Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdallah Ally Mtolea (40 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami kwanza nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Temeke kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuwatumikia. Nawaahidi tu wasiwe na wasiwasi, nitawatumikia kukidhi mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeipitia hii hotuba ya Mheshimiwa Rais na yako mambo ameyataja, lakini vizuri tungependa tuyaongezee nyama ili Serikali inapokwenda katika utekelezaji wake, basi iweze kuyatekeleza haya kwa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la afya. Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya afya hasa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam. Serikali iliwahi kuzipandisha hadhi hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala kuwa katika hadhi ya Hospitali za Mkoa, lakini baada ya kuzifanyia hivyo, haijawahi kuzipa support kwa maana ya kuzihudumia kama Hospitali za Mkoa na badala yake majukumu hayo yameachiwa Halmashauri, na kwa uwezo wa Halmashauri zetu imekuwa ni vigumu kuhakikisha inaboresha huduma katika hospitali hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana sasa hivi hospitali hizi za Temeke, Amana na Mwananyamala zimebaki kuwa kama sehemu ya mifano mibaya, yaani ukitaka kutoa mifano mibaya au kuonesha watu kwamba huduma mbaya hospitalini zinapatikana wapi, basi ni vizuri ukawapeleka katika hospitali hizi, maana watashuhudia wagonjwa wanalala chini, dawa hakuna, au wengine wakilala watatu watatu kwenye vitanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali hii ya Awamu ya Tano ikahakikisha kwamba matatizo ya vitanda, wauguzi na dawa hospitalini yanakwisha kabisa. Tupatiwe vitanda vya kutosha katika Hospitali ya Temeke, tupate madawa, wananchi watibiwe pale; na wakifika waone kwamba wamefika sehemu salama na magonjwa yao yatakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni elimu. Serikali imeanza kwa kuondoa michango na ada, lakini hili ni suala dogo sana katika matatizo ya elimu yanayoikabili nchi hii. Bado hizi shule, hasa Shule za Msingi. Kwa Dar es Salaam tu ukitembelea Shule za Msingi utagundua
kwamba shule zina matatizo makubwa, achilia mbali tatizo la madawati, lakini majengo yenyewe, mapaa yametoboka, sakafu zimekwisha. Kuna madarasa ukipita unaweza kufikiri kwamba hapa ni kituo cha kuwekea ng‟ombe kabla hawajakwenda kuchinjwa, lakini kumbe ni
madarasa hayo, watoto wanakwenda kusoma pale. Unajiuliza, mtoto huyu anawezaje kuipenda shule akiwa anakaa chini, hana madawati, sakafu imeharibika na juu kunavuja?
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tunakoelekea katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali iamue jambo moja, itoe mikopo ya elimu kuanzia Shule za Msingi ili mzazi aweze kuchagua shule ya kumpeleka mtoto wake kulingana na viwango vya ufaulu na siyo kwa sababu tu hana ada.
Hii itatusaidia kuondoa ile gap ya nani anasoma katika shule nzuri na nani asome katika shule mbaya. Maana yake anayesoma katika shule nzuri ndiye atafanikiwa; na hao ni watoto wa matajiri; hao ambao wanasoma kwenye shule hi zo mbovu, hawawezi kufanikiwa, tunaua vipaji
vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa napenda Serikali ilichukulie hili kama jambo muhimu sana. Tuondoe madaraja ya elimu kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake alizungumzia suala la Mahakama Maalum kwa ajili ya Mafisadi, lakini amesahau pia kuzungumzia Mahakama Maalum ya wale wanaowatesa na kuwaua ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu tumekuwa na hili tatizo. Albino wanauawa, wanakatwa viungo vyao, na hizi kesi zao zinachelewa sana Mahakamani. Mwisho wa siku hata wale wachache ambao wamehukumiwa, hasa waliohukumiwa vifungo vya kunyongwa hadi
kufa, inasemekana hakuna aliyewahi kunyongwa. Hiyo ni kwa sababu kabla ya utekelezaji wa hiyo adhabu, Mheshimiwa Rais anahitaji kusaini kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya kikatiba.
Sasa tumtake Rais huyu wa Awamu ya Tano atuoneshe mfano kwamba na yeye anachukizwa na mauaji ya albino. Atie nguvu kuhakikisha kesi zile zinasikilizwa na zinafika mwisho haraka. Waliohukumiwa kunyongwa, wanyongwe mpaka kufa ili jamii ione kwamba kweli Serikali imeamua kukomesha tatizo la mauaji ya albino. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa sisi tunaokaa Dar es Salaam hasa pale Jimboni kwangu Temeke ambako ni moja kati ya maeneo ambayo yameathirika na matumizi haya ya dawa za kulevya, hatuamini kama kweli Serikali imewahi kuchukua jitihada za dhati au ina mipango ya dhati ya kukomesha uingizwaji na usambazwaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa uingizaji wa dawa za kulevya katika nchi hii haujawahi kuyumbishwa hata kidogo. Mfumo wa kuingiza mafuta ya petroli ukiyumba, siku mbili tu utaona watu wanahangaika kutafuta mafuta. Mfumo wa chakula ukiyumba, utaona watu
wanahangaika kutafuta chakula, lakini niwahakikishieni, hatujawahi kuona hawa watumiaji wa dawa za kulevya wakihangaika kutafuta dawa hizo. Maana yake mfumo wa kuingiza na kusambaza haujawahi kuyumbishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaitaka Serikali hii ya Awamu ya Tano kuweka jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba inadhibiti uingizaji wa dawa za kulevya, lakini pia usambazaji huko mitaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku tunapishana na polisi na magari yao hayo maarufu kama defender, wamekamata wauza gongo na wauza bangi, lakini hatuoni wakikamata hawa wanaouza dawa za kulevya. Huwezi kuniambia kwamba wanaouza haya dawa za kulevya
wanajificha sana, kwa sababu wale watumiaji wenyewe muda wote unawakuta kama wameshalewa, lakini akizunguka nyumba ya pili, ya tatu ameshapata, anatumia tena. Ni kwa nini Serikali haiwaoni? Kwa nini isidhibiti huku kwa wauzaji wadogo wadogo ambao ndio
wanaotuharibia vijana wetu na ndugu zetu? Kwa hiyo, tunaomba Serikali ya Awamu ya Tano iweke macho sana katika kukomesha
uingizaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni hili la amani na usalama. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake pale ukurasa wa kumi amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wananchi (CUF) na CCM zinafanya jitihada ya kuondoa tatizo
la kisiasa lililopo Zanzibar. Hapa ukiangalia kauli hii ni kama vile Mheshimiwa Rais anajitoa katika kushughulikia tatizo la Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, unawezaje kuiachia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ishughulikie tatizo la Zanzibar wakati tatizo lenyewe linahusu kuiweka Serikali madarakani? Serikali imemaliza muda wake, Serikali nyingine haitaki kutangazwa. Tumtake Mheshimiwa Rais ambaye kimsingi wananchi tuna imani naye kubwa sana, ameanza kuonesha kwamba analolisema analitekeleza. Hebu aamue sasa kusema kwamba aliyeshinda katika uchaguzi wa Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2015 atangazwe kuwa Rais. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Uchaguzi haujaisha! (Makofi)
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuona suala la Zanzibar kama ni la Zanzibar, lakini hili suala siyo la Zanzibar, ni suala la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii heshima ya amani na usalama ambayo Watanzania tunayo leo ni kwa sababu
nchi nzima iko salama. Sehemu moja ikianza kutumbukia katika machafuko, hakuna atakayekuwa salama hata huku kwetu. Kwa hiyo, tulichukulie hili jambo kama suala la Kitaifa na siyo suala la kisiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anafahamu kilichotokea katika uchaguzi wa Zanzibar. Mshindi kapatikana na kama kuna matatizo kwenye baadhi ya Majimbo, uchaguzi urudiwe kwenye Majimbo hayo ambayo yana matatizo, siyo uchaguzi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Serikali hii, tumwombe Mheshimiwa Rais ahakikishe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtolea, ahsante. Naomba umalize.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumwombe Mheshimiwa Rais ahakikishe mshindi kwa uchaguzi wa Zanzibar anatangwazwa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia kidogo katika bajeti ya Wizara hii ya Katiba na Sheria kwa niaba ya wananchi wa Temeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nioneshe masikitiko yangu makubwa kwa Bunge lenyewe kwa sababu Bunge limeunda Kamati na miongoni mwa Kamati ambazo limeziunda limeunda Kamati ya Sheria Ndogo. Kwa uelewa wa kawaida, Kamati ya Sheria Ndogo ilikuwa iwe Kamati pacha ya Katiba na Sheria. Kwa hiyo, ilikuwa tutegemee hapa wakati Kamati ya Katiba na Sheria inawasilisha pia kungekuwa na wasilisho kutoka Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Kamati ya Sheria na Katiba imejikita katika sheria mama ambapo utekelezaji wa hizi sheria mama upo chini ya sheria ndogo ndogo ambazo ziko nyingi na hizo ndizo zinazowagusa Watanzania. Kwa kukosa nafasi ya kuzisemea sheria ndogo hizo katika Bunge hili si jambo zuri. Mwishoni unajiuliza hivi hii Kamati ya Sheria Ndogo yenyewe ikasemee wapi maana Kamati zote zimekuwa connected na Wizara na zinapata nafasi ya kuwasilisha hapa isipokuwa Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumza kwamba tunataka tutengeneze Taifa la kijani kwamba mwanamama Mtanzania aache kutumia mkaa atumie gesi unazungumzia sheria ndogo ndogo zitakazosimamia uagizaji wa gesi hiyo ili ipatikane kwa bei nafuu. Usipopata nafasi ya kuzisemea hapa unakwenda kuzisemea wapi ili uhakikishe kwamba hilo Taifa la kijani linakuja? Unaposema kwamba gharama ya ndege hapa nchini imekuwa kubwa unazungumzia uagizaji mbovu wa mafuta ya ndege ambapo waagizaji wanajiwekea bei zao wenyewe. Hapo unahitaji sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia haya ili Mtanzania aweze kusafiri hapa ndani ya nchi kwa tiketi za bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Land Registration Act inampa mamlaka Waziri kuweka kanuni na sheria ndogo ndogo za kusimamia vibali vya makazi. Katika hili, pale Dar es Salaam pana changamoto sana na hasa jimboni kwangu. Vile vibali vya makazi vimeainisha kwamba watu wanaokaa mita 60 kutoka kwenye reli ya TAZARA hawastahili kupewa hivyo vibali vya makazi. Hapa wanasimamia Sheria Ndogo ya mwaka 1995 inayoongeza eneo la kuachwa wazi kutoka kwenye reli lakini hao watu ambao wananyimwa vibali hivyo wamekuwepo hapo kabla ya sheria hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wakazi pale kwenye Kata za Mtoni, Azimio, Tandika, Kilakala, Yombo Vituka na Sandali ambao toka mwaka 2002 nyumba zao zimewekwa alama ya ―X‖ na watu wa TAZARA wakisimamia hiyo sheria ya mwaka 1995 inayowataka wahame bila kulipwa wakati watu hao walikuwepo pale kwa muda mrefu. Tunapoacha kuzijadili hizi sheria ndogo tunawaacha Watanzania walio wengi kwenye matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri mkalitazama hili kwa kushirikiana na Wizara hii ili tuone haya mambo tunakwenda kuyashughulikia kwa namna gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee kabisa nimpongeze sana Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa namna ambavyo amewasilisha hotuba yake yenye mashiko, iliyojaa facts na imedhihirisha kama kweli imewasilishwa na Wakili msomi. Suala la watu wanaipokeaje, hilo si jukumu lake, yeye amewasilisha na ni ukweli utaendelea kubaki kuwa ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na hili suala mnaliita kiporo, suala la Katiba Mpya. Mchakato huu wa Katiba Mpya wakati unaanza kwanza harakati zake hazikuwa za muda mfupi, zilianza muda mrefu na hazikufanywa tu na wanasiasa zilifanywa na taasisi mbalimbali. Baadaye Serikali ya Awamu ya Nne iliona kwamba kweli kuna umuhimu wa kupata Katiba Mpya kwa sababu jambo hili mnakuwa mnatafuta muafaka wa kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato ulianza vizuri lakini ulikuja kuharibika kwenye Bunge la Katiba. Hatua za awali za ukusanyaji wa maoni zilikuwa ni nzuri kweli kweli lakini ilipofika kwenye Bunge la Katiba mchakato ule uliharibikia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Taifa hili na Serikali hii ya Awamu ya Tano inatamani kuendeleza muafaka huo wa kitaifa kwamba hili Taifa lipate Katiba Mpya, ni vizuri mchakato huo ukarejewa kuanzia pale kwenye Bunge la Katiba na Mheshimiwa Rais ana mamlaka hayo. Kwa mujibu wa kifungu cha 28(2) cha Sheria Na. 83 ya 2011 maarufu kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inampa mamlaka hayo Mheshimiwa Rais kuweza kuliita tena Bunge la Katiba na kujadili mapendekezo yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Kama kweli wote nia yetu ni moja tunakwama wapi? Ndugu zangu wana CCM jambo hili litawajenga ninyi. Mnapoanzisha mchakato, mkausimamia na ukafika mwisho mnajitengenezea heshima ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo likiishia kati mnawapa wasiwasi sana Watanzania. Jana tumepitisha hapa bajeti ya Wizara ya Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema anataka kulitoa jembe la mkono na kuliweka makumbusho, watu wanahoji, mmeshindwa kulitoa jembe la mkono kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi unawezaje kulitoa shambani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nia ni hiyo, watu waliofanya marketing wanajua, kile kinachopepea kwenye bendera kinapeleka ujumbe mzuri sana kwa wananchi. Kumbe tungeanza kwenye bendera ya Chama cha Mapinduzi kuondoa nyundo na jembe la mkono tukaweka computer na trekta ili kuonyesha kwamba kile tunachokihubiri ndicho tunachokisimamia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ishauri Serikali hii iuanzishe mchakato wa Katiba Mpya kuanzia kwenye Bunge la Katiba. Kuupeleka mbio mbio kweli tutafanikisha tutaileta Katiba lakini itakuwa si Katiba ambayo wananchi walikuwa wakiitarajia na hili haliwezi kutusaidia, tutakuwa tukiendelea kuimba Katiba Mpya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni huu mrundikano wa kesi. Mrundikano wa kesi mahakamani umekuwa ni mkubwa sana na work load kwa Majaji na Mahakimu ni mkubwa. Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa kwamba ni kesi 200 kwa Jaji, huo si mzigo mdogo, huo ni mzigo mkubwa sana. Inafika mahali labda shahidi hajatokea siku moja Jaji anakuambia mimi nina kesi nyingi msinisumbue, mimi ninaendelea tu. Sasa haya mambo ya kutafuta haki za watu huwezi kuyapeleka namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuone katika bajeti hii kwamba kuna vifungu vya kutosha kuweza kuongeza Majaji na Mahakimu ili kesi hizi ziweze kuisha. Kusema tu kwamba tunahitaji twende kwenye zero case bila kuwa na Mahakimu na Majaji wa kutosha maana yake utakwenda kulazimisha Majaji na Mahakimu waliopo wazimalize hizo kesi kwa namna yoyote ile na justice haitaki namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni uchakavu wa majengo. Majengo ya mahakama yanatia aibu kweli kweli. Kibaya zaidi nature ya hao wanaofanya kazi kwenye hayo majengo mabovu ni kuwa watu nadhifu. Tunawafedhehesha sana kuwarundika Majaji na Mahakimu kwenye vijumba vya hovyo, vyenye joto la ajabu na kwa unadhifu wao wamevaa tai na suti kubwa, kwa nini tunawatesa watu hawa?
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Wizara hii ikajipanga, iombe fedha ya kutosha kuhakikisha kwamba wanawatengenezea Majaji na Mahakimu majengo yenye heshima ya kuwa ofisi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa uwezo wa kunipa nafasi ya mimi kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara kwa niaba ya wananchi wa Temeke na kwa maslahi mapana ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukimsikiliza hapa Mheshimiwa Waziri ni kwa namna gani anapenda kuiona Tanzania ambayo imesheheni uwekezaji katika sekta mbalimbali ili kuifanya nchi hii iwe ya kipato cha kati. Hili ni jambo zuri na kila mtu angependa siku moja kuiona Tanzania hiyo. Wakati pia tunajipanga kuwakaribisha wawekezaji kwa kiasi kikubwa, ni vizuri pia tukawa na mpango maalum wa kuona ni kwa namna gani tutawasimamia wawekezaji hao ili uwekezaji wao uwe na tija kwa Taifa hili na kwa wananchi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano michache ya wawekezaji ambao sasa hivi wapo, inatutia mashaka kweli kweli. Haioneshi kama uwekezaji wao una tija na malengo mazuri kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jimboni kwangu Temeke, eneo la viwanda Chang‟ombe lina wawekezaji wengi, lakini kwa masikitiko makubwa yamekuwa ni maeneo ya mateso kwa Watanzania, maeneo ya mateso kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wananyanyaswa kwa kiasi kikubwa sana katika viwanda na makampuni hayo, kwa kulipwa mishahara midogo sana, kufanyishwa kazi ngumu kwa masaa mengi, hawana vitendea kazi; unamkuta mtu katika kiwanda pengine cha kuyeyushia chuma hana vifaa vya kufanyia kazi. Yupo tumbo wazi, mikono mitupu, hana mask, anafanya kazi kwenye moto mkubwa kiasi hicho. Wawekezaji wanawaambia kabisa, kama hutaki kazi acha, kuna wenzio 300 mpaka 400 wanasubiri hiyo kazi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inapofikia mahali wawekezaji wanawanyanyasa wananchi kwa sababu tu kuna tatizo kubwa la ajira, ni lazima tufikirie mara mbili, ni namna gani tujipange tuweze kuufanya uwekezaji huu uwe na tija kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tungependa tuwe na wawekezaji wenye masikio yanayosikia wawekeze kwa kufuata sheria na taratibu za nchi hii. Hapo hapo Chang‟ombe, kuna wawekezaji wamejenga viwanda na ma-godown yao juu ya mifereji ya kutiririsha maji machafu. Yaani wanaziba miundombinu ya kutolea maji mitaani kwa maana ya uwekezaji. Unajiuliza, ni kweli tunasimamia huu uwekezaji? Kwa hiyo, kuna wananchi pale Chang‟ombe kwa muda wa miaka 12 sasa, kila ikinyesha mvua kwao ni mafuriko, kwa sababu tu kuna watu wamejenga magodauni yao na viwanda vyao, wameziba mifereji ya maji na hakuna mtu wa kuwaambia kwamba hili mnalolifanya ni kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi, wanatiririsha maji ya kutoka viwandani yanaingia mitaani unajiuliza hawa wanaoitwa NEMC wako wapi? Wanaandikiwa barua, wanapigiwa simu, hakuna kitu wanachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akafahamu kwamba Taasisi zinazomzunguka zina mchango mkubwa sana wa kuzifanya ndoto za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati, zitimie au zifeli. Ni vizuri akaziangalia tena upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Sandali ambayo nayo ipo katika Jimbo hili hili la Temeke, ambayo inapakana na viwanda vya Vingunguti vilivyoko katika Jimbo la Segerea, kuna mfereji unaotiririsha maji ya sumu yanayonuka vibaya na yanayoathiri mazingira kuanzia Januari mpaka Desemba. Wananchi wa Mitaa ya Mamboleo „A‟, Mamboleo „B‟, Kisiwani, Usalama wakijenga nyumba ukaezeka bati leo, baada ya miezi sita, zile bati zinakuwa zimetoboka zote na ukizigusa zile kuta za nyumba, yale matofali yanamong‟onyoka. Sasa jiulize, afya za wananchi wa hapo zikoje? Kama mabati yanatoboka hivyo, afya za wananchi zikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akimaliza bajeti yake hapa, afanye utaratibu afike Temeke ajionee. Twende nikakuoneshe yanayofanyika, uone wananchi wanavyoteseka na uwekezaji ambao tunautaka uingie sasa hivi. Upite na kwenye ma-godown uone. Kwa mfano, kwenye viwanda labda vinavyotengeneza unga, wakisikia watu wa TBS wanakuja, siku hiyo utatengenezwa unga maalum kwa ajili ya kuwaonesha TBS, lakini siyo ule unaotengenezwa kila siku. Kwa hiyo, kumbe hata afya zetu kwenye hizi bidhaa zinazozalishwa, ni matatizo (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna raia wengi wa kigeni wasiokuwa na documents za kukaa hapa nchini, wamefungiwa kwenye hayo ma-godown wanafanya kazi ambazo Watanzania wangezifanya. Kwa hiyo, kuna miradi mikubwa ya watu, kuwaficha watu, kuwatumikisha wakidhulumu nafasi za Watanzania. Lazima tuyatoe haya, ndiyo uwekezaji utakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hawa watu wa viwanja vya biashara vya Saba Saba na uwanja wa Mpira wa Taifa; uwanja mkubwa wa Taifa na Uwanja wa Uhuru; hawa watu hawalipi kodi. Hawalipi malipo wanayostahili kuilipa Halmashauri ya Temeke. Hawalipi property tax wala service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Halmashauri iweze kutekeleza majukumu yake ya kuboresha huduma za kijamii ni lazima ikusanye kodi. Unapokuwa na wawekezaji au watu wanaofanya biashara ambao hawakulipi, unakuwa ni mzigo mkubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa nafasi yake, aongee na hawa watu wa Saba Saba na Uwanja wa Taifa. Tumewapelekea invoice kwa muda mrefu na hawajalipa. Sasa akawaambie nitawajazia watu siku siyo nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawakusanya wananchi wa Temeke twende tukazuie kufanya biashara zao, twende tukazuie mechi zisichezwe Uwanja wa Taifa. Najua tutapigwa sana mabomu, lakini I am very proud kwamba watu wa Temeke wakilitaka lao, hawaogopi mabomu. Kwa hiyo, tutayafanya hayo endapo wataendelea kukaidi kutulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia fedha za Halmashauri kusafisha yale mazingira baada ya mechi kuchezwa, baada ya maonesho ya Saba Saba; kwa nini tutumie fedha yetu na wao hawataki kuchangia? Hatuhitaji uwekezaji wa namna hiyo. Kwa hiyo, wafikishie taarifa, waambie kwamba tutakuja tuyafanye hayo. Tutazuia moja kati ya maonesho Uwanja wa Saba Saba, lakini tutazuia moja ya mechi Uwanja wa Taifa nao waione hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wakati wengine wanahitaji viwanda, sisi Temeke tunahitaji masoko. Tuna viwanja vikubwa vya kujenga masoko kwenye kila Kata na wafanya biashara wako tayari kufanya biashara katika masoko hayo. Tuletewe wawekezaji watujengee masoko ya kisasa na fedha yao itarudi haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waambie NSSF waache kujenga madaraja, waje wawekeze kwenye masoko, fedha yao itarudi haraka sana. Waambe National Housing waache kwenda kujenga majumba maporini wanahangaika kutafuta wapangaji, waje kuwekeza sokoni.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi lakini pia nikupongeze kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeza sana Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni ukweli na itakuwa busara sana Wizara ya Afya ikaichukuwa na kuyatumia yale yote ambayo yameainishwa mle. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameahidi kutupatia vituo vya afya kwenye kila kata. Kwa hiyo, hili ni deni ambalo Serikali ya Awamu ya Tano tunaidai. Tulikuwa tunategemea katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa ita-reflect moja kwa moja kwenye ahadi ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ama amezitaja au hakuzitaja lakini nataka Wizara ijue kwamba sisi kama Watanzania tunategemea kuona vituo vya afya kwenye kila kata. Mimi nikuambie tu Temeke ambako nina kata 13 tuna kituo cha afya kimoja na Hospitali ya Temeke kwa hiyo nakudai vituo vya afya 12. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakati wako nitakufuata uniambie tunavipataje ndani ya miaka hii mitano. Kama ni kupata viwili kila baada ya mwaka, kupata vitatu kila baada ya mwaka itakuwa ni jambo zuri. Kimsingi tunahitaji ahadi mlizozitoa zitekelezwe kwa sababu wananchi wanazisubiria. Laa kama mnaona yale mlioyaahidi hayawezi kutekelezeka basi isemwe ili tujue kwamba tunatafuta source zingine kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kwa sababu sisi kama Wabunge bado tuna nia thabiti ya kuwasaidia wananchi kuhakikisha kwamba huduma ya afya inapatikana katika maeneo yao ya karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilitaka kuishauri Wizara ya Afya, wakati inafanya allocation au namna ya kuzisaidia hizi hospitali izingatie sana mazingira ya kijiografia. Sisi katika Hospitali ya Temeke tunapata taabu sana pale kwa sababu muda wote hospitali inazidiwa na wagonjwa kwa sababu tu ya mazingira ya kijiografia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Temeke inapakana na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania kwa maana ukitoka Temeke sasa ndiyo unaelekea Kusini. Kwa jiografia tu mbaya ya Mkoa wa Pwani, nasema jiografia mbaya kwa maana Mkoa wa Pwani umekatwa kati na Mkoa wa Dar es Salaam. Sasa mtu hawezi kutoka na mgonjwa labda Utete akampeleka Tumbi - Kibaha yaani avuke Temeke, haiwezekani maana yake atamshusha Temeke. Mtu hawezi kutoka na mgonjwa Kibiti akaipita Temeke aende Tumbi - Kibaha atamshusha Temeke halikadhalika na Mkuranga. Kwa hiyo, kumbe Hospitali ya Temeke haihudumii tu watu wa Temeke, inahudumia na watu wa mikoa ya jirani. Sasa tunapofanya zile allocation tuangalie mazingira haya ya kijiografia kwa sababu sisi tunakuwa tumezidiwa si kwa maana ya wakazi wa Temeke lakini kwa maana ya jirani zetu na unafahamu suala la huduma ya afya huwezi kumwambia mtu kwamba wewe hutokei Temeke nenda huko, kwa hiyo lazima wote tuwasaidie pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wizara mlizipandisha daraja hizi hospitali za Temeke, Ilala na Mwananyamala, cha ajabu bado mmeuacha mzigo kwa halmashauri. Serikali irudi na itekeleze majukumu yake kwenye hizi hospitali kwa ni mzigo mkubwa sana kwa Halmashauri. Unaita Hospitali ya Mkoa halafu inahudumiwa na Halmashauri, vyanzo vyetu havitoshelezi kuzihudumia hizi hospitali. Ni lazima Serikali itekeleze wajibu wake kuhakikisha kwamba hizi hospitali zinakuwa na wafanyakazi, wataalam na vifaa tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana mpaka leo mwana mama anapokwenda kujifungua abebe na vifaa vidogo vodogo vya kwenda kumsaidia kujifungua hospitalini. Huu ni udhalilishaji mkubwa wa mama zetu. Kwa nini Serikali ishindwe hata kuweka vifaa vidogo vidogo kama groves, sindano, uzi, beseni, kweli? Miaka zaidi ya 50 kweli tunashindwa kupata sindano za mama kujifungulia?
Kwa hiyo, wako kina mama wengine wanadhalilika, wanajifungulia kwenye daladala kwa sababu tu hakwenda hospitali mapema alikuwa hajatimiza hivyo vifaa vya kwenda kujifungulia. Hebu tujaribu kuyatengeneza haya mazingira ya kujifugulia akina mama yawe mazuri na yenye staha kwa ajili ya kulinda heshima ya mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa uwezo wa kunisimamisha mahali hapa ili na mimi kidogo niweze kusema machache juu ya Serikali hii. Of course ina-bore kumshauri mtu au unapojiandaa kumshauri mtu ambaye unaamini hashauriki. Inafika tu wakati huna jinsi unahitaji kufanya hivyo hata kama hashauriki ni wajibu wetu kuendelea kuiambia Serikali labda kunaweza kutokea muujiza mwaka huu au miaka michache hii ambayo mnamalizia muda wenu wa kuwa madarakani kwani miaka michache ijayo sisi ndiyo tutakuwa madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu waliotangulia katika Mabunge haya wamesema sana, wameishauri sana Serikali, lakini hakuna hata moja wanaloweza kulichukua. Muda wote wao wanajenga ile defensive mechanism kwa kupinga kila kitu na kila ushauri mzuri ambao Kambi hii imekuwa ikiwashauri. Jana hapa tumesikiliza hotuba nzuri kutoka Kambi hii ikiishauri Serikali lakini bado wanazibeza, wanazifumbia macho ili waendelee kujikita katika ile misingi mibovu na mambo mabovu ambayo mara nyingi wamekuwa wakiyashughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitendo cha ajabu kwa Serikali hii toka imeingia madarakani yaani jambo kubwa la ubunifu ambalo wao wamelifikiria ni kuhakikisha tu kwamba wanazima matangazo ya moja kwa moja ili wananchi wasiweze kuliangalia Bunge. Ni aibu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tulipokuwa tukisikiliza Baraza Jipya la Mawaziri likitangazwa tunaona kina Nape wanachaguliwa tulikuwa na matumaini makubwa sana kwamba sasa tutaona Serikali ikiendeshwa kisasa zaidi, lakini kwa ajabu leo namwona Ndugu yangu Nape mishipa ya shingo ikimtoka hapa kutetea eti ni sahihi kutoonyeshwa live kwa Bunge, ni ajabu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si kwamba Serikali hii haitambui mchango wa waandishi wa habari au mchango wa waandishi kuonyesha vitu hivi live kwa sababu wao wakati wanaenda kwenye zile ziara zao wanazoita za mishtukizo, za kutumbua majipu ambazo of course wanakwenda tu kukuna vipele na siyo kutumbua majipu kwa sababu majipu hayajatumbuliwa, wanaongozana na makundi makubwa ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwakuta utafikiri pengine wasanii wanakwenda location ku-shoot movie kumbe wanatambua kwamba unapofanya jambo lolote unahitaji wananchi walione, unahitaji kusikika, unahitaji kuonekana wananchi waone unafanya kitu gani, leo hapa mnalifunga Bunge hili wananchi wasione. Hili ni tatizo kubwa lakini ukweli utaendelea kubaki palepale kwamba huwezi kupambana kuirudisha nyuma teknolojia ya mawasiliano. Teknolojia inazidi kwenda mbele, inazidi kuendelea na huwezi kutumia mikono kuizuia. Kwa hiyo, itafika mahali haya mnayoyaficha wananchi watayaona tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii inaongea sana, lakini yale wanayoyaongea ukitaka kuyaweka katika utekelezaji unaona kwamba hizi ni ndoto na hivi vitu vitaendelea kubaki ndoto haviwezi kutekelezeka. Tunaimba hapa suala la afya, wananchi wanategemea waone mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, wananchi wapate huduma za afya katika maeneo ya karibu, wahudumiwe kwa uwiano unaostahili lakini bado Serikali hii haijaonesha dhahiri ni kwa kiasi gani itakwenda kutuwekea vituo vya afya kwenye kila kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti zinazoletwa hapa ni bajeti za kujenga vyoo siyo za kwenda kutuwekea vituo vya afya kwenye kata zetu. Ni bajeti ndogo ambayo itaweza tu kujenga vyoo au kujenga uzio na mwisho wake mtatumia fedha nyingi kuupeleka mwenge ili uende ukazindue vyoo hivyo.)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta tuna Serikali ambayo iko tayari kutumia nguvu nyingi kwenye vitu vidogovidogo lakini haiwezi kutumia nguvu nyingi kwenye mambo makubwa. Ukiwaambia kwenda kuzindua choo wataidhinisha mabilioni ya fedha uende Mwenge kule ukamulike uzindue ujenzi wa choo. Choo kinajengwa kwa shilingi milioni tano unapeleka mwenge ambao unatumia zaidi ya bilioni 120. Wakati mwingine unafikiria kwamba inawezekana hii Serikali inaamini kwenye nguvu za giza!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa akili ya kawaida unawezaje kuuthamini moto ndiyo uutembeze nchi nzima kwa fedha nyingi, lakini unaacha kuyafanya yale mambo ya msingi? Nishauri tu kwamba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi iko madarakani si kwa sababu mmewaloga Watanzania kwa kuwapitishia Mwenge wa Uhuru. Mko madarakani kwa sababu ninyi ni wazuri sana wa kuiba kura wakati wa uchaguzi. Itoshe mkajiamini na mkajikita katika sifa hiyo ya kuiba kura. Huu mwenge uwekeni mahali, uwekeni makumbusho uendelee kubaki pale kama alama nyingine za kawaida, lakini tusitoe fedha kwa ajili ya kuutembeza moto ambao unaharibu vipindi vya wanafunzi mashuleni, wanakaa kuusubiria mwenge lakini pia moshi wa mwenge unachafua mazingira na unaathiri afya za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri jana inajaribu kuwatia moyo wananchi kwamba kuna fedha, vikundi sijui vitaboreshwa, mikopo na vitu vya namna hiyo. Wakati unakwenda kwenye kuahidi kwanza angalia yale ambayo yanaendelea kufanyika katika jamii unayasimamia kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, wajasiriamali wamekuwepo kabla ya Wizara hizi hazijaanza kutenga hizo fedha, wananchi kwa jitihada zao wenyewe wamejikita katika ujasiriamali. Nichukulie mfano tu watu ambao wameamua kujikita na kujiajiri katika shughuli za bodaboda ambazo zimetoa ajira kwa kiasi kikubwa sana kwa vijana pale Dar es Salaam. Cha ajabu Serikali badala ya kuwawekea miundombinu mizuri ili waweze kuzifanya shughuli zao kwa tija sasa hivi Serikali inatumia Jeshi la Polisi kuwatesa vijana wa bodaboda utafikiri ni majambazi, wezi au siyo watu ambao wanastahili kutunzwa na kuhudumia katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wa bodaboda wanavamiwa katika vituo vyao, polisi wanawachukulia bodaboda zao wanazipakiza kwenye magari wanazipeleka kituoni, eti wanataka kwenda kuwauliza tu kama wana leseni…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali na ndani ya bajeti hii mlishauri Jeshi la Polisi likome mara moja tena likome kwelikweli na likome hasa kuwanyanyasa hawa watu wa bodaboda. Wawaache wajasiriamali hawa ambao wamekopa fedha na kujiajiri waweze kufanya shughuli zao na zilete tija kwao na kwa familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa majumuisho ya Waziri nitapenda pia atuambie ni kwa nini wale pensioners toka wamepandishiwa malipo yao mapya Sh. 100,000/= kwenye bajeti ya mwaka jana wale ambao hawalipwi moja kwa moja kupitia Hazina hawajawahi kulipwa hayo malipo yao mapya mpaka leo. Hii fedha iko wapi? Kwa nini hawalipwi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Walimu waliosimamia mitihani katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke mwaka 2015 mpaka leo hawajalipwa fedha zao, fedha hiyo iko wapi? Tunahitaji hayo majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake tuone hizo fedha zimekwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi wananchi kwa kweli wameichoka na ninyi wenyewe mnafahamu. Kumbukeni jitihada kubwa mlizofanya kutengeneza matokeo ya Bara na hata kulazimisha matokeo ya Zanzibar, kulazimisha uchaguzi ambao haukuwa na sababu ya kuwa uchaguzi kwa sababu uchaguzi ulishafanyika. Sasa mtatumia mabavu ya kubaki madarakani mpaka lini, wananchi hawa wanajitambua na wanafahamu nani wanataka awaongoze. Hata ninyi wenyewe hamuoneshi dalili kama kweli mnahitaji kubaki madarakani kwa sababu mahitaji ya wananchi mnayajua, kwa nini basi kama mnapenda kubaki madarakani msifanye kazi kwa bidii wananchi wakaona kwamba ninyi mnafaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, mna bahati nzuri sisi hatufichi mbona tunasema mambo mazuri ni haya, ni haya, ni haya, mmekaa madarakani chukueni haya mazuri tunayoyasema muyatekeleze kule. Sisi tunapambana kwa sababu tunajua hii nchi ni yetu sote. Mambo yakiwa mazuri kwa wananchi ni kwa ajili ya Tanzania, acheni ubinafsi, acheni ubinafsi Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Naibu Spika, siiungi mkono hoja hii hata kidogo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Ardhi. Nakuhakikishia tu, hata hawa wageni wangu 16 uliowataja hapo, wafanyabiashara wa furniture kutoka Keko wamekuja maalum kwa ajili ya kikao na Mheshimiwa Waziri, pamoja na viongozi wa Shirika la Nyumba kwa ajili ya kuzungumzia changamoto zetu zinazohusiana na masuala ya ardhi pale Temeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na heshima yote hasa ya ushirikiano ambayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akinipatia, bado niseme kwamba Mheshimiwa Waziri anahitaji kuwaaangalia kwa makini sana watendaji wake katika Wizara hii. Bado kuna watendaji wengi ambao wanaonyesha kutokuwa na dhamira nzuri na wanaamini kwamba ukiwa mtumishi kwenye Wizara ya Ardhi, basi umepata goli la kutokea au umepata sehemu ya kutajirikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kurasini ardhi yake sasa hivi inasimamiwa na Wizara ya Ardhi, siyo Halmashauri tena, kwa sababu kuna mpango maalum wa kulifanya eneo lile liwe mbadala au lisaidie shughuli za bandari pale, lakini pia kuna ule uwekezaji mkubwa wa EPZ. Kwa hiyo, maamuzi mengi pale tunategemea yafanyike kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Wizarani sasa baadhi ya watumishi wasiokuwa na nia njema wamegeuka kuwa madalali wa eneo hilo. Nitatoa mifano michache tu. Eneo la Mabwawani; hili linaitwa Mabwawani kwa sababu DAWASCO ndiyo wanatupa majitaka katika eneo hilo, wanamwaga pale. Kwa hiyo, miaka ya 1980 kwanza ilikuwa ni sahihi kwa sababu hiyo sehemu ilikuwa bado haijachangamka, haukuwa mji, lakini kwa sasa pale ni mji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa DAWASCO, miundombinu yao yenyewe ya kuchakata zile taka imekufa. Kwa hiyo, kinamwagwa kinyesi kibichi pale na hilo eneo limezungukwa na makazi ya watu; watu wanakaa pale. Kwa hiyo, ikinyesha mvua, yale mabwawa yanatapika, ule uchafu wote unaingia kwenye makazi ya watu. Wananchi wa pale kwa kutambua ile kero, wakamtafuta mtu, bwana, njoo tununue hapa sisi tuondoke; tulipe gharama yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule mtu alikuwa tayari kuwalipa ili wale wananchi waondoke. Alipokuja akaamua afuate utaratibu kuja Halmashauri kwamba pale nataka niwanunue. Halmashauri wakamwambia kwamba hilo eneo linasimamiwa na Wizara. Kwa hiyo, hebu nenda Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akaandika barua akapeleka Wizarani. Wizara wakamwambia, basi ngoja tuje tufanye uthamini hapo, lakini kwa sasa hatuna fedha ya kuwaleta wathamini kuja kufanya uthamini hapo. Kwa sababu wewe ndio unataka kununua, tupatie shilingi milioni 25 tufanye uthamini. Yule bwana akalipa ile shilingi milioni 25 kwenye akaunti ya Hazina, hela imeingia Wakafanya uthamini ili awalipe wananchi waondoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya fedha ile kulipwa, Wizara inamwambia yule mtu, kwamba tutafanya uthamini wenyewe, kwa hiyo, hela yako tutakurudishia, ambapo mpaka leo haijarudi na ni miaka miwili imepita. Nilikuja ofisini, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, akamwita Kaimu Mthamini, anaitwa Evelyne yule mama, akaja pale, akasema, aah hii pesa tunairudisha. Mpaka leo nakuhakikishia hiyo hela haijarudi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi siyo suala la kurudisha pesa, ni kwamba wale wananchi wanataabika na wanahitaji mwekezaji awalipe, waondoke pale. Wizara sasa inasema kwamba lile eneo maana lile eneo limegawa kuna upande wa eka nane na upande eka nne. Wanasema zile eka nne kwa sababu zina mabwawa ya DAWASCO, tumempa DAWASCO ndio atawalipa fidia. DAWASCO amekaa hapo miaka yote, ameshindwa kuwalipa fidia, leo unampa hilo jukumu DAWASCO eti awalipe fidia, DAWASCO wameiweka wapi hiyo hela? Mfuko gani wa DAWASCO una hela ya kumlipa mtu fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni haraka kwa sababu wale wananchi pale wapo kwenye mazingira magumu. Tunahitaji mtu aje awalipe, waondoke wakatafute maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu kwa akili ya kawaida, tunasema hapa tuna mradi mkubwa wa EPZ, hapo unampa DAWASCO aendelee kuboresha eti amwage taka; au ndiyo mnatuchulie poa watu wa Temeke; hapa nyumba, hapa choo? Hiyo moja. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri sasa ikawaandikia barua Wizara, njooni mfanye uthamini basi haya maeneo, wananchi wajue tu kwamba hapa hivi tunalipwaje? Barua ikaenda Wizarani, ikakaa kweli kweli! Mpaka mimi nimekuja tena Wizarani, Mthamini akasema aah, nawajibu. Akajibu kwamba Halmashauri ifanye uthamini wenyewe, sisi hatuna wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dana dana zinaendelea ili mradi tu hilo jambo lisifike mwisho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nataka upate hiyo picha na ujue kwamba pale kuna matatizo na tuna kazi kubwa ya kufanya. Kwa hiyo, sitachoka kuja ofisini kwako tuhakikishe hizo kero tumezimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri iliwahi kutoa barua ya kuwataka Halmashauri wakavunje pale; kuna lile jengo linaitwa Monalisa, lile godauni pale Toroli; yule Oil Com kiwanja chake kamaliza, akaingia tena barabarani, kajenga fence kwa pembeni na kwa nyuma kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, amezuia njia sasa za gari. Kwa kule nyuma watu wanalazimika kuhama nyumba zao kwa sababu vyoo vimejaa lakini huwezi kupeleka gari ya kunyonya taka, anayeitwa mwekezaji kazuia njia. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, hata ghorofa ulilolivunja ni kwasababu uliamua livunjwe. Ukimpelekea barua Halmashauri ndiyo akavunje, hilo haliwezi kutekelezeka, kwa sababu inawezekana kabisa kwenye ule ujenzi huyo Halmashauri ndio ana mkono wake. Kwa hiyo, kwenye hizi kero ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja, nakuomba Mheshimiwa Waziri husichoke. Uingie kwa miguu yote miwili, twende tukaokoe hawa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni tatizo la mpaka kati ya Temeke na Ukonga kule, limekuwa ni la muda mrefu sana na limesemewa hapa kwa muda mrefu. Halmashauri ya Jiji pia walilishughulikia na sasa hivi lipo Wizarani kwako.
Tunawaomba mje tumalize ule utata pale. Msitake kunigombanisha na Mheshimiwa Waitara, sisi wote team UKAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mje mtusaidie, mpaka wetu pale ujulikane sasa, ili tatizo lifike mwisho. Hatuna ugomvi, mkija tu, tutayamaliza kwa sababu mimi na Mheshimiwa Waitara wote ni ndugu moja. Kura zake zikija kwangu siyo tatizo na zangu zikienda kwake, wala halina utata. Yawekezana zamani ilikuwa tatizo sana kwa sababu ya watu kutetea kura zao zisihame. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri uje tuweze kulifanyia kazi jambo hili kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, issue za Kurasini nahitaji Mheshimiwa Waziri uje hasa uzione. Issue ni nyingi, watu wanadhulumiwa, watu wanaishi kwenye maisha ya taabu! Eneo moja pale lilikuwa na soko, pembeni huku kote watu wameshaondoka, ni fence tu sasa hivi hapa watu wanasubiri uwekezaji. Sokoni pale hakuna biashara inayofanyika na watu ndio wanaendesha maisha yao pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na hili nimelisema hapa mara kadhaa, suala la watu waliokuwa pembeni ya reli ya TAZARA. Wizara yako imesema kabisa zile mita 60 pale wahame...
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Dkt. Nagu fujo hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika Wizara hii inayoshughulikia maji. Inasikitisha sana kuona kwamba tunatengeneza madaraja kwa namna ambavyo tunapata maji katika nchi hii. Sisi kwenye Jimbo la Temeke tunaonekana kama watu wa daraja la tatu ambao hatustahili kuwekwa kwenye mpango wa kutumia maji matamu maji ya bomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote mipango ambayo inaigusa Temeke ni ile ya visima, maji ya visima ni yale ambayo yanakuwa na asili ya chumvi chumvi na haya ndiyo maji ambayo watu wa Temeke tunakunywa. Ukipikia chai ile chai inakuwa ina utamu wa chumvi na sukari, kwa hiyo lazima utumie sukari nyingi zaidi ili upate utamu wa chai. Ni vizuri Wizara ikaangalia mgawanyo ulio sahihi wa watu wote Dar es Salaam kupata maji ya bomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii mipango zikitajwa hapa Kata za Jimbo la Temeke zinatajwa zile ambazo pengine zinapakana pakana na Ilala hivi, ndio labda ziingizwe kwenye huo mpango. Inatajwa hapa Kurasini, inatajwa Keko, inatajwa Chang‟ombe, lakini tunaacha eneo kubwa lenye watu wengi ambalo limejikita katika kutumia maji ya visima, tena siyo vile visima virefu, Visima vingi ni hivi vya watu binafsi, vinavyomilikiwa na watu binafsi ni visima vifupi havijachimbwa kiutalaam, unakuta hapa ni choo, hapa kimechimbwa kisima, ndiyo maana kila siku kipindupindu kikiingia Dar es salaam lazima kitafikia Temeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Mheshimiwa Waziri akatuangalia kwa jicho lingine, atuangalie kwa jicho la huruma, basi aje hata na mpango tu mzuri kwamba kwa sababu visima vingi ni vifupi ambavyo maji haya si salama basi kuwe na utaratibu wa kuwekea dawa visima hivi, utaratibu ambao hautotugharimu sisi wanywaji. Serikali hilo ni jukumu lao kuhakikisha haya maji yanakuwa treated ili wananchi wao waweze kunywa maji yaliyo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo, lakini bado tunahitaji kuwe na mpango maalum wa kupata maji ya bomba, amezungumza hapa Mbunge wa Rufiji, kama Serikali kweli ina nia ya kufikisha maji Dar es Salaam iweke fedha kwa ajili ya huu mradi, kutoka Rufiji kuja Dar es Salaam sio mbali na tutapata maji ambayo yatatumika Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Dar es Salaam. Kwa Dar es Salaam si kwa maana ya Temeke peke yake, hata maeneo ya Kinondoni, maeneo ya Ubungo wanaweza kutumia maji haya kutoka Rufiji na yakawa mazuri zaidi na mengi kuliko haya ambayo tunahangaika nayo kutoka Ruvu, kwa nini Serikali haijikiti uko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa Wizara hii itoe kipaumbele sana kuhakikisha kila mtu anapata maji na yaliyo safi na salama kwa wingi. Ukikatika umeme tu Dar es Salaam, ukikatika umeme Temeke basi ujue siku hiyo hakuna maji kwa sababu ili watu wapampu maji lazima wanahitaji ule umeme. Kwa kuwa maji yenyewe ni visima vimechimbwa na watu binafsi hawana matenki makubwa ni matenki ya lita 2,000, lita 5,000, kwa hiyo, ukikatika umeme hatuna maji, tunasubiri huku tumepanga foleni mpaka usiku umeme ukirudi kama tuko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Temeke pia tunataka tuishi maisha ya kimjini jamani, tunaomba tupatie maji. Haya ndiyo mambo wanayoyataka wananchi, tena wale wananchi wa kawaida kabisa wakati wa kampeni tunawapelekea tisheti na kapero. Shida yao siyo hivyo, shida yao ni maji haya, basi Serikali iweke fedha za kutosha kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji, lita elfu moja kwa Temeke tunazinunua kwa sh. 3,500. Maana yake familia ya watu wawili tu kwa mwezi mnalipa maji zaidi ya shilingi…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kulishukuru Bunge hili kwa maana ya Wabunge wote Mheshimiwa Spika na Mawaziri kwa namna ambavyo walinifariji mimi na familia yangu wakati nilipompoteza Mzee wangu mwezi Novemba mwaka jana. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka nijielekeze kwenye taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo. Imeonesha kuna umuhimu mkubwa sana wa Serikali kutunga Kanuni na Sheria Ndogo katika kuzisimamia rasilimali lakini wakati mwingine pia kuzipatia vipato Halmashauri. Mbali na changamoto ambazo Kamati imezionesha hapa za uandishi, uchapishaji, naliona tatizo lingine kubwa ambalo lipo katika utungaji wa hizi Kanuni na Sheria Ndogo kwenye Wizara lakini pia kwenye Halmashauri. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la kutokuwasiliana kwamba Kanuni au Sheria Ndogo inayotungwa na Wizara moja katika kulidhibiti jambo fulani haiangalii kitu gani kinafanywa na Wizara nyingine. Kwa mfano, watu wa NEMC wanaweka sheria za kudhibiti ukataji wa miti kwa maana ya matumizi ya mkaa na vitu vya namna hiyo. Watu wa Maliasili na wao pia wanatunga sheria za kuhakikisha kwamba wanalinda maliasili za nchi hii. Hata hivyo, unapotunga Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Mkaa lazima uangalie Wizara inayoshughulikia mbadala wa nishati inafanya kitu gani Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeona hapa kwa mfano Wizara ya Nishati inasema kwamba ina gesi ya kutosha lakini kwa sasa gesi hiyo haijaanza kutumika majumbani inasubiri TPDC wajenge miundombinu ya kuifikisha gesi hiyo majumbani. Jambo ambalo kwa maana ya kuipendezesha presentation linavutia sana, lakini ukija kwenye uhalisia unagundua hili jambo haliwezi kutekelezeka ndani ya miaka 50 au 100 ya hivi karibuni. Kwa sababu tukumbuke kujenga tu miundombinu ya kusambaza maji safi na maji taka mpaka leo hatujaweza kueneza nchi nzima, unawezaje kutegemea ndani ya muda mfupi kwamba TPDC watajenga miundombinu ya kuisambaza gesi nchi nzima? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta yanayofanyika huku sasa yanasababisha matumizi ya mkaa yaendelee kuwa makubwa. Sasa kule tena mnatunga Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Mkaa maana yake bei ya mkaa itazidi kupanda na anayeteseka hapa ni mwananchi. Kwa hiyo, ugumu wa maisha tunausababisha na namna ambavyo tunasimamia hizi rasilimali zetu. Kwa hiyo, ni vizuri Wizara au Serikali ingekuwa yenyewe inaangalia hali halisi ikoje kabla haijatunga Sheria Ndogo kwa ajili ya kuzuia jambo fulani. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia inapotokea migogoro ni vizuri Serikali ikaenda haraka kutunga Sheria na Kanuni kwa ajili ya kumaliza migogoro hiyo. Vinginevyo inakwenda kuligawa Taifa katika hali ya kubaguana. Tazama migogoro iliyopo katika masuala ya ardhi. Ukienda sehemu ukikuta viongozi ni wakulima wanasema wafugaji wametuingilia na ukienda maeneo mengine wanasema kwamba wakulima wametuingilia. Matokeo yake tunaanza kuchukiana kwa kubaguana, huyu ni mkulima, huyu ni mfugaji. Mfugaji anamwingilia mkulima, mkulima analalamika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa mlisikia Mheshimiwa Mbunge mmoja amesema migogoro hii haishughulikiwi kwa sababu Waziri wa Kilimo ni mfugaji kwa hiyo anawaacha wafugaji waendelee kulisha kwenye mashamba ya wakulima. Sasa haya mambo ya kutosimamia vizuri rasilimali ndiyo inakuwa chanzo cha kuzibadilisha rasilimali ambazo zilikuwa neema zianze kuwa laana kwenye Taifa hili na hivi viashiria tayari vimeanza kuonekana. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama rasilimali zetu, tuna rasilimali ardhi, gesi, madini na tuna rasilimali watu. Kwenye ardhi tayari wakulima na wafugaji wanagombana. Kwenye gesi tumeona yaliyotokea Mtwara, kwenye madini unaona wachimbaji wadogo na wachimbaji wakubwa wana migogoro. Kwenye rasilimali watu ndiyo hivyo, mtu mmoja anaweza kunyanyuka anawaambia nyie mnauza madawa ya kulevya. Hivi ni viashiria vya kuona kwamba sasa rasilimali zetu zinageuka kutoka neema kwenda kuwa laana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuishauri Serikali mambo mawili, matatu. Awali ya yote kwanza niwape pole wananchi wangu wa Temeke kwa changamoto wanazozipata kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Jijini Dar es Salaam. Niwaombe tu tuendelee kuomba kwamba ziendelee kunyesha mvua zenye neema na wala zisiwe zile zenye balaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maeneo machache hasa katika ukurasa wake wa 15 mpaka ukurasa wa 18 ambapo anazungumzia masula mazima ya uwezeshaji, ajira na mahusiano kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba bado ratio ya Watanzania wasiokuwa na ajira imezidi kuongezeka na mpaka sasa takwimu bado zinatuonesha kwamba zaidi ya watu laki nane wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka na takribani watu 50,000 pekee ndio hubahatika
kupata nafasi za kazi na hapa haijalishi zile ajira bora au ajira ilimradi ajira. Ukweli bado upo pale pale kwamba hata hao wachache ambao wanapata nafasi za ajira mazingira yao ya kufanya kazi bado ni magumu sana. Wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwenye magodauni, viwandani bado wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, wanafanya kazi katika mazingira ya unyanyasaji mkubwa, wanafanya kazi bila kuwa na protective gears, kuwa na vifaa vya kuwazuia na hatari zozote ambazo zinaweza kujitokeza katika mazingira yao ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo bado pia hakuna vyama vya wafanyakazi katika sehemu za kazi ambazo zinaweza kutetea maslahi ya wafanyakazi. Naitaka Serikali ihakikishe kwamba kila sehemu ambayo watu wanafanya kazi kuwe na chama cha wafanyakazi. Jambo hili wanapoachiwa wafanyakazi wenyewe wajiundie vyama vyao wanapata changamoto kubwa, wanapata upinzani mkubwa kutoka kwa waajiri kwa sababu waajiri hawataki kuona kuna vyama vya wafanyakazi kwa sababu vitadai maslahi ya wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi ni vizuri akaunda taskforce ambayo itasimamia uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi kila eneo ambapo kuna wafanyakazi wanafanya kazi katika eneo hilo, kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kuweza kutetea maslahi ya wafanyakazi kama hakuna chama cha wafanyakazi katika hilo eneo husika. Hao ndio watakaoweza kuhakikisha kwamba wafanyakazi maslahi yao yanaboreshwa, lakini pia mazingira yenyewe yanakuwa rafiki na wezeshi kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo kubwa sana la fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi za jamii. Kumekuwa na kero kubwa na kelele nyingi sana kwa wafanyakazi huko mtaani. Katika Bunge la Kumi ilipitisha sheria hapa ya kuondoa fao la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya kijamii. Hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa wafanyakazi. Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi sisi ambao tumefanya kazi katika private sectors hatukuwa hata siku moja tuna malengo ya kufanya kazi mpaka uzeeke. Unafanya kazi kwa malengo, kwamba ufanye kazi labda miaka mitano au sita uache kazi uende ukajiajiri mwenyewe. Unategemea baada ya kuacha kazi uende ukalitumie fao lako la kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii upate fedha uende ukafanye uwekezaji mwingine, uendeshe maisha yako kwa kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wafanyakazi hawezi kwenda ku-access fao la kujitoa eti mpaka wafikishe miaka 55, nani ana uhakika wa kesho? Kwa hiyo yapo mambo mazuri ambayo yamefanywa na Bunge la Kumi lakini yapo pia mambo mabaya ambayo yamefanywa na Bunge la kumi. Ni wajibu sasa wa awamu hii kuyarekebisha yale mabaya kwa maslahi ya wananchi wetu. kwa hiyo, nilikuwa nategemea katika bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri aje hapa na mpango wa kutaka kuileta sheria hiyo Bungeni, ili tuifanyie mabadiliko turudishe fao la kujitoa kwa wafanyakazi katika mifuko ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni kweli Serikali inaamini kwenye yale ambayo inayahubiri, tunahubiri hapa kuijenga Tanzania ya viwanda. Hatuhitaji hivyo viwanda vijengwe na wageni, tunahitaji Watanzania wenyewe ndio waweze kuvijenga viwanda hivyo, ili viwanufaishe Watanzania. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Mwijage, anakwambia kwamba, ukiwa na milioni 15, milioni 20, milioni 30 una uwezo wa kuanzisha kiwanda chako.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtu ambaye anadai fedha zake NSSF au PPF ambazo zinaweza kuwa milioni 30 au milioni 40 anaweza kumbe na yeye kuanzisha kiwanda chake. Leo unapomzuwia kuweza kuchukua fedha yake eti mpaka atimize miaka 55 maana yake ni kwamba hamtaki vijana wa nchi hii sasa wamiliki viwanda wakiwa na umri mdogo, sasa, kwa nini Serikali iwazuie vijana kutajirika wakiwa na umri mdogo?. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu ambao wako makazini leo ni kati ya miaka 25 mpaka miaka 35. Kumbe huyu anaweza kupata fedha yake na akaamua kuachana na ajira akaenda kuwekeza kwenye viwanda. Leo Serikali inamzuia mtu huyu asimiliki kiwanda kwa sababu tu eti hajafikisha miaka 55. Hii haiwezi kuwa sahihi. Kwa hiyo, nizidi kuishauri Serikali ilete hapa hiyo sheria ili tubadilishe turudishe fao la kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni utumiaji wa dawa za kulevya. Nashukuru sana kwa jitihada ambazo zimeanza za kuanzisha vituo vile vya kutoa dawa za methadone, kwa kuwasaidia wale ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya ili waweze kuacha matumizi hayo taratibu. Ukweli ni kwamba, inaonekana kama hivyo vituo vilikuwa tu vya majaribio, dawa hizo zinatolewa kwa ubaguzi mkubwa. Waathirika wanapokwenda wanatengwa, wanaambiwa kwamba wale ambao wanatumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga ndio wanapewa hizo dawa za methadone, lakini wale ambao bado wanatumia ile njia inayoitwa cocktail, wao hawapewi dawa hizo za methadone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachotokea ni nini; wale wanaotumia cocktail ambao na wenyewe wana nia ya kujitoa kwenye dawa za kulevya, wanalazimika sasa na wao kuanza kutumia ile njia ya kujidunga, ili waweze kupata hizo dawa. Hiyo njia ya kujidunga ni njia hatari sana, sasa kama kweli lengo ni kuwasaidia vijana wetu kwa nini tuwabague? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuongeze tuongeze uwezeshaji, tuongeze hizo dawa ziwe za kutosha, ili kila aliyekuwa tayari kuachana na dawa za kulevya aweze kupata hizo dawa na aache, tuache kuwatenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, ni vizuri hivi vituo vikasogezwa karibu na maeneo ya watu. Kwa mfano katika Jimbo la Temeke, sehemu pekee ambazo hizo dawa zinatolewa ni kwenye Hospitali ya Temeke. Sasa kwa nini huduma hii isisogezwe kwenye kila kata? Sisogezwe kwenye kila zahanati kuwe pia na huduma hii ya kutoa hizo dawa za methadone? Kwa sababu, hawa waathirika wanapotembea umbali mrefu kuzipata hizi dawa, wakati mwingine wanashindwa kwenda kwa hivyo, wanakatiza zile dozi. Kwa hiyo, kama lengo la Serikali ni kuwasaidia hawa vijana, basi wahakikishe tunakuwa na dawa za kutosha, lakini pia hivi vituo vinasogea kwenye maeneo ambayo wananchi ndiko wanakotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho nililokuwa nataka kuchangia hapa ni kuhusu utendaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa masikitiko makubwa sana Ofisi hii ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika hizi siku za karibuni imekuwa ni ofisi yenye vituko na kufanya mambo ya ajabu, tofauti na majukumu ya Ofisi hii yanavyotakiwa kufanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia ofisi hii ikiviamulia vyama nani awe kiongozi wa chama hicho kwa vile tu Msajili labda pengine ana maslahi yake binafsi. Sitaki kuzungumzia namna ambavyo amemrudisha Profesa Lipumba, eti awe Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi –
CUF kwa sababu kesi iko Mahakamani. Pia juzi tu hapa amemrudisha mtu kumfanya awe ndiye makamu mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi wakati hakuwa na sifa wala hakustahili kuwa hivyo. Sasa tunataka kuuliza haya mabadiliko ya majukumu na nguvu ya Msajili wa Vyama vya Siasa yametoka wapi na yameanza lini na kwa maslahi ya nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyotambua sisi, Msajili wa Vyama vya Siasa ni Karani tu wa kutunza kumbukumbu za vyama vya siasa. Lakini leo anajipa nguvu kubwa na kuvipangia vyama nani aweze kuviongoza. Lakini amekwenda mbali zaidi, juzi hapa kati ameshirikiana na wahuni wachache kutoa ruzuku ya Chama cha Wananchi – CUF kuipeleka iende huko mtaani iende ikaliwe. Sasa tunajiuliza, hivi fedha za Serikali ambazo ni fedha za walipa kodi wa nchi hii, zinawezaje kutolewa bila utaratibu na zikaingia mtaani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote mwananchi wa Temeke hasa wakazi wa chang’ombe na Keko wanamshukuru Mheshimiwa Mpina kwa ziara zake zilizotokana na kero ya muda mrefu katika eneo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo bado nguvu kubwa ya kukomesha wachafuzi wa mazingira inahitajika. Bado baadhi ya viwanda vinatiririsha maji machafu kwenda mitaani na baharini. Tafadhali Mheshimiwa Mpina usichoke kuja Temeke ili tuzitatue kero hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda Mheshimiwa Waziri ashauriane na Waziri wa TAMISEMI ili watoe maelekezo kwa Halmashauri kuwa Kamati ya kutoa vibali vya ujenzi imjumlishe na Afisa Mazingira wa Halmashauri badala ya Mganga Mkuu. Hii itasaidia kuhakikisha hakuna kibali cha ujenzi kitakachotolewa bila tathmini ya mazingira. Kwa sasa hali hii ni mbaya na vibali hutolewa hata katika maeneo oevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katiba mpya, Wizara haina muda tena wa kusubiri kuanza kumalizia mchakato wa kupata katiba mpya. Kama bajeti hii ya 2017/2018 haitatenga pesa kwa ajili ya jambo hili, maana yake Watanzania wasitegemee tena kupata katiba mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho ya sheria, Serikali ilete Muswada Bungeni kwa ajili ya kubadilisha sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2011 na ile ya kura ya maoni ya 3013 ili iendane na hali ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zuio la shughuli za kisiasa, Serikali itengue zuio lake la kuwakataza wanasiasa kufanya mikutano ya kisiasa kwani kwa kufanya hivyo inavunja sheria ya vyama vya siasa. Ni haki ya msingi ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo chakavu, Wizara itafute vyanzo vyake vingine ili ipate fedha za kujenga na kukarabati majengo ya mahakama hasa Mahakama ya Mwanzo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia machache katika mjadala unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka salama na kunipa nguvu za kusimama mahali hapa asubuhi ya leo ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, pia naungana na Watanzania wengine wote kutoa pole kwa familia za marehemu waliopoteza maisha mwishoni mwa juma hili na tumwombe Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, lakini atupe nguvu na subira sisi wafiwa katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Spika, nianze na TBC. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza mambo mengi ya kuona namna gani anaweza kuiboresha TBC, lakini kwa maana ya kupanua usikivu wake na muonekano wake na kuiboresha yenyewe mambo ambayo yanahitaji sana fedha. TBC hii haihiitaji tu maboresho kwenye mambo ambayo yanatumia fedha inahitaji pia maboresho ya weledi na kujituma kwa wafanyakazi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TBC imekuwa kituko na inashindwa kubeba hasa ile nafasi yake kama chombo na chanzo cha kutoa habari kwa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, habari ambazo zinarushwa na TBC kwanza zinakosa mvuto, watangazaji wenyewe ile kuchangamka tu, kwa sababu kuchangamka hakuhitaji Wizara ikutengee fedha ili uchangamke ukiwa studio. Mtangazaji anafanya kazi kama kalazimishwa, matokeo yake hata wanapozungumza habari za burudani ambazo ni za kufurahisha bado zinaonekana kama habari za msiba ambazo zinatia huzuni.

Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ya kiweledi ambayo yanahitaji tu usimamizi mzuri na wafanyakazi hawa waambiwe kwamba TBC ndiyo chombo kinachotegemewa na wananchi. Kama hakuna mvuto wa kuingalia television hiyo, hivi mtu ata-tune vipi kwenye television ambayo haimfurahishi hata kwenye mambo yale ya kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukweli wa habari ambazo zinatangazwa na TBC, hivi juzi juzi hapa tulishuhudia kabisa habari ya kupikwa kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump amesifia na kupongeza kazi zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Ni jambo zuri, lakini ukweli wenyewe wa habari ile ilikuwa ni ya kupikwa haikuwa ya kweli kutoka Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sasa unajiuliza, hivi jambo dogo kama hili TBC wanashindwa ku-cross check, kuthibitisha kwamba habari hiyo ni ya kweli! Tuna Ubalozi wa Marekani kutoka Bamaga kwenye Ofisi za TBC kwenda Ubalozi wa Marekani hazifiki hata kilometa tano. Hivi TBC ilishindwa kitu gani kwenda Ubalozi wa Marekani kuthibitisha kama kweli kuna habari hiyo ili watulishe habari ambazo ni za kweli na uhakika badala ya kutulisha habari za kupikwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa na wewe habari za kukanushwa kwa taarifa ile ulizipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya sasa ndiyo yanawafanya Watanzania waache kuitegemea TBC kama chanzo cha taarifa na badala yake sasa tumejikita kwa ITV na Azam TV kwamba sasa zimekuwa kama television za Taifa badala ya TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri tu wakajitazama wenyewe ili waaminike na watu wengi wa- tune kwenye TBC, ni lazima wabadilishe namna ambavyo wenyewe wanafanya kazi zao za kila siku katika kituo hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la ving’amuzi; wakati tunaimba kwamba tunabadilika kutoka analogue kwenda digital, zilikuja concerns kwamba watu watakaposhindwa kulipia ving’amuzi vyao watakosa kuangalia television na Serikali ilituaminisha kwamba kila muuza ving’amuzi atalazimika kuhakikisha kuna local channels angalau tano ziwe zinaonekana hata pale ambapo king’amuzi kitakuwa kimemaliza bundle lake. Kitu hiki sasa hivi hakipo.

