Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Ally Mtolea (46 total)

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kutokana na majibu haya yasiyokuwa na tija kwa wananchi wa Temeke yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatushawishi sasa kwenda kuidai haki yetu Mahakamani, naomba niulize maswali matatu ya nyongeza. (Kicheko)
Samahani naomba niulize maswali mawili ya nyongeza moja lina sehemu (a) na (b).
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtolea nadhani utakuwa umeziangalia Kanuni kuhusu maswali, ukiuliza swali moja lenye (a) na (b) kwa sababu ni nyongeza utakuwa umeshauliza hayo mawili, tafadhali.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilwa ilijengwa chini yakiwango, na Serikali ilimwamulu mkandarasi airudie kwa gharama zake mwenyewe. Ujenzi huo wa chini ya kiwango ni pamoja na mitaro iliyo pembezoni mwa barabara hiyo, mvua zilizonyesha tarehe 14 na tarehe 15 Disemba, mitaro hiyo ilishindwa kuyabeba maji vizuri na ikapasuka ikapeleka maji kwenye makazi ya watu maeneo ya mtaa wa Kizinga katika Kata ya Azimio pale Mtongani na nyumba 40 ziliharibika vibaya.
Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuwatuma wataalam wake kwenda kufanya tathmini na kuwalipa wananchi walioathirika na tukio hilo?
Swali la pili, hivi tunavyozungumza hivi sasa kuna taharuki kubwa imezuka kwa wakazi wanaokaa pembezoni mwa barabara ya Davis Corner - Jet Rumo ambapo wananchi waliokuwa pembezoni mwa barabara hiyo wanawekewa alama za „X‟ kwamba wavunje nyumba zao ambao kimsingi zimejengwa kihalali kwa sababu wakati wa upanuzi wa barabara walilipwa mita 15 na Serikali ilikuwa haina pesa ya kuwalipa mita nyingine 15 kukamilisha mita 30 kila upande.
Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa yuko tayari sasa kuamulu zoezi linaloendelea katika Kata ya Vituka, Buza, Makangarawe na Tandika hivi sasa, lisimame mpaka yeye na mimi tutakapokwenda kukaa na wananchi na kujua nini tatizo la pale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, maswali uliyoyauliza yanahusu masuala ya fidia ambayo inashughulikiwa chini ya sheria maalum chini ya Wizara ya Ardhi. Tumekubaliana kwamba tukutane wote sisi na Wizara ya Ardhi, tulichunguze hilo suala ulilolileta ili hatimaye tukupe majibu sahihi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Upatikanaji wa gesi na mafuta katika nchi hii ulileta matumaini kwa Watanzania kwamba sasa watapata fursa ya kupata ajira katika shughuli hizo. Kwa kuwa Serikali inakiri kabisa kwamba ni muhimu hii kozi kuwa inatolewa hapa nchini ili Watanzania waweze kupata uwezo wa kuajirika au kupata ajira katika sekta ya mafuta na gesi na mpaka leo Serikali ndiyo bado iko kwenye mchakato wa kuanzisha kozi hii. Nataka kufahamu, Serikali kwa nini ilianzisha uchimbaji wa gesi na utafutaji wa mafuta hapa nchini wakati bado haijajenga uwezo kwa Watanzania kutumia fursa hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika sheria zinazosimamia shughuli za bandari inazitaka meli zikishaweka gati kwenye bandari zetu theluthi mbili ya wafanyakazi wanaoenda kutoa huduma kwenye zile meli wawe ni Watanzania. Kwa sasa meli zote zinazoingia zinakuja na wafanyakazi wake na hivyo kuwakosesha ajira Watanzania wanaotegemea ajira kwenye bandari zetu. Je, ni lini Wizara hii itaivunja hii Bodi ya SUMATRA na kuiunda tena upya ili iweze kusimamia majukumu yake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea na kwa kweli Watanzania wote wanafahamu kwamba Chuo cha Bandari tunachokiongelea pamoja na DMI ni hatua ya nyongeza. Mafunzo kwa ajili ya utaalam wa masuala ya mafuta na gesi yalishaanza kutolewa muda mrefu katika Chuo cha Dodoma pamoja na Chuo cha Madini na wahitimu wameshaanza kutoka. Kwa hiyo, nachomueleza Mheshimiwa Mbunge ni kwamba katika chuo hiki tunaongeza mafunzo. Kitu ambacho ni kipya katika chuo hiki ni yale mafunzo ya usalama ambayo yatafanyika katika Chuo cha DMI na wenzetu wa Norway wametuahidi kutuimarisha katika eneo hili ili tuwe nchi ya pili kwa Afrika kutoa mafunzo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, hata sisi tumepata malalamiko kutoka kwa Mabaharia na kwa kweli tumehangaika nao sana na nadhani wanatuelewa kwamba tafsiri ya ile sheria unayoongelea haiko hivyo kama inavyotafsiriwa. Tunaomba tuipitie hiyo sheria upya pamoja na Sheria ya SUMATRA ili tukipate kile tunachokitaka yaani sisi, Mabaharia na Waheshimiwa Wabunge.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba limekuwa likiwapa notice wafanyabiashara eneo la Keko Furniture ambao wanafanya biashara chini ya majengo ya National Housing kwamba wahame wakatafute sehemu nyingine ya kufanyia biashara ili shirika izikarabati nyumba zile na iweze kuwapangisha wapangaji wengine. Wafanya biashara hawa ni zaidi ya 300 na shirika linataka liwafukuze ili lipangishe watu wasiozidi 50. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari sasa kulishauri Shirika la Nyumba wawe flexible badala ya kuwafukuza hawa watu 300, wavunje zile nyumba wajenge mabanda ambayo yatawa-accommodate hawa wafanyabiashara ili wawe wapangaji wao? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na mchezo mchafu, watu ambao hawakai kwenye nyumba zile lakini ndiyo wanaonekana wapangaji wa nyumba za National Housing, kisha wao wanawapangisha watu wengine kwa gharama kubwa. Je, shirika litakuwa tayari sasa kufanya uhakiki wa kuhakikisha kwamba anayekaa kwenye nyumba ndiye ana mkataba na National Housing ili kuzifanya nyumba hizo zisiwe za gharama kubwa na zitumike na watu wenye mahitaji nazo? Ahsante.
Naibu Spika, ni kweli hayo anayoyasema ya wafanyabiashara wa Keko Furniture na hata juzi alikuja mmoja kuonesha vifaa vya hospitali hapa, nawajua, lakini kwa ufupi ningemshauri, mimi na yeye na baadhi yao tukipata fursa tukutane maana majibu yanaweza kuwa marefu hapa, tuone namna ya kutekeleza kwa pamoja ili kuwawezesha hawa vijana wafanyabiashara 500 waendelee kujiajiri katika eneo hilo. Sasa tutoke nje tuzungumze zaidi badala ya kukujibu hapa maana nitajibu majibu marefu sana, tutafute muafaka wa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ni kweli shirika linafanya uhakiki. Hivi sasa ukiomba nyumba ya Shirika la Nyumba hupati, yule aliyepo anampa funguo mwenzake na hata wafanyabiashara wa maduka makubwa kama Samora na kadhalika wengine wanakula kodi za mtu wa tatu. Hilo nalijua na nimeshatoa maelekezo, kama unavyosema Mheshimiwa Mtolea, kwa National Housing wafanye uhakiki ili wachukue kodi kwa mpangaji na isitokee mtu mwingine kuchukua kilemba cha mpangaji. Kwa hiyo, hilo tunalifanyia kazi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, akina mama lishe na akina baba lishe pale Temeke wanakaribia kufilisika toka tatizo la bei ya sukari kupanda lilivyoanza! Hawakushawishika kupandisha bei ya vyakula wanavyouza kwa sababu walitegemea tatizo hili la sukari litakuwa ni la muda mfupi, lakini mpaka leo hawajui ni lini tatizo hili litakwisha. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna umuhimu wa yeye kila siku kutoa status update ya sukari hapa nchini kila tunapoingia hapa Bungeni?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru akinamama lishe kwa kuwa watumishi wa Mungu. Hawana hulka ya kutafuta faida wanatoa huduma, watafurahi duniani na mbinguni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la msingi ni kwamba Mwijage nitoe status ya sukari, kila siku nakubali kabla hatujaahirisha mchana huu nitatoa status ya mgao wa sukari kwa nchi nzima.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwa pensioners ambao hawalipwi kupitia Hazina moja kwa moja kwamba, vile viwango vipya vya malipo hawajaanza kulipwa mpaka hii leo. Na haya malalmiko yamekuwa ni ya muda mrefu sana. Naomba commitment ya Serikali ni lini wastaafu hawa wataanza kulipwa viwango vyao vipya pamoja na arrears zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu ni kwamba watumishi wote ambao wanalipwa kupitia Hazina walianza kulipwa fedha zao za nyongeza tangu mwaka jana mwezi wa saba, 2015. Kwa mifuko ambayo haijaanza kulipa kama ambavyo nilisema mwanzo, nyongeza hizi, sasa hivi Bodi za Mifuko hii zinamalizia kufanya maamuzi, ili waweze kuanza kulipa nyongeza ambayo ni ya 50,000 kama ilivyotangazwa na Serikali.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo lililopo la msongamano wa mahabusu kwenye Gereza la Tabora linafanana kabisa na tatizo lililopo kwenye Gereza la Keko lililopo Jimbo la Temeke katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Mbaya zaidi ni kwamba, miundombinu ya majitaka ndani ya gereza imekufa na hivyo sasa vinyesi kutoka gerezani vinatiririka mpaka mtaani na kuhatarisha afya za mahabusu na wakazi wa maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maelezo Mheshimiwa Waziri amesema bilioni tatu iliyotengwa kwa ajili ya kukarabati magereza haijalitaja Gereza hili la Keko. Sasa nataka kujua, Mheshimiwa Waziri anawaambia nini wakazi wa maeneo ya Keko wanaolizunguka gereza lakini na mahabusu waliopo ndani ya Gereza la Keko, waendelee kukaa katika mazingira hayo mpaka lini?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshapokea concern ya Mheshimiwa Mbunge na kwa kuwa katika ratiba ya ziara zangu natarajia kuzungukia na magereza yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam, nitafika na Gereza la Keko na baada ya hapo kama Wizara tutakaa kuangalia hali hiyo na namna ya kulifanyia kazi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto za mahospitalini zimekuwa nyingi na moja kati ya kero kubwa ambayo wananchi wanaipigia kelele ni kile kitendo ambacho mwananchi akiuguza mgonjwa wake na hatimaye akapoteza maisha haruhusiwi kuchukua mwili wa marehemu mpaka alipe gharama za matibabu ambazo kimsingi hazikumsaidia mgonjwa wake mpaka amefariki dunia. Kitendo hiki kinatengeneza taswira mbaya kwa wananchi kuonesha kwamba Serikali haijali utu na haithamini utu wa wananchi wake.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba endapo mwananchi atafiwa na mgojwa wake lile deni la matibabu asamehewe ili familia ijikite tu katika kushughulikia suala la mazishi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba kwanza nakanusha kwamba Serikali haithamini utu wa Watanzania, hapana Serikali ina thamini sana utu wa Watanzania wote na ndio maana ikaweka utaratibu mzuri sana wa kutoa huduma za afya kwa watu wote hata wasiojiweza. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana ambazo zinawapa usawa wa huduma tena bure kwa kuwahudumia takribani asilimia 67 ya wagonjwa wote hapa nchini bure bila gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa wale wachache ambao wanatengeneza hiyo asilimia 33 ya wanaochangia huduma za afya, kama itajitokeza kwa bahati mbaya baada ya kuhudumiwa akafariki halafu Sheikh Mtolea unasema sasa pale ndio utu wake unaanza, sio sahihi. Utu wa Mtanzania upo akiwa anaumwa, akiwa anahudumiwa kwenye hospitali na hata ikatokea bahati mbaya umauti ukamkuta utu uko pale pale. Lakini gharama za mtu ambaye amekwishahudumiwa iwe alipona ama kwa bahati mbaya alipoteza maisha; zipo pale pale ni lazima ziwe compensated na Serikali haiwezi kuziondoa.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme lililopo Mtwara na Lindi linafanana kabisa na hali ilivyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke hasa katika Kata za Kurasini, Mtoni, Keko, Chang’ombe, Tandika Sandari, Buza na
