huu imezidi kupungua. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tumeanzisha TARURA ili ikasaidie kujenga barabara za vijijini na mijini, lakini ukiangalia kwa jinsi ambavyo bajeti ya TARURA inapungua, tutashindwa kujenga barabara ambazo amesema mwenyewe hapa kuna kilometa 108,000; kwa kweli kwa pesa hii itakuwa shida sana kuisaidia TARURA. Hivyo, naungana na Wabunge wenzangu waliosema kwamba, TARURA iongezewe fedha. Hii asilimia ya kugawana, mgawanyo wa kwake TARURA na TANROADS kwa kweli uangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa TARURA inakwenda mbali na mzunguko wake ni mkubwa na vijijini, niombe basi tuone namna ya kufanya, tuiongezee fedha na fedha hizi tupange asilimia. Sasa hivi inaonekana ni asilimia 30, ni ndogo sana, tuongeze basi asilimia hizi angalau ziende 40 au 50. Nashukuru TARURA kwa mwaka huu wamenisaidia, wamejenga madaraja mawili na nimeona kwenye bajeti hapa kuna Daraja la Qambasiro na calvat ya Gidimadoy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe, kuna barabara mbili ambazo kwa kweli, hazipitiki sasa hivi. Barabara ya Masieda kwenda Mongo wa Mono kufika mpaka Yaeda Chini, wako Wahdzabe kule sijawahi kuwafikia, barabara haipitiki kabisa. Niombe Ndugu yangu aangalie kwenye bajeti hii tupate barabara ile, lakini kuna barabara nyingine kutoka Masieda kupitia Laghangesh kwenda Yaeda Chini, naomba barabara ile aiangalie vizuri, iwekewe fedha ili walau hata sisi tuwe na namna ya kutembea. Nami napigania na ku-support uongezaji wa asilimia za barabara katika TARURA ili basi barabara hizi ziweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimeangalia, ndugu zangu wapinzani au upande wa Gaza wanasema, kwa nini nimesoma mstari wa Biblia, nimetaka hata washukuru. Nimeangalia kuna mzungumzaji mmoja hapa kabla yangu ame-quote maneno ya mtu anayeitwa mwanazuoni na amesema yeye mwenyewe uzalendo kwanza na nini maana ya uzalendo ku-support nchi yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeangalia kwenye mpango wa bajeti ya mwaka huu, ukiangalia Rombo kwa Mheshimiwa Selasini pale, kapewa hospitali. Sasa sijaona kwa nini watu hawa hawashukuru mara nyingi? Nami nawaza humu kwa nini shukrani zisitokee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda Kilombero kumepewa milioni 500, lakini ukienda Arusha AICC pale kumepewa milioni 500, ukienda Ubungo wana fedha pale, ukienda Kigoma wanayo. Sasa huwa nawaza humu ndani, jamani hata shukrani kidogo tu hakuna? Nadhani wakati fulani yako mambo ambayo hayaendi vizuri tuseme, lakini mambo ambayo yanaenda vizuri tushukuru, hata kwa jambo moja tu. Ndio maana mara nyingi ni lazima kushukuru, tusiposhukuru ndugu zangu hata Mheshimiwa Waziri na wanaofanya kazi chini yao wataona kama vile hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa pamoja na shukurani hizi naomba nielezee ahadi za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anapita aliahidi kilometa tano pale Hydom na kilometa mbili Dongobesh na Mheshimiwa Waziri nina hakika amefika Dongobesh na Hydom, ili Rais wetu asionekane kwamba, ameahidi na hajatekeleza, niombe basi katika bajeti ya mwaka huu atenge hata kilometa tatu au mbili, ili walau tuonekane tunaanza kujenga barabara zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli barabara zetu hazina lami, nami nashukuru Mungu walau naona mpango wa Serikali wa kuweka lami katika wakati ujao, lakini naomba basi kipindi hiki cha mwaka huu wa 2019 kwenda 2020 kwa kweli, tuione lami ya Hydom ikiwekwa kwenye bajeti hii. Mheshimiwa Waziri nimempelekea maombi na naomba maombi haya ayachukue, aniwekee lami kilometa zile zilizoahidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi naomba kuna shule ya sekondari ambayo wananchi wanaijenga kule Maretadu, wanajenga kidato cha tano na cha sita kwa fedha zao. Tumejenga madarasa manne na tumejenga bwalo, sasa naomba tu fedha za kumalizia ili mambo yaende vizuri. Kwa nini nashukuru? Principle ya kushukuru ni hivi unaposhukuru maana yake unaomba mara ya pili. Niombe ndugu yangu fedha atuwekee pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu pia katika ugawaji wa vijiji na kata. Inawezekana kweli kukawa hakuna bajeti ya namna hii, lakini waangalie kuna vijiji ambavyo vimeshakuwa vikubwa na vingine vitongoji vina shule ya msingi na wanahitaji kuona kwamba, wanapata uongozi wao. Katika hili wafikirie, nina kata mbili za Maretadu kule na Haidereri wameanza kujenga shule zao za vitongoji na wako vizuri na wanaendelea kufanya kazi hii ya kui-support Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kuunga mkono hoja. Pili, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa kufanya kazi ambayo inaonekana kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake, Mheshimiwa Eng. Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa, kwa kweli wamefanya ziara kwenye eneo langu, Mungu awabariki sana, chapeni kazi, mimi nawapongeza mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia kwa minara ambayo kimsingi nimepata kwenye jimbo langu, mawasiliano walau yameanza kuonekana. Niwaombe sasa uko mnara ambao uko Maga na mwingine Dinamo haujawaka bado, imekaa miaka miwili pale. Najua mki-press kidogo tu ile minara itafanya kazi na mawasiliano yataongezeka na kwa ajili hiyo niwashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia nimeona kwenye hotuba hapa wametuwekea fedha kidogo kwa ajili ya barabara ya kutoka Dongobesh kwenda Babati itajengwa kwa kiwango cha lami na ile ya Mogitu – Haydom, niwashukuru sana. Sasa nilete ombi ambapo nimeona pia mmeweka kidogo na mmeizingatia barabara hii ya Karatu – Haydom – Sibiti, kwa kweli barabara hii tumeomba kwa miaka mingi sana; Mbulu imezaliwa 1905, mpaka leo kwa kweli haina barabara ya lami kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbulu hii imezaa Karatu ina barabara ya lami; imezaa Babati ina barabara ya lami; imezaa Hanang ina barabara ya lami. Kwa hiyo, Mbulu imekuwa wilaya mama tangu mwaka huo wa 1905, nashukuru kuona walau sasa inakumbukwa na nimeona hela kidogo mmeiweka humu. Nasikitika kuona mchangiaji mmoja ni rafiki yangu sana, Mheshimiwa Waziri wewe msamehe tu, amekuwa akisema unajenga barabara kama kitu kinachoitwa nywele, unajenga kwa huku unakata kwa huku, mimi nikuombe msamehe ni kaka yangu, hana tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe anzia kujenga barabara hapo ulipopanga. Kama tumeomba kwa miaka mingi namna hii barabara ya lami ijengwe kutoka Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti, mimi nikuombe jenga hapo ulipoanzia ukianzia Mbulu kwenda Haydom sawasawa, jenga; ukianzia labda Haydom kuja Mbulu, jenga na Mungu akubariki sana. Nimeona hela kidogo umeweka, sasa mimi nikuombe; ongeza kidogo hela hii ili barabara nayo ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mbulu imesahaulika sana. Kwa nini nasema hivi? Leo ukitaka kupita kwenda Shinyanga na hata ukitoka Simiyu lazima upite Singida, hakuna njia ya mkato kwenda Arusha, kwa hiyo kiuchumi tunaitegemea sana barabara hii ya Karatu – Mbulu
