Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Silafu Jumbe Maufi (53 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii. Kwa kuwa siku ya leo ni siku yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuipata nafasi hii ya kuwawakilisha akina mama wanawake wa Mkoa wa Rukwa. Mwenyezi Mungu, nakushukuru sana.
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, awali ya yote, napenda kuwakumbusha kuhusu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli. Kwa kweli hotuba ile ilikuwa ni hotuba ambayo imesheheni kila upande wa Tanzania hii na kila Jimbo la Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba niwakumbushe ndugu zangu wa Chama cha Mapinduzi kwamba, daima mtoto huwa anapiga madongo ya kila aina kwenye mti wenye matunda au mti wenye neema kwao. Mtoto hawezi kutupa madongo yoyote kwenye mti ambao hauna kitu. Kwa hiyo, haya madongo tunayoyapata kutoka upande wa pili, ni ashirio tosha kwamba mti wa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake imefanya kazi. Hivyo sasa tunahitajika tukaze buti ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, katika hotuba ya Rais iliweza kugusa kila eneo ambalo kwa namna moja au nyingine limegusia hatua ambazo zinahitajika kufikiwa kwa wananchi wetu wa Tanzania. Sasa basi, kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshabainisha nini ambacho anachotakiwa kufanya kwa wananchi wa Tanzania ili waweze kupata uchumi wa kati; kwa hiyo, hatuna budi kumuunga mkono na kuifanya kazi hii ili iwe na maendeleo kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Ndugu zangu, leo tuna shughuli ya kuzungumzia juu ya Mpango wetu wa kazi ambayo tunahitajika kuifanya ndani ya mwaka 2016/2017. Mpango huu ni mzuri, ni Mpango ambao umeainisha nini ambacho Chama cha Mapinduzi imesema itafanya ndani ya miaka yake mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, Mpango huu umeona tatizo ni nini? Mbona maendeleo yetu hayakamiliki? Imebainika kwamba tatizo ni mapato. Sasa Serikali imeelekeza kukusanya mapato na hatimaye kuyarejesha mapato hayo kwa wananchi kwa maendeleo yao. Hilo ni jambo zuri na tunaomba tuliunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulizungumzia suala la afya. Tuliamua ndani ya Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010/2015 kuweka zahanati katika vijiji vyote na kazi hiyo wananchi wameweza kuunga mkono na kujenga hizo zahanati. Tatizo, zahanati hizi haziko katika ramani inayofahamika, kila kijiji wamejaribu kutengeneza zahanati kufuatana na nguvu ya mapato waliyokuwanayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake tumepata tatizo kubwa katika zahanati hizi kwa sababu eneo la kujifungulia limewekwa karibu na eneo la OPD, limewekwa karibu na eneo ambalo watu wa kawaida wanasubiri madaktari, ndipo palipo na chumba cha kuweka akina mama waende kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri wa Wizara inayohusika, kazi ile ya kujifungua akina mama wana kazi pevu na bora iwe usiku kuliko ikiwa mchana. Mifano tunayo, zahanati ya Kisumba, kwa kweli ile ramani siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba katika Mpango wetu uainishe dhahiri nini watafanya katika suala zima la kuhakikisha wanatembelea ama wanaweka mpango mkakati wa kuhakikisha ramani zilizotengenezwa hivi sasa ziboreshwe ili akina mama tupate eneo la kuifadhiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, zahanati nyingi hazina vitanda vya kuzalia, hakuna vyumba vya kupumzikia, kwa maana ya kwamba hakuna vitanda vya kupumzikia. Tunaomba tupate vitanda hivyo. Siyo hilo tu ndani ya afya, zahanati zetu nyingi hazina umeme. Pamoja na kwamba kuna umeme wa REA, lakini bado hawajaunganisha kwenye zahanati zetu. Solar zilizopo zimeharibika na hakuna mtu tena wa kutengeneza zile solar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuunganishwe na umeme wa REA, katika zahanati zetu zote. Siyo hilo tu, maji hakuna kwenye zahanati zetu. Tunaomba Mpango Mkakati wa kuhakikisha kwamba zahanati zetu zinapata huduma ili akina mama waweze kujihifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu suala la elimu. Tumeamua kuboresha elimu yetu na iwe elimu bora, lakini kuna maeneo ambayo tumeanza kuweka utaratibu wa watoto wetu waweze kujifunza teknolojia ya kisasa, kwa maana ya kwamba wamepeleka computers katika shule zetu za sekondari. Naomba mipango iwekwe ya kutosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza, mfano Sekondari, darasa lina watoto 40, lakini kuna mikondo miwili; na mikondo hiyo miwili ni watoto 80, zinapelekwa computer 10 ambazo hazitoshelezi. Naomba tuliangalie hilo katika utaratibu. Mifano tunayo, pale Sumbawanga kuna shule za sekondari za Kizito na Mazu wana computer 10 na watoto wako 80, watafanya nini wakati wa mitihani yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni barabara. Maendeleo ya huduma za jamii katika Mikoa ya pembezoni tumekuwa nyuma. Mimi nasikitishwa sana ninaposikia wenzetu wenye barabara, wanaongezewa barabara za juu, wanaongezewa barabara ziwe sita, wapite barabara watu sita. Kwa kweli mimi nasikitishwa sana kwa suala hilo. Maadamu tumeamua kwanza tuunganishe Wilaya, tuunganishe Mikoa, zoezi hili ndugu zangu bado halijakamilika. Sasa kama halijakamilika, huyu aliyekamilika kuongezwa na katika Wilaya zake zimeunganika, Mikoa ya jirani ameunganika; nchi za jirani ameunganika; kwa nini aongezewe tena mradi wa barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tuelekeze Mkoa wa Rukwa. Hatujaungana na Katavi, hatujaungana na Kigoma wala na Tabora. Nawaomba ndugu zangu, huo Mpango uje ukionyesha mikakati, tunajitengeneza vipi kuhusu hizi barabara kuweza kuunganika? Vilevile Mkoa wa Rukwa, tumeungana na nchi ya Zambia barabara haijakamilika, nchi ya Zaire bado barabara haijakamilika. Tunaomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji, tuna mradi mkubwa sana pale Mkoa wa Rukwa karibia shilingi bilioni 30, lakini mradi ule bado haujakamilika, bado pale mjini watu wanahangaika na maji; bado vijijini vya jirani vinahangaika na maji, tuanomba Mpango unaokuja, huo mwezi wa tatu, uwe umekamilika ili na sisi tuweze kupata maji katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ardhi, tunaomba wataalam wa upimaji wa vijiji, hawapo wa kutosheleza na hata vifaa vyake havipo vya kutosheleza. Tunaomba tuhesabu ili tuweze kukamilisha.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kiasi katika suala zima la bajeti hii iliyowasilishwa asubuhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa shukurani za dhati na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Vile vile nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nisipompongeza Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi wanayoifanya, nasema big up. Pia napenda kutoa shukrani za dhati kwa akinamama wa Mkoa wa Rukwa walioniwezesha kuingia katika jengo hili na kuweza kuwazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati za Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika kutambua na kujipanga na kuona kwamba wanahitaji kufanya nini katika kukinga na kuyaboresha mazingira ya nchi yetu ili iweze kuwa katika maendeleo ya wananchi kwa ujumla, nawapongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyeketi, napenda kuzungumzia suala la mazingira na hasa katika Mkoa wetu wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa kwa maana ya jina la Mkoa wa Rukwa imetokana na Ziwa Rukwa tulilonalo. Ziwa hili linaanza kupoteza kina cha Ziwa lile kutokana na maporomoko ya mito inayotoka milimani kuanzia Mlima Liambaliamfipa mpaka milima inayozunguka ziwa lile; kuna mito mingi mno ambayo inatiririka kiasi cha kuchukua udongo na kujaza katika lile ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu Wizara imejipanga vipi katika kulinusuru ziwa hili lisiweze kupotea na Mkoa wetu wa Rukwa ukakosa kupata jina. Naomba Serikali ifikirie namna ya kuweza kuyakinga haya maji kwa namna moja au nyingine yakaweza kutusaidia katika suala zima la umwagiliaji au Serikali iweze kukinga maji haya wakayaweka mahali ambapo wanaweza wakafanya utaratibu wa kuyasambaza na kuya-treat, hatimaye kuyasambaza kwa wananchi wetu na kupata maji safi na salama. Kwa kufanya hivyo, itakuwa imewasaidia akinamama wangu wa sehemu ya Bonde la Rukwa kupata maji kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linapelekea hili Ziwa letu kuwa na kina kifupi ni mifugo mingi iliyoko katika Bonde la Rukwa. Bonde la Rukwa lina mifugo mingi na mifugo mingine ni kwamba wakati wa mnada wa Namanyere kupeleka ng‟ombe Mbeya ni lazima watapita barabara ya bondeni na barabara ile ni barabara ya vumbi inayotoka Nyamanyere hadi Kibaoni, Kibaoni mpaka Mtowisa, Mtowisa –Ilemba, Ilemba - Kilyamatundu hadi kufikia Kipeta na hatimaye kuondoka kuingia Chunya - Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ng‟ombe wale wanaweka tifutifu, wakati wa mvua, lile tifutifu ambalo ni udongo unachukuliwa na maji na kupelekwa katika Ziwa Rukwa. Sasa Wizara ina mpango gani wa kushauriana na Wizara husika kuhakikisha barabara ile ya kutoka kibaoni hadi Kilyamatundu kuelekea Kamsamba iwe ni ya lami badala ya kuwa ya vumbi ili isiendelee kujaza udongo katika ziwa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu mzima wa mazingira sehemu yetu ile ya Rukwa ni kutokana na akinamama kuingia mle na kukata miti na kuitumia kama nishati. Sasa tunaomba nishati mbadala kwa lile Bonde la Rukwa kwa kuhakikisha kwamba umeme unapatikana. Umeme ukipatikana mama zangu watapata nishati mbadala na hatimaye ile miti itaweza kukua na kuhifadhi mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naweza kuzungumza katika suala zima la mazingira ni suala zima la utafiti. Karibu Wizara zote ambazo nimewahi kuzisikia na ninazoendelea kuzisikia, daima huwa wanaweka utafiti, tathmini, katika sehemu ambazo kwamba zimekwisha piga hatua. Kwa nini wasifanye utafiti na wakafanya tathmini ya maendeleo ya jambo katika Nyanda za Juu Kusini ambapo tuko pembezoni tumechelewa kwa kila kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa utafiti uelekee upande wa Nyanda za Juu Kusini ili na sisi tuwe makini, tuweze kuelewa nini elimu ya mazingira, tunatakiwa kufanya nini kuhusiana na mazingira yetu na sisi tusije tukawa jangwa kama mikoa mingine ambayo imetajwa ndani ya taarifa hii ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio yaliyokuwa yamekadiriwa katika Wizara hii hayatoshelezi mahitaji. Hayatoshelezi mahitaji kwa nini? Kwa sababu suala la mazingira ni suala pevu na ni suala pana ambalo kila Wizara ikitamkwa humu ndani, maendeleo yake huhitaji mazingira yake yawe ni bora zaidi. Sasa suala la mazingira ni suala pana ambalo linahitaji kuwa na bajeti kubwa ya kutosha. Mheshimiwa Waziri Januari sitaona ajabu kabla ya mwisho wa mwaka ukaomba tukuongezee bajeti ya utekelezaji wako. Sasa naomba, Serikali ione uwezekano wa kuiboresha hii bajeti ili iongezeke, tuweze kupata uhakika wa kuweza kuiendeleza vizuri Wizara yetu hii ya Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Wizara hii ya Mazingira katika wilaya zetu na mikoa yetu hawa watu hawaonekani kutokana na kazi nzito iliyoko ya Mazingira. Nawaomba tuongezewe idadi ya watumishi ili watumishi hao waweze kujigawa kuweza kutoa elimu kwa wananchi wetu kuhusu suala zima la mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na hawa wataalam, ni vema wakatengewa fungu la kutosha kupata elimu ndani na nje ya nchi ili waweze kwenda na nyakati zinavyoweza kusomeka katika suala zima la mabadiliko ya tabianchi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kupewa taarifa rasmi na Mheshimiwa Waziri mhusika hasa kuhusu kuhakikisha kwamba Ziwa letu la Rukwa linakingwa na linaweza kuboreshwa na hatimaye kuwa ziwa zuri na kuweza kuimarika, kwa sababu Ziwa Rukwa lina mamba wengi mno. Suala la Mamba pia ni suala la Maliasili, kwa hiyo tunawaomba muwalinde mamba hawa wasiweze kupotea ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba Mheshimiwa Waziri mhusika aweze kuniambia ni mikakati ipi ambayo imewekwa au anayotarajia kuifanya kuboresha mazingira yanayoanza kupotea katika Nyanda ya Juu Kusini na hususani Mkoa wetu wa Rukwa ndani ya Ziwa letu la Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Elimu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nguvu kwa kuniwezesha mimi kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati na kumpongeza ndugu yangu Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri ambayo ameanza nayo katika kipindi hiki kifupi na kuleta matumaini kwa wale wanohitaji elimu bora katika nchi hii, ahsante sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kutoa shukrani kwa dada yangu Stella Manyanya Naibu Waziri. Awali ya yote tunamuomba Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema mama yetu mpenzi na mwanga wa milele umwangazie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika suala zima la msingi wa elimu. Elimu ni kila kitu ndugu Waheshimiwa Wabunge, hakuna kitu ambacho kitakachoanzishwa ama kitakachofanyika katika nchi au mahali popote pale pasipokuwa na elimu, kwa hiyo elimu ndio msingi wa maisha yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninapenda kuzungumzia kwenye suala zima la elimu ya awali. Tumeweza kuanzisha madarasa katika shule za msingi madarasa ya awali lakini bahati mbaya walimu husika na kufundisha madarasa yale ya awali hawapo walimu hao na kama wapo hawatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia kwamba, hawapo ni kwa sababu katika shule zetu walimu wakuu wanachukulia sifa ya kumpatia mwalimu kufundisha darasa la awali ni mwalimu ambaye amefundisha kwa muda mrefu au ni mwalimu ambaye amebakiwa na miaka miwili au mitatu ya kustaafu ndio anayoelekezwa kwenda kufundisha watoto wa somo la awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hilo sio sahihi, tunaomba Serikali ijipange na ijitoe kuhakikisha ya kwamba inaandaa walimu wa kwenda kufundisha watoto wetu wa madarasa ya awali kwa sababu ndio msingi wa elimu. Bila kuwa na msingi bora ni dhahiri kusema ya kwamba uinuaji wa elimu bora na mafunzo bora katika nchi yetu hautawezekana kwa sababu watoto hawa watakuwa hawajapata msingi bora wa ufundishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Serikali, ninaomba Wizara iweke utaratibu maalum wa kufuatilia kwanza, kufatilia katika shule zetu za msingi kuona ile elimu inayotolewa kwa watoto wetu kama inaafiki ama inaswii katika kuhakikisha kwamba wanapata elimu bora. Hapo ndipo tutakapoonda kwamba kweli tumedhamilia kuinua elimu bora na mafunzo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu watoto wasichana, wasichana ni kwa maana ya kwamba, hao ndio watakaokuwa wakina mama wa kesho kama sio wakina mama wa leo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia ni ujenzi wa mabweni ya shule za sekondari. Ninawaomba Serikali iliweka msukumo wa kujenga sekondari kila kata na tumejenga sekondari kila kata na katika sekondari zile kuna watoto wasichana na watoto wa kiume, lakini hawa watoto wasichana ambao akina mama wa kesho wanakuwa na mitihani walimu wanawapa mimba, wananfunzi wenzao wanawapa mimba, sisi wenyewe wakubwa tunawapa mimba kwahiyo hawa watoto wanakuwa na mtihani mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ione umuhimu wa kukamilisha mabweni ya watoto wasichana katika mashule yetu kuhakikisha kwamba samani zinakuwemo ndani ya mabweni hayo vitanda, magodoro na kadhalika ili kujenga mabweni yale yawe ni rafiki kwa watoto wetu wasichana ili angalau wapunguze ile taratibu ambayo wanaopata mimba ambazo zisizokuwa na wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la hawa akina dada, wale wanaowapa mimba wanapobainika ninawaomba wapatiwe adhabu kali tena kali sana. Kwa sababu wanapunguza muonekano wa wale akina mama katika mafunzo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba ninaiomba Serikali hawa watoto wanaopata mimba ninawaomba wawaandalie fursa muafaka wa kuwawezesha hawa watoto wanapomaliza kujifungua, watoto wabaki wazazi wao, wao waendelee na masomo jamani, hili limekuwa ni kilio cha kila mara sasa limefikia wakati kwa Mama Ndalichako nafasi kwa Mama Manyanya mmepewa ninyi wanawake kwa sababu mnauchungu na watoto.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike, tuwaonee uchungu hawa watoto wa kike na tunajua ya wazi kwamba, ukimuelimisha mwanamke mmoja umeelimisha jamii nzima. Sasa kwanini tuwapoteze hawa kwa kuweza kuja kuendeleza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuweke fursa maalum ya kuhakikisha hawa watoto wa kike wanapomaliza kujifungua watoto wanawaacha nyumbani wao wanaendelea na masomo ili tuweze kupata maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kulizungumzia suala zima la wanasayansi. Tumesema nchi yetu itakuwa ni nchi ya viwanda, tuanze na viwanda vidogo vidogo, lakini hatuwezi kuwa na viwanda endelevu ikiwa hatuna wataalam wa kisayansi, ni lazima tuandae wanasayansi wa kuja kuendesha hivi viwanda vyetu, ili viwanda vyetu visiweze kufa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanyaje basi, tumeanzisha maabara katika shule za sekondari zote, lakini maabara hizi katika mashule yetu yana changamoto, changamoto iliyopo ni walimu wa sayansi hatuna. Vifaa vya sayansi katika maabara yetu havipo na ukiachia Halmashauri uwezo wa kununua vifaa vile ni aghali sana hawawezi Halmashauri kuweza kutekeleza na kuweka katika maabara zote za Sekondari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali natunamuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atuaeleze amejipangaje na uwekaji wa vifaa au samani za maabara katika mashule yetu ili tupate walimu wa kutosha na hatimaye tupate wanasayansi wa kuja kuendeleza viwanda vyetu hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri ni vyema wakaweka utaratibu maalum wa kuweka vivutio kwa walimu hawa wa sayansi, na kuweka vivutio kwa wanafunzi hawa wanaopenda sayansi, vinginevyo tutaweza kupoteza maana ya kuhakikisha kwamba, tunajenga viwanda katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika suala la walimu, walimu wanaokuja katika maeneo yetu kama sisi Mikoa yetu ya pembezoni Mkoa wa Rukwa, kwenda kule vijijini wamekuwa na taratibu za kuja ku-report wakishaingia kwenye payroll wale walimu wana-disappear katika yale maeneo kwa sababu mazingira yale ni mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikuwepo utaratibu na hata na baadhi ya Mikoa walijaribu kuanzisha taratibu hizo za kuwawezesha walimu hawa kwenda kuishi kule mfano Rukwa walianzisa Nyerere Fund ambayo kwamba sasa hivi hai-operate vizuri, lakini vilevile na Serikali wangeweza kuweka package nzuri ya kuhakikisha kwamba huyu mwalimu anapokwenda kule anakwenda katika ukamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Rukwa walikuwa wanapewa vitanda, magodoro, vyombo na sehemu kidogo ya kwenda kuanzia maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Wizara iweze kuona suala hili ili tuwe na walimu hawa katika shule zetu, katika ukamilifu. Walimu wanafanya kazi moja kubwa mno, sisi sote hapa tusingekuwepo kama kungekuwa hakuna mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi tunachokiomba hii Wizara ya TAMISEMI imepewa mambo mengi mno, kwa sababu changamoto zote za walimu, changamoto za wanafunzi zipo TAMISEMI, lakini wanaolaumiwa ni Wizara ya Elimu, tunaomba hii Wizara ya Elimu ijitegemee kwa sababu ina mambo mengi ya kuweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wameanza Tume ya Walimu lakini bado haitoshelezi mahitaji, tunahitaji elimu iwe na Wizara inayojitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenykiti, lingine ni kuhusu na VETA Mkoa wa Rukwa umeanzishwa nadhani ni mwaka 1974 ama ni 75 lakini mpaka hivi leo Mkoa wa Rukwa hatuna VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la saba, tunao vijana wengi wanaomaliza darasa la 12 lakini wanakuwa hawana mahali pa kushika, hawawezi kujiajiri na wala hawawezi kuajiriwa. Kwa hiyo tunaomba katika Bajeti hii ya 2016/2017 katika mipangilio yao wafanye utaratibu wa kuanzisha VETA katika Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na napenda kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa jitihada na matarajio makubwa ya nchi kuwa na Viwanda na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Watendaji wote walioteuliwa nae, kwa kasi yenye uchungu wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania kwa kuwapatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Madhumuni ya kuanzisha SIDO ni kuwezesha kutoa ushauri na mafunzo kwa vijana wetu wajasiriamali kuboresha uwezo wa kujiajiri kwao. Lakini Mkoa wa Rukwa kuna mapungufu ambayo yamekwamisha utekelezaji wa ufanisi na wenye tija wa SIDO kwa vijana na wajasiriamali wetu.
Majengo yapo, mashine zilizokuwepo hazipo kwa sasa, ambazo zilitoa ajira na mafunzo kutokana na hali hiyo majengo yamepangishwa kwa wafanyabiashara wa mashine za kukoboa mpunga na kusaga unga. Naomba Serikali kufuatilia majengo hayo na kurejesha mashine zilizokuwepo ili kufufua SIDO madhumuni yake kwa vijana na wajasiriamali wengi wao ni kina Mama.
Mapungufu yafanyikayo SIDO-Rukwa, kwa namna watoavyo mafunzo kwa vijana wetu na wajasiriamali kwa kufanya mchango kutoka kwa washiriki hao ndiyo wafanye maandalizi ya mafunzo. Inakatisha tamaa na mafunzo hupatikana kwa wachache. Serikali ipange fungu maalum la kuendesha mafunzo kwani watalamu wapo bila ya kufanya hivyo watakuwa wanapata mishahara bure.
Serikali kuona umuhimu kwa Mkoa wa Rukwa kufufua SIDO kwa kuhakikisha majengo yake yanarejeshewa mashine zake na vijana, akina mama wajasiriamali waweze kufaidika na uwepo na SIDO Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa wapo vijana wa kutosha wanaomaliza elimu ya msingi na Sekondari wanakosa elimu ya kujiajiri, wanajishirikisha kwenye Ujasiriamali pasipo na uwelewa wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo. Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wametenga eneo la kujenga chuo cha VETA lakini hakuna kinachoendelea. Ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kujenga Chuo hiki kwa maslahi ya Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Waziri napenda kupata utaratibu na mikakati ya kufufua SIDO-Rukwa na ujenzi wa VETA-Rukwa katika kutukwamua huku pembezoni ambako hakuna hata viwanda vya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza jitihada za kuendeleza michezo ingawa haijafika mahali inapotakiwa kwani tunaporomoka Kitaifa na Kimataifa kwa sababu vijana wetu hawana maandalizi ya awali na endelevu kwa fani maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo ya michezo haikidhi mahitaji katika kuimarisha miundombinu na mazingira kwa kuleta ufanisi katika michezo. Kwa ujumla bajeti ya Wizara haitoshi, inahitajika kuangaliwa upya mwaka ujao wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuandaa watalaam wa kuwaandaa vijana wetu shuleni kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari. Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya pekee hakitoshi kuandaa watalaam wa kutosha kuwasambaza kwenye shule hapa nchini, ni vema Serikali kuona umuhimu wa kupandisha daraja vituo vya michezo kuwa vyuo vya maendeleo ya michezo kuongeza hao watalaam ili kuinua michezo na Taifa kufahamika duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamishwa kwa nini Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya na vituo vya michezo Arusha na Songea hawakuwekewa makadirio ya mishahara 2016/2017?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhuru wa vyombo vya habari vilivyokithiri hapa nchini kwa upande wa magazeti ambayo baadhi yana poromosha maadili ya vijana wetu, Serikali ni bora kusitisha usajili wa magazeti na kuyafuta yanapobainika kwenda kinyume na maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, umeme ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na ajira kwa wananchi wetu. Bado naendelea kuzungumza kuhusu Mikoa ya Pembezoni kwa kuchelewa kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa tunao umeme wa jenereta unaosaidiana na umeme kutoka Zambia ambao una changamoto zake, naomba Serikali kuona umuhimu wa kutuunganisha na grid ya Taifa kutokea Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la usambazaji wa umeme vijijini huu wa REA, tukaongeze kasi kwa mikakati maalum kuharakisha vijiji vya mipakani kupata umeme huo, Kata zifuatazo Kabwe, Mirando, Kipili, Wampembe, Kala, Kasanga, Wampambwe, Sopa, Katete, Mambwenkoswe. Vilevile vijiji vya Bonde la Rukwa ukizingatia ni wakulima wazuri wa mpunga na alizeti wanahitaji kuwa na mashine za kukoboa mchele na kusindika alizeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kuwa bajeti ya nishati haikidhi mahitaji kwa Mkoa wa Rukwa, baada ya kukamilika kwa barabara ya Tunduma, Sumbawanga ambayo ni mwanzo wa kufunguka Mkoa wa Rukwa. Naomba Serikali kuangalia Mkoa huu kwani unahitaji kupiga hatua kwa maendeleo ya wananchi wake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uteuzi wa Waziri na Naibu Waziri kwa Wizara hii na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwani ni watendaji wenye weledi mkubwa kwa kujituma kwao na kujitoa kwao katika kupatikana utatuzi wa mambo yanayowakera wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuendelea kujipanga na kuandaliwa sheria maalum ya kuwawezesha wawekezaji kutoa mchango wa maendeleo ya huduma za jamii kwenye vijiji vinavyomzunguka hilo liwe mojawapo ya sharti maalum kwa mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinaongezeka ndani ya Wizara hii kwenye maeneo yetu ya vijiji, miji na majiji ni upungufu wa watumishi ukizingatia hadi sasa ni asilimia 24 tu kati ya mahitaji yanayohitajika kuanzia Halmashauri hadi Wizara. Ushauri kwa Serikali ni uwepo uthibitisho wa kuthubutu kuongeza ajira na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na mtandao wa dunia. Angalau kwa asilimia 50 ya watumishi, wanaohitajika tupate ufanisi katika nyanja zote na tuepukane na migogoro iliyokithiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wamekuwa na migogoro ya wawekezaji na vijiji, panaposhindikana kulipwa kwa fidia ndani ya muda wa uthamini, ni vema Serikali kuona mwelekeo wa kuwapimia wawekezaji nje ya maeneo ya wananchi kwani wao wana uwezo wa kuweka huduma zote za jamii, popote watakapowekwa kuliko kuwachanganya wananchi na kuwazorotesha maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu kuliko yote na kuwezesha yote yaliyopangwa kutekelezwa ni kuhakikisha fedha zilizopangwa kutolewa kwa wakati na katika ukamilifu kama Bajeti iliyopangwa na kuidhinishwa na Bunge hasa shilingi 20,000,000,000 kwa miradi ya maendeleo, kwa nini tumekuwa na viporo vingi vya miradi ndani ya nchi yetu ambayo inawadhoofisha wananchi. Ingawa kiasi hicho hakitoshelezi kwa maendeleo ya jumla kwa Wizara hii. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote chini ya Katibu Mkuu wa Wizara katika kipindi kifupi wameweza kufanya kazi ya kuwapa matumaini makubwa wananchi, ingawa matatizo ni mengi kwenye sekta ndani ya Wizara hii. Pamoja na yote tunapaswa kuwa na subira ya kujipanga na kuweka miundombinu ya mikakati ya kusafisha matatizo yaliyopo kwa kuyaweka katika kipaumbele ndani ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatana na hali halisi ya wananchi kuongezeka na ardhi/nchi ipo vilevile ni dhahiri haya mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42 yawezekana yamepotea au kupungukiwa sifa ya kuwa mapori ya akiba au mapori tengefu. Nashauri Serikali kufanya utafiti wa kukagua maeneo hayo na kupata idadi halisi ya uhalisia uliopo sasa na tupatiwe idadi na orodha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu tunaitumia wananchi katika shughuli mbalimbali na kuendelea kupungua kutokana na ukosefu wa nishati mbadala na kusababisha baadhi ya watumishi wa maliasili kuwa wasumbufu kwa wananchi wetu. Mazao ya misitu yamekuwa yanawanufaisha wachache na kukosesha mapato kwa Serikali. Ni vyema tukaweka mkakati wezeshi wa kupunguza usumbufu wa tozo zinazoingiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA inajitahidi katika kujenga mahusiano mazuri na wananchi wetu, nashauri badala ya makusanyo yote kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu, ni vyema wakabakiwa na hata asilimia 30 ili kuboresha shughuli wazifanyazo kwa wananchi wanaozunguka maeneo yao ya huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii una mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa. Mkoa wa Rukwa una vivutio kadhaa, mfano, Kalambo Falls. Tunahitaji vivutio vipitishwe na kutambuliwa na kufanyiwa matangazo, huku miundombinu ya kufikia kwenye eneo inafanyiwa kazi. Barabara ya kiwango cha lami (Matai – Kisumba – Mpombwe (Kapozwa) – Kalambo Falls) kwani eneo hilo linatumiwa zaidi na utalii wa Zambia kuliko Tanzania wenye eneo kubwa linalovutia katika kuyaona maporomoko hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuona umuhimu wa kukuza utalii wa Nyanda za Juu Kusini (Rukwa), kubadilisha mwelekeo wa Mashariki na Kaskazini. Nchi hii pande zote kuna vivutio vya utalii. Naomba Waziri atuthibitishie vivutio vyetu vitatambuliwa lini ili watalii wafike na tuongeze Pato la Taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha na kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SILAFU JUMBE MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza jitihada ya kazi nzito ifanyikayo katika kuendeleza, kuilinda na kujenga hasa mahusiano nchi za nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki. Waziri na jopo lake kwa kazi yenye matumaini kwa nchi yetu ya uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Serikali kuona upya namna ya kujipanga na kuweka bajeti yenye tija hasa katika kuwezesha ujenzi wa mahusiano wa nchi za nje, kwa kupata wataalam wa kuwajengea uwezo vijana wetu na kusimama wenyewe na hata upatikanaji wa Wawekezaji mahiri ambao wakitumia malighafi zilizopo na wanapoondoka viwanda vyetu kuendelea kuzalisha, yaani tuweze kubakiwa na viwanda mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuona umuhimu wa kuweka msukumo wa kusimamia ongezeko la bajeti kuwezesha nchi yetu kupiga hatua sasa ya kuwajenga vijana wetu, kwa kukiwezesha Chuo cha Kidiplomasia kwa kuongeza idadi ya udahili, tukifahamu kuwa chuo hiki Tanzania ni kimoja tu hivyo kipanuliwe au kuwa na branch kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi za Mabalozi wetu huko nje, kuendelea kupanga na makazi ya Mabalozi, ni suala la kuangaliwa upya, madamu tunazo Taasisi na Mifuko ya Jamii inaonesha uwezo wa ujenzi wa majengo makubwa,
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
222
kwani hawawezi kupewa ukandarasi wa ujenzi wa majengo hayo. Ni lini sasa Serikali itayafanyia kazi na kuondokana na utaratibu wa upangaji huko nje, kwani wao kwetu wanajenga?
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa wananchi katika kusafiri kwenda nchi za nje, kuna urasimu sana, kuliko wanaoingia nchini na sasa idadi yao inatisha na wote wanakuwa ni wafanyabiashara na wawekezaji na baadhi yao kuwa wahalifu nchini. Serikali inalazimika kuongeza nguvu zaidi ya kiusalama katika maeneo yote na kudhibiti hii hali ya mwingiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kutoa shukrani kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunipatia afya njema na leo hii kuweza kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu kuzungumza haya nitakayozungumza muda si mrefu. Nakutakia kila la kheri, Mwenyezi Mungu akupatie afya njema, akupatie wepesi kutokana na kazi nzito unayoifanya. Ujue ya kwamba tunakuombea na tunaendelea kukuombea upate afya hiyo mpaka mwisho wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu bajeti ya Serikali. Nadhani wataalam tuliokuwa nao waliweza kujifunza katika kipindi kilichopita cha Awamu ya Nne na kufuatana na kasi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuhitaji kuweka asilimia 40 ya fedha kwenye maendeleo ya wananchi wake basi itawekwa msingi madhubuti kuweza kumhakikishia Rais huyu kusimama kwa miguu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya nimeona kila Mbunge anayesimama hapa hayuko rafiki na bajeti hii, sijui hii Wizara haikuwa makini kufikiria na kuona hii kasi ya Mheshimiwa Rais itakwendaje ama itaanzaanza vipi katika kuhakikisha kwamba asilimia 40 inapatikana na maendeleo ya wananchi yanapatikana. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu Wizara hii imekwenda tofauti na Kamati ya Bajeti jinsi ilivyotoa mapendekezo yake, hii inaashiria wazi kwamba Wizara haikuona umuhimu wa Kamati hii kufanya kazi kwa niaba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nastaajabu kwa nini ameileta bajeti hii kwetu na sisi Wabunge wenzetu walikataa mapendekezo yao? Kama kweli aliona thamani ya Wabunge kwamba lazima wapitishe bajeti hii basi angehakikisha mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yanazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala la afya. Tunafahamu wazi kabisa kwamba afya ya mtoto mama ndiye anayesimamia siyo hilo tu mama ndiye anayesimamia hata malezi ya baba. Baba akiugua ndani ya nyumba mama ndiye mwajibikaji wa kuhakikisha afya ya baba inakuwa katika usalama na hali kadhalika ya mtoto. Sasa mama huyu tunamwekea mazingira ambayo siyo mazuri kwake, tunaendelea kumuongezea mzigo juu ya mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia nini? Nazungumzia zahanati. Ukichukulia mfano wa Wilaya ya Sumbawanga Mjini kuna kata saba zinazozunguka mji ule lakini hazina kituo cha afya, zina zahanati lakini baadhi ya zahanati kwenye vijiji ni maboma ambayo bado hayajakamilika. Halafu Waziri wa Fedha anasema hakuna fedha ambazo zimewekwa kwa ajili ya kukamilisha zahanati hizi, kwa ajili ya kukamilisha vituo hivi ili huyu mwanamama awe na huduma ya afya karibu na yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Wizara hii kwa sababu inafahamu wazi kanuni sijui sheria ya 106 inayosema kwamba sisi kama Bunge hatuwezi kubadilisha kifungu chochote labda ndiyo maana amekuwa na kichwa cha kusema kwamba hata wakisema hayawezi kubadilika kwa wakati huu. Sisi tunasema ni vyema Wizara ikawa na ushauri mzuri ama ikawa na maelekezo mazuri na kutukubali sisi Wabunge kama ndiyo tunaosimamia Serikali katika kuiongoza nchi hii. Waziri akienda kinyume na ukweli huo hatakuwa rafiki wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kama amekosea kipindi hiki tunaomba kipindi kinachokuja aje na fungu maalum la kuhakikisha miundombinu ya zahanati, miundombinu ya vituo vya afya inakamilika kwa maana ya theater ili akina mama waweze kufanyiwa upasuaji wakati wa zoezi la kuongeza idadi ya wananchi wa Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu shilingi milioni 50 kwa vijiji ambapo shilingi bilioni 59 zimetengwa. Imesemwa hapa kwamba hazitasambazwa nchi nzima bali watachukua maeneo maalum kama pilot program. Mimi nasema Mheshimiwa Rais alisema ni kwa nchi nzima leo hii tukisema tunachukua baadhi ya mikoa iwe ndiyo shamba darasa la hizi shilingi milioni 50 ndani ya vijiji vyao tutakuwa hatujawatendea haki wengine. Ushauri wangu kama ni kutafuta mashamba darasa ya kuona hii shilingi milioni 50 itakwendaje basi ni vyema hizi shilingi bilioni 59 zigawanywe ili kila Jimbo waweze kupata vijiji viwili ama vijiji vitatu viwe ni pilot program katika maeneo hayo ili na wale ambao wanawazunguka waweze kujifunza nini makosa ya wenzao kuliko ukisema kwamba pilot program inakuwa Tanga mimi niko Rukwa wapi na wapi? Tunaomba tuweke kwa kila Jimbo ili tuweze kupata pilot area ya kujifunza sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la asilimia 10 halikuweza kutekelezeka kwa sababu ndani ya Kamati ya Bajeti ama Kamati ya Fedha ya Halmashauri hakuna anayelizungumzia wala hakuna anayelifuatilia wala hakuna mwenye uchungu nalo. Kwa nini? Ni kwa sababu Wabunge wa Viti Maalum ama Waheshimiwa Madiwani wa Viti Maalum kwenye ile Kamati hawamo na ndiyo wenye uchungu na vijana na akina mama wenzao. Naomba Wizara inayohusika isiwe na kigugumizi itoe tamko rasmi kwamba hawa Madiwani wa Viti Maalum na Waheshimiwa Wabunge waingie kwenye Kamati ya Fedha za Halmashauri wakazungumzie na kufuatilia asilimia yao 10. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya bajeti yetu tumesema Wizara ya Utalii ndiyo ambayo inaleta fedha za kutosha takribani asilimia 25 lakini mazingira yanayotengenezwa kwa huu utalii si rafiki. Badala ya kupata zaidi ya asilimia 25 ni dhahiri katika kipindi kifupi tutapata chini ya asilimia 25 na kwa maana hiyo uchumi wetu utaanguka. Nasema hivyo kwa sababu wenzetu wa Kenya katika bajeti ya mwaka 2016/2017 wametenga shilingi bilioni 90 sisi tumeweka shilingi bilioni 135 lakini si kwa utalii peke yake ni pamoja na Maliasili na Utalii. Kama wakigawana pasu hawa kila mmoja anapata shilingi bilioni 67.
Hii saa inasema uongo sasa. Naomba kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naunga mkono Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018, pamoja na kutofahamishwa rasmi mafanikio na upungufu wa utekelezaji wa mwaka 2016/2017 hadi sasa ili kutupa picha kwa mapendekezo ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka asilimia 40 ya bajeti kwa maendeleo lakini hadi sasa fedha hizo hazijafika kwenye Halmashauri zetu na kupelekea kuzorota kwa utekelezaji wa maendeleo kwenye huduma za jamii kama afya, maji na umeme. Nashauri katika kipindi hiki, kabla ya kufika mwaka 2017/2018, kuboresha mwenendo wa usambazaji wa fedha za maendeleo kwa angalau asilimia 75 kwa miradi ya maji, afya na umeme kwani huduma hizi zinawagusa wananchi wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kusonga mbele na kuendelea kuweka mazingira ya malalamiko kwa baadhi ya viongozi na wananchi kwa maendeleo yao kiuchumi, nashauri Serikali kujikita zaidi kujenga mikakati ya kufufua mazingira bora ya kilimo, biashara na fursa za ajira binafsi kwa vijana wetu. Pia kuwepo na uratibu wa malalamiko na kuyapanga kwa utekelezaji ili kuepusha malalamiko kujirejea ndani ya mipango yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mapendekezo haya ya Mpango wa mwaka 2017/2018.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
HE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutoa pongezi kwa Wizara kufanya kazi nzuri hadi sasa, napenda kuzungumzia barabara zifuatazo ambazo zimekuwa zikiombewa fedha kwa Serikali Kuu katika kuongeza nguvu kwenye Halmashauri kuzifanyia kazi pasipo na mafanikio:-
(i) Kitosi – Wampembe – kilometa 68, imepewa shilingi milioni 84 ambazo ni pungufu na fedha za 2016/2017 ni dhahiri kwa barabara hii hazikidhi mahitaji na ndio maana kuna maombi ya kuchukuliwa na TANROAD.
(ii) Nkana – Kala – kilomita 67, kijiografia Halmashauri haiwezi kuifanyia huduma katika ukamilifu wake. Serikali Kuu ni vema kuiangilia vinginevyo kwa maslahi ya wananchi wetu.
(iii) Namanyere – Ninde – kilomita 40, imekuwa ni barabara yenye maombi maalum kila mara, hii ya milioni 350 haijakamilishwa na barabara haijakamilika, hivyo Kata ya Kala haijafunguka. Tunaomba kuongezewa fedha ambazo zitakamilisha barabara hii kwa sasa.
(iv) Kasu – Katani – Miyula – kilomita 24, Mkoa wa Rukwa ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka kwa chakula na biashara na wahusika zaidi ni akinamama na vijana wao. Barabara hii imekuwa ni mzigo mzito kwa Halmashauri na kuwa kero kwa wananchi wetu kutowawezesha kufika kwenye soko na kusababisha mazao kuharibika. Tunaomba Serikali Kuu kuwawezesha kiwango fulani Halmashauri ya Nkasi kuweza kuimarisha barabara hiyo kwa kunusurisha vifo kwa akinamama kufuata huduma ya afya. Kuwainua wananchi kiuchumi, kuwarahisishia kufika kwenye soko kwa uharaka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri; kwa kuwa kila Mbunge anazungumzia kupandishwa kwa barabara zao na kwenda chini ya TANROAD na Serikali kuona Bodi ya Wakala ya Barabara Vijijini kuanzishwa kwa tatizo hili. Naomba kutoa ushauri wangu kuwa kutokana na kazi zenye tija kubwa na uimara wake ni vema:-
- TANROAD ikaongezewa fedha kutoka bilioni 30 kutokana na kazi kubwa wanayofanya.
- Vema TANROAD kuongezewa rasilimali watu na rasilimali fedha, kwa kuzingatia kuwa huduma zao zitalazimika kufika hadi barabara za vijijini (barabara zote zilizopo hapa nchini) hakuna sababu ya kuanzisha Bodi ya Wakala wa Barabara Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano; napenda kuzungumzia Kata ya Kala kwa ujumla wake ndani ya Vijiji vya King’ombe, Mlambo, Kapumpuli, Mpasa, Kilambo, Lolesha, Kala na Tundu.
- Hawana mawasiliano ya simu na barabara.
- Eneo hili ni mpakani mwa nchi yetu na DRC – Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuona umuhimu wa kushauri na kuelekeza kampuni kadhaa maeneo hayo, nao wapate mawasiliano ya simu, ukizingatia usalama kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii, bali bajeti inakuwa finyu na kutokana na umuhimu na uharaka wa maendeleo haya kwenye Mkoa wa Rukwa ndiyo maana tunaomba Wizara kuongezewa fedha na miradi husika kukamilika ndani ya muda mfupi na kwa kiwango cha kudumu muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kutenga fedha za matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe na udongo zipatazo shilingi 1,350,906,000.
(i) Ntendo – Muze – kilomita 8, shilingi milioni 249,245
(ii) Muze – Mtowisa – kilomita 7, shilingi milioni 218,089
(iii) Mtowisa – Ilemba – kilomita 20 shilingi milioni 623,111
(iv) Ilemba – Kaoze – kilomita 8.36 shilingi milioni 260,461
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi ni maeneo ya ndani ya barabara ya Kibaoni – Muze – Mtowisa – Ilemba – Kaoze – Kilyamatundu – Kamsamba – Mlowo, ambayo inaunganisha Mikoa ya Katavi – Rukwa – Songwe. Kwa azma ya Serikali ya kuunganisha mikoa hapa nchini. Naomba sasa ijipange kwa kuitoa barabara hii kwenye bajeti ya kuitengeneza kwa kiwango cha changarawe na udongo na kuiweka kwenye fungu la barabara za kiwango cha lami ili mikoa hii iweze kuunganishwa.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanja cha ndege Sumbawanga. Nashukuru kwa kutengewa fedha milioni 18,400. Tunachoomba ni ukamilifu wa malipo ya fidia ya wananchi wanaotoa majengo yao kuachia upanuzi wa kiwanja hicho kwa wakati na thamani ya fedha zao kwa sasa. Tunaomba usimamizi wa ujenzi huo kuwa wa karibu zaidi na kukamilika mapema kwa kiwango takiwa ili wananchi wa Rukwa waondokane na usumbufu na adha kadhaa za kukimbilia Songwe Airport.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia afya nami kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nisipomshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Kwa kweli amefanyakazi kubwa na kazi nzuri na tarajio jema kwa wananchi wa Tanzania kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwashukuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamefanya kazi nzuri ambayo sikutarajia kabisa katika kipindi hiki kifupi kuweza kuifanya kazi kubwa hii ndani ya afya katika nchi yetu. Wakati akisoma mdogo wangu Mheshimiwa Ummy taarifa yake ya Wizara, kwa kweli ameni-impress na kujua ya kwamba kumbe yeye ni bush doctor lakini kwa kweli ni daktari kamili, kwa jinsi anavyoifanya kazi yake kwa kuipenda na kuifahamu Wizara ya Afya na kweli ameishika na kuhakikisha kwamba anaifanyia kazi njema katika kipindi chake hiki cha uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala la maendeleo ya jamii. Kitengo cha Maendeleo ya Jamii kimesahaulika hivi sasa ndani ya utekelezaji wake wa kazi. Maendeleo ya jamii ilikuwa kila mwaka wanaketi Maafisa Maendeleo ya Jamii kukaa pamoja, kushauriana, kuelekezana na hatimaye kupeana ubunifu wa kuweza kuitekeleza Wizara yao, tatizo vikao hivi sasa hivi havifanyiki ikidaiwa kwamba bajeti ni finyu. Ninaomba vikao hivi virejee ili maendeleo ya jamii iweze kufufuka tena upya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya jamii ni kitengo ambacho kinatoa elimu kwa akina Mama katika kuhamasisha ujasiriamali, kuwahamasisha akina mama kiuchumi, kuelekeza akina mama umuhimu wa kujiunga na tiba, umuhimu wa kujiunga na bima, umuhimu wa mikopo na namna ya utekelezaji wa mikopo hiyo ya vyombo vya fedha na SACCOS na kadhalika. Tatizo ni kwamba hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii hawana vitendea kazi, hawana usafiri na hata alivyozungumza Mheshimiwa Waziri ya kwamba wasitumie magari ya miradi ya UKIMWI na kadhalika, ajue wazi ya kwamba maendeleo ya jamii hawana usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa hatuna usafiri, Wilaya zote hazina usafiri na hata ngazi ya Kata hawana usafiri hata wa pikipiki. Mimi ninavyoelelwa ni kwamba, Maafisa Maendeleo ya Jamii siyo desk officers, hawa ni field officers, wanahitaji kwenda kwenye maeneo, wanahitaji kupatiwa usafiri, vinginevyo watatumia nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri wana mambo mengi, wanawapa usafiri kwa kubahatisha, lakini wakiwa na usafiri wao watu wa maendeleo ya jamii watafanya kazi nzuri kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninapenda kuishukuru Serikali yangu kwa kutoa ajira takribani kwa wananchi 52,000; ninaomba katika hawa 52,000 hebu tuangalie ajira ya Maafisa Maendeleo ya Jamii. Hatuna Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Rukwa ndani ya kata 97 ukiacha zile zilizoongezeka tunao Maafisa 51 tu, tuna upungufu mkuwa wa Maafisa Maendeleo ngazi ya Kata, tuna upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ngazi ya vijiji na tunao upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo wa Wilaya ya Nkasi na Wilaya ya Kalambo bado wana kaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hawa Maafisa Maendeleo wa Jamii wa Wilaya ya Nkasi na Kalambo wapatiwe uthibitisho kamili wa Maafisa Maendeleo wa Wilaya yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu suala la afya. Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi tuko mbali na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ambayo iko Mbeya. Tumekubaliana Mikoa hii miwili tuweze kujenga hospitali ya rufaa kati ya Rukwa na Katavi na tumeweza kupata eneo la hekari 97 kuijenga hospitali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa awamu ya awali imetupatia shilingi bilioni moja kwa maana ya kulipa fidia ya wananchi wetu waliokuwa katika lile eneo, ninashukuru sana kwa ngazi hiyo mliyoifikia. Kutokana na Halmashauri zetu kutokuwa na pato la kutosha, tunaomba Serikali Kuu iweze kuongeza hatua inayofuata ya uchoraji wa ramani na ujenzi wa hospitali ile iweze kuanzishwa katika Mkoa wetu wa Katavi na Mkoa wa Rukwa haraka iwezekanavyo ndani ya kipindi hiki tuweze kuifungua hiyo Hospitali ya Kanda ambayo ni hospitali ya Rufaa kwa Mikoa hii miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine katika upande wa afya ni upungufu wa madaktari. Katika Hospitali ya Mkoa tunao madaktari 20, kati ya madaktari 20 tunaowahitaji tunao madaktari 12 tu ambao hawakidhi mahitaji. Upande wa Madaktari Bingwa, tunao madaktari watano lakini tuna uhitaji wa Madaktari Bingwa 15 waweze kukidhi pale. (Makofi)

