Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mussa Azzan Zungu (2 total)

MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Mafuriko yanayotokea katika Mji wa Bukoba husababisha uharibifu mkubwa wa chakula, mali, barabara na hata kusababisha vifo kwa watu na mifugo; mafuriko hayo husababishwa na Mto Kanoni kujaa mchanga na takataka:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea kero ya mafuriko kila mwaka ikiwemo kusafisha na kuongeza kina cha Mto Kanoni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, chanzo cha uchafuzi wa Mto Kanoni unaosababisha mto huo kujaa mchanga na taka ngumu zinazopelekea wakati wa masika maji kujaa na kuleta athari za mafuriko kwenye makazi ya watu, ni kuwepo kwa shughuli za kibinadamu pembezoni na ndani ya mto zikiwemo; ujenzi wa nyumba, ujenzi wa karo za maji taka, kilimo (mashamba), ujenzi na utumiaji wa mazizi na vyoo, ufuaji, uogaji na uoshaji wa magari na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Bukoba imeanza kuchukua hatua za muda mfupi kwa kupiga marufuku na kuondoa shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mto kama zilivyobainishwa hapo juu, pamoja na kuhakikisha eneo la hifadhi ya mto kisheria, linasafishwa.

Aidha, hatua nyingine ambazo Halmashauri inaendelea kuchukua ni pamoja na kuondoa miti yote isiyokuwa rafiki wa mazingira iliyokuwa imepandwa ndani ya Mto Kanoni na kupanda miti rafiki wa mazingira, kufuatilia ubora wa maji ya mto na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kupitia redio, mikutano ya hadhara, semina na makongamano. Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Bukoba inaendelea kuwahamasisha wananchi kujitolea kupanda miti ili kuhifadhi kingo za mto na uondoaji wa mchanga unaosababisha kupungua kwa kina cha mto kunakosababisha mafuriko wakati wa masika.
MHE. ZAINABU M. AMIRI aliuliza:-

Mboga za majani ni lishe bora kwa afya ya binadamu na wakulima wengi wa mbogamboga hasa Jijini Dar es Salaam wanatumia maji yasiyo salama kwa ajili ya kumwagilia na huenda maji hayo yana kemikali zinazoweza kupelekea mbogamboga hizo kudhuru afya za wananchi badala ya kuziimarisha:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji safi na salama wakulima hao wa mbogamboga?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mboga za majani ni lishe bora kwa afya ya binadamu na wakulima wengi wa mboga hizi waliopo Jiji la Dar es Salaam hutegemea Bonde la Mto Msimbazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao. Hata hivyo, Mto Msimbazi unaendelea kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo cha mbogamboga kando ya mto huo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kuhusu hifadhi ya vyanzo vya maji na kutekeleza mipango na shughuli mbalimbali kwa ajili ya kulinda mazingira ya mto huo yasiharibiwe.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mradi wa kuboresha Bonde la Mto Msimbazi ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na uharibifu wa mazingira katika mto huo. Mradi huu unalenga kupunguza athari za mafuriko, kudhibiti mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na shughuli za binadamu kando ya mto huo, kujenga uwezo wa jamii inayozunguka Mto Msimbazi kuendelea na shughuli za kiuchumi pasipo kuathiri mto, kupanda miti kwa ajili ya hifadhi ya mazingira ya mto, kuweka mkakati wa udhibiti wa taka ngumu katika mazingira ya Mto Msimbazi na kujenga mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo kuendeleza shughuli zao pasipo kuathiri mazingira ya mto huo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuboresha mazingira ya Bonde la Mto Msimbazi, tunategemea kwamba uchafuzi wa mazingira katika mto huo utapungua. Hata hivyo, Kifungu cha 57 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 kinazuia shughuli za kudumu na ambazo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya utunzaji wa bahari au kingo za mto na mabwawa katika eneo la hifadhi mita 60 kutoka vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, aidha, sheria hii inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira kuandaa mwongozo wa matumizi endelevu wa eneo hilo. Kwa muktadha huo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa rasimu ya mwongozo wa mita 60 wa kuhifadhi vyanzo vya maji. Rasimu hii inaainisha matumizi endelevu ya eneo la mita 60 kutoka vyanzo vya maji ikiwemo shughuli za kilimo kando na vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Zainabu Mndolwa Amiri kwamba Serikali itaendelea kuboresha Sera, Sheria na Kanuni ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na usimamizi thabiti wa mazingira ya nchi yetu. Aidha, ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge watakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kuzingatia sheria zilizopo katika kufanya shughuli za maendeleo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuhifadhi mazingira na kuboresha ustawi wa jamii.