Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Stella Ikupa Alex (27 total)

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana ndiyo kundi muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa letu, je, Serikali ina mpango ganiwa kuwapatia vijana nchini wakiwemo wa Mkoa wa Singida vitendea kazi na mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha kujikita katika shughuli za ujasiriamali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina Maafisa Maendeleo vijana kote nchini lakini maafisa hawa hawana vitendea kazi kuweza kuwafikia vijana wengi walioko vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha Maafisa vijana hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Aysharose kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutetea maendeleo ya vijana katika Mkoa wa Singida na mimi binafsi nimeshuhudia kwa sababu alishanialika kuwa mgeni rasmi kwenye mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana wa Mkoa wa Singida. Naomba aendelee hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi hatuna shida ya kuwasaidia vijana wetu vitendea kazi na mikopo na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu ni ofisi ambayo inasimamia suala zima la uwezeshaji wananchi kiuchumi, kama nilivyosema tunayo mifuko 16 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na mimi, tutaendelea kumuelekeza jinsi ya kufanya pamoja na kutumia mfuko wa maendeleo ya vijana kutoka katika Halmashauri zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ni kwa kiasi gani tutawasaidia Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuweza kusimamia shughuli za maendeleo ya vijana. Ni hivi juzi tu Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alinialika na tulianza kikao cha kwanza cha kuwapa nguvu na kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii nchi nzima. Tutaendelea kufanya hivyo kwa Maafisa Vijana pia katika nchi nzima ya Tanzania. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jana tu nilimpongeza Waziri Mkuu kwenye twitter kwa tamko lake ambalo limesema kila Wizara na Idara itoe taarifa kila mwaka imetenga kiasi gani kwenye kuimarisha huduma kwa watu wanaoishi na ulemavu. Nafikiri hili ni tamko zuri sana na linafaa kupongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imejipangaje, utaratibu huu tutaanza kuuona katika mwaka huu wa fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu kama Serikali tumeu-plan kwamba uanze kuonekana katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. (Makofi)
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa hawa walemavu ili waweze kupata hizi ajira na huduma zingine mbalimbali ni lazima wapiti shule, vyuo na taasisi zingine ili waweze kukubalika katika hili eneo la ajira. Sasa kwa kuwa wanapitia katika shule mbalimbali ambazo zina matatizo mengi na inawafanya wasiweze kupata elimu vizuri kwa mfano Shule ya Viziwi Kigwe ambayo hakuna maji kwa muda mrefu na shule ile ni ya kitaifa na inachukua wanafunzi wengi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea maji wanafunzi wa shule ya wasiosikia Kigwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali niseme kwamba hilo tumelichukua na kwa sababu ni suala mtambuka, tutafanya mawasiliano ndani ya Serikali kwa maana Wizara ya Maji ili tuweze kuona jinsi gani tunaweza tukapeleka maji katika Shule ya Kigwe, ahsante. (Makofi)
HE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naishukuru Serikali kwa majibu yake, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja natambua jitihada za Serikali za kuweka mfumo kwa ajili ya kuwafikia walemavu, lakini suala la mfumo ni moja na suala la kufikisha huduma wanazohitaji kwa maana ya kuwafanyia upendeleo chanya (positive discrimination) ni lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kwa namna gani Serikali sasa imeweza kuwafikishia rasilimali fedha na rasilimali mafunzo watu wenye ulemavu kwenye vikundi vyao, tofauti na kuwajumuisha kwenye vikundi vingine ambapo mahitaji yao mahususi hayawezi kutimizwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa namna gani na kwa kiwango gani Serikali inadhani inaweza kuwapatia nafuu kwenye yale mambo ya msingi kwa mfano Bima ya Afya. Tuchukulie mfano mlemavu wa ngozi akipata ruzuku kwenye bima ya afya una uhakika wa kuhakikisha anakingwa kwa bima, kitu ambacho anakihitaji kama Watanzania wengine lakini yeye anakihitaji zaidi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia na kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linauliza ni jinsi gani Serikali imeweza kuwapatia vikundi vya watu wenye ulemavu fedha. Niki-refer kwamba swali lake lilikuwa linauliza kwa habari ya vijana; kuna mfuko wa maendeleo ya vijana ambao mfuko huu unawawezesha vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee kidogo kwamba kinachotakiwa kufanyika ni kwamba vijana wanatakiwa wajiunge kwenye vikundi, wakishajiunga kwenye vikundi mbalimbali, kwenye maeneo yalipo wanatakiwa pia kuwe na SACCOS. Kwa hiyo, kama Serikali tunapeleka hela kwenye zile SACCOS halafu baada ya kupeleka hela kwenye zile SACCOS vile vikundi vinapewa kupitia zile SACCOS.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo kikubwa ambacho kinapatikana kwenye hivi vikundi ni kwamba wakati ule wa kurejesha wanatakiwa warejeshe riba ya asilimia 10. Katika hiyo riba ya asilimia 10, asilimia tano inabaki kwenye kikundi husika, asilimia mbili inabaki kwenye Halmashauri na asilimia tatu inaenda Serikalini. Kwa hiyo, hiyo ni njia mojawapo ambayo kama Serikali tunavipatia hivi vikundi fedha lakini pia kuna hii mifuko ya uwezeshaji kiuchumi wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kikubwa ambacho ninapenda niongelee hapa, nitoe wito kwa Halmashauri mbalimbali wawahamasishe watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi, kwa sababu hizi hazitolewi kwa matu mmoja mmoja. Wawahamasishe watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi, yakiwepo makundi ya vijana lakini pia na makundi mengine ambayo sio ya vijana ili waweze kunufaika na hizi fedha ambazo zinatolewa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameongelea kwa upande wa afya, kwa upande wa afya ametolea mfano wa watu wenye ualbino. Kwa upande wa watu wenye ualbino tayari Serikali imekwisha kuziagiza Halmashauri kwamba zinapoagiza dawa kutoka MSD zihakikishe zinajumuisha mafuta ya watu wenye ualbino katika madawa ambayo wanaagiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jingine la pili ameongelea kwamba kwanini Serikali haitoi bima ya afya kwa watu wenye ulemavu. Niseme wazi kwamba Serikali, hicho ni kitu ambacho kama Serikali tunakichukua, hatuna specific kwamba hii ni bima ya afya kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Lakini watu wenye ulemavu wasiokuwa na uwezo wanatibiwa baada ya kutambulika kwamba hawa watu hawana uwezo wa kugharamia mahitaji yao. (Makofi)
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa takwimu hizo zinatokana na sensa ya mwaka 2012 na Tanzania sasa inakadiriwa kuwa na watu wasiopungua milioni 50, hii inaonesha wazi kwamba Serikali haina takwimu sahihi kwa sasa.
Swali langu la kwanza, Serikali haioni kwamba kukosekana kwa takwimu sahihi kunapelekea kushindwa kuwapatia mahitaji yao ipasavyo?
Swali langu namba mbili, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kufanya takwimu ili kuweza kupata idadi kamili ya watu wenye ulemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana mdogo wangu kwa ajinsi ambavyo anafuatilia masuala ya watu wenye ulemavu, lakini pia na yeye ni mdogo wetu yaani mdogo wa watu wote wenye ulemavu kwa sababu dada yake ni kiziwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa takwimu kwa watu wenye ulemavu, na sambamba na hilo kama tunavyofahamu, sensa inafanyika kila bada ya miaka 10 ambapo kutokana na kwamba ilifanyika mwaka 2012 kwa hiyo tunategemea sensa nyingine ifanyike mwaka 2022; lakini kwa sababu ya umuhimu wa jambo hili yaani takwimu kwa watu wenye ulemavu tayari Serikali imeshaanza kufanya mazungumzo na kuangalia ni jinsi sasa tunaweza kupata takwimu hizi kabla ya wakati huo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Khadija Nassir Ali kwamba hili suala Serikali imeliangalia kwa umuhimu wake kabisa kwa sababu ni makusudi na nia ya Serikali kuona kwamba inapanga bajeti zake kulingana na uhalisia wa mahitaji ya watu wenye ulemavu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwaficha watoto ambao wamekuwa na ulemavu na hivyo kukosa haki za msingi kama afya na elimu. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu wazazi na walezi hawa ambao wanawakosesha hawa watoto? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kuhusiana na umuhimu wa kwamba kila mtoto mwenye ulemavu anawajibika ama ana fursa sawa na watoto wengine ambao hawana ulemavu. Kwa kuliona hilo hivi ninavyozungumza tayari kuna zoezi linaendelea la kuwatambua watoto wenye ulemavu kila mahali nchini ili kuona sasa ni jinsi ya kuhakikisha kwamba hawafichwi tena ndani na wanapatiwa huduma kama watoto wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili linafanyika. Hata hivyo niendelee kutoa rai kwa wazazi wote nchini pamoja na walezi kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wanawapatia fursa sawa na watoto ambao hawana ulemavu. Mtu mwenye ulemavu ni sawa na mtu mwingine ambaye hana ulemavu, akiwezeshwa anakuwa anaweza. Kwa hiyo, nitoe rai sana na niwaombe wazazi pamoja na walezi kulizingatia hilo kuona kwamba watu wenye ulemavu wako sawa pamoja na watu ambao hawana ulemavu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Watoto wanaozaliwa na ulemavu nao wanastahili kupata elimu kulingana na ulemavu walio nao. Sisi pale Temeke tuna Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu ambayo inatoa elimu ya msingi kwa watoto wenye ulemavu kutoka sehemu mbalimbali za nchi, lakini ukweli ni kwamba shule ile inakabiliwa na changamoto nyingi za vifaa wezeshi kwa wale walemavu, lakini pia mazingira yenyewe ya shule. Nilitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuisadidia shule ile ili watoto wasome kwenye mazingira rafiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kaka yangu Mtolea, Shule ya Salvation Army nimefika pale na nimejionea mazingira yalivyo. Kwa hiyo kama shule zingine ambavyo tumekuwa tukifanya kuhakikisha kwamba zinapata vifaa saidizi na Shule ya Salvation Army tutahakikisha kwamba itaendela kupata vifaa saidizi sawa na shule zingine ambazo tumekuwa tukigawa vifaa saidizi kama Serikali. (Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mtolea kwamba shule hii na yenyewe itaendelea kupata vifaa saidizi kama ambavyo shule zingine zimekuwa zikipata. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa pia kuongezea na kulihakikishia Bunge lako kwamba Wizara ya Elimu imekuwa ikinunua vifaa visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Katika bajeti ambayo tutakuja kuiwasilisha Bungeni tarehe 3 na 4 Mei, 2018 pia tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha kwamba shule hiyo pamoja na shule nyingine ambazo zina wanafunzi na ambao wanahitaji visaidizi watapatiwa ili waweze kujifunza kwa ufanisi. (Makofi)
MHE. MWAMTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kuniona. Kwa kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kwenye suala la ubakaji, je, Serikali imejipanga vipi kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikihakikisha ulinzi kwa watu wenye ulemavu kila iitwapo leo. Kwa hiyo, niseme kwamba hata hili la ubakwaji kwa watoto wenye ulemavu Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inawapatia ulinzi. Hata hivyo si hilo tu, mtu ambaye atabainika kwamba amefanya kitendo hicho kwa mtu mwenye ulemavu atachukuliwa hatua kali na hatua stahiki kama inavyostahili ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sambamba na ufutwaji wa kodi wa vifaa vya watu wenye ulemavu, je, ni lini Serikali itawagawia bure walemavu kwenye kaya maskini vifaa vya uhafifu hauoni kwa watu wenye ulemavu wa macho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kadri vinavyokuwa vinapatikana, kwa hiyo, hili ambalo ameliuliza dada yangu Sophia nimhakikishie tu kwamba Serikali itaendelea kutoa vifaa hivi. Hata hapa, muda mfupi uliopita kama wiki mbili/ tatu/mwezi mmoja uliopita tumekuwa na hilo zoezi la kugawa vifaa hivi saidizi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya hivyo kupitia bajeti zake lakini pia kupitia wadau mbalimbali wanajitokeza kusaidia kundi hili la watu wenye ulemavu (Makofi).
