Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shally Josepha Raymond (88 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mkaguzi Mkuu huwa anakagua mashirika mengine, lakini ningependa kujua au kwa niaba ya wengine pia, yeye huwa anakaguliwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkaguzi Mkuu naamini yeye pia hujikagua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii.
Kwa kuwa, ndizi ni kati ya zao ambalo linatumika sana nchini lakini kipimo chake kimekuwa na tatizo na wakulima wa ndizi wanapunjika sana zikiwemo ndizi kama mishale, minyenyele, mlelembo, toke, kitarasa na mtwishe. Mheshimiwa Waziri anatueleza nini kuhusu soko la bidhaa kama hiyo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ndizi zimenilea, lakini msema kweli ni mpenzi wa Mungu, sijui international standard za kupima ndizi, nitakwenda kuwa task watu wa TBS na watu wa vipimo kusudi tuweze ku-establish kipimo standard cha ndizi. Lakini kitakachoamua bei nzuri kwa mkulima ni soko la ndizi, watu wa (TAHA) Tanzania Horticulture, chini ya ndugu Jacquline wanatafuta soko la ndizi nje ya nchi, na tumeshapata soko ambalo tunahitaji kuuza nje ya nchi tani 50 kwa wiki. Kwa hiyo tunawasiliana na mama Raymond kusudi tuweze kumuunganisha na Jacquline tuone kama Kilimanjaro mnaweza kulima kusudi kupeleka nje ya nchi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa kuna mtazamo kwamba kila kundi kufungua benki ndiyo jibu la huduma ya benki, siyo jema; na kwa kuwa hapa tulipofikia, huko nyuma tulikuwa na Benki ya Posta ambayo iko kila mahali na watumiaji wa benki ni hao hao wananchi wa eneo lile; je, ni kwa nini sasa Serikali isiipe uzito Benki ya Posta ikasambaa kote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika benki ambazo zinakuja juu sasa ni Benki yetu ya Posta. Tumeiwezesha vizuri, Menejimenti yake imekaa vizuri sasa, imezindua huduma nyingi ambazo hata benki nyingine kubwa za kibiashara zimeshindwa kuanzisha huduma hizo. Kwa hiyo, ni imani yangu kubwa Benki ya Posta ndani ya muda mfupi ujao itarejesha hadhi yake ndani ya nchi yetu ya Tanzania.
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuiunga mkono Benki yetu ya Posta, tufungue akaunti kule, tuiwezeshe sisi kama shareholders muhimu ili Benki ya Posta iweze sasa kurejea. Tuko vizuri na inakimbia Mheshimiwa Shally, itafungua matawi yake sehemu zote nchini.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa
kuwa katika swali la msingi linazungumzia pombe za kienyeji na pombe za
kienyeji katika Taifa letu ni nyingi ikiwemo mbege, kimpumu, ulanzi na pombe
nyinginezo. Ni lini sasa hawa watu wa viwango vya kuandika kilevi kilichoko
kwenye pombe ikiwemo TBS wataingia katika maeneo husika ili kuweza kujua
kwamba ni kiwango gani cha ulevi kinachoruhusiwa katika pombe za kienyeji?
NAIBUWAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna pombe mbalimbali. Kuna mbege, kuna
ulanzi na nyinginezo, bahati mbaya pombe hizi hazijawekwa katika viwango
stahiki na ndiyo maana maeneo mengine utakuta kuna kesi mbalimbali
zimejitokeza. Baadhi ya watu saa nyingine wamekunywa pombe, pombe ile
imewadhuru na matukio haya tumeona kwamba yametokea maeneo
mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwa sababu sasa hivi tuna Wizara
ambayo inafanya kazi vizuri zaidi na hususan suala zima la viwanda na naamini
wenzetu sasa wa TBS watachukua jukumu lao katika maeneo mbalimbali
kuhakikisha ni jinsi gani tunafanya kurekebisha utaratibu mzuri hasa katika hivi
vikundi vidogovidogo vinavyojihusisha na pombe za kienyeji, lengo kubwa ni
kumlinda Mtanzania anywe kitu kinachoridhisha maisha yake lakini na afya yake
ya msingi vilevile.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya hatua husika za mradi huu, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri ametueleza kuhusu awamu ya kwanza inayotarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Je, huo ndiyo wakati ambapo mabomba ya Same yatafungua maji hayo na kuona maji yakitiririka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Same haiko vizuri kifedha kuwasaidia watu wa Same ambao mpaka sasa hawana maji safi na salama zikiwepo Kata za Njoro, Same Mjini, Makanya na Hedaru. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapatia fedha za kuchimba visima virefu ili watu hao wapate maji safi na salama wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi huo mwaka 2019?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la msingi limezungumzia mradi wa Same-Mwanga-Korogwe kwamba ifikapo mwaka 2019 utakuwa umekamilika kwa maana kwamba maji tayari yatakuwa yamefika Mwanga na yatakuwa yamefika Same, yatafunguliwa wananchi wanaanza kupata maji na miradi hiyo inaendelea vizuri na fedha zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kuhusu Same, katika bajeti hii tuliyonayo kwa sasa na ninyi Waheshimiwa Wabunge mliipitisha, tulihakikisha kila Halmashauri tumeipatia fedha ili Waheshimiwa Wabunge na Madiwani katika Halmashauri zao wapange miradi kutokana na hiyo fedha ambayo tumeituma kwenye Halmashauri. Kwa bahati nzuri Halmashauri ya Same ilipewa Sh. 663,847,000 kwa ajili ya miradi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Halmashauri hizi sasa zinao uwezo, zitekeleze miradi kutokana na fedha hii kwa kuchimba visima au maji ya mtiririko kutokana na hali ya mazingira ya Halmashauri husika ili kuhakikisha wananchi wanapata maji. Mwaka huu wa fedha unaokuja tutaendelea kutenga fedha kwenye Halmashauri ili wao wenyewe waweze kutekeleza miradi ya kuwapelekea maji wananchi wao.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Waziri ametueleza kwamba shida kwenye kuwekeza hisa iko kwenye elimu kwa umma; na kwa kuwa ametutajia kwamba wanaonufaika na lile dirisha dogo zaidi ni makampuni. Nilikuwa naomba kuuliza kwa kuwa wengi wa wajasiriamali ni wadogo wadogo wakiwepo wale wamama wa Kilimanjaro na mpaka sasa elimu ya hisa inatoka tu labda kutokea Benki ya CRDB kupitia matawi yake, ni lini sasa mabenki mengine yaliyotajwa pamoja na TOL, TCC, NMB watatoa elimu ya hisa kupitia matawi yao yaliyo huko mikoani?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sikusikia vizuri jina la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza haya mashirika na taasisi ambazo nimezitaja, linalonufaika na dirisha dogo, mashirika haya, hisa zao zile wao ndio wanapopata faida wanawagawia wanahisa wao. Kwa hiyo, wananchi wadogo wadogo wananufaika kupitia hizo taasisi ambazo zinanufaika na hilo dirisha dogo. Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa swali dogo la pili nitumie nafasi hii kuyashauri mashirika yote yanayohusika na benki hizi kuongeza elimu katika matawi mbalimbali ili wananchi waweze kupata elimu na kunufaika na hilo dirisha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika,
ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hadhi ya Hifadhi ya
Ngorongoro inafanana kabisa na hadhi ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, mlima ambao ni mrefu sana, mlima ambao unaingiza kipato kikubwa kwenye utalii, mlima ambao ni wa pekee wenye theluji katika nchi za tropic.
Je, Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha
kwamba wanaozunguka mlima ule wanaweza kuwekwa katika hali ambayo wataendelea kuutunza ili ile theluji isije ikayeyuka yote na ule mlima ukabakia katika ubora wake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kwa maana ya sifa za uhifadhi, lakini pia faida za kiuchumi zile za Ngorongoro zinafanana kwa karibu sana na za hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Sasa kuhusu swali lake nini Serikali itafanya ili kuweza kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi kwa faida za kiuchumi Kitaifa lakini pia kwa faida ya jamii inayoishi kwenye maeneo haya ya Hifadhi ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwanza Serikali inatambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na kwa kweli tunatoa wito kwa wananchi wanaoishi katika eneo hili la Mlima Kilimanjaro waweze kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba uhifadhi unaimarishwa katika eneo la Kilimanjaro. Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali ni kuendelea kusimamia sheria iliyopo lakini pia tunakaribisha maoni kutoka kwa wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo hata wengine waweze kutusaidia ili kuweza kupata maoni ya
wananchi yatakayotuwezesha kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali kwa kutambua wanawake inakuwa vigumu kupata mikopo kwenye mabenki, imekuwa ikitoa hela na wakati mwingine pia ikipeleka kwenye mabenki, lakini wanawake wanakopeshwa kupitia kwenye vikundi vyao zikiwemo mabilioni ya JK.
Swali langu nauliza, wanawake wa vijijini hawakunufaika na hizo hela, sasa Serikali inafanyaje kuhakikisha kwa kuwa zile hela ni za mzunguko na bado tuna amini zipo, zitawafikiaje wale wanawake wa vijijini?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi wote ni wajumbe katika zile Halmashauri zetu na mikopo inapopitishwa inapitia katika vikao vya Baraza la Madiwani.
Kwa hiyo, mimi naomba pale ambapo tunapitisha vikundi vyetu viweze kupewa mikopo ni lazima tuzingatie pia tunao akina mama wanaotoka katika maeneo ya Vijiji ili na wao waweze kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la mabenki, benki wana masharti yao ambayo yanatakiwa yatimizwe, kwa hiyo tujaribu kuwaelimisha wakina mama ili waweze kukidhi vigezo vinavyotakiwa na mabenki na sisi wenyewe tuwe mstari wa mbele katika kuangalia ni vikundi vipi ambavyo vimekidhi vigezo hivyo na tuawasidie katika hatua za kuweza kupata mikopo either kutoka katika benki au kutoka katika Halmashauri kupitia ule Mfuko wa Wanawake na Vijana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ili wananchi waupende ushirika ni pamoja na kuona kuwa mali zao ziko salama na wananufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza Serikali, kwa Vyama vya Ushirika ambavyo mali zake zimetapanywa yakiwemo mashamba, viwanja, nyumba, hususani KNCU, Serikali inasaidiaje ili kurejesha mali hizo ili wananchi wanufaike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inasaidiaje mikataba mibovu iliyoingiwa na Vyama vya Ushirika na wale ambao wamechukua mali za vyama hivyo iletwe ili irekebishwe wananchi hao waweze kuona sasa ushirika wao unaendelea vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba baadhi ya mali za Vyama vya Ushirika zimetapanywa na hazitumiki kwa utaratibu unaotakiwa na ndiyo maana Wizara yangu kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika nchini kote kwa sasa wanafanya tathmini kuhusiana na mali zote za Vyama vya Ushirika ili kujua ni zipi ambazo hazitumiki, zipi ambazo zimeingia mikononi mwa watu binafsi kinyume na taratibu, kwa lengo la kuhakikisha kwamba zile ambazo zimechukuliwa kinyemela ziweze kurudi, lakini vilevile ili mali hizo za ushirika ikiwa pamoja na ardhi ziweze kutumika katika mazingira ambayo yanaleta tija zaidi na kwa manufaa ya ushirika na wana ushirika wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la pili kwamba tunafanyaje kurejesha mali ambazo zilichukuliwa kinyume na taratibu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tokeo Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, tumechukua hatua kadhaa za kuhakikisha kwamba uovu uliokuwa ukifanyika katika Vyama vya Ushirika hautokei tena. Kwa hiyo, wale wote ambao wamehusika katika kufanya ubadhirifu na upotevu wa mali za ushirika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao nao wanakuwa ni sehemu ya ubadhirifu huo tumeendelea kuwachukulia hatua. Ni hivi karibuni tu tumevunja Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi. Vilevile mmesikia yaliyotokea Nyanza, jitihada zinaendelea kurudisha mali za Ushirika wa Nyanza. Pia tunajitahidi kuendelea kusaidia vyama vingine ambavyo siku za nyuma kimsingi taratibu zilikiukwa na mali zao kwenda nje kwa watu binafsi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maswali haya na jitihada za Serikali, naomba niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wahamasishe wanaushirika wawaeleze kwamba ushirika ni wa kwao, Serikali yenyewe inasaidia. Kwa hiyo, inatakiwa wenyewe wawajibike kuhakikisha kwamba mali za ushirika zinalindwa na pale kasoro zinavyotokea basi watoe taarifa kwa Serikali ili tuweze kuchukua hatua.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika jibu lake la msingi amekiri kwamba kuna miradi 114 ambayo imekuwa haiendelei au imeharibika kabisa na katika miradi hiyo 114 mmojawapo ninaoufahamu mimi ni ule wa Kili Water kule Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali itahakikisha imeukarabati mradi huo ili kuondoa adha ya Wanawake wa Tambarare ya Rombo kubeba ndoo za maji Alfajiri na mapema walio katika Kata ya kule Ngoyoni, Mamsera chini pamoja na wale ambao wako kule pembeni ya Ziwa Chala?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tambarare yote ya Mkoa wa Kilimanjaro imekumbwa na adha hii ikiweko Wilaya ya Mwanga, Same Mjini mpaka kule Hedaru. Ni lini sasa Serikali itakamilisha ule mradi wa maji wa Ziwa la Nyumba ya Mungu ambao utapeleka maji kupitia Mwanga, Same, Hedaru mpaka Mombo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali kumpongeza sana Mbunge kwa maana kwamba anafuatilia kuona namna gani miradi hii inawea kuathiri matumizi ya wananchi kwa maana kwamba maji yamekuwa yanapungua kwa namna hali ya hewa inavyobadilika. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni la msingi lakini pia ni lazima tuchukue hatua. Hatua mojawapo ni lazima sisi sote tuhakikishe kwamba tunalinda vyanzo vya maji lakini pia tupande miti ambayo ni rafiki lakini pia tuvune maji ya mvua kwasababu rasilimali za maji zinapungua mwaka hadi mwaka kama hatuchukui hatua yoyote ya kukabiliana na tatizo hilo. (Makofi)
Sasa kuhusu mradi ambao unasema ni lini utakarabatiwa, Mkoa wa Kilimanjaro Serikali kwa mwaka huu wa 2017/2018 tumetengea shilingi bilioni 8.95 kwa ajili ya kumaliza miradi inayoendelea lakini pia kukarabati miradi ambayo ipo haifanyi kazi katika kiwango kwahiyo watumie fddha zile katika kuangalia vipaumbele na kuona kama wanaweza kukarabati kwa mwaka huu wa fedha vinginevyo wapange katika mwaka wa fedha unaofuata.
Kuhusu swali lake la pili, mradi wa Nyumba ya Mungu kupeleka maji Mwanga mpaka Same, sasa hivi mkandari huko mwanzo alikuwa anusua sua lakini sasa hivi anakwenda kwa kasi na nina uhakika kwamba mradi ule utakuja kukamilika lakini pia tumeanza na awamu nyingine ya kupeleka maji kule Same nayo Mkandarasi yupo site na kazi inakwenda vizuri. Serikali inafuatilia kwa nguvu zote ili miradi hii iweze kukamilika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa uhusiano wa benki na mtu wa kawaida ambaye hafanyi biashara, ni kuweka hela yake ili apate faida na pia kwa usalama; na sasa hivi tunashuhudia kwamba hata mitandao ya simu mtu unaweza ukawekeza hela yako. Ni lini sasa benki hizi zitakaa chini na kuona kwamba kuna umuhimu wa kuongeza faida (interest rate) kwa wale wanaoweka hela zao kwenye savings account?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema tangu mwaka 1991 nchi yetu iliingia katika soko huru katika masuala ya kifedha nchini na interests zinazopangwa na mabenki yetu katika savings accont huwa zinawekwa kulingana na uhalisia wa soko. Ina maana faida inapatikana kwa mabenki na kwa wananchi. Kwa kumbukumbu ambazo tunazo Wizara ya Fedha na Mipango, interest hii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe angalizo kwa mabenki yetu kuangalia kwamba wana balance interest wanayotoza waone interest wanayowapa wananchi kwa kuweka pesa hizi katika akaunti zao hasa savings account.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika katika hili mabenki yetu yanafanya kazi vizuri kuhakikisha wao wanapata na wateja wao ambao ni wananchi wanapata vizuri kwa kuwa tupo katika soko huria na wanapambana kuweza kupata wateja kuweka pesa katika benki zao.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Swali langu linahusu umbali wa wananchi hawa na benki zao. Kwa kuwa benki hizo zina nia nzuri ya kuwakopesha, lakini tatizo ni wananchi wanakoishi ni mbali na zile benki, kwa sababu benki nyingi zimefunguliwa mijini na nyingi zinafanya kibiashara zaidi.
Ni lini sasa Serikali itawasiliana na hizi benki zifungue matawi yao kule vijijini zikiwemo kule Mamba Miamba kule Same na kwingineko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tunashukuru sana kwa concern yake ya kuona kwamba wananchi wengi wanahitaji huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama Serikali hatua ambazo zinaanza kuchukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba mabenki haya ya biashara yanakwenda kutafuta wateja maeneo ya pembezoni ili sasa watu wengi zaidi wapate fursa ya kuweza kupata huduma hizi za kifedha.
Kwa hiyo, naamini kabisa katika mipango ile ya Serikali ambayo mojawapo kubwa lililofanyika mwaka 2015 ni kuhakikisha kwamba fedha ambayo ilikuwa ni ya Mashirika ya Umma ambayo mabenki mengi walikuwa wanaitegemea, ilirudi Benki Kuu sasa ili mabenki waende kuwatafuta wateja wengi zaidi. Kwa kufanya hivyo pia itasaidia sana mabenki haya kwenda katika maeneo ya pembezoni ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukua hilo na kazi inaendelea kufanyika, kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma hii ya kifedha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya tambarare ya Kilimanjaro yana shida ya maji safi na salama. Ni lini sasa Serikali itatumia Lake Chala ili kuyapatia maeneo ya tambarare maji vikiwemo vijiji vya Mahida, Malawa, Ngoyoni, Ngareni, Holili na kwingineko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari na inatekeleza miradi mingi ya maji na mipango kemkem ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutoa maji kutoka Lake Chala, naomba tushirikiane na Halmashauri yako ambayo hilo bwawa liko katika hiyo Halmashauri ili tuone jinsi gani tunaweza tukafanya utafiti na kuweka fedha kuhakikisha vijiji vinavyozunguka sehemu hiyo vinapata maji.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali la nyongeza. Serikali iko moja nayo ni Serikali Kuu na hao wote waliotamkwa wanatekeleza kutokana na maagizo ya Serikali Kuu. Je, inakuwaje pale ambapo hela hazipelekwi za kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali inafuatilia vipi kuepusha migongano hiyo kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo fedha za kutekeleza mradi fulani hazijapelekwa zote mawasiliano yanafahamika kati ya waliopokea na waliopeleka. Kwa hiyo hayo yanakuwa ni maelezo sahihi wakati wa tathmini kwamba hatukuweza kutekeleza vizuri mradi huu au hatukukamilisha kwa sababu fedha imekuja nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hiyo ni mawasiliano ya ndani ya Serikali na mara nyingi imefanyika; lakini kitu kimoja kizuri kwa upande wa Serikali za Mitaa ni kwamba wanapopewa wakati mwingine fedha imezidi au imechelewa kuja imekuja mwishoni mwa mwaka wa fedha wenzetu wanaruhusiwa kubaki na fedha ile halafu mwezi wa Saba wanakaa kwenye vikao vyao rasmi wanazipitisha kwa ajili ya matumizi yaliyovuka mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili kwamba tunafuatiliaje mgogoro; Serikali ina macho usiku na mchana. Kule kule ziliko Serikali za Mitaa wapo waangalizi wa Serikali ambao wanakusanya taarifa kila siku asubuhi na mchana kwa masaa yote. Kwa hiyo kama kuna harufu yoyote ya mgogoro Serikali Kuu huwa inapata taarifa hizo mara moja. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Ni takribani miaka kumi sasa toka hili swali linaulizwa. Nakumbuka lile Bunge la Tisa niliuliza hili swali
mwaka 2007 na Bunge la Kumi aliuliza Mheshimiwa Maida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la Serikali siku zote ni kwamba muswada unaandaliwa. Ni lini sasa muswada huo utaletwa hapa Bungeni ili uweze kupitishwa kama sheria?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mbunge najua una imani na mimi. Sasa upele umepata mkunaji, safari hii unaletwa chini ya uongozi wangu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hali ya kusuasua kwa huu mradi wa Mande, Tela kunafanana kabisa na miradi mingine iliyo katika maeneo ya tambarare ya Mkoa wa Kilimanjaro, ukiweko ule mradi wa Mwanga mpaka kule Hedaru mpaka Mombo. Ni lini sasa Serikali itatupa muda muafaka wa kukamilika kwa miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Tunapozungumzia suala la maji, maji hayana mbadala, si kama wali, ukikosa wali eti utakula ugali. Kwa hiyo kuna haja kubwa sana ya kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati lazima kuwe na ufuatiliaji na usimamizi wa karibu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga katika kufuatilia na kusimamia miradi hii kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji kwa muda muafaka uliopangwa. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa uwezo wa Halmashauri unatofautiana na Halmashauri nyingine ni duni kabisa hazina kipato zikiwepo Halmashauri za Hai, Siha, Rombo na kwingineko; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kufanya top up ili nia yao njema ya kuwezesha wanawake na vijana ifanane Tanzania nzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la mama ni zuri, Halmashauri zingine pato lake ni dogo lakini kutokana na wazo hilo zuri ndiyo maana Serikali ina mifuko mingine ya ku-top up. Kuna Mfuko kutoka katika empowerment programu yetu ambayo inasaidia na tuna fedha nyingi sana hapa, takribani kuna Mifuko 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni wazo zuri lakini Serikali imeshachukua initiative tayari, Mifuko hiyo ipo, isipokuwa jamii yetu wakati mwingine hawana taarifa sahihi kuhusu mifuko hiyo. Ndiyo maana sasa wakati programu hii inaendeshwa hapa Dodoma takribani mwezi mmoja uliopita uwezeshaji huo umeshatolewa na tumewaelekeza sasa Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii waweze kushuka katika grassroot ili kuweza kuwaelimisha wananchi ni wapi watapata hizi fedha na uwezeshaji ili kujiinua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wazo zuri na Serikali hivi sasa inaendelea ku-top up isipokuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wafanye kazi yao sasa kuhakikisha jamii sasa inapata uelewa wa kutosha juu ya mifuko hii ili waweze kupata uwezeshaji wa kutosha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante; nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya ufafanuzi. Kwa kuwa tumeshuhudia kwenye luninga wakiteketeza vifaa hivi na wanaoingiza kupata hasara, Je, ni hatua gani zaidi zinazochukuliwa kwa wale wanaoingiza ili kukomesha hali hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vifaa bandia havitoki tu nje ya nchi, vingine vinatengenezwa humu humu nchini. Mimi naomba kujua ni hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kukomesha kabisa vifaa hivyo, vikiwemo viatilishi, pembejeo za kilimo, vipodozi vya kina mama, na hata vingine ambavyo si rahisi kutamka hapa hadharani? Naomba kujua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza nakiri na amekubali jibu kwamba kweli vile vifaa vinateketezwa na yeye mwenyewe ameona; lakini ni hatua gani zinachukuliwa sasa kwa wale ambao wameshikwa na hizo bidhaa bandia.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tunazo sheria nchini, yule anayeshi kwa na vifaa bandia ni kwamba anapata stahili kulingana na sheria. Wakati mwingine wanatozwa faini na pengine inaweza hata zaidi ya hiyo akapewa adhabu stahiki.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili amesema kwamba hivi vifaa bandia sio kwamba vinatoka nje ya nchi tu, kuna vingine vinatengenezwa humu ndani. Kwa mfano, kama vipodozi wapo watu wanachanganya vipodozi na wamewaathiri sana wale ambao wanatumia.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kufunga viwanda vile ambavyo havijasajiliwa na mara nyingi hivi vitu ambavyo vinafanywa ambavyo havipo katika viwango vinafanywa na viwanda bubu. Kwa hiyo, Serikali inafanya ukaguzi, kama tulivyojibu katika swali la msingi ili kuhakikisha kwamba hawa wote wanaofanya hivyo wanakamatwa na wanapewa adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria na viwanda vinavyojihusisha na hivyo tayari vinafungwa ili kuhakikisha kwamba suala hilo haliendelei. Vilevile pia nimeongea na Mheshimiwa Waziri akasema kwamba wanatarajia kuleta sheria itakayotoa adhabu kali zaidi hasa kwa hawa watu ambao wanatengeneza vitu bandia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri ametueleza kwamba takwimu za mwaka 2014 miaka minne nyuma zinaonesha kuwa vijana 65,614 hawakupata ajira. Naamini kabisa baada ya miaka hiyo idadi hiyo imeendelea kuongezeka. Swali la kwanza; je, ni nini hasa kinawachofanya wahitimu washindwe kuajiriwa au kujiajiri?
Mheshimiwa Spika, swali l a pili, ni hatua zipi mahususi zinazochukuliwa na Serikali kuwawezesha au kuwajengea wahitimu hao mazingira wezeshi ya kuajiriwa au kujiajiri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameulizia kuhusu ni kwa nini sasa watu hawa wanashindwa kupata fursa ya kuajiriwa au kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, jibu lake ni kwamba katika nchi yoyote duniani suala la ajira limekuwa ni suala ambalo limekuja na changamoto nyingi sana, kutokana na kwamba nafasi za ajira zinazozalishwa na idadi ya watu ambao wana uwezo wa kufanya kazi vinakosa uwiano. Kwa hiyo, kama Taifa tunaendelea kuwa na mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunakuja na mipango madhubuti ya kufanya nguvu kazi yetu hii kubwa iweze kupata nafasi ya kuajirika.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti ya mwaka 2014 ambayo wanaiita Integrated Labour Force Survey inasema takribani watu wa kuanzia miaka 15 na kuendelea ambayo ndiyo working age population, ambao wana uwezo wa kufanya kazi kila mwaka wanaojitokeza ni wengi zaidi kuliko nafasi za ajira.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika kujibu swali lake la pili, niseme tu kwamba kama Serikali tumeona kabisa suala la kwanza la kuweza kukabiliana na changamoto hii hasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu, tumekuja na utaratibu wa kwanza wa kuzindua mpango maalum wa mafunzo ya uanagenzi na mafunzo ya vitendo ambao Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua mwaka jana ambao unamfanya mhitimu yeyote wa Chuo Kikuu....

