Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwantum Dau Haji (31 total)

MHE. MWANTUMU D. HAJI aliuliza:-
Vijana ndiyo nguvu kazi ya kutegemea katika Taifa hili na ulimwenguni
kote. Kwa bahati mbaya, vijana wetu wengi wameathirika sana na madawa ya
kulevya kiasi kwamba, badala ya kuwa nguvu kazi, imekuwa ni mzigo mkubwa
kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Je, Serikali imejipanga vipi kuona inawanusuru vijana katika janga hili?
MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI - NAIBU WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA,
VIJANA NA WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la
Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa, matumizi ya dawa za
kulevya yana madhara mengi kwa watumiaji, familia na jamii kwa ujumla. Ili
kuwanusuru vijana wetu na madhara hayo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
1. Kuongeza juhudi za dhati za kimkakati za kuhakikisha za kuhakikisha wale
wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanakamatwa na
kuadhibiwa vikali kupitia Sheria Na. 5 ya mwaka 2015.
2. Kuendeleza huduma njema na endelevu ya Serikali ya kutoa matibabu
kwa watumiaji wa dawa za kulevya katika hospitali na vituo vya
wagonjwa wa akili nchini, ili kuwasaidia watumiaji wa madawa hayo
kuacha.
3. Kuendelea kuratibu na kusaidia kusambazwa kwa nyumba za ushauri
nasaha na upataji nafuu (Sober Houses) na huduma za kuwafikia
watumiaji katika miji mbalimbali nchini.
4. Kuanzisha huduma ya tiba kwa kutumia dawa ya methodone katika
hospitali zetu.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kwa kuwa barabara kuu kwenda mikoani zina foleni na tukiangalia barabara hizo zinatumika na magari mengi ya mizigo ambayo mara nyingi huwa ni chanzo cha ajali na Watanzania wengi kupoteza maisha:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizo zinapungua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyowahi kujibiwa swali la msingi namba 13, 74, 75 na 167, katika Mikutano mbalimbali ya Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zipo sababu nyingi za vyanzo vya ajali za barabarani nchini. Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa, sababu hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu:-
Kwanza, sababu za kibinadamu kama vile ulevi na uzembe zinazochangia asilimia 76 ya ajali zote.
Pili, ubovu wa vyombo vya usafiri zikiwemo hitilafu za kiufundi na mfumo wa umeme wa magari unaochangia asilimia 16.
Tatu, mazingira ya barabara yaani ubovu, ufinyu na usanifu mbaya wa barabara zetu unachangia asilimia saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa, suala la msongamano wa magari ambao linahusiana zaidi na mazingira ya barabara linachangia kiasi kidogo cha ajali ikilinganishwa na sababu zingine nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajali nchini ni tatizo ambalo kutokana na madhara yake kwa umma, Serikali itaendelea kukabiliana nalo kwa nguvu zote. Kwa kuzingatia hali hii, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani likishirikiana na wadau wengine wa usalama barabarani limechukua hatua zifuatazo:-
(1) Kusimamia kwa karibu mifumo ya sheria ukiwemo utaratibu mpya wa malipo ya papo kwa papo (notification) kwa njia ya kielektroniki ulioanzishwa hivi karibuni katika Jiji la Dar es Salaam na baadaye kutumika kwa nchi nzima.
(2) Kunyang‟anya leseni za madereva wazembe wanaorudia kutenda makosa ya usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani pindi wanaposababisha ajali.
(3) Kuwafukuza au kuwabadilisha kazi Askari wa Usalama Barabarani wanaotuhumiwa kujihusisha katika vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikichochea ongezeko la ajali barabarani.