Jambo lingine katika upande wa afya ni kuhusu vituo vya afya na zahanati. Tunazo zahanati na vituo takribani 54 ambavyo vimejengwa lakini bado havijakamilika. Tunaomba Serikali iweze kuhakikisha ya kwamba haya majengo ambayo hayajakamilishwa 54, zahanati zikiwa 48 na sita ikiwa ni vituo vya afya viweze kukamilishwa ili viweze kutoa huduma kamili na hatimaye kuondoa msongamano katika hospitali ya Mkoa ambayo hivi sasa ndiyo inaifanya hiyo kazi ili akina mama na watoto vifo viwe vichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa vifo vya akina mama na watoto kwa kweli vimekithiri na tuna kila sababu ya kuweza kuhakikisha vinapungua kama siyo kuisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala la 10 percent za Halmshauri; wakati TAMISEMI ikizungumza, ilisema kwamba itatoa waraka kupeleka kwenye Halmashauri kuhakikisha ya kwamba wanafungua mifuko na hizo fedha za asilimia 10 zinapatikana na zinagawiwa katika vikundi vinavyohitaji vya akina mama na vijana. Tunaomba waraka huo kutoka TAMISEMI utoke ili Halmashauri ziwe na uhakika wa kutoa hizi asilimia 10 na Wabunge wa Viti Maalum tupate hizo nakala za waraka huo ili tuweze kufuatilia hizi fedha kama zinatoka na kuwafikia walengwa wanaohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalopenda kulizungumzia ni kuhusu ziara ya Mheshimiwa Waziri. Waziri alikuja Mkoa wa Rukwa bahati mbaya jioni yake akapata dharura ikabidi arudi Dar es Salaam na ziara yake ikafutika, hivyo tunamuomba Mheshimiwa Waziri urejee tena katika ziara yako ya Mkoa wa Rukwa ili uweze kufahamu changamoto za afya katika Mkoa wa Rukwa, kwa sababu Mkoa wa Rukwa hatuna hata Wilaya moja yenye Hospitali ya Wilaya, tuna Hospitali Teule tu, tunahitaji kuwa na Hospitali ya Wilaya.