Mheshimiwa Spika, kwanza tumekuja na framework hiyo ambayo hivi sasa tutaanza kuwachukua wahitimu wa vyuo vikuu kwa kwenda kuwa-attach katika mashirika mbalimbali, kampuni mbalimbali, waende kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu, hilo ni eneo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, tumekuja na utaratibu wa kubadilisha mindset kwa mujibu wa sera ya ajira inasema ajira ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato. Kwa hiyo, tunawatoa sasa wale wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu kutoka kwenye kufikiria kuajiriwa moja kwa moja ofisini na kubadilisha mtazamo kwenda kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji na biashara.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeandaa mazingira wezeshi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili vijana hao waweze kupata fursa na kupata mitaji na maeneo ya kufanyia shughuli zao. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena. Nianze kwa kumshukuru sana Naibu Waziri aliyepata muda wa kuitembelea barabara hiyo na Mheshimiwa Anne Kilango mnamo tarehe 8 Agosti. Mheshimiwa Anne Kilango anatuma salamu na anasema ahsante sana na nadhani aliiona kazi kubwa hiyo. Pamoja na shukurani hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ni adui mkubwa sana wa barabara ya lami na baada ya mvua kila wakati vile vipande vya lami vilivyojengwa katika eneo husika zikiwemo zile kilomita tatu Kihurio, kilomita tano kisiwani, kilomita tano Ndungu zinaendelea kumomonyoka kila wakati. Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kufanya haraka kuunganisha vipande hivyo ili lami ile iliyowahi isifagiliwe kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wote wa Kilimanjaro ilionekana wazi kwamba katika vikao vya RCC Same iko nyuma sana kwenye miundombinu ya barabara na barabara iliyotajwa hapa ni barabara muhimu ambayo pia ina Mbuga za Wanyama. Je, ni lini sasa, baada ya upembuzi yakinifu Serikali iko tayari kupeleka hela hiyo mapema ili zoezi hili lifanyike kwa sababu hii ni ahadi ya Waheshimiwa wagombea Marais toka Awamu ya Nne na Awamu ya Tano? Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo anafanya kazi zake kutetea Mkoa wa Kilimanjaro na wananchi wake kwa ujumla. Swali lake la kwanza ni kweli kwamba mvua au maji ni adui mkubwa sana wa barabara zetu na hasa zile za lami na hata zile ambazo si za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la awali, kwamba baada ya usanifu wa kina kukamilika na kujua gharama tutatangaza tena tutampata mkandarasi, tukishampata mkandarasi hatua za haraka za kutafuta pesa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, sisi tunasubiri taarifa za kitaalam, zitakapokuwa tayari na kujua gharama hatutachukua muda mrefu kama Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na tutaendelea kuilinda hiyo barabara kwa pesa tulioitenga kwenye bajeti ya mwaka huu. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na niseme wazi nimeyaelewa sana majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na majibu hayo mazuri na ufafanuzi huo, wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro wamehamasika sana kwenye SACCOS na sio vikundi vya ambao wameshapata maradhi tayari, bali ni vikundi vya akinamama ambao wanafundishana mambo mengi ikiwemo ujasiriamali, scheme za elimu pamoja hiyo kujiunga na NHIF. Ni muda mrefu sasa toka mwaka jana wameandikiwa barua kusitisha zoezi hilo, lakini kwao imekuwa ni usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri haoni kwamba itakuwa sasa ni usumbufu wale akinamama kurudi kuanza upya, badala ya kuweka muendelezo kwamba walikuwepo kwenye NHIF na waendelee?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sina maelezezo kamili kuhusiana na hivi vikundi vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaviongelea, mimi nimuombe sana Mama Shally Raymond baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu tuonane anipe maelezo na mimi nimtume Meneja wangu wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro aende akavitembelee na kuvikagua vikundi, kwa sababu tunapozungumzia vikundi vya washirika na vikundi hivi vya SACCOS ni vikundi ambavyo na sisi tumekuwa tunavihamasisha vijiunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotaka tuweze kupata maelezo kidogo tuweze kubaini changamoto zilizopo na tuweze kuchukua hatua kwa haraka zaidi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Serikali na ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Moshi Vijijini ina skimu ya umwagiliaji inayoitwa Lower Moshi Irrigation ambayo ilifadhiliwa na Japan, lakini skimu hiyo sasa iko taabani kwa sababu ya upungufu wa maji na miundombinu mibovu na imesababisha kupungua sana kwa zao la mpunga. Ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kutuchimbia visima au mabwawa ili kuongeza maji ili skimu hiyo iweze kuwa endelevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ni wengi sana wanategemea mpunga kutoka eneo hilo la Lower Moshi, ni lini sasa Serikali itafanya jambo la dharura kutupelekea wataalam hao ili hali irudi kama ilivyokuwa siku za awali? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya maji. Lakini pia hata masuala ya umwagiliaji na hasa kwa eneo la Lower Moshi. Lakini katika hoja zake mbili naomba kumjibu kwamba ni kweli tunayo taarifa kwamba Lower Moshi Irrigation ilijengwa miaka ya nyuma na Serikali ya Japan na ilifanya kazi kubwa sana kule Moshi ya kuzalisha mazao ya mpunga. Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni kweli maji yamepungua na ndiyo maana huu mpango kabambe ambao tunaukamilisha tutahakikisha ama tunachimba visima na bahati nzuri Kilimanjaro kule chini ya ardhi maji ni mengi au tunajenga mabwawa ili kuvuna maji ili wananchi wale. Lakini pia miundombinu ya Lower Moshi pia kidogo imechakaa, tutahakikisha pia tunaiboresha ili wakulima wale waendelee kufaidi matunda ya kilimo.
Kuhusu suala la wataalam kama ambavyo nimejibu katika suala la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza suala la wataalamu Mheshimiwa Shally Raymond tunalifanyia kazi na tumeelekeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji itaajiri wataalam wa umwagiliaji kwa ajili ya kutengeneza scheme za umwagiliaji. Lakini baada ya kutengeneza kwa sababu utekelezaji wake utafanywa na Halmashauri tumeelekeza pia Halmashauri nao iajiri wataalamu wa umwagiliaji ili wakati wanapojenga wawe wanatoa taarifa jinsi miundombinu inavyobadilika ili tuweze kwenda vizuri.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu ya msingi Naibu Waziri amesema kwamba tatizo ni pia uelewa mdogo wa wananchi kuhusu kutunza mazingira. Kwa kuwa sasa Mlima Kilimanjaro ile theluji inaendelea kuyeyuka na mazingira yamekuwa kame muda wote lakini wanawake na vijana wa Kilimanjaro wapo tayari kuungana na Wizara hiyo katika kuboresha mazingira hayo. Ni lini sasa hii Wizara ya Mazingira itawezesha wanawake na vijana wale kiuchumi ili wapate miche waweze kuotesha miti kwenye mashamba yao kuzunguka mipaka na pia kwenye barabara inayoelekea Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la shemeji yangu Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika Mlima Kilimanjaro kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo maeneo mengi yameathirika ni pamoja na theluji ambayo imekuwa ikipamba ule mlima kule juu unakuwa ni kivutio katika masuala ya utalii. Pia tumeendelea kusisitiza kupitia Halmashauri za Hai, Rombo, Moshi Vijijini pamoja na Moshi Mjini kuhakikisha kwamba wanapanda na kuhifadhi miti. Hawa akina mama ambao amesema mimi nipo tayari kabisa kuja kwa hao akina mama japo hakuwasema ni wengi kiasi gani ili na mimi pengine niambatane na akina baba wengi kidogo kuja kuonana na hao akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Shally, baada ya Bunge hili, naye ni shahidi nilipokuwa Kilimanjaro nilimpa taarifa na kukupigia simu kwamba aje tushughulike na mazingira. Aliweza kuja na akanipa msaada ambao kwa kweli mpaka leo bado naukumbuka. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE.SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same, Kata ya Makanya yanapatikana madini ya gypsum, madini hayo Tanzania nzima yanapatikana Manyoni, Pindilo na Makanya kwenyewe. Hata hivyo, miundombinu ya hapa ni mibaya sana na wachimbaji hao ni wachimbaji wakiwemo akinamama na akinababa. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wachimbaji hao wakati tunapoelekea kwenye Sera ya Viwanda na Biashara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kama Serikali tunazidi kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo tunawawezesha kimiundombinu, kimitaji na kuwasaidia kiteknolojia ili waweze kuchimba na waweze kujipatia kipato chao. Ni kweli kabisa hayo madini ya gypsum ni madini ambayo ni muhimu na yahahitajika katika soko la dunia na baadhi ya nchi za jirani wanahitaji madini hayo na kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali pamoja na kupitisha sheria ile ya mwaka jana ya Marekebisho ya Sheria ya Madini tumetaka kwamba madini yote ya gypsum tuweze kuwasaidia wachimbaji waweze kuchimba na kuya-process ili kusudi wapeleke kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi pamoja na Wizara nyingine tunasaidiana kupeleka miundombinu kwa maana ya maji, umeme, barabara kwa wachimbaji wadogo dogo ili waweze kuchimba vizuri na kwa gharama ndogo ili waweze kupata faida. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa alisambaza mitamba bora katika maeneo yote ambayo yanafanya zero grazing. Kwa kuwa ni muda mrefu sasa na cross breeding imeshafifisha mazao yale ni lini sasa Serikali itaweza kuboresha na kutawanya mitamba bora, vifaranga bora vya kienyeji na vifaranga bora vya samaki katika maeneo ya wafugaji kama Kilimanjaro ambapo kuna wanawake wengi sana ambao ni wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza swali ni zuri sana juu ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasambaza mitamba bora kwa wafugaji hasa akina mama wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa zima. Progamu hii Serikali tunayo kupitia mashamba yetu ya mifugo yaliyosamba nchi nzima tunafanya kazi hii. Kwa mfano tu ni kwamba hivi karibuni kupitia dirisha letu la sekta binafsi tumewawezesha Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoani Tanga yaani TBCU, wamekopeshwa pesa na Benki yetu ya Kilimo ili waweze kununua mitamba bora 300 ambapo kufikia tarehe 30 ya mwezi huu mitamba ile itaenda kusambazwa kwa wafugaji wote wa Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tuko tayari kuhakikisha kwamba na wafugaji wengine kote nchini wanapata fursa hii. Shime wafugaji wote wa ng’ombe wa maziwa, kuku hata wale wa samaki wajiunge katika vikundi ili waweze kutumia fursa hii inayopatikana kupitia dirisha letu la ukopeshaji la Benki ya Kilimo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Wauguzi wanaofanya kazi katika Wodi za Wagonjwa wa Akili, wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi sana kwa sababu wagonjwa hao mara nyingi wako hyper:-

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwakatia Wauguzi hao bima ya maisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, matibabu ya afya ya akili ni taaluma na wataalam wetu hawa wamepata mafunzo mazuri tu ya jinsi gani ya kuweza kuwatibu wagonjwa hawa wenye matatizo ya afya ya akili katika hatua zile za awali ambazo sisi mara nyingi katika lugha ya kitaalaam tunaita acute phase, lakini vilevile katika hatua ya mwendelezo wa yale matibabu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba wataalam wetu wako vizuri na ndiyo maana hujawahi kusikia kwamba kuna muuguzi wala daktari amefariki au amepata kipigo kikubwa kutokana na kuhudumia wagonjwa hawa wa afya ya akili. Kwa hiyo, kwa sasa hatuna evidence ya kutosha ya kusema kwamba sasa watu wote ambao wanatoa huduma za afya kwa wagonjwa wa akili tuweze kuwakatia bima ya maisha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimeyapokea.

Swali la kwanza; kwa kuwa Benki ya Kilimo mpaka sasa haijaweza kuwa katika Mikoa yote na hizo benki nyingine alizozizungumzia kama NMB na alitaja benki mbili zote hizo ni Commercial na zinahitaji wewe unayekwenda kukopa lazima uwe na dhamana na wanawake wengi hawana nyumba wala hawana dhamana ambazo zinatambulika kibenki: Je, Serikali iko tayari ku-guarantee mikopo hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tatizo katika kilimo ni pamoja na mbegu bora na mara nyingi unakuta kwamba mbegu hizo ni ghari na pia siyo rahisi kumfikia mkulima. Ni lini sasa mbegu hizo zitagaiwa kwa wanawake hao kupitia katika Kata zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Shally Rymond anataka kujua kwamba kwa sababu benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa na kwamba hizi benki nyingine ni za kibiashara, anataka kujua mikakati ya Serikali kama iko tayari kudhamini mikopo hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali tupo tayari na tulishaanza na ndiyo maana kama alivyosema Benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa, ni kwa sababu hii ni Benki ya Maendeleo, ni benki ya kimkakati na lengo lake ni kuwasaidia wakulima kupitia madirisha mbalimbali ya Taasisi za Fedha. Moja, tulichokifanya, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tumedhamini mikopo yote ambayo inayotolewa na Benki ya NMB ili kwenda kwenye Sekta ya Kilimo hususan pamoja na akina mama.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba ni lini Serikali itatengeneza mazingira ya mbegu hizi zikapatikana katika ngazi za Kata ili wanawake wazipate kiurahisi?

Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba Serikali siku zote kwamba tuko tayari. Mbegu hizi kupitia Shirika letu la Mbegu (ASA) na Taasisi nyingine binafsi na mawakala mbalimbali, tumeweka mazingira mazuri kwamba mbegu hizi zinapatikana Tanzania kote, siyo kwa kwenye Kata tu, mpaka ngazi za vijiji kwa kuzingatia mahitaji. Kama kuna mahitaji maalum katika eneo unalotoka, baada ya Bunge hili tuone ili tuwaelekeze wenzetu wa ASA ili waweze kupeleka mbegu haraka iwezekanavyo ziwafikie wakulima.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa njema ni vyema zikawa na sauti, leo asubuhi kuanzia saa 12.00 TBC haikuwa na sauti kabisa na hakuna namba yoyote iliyokuwa inaonesha pale tupige kwa dharura wale ambao tuna ving’amuzi vya Azam TV.

Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini na wakati walipokuja kurudi kutupatia sauti saa 1:10 asubuhi hawaku- apologize?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hata mimi mwenyewe nimeona hiyo hitilafu ikitokea leo, lakini siyo leo tu imekuwa ikitokea mara kwa mara kwa sababu TBC, television yenu ya Taifa sasa hivi ipo katika programu ya mageuzi makubwa sana kiteknolojia ndiyo maana muonekano wa TBC sasa hivi ni bora kupita miaka iliyopita nyuma na naomba ndani ya mwezi mmoja mtaona hata background, nyuma ukiangalia TBC haitatofautiana sana na CNN. Kwa hiyo, kaa mkao wa kuangalia Television ya Taifa.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu yao mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; sasa hivi ni takribani miaka 53 toka tumepata uhuru na majiko haya yamekuwa yakitumika pamoja na athari zake. Je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha kampeni mahususi ya kutokomeza matumizi ya majiko ya mafiga matatu katika shule za sekondari, vyuo, primary na kote huko ili kuondoa athari hizo kama ilivyofanya kampeni ya kuboresha maabara na kuleta madawati kwa shule zote hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna makampuni binafsi ambayo yanasambaza gesi hizo za kupikia (liquid gas) na pia kwenye mitungi midogo ambayo ni affordable ikiwemo Mihan na Oryx. Sasa Serikali iko tayari kushirikiana na makampuni hayo ili kupunguza athari za moshi unaowaumiza sana akina mama walioko vijijini na kwingineko na bado hawajapata elimu ya matumizi ya majiko hayo kwamba wanaumia ili waweze kupatiwa majiko hayo kwa bei nafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa mama yangu Shally Raymond. Kwanza nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye eneo lake la Mkoa wa Kilimanjaro hususan kwa masuala ya wanawake na inadhihirisha kwa swali hili ambalo ameliuliza linalohusiana na masuala ya majiko ya mafiga matatu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza la nyongeza ameulizia kama Serikali ipo tayari kuanzisha kampeni ya kuondokana na majiko haya hususan katika shule za sekondari na msingi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tunatambua kwamba majiko haya ya mafiga matatu yana athari ya kimazingira na kiafya lakini kwa kuwa tumelitambua hilo, Serikali pia ina mpango wa usambazaji wa gesi asilia katika mikoa mbalimbali ambapo imeanza na mikoa saba ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga, Dodoma na Morogoro lakini sambamba na hilo, Serikali pia imekuwa iki-support makampuni yanayohusiana na gesi ya LPG.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa hatua hizi zinaendelea katika kuhakikisha kwamba kwanza gesi asilia inasambazwa katika maeneo mbalimbali ambayo ina bei nafuu, lakini pili kwa kushirikiana na makampuni yanayoingiza nchini LPG ili iweze kushusha bei, nina uhakika kwamba tutafikia hatua hiyo ya kupeleka nishati hii ambayo itatumika katika shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, pia kuna makampuni mbalimbali ambayo yanashirikiana katika suala zima la usambazaji wa nishati jadidifu katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, nitoe wito tu katika makampuni hayo kuendelea kuiunga mkono Serikali ili iweze kufikia hatua ya kutangaza hiyo kampeni na ni jambo jema. Namwomba yeye pamoja na Wabunge wote wa Viti Maalum, Wabunge wote na wananchi mbalimbali tuhamasishe utunzaji wa mazingira na utumiaji wa nishati mbadala hasa katika kupikia ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli yapo makampuni kama nane ambayo yanahusika na masuala ya uingizaji wa gesi ya LPG ikiwemo Oil Gas Tanzania Ltd, Taifa Gas, Mount Meru Gas lakini pamoja na hayo kuna Lake Gas, Oilcom na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nini Serikali imefanya? Tumeona kwa kuwa kiwango cha matumizi ya LPG kimeongezeka kutoka kwa mfano tani 90,000 mwaka 2016 mpaka tani 147,000 mwaka 2018. Kwa hiyo, ni wazi matumizi yameongezeka, kwa hiyo, tulichofanya, tunatafakari namna ambavyo gesi ya LPG inaweza ikaingizwa kwa mfumo wa uagizwaji wa pamoja. Tupo katika mazungumzo na wadau wa makampuni haya na taasisi mbalimbali ili kuwezesha kuweka mazingira wezeshi ambayo yataisaidia hata EWURA kuweza kupanga bei ambayo inaweza ikawasaidia watanzania kutumia gesi hii ili kulinda mazingira yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa makampuni ambayo yanaagiza; kwanza nawapongeza kwa uwekezaji wanaofanya, waendelee kujenga miundombinu katika mikoa mbalimbali ili hii gesi ya LPG iweze kuwafikia Watanzania wote. Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi ili kuwezesha huduma hii ipatikane kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naishukuru serikali kwa majibu mazuri, lakini pia naipongeza kwa kurejesha mali za ushirika mikononi kwa washirika wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu. Kwa kuwa elimu ya ushirika ni elimu ambayo inahitajika sana kwa wananchi na hasa tukizingatia ambavyo ushirika nchi hii umekuwa ukipata misukosuko hadi umefikia kutoka kwenye wizara mpaka hadi kwenda idara; na kwa kuwa nchi hii ina bahati sana kuwa na Chuo Kikuu cha Ushirikia pale Moshi, na wote washirika wanatakiwa kupata elimu.

Ni lini sasa serikali italeta muswada Bungeni kubadili mafunzo kwa wote wale ambao wanashiriki ushirika waende kwenye chuo kile kusomeshwa na kuelewa ushirika nini kama alivyoeleza Naibu Waziri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya elimu ya ushirika miongoni mwa viongozi wa ushirika vilevile na wanachama wa vyama vya ushikirika. Wakati tunapitia, na tutakapoleta sheria ambayo tunatarajia kuileta katika Bunge lango Tukufu. Wizara ya kilimo sasa hivi imeamua kuanzisha mkakati wa kutoa elimu ya ushirika kwa kukihusisha Chuo cha Ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita tumeanza na vyama vikuu vya ushirika, viongozi wote walikuwa hapa Dodoma, na sasa hivi watalaamu kutoka Chuo cha Ushirika Moshi wamekatiwa zones kwenda kutoa elimu katika vyama vya msingi vilivyopo katika wilaya zetu na mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nitumie nafasi hii kusisitiza ofisi za serikali za wilaya na mikoa zitoe ushirikiano kwa Warajis wa Mikoa na walimu walioletwa katika mikoa kwa ajili ya kutoa elimu kwa vyama vikuu na vya msingi vilivyopo katika wilaya zetu. Tumewekeana deadline kufika mwezi wa Aprili wataalamu hawa waliogawana katika zones sita watakuwa wamefika katika wilaya zote na mikoa yote kuanza kutoa elimu ya ushirika kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwanza kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutoa elimu bure ambayo imewezesha kila mtoto sasa atoke akasome na hakuna dadalea tena nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la msingi nimesisitiza elimu ya msingi kuwezesha wanafunzi kwenda kufanya kazi zao baada ya masomo kwa wale ambao hawataendelea. Naomba kuuliza maswali kwa Serikali, la kwanza, kwa kuwa wanafunzi hao tunaowaona barabarani na nyie mkiwa mashahidi wanatoka nyumbani alfajiri saa kumi na moja na kurudi nyumbani saa kumi na mbili hoi bin taabani, kwa maana muda mwingi wako shuleni na shuleni ndiko wanakoweza kufundishwa, kwa nini sasa katika elimu ya msingi walimu wasiwe na mtaala ambao watafufua zile bustani ndogondogo toka wakiwa wadogo wawe na interest ya kilimo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kipindi cha nyuma tulikuwepo na sekondari za mchepuo, tulikuwa na sekondari ya mchepuo wa kilimo, mchepuo wa biashara, mchepuo wa sayansikimu na kadhalika. Baada ya hayo yaliyotokea hapo katikati na michepuo ile kufutia, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kurejesha tena aina ile ya mitaala ili mwanafunzi akitoka pale pamoja na kulelewa nyumbani na wazazi, kulelewa shuleni, lakini taifa ka kesho liwe bora kama nyie mlio hapa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na umuhimu wa Serikali kurejesha bustani mashuleni, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sehemu kubwa wanafunzi bado wanapata fursa za kujifunza kilimo kidogo kidogo hasa maeneo ya vijijini lakini changamoto wote tunafahamu ni maeneo ya mjini ambapo ardhi ni changamoto kubwa. Ndiyo maana tunaendelea kusisitiza kwamba jamii, familia waisaidie Serikali nao waweze vilevile kutoa stadi hizo kwa vijana, kwa sababu lazima tuseme pia kwamba maisha ya kisasa yanahusika kwa kiasi kikubwa katika kuondoa ari na hamasa ya vijana kujihusisha na vitu kama hivyo. Wazazi wengi wanapenda watoto wao wakacheze na play station, kuangalia TV, video games kuliko kujifunza stadi za maisha. Ndiyo maana tunasema, ndiyo Serikali itaendelea siyo tu kuboresha mitaala lakini kuweka mazingira wezeshi ili wanafunzi waweze kupata hizo stadi za kazi lakini kama nilivyosema ni jukumu letu wote. Kwa hiyo, tunomba tusaidie ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kubadilisha mitaala ili turudi nyuma, naomba nichukue mawazo yake, siyo baya tutaendelea kuboresha mitaala yetu ili iweze kutoa elimu bora na yenye manufaa kwenye vijana wetu. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniona sambamba na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali wilayani Moshi Vijijini kuna shule ya viziwi ya Vona wamejitahidi kwa muda mrefu sana kupata ushirikiano na Serikali lakini imeshindikana. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kufuatana na mimi mpaka Vona ili aone ni jinsi gani Serikali itaisaidia shule hiyo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari sana kuambatana na mwalimu tukatembelee watoto wetu hao wazuri tukaone mazingira hayo na ni kuhakikishie Mheshimiwa Mbunge huo ushirikiano uliokosekana sasa utapatikana. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa benki hii ilikuwa na matawi Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, na kwa kuwa benki hii ilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 100 na familia hizo na wafanyakazi hao mpaka sasa hawajui hatma yao, familia hizo zinateseka kulipa ada, kulisha ndugu na kadhalika.

Je, ni lini sasa wafanyakazi hao watafahamishwa hatima yao kwa sababu pia hawawezi hata kwenda kuomba kazi mahali pengine popote?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye majibu ya msingi na majibu ya nyongeza ambayo nimemjibu Mheshimiwa Jaku Hashim, baada ya kuwa tumemaliza majadiliano na Benki Kuu ya Cyprus na kuingia sasa kwenye mchakato wa kuhakikisha kila mwenye haki yake anapata haki yake ni imani yangu na wafanyakazi hao wa iliyokuwa Benki ya FBME Limited watapata haki yao, nimesema wazi mwezi wa Septemba, baada ya Mahakama za nchini Cyprus kurejea kazini basi yote hayo yatajulikana na kila mmoja atapaa haki yake na kwa wafanyakazi kwa sababu waliajiriwa na Benki hii ambayo ilikuwa na Makao Mkuu hapa nchini, basi sheria zetu za kazi na ajira zitatumika ili kila mtumishi aweze kupata haki yake.(Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwenye awamu ya tatu nyumba za Serikali ziliuzwa na nyingi zilikuwa zile za Shanti Town kule Moshi, Oysterbay Dar es Salaam, Gangilonga na Wilolasi Iringa na hapa Kilimani Dodoma na kwingineko. Nyumba hizo zilikuwa ni za makazi na zilikuwa ni eneo tulivu sana zikiitwa uzunguni. Lakini nyumba hizo ndiyo zimegeuka sasa ni Bar, ni maeneo ya kuoshea magari kule Moshi Shanti town zinasumbua wananchi na watoto hawalali. Ni lini sasa Serikali italeta sheria hapa Bungeni kama zile sheria za awali hazifuatwi ili zikatazwe kabisa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli hii ni kero kubwa sana mpaka hivi leo asubuhi nilikuwa naongea na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo kwamba ukiangalia kuna jengo la sinema karibu ya Shule ya Sekondari ya Arusha Girls na Shule ya Sekondari nyingine katikati, inaonekana badala ya kuweka jengo la sinema la kawaida sasa imekuwa sehemu ya night club na mambo vuruguvurugu hata hivyo kuhatarisha hasa madhara makubwa kwa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Spika, lakini maeneo hayo uliyoyazungumza ni kweli mkakati wa Serikali nadhani sheria ipo isipokuwa ni enforcement ya hizi sheria tu ndiyo inatakiwa. Kikubwa zaidi niwaelekeze viongozi wetu katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ambao ni Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya palepale ninaimani wakizingatia vizuri eneo hili la kusema kuleta utulivu katika maeneo yao ninaamini kwamba jambo hili halitokuwa na mashaka. Kwa hiyo, niwaagize wakuu wa mikoa wote sasa waanze kufanya ufuatiliaji wa karibu kukomesha vitendo hivi vya hovyo vinavyotokea katika mazingira yetu ambao siyo jambo jema katika Taifa letu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante awali ya yote naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na juhudi zote ambazo zimeshafanyika na zinaendelea kufanyika. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina taasisi zake ambazo zinashughulikia matatizo yao ikiwemo mirembe hapa Dodoma na Lushoto na kituo kilichopo Lushoto. Lakini taasisi hizo zina mapungufu katika rasilimali watu, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuwezesha taasisi hizo ili wanapozidiwa na wagonjwa hao waweze kupatiwa matibabu hayo kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili , madawa ya kulevya yana urahibu na pia yanaleta msongo wa mawazo ambayo yanapelekea vijana hawa au wote waliotumia kuwa katika hali ngumu sana ya kimaisha hata pale wanapotoka nje ya vituo ambavyo walikwenda kwa rehab.

Sasa Serikali ina mpango gani kuwezesha Chuo chetu cha Ustawi wa Jamii Tanzania ili waweze kupata wataalam ambao watakuwa wanapita au wanasambazwa katika mikoa yote kwenda kuwashughulikia vijana hawa ambao wameshapata shida hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niungane na Watanzania wote lakini vilevile niungane na Waheshimiwa Wabunge wote na hasa Kamati ya UKIMWI na Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kuwashukuru wadau wote ambao wameshirikiana na Serikali katika kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa kwa kiasi kikubwa, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue hatua nyingine kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya dhati na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inaondokana na tatizo la dawa za kulevya nchini. Mapambano haya ambayo yameongozwa na mamlaka yamesaidia kwa sasa kwa mujibu wa takwimu na tafiti tulizozifanya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchi tumeweza kufanikiwa kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya nchini kwa asilimia 95, baada ya kufikia hatua hiyo sasa tunakabiliana na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza tunakabiliana na suala zima la harm reduction kuhakikisha tunawarejesha katika hali nzuri waraibu wote ambao walikubwa na matatizo hayo. Yapi ambayo ni mpango wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo tumelifanya Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mamlaka ni kufungua kituo kikubwa cha tiba hapa Dodoma katika eneo la Itega ili warahibu wote ambao wataonekena wanahitaji matunzo ya ziada kupitia nchi nzima waweze kufanikiwa hapo, lakini kupitia madirisha ya hospitali zetu za rufaa katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa, madirisha ambayo yanahudumia wagonjwa wa matatizo ya akili yatatumika pia kutoa tiba ya methadon ili kuwahudumia warahibu wote ambao watapatikana kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu tumegundua warahibu wakitoka kwenye urahibu wanatakiwa wapatiwe shughuli mbalimbali za kufanya ili wasahau shughuli ile ya utumiaji wa dawa za kulevya, lakini waende katika shughuli ambazo zitawaongezea kipato. Ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo programu ya kukuza ujuzi, sasa tunataka kuwachukua na warahibu wote waliotengemaa tuwafundishe ujuzi, waweze kujiajiri, waondokane na matumizi ya dawa za kulevya, wawe raia wema na wachangie uchumi na maendeleo ya Taifa lao na maendeleo yao wao wenyewe. Kwa hiyo, nalishukuru sana Bunge na Watanzania wote kwa kazi nzuri ya kupambana na dawa za klulevya nchini. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majibu ya Serikali yameeleza bayana kwamba uwiano wa mapato katika kila Halmashauri ni tofauti na hata wingi wa watu ni tofauti; na kwa kuwa shida hii ya mikopo ya akinamama bado inaonekana ni kubwa; je, ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kuongeza asilimia ya mikopo kwa akinamama kutoka asilimia nne kwenda asilimia 10? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna uwiano tofauti wa mapato ya ndani ya Halmashauri, lakini hoja ya kuongeza kiwango cha ukopeshaji kutoka asilimia 10 kwenda juu zaidi ni jambo ambalo linahitaji kufanyiwa tathmini na kuona uwezekano wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majukumu haya ya asilimia 10, ikumbukwe pia mapato ya Halmashauri yanahitajika pia kuboresha miundombinu mbalimbali kama ujenzi wa vituo, ukarabati wa madarasa, ujenzi wa madarasa na huduma mbalimbali za wananchi. Kwa hiyo, ni jambo ambalo linahitaji pia kufanyiwa tathmini kuweza kuona faida zake na kuweza uona namna gani litaboresha huduma kwa ujumla katika halmashauri na katika vikundi hivi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme tunachukua wazo la Mheshimiwa Mbunge, tutalifanyia tafakuri na kuona njia bora zaidi ya kuboresha mfumo huu wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kipekee zaidi namshukuru Mungu kwa fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la msingi nimeuliza sehemu ya Serikali kama ruzuku. Nikiri kwamba nimepokea majibu ya Serikali, lakini naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana na mimi kwamba kuku wa kienyeji ndio mradi wa chini kabisa wa mwananchi yeyote kumudu Tanzania. Kila kaya ingepata kuku wa kienyeji tungeboresha hata chakula chetu sisi wenyewe na pia miradi kwa akinamama. Nimeambiwa hapa kwamba bei ya ruzuku ni shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= naomba niseme kwamba hiyo ndio bei ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali kama Serikali inatoa ruzuku gani ili kila kaya ipatiwe vifaranga hivi vya kienyeji ambavyo pia Serikali inatakiwa kutoa elimu, vifaa vya kulishia kuku hawa, vyakula vya kulishia ikiwemo starter, growers na pia dawa za kuku hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa swali hili nimekuwa nikiliuliza kwa awamu zote na sasa ni mara ya tatu niko Bungeni na jibu linajibu kwamba wako wanafanya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 15 ya utafiti kwa nchi ambayo ina Chuo cha Kilimo na Mifugo kama ilivyo SUA ni jambo ambalo halikubaliki. Swali, ni lini sasa Serikali itawezesha Wabunge wote Viti Maalum wakafanye miradi hii ya kuku wa kufuga kwenye mikoa yao? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini pia, nichukue nafasi hii kumshukuru sana mama yangu Mama Raymond kwa swali lake hili ambalo ameendelea kuliuliza kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba Serikali inatoa ruzuku gani, ili bei ya vifaranga hao tunaowauza angalao iwe chini kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hiyo bei ya shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= kuna ruzuku ndani yake, kwa sababu bei ya kifaranga ni shilingi 2,200. Sasa badala ya kuuzwa shilingi 2,200 Serikali kwa kushirikiana na kampuni nilizozitaja wanatoa ruzuku ili kwamba wahitaji wa vifaranga hawa wawapate kwa bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali pamoja na wadau wake tunatoa ruzuku. Sasa kama bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500 bado ni kubwa, hilo linaweza kuwa ni suala lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili kama ulivyoelekeza, basi tutaona ni kwa namna gani Wabunge wa Viti Maalum tuwapeleke Naliendele mahali ambapo tunafanya utafiti, ili waelezwe kitaalamu utafiti huo unachukua muda gani na kwamba utaisaidia nchi hii baada ya muda gani. Nadhani itakuwa ni suala la msingi sana, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kiu ya wananchi wa Makambko inafanana kabisa na kiu ya wananchi wa Same. Mradi umechukua muda mrefu na wakati wa kampeni alipopita Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati huo akiwa Naibu Waziri na sasa Waziri ndugu yetu Aweso, aje mara moja na yeye akasema yale yale maneno ya kutokushika kidevu lakini uchezee kitambi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, je, ni lini wananchi hao wa Same watasambaziwa maji?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana mama yangu Shally Raymond, amekuwa mpiganaji mkubwa sana hususan wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro; Moshi, Same na Mwanga waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, moja ya miradi ambayo ilikuwa imechezewa na wakandarasi wababaishaji ni Mradi wa Same – Mwanga na nilipata nafasi ya kwenda katika mradi ule, tumekwishawaondoa wakandarasi wale. Kubwa kazi hii tumeweza kuwapa wenzetu wa DAWASA kuona tunaweza kuifanya kwa force account, mwisho jana Katibu Mkuu alikuwepo huko, tumewekeza nguvu zetu kuhakikisha mpaka Desemba mradi ule uwe umekamilika na wananchi wale waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naipongeza Serikali kwa usambazaji wa maji ya Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo lililo katika ukanda huo linafanana kabisa na lile la Rombo na wanawake hawa wamezeeka sasa na kutoka upara kwa ajili ya kubeba maji:-

Ni lini sasa Wizara hii itaona ni wakati muafaka wa kusambaza maji ya Lake Chala kwa wale wananchi wa Rombo katika Mji ule wa Holili, Kata za Mahida, Ngoyoni na tambarare yote ya Rombo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maeneo ya Rombo Mheshimiwa Shally nimeshafika. Nimeacha maagizo ya kutosha na hata miradi ambayo ilikuwa inasuasua pale niliacha maagizo na utekelezaji unaendelea. Nikutoe hofu kwamba nitarudi tena kuhakikisha ule mradi mkubwa tunakwenda kuutekeleza

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yangu, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri pamoja na Mbunge Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wote mmekuwa mkifuatilia kwa jitihada kubwa. Hatutawaangusha. Sisi Wizara hatutakuwa kikwazo kwenu kwa sababu tunahitaji Wana-Rombo waweze na wao kupata ladha ya mageuzi makubwa ambayo yako ndani ya Wizara ya Maji. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza; kwa kuwa katika majibu yake ya msingi ameeleza wazi kwamba, Zimamoto huwa wanahusika sana katika kutuliza moto huo endapo majanga yanatokea. Hata hivyo, sio siri mara nyingi Jeshi hilo likifika linakuta magari hayana maji au wamechelewa sasa swali langu kwa Serikali, imejipangaje kuimarisha Jeshi hilo la Zimamoto ili wawe more efficient? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mioto hiyo ipo katika maeneo yetu tunayoishi au vijijini au kwenye kata zetu au mitaa yetu, lakini wananchi hao nikiweko mimi hatujapatiwa mafunzo ya kutosha kwenye kuzima mioto mikubwa kama hiyo. Wengi ni waathirika wa maeneo hayo na sitaki kurudi nyuma kukumbusha vilio vya Shauritanga na mashule mengine ambayo sitaki kutaja ikaja kuharibu sifa za shule hizo kupata wanafunzi. Je. Serikali itatoa lini mafunzo na kwa msisitizo kabisa ili watu hawa wapate elimu ya kusaidia kuzima mioto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nachukua fursa hii kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza, je, ni nini sasa Serikali inafanya au hatua ambazo inazichukua katika kuhakikisha kwamba inapunguza haya majanga ya moto ambayo yanajitokeza mara kwa mara? Ziko hatua nyingi ambazo kama Serikali tumezichukua ili kuona namna ambavyo tunapunguza, hatuwezi kuondosha moja kwa moja kwa sababu, mengine yanakuja, lakini tunapunguza. La kwanza, ni kuendelea kutoa elimu ama kuendelea kutoa taaluma kwa jamii, kwa sababu tunaamini jamii ikipata taaluma ama ikishiba taaluma ya kutosha majanga haya yatapungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunaendeleza ukaguzi wa majengo. Yapo majengo lazima tuyakague kwanza, yako majengo ya binafsi, yako majengo ya Serikali na yako majengo mengine. Kwa hiyo, tunakuwa tunafanya ukaguzi wa kwenye majengo ili kuona namna ambavyo tunawaelimisha namna ya kujikinga na haya majanga ya moto. Kikubwa zaidi tunao mpango na tumeshaanza, wa kuongeza visima vya dharura kitaalam tunaviita fire hydrants ili ikitokezea taharuki kama ya moto tuwe tuna maeneo ya kuweza kuchota maji na kuweza kuokoa maisha ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba Je. taaluma huko vijijini inafikaje? Tunavyo vitu vingi ambavyo tumeviandaa ambavyo vinaendelea kutoa taaluma, tunazo zile fire clubs ambazo ziko huko vijijini kwenye kata kwenye vijiji, kwenye shehia ambazo zinaendeleza kutoa taaluma kwa watu. Pia hivi karibuni nimewahi kusema sana tu, hivi karibuni tulifanya makubaliano na watu wale wa skauti ambao wengi wao ni wanafunzi na wako vijijini huko ambao wanafanya kazi kubwa ya kuendelea kutoa taaluma na kuelimisha jamii namna bora ya kujikinga na haya majanga. Vile vile kuelimisha jamii namna bora ya kutoa taarifa mapema kwa sababu changamoto inakuja kwenye utoaji wa taarifa. Nakushukuru sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri ametueleza kwamba kwa kipindi kifupi Serikali imewekeza pale takribani shilingi milioni 130 hivi kwa kuweka changarawe na kukarabati. Hata hivyo, kila baada ya ukarabati huo, mvua ikija inazoa changarawe zile na shida inabakia palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shida ambazo mwenye swali alishazizungumzia, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuanza kuweka lami katika kilometa chache chache ili shida hiyo ya kupoteza hela za Serikali iishe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba tunatuma wataalam wa TARURA pale wakafanye tathmini na baada ya tathmini hiyo watakayotuletea ndiyo tutafanya maamuzi ya kwamba sasa ijengwe hilo lami kama ambavyo nilimjibu mwenye swali la msingi, ama tuweke kiwango cha changarawe. Kitu ambacho nina uhakika nacho ni kwamba Serikali yetu ni makini na inasikia, lengo lake ni kuhakikisha barabara hiyo inapitika kwa wakati wote. Ahadi zetu siyo za uongo, tuko hapa kwa ajili ya kufanya kazi na tutahakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninakubaliana na aliyosema Naibu Waziri:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hizi ziko kwenye tambarare ya Kilimanjaro na mvua zote zinazonyesha mlimani zinashuka chini na kufagia changarawe yote iliyowekwa na TARURA. Na kwa kuwa, Barabara ya kutoka Hai kwenda Rundugai inaunganisha Barabara ya TPC ambayo ni ya lami.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kabisa kuanza barabara hiyo kwa lami kuliko kila wakati kumalizia hela za Serikali kwenye changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Kilimanjaro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza concern njema kabisa yenye nia njema. Niseme kwamba, tumelipokea ombi lako tutakwenda kufanya tathmini, ili tuingize katika mipango inayofuatia ya kuhakikisha tunaiondoa hiyo adha. Sio kila wakati tu hizi barabara zetu zikawa zinaondolewa na mvua kutokana na ile changamoto ya udongo au kifusi kwa hiyo, tunachokitaka sisi ni kuhakikisha kwamba, hizi barabara zinatengenezwa katika kiwango ambacho muda wote zitakuwa zinapitika.

Kwa hiyo, nilipokee hilo na tutaliingiza katika mpango, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Kwa kuwa, azma nzima ya kuondoa malaria siyo kupunguza bali ni kumaliza kabisa na Zanzibar wamefanikiwa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kugawa viuadudu hivyo wakati wa weekend zote za kufanya usafi majumbani kwa watu? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa Kamati ya Bunge ilipotembelea kwenye kiwanda hicho ilikuta bado Halmashauri nyingi hazijalipa mikopo ambayo walichukua. Ni lini sasa Serikali italipa ili kiwanda kile kiweze kuendelea vizuri. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE
NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunaelekea kwenye elimination na ndiyo mkakati wa Serikali na tumejipanga pamoja na wadau wetu kwamba tunapata fedha kwa ajili ya kufanya haya masuala ya kununua hivi viuadudu endelevu kwa ajili ya kuelekea kwenye elimination. Kwa mfano, Serikali ya Uswiss kwenye mpango wake wa Miaka Nne, 2021- 2024 kuna bilioni 4.4 zimetengwa ambapo bilioni 3.7 zitatumika kununua lita 284,810 kwa ajili ya utekelezaji huo. Sasa hivi tunaandika andiko ambalo litagharimu bilioni 294 kwenye Mwaka wa Fedha ujao tutalileta kwa wastani wa bilioni 59 kila mwaka tuweze kuwa na utaratibu wa kuwa tunapuliza haya mazalia mpaka kila kitu kiishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haya masuala ya Halmashauri kutokulipa kama nilivyosema kwenye jibu la msingi zimetengwa bilioni 2.7 tutasimamia walipe yale madeni lakini waendelee kuchukua na kupewa viuadudu vingine vya ziada. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika maeneo ambayo ameyasema Waziri kwamba yatajengewa scheme za uhakika, sikumsikia akitaja eneo la Ruvu Tambarare ya Same na Mto Ruvu huwa unaharibu sana eneo hilo. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea watu wale scheme ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mama Shally kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sijataja maeneo ya Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro; ni moja ya maeneo ambayo ni potential, kwa hiyo nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge waweze kutuvumilia, tumeunza huu mchakato na wenzetu wa Wizara ya Fedha na baada ya bajeti tutakuwa tuna kikao cha pamoja kwa ajili ya kuchagua maeneo yote ambayo yatakuwa ni ya miradi ya kielelezo katika umwagiliaji. Kwa hiyo, kila ambapo kuna potential na upande wa Kaskazini ni eneo muhimu sana kwetu kwa ajili ya uzalishaji. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini niseme wazi kwamba ninapotamka zao la kahawa aina ya Arabic katika Mkoa wa Kilimanjaro ni zao dume, ni zao ambalo linawapatia wanaume kipato. Wakati zao hili linapauka, wanaume wote sasa wanakwenda kuwabana akina mama kwenye zao lao la migomba, kwenye zao lao la mbogamboga, maharage na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi niliomba kuelezwa ni nini makubaliano ya kibiashara kati ya Serikali na wafanyabiashara wenye estates? Kwa sababu wale ndio wenye mashamba makubwa ya kahawa yanayozunguka wakulima wadogowadogo, estates hizo zikiwemo Tchibo, Machare, Kikafu na kadhalika.

Sasa ni lini Serikali itakubaliana na wakulima hao wa ma-estate wawasaidie hawa wakulima wadogo wadogo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; sina tatizo wala shida kabisa na uzalishaji wa miche kutoka TaCRI, lakini TaCRI ni kituo kimojawapo tu kinachozalisha miche pamoja na hiyo mingine aliyosema Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, je, Naibu Waziri yuko tayari sasa kufuatana na mimi mama yake, mguu kwa mguu twende katika mashamba ya wananchi tuone ambavyo zao hilo limepauka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mama Shally Raymond kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, suala la kufuatana na Mheshimiwa Mama Shally kwenda Mkoa wa Kilimanjaro, nimhakikishie niko tayari na tutapanga mimi na yeye kwa sababu nina wajibu kwake, ni mama yangu, kanilea miaka mitano nikiwa next kwake. Kwa hiyo, nitakwenda na nitazunguka naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuingia mikataba na estates, kwanza mikataba ni willingness kati ya mtoa huduma na anayeombwa kutoa huduma, kwa hiyo, sisi kama Serikali pale ambapo watu wako tayari kuingia mikataba na Taasisi yetu ya TaCRI kwa gharama nafuu ambayo siku ya mwisho haitaweza kumuumiza mkulima na conditions ambazo haziwezi kutuumiza, tuko tayari.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi tuna programu kubwa ya kuzalisha zaidi ya miche milioni 20 ya kahawa ambayo tutaigawa katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa hiyo, kwa wafanyabiashara ambao wako tayari kuingia kwa conditions ambazo ziko wazi na TaCRI, sisi wala hatuna tatizo juu ya hilo na ndiyo maana tumetaja baadhi ya taasisi ambazo tumeshaingia nazo makubaliano na baadhi ya wakulima ambao tutaingia nao makubaliano. Lakini tukienda pamoja kama tutakutana na hao wenye estates kubwa tutajadiliana namna ya kufanya.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniona. Nadhani mtakubaliana nami kwamba hizi barabara zinajengwa ili kuwapa watu urahisi wa maisha na kuwawezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Kalali – Nronga ni barabara ambayo ina kona nyingi, ni ndefu na ina milima, ni chini tu ya Mlima Kilimanjaro. Huko Nronga ndiyo kwenye kile kiwanda kikubwa cha maziwa ya mgando ambayo pia yananywewa hapa Dodoma. Swali langu kwa Wizara, ni lini sasa barabara hiyo itaanza kutengenezwa kidogokidogo kwa lami ili wamama wale waweze kuteremsha maziwa yao mpaka mjini na kufika huku Dodoma kwa ajili ya afya za watu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachokieleza Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara ya Kalali – Nronga ambayo inapita pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro kule chini imeharibika na tunahitaji fedha ya kutosha kuendelea kuijenga na ombi la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba wanahitaji sasa ianze kujengwa polepole kwa kiwango cha lami. Niseme tu kwamba kulingana na bajeti yetu kadri itakavyoongezeka, tutalipokea na tutaliweka katika mipango yetu ya baadaye kuhakikisha barabara hii inatengenezeka ili iweze kutoa huduma kwa urahisi kwa wananchi wa eneo husika. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Naibu Waziri amesema kwamba magunia ya katani ni ya adimu na yanahitajika sana; na kwa kuwa Mkoani Kilimanjaro ikiwemo Same, Mwanga ni wakulima wazuri wa katani lakini katani hiyo haipati namna ya kuhifadhiwa. Je, ni kwa nini Serikali haioni uharaka sasa kuzungumza na Mohamed Enterprise ambaye pia alimiliki mashamba hayo na akamiliki kile kiwanda ili waweze kutengeneza magunia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametutajia kuwa kuna viwanda nane na vitatu ndiyo vipo active lakini magunia haya yanatumika kwenye kuweka kahawa na Mkoa wa Kilimanjaro unalima kahawa na magunia wanaagiza kutoka nje. Je, Serikali inasema nini kuhusu hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema ni kweli kuna changamoto katika zao la mkonge kwa maana ya uchakataji. Sasa hivi Serikali inafanya juhudi kwanza kuongeza uzalishaji wa mkonge kwa maana ya malighafi, lakini pia kuhakikisha wazalishaji kwa maana ya wachakataji kwenye viwanda wanaendelea. Ndiyo maana tumesema moja ya kazi tunazozifanya ni kuwapa vivutio maalumu ikiwemo kuwalinda wazalishaji wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimueleze tu Mheshimiwa Shally Raymond kwamba huyu mwekezaji METL kwa maana Mohamed Enterprise tayari tumeshaanza kumpa baadhi ya mikataba kwa ajili ya kuzalisha vifungashio kwa maana ya magunia hayo katika zao la korosho. Hii ni mojawapo ya mipango ambayo tunadhani kwa sababu ana uhakika wa soko maana yake atapata mtaji na kuendelea kuzalisha kwenye viwanda hivyo vingine. Kiwanda cha Morogoro tayari kinazalisha tunaamini ataendelea kuzalisha pia katika kiwanda hicho cha Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, kama ambavyo nimesema tumeshaanza kuwapa vivutio maalum ikiwemo kuwapunguzia baadhi ya kodi kwa magunia haya ambayo yanaenda kufanya kazi kwenye vifungashio katika mazao ya kilimo. Kwa hiyo, ameanza na korosho tunaamini akiendelea kuzalisha sasa ataenda kwenye vifungashio kwa ajili ya zao la kahawa na mazao mengine. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Niseme nimepokea kwa furaha taarifa njema za magari 369 ya Polisi yatakayokuja. Swali langu. Je, katika magari hayo na ukizingatia kwamba, Kilimanjaro ina kata 169 na za mlimani ziko kama 110 zikiwemo kata za kule Siha, zikiwemo kata za Moshi Vijijini, Kata za Same, Kata za Mwanga na Kata za kule Rombo. Je, Serikali iko tayari sasa kupatia zile kata za mlimani ambazo haziko mjini magari hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, inasogezea wananchi huduma za ulinzi na usalama popote walipo. Moja miongoni mwa mambo ya msingi ambayo Serikali imeazimia kufanya kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunatengeneza vituo vya polisi, lakini pili kuwatafutia magari ya polisi ambayo yatakwenda kufanya doria katika maeneo mengi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, miongoni mwa maeneo ambayo yatafika haya magari tutajitahidi sana maeneo hayo ameyataja na huko kwenye mkoa wake magari haya yafike ili yaweze kutoa huduma. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jina langu ni Shally Josepha Raymond. Namshukuru Mungu sana kwa nafasi hii ya kupatiwa majibu haya mazuri na Serikali na nikuombe sasa niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amenieleza wazi, kuwa sasa hivi wakulima wanalima kutokana na wao wenyewe walivyoamua. Maamuzi hayo ni mazuri sana, lakini swali langu la kwanza la msingi; kwa kuwa Serikali imeamua sasa kila mazao yanayolimwa yawe zaidi kibiashara na nchi hii utakuta kwamba shida kubwa ni mbegu. Wakulima wako tayari kulima sasa hasa mazao ya mbogamboga na TAHA iko kazini masaa 24 kutoa msaada kwa wakulima wa mbogamboga. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa ruzuku kwa mazao hayo yakiwemo maparachichi, alizeti, mbogamboga zozote ambazo zinalimwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wanawake wa Kilimanjaro wako tayari kulima kwenye vihamba vyao na Taasisi za Kilimanjaro za elimu, yakiwemo mashule yana mashamba ambayo yanalimwa mara moja tu mahindi lakini mwaka wote mzima yanakuwa hayana kitu. Je, Serikali iko tayari sasa kuwasaidia wakulima hao na wakina mama wa Kilimanjaro, kulima maparachichi kwa wingi na Taasisi hizo kuchimbiwa mabwawa ili mashamba yale yasikae idle mwaka mzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza la kuhusu mbegu na ruzuku, ushauri huo tumeupokea tutakwenda kuufanyia kazi. Isipokuwa tu nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeendelea kukiimarisha Kituo chetu cha Utafiti wa Kilimo kwa maana ya (TARI). Hata ukiangalia bajeti imeendelea kuongezeka kwa sababu tunataka tufanye utafiti wa mbegu bora na zenye tija, ili mkulima wa Tanzania anufaike na kilimo kiwe cha tija.

Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba eneo hili pia tumelipa kipaumbele na tunaendelea kuhakikisha kwamba, TARI inajengewa uwezo ili kuja basi na tafiti ambazo zitatusaidia katika kilimo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili la kuwasaidia katika eneo la maparachichi hasa katika Taasisi zenye mashamba ambayo hayatumiki muda wote. Kama nilivyosema dhamira ya Serikali katika sekta ndogo hii ya kilimo cha mazao ya bustani na mbogamboga ni kuhakikisha tunaipeleka mbele parachichi. Kwanza kwenye kuongeza uzalishaji wetu kwa sababu hivi sasa kama nchi tunazalisha tani 48,000 kwa mwaka. Lakini lengo letu ni kwamba ifikapo mwaka, 2025 tufikishe tani 140,000 ya parachichi na tuongeze pia ku-export parachichi nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili hayo yote yaweze kutokea lazima tuweke mkazo mkubwa kuhakikisha kwamba tunasaidia kilimo hiki kukua. Hivyo, kwa wanawake wa Kilimanjaro ambao Mheshimiwa Mbunge amewaulizia swali hili, nataka tu nimwahidi ya kwamba, mimi niko tayari kuandaa ziara maalum katika maeneo yote ambayo umeyataja, tuyapitie kwa pamoja na vile vile tuimarishe vituo vyetu ili mpate miche ya kutosha, basi waweze kulima parachichi kwa sababu soko limeshakuwa kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante; zao la parachichi limekuweko nchini miaka nenda rudi na hata mikoa mingine likiwa ni chakula cha mbwa; hadi majuzi Serikali ilivyoanza kuona kwamba ni zao la kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatuambia nini sasa kujenga kiwanda cha kuchakata parachichi katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo maparachichi mazuri sana yako kule Rombo, Mwika, Kahe na kwingine ambapo yanatupwa tu hadi leo?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge kutoka Kilimanajro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzo azma ya Serikali ni kuhakikisha tunaongeza ujenzi wa viwanda kwa kuweka mazingira wezeshi. Kilimanjaro ni moja ya maeneo ambayo yanalima kwa wingi sana parachichi hivyo basi ombi letu ni kuhakikisha na sisi kama wawekezaji tuanze kutumia fursa, kwanza tunaweka miundombinu kupitia SIDO changamoto kubwa tuliyonayo ni collection centers kutunza katika vyumba vya ubaridi matunda yale ili yaweze kuchukuliwa na wenye viwanda. Kwa hiyo kupitia SIDO tutaenda kuhakikisha sasa kunakuwa na ofisi katika ngazi za Halmashauri au Wilaya ili kupunguza upotevu wa mavuno ya matunda yanaposubiriwa kupelekwa kwenye viwanda ambavyo tayari viko nakushukuru sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Waliokuwa Bungeni kabla yetu waliona busara kwamba asilimia 10 iende kwa wanawake, na baadae sasa makundi yale yalivyobainika ikaonekana ile ile asilimia 10 igawanywe kwa walemavu na vijana.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wanawake wakabaki na ile asilimia 10 na yale makundi mengine yakapatiwa asilimia yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mikopo ya Ujasiriamali iliyopitishwa na Bunge hili mwaka 2019 inaelekeza asilimia 10 kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Ni kweli kwamba tulianza na asilimia 10 kwa wanawake, lakini baada ya tathimini ya makundi yenye uhitaji wa kujengewa uwezo wa ujasiriamali yaliongezeka makundi ya vijana pamoja na makundi ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, makundi haya yote ni muhimu kujengewa uwezo katika jamii yetu. Hata hivyo tunachukua wazo lake kuendelea kufanya tathmini. Lakini kabla hatujafikia hatua hiyo tunafanya tathmini ya ufanisi, changamoto na mafanikio ya hii asilimia 10, kwa maana ya 4:4:2, na baada ya hapo tutaona maeneo gani tuboreshe ili tuweze ku-accommodate mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, ni lini sharti litawekwa sasa baada ya kutoa mwongozo huo (Building Regulations) ya majengo yote ya Serikali na hata ya watu binafsi kuwa na makingamaji ili waweze kuihifadhi hayo maji ya mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa maji hayo yanaharibu sana barabara wakati wa masika, hasa maeneo ya mlimani kama ya Wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro na yanaosha kabisa ile changarawe kwenye barabara: Ni lini mitaro mikubwa itajengwa katika barabara hizo ili iwe salama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya, lakini kubwa ambalo nataka nimhakikishie kupitia Wizara yetu ya maji tumeshatoa maelekezo na tumekubaliana kwamba mvua isiwe maafa, mvua iwe fursa. Kwa hiyo, moja ya mkakati wetu ni kuwa na ushirikiano na Wizara nyingine, kwa maana ya Wizara ya TAMISEMI. Mwananchi kule anapotaka kujenga nyumba yake, basi uwekwe utaratibu namna gani anaweza kuvuna maji ya mvua ili aweze kuondokana na matatizo ama changamoto ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kikubwa, Wizara ya Maji itashirikiana na Wizara nyingine ikiwemo Wizara ya TAMISEMI ili kuhakikisha wananchi wetu nyumba wanazojenga wanaweka miundombinu ya uvunaji wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, tumeona baadhi ya maeneo mbalimbali mvua inaponyesha inaleta maafa na kuleta athari mbalimbali. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais katika Wizara yetu ya Maji ni juu ya ujenzi wa mabwawa ili kuhakikisha kwamba tunavuna maji na kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kujenga miundombinu ili mvua zinaponyesha zisilete athari na badala yake iwe fursa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwakuwa tumekuwa tukishuhudia kila mara vitu hivyo au vipondozi hivyo, vyakula hivyo vikichomwa katika maghara na kwa gharama kubwa sana. Je, ni nani anayegharamia, kwasababu yule aliyenyang’anywa tayari ameshafilisika?
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond (Mb) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, kwamba kwa utaratibu anayetakiwa kugharamia uharibifu wa bidhaa hizo fake au vipodozi ni yule ambaye ameingiza, kwa maana ya aliyekiuka sheria ya uingizaji wa bidhaa, kwasababu zidhaa zote ambazo zinaruhusiwa kuuzwa katika masoko ya Tanzania hasa vipodozi lazima viwe vimesajiliwa. Kwamba, kama vimeingizwa kinyume na sheria hiyo yeye ndiye atakayetakiwa kulipa ili kuhakikisha anafidia gharama hizo za kuharibu vipodozi, nashukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa watoto njiti hao wana haki kabisa kama alivyosema mwenye kutujibia maswali kutoka Serikalini.

Ni kwa nini sasa basi Serikali hailipi gharama ya mtoto huyo wakati ambapo yuko hospitali na inalazimu wazazi kulipa mpaka milioni tano ikiwemo Muhimbili Hospital? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, niseme kwanza moja kwa mwaka huu kwenye bajeti zimetengwa bajeti ya kujenga vituo vya watoto njiti 100, lakini katika module yetu ya kawaida pamoja kwamba hakuna sheria ambayo imetunga kwamba unampa mama huyu likizo, lakini kuna utaratibu wa ndani umekuwa ukifanyika wakati wote ambapo mama akitokea namna hiyo madaktari wanaandika na anapewa huduma.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye suala lako la kusema kwamba Serikali kwa nini hawalipii, kwenye mfuko wa bima kweli kulikuwa na changamoto hiyo kwamba anatokea mtoto njiti, lakini anatakiwa afanyiwe hivyo, lakini inaandikwa na sasa hivi tumeshaondoa hiyo na watoto njiti wanalipiwa na watoto chini ya miaka mitano huwa wanalipiwa bure kama sio bima. Kwenye mfuko wa bima ndio kulikuwa na shida na hiyo shida imeshamalizwa sasa hivi, watoto njiti wanahudumiwa kama kawaida.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, mtoto njiti akizaliwa pale Muhimbili Hospital, anatakiwa alelewe mpaka afika ule umri ambao sasa mimba ingekuwa term na mtoto azaliwe na wengi wanakuwa na complication, lakini suala alilojibu Naibu Waziri mimi mwenyewe nilishafikisha kwake maombi ya kufadhili mtoto njiti ambaye alipitishwa kwangu na anaijua hiyo kesi ilifika mpaka shilingi milioni tano, ni watoto wa kawaida pamoja na hata wale waliokuwa kwenye insurance kama alivyoeleza yeye. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli alishanifikishia, mara nyingi kuna wenzetu kulikuwa na shida kweli Muhimbili, watoto wakipata matatizo si watoto tu hata wazee na watu wengine imekuwa kwamba wanakuwa-charged hasa hao watoto chini ya miaka mitano. Lakini tulipiga simu kwa sababu ni suala kisheria na halikuwa exempted na sasa tumeweka mfumo ambao hayo mambo hayajitokezi tena. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwa ajili ya mradi mmoja tu, mradi wa Mwanga, Same, Korogwe. Ukitaja Moshi, katika Mkoa wa Kilimanjaro, Mji mkubwa unaofuata ni Same, lakini takribani ni miaka kadhaa toka tumepata uhuru same haijawahi kupata maji safi na salama na wanaogea maji ya kununua mpaka leo.

Je, ni lini sasa ule mradi ambao tuliambiwa ungekamilika mwaka jana Septemba utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally, Mbunge Viti Maalum kutoka Kilimanjaro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Same -Mwanga ni mradi ambao ni mkubwa na umetumia fedha nyingi na sisi kama Wizara tumefuatilia kwa karibu na tayari kazi zinaendelea. Hivyo nipende kusema mradi huu utakamilika ndani ya wakati kwa namna ambavyo usanifu unaonesha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, nchi yetu inauza ngozi ya bilioni 10 tu kwa mwaka, lakini nchi hii-hii ndiyo ambayo imebarikiwa kuwa na mifugo mingi zaidi.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuongeza uzalishaji huo kwenye hivyo vituo viwili ambavyo vina-process mpaka mwisho ikiwepo Himo Tanneries na Moshi Leather Industries ili waweze kukidhi uhitaji wa nchi hii baada ya kufunguliwa kiwanda cha uzalishaji wa Kilimanjaro International Leather Industries?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ina mkakati gani kutoa elimu kwa wananchi wake ili kuhakikisha kwamba, mifugo inatoa ngozi bora na salama katika kipindi chote cha mwaka, ili kutoa ajira zaidi kwa vijana, wakiwemo vijana wa Kilimanjaro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli lengo letu kama Serikali ni kuona uzalishaji kwenye viwanda vyetu vya ndani unaongezeka, jitihada kadhaa zinafanywa, ikiwemo kuondoa changamoto na kuboresha mazingira ya biashara. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kushughulikia changamoto hizo ikiwa ni pamoja na ile ya kuondoa tozo na kodi mbalimbali zenye kuweka mkwamo wa upatikanaji wa malighafi na ushindani kwenye biashara. Baada ya kuyafanya haya tunayo imani kuwa, viwanda vyetu sasa vitapokea malighafi nyingi kutoka kwa wazalishaji ili kuviwezesha kufanyakazi yake kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; ni mkakati gani juu ya elimu ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga fedha, mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachunaji wa ngozi, lakini pia vilevile kununua vifaa kama computers, ili tuweze kuwa na record ya uzalishaji sahihi wa ngozi na hatimae kuwawezesha kuwaingiza katika masoko ikiwemo viwanda vyetu ambavyo vinazalisha hapa nchini, ambavyo tayari Mheshimiwa Shally Raymond ameshavitaja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kutibu maji ni gharama sana ili yafikie hatua ya kuwa maji safi na salama na wananchi kuyatumia kwa uhakika, lakini maji hayo hayo yanayogharamiwa sana na Mamlaka za Maji na RUWASA na wote ambao na Wizara pia yanatumika kuonyeshea magari, yanatumika kwenye kuzima moto, yanatumika kwenye kufrashi vyoo.

Je, ni lini sasa Serikali hii ya Tanzania italeta mpango mzuri wa kutumia maji safi na salama kwa ajili ya wananchi na maji hayo mengine kwa ajili ya takataka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Wizara ni kuhakikisha maji yote ambayo yanatumia gharama kubwa katika kuyatibu yaweze kutumika kwa matumizi sahihi ya majumbani na kwa kazi kama alizozitaja za uoshaji wa magari, tayari Wizara tuna mpango wa kuona kwamba raw water, maji ambayo bado hayajatibika yaweze kutumika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa mafuriko au maporomoko yale ya milimani kipindi cha mvua yanaleta maji yote tambarare na barabara inayotoka Same mpaka Bendera inakuwa haipitiki, wakati mwingine hasa kuanzia Ndungu mpaka Bendera kwenyewe.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuifanya na kuipasisha barabara hiyo ijengwe kwa lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua adha ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza na ndio maana katika mkakati wa Serikali tumeongeza fedha ili tuhakikishe kwamba hizi changamoto ambazo Wabunge wamekuwa wakizieleza humu ndani tunazitatua. Kwa hiyo, na hilo tumelipokea tutaliweka katika mipango yetu, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa nimekuwa nikifuatilia sana mbegu za parachichi katika Bunge hili kwa kipindi kirefu; na kwa kuwa leo nimeambiwa itazalishwa miche milioni 20 ya ruzuku; na kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo Siha, Hai, Rombo, Mwanga, Same na Moshi Vijijini, wote wanasubiri miche hiyo kwa hamu, naomba kujua, mgao wetu ni miche mingapi kwa hii awamu itakayotoka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa parachichi lina wadau wengi sana, naomba pia kufahamu, Serikali imejiunganishaje na wadau hao ili kupata soko la uhakika la parachichi ambalo ni perishable, kwa kipindi hicho ambacho kipo na kinachoendelea katika soko la nje na ndani? Naomba kufahamu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wakulima wa parachichi katika Mkoa wa Kilimanjaro. Katika maswali yake; la kwanza, mgao utatokana na mahitaji. Siyo rahisi sana kutamka hapa Bungeni kwamba nitapeleka miche mingapi katika Mkoa wa Kilimanjaro, lakini mahitaji yataamua miche mingapi iende katika Mkoa wa Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge avute Subira, tukianza zoezi hili, najua tutakuwa pamoja, yale mahitaji ya wakulima Mkoa wa Kilimanjaro tutahakikisha kwamba tunayafikia ili wakulima waendelee kulima kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu soko la uhakika, katika eneo ambalo tumelifanyia kazi la utafutaji wa masoko katika mazao yetu ni pamoja na parachichi. Hivi sasa tarehe 25 Novemba, 2011 Mamlaka ya Afya ya Mimea India walitupatia kibali cha kupeleka parachichi India, na hivi sasa wakulima wetu wameanza kupeleka parachichi India. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tunauza parachichi yetu Afrika ya Kusini. Pia tunakamilisha mazungumzo na China juu ya phytol-sanitary, tutaanza pia kupeleka parachichi yetu pia China. Hivi sasa ninavyozungumza, wazalishaji wetu wadogo wadogo wameshapata masoko ya uhakika kule Hispania na Marekani pia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya soko, soko la uhakika lipo, isipokuwa tulikuwa tuna changamoto moja ambayo tumeshai-address hivi sasa, ilikuwa ni lazima zao letu li-meet international standard, na hivi sasa tunayo maabara yetu pale Arusha ambayo tumeiboresha na hivi sasa tumepata accreditation ambayo ni namba 17025. Kwa hiyo, zao lolote ambalo linatoka Tanzania hivi sasa lina uhakika soko nje ya mipaka ya Tanzania. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, tatizo hili ni kubwa kiasi ambacho sasa hivi watu wanaishia Mirembe badala ya kutibiwa wakiwemo wanaume wanaopigwa na wake zao, wakiwepo watoto wa shule ambao wanajeruhiwa na wenzao au na walimu.

Je, ni lini hasa Serikali itaona ni wakati muafaka wa kutoa hata mafunzo hadharani wakati wanaposhughulikia hizo ajira?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu kama nilivyoeleza Wizara imejipanga kuhakikisha tunatoa elimu kwa wananchi wote hasa wale ambao wanakuja katika sehemu zetu husika wana matatizo ya saikolojia basi tunawapa elimu na tumejipanga kwamba tutakapopa wafanyakazi wengi basi elimu hiyo tutaitoa kwa kila mikoa na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata elimu hii ili kuondokana na matatizo ya saikolojia na kuondokana na msongo wa mawazo. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo lililo kwenye milima ya Iringa linafanana kabisa na tatizo lililoko tambarare ya Mlima wa Kilimanjaro kwa ajili ya mabadiliko ya tabia nchi. Je, Serikali itaungana lini na wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro, ambao wako tayari sana kurejesha uoto huo kwa kuotesha miti katika vihamba vyao, hususani miti ya matunda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS - MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lake ni kweli tunajua kwamba wanawake ama vikundi mbalimbali wakiwemo wanawake, wanaimarisha sana suala la mazingira kwa upandaji miti, pamoja na na miti ya matunda. Serikali inaahidi kutoa motisha kwa wale ambao watafanya vizuri kwenye kampeni yetu kapambe ambayo itamalizika tarehe 30 Juni.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wengi wanaochukua mikopo hiyo ni pamoja na kinamama ambao wanakuwa na vikundi vyao vya vikoba, lakini hela zao huwa zinazunguka kwenye makasiki na wakati mwingine kasiki linaibiwa.

Ni lini sasa Serikali itazungumza na mabenki ili waweze kuongezewa angalau asilimia moja ya kuweka kwenye account zao kuendesha viofisi vidogo dogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba akina mama na vikundi vingine na hususani akina mama wanakopa lakini pia wana shughuli za vikoba, na kuna risk hizo za mara nyingine kupoteza fedha kwa njia mbalimbali. Nimepokea wazo lake, tumepokea kama Serikali tutalifanyia tathmini kuona namna ya kuongea na benki ili tuone njia sahihi ambayo inaweza kufanyika kunusuru changamoto.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kutokana na majibu ya msingi ya swali hilo, Mheshimiwa Waziri ameendelea kusisisitiza kwamba mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi; na kwa kuwa hiyo dhana ya vikundi imekuwa ni mwiba sana kwa wale akina mama wa Kilimanjaro wanaotaka kuchukua mikopo hususan wale ambao wako katika ujasiriamali.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kurekebisha kipengele hicho ili mikopo hiyo itolewe kwa mtu mmoja mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuipitia sheria na kanuni ya mikopo ya asilimia kumi. Katika kupitia kanuni hii tayari tumeshaanza kufanya tathmini kwa kina ili kuona maeneo gani yanahitaji kuboreshwa zaidi likiwemo suala la kuona uwezekano wa mtu mmoja kupata mkopo badala ya vikundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya tathmini hiyo, tutafanya maamuzi na kuona utaratibu sasa utakuwa wa aina gani. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa mikopo hiyo kutokuwa na riba ni kivutio kikubwa sana kwa wale ambao hawana uwezo; na wakati huo huo wanawake wana vikoba: Je, Serikali inaonaje sasa kama wale wa vikoba watapatiwa mikopo hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sheria ya mikopo ya asilimia kumi imeeleza kwamba wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanaweza kukopeshwa wakijiunga kwenye vikundi vyao na mkopo huo hauna riba. Kwa hiyo, kama wanawake walio kwenye vikoba ni sehemu ya kikundi cha wajasiriamali bila kujali kwamba wapo kwenye vikoba au la, wataweza kukopeshwa fedha hizo kwa utaratibu huo na kufanya shughuli zao ili kujiletea maendeleo, ahsante. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wengi wanalalamikia sana bili kubwa za maji pale ambapo hata hawatumii maji nikiwemo mimi, ilhali hatupo hapa Dodoma naletewa bili kubwa. Ni lini sasa Wizara ya maji italepa prepaid meters kwa wengi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, prepaid meters tunaendelea kufunga maeneo mbalimbali. Kwa hiyo naomba niseme tu Mheshimiwa Mbunge, tuendelee kuwasiliana, hata wewe ukihitaji leo unaweza ukafungiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile bili kubwa hizi za maji Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote naomba niseme kwamba, tuangalie miundombinu yetu. Wakati fulani ni wewe mhusika peke yako ndiye unaepata bili kubwa kwa sababu, labda mita yako hapo nje inapitisha hewa au kuna tatizo la uvujaji. Kwa hiyo hizi bili kubwa naomba tutoe taarifa kwa mafundi wetu, ili tuweze kuzidhibiti.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu ya msingi ameitaja Boloti ambayo iko Siha na Ikuini ambayo iko Rombo tu; lakini kwenye swali langu niliuliza tambarare yote ya Mkoa wa Kilimanjaro. Sasa, ni lini wataweza kujenga mabwawa hayo Undugai katika Wilaya ya Hai, Arusha chini kule Chekereni Wilaya ya Moshi Vijijini na Kahe na kule Mwanga ikiweko na Ruvu kule Same?

Mhehimiwa Spika, swali la pili; ni lini mabwawa hayo yanayojengwa na yanayotarajiwa kukarabatiwa yatatumika kufundishia wananchi kutumia drip irrigation ambayo ni umwagiliaji wa matone ili uweze kuwa na tija kwa mazao ambayo yatakuwa yameoteshwa wakati wa ukame?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha maeneo yote yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa tuweze kuyafanyia kazi ili wananchi wetu waweze kulima mwaka mzima, ni muondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti yetu ambayo tutakuja kuisoma hapa tumeitengea eneo hili fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunapitia maeneo yote ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro katika maeneo ambayo ameyataja.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, teknolojia ya umwagiliaji wa matone ni kati ya teknolojia ambayo inatumika katika maeneo mengi sana hivi sasa nchini, na sisi kama Wizara ya Kilimo tunaiunga mkono. Isipokuwa tu katika Mabwawa ambayo ameyatamka teknolojia hii huwa inaendana na aina ya mazao yanayolimwa. Kwa hiyo kama mazao yanayolimwa yatakuwa yanahitaji teknolojia hii tumeshaanza, na ukienda katika Bwawa letu la Chinangali hapa Dodoma tayari kuna umwagiliaji wa matone katika zao la Mzabibu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Polisi wote nchini wanapitia Shule ya Polisi Moshi inayojulikana kama CCP, shule hiyo ni chakavu, mbovu, barabara hazipitiki na wakija wageni wanapitishwa kwenye geti kubwa na sio hili la Moshi Sekondari. Je, ni lini sasa Serikali itakarabati chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, nimekitembelea Chuo cha Polisi Moshi na kubaini uchakavu anaousema na kupitia ziara yangu tulikubaliana na uongozi wa Manispaa ya Moshi kupitia Mamlaka ya Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa sababu chuo hiki kipo kwenye himaya yake waanze kutenga fedha. Nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara kuu inayoingia tayari ukarabati umefanyika na tutaendelea kufanya ukarabati huo kwenye barabara zote nyingine zilizopo kwenye chuo hicho, nashukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Denmark kuna daraja linalounganisha Odense na Sealand na lilichukua muda mfupi sana kujengwa.

Je, Serikali inatueleza nini katika kupeleka mtu kama mwenye swali lake Mwantumu Dau Haji kwenda kulishuhudia ili tufupishe hayo maneno ya mazungumzo yalifanyika, yalifanyika kwa muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazungumzo yalifanyika Mwezi Machi mwaka huu na huu ni mwezi Aprili. Kwa hiyo, kwa mradi mkubwa kama huu na daraja ambalo linaunganisha linategemewa liunganishe Bara na Zanzibar yako mambo mengi sana ambayo yatafanyika. Moja ya eneo ambalo tunafahamu ni Denmark lakini hata China wana madaraja mengi marefu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla Serikali haijaanza kutekeleza lazima watajiridhisha kwa mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na teknolojia mbalimbali ambazo zimetumika katika nchi nyingine ambazo wana madaraja marefu kama haya. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Gereza la Karanga lililopo Mkoani Kilimanjaro ni katika yale magereza ya awali sana Tanzania. Miundombinu yake ni chakavu na hasa nyumba za wafanyakazi. Je, ni lini Serikali itatupa kipaumbele kukarabati gereza hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Karanga tunatambua ni chakavu na ni la muda mrefu, lakini ni gereza ambalo angalau lina miradi ya maana ikiwemo hiki Kiwanda cha Viatu. Jambo moja ambalo namuahidi Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba kupitia mapato yao ya ndani ikiwemo ya uuzaji wa viatu, waanze ukarabati lakini ngazi ya Serikali Kuu wataenda kutenga fedha kwa ajili ya kukrabati magereza makongwe ikiwemo Gereza la Karanga kadri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa mafanikio makubwa ya kilimo Israel ni yale ya Kibbutz Farms na vijana wa kitanzania waliofanikiwa nadhani hayo ndiyo pia wanaenda kujifunza: Je, Serikali iko tayari sasa kutumia vijana hao kuwarejesha katika maeneo yao ya vijijini kwa sababu Watanzania wengi na karibu wote ni wakulima wadogo wadogo ili wanufaike?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama Shally Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi na maswali aliyouliza Mheshimiwa Cosato, namna ya kuwatumia vijana hawa ni lazima tuwe na mfumo wa ugharamiaji kwa sababu huwezi kutaraji kumpeleka kijana kijijini ukamwambie akatoe elimu bila kuwa na mfumo wa ugharamiaji.

Mheshimiwa Spika, tumepokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge na wadau wengi wa sekta ya kilimo namna ya kuwatumia vijana walioenda Israel, walioenda nje lakini wapo vijana ambao wamesoma katika vyuo vyetu, wamesoma kilimo na wana utaalam wa kilimo cha kisasa, lakini bado wapo mtaani. Kwa hiyo, kama Wizara, tunapoenda kupitia mapitio ya sheria ambayo tutaileta ndani ya Bunge lako tukufu ya Irrigation and Extension Services, tuta-incorporate component ya vijana ambao wana elimu ya extension namna ambavyo watatumika na namna gani tutakuwa na mfumo mzuri wa ugharamiaji wa huduma zao.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio cha maji safi na salama Tanzania ni kama wimbo wa Taifa na wanaoteseka zaidi ni wanawake. Sasa hivi tunavyoongea ni masika na maji yanapotea na hakuna kinachoendelea kutoka Serikalini.

Je, ni lini sasa Serikali itatumia kuvuna maji haya ya mvua kuwaponya wanawake wa Makanya, Hedaru, Hundugai, Ngoyoni na Holili kule Kilimanjaro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni tabia ya maji ya mvua kupotea, lakini sasa hivi Wizara tumejipanga kujenga mabwawa maeneo yote ambayo yamekuwa na mafuriko na maji yanapotea kuelekea baharini. Tutachimba mabwawa Mheshimiwa Mbunge na tayari mitambo tunayo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu fedha nyingi kutumika kuleta mitambo mikubwa mitano ya kuchimbia mabwawa.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu spika, swali la kwanza. Kwa kuwa maji chini ya ardhi ni Pamoja na chemchem zinazofumuka wakati wa masika na kupotea wakati wa kiangazi hasa mkoani Kilimanjaro;

Je, Serikali inazitambua na kuziwekea udhibiti chemchem hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa utafiti wa Chuo Kikuu cha SUA kimebaini kuwa maji chini ya ardhi yanapungua sana lakini Serikali haijaweza kudhibiti maji ya mvua ya kila msimu na kila mwaka yanayotiririka na kutuharibia barabara. Serikali ina mpango gani sasa wa kufanya project ambayo itaweza kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, chemchem zote za Mkoa wa Kilimanjaro ni chemchem ambazo zina manufaa makubwa katika kuongeza maji katika miradi yetu inayoenda kwa wananchi. Hivyo tunailinda na kuidhibiti na tunaitambua vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu maji chini ya ardhi hupungua na sasa maji yanapotea. Hapa tumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hasssan, tuna mitambo mitano ya kuchimba mabwawa na lengo la kuchimba mabwawa haya ni kuhakikisha maji yote ya mvua tuweze kuyatunza kwa ajili ya mhitaji wakati wa kiangazi. Tunataka kuonesha kwamba mvua ambazo Mwenyezi Mungu anatupatia siyo laana bali ni baraka na yanakwenda kutumika vizuri.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kati ya waliopata sifa ni pamoja na wanawake na kaya nyinginezo za Mkoa wa Kilimanjaro ambao walipewa sasa ajira za muda, lakini baada ya kufanya ajira hizo vizuri hawajalipwa kwa vipindi viwili sasa.

