Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwanne Ismail Mchemba (40 total)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye kutia matumaini makubwa, naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara hizi zimeathirika kiasi kikubwa wakati huu wa mvua ambazo zimenyesha kwa wingi na kwa kuwa mpaka hivi sasa barabara hizo hazipitiki, je, Serikali iko tayari kutengeneza sehemu korofi ili usafiri uendelee kama ilivyokuwa zamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza kwamba vijana wetu wa TANROADS pamoja na Mameneja wa TANROADS Mkoa hivi sasa waelekeze nguvu katika kufungua mawasiliano kwa sehemu zote zilizoathiriwa na mvua. Hii ikiwa ni pamoja na barabara hii ya Nyahua - Chaya ambayo imekatika kwa kipindi kirefu kidogo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, humu ndani maswali yote huwa yanaelekeza nyumba za Polisi. Je, Waziri anasema nini kuhusu nyumba za Askari Magereza hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia tuna tatizo la upungufu wa nyumba katika Jeshi la Magereza. Kama ambavyo ipo katika Jeshi la Polisi, pia iko programu ya ujenzi wa nyumba ambazo zinakwenda sambamba na hizi za Polisi, kwenye Polisi tuna nyumba 4,136 na Magereza tuna nyumba takribani 9,500 kama nitakuwa sijakosewa sawasawa takwimu zake. Kwa hiyo, tunatambua hiyo changamoto na zipo katika hatua nzuri tu za utekelezaji naamini kabisa katika kipindi cha miaka mitano hii, tutaanza kuona miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba hizi pindi mipango ya upatikanaji wa fedha na taratibu za kifedha kupitia Hazina itakapokamilika basi nyumba za Polisi na Magereza kwa pamoja zitakwenda sambamba.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa nchi ya Tanzania ilikuwa koloni la Mwingereza na hivyo kuwa na mahusiano mazuri mpaka hivi sasa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuishawishi sasa Serikali ya Uingereza ili waweze kurejesha huduma hiyo hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huu mpya wa Serikali ya Uingereza ni wa duniani kote, siyo kwa Tanzania tu. Kwa hiyo, siyo kwamba ni sisi pekee ndio tumebanwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimweleze tu kwamba kuhamishwa kwa Kituo cha Kuchakata Visa za Uingereza kwenda Pretoria nchini Afrika Kusini hakujaathiri utoaji wa visa. Sana sana kinachotakiwa kwa sasa ni kwamba ujipange mapema, ufanye maombi mapema, lakini kimsingi muda umebaki vilevile, gharama ni zile zile. Kwa hiyo, wao walichofanya ni kupunguza gharama zao za kuchakata visa kwa kuhakikisha kwamba wanaipa Kandarasi Kampuni ya Tele-Performance, badala ya wao wenye kufanya hiyo kazi. Kwa hiyo, namhakikishia tu kwamba hakuna madhara makubwa ambayo yametokea kwa sababu hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Naibu Waziri amesema kwamba watumishi ambao wameajiriwa na ushirika huo wanapewa semina mbalimbali za kitaalamu na kwa kuwa kama tunavyofahamu suala la hesabu kwa nchi yetu ni tatizo, hawajui hesabu, je, Serikali inajua kwamba mpaka hivi sasa wanunuzi wa tumbaku ambao wamejitawala wanadaiwa na wakulima shilingi bilioni 14 za mwaka 2014/2015 ambazo hawajalipwa mpaka sasa? Je, Serikali inasemaje kufuatilia suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mpaka hivi sasa soko la mwaka huu halijaanza, linasuasua na unapochelewa kupima tumbaku maana yake unapunguza kilo za tumbaku. Je, Serikali inasema nini kufuatilia suala la soko la tumbaku kwa sasa hivi ili liweze kukamilika kwa muda muafaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama anavyosema kwamba wakulima wa tumbaku wa Tabora na wa mikoa mingine wanadai fedha nyingi, wanawadai vyama vya ushirika pamoja na wanunuzi wa tumbaku. Serikali imekuwa ikiendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba fedha hizi zinalipwa. Tayari mafaili ya watu waliohusika na ubadhirifu mkubwa katika Mkoa wa Tabora yameshawasilishwa Polisi taratibu nyingine ziendelee ili wahusika waweze kupelekwa mbele ya sheria ikiwezekana wakulima waweze kupata fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu soko la tumbaku, ni kweli kama Mheshimiwa alivyosema kwamba suala la soko la tumbaku bado linasuasua na Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya njia mbalimbali ili kuhakikishia wananchi kwamba soko halitapata shida. Jitihada hizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanapatikana wanunuzi wengine wa tumbaku ili kuondoa ukiritimba wa wanunuzi wachache ambao mara nyingi wao ndiyo wanaoamua bei lakini vilevile wao pekee ndiyo wanaendesha soko la tumbaku. Tunaamini kwamba wanunuzi wengine wakipatikana itaondoa tatizo hili na italeta ushindani na hivyo kuondoa tatizo katika bei na soko la tumbaku.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishaahidi kwamba tukitoka kwenye Bunge hili tutaenda Tabora na maeneo mengine kwa wadau wa tumbaku tujadiliane namna bora ya kuboresha zao la tumbaku. Nimhakikishie tu kwamba pamoja na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kuhama, ambaye ndiye aliyetoa ahadi, ahadi ile ilikuwa ni ya Wizara na iko pale pale. Niwahakikishie tu kwamba tukimaliza bajeti Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ataelekea Tabora kwa ajili ya kwenda kuongea na wadau kuhusu masuala ya tumbaku.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa ongezeko la ajira kwa watoto wadogo ni kubwa sana hapa nchini; na kwa kuwa tatizo hilo kuchangiwa na kuvunjika kwa ndoa kwa kutokuwa na msingi na kuachiwa akina mama kulea hao watoto. Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka kuleta mabadiliko ya sheria ya mwaka 1971 ili wanawake na watoto hawa waweze kupata haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa TASAF III imeonesha mpango mzuri sana na mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwenye mashamba makubwa watoto hao wapo wengi na wanaonekana kama vile kwenye mashamba ya tumbaku, kahawa, chai, pamba na kadhalika, je, Waziri yuko tayari kuwakusanya hawa watoto na kuwapa elimu ya kutosha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa swali lake la kwanza kuhusiana na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, bahati nzuri suala hili limekuwa likizungumzwa katika nyakati mbalimbali na hata katika Bunge hili na Mkutano huu wa Tatu, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria amelisemea sana, lakini vilevile Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto pia ameweza kulizungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kurudia kwa mara nyingine tena, ni kweli sheria hii ilionekana kuna upungufu. Ukiangalia viko baadhi ya vifungu vinavyoruhusu masuala mazima ya ndoa za utotoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kutambua kwamba katika masuala haya ya ndoa kuna mkanganyiko wa masuala ya kimila na kidini, ikaonekana kwamba ni vema suala hili likapatiwa suluhu kwa kupata maoni ya wananchi wengi zaidi kupitia mchakato wa White Paper. Mwanzo wakati zoezi hili Wizara ya Katiba na Sheria ilipotaka kulianza, taratibu zote karibia zilikuwa zimeshakamilika, lakini ikawa imeingiliana na mchakato wa Mabadiliko ya Katiba. Ikaonekana itakuwa si wakati mzuri kuwachanganya wananchi, huku wanatakiwa watoe maoni kuhusiana na Katiba Mpya lakini wakati huo huo unawapelekea zoezi lingine kuhusiana na marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Vilevile ilionekana kwamba huenda wakati ule kwenye kukusanya maoni ya Mabadiliko ya Katiba wananchi wangeweza kulisemea jambo hili lakini kwa kiasi kikubwa halikusemewa sana. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria bado wanasubiria wakati mzuri zaidi wa kuweza kulipeleka lakini ni lazima liende kupitia Waraka wa Maoni kupitia White Paper.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwa watoto ambao wamekuwa wakifanya ajira mbalimbali za utotoni, niseme tu kwamba kupitia Wizara ya Kazi kwa Mheshimiwa Jenista, wamekuwa wakifanya kazi hii na wanaendelea kufanya kazi hii kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wako katika ajira za utotoni wanaelimishwa, lakini zaidi kuhakikisha kwamba wazazi wao wanapewa elimu hii. Ndiyo maana kupitia TASAF kama nilivyoeleza, nichukulie tu kwa upande wa Zanzibar, zaidi ya watoto laki moja na mbili wamekuwa wakinufaika na ruzuku hii ili kuwawezesha kwenda shule.