Katika kuhangaika kutafuta hospitali ya Wilaya, tuliweza kuomba majengo ambayo yako chini ya TANROADS yaliyokuwa kambi ya kujengea barabara bahati mbaya inasemekana kwamba majengo yale ni madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na juhudi uliyonayo Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla, nina imani kwamba mtasimamia kuhakikisha Mkoa wetu wa Rukwa tunapata hospitali za Wilaya katika Wilaya zake zote nne ambazo kwa sasa hatuna hizo hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonekana ya kwamba Mkoa wa Rukwa tuko mwisho, tuko pembezoni, bila ya kuwa na afya bora itakuwa ni hatari, sisi ndiyo wazalishaji tunaowalisha katika nchi hii ya Tanzania. Hivyo tunawaomba kabisa kwamba tujaribu kuangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika upande wa afya ni huduma ya damu salama, akina mama na watoto ndiyo wanaohitaji kuhakikisha kwamba wanapata huduma salama na huduma salama ni damu, damu kwetu kuna tatizo la chupa za damu, sasa katika hizi chupa 250,000 sijui Mkoa wa Rukwa una kiasi gani cha hizo chupa, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili ni kwamba, vituo vyetu vya afya havina majokofu ya kuhifadhi hiyo damu salama na wale wataalam wa kukusanya damu salama wengi wao hawajapata mafunzo, hivyo ni kwamba hawapo ambao wanaweza kukusanya damu salama na kuhakikisha kwamba wagonjwa wetu wanapata damu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunawaomba mtoe mafunzo kwa wale wataalam wanaoshughulika na damu salama...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na big up.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii, awali ya yote ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya na nguvu na vilevile nawashukuru kina mama wa Mkoa wa Rukwa kuendelea kuniamini na mimi ninawaambia ya kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutoa shukrani za dhati na pongezi nyingi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara hii ni pana na ni Wizara ambayo inahitaji nguvu zaidi kuiongezea ili iweze kufanya kazi yake vizuri. Napenda kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Waziri Maghembe na Naibu wake ndugu Makani, wanafanya kazi ni nzuri na kazi ni nzito, na wamejitoa kwa kuweza kuisaidia Tanzania hii katika suala zima la maliasili na utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwapaka matope ya namna moja au nyingine ni kutokana tu na baadhi ya watumishi ndani ya Wizara hii wamekuwa si waaminifu na si waadilifu, ndiyo wanaopelekea Waziri huyu na Naibu wake kupewa matope hayo. Lakini matope hayo hayawastahili hata kidogo kwa sababu ya kwamba wanafanya kazi yao vizuri katika wakati huu mgumu. (Makofi)

Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa Rais wetu kutokana na jinsi anavyoweza kuimudu nafasi yake na kuisaidia Wizara yetu ya Maliasili kutuletea ndege ili utalii uweze kukomaa ndani ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la mkaa. Mkaa sisi sote Wabunge humu ndani tumetumia mkaa na bado tunaendelea kutumia mkaa, wananchi wa Tanzania wengi wao takribani asilimia 96 wanatumia mkaa na hata hiyo miji na majiji ambayo wanaotumia umeme na gesi lakini bado wanatumia mkaa, mathalani Dar es Salaam wanatumia mkaa wa takribani asilimia 91 pamoja na kuwepo na umeme na gesi, kwa sababu umeme na gesi ni gharama na umeme na gesi hauna uzoefu kwa wananchi wetu wa Tanzania kwa sababu ndani ya miaka yao yote hii wametumia mkaa na kuni. Kwa hiyo, ninaomba tuzungumzie suala la mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Maliasili, Utalii na Ardhi, nimetembelea Morogoro Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Kilosa na Morogoro Vijijini, upo mradi ambao unaendeshwa pale, mradi ambao unaitwa Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS). Huu mradi ni mradi mzuri ambao tunasaidiana na wenzetu wa Uswis nimeuona utakuwa ni jibu sahihi la kutunza misitu yetu na suala lile la Wizara ama suala lile la Serikali kuzuia kuchomwa mkaa halitaweza kuwepo tena, bali watu wataendelea kuwa na mkaa na kuutumia mkaa. Watautumiaje, hawa ndugu zetu wanaleta mkaa endelevu, ni kwamba wanaelezwa namna ya kukata miche ya mkaa ndani ya misitu wakiacha miche ambayo ina viota vya ndege, miche inayotumika kurina asali, na miche ya mbao. Wanaitenga, wanachukua miti inayostahili kukatwa na kutengenezwa mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameoneshwa namna ya kuchoma, uko namna kuchoma, namna ya chupa na namna ya box kwa kweli utaalam huu unapelekea hawa wachomaji wa mkaa wanapata mkaa mwingi wa kutosha, takribani gunia 50 mpaka gunia 60, na hii sehemu ambayo wanakata baada ya miaka mitatu wanaacha sehemu ile na sehemu ile inakuwa inapata maoteo, na yale maoteo yanarudisha msitu mapema zaidi kulikoni ule utaratibu tunaosema wa kukata mti, panda mti. Kwa sababu tunapanda miti kwa sababu uoto wake na ukomavu wake haupo, unakuwa ni asilimia ni ndogo sana, lakini hii ya maotea inaonekana kana kwamba ule msitu unarudi kama ulivyokuwa zamani na hatimaye unaweza kuwasaidia wanachi kuendeleza mkaa endelevu katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ushauri wangu kwa Serikali, ninaomba mradi huu kwa sababu unachukua muda mrefu, ni vyema Serikali ikaongeza mkono katika mradi huu ili mradi huu ukatawanishwe katika kanda zetu za nchi yetu. Tuna kanda nane za nchi yetu, kwa hiyo katika kanda zile nane wakapeleka utaalum huu wa mkaa endelevu. Ili huu mkaa kwa kweli ni rafiki mzuri sana wa utunzaji wa misitu yetu na mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba kabisa kwamba hata mapato ya Serikali yatapatikana kwa sababu yanakuwa na hesabu kwa sababu tanuru moja ni gunia 50; kwa hiyo, watajua Wilaya inapataje, Taifa linapataje, kwa bei ambayo inakubalika. Lakini tukiacha uholela ndio maana tunapelekea kwamba, Wizara yetu inasitisha, lakini inasitisha kwa sababu ya nini, wananchi hawa wanatumia mkaa na mkaa unatumiwa sana na akina mama na hata hii biashara ya mkaa ni kina mama, tunasema kina mama tunawatua ndoo, sasa tukiziba ziba hii mikaa bila kutumia utaratibu huu ni dhahiri kusema kwamba Serikali inaleta mzigo mwingine kwa akina Mama, wa mama watabeba ndoo ya maji, na watabeba tena na mzigo wa kuni ambao kwamba sio sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tanaomba tuwasaidie kina mama kwa kuongeza nguvu katika mradi huu, ili mradi huu uwe ni endelevu na tupate mkaa endelevu kwa wananchi wa Tanzania, kwa sababu mbadala wa mkaa katika nchi hii bado haujapatikana. Kwa hiyo, ninawaomba ndugu zangu tukubaliane na wewe Waziri Maghembe najua ni makini na msikivu, ninaomba huu mradi uje utoe semina kwa Wabunge wote hapa Bungeni, kabla ya Bunge halijaisha ili tukitoka wote na uelewa tutakwenda kutoa maelekezo kwa watu wetu kule na hatimaye na wao watafuata huu mkaa endelevu na sisi tutaweza kuokoa misitu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo kupanda miti itakuja kwa hiyo milima ambayo tuliyoiacha sasa hivi imeshakuwa ni kipara, lakini kwa sasa hivi kwa ile misitu tuliyokuwa nayo ni lazima tuweze kuweka utaratibu huo. Lingine ndio kusema ya kwamba mkaa ujitegemee katika maeneo yao, hao watu wa mjini Dar es Salaam watapata mkaa kutoka wapi, wakati mkaa wa Dar es Salaam unatoka Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu amabo unaweza kujibu hoja kwamba miti yote haina misitu kwa hiyo hawatakuwa na mkaa, lakini katika miji yote takribani asilimia 91 watu wa mijini wanatumia mkaa. Kwa hiyo nawaomba kwamba utaratibu uwepo, mkaa uingie mijini na iwezekane kuhakikisha kwamba akinamama hawa wanatokana na adha hiyo. Tunavyozuia tunapelekea bei ya mkaa kupanda, sasa hivi Dar es Salaam ni 73...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepongeza wakati wa kuchangia moja kwa moja Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana kwa dhati bajeti ya kitengo cha utangazaji wa utalii wetu kupewa kipaumbele ndani ya utalii kwa kutangazwa mapema vivutio vyetu kwani kuchelewa kwetu kunapelekea nchi jirani na vivutio hivyo kuvitangaza ndani ya nchi zao kama Kenya - Mlima Kilimanjaro au Zambia - Kalambo Falls(Rukwa) ni hatari na kutupunguzia mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuweke timu maalum ya kufuatilia vivutio hapa nchini na kutimiza taratibu kwa uharaka na kuvitangaza kwa kwenda sambamba na utekelezaji wa kuweka mazingira rafiki ya kuwafikisha watalii kwenye maeneo hayo. Tunashukuru Mkoa wa Rukwa Serikali kulishughulikia eneo la Kalambo Falls kuweka miundombinu, kasi hiyo iongezeke kukamilisha zoezi tuanze kupokea mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni muhimu sana kutekelezwa kikamilifu na Wizara ya Fedha kwa maana ya Hazina hutoa fedha kwa kufuata maidhinisho ya Bunge kwa hii Wizara kwani ina mchango mkubwa na unaweza kuongeza Pato la Taifa ikiwa itasimamiwa ipasavyo kwa maslahi ya nchi. Penye rupia penyeza rupia. Mfano, mwaka 2016/2017 kuliidhinishwa fedha za miradi ya maendeleo shilingi bilioni mbili na zikatolewa shilingi milioni 156.6 sawa na asilimia nane kwa fedha za ndani na nje wakatoa asilimia 82. Hali hii tunahitaji mabadiliko makubwa kwani sisi ndiyo wenye uchungu na haya maendeleo, kilio na mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio yetu sasa ni kwa Wizara hii pamoja na upana wake, lakini ina maslahi makubwa kwa nchi na maendeleo kwa watu wake, hivyo bajeti ya mwaka 2017/2018 ya shilingi bilioni 51.8 itatoka hata asilimia 75, kwani tunahitaji kwenda kwenye nchi ya viwanda na uchumi wa kiwango cha kati na mafanikio yake mengi ni ya muingiliano na Wizara kadhaa, hivyo ni mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho tunaomba hizo changamoto zilizofuatiliwa na timu ya pamoja za Wizara husika, taarifa hiyo ikafanyiwe kazi kwa mujibu wa taratibu na hatua husika. Ikibidi hadi Bunge tuletewe ili tuweze kufanya marekebisho kwa lengo la kuondoa malalamiko ya wananchi wetu na haya matope tunayopakana viongozi wa kisiasa na Kiserikali.

Mheshimwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mnyimi wa fadhila kama nisipomshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi hiki kifupi kwa wananchi wa Tanzania. Mwenyezi Mungu ampatie afya, ampatie nguvu na ampatie uwezo wa kuendelea kuifanya, ili adhma yake iweze kutimizika kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kwa mwaka huu kwa kweli imefanya kitu ambacho kimewagusa wananchi wa Tanzania na hususan wananchi na akinamama wa Mkoa wa Rukwa. Bajeti ni nzuri na bajeti hii tukiisimamia nina imani kabisa kwamba itatekelezeka kwa asilimia kubwa zaidi na hatimaye kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la maji. Maji imekuwa ni kizungumkuti, maji imekuwa ni suala tete kwa akina mama, ni suala tete kwa wananchi wa Tanzania. Mimi napenda kutoa ushauri kwa Wizara yangu ya Afya na Wizara yetu ya Fedha kwamba tunaomba hii shilingi 40 naomba tuongeze tena shilingi 10 iwe shilingi 50. Kwa sababu hii fedha inahitajika kurudisha deni la Serikali, inahitajika kuleta umeme na inahitajika kuleta maji.

Mheshimiwa Mwenyekii, tunasema kwamba tunatua ndoo ya akina mama kichwani, lakini ukiangalia karibia asilimia 60 vijijini na vitongoji hakuna maji safi na maji salama. Mfano Mkoa wa Rukwa, ningeomba Serikali iangalie umuhimu wa kuangalia kutoa maji katika Lake Tanganyika. Lake Tanganyika maji yako ni mazuri, lakini tatizo ni kwamba, hayajawekewa mradi wa kuyaleta kwa wananchi. Mwambao wote huko wa Lake Tanganyika kuanzia Kala mpaka Karema, (Katavi) hakuna maji salama na maji safi, lakini Lake Tanganyika iko pale! Tungeiomba Serikali ikaangalia mradi wa kutoa maji Lake Tanganyika kwenda kwa wananchi wetu ili kinamama waweze kupumzika na suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba, tunatua ndoo ya mama, kama tunatua kweli ndoo ya mama, lakini mimi naona kuna wasiwasi wa kumpatia tena mzigo mwingine. Mzigo mwingine ni mkaa, nilizungumza katika mchango wangu wa msingi katika maliasili na utalii tukasema ya kwamba ni vema tukapewa semina Wabunge kuhusu mkaa endelevu ambao ni rafiki wa misitu, ili tukiuelewa ikawa ni faida kwa akinamama wasipate mzigo wa pili kabla ya kutuliwa ndoo ya maji kichwani. Kwa maana hiyo, tunaiomba Serikali tuongeze hiyo shilingi 10 iwe shilingi 50 ili iweze kutoa tatizo hili ambalo linakuja la pili kwa akinamama zetu kuwa mzigo wa pili ndani ya kichwa chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaloomba lingine ni kwamba, ni kuhusu suala zima la barabara. Mkoa wa Rukwa tumechelewa, Mkoa wa Rukwa tulisahaulika kuhusu barabara. Hadi hivi sasa bado hatujaungana na Katavi, bado hatujaungana na Kigoma, bado hatujaungana na Tabora. Ninaomba kwa sababu tunakubali kuunga Mikoa yetu na hizi fedha zinatoka katika Serikali yetu ya ndani, kwa hiyo, tunaomba fedha hizi zitoke katika ukamilifu wake ili tuweze kuunganika na Mikoa yetu ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mkoa wa Rukwa tunaungana na Kongo, tunaungana na Zambia, tunaomba Matai-Kasanga na Matai-Kasesya hizi barabara zikamilike. Kukamilika kwa barabara zitawasaidia akinamama kwenda kwenye masoko ya mazao yao hali kadhalika kwenda kupata huduma ya afya kwa sababu Mkoa wa Rukwa hatuna Wilaya hata moja yenye Hospitali ya Wilaya, zote tuna Hospitali Teule kwa maana ya Vituo vya Afya; kwa hiyo, akina mama wanatoka huko wanakuja Mkoani kuja kupata huduma ya afya, tunaomba hizi barabara, hizi fedha za ndani zitoke katika asilimia hata 75 angalau hizi barabara sasa ziweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninapenda kuzungumzia suala zima la elimu. Tunao watoto wetu walemavu, hawa watoto wetu walemavu wanahitaji kupata elimu, lakini vifaa vyao vya kufundishia ni vifaa vyenye gharama kubwa zaidi, Halmashauri hawawezi na hata wazazi kuchangia hawawezi. Lakini juzi nimesikia kwa Mheshimiwa Waziri akisema kwamba Waziri Mkuu amepokea vifaa vya elimu. Naomba hivyo vifaa vya elimu ya kufundishia viweze kupelekwa shule ya Malangali ya Watoto Viziwi, Vipofu pamoja na Albino hali kadhalika shule ya Mwenge ambako kuna watoto wenye mtindio wa ubongo waweze kupelekewa vifaa hivyo, waweze kupata elimu nao waweze kujiunga na sisi katika maendeleo ya jamii ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la shilingi milioni 50. Shilingi milioni 50 tumeizungumza na inawezekana kutekelezeka. Kutokana na kasi ya Rais wetu kuhakikisha kwamba, rasilimali ya nchi hii tunaitumia Watanzania, nina imani kabisa kwamba, hizi shilingi milioni 50 za kila kijiji zitapatikana kutokana na jitihada iliyopo katika Serikali yetu.

