Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Issaay Zacharia Paulo (105 total)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili.
Kwanza, kwa kuwa mipango hii ya bajeti tunayoijadili sasa hivi katika Bunge letu inahitaji sana kada hizi za Watendaji na kwa kuwa nafasi nyingi katika kada hizi ziko wazi, je, ni kwa nini Serikali isione umuhimu mkubwa wa kutoa nafasi kwa wale vijana waliomaliza Vyuo vya Serikali za Mitaa na Vyuo vya Utawala, wakaanza kujitolea katika kipindi hiki cha mpito kutegemeana na makubaliano yao katika Serikali za Mitaa hususan kwenye maeneo yao, ili baadaye waweze kuingia katika mfumo wa ajira?
Pili, ni kwa nini sasa Serikali isione inapaswa kutenga fedha za kutosha katika kuwezesha ofisi za Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa sababu fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika ngazi za chini zinatumika kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uendeshaji katika ofisi hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issaay ambapo katika suala lake la kwanza alitaka kujua kwamba ni kwa nini Serikali isitoe fursa au nafasi kwa hawa WEO na VEO ambao wanajitolea katika kipindi hiki cha mpito.
Mheshimiwa Naibu Spika suala zima la kujitolea au la liko mikononi mwao katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Kwa hiyo, nitoe tu rai kwa Mheshimiwa Mbunge, mipango hiyo wanaweza wakaifanya na kuitekeleza huko chini kabisa katika Mamlaka zao za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika kama ambavyo nimesisitiza, ni kutokana tu na ufinyu wa nafasi na wigo wa kibajeti, katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo nilieleza tumepanga kuajiri ajira mpya, nafasi 71,496 na katika nafasi hizo kwa ujumla wake katika WEO na VEO na nafasi zinginezo kwa upande wa Mbulu watapata nafasi 466, vile vile tutawapandisha vyeo katika promotion nafasi 1066. Kwa hiyo, nimwombe tu waendelee kuwa wavumilivu kipindi hiki na kama nilivyoeleza mwezi huu wa Tano ajira hizo zitaanza kutekelezwa na ni imani yangu watatekeleza kwa wakati, ili nafasi hizo ziweze kuzibwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kwa nini sasa Serikali isiweze kutenga fedha za kutosha kuziwezesha Kata hizi ziweze kufanya kwa ukamilifu niseme tu kwamba, mipango ya kibajeti kutokana na uwezo tulionao, Halmashauri zenyewe zinashirikishwa katika mpango mzima wa maandalizi ya bajeti. Kwa hiyo, niwaombe tu wahakikishe kwamba wanapokuwa wanapanga mipango yao wanaweka vipaumbele katika kuziwezesha Kata hizi kuwa na fedha ambazo zitaweza kufanya majukumu yao ya msingi, lakini kwa sasa inawezekana zisitoshe kabisa na ni kutokana na wigo wa bajeti.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri akiwa Mbulu aliwaahidi wananchi wa Mbulu kwamba Halmashauri ya Mbulu itafute jengo kwa ajili ya Mahakama. Namuomba Mheshimiwa Waziri katika mwaka huu wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu itafanikiwa kwa kuwa ina kesi nyingi za ardhi ili Baraza hilo liweze kuzinduliwa na tayari Hamshauri imepata jingo.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, rafiki yangu anajua majibu lakini anataka nirudie ili watu wake wasikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishakwenda, nimetangaza kwamba tutazindua Baraza la Mbulu mwaka huu, bahati mbaya sana majengo waliyotupa yalikuwa na „mushkeli‟ kidogo, Katibu Mkuu wangu ameandika barua kuomba majengo mengine, nafikiri yakirekebishwa hayo majengo, nimeshamuahidi na nimeshawaahidi watu wa Mbulu kwa sababu nimekwenda mwenyewe na Serikali hii haifanyi longo longo inafanya mambo ya uhakika, kwa hiyo tutazindua hilo Baraza mwaka huu la Mbulu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina shule ya viziwi kule Dongobesh na pia ina Kitengo cha Elimu ya Watoto Walemavu katika Shule ya Msingi Endakkot na kwa kuwa kundi hili ni kubwa katika jamii; je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kuweka Kitengo cha Elimu kwa Walemavu katika kila halmashauri kwa shule mojawapo ili kundi hili lililokosa nafasi wapate huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kuna umuhimu mkubwa sana kwa kila halmashauri kuwa na shule yenye kitengo cha watu wenye ulemavu. Hata hivyo, niseme tu kwamba, kuwa na kitengo ni kitu kimojawapo, lakini kuangalia hivyo vitengo vikafanya kazi iliyokusudiwa ni hatua ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningetamani kuona kwamba, kwanza kila halmashauri iwatambue hawa watoto wenye ulemavu pamoja na mahitaji yao yanayohusika. Baada ya hapo, katika hizo shule zinazotengwa, naomba ziwasilishwe kwenye Wizara yetu pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuona kwamba vinawekwa vifaa vinavyohusika na kukidhi mahitaji yanayostahili, tukifanya hivyo tutakuwa tumetatua matatizo makubwa ya watu wenye ulemavu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbulu yenye majimbo mawili, tuna vituo vya afya ambavyo havijakamilika takribani vituo vitano. Kwa mfano, Tarafa ya Nambisi ina kituo cha afya ambacho hakina hadhi, Tarafa ya Daudi na Tarafa ya Dongobesh.
Je, ni kwa nini Serikali isichukue hatua za makusudi kukagua vituo vyote vya afya, na kwa kuwa Waheshimiwa Madiwani katika bajeti ya Halmashauri hawawezi kupitisha bajeti ikaenda kwenye kituo kimoja ili Serikali itenge fedha za kutosha kwa kila Halmashauri, kwa kila mwaka walau kuwa na kituo cha afya kitakachotengewa fedha kutoka Hazina, nje ya bajeti ya Halmashauri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa hoja muhimu sana ambayo ni muhimu sana imesaidia kuibua mambo mbalimbali, Mheshimiwa Zacharia alikuja pale ofisini, na alizungumzia suala zima la maboma ambayo yapo katika Jimbo lake ambayo hayajakamilika.
Ninakushukuru Mheshimiwa Mbunge, ulivyokuja pale ofisini siku ile na Mheshimiwa Jitu na Mheshimiwa Issaay pamoja, katika suala zima la maboma pia suala zima la watendaji, miongoni mwa hoja ambazo mmenisaidia ni kuweza kuangalia tutafanya vipi sasa tuweze kumaliza maboma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili nimezungumza wiki iliyopita tumeelekeza Halmashauri zote zibaini yale majengo yote ambayo hayajakamilika, tunayapangia mpango mkakati maalum kama Serikali, nimesema tulikaa katika utatu, Wizara ya Afya, TAMISEMI pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti kubaini maboma yote na tumeshatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote huo ndiyo mkono wa Serikali sasa, maboma yote yatabainika, lakini tunachotaka kufanya ni angalau kila Halmashauri kwa kila mwaka japo angalau tujenge kituo cha afya kimoja kilichokamilika. Lakini sambamba na hilo, jinsi gani tutafanya kuimarisha zahanati yetu, mwisho wa siku tunakwenda katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ulivyokusudia kupeleka huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge, nikwambie kwamba ni mpango wa Serikali na tunaendelea nao na hili litaendelea kufanikiwa ndani ya kipindi chetu cha bajeti ya miaka mitano hii.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo nilitaka niongezee kidogo juu ya jambo hili la huduma ya afya ya msingi kwa namna ambavyo linaulizwa mara nyingi na imekuwa concern kubwa sana ya Waheshimiwa Wabunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wakati tunajumuisha Bajeti ya Serikali juzi, ni kweli kwamba tuna vituo vya afya vichache, tangu tumepata uhuru tumeweza kujenga vituo vya afya vya Serikali takribani 470 tu. Lakini maeneo ya utawala yamekuwa yakiongezeka Wilaya zimeongezeka Halmashauri zimeongezeka, Mikoa imeongezeka na hivyo ni lazima tufanye utafiti, tufanye tathmini ya namna catchment zilivyokaa ili tuweze kuja na mpango mzuri sana ambao utajibu maswali mengi sana ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyo sasa waridhike na Waheshimiwa Wabunge watuamini tunaendelea kufanya mchakato huo wakufanya tathmini tukishirikiana na Wizara ya Afya na kama nilivyosema juzi kwamba tukiamua kwa Halmashauri 181 tulizonazo nchini, tukasema kila mwaka tujenge kituo kimoja, kwa miaka mitatu tutakuwa tumejenga vituo 543, vituo 543 ni zaidi ya vituo tulivyovijenga vya afya toka tupate uhuru ambavyo ni 470.
Kwa hiyo, nasema Waheshimiwa Wabunge hili tunalichukua pamoja na uchache wa fedha kama mnavyosema lakini kwenye mpango huo tunaokubaliana Wizara ya Afya tutakuwa pia tuna-package ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tuna-fund siyo tu kwa maana ya ujenzi lakini pia kwa maana ya vifaa tiba, pia na wataalam.
Waheshimiwa Wabunge, hivyo, niwaombe sana tuvumiliane tuende kwa style hiyo ninaamini baada ya miaka mitano mtakuwa na kitu cha kusema kwa wananchi waliowachagua.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nami naomba kuuliza maswali madogo mawili. Swali langu la kwanza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri…