Mheshimiwa Spika, usilipolipia king’amuzi huna channel utakayoiona na hata vile ving’amuzi vichache ambavyo wanaweka channel, basi hazizidi mbili. Ving’amuzi vingi usipokuwa na bundle hakuna channel yoyote utakayokuwa unaiona.

Mheshimiwa Spika, sasa Watanzania wanakosa fursa ya kuangalia television kwa sababu tu tumeingia kwenye digital. Sasa hili jambo ni la kisheria, linahitaji tu kusimamiwa kuhakikisha kwamba hizi sheria zinatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaouza ving’amuzi mnawafahamu, TCRA wako wapi? Kwa nini wasiangalie kama kweli zinakidhi hayo matakwa ya kuwa na local channels angalau tano ili ziwe zinaonekana pale ambapo watu watakuwa hawajalipia ving’amuzi vyao?

Mheshimiwa Spika, maisha yamekuwa magumu sana, siyo kila mmoja anaweza kulipia king’amuzi kila mwezi. Kuna miezi mingine mtu anashindwa kulipia. Sasa anaposhindwa kulipia, basi asikose uhuru wake wa kuangalia television. Kwa hiyo, tuwasaidie Watanzania hawa waendelee kuangalia television zao zisiendelee kubaki kama mapambo ndani ya nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni usalama wa waandishi wa habari. Kumekuwa na matukio hapa karibuni ya kuvamiwa waandishi wa habari wakiwa wanafanya shughuli zao.

Mheshimiwa Spika, najaribu kunukuu uvamizi uliofanyika katika kituo cha Clouds, lakini pia tukio lingine la kuvamiwa waandishi wa habari kwenye mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Chama cha Wananchi, CUF kule Mabibo. Matukio haya siyo ya kuyabeza, kwa sababu hao waandishi maana yake sasa hivi usalama wao wanapokuwa kazini umekuwa ni wa mashaka sana. Haturidhishwi kabisa na namna ambavyo Serikali ina-react katika kuyakabili matatizo haya. Serikali ina-react very light kama vile haya matukio siyo mazito kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, tunapowafanya waandishi wawe na wasiwasi katika kutekeleza majukumu yao, tunapoteza zile nguvu zao na commitment zao katika kufanya kazi zao kiweledi zaidi. Ni lazima Serikali iwe na mpango madhubuti kabisa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira yaliyo salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni hapa kwenye suala la michezo, kwenye ukurasa wa 44 Mheshimiwa Waziri ameelezea sana michezo lakini amejikita zaidi kuelezea mpira wa miguu. Serikali isituaminishe kwamba tunapozungumzia michezo kwenye nchi hii, basi tunazungumzia mpira wa miguu pekee. Kuna michezo mingi katika nchi hii na ni lazima Serikali iisimamie yote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa Mheshimiwa Waziri anazungumza tu hamasa za kuhakikisha Serengeti Boys inafanikiwa. Kuna michezo mingi zaidi ya huo ambao Serengeti Boys wanaucheza, sasa hao wanamichezo wengine Serikali inawasaidiaje? Tusisubiri tu mtu kashinda mbio huko, ndiyo tunamchukua tunamleta Bungeni hapa tupige naye picha. Tumewekeza nini katika kufikia mafanikio hayo?

Mheshimiwa Spika, tunawekeza kwa Serengeti Boys lakini sifa tunataka kuzichukua kwa watu wanaokimbia riadha, hili haliwezekani. Ifike mahali tukubali kabisa huu mchezo wa mpira wa miguu umeshatushinda, hatuwezi kufanikiwa, figisu zilizopo TFF ni nyingi. Tazama sasa hivi kuna mbinu za makusudi zinazofanywa na TFF kuhakikisha kwamba Simba inapata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani limetengenezwa zengwe kwa sababu TFF inaelekea kwenye uchaguzi wake, wameambiwa kwamba kwa sababu kwa miaka minne Simba haijashiriki mashindano ya Kimataifa, mtakosa kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi TFF na wenyewe wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha eti Simba iwakilishe Taifa kwenye mashindano ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yana ushahidi usiofichika. Duniani kote matokeo ya uwanjani yanaheshimika, hata kama kuna matatizo yametokea, wanaadhibiwa waliosababisha matatizo hayo, lakini siyo kuhamisha point kutoka timu moja kuzipeleka kwenye timu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuchezea haya matokeo ya mezani, yanaonekana tu hapa Tanzania, lakini huko kwingine kote mpira wa miguu watu wanaheshimu matokeo ya uwanjani.

T A A R I F A....

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipokea kabisa taarifa aliyotoa Mheshimiwa Bulaya, naipokea kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Spika, jambo hili siyo hapo tu. Siyo kwenye point tatu za KageraSugar, hawa Simba wameonyeshwa kubebwa kwenye maeneo mengi. Mechi ya kwanza Simba imecheza na Mbao, zikaongezwa dakika nne na refa akazidisha dakika mbili tena. Mechi ya pili, Simba imecha za na Mbao, refa akaongeza dakika saba, lakini kwenye kucheza zikaongezeka dakika kumi zaidi. Leo hii Mbao FC imeingia fainali na Simba kwenye Kombe la FA tayari viwanja vimebadilishwa mara mbili zaidi.

T A A R I F A...

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi tunachotaka kumtaarifu ni kwamba ukimpa mtu kadi tatu mfululizo anatakiwa a-miss mechi moja mwishoni. Kingine, pilipili usiyoila wewe yakuwashia nini? Kwa sababu Kagera siyo Yanga. (Makofi/Kicheko)

Taarifa......

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, naamini kabisa kwamba pamoja na madaraka makubwa uliyopewa na Kanuni ya tano, lakini pia unaitumia hiyo Kanuni ya tano kwa kuheshimu pia Kanuni ambazo zinanilinda mimi katika uchangiaji na unafahamu tunapochangia hapa tunakuwa tumejipanga, tumejiandaa kwa muda mrefu ili tufikishe kilio cha Watanzania na Serikali iweze kukifanyia kazi. (Makofi)

Pili, zimetoka taarifa hapa sasa sijui unanipa nafasi na zenyewe kwanza nizipokee au nizikatae japo kwa dakika moja au unanisaidiaje katika hili?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona dakika hizi za lala salama nami niweze kuchangia mawili matatu katika Wizara hii inayoshughulika na mambo ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotokea mjadala hapa wa kuitaka Serikali ibadilishe Sheria ya Ndoa ili ukomo au mwanzo wa umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18 na kwenda juu kuna kundi huwa linapinga sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kundi hilo linalopinga kupandisha ukomo wa kuolewa watoto wa kike ndiyo hilo linapinga watoto wanaopata ujauzito kurudishwa tena shuleni. Tafsiri tunayoipata hapa ni kwamba kumbe wabakaji na wanaotutilia mimba watoto wetu inawezekana wengine wapo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge kama wazazi, mtu kuanza kupinga kumpa fursa mtoto wa kike ambaye pengine alifanya kosa kupata mimba au ilitokea bahati mbaya amebakwa, unasimama mapovu yanakutoka hapa eti hutaki mtoto huyu kurudi tena shuleni ni jambo la aibu sana.

TAARIFA...

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza unaposema Bunge lililopita maana yake una-refer Bunge la Kumi, Bunge la Kumi Mheshimiwa Mchengerwa hakuwa Mwenyekiti na wala hakuwa Bungeni.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya maisha tunayoishi hatushindani kutokufanya makosa, tunashindana kwa namna gani unajifunza kutokana na makosa ambayo umeyafanya. Hivi ni nani amefanya kosa la makusudi kati ya aliyebakwa akapata au kijana anayejifunza kuvuta dawa za kulevya? Serikali hii juzi tumepitisha hapa bajeti ya Wizara ya Afya, Serikali inatenga pesa kwa ajili ya vituo vya methadone, inatumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwapa fursa vijana ambao wametumia dawa za kulevya sasa wanatafuta nafasi ya kujifunza kutokana na makosa yao, wanatafuta nafasi ya kujirekebisha ili wawe raia wema. Ndiyo kazi ya Serilkali kuwajengea miundombinu wananchi ili waweze kuwa wananchi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtoto aliyepata mimba ama kwa kubakwa au kwa kurubuniwa unamnyimaje fursa ya kurudi shuleni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusimalize maneno kwa sababu tu mtoto wako anasoma shule nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwe wageni wa nchi hii, Waziri wa Elimu anafahamu, moja ya changamoto kubwa za elimu katika nchi hii ni kwamba hizo shule ziko mbali na watoto wetu wanakoishi. Watoto wanatembea umbali mrefu kuzifuata shule, hakuna hostel za kutosha kwamba hawa watoto wakae hostel wasome huko mpaka wamalize shule zao. Mtoto anapewa lift ya bodaboda mwaka mzima, hivi mtoto huyu kweli ana ujasiri gani atakataa kutongozwa na dereva wa bodaboda anayempa lift kwa mwaka mzima? Wewe mtu mzima pamoja na Ubunge wako hapa ukipewa lift mfululizo siku 30 tu lazima mtakuwa bwana na bibi. Leo mtoto mdogo, watoto hawa wadogo wanarubuniwa, wanapata mimba, tunashindwa kweli kuwa na huruma kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukru sana na ukijiona unanyeshewa wewe ingia ndani, ujue upo nje, ndiyo maana manyunyu yanakukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ambayo watoto wetu wanakwenda shuleni siyo rafiki kiasi hicho, kwamba unaweza ukadhibiti wasipate mimba. Wakati Serikali inaendelea na jitihada zingine za kuhakikisha watoto watakuwa wanapata hostel, shule zitakuwa karibu na makazi yao, pia tuwape fursa wale ambao tayari wameshapatwa na matatizo. Inatugharimu kiasi gani...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Nami niungane na waliotangulia kusema Wizara imefanya vizuri kuleta mikataba hii ili iweze kuridhia sasa kwa kuwa imechelewa kufanya hivyo kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji sasa kuwa na uangalifu wa hali ya juu kwamba lengo la kuridhiwa kwa mikataba hii ni kupunguza wimbi la uharamia huko baharini hasa bahari kuu. Sasa tunapokwenda kutoa vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua wavuvi wetu tunahitaji kuwa na umakini wa hali ya juu sana kwa sababu vinginevyo wahalifu kutoka Mataifa mengine watajipenyeza na wao wapate vitambulisho hivi kutoka nchini kwetu ili waende kuvitumia vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, hatupaswi kuweka urasimu mkubwa ambao utawafanya sasa wavuvi wetu kwa maana ya Watanzania ambao wanastahili kupata vitambulisho hivi waanze kupata usumbufu mkubwa wa kuvipata, ni lazima tutengeneze utaratibu mzuri ambao hautakuwa na usumbufu ili wavuvi wetu waweze kuvipata vitambulisho ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhia ni jambo moja, tunahitaji pia sasa iletwe sheria ambayo tuje tuipitishe hapa kwa ajili ya utekelezaji wa mikataba hii. Kwa sababu kama tutairidhia leo, lakini sheria ya kusimamia utekelezaji wake na wenyewe utachukua miaka 10 bado tutakuwa hatujaenda kumaliza tatizo, Kwa hiyo, niishauri Serikali ifanye hivi kwa wakati.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono mawazo mazuri ya Kambi Rasmi ya Upinzani hapa Bungeni kwa namna ambavyo wameichambua kwa kina bajeti hii lakini kwa kutoa mawazo mbadala ili Serikali waweze kuyachukua na kuiboresha bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa naamini siyo jambo geni kwa Serikali kuchukua mawazo ya Upinzani na kuyafanyia kazi kwa sababu hata Mheshimiwa Rais ameanza kuonesha njia kwa kuyachukua yale mawazo mazuri ambayo upande wa Upinzani tukiyatoa na kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze sana viongozi wetu wa Kambi kwa pamoja Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa James Mbatia na Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali kwa namna ambavyo wanatu-groom vizuri ili tuendelee kutoa michango hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami pia ni miongoni mwa wanaoshangazwa na bajeti hii. Kama ambavyo mnasema bajeti ya kihistoria maana yake imeduwaza wengi na mimi pia ni miongoni mwa watu ambao tumeduwazwa na bajeti hii hasa kwa kutotarajia kuona kwamba bajeti ingeongezeka kufikia shilingi trilioni 31.7 wakati ya ile shilingi trilioni 29 tulishindwa kufikia. Naona ni kama vile mgonjwa ambaye ameshindwa kunywa uji sasa tunampatia pande la mhogo. Kwa mtazamo huo unaona kabisa tunatengeneza bajeti ambayo hatuwezi kwenda kuitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifikiri baada ya kuona kwamba bajeti ya 2016/2017 tumeshindwa kuitekeleza hata kwa asilimia 40, Serikali ingerudi nyuma na kujiuliza wapi ilikosea. Kwa sababu unapokuwa na bajeti ambayo unashindwa kuifikia maana yake ama mli-overestimate kwamba makadirio mliyoyafanya yalikuwa makubwa kuliko uwezo halisia. Kwa hiyo, nilitegemea leo bajeti yetu ishuke kwenye shilingi trilioni 29 iende kwenye uhalisia badala ya kuipandisha kuipeleka kwenye shilingi trilioni 31.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu moja ya vitu ambavyo vimechangia bajeti yetu 2016/2017 ku-fail ni mazingira mabovu tuliyonayo sasa kati yetu na wahisani wetu. Mazingira hayo bado hayajaondoka, mazingira yetu hayawavutii wahisani kuendelea kutupatia zile fedha ambazo walikuwa wakiahidi. Kwa hiyo, maana yake hata kwenye bajeti hii tunayoendelea nayo na yenyewe itapata changamoto zilezile ambazo bajeti ya 2016/2017 ilizipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wahisani hawaridhiki na uchaguzi wa Zanzibar ulivyoendeshwa. Tuliyasema haya wakati tunachangia bajeti ya 2016/2017, kwamba haya mazingira yaangaliwe. Tumekuwa tukijinasibu kwamba sisi ni kisiwa cha amani, kisiwa cha utulivu lakini kiukweli mazingira ya siasa za Zanzibar hayaoneshi kama kweli sisi ni watulivu na tuna amani kiasi hicho. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri ili yale makandokando yaliyozunguka yaweze kuondoka na wahisani hawa waendelee kutuamini na kutuletea misaada yao kama ambavyo ilikuwa hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili mambo mengine haya ya kuiminya demokrasia. Bado demokrasia katika Awamu hii ya Tano imeendelea kuminywa hapa nchi, tunazuiwa kufanya mikutano ya kisiasa. Kwa mfano, mikutano ya kisiasa ipo kwa mujibu wa sheria. Sheria iliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi inavitaka vyama kuendeleza mitandao yao huko nje. Leo mnaambiwa kwamba msifanye mkutano ya kisiasa kwamba kila mtu afanye mkutano kwenye eneo lake aliloshinda.

Mheshimiwa Spika, tuna vyama vilivyosajiliwa zaidi ya 22 si kila chama kimeshinda uchaguzi, kuna vyama havina hata mjumbe wa Serikali ya Mtaa, huyu akafanyie wapi siasa yake? Kwa nini huyu abanwe kufanya siasa? Kwa nini tutenge kwamba watu walioshinda tu ndiyo wafanye siasa wengine wakafanyie wapi? Ni lazima na wao wafanye siasa ili uchaguzi ujao waweze kushinda wapate wawakilishi kwenye nafasi hizo. Sasa tunapowanyima nafasi watu hawa tunaiminya demokrasia kwa upana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi wasiwasi uko wapi, kama sisi Wapinzani tunasema uongo tufanye kwamba CUF tumefanya mkutano pale Mwembe Yanga Temeke tukasema kwamba maisha ni magumu kwa Watanzania, si kesho CCM na wenyewe wafanye mkutano Jangwani waseme maisha ni mazuri. Kwa sababu hii siasa tunayoifanya ni vita ya maneno tu, hasira zinatokea wapi? Mwenzio akisema hivi na wewe sema lile unaloliona la ukweli, halafu wananchi watakwenda kutupima 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niishawishi Serikali na naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri amepata Uwaziri kama mtaalam na siyo kama mwanasiasa japokuwa ameanza kuonesha interest za kulitaka Jimbo la Buhigwe, nikutakie kila la kheri, lakini kwenye haya mambo ambayo ni ya kisiasa lakini yanaharibu uchumi aiambie ukweli Serikali kwamba tubadilishe mazingira haya wahisani hawa waendelee kutusaidia, lakini akiyakalia kimya mwisho wa siku mzigo unakuja kubebeshwa wewe. Watu wanaamini Mheshimiwa Waziri ni mtaalam mzuri sana, amefanya kazi ya kuishauri Serikali ya Awamu ya Nne na ilifanya vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iweke mazingira sawa ili wahisani waendelee kutoa zile pledges zao kama walivyokuwa wanafanya kwenye awamu zilizopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ahadi za Mheshimiwa Rais, naamini kabisa Serikali hii inafanya kazi za kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni zake kutoa milioni 50 kwenye kila mtaa.

Tunakwenda kwenye bajeti ya mwaka wa pili huu hiyo milioni 50 haionekani, huku ni kumgombanisha Mheshimiwa Rais na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama wana wasiwasi wa utekelezaji wa hiyo ahadi wangechagua hata pilot regions au districts kwamba hizi wilaya mbili au tatu tupeleke hizo milioni 50, tuzisimamie tuone utekelezaji wake utakuwaje. Hata Watanzania wangeona ile nia ya kweli ya kutekeleza ahadi hiyo, lakini wamekaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais pia aliahidi kutoa laptop kwa Walimu wote leo tunakwenda kwenye bajeti ya mwaka wa pili huu, tumepitisha hapa Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI hakuna hata moja imetenga fedha kwa ajili ya hizo laptops za Walimu na hii ni bajeti kuu pia hili halizungumziwi. Kwa nini tunamgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi wake? Naitaka Serikali imsaidie Mheshimiwa Rais kutekeleza ahadi zake ili aendelee kunukia na kupendeza mbele ya macho ya watu aliowaahidi na walimpa kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nataka kuchangia hapa ni namna ambavyo Serikali inazidi kupoka madaraka kutoka kwenye Serikali za Mitaa. Mwaka jana wametuchukulia Property Tax kibaya zaidi siyo kuzichukua hizo Property Tax lakini hazikukusanywa. Mpaka tarehe 31 Machi, Serikali ilikusanya asilimia 20 tu katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hata hao watumishi wenyewe wa kwenda kukusanya TRA hawana kwa maana hawajajipanga, wanaazima humo humo kwenye Halmashauri ndiyo wapate watu wa kwenda kuwakusanyia. Kama walikuwa hawajajipanga kwa nini wanalichukua jukumu hili, kwa nini wasiendelee kutuachia sisi tukakusanya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hapa badala ya kujikita kwanza wajipange vizuri kwenye kukusanya Property Tax

wameongeza na mabango pia maana yake wanakwenda kuziua Halmashauri zetu kwa kutunyang’anya vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja hii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia katika Taarifa za Kamati hizi mbili, lakini nazipongeza sana Kamati hizi mbili, zimefanya kazi nzuri kwa kadri walivyoweza. Wamegusa maeneo mengi ambayo kimsingi yanaigusa jamii yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali tu ya kuongezea, nami nina machache ya kuongezea ili tutakapoishauri Serikali, basi tuzidi kuboresha huduma za jamii kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hii ambayo kwenye Kamati ya UKIMWI umesema ni gender based violence. Vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vimekuwepo kwa muda mrefu. Mtakumbuka Bunge hili na Tanzania kwa ujumla ilionesha kukasirishwa sana na vitendo vile vya uuaji wa vikongwe, mnakumbuka Wanyamwezi walikuwa wanawaua vikongwe huko, sheria ikasimama kwamba watu hao waadhibiwe kiasi kwamba wengine hawatoiga. Pia matukio yale ya kuuawa kwa albino na kukatwa viungo, kama Taifa tuliungana pamoja kulaani vitendo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna jambo la ubakaji hasa kwa watoto wadogo. Matendo ambayo yametokea mwaka 2017 yametuvunja nguvu sana sisi wapigania haki za watoto na jinsia. Kwanza Serikali ilikataa watoto wa kike wanaopata ujauzito wasirudi mashuleni. Kwetu lilikuwa pigo namba moja, lakini mwisho wa siku Serikali ikaamua hivyo. Kwetu imetunyong’onyeza sana kwa sababu tunaona watoto hawa ambao hawakupata hizo mimba kwa makusudi, zilikuwa bahati mbaya, wanakosa fursa ya kujiuliza tena na kurudi shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi kwenye maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, ukatoka msamaha kwa Babu Seya na wenzake, watu ambao pasipo na shaka mahakama zilithibitisha kwamba hawa watu ni wabakaji. Sasa tunapokuwa tunasamehe wabakaji, wapi ulinzi wa watoto katika Taifa hili? Tunawafundisha nini? Misingi yetu ya kukomesha vitendo hivi imepotelea wapi sasa? Tunakwenda mbali zaidi, tunawachukua, tunawapeleka Ikulu, tunawapandisha kwenye majukwaa wafanye show, tunawaona kwamba ni kioo cha jamii, wanafundisha nini? Mnataka watoto wajifunze nini kutoka katika hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua mamlaka makubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo chini ya Ibara ya 45 ya kuwafutia watu vifungo, lakini kufuta kifungo hakuondoi kuwa wewe ni mkosaji katika kosa fulani na mtatambua mwenye nguvu ya ku-justify kwamba huyu amekosa, huyu ana hatia ya jambo hili, ni mahakama peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam ilithibitisha hilo pasipo na shaka, lakini walikata Rufaa kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na yenyewe pia ikajiridhisha kwamba hawa watu ni watuhumiwa katika kosa hilo. Wakaenda Mahakama ya Rufaa, Mahakama ya mwisho kabisa katika nchi hii; na yenyewe ikajiridhisha pasipo na shaka hawa ni wabakaji. Leo tunawachukua, tunatembea nao majukwaani. Je, mnataka siku ya mwisho tukiwauliza watoto kwamba ukiwa mkubwa unataka kuwa nani, aseme nataka kuwa mbakaji? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo taarifa, lakini yawezekana humu ndani tukawa tunafana kiumri lakini tukatofautiana sana katika vichwa vyetu. Kwa hiyo, ni lazima haya pia tuyazingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu mtoa taarifa, siyo nia yangu hata siku moja kuwa kituko ndani ya Bunge hili kama ambavyo wewe unataka niwe. Mimi nimeletwa hapa na wapigakura wa Jimbo la Temeke, moja kati ya Majimbo yaliyo mjini, moja kati ya majimbo ya watu waliokwenda shule, wanaojitambua na wanaojiheshimu.

Kwa hiyo, ninawakilisha group moja tofauti sana na group ambalo labda wewe unakuja kuliwakisha hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba ni lazima tuwe na jambo linalofanana, tuwe na nia moja. Tunapoamua kupabambana na mambo maovu, tupambane nayo kweli kweli. Mumshauri Mheshimiwa Rais afanye mambo ambayo wananchi ndio wanayataka. Mkipoteza naye anapotea, mnaipoteza Serikali, mnalipoteza Taifa na mnakipoteza chama chenu ambapo kimsingi kimeshapotea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine...

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii. Naomba nisiendelee hapa, panaweza pakamliza mtu, ni kipande kizito sana hiki kukizungumzia hasa sisi ambao tunawajali watoto wa Taifa hili. Naomba niende kwenye mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezunguzwa pia suala la utoaji wa huduma hii ya methadone kwa wale warahibu wa dawa za kulevya. Dawa hizi au huduma hii inatolewa kwa ufadhili wa asilimia 100 na siyo kwamba huduma hii inatolewa kwa kiasi ambacho kinaridhasha, bado uhitaji wa huduma hii ni mkubwa kuliko ambavyo huduma yenyewe inatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vituo wanajaribu kuwachuja ili kupunguza wingi wa watu watakaowahudumia. Sasa hivi wanawapa dawa hizi wale tu ambao wanatumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano. Zile njia nyingine, yaani kama mtu anatumia dawa za kulevya kwa njia nyingine kama zile za kunusa, kwa maana wanasema sniff au ile cocktail wao wanaambiwa ninyi bado hamjafia katika kiwango cha kupata huduma hiyo. Sasa kinachotokea ni nini? Kwa sababu vijana hao wana mwitikio mkubwa wa kujitoa katika matumizi ya dawa za kulevya, nao sasa wanaruka hizo hatua, wanatoka kwenye cocktail, wanatumia sindano ili wa-qualify kwenda kupata hiyo huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni hatari kwa sababu kwenye matumizi ya kutumia sindano ndiyo huko mnakutana na maambukizi ya magonjwa ya UKIMWI pamoja na magonjwa mengine. Sasa ni vizuri Serikali na yenyewe ikatia mkono ili kuifanya huduma hii ili ipatikane kwa kiwango cha kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia Waziri Mkuu wakati anafungua Kituo cha Methadone pale Hospitali ya Rufaa Mbeya mwezi Juni, 2017 akiziagiza hospitali zote za mkoa ziwe na Vituo vya Methadone; lakini kuviagiza peke yake bila Serikali kutenga fedha, hili agizo litatekelezwaje? Mwenyewe pale akasikia, wanasema kwamba Kituo cha Methadone cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitakuwa kinahudumia watu kutoka Njombe, Songwe, Iringa na Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anatokaje Songwe, Njombe kwenda kula dawa Mbeya na kurudi kila siku? Kwa sababu hizi dawa hupewi ukale nyumbani, ni lazima ukazilie kituoni na za kila siku. Vituo vinapokuwa mbali, inakuwa ni mzigo sana, hawa watu hawataweza kuzifuata. Ndiyo matokeo yake, wote hawa wanasafiri wanakuja kukaa Temeke sasa, tunaonekana Temeke ndio tuna warahibu wengi. Tusaidiane huu mzigo uweze kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vitendo vya ushoga na usagaji. Hili tatizo linazidi kukua hapa nchini. Kwenye shule za msingi, sekondari za day na za bweni vitendo hivi vinaendelea kinyemela. Watoto sijui wanajifunza wapi, sijui ni mitandao, lakini wanalawitiana kiasi ambacho hawa wanakuja kujijenga kuja kuwa mashoga wa baadae. Vilevile kuna watu wanajitangaza kabisa mitandao na mitaani kwamba wao ni mashoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Serikali badala ya kwenda kupambana na watu ambao eti wanavaa nguo fupi au wana-post picha za uchi mitandaoni, kwa nini tusipambane kwanza na mashoga na wasagaji? Tupambane na hawa ambao kwanza wanajitangaza kwa sababu ndio wanatengeneza, wanavutia watoto wengine wadogo waweze kujifunza hayo mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunawachukua watoto wa kike kwenda kuwapima mimba randomly kwa kuwashtukiza, tuanze na utaratibu wa kwenda kuwapima watoto wote kama wameshaingiliwa ili watutajie nani kawaingilia tuweze kuchukua hatua. Vinginevyo tatizo hili ninazidi kuwa kubwa nchini na itafika mahali tutaanza kukimbiana hapa. Hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni tatizo hili la kifua kikuu. Ugonjwa huu wa kifua kikuu sioni kama Serikali imeanza kuuchukua kwa nguvu inayostahili, lakini kuna tatizo kubwa la maambukizi ya ugonjwa huu wa kifua kikuu hasa sehemu hizi za mikusanyiko kwa maana ya huko migodini, sehemu za burudani, kwenye viwanja vya mipira ambako mikusanyiko ya watu inakuwa ni mikubwa. Ikiwa kuna watu wawili au watatu wana ugonjwa huu wa kifua kikuu ni rahisi kuusambaza kwa watu wengine. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikawa na mpango mahususi katika maeneo yote ambayo yana mikusanyiko, tuone ni namna gani tunapambana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni kule kuharibika haribika kwa CT-Scan katika Hospitali ya Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tatizo hili haliishi? Kila wakati lazima usikie CT-Scan imeharibika. Watu wanasafiri kutoka mikoa mbalimbali kupeleka mgonjwa Muhimbili, anafika pale mgonjwa ana hali mbaya, anaambia wiki hii yote CT-Scan imeharibika, kwa hiyo, usubiri. Watu wanapoteza maisha kila uchao. Kwa nini Serikali haiangalii jambo hili? Kama hiyo CT-Scan moja haitoshi, kwa nini tusiwe na nyingine standby? Hebu tutambue kwamba hili tatizo ni kubwa sasa na ifike mahali tuone tuna mkakati mahususi kwa ajili ya kulingamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja zote hizi mbili.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua kukabiliana na Upotevu wa Mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia Azimio hili japo kwa uchache kwa hizi dakika chache ambazo umetugawia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napatwa na mshituko mkubwa kuona ni kwa nini tunaanza kupongezana mwanzo wa safari, tumezoea kupongezana pale kazi inapokamilika. Kuundwa kwa Tume hakujaanza leo, hakujaanza jana, nikiwa niko mwanafunzi sekondari miaka ya 1997-1998 tulikuwa tunaona Mheshimiwa Benjamin Mkapa aliunda Tume zikafanya kazi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume zikafanya kazi, hawa wote tungeanza kuwapongeza pale tu walipounda Tume mwanzoni kabla ya kazi kukamilika tungekuwa tuko wapi? Lazima tuache kazi ifanyike, madini bado yanaibiwa kwa kiasi kikubwa migodini leo tukianza kupongeza kuzuia makinikia peke yake tunakuwa tunakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maisha kuna vitu viwili vya kuchangua ama uchague kuwa mtendaji au uchague kuwa mshangiliaji. Bunge tunaamua kuwa washangiliaji, hili ni jambo la kusikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliamua kubeza hoja nzito zinazohusu kuyalinda madini yetu wakati muafaka, akina Peter Serukamba hawa walipiga kelele hapa, Hamisi Kigwangalla huyu alikamatwa na kuteswa huko kwa sababu ya madini, John Mnyika, Tundu Lissu, Zitto Kabwe walizungumza mambo haya na tuliamua kuwabeza. Leo kwa sababu imepigwa ngoma na tunayempenda tumeamua kuishangilia, tunaishingilia kwa sauti nzito nzito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitendee haki Bunge hili, tunapoingia hapa Bungeni tuvae viatu vya Kibunge tuenee ili tuishauri Serikali na tusijigeuze kuwa washangiliaji tu wa Serikali. Inasikitisha sana, tukilichukulia jambo hili rahisi rahisi kama vile limekwisha na kilichofanyika ndiyo kinatosha tunapoteza rasilimali za nchi hii. Kama Bunge tukae na tuone kwamba kama Rais ana nia nzuri kiasi hiki na sisi Bunge tumsaidie kwa ku-pressurize sheria zote za mikataba tuzifanyie amendments hapa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapande ya dhahabu bado yanaendelea kuondoka na kwa sababu tayari hizi indicator za kuzuia zimeanza, tukichukua muda mrefu kabla hatujayazuia haya, watu wataongeza speed ya kuziiba kwa sababu wanajua mwisho wao unakaribia. Tuongeze nguvu ya kuzuia rasilimali zetu ziache kuibiwa, kupongezana ni jambo dogo sana, tunaweza kupongezana wakati wowote na wala siyo lazima tukapongezana kwenye Bunge, tunaweza kupongezana kwenye mabaraza ya kahawa, tunaweza kupongezana… (Makofi/Vigelegele)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwneyekiti, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa uwezo wa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti inayohusu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nianze kwanza kwa kutoa pole kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hasa wapiga kura wangu wa Temeke kwa mvua kubwa ambazo zinakwamisha shughuli zao za kila siku kwa namna moja au nyingine. Niiombe pia Serikali baadhi ya maeneo madhara yamekuwa makubwa kwa sababu ya wao kutotimiza wajibu wao vizuri. Kama pale kwenye barabara ya Mandela kwenye mataa ya Serengeti ambapo kuna shule ya sekondari ya Kibasila mifereji ya barabara imeshindwa kubeba maji yale ya mvua matokeo yake maji yote yanakwenda kwenye shule ile. Sasa hivi naambiwa madarasani maji ni ya kiuno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna barabara ya Jet Lumo - Davis Corner na yenyewe pia Serikali haijaitengea fedha ya kumalizia toka mwaka wa fedha uliopita na mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, mitaro iliyochimbwa mkandarasi hajamalizia, maji yanakwenda kwenye makazi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi kwenye hoja mimi nina machache tu na haya machache nayazungumza kwa sababu mara zote yanazunguka kichwani kwangu siyapatii majibu.

Moja, mara kadhaa nimekuwa nikiona vitabu vikiandika kwamba pande mbili za Muungano zilikaa kujadili Muungano. Huwa nafahamu sana upande wa Zanzibar wana Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo, huwa linakaa linakusanya kero na linawapa Wajumbe wake kwamba hizi mwende mkazisimamie kwa maslahi ya Zanzibar. Sijui wanaotoka upande wa Tanganyika huwa wanakaa wapi, wanaambiwa na nani kwamba hizi ndiyo hoja za Tanganyika mwende mkazipiganie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili huwa sielewi kwa nini tunavunja Katiba hasa tunapokwenda kwenye sherehe za Mapinduzi. Kwenye sherehe za Mapinduzi mtakumbuka ukiacha ile ya mwaka 2016 ambayo Mheshimiwa Rais hakwenda alienda Shinyanga, mara zote Mheshimiwa Rais akihudhuria pale tunamvua madaraka yake tunamvalisha Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye anapanda motorcade, anapigiwa mizinga 21 lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano mwenye hadhi hiyo amekaa pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo mawili ndiyo nilikuwa hasa nataka kuyazungumzia. Sasa nianze na la kwanza. Kwanza nawapongeza sana wenzetu Wazanzibari kwa namna ambavyo wamekuwa wamoja wakiipigania Zanzibar yao. Mara kadhaa tumeona hata wakiwa hapa ndani linapokuwa jambo ni la Zanzibar wanalipigania bila kujali wanatokea upande upi wa kisiasa na ndiyo maana wenzetu wanafanikiwa. Wametujengea picha kwamba sasa hata Serikali inafikiri kushughulikia kero za Muungano ni kwenda kujibu hoja za kutoka upande mmoja tu wa Zanzibar, wanahisi kwamba Tanganyika hakuna kero. Tanganyika kuna kero nyingi, lakini hatuna pa kusemea kwa sababu hakuna chombo ndani ya Tanganyika ambacho Watanganyika watakaa, watasema kwamba kero zetu au tungependa Muungano wetu uwe hivi. Sasa tumekataa kwenda kwenye Katiba Mpya, lakini kwa nini tusitafute mazingira ambapo Watanzania na wenyewe watapata kusema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namnukuu Msomi Profesa Palamagamba Kabudi ambaye kwenye hii Serikali ya Dodoma yeye ni Waziri wa Katiba na Sheria, siku moja aliwahi kusema siku moja kwamba kwenye kero za Muungano yeye haofii kero za kutoka Zanzibar kwa sababu nyingi ziko mezani na zinajadiliwa, anapata wasiwasi sana na Watanganyika ambao muda mrefu wamekaa kimya na kimsingi hatujakaa kimya, lakini tunasemea wapi? Hakuna kikao chochote mahali popote Watanganyika wanaweza wakakaa wakasema tunataka haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Muungano huu uwe na tija, bora na imara ni lazima tupunguze manung’uniko kutoka kwenye pande mbili za Muungano. Muungano wenye manung’uniko hauwezi kuwa na afya. Japo kuna taswira zile kwamba watu ambao wanataka kuufanyia marekebisho Muungano ndiyo wanaonekana kama hawapendi Muungano lakini kiukweli hata nyumba yako kama unaipenda sana utakuwa unaifanyia ukarabati ili iendelee kuwa nzuri wakati wote. Kwa hiyo, msiotaka tuujadili Muungano na kujiaminisha kwamba Tanganyika haipo na wala haikuwepo, ninyi ndiyo hamuutaki Muungano kwa sababu bado hitaji la Watanganyika kukaa na kusema linaendelea kuwa la msingi. Sasa ni vizuri hili kama ni jipu Serikali mlimiliki jipu hili ili mpange hata tarehe ya kulipasua, mkiacha wananchi walimiliki watakuja kulipasua siku ambayo ninyi hamjajiandaa kushika usaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwafurahisha Watanganyika siyo kuwabana Wazanzibari, ni kuwaacha Watanganyika nao waseme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuufurahisha upande huu huku, siyo lazima kuwaminya Wazanzibari kwamba labda wakitaka kujiunga na FIFA tuwakatalie, wakitaka kujiunga na IOC tuwakatalie, hapana. Tuwaunge mkono ikiwezekana wapate hata mamlaka kamili lakini na upande huu pia tupate pa kuzisemea kero zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa upande huu ambao hutaki niwaite Watanganyika, wa upande huu, kuna mambo ambayo kwa kweli… (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama muda wangu unanitunzia maana unani- interrupt sana wakati si lazima niseme Tanzania Bara, nikisema upande huu, huku ni Bara. (Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo naliacha kama halikufurahishi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha mwisho nachotaka kusema kwa nini tunayapora mamlaka ya Rais tunapomtaka ahudhurie Sherehe za Mapinduzi? Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 33(1) na (2) inamtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ndiye Kiongozi Mkuu wa nchi hii, ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali na ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote, lakini anapokwenda kwenye Sherehe za Mapinduzi yeye anaingia wa pili na Mheshimiwa Dkt. Ali Shein anaingia mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Wakati Mheshimiwa Dkt. Ali Shein anaingia, Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ndiye mwenye hadhi ya kuwa wa mwisho inabidi asimame kumkaribisha anayeingia, hakuna itifaki ya namna hii duniani hapa. Ingekuwa ni busara kwenye sherehe zile Mheshimiwa Rais asiende, anaweza kwenda Naibu Waziri wa Mazingira akawakilisha Serikali ili Mheshimiwa Dkt. Shein anapoingia awe mkubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kusimama mahali hapa ili tuweze kuishauri Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili baadae iweze kufanya kazi vizuri na maendeleo yawafikie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache sana, mimi nilikuwa na mapendekezo matatu tu ambayo nataka kuikabidhi Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili wayafanyie kazi.

La kwanza, napendekeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi iangalie uwezekano wa kuiunganisha Wizara ya Kilimo na Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili, nataka Serikali ikubali sasa ili tuelekee kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo na kuijenga Tanzania ya viwanda basi tukubaliane kupiga marufuku uagizaji wa vyakula na malighafi zingine ambazo zinaweza kuzalishwa hapahapa nchini. (Makofi)

Pendekezo la tatu, ni kupendekeza Chama cha Mapinduzi ambao ndiyo marketing manager wa sera zinazotekelezwa na Serikali wabadilishe logo yao, wabadilishe nembo ya jembe na nyundo ambayo haihamasishi mapinduzi ya kilimo hapa nchini. Naomba niyajadili haya bila kufuata mpangilio wa namba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilipoanza kusema wanataka kuitengeneza Tanzania ya viwanda, hatukuwa tunategemea kwamba tujenge viwanda ambavyo havitatumia malighafi zinazotoka shambani. Tuliamini kwamba Tanzania ya viwanda ni viwanda vile ambavyo vitatumia malighafi zinazozalishwa mashambani ili ziweze kuzalisha bidhaa ziweze kupandisha thamani mazao yetu na Mtanzania huyu ambaye anaitwa mnyonge ambaye kimsingi ametiwa unyonge na Serikali ya Chama cha Mapinduzi aweze kubadilisha maisha yake yale bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukasema ili haya yafanye kazi vizuri, ni lazima Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ziwe zinafanya kazi kwa pamoja. Kitendo cha kutengana kwa Wizara hizi ndiyo unakuta anakuja Waziri wa Viwanda anakusomea hapa kwamba wamejenga viwanda vingi, lakini ni viwanda vya kutengeneza kandambili, viwanda vya kutengeneza mabeseni, viwanda vya kutengeneza mabanio ya nywele, viwanda vya maji, vitu ambavyo havitusaidii kuboresha mazao yanayotoka shambani. Kama wangekuwa wanafanya kazi kwa pamoja maana yake kwenye mafanikio ya Wizara ya Viwanda angekuja angesema kwamba tulikuwa tunazalisha mafuta ya kula asilimia 30 tu ndani sasa tumepandisha tunazalisha mafuta ya kula kwa asilimia 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tunaona pia kwenye viwanda kwamba zao la chikichi limetengewa fedha kubwa ili uzalishaji wa malighafi za kutengeneza mafuta zipatikane ndani. Tusingekuwa tunaona kwenye kilimo wakulima wa ufuta wanalalamika kwamba hawana soko la uhakika, tusingekuwa tunalalamika kwamba eti kuna mafuta ghafi yamekwama bandarini yanataka kuingizwa huku ndani tunaanza kupiga kelele hapa inaharibu muda wetu wa kufanya mambo mengine kama malighafi hizo zingekuwa zinazalishwa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi imepiga hatua kwenye mapinduzi ya viwanda bila kupitia kipindi kigumu. Ukienda India watakuambia tulisimamisha kuagiza magari kutoka nje kwa sababu tulitaka tuzalishe ya ndani kwanza ili soko letu la ndani lote litumie magari ya ndani.

Ukienda China hivyo hivyo, sisi hapa bado tunaagiza sukari, mafuta, soya, mihogo mikavu kutoka nje, tunashindwa nini kulima hapa? Tupige marufuku uagizaji wa mazao haya kutoka nje, hata kama tunazalisha mafuta kwa asilimia 30 tuitumie hiyo hiyo, tutaona namna gani kumbe tunaweza tukaongeza, tunaweza tukatengeneza fursa kuzalisha hapa nchini. Hatuwezi kufa kwa kukosa mafuta ya kula, hatuwezi kufa kwa kukosa sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sukari siyo kwamba tunashindwa kulima hapa ndani, ni ukiritimba tu wa kulinda viwanda vikubwa. Ukienda kule Kilombero kila mwaka miwa inalala shambani mnunuzi hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkulima wa miwa kule Kilombero, tunalima miwa hatuwezi kupanga bei sisi anapanga bei anayekuja kununua. Yeye ndiye anapanga bei ya namna gani atautoa huo muwa wako kutoka shambani kuupeleka kiwandani kwake na namna ya kulipa pia anachangua yeye kwamba nakulipa kwanza asilimia kumi, hii asilimia kumi nyingine nitakulipa mwezi unaofuata yaani mkulima unakuwa kama unasaidiwa wakati unauza mazao yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo mfanyabiashara mmoja alijaribu kujenga kiwanda kidogo cha kutengeneza Sukari pale Sanje akapigwa vita mpaka akafunga kiwanda. Kwa hiyo, kuna mikakati ya makusudi kuhakikisha hakuna viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sukari vinajengwa ili wale ma-giant wakubwa ndiyo waendelee kuzalisha sukari hiyo kidogo ili mwisho wa siku Serikali itoe vibali vya kuagiza sukari kutoka nje wapewe wao ndiyo waingize wapate faida kubwa, hatuwezi kuitengeneza Tanzania ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni nembo ya Chama cha Mapinduzi, tunasema tunataka kwenda kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo lakini wewe Mheshimiwa Waziri unasimama kunadi kwamba tunataka tuachane na jembe la mkono huku umezungukwa na watu waliovaa t-shirt ambazo zimebeba jembe la mkono na nyundo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni brand, namna ambavyo umeiweka brand yako ndiyo itasaidia kukutangaza kwamba wewe una malengo ya kuelekea wapi. Huwezi kubeba brand ya jembe na nyundo halafu utake ikupeleke kwenye kilimo cha kutumia matrekta. Hebu mkae, mnaweza kulichukua hili kama jambo la kisiasa, lakini hii siyo siasa, ndiyo ukweli, kilimo ni biashara. Watu wanataka kulima, wanataka wabadilike kutoka kwenye jembe la mkono watumie kilimo cha kisasa, unawapelekaje kwa kuvaa jembe la mkono?

Anzeni kubadilisha mindset zenu ndiyo mtaweza kulisimamia jambo ambalo mnataka kulitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana mmeamini kwamba kila mambo mnayoyasema huwa hayatekelezeni, lakini I assure you, Tanzania ya viwanda inawezekana. Mpaka leo bado unapita hapo Dumila unakuta nyanya zinaoza, ni kwa sababu wenyewe hamuamini kwenye jambo ambalo mnalisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anzeni kwanza kubadilisha mitazamo yenu kama Serikali muamini kwamba tunataka tujenge Tanzania ya viwanda lakini kwa kutumia malighafi zinazolimwa shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana watu wanapiga kelele leo, amesema hapa Mheshimiwa Qambalo kuwa Mheshimiwa Waziri ambaye uko ndani ya Serikali huna tofauti na mimi Waziri Kivuli, wote tunaongea maneno matupu ambayo hayaendi kwenye utekelezaji. Kama huna bajeti, bajeti inashuka kila siku, utatekeleza vipi hiyo mipango yako? Wanatushinda Rwanda, wametenga bajeti ya shilingi trilioni saba kwa ajili ya kilimo, nchi ndogo kama ile, sisi tunatenga shilingi bilioni 170, hiyo si nauli tu ya Waziri kutembelea mikoani, itatusaidia kitu gani? Bado Waziri unataka kudanganya watu hapa kwamba eti NFRA itanunua mazao yote ambayo yamesalia huko mikoani, hii haiwezekani.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. ABDALLAH S. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye azimio hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wala hatubishani Dodoma kuwa Jiji au siyo Jiji, au Dodoma Kuwa Makao Makuu au siyo Makao Makuu. Tayari hapa ni Makao Makuu na tayari imetangzwa kuwa ni Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji kuwa Jiji is not honorarium privilege, ni vigezo, yaani Mji unakuwa Jiji kwa kuwa na vigezo. Mheshimiwa Simbachawene amekuwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI anafahamu Majiji yana sifa gani na Dodoma imepungukiwa sifa gani. Sasa kumuunga mkono Rais kwa hili alilolifanya ya kuifanya Dodoma iwe Jiji kabla haijawa na vigezo vya kuwa Jiji ni kutekeleza vigezo vile kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea azimio linalokuja hapa liwe la Bunge kuitaka Serikali itenge fedha za kutosha sasa ili twende tukaijenge Dodoma iwe na sifa ya Jiji. Tukisema tu tunapongeza kwamba tayari tumeambiwa na sisi ni Jiji, uneweza ukaitwa Jiji lakini bado ni kijiji. Hii haikusaidii! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma ambayo leo ni Jiji haina hata stand ya magari kutoka mkoani; Dodoma ambayo leo ni Jiji haina hata stand ya Daladala, zinasimama kokote tu, zinajipanga humo barabarani. Sasa tunahitaji fedha kuhakikisha Dodoma inapangika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu pekee ya adventure hapa Dodoma ni Mnadani. Mnadani ni kuchafu ajabu! Halmashauri inashindwa hata kutengeza basi. Sawa, tutakuja kuumwa kipindupindu hapa kwa sababu hatuna sehemu nyingine ya kwenda. Weekend lazima uende Mnadani. Unaenda kula, maeneo ni machafu. Halmashauri ibadilishe mindset zake kwamba sasa hivi hapa ni Jiji. Sasa Jiji lina heshima yake na Jiji ni vigezo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawataka Waheshimiwa Wabunge wa Dodoma watumie fursa waliokuwa nayo kuwa-lobby Waheshimiwa Wabunge hapa tuilazimishe Serikali kutenga fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hazipitiki huko, ikinyesha mvua ni tope kila sehemu. Fedha ya Halmashauri huwezi kujenga barabara zote hizo kwa kiwango cha lami. Barabara ya kilometa moja sasa hivi kwa lami ni kati ya shilingi milioni 900 mpaka shilingi bilioni 1.3. Halmashauri ya Dodoma mna fedha hiyo ya kujenga hizo barabara? Hamna! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vya maji bado ni kile kile vya Mzakwe, watu wanaongeza, Mji unapanuka, hakiwezi kutosha. Leo mnagawa viwanja, Halmashauri iko busy kutangaza kugawa viwanja. Nendeni mkajenge miundombinu kule watu watakimbilia wenyewe. Unauza viwanja au mnauza mashamba sasa? Kwa sababu ili muuze viwanja na watu wavikimbilie ni lazima mtengeneze barabara, mpeleke umeme, pelekeni miundombinu ya maji, watu watahamia. Leo hata ukijenga kule Mtumba utaenda kukaa? Huwezi kwenda kukaa, tutaendelea kubanana hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri Waheshimiwa Wabunge wa Dodoma mjipange vizuri ili tuweze kuwasaidia tuijenge hii Dodoma. Nasi tunakaa hapa, shughuli zetu tunazifanya hapa, tungependa pawe na hadhi ya Jiji na siyo hii blah blah tunayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia machache katika bajeti hii. Kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya, nimeweza kumaliza Mfungo wa Ramadhani mimi na wapiga kura wangu wa Temeke na leo tunahitimisha siku za ziada sita katika kuukamilisha ule Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja iliyokuwa mbele yetu, nina mambo matatu tu ya kuyagusia endapo muda utanitosha. Kwanza, nitapenda kugusia pato la kila Mtanzania, mfumuko wa bei na mwisho nitamalizia na hujuma ya Serikali dhidi ya zao la korosho kule Mikoa ya Lindi na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla Mheshimiwa Waziri hajawasilisha hotuba ya bajeti yake, alitangulia kutoa Taarifa ya Hali ya Uchumi hapa nchini. Katika kuizungumzia hali ya uchumi hapa nchini yako mambo ambayo yameandikwa kwenye kitabu hiki ukiyasoma kama Mtanzania kwa kweli hayaeleweki. Nadhani Mheshimiwa Waziri alikuwa analenga kuwafurahisha pengine Wazungu, World Bank au IMF ili Serikali iendelee kupata sifa za kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, anasema Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kupandisha pato la Mtanzania mmoja mmoja kutoka Sh.2,086,000 mpaka Sh.2,275,000. Maana yake Mtanzania mmoja sasa pato lake limepanda kutoka Sh.5,700 kwa siku mpaka Sh.6,300 kwa siku. Nikajiuliza hii ni sifa au ni kejeli? Kwa sababu kipimo cha pato la Mtanzania ni kumwezesha kupata milo mitatu. Sasa kama tunajisifu kwamba tumemuwezesha Mtanzania kupata Sh.6,300 kwa siku, hiyo itakuwa ni kejeli, haiwezi kuwa sifa, kwa sababu Sh.6,300 huwezi kupata angalau mlo mmoja uliotimilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikajaribu kuingia sokoni, nikanunua tembele la Sh.1,000 kwa maana ya mafungu mawili, nikanunua unga nusu kilo Sh.1,200, nikanunua mkaa kipimo kidogo Sh.3,000, nikachanganya na pilipili, nyanya na kitunguu Sh.6,300 imekwisha sijapata mafuta ya kula na chumvi nikaombe kwa jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaleta bajeti ambayo ni ya kumwezesha Mtanzania kupata ugali na tembele la kuchemsha ndiyo uwe mlo wake mmoja wa siku nzima, nikagundua kwa nini Mheshimiwa Waziri pia alisema, akiwadhihaki tena kwamba umri wa Watanzania average ya kuishi ni miaka 64, it is obvious. Kama mlo wako wenyewe ni mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha, utawezaje kuishi zaidi ya miaka 50? Hapo hujaumwa, yaani uombee usiumwe na hiyo familia iwe ni wewe ni mkeo au mke na mume ndiyo mtapata huo mlo mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni dharau kwa Watanzania na ndiyo maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi mnapenda sana sifa, mkisimama majukwaani muda wote mnajisifu, tumenunua Bombardier, tunajenga standard gauge, stiegler’s gorge, hata siku moja hamjawahi kusema kwamba mmemwezesha Mtanzania sasa anaweza kupata mlo mmoja wa ugali na tembele la kuchemsha ni kwa sababu mnatambua hii siyo sifa, ni kejeli lakini kwenye kitabu hiki mmeiandika. Ndiyo maana nikasema, kitabu hiki pengine kilikusudia watu wengine nje ya nchi hii lakini siyo kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pato linakwenda sambamba sana na mfumuko wa bei. Mtanzania leo hata ukimwezesha apate Sh.20,000 kwa siku, kama haitoshi kumwezesha kupata milo mitatu, ni sawasawa na bure. Kwenye Taarifa ya Hali ya Uchumi Mheshimiwa Waziri anasema, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kupunguza mfumuko wa bei. Nikajiuliza, ni bei za vitu gani ambazo Serikali imedhibiti? Ni bei ya chumvi, biscuit au ya Big G?

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake kwa sababu anakiri kwamba kweli kwenye huo huo wastani, Watanzania hawapati milo mitatu, mpaka tusubiri mwaka 2025 tutapata milo mitatu. Kwa hiyo, yupo sahihi, ananiunga mkono kwa hiki nachokisema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nikasema pato la mtu mmoja mmoja kama halimwezeshi kupata milo mitatu kwa kesi yetu hapa Tanzania, hata kama atakuwa anapata Sh.20,000 haiwezi kumsaidia. Ndiyo maana nikasema huo mfumuko wa bei wanaosema wanau-control ni upi? Kwa sababu kama mfumuko wa bei ungekuwa controlled vizuri, Mtanzania hata angepata Sh.2,000 kwa siku, angeweza kumudu milo mitatu. Sisi kesi yetu ni milo mitatu tu hapa, wala siyo kiasi gani kinaingia mfukoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wamepunguza mfumuko wa bei mwaka 2017, Serikali ya Awamu ya Tano wakati inaingia madarakani bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa Sh.1,200, mwaka 2017 bei ya sukari ika-shoot kutoka kilo Sh.1,200 mpaka Sh.2,500/=. Wakalieleza Bunge hili na Taifa hili kwamba hiyo ni hujuma ya wafanyabiashara wameficha sukari kwenye godown na kwamba wataitafuta kwa gharama yoyote ili bei ya sukari irudi kwenye bei yake ya kawaida. Leo ni mwaka 2018 hawajarudi kutuambia walipata sukari kiasi gani kwenye godown na wameipeleka wapi? Cha ajabu zaidi, bei sasa imekwenda mbali zaidi, kilo ya sukari leo ni zaidi ya Sh.3,000. Sasa unajiuliza, bei ambayo wanai-control ni ya vitu gani, mbona hatuioni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu hapa ikatoea tena crisis ya mafuta ya kula na Mheshimiwa Waziri Mkuu akaahidi hapa ametoa siku tatu. Utakumbuka maelezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yalikuja baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara kutoa tamko hapa Bungeni kwamba malighafi ya mafuta iliyopo nchini haiwezi kusababisha bei ya mafuta ipande, hata kama ile meli itachelewa kupakua mafuta. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kupitia maelezo hayo akasema hapa, natoa siku tatu, mafuta yaliyofichwa yatoke. Mpaka leo bei ya mafuta ipo juu, haijashuka na hatujapewa taarifa yoyote. Tukisema tuna- control mfumuko wa bei, ni bei za vitu vipi? Hivi vitu ndiyo vinagusa maisha ya Mtanzania ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita hapa lilipandisha bei ya mafuta ya taa kwa sababu ya kukomesha uchakachuaji. Walisema kabisa kwamba wanafanya hivyo kama temporary solution ya ku-control uchakachuaji wa mafuta, kwa hiyo, bei ya mafuta ya mafuta ya taa ifanane na bei ya diesel. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, EWURA sasa hivi inatumia mbinu za kisasa na teknolojia za kisasa, lakini bado eti tunaacha bei ya mafuta ya taa iwe sawa na ya diesel kwa ajili ya ku-control uchakachuaji. Kwa nini tumtese Mtanzania asiyekuwa na gari kwa sababu ya kulinda maslahi ya wenye magari? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kengele ya kwanza. Naomba dakika tatu basi nimalizie hujuma ya Kusini.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kusema machache katika taarifa hizi za Kamati mbili zilizowasilishwa hapa Bungeni leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimejifunza jambo leo na hili ni kuonesha ni kwa kiasi gani sasa kazi nzuri zinazofanywa na Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, zinakubalika pande zote, kwamba hata wale ambao hapo awali walikuwa wakibeza yale makubwa anayoyafanya sasa unaona wameanza kuyakubali kwa njia nyingine tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijakuja hapa nilipitia Hansard za Bunge kuona maoni ya Wabunge wakati wa mjadala wa IPTL ulipokuwa ukijadiliwa hapa Bunge. Yalikuwa ni maoni ya Kambi ya Upinzani kwamba tuachane na miradi midogo midogo ya kutengeneza umeme nchini tuje na miradi mikubwa, hata kama nchi itasimama kufanya shughuli nyingine kwa miaka mitano, lakini ikitatua tatizo la umeme, huo utakuwa uamuzi wa basara sana. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Yes! Yes!

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikarudi nikaangalia Hansard za Bunge la Bajeti mwaka jana. Waliotoa maoni hayo wakati Serikali imeanza kuzungumzia suala la Stiegler’s gorge, wakaanza kusema kwamba mradi huo si sahihi kwa sababu unaharibu mazingira. Leo tumekuja hapa tena tunasikia hoja zinazidi kubadilika ninachomaanisha kwamba mradi huo sasa sio sahihi mkandarasi aliyepewa hana uwezo wa kujenga. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inakuja hoja nyingine mpya kwamba mradi huo Watanzania wasiutegemee kesho au kesho kutwa nani alisema mradi mkubwa kama huu unaweza ukajengwa ndani ya mwaka mmoja? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mmmh!

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza kuona ni kwa namna gani Watanzania wanaanza kukubali na kuzielewa kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Sasa hili ni jambo zuri kwa sababu umeme ambao unakuja kujengwa kwenye nchi hii, unakwenda kuondoa matatizo mengi ambayo yamekuwa yakiisumbua nchi kwa muda mrefu. Wakati mradi huu ukiendelea miradi mingine ya kuimarisha umeme inaendelea kufanywa ili Tanzania isiwe gizani wakati wa kusubiri mradi huu. Watanzania wanaelewa kwamba tunakoelekea sasa tunakwenda kulitatua tatizo hili moja kwa moja. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa maamuzi haya magumu wanayoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa suala hapa pia la LNG na kuna msemaji mmoja alitoa taarifa kwamba wananchi wasahau kuhusu LNG kwa sababu baada ya sheria mpya za kutunza rasilimali za nchi hii zilizotungwa mwaka 2017, hakutokuwa na mtu atakayetamani kuja kufanya miradi ya LNG.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri haya masuala ya gesi ni masuala sensitive sana si kila mmoja anaweza kuyasema yana technicalities zake. Taifa halikuwa likitafuta Mkandarasi kwa ajili ya kujenga LNG, lakini waliokuwa wakifanya kazi ya gesi kwenye Kitalu Block one na Block two baada ya kugundua gesi nyingi wakasema hii gesi huwezi kuiuza hapa ndani ni lazima itengenezewe plant za LNG iuzwe nje. Serikali ikawaambia badala ya Block one kujenga LNG yake na Block two kujenga LNG yake, shirikianeni mjenge plant moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana kwamba Equinor ambao zamani walikuwa wakifahamika kama Statoil wakishirikiana na ExxonMobil ambao ndio wako block one washirikiane na Shell ambaye ndio alinunua hisa za British Gas (BG) ambaye na yeye anashirikiana na Ophir Energy na Pavilion Energy kwamba hawa washirikiane kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati Statoil ambao ni Equinor leo wanahangaika na hili Shell alikuwa busy na Plant ya Msumbiji, kwa hiyo wakawa hawashirikiani vizuri. Equinor wakaamua kupambana kuishauri Serikali iwaruhusu wajenge plant yao wenyewe na mwezi wa Disemba Serikali imeridhia kwamba nyinyi Equinor mnaweza kuendelea na plant yenu. Leo mtu akisema hapa wananchi washukuru Mungu kuhusu LNG maana yake anazungumza jambo asilolijua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niishauri tu Serikali hapa sasa kwa sababu mradi wa LNG ni mkubwa na kwa kuwa mmewaruhusu Equinor kuendelea na LNG basi kiundwe kitengo maalum cha kushughulika na hiyo LNG kama ilivyofanywa kwenye Stiegler’s gorge. Kwamba kumekuwa na kitengo maalum kinashughulikia uendelezaji tu wa Stiegler’s gorge na kwenye LNG vile vile kiundwe kitengo cha namna hiyo ili hawa Equinor wawe na mtu ambaye wanadili naye moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya mambo ya gesi usipoyajua kwa kweli yatakusumbua na ndio maana mtu anaweza kuja hapa akahoji, bomba kubwa la gesi mpaka leo utilization yake ni 7% tu, hiyo ndio sahihi kwa sababu bomba lile halikujengwa ili lijae ndani ya miaka miwili. Kwa sababu kama lingejaa ndani ya miaka miwili ndio ingekuwa hasara. Lile bomba linatakiwa lisijae hata ndani ya miaka
20. Kwa hiyo, kama leo liko 7% maana yake ujenzi ule uliona mbali zaidi na tuna sababu ya kuipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Watanzania waanze kuzoea vitu vikubwa vinavyojengwa kwa fedha za ndani, yale mengi ambayo tulikuwa tukiamini huko nyuma kwamba hayawezi kutekelezeka ndani ya Awamu ya Tano yanatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye Kamati nyingine ya Ulinzi na Mambo ya Nje…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie machache kwenye mjadala ulio mezani asubuhi ya leo. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya nzuri siku ya leo, lakini niendelee kumwomba anilinde kunipa afya njema mpaka siku nitakayopiga kura ya bajeti ili nami kwa mara ya kwanza niweze kuwatendea haki wananchi kwa kupiga kura ya ndiyo kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze sana Serikali kwa namna ambavyo imemwaga miradi mingi Majimboni kwetu katika kuboresha huduma za jamii. Imeweka fedha nyingi sana kwenye miradi ya afya na huduma za afya kwa kweli zimeboreka kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, ulikuwa ni utaratibu wa kawaida wamama wanapoenda kujifungua, kubeba vifaa vya kujifungulia, kubeba mabeseni na vitu vya namna hiyo, jambo ambalo kwa sasa limekuwa ni historia. Wamama wanakwenda kujifungua, wanapata huduma zote hospitalini na hawachajiwi. Jambo hili limekuwa ni la kihistoria na wananchi wa Temeke wanaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imejikita katika kuboresha huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwenye huduma za afya, lakini pili, kwenye uboreshaji wa miundombinu. Nikitolea mfano tu wa huko huko Jimboni kwangu Temeke, kuna ujenzi mkubwa wa miundombinu, achilia mbali daraja la juu (flyover) ambalo limerahisisha sasa foleni zilizokuwa zikiwakabili watu wakati wakwenda Airport, lakini barabara nyingine zinazoungana na zenyewe pia zinaendelea kujengwa. Wakandarasi wako site wanaboresha miundombinu. Tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hili lakini Waziri Mkuu na Ofisi yake kwa namna ambavyo wanakuja kusimamia na kuhakikisha kwamba ujenzi na matumizi ya fedha hizi za Serikali unakuwa ni wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze sana Tume ya Uchaguzi kwa namna ambavyo wamekuwa wanafanya kazi zao vizuri. Tume ya Uchaguzi inafanya kazi zake vizuri na mfano mkubwa ni kwenye chaguzi hizi chache ambazo zimepita hivi karibuni ambavyo wamezisimamia vizuri. Sisi Wandengereko huwa tuna usemi wetu tunasema, “maiti ya Kimakonde haikosi mchawi.” Ni kwa maana pamoja na kazi nzuri mnayoifanya, bado wapo watu ambao wataendelea kuwakosoa. Wanaowakosoa kwa kusema kwamba Tume ya Uchaguzi inapendelea, ni hao hao ambao nanyi mliwahi kuwatangaza na leo ni Wabunge huku. Kwa hiyo, hayo…

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Tusikie taarifa.

T A A R I F A

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza, mimi binafsi amenishtua kidogo aliposema maiti ya Mmakonde haikosi mchawi. Nataka ufafanuzi, atufafanulie tafsiri yake ni nini hapo? Ahsante.

MWENYEKITI: Hilo ni swali, mtaeleza huko nje. Endelea Mheshimiwa.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sasa ombi langu kwa Tume ya Uchaguzi, nilikuwa nataka sasa iende mbali zaidi. kwa kuwa imefanikiwa katika usimamizi wa taratibu za uchaguzi, iende mbali kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mambo ambayo viongozi waliochaguliwa unaendelezwa hata baada ya wao kumaliza muda wake. Kwa mfano, tunapopata viongozi mahiri kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye anaanzisha vitu vingi vikubwa, tena vyenye tija kwa Taifa ambavyo vingine vitakuwa bado havijakamilika wakati muda wa miaka 10 unakwisha, ni vizuri Tume ya Uchaguzi ikaandaa mfumo ambapo atakayekuja sasa madarakani naye asianze na vitu vipya, aendeleze yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kuweka Makao Makuu Dodoma. Mpango huu ni endelevu, nyumba na Ofisi za Serikali zinaendelea kujengwa, zipo zitakazokamilika na zipo ambazo zitakuwa hazijakamilika mpaka Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anaondoka madarakani. Sasa tusipoweka mfumo mzuri kwamba anayekuja naye aendelee mle mle, maana yake anaweza akaja mwingine akaanzisha vitu vipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tumeweka sheria ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu, lakini sheria zinabadilika, maana yake afadhali lingekuwa ni jambo la kikatiba, utaratibu wake kidogo ni mgumu, lakini sheria zinaweza zikaja amendments zikabadilisha tukarudi tena Dar es Salaam. Jambo hili litakuwa ni hasara kubwa kwa Taifa. Sasa ni vizuri mambo haya yakawekewa utaratibu mzuri.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtolea, taarifa.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mtolea kwa ushauri ambao ametoa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba angependa sana kuwe na utaratibu ambao utawafanya viongozi ambao amesema mahiri baadaye na wao vitu ambavyo wamevianzisha ili viendelee. Akumbuke kwamba hata waliomtangulia Mheshimiwa Dkt. Magufuli viko walivyovianzisha naye aliviacha. Kwa mfano, miradi ya gesi ambayo Serikali ya nchi hii ilizunguka nchi nzima kuwaambia Watanzania kwamba sasa gesi ikishapatikana tutakuwa hatuna tena tatizo la umeme katika Taifa hili…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka!

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: …lakini ameacha na sasa hivi tuna mradi wa Stiegler’s Gorge unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtolea.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipuuze hiyo taarifa kama ambavyo nampuuzia na yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyetiki, ninachozungumza ni kwamba, tunahitaji mambo ya msingi, mambo makubwa ambayo yameanzishwa hivi sasa ambayo kila Mtanzania anayaona na anakubali kwamba yana tija kwa kizazi hiki na kizazi kijacho yaweze kuendelezwa. Yasiishie pale ambapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli atamaliza muda wake. Kama tunashindwa kumwongezea muda yeye aendelee, basi tuwe na mfumo ambayo Ofisi kwa maana ya Rais kama taasisi itaendeleza yale ambayo aliyaanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu si muda wa sisi kwenda mbele na kurudi nyuma tena, tumeshapiga mark time kwa muda mrefu. Sasa hivi tumepata mtu ambaye ametuonesha njia, ni vizuri tukaenda nae. Watu kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hawazaliwi kila wakati, akipita huyu, inaweza kupita miaka 50 au miaka 100 tusipate mtu mwenye maono ya namna hii. Kwa hiyo ni vizuri tukaona kwamba, haya maono yake... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niwapongeze sana Mawaziri wanaosimamia Wizara hii kwa namna ambavyo wanajitoa kuhakikisha wanasimamia Muungano, lakini pia upande wa mazingira. Waendelee kufanya ziara nyingi kwa sababu mazingira kwa kweli yameharibika kwa kiasi kikubwa na Muungano unahitaji kusemewa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu kuna tatizo moja; kuna mtaro mmoja unatiriri nafikiri ni maji ya sumu, nimeshawahi kulizungumza hili hapa Bungeni na leo ni mara ya pili. Kwenye Kata ya Sandari kule Temeke Mikoroshini, kuna mtaro wa mfereji wa Mpogo, yake maji yanaoneka yanatoka kwenye moja kati ya viwanda vilivyoko Vingunguti, nyumba zilizokuwa pembeni bati zinaharibika na matofali yanamung’unyuka. Hali hii inaonesha kabisa kwamba pale kuna sumu inatembea na kama matofali yanamung’unyuka maana yake afya za watu wanaoishi pale ziko kwenye hii changamoto kubwa. Kwa hiyo, naomba hili jambo walichukue na walifanyie kazi kwa haraka. Sisi kama Halmashauri tumeshatenga fedha ya kuujenga ule mfereji, lakini haiondoi ukweli kwamba maji yanayotiririka yanakuwa na sumu. Hilo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naitaka Wizara wawe wanatupa taarifa za mara kwa mara za uchafuzi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam. Tunapata taarifa ambazo zinaleta sintofahamu kidogo, kuna wakati tunaambiwa kwamba mabonde yale hayafai hata kwa kulima mbogamboga za majani, kuna wakati tunaambiwa water table ya Dar es Salaam yote imechafuka hata maji ya visima tunayoyatumia si mazuri. Sasa ni vizuri wakawa wanatuandalia taarifa za wazi na za kina ili tujue kitu kipi tufanye na kitu kipi tusifanye. Maana yake sasa tukienda sokoni tunaogopa michicha tunaogopa matembele, tunahisi yamelimwa kwenye yale maeneo ambayo yana sumu. Ikiwezekana waweke hata mabango tujue kwamba eneo hili linastahili, eneo hili halistahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sheria ambazo zinatumika na NEMC kwa kuwaadhibu wanaochafua mazingira, ziangaliwe upya, inawezekana ni za Ulaya sana. Kwa mfano, mtu mwenye garage anatakiwa awe amesakafia na kuwe na system ya kutofautisha maji na oil. Garage zetu nyingi hazijasakafiwa, kwa hiyo kinachofanyika ni kama tumetengeneza mwanya wa watu kupiga fedha. Leo mtu anapelekewa notice kwamba hii garage uisakafie ndani ya siku 14, jambo ambalo haliwezekani. Akija siku ya pili, yule mtu atakachofanya ili asitozwe faini ya milioni tano, atamuona tu pembeni huyu mtu, kwamba bwana usiniandikie, chukua hii milioni moja, chukua hii laki mbili, sasa watu wataishi hivi mpaka lini? Lazima tuwe na sheria ambazo zinaendana na mazingira yetu, je tuna uwezo kwenye kila car wash kuwa na hiyo system ya kuchuja maji na oil. Magari yetu yenyewe ya mitumba, likisimama tu hapo linavuja oil, mtu anatakiwa awe na system ya kuchuja hiyo kitu, hii inawezekana vipi? Kwa hiyo, tuziangalie hizi sheria kama kweli ni rafiki na zinaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni la Muungano; nimeshtushwa sana, mtu aliyesimama hapa kusema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haiutaki Muungano tena na yeye anasimama akitoka CUF. CUF wanaamini kwenye madaraka kamili, mamlaka kamili, mamlaka kamili maana yake Zanzibar isimame kama nchi tofauti na Tanzania Bara isimame kama nchi tofauti, sasa hapa ni nani asiyeupenda Muungano? Kwa hiyo, nafikiri kwenye jambo hili la Muungano, ni vizuri tukawa wakweli, kwamba hizi nchi mbili, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, zinahitajiana sana whether tuko ndani au nje ya Muungano. (Makofi)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumekubali tuko ndani ya muungano ni vizuri….

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mamlaka ya Zanzibar ambayo ni kupata fursa zaidi za kiuchumi hususan katika nyanja za kimataifa, haliharamishi kutokuwepo Muungano. Tuna mifano mingi, tuna European Union, ni Muungano una nchi kadhaa, lakini kila nchi si ina mamlaka yake! Kwa hiyo, suala la kujadili, Mheshimiwa Mtolea, suala la kusema kwamba eti kwa sababu kuna watu wanazungumzia suala la kwamba Zanzibar iwe na mamlaka kamili, hawataki Muungano, hii siyo sahihi. Suala la mamlaka kamili ni suala la kuwepo kwa Serikali tatu….

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mtolea endelea.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siipokei hiyo taarifa yake. Tunapozungumzia Muungano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumzia kitu tofauti sana. Huwezi kufananisha na miungano mingine hiyo sijui ya European Union na sehemu nyingine. Huu ni muungano wa kipekee, una historia ya kipekee na mazingira yake ni ya kipekee. Sasa ukianza kusema kwamba tunakosa fursa, si kweli na wakati mwingine eti mtu anasema kwamba tumechoka kubebwa kwenye koti la Muungano, hivi aliyebebwa anaweza akaanza kuchoka kabla ya aliyembeba? Maana yake aliyekubeba anavumilia kwa sababu anafahamu thamani ya anachokifanya. Mama akimbeba mtoto, si kwamba eti mtoto aanze kuchoka eti mama hajachoka, lakini Mama anaendelea kumbeba kwa sababu anajua ni jukumu lake na ndicho Tanzania Bara wanachokifanya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijalia uhai na kuanza Mfungo wa Ramadhani vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali hasa Wizara ya Afya kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya ya kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinakuwa katika mikono salama. Uwekezaji mkubwa mnaufanya kwa maana ya kutenga fedha, kuzipeleka na kuzisimamia lakini kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinapatikana na wauguzi wanakuwepo. Hili ni jambo kubwa, muendelee kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nisiache kumshukuru Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji ambaye aliamua kwa makusudi katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani yeye akishirikiana na wanawake wanaofanya kazi na Benki ya UBA walijitolea kuleta mashuka katika Hospitali ya Temeke. Wananchi wa Temeke wanakushukuru sana na kwao hawakuoni tu kama kiongozi lakini wanakuona kama ndugu yao wa karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri Mkuu ambaye alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Temeke. Ziara yake imekuwa na tija sana, amerekebisha mambo kadha wa kadha lakini pia alisisitiza baadhi ya mambo ambayo Wizara ilibidi muendelee kuyashughulikia. Moja, ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunapata mashine ya kufulia katika Hospitali ya Temeke. Ni kweli hakuna tatizo la kufua kwa sababu wanakwenda kufua Muhimbili lakini kwa upekee wa Hospitali ya Temeke ambayo pia ni kituo cha magonjwa ya mlipuko si vizuri sana wakawa wanaenda kufua katika eneo linguine. Ni vizuri kwa ubora ambao mmeboresha hospitali ile basi tungekuwa pia na mashine za kisasa za kufulia ili shughuli zote zifanyike pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hospitali ile haijakabidhiwa kwa Wizara wakati ilipokuwa chini ya Halmashauri tulianza kujenga jengo la emergency kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa lakini pia na Ubalozi wa China. Sasa wakati tunakabidhi ujenzi ule ulikuwa bado haujakamilika na mpaka leo umesimama. Si vizuri kwa wadau wa maendeleo ambao wametuchangia halafu waone lile zoezi haliendelei. Tunaomba katika hiyo shilingi bilioni 10 ambayo Mheshimiwa Waziri umesema unayo basi tuelekeze hiyo shilingi milioni 100 iende pale ikamalize lile jengo la emergency.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto ya generator upande huu wa utawala. Hii imekuwa ni tatizo sana kwamba umeme unapokatika madaktari wanakosa standby generator ya kuwasaidia kwa sababu ile generator kila siku imeharibika. TEMESA wanaambiwa kwamba ile generator imekufa watoe kibali ili hospitali ikanunue generator lakini hawataki kila siku wanataka wawe wanalitengeneza baada ya siku mbili limekufa. Naomba mtusaidie waambieni hao TEMESA watoe hicho kibali hospitali ikanunue generator nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwashukuru kwa hayo mazuri mnayoyafanya, nina kero moja nataka niifikishe na hii ni kero kubwa kwa wananchi siyo tu wa Temeke lakini yawezekana ni Watanzania nzima na hili ni tatizo la kuzuia maiti eti kisa kuna deni hospitali. Kumekuwa na utaratibu huo hasa katika Hospitali ya Muhimbili na Mloganzila kwamba marehemu anapofariki kama anadaiwa iwe Sh.20,000, Sh.100,000 au kiasi chochote maiti inazuiwa isitoke hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si la kibinadamu, linaondoa utu ambapo kama Watanzania tulizoea kuheshimu maiti. Hata barabarani maiti ikiwa inapita, unasimama unaacha maiti ipite. Huu ujasiri wa mtu kuzuia maiti unatoka wapi? Kwa nini maiti izuiliwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye mazingira ya kawaida kabla hatujaenda kuzika huwa tunatangaza jamani anayemdai marehemu ajitokeze, tunamkabidhi kwa ndugu wa marehemu wataendelea na shughuli za kudaiana baadaye lakini sisi tunaenda kuzika. Wengine kuzika ni ibada na sisi Waislamu tunasisitizwa mtu akishafariki awahishwe akazikwe lakini leo tunashindwa hata kuitekeleza hii ibada yetu kwa sababu badala ya kuchukua maiti mkazike mnaanza kupita na daftari la kukusanya michango.

T A A R I F A

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nafikiri Mheshimiwa Mbunge anachanganya, nimesema hapo awali kwamba ni utaratibu kabla hatujaenda kuzika tunatangaza wanaomdai marehemu wajitokeze, wanaodaiwa na marehemu wajitokeze, kisha tunawakabidhi kwa familia waendelee na taratibu za kulipana lakini hatuzuii kwenda kuzika. Sasa sijui yeye anazungumzia Uisalamu katika kitabu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kwamba, kwanza wakati mwingine unakuta maiti inayozuiliwa kwenye hospitali hiyo kwa sababu anadaiwa Sh.120,000 tayari labda ameshaugua hapo miezi miwili na bili nyingine ameshalipa yaani unakuta mgonjwa ameshalipa zaidi ya shilingi milioni 2 siku anakufa kwa sababu tu kuna siku mbili za mwisho bili yake haikulipwa eti tunazuia maiti, hii siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuweka fedha nyingi kwenye huduma za afya na kutatua kero za wananchi haiendani na jambo hili linalofanyika la kuzuia maiti hospitalini. Dhamira ya kuwekeza katika hospitali si kufanya biashara ni kuboresha huduma lakini hata ingekuwa biashara mabenki haya yanakopesha hayadai maiti, mtu akifa deni lile limekufa inakuwaje hapa hospitalini? Tulitegemea sasa hivi tuwe tunakwenda mbele zaidi kwamba mgonjwa ambaye ameugua miezi miwili, mitatu hospitali na alikuwa analipa bili akifa hospitali hata itoe incentives ya kusafirisha ile maiti kwa sababu alikuwa wa kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaonekana anaguswa na maisha ya wananchi lakini anaguswa pia na misiba inayotokea, ndiyo maana hata kwenye hotuba ameanza kwa kuwapa pole watu ambao wamepoteza ndugu zao. Sasa kauli hii haiwezi kuleta tija endapo bado maiti za watu zinazuiliwa hospitalini. Siyo kila jambo tumwachie mpaka Mheshimiwa Rais ndiyo siku asimame atoe maamuzi, hili mbona liko ndani ya mikono yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anachapa kazi sana, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndungulile namfahamu ni mtu ambaye amenyooka sana, anapenda kuhakikisha kwamba kero za wananchi zinaondoka, kwa nini hili hatuliangalii na linabaki kuwa kero Mloganzila na Muhimbili peke yake? Kwa nini hatulalamikii Temeke, Ilala au Mwananyamala kwani huko watu hawafi, kote huko watu wanafariki kila siku lakini haya hayatokei, mtuondolee na hili katika hizo hospitali mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuamini kwamba hizi maiti zinazozuiliwa eti zikiachiwa ndio Mloganzila na Muhimbili zitapata hasara sana zitashindwa kutoa huduma sio kweli. Lakini kama tatizo ni fedha leo tuna makapuni haya ya bima za afya yanapata fedha kutokea kwa wagonjwa wanaopelekwa hospitalini. Na ni mara chache utasikia haya makampuni ya bima za afya yanafanya hiyo cooperate social responsibilities maana yake hata ile asilimia moja ya faida ambayo wanatakiwa kutoa kwa jamii hawatoi. Kwa nini msiweke utaratibu basi wailekeze huko iwe ina fidia hawa watu ambao hawana watu… (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa hiyo naipokea lakini nizidi kutoa angalizo kwamba, Serikali yetu imejikita katika kuondoa kero kwa wananchi hasa wananchi maskini na wanaoshindwa kutoa maiti zao kwa kuzuiliwa huko hospitalini wala sio matajiri ni wananchi maskini twende tukawasaidie tuondoe hii kero nakushuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona, na nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini hata hivyo na mimi nisijifanye kuwa mpofu wa kutoona kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, pamoja na timu nzima ya Wizara hii ya kuhakikisha wanaitoa Tanzania gizani na kuiweka kwenye mwanga safi wa umeme, tena umeme ulio nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara na Serikali kwa ujumla, changamoto huwa haziishi, na kwa dakika hizi chache nilipenda niwasilishe changamoto ya kukatika katika kwa umeme katika Jiji la Dar Es Salaam.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kero kubwa hata baada ya ile ya migao ya kawaida kumalizika, migao ile ya umeme tuliyoizoea miaka ya nyuma, bado Dar Es Salaam kumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme. Ni ngumu sana ukae siku nne mfululizo bila kusikia umeme umekatika. Niliwahi kuuliza maswali hapa mara kadhaa, Mheshimiwa Waziri mwanzo alisema kwamba kwa kesi ya Temeke wanajenga substation nyingine Mbagala na Kurasini ambazo zitaondoa tatizo hili. Hata hivyo, Substation ya Mbagala ilimalizika na ndani ya mwezi mmoja tu ikawa tayari imeshazidiwa. Sasa hivi ukiuliza wanasema kwamba tunasubiri Substation ya Kurasini ambayo ilikuwa imelenga kusaidia watu wa Kurasini na watu wa Kigamboni; sasa maana yake ni kwamba bado hatujapata dawa ya kulitatua tatizo hili, na Dar Es Salaam ndilo soko kubwa la umeme ambao TANESCO wanaouza.

Mheshimiwa Spika, utagundua kwamba sasa hivi kuna megawatt 600 kati ya megawatt 1,600 zipo Dar Es Salaam. Sasa kama watumiaji wenyewe bado wanaendelea ku-experience kukatikakatika kwa umeme maana yake kuna tatizo la msingi ambalo ni lazima Wizara ije na mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba inakwenda kulitibu. Ukipiga simu kwenye vituo hivyo vya TANESCO wanakwambia kwamba eneo hilo umeme unakatikakatika kwa sababu Transformer imezidiwa, huko kwa sababu kuna nguzo imedondoka; tafsiri yake ni nini? Ama hatujui tuna idadi gani ya wateja wanaohitaji umeme Dar es Salaam na je, ongezeko la wateja katika Jiji la Dar es Salaam ni wangapi kwa mwaka? Ili tunapoweka Transformer iweze angalau kuhimili ongezeko hilo la wateja angalau kwa miaka miwili mitatu; sasa badala yake kila kitu kimezidiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini uchakavu wa hizo nguzo na miundombinu yote ya umeme katika Jiji la Dar Es Salaam ni tatizo. Kwa hiyo ni vizuri Wizara wakati inafanya kazi nzuri ya kuongeza umeme na kusambaza katika mikoa mingine pia iwe na mpango wa kuhakikisha kwamba itanarabati miundombinu ya kusambazia umeme kwenda kwa wateja katika Jiji la Dar Es Salaam, ili wateja wa Dar Es Salaam waiingizie fedha nyingi TANESCO; kwa sababu kwa uwekezaji huu mkubwa ambao Wizara na Serikali unaifanya ni lazima TANESCO ifanye kazi kibiashara, kuuza umeme kibiashara, ili ipate faida kwa sababu hatimaye mtakuwa na jukumu la kuilea hiyo miundombinu yote ambayo leo inajengwa.

Mheshimiwa Spika, sasa msipofanya kazi kibiashara na mkatengeneza faida, mkaliachia soko lenu liwe linapoteza mapato maana yake na ninyi pia mnapoteza; kwa sababu umeme unapokatika Dar Es Salaam, kwenye eneo lolote hata kwa nusu saa tu maana yake na TANESCO mnapoteza kwa sababu umeme utakuwa hautembei. Kwa hiyo zile gharama zitakuwa haziongezeki, Kwa hiyo ni vizuri mkaliangalia hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ningependa mpango madhubuti kabisa wa kuhakikisha tunakwenda kulitatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme Dar Es Salaam. Tunapokuwa na umeme wa ziada kwamba tuna umeme mwingi tuliozalisha kuliko tunaoutumia, lakini kama bado umeme huku unakatika katika wananchi hawawezi kuona hicho tunachokizungumza; kwa sababu kama kweli tuna umeme wa kutosha kwa nini basi unakatika katika?

Kwa hiyo hizi sababu ndogo ndogo, za miundombinu za Transformer, tuhakikishe tunazimaliza ili watu waendelee kuutumia umeme, tena umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru wa kunipa nafasi lakini nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu Allah Subhanahu Wataala kwa kutujalia afya njema na kuweza tena kupata fursa ya kuchangia katika bajeti ya mwisho kabisa katika kupindi hiki cha kwanza cha kukitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja na nina tambua kazi nzuri zinazofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu akishirikiana vizuri na Mawaziri wake Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Angela, Wasaidizi wake Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa mmefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na haya mimi leo nina jambo moja tu, na jambo hili ninalielekeza kwa msajiri wa vyama vya siasa. Mheshimiwa Spika mwaka jana tuliboresha sheria ya vyama vya siasa na kuumpa nguvu sana msajiri wa vyama vya siasa ili awe meno katika kuvisimamia vyama vya siasa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nijue ni lini msajiri wa vyama vya siasa atakuwa amejiridhisha kwamba matukio ya fujo siasa za chuki kuamsha mihemuko ya hasira kwa wananchi zinazofanywa na Chama cha Demokrasia na Mandeleo CHADEMA kuwa ni sababu za tosha ya kukifuta chama hiki.

WABUNGE FULANI: Aaah tulia wewe!

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, chama hiki kimesababisha fujo nyingi na moja kati ya fujo iliyofanyika tarehe 16 Februari, 2018 iliyopelekea kifo mdogo cha Akwilina Akwiline Bafutah. Hapa nina hukumu ya Kesi ya Jinai Namba 112 kesi ya mwaka 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, kwa faida ya Bunge lako naomba kunukuu Shauri Na. 4 katika kesi hiyo, kesi hiyo ilikuwa na mashauri 13. Na. 4 inasema hivi:-

“Particularly of the force account are that on 16th February, 2019 along Kawawa Road at Kinondoni Mkwajuni area within Kinondoni district in Dar es Salaam Region jointly and together with more than twelve other persons not in quote having riotously assembled in disobedor of proclamation to dispense made SP Gerald Thomas Nginja failed to dispence...”

SPIKA: Labda jambo moja Mheshimiwa shauri hilo limekatiwa rufaa au halijakatiwa rufaa?

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, halijakatiwa rufaa.

SPIKA: Nawauliza upande huu.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, notes ya rufaa imeshatolewa na rufaa imeshakatwa kwa hiyo namshangaa anavyohaika tena…

SPIKA: Basi liruke tu…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, endelea tu halafu utafisiri kwa Kiswahili baada ya hicho kingereza.

SPIKA: Kwa ajili ya taarifa hii ambayo tumeipata. Endelea ana hoja yako.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, naendelea na hoja yangu kwa maana niache kunukuu kwa sababu wametoa notes ya rufaa na rufaa haijashikiliwa na kwa sasa hukumu halali ya public ni public document inaweza kutumika mpaka mahakama nyingine itakavyosema vinginevyo ndio maana nimeichukua hapa kuinukuu.

WABUNGE FULANI: Endelea endelea!

