Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zainab Athuman Katimba (16 total)

MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ilifanya ongezeko la fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu kwa shilingi 1,000 kutoka shilingi 7,500 mpaka shilingi 8,500 katika mwaka wa fedha 2015/16 ongezeko ambalo haliendani na kasi ya mfumuko wa bei uliorekodiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoka aslimia 4.2 Februari, 2015 mpaka kufikia asilimia 5.6 Februari, 2016:-
Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha hizo kufikia shilingi 10,000 kwa siku ili kuendana na kupanda kwa gharama za maisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya utafiti juu ya gharama halisi za maisha ya wanafunzi ambazo hujumuisha gharama za chakula na malazi. Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilifanya utafiti katika vyuo vyote nchini ili kujua gharama halisi ya chakula na malazi. Utafiti huo ulionesha kuwa gharama hizo zilikuwa kati ya shilingi 8,000 mpaka 8,500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka miwili, Wizara yangu itafanya utafiti mwingine, ili kubainisha gharama halisi za chakula na malazi. Matokeo ya utafiti huo yatatumika kupanga viwango vya fedha atakazolipwa mwanafunzi kwa kuzingatia gharama halisi pamoja na upatikanaji wa fedha.
MHE.PETER J. SERUKAMBA (K.n.y MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Mwaka 1993 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (Youth Development Fund – YDF) ili kutoa mikopo kwa vijana nchini. Mwaka 2013/2014 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 6.1 na mpaka mwezi Machi, 2014 jumla ya shilingi bilioni mbili zilitolewa na Serikali.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuwaeleza vijana nchi nzima kuwa ni vijana wangapi na wa maeneo gani ambao wamenufaika?
(b) Je, maisha ya vijana waliopewa fedha hizo yamebadilika kwa kiasi gani ili tuweze kupima haja ya mfumo huo na usimamizi wake?
(c) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuangalia upya mfumo uendeshaji wa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum na kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia utaratibu huu, vijana huwezeshwa kujitegemea, kupunguza umaskini wa kipato na kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vikundi vya vijana 309 kutoka Hamlashauri mbalimbali nchini vilifaidika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kupata mikopo yenye jumla ya shilingi 1,867,899,520 ambako mpaka sasa tayari SACCOS za vijana kutoka katika Halmashauri 94 zimepatiwa mkopo huu.
Vijana hawa pia hupatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa miradi, utunzaji wa fedha na utafutaji masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za mkopo zitokanazo na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa msingi mzuri katika kuandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kupitia fedha hizo, vikundi vingi vya vijana vimefanikiwa kukuza vipato vyao kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, usindikaji wa mazao na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo. Aidha, shughuli hizo zimefanya vijana waachane na utegemezi na badala yake kutumia muda wao mwingi katika uzalishaji na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vikundi vya mfano ambavyo kupitia mfuko huu vimekuwa kielelezo cha dhati katika kubadili mtazamo wa vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao. Vikundi hivyo ni pamoja na THYROID Group kutoka Halmashauri ya Chunya kinachosambaza taa za solar vijijini, MIRANACO Group kinachomiliki duka kubwa la dawa za binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, Maswa family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha uendeshaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini mbalimbali mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za kiutendaji zinazojitokeza. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali inapitia upya muongozo wa utoaji fedha kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana wa mwaka 2013 ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kuanzisha viwanda vidogo katika kuendana na sera ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
MHE. PETER J. SERUKAMBA (K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Shule za Sekondari za Umma zimeendelea kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne na sita, ambapo kwa mwaka 2015 katika matokeo ya kidato cha nne watahiniwa waliopata daraja la nne ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 na waliopata daraja la sifuri ni 113,489 sawa na asilimia 32.09:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi katika kuboresha mazingira ya kujifunzia katika Shule za Umma za Sekondari nchini ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya madarasa, mabweni na maabara?
