Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mussa Azzan Zungu (16 total)

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nataka kujua tu, Serikali inipe majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuzuia branding za Tanzanite externally, nayo yana sovereign ownership ya Tanzania na kuthibiti mapato ya Serikali; kulikuwa na Mkataba ambao ulisainiwa Afrika Kusini mwaka 2003 unaitwa Kimberley Process. Certification ya madini haya ilikuwa pamoja na Diamonds, kipindi kile kulikuwa na conflict diamonds, lakini waka-incorporate na madini ambayo yana thamani kama Tanzanite.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, je, Tanzania tumo katika mkakati huo wa certification ya Tanzanite ili kudhibiti sovereign ya mali hii ibaki nchini na itambulike kuwa ni mali ya Tanzania tu? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Kimberley Code yenyewe ilikuwa controversial. Kuna wengine waliikubali, wengine wameikataa, ikaanzishwa nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jibu la kifupi ni ndiyo tunataka Tanzanite. Hata Ofisi yetu ya London, wale wafanyakazi wa kwetu kule waliokuwa wanasimamia uuzaji wa diamonds, wakiwa wana Ofisi London, tuliifunga, tunataka haya madini yauzwe nchini hapa. Jibu ni ndiyo!
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na rubani kuwa mmoja na risk za ndege hizi zimewekwa kwa mazingira kwa Rubani mmoja anaweza kurusha hizi ndege kwa kitalaam, lakini liko tatizo la baadhi ya viwanja vyetu kutokuwa na mitambo ya Precision Approach Path Indicator, kutokuwa na mitambo ya Visual Approach Slope Indicator na hizi ni kwa Rubani licha ya kuwa anayo mitambo ya Eye Rescue ya ndege yake, lakini anahitaji Visual Support.
Je, Serikali sasa itafanya nini kuhakikisha System hizi za taa, visually kumsaidia Rubani kuweza kutua, kuokoa maisha ya watu na kumuokoa yeye mwenyewe?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya viwanja vyetu vina matatizo ya vifaa, lakini Serikali tumejipanga kuhakikisha viwanja vyetu vyote ambavyo vinatumika kwa sasa hivi viwe na vifaa vya kisasa kuhakikisha kwamba kuna usalama wa kutosha kwa ajili ya abiria wetu wanaosafiri katika viwanja hivyo vya ndege.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa spirit hiyo hiyo ambayo Serikali imeiona ya kuweka mahusiano na Israel kwenye masuala ya kiuchumi, Morocco nayo vilevile iko tayari kutaka kuisaidia Tanzania kwenye masuala ya diplomasia ya uchumi. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kushirikiana na Serikali ya Morocco; najua Ubalozi upo, lakini bado Ubalozi huu haujakomaa vizuri wakati wenzetu pale Morocco wako tayari kuisaidia nchi yetu kwenye masuala ya kiuchumi wakiwa na uwezo mkubwa sana kwenye masuala ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe kwamba Ubalozi wa Morocco upo na sijaelewa jinsi alivyoliweka kwamba haufanyi kazi vizuri, lakini labda pengine angetoa ufafanuzi zaidi. Lakini kwa vile nipo nitaonana nae anieleze kwamba, alikuwa na maana gani. Lakini kama kuna tatizo, sisi kama Wizara, tutalishughulikia na sisi tunajua kabisa kwamba tunafanya kazi vizuri na Morocco na kazi inasonga mbele.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru.
Katika Awamu ya Nne, Serikali ya Ujerumani ilileta maombi nchini mwetu kutaka kufanya ukarabati meli ya MV Liemba ambayo ipo toka Vita Kuu ya Kwanza kama sentiment value ya Serikali ile walitoa offer ya kuitengeneza na kui-refurbish na kuifanya i-comply na sea worthiness kwa asilimia mia moja lakini hawakupewa jibu sahihi.
Je, Serikali mko tayari kukaa nao tena ili sasa offer ile iweze kufanywa na meli ile iweze kutengenezwa na ili iweze kutoa huduma kwa uhakika kwa wananchi wa Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na mpango na sasa hivi mpango huo upo, mimi mwenyewe kama mwezi mmoja uliopita nilikuwa na mazungumzo ya kina na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, mpango huo upo na tunaendelea nao ili MV Liemba ambayo imedumu kwa muda mrefu iweze kufanya kazi kama inavyopaswa.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru. Pamoja na mikataba ya bodaboda na bajaji, mikataba ni fursa za hawa vijana kufanya kazi katika miji. Sera ya MKURABITA ni mkakati wa kurasimisha biashara za wanyonge ziwe rasmi. Bodaboda na bajaji hizi baada ya mikataba hii wanapata tabu sana kufanya biashara katika miji na hasa kwenye barabara kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua na kuwajali wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini Mamlaka za Halmashauri bado zinazuia vijana hawa wasifanye biashara kwa uhakika na kuwatia hasara sana. Yako malalamiko, madalali wanaokamata bajaji na bodaboda wanaruhusu bodaboda zao tu ziingie mjini.
Je, Serikali sasa kwa kutambua sera MKURABITA wanaonaje sasa hili jambo liruhusiwe na hawa vijana wapate uhalali wa kufanya biashara katika miji yetu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo yanatofautiana, ni case by case Mikoa kwa Mikoa na Wilaya kwa Wilaya, lakini Mheshimiwa Zungu ame-raise jambo la msingi sana. Naomba Ofisi yangu ilichukue jambo hili kwa ajili ya kuliwekea utaratibu mzuri tuangalie jambo gani lifanyike katika eneo gani ili mradi tufikie muafaka kwa ajili ya vijana wetu. (Makofi)
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa namna inavyofanya maendeleo nchini, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa namna yeye na timu yake wanavyohangaikia maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Waziri akisema juu ya barabara za lami na mabomba kuanzia Buguruni kwenda Vingunguti, sikumsikia akisema kwenye eneo ambalo kodi ndiko zinakokusanywa, kuanzia Buguruni kurudi mjini. Je, maeneo haya ya Buguruni kurudi mjini barabara za lami na maji vipi Mheshimiwa Waziri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli jambo la maji na barabara ni mtambuka lote kwa pamoja nafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Zungu kwanza kuhusu suala la hiyo mitandao ya barabara na maji tumetoa maelekezo, lakini hata hivyo tukija katika upande wa barabara, Mheshimiwa Zungu ofisi yetu itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba Jimbo lile la Ilala kupitia Mradi wa DMDP jimbo lako litaweza kuwa linang’ara zaidi kwa sababu hili ni jukumu la ofisi yetu, na kwa vile unapigana sana kwa wananchi wako, jambo hili tunalibeba na tunalisimamia kwa nguvu zote kwa kipindi hiki.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge wa Segerea, Mheshimiwa Bonnah Kaluwa kwa kazi nzuri za miundombinu anazofanya kwenye jimbo lake. Hivi karibuni alikuwa na ziara na Waziri wa Ujenzi kutazama miundombinu kwenye jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Segerea na Mkoa wa Dar es Salaam, naomba kujua ni lini sasa Serikali itaweka mkazo kwenye barabara za Jimbo la Ilala ambalo ndilo linabeba magari yote kutoka maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri, TAMISEMI kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Zungu kwa kufuatilia kwa pamoja na maeneo mengine. Kama alivyosema nimekuwa na ziara Segerea Jumamosi, nimezitembelea barabara ambazo pia ziko chini ya TARURA ili kuweza kuona changamoto zilizopo ili kwa upande wa Serikali tuweze kuona namna sahihi ya kuweza kuzitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwa maana ya kupunguza msongongamano katika Jiji la Dar es Salaam hususani Ilala, kama tulivyopitisha bajeti tunaendelea na ule mkakati wa kupunguza msongamano. Tutakuwa na BRT III na IV lakini pia ipo mbioni BRT V na VI ili hatimaye msongamano katika Jiji la Dar es Salaam uweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira na wakati mwingine tunaweza kupeana mrejesho ili aone namna tulivyojipanga. Kwa kweli BRT I na II imefanya vizuri na imekuwa na rekodi nzuri kitaifa na watu na mashirika mengi yapo tayari kuja ku-support tutakwenda mpaka BRT V na VI.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka kuwaambia tu Waheshimiwa Wabunge kuwa humu ndani kaingia mnyama mkali sana, lakini tuko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali jana ilitoa kauli kuwa ili Tanzania ifanikiwe katika michezo ni lazima wachezaji wa timu ya youth watoke kwenye shule. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Walimu kwenye shule, ili tuwe na oriented result youth team ya Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala na naungana naye kwenye furaha yake ambayo naijua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Zungu kwamba shule yetu au chuo chetu cha michezo pale Malya - Mwanza Serikali inakiboresha; na tutapeleka Walimu kwa awamu ili wakafundishwe, ukiacha wale ambao wanasoma kutoka mashuleni, tunataka tupeleke Walimu ambao watafundishwa masomo ya michezo kwa muda ili waje kuboresha michezo kwenye shule zao wanazofundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tuna Walimu ambao wana uzoefu wa michezo, wengi tu ambao wanafundisha na Walimu wa michezo wako wachache. Nataka nitoe rai kwa Maafisa Elimu wote nchi nzima, kwamba Walimu wetu ambao wanafundisha michezo, wale ambao hawana cheti cha michezo basi wawape kipaumbele kuwapeleka kwenye chuo chetu cha michezo ili hatimaye tupate timu nzuri kwanza ya UMITASHUMTA na timu nzuri ya UMISETA ambayo itakuwa inapambana vizuri na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumeona mwaka huu zimepambana timu zetu za vijana na kushinda huko nje, inawezekana kabisa tukapata Timu ya Taifa bora kabisa kutoka kwenye shule zetu na vyuo vyetu baada ya muda mfupi ujao.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara za Jimbo la Ilala zote za Mjini ni mbaya, na tukamuita Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo akaja akashuhudia, wakaitwa watu wa TARURA wote wakashuhudia, lakini mpaka leo barabara za Kalenga, Mindu, Mchikichi, Pemba, Aggrey, Likoma, Bonde, Mali, Utete, Morogoro, Kikuyu, Mafuriko, pamoja na barabara ya Pemba; barabara hizi zote; na barabara zote hizi ndiyo sehemu ya uchumi wa Dar es Salaam na huchangia asilimia 70 ya mapato ya Taifa katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali ione umuhimu wa kuboresha kiundombinu hii ili wananchi waendelee kulipa kodi vizuri.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nawe ni shuhuda jinsi ambavyo Mheshimiwa Zungu anazifahamu barabara, amezitaja nyingi kweli kweli. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Zungu ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara ndani ya Jiji la Dar es Salaam zinajengwa na kuboreshwa kwa kiwango kikubwa. Ndiyo maana kwa kupitia mradi wa DMDP imetengwa jumla ya shilingi bilioni 660 na zitajengwa kilomita 210.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa barabara ambazo Mheshimiwa Zungu amezitaja zitakuwa ni miongoni mwa barabara ambazo zitajengwa. Tuko kwenye hatua nzuri, baada ya muda si mrefu tutakuwa tumeshaweka Mkandarasi kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hizo.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Michezo ni pamoja na viwanja. Naipongeza sana Serikali kwamba tuna uwanja mzuri sana, Uwanja wa Taifa, lakini uwanja ule kwenye eneo la VIP na juzi wananchi wote na Mheshimiwa Rais walikwenda pale kushuhudia mechi ya Simba na mechi ya Kagera. Eneo lile halina kibanda au kinga ya jua au mvua wakati hali ya hewa inabadilika.
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kuwa eneo lile sasa linawekewa kibanda maalum kuzuia mvua kwa watazamaji wa kawaida na viongozi wa Kitaifa watakapokwenda kutazama mpira?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kuna upungufu katika Uwanja wetu wa Taifa na ndiyo maana tulipokuja mbele ya Bunge lako tukufu kuomba tutengewe pesa kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Taifa, hiyo ni moja ya upungufu ambao utatatuliwa kwa pesa ambayo tumeiomba na ambayo inakidhi viwango vya CAF na FIFA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata walipokuja juzi, tulipowaeleza kwamba matarajio yetu ni kutumia hiyo shilingi bilioni moja kwa ajili ya marekebisho ya aina hiyo katika Uwanja wa Taifa, walitukubalia. Kwa hiyo, mabadiliko kama hayo tuyategemee katika Uwanja wa Taifa katika muda sio mrefu kutoka sasa.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na mahitaji makubwa ya barabara nchini, bado gharama za ujenzi wa barabara Tanzania ni kubwa mno ukilinganisha na mataifa mengine. Utakuta hata mjini barabara moja ina-cost mpaka shilingi bilioni 1.4, hakuna madaraja hakuna ma-culvert. Ni lini sasa Serikali ita-revisit gharama zake za ujenzi wa barabara ili iweze ku-save pesa na zitumike kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa barabara unaonekana gharama ni kubwa. Sisi kama Serikali tunachukua hatua kufanya mapitio ili kuona kwa kiasi kikubwa tunapunguza hizi gharama.
Mheshimiwa Spika, gharama kubwa zinaweza kusababishwa na interest, bei ya vifaa, teknolojia na usimamizi. Kwa upande wa Serikali tumejipanga ili kuhakikisha kwamba kwanza taasisi zetu ambazo zitakuwa zinasimamia ubora na gharama, kwa mfano tunafanya mapitio ili tuone Baraza la Ujenzi (NCC) tunalifanyia mabadiliko makubwa ili sasa lije na utaratibu wa kutazama hizi gharama za miradi ili uwiano wa ujenzi wa barabara uwe mzuri. Kwa sababu pia Serikali sasa inalipa kwa haraka wakandarasi hili eneo la interest litapungua lakini pia kwa sababu teknolojia inabadilika, sasa hivi tumekuja na teknolojia mpya na wataalam wetu katika Wizara tunaendelea kuwapeleka kujifunza teknolojia hii, teknolojia hii pia itakuwa muarobaini.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa ujumla wake kwamba sisi kama Serikali tunaona kuna variance kubwa kati ya barabara na barabara pia kati ya maeneo na maeneo lakini pia ule utaratibu wa manunuzi tunaendelea kuutazama ili mwisho wa safari tuje na muarobaini wa kupunguza gharama za barabara. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tumeona kwamba iko haja ya kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara nchini unakuwa na gharama ya chini lakini itatupa fursa ya kuweza kutengeneza barabara nyingi zaidi kama control ya cost itakuwepo. (Makofi)
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Zao la mawese ambalo ndiyo mchikichi linazalisha vilevile petroli na mafuta ya kula. Nchi ya Malaysia ambayo imechukua mbegu hii Tanzania ina mafanikio makubwa sana ya zao hili. Je, Serikali namna ilivyofanya sasa kupeleka zao la korosho kila mkoa, kwa nini kusiwe na affirmative action ya kupanda michikichi siyo chini ya milioni 30 ili Serikali i-benefit na zao hili ambalo ni zuri kwa uchumi wa nchi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zungu, Mbunge wa Ilala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu tu kwamba sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha zao hili la mchikichi ambalo linatoa mafuta ya mawese linafanikiwa kwa kasi. Kama Wizara ya Kilimo tuna programu yetu ya Supporting Indian Trade and Investment in Africa (SITA), kuhakikisha kabisa zao hili la mchikichi nalo linatiliwa mkazo na liweze kufanya vizuri. Ahsante.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa swali. Kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada zake za mikakati ya ajira kwa vijana na Sera ya Vijana.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo liko eneo ambalo Serikali kama wakitilia mkazo na kulifuatilia; sehemu ya hand- looming. Huu ni mtambo mdogo sana ambao unatumika hasa na nchi ya India ku-create ajira kwa vijana na wananchi wa kawaida kwa kufanya biashara ndani ya vyumba vyao. Haihitaji umeme wala teknolojia yoyote zaidi ya kuwa na chumba na mtu mmoja unapata nyuzi wanatengeneza gray cloths na vile vitambaa wanauzia viwanda vya kutengeneza nguo; na matokeo yake wanapata kati ya laki moja na nusu mpaka laki mbili kwa siku. Je Serikali ina mkakati gani wa kutazama eneo hili la ku-create ajira badala ya kuacha vijana wengi ambao sasa hivi hiyo nguvu kazi zinapotea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri mzuri wa Mheshimiwa Mbunge wa lengo la kuongeza ajira hasa kwa vijana. Kwa kuongezea tu na sisi kama Serikali tuliona pia tuna jukumu la kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana wengi. Ndiyo maana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu hivi sasa tunaendesha programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imeanza mwaka 2016 mpaka 2021 lenye lengo la kuwafikia takribani vijana milioni 4.4 nchi nzima ili vijana kupitia ujuzi mbalimbali waweze kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Spika,kwa hiyo fursa aliyosema Mheshimiwa Mbunge tunaichukua na tutaiboresha ili vijana wengi zaidi waweze kupata ajira.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tunachimba visima kwenye maeneo yetu. Kisima cha mita 100 kina-cost takribani shilingi milioni saba, lakini ukienda Halmashauri kisima cha mita 100, gharama zinazolipwa ni zaidi ya shilingi milioni 35 kwa kisima kimoja. Visima hivi 23 ambavyo vinataka kuchimbwa Tarime vitagharimu siyo chini ya shilingi milioni 900 kwa bei za Wakandarasi na bei za hao wanaokwenda huko kwenye Halmashauri zao.

Je, Serikali sasa lini ita-revisit bei hizi na kutoa bei elekezi kuhakikisha pesa za Serikali zinaokolewa na ubadhirifu ili wananchi wapate maji kwa bei nafuu ambapo yanaweza kupatikana kwa shilingi milioni saba tu kwa kisima cha mita 100?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Zungu kwa swali lake zuri sana lakini kubwa tukiri kwamba kulikuwa kuna ubadhirifu mkubwa sana hasa katika miradi ya maji. Sisi tumeona hilo na ndiyo maana tukaanzisha Wakala wa Maji Vijijini na tuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kutupitishai Muswada wetu na sisi tumejipanga katika kuhakikisha tunasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na gharama nafuu, sisi tunataka tuuongezee uwezo kwa Wakala wa Maji wa Uchimbaji Visima (DDCA) katika kuhakikisha tunawapa vifaa vya kutosha ili uchimbaji wake uwe nafuu uweze kuendana na watu binafsi. Ahsante sana.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naipongeza Serikali kwa mradi wake wa kuleta mpango wa DNDP kwenye Mkoa wa Dar es Salaam. Jimbo la Ilala tumepata Kilometa mbili tofauti na maeneo mengine wamepata zaidi ya Kilometa 40.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha barabara za kata zote 10 za Jimbo la Ilala ili ziweze kuonekana za kupitika kwa sababu ni katikati ya mji na zinasaidia kupunguza msongamano katikati ya mji kuelekea pembezoni mwa mji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M.WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna miradi inaendeshwa katika Mji wa Dar es Salaam, UNDP na sasa kilichobaki, baada ya kutengeneza barabara nzuri zaidi, ni vingumu zaidi barabara za pembezoni zikawa nzuri. Sasa kwa sababu Mheshimiwa Mbunge tupo wote Ilala na tunampongeza Meneja wa TARURA kwamba ni msikivu sana, tutawasiliana naye tuone mipango iliyopo na sisi tuishi kama Wabunge wa Dar es Salaam ili kuwezesha mipango ya kukamilisha barabara zetu na hasa wakati wa mafuriko watu wa Dar es Salaam wasiweze kupata shida zaidi.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Athari ya moshi ni sawa na athari ya umeme unaopita juu ya nyumba za wananchi. Kuna mradi Mchikichini, Mtaa wa Ilala Kota eneo la Baghdad ambapo TANESCO walikubaliana na wananchi kupitisha umeme mkubwa sana juu ya nyumba zao lakini kwa kigezo cha kuwalipa fidia. Umeme umepita, umeme ulikuwa usiwashwe mpaka fidia ilipwe, lakini umeme umewashwa na fidia haijalipwa, watu wako chini ya umeme mkubwa na wanaathirika kiafya.

Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kujua ni lini sasa Serikali au TANESCO itawalipa fidia wananchi hawa wa Mchikichini ambao wako hapo kwa zaidi ya miaka 50, huduma zote wanapata pale. Kuna kigezo kililetwa kuwa eneo lile ni hatarishi. Wananchi hawa wamekaa hapa miaka 50 wana huduma za maji, umeme na wanalipa bili zote na kikubwa kabisa inapokuja uchaguzi maboksi ya kura yanapelekwa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na TANESCO wawafikirie wananchi hawa ambao ni masikini, wawalipe fidia waondoke ili waondokane na athari ya kuathirika na umeme huu mkubwa katika nyumba zao. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zungu kwa kuulizia na kufuatilia masuala ya fidia kwa wananchi Mchikichini. Ni kweli kabisa wananchi wa Mchikichini walipitiwa na umeme mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala miaka sita ama saba iliyopita. Ni kweli katika eneo hilo bahati nzuri sana eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Dar es Salaam lakini ni kweli wananchi hao wanatambulika na kwamba walikuwa wakidai fidia.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunafanya majadiliano ya kina sana na Manispaa ya Ilala ili kuhakikisha kwamba wananchi ambao wanadai fidia ni wale ambao kweli waliathirika na fidia. Pili kwa sababu eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa, tunafanya mazungumzo ili wananchi hao waendelee kupata haki yao kulingana na wanavyostahili.

Mheshimiwa Spika, la pili, nampongeza Mheshimiwa Zungu, wiki mbili zilizopita tumekaa na Mheshimiwa Zungu kupitia kwa Kamishna wetu wa Nishati na tumefanyia kazi kwa kina suala hili. Wananchi hao tunawasihi wawe watulivu wakati suala hili linafuatiliwa kati ya Wizara na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili waweze kupatiwa haki yao ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana. (Makofi)