Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Mussa Azzan Zungu (6 total)

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushuru japo swali hili lilikosewa na kwa sababu hakukuwa na muda wa kufanya marekebisho na bahati nzuri Mheshimiwa Kandege anajua mazingira ya pale vizuri. swali langu Mheshimiwa lilihusu Zahanati ya Nyamwaga ambayo Halmashauri ya Wilaya imejenga majengo kumi wodi theatre, mochwari na tukaiomba iwe-upgraded kuwa Hospitali ya kwanza sasa ya halmashauri kwa sababu ina mazingira yote yanayoruhusu. Wewe tulikwenda pale na Waziri Mkuu unapajua, tumepeleka vifaa vya milioni mia tatu, swali langu linauliza ni lini, Zahanati ya Nyamwaga ambayo inazidi hata Hospitali ya Wilaya itafanywa kuwa Hospitali ihudumie wananchi kama hospitali na ipolekewe Wataalamu kwa sababu vifaa vipo? Ndio swali hilo na wewe unapafahamu vizuri pale.
MWENYEKITI: Lakini silo uliloliuliza, wewe umeuliza swali lingine, na Serikali imekujibu swali lako, sasa wewe umekuja na swali jipya, sasa nakubaliana na wewe, maswali ya Afya ni muhimu jimboni mwako na nakushukuru umelitolea, Mheshimiwa Waziri baadaye kaa na Mheshimiwa Mbunge mueleze majibu namna gani mnaweza ku-coucas na kujibu, hongera kwa swali zuri.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anatoa majibu yake ametaja kama mamlaka nne hususan kwenye suala la mchanga. Ametaja Wizara ya Mazingira ambayo kuna NEMC, ametaja Wizara ya Nishati na Madini, ametaja halmashauri lakini vilevile kuna kitu kingine kinaitwa Bonde ama Pwani Ruvu Bonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya usimamizi wa mito yetu ni kutokana na ukweli kwamba si NEMC, si halmashauri, si Wizara ya Nishati na Madini ina mamlaka ya moja kwa moja ya ku-deal na masuala ya mchanga. Ni Pwani Ruvu Bonde ambayo ofisi zake ziko Morogoro ndiyo inaingia mikataba na watu wa kuchimba mchanga kwenye halmashauri zetu. Wananchi wetu wakipata mafuriko wanaenda halmashauri wakijua halmashauri inaweza ikawasaidia, wanajua NEMC inaweza ikawasaidia lakini ukweli ni kwamba Pwani Ruvu Bonde ndiyo inafanya kila kitu na kuchukua mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu kwa Serikali, kwa kuzingati hizo changamoto nilizozizungumza ni lini sasa mtabadilisha sheria zilizopo ili kuwe na mamlaka moja yenye usimamizi ili hili suala liweze kudhibitiwa vizuri? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, takataka za Dar es Salaam pamoja na maelezo yote mazuri na matamu uliyoyeleza ni ukweli kwamba Dar es Salaam yenye wakazi wasiopungua milioni tano, yenye majimbo kumi ya uchaguzi, yenye wilaya kubwa tano lina dampo moja tu ambalo liko Pugu Kinyamwezi; na dampo hilo liko katika hali mbaya sana. Sasa nilitaka Serikali ilieleze Bunge hili Tukufu ina mkakati gani wa kuhakikisha…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima malizia swali lako.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Serikali katika majibu yake inipe majibu serious, kwamba ina mpango gani wa kujenga madampo mengine makubwa. Kama inashindwa kujenga katika kila jimbo basi at least kila wilaya iwe na dampo kubwa ili taka ziweze kwenda kutupwa kwa uharaka na kuzuia uchafu. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza nasimama kwenye upande wa Serikali, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia wote viumbe vyake. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kuwa na imani kubwa sana na mimi kuniweka kwenye wizara nyeti kama hii, lakini mafanikio yangu na mafanikio yetu wote ni kushirikiana, tufanye kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nitajibu swali namba mbili la Mheshimiwa Mbunge Halima Mdee. Ni kweli crisis ya taka katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kubwa, si ndogo na Dar es Salaam inakuwa sasa hivi kwa asilimia kubwa sana. Kwa miaka miwili ijayo Dar es Salaam itakuwa na population siyo chini ya watu milioni nane mpaka tisa na dampo ni moja. Juzi mimi nimekwenda kwenye dampo, hali ya dampo ni mbaya lazima tukiri ni mbaya, miundombinu ni mibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatua zimeshachukuliwa. Halmashauri ya Jiji imeshatoa fedha kujenga barabara ya lami katika eneo lote la dampo lakini baada ya hapo kuna mradi ambao unafadhiliwa na donors wa bilioni 75 fedha ambazozimeshakuja. Fedha hizi zimeshawekwa ili ziweze kuboresha dampo jipya la kisasa ambalo litaweza kubeba taka zote za Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nim-assure Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko kazini na Serikali iko makini kuhakikisha kuwa dampo hili linajengwa na fedha ziko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu haya namwambia akae chini sasa. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali dogo la kwanza la Mheshimiwa Halima Mdee. Kwanza nakubaliana naye, wanaotoa kibali na siyo cha kuchimba mchanga cha kusafisha mto ni Bonde. Ukishautoa ule mchanga kwenda nje maana yake Wizara ya Madini wanatoa kibali kingine kwa hiyo unapaswa kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Ofisi ya Makamu wa Rais kwa maana ya kupitia NEMC tunaowajibika sasa kusimamia athari ya mazingira na uhidhi wa maeneo hayo. Sasa nakubaliana naye kwamba umefika wakati lakini pia Ofisi ya Makamu wa Rais ilishaunda Kamati na kamati hii ilijumuisha wadau wote na imekuja na mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mapendekezo ni kuwa sasa na mbadala wa mchanga, hasa kwenye maeneo ya ujenzi sasa hivi, kwenye kokoto ile vumbi ya kokoto ianze kutumika barabarani ili iweze kutumika badala ya mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hata tunapojenga haya majengo yetu sasa tunaanza kutumia vyuma; na baada ya hapo kamati ile pia imependekeza iwepo sasa sheria maalumu na kuwe na bodi moja mbayo inaweza kusimamia zoezi hili. Kwa hiyo nakubaliana naye. Nashukuru.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu wa Wizara ya Mazingira nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge kwamba hata sisi kwa upande wa Wizara ya Madini tunatoa leseni za uchimbaji wa mchanga tofauti na leseni nyingine. Leseni nyingine tunatoa miaka kumi ya uchimbaji wa madini mengine na leseni nyingine tunatoa kwa muda wa miaka saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leseni ya uchimbaji wa mchanga tunatoa kwa muda wa mwaka mmoja mmoja. Maana yake nini; ni kwamba kila tunapotoa leseni katika maeneo fulani basi tunaangalia vilevile na athari za mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira, na tunapoona kwamba eneo hili halifai basi kwa mwaka unaofuata hatutaweza kutoa leseni hiyo. Kwa hiyo tunatoa muda mfupi mfupi huku tuki- monitor mazingira yanavyokwenda katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunapotoa sisi leseni za uchimbaji tunategemea kabisa na mamlaka nyingine ikiwemo mamlaka za halmashauri na mamlaka nyingine ambazo zinalinda mabonde, tunashirikiana kwa pamoja katika kutoa vibali. Tunapokuwa tunaona kwamba eneo hili tunakubaliana kwamba mtu achimbe mchanga tunakuwa tumekubaliana kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoona kwamba kuna athari inaweza kutokea katika uchimbaji wa mazingira, basi mamlaka ile nyingine tunashirikiana nazo kuhakikisha kwamba tunafuata maamuzi ambao wanaona na wao kwamba kuna athari au hakuna athari katika maeneo yale ya uchimbaji wa mchanga. Ahsante sana.
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa nikauliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri tunajua ama ni ukweli kwamba mazingira hasa kwenye upande wa carbon and mission ni nchi ambazo zilizoendelea ndio zinazo- emit hii carbon na athari kubwa inatokea kwa nchi ambazo zinaendelea ikiwemo Tanzania. Lakini nchi hizo ambazo zinaharibu sana mazingira haya zimekuwa zinasita kutoa finance kwenye climate change. Labda Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipangaje kuhakikisha kwamba inapambana katika kukabiliana na matatizo haya ya climate change ikiwemo mitigation adaption? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri ni kweli kuna baadhi ya nchi kubwa duniani ambazo zimejitoa kwenye mkataba huu wa tabianchi kutokana na maslahi yao binafsi, lakini vilevile nchi zilizobakia zikiongozwa na Ufaransa na Qatar na nchi zingine wameanzisha mfuko wa one bilioni 100 Us dollars ambazo zitatumika kwa nchi zote ambazo zitahitaji pesa hizi kuboresha mazingira katika nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hatuko nyuma tulishaanza mkakati wa kuziomba pesa hizi na program mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inafaidika na pesa hizi na kulinda mazingira. Programu ya kwanza ni kuhakikisha tunapanda miti Mlima Kilimanjaro zaidi ya miti bilioni moja ili kulinda barafu ambayo ipo katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri saa ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu swali hili nina maswali ya nyongeza mawili. La kwanza nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akiongelea charcoal briquettes bada la mkaa wa kawaida kutumia charcoal briquettes ambao utengenezaji wake sio lazima utumie miti unatumia majani ya miti, majani ya kawaida haya kuweza kutengeneza mkaa huo ambao una nguvu kuliko mkaa wa kawaida.

Je, ni lini Serikali itaanza kuhamasisha wananchi waaanze kuchoma charcoal briquettes badala ya kutumia miti kuchoma mkaa hilo la kwanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nimefurahishwa sana na majibu ya nyongeza ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwenye swali la nyongeza la swali namba 68 kuhusu kupanda mamilioni ya miti kwenye Mlima Kilimanjaro ili kuupunguzia climate stress huu Mlima Kilimanjaro.

Je, ni lini Serikali itaanza kampeni hiyo ya kupanda miti sio tu kwenye Mlima Kilimanjaro bali nchi nzima wananchi waanze kupanda miti? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa swali la pili mkakati unaandaliwa sasa hivi wa kupanda miti katika Wilaya zote na sasa sio kupanda miti tu, kupanda na kuitunza miti ili isije ikafa. Mara nyingi sana halmashauri wanahamasika kupanda miti lakini baada ya muda mfupi miti ile inakufa na tutaweka aina maalum ya miti kwa Wilaya ambayo itakayoweza kufaa kuna miti mingine haifai kwenye Wilaya mbalimbali, miti hii inapandwa kwa gharama kubwa na inakufa. Kwa hiyo, program kaguzi tutaanza tutashirikiana na halmashauri zote kuhakikisha miti inapandwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu, nchi yetu imebarikiwa kuwa na asilimia 39.9 kuwa ni misitu, misitu hii inapotea. Kuanzia mwaka 1990 mpaka 2010 tumeshapoteza takribani hekta milioni nane ya misitu na hii ni hatari kubwa sana kwa Watanzania tuhakikishe tuache kukata miti tutunze miti kama fursa ya kibiashara, tutumie miti badala ya kukata tuweke mazao ya nyuki. (Makofi)
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante halmashauri zimekuwa zikichukua hatua kali sana kwa hawa wafanyabishara wa mkaa hususani katika mikoa ya pembezoni.

Sasa nataka nifahamu mkakati wa Serikali pamoja na juhudi ambazo mnazifanya za kuhakikisha tunatunza mazingira na ukizingatia uuzaji wa gesi bado ni gharama kwa mwananchi ambaye hana kipato kikubwa. Serikali mna mkakati wa gani wa kuhakikisha haya matumizi ya gesi kwa bei ya chini yanaenda sambamba na kupunguza gharama za manunuzi ya mkaa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kuleta gesi wananchi watumie umeshanza. Napongeza Wizara ya Nishati Pardot Project imeshaanza na imeshaanza kuonesha gharama ni za chini na hivi karibuni Wizara ya Nishati itaanza mkakati kuhakikisha gesi tunapitisha katika nyumba zote Dar es Salaam na tukitoka Dar es Salaam tunakwenda mikoa mingine Iringa kwa Msigwa kule. (Makofi)
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mto wa Kanoni kwa sasa umejaa sana mchanga na kina kimepungua sana, kwa watu wenyewe itakuwa si kazi rahisi kuondoa mchanga na zitahitajika fedha nyingi sana; pamoja na hatua zilizoainishwa kwenye jibu la swali ambazo ni za muda mrefu:-

Je, ni kwa nini Serikali isiwasaidie sasa hawa watu wanaohangaika na mafuriko kila mwaka kwa kutoa fedha kiasi za kuanza kusafisha mto huu angalau mara moja kwa mwaka?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, awali yote napenda kumshukuru Mheshimiwa Benadetha kwa kufuatilia kwa kina suala hili na kutupatia taarifa za kina kuhusu changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikiashia Mheshimiwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu na inajali wananchi wake. Hivyo, Serikali inalichukulia kwa uzito suala hili na tunawasiliana na mamlaka husika ikiwemo Halmashauri ya Bukoba Mjini kuona namna bora na ya kudumu ya kutatua changamoto ya kujaa mchanga katika Mto Kanoni ili kuondoa kero ya mafuriko ya mara kwa mara.