Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdallah Ally Mtolea (9 total)

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Kufuatia upanuzi wa barabara ya Kilwa mwaka 2002 wapo wananchi 80 waliolipwa maeneo ya Kongowe mwaka 2008 na wengine 111 walilipwa baada ya hukumu ya shauri lililofunguliwa na ndugu Mtumwa.
Je, Serikali itakamilisha lini malipo ya fidia ya nyumba zote zilizobomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili linaulizwa mara saba na Wabunge mbalimbali wa Temeke ikiwa ni pamoja na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ninawaombeni Waheshimiwa Wabunge tunapotoa majibu ni muhimu tukawaeleza wananchi majibu hayo na tukienda nje ya hapo tutakuwa tunarudia rudia na sisi wengine hatujisikii vizuri tunaporudia kutoa majibu .
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa wananchi wanaodai fidia kutokana na nyumba zao zilizokuwa zimejengwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ya Kilwa ambayo ilibomolewa mwaka 2002 kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 167 ya mwaka 1967.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nyumba hizo zilijengwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara na hivyo kukiuka Sheria ya Barabara namba 167 ya mwaka 1967, Serikali haina mpango wa kuwalipa fidia wamiliki wa nyumba hizo kwa kuwa hawastahili kulipwa fidia.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Ili Watanzania wanufaike katika ajira zinazotokana na shughuli za uchimbaji wa gesi na mafuta wanatakiwa kuwa na cheti cha Basic Off Shore Safety Certificate ambacho kwa sasa hakipatikani katika vyuo vya hapa nchini:-
Je, ni lini Serikali itakiwezesha Chuo cha DMI (Dar es Salaam Marine Institute) kianze kutoa kozi hizi ili wananchi wote waweze kupata cheti hiki ili waweze kuajiriwa katika shughuli za gesi na mafuta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Bandari kinachosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta na gesi kutoka hapa nchini kikiwemo Chuo cha DMI yaani Dar es Salaam Marine Institute na Norway, kinakamilisha maandalizi ya kuanza kutoa mafunzo na kujenga miundombinu inayotakiwa ili kuendesha mafunzo ya usalama katika sekta ya mafuta na gesi. Kutolewa kwa mafunzo hayo hapa nchini kutaongeza fursa ya ajira kwa wahitimu wetu kufanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi lakini pia kupata wanafunzi kutoka nchi jirani zenye viwanda vya mafuta na gesi kama Uganda, Sudan na Kenya. Tunategemea ifikapo Disemba, 2016 mafunzo hayo yatakuwa yameanza kutolewa na Chuo cha Usimamizi wa Bandari. Mafunzo yatatolewa kwa kufuata mitaala ya kimataifa na hivyo wahitimu watapewa vyeti vinavyotambuliwa Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Chuo cha DMI (Dar es Salaam Maritime Institute) kitaendelea kufanya maandalizi muhimu ya kumpata mtaalamu wa kufanya tathmini ya vifaa vya kufundisha kama vile helikopta dunker, bwawa la kuogelea, smoke house na kadhalika ili kuanzisha mafunzo hayo.
MHE. ABDALLAH H. MTOLEA aliuliza:-
Bunge liliridhia nyumba za NHC zilizowekwa katika kundi A ziuwe, kundi B zikarabatiwe, kundi C zijengwe upya:-
Je, kwa nini hadi leo baadhi ya nyumba zilizoagizwa kuuzwa hazijauzwa kwa wapangaji wake?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba swali hili limekuwa likiulizwa sana kwenye Bunge hili, lakini nataka nimjulishe mdogo wangu, Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea kwamba hakujawahi kutolewa uamuzi rasmi wa Serikali wala Bodi ya Shirika au halijawahi kuwepo azimio rasmi la Bunge hili kufikishwa Serikalini kutaka Serikali kufikiria kuuza nyumba hizo ulizozitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa mwaka 2010 ulionesha kuwa nyumba zinazomilikiwa na National Housing zina tija kubwa kwa Shirika na Taifa, hivyo nyumba hizo zilizotajwa hazitauzwa kwa kuwa ziko kwenye maeneo yenye thamani kubwa na ni mtaji wa kuliwezesha shirika kujenga nyumba nyingi zaidi zitakazowanufaisha wananchi wote na si wapangaji wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la sasa la shirika ni kuendelea kuzifanyia matengenezo nyumba zake na kuvunja nyumba kama hizo ambazo mamlaka za manispaa na halmashauri mbalimbali zimezi-condemn nyumba hizo na zile zilizochakaa vilevile ili kujenga nyumba mpya za kisasa zitakazotoa fursa zaidi kwa Watanzania wengi kuuziwa wakiwemo wapangaji hao.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Serikali iliipandisha hadhi Hospitali ya Temeke kuwa Hospitali ya Mkoa ambayo sasa inastahili kuhudumiwa na Wizara badala ya Halmashauri ili huduma inayotolewa hapo ifanane na hadhi ya Hospitali ya Mkoa.