Kwa hiyo, ni imani yangu bado kupitia Serikali kwa ujumla wake na mipango mbalimbali na TASAF ikiwemo tutahakikisha tunatoa elimu hii, lakini vilevile kuona ni kwa namna gani watoto wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo. Nakushukuru.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi name niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la Mwanza linafanana na tatizo la Tabora Manispaa, Kata ya Malolo na mpaka sasa hawajalipwa fidia ya aina yoyote na wakati huo huo Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliwahi kufika na kutoa agizo. Je, Serikali inasemaje kuhusu kulipa fidia ya hawa wakazi wa Kata ya Malolo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama nilivyosema katika majibu ya awali ambayo nilikuwa naongezea kwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI), nimesema Wizara imejipanga katika kupitia; kwa sababu tumekusanya madai haya au migororo na fidia anazozisema mengi yako katika ile orodha tuliyoichukua. Kwa hiyo, tutakachofanya sisi ni kukumbusha taasisi zinazohusika na fidia hiyo ili waweze kulipa, kwa sababu ni nyingi kweli zimekaa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna namna nyingine ya kufanya kwa sababu Serikali haiwezi kulipa fidia ambayo inadaiwa taasisi au maeneo mengine tofauti. Kwa hiyo, tutakachofanya sisi ni kupeleka kumbukumbu za kuwakumbusha wahusika na pale ambapo Serikali inahusika yenyewe basi itajipanga namna ya kuweza kuilipa.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo. Kwa kuwa matatizo ya Wilaya ya Nkasi yanafanana na matatizo ya Mkoa wa Tabora na kwa kuwa nyumba za Polisi na Magereza za Mkoa wa Tabora ni mbovu sana ikiwa ni pamoja na miundombinu ya vyoo. Pamoja na kipaumbele katika Mkoa wa Tabora yuko tayari twende naye kwa gharama zangu akaone hali halisi ya vyoo?
NAIBU WAZIRI WA MAMABO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari lakini siyo kwa gharama zake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri nilikuwa na ratiba ya kutembelea Tabora pamoja na Rukwa katika kipindi hiki kwenye ile ziara yetu pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotokea huko kwenye kambi za makazi ya waliokuwa wakimbizi. Basi tutaunganisha ziara hiyo weekend moja kabla hatujaondoka Dodoma, tuwasiliane baadaye kwa ajili hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wengi wamejitolea kujenga maboma ambayo wamejitolea kujenga zahanati, nyumba za Walimu na mpaka sasa halmashauri hazijaweza kukamilisha. Je, ni lini sasa Halmashauri zitakamilisha miradi ambayo ni viporo ambavyo wananchi wameweza kujenga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maboma ni mengi na kumbukumbu yangu kati ya tarehe 12 na 13 nilikuwa kule Tabora katika Mkoa wako na nishukuru sana ushirikiano wako japokuwa ulikuwa na changamoto za kuuguliwa. Katika kupita huko huko katika Mkoa wa Tabora lakini na mikoa mingine tatizo la maboma limekuwa ni kubwa ndiyo maana katika maelekezo yetu tumeagiza kwanza lazima tumalize vile viporo vya mwanzo. Kama maboma ya ujenzi wa zahanati, nyumba za Walimu lazima tumalize hilo kwanza.
Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana mtaona katika maelekeo ya bajeti yetu itakayokuja ya mwaka mwingine wa fedha unaokuja, tutahakikisha suala zima la maboma sio suala katika sekta ya elimu peke yake hali kadhalika katika sekta ya afya tumalize hayo halafu ndiyo tuweze kuanza upya. Haiwezekani wananchi wamefanya nguvu kubwa za kutosha halafu nguvu zikapotea bure; Serikali imeliona hilo na ndio maana tuna mpango mkakati mpana sana kuondoa kero hiyo katika Jamhuri yote ya Tanzania.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali madogo ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa ugonjwa huu ni wa kitaalam zaidi na kwa kuwa elimu yake haijatolewa kikamilifu; je, Serikali iko tayari kutoa elimu kwenye vituo vya afya, zahanati na Wilaya wanapohudhuria kliniki wakina mama. Kwa sababu waathirika wakubwa ni wakina mama, je, Serikali inasema nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa ugonjwa huu dawa zake zina gharama sana, je, Serikali iko tayari kuzitoa dawa hizo bure ili akina mama na wananchi wote waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu elimu Serikali tayari inatoa elimu kuhusiana na ugonjwa wa sicklecell na magonjwa mengine yote kwa kina mama kwenye kliniki ya uzazi pindi akina mama wanapokwenda kuhudhuria, aidha wao wenyewe kwa mahitaji yao mbalimbali ama watoto wao walio chini ya umri wa miaka mitano, kwa hiyo, elimu inatolewa.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa kwenye kutoa elimu ipo kwenye kutoa elimu kwa vijana ambao wanatarajia kushika mimba siku za usoni. Changamoto hii ni kwamba bado katika nchi yetu hatubajeti sana fedha kwa ajili ya kinga zaidi kwa kweli tunatumia fursa ya kliniki na watu wanaokwenda hospitalini ama fursa ya shule kutoa elimu ya afya kwa umma, kama tungepata fursa ya kibajeti ya kuweza kufanya hivyo tungeweza kufanya.
