Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Abdallah Ally Mtolea (1 total)

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru kwa majibu yako mazuri, lakini pamoja na hayo, hizi tozo zinazotokana na ardhi kwa maana ya Property Tax na Service Levy, it‟s just a peanut kwenye uwekezaji ambao umekuwa ukifanyika. Kwa mfano, katika uwekezaji wa EPZA ambao unafanyika katika Kata ya Kurasini kwenye Halmashauri ya Temeke; ardhi ambayo Halmashauri tumeitoa, kwa sasa ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 100. Unatoa ardhi ya shilingi bilioni 100 halafu uende ukasubiri mrejesho kwa kupitia Property Tax na Service Levy vinakuwa havifanani. Hivi kweli Ofisi yako haioni umuhimu wa kuifanya Halmashauri ya Temeke kupata angalau hisa 10 katika uwekezaji huu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Wakati huu tukiwa tunafanya mabadiliko makubwa na mapitio makubwa kwenye uwekezaji katika maeneo yote, tunaanza kugundua baadhi ya changamoto ambazo zinajitokeza, lakini pia usimamizi wa maeneo hayo pia tumeanza kuona kwamba upo umuhimu wa mamlaka yenyewe kuwa inaweza kuweka mipango yake ili iweze kupata manufaa ya uwekezaji uliopo. Moja kati ya mifano niliyonayo kwenye Halmashauri ya Temeke ni pale Temeke mwisho eneo ambalo mmebomoa majengo na sasa mmepata mwekezaji wa kampuni moja ya Kichina.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ndiyo inafanya maamuzi ya uwekezaji ule na ndiyo aina nyingine ya uwekezaji nilioutaja kwamba Halmashauri inaweza kunufaika zaidi. Sasa hivi mpo kwenye mjadala wa manufaa yenyewe na tozo ambazo mtazipata kutoka kwenye kampuni ile. Kwa hiyo, utaratibu ule pamoja na usimamizi wa Halmashauri yenyewe, lakini bado Serikali sasa tunataka tuipeleke ili iweze kuona kwamba je, Halmashauri yetu inaweza kunufaika?
Mheshimiwa Spika, ninachoweza kusema sasa ni kwamba, Serikali inaandaa utaratibu wa kusimamia uwekezaji wa namna hii ili Halmashauri zetu za Wilaya, Manispaa ziweze kupata tija kwenye uwekezaji ambao sasa tumefungua milango kwa wingi na watu wengi wanaingia kwa ajili ya uwekezaji ili Halmashauri zetu zisiweze kukosea.
Mheshimiwa Spika, wito wangu kwa Halmashauri zote nchini na Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani, tuzingatie sana kwamba uwekezaji huu unaofanyWa kwenye maeneo yetu unaleta tija kwenye Halmashauri zetu na lazima tusimamie hilo kwa pamoja na Serikali itaanza kufanya ufuatiliaji wa kina kuona kuwa uwekezaji ule kwenye Halmashauri zile za Wilaya unawaletea tija Wanahalmashauri hiyo wakiwemo Baraza la Madiwani ambao ndiyo wasimamizi wakuu. Kwa hiyo, tutaendelea kufuatilia uwekezaji huu tuone tija ambayo inaweza kupata pia Halmashauri zetu kote nchini.