(4) Kutoa elimu na namba za simu za viongozi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa wananchi ili wafahamu haki zao wanapokuwa abiria au watumiaji wa barabara na kutoa taarifa wanapotendewa isivyo halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwaagiza madereva na watumiaji wengine wa barabara kote nchini kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kutoa taarifa za dereva, askari au mtu yoyote anayekiuka sheria za barabarani au taratibu za kazi kwa makusudi ili hatua stahiki zichukuliwe.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la wagonjwa wa kisukari na miongoni mwa waathirika ni wanawake wenye kipato cha chini:-
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kisukari katika zahanati na vituo vya afya vya Serikali ili kusaidia watu wasio na uwezo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa ugonjwa wa kisukari ni moja ya magonjwa yasiyoambukizwa yanayoongezeka kwa kasi hapa nchini. Kitaalam imethibitika kuwa moja ya sababu kubwa ya ongezeko la ugonjwa wa kisukari hasa kwa watu wazima linatokana na mtindo wa maisha kama vile kutokufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika,ugonjwa wa kisukari unahitaji wataalam wenye ujuzi wa kumchunguza mgonjwa na kuhakikisha maendeleo yake ya kiafya yanakuwa mazuri na pia kubaini magonjwa yatokanayo na kisukari na kuyadhibiti mapema kabla hayajaleta madhara kwa mgonjwa. Madhara yake mara nyingi ni kama vile kukatwa mguu, athari kwenye macho, figo na moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sasa huduma za matibabu ya kisukari zimekuwa zikipatikana katika ngazi ya Hospitali ya Wilaya. Hii imetokana na ukosefu wa watumishi wenye ujuzi na weledi wa kuhudumia wagonjwa wa kisukari katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya. Pia mwongozo wa matibabu yaani standard treatment guidelines umeelekeza dawa za kisukari kupatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Wilaya na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho yanayoendelea katika sekta ya afya ikiwemo kutoa mafunzo kwa watoa huduma katika ngazi za zahanati na vituo vya afya, Serikali itaanza kutoa huduma za matibabu ya kisukari katika ngazi hizo kwa awamu kuanzia kwenye vituo ambavyo watoa huduma wamepata mafunzo. Mpaka sasa watumishi wapatao 150 wamepewa mafunzo kuhusu matibabu ya akinamama wajawazito wenye matatizo ya ugonjwa wa kisukari. Pia mwongozo wa matibabu utafanyiwa mapitio na Wizara yangu ili uendane na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwapima wagonjwa wa kisukari zinakuwepo katika vituo vyote vya huduma za afya zenye kliniki za wagonjwa wa kisukari katika halmashauri zote zilizopo hapa nchini. Pia utoaji wa Huduma za Mkoba (Outreach clinics) utaimarishwa katika maeneo yasiyo na kliniki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa IV wa Afya wa mwaka 2015 – 2020, mwelekeo ni kuongeza kasi ya kuzuia kuongezeka kwa wagonjwa wa kisukari kupitia uelimishaji kwenye jamii na mashuleni. Pia uhamasishaji wa kula vyakula visivyoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari na kufanya mazoezi. Vilevile utambuzi wa mapema wa ugonjwa na kupata matibabu mapema kupitia mifumo iliyopo ni mambo ya kipaumbele katika miaka mitano ya kutekeleza mpango mkakati wa sekta ya afya.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Askari wa usalama barabarani ndio wenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, lakini kwa sasa askari hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha askari wa usalama barabarani wanakuwa waadilifu na hawajihusishi na vitendo vya rushwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mhehimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi limekuwa na mikakati ya kuhakikisha askari wa usalama barabarani hawapokei rushwa kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Kutoa elimu wa askari wote wakiwemo wa usalama barabarani juu ya madhara ya rushwa katika mabaraza, kwenye komandi na vikosi, ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa askari kabla ya kuingia kazini na baada ya askari kutoka kazini.
(ii) Kutoa namba za simu za viongozi wa polisi, viongozi wa mamlaka nyingine za ulinzi na usalama kwa umma.
(iii) Mfumo wa kutoa notification kwa kutumia mashine za kielektroniki ambayo nimoja wapo ya mkakati wa kukomesha rushwa barabarani.
(iv) Kusambaza mabango katika maeneo mbalimbali yanayopiga vita rushwa.
(v) Kuanzishwa kwa masanduku ya maoni ili kutoa malalamiko katika vituo vya polisi.
(vi) Kuwasimamia na kuwakagua mara kwa mara askari hawa katika maeneo yao ya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mikakati hiyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuhusu huduma ya mabasi yaendayo kasi pale umeme unapokatika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala wa mabasi yaendayo haraka umejipanga vizuri kwa kuweka jenereta moja katika kila kituo kikubwa, ambalo hutumika kama chanzo cha umeme pale umeme wa TANESCO unapokatika. Vituo vikuu vilivyowekewa jenereta ni vya Kimara, Ubungo, Morocco, Kivukoni, Gerezani na katika karakana iliyopo Jangwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia kupitia DART imeweka betri za kutunza umeme (backup batteries) katika vituo vyote vidogo 27 ili zitumike kama chanzo cha umeme, pale umeme wa TANESCO unapokatika.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo. Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2007 na mkakati wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua, kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu, ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika suala zima la kuleta maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo kwa kuandaa mpango mahususi wa sekta ya kilimo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mpango wa Taifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo. Katika utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo limezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo, kuongeza tija kupitia kilimo cha umwagiliaji na teknolojia bora za uzalishaji kupitia kilimo shadidi, kuboresha mfumo wa upatikanaji wa mbegu bora, kuwekeza katika utafiti wa mazao ya kilimo, kutumia sayansi na teknolojia za kisasa katika kilimo kulingana na misimu na hali ya ukame na msingi mingine inayolenga kuweka mbinu mbadala za kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu ya matumizi ya ardhi pamoja na masharti maalum yanayotakiwa katika mapori yetu hususan kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka hifadhi na mapori tengefu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya hifadhi na mapori tengefu yametengwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Aidha, uwekezaji katika hifadhi, mapori ya akiba na tengefu, maeneo ya wazi yenye wanyamapori, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi na Wanyamapori (WMAs) husimamiwa na sheria hiyo. Sheria na Kanuni husika hutoa taratibu za usimamizi wa maeneo hayo muhimu kwa maslahi ya uhifadhi, maliasili na mazingira, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi kupitia matumizi endelevu. Mwekezaji anapaswa kupata kibali na leseni ya kumruhusu kuendesha shughuli za utalii kutoka mamlaka zinazohusika kabla ya kuanza biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali inapitia upya kanuni na taratibu za uwekezaji katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu, miongoni mwa kanuni zinazopitiwa ni pamoja na Kanuni ya Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs).
Aidha, Serikali iko katika hatua za mwisho katika maandalizi ya kanuni za maeneo ya mapito (shoroba) ya wanyama na mtawanyiko wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuepukana na migogoro ya ardhi baina ya wanavijiji, wawekezaji na Mamlaka za Hifadhi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA (K.n.y) MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inarejesha kasi ya kupambana na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mantumu Dau haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza kasi na harakati za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini baada ya Bunge lako Tukufu kutunga Sheria mpya ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015. Sheria hii imeipa Serikali Mamlaka ya kuanzisha chombo chenye nguvu cha kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, ambacho kiliundwa rasmi mwezi Februari mwaka 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka hiyo imepewa nguvu Kisheria ya kuweza kukamata, kupekua, kuzuia mali na kuchunguza mashauri yote ya dawa za kulevya na makosa mengine yanayohusiana nayo ikiwemo mali zitakazothibitika kupatikana kutokana na dawa za kulevya. Hata hivyo, Serikali katika kuongeza kasi ya kupambana na dawa za kulevya, mwaka 2017 ilifanya marekebisho makubwa ya sheria hiyo na kuipa nguvu maradufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu kuundwa kwake hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2018, Mamlaka imekwishakamata jumla ya watuhumiwa 11,071; kati ya hao, watuhumiwa 3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya na tayari wameshafikishwa Mahakamani. Kutokana na kuongezeka kwa kasi ya kupambana na dawa za kulevya imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa cha matumizi ya madawa ya kulevya nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kushiriki kikamilifu katika juhudi za Serikali za kupambana na dawa za kulevya kwani madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo kwa namna moja ama nyingine yanatuathiri sote kwa njia mbalimbali ikiwemo kuongeza vitendo vya uhalifu, matumizi ya Serikali katika kuwahudumia waathirika pia.
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini bado ni tatizo kubwa:-
Je, Serikali inasema nini katika kupambana na wanaume wanaodhalilisha wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kuipongeza sana Timu ya Simba. Wahenga wanasema; mla mla leo, mla jana kala nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa lipo ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa mujibu wa matukio yaliyoripotiwa katika vyombo vya dola na vyombo vingine vya umma. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau inachukua hatua zifuatazo:-
Moja, Serikali imezindua Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Vitenda vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa mwaka 2017/2018
– 2021/2022. Kupitia mpango huu, Serikali imedhamiria kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ukeketaji wa watoto wa kike kutoka asilimia 15 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia saba mwaka 2022. Utekelezaji wa mpango huu umeanza kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mikoa yote na baadhi ya Asasi Zisizo za Kiserikali yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kutekeleza mpango huu.
Pili, tumeanzisha madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi ambavyo kwa sasa tuna jumla ya madawati 417 ambayo yamewezesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kujiamini na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti kwa watoto na udhalilishaji wa wanawake katika maeneo yao.
Tatu, tumeanzisha vituo vya one stop center na vituo hivi vimekuwa na madawati ya polisi, ushauri nasaha na huduma za afya katika eneo moja, tofauti na sasa ambapo wahanga inabidi waende kwanza polisi wachukue fomu waende hospitali wapate ushauri nasaha, jambo ambalo linapoteza muda. Vituo hivi tumevianzisha katika Hospitali ya Amana kule Mbeya; Hai, Mkoa wa Kilimanjaro; na Kahama katika Mkoa wa Shinyanga.
Nne, Serikali inaendelea kuhamasisha utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Adhabu, Sura Na. 16 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 na kuhimiza wazazi, walezi, jamii na wahanga wa vitendo vya ukatili kutokaa kimya pindi wanapoona watoto au mwanamke anafanyiwa vitendo vya ukatili ili kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaowatendea watoto na wanawake vitendo hivyo vya kinyama vinavyopelekea madhara ya kimwili, kiafya, kisaikolojia, hata kifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2017, Jeshi la Polisi limeripoti jumla ya matukio 41,416 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake. Kati ya matukio hayo, matukio 13,457 ni ya ukatili wa kijinsia kwa watoto. Serikali inakemea udhalilishaji na ubakaji wa aina yoyote kwa wanawake na watoto. Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawashawishi na kuwashauri wananchi kutomaliza mashauri yaliyopo katika vyombo vya dola katika ngazi ya familia.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na ucheleweshaji wa mishahara kwa watumishi wa umma:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Waraka wa Hazina Na.12 wa mwaka 2004, watumishi wa umma wanatakiwa kulipwa mishahara yao kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi. Kumbukumbu za malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma zinaonyesha kuwa, kuanzia Julai, 2017 hadi Agosti, 2018 watumishi walilipwa mishahara yao kati ya tarehe 20 na 24 ya kila mwezi. Hivyo basi, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kuwa hakuna ucheleweshaji wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma.
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-
Kilimo cha Tanzania hutegemea mvua za msimu ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuathiri shughuli za uzalishaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo, Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2007 na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012 katika sekta mbalimbali ikiwemo na sekta ya kilimo. Mipango hii kwa sekta ya kilimo imejikita katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza upotevu wa maji ili kuepuka kilimo cha kutegemea mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mipango hii inaelezea namna ya kubadili vipindi vya upandaji mazao ya misimu ili kuendana na mabadiliko ya misimu ikiwa ni pamoja na kupanda mazao na mbegu zinazohimili ukame, kuboresha mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na kuweka mifumo mbadala ya kilimo ili kuongeza uzalishaji. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais ipo katika mchakato wa kukamilisha kuandaa mpango endelevu wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Plans). Mpango huu utakapokamilika utawezesha nchi kuwa na mipango itakayowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta muhimu ikiwemo sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa inashirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji katika kuandaa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Kilimo. Mipango iliyoandaliwa ni pamoja na:-
Moja, Mpango Mahususi wa Sekta ya Kilimo katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Tanzania Agriculture Climate Resilience Plan); pili, Mpango wa Kitaifa wa Kilimo Rafiki cha Mabadiliko ya Tabianchi (National Climate Smart Agriculture) na programu mbalimbali za uendelezaji wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mipango na programu hizi katika sekta ya kilimo, suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo imezingatiwa hasa kwa kusisitiza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo (suala la kuongeza kilimo cha umwagiliaji).
MHE. MWATUM DAU HAJI aliuliza:-

Kuna baadhi ya Askari Polisi kupandishwa vyeo lakini hawapati stahili zao kama inavyotakiwa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia askari hao stahiki zao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa upandishaji vyeo kwa Askari Polisi hutekelezwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi ikiwemo kupandishwa vyeo baada ya kuhudhuria na kufaulu mafunzo stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa Jeshi la Polisi kama ilivyo kwa Wizara na Idara nyingine za Serikali lilihusika na zoezi la uhakiki wa watumishi, zoezi ambalo pia lilisitisha marekebisho yoyote kwenye daftari la mishahara, ajira mpya pamoja na upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Serikali. Baada ya zoezi hilo kukamilika tayari Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali zaidi ya 8,440 waliokuwa na madai mbalimbali yakiwemo stahiki za kupandishwa vyeo wamesharekebishiwa mishahara na stahili zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wapatao 2,143 kati ya 3,089 waliopandishwa vyeo mwezi Juni, Septemba na Disemba, 2018 wamerekebishiwa mishahara yao. Hata hivyo taratibu za kukamilisha kuwarekebishia Askari waliobaki zinaendelea ili kuhakikisha kuwa Askari wote waliopandishwa vyeo wanarekebishiwa mishahara yao kulingana na vyeo vyao vipya.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Kuna wagonjwa wa Kisukari, Shinikizo la Damu na Kansa wanapata shida kubwa ya kiafya:-

Je, Serikali ina mpango gani katika kuwapatia huduma ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisukari, Shinikizo la Damu na Saratani ni kati ya magonjwa yajulikanayo kama magonjwa sugu au magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka sana duniani kote ikiwa ni pamoja na Nchi Zinazoendelea, Tanzania ikiwepo. Ongezeko hili lilianza kuonekana tangu miaka ya tisini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sera ya Afya ya Mwaka 2007, ilitoa tamko la kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, mnamo mwaka 2009, Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilianzisha kitengo cha kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kutengeneza mpango mkakati wa mwaka 2009 – 2015 na hivi sasa tunatekeleza mpango mkakati wa mwaka 2016 – 2020. Mwongozo huu unatekelezwa kuanzia ngazi ya hospitali ya kanda hadi zahanati. Huduma za Magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la Damu pamoja na Saratani ni huduma ambazo katika hatua za awali zinapatikana katika ngazi ya kituo cha afya. Mgonjwa anapokuwa na magonjwa haya ambayo yapo katika hatua ya juu, hulazimika kupatiwa huduma za matibabu ambazo zinapatikana Hospitali za Kanda, Taifa, Rufaa za Mikoa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeboresha huduma ya magonjwa ya moyo ikiwemo Shinikizo la Damu kwa kufungua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali za Ocean Road, Bugando, KCMC, Benjamin Mkapa na ipo mbioni kufungua huduma za saratani katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya ili kupunguza mzigo kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambayo kwa miaka mingi ni yenyewe pekee imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa hao. Aidha, Serikali iko mbioni kuanzisha programu ya magonjwa yasiyoambukiza kama ilivyo kwa Programu za UKIMWI, TB na Malaria ili kufikisha huduma hizi katika ngazi ya zahanati na kuzipa mwonekano wa kipekee huduma za magonjwa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, natoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanajikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki, kula mlo unaofaa, kutotumia tumbaku na bidhaa zake na kupunguza matumizi ya pombe.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Dalili za maji safi na salama kuchanganyika na maji chumvi (bahari) zinatishia ustawi. Je, nini utatuzi wa tishio hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa maji safi na salama kuchanganyika na maji chumvi bahari yanatishia ustawi wa jamii na kilimo. Hali hiyo inasababishwa na athari ya mabadiliko ya tabianchi, kutokana na kuongezeka kwa joto la dunia linalosababisha na kuyeyuka kwa barafu kwenye ncha za dunia na kwenye vilele vya milima mirefu. Kuyeyuka huko kwa barafu kunasababisha maji kutiririka kwenda baharini na kuongeza ujazo wa maji ya bahari na kusambaa katika maeneo ya mwambao ambayo yana shughuli muhimu za kijamii kama vile visima vya maji, kilimo na miundombinu muhimu ambayo huingiliwa na maji chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya sita ya jopo la watalaam inaonesha kuwa ujazo wa bahari umeongezeka kwa sentimita 19 katika miaka ya hivi karibuni na kusababisha mmomonyoko wa kingo za bahari na baadhi ya maeneo ya Pwani yameingiliwa na maji chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utatuzi wa kudumu wa suala hili unahitaji ushirikiano wa Kimataifa hususani katika kupunguza gesi joto ambazo huchangia ongezeko la joto duniani ambalo husababisha mabadiliko ya tabia nchi. Kwa kuwa suala la kupunguza gesi joto sio rahisi kufikiwa katika kipindi kifupi nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinahimiza kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuchimba visima vipya, kupanda miti ya mikoko katika maeneo ya kandokando ya bahari, kujenga kuta na makinga maji pale panapowezekana na kuhamasisha shughuli za kilimo kufanya katika maeneo mengine ambayo hayajaathirika. Sambamba na suala la kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, nchi zinazozalisha gesi joto kwa wingi zinahimizwa kupunguza gesi joto ili kuzuia athari zaidi za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza:-

Kasi ya mmomonyoko wa ardhi na uhaba wa udongo katika Visiwa vya Unguja na Pemba inatishia uhai wa Visiwa hivyo:-

Je, ni hatua zipi za makusudi zimechukuliwa katika kuvinusuru Visiwa hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba nichukue fursa hii sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Visiwa vya Unguja na Pemba vina maeneo takribani 148 yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi (Pemba 125 na Unguja 23). Athari hizi ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe na kuingia kwa maji ya bahari katika mashamba na makazi ya watu. Ili kuvinusuru visiwa hivi dhidi ya athari ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali kupitia miradi inayofadhiliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari ya mabadiliko ya tabianchi (LDCF) ambao umetekelezwa mwaka 2012 - 2018, shughuli zifuatazo zimefanyika: Ujenzi wa kuta mbili za mita 25 kila moja katika eneo la Kisiwa Panza - Pemba na ujenzi wa makinga bahari (gloynes) matano ya wastani wa urefu wa mita 100 kila moja katika eneo la urefu wa mita 538 Kilimani
– Unguja; upandaji mikoko Pemba maeneo ya Kisiwa Panza hekta 200, Tumbe hekta 10, Ukele hekta 7 na Tovuni hekta 1; na upandaji mikoko Unguja maeneo ya Kisakasaka hekta 8 na Kilimani hekta 1.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia Mradi wa Kupunguza Uhalibifu wa Ardhi na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula katika Maeneo Kame nchini mwaka (2017 - 2022), shughuli zifuatazo zinategemewa kufanyika katika maeneo ya Micheweni, Kata ya Micheweni na Kiuyu Maziwang’ombe ambazo ni: Kujenga makinga maji katika mashamba (dykes) ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba; kutoa elimu kuhusu kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mashamba darasa; upandaji wa miti ili kuhifadhi udongo na kutunza mazingira; na uanzishaji wa biashara ndogo ndogo ili kuwezesha jamii kuwa na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi; kudhibiti mmomonyoko wa udongo; na kukabiliana na uhaba wa udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za ujenzi wa jengo jipya la kisasa la Askari Polisi wa Makunduchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi ya askari katika eneo la Makunduchi na katika Mkoa wote wa Kusini Unguja. Eneo la Makunduchi lina jengo moja la ghorofa la makazi ya familia nne za askari lililorithiwa toka Serikali ya Mkoloni na Mahanga mawili yanayotumiwa kwa makazi ya askari. Makazi haya ni sawa na asilimia 10 tu ya mahitaji halisi. Kwa kutambua changamoto hii, Serikali imeanzisha ujenzi wa nyumba za makazi ya familia 12 za askari polisi katika Mkoa wa Kusini Unguja. Aidha, Serikali kwa kupitia jeshi la polisi na kushirikiana na wadau imeanzisha ujenzi wa kituo cha polisi cha Daraja B huko Dunga, kituo hiki kimefikia hatua za mwisho kumalizika.
MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kusini Unguja ulianza mwaka 2008 na gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi 225,000,000/= mpaka kukamilika kwake. Mpaka sasa ujenzi huu uko kwenye hatua ya msingi na unagharamiwa na Serikali kupitia bajeti ya maendeleo, na ujenzi umekwama kwasababu ya kukosekana kwa fedha za kutekeleza mradi wa ujenzi kutokana na ufinyu wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imo katika kufanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa ulinzi na usalama pamoja na wananchi, ili kuchangia na kukamilisha mradi huo, ili uweze kuwasaidia wananchi na shughuli za ulinzi na usalama ziweze kupatikana katika eneo hilo la Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja. Ahsante sana.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoa mafunzo ya ujasiriliamali kwa Watu Wenye Ulemavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo : -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia bajeti ya kila mwaka wa fedha imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuwezesha mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu waliopo katika ngazi mbalimbali, zikiwemo halmashauri zote nchini. Tumekuwa tukifanya hivi ili kusudi watu wenye ulemavu wanaopewa fedha hizi waweze kuzifanyia kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imekuwa ikiendelea kushirikiana na wadau, na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu kwneye fani mbalimbali lengo la kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kuwaingizia kipato. Kwa mfano, katika mkoa wa Dar es Salaam pekee, kwa mwaka 2019/2020, zaidi ya wajasiriamali wenye ulemavu wapatao 160 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na uanzishaji wa miradi endelevu. Mafunzo haya yalihusisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Benki Kuu ya Tanzania, mifuko yetu ya hifadhi ya jamii NSSF, Benki ya Exim, Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), na Vyama vya Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu katika mafunzo ya ujasiriamali umekuwa ukiendelea kufanyika kupitia vyama vyao wakati wa matukio mbalimbali kama maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu lakini vile vile tumekuwa tukiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo mbalimbali kwa mfano kule Mbeya – Kyela tunashirikiana na wenzetu wa trade craft exchange na mashirika mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO K.n.y. MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana katika Halmashauri wanapewa mikopo ya asilimia tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 23 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya asimilia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa kutoa mafunzo kwa vikundi vilivyokubaliwa kupata mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Kanuni hiyo Serikali ilikwishaanza kutoa elimu ya ujasiriamali na katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetoa mafunzo kwa vikundi 11,915 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambavyo vilipewa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini. Mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, utunzaji fedha, uendeshaji na usimamizi wa miradi, utoaji taarifa na usimamizi wa marejesho ya mikopo. Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa itaendelea kutoa elimu kwa vikundi hivyo ili kuvijengea uwezo wa kuendelea kukua na kutumia ipasavyo fursa mbalimbali za kiuchumi katika maeneo yao, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali imepanga kuanza kukarabati majengo ya Kituo cha Polisi Makunduchi.?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Makunduchi pamoja na nyumba za makazi ya Askari ambayo ni jengo la ghorofa moja linaloishi familia nne na mahanga mawili ya familia kumi na sita. Tathmini kwa ajili ya ukarabati imeshafanyika na jumla ya Shilingi 110,093,400 zinahitajika. Ukarabati huo ni wa kubadilisha paa, dari, mfumo wa maji safi na taka pamoja na kupaka rangi. Jeshi la Polisi linatafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo ikiwa ni pamoja na majengo mengine ya vituo na makazi ya askari yaliyokwisha fanyiwa tathmini. Nakushukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama wafanyabiashara ili wafanye biashara zenye tija?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wadogo wakiwemo akinamama kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi na kuchukua vitambulisho vya wajasiriamali na kurasimisha biashara zao. Mikakati ya Serikali ni kuendelea kuwasaidia akinamama wafanyabiashara kupitia mikopo inayotolewa na Mifuko ya Uwezeshaji ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wafanyabiashara Wananchi (NEDF) chini ya Shirika letu la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wajasiriamali (SME Credit Guarantee Scheme) unaoratibiwa na pia SIDO kwa kushirikiana na Benki ya CRDB.

Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ikiwemo majengo ili wapate sehemu tulivu za kukuza biashara zao. Kuanzia Julai, 2015 hadi Machi, 2021, Serikali kupitia Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wajasiriamali pekee imekwishawapatia akinamama wafanyabiashara mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 310. Aidha, Wizara inakamilisha mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya mwaka 2003 ili iweze kuendana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ya sasa. Nakushukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, ni kwa nini ugonjwa wa TB hauwezi kuonekana kwa mara moja unapompata mwathirika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ugonjwa wa TB huchelewa kuonekana kutokana na tabia na mwenendo na vimelea vya TB kuzaliana taratibu mwilini na mara nyingi hudhibitiwa na kinga ya mwili wa aliyeambukizwa. Hivyo kila mgonjwa ataanza kuonesha dalili za ugonjwa kutegemea hali ya kinga ya mwili wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya kupimwa mara tu wanapojisikia dalili zifuatazo; homa za mara kwa mara, kikohozi cha wiki mbili au zaidi, kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu, kupungua uzito kwa haraka bila sababu ya msingi na kutokwa jasho jingi hasa usiku. Aidha, ninashauri jamii iwe na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kutambua magonjwa mapema na hatimaye kuanza matibabu mapema. Ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza Wananchi wengi zaidi kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwntumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaendelea katika maeneo ya Mamlaka 186 ikiwa ni Halmashauri 184 za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kipindi hiki, idadi ya walengwa iliyobaki awali ya asilimia 30 ya Vijiji, Mitaa pamoja na Shehia 7,217 ambazo hazikufikiwa katika kipindi cha kwanza imeongezwa. Jumla ya kaya 498,091 zilizokidhi vigezo zimeandikishwa na kuingizwa kwenye mifumo ya taarifa za walengwa. Aidha, Kaya mpya na ambazo zilikuwemo kwenye Mpango, zinafanya jumla ya idadi kuu ya walengwa kuongezeka na kufikia kaya 1,279,325.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma za kipolisi jirani na maeneo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa madhumuni ya kupeleka huduma za polisi jirani na wananchi, Jeshi la Polisi linatekeleza utaratibu wa kuwapangia kazi Wakaguzi wa Polisi kwenye maeneo ya kata na shehia zote hapa nchini. Mpaka sasa Wakaguzi wa Polisi 2,552 wameshapelekwa kwenye kata hizo 2,552 na...Sorry, naomba kurejea eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linatekeleza utaratibu wa kuwapangia kazi Wakaguzi wa Polisi kwenye maeneo ya kata na shehia zote hapa nchini. Mpaka sasa Wakaguzi 2,552 wameshapelekwa kwenye kata na 288 wameshapelekwa kwenye shehia kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Wakaguzi wa Polisi wanaopangwa kwenye kata na shehia ni kusimamia hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao na kushirikiana na wananchi kuanzisha na kusimamia vikundi vya ulinzi shirikishi, kushiriki vikao na mikutano ya vitongoji, vijiji, shehia na kata na ward ili kutatua changamoto za uhalifu na migogoro katika jamii, pia hushiriki kwenye mikutano ya kamati za maendeleo za kata ili kutoa ushauri kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama, nakushukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja litakalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazungumzo kuhusu ujenzi wa daraja litakalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar yalishaanza kwa kuzihusisha Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya ujenzi kwa upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa upande wa Zanzibar, ambapo mnamo tarehe 11 Machi, 2023 kwa pamoja walikutana na Wawekezaji Kampuni ya China Overseas Engineering Group Company waliokuwa wameonesha nia ya kujenga daraja hilo. Yatokanayo na kikao hicho bado yanafanyiwa kazi kwa pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar, ahsante.
MHE. MWATUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza gari lingine la polisi wilaya ya Kusini Unguja kwani gari moja lililopo halikidhi mahitaji?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi wilaya ya Kusini Unguja, katika mkoa wa kusini Unguja una magari manne ambayo yote ni mazima na yanatumika kutoa huduma katika eneo hilo. Magari hayo ni PT 4807 Ashok Leyland ambalo liko kituo cha Polisi Kizimkazi, PT 4808 Ashock Leyland ambalo liko Kituo cha Polisi Paje, PT 1906 Toyota Land Cruiser ambalo lipo Kituo cha Polisi Paje, PT 3860 Toyota Hilux Double Cabin ambalo liko kituo cha Polisi cha Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023 imetoa kiasi cha fedha shilingi billioni 15 kwa ajili ya Jeshi la Polisi ili kununulia pikipiki pamoja na magari ambayo yamepangwa kugawiwa kwenye mikoa na wilaya zote nchini.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kudhibiti vyombo vya baharini vinavyozidisha mizigo na abiria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyombo vikubwa ikiwa ni vyombo vyenye urefu zaidi ya mita ishirini na nne. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania TASAC linajukumu kisheria kufanya ukaguzi wa michoro ya meli kabla ya hatua ya ujenzi kuhakikisha mstari wa ujazo (load line) umewekwa kwenye kina sahihi cha meli, kisha Msajili wa meli anathibitisha michoro hiyo na kutoa ruhusa ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TASAC kufanya ukaguzi kipindi cha ujenzi wa meli. TASAC hufanya Ukaguzi kuhakikisha Meli inapakia mizigo bila kupitiliza mstari wa ujazo uliothibitishwa na Msajili, na endapo itabainika kuwa meli imezidisha ujazo wa abiria, mizigo au vyote kwa pamoja itakuwa imetenda kosa kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, meli hiyo itapaswa kuzuiliwa bandarini na Mamlaka ya Bandari Tanzania itajulishwa ili kusitisha kutoa kibali kwa meli hiyo hapo bandarini. Kwa hatua zaidi, TASAC humtoza mmiliki au nahodha wa meli faini na kisha kusimamia upunguzwaji wa abiria, mizigo na vyote kwa pamoja kisha kuruhusu meli hiyo pindi Mkaguzi atakapojiridhisha kuwa Meli ipo salama kwa kuanza safari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vyombo vidogo vyenye urefu chini ya mita ishirini na nne, TASAC inajukumu kisheria kufanya ukaguzi wa vyombo vidogo na kutoa leseni ya uendeshaji inavyotaka ujazo wa abiria au mizigo unaostahili kuzingatiwa katika uendeshaji wa chombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, endapo itabainika kuwa chombo kimezidisha ujazo wa abiria au mizigo, nahodha atakuwa ametenda kosa kisheria na chombo hicho kitazuiliwa bandarini au mwaloni ili kulipa faini na TASAC kusimamia upunguzwaji wa abiria au mizigo kabla ya kuruhusu chombo kuendelea na safari, ahsante.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya bei ndogo za mazao pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wakulima wanapata bei shindani na masoko ya uhakika. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza tija kwenye uzalishaji kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo, utafiti, huduma za ugani, matumizi ya teknolojia na kurasimisha Sekta ya Kilimo Mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko; kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji kwa lengo la kutangaza bidhaa na maeneo ya uwekezaji katika sekta ya kilimo; kushirikiana na Sekta Binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya masoko; kuimarisha mifumo ya kielektroniki ambayo itawezesha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakati; kutoa mafunzo kuhusu kilimo biashara kwa Maafisa Ugani na Wakulima na kuendelea kufungua masoko mapya katika nchi mbalimbali kwa kufanya tafiti za mahitaji kwa nchi husika.
MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha na kuwainua kiuchumi wanawake wasiojiweza?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha mifuko na programu za uwezeshaji kwa lengo la kuwawezesha na kuwainua wananchi kiuchumi wakiwemo wanawake wasiojiweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini - Awamu ya Pili kwa kuhawilisha ruzuku ili kuwawezesha wananchi wasiojiweza ikiwemo wanawake kupata mahitaji ya msingi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wanawake wasiojiweza kutumia fursa za uwepo wa mifuko na programu za uwezeshaji ili kuanzisha na kuendeleza biashara zao, nakushukuru sana.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha Shilingi 43,000,000 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga kilichoko Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha hizo ili kumalizia ujenzi huo, kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi na wadau, hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha Shilingi 43,000,000 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga kilichoko Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha hizo ili kumalizia ujenzi huo, kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi na wadau, hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024.