– Haydom – Sibiti. Barabara hii inakwenda kwenye majimbo tisa ambayo kimsingi hayana lami kabisa. Mimi leo ukimwambia hata mwanafunzi lami inafananaje hawezi kuijua kwa sababu wala hasafiri, ukijua hiyo basi ujue kwamba lami hakuna kwenye maeneo yetu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimeshukuru sana na itakuwa mara ya kwanza kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu barabara hii imeonekana kwenye kitabu hiki. Kutokana na haya yaliyoonekana hapa isije ikaishia kwenye vitabu na kwa sababu Rais aliahidi na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Jimbo la Mjini, Jimbo la Singida kule Iramba na kila mahali naomba imalizike kwani inahitajika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kwanza inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara lakini isitoshe inaunganisha Mkoa huu wa Manyara na Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa kuweka barabara hii utakuwa umetimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais lakini pia utakuwa umefungua eneo la uchumi ambao unatokea maeneo haya barabara ilikopita. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana na nikuombee Mungu udumu na Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitafurahi sasa kuona barabara hii inajengwa, itajengwa wapi mimi sijali, anzia kipande chochote. Muungwana anasema unapoanza jambo unaonesha nia ya dhati kwamba unajenga. Naona kwamba hela ni kidogo lakini kwa kuwa mimi ni muungwana sana na ni Mkristo, naomba nikupongeze hata kama umeweka kidogo lakini nimeona umeweka na Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika suala la mawasiliano. Leo tunasajili laini za simu kwa kutumia Vitambulisho vya Taifa lakini ukiangalia wenzetu wa NIDA, Tume ya Taifa na Uhamijaji ni kama wanafanya kazi zinazofanana. Mimi nishauri tu unaposajiliwa kwenye kitambulisho kimoja kwa mfano Kitambulisho cha Taifa wanapochukua finger prints (alama ya vidole) basi iwe tu katika kumbukumbu moja kwa sababu sisi tuna Data Center moja Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, National Data Center itumike vizuri ili huyu wa NIDA akichukua particulars (kumbukumbu) za mtu, kumbukumbu hizo zitumike kwenye NIDA, Tume ya Taifa na Uhamiaji. Kwa maana hiyo basi mtakuwa mmesaidia kuondoa usumbufu kwa mwananchi ili wakati wa kupiga kura pia alama ya vidole akishaweka inaonekana kila mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nilete ombi jipya kwako; tunayo Hospitali ya Haydom ambapo kimsingi barabara ile ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti inaelekea, tuna uwanja wa ndege uko pale na ni muhimu sana. Mheshimiwa Waziri naomba kabisa utuangalie, tuwekee kilometa chache katika kujenga Uwanja wa Ndege wa Haydom ili basi wanapokuja wagonjwa, maana hospitali ile ni ya rufaa na inakwenda kuwa ya kanda, utakuwa umesaidia wagonjwa wakitua pale waweze kufika kwa urahisi katika huduma hii ya kibingwa ya hospitali, nikuombe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nishukuru sana kwa kupata nafasi hii na nirudie kukupongeza sana na Mungu akubariki kwa sababu nimeona barabara hii umeiweka. Naamini mwaka huu 2019 kwenda 2020 utajenga barabara ya lami kutoka Mbulu – Haydom – Sibiti na Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kushukuru Mungu kupata nafasi hii lakini pili nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambaye kimsingi anatenda vizuri sana na Waheshimiwa Mawaziri wake hasa Waziri Mpango na Naibu wake, mtani wangu, Naibu Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usiposema ukweli hautajulikana. Miradi hii ambayo nimeisoma hapa katika hali hii ya uchumi na imeelezwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri. Naomba tu leo nisome mistari ya Biblia kutoka Yohana 20:27, inasema: “Kisha akamwambia Tomaso, leta hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye”. Haya ni maneno ya Yesu mwenyewe wakati anawaeleza Mitume wake ambao hawakuamini mambo ambayo yalikuwa yanatendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango maneno haya yampe faraja huko anakoelekea maana ni vigumu sana kwa wengine kueleza habari ya Stigler’s, SGR au ndege. Hii ni miradi ya kimkakati ambayo imesemwa na nchi hii ili kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati, hali hii isipokuwepo namna gani tutaendelea? Kwa hiyo, mimi nikupongeze naendelea hivyo hivyo. Najua wengine watakwambia acha hii, watabeza sana lakini maneno haya ya Biblia kutoka Yohana yaendelee kukutia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukupa moyo sasa nijielekeze kwenye kilimo. Kwa kweli nipongeze walau kwa namna fulani mwaka huu imeonyeshwa jinsi ambavyo tutaelekea kwenye eneo hili la kilimo. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanategemea sana kilimo na ukiangalia imeanza kupanda kutoka asilimia tatu kwenda asilimia nne. Sasa basi ni vyema tukaelekeza mipangilio yetu katika eneo hili la kilimo kwa sababu ukiangalia ipo miradi mingi ambayo inatekelezwa hasa masuala ya mabwawa ambapo mengine yamefanya kazi lakini mengine bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kulingana na nchi yetu hatuna mvua za kila mara, mvua zetu zinahesabika ni wakati wa masika, tukiwekeza katika mabwawa kilimo chetu kitakuwa na uhakika kwa sababu tutanyeshea wakati mvua hakuna. Kwa maana hiyo basi, Serikali ikijielekeza katika kujenga mabwawa mengi ni wazi kwamba baadaye wakulima wetu wanaweza kuendelea kulima kilimo cha kumwagilia ambacho kina uhakika wa kupata maji na hivyo tukaweza kusonga mbele zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule jimboni nina bwawa moja ambalo kimsingi lina shilingi bilioni moja lakini bado halijakamilika linahitaji shilingi milioni mia nne (400) tu. Kwa msingi huu, kama Serikali ikijelekeza moja kwa moja katika eneo hili la mabwawa ikamalizia mabwawa yote ambayo imeshaamua kuyajenga basi asilimia tatu kwenda nne itakuwa tano kwenda sita. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ijielekeze upande huu kwa sababu ndiyo maeneo ambayo ukigusa utakuwa umesaidia pia katika eneo hili la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nishukuru sana Serikali na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa eneo hili la afya. Kwa eneo la afya mambo yameenda vizuri hata kama siyo kwa asilimia 100, vituo vya afya na hospitali zimejengwa lakini niombe sasa tujielekeze katika vifaa tiba. Tukishapata vifaa tiba Tanzania itakuwa imesaidika sana kwani Watanzania watapata afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, tuongeze pia watumishi, wafanyakazi wakishapatikana kwenye maeneo haya basi Tanzania tutasonga mbele. Sehemu ambayo ina mkosi yaani inasababisha kushuka kwa uchumi wa kawaida wa mtu mmoja kule vijijini ni habari ya afya kwa sababu ni ghali lakini tukijielekeza kwenye vifaa tiba na watumishi Tanzania itakwenda mbele sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka kusemea habari ya miradi ya maji, tunajua wazi kwamba miradi ya maji tumeiahidi kwenye ilani ya Uchaguzi na kwa maeneo mengi imetekelezwa lakini yako maeneo machache ambayo kimsingi utakumbuka wakati wa kampeni tulisema tunamtua mama ndoo kichwani. Hii inawezekana ikiwa tu pale ambako miradi hii itatembelewa kwa ukaribu sana na Watendaji wa Serikali. Iko miradi mingine imekaa kwa muda mrefu na hata kwenye jimbo langu lipo na iko mingi lakini tukielekeza maeneo haya tukaweka usimamizi wa kutosha ni wazi miradi hii itakwisha na Tanzania wananchi watapata maji na asilimia ambayo inaonekana hapa itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalopenda kusema ni habari ya mgawanyo wa TARURA na TANROADS kwa 30% kwa 70%. Niombe, ipandisheni asilimia hii kutoka 30 kwenda hata 40% au 50% ili walau barabara za vijijini zikaweza kupitika na baadaye malighafi kwa sababu inatoka vijijini iweze kufika mjini. Tukifanya hivyo basi ni wazi kwamba uchumi wa Tanzania utapanda na hali kadhalika barabara zetu zitakwenda mbele. Mheshimiwa Mpango nikuombe sasa, kuna barabara ya Mbulu – Haydom – Sibiti; hii kwa kweli mara nyingi nimejaribu kuisema nimeiomba kweli kweli, nimeona mambo yameshakuwa mazuri, imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, imeanza kuwekewa fedha, mwaka huu nikuombe ionekane walau kwenye mipango yako basi. Ikiwekewa fedha na katika hali hiyo ukituwekea fedha bwana utakuwa umefufua eneo ambalo kwa kweli kwa uchumi wa Kanda yetu kule utakuwa umefungua sana na nina hakika katika hali hiyo mambo yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ajili ya elimu bure. Eneo hili la elimu bure hata kama hauoni kwa macho hakika sasa hivi ukiangalia wanafunzi au watoto wengi wameandikishwa shuleni wengi sana. Hebu fikiri kama Mheshimiwa Rais asinge support hii elimu kuwa bure watoto wangapi wangebaki kule vijijini hawana namna ya kujitosa katika elimu. Kwa hiyo ukiangalia kiwango kile cha watoto waliojiandikisha mwaka wa awali, ni wazi kwamba tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu amefanya kazi kubwa sana. Na hii ndugu zangu wapendwa kama hamuoni mtaona wapi? Ni vema tukawapongeza pia Serikali hii, kwa kweli Rais huyu ameamua kufanya kweli na hii kweli yake tumpe big up sana na iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kweli nielezee habari ya REA, ukweli ni kwamba Serikali inafanya vizuri kwa upande wa REA. Kwa kweli katika hali hii Tanzania itakwenda mbele, sisi vijijini sasa hivi tunapata umeme ni wazi kwamba tuipongeze na kuisaidia Serikali yetu iweze kwenda mbele zaidi. Zipo changamoto chache, kuna maeneo machache tu ambako REA haikufika wakandarasi wanakosa fedha, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango elekeza mipango hii pale ili REA nao iende mbele zaidi vijiji viwe vingi na hatimaye pawe na kile kinachoitwa ujazilizo katika maeneo yetu. Maana yake maeneo ya vijijini sasa hivi kwa bahati mbaya sana imefika kwenye maeneo ya Kata tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri pamoja na mipango hii ikielekea na namna hii kufika mwaka 2020/ 2021 tutakuwa tumefika maeneo mengi sana na wananchi watakuwa wamepata umeme. Leo hii Television zinaonekana vijijini jambo ambalo kwa miaka iliyopita ilikuwa hakuna, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais nakuombea Mungu akubariki sana uendelee mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana ahsante sana kwa mchango naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. FLATEY G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kusema jioni hii ya leo. Kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa kutujalia na kutupatia uhai, lakini pia nikishukuru chama changu kwa kunichagua na kuniteua jina langu na kupigiwa kura na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini. Niwashukuru sana kwa kunipa kura na kunileta humu ndani. Nikushukuru na wewe sasa kuwepo tena kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu wa kuchangia hizi hotuba mbili za kufunga Bunge la Kumi na Moja na kufungua la Kumi na Mbili, ukiangalia sasa jinsi ambavyo Rais wetu anavyofanya kazi mimi namuombea Mungu ampatie afya njema, aendelee kumpa nguvu ili hizi ndoto ambazo amekuwa akizizungumza katika hotuba yake Mungu asaidie na sisi tumsaidie twende naye kufanya Tanzania ambayo sasa tumeingia kwenye uchumi wa kati, twende zaidi ili wananchi wetu waondokane na kero ambazo zipo katika maisha ya kawaida ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu dakika ni chache naomba niende kwenye upande huu wa kilimo. Ukiangalia ukurasa ule wa 27 kilimo chetu wananchi wanakitegemea sana, zaidi ya asilimia 75 wanategemea kilimo. Sasa naomba nishauri kwa sababu Wizara sasa ndio wana kazi ya kuhakikisha kwamba wanaangalia ile vision ya Mheshimiwa Rais wakati anaitoa hotuba hii. Ukiangalia leo mvua zinanyesha na mimi niishauri Wizara nayo iangalie iende katika kuwekeza kuzuia maji yanayotokana na mvua na kuchimba mabwawa, ili mabwawa yanapochimbwa basi itasaidia zaidi kufanya kilimo cha uhakika. Tukichimba mabwawa, tukaweka fedha na fedha hizi tukasaidia kuziwekeza katika mabwawa na maeneo mengi ya wafugaji na wakulima mabwawa haya yatatumika kwa mambo mawili, kwanza yatanywesha mifugo, lakini pili tutakuwa na kilimo cha uhakika wa kupata mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Mheshimiwa Rais amezungumza sana na ameahidi kwamba, katika wakati huu atahakikisha pembejeo zinafika kwa haraka. Na pia, ukiangalia