Kwa hiyo, ninaomba Serikali iweke tu utaratibu wa namna ya kuzisimamia na namna ya kuzifikisha kwa walengwa na wale wanaohusika ili ziweze kufanya kazi ya maendeleo. Nina imani kabisa kwamba jitihada ya Rais wetu Magufuli atasimamia ahadi zake kwa sababu hili alikuwa akilizungumzia sio kwa kuombea kura, alikuwa analizungumzia kwa kutaka kuhakikisha kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami kuzungumza na Bunge lako Tukufu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya ya kuweza kusimama leo hii katika kuzungumzia suala zima la Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyojitokeza mbele kabisa kuhakikisha ya kwamba anaboresha na kuweka maisha bora kwa askari wetu Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mnyonge mnyongeni na haki yake mpeni. Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi kwa hali ngumu sana, lakini inafanya kazi kwa weledi na kuthibitishia Watanzania kuwa katika amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao Wanajeshi, Polisi, Zimamoto, Uhamiaji na Magereza, wote hawa wako karibu na wananchi wa kawaida na wanashirikiana na wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, Mambo ya Ndani ni msingi wa amani na utulivu wa nchi yetu. Bila hawa, hii amani tunayojivunia hivi sasa tusingejivunia hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tusione kigugumizi na wala tusione aibu, ni lazima tuseme kwa ukweli kabisa kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi yake vizuri na kwa weledi, iliyobakia kwetu sisi ni kuwaunga mkono ili bajeti yao hiyo wanayoipata na hiyo walioyoiunda iweze kuongezeka na waweze kufanya kazi yao vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima la bajeti. Bajeti ya 2017/2018 tuliweza kutenga, lakini Wizara ya Fedha imetoa kwa asilimia 28 tu kwa miradi ya maendeleo. Naomba Wizara ya Fedha, hii asilimia 28 ni ndogo sana, naomba wajitahidi kwa Jeshi la Polisi ama kwa Wizara ya Mambo ya Ndani waweze kupata bajeti yao kamilifu. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana. Bila usalama na amani hata hayo mengine tusingeweza kuyafanya. Mengi wameyasema wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Ndani ipatiwe kwa asilimia mia moja bajeti yao wanayoipanga na kwanza hata hii bajeti tuliyoiweka haikidhi mahitaji ya Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la makazi. Napenda ku-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe katika Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Tumetembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara; nyumba za Wanajeshi wetu kwa kweli siyo nzuri, haziridhishi, ni kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe maamuzi magumu, kama ilivyotolewa maamuzi kwa Uhamiaji hapa Dodoma kuhusu kununua nyumba pale Iyumbu, basi tunaomba na Wizara ya Mambo ya Ndani wachukue jukumu la kununua nyumba kwa Askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba zilizojengwa na National Housing ambazo wanasema kwa bei nafuu, lakini siyo bei nafuu na wananchi wameshindwa kuzinunua. Naomba hizo nyumba zinunuliwe na Serikali kwa Wanajeshi wetu ambao hawana nyumba za kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba zitolewe ramani maalum za kujenga nyumba za Wanajeshi yetu kwa sababu nyumba zile walizonazo siyo za kuishi binadamu ni nyumba za kuishi mifugo. Tunaomba nyumba za kuishi binadamu zitolewe kwa kila mkoa na kila mkoa upewe idadi maalum kwa kila mwaka wajenge nyumba ngapi; ili tuweze kutathmini baada ya hii miaka miwili na nusu ni mkoa upi utapata ushindani wa kujenga nyumba za kutosha za Wanajeshi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalopenda kulizungumzia ni kuhusu kupandisha madaraja Askari. Kwa kweli inachukua muda mrefu sana kupandishwa madaraja Askari hawa na wale wanopandishwa madaraja inachukua muda kuwapatia fedha zao stahiki kwa daraja walilopandiswa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuna Askari ambao wanastaafu. Mtu anapostaafu kwa mujibu wa Jeshi wanapewa likizo ya kustaafu. Likizo ya kustaafu ni miezi minne. Kipindi hiki cha miezi minne kinatosha kabisa kumwandalia mafao yake ili akimaliza tu likizo yake, anapoanza kustaafu, fedha yake inapatikana; lakini tangu mwaka jana, Askari wamestaafu mpaka hivi leo wanatimiza sasa ni mwaka hawajapata mafao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Jeshi liweze kuwapatia fedha yao. Hii ni kutokana na kwamba kile kifungu cha matumizi ya kawaida na matumizi mengineyo hakifiki kwa wakati kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na kinafika kikiwa hakikidhi mahitaji kwa wenyewe katika kutekeleza mahitaji hayo yote. Kwa hiyo, nawaomba Wizara ya Fedha, wawape fungu hili katika ukamilifu wake ili waweze kulipa madeni ya hao Maaskari wanaolalamika; wengine wana hali duni na wanaweza wakapoteza maisha kabla hawajapata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iweze kuhakikisha kwamba fungu hili kwa Majeshi yote; Zimamoto, Uhamiaji, Magereza na Polisi wapelekewe katika ukamilifu ili waweze kuondoa matatizo ya Wanajeshi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu suala la kiwanda. Tunacho kiwanda Morogoro kinachotengeneza sare za Polisi na wafungwa. Tunaomba viwanda hivi viweze kuongezwa au viwezeshwe na Serikali ili viweze kuzalisha kiasi cha kutosheleza wananchi na Wanajeshi wetu katika nchi yetu. Tunawajua idadi yao. Wanajeshi hawa wakipata angalu pair mbili zinaweza zikawasaidia. Vile vile kiwanda cha viatu kiongezwe ili kiweze kutoa viatu kwa Wanajeshi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda Lindi na Mtwara, tumekuta baadhi ya Askari viatu vyao kwa kweli tulisikitika sana. Tulisikitika mno! Kwa hiyo, tunaomba hiki kiwanda kinachotaka kujengwa hivi sasa kitakachoweza kuzalisha jozi 4,000, naomba kianzishwe mara moja ili Wanajeshi wetu waweze kupata vifaa vya kutumia katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nashukuru na kutoa pongezi sana kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya. Ila naomba kwa Serikali yangu sikivu, suala la mazingira yetu Mkoa wa Rukwa, Bonde la Rukwa, Bonde la Tanganyika, kwa kweli hali siyo nzuri kimiundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, tunahitajika tupate Vituo vya Polisi. Vituo vya Polisi vipo lakini havina amari. Kwa hiyo, wako Askari wanalinda bila kuwa na silaha, lakini wananchi wao wa kule wanazo silaha na ndiyo maana mauaji katika Bonde la Rukwa yanaendelea. Kwa sababu hakuna amari katika vituo vyetu, inaweza kuleta matatizo, Polisi wetu wanashindwa kufanya kazi iliyokuwa katika ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani ione umuhimu wa kuweka amari katika hivi Vituo vyetu vya Polisi vilivyokuwa kule Bonde la Rukwa. Vinginevyo, nadhani zile silaha zao wanaweka mahali pasipokuwa salama na kwa maana hiyo inahatarisha vile vile katika suala zima la ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba Wizara yetu ya Mambo ya Ndani iweze kupewa fedha kamilifu katika mwaka huu wa 2018/2019 ili iweze kutimiza majukumu yake katika ukamilifu wake. Kutokana na kazi ngumu wanayoifanya Polisi wetu, ndiyo maana maneno mengi yanazungumzwa. Daima mti ukiwa na matunda hupopolewa na mawe, mti usiokuwa na matunda mazuri hakuna mtoto hata mmoja atakayeupopoa mawe. Kwa hiyo, maneno mengi haya tunayozungumza Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani ni dhahiri kusema kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu zangu wa Zimamoto waweze kuongezewa vituo na vile vile waweze kupewa magari angalau nusu ya vituo viwepo na nusu ya magari ya vituo hivyo yaweze kupatikana, kwa sababu wananchi wetu wanaendelea kujenga majumba na hatimaye kufikisha miji yetu kuwa scattered, inakosekana miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, likitokea la kutokea, Zimamoto hawawezi kuingia kwa urahisi mle ndani. Kwa hiyo, tunachokiomba ni kwamba, hawa watu wa Zimamoto wapewe vituo vya kutosha angalau nusu ipatikane na hali kadhalika magari yaweze kupatikana ili waweze kutusaidia vizuri ndugu zetu hawa wa Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni kuhusu watu wa Uhamiaji. Watu wa Uhamiaji kwa kweli katika nchi yetu hii ya nchi nane zinazotuangalia wanahitaji kupewa nguvu ya ziada na nguvu ya ziada ni kuhusu na magari yao na nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachokiomba ni kwamba hawa watu wana doria, Polisi wana doria, Magereza wana doria, Zimamoto wana doria na Uhamiaji wana doria. Vile vile wana suala la kufuatilia makosa mbalimbali katika kufanya msako wa kuangalia Wahamiaji, wahalifu na kadhalika. Sasa watu hawa wana dharura mbalimbali, lakini hawana magari na wala hawana mafungu ya mafuta ya kukamilisha shughuli zao hizo na ni shughuli muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani waone umuhimu kwamba sasa umefika wakati wa kuhakikisha watu hawa wanapata magari ya kutosha, mafungu ya mafuta ya kutosha. Vile vile wanafanya kazi na baada ya saa za kazi, pamoja na kwamba ni saa 24, lakini hawa ni binadamu, tujaribu kuweka na motisha kwa watu hawa wakati wa kufanya kazi zao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo pia naomba ndugu zangu Serikali, najua kila Wizara huwa inapewa ukomo wa bajeti, lakini kwa majeshi yetu tunaomba ukomo uangaliwe kwa Serikali. Ukomo ni mdogo na kazi wanayoifanya ni kubwa zaidi. Kwa hiyo, naomba ukomo wa miradi ya maendeleo, ukomo wa shughuli za kawaida uangaliwe upya na kuwaongeza nguvu ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuunga mkono hoja na nawapongeza sana Makamishna wote, Waziri na Naibu wake na wataalam wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani, aluta continua, big up!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuzungumza mbele ya Bunge lako tukufu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia afya na nguvu na kuweza kusimama leo hii mbele ya Bunge lako na kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuzungumzia suala zima la bajeti ya elimu. Bajeti ya elimu imeweza kufanyiwa kazi kwa mwaka 2017/2018 na kuweza kupatikana kwa asilimia 65 ndani ya matumizi ya kawaida na asilimia 68 katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini elimu ni kila kitu, bila kuwa na elimu huwezi kupata maendeleo yoyote katika maisha ya mwananchi, ni lazima apate elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninaiomba Hazina ijipange kwa ukamilifu angalau kwa Wizara ya Elimu iweze kupata bajeti yake kwa asilimia 85 ili waweze kutekeleza mambo yao kwani wana changamoto nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Mkoa wetu wa Rukwa tuna mapungufu ya madarasa, tuna mapungufu ya matundu ya vyoo, tuna mapungufu ya nyumba za walimu na vilevile tuna mapungufu ya maabara pamoja na vifaa vya maabara. Ukiachia mbali suala zima la upandishaji wa vyeo vya walimu na hata kuhakikisha kwamba wanapata stahiki zao zilizo sahihi katika Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanakosa hata ule motisha na kufanya kazi yao katika uweledi na kufanya kazi yao katika hali iliyo nzuri zaidi. Kwa hiyo, ninaiomba Hazina kuweza kutoa fedha za kutosha kutokana kufuatana na jinsi bajeti tutakavyoipitisha hapa leo ili kuhakikisha kwamba elimu waweze kutimiza malengo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilikuwa naomba Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba inajikita sana katika elimu ya awali. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuseme kwa kweli kabisa kwamba lugha yetu ya Tanzania ni kiswahili, lakini lugha ya kiingereza ni muhimu kwa watoto wetu. Kwa hiyo tunawaomba Wizara ya Elimu tujikite kuhakikisha kwamba haya masomo ya awali (chekechea) waanze na lugha ya kiswahili na lugha ya kiingereza mpaka kuendelea huko mbele. Kufikia hapo ndiyo kusema ya kwamba walimu wanafundisha shule za chekechea naomba wafanyiwe maandalizi mazuri ili waweze kwenda kuwaandaa watoto wetu katika elimu ya awali ambao ndiyo msingi wa kuibua elimu bora ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima lililozungumzwa katika ukurasa 143, kuhusu nyumba za walimu. Suala la nyumba za walimu ni tatizo la nchi nzima. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri na Wizara yake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika Mama Ndalichako na timu yako mnafanyakazi pamoja na changamoto zilizopo hamyumbi na wala hamtikisiki ilhali kwamba mnafanyakazi kwa pamoja. Ninawaomba hizi nyumba 40 zimetajwa katika shule kadhaa na Rukwa tumetajiwa shule moja ya Kasanga. Lakini nilikuwa naomba, kwa kuwa bajeti hii tumechelewa kuwekewa zaidi ya shule mbili/tatu kwa Mkoa wa Rukwa ninaomba awamu ijayo Mkoa wa Rukwa uweze kuangaliwa katika kuhakikisha kwamba tunajenga nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mnajenga nyumba za walimu katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi, hata sisi kwetu Mkoa wa Rukwa ziko sehemu hizo; Milepa, Kaoze, Kipeta, Ninde, Wanpembe, Kala, Senga, Molo ni maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi. Ningeomba kwamba tuweze kupatiwa nasi vilevile ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu wawepo wa kutosha ili watoto wetu waweze kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kuzungumzia suala la usafi wa mazingira. Usafi wa mazingira shule zetu za msingi na sekondari katika upande wa vyoo kwa kweli hauridhishi, unasikisitisha sana na kwa kuwa Wizara imeamua kujenga madarasa 2,000 na matundu ya vyoo 2,000, hata wakijenga 10,000 lakini hayatakuwa bora zaidi ikiwa kwamba hatuna huduma za maji katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Hazina (Wizara ya Fedha) wahakikishe kwamba zile shilingi bilioni
17.033 ambazo wizara imeweka kama bajeti yao 2018/2019 fedha hii itoke kwa sababu imeshawekwa hapa, lakini ingeongezeka ikawa ni kubwa zaidi kwa sababu zoezi walilonalo kuhusu vyoo vya shule kwa kweli eneo ni kubwa zaidi na vyoo kwa sababu vinahitaji maji na maji hayapo shuleni wanahitaji kuweka miundombinu ya maji, aidha, ya kukinga maji ya mvua au kuhakikisha kwamba wanaweka mifereji na kufikisha maji katika shule zetu zote za nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni zoezi kubwa, kwa hizi shilingi bilioni 17 kwa kweli ni ndogo zingeweza zikaongezeka ili wakaweza kufanisha hili zoezi ambalo ni gumu na tete kwa watoto wetu; na hasa watoto wetu wa kike hawawezi kuzihifadhi kwa sababu zile siku zao tatu au siku zao tano wanakosa maji katika maeneo yao ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napenda vilevile kuzungumzia suala la ujenzi wa shule za mikoa. Imetajwa mikoa saba inayojengewa shule, ninawaomba kwamba hata Mkoa wa Rukwa nao unahitaji kuwa na shule. Tuna shule chache na hata shule za sekondari za wasichana hatuna. Tunayo sekondari ya wasichana moja ambayo ni ya dhehebu ya wenzetu wa kikristo iko pale Kizwite, lakini tunahitaji kupata shule za sekondari za wasichana hata mbili, tatu kwa Mkoa wetu wa Rukwa na mjue wazi kabisa kwamba Mkoa wa Rukwa ulikuwa uko pembezoni na imechelewa na mambo mengi. Kwa hiyo suala la elimu ni mojawapo.

Kwa hiyo, tunawaomba kipindi kijacho, naomba katika ujenzi wa sekondari hizo za mikoa na Mkoa wa Rukwa uwemo katika mipangilio hiyo ya kikao kinachokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya ukurasa wa 126 wa hotuba wamezungumzia suala la ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi. Ninashukuru kuona Mkoa wa Rukwa nao umo miongoni mwa hiyo mikoa, tunashukuru sana Wizara. Lakini je, hii shule ya ustadi inakwisha lini? Ni ndani ya mwaka huu wa 2018/2019 ama zaidi ya mwaka mmoja? Kwa hiyo, tunapenda kufahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naifahamu wazi kwamba ndugu zangu wa Wizara ya Elimu tulishazungumza mara nyingi sana ndani ya Bunge hili kwamba Mkoa wa Rukwa hatuna Chuo cha VETA. Tunaomba Chuo cha VETA nayo inaanza lini kujengwa pale katika Mkoa wetu wa Rukwa ili vijana wetu wa darasa la saba na darasa la kumi na mbili waweze kupata mahali pa kuweza kupata stadi na kuweza kujiajiri wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nililokuwa napenda kulizungumzia ni kuhusiana suala ya walimu. Walimu wanahitajika kupata motisha. Lakini pamoja na hivyo Wizara imeelekeza katika ukurasa wa 123 kwamba kuna fedha zimetengwa, takribani trilioni moja ambazo watazitumia kwa kuhusu na kutoa na motisha kwa Halmashauri na kwa shule mbalimbali ili waweze kuonesha nguvu ya kuongeza elimu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, lakini tatizo linakuja ubora wa hizi Halmashauri na kupata motisha hizo na ubora wa hizi shule kupata motisha hizo kwa walimu wale kutaendelea na kuwezekana kuwepo kuwa na bora zaidi ikiwa Idara ya Ukaguzi ikiwezeshwa. Hawana magari, hawana mafungu ya kujiendesha wao wenyewe katika suala zima la ukaguzi. Ukaguzi si maafisa wanaokaa ofisini, ukaguzi ni watu ambao wanakwenda field si kwa ratiba maalum hata wakati mwingine kuvamia zile shule na kuona zinaendelea namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba hiyo motisha iliyokuwa imetengwa ninaomba Hazina itoke ili kwamba wale watakaoshinda na wale watakaoshindwa waweze kuhamasika ili na wao pia kipindi kichokuja waweze kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusiana na ubora wa elimu. Ubora wa elimu ni mambo mawili; wale wanaoandaliwa na wale wanaowaandaa hao wanaoandaliwa. Kwa hiyo tunaomba elimu waweze kuangalia kitu hicho wale wanaowaandalia hawa wanaoandaliwa wawe katika ubora zaidi na katika ukamilifu zaidi. Na hawa watu wapo tunao walimu walimaliza kusoma vyuoni wako mitaani hawajapata bado ajira, tunaomba hao walimu wato…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima nashukuru kwa kunipa nafasi hivyo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuzungumza kiasi, nadhani hata dakika 10 hazitofika kwa sababu mambo mengi yamekwisha kuzungumzwa ambayo nilikuwa nimeyaandaa kuyazungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa moyo wa dhati aliounesha kwa majeshi yetu ya Tanzania kuhakikisha ya kwamba wanaboreshewa nafasi zao za kufanyia kazi hali kadhalika na makazi yao. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaunga mkono kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakuu wote wa Majeshi wa JWTZ na JKT kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uzalendo. Nasema ya uzalendo kwa sababu hawa ndugu zetu kwa kweli maisha yao katika mazingira yao na wanapoishi kwa kweli majumba yao siyo mazuri na hata maeneo yao ya kazi siyo mazuri na makazi siyo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iweze kuwaongezea mfuko katika fungu la maendeleo kwani hawa watu wameonyesha uzuri wao wa ujenzi katika uzio wa Tanzanite. Wameonekana kwamba ni watu bora na wanaoweza kusimamia kitu katika muda mfupi na kuweza kukamilisha. Ni vema ndugu zetu wakaongezewa fedha za mafungu ya maendeleo ili waweze kukarabati, waweze kujenga miundombinu yote inayowahusu katika upande wa Jeshi kwa ukamilifu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali au Wizara ya Fedha katika suala zima la kuweka ukomo wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi kwa kweli ukomo ule siyo mzuri. Kwa mfano, mwaka huu walikuwa wamewekewa ukomo wa trilioni 1.9 lakini bajeti ya ulinzi bajeti ya Wizara ni trilioni 2.8. Nawaomba Wizara ya Fedha, kabla hawajafanya jambo lolote lile katika makusanyo yao ya fedha na kuzigawa fedha hizo, katika
kuziweka kwenye ukomo, waangalie kwa jicho la pekee Wizara ya Ulinzi. Ulinzi ni kila jambo, ulinzi ni kila kitu, bila ulinzi mengine yote hayawezi kuyafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hivyo hata katika Wizara ya Mambo ya Ndani, nilizungumzia suala la Wanajeshi, tusiweke ukomo jamani, wanafanya kazi ngumu ni ngumu sana. Wanajeshi wana hali ngumu sana bila wao tusingekuwepo hapa. Mimi leo asubuhi nilipokuwa nakuja Bungeni nilipowaona wenzangu wa Jeshi nikasema leo ni usalama mtupu katika Bunge letu. Kwa hiyo, wanajeshi tunawapongeza na tunawatakia kila la heri katika maisha yenu katika kazi ngumu mnayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara waone umuhimu kabisa katika bajeti hii waliyoiomba Wizara ya Ulinzi kwanza ni ndogo. Wamefanya hivyo kwa sababu ya ukomo, naomba hii bajeti waliyokuwa wameiandika itolewe yote asilimia mia kwa mia, wala pasiwe na mjadala wa kuiacha hii sehemu fulani, kwa sababu mwaka jana wametoa asilimia takribani 80, lakini hii asilimia 20 iliyobaki pia nayo tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kabla ya tarehe 30 Juni, fedha hii iweze kupelekwa katika Wizara ya Ulinzi ili waweze kukamilisha malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la maendeleo. Katika suala la maendeleo mwaka 2017/2018, katika Mashirika yetu Mzinga tulipata asilimia 38 na Nyumbu tulipata asilimia saba ni aibu. Nasema ni aibu kwa sababu hawa watu wanachokifanya wanafanya kitu ambacho kina maslahi kwetu. Wanapunguza gharama ya utengenezaji wa vifaa mbalimbali kwa Taifa na kupunguza gharama ambayo inatoka nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi ni vema tukawapa fedha zao kamili ili waweze kukamilisha malengo yao. Kwa maana hiyo Wizara katika Fungu Namba 38, mwaka 2017/2018 tulipata asilimia 41. Sasa naomba hizi bilioni nane za 2018/2019, zitoke zote. JKT - Fungu 39, bilioni sita na pia Wizara bilioni 220, naomba zitoke zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba Wizara ya Fedha, sijui kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mwinyi ni mtu mtaratibu, mkarimu ambaye hataki vurugu ndiyo maana labda wanambana hizi fedha hazitoki zote. Naomba ndugu zangu msimchukulie ukimya wake na upole wake kutoweza kumpa katika ukamilifu, naomba mumpatie kwa asilimia 100 fedha zake za mafungu yake aliyoomba kwa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la JKT. Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha elimu bure. Baada ya kupitishwa elimu bure vijana wetu wengi ambao wanamaliza darasa la saba, wanamaliza darasa la 12 wanakuwa wako mitaani na hawana mahali pa kwenda. Tunaomba vijana hawa waweze kuchukuliwa kwenda kujiunga na JKT ili waweze kupata uzalendo wa nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya wanaochukuliwa kutoka kwenye Mkoa hawazidi vijana 100, kila wanapokuwa wanafanya reshuffle ya kusaili vijana wa JKT wanachukua chini ya 100. Naomba hii idadi iweze kuongezwa kwa kila mkoa, idadi iwe ni kubwa kwa sababu tumeamua kuongeza Kambi za JKT, kwa hiyo, tunaomba tuongeze idadi ya watoto wanaochukuliwa kwenda JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kutoa shukrani za dhati, nilipoingia Bungeni niliulizia suala la Kambi ya Luwa na Kambi ya Milundikwa kwamba yawe ni Kambi za Jeshi. Nashukuru kwamba sasa zimerejeshwa kuwa ni kambi za JKT, kwa maana hiyo nawashukuru sana kwa maamuzi hayo ili vijana wengi wa Mkoa wa Rukwa nao watapata nafasi ya kujiunga na JKT. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kutoa pongezi za dhati kwa Wanajeshi wetu kwa kazi nzito wanayoifanya. Naiomba Serikali yangu sikivu, kwa heshima na taadhima kubwa, tujaribu kusukuma yale mashirika na zile taasisi na zile Wizara ambazo zinadaiwa na SUMA JKT, naomba walipe madeni hayo. Walipe madeni hayo kuhakikisha kwamba ndugu zetu wa SUMA waweze kuendeleza shughuli wanazoziendeleza za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa sijawahi kununua trekta kwa sababu matrekta yalikuwa na bei kubwa, lakini leo baada ya JKT SUMA kutoa matrekta nimeweza kununua trekta na wamewasaidia sana wakulima wadogowadogo wenye kipato kidogo kuweza kulipa by installment na kuweza kukamilisha matrekta yale na sasa hivi wanalima kwa tija inayokubalika kwa hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kama tunavyosukuma madeni ya TANESCO, kama tunavyosukuma madeni ya maji, basi naomba tusukume na madeni ya SUMA JKT ili waweze kujiendeleza na waweze kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa heshima na taadhima napongeza Jeshi langu la Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya nasema kwamba Aluta Continua na big up, hamna matatizo tuko pamoja na ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SILAFI J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuzungumza machache katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipatia pumzi na afya ya kuweza kusimama tena katika mwaka huu wa 2019 niweze kuzungumza haya yafuatayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, natoa pongezi za dhati kwa mdogo wangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kujituma na kujitoa kwa maslahi ya kuhakikisha kwamba elimu bora kwa Watanzania inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuzungumza hayo lakini napenda kumuarifu Waziri wa Fedha, Wizara ya Elimu ni vyema ikaangaliwa kwa jicho la namna yake la kuhakikisha ya kwamba ukomo wa bajeti unaongezwa. Nasema hivyo kwa sababu ina miradi mingi na mizito ya kutekelezwa ili kuiweka elimu katika hali inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima la miradi ya maendeleo. Fedha ya miradi ya maendeleo ya mwaka 2018/2019 haikuweza kutoka yote na vilevile nina wasiwasi hata mwaka wa fedha 2019/2020 zinaweza kutoka na kukidhi mahitaji katika maendeleo ya Wizara yetu ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la maboma. Kuna maboma kadhaa ndani ya mikoa yetu ya madarasa, shule za msingi na shule za sekondari hali kadhalika nyumba za walimu. Maboma haya yamejengwa kwa nguvu za wananchi lakini Serikali yangu haijaongeza mkono wake katika kuhakikisha kwamba maboma yote yanakamilika ili watoto wetu waweze kupata nafasi ya kujifunzia. Kwa hiyo, tunaomba Wizara hii iongezewe ukomo wa bajeti ili waweze kuweka bajeti yao katika mahitaji yanayohitajika ili maboma yetu yaweze kukamilika yote pamoja na jitihada waliyofikia ya kukamilisha maboma hayo kadhaa. Kwa hiyo, tunaomba fedha za maendeleo ziweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nnapenda kuzungumzia suala la madarasa lakini shule ni choo, bila kuwa na vyoo vya kutosha kwa maana ya matundu ya kutosha kwa watoto wetu watapata maradhi mengi ya kuambukiza. Kwa hiyo, tunawaomba Wizara hii iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba vyoo vya shule vinaendana na idadi ya wanafunzi waliopo hasa ukizingatia kazi nzuri aliyoifanya Rais wa Jamhuri wa Tanzania Dkt. Magufuli kuhusu elimu bure, ni dhahiri kusema kwamba wanafunzi wameongezeka katika shule zetu lakini vyoo vimebakia vilevile. Sasa hivi vyoo vingi vimejaa, tukiwaambia Mabwana Afya wakazungukie shule bila shaka nyingi zitafungwa kwa sababu vyoo vyao haviko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuweka mkakati maalum wa ujenzi wa vyoo vya watoto shuleni. Pia tunaomba waweke choo maalum kwa watoto wetu wakubwa wa kike hasa katika shule za sekondari kwani zimekuwa na matatizo makubwa. Hali kadhalika vyoo vinavyojengwa ni maji, tunaomba utaratibu wa kuweka miundombinu ya maji katika shule zetu uweze kupewa kipaumbele ili vyoo vyetu hivyo vitakavyojengwa viwe katika hali ya usafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la idadi ya wanafunzi. Idadi ya wanafunzi imeongezeka ndani ya madarasa yetu na kufikia walimu kufanya kazi ya ziada. Kwa kweli mimi napongeza sana kazi kubwa wanayoifanya walimu wetu pamoja na hali ngumu wanayofundishia lakini bado watoto wetu wanafaulu, wanakwenda sekondari, high school na vyuo vikuu lakini kazi ya walimu ni ngumu. Katika kipindi hiki cha miaka mitatu cha ongezeko la wanafunzi katika madarasa yetu na mwalimu kujikuta ana watoto zaidi ya 60 ndani ya darasa lakini bado anaifanya kazi ile. Hata hivyo, mishahara yao haijaongezeka na ni midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibuni kila Mbunge aliyesimama hapa amezungumzia mishahara ya walimu, kweli wamefanya kazi nzuri ndani ya hii miaka mitatu, tunaomba tuangalie madaraja yao na tuhakikishe ya kwamba tunawaongezea mishahara yao ili kuwatia morali walimu hawa waweze kufanya kazi nzuri zaidi na kazi iliyotukuka, pamoja na kazi hiyo ya kutukuka wanaifanya hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala zima la kuhakikisha ya kwamba tunaongeza ajira, tunashukuru kwa hizo nafasi elfu nne, lakini nafasi elfu nne katika mahitaji ya milioni 60, kwa kweli haijafanyika kazi yoyote. Tunaomba tuongeze nguvu ya kutoa ajira kwa walimu, walimu wapo, wako kwenye mitaa yetu, hata kana kwamba walimu wengine wanashindwa kwenye maeneo hayo kutokana na mazingira, lakini bado mazingira yale tuliyokuwa nayo sisi kule hasa mikoa ya pembezoni, vijijini, wako walimu waliomaliza vyuo wako mitaani, nao hawajaweza kupata nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba basi, kama wengine hawawezi kuja kwenye mazingira yale ya pembezoni, kule vijijini, basi walewalioko kule naomba wapewe kipaumbele waweze kupata ajira ya ualimu, kwa sababu wanazoea mazingira yale na wamo ndani ya mazingira yale, waendelee kuwafundisha wenzao nao waweze kupata elimu iliyokuwa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ongezeko la ajira ya walimu, bado tuko nyumba, tunaomba mshirikiane na ndugu wa TAMISEMI, tuweze kupata ajira ya kutosha kwa walimu kwani tunawahitaji sana, hasa sisi mikoa ya pembezoni. Ninasema sisi mikoa ya pembezoni, hata shule za private kule ziko ni chache, ziko mbili tatu, kwa hiyo, bado tunahitaji walimu, kwa hiyo, tunaomba walimu waweze kupatiwa kipaumbele waweze kuongezewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nilikuwa nazungumzia upande wa watoto walemavu, kuna watoto walemavu maalbino, ambao wenye ufinyu wa uono, lakini wanahitaji kusoma, kuna baadhi ya wanafunzi albino, wamechanganyikana na wanafunzi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapokuwa wanasoma katika kuandika ama wanapokuwa kwenye mitihani, wakati wa kuandika, wao wanakwenda taratibu mno, wenzao wanakwenda harakaharaka, kwa sababu hatuna shule maalum katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba kwamba ile mitihani wao wawekwe peke yao watu wa albino, halafu wale walemavu wakae pekee yao na wale wengine wawe peke yao na pia waongezwe mudu wa kufanya mitihani yao na wao waweze kufanya vizuri kama wanavyofanya wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lililokuwa napenda kuzungumzia ni kuhusu katika mukoa wetu wa Rukwa, katika Mkoa wetu wa Rukwa, tuna bahati ya shule kama tatu zina walemavu, wa mtindio wa ubongo, maalbino, viziwi na vipofu. Shule ya Malangali, Shule ya Katandara B, na Mwenge B, lakini walimu tunakuwa nao ni wachache ambao ni walimu wa taaluma, tunaomba walimu wa taaluma wapatikane katika shule hizo za Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hawa watoto wanahitaji kupewa chakula mashuleni kwao, lakini bahati mbaya, Serikali yangu imetoa bilioni 22, chakula cha shule hizi, ambazo kwamba ni watoto kwa mwaka mzima. Wao hali halisi kwa maana ya Katandara, kwa maana ya Shule ya Mwenge B, na kwa maana ya Malangali, ni takribani bilioni 72, ndiyo hali halisia ya kuweza kupatikana kwa chakula kwa wale watoto. Lakini wanapata bilioni 22 ambazo kwamba hazikidhi mahitaji, tunaomba waongezewe ili watoto wale waweze kupata chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na shule za stadi, shule za stadi, ufundi stadi wa mashule, tunazo shule kadhaa katika Mkoa wetu wa Rukwa Katandara, Mwaze, Matai na kadhalika. Lakini shule hizi wanafunzi wale hawana vifaa vya vitendea kazi, yaani vya kufundishiwa na vya kufundishika, hawana vitendea kazi. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba wapewe vitendea kazi, wapewe vitu vya kwenda kufundishiwa pale, wale ambao kwamba hawawezi kwenda sekondari kuendelea na masomo… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. (Makofi)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja, asilimia mia kwa mia, naomba tuangaliwe Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote ninaunga mkono hoja kwa asilimia zote. Napenda kuwapongeza Waziri na Katibu Mkuu wake kwa kusimamia, kuiongoza na ufuatiliaji wao wa karibu zaidi wa majukumu ya Wizara yao, pamoja na changamoto zote na ukosefu wa kupatiwa bajeti katika ukamilifu wake kama ilivyopitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumza kwa uchungu kuhusu Mkoa wetu, hapo awali tulikuwa na makambi ya JKT Milundikwa na Luwa, Rukwa ambayo yalitusaidia kuwaweka vijana wetu ndani ya maadili ya uzalendo na ulinzi uliotukuka wa ushirikishwaji na wananchi wetu, sasa kama itakuwa Serikali (Hazina) haitoi fedha za kukidhi mahitaji kwa angalau asilimia 75 kwa umuhimu wa Wizara hii, kwani hawana masaa maalum ya utumishi wao, hivyo kuna umuhimu wa kupewa fedha za maendeleo kwa asilimia hiyo ili makambi haya yakarabatiwe na kuanza kutumika mapema, kwani vijana wanaongezeka mitaani/Vijijini baada ya kumaliza masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 zimetolewa fedha za maendeleo shilingi 35,900,000,0000 ikiwa ni asilimia 14.5 ya bajeti iliyoidhinishwa mwaka 2017/2018. Bajeti imepungua kwa shilingi 29,000,000,000 kwa bajeti ya mwaka 2016/2018 iliyokuwa shilingi 248,000,000,000 na sasa kuwa 219,000,000,000 kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba fedha za maendeleo ni vema zikatolewa kwa wakati na katika ukamilifu wake, kutokana na umuhimu wa:-