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru. Naomba kuuliza, ni kwa nini Wizara ya Ujenzi haijaweza kupitisha barabara mpya za Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kwa kuwa mji wetu wa Mbulu ni mji mkongwe kuliko miji yote Tanzania? Naomba kauli ya Wizara kuhusu barabara hizi mpya kwa kuwa sasa magari yameongezeka sana katika Wilaya zetu. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ambayo ni ya lami kwa pale Mbulu Mjini. Vilevile Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu kwamba katika bajeti ambayo tunashukuru sana mliipitisha hapa Bungeni, kuna bajeti ya kutekeleza baadhi ya barabara ambazo ziko ndani ya Wilaya ya Mbulu; na ninamhakikishia kwamba tutatoa kipaumbele ili fedha zile zilizotengwa kwa ajili ya kujenga barabara za Wilaya ya Mbulu na Wilaya nyingine tutazitekeleza kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujalia nguvu za kifedha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Ni kweli kuwa taifa letu lina changamoto kubwa ya ajira kwa vijana. Kwa kuwa vijana hawa wengi wako kwenye mazingira ya vijijini, ni kwa nini sasa Serikali isianzishe Jukwaa la Vijana katika Halmashauri zetu ili vijana wetu walioko vijijini na wale walioko kwenye miji midogo kama Mbulu na kwingineko waweze kujadiliana na Maafisa Uchumi, Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii changamoto na fursa zilizoko na jinsi vijana wetu wanavyoweza kupata ajira zile ambazo si rasmi kutokana na ukosefu wa ajira? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa jana ilipitishwa sheria hapa ya uundwaji wa Baraza la Vijana ambayo lengo lake mahsusi kabisa lilikuwa ni kwenda kusaidia kuyakusanya mawazo ya vijana na kuwashirikisha vijana katika kutatua kero na changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili. Kwa sasa Wizara ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kanuni ambazo zitatoa mwongozo ni namna gani Mabaraza haya yataanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mabaraza haya kuanzia katika ngazi ya kata na kuja mpaka taifa itakuwa ni kusikiliza na kujadili na vilevile kuwa sehemu ya kuwasilisha Serikalini na ushauri na matatizo ya vijana. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na hayo yote lakini sisi kama Wizara tumeendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Halmashauri. Kwanza kabisa, kwa kuendelea kusisitiza kwamba kila Halmashauri nchi nzima ihakikishe inaanzisha SACCOS ya vijana ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata mikopo na mitaji kwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2014 Wizara pamoja na Wakuu wa Mikoa wote tulikutana hapa Dodoma. Lengo kubwa la mkutano wetu hapa Dodoma lilikuwa ni kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana hasa vijana wa pembezoni kwa maana ya vijijini ili tuanzishe kitu kinachoitwa Youth Special Economic Zone ambayo itakuwa ni sehemu kwa ajili ya vijana kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba aendelee kutupa ushirikano, sisi tupo tayari kushirikiana na Halmashauri kutatua changamoto za vijana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kufahamu, kule Jimboni Mbulu kuna Bwawa la Dongobesh lililokamilika takriban miezi sita. Mkandarasi ameshaleta certificate yapata miezi miwili. Waheshimiwa Mawaziri wanajibu majibu hapa, lakini kule Wizarani hakuna mchakato wa kuwalipa hao Wakandarasi. Naomba, kama itawezekana, Waziri ana kauli gani kumlipa Mkandarasi wa Bwawa la Dongobesh?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Dongobesh ni kweli ujenzi wake umeshakamilika, kilichobaki ni miundombinu ili lile bwawa sasa liweze kufanya kazi kwenda kumwagia kwenye mashamba. Tumeweka utaratibu kwamba certificate zifike. Wiki iliyopita niliongea na Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka wiki iliyopita certificate zilikuwa hazijawasilishwa katika Wizara, lakini tunaendelea kufuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshamwagiza Mkurugenzi wa Maji Vijijini ili aweze kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbulu Vijijini ili waweze kuangalia hizi certificate ziko wapi, kwa sababu kule wanasema zimetumwa, lakini Wizarani hazijafika. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala tunalifanyia kazi na pindi certificate zikifika hela tunazo, tunalipa, ili hili bwawa liweze kukamilishwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusu vyuo hivi viwili vilivyoko Wilayani Mbulu, nami naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa katika Chuo cha MCH - Mbulu hadi sasa wanafunzi wetu wamesitishiwa huduma ya chakula kutokana na madeni makubwa walionayo wazabuni. Je, ni lini Serikali itarudisha huduma hiyo ya chakula ili wanafunzi wetu wasome kwa amani? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu kuna jengo la ghorofa lililojengwa takribani miaka mitatu na liko chini ya kiwango na kwa sasa halitoi huduma iliyokusudiwa. Je, Serikali inachukua hatua gani kuja kubomoa hilo jengo na kujenga jengo lingine jipya ili liweze kutoa huduma kwa hospitali yetu na chuo kwa ujumla?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza linahusu chakula kwa wanafunzi wa Chuo cha Mbulu. Kwa mwaka mmoja uliopita, Serikali iliondoa utaratibu wa kupeleka bajeti ya chakula kwenye vyuo vyote vya MCH nchini na vyuo vyote ambavyo viko chini ya Serikali na badala yake huduma hizo zimekuwa zikitolewa na sekta binafsi kwa makubaliano na miongozo maalum inayotolewa na Serikali. Kwa maana hiyo, chuo hiki kinapaswa kifuate utaratibu huo mpya wa Serikali ili wanafunzi wapate huduma hiyo kutoka kwa washitiri binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la jengo, kwa sababu ni swali jipya na jengo hilo silifahamu vizuri, naomba nisitoe commitment yoyote ile, ila nimuahidi tu Mheshimiwa Issaay kwamba tutaongozana ama nitamkuta Jimboni baada ya Bunge la bajeti ili nilitembelee jengo lenyewe, nijue ni mradi wa nani, chanzo cha fedha za kutekeleza mradi huo ni kipi na niweze kujua nitamshauri vipi yeye pamoja na uongozi mzima wa Halmashauri ya Mbulu ili tuweze kuona mradi huo ukitekelezeka kwa manufaa ya umma.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na nimpongeze Naibu Waziri kwa maelezo ya swali la msingi. Tatizo la ujenzi holela wa miji katika Tanzania yetu inakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha, watumishi kwa maana ya Maafisa Mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu takribani miaka sita tulikuwa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe wa Master Plan ya Mji wa Mbulu na hatimaye kushindikana, hivyo ni kwa nini Serikali isifanye mapitio upya kuona rasilimali watumishi kwa maana ya wataalam wa Mipango Miji, fedha za kuhakikisha kwamba miji midogo na miji mikubwa inayopanuka inafanyiwa utaratibu wa mipango miji ili nchi yetu isikumbwe mara nyingi na bomoabomoa zinazojirudia mara nyingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na ndiyo maana hapa mwanzo nimezungumzia hii programu kubwa ambayo kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaanza nayo hivi sasa na hii maana yake haitogusa maeneo yale ya pembezoni, isipokuwa yale maeneo ya mipakani kwanza ndiyo yatakuwa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivi kwa nini, ni kwamba ukipita nchi mbalimbali, maeneo yaliyopangwa yatafurahisha hata unaposhuka katika ndege unapoona jinsi gani mji umepangwa vizuri na bahati mbaya sana katika maeneo yetu mbalimbali miji yetu imekuwa ikijengwa katika squatter na ndiyo maana tumetoa maelekezo hasa kwa Maafisa Mipango Miji wa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa haipendezi, kwa mfano, eneo kama la Kibaigwa ndiyo kwanza linakua na Afisa Mipango Miji yupo pale, anaacha tu ujenzi unaendelea, ndiyo sababu tumetoa maelekezo kwamba kila Afisa Mipango Miji ahakikishe kwamba kupimwa kazi yake na Wakurugenzi tumewaagiza hili, katika zile performance appraisal za Maafisa Mipango Miji wahakikishe jinsi gani wametumia taaluma zao kuhakikisha miji yetu inayokua inapangwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imejipanga tutatafuta funds, lakini vilevile tutatumia human resources tulizonazo kuhakikisha kwamba watu wetu wanawajibika. Hata hivyo, tunakiri kwamba Maafisa Mipango Miji bado wapo wachache tutajitahidi kutafuta uwezekano wa kadri iwezekanavyo kuongeza nguvu kazi hii ilimradi maeneo yetu yaweze kuwa maeneo rafiki kama nchi ya Tanzania ambayo inakwenda katika Awamu ya Tano ambayo inakwenda kwa kasi zaidi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue nafasi hii kuuliza maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa kilio cha barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara – Mbulu ni ya muda mrefu na kwa kuwa barabara hii ndiyo inaunganisha Mji wa Babati na Mji wa Arusha kwa ajili ya wananchi wa Mbulu na kwa kuwa taarifa anayosoma Mheshimiwa Naibu Waziri ni taarifa aliyoandikiwa; wakati wa bajeti tulikubaliana fedha zote, karibu shilingi bilioni moja na milioni 200 zitumike kujenga daraja la Magara, na kwa sasa fedha zinazozungumzwa, shilingi milioni 300, ni hela ndogo sana.
Je, ni lini Naibu Waziri au Waziri mwenyewe mwenye dhamana ya Wizara hii atafanya ziara kujionea hali halisi ya mateso wanayopata wananchi wa Mji wa Mbulu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika uwanja wa Mbulu Mjini, aliahidi kuweka kilometa tano za lami katika Mji wa Mbulu kutokana na Mji wa Mbulu kuwa Mji mkongwe sana na kwa kuwa Rais aliahidi kwamba ahadi hii itatekelezwa katika bajeti ya mwaka 2015/2016.
Je, ni kitu gani kilipelekea ahadi ile isitekelezwe mpaka leo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nitakuwa nimefika katika hiyo barabara na nitakujulisha lini, lakini kwa vyovyote itakuwa ni kabla ya mwezi Januari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, ni suala la ukosefu wa fedha ndilo lililosababisha kipindi kilichopita kilometa tano za barabara hiyo zilizoahidiwa zisijengwe.
Naomba tu nikuhakikishie kwamba tunachukua kwa umuhimu mkubwa na tutaitekeleza hii ahadi ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne pamoja na wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi walizitoa, nikuhakikishie kwamba tutazitekeleza.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwezesha elimu bure, upatikanaji wa madawati na pia watumishi hewa kuondolewa, naomba kufahamu, kwa sasa Watanzania wengi hasa akinamama katika SACCOS zao wamekuwa na hamu kubwa ya kufanya biashara. Je, Serikali inachukua hatua gani kuwezesha SACCOS za akinamama katika halmashauri zote zipate hela za kutosha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ikumbukwe kwamba sote humu ndani Waheshimiwa Wabunge sisi ni Wajumbe katika Mabaraza yetu ya Halmashauri, hivyo tunatoa asilimia tano katika mapato ya halmashauri na hayo ni katika kuimarisha vikundi vyetu vya VICOBA pamoja na SACCOS zilizopo ndani ya halmashauri zetu. Nitoe wito tu kwa Waheshimiwa Wabunge, tusimamie kwa ufasaha asilimia hizo tano za mapato ndani ya Halmashauri zetu ili ziweze kuwafikia wananchi wetu hasa akina mama na vijana ili kuweza kuinua uchumi wao.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue nafasi hii kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri hayakugusa ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika barabara ya Mji wa Mbulu na ahadi hiyo iliwagusa wananchi wa Mji wa Mbulu wakati wa uchaguzi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia nini kuhusu utekelezaji wa ahadi hii ambayo imesahaulika, hadi sasa mwaka mmoja umeisha baada ya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii hatujaisahau. Tulichokifanya katika mwaka wa kwanza ni kutekeleza barabara zile ambazo wakandarasi walikuwa wameondoka site kwa kutolipwa madeni yao, na unaona kwamba sasa hivi tumefanya kazi kubwa sana na barabara nyingi zinaanza kukamilika baada ya kulipa madeni ambayo walikuwa wanayadai. Nimhakikishie, kuanzia bajeti ijayo, tunaanza sasa, kwanza kukamilisha zile barabara zilizobakia za nyuma ili tusiwe tunadaiwa daiwa riba pamoja na usumbufu, lakini vilevile tuanze sasa kwa kiwango chochote tutakachoweza kwa mwaka ujao wa fedha barabara zile mpya tulizoziahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie katika safari yangu ambayo Mheshimiwa Massay tumekubaliana tutafika mpaka Mbulu na ninadhani nitalala Mbulu Mjini ili tuliangalie hilo kwa undani pamoja na hayo matatizo matatu makubwa ambayo nimeyaongea kabla.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri niwashukuru Naibu Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa kuja Mbulu na kutembelea baadhi ya Halmashauri za Wilaya ya Mbulu na vituo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali la msingi muuliza swali alitaka pia mpango mkakati wa Serikali kuajiri kada za afya kwa maelezo ya swali la msingi. Je, Serikali ina mkakati gani na ajira ya kada za afya ili kupunguza tatizo
hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ongezeko la asilimia 9.7 ni dogo sana ukilinganisha na tatizo la huduma ya afya hususan dawa na vifaa tiba katika nchi yetu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kukaa chini na kwenda katika Halmashauri zote nchini kufanya tafiti ili waweze kuleta mpango mkakati wa kuondoa tatizo la
upungufu wa dawa na vifaa tiba katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mpango mkakati wa Serikali ni suala zima la ajira kama tulivyosema. Niseme wazi kwamba ajira zilisimama kwa lengo mahususi kutokana na mipango ya Serikali na hapa juzi mnaona kwamba mchakato wa ajira za elimu hasa walimu wa sayansi umeanza lakini sio muda mrefu kwa kadri Ofisi ya Rais, Utumishi itakavyokuwa imejipanga itatoa vibali vya ajira kwa ajili ya sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuondoe hofu katika suala hilo kwa sababu tunajua wazi kwamba kweli tuna changamoto ya wahudumu mbalimbali hasa katika sekta ya afya katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la
mpango mkakati ni kweli, kwanza naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge leo hii ukifanya reference katika Halmashauri zetu kuna ma-DMO wengi sana walikuwepo hapa Mkoani Dodoma. Lengo ni kuhakikisha sasa tunatengeneza mipango mizuri na sio ile mipango ya mezani peke yake; tunatengeneza mipango mizuri ya kwenda kujibu matatizo ya afya katika maeneo yetu. Leo hii tumesema fedha zitakwenda moja kwa moja mpaka katika kituo cha afya
na zahanati; tumepata akaunti zote za vituo vya afya katika nchi yetu; huo ni mpango mkubwa kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo naomba
niwaeleze ndugu zangu wakati mwingine tuna tatizo kubwa la usimamizi wa rasilimali fedha. Katika mwaka 2016/2017, mpaka mwezi Julai kuna outstanding fedha ambazo ni za Basket Fund hazijatumika karibu bilioni 20. Katika Mkoa wa Manyara peke yake kuna karibu milioni 500 mpaka mwezi Julai zilikuwa hazijatumika. Mpaka tunapozungumza leo hii bajeti yetu ya mwaka huu Basket Fund ni zaidi ya shilingi bilioni 106.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mpaka mwezi
Desemba fedha zile ambazo zimekuwa accrued ambazo hazijatumika na fedha zilizoingia ni takriban shilingi bilioni 71; kati ya fedha hizo 71, fedha ambazo zimetumika mpaka hivi sasa ni asilimia 55 tu mpaka mwezi Desemba, nini maana
yake? Fedha zipo katika Halmashauri yetu lakini dawa hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwasihi Waheshimiwa
Wabunge kwamba tuhakikishe katika Halmashauri zetu fedha za Basket Fund tuwabane ma-DMOs na wahasibu wetu tuweze kuzibainisha ziende zikanunue dawa na vifaa tiba; lengo kubwa ni kumwokoa mwananchi wa Tanzania.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Hivi sasa Serikali inatumia gharama kubwa sana katika kuanzisha mabwawa mapya kupitia maji ya mvua; lakini rasilimali hizi za asili nyingi zimeelekea kutoweka, kwa hiyo, nilidhani Serikali pia itakuwa na mkakati.
Mheshimiwa Spika, hivyo nina maswali madogo mawili, la kwanza, fedha zilizotajwa katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 hazikuweza kupatikana hadi sasa na hivi sasa tunaingia Bajeti ya Mwaka 2017/2018, lakini hali inayotishia ziwa hili inaonesha hivi punde litakauka; je, Serikali itatoa lini fedha milioni mia moja kupitia Mradi wa DADP’s ambayo imekusudiwa kwa nia njema katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amewajibu Watanzania pamoja na mimi na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma timu ya wataalam kupitia maziwa yote ya asili katika nchi yetu ili iweze kutoa ushauri wa kitaalam na kuchukua hatua za kunusuru maziwa hayo kwa haraka na wataalam hao watakwenda lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba baada tu ya kupata swali lake hili nilifanya ziara katika Mkoa wa Manyara na kati ya maziwa ambayo nilikwenda kuyaona ni Ziwa Babati, tukiwa na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Mheshimiwa Pauline Gekul pamoja na Mheshimiwa Jitu Soni, na bahati mbaya siku ile Mheshimiwa alipata ajali, pole sana, lakini Mwenyezi Mungu alitusaidia.
Mheshimiwa Spika, basi niseme kifupi kwamba, bajeti haijakwisha, Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la kwanza kwamba fedha hazijapatikana, milioni 100 lakini leo tuko Aprili na bajeti yetu inakwisha Juni. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba sisi tunafanya kila linalowezekana kama Serikali kuhakikisha fedha hizo zimefika ili zifanye kazi iliyokusudiwa; na zile nyingine zilizopangwa kwa ajili ya kazi nyingine inayofuata.
Mheshimiwa Spika, la pili, timu ya wataalam itakwenda lini; hili namhakikishia kwa sababu hili sasa nimeahidi kwa niaba ya Serikali, kwamba tutafanya tathmini katika maziwa yetu. Tunaelewa changamoto ambayo sasa vyanzo vya maji vimekabiliwa, mito mingi inakauka, maziwa yetu mengi yanakauka, mabwawa yetu mengi yanakauka.
Kwa hiyo, sisi kama wenye dhamana hii ya kusimamia mazingira, kwa dhati kabisa tumeamua na katika bajeti ya mwaka huu wa fedha inayokuja mtaona jinsi ambavyo tutaanza kushughulikia vyanzo vya maji, kurudisha uhai wa
vyanzo vya maji ili viweze kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuahidi kwamba niliyowaahidi kwenye maziwa ambayo nimeyataja kwanza wataalam watakwenda tena waliobobea kutoka kwenye sekta zote ambao wako competent na wataweza kutushauri kama Serikali ili tuweze kuja na mpango sasa madhubuti wa kuhakikisha kwamba maziwa yetu yanaendelea kubaki.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mji mkongwe wa Mbulu ni mji wa zamani. Umekumbwa na tatizo kubwa la maji hivi karibuni, lakini tatizo hili la miradi ya maji kusuasua katika utekelezaji limeikumba Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Serikali mwaka huu ilitenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa maji Mbulu Mjini. Mradi huu hadi sasa utaratibu umeshafanyika wa tenda kwa kupitia Mamlaka ya Maji Mji wa Babati, lakini hakuna hatua iliyofikiwa umebaki mwezi mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana, alifika Mbulu akafanya ziara. Mradi wa Maji ulioko katika kijiji cha Moringa Daudi una takribani miaka minne, hadi sasa mradi huo umeshindikana kukamilika na mkandarasi alimdanganya Mheshimiwa Naibu Waziri alipotembelea site.
Je, ni hatua gani ichukuliwe kwa mkandarasi wa namna hii ambaye alimdanganya Mheshimiwa Waziri hadi leo ni miezi minne hajakamilisha mradi huo, ambapo aliahidi mbele ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba nijibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge, kwa mujibu wa Kanuni. Maana ameuliza maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za mkataba zinashughulikiwa kwa masharti yaliyoko ndani ya mkataba. Kwa hiyo, naomba tuwasiliane mimi na wewe ili tuone huyu mkandarasi ni wapi ambapo ameteleza tuweze kushauri. Kwa sababu mkataba huo umesainiwa na Halmashauri yake, Wizara ya Maji na Umwagiliaji iko tayari kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kwamba tunashauriana ili kumfanya huyu Mkandarasi aweze kutekeleza miradi. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, hivi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu katika majimbo yote mawili tulikuwa na mradi wa maji takribani zaidi ya miaka minne na hao wamekosesha Halmashauri zetu kupata mpya za miradi ya maji. Ni kwa nini sasa Serikali isitoe maelekezo ya Waraka kwa Halmashauri za Wilaya kwa jinsi ambavyo watajiondoa katika mikataba ya awali ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Halmashauri yake naijua, tena mikataba hiyo imeingiwa wakati na yeye mwenyewe akiwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri. Tumeanza kutoa fedha na tumetoa maelekezo kwamba kwanza tukamilishe ile miradi ya awali ambayo ilikuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la mikataba ni la Mkurugenzi mwenyewe aliyeingia mikataba, clauses za kuhudumia mikataba ziko ndani, termination ziko ndani namna gani ziko ndani, suala la mikataba haliwezi kujadiliwa Bungeni, ni la yeye mwenyewe Mkurugenzi ambaye aliingia mikataba hiyo; na condition ya mikataba ipo pale na taratibu zote zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge amwambie Mkurugenzi wake aiangalie mikataba vizuri, madirisha ya jinsi ya kutoka yapo ili kuachana na huyo mkandarasi ambaye ameshindwa kazi ili kuweza kuingia na mkandarasi mwingine.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na riba kubwa inayotozwa kwa wafanyabiashara wadogo lakini pia wafanyabiashara wadogo wanachangamoto kubwa ya tozo za ada na ushuru katika makundi haya ya bodaboda, mama ntilie na wauza mbogamboga. Na kwa kuwa Serikali yetu kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliahidi Itazitazama upya tozo hizi ambazo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo, sasa ni lini Serikali yetu itatazama upya tozo hizi ili wafanyabiashara wadogo waweze kupunguziwa mzigo mkubwa katika uendeshaji wa biashara yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Bunge lako Tukufu limeona kupitia Wizara ya Kilimo kuna tozo ambazo zimependekezwa nyingi tu kuondolewa, ambazo serikali iliahidi kuziondoa. Na nyingine ambazo haziko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko kwenye mchakato wa kuandaa Tax Measures na Finance Act, 2017, hivyo tuvute subra, yote haya ambayo Serikali yetu iliahidi yote yatatekelezwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wetu, hali hii ya makorongo na jiografia inayobadilika kutokana na tabianchi imesababisha jamii yetu hasa akinamama kukosa huduma za afya, watoto na wanafunzi kukosa masomo na kwa kuwa ni tatizo la nchi nzima, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuona ni namna gani hata madaraja ya dharura kama yale ya chuma kuwekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sasa hivi tunabadilika kutoka Watendaji wa Halmashauri na barabara zote zinazohudumiwa na Halmashauri zinapelekwa kwa Wakala wa Barabara za Vijijini. Je, ni kwa namna gani Serikali itatazama suala hili kutokana na kwamba fedha zinazotengwa ni kidogo sana kulingana na fedha za Mfuko wa Barabara kwa zile barabara zilizokuwa zinahudumiwa na halmashauri za wilaya katika maeneo ya vijijini ili fedha zitakazotengwa kwa dharura ziweze kusaidia tatizo hili na jamii ipate huduma stahiki na kwa wakati kuliko sasa ambavyo inapoteza maisha katika hali ya dharura na mvua nyakati za masika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika nchi yetu kuna maeneo mbalimbali yanaathirika sana, na hasa katika Mkoa ule wa Manyara. Nikiri wazi kwamba eneo lile lina changamoto kubwa sana na wakati mwingine mvua ikinyesha utakuta sehemu nyingine mpaka mito inahama. Hali hiyo inajitokeza hata katika Mkoa huu wetu wa Dodoma na Mkoa wa Morogoro maeneo ya Gairo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa suala la upatikanaji wa madaraja ya chuma naomba tu niseme kwamba jambo hilo tumelipokea, japokuwa siwezi kusema kwamba hilo daraja litapatikana lini; lakini kwa haja ya kusaidia wananchi nadhani ngoja tuliweke hilo katika vipaumbele vyetu. Katika maeneo ambayo mwanzo yalikuwepo madaraja hayo, lakini leo hii yametengenezwa madaraja mengine, yale madaraja ambayo ni ya chuma yaliyohamishwa kule, tutaangalia jinsi ya kufanya, kwa kushirikiana na wenzetu wa TANROADS katika maeneo mbalimbali ili kuisaidia jamii yetu hasa kule Mbulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la TARURA na bajeti; ni kweli katika fedha zinazokwenda za Mfuko wa Barabara; kwa sababu kuna ule mgawanyo wa sheria ambapo sheria ya TANROADS ni tofauti na sheria za halmashauri; lakini tumeunda Wakala mpya ambao una mikakati vile vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine linalofanyika ni suala zima la resource mobilization, kutafuta fedha, kwa hiyo naamini; katika kipindi hiki ambacho TARURA inaanza sasa naomba Waheshimiwa Wabunge muwe na imani, kwamba kazi nzuri itafanyika na mtakuja kuona kwamba kuna faida kubwa sana kwa kuanzisha Wakala huu; ambapo iliainishwa wazi katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwamba lazima katika kipindi hiki Wakala uanzishwe. Sisi jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tutasimamia Wakala huu ili uweze kufanya kazi vizuri ili wananchi waweze kupata huduma vizuri
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa Wilaya kongwe hapa nchini. Wilaya hiyo kongwe huko mbele ilikuwa na kiwanda cha kutengeneza vigae vya kuezeka maghorofa na pia kulikuwa na kiwanda kilichokuwa kinamilikiwa cha kutengeneza chokaa na gypsum powder. Hivi sasa hivyo viwanda havifanyi kazi.
Je, ni lini Wizara itaenda Mbulu ili ikae na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Vijijini waweze kufufua viwanda hivi ambayo vilianzishwa na wenzetu huko awali?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Issaay, kuhusu vifaa vya madini ya ujenzi, kwa mamlaka niliyonayo namuagiza Mkurugenzi anayeshughulikia viwanda aandae safari ya wataalam kwenda kuangalia fursa zilizoko kule na awapeleke wawekezaji kule Mbulu kusudi mimi nikienda, niende kufungua na kuzindua kiwanda hicho.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii niseme kwamba kwanza Serikali haitutendei haki sisi Wabunge. Neno italipa fedha au kifuta machozi pindi hela itakapopatikana haliwafurahishi Watanzania kwa tukio lililotokea la Watanzania kupoteza maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kadhia hii kwa Jimbo la Mbulu Mjini ina changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa Askari Wanyamapori na pia ratiba isiyoonekana ya wenzetu wa TANAPA na jamii zinazopakana na mipaka ya hifadhi na makazi ya watu. Tukio hili la mwaka 2015 lilipoteza maisha ya wananchi saba, siyo watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine niishukuru Serikali kwa sababu, Mheshimiwa Waziri ameleta tu majibu ambayo hajayafanyia kazi kwa sababu, hadi sasa muda mchache uliopita, kama miezi miwili, mitatu, Serikali tayari imetoa fidia kwa wahanga hao wapatao wanne, lakini wale wengine hawakupatiwa hata fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu sasa, kwa kuwa tatizo hili linagusa maisha ya Watanzania, je, ni kiasi gani cha fidia au cha kifuta machozi kinatolewa kwa wale wote waliopoteza maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kwa kuwa tatizo hili linavunja mahusiano kati ya wananchi na wenzetu wa TANAPA ama Serikali, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuandaa ratiba rasmi itakayowaunganisha wadau wa mpakani katika Tarafa yangu ya Daudi ili waweze kujadiliana matukio yanayotokea na hatimaye kudumisha uhusiano kati ya Shirika la TANAPA na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kama alivyosema tayari Serikali imekwishaanza utaratibu wa kulipa bakaa au madeni ambayo yamekuwepo ya muda mrefu yanahusiana na kifuta jacho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sana madeni haya yamekuwa hajalipwa, lakini napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwa ujumla kwamba Serikali katika awamu hii imeshalipa madeni yaliyokuwa yanafikia kiasi cha shilingi bilioni 2.1 na hata sasa kuwa yamebaki jumla ya shilingi takriban milioni 500 peke yake. Mbulu ni mojawapo kati ya Wilaya ambazo zimelipwa malipo hayo na jumla ya fedha kiasi cha shilingi milioni 7,100,000 zimelipwa kwa madhumuni hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza; la kwanza, anazungumzia ni kiasi gani cha fedha kilichobaki kwa ajili ya malipo kwa Halmshauri ya Wilaya ya Mbulu? Katika takwimu nilizonazo, nina takwimu za ujumla wa kiasi chote ambacho fedha zinadaiwa kwa Serikali, lakini mahususi kwa ajili ya Mbulu, ukiacha hiki nilichotaja, kilicholipwa tukionana mchana naweza kumpa taarifa juu ya kifuta jasho na kifuta machozi kilichobaki kwa ajili ya Wilaya ya Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili la kuweka ratiba na utaratibu wa kuweza kujadiliana, kuisharisha mahusiano zaidi baina ya TANAPA na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi, hili ni jambo jema na Serikali inalipokea. Tutakwenda kufanya hivyo na tutamshirikisha Mheshimiwa Mbunge ili kuona kwamba tunaimarisha zaidi mahusiano hayo kwa ajili ya uendelevu katika utaratibu mzima wa hifadhi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Waziri wa Maji na Waziri wa TAMISEMI kwa kuteua Bodi ya Maji na pili kuwatuma wataalam kule Mbulu kwa ajili ya suala hili la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Mbulu na hasa Mji wa Mbulu, hali ya maji imekuwa mbaya kwa takribani sasa miezi sita. Katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tulitenga fedha shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya utafiti na usanifu wa maji katika Mji wa Mbulu. Je, ni lini mpango huu sasa Wizara itatusaidia ili tuweze kupata maji ya uhakika kuepukana na adha hii ya ukosefu wa maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubaini upungufu katika Halmashauri yake nilimwelekeza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji BAWASA, ameenda kule kuangalia, akagundua matatizo mengine ni madogo sana, ni pampu tu zimekufa zinahitaji matengenezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ameshaandaa quotation na wiki hii nakutana naye ili tuweze kumpatia hela akafanye kwanza ufufuaji mdogo ili wananchi wapate maji, lakini baada ya hapo tutatekeleza mradi mkubwa kuhakikisha kwamba Halmashauri yake na kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi tunapata asilimia 95 ya huduma ya maji.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Mjini limekuwa na migogoro ya ardhi hususani shule zetu za msingi na sekondari na kwa sasa karibu shule mbili ziko mahakamani kwa ajili ya kutetea ardhi zake.
Je, Serikali haiwezi kuchukua utaratibu sasa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote ya shule za msingi na sekondari nchini zinapata kupimwa ili ziweze kuepukana na adha hii ya migogoro ya ardhi kwa taasisi hizi za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema, Serikali inahitaji kupima hayo maeneo naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna mkakati na maelekezo madhubuti ili taasisi zote za umma hususani shule kuhakikisa kwamba maeneo yao yote yanapimwa na kupatiwa hati ili kuondoa migogoro ambayo inaweza ikatokea pamoja na uvamizi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Waziri kwa kuteuliwa kwake pamoja na Mawaziri wengine wote.
Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali ilikuwa na nia njema ya kuajiri watumishi 52,000; je, Serikali sasa itatekeleza mpango ule wakati gani ili vijana wetu waliopo mitaani waweze kupata nafasi ya ajira?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baada ya mchujo wa watumishi hewa, Mheshimiwa Rais ametoa idhini, Serikali imeidhinisha waajiriwe watumishi wapya 15,000, hilo zoezi linafanyika. Pia katika mwaka huu wa fedha kuna kibali cha kuajiri watumishi 52,000, zoezi hilo litaendelea, nataka nihakikishe kwamba nafasi na fedha za kuwalipa zipo, kazi hiyo itatekelezwa. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi mimi ni kwa namna gani Serikali itoe utaratibu wa jamii, Halmashauri na Serikali Kuu kuweza kuweka nguvu pamoja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu hivi sasa maboma yaliyo mengi katika Halmashauri zetu yamechukua miaka mingi ningeomba basi Mheshimiwa Waziri atume wataalamu kwa baadhi ya maeneo machache ili kunyambulisha ni gharama gani zitakazotumika katika ujenzi wa nyumba hizi za walimu na tuwe na lengo kwa kila Halmashauri kwa zile nyumba ambazo ziko katika lenta ili tuweze kukamilisha kuungana na wananchi. Nashukuru.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Issaay nadhani swali lake limejenga katika kujenga suala zima la ushauri na kiufupi kwamba ushauri huu tumeuchukua ndio maana tuliongeza bajeti katika mwaka huu wa fedha kutoka shilingi bilioni 150 npaka kufika shilingi bilioni 246 kwa lengo kubwa kuweza kuhakikisha eneo hilo tunalifanyia kazi. Lakini tunafanya kazi hilo katika maeneo yote sekta ya afya na sekta ya elimu ambapo Mheshimiwa Issaay ndio ulikuwa umejenga hoja ya msingi kipindi cha Bunge lililopita.
Kwa hiyo, naomba niseme tutalichukua hili naamini kwa pamoja tukishirikiana lakini hata hivyo nipende kuwapongeza Wabunge hasa wanaotumia Mfuko wa Jimbo na kwa kushirikiana na maeneo yao ambapo katika tembea yangu nimekuta miradi mingi ambayo Wabunge kupitia Mfuko wa Jimbo wameingiza fedha kuhakikisha nyumba za walimu na madarasa yanafanyika hivyo, kwa hiyo nawapongeza sana kwa hali hiyo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na hatua kubwa inayochukuliwa na Serikali yetu.
Je, kutokana na gharama kubwa inayotumika ya matengenezo ya kawaida katika barabara hii inayounganisha mikoa minne kwa kiwango cha changarawe na kwa kuwa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri hakueleza mkataba huu unaisha lini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuharakisha kazi hii ya usanifu ili barabara hii ipate kutengenezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais aliahidi ahadi nyingi wakati wa kampeni kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za wananchi. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu aliahidi kilometa tano kwa barabara ambazo zinamilikiwa na Serikali za Mitaa wakati ule. Kwa kuwa sasa barabara zile zimehamia kwa TARURA, je, ni nani atakayetekeleza ile ahadi ya kilometa tano katika barabara zile kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa haziko tena kwenye utaratibu wa kuzihudumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana hii barabara muhimu ambayo inaunga mikoa mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba kwanza barabara hii pia inafuatiliwa na Waheshimiwa wa mikoa hii. Mheshimiwa Flatei Massay naye anaifuatilia sana barabara hii tumezungumza, lakini wako Wabunge wa Mkoa wa Singida, wako Wabunge wa Simiyu wanafuatilia hii barabara muhimu sana. Na sisi upande wa Serikali, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, tumeanza ujenzi katika Mto Sibiti, sehemu ambayo ilikuwa ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa sasa kwanza wananchi wanapita. Wakipita katika barabara hii kwa mtu ambaye anaenda Karatu tuna-save zaidi ya kilometa 400, kwa mtu anayekuja Singida tuna-save zaidi ya kilometa 200; tuna-save muda, lakini pia tuna-save gharama mbalimbali.
Mheshimiwa NAibu Spika, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, Serikali imechukua hatua kuhakikisha kwamba ujenzi wa daraja utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu, tutakuja kwenda haraka katika ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za kilometa tano, ninajua kwamba nchi nzima ziko ahadi ambazo sisi kama Serikali tunaendelea kuzitekeleza, ikiwepo ahadi ambayo imetolewa huko Mbulu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga tunaendelea kuratibu kuona kwa kiasi sasa tunapoenda nusu ya kipindi cha miaka mitano tumetekeleza ahadi ngapi ili tuweze kukamilisha ahadi hizi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais wetu; na pia pamoja na harakati kubwa ya kuwajengea Watanzania nia njema ya kulipa kodi; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa Uchaguzi na katika Kampeni zake aliahidi kuondolewa kwa tozo ndogo ndogo kutokana na wafanyabiashara wadogo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kuwa ina kila sababu ya kutazama upya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na makundi gani yanasamehewa katika hizo tozo ndogo ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, katika vipindi tofauti, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais na timu zote tulipokuwa tukinadi ilani na Mheshimiwa Rais aliahidi kundoa hizi tozo ndogo ndogo ambazo zimekuwa kero kwa wananchi; kwamba mboga mboga, nyanya nini imekuwa ni kero kubwa zaidi. Kwa sababu kodi hizi zinatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Sura Na. 290, ndiyo maana tumefanya maelekezo sasa; kuna mchakato unakwenda kwa ajili ya kurekebisha sheria zetu tuone ni jinsi gani sasa tutakusanya katika kodi zile kama crop cess na maeneo mengine lakini kuondoa usumbufu kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili lipo katika mchakato na wadau mbalimbali ndiyo wanaweka maoni yao sawasawa na mwisho wa siku sheria hiyo itakuja katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tuipitishe sisi sote kwa pamoja, tufanye amendments, tushauri, turekebishe, mwisho wa siku ni kwamba mwananchi wa kawaida atakuwa ameguswa na matamko ya Mheshimiwa Rais alipokuwa akinadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama tulivyoelekeza.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza swali dogo. Kwa kuwa sasa kuna wimbi kubwa la ujenzi wa vituo vya afya katika ngazi za kata, kwa mfano, Wilaya yetu ya Mbulu ina tarafa tano, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kupitia tarafa zote hizo tano na kuona ni kituo gani cha afya chenye mahitaji madogo ya fedha ili iweze kutoa huduma kwa kutengewa fedha za kutosha? Kwa mfano tarafa zote zina vituo vingi lakini hakuna kituo kinachotoa huduma stahiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tumeupokea kwanza na ndiyo maana wiki iliyopita kamati ya Bunge ya Bajeti, Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya tulikuwa tuna kikao cha pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikao kile kililenga kubaini kwanza maboma yaliyokuwepo yote kabla hayajakamilishwa. Najua Mheshimiwa Mbunge una-concern kubwa ya maboma katika maeneo yako. Tumefanya tathmini ya maboma yote yaliyojengwa, lakini hayajakamilika, pia tathmini ya zahanati na tathmini ya vituo vya afya vina hali gani. Lengo letu ni kuwa na kituo cha afya ambacho mtu hata huduma za operation ziweze kufanyika vizuri katika maeneo husika. Kwa hiyo, jambo hilo sasa tumelifanya kwa pamoja na Kamati ya Bunge imeelekeza. Lengo kubwa ni kupata fedha za kuboresha huduma ya afya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba kinachotakiwa kufanyika ni wataalam wetu na Wabunge wetu kutushauri, kwamba ikiwezekana tu-review ramani za majengo yetu. Wakati mwingine inaonekana kujenga kituo cha afya gharama yake inakuwa kubwa kumbe inawezekana kwamba, isiwe friendly kwa mazingira husika. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Serikali tunalifanyia kazi na kwamba tutateua baadhi ya vituo, tuviweke katika hadhi nzuri ili viweze kutoa huduma bora na viwe kimbilio ya wananchi katika maeneo yao.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana. Tatizo hili la wazabuni kushinda tender na baadae kuchelewesha huduma kwa Watanzania kwa muda uliokusudiwa imekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. Mifano ya wazi zipo katika Halmashauri za Wilaya ya Mbulu kwa miradi ya maji na miradi ya afya. Mifano hiyo ni kama ambavyo kupewa tender makampuni ambayo hayana uwezo na hatimaye baadaye kuchelewesha huduma hizi. Je, Seriakli yetu sasa kutokana na hali hii ambapo tenda hutolewa na wataalam ndani ya Halmashauri, inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma kwa wakati uliokusudiwa kutokana na muda wa mikataba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nilichozungumzia kwenye korosho ni zile taratibu ambazo tumeweka kwa ajili ya korosho, lakini ukweli wa mambo, kuna utaratibu wa kawaida wa kisheria kuhusiana na mambo ya tender. Sheria yetu ya manunuzi inaweka wazi namna tender inavyotakiwa kuendeshwa, lakini vilevile inaweka masharti kuhusiana na utekelezaji wa miradi kwa yule ambaye ameshinda tender na kwa vyovyote vile hairuhusiwi kisheria mtu ambaye ameshinda kutelekeza ile kazi kama kuna mapungufu ambayo yametokea ni vizuri kuangalia katika kesi zenyewe ili wale ambao wamehusika waweze kuchukuliwa hatua za sheria.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na changamoto nyingi zilizokuwa zinakabiri kundi hili la walimu, moja ya changamoto kubwa inayokabili kundi la walimu ni mazingira magumu ya kufanyia kazi. Na kwa kuwa hivi sasa Serikali yetu inatekeleza mpango kabambe wa vituo vya afya kwa nchi nzima, je ni kwa nini Serikali isione umuhimu sasa wa kushirikiana na jamii, Halmashauri na Serikali Kuu ili kuona ni namna gani kwa kila Halmashauri katika mwaka wa fedha tunajenga nyumba kadhaa za walimu hasa mazingira yale ya vijijini ili walimu waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Zacharia Issaay kwa swali lake zuri na ninaomba sasa kumjibu kwamba Serikali inakubaliana kwamba kuna maeneo ambayo kweli yana mazingira magumu hasa maeneo ambayo yapo mbali na Makao Makuu ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo hayo yanahitaji mkakati maalum, na kama tulivyoeleza katika mipango mingi ya Serikali, ni kwamba tunaomba sana ushiriki wa jamii katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na miundombinu ambayo inavutia walimu waendelee kukaa katika maeneo hayo na miundombinu hiyo ni pamoja na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili natoa wito kwamba halmashauri zote ziweke kipaumbele kwenye maeneo ambayo yapo mbali zaidi na halmashauri kwa kutenga kwanza fedha/mapato ya ndani kabla hatujapeleka sisi kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha maboma. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naipongeza Serikali kwa hatua kubwa inayochukua ya kutekeleza miradi ya barabara nchini.
Swali langu dogo, katika utaratibu wa awali nilijibiwa hapa Bungeni kwamba barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga iko katika hatua ya mwisho a kupatiwa fedha za usanifu kina.
Je, Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetenga kiasi gani kwa ajili ya kufanya usanifu wa Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, anaifuatilia sana hii barabara na anajua umuhimu wake. Barabara hii itakuwa kwa kweli ni dawa kwa ajili ya kusaidia uzalishaji katika eneo hili. Nafahamu hatua ile ya awali ya usanifu imekuwa ikiendelea, lakini katika mwaka huu wa fedha unaokuja tutaendelea na kuhakikisha kwamba utaratibu wa kukamilisha michoro na ujenzi wa barabara hii unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ila nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo ya Simiyu, Shinyanga na maeneo ya Arusha na Singida kwamba ule ukamilishaji wa ujenzi wa lile daraja pale Sibiti unaendelea. Vile vyuma vilivyokuwa vinasubiriwa kwa muda mrefu vilishafika, kwa hiyo sasa kipande kile tutaweza kupita wakati tunakamilisha hii hatua ya michoro na kuanza huu ujenzi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, ile kasi ya kukamilisha kazi hii inaendelea vizuri, na kwamba hii barabara sasa iko kwenye hatua nzuri ya kuanza ujenzi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo la Mbulu Mjini mipaka yake kwa asilimia 50 inazungukwa na misitu ya asili na maji wanayotumia viumbe wakiwemo binadamu yanatoka katika misitu hiyo. Hivi sasa maji hayo yameanza kupungua ndani ya misitu. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam watakaofanya utafiti katika misitu inayozunguka Jimbo la Mbulu Mjini ili iweze kufanyia kazi taarifa yake ya utafiti kwa ajili ya kushauri jamii inayozunguka misitu hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kusema tu Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba ameshafika Ofisini kwangu siyo mara moja na suala hili tumelizungumza, tumeliweka wazi, tumesema kwamba nina maslahi kwa wananchi wa Jimbo lile. Kwa hiyo, ni lini tunaenda? Jibu ni lile lile ambalo nilisema kabla; nimemwambia Ofisini na narudia tena hapa kwamba mara baada ya Bunge hili la bajeti, nina ziara ndefu sana, ratiba hiyo inahusisha pia Jimbo lake. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii ya madini kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wa Jimbo la Mbulu Mjini, ni kwamba wanakosa mitaji, lakini pia uchimbaji wao ni wa kubahatisha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia fursa za uwezeshaji, lakini pia na vifaa vya kubaini madini yako wapi na njia rahisi ya uchimbaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwamba, wachimbaji wadogo wanakumbana na tatizo kubwa la kuwa na mitaji midogo. Sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba, wachimbaji wadogo tunakwenda kuwasaidia, ili waweze kupata mitaji ya kuweza kuchimba na waweze kuchimba kwa kupata faida, na sisi kama Serikali tuweze kupata maduhuli na kodi kutokana na uchimbaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wachimbaji wadogo wengi wanachimba kwa kubahatisha. Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na Geological Survey of Tanzania taasisi ambayo chini ya Wizara ya Madini, tuna mkakati kabambe wa kuhakikisha tunafanya tafiti mbalimbali. Tafiti ambazo zitaonesha ni wapi kuna madini ya kutosha na kuweza kuwapa ushauri wachimbaji wadogo kuchimba maeneo ambayo yana madini ili kuepukana na tatizo la kuchimba kwa kubahatisha. Wanatumia fedha zao za mfukoni, wengine wanauza hadi mali zao, ili waende wakachimbe maeneo ambayo hayajafanyiwa utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumejipanga vizuri, tunafanya tafiti za kutosha na tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo, ili waweze kuchimba maeneo ambayo yana madini na waweze kuchimba kwa teknolojia nzuri ya kisasa na nyepesi, ili waweze kupata tija na waweze kuendesha maisha yao vizuri zaidi, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mbulu, kwanza kuishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Daudi na Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Kituo cha Afya cha Dongobeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba pamoja na shukrani hizi ninazotoa, naishukuru pia Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ambayo iko kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbulu takribani shilingi bilioni moja na nusu katika bajeti ya mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili sasa; upungufu huu wa watumishi umepelekea watumishi waliopo kufanya kazi ya ziada kutokana na kwamba hospitali hii ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu iko mpakani mwa Halmashauri ya Babati, Halmashauri ya Karatu na Halmashauri ya Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapokea huduma wa afya katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu, karibu asilimia 30 wanatoka kwenye maeneo ya pembezoni, hali inayopeleka watumishi walioko kufanya ya ziada.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali iniambie inachukua hatua gani sasa kuongeza fedha za OC kwa ajili ya wale watumishi wanaofanya kazi ya ziada ili waweze kuwahumia wananchi wetu wanaotoka ndani ya Halmashauri ya Mbulu na Halmashauri nyingine za jirani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa sasa fedha zinazotengwa za dawa na vifaa tiba ni kidogo kulingana na idadi ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini na kwa kuwa wale wanaotoka nje ya Jimbo la Mbulu Mjini hawapo kwenye mpango huu; Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kutazama takwimu ya wananchi wanaopokea huduma ya Afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazipokea pongezi alizotoa kwa kazi ambayo inafanywa na Serikali, lakini ameuliza maswali mawili. La kwanza ni suala zima la kutoa allowance kwa wale watumishi wachache ambao wanalazimika kufanya masaa ya ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba kila Mtumishi na hasa wa sekta ya afya pale anapofanya kazi masaa ya ziada, ndiyo maana kuna kipengele cha on-call allowance ili waweze kulipwa stahili zao na wahakikishe kwamba wanafanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba kibali cha kuweza kuwaajiri watumishi 25,000. Kibali hiki kitakapokuwa kimepatikana ni imani yangu kubwa Hospitali yao ya Mbulu nayo itapata watumishi kama ambavyo ameomba watumishi 91, ni ukweli usiopingika kwamba itapunguza uhaba uliojitokeza kufikia sasa hivi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja ya changamoto inayokabili sana Mji mkongwe wa Mbulu ni pamoja na barabara ya Magara - Mbulu kupita katikati ya Mji Mkongwe wa Mbulu. Kwa kuwa jambo hili linaathiri uchumi wa wananchi, je, Serikali ina utaratibu gani sasa ikiwemo Mji wa Mbulu na miji mingine nchini namna ya kupata barabara ya mchepuo katika miji yetu ikiwa ni pamoja na athari za kiuchumi lakini pia na jiografia ya miji hiyo inavyokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba tunatazama sana maeneo haya kadri yanavyokua na anatambua ziko barabara ambazo zitakuja kuunganisha Mbulu Mjini. Nampongeza sana kwa kufuatilia, anajua tutatoka Mbulu Mjini kwenda Karatu, tutakwenda kutoka Mbulu kupitia Magara kama alivyosema na kuja Mbuyu wa Mjerumani. Vilevile ipo barabara kubwa ambayo itakuwa inakwenda Katesh – Dongobesh. Sasa barabara hizi zinavyokuja kuunga Mbulu, tunazitazama pia ukuaji wake na kuweka barabara za mchepuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mbalimbali katika miji kama alivyosema, tunayatazama yakiwemo maeneo ya Songea. Najua ndugu yangu alikuwa anafuatilia kilometa 11 zile, lakini maeneo mbalimbali ukienda Mwanza, tunayatazama ili kupunguza msongamano katikati ya mji. Zipo barabara ambazo zimekamilika kwa ajili ya mchepuo. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kupitia Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa inayofanya Wizara hii. Pili niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa tatizo kubwa linalowakabili akina mama wajane, watoto, ambao wamepoteza wapendwa wazazi wao ni katika tatizo hili la kesi na mashtaka ya ardhi; na kwa kuwa familia nyingi zinazopata matatizo hayo hazina uwezo wa kifedha kuweka wanasheria. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali itatafuta msaada wa kisheria kwa akina mama wajane na watoto warithi wa ardhi katika familia mbalimbali zinazopoteza wazazi wao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Wizara yameniridhisha kwa kiasi kikubwa, je, ni kwa namna gani Wilaya ya Mbulu ambayo hivi sasa kesi nyingi zinazoendeshwa katika Baraza la Ardhi la Babati zinapata nafasi ya fursa ya kupimiwa ardhi kwa msaada wa Serikali, wananchi na wadau wengine ili tatizo hili la mashtaka mengi ya ardhi katika Baraza la Babati yapungue na hata kwa Mbulu kwa sababu hata tukipata Baraza bado tatizo litakuwa kubwa kwa mashtaka yatakayoendelea kutokana na hali hii ya kunyang’anyana ardhi kwa wale wenye uwezo na wasio na uwezo? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali inao mkakati wa kutoa msaada wa kisheria kwa makundi kadhaa yenye shida kama hizi, lakini kwanza kwa Mbulu tulifikiri kitu cha muhimu tusogeze huduma na kuanzisha Baraza la Ardhi kwa sababu tusingeweza kufikiria huduma za kisheria wakati huduma yenyewe haitolewi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba kwanza atuvumilie, mwaka huu Mungu akipenda lazima lile Baraza ambalo amelipigania kwa muda mrefu Mbulu Mjini litaanzishwa.
Mheshimiwa Spika, pia lile Baraza la Babati linaendelea kufanya kazi. Tutahakikisha kesi zote za Mbulu ambazo ni nyingi sana, tukishamuweka pale Mwenyekiti pale Mbulu kesi zote za Mbulu zitarudi Mbulu kutoka Babati ili angalau iwarahisishie hawa akina mama na watu wasio na uwezo waweze kupata hii huduma karibu na mahali wanakoishi. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara kwa hatua inayochukua. Tatizo linaloikumba Ziwa Babati kadhalika linaikumba Ziwa Tawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na kwa kuwa tatizo hili ni tatizo mtambuka kwa nchi nzima.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuunda wataalam kwa nchi nzima na baadae kuzitafutia fedha za kunusuru maziwa hayo ili yaweze kuendelea kutoa huduma kwa jamii na viumbe wengine hai?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu kwenye swali la msingi nimeeleza tarehe 4 Septemba kimefanyika kikao cha wadau ambapo Waziri alikuwa amekisimamia na moja ya mambo ambayo wamejadili ni mkakati wa kuhakikisha kwamba wanaondokana na tatizo hili la magugu maji.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huu tutaendelea nao na baada ya kuweka ule mkakati basi tutahakikisha kwamba tunaweza kuondoa tatizo hilo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nashukuru kwa majibu ya Wizara kwa maswali yote yaliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapata miaka kadhaa sasa bidhaa hii ya sukari nchini inapanda bei kila inapofika mwezi wa tatu na inampa wakati mgumu mlaji katika gharama kulingana na hali ya uchumi ya Mtanzania wa chini.
Je, ni kwa nini Serikali isitazame namna ya kuzalisha sukari hii ikamudu katika ule muda wa sukari kupanda kila mwaka kuanzia mwezi wa tatu ili kila Mtanzania kwa wakati mmoja aweze kupata bidhaa hii kwa bei nafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wawekezaji au wazalishaji wa sukari ni wafanyabiashara binafsi na Serikali imekuwa haiwaingilii sana katika upangaji wa bei, lakini tunawaomba fursa hii wanayoipata ya kulindwa wasiitumie vibaya. Tumefanya hivyo kwa viwnada vya saruji, tumeelewana vizuri na ninatoa rai kwao iwe ni mwiko kupandisha sukari kiholela.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa hivi sasa mashtaka mengi ya walimu yanachukua muda mrefu na kwa kuwa walimu hawa wanalipwa mishahara na kitendo kinachofanya wasitoe mchango wao.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutoa waraka au maelekezo ya mashtaka haya kuchukua muda mfupi ili walimu warudi kwenye masuala yao ya utumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya maeneo kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge mashauri yamechukua muda mrefu. Hata hivyo utaratibu mwingine unaosababisha mashauri kuchukua muda mrefu ni kwa sababu kutakuwa na baadhi ya mambo ambayo yanahitajika katika huo mchakato wenyewe wa kusikiliza hayo mashauri. Mimi napenda niungane naye, kwamba tutatoa maelekezo hivi karibuni; kwa mashauri ambayo yako shuleni ambayo hayahitaji gharama kubwa na yako chini ya Mwalimu Mkuu wa shule yaweze kusikilizwa haraka iwezekavyo. Mashauri ambayo yako kwenye halmashauri ya wilaya au katika wilaya kwa Katibu Msaidizi tutatoa maelekezo hivi karibuni ili kusudi kasi yake iweze kuongezeka ya kusikiliza.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kushukuru Serikali kwa kujenga vituo vya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa ziara yake pamoja na muda huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani amejitahidi kwenda Mbulu na kuona changamoto zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Halmashauri ya Mji wa Mbulu ina Tarafa tatu; Tarafa ya Nambis katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu haina hata kituo kimoja cha afya. Changamoto kubwa inayowakabili wakina mama wa Tarafa ya Nambis katika hali ya kupata huduma ya uzazi salama. Je, ni lini sasa Serikali itatupa fedha na ahadi ya Mheshimiwa Waziri ya kwenda kwenye ile Tarafa ya Nambis ambako wananchi wengi na hasa akina mama wanapata tatizo kwenye uzazi?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Issaay kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini kwa kweli kazi yako inaonekana na imetukuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la kupata kituo cha afya katika Kata ambayo haina Kituo cha afya tumeshirikiana na wenzetu wa TAMISEMI tayari kuna mpango wa kuhakikisha kwamba kata ambazo hazina vituo vya afya zinakuwa na vituo vya afya na vijiji ambavyo havina zahanati vinakuwa na zahanati.
Mheshimiwa Menyekiti, lakini naomba nitumie Bunge lako tukufu kutoa angalizo, sera ya afya inasema kituo cha afya kila kata na zahanati kila kijiji, lakini tunafanya mapitio ya sera ya afya. Tutatoa vigezo kwamba kituo cha afya kila Kata kwa kuzingatia jiografia ya eneo husika, idadi ya watu na burden of disease (aina ya magonjwa ambayo yanapatikana katika eneo hili) kwa sababu sasa hivi barabara nzuri lakini pia kuna mawasiliano ya simu.
Kwa hiyo, sitaki kuwadanganya Wabunge kwamba tutakuwa na vituo vya afya kila kata, haitawezekana. Tutaweka vigezo ili tuone ni kata zipi ambazo zitakuwa na vituo vya afya.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutoa kifuta machozi takribani milioni nane kwa ajili ya wananchi waliopoteza maisha yao na wale walioathiriwa na wanyama wakali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwaka 2016 Serikali iliahidi kufanya ziara katika Tarafa ya Daudi na Tarafa ya Ndekoti kwa ajili ya wananchi ambao mali zao na mazao yameharibiwa na wanyama wakali, lakini hadi sasa Serikali haijatimiza ahadi yake hiyo kwa kuwa wale waliokuwa kwenye Wizara walibadilishwa.
Je, ni lini Serikali itafanya ziara katika Tarafa ya Daudi na Tarafa ya Ndekoti kwa ajili ya wananchi ambao mali zao zimeathiriwa na wanyama ikiwemo mazao na hawajapata kufidiwa hadi sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba inawezekana kulikuwa na ahadi ya kwamba viongozi wa Kitaifa wataenda kutembelea katika lile eneo.
Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata kama viongozi wa kitaifa hawajafika, bado wapo Watendaji wetu ambao lazima wafike katika yale maeneo na wahakikishe kwamba wanahakiki mali zilizopotea, wanahakiki uharibifu uliofanyika kusudi wale wananchi wanaostahili kupewa kile kifuta jasho au kifuta machozi, waweze kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa nafasi hii, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba leo hii nitawaagiza watendaji wafike katika lile eneo ili wakutane na hao wananchi, wafanye tathmini na tuone ni kiasi gani wananchi wale wanastahili kulipwa kwa mujibu wa kanuni zetu tulizonazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utayari, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakuwa tayari, tutakuja pia kuhakikisha kwamba haya yote yanatekelezeka na wananchi waweze kuona kwamba Serikali yao inawajali vizuri. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Katika Jimbo la Mbulu Mjini kuna maporomoko ya Haino katika Tarafa ya Nambisi, Kata ya Nambisi. Maporomoko hayo ambayo wataalam kutoka Serikalini na taasisi mbalimbali zisizo za Serikali wameendelea kuyatembelea; na kwa kuwa, tuna mahitaji makubwa ya uzalishaji wa umeme nchini, je, ni lini Mheshimiwa Waziri na Wizara yake watatembelea maporomoko ya Haino ili yaweze kutoa mchango wake katika sekta ya umeme kwa nchi nzima na hususan Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issaay, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunatambua uwepo wa maporomoko haya ambayo kwa mujibu wa tafiti mbalimbali yana uwezo hata wa kuzalisha Megawati 5,000. Kupitia Serikali na TGDC tuna mpango wa kuhakikisha kwamba tunazalisha Megawati 200 kupitia maporomoko mbalimbali ambayo yataleta nishati ya joto ardhi ifikapo 2025, naomba nimkubalie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali kupitia Wizara ya Nishati tutafanya ziara katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye jibu lake kwamba kwa mwaka huu kuna maeneo kama 50 ambayo yatafanyiwa tafiti likiwemo eneo la maporomoko hayo katika Jimbo la Mbulu Mjini. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu swali hili lilikuwa la mwezi wa Pili mwaka huu. Hivi sasa ni kweli, barabara hizo nilizozitaja zimefanyiwa matengenezo, lakini kwa kuwa, sasa fedha zinazotengwa kwa wenzetu wa TARURA kutengeneza hizi barabara za vijijini ni kidogo sana je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kutafuta vyanzo vingine na kuhakikisha kuwa, barabara zote zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini, anaweza kupatiwa fedha za kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi wote Wabunge humu ndani ni mashahidi, maeneo mengi yanayopata makorongo makubwa katika halmashauri zetu na majimbo yetu yanahitaji mdaraja makubwa. Fedha zinazotolewa kwa wenzetu wa TARURA ni kidogo sana kiasi kwamba, hata kama wangepewa fedha makorongo hayo hayapo katika jiografia au mtandao wa barabara wanazohudumia wenzetu wa TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni ni wakati wa kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayohitaji madaraja makubwa ambayo ni kikwazo kwa huduma za kijamii zikiwemo kliniki za akinamama, huduma za afya na elimu zinapatiwa mpango mkakati wa kujengewa madaraja hata ya chuma? Kwa kuwa, eneo hilo ni tete na…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, fedha ambazo tunazipata kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima, ikiwemo pesa za TANROADS na TARURA ni kidogo. Sasa hivi uwezo wa fedha tunazopata ni asilimia 57 ya mahitaji. Hata hivyo niseme tu kwamba, kati ya fedha tunazozipata asilimia 90 zinakwenda kufanya matengenezo ya barabara, kwa hiyo, utaona kwamba ni asilimia 10 tu ndiyo inayokwenda kujenga barabara mpya. Kwa hiyo iko haja ya kuongeza fedha kwenye matengenezo ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, lile zoezi la kutambua network ya barabara kwa upande wa wenzetu wa TARURA, limefanyika, lakini kulikuwa na changamoto ya data ambazo zilipatikana; ikalazimika TARURA waende maeneo husika ili tuweze kuzitambua barabara zote ili sasa mgawo wa fedha na mahitaji ya fedha tuweze kuyaona kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo ambavyo vinatumika ni pamoja na urefu wa mtandao wa barabara, tunatumia vigezo pia vya aina ya barabara, kama ni barabara ya lami, barabara ya changarawe, barabara ya udongo na hali ya barabara ilivyo na idadi ya magari yanayopita katika maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga na TARURA wanafanya kazi nzuri na ni kesho tu tunategemea taarifa itawasilishwa TAMISEMI, itawasilishwa kwenye Mfuko wa Barabara na upande wa kwetu kwenye Wizara, ili tuangalie mahitaji yetu halisi na tuweze kuomba fedha zaidi kukamilisha maeneo ambayo ni korofi. Kwa hiyo, kazi inaendelea ya kuhakikisha barabara zetu tunaziboresha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Mwaka 2015/2016 wanyama wakali walipoteza maisha ya wananchi watano katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Hivi sasa Halmashauri ya Mbulu toka ianzishwe mwaka 2015 haina Maafisa wa Wanyamapori. Je, ni lini Serikali yetu itatusaidia kutupatia Askari wa Wanyamapori katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na upungufu wa wafanyakazi katika maeneo mengi ikiwemo Maafisa Wanyamapori. Katika jitihada ambazo zinafanyika sasa hivi tumeweka kwenye bajeti inayokuja kuangalia kama tunaweza kupata wafanyakazi wachache ambao tutawasambaza katika wilaya mbalimbali hapa nchini. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira hilo likikamilika tutafikiria Wilaya ya Mbulu ili waweze kupata wafanyakazi hao.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Hivi sasa nchi nzima hatuna vitabu vya elimu ya msingi kwa darasa la nne hasa mitalaa mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wanafunzi hawa wanatarajia kufanya Mitihani ya Taifa hivi punde mwisho wa mwaka huu, Serikali ina utaratibu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama majibu ya Serikali hayatatosheleza kwa umma wa Watanzania na sisi Wabunge, basi tuahirishe mjadala ulioko mezani tukajadili jambo hili kwa manufaa mapana ya nchi yetu. Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge sidhani kama ni sahihi, kwa sababu ni karibu wiki mbili au tatu zimepita Wizara imesambaza vitabu vya darasa la kwanza mpaka darasa la nne kwa Halmashauri zote nchini. Sasa kwa hali hiyo, nina imani kwamba vitabu vipo katika mashule na hapana huo upungufu anaozungumza kwa sasa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mpango unaotekelezwa sasa wa kilomita 0.4 ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na kwa kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ni kilomita 5 katika Mji wa Mbulu, nini majibu ya Serikali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa Rais atakuwa anataka ahadi hiyo iwe imetekelezwa na mimi nimeshatimiza wajibu wangu wa kuikumbusha Serikali mara kadhaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni kweli Mji wa Mbulu ni mji mpya ulioanzishwa lakini ni Halmashauri au Wilaya kongwe katika ya Wilaya kongwe Tanzania. Kwa hivi sasa Mji wa Mbulu una kilomita 1.8 katika mitaa yake kwa kiwango cha lami. Kwa kuwa hali ya barabara na madaraja katika kata kumi ukiacha kata zingine nane za vijijini ni mbaya; na kwa kuwa TARURA wanapewa fedha kidogo sana hivyo kushindwa kutekeleza mahitaji yaliyoibuka, nini kauli ya Serikali kuwezesha miundombinu ya barabara katika Miji wa Mbulu pamoja na ahadi hiyo ya Rais?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge Zakharia, Mbunge wa Mbulu Mji maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, naomba nimhakikishie kwamba hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, kipenzi cha Watanzania, namhakikishia kabla ya 2020 ahadi hii itakuwa imekamilishwa ili Mheshimiwa Rais atakapoenda kuomba kura kwa awamu nyingine kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi, asipate vikwazo kwa wananchi wa Mji wa Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anapenda kujua tuna mpango gani, nitoe maelekezo kwa TARURA Mkoa na Wilaya yake ya Mbulu kama hali ya mji huu ni mbaya kiasi hicho wafanye mchakato walete maandishi hapa tujue namna ya kufanya ili tuweze kuboresha wakati tukisubiri kutafuta fedha nyingi zaidi za kuboresha Mji wa Mbulu. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, moja ya tatizo linalopoteza morality ya utendaji kazi katika watumishi wetu wa umma ni pamoja na kutokuweka wazi namna ambavyo Serikali italipa madeni ya huko nyuma ya watumishi wetu; na kwa kuwa kwa jambo hili watumishi wanakosa moyo wa kufanya kazi, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kukaa na vyama vya wafanyakazi ili waweze kuona namna gani ya kutatua tatizo hili la madeni ya huko nyuma ili watumishi wetu wote waweze kufahamu namna ambavyo Serikali kama mlezi wao na mwajiri wao itawatendea katika jukumu hili la kulipa madeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshafanyia kazi madai ya Walimu na watumishi wengine na ilishakutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na utaratibu upo wa kuweza kulipa fedha hizi. Kwa sasa hakuna mgogoro kati Serikali na wafanyakazi, madeni yanajulikana. Tunatafuta fedha na uwezo wa Serikali kuanza kulipa madeni haya. Hata hivyo tunalipa kila muda, sio kwamba bajeti ni kubwa kiasi hicho, kwa hiyo madeni yanalipwa, lakini pia tumeshakubaliana namna ya kwenda, deni halisi linajulikana kwamba kila mtu anadai kiasi gani na hilo linafanyiwa kazi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa kwa nchi nzima na kwa kuwa baadhi ya familia ambazo zina watoto hawa ni watu wenye uwezo, wametelekeza kutokana na matatizo mbalimbali ya kifamilia:-

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutafuta namna ya kutafuta msimamizi halisi wa sheria hii kwa ngazi ya Wilaya na Ofisi za Ustawi wa Jamii ili kuweza kuleta tija kwa kundi hili muhimu sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi Serikali ya Tanzania imeridhia Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Mtoto na ndiyo maana tuna Sera ya Mtoto ya Mwaka 2008 na vilevile tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009. Sheria hii imeainisha kwa kina sana haki hizi za mtoto. Niseme tu kwamba sheria ipo na imeainisha adhabu ambazo zinaweza zikatolewa endapo haki za mtoto zitakiukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo inatukabili ni idadi ndogo ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali katika Halmashauri zetu. Nasi kama Serikali tumeliona hilo, tunaendelea kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi Jamii wetu katika Halmashauri ambapo wapo lakini vilevile dhamira ya Serikali ni kuongeza idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii ili waweze kusimamia jukumu hili la kuweza kuhakikisha kwamba haki za watoto zinalindwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Mpango wake wa Bajeti ilipanga minara minne katika Jimbo la Mbulu Mji, katika Kata za Murray, Nahasey, Masqaroda na Gunyoda. Hadi sasa ni mnara mmoja kule Murray umeanza kujengwa. Je, ni lini Serikali itajenga minara mitatu iliyobaki kwenye Kata za Masqaroda, Nahasey na Gunyoda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mimi mwenyewe nimewahi kutembelea Mbulu Mjini na nikaona maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto ya mawasiliano na hasa eneo la Masqaroda, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lile eneo kuanzia mwezi Februari mwanzoni minara itaanza kusimikwa kama tulivyopanga kwa sababu wakandarasi tuliowapatia kazi hiyo wameshatuhakikishia kama Serikali kwamba wameshajipanga kwa ajili ya kuanza kutekeleza kuanzia mwezi Desemba, mwezi Januari na mwezi Februari katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa hospitali ya Mji wa Mbulu inategemewa na kata zinazopakana kutoka Wilaya ya Babati, Karatu na hata upande wa Jimbo la Mbulu Vijijini; na kwa kuwa hospitali hii inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za uendeshaji hali inayopelekea wagonjwa kujigharamikia wakati wa rufaa na ukosefu mkubwa sana wa dawa. Mheshimiwa Waziri ameshafika mara kadhaa na sasa hivi tuko kwenye mpango wa bajeti wa 2020/2021. Je, Serikali ina mkakati gani wa kusaidia hospitali ya Mji wa Mbulu kwa kuiongezea fedha za uendeshaji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Vituo vya Afya ya Daudi na Tlawi tayari vimeanza kutoa huduma, tunaishukuru sana Serikali. Pia nia ya Serikali ni njema kujenga Kituo cha Afya katika Tarafa ya Nambis ambapo vijiji vyake baadhi vina umbali wa kilomita 30 mpaka 40 kwenda hospitali wa Mji wa Mbulu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka maombi niliyowasilisha ya gari la ambulance kutafutwa haraka ili wananchi wa kata hizo za Nambis na maeneo mengine ya pembezoni wapate huduma ya usafiri haraka kwenda kupata matibabu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Zacharia Paul Issay, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na pacha wake Mheshimiwa Flatei Massay hapa karibuni tulienda kufanya ziara katika Halmashauri hizi mbili na niwapongeze Wabunge hawa wamefanya kazi kubwa sana ya kusimamia miundombinu kwa fedha ambazo tumepeleka kule.

Mheshimiwa Spika, ni kweli hospitali ya Mheshimiwa Mbunge siyo suala la mgao wa fedha peke yake hata hali ya majengo haipendezi. Ndiyo maana kwa ombi la Mheshimiwa Mbunge nilipendekeza na nilielekeza kwamba zile shilingi milioni 500 sasa zianze kuibadilisha Hospitali ya Mbulu kwa sababu tunajua itakapokuwa na mazingira mazuri hata suala zima la ukusanyaji wa mapato litaongezeka. Hata hivyo, ni azma ya Serikali Mheshimiwa Mbunge wala usihofu tutaangalia nini kifanyike kuhakikisha mgao wa dawa katika eneo lile ambapo tunajua fedha nyingi sana zinaenda vijijini kuwasaidia Halmashauri ya Mbulu Mjini kuweza kuongeza ule mfuko wao wa dawa ili waweze kupata huduma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ajenda ya upatikanaji wa ambulance, naomba nimhakikishie tutashirikiana na dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya pale tutakapopata gari aina yoyote tutawapelekea. Kwa kweli nimefika kule na nimeona changamoto kubwa katika eneo hilo lazima tupate usafiri.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa madaraja katika maeneo mengi nchini ikiwemo Jimbo la Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Gunyoda katika Jimbo la Mbulu Mjini linahitaji zaidi ya shilingi milioni 700 na hadi sasa ni mwaka wa nane (8) Serikali ikiombwa kujengwa daraja hilo. Je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kuja na mpango mkakati kupitia TARURA na TANROADS ili kuainisha baadhi ya madaraja ambayo yanakwamisha huduma za jamii ili kuweza kutatua tatizo hili kwa nchi nzima?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Issaay tumeshafika Jimboni kwake takribani mara kadhaa na mwezi mmoja na nusu uliopita nilikuwa kule na kweli wana changamoto hizo. Nadhani kwa juhudi yake aliyoifanya na mwenzake kule Mheshimiwa Flatei walikuwa na changamoto kubwa la Daraja la Magara ambapo leo hii Serikali imeshasikia na kuweza kujenga lile daraja la Magara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? Ni mpango wa Serikali maeneo yote yenye vikwazo aidha kupitia TARURA au kupitia TANROADS kuondoa changamoto zilizopo na mpaka sasa kazi kubwa imefanyika maeneo mbalimbali. Nimtoe hofu Mheshimiwa Zacharia ni mpango wa Serikali kupitia TARURA na TANROADS kuhakikisha tunaondoa vikwazo kwa wananchi ambao wanashindwa kusafiri katika maeneo hayo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la makorongo na mahitaji ya madaraja katika majibo ya vijijini imekuwa kubwa sana na kwa kuwa maeneo haya yanatatiza na kuzuia huduma za jamii nyakati za masika, katika Jimbo la Mbulu Mji kuna Daraja la Gunyoda linalounganisha Halmashauri ya Mbulu Mjini na Halmashauri ya Mbulu Vijijini; mahitaji ya ujenzi wa daraja lile ni zaidi shilingi milioni 600 na kwakuwa fedha tunazopata kutoka TARURA kwenye jimbo la Mbulu Mji ni shilingi milioni 600 na hazitaweza kusaidia ujenzi wa daraja hilo pamoja na maeneo mengine nchini. Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka mpango mkakati kwa kuainisha baadhi ya maeneo hayo ili tuweze kutatua tatizo hili linalokwaza jamii katika kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema katika swali lake kuna maeneo ambayo yanauhitaji maalum na kiasi cha fedha ambacho kinatakiwa kitumike kingi na yeye mwenyewe katika swali lake anasema kiasi ambacho TARURA Wilayani kwake wanapangiwa kiasi kidogo, ni vizuri tuendelee kushirikiana tuone maeneo hayo ili tuwe na mpango mahususi katika kuhakikisha sehemu ambazo inahitajika fedha nyingi ili kuwe na andiko maalumu kwa ajili ya kutatua maeneo yenye matatizo makubwa kama hayo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu na Serikali nzima, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kazi kubwa wanayofanya katika nchi yetu hususani Jimbo la Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu madogo ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mahitaji ya umeme katika Jimbo la Mbulu Mji ni makubwa; na kwa kuwa Jimbo la Mbulu Mji sehemu nyingi zilikosa umeme wakati wa REA I na II. Je, sasa Serikali inachukua hatua gani kwa wale wananchi ambao hadi sasa wameendelea kuachwa na umeme umeshapita kwenye maeneo yao na maombi yao hayajibiwi na Ofisi yangu ina orodha kubwa sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mahitaji ni makubwa sana ya chombo kinachoitwa UMETA (Umeme Tayari) na kwa kuwa majengo mengi katika Jimbo la Mbulu Mjini yako mbalimbali kwa maana ya nyumba za wananchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta chombo hiki cha UMETA kwa kiasi kikubwa ili kuwapatia wananchi umeme ambao wana uhitaji mkubwa sana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini. Nampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo lake hususani katika kufuatilia sekta ya nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ameuliza Serikali ina mpango gani kwa kuwa mahitaji ya umeme ni makubwa na kwa maeneo mbalimbali ambayo hayajafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Serikali yetu kuna Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B ambapo Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa 16 ambayo itahudumiwa. Kwa sasa Mshauri Elekezi Multiconsult na Norplan wanaendelea kuhakiki vitongoji katika maeneo mbalimbali. Mradi huu utafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa Euro milioni 100 na unatarajiwa kuanza mapema mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sambamba na miradi ya REA III ambayo itaendelea kupitia TANESCO, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada hizi na huu Mradi wa Ujazilizi kwenye maeneo ambayo umepita vitongoji vimeachwa, Jimbo lake la Mbulu Mjini nalo litazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia masuala ya kifaa kinachoitwa UMETA. Kwanza Serikali kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA III, Mzunguko wa Kwanza vimetoa UMETA 250 kwa kila mkandarasi ambapo vinagaiwa bure kwa makundi maalum. Sambamba na hilo, kwa kuwa tumeona uhitaji ni mkubwa Shirika la TANESCO na REA wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha UMETA inapatikana kwa bei nafuu ambayo ni Sh.36,000 ambapo kila mwananchi ana uwezo wa kumudu.