(b) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta
kazi Bodi ya Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kutokana na kushindwa kusimamia ubora wa elimu nchini ambayo ni moja ya jukumu lake?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua zilizokuwa shule za vipaji maalum za Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha zilizowahi kufanya vizuri miaka ya 1990?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) Serikali imekamilisha uboreshaji wa Shule za Sekondari 792 kwa kukarabati miundombinu na kuweka samani; shule 264 ziliboreshwa katika awamu ya kwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 56; na shule 540 katika awamu ya pili kwa gharama ya shilingi bilioni 67.8 na zote zimekamilika. Ukamilishaji wa ujenzi wa shule hizo, umesaidia katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia katika Shule za Sekondari za Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ubora wa elimu linajumuisha mambo mengi ambayo yanahusisha kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia jambo ambalo linatekelezwa kupitia mipango na bajeti kila mwaka. Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inasimamia udhibiti wa ubora wa elimu ikishirikiana na taasisi nyingine zinazotekeleza Sera ya Elimu Tanzania. Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha elimu nchini, hatuoni sababu ya kuvunja Bodi hiyo, badala yake tutaendelea kuiwezesha kutekeleza majukumu yake vizuri zaidi kwa kushirikiana na taasisi nyingine.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea
na ukarabati wa shule kongwe zote 89 nchini zikiwemo Ilboru, Kilakala, Mzumbe na Kibaha. Mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali ilitoa shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe na shilingi bilioni 3.5 zilitolewa na kutumika kukarabati shule saba za ufundi za Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma, Bwiru Boys na Ifunda. Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) itakarabati shule kongwe 11 zikiwemo za vipaji maalum za Mzumbe, Ilboru, Kilakala, Tabora Boys, Tabora Girls, Pugu, Nganza, Mwenge, Same na Msalato.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
(i) Je, Serikali ina mkakati gani mahususi katika kuboresha mazingira ya kujifunza katika shule za umma za sekondari nchi nzima ikiwa ni pamoja na ukarabati wa majengo, madarasa, mabweni na maabara?
(ii) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta kazi Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kwa sababu imeshindwa kusimamia ubora wa elimu nchini?
(iii) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua shule zilizokuwa za watoto wenye vipaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), refu sana, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule za umma za sekondari nchini. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) ulianza kutekelezwa mwaka 2004 hadi mwezi Disemba 2016, jumla ya shule za sekondari 792 zimejengwa na kukarabatiwa miundombinu yake na kuwa shule kamili kwa gharama za shilingi bilioni 123.8.
Aidha, katika kipindi hicho jumla ya maabara 6,287 sawa na asilimia 60.52 ya lengo zimekamilika kati ya maabara 10,387 zilizohitajika. Kupitia Mpango wa Lipa kwa Matokeo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 21.9 zimeidhinishwa kwa ajili ya upanuzi wa shule 85 za sekondari na shule 19 za msingi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya vyumba vya madarasa 320, mabweni 155 yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila moja na matundu ya vyoo 829 yatajengwa.
(b) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Elimu Tanzania huchangia katika kukuza ubora wa elimu nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi chuo kikuu. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa fedha za kutosha kuwezesha kutekeleza miradi mingi zaidi kama inavyotarajiwa na wananchi katika maeneo mengi nchini.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzikarabati shule kongwe 89 zikiwemo shule nane za wanafunzi wenye vipaji maalum kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Mradi huu utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni 89 hadi kukamilika unatekelezwa kwa awamu. Hadi kufikia Julai, 2017 jumla ya shule kongwe 43 zimekarabatiwa na shule 20 zitakarabatiwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kupiga marufuku uingizwaji wa nyama kutoka nchi za nje ili kuruhusu ukuaji wa viwanda vya nyama nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika baada ya Ethiopia. Aidha kumekuwepo na uingizaji wa nyama ya ng’ombe, nguruwe na kondoo kwa wastani wa tani 2,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2013 hadi 2015. Hata hivyo kiasi hicho kimepungua kuanzia mwaka 2016 tani 1,182.79 na mwaka 2017/2018 tani 1,225 kutokana na kuwepo kwa machinjio na viwanda 23 vyenye uwezo wa kuzalisha tani 44,820.6 za nyama na bidhaa zake kwa mwaka zenye ubora linganifu na nyama inayotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2016/2017 jumla ya nyama tani 2,608.93 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 5,679,217.28 iliuzwa katika nchi za Oman, China, Hong Kong, Dubai na Vietnam. Vilevile idadi ya machinjio nchini kwa sasa ni 1,632 na yana uwezo wa kuchinja nyama kiasi cha tani 625,992 kwa mwaka.