Je, ni lini, Serikali itatoa malipo hayo ili malalamiko yaondoke katika mioyo yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyomgeza la Mheshimiwa Shally Raymond kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni taarifa na nimeisikia sasa kutoka kwake kwamba Mkoa wa Kilimanjarpo kuna wale ambao waliofanya kazi za TASAF za miradi ya kipindi maalumu na kwamba bado hawajalipwa basi acha tukalifanyie kazi halafu tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa kuna smoke detecters ambao ndio utaaalamu wa kisasa wa kujua kama moto unakuja. Kwa nini Serikali haioni ni muhimu chombo hicho kuwekwa katika kila jengo la shule au taasisi inayojengwa ili waweze kupata alert?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond hili la smoke detectors. Kama nilivyokuwa nimeshazungumza hapo awali tutashikiana kwa karibu na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kuona sasa ni namna gani tunaweza kuhakikisha majengo yote ya shule zetu yanakuwa ya smoke detectors hasa zile shule za bweni ambazo zina wanafunzi wanaolala pale muda wote.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Manispaa ya Moshi, barabara inayotoka YMCA kwenda KCMC ni barabara ambayo ina msongamano mkubwa sana. Kuna Chuo cha Ushirika, kuna Chuo cha CCP Moshi na kuna Chuo Kikuu cha Katoliki, lakini kwenda pale hospitali kwenyewe watu wanaoenda kuona wagonjwa wanachelewa na wakati mwingine pia wanapata matatizo; bajaji zimo humo humo, bodaboda zimo humo humo, vi-hiace na hata magari binafsi; kutokana na majibu ya msingi, kwamba vikao vifanyike na ni matakwa ya sheria, vyote vimeshafanyika: ni lini Serikali itaona umuhimu na udharura wa kubadilisha barabara hiyo kutoka TARURA kwenda TANROADS? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya YMCA kwenda KCMC katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi. Tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuona hatua zipi ambazo wamezifikia katika kwenda kupandisha hadhi barabara hii kuwa barabara ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba haya ni matakwa ya kisheria, na yakishapita kutoka kwenye vikao hivi vyote na vikipitishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa ambaye ni Mkuu wa Mkoa, sasa yanakwenda kwenye mamlaka ya Waziri wa Ujenzi ambaye ndiye mwenye dhamana ya barabara. Kwa hiyo, Serikali inalichukua na tutakaa na wenzetu wa barabara kuona imefikia wapi?
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali inaendelea na maboresho na VICOBA ni vikundia ambavyo wananchi ususani wanawake wa Kilimanjaro wameshamiri sana; ni kwa nini VICOBA visiusishwe sasa katika mikopo hii ya asilimia 10?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa nikisema awali maboresho haya yanafanyika kwanza ni kutokana na maagizo aliyoyatoa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya kuangalia upya utoaji wa mikopo hii kwa vikundi. Kwa hiyo, naamini katika timu ambayo inafanya kazi watapitia pia hili la VICOBA kuona uwezekano au upi ni urahisi kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa waboreshaji wakubwa wa mazingira ni wanawake wakiwemo wanawake wa Kilimanjaro wnaaouzunguka mlima; na kwa kuwa hawa watu wanaotoa CSR wankwenda zaidi kwenye miradi mikubwa wakiacha kugawa miche na kuhakikisha kuwa miche ile inatunzwa na kuweza kufikia katika hali ya kurudisha uoto wa asili. Je, ni lini sasa taasisi hizo ikiwemo TFS wataweza kushirikiana na wanawake wa Kilimanjaro ambao wana nia sana ya kuboresha mazingira hayo kutokana na jambo alilolifanya Mheshimiwa Rais la Royal Tour kugawa miche ya matunda na miche ya kuboresha mazingira na kurejesha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira maeneo hayo hasa yanayozunguka Mlima wa Kilimanjaro. Uharibifu ambao unasababishwa na shughuli za kibinadamu na hapa tunataka tuchukue fursa hii tutoe maelekezo tuwaambie wananchi, tuwashauri sana, waache kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo haya zikiwemo za ufugaji na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutajitahidi tupeleke fedha kwa Mkoa huu wa Kilimanjaro, hasa kwa akinamama, lengo na madhumuni ikiwa ni kuweza kurejesha ile hali katika ule Mlima Kilimanjaro. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali sasa itapeleka vifaranga bora vya mbuzi, kuku na ng’ombe ili kuboresha mikopo hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweza kuona ni namna gani tunapata mbegu bora kwa ajili ya kupeleka kwenye vikundi hivi ili waweze kufanya ufugaji ambao una tija na ambao utawaongezea kipato vilevile.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa tatizo la maji kutiririka hovyo wakati wa mvua ni tatizo kubwa sana kwa maeneo ambayo yako kwenye milima ukiwemo Mkoa wa Kilimanjaro.

Ni lini sasa Serikali italeta muswada hapa Bungeni ili nyumba zote zinazojengwa ziwekewe vikinga maji na kutumia maji yale ya mvua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuleta muswada niseme nimelipokea, lakini sisi kama Wizara tayari tumejipanga na kuona kwamba mabwawa tutakayoyachimba tutaweka kwenye maeneo yote ambayo ni korofi kwa sasa, na tumshukuru Mheshimiwa Rais ameweza kutupatia vitendea kazi, tumeshanunua seti tano kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa.

Mheshimiwa Spika, lakini hilo aliloliongea Mheshimiwa Mbunge naomba niseme nimelipokea.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa ukosefu wa nyumba unasababisha walimu na hao wafanyakazi wa Serikali kuchelewa, lakini katika vijiji vingine kuna nyumba za wananchi ambazo hawaishi huwa wanakuja tu wakati wa sikukuu ikiwemo Christmas. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuziagiza Halmashauri ziingie mkataba na hawa watu wenye ma–bungalow huko vijijini ili waweze kupatia wafanyakazi nyumba za kuishi?

Swali la pili, upungufu ulioandikwa ni mkubwa sana, hata tungejenga kwa miaka 10 bado hatutatosheleza. Serikali inasema nini sasa kuongeza hela zaidi katika mfuko huo wa ujenzi ili hii kazi iende kwa uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza kuhusu Serikali ina mpango gani kuingia mkataba. Hili ni jukumu ambalo linaachiwa Halmashauri wenyewe kuweza kuingia mikataba na wenye nyumba ambazo hazitumiki na naamini hili Mheshimiwa Mbunge amelileta kwa sababu kule Mkoa wa Kilimanjaro wengi wanakuwa wapo katika Mikoa mingine na wanarudi kipindi cha mwisho wa mwaka. Kwa hiyo, tutakaa na kuona ni namna gani tunaweza tukazungumza na Halmashauri ambazo zina mazingira kama ya Mkoa wa Kilimanjaro, kuona ni namna gani wanaweza kuingia mikataba hii kwa ajili ya kuweza kuwaweka watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la hela ya ujenzi. Ni wajibu wa Halmashauri kuanza kuweka fedha, kutenga fedha katika mapato yao ya ndani kwa ajili aya ujenzi wa nyumba za watumishi wa kada ya elimu na afya. Serikali Kuu tayari imeshachukua jukumu kubwa sana, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa maboma, madarasa katika Halmashauri hizo na ukamilishaji wa maboma lakini vilevile katika afya ameshapeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.

Kwa hiyo, ni wajibu wao sasa kuanza kuunga mkono jitihada zile za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukamilisha maboma yaliyojengwa na wananchi kwa ajili ya nyumba za watumishi wa umma. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa uhitaji wa kuongeza thamani kwenye zao la korosho Mtwara unafanana kabisa na uhitaji wa kuongeza thamani kwenye zao la ndizi Kilimanjaro.

Je Serikali ina mpango gani kuwasaidia wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro mashine hizo za SIDO ili waweze kuongeza thamani kwenye zao la ndizi kwa kutengeneza clips na vitu vingine vinavyotokana na ndizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha ya kwamba mazao yetu ya kilimo yanachakatwa ili kuongeza thamani na vilevile kuongeza kipato kwa wazalishaji au wakulima wetu na tupo katika mkakati wa pamoja sisi pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha kwamba tunatumia taasisi zetu za ndani kama CAMARTEC, TIRDO na SIDO kutengeneza mashine ndogo ndogo na ambazo zitakuwa zina bei rahisi ili kuweza kuwafikia wakulima wengi zaidi kuongeza thamani ya mazao haya.

Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakulima pia wa ndizi wa Mkoa wa Kilimanjaro hasa akina mama na wenyewe pia tutawaweka na kuhakikisha kwamba na wenyewe wanafanya kazi ya uchakataji.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ili mwanafunzi afikie kupata division zero au four ni pamoja na ufatiiaji hafifu wa masomo yake. Wazazi wanatakiwa wahudhurie mikutano ya shule wanapoitwa nakadhalika: Ni lini sasa Serikali italeta Muswada hapa Bungeni kuhakikisha kwamba tunatunga sheria ya wazazi kufatilia masomo ya watoto wao mashuleni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu ni suala ambalo linahusu pande karibu tatu; upande wa kwanza ni wanafunzi yeye mwenyewe, upande wa pili ni wa wazazi kama Mheshimiwa Mbunge alivyoshauri na upande wa tatu ni wa walimu au Serikali kwa ujumla. Kwa vile amezungumza hapa suala la kuleta Muswada Bungeni wa kuangalia namna gani tunaweza kuwabana wazazi ili waweze kufuatilia maendeleo ya watoto wao katika elimu, naomba tuubebe ushauri huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba katika shule zetu kunakuwa na Kamati mbalimbali za kufuatilia maendeleo ya shule pamoja na wanafunzi kwa ujumla. Kwa hiyo, nadhani Kamati zile sasa zinatekeleza wajibu huu, lakini kwa vile ni wazo au ushauri ambao ameutoa, acha tuuchukue kama Serikali twende tukafanye tathmini, halafu kama tukiona kama kuna umuhimu wa kuleta Muswada huo, tuweze kuleta hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nashukuru kwa majibu haya mazuri; lakini kwa kuwa Serikali imeelemewa sana na jambo hili, ina mpango gani sasa au ina vivutio gani kwa sekta binafsi kuzalisha mbegu hizo za malisho pamoja na kuzalisha madume bora ya mbegu? (Makofi)

Swali la pili kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa mitamba bora, mbuzi mapacha, pamoja na vifaranga vya kuku vilivyoboreshwa kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanasubiri kwa muda mrefu hata wakati wa kampeni walimuomba Waziri Mkuu alipokuja kufungua kampeni ya Mkoa wa Kilimanjaro. Serikali iko tayari sasa kutoa vitu hivyo kwa ruzuku kwa wanawake hao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni juu ya vivutio tulivyoviweka; Serikali imejipanga mara baada ya kupokea maoni ya wadau juu ya kuweza kuweka vivutio kwenye upande wa uzalishaji wa mbegu za malisho, lakini na upande wa uzalishaji wa ng’ombe bora kwa maana ya madume ya mbegu kwa kuondoa baadhi ya tozo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ng’ombe bora Serikali imeondoa tozo ya import ya ng’ombe wanaotoka nje ya nchi tulikuwa tukilipisha shilingi 10,000 kwa ajili ya ng’ombe kumkagua na sasa Wizara imependekeza kuondolewa kwa tozo hii na bado tupo katika mazungumzo ndani ya Serikali ya tozo kwa upande wa mbegu za kutoka nje za malisho ili kusudi na zenyewe ikiwezekana ziweze kuondolewa ile tozo na wawekezaji waweze kuweza kufanya kazi hii kwa ufasaha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni juu ya jambo linalohusu Mkoa wa Kilimanjaro na akinamama kupata ng’ombe wa ruzuku. Katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imejipanga kuyaimarisha mashamba ya uzalishaji wa ng’ombe bora na ili tuweze kuwasambaza kwa wafugaji kote nchini. Nina imani kuwa akinamama wa Mkoa wa Kilimanjaro watakuwa ni miongoni mwa wanufaika, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na nakuomba kwa ruhusa ya kiti chako nitangulize shukrani kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa tamko lake la jana kwamba sasa mradi wa Mwanga, Same, Korogwe unakwenda kuanza tumepata usingizi watu wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo naomba nimuulize sasa Naibu Waziri; je, ni lini mradi mkubwa wa chanzo cha maji cha Ziwa Chala ambao utawapatia maji wananchi wa Holili, Ngoyoni, Chala na wengine tambarare ya Rombo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mradi wa Ziwa Chala unatarajiwa sana kuona kwamba unakwenda kutatua tatizo la maji, lakini Ziwa Chala tukitaka kutumia mradi ule maana yake ni mradi wa ku-pump, ni mradi ambao utaleta gharama kubwa na matokeo yake wananchi watalipa huduma kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, lakini tayari kuna miradi mitatu pale ya gravity inayoendelea kujengwa katika Mji wa Rombo na tunatarajia miradi hii ikija kukamilika kwa sababu ni miradi ya miserereko itakuwa ni miradi rafiki kwa wananchi na tatizo la maji linakwenda kukoma.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la kukatika umeme katika Manispaa ya Morogoro linafanana na tatizo lililopo katika Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro, hususan Kata ya Uru Kusini; ni lini sasa TANESCO itarekebisha tatizo hilo kabisa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tatizo la kukatika kwa umeme halipo tu Morogoro na Kilimanjaro, limekuwepo kwa Tanzania nzima. Serikali tumechukua hatua. Mwanzoni tulianza na upungufu wa Megawati 421 wastani hapo. Mpaka kufikia leo tumefanikiwa kupunguza upungufu kwa wastani wa Megawati 218. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, nilieleza hapa kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere tumefikia 94.01% na tumeshaanza majaribio. Pia, nimesema hapa tumeongeza uzalishaji kwenye visima vetu vya Songo Songo pamoja na Madiba ili kuweza kuongeza gesi ili tuweze kupunguza changamoto hii ya upatikanaji wa umeme. Tayari tunafanya matengenezo kwenye mitambo yetu yote ili kuboresha hali. Nina uhakika Waheshimiwa mmeona hali ya upatikanaji wa umeme imeanza kutengemaa.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie tutaendelea kufanya kazi hii nzuri ili kuhakikisha tunaiondoa nchi katika changamoto ya umeme, ahsante. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; bei ya maji pale Same sasa hivi ni kati ya shilingi 4,000 mpaka shilingi 5,000 kwa ndoo na adha hii inawakumba sana wanawake wa Same; ni lini sasa Mradi wa Mwanga – Same – Mombo utakamilika ili waweze kupunguza adha hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa mama yangu kuhusu Mradi wa Same – Mwanga – Korogwe; mradi huu kwa sasa hivi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ameweza kutuwezesha na wakandarasi wote kwenye kila kipengele wapo kazini. Kufikia mwezi Juni, 2024 tunatarajia mradi uwe umekwisha. Mpaka leo hii mradi upo asilimia 86.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; bei ya maji pale Same sasa hivi ni kati ya shilingi 4,000 mpaka shilingi 5,000 kwa ndoo na adha hii inawakumba sana wanawake wa Same; ni lini sasa Mradi wa Mwanga – Same – Mombo utakamilika ili waweze kupunguza adha hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa mama yangu kuhusu Mradi wa Same – Mwanga – Korogwe; mradi huu kwa sasa hivi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ameweza kutuwezesha na wakandarasi wote kwenye kila kipengele wapo kazini. Kufikia mwezi Juni, 2024 tunatarajia mradi uwe umekwisha. Mpaka leo hii mradi upo asilimia 86.