sasa kwa hali ya saa hizi tusipoweza kuishauri Serikali vizuri na mimi naomba niwashauri, ukiangalia leo hii bei ya mbegu katika maeneo yetu ni kubwa zaidi kuliko debe moja. Kwa mfano, kilo moja saa hizi au mbili katika mfuko mmoja ni shilingi 13,000/= mpaka shilingi 14,000/=. Debe unapokuwa umevuna mazao linakuwa na shilingi 6,000/=; kwa hiyo, basi mimi nishauri tuone namna gani pia ya kuanzisha mashamba ya mbegu humu nchini kuliko mbegu kutoka nje ya nchi kuja kuuzia huku. Kwa nini tusizalishe mbegu sisi tukawauzia wakulima? Na hili linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini linguine kutokana na muda twende kwenye TARURA. Mimi nina kilometa 1,300 kwenye Jimbo la Mbulu Vijijini, tunapata shilingi milioni 696 haziwezi kutengeneza barabara hii. Sasa niombe wakati tunatunga sheria ya kuisaidia Serikali kutumia mfumo huu wa bei ya soko yaani force account, kwa kutumia miradi hii ya afya na miradi mingine ya kujenga majengo ya shule wataalam hawakukubali sana; mimi niombe Serikali ije na mpango, ione namna gani ya kusaidia hii TARURA maana tunaweza kuwa katika ukandarasi tunapigwa sana. Sasa ili kuona namna ya kusaidia Serikali hebu tujaribu twende kwenye force account pia kwenye TARURA naamini katika njia hiyo tunaweza kusaidika.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia barabara zetu nazo zimekuwa na halimmbaya sana, ni ngumu. Tuone namna gani mwaka 2016 tumezungumza Habari ya TARURA, mwaka 2017 tumezungumza hivyo, mwaka 2020 tumezungumza hivi hivi, tunaenda mwaka wa 2021 naomba sasa tufanye namna ya maamuzi makubwa tuamue ili TARURA ikafanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona muda umeisha, basi kwa sababu, muda umeisha tutakutana kwenye mpango, niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anazofanya kwa umahiri mkubwa. Namuombea Mungu azidi kumtia nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo ahadi za Mheshimiwa Rais katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambayo ni barabara ya lami toka Mbulu – Haydom - Sibiti. Naomba itengwe fedha ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Haydom - Mbulu maana hatuna kabisa lami katika Jimbo la Mbulu Vijijini. Kwa kutekelezwa kwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli itakuwa imetatua kero kubwa ya wananchi ya kushindwa kufika katika Hospitali ya Haydom. Pili, kwa kufanya hivyo mtakuwa mmetekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Dongobesh. Tunaomba tupewe fedha za kujenga Kituo cha Afya Maredadu maana wananchi wameshajenga katika hatua ya mwanzo ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la kutomalizika kwa miradi ya maji katika Jimbo la Mbulu Vijijini, mfano mradi wa Arri – Harsha na Tumati Mungasharq. Tunaomba msukumo wa Serikali katika miradi hii ya maji. Nashauri pawepo na Mamlaka za Maji za Mikoa ili ziweze kuisimamia miradi ya wilaya kwa ukaribu zaidi na certificate zilipwe kwa wakati.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Nianze kutoa mchango wangu katika Mpango huu wa mwaka mmoja na miaka mitano na nataka kwenda kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukiangalia kilimo cha umwagiliaji katika nchi yetu tunalima hekari 461,376. Kilimo cha uhakika duniani kote lazima utumie umwagiliaji na ukimwagilia maana yake una maji ya uhakika na unaweza kunyeshea na mazao yakaiva kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hali halisi kwa sasa Tanzania mvua zinanyesha na hapa Dodoma unaona mchana kutwa mvua imekuwa ikinyesha, lakini hakuna namna yoyote tunayofanya, kama nchi kuweza kuzuia maji haya. Nashauri katika Mpango huu, Serikali ije na mpango mzuri iweke hela kwenye kilimo, wananchi waweze kutengenezewa mabwawa ili haya maji ambayo yanatoka katika mbingu yanapokuja ardhini yaweze kutiririka kwenye mabwawa, yahifadhiwe na badaye wakulima wetu waweze kunyeshea mashamba na Tanzania tutaokoka kwa kuwa na mashamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mvua hizihizi ndiyo zinazoenda kuharibu barabara. Tumekuwa tukilalamika hapa tangu hotuba ya Rais kwamba TARURA iongezewe fedha, lakini tungekuwa na namna ya kuzuia haya maji yaende kwenye mabwawa badala ya barabarani, ni wazi ni rahisi sana kuweza kutumia maji haya ambayo yapo katika nchi yetu kufanya kilimo cha umwagilia. Maji haya yanaharibu barabara. Yanapoharibu barabara maana yake ni kwamba Serikali hiihii pia tunaanza kuilaumu itafute pesa za kutengeneza barabara, kumbe tungeweza kuwa na mpango mzuri wa kuhifadhi maji yanayotiririka, ili maji haya yakaweza kunyeshea mashamba na wakati huohuo tutakuwa tumezuia maji haya yasiende kwenye barabara kuleta uharibifu. Kwa hiyo, nadhani Waziri Mpango na Serikali yake waone namna gani kusaidia kuweka fedha ya kutosha katika uwekezaji kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti zote zilizopita hazikuonesha wazi kabisa kwamba tumewekeza kwenye kilimo. Kwa mfano leo, AMCOS na mashirika madogo madogo ya wakulima yamekuwa yanakopeshwa ili kulima lakini wakati huo wanawekewa insurance ya pembejeo hizo, lakini wakati huo wanaenda kudaiwa wakati ambapo Serikali huku hatujawawezesha bado kwa kuwawekea namna nzuri ya kupata mavuno kwenye mashamba yao. Ni lazima tuhakikishe kwamba tunapowakopesha wakulima, wakati huo tumeshawawekea mazingira mazuri ya wao kuzalisha, vinginevyo tutakuwa tuna madeni na tunawadai hawa wenye AMCOS lakini hawataweza kulipa. Nadhani masuala haya yanapaswa kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, pembejeo. Leo hii Tanzania kama nchi, pembejeo zetu zote tunatoa nje. Kwa mfano, mbegu zetu nyingine zinatoka Kenya, Uganda lakini ombi langu kwa nini tusianzishe mashamba ya mbegu katika nchi yetu ili mbegu zisitoke nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati nachangia kwenye Hotuba ya Rais, mbegu zinatoka nje kwa gharama kubwa, ikija hapa kwetu tunauziwa shilingi 13,000 mpaka shilingi 15,000 kwa mfuko. Ni wazi kabisa kwamba mwananchi wa kijijini kule kwa kupanda eka nyingi anahitaji kuwa na investiment ya kutosha. Tukiwa na mashamba ya mbegu hapa nchini ni wazi kwamba mbegu zitakuwa za bei nafuu na zitaongeza ubora katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya barabara katika nchi zote ndiyo inayosaidia uchumi wa nchi kupanda. Katika Mpango huu, naomba muangalie barabara kubwa zinazoleta uchumi katika nchi hii. Kwa mfano, kuna barabara ambayo kila siku tumekuwa tukiisema hapa, hii ya Karatu - Mbulu - Dongobesh - Haydom - Simiyu - Bariadi.

Kwa hiyo, barabara kama hizi zikifunguliwa na zikaonekana kwenye Mpango, kwa sababu, ukiangalia kwenye Ilani ya Chama ipo, kwenye Hotuba ya Rais ipo, lakini namna ya kuweka mpango sasa hii barabara ianze kujengwa ndiyo inakuwa kigugumizi, kwa hiyo, kupanga ni kuchagua. Ukipanua hili eneo la Tanzania kama nchi ukawekeza hela kujenga zile barabara za upande ule, kwa hiyo, unapozunguka nchi hii mazao yanatoka kijijini kwenda viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nikuambie ukweli viwanda vyetu vipo, lakini ukimuuliza Waziri wa Viwanda atakuambia hakuna malighafi, lakini nenda kijijini kwa mfano Haydom utakuta alizeti ipo. Itafikaje kiwandani, haiwezekani kwa sababu barabara za kule ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika ni kidogo sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwa Ulinzi na Usalama wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Masauni, sisi Jimbo la Mbulu Vijijini tumejenga Kituo cha Polisi cha Yaeda Chini na kukimaliza kabisa tumebakia na nyumba za Walimu ili kituo kianzishwe hapo Yaeda Chini kwani wananchi wamejenga ili kupata usalama wa watu na mali zao. Sababu za kujenga kituo pametokea mauaji ya raia hapo nyuma bila watuhumiwa kufikishwa Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, kuna wizi wa mifugo ambao unaendelea, mifugo mingi imekuwa ikiibiwa na ikawaacha wananchi wakiwa hawana nchi zao ndiyo maana wameamua kujenga kituo cha polisi. Wanawake wengi wamekuwa wanabakwa sana hii ni kutokana na taarifa ambazo zipo. Ili kupunguza tatizo hilo tume ambazo zipo ili kupunguza tatizo hilo tumeamka kujenga kituo cha polisi ila tumeishiwa na nguvu za kuweza kuchangia hela na nyumba za askari tusaidieni hata nyumba moja. Mimi Mbunge nimechanga milioni nane za ujenzi wa kituo hiki cha polisi kushirikiana na wananchi. Ombi langu tupatiwe fedha za ujenzi wa nyumba za askari.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza nianze kuwapongeza Wizara hii ya TAMISEMI, nimpongeze Mheshimiwa Ummy kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Festo hongereni sana. Najua nyinyi ni wachapakazi na kwasababu tumeshafanyakazi kwa awamu, yaani miaka mitano iliyopita najua uchapakazi wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si vibaya nikushukuru sana Mheshimiwa Ummy ulipokuwa Waziri wa Afya kwa kweli ulifanya kazi vizuri na najua utendaji wako wa kazi. Niishukuru pia Serikali kwa kunijengea Hospitali ya Halmashauri ambayo kimsingi haikuanza kazi ila kwa kweli imemalizika lakini yapo mambo machache ambayo tungependa yakamilike. Ziko fedha ambazo kimsingi zilishafika kwenye account za halmashauri lakini bahati mbaya sana fedha zile zimeondoka kutokana na kwamba muda wa bajeti ulishafika kwa hiyo, wakati wa mwaka mwingine fedha zikachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe zile fedha zikirudi basi hospitali hiyo itakamilika na hatimaye kuanza kazi kwasababu ni hospitali hiyo tunaitegemea tu ya Halmashauri ya Mbulu. Na kwa hiyo, nishukuru sana lakini kingine nikushukuru pia kwa kituo cha afya cha Dongobeshi ni hicho kituo kimoja tu. Lakini ombi langu unajua unaposhukuriwa Mheshimiwa Waziri tuna principal za kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wakristo kuna sala ya Baba Yetu tunasema Baba uliye Mbinguni unamshukuru Mungu, unasema jina lako litukuzwe unamshukuru Mungu, unasema mapenzi yako yatimizwe unamshukuru Mungu lakini baadaye huyu Mungu unamuwekea ombi unasema utupe riziki za kila siku sasa Mungu anapenda sifa na anamjalia mja wake anapomuomba. Sasa nimekusifia na nyinyi mawaziri ili haya maombi yapitie hii sala na mtume basi huko vijijini ili mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu ni kujengewa vituo vya afya, Mbulu vijijini kama Jimbo tuna kituo kimoja tu acha afya kama Mke wa Mkristo kwa hiyo maana yake ni huyo tu, Wadongobesh ndiyo kituo kimoja. Na sisi kama Halmashauri ya Jimbo la Mbulu Vijijini wananchi wamejenga Vituo vya Afya vipo hatua mbalimbali; kuna Kituo cha Afya cha Getere ambao wameshazeeka kwa hiyo, tukipata fedha kidogo tunamalizia. Kuna kituo cha afya cha Maretadu na tuna zahanati nyingi tumeshajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ujue kwamba tukishajenga vituo hivi mkishatupatia zile fedha na sisi watumiaji wazuri wa fedha mkishatupa katika halmashauri yetu. Kuna Zahanati ya Galabadi, Zahanati ya Halsha, kuna Zahanati ya Hanaj na maboma mengine ambayo yapo kimsingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pia nishukuru umetupa fedha katika zahanati tatu nimeziona juzi. Lakini mkituongezea basi ni wazi kwamba kwa jimbo la Mbulu vijijini tunaweza kuihudumia wananchi wetu kwa afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Wizara hii ya TAMISEMI saa hizi majimbo yetu ya vijijini yameanza kuwa na kata zake ni kubwa, kwa miaka zaidi mitano tunaenda mwaka wa sita hapajatokea kabisa ugawaji wa Vijiji na Vitongoji na Tarafa. Sasa niombe muangalie kwenye bajeti yenu ijayo muweze kutenga fedha za kugawa Vijiji na Vitongoji na Kata kwasababu zimekuwa kubwa sana hazitawaliki. Na sisi tuna Tarafa ambayo tunaiomba sana mara nyingi tunaleta maombi kwenye tuna Tarafa tunaiita ya Hedayachini kule kuna Wahadzabe eneo lao ni kubwa sana ina kilometa 245. Kwa hiyo, ni Tarafa ambayo kwa kweli ukiangalia tunahitaji jambo dogo tu kuwapatia ule uwezo wa kugawanya Tarafa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na TARURA, umezungumza katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umeonyesha kwamba kuna jambo la ugatuaji wa madaraja D by D nitaizingatia sana. Lakini ni ngumu kwasababu moja kwenye Jimbo la Mbulu vijijini kwa sababu tu ya miundombinu ya barabara ambayo kimsingi haiwezi kwasababu kwanza TARURA pesa zake zinazopatikana ni kidogo sana, sisi kwa mara ya mwisho tumepewa milioni 671 na tuna barabara zetu zenye urefu wa kilometa 1,093.7. Kwa fedha hizi kwa kweli hatuwezi kujenga hizi barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo korofi ambayo kimsingi imekuwa na shida tunatakiwa tujenge madaraja kumi yenye jumla ya shilingi bilioni 11 hasa umepewa Milioni 66. Nimpongeze sana Meneja wangu wa TARURA wa Wilaya anajitahidi sana kufanya kazi na nishukuru umempa gari lakini shida iliyopo pale ni kwamba hakuna namna yoyote ya kujenga hizo barabara. Lakini nishukuru sasa pamoja na hayo yote nimeona kuna kama kamilioni kadhaa kameongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hasa niombe tumeweka madaraja yetu mfikirie namna ya kuyajenga kwasababu kuna shule kama saba sasa haziendeki kutokana na miundombinu. Kuna daraja la Masyeda, kuna daraja la Getere na Miodad hayawezi kabisa kupitisha wanafunzi na kwasababu mvua ikinyesha tu hizo shule tena hazifikiki kwasababu umbali ule na makorongo yamejaa. Kwa hiyo, naomba TAMISEMI wafikirie na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi tumeleta maombi ya kupandisha mji wetu wa Haydom kuita Manispaa aah na ni hii mji wa Haydom. Tumeleta maombi yetu na Mji wa Dongobesh tumeleta maombi tufikirie na hilo lakini mwisho kabisa najua dakika zimekwisha tuna ahadi za kilometa 5 ya mji wa Haydom, tuliahidiwa na viongozi wetu naomba tumejenga kilometa 1.8 naomba sasa tuweke fedha ili walau zile kilometa za ahadi za Mheshimiwa Rais ziweze kutimilizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa nishukuru pia kwa utendaji wenu wa kazi lakini niwakumbushe pia pamoja na wewe Mheshimiwa Ummy unakumbuka umefika Haydom na umefika Dongobesh zile ahadi zetu tulizoziweka pale ukanisaidie sana kuzitimiza na kwasababu umeingia TAMISEMI Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea mchana huu wa leo. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Awesso na dada yangu Mheshimiwa Eng. Prisca kwa kazi wanazofanya kwenye Wizara hii. Ninakupongeza kwasababu ninajua jinsi ambavyo umesumbuka na Wizara hii, tangu ukiwa Naibu Waziri na sasa Waziri. Nataka nikupe moyo najua kuna changamoto, Biblia inasema namna hii kwenye kitabu cha Mwanzo mstari wa 1 na nikuambie tu unashughulika na kazi ya uumbaji ujue hilo unapotafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwanzo anasema kwenye mstari ule wa 1, hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na nchi, nayo nchi ilikuwa tupu na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, na roho ya Mungu ilitulia juu ya uso wa maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Awesso jua unazungumza na unafanya kazi katika hali ya uumbaji. Nakumbuka unapotembea kutafuta maji, unaposaidia kuipa maji nchi ujue kwamba unasumbuka na kazi ambayo Mungu aliifaya hapo mwanzo. Na nikuombee Mungu akusaidie katika hayo. (Makofi)


Mheshimiwa Spika, lakini sasa umekuja Mbulu Vijijini nakushukuru, sasa ujue hiyo kazi Mbulu Vijijini inahitajika sana hiyo ya uumbaji kutafutia watu maji na katika slogan zetu tumewahi kusema maji ni uhai. Kwa hiyo, bwana, tusaidie tupe uhai katika Mbulu Vijijini. Ninashukuru nimeona kwenye bajeti imetengwa bilioni 2,300,000,000/= hii ni wazi kwamba, tunafanya kazi hii na niishukuru sana Serikali umetusaidia sana kwenye visima vya pale Haydom. Sasa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ameitoa pale Samia Suluhu Hassan ya kutoa maji katika Ziwa Madunga kuleta katika Mji wa Dongobesh. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nishauri kiujumla, hii kuchimba visima naomba Wizara iangalie Je. ni njia sahihi ya kuwapatia watu maji? Maana visima vidogo vidogo wanavyochimba ninahakika katika maeneo mengi visima vile vimekufa kwasababu, tu maji maeneo mengine yanachimbwa na wanakutana na mwamba basi hela inakuwa imetumika zaidi. Kwa nini Wizara isiende ikachukue maji kwenye sehemu yenye ziwa ikapeleke kwenye vijiji pakawa na usambazaji, kuliko kila mahali kuchimba visima ambavyo baadaye vinakauka na hali kadhalika Serikali inakuwa imeharibu hela pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe Wizara ione namna hii kwamba, tunapochimba visima hivi vinatusaidia sana? Au kuchukua maji kwenye Ziwa na kuyasambaza? Nadhani tukichukua maji kwenye maeneo yenye Ziwa tukasambaza maji, fedha ya Serikali itatumika na watu wengi watapata maji kwa maeneo mengi. Sasa niombe kwenye bajeti yetu naona kuna vijiji umeviweka vingine si vya Jimbo langu na nimeshakuambia tangu jana wataalam wako waangalie, waweke visima vilivyo na majina yaliyopo kwenye Jimbo langu la Mbulu Vijijini. Naomba nikutajie sina hakika kama Hansard itashika lakini najua tutaongea baadaye.

SPIKA: Haya mjiandae Waheshimiwa Wabunge anataja majina. (Makofi)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kuna kisima cha Gembaku, kuna kisima Getanyamba, Qaloda, Edahagichani, Maheri, Maretadu, Endadubu, Galoda, Dotina, Labay, Ng’orati, Garbabi, Qatabela, Qheteshi, Endaanyawish na Endaharqadat. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ndugu yangu mpendwa hivi ndio vijiji vyangu, lakini vijiji ulivyoviweka sio vya kwangu kabisa, angalia kitabu chako cha bajeti. Wataalam waangalie vijiji walivyoweka si vya kwangu lakini waviweke basi hivi nilivyovitaja kwasababu, najua ndivyo vilivyoombwa katika bajeti toka Wilayani.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana naamini atakuwa amevishika na ndugu yangu Awesso ni kijana mzuri sana na slogan zako nazipenda. Bwana sikufichi na kule kwetu nawapongeza sana wataalam wa maji wamejitahidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji katika Mkoa wa Manyara kuna shida kubwa sana ni asilimia 53 kwa Mkoa wa Manyara unaopata maji. Kwa hiyo, ni chini ya asilimia ya nchi. Lakini pia, Jimbo la Mbulu Vijijini tuna asilimia 59 si mbaya sana lakini si nzuri sana. Lakini ukiangalia pale Haydom Mheshimiwa Aweso, uliahidi mwenyewe kisima kichimbwe mpaka leo kisima hakijachimbwa bwana. Haydom pale tuna asilimia 52 tu ya wakazi wanapata maji basi nikuombe sana angalia maeneo hayo. Lakini Haydom na Dongobesh tumeomba mtusaidie tupatieni Mamlaka ya Maji kwasababu, kuna jumuiya ya watumia maji wana hela nyingi sana pale zaidi ya milioni 400, ukiwaacha wale wananchi watumie ile hali ya watumia maji hainogi sana kwa sababu pale hawana wataalam wanaofanya kazi hiyo sio wakuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, lakini Haydom na Dongobesh tumeomba mtusaidie tupatieni Mamlaka ya Maji kwa sababu kuna Jumuiya ya Watumia Maji wana hela nyingi sana pale zaidi ya shilingi milioni 400, ukiwaacha wale wananchi watumie utaratibu ule wa watumia maji hainogi sana. Nasema hivyo kwa sababu pale hawana mafundi na wataalam wanaofanya kazi hiyo sio wa kuajiriwa kwa hiyo kudhibiti ile fedha kwa kweli hali si njema. Nikuombe sana uone jambo hili kwa sababu ni mji mkubwa unakua na kuna hospitali kubwa ya Rufaa ya Haydom.

Mheshimiwa Spika, suala kubwa zaidi ni units za maji, imekuwa kero sana katika Mji wa Haydom na Dongobesh, unit imekuwa Sh.2,000. Mheshimiwa Waziri utakapofikia hatua ya kupelekea pre-paid machine za kulipia maji, nikuombe kabisa anzia na hiyo miji ya Haydom, nafikiri mambo yatakwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, suala lingine DDCA wamechimba visima tisa hawajapeleka maji yaani wamechimba pump wakazifunika. Niombe wazipeleke zile pump ili watu wapate maji. Wananchi wanapoangalia pump inakuwa taabu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais ametusaidia sana katika kutuletea fedha za elimu, hasa katika Majimbo yetu, kwenye shule za Msingi, shule za Sekondari na sasa ndiyo hili tatizo linajitokeza hapa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuunga mkono mara moja hoja hii ya Mheshimiwa Ezra. Kwa sisi ambao tunaabudu katika Biblia, maneno ya Mungu yanasema hivi kwenye Mithali 4 Mstari wa 13, “Mkamateni sana elimu msimuache aende zake, mshike maana yeye ni uzima.” Kama haitoshi Biblia inasema tena kwenye Kitabu cha Hosea, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimenukuu tena kwenye neno…

SPIKA: Sasa ngoja nikusaidie kidogo, ni watu wangu wanaangamizwa, sio wanaangamia, watu wangu wanaangamizwa.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, sawasawa. Kwa kukosa maarifa na maarifa yanaletwa na elimu. Kwenye misahafu, amenisaidia hapa Mheshimiwa Nahodha, Mtume anasema hivi, tafuteni elimu mpaka China. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa nimejaribu kuangalia na kwenye Biblia yangu hapa nimefungua neno elimu limeandikwa mara 300 kwa umuhimu wake, neno tu elimu. Nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Rais wetu cha ‘‘Maisha Yangu Malengo yangu au Maisha Yangu Dhamira Yangu’’ amendika, yeye mwenyewe nanukuu: “Mimi leo ni Rais nisingefika hapa bila elimu” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yangu ni kuonesha jinsi ambavyo elimu imepewa kipaumbele kwenye Biblia na Misahafu pia kwa viongozi wetu wa nchi. Tumeona sisi hapa leo hii, mimi kule Jimboni wanafunzi wengi wa vyuo wamerudi sasa kwa sababu kwa kweli hawana mikopo na hawawezi kuendelea bila mikopo. Ukiangalia bajeti ya mwaka jana, amesema Mbunge mmoja hapa na nimesoma ni zaidi ya Bilioni 427, tena mwaka huu Bilioni 570. Ni lazima sasa Serikali ije na projection tunapokwenda kwenye miaka ya bajeti tuhakikishe kwamba tatizo hili halijirudii tena, kwa sababu hili ni bomu na bomu hili linakuja pale ambapo sasa tunaendelea kukatishana tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika familia zetu maskini watu wengi kwa kweli kwa sasa wameshauza mashamba, wameuza ardhi, wamefanya mambo mengi kufikisha watoto katika level hii ya University. Sasa inapofika mtoto anakosa fedha ya mkopo ili kuendelea na masomo yake, hasa akiwa mwaka wa pili au mwaka wa tatu na kurudi nyumbani, hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, ukiangalia sasa hivi katika zile sifa za kupata mkopo, awe yatima, awe fukara, asiwe na wazazi, haya yote Serikali haina uwezo wa kujua moja kwa moja na kama inao basi maana yake ni kwamba, hali yetu imeshakuwa mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba hii Bodi ya Mikopo ivunjwe mara moja kwa sababu inaonekana sasa haina namna ya kutusaidia, lakini pili utaratibu huu wa kuona namna gani ya kupata mkopo kutoka mtoto wa fukara au masikini utaratibu huu uangaliwe upya kwa sababu, inaonesha kabisa hali ni mbaya kule kwenye maeneo yetu na wananchi wanapata shida.

Mheshimiwa Spika, pia tuone tutafute hela ya dharura ili watoto hawa waweze kwenda shule, tusipofanya hivyo tutakuwa tumezalisha watoto ambao baadae hawawezi kuwa viongozi. Kwa mfano, ametoa mfano mtu mmoja hapa, Rais wetu wa Kwanza, Baba wa Taifa, ameenda shule na wakati ule bahati nzuri shule ilikuwa bure na ametoka kwenye familia tunayoijua. Rais wa Pili, Rais wa Tatu, Rais wa Nne na Rais wa Tano, bila ya elimu asingeweza kuwa Rais na huyu wa Sita kaenda sana, unajua leo hii bila elimu kwa nafasi hii ya Urais watoto wetu wale fukara hawawezi kuwa viongozi.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba Wabunge leo hii tusimame, tuungane kwa jambo hili, Serikali ije na fedha ya dharura kuwasaidia watoto hawa ambao wako nyumbani wanaotakiwa kwenda vyuo sasa. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga hoja hii mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fursa ya Elimu Bure. Pamoja na kusaidiwa na Serikali, tuna shule ambazo ni za zamani sana hasa Mbulu DC mfano Shule ya Msingi Maskaroda inahitaji ukarabati kwani majengo yake ni ya zamani, tangu 1955 na watoto ni wengi. Tunaomba Wizara ione namna ya kusaidia ujenzi wa madarasa. Pia katika Sekondari wananchi wa Maretadu wamejenga Sekondari ya Kidato cha Tano bwalo na madarasa manne. Tunaomba msaada wa kuongeza bwalo kwani wananchi wameamua kuchangia majengo ili kusaidia kuanzishwa kwa Kidato cha Tano na Sita Mbulu DC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule maalum zipewe kipaumbele katika bajeti ya Waziri wa Elimu kwani bila kufanya hivyo wanasahaulika sana. Hivyo naomba zipewe kipaumbele. Mfano, Shule ya Viziwi Dongobesh na nyingine zilizomo katika nchi. Walimu wanahitajika sana katika shule hizi za walemavu hasa wale wenye ujuzi wa kuunda hao watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Sekondari Mbulu DC zimejengwa na wananchi, zinahitaji msaada wa kujengewa madarasa na nyumba za walimu, mfano Dr. Olsen Sekondari ina wanafunzi wengi na hawana madarasa na bweni; na watoto wa Kidato cha Tano na Sita wanapata taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za Walimu wa Sayansi ni kubwa sana katika Shule nyingi za Sekondari, hivyo kupelekea ufaulu kuwa chini. Hivyo tunaomba Walimu wa Sayansi waongezwe ili kukidhi haja hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nitoe pongezi zangu kwa Serikali ya Awamu ya Tano, pia kwake Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. F. Ndugulile, kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani hizi, naomba nikumbushe jambo moja kwamba Dongobesh, Kituo cha Afya na Jimbo la Mbulu Vijijini hatuna kabisa gari la wagonjwa (ambulance) la kuwahudumia wananchi. Pia Mheshimiwa Ummy akumbuke ilikuwa ahadi yake pale Dongobesh baada ya ziara yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli nakubali kazi wanayofanya Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Faustine, wamefanya ziara ya kuona changamoto za Mbulu Vijijini. Pia tumejengewa kituo kimoja cha afya cha Dongobesh, ahsanteni sana. Hospitali ya Halimashauri ya Wilaya inajengwa, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaombea Mungu warudi tena katika nafasi zao baada ya mwaka 2020 katika Uchaguzi Mkuu. Mungu atujalie, ahsanteni.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kuleta Muswada huu ambao kimsingi unaonesha una matumaini kwa wananchi wetu hasa kwa sehemu hii ya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapotazama neno “utafiti,” napata mwamko mzuri wa kuona kwamba sasa Serikali imekuja na mpango mzuri wa kusaidia jamii yetu; maana ni nini maana ya utafiti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema “utafiti,” maana yake ni uchunguzi kuhusu jambo fulani kwa undani. Sasa kwa kuwa, naamini wakulima wetu hasa katika maeneo yetu tumekuwa na mambo mengi ambayo tuna matarajio hasa kuhusu kilimo; na leo Serikali wanapoleta Muswada huu, mimi kwa kweli kama mdau wa kilimo, nimefurahia sana hali hii. Hata hivyo yako maeneo machache ambayo nilipenda kushauri na kuchangia kama mchango wangu humu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo hili la uwakilishi. Wameonesha kwamba kuna mwakilishi mmoja wa wakulima, lakini nilikuwa napenda kuona kwamba, kwa nini asiingizwe hata wa pili? Tatizo liko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda moja kwa moja katika hizi Kanuni za Utafiti. Nimezisoma hapa vizuri sana, lakini ukiangalia na pia, hawa wanaoingia humu; kwa mfano, ukimwangalia kama Mkurugenzi anayetegemea kuteuliwa hapa, anatakiwa awe na sifa na hii inayoonekana kwenye Muswada huu wa sheria ya Kiswahili kwenye page ya 41 Kifungu cha 8(c) inaonesha kabisa mtu huyu lazima awe na uzoefu au ujuzi uliothibitika wa miaka 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kabisa kwamba kuna hali ya kupunguza idadi hii ya miaka. Napendekeza kwamba, kwa kuwa miaka 10 ni sawa sawa na miongo miwili ya Mbunge, kwa mfano, mimi nimeingia hapa leo, kwa miongo hii 10 ndiyo unampata mtu ambaye anaweza kuwa na sifa ya kuingia humu kama Mkurungezi. Naishauri Wizara ione namna ya kupunguza huu uzoefu. Kwa nini nasema hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba muda huo nauona ni mwingi sana; kwa nini isifanywe hata miaka mitano? Uzoefu ukachukuliwa kutoka sasa na mtu basi akaajiriwa kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, utafiti ni jambo zuri sana, lakini zipo tafiti nyingi ambazo zimefanyika maeneo mengi katika vyuo vingi, zimekuwa zikiachwa. Naishauri sasa Wizara ijielekeze na Serikali iweke mazingira mazuri ya hawa watafiti wetu ili wanapofanya utafiti, basi utafiti huu uchukuliwe kwa jinsi ambavyo wanaweza kupewa motisha. Maeneo mengi kwa nchi nyingine vijana wengi wanaingia katika utafiti kwa sababu wanajua wakifanya utafiti, utafiti huu ukazaa matunda, utafiti pia unalipa kwa maana ya kwamba wanaweka kwenye kumbukumbu za vitabu. Kwa hiyo, niliona niseme haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye taasisi za utafiti naomba kabisa ianzie chini. Hata utafiti huwa unazoelekea; pawe na co-ordination. Utafiti na tafiti nyingine huwa zinakaribiana, hata kama ukiwa utafiti wa sayansi ya kilimo, lakini kuna utafiti wa biolojia, kuna tafiti zote hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri paundwe chombo ambacho kitasaidia ku-coordinate tafiti hizi. Hii ikishafanyika itakuwa ni jambo zuri ambalo litasaidia watafiti wetu wa hapa nchini kuwa na muunganiko mzuri wa kufanya tafiti zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tafiti sijaona mahali ambapo panaonesha tafiti hizi zitasaidiaje wananchi wetu? Nawapongeza sana, kwa sababu sisi wakulima tuna matatizo mengi sana, lakini labda matatizo yatatusaidia sasa katika tafiti hizi. Kwa mfano, yapo maeneo mengi ambayo wananchi wetu wanakuwa na kitu kinachoitwa maeneo ya kulima, lakini hawajui kwamba mbegu gani hasa inaweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba, maeneo hayo nitashukuru sana kama tafiti zitasaidia pia kuona kwamba katika maeneo yote ya kule vijijini hawa watafiti watatusaidia, hivi ni mbegu gani na inafaa katika eneo hili? Kwa mfano, maeneo labda ya Babati au eneo fulani na udongo huu wa maeneo haya: Je, unafaa kwa zao gani? Nina uhakika kwamba watafiti hawa wakifika mahali hapo, basi Tanzania yenye kutakiwa kuwa na uchumi wa kati, labda tutaupata kwa njia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo la fedha. Nimeona hapa kwenye eneo la (h), bodi hii inatakiwa kutafuta fedha, ni kweli. Naomba katika bajeti ya Serikali, Serikali ijielekeze yenyewe kutenga bajeti katika utafiti. Usipotenga bajeti na sisi Wabunge tukawa hapa tunapitisha sheria hii leo, kwa makofi, tutatafuta namna ya kuunda Bodi, tunaajiri Wakurugenzi lakini mwisho kama sisi Wabunge hatutatenga bajeti ya kuwezesha utafiti, sina uhakika kama utafiti huu utazaa matunda ya kwenda moja kwa moja kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika bajeti ijayo; najua bajeti imeshapita; Serikali iweke mazingira wezeshi na kutenga bajeti ya kuwasaidia hawa watafiti ili bajeti itakapokuwa wezeshi, utafiti utafanikiwa; na maeneo haya yatakuwa na afadhali kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze tena kuiomba Serikali; mara nyingi tunakwenda kusoma masomo haya ya utafiti kwenye high level, lakini ushauri wangu, kwa nini basi usianze huku chini? Nchi za wengine, wanaanza utafiti kwenye masomo ya msingi kabisa na mtu akifika sekondari amekomaa kwa jambo la utafiti. Kwa hiyo, kunakuwa na co-ordination kutoka maeneo haya; tutakuwa tunahamasisha vijana wetu kufanya utafiti. Waingereza wana msemo wao wanasema, “if you have no research, you have no right to speak.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii basi, naipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu. Kubwa zaidi naomba Wizara pia itusaidie; hawa watafiti wanaofanya mambo ambayo yanaonekana yapo vizuri, tuwe na mpango basi wa kuisaidia bodi hii na watafiti wa nchini kwetu kuwapa tuzo, pawepo na tuzo. Katika historia ya Tanzania sijaona mahali popote hata kwenye Muswada nimeangalia, hakuna mahali pa kumpa hata motisha mtafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia haya ili hata haya yakawe yanawezekana kwamba mtafiti apewe na motisha na Serikali yenyewe. Ahsante sana.