maeneo yote ya Yombo ambapo kila siku ni lazima umeme ukatike na pale inapokuwa na hali ya mawingu au mvua basi umeme hukatika kwa muda mrefu zaidi. Sasa wananchi wa Temeke wangependa kusikia majibu ya Serikali, ni lini tatizo hili litakoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika kujibu swali la nyongeza katika Mkoa wa Kilimanjaro, mtekelezaji anayerekebisha mitambo pamoja na miundombinu katika maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni pamoja na Kiwalani
ni mradi mmoja. Lakini katika maeneo ya Temeke mwezi uliopita nilifatana na Mheshimiwa Mbunge wa Temeke, nimeenda kukagua mradi wa Temeke na Kurasini. Kinachofanyika sasa wanaimarisha na kuweka vikombe vipya kwa sababu maeneo ya Temeke, Kurasini yamezidiwa. Kwa hiyo, tunaongeza nguvu ya umeme ya kilovolti 220
kutoka 132, lakini kadhalika tunafupisha umbali wa nyaya uliokuwepo wa zaidi ya kilometa 57 ili ziwe chini ya kilometa 50 katika maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni pamoja
na Kiwalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa utaratibu wa
kukamilisha tarehe 27 Aprili, 2017 mradi utakamilika. Kwa hiyo, baada ya kukamilika kwa mradi huu maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni na maeneo ya jirani tatizo la umeme
litapungua sana kwa kiasi kikubwa.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa suala la usafiri Jijini Dar
es Salaam hasa public transport ni jambo nyeti na linawagusa wananchi wote kwa ujumla wao; kwa mazoea katika Majiji ya wenzetu Ofisi za Mameya zinahusika sana katika kusimamia usafiri katika Majiji yao. Kwa mfano katika Jiji la London Ofisi ya Meya wa Jiji la London inahusika mpaka kupanga ratiba za treni, ratiba za mabasi na route zenyewe.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua kwanini katika Jiji la Dar es Salaam Ofisi ya Meya haihusishwi kwa namna yoyote
katika upangaji wa route au kusimamia usafiri katika Jiji la Dae es Salaam?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TA WALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimwa Spika, ni kweli huo ndiyo utaratibu wa Majiji mengi, lakini tatizo letu hapa ni historia ya UDA na Jiji la Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam waliziuza hizi hisa kwa Kampuni ya Simon Group. Tumejaribu kutafuta namna ya kusaidia, ni Serikali Kuu ndio tuliojitahidi kurudisha asilimia 49 za kwetu maana za zenyewe zilitaka kupotolea huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kusema ukweli nimpongeze sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika jambo hili
tumeshirikiana vizuri. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa guidance zake mpaka tumeweza hata hizo asilimia 49 zenyewe zilikuwa ni kiini macho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Waheshimiwa Wabunge tukumbuke pia historia ya UDA ilivyokuwa, kilikuwa ni kitu
ambacho kimetupwa, kimeachwa huko lakini baadaye kimerudi na kuwa kitu chenye thamani leo ndiyo tunasema.
Waulize wao Jiji la Dar es Salaam wapo, wamewahi kwenda hata Mahakamani kudai kwamba uuzaji huu sio halali? Na kama walikwenda je, ilikuwaje? Na matokeo ya kesi yalikuwaje, mbona sasa hawasemi kwamba tunataka kuappeal?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana, Jiji la Dar es Salaam is a legal entity. Wao wanaweza kushtaki na
kushtakiwa, wasije hapa Bungeni, maana walipouziana hawakuleta hapa Bungeni tukapitisha. Waende wakatafute
kama hawakuuza sawasawa waone wanavyoweza kufanya, lakini kwa sasa sisi kama Serikali Kuu tumeweza kurejesha asilimia 49 ya hisa zetu na zinaendeshwa kwenye mikono ya Serikali na tume-win tender ya ku-operate mabasi ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na huyo mwekezaji binafsi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa lengo la kuboresha nyumba hizi za National Housing ni kuwaondolea bugudha wapangaji wanaoishi katika nyumba hizo; sasa pale kwenye nyumba zilizoko Keko Juu, Kata ya Keko njia panda ya kwenda Uwanja wa Taifa wapangaji katika nyumba nne kati ya nyumba Nane zilizokuwa pale waliwahi kupewa notice ya kutaka kuhama bila sababu za msingi na wapangaji wakaamua kwenda mahakamani. Mpaka tunapozungumza sasa kesi hiyo ipo mahakamani. Mahakama imesema kwamba wakati kesi bado inaendelea pande zile mbili kati ya National Housing na wapangaji sizibughudhiane, lakini mara kwa mara...
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye swali. Kinachoendela sasa kila baada ya muda mfupi National Housing wanawatuma madalali kupeleka notice kwa wapangaji wale. Kwa kuwa, kesi ipo Mahakamani na kuwapelekea notice ni kuwabughudhi wapangaji wale na kuingilia Mahakama, Mheshimiwa Waziri anaweza kutoa kauli hapa leo ya kuwaambia National Housing waache kuwabughudhi wapangaji wale mpaka kesi itakapoisha?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba Wizara kama Wizara haiwezi kutoa kauli hapa kwa maamuzi ambayo yako nje ya muhimili wa Bunge. Maamuzi ya Mahakama yatabaki kama yalivyo na kwa maana hiyo yale yaliyoagizwa na Mahakama ndiyo yatakayoendelea kuheshimiwa mpaka hapo uamuzi sahihi utakapokuwa umetoka.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na heshima kubwa ninayompa Mheshimiwa Mwijage, lakini nasikitika kwa majibu yake mepesi kiasi hiki na hii ndiyo inayothibitisha mawazo ya baadhi ya watu ambao wanafikiria kwamba mradi huu ukitekelezwa basi utakuwa umeathiri zoezi zima la kujenga viwanda katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia ambayo Mheshimiwa Waziri anaizungumza hapa ililipwa zaidi ya miaka saba nyuma na mpaka leo bado eneo hilo liko wazi, hakuna hatua yoyote nyingine iliyopigwa baada ya ulipaji wa fidia.
Sasa swali la kwanza, kwa kuwa bado kuna malalamiko makubwa kwa waliohamishwa katika eneo hilo kwamba hii fedha shilingi bilioni 101 inayotajwa hapa inawezekana kabisa haikuwafikia waliostahili kufikiwa kwa maana ya waliohamishwa katika eneo lile na bado wanalalamika mpaka leo, je, Mheshimwa Waziri atakuwa tayari sasa kufungua milango ya majadiliano na wanaodai fedha hizi ili aweze kuona wapi zilipopotelea? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu ni kwa muda mrefu Wizara imeshindwa kumpata mbia wa kuendeleza eneo hilo labda kwa sababu ya urasimu ambao upo kwenye Wizara, je, atakuwa tayari sasa kuwakabidhi Halmashauri ya Temeke ambayo iko aggressive zaidi kuona ule mradi unatekelezwa watafute mbia na waweze kuendeleza eneo hilo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo fidia imelipwa siku nyingi na watu wote wamelipwa, ambao hawajalipwa ni watu watatu kwa sababu mtathmini hakufanya hakufanya kazi hiyo. Kazi niliyofanya, nimemuagiza DG wa EPZA aende kwa Mkuu wa Wilaya na Mamlaka ya Kata kusudi wakae na watu wao waweze kufidiwa. Wale watu hawakufidiwa kwa sababu mthamini hakuwathamini. Mimi nimeona busara hiyo na watu wamezungumza na mimi nimeagiza kwamba wafidiwe. Kwa hiyo, eneo lile liko tayari kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kwamba eneo limekaa siku nyingi, inanirudisha kwenye historia, kazi ninayofanya ndiyo muhimu kwako kukueleza kwamba sasa kazi ninayofanya, eneo limetangazwa, wawekezaji wako tayari na ili uweze kujenga pale unafuata sheria za manunuzi na ndizo tunazozifuata. Hata Halmashauri yako ikija kujenga itafuata sheria za manunuzi. Lakini nikupe imani kwamba Kurasini ambalo ni eneo lako la Jimbo itakuwa sehemu nzuri ya viwanda lakini la muhimu kwa wale wenye mashaka na mimi ni kwamba bidhaa zitakazozalishwa pale zitauzwa kwa jumla, hazitauzwa Kariakoo wala Temeke. Lazima eneo lile litoe ajira na mafunzo kwa vijana wako wa Temeke na Tanzania kwa ujumla. Hayo ndio maslahi yako, maslahi yako ya viwanda iwe ajira mengine yatafuata baadaye.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Matatizo yaliyopo katika Mikoa ya Simiyu, Dodoma na Shinyanga yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Halmashauri ya Temeke, pia hatuna maji. Mheshimiwa Naibu Waziri anakumbuka kwamba, Halmashauri ya Temeke si wanufaika wa maji yanayotoka Mto Ruvu hivyo, hatuna mfumo wa mabomba na tunatumia maji ya kisima na taarifa za wataalam zinasema kwa sababu Halmashauri…

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, mfumo wa maji taka umechanganyika na mfumo wa maji safi ya kisima tunayotumia Temeke. Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha kwamba, mnatuletea maji ya bomba Temeke, ili tuachane na kunywa haya maji machafu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Temeke kwanza tunao mtambo wa maji wa Mtoni, ila kweli kwamba, maji yanayotoka pale ni machache. Hata hivyo, tayari tunakamilisha uchimbaji wa visima 20 Kimbiji na Mpera na sasa hivi tunatafuta fedha na tunayo ahadi kutoka Benki ya Dunia, ili tuweze kuweka miundombinu ya usambazaji kuhakikisha kwamba, maeneo yote yale Mheshimiwa Mbunge Temeke na Mbagala yaweze kupata maji safi na salama. Kwa hiyo, ni suala la wakati tu, tayari maji tunayo, tunachoshughulikia ni kupata fedha za kusambaza miundombinu ili wananchi wake waweze kupata maji safi na salama.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea majibu ya Serikali yaende mbali zaidi, kwamba mbali ya kuelezea huu utaratibu lakini ijiridhishe kama kweli huo utaratibu unafuatwa. Wastaafu wa Zanzibar wamekuwa wakilipwa kwa mikupuo mitatu, maana yake ni miezi minne badala ya miezi mitatu, mitatu kama utaratibu unavyosema.
Je, ni lini Serikali itaanza kuwalipa kwa miezi mitatu badala ya miezi minne kama utaratibu unataka?
Swali la pili, Bunge la Kumi lilipandisha viwango vya pensheni vya kima cha chini kutoka shilingi 50,000 kwenda shilingi 100,000, mpaka leo baadhi wastaafu hawa baadhi ya wastaafu hawajawahi kulipwa hicho kiwango kipya. Tuliwahi kuuliza hapa na Naibu Waziri wa Fedha akasema kwamba kufika Februari, 2016 wangeanza kulipwa viwango hivyo vipya pamoja na arreas zao. Nataka kujua kwa wale wastaafu wote ambao hawalipwi kupitia Hazina ni lini wataanza kulipwa viwango vipya vya shilingi 100,000?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza kwamba wastaafu wa Zanzibar wanalipwa miezi minne, minne, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba hata wastaafu wa Bara waliokuwa wakilipwa na Hazina walikuwa wakilipwa miezi mitatu mitatu na sasa hivi kuanzia Oktoba 2016, wanalipwa mwezi mmoja, mmoja na tulipokuwa tunafanya uhakiki wa wastaafu wetu, zoezi ambalo linaendeshwa na Wizara ya Fedha tumekuwa tukikusanya mawazo yao kwamba nini wanapendelea na tutakapokuwa tumekamilisha utafiti huo tutakaa chini na kuweza kutoa maelekezo ya Serikali kwamba watalipwaje. Hivyo, hii inakwenda kwa wastaafu wa Zanzibar kwamba na wao tutachukua maoni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba Serikali imekuwa ikifuata sheria katika kulipa mafao haya, lakini pia kuweza kuchukua mawazo ya wastaafu hawa kwa sababu wao ndiyo wafaidika. Kwa mfano, hii ya sasa hivi hii ya kwenda mwezi mmoja, mmoja kwa wastaafu wa Bara wamekuwa wakilalamika kwamba ile miezi mitatu, mitatu japo kuwa ni wao ndiyo walipendekeza na sheria yetu ikaruhusu lakini wanalalamika kwamba wanakosa kupata mikopo kwa sababu cash flow haiko vizuri. Serikali imewasikiliza na kuanza kulipa mwezi mmoja mmoja na hao wa Zanzibar pia tutasikiliza tutaangalia na sheria zetu wataweza kulipwa kwa vile ambavyo wao wanapendelea na sheria yetu inaruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swalli la nyongeza ya shilingi 50,000 nakumbuka nilijibu hapa katika hapa katika Bunge lako Tukufu, kwamba wale wastaafu wote wanaolipwa na Hazina nyongeza yao walianza kulipwa na wote wanalipwa shilingi 100,000 kwa sasa. Kwa wale wanaolipwa na mifuko nililiambia Bunge lako Tukufu kwamba baada ya kutolewa agizo lile la Serikali, Bodi ya Wakurugenzi wa Mifuko husika, walitakiwa kukaa na kuweza kukubaliana ni lini wanaanza kulipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwaambie wastaafu wote nchini, kwamba hii tuliyoisema shilingi 50,000 kwenda shilingi100,000, moja kwa moja ilikuwa ni wale wastaafu wanaolipwa na Hazina. Wale wa mifuko, Bodi zao za Wakurugenzi watafanya tathmini na wataanza kuwalipa kama ambavyo mfuko wetu wa PPF wameshafanya tathmini na sasa tangu Januari 2017, wameanza kulipa shilingi 100,000 kwa wastaafu wote wa kima cha chini.(Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANAM AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kwanza niwapongeze Naibu Mawaziri wote wawili kwa majibu mazuri ya nyongeza.
Naomba niongeze jambo moja tu dogo nilialifu Bunge lako Tukurfu kwamba SSRA wameshamaliza kufanya tathmini ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yote katika nchi yetu ya Tanzania pamoja na PPF kuanza kulipa kima cha chini cha pensheni cha shilingi 100,000 pia Mfuko wa NSSF na LAPF wameshakamilisha tathmni hiyo na wao wameshaanza kuendelea na mchakato huo wa kupandisha kima cha chini. Kwa hiyo, Serikali imeshatekeleza agizo hilo kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa malipo hayo sasa umeanza kufanyika hata kwenye Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nionyeshe masikitiko yangu makubwa kwa majibu ya Serikali, lakini natambua ugeni wa Mheshimiwa Naibu Waziri na nimhakikishie kwamba hayo majibu ambayo umeandaliwa yana mapungufu makubwa.
Je, utakuwa tayari kwenda field kutembelea ukajionee hali halisi iliyopo katika mradi huu kwa sababu sio kweli kwamba umekamilika?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na matatizo makubwa ya kukatikakatika kwa umeme na hasa kunapokuwa na dalili za mvua au mvua inaponyesha. Je, tatizo hili la kukatikakatika kwa umeme litakwisha lini katika Halmashauri ya Temeke?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi mwenyewe binafsi Jumapili nilifanya ziara ya kutembelea miradi hii na nilipita pamoja na TANESCO. Tulikuwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme (TANESCO) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke tuliitembelea. Katika majibu yangu ya msingi nimeainisha miradi ambayo haijakamilika na mradi ambao haujakamilika ulikuwa Masista Magogo Na. 2 na Na. 3 ambao utakamilika Disemba 2017.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba miradi hiyo kwa kweli nimeiona lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba wakati miradi inakuwa designed scope yake na tunatambua maeneo ya Mbagala na Wilaya ya Temeke na Kigamboni ujenzi wa makazi unaongezeka kwa kasi, kuna maeneo yameongezeka wananchi wengi wamejenga. Kwa hiyo, scope ile imewaacha nje kwa hiyo unaona kwamba mahitaji yameongezeka kuliko ambavyo scope ilizingatiwa. Kwa hiyo, nimthibitishie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwa Wilaya ya Temeke litaisha lini. Ni kweli kuna tatizo la kukatikakatika kwa umeme maeneo ya Temeke, Mbagala, Yombo Dovya, Buza na Kigamboni. Serikali kupitia TANESCO imekuwaikitekeleza miradi mbalimbali, hata mwaka huu wa fedha imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.2.
Mheshimiwa Spika, sambaba na hilo kuna ujenzi wa miradi inayoendelea chini ya Mradi wa TEDAP (Tanzania Energy Development and Access Expansion Project). Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa msongo wa KVA 232 unaotoka Gongolamboto mpaka Mbagala na ujenzi wa kituo kikubwa cha kupoozea umeme chenye MVA 50.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia kuna ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovoti 132 ambao unatoka Mbagala unaelekea Kigamboni, ujenzi wa msongo wa umeme unaotoka Kurasini kuelekea Kigamboni. Kwa hiyo, jitihada zote hizo na tatizo linasababishwa na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme Mbagala na ndio maana unakatikakatika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kutokana na kazi zitakamilika Desemba 2017 na kuanzia Disemba, 2017 nakuthibitishia kwamba tatizo la kukatikakatika kwa umeme kwa Wilaya ya Temeke litakuwa limepungua na litaisha kabisa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Hospitali ya Ocean Road ambayo ndiyo maarufu na inafanya kazi kubwa ya kuhudumia wagonjwa hawa wa saratani ndiyo hospitali ya siku nyingi na miundombinu yake pia ni ya kizamani lakini idadi ya wanaopata huduma hapo imeongezeka maradufu. Mbali na hayo hospitali ile haifikiki kirahisi kwa sababu iko pembeni na vituo au barabara za usafiri wa umma kwa maana ya daladala. Hivyo, wananchi wanatakiwa kutembea umbali mrefu kwa zaidi ya kilometa moja kufika hospitalini pale umbali huu si rafiki kwa mgonjwa au watu wanopeleka wagonjwa hospitali. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hospitali nyingine kubwa ya kisasa jijini Dar es Salaam ili kuzihamisha huduma hizi za magonjwa ya saratani ziweze kufanyika katika kituo kimoja kikubwa na cha kisasa?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hatuna mpango kwa kweli wa kujenga kituo kingine cha kutoa tiba ya saratani katika Jiji la Dar es Salaam, kwa sababu kituo cha Ocean Road kinajitosheleza na kinajitosheleza kwa maana ya kutoa huduma kwa Kanda nzima ya Mashariki na hata wagonjwa wanaotokea Kanda ya Kati wanaweza wakapata huduma zao pale Ocean Road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ni moja kituo kile hakipaswi kuwa kama hospitali ya kwenda kila siku, kile kituo ni kituo cha rufaa. Kwa sasa kilikuwa ni kituo pekee cha rufaa cha Kitaifa lakini kwakuwa toka tumeingia Awamu ya Tano tumeanzisha utaratibu wa kufungua vituo vingine kwenye satelites/kwenye Kanda zote kwa maana ya Kanda ya Kusini pale Mbeya, Kanda ya Ziwa pale Bugando na Kanda ya Kaskazini pale KCMC ndio maana sasa tunakichukulia kituo hiki cha Ocean Road kama cha Kanda hii ya Mashariki na Kanda zozote zilizo karibu na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ile ya saratani inayotolewa pale ni ya rufaa ni huduma ya ngazi ya juu kabisa, kwa hivyo kwa vyovyote vile hatuwezi kusambaza huduma hizi kila sehemu kwamba tuweke na upande mwingine, hapana. Hospitali kubwa zipo nyingi Dar es Salaam ikiwemo ile mpya ya Mloganzila ambayo itatoa huduma nyingine zozote pembeni lakini siyo huduma za saratani kwa sababu gharama za kuanzisha kituo cha saratani ni kubwa sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta hizi zisizo rasmi na hapa nawalenga hasa wale wanaofanya kazi za daladala kwa maana ya madereva wa madaladala na makondakta wao na hii ni sekta ambayo imeajiri vijana wengi na watu wengi. Kimsingi wana malalamiko mengi ya haki za wafanyakazi, kwamba hawapewi stahiki zao. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, atakuwa tayari kukutana na Madereva na Makondakta wa daladala ili asikilize kero zao na uweze kuzipeleka Serikali kwa ajili ya kuzishughulikia, ukianzia Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii kama Wizara tumekuwa tukiifanya, tutaendelea kuifanya na nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nipo tayari kukutana nao na kujadiliana nao kuhusu haki ambazo zinawahusu. (Makofi)
MHE ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji liliko Msalala linafanana na tatizo la mji liliko katika Halmashauri ya Temeke ambayo kwa kiasi haina mfumo wa maji ya bomba. Hata hivyo bomba kubwa la maji kutoka Mto Ruvu linalopeleka maji katika Kambi ya Jeshi ya Navy linapita Temeke.
Sasa ni lini Serikali itatoa matoleo kutoka kwenye bomba lile ili wananchi wa Kata za Mtoni, Azimio, Tandika, Makangarawe pamoja na Buza nao waweze kupata maji kutoka kwenye bomba hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri, lakini nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jukumu la kuwapatia wananchi maji ni jukumu letu sisi Wizara ya Maji na kwa kuwa sisi ni Wizara ya Maji na si Wizara ya ukame tupo tayari kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. Mheshimiwa Mbunge nataka nikuhakikishie Jumatatu mimi naanza ziara katika mkoa wa Dar es Salaam, na katika maeneo nitakayotembelea nitafika Temeke tuangalie namna bora ya kuweza kuwapatia wananchi wako maji. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu hayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri na amekiri kabisa kwamba TFDA wanashindwa kukusanya wenyewe kwa sababu ya changamoto ya rasilimali watu pamoja na vitendea kazi vingine na Halmashauri inakwenda kukusanya tozo hizo kwa kutumia rasilimali watu zake, magari yake na muda lakini mwisho inapata asilimia 40 na yule ambaye amekaa tu maana ya TFDA anapata asilimia 60. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu sasa wa kubadilisha Halmashauri ibaki na asilimia 60 na TFDA apate asilimia 40? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tabia chafu kati ya wanaouza na kuzalisha vyakula kwa maana vyakula vinapokuwa vinakaribia kumaliza muda wake wa matumizi, wanakwenda kuwauzia kwa nusu hasara watu wenye migahawa au hoteli ili waweze kuvitumia. Ndiyo maana imekuwa ni kawaida sasa kusikia mtu amekula sehemu fulani na amepata food poison, kwa sababu vyakula vinavyotumika kwa maana ya vyakula ghafi vinavyotumika kuandalia vyakula katika hoteli na migahawa mingi vinakuwa ama vime-expire au vimekaribia sana kumaliza ule muda wake wa matumizi. Je, TFDA inafanya jitihada gani kuhakikisha kila chakula ghafi kinachotumika kuandalia chakula hotelini kinakuwa ni salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kuhusu tozo za makusanyo mbalimbali ya ukaguzi, usimamizi wa maeneo ya biashara zinazohusiana na sheria hii niliyoitaja Sura 219, kwa kawaida yanabaki kwenye Halmashauri kwa asilimia 100. Sijui wewe umeitoa wapi hiyo asilimia 60 lakini sheria ninayo hapa nimekuwa naiperuzi tu wakati unauliza swali lako, inasema mapato yote yanayokusanywa kwenye Halmashauri yanabaki kwenye Halmashauri wala hayachukuliwi na TFDA. Kazi ambazo zimekuwa delegated ni pamoja na kukagua groceries, restaurants, bar, mashine za kusaga na kukoboa na fees zote ambazo zinakusanywa zinabaki kwenye Halmashauri zenyewe. Kwa hiyo, wala hakuna cha asilimia fulani kwamba inaenda TFDA, hapana, sheria inasema hivyo, naomba uipitie ukitaka naweza nikakupa ukaitazama.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu usalama wa malighafi ambazo zinaenda kutengeneza vyakula kwenye restaurants kwamba ni mdogo, hapana, sikubaliani na wewe kwa sababu kiukweli kama kuna mamlaka iko makini katika nchi yetu, ambazo mimi na zifahamu vizuri ni pamoja na Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipondozi. Hawa watu wako makini sana na ni kwa sababu wanajua jukumu lao linahusu afya za Watanzania. Wakivurunda tu wao maana yake vyakula feki ama dawa feki zitaingia nchini na mwisho wa siku Watanzania wataumia na Watanzania wakiumia itakuwa kelele nchi nzima, kila mtu atajua kwamba sehemu fulani kuna chakula fulani kimeingizwa na ni kibovu na kinasababisha madhara kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kama kuna mamlaka haina compromise ni pamoja na TFDA. Kwa kweli hawana compromise, hata mimi leo nikisema nazalisha juice kuja kunikagua watanikagua kwa umakini wa ajabu na hawatabadilisha matokeo kwa sababu wakibadilisha matokeo tu itajulikana.
Mheshimiwai Naibu Spika, namhhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa usalama wa afya za Watanzania uko kwenye mikono salama ya TFDA. Kama inatokea food poisoning kwenye maeneo wanapouza chakula basi ni aidha uandaaji wa chakula ama uandaaji wa vyombo lakini sio zile ingredients ambazo zimekaguliwa na TFDA.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, umekuwa ni utaratibu wakati wa mtihani wa kidato cha nne Serikali inapeleka askari tena askari wenye silaha kwenda kuwasimamia watoto wakati wanafanya mtihani. Kitendo hiki kinawatia uoga wanafunzi kwa sababu hawajazoea kusimamiwa na askari wakati wakifanya mitihani au wakati wanajisomea, hivyo wanapoteza concentration katika mitihani na hii inawapeleka wengine kufeli.
Je, Serikali haina njia mbadala ya kuhakikisha kunakuwa na ulinzi lakini usiotisha kama vile kuweka askari ambao hawana uniform na hawana silaha ili waweze kuwasimamia watoto hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaaminishwa kwamba mtihani wa mwisho sio pekee ndiyo unaomfanya mtoto afaulu katika mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne, kwamba continuous assessment inachukua asilimia 50 na mitihani ya mwisho inachukua asilimia 50, kama hili ni kweli kuna sababu gani ya kuweka ulinzi mkubwa wakati wa mtihani wa mwisho wakati ule unachangia tu asilimia 50? Je, ulinzi huo pia unawekwa kwenye zile continuous assessment ili kufanya usawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi tunapoweka ulinzi lengo si kuwatisha watahiniwa bali kuhakikisha kwamba mazingira hayo yanakuwa salama kabisa. Kama ambavyo imeshuhudiwa katika siku za karibuni, hali ya uhatarishi imekuwa ikijitokeza katika aina tofauti tofauti. Kwa kweli siamini kama wanafunzi wa Kitanzania wanaweza wakamuogopa askari kwa sababu ni maisha yao ya siku zote, hawezi akawa hamuoni kabisa askari, karibu kila mahali nchi hii imeimarisha ulinzi na askari kama polisi tuko nao siku zote tena kuna ulinzi jumuishi na shirikishi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa misingi hiyo mimi nadhani kwamba lengo la muhimu lieleweke kwamba ni kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira salama kabisa ambayo wanafunzi wale badala ya kuogopa askari kwao ni suala la usalama ili wafanye mitihani yao bila kupata uhatarishi wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kupimwa kwa kufuata matokeo endelevu (continuous assessment), ni kweli tumekuwa tukifanya hivyo na hiyo haiwezi kuwa ndio sababu ya kusema kwamba kwa sababu marks tunazozitegemea mwishoni ni asilimia 50 tu, basi tusiwawekee mazingira ya usalama. Tutaendelea kufanya hivyo, na kwa sababu umetoa hoja hiyo, tutafanyia kazi kama tukiona kweli mwanafunzi anaogopa sana askari tutajua namna bora zaidi ya kufanya.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika nakushukuru kunipa nafasi na mimi kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kabisa kwamba kuna mialo ambayo haijasajiliwa na inasafirisha abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Nataka kujua Serikali kupitia SUMATRA na TPA wanatumia utaratibu gani kuhakikisha kwamba vipimo vya kuhakikisha kwamba mizigo na abiria wanaoingia kwenye vyombo vya usafiri vinakwenda sambamba na uwezo wa chombo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, bado kuna vyombo vingi vibovu na visivyokuwa na life jacket vinafanya safari za kubeba abiria kutoka Pwani ya Tanga kwenda Pemba; kutoka Pwani ya Dar es Salaam kwenda Unguja na kutoka Pwani ya Mkoa wa Pwani kwenda Mafia na sehemu zingine za jirani kama visiwa vya Comoro. Vyombo hivi vinafanya safari usiku vingine vinapotea na hata kumbukumbu hatuna. Serikali ina mpango gani wa kudhibiti safari za usiku za vyombo vibovu vinavyosafirisha abiria ili visiweze kufanya hivyo kunusuru maisha ya Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba vyombo vyote vya majini kuanzia wakati vinatengenezwa kuna loading mark huwa inawekwa yaani chombo kikielea majini hakitakiwi ile loading mark izame chini, hicho ndicho kitu cha kwanza ambacho vijana wa SUMATRA wanakitumia katika kuhakikisha kwamba chombo hiki kinachokwenda kuelea majini na kusafirisha abiria na mizigo hakijazidisha abiria wala mizigo, kwa kukagua ile loading mark.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu suala la ni namna gani tunaweza kudhibiti, na vile vile vyombo hivi vinavyosafirisha abiria kati ya Tanga, Dar es Salaam na Zanzibar tunavidhibiti vipi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijana wetu wa SUMATRA wapo katika mialo, mialo ile iliyosajiliwa. Labda tu nichukue fursa hii kukiri na mara nyingi nakiri kwamba kuna mialo ambayo haijasajiliwa, na mingine hatuijui.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo ndiyo maana tumeweka usimamizi kwa kutumia viongozi wetu kamati za ulinzi na usalama za Mikoa yote ya Pwani na Zanzibar wanakutana kila baada ya miezi, na wakati mwingine miezi sita wanakutana na mikoa mbalimbali katika hii mikoa ya ukanda wa Pwani pamoja na Zanzibar ili kujadili na kuhakikisha kwamba wanaitambua ile mialo yote ambayo haitambuliki. Mialo hiyo ndiyo inayotumika mara nyingi kusafirisha mizigo usiku bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Spika, niwaombe tu nanyi Waheshimiwa Wabunge tuhamasishe watu wetu wasitumie hii mialo ambayo haijasijiliwa, kwa sababu kwanza ni hatali lakini pili inapoteza mapato yetu kwa sababu hii mialo tunaitumia vilevile kukusanya kodi zinazotusaidia kuleta huduma mbalimbali za jamii na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana tusaidiane ili kuhakikisha mialo hii ambayo inaoparate illegally tuidhibiti kwa pamoja tukishirikirikiana na nyinyi Waheshimiwa Wabunge, muwaelimishe watu wenu. Kwa sababu hatimaye hawa watu wanatoka katika maeneo yetu. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwaadhibu wale wote wanaofanya vitendo vya udhalilishaji, lakini watoto hawa wanaofanyiwa udhalilishaji wanapata madhara ikiwemo kuambukizwa magonjwa na kupewa mimba. Je, Serikali ina jitihada gani za kuhakikisha watoto hawa ambao wamepata maradhi au wamepata mimba wanasaidiwa ili kutimiza ndoto zao za maisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua ambazo nimetoka kuzieleza na ambazo Waheshimiwa Mawaziri wametoka kuzisema za kuchukua hatua kuhusiana na wahusika ambao wanafanya matendo hayo ya udhalilishaji, nami niendelee kutoa rai tu, changamoto ya kuyafikisha mashauri haya Mahakamani mojawapo ni kwamba ndugu na wazazi wa watoto wale wanakubaliana na mtuhumiwa kuyamaliza mashauri yao nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba udhalilishaji wowote wa mwanamke na mtoto masuala haya yasimaliziwe mtaani, badala yake yaweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Sisi kama Wizara na Serikali tutaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba matibabu kwa wale ambao watakutwa wameathirika na virusi vya UKIMWI, kwa sababu huduma za tiba ya UKIMWI zinatolewa bure na Serikali na pale itakapothibitika kwamba binti yule ameweza kupata ujauzito basi huduma za afya kwa wajawazito ni bure kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, sipingani na mpango huu wa Serikali katika kuzichukua moja kwa moja hospitali hizi, hasa ukizingatia Halmashauri zetu sasa hivi zina hali mbaya kichumi kutokana na vyanzo mbalimbali kuondolewa. Nataka kujua sasa, mfumo wa utumishi baada ya kuzichukua hizi hospitali utakuweje kwa maana za mamlaka za kinidhamu kwa watumishi waliokuwa wakifanya kazi kwenye hizi hospitali? Hilo moja.