Kwa hiyo, niendelee kutoa maelekezo kwa niaba ya Waziri wa Nishati, TANESCO na REA kuendelea kusambaza UMETA hasa kwenye taasisi za umma ambazo hazina mahitaji makubwa na wananchi wa kawaida. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Hospitali ya Mji wa Mbulu ni Hospitali iliyokuwa inahudumia Wilaya ya Babati, Karatu na Mbulu. Hospitali hiyo iliyojengwa toka enzi za koloni imekabiliwa na changamoto lukuki, moja ya changamoto iliyoko ni uchakavu wa gari la ambulance, na kwa kuwa Hospitali hiyo iko mpakani mwa Jimbo la Mbulu Vijijini, Jimbo la Karatu na Jimbo la Babati na Hospitali za Rufaa ni Haydom na KCMC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mbulu inashindwa kusafirisha wagonjwa wake, kutokana na upungufu wa wataalamu na vifaa chakavu.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri ataisaidia Hospitali ya Mji wa Mbulu kuipatia gari la ambulance?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Issaay kwa swali lake zuri, kuhusu hali ya Hospitali ya mji wa Mbulu hasa upatikanaji wa gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeagiza na yanakaribia kuingia nchini magari ya wagonjwa hamsini kwa hiyo naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha gari moja linaenda Mbulu na kwa Waheshimiwa Wabunge ambao labda mnataka pia kuomba Ambulance, tumeagiza tena ambulance hamsini, kwa hiyo tunatarajia kuwa na magari ya wagonjwa mia moja, tutayagawa katika maeneo ya vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo nitaomba tu wenye maswali kidogo watuvumilie tutakapoleta orodha ya mgao wa Ambulance basi tutaweza kuongeza zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Daudi na Tlawi. Hata hivyo, katika swali langu la msingi nilikuwa nimeomba kituo hiki kwa ajili ya tarafa kwa sababu Jimbo la Mbulu Mjini lina tarafa tatu, tarafa mbili zimeshapata vituo vya afya ambavyo ni vituo pekee katika Jimbo la Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Tarafa ya Nambis ambayo iko pembezoni kama sehemu ya vijijini haina kituo cha afya na ina zahanati mbili tu katika kata hizo nne. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutafuta fedha za dharura ili walau zahanati moja katika zile mbili kwenye tarafa hiyo ikapandishwa hadhi na kuongezewa majengo na miundombinu mingine ya huduma ili wananchi hao wapunguziwe adha ya kusafiri mbali na huduma bora zaidi za afya?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; katika mpango wa awali wa vituo viwili vya afya; Kituo cha Afya Tlawi na Kituo cha Afya Daudi, Serikali ilikuwa na nia njema ya kupeleka vifaatiba na vitendeakazi vya milioni 440. Je, ni lini sasa Serikali yetu itakamilisha upelekaji wa vifaa hivi vya milioni 440 katika Vituo vya Afya Daudi na Tlawi ili kuweza kuboresha huduma ya afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Zacharia amekuwa ni mfuatiliaji sana na hata wiki iliyopita tulikuwa pamoja kujadili mambo mbalimbali katika jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, saula la jinsi gani tupate fedha za haraka, naomba Mheshimiwa Mbunge nikuahidi kwa sababu kwanza ufahamu kwamba juzijuzi tulikuwa twende wote pamoja kule Jimboni Mbulu lakini kulikuwa na mkutano ule wa Ma-DC ambao ulikuwa unafanyika tumeshindwa kwenda. Kwa hiyo, ahadi yetu tunatarajia Mwezi wa Sita tutaenda hata ikiwezekana site hiyo tutaweza kufika. Lakini kikubwa zaidi tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo tutafute fedha kuisaidia hilo eneo ambalo umezungumza kwa lengo kubwa la kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, agenda ya vifaatiba ni kweli tumejenga vituo takribani 352 na katika vituo hivyo vituo 44 vya kwanza vimeshapata vifaa lakini vituo vingine bado vifaa vinakuja. Kwa hiyo, tutafanya kila liwezekanalo vituo vyote 352 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo Mheshimiwa Rais amevijenga vyote vitapata vifaa kwa lengo kubwa wananchi waweze kuhudumiwa vizuri. Kwa hiyo, usipate shida Mheshimiwa Issaay, tunalifanyia kazi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Swali langu, barabara hii iliyojibiwa na Serikali muda huu ina miaka miwili kwenye bajeti ya Serikali na barabara hii tumeiombea kura kwa maeneo yote ya Majimbo matano ambamo barabara hii inapita.

Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu kwa majibu ya Wizara kwa kuwa tumebakiza miezi minne ya bajeti ya mwaka huu wa fedha unaoisha. Je, Serikali haioni kuwa kitendo cha kuombea barabara hii kura kutoka Karatu, Mbulu Mji, Mbulu Vijijini mpaka Maswa inawapa changamoto na imani ndogo wananchi wanaotuchagua na kutufikisha hapa tulipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara hii ninayoizungumza sisi Mbulu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi na viongozi wengine wakuu, walipokuja kwenye kuomba kura walitegemea sana kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa barabara hii kuanzia Jimbo la Karatu, Jimbo la Mbulu Mji na Jimbo la Mbulu Vijijini hadi huko Maswa. Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa kujibu kiu na imani ya wananchi wa Majimbo yote matano kwa barabara hii ambayo ni muhimu iliyoko juu ya bonde la ufa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza, lakini nimshukuru Mungu sana na nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani kunipa nafasi ya kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, napenda nimjibu ndugu yangu wa Mbulu kwamba anafahamu na wananchi wa Mbulu na Manyara kwa ujumla wanafahamu juhudi za Serikali kuweza kuwakwamua wananchi kwa kujenga na kuimarisha barabara za maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba katika juhudi za kuwasaidia wananchi wa Mbulu tumejenga daraja la maghala kwa gharama kubwa na wananchi sasa wanapita.

