Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Taska Restituta Mbogo (32 total)

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa Mikoa ambayo haina kiwanda hata kimoja;
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda katika Mkoa wa Katavi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana wa mkoa huo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na taarifa ya sensa ya viwanda iliyofanyika mwaka 2015 ni kweli kuwa Mkoa wa Katavi hauna viwanda vikubwa. Hata hivyo, Mkoa huo una jumla ya viwanda vidogo 221 ambapo kila kiwanda kina uwezo wa kuajiri wafanyakazi wasiozidi 10. Aidha, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) linatoa huduma katika viwanda vidogo vya usindikaji wa vyakula na asali vipatavyo 26, viwanda vidogo vya kukoboa mpunga tisa, viwanda vya kusaga unga 11 na viwanda vidogo vya kubangua karanga saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha na kuboresha mazingira yanayovutia wawekezaji wa ndani na nje, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Katavi kuwa, tutaongeza juhudi za kutekeleza jukumu la kuhamasisha viwanda kwenda Katavi. Aidha, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wadau wote wa maendeleo kusaidiana na Serikali kuhamasisha ujenzi wa viwanda Mkoa wa Katavi kwa kulenga malighafi zinazopatikana sehemu hiyo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia SIDO imeendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi wakiwemo wanawake na vijana. Kati ya mwaka 2007 mpaka 2015 SIDO ilitoa mafunzo yenye nia ya kutoa maarifa na kujenga uwezo wa stadi kwa wajasiriamali wapatao 520. Mafunzo hayo yalitolewa katika nyanja zifutazo:-
Utengenezaji wa mizinga ya nyuki ya kisasa, usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa sabuni, utengenezaji wa chaki, mafunzo juu ya ujasiriamali, utengenezaji wa majiko ya kisasa yanayotumia nishati ndogo, mfumo wa ufuatiliaji bidhaa za asali, utengenezaji wa mitambo ya kukausha mazao ya kilimo yanayotumia nishati ya jua na usimamizi wa masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, SIDO imekwishapata ofisi ya kufanyia kazi katika Mkoa wa Katavi kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi. Hatua hiyo itapanua wigo wa utoaji mafunzo ya ujasiriamali na usindikaji wa vyakula kwa wanawake na vijana katika Mkoa wa Katavi.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaainisha kuwa, mtu akifika umri wa miaka 18 huyo ni mtu mzima na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, Ibara ya 13 inasema umri wa msichana kuolewa ni miaka 15 na mvulana kuoa ni miaka 18:-
Je, ni lini Serikali itaifanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa, ili watoto wa kike wasiolewe na umri mdogo kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa, kumekuwa na mkanganyiko kati ya Sheria hizo mbili, hususan kuhusu umri wa kuolewa, kwani Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 katika Kifungu cha nne imetafsiri mtoto kuwa ni mwenye umri chini ya miaka 18, ingawa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, Kifungu cha 13, kinaruhusu mtoto wa chini ya miaka 15 kuolewa. Serikali ilishaanza kufanyia kazi marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 baada ya kupokea taarifa ya Tume ya Kurekebisha Sheria ya mwaka 1996 kuhusu sheria kandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya kazi zilizofanyika ni pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa Waraka Maalum wa Serikali (White Paper) kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sheria hiyo. Kwa sasa Waraka huo Maalum upo katika ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutolewa maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hii, Serikali pia, imefanya juhudi nyingine, kama vile kutungwa kwa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009, iliyofuta vipengele vya 161 mpaka 166 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971. Ili kuweka tafsiri moja ya mtoto kuwa ni chini ya umri wa miaka 18. Hatua hii inaifanya sasa Sheria ya Mtoto kutumika katika mashauri mengi yanayohusu haki za mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kutambua thamani na haki za makundi yote katika jamii Serikali imeweka Ibara Maalum ya 57 inayohusu Haki za Watoto katika Katiba inayopendekezwa. Hivyo, endapo Katiba inayopendekezwa itapitishwa basi taratibu zitafuata za kufanyia marekebisho Sheria zote kandamizi kwa wanawake na watoto.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta mradi wa maji Ziwa Tanganyika ili maji yaweze kuvutwa mpaka Mpanda na Mkoa wa jirani wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto za upatikanaji wa maji nchini. Hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto ya maji katika Mikoa ya Rukwa na Katavi zimegawanyika katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mfupi, Serikali imekamilisha usanifu na uandaaji wa kabrasha za zabuni kwa ajili ya mradi wa maji kwa Mji wa Inyonga Mkoa wa Katavi, Miji ya Chala, Laela, Namanyere na Matai katika Mkoa wa Rukwa.