Sasa tunashirikiana na wadau mbalimbali kama Chama cha Kitaifa cha Sickle Cell ambacho kinatoa elimu nchi nzima kuhusiana na ugonjwa huu, pia kuna taasisi ya utafiti iko pale Muhimbili nayo inatoa elimu kwa umma nchi nzima kuhusiana na ugonjwa huu. Kwa vijana ambao wanatarajia kwenda kujifungua ama wanapata mwenza ni vema wakapima kama wao ni carriers wa sickle cell ama laa. Kwa sababu carrier wa sickle cell akiona na carrier wa sickle cell wakashika mimba maana yake mtoto ana hatari ya asilimia zaidi ya 25 ya kupatwa na ugonjwa huu kama homozygous yaani kuwa na sickle cell ambayo imekomaa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na gharama za matibabu ya sickle cell hapa nchini, ugonjwa wa sickle cell napenda kumpa taarifa yeye, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba ni miongoni mwa magonjwa ambayo kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Taifa ya mwaka 2007 ugonjwa wa sickle cell unatibiwa bure. Tiba ya sickle cell ni bure kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya, sasa hivi kuna taasisi imetufuata inataka kutekeleza huo mradi wa kutoa elimu kwa umma nchi nzima ili kuwa-screen watu wote wajue hali zao kuhusiana na sickle cell kama wao ni carrier ama siyo carriers.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Mlele linafanana sana na tatizo la Tabora Manispaa, Uyui pamoja na Kaliua, je, Serikali inasema nini kuhusu kukamilisha au kuandaa mpango wa kukamilisha hospitali ambazo hazipo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, Serikali kama tulivyosema kipaumbele chake ni kuhakikisha huduma ya afya inapatikana na ndiyo maana siwezi ku-disclose
information zote, lakini kuna juhudi kubwa sana inafanyika lakini kiukweli ni kwamba kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kwanza kipaumbele cha kwanza kinawekwa na Halmashauri, japokuwa mnajua kwamba katika suala zima la cealing ya bajeti wakati mwingine ile cealing ikishaondoka vipaumbele vingine vinakwama, lakini tutaangalia jinsi gani tutafanya, lengo letu kubwa ni kwamba wananchi katika kila
maeneo waweze kupata huduma. Na ndiyo maana tunafanya harakati mbalimbali kufanya marekebisho makubwa katika sekta ya afya lakini imani yangu ni kwamba tutafika mahali pazuri tutasimama vizuri. Kwa hiyo wananchi, ndugu zangu wa Tabora ambao wengi ni watani wangu naomba msiwe na hofu kwamba Serikali yenu iko nanyi kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa mazuri.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wananchi wengi
wamekuwa waoga kwenda kwenye kituo cha polisi hususan wanawake na kwa kuwa maeneo mengi hayana vituo vya polisi hususan vijijini. Je, Serikali iko tayari sasa kugatua madaraka kwa Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili waweze kupata matibabu pale wanapopata ajali?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuona uhalisia unaotokea kwenye grass root. Niseme tu tumepokea wazo hilo, itabidi tuongee na wenzetu wa TAMISEMI kwa sababu likiamuliwa kufanyika katika msingi huo kuna vitu ambavyo lazima tujiridhishe navyo na aina ya maumivu ambayo yanaweza yakatumika kwenye ngazi ya viongozi wetu wa Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu ambacho huwa tunakiepusha na kulazimisha ipitie polisi hasa ni kwa wale ambao wanaweza wakafanya makosa makubwa kwa mfano, mtu aliyeenda kuiba akawa amejeruhiwa angetamani sana asipitie polisi aende moja kwa moja hospitalini. Kwa hiyo, huwa tunaona apitie polisi na wale
wengi wanaokwepa kupitia polisi tunakuwa tunajua watakuwa wana vitu wanavyovihofia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa vitu ambavyo
vimefanyika katika ngazi ya familia labda mtu amepata ajali ya kawaida katika ngazi ya familia ama katika eneo na anafahamika, ana kumbukumbu nzuri za kutokuwa na vitendo vya kihalifu ni maeneo ambayo tunaweza tukaongelea tukaenda katika taswira hiyo aliyoisemea Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kituo cha afya cha Manonga jengo lake la upasuaji limekamilika; na kwa kuwa mpaka sasa hakifanyi kazi, je, Serikali ni lini, itapeleka vifaa vya upasuaji katika kituo hicho cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna tatizo katika kituo cha afya cha Manonga, pia tulikuwa na tatizo hili katika vituo vya afya mbalimbali ambapo tulivijenga kupitia mradi wa ADB, bahati nzuri tumepata mafanikio katika Mkoa wako katika kituo cha afya cha Itobo na Bukene vimeshaanza kufanya kazi, Manonga pale vifaa vilikuwa bado havijakamilika. Hivi sasa tunaendelea kuangalia ni jinsi gani tufanye kwa sababu pale kulikuwa na mapungufu ambayo yalijitokeza huku, katika suala zima mchakato wa ujenzi ule kuna mambo mengine hayakwenda sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inalichukua hili tuangalie nini tufanye ili kituo cha afya cha Manonga kiweze kukamilika vizuri kuwa na vifaa pale na wananchi wa eneo lile wajisikie kwamba wana viongozi wao Mbunge wao Mheshimiwa Mwanne Mchemba na Mheshimiwa Gulamali wanawawakilisha huku. Sasa Serikali tumelichukua hili kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ajali hizi za wanaoendesha vyombo vya moto ni nyingi sana hapa nchini, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kila anayehitaji leseni anakuwa na bima ya afya ili waweze kurahisisha matibabu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mchemba kwa concern hiyo ya vijana wetu, tumelipokea kama Serikali na tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Afya. Lakini kubwa si kwa anayehitaji leseni, tunaongelea kwa wale ambao wanafanya ile shughuli yenyewe. Kwa sababu kwenye leseni kuna kuwepo na vitu vya aina mbili, kuna yule anayemiliki na kuna wale wanaoendesha ambao ndio wamekuwa wakipata zaidi ajali kuliko wale wanaomiliki bodaboda zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na viongozi wa vijiwe hivi tumeendelea kuwaelekeza kwamba wahakikishe katika makundi yale wanatambuana wale wanaohusika na akiongezeka ambaye hayuko kwenye kijiwe chao na hawajui kuhusu leseni zao, nao wachukue wajibu huo kwa sababu kwa kweli ni jambo ambalo linatoa ajira, lakini limekuwa likitugharimu sana maisha ya vijana wetu hawa wanapofanya kazi hizo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Wilaya ya Uyui tayari ina eneo kubwa ambalo wawekezaji wanaweza wakalitumia. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapeleka wataalam kuhakikisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wawekezaji wengi hapa nchini hukiuka maandiko au mikataba wanayoingia na Serikali. Je, Serikali iko tayari sasa kuipitia upya ile mikataba na kuivunja kabisa mikataba ambayo wameingia hapa nchini kwa mfano Kiwanda cha Manonga na Kiwanda cha Nyuzi? Je, Serikali inasema nini? Je, Waziri yuko tayari sasa kwenda kuviona viwanda hivyo jinsi walivyoviharibu? Naomba majibu. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Uyui, kwenye kongamano nililolisema ambalo analisimamia Mkuu wa Mkoa na Meneja wa Tan Trade na mimi nitakuwepo. Kwa hiyo, nitakwenda Uyui na wataalam tutaangalia hali itakavyokuwa na tutaweza kuwashauri namna ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si wawekezaji wote wanakiuka, mmoja anayekiuka umlete tutamshughulikia, ni case by case. Wawekezaji si wabaya, wawekezaji ni wazuri lakini yule anayekiuka tutamshughulikia kulingana na tukio lenyewe.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yamekidhi lakini naomba niongeze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Tabora una historia nyingi sana ukizingatia pia na historia ya Baba wa Taifa, lakini wakati anajibu majibu yake Baba wa Taifa hakuwepo, hawakuongeza, kwa hiyo, niombe Wizara ya utalii iongeze kuitangaza historia ya Baba wa Taifa.
Lakini lingine kuna historia ya miembe ambayo ina umri wa miaka 100 nayo ipo kwenye njia ya watumwa. Kwa hiyo niombe niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa hivi sasa njia ya utmwa inatambulika, je, Serikali iko tayari kuikarabati ile njia kutoka Tabora hadi Kigoma - Ujiji ili iwarahisishie watalii kupita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine, je, Serikali iko tayari kuwatuma wataalam kuhakikisha vivutio vyote ambavyo vipo katika Mkoa wa Tabora vinaorodheshwa? Ukilinganisha na mapato yaliyopatikana tangu 2013 mpaka 2017 ni milioni mbili, milioni mbili kuna nini? Kwa hiyo nasema kwa uchungu kwamba bado tunahitaji utangazaji wa utalii kwa Mkoa wa Tabora ni muhimu sana naomba izingatiwe, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukarabati hii njia ambayo inatoka Tabora hadi Kigoma hili tutalifanyia kazi, tutaangalia kadri upatikanaji wa fedha utakavyokuwepo katika bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, kuhusu kuorodhesha vituo, ni kweli kabisa Tabora ina historia ndefu sana ikiwa ni pamoja na hiyo aliyoisema ambapo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliweza kusoma katika Mkoa ule na mambo mengine mengi na mimi mwenyewe nimefika katika yale maeneo, nimetembelea na nimeyaona. Kwa hiyo orodha tuliyonayo ni kubwa na tutaendelea kuifanyia kazi, kuiuhisha ili tuweze kuongeza mapato yatokanayo na utalii katika Mkoa huu wa Tabora.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na jitihada zote zinazofanywa na Serikali kutatua tatizo la makazi ya askari. Je, kwa kipindi hiki cha 2017/2018 Mkoa wa Tabora umetengewa kiasi gani?
Swali la pili, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Congo na kwa kuwa hivi karibuni pia wamesema kwamba baadhi ya wakimbizi wale wametawanyika katika Mkoa wa Kigoma inawezekana wakaja na Mkoa wa Tabora. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwanne Mchemba kwa swali lake zuri la pili la nyongeza kutokana na changamoto ya mfumuko wa Wakimbizi ambao wanaingia nchini kutoka DRC hasa kutoka katika maeneo ya Kivu kutokana na changamoto ya hali ya usalama nchini DRC. Kabla sijatoa ufafanuzi wa swali lake hilo la pili nimjibu kwamba kwa bajeti ambayo nimeizungumza ya maendeleo ambayo nilisema ni takribani bilioni 12.3 ya mchanganuo mbalimbali ikiwemo shilingi bilioni 7.2 ya Magereza ni fedha ambazo zimetengwa kwa maendeleo nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Jeshi la Magereza hakuna utaratibu wa sub vote kwenye Jeshi hilo ingawa Jeshi la Polisi ipo lakini kwa ujumla kwa mwaka huu wa fedha hakuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya mradi wa maendeleo kwa Tabora specifically, lakini kwa sababu tunatambua kwamba kuna maeneo mengi nchini ambayo kuna majengo mengi ya Polisi ambayo yapo katika hatua za mwisho kukamilika, kwa mfano, kule Mtambaswala
- Mtwara, Njombe, Mabatini Mwanza, Musoma na kadhalika, kwa hiyo fedha hii ya maendeleo mwaka huu tunataka tuilekeze katika majengo ambayo tayari yapo katika hatua za mwisho kukamilika kabla hatujaanza miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii sasa kuweza kuzungumzia hoja yake ya pili muhimu ya wimbi la wakimbizi kutoka DRC. Mpaka hivi naomba nitoe taarifa rasmi kwamba Wakimbizi ambao wametoka DRC kuingia nchini tokea Januari wanakadiriwa kufika zaidi ya 2,500 na katika hao takribani wakimbizi 1,960 tayari wameshakuwa wamehifadhiwa katika Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu na wengine 300 na zaidi wapo kwenye vituo vya kupokelea Wakimbizi. Changamoto ambayo amezungumza ya kwamba kuna baadhi ya wakimbizi ambao wamekuwa wana desturi aidha ya kutoroka kwenye makambi kutoka DRC na kuingia mitaani ama kupita njia za panya kuingia nchini kwetu kwa kisingizio cha machafuko DRC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe kauli ifuatayo, jambo la kwanza nataka nitoe angalizo ama onyo kali kwa wakimbizi kama hao kuacha desturi hiyo. Tumeshatoa maelekezo katika vyombo vyetu vya usalama nchini kuhakikisha jambo la kwanza kwa Idara ya Uhamiaji kuendelea kufanya msako kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, ikiwemo Jeshi la Polisi hasa katika Mkoa wa Kigoma ambao una changamoto kubwa sana ya wakimbizi, hii inadhihira na takwimu ambavyo zipo kwa mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, takribani asilimia 30 ya wahamiaji haramu waliokuja Tanzania wametokea katika Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, tumewekeza nguvu nyingi sana katika Mkoa wa Kigoma kuhakikisha kwamba inadhibiti wimbi la wahamiaji haramu kuingia. Vilevile tumetoa maelekezo kwa Idara ya Wakimbizi ambayo ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha kwamba inafanya uhakiki na kuimarisha ulinzi katika makambi yetu hasa Kambi ya Nyarugusu ambayo ndiyo kambi ambayo inapokea wakimbizi kutoka DRC ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao watakiuka sheria na utaratibu wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ya wakimbizi kwa kushtakiwa ili baadaye sheria ichukue mkondo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na swali lake la pili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Busega linafanana na tatizo la Mkoa wa Tabora, hususan Tabora Manispaa; na kwa kuwa tuna bwawa la Kazima ambalo kina chake ni kifupi: Je, Serikali ipo tayari sasa kukarabati bwawa hilo ili tuweze kupunguza tatizo la maji Mkoa wa Tabora hususan Tabora Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la Kazima lilijengwa mwaka 1946 na bwawa hili lilijengwa na watu wa reli kwa ajili ya kupata maji ya kupoza engine zile ambazo zilikuwa zinatumia mkaa. Mwaka 1990 matumizi yalibadilika baada ya kupata engine ambazo zinatumia diesel, kwa hiyo, ikaamuliwa bwawa hili liwe linatumika kwa ajili ya maji ya kunywa. Sasa hivi linamilikiwa na Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Tabora (TUWASA) na linazalisha lita milioni 1,400 ya maji safi na salama kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka imeomba shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha lile tuta kwa sababu mwaka huu maji yalijaa sana, lakini pia lipo shirika linalohudumia maeneo ya Lake Tanganyika. Mamlaka wameomba ili waweze kulikarabati lile bwawa liendelee kuhimili kuweka maji mengi na kuendelea kuwahudumia wananchi wa Tabora. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwanne nikuhakikishie kwamba suala hili linafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba bwawa hili linakarabitiwa.
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naitwa Mwanne Ismail Nchemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tatizo la Wakimbizi wa Katumba linafanana na tatizo la Wakimbizi wa Ulyankulu na kwa kuwa hawakufanya uchaguzi wa Madiwani. Je, Serikali inasema nini, ni lini utafanyika uchaguzi wa Madiwani katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hao ni wananchi wake, akiwa Mbunge wa Viti Maalum ana kila sababu ya kuona maeneo hayo yanafanyika uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka swali hili nilijibu katika Mkutano wetu wa Bunge uliopita, nilisema pale kuna takribani Kata tatu uchaguzi haujafanyika kwa sababu za msingi, bado suala zima la utengamano linaendelea na pale sasa hivi bado Jeshi na Wizara ya Mambo ya Ndani wanaendelea kumiliki eneo lile. Utararibu utakapokamilika jukumu letu kubwa watu wa TAMISEMI baada ya ule mtangamano kuwa vizuri zaidi na eneo lile sasa rasmi likishakuwa chini ya TAMISEMI, mchakato wa uchaguzi sasa utaendelea ili watu wa pale wajikute nao wana Serikali yao halali iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Namba 292
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkoa wa Tabora Wilaya mbili hazina Hospitali za Wilaya, Sikonge na Tabora Manispaa na viwanja tayari vipo, je, Serikali inasema nini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la la Mheshimiwa Mwanne Mchemba, ambaye wakati tumefanya ziara kwenda Kilolo yeye ndio alikuwa Mwenyekiti wa Kamati na akashuhudia kazi njema ambayo inafanywa na Serikali, Hospitali ya Wilaya ya Kilolo itakuwa miongoni mwa hospitali za kutilia mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika swali lake anasema Serikali inasema nini kuhusiana na Wilaya mbili za Sikonge na Tabora Mjini ambazo hazina Hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya mwanzo, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hakuna hospitali za wilaya zinajengwa ili kupunguza mlundikano wa wagonjwa kwenda katika Hospitali za Rufaa ili wale ambao wanaweza kutibiwa katika Hospitali za Wilaya waweze kutibiwa. Naomba niiombe Halmashauri, ni vizuri na wao wakaonesha kwamba ni hitaji la wananchi kwa hiyo na wao katika vyanzo vyao vya mapato waanze pia ujenzi ili na Serikali Kuu tuweze kushirikiana nao.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa uanzishwaji wilaya ni wa muda mrefu na hili swali sasa ni la mara nyingi tunauliza; kwa kuwa Ulyankulu ilikuwa na makazi ya wakimbizi, na ambao wapo mpaka sasa, na kwamba vile vile wapo wakimbizi ambao wamepewa uraia na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu na kuwa na watu wengi.
Je, Serikali haioni hilo? je, ni lini sasa inaweza ikaamua kwa maksudi kuhakikisha kwamba wilaya ile sasa inakuwepo baada ya kukamilisha vigezo vyote tulivyovileta. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pale awali, mapendekezo ya kwanza yalivyokuja ikaonekana kuna mapungufu ya idadi ya watu, hii ndiyo iliyokuwa miongoni mwa vigezo ambavyo vilifanya isi-qualify kipindi kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amekiri hapa kwamba kuna baadhi ya makazi ya wakimbizi, nadhani takriban kata tatu, zimesababisha kuwepo kwa sasa idadi kubwa sana ya watu katika maeneo hayo ambayo sasa wamesajiliwa kuwa kama raia wa Tanzania. Hata hivyo utaratibu ni ule ule kwa sababu lile jambo la mwanzo lilidondoka haliku--qualify. Kwamba kama tunaona idadi sasa hivi inatosha twende na michakato ile ile kama nilivyosema awali, kwamba ipitishwe katika vikao vya kisheria ambavyo katika Ward C, DCC pamoja na RCC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikifika kwetu sisi, tutawatuma wataalam kuja kufanya verification, iki-qualify biashara imekwisha. Kwa hiyo mama Mwanne Mchemba naomba nikutoe shaka katika hilo, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itasikiliza jambo hili na kwa kupitia document zote zilizotumwa kutoka kwenu tutalifanyia kazi jambo hili. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kituo cha afya cha Manonga kimekamilika na kwa kuwa mpaka sasa vifaa havijapelekwa. Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri watapeleka vifaa hivyo kwa ajili ya wodi ya upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo cha afya cha Manonga kimekamilika na nakumbuka vituo vile vilikuwa ni miongozi mwa vituo ambavyo tumetengeneza kwa African Developmnet Bank na vituo vile tulitengeneza pale Bukene katika Mkoa wake, hali kadhalika hapa Itogo, lakini bahati mbaya Manonga vifaa vilikuwa havijafika, hata kwa ndugu yangu Mheshimiwa Cecil Mwambe pale kulikuwa na kazi tumefanya katika kituo cha Chiwale, vinafanana katika kesi kama hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manonga kulikuwa na kesi maalum kwamba vifaa havikufika na kwa sababu jambo lile lilikuwa na bajeti yake maalum, naomba niseme kwamba tunalichukua na tutalifanyia kazi kwa haraka sana kwa sababu bajeti yake ilikuwepo ili vifaa vile viweze kufika, wananchi wa Manonga waweze kupata huduma kama ilivyokusudiwa katika mradi ule.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, mradi huu umeleta mabadiliko makubwa sana hapa nchini hususan Tabora; na kwa kuwa fedha zinazotolewa ni kwa awamu na kidogo kidogo. Je, Serikali iko tayari sasa kupeleka fedha hizo vijijini ambako tayari wananchi wana uelewa wa kutumia masoko hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, mantiki hasa ya mradi huu ni kwenda kusaidia katika miundombinu ya masoko na barabara hasa katika maeneo ya vijijini. Lengo kubwa hapa ni kusaidia katika kuongeza thamani ya kile ambacho kinafanywa na wakulima. Kwa hiyo, nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba upelekaji wa fedha katika miradi hii unategemeana pia na vigezo ambavyo vimewekwa kwa kila Halmashauri kuweza kuvifikia. Kwa hiyo, tumeendelea kufanya hivyo na tayari mradi huu kama nilivyosema hapo awali umekwishatoa fedha nyingi sana kwa ajili ya huduma hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo mengine, wale ambao wamekidhi vigezo, fedha hizi zimekuwa zinatoka kwa wakati kwa ajili ya kwenda kusaidia huduma hizi zipatikane kiurahisi. Nimwondoe hofu kwamba fedha hizi zinafika na zinakwenda kwa wakati katika kusaidia malengo yaliyokusudiwa.
MHE. MWANNE J. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora walisumbuliwa sana katika suala la ununuzi wa bei ya tumbaku. Je, Serikali imejipangaje kuhusu suala la ununuzi wa tumbaku kwa bei nzuri ili isijirudie kama ilivyokuwa mwaka 2007?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi kwa upande wa zao la tumbaku tuna wanunuzi wakuu wanne. Hata hivyo kama Serikali tumejipanga kutafuta masoko mengine nje ya nchi, tumeweza kuongea na nchi ya Vietnam, China na Singapore; na naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako tukufu kwamba mpaka sasa hivi nchi ya Singapore tumeweza kufanikiwa na watanunua tani 1,000 kwa msimu huu. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kuuliza swali dogo. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini kwa kuwa huu sio mchango ni maswali ya nyongeza mimi naomba niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa TASAF inafanya kazi nzuri sana hapa nchini na kwa kuwa TASAF imefanya kazi maeneo mengi sana hapa nchini kama vile upande wa afya, elimu sasa hivi TASAF inasimamia wanafunzi kwenda shuleni ambao zamani walikuwa hawaendi kutokana na kupunguza umaskini. Lakini nimesema hivi kwa uchungu kwa sababu gani TASAF kazi inayofanya haichagui vyama, haina mpango wa vyama tumeshuhudia Pemba, tumeshuhudia Unguja na tumeshughulikia na hapa Tanzania vyama vyote sichangii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize swali kwa kuwa TASAF inafanya kazi nzuri, je, Serikali ipo tayari kuwaongezea fedha ili wakidhi haja zote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kumshukuru Mheshimiwa Mchemba kwa pongezi alizolitoa kwa TASAF na sisi tutaendelea kuchapa kazi zaidi, lakini kuhusu swali lake kwamba je, TASAF iko tayari kuwaongezea fedha? Nataka niseme kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya TASAF ni ya kuwafikia walengwa wote wanaohitaji kusaidiwa, mpaka sasa tumefikia walengwa asilimia sabini ndio maana kuna vijiji TASAF haijafika, kuna vijiji TASAF imefika lakini hatujawapata walengwa wote, huu mpango wa TASAF uko sehemu “A” na “B”. sehemu a ndio hii tunayoitekeleza sasa, TASAF ya Awamu ya Tatu “B” malengo ya Serikali ni kuwafikia walengwa wote, na ili kuwafikia walengwa wote ni dhahiri lazima tuongeze fedha.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, Serikali imekiri kutokuwa na nyumba ya mahabusu au kutokuwa na mahabusu ya wanawake katika Wilaya ya Igunga na kuwasababishia ndugu kutokuwasalimia na kutokujua afya zao kwa hao mahabusu ambao ni wanawake na kuwanyima haki zote.
Je, Serikali iko tayari kujenga mahabusu maalum ya wanawake kama dharura ili kuwaondolea adhabu wanayoipata wanawake na usumbufu wa kutoka Igunga kwenda Nzega mara kwa mara? Naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nilizungumza wakati najibu swali la msingi kwamba ujenzi wa gereza hili ambao ulianza mwaka 2003 haujakamilika na nilisema kwamba utakapokuwa umekamilika basi changamoto ya mahabusu kwa wanawake itakuwa imepatiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge astahamili wakati ambapo tunajiandaa kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga gereza hili ili tuweze kupata ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kuna jitihada ambazo tumeweza kuchukua katika baadhi ya maeneo mengine nchini ambapo tumeweza kutumia rasilimali za maeneo husika pamoja na wafungwa na nguvu na ushirikiano wa wananchi pamoja na Wabunge wa maeneo husika kuhamasisha katika ujenzi wa mabweni. Naomba nichukue fursa hii kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara rasmi katika gereza hili ili tushirikiane pamona na Mbunge wa Jimbo hilo kuona jinsi gani tunaweza tukafanya kutafuta njia za hatua za dharura kuweza kukabiliana na changamoto hii wakati tukisubiri fedha za bajeti za ujenzi wa gereza hili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Tabora Manispaa haina Hospitali ya Wilaya, je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kukosekana kwa Hospitali ya Wilaya na hata kwenye bajeti hii haikuwekewa, je, nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, utakabaliana na mimi kwamba swali hili linaulizwa kwa mara ya tatu kama si mara ya nne, kuhusiana na suala zima la uwepo wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora ili Hospitali ya Mkoa ya Kitete iweze kupata pahali pa kupumulia. Kama ambavyo imekuwa nikijibu ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba ili Hospitali ya Wilaya ambayo imeshaanza kujengwa, iendelee kujengwa. Ni suala tu la kibajeti, hali ikiruhusu hatuwezi kuacha kujenga Hospitali ya Wilaya ndani ya Manispaa ya Tabora ili Hospitali ya Kitete iweze kupumua.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa gereza la Uyui Mkoa wa Tabora ni kongwe linafanana na gereza la Mng’aro. Kawaida ya gereza lile lilitakiwa kuchukua wafungwa 1,360 lakini mpaka ninavyosema hivi sasa lina wafungwa 1,860. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua gereza au kuwapunguza wafungwa waende sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la msongamano wa wafungwa ni suala pana na niseme bora nizungumze kwanza kwa ujumla wake kabla sijaenda specifically kwenye gereza la Uyui kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza, maana yake naona masuala yote yanaingiliana katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imsingi suala hili nimekuwa nikilijbu mara kadhaa katika kipindi cha nyuma kwamba tunaweza tukatatua tatizo la msongamano wa wafungwa kama ambavyo Serikali tunavyofanya kwa kufanya mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, tunapanga bajeti ya kuongeza mabweni yetu na kazi hiyo inaendelea kadri ya hali ya uwezo wa kibajeti utaporuhusu. Katika kipindi cha miaka mitano tumefanya hivyo katika magereza, nadhani takribani mawili kama sikosei.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunatumia sheri zetu zile tatu ama nne, Sheria ile ya Parole, Sheria ile ya Community Services pamoja na kutumia vile vile mamlaka ya kikatiba ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo haya ni mambo ambayo tunayafanya kimsingi kupunguza msongamano wa wafungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba tunafanya kila linalowezekana kupitia vyombo vingine vya dola kusimamia sheria. Ndiyo maana jeshi letu la polisi sasa hivi linafanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuepukana kufanya makosa ambayo yanaweza kuepukika ili kuweza kupunguza msongamano katika magereza yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, specifically kuhusiana na kwenye gereza la Uyui, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo nimezungumza kwenye majibu yangu mengine haya mawili utaratibu ndio huo huo tu, aidha bajeti ya Serikali au utaratibu wa kuweza kutumia rasilimali za eneo husika kuweza kufanya marekebisho madogo madogo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya kutoka Puge – Ndala – Nkinga – Ziba inapita kwenye hospitali kubwa sana za Mission, je, ni lini sasa hizo barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, hii barabara tumeizungumza mara nyingi sana ili tuweze kuiweka kwenye usanifu. Nami nitumie nafasi hii kumkumbusha tu kwa sababu niliongea na Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Tabora kwamba kipande hiki cha barabara ni muhimu na anawatambua kwamba wananchi wengi wanakwenda Nkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni muhimu sana kwa barabara kuja Ziba kwa sababu wananchi pia wanatoka maeneo ya Tabora wengine wanakuja Nkinga kutokea Ziba. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tutaiweka kwenye mpango ili barabara iweze kutengenezwa na pia iweze kuongeza huduma muhimu katika maeneo haya.
MHE. MWANNE I. NCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa station hizo zina Vituo vya Polisi na kwa kuwa kwa muda mrefu sana Vituo hivyo vya Polisi havija pata msaada wa kukarabatiwa, pamoja na nyumba zao ni chakavu, mbovu, hazifai. Je Serikali iko tayari sasa kutenga fedha rasmi kwa ajili ya ukarabati wa Vituo hivyo vya Polisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye program ambayo imewekwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na ukarabati wa station watakarabati na Vituo vya Polisi ambavyo vipo kwenye station mbalimbali. Kwa hiyo tunamwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati mchakato huo utakapoanza hivi karibuni hivyo vituo navyo vitakarabatiwa.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aomba niiulize Serikali, kwa kuwa Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora hakifanyi kazi; na kwa kuwa mpaka sasa kimeiondolea Tabora kupata mapato ya uhakika na vijana kupata ajira: Je, Serikali iko tayari sasa kukinyang’anya na kukirejesha kiwanda hicho Serikalini? Hakifai kabisa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kimsingi Kiwanda hicho kimezungumzwa siku nyingi na mmekuwa mkikifuatilia. Niseme tu kwamba kabla ya kukirejesha kiwanda Serikalini, hatua ya kwanza ni sisi kukitembelea na kujiridhisha, kwa nini hakiwezi kufanya kazi zake inavyopaswa, ikizingatiwa kwamba Tanzania ni nchi ambayo inalima pamba kwa wingi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapomaliza Bunge, nitatembelea kiwanda hicho ili kujiridhisha na niweze kutoa ushauri Serikalini juu ya utekelezaji utakaofuata. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya ukarabati katika shule za sekondari yanafanana na shule za msingi, Mkoa wa Tabora katika Manispaa ya Tabora, Shule ya Kanyenye iliezuliwa karibuni madarasa manne tangu mwaka 2018 Machi, mpaka leo haijafanyiwa ukarabati, wanafunzi wanapata taabu. Nini kauli ya Serikali kwa leo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nipokee maombi na maelekezo ya Mheshimiwa Mbunge tutayafanyia kazi. Mpaka Bunge lijalo tutakuwa tumepata majibu ya tatizo hili katika eneo la Tabora. Ahsante.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo yanaridhisha na yanakidhi swali langu, naomba niulize maswali mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mpaka sasa Bodi ya TAWA haijakabidhiwa rasmi uendeshaji wa shughuli hiyo ili waweze kutekeleza mipango waliyotarajia. Ni lini sasa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itawakabidhi TAWA ili waweze kufanya kazi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari tuongozane siku ya Jumamosi akaone hali halisi ambayo naizungumzia? Ahsante?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwanne Mchemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumpongeza kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa karibu sana kuimarishwa kwa bustani hii kama chanzo cha mapato cha Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza, naomba kumhakikishia kwamba taratibu za kukabidhiwa kwa TAWA zimekamilika na ndiyo maana mshauri mwelekezi amepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Tabora kwenda kuangalia bustani hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la dogo nyongeza. Kwa kuwa Serikali imetamka Vituo vya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na kadhalika, lakini Mkoa wa Tabora una historia kubwa, nilitegemea kwamba leo Mheshimiwa Waziri atatamka kwamba Tabora nayo iwemo katika orodha ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa. Nasema hivi kwa sababu uhuru na maelekezo mengine yote ya Baba wa Taifa yalitoka Mkoa wa Tabora, karata tatu zimetoka Mkoa wa Tabora. Baba Taifa ameacha historia kubwa katika Mkoa wa Tabora kwa kusoma na kadhalika.

Kwa hiyo, kwa kutokuweka orodha ya Kituo cha Tabora kukitambua rasmi kwa kweli hawautendei haki Mkoa wa Tabora. Je, ni lini sasa Serikali itaingiza katika orodha ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa kwenye vituo hivyo ambacho vimetamkwa hivi leo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Mwanne Nchemba, mama yangu kwa maswali ya nyongeza. Napenda nitumie fursa hii kumhakikishia kwamba kwa suala hili la uhifadhi wa Kumbukumbu za Mwalimu Nyerere kitu ambacho kama Wizara tunafanya, kwa sababu tulitaka tufanye katika mapana makubwa, tunayo sasa hivi Programu yetu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.

Kwa hiyo, kupitia hiyo pragram Mkoa wa Tabora ni mkoa mmojawapo kati ya mikoa 15 ambayo imeteuliwa na Wizara ili kuweza kuyabaini yale maeneo maalum ambayo yallitumika katika ukombozi wa Bara la Afrika. Kwa hiyo Mkoa wa Tabora upo, lakini ni katika ile Program kubwa ya Ukombozi wa Bara la Afrika. Ahsante.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa barabara za lami, Mkoa wa Tabora sasa hivi tuna matatizo makubwa ya mafuriko. Mafuriko ni makubwa, naomba Serikali itambue kwamba Tabora nayo ni miongoni mwa mikoa yenye mafuriko.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Tabora Manispaa, Kata ya Ipuli ambayo tunaitwa Freemason au Chuo cha Utalii pamoja na Malolo wananchi mpaka sasa wako nje, wanateseka kutokana na kutokuwa na miundombinu ya mifereji inayopitisha maji mengi. Mifereji iliyopo ni midogo mno, nimeomba univumilie kwa sababu hali tuliyonayo sasa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora hususan Manispaa wana matatizo makubwa.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Naibu Waziri aende Tabora akutane na Wahandisi wa TANROADS pamoja na TARURA ili watafute njia gani mbadala ya kuwasaidia wakazi wa maeneo hayo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanne Mchemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimwa Mbunge maeneo mengi tumepata adha ya hizi mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha. Nitumie nafasi hii nimpe pole Mheshimiwa Mbunge lakini pia niwape pole wananchi wa Tabora Mjini. Natambua maeneo haya uliyoyazungumza ya Ipuli na Malolo kuna shida na nakubaliana na ushauri wako.

Tunaendelea kufanya uratibu wa maeneo yote nchini kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kama nilivyozungumza hivi karibuni wakati nikijibu swali la Korogwe Mjini tuwe na ushirikiano kama Mbunge unavyosema wenzetu wa TARURA na TANROADS na upande wa Mipango Miji tushirikiane ili miji yetu hii inayokua kwa kasi lazima tuje na mipango mizuri ya kudhibiti maji ya mvua hususan tunapopata mvua nyingi namna hiyo. Kwa hiyo, nakubaliana na ushauri wako nitakwenda Tabora kufanya hivyo kama ulivyoshauri.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa jengo la ICU muhimu sana na kwa kuwa mradi ule mpaka sasa hauna fedha na Serikali imesema itatenga fedha mwaka huu wa fedha, je, Serikali iko tayari kupeleka angalau hizo milioni 200 za dharura?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa idadi ya watumishi ni ndogo sana hususan kitengo cha nursing, je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuongeza angalau watumishi sita katika Hospitali ya Wilaya?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na maswali hayo, nipongeze sana majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanne Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tabora, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali, naomba tupokee pongezi ambazo Mheshimiwa amezitoa. Kipekee naomba na mimi nimpongeze kwa jinsi ambavyo amekuwa akipigania kuhakikisha afya na hasa ya akina mama inaboreshwa katika Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza anaomba walau Serikali itoe jumla ya shilingi milioni 200 za dharura. Hata hivyo, katika majibu ya msingi na swali la msingi kinachoombwa ili kumalizia majengo yote mawili ni jumla ya shilingi milioni 200. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali, tumeahidi kwamba katika bajeti ya 2020/2021 tunaenda kutekeleza na hii inatokana na baadhi ya maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika Hospitali ya Urambo ambapo sasa hivi hata makusanyo yanayokusanywa pale ni mengi. Naomba Mheshimiwa aendelee kuiamini Serikali, tutatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaomba kuongeza idadi ya watumishi walau sita. Juzi Waziri mwenye dhamana amejibu akieleza namna ambavyo Serikali inaenda kutoa jira zisizopungua 45,000. Katika watumishi watakaoajiriwa upande wa afya, hakika nimhakikishie Mbunge na Tabora kwa ujumla wake hatutaisahau. (Makofi)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuhakikisha kwamba usalama wa barabarani unasimamia mazingira yote. Kwa kuwa usalama barabarani wanafanya kazi kubwa na kwa kuwa waendesha bodaboda kwa sasa pamoja na kupunguza ajali, wapo wanaovunja sheria na baada ya kuvunja sheria wao pia wanakuwa vyanzo vya watu kupata ulemavu: Je, Serikali inatoa adhabu gani kali kwa hao ambao wanavunja sheria?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha inasajili bodaboda zote hapa nchini ili kupunguza uhalifu na kupunguza ajali pale inapotokea wale wenye bodaboda wanapokimbia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, aina ya adhabu zipo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani lakini inategemea pia aina ya kosa la mhusika. Hata hivyo nikiri kwamba inawezekana adhabu hizo sasa hivi zikawa zimepitwa na wakati, ndiyo maana tupo katika hatua za mwisho za mchakato wa marekebisho makubwa ya Sheria za Usalama Barabarani. Ni imani yetu kwamba sheria hiyo itakapokamilika, inaweza ikasaidia sasa kuweka adhabu ambazo zitawabana zaidi wavunjifu wa sheria za usalama barabarani hususan waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la usajili, nimhakikishie kwamba tupo katika hatua za kuanza mchakato huo tukiamini kwamba utaratibu huo utasaidia sana katika kupunguza malalamiko ya baadhi ya waendesha bodaboda ya uonevu wanaofanyiwa dhidi ya baadhi ya Askari wetu, lakini pia itasaidia sana kuweza kuwadhibiti na kuwakamata pale ambapo wanafanya makosa hayo kwa urahisi na uvunjifu wa Sheria za Usalama Barabarani kwa wanaotumia bodaboda.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mafupi ya nyongeza. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo inafanywa kwa ajili ya mambo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa kuwa alipokuwepo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, alikuwa ameandaa na alishawatayarisha wawekezaji kutoka nchini China ambao walikuwa tayari kuwekeza katika Kiwanda cha Tumbaku, kwa bahati mbaya waliishia Dar es Salaam na kulikuwa na matatizo ya Uhamiaji: Je, Waziri yuko tayari sasa kuwafuatilia hawa wawekezaji wa Kichina ambao walikuwa tayari kabisa na maeneo yalitengwa ili waweze kuja kuwekeza kwenye zao la tumbaku?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, amefanya jitihada kubwa na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwa kuboresha maeneo katika mkoa mzima na Wilaya zote: Sasa je, Waziri yupo tayari sasa kuwaleta wataalamu rasmi ili kuweza kuainisha hayo maeneo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tunashukuru kwa pongezi na nikuhakikishie tutaendelea kufanya kazi nawe pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine pamoja na mikoa yetu katika kuhakikisha kwamba tunachochea na kuvutia uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kweli nimefahamishwa kwamba alikuwepo mwekezaji kutoka China ambaye alikuwa na nia ya kuwekeza Kiwanda cha Tumbaku Tabora. Mpaka sasa tumeendelea kumfuatilia, lakini bado hajaonyesha nia.

Napenda kusema kwamba tutaendelea kumhamasisha yeye zaidi na kutafuta wawekezaji wengine zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Viwanda pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili katika swali lake la pili kuhusiana kuleta wataalam, kwanza napenda kuwapongeza Mkoa wa Tabora kwa kutenga ardhi hiyo ya zaidi ya ekari 42, lakini kipekee napenda kusema tu kwamba ni takribani asilimia tano ndiyo tayari inakidhi vigezo. Imewekwa ardhi kubwa, mfano ukiangalia Kaliuwa, wana zaidi ya ekari 37,201, lakini ni asilimia tano tu ya Mkoa mzima wa Tabora katika maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa, ndiyo ambayo tayari yalimewekewa miundombinu wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi pamoja na Mkoa husika wa Tabora kwanza kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanawekewa miundombinu wezeshi lakini pia kuhakikisha Halmashauri nazo zinaendelea kutenga fedha ili miundombinu iweze kutengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza sana kipekee Halmashauri ya Nzega ambao tayari kwenye bajeti yao wameweka zaidi ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya suala zima ya upimaji. Kwa hiyo, natoa rai kwa Halmashauri nyingine saba zilizobakia na nyingine nchini, basi wajitahidi kutenga fedha katika bajeti yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala zima la kuleta wataalam, nimhakikishie kwamba tuko tayari kuleta wataalamu, lakini zaidi niwapongeze Halmashauri zile nane, kila moja imekuja na mradi wake wa kimkakati; wako ambao wana mradi wa machinjio, wako ambao wana mradi wa mashamba ya mifugo, kuweka kiwanda cha usindikaji na utengenezaji wa vyakula vya mifugo pamoja na sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza mikoa yote na Halmashauri zote ambazo tayari wameweza kubuni miradi ya mikakati. Nawaomba waendelee kufuatilia, washirikiane na Wizara ya Kilimo pamoja na Benki yatu ya Kilimo na benki nyingine za kimaendeleo ili kuweza kupata mitaji ya kuweza kuwekeza. Nakushukuru.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Tabora kuna karakana kubwa ambayo ipo tangu wakati wa mkoloni na kwa kuwa sasa kuna ujenzi wa standard gauge. Je, Serikali iko tayari sasa kuboresha karakana hiyo kupeleka mitambo ya kisasa ili iendane na treni hiyo ambayo ni ya kisasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunayo karakana kubwa kabisa ya matengenezo ya vichwa vya treni maeneo ya Tabora na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia TRC bado ina mpango wa kuendelea kuirekebisha karakana ile na tunamhakikishia kwamba tutaongeza vifaa na iko kwenye mpango ambao tunakwenda kuutekeleza kuanzia mwakani mwezi wa pili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya Puge - Ziba - Manonga hufanyiwa matengenezo mara kwa mara na kutoa gharama kubwa sana ya matengenezo hayo, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kujenga barabara hii kwa awamu kama ifuatavyo; kujenga kutoka Puge - Ziba - Manonga kwa kiwango cha lami angalau ianzie Ndala mpaka Ziba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanne Mchemba kwa sababu barabara hii ameifuatilia sana na imezaa matunda kwa kweli kwa sababu maeneo yote korofi tunafanya matengenezo makubwa ikiwepo ujenzi wa daraja kubwa kabisa katika Mto Manonga. Nia ya Serikali ni kuboresha maeneo haya. Kwa sasa Serikali ilikuwa inaendelea kuunganisha mikoa na Mkoa wa Tabora umeunganishwa na mikoa mingine kwa maana ya Tabora kwenda Shinyanga kuja Singida. Uvute subira tu kidogo tumeiweka kwneye mpango barabara hii na sasa eneo hili unalolisema la kutoka Ndala kwenda Ziba ni eneo muhimu ambao linapita kwenye Hospitali ya Nkinga, tutaliangalia ili tukipata fedha tuanze na eneo hili ambalo pia lina shughuli nyingi za kiuchumi. Ahsante sana.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo inafanya kukamilisha Vituo vya Afya ambavyo mimi mwenyewe kama Mjumbe wa Kamati hiyo nimejionea kwa macho yangu mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu sasa, kwa kuwa Kituo cha Afya Simbo kimekamilika na bado hakijaanza kazi, je, ni lini sasa hivyo vifaa tiba vitapelekwa haraka sana ili kuwapunguzia adha wagonjwa ambao wanakimbilia kwenda Hospitali ya Private ya Nkinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchemba, Makamu Mwenyekiti wa Kamati yetu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nipokee pongezi kwa niaba ya Wizara na yeye mwenyewe amekuwa shuhuda amejionea kwa macho yake, lakini katika swali lake anauliza lini Kituo cha Afya hicho ambacho kimeshakamilika kitaanza kutoa huduma kama ambavyo Serikali imekusudia. Naomba nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge tayari fedha tumeshalipa MSD na vifaa vinanunuliwa moja kwa moja kutoka mtengenezaji, kwa hiyo wakati wowote vifaa vikishakamilika, lakini pia kumekuwa na changamoto ya Wataalam wa kutoa tiba kwa ajili ya usingizi anesthesia, tayari wamepelekwa Bugando mmoja na mwingine amepelekwa Muhimbili ili vifaa vitakapofika na wataalam waweze kutoa huduma ili wananchi wasihangaike kutembea umbali mrefu. (Makofi)