Mheshimiwa Spika, lakini siyo hivyo tu tumejenga daraja la Sibiti kwa nia ya kuwanusuru wananchi katika maeneo hayo, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wanafahamu na wanaona na maboresho ya barabara katika barabara hizi ukitoka Karatu kuja Mbulu kupita Kilimapunda barabara zimeimarishwa ili kuwasaidia wananchi katika uzalishaji kwa ajili ya utalii, kwaajili ya kilimo na nataka kusema hivyo kwa ajili ya vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali inafanya juhudi kubwa kuwasaidia wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hata hizo kilomita 50 ambazo zimewekewa mpango kazi wa kujengwa, kilomita 50 ilikuwa ni kipaumbele kwa kuwasaidia wananchi ambao kuna sehemu kubwa wanazalisha mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika,kwahiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi niwatoe tu hofu, mpango ambao upo, majibu mazuri ya Naibu Waziri aliyoyajibu hapa ikitekelezwa kwa kweli wananchi tunaenda kuwasaidia sana. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Niishukuru Serikali kwa mpango wake wa kujenga mahakama kule Mbulu, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbulu iko ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 30 na kwa kuwa barabara hiyo ya kwenda Haydom iko kwenye mpango wa kutangazwa tender kwa kiwango cha lami. Je, Serikali ni lini itakuja kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ili kuondoa kadhia hii ambayo itasababisha huduma kusimama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia na ninajibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali tunatambua changamoto ya ulinzi au changamoto ya ukosefu wa Kituo cha Polisi hilo eneo ambalo Mheshimiwa amelitaja, lakini kikubwa nimuambie kwamba moja ya miongoni mwa kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inawapelekea wananchi huduma za ulinzi na usalama. Nimhakikishie mbele ya Bunge lako hili kupitia Wizara yetu, Kituo cha Polisi Mbulu kitafika na wananchi wataendelea ku- enjoy ama kupata huduma za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya miundombinu inayoikabili Jeshi la Polisi nchini inaikabili sana Wilaya ya Mbulu. Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Mbulu kilijengwa mara baada ya uhuru, kwa sasa kina uchakavu mkubwa. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili la uchakavu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Mbulu na makazi ya askari katika Wilaya yetu ya Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kama Serikali na Wizara ni kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama wa nchi unaenea kila mahali. Hilo la kujenga vituo vya polisi na kuvipatia magari, yote ni sehemu ya jukumu na wajibu wetu. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge, awe na subira kidogo kwa sababu kasungura bado kadogo lakini kakija kakichononoka kidogo, basi hilo ni jambo ambalo linawezekana na tukipata fedha ya kutosha, basi tutampelekea kituo cha polisi na huduma nyingine za polisi katika Jimbo lake. Nashukuru.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa Serikali italeta mashine za CT-scan na MRI kwa ajili ya Hospitali za Mikoa hususan Mkoa wa Manyara kwa kuwa gharama ni kubwa za wagonjwa wa magonjwa makuu kwenda kwenye Hospitali za kKnda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kutoka Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema hata kwenye bajeti ya mwaka huu Serikali imejipanga, siyo tu kuweka CT-Scan kwenye hospitali za kanda, bali pia kwenye hospitali za mikoa. Tayari Hospitali ya Mkoa kama Mwananyamala; na sasa hivi tunavyozungumza nilikuwa naongea na Meneja wa MSD, kuna CT-Scan mbili ambazo ziko njiani kwa ajili ya kufunga kwenye hospitali mbili za mikoa; na jinsi fedha zitakavyokuwa zinapatikana, Serikali itahakikisha kwamba hospitali zote za mikoa zinapata CT-Scan na hasa tutazingatia umbali kutoka CT-Scan moja kwenda nyingine ili kuhakikisha kwamba zinawekwa kwenye angle ambazo zitapunguzia wananchi adha ya kwenda mbali kufuata CT-Scan.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Naibu Waziri, tatizo hili la watoto kutelekezwa limekuwa kubwa sana kuzalisha watoto wa mitaani.

Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kutazama upya sheria za kuzuia uwepo wa watoto wa mitaani kwa ajili ya wale wanaotelekeza watoto? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Issaay kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua kwamba tatizo hili ni kubwa na tunakiri kwamba kuna haja ya kufanya kitu cha ziada hapa kuweza kulidhibiti. Niseme kuelekea tarehe 16 Juni, 2021 tunapokwenda kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika, hili nalo tutaliangalia tuliwekeje. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana; pamoja na majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo yanaeleza ni walimu kumi tu wa sayansi walioajiriwa kwa muda wa miaka mitano hali inayopelekea wanafunzi wengi wa Jimbo la Mbulu Mji na maeneo mengine nchini kushindwa kufanya mazoezi ya sayansi, na kwa kuwa tatizo hili limewagharimu wananchi kwa muda mrefu kwa ajili ya kuwachangia walimu wa kujitolea katika shule za Halmashauri ya Mji wa Mbulu.

Nini kauli ya Serikali ya kutusaidia walau tatizo hili linapungua katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu pamoja na maeneo mengine nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa tupo kwenye mchakato wa ajira na majibu ya awali nilipofuatilia Wizarani walikuwa wamesema tuna walimu wengi wa sayansi na tatizo hili limewagharimu wanafunzi hao wasifanye vizuri.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa nafasi pekee ya kuondoa walau kiasi kikubwa cha upungufu wa walimu kwa shule za sekondari katika Jimbo la Mbulu Mji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza alikuwa nataka kujua kauli ya Serikali ya kupunguza tatizo la walimu wa sayansi hususan katika eneo lake lakini na maeneo mengine nchini; ni kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba Serikali itaendelea kuajiri walimu na tutaendelea kuangalia kada mbalimbali hususan kada za walimu wa sayansi pamoja na wataalam na mafundi sanifu wa maabara ili tuweze kuwasaidia.

Kwa hiyo, miongoni mwa vigezo ambavyo tumevizingatia sana ukiacha vile vigezo vya awali ambavyo tulivitaja ikiwemo watu kukaa muda mrefu ambao hawajapata ajira, lakini miongoni mwa vigezo ambavyo tunavitumia sasa hivi ni pamoja na ku-consider walimu wa sayansi katika ajira hizi ambazo tutazitoa hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nimtoe wasiwasi tu kwamba Serikali tutaendelea kuwapanga katika maeneo yote ikiwemo katika eneo lako la Mbulu Mji. Kwa hiyo, hilo niahidi kwa Wabunge wote kwamba tutazingatia Majimbo yote katika kipindi hiki kuwaletea walimu wa sayansi lakini hatutawaacha na walimu wa arts ambao wamesoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba alitaka tu kujua ni namna gani tunawasaidia kuwatoa. Jukumu kubwa ni kwamba Serikali itaendelea kuajiri kulingana na upatikanaji wa fedha na kadri tutakavyoajiri ndivyo ambavyo tutaendelea kuwapanga, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mgawanyo huu ulifanyika mwaka 2015/2016, ni miaka mitano, sita sasa; na kwa kuwa hadi sasa hakuna tamko la wazi la Wizara kuwasilishwa mbele ya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri zote mbili ili kuondoa hali ya madeni mbalimbali na rasilimali nyingine na mkanganyiko uliopo: -

Je, ni lini sasa Wizara itawasilisha mgawanyo huu kwa waraka maalum wenye GN mbele ya Mabaraza hayo mawili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika mgawanyo wa rasilimali tulizopokea ni pamoja na watumishi; Halmashauri ya Mji Mbulu sasa inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi takribani miaka sita sasa kwa ajili ya hizo asilimia 40 ambapo wengine wamestaafu na wengine wamefariki kwa sababu mbalimbali: -

Je, lini sasa Serikali itaondoa tatizo hili la upungufu wa watumishi hawa angalau kwa awamu katika sekta mbalimbali katika Halmashauri yetu ya Mji wa Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay katika swali lake la kwanza alikuwa tu anataka kwamba kujua ni lini Serikali itatoa tamko la wazi ambalo litawasilishwa katika mabaraza ili kutoa waraka maalum ili hizi Halmashauri mbili ziweze kujua sasa zimeshagawanyika rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, kwa sababu jambo hili limefanyika muda mrefu, ninaiagiza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba waandike hili tamko la wazi haraka iwezekanavyo na ndani ya miezi mitatu jukumu hilo tutakuwa tumeshalifanya na mabaraza hayo mawili yatakuwa yamekaa ili wawe wanajua kabisa rasmi wameshaganyika. Kwa hiyo, ndani ya miezi mitatu tutakuwa tumeshalitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni kero ya watumishi wachache katika eneo lake na anataka kujua Serikali itatatua lini tatizo hili; niseme tu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, tutashirikiana kwa Pamoja, kwa sababu wanaotoa kibali cha kuajiri watumishi ni Ofisi ya Raisi Utumishi na Utawala Bora na sisi jukumu letu ni kupata hao watumishi na kuwapangia vituo na maeneo ya kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale ambao tunaendelea kuwajiri kama ambavyo tumekuwa tukiendelea kuajiri walimu, tumekuwa tukiendela kuajiri watumishi katika kada ya afya, tunaendelea kuwaleta katika Halmashauri zetu nchi kwa kadri tutakavyokuwa tunapata kulingana na kibali tunavyopewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuleta watumishi katika eneo lako kwa kadri tutakavyokuwa tunapewa kibali na bajeti ya Serikali inavyohitaji. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kupitia Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; nini kauli ya Serikali kwa kuwa Daraja la Gunyoda limepoteza maisha ya wakazi wa Jimbo la Mbulu Mji hasa nyakati za masika? Kwa kuwa daraja hilo ni kubwa na linaunganisha halmashauri mbili imekuwa kikazo kikubwa sana kwa huduma za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tatizo la kuongezeka kwa makorongo katika nchi yetu limekuwa kubwa na tatizo hili linachochewa na mabadiliko ya tabianchi. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma Watalaam wa Wizara, Mkoa na Halmashauri zote nchini ili wafanye mapitio upya katika maeneo haya ili waandae mpango wa kuzuia kuongezeka kwa makorongo, lakini pia na ujenzi wa maeneo ambayo yatapewa kipaumbele katika bajeti za Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza anataka kauli ya Serikali juu ya hilo korongo ambalo linatakiwa kujengwa daraja. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Serikali ya Awamu ya Sita, moja ya kazi yake kubwa ambayo tumekubaliana kuifanya sasa hivi ni kuunganisha maeneo yote kwa kujenga madaraja hususani katika maeneo korofi. Kwa hiyo na daraja hili katika mpango wa fedha wa mwaka unaofuatia tutaliweka katika vipaumbele vyetu kuhakikisha daraja hili na lenyewe linapatiwa fedha ili liweze kujengwa kwa umuhimu ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema hapa kwamba daraja hili linaunganisha halmashauri mbili kwa maana ya Mbulu Mji na Halmashauri ya Mbulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lilihusu maongezeko ya makorongo, akawa anataka Serikali tufanye tathimini upya kwa kutuma watalaam ili tuweze kuzuia uendelezaji huu. Moja; nipokee kama ushauri kwamba sisi kama Serikali tumepokea, lakini la pili; ni kwamba kwa hivi karibuni tulishawatuma wahandisi wetu nchi nzima kukagua na kuanisha maeneo yote korofi hususani madaraja ili tuweze kuyatengea bajeti na yaweze kupitishwa. Kwa hiyo na hili ni sehemu ya mapendekezo ambayo ameyatoa na sisi tunaendelea kuyapokea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Shule ya Msingi ya Endakoti katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ina wanafunzi 40 wa elimu maalum. Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1929 inakabiliwa na changamoto ya miundombinu. Je, ni lini Serikali itatekeleza azma yake ya kuteua shule mojawapo kila halmashauri itakayochukua wanafunzi wa elimu maalum ili vitengo hivyo viboreshwe kupata miundombinu na huduma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zacharia kwa kuona umuhimu wa watoto wetu hawa kuweza kupata mazingira wezeshi na miundombinu wezeshi ili kuweza kufikia ndoto zao. Suala la uboreshaji wa mazingira ni suala endelevu na nadhani tumeona kwenye Serikali yetu kwenye kipindi hiki kifupi kilichopita zaidi ya trilioni 1.3 tulizozipata zimeweza kwenda kwenye eneo kubwa sana la miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika kipindi kijacho, kwa vile sasa tunaandaa bajeti, tutahakikisha kwamba, maeneo haya ambayo yanachukua wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum tutakwenda kuyafanyia kazi na kuyapa kipaumbele kuhakikisha kwamba, yanapata miundombinu wezeshi, lakini vilevile na Walimu wa kutosha kwa ajili ya kuwafundisha watoto wetu. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi: -

Mheshimiwa Spika, yapata zaidi ya mwaka mmoja sasa mamlaka za Serikali za Mitaa, hususan Madiwani, hawakuweza kupata semina kwa ajili ya kuwajengea uwezo. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kutoa semina kwa Waheshimiwa Madiwani kote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Serikali kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa mara baada ya Madiwani kuchaguliwa katika mwaka 2020, maelekezo yalitolewa wakurugenzi kuhakikisha Madiwani wanapewa mafunzo kwa taratibu ambazo walijipangia wao katika halmashauri husika. Na mpaka sasa Madiwani wengi wamepata mafunzo, lakini ni kweli kuna baadhi ya halmashauri hazijafanya mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kusisitiza kwamba, halmashauri zifanye mipangilio ya ndani ya halmashauri kuhakikisha kwamba, Madiwani wanapata mafunzo hayo, lakini pia, kushirikiana na chuo chetu cha Hombolo cha mafunzo ya Local Government, ili kuhakikisha Madiwani wetu wanajua majukumu yao na mipaka yao ili kuboresha utendaji.

Kwa hiyo, jambo hilo ni endelevu litaendelea kufanyika katika ngazi ya halmashauri, ili kuhakikisha kwamba, utumishi unakwenda vizuri. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom – Mkalama – Meatu ni barabara muhimu sana kwa wakazi wa majimbo hayo niliyoyataja.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema barabara hii ya kutoka Karatu – Mbulu – Hydom - Sibiti kuja Lalagwa – Maswa – Kolandoto ni barabara ambayo inaunganisha mikoa mingi, tayari tupo kwenye manunuzi kipande cha Mbulu – Hydom. Pia Daraja la Sibiti kama nilivyojibu kwenye maswali mengine limeshakamilika na tunategemea kuongeza kilometa 20 pande zote kwenye barabara hiyo. Hali kadhalika, kuanzia Kolandoto tupo kwenye mpango wa kutafuta fedha kuanza ujenzi kutokea Kolandoto kwenda Sibiti. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitangulize masikitiko makubwa ya majibu ya Serikali. Mheshimiwa Naibu Waziri aliyejibu swali hili alijibu swali hili hili katika Bunge lililopita. Leo nilipoona swali hili limerudishwa kwa makosa kutoka swali lile la kwanza nililopenda kuuliza nikaacha kwa sababu nimetumiwa jana jioni. Lakini majibu yaliyotolewa ni tofauti kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri aliyoyatoa kule mwanzo kwenye Bunge lililopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi niiombe tu Serikali kwamba, tunachouliza hapa ni ujenzi wa Daraja la Bunyoda ambalo Serikali imepigiwa kelele kwa miaka tisa. Na Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa majibu mazuri sana kwenye Bunge lililopita, kwamba usanifu wa daraja hili ni bilioni moja na milioni mia mbili. Leo jibu lililokuja ni kwenda kufanya usanifu upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani kama Mheshimiwa Waziri atarejea kwenye majibu yake arejee, lakini kwa Bunge hili linalokuja daraja hili lisipowekwa kwenye bajeti, nadhani nitakuwa naunga mkono bajeti ambayo haina tija kwa wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ninaomba majibu ya kina ya daraja hili kujengwa kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu ndani ya Bunge hili, akisema katika mwaka wa bajeti wa 2022/2023 daraja hili litatengewa fedha bilioni moja na milioni mia mbili ambapo usanifu wake uko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pil; eneo la Mbulu Mji lina kata 10 vijijini na kata saba mjini. Eneo lote la vijijini lina makorongo makubwa. Ni lini wataalam wa TARURA na TAMISEMI watakwenda katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ili waweze kujua namna ya kuweza kutatua tatizo la makorongo linalokabili maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika maeneo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, baadhi ya maelezo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatoa tuliyatoa katika Bunge lako Tukufu, na nilishatoa maelekezo katika ngazi za chini. Kwa hiyo kitu ambacho walikuwa wameshatueleza ni kwamba walikuwa bado hawajafanya usanifu, isipokuwa walitupatia zile gharama za awali, kwamba wanakadiri daraja lile litagharimu bilioni moja nukta mbili. Kwa hiyo sisi ambacho tunahitaji ni exactly figure ili tuweze kuliweka katika bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipokee maoni na maelezo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Mbunge, na niahidi kwamba nitalifanyia kazi, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu haitakuwa tayari kulidanganya Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo hilo hatutalipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto nyongine za wananchi wa Jimbo la Mbulu kumaliza matatizo ya makorongo kwa kujenga madaraja pamoja na kurekebisha barabara, Mheshimiwa Mbunge na hili tumelipokea, tutaendelea kufanya usanifu pamoja na tathmini na kama ambavyo kiti chako kilieleza siku zilizopita uliopita, tathmini ya awali tumeshaifanya, bado tunakwenda kufanya tathmini ya kina ili kujua ukubwa wa matatizo katika maeneo yote nchini ikiwemo Jimbo la Mbulu, na sisi tutachukua hatua ya kuyakamilisha. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mahitaji makubwa ya wananchi ni kupata vitongoji vipya na vijiji vipya; na kwa kuwa mchakato huu haueleweki sana kwao, sisi tunalalamikiwa: Je, Serikali ina utaratibu gani sasa wa kugawa vijiji na vitongoji na mitaa ili kurahisisha huduma kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna mahitaji ya kugawa vijiji, vitongoji, kata na mara nyingine hata Halmashauri katika nchi yetu, lakini kama nilivyotangulia kujibu kwenye maswali ya msingi kwamba kipaumbele chetu sasa Serikali ni kuboresha kwanza miundombinu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, utaratibu ni kwamba wananchi wanafanya vikao vyao vya Halmashauri za Kijiji na kwenda DCC na RCC na baadaye kuwasilisha maombi Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, namwombe Mheshimiwa Mbunge waanze taratibu hizo za kisheria wakati tukisubiri maamuzi ya Serikali kuja kugawa maeneo mengine ya kiutawala. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza; kwa kuwa tunaelekea robo ya pili ya mwaka wa fedha sasa na jiografia ya Mlima Magara ni ngumu sana utekelezaji wake wakati wa mvua; je, Serikali imefikia hatua gani katika mchakato wa hiyo kilometa moja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Barabara ya Magara – Mbulu ina jiografia ngumu kuliko sehemu yoyote nchini na hizo kilometa 44 zilizobaki zimefanyiwa usanifu tayari kwa miaka mitatu. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mpango wake wa lami wa kilometa 44 katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuanzia Novemba mwaka huu barabara hii itakuwa imeanza kujengwa kwa kiwango cha zege kwa sababu taratibu zote za zabuni zimeshakamilika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuanza kujenga barabara yote, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kilichokuwa kimefanyika ulikuwa ni usanifu wa awali na atakubaliana nami kwamba wakati Makamu wa Rais anafungua Daraja la Magara mwezi Machi mwaka huu aliagiza barabara ile ikamilike na Juni mwaka huu ndiyo usanifu wa kina umekamilika. Kwa hiyo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili ijenge kilometa hizi 44 kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Bwawa la umwagiliaji la Edayaya Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilifanyiwa usanifu toka 2009; je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja kati ya mikakati ambayo tumeiweka hivi sasa kama Wizara, tumeiagiza Tume ya Umwagiliaji wa Taifa ku-take stock ya miradi yote ya umwagiliaji katika nchi yetu ya Tanzania ile ambayo ilishafanyiwa upembuzi yakinifu ambayo ilishafanyiwa usanifu na baadaye kinachofanyika ni kwamba tutakwenda katika mradi mmoja baada ya mwingine iko miradi ambayo inahitaji fedha kidogo na iko miradi ambayo inahitaji fedha nyingi.

Mheshimiwa Spika, kupitia maelekezo haya ambayo Mheshimiwa Waziri ameyatoa, Tume hivi sasa wameanza zoezi hilo. Tutaipitia miradi yote na hivi sasa tunayo miradi 51 ambayo imeshatangazwa kupatikana kwa wakandarasi, naamini kupitia utaratibu huu ambao tumeuanzisha, tutaifikia miradi yote ikiwemo mradi ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hivi sasa wanafunzi wa vyuo vya afya nchini kwa ngazi ya cheti na diploma wanasoma kwa ghrama kubwa. Je, ni kwa nini sasa Serikali isione namna ya kuwapunguzia wanafunzi hawa gharama katika masomo yao ya fani ya afya kwa ngazi ya cheti na diploma ili wazazi waweze kumudu gharama zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issaay, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri kwamba ni kweli kwamba upande wa elimu ya tiba ada zimekuwa ni kubwa, lakini wakati tunatoa bajeti yetu hapa, wenzetu au benki yetu ya NMB ilitoa ufadhili wa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kada hizi za kati. Kwa hiyo, eneo la kwanza naomba wazazi na walezi wa wanafunzi hawa waweze kuifikia benki hii ili waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tuko katika mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunafikia kada hii ya kati pindi tutakapoongeza bajeti kwa ajili ya wanafunzi hawa kupata mikopo vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ni miaka minne sasa nikiendelea kutetea ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu. Kwa kuwa, sasa mahakama ya Wilaya inapitiwa na ujenzi wa barabara ya lami. Je, ni lini Serikali itatekeleza azma yake ya ujenzi wa Mahakama yetu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kutoka Mbulu. Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa Wilaya ambazo ziko kwenye mkakati wa kujengewa Mahakama kwa kipindi hiki cha fedha cha 2022/2023. Kwa hiyo taratibu za kupata Mkandarasi kwa ajili ya zoezi hilo zinaendelea. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa, sasa ni miaka miwili toka Serikali itoe fedha za ukarabati wa Chuo cha Maendeleo Tango - FDC Mbulu na kwa kuwa tayari mradi wa awali umeshatekelezwa.

Je, ni lini Serikali yetu itatoa tena fedha ya ukamilishaji wa majengo hayo ya Chuo cha Tango FDC kwa awamu ya pili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mbunge wa Mbulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika majibu yaliyopita katika Chuo cha VETA kule Bunda ni hivyo hivyo kwa upande wa wenzetu wa Tango.

Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza katika fedha ambazo tulizipata za UVIKO – 19 zaidi ya Shilingi Bilioni 6.8 zimekwenda kununua vifaa kwa ajili ya vyuo hivi vya FDC (54) kote nchini, ambapo Chuo hiki cha Tango nacho vilevile kimezingatiwa.

Mheshimiwa Spika, vifaa hivi tayari tunavipeleka kwenye maeneo haya ya vyuo, vilevile upanuzi wa vyuo hivi tumeuingiza kwenye bajeti yetu ya mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo, maeneo haya yote tutakwenda kuyafanyia kazi kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinatoa taaluma ile ambayo inatakiwa katika maeneo husika.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naipongeza Serikali na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika Jimbo la Mbulu Mji. Swali langu ni dogo: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutekeleza mpango wake wa bajeti wa miaka miwili wa Kata za Gunyoda, Silaloda na Marang kuweka minara kwa kuwa alijionea hali halisi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini kuwa kata hizo ambazo amezitaja tayari ziko katika mchakato wa zabuni ambayo imefunguliwa jana. Kwa hiyo, tunaamini kwamba mchakato wa evaluation utakapokamilika, tutaelewa kwamba ni mtoa huduma gani ambaye amepatikana kwa ajili ya Mbulu Vijijini? Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Halmashauri ya Mji wa Mbulu iliko soko na stendi ni mahali pamoja kwenye kiwanja kimoja hali inayohatarisha watumiaji wa huduma na wapokea huduma katika eneo hilo.

Swali la kwanza; je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu kusogezwa kwenye kundi la pili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa tatizo hili ni kubwa na tumesubiri mradi huu kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri ana kauli gani ya kuweza kufika Mbulu na wataalam wa TAMISEMI ili waone tatizo lenyewe kwa undani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini , kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kikubwa ni kwamba makundi yote matatu yatapatiwa hizo fedha za TACTIC na miradi yote iliyoainishwa itajengwa. Jukumu kubwa tunalolifanya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sasa ni kuhakikisha miradi hii inatekelezeka kama ambavyo imepangwa katika mkakati tulionao. Niwahakikishie tu hata wale wa tier one kwa maana ya kundi la kwanza, miradi yao inaanza kutekelezeka katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi kuchelewa, niko tayari kwenda Mbulu pamoja na wataalam kwenda kujionea haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumza, ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tunaishukuru Serikali kwa kutoa chakula cha gharama nafuu. Je, Serikali ina mkakati gani kwa kaya ambazo hazina uwezo wa kununua chakula kwa sasa ili itoe chakula cha msaada?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo taratibu ambazo huwa zinapelekea Serikali kufikia hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiomba, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, zipo taratibu za kwenda ofisi ya Waziri Mkuu ambayo pia wao wamekuwa wakiwasiliana nasi juu ya namna ya kupeleka chakula hiki cha msaada katika baadhi ya maeneo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Kwa kuwa tatizo la usambazaji wa umeme kupitia Wakandarasi wa REA III mzunguko wa pili imekuwa tatizo kubwa katika Majimbo yetu. Je ,Wizara haioni umuhimu sasa wa kutusikiliza Kikanda kuona matatizo yalivyo kwenye Majimbo yetu katika mradi huu wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swalil la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilikuwa nyingi, zile za ndani ya uwezo na nje ya uwezo. Changamoto zilizo ndani ya uwezo zote tumeshazitatua. Siku chache zilizopita Mheshimiwa Waziri aliitisha kikao cha Wakandarasi wote na kutoa maelekezo, tayari wenzetu wa REA wameshapita kwenye Mikoa takribani Saba au Nane ambayo tuliona iko nyuma zaidi kuhakikisha kwamba wao, watu wa REA na watu wa TANESCO kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa lakini na Waheshimiwa Wabunge pia mlipata mialiko kwenye hayo maeneo tukae kwa pamoja ili tuone tatizo liko wapi na tuweze kusukuma shughuli hii ili tuweze kuikamilisha kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewekeana makubaliano na tunaamini ndani ya muda tutayatekeleza na tutakamilisha kazi hizo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi; je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya Karatu-Endabash-Mbulu kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja tumeshaanza kuijenga kuanzia Mbulu hadi Garbab na tunaendelea. Zabuni ziko zilishafunguliwa zinafanyiwa evaluation kutoka Labay kwenda Hydom. Kwa hiyo tayari tumeshaanza hiyo barabra lakini pia ni barabara ambayo imeingia kwenye mpango wa EPC+F na evaluation zinaendelea.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru Serikali kwa kibali cha ajira ya zaidi ya nafasi 30,000. Katika nafasi zilizotangazwa hatuna kada ya Watendaji wa Vijiji na Kata.

Je, Serikali ni lini itatoa kibali cha ajira kwa Watendaji wa Kata na Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo mbioni kuwaajiri Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata na muda si mrefu tayari tutaanza kuweza kuwa-post wale Watendaji wa Kata kwenye maeneo yenu lakini vilevile bado tena narudia rai yangu kwa waajiri ku- compile orodha ya mahitaji yao kwenye Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata na kuiwasilisha TAMISEMI kwa wakati ili waweze kuileta Utumishi ili pale zoezi hili la kuajiri hawa linapoanza basi tuweze kufidia maeneo yote ambayo yanauhitaji wa watendaji hao.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwa kuwa viwanda vilivyotajwa ni viwili tu nchini: Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kuhamasisha wawekezaji wengine ili uzalishaji wa mbolea nchini uwe mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, moja kati ya mikakati tuliyonayo hivi sasa ni kuendelea kuwakaribisha wawekezaji wengi zaidi wa viwanda vya mbolea ili kwa pamoja tusaidiane kutatua changamoto iliyoko hivi sasa ya upatikanaji wa mbolea. Tunaamini katika misimu michache inayokuja, kiwanda cha Itracom na Minjingu ambacho sisi kama Wizara tumewasaidia kuzungumza na Benki za TADB na CRDB kuongeza expansion, tutakuwa tumetatua changamoto hii ya upatikanaji wa mbolea kwa kiwango kikubwa sana. Pia bado tunakaribisha makampuni mengine, na kama Serikali tunaendelea pia kukaribisha makampuni mengi zaidi ili tuondokane na changamoto hii ya upatikanaji wa mbolea hapa nchini.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua kubwa ya wahitimu nchini wa sekta ya elimu, zaidi ya asilimia 70 ya wahitimu wa vyuo nchini ni walimu.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati mwafaka sasa wa kuhamasisha fani nyingine ili vijana wetu wanapomaliza kidato cha nne waweze kusoma fani nyingine kwa mazingira wezeshi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo anazungumza Mheshimiwa Mbunge ni kweli, na kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, kwa vile sasa tunafanya mapitio ya sera, sheria pamoja na mitaala yetu ambayo tunakwenda kuhakikisha kwamba maeneo mengi ambayo yanabeba fani za ufundi tunakwenda kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi katika eneo hilo, kwa vile amesema wengi ni walimu hata huko huko kwenye ualimu nako tukiweka na stadi zlie za kazi tunaweza tukaondoa changamoto hiyo ya ajira.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la huduma bure kwa wazee, akina Mama na Watoto limekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi yetu, na kwa kuwa wote tulioko hapa ni wazee watarajiwa leo, kesho, keshokutwa na mtondo go.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kutoa waraka wa wazi kwa ajili ya jambo hili la huduma katika makundi niliyoyataja?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tunapokea ushauri wa Mbunge na labda niseme tu kidogo kwamba, kwa mfano tunazungumzia tu wazee walioko kwenye mfumo ambao ni wastaafu 149,000 ukiwaangalia sasa hivi kwa mwaka tu wanatumia Bilioni 61 kwenye kupata huduma za afya ambayo ni asilimia 82 tu wao ndiyo wagonjwa. Kwa maana hiyo, ukizungumzia wazee wote kwenye nchi nzima nalo ni tatizo kubwa na nakubaliana naye kwamba inahitajika hela nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama ambavyo nimesema swali la kwanza la msingi tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ili kuhakikisha kwamba hayo mambo yanafuatiliwa kwa ukaribu lakini tunawaomba wenzangu Wabunge na sisi tufatilie kwa karibu kuhusu wanavyohudumiwa wazee na mkiona kwamba hawahudumiwi tupaze sauti kwa pamoja, lakini sisi tutaelekeza sheria na kusimamia na kuwaadhibu ambao wanaacha kutekeleza maelekezo ya Serikali.(Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali. Swali langu la msingi liliuliza kada zote hadi sasa kada za watendaji wa kata, vijiji na mitaa hazijapata kibali. Halmashauri ya Mji wa Mbulu ina upungufu wa watendaji wa kata, vijiji na mitaa zaidi ya 70, ni miaka mitatu sasa.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri watumishi hawa katika Halmashauri wa Mji wa Mbulu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa waalimu wa sayansi katika mgawo wa ajira mbili zilizopita za Serikali hawakupatikana katika Halmashauri wa Mji wa Mbulu kwa kigezo cha kuona waalimu wa sanaa ni wengi na wanafunzi wameendelea kukosa masomo ya sayansi. Je, Serikali ina mkakati gani au inakusudia kugawa walimu wangapi wa sayansi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kada ambazo hazijatangazwa kwa maana ya watendaji wa kata wa vijiji na mitaa lakini na kada nyingine zote zitaendelea kutangazwa kwa awamu kwa sasa tumeanza na sekta ya afya na elimu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge lengo la Serikali ni kuhakikisha kada hizo nyingine pia zinaajiriwa. Lakini pamoja na hiyo bado halmashauri zimeendelea kuajiri watendaji kupitia mapato ya ndani, baadhi ya halmashauri wataendelea kufanya hivyo kwa vibali vya Serikali Kuu pia kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na walimu wa sayansi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi ambazo tayari zimetangazwa za walimu 9800 tutaenda kuhakikisha tunapeleka walimu wa sayansi katika maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi wa walimu wa sayansi. Kwa tathmini hiyo tumeshaifanya na tutampa kipaumbele katika Jimbo lake la Mbulu Mjini, ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa swali hili zuri sana la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge, kwanza naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, kwa kibali ambacho Mheshimiwa Rais amekitoa cha kuhakikisha tunatoa ajira 32,604 ambazo zilipangwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022, baada ya kutoa ajira zile za kipaumbele kwenye sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta zile nyingine ambatanishi. Mheshimiwa Rais kupitia ofisi yetu ameridhia sasa kada zile nyingine za watumishi zilizobakia ikiwemo hao watendaji wa vijiji na kata ziweze kufanyiwa mgao kwenye ajira 7,792 ambapo bado hizo zinasimamiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba waajiri wote nchini wahakikishe tu wanapanga majukumu sahihi kwa watumishi wote wapya watakaoajiriwa ili waweze kuongeza tija na kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Karatu – Mbulu kilometa 76 kama ilivyowekwa kwenye bajeti ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti ndiyo barabara ambazo kati ya zile barabara saba ipo kwenye mpango huu wa EPC+F. Kwa hiyo, kama itakavyokuwa imekamilika basi kilometa hizo 76 itakuwa ni sehemu ya ujenzi wa hiyo barabara.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Samahani sana, naona hata majibu yaliyotolewa hayana uhalisia kabisa. Nafasi tano kwa wapishi nchi nzima na nafasi 200 za makatibu muhtasi kwa ajili ya shule ya sekondari. Katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema pia eneo hili la ajira kwa halmashauri zimepewa nafasi. Hakuna Halmashauri hata moja nchini inaajiri kada hizo.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa wazazi wengi nchini wamebeba mzigo mkubwa wa kulipa michango kupitia watumishi hawa ambao wanalipwa kwa michango ya wananchi; na kwa kuwa katika shule zetu familia moja inaweza kuwa na watoto wawili, watatu mpaka wanne, Serikali haioni kuwa ni wakati muhimu na muafaka wa kuweza kuongeza ikama ya ajira hii kwa ajili ya watumishi hawa ili kupunguza mzigo kwa wazazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika kibali cha ajira kilichotolewa juzi Serikali haikutoa kipaumbele kwa ajili ya Walimu wa kada ya kilimo…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, je, ni kwa nini Serikali haiweki kipaumbele kutoa kibali kwa Walimu wa mchepuo wa kilimo ili vijana wetu waweze kupata stadi za klimo kutoka shule za sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu tulizotoa ni takwimu sahihi na usahihi wake unakuja kutokana na ukweli kwamba, Mheshimiwa Mbunge ajira hizi zinatokea kwenye halmashauri zetu. Halmashauri ndizo zinazoomba na sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi, tunapokwenda kuomba Kibali tunaomba kwa ikama iliyoombwa tukiangalia na Bajeti ambayo imepitishwa na Bunge lako. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwanza apate kufahamu kwamba kilichoelezwa hapa ni kutokana na taarifa zilizoombwa kutoka katika maeneo yetu ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, pia pamoja na hilo tunakubaliana kiukweli kwamba hitajio la kuongeza ikama kwa ajili ya ajira hizi ambazo zimeelezwa ni jambo la msingi na sisi kama Serikali tumelisikia. Pia nimwombe tena Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, tunapokwenda kutaja vipaumbele vya maeneo yetu ya kiutawala kwa maana ya halmashauri, basi tuangalie kwamba hii ni sehemu moja wapo ya eneo muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili, juu ya walimu wa mchepuo wa kilimo. Ameeleza hapa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, wakati anatoa taarifa juu ya idadi ya nafasi za ajira zilizotolewa, iko nafasi ya ajira za Walimu, ziko nafasi za eneo la afya. Katika eneo hili la elimu naamini kabisa kama kipaumbele ndani ya halmashauri zetu kitaainishwa wazi, kwamba tunahitaji Walimu watakaokwenda kusaidia kusimamia eneo la kilimo, basi sisi kama Serikali sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tuko tayari kwenda kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba malengo ya kuhudumia wananchi wetu yanakamilika. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa zoezi la ukaguzi wa ubora wa dawa linafanyika katika vituo vya wauza dawa nchini, kitendo ambacho kinaleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara hawa;

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa ubora wa dawa katika hatua za mwanzo kwenye viwanda ili wafanyabiashara wasipate hasara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, moja ni kwamba, kwenye kudhibiti suala la dawa na wafanyabiashara ya dawa wenzetu wakati mwingine wanaangalia kutengeneza faida kuliko usalama wetu sisi watumiaji. Kwa hiyo suala la wao kuendelea kusimamiwa kwa nguvu na kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu ni lazima tuwasimamie namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekuwa na mjadala wa kuhakikisha sasa badala ya kuwepo na wafamasia kwenye maduka ya dawa ambao wanaweka vyeti vyao, tubadilishe hiyo sheria iwe sasa mfamasia anaajiriwa kwenye duka husika na anakuweko pale kuhakikisha usalama unakuweko, na hasa kazi ya ukaguzi inakuwepo kwa mambo ambayo hayaendani na utaratibu yanazuiliwa mapema.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, swali langu ni dogo; kwa kuwa huduma ya treni ya mwendokasi nchini inasubiriwa kwa hamu kubwa sana.