Pia masoko ya nyama inayozalishwa ndani ya nchi yameongezeka ambapo inauzwa katika hoteli za kitalii, maduka maalum (super markets) na migodi yote nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inafanya tathmini ya kina kuhusu biashara ya mifugo na mazao yake ili kujua kwa uhakika kiasi cha nyama kinachoingizwa nchini, masoko na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha nyama na mazao yenye ubora na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha, kuchakata na kusindika nyama na bidhaa zake zenye viwango na ubora unaokubalika. Pia, imeweka mapendekezo ya kuongeza tozo ya uingizaji wa nyama na bidhaa zake ili kuleta ushindani wa haki katika soko la ndani utakaowezesha kukua kwa viwanda vya ndani, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa uingizaji wa nyama kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba wizara inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kuufanyia kazi na kwa kuzingatia matokeo ya tathmini tunayoendelea hivi sasa.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunikumbusha, naomba isomeke dola za kimarekani 5,679,217.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Charles Kitwanga alikaririwa na vyombo vya habari mwezi Desemba, 2015, akiliagiza Jeshi la Polisi kumkabidhi majina ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ambazo ongezeko lake nchini lina athari hasi dhidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa:-
(a) Je, ni hatua gani zimechukuliwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwafikisha Mahakamani wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wanaojiingiza kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya nchini?
(c) Je, ni vijana wangapi kwa nchi nzima ambao kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita wamepatiwa tiba kusaidiwa kuondokana na utegemezi wa dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kati ya Oktoba, 2015 hadi Aprili, 2017 Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 9,140 wa dawa za kulevya ambapo watuhumiwa 14,410 kesi zao zinaendelea Mahakamani na zipo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 2,401 walikutwa na hatia, watuhumiwa 615 waliachiwa huru na watuhumiwa wengine 13,071 kesi zao ziko chini ya upelelezi.
(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kupitia Programu ya kuzuia uhalifu limeendelea kutoa huduma ya urekebishaji kwa waaathirika wa dawa za kulevya. Kwa kutumia vikundi mbalimbali vya michezo chini ya miradi ya kuzuia uhalifu kama vile familia yangu haina mhalifu na klabu ya usalama wetu kwanza.
(c) Mheshimiwa Spika, vijana 3,000 walipatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Vijana wengi wanakosa sifa za kuajiriwa kwa kukosa uzoefu kazini.
Je, Serikali haioni haja ya kutungwa kwa Sera ya Mafunzo kwa Vitendo Kazini kwa wahitimu wa elimu ya juu na vyuo vya ufundi (Internship Policy for Higher Learning Institutions and Technical Colleges Graduates) ili vijana waweze kupata ujuzi utakaoendana na mahitaji ya soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha pengo la ujuzi (skills mismatch) kati ya ujuzi walinao wahitimu na ule unaohitajika katika soko la ajira unazibwa. Ni kweli Serikali imeona kuna haja ya kuwa na miongozo ya kisera kama alivyoshauri Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba ambapo kupitia ofisi yangu tumeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu (National Internship Guidelines). Mwongozo huu unasaidia wadau kuandaa, kutekeleza, kusimamia na kuratibu mafunzo ya uzoefu kazini kwa wahitimu. Mwongozo huu ulizinduliwa mwezi Septemba, 2017 na kuanza kutumika rasmi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 zaidi ya nafasi 750 zimetolea na waajiri mbalimbali kuwezesha wahitimu kufanya mafunzo kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, kufanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kuendana na mahitaji ya sasa. Sera mpya pamoja na mkakati wa utekelezaji wake ipo katika hatua za mwisho ambapo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2018. Miongoni mwa matamko mahsusi ya sera hii ni pamoja na kusisitiza kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu wa vyuo. Baada ya kupitishwa sera hii, suala la mafunzo ya vitendo kazini kwa wahitimu litawekwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa programu ya mafunzo kazini kwa wahitimu kwa kutoa fursa kwa vijana wahitimu kujifunza katika maeneo yao ya kazi.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, kuna utafiti wowote uliofanyika ili kubaini kama adhabu ya kuchapa wanafunzi inaongeza kiwango cha elimu na ufaulu katika shule zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi ya Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, zipo tafiti mbalimbali za kielimu kuhusiana na matumizi ya viboko kama njia ya kurekebisha tabia na mwenendo wa mwanafunzi katika kudhibiti nidhamu shuleni. Hata hivyo tafiti hizo zimegawanyika katika makundi makubwa matatu ambayo ambapo zipo zinazokubaliana zinazokataa na zenye msimamo wa kati juu ya matumizi ya adhabu juu ya matumizi ya adhabu ya viboko kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa na Hamza Bakari na Mpoto Tanzania mwaka 2018 unakubaliana na matumizi ya adhabu ya viboko kama njia ya kudumisha nidhamu na hatimaye kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika ujifunzaji.