Je, ni lini Serikali itaanza kuihudumia hospitali hiyo kwa kiwango kinachostahili ili kuipunguzia mzigo Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Serikali iliipandisha hadhi Serikali ya Temeke kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hiyo ni moja ya hospitali tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam zilizopandishwa hadhi kuwa Hospitali za Rufaa za Mkoa ikiwa ni pamoja na Hospitali za Mwananyamala na Ilala. Lengo ni kuhakikisha kuwa huduma za afya za kibingwa zinawafikia wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mheshimiwa Spika, katika mwendelezo wa kuboresha huduma za kibingwa kwa wananchi, tarehe 25 Novemba, 2017 Hospitali ya Temeke ni miongoni mwa hospitali 23 za Rufaa za Mikoa ambazo zilikabidhiwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka TAMISEMI wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua Hospitali ya Mafunzo ya Mloganzila. Wizara yangu imekabidhiwa hospitali hizi kutoka TAMISEMI tarehe 15 Machi, 2018.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha hospitali hii inatoa huduma kulingana na hadhi iliyopewa, Serikali imeweka vipaumbele vya kuboresha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na:-
• Vipaumbele vya kuongeza madaktari bingwa wanane katika fani za magonjwa ya akinamama, upasuaji, mifupa, mama na watoto na magonjwa ya ndani. Hospitali ya Temeke kwa sasa ina wataalam hao.
• Kuhakikisha upatokanaji wa dawa na vifaatiba.
• Kuhakikisha mipango ya hospitali inawekwa wakiasaidiana na Wizara katika kukarabati vyumba vya upasuaji, maabara na vyumba vya wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha hospitali hii ili kukidhi mahitaji ya wananchi kulingana na uwezo uliopo.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Tarehe 9 Desemba, 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere alisema tutauwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike nchi nzima na kuleta upendo, amani na kadhalika:-
Je, utaratibu huu wa kukimbiza Mwenge nchi nzima kila mwaka umetoka wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tarehe 9 Desemba mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema nanukuu;
“Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima palipojaa dharau.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima kila mwaka ulianzishwa mwaka 1964 baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa nchi mbili zilizokuwa zinaitwa Tanganyika na Zanzibar. Utaratibu huu ulianzishwa kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1992 mbio za Mwenge wa Uhuru zilitumika zaidi kueneza na kuwakumbusha Watanzania falsafa inayotoa misingi ya sera ya ndani ya nchi yetu baada ya kupata Uhuru. Misingi hiyoni kujenga Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu na usawa wa binadamu; na mbio hizi zilihasisiwa na Baba wa Taifa mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, pili, katika karne ya 20, kwa kutumia falsafa yake, mbio za Mwenge wa Uhuru zilitumika kumulika hata nje ya mipaka ya nchi yetu ili kuhamasisha vita vya ukombozi dhidi ya ukoloni mkongwe, dhuluma, ubaguzi na hasa katika Bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika, tatu, wakati tunaingia katika karne ya 21, mbio za Mwenge wa Uhuru baada ya kutimiza azma yake ya awali ya uhamasishaji wa msingi wa utaifa wetu na ukombozi wa Bara la Afrika, mbio hizi ziliendelea kukimbizwa nchi nzima kwa lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya maadui ujinga, maradhi na umaskini katika nchi yetu. Kupitia utaratibu huu Mwenge wa Uhuru umekuwa ni chombo muhimu cha kuchochea maendeleo ya wananchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la amani, haki, utu, muungano wetu na maendeleo kwa wananchi halina mipaka ya kijiografia wala muda maalum wa kulishughulikia. Hivyo, Serikali inaona ni muhimu kuendelea na utaratibu wa kuukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima kila mwaka ili uendelee kufanya kazi ya kuimarisha misingi ya Taifa letu na kuhamasisha maendeleo ya wananchi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-