Katika usanifu huo, vyanzo mbalimbali vimeainishwa vikiwemo mabwawa, chemchemi na visima virefu. Aidha, kwa Mji wa Mpanda, Serikali imetekeleza mradi wa maji wa Ikolongo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuboresha hali ya huduma ya maji Mjini Mpanda. Mradi huu umekamilika mwezi Julai mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imejielekeza katika kutumia vyanzo vya maji vya Ziwa Tanganyika na mito mikubwa kwa ajili ya kuhudumia Miji ya Mpanda na Sumbawanga, Miji mingine pamoja na vijiji vitakavyokuwa kando kando ya Bomba kuu. Hivyo Wizara imeziagiza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpanda na Sumbawanga kufanya tathmini ya awali na kuiwasilisha Wizarani ili kuweza kuajiri wataalam washauri watakaofanya usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Majisafi Sumbawanga wameshaandaa andiko hilo na Mamlaka ya Majisafi Mpanda pia nao wameandaa andiko hilo ambalo linawasilishwa mwezi Februari mwaka 2017. Kazi ya usanifu itaanza wakati wa utekelezaji wa programu ya maendeleo ya Sekta ya Maji, Awamu ya Pili iliyoanza Julai, 2016.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa ambayo ina vivutio vingi vya utalii kama vile Mbuga ya Katavi yenye wanyama wengi, kivutio cha pekee cha twiga weupe ambao hawapatikani mahali pengine popote duniani:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukitangaza kivutio hiki pekee cha utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vingi vya utalii, vikiwemo Mbuga ya Wanyama ya Katavi, Mti wa Mzimu wa Katavi pamoja na vivutio vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Bodi ya Utalii Tanzania na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, imekuwa ikitangaza vivutio vya utalii vya Katavi kwa ujumla wake kupitia mitandao na tovuti mbalimbali za kijamii. Aidha, Majarida ya Utalii ya TANAPA na TTB yanayotolewa kwa lugha za Kiswahili, Kingereza, Kidachi, Kichina, Kifaransa na Kirusi ni sehemu ya njia zitumikazo katika kutangaza utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Majarida hayo ni Selling Tanzania na Explore Tanzania yatolewayo na TTB na TANAPA Today na Hifadhi za Taifa Tanzania au Tanzania National Parks yanayotolewa na TANAPA. Aidha, TANAPA hutangaza pia utalii kupitia kipindi maalum kiitwacho Hifadhi za Jamii za Taifa kilichorushwa na Kituo cha Luninga cha Taifa (TBC). Kipindi hiki hurushwa kila wiki na kupitia kipindi hiki vivutio vinavyopatikana Hifadhi ya Taifa ya Katavi, kikiwemo kivutio pekee cha twiga weupe hutangazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda kulikofuatiwa na ujio wa Ndege za Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) kutasaidia sana kuongezeka kwa idadi ya watalii ambao watatembelea maeneo mbalimbali Mkoani Rukwa, ikiwemo Hifadhi ya Katavi. TTB na ATCL wanakamilisha matayarisho ya kuanzisha safari maalum za siku za mwisho za juma na siku za sikukuu kwa lengo la kuhamasisha na kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Bodi ya Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa la TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kuboresha mbinu zilizopo na kubuni mbinu mpya, ili kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii na hatimaye kuvutia watalii wengi zaidi katika sekta ya utalii nchini.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, ipo karakana ya kutengeneza ndege (hangar) ambayo ilijengwa na Serikali ya Uholanzi, lakini sasa hivi haitumiki.
(a) Je, ni lini Serikali itafufua karakana hiyo ili ndege zetu za Bombardier na nyingine ziweze kufanyiwa matengenezo hapo?
(b) Je, ni nani mmiliki wa uwanja huo wa ndege?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye Sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, karakana ya kutengeneza ndege ya KIMAFA iliyopo Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro kwa sasa inaendeshwa na kusimamiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Mheshimiwa Naibu Spika, Karakana hiyo ilijengwa mwaka 1980 na kukabidhiwa rasmi kwa Serikali mwaka 1985 na ina uwezo wa kuhudumia ndege kubwa aina ya B747’S au ndege tano aina ya B737’S kwa wakati mmoja. ATCL inaendelea kuifanyia matengenezo karakana hiyo ili iweze kurudi kwenye ubora wake na kutoa huduma za matengenezo ya ndege.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) ni kati ya viwanja 59 vinavyomilikiwa na Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kiwanja hiki kinaendeshwa na Kampuni ya Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege ya Kilimanjaro (Kilimanjaro Airports Development Company – KADCO) ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Aidha, taratibu za kuunganisha KADCO na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ili kuwa na taasisi moja inayosimamiwa na viwanja vya ndege nchini zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu 2018.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Mkoa wa Katavi hauna umeme wa Gridi ya Taifa. Je, ni lini Mkoa huo utapatiwa umeme wa Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Mikoa ya Kusini Magharibi ikiwemo Katavi, Kigoma na Rukwa kuunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa. Serikali kupitia TANESCO imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa Gridi Msongo wa kilowati 400 yenye urefu wa kilometa 1,080 kutoka Mbeya – Sumbawanga – Mpanda – Kigoma hadi Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, mtaalam mshauri amekamilisha kazi ya kudurusu taarifa ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuhuisha mradi kutoka kilovoti 220 hadi kilovoti 400. Utekelezaji wa ujenzi wa mradi huu utaanza mwezi Desemba, 2017 na kukamilika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Mkoa wa Katavi utaanza kupata umeme wa Gridi ya Taifa. Gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 664.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Wabunge wa Viti Maalum ni sawa na Wabunge wengine wa Majimbo kwa sababu hakuna tofauti ya kiapo cha Wabunge wa Majimbo na wale wa Viti Maalum.
Je, ni kwa nini Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Vikao vya Kamati ya Fedha za Halmashauri zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 75 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 kifungu cha 47 pamoja na kifungu cha 40(2)(c) cha Kanuni za Kudumu za Halmashauri za mwaka 2014 na Kanuni za Kudumu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kifungu 41(1) zinazotaja Wajumbe wa kuingia kwenye Kamati ya Fedha na Mipango kuwa ni Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti; Naibu Meya au Makamu Mwenyekiti, Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha Majimbo katika Halmashauri hiyo; Wenyeviti wa Kamati za Kudumu katika Halmashauri; Wajumbe wengine wasiozidi wawili watakaopendekezwa na Mwenyekiti au Meya na kupigiwa kura na Baraza la Madiwani la Halmashauri, mmoja kati yao akiwa mwanamke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye vikao vya Kamati za Fedha za Halmashauri kwa sababu hawajatajwa kwenye orodha ya Wajumbe iliyoainishwa na kifungu cha 41(1) na kifungu cha 40(2) cha Kanuni za Kudumu za Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mwaka 2014, zinazofafanua mahitaji ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 75 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 kifungu cha 47.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Kumekuwepo na mkanganyiko wa elimu ya msingi nchini ambapo kuna sera inasema Elimu ya Msingi ni kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba na nyingine inasema elimu ya msingi ya Mtanzania ni kuanzia darasa la kwanza mpaka la kumi na mbili. Je, Serikali inasema nini juu ya suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa elimu Tanzania ni utaratibu uliowekwa ili kufikia malengo na dira ya elimu katika maeneo husika. Mfumo unajumuisha elimu ya awali ambayo ni miaka miwili, elimu ya msingi miaka saba, elimu ya sekondari miaka minne na elimu ya juu miaka miwili na miaka mitatu au zaidi elimu pia ya ya juu. Aidha, kwa sasa mfumo wa elimu wa Tanzania unasimamiwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 1978 Sura Namba 353. Sheria hii inabainisha wazi kuwa elimu ya msingi ni kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusisitiza kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza na kusimamia elimu kwa kutumia sheria hiyo ambapo elimu ya msingi ni kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Tanzania inayo makabila yapatayo 124 yanaongea lugha tofauti na yanazo mila tofauti ambazo wamekuwa wakiziheshimu tangu enzi za mababu:-
(a) Je, ni lini Serikali itaandika lugha za makabila hayo ili yasiweze kupotea kwenye uso wa dunia?
(b) Je, ni lini Serikali itaandika historia kwa kila kabila nchini ili vijana wanaokua waweze kujua tamaduni za makabila yao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ni msimamizi na mratibu wa shughuli mbalimbali za utamaduni nchini. Aidha, kwa mujibu wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997, jamii ndiyo mmiliki wa utamaduni, hivyo wajibu wa kufanya tafiti, kuorodhesha na kuandika historia za kila jamii ni wetu sote.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake inaendelea na utaratibu wa kukusanya tafiti za lugha za jamii mbalimbali zinazofanywa na wadau wanaojishughulisha na ustawi wa lugha nchini na inaandaa kanzidata ili lugha hizo zisipotee kwenye uso wa dunia. Hadi sasa lugha za jamii 38 zimeshakusanywa na kufanyiwa tafiti na zimehifadhiwa kwa njia ya kamusi. Ikumbukwe kuwa lugha ni sehemu ya utamaduni wa Taifa lolote lile.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali na wadau mbalimbali wameandika na wataendelea kuandika historia za jamii, mila na desturi zake. Kwa sasa, karibu kila jamii imekwishaandika historia ya mila na desturi zake. Wizara inaendelea na utaratibu wa kukusanya maeneo ya kihistoria ya jamii mbalimbali hapa nchini na kuyahifadhi kwa njia ya TEHAMA. Vitabu vya historia na maandiko hayo yanapatikana katika Ofisi za Idara ya Nyaraka za Taifa, maktaba pamoja na maduka mbalimbali ya vitabu nchini.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-

Tanzania haina wauguzi walisomea kuhudumia watoto njiti.

(a) Je, ni lini sasa Serikali itasomesha wauguzi kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti?

(b) Je, kuna hospitali ngapi na vituo vya afya vingapi nchini vyenye chumba atamizi (incubator)?

(c) Gharama za kuwatunza watoto njiti ni kubwa na wanakaa hospitali muda mrefu kwa miezi mitatu hadi minne, je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya kuwahudumia watoto njiti yapo katika Mtaala wa Mafunzo ya Wauguzi na Madaktari na wanafundishwa wakiwa vyuoni. Ili kuboresha ufanisi katika kuwahudumia watoto njiti na upatikanaji wa elimu hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, imetengeneza mtaala wa mafunzo haya utakaotumika kuwafundishia wauguzi waliopo makazini kuanzia mwezi Februari, 2019 nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia Mafunzo ya Huduma Muhimu kwa Watoto Wachanga (Essential Newborn Care), watoa huduma kwa maana ya Madaktari na Wauguzi 1,453 kutoka vituo vya kutolea huduma 653 katika Mikoa ya Tabora, Simiyu, Shinyanga na Kigoma walio makazini wameshapata mafunzo. Lengo ni kutoa mafunzo haya katika mikoa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma atamizi kwa maana incubators hutolewa kwa watoto wote njiti pamoja na walio na uzito pungufu ili kuzuia kupoteza joto ambapo kwa sasa huduma hii inapatikana katika baadhi ya hospitali za Mikoa na Halmashauri tu. Mpaka sasa ni hospitali za mikoa 20 pamoja na Hospitali 24 za Halmashauri ambazo zina vyumba vyenye huduma atamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa Serikali ni kuhakikisha huduma za kumhudumia mtoto njiti zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma. Serikali inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya huduma za afya ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na mtoto njiti. Aidha, elimu kuhusu maandalizi kwa ajili ya kujifungua hutolewa kwa wazazi, mama na mwenza wake, wakati wa kliniki za ujauzito ikiwa ni pamoja na matunzo ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua.

Hivyo, Serikali haina kusudio la kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaojifungua watoto njiti. Wizara itaendelea kuboresha miundombinu ya kuwatunza watoto njiti katika vituo vya kutolea huduma za afya na kutoa elimu ya kulea watoto njiti kwa jamii.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mkoa wa Katavi unapata mvua za masika kuanzia mwezi Septemba na Oktoba lakini mara nyingi pembejeo zimekuwa zikichelewa kupelekwa wakati mwingine hadi mwezi Novemba:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kwa wakati pembejeo Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) kuagiza mbolea ya kupandia (DAP) na mbolea ya kukuzia (UREA). Mfumo huo unawezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu na kudhibiti upandishaji wa bei za mbolea kiholela.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha zabuni ya kuagiza mbolea tani 280,000 ambapo tani 170,000 ni mbolea ya kupandia na tani 110,000 ni mbolea ya kukuzia kwa ajili ya msimu wa 2019/2020 kupitia mfumo wa BPS. Mbolea hiyo inatarajiwa kufikishwa hapa nchini mwezi Agosti, 2019 na kusambazwa kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingine nchini kabla ya mwezi Septemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ziada ya mbolea iliyopo nchini inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali kulingana na msimu wa kilimo, ambapo hadi tarehe 30 Machi, 2019 kulikuwa na mbolea tani 147,913 za mbolea zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeyaelekeza makampuni yanayoingiza na kusambaza mbolea ya Premium Agrochem, OCP na Export Trading Group kuhakikisha kwamba ifikapo Julai, 2019 kampuni hizo ziwe na maghala ya kuhifadhia mbolea na mawakala wa kusambaza mbolea katika mikoa inayotumia mbolea kwa wingi ukiwemo Mkoa wa Katavi ili kuondoa changamoto ya upungufu wa mbolea kwa wakulima katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelielekeza Shirika la Reli Tanzania kutoa kipaumbele cha kusafirisha mbolea ili kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja na gharama nafuu ili kumfikia mkulima kwa wakati na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakusanya mahitaji ya mbegu bora na viuatilifu katika mikoa mbalimbali ili kuhamasisha kampuni na wafanyabiashara kupeleka pembejeo hizo kwa wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza na wakati na kwa kuuza kwa bei ya mauzo na bei nafuu.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Watanzania wengi wanaoishi nje ya nchi wamejikuta ni raia wa nchi wanazoishi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kazi lakini si kwamba hawaipendi Tanzania:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatambua Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine ili waweze kukuza uchumi wa nchi na kusaidia ndugu zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia masuala yanayohusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) pasipo kubagua wale waliochukua uraia wa nchi nyingine kwa lengo la kuhakikisha kuwa mahitaji yao ya kikonseli yanashughulikiwa na pia kuongeza ushiriki wao katika kuchangia maendeleo ya nchi na ndugu zao.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeweka mikakati mbalimbali ya kuwatambua diaspora katika kukuza uchumi. Mikakati yao ni pamoja na kuhimiza diaspora kujisajili kwenye Balozi zetu na maeneo ya uwakilishi; kuratibu makongamano ya diaspora ndani na nje ya nchi; kuratibu mikutano ya diaspora na viongozi wa Serikali wanapofanya ziara za kikazi nje ya nchi; kuhamasisha diaspora kuunda na kusajili jumuiya zao na kuwahimiza kuwa washawishi wazuri wa uwekezaji kutoka mataifa mengine kuja kuwekeza nchini.

Mheshimiwa Spika, idadi ya diaspora wa Kitanzania nje ya nchi inakadiriwa kuwa ni zaidi ya milioni moja, ambapo idadi ya diaspora waliojisajili kwa hiari kwenye Balozi zetu na maeneo ya uwakilishi ni takribani laki moja. Aidha, diaspora hao wamekuwa wakimiliki akaunti kwenye taasisi mbalimbali za kifedha kama vile Benki za Azania, CRDB, NMB, Stanbic na pia kuwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF, ikiwa ni pamoja na kumiliki nyumba 166 zilizouzwa na Shirika la Nyumba la Taifa zenye thamani ya shilingi bilioni 5.5 hadi kufikia Februari, 2019. Pia diaspora wameleta mafanikio makubwa kwa ndugu zao na taifa kwa ujumla kwa kuchangia sekta mbalimbali kama vile afya ambapo tumekuwa tukipokea wataalam wa afya na magonjwa yenye kuambukiza na yale yasiyoambukiza kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, tunao mfano mzuri katika sekta ya afya ambapo Novemba, 2019 tulipokea msaada wa sanamu ya vitendo (simulative manikin) kutoka kwa Jumuiya ya Watanzania Wanaoishi Uingereza yenye thamani ya shilingi milioni 100; vitabu vya afya vyenye thamani ya shilingi milioni 30 vilivyogawiwa katika Maktaba Kuu ya Shirika la Elimu Kibaha, Taasisi ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Namanyere iliyopo Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, Mbeya pamoja na Pemba.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

TBC ni Shirika la Umma na hutangaza habari na vipindi mbalimbali ili Watanzania wasikie kwa Lugha ya Kiswahili; Tanzania pia ina wageni kutoka nchi mbalimbali duniani waishio nchini. Lakini TBC limekuwa likitangaza taarifa za habari na vipindi vyake vingine kwa lugha ya Kiswahili tu; zamani kulikuwa na kipindi cha External Service kilichokuwa kikitangazwa kwa Lugha ya Kiingereza ili wageni waishio nchini wasikie lakini sasa hivi hakipo.

(a) Je, ni kwa nini TBC ilifuta kipindi cha External Service kilichokuwa kikitangaza taarifa ya habari kwa Lugha ya Kiingereza?

(b) Je, kwa kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili tu hatuoni kwamba tunawanyima wageni fursa ya kujua kinachoendelea nchini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Taska Restituta Mbogo Mbunge wa Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Idhaa ya External Service ya Radio Tanzania Dar Es Salaam ilianzishwa rasmi wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi za kusini mwa Afrika ikiwepo, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola, Afrika ya Kusini. Viongozi wa wapigania uhuru katika nchi hizo waliishi na kuratibu harakati za ukombozi kutokea Tanzania ambapo walirusha ya Radio ya kuhamasisha wananchi wao kushiriki katika mapambano hayo kupitia Idhaa hiyo ya External Service. Baada ya nchi hizo kupata uhuru, Idhaa hiyo haikuendelea tena na hayo matangazo yake.

(b) Hata hivyo, kwa sasa TBC kupitia stesheni yake ya TBC International inayopatikana katika masafa ya 95.3, hutangaza kwa lugha ya Kiingereza. Aidha, TBC1 pamoja na TBC Taifa zinarusha baadhi ya vipindi kwa Kiingereza. Kwa mfano TBC1 ina vipindi maarufu “This Week in Perspective” na “International Sphere” na TBC Taifa ina vipindi ya”Breakfast Express”, “Daily Edition”, “Day Time” Overdrive kwa Kiingereza. Vipindi hivi huzungumzia masuala mbalimbali yakiwepo ya kisiasa, kiuchumi, pamoja na kijamii.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kwa kutangaza taarifa ya habari kwa lugha moja ya Kiswahili kunawanyima wageni fursa ya kujua masuala mbalimbali yanayoendelea hapa nchini. Lakini yapo magazeti mbalimbali yanayochapisha habari hizo zinazotokea nchini kwa lugha ya Kiingereza. Magazeti hayo ni pamoja na Daily News, The Guardian, The Citizen.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mtoto mwenye ugonjwa wa sickle cell hutakiwa kupata matibabu mfululizo ambapo kwa familia zisizo na uwezo hushindwa kulipia gharama za matibabu na hivyo kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wagonjwa wa sickle cell kupata matibabu bure?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa watoto wenye ugonjwa seli mundu au kwa jina la kitaalam sickle cell, wanahitaji matibabu mfululizo kwani huwa wanapata upungufu wa damu na maumivu ya mara kwa mara. Familia, jamii na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitahidi sana kuwahudumia watoto hao kwa kuwapatia mahitaji maalum. Hata hivyo, misaada hiyo haikidhi mahitaji ya wagonjwa wote na kuna baadhi ya familia hazina uwezo wa kuwahudumia watoto wenye seli mundu.

Mheshimiwa Spika, kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeandaa mwongozo wa kutoa msamaha kwa makundi tofauti yasiyo na uwezo likiwepo kundi la watu wenye magonjwa sugu kama sickle cell. Kwa kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, familia zisizo na uwezo huhakikiwa na kupatiwa kibali cha huduma bila malipo. Aidha, Serikali inaanzisha Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza (National Non-Communicable Diseases Control Programme) ambayo ugonjwa wa sickle cell utakuwa ni moja ya magonjwa yatakayokuwa yakiratibiwa kitaifa.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Mkoa wa Katavi hauna kifaa cha kumsaidia kupumua mtoto aliye dhaifu (ambubag):-

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi kifaa hicho?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ambu bag na maski ni vifaa vinavyompatia hewa mtoto mchanga aliyezaliwa na tatizo la kushindwa kupumua na ni moja ya afua inayolenga kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini. Serikali imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha siyo tu kuna watoa huduma wenye ujuzi, lakini pia dawa na vifaa tiba muhimu vinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya hapa nchini. Kwa kipindi cha mwaka 2018, Serikali ilipokea na kusambaza vifaa mbalimbali vya kumsaidia mtoto mchanga mwenye matatizo ya kupumua ikiwemo ambu bag na maski 3,735. Vifaa hivyo vilipekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya 3,500 katika Halmashauri 109 za mikoa 16 ya Tanzania Bara. Usambazaji huo ulienda sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma namna ya kutumia vifaa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inategemea kupokea ambu bag na maski nyingine 2,500 ambazo zitasambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwenye mikoa ambayo haikupata mgao hapo awali. Utaratibu wa ugawaji wa vifaa hivyo umeandaliwa kupitia Bohari ya Dawa (MSD) ambapo Katavi imeorodheshwa katika mgao huo. Nizitake mamlaka husika kuagiza vifaa hivyo kutoka Bohari ya Dawa. Aidha, Bohari ya Dawa itaendelea kuvinunua vifaa hivyo ili vipatikane sambamba na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ikiwemo afya ya watoto wachanga.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itasomesha wataalam wa Court Reporter na Stenographer ili Mahakama zetu ziwe na wataalam hao?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa kusomesha wataalamu waandishi wa Stenographer (Stenographer na Court Reporters) ambao hufanya kazi za uandishi wa maelezo ya mijadala ya wakati wa uendeshaji wa kesi Mahakamani. Kazi hizo kwa sasa zinafanywa na Waheshimiwa Majaji na Waheshimiwa Mahakimu.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuangalia utaratibu mzuri wa kuwatumia wataalamu hawa ambao kwa sasa hawapo katika Muundo wa Utumishi wa Mahakama. Baada ya kukamilika kwa utaratibu unaoangaliwa na kuingizwa kwenye Muundo wa Utumishi wa Mahakama, Wizara itaandaa mpango wa mafunzo kwa wataalamu hao kuanza kuwasomesha rasmi tayari kwa kuanza kuwatumia kwenye Mahakama zetu hapa nchini. Ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70, ambapo ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 zimetumika na bilioni 5.85 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 na zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari, 2022. Ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa umeme wa Grid ya Taifa Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Njia Kuu ya Kusafirisha Umeme wa Gridi ya Taifa wa msongo wa kilovolti 132, yenye urefu wa kilometa 381 kutoka Tabora hadi Katavi. Mradi huu unahusisha pia ujenzi wa vituo vitatu vya kupoza umeme vya msongo wa kilovoti 132 kwenda 33 vya Ipole, Inyonga na Mpanda. Ujenzi wa Mradi unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2023. Gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 64.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa mradi mwingine wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka Iringa - Mbeya – Sumbawanga – Mpanda hadi Kigoma yenye urefu wa kilometa 1,232, unatarajiwa kuanza Novemba na kukamilika mwezi Oktoba, 2024. Gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 470.42.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Umeme wa Grid ya Taifa katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa Gridi ya Taifa wa msongo wa kilovolti 132 yenye urefu wa kilometa 381 kutoka Tabora hadi Katavi na ujenzi wa vituo vitatu (3) vya kupoza umeme vya msongo wa kilovolti 132/ 33kV Ipole (Sikonge), Inyonga (Mlele) na Mpanda (Mpanda Mjini).

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa majengo ya kudhibiti mfumo wa umeme (Control Building) ya Ipole, Inyonga na Mpanda yamekamilika. Upimaji wa mkuza (wayleave) kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme (Transmission Line) kutoka Tabora hadi Katavi umekamilika. Zoezi la uthamini wa mali za wananchi katika maeneo yanayopitiwa na mradi limekamilika kwa Wilaya za Mlele na Mpanda Mjini na zoezi hilo linaendelea kwa Wilaya za Tabora, Uyui, na Sikonge na litakamilika mwishoni mwa mwezi wa Novemba, 2021. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti, 2023.

Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni shilingi bilioni 64.9 na fedha hizi zote ni fedha za ndani na ujenzi unafanywa na Wataalamu wa Shirika la TANESCO.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Mpanda kwenda Karema kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mpanda – Kagwira - Karema yenye urefu wa kilometa 122 ambapo kipande cha Mpanda – Kagwira chenye urefu wa kilomita 10, ni sehemu ya barabara Kuu na sehemu ya Kagirwa – Karema yenye jumla ya urefu wa kilometa 112 ni barabara ya Mkoa.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Machi, 2021 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ilisaini Mkataba na Kampuni ya M/s Crown Tech. Consultant Ltd. kwa ajili ya kufanya Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kagwira – Karema yenye urefu wa kilometa 112 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami na kazi hii inategemea kukamilika mwezi Aprili, 2022.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto wa mitaani ambapo kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: alijibu: -

Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na ongezeko la watoto wa mitaani hivi karibuni. Hii inatokana na sababu mbalimbali za kifamilia.

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza watoto wa mitaani Serikali inafanya mikakati ifuatayo: -

Kuimarisha Kamati za Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Watoto katika ngazi za jamii ambapo hadi sasa kuna jumla ya Kamati 18,186 katika ngazi za taifa, vile vile kutoa elimu kwa wazazi au walezi kuhusu malezi chanya ya watoto kupitia Ajenda ya Taifa ya uwajibikaji wa Wazazi katika malezi ya watoto kwenye familia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikifanya zoezi la kuwatambua na kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani kwa kuwarudisha katika familia zao.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya watoto ambao familia zao hazipatikani Serikali imekuwa ikiwapeleka katika makao ya watoto yanayomilikiwa na Serikali na yale yanayomilikiwa na taasisi binafsi, ambako wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na kuwaandalia mazingira ya kujitegemea kutokana na uwezeshaji wa elimu ya ufundi na mitaji ya kuanzia maisha.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa viongozi na jamii kwa jumla kutimiza wajibu wao katika kuimarisha malezi chanya ya watoto katika familia.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, ni chombo gani kinadhibiti vyuo binafsi vinavyodahili walimu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ndiyo yenye jukumu la kuthibiti ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo vya ualimu vya binafsi nchini. Mamlaka haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kifungu cha 25 na marekebisho yake kifungu cha 10 cha mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vyuo vikuu binafsi vinavyodahili walimu nchini, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ndio chombo chenye mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo hivyo. Mamlaka haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura Na. 346 ya Sheria za Tanzania, nakushukuru.
MHE. BAHATI K. NDINGO K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Bima za Afya za Wazee ili ziweze kutumika wakiwa nje ya Mikoa ambayo wamepewa Bima hizo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa wote, Serikali inaelekeza vituo vyote vya huduma kuwapatia huduma wazee wasio na uwezo waliotimiza vigezo hata wakiwa nje ya maeneo yao. Ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Bima za Afya za Wazee ili ziweze kutumika wakiwa nje ya Mikoa ambayo wamepewa Bima hizo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa wote, Serikali inaelekeza vituo vyote vya huduma kuwapatia huduma wazee wasio na uwezo waliotimiza vigezo hata wakiwa nje ya maeneo yao. Ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuruhusu Mabasi ya Abiria yanayopita Wilayani Sikonge kuendelea na safari badala ya kuyalazimisha kulala?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Mbogo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mabasi ya abiria yanayokwenda Mpanda Mkoa wa Katavi ambayo yanapita Wilaya ya Sikonge zaidi ya saa nne usiku hushauriwa kulala Sikonge kwa sabubu za kiusalama. Eneo hilo lina pori la hifadhi kuanzia Sikonge hadi Inyonga lenye urefu wa kilometa 161 na halina mtandao wa mawasiliano. Hivyo si salama kupita nyakati za usiku mkubwa.

Mheshimiwa Spika, ili kuepuka adha ya kutakiwa kulala Sikonge, wamililki wa mabasi ya abiria wanashauriwa kupanga safari zao ili wapite katika maeneo hayo yenye changamoto mapema zaidi. Mabasi hayo yanaweza kuomba kuanza safari zao hasa kutoka Dar es Salaam saa tisa au saa kumi Alfajiri na Serikali itaafiki maombi yao.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mpanda hadi Karema kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya kilometa 10 ya kutoka Mpanda hadi Kagwira na kwa sehemu iliyobaki ya kuanzia Kagwira hadi Karema (kilometa 112) zabuni za kuwapata Makandarasi zilitangazwa tarehe 20 Aprili, 2023 na zimepangwa kufunguliwa tarehe 31 Mei, 2023, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Bandari ya Karema itafunguliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuwa ujenzi umekamilika kwa asilimia 87?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeshakamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema na huduma katika bandari hiyo zimeanza kutolewa rasmi kuanzia tarehe 1 Septemba, 2022 baada ya kufanyiwa uzinduzi na Mkuu wa Wilaya ya Ziwa Tanganyika. Bandari hiyo inahudumia abiria na shehena mbalimbali za ndani ya nchi na zile zinazosafirishwa kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
MHE. TASKA R. MBOGO, aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Mkongo wa Mawasiliano katika eneo la Sikonge hadi Inyonga?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuwa ni muhimili wa mawasiliano hapa nchini. Katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuanzia Tabora – Sikonge – Inyonga – Majimoto – Kizi wenye urefu wa Kilomita 369.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hadi sasa Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imesaini mkataba na Mkandarasi kwa ajili ya kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika maeneo hayo. Hatua za utekelezaji zimeanza ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2024.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa meli tatu kwa ajili ya Ziwa Tanganyika kama ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imetenga bajeti katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa meli mpya mbili; meli moja ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli moja ya kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 katika Ziwa Tanganyika. Kwa sasa MSCL ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na mkandarasi ili kuwezesha kuanza ujenzi wa meli hizo. Mikataba ya ujenzi wa meli hizo inatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa Juni, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, jitihada zinafanywa na Serikali za kukarabati Meli ya MV Liemba. Kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na mkandarasi kabla ya mkataba wa ukarabati wa Meli ya MV Liemba kusainiwa, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Mpanda hadi Uvinza, yenye kilometa 159, utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Mpanda hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 194 kwa awamu. Ujenzi wa Barabara ya Mpanda hadi Vikonge kilometa 37.6 umekamilika na ujenzi wa sehemu ya Vikonge hadi Luhafwe kilometa 25 unaendelea. Mkataba wa ujenzi wa sehemu ya Luhafwe hadi Mishamo unatarajiwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023. Kwa sehemu iliyobaki ya Mishamo – Uvinza kilometa 94, Serikali iko kwenye mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuruhusu bakaa ya fedha za Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Tabora – Koga hadi Mpanda zitumike katika ujenzi wa sehemu hii, ahsante.
MH. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Katavi wanapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Katavi ni wastani wa asilimia 71 kwa vijijini na asilimia 60 kwa mijini. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 42 katika Wilaya zote za Mkoa wa Katavi lengo likiwa ni kuhakikisha Wananchi wanapata maji safi na salama. Miradi hii ni pamoja na mradi wa maji Karema kwa kutumia Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Tanganyika unaotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2022. Vilevile Mji wa Mpanda utanufaika na utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itaajiri Mtaalamu Mshauri wa kufanya usanifu kwa kutumia vyanzo vya Ziwa Tanganyika ili kuwapatia maji wananchi wa Wilaya za Tanganyika, Mlele, Mpanda na maeneo ya karibu na kufikia lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025.
MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Watanzania wote wanajua kusoma na kuandika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kulingana na ripoti iliyotolewa na NBS, kwa sensa ya mwaka 2022 Tanzania imefikia kiwango cha asilimia 83 cha kujua kusoma na kuandika miongoni mwa watu wazima (miaka 15 na kuendelea), ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.3 kutoka asilimia 78.1 cha sensa ya mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Watanzania wote wanajua kusoma na kuandika, Serikali imeendelea kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo kuondoa vikwazo vya kupata elimu kama vile kutolewa kwa elimu ya msingi bila ada, elimu ya lazima sasa kuwa ya miaka 10, kutekeleza programu zenye lengo la kuwafikia Watanzania waliokosa fursa za elimu. Kwa mfano, Elimu ya Watu Wazima na ujifunzaji endelevu, utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kusoma pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha masomo kwa sababu mbalimbali kurudi shuleni na kuendelea na masomo (re-entry program) kupitia Waraka Na. 2 wa mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, pamoja jitihada hizo, Serikali imeendelea kuboresha huduma za maktaba nchini katika ngazi za mikoa, wilaya na shule, ikiwa ni pamoja na maktaba mtandao, ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi katika maeneo mbalimbali kupata huduma ya kusoma huko waliko.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa lengo la kuongeza fursa kwa Watanzania wengi zaidi kujiunga na Elimu ya Watu Wazima, nakushukuru.