Hata hivyo, tafiti zilizofanywa na Maria Jose Oganda na Kirrily Pells, 2015 (Ethiopia, India, Peru na Vietnam) na Josephine Invocavity, 2014 uliofanyika Tanzania zinasema adhabu ya viboko haina tija na husababisha madhara ya kisaikolojia na kimwili kwa wanafunzi. Aidha, tafiti zilizofanywa na Lomasontfo Dlamini na wenzake 2019 (Swaziland) na Yusuph Maulid Kambuga na wenzake, 2018 (Tanzania) zinasema adhabu ya viboko inaweza kutumika pamoja na njia nyingine ili kudhibiti nidhamu kwa wanafunzi kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni.

Mheshimiwa Spika, katika shule zetu adhabu ya viboko hutumika pale mwanafunzi anapofanya utovu wa nidhamu uliokithiri na hutolewa kwa utaratibu maalum. Kanuni ya 3(1) ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 Marejeo ya mwaka 2002, inasema kuwa adhabu ya viboko shuleni itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Aidha, Waraka wa Elimu Namba 24 wa mwaka 2002 unaelekeza kuwa adhabu ya viboko itatolewa na Mwalimu Mkuu au walioteuliwa kwa kuzingatia ukubwa wa kosa, jinsia, afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja. Hivyo Serikali itaendelea kusisitiza matumizi sahihi ya adhabu kwa wanafunzi ili kuleta tija katika ufundishaji na ujifunzaji.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Serikali ina mpango wa kufikia uzalishaji wa zaidi ya megawatts 5,000 za umeme ifikapo 2020.

Je, ni mkakati gani umewekwa ili kufikia lengo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athumani Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Tanzania inajenga uchumi wa viwanda, Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 imeweka mipango ya kuzalisha umeme wa kutosha na unaotabirika. Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeweka mpango wa kuzalisha umeme wa megawatts 5000 ifikapo mwaka 2020. Kufutia mpango huo, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme kutokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo maji, gesi asilia na jua. Miongoni mwa miradi ya kuzalisha umeme inayotekelezwa ni pamoja na upanuzi wa mradi wa kufua umeme kwa kutumia gesi asilia Kinyerezi I kutoka megawatts 150 za sasa na kufikia megawatts 335. Utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2019.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya kufua umeme kwa gesi asilia ni Kinyerezi II, megawatts 240 ambao utekelezaji wake umekamilika mwezi Aprili, 2018, badala ya 2019 inayosomeka hapo na mradi wa kuzalisha umeme wa Mtwara wa megawatts 300 unaotekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA). Mradi huu unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Machi, 2019.

Mheshimiwa Spika, mwezi Disemba, 2018, Serikali ilianza kutekeleza mradi za kuzalisha umeme wa kutumia nguvu ya maji (Stiegler’s Gorge) megawatts 2,115 pamoja na mradi wa Rusumo, megawatts 80. Miradi mingine itakayoanza kutekelezwa hivi karibuni ni mradi wa Ruhudji, megawatts 358, mradi wa Rumakali, megawatts 222 na mradi wa Kakono, megawatts 87. Miradi hii inatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia itatekeleza miradi ya kuzalisha umeme wa nguvu za jua megawatts 150 (Kishapu), upepo megawatts 100 (Singida) na miradi ya Makaa ya Mawe megawatts 600.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi hii itaongeza umeme katika gridi ya Taifa kutoka megawatts 1602 kutoka kwenye vyanzo vilivyotumika kuzalisha umeme kwa sasa na kufikia megawatts 10,000 ifikapo 2025.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wakuleta Bungeni marekebisho ya Sheria ili kupunguza kiwango cha ushahidi kwenye kesi za ubakaji na hasa ubakaji wa Watoto?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushahidi katika kesi za daawa ya jinai hususan kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 yanaadhibiwa kwa mujibu wa Kifungu cha 130(1) na 13(2)(e) cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 20. Makosa haya kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi yanahitaji kuthibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote ili mtuhumiwa atiwe hatiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kiwango cha kuthibitisha mashauri ya jinai pasipo kuacha shaka yoyote, kiwango cha ushahidi kitategemea mazingira ya kosa husika na namna yalivyotendeka na mashahidi walioshuhudia kutokea kwa tukio hilo. Sheria haijatoa masharti ya idadi ya mashahidi wanaotakiwa kutoa ushahidi. Hivyo, kila kesi huangaliwa kwa kuzingatia mazingira yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo na kwa lengo la kumlinda mtoto aliyeathirika na tukio la ubakaji, mwaka 2016 Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho katika Kifungu cha 127 cha Sheria ya Ushahidi kwa kuondoa masharti ya kumhoji mtoto ili kupima ufahamu wake na badala yake kuweka masharti ya Mahakama kujiridhisha kuwa mtoto ana uwezo wa kusema ukweli pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inaendelea na itaendelea kufanya maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai ili kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha usikilizwaji, siyo tu wa mashauri ya namna hii, bali mashauri yote yanayohusu makundi ya watu katika jamii yetu ili kulinda utu wao ikiwemo watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wanaoathirika na vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji. Ahsante.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, ni kwa kiasi gani Serikali imeweka mikakati ya kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania kijiografia ipo katika ukanda wenye mvua za kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI, alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kimojawapo katika kuongeza uhakika wa upatikanaji wa maji kwa wananchi ni maji ya mvua. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilizielekeza Mamlaka za Serikali za Mtaa kutunga sheria ndogo ndogo ili kuhamasisha na kushauri kuwa nyumba zote zinazojengwa ziwekewe miundombinu kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uhaba wa maji bado ni changamoto katika nchi yetu, Serikali inaendelea kuhimiza na kuhamasisha jamii kwa kutoa elimu ya utaratibu wa uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa, malambo na uvunaji wa maji ya paa. Katika utekelezaji wa Programu ya kuendeleza Sekta ya Maji nchini, uhamasishaji umefanyika kwa kujenga matenki ya mfano ya kuvuna maji ya mvua katika maeneo ya shule na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji imeandaa Mwongozo wa Uvunaji wa Maji ya Mvua ambao utasambazwa na kutumika nchi nzima. Mwongozo huo umeainisha mbinu mbalimbali za kuvuna maji ya mvua katika Kaya na Taasisi. Mwongozo utatumika katika kupanga, kusanifu, kujenga na uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND (K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-