(i) Kukamilisha ukarabati wa makambi ndani ya mwaka 2017/2018, kuchelewa zaidi kutatuathiri.

(ii) Tuondokane na migogoro ya wananchi waliochukuliwa maeneo yao kwa matumizi ya Jeshi, walipwe fidia zao waweze kujiendeleza. Hizo bilioni 27 ni muhimu kwa sasa kabla ya Juni, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya kukamilisha makambi ni kuwajenga vijana wetu kiuzalendo, kiulinzi na naishauri Serikali inapohitaji kuajiri Polisi, Wanajeshi, Maafisa Usalama wa Taifa, Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Magereza usaili ufanyike kwa vijana waliopitia JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana wanaopitia JKT baadhi wanabaki mitaani/vijijini ni bora vijana hawa wakaunganishwa kwenye huduma za ulinzi za SUMA Guard badala ya kurudi kujiunga na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada zake za vitendo kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya viwanda. Napongeza kazi nzuri inayofanywa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ya kufufua na kujenga viwanda, huku akihamasisha wawekezaji kuingia nchini na kufanyika kwa biashara ya kiushindani kwa maendeleo ya wananchi wetu. Natoa pongezi za dhati kwa Wizara hii kwa jinsi wanavyojitoa kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni wakulima bora na wazalishaji kwa ziada kubwa na kuchangia chakula kwa Taifa letu. Mkoa wa Rukwa tuna viwanda vidogo vinavyoendeshwa na sekta binafsi na tangu 2015 hadi sasa tuna viwanda 137 vyenye ajira ya 411 (mpya).

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamekuwa wanapata mfumuko wa bei ya unga pamoja na kuwa na mahindi ya kutosha. Hivi sasa bei ya unga Mkoa wa Rukwa sokoni kilo moja ni Sh.1500, kilo tano ni Sh.8,000/= na kilo 25 ni Sh.37,000/=. Naomba Serikali kuwawekea mazingira bora hawa wenye viwanda hivi vidogo kuzalisha kwa wingi na kupelekea kuteremsha bei ya unga. Pia mahindi yaliyomo ndani ya maghala ya Taifa ya miaka iliyopita yatolewe na kuuziwa wenye viwanda vya unga (sembe) kuliko kuharibika. Tunaomba wawekezaji waelekezwe Rukwa tupate ajira kwa vijana wetu na kuteremsha mfumuko wa bei ndani ya soko kwa maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu wengi wanakimbilia kufanya biashara mbalimbali ila hawana uelewa wa uendelevu wa biashara zao. Tatizo ni upungufu wa rasilimali watu katika maeneo yetu, Maafisa Biashara kuwa wahusika na leseni za biashara badala ya kuwainua wafanyabiashara kuwa na biashara zenye tija. Naomba Serikali kutoa ajira kwani tunao vijana waliohitimu kwenye vyuo vyetu vya CBE ili tupate wataalam wa kukidhi mahitaji, tupate wafanyabiashara watakaoendana na ushindani wa kiulimwengu na wa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri kwamba kwa kuwa tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, ni vema maeneo kama Rukwa tuhakikishe tunawaimarishia Chuo cha VETA na kuboresha Kituo cha SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waziri wa Viwanda kutuangalia sisi wa mikoa ya pembezoni kwa bidhaa kadhaa kuwa na bei za juu mfano sukari kilo moja ni Sh.2,200/=, sementi mfuko ni Sh.14,000/=. Kutokana na maeneo ya ujenzi wa viwanda yapo, tunaomba kuelekezewa wawekezaji wa kujenga viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza jitihada ya Serikali kwa wafadhili kwa utekelezaji wa kusambaza maji mijini na sasa tuongeze nguvu katika kusambaza maji vijijini, kwani kuna wananchi kwa asilimia kubwa zaidi ya asilimia 70 wanahitaji maji, ingawa hadi sasa tumefanikiwa kwa asilimia19.8 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo ambazo hazikidhi mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kweli tumedhamiria kwa dhati kuwatua ndoo kichwani akinamama, Serikali isingepunguza bajeti ya maji kutoka sh.939,631,302,771/= hadi sh.648,064,207,705/=, kwa mwaka 2017/2018 bali kuongezea au tukabakia na bajeti ya 2016/2017 na kuendeleza mikakati ya kutatua upatikanaji wa fedha za kuwezesha tatizo la maji kutoweka kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kala, Kipili, Kirando, Katete na Wampembe, Kabuve, Samazi ni maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, lakini hawana maji safi na salama. Kata ya Muze, Mtowisa, Mfinga, Zimba, Milepa, Ilemba, Kalumbaleza maeneo ya bonde la Rukwa wakiwa na Ziwa Rukwa hawana maji safi na salama. Vile vile Kata ya Mambwe, Nkoswe, Mambwe Keunga, Ulumii, Mnokola, Mwazye, Katazi, Mkowe, Kisiimba, Mpombwe maeneo mengi haya hakuna maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bajeti ya 2017/2018, kwa mchanganuo wa fedha za maendeleo kwa Mkoa wa Rukwa wa sh.4,307,846,000/= hazitatosheleza mahitaji, kwani kutoka kwake zote ni ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nashauri kwa ujumla kwamba tozo ya sh.50/= ni vema ikaongezeka hadi kufikia shilingi 100/= ili makusanyo yake yaelekezwe kwenye mahitaji ya maji, kama tulivyoamua kwenye umeme na miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema tukawa pia na Wakala wa Maji Vijijini ambaye atasimamia na kufuatilia utekelezaji wa usambazaji wa maji hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mvua, kuwepo na utaratibu wa kuvuna maji na kuandaa mabwawa ya kuhifadhia maji. Maji yanayoporomoka kutoka milimani hadi bonde la Rukwa na kuingia Ziwa Rukwa na kujaza udongo na kupunguza kina cha Ziwa hilo, ni vema utaratibu ukawepo wa kuyakinga (kuyavuna) maji hayo yakasaidia wananchi kupata maji safi na salama na pia wananchi watakuwa na kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ya Fedha ihakikishe Wizara ya Maji na Umwagiliaji inapatiwa fedha kwa asilimia 75 kama siyo wote, kwa utekelezaji wa utatuzi wa maji kwa wananchi wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote. Kwa umakini wao ndani ya Wizara hii, kwa matokeo mazuri hadi sasa kwa wananchi na kuwapa matumaini ndani ya changamoto zao za ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto nyingi za ardhi kwa wananchi wetu na kupelekea miji yetu kuwa na majengo ndani ya ujenzi holela na maeneo yasiyopimwa yanaleta magomvi kwa wananchi wetu, mandhari ya mji itakuwa siyo nzuri kiusalama na malalamiko ya wananchi hayapati ufumbuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Waziri kwa umahiri wake aone uwezakano wa kuteua Kamati za Kugawa Ardhi ngazi ya Wilaya haraka iwezekanavyo, kwani Mkoa wa Rukwa unachipukia kukua na wananchi kuwa na kasi ya maendeleo yao na Wilaya moja (Nkasi) tu ndio yenye Kamati ya Kugawa Ardhi. Wilaya ya Kalambo na Sumbawanga tushughulikiwe, hali mbaya hivi sasa, miji yetu itashindikana kupangiwa hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa upo pembezoni, lakini kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri zilivyotekeleza katika kutoa Hati miliki, Vyeti vya Ardhi ya Kijji, Hati Miliki za kimila. Ukurasa Na. 109 umedhihirisha kwenye jedwali Na.4 kwa Mkoa wa Rukwa haujafanya vizuri ni kutokana na rasilimali watu na rasilimali fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mkoa wa Rukwa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi, tukifahamu wazi kuwa tupo mpakani mwa nchi mbili (Zambia na DRC) ni vema tukavihakikisha vijiji vyetu na wenye maeneo kuwa na hatimiliki. Ni vema ukawekwa kipaumbele kwa mikoa ya pembezoni inayopakana na nchi mbalimbali, kupimiwa ardhi yao na kuipanga, kuepukana na migogoro ya ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuona umuhimu wa kupatiwa kibali cha kuajiri Maafisa Ardhi wa kutosha kwenye Halmashauri na vitendea kazi kulingana na mahitaji ya nchi kwa hii bidhaa adimu ya ardhi, kwa kila sekta. Ni vema Wizara ikaweka malengo ya utekelezaji kwenye Halmashauri na kufuatiliwa na kutathminiwa ili kila mmoja aweze kuwajibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa uongozi wake wa kuwathamini wananchi kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kuona inapunguza gharama ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta, kama ilivyo mikoa kadhaa ya nchi ikiwemo Mkoa wa Rukwa, Katavvi na kadhalika. Tunaomba kuunganishwa na gridi ya Taifa kwa sasa takribani mikoa yote. Mfano Rukwa tunatumia mafuta na umeme wa kutoka Zambia. Hii harakati ya kuanzisha viwanda tunahitajika kuwa na umeme wa kutosha na kukidhi haja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mikoa ya Kusini kuna nafaka za kutosha, tunahitaji kuziongeza thamani, hivyo umeme ni muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia umeme REA III ufikishwe kwenye vijiji na vitongoji vyote nchini, kwa hatua ya sasa, ikamilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza jitihada ya Serikali katika kutatua matatizo, migogoro na changamoto zinazokabili ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi kwa asilimia 80 wanatumia nishati ya kuni na mkaa na kuyumbisha uhifadhi wa misitu yetu hutupatia matatizo kadhaa kama vile ukosefu wa mvua, kutoweka kwa vyanzo vya maji pamoja na mito kukauka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado umeme na gesi kuwa na gharama kubwa na kutokuwepo ama nishati hizo hazijasambaa nchi nzima na zikiwa ndiyo nishati mbadala kwa wananchi wetu. Hivyo, ni vyema Serikali ikaharakisha kuleta Muswada wa Sheria ya Mbegu za Miti kuwa na bei rafiki na wezeshi kwa wananchi ili kuwawezesha wananchi kupanda miti ya muda mfupi kwa wingi na kuwezesha kuitumia kwa nishati na kurejesha misitu yetu kwa miti ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Mbegu za Miti wapewe Bajeti ya kutosheleza kuweza kufanya utafiti wa mbegu za miti na kubainisha upevu wa miti katika muda mfupi kwa kuharakisha kuondoa usumbufu utakaojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti unaenda sambamba na kuwa na maabara bora zenye vifaa vya kisasa viendavyo na wakati uliopo na kuharakisha matokeo ya ubunifu wa wataalam wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bado upatikanaji wa nishati mbadala kwa wananchi, basi Serikali ni vema ikawa na udhibiti kwa watumishi wanaotoa usumbufu, kujenga kero na chuki kwa Serikali na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara/Serikali inajitahidi kushughulikia migogoro ya ardhi na hifadhi zetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kujipanga kwa kuboresha majiji katika muonekano wake ni sawa, ila nashauri Serikali kwa hii miji inayokua au inayoanza nayo ni vyema ukawepo mpango kabambe wa kuipima na kuipanga kwa ajili ya mwonekano endelevu kuelekea mji au jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa hivi miji inakuwa changanyikeni na kutokuwa na miundombinu, kwa mfano Sumbawanga, Kigoma, Tabora, Mpanda na kadhalika, hivyo matumizi bora ya ardhi iwe ni zoezi kwa vitendo kila eneo la hapa nchini na kufanyiwa tathmini kwa
kipindi kifupi ili kuleta ufanisi na matokeo ya kuonekana na kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wananchi na hifadhi, wafugaji na hifadhi, wakulima na wafugaji sasa ni wakati wa kutokana nayo. Serikali ichukue hatua ya uthubutu kabisa wa kushughulikia tatizo hili la migogoro liweze kutoka ndani ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara husika kwa namna moja au nyingine kukutana na wamekwishafanya hivyo ni vema wakatoa makubaliano yao ya utekelezaji mapema; kama ni kubadili sheria lifanyike; kama kuwekwa kanuni ziwekwe na kupitishwa; mpango wa matumizi bora ya ardhi kuwekwa kwenye sheria lifanyike na kama kufutwa kwa baadhi ya sheria zifutwe na kadhalika

Mheshimiwa Mwenyekiti, kucheleweshwa kwa taarifa ya kikao cha pamoja cha Wizara husika kwa Bunge ili kufanyia kazi na kurejesha kwa jamii kwa utekelezaji ni hatari. Ni vyema sasa tukakamilisha zoezi hili la kufuta au kupunguza migogoro na kujenga imani kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kurejea kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais wetu ya kuwatua ndoo ya maji kichwani wanawake, ambayo Wizara imejipanga kuifanyia kazi lakini itachukua muda mrefu kufikia vijijini ambako wananchi wengi wazalishaji wanakoishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kuelewa kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi cha kukubali ushauri wa Sh.100 kwa lita ya dizeli na petroli, kwa ajili ya Mfuko wa Maji Vijijini. Kwa sasa na kuelekeza nguvu zaidi ya utekelezaji wa ukamilifu wa miradi ya maji kwani hata vyanzo vya maji vipo vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ushauri huu wa Sh.100 utekelezwe ili kuharakisha kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais ya kuwatua ndoo wanawake. Ukimtatulia tatizo la maji mwanamke utakuwa umeitatulia jamii nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Maji zinasisitiza umuhimu wa uwakilishi wa mwanamke ndani ya Kamati hiyo. Tunashauri kuanzishwa na kamati za kutunza vyanzo vya maji vijijini zenye ushirikishi wa wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwepo na ufuatiliaji na uthamini wa vyanzo hivyo na kuviweka katika madaraja ya ushindani ambako kutahamasisha utunzaji wa vyanzo na kuwa endelevu. Tutaepukana na ukosefu wa maji na wananchi watapata maji safi na salama kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndilo tegemeo letu hapa nchini kwa ajili ya upatikanaji wa bidhaa ndani ya viwanda vyetu vya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuendelea kuchambua na kuona namna ya kuteremsha bei na kuboresha utaratibu rafiki zaidi kwa wakulima wetu katika upatikanaji wa pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kuona umuhimu wa kuongeza Maafisa Ugani wa kukidhi mahitaji na kuleta tija kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri tunavyojipanga kuboresha kilimo na kuzalisha kwa ziada na kuingiza kwenye biashara na kukosa soko kutokana na nchi zinazotuzunguka nao kuanza kuzalisha hayo mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wataalam wa uwekezaji kuona utaratibu wa kukinzana na hali ya wakulima kuhangaika na mazao yao na kuona kilimo ni tatizo kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kujikita kwenye pambano la kuufuta ugonjwa huu wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030. Tunashauri kwa sasa tumekwisha toa elimu ya kutosha, ni vyema tujikite kuwahudumia waathirika kwa ukamilifu zaidi. Serikali kuongeza bajeti kwa fedha zetu bila kusubiri fedha za wafadhili, hatathamini ifanyike kila mwaka kwa kila mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni vyema ikafanye maamuzi magumu kwa kutoa ajira ya kukidhi mahitaji kwenye upungufu wa watumishi vitendea kazi, rasilimali fedha, angalau kwa asilimia 75 ndani ya huduma ya afya, elimu – VETA, msingi na sekondari. Kwani hatua hii ngumu inawezekana ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili gonjwa limekuwa na NGO’s nyingi wakichukuliwa kuwa ni eneo la kupatia mapato, hivyo uwepo uchunguzi na kuweka vigezo vya kusababisha upunguzaji wa hizi NGOs kuelekea mwaka 2030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pawepo na utaratibu wa kuwadhibiti watu au familia zinazowanyanyapaa wenzao miongoni mwao, wanaobainika kuwa waathirika wa UKIMWI au madawa ya kulevya. Kutungwe Kanuni maalum ya kuwaweka hatiani na kupatiwa adhabu ya kutowajibika ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ambao wanasambaza gonjwa hili na kufikia kuwasababishia vifo, nao kuendelea kutamba. Wahusika hawa wanaumiza moyo kwa baadhi ya wananchi na kuchukua sheria mkononi. Ni bora Serikali ikaona namna ya kuwawajibisha watu hawa na walio ndani ya jamii yetu. Suala hili ni siri kubwa inahitajika katika kutolewa kwake taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa kunipa nguvu ya kuweza kuchangia kwa maandishi angalau kutimiza azma yangu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa kazi njema ifanyikayo ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa miaka hii miwili na nusu chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakishirikiana na mtendaji wao mkuu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, katika lengo la kuwainua wananchi wetu kiuchumi, kuondoa umaskini na kwa jitihada ya kuanzisha na kuimarisha miundombinu yote ya kufanikisha uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu suala la ajira. Katika ukurasa wa 20, aya ya 37 ya hotuba amesema Serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa tathmini ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi, kusajili, kusuluhisha na kuamua migogoro katika maeneo ya kazi. Sasa huu utaratibu uliopitishwa wa kuwaondoa watumishi wa darasa la saba ambao wamefanya kazi nzuri kuanzia Awamu ya Kwanza na jitihada zao ndio zimetufikisha hapa ndani ya Awamu ya Tano siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali tusizue mgogoro ambao tunalazimika wenyewe kuushughulikia kuupatia ufumbuzi. Kwanza miongoni mwao wanastaafu sasa na wataendelea kustaafu, ni bora kwa busara kuanzia sasa tuendelee na utaratibu huo unaohitajika kwa wakati huu. Hata wakati ule walikuwepo kwa uchache wao, lakini hawakuwa na wito wa kazi hizo na darasa la saba walizichukua. Narudia tena tuwaache wamalizie muda wao wa utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu barabara, ukurasa wa 44-45. Naipongeza Serikali yangu kwa jitihada ya kujenga miundombinu ya barabara hapa nchini kwa jitihada ya kuunganisha wilaya na mikoa hata na nchi jirani. Napenda kukumbushia kwa Serikali hii sikivu kwamba mikoa ya pembezoni ilisahaulika na msukumo wa maendeleo ya barabara ulichelewa kuwafikia ndio maana maendeleo yao bado yanasuasua katika nyanja zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Daraja la Momba kujengwa na kuunganisha Chunya (Kamsamba) na Rukwa (Kilyamatundu) lakini barabara zake kuelekea Chunya na kuelekea barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga ni za udongo, hivi Serikali inaonaje na barabara hizo kuwa za kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeweza kupita Mlima Kitonga na Mlima Nyang’oro ambayo awali ilitupatia wananchi shida sana ya kupita na kuchukua muda mrefu, lakini sasa naishukuru Serikali yangu imetatua tatizo na milima hiyo inapitika na usafiri wake kwa wananchi umewarahisishia na kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na wepesi kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuangalia na barabara za milima inayoteremka mabonde ya Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika kwa kuanza na hatua za awali kuelekea kiwango cha Kitonga na Nyang’oro ili wananchi wa maeneo hayo wafaidike na matunda ya Serikali yao na ikumbukwe tunapakana na nchi ya DRC – Congo na Zambia. Pia tunaomba jitihada kubwa kuongezeka kwa sasa kwani zinasuasua za Mkoa wa Rukwa kuunganishwa na Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora na nchi za Zambia na DRC – Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kutoa tamko au mwongozo wa TARURA kushirikiana na Mabaraza ya Halmashauri kwani kule wanawashirikisha wananchi wa maeneo husika kufanya kazi. Pasipo kufanya hivyo kazi yao itakuwa ngumu au itawagharimu sana wakikosa ushirikiano wa awali kabla ya utekelezaji wao kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu maji, ukurasa wa 52 – 53. Maji ni uhai wa viumbe wote duniani na ndiyo eneo nyeti linalohitajika kufanikisha mengine yote. Tunajitahidi kuanzisha miradi ya maji ambayo bado haijakidhi mahitaji kwa kutoa matokeo mazuri, imekuwa ni miradi ya kunufaisha hao wanaoifanya siyo walengwa (wananchi). Mradi haujatoa matokeo mhusika keshalipwa mabilioni ya pesa, siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, taasisi zetu za majeshi hawana maji na ndiyo tunawategemea kwa ulinzi na usalama, mchana na usiku ndani ya nchi na nje. Pia shule na vyuo kukosa maji ni janga la kipekee. Matatizo ya taasisi za majeshi na shule kukosa maji yamekithiri Lindi, Mtwara, Rukwa, Ruvuma kwa ujumla mikoa ya pembezoni mwa nchi yetu, tuangalieni kwa huruma, tusijutie kuwa pembezoni ni tatizo kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri wakandarasi ambao hawana uwezo wa kuchimba visima na kupatikana maji kwa lengo la eneo husika wasipewe kazi na apewe muda wa kipindi maalum cha maji kupatikana na ndipo akubalike kupewa mradi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni afya, ukurasa wa 54. Tunashukuru jitihada ya Serikali na kujituma kwa Waziri mwenye dhamana kuhakikisha huduma ya afya inasonga mbele. Hata hivyo, jitihada hii ya kuongeza idadi ya vituo vya afya nchini tunaomba iende sambamba na ujenzi wa Hospitali za Wilaya kwani Mkoa wa Rukwa hakuna hata wilaya yenye hospitali pamoja na kuanzishwa mwaka 1974.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kushirikiana na wataalam wake kuona umuhimu wa Wabunge wa Viti Maalum kupatiwa angalau nusu ya Mfuko wa Jimbo kwa wastani wa idadi ya majimbo yaliyomo ndani ya mkoa anaoishi. Kwani Mbunge wa Viti Maalum na Mbunge wa Jimbo hawatofautiani kwenye majukumu ingawa wa Viti Maalum anazunguka mkoa mzima na kuwajibika ndani ya majimbo yote ya Mkoa. Sio ndani ya chama changu, wananchi na Serikali hawatutenganishi wanatuhesabu Wabunge tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa kazi nzuri ifanyikayo na uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Pia Waziri na Naibu Waziri wa Afya na timu yao nzima nawapongeza kwa kujitoa na kujituma kwa dhati katika nafasi zao kiutendaji kazi, wameonesha uweledi na uzalendo kwa dhati ya huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tuna wananchi takribani milioni 55, Serikali inajitahidi sana kwa upatikanaji wa dawa kwa uponyaji wa maradhi kadhaa. Kufuatana na hotuba inadhihirisha mapungufu ya rasilimali watu yaani watumishi na maandalizi yao yanachukua muda mrefu. Tunaomba Serikali kujipanga kwa kuwasambaza wataalam waliopo ambao wamerundikana kwenye miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya. Vijijini tumekuwa na upungufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili Serikali kuangalia stahiki za wataalam wa afya ili waendelee kutoa huduma kwenye zahanati za Serikali, kwani tunawasomesha kwa pesa nyingi lakini wanakosa ajira na stahiki bora wanakwenda kwa watu binafsi au hata nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala zima la mapungufu makubwa ya rasilimali watu yaani watumishi wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana upigie jicho la pekee na kutatua mapugnufu ya maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kwani watu hawa ni wa muhimu ndani ya maeneo yetu. Wananchi wetu wanahitaji kupatiwa uwelewa na ufahamu wa maendeleo yao, hasa kina mama ndio chachu wa kila kitu ndani ya Kaya, Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa matumizi ya bima ya afya ni pamoja na kuinua uchumi na kuachana na umaskini. Katika Mkoa wa Rukwa, Maafisa Maendeleo ya Jamii tuna mahitaji ya 158 tulionao ni 50 tu; katika Halmashauri ya Sumbawanga mahitaji ni 39 waliopo 15 kwa pungufu ya 24; Nkasi mahitaji ni 34 waliopo 10 kwa pungufu 24; Manispaa mahitaji ni 33 waliopo 13 kwa pungufu ya 20 na Kalambo mahitaji ni 29 waliopo 13 kwa pungufu ya 16.

