Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Silafu Jumbe Maufi (8 total)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI kuhusu swali langu, nina swali la nyongeza.
Pamoja na jitihada na changamoto walizonazo na kuhakikisha kwamba masomo haya yanapatikana katika maeneo yetu ya Rukwa na hasa katika Mikoa yetu ya pembezoni. Kwa kuwa tumechelewa kupata elimu hii na speed ambayo wanakwenda nayo naona kana kwamba haitaweza kuleta mafanikio mazuri kwa mikoa yetu ya pembezoni. Swali langu dogo napenda kuuliza kwa niaba ya Mkoa wa Rukwa, ni lini sasa Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo masomo hayo yatafikishwa kwani Makao Makuu ya Wilaya hizi umeme umekwishafika?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tukiri kwamba suala la kompyuta sasa hivi na elimu ya TEHAMA ni jambo la msingi sana kama tunataka twende katika maendeleo ya kasi. Tumejielekeza sasa hivi, kama jibu langu la msingi lilivyosema kwamba, tutatumia kila liwezekanalo kuhakikisha tunawezesha vijana katika shule hizi kupata elimu hii ya kompyuta.
Suala la Nkasi na Kalambo ni kweli, katika maeneo mbalimbali ambayo tunataka tuyape nguvu hasa ukiangalia mkoa huu una changamoto kubwa sana, jambo hili hata Mheshimiwa Keissy na Mbunge wa Viti Maalum huwa eanalizungumzia sana, siyo hilo tu na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nieleze wazi katika michakato ambayo tutaifanya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sababu Mkoa wa Rukwa ni Mkoa wenye changamoto kubwa sana, tunaita mikoa ya pembeni, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo katika program zetu Wilaya hizi tuwape kipaumbele, kwa sababu maeneo mengine ya mijini kama vile Dar es Salaam, Arusha na Mikoa mingine ni rahisi zaidi vijana ku-access mambo ya kompyuta kuliko mikoa ya pembezoni. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa na hasa katika Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya kitaalam ambayo kwa namna moja au nyingine akina mama zangu wa Mkoa wa Rukwa na hususan wa Bonde la Tanganyika, bado hawajatendewa haki. Tunasema ya kwamba tunazuia magonjwa na vifo vya wamama na watoto, katika maeneo haya hatutakuwa tumezuia vifo vya akina mama na watoto, bali tutaendeleza vifo hivyo.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Waziri anahusika vilevile na suala zima la mawasiliano, afahamu ya kwamba kata ya Kara haina mawasiliano ya barabara na wala haina mawasiliano ya simu. Huu utaalam wa TARURA watakuwa wamewapa umuhimu upi wa kuweza kuyafanyia kazi katika hizi barabara zetu za Ziwa Tanganyika na vilevile zinazoelekea kwenye barabaa za Ziwa Rukwa ziko katika hali hiyo hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kupata majibu yaliyokuwa sahihi hasa kuhusu akina mama zangu wa Bonde la Tanganyika na Bonde la Rukwa, wanasaidiwa vipi juu ya hizi barabara na hao ndugu wa TARURA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi kwa namna anavyoshirikiana na Wabunge wenzake katika kufuatilia masuala mbalimbali ya maendeleo ya watu wa Mkoa wa Rukwa na vilevile Mkoa wa Katavi. Sina uhakika kwa nini wanashirikiana wakati ni watu wa mikoa miwili tofauti, lakini nadhani ni kwa sababu maeneo yao yanafanana. Mara nyingi barabara anazoziongelea nyingine zinaunganisha mikoa yote hii miwili, kwa mfano, barabara zinazoenda kwenye Ziwa Rukwa zinapita katika mikoa hii yote miwili.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie, kama ambavyo tumeweka katika bajeti, barabara hizo tutazishughulikia kwa kadiri bajeti ilivyopangwa. Kwa mfano, barabara inayounganisha mikoa hiyo miwili, lakini vilevile na Mkoa wa Songwe anafahamu kwamba tumeanza kujenga daraja linalounganisha mikoa hiyo na tukishamaliza kujenga daraja, tutaanza sasa kuiangalia barabara yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kubwa nimhakikishie kwamba Serikali inafahamu sana na wala haina nia hiyo anayoiongelea. Barabara hizo zitashughulikiwa na TARURA kwa kiwango na kwa kasi ile ile ambavyo angetegemea kwa kuzipandisha hadhi. Kwa sababu TARURA na TANROADS kwa sasa wana hadhi sawa na uwezo sawa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata kwenye upande wa rasilimali fedha nako huko tunakuangalia, ili kuhakikisha taasisi hizo mbili zinatekeleza ahadi zetu na ahadi za viongozi katika maeneo hayo ambayo yameulizwa kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru hayo majibu niliyopewa na Mheshimiwa Waziri, lakini niliuliza swali kwamba kufufuliwa Kambi ya JKT, sikuuliza swali la kwamba mabadiliko ya matumizi ya Kambi ya JKT, la hasha. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa tunajua wazi kwamba kujiunga kwa vijana wetu kwenye JKT ndiko ambako kuna chachu ya kuwawezesha wao kujiunga na Polisi, kujiunga na JWTZ na kadhalika. Sasa je, ni sababu zipi zilizopelekea kutoka JKT na kuwa Kikosi cha Jeshi na kusababisha Mkoa wetu wa Rukwa kukosa Kambi ya Jeshi?
Swali la pili, je, vijana wetu ambao wanauhitaji wa kujiunga na JKT wa Mkoa wa Rukwa kutokana na wingi wao wa kila mwaka kuongezeka ndani ya jamii, je, hawa vijana watanufaika vipi na vikosi hivyo ambavyo vimebadilishwa makambi yao kuwa ni vikosi vya Jeshi au watajengewa Kambi ya Jeshi upande gani? Naomba uniambie katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge kwa kuguswa kwake na vijana hasa hasa wa Mkoa wa Rukwa na hoja yake ya kutaka vijana wapate fursa hiyo, lakini nimhakikishie tu ninapojibu maswali yake yote mawili kwa pamoja ni kwamba Kambi la Jeshi kubwa hasa linaloangaliwa ni suala la kibajeti.
Natambua katika nchi nzima vijana wengi hata maeneo ambako kuna Kambi wengi sana wanajitokeza kuomba nafasi hizo, unaweza ukakuta Wilaya ambako wamejitokeza vijana kama 500, idadi inayotakiwa kupatikana labda ni 50 mpaka 60 kwa maana hiyo sisi kama Serikali tunapokea tu hoja ya Mbunge na uhitaji mkubwa huo wa kuona vijana wanataka kujitolea kwenda kujenga Taifa ili tuliangalie kwenye upande wa bajeti kwasababu kwenye upande wa makambi hilo ni jambo rahisi tu ambalo wanaweza wakakaa tu katika Kambi yoyote ile na mafunzo haya yakaendelea kama ambavyo inafanyika katika mikoa mingine.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu suala hili, bahati nzuri mwenyewe anayezungumza ni ametoka Mkoa wa Rukwa, kwa hiyo, barabara hii anaifahamu vilivyo. Akina mama wengi na watoto wanapata shida kwenye barabara hii wanapokuja kupata huduma ya afya Namanyere.
Napenda kuiuliza Serikali, je, ina mpango gani kwa hivi sasa kwa sababu tupo katika kipindi cha bajeti kuweza kutenga fedha za kutosha kuikamilisha hii barabara badala ya kuendelea kutengeneza maeneo korofi kila mwaka hadi mwaka na kuonekana kana kwamba ni mradi wa Serikali? (Makofi)
Swali la pili, ninapenda kuiomba Serikali ijaribu kuona hizi barabara zetu za Bonde la Lake Tanganyika na Bonde la Lake Rukwa, barabara hizi ni tata, zinahitaji matengenezo yaliyokamili kama vile Kitonga na inavyoelekea kutumika katika kipindi chote cha mwaka mzima.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba barabara hii ina changamoto kubwa maana kuna maeneo ambayo kuna milima mikubwa sana na azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Ninde wanapata barabara inayoweza kupitika kwa vipindi vyote.
Mheshimiwa Spika, kabla ya hapo ilikuwa hakuna barabara kabisa na ndiyo maana Serikali kwa kulitambua hilo ikaanza kutenga kiasi cha shilingi milioni 350 na maeneo yaliyokuwa korofi zaidi ilikuwa ni maeneo ya madaraja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ilimradi madaraja yameshajengwa ambayo ndiyo yalikuwa ni changamoto kubwa sana, nia na azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yaliyobaki yataweza kutengenezwa kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
Katika swali lake la pili, ameongelea Ukanda wa Ziwa Rukwa. Sifa ya Ukanda wa Ziwa Rukwa na hii barabara aliyoitaja ya kwenda Ninde hazina tofauti sana na Mbunge, Mheshimiwa Malocha amekuwa akiipigia kelele sana na kwa mara ya kwanza Serikali imesikia kilio chake na barabara hii inaweza kuimarishwa ili iweze kupitika katika kipindi chote.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya kuiuliza Serikali yangu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mikoa hii ya pembezoni Serikali imekuwa inasuasua kuwapelekea huduma zinazohitajika kwa maendeleo ya jamii. Napenda kuiambia Serikali kwamba huu uzoefu walioupata kutoka Ziwa Victoria kupeleka maji Shinyanga, Tabora, Simiyu na kadhalika naomba basi uzoefu huu wakaupeleke katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii speed ya kupeleka maji katika Mji wa Ujiji ni ndogo sana, haina matunda mazuri kwa mikoa hii mitatu. Je, Serikali inasema nini katika kuhamisha uzoefu huu wa Ziwa Victoria na kuuweka katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni kwamba inatumia fedha nyingi za kuchimba visima virefu katika vyanzo ambavyo havina uhakika, inaonaje ikatumia vyanzo hivi ambavyo ni vya uhakika…
Mheshimiwa Spika, ni katika kujenga hoja na kuweka mambo sawa. Napenda kufahamu ni lini hii awamu ya pili itaanza ili hivi vyanzo vya uhakika vya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa vifanyiwa kazi ili wananchi wa Rukwa wapate maji ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge na ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua changamoto kubwa sana ya maji katika eneo lake. Sisi kama Wizara tupo tayari sasa kutoa ushirikiano na uzoefu wetu katika kuhakikisha wananchi wake wa maeneo ya Rukwa wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe sisi ni Wizara ya Maji na siyo Wizara ya Ukame, tupo tayari kuwapatia maji wananchi wa Rukwa.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza jitihada, nipo tayari kufanya ziara maeneo ya Mheshimiwa Mbunge ili kuangalia namna ya kuweza kutatua tatizo hili kwa haraka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri katika swali langu la msingi, mimi kama Mheshimiwa Mbunge wa Bunge hili la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na bahati nzuri kwa rehema zake Mwenyezi Mungu, jana tu tumepitisha sheria ya kuiwezesha Serikali kuingia ubia na mashirika binafsi katika maendeleo ya wananchi wetu wa Tanzania.
Je, kwa nini Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa wao kuingia ubia na sekta hii binafsi yenye viwanja hivi vinavyomikiwa na hawa watu ambao ni viwanja vyao vya halali? Kwani wamevijenga kwa muda mrefu na wanasuasua katika kuviendeleza viwanja hivi ili waweze kuingia ubia waweze kuvikarabati na watoto wetu wapate afya njema na waweze kupata ajira katika maendeleo yao.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali inipatie majibu kwa hilo swali dogo ambalo nimeliuliza kwa wakati huu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba moja kati ya mkakati wa kuendeleza michezo mbalimbali nchini ni pamoja na kuwa na miundombinu rafiki ya kuwafanya washiriki wa mchezo husika kuweza kushiriki kwa ufanisi mkubwa. Ni dhamira ya Serikali kuendeleza viwanja vingi vya michezo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mbunge wa kushirikisha sekta binafsi na wadau mbalimbali, sisi kama Serikali tuko tayari. Lengo letu ni kujenga mazingira rafiki ya kufanya michezo mbalimbali iliyo na miundombinu ambayo itatoa fursa kwa washiriki wake kushiriki kikamilifu.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini bado napenda kufahamu kwamba, ikiwa mikoa na wilaya zimeweza kutanganza fursa ambazo zimo ndani ya mikoa husika, lakini bado mikoa ile ama wilaya zile zinasuasua katika kupata wawekezaji; Je, Serikali haioni umuhimu wa wao wenyewe kwenda kusukuma katika mikoa ile na wilaya zile kuweza kupata viwanda hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili la nyongeza, napenda kufahamu kwamba wanapewa muda upi wa utangazaji wa fursa na kama fursa haina majibu Serikali inachukuwa mkakati gani katika mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maufi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuupongeza sana Mkoa wa Rukwa umekuwa ukifanya makongamano mbalimbali ya kuhamasisha uwekezaji na makongamano hayo kwa kweli yamekuwa yakiza matunda. Kwa mfano, wameweza kuhamasisha na kupata kiwanda cha kusindika unga wa mahindi, Kiwanda cha Energy, vilevile wameweza kuhamasisha na mpaka kuwezesha mradi wa makaa ya mawe kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali hatuiachi mikoa peke yao isipokuwa mikoa yenyewe kwa sababu inazo fursa hizo kwa karibu zaidi inapohamasisha inaungana na Serikali Kuu kuona kwamba hawa wenye viwanda waweze kwenda kuwekeza huko. Sisi kwa kutumia Tantrade, TIC na Wizara kwa ujumla kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji tumekuwa tukiendelea kuhamasisha wenye viwanda au wawekezaji mbalimbali kwenda kwenye maeneo hayo.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kutoa majibu mazuri katika swali langu namba 396, lakini kutokana na mfumo dume tulionao katika nchi yetu ya Tanzania, hizo sheria kihalisia hazitekelezeki ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba elimu haijawafikia wananchi wetu na hususan akina mama wenzangu ndiyo wanaonyanyasika sana na sheria hizi, inapofika wakati wa mirathi mama anakosa kupata haki iliyokuwa sahihi. Ifahamike wazi ya kwamba Wizara inasema inapitia RITA, hiyo RITA huenda ikawa iko Dar es Salaam, lakini katika Mkoa wa Rukwa na Mikoa mingine RITA hiyo haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kuuliza swali langu; je, Wizara au Serikali ipo tayari kuweka mkakati maalum wa kutoa mafunzo endelevu na hasa kwa kina mama kuelewa haki zao katika kuhakikisha kwamba wanatimiziwa haki zao? Kwa sababu wanahitaji uwakilishi wa sisi Wabunge ni dhahiri kusema ya kwamba…(Makofi)

SPIKA: Sasa swali.

MHE. SILAFU J. MAUFI: ...hata Wabunge elimu hiyo hawana; je, wako tayari Serikali kutoa mafunzo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wanawake hawa wajane wamekuwa ni wengi, wanaume wagane ni wachache kwa sababu mwanaume mgane ni wa dakika mbili baada ya muda anaweka mke mwingine ndani, kwa hiyo, anakuwa siyo mgane tena, lakini mjane anaendelea kuwa mjane. (Makofi)

Kwa kuwa wako wengi na wako katika makundi mbalimbali; je, Serikali inaona mkakati gani wa kuwawekea mpango wa kuwawezesha kimkopo ili kina mama hawa waweze kujendeleza na kuhudumia familia zao? Naomba majibu hayo. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, mimi naungana mkono na mama, kwa kweli katika utekelezaji wa sheria hizi hasa za mirathi akina mama wamekuwa siyo tu wanasumbuliwa, lakini wanabaguliwa. Tatizo hili linajionesha kadri tunavyokuwa mbali na miji hasa kwa akina mama walioko vijijini. Ni kweli kwamba katika mfumo dume, zile mali mara nyingi ziko chini ya mwanaume na wanawake inapokuja kwenye mirathi wanawekwa pembeni au ndugu wa yule aliyefariki mwanaume wanamnyanyasa yule mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaona umuhimu na ninakubaliana na wewe kwamba RITA ipewe jukumu kubwa la kuelimisha wananchi wote kwa ujumla, naomba mashirika mbalimbali ya akina mama tushirikiane katika kueneza elimu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana kwamba mbali na elimu hizi za vipeperushi au machapisho kuna haja ya kuwa na mkakati maalum, mkakati ambao hata Wizara yangu, Majaji, Hakimu watakuwa wanaelezwa na kushirikiana na utawala kwa ujumla katika Mikoa na katika Wilaya. Pendekezo hili na jinsi lilivyoungawa mkono hapa nitalipa kipaumbele katika Wizara yangu, ahsante sana. (Makofi)