(a) Je, Serikali ipo tayari kuwaeleza Watanzania hususani vijana kuwa hatua gani zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwahukumu wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana waliotumbukia kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Naibu Spika, tokea Awamu ya Tano iingie madarakani imewabaini na kuwakamata watuhumiwa kama ambavyo inaorodheshwa hapa chini. Watumiaji wa dawa za kulevya za viwandani mwaka 2016 idadi ya makosa ni 679 na watuhumiwa waliokamatwa ni 1,269 ambao kati ya hao wanaume ni 1,127 na wanawake 142; mwaka 2017 idadi ya makosa ni 902 ambapo watuhumiwa 1,578 walikamatwa kati ya hao 1,485 ni wanaume na 93 ni wanawake; mwaka 2018 makosa yalikuwa ni 702 ambapo watuhumiwa 886 walikamatwa kati ya hao 796 ni wanaume na wanawake walikuwa 90 na mwezi Januari, 2019 hadi Machi, 2019 jumla ya makosa yalikuwa ni 133, watuhumiwa waliokamatwa ni 174 kati ya hao 162 ni wanaume na 12 ni wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, madawa ya mashambani kwa maana ya mirungi na bangi; mwaka 2016 jumla ya makosa ya madawa ya mashambani ni 10,375 ambapo watuhumiwa walikuwa ni 26,031, kati ya hao wanaume 23,872 na watuhumiwa wanawake walikuwa 2,159; mwaka 2017 makosa ya madawa ya kulevya yalikuwa ni 8,956 na watuhumiwa walikuwa 12,529 wakati wanaume walikuwa 12,529 na wanawake walikuwa ni 1,112; mwaka 2018 makosa yalikuwa ni 7,539 watuhumiwa walikuwa 9,987 ambapo wanaume walikuwa ni 8,935 na wanawake walikuwa ni 1,052 na Januari, 2019 hadi Machi, 2019 makosa yalikuwa 1,842 ambapo wanaume walikuwa 2,340 na wanawake walikuwa 202.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi watuhumiwa wamepelekwa mahakamani na wengine upelelezi wa kesi zao na mashauri yao unaendelea na uko kwenye hatua tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi kupitia programu ya kuzuia uhalifu limeendelea kutoa huduma ya urekebishaji kwa waathirika wa dawa za kulevya kwa kutumia vikundi mbalimbali kama vile vya michezo nchini chini ya miradi ya kuzuia uhalifu kama vile familia yangu haina uhalifu na klabu ya usalama kwetu wetu kwanza.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanyia maboresho Mfumo wa Elimu Tanzania?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la uboreshaji wa utoaji wa elimu katika nchi yoyote ni endelevu, ambalo hutegemea mabadiliko yanayotokea katika nchi kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii, pamoja na ulinganisho wa maendeleo ya sayansi na teknolojia. Katika nchi yetu, suala hili la uboreshaji wa mifumo ya elimu limekuwa likifanyika na hutegemea tathmini mbalimbali za kitaalamu zinazofanyika kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Spika, mfano elimu ya sekondari ya chini (O level) kutambuliwa kuwa ni sehemu ya Elimumsingi kwa watoto wetu na inatolewa bila malipo ya ada. Aidha, katika elimu ya ualimu tumeongeza miaka ya kumwandaa mwalimu wa elimu ya awali kutoka miaka miwili kuwa miaka mitatu. Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeendelea na uimarishaji wa elimu yetu kuwa ya umahiri (competence based) kutoka katika mfumo wa awali ambao ulimwandaa mhitimu kwa nadharia bila mafunzo kwa vitendo ya kutosha. Uboreshaji huu umefanyika sambamba na uimarishaji wa mitaala katika ngazi zote.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi, Serikali imeunda Mabaraza ya Ujuzi ya Kisekta ambayo yanakuwa kiungo kati ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na wadau, vikiwemo viwanda na waajiri. Mabaraza hayo yatahakikisha kuwa mitaala inayotumika inakidhi mahitaji ya wadau na soko la ajira. Katika ngazi ya elimu ya juu, Serikali imeendelea kuhuisha na kuanzisha programu mbalimbali zinazotolewa ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali, imeanzisha vituo atamizi katika taasisi za elimu ili kuhakisha wahitimu wanapata fursa za kulea mawazo na ubunifu wao. Maboresho haya yanalenga kuimarisha umahiri wa wahitimu wetu ili waweze kuajirika na pia kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa Mfumo wa Elimu unakidhi mahitaji ya soko Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha baadhi ya Sheria kandamizi kwa Wanawake ili ziendane na wakati?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu nasimama mbele ya Bunge lako kwa mara ya kwanza. Pia niwashukuru wananchi wa Kavuu kwa kunidhinisha kuwa Mbunge wao. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona nafaa kuwakilisha Wizara hii ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Mkoa wa Kigoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kabla ya kujibu swali la msingi, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali haina sheria kandamizi. Sheria zote zinazotumika nchini zilitungwa na Bunge lako Tukufu ambalo halijawahi kutunga sheria kandamizi. Aidha, Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na watu wake, imekuwa ikiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuziboresha sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wakati tulionao na mahitaji ya sasa, Serikali imeanzisha mchakato wa kuzipitia baadhi ya sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kuendana na wakati. Hivi sasa, Serikali kupitia Wizara imeandaa Muswada wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Ndoa utakaowasilishwa katika Bunge lako Tukufu ili kuiboresha, kwa lengo la kulinda makundi ya wanufaika na sheria hii. Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi na Sheria za Kimila. Hatua hizo zikikamilika, Muswada wa Mapendekezo ya kuzirekebisha sheria hizo utawasilishwa kwenye Bunge lako Tukufu ili Wabunge wapate nafasi nzuri ya kujadiliana na kuyapitisha marekebisho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ipo katika mabadiliko makubwa ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya sheria zetu ikiwemo kuzitafsiri kwa Kiswahili lakini pia kuweka vipengele kwenye sheria hizo vya kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili jambo ambalo litaleta tija kubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Tunawaomba Wabunge kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hili kwa lengo la kuimarisha utawala wa sheria na upatikanaji wa haki nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-

Kijiographia Tanzania ipo kwenye ukanda wenye mvua za kutosha:-

Je, Serikali imejizatiti vipi kuhamasisha zoezi la uvunaji wa maji ya mvua kwa matumizi ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Nchi yetu ipo kwenye ukanda wa mvua za kutosha, hivyo ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ni muhimu kwa kuwa itawezesha kuwa na maji ya uhakika kwa kipindi chote cha mwaka bila kujali hali ya hewa. Vilevile, miundombinu hiyo ni muhimu kwa kuwa itawezesha kudhibiti mafuriko na pia kuokoa miundombinu, ikiwemo ya kuhudumia maji pamoja na mali na maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza azma hiyo mkakati mwingine ni Wizara ya Maji kukutana na TAMISEMI kwa lengo la kuhusisha mashule, kujenga gats za maji na matenki, pia kuhamasisha wananchi wanapojenga nyumba zao waweke miundombinu rafiki ya kukusanya maji, lengo zoezi liwe shirikishi. Aidha, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa ukarabati wa mabwawa kwa kila wilaya, hususan katika wilaya kame.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 Wizara imekamilisha ukarabati wa mabwawa ya Mwadila lililoko Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu, usanifu kwa ajili ya kukarabati mabwawa matatu ya Itobo lililoko Wilaya ya Nzega, Ingekument lililoko Wilaya ya Monduli na Horohoro lililoko Wilaya ya Mkinga na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili ya Muko na Chiwanda yaliyoko Wilaya ya Momba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, usanifu wa Malambo ya kunyweshea mifugo sita, umekamilika katika mwambao wa barabara kuu ya Dodoma Babati, ikihusisha Wilaya ya Bahi malambo mawili na Chemba malambo manne. Vile vile, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga mabwawa ya kimkakati ya Kidunda Mto Ruvu, Falkwa katika Mto Bubu na Ndembela Lugoda katika Mto Ndembela.
MHE. SALMA R. KIKWETE K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa Bungeni ili kurekebisha Vifungu vya Sheria vinavyohusu Mtoto wa Kike kuolewa akiwa na umri chini ya miaka 18?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali wa yote, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi za ufuatiliaji kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kutaka kujua ni lini Muswada huu utawasilishwa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa Muswada wa Sheria ya Ndoa ulifikishwa kwenye Kamati ya Katiba na Sheria mwezi Februari, 2021 kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani katika Kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi Rebecca Gyumi, Rufaa Na. 204 ya 2017 na Na.5 ya 2016 ya Mahakama Kuu iliyotaka Sheria ya Ndoa ifanyiwe marekebisho ili mtoto wa kike aolewe akiwa na miaka 18. Kamati baada ya mapitio iliona upo uhitaji wa ushirikishwaji wa wadau wengi zaidi ili kupata maoni zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kushirikisha wadau ambapo hadi sasa Serikali imeweza kufanya mikutano na Viongozi wa Dini katika Mkoa wa Dar es Salaam mwezi Machi, 2021.

Mheshimiwa NaibU Spika, mMkutano wa pili ulifanyika Jijini Dodoma tarehe 2 Julai, 2021 uliojumuisha Wabunge wa Mkoa wa Dodoma na Viongozi wa Halmashauri ya Mkoa wa Dodoma. Kurejeshwa kwa Muswada huu Serikalini kulitokana na unyeti wa jambo lenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali itakapokamilisha michakato iliyoelekezwa na Kamati ya Bunge lako Tukufu, Muswada huu utawasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kisha kuwasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya Kutunga Sheria husika. Ahsante.