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, katika shauri hili Na. 4 fujo zao za kukataa amri halali ya polisi zikasabisha kifo cha huyu binti Akwilina Akwilini Bafutaa. Lakini kibaya zaidi chama hiki hakionyeshi kujutia tukio hili, hukumu hii ilivyotoka chama hiki tulitegemea kama viongozi wa wananchi wangetoka kwenda kuiomba samahani na kuipa pole familia ya huyu binti marehemu. Lakini wao wakaanza kufanya vikao na waandishi wa habari vya kisiasa vya kujijenga kisiasa wakafanya vikao asubuhi mchana na jioni wakawa wanawaita waandishi wa habari wakilia kwa furaha ya shauri hili kuisha. wakati hawa wanalia kwa furaha mama wa marehemu Akwilina analia kwa uchungu. Wakati hawa wanafuata machozi ya furaha mama yake marehemu Akwilina hana mtu wa kumfuta chozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama sio sisi wakumesemea mama Akwilina ambaye amempoteza mtoto kwa fujo za CHADEMA ni nani mwingine anaweza kumsemea? Kwa hiyo, majigambo waliyokuwa wakifanya mbwembwe za kuchangishana fedha walizokuwa wazikifanya hazikuwa zinafanywa dhidi ya CCM, hazikuwa zinafanya dhidi ya Serikali zilikuwa zinafanya dhidi ya mama yake Akwilina aliyepoteza mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya kama msajiri wa vyama vya siasa anaendelea tu kuyaangalia tunakwenda wapi? Na mimi nikukumbushe hizi hatua za kuachana na ubinadamu wanapiga kila siku, walianza kila ikitokea msiba labda wa CHADEMA aaah! Labda au wa Mbunge wa chadema au mwana CHADEMA mwenzao wakawa wanageuza misiba hiyo sio kuwa sehemu ya mbaombolezo bali kuwa jukwaa la kisiasa.

Mheshimiwa Spika, nikukumbushe wakati wa msiba wa marehemu Kasuku Bilago, wewe na ofisi yako mlikuwa mkishirikiana vizuri na familia ya marehemu Bilago. Ukafunga safari hapa mpaka Kankongo kwenda kuzika kwa tarehe ambayo umepanga. Kufika kule CHADEMA wakaairisha ule msiba usizikwe siku ile ili wewe usizike wao waweze kufanya siasa siku inayofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiendelea kuyavumilia haya tunatengeneza siasaya aina gani? Ifike mahala msajiri awe mkali asilichoshe jeshi la polisi kufanya vitu ambavyo na yeye pia ana nafasi ya kuweza kuvifanya. Maadili ya vyama vya siasa yanasimamiwa na msajili iwa vyama vya siasa yanasimimiwa na msajiri wa vyama vya siasa. Hapa katika haya mauaji ya marehemu Akwilina wenyewe walipanga wafe watu 200, ukisoma shauri Na. 10 ambalo ameshtakiwa Mheshimiwa Mbowe peke yake katika kesi hiyo hiyo, muendesha mashtaka ana mnukuu wakati anawaanda sasa ili watoke wakati wanaingia mtaani kwamba wafe angalau watu 200.

Mheshimiwa Spika, ule ulikuwa ni uchanguzi mdogo wa jimbo moja Kinondoni akafa mtu mmoja katika target yao ya watu 200. Tunaelekea uchaguzi mkuu kila kata kutakuwa na uchaguzi kila jimbo litkauwa na uchanguzi nchi nzima itakuwa na uchanguzi hivi unajua wamepanga kuua watu wangapi? Lakini wewe mwenyewe ni shaihidi baadhi ya Wabunge hapa mara kadhaa wanasimama wanasema mimi nisingetangwa kama watu wawili wasingekufa mimi singetangazwa kama watu watatu wasingekatwa miguu. Haya yote ni mwendelezo wanayoyapanga wenzetu, sisi tunapanga kwenda kushinda majimbo wao wanapanga kwenda kuua watu msajili wa vyama vya siasa yupo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya mambo ni lazima kama Bunge tuamue, tuamue kwamba tunalaani siasa hizi zinazofanywa na CHADEMA. Hata kama msajili atachelewa, lakini sisi kama Bunge part yetu tuifanye. Nilikuwa hata ninapata hisia kwamba mwishoni wa mchango huu nitoe hoja angalau tukatoe pole kwa familia ya Akwilina kwa kilichotokea tukamfute chozi huyu mama haiwezekani anaonewa mtu mmoja anashambuliwa na taasisi fulani tena ya viongozi wengine ni Wabunge halafu tukaa kimya tu ni lazima huyu mtu afutwe chozi. Na wakumfuta chozi sio hawa waliosababisha mauaji ya mwanae ni sisi tunayeyaona haya kwa mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiyaacha haya mambo na msajili akaendelea hivi hivitutaipeleka hii nchi kubaya. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii, bado napenda kuikumbusha Serikali kupitia Wizara hii kumaliza kulipa fidia Kurasini. Tathmini imefanywa muda mrefu lakini hadi leo wananchi wale hawajalipwa fidia hiyo pamoja na mapunjo yao. Fidia inapokaa muda mrefu huleta matatizo kwa raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri awahimize NHC kuharakisha makubaliano yetu ya kujenga jengo la biashara ya fenicha pale Keko.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kuhusu suala la makokora. Zoezi la uchomaji moto nyavu za asili zenye macho madogo madogo linaathiri uchumi wa wavuvi wa dagaa ambao hawana uwezo wa kununua nyavu maalum za macho madogo za kuvulia dagaa. Serikali iwatambue wavuvi wa dagaa na iwasaidie kuwapatia nyavu hizo ili waepuke kutumia makokora badala ya kutumia mabavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niongelee suala la kuzuia usafirishaji wa viumbe hai. Sasa ni zaidi ya miaka miwili toka Serikali izuie usafirishaji wa viumbe hai kama mijusi, panzi na kadhalika. Zoezi hili linawaumiza wajasiriamali wa shughuli hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa pili wa Hotuba ya Waziri Mkuu ameonesha kero za Muungano na jitihada za kuzitatua. Naomba kuishauri Serikali isishughulikie kero za Zanzibar peke yake, ni vema kukawa na utaratibu wa kuziangalia kero za Tanganyika na iache kuipendelea Zanzibar. Kwa mfano, katika sherehe za Mapinduzi, Dokta Shein hupigiwa mizinga ishirini na moja wakati yeye sio Amiri Jeshi wa Tanzania. Jambo hili linatukera Watanganyika na linamshusha hadhi Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jambo hili halihitaji mabadiliko ya Katiba, basi Serikali iache kumshauri Rais kuhudhuria sherehe hizo kama tunataka Dkt. Shein ndiye awe mgeni rasmi ili itifaki iweze kuzingatiwa na kama Rais wa Jamhuri atahudhuria, basi yeye ndiye awe mgeni rasmi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuikumbusha Wizara hii kutenga pesa kwa ajili ya kumalizia barabara za ring roads ambazo ujenzi wake haujakamilika. Barabara ya Davis Corner – Jet Lumo inayounganisha Temeke na Jimbo la Segerea (Ilala), barabara hii haijatengewa pesa kwa mwaka wa tatu sasa. Hili sio jambo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara itenge fedha za kuimalizia barabara hii ili lengo la kupunguza kero ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam itimie. Tafadhali naomba pesa kwa ajili ya barabara hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo mpya imeibuka mpakani Tunduma inaitwa tozo ya uzito wa mizigo inayotokea Zambia ambapo lori moja hulipishwa hadi shilingi 400,000. Hii ni kero mpya na inachangia kuongeza gharama za uzalishaji kwa viwanda vya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hili la Kurasini Logistic Centre. Natambua jitihada binafsi za Mheshimiwa Waziri lakini sina budi kuliingiza katika rekodi ili nguvu iongezeke katika kulishughulikia suala hili hasa ukizingatia pesa nyingi ya Serikali iliyoingia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho ni unyanyasaji wa TRA dhidi ya wafanyabiashara kwa kuwakadiria kodi kubwa kuliko hata mitaji yao kimakosa na wanapotakiwa kuhakiki inachukua muda mrefu sana na kuathiri uzalishaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, katika Soko la Samaki la Kimataifa la Dar es Salaam zaidi ya asilimia 75 ya samaki wanaouzwa pale ni samaki kutoka nje ya nchi. Jambo hili ni baya na linahitaji kuangaliwa upya ili tuweze kuwalinda wavuvi wa ndani. Kibaya zaidi wamiliki wa viwanda vya samaki ndio waagizaji wakubwa wa samaki kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, zoezi la ukamataji nyavu za kienyeji maarufu kama makokoro linawaonea wavuvi wa samaki wadogo yaani dagaa kwa kuwa dagaa hawawezi kuvuliwa na nyavu nyingine tofauti na nyavu za macho madogo. Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia wavuvi wa dagaa nyavu maalum za kuvulia dagaa, maana bei yake ni kubwa na wavuvi wetu hawawezi kumudu.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wakandarasi waliotoa huduma Serikalini limekuwa tatizo kubwa. Wizara imekuwa ikirudia uhakiki hata katika fedha au madai yaliyohakikiwa. Kwa mfano mkandarasi Tanzania Printing Services (TPS) waliotoa huduma ya printing Ofisi ya Waziri Mkuu hadi leo ni zaidi ya miaka miwili kampuni hii haijalipwa kiasi cha shilingi 740,000,000 zilizohakikiwa kati ya shilingi bilioni mbili anazodai.

Mheshimiwa Spika, binafsi nimeongozana na mfanyabiashara huyu Wizarani bila mafanikio, kila mtu anasema file bado lipo internal auditors. Hivi ni lini usumbufu wa kulipa wakandarasi utakoma?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni usumbufu kwa wafanyabiashara. Leo pale mpakani mwa Tanzania na Zambia imeanzishwa tozo mpya inayoitwa weight and measure ambapo lori moja hutozwa kati ya shilingi 640,000 kwa kupita tu pale.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linaongeza gharama za uzalishaji na hivyo kuzifanya bidhaa za Kitanzania kuwa ghali na kushindwa kuhimili ushindani wa soko.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kwa uchache sana niweze kuchangia kidogo kuongezea kwenye yale ambayo jana niliwasilisha kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna watu walikuwa wanasema hapa wanaomba tuaminiane, mimi niwaambie tu suala la kuaminiana siyo suala la kusimama na kusema, tunaaminiana kwa vitendo, ukifanya vitendo unaijenga imani automatically na ukiona kuna tatizo la imani kati ya Serikali na wananchi, maana yake tatizo lipo upande wa Serikali kwa sababu Serikali ndiye mtendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunajadili Muswada huu tunahitaji kujua, kweli huu muswada umeletwa hapa kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa au kwa ajili ya maslahi mapana ya Mtawala, na kabla hatujafika huko kwanza tuangalie Muswada huu wa Sheria ya Kupata Taarifa, lazima tuanze kuangalia mambo machache ambayo yameizunguka tasnia hii ya habari kabla hatupitisha muswada huu, ili tunachokipitisha hapa kisijekuwa ni mwendelezo wa kuwakandamiza zaidi watu wanaohusiana na vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hapa, vyombo vya habari vikifungwa, magazeti yakifungiwa na kosa linaweza kuwa pengine ni la mtu mmoja au mhariri au mwandishi hakufanya kazi yake vizuri, lakini linafungiwa gazeti lote. Katika kipindi hiki ambapo nchi ina tatizo kubwa la ajira, unalifungia gazeti, kuna mtu kazi yake ilikuwa ni kufagia tu ile ofisi inayotolewa lile gazeti anahusika vipi kwenye machungu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekitii, kwa hiyo tunahitaji kufikiria zaidi wakati tunazitunga hizi sheria ili zisiende kuwatesa watu ambao hawakustahili kuteswa, unaangalia hapa kwa mfano hii sheria imekuja imetoa adhabu kali kweli, moja ya adhabu ambayo inayotolewa hapa ni kifungo cha miaka 15 mpaka miaka 20, hiki kifungo ni kikubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba nchi yetu yenyewe inakabiliwa na tatizo la mlundikano wa wafungwa magerezani na hao wafungwa wamejazana huko kwa sababu kila sheria tunayoitunga haiweki adhabu mbadala inakimbilia tu kuwaapeleka watu gerezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nategemea hii sheria kwa kuwa inawahusu wengi ni wataalamu ambao watakuwa ni watumishi, wataalamu wa habari, ndiyo wanaoguswa na sheria hii tuwape adhabu mbadala, adhabu iwe ni mtu kumfungia kufanya ile shughuli japo kwa mwaka mmoja, miaka miwili siyo kumpeleka gerezani, tumsaidie Waziri wa Mambo ya Ndani kupunguza wafungwa magerezani. Unamfunga mtu miaka 15 kisa tu alikosea kutoa taarifa kwa nini usimfukuzishe tu kazi, kwa nini asikae nje tu ya hiyo ajira yake kwa miaka miwili au mwaka mmoja, ni adhabu ya kutosha sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri uangalie hii adhabu ulizoziweka hapa wala haziwezi kuwa applicable, zitawatesa watu, tuwape watu adhabu zinazolingana na taaluma zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata taabu tena kwenye hizi siku 30 za kusubiria hizi taarifa. Mwanzo unapousoma Muswada huu unaona pengine huu Muswada una lengo zuri labda una lengo la ku-compel government iweze kutoa taarifa lakini sasa unapoweka hii turn around ya siku 30 unaona ile nia njema ya Serikali inaondoka! katika karne hii ya sayansi na teknolojia unawezaje kusubiri taarifa kwa siku 30?
Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu tu kufikiria kwa sauti kwamba labda Askari Polisi Mpelelezi anahitaji kupata taarifa za kitabibu za binti aliyebakwa, kama daktari kwa maksudi ataamua kumzungusha kwa kutumia loophole zilizopo katika sheria hii hizo taarifa zinaweza zikatoka wakati huyu binti emeshajifungua, kama siku hiyo alipata ujauzito. (Makofi)
Sasa tukiiangalia hi kwa maana tu ya kuya-target magazeti, tukumbuke kwamba kuna vitu vingine vingi vya kijamii tunavisahau na watu watakuja kuumia.
Kwa hiyo naomba turn around time ya kupata hizi taarifa iwe ni ndani ya saa 24 kama taarifa imeombwa kwa njia ya kielektroniki, lakini kama imeombwa kwa njia ya barua ya maandishi ndiyo iweze kuchukua siku saba kwa sababu ndio utaratibu wa kawaida kwenye ofisi zenu barua zinajibiwa ndani ya siku saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taarifa tunapoziomba tunaziomba kwa sababu zipo na mnazo, hatuombi hizi taarifa ili muende mkazitafute halafu ndiyo mzilete. Lakini kwenye sheria mnasema hizo siku 30 ni za mtoa taarifa kujibu kwamba hiyo taarifa ipo au hiyo taarifa haipo au hiyo taarifa anaweza kuitoa yote au kuitoa sehemu, hivi majibu haya yanahitaji siku 30.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana ukija utuwekee wepesi katika kuzipata hizi taarifa, tuzipate hizi taarifa tukiomba kwa njia ya kielektroniki zije ndani ya masaa 24 na kama kwa maandishi basi zije siyo chini ya siku Saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na mimi kuweza kushiriki shughuli za Bunge toka mwanzo mpaka hii leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuipongeza kwa dhati Kambi ya Upinzani kwa namna ambavyo haikati tamaa kuishauri Serikali na kuendelea kuipa mambo mazuri ambayo kama Serikali itayachukua kwa ukamilifu wake nchi hii itapiga hatua kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge hili linapitisha Azimio la Kumpongeza Rais John Pombe Magufuli niliwatahadharisha sana Serikali na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwamba matumizi mabaya ya wingi wao hapa Bungeni kushabikia au kuzomea mambo mazuri ambayo Kambi ya Upinzani wamekuwa wakishauri kwa sababu tu yanaanzia huku Upinzani haulitendei haki Taifa hili na italeta madhara makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru jana Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha kwenye hoja ya jana alim-quote Mwalimu Nyerere akisema kwamba; Taifa linapokuwa linaibiwa tunaibiwa sote, haibiwi CCM, hawaibiwi Upinzani. Taifa linapokuwa linafanya vizuri tunanufaika sote. Tukiyazingatia maneno yale na tukayafanyia kazi tutakuja kugundua kwamba sisi ni watu wamoja, tunafanya kazi moja kwa ajili ya kulijenga Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu mjadala huu leo unachukuliwa kama wazo jipya la nchi hii kutaka kuzitetea rasilimali zake lakini kimsingi kelele hizi zimeaanza kupigwa hasa na Upinzani huku muda mrefu. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwepo kabla yetu kwa maana walifanya kazi kubwa sana. Hata mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ni kwa sababu ya kelele nyingi zilizopingwa na Kambi ya Upinzani kwa maslahi ya Taifa hili. Hazikuishia hapo, tuliendelea kupiga kelele mpaka hivi tunavyokwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikitika sana jana Mbunge mmoja hapa anasema kwamba kwenye nchi hii hakujawahi kuwa na sheria ya kutaka ku-review mikataba, si kweli! Sheria hii ya Madini ya mwaka 2010, Kifungu cha 12 kinatoa mwanya huo kwamba Serikali kila baada ya miaka mitano inaweza kukaa na wawekezaji kujadili kuhusu mikataba hiyo. Serikali hii ituambie ndani ya miaka mitano, kumi iliyopita imeitekeleza sheria hiyo kwa ukubwa upi? Kwa hiyo, yawezekana wakati mwingine tunasimama na kutaka kutunga sheria mpya kumbe tatizo siyo uwepo sheria, tatizo ni namna ambavyo Serikali inazisimamia sheria hizi. Kwa hiyo, tunaweza tukaendelea kutunga sheria hapa kila siku, lakini kama hatutaungana Bunge kama kitu kimoja kuisimamia Serikali iweze kuzitekeza sheria hizo bado tutakuwa hatuna tunacholisaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hapa nilitegemea tuungane kama Bunge, tunasema maslahi mapana ya Taifa hili tunapozungumzia rasilimali za Taifa hili, tunapozungumzia madini ya nchi hii haliwezi kuwa suala la kuletwa Bungeni kwa Hati ya Dharura. Tunahitaji kulipa Taifa hili muda wa kutosha kujadili, haraka haraka haijawi kuwa na baraka hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mimi nilikuwa nacheka, nina kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Doto Biteko aliisoma jana hapa, yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa ile Kamati Maalum aliyoiunda Mheshimiwa Spika na hiki ni kitabu kimesomwa na Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria. Wenyeviti hawa wakati wa kusikiliza wadau tarehe 1 Julai, 2017, walikaa meza moja kusikiliza wadau, hawakukaa maeneo tofafuti. Hata hivyo, Mheshimiwa Doto Biteko anasema wadau waliotoa maoni mbele yake, ameandika humu ni wadau 26 na wadau 10 waliandika. Mheshimiwa Mchengerwa anasema wadau 12 ndio walitoa maoni mbele yake, mnayo huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya humu. Wenyeviti hawa walikaa meza moja na huwezi kuniambia eti kwenye eneo lake watu wanaopika …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtolea kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawasawa za Bunge,.....

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri hata kwenye maelezo yako unatumia neno huenda mimi nasoma vitabu hivi vimeletwa hapa…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtolea,....

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi haya niyaache niende mbele, lakini ndiyo tatizo ninalotaka kulizungumzia linatokana na hayo hatutaki kujifunza kukubali ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na sasa acha nijikite katika kutafuta sifa tu niachane na haya mambo ya kukosoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri toka jana naona unarekebisha kauli ambayo imesemwa na Jamii Forum kwamba si kweli sheria tunayoitunga haitashughulikia mikataba ya nyuma. Kama Jamii Forum wamesoma kifungu kinachopendekezwa, kifungu cha 11 Jamii Forum watakuwa wako sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisome Kifungu hiki cha 11 kinasema:

“Notwithstanding the provisions of this Act and any other Written laws, all development agreements concluded prio to the coming into force of the section shall, subject to the provisions of the Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017 remain in force”, unless hili neno la mwisho la remain in force limeondolewa. Kama Mheshimiwa Waziri atakuwa ameleta Jedwali la kuondoa neno hili, ndicho anachokisema kama kilivyosemwa kwenye Kifungu cha Pili cha hii Unconscionable Terms ndiyo kitakuwa kiko sahihi. Kwa sababu kule kwenye section two ndiyo inamalizia kwa kusema kwamba sheria hizi zitatumika after and before, kwa ku-quote hapa na kuongezea hii remaining in force kinabadilisha hayo ambayo wewe umeyakusudia.

Mheshimiwa Waziri utakuja kujibu kwenye majibu yako lakini hata hivyo ninakusaidia nita-move Schedule of Amendment. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilinde pia, Mheshimiwa Waziri atakuwa na nafasi yake, atakuja kuyajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, muundo wenyewe wa hapa ndani kuongea unatazama huku, kwa hiyo kuna wakati unamtazama Waziri na kuna wakati nakutazama wewe, ni jambo ambalo haliepukiki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pia, nimesema hapa kwamba ile Sheria ya Madini ya mwaka 2010, kipengele

cha 12 kilikuwa kimejitosheleza zaidi kuliko Kifungu cha 100E sub section (2), (3) na mapendekezo yake, inazungumzia stabilization of agreement ni kweli. Ukisema kwamba review iwe time to time, inaweza kuwa baada ya miaka 10 baada ya miaka 20 ikawa time to time, kule kwenye 12 kwenye sheria ya mwanzo kilikuwa kimesema vizuri miaka mitano na huwezi kwa nature ya mikataba hii ya kimadini huwezi ukafanya review ndani ya muda mfupi zaidi ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, investment yenyewe tu wakati mwingine inachukua zaidi ya hiyo miaka mitano, ni vizuri tukajikita pale pale kwenye miaka mitano badala ya kwenda kuibadilisha tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la kuwa na hiyo asilimia 16 mpaka asilimia 50 ni jambo zuri sana kwamba Serikali ianze kupata hizo share. Hapa ukisoma ongezeko hili au pendekezo hili ni kama vile tunavyozungumzia madini tunazungumzia dhahabu pekee yake, wakati si kweli! Kuna madini mengi na madini mengine ni ya kipekee sana huwezi kuanza na asilimia 16 na hata sasa hivi yapo maeneo ambayo Serikali ina hisa nyingi zaidi ya hizi ambazo zimependekezwa hapa. Kwa hiyo, ningependa Mheshimiwa Waziri kwa maslahi mapana ya nchi hii ayafanyie marekebisho maeneo haya ili tuweze kwenda sawa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema naiheshimu sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu nilishirikiana nayo vizuri. Hata wakati nikiwa na kesi ya uchaguzi ofisi hii ilionesha uwezo mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunashinda kesi na tukashinda kesi. Lakini nimesikitishwa sana kuona wanaleta muswada mwepese kiasi hiki. Muswada huu umekuwa mwepesi mno, sheria ambazo zinafanyiwa marekebisho hapa zina changamoto nyingi kuliko ambazo Mwanasheria Mkuu ameamua kuja kuzifanyia marekebisho hapa.


Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani amedonyodonyoa vitu vichache ndivyo amevileta vifanyiwe marekebisho wakati ndani ya sheria hizo kuna vitu vingi vyenye changamoto nyingi kwa wananchi ambavyo kama angeamua kutumia uwezo wao ule ambao mimi ninautambua wakaingia ndani kwenye miswada hii, wangetuletea vitu vizito hapa na ungeona Bunge hili limejaa kwa sababu kila Mbunge angekuwa na hoja ya kutaka kuchangia kwa sababu vitu vilivyoletwa vingekuwa vinawagusa wananchi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wamejaribu kuchukua vitu vichache, sijui ni kwa sababu gani. Hata wakati naadika hotuba hii ya Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, tumepata shida sana kwa sababu vitu vingi ambavyo tulitegemea Serikali ivilete hapa hawajavileta, wameleta vitu vyepesi, kwa faida ya nani, hiyo hatuwezi kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tu; Serikali hii ya Awamu ya Tano imekuwa ikijinasibu sana kwamba ni Serikali inayobana matumizi, Serikali ambayo inaheshimu value for money, lakini kwa nini hawalitendei haki Bunge hili? Kikao hiki cha leo kujadili muswada huu, value for money haipo kwa sababu kikao ni kikubwa lakini kinajadili kitu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kila siku anapiga kelele kwamba anakerwa na utitiri wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, amelisema hili mara kadhaa. Na Serikali hii Mawaziri, Mwanasheria Mkuu ndio watu wa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha wanaharakisha mchakato wa kupunguza hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili iwe michache, ama uwe mmoja au miwili ili kile kilio chake na ile kero yake iweze kuondoka. Lakini ni kwa kiasi gani katika mabadiliko haya wamesaidia kuondoa hiyo kero ambayo Mheshimiwa Rais anaipigia kelele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninaamini toka Mheshimiwa Rais ameanza kukerwa na utitiri huu wa Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii, tayari SSRA wameshakwenda mbali kwa maana ya kufanya research na kuandaa maandalizi


mbalimbali ili hilo liweze kufanyiwa kazi. Lakini muswada unaletwa leo hapa mambo hayo hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku Waheshimiwa Wabunge hapa wanapiga kelele kuhusu fao la kujitoa. Wananchi wanalalamika, kwa nini wananyimwa fursa ya kujitoa kwenye Mifuko ya Jamii, wachukue fedha zao waende wakafanye shughuli nyingine. Serikali hii ndiyo inanadi kwamba inataka kuijenga Tanzania ya viwanda, Tanzania ya viwanda inahitaji mitaji, tunasema hapa kila siku. Mtu ambaye ameshafanya kazi miaka yake kumi anaona kwamba kilichopo kwenye mifuko ya jamii akilipwa kinamtosha kufanya mtaji, kinamtosha kutengeneza kiwanda chake, kwa nini unamzuia mpaka afikishe miaka 55, miaka 55 ni muda wa uzee, muda wa kula mafao, muda wa kumpizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka fedha sasa hivi ili tuweze kuwekeza, watu hao wakifika hiyo miaka 55 wawe tayari walishakuwa matajiri, au mnataka hiyo Tanzania ya viwanda wanufaike akina nani? Kama mnataka Watanzania ndio wanufaike, wapeni mafao yao. Mnazuia fao la kujitoa kwa sababu gani? Mnataka fedha ziendelee kubaki kwenye hiyo mifuko ya jamii kwa matumizi yapi? Au ndiyo hizo huwa mnazikopa wakati wa kampeni mnatushinda sisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna changamoto nyingi sana huko kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Mifuko yenyewe hiyo inafanya uwekezaji wa hasara katika maeneo chungu nzima, hayo yote yanatokana na mapungufu ya kisheria. Tulitaka Serikali sasa iende mbali iangalie kwamba kwa sababu hizi fedha ni za wananchi, mifuko hii inakwenda kufanya uwekezaji, inapata hasara, hiyo hasara ni ya nani, kwa nini hasara inapatikana, kwa inaendelea kuwekeza katika miradi ya hasara? Hayo yote ni mapungufu ya sheria, ndiyo tulitegemea hapa Mheshimiwa AG aje na muswada mzito uliojaa nyama za namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio tu kwenye hiyo Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini hata kwenye ile Sheria ya


Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi; kuna migogoro ya ardhi kwenye nchi hii kila kona lakini marekebisho yaliyoletwa hapa yenyewe ni machache sana. Hayatibu ile migogoro, hayaendi mbali kuhakikisha kwamba tunapata sheria ambayo itakwenda kutibu migogoro…

T A A R I F A . . .

Siipokei hiyo taarifa na kwa bahati mbaya sana anayetoa taarifa hii ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ambaye aliongoza vikao vya kukubali muswada huu mwepesi uweze kuja hapa Bungeni. Kwa hiyo, taarifa yake ni kutetea tu haya ambayo ninaya- challenge hapa. Sasa ni vizuri angemuandikia Mwanasheria Mkuu ili wakati wa kuja kujibu, ndio angeweza kuyatolea maelekezo haya ambayo anafikiri alisahau kuyaingiza kwenye hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia changamoto katika uwanda mzima wa masuala ambayo yanahusu ardhi, kwamba marekebisho haya yangekwenda mbali zaidi kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa upana wake, sio kwa kiwango hiki kidogo ambacho Mheshimiwa AG ameleta hapa. Unapofanya maboresho kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya unaacha kugusa Baraza la Ardhi la Kata, unakuwa hujalisaidia lile Baraza kwa sababu kesi za ardhi, migogoro ya ardhi, huwezi kwenda hatua nyingine yoyote – kwenye Baraza la Wilaya au Mahakamani kama hujaanza kwenye Baraza la Ardhi la Kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima unapofanya maboresho yoyote uanzie kule chini ambapo ndipo migogoro yenyewe inaporipotiwa. Kufanya marekebisho kwenye Baraza la Ardhi peke yake maana yake sasa utakwenda kurundika kesi nyingi zikakae pale Baraza la Ardhi la Wilaya halafu ziwe zinachelewa kufikiwa maamuzi, hii utakuwa bado hujawasaidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Waziri wa Ardhi mwenyewe akisema kwamba wapo watu, kwa kutumia fedha zao, wamejenga kwenye viwanja vya watu. Serikali yenyewe hii imekuwa sio sikivu kwa kuheshimu misingi ya sheria hizo hizo za ardhi, wamekwenda kubomoa pale Kimara nyumba za watu ambao wengine tayari wana stop order ya
Mahakama. Sasa kama Serikali yenyewe ni sehemu ya kutoheshimu amri za Mahakama au Mabaraza haya ya Ardhi, nani mwingine atakwenda kuheshimu? Sio kwamba tunailaumu Serikali, tunalaumu sheria ambazo zinaacha hizo nafasi za hayo mambo kuweza kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tazama ukubwa wa eneo ambalo linachukuliwa, watu wamebomolewa ili ijengwe barabara, unajiuliza ni barabara au viwanja vya mpira, robo kilometa. Watu wamevunjiwa eneo lile ni robo kilometa, inajengwa barabara ya aina gani. Ni kweli tunahitaji ile ardhi kwa ajili ya barabara au ni kwa ajili ya kukomoana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya yote yanaweza kutibiwa na kuwa na sheria nzuri inayomlinda mwananchi. Sio tuwe na sheria ambayo inahalalisha maovu ambayo yanaweza kufanywa na Serikali yaonekane kwamba ni halali, hapo hatuwagusi wananchi. Kwa hiyo mimi niseme kwamba tunahitaji marekebisho ambayo yatawagusa wananchi.

Mheshimiwa Menyekiti, sheria zina mapungufu makubwa, maeneo yameandikwa kabisa hapa pana mgogoro pasijengwe, lakini upande mmoja wa mlalamikiwa kwa sababu una fedha unakwenda unajenga, wananchi wanapata taabu, wananchi wanateseka. Bunge hili kwa kutumia mamlaka yetu ya kutunga sheria tuishauri Serikali ituletee sheria ambazo zitaigusa jamii ya Watanzania kwa kiasi kikubwa ili tupunguze migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru, lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu ya kusimama hapa na kukupa nguvu wewe ya kuniona na kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo katika Muswada ambao uko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli zilikuwa kelele zetu za muda mrefu sana kutaka marekebisho haya yaje ili tuweze kufanya maboresho katika hii mifuko ili Watanzania walio wengi wale ambao wapo katika ajira waweze kuona mwanga wa maisha yao ya kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulihitaji kweli kupunguza utitiri wa mifuko, lakini tulihitaji kuboresha maslahi yaliyomo kwenye mifuko iliyopo. Sasa tungeweza kuipongeza Serikali kwa kuleta muswada, lakini kuuleta muswada peke yake bila kuzingatia vile vilio vyenyewe vilivyokuwa vikipigiwa kelele na sisi Wabunge kwa niaba ya Watanzania, haisaidii sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuja kugundua kwamba kuna mafao mapya ambayo yanaanzishwa, lakini kuna mafao ya muhimu yaliyokuwepo yameondolewa. Sasa hili siyo jambo jema sana, kwa sababu lengo ilikuwa ni kupunguza malalamiko ya watu. Sasa huwezi kupunguza malalamiko ya watu kwa kuondoa vile vitu vizuri ambavyo vilikuwa vikiwagusa katika maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona hapa limeondolewa lile fao la afya (health benefit). Utagundua kwamba katika kipindi kilichopita ambapo fao la kujitoa lilikuwa limeondoka, wanufaika hawa walikuwa angalau wanaenda wanapata
ile huduma ya afya. Sasa hivi hilo fao limeondolewa, kinaletwa kitu kinachoitwa unemployment benefits ambayo na yenyewe inaelea juu juu, hujui mtu huyu mnufaika atapata kitu gani? Unaambiwa kwamba kujua ni namna gani itakokotolewa, Waziri atakuja kutunga regulations. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndio wenye kazi ya kutunga sheria na siyo vizuri tukatunga sheria ya kumruhusu Waziri aende akatunge sheria. Tunatakiwa tumalizie hapa, tuwekewe hiyo hesabu ya kukokotoa ili tujue mtu akiwa amepoteza ajira, wakati anatafuta ajira, anapata kiasi gani? Tunajijua wenyewe, ukiiacha tu hivi na kusema Waziri atatunga regulations, inaweza kuchukua miaka mitatu au minne hapa hiyo regulation haijatungwa. Tuna hiyo mifano. Sasa hapa hata ile kazi yetu ya Kibunge ya kutunga sheria yenyewe haikamiliki katika kuweka mafao ambayo yanaelea kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kifungu cha 31(2) kinatambua kwamba kuna Mtanzania kwa namna moja au nyingine atalazimika kuondoka hapa nchini, ama ataacha kazi au atapata kazi kwenye nchi nyingine na sheria inatambua kabisa kwamba mtu huyu anaweza akaenda akarudi au akaenda asirudi. Mnatuletea hiyo special lump sum benefit na yenyewe ni kiasi gani? Mtu kama anaondoka nchini, bado unataka akuachie hela yake, ufanye nayo nini? Kwa nini humpi hiyo hela yake akaondoka nayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaona muswada umekuja na mambo mengi ambayo hayajakamilika, yaani vitu viko nusu nusu. Miswada ya namna hii kwa kweli haitusaidii. Vilevile inatunyima fursa na sisi kama Wabunge kuitunga sheria ambayo tukimaliza tu, Mtanzania atakuwa anaguswa moja kwa moja. Sasa hata tukishaipitisha hii leo hapa, bado kazi kubwa anaachiwa Waziri. Kwa hiyo, sisi tunakuwa bado hatujafanya ile kazi yetu ya kimsingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ukienda kwa mfano pale kifungu cha 57(1) kinasema hivi, kwa ufupi tu nikisome. Anasema: “The board shall at interval of three year or at any other intervals...” sitaki kuendelea huko. Hivi ukisema “the body shall’, halafu unasema at interval of three year or any intervals;” sasa hapo “shall” ilikuwa na kazi gani? Kwa sababu unapoweka “shall” ni lazima ukasisistize lile jambo, lakini kumbe jambo lenyewe bado linaendelea kubaki ni discretion ya mtu ambaye atafanya hayo maamuzi. Kwa nini tunatumia “shall”? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekwenda mbali zaidi mkaongeza kifungu kingine cha 57(2), mnazidi kusisitiza hilo hilo kwamba kumbe hii actuarial valuation siyo jambo la msingi kwenu. Sasa kama siyo jambo la msingi, kwa nini mnalirudia, mnaliandika halafu mnalitoa? Mngechagua moja au kuliweka au kutoliweka kuliko kufanya namna hii. Maana yake hapa tutaonekana sasa kama tumekuja kupitisha mafao ya kijanja kijanja hivi, jambo ambalo siyo zuri kwa Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri, hiki kifungu, maana yake hata kwenye drafting tu ya mambo haya ya kisheria hapa inatudhalilisha. Kwa hiyo, mnaweza mkaenda kuifanyia marekebisho au mkaondoa kabisa hiyo sub-section two, kama hamtaki ku-edit hiyo sub-section one.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kusisitiza kwamba kitendo cha kutokuwa na kikokotoo katika Muswada huu kimeondoa ile maana nzima ya sisi kuja kutunga sheria na kuwasaidia hao wanufaika wa hii wa mifuko ili wajue ni kitu gani watakipata baada ya kuwa wamepoteza ajira kabla ya kutimiza hiyo miaka 50. Fao lao la kujitoa bado linahitajika sana na kelele za Watanzania katika hili hazitaisha. Nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2018
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi kuchangia walau kwa uchache katika muswada uliokuwa mbele yetu, lakini kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, lakini nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kumjaalia afya inayoimarika Mheshimiwa Tundu Lissu ambayo siku kama ya leo mwaka jana dakika chache tu kutoka sasa alinusurika kifo kutoka kwenye shambulio lililotokea hapa Mjini Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotanguliza kusema na mimi nina machache tu ya kuchangia katika hili na kubwa ni kuendelea kushangazwa kwangu na namna ambavyo tuna misuse nafasi ya kufanya mabadiliko ya sheria mbalimbali, kwamba miswada inayoletwa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya sheria ina donyoadonyoa tu vitu vidogo vidogo na kuacha vitu vingine, jambo ambalo linatupelekea baada ya muda mfupi tuone tena inaletwa tena sheria hizo hizo kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hii sheria inayofanyiwa mabadiliko ya TLS mbali ya hiki kitu kimoja labda kwa maslahi mapana ya Serikali ndio wamekuja kufanyia marekebisho wameacha vitu vingi ambavyo TLS ilikuwa ikivilalamikia. Kwa muda mrefu TLS ilikuwa ikilalamika kwamba kulazimishwa kufanya Mkutano wa nusu mwaka kwao ni gharama kubwa na ni mzigo mkubwa kwa TLS imepeleka malalamiko hayo Serikalini, Mheshimiwa Waziri anafahamu, AG anafahamu lakini humu wanashindwa kuyafanyia marekebisho na muswada umekuja kwa ajili ya marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanalalamika kuhusu chapters kupewa nguvu na zenyeweziwe active kuweza kuisaidia TLS kufanya kazi zonal wise, hili haliletwi na haya ni malalamiko ya TLS. Sasa unajiuliza haya mabadiliko yanayokuja kufanywa yanakuja kufanywa kwa ajili ya akina nani? Lakini mmegusa marekebisho wa muundo wa bodi, mnaacha pia kufanya marekebisho ya functions za bodi ambazo zina muingiliano mkubwa na functions za secretariat za TLS. Sasa kama kweli azma ya Serikali ni kuleta marekebisho kwa ajili ya kuboresha sheria kwanini mnadonyoa donyoa? Kwa nini hamleti marekebishao ambayo yatakamilisha marekebisho makubwa ili TLS waweze kufanya kazi yao kwa umakini. Sasa tunaleta sheria kwa ajili ya kuwalenga watu, hapa hatulisaidii Taifa na ukisoma haya marekebisho, moja kwa moja utaona kwamba lengo la Serikali sio kutaka kuwaondoa wanasiasa katika nafasi za uongozi, lakini lengo lao ni kuhakikisha kwamba TLS inakuwa ndani ya mkono wa Serikali. Sasa hatuwezi kwenda namna hii na ndiyo maana unaona kwenye amendment hii hii iliyoletwa hapa huku ya TLS unaambiwa mwanasiasa asiwe kiongozi wa TLS, lakini sheria nyingine hapa inamtaka tena mwanasiasa amteue Wasii Mkuu; Wasii Mkuu ndiyo anasimamia Bodi za Vyama vya Siasa. Yeye anateuliwa na mwanasiasa, unategemea afanye haki? Kama kule TLS umeona hii haki inakosekana, huku inapatikanaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kesi Mahakamani, iko kesi ya madai namba 13 ya mwaka 2017 ya Ally Saleh Vs Vita na AG yuko miongoni mwa washtakiwa hiyo kesi, anafahamu. Yanayodaiwa humo ni hizo hizo influence za kisiasa kuvivuruga vyama vingine. (Makofi)

Sasa kwa nini tunaliona hili kule tu TLS? Lakini kama kweli Serikali imefika mahali pa kutambua kwamba kada wa chama fulani anaweza asitende haki kwa watu wengine kwa nini basi hamlet muswada wa ku-amend Tume ya Uchaguzi, haya si yako na si mnafahamu kwamba returning officers wote ni makada wa Chama cha Mapinduzi na haya malalamiko ya Watanzania kuporwa haki zao kwenye chaguzi sio ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kabudi umekusanya maoni ya Katiba Mpya unafahamu kilio hiki kilivyokuwa kikubwa, leo umepewa fursa kama Waziri, leta muswada sasa tubadilishe tuwe na Tume Huru Uchaguzi kwa sababu wale wanasiasa ambao ndiyo wanatangaza matokeo kwenye chaguzi ni makada wa CCM, tunacheza nao mechi moja, refa wa kwenu na ninyi mko humo humo, mnaachaje kushinda? Kwa CCM wao ni rahisi tu ni
kujidondosha tu eneo la penalty mnapata penalty kwa sababu refa wa kwenu. (Makofi)

Sasa hatuwezi kwenda namna hii na mkumbuke yanapoporwa matokeo ya uchaguzi hamtupori wagombea, mnawapora wananchi na sisi kama vyama vya upinzani kwa muda mrefu tumekuwa tukifanya kazi ya kuwazuia wananchi wanapoporwa kutochukua hatua mikononi. Sasa itafika mahali na sisi tutachola kuwazuia, hatutawatuma wachukue hatua mikononi lakini tutachoka kuwazuia wasichukue hatua na hili litakuwa baya kwa sababu na wao watafika mahali watachoka huku kudhulumiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla Taifa halijaingia huko kubaya tumieni fursa ya kufanya amendment hata kama hamtaki mchakato wa Katiba Mpya uendelee basi fanyeni amendment kwenye yale maeneo ya msingi ili haki iweze kutendekea. Ninyi mkimuona mtu anafanya sawa tu, hapa mnamuona Fatma Karume anafanya sawa tu inawauma! Sasa pale ambapo mnapendelewa ninyi sisi mnafikiri inatuuma kwa kiasi gani? Sasa na sisi wote tuko kwenye nchi yetu hii tunahitaji usawa. (Makofi)

Kwa hiyo tuitumie fursa ya kufanya hizi amendment kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa na sio kuwashughulikia watu kwa sbabu haya mabadiliko ukiyasoma tu unaona kabisa hapa yaani unapata picha ya Tundu Lissu, unapata picha ya Fatma Karume. Fatma Karume sio mwanachama wa chama chochote pengine lakini kwa sbaabu tu anasimama kwenye anayoyaamini kwenu inakuwa tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni matumizi mabaya ya Bunge lako, haya ni matumizi mabaya ya fursa ya kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, linazungumzwa hapa suala la kumpa nguvu Mwendesha Mashtaka ya kukamata mali. Ukisoma marekebisho hayo unashindwa kutofautisha nani mwenye jukumu la kuhukumu sasa, kwa sababu hapa
unapofunga akaunti ya mtu kwa sababu tu unamtuhumu, hivi hii sio adhabu? Si tayari umeshaanza kumuadhibu? Yaani mtuhumiwa sasa anaanza kuadhibiwa kabla Mahakama haijamuadhibu. Hili haliwezi kuwa sawa! Tunaliangalia ndiyo tunarudi pale pale kwamba tunatunga sheria kwa kuwaangalia watu namna gani tutawakomesha badala ya kuangalia sheria hii italinufaisha vipi Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la kuhukumu ni la Mahakama, kutuhumiwa mtu yeyote anaweza kutuhumiwa. Leo una-freeze akaunti, akaunti ya mtu ukiifungia kumuathiri yeye tu uliyemlenga kuna watu wanakwen da shule wanalipiwa ada, kuna watu wanalipwa mishahara, wewe unaifunga, unawaathiri watu wengi kisa tu unamtuhumu na watu tunatuhumiana kisiasa hapa, watu wangapi wako magerezani, watu wangapi wana kesi hapa za kubambikiwa, leo una-freeze akaunti zao, mbona tunataka tupeane pressure tu bure. Hebu tutunge sheria kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi. Tuache kuwalenga watu halafu ndiyo tunakuja kufanya amendment. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tawala zinapita, leo tupo kwenye hii Awamu ya Tano, itakuwa Awamu ya Sita. Sio kila anayekuja atakuwa na mtazamo ule ule. Tutakuwa tuna kazi ya kuzipa viraka vya sheria kila mwaka kila tunapobadilisha viongozi. Hili sio jambo jema kwa Taifa ambalo linataka kwenda mbele hasa linalotaka kuweka misingi ya kisheria na utawala bora inafanya mabadiliko kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi na sio kwa ajili ya kuwalenga watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nitoe mchango wangu katika Muswada ulio mezani hii leo.Nianze na nyongeza iliyowekwa ya Kifungu cha 41(A) kwenye Sheria ya Mahakama ya migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, nahisi ni typing error na siyo kwamba ndivyo walivyokuwa wamekusudia, wanasema kwenye Kifungu hiki kwamba Jaji Mkuu kwa kushauriana na Waziri wa Sheria na Katiba na Mwanasheria Mkuu, wakishashauriana ndiyo wanaweza kuruhusu kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali juu ya hii extended jurisdiction. Kitendo cha kusema Jaji Mkuu kwa kushirikiana na Waziri wa Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu peke yao maana yake wanamweka nje Waziri wa Ardhi na kwenye Sheria zote za ardhi anatajwa mtu wa kufanya naye consultation ni Waziri. Waziri kwenye Sheria hizi anakuwa ni Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa wamekwenda moja kwa moja kwa kusema kwamba ni Waziri wa Katiba na Sheria ambavyo ukishamtaja Mwanasheria Mkuu yuko mle it is automatically kwamba Waziri wa Katiba na Sheria na yeye yumo. Kwa hiyo, walioachwa hapa ni Waziri wa Ardhi na tukikubali ibaki hivi maana yake sasa Waziri wa Ardhi yeye atakuwa anasikia tu tangazo limetolewa gazetini la kufanya marekebisho kwenye mambo ambayo yeye anayasimamia lakini hakushauriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele hiki nafikiri kimekaa vibaya sasa na kwa bahati mbaya sikufanya amendments na hapa ilitakiwa tu ibaki Waziri, isiwe Waziri wa Katiba na Sheria. Kwa hiyo ni vizuri wakaliangalia hili ka tafsiri zao wasomi waone wataiondoa hiyo ya Katiba na Sheria ibaki Waziri tu ili awe anaingia Waziri wa Ardhi. Atakuja kujibu Mheshimiwa Waziri asiwe na midadi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado tatizo letu linarudi pale pale; ijumaa nilikuwa nachangia hapa kwamba hizi fursa za kufanya amendments kwenye hizi Sheria hatuzifanyi ipasavyo, tunadonyoa donyoa tu. Kwa mfano; unapokuja kugusa sheria inayohusu migogoro ya ardhi, migogoro ya ardhi katika nchi hii ni mingi kweli kweli, kesi za ardhi ni nyingi sana. Wananchi wanaonewa kweli kweli kwa sababu wka sasa kesi za ardhi ni kati ya wenye fedha dhidi ya wasiokuwa na fedha ndiyo migogoro ya ardhi, lakini hii inatakiwa ianzie kwenye Baraza la Ardhi la Kata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Baraza hilo ukimkuta mtu amesoma sana atakuwa amemaliza darasa la saba, lakini wengi wanaochaguliwa kuunda hayo Mabaraza siyo watu wenye weledi mkubwa wa mambo ya kijamii tu, mambo ya kawaida, wala hayo mambo yenyewe ya ardhi, lakini kesi ndiyo zianzie huko. Pia hata mazingira wanayofanyia kazi siyo rafiki ya kuonesha kwamba haki pale inaweza kutendeka. Anaweza akaja mmoja kati ya wanaogombana, yeye kwa sababu ana hali nzuri ya kifedha ndiyo atagharamia hicho kikao, ndiyo atawabeba hao wajumbe kwenye gari lake kwenda kwenye site kupima hiyo mipaka, wakati huo mlalamikaji au mlalamikiwa mwingine ambaye hali yake ni hohe hahe na yeye ataomba lift humo humo. Katika mazingira ya namna hiyo huwezi kutegemea haki itendeke.

Mheshimiwa Spika, sasa tulitegemea wanapokuja na Muswada kwenye ardhi, maana yake mngekuja na Muswada ambao unakwenda sasa kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi, lakini badala yake wamekuja kugusa vipengele vichache sana ambavyo bado haviwezi kutatua msongamano wa kesi za ardhi zilizoko kwenye Mabaraza ya Kata, zilizopo kwenye Mabaraza ya Wilaya, kwa sababu hata akimpa mamlaka huyu Hakimu Mkazi bado anataka tu aondoe lile rundo la kesi lililopo kwenye Baraza la Wilaya lihamie kwake. Hii bado haiwezi kumaliza migogoro.

Mheshimiwa Spika, sasa tulitaka kwanza walete Sheria ya kuondoa mfumo uliopo sasa kwamba kesi ziwe ni kesi, zishughulikiwe na Mahakama za kawaida, waziwezeshe mfumo wa Mahakama wa kawaida ndiyo ushughulikie hii migogoro ya ardhi, kwamba watu badala ya kuanza kwenye Mabaraza ya Kata ni afadhali waanze kwenye Mahakama za Mwanzo endapo watazipa nguvu hiyo ili zianze kushughulikiwa kisheria kuanzia hatua ya awali. Leo zinashughulikiwa kienyeji kwenye hatua ya awali, halafu hilo file ndiyo linakwenda mpaka Mahakama Kuu mpaka Mahakama ya Rufaa, watu wana-refer kwenye vitu ambavyo vilifanywa na watu ambao hawa weledi wa mambo ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kesi za ardhi hazihitaji tu haya mapatano ya kawaida, zinahitaji sana usuluhishi wa kisheria. Sasa lazima tuisaidie nchi hii kwa kuweka sheria ambazo zitamsaidia mwananchi. Juzi wakati Rais yuko Serengeti alikutana na mama mmoja akimlilia kuhusu alivyodhulumiwa haki zake za ardhi. Sasa huyo ni yule ambaye alipata fursa ya kuonana na Mheshimiwa Rais akapeleka kilio chake na Mheshimiwa Rais kwa uchungu sana akaona kweli hapa pana tatizo. Watu wa namna hii wako wengi sana katika nchi hii ambao haki zao zinapotea, lakini hayo Mabaraza ya Kata yanaingiliwa sana na Wanasiasa na wateule wengine mbalimbali. Ziko kesi zinashughulikiwa kwenye haya Mabaraza anakuja Mkuu wa Wilaya anasema hiyo kesi isimame na kweli inasimama.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, pale Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa aliwahi kuyazuia Mabaraza yote ya Ardhi Dar es Salaam yasifanye kazi na yalikaa kimya karibuni mwaka mzima, yanavyokaa kimya haki za watu zinapotea. Sasa tulitegmea mkwamo huu, matatizo haya yataondolewa na mabadiliko ya kisheria kwenye mfumo ambao tunaishi nao, lakini wasomi wanakuja hapa hawagusi huko bado wanatuachia migogoro ya ardhi iendelee kutatuliwa na Mabaraza ya Kata ambayo watu hawana uwezo huo.

Mheshimiwa Spika, sasa hili ni tatizo na tatizo hili ni kubwa sana kwenye hizi amendments. Kila zinapokuja hizi amendments hazimalizi matatizo. Kwa hiyo, tusaidie siku nyingine tukatae yakija marekebisho hapa yanadonyoa donyoa tu vitu viwili, vitatu tuseme hapana, hebu waende wakajipange waje hiyo sheria waifanyie marekebisho yote. Kwa mfano, wamegusa hapa suala la kuondoa techinicaliries kwenye Mahakama. Ni jambo jema sana kwa sababu kweli kulikuwa na mkwamo mkubwa, ilikuwa sasa hivi ukienda Mahakamani husikilizi tena watu wakibishana kuhusu ku- prove tatizo liko wapi, bali wanabishana kwenye technicalities, kwa hiyo iliondoa ladha kabisa ya kwenda Mahakamani.Sasa kama hili limeondolewa ni jambo jema, sasa kwa nini na huku wasifanye hivyo?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunayoyategemea kutoka kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Profesa Kabudi, ni makubwa sana kuliko anayotuletea. Tunayotegemea kutoka kwa Mwanasheria Mkuu ni makubwa sana kuliko ambayo anatuletea hivi sasa. Kwa hiyo, ni vizuri waisaidie nchi hii kwa kuondoa matatizo ambayo yapo kwenye masuala haya ya kisheria.