Serikali inajitahidi kujenga barabara ili kupunguza foleni pamoja na kurahisisha usarifi na usafirishaji, lakini barabara zinawekwa matuta ambayo siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri jambo linalosababisha baadhi ya watumiaji wa barabara hizo kuzikimbia, kwa mfano, matuta yaliyowekwa katika barabara ya Msata – Bagamoyo:-

Je, matuta ni sehemu ya alama za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, alama za barabarani hutumika kutoa ujumbe wa matumizi sahihi ya barabara katika eneo husika. Alama hizo huwekwa kwenye milingoti pembezo mwa barabara au huchorwa katika uso wa barabara kutoa tafsiri sahihi ya matumizi ya barabara. Hata hivyo, kutokana na baadhi ya madereva kutozingatia alama za barabarani hususan, alama za ukomo wa mwendo (speed limit), Serikali hulazimika kujenga matuta katika maeneo ambayo ni hatarishi ili kuwalazimisha madereva kupunguza mwendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua kuwa baadhi ya matuta ya barabarani siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri, Serikali iliandaa mwongozo wa usanifu wa barabara wa mwaka 2011 Road Geometric Design Manual, 2011 ambapo pamoja na mambo mengine, imeweka viwango bora vya ujenzi wa matuta barabarani. Kwa kuzingatia mwongozo huo, Wizara yangu kupitia TANROADS imepitia upya matuta yote yaliyojengwa katika barabara kuu hapa nchini na kubaini kuwa matuta 323 siyo rafiki kwa vyombo vya usafiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya uboreshaji wa matuta hayo inaendelea ambapo hadi sasa matuta 281 yemerekebishwa. Baadhi ya barabara ambazo matuta yamerekebishwa ni Kibaha - Mlandizi (6), Morogoro – Iringa (12), Mara – Simiyu (matuta 12), Igawa – Songwe (matuta matatu), Uyole – Kasumulu (matuta mawili) Mwanza – Simiyu (matuta tisa), Shelui – Nzega (matuta matano), Singida – Manyara (matuta 23), Mtukula – Bukoba (matuta saba) pamoja na maeneo mengine kwa ujumla (matuta 202).

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwa ujumla kuwa matuta yote ambayo hayastahili kuwepo barabarani yataondolewa na yale ambayo hayakidhi kiwango yatajengwa upya. Aidha, natoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia alama za barabarani ikiwemo alama za ukomo wa mwendo (Speed limit).
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati gereza la Keko ambalo miundo mbinu yake imechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge Wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Keko ni moja ya magereza yaliyojengwa wakati wa mkoloni, hivyo hata miundombinu yake imekuwa ni ya muda mrefu inayohitaji ukarabati. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya jitahada za ukarabati kulingana na fedha inavyopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilifanya ukarabati wa mfumo wa maji taka kwa kuchimba mashimo ya kuhifadhia majitaka baada ya mashimo yaliyokuwepo kuzidiwa kutokana na idadi kubwa ya wahalifu waliomo ndani ya gereza hilo.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-

Baadhi ya mechi za mpira wa miguu za Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019 zilichezwa bila kuwepo kwa gari la wagonjwa uwanjani na kusababisha wachezaji walioumia kulazimika kukimbizwa Hospitali kwa kutumia magari ya kawaida:-

(a) Je, Serikali ina taarifa juu ya tatizo hilo?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kosa hilo halitokei tena viwanjani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu na sharti la kuwepo kwa magari ya wagonjwa viwanjani ili kuhudumia wachezaji na hata watazamaji wanaopatwa na dharura kubwa za kiafya na dharura inayohitaji huduma haraka ya matibabu. Aidha, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) linaheshimu Kanuni hiyo pamoja na kwamba utekelezaji wake katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu unakawamishwa na uhaba wa magari ya wagonjwa ambayo huchelewa kufika uwanjani siyo kwa makusudi bali ni kwa kutingwa na huduma zingine za tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, ni mechi ya Mbao FC dhidi ya Coastal Union iliyochezwa katika Uwanja wa CCM-Kirumba ambapo mchezaji aliumia kipindi cha kwanza lakini gari la kubebea wagonjwa lilikuja kipindi cha pili kutokana na gari hilo kuwa na majukumu mengine Mkoani hapo. Hali hii inasababishwa na ukweli kwamba hakuna Chama cha Soka cha Mkoa kinachomiliki magari ya wagonjwa, magari yote yanapatikana kwenye Halmashauri husika, baadhi ya hospitali za Serikali na asasi zenye magari ya wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, natoa wito kwa Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na mamlaka nilizozitaja kwenye huduma hii ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa kukosa huduma hiyo inapohitajika. Aidha, nawahimiza TFF na uongozi wake wa Mikoa kujiongeza kwa kufikiria njia rahisi zaidi za kubebea majeruhi kama vile pikipiki maalum za miguu mitatu au miwili kwenye mechi za ligi ya chini ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa majeruhi kucheleweshwa kupelekwa hospitalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ISSA A. MANGUNGU (K.n.y. MHE. ABDALLAH A. MTOLEA) aliuliza:-

Eneo la kipande cha barabara ya Kilwa – Rangi Tatu – Kongowe limeharibika vibaya na kusababisha foleni na ajali nyingi.

(a) Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kikamilifu kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero hizo?

(b) Je, ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kipande hicho kwa njia nne mpaka Kongowe itaanza lini?

(c) Daraja la Mto Mzinga katika kipande hicho lipo katika hali mbaya na hatarishi: Je, ni lini Serikali itajenga daraja jipya kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a),( b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara katika Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kushughulikia tatizo la msongamano wa magari katika Jiji hilo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kwa awamu ya pili, (BRT Phase II) ambao unahusisha barabara ya Kilwa kuanzia Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu. Kazi za ujenzi wa barabara na vituo vya mabasi ulianza mwezi Mei, 2019 na umepangwa kukamilika mwaka 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usanifu kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Kilwa kuanzia sehemu ya Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe yenye urefu wa kilometa 3.8 kutoka njia mbili kuwa njia nne. Usanifu huo unahusisha Daraja la Mzinga. Baada ya kukamilika kwa usanifu huo, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi.