Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwantum Dau Haji (15 total)

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru kwa siku hii ya leo adhimu kwa kunijalia kunipa nafasi hii katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa leo hii ni siku yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, nishukuru viongozi wangu wote walioniwezesha kufika hapa pamoja na Mwenyezi Mungu; nimshukuru Rais wangu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa ushindi alioshinda wa kishindo siku ya tarehe 20 Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru na wadau wangu walioniwezesha wa Mkoa wa Kusini Unguja, kuniamini na kunithamini wakanipa kura zao ili niwe Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Unguja. Nasema sitawaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia suala la Wizara hii ya Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa. Kwanza niseme, alisimama mwenzangu hapa akazungumzia kwamba Jeshi limepindua Zanzibar. Jeshi halijapindua Zanzibar! Nataka kuuhakikishia ukumbi huu kwamba Serikali ya Mapinduzi tarehe 20…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, Mwantumu, hiyo kauli ilifutwa asubuhi. Kwa hiyo, tuendelee. (Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuendelea kuchangia, kuna ndugu zetu wa polisi ambao ni trafiki na pamoja…
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Usinishuhulishe!
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa jitihada zao wanazozifanya katika Serikali ya Muungano huu wa Tanzania ninawapongeza kwa dhati. Hufanya kazi zao kubwa sana, kuimarisha Muungano ndiyo maana tumekuwa na utulivu, amani na uhuru wa nchi yetu. Nawaomba wazidi kulinda Muungano, wasirudi nyuma na wala wasitetereke. Waulinde, wausimamie na wautetee kwa maslahi ya nchi yetu na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea katika huduma za jamii, mfano afya, ujenzi na utalii kuwa karibu na wananchi kutoa mafunzo ya ulinzi ili wananchi wazidi kufaidika na kujijengea kwenye harakati za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Kusini Unguja tuna ulinzi wa uhakika kwenye Jeshi la Ulinzi na wanatusaidia vikubwa kutulinda na wala hatuna tatizo tunakwenda nao vizuri, tunashirikiana nao vizuri na ndiyo tumejivunia mpaka leo hii tumefikia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichangie kuhusu suala la ujenzi wa Kituo cha Mkoa cha Polisi Jumbi; kuna Kituo cha Mkoa wa Kusini Unguja kilikuwa kinafanya kazi pale Fuoni lakini Kituo kile kilihamishiwa Mkoa wa Kusini, Wilaya Kati pale Jumbi. Naomba Mheshimiwa Waziri, kwa udhati wako wa moyo, kwa imani yako, utusaidie kituo kile kiwe na jengo imara, lenye mvuto na pale lilipo ni njiani basi paonekane kwamba pana jengo la Kituo cha Polisi; na watu wote wanaopita pale wajue kwamba hili ni jengo la polisi la Mkoa wa Kusini Unguja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jitihada na busara zake jinsi anavyoliendesha Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MWANTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali yangu chini ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufulikwa jinsi anavyoisimamia Serikali yake, nasema ahsante. Pia nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kusimamia vyema Wizara yao kikamilifu, nawapongeza sana, Mwenyezi Mungu awasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu huduma ya afya ya uzazi na watoto. Vifo vitokanavyo na uzazi bado vinaendelea japokuwa vimepungua lakini wajawazito wengine hawana elimu kutokana na umbali kutoka wanakoishi mpaka kwenye vituo vya afya. Kwa hiyo, naishauri Serikali wapatiwe huduma elekezi, japo wauguzi wa vituo mbalimbali wasogee vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wajawazito wengi wanapata operesheni, kwa nini iwe hivi? Watoto wengi sasa wanaozaliwa afya zao zinakuwa si nzuri. Aidha, wamekuwa wadogo sana au wamelegea. Mzazi anahangaika mpaka anachoka. Huduma wodini madaktari wanajitahidi sana, lakini wodi ndogo hazina ukarabati, vitanda vidogo, inafikia hatua kitanda kimoja wazazi watatu au wawili, hivi na magonjwa kila mtu na yake ukizingatia maambukizi ni mengi. Kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye juhudi zake ili ipanue wodi au ukarabati kwenye hospitali zetu zilizokuwa zimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na vilevile nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu ndogo kwa hiyo siwezi kusema mlolongo mkubwa. Naipongeza hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa hotuba hii ambayo ni nzuri, aliyoipanga na haina mjadala, isipokuwa kuna mambo tu madogo madogo yaweze kuwekwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha Polisi Daraja ‘B’ Mkokotoni Unguja kina asilimia 60 na haya ninayozungumza yamo katika hotuba hii. Kituo hiki kina asilimia 60 Mkokotoni tayari kimeshakuwa kimefanikisha, lakini kuna vituo humu nchini ambavyo havina hadhi na havina mashiko. Tukizingatia katika Mkoa wangu wa Kusini Unguja kituo hiki cha Paje ambaye hapa kidogo mwenye hili Jimbo alilizungumzia lakini hakulitoa sahihi sana. Kituo kile hakina hadhi na ukipita pale utahisi kama hiki siyo kituo cha Polisi, kama wenyewe watakuwa hawapo pale nje basi huwezi hudhani kwamba hiki ni kituo cha Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo pia hiki kilikuwa kimo ndani ya mgao kwamba kitengenezwe na kiwe kituo cha hadhi cha Wilaya ya Kusini, naomba kama hili suala kweli lipo basi hiki kituo kiweze kutengenezwa kwa sababu ukanda mzima ule ni ukanda wa watalii na watalii wote waliopo kile kituo hiki ndicho kinachohusika kuanzia Jambiani hadi Michamvi. Naomba kituo hiki kitengenezwe kuwa kituo cha hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MWATUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya. Nishukuru ukumbi huu leo wote tuliopo hapa pia tupo wazima wa afya mpaka hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba kuchangia Hotuba hii ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nachangia kuhusu JKT hasa kwa vijana na kule kwetu Zanzibar. Kule Zanzibar kuna vijana wetu ambao wanakwenda JKT na wanakuwa wazuri tu wakirudi kule wameiva, lakini wakifika kule wanakuwa hawana ajira rasmi za kujiajiri, wanahangaika isipokuwa ajira zao ziwe mikononi mwao. Vijana hawa wanakuwa wanatupigia kelele sana sisi wazazi au kama hivi sasa mimi ni Mheshimiwa, lakini huko nyuma nakumbuka sisi Wabunge waliopita walikuwa wanapata hizi ajira kama kwa mtoto wake au mtoto wa ndugu yake lakini ajira walikuwa wanapata kwa mtu mmoja mmoja, kwa hiyo zoezi hili limeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba hili zoezi lirudi tena sisi Wabunge tuwe mfano wa kupata kwa kila mtoto kama mmoja mmoja au katika jamii tulizonazo wapate ajira hizi za Jeshi ili na wao wajiajiri na wajisikie. Na wanakuwa na hamu sana ya kwenda Jeshini, lakini ajira kama tunavyozungumza ni ngumu. Hili lirudi na lizingatiwe sana ili wale vijana wawe na imani na Nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwapongeze Jeshi kwa kazi zao wanazozifanya na hasa jana tu, wakati mimi nakuja huku Bungeni nipo maeneo ya Mlandizi, ilitokea ajali mbaya kati ya basi la Tanga na coaster inayotokea Morogoro, walisaidia roho za binadamu pale… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. MWATUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siikubali kwa sababu mimi sikusema kwamba huyo Mbunge ndiye anayetoa hiyo ajira hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesikia, mimi naomba kwamba sisi Wabunge hivi sasa tunaomba kwamba zikitokea hizi ajira za Jeshi basi kama kuna uwezekano tuzipate ili tuwasaidie wale vijana na wale watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na hotuba yangu hii…majimboni, hata ikiwa majimboni ikiwa kwa jamii lakini tunaomba kwamba tupatiwe na sisi hizi ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi jana limeokoa roho za binadamu pale Mlandizi kati ya basi la Tanga na basi la coaster linalotokea Morogoro, ana-overtake basi la Tanga kwa bahati yule amejitahidi kulivusha lakini hakufanikiwa likaenda uso kwa uso dereva katoka miguu hana. Kwa hiyo, pale watu walishindwa kumtoa kila mmoja na imani yake basi walitokea vijana wetu hawa wa Jeshi na wakaenda pale wakaokoa roho zile wakawakwamua na palepale ikatokea gari wakapelekwa hospitali. Mimi ninawashukuru sana na ninawapongeza sana kwa kitendo kile walichokifanya jana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Dakika zangu umenipatia chache lakini hizi hizi naona zinaweza kutosha kidogo kwa mambo niliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa na hali ya uzima na afya na kutujaalia kuwa na mfungo wa Ramadan na leo ndiyo kwanza siku ya kwanza. Kwa hiyo Mungu atusaidie tuifunge Ramadan kwa salama ana amani na tupendane sote humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake ya Wizara ya Afya iliyojaa maono, haina mjadala. Mzungu amesema no discussion. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea, dakika zangu tano nataka kuzungumzia suala la mradi wa magonjwa yasiyo ambukizika. Kuna magonjwa yasiyo ambukiziki ni magonjwa ya sukari, presha pamoja na magonjwa ya shinikizo la damu. Magonjwa ya sukari haya ni magonjwa tutasema mfano kama yanapunguza ile hofu ya mgonjwa hasa atakapokuwa anapata dawa zake za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wagonjwa wa sukari ambao wagonjwa hawa wa sukari na presha zinaendana pamoja na shinikizo la damu lakini wagonjwa hawa wengine wanyonge, maskini hawana hata ile bima ya kuweza kununulia zile dawa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, dawa ziko nyingi sana nakupongeza sana lakini hizi dawa kama huna pesa au huma bima unakuwa huwezi kuzinunua baadhi ya dawa nyingine maana kuna dawa nyingine zinashusha hata sukari, unapata nne, tano, saba, nane lakini kuna dawa nyingine zinakuwa hazishushi. Sukari ile inakuwa inapanda pamoja na presha hasa kuna dawa hizi za mizizi ambazo tunapewa humu nje. Dawa zile Mheshimiwa Waziri yanaua kongosho la eucilin kwa hiyo, yanapoua lile kongosho la eucilin basi uhakikishe wewe mgonjwa wa sukari tayari umeshapata ganzi, tayari umeshapata hofu, tayari unakuwa huna nguvu za mwili ambao ukaweza kufanya harakati zako ulizokuwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nakuomba naiomba Serikali yangu hivi sasa hivi kwamba itafute dawa ambazo zipunguze gharama ili na wale wengine waliokuwa hawana zile bima au hawana ile pesa waweze kuzinunua hizi dawa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwantumu Dau.

MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa suala langu hili la kuhusu magonjwa yasiyoambukizi ni hili. lakini la pili, nataka kuzungumzia…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwantumu muda wako umekwisha nashukuru sana kwa mchango mzuri. (Makofi)

MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja lakini mmenipa dakika kidogo. Ahsante sana, pia nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia siku hii leo, Ijumaa ndiyo siku yangu adhimu aliyoniwekea kipindi hiki ili niweze kuchangia Wizara hii ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake.

Mheshimiwa Waziri, Mama Ummy, mwanangu nakushukuru sana na nakushukuru kwa jitihada zako unazozitendea Wizara hii ya Afya na ninakushukuru kwa jitahada zako kwamba umefika pia nami kunisaidia kufika Ocean Road kumpeleka ndugu na akapata uzima kuhusu cancer. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu tano, kwanza niingie suala la ukatili dhidi ya watoto na wanawake nchini. Ukatili wa watoto na akina mama umezidi hapa nchini kwetu. Umezidi mno, umekithiri, maana yake sijui mtu afanye nini hasa! Nataka kuishauri Serikali, hili suala wasilitizame kwa jicho tu hivi, waangalie kwa kina ili hili suala la udhalilishaji wa watoto na akina mama lifanyiwe kazi ili liondoke katika nchi hii. Inawezekana kwa nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama na mtoto katika kuimarisha huduma ya afya, lazima aimarishe kwa jitihada zake na uwezo wake ambao anao. Mama anakwenda hospitali hana mbele wala nyuma, ana mtoto wake anaumwa, pengine naye pia anaumwa, anakwenda pale, hana hata shilingi. Bima ya afya pia hana, anafika pale anaandikiwa madawa anakwenda akahangaike nje ili apate pesa zimsaidie mtoto. Kuimarisha huko ndiyo kunaendelea? Hakuna. Kwa hiyo, jitihada ya Serikali itazame vilevile kwa jicho la huruma mama na mtoto waweze kusaidiwa waweze kuimarisha afya zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na uboreshaji wa huduma ya vituo vya afya; vituo vya huduma ya afya hapa nchini niseme Wizara imejitahidi sana, lakini kwa kuingilia ndani ukaitazama katika huduma zetu za afya ndani ya madaktari wengine wanakuwa madaktari, maana yake ni kama wanawanyanyasa wale wanaohitaji huduma, wanaokwenda pale kutibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ashakwenda pale anaumwa, lakini daktari anajifanya kama yeye ni daktari, amesoma na uwezo wake, basi kumhudumia yule mtu aliyekwenda pale, mnyonge, maskini, anamnyanyapaa.

Anaona kama hakwenda mgonjwa pale. Anapiga simu au kama ana kikaratasi chake, anaendelea kusoma. Wengine utakuta wanachukua simu wanachapa zile karata katika ile simu, mna zile karata wanacheza. Mtu hajui huku kama kaja mgonjwa anaumwa amhudumie. Hilo limo katika vituo vyetu, nakuomba uliangalie kwa kina katika vituo vyako hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapokwenda kutembelea uangalie vizuri madaktari wetu. Sisemi kama hawafanyi vizuri, wanafanya vizuri, tumewapongeza humu sana, lakini suala hilo madaktari wengine wanafanya. Jitahidi katika kutembelea vituo vyako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, kuna ukurasa wa 14 aya 22 - afya na usafi wa mazingira. Kuna mazingira mengine katika vituo vyetu ambavyo tunakwenda kuingilia kama vituo vya mabasi, huduma za vyoo sio nzuri. Huduma ni mbaya, hazina usafi, utoke huku uende ukachukue maji uingize ndani ndipo uende ukafanye huduma yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara izingatie suala hili na hivi vyoo vitembee hasa ili kwenda kutizama juu ya huduma zilizokuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja Wizara ya Afya. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana niugane na wenzangu ambao waliosimama katika Bunge lako hili Tukufu kuichangia TAMISEMI na Serikali za Mitaa. Kwa kuzungumzia moja kwa moja, nazungumzia kwenye hoja maana nisemi Mheshimiwa Ummy Mwalimu nimpongeze na nimshukuru sana kwa kuletwa kwenye kamati hii na kwa kweli umeonekana mtu mahiri wa kuja kwenye kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naanza kutangulia kusema kwamba kuna watumishi wengi katika halmashauri ambao hao watumishi wa umma hawajapata stahiki zao kwa kipindi kirefu. Suala hili la watumishi wa umma ambao waliokuwa awajapa stahiki zao toka kipindi cha miaka ile mitano tuliyopita tulikuwa tunazungumzia wastahiki hawa wa umma katika Serikali yetu. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali yangu ili hawa watumishi waliokuwa wameacha kazi zao wapewe stahiki zao kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuzungumzia suala la kuunganisha vikundi vya watu wenye ulemavu au watu wa mahitaji maalum, tumetembelea katika halmashauri katika kamati yangu hii tumewaona vikundi mbalimbali ambavyo vilivyokuwa havijaunganisha kwenye halmashauri zile watu wenye ulemavu ili wakaweza kufanya kazi zao katika vikundi vyao na ile asilimia yao mbili wanayoipata, bado awajakaa kabisa wakaweza kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, vilevie napenda kuishauri Serikali waweze kuwapatia mafunzo watu wenye ulemavu ili waweze kujisaidia nakujikwamua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho nazungumzia kuhusu TASAF, TASAF kusaidia wananchi wanaonufaika ruzuku za Kaya Maskini, hii TASAF tulikuja tukaitia baraka hapa katika Bunge lako Tukufu na kwa bahati hii TASAF ipo katika halmashauri lakini napenda kusema kwamba ninaishauri Serikali TASAF izidi kufanya kazi zao kwa urefu zaidi ili waweze wale watu wa Kaya Maskini wapate na wao kunufaika, na vilevile wawapatie vikundi mbalimbali katika ndani ya hii TASAF ili na wao waweze kufanya kazi zao vizuri na waweze kujikwamua kiumaskini.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kuunga hoja mkono asilimia mia moja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya kwa wakati huu na pindi hizi kusimama katika Bunge hili Tukufu ili kuichangia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu wake kwa kazi zao nzuri wanazozifanya na kuzitekeleza katika masuala yao ya utendaji wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kuhusu suala la hali ya usalama barabarani, hali ya usalama barabarani ni nzuri na niwapongeze sana maaskari wetu wanafanya kazi nzuri, wanajitahidi kuifanya kazi hii ya barabarani lakini kuna suala la barabarani la kuhusu yale mataa. Katika vile vitengo vya mataa pale wananchi wanakuwa wanakasirika sana baadhi yao madereva. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taa zile zimewekwa pale ili kupitisha zile gari lakini askari wanatoka wanakwenda kusimama pale kuzipeleka zile gari kwa mikono na kasi, imekuwa wanaungana msururu mkubwa sana huku wa magari na muda mrefu sana watu wanapeleka wakati zile taa pale zipo zina kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumwambia Waziri kwamba lile suala walizingatie kwa kina wale askari. Hatutaki kwamba wasiwepo, wawepo maana wapo kwenye kutengeneza suala la usalama lakini wanapokuwepo pale wakae pembeni wangalie zile gari na zile taa zinazopitisha; kuna taa kijani, nyekundu lazima utajua hii nyekundu sasa hivi kule siendi lakini hii kijani ni yangu mimi lakini ndio ataposimama kuleta zaidi msongamano wa magari katika sehemu hiyo ya mataa barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu mradi wa ujenzi wa majengo na vituo vya polisi. Nilizungumzia suala hili hapa katika Bunge hili Tukufu, nikalizungumzia suala la vituo vya polisi ambavyo havina hadhi na mpaka hivi sasa bado vituo havijawa na hadhi hasa katika Mkoa wa Kusini Unguja. Mkoa wa Kusini ni mkoa mama, Mkoa wa Kusini unajulikana kila kitu kwamba ule mkoa ni mkoa wa utalii lakini vituo vya polisi bado havijawa na hadhi na hili nililiomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tena hii Wizara ya Mambo ya Ndani kwamba Mheshimiwa Waziri anasikia na Mheshimiwa Naibu Waziri nimshukuru kwamba alitembelea huu Mkoa wa Kusini lakini alikwenda akatembelea kuhusu suala la madawa ya kulevya, vile vituo navyo pia kaviona, hali ni mbaya. Vituo vya Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kusini kituo cha Paje bado hakijawa kituo na pale ukatarajia ni msafara mkubwa sana wa gari zinazokwenda kwenye suala la utalii. Wilaya ya Kati Jimbo la Chwaka kituo chao cha polisi wamejitahidi, niwapongeze. Wamejenga kwa nguvu zao wenyewe, hawakusaidiwa na Serikali wala na mtu. Kituo kipo kizuri, kinang’ara na hivi sasa hivi kinafanya kazi kituo kile, hakina wasiwasi. Akamatwe mwanamke kama hivi apelekwe mahabusu basi chumba chake kawekewa maalum cha kwenda kuhifadhiwa, Kituo cha Polisi kile cha Chwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nishukuru kwamba Kituo cha Polisi cha Makunduchi tayari sasa hivi kimeweka foundation, nishukuru. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri kwamba vituo hivi nilivyovitaja hapa ajitahidi katika kuviendesha na katika kutekeleza huu mpango wao waliouweka wa kuhusu utengenezaji wa vituo hivi vya kwenye mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie kuhusu uboreshaji wa maslahi ya askari, maslahi ya askari bado hayajawa moja kwa moja mazuri, yanatoka lakini kuna askari ambao wanapandishwa vyeo, mfano koplo au sergeant, koplo yule anayepandishwa cheo kwenda u- sergeant basi bado maslahi yao yanakuwa yameganda kwenye ule ukoplo, hawajapata maslahi yao mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala nililileta mpaka kwenye swali langu la msingi , lakini bado sikuwa nimejibiwa lolote mpaka sasa hivi. Naomba sasa nilizungumzie hili suala, kwamba maslahi ya polisi wale ambao walikuwa wamepandishwa vyeo, u-sergeant na ukoplo, wafanyiwe haraka maslahi yao wanapopandishwa vyeo vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuwa na mengi, nizungumzie hayo ambayo nimeyaweka ndani ya nafasi yangu na ndani ya moyo wangu kwamba niyatoe leo hapa katika Bunge lako Tukufu, naomba kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa ruhusa yako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uzima na afya hata kurudi tena jioni hii na kuanza kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza napongeza kusainiwa kwa hati tano za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi mfano kushirikishwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye masuala ya kitaifa na kikanda. Suala hili tunashukuru sana kwamba limeondoa kero hizi na sasa hivi hivi tuko katika Muungano wa uhu na haki ambao hauwezi kupingika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu kuratibu masuala ya kiuchumi na kijamii hasa suala hili la TASAF Awamu hii ya Tatu. TASAF Awamu hii ya Tatu kuna jambo hawajalitekeleza na kipindi kile tulichopita walikuwa wanafanya semina kule Zanzibar na wanashirikisha Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi wengine lakini pia walitushirikisha na sisi Wabunge wa Zanzibar tunapewa semina na kupata mafunzo elekezi ili kwenda kuwafanyia wajasiriamali. Kwa hiyo, naomba hizi semina zifanyike tena kwa hii awamu ya tatu na washirikishe viongozi kama vile walivyoshirikisha mwanzo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la mazingira. Kule kwetu katika Mkoa wetu wa Kusini kuna Kijiji kinaitwa Marumbi. Kijiji kile kutokana na tabianchi maji yakajaa hadi kufikia kubomoa makaburi kwa sababu kule wanazikia maeneo pwani. Kwa hiyo, kutokana na tabianchi maji yalipanda juu na kuvunja makaburi yale. Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilichukua hatua lakini sehemu nyingine bado maji yanachimbuka. Kwa hiyo, naomba suala hili lifanyiwe kazi tena na kama kuna uwezekano Mheshimiwa Waziri tuungane twende katika Mkoa wa Kusini Kijiji cha Marumbi akaone hiki nachokiongelea ikiwa ni pamoja na upandaji wa koko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia kuhusu suala la Bodi ya Mkopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Suala la mikopo ya elimu ya juu watoto wetu wanapokuwa wanataka mikopo hili suala linakuwa kubwa na linakuwa zito, wanahangaika kwa kuwaona kwa macho yetu mpaka wakaipata ile mikopo basi wanakuwa wako hoi. Kwa hiyo, naomba Bodi hii ifanye kazi zake vizuri, watoto wanapotaka mikopo ili kwenda kujisomea basi wafanyiwe kiurahisi. Wanapokwenda kule benki wasihangaike wapate pesa zao za mikopo na waende wakafanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa ruhusa yako nami napenda kuongelea katika taarifa hizi mbili za Wizara ya TAMISEMI na Serikali za Mitaa. Kwanza niweze kumpongeza Waziri wangu Mheshimiwa Jafo pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuchika.

Vilevile niwapongeze na Manaibu wake wote aliokuwa nao jinsi wanavyoweza kufanya kazi. Pia nampongeza mama yangu Mary Mwanjwela kwa kuteuliwa kuwa Naibu wangu wa TAMISEMI na Serikali za Mitaa. (Makofi)

MWENYEKITI: Hebu jina likae, vizuri Mheshimiwa Mwantumu. Mheshimiwa Mwanjelwa.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwanjelwa nakupongeza sana, kuwa Naibu wangu wa Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye mchango wangu, kwanza nianze kuzungumzia suala la TARURA. TARURA ni chombo ambacho kinafanya kazi vizuri na wanafanya kazi kwa juhudi kubwa, lakini kila anayesimama hapa anaisifu TARURA. Katika kutembelea miradi yetu, nimeiona TARURA kama kweli inafanya kazi tulipokwenda Mtwara na nimeziona barabara zile za TARURA jinsi zinazofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokiona pale juu ya zile barabara, kuna barabara zimejengwa 2017 tu, lakini tayari zimeshaanza mashimo. Katika kuangalia barabara zile, mimi nahisi yale malori yetu ambayo yanasimama katika barabara, yanamwaga oil. Zikishamwaga oil, zile barabara zinavimba, zinafanya mashimo halafu utaziona zipo kwenye uchakavu, kumbe zile barabara bado zingali mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuogelea katika suala hili napenda Serikali ifanye juu chini kutokana na zile barabara za TARURA na yale malori jinsi yanavyomwaga ile oil waweze kuzifuatilia na kuzifanyia utaratibu kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niogelee katika suala la mradi wa TASAF. Kila ninaposimama nazungumzia mradi wa TASAF, nawapongeza sana kwa sababu wanafanya kazi nzuri na kila siku nikisimama huwa nawaambia big up, maana wanafanya kazi kwa hali na mali, watu wetu ambao waliokuwa wanyonge hivi sasa hivi wana wanajisikia kutokana na TASAF inavyofanya kazi. Wale watu wanapata pesa za TASAF, kisha wanafanya miradi yao na ile miradi yao inaonekana; kuna wengine wana ufugaji wa mbuzi, kuna wengine wanajenga nyumba zao, wanapata kustirika na wengine wanapeleka watoto wao shuleni. Kwa hiyo, naomba sana, TASAF isije ikaondolewa maana tayari ni mkombozi wa wanyonge katika Tanzania yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niogelee pia kwenye suala la uzazi salama; hivi sasa hili neno lazima tuliweke mbele kutokana na watoto wetu. Uzazi salama, watoto wanapokuwa wamezaliwa na wazazi wao tayari wanakuwa wanashughulikiwa na watoto wale kila mmoja anapata haki yake kwa mama yake. Hata hivyo, kuna suala nimeliona kwa macho yangu Dar es Salaam, kuna watoto ambao wanapelekeshwa na wazazi wao, wanakaa pembeni ya barabara na wanatumwa watoto wa miaka minne waje pale kwenye barabara zile, gari zinapokuwa zimepaki, kuja kuomba pesa. Hapa tayari wale watoto wameshakuwa wanaanza kudhalilika, maana wazazi wamekaa pembeni watoto wao ndio wanaotumikishwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye juhudi juu chini, juu ya kazi zao wanazozifanya, maana inaonekana limepungua sana suala lile la ombaomba na kuwatumikisha watoto, lakini bado hili suala linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niogelee katika suala la Bodi ya Mishahara ya Watumishi wa Umma. Bodi hii nimeangalia hapa vizuri tu katika taarifa ya Mheshimiwa Mkuchika kwamba kuna watumishi wa umma ambao wanafanyiwa utaratibu wa mishahara yao wapate kulipwa maslahi yao kiuhakika. Hata hivyo, bado watumishi wa umma wanasikitika hawapati mishahara yao kikamilifu na bado wanasikitika hawajaongezewa mishahara. Mishahara yao bado haijaongezwa na bado inakawia kuingizwa ili wajikwamue kimaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wangu kwa hii leo nilikuwa nataka nijikite katika masuala hayo. Pia nataka kumpongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa jitihada zake anazozichukua hivi sasa kuzungukia mikoa yote na kesho tukijaaliwa tunaambiwa yuko hapa Dodoma. Kwa hiyo, nampongeza sana pamoja na Makamu wake, wanafanya kazi vizuri, waendelee kufanya kazi ili wazidi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Muungano wetu na changamoto. Kwanza ni suala la biashara na ajira katika Taasisi za Muungano, napenda kuishauri Serikali kuhusu masuala haya bandari tuachiwe biashara ndogondogo tupitishe bila pingamizi. Pili, ajira nazo zikitokea kuhusu Muungano tupewe japo kama Tanzania watu kumi basi tupatiwe watu wanne kwa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuhamia Dodoma. Utekelezaji wa zoezi hilo unaimarika Watumishi wa Umma na Taasisi mbalimbali wamehamia Dodoma.

Miundombinu hasa barabara za ndani hasa kama Area D’ barabara ni mbovu mno. Naishauri Serikali yangu izione barabara hizo au TBA nao wanahusika kuhusu hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Naishukuru Serikali kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji ambao unatoa mikopo kupitia vikundi vya vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na makundi mengine. Naomba Mfuko huu uimarike uzidi kusaidia mpango huu hasa kusaidia wanawake ili wajikwamue kiuchumi na kuondoa umaskini na kudhalilika kijinsia pia vijana kupata asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la vita dhidi ya dawa za kulevya. Madawa ya kulevya nchini ni tatizo. Vijana tunaowategemea ndiyo wanaoathirika hapa nchini licha ya Serikali kujitahidi juu ya suala hili bado ijitahidi kupatiwa vituo vya Sober House ili kuwapatia masomo na ujasiriamali waondokane na kadhia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara za vijijini na mjini. Wakala wa Barabara TARURA, ufanisi wao ni mdogo hawajengi barabara za kiwango wanakuwa wanafyeka tu, madaraja mabovu yakipata dhoruba za mvua yanakatika. Serikali sasa inaanza kupata hasara kubwa. Nashauri Serikali yangu Halmashauri ziwasimamie TARURA utendaji wao wa ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyojaa mashiko na mambo yote nasema ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya. Pia namshukuru kuwa na uhai na uzima wa kusimama kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa jitihada kubwa wanazozichukua kufanya kazi zao hizi za Wizara ya Mambo ya Ndani. Naendelea kuzungumzia suala la amani na utulivu na usalama. Wenzangu wengi waliosimama wamezungumzia suala hili lakini kila mmoja kazungumzia kwa mtazamo wake.

Mheshimiwa Spika, mtazamo wangu ninaouzungumzia ni kwamba usalama, amani, utulivu umeimarika, Jeshi la Polisi wanafanya kazi kubwa sana kuhusu suala hili la amani na utulivu. Hivi sasa hatuna wasiwasi wa kwamba nina safari yangu hivi sasa saa tatu nitoke nirande, basi huko njiani labda nitakutana na jambo gani. Unitembea kifua mbele, unakwenda kutoka hapa Dodoma mpaka Dar es Salaam bila ya wasiwasi na tunafika salama salimini Dar es Salaam na magari yanakwenda bila kuzuiliwa. Kwa hili, nalipongeza Jeshi la Polisi liendelee kufanya kazi hii kubwa sana wanayoifanya ili tupate amani na utulivu na tujitanue katika Tanzania yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumzia suala la ujenzi wa makazi na Vituo vya Polisi. Kwa kweli Serikali imechukua jitihada; na sasa hivi nilivyoipitia hotuba hii, inazungumzia kwamba kila mkoa utajengwa nyumba ishirini ishirini.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli sisi Mkoa wetu wa Kusini kuna nyumba pale Paje na kuna baadhi ya nyumba zile nne pale tayari zilishakuwa zinakalika na nyingine bado kidogo kupauliwa. Nasema hivi, nyumba zile ziendelee kuboreshwa ili Polisi wapate kukaa vizuri waweze kufanya kazi zao vizuri na hasa ukizingatia ukanda ule ni wa watalii. Hili nalizungumza kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado vituo havijakarabatiwa. Kwa Mkoa wetu wa Kusini kuna vituo baadhi tu; kuna Kituo cha Dunga tayari kiko kinajengwa, kuna Kituo cha Chwaka tayari kinafanya kazi; lakini kuna baadhi ya vituo bado havifanyi kazi vizuri, havijakarabatiwa ukaridhika Polisi wako katika mazingira mazuri juu ya vituo vile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Makunduchi wameweka foundation toka 2015, foundation ile mpaka leo bado haijapata msaada wowote. Serikali haijaweza kuinyanyua ili kile kituo kiendelee kiwe cha kisasa. Bado Serikali, juu ya jitihada zake inazozichukua lakini bado haijafikia malengo hasa tunayoyataka.

Mheshimiwa Spika, nasema Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake waifanye hii kazi hasa kwa Mkoa wangu wa Kusini na huu mkoa ni mkubwa sana, maana mkoa huu ni mkoa wa watalii. Watalii wote wanapokuja Kusini Unguja, basi lazima wafike Chwaka, Paje, Makunduchi, Jambiani, kote huko kuna vikazi vyao vya kupita wakienda wakafanya utalii wao.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mafao ya polisi na mahitaji yao ambayo polisi wanapokuwa tayari wameshapandishwa vyeo, basi polisi anapandishwa cheo na anakaa muda mrefu bado hajapata stahiki yake inayotakiwa. Hili nimeshalizungumzia mpaka katika swali langu la msingi, nikazungumza kwamba mafao ya polisi ni bado, polisi wanalalamika mafao bado hawajayapata.
Mheshimiwa Waziri …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwantumu Dau.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, Mheshimiwa Waziri anapokuja hapo aje atuambie kuhusu habari ya mafao ya polisi, maana alisema mpaka mwezi wa Tano itakuwa tayari hapa. Kwa hiyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakulima vijijini wanapata tabu sana kuhangaika kulima chakula chao, matokeo yake hawafanikiwi kutokana na wanyama kuingia mashambani wakavuruga mazao hayo, jambo ambalo linawarudisha nyuma kuendelea na harakati zao za maendeleo. Napenda kuishauri Serikali kuwa, wafugaji wanaofanya vitendo hivi wachukuliwe hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za jamii kama elimu; Serikali inatekeleza kikamilifu mafanikio ya elimu licha ya juhudi za Serikali wanazozifanya, kuna watu wachache wanarejesha nyuma Serikali yetu hasa uvujaji wa mitihani nchini. Kuna sehemu mitihani ilichelewa kufanywa, nishukuru Serikali yangu kwa jitihada zake, mithani imeendelea kufanywa, lakini napenda kuishauri Serikali suala hili waliangalie kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira na vijana; nguvu kazi za vijana ni muhimu sana kuwezeshwa nchini, asilimia yao wanayopata wanaifanyia kazi kubwa lakini changamoto zao katika kazi zao ni kwamba hawana soko madhubuti la kuuza vitu vyao. Sasa basi, naomba Serikali Tukufu ilione suala hili na iwapatie soko la uhakika ili waondokane na tatizo hili . Sasa nimpongeze Waziri Mkuu na watendaji wake kwa jitihada nasema asanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya wakati huu. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kunirejesha tena kwa mara ya pili katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikupongeze wewe maana kipindi kile tulikuwa pamoja tumefanya kazi pamoja, pamoja na Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze na Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteua na kuniamini na kunirejesha tena katika Bunge hili Tukufu. Kwa kweli tushukuru Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mfupi, tuna mengi ya kusema, lakini tutapopata ndio tumefanikisha. Mpango huu umefika kwa wakati muafaka na Mpango huu mambo yake mengi yaliyokuwamo humu yamejikita pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais, yameendana pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kuchangia kuhusu Mpango huu, kwanza huu Mpango nataka kusema umefika wakati muafaka na hili suala langu ambalo ninalolitaka kulisema hapa hivi sasa na suala hili la muda mrefu na suala hili linanikereketa, nikienda nikirudi bado lipo ndani ya nafsi yangu, lakini hivi sasa hivi nataka kulitoa katika Mpango ambao uliofika hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu sehemu ya Muungano, sehemu ya Muungano kuna magereza ya Zanzibar pamoja na magereza ya Bara. Magereza ya Zanzibar na magereza ya Bara, magereza ya Bara yanafanya kazi kwa wakati wake na magereza ya Zanzibar yanafanya kazi kwa wakati wake. Naomba kwa Mpango huu ili kuunganisha huu Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, je, haiwezekani magereza haya yakaweza kuunganishwa, ikawa kitu kimoja kama ilivyo Polisi na Jeshi? Hilo lilikuwa linanikereketa na leo hii limefika mahali pake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kuhusu suala la afya; suala la afya na wagonjwa na sukari, shinikizo la damu pamoja na pressure. Magonjwa haya yametawala nchini, yako mengi, haya magonjwa hayaambukizi, lakini ni magonjwa sugu, yanaumiza na wala hayana dawa. Maana kuna wenzetu ambao wamepata maradhi haya wanyonge, maskini, hawana kipato cha kuweza kujiwezesha ili kujitibu magonjwa hasa shinikizo la damu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa una sukari, ukiambiwa usile hiki, usile hiki unaweza ukapona, ukaifuata miiko yake, lakini shinikizo la damu gumu. Kwa hiyo naomba Mpango huu pamoja na Serikali yangu iweze kuwaona wagonjwa hawa wa sukari, pressure pamoja na shinikizo la damu ili wawezeshwe wapate dawa za kuweza kujitibu ili waendelee na wao kufanya kazi zao kama tunavyozifanya hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu Chuo cha Hombolo; hiki chuo kizuri nilikwenda nikakitembelea, kizuri sana na kina mambo yote ya sayansi na teknolojia. Hata hivyo, hiki chuo kiko mbali. Sasa umbali wake ni nini? Ni kuhusu barabara ya kuendea Hombolo kwani ni mbovu, chafu, haifai. Naomba barabara ya Hombolo kwa Mpango, Mwenyezi Mungu akatujalia, basi barabara ile mwaka huu iwezeshwe, itengenezwe ili watoto na siye tuweze kuwapeleka kule ili waweze kwenda kusoma katika kile Chuo cha Hombolo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia kuhusu suala la ukosefu wa nyumba za askari; ukosefu wa nyumba za askari ni mkubwa hasa kwa Mkoa wetu wa Kusini, Mkoa wetu wa Kusini una wilaya mbili, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini, lakini Wilaya ya Kusini ni mkoa bora, ni mkoa mama ambao unaweza kuchukua watalii wakawa wanakwenda kutalii katika wilaya ile, lakini nyumba za askari hakuna na wala hawana mahali pa kukaa, wanahangaika hangaika isipokuwa kituo kidogo kipo Paje, pale kidogo lakini Jambiani hakuna Kituo cha Polisi, naomba napo kiende kikajengwe kituo cha polisi…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kengele imeshagonga.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: …ili na wao waweze kujisikia. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWANTUM DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, kuna suala la watu wenye ulemavu na wanawake na vijana ambao bado hawajitambui kuhusu vikundi na asilimia kumi na mikopo ya VICOBA. Mikopo yao hawawezi kurejesha marejesho katika Halmashauri zao, wanajisahau na kupelekea madeni makubwa kwenye mabenki na Halmashauri kukaa na madeni hayo kwa kweli hili lionekane na Serikali, lakini pia naishauri Serikali ifanye juu chini iwafanyie semina au mafunzo kwenye Halmashauri zao ili wajue nini maana ya mikopo na wajue kuwa kuna wenzao wanasubiri pesa ile ya marejesho.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la walemavu huwa hawataki kukaa vikundi kutokana na matatizo yao ya kuwa wako mbali mbali kukutana inakuwa vigumu, kwa hiyo asilimia mbili hii inakuwa haina kazi kubwa katika Halmashauri zao.

Mheshimiwa Spika, vilevile watu wenye ulemavu hawana ushauri kuhusu Corona, bado hawafahamu kitu wapowapo tu. Kwa kweli hili Serikali ilitambue na kuwapatia ufahamu walemvu.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la vijana na kuhusu ajira; vijana wengi hawajui kuhusu ajira, wanakwenda wapi vijana, wanazurura zurura vibaya huko nchini. Serikali ilione hili na ajira zikitoka zinakuwa kidogo, wasaidiwe vijana hao.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la madawa ya kulevya pamoja na jitihada zake bado hili janga la madawa lipo, vijana wanateketea Serikali ichukue jitihada kubwa ili liondoke kabisa.

Mheshimiwa Spika, sasa nimpongeze Rais wangu Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli kwa jitihada zake anazoendelea kuzifanya nchini pamoja na watendaji wake wote wana chapa kazi kweli.

Pia nikushukuru wewe Spika kwa jitihada zako unavyolisimamia Bunge tukufu, kwa kweli wewe ni mfano wa kuigwa. Nimshukuru Waziri Mkuu kwa umahiri wake wa kazi zake anazozifanya kwa kweli yeye ni mfano wa kuigwa pamoja na Mawaziri wenzake wote wanachapa kazi kweli.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuleta maoni yangu niloyaona, ahsante na naomba kuwasilisha.