Mheshimiwa Spika, la pili, wakati Wizara inapanga namna gani ya kuzihudumia hizi hospitali, huwa inaangalia idadi ya watu katika eneo husika, mfano kwa Hospitali ya Temeke mnaangalia idadi ya watu katika Wilaya ya Temeke, lakini ukweli ni kwamba Hospitali ya Temeke haihudumii tu watu wa Temeke, inahudumia na maeneo jirani kwa sababu ya jiografia yake ilivyo, maeneo kama ya Kigamboni, Mkuranga na sehemu nyingine kama Kibiti na Rufiji.
Je, Wizara mmelizingatiaje hili, ili kuhakikisha sasa huduma mtakazozitoa katika Hospitali ya Temeke zitaenda sambamba na idadi kubwa ya watu wanaopata huduma katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sisi ndani ya Wizara baada ya kukabidhiwa hospitali hizi tumefanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji ya miundombinu ya kiutumishi ya hospitali hii. Niseme tu kwamba kuna maboresho makubwa ambayo tumeyafanya ndani ya Wizara kwanza; kwanza, kuanzisha section maalum ambayo itakuwa inasimamia Hospitali za Rufaa na za Mikoa katika Idara ya Tiba.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika Idara Kuu ya Utumishi tumefanya mabadiliko, tutakuwa na Mkurugenzi Msaidizi ambaye naye atakuwa anasimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tumefanya maboresho vilevile katika Hospitali za Rufaa za Mikoa baada ya kuitwa Waganga Wafawidhi. Matarajio yetu ni kwamba sasa wasimamizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa watakuwa wanaitwa Wakurugenzi kamili na watapata hadhi hiyo na taratibu zote hizo tumeshazikamilisha.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Nidhamu bado yako chini ya Mabaraza ya Taaluma ambayo nayo yako chini ya Ofisi ya Mganga Mkuu. Kwa hiyo, Mamlaka za Nidhamu zitaendelea kufanya kazi kwa mujibu ule ule, hata pale wakati zikiwa TAMISEMI, mamlaka ya nidhamu yalikuwa bado chini ya Wizara ya Afya chini ya mabaraza, chini ya Mganga Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mtolea, ni kweli Wilaya ya Temeke ina watu takribani milioni 1.6 na Hospitali ya Temeke imekuwa ikiwahudumia wananchi wengi pamoja na Wilaya nyingine za jirani. Serikali inatambua hilo, tutazingatia hilo, lakini sambamba na hilo tunaboresha mnyororo wa utoaji huduma kwa maana ya kuboresha vituo vya afya, kujenga Hospitali za Wilaya na zahanati ili sasa ule mnyororo wa rufaa uweze kuwa kamili na kuhakikisha kwamba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inafanya kazi ya rufaa ya mkoa.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Watoto wanaozaliwa na ulemavu nao wanastahili kupata elimu kulingana na ulemavu walio nao. Sisi pale Temeke tuna Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu ambayo inatoa elimu ya msingi kwa watoto wenye ulemavu kutoka sehemu mbalimbali za nchi, lakini ukweli ni kwamba shule ile inakabiliwa na changamoto nyingi za vifaa wezeshi kwa wale walemavu, lakini pia mazingira yenyewe ya shule. Nilitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuisadidia shule ile ili watoto wasome kwenye mazingira rafiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kaka yangu Mtolea, Shule ya Salvation Army nimefika pale na nimejionea mazingira yalivyo. Kwa hiyo kama shule zingine ambavyo tumekuwa tukifanya kuhakikisha kwamba zinapata vifaa saidizi na Shule ya Salvation Army tutahakikisha kwamba itaendela kupata vifaa saidizi sawa na shule zingine ambazo tumekuwa tukigawa vifaa saidizi kama Serikali. (Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mtolea kwamba shule hii na yenyewe itaendelea kupata vifaa saidizi kama ambavyo shule zingine zimekuwa zikipata. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa pia kuongezea na kulihakikishia Bunge lako kwamba Wizara ya Elimu imekuwa ikinunua vifaa visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Katika bajeti ambayo tutakuja kuiwasilisha Bungeni tarehe 3 na 4 Mei, 2018 pia tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha kwamba shule hiyo pamoja na shule nyingine ambazo zina wanafunzi na ambao wanahitaji visaidizi watapatiwa ili waweze kujifunza kwa ufanisi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo lililopo katika Jimbo la Segerea linafanana pia na lililopo katika Jimbo la Temeke ambapo katika Kata za Buza, Tandika na Kata 14 Temeke barabara zimeharibika sana na hasa baada ya mvua hizi. Kwa kuwa kata hizi hazipo katika ule mpango DMDP, nilitaka kujua Serikali ina mpango gani kwenda kukarabati barabara za mitaa katika kata hii angalau kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba baada ya mvua kunyesha maeneo mengi miundombinu yake imeharibika na hasa kwa Jiji la Dar es Salaam ambapo mvua zimenyesha nyingi sana.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya tathmini ya uharibifu uliotokea ili tujue hatua za dharura za kuchukua ili wananchi waendelee kutumia barabara katika hali nzuri.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu ya 2014 ya Elimu Bila Malipo inaonekana kuwa ni sera ya ubaguzi ambayo inawabagua watoto wanaosoma kwenye shule binafsi. Mbali tu ya kuwalipisha ada za mitihani lakini sasa Serikali imekwenda mbali kwamba wanaosoma shule binafsi hawawezi hata kupata mikopo ya elimu ya juu. Hivi ni kigezo gani Serikali imekitumia cha kujiaminisha kwamba watoto wanaosoma shule binafsi ni watoto wa matajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwaa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Sera ya Elimu Bure ni ya kibaguzi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sio ya kibaguzi bali elimu bure tunazungumzia katika sekta ya umma. Kwa hiyo, lazima tutofautishe sekta ya umma na sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na watoto ambao wamesoma shule binafsi kutoruhusiwa kupata mikopo ni suala tu la kuangalia kwamba kati ya mtu ambaye anaweza kulipa milioni mitatu au milioni nne kwenda shule ya msingi na sekondari na yule ambaye hawezi, ni yupi utamuangalia wakati wa kutoa mkopo? Ni suala la kuangalia nani mwenye mahitaji zaidi siyo suala la kibaguzi. Bajeti iliyopo ni kidogo na wahitaji ni wengi lazima tuchague na tunatoa zaidi kwa wale ambao wanahitaji zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa wanafunzi wale ambao wamepata bahati ya kusomeshwa labda na wafadhili, Serikali haiwanyimi mikopo, tunachotaka ni ushahidi kwamba kweli wamefadhiliwa. Tutahitaji barua kutoka kwa mfadhili kuonyesha kwamba mwanafunzi amefadhiliwa. Kwa hiyo, sio ubaguzi ni suala tu la ni namna gani tunafanya kazi ili huduma hiyo ya elimu iweze kutolewa kwa wote kwa usawa. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Njia zinazotumika kuzitangaza fursa zinazopatikana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa ni zile zile ambazo zinawafikia tu watu wanaoishi mijini na wachache waliopata shule ya kutosha, lakini elimu hiyo haiwafikii watu walio vijijini na hasa wanaoishi mipakani ambao wangependa sana kuzijua hizi fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kujua Serikali ina mpango gani tofauti wa kuhakikisha fursa zinazopatikana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaelezwa kwa wazi na kwa kina na kuwafikia Watanzania wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nchi wanachama zinabadilisha sheria zao ili wananchi waweze ku-enjoy fursa zilizokuwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wenyewe wana kaulimbiu yao wanasema Chungulia Fursa. Sasa Watanzania walichungulia fursa zilizopo ndani ya Afrika Mashariki wakalima mahindi kwa kiasi kikubwa ili waweze kufaidi Soko la Afrika Mashariki kwamba wauze mahindi ndani, lakini wauze mahindi nje ya nchi hii kwa maana kwenye nchi za Afrika ya Mashariki. Serikali ya Tanzania ikapiga marufuku mahindi kuuzwa nje ya nchi.
Je, Serikali haioni kwamba inawanyima Watanzania fursa za ku-enjoy Soko la Afrika ya Mashariki? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunawafikiaje wananchi walio katika vijiji? Hakuna tofauti ya kuwafikia wananchi walio katika vijiji kama tunavyowafikia katika kampeni zetu, katika kutangaza sera za Serikali kwa kutumia vyombo vilivyopo na njia zilizopo. La kwanza, ni kutumia redio na television. Wananchi wengi siku hizi wanazo redio na wengine wanatazama television.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya pili ambayo tunaitumia kuwafikia wananchi wetu ni kufanya makongamano katika maeneo ya vijijini, hasa yale ambayo wananchi wamekuwa karibu na miji. Hili limekuwa na mafanikio mazuri sana kwa sababu, wananchi wengi wamekuwa wakifuatilia kwa makini siyo tu redio, na warsha ambazo zinapelekwa kwao. Na hii tumeanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba Serikali yetu ina mkakati wa kuhakikisha kwamba tunacho chakula cha kutosha katika nchi yetu. Baada ya hapo hakuna kizuizi cha kuweza kuuza mahindi nje ya nchi. Sasa hivi kuna utaratibu wa kutengeneza maghala na kufanya tathmini inayoeleweka kwamba chakula cha kila mkoa au kutoka mkoa hadi mkoa kinaweza kukidhi mahitaji ya wananchi. Baada ya hapo, hakuna kizuizi cha kuweza kuuza mahindi nje ya mipaka yetu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la miundombinu hii ya maji halipo tu Wanging’ombe lipo pia pale Temeke ambako miundombinu ya maji taka pale Kurasini imekufa kabisa na sasa hivi mazingira yale kwa kweli yanatia kinyaa kwa sababu vinyesi vinatapakaa nje. Wizara ilisema kwamba wanataka wajenge mitambo ya kisasa ya kuchakata taka na nimeona wameanza kulipa fidia japo kidogo kidogo sana. Sasa kwa sababu jambo hili ni la hatari linaweza kusababisha magonjwa mlipuko pale, Wizara ina mpango gani wa kuanza kujenga mitambo hiyo mipya haraka?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekit, kwanza nimshukuru amekiri kwamba na fidia tumeanza kulipa na tumeshapata fedha kutoka Serikali ya Korea Dola milioni 90. Kwa hiyo, wakati wowote tunatangaza tenda tuanze utekelezaji wa mradi huo. Hata hivyo, katika kipindi kuna miradi midogo midogo tunayotekeleza ili kuhakikisha kwamba suala la kipindupindu haliwakuti wananchi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli Serikali imetoa elimu kwa wananchi wanaoishi mikoani juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, lakini kituo cha kuhudumia wagonjwa wa Ebola endapo watapatikana kipo pale Temeke. Sasa kwa nini Serikali haioni haja ya kutoa elimu hiyo ya uelewa kwa wananchi wa Temeke pia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo cha Isolation Center kwa magonjwa haya hatarishi kipo pale Temeke, watoa huduma wetu katika Hospital ya Temeke wameshapewa Elimu hiyo na tutaendelea kutoa elimu kwa ujumla kwa wananchi wote ikiwa ni pamoja na wananchi wa Temeke kuhusiana na athari za ugonjwa huo.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali yanaonesha kwamba kumbe Tume ya Uchaguzi haiandikishi watu kwa kufuata vigezo bali inaandikisha yeyote atakatejitokeza na mzigo wa kuangalia nani ana vigezo na nani hana unabaki kwa wananchi kwamba waweke pingamizi, jambo hili siyo zuri.
Sasa Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Tume ya Uchaguzi inapoandikisha wapiga kura ifuate vigezo vilivyoainishwa kisheria? Hilo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kutokana na harakati za kiuchumi sasa hivi zilivyo duniani Watanzania wanaishi katika mataifa mbalimbali na wangependa kuendelea ku- enjoy ule Utanzania (utaifa) wao. Serikali ina mpango gani wa kuruhusu uraia pacha ili Watanzania walio nje na wenyewe waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama watanzania wanaoishi Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, KWA swali la kwanza, si kweli kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiwa inawaandikisha Watanzania kushiriki kwenye uchaguzi haifuati vigezo vilivyowekwa. Kwa mujibu wa Katiba yetu na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, vigezo vimewekwa vya nani anapaswa kuandikishwa kwenye daftari la kupiga kura na ndiyo maana kifungu cha 24 cha sheria hiyo kimetoa mwanya kwa mtu yeyote ambaye ana pingamizi kwa mtu aliyeandikishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake si kwamba tume sasa inamchukua kila mmoja tu lakini kwa mujibu wa kifungu hicho imetoa nafasi hiyo ili yeyote mwenye pingamizi awasilishe pingamizi hilo kwa Tume lifanyiwe kazi na kama mtu hana sifa ataondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uraia pacha limezungumzwa mara zote, suala hili ni la Kikatiba muda utakapofika na itakapoonekana inafaa basi ninaamini sisi sote kama Wabunge na nchi kwa ujumla tutaenda katika mwelekeo huo, lakini kwa hivi sasa Katiba na sheria zetu haziruhusu uraia pacha. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la ubovu wa viwanja limekuwa kubwa sana hapa nchini. Sasa Serikali haioni kwamba huu ni wakati sahihi sasa wa kuanzisha Wakala wa Kusimamia Viwanja vya Mpira ili iwe inasimamia ubora wa viwanja vyote vya mpira hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO): Mheshimiwa Spika, chini ya Wizara pamoja na Shirikisho la Michezo Tanzania kwa maana TFF iko Idara maalum ambayo inasimamia ubora na vigezo vya viwanja ambavyo vitatumiwa katika michezo mbalimbali. Utaratibu uliowekwa ni kwamba iko international standard ambayo inavitaka viwanja mbalimba viwe vina sifa zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa Kiwanja cha Mpira wa Miguu, kwa mujibu wa international standard kinatakiwa kiwe kati ya mita 100 mpaka mita 110 na upana wake uwe ni mita 64 mpaka mita 75. Kwa hiyo, tunayo Idara chini ya TFF na kwenye Wizara ambayo kazi yao ni kushughulikia viwanja ambavyo vitakuwa ni bora.
Mheshimiwa Spika, pia kwa wazo ambalo ameleta Mheshimiwa, naamini kazi kubwa ambayo tutafanya kama Serikali ni kuboresha Idara zetu za ndani ili ziendelee kufanya utaratibu kuhakikisha kwamba tunakuwa tuna viwanja bora zaidi vya watu kuchezea.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wizara na Baraza la Michezo zimekuwa zikiweka nguvu katika kuushughulikia mchezo mmoja tu wa mpira wa miguu na kusahau michezo mingine na ndiyo maana hata wakati uwanja mkubwa wa Taifa unajengwa, tuliambiwa kwamba inajengwa sports centre, lakini imejengwa football ground. Kwa maana hiyo, wenye michezo mingine wanashindwa kutumia miundombinu hiyo. (Makofi)
Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutenga ukumbi mmoja kati ya kumbi zilizokuwa kwenye Uwanja wa Taifa kuwa Boxing Academy ili wacheza ngumi na wenyewe waweze kupata sehemu ya kufanya michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna jumla ya michezo 38 iliyosajiliwa hapa nchini na tuna michezo mipya kabisa tisa ambayo mingine nikiitaja hapa wengine hatuwezi kuielewa. Kwa hiyo, kutokana na hiyo, sisi Kiwizara tunapanga mipango yetu kwa mahitaji na jinsi ambavyo michezo yenyewe inavyoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba kuna mchezo mwingine tunaupendelea, hapana, ni kutokana na wadau wenyewe.
Kwa mfano, leo hii hatuwezi tukasema tuweke katika mipango yetu namna ya kuendelea na mchezo wa freese B ambao ni mchezo wa kisahani umeingia nchi, kuna mchezo wa kabadi, kuna mchezo wa kengele (goal ball), kuna mchezo wa roll ball, kuna mchezo wa wood ball; sasa hiyo michezo tunawategemea wadau mwiendeleze ifikie kiwango ambacho tunasema tunaweza kuwa na ushindani katika nchi hii na tukaweza kuifanyia utaratibu kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Mtolea ni zuri kwamba tuna maeneo makubwa sana Uwanja wa Taifa, lakini pale penye mahitaji, wadau wenyewe waeleze na sisi tunaweza kutoa maeneo hayo kuweza kuyaendeleza kwa michezo mingine.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo kwenye Chuo cha Maendeleo Kilwa zinafanana kabisa katika changamoto zilizopo katika Chuo cha Bandari kilichopo Tandika pala Temeke ambako chuo hicho kilianza kufundisha wanafunzi kabla hakijapata ithibati, hivyo wanafunzi wote walio-graduate kuanzia mwaka 2016 kurudi nyuma hawakupewa vyeti vyao mpaka hivi leo. Jambo hili limezua mtafaruku mkubwa, wanafunzi hawa hawajui hatima yao, wanashindwa kuendelea na masomo zaidi na wanashindwa kupata ajira. Nilitaka kujua kauli ya Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi hawa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema kwamba kuna changamoto katika Chuo cha Bandari. Changamoto hiyo imeshafika Wizarani kwetu na kwa sasa tunaishughulikia na wanafunzi watapatiwa majibu muda si mrefu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tatizo hili la ajira halipo tu kwa wahitimu wa vyuo vya ufundi, lipo pia kwa wahitimu wengine wa vyuo vikuu hapa nchini. Kwa kuwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu tayari ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, kwa maana hiyo ni watu ambao wanaaminika. Kwa nini Ofisi ya Waziri Mkuu isishirikiane na Wizara ya Elimu kuandaa mikopo ya wahitimu ya kuanzia maisha pale ambapo wanamaliza masomo yao ili waweze kujitengenezea fedha ambazo zitasaidia kuendesha maisha yao lakini kurejesha mikopo waliyokopa wakiwa vyuoni. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuendelea kuwakusanya vijana wahitimu wa vyuo vikuu katika makundi tofauti tofauti na mmoja mmoja ambao wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi na lengo letu ni kuweza kusaidia kufikia malengo yao. Chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunalo Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ambapo ndani ya Baraza lile tuna mifuko zaidi ya 19 inayotoa mikopo na grants. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa vijana wote nchi nzima hasa wahitimu wa vyuo vikuu wenye mawazo mbalimbali ya kibiashara, watumie fursa ya uwepo wa Mfuko wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na mifuko mingine ili waweze kujikwamua kiuchumi. Naamini kabisa kwa kutumia Baraza hili itasaidia sana wao kuweza kupata sifa ya kupata ajira lakini vilevile na kutengeneza kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili huwa napenda kutoa mfano na naomba nirudie mfano wangu, tunao vijana waliomaliza Chuo Kikuu cha Sokoine pale Morogoro ambao walipohitimu walijiunga pamoja, wakaunda kampuni, sisi kama Serikali tukawapa dhamana ya mkopo na hivi leo wanafanya kazi kubwa sana katika kilimo cha mboga mboga hapa nchini na wameanza kuwaajiri mpaka vijana wenzao. Kwa hiyo, natoa rai kwa vijana wengine wote kufuata mfano huo na inawezekana kabisa kutimiza malengo yao.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la barabara ya Bukoli - Kahama linafanana kabisa na barabara ya Davis Corner – Jeti Lumo ambayo ipo kwenye ule mpango wa barabara pete za Dar es Salaam kwa ajili ya kupunguza foleni. Mkandarasi Nyanza Construction alipewa pesa ya kujenga kipande kidogo tu cha kutoka Tandika - Yombo Dovya – Makangarawe – Buza - Mwisho wa Lami, kipande kilichobaki cha kutoka Mwisho wa Lami - Jeti Lumo bado hakijafanyiwa kazi na kina mashimo makubwa. Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili mkandarasi amalize kujenga barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna mradi huu wa Davis Corner - Jeti Lumo na natambua pia kuna kiasi ambacho kimeshatengenezwa. Matumaini yangu baada ya kukamilisha kipande hiki sasa ile safari ndefu ya kuitengeneza barabara hii imeshaanza. Tulikuwa na shida kidogo ya kuendelea kulipa wakandarasi lakini mpaka hivi navyozungumza karibu wakandarasi wote nchi nzima wamelipwa. Kwa hiyo, kwetu sisi ni fursa ya kuendelea kufanya matengenezo ya barabara. kwa hiyo, nafikiri hata baada ya kikao tuzungumze ili tuone kwamba hiki kipande kinachobakia tuweze kuona kwamba kinaweza kukamilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba hizi barabara za Dar es Salaam na mzunguko wake zinaweza kutengenezwa. Pia kuna fedha ambazo zimeendelea kutolewa ili kuhakikisha kwamba kazi hazisimami na hasa baada ya mvua hizi kupungua tunarejeshea maeneo ambayo yalikuwa yameharibika ili waanchi wasipate adha. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Dar es Salaam na maeneo yote kwamba tumejipanga vizuri kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Hali ya vituo vya Polisi vya Kata pale Temeke ni mbaya sana, mapaa yameoza kabisa na Polisi muda mwingi wanafanya kazi chini ya miti badala ya kukaa kwenye ofisi kwa sababu hazikaliki. Hata hivyo, hata zile ofisi chache ambazo tumezijenga kwa nguvu za wananchi kama pale Makangalawe na Buza ambazo tumeshindwa kumalizia vyumba vya mahabusu na vya kutunzia silaha Serikali nayo imeshindwa kuvimalizia ili viweze kufanya kazi masaa 24. Sasa labda kwa sababu Mawaziri hawafahamu hali halisi iliyopo huko kwenye vituo hivyo ndio maana kila siku wamekuwa wakisema wanasubiri bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa kadri watakavyoweza kujipanga ni lini watakuwa tayari kuja kufanya ziara Temeke ili wakajionee hali halisi ya vituo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si sahihi kwamba hatufahamu au hatujafika. Binafsi nimeshafanya ziara katika Jimbo lake na Wilaya yake na nimeshiriki katika ujenzi wa kituo pale nimesahau jina la kile kituo, lakini ni maeneo ya Mbagala. Hali kadhalika nikashiriki katika uzinduzi wa kituo kingine cha Polisi nikizindua maeneo ya kule Wilaya hiyo ya Temeke lakini Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kwamba hali ya vituo vya Polisi vya Temeke tunaifahamu vizuri, kwa sababu physically nimekwenda na nimeshuhudia na tumeshiriki na wananchi kuweza kufanya kazi ya kuvijenga na kuvikarabati vituo vingine ambavyo ni vichakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ningemwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie ni kwamba, naye aendelee kuunga jitihada zetu hizi mkono kwa sababu si rahisi kuweza kukabiliana na changamoto hizi za vituo kwa wakati mmoja. Ndio maana tunafanya kazi hizi kwa awamu na kuhamasisha wadau kama sio wananchi na Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo niliwapongeza Waheshimiwa Wabunge waliopita hapa, Mheshimiwa Getere, Mheshimiwa Ntimizi katika suala hili hili la msingi ambalo nimejibu, basi na Mheshimiwa Mtolea naye tunakukaribisha aweze kuhamasisha wananchi hata kama akiamua fedha yake ya Mfuko wa Jimbo aingize katika kukarabati vituo hivi, tutamshukuru sana.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kweli udhamini katika soka la wanawake hauridhishi na league ya mpira wa miguu ya wanawake inaendeshwa katika mazingira magumu sana. Ni kwa nini isiwe ni lazima kila udhamini unaopatikana kwa league ya wanaume uende sambamba na udhamini pacha wa league ya wanawake? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba udhamini kwa timu za wanawake siyo mkubwa kama ulivyokuwa kwenye timu za wanaume, lakini lazima tuangalie historia kwamba league kuu nchi hii miaka 50 iliyopita ilianza kwa wanaume tu na tulianza na timu chache tu kama sita, lakini sasa hivi tuna timu 16 na mwaka ujao tutakuwa na timu 20. Kwa hiyo, imeongezeka ukubwa na udhamini wake lazima tuupiganie nao uwe mkubwa vilevile. Sasa hivi ndiyo tumeanza na ligi ya wanawake, tumepata udhamini mdogo, lakini tunaendelea na juhudi kuongeza ukubwa wa udhamini wa timu za wanawake kulingana na ukubwa wa league yenyewe.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu suala la kilimo na matumizi ya tumbaku, kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Afya imeridhia Sera ya Umoja wa Mataifa ya kupiga vita matumizi ya tumbaku; lakini Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inahamasisha kilimo cha tumbaku. Sasa nataka kujua kauli ya Serikali, ni upi hasa msimamo wetu kuhusu kilimo na matumizi ya tumbaku hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoongea Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kwamba katika Shirika letu lile la WHO wanapiga vita tumbaku na hususani katika masuala mazima yale ya afya lakini vile vile na mazingira na suala zima la child labour. Naomba nichukue fursa hii kipekee kabisa kusema kwamba nicotine yetu sisi kwenye tumbaku ni ndogo. Hata hivyo, niase wakulima wote nchini, kwamba wasitegemee tu zao la tumbaku vile vile kuna mazao mengine mbadala ambayo na yenyewe wanapaswa wawe wanazingatia na kuyalima pia. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wanahitaji umeme tena umeme wa uhakika lakini tumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme katika Mkoa mzima wa Dar es Salaam na hasa kule Temeke; na mwaka jana Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi hapa kwamba kufikia Disemba 2017 tatizo la kukatika kwa umeme litakuwa limekwisha, leo ni mwezi wa nne mvua zinanyesha na umeme unakatika sana Jijini Dar es Salaam. Serikali mnatuambia nini kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kwanza napenda nitoe taarifa katika Bunge lako hili, katika maeneo ya Mbagala na Gongolamboto kulikuwa na kero kubwa sana ya kukatika kwa umeme, wiki mbili zilizopita tumejenga sub - station imekamilika na kwa hiyo Mbagala sasa nina amini wanapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, umeme huu wa Mbagala ambao ni wa gridi naishukuru sana Serikali yetu, tumeanza sasa kuunganisha umeme wa gridi kutoka Mbagala kwenda Ikwiriri kupitia Kibiti mpaka Somanga Fungu na umeme huu wa Mbagala ambao unatoka kwenye Gridi ya Taifa ndio tunaunganisha katika Mikoa yote ya Mtwara na Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia mwezi uliopita nitoe taarifa katika Bunge lako kwamba hata Mikoa ya Mtwara na Lindi sasa itakuwa inapata umeme wa gridi badala ya umeme wa mashine inayotumia sasa. Hizo mashine zilizopo sasa zitatumika tu kama mashine za ziada. Kwa hiyo nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu inanisaidia sasa kutoa taarifa kwa wananchi wa Mbagala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kukatika kwa umeme kunatokana na sababu nyingi, sio sababu ya kuwepo kwa umeme au miundombinu, wakati mwingine ni kasoro ndogo ndogo, tunakiri kabisa zipo changamoto za maeneo machache kukatika kwa umeme katika baadhi ya nyakati za mida. Tutashirikiana na Waheshimiwa Wabunge kutatua matatizo hayo. Tunachoomba tupate taarifa inapotokea itilafu ya namna hiyo, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa wananchi wa Mbagala kwa sasa wanaendelea kupata umeme wa uhakika zaidi. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze sana Serikali kwa usimamizi makini wa barabara ambao ndiyo ulibaini kwamba barabara hii ilijengwa chini kiwango na kumtaka mkandarasi airudie kwa gharama zake hata hivyo nina maswali mawili madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, baadhi ya mitaro iliyojengwa katika barabara hii inapeleka maji kwenye majumba ya watu hasa maeneo ya Mtoni kwa Azizi Ally na Mtoni Mtongani. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kuwapeleka wataalam kwenda kuiangalia upya mifereji hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali itamalizia kipande cha kutoka Mbagala Rangi Tatu mpaka Kongowe kwa ujenzi wa barabara mbili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza pongezi alizozitoa nazipokea. Pili, kuhusu mitaro kupeleka maji majumbani, sisi kama Serikali tutashirikiana na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuhakikisha kwamba tunayatazama vizuri maeneo ambayo yana matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuendelea na ujenzi wa barabara kutoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Kongowe, niseme tu kwamba Serikali inayo mipango ya muda mrefu kuboresha barabara hii.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambapo imekiri uwepo wa matuta hayo ambayo siyo rafiki barabarani na wameanza kuchukua jitihada, nilitaka kujua ni lini sasa Serikali itakuwa imemaliza kuyapitia na kuyarekebisha matuta yaliyopo kwenye barabara ya Msata – Bagamoyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hivi karibuni Jeshi la Polisi kwa kupitia Kitengo chake cha Usalama Barabarani, wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuwadhibiti madereva wakorofi. Je, pamoja na kazi nzuri hii ya Jeshi la Polisi bado tunaona kuna tija ya kuendelea kuweka matuta kwenye barabara kuu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, tunaendelea kuyatoa matuta yote ambayo yameonekana kwamba hayafai kulingana na mwongozo ambao tumeutoa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mtolea kwamba muda siyo mrefu tutakamilisha kazi hii kwa sababu mpaka hivi ninavyoongea, tuko karibu asilimia 90 ya matuta yote ambayo tuliyatambua kwamba ni hatarishi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira kwa sababu kuyatoa matuta haya pia ni gharama; tutaendelea kuyatoa matuta yote sehemu hiyo uliyosema kutoka Msata kwenda Bagamoyo na maeneo mengine nchini. Kwa hiyo, vuta subira kasi yetu ni nzuri, tutayatoa matuta yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mtolea kwa kutambua na kuona udhibiti wa madereva tunaoufanya Serikali kupitia Mambo ya Ndani na sisi upande wa ujenzi. Mimi kama Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, tunahakikisha kwamba kwanza wananchi wanabaki salama, watumiaji wengine wa barabara wanabaki salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa tutaendelea kufanya udhibiti ili kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama kwanza, halafu tuendelee na hatua nyingine. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuhakikisha watu wetu wanakuwa salama. Kwa hiyo, tutaendela kudhibiti na kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali lwa kwanza, kama ambavyo Serikali inakiri umuhimu wa kituo hiki lakini ni muda mrefu sasa majibu yamekuwa ni haya haya kwamba bajeti itakaporuhusu, bajeti itakaporuhusu. Juzi tumepitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani na ujenzi wa kituo hiki haupo kwenye bajeti hiyo. Sasa nataka kujua Mheshimiwa Naibu Waziri anavyotuambia tusubiri bajeti itakaporuhusu ni bajeti ipi anayoizungumzia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wamekuwa wakijitahidi kujenga vituo vya polisi lakini vingi havifanyi kazi kwa saa 24 yaani havipewi hadhi ya kufanya kazi saa 24. Kwa mfano, Kituo cha Polisi cha Buza ambacho wananchi wamekijenga kwa kiwango cha hali ya juu lakini mpaka leo ni miaka mitano bado kinafanya kazi kwa saa 12 tu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kutoa amri kituo hicho kianze kufanya kazi kwa saa 24?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikijibu swali lake la kwanza kwamba bajeti ya mwaka huu haikuhusisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbagala. Hata hivyo, si Kituo cha Polisi Mbagala tu, vituo vya polisi vingi havikuhusishwa sababu ni kama nilivyozungumza mwanzo kwamba hatuwezi tukategemea bajeti ya mwaka mmoja itatue changamoto ya vituo vyote au maeneo yote. Kwa hiyo, kazi hii itaenda kwa awamu na kituo hiki kama hakijaweza kupata fursa katika bajeti hii basi kinaweza kupata fursa katika bajeti zinazokuja. Cha muhimu atambue Serikali inathamini na inatambua juu ya umuhimu wa ujenzi wa kituo hiki hasa ukitilia maanani changamoto za usalama katika Mkoa wa Kipolisi Temeke na Wilaya ya Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwanza niwapongeze yeye pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke kwa ujumla wao kwa jitihada zao kubwa ambazo wanachukua katika kusaidiana na Serikali kupunguza changamoto ya vituo vya polisi. Nami ni shahidi kwani nimeshiriki katika programu mbalimbali ikiwemo programu ya uchangishaji fedha wa kituo cha Chamanzi, ambapo sasa kipo katika hatua nzuri ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nimhakikishie kwamba tutakapomaliza kujenga vituo hivi madhumuni yake ni vitumike kama ilivyokusudiwa. Hoja ya kutumika saa 24 inategemea na aina ya kituo. Kwa mujibu wa PGO kuna Class A, B na C. Kuna vituo ambavyo vinapaswa vitumike kulingana na category ya class ya kituo hicho kwa muda wa saa 24 na viko ambavyo havipaswi kutumika kwa muda wa saa 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo ambacho amekizungumza ni Class C, kwa hiyo, hakiwezi kutumika kwa saa 24. Si kwa sababu labda hatuna askari wa kupeleka ama tumekitelekeza au hatuoni umuhimu huo lakini ni kwa sababu ya aina ya kituo na utaratibu ambao tumejiwekea kwa mujibu wa PGO.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la wanadiplomasia kutolipa kodi za pango halipo tu Arusha lakini pia lipo kwenye baadhi ya Balozi. Kwa mfano, Ubalozi wa Palestina nchini umepanga katika jengo linalomilikiwa na Halmashauri ya Temeke toka mwaka 2003 na mpaka leo hawajawahi kulipa kodi hata shilingi moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri imejaribu kufuata hatua mbalimbali za kudai ikiwa ni pamoja na kuripoti ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje lakini hakuna lolote lililofanyika. Tunahofia kuwaondoa kinguvu kwa sababu ya kulinda hiyo image ya ushirikiano wetu. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari leo kuwapa notice Ubalozi wa Palestina kwamba ndani ya miezi mitatu kuanzia leo wahame katika jengo hilo huku Halmashauri ikiendelea na taratibu nyingine za kudai deni lao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kuna utaratibu wa kidiplomasia wa kudaiana kati ya Serikali na Serikali na kwa vyovyote haiwezi ikawa kwa kupitia matamko ya Bungeni. Kwa hiyo, naomba tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala linafanyiwa kazi. Madeni yapo kila mahali, ni kawaida, awe na subira, nina hakika Serikali italifanyia kazi na changamoto hii itaondoka.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili naliuliza kwa mara ya pili, niliuliza kwa mara kwanza kwama 2016 na Serikali kweli ni sikivu ilifanya ukarabati mdogo mwaka 2016/2017. Hata hivyo, ukarabati huo haukumaliza tatizo kwa sababu bado maji taka yanachirizika kutoka gerezani kwenda kwenye makazi ya watu na ni hatari zaidi kwa kipindi hiki cha mvua ambayo maeneo hayo mengi yamefurika na maji ya mvua. Kwa hiyo kuna hatari kubwa ya kutokeza magonjwa ya mlipuko.

Je, Serikali ipo tayari sasa kama hatuwezi kujenga mashimo ya kutosha basi tuzibe zile njia zisitiririshe maji kwenda kwenye makazi ya wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, gereza hili ni gereza VIP ni gereza ambalo limejengwa kwa upekee sana ukifananisha na magereza mengine, ndio maana huhifadhiwa watu maarufu au wenye kesi kubwa kubwa, je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kulitazama gereza hili kwa jicho lingine ili watenge fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa gereza lote kwa pamoja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze wakati ule alivyoleta hoja yake ya changamoto ya gereza hili na yeye ameona uungwana wa kuipongeza Serikali kwa kutilia maanani yale aliyoeleza hapa Bungeni na tukayafanyia kazi. Nimhakikishie kwamba kama ambavyo tumefanya kipindi kile na haya ambayo ameyazungumza sasa hivi na yenyewe tatayachukua ili tuweze kuyafanyia kazi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali hata hivyo bado kuna changamoto mbili, tatu. Kwa mfano, madaktari wote wanaojitambulisha kama madaktari wa timu wanapokwenda na timu uwanjani, wengi siyo madaktari ni mashabiki tu ambao wanebeba hiyo mikoba ya first aid na hii ni hatari kwamba inapotokea matatizo wanakuwa hawana utalaam wa kutoa huduma ya kwanza viwanjani. Je, Serikali itakuwa tayari kuwashauri sasa TFF na Bodi ya Ligi kuwatambua madaktari wenye sifa ndiyo wapewe hiyo nafasi ya udaktari wa kuingia na timu viwanjani? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wachezaji wengi hawana bima za afya jambo ambalo linapelekea wanashindwa kujituma mazoezini na viwanjani kwa kuhofia kuumia. Serikali itakuwa tayari kuwashauri pia TFF badala ya kupoteza muda mwingi kuchunguza Makocha wamevaa nini sasa wakaongee na mashirika ya bima za afya ili waweze kuwapa bima za afya wachezaji?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa ni mdau mkubwa sana wa michezo na hivi majuzi


tumeshuhudia timu yake ya Umoja wa Vijana wa Temeke ikishinda kwenye Mashindano ya Ndondo Cup kwa msimu wa mwaka 2019. Kwa hiyo, hongera sana Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya msingi amezungumzia suala zima la madaktari wa timu kwamba wengi wa madaktari wa timu hawana vigezo au sifa za kuwa madaktari. Suala la timu zote kuwa na madaktari ni takwa la kikanuni. Nitumie fursa hii kwanza kuwataka wasimamizi wote wa vilabu nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanatumia madaktari ambao wana sifa za kuwa madaktari kwa sababu tunajua kwamba yako matatizo mbalimbali ambayo huwa yanawapata wachezaji pindi wanapokuwa kwenye mazoezi na kwenye michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Mbunge ametaka tuwashauri TFF wanatambua na kuhakikisha kwamba vilabu vyote vinakuwa na madaktari ambao wana sifa. Nitumie fursa hii kuwataka TFF kuhakikisha kwamba suala hili kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba ni vyema wakasimamia kuhakikisha kwamba vilabu vyote vinakuwa na madaktari wenye sifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili ametaka kujua kuhusiana na bima za afya. Suala la afya za wachezaji sisi kama Wizara tunalisimamia na ndiyo maana kwenye mashindano yote tunahakikisha kwamba kabla wachezaji hawajaenda kwenye mashindano wanapima afya zao. Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua kwamba kwa nini sisi kama Serikali tusiwashauri TFF waongee na mashirika ya bima za afya ili wachezaji waweze kupatiwa bima za afya, ushauri huu mzuri na sisi kama Wizara tumeupokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba TFF wameuchukua na wataufanyia kazi kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba kuhakikisha kwamba wachezaji wote wanakuwa na bima za afya. Suala la bima ya afya siyo tu wachezaji peke yake ni Watanzania wote na tumeona namna ambavyo Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba bima ya afya inakuwa jambo la msingi kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naipongezs Serikali kwa kazi kubwa inayoendelea ya ukarabati na ujenzi wa barabara mbalimbali pale Wilayani Temeke. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara kutoka Keko Furniture mpaka kwenye geti la Chuo Kikuu cha DUCE imekuwa na mashimo makubwa na imekuwa ni usumbufu kwa wanaotumia barabara hiyo ikiwa ni sambamba na kipande cha barabara ya Devis Corner, Jet corner hasa kipande cha kutoka Lumo mwisho mpaka Jet corner, vimekuwa na mashimo mengi sana na barabara hizi ziko chini ya TANROADS: Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuiagiza TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kuziba mashimo katika barabara hizi haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, barabara nyingi zilizo chini ya TANROADS na TARURA hasa barabara ya kutoka Temeke Veterinary kupitia Mwembe Yanga mpaka Tandika na barabara zote zinazoingia Tandika barabara zote katika Kata ya Temeke 14, Kata ya Sandali na Kata ya Buza hazipitiki kabisa; na uwezo wa Halmashauri ya Temeke kuzikarabati barabara hizi zote kwa kipindi hiki umekuwa ni mgumu: Je, Wizara yako kama mdau mkubwa wa miundombinu, ina mpango gani wa dharura wa kuisaidia TARURA kukarabati barabara hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli baada ya mvua nyingi hizi kunyesha barabara zetu nyingi zimeharibika kwa kiasi kikubwa. Nianze tu kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anafanya kazi kwa ushirikiano. Na mimi nimetembelea barabara hizi ikiwemo hii barabara ya Keko Furniture - DUCE nimeipita tena ni wiki ya juzi tu kuona hali ilivyo mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge na kwa maelekezo yangu kama tulivyojipanga ni kwamba tutarejeshea miundombinu ya barabara hii mvua zitakapopungua. Inakuwa siyo rahisi wakati huu mvua nyingi zinaendelea kunyesha kufanya ujenzi wa kiwango cha lami kwa maana ya kurudishia sehemu zilizoharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri, ndiyo maana tumeendelea kuyatambua maeneo yote ambayo yanahitaji kufanyiwa matengenezo na tutarudi kufanya matengenezo mvua zitakapopungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu pia barabara hii ambayo ameitaja ya Tandika na kimsingi barabara ambazo ziko TARURA, niseme tu kwa ujumla kwamba tunao utaratibu wa kushirikiana kama Serikali kwa upande wa TARURA na TANROAD. Inapokuwa tumepata dharura (emergency) au shida kama wakati huu, tunafanya kazi kama timu moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, tutashirikiana na wenzetu wa TARURA kuhakikisha kwamba mvua zikipungua tutafanya urejeshaji wa miundombinu muhimu katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofanya, nami namwahidi kumpa ushirikiano mkubwa; tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba tunawahudumia vizuri wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Muheza linafanana kabisa na tatizo lililoko pale Kurasini ambapo nyumba zilizokuwa za TRC zilikabidhiwa kwa TBA na TBA iliwauzia wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo, lakini sasa hivi baada ya TRC kuwa vizuri imeenda tena kuzidai nyumba zile na kuwavunjia vibanda wale watu ambao wamenunua nyumba hizo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inakwenda kutatua tatizo hili kwa kuwataka TBA kuwapa hati wale wote walionunua nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, uko utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi pale ambapo wanapopisha maeneo kwa ajili ya maendeleo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mtolea nikuhakikishie tu kama wananchi hawa walipewa hizi nyumba kihalali na wanastahili kulipwa, ni kwamba utaratibu uleule wa kupisha maeneo kwa ajili ya maendeleo utatumika kwa ajili ya kuwatazama hapo, lakini kwa sababu suala hili umelileta hapa naomba nilichukue kama mahususi ili tuangalie nini kilitokea na ili haki iweze kutendeka kwa wananchi hawa. Ahsante sana.