Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Silafu Jumbe Maufi (11 total)

MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali imeamua kutoa elimu ya kompyuta kwenye shule za sekondari nchini lakini vifaa vya kufundishia havitoshelezi na hata Walimu ni wachache katika maeneo mengi ikiwemo Mkoa wa Rukwa, ambapo ni shule mbili pekee za Mazwi na Kizwite Sekondari ambazo zimeshaanzishwa:-
Je, Serikali ina mpango mkakati upi wa kufanikisha ufundishaji wa somo hilo kwa tija?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa elimu ya kompyuta mashuleni umeanza kufanyika kwa baadhi ya shule zenye mazingira yanayowezesha somo hilo kufundishwa. Changamoto zilizopo ni uhaba wa Walimu, ukosefu wa umeme hususani maeneo ya vijijini na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Serikali inakabaliana na changamoto hizo kwa kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), pamoja na kuhakikisha somo la Kompyuta linafundishwa katika Vyuo vya Ualimu ili kuwaandaa walimu watakaofundisha somo hilo mashuleni. Kuhusu upatikanaji wa vifaa mashuleni Serikali inashirikiana na Kampuni ya Microsoft ambayo imeonesha nia ya kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa muda mrefu wa Serikali ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji mashuleni hususani masomo ya sayansi. Kwa msaada wa Kampuni ya Microsoft imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa shule 50 katika Mikoa 25. Kwa Mkoa wa Rukwa shule zilizochaguliwa ni shule ya Sekondari ya Kizwite na Mazwi. Shule hizi mbili kila Mkoa ni vituo vya mafunzo kwa Walimu ili kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa kutumia TEHAMA. Kituo cha Mazwi kinaanza kufanya kazi kuanzia Julai, 2016 ambapo kitapewa vifaa vyote muhimu vitavyohitajika katika mafunzo hayo.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Wananchi wamehamasika kujenga zahanati kwenye vijiji vyao lakini baadhi hazijakamilika na hata zile zilizokamilika hazijafunguliwa bado na watumishi nao hawatoshelezi mahitaji; hali hii inasababisha hospitali za mkoa ambazo ndizo za rufaa kuwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya Wilaya hazina Hospitali za Wilaya.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani ya utekelezaji wa kutoa unafuu wa uchangiaji huduma kwa akina mama wajawazito wanaoenda katika Hospitali za Rufaa?
(b) Je, ni lini Serikali itachukulia afya kuwa ni kipaumbele cha nchi hasa ikizingatiwa kuwa afya ni kila kitu katika maisha ya mwanadamu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu (a); Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma za akina mama wajawazito katika vituo vya ngazi zote ni bure na hazipaswi kuchangiwa. Aidha, mwongozo wa uchangiaji pia umesisitiza utekelezaji wa sera hii. Ili kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma wanazozihitaji Wizara inahakikisha wanakuwa na vifaa muhimu vya kujifungulia, ambapo vifuko maalum vyenye vifaa vya kujifungulia (delivery packs) vitasambazwa kwa wanawake 500,000 nchi nzima kulingana na uhitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu (b); siku zote Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele kwa sekta ya afya katika nyanja zote na ndiyo maana Serikali inatoa huduma ya afya bure kwa watu wasiojiweza na kwa usawa kwa wote. Sekta ya afya imeendelea kuwa ya kipaumbele kwa Serikali kwani katika mgao wa bajeti ya mwaka 2016/2017 imekuwa ya tatu kwa kutengewa asilimia 9.2 ya bajeti yote.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. SILAFU J. MAUFI) Aliuliza:- Rukwa ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha mazao ya chakula hasa mahindi na mpunga kwa wingi na hivyo kusaidia upatikanaji wa chakula kwa Taifa. Maeneo mengi ya kilimo katika mkoa huo ikiwemo Bonde la Rukwa yanakabiliwa na changamoto ya barabara mbovu na hivyo wakulima kushindwa kusafirisha mazao yao kwa wakati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za Kibaoni (Katavi) – Muze (Rukwa) – Kilyamatundu – Kamsamba (Songwe) hadi Mlowo, Sumbawanga – Muze, Kalambazite – Chambe (Ilemba) na Miangalua – Kilyamatundu (Kipeta) kwa kiwango cha lami ili wakulima wasafirishe mazao yao kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge Viti Maalum wa Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibaoni – Kasansa – Kilyamatundu – Kamsamba hadi Mlowo ni miongoni mwa barabara zinazounganisha Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii ni muhimu katika uchumi wa nchi kwa kuwa inapita katika Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu sana kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Aidha, barabara za Ntendo hadi Muze, Kalambazite hadi Ilemba na Miangalua hadi Chombe hadi Kipeta ni muhimu katika usafirishaji wa mazao ya kilimo katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi imeanza kuchukua hatua za dhati za kuhakikisha kuwa barabara hizi zinapitika katika majira yote ya mwaka. Katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, Serikali ilitenga jumla ya Sh.3,989,030,000 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara hizo pamoja na madaraja yake.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imedhamiria kuanza ujenzi wa Daraja la Momba ambalo linaunganisha barabara ya Sitalike – Kibaoni – Muze – Ilemba hadi Kilyamatundu na Kamsamba hadi Mlowo ambayo ni kiungo muhimu kwa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe. Daraja hili limetengewa jumla ya Sh. 2,935,000,000 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 na limeombewa Sh. 3,000,000,000 katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe kuwa Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi kiuchumi na kijamii na inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hizo ili hatimaye zijengwe kwa kiwango cha lami.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Kata ya Kula ipo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika umbali wa takribani kilometa 50 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi huku kukiwa hakuna barabara ya kuunganisha kata hiyo yenye mawe mengi na miteremko mikali kufika huko.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuzichukua barabara zenye kuelekea Bonde la Ziwa Tanganyika na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuna barabara tatu zinazoelekea katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ambazo zinaunganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi. Barabara hizo ni Nkana – Kala ambazo urefu wake ni kilometa 67, Kitosi - Wampembe yenye urefu wa kilometa 68 na Namanyere hadi Ninde yenye urefu wa kilometa 60 ambazo pia zinaunganisha Makao Makuu ya Kata za Kala, Wampembe na Ninde. Barabara zote hizi zinasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kupandisha hadhi barabara mbili kati ya tatu nilizozitaja, tayari yamewasilishwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Tathmini ya Wizara baada ya kuyapitia maombi hayo ilibainisha kuwa Barabara za Nkana hadi Kala yenye urefu wa kilometa 72 na Kitosi hadi Wampembe yenye kilometa 68 hazikidhi vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa barabara ya mkoa. Hivyo ilipendekezwa zibaki katika hadhi ya sasa. Kwa upande wa barabara ya Namanyere hadi Ninde yenye kilometa 60, kumbukumbu za Wizara zinaonesha haijawahi kuombewa kupandishwa hadhi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), barabara zote zitaendelea kuhudumiwa na TARURA chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
MHE. SILAFU J. MAUFI
Serikali imerejesha mafunzo ya JKT nchini. Je, ni lini Kambi ya JKT ya Luwa Mkoani Rukwa itafufuliwa ili kuandaa vijana wetu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Maufi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Luwa JKT ilifufukiwa na sasa kimekuwa Kikosi na kimepewa namba 846 Kikosi cha Jeshi yaani 846 KJ kuanzia tarehe 01 Desemba, 2016.
Aidha, vikosi vilivyoanzishwa sambamba na kikosi hicho ni pamoja na Kikosi cha Jeshi 826 kilichopo Mpwapwa hapa Dodoma, 839 Kikosi cha Jeshi kilichopo Makuyuni, Mjini Arusha, 845 Kikosi cha Jeshi kilichopo Itaka, Mkoani Songwe na 847 Kikosi cha Jesi kilichopo Milundikwa, Mkoani Rukwa.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali ilitoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi hadi Ninde yenye urefu wa kilometa 40 lakini hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo bado haujakamilika kwa muda mrefu sasa.
(a) Je, ni lini Serikali itachukua hatua kwa kufuatilia na kuchunguza matumizi ya fedha zilizotolewa na kuchukua hatua ili ujenzi wa barabara hiyo uweze kukamilika?
(b) Je, ni lini wananchi wa Ninde wataondokana na changamoto ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Namanyere - Ninde yenye urefu wa kilomita 60 katika mwaka wa fedha 2014/2015 ilitengewa shilingi milioni 350 za kufanyia matengenezo kama ifuatavyo:-
• Ujenzi wa daraja moja lenye urefu wa mita 20 kwenye Mto Lwafi kwa shilingi milioni 73.69;
• Ujenzi wa daraja moja lenye urefu wa mita 50 kwenye Mto Ninde kwa shilingi milioni 33.922 ;
• Ujenzi wa madaraja mawili yenye urefu wa mita tano kila moja kwenye msitu wa Lwafi kwa shilingi milioni 26.65; na
• Kuifungua sehemu iliyokuwa imebakia ya barabara ya urefu wa kilometa 25 kwa kufanya matengenezo kwa kiwango cha udongo na kujenga makalvati mistari 15 kwa shilingi milioni 154.735 pamoja na gharama za usimamizi jumla ya shilingi milioni 61.003.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kupambana na changamoto ya barabara kwa wananchi wa Ninde kwa kuitengea fedha za matengenezo barabara hiyo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 shilingi milioni 44.58 zilitengwa kwa ajili ya kufanyia matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilometa mbili. Aidha, mwaka wa fedha 2016/2017 shilingi milioni 20 zilitengwa na kutumika kuimarisha sehemu korofi zenye urefu wa mita 500.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanyia matengenezo barabara hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili iweze kupitika na kuondoa tatizo la usafiri kwa wananchi wa Ninde na maeneo jirani.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Kumekuwa na changamoto katika kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma pamoja na kuwa Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa yako katika mikoa hiyo.
Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuanzisha mradi wa maji kutoka kwenye vyanzo hivyo na kusambaza kwa wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuboresha huduma ya maji kwa wananchi, Serikali imeanza kutekeleza miradi ya kutoa maji katika maziwa makuu nchini kupeleka kwa wananchi wanaozunguka maziwa hayo. Katika Mkoa wa Kigoma, Serikali inatekeleza mradi unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 42 kutoka Ziwa Tanganyika kwenda katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na jitihada za kutumia vyanzo vya maji vya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma. Hivyo, Wizara imeziagiza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za mikoa husika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya maji na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya miradi ya maji itakayotumia vyanzo hivyo. Utekelezaji wa miradi hiyo ni kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili (WSDP II).
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali inafahamu kuwa michezo ni afya na ni ajira pia, lakini mikoa kadhaa hapa nchini ina viwanja visivyokidhi hadhi ya kitaifa na kimataifa na hata kasi ya kuibua vipaji vipya imedorora katika Mikoa ya Rukwa, Tabora, Iringa, Kigoma na kadhalika.
Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo kuvikarabati na kuviboresha kufikia hadhi stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba ujenzi wa miundombinu ya michezo ni jambo muhimu sana katika kuendeleza vipaji vya wanamichezo na ndiyo sababu ya Serikali kujenga viwanja changamani vikubwa viwili nchini ambavyo ni Kiwanja cha Uhuru na Kiwanja cha Taifa, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kazi ya ujenzi wa kiwanja kikubwa cha Ngamani cha tatu Jijini Dodoma yanaendelea. Hata hivyo Serikali haiwezi peke yake kujenga miundombinu ya kisasa kwa michezo yote bila mchango wa Halmashauri zetu, taasisi za umma, asasi na kampuni binafsi na vilevile mashirikisho na vyama husika vya michezo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, pale penye jitihada bayana za kujenga miundombinu ya michezo, Serikali daima imekuwa mstari wa mbele kusaidia juhudi hizo. Utaratibu mkubwa wa viwanja vya Kaitaba - Kagera na Nyamagana - Mwanza, ni matokeo ya mazingira mazuri ya ushirikishaji yaliyowekwa na Serikali kati ya wadau soka, Shirikisho la Soka nchini na Shirikisho la Soka la Dunia.
Aidha, ukarabati mkubwa wa viwanja vya Namfua - Singida; Samora Machel - Iringa na Majaliwa Stadium - Ruangwa ni matokeo ya mazingira mazuri ya ushirikiano yaliyowekwa na Serikali kati ya wadau, TFF na Wizara yenye dhamana ya michezo. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge) kwa kuonesha mfano wa kuhamasisha Halmashauri yake na wananchi wa Ruangwa kuunganisha nguvu na kujenga uwanja wa Majaliwa Stadium. (Makofi)
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-

Mkoa wa Rukwa umeanzishwa mwaka 1974 lakini hadi sasa hakuna viwanda vikubwa vilivyowekezwa na kuwekewa mikakati na Serikali na viwanda vilivyopo ni vya watu binafsi:-

(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya kujenga viwanda au kupeleka wawekezaji ambao watajenga viwanda vikubwa Mkoa wa Rukwa ili kutoa ajira kwa vijana?

(b) Mazao yanayolimwa Mkoa wa Rukwa yanapewa bei kiholela na kufanya maisha ya wananchi kuwa magumu: Je, ni lini Serikali itaingia mkataba na viwanda vya uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Jukumu la Serikali katika ujenzi wa viwanda ni kuwepo mazingira rafiki na wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza na kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kuzalisha na kufanya biashara. Msimamo huo wa kisera unaihusu mikoa na sekta zote za kiuchumi. Kwa msingi wa utaratibu huo wa kisera, Serikali imeelekeza nguvu zake katika kujenga na kuboresha miundombinu wezeshi na saidizi hususan umeme barabara, maji na mawasiliano. Aidha, katika kuhamasisha uwekezaji, Serikali imeitaka mikoa yote nchini kuandaa Taarifa za fursa za uwekezaji zilizopo (Regional Profiles) katika maeneo yake na kuvitangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pPia Serikali imeanzisha Mkakati wa zao moja Wilaya Moja (ODOP) ili kila Wilaya nchini ijielekeze katika kuendeleza angalau zao moja litakalovutia uwekezaji wa viwanda. Mkakati huu utasaidia kila Wilaya zikiwemo za Mkoa wa Rukwa kuwa na kiwanda angalau kimoja kinachotumia rasilimali zilizopo katika wilaya hizo. Hivyo, natoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote tushirikiane kuainisha fursa zilizopo na kuzitangaza kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mkataba hapa Tanzania kwa sasa kinatumika katika baadhi ya mazao yakiwemo miwa na tumbaku. Katika utaratibu huo wakulima hukubaliana na wanunuzi/viwanda kupewa baadhi ya huduma zikiwemo pembejeo kwa masharti ya kuwauzia mazao hayo na gharama za huduma au pembejeo hizo hukatwa wakati wa malipo. Katika utaratibu huo Serikali haihusiki moja kwa moja katika kuingia mikataba hiyo bali Maafisa Ugani huwasaidia wakulima kuangalia iwapo mikataba husika itakuwa na tija. Tunawahimiza wananchi kuwa makini wakati wa kuingia mikataba hiyo na wanunuzi. Aidha ili kupata nguvu ya soko, ni muhimu kuuza mazao kupita vyama vya ushirika.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-

Mgane anapobaki na watoto hundi zinazolipwa kama kuna malipo huandikwa kwa jina lake, lakini kwa wajane huwa ni tofauti, anapewa masharti ya kulipiwa mahakamani na awe na muhtasari wa kikao cha upande wa mwanaume na ndipo malipo yafanyike kwa mgao maalum.

(a) Je, kwa nini mjane asiandikwe jina lake kwenye hundi na asimame na watoto wake kwa kupewa haki hiyo?

(b) Je, Serikali haioni kama inamnyanyasa mjane?

(c) Kama ni sheria; je, Serikali haioni kwamba ni wakati wa kuiangalia upya sheria hiyo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, masuala ya mirathi yanasimamiwa na Sheria ya Mirathi, Sura ya 352. Sheria hii inatoa utaratibu mzima unaohusu masuala yote ya mirathi, wosia, kufungua mashauri ya mirathi, usimamizi, pingamizi la msimamizi au msimamizi anapofariki au asipotendewa haki.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, sheria za nchi zinatambua kuwa mirathi na usimamizi wake unaweza kuongozwa na Sheria ya Kiislam au Sheria ya India ya mwaka 1885 kwa wasiokuwa waislamu. Matumizi ya sheria hizi yanaangalia maisha ya marehemu, dini na namna marehemu alivyozikwa. Pia sheria hizi zinaeleza namna mali itakavyopaswa kugaiwa kwa wanufaika huku ikiainisha kila mnufaika kwa kiwango anachopata.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu inajali na kutambua kuwa binadamu wote ni sawa na hii imeelezwa katika Ibara ya 12(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 13(2) ya Katiba inatoa marufuku kwa sheria yoyote kuweka shauri lolote lile la kibaguzi katika matumizi yake.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo hakuna sheria yoyote inayompa mgane haki zaidi mjane au kwa namna yoyote kuonesha ubaguzi. Hata hivyo, utaratibu unaofanyika unatamka msimamizi wa mirathi kuwasilisha mchanganuo wa malipo na hundi huandikwa kwa wanufaika wote pasipo kujali jinsia zao.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa na sheria nzuri, kumekuwa na uelewa mdogo miongoni mwa baadhi ya wananchi kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazohusu masuala ya mirathi. Wizara yangu kupitia RITA na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu mirathi na maendeleo na kubuni mbinu zitakazosaidia ili elimu ya mirathi iwafikie wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu, ninaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika kuchangia jitihada za Serikali katika kufikisha elimu ya mirathi kwa wananchi wetu katika maeneo yetu yanayotuhusu, ahsante.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-

Serikali inatambua vivutio kadhaa vya utalii ikiwemo Kalambo Falls Mkoani Rukwa. Hata hivyo, barabara ya kuelekea maporomoko hayo kutokea Kijiji cha Kawala hairidhishi.

(i) Je, Serikali ina mpango gani wa kuiboresha barabara hiyo itakayokuwa ikitumika na watalii?

(ii) Je, kwa nini kipande hiki chenye urefu wa kilometa 12 kuanzia barabara ya Kijiji cha Kawala kisiwekewe lami?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya matengenezo ya kilometa 6.5 za barabara ya Kalambo Falls kwa kiwango cha changarawe na kujenga makalvati kwa gharama ya shilingi milioni 160.8 ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika katika kipindi chote cha mwaka.

(b) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya usanifu wa kina wa kipande cha barabara ya kutoka Kijiji cha Kawala hadi Kalambo Falls chenye urefu wa kilometa 12 ili kubaini gharama halisi zinazohitajika kwa ajili ya kujenga kipande hicho cha barabara kwa kiwango cha lami.