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa baadhi ya watoto wanaosoma katika kituo hiki au Shule ya Buhangija wengi wao wametelekezwa kabisa na wazazi wao, kwa maana ya kwamba wazazi wakati ule wa mauaji waliwafikisha watoto wao getini katika ile shule na kuwaacha; na hivi sasa wakati wa likizo na muda wote yamekuwa ni makazi yao katika kituo hiki; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba angalu siku moja basi, watoto hawa wanawapata wazazi wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu ameeleza idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi waishio kwenye shule ya Buhangija; je, ina mpango gani pia wa kuhahakisha kwamba tunapata idadi kamili ya watu wenye ualbino na hata watu wengine wenye ulemavu ili basi tunapopanga au tunapotunga sera/ sheria kujua kwamba idadi kamili ya watu wenye ulemavu Serikali iweze kupeleka maendeleo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kilikuwa kinafanywa na Serikali baada ya kutokea lile wimbi la mauaji kwa watu wenye ualbino ilikuwa ni kunusuru maisha yao kama nilivyosema, kwa kuweka kwenye vituo mbalimbali, lakini sasa hivi kitu ambacho kimefanyika Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na vitongoji pia na halmashauri ambako wanatoka iliweza kuangalia jinsi gani hawa watu wanaweza wakarudishwa kwenye familia zao kwa kuangalia usalama na kama ile hali inakuwa imeisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa upande wa Kituo cha Buhangija na vituo vingine, Serikali ambacho inafanya sasa hivi ni kutembelea hivi vituo, lakini kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kama itabainika kwamba kuna watoto wako kwenye hivi vituo, basi Serikali itafanya utaratibu wa kuwapata wazazi wao ama walezi wao ama familia zao na kuweza kuwarejesha kwenye familia zao ama wakati wa likizo sasa waweze kurudi kwenye famila zao kama ambavyo ilivyo kwa watoto wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilijibu kwenye swali la Mheshimiwa Khadija Nassir na wakati pia natoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba sensa inafanyika kila baada ya miaka kumi. Ilifanyika mwaka 2012, lakini pia itafanyika mwaka 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kwa kuona umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watu wenye ulemavu kwa ujumla wake, wakiwemo watu wenye ualbino, basi inaandaa mpango ambapo yaani inafanya majadiliano ya ndani kwa kuona kwamba ni jinsi gani sasa tunaweza tukapata takwimu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaweka mipango, kwa hiyo, tutawatumia Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji ili kuweza kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu kutoka kwa pacha wangu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Watu Wenye Ulemavu ni haki na ni wajibu kwa sababu liko katika makubaliano ya utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006, ambao ni matokeo ya Sheria Namba 9 ya mwaka 2010. Hata hivyo tangu Baraza lilivyoteuliwa tayari limeshamaliza muda wake, lakini mpaka hivi sasa bado Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana hawajateua tena na kulitangaza Baraza ili liweze kushughulikia changamoto na tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuweza kuisaidia na kuishauri Serikali, katika suala zima la watu wenye ulemavu.
Ningependa kufahamu ni lini sasa Serikali itaunda hilo Baraza na kulitangaza ili liweze kufanya kazi zake na liweze pia kuishauri Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa maswala ya watu wenye ulemavu sasa tayari yapo kwenye Wizara hii husika katika Ofisi ya Waziri Mkuu na katika vyama hivi vya watu wenye ulemavu na kutokuwepo kwa hilo Baraza, imekuwa ni changamoto pia kwamba Serikali, haivisaidii kwa kiasi kikubwa hivi vyama; kwa mfano, Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo mpaka sasa hakina viongozi na matokeo yake ni kwamba mambo hayaendi kama yalivyo sawa, wameunda Kamati.
Sasa je, ni lini wataona umuhimu wa kuvisaidia hivi vyama kuvipa ruzuku kama ilivyokuwa hapo awali viweze kufanya mambo yao katika utaratibu unaotakiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maswali yake mawili nikianza na hili la kwanza, nikiri wazi kwamba kweli muda wa wajumbe wa Baraza la Ushauri umekwisha na sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ofisi yenye dhamana na masuala ya watu wenye ulemavu tayari tulishaviandikia vyama mbalimbali vyote. Kwa maana ya kwamba sisi kama Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hatuwateui wale wajumbe kutoka hewani, lazima tushirikishe vyama husika na wadau mbalimbali. Kwa hiyo sasa hivi hatua iliyopo, ni kwamba tayari barua tulishasambaza kwa vyama, na vyama tayari vimesha-respond kwa kutuletea majina mbalimbali. Sasa hivi kinachoendelea ni mchakato wa ndani wa ofisi yetu kuhakikisha kwamba sasa tunateuwa watu ambao wateweza kweli kusaidia watu wenye ulemavu, kwa masuala yanayowahusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali lingine ameuliza suala la ruzuku. Nipende kumthibitishia kwamba Serikali yetu ina nia ya dhati kabisa, katika kuhakikishwa kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili la ruzuku, tukiangalia huu Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu, ambao sasa katika jibu langu la msingi nimeshaliongelea kwamba tuko katika hatua nzuri, kwamba tumekwisha kutenga fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa huu mfuko. Miongoni mwa kazi za huu mfuko ni pamoja na kuhakikisha kwamba hivi vyama ikiwemo pamoja na ruzuku za vyama zinatekelezeka vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi ruzuku zitaendelea kutolewa kwa vyama pindi huu mfuko utakapokaa vizuri, na pindi ambapo zoezi zima la uteuzi wa wajumbe utakapokamilika.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi na naomba uniruhusu nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Stella Ikupa. Tangu amechaguliwa, amekuwa ni faraja na sauti yenye matumaini kwa walemavu wenzake na bidii yake ya kazi hapa Bungeni sote tunaiona. Kwa hiyo, namwombea Mwenyezi Mungu aendelee hivyo hivyo kwa sababu hata sisi walemavu watarajiwa tunawiwa kwake. (Makofi)
Sasa swali langu, katika jimbo langu kuna Chama cha Walemavu na kilikuwa kinapata ufadhili kutoka kwa mama mmoja Elizabeth kutoka Sweden. Chama hiki kiliingia kwenye mgogoro wa uongozi na kusababisha yule mfadhili akarudi nyuma, na baadhi ya walemavu pia wakarudi nyuma, kwa sababu ya kugombea baadhi ya vitu ambavyo walikuwa wanafadhiliwa.