Je, ni lini shirika hili litaanza kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Reli yetu ya TRC hususan katika mradi wetu wa SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma awamu ya kwanza tutaanza kutoa huduma kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro. Hivi ninavyosema tumeshafanya testing katika vituo vyote signal na treni la Mkandarasi na kwa maana hiyo tunachosubiria sasa ni kuja vichwa na hivi vichwa tunategemea vitakuja ndani ya mwezi ujao ili ianze kufanya hii station ya SGR, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa tatizo hili la uhaba wa hosteli katika shule za Serikali nchini limekuwa kubwa sana;

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuwa una haja kubwa ya kupeleka timu katika halmashauri zote ili kuratibu na kuona upungufu ulivyo mkubwa na hatimaye kuja kuiweka kwenye mipango ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimpongeze Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kwa maoni ambayo ameyatoa. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeyasikia na hivyo itayafanyia kazi kwa kuunda timu maalum ambayo itazunguka maeneo yote ili ipitie na kugundua ukubwa wa changamoto ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipande cha barabara ya lami kutoka Mbulu Garbabi, kazi ya Mkandarasi imesimama kwa miezi minne; je, ni lini mkandarasi yule ataanza kazi ile rasmi ili barabara hiyo iweze kutekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema hii, ni kweli kulikuwa kuna changamoto ya mvua na pia mkandarasi alikuwa hajalipwa fedha zake alizokuwa anadai. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunavyoongea sasa hivi mkandarasi ameshaanza kazi ya Mbulu kwenda Garbabi na tunategemea muda wowote kuanzia sasa tutasaini mkataba wa Labay kwenda Haydom, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi. Naishukuru Serikali kwa majibu. Je, Serikali haioni kuwa sasa shule zetu za sekondari za kata zimekuwa na wanafunzi wengi wasiopata kuendelea na masomo ya juu na kwa hiyo, vijana hao wangekuwa sehemu moja ya kuwajengea uwezo wale wanafunzi walioko shuleni kwa kuanzisha mashamba madogo ya majaribio na mafunzo katika shule hizo katika kanda na wilaya zetu? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna mchakato unaendelea wa mapitio ya sera ya elimu, nami naishukuru Wizara ya Elimu kuweza kuchukua component ya agriculture kuwa sehemu ya mapitio haya ya sera. Mawazo kama haya tutaendelea kuyapokea na siwezi kutoa commitment sasa hivi kwamba tutaanza kuweka mashamba darasa katika kila sekondari, lakini ni wazo na ninashukuru, nasi kama Serikali tumelipokea.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimehudumu kwenye Kamati hii miaka miwili na nusu, Jeshi letu la Polisi linakabiliwa sana na uchakavu wa muindombinu ya vituo vya Polisi pamoja na makazi ya Askari kote nchini ikiwemo Jimbo la Mbulu Mji Manyara.

Je, ni mkakati upi wa Serikali wa kuondoa tatizo la uchakavu wa majengo ya Askari kote nchini?
NAIBU WAZIRI WA AMAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba baadhi ya vituo vya Polisi majengo yake ya vituo ni chakavu na nyumba za Askari ni chakavu. Kwa msingi huo Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi limeandaa mpango mkakakti wa miaka 10, kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vituo vilivyochakaa na nyumba Askari zilizochakaa, kwa hivyo kama eneo lako Mheshimiwa Mbunge pia lina changamoto hii litafikiwa. Tunashukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa matibabu ya ugonjwa wa figo nchini yakemkuwa na gharama kubwa sana na kwa kuwa bima ya afya kwa sasa haitoi huduma ya ugonjwa huu; je, ni utaratibu upi mbadala wa Serikali ili kusaidia kundi la wananchi wa ngazi za chini kwa sababu ugonjwa huu unawakabili rika mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda nimwambie kaka yangu kwamba bima ya afya inatoa huduma hiyo, ndio maana katika presentation tuliyowasomea Wabunge, utaona eneo linalotumia fedha nyingi kwenye eneo la bima ni eneo hilo, lakini liawezekana Mbunge anamaanisha Bima ya Afya ya CHF ambayo ndio iko kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ile bima ya afya ya CHF na tulitaka tuitafute namna ya kuiboresha iweze kuwapa wananchi manufaa mazuri zaidi. Kama ambavyo nimesema kwenye maswali ya nyongeza, kwamba utaratibu ni ule ule. Niendelee kusisitiza Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuendelee kuwa mabalozi wazuri wa bima ya afya kwa watu wote kwa sababu ndipo tutakapoweza kupata suluhisho la kudumu kwa matatizo haya.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ni Mahakama chakavu sana iliyojengwa toka enzi za mkoloni; na ni miaka mitatu nimekuwa nikiendelea kuomba ujenzi wa Mahakama hiyo: Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea Mahakama Wilaya ya Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Issaay Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha, miongoni mwa maeneo tutayokwenda kujenga, tunategemea kujenga Mahakama 18 za Wilaya. Wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa Wilaya ambazo tutajenga Mahakama hii. Kweli eneo lao lile, jengo la Mahakama lipo pembeni ya barabara na kimsingi linatakiwa litoke pale. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba huu mpango tunao na tutajenga katika mwaka huu wa fedha. Upo kwenye list yetu. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Changamoto hii ya ukosefu wa dawa imetugharimu sana kwa wananchi: Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuweka alama dawa za Serikali ili kudhibiti upotevu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kuweka alama limekuwa ni endelevu na dawa zote za MSD zimekuwa na alama. Ninachoweza kumwomba Mheshimiwa Mbunge, kwenye Baraza la Madiwani suala la dawa na vifaa tiba liwe ni ajenda ya kudumu. Pia nawaomba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hilo liwe ni ajenda ya kudumu, kwa sababu ni ukweli kwamba upungufu mkubwa unasababishwa na matumizi mabaya ya fedha yanayopatikana baada ya kuuza huduma na dawa zenyewe, na pia baadhi ya dawa kuibiwa kwenye vituo vyetu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na hatua hiyo ya kuanza ujenzi. Mimi nina swali moja tu.

Mheshimiwa Spika, katika Tarafa ya Nambisi kuna Mahakama chakavu katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Je, utaratibu wa Serikali ukoje wa kukarabati majengo ya Mahakama katika Tarafa zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa pongezi hizo.

Mheshimiwa Spika, mhimili wetu wa Mahakama una mpango wa miaka mitano wa kukarabati na kujenga majengo ya Mahakama kote nchini na katika mpango huu Mtendaji Mkuu wa Mahakama akishirikiana na Watendaji wa Mikoa wanafanya wanafanya utafiti katika Tarafa zote nchini zaidi ya Tarafa 500 na Kata zaidi ya 3,000 kuona ni wapi ambapo kuna mashauri mengi na umbali, tafiti hii tutakapokamilisha tutakuja sasa na list ya kwamba wapi tuanze.

Mheshimiwa Spika, ninafahamu kwamba hata Nambisi ambako Mheshimiwa Mbunge amepataja kuna uhitaji naomba avute subira tuweze kukamilisha tafiti hii halafu tutamwambia kama hapo tutakwenda kujenga. (Makofi)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naishukuru Serikali kwa kuwa tayari Mkandarasi wa REA katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ameshasimika nguzo kwenye vijiji vyote yapata miezi minne. Je, ni lini sasa wananchi wale wa Vijiji vya Mbulu Mjini watapewa umeme kwa kuunganishiwa nyaya na kuunganishiwa umeme kwenye makazi yao?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema miradi yote ya REA three round two itakamilika kufikia Desemba mwaka 2023 lakini kwa nyakati tofauti tofauti vijiji mbalimbali vitaendelea kuwashiwa umeme. Kama alivyosema Mheshimiwa Issaay hayo maeneo ambayo tayari wameshasimika nguzo tunatarajia kwenye mwezi mmoja mpaka miwili tayari kazi itakamilika wakati maeneo mengine tunaendelea kuchimba, kusimika nguzo na kuunganisha umeme, lakini ifikapo Desemba kazi yote itakuwa imekamilika.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali; je, mpango ukoje kwa Bima ya Afya kwa Wote kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa hawa wa magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa bima ya afya ulikuja hapa kwa ajili ya sisi kuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuweza kabisa kuboresha mambo mengi ambayo yangeweza kusaidia pamoja na eneo hili tunaloliona. Kwa hiyo kikubwa mimi na wewe tuendelee kushirikiana kuona ni namna gani tunapambana kupeleka Muswada wetu wa Bima ya Afya kwa Wote uweze kurudi na iwe ajenda ya Mbunge ya kudumu na ajenda ya kudumu ya Wabunge ili wananchi waweze kupata huduma tukija na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara – Mbulu ni muhimu sana inayounganisha Mkoa wa Manyara na Wilaya za Mbulu na Mji wa Arusha: Je, kwa nini Serikali imeshimdwa kutekeleza eneo la mlima Magara ambalo lina jiografia ngumu sana na inatumia gharama kubwa kwa kiwango cha changarawe? Lini itaweka lami mlima Magara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara hadi Mbulu ni barabara ambayo inapita kwenye escarpment. Mheshimiwa Mbunge atakuwa ni shahidi kwamba tunachokifanya sasa hivi, ni kukamilisha eneo lote la ule mwinuko kujenga kwa kiwango cha lami au kiwango cha zege. Baada ya kukamilisha hayo maeneo ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa, mpango sasa ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami, kwani usanifu tayari umeshafanyika, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa posho ya Waheshimiwa Madiwani inayotumika hivi sasa ni shilingi 350,000 imekaa takribani miaka kumi sasa.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza posho ya waheshimiwa Maadiwani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa halmashauri nyingi nchini zinapata mapato madogo, ikiwemo halmashauri ya Mbulu, na kushindwa kulipa posho ya wenyeviti wa vijiji na mitaa;

Je, Serikali haioni kuwa ndio wakati muafaka wa kutazama jambo hili ili kila halmashauri nchini zitekeleze takwa hili la kikanuni kwa mujibu wa huduma wanazotoa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issaay, kwanza kuhusu hili la posho kuwa zimekuwa ni za muda mrefu. Mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Serikali kuu ilichukua jukumu la kulipa posho hizi Madiwani moja kwa moja kutoka hazina, hivyo, kuwapunguzia mzigo mamlaka hizi za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupunguza hilo, na kwa sababu ni jambo la kisheria na Mheshimiwa Issaay ni Mheshimiwa Diwani kwenye halmashauri yake ilitakiwa wakae ili zile fedha am,bazo wanafanya saving baada ya Serikali Kuu kuchukua la kulipa posho za Madiwani waone ni namna gani wanatenga kwa ajili ya wenyeviti wao wa vijiji na wenyeviti wao wa mitaa n.k.

Mheshimiwa Spika, pia, fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa kutoka Serikali kuu. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi kwenye miundombinu, afya na elimu. Hivyo, halmashauri nyingi zimepunguziwa ule mzigo mkubwa. Ni wajibu wao kutenga na kuhakikisha wanalipa kama inavyosema Sheria ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nikimalizia kujibu swali lake la kwanza la nyongeza, mwaka huu wa fedha tunaokwenda kuuanza wa 2023/2024 Serikali Kuu vile vile, imewapunguzia mzigo halmashauri zote nchini kwa kuanza kulipa zile stahiki za wakuu wa idara, na zitaanza kulipwa moja kwa moja na Serikali kuu. Hivyo, kuwaacha halmasahuri kuwa na uwezo wa mapato zaidi na kuweza kutenga fedha za kulipa wenyeviti hawa na madiwani vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, linalohusu mapato kuwa madogo. Halmashauri huanzishwa kwa mujibu wa sheria; na moja ya kigezo kikubwa cha uanzishwaji wa halmashauri au mamlaka za Serikali za mitaa ni uwezo wake wa kukusanya mapato. Vile vile, huwa wanaainisha vyanzo zaidi ya 30. Na kwa mujibu wa Sheria ile Na. 287 ya Mamlaka za Wilaya, 288 Mamlaka za Miji inaelezea wazi. Vile vile, Sheria ile ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Kifungu cha (6) (7) (8) na (9) inaelezea wazi namna ambavyo wanatakiwa kubanana kuweka mapato yao sawa.

Mheshimiwa Spika, ukisema kila kitu kichukulliwe na Serikali Kuu ina maana dhana nzima ya D by D inakuwa imeondoka.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hivi sasa kampuni ya Kichina inatekeleza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbulu kwenda Garbabi kilometa 25, lakini barabara hiyo kwa jiografia ya milima inahama kwenda nje ya mita 22.5 kutoka katikati ya Barabara: Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kwenda kuwaelimisha wananchi ili tujue wanaofidiwa na wasiofidiwa ndani ya corridor hiyo ya barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyo utaratibu kwamba pale ambapo tunajenga barabara tunatumia sheria za barabara na hasa kwenye kutoa fidia. Kwa wananchi ambao wako ndani ya mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kwa pande zote wanakuwa wako kwenye hifadhi, lakini wale ambao wako mita 7.5 kwa pande zote ambazo zimeongezeka, barabara inakuwa imewafuata, na hao kwa kweli wanatakiwa wafanyiwe tathmini, waainishwe na walipwe fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina hakika kama hivyo ndivyo, Mheshimiwa Mbunge suala hilo litafanyika kwa hao wananchi wa Mbulu hadi Garbabi, ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na tatizo kubwa la Wakandarasi kushindwa kuchimba visima. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Mkandarasi ana miezi sita, ameshindwa kuchimba visima vya Aicho, Boboa na Titimu:-

Je, Serikali imefikisha hatua gani kuleta mitambo ya kila mkoa kuchimba visima vyetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, ametupatia fedha ya kutosha, taratibu zote zilishafanywa. Kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha tunatarajia mitambo ile yote iwe imeshafika Tanzania na iweze kwenda kufanya kazi inayokusudiwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Gereza la Mbulu lilijengwa toka ukoloni, na kwa kuwa gereza hilo haliko kwenye magereza yaliyotajwa hivi sasa kwenye mpango wa ujenzi. Je, ni lini Serikali itajenga upya gereza la Mbulu na makazi ya Askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kusema katika jibu la msingi kulingana na upatikanaji wa fedha tutaendelea kukarabati magereza yote yaliyochoka ikiwemo hili gereza la Mbulu. Lakini kwa mwaka huu wa fedha tumebainisha magereza yaliyotengwa kwa sababu ya ndio fedha tuliyopata lakini kwa miaka ijayo gereza lake pia litafikiriwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, baadhi ya vyuo nchini vinakabiliwa na ukosefu wa viwanja vya michezo.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka Wizara kupita kwenye Wilaya zote na Mikoa kuona viwanja vilivyopo na namna ya kushirikiana na wadau? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Issaay kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukakubali kwamba kuna changamoto ya viwanja kwenye maeneo yetu ya vyuo, tunaomba tubebe/tuchukue ushauri huu wa Mheshimiwa Issaay ili tuweze kwenda kufanya tathmini namna gani tunaweza kushirikiana na wadau wengine kuweka kufanya maendeleo ya viwanja kwenye vyuo vyetu. Nakushukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza swali hili lilikuwa limeulizwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu niliuliza mimi mwenyewe na ninakushukuru kiti chako kuamua Wizara ijibu na leo amekuja kuleta majibu.

Nina maswali madogo mawili ya nyongeza, swali la kwanza, kwa kuwa sasa Halmashauri ya Mji wa Mbulu haina jokofu kwa muda wa mwaka mmoja au zaidi ya mwaka sasa, na kwa mapato yetu ya ndani hatuwezi kununua jokofu hilo linalohitaji takriban Milioni 70.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutununulia hilo jokofu ili hospitali ya Mbulu ipate huduma hiyo na kuondoa adha hiyo kwa wananchi?

Swali la pili, kwa kuwa kumeonekana kuna gharama kubwa sana ya uagizaji wa dawa na vifaatiba nchini kupitia Wakala wa MSD Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kutazama gharama hizo ili kuona namna mbadala ya kupunguza gharama kwa Serikali na kutoa huduma hiyo kwa Umma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Kwanza ninampongeza kwa ufuatiliaji wake makini wa hili suala kwa ajili ya Wilaya yake. Kwanza ameshafika Wizarani na nimhakikishie kwamba majokofu yameshafika MSD siku tatu zilizopita, kwa hiyo mpaka mwisho wa wiki itakuwa jokofu la kubeba miili 12 litakuwa limefika Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kuelekea kwenye hospitali yake ya Wilaya.

Swali lake la pili ni suala la gharama ya bei ya MSD kuwa ni ghali. Kwanza nimwambie MSD ni Shirika la Serikali na kweli huko nyuma kulikuwa na tatizo hilo lakini halipo sasa hivi, ndiyo maana Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa fedha na tumejenga viwanda kule Idofi ambavyo vinazalisha dawa pamoja na gloves ukienda sasa hivi MSD ukilinganisha na bei zilizopo mtaani, MSD ni bei rahisi kuliko ilivyo mtaani. Kwa hiyo, hilo tatizo limesha tatuliwa na linaendelea kufanyiwa kazi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako niseme tu moja kwenye eneo hili la mortuary, Mbunge wa Meru amejenga yeye mwenyewe mortuary kwa asilimia 80 kwa fedha zake na niipongeze Halmashauri yake ikachangia asilimia 20 iliyobaki na katika majokofu yanayokuja, jokofu lako linakuja na Mbunge wa Makete.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Miezi nane sasa au saba, mkandarasi wa REA katika Jimbo la Mbulu Mji amesimika nguzo, hajaweka waya wala kuwasha umeme.

Je, ni lini mkandarasi huyo atafunga waya na kuwasha umeme katika Jimbo la Mbulu Mji? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia, Mbunge wa Mbulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kulitokea changamoto katika mradi unaoendelea wa REA wa kupanda kwa bei za vifaa ikiwemo transfoma na waya ambayo ilipelekea wakandarasi kuchelewa kukamilisha kazi walizokuwa wamepangiwa kufanya. Bahati nzuri Serikali imekaa na wakandarasi, tumepanga fedha za ziada kufidia gharama zilizoongezeka, tumeingia mikataba mipya na sasa kazi itaenda kwa kasi zaidi kukamilisha yale maeneo ambayo yalikuwa yamesimama.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu wake pamoja na watendaji wa Wizara ya Umwagiliaji. Kwanza nichukue nafasi hii pia kumwomba Mheshimiwa Waziri je, ni lini atafanya ziara katika eneo hilo la skimu ya umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa shukrani na pongezi. Nimuahidi tu baada ya Bunge la Bajeti tutakwenda pamoja kuangalia mradi huo.