Mheshimiwa Naibu Spika, maafisa ustawi wa jamii ni wachache sana tena sana ukizingatia uhitaji kwao ndani ya jamii katika suala zima la kukinga. Unahitajika uelewa huu awali kwa wananchi wetu kuliko tiba ni gharama kubwa. Hali halisi kwa mkoa wetu kwa maafisa ustawi wa jamii ni mkoa mmoja, Kalambo mmoja, Sumbawanga wawili, Manispaa watatu, hospitali ya mkoa wanne. Ifahamike mkoa wa Rukwa una kata 97 na mitaa 172 tu na Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa. Tunahitaji kuiomba Serikali kuona umuhimu wa kutoa ajira kwa watumishi wa kada hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara kuona namna ya kuwasaidia na kuwatatulia Idara ya Maendeleo ya Jamii changamoto zifuatazo; usafiri (magari, pikipiki), vifaa vya uandishi (stationary), uhaba wa fedha za mikopo za Mfuko wa WDF toka mapato ya ndani (Wizara kulitolea maombi kwenye Serikali na ufuatiliaji wa karibu kwa maslahi ya watumishi hawa).

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali kuona umuhimu wa kutoa taulo kwa watoto wetu mashuleni kwani tunazo pamba za kutosha kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa pamba hapa nchini, tuna kila namna ya kuzalisha taulo hizi na wanafunzi wa kike waweze kujistiri katika kipindi cha miaka nane kabla ya kwenda chuo angalau tuwawezeshe Watanzania hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi kubwa ya dhati kwa kazi nzuri chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, bila kusahau kwa Waziri mwenye dhamana wa Wizara hii pamoja na Naibu Mawaziri kwa kushirikiana na wataalam, watumishi kwa ujumla wa timu hii imefanya kazi nzuri kwa nchi yetu na kwamba wametutendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na mawasiliano kwa mitandao kadhaa na yote yanatoa huduma ya kibenki, lakini mtandao wa Vodacom – Mpesa kumekuwa na wizi wa fedha, mteja akikosea namba akiwa ametuma fedha akitoa taarifa Vodacom jibu kuwa fedha hizo zimekwishatolewa na mhusika hana salio hivyo hesabu maumivu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ni wizi kwani hawezi kufuatiliwa huyo mhusika anapokuwa na fedha hiyo basi irejeshwe kwa mteja aliyetoa taarifa, kuliko kumjibu hivyo au kwenda kuripoti polisi. Ni vema Wizara kuingilia kati kwani wakati mwingine ni pesa ya ada kwa wanafunzi vyuoni, kwa majibu hayo, hivyo mwanafunzi hatasoma chuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano ni muhimu kwani ni kiunganishi madhubuti kwa wananchi wetu hasa waliopo mipakani kuwa na mitandao yenye mitambo mikubwa kwa kuwa huwa wanaingiliana na mitandao ya nchi jirani hasa Zambia na Bujumbura. Mfano; Kata ya Kala, Kata ya Wampembe, kata ya Mambwenkoswe (Rukwa), mitandao inayumba. Tunaomba Wizara kuangalia mawasiliano kwa mikoa ya pembezoni, Bonde la Tanganyika na Bonde la Rukwa kuwa na mawasiliano kamili kuanzia milimani tuteremkapo bondeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi sana katika kuiunganisha nchi yetu, lakini wananchi wetu asilimia kubwa na wazalishaji wakuu hawana barabara (vijijini) na sasa na TARURA asilimia 30, hatutakuwa tumetenda haki kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda, hivyo ni bora wakati huu tukachukua maamuzi magumu ya kuwapa asilimia kubwa TARURA. Tuwaunganishe wazalishaji hawa tusonge mbele kwenye azma ya maendeleo ya nchi hii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa msemaji wa kila mara katika Bunge hili kuhusu na barabara zinazoteremka kwenye mabonde ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa sasa zimefikia mwisho wa kuendelea kuwa za changarawe/ udongo au kuweka viraka vya sementi na matengenezo ya maeneo korofi haya mara kwa mara kwa sasa basi. Tunaomba Serikali kuzingatia na kuzitengeneza kwa kiwango cha lami kama Milima ya Kitongo na Nyang’oro kuliko kuendelea kupanga bajeti kila mwaka kama 2018/2019 kwa kilometa 108.0 shilingi milioni 3,315.852 na kadhalika. Tuziangalie kwa huruma tupo pembezoni, tumechelewa kimaendeleo pamoja uzalishaji mkubwa wa chakula na biashara kwa ndani ya nchi na nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kusahau barabara ya Kibaoni (Katavi) hadi Kilyamatundu – Miangalua (Rukwa), ukifahamu Serikali inajenga daraja kubwa la Mamba (Rukwa/ Songwe) halafu barabara zake changarawe/udongo hali hii ngumu na haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali na Wizara kiutalaam wana haja ya kuinua Shirika la TTCL na kuweza kujiendesha, basi ni bora kuhakikisha kwa kuliwezesha kusambaa nchi nzima na vifurushi vyao kuwa rafiki kwa wananchi wetu, pamoja na simu zao kuwa na uwezo wa huduma zote za kimtandao kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi, na Serikali tusiendelee kuingizamitandao kutoka nje, naomba nguvu kubwa tuelekeze TTCL iweze kusimama na tujivunie shirika letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada ya Serikali chini ya Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wote ndani ya Wizara hii wanafanya majukumu yao kwa tija na ufanisi katika kurejesha heshima na sifa za Kitaifa kwa nchi yetu. Napenda kupata ufahamu kwa nini bajeti ya 2018/2019 imepungua kwa asilimia 15.4 kwa Sh.5,136,989,000/= kwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, bajeti ya mishahara ya mwaka 2018/2019imepungua kwa asilimia 11.7 kutoka Sh.17,276,616,000/= na kufikia Sh.15,253,265,000/= je, ni kutokana na punguzo la watumishi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kilichosababisha bajeti ya matumizi mengineyo kuongezeka kwa asilimia 50.8 ya Sh.4,780,331,000/= kutoka lengo la 2017/2018. Wakati bajeti ya miradi ya maendeleo ni Sh.8,700,000,000/=, pungufu ya Sh.696,410,000/= ya bajeti ya matumizi mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunahitajika kuendeleza na kuimarisha maendeleo ya utamaduni na sanaa, maendeleo ya sanaa na maendeleo ya michezo na kutuwezesha kuibua vipaji vya aina zote na kuitangaza nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja na kabla ya kuzungumza lolote napongeza jitihada ya Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na baadhi ya wataalamu kwa kazi nzuri waifanyayo kwa wananchi wa Tanzania na jinsi wanavyomuunga mkono Rais mpendwa kwa jitihada zake za kumtua ndoo mwanamke kichwani na kwa kuhakikisha maji yanapatikana ndani ya mita 400. Mola awape wepesi na nguvu ya kufikia azma ya Rais wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni kati ya mikoa ambayo inakumbwa na magonjwa ya mlipuko kila mara kutokana na kutokuwa na visima virefu vya maji safi na salama hasa vijijini. Wananchi hutumia maji ya visima vifupi, madimbwi, mito na Ziwa Rukwa ambayo ni maeneo yasiyo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia ukurasa wa 267 hadi 279 kuna orodha ya visima 225 lakini hakuna kisima hata kimoja kwa Mkoa wa Rukwa. Tunaomba hawa Mawakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) wafike na Mkoa wa Rukwa kwa zoezi hili la uchimbaji wa visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu wa maji nchi nzima na kuwa na miradi kadhaa ya maji ambayo bado haijakamilika na iliyokamilika hakuna maji na wakati pesa ya Serikali inakuwa imetolewa na huku haitoshelezi mahitaji, tunaomba miradi ambayo haijakamilika itambulike na kuandaliwa mpango mkakati maalum wa kuikamilisha. Kwa ile miradi iliyokamilika na haina maji na pesa ya Serikali imetolewa ni vema wahusika wachukuliwe hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kuona namna ya kuvuna maji ya mvua kwani mafuriko yamekithiri hapa nchini. Tutafute namna ya kuyavuna kuliko kupotea bure na kuyatumia kwa matumizi ya majumbani, mabwawa ya mifugo na hata umwagiliaji. Kwa matumizi ya maji safi na salama, kwa matumizi ya majumbani kwa wananchi wetu, ni vema Serikali kukubaliana na mapendekezo ya kuongeza shilingi 50 kwenye mafuta ya dizeli na petroli ili Mfuko wa Maji uwe na fedha za kutosha. Fedha za Mfuko wa Maji kwa Mkoa wa Rukwa shilingi 4,101,400,911 hazitoshelezi mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tufanye ukaguzi wa miradi kabla ya kuiendeleza. Aidha, uwepo ukaguzi wa kila hatua ya miradi kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali kuwa tete ya upatikanaji wa maji kutolingana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali na mahitaji halisi ya wananchi wetu, nashauri wataalam waliopo ni vema wakatathminiwa kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa dhamira ya Rais kuwatua akina mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara kwa jinsi wanavyojituma katika jitihada ya kuusimamia na kuutekeleza kwa vitendo uchumi wa viwanda nchini, pamoja na changamoto zote na utofauti wa uelewa wa nini ni kiwanda kwa wananchi, baadhi ya wenzetu wa upande wa pili, ni vema yakatolewa maelezo ya ufafanuzi kwa lugha nyepesi ya nini ni kiwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa wananchi wanashughulika wao wenyewe bila ya kusukumwa katika shughuli za kilimo mahindi, mpunga, maharage, ulezi, alizeti, miwa, ufuta na kadhalika. Utaratibu wa kuuza mahindi nje ya nchi, natoa ushauri Serikali kutoa kiasi maalumu na kiasi kikubwa yaongezwe thamani (unga) wa kuuzwa huko. Kuongeza pato kwa mkulima na Taifa letu, mfano asilimia 25 kwa asilimia 75 au asilimia 45 kwa asilimia 55 kwa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo mema yaliyofuatia zoezi la wafanyabiashara ndogo ndogo kutengewa maeneo katika ukurasa 43 - 44 ndani ya hotuba ya Waziri kwa mikoa minne kati ya 26 hii kasi ndogo, kwani wafanyabiashara ndogo ndogo ni eneo pana kwa vijana wetu la kujiajiri, hivyo tunahitaji kuongeza kasi, kwani tutawakatisha tamaa vijana na kusababisha wakajiunga na mambo yasiyostahiki kwao na Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali/Wizara kufuatilia zoezi hili ndani ya muda wa miezi sita ya mwaka 2018/2019 kwani ni kero iliyokithiri ndani ya nchi kwa hawa wafanyabiashara ndogo ndogo na ni sehemu kubwa ya wapiga kura wetu ili tuachane na hii changamoto. Pia Serikali
kuangalia namna sahihi na rafiki kwa wafanyabiashara kuhusu na malipo ya VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa 29 - 30 wa hotuba inazungumzia suala la usindikaji wa mafuta ya alizeti ingawa tuna pamba, karanga, ufuta na kadhalika, kwa mchanganuo wa hizi mbegu zitolewazo mafuta, ndiyo asilimia 30 ndani ya hayo mahitaji yetu ya tani 700,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuona umuhimu wa dhati na kulegeza masharti kwa viwanda vya mafuta ya pamba na alizeti ambayo tunayatumia sana nchini kuongeza idadi ya viwanda kutoka 21 na kuongeza idadi ya viwanda vidogo kutoka 750 kwa kuweka lengo hadi tufikapo mwaka 2020 tufikie uzalishaji wa asilimia 45 ya mafuta ya kula, kwani mazao hayo yanazalishwa kwa wingi hapa nchini ni kuwaongezea uwezo wa kilimo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuweka mkazo kwa wafanyabiashara wote watakaohusika kwa namna moja au nyingine yaani chakula, mafuta na sukari kwa ndugu zetu wa Kiislamu ili waweze kutimiza ibada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni pana inayohusika na idadi kubwa ya wananchi wanaoshiriki kwa upatikanaji wa chakula na kibiashara katika uchumi wa wananchi hao. Kutokana na uzito wa Wizara hii, sina budi kutoa shukrani za dhati na pongezi kwao Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa kada mbalimbali kwa kazi nzito waifanyayo kuhudumia wananchi, pamoja na uchache wa bajeti yao na bado Wizara ya Fedha inawasilisha kwa fedha za miradi ya maendeleo kwa asilimia 18 kwa fedha zilizoidhinishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatari kwa watekelezaji na wasimamizi wa kilimo chetu nchini. Hivyo, Fungu 43 kwa mwaka 2017/2018 ya tengeo la shilingi 150,253,000,000 na kupelekewa shilingi 27,231,305,232.69 ambayo ni 18%. Tunaomba kwa mwaka 2018/2019 fungu hili liweze kutekelezewa kwa angalau 65% kama sio 75% kutokana na shilingi 162,224,814,000 ili tuweze kuboresha zaidi maendeleo ya kilimo chetu nchini na kuweza kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kusubiri mvua za msimu ambazo zinaendelea kupungua na kutokukidhi haja ya kuivisha baadhi ya mazao kwenye baadhi ya maeneo hapa nchini na kurudiarudia kila mwaka na wananchi wa maeneo hayo kupata shida ya upatikanaji wa chakula, kwani kinakuwa kwa gharama kubwa na wengine kushindwa kukipata na kuwasababishia kubadili utaratibu wa kutumia chakula kwa mlo mmoja kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inafahamu maeneo hayo, lakini urasimu wa utekelezaji kwa wataalam wetu wa kuchukua muda mrefu wa utafiti wa kufanyia kazi kwa wakati bado maeneo hayo hayana mavuno mazuri. Wataalam waweke mikakati ya makusudi ya kukabiliana na uharibifu wa hali ya hewa kwa kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuhakikisha maji ya mvua yanavunwa, tusikubali maji haya yakapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Bonde la Rukwa linapokea maji mengi kutoka Ufipa ya Juu na kwenda moja kwa moja Ziwa Rukwa na kujaza udongo na kusababisha ziwa kujaa udongo na kina chake kupungua na maji kupotea. Maji hayo yakingwe kwenye mabwawa kadhaa yatasaidia kilimo cha umwagiliaji, maji ya kutumiwa na wananchi, mifugo na viwanda vidogovidogo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la ushirika kwa sasa wananchi wengi na ambao wanaumia na utekelezaji wa viongozi waliotangulia kutokutenda haki, hasa kipindi cha hapa kati, kunawakatisha tamaa kwa kuendelea na suala la kuendelea na ushirika. Ushauri ni bora sasa ukafanyika kwa kina uchambuzi wa viongozi wetu ndani ya ushirika kwa kila eneo hapa nchini, ikibidi tupate viongozi tofauti kabisa. Ushirika tulionao tuone utaratibu wa kuunda muundo tofauti na tulionao ambao hauna usimamizi na ukaguzi wa karibu na chombo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa jitihada zote zinazoendelea kwa kuendeleza kilimo, lakini bado uchelewesho wa mbolea na pembejeo kwenye maeneo kwa kuzingatia na msimu wao kuanza. Nashauri pembejeo na mbolea uwepo utaratibu wa kuwa ni bidhaa zinazokuwepo ndani ya maduka yetu mwaka mzima. Kwa kuwa ni mwanzo, tunaomba Wizara kutoa maombi Serikalini ya kusogeza huduma hiyo angalau kwenye kuunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza kwa kazi nzito waifanyao Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na baadhi ya wataalam wafanyao kazi kwa weledi na kwa maslahi kwa nchi yetu. Wizara hii inatoa pato au inachangia kwa asilimia ya kutosha kwenye pato la Taifa. Kama miundombinu yake ikiboreshewa ipasavyo na kwa kukubali maoni, ushauri wa Wabunge na Kamati husika ni dhahiri pato la Taifa litaongezeka hadi asilimia 10 -15.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii imekuwa na upungufu wa watumishi wenye mafundisho sahihi kwa kada mbalimbali za kutoa huduma kwa watalii na wabunifu wa shughuli kadhaa za kuwavutia watalii kwenye maeneo yetu kuzingatia mazingira yetu. Vyuo vya Utalii kuongezeka kwa idadi ya usaili na miundombinu ya kuikabili hali na mahitaji ya wataalam. Mitaala iendane na mahitaji ya kuwa na utalii endelevu uendao na wakati wa maendeleo ya utalii ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba eneo kubwa la utalii linahitajika ulinzi na usalama kwa wageni na nchi kwa ujumla wake, ni vyema usaili wa watumishi wa Wizara hii watokane na vijana wa JKT pia.

Mheshimiwa Spika, bado Serikali haijasambaza nishati mbadala kwa matumizi ya wananchi wetu kwa huduma mbadala ya nishati ya kuni na mkaa. Ni vema Wizara ikajikita katika kuhakikisha tunapata umeme wa kutosha na gesi na kupelekea gharama yake kuwa rafiki kwetu na wananchi kuelimika na kuikubali hali ya matumizi hayo kutapunguza uharibifu wa misitu yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati huu tunalazimika pia kuangalia tozo zitolewazo kwa wajasiriamali wa uuzaji wa mkaa mpaka afikishapo mjini kutoka vijijini ni kubwa ukichanganya na changamoto azipatazo katika kuupata mkaa na kuusafirisha.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya watumshi wakusanyao maduhuli ya misitu vijijini si waaminifu, ni bora uwepo utaratibu wa kutumia mashine za kieletroniki, kudhibiti makusanyo hayo kwa kuwapa malengo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumekubaliana kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini, tunaomba Wizara kuwa na utaratibu wa awali kabisa kuimarisha miundombinu (barabara) inayoelekea kwenye maeneo ya vivutio vilivyobainishwa kwenye maeneo yetu, naomba ushauri kuzingatiwa. Kwa mfano barabara inayoelekea Kalambo Falls – Rukwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, napongeza kwa dhati jitihada za Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wakuu wa Wizara hii kwa kazi ngumu sana waifanyayo kwani mahitaji ni makubwa kuliko pato tulilinalo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu fedha za maendeleo, naomba kufahamishwa ni namna gani Serikali itafanya au inaona huu upungufu na kuweka mikakati gani ya makusudi ili tuachane na kutegemea mapato ya nje kwa maendeleo yetu. Kwani fedha za maendeleo kwa mwaka 2017/2018 tulikuwa na shilingi bilioni 1,382.98 za ndani na nje shilingi 46,108,149,741 (46.11) na sasa mwaka 2018/2019 ni shilingi bilioni 1,266.03 za ndani na shilingi bilioni 29.18 ni fedha za nje. Ndiyo kusema fedha za nje zikikoma maendeleo yetu nchini yatayumba. Ni vyema Wizara ikaweka mikakati yenye tija zaidi kuongeza mapato ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni rasilimali kwa mapato yetu. Naomba tufanye utafiti wa rasilimali za nchi zilizopo kila pande ya nchi yetu kuzibainisha na kuzichimba na kuziongezea thamani hapa nchini kabla ya kuziuza nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu usambazaji wa mafungu ya fedha kuzingatia bajeti iliyopitishwa, hata kwenye mafungu ya Wizara ya Fedha hazikutolewa na baadhi hazikufika asilimia 85. Hii ni dhahiri Wizara nyingine ni dhahama kwa kutekelezewa. Tunaomba Wizara ione namna ya kukusanya mapato ya ndani na kutoa kikamilifu kwenye mafungu ya maendeleo kwa kila Wizara na kwa wakati kama jinsi yalivyopitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa msisitizo wa kuendelea kufanya uhakiki ulio sahihi kwa wakandarasi na wazabuni wetu na kufanyiwa malipo kwa ukamilifu ili tuweze kukamilisha miradi ya maendeleo yetu na ufanikishaji wa huduma ndani ya taasisi zetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana tena sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na Mola ampe maisha mema na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo ni Waziri wa kuigwa kutokana na jinsi anavyofanya kazi kwa kushirikisha zaidi na walengwa hadi ngazi ya awali, hafanyi kazi za mezani. Mola ampe nguvu na afya atimize azma yake. Pamoja na timu yake ya Wizara yake wanashirikiana vyema na waendelee hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mkuchika kwa kazi nzuri sana, ingawa bado ana jukumu kubwa kwa mazingira ya upungufu wa watumishi katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mengi kufanyika vizuri, bado tunahitaji kazi ifanyike na hasa kwa mikoa ya pembezoni na kufuatiwa na miji kupanuka na wananchi kuibukia kujenga majengo yao kwa maendeleo yao na kuwaonesha kasi yao kubwa na kuacha Serikali nyuma. Mfano Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TAMISEMI ishirikiane na Wizara husika kupatikana kwa vyombo vya upimaji ardhi, ili miji ipangwe na tusiwe na maeneo yasiyo na mpangilio. Zoezi la matumizi bora ya ardhi kwenye mikoa yetu lifanyiwe kazi na kutathmininwa kila mwaka ili tuondokane na migogoro ya wakulima na wafugaji, pia na hifadhi zetu na miji yetu isivurugike kimpangilio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TAMISEMI kuona umuhimu wa kuongeza asilimia ya fungu la fedha za maendeleo ya ujenzi wa barabara za vijijini kwa TARURA. Barabara hizo ni nyingi na zinaongezeka siku hadi siku, kwa jinsi wananchi wanavyoongezeka kwenye maeneo na kuibuka vitongoji na vijiji kupanuka. Hivyo tunahitaji TARURA kuwa na nguvu kubwa kwa utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia barabara za vijijini ni za muhimu sana kwa wakulima, kusafirisha mazao yao kuwapeleka sokoni na viwandani. Akinamama ndiyo wazalishaji hasa wanahitaji barabara kuwawezesha kufika sokoni, hospitali na kupunguza vifo vyao na watoto. Bora TARURA kupata asilimia 65 angalau kwa kuanzia kwani TANROADS hupata wao na wafadhili na marafiki wa nchi na mikopo ya nchi kuendeleza barabara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tena sana pamoja na kutokuwa na mapato ya kutosha na kutoa nguvu ya mwelekeo wa bajeti kuwa yenye matumaini makubwa kwa maendeleo. Bado tunaomba Wizara kuona uhitaji wa watumishi kwenye maeneo ya awali waliko wananchi wetu ambao wazalishaji wa mazao ya chakula na malighafi ya viwanda vyetu. Wanahitaji zahanati, vituo vya afya, majengo yapo na yanaendelea kujengwa lakini watumishi hawapo, wanahitajika wataalam husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure; inatuhitaji kujenga madarasa, tunaomba Serikali kuwaunga mkono wananchi kuyakamilisha madarasa haya na miundombinu yote ya shule. Maafisa Maendeleo wa Mitaa/Vijiji na Kata na Maafisa Ugani kuhakikisha wataalam hawa kuwepo katika maeneo hayo kwa nchi nzima kwa maendeleo ya wananchi wetu. Pia, wapewe usafiri kurahisisha kazi yao ya kuwatembelea walengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la watoto kwenda shule kutokana na elimu bure, Wizara tunahitajika kuajiri Walimu wa shule za msingi na kuwapeleka Walimu kuwa na watoto (wafanyakazi) 45 kuliko ilivyo sasa zaidi ya 100 siyo vyema. Utaratibu wa ujenzi wa nyumba za Walimu ufanyike kwa kila mkoa kwa kuigwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado halmashauri zetu zinafanya vikao vya Mabaraza wakati wa ratiba ya Bunge na Kamati za Kudumu za Bunge. Hali hii inasababisha Wabunge kutohudhuria vikao hivyo, waskati mwingine inamgharimu pakubwa Mbunge kuhudhuria. Pia tunaomba posho ya Madiwani kuangaliwa upya na wasaidizi wao Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa, kwani kazi yao ni kubwa kwa usimamizi wa ufuatiliaji wa miradi na maendeleo kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
MakadirioMakadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhakika Wizara hii inafanya kazi kama mchwa kutokana na hali iliyopo katika suala zima la matumizi bora ya ardhi kwa nchi yetu na kujikuta na migogoro kila upande na inayoendelea kupatiwa ufumbuzi. Utekelezaji huu unatokana na umahiri, weledi wa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na baadhi ya watumishi wazalendo wapendao maendeleo ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchini mwetu tuna mtihani mkubwa wa matumizi bora ya ardhi na kupanga nchi yetu na kuiepusha na migogoro ya wananchi wetu. Hadi mwaka 2016/2017 tuliweza kuwa na wahitimu 559 tumejitahidi na kufikia 787 mwaka 2017/2018 kwa nyongeza ya watahiniwa 228.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ichukue maamuzi ya makusudi ya kuomba majengo kadhaa UDOM na kuendesha mafunzo ya wataalam wa ardhi huku tukiendelea na kuboresha miundombinu ya vyuo vyetu. Upungufu ni mkubwa kwa mahitaji yake, ukiangalia nchi ni kubwa na wananchi wanaongezeka kwa kasi kubwa kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ya upimaji wa ardhi nchini imekuwa ya kusuasua kutokana na wataalam, pia vifaa husika. Pamoja na jitihada za Serikali na Wizara kuanzisha utaratibu wa kufungua ofisi husika kwa ngazi ya kanda, bado vifaa havijafika na wataalam wa kutumia vifaa hivyo bado hawajaandaliwa. Katika maonesho tumekutana na kampuni husika na upimaji ardhi wenye vifaa vya kisasa. Gharama ya ununuzi wa vifaa hivyo ni bei rafiki. Kwa chombo cha shilingi milioni 50 wao wanauza shilingi milioni 16. Je, Serikali haioni umuhimu wa kudhamini Halmashauri kupata vifaa hivyo kutoka kampuni hiyo waweze kuwa na vifaa vyao na kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya fedha ni vema ikaona umuhimu wa kuwasilisha fedha zote zinazopitishwa kwenye Bajeti ya Wizara ya Ardhi ili nao wafahamu kuwa ni wadau wa kupiga vita migogoro ya ardhi na uimarishaji wa matumizi bora ya ardhi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ni vema ikaona namna ya kutoa maelekezo ya ulipaji wa gharama ya viwanja kwa wananchi wetu wa kawaida. Pamoja na kuchukua kwao viwanja vidogo, bado uwezo wa gharama anayotakiwa kulipa ni mtihani kwao kwa kipindi cha mwezi,

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wana kiu ya maendeleo, naomba tuwape muda watimize ndoto zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kukubaliana na ushauri wa kuzitenganisha Wizara ya Nishati na Madini kwa maslahi ya Taifa. Hii yote ni jitihada ya kupambana kwa kufahamu rasilimali za nchi zenye maslahi ya wananchi na kunufaika nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza kwa uteuzi wa Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Katibu Mkuu. Ni watu wenye mwitikio wa kujituma, kujitoa kwa uzalendo uliotukuka kwa maendeleo ya nchi na utendaji wao ambao unaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO nimeisikia muda mrefu nchini ikiwa inahusika na madini, lakini matunda yake hayana afya kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni vyema ikaangaliwa upya katika mfumo wake wa utendaji na usimamizi kwa maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina madini kadhaa na wananchi wengi wanajihusisha na uchimbaji mdogo mdogo wa kupata madini yanayofahamika na yasiyofahamika na hapa ndipo wananchi ambao ni wachimbaji wadogo wanadhulumiwa na watalaamu wachache tulionao. Mkoa wa Rukwa kuna wachimbaji wadogo kwenye milima ndani ya Kijiji cha Kastuka, hawayafahamu hayo madini lakini wachimbapo wanayaleta Dar es Salaam na bado wanaendelea na kazi hiyo, ndiyo kusema wataalaam wameyafahamu. Tunaomba Wizara iweke utaratibu wa kitengo maalum kuzungukia nchi nzima na kubaini madini yanayopatikana kila Mkoa na kuwekwa takwimu sahihi ya madini tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ijipange vyema na suala zima la uchenjuaji wa madini hayo kwa kuyaongeza thamani na kutambua kwa kuchanganua aina za madini moja moja. Kwa umakini huu, ukizingatiwa, tutafahamu thamani ya madini yetu na kuwa na mchango mkubwa kwa pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na njia nyingi za panya za kutorosha madini yetu katika kutafuta soko zuri kwa wachimaji wadogo. Tunaomba Serikali kurejesha utaratibu wa Soko la Dhahabu la Benki Kuu kwani wanatapeliwa na walanguzi na bei wanayoipata ni ndogo, huku kazi waifanyayo hadi kuipata mali hiyo ni ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa 21 wa hotuba ya Wizara, pamezungumzia suala la usimamizi wa matumizi ya baruti na udhibiti wa matumizi ya baruti kwenye shughuli hizo mbalimbali kwa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama na kwa madhumuni yaliyokusudiwa. Sikuona ni namna gani wananchi wanaozunguka maeneo yanayotumia baruti na majengo yao kuathirika, wanalipwaje fidia na wahusika au wanahudumiwa vipi na wahusika?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa tuna hao wahusika wa matumizi ya baruti katika kupasua mawe na kutengeneza kokoto, changarawe na kadhalika. Wananchi wanaozunguka eneo hilo, nyumba zao zimepata nyufa kadhaa na kupunguza uimara. Ni vyema Serikali ikaona namna ya kuwaangalia wahanga hawa. Pia uwepo msukumo wa hao wahusika kwa mchango wao kwa maendeleo ya huduma za jamii kuwa ni lazima, siyo hiari au mahusiano ya viongozi kwa matakwa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa madini yanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuchangia pato la Taifa, hivyo tunaomba Wizara ya Fedha kuweka jitihada ya makusanyo na kuwapelekea Wizara ya Madini bajeti ya Maendeleo ya shilingi 19,620,964,000 ambazo asilimia kubwa ni fedha za ndani. Ni matumaini yetu kwamba wachimbaji wadogo na wananchi wetu watanufaika na kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujengewa ofisi ya madini kwenye mikoa yenye madini kuliko kuwa na Ofisi Dar es Salaam, ndipo Wizara itakuwa na shinikizo la kuandaa wataalam na kuwasambaza mikoani au kwenye kanda kwa kuanzia. Tutaimarisha wachimbaji wetu, tutawadhibiti walanguzi na matapeli na mapato yatafahamika na kuyasimamia kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi. Waziriwa TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo,Naibu Mawaziri wake, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wanafanya kazi iliyotukuka na kwa ufanisi na maendeleo yaoonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri George Mkuchika na timu yake wamejitahidi kuweka hali sawa ya utawala bora na kutoa vibali vya ajira na kujaza nafasi za utumishi za kada mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotoka ndani ya mapato ya Halmashauri zetu, kazi hii inaendelea ndani ya Halmashauri zetu kwa kiwango tofauti. Tunaomba Waziri, Mheshimiwa Jafo kwa umahiri wake kuona umuhimu wa kutoa usafiri wa pikipiki angalau kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Vijiji na Mitaa na ngazi ya Wilaya (Halmashauri) na Mkoa wapatiwe magari kuliko kutegemeahurumaya Wakurugenzi wao. Pia tunaomba ajira ya Maafisa Maendeleo ya Jamii, kwani wana kazi kubwa ya kuelimisha wananchi hasa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuunda vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote wa Wizara hii kwa kufanya kazi yao ya udhibiti wa uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa dhati na weledi pamoja na kutopelekewa fedha kama zilivyopitishwa na kuidhinishwa na Bunge kutoka Hazina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu eneo kubwa limeathiriwa na uharibifu wa mazingira na tabianchi na kupelekea vipindi vyetu vya masika (mvua) kubadilika na mvua kuwa ndogo na mazao ya mahindi, mpunga na kadhalika kukosa maji (mvua) na kufanya uzalishaji kuwa mdogo. Mfano mwaka huu mazao yamekubwa na ukame, hivyo nashauri Serikali ijipange namna ya kukabiliana na ukosefu wa chakula nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kila Halmashauri kubaini miinuko (milima) iliyokuwa kipara yaani hakuna miti kuweka mkakati wa kupanda miti na kuweka kanuni za kulinda miinuko hiyo. Pia, kwa vile athari ni kubwa kwa nchi, ni vema bajeti ya Wizara hii katika Fungu 31 na 26, zikatolewa kwa asilimia zaidi ya 85 kwani hali ya mazingira yetu ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yasipoboreshwa kwa uharaka zaidi, lengo la maendeleo ya uchumi wa viwanda halitakuwa lenye mafanikio na endelevu kwa vizazi vijavyo. Tufanye jitihada za kufufua na kuboresha mazingira ili tupate mvua za kutosha na kupunguza athari za upepo (kuezuliwa na kubomoa majengo) ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri tupate Maafisa wa Mazingira wa kutosha ili watoe elimu na iwe elimu endelevu kwa wananchi wetu na tuwe na ushindani kwenye Halmashauri zetu. Wataalam hawa wasiwe na urasimu mkubwa wa kufikisha mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mazingira kutokana na waliyoyaona katika utekelezaji wao wa majukumu ili kusaidia kutatua changamoto za mazingira katika maeneo yao. Tuwe na kanuni na miongozo ya kurejesha hali ya mazingira yetu kwa haraka tusiwe na urasimu? Chelewa chelewa tutakuta mazingira yameharibika kwa kiasi kikubwa na kuwa jangwa na gharama ya kuyarejesha itatushinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali tushughulikie haraka suala hili, hali ni mbaya sana. Naomba tuone umuhimu wa kuongeza bajeti yetu ndani. Pia tuweke mikakati maalum ya kupanda miti rafiki ya kulinda mazingira na vyanzo vya mito, maziwa na bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Rukwa nalo limejazwa na udongo unaoteremka kwenye milima na kushuka kwenye Bonde la Rukwa hadi kuingia Ziwa Rukwa. Hivyo nalo liko mbioni kina chake kutoweka. Naomba nalo lipewe kipaumbele ili kulinusuru na hali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, suala la mazingira tuliangalie upya na kuliwekea mikakati kwani tunahitaji mazingira kwa ajili ya urithi wa vijana wetu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, natoa shukrani na pongezi za dhati kwa Rais kutokana na utekelezaji wake kwa maendeleo ya nchi kwa wananchi wake. Jinsi anavyowasimamia na kuwaelekeza wasaidizi wake katika kutimiza majukumu yao kwa mafanikio ya wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waziri na Naibu Waziri bila kuwasahau Katibu Mkuu na wataalam wote ndani ya Wizara kwa kusimama na kutekeleza majukumu yao na kutuwezesha wananchi na wadau wapenda michezo utamaduni na sanaa kufarijika na kuwa na matumaini makubwa kwa kusonga mbele na michezo, sanaa na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa ushauri kwamba inasikitisha kila vijana wanapojitahidi kufanya vizuri wanaishia kwenye robo fainali. Naomba nasi tuwachukue vijana wetu kipindi chote na haya mazoezi ya kila siku kama ajira kwao, hadi mashindano yawakute humo humo, kuliko tunavyofanya mazoezi ya matukio, ni kazi ngumu ndiyo maana tunaishia mahali duni. Hivyo tubuni kitu cha kuzalisha ili tupate mapato ya kuwalipa kila mwezi hawa wachezaji ili wafanye mazoezi ya kuleta ushindi kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba chuo cha kuandaa wataalam wa michezo, sanaa na utamaduni kuboreshwa na kuongezewa wigo ili tupate uelewa zaidi ya kiwango cha juu, tunahitaji nasi Tanzania tuwe mfano ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la wacheza sanaa wa upande wa watoto wa kike, mavazi yao hayana maadili mema. Ni vema uwepo utaratibu wa kufunika miili yao kuanzia kifua hadi chini ya magoti yao na wakacheza vizuri tu. Kwa mfano wanaume wanacheza vizuri na wakati mwingine zaidi ya wa kike huku wakiwa wamevaa kamilifu. Tunaomba sasa wakati umefika turekebishe sheria, kanuni na taratibu zitakiwavyo kuhusu mavazi ya watoto wa kike yatumikayo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba uwepo utaratibu kwa wachezaji wasanii na utamaduni kuwekewa bima ya afya. Pia uwepo utaratibu wa kuwaelimisha kila mara, waepukane na utumiaji wa madawa ya kulevya. Tunapendekeza tunapohitaji kutoa zawadi kwa vijana wetu ni vema tukaendeleza zawadi ya Rais aliyotoa hivi karibuni ya viwanja na hatimaye tuweze hata kuwajengea nyumba za bei nafuu kuliko pesa hatimaye wanakimbilia kununua vitu vya anasa, visivyo na faida baadaye.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza wote Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na wataalam wote ndani ya Wizara kwa kazi nzuri iliyotukuka kwa nchi yetu na wananchi wake. Pia, pongezi za dhati kwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jinsi anavyoyajali majeshi yetu. Hivyo, nasi wawakilishi tuna kila sababu tukubaliane na tuunge mkono jitihada za Rais kwa kazi kubwa anayofanya kwa majeshi yetu kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu hasa makazi, ofisi, sare na miundombinu mingine kutokarabatiwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa ushauri kwa Serikali yangu sikivu kuisukuma na kuisisitiza Hazina kutoa fedha zote za maendeleo zinazopitishwa na Bunge kwa bajeti ya Wizara hii kwa Mafungu yote 14, 28, 29, 93 na 51 ili Wizara iweze kutatua changamoto zinazowakabili ambazo ni sugu kwa sasa. Kwa kuwa, hakuna fedha ya maendeleo zilizotoka kwa mwaka 2018/2019 za shilingi bilioni 1.027 na kwa kuwa mwaka haujakamilika ni vema zikatolewa kwa sasa. Mfano Chuo cha Polisi Kidatu kutokana na kutotolewa fedha za maendeleo kimechakaa na kupelekea kupunguza idadi ya wanachuo wanaodahiliwa chuoni hapo na zinahitajika shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ukarabati.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni nyeti kiutendaji na tunahitaji wanajeshi wetu kuwa na mpangilio mzuri wa maisha ya kila siku, hivyo maji na umeme ni huduma muhimu kwao. Ni vema tuweke mkakati madhubuti wa kuhakikisha madeni yote ya huduma hizo yanalipwa kikamilifu na yasijirudie.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu na kazi ngumu waifanyayo wanajeshi wetu na changamoto lukuki walizonazo ambazo zinawadhoofisha lakini inabidi wafanye kazi ya ziada katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi na umakini mkubwa. Wizara inatambua uzito wa changamoto hizo kwa majeshi yetu lakini inapoandaa bajeti wanajielekeza zaidi na ukomo wa bajeti waliopewa na Hazina. Nachokiona ni kwamba ukomo wa bajeti wa sasa haukidhi mahitaji na hawawezi kupata ufumbuzi wa changamoto walizonazo kwa wakati na ukizingatia tabia iliyodumu kwa Hazina kutotoa fedha za maendeleo kwa wakati na zote kama zilivyopitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu wa jana, napenda kuongeza kwa haya yafuatayo kwa maslahi ya Mkoa wetu wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa tunayo maboma kadhaa na majengo ya nyumba za walimu, madarasa, vyoo na maabara jumla ni 208 lakini kati yake maboma 177 ya maabara bado hayajakamilika na kupelekea wasiwasi wa kupata mafunzo kamilifu ya sayansi kwa watoto wetu. Tunaomba Mkoa wa Rukwa utizamwe kwa jicho la pekee hasa mkizingatia tupo pembezoni nasi tulichelewa katika suala zima la elimu, tumekuja kuibukia hivi sasa. Tunaomba fedha iliyoandaliwa kuhusu ukamilishaji wa maboma ya majengo ya elimu, Mkoa wa Rukwa tuwemo katika mgao wa fedha hizo kwa zaidi ya nusu ya maboma hayo ya maabara kwa makusudi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumzia kuhusu matatizo ya kiwango cha pesa zitolewazo kwa ajili ya chakula kwa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum, kwa shule zetu za Mkoa wa Rukwa, tunazo pale Kata za Ndala B, Mwenge A na Malangali kwa mwaka fedha zinazotolewa na Serikali ni kiasi cha shilingi bilioni 22 wakati mahitaji halisi ni shilingi bilioni 72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachohitaji kuongezea hapa ni usalama wa shule hizi hasa Shule ya Walemavu Malangali. Malangali ni shule ya bweni lakini haina uzio na watoto ambao ni wenye ualbino wanakuwa katika wasiwasi wa maisha yao na hata walimu wao wanakuwa na kazi ya ziada ya ulinzi wa watoto hao. Tunaomba Serikali ione umuhimu wa ujenzi wa uzio wa shule hiyo kwani ni shule inayosaidia na mikoa ya jirani na wakati wa likizo wengi wao hawaendi majumbani kwa kuhofia usalama wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuweka msisitizo kuhusu Chuo cha FDC - Chala kwa kuwa majengo hayo yanahitajika kurejea kwenye umiliki wa Askofu wa Kanisa la Katoliki, ingawa miundombinu yake imechakaa kwa kiasi kikubwa sana, wananchi wametoa eneo na majengo kadhaa yameanzishwa kwa nguvu za wananchi. Kwa kuzingatia na kuheshimu mchango wa wananchi wetu, tunaomba mgao wa fedha hizo za kukarabati Vyuo vya FDC kwa Mkoa wa Rukwa zielekezwe kwenye eneo hili tukamilishe Chuo chetu cha FDC mbadala wa Chuo cha FDC – Chala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wa afya kwa kazi nzuri zilizotukuka na kumuunga mkono wa dhati Rais Dkt. J.P. Magufuli na kuwezesha kuwa na matumaini ya kutimiza azma yake kwa akinamama na watoto hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana Mkoa wa Rukwa wamepatiwa pesa kwa ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya zote nne na kuanza maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa. Ombi letu ni Wizara ya Afya kutoa msukumo kwa TAMISEMI kuhakikisha wanaunga mkono jitihada na nguvu za wananchi katika kuyakamilisha maboma ya majengo ya zahanati yapatayo 50. Pia tunaomba vifaa tiba kwa wakati, ili zahanati takribani 15 zilizokamilika zipatiwe watumishi na zianze kazi kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kujengewa vituo vya afya vya kihistoria na bajeti ya 2019/2020 tumeongezewa vituo viwili ndani ya mkoa, ingawa bado mahitaji ni makubwa kwa Mkoa wa Rukwa kwani tupo pembezoni mwa nchi yetu (Congo DRC na Zambia). Tunaomba vifaa tiba na watumishi wa kukidhi mahitaji kwani majengo mazuri bila kuwa na hayo mahitaji hatutakuwa tumewafikishia wananchi huduma njema kwao.

Naomba Wizara kuona umuhimu wa Vituo vya Afya – Sopa, Kitete, Kala, Kabwe na kadhalika. Tuzingatie jiografia ya Rukwa ni mtihani kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kwa hali halisi ya Waziri, bado Mkoa wa Rukwa tunaomba kuangaliwa kwa jicho la aina yake kwani, akinamama na vijana wameibuka katika kuinua uchumi wao kwa kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, tatizo lililopo ni elimu kwao, lakini Maafisa wa Maendeleo ya Jamii hawakidhi mahitaji. Si rahisi mmoja kushika vijiji viwili au mitaa sita au kata tatu, utendaji wao unakuwa hauna ufanisi na hata tija haipo. Tunaomba ajira itendeke kwa sasa, watumishi hawa ni muhimu sana vijijini, mitaani kwa afya, uchumi, maendeleo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, maafisa hawa hawana usafiri. Tunaomba usafiri kwao na pikipiki kwa vijiji, mitaa na kata, magari kwa ngazi ya wilaya na mkoa kwani sasa inategemea huruma ya Mkurugenzi au RAS. Tunawarudisha nyuma kiufanisi kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba upande wa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii kuwa na ukaimu kwenye nafasi zao. Tunaomba eneo husika kuona kama vigezo vinakubalika waweze kupata nafasi hizo kikamilifu, ili wafanye kazi kwa tija na ufanisi uliotukuka kwa maslahi ya nchi yetu, hususan Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Duniani, Mkoa wa Rukwa, alitoa ahadi ya kutoa ambulance ya Manispaa na Hospitali ya Mkoa, hivyo tunasubiri bado hizo ambulance mbili. Tunaomba Waziri aone namna ya kutimiza ahadi hii, kwani akinamama wanayumba sana kwa huduma hii ya usafiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwa hatua iliyofikiwa hadi sasa. Tunaomba kasi kuongezwa ili tufanane na mikoa iliyokamilishiwa kwa asilimia 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tunaomba utaratibu wa Bima ya NHIF ukamilishwe haraka kwa kutolewa kwa wananchi wote kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Wizara hii kwa ujumla wao kwa maslahi ya wananchi wetu, ni wizara pana ndani ya utekelezaji wake, hivyo nasisitiza na kukubaliana na Kamati na kupongeza kwa kuongezewa bajeti, lakini ni bora zaidi ikiwa Hazina watazitoa zote au kwa asilimia zaidi ya 85.

Mheshimiwa Spika, kwani tunatarajia kuinua utalii ambao unatupatia mgawo wa zaidi ya asilimia tano ya pato la Taifa, pia kurahisisha mawasiliano ya barabara kwa uchumi wa nchi yetu. Tunashukuru jitihada ya Serikali ya kutuunganisha na nchi jirani kwa barabara ya kiwango cha lami, Sumbawanga – Matai – Kassanga (DRC CONGO), Matai – Kasesya (Zambia). Ombi, tunaomba kasi kuongezwa kwa ukamilifu wa barabara hizi pamoja na kuwemo kwenye bajeti iliyobainishwa ukurasa wa 257, tunasisitiza fedha za miradi ya maendeleo kutolewa zote na kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, hali ya barabara ya bonde la Rukwa kutoka Kibaoni hadi Kilyamatunda ina hali ngumu kutokana na maji yanayoporomoka kutoka mlimani na kuelekea Ziwa Rukwa, yanakuwa na nguvu na kukokota miti mikubwa na kuhatarisha madaraja katika barabara hiyo yote na yote yameharibika na kupelekea kila mwaka kurekebishwa maeneo korofi na kuendelea kutumia pesa nyingi za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo na ushauri, barabara hii ni kutengenezwa kwa kiwango cha lami na ujenzi wa madaraja makubwa na madhubuti, ndiyo suluhisho lake. Pamoja na Bajeti iliyopendekezwa kwa baadhi ya maeneo katika ukurasa 302, Ntendo – Muze, Ilamba – Kaoze, Kasansa – Kilyamatundu, Mtowisa – Ilemba, ni matumaini yangu, ushauri wa muda mrefu wa ujenzi wa barabara hii kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa, tuna Kiwanja cha Ndege, Sumbawanga ambacho kinafanyiwa ukarabati na kuongezwa urefu wa uwanja huo, kwa kiwango cha lami, ili nasi tupate usafiri wa Anga. Ombi, tunaomba kasi kuongezwa katika kuendeleza ukarabati huo, ambao haujaonekana ipasavyo, kwani tuna kiu kubwa na kukamilishwa mradi huo kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, bado nasisitiza Wizara kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu wa kuzijenga barabara za mabonde ya Rukwa na Tanganyika kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya tuonayo katika hali halisi kwa usimamizi uliotukuka wa Waziri na ushirikiano wa makamanda wake. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni Jemadari Mkuu mwenye upendo wa Jeshi na nchi yake kwa ujumla na ndiko kunakopelekea amani kuimarika na kudumu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za maendeleo zinazopangwa na kuidhinishwa na Bunge ziweze kutolewa katika ukamilifu wake, kwani mwaka 2018/2019 hadi Machi, 2019 zimetolewa asilimia 41.8 ambazo hazitendi haki kwa Jeshi kwani kazi yao ni ngumu na hali hiyo wanahitaji kubadili na kuboresha maeneo yao ipasavyo ili wawe wepesi na katika mazinigira mazuri ya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti ni muhimu sana kwani utatuwezesha kufanya mambo yetu kwa ufanisi na tija, kwenye mashirika yetu (Nyumbu na Mzinga) ya Jeshi kuendelea kuwapatia kipaumbele chao. Hivyo tunaomba pesa inayoidhishwa ikatolewa kwa asilimia 85 kuliko hii hali ya asilimia 10 hadi sasa haina mshiko kwa Jeshi letu (2028/ 2019).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa wananchi na Jeshi letu la wananchi katika kutwaliwa maeneo na ulipaji wa fidia ni kizungumkuti kwa sasa. Mgogoro huu hauwezi kuwa wa kudumu hapa nchini kwani unatatatulika hivyo unaweza ukatoweka kabisa, kutokutoa pesa inayoidhinishwa kwa ukamilifu na wakati ili waweze kutathimini maeneo hayo na kuyalipia fidia ambayo haiwi na manung’uniko kwa wanaolipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya mwaka 2018/2019 hayakuweza kulipwa kwa wahusika na Jeshi halikufanya kazi kwa wahusika kutokana na asilimia 14.32 ya bajeti iliyotolewa. Tunaomba bajeti ya mwaka 2019/2020 kutolewa kwa ukamilifu ili maeneo ya Jeshi yatambulike na wananchi wasiwe na manung’uniko yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikitishwa sana na makazi ya wanajeshi wetu hapa nchini na kazi yao ngumu waifanyao na hawana muda maalum wa kazi yaani wapo mchana na usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tukiona bajeti ya Fungu 57 inatolewa kwa 1.47% ya mwaka 2018/2019 hadi sasa inasikitisha kwani dalili hii haioneshi kama tuna nia njema ya kuboresha makazi ya wanajeshi tukimuunga mkono Raisi wetu. Tunaomba pesa ya Fungu 57 itolewe kwa nia njema kwa asilimia kubwa zaidi tuwatolee tatizo hili la mazingira mabovu ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kutambua kuwa kilimo ni uti wa mgongo kwa nchi yetu, kwa nini wananchi zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Ambao wengi wao ni waelewa wa uwezo wa kati wa kuwa na maeneo makubwa na uzalishaji kuwa wa wastani, ni dhahiri wanahitaji kupewa elimu na kufanyiwa utafiti wa udongo kwa mazao yao, kutokukana na uchovu wa udongo wao. Hivyo Taasisi yetu ya TARI inahitajika kupatiwa fedha za kutosha kwani, hivi sasa tunahitaji utaalam wao zaidi ndani ya nchi yetu, hasa Mkoa wa Rukwa kwani mwaka 2018/2019 baadhi ya wakulima wamepatiwa mbegu zisizo bora na pembejeo kuwa feki na kumpatia hasara kubwa mkulima wetu.

Mheshimiwa Spika, nasikitika ndani ya ukurasa 20-23, TARI wameandaa nyenzo tatu za kumsaidia mkulima kufanya uamuzi wa kuboresha uzalishaji wa zao la mhogo, hakuna maeneo ya Mkoa wa Rukwa katika kufanikiwa na utafiti huo wa TARI kwa wakulima wetu wa mhogo - mwambao wa Ziwa Tanganyika, Kala, Wampembe, Kisumba-Kasanga, Karogwe, Kabwe, Kirando, Kipili, Mpombwe na kadhalika. Tunahitaji msaada wa zao hilo, kwani hatuna Maafisa Ugani wa kutosheleza mahitaji.

Mheshimiwa Spika, upungufu wa Watafiti na Maafisa Ugani tulishughulikie katika ajira yao ili tuboreshe kilimo chetu. Vijiji zaidi ya elfu 15, Maafisa Ugani ni elfu saba ni kujidanganya wenyewe.

Mheshimiwa Spika, ndani ya ukurasa wa 25, kuhusu mazao ya jamii ya mikunde, inalimwa kila pande ya nchi yetu na wananchi hutumia kama mboga kwenye chakula kikuu kwa kila upande. Uzalishaji wake unashuka pamoja na kutumika eneo kubwa la kuzalishia ni ukosefu wa mbegu bora. Bado uwezo ni mdogo wa TARI kuzalisha mbegu bora, si sahihi kwa wakulima 10,160,577 tu ndiyo wanufaika wa mbegu bora za aina ya mikunde. Ni vema nguvu ya rasilimali fedha kuandaliwa upya kwa maslahi ya wakulima wa nchi hii. Kuinua tija kwa wakulima wetu, hatuwezi kuwa tegemezi wa ukulima wetu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba uwepo utaratibu maalum wa ujenzi wa maghala makubwa na vihenge vikubwa vya kutosha kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa. Majengo hayo ya Serikali yanapohifadhiwa mazao hayo hakuna uharibifu mkubwa, kuliko tunavyohifadhi wakulima wenyewe mazao uharibika na kupata hasara.

Mheshimiwa Spika, utafiti na ukaguzi wa karibu zaidi wa pembejeo za kuhifadhi mazao, nyingi ni fake. Asilimia 14.5 ya utekelezaji wa vihenge nchini, ni wa hali ndogo sana ambayo inakatisha tamaa kwa wakulima wanapoharibikiwa mazao yao. Tuongeze nguvu na usimamizi wa karibu. Pia Mkoa wa Rukwa tufikirie kuletewa hivyo vihenge vya kututosha. Tunasisitiza tujipange hasa na ujenzi wa maghala makubwa, kwa ajili ya stakabadhi ghalani ni zoezi limpatialo mkulima faida kwa mazao yao.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza wote ndani ya Wizara katika utendaji wao wa kazi nzito kutokana na wengi wao ambao ni wafugaji na wavuvi ni wananchi wa kawaida, ambao wanahitaji kupewa elimu ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi na tija kwa mapato yao. Hivyo hazina waone umuhimu wa kuongeza ukomo wa bajeti na fungu la miradi ya maendeleo kuweza kutolewa kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, napenda kuona umuhimu wa vikundi vya akina mama wanaojikita kwenye ufugaji wa kuku kama miradi ya kuwapatia uchumi kwa kupambana na umasikini. Akina mama wamekuwa na uwezo mdogo wa kufuatilia vifaranga na utunzaji wa vifaranga hivyo hadi kufikia kutoa mazao tarajiwa ya mayai au nyama, kuwa na gharama kubwa. Tunaomba Wizara/Serikali kuona utaratibu bora wa kuboresha utunzaji wa kuku wa kienyeji ili kuweza kuzalisha mayai na kutoa nyama kwa mahitaji makubwa kwa wananchi wetu, na kwa kuwa hawana gharama kubwa na wanastahimili madhara stahili kwa wastani mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wamekuwa wanasafiri sana maeneo mbalimbali ili kutafuta malisho. Hivi kwanini Serikali isiweke utaratibu wa mashamba ya malisho na yakafahamika na kuwaelimisha wafugaji kulima mashamba hayo kwa idadi ya mifugo yao? Pia tuone utaratibu wa kuboresha mifugo ya asili kulika kupandikiza wa kutupatia mifugo chotara na kusababisha kupotea kwa mbegu ya asili ya mifugo yetu.

Mheshimiwa Spika, jitihaa ya Wizara kutuwezesha kupata samaki wakubwa na wenye tija wa kuwapatia mapato ya kutosha wananchi wetu. Kikubwa tutoe elimu kwa wahusika na uvuvi na ufugaji kwa maendeleo na kukuza uvuvi na ufugaji bora nchini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri yenye tija kwa taifa letu. Mheshimiwa Waziri ninakuombea Mungu aendelee kukupa afya, nguvu na wepesi ndani ya utekelezaji wa majukumu yako kwani chini ya uongozi wako Wizara imetulia na unawajibika kwa maslahi ya kuachia urithi watoto wetu na kusababisha kuongeza gawio kwa Pato la Taifa. Tumeweza kubainisha maeneo kadhaa ya vivutio hapa nchini kwa nia ya kupanuwa wigo wa utalii. Tatizo ni kuhakikisha tunaweka mazingira madhubuti ya kuweka miundombinu yote kwa kuanzia kabla ya kutangaza ili wakiingia watalii wasiwe na kigugumizi tena cha kurudi au hata kushawishi wengi kutokana na kukuta ubovu wa miundombinu. Mfano Rukwa kuna Kalambo falls, ni kivutio kikubwa ndani ya Afrika Mashariki na Kati lakini hakuna barabara na hoteli, vyoo na maeneo ya kupumzika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kilimo Rukwa ni Oktoba – Novemba mvua zinachanganya na kwa wananchi wetu kilimo ndio mradi mkuu kwa kuzalisha chakula na mazao ya ziada kwa biashara. Wanapojitokeza wanyama waharibifu kunakuwa na hasara kubwa kwa wananchi wetu na maafisa kuwa na uvivu wa kuyatembelea mashamba yaliyoathirika kwa wakati na kwa eneo zima, wamekuwa wanawahadaa wakulima na hatimaye kuwa na chuki na Serikali yao. Mfano kijiji cha Kisumba – Katanga Kisumba, Wilaya ya Kakumbo – Rukwa. Wakulima wa alizeti walioingiliwa na wanyama ni 140 lakini waliolipwa ni wakulima 60, wengine hadi leo hawajalipwa. Tunaomba Wizara na kitengo husika kufuatilia malalamiko ya wakulima na kuwa shughulikia malipo ya fidia zao ili zitoke; ni kero kubwa sana huko vijijini, maafisa waachane na rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu wote tunakubaliana kuwa asali kwa sasa ina soko ndani na nje kwa matumizi ya kakwaida kwa afya zetu. Maadamu misitu tunayo nashauri wale mabwana nyuki tulionao wawe na kazi ya kutoa elimu, uelewa na kushauri makundi mbalimbali na kuunda makundi ya ujasiriamali kwa vijana na akina mama ili kuweza kuifanyia shughuli hiyo. Kwani ni mradi ambao unajizalisha wenyewe na maafisa wanafahamu maeneo yenye tija hiyo. Mikoa, wilaya, kata na vijiji ambavyo vina mwelekeo huo kwa uzalishaji wa asali kuwa na viwanda vya kuchuja na kufungasha kuingiza sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ziwa Rukwa kuna mambo mengi sana lakini kutokana na uharibifu wa mazingira na shughuli za kibinadamu na mito kuporomosha maji kwa wingi na udongo moja kwa moja kwenye Ziwa sasa kina cha maji katika Ziwa Rukwa kinapungua na mamba kutawanyika na kuathiri wananchi wetu. Ushauri, mamba waweze kuvunwa, washirikiane na Wizara ya Maji, Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Tuweze kuvuna maji kwa umwagiliaji, mabwawa nakadhalika. Tuliokoe Ziwa na usalama wa wananchi wetu upatikane kwao dhidi ya mamba. Tunaomba Hazina kuitoa pesa iliyopendekezwa ya maendeleo ya Bilioni 48.889 yenye ongezeko la asilimia 66, tunahitaji matokeo chanya yajioneshe kwenye gawio la Pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kuwawezesha Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kujituma na kujitoa kwa maslahi ya maendeleo ya kuwasambazia umeme wananchi hadi vijijini na vitongoji vyote nchini hadi sasa wana asilimia ya kuridhisha na matumaini ya kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya ahadi ifikapo mwaka 2025 umeme uwafikie wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani za dhati kwa Meneja wetu wa TANESCO, Ndugu Chambua kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na changamoto zilizopo ndani ya Mkoa wa Rukwa.

(1) Wakandarasi hawajapatiwa nyongeza ya vifaa vya kupeleka umeme kwenye Taasisi za Serikali (zahanati, vituo vya afya, shule za msingi na sekondari zetu).

(2) Nguzo zilizosambazwa zisiwe picha kwa wananchi, ni vyema zikakamilishiwa zoezi na umeme kupatikana

Mheshimiwa Spika, pamoja na shughuli na jitihada za Waziri na Naibu Waziri kwa moyo wa dhati wa kuitumikia Wizara hii, bado Mkoa wa Rukwa tunahitaji umeme kwani kazi iliyofanyika bado vijijini Mwambao wa Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa bonde zima, mpakani mwa Zambia na Congo DRC hali ni ngumu bado. Tunaomba umeme vijijini zaidi, tunashukuru hiyo jitihada ya kupatiwa umeme wa gridi ya Taifa kuingia Sumbawanga ni tija ya pekee kwetu.

Mheshimiwa Spika, tunaomba jitihada iongezeke kwa kusambaza umeme Mkoa wa Rukwa na kutuwezesha kwa kuongeza nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika suala zima katika suala zima la Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuendelea kumwombea heri na baraka na apate wepesi Mheshimiwa Spika wetu, afya yake iendelee kuwa njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Ardhi, kwa Waziri mwenyewe, Naibu Waziri na Kaimu Kamishna Mkuu ambaye ni Mthamini Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzito waliyoifanya na kukubaliana kwamba sasa ni wakati muafaka wa sheria hii kuweza kuletwa katika Bunge hili ili kuweza kujadiliwa na hatimaye kupitishwa ili iweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 52 cha uhalali wa uthamini wa masuala kwa wananchi wetu ilikuwa ni kazi nzito sana na ikajenga kero miongoni wa wananchi, lakini kwa sasa kutokana na speed aliyonayo Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wakifuata speed ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ni dhahiri kusema kwamba sheria hii itaweza kuwa-push na kuifanya kazi yao katika ukamilifu tunaouhitaji na unaotarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la ulipaji wa fidia. Hili suala la ulipaji wa fidia ndani ya miaka miwili na ulipaji wa ribandani ya miezi sita litaweza kutoa ufafanuzi mzuri kwa wananchi wetu na kuleta muafaka wa kuweza kuona kwamba Serikali yao ni kweli ni Serikali ya wanyonge. Hili suala la thamani; uthamini ulikuwa ukifanyika toka huko awali, ulikuwa upo, lakini walikuwa wamechanganywa pamoja na ma-surveyor. Sasa hivi hii sheria itakuwa ni ma-valuer peke yao ambao watakuwa wanaitumia kwa maana ya kuweka ufanisi na weledi katika kazi yao ya uthamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi ninachoomba na ninaamini ya kwamba katika taarifa hiyo uliyotuletea ni dhahiri kusema kwamba Wizara imekubaliana na mapendekezo ya Kamati ya kuzungumza kwamba huyu Mthamini Mkuu awe huru. Hapa imethibitisha wazi ya kwamba ni huru kwa sababu atateua wenzie wa kumsaidia kazi kwenye eneo la kanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Sheria hii ni nzuri, ninaiomba Serikali katika kifungu cha 5 kinachuhusu kuteua Wathamini Wasaidizi, ni vyema suala hili likafanyiwa kazi na hizo sifa ni sahihi kwa sababu hao Wathamini wapo tokea awali isipokuwa Bodi ndiyo ilikuwa haipo. Sasa Bodi ya Wathamini imepatikana; na katika mchanganuo na ushirikiano uliowekwa kwa kila sekta inayotakiwa katika suala zima la uthamini, wamo katika Bodi. Kwa maana hiyo ndiyo kusema ya kwamba wale Wathamini walioko wa miaka mitano hawatakuwa wazee peke yao, watakuwa ni pamoja na vijana watakaotimiza hivyo vigezo vinavyohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba katika kipengele hiki cha namba 5 kwa utaratibu chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma wangefanya haraka iwezekanavyo kuwateua hawa Wathamini Wakuu Wasaidizi ili Mthamini Mkuu aweze kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima katika Ibara ya 8(1) mpaka (4) ambacho kinapelekea kwamba Wathamini Wasaidizi wa Kanda watakuwepo katika Kanda. Naomba katika uteuzi wa Wathamini hawa, naomba kila Halmashauri ya nchi hii wapate Wathamini angalau wawili, watatu kwa sababu migogoro mingi ambayo imeorodheshwa na Wizara ya Ardhi, iliyopo katika orodha ya migogoro, migogoro mingi iko kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba Wathamini wawepo katika Halmashauri zetu ili wale Wathamini Wakuu Wasaidizi wa Kanda waweze kusaidiana nao katika ile migogoro inayowahusu kutatuliwa mmoja baada ya mwingine; ili migogoro ile ikianza kutatulika ni dhahiri ya kusema kwamba hii miaka miwili ya uthamini kuanzia sasa itakwenda vizuri na hatimaye tutakuwa tumefuta migogoro yote na hatutakuwa tena na migogoro mingine mipya itakayooana ama kushahibiana na ile ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba ni kwamba Sheria hii ya uthamini ni nzuri na kuweza kumpatia Mthamini Mkuu kuweza kuteua Wathamini Wakuu Wasaidizi na Wathamini ambao wataidhinishwa katika maeneo yetu. Hii inamaanisha ya kwamba katika kifungu cha 11(1), kinampa mamlaka ya kuweza kukasimu mamlaka yake, kinampa mamlaka kuteua. Katika kuteua mamlaka ile, anaweza akafikia kutoa agizo la jukumu lake yeye la kusaini hati. Sasa akimtafuta mtu ambaye sio wa ngazi yake itakuwa ni tofauti na sheria ambayo tumeitunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba ni kwamba wale Wathamini Wasaidizi wabakie vilevile kwa sifa zile zile za kifungu cha 5 ili waende sambamba na Mthamini Mkuu na ili atakapowakasimia madaraka ya kazi zake, ziwe zinakwenda kwa mtu muafaka anayehitajika kuifanya kazi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza mafungu hayo matatu, napenda kusema kwamba hii sheria ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba tukubaliane kwamba itatatua matatizo yaliyopo na itafuta kabisa matatizo haya kujirejea tena kwa wananchi wetu. Hivyo, naomba tuiunge mkono kwani speed ya Mheshimiwa Waziri na speed ya Mheshimiwa Rais na speed ya Naibu Waziri katika kutatua matatizo ya hawa wananchi nina imani kabisa ya kwamba itaweza kwisha na sisi tutakuwa tumepumua na hii sheria itatoa pumzi kwa wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile itamuunga mkono Mthamini Mkuu kwa sababu sasa hivi Wizara hii ina Mthamini Kaimu; yaani Kaimu Mthamini Mkuu. Kutokana na hali hii ya sheria hii ya kumpa uhuru wa kufanya kazi hii, nina imani kabisa ya kwamba katika kifungu 52 atakitimiza kwa kazi ngumu hiyo, ataitimiza kwa weledi mkubwa na uaminifu mkubwa ili aweze kujithibitishia yeye mwenyewe kwa Mheshimiwa Rais aweze kumteua na kuwa Mthamini Mkuu wa Serikali katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kabisa kwamba sheria hii imefika wakati muafaka wa kutatua matatizo ya wananchi wetu na kwa hiyo, tuiunge mkono iweze kupita tuondokane na matatizo kwa wananchi wetu, ahsante sana.