Sasa nataka nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri, je, uko tayari utakapopata nafasi kuja Rombo ili tusaidiane kutatua ule mgogoro na kuwaweka wale walemavu vizuri katika chama chao. Ili wale wafadhili waweze kurejea na kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo ameeleza kwamba anashughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kwenye jimbo lake. Nimhakikishie kwamba baada ya Bunge hili nitaendelea na ziara, na miongoni mwa ziara ambazo nitafanya kama alivyoniambia au kama alivyoniomba, nitafika kwenye jimbo lake kwa ajili ya suala ambalo amelieleza mbele yako. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, niipongeze Serikali kwa majibu mazuri ya kitakwimu na naamini kwa majibu haya na kuonesha kwamba tuna walemavu zaidi ya milioni mbili, itasaidia Serikali yetu kuja na mpango mkakati wa namna gani ya kuwasaidia. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa, hapo Dar es Salaam Mkuu wetu wa Mkoa alileta mpango kuleta vifaa vya kuwasaidia walemavu na walemavu wengi sana wakajitokeza, ikionesha kwamba kuna shida hiyo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inawajengea uwezo walemavu, kwa maana wa viungo kuwaletea viungo ili wawe na uwezo wa kujitegemea wenyewe na wale wa kusikia wapate viungo vya kusikia ili waweze kujitegemea wenyewe na walemavu wengine? Pia, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo ili kupunguza athali ya ulemavu kwa kutumia viungo bandia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa mbona umeuliza kwa nini mbili hapo, kuna swali lingine tena! Maswali ni mawili tu na umeshataja kwa nini mbili, kwa hiyo maana yake maswali yako mawili, maana nisije nikakosea kanuni hapa itakuwa balaa. Mheshimiwa Ikupa Stella Alex, majibu!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa Kinondoni kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeza Mheshimiwa Maulid Mtulia kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya watu wenye ulemavu. Pia naomba niweze kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imekuwa na mipango mingi kwa upande wa uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi. Kwa sababu tunafahamu kwamba, mtu mwenye ulemavu, kulingana na aina yake ya ulemavu, asipowezeshwa kwa upande wa vifaa visaidizi, hawezi kujimudu. Kwa kuliangalia hilo, Serikali imekuwa ikitenga bajeti, lakini pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tumekuwa tukigawa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa kundi hili la watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha kwamba wanaweza kufanya vizuri kama ambavyo nimeongea kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba tumekuwa tukihakikisha kwamba tunawajengea uwezo kwa kuwawezesha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuhakikisha kwamba pia hata programmes ambazo tunakuwa tunaziandaa zinakuwa ni jumuishi kwa watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, suala la vifaa kwa watu wenye ulemavu, tumekuwa tukilifanya kama Serikali. Tunaona hata katika shule zetu, tumekuwa tukitenga bajeti ambayo tunanunua vifaa visaidizi na kuvigawa kwenye shule zetu, lakini haviishii tu kwenye shule, tunavipeleka hata kwa watu ambao siyo wanafunzi.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka niongezee kidogo katika majibu hayo. Kwanza Serikali imeondoa kodi katika baadhi ya vifaa saidizi kwa kutambua kwamba kuna kikundi ndani ya nchi yetu ambacho wanavihitaji vile vifaa na vinaweza vikawasaidia kuwa na maisha bora, kodi hizo katika baadhi ya vifaa zimeondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nilikuwa nataka niwape taarifa tu Waheshimiwa Wabunge, kuanzia mwezi huu wa Aprili, Hospitali ya Mifupa MOI, wataanza zoezi la kufanya upimaji pamoja na kutoa vifaa, viungo bandia kwa baadhi ya wale walemavu ambao wanavihitaji. Kwa hiyo, naomba kupitia Waheshimiwa Wabunge kutoa taarifa kwa watu hawa ambao wanahitaji viungo bandia, basi kufika katika Hospitali ya Taifa, MOI kwa ajili ya kuweza kupata vifaa hivyo. Hata hivyo, katika masuala ya vifaa vya usikivu tumekuwa tunaendelea na kampeni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili vya kupandikiza vifaa vya usikivu, lakini vilevile kutoa vifaa saidizi kwa wale watoto ambao wanahitaji vifaa hivyo.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo moja la nyongeza. Kwa kutambua mahitaji makubwa ya walemavu wananchi wa Moshi Vijijini kwa kushirikiana na Padri Apolnarys Ngao ambaye anaishi Ujerumani na marafiki zake kule Ujerumani, tunajenga kituo kikubwa cha walemavu kule Parokia ya Mawela. Naomba kumuuliza Waziri kama atakuwa tayari kuja kuona hii jitihada, kuitambua na kuhamasisha michango zaidi ili kuweza kufanikishi hii nia njema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anthony Komu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ameomba niweze kwenda kwenye hicho kituo ambacho kinaandaliwa sasa hivi, kwanza niwapongeze kwa hilo wazo jema kwa kundi hili la watu wenye walemavu. Mimi nikiwa kama Naibu Waziri mwenye dhamana hiyo, naomba niseme kwamba niko tayari.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanywa na Serikali, kundi la watu wenye ulemavu limeongezeka na ni walemavu wa tofauti. Je, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakubali kukutana na makundi hayo ili iwe rahisi kuwasaidia kwa sababu wana changamoto zinazotofautiana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, Balozi wa Watu Wenye Ulemavu, lakini pia babu yangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mwamoto, hajaanza leo kuhakikisha kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanakaa sawa, toka akiwa DC anafanya hivyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nimefanya ziara nyingi hapa Tanzania kwenye mikoa mingi na katika zile ziara zangu, ni lazima nikutane na makundi ya watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, niko tayari kwa hilo ambalo amelizungumza.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikia vigezo ambavyo vinatumika katika kutoa mikopo. Pia nafahamu katika maeneo yetu tunavyo vikundi vya wajasiriamali vikiwemo vikundi vya VICOBA na SACCOS. Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kufikisha elimu hiyo kwa walengwa na hasa walioko vijijini ili kuwawezesha wana VICOBA na SACCOS kunufaika na mikopo hii ambayo inatolewa na Baraza la Uwezeshaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nimekuwa nikisikia kwamba kuna Baraza la Uwezeshaji wa Taifa, napenda kujua haya Mabaraza yapo na ngazi za Mkoa, Wilaya na hadi ngazi za Kata ili wana vikundi wale waweze kuyatambua na kupata mikopo kupitia Mabaraza hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sikudhani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Sikudhani kwa jinsi ambavyo ameendelea kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wanapata manufaa ya yale yanayotendeka ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Sikudhani ni Mbunge wa Viti Maalum lakini tunaona anatetea wananchi kwa ujumla wake. Mheshimiwa Sikudhani, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nije kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, ameuliza ni njia zipi ambazo Serikali inazitumia kuhakikisha kwamba elimu hii ya uwepo wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ama fursa ambazo zinazopatikana ndani ya Taifa letu inawafikia wananchi wetu. Serikali siyo kwamba ina mikakati bali imekuwa ikifanya kwa kutumia media, tumekuwa tukitumia media mbalimbali kuhakikisha kwamba taarifa hizi za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinawafikia wananchi. Sambasamba na hilo Serikali kila mwaka tumekuwa tukitumia maonyesho mbalimbali ambapo katika mwaka wa fedha uliopita 2018 maonyesho haya yalifanyika Mkoani Mbeya lakini pia mwaka huu wa fedha maonyesho haya mwezi Oktoba yatafanyika Mkoani Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukifanya makongamano pamoja na semina mbalimbali. Katika makongamano haya tumekuwa tukishirikiana na Wakuu wa Wilaya kwenye Wilaya mbalimbali. Kupitia makongamano haya, tumekuwa tukienda na hii Mifuko yetu na kutoa elimu kwa wananchi wetu na wale ambao wanakuwa tayari basi wanapata mikopo palepale wakati wa maonyesho hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine tulio nao ni kwamba umeandaliwa Mwongozo wa kuipima Mifuko hii ni kwa jinsi gani inafanya kazi. Kipimo kimojawapo ni kuangalia ni kwa jinsi gani imetoa fedha kwa wananchi wetu au ni kwa kiasi gani imefikia wananchi wetu. Kwa hiyo, mikakati tuliyo nayo ndani ya Serikali ni mingi na Mwongozo huu utazinduliwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ameuliza Mabaraza haya yako katika ngazi zipi. Mabaraza haya yako kwenye ngazi za Halmashauri kupitia Waratibu. Tuna Waratibu mbalimbali ambao wanaratibu masuala haya ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu yake ya kuridhisha, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru unaleta maendeleo ni sawa lakini kuna changamoto na kuna hasara kubwa, kwa sababu mkesha wa Mwenge unapolala unakuwa kishawishi na maambukizi makubwa mapya ya UKIMWI jambo ambalo linapelekea vijana wengi kuathirika. Je, kwa nini Serikali haiweki mfumo mwingine kwa kulaza Mwenge huu kwenye Vituo vya Polisi au Ofisi za Halmashauri ili kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI kwa vijana wetu? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgeni, hilo la UKIMWI halina uthibitisho.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watu wanalazimishwa wakalale kwenye mkesha wa Mwenge wakiwemo wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara. Je, hii ni kwa mujibu wa kanuni au sheria gani? Nataka kufahamu kuhusu suala hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niuambie umma wa Watanzania kwamba Mwenge una faida kubwa sana. Pia niuambie kwamba hakuna Taifa ambalo halina chimbuko lake. Mwenge ni chimbuko la Watanzania na ni utamaduni wetu. Hivyo, Mwenge utaendelea kuwa chombo muhimu na alama ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba mkesha wa Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU, siyo kweli, kwa sababu kitu kimojawapo ambacho kinafanywa na Mbio za Mwenge ni kuelimisha mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya UKIMWI, Malaria pamoja na Kupambana na Dawa za Kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala haya ya UKIMWI, tunaelimisha nini kupitia Mwenge? Tunaelimisha kwamba ni lazima Watanzania wapime wafahamu afya zao, matumizi sahihi ya ARV’s na kuondoa unyanyapaa kwa waathirika wa magonjwa ya UKIMWI. Suala lingine ni mabadiliko ya tabia, Watanzania tunapaswa tubadilike tabia ili kuondokana na maambukizi mapya ya VVU. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Mwenge unasababisha maambukizi ya VVU kupitia hii mikesha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza amesema kwamba watu wanalazimishwa kwenda kwenye hii mikesha, siyo kweli. Hakuna mtu anayelazimishwa, kila mtu kwa mapenzi yake anaenda kwenye mkesha wa Mwenge. Mimi mwenyewe nilikesha hakuna mtu ambaye aliniambia Ikupa njoo ukeshe kwenye Mwenge, nilienda nilikesha.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanafunzi mbalimbali wanakwenda kwenye mikesha hiyo kutokana na hamasa ambazo zinafanywa na mbio za Mwenge. Kwa hiyo, hamasa za mikesha hii ndiyo zinafanya watu wanajitokeza kwenda kukesha na kusikiliza ni nini kimefanywa na Serikali yao lakini pia kujua ni nini kinaendelea kutekelezwa na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Serikali imezuia mikesha ikiwemo ngoma na mambo mengine ili kuondokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, hiyo ni dhahiri kabisa. Pili, kazi ambazo zinafanywa na Mbio za Mwenge zinaweza kufanywa na baadhi ya Watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali na tumeshuhudia uzinduzi wa miradi ya aina mbalimbali ukifanywa na watendaji hao. Je, kwa kuwa condom zimekuwa zikigaiwa maboksi na maboksi katika mikesha ya Mwenge, hamwoni sasa kuna haja Mwenge wa Uhuru ukawekwa makumbusho badala ya kutembezwa katika maeneo mbalimbali? (Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeweza kujibu wakati najibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mwengenge wa Uhuru una mambo mengi, mwenge wa uhuru ni tochi ambayo inaangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yanafanwa na mwenge wa uhuru kama ambavyo nimesema. Hii itaendelea kuwa alama yetu. Mbio hizi zitaendelea kukimbizwa kila mahali kwa sababu mwenge huu wa uhuru tukisema kwamba tunauhifadhi, je, hii miradi, kwanza nikielezea faida moja, mwenge wa uhuru unakagua miradi mbalimbali, miradi ambayo kama mwenge wa uhuru usingepita; sasa hivi tunaona kwamba Wakandarasi wengi wamekuwa wanahofu, wanajitahidi kuhakikisha kwamba mwenge unapofika mahali pale, ukute ule mradi wake uko vizuri. Sasa kama tukisema kwamba tuuhifhadhi huu mwenge wa uhuru, Mheshimiwa Mbunge nadhani tutakuwa hatujafanya kitu. Faida ambazo zinapatikana na mwenge wa uhuru ni kubwa kuliko vile ambavyo tunafikiria. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, amefanya kazi nzuri sana na ametoa majibu fasaha kabisa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, napenda tu niwakumbushe na niwarudishe kwenye dhana yenyewe ya mwenge wa uhuru. Tunapokwenda kwenye dhana ya mwenge wa uhuru tujue falsafa yake na chanzo chake ndani ya Taifa letu. Sasa tukifika mahali hapo, nadhani sisi wote tutakuwa na uelewa wa pamoja. Tukumbuke kwamba, chombo hiki mwenge wa ukuru ni ukumbusho wa uhuru wa Taifa letu la Tanzania ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa hili la Tanzania, ukiwa na falsafa ya kujenga umoja, mshikamano, ukombozi ndani ya Taifa letu na Bara zima la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenge huu umekimbizwa miaka hii yote na faida ya kuendelea kuenzi falsafa ya Baba wa Taifa imekuwa ni mfano mzuri hata kwenye Mataifa mengine kwenye Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona, ziko nchi katika Bara la Afrika kwa sasa nao wameanza kuwa na mienge yao katika matukio ya Kitaifa ambayo yanaashiria mambo yao ya msingi na ya muhimu kabisa katika Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, hakuna jambo linalofanywa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambalo halijaratibiwa kwa faida ya Watanzania tu ni kwa faida ya Taifa letu na nchi nzima kwa ujumla, hata Mataifa ambayo yako nje ya mipaka ya nje ya mipaka ya nchi ya Tanzania. Tuungane pamoja, tuenzi falsafa ya mwenge wa uhuru, tumuenzi Marehemu Baba wa Taifa na chombo hiki ni muhimu katika historia ya ukombozi wa Taifa letu. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakipata shida sana wanapokwenda kutibiwa katika hospitali zetu kwani kumekuwa hakuna mawasiliano kati ya daktari na mtu mwenye ulemavu kwa sababu ya daktari kutojua lugha za watu wenye ulemavu. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaweka mkalimani kati ya daktari na mtu mwenye ulemavu ili aweze kutibiwa kile ambacho anatakiwa kutibiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala ambalo ameliuliza Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba tuna upungufu wa wakalimani wa lugha ya alama. Wizara ya Afya ilishatoa maelekezo kwamba kwa kuwa sasa hivi tunajiandaa na tunawaandaa wakalimani wa lugha za alama basi watu wenye ulemavu wanapoenda hospitali waruhusiwe kwenda na watu ambao wanawaamini ili mawasiliano yaweze kufanyika vizuri kati ya mtu mwenye ulemavu na daktari ama na mtu anayemhudumia.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kitu chema kinaanza nyumbani basi napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa nini lugha ya alama haianzii hapa Bungeni pale juu tukawa na mkalimani maana hii haioneshi kwamba kweli tunataka mabadiliko kwa sababu Bunge lilitakiwa liwe mfano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Saleh, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo wakalimani wa lugha ya alama wawili. Hata sasa hivi tunavyozungumza haya yanayoendelea hapa yanatafsiriwa kwa lugha ya alama. Ahsante.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Tanzania ni nchi wanachama wa UN na tuliridhia na kusaini Mkataba wa Haki za Walemavu. Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kupeleka Ripoti ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu UN ili sasa tuweze kuona way forward ya wenzetu ambao wana ulemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khadija Nassir, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kweli iliridhia Mkataba huu wa Kimataifa na inatambua kwamba iko haja sasa ya kupeleka UN Ripoti ya Utekelezaji wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu. Ripoti hii inaandaliwa, ipo kwenye hatua za mwisho na karibia itawasilishwa. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyozifikia Halmashauri zetu na kutoa maelekezo namna ya kuitekeleza mahitaji ya watu wenye ulemavu. Nilikuwa nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mkakati wa kuanzisha kanzidata nilitaka kufahamu ni utaratibu gani unaotumika kuwapata wahitimu wenye ulemavu ili waweze kuingizwa katika kanzidata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili katika Halmashauri zetu kuna vikundi vya wajasiriamali wenye ulemavu wakiwepo mafundi selamala, lakini wameshindwa kupata masoko katika ofisi za umma. Nilitaka kufahamu Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia kupata masoko ili waweze kukuza mitaji yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya Mbunge wa Viti Maalum, pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Leah kwa jinsi ambavyo amekuwa akihakikisha kwamba watu wenye ulemavu Mkoani Simiyu wanaenda vizuri. Nilienda ziara Mkoani Simiyu tulikuwa naye na kuna mambo niliahidi na niliweza kutekeleza pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza ameuliza kwamba ni utaratibu gani ambao Serikali tunautumia kuwapata wahitimu hao wenye ulemavu na kuweza kuwaingiza kwenye kanzidata yetu.

Awali ya yote tuliweza kuviandikia vyuo vyote vya elimu ya juu pamoja na vyuo vingine ambavyo vinatoa mafunzo kwamba watu wenye ulemavu wanapohitimu basi Ofisi ya Waziri Mkuu kuna kanzidata ambayo tunawaingiza na kuweza kuwapatia ajira. Lakini njia nyingine ambayo tumekuwa tukiitumia ni watu wenye ulemavu mara nyingi wamekuwa wakipiga simu na wakija ofisini wao wenyewe physically kwa ajili ya kutafuta ajira. Kwa hiyo, wanapokuja pale ofisini tunapata zile details zao na kuweza kuwaingiza kwenye kanzidata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiongee tu kwa kifupi kwamba kanzidata hii imekuwa na manufaa makubwa, hata mwaka jana tuliweza kupata walimu ambao waliajiriwa pale nafasi za ajira zilipotangazwa kupitia kanzidata hii. lakini pia sasa hivi tuna programy ya internship kwa vijana na tunaposema vijana ni pamoja na vijana wenye ulemavu na tunaposema vijana ni pamoja na vijana wenye ulemavu. Kupitia kanzidata hii tumepata wahitimu wenye ulemavu zaidi ya 100 ambao watanufaika nah ii program ya internship. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kwamba ni kwa jinsi gani Serikali inafanya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata masoko ya bidhaa zao, tumekwisha kuzielekeza Halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya biashara za watu wenye ulemavu, lakini pia masoko ambayo yamekuwa yakiandaliwa sasa hivi tumesisitiza kwamba miundombinu ni lazima iwe rafiki kwa watu wenye ulemavu, lakini pia ndani ya hayo masoko wahakikishe kwamba kunakuwa na maeneo ambayo ni maalum kwa ajili ya watu wenye ulamavu. Mikakati ya Serikali iko migni lakini kwa ufupi ni hiyo. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali na hasa katika sekta ya elimu imefanikiwa kuajiri walimu wengi wenye mahitaji maalum, lakini changamoto kwa walimu hawa wanaoajiriwa tatizo kubwa ni vifaa maalum ambavyo vinawasaidia hasa walimu wasiioona, changamoto ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha kwamba walimu hawa wanaoajiriwa kwanza wanapelekwa katika shule zenye miundombinu rafiki, lakini pia vifaa hivyo kwamba wanawasaidia ili waweze kufanya kazi zao kwa ufasaha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mwongozo wa watumishi wenye ulemavu na mwongozo huu tumekuwa tukiutumia kuhakikisha kwamba mtumishi yeyote mwenye ulemavu anapata mahitaji yake ya msingi kwa mujibu wa yale ambayo yameelekezwa ndani ya mwongozo.

Kwa upande wa walimu wenye ulemavu tumekuwa tukielekeza ama mtu mwenye ulemavu yeyote si walimu peke yake, lakini mtu mwenye ulemavu yoyote anapokuwa anafika mahali akaajiriwa basi yeye ni wajibu wake na ndio mwongozo unavyosema kwamba ni wajibu wake kuweza kueleza mahitaji yake kwa mwajiri wake kwamba ili aweze kutekeleza majukumu yake basi mahitaji yake ya msingi ni nini na pale ambapo mwajiriwa huyu anapeleka mahitaji yake kwa mwajiri sisi kama Serikali tumekuwa tukifanya ni sawa na ambavyo tulikuja hapa Bungeni tulikaa na uongozi pia wa Bunge tukiwa Wabunge tukaeleza kwamba kama Wabunge wenye ulemavu tuna mahitaji gani na ili ufanisi wetu katika kazi uweze kwenda vizuri basi Bunge lifanye nini ili tuweze kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya Serikali haya yamekuwa yakifanyika, walemavu wa viungo wamekuwa wakipatiwa usafiri, lakini pia na wengine kulingana na mahitaji yao. (Makofi)
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kifungu cha 31 kinataka waajiriwa waajiri wote kuajiri angalau asilimia tatu ya watu wenye ulemavu. Ni nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Bunge ambalo ndio chombo kinachotunga sheria kinatimiza matakwa haya ili kutoa mfano kwa waajiri wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza Bunge kama nimemuelewa vizuri ameuliza kwamba ni nini sasa kwamba Bunge ili lioneshe mfano nadhani sasa hilo ni suala uongozi wa Bunge kwamba ni kwa jinsi gani sasa Bunge litafanya ili kuonesha mfano kwa kuajiri watumishi wenye ulemavu kwa kuzingatia sheria kwamba asilimia tatu ni lazima iwe ni watu wenye ulamavu. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutendea haki sana kiti chake na kujibu maswali mazuri yaliyoulizwa kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kupitia Tume ya Huduma za Bunge ambayo ndio yenye Mamlaka ya Ajira katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ajira kwa watu wenye ulemavu pia zimekuwa zikizingatiwa na kama Waheshimiwa Wabunge mtaona mnapishana na watumishi wengine baadhi ya watumishi kwenye Ofisi ya Bunge wakiwa wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kuweza kupitia hizo quota na viwango vinavyotakiwa kisheria yako mambo mengi ambayo pia yanatakiwa kuzingatiwa kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma. Hata hivyo Tume ya Utumishi wa Bunge itaendelea kuzingatia sheria nyingine pamoja na sheria hii ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu ili kuhakikisha kwamba kadri watu wenye ulemavu wanavyoweza kutoa huduma na kuajirwa katika taasisi za Serikali na sekta binafsi waendelee kupewa nafasi na haki sawa kama Watanzania wengine. (Makofi)
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali ambayo kwa kiasi fulani yanatoa mwangaza kidogo na yanaonesha matumaini katika maelezo sijui kwenye utendaji itakuwaje. Pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kulitamka jina langu kama vile ambavyo linatakiwa litamkwe, hakulikosea hiyo ndio asili ya jina Muhammed Amour Muhammed.

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tunategemea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka nchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ratio ya uwazi kabisa katika kutoa ajira Serikalini kwa watu wenye ulemavu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, watu wenye ulemavu nao ni watu kama wengine, wanasafiri wanaenda kwenye viwanja vya michezo kama football na kadhalika tunawaona mara nyingine wanapata tabu bandarini pale, saa nyingine airport na mara nyingine kwenye vituo cha mabasi. Je, Serikali imejipangaje katika kuweka miundombinu wezeshi kwa watu wenye uleamavu katika maeneo kama yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge vile ambavyo anafuatilia masuala haya ya watu wenye ulemavu. Ameulizia kuhusiana na ratio ni kwa jinsi gani Serikali ina weka ratio ya ajira kwa watu wenye ulemavu. Bunge letu Tukufu lilitunga Sheria Na.9 ya mwaka 2010, ndani sheria imeelezwa wazi kwamba watu wenye ulemavu ni kwa jinsi gani wanatakiwa kuajiariwa. Mwajiri yoyote mwenye watu kuanzia 20 na kuendelea, basi 3% inatakiwa kuwa ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, kwa hili lipo wazi na niendelee kuwasihi na kuhawamasisha waajiri kwamba waweze kuitekeleza sheria hii kwa sababu sheria hii ya watu wenye ulemavu ni sawa na sheria zingine na pia inapobidi sheria itachukua mkondo wake wa yule ambaye atakuwa hatekelezi.

Mheshimiwa Spika, vile vile ameuliza ni kwa jinsi gani Serikali inahakikisha kwamba usafiri kwa watu wenye ulemavu unakuwa ni rafiki. Mimi mwenye nimefanya ziara katika maeneo kadhaa ikiwemo airport, lakini pia tumeendelea kusisitiza na kuweka mkazo kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa rafiki. Katika airport kwa hapa nchini tunahakikisha kwamba kunakuwa na wheelchair lakini kunakuwa na zile ambulift kwa ajili ya kubeba watu wenye ulemavu pamoja na wazee.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia kwenye maeneo ya usafiri wa umma ikiwemo huu usafiri wa kawaida hiyo ni changamoto ambayo nikiri wazi tunaendelea kuifanyia kazi kwa kuendelea kuelekeza wamiliki wa vyombo hivi kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia habari ya huduma stahiki na sasa hivi mobility ni huduma stahiki kwa watu wenye ulemavu. Swali langu linakuja kwamba, je, haoni ni wazo nzuri sasa kwamba Serikali itoe agizo kwamba katika parking lots katika public spaces kunakuwa na uhakika wa nafasi ya kuwekwa maalum kwa watu wenye ulemavu ambao aidha wanaendeshwa au wanaendesha wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Ally Saleh kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huu ni ushauri mzuri ambao tunaupokea, lakini pia kama serikali tayari tumekwishaanza kufanya hivyo, hata tukienda kwenye airport mpya ambayo tumeijenga pale Dar es Salaam tumeona kabisa kuna parking maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Pia hata kama ukienda maeneo mengine hili limekuwa likifanyika, lakini tunapokea kama ushauri ili tuendelee kuhamasisha maeneo mengine kuwa na parking maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Vile vile kwa Watanzania wote ambao wananisikia waweze kulitekeleza hili kuhakikisha kwamba parking za watu wenye ulemavu zinakuwepo. Kwa kweli inakuwa ni usumbufu mtu mwenye mwenye ulemavu akifika akikuta magari yamejaa anaanzia kuhangaika na hasa akiwa anaendesha yeye mwenyewe. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo, ningependa kufahamu tu kwamba, ni lini sasa Serikali itaanza kutoa ruzuku hasa kwa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya Vyama vya Watu Wenye Ulemavu badala ya vyama hivyo kutegemea wafadhili. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Mollel, pacha wangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimewahi kujibu mara kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu, kama Serikali tukiwa tunaahidi Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu utakapotengewa fedha ndipo ambapo hivi Vyama vya Watu Wenye Ulemavu vitaweza kupatiwa ruzuku. Pia niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika bajeti ya mwaka huu, fedha zimeweza kuwekwa kwenye Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu na hivyo basi tunasubiri uzinduzi ufanyike, baada ya hapa ruzuku hizi za Vyama vya Watu Wenye Ulemavu zitaendelea kutolea.

Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu kuwa wabunifu, kama ambavyo Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo ameendelea kusisitiza jinsi gani ya vyama ama maeneo mbalimbali kuweza kujitegemea. Kwa hiyo pia niombe ubunifu kwa viongozi wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu ili kuwa na miradi na si